Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Felister Aloyce Bura (28 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kazi nzuri, kadhalika na Watendaji wa Wizara hii. Suala la Makaa ya Mawe, Mchuchuma na chuma cha Liganga, Ludewa ni la muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hakuna maelezo yanayojitosheleza kuhusu utekelezaji wa mradi. Kila kipindi cha bajeti, maelezo ni hayo hayo ya Kamati ya Watalaam kupitia mapendekezo ya mwekezaji. Serikali ieleze Bunge lako Tukufu tatizo la uwekezaji Mchuchuma na Liganga. Tunajenga reli tunahitaji chuma! Tutaagiza chuma kutoka nje ya nchi wakati Mungu katujaalia chuma Liganga!

Mheshimiwa Naibu Spika, CAMARTEC ni kiwanda kinachotengeneza zana za kilimo. Hata hivyo, vifaa vya CAMARTEC havipatikani kwa wingi kwa wakulima; wangeweza kufanya kazi kubwa na kwa wepesi zaidi kwa kutumia vifaa vya CAMARTEC; vifaa vya kupandia, kupalilia, kuvunia na kuchakata mazao. Kwa kuwa viwanda vingi vya hapa nchini vinategemea malighafi ya mazao ya hapa nchini, naomba Serikali kuhakikisha kuwa vifaa vinavyoweza kumrahisishia mkulima kazi, viuzwe kwa wingi na kwa bei nafuu kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania tunatamani kuwa na viwanda vingi kila Wilaya au kila Mkoa, lakini je, tumejiandaa vipi kuhusu malighafi, barabara, umeme, mifugo bora, mazao bora na yanayolimwa mwaka mzima na kadhalika? Maandalizi yanahitajika sana kwa wananchi kulima mazao bora yanayolimwa mwaka mzima, ufugaji wa kisasa na umeme usio na shaka kwa wenye viwanda na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiamini Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo ni kukumbushana mambo muhimu kwa maandalizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, waliouziwa viwanda na kuvigeuza maghala na vingine havitumiki kabisa: Je, Serikali inasema nini juu ya viwanda hivyo? Naomba maelezo ya Kiwanda cha Maziwa Utegi, Rorya kilichobinafsishwa na kilikuwa na mali nyingi na mpaka sasa hakifanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tuna mifugo ya kutosha na tungeweza kuuza bidhaa/mazao ya mifugo na kuingiza fedha nyingi nchini. Tatizo letu ni viwanda vya mazao ya mifugo. Hatuna viwanda vya nyama, ngozi, maziwa na kadhalika. Serikali ina mpango gani wa kuanzisha viwanda vya kusindika nyama, maziwa na ngozi? Viwanda vilivyopo vya watu binafsi havikidhi mahitaji ikilinganishwa na mifugo iliyopo. Naamini tukitumia vizuri Sekta ya Mifugo kelele/ ugomvi kwa wakulima na wafugaji ungekwisha kwa amani na kwa urahisi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inafanya kazi nzuri kwa maendeleo ya Taifa hili. Mifuko hiyo imejenga majengo makubwa mazuri katika miji yetu; na kwa sababu mifuko hiyo, inatarajia kujenga viwanda katika maeneo mbalimbali. Kwa taarifa zisizo rasmi, Mfuko wa PSPF haupo vizuri sana kifedha: Je, utakuwa na uwezo wa uwekezaji kama Hotuba ya Mheshimiwa Waziri inavyojieleza ukurasa wa 170?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na nichukue nafasi hii kuunga mkono azimio ambalo lipo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tangu mwaka 1973 Mji huu wa Dodoma ulishapangwa kuwa Makao Makuu. Umechukua muda mrefu sana takribani maisha ya mtu mzima Serikali ya Tanzania kuhamia katika Mji wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kwa maamuzi haya ya haraka na mazito aliyoyachukua kuhakikisha kwamba Serikali sasa inahamia Dodoma. Naamini Marais waliomtangulia awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne walifanya kazi kubwa ya maandalizi, naye amekuja kuhitimisha lile lililokuwa hamu ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ramani au master plan iliyojenga Abuja Nigeria, ilikuwa master plan ya Mji wa Dodoma. Ukienda Abuja, unaiona Dodoma ambavyo ingekuwa katika miaka hiyo. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwamba amewachukuwa wataalam wengi wa ardhi, amewapeleka maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba Mji wa Dodoma unakuwa tofauti na mikoa mingine kwa sababu ni Mji Mkuu uliosubiriwa kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena Mheshimiwa Rais kwamba ametoa fedha kwa ajili ujenzi wa stand ya mabasi ya kisasa ambayo litajengwa katika eneo la Nane Nane.

Pia tunajenga uwanja wa michezo wa kisasa ambao utajengwa hapa Dodoma na utachukua takribani watu zaidi ya 100,000. Pia tuna soko la kisasa ambalo halijawahi kujengwa Tanzania katika Mkoa wowote, ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi na ameomba msaada kutoka kwa watu wa Morocco kwa ajili ya ujenzi wa uwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa Muswada wa Sheria uje kwa ajili ya kuutambua sasa Mji wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali. Naiomba sasa Serikali ifanye haraka kuleta huo Muswada ili sasa Dodoma hata atakapokuja Rais mwingine asiyependa Mkoa wa Dodoma au Mji wa Dodoma, basi asipate nafasi ya kuhamisha Makao Makuu kupeleka Mkoa mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana hili azimio na ninaunga mkono azimio hili lililoko mbele yetu.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema aliyonijalia. Nawashukuru wanawake wa Dodoma kwa kunipenda tena na kunichagua kuwa Mbunge lakini pia Chama changu cha Mapinduzi.
Nawapongeza sana Watanzania kwa uamuzi wa dhati walioufanya kwa kuichagua tena CCM kuitawala nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Goodluck amenifurahisha, nampongeza sana. Tunachofanya leo ni kuisaidia Serikali. Wameleta mwelekeo wa Mpango na tunatakiwa tujadili na kuwapa mawazo mapya ni wapi wanaweza wakapata mapato zaidi ili matumizi yaendane na mapato. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, hiyo ndiyo kazi kubwa tuliyonayo hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma taarifa ya Serikali na nimeona jinsi sekta ambayo Watanzania ni wengi ilivyochangia kwa kiasi kidogo sana, 4% ya pato la Taifa, ni sekta ya kilimo, uvuvi na misitu. Najiuliza kwa nini sekta ya kilimo na ufugaji ichangie kidogo? Tanzania kila kona kuna ugomvi wa wakulima na wafugaji ina maana tuna mifugo mingi ambayo haileti faida ndani ya nchi, haichangii kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa. Ndiyo maana mifugo, kilimo, misitu, uvuvi imechangia 4% tu. Lazima tutafute ni wapi tulipokosea mpaka sekta hii isichangie pato la Taifa kwa kiasi kikubwa. Kuna mazao yanayotokana na mifugo mfano maziwa, ngozi, nyama na kuna mifugo mingi sana ndani ya Tanzania. Nadhani Serikali itafute sasa namna ya kushughulikia matatizo yaliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suluhisho siyo kupima ardhi ni kuwasaidia wafugaji kupunguza mifugo. Nilikwenda Mkoa wa Arusha kipindi fulani tukaambiwa, tena alisema mfugaji mwenyewe yeye ana ng‟ombe 10,000. Kama mtu mmoja ana ng‟ombe 10,000 na hana jinsi ya kupunguza mifugo yake lazima ugomvi wa wakulima na wafugaji utaendelea lakini hatuwezi kuona faida ya kuwa na mifugo mingi. Vilevile hatuwezi kuona faida ya wavuvi wakati maziwa tunayo yamezunguka nchi yetu; tuna Ziwa Tanganyika, Ziwa Viktoria lakini tuna bahari. Nadhani Serikali iangalie namna ya kutumia sekta hii kuzalisha kwa wingi. Tupate viwanda vya nyama, viwanda vya maziwa, viwanda vya kusindika samaki, viwanda vya matunda, tutaona ugomvi wa wafugaji na wakulima hautakuwepo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumemuudhi Mwenyezi Mungu, siku hizi mvua hainyeshi inavyotakiwa. Kwa hiyo, tukiendelea na kilimo cha kutegemea mvua hatutafika mbali. Ndiyo maana mvua isiponyesha vizuri baada ya muda mfupi wananchi wetu wana njaa. Kwa hiyo, lazima tutafute namna ya wakulima wetu kuwa na ukulima endelevu. Bila hivyo, kila mwaka tutakuwa tunalia hatuna chakula, sekta ya kilimo haijachangia kwa kiasi kikubwa lakini hatuna mipango mizuri kwa wakulima na kwa wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna fukwe nzuri sana kuanzia Mtwara hadi Tanga, tunaweza kuzalisha kupitia fukwe zetu. Siyo lazima Serikali ifanye, tunaweza tukaingia ubia na watu binafsi. National Housing ni mfano mzuri, wana ubia na makampuni na watu binafsi na tunaona National Housing inavyofanya kazi kubwa katika nchi hii. Kwa nini tusiungane na sekta binafsi katika kuhakikisha kwamba nchi yetu tunapata mapato ya kutosha kwa ajili ya huduma za jamii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna madeni mengi. Wakandarasi waliotengeneza barabara wanatudai, wanaopeleka vyakula katika shule, inawezekana Mheshimiwa Magufuli amelipa hilo deni, lakini kipindi cha nyuma tulikuwa tunadaiwa na Walimu walikuwa wanadai kwa sababu hatuna mapato ya kutosha. Pia matumizi yetu, hata ukiangalia taarifa ya Waziri, ni makubwa kuliko mapato tuliyonayo, kwa nini matumizi yetu yasiendane na mapato? Hata kama nakisi inakuwepo, isiwepo nakisi kubwa kama iliyopo kwenye ripoti ya Serikali. Tusipoangalia namna tunavyotumia na namna tunavyopata mapato kwa kweli tutabaki kila siku miradi yetu ya maendeleo haikamiliki tukitegemea fedha kutoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaolima Nyanda za Juu Kusini wanalima vizuri lakini masoko pia bado shida. Mwaka jana walipiga kelele sana mahindi yanaoza Mbeya, Iringa, Rukwa na Ruvuma. Lazima tutafute masoko ya uhakika kwa wakulima wetu. Tanga kuna matunda mengi lakini hawana soko, hakuna kiwanda. Bado kuna haja ya kuwa na uhakika wa masoko ya wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeangalia pia Kitabu cha Wizara, suala la utalii sikuliona vizuri. Kwa sababu utalii unachangia kwa asilimia kubwa katika pato la nchi yetu lakini sikuona mikakati iliyowekwa na Serikali kwa ajili ya kutangaza utalii wa ndani na wa nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze pia kuhusu retention kwa mashirika haya yanayoshughulika na mambo ya utalii; ukiondoa retention kwamba fedha zote ziende Hazina, TANAPA itakufa, Ngorongoro itakufa. Kwa hiyo, niombe kabisa suala la retention liangaliwe kwa mashirika ambayo aidha hayafanyi vizuri, lakini mashirika kama TANAPA, Ngorongoro, ambayo retention inawasaidia pia kutengeneza miundombinu kwa ajili ya watalii naomba retention yao wasinyang‟anywe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja nirudi kwangu Dodoma ambako wanawake wanapata tabu ya kubeba ndoo na kuamka alfajiri kwa ajili ya kutafuta maji. Suala la maji Wilaya ya Bahi tumeongea tumechoka. Tuliomba shilingi milioni 500 mwaka jana mpaka bajeti imemaliza muda wake mpaka tukaanza bajeti nyingine hatujawahi kuona hayo maji. Bahi maji ni ya chumvi mno hayafai kwa matumizi ya binadamu. Niiombe Serikali, wanapoangalia namna ya wananchi au miji ile midogo iliyoanza hivi karibuni kupata maji suala la Bahi lisiwekwe pembeni. Shida ya maji Kondoa ni ya muda mrefu, tumeshalizungumza mpaka tumechoka. Suala la maji Wilaya ya Chemba wameshindwa hata kujenga Wilaya, hakuna maji pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Waziri wa Maji atakumbuka tumepiga kelele sana kuhusu suala la kilimo cha umwagiliaji na tuliambiwa bwawa kubwa sana linachimbwa pale Farkwa na bwawa lile lingesaidia wakulima wa mpunga wa Bahi, wakulima wa Chamwino, wakulima wa Chemba na baadhi ya wakulima wa Kondoa lakini mpaka navyozungumza hilo bwawa utaratibu wa kujengwa sijauona. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ni kengele ya pili, lakini taarifa hii haina mpango wa Serikali kuhamia Dodoma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema aliyotujalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza hotuba za Mawaziri, Mwenyekiti wa Kamati, Kambi ya Upinzani na kuna hotuba nzuri ambazo zinaleta msisimko kwamba, Watanzania hakika Rais hakukosea kuwateua hawa Mawaziri kuwa Mawaziri katika Wizara wanazozihudumia. Niwahakikishie tu wale ambao wana wasiwasi kwamba, watumishi hewa wataendelea katika Serikali yetu, haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale waliokuwa wanakwamisha tatizo hili la watumishi hewa kuondoka katika Serikali yetu wameondoka na wengine tunao humu humu ndani. Naomba pia Serikali iangalie namna sasa ya kuhakikisha kwamba hizi milioni 50 ambazo zitakwenda kila Kijiji ziwe na utaratibu maalum wa kuzifuatilia. Vijana au wanawake na makundi mbalimbali ambayo yamekwishaunda SACCOS yao na SACCOS yao ina uongozi unaoaminika, wao wapewe hizi milioni 50 kwa utaratibu maalum ambao pia utaruhusu kufuatiliwa kwa karibu kwa sababu hizi hela najua ni revolving fund, wengine watahitaji hizi fedha kwa ajili ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi kabla hazijatolewa makundi yapate elimu nzuri na zaidi ya yote yawe na uongozi, pia zifuatiliwe kwa karibu kuhakikisha kwamba, hazitumiki ovyo kama fedha ambazo zimewahi kutolewa na Serikali na hatukujua zimetumikaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Manispaa yangu ya Dodoma Mjini, tuna upungufu wa watumishi 590 wa kada mbalimbali. Kukosekana kwa Watumishi hawa kunafanya maendeleo yasifuatiliwe kwa ukaribu zaidi. Mheshimiwa Waziri unayehusika na utumishi wa umma nakuamini kwa kazi zako nzuri na ofisi yako kwa sasa naiamini, kwamba tutakapoleta barua kwani tuliandika barua mwezi wa Machi mwaka huu hatutajibiwa, naomba sasa nitakapokuletea hiyo copy ya barua uhakikishe kwamba wale watumishi wa kada mbalimbali katika Halmashauri yetu ya Manispaa ya Dodoma tunawapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ukosefu wa Walimu 105 wa Sayansi na Walimu wa sayansi wamesomeshwa hapa UDOM (University of Dodoma), siyo vizuri Manispaa ya Dodoma tukakosa Walimu 105 wa Sayansi ambao wangewasaidia wanafunzi wetu. Sasa hivi tunajenga maabara na maeneo mengine katika Manispaa yetu tumekwishakamilisha maabara, lakini Walimu 105 hawapo. Nakuomba Waziri unayehusika na Wizara hii tusaidie kupata Walimu hao 105 na wale watumishi 590 hasa wa kada za chini ambao ni watendaji katika vijiji vyetu, watendaji katika mitaa yetu, watusaidie katika kusimamia maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Dodoma haina ofisi. Tunafanya kazi katika shule iliyokuwa Sekondari ya Aghakan na wameshatuandikia barua wakitaka majengo yao. Iko siku tutakuta vifaa na samani na kila kitu vikiwa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kupewa barua na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi Dkt. Kawambwa kwamba tunapewa ofisi ambayo inatumika na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa sasa, lakini kwa sababu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hana ofisi na jengo lake linalojengwa kila mwaka tunaomba fedha, lakini fedha zinazoletwa ni kidogo mno hazisaidii kitu chochote, naiomba Serikali yetu sikivu, tumeomba pesa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Manispaa, tumeomba pesa kwa ajili ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, tunaomba hata kama ni floor moja ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hata kama ni ground floor, basi ijengwe imalizike ili Mkuu wa Mkoa aweze kuhamia kwenye Ofisi yake na Halmashauri ya Manispaa wapate ofisi yao. Pale tunapofanya kazi kama Manispaa huwezi kuongeza hata kibanda cha mlinzi kwa sababu majengo yale siyo ya kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, hata hospitali ya Wilaya hatuna. Tumeomba bilioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya, Dodoma imekua, watu wako wengi, Wabunge wenyewe mmeongezeka, kwa hiyo hatuna hospitali ya Wilaya. Naomba sana kwamba zile bilioni 25 tulizoziomba, basi tufikiriwe kupewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wilaya ya Bahi hawana Hospitali, asilimia 80 ya wagonjwa wanaokuja Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wanatoka Wilaya ya Bahi, kwa sababu hawana hospitali ya Wilaya. Naiomba Serikali yetu sikivu waone namna ya kujenga Hospitali ya Wilaya Bahi na hospitali ya Mkoa ibaki kama hospitali ya rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maslahi ya Watumishi wa kada za chini sasa kwa sababu Mheshimiwa Rais ameagiza kwamba kusiwepo madeni kwa watumishi kama Walimu, Manesi, Maafisa Ugani, Polisi na kadhalika, Serikali ione kwamba madeni yale ya nyuma ambayo wanadaiwa na watumishi yahakikiwe na kama yamekwisha hakikiwa basi Watumishi walipwe haki zao maana naiamini Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwamba inafanya kazi kwa uhakika na kwa juhudi nyingi, kuhakikisha kwamba watumishi wanapata maslahi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu ya Chamwino tuna jengo la Halmashauri pale. Lile Jengo Mkandarasi anadai bilioni tatu ili kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Naomba sana Serikali ikamlipe Mkandarasi anayejenga Ofisi ya Halmashauri ya Chamwino ili watumishi wale wawe katika jengo moja, kwa sababu Watumishi wa Wilaya ya Chamwino wamesambaa, wengine wako Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, wengine wanafanya kazi kwenye nyumba za watu binafsi, wengine wapo kwenye nyumba zisizoeleweka, lakini Mkandarasi akipata bilioni tatu alizoziomba jengo lile litakuwa limekamilika.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yetu ya Chemba pia hatuna Hospitali, hatuna nyumba za Watumishi, hatuna maji, hatuna kitu chochote. Naiomba Serikali yetu sikivu sasa ione namna kwa sababu Wilaya ya Chemba ni Wilaya mpya. Pia tuna mradi wa umwagiliaji wa maji wa GAWAE tuliomba milioni 533. Naiomba Serikali ione namna ya kupata hizi fedha ili kazi ya umwagiliaji kwa wananchi maana Dodoma ni Mkoa kame sasa iweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kuwashusha wanawake wa Wilaya ya Bahi ndoo vichwani. Tuliomba shilingi milioni 400 kuvuta maji kutoka katika Kijiji cha Mkakatika. lakini tulipewa milioni 100 tu. Naiomba Serikali katika bajeti hii itukumbuke tunatamani wanawake wa Wilaya ya Bahi katika eneo la Makao Makuu ya Wilaya wapumzike kubeba ndoo vichwani. Tukipata milioni 400 tutapata maji Bahi katika Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia hotuba za upande wa pili katika Bunge hili wakijinasibu kwa mambo mengi, kwamba Serikali inagawa maeneo na kulipa watumishi pesa nyingi na kuweka miundombinu badala ya kusimamia miradi michache ya maendeleo, hatuwezi kuacha kuwalipa watumishi, miundombinu ndiyo maendeleo…
(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda mchache sana. Nimeangalia katika hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuangalia fedha za zahanati, sikuona mahali popote ambapo kuna fedha za ujenzi wa zahanati na Wizara ya Afya pia sikuona fedha za ujenzi wa zahanati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utumie Kiti chako, Kamati ya Bajeti irudi ikapange fedha za zahanati nchi nzima. Tukitaka mafanikio katika kazi zetu ni lazima tufuate utaratibu uliowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Bima ya Afya, Mkurugenzi aliyekuwepo Mr. Humba alistaafu mwaka 2013, akakaimishwa Miss Mdee akatolewa, akakaimishwa mwingine Mr. Mhando akatolewa. Bima ya Afya haina Bodi, jamani tunategemea ufanisi hapo kweli! Hatuwezi kupata ufanisi! Wale watumishi kila mtu anaogopa kutumbuliwa! Mheshimiwa Waziri amteue Mkurugenzi Mkuu wa Bima ya Afya, Bodi ya Bima ya Afya iko chini ya mamlaka yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya MOI aliyeko anakaimu, tunategemea ufanisi kutoka wapi? Taasisi ya J. K. Kikwete, taasisi ile aliyeko Profesa Janabi anakaimu. Tunategemea ufanisi kutoka wapi? Kuna kazi gani au kuna kazi gani kuwateua wale kama wanafaa? Hakuna Bodi ya Muhimbili. Mkurugenzi wa Muhimbili anakaimu. Tunategemea ufanisi kutoka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali yetu ya Mirembe ina Manesi 89 kati ya Manesi 700. Jamani wale wana-deal na watu wasio na akili timamu. Siku moja Nurse, tena mwanamke, aliniambia mgojwa wa akili alitaka wafanye ngono. Nurse anafanya kazi tangu saa 1.00 mpaka saa 12.00 anawahudumia wagonjwa 20 kwenye wodi moja. Wagonjwa wenyewe hawana akili timamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ummy nampenda sana, lakini ataniambia ni lini atawapeleka wafanyakazi Mirembe? Bodi ya Mirembe haipo! Kwa hiyo, hata ufanisi mkubwa hauwezi. Wale watu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Hebu awafikirie watu wa Hospitali ya Mirembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali yangu ya Mkoa wa Dodoma aliitembelea Mheshimiwa Waziri wiki iliyopita na tukamwonyesha jengo ambalo lipo mbele yake, lile jengo la wodi ya wazazi lina vitanda 180, wodi inayotumika sasa hivi ina vitanda 18 tu, wanawake waliozaa wanalala wawili wawili. Siyo haki!…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu wangu kwa kunipa nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi pamoja na timu yake kwa kazi nzuri anayoifanya, hakika Mheshimiwa Lukuvi anatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia juu ya Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi. Nadhani wakala ilianzishwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na hasa wale wenye kipato kidogo; lakini ofisi za wakala ziko Dar es Salaam, wakala hana ofisi wilayani, mikoani lakini wananchi wenye shida ya kujenga nyumba zenye gharama nafuu wako wilayani, wako vijijini, wako mikoani. Sasa sijui ofisi hii inafanya nini Dar es Salaam na hata katika wilaya zetu hatujawahi kuwaona wala kusikia habari zao, tunazisoma habari za kwenye vitabu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wakala hawa waje Dodoma; Dodoma tuna mahitaji makubwa ya kujenga nyumba za gharama nafuu na hasa kwa matofali haya ya kufungamana; vijana wapo watapata ajira kutokana na kazi hii ya kufyatua hayo matofali, watajenga nyumba za kudumu, nzuri ambazo hazitawasumbua kujenga tena baada ya kipindi kifupi. Naomba wafanye kazi hiyo Dodoma kama mkoa wa mfano na wananchi watafaidika na shughuli watakazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie pia pