Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Vicky Paschal Kamata (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa ninamshukuru Mungu kwa afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nianze kwa kusema kwamba ninaunga hoja hii mkono kwa asilimia mia moja lakini pia ninampongeza sana Profesa Muhongo kwa kurudi tena katika Wizara hii. Imani kubwa aliyokuonyesha Mheshimiwa Rais John Joseph Pombe Magufuli, ni imani kubwa ambayo Watanzania wengi tulioko huko nje pia tunayo kwako pamoja na Naibu wako Dkt. Kalemani. Tuna imani kubwa sana, kwamba kazi itafanyika na matokeo yataonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza na narudia tena kusema kwamba Rais amekuamini Profesa Muhongo, amekurudisha kwa sababu anakujua. Tunataka kwenda kwenye uchumi wa kati ambao unategemea viwanda. Mheshimiwa Mwijage, Profesa Mkenda pamoja na Dkt. Meru hawana muujiza wowote ule watakaoweza kuufanya ili Tanzania iwe kweli ya viwanda iwapo ninyi hamtafanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba umeme wa uhakika unapatikana ili kuwezesha Tanzania ya viwanda iweze kufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi na Kamati yangu tulienda Arusha, tulitembelea Kiwanda cha kutengeneza transfoma, TANELEC. Kiwanda kile kinafanya kazi nzuri sana, kinatengeneza transfoma zenye obora mkubwa sana. Transfoma zile zinanunuliwa Kenya, Uganda na nchi nyingine lakini sio Tanzania, kwa maana ya kwamba TANESCO hainunui zile transfoma zenye ubora mkubwa. Wananunua transfoma kutoka India, zinakuja hapa zinafika kwa gharama kubwa pengine kuzidi hizi za hapa kwetu na bado hazina ubora wa kutosha, zinalipuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajumbe wengi wameeleza kwamba kwenye maeneo yao yametokea matukio ya hatari sana kwa sababu zile transfoma zimekuwa zikilipuka, wanashindwa kununua transfoma kutoka TANELEC. Kamati yangu ilipata uchungu sana baada ya kujionea kazi nzuri ya kiwanda kile, lakini kuna malalamiko na changamoto kubwa wanazokutana nazo. Kamati ilipata uchungu na ilipata hasira sana. Ninaamini kama kamati yangu ingekuwa na mamlaka, ingekuwa na uwezo siku ile ile tungeweza kutumbua majipu fulani fulani.
Lakini tulijiuliza, kama tunaweza kumtumbua Mkurugenzi wa TANESCO tukamuita jipu, tutakuwa tunamuonea kwa sababu tatizo sio Mkurugenzi wa TANESCO, tatizo si Idara ya Manunuzi, tatizo ni Sheria ya Manunuzi. Sasa kama tunazo sheria ambazo zinakuwa kikwazo, sheria ambazo hazitusaidii, tunataka kukimbia sheria zinatufunga miguu tushindwe kwenda tunakoenda, kwa nini hizo sheria zisiletwe haraka tuzifanyie marekebisho ndani ya Bunge hili? Tuifanyie marekebisho hiyo Sheria ya Manunuzi kusudi tuweze kufanya kazi vizuri kwasababu hii Sheria ya Manunuzi imekuwa kichaka, tutakuwa tunawaonea watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikasirika sana siku ile na Mkurugenzi wa TANESCO tukasema kwanza yeye ni Mjumbe wa Bodi inawezekanaje wanunue transformer India zenye ubora mbovu? Lakini tunakuja kujua kumbe si yeye, tatizo ni sheria yetu ambayo tuliipitisha wenyewe humu. Sasa tulete hiyo sheria haraka sana ifanyiwe marekebisho kusudi tuweze kufanya kazi vizuri na TANELEC iweze kuuza transfoma zake hapa hapa Tanzania; na kiwanda chetu kama kweli tunataka Tanzania iwe ya viwanda basi tuanze na viwanda vilivyomo humu kuvipa uwezo wa kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ningependa nizungumzie wachimbaji wadogo wa Geita. Mheshimiwa Profesa Muhongo na kaka yangu Dkt. Kalemani; tena Dkt. Kalemani unaona kabisa hali halisi ya watu wako wa Geita maana wewe