Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Felister Aloyce Bura (39 total)

MHE. FELISTER A BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Dodoma ilijengwa mwaka 1923 na ilipojengwa ilikuwa na wakazi wasiozidi elfu hamsini lakini kwa sasa Dodoma ina wakazi takribani laki sita na majengo yako vilevile wala hayajaongezeka. Bima ya Afya waliamua kujenga jengo kwa ajili ya kupunguza wingi wa watu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambalo lina miaka mingi halijakamilika, limekabidhiwa lakini hakuna samani ndani yake.
MWENYEKITI: Uliza swali sasa.
MHE. FELISTER A. BURA: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuishawishi Bima ya Afya ambayo ipo chini ya Wizara yake kuleta samani na kukamilisha jengo lile ili lianze kutumika kwa wagonjwa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Bura kwa swali lake la nyongeza. Sisi hatuna shida na kuishawishi taasisi ya NHIF kuwakopesha Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, lakini ukweli utabaki palepale, narudia tena ukweli utabaki palepale kwamba hospitali hizi za mikoa zipo chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Naomba Waheshimiwa Wabunge tunapohudhuria vikao vya RCC tuikumbuke sekta ya afya kwa kushawishi bajeti maalum za mikoa na hata bajeti za kawaida za mikoa kwa kiasi kikubwa zielekezwe kwenye kuboresha hospitali zetu ikiwa ni pamoja na utanuzi wa majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la mikopo NHIF ni suala la kibiashara zaidi. Kama hospitali husika ina makusanyo na vigezo vinavyotosha kuwezesha kupata pesa kwa mkopo kutoka NHIF basi uongozi wa hospitali husika utafanya mazungumzo ya kibiashara ambayo yana faida kwa pande zote mbili baina ya wao wenyewe. Hili wala siyo suala la sisi kama Wizara kwenda kuishawishi NHIF kwa sababu mambo haya yanahusu fedha na fedha zinataratibu zake.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa barabara hii ni sehemu ya Great North Road iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na Watanzania; na kwa kuwa ni sehemu ya Tanzania tu ambayo haijakamilika mpaka sasa; na kwa kuwa baadhi ya Wakandarasi wanasuasua; kazi zimesimama kwa baadhi ya maeneo; je, Serikali inatuhakikishiaje Watanzania kwamba barabara hii itakamilika kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati akiwa Waziri wa Ujenzi katika Mkutano wa Wadau uliofanyika Saint Gaspar aliwaahidi Wanadodoma kwamba atajenga ring roads ili magari yanayotoka mikoa mbalimbali yaishie nje ya Mji kupunguza msongamano wa magari; je, ni lini upembuzi yakinifu utaanza kwa ajili ya kujenga barabara hizo za ring roads?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kuhusiana na kipande kilichobakia cha Msalato na vipande vichache vilivyobaki vya kukamilisha hii barabara ya North Great Road, kwa vyovyote vile muda si mrefu barabara hii itakuwa imekamilika na naomba kumhakikishia hilo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la ring roads, aliyeahidi ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ujenzi, hivi sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda tu nimjulishe; hapa nina ramani nitamwonesha, labda kwa niaba ya wengine, hasa Waandishi wa Habari... (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, tayari tuna mpango mkubwa kabambe wa kujenga za ring roads ndani na nje ya Manispaa ya Dodoma katika kipindi cha miaka mia moja ijayo. Mpango huu utatekelezwa kwa kadiri mahitaji yanavyokuja. Barabara ambazo tunazo hapa za miaka mia moja ijayo, ziko barabara nane kubwa na jumla yake ni Kilometa 147.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mgogoro uliopo kati ya Wananchi wa Buger na Hifadhi ya Taifa ya Manyara ni sawasawa na mgogoro uliopo kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi wa vijiji 11 vya Wilaya ya Kondoa. Katika mgogoro huo wananchi wameuawa, Askari wa Hifadhi ya Mkungunero wamekufa na mgogoro huu ni wa muda mrefu na tumeiomba Serikali washughulikie mgogoro huo na wananchi wanaomba kilometa 50 tu ili mgogoro umalizike.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri waliopita wametembelea na wamefanya mikutano na wananchi wa vijiji 11 wa Wilaya ya Kondoa pamoja na Chemba. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini mgogoro wa wananchi wa Wilaya ya Kondoa, vijiji 11 utaisha kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi hao?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza kuhusu Mbuga ya Mkungunero. Wizara yangu pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, imeandaa mpango wa kupima maeneo yote ambayo yana mgogoro kati ya wananchi na Hifadhi za Taifa ili kufanya juhudi za kutatua matatizo haya moja kwa moja.
Mh
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali
la nyongeza.
Pamoja na njaa iliyowakumba wananchi wa Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Chemba,
Kondoa na maeneo mengine ya ukame katika Mkoa wa Dodoma, lakini mvua iliyonyesha na
inayoendelea kunyesha imeleta mafuriko makubwa kwa baadhi ya vijiji na vyakula ambavyo
wananchi walikuwa navyo vimesombwa na maji, mahitaji ya ndani, magodoro, vitanda,
vyombo vimesombwa na maji.
Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao kwa kushirikiana na Wabunge?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU:
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekumbwa na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha majanga
ya mafuriko katika maeneo tofauti katika nchi yetu ya Tanzania. Sisi wenyewe kama Serikali
tumekuwa tukitembelea maeneo hayo nakuona madhara yaliyopatikana.
Mheshimiwa Spika, inawezekana tukaweza kufanyakazi ya kuwasaidia Watanzania kwa
namna ile ambayo Serikali ina uwezo kwa sasa. Kwa hivyo, naomba niwahakikishie
Waheshimiwa Wabunge, tutajitahidi kuendelea kufanya tathmini na kuona tunafanya nini
kutoka eneo moja hadi jingine, lakini ninaziomba kamati za maafa kwenye ngazi ya Kata, ngazi
ya Wilaya, ngazi ya Mkoa kuona yale yanayoweza kufanyika ndani ya uwezo wao, na
yanayoshindikana wayalete Serikalini ili tuweze kushirikiana kwa pamoja.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili na kwa kuwa vyuo vikuu vinazalisha vijana asubuhi na jioni wenye elimu nzuri ya kufanya ujasiriamali, lakini tatizo ni wapi watapata mikopo kwa njia rahisi zaidi na kwa riba nafuu zaidi? Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia hawa vijana kupata mikopo kwa urahisi na kwa riba nafuu zaidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ajira ambayo ni rahisi kwa vijana na hasa kwa wanawake pia ni kilimo; lakini kilimo kinacholimwa kwa sasa hakina tija; kwanza, masoko hayapo kwa urahisi, mazao mengine yanaoza mashambani; lakini la pili, maeneo ya kulima. Vijiji vingi havijatenga maeneo kwa ajili ya kilimo kwa vijana na hata kwa wanawake ambao wameshajiunga kwenye vikundi mbalimbali. Je, Serikali iko tayari kutenga maeneo na kuzihimiza Halmashauri zetu kutenga maeneo kwa ajili ya vijana na hata kwa wanawake ambao wako tayari kuwa wajasiriamali kupitia kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na la kwanza la mikopo na mitaji kwa wahitimu wa elimu ya vyuo vikuu na elimu ya juu, ni kweli natambua kwamba vijana wengi sasa hivi wanapenda kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali hasa kilimo, lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ukosefu wa mitaji na mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeliangalia hili kwa macho mawili na katika mtazamo wa mbali kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapata fursa ya mikopo na mitaji kwanza kabisa kupitia Mfuko wetu wa Maendeleo ya Vijana ambao umekuwa ukikopesha makundi mengi ya vijana kupitia SACCOS ambazo ziko katika Halmashauri zetu. Vilevile tumeendelea kuwa na msisitizo kwa kuwataka vijana hawa wajiunge katika makampuni na vikundi mbalimbali ili waweze kupata fursa ambazo zinatokana na mikopo na mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunayo program maalum sasa hivi kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, ambapo tuna program ya Kijana Jiajiri inahusisha young graduates, wanaandika proposals zao wanazi-submit katika baraza na baadaye wanapatiwa mikopo na mitaji. Pia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imezungumza kuhusu kuwawezesha vijana wakae katika vikundi na makampuni kutumia fani zao na taaluma zao mbalimbali ili waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu rai kwa vijana wote wale wa vyuo vikuu na wahitimu wa elimu ya juu kutumia fursa hii ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mikopo inayopita katika Halmashauri zetu kwa kukaa katika vikundi na makampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, limeulizwa swali kwamba Serikali ina nia gani ya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kilimo? Mwaka 2014, Wizara yetu ilikutana na Wakuu wa Mikoa wote nchi nzima hapa Dodoma na likatengenezwa azimio, ambapo moja kati ya kilichoamuliwa ni kutengeneza kitu kinaitwa Youth Special Economic Zone, ni ukanda maalum ambao utakuwa unasaidia utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana. Mpaka sasa tayari ekari 8000 zimeshatengwa nchi nzima kwa ajili ya maeneo haya ili vijana waweze kufanya shughuli za kilimo na biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumezungumza na Waziri wa Kilimo, yako mashamba makubwa ya Serikali ambayo wanayafanyia utaratibu sasa hivi nayo tuweze kuyatenga kwa ajili ya kuwagawia vijana waweze kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yetu ya Kondoa haina ultra sound na kuna Kata zaidi ya 30, lakini wanawake wanapopata shida, wanaletwa Dodoma Mjini. Kituo cha Afya cha Chamwino lkulu, kiko katika geti la Ikulu pale Chamwino hakina ultra sound, na wanawake wanatoka kilometa 50, 80, 90 wakija Dodoma Mjini,kwa ajili ya matibabu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuongea na Bima ya Afya ili tupate mkopo huo wa shilingi milioni 72 kwa haraka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali iko tayari kuisaidia Hospitali ya Kondoa, ambayo pia haina kifaa tiba hicho; na wanawake wengi wa Kondoa, wanabebwa kilometa 150 kuja Dodoma Mjini kwa ajili ya ultra sound. Je, wako tayari kuisaidia hospitali hii ya Kondoa wakapata kifaa hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tarehe 24 Februari katika ziara yangu katika Wilaya ya Chamwino niliweza kufika Chamwino soko la Bwigiri na kuangalia ujenzi wa Halmashauri ya Chamwino. Nilipofika pale kweli nilitembelea majengo yote na kuangalia kituo cha afya kile kikoje, na kwakweli na mimi sikuridhika, ndiyo maana nikatoa maelekezo siku ile ile, kwamba kinachotakiwa sasa tuangalie jinsi gani kituo kile kitapata ultra sound. Na bahati mbaya wakati ule bajeti ilikuwa haijaanza, na niliwaelekeza kwamba ikiwezekana waangalie kupitia mfuko wa Bima ya Afya, hali kadhalika katika mpango wao wa bajeti. Lakini kwa bahati mbaya kutokana na ukomo wa bajeti walishindwa kungiza katika bajeti yao.
Mheshimia Naibu Spika, lakini hata hivyo katika maagizo yangu niliyoyatoa nimshukuru sana DMO wa Chamwino na timu yake ya Mkurugenzi kwamba waliweza kufanya utaratibu wa kuwahusisha wenzetu wa NHIF. Na mchakato huu upo mbioni na mimi nina imani kwamba ombi lako Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari, ni kwamba tulishakuwa tayari ndiyo maana nikaagiza. Kwa hiyo, jukumu letu kubwa ni kuendelea kupambana ili wenzetu wa NHIF waweze kusaidia Kituo cha Afya Chamwino.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala zima la Kondoa; ni kweli kutoka Kondoa mpaka hapa ni mbali; na pale ultra sound hakuna, kama Serikali tumeliona hili. Lakini vilevile naomba nisisitize jambo hili jamani; kwamba mambo haya wakati mwingine yote lazima yaanze katika mchakato wetu wa bajeti. Kama bajeti katika vipaumbele inawezekana hatukuweka ultra sound inaonekana kwamba sisi wenyewe tumedhulumu vityo hivyo. Kwa hiyo, jukumu langu kubwa mimi ni kuwasisitiza ndugu zangu Wabunge, tunapoweka katika mchkato wa bajeti tuangalie kipi kipaumbele cha zaidi? Tupunguze yale mambo mengine ambayo hayana maana tuweke katika sehemu ambayo moja kwa moja tunaenda kumsaidia mama na mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama Serikali tumelisikia hili na kwamba tutawahusisha wenzetu wa NHIF ili kama itawezekana waangalie ni jinsi gani waipe kipaumbele Hospitali ya Kondoa. Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kuwa Mheshimiwa Mbunge yuko makini katika hili, najua tutashirikiana na wenzetu wa NHIF. Na siku ile alizungumza pale katika Hospitali yetu ya General, wenzetu watalisikia hili watatupa kipaumbele pale Kondoa.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wa Shabiby round about, Arusha Road walifanyiwa tathmini mwaka 2006 na waliambiwa wakati wowote Serikali itabomoa nyumba zao na kujenga barabara pale lakini mpaka leo wananchi hawa hawajalipwa na huu ni mwaka wa 10 hata choo kikibomoka hawajengi. Naomba Waziri aniambie, ni lini wale watu watalipwa fidia zao halali kwa maana zinazostahili kwa leo ili waondoke?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILANO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba umenizuia kusema yale yaliyopo ndani ya roho yangu lakini naomba uniruhusu, unafahamu fika Mheshimiwa Felister Bura…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwa sababu muda wetu ni mfupi ndiyo maana nimekusaidia kuwatangazia wote kwamba sifa zile zinamwendea kila Mbunge hapa ndani ili wewe uendelee tu kujibu maswali. (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa juhudi za Mheshimiwa Felister Bura, hivi sasa tunaendelea kukamilisha kilomita nane za lami eneo la Msalato na kwa juhudi zake hizo hizo namhakikishia tutaendelea kuhakikisha tunawalipa fidia hawa watu ambao wanahusika katika hilo eneo. Kama ambavyo nilijibu awali, hakuna sababu ya kufanya tathmini upya badala yake ile formula ya kuongeza riba ndiyo inayotumika na hawa watu watalipwa haki yao bila matatizo yoyote mara fedha zitakapopatikana.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi suala la Pori la Mukungunero ni tofauti na maeneo mengine kwa sababu mauaji yamekwishatokea, maaskari watatu walikwishauawa pale, wananchi walishaandika barua mpaka kwa Waziri Mkuu na Waziri Mkuu akapeleka suala hili Wizara ya Maliasili lakini tangu mwaka 2013 suala la Mukungunero halijashughulikiwa. Naomba suala la Mkungunero sasa litazamwe kwa jicho lingine la haraka. Je, ni lini sasa Wizara ya Maliasili itaishughulikia barua iliyoandikwa kwao na Waziri Mkuu aliyepita?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, jibu fupi kabisa, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge swali lake la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa maelezo aliyoyatoa ni wazi kwamba suala hili la Mkungunero, kwa jinsi swali lilivyoulizwa na uhalisia ulivyo lina upekee kama ambavyo na yeye ameweza kubainisha. Kwa hiyo, ushughulikiaji wa suala hili ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii unavuka mipaka, unahusisha masuala yanayohusiana na Wizara ya Mambo ya Ndani. Hapo unahusisha polisi na mambo mengine ya utendaji wa Kiserikali lakini nje ya mipaka ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Hata hivyo, kwa sababu ni suala linalohusiana na Wizara ya Maliasili na Utalii basi tutakwenda kuona namna ambavyo tunashirikiana na vyombo vingine ambavyo vinahusika katika kuweka msukumo kukamilisha ushughulikiaji wa changamoto hii.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa lengo la Serikali la kuanzisha benki hii ni kuwasaidia wanawake wanyonge waliopo vijijini; na kwa kuwa masharti ya Benki ya Wanawake haina tofauti na masharti ya mabenki mengine; na kwa kuwa riba inayotozwa na benki hii pia haina tofauti na riba inayotozwa na mabenki mengine. Je, lengo la Serikali la kuanzisha benki hii kuwasaidia wanawake wanyonge limefikiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wanawake wengi wao wapo vijijini na benki hii haijaweza kuwafikia wanawake hao wa Tanzania waliopo vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanawake wengi wanyonge waliopo vijijini wanafikiwa na huduma ya benki hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, (a) swali lake linahusu riba ya benki hii kuwa sawa na riba inayotolewa na mabenki mengine. Majibu yetu ni kwamba mwezi Machi mwaka huu wakati tukisherehekea sherehe ya Siku ya Wanawake Duniani, Waziri wa Afya alitoa agizo tena kwenye mkutano wa hadhara kwa Mkurugenzi wa Benki hii kwasababu kipindi hicho hakukuwa na bodi, waweze kulishughulikia suala hilo, ili kutengeneza dirisha maalum ambalo litawafikia wanawake wa nchi hii na mikopo yenye riba nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa msimamo wetu ni kwamba bodi ambayo tayari Mheshimiwa Waziri ameiunda inalishughulikia suala hilo na tutatoa majibu baada ya kupata mwongozo kutoka kwa bodi husika ni namna gani wametekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wanawake wa vijijini watafikiwa na benki hii lakini pia pamoja na benki nyingine lakini pia pamoja na schemes nyingine za kuwawezesha wanawake kujiendeleza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Na ndiyo maana kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 Serikali imeanzisha mpango wa kupeleka shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji kwa ajili ya kuwafikia makundi mbalimbali ya kujijenga kiuchumi. Benki yetu itaendelea kushirikiana na benki nyingineza kijamii kama hizi community banks na benki nyingine kubwa ili kuweza kutoa mikopo kwa wanawake.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililoko Mara la ambulance ya kuwachukua wagonjwa, ni sawasawa na tatizo lililopo Wilaya ya Kondoa ambako Kituo cha Afya cha Wilaya ya Kondoa hakina ambulance kwa muda mrefu sasa; iliyopo ni mbovu ya mwaka 2008 na inahitaji matengenezo makubwa sana kiasi kwamba Halmashauri haiwezi kumudu. Je, Serikali iko tayari kutuletea ambulance Wilaya ya Kondoa ili wagonjwa ambao wanatakiwa kupata Rufaa ya kuja Dodoma Mjini wapate usafiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tumelisikia suala zima la request katika Wilaya ya Kondoa. Niseme wazi, ukiangalia hata katika database ya mwaka huu, katika Halmashauri ambazo ziliomba kupata ambulance zilikuwa 18, katika kumbukumbu yangu ya karibuni. Hili sina hakika hapa kama tuliweza kuliainisha katika mpango wetu wa bajeti wa Halmashauri ya Kondoa kwa mwaka huu wa fedha, lakini tutaenda kuliangalia. Kama Kondoa haipo, itabidi tujipange kwa pamoja, tuone ni jinsi gani tutafanya katika mchakato wa bajeti ambao utaanza siyo muda mrefu; na mpango wake tumeujadili hapa siyo muda mrefu, tujadili kwa pamoja kwa sababu hii needs assessment inaanzia kutoka katika vikao vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapolifanya hivi na kwa sababu jambo hili ni pana na ninavyojua, mgonjwa kutoka Kondoa mpaka aletwe Hospital ya General hapa Dodoma ambapo ni mbali sana, tuna kila sababu kuwezesha eneo hilo lipate vifaa vizuri hasa ambulance kuwafikisha wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Felister Bura kwamba, hili tutaliangalia kwa upana wake, tuone ni jinsi gani tutafanya ili eneo lile lipate huduma bora.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa kupanua uwanja wa ndege wa Dodoma, lakini upanuzi huo umeathiri sana barabara ya Area D round about ya Shabiby, na wananchi wanaotoka Area D na Majengo Mapya
hurudi mpaka Kisasa kuja mjini kilometa nyingi.
Je, Serikali iko tayari kujenga barabara nyingine ya
lami kuwapunguzia safari ndefu wananchi wanaokaa maeneo ya Area D na Majengo Mapya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunahitaji kuangalia upya namna Area C na Area D inavyoweza kufikika ukitokea Dar es Salaam bila mzunguko huo mkubwa kwa kuhakikisha tutapata barabara nyingine badala ya ile ambayo sasa hivi imefungwa kwa ajili ya kiwanja cha ndege. Kwa hiyo, namhakikishia Serikali nayo inalifikiria na tutalifanyia kazi kwa haraka hilo.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa uamuzi wa kufungua Benki ya Maendeleo ya Kilimo Mkoani Dodoma na kukubali kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wadogo Mkoani Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeanzishwa kwa malengo ya kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa masharti nafuu na kwa haraka zaidi. Je, Serikali iko tayari kupunguza sasa riba ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili wakulima wengi wapate kufaidika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni mkombozi kwa wakulima. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba mikoa yote wanapata matawi ya benki hii ili wakulima wasihangaike kwenda Dar es Salaam na Dodoma kufuatilia mikopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Felister kwa kuwa mbele katika kufuatilia miradi ya maendeleo ndani ya Mkoa wetu wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameuliza kuhusu kupunguza riba. Kwanza nimkumbushe kwamba Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo ilianzishwa kwa malengo makuu mawili. Moja ni kuchangia utoshelezi na usalama endelevu wa chakula nchini na pia kusaidia mapinduzi ya kilimo kutoka katika kilimo cha kujikimu na kwenda kilimo cha kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza malengo haya, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili iweze kufanya kazi hizi ni lazima iwe na mtaji wa kutosha na pia imekuwa iki-lobby katika taasisi nyingine za kifedha ili ziweze kutoa mikopo katika sekta ya kilimo. Benki hii ili iweze kupata mtaji wa kutosha sasa hivi Serikali imeshairuhusu Benki ya Maendeleo ya Kilimo iweze kupata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na iko mbioni kuupata na nina uhakika itaweza kutoa mikopo hii kwa bei nafuu kwa wakulima wetu wadogo wadogo na wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ili kutimiza pia malengo haya Benki yetu ya Kilimo iliandaa mpango wa biashara wa miaka mitano ambao umeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2017 - 2021. Katika kutekeleza mpango huu wa biashara wa Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo imedhamiria kufungua ofisi sita za kikanda ndani ya Tanzania, ambazo ni Kanda ya Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa Viktoria pamoja na Zanzibar. Baada ya kufunguliwa ofisi hizi za kanda nchi nzima ni imani yetu sasa tutaweza kuwafikia wakulima wetu kule walipo.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Kibaigwa unakua
kwa kasi sana na kwa sasa mji ule ni Mji Mdogo. Hata hivyo, kwa kuwa hatuna watumishi wa kutosha na mji ule haujafanywa kuwa mamlaka, naiomba Serikali sasa ituambie ni lini Mji wa Kibaigwa utapewa mamlaka ili waweze kupanga shughuli za mji wao na kupewa watumishi wa kutosha kuendeleza Mji ule Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, toka asubuhi nimesema leo kuna utaratibu wa kuhamisha goli katika uwanja. Naomba nikuambie Mheshimiwa Felister Bura kwamba hoja yako imesikika na lengo letu ni kupanga miji hii yetu yote vizuri, kuna Kibaigwa, Kibakwe na maeneo mengine katika Mkoa wako wa Dodoma najua inakua kwa kasi sana. Hata hivyo, wakati tunajielekeza katika mipango ya Mamlaka ya Miji Midogo tutajielekeza jinsi gani tupate watumishi kuweza kuziba nafasi hizo ili wananchi wetu wapate huduma vizuri. Nakushukuru sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama tena kwa sababu jambo hili limekuwa likiwagusa Waheshimiwa Wabunge wengi na katika maeneo mengi na hasa pale inapoanzishwa Mamlaka za Miji Midogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiutaratibu mwenye dhamana ya kuendeleza miji hii kuweza kuanza kufanya shughuli zake inapokuwa imeanzishwa Miji hii Midogo ni Halmashauri Mama. Kwa hiyo, inapokuwa Serikali tumekubali kwamba mji huo uanze mipango yote na utaratibu wa uanzishwaji unaanzia kwenye Halmashauri Mama kuijengea uwezo Halmashauri hiyo ya Mji Mdogo ili iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwasihi Waheshimiwa Wabunge kwamba mipango yote itapaswa iingie kwenye mipango ya Halmashauri Mama na ndipo sasa kwa yale maeneo ya upungufu wa watumishi Serikali inaweza kuwaleta. Hata hivyo, kama hakuna bajeti au mpango kutoka kwenye Halmashauri Mama sio rahisi kwa Halmashauri hizo za Miji Midogo kuweza kuanza.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi, kwanza naipongeza Serikali kurudisha Ardhi ya Dodoma mikononi mwa wananchi yaani Baraza la Madiwani. (Makofi)
Kwa kuwa CDA imevunjwa na ndio mamlaka iliyokuwa na madaraka juu ya ardhi ya Dodoma na wakati inavunjwa wapo wananchi ambao walishapata barua za kumiliki ardhi, lakini walikuwa hawajaonyeshwa maeneo yao na wapo wananchi ambao wanalipa kidogo kidogo pale CDA, je, Serikali imeweka utaratibu gani wa dharura wa kuhakikishwa kwamba wananchi wa Manispaa ya Dodoma wanahudumiwa wakati taratibu zingine zinaendelea?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunashukuru kwa Mheshimiwa Mbunge ku- recognize kwamba kilio cha wananchi wa Dodoma katika hilo, lakini jambo la pili government works on papers, hakuna haki mtu itayopotea. Kwa hiyo, Serikali itaandaa utaratibu wowote ambao unawezekana na kikosi kazi kwa mujibu Serikali itakavyokuwa imejipanga naomba muondoe hofu kwamba Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo jambo hili inaisimamia vizuri tutakuja kutoa taarifa hapa iliyokuwa rasmi juu ya jinsi gani jambo hili linatekelezeka na wananchi wote wa Dodoma wasiwe na hofu kila jambo litakuwa limewekwa vizuri kwa utaratibu wa Kiserikali.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa majibu ya nyogeza kwa niaba Waziri wa Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuhusiana na swali lililoulizwa na Mheshimiwa Bura kama ifuatavyo:-
Naomba niwahakikishie wananchi wa Dodoma kwamba mbali na kuvunjwa na CDA huduma zote za ardhi zinaendelea chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma na watumishi waliokuwa wakifanya kazi sekta ile wapo ambao wataendelea na kazi hiyo na wale ambao walikuwa wamelipia nusu ya maeneo yao wataendelea na utaratibu huo mpaka pale watakapokamilisha kulingana na makubaliano waliopeana awali.
Aidha, wale wote ambao wana zile hati ambao si
hati miliki ambazo tunazitambua kutakuwa na utaratibu wa kubadilishiwa na kupewa zile hati ambazo watapewa muda wa miaka 99 kuanzia pale alipopewa awali. Kwa hiyo, wasiwe na hofu Wizara imejipanga vizuri na kila mmoja atapata haki yake kadri utaratibu wa ofisi ilivyopanga.(Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chemba ni kati ya Wilaya mpya katika Mkoa wetu wa Dodoma. Ukitoka Kondoa kwenda Chemba ni zaidi ya kilomita 50 na ukitoka Dodoma Mjini kwenda Chemba ni zaidi ya kilomita 100 lakini Kituo cha Afya kilichopo pale hakikidhi mahitaji na Kituo cha Bahi ambacho kinahesabika kama Hospitali ya Wilaya bado kina upungufu makubwa. Je, lini Serikali itaungana na wananchi wa Chemba kuhakikisha kwamba Makao Makuu ya Wilaya inapata hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini ni kwamba mpango wa Serikali wa mwaka huu imetengwa shilingi milioni 23 ambayo ni kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya maandalizi ya awali lakini tumeshaingiza katika mpango mwingine na vilevile wenzetu wa Chemba wako katika mchakato wa kushirikisha National Health Insurance Fund katika jambo hilo. Kwa hiyo, naomba tuseme kwamba mipango hii yote itaenda kwa pamoja kusaidia Chemba iweze kupata kituo cha afya. Hata hivyo, ndiyo maana tunaamua kufanya ukarabati mkubwa katika Kituo kimoja cha Afya cha Chemba na Bahi tupunguze referral system ili kusaidia wananchi kupata huduma za upasuaji wakiwa katika maeneo yao.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali na kuipongeza kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa kwa kiwango cha lami. Naamini mwaka ujao wa fedha barabara hii itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali; kwa kuwa mji wa Dodoma na viunga vyake unakua kwa kasi sana kutokana na Serikali kuhamia Dodoma, na kwa kuwa tusingependa mji wa Dodoma ukawa na msongamano kama Dar es Salaam; je, Serikali iko tayari na ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kwamba barabara za mzunguko katika mji huu zinaanza kujengwa kupunguza Msongamano unaoweza kuwepo mji utakapokua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, ni lini Serikali itajenga barabara nyingine baada ya barabara iliyokuwa inatoka Shabiby Petrol Station na Area D kufungwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege na sasa wananchi wa Area D, Mlimwa, Majengo Mapya na maeneo mengine wanazunguka mpaka Swaswa ndipo waje mjini, je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba Dodoma ndiyo makao Makuu na mpango mzima wa kuhamia Dodoma unaendelea. Pia Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha barabara zake ili kuondoa usumbufu ambao unaweza kujitokeza kutokana na ukuaji wa mji wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshaweka mkandarasi kwa ajili ya usanifu wa barabara za mzunguko za Dodoma ambazo zitakuwa na ukubwa wa kilometa 96. Tulitenga fedha kiasi cha shilingi 959,812,000 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba usanifu unakamilika; na usanifu wa barabara za Dodoma utakamilika mwezi wa tano mwaka 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua iliyofikiwa sasa hivi tuko zaidi ya asilimia 25 ya zoezi la usanifu na mimi ni wito wangu tu kwa maana kwamba hii kazi isimamiwe vizuri na upande wa TANROADS iliusanifu ukamilike ikiwezekana mapema kabla ya muda huu ili harakati za kutafuta fedha na kujenga barabara za mzunguko wa Dodoma ziweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, tunatambua usumbufu ambao unajitokeza na sasa hivi pia tunaona kuna foleni zimeanza kuonekana. Hii barabara anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ambayo inaleta usumbufu kwa wakazi la eneo la Area D, Mlimwa na Majengo Mapya kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema ninatambua urefu wa kilometa kama mbili; barabara hii mawanzoni ilikuwa inasimamiwa na CDA kabla haijavunjwa. Kwa hiyo, upande wa Serikali tumechukua jukumu la kuhakikisha sasa kipande hiki cha barabara kinatengenezwa haraka ili Waheshimiwa Wabunge wakiwa Dodoma pamoja na wananchi wa Dodoma kwa ujumla wasipate shida kutokana na shida ambayo imejitokeza baada ya ujenzi wa uwanja ule wa ndege kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zoezi la kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha kipande hicho pamoja na kusimamia maeneo ambayo yametengewa fedha kwa tija tutapokuwa na balance kidogo imebakia tutaanza kupeleka eneo lile ili barabara iweze kujengwa, Ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, takribani zaidi ya vijiji 12 vinavyozunguka Pori la Akiba la Mkungunero hawafanyi kazi ya kilimo kwa sababu ya mgogoro mkubwa ambao umedumu zaidi ya miaka 10, kati ya wafanyakazi wa pori la Akiba la Mkungunero na wakulima wanaozunguka pori lile. Suala hili limeshafika Serikalini, lakini hakuna hatua zinazochuliwa. Wabunge wa Majimbo Mheshimiwa Juma Nkamia na Mheshimiwa Dkt. Ashatu wanapata shida sana wakati wa kampeni na hata wakati wa kuwatembelea wananchi wao.
Je, ni lini sasa matatizo haya yatakwisha mpaka halisi wa pori la Mkungunero litabainishwa ili wakulima wale wafanye kazi yao kwa uhuru na kwa amani?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na tatizo la muda mrefu la vijiji hivi 12 katika pori la Akiba la Mkungunero ambapo wananchi walikuwa wanagombania mipaka, hili ni mojawapo ya eneo ambalo Kamati ya Kitaifa imeyapitia na wenyewe tumeipitia tumeona kweli kuna mgogoro ambao unatakiwa kutatuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kumuomba Mheshimiwa Felister Bura kwamba katika hili eneo Serikali iliagiza kwamba maeneo yote yenye migogoro yawekewe mipaka na muda wa mwisho ulikuwa ni tarehe 31 Desemba, 2017. Hivi sasa tunafanya tathmini kupitia maeneo yote sio tu katika eneo hili la Mkungunero, katika mapori yote ya akiba na mengine yote kuangalia baada ya kuweka mipaka na vigingi katika haya maeneo ni maeneo yapi ambayo yana migogoro, ni maeneo kiasi gani tunatakiwa tuyaachie ama tuendelee kuyahifadhi na wananchi watafutiwe maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya yote kukamilika basi Waheshimiwa Wabunge watajulishwa na hatimae tutajua kabisa kwamba wananchi sasa watatatuliwa haya matatizo na hili tatizo la Mkungunero na vijiji hivi 12 vyote vitakuwa vimepata ufumbuzi wa kudumu.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kero ya maji iliyopo Nyang’hwale inawasumbua sana wanawake wa Wilaya ya Kongwa na Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuuliza mara nyingi ukipita hapa jirani yangu kuhusu Wilaya ya Kongwa na ukaniambia umetoa fedha kwa ajili ya maji Wilayani Kongwa. Visima vinavyotoa maji Wilayani Kongwa havizidi vitatu, visima vingine vilivyobaki vilivyochimbwa na World Bank havitoi maji. Ni jana tu nimeongea na Mkurugenzi wa Kongwa akaniambia shida ya maji ya Kongwa ipo palepale, maji yanayotoka ni kwa maeneo machache sana.
Naomba leo Naibu Waziri aniambie maji yatatoka lini Kongwa ya kuwatosha wanawake wa Kongwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nina umakini mkubwa sana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa nimeifanyia kazi sana tangu nakuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Ni juzi tu nilipeleka mtambo wa kuchimba visima Kongwa na kwamba tayari kuna visima vya kutosha ambavyo vimechimbwa lakini siyo kwamba tumekamilisha Jimbo zima au Halmashauri nzima ya Kongwa, kwa hiyo, tunaendelea. Kama bado kuna maeneo yanahitaji kupata visima tupo tayari kuendelea kuchimba na hasa kwa kuzingatia kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 tumeweka fedha tena kwa ajili ya kuendelea kuwapatia akina mama maji.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie mama yangu Mheshimiwa Bura kwamba sisi tumedhamiria kuhakikisha kwamba kweli tunamtua mama ndoo kichwani. Yule ambaye hatatuliwa ndoo kichwani ni kwamba atakwenda kuchota maji umbali usiozidi mita 400 kutokana na sera yetu. Kwa bahati nzuri na mimi mwenyewe naishi Dodoma Mama Bura, kwa hiyo, tutakuwa pamoja na kwa vyovyote vile tuambatane tukaangalie maeneo mengine ambayo hayana ili tuweze kuyapatia maji. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ili kulinda Kiti cha Spika kwa sababu wewe huwezi kuuliza swali la nyongeza, naomba nikiri kwamba Mji wa Kongwa tumepata kisima ambacho kinatoa maji mengi. Sasa hivi kinachotakiwa ni kupeleka fedha ili tuweze kujenga miundombinu. Naomba nikuahidi kwamba tutapeleka fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ili wananchi wa Kongwa waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ilianzishwa zaidi ya miaka Kumi iliyopita na Halmashauri hii Makao yake Makuu yako karibu sana na Chamwino Ikulu. Kwa hiyo, nilitegemea Serikali ingeliangalia hili suala kwa jicho la kipekee kabisa. Idara za Halmashauri hii zimetawanyika, ukitoka Ofisi ya Mkurugenzi hadi Ofisi ya Ardhi ni kilometa tano.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka Ofisi ya Mkurugenzi hadi Idara nyingine ambazo nyingine ziko kwenye shule za msingi, nyingine ziko kwenye nyumba za watu binafsi kwa hiyo, ufanyaji kazi na huduma kwa wananchi uko katika hali ngumu kabisa kutokana na jengo lile kutokamilika. Halmashauri waliwafuata TBA wakafanya tathmini wakaona kwamba, zinahitajika shilingi…

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa shilingi bilioni 2.3 na Serikali imetenga shilingi milioni 600 tu kukamilisha lile jengo.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha za kutosha kwa ajili ya lile jengo la Halmashauri na likamilike kwa wakati, japo floor ya chini, ili watumishi wahamie wakafanye kazi pale?
Swali la pili, Halmashauri ya Chemba iliomba shilingi milioni 950 kwa mwaka huu wa fedha na wamepata shilingi milioni 450 tu. Je, shilingi milioni 500 zilizobaki watapata lini ili waendelee na ujenzi wa jengo la Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, watumishi wa Halmashauri ya Chamwino wanapata shida kubwa sana na hili tunalijua wazi. Ninajua kwamba mkataba wa kwanza wa mkandarasi wa kwanza umevunjwa lakini commitment ya Serikali iko pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali mpaka hivi asubuhi na-cross check pale tumeshapeleka shilingi milioni 750 hivi sasa. Kama ulivyosema tathmini iliyofanywa na TBA imeonekana kumaliza lile eneo la ground floor peke yake karibu ni shilingi bilioni mbili. Hata hivyo, nimeongea nimeongea na Kaimu Mkurugenzi pamoja na Engineer leo wafike ofisini kwangu kuangalia way forward tunafanyaje kwa sababu tathmini iliyofanywa gharama yake ni kubwa, lakini Engineer na timu yake wanasema kwa kutumia wao utaalamu wao pale ile shilingi milioni 750 wataweza kumaliza ile ground floor na hivi sasa tunajielekeza kuangalia jinsi gani fedha zitumike vizuri.
Kwa hiyo, nimemuagiza Kaimu Mkurugenzi na Engineer leo hii wanakuja kukutana na wataalam katika ofisi yetu tuangalie tufanye nini ili tumalize ile ground floor.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ujenzi pale Chemba, ni kweli tumepeleka shilingi milioni 500 mpaka hivi sasa, tunachotaka kufanya ni kuhakikisha kwamba, fedha tunazipeleka maeneo haya na maeneo mengine tofauti, lengo kubwa ofisi hizi ziweze kukamilika na watumishi wetu wapate maeneo mazuri ya kufanya kazi. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kutupa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya cha Bahi. Kituo hiki kinawahudumia wananchi wengi sana kwa sababu mji ule unaendelea kupanuka kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tulilonalo, upanuzi unafanyika lakini hatuna vitendea kazi, watumishi walioko pale ni Manesi wanne tu na yuko Daktari mmoja na Matabibu wachache sana ambao hawakidhi mahitaji ya wagonjwa wanaokwenda katika kituo kile cha afya. Ni lini sasa Serikali italeta watumishi na vitendea kazi vya kutosha kwa ajili ya huduma za Kituo cha Afya cha Bahi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimshukuru Mheshimiwa Bura kwa sababu yeye amekuwa Msemaji wa Mkoa wa Dodoma kwa nafasi yake ya Viti Maalum na anautendea haki sana mkoa huu. Naomba ku-declare interest, jengo ambalo tumemaliza hivi sasa katika Hospitali ya General, amefanya kazi kubwa sana kuhakikisha tumepeleka pesa na hivi sasa tumepeleka karibuni shilingi bilioni mbili hospitali ile inapata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, eneo la Bahi kweli tumeboresha kituo kile cha afya lakini siyo hivyo tu kwa kelele zake na za Mbunge wa Bahi mwaka huu tunakwenda kuanza ujenzi wa hospitali mpya za Wilaya za Bahi, Chemba pamoja na Chamwino. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo, wenzetu kupitia Utumishi kabla ya Juni, kuna mpango mkakati kupata watumishi wapya katika sekta ya elimu na sekta ya afya. Pia kwa vile tunajua Bahi ni pumulio la makao makuu yetu ya nchi kwa maana ya hapa Dodoma tutajitahidi kuhakikisha tunawapeleka watumishi wa kutosha ikiwa lengo kubwa ni wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)
MHE. FELISTER A BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maporomoko ya Ntomoko ni janga kwa wananchi wanaoishi kandokando ya maporomoko haya. Wananchi wa Wilaya ya Chemba vijiji kumi na vijiji vitatu vya Wilaya ya Kondoa wamesubiri mradi huu kwa muda mrefu sana na fedha zilishatolewa zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya kukarabati mradi ule, watumishi ambao walizembea mradi ule hawajachukuliwa hatua yoyote. Wananchi wanateseka na hakuna jibu lolote linaloonesha kwamba hivi vijiji vitapata maji hivi karibuni.
Je, watumishi waozembea na wakapoteza zaidi ya shilingi bilioni mbili na kufanya mradi huu ukasimama wamechukuliwa hatua gani?
Swali la pili, mradi huu umekwishatembelewa na viongozi wengi na tumekwishachangia mara nyingi na Wabunge wa maeneo yale mimi na Mheshimiwa Juma Nkamia na Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji sasa hivi hatueleweki kwa wananchi.
Je, kuna mkakati gani wa haraka wa kuwapatia wananchi wa vijiji vile maji ili wasiendelee kuhangaika kwa sababu hata DUWASA wenyewe hawajapata fedha kwa ajili ya ule mradi? (Makofi)
NAIBU WA WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze Mama yangu Felister Bura kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ambalo nashukuru sana ni taarifa ambayo amenipa kama Naibu Waziri wa Maji, nataka nimhakikishie fedha za Serikali haziliwi bure. Kama kutakuwa na watumishi ambao kwa kuzembea au kwa maksudi fedha zile zimepotea, tutafanya mawasiliano ya haraka na watu wa Kondoa katika kuhakikisha hatua za haraka zitachukuliwa kwa watumishi wale ambao wamefanya uzembe wananchi waweze kupata taabu.
Swali lake la pili, amesema huu ni mradi wa muda mrefu sana nataka nimuhakikishie sisi ni Wizara ya Maji na jukumu letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama yenye kuwatosheleza na ndiyo maana tumeahidi kwamba katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 tumeshatenga fedha ili katika kuhakikisha mradi ule uweze kukarabatiwa kwa haraka ili wananchi wake waweze kupata majisafi salama na ya kuwatosheleza. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kumfahamisha Mheshimiwa Felister Bura kwamba kuna hatua za dharura ambazo tunaendelea nazo, tunachimba visima katika vijiji vyote eneo la Kondoa na tumeshaanza na visima 15 ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yanayoelimisha umma juu ya ugonjwa wa Ini, ugonjwa ambao ni hatari kama alivyoeleza mwenyewe Naibu Waziri kwamba, ugonjwa huu unaweza ukaambukizwa kwa kujamiiana, kwa mama kumuambukiza mtoto wake mchanga, kudungwa au kujidunga sindano na mama kumwambukiza mtoto anapojifungua. Ni ugonjwa hatari sana ambao wananchi wengi hawaujui na hawajui namna ya kujikinga. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kutoa elimu kama inavyotoa juu ya ugonjwa wa malaria, kifua kikuu na maradhi mengine ili wananchi wajiepushe na wawe na elimu juu ya ugonjwa huu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo kwa zahanati na vituo vya afya kuwa na uwezo wa kupima ugonjwa wa Ini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Moja, ametaka kujua Serikali tunafanya nini katika kuelimisha jamii. Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii kupitia vitengo vyake vya elimu kwa umma imekuwa inaandaa majarida na machapisho mbalimbali ambayo tumekuwa tunayatoa kwa umma na kwa kupitia katika Vyombo vya Habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tumekuwa tunatoa elimu hii katika kliniki mbalimbali lakini kutokana na umuhimu wa ugonjwa huu, tutajaribu kuongeza juhudi zaidi kuhakikisha kwamba wigo wa elimu hii unapanuka na kuweza kuwafikia Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili alitaka kujua wigo wa upimaji. Kwa sasa upimaji wa ugonjwa huu unafanyika katika ngazi ya Wilaya kwenda juu kwa aina ya vipimo ambavyo tulikuwa navyo, lakini kwa sababu teknolojia imekua sasa hivi na vipimo vya haraka (rapid test) zimeweza kupatikana, Serikali inatafakari sasa upatikanaji wa vipimo hivi katika ngazi nyingine za chini ili upimaji wa ugonjwa huu uweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nitoe rai kwamba maambukizi ya Hepatitis B yanafanana na maambukizi ya UKIMWI na nawaomba sana wananchi tuwe tunajenga tabia ya kupima ili tuweze kutunza maini yetu.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma na wananchi ambao wanaishi karibu na uwanja ule nyumba zao ziliwekwa alama ya “X” kwa maana kwamba zile nyumba zitavunjwa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege. Hata hivyo baadhi ya wananchi wamelipwa na baadhi ya wananchi hawalipwa fidia kutokana na nyumba zao kuwekwa alama “X”. Naomba kujua ni lini wananchi ambao hawalipwa watalipwa fidia ili waende wakayafanye maendele ya ujenzi wa nyumba kwenye maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimtaharifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia kesho hao wananchi ambao wanadai fidia zao wataanza kulipwa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Naibu Waziri kwa kuteuliwa lakini pia nimpongeze kwa majibu mazuri aliyonipatia. Pamoja na majibu hayo mazuri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Taifa hili hutumia fedha nyingi sana kuagiza mafuta ya kula ukiachilia mafuta ya petroli, lakini nchi hii ina uwezo wa kuzalisha mafuta ya kutosha ya kula na tukaacha kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi. Katika nchi yetu kuna viwanda vingi vinavyokamua mafuta kwa mfano, Kiwanda cha Mount Meru ambacho kina uwezo wa kukamua mafuta tani 400,000 lakini kwa sasa wanapata tani 40,000 tu ukiachilia viwanda vingine.
Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwamba Mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara wanawekwa kwenye mkakati maalum wa kuzalisha mazao ya mafuta na hata Mkoa wa Kigoma unaozalisha mafuta ya mawese, kwamba sasa mkakati uwekwe kwa kupata mbegu bora kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayozalisha mafuta, ni mkakati gani umewekwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sisi wananchi wa Dodoma ni wakulima wazuri sana wa zabibu na tunazalisha mara mbili kwa mwaka lakini hatuna soko. Zabibu zinaoza mashambani kwa sababu wakulima wamekosa masoko. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba zabibu zote zinazozalishwa na wakulima zinapata soko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kutaka kujua mkakati wa Serikali kwa ajili ya kuweza kuzalisha mazao ya mbegu ya mafuta hapa nchini ili kumaliza tatizo la mafuta hapa nchini ili kuokoa fedha za kigeni. Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 4 Juni, 2018 ilizindua Programu Maalum ya Kuendeleza Kilimo, kwa Kiluguru tunaita ASDP II ambapo lengo lake ni kuongeza uzalishaji na tija kwa ajili ya mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mpango huo Mheshimiwa Waziri Mkuu alianza utekelezaji huo tukaenda Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya kuzindua na kuendeleza kilimo cha mchikichi, ikafuatiwa na kikao cha wadau kilichofanyika tarehe 24/05 pale Morogoro kwa maana ya kampuni yetu ya uzalishaji mbegu ya ASA, Kampuni ya Utafiti wa Mbegu (TARI) pamoja na Kampuni ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI) wamepanga mikakati na tumekubaliana kama Serikali kuanza kufufua zao la mchikichi kwa ajili ya kuzalisha ndani ya miaka minne miche milioni 20 ili kumaliza tatizo hilo sambamba na kuongeza mbegu bora katika zao la alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu zabibu, kwanza nimpongeze Mheshmiwa Mbunge kwa kuwatetea watu wake wa Dodoma ambao ni maarufu kwa kilimo cha zabibu hapa nchini lakini ni kweli bei ya wine inayotokana na zabibu ya Tanzania ipo juu kuliko ya wine zinazotoka nje ya nchi. Hii inatokana na sababu ya gharama kubwa za uzalishaji hapa nchini na tija ndogo wanayopata wakulima, wanatumia gharama kubwa lakini wanapata faida ndogo. Serikali tumeliona hilo na kwa sasa tunapitia na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuangalia mfumo wa kodi zetu na ushuru ili kupunguza gharama za uzalishaji kuwezesha wine hii kuuzwa kwa bei nafuu ili soko liwe la uhakika. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwanza tunaishukuru Serikali kwamba tumechimbiwa visima vinne kupitia Halmashauri ya Mji wa Kondoa. Pamoja na visima hivyo ambavyo vimechimbwa bila ukarabati wa miundombinu ya maji, uchimbaji wa visima hivi havitawasaidia sana wananchi wa Kondoa Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo katika bajeti iliyopita tuliomba fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo. Naomba kujua Serikali imetenga fedha kiasi gani kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya zamani ukizingatia kwamba maeneo kama Kwapakacha, Kilimani na Bicha katika uchimbaji wa visima hivyo kuna maeneo watatumia miundombinu ya zamani? Je, Serikali iko tayari kujenga baadhi ya miundombinu ili wananchi wa Kondoa Mjini wapate maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ahadi ya ukarabati wa miundombinu ya maji katika Mji wa Kondoa ni ya ahadi ya viongozi wa Kitaifa na hasa waliotembelea Kondoa Mjini mwaka jana akiwemo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, ahadi hizo zitatekelezwa lini? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninavyosema mara nyingi, nia ya Serikali ni kuhakikisha kila eneo tunapeleka maji safi na salama. Kwa upande wa Kondoa Mjini sasa hivi tuna mradi ambao utahakikisha kwamba tunapeleka maji kila eneo la Kondoa Mjini ambapo kama nilivyosema kwenye swali la msingi kwamba sasa hivi tunajenga miundombinu ya kilomita 9.12, tunajenga miundombinu ya kusambaza maji kilomita 30.172 kwa sababu kuchimba visima ni jambo lingine na kuweka miundombinu ni jambo linguine. Kwa kulijua hilo, Serikali tunaendelea sasa hivi kujenga miundombinu hiyo tuhakikishe mwananchi kila eneo anapata maji safi na salama. Tunategemea mradi huu utamalizika hivi karibuni na wananchi watapata maji hayo.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dodoma linakua kila kukicha na uwezo wa DUWASA kuwahudumia wananchi wa Dodoma unapungua kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali. Wananchi wanaoishi Ntyuka, Ng’ong’ona, UDOM, Mtumba hawana maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watu wanaohamia Dodoma na walioko Dodoma wanapata maji safi na salama kwa wakati? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki hii nimeshuhudia utiaji wa saini wa mradi wa kupeleka maji katika mji wa Serikali pamoja na eneo la Mtumba, kwa hiyo, maji yatapatikana. Hata hivyo, chanzo cha Makutopora Mzakwe kina uwezo wa kutoa lita milioni 61.5, kwa hiyo, maji yapo na sasa hivi tunazalisha lita milioni 46. Kwa hiyo, maji bado tunayo Mheshimiwa Mbunge. Sasa hivi tunaweka mradi wa kusambaza maji ili tuweze kufika maeneo yote aliyotaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza Swali la nyongeza. Kama ilivyo Morogoro kwamba kuna vivutio kwa watalii ndivyo ilivyo kwa Mkoa wa Dodoma ambako Wilayani Kondoa kuna michoro ambayo haipo Tanzania na michoro ile iko katika mapango ya Kolo na Pahi, lakini vivutio vile havijawahi kutangazwa na Serikali.
Je, Serikali ina mkakati gani? Pamoja na Wabunge wa Kondoa kuhangaika kuleta watalii, lakini bado haitoshelezi kama Serikali haitatia mkazo kutangaza vile vivutio.
Je ni lini sasa au Serikali ina mkakati gani kutangaza michoro ile ya mapango ya Kolo, Pahi na maeneo mengine katika Wilaya ya Kondoa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba nichukue nafasi hii kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Felister Bura na Wabunge wote wa Mkoa wa Dodoma kwa jinis ambavyo wamekuwa wakilifanyia kazi hili suala. Hivi sasa tunajua kabisa kwamba Dadoma ndiyo Makao Makuu ya nchi na kweli lazima tuziimarishe hizi hifadhi zetu na maeneo maengine ya Utalii ili kuweza kuvutia watu mbalimbali kuja kuwekeza katika Mkoa huu wa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho tunategemea kukifanya katika kutangaza yale maeneo ya michoro ya Miambani kule Kondoa; yaani Kolo na pale Pahi; jitihada ambazo tunaweka kuanzia tarehe 1 Julai, 2018 tunategemea kuanzisha studio ya kutangaza utalii yaani kutangaza vivutio vyote nchi nzima. Hiyo ni pamoja na hilo eneo, tutalitangaza vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tunategemea kuanzisha channel maalum kupitia TBC ambayo itakuwa inahusiana na masuala ya utalii. Kwa kutumia hilo basi, tunaamini kwamba basi matangazo, wananchi wengi wa ndani na wa nje wataweza kupata fursa ya kuweza kujua vivutio vyote tulivyonavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, tunategemea kutumia viongozi mbalimbali mashuhuri pamoja na mambo mengine mengi kutangaza ndani ya nchi na nje ya nchi kwa kutumia mitandao ya facebook, twitter na mambo mengineyo ili kusudi vivutio vyote vieleweke kwa watanzania lakini kwa watu wote walioko nchi za nje waweze kuijua Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii niseme kwamba sasa hivi Tanzania tumepata taarifa kwamba sasa imekuwa ni nchi inayoongoza kwa safari Afrika kupitia Serengeti. Kwa kweli huu ni ufahari mkubwa na Dodoma nayo itafaidika sana na haya mambo ambayo tunakwenda kuyafanya.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Watoto wakike wengi wanaoshindwa kuendelea na masomo baada ya kumaliza kidato cha nne na cha sita wanaolewa kwa kukosa fursa ya kujifunza katika vyuo vyetu vya ufundi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha kambi la vijana ili hawa watoto wanaomaliza kidato cha nne wakiwa wadogo na hawaruhusiwi wakiwa chini ya miaka 14 au wakiwa na miaka 14 wakajifunze shughuli za ufundi, ufugaji bora wakajifunze ujasiriamali na mambo mengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) : Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi ya Waziri Mkuu ina program ya ukuzaji ujuzi nchini ambao lengo lake kubwa ni kuhakikisha tunaisadia nguvu kazi yetu hasa vijana wengi kupata fursa ya kujifunza kwa vitendo hasa katika mafunzo mbalimbali ya ufundi. Program hii inaendelea na mpaka ninavyozungumza hivi sasa takribani vijana 22,000 nchi nzima wameshawasilisha maombi. Kwa hiyo, ni program ambayo inawagusa watu tofauti tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni program endelevu mpaka mwaka 2021 tutaendelea kuwachukua watoto wengi hasa wa kike kuingia kwenye program hii kujifunza ili waweze kujitegemea. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kondoa kuna michoro ya mapangoni Kolo – Kondoa Irangi,na michoro hii ni urithi wa dunia kama alivyosema yeye mwenyewe Naibu Waziri, na mpaka sasa wananchi wa Kondoa na hata watanzania hatujafaidika vizuri na michoro ile kwa sababu haijatangazwa ipasavyo.

Je, Serikali ina mikakati gani ya kutangaza michoro ya mapangoni pale Kolo-Kondoa Irangi ili wananchi wa Kondoa wafaidike na Watanzania wote kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye swali la msingi kuhusu Kilwa, maeneo mengi sana haya ya malikale yalikuwa hayatangazwi na sasa wizara yetu imechukua hatua ya kuyagawa kwenye taasisi zake 4 ambazo ni TANAPA, TFS, Ngorongoro pamoja TAWA. Eneo hili la Kolo-Kondoa tumewapa watu waTFS ambao watafanya kazi zote za uendelezaji ikiwa ni pamoja kuandaa mazingira lakini na kutangaza ili kufanya eneo hilo liweze kufikika na kuvutia watalii.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo nyongeza. Tangu mwaka 2017 mwezi wa Pili, huu ni mwaka wa tatu jengo hili halijawahi kutumika baada ya kulikabidhi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Wananchi wanatoka kilometa 30 kufuata huduma Dodoma Mjini badala ya kwenda Bahi ambayo ndiyo Wilaya iliyopo Tarafa ya Chipanga. Wananchi wanateseka kwa sababu hawana mahali pa kupeleka wahalifu wanapokamatwa. Je, Serikali iko tayari sasa kufanya ukarabati kwa mwaka huu wa fedha katika jengo hili ambalo tulikabidhi litumike kama Kituo cha Polisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari sasa aandamane pamoja nami baada ya Bunge hili twende akaongee na wananchi ambao wamekaa kwa muda mrefu wakisubiri jengo lile litumike kama Kituo cha Polisi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Bura kwa namna ambavyo anachapa kazi kwa umahiri na juhudi kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma. Ndiyo maana Mheshimiwa Bura namfananisha na kumlinganisha na mama mmoja kwenye Biblia naitwa Ester. Mama huyu akiwa bikira alipata kibali machoni pa Mfalme Ahasuero wa kule Shushani Ngomeni. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bura amepata kibali kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika kuwafanyia kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, ni kweli kwamba Kituo hiki cha Polisi cha Chipanga kina matatizo ambayo tumeyafanyia tathmini. Namhakikishia Mheshimiwa Bura awe na amani, kwamba kituo hicho baada ya kufanya tathmini, tutatenga fedha kwa ajili ya kwenda kukikarabati ili kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Chipanga katika Wilaya ya Bahi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Felister Bura nikukuhakishie kwamba huko unakotaka twende labda wewe ndio umechelewa, mimi niko tayari hata leo hii ukitaka tutakwenda wote kule Bahi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe wito kwa Mabaraza ya Madiwani kote nchini kwamba katika Ilani hii ya CCM, Ibara ya 146 chama kimeelekeza Serikali zake mbili kwa maana ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu. Nawaomba Waheshimiwa Madiwani, kwenye makusanyo ya ndani watenge pia fedha kwa ajili ya kujenga Vituo vya Polisi pamoja na nyumba za askari ili tuweze kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora kwa wananchi hapa nchi. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa ongezeko la watu na hasa Jiji la Dodoma limekuwa kubwa baada ya Makao Makuu kuhamia Dodoma, je, Serikali ina mpango kabambe au mkakati gani wa kuhakikisha kwamba maji ya Ziwa Victoria yaliyofika Tabora yanafika Dodoma kuwasaidia wananchi wa Dodoma kutokana na upungufu wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Bura kwa swali lake zuri sana, sisi kama Wizara ya Maji tunatambua kabisa sasa hivi kumekuwa na ongezeko kubwa sana katika Mkoa huu wa Dodoma, lakini jitihada kubwa ambazo tulizozifanya sasa hivi, uzalishaji wetu zaidi ya lita milioni 55, lakini mahitaji lita kama milioni 44. Kwa hiyo, tuna maji kwa kiasi kikubwa, kubwa ambalo tunaloliona hapa ni suala zima la usambazaji, lakini itakapobidi tutafanya kila jitihada katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji na wananchi wa Dodoma wasipate tatizo hilo.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, kama uhitaji wa Walimu wa Sayansi kwa Mkoa wa Dodoma ni 916. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba uhitaji wa Walimu wa Sayansi ambao ndio Madaktari na Wahandisi na Wauguzi unakamilika kwa kuwaajiri Walimu wanaotesheleza mahitaji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na uhitaji mkubwa wa Walimu wa Sayansi kwa shule za sekondari, kuna uhitaji mkubwa wa Walimu wa shule za msingi. Kwa mfano, Wilaya ya Kongwa kuna uhitaji wa Walimu 1,088; Chemba, Walimu 786; Kondoa, Walimu 618; Dodoma Jiji, Walimu 656, hapo ni Wilaya nne tu nimezitolea mfano. Je, ni lini sasa Serikali itaamua sasa kuwaajiri Walimu wa shule ya msingi kwa sababu elimu ya msingi ni kujenga msingi wa mwanafunzi, Je, Serikali iko tayari kuwaaajiri Walimu wa kutosha pamoja na halmashauri zetu kujenga miundombinu, Jiji wamepanga bilioni 8.3 kwa ajili ya kujenga miundombinu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari. Je, serikali iko tayari sasa kuwaajiri na Walimu wa shule za msingi ili kukidhi mahitaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felister Bura, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli swali lake la kwanza anauliza upungufu mkubwa Walimu na naomba nikiri kwamba ni kweli kwamba tuna uhitaji mkubwa sana wa Walimu wa Hesabu na Sayansi, takribani nchi nzima na Wilaya zote na Wahesimiwa Wabunge wote hawa ukiona wanapiga makofi wanazungumza hilo. Hii ni ajira ya awamu ya kwanza, bado tathimini ile ya Walimu hewa na wengine, hii tumeomba kibali kupata Walimu 8,500 kama nilivyosema, lakini tunatarajia kupa kibali kingine mwezi wa Tano au wa Sita ambao watakuwa wengi zaidi ya hawa. Kwa kweli makusudi yetu ni kulenga kuajiri Walimu wengi wa Hesabu na Sayansi, lakini kama nilivyosema pale ambapo wana mahitaji makubwa sana, kwa mfano, unakuta kuna shule haina Mwalimu wa Hesabu, haina Mwalimu wa fizikia na kemia tutazingatia maeneo yenye upungufu mkubwa zaidi wakati tunapeleka Walimu hawa katika shule zetu za sekondari.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameuliza ajira ya Walimu wa shule za msingi. Katika hao niliowataja Walimu 4,500 nimesema 1,300 ni masomo ya sayansi na hisabati, maana yake Walimu 3,200 wanaobaki wote hawa ni Walimu wa shule ya msingi pamoja na Walimu wa watoto wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, tutazingatia kupeleka pia na Walimu wa shule za msingi katika maeneo mbalimbali ambayo yana upungufu mkubwa. Tumefanya mawasiliano na Waheshimiwa Wabunge, wanafahamu, tutalizingatia, lakini tukipata kibali mwezi wa Tano kama nilivyosema au wa Sita tutazingatia maeneo gani ya kwenda.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna upungufu mkubwa, lakini tuna maelekezo mengine ambayo kama kutakuwa kwa mfano kwenye vibali vya muda, tukianza kutangaza nafasi unakuta pia inakuwa ni pungufu. Tumetoa vibali vya muda, Walimu ambao wamesoma masomo ya sayansi na hesabu lakini sio Walimu wanapata mafunzo ya muda mfupi ili waweze kuziba gape hili la Walimu wa Sayansi na Hisabati. Ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri ambayo tumeyapata. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, tunaipongeza Serikali kwa uamuzi wa kujenga Kituo Kikuu cha Kumbukumbu Wilayani Kongwa kwa sababu Kongwa ina historia ya wapigania uhuru. Je, kituo hicho kitaanza kujengwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ushirikishwaji wa wadau huharakisha shughuli za maendeleo na nimeona katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wadau wameshirikishwa, Wachina wamejenga majengo mazuri na makubwa pale chuo kikuu Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango wowote wa kushirikisha wadau ili jengo hilo likamike katika uongozi wa Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Felister Bura kwa niaba ya Mheshimiwa Livingstone Lusinde kwa maswali yake mazuri ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilianza na kwanza ameanza kwa kutoa pongezi kwa Wizara, tumepokea pongezi hizo. Vile vile swali lake la msingi la kwanza ametaka kujua, je, ni lini kituo hicho kitaanza kujengwa rasmi. Tayari ujenzi wa hiyo kituo ulishaanza na tulishaanza tangu mwaka 2015 ambapo ukarabati wa hicho kituo ulianza. Hata hivyo, kwa sababu ni suala la kibajeti na kwenye bajeti yetu ya mwaka jana kuna fedha ambayo ilitengwa kwa ajili ya kwenda kukarabati kituo hicho. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuweza kumhakikishia Mheshimiwa Bura kwamba ukarabati wa hicho kituo na kuweka miundombinu mingine unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kwa sababu lengo la Wizara ni kuhakikisha kwamba hicho kituo kinakuwa pia center kwa ajili ya masuala mazima ya utalii. Kwa hiyo mipango ambayo ipo pale ni mikubwa mpango mmojawapo ni kuhakikisha kwamba tunajenga kituo cha ndege lakini vilevile tuweze kujenga hotel za five stars pale ili kiweze kuwa kituo kikubwa cha masuala ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake pili ametaka kujua kwamba kuhusiana na kuweza kushirikisha wadau. Kama ambayo nimejibu kwenye jibu langu la msingi ni kwamba sisi kama Wizara suala hili hatufanyi peke yetu tumekuwa tukishirikiana na wadau. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuweza kuwahamsisha wadau mbalimbali waweze kushiriki katika kuhakikisha kwamba tunatunza hizi kumbukumbu za Mwalimu Nyerere. Ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na shughuli nyingi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wawekezaji wengi wameamua kuja Dodoma na Serikali yenyewe inakuja Dodoma na vyuo vikuu vingi vinajengwa Dodoma, hasa maeneo ya Nala; na kwa kuwa, maeneo ya pembezoni kama vile Bahi, Wilaya ya Chamwino na maeneo mengine yanahitaji maji kwa ajili ya wawekezaji, je, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba, hao wawekezaji na wananchi wanaozunguka maeneo hayo hawakosi maji kwa ajili ya matumizi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, maji ya Ziwa Victoria yameshaletwa mpaka Nzega na kuna taarifa hayo maji yanakuja mpaka Igunga. Je, Serikali haioni kwamba, suluhu ya kudumu kwa ajili ya mahitaji ya Dodoma ni kuleta maji ya Ziwa Victoria ambayo yatasaidia pia Mkoa wa Singida na Dodoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Felister Bura amekuwa mpiganaji mkubwa sana, hususan kwa changamoto ya maji katika Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho nataka niwahakikishie wakazi wa Dodoma kupitia uongozi mahiri wa kiongozi wetu wa Wizara ya Maji, Profesa Makame Mbarawa, tumekwishaliona hilo. Moja kuwaagiza DUWASA katika kuhakikisha kwenye makusanyo yao ya ndani asilimia 30 wahakikishe wanachimba visima virefu maeneo ya pembezoni ili wananchi wa Dodoma waweze kupata huduma ya maji.

Pili, mpaka sasa tumekwishalipa fidia katika Bwawa la Farkwa kwa wananchi wale ili tuweze kujenga Bwawa la Farkwa. Katika kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo la maji katika Mkoa huu wa Dodoma tumeshaanza kuanzisha timu ya kufanya study ya namna gani ya kuanzisha standard gauge kubwa katika miradi yetu ya maji. Moja ni katika kuhakikisha tunaandaa standard gauge ya kuyatoa maji Ziwa Victoria hadi kuyaleta hapa Dodoma. Subira yavuta heri. Heri itapatikana katika kuhakikisha kwamba, Mradi wa Ziwa Victoria unafikisha maji hapa Dodoma. Ahsante sana.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kujua kwamba Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa ufugaji wa wanyama; ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda na mifugo mingine, lakini cha ajabu ni kwamba hatuna kiwanda cha kuchakata mifugo hiyo na sasa hivi Serikali imehamia Dodoma na tuna ranchi ya Kongwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili alijibu kwa umakini zaidi, tuna ranchi pale Kongwa. Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wafugaji wa Dodoma, Shinyanga, Tabora, Mwanza wanaleta mifugo yao Dodoma pale ranchi ya Kongwa, ambapo ombi langu kwa Serikali ni kujengwa kwa kiwanda cha kuchakata mifugo pale Kongwa Ranch ili wananchi wa Mwanza, Shinyanga, Dodoma na Singida wapate mahali pa kuuza mazao ya mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kiwanda cha kuchakata mifugo pale Ruvu kilianza tangu mwaka 2007 na sasa ni miaka 12 kiwanda kile hakijakamilika na fedha nyingi zilishatumika kwa ujenzi wa kiwanda kile; naomba kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba kile kiwanda cha Ruvu pia kinaanza kazi sambamba na kiwanda kitakachojengwa Kongwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Tanzania ni nchi ya pili kwa mifugo katika Bara la Afrika. Suala la kutokuwa na kiwanda, naomba tu niliambie Bunge lako Tukufu kwamba tunavyo viwanda katika nchi yetu vinavyochakata mazao ya mifugo, kwa mfano, tunacho kiwanda cha Chobo Investment pale Mwanza kinachomilikiwa na kijana Mtanzania mzalendo ambacho kina uwezo wa kuchakata ng’ombe wasiopungua 500 kwa siku na mbuzi wasipungua 1,000 kwa siku moja. Vile vile tunacho kiwanda cha Serikali hapa hapa Dodoma kinachoitwa TMC.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bura angependa kuona kuwa viwanda hivi vinachakata mazao ya wafugaji katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Dodoma. Naomba tu nimhakikishie kuwa kiwanda cha TMC kilichosimama kwa muda kiasi, Serikali imejipanga vyema na tayari tumekirudisha katika utaratibu wa ndani ya mikono ya Serikali kwa lengo la kuhakikisha kiwanda kile kinaendelea na kazi ya kuchinja na kuchakata mifugo ya maeneo haya ya Dodoma, Singida, Shinyanga na Mwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema zaidi, pale Shinyanga tunacho kiwanda cha siku nyingi zaidi cha Tanganyika Packers ambacho kilichokuliwa na wawekezaji, tumekirudisha pia Serikalini kwa lengo la kuhakikisha kuwa kinaendelea kuchakata mifugo ya wafugaji wetu na kuuza ndani ya nchi na ziada kuweza kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na ujenzi wa kiwanda katika eneo la Ruvu. Kama nilivyojibu katika swali la msingi, ni kwamba NARCO tumeingia ubia na kampuni ya NIKAI ya kutoka Misri ambayo sasa itachukua jukumu hili lote ikiwa ni pamoja na kile kiwanda ambacho tulikianzisha pale mwanzo kuhakikisha kwamba kiwanda hiki kinajengwa kwa pamoja na kuweza kuchinja na kuchakata mazao ya mifugo inayotokana na wafugaji wetu katika Taifa letu.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Dodoma ni Jiji ambalo lina vijiji na lina vijiji 34 ambavyo tulikwishapeleka ombi kwa Wizara na Mbunge wa Jimbo hili aliwahi kutembelea maeneo hayo pamoja na Waziri mhusika na tuliomba kupatiwa umeme wa REA. Naomba wananchi wajue ni lini sasa vile vijiji 34 ambavyo tuliviombea umeme wa REA vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la mama yangu, Mheshimiwa Felister Bura kuhusu vijiji 34 vya Jiji la Dodoma ambavyo vinahitaji umeme wa REA. Kwanza nimpongeze yeye mwenyewe kwa kazi nzuri ya kuwasemea wanawake wa Dodoma lakini pia nimpongeze Mbunge wa Jimbo naye Mheshimiwa Mavunde amekuwa akifuatilia na tumefanya ziara katika Jimbo lake hili la Dodoma Mjini, Mheshimiwa Waziri na mimi mwenyewe tumetembelea Jimbo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu hivi vijiji 34 vipo katika Mpango wa Ujazilizi Awamu ya Pili. Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa tisa na tunakamilisha taratibu za manunuzi na kuanzia kipindi hiki cha mwezi wa Septemba na Oktoba tutakuwa tumeshawapata wakandarasi na kuwakabidhi site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilitaarifu Bunge lako kwa kuwa Dodoma sasa imekuwa ni Jiji na ni Makao Makuu ya Serikali, kwa kweli moja ya mikoa ambayo iko katika kipaumbele cha kusambaza miundombinu ya umeme Mkoa wa Dodoma nao upo. Hata tulivyowaelekeza TANESCO kuendelea kuwaunganisha wananchi kwa bei ya Sh.27,000, Mkoa wa Dodoma nao mpaka sasa zaidi ya wananchi 4,000 wameunganishwa hususani katika maeneo ambayo ni pembezoni mwa mji. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge Dodoma ni kipaumbele na tutaendelea kufanya kazi hiyo kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii uliyonipa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tabu wanayopata wananchi wa Urambo, wanapata wananchi wangu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jimbo la Kibakwe, Kata ya Mlunduzi ambayo ina zahanati tatu na zahanati hizi majengo yameshakamilika lakini milango, madirisha, ceiling board havijawekwa, kwa hiyo wanawake na watoto wanapata shida wakitafuta matibabu mbali na maeneo yao wakati majengo yako pale. Je, ni lini Serikali itakamilisha majengo yale ya zahanati ya Kata ya Mlunduzi, Jimbo la Kibwakwe ili wananchi wa pale waweze kupata huduma ya karibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Felister Bura, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hicho anachosema Mheshimiwa Mbunge ndiyo uhalisia maana yeye mwenyewe anakiri kwamba almost ni kama majengo yamekamilika imebaki vitu vichache tu ili kukamilisha majengo hayo. Naomba nichukue fursa hii kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji ahakikishe kwamba tathmini inafanyika kwa sababu katika hayo ambayo anayasema ni pesa kiasi kidogo sana kinahitajika ili kuweza kukamilisha zahanati hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimtoe wasiwasi. Kama kuna mikoa yenye neema kwa sasa hivi ambayo watumishi wengi wa Serikali wanapenda kuhamia ni pamoja na Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo, adha ya ukosefu wa watumishi kwa Dodoma itabaki ni historia.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, elimu ya msingi ni kumjengea mtoto uwezo wa kujua, wa kuelewa na wa kuendelea na maisha ya elimu na ujuzi katika siku za mbele; na unapoacha kumpa mwanafunzi wa shule ya msingi mwalimu wa kumsaidia hata huko sekondari hawezi kufanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, tuliomba walimu 4,410 lakini tumepewa walimu 699 hata nusu ya kiwango tulichoomba hatujapata; na hapo kuna walimu waliostaafu, waliotolewa kwa vyeti fake, kuna wanaougua ambao wamesafishwa kwa ajili ya kuugua. Walimu 699 hawakidhi mahitaji ya walimu wa shule za msingi na kutokana na ujio wa makao makuu kuna uhitaji mkubwa sana wa walimu wa shule za msingi.

Serikali ina mkakati gani sasa wakuongeza walimu wa kutosha katika mkoa wetu wa Dodoma?

Mheshimwa Spika, swali la pili, tuna walimu 203 ambao wamestaafu ambao mahitaji yao ya fedha wanazotakiwa kulipwa ni shilingi milioni 260. Walimu hawa tangu mwaka 2014 hajalipwa stahili zao na wamekwishastaafu wapo nyumbani.

Ni lini sasa Serikali itawalipa walimu hawa 203 ambao wamestaafu wameshindwa kurudi kwao kutokana na kutolipwa stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA W. WAITARA): Mheshimwa Spika, ni kweli kwamba tulipata kibali cha kuajiri walimu 4500 lakini uhitaji wa walimu wa shule za msingi ni zaidi 66,000; uhitaji wa walimu wa sekondari ni zaidi ya 14,000; walimu 3,088 tuliwapeleka shule za msingi na walimu waliobaki ndio tulipeleka sekondari. Kwa hiyo katika hesabu hiyo katika hali ya kawaida lazima kutaendelea kuwa na upungufu na kuna Halmashauri na shule nyingine hazikupata walimu kabisa, huo ndio ukweli.

Mheshimwa Spika, lakini kama nilivyosema kwenye swali lililotangulia tuliomba kibali cha kuajiri walimu tukipata kibali hicho tunaongeza walimu lakini tutapeleka maeneo ambayo wana uhitaji makubwa ikiwepo na Mkoa wa Dodoma.

Mheshimwa Spika, swali la pili anauliza walimu wastaafu; malipo ya stahiki za walimu ziko za aina mbili, kuna malipo yanayolipwa na Halmashauri zetu lakini pia kuna malipo ambayo yanatoka katika Serikali Kuu. Katika Mkoa wa Dodoma amezunguzumza walimu 203 lakini sisi tunajua kwamba tuna walimu hapa 599 katika Mkoa huu ambao wamestaafu na wadai fedha zaidi ya shilingi milioni 652. Lakini madi yalipokuja TAMISEMI yamerudishwa kule kwa mambo manne.

Moja, ni kwamba madai hayo pia yanabidi yahakikiwe kamati za ukaguzi za mikoa na halmashauri hazikufanya hivyo; lakini jambo la pili kwa mfano nauli za walimu inabidi Wakurugenzi walipe. Wakurugenzi hawakuwa wameonesha wana mkakati gani wa kulipa walimu wastaafu fedha kutoka kwenye mipango ambayo ni maelekezo ya Serikali; lakini jambo la tatu ni lazima fedha hizo baadhi ya watumishi waliomba wameletwa kwamba wadai wengine wanastaafu mwaka 2019 yaani mwaka Juni kimsingi walikuwa hawajastaafu. Sasa tulipoangalia namna ya ukokotoaji wa zile nauli kwamba nani analipwa nini kutoka wapi kwenda ilikuwa imekosewa.

Mheshimwa Spika, kwa hiyo tukarudisha madai hayo katika viongozi wetu wa Mikoa na Halmashauri wayafanyie kazi tutawasiliana na Wizara ya Fedha, ukweli ni kwamba wataafu wa Serikali wakiwemo na walimu baada ya kufanya kazi kubwa kutumikia taifa hili kwa unyenyekevu mkubwa na uaddilifu mkubwa ni lazima walipwe stahiki zao.

Kwa hiyo, naomba kwa Wakurugezi wahakikishe kabla ya kuleta madai ni lazima wahayahakiki ili kondoa usumbufu ambao walimu wetu na wastaafu wengine wanaupata, ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu Mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya Nyongeza. Kwa kuwa Mfalme wa Morocco alikubali kujenga Uwanja wa Michezo wa Kimataifa hapa Dodoma:

Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari kuwasiliana na Serikali ya Morocco ili ujenzi uanze mapema iwezekavyo?

Kwa kuwa Dodoma ndiyo Makao Makuu: Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanja vingine vya michezo ili ikiwezekana Tanzania ije ipate nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Michezo ya Kimataifa.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, mawasiliano baina ya Serikali mbili za Tanzania na ile ya Morocco yanaendelea na ni tumaini letu kwamba muafaka utafikiwa mapema iwezekanavyo kuhusu mradi huu wa ujenzi wa uwanja wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa bado mpango wa kujenga uwanja mpya wa Dodoma unaendelea, Mheshimiwa Mbunge avute subira kwa sasa Serikali ikamilishe kwanza mradi huo na kisha Serikali itaweza kufikiria kujenga viwanja vingine zaidi na siyo lazima iwe Dodoma pekee, bali hata miji mingine inayozunguka Makao Makuu ya nchi itafikiriwa.