unatoka Geita, wewe ni Mbunge wa Chato. Maisha ya wananchi wa Geita ni magumu na Serikali imekuwa ikiahidi kila siku kwamba itawapa maeneo ya kuchimba lakini sielewi tatizo ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Muhongo ulianza vizuri sana kipindi kile, uliwapa matumaini makubwa sana wananchi wa Geita hususani hawa watu ambao wanachimba, walijiunga kwenye vikundi vya SACCOSS mpaka leo vikundi vinakufa kwa sababu hakuna maeneo ya kuchimba. Naamini pale ulipoishia kipindi kile baada ya matatizo yale kutokea, umerudi tena, ni kwa mpango wa Mungu na kwa makusudi mazuri na nia njema ya Rais kwamba uwasaidie wachimbaji wadogo wadogo wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa taarifa nilizonazo, lile eneo la STAMICO lina-expire Julai, 2016 yaani mwaka huu, tuna mwezi mmoja tu lile eneo lina-expire. Huoni umuhimu Mheshimiwa Waziri wa kuwapatia sasa wananchi hilo eneo la STAMICO ili waweze kugawana SACCOSS zile ziweze kuanza kufanya kazi? Wananchi wa Geita wanategemea uchimbaji, sasa hawafanyi kazi matokeo yake watu wanaanza kufanya vitendo vya uhalifu kwa sababu hawana kazi za kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninaomba sana kupitia bajeti, nina uhakika bajeti hii itapita kwa sababu ni nzuri na tena kama ulivyosema asilimia 94 ni kwa ajili ya maendeleo, kwahiyo ninaamini kabisa Geita itapewa kipaumbele.
Mheshimiwa Muhongo juzi umeenda umekutana na Watanzania wanaoishi Geita, umewapa matumaini na umerudisha imani kubwa, wana imani na wewe na mimi Mbunge wao nasema waendelee kuwa na imani na wewe kwa sababu wewe ni mnyoofu, ni muadilifu na ahadi zako hazipindi pindi. Nina uhakika safari hii maeneo ya wachimbaji wadogo yatapatikana, tukianza na hilo linalo-expire mwezi Julai.
Lakini vilevile Mheshimiwa Muhongo unauwezo wa kwenda kuzungumza na GGM. GGM wamehodhi maeneo makubwa sana. Kuna lile eneo la Nyamasagata, kuna la Semina, kwanini usiongee na GGM wakawagawia haya maeneo, wakawaruhusu basi hata wakachimba kwa sababu wenzetu wa Ghana wamewezaje wachimbaji wadogo na wakubwa kuogelea kwenye bwawa moja bila kuleta madhara yoyote? Ni utaratibu tu uwekwe, hawa wachimbaji wadogo wachimbe na hawa wakubwa pia wachimbe, hawa wadogo kwanza wanachimba kwanza hawana vifaa vikubwa kwa hiyo hawawezi wakachukua dhahabu nyingi ya hawa wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itawasaidia tu kuweza kuendesha maisha yao ya kawaida na kelele pia zitakwisha. Nikuombe Profesa Muhongo na Naibu wako, Katibu Mkuu; sisi tuna imani kubwa sana na ninyi, kwa hiyo ninaamini kabisa, mara baada ya hii bajeti kupita, utafika Geita, utawasaidia wachimbaji wadogo, SACCOSS zitaanza kufanya kazi na Geita itafanana kwamba huu kweli ni mji wa dhahabu maana maisha wanayoishi Watanzania pale kwa kweli hayaridhishi hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijagongewa Kengele pia nipongeze na mimi kidogo umeme wa REA. Kwa kweli kwa Mkoa wetu wa Geita mmejitahidi, tunakwenda vizuri, lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo nguzo zimepita muda mrefu sana na mpaka sasa imefikia mahali wananchi wanaanza kupata hasira wanataka kukata zile nyaya kwamba kwa nini umeme umepita umeenda maeneo mengine na sisi tumerukwa, na sisi tuko kwenye kata ambayo ni makao makuu ya kata? Kuna vituo vya afya pale, kuna sekondari pale, kuna shughuli nyingi za maendeleo ziko pale lakini umeme umepita juu. Juzi juzi nilikuwa naongea na Diwani wa Nyaruyeye, kaniambia kweli nimekuwa na kazi kubwa ya kuzuia watu kwenda kuangusha zile nguzo kwa sababu zimepita hapa muda mrefu na sisi hatuna umeme.
Kwa hiyo, ninaamini kabisa baada ya bajeti hii kupita, maeneo ya Nyaruyeye, Nyarugusu na mengineyo yote ambayo bado hayajapatiwa umeme lakini nguzo zimepita basi ule umeme ushuke ili watu wote tuweze kunufaika na huo umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo machache, narudia tena kupongeza Wizara hii na kuwatakia kila la heri, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Nami nianze kwa kuunga hoja mkono na kumpongeza sana Waziri na Naibu Waziri kwa hotuba yao nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hifadhi zetu kuna madini mengi sana na ili Mtanzania aweze kuyachimba lazima apate kibali kutoka kwa Wakala wa Misitu. Akishakipata kile kibali anatakiwa kulipia ada milioni moja kwa mwaka na kama ana hekta kumi ina maana atalipa milioni kumi. Vilevile anatakiwa kulipia leseni 800,000 kila mwaka. Wakati huo huo anatakiwa kulipa asilimia nne kama loyality.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maombi ya wachimbaji wadogo wa Geita wamenituma nimweleze Waziri kwamba wanaomba sana kwamba hili haliwasaidii wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu ada ile ni kubwa, lakini pia wanachangia maendeleo siyo kitu kibaya, kwa kuwa wanachangia maendeleo basi wafikiriwe kupunguziwa. Hilo ni ombi maalum kutoka kwa wachimbaji wadogo wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumzie kidogo hili jambo ambalo limezungumziwa sana na Wabunge wenzangu linalohusu wafugaji. Mimi pia ni mfugaji na nimetoka sehemu ya wafugaji. Naungana mkono na wale wenzangu wanaosema kweli kuna umuhimu wa kuwashawishi wafugaji wetu kuona kama inawezekana wakapunguza hii mifugo ambayo pengine imekuwa mingi kama ambavyo mnasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini natofautiana na wenzangu kwa namna wanayosema mifugo hii ipinguzwe. Isipunguzwe kwa kuwaumiza hawa wafugaji lakini ipunguzwe kwa kuwanufaisha, huo upunguzaji uwe na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kaka yangu Dotto aliongea na mimi nilipata uchungu sana. Inaumiza kuona mfugaji anauliwa mifugo yake ng‟ombe sitini, ishirini, thelathini, yaani hiyo ni torturing ya aina gani? Yaani jiweke tu kwenye viatu vya huyo mfugaji maumivu aliyoyapata, achilia mbali hasara kwamsababu mtu anapofuga kitu tayari anammapenzi nacho. Mimi ni mfugaji nina mbwa kama wanne nyumbani kwangu. Hivi juzi kuna mbwa mmoja, amekufa katika mazingira ambayo mimi sikuyaelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hao mbwa nilikuwa nampenda sana yule mbwa, amekufa sikuelewa amekufaje, mpaka hivi ninavyozungumza ameniuma na ni mbwa tu mmoja, hebu fikiria hawa ng‟ombe sitini ana maumivu kiasi gani? Yapo mengi ya kuwasaidia wafugaji wetu wakafuga katika hali nzuri na wakanufaika na mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri akae vizuri na Waziri wa Mifugo, wakae vizuri na Waziri wa Ardhi, wakae vizuri pia na Waziri wa Viwanda waje na Mkakati Maalum wa kuwasaidia hawa wafugaji ili wasije wakajiona kwamba kumbe kufuga katika nchi hii ya Tanzania ni mateso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa Serikali ikishirikiana na hawa wafugaji ambao wana mifugo mingi na wana pesa nyingi, wanaweza wakawasaidia hata wakaenda kujifunza kwa wenzetu Netherland wanafugaje! Ufugaji wao utakuwa ufugaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nilikuwa najaribu ku-google kidogo asubuhi, nijaribu kuona wenzetu walifanyaje. Netherland wanafuga na ufugaji wao una tija, sitaki kujilinganisha nao kwa sababu wenzetu wako mbali sana, lakini bado tunaweza tukajifunza kutoka kwao. Serikali ikawasaidia hawa wafugaji, ikachukua labda kila mkoa ambao una wafugaji wengi wakachukuliwa kumi au kumi na tano ama ishirini wakaenda kule Netherland wakaenda kujifunza, kuna teknolojia nzuri kabisa ambayo wakirudi nayo hawa wafugaji watakubali wenyewe kwa kusema kwamba tunapunguza mifugo na sisi tunafuga kisasa na ufugaji wetu uweze kuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanayo teknolojia nzuri sana ambayo siwezi kuizungumza hapa, nimejifunza mimi leo hii, lakini naamini Mheshimiwa Waziri akiifanyia kazi, akashirikiana na hawa wafugaji; kwanza wana pesa wanaweza hata wao wenyewe wakajilipia ndege na hoteli kule wakaenda kujifunza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile vijana wetu wanaosoma vyuo vikuu, wanaosomea mambo ya kilimo, tuwapeleke nje wakasome. Hili jambo hatuwezi tukaliondoa haraka sana bali taratibu, kama kweli tunataka ufugaji upungue, watu wasifuge ng‟ombe elfu thelathini, wasifuge ng‟ombe wengi kiasi hicho, tusiwakatili ghafla sasa kwamba mnaanza kufuga ng‟ombe watano, mwisho kumi, hapana. Taratibu, taratibu kwa kuanza na mind set zao, tuwaelimishe kwanza kwa kuwapa hiyo exposure, waende wakajifunze, warudi na vijana wetu wanaosoma pia watatusaidia kuhakikisha kwamba ufugaji wetu unakuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilivyosema Mheshimiwa Waziri akae na Wizara hizo kwa maana ya Wizara ya Ardhi, Wizara ya Viwanda bado naona kuna umuhimu wa kutengewa maeneo. Watengewe maeneo maalum ili waweze kulisha mifugo yao wakati tukiendelea huko kwenye teknolojia ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo kuhusu suala la utalii, nilipokuwa naangalia hiki kitabu ukurasa wa 15 nimeona jinsi ambavyo, (sintasoma) lakini nimeona jinsi ambavyo utalii umeweza kuchangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa, nawapongeza sana. Ninaamini bado kuna vitu vya ziada vya kufanya ili utalii huu uweze kutuletea pato kubwa sana kwenye Taifa letu na kukuza uchumi wa nchi yetu. Kwa mfano, tukiamua kumleta Jay Z na familia yake hapa, tukamleta David Beckham na Victoria Beckham hapa, tukakubaliana nao kabisa kwamba hiyo tour yao iwe broadcasted na vyombo vyote vikubwa vikaimulika Tanzania kwa siku zote watakazo kaa hapa, Serikali mkakubali kabisa kuwa-host, wakawa kila mahali wanapoenda vyombo vyote viimulike Tanzania, ninaamini watajua Mlima Kilimanjaro uko Tanzania maana sasa hivi tunalalmika tu, ooh, Kenya wanasema Mlima Kilimanjaro uko kwao, ili tuioneshe dunia kwamba mlima Kilimanjaro uko Tanzania tukubali kuingia gharama kama hizo, tuwalete watu maarufu duniani, watembelee Mlima Kilimanjaro, vyombo vyote vikubwa vya habari vimulike nchi yetu, kila mahali wanakoenda wamulikwe, itaonekana kumbe Mlima Kilimanjaro uko Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unyayo ambao yule binti wa Kenya alikurupuka akasema sijui Olduvai Gorge iko Kenya tutawa-prove wrong kwamba kumbe haiko Kenya iko Tanzania kwa kuwaleta watu mashuhuri wakatembelea hayo maeneo. Waende Rubondo, Rubondo - Geita kuna hifadhi zetu nzuri sana pale, lakini haijulikani. Wakija watu kama hao wakatembelea hata hivi vivutio vyetu ambavyo havijulikani itakuwa mojawapo ya kuvitangaza na watalii wengi watakuja na mwisho wa siku tutapata pesa nzuri sana. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema Tanzania hii ndiyo nchi pekee tunatoa Tanzanite, ninasikitika sana kuona kwamba hatujitangazi kwamba hata hii Tanzanite inatoka kwetu. Hao hao akina Jay Z wakija hapa wakaenda kwenye duka moja hapo Arusha itajulikana kumbe Tanzanite inatoka Tanzania. Camilla alikuja hapa na Prince Charles wakenda pale Cultural Heritage wakanunua Tanzanite nyingi, lakini hakuna mtu aliyejua kwamba wamekuja lakini kama tungekuwa tuliongea nao, tukafanya utaratibu, wakaonekana wakiwa kwenye lile duka walilonunua zile Tanzanite tayari tungekuwa tumeonesha dunia kwamba Tanzanite iko kwetu na tayari tungevutia watu wengi kuja kutalii hapa nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa utalii unaweza ukawa chanzo kikubwa sana cha mapato kuliko hapa huu ukurasa wa 15 unavyosema. Naamini tunaweza kufanya vizuri zaidi na zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nimpongeze Waziri na nimtakie kila la kheri nikiamini kwamba atayazingatia hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii iliyoko mbele yetu. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusisima tena katika Bunge hili na kuweza kuchangia bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Ummy, Waziri wa Afya, Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Katibu Mkuu na Viongozi wote, Watalaam wetu mbalimbali wa sekta hii ya afya, kwa jitihada kubwa wanazozifanya kuhakikisha kwamba afya ya Mtanzania inazidi kuimarika ili tuweze kufanya kazi na kuleta maendeleo kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo naomba pia niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wenzangu jambo moja. Waheshimiwa Wabunge kazi yetu ni kuisimamia Serikali na kuishauri Serikali, nadhani hiyo ndiyo kazi yetu kubwa. Pia naamini kabisa kwamba sisi kuwa ndani ya Bunge hili siyo kwa sababu tuna akili kuliko wale tuliogombea nao tukawashinda, wala siyo kwamba sisi ni bora zaidi ya wale tuliogombea nao tukawashinda isipokuwa ni kwa neema tu. Mungu amepanda sisi tuingie kwa kipindi hiki tufanye hiyo kazi ya kuishauri Serikali na kusimamia siyo kuisifia Serikali au kuibomoa, hapana! Kuisimamia na kuishauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye hilo kwa kuwa nimewakumbusha na nashukuru makofi haya ni kwamba kweli mnaungana na mimi kwamba kazi yetu ni hiyo kusimamia na kuishauri, basi tuifanye kwa uaminifu na Mungu wetu atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii maarufu Guantanamo na nilipata bahati ya kufanya ziara katika Mkoa wa Mbeya na Iringa ambapo tulikuwa tunakwenda kukagua miradi ambayo ilikuwa imeidhinishiwa pesa kwa bajeti ya 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Lungemba kilichopo Mufindi – Iringa. Chuo kile kilikuwa kimetengewa milioni 258 kama nakosea nitarekebishwa na Wajumbe wenzangu lakini nina uhakika ni milioni 258 zilitengwa na tukaidhinisha pesa zile ziende kwa ajili ya mradi ule ili hiki Chuo cha Maendeleo ya Jamii huo mradi uweze kukamilika, tuweze kudahili wanafunzi wa kutosha ili waje watusaidie huko maana tunaitaka Tanzania ya viwanda, tunataka Tanzania kufikia uchumi wa Kati kwa kutegemea viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawategemea sana hawa Maafisa Maendeleo washuke kule chini kwenye Kata zetu, wafanye hiyo kazi ya kuhamasisha maendeleo, wawe chachu kwa sababu watakwenda kule wakiwa wameelimishwa vya kutosha, wakatusaidie kule chini, kuhamasisha maendeleo kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kule pesa zile ambazo tumeidhinisha Bunge la Bajeti mwaka jana mwaka wa 2017/2018 pesa hazijakwenda mpaka tulivyoenda kukagua huo mradi na mpaka juzi ambapo tunajadili tena, tunachambua bajeti ya hii 2018/2019, taarifa tulizokuwa nazo mpaka dakika ya mwisho juzi hapa ni kwamba zile milioni 258 hazijakwenda mpaka sasa hivi tunapojadili bajeti nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole, kiko Mbeya. Chuo hicho kilikuwa kimetengewa zaidi ya milioni 216, tumefika kule pesa hazijakwenda mpaka mwisho sasa tunaingia bajeti nyingine 2018/2019 pesa hazijakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda hospitali ya Rufaa ya Mbeya, hii ni hospitali ya Kanda inahudumia mikoa saba, hospitali hii tuliidhinisha kwenye Bunge hili bilioni 200 kwa ajili ya kununua madawa na kazi zingine huko nafikiri na ujenzi wa jiolojia, kitu kama hicho mtanirekebisha wataalam ambao mnajua, lakini bilioni 200 tumeidhinisha kwenye Bunge hili. Mpaka tunaenda kuukagua ule mradi bilioni 200 zilikuwa hazijakwenda na mpaka juzi tunachambua bajeti hii ya mwaka mwingine 2018/2019, pesa zile hazijakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu ni kuisimamia Serikali na kuishauri sasa tunashauri zile pesa ziende hata kama mimi namheshimu sana Mheshimiwa Ummy na naamini wana dhamira ya dhati pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu wanafanya kazi kwa dhati, sasa sisi kama kazi yetu ni kusimamia kweli Serikali, ni kuishauri kweli Serikali, pesa ambazo tunakuwa tumepitisha humu ziwe zinaenda kule kutekeleza miradi ili hata uhalali wetu wa kuwa humu ndani uweze kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana kama tunaisimamia Serikali, tunaishauri, halafu tunaidhinisha pesa haiendi mpaka dakika za mwisho, tunakuja kujadili bajeti tena kwa mwaka mwingine, tunaidhinisha tena pengine hazitaenda tena. Kama zile za mwaka jana hazijakwenda tuna uhakika gani hizi tunazoidhinisha leo zitakwenda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, tusionekane kama rubber stamp, maana huko nje jamani credibility ya Bunge letu inaondoka watu wanafuatilia Bunge, watu wanafuatilia Bunge hili tutake, tusitake na wakija wakaanza kutudhihaki kama akina Pascal Mayala tusiwalaumu kwa sababu wao wanaamini kazi yetu ni kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapoishauri tunatakiwa tuhakikishe kwamba tunaidhinisha pesa mwaka unaofuata au muda unaotakiwa pesa zikiwa zimeshaenda au hazijaenda tuwe na haki ya kuuliza na tujibiwe tu vizuri siyo kwa lengo la kubomoa bali kwa lengo la kujenga. Nimesema kazi yetu ni kuishauri na kuisimamia, siyo kuibomoa wala kusifia siyo kazi yetu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mimi nitaunga hoja hii mkono bila wasiwasi, lakini naomba tunapoidhinisha pesa ziwe zinaenda na kama kunakuwa kumetokea mabadiliko yoyote ya matumizi basi Bunge hili si ndiyo linatakiwa pia liidhinishe hayo mabadiliko? Kwa hiyo, kama kuna mabadiliko, tuidhinishe sasa hayo mabadiliko kwamba hii pesa haitaenda tena kwenye kile Chuo cha Maendeleo lakini tutaitumia kwenye one, two, three, four iende hivyo, ndiyo hivyo ndugu zangu tutafika, vinginevyo hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani sana na Mheshimiwa Ummy, nina imani sana na Serikali hii kupitia Wizara ya Afya, naamini kabisa kwamba bajeti hii itapita lakini msisitizo sasa tukubaliane kabisa, tunapopitisha ziende kweli. Naomba pia kwa ajili ya Mkoa wangu wa Geita. Mkoa wa Geita tuna ujenzi wa hospitali ya Mkoa na mpaka sasa hivi jitihada kubwa zimeshafanyika Mheshimiwa Ummy, rafiki yangu anajua. Kwa hiyo, tunaomba hizi pesa ambazo tunazipitisha sasa hivi hapa, ziende ili ile hospitali ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatuna ma-specialist kwenye hospitali yetu ya Mkoa, tunaye mmoja tu na uhitaji kwa Mkoa wa Geita ni Specialist 24. Wauguzi tunao watatu katika Mkoa mzima, tunahitaji Wauguzi 30. Kwa hiyo, naomba sana Serikali yetu hii sikivu, basi isikie yale ambayo tunayapitisha humu yaende ili tuweze kuufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mungu kwa kututia nguvu na kutuvusha salama katika kipindi kigumu ambacho kilikuwa ni cha kuuguza na hatimaye kumpumzisha mahali pa milele mama yetu mpendwa Paulina. Nimshukuru pia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa upendo, huruma na utu wema aliotuonesha katika kipindi cha kuuguza na hata mpaka mama alipofariki na hata baada ya kumpumzisha katika nyumba ya milele ameendelea kutupa faraja mimi na kaka yangu kwa kutupa maneno ya imani ambayo yametupa nguvu hata tunaweza kuendelea kustahimili kuishi bila mama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya pamoja na mama yetu mpenzi, Mheshimiwa mama Salma. Nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote, Wabunge, Spika, kaka yangu Rashid Shangazi pamoja na Joseph wa Faraja Fund. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana viongozi wote wa dini, madaktari wote wa Muhimbili na Bugando, wananchi wote wa Geita, wananzengo wenzangu wa Mbweni pamoja na Mpigi kwa faraja kubwa ambayo wametupa na Watanzania wote kwa pamoja ambao wameweza kutufariji na sasa tunaendele vizuri, tunamshukuru Mungu. Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie. Apumzike kwa amani.

WABUNGE FULANI: Amina.

MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu baada ya kuwa nimekipitia kitabu hiki vizuri na kwa kweli niipongeze sana Serikali kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kutaka kututoa hapa tulipo na kutupeleka mbele zaidi kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauanzia kwenye ukurasa wa 53. Ukurasa wa 53 unazungumzia mambo ya elimu bila malipo. Nitasoma kidogo: “Serikali inatekeleza kwa mafanikio makubwa mpango wa Elimumsingi bila malipo. Mpango huo una lengo la kuhakikisha kila mtoto wa Tanzania mwenye umri wa kwenda shule anapata haki ya kupata elimumsingi bila kikwazo cha ada na michango mingine.

Katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali imetumia shilingi bilioni 711.22 kutekeleza mpango huu. Katika mwaka 2018/2019, Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 166.44 hadi Februari, 2019, kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Elimumsingi bila malipo hapa nchini. Utekelezaji wa mpango huo, umeongeza idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika shule za msingi na sekondari”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kusema, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kubuni jambo hili ambalo ni muhimu na lenye tija kubwa sana kwa nchi yetu kwa ajili ya kizazi chetu cha leo na kijacho. Naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kuwa kila jambo jema kubwa la namna hii linapokuwa linaanzwa kwa mara ya kwanza huwa halikosi changamoto mbalimbli na kwa kuwa mimi kama Mbunge kazi yangu ni kuishauri Serikali, napenda nishauri machache kwenye elimu bila malipo. Kwanza kabisa, kwa kanuni iliyowekwa kwamba pesa inayopelekwa shuleni inaenda kulingana na idadi ya wanafunzi katika shule husika. Kwa mfano, Shule ya Msingi Bunge ina watoto 150, nitolee mfano tu, kwa kuwa TAMISEMI inatoa Sh.10,000 kwa kila mtoto na katika Sh.10,000 hiyo, Sh.4,000 inabaki TAMISEMI kwa ajili ya kununua vitabu, Sh.6,000 ndiyo inaenda kule shuleni, sasa Sh.6,000x150 kwa mwezi nadhani inakimbilia kwenye Sh.75,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipiga mahesabu ya matumizi kwa ile shule husika bado kuna changamoto kidogo kwamba inakuwa haitoshelezi. Kila shule kwa ajili ya usalama wa vifaa vilivyoko pale ni lazima kuwa na mlinzi. Mlinzi kwa vyovyote hawezi kulipwa chini ya laki moja, itakuwa ni laki moja na point. Shule yoyote ni muhimu na ni lazima kama ikibidi iwe na umeme, kama haina umeme basi lakini iwe na maji maana ni muhimu sana. Kwa hiyo, bili za umeme, bili za maji zitatoka kwenye hiyo hiyo Sh.75,000 kitu ambacho unaona kabisa bado kinakuwa ni kigumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mkuu wa shule huyu Mwalimu Mkuu kila mwezi anatakiwa aende hata mara mbili au ikibidi hata mara tatu kuhudhuria vikao na Afisa Elimu labda ameitwa au ameitwa na Mkurugenzi kwenye Halmashauri, atategemea ile ile Sh.75,000 ndiyo imsaidie yeye kwenda mpaka kule na wakati mwingine ni mbali inabidi alale, hakuna posho ambayo anaipata ya kwenda kulala au usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo, kuna hii michezo ya UMITASHUMTA ambapo anatakiwa huyu Mwalimu Mkuu achekeche akili yake ahakikishe kwamba watoto wanashiriki michezo kuanzia kata, wilaya, mkoa na mpaka taifa. Kwa taarifa nilizonazo ni kwamba mwaka huu Mtwara ndiyo michezo inafanyika kitaifa. Katika hiyo Sh.75,000 yake, atafanya muujiza gani ili watoto hawa waweze kushiriki vizuri michezo kwenye kata, waende kwenye wilaya, washiriki kwenye mkoa, anunue jezi na mipira, kwa kweli kiuhalisia inakuwa bado ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado huyu huyu Mwalimu Mkuu anatakiwa adurufu internal exams, test, wakati mwingine hata ku-print repoti kwa ajili ya watoto hawa wapeleke kwa wazazi wao, zote zinahitaji pesa ambayo inatoka kwenye ile Sh.75,000. Maelekezo yaliyotoka TAMISEMI pia yanaeleza kwamba pesa hiyo hiyo kama kuna marekebisho madogo madogo Mwalimu Mkuu aitumie hiyo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ijaribu kufanya upya calculation ili tupate ile initial cost ambayo itasaidia kujua pamoja na kwamba tunaenda na uwiano wa shule, pesa inatolewa kwa ajili ya watoto 100, kuna shule nyingine zina watoto 1,000 tunatoa hiyo lakini lazima tuangalie vitu ambavyo ni vya muhimu. Kwa mfano, issue ya mlinzi, Mkuu wa Shule asiwe na hiyo headache kwamba nitatoa wapi hela ya kumlipa mlinzi mwisho wa mwezi umefika. Ikija bili za maji, umeme, kuna mpishi wa uji, Mwalimu Mkuu anaumia kichwa, kidogo inasumbua na kwa kweli inakuwa ni burden kwenye hizi shule ambazo tumelenga kuzisaidia. Kama tunataka elimu bora na tumeanzisha mpango huu mzuri kabisa wa Elimu bila malipo, basi tupeleke na haya marekebisho madogo madogo viende kwa pamoja ili tuweze kulifikia lengo la kutoa elimu bora, siyo tu elimu bila malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, napenda kuishauri Serikali yangu kupitia upya kuangalia kupandishwa kwa madaraja ya walimu. Ni muda kidogo walimu hawajapandishwa madaraja na increments za mishahara na yenyewe inaweza ikapunguza kidogo morale ya kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa lengo letu ni jema, tunataka watoto wetu wapate elimu iliyo bora, basi tujaribu kuangalia makandokando haya ambayo yanaweza yakakwamisha kutupeleka kwenye ile elimu bora tunayoitaka, tuhakikishe tunarekebisha hizi changamoto ambazo nimezizungumzia. Nina imani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwamba ushauri huu nilioutoa utafanyiwa kazi kwa sababu naamini pesa ipo, tutajaribu kurekebisha hayo ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, mchango wangu ulikuwa ni mdogo, naomba muuzingatie. (Makofi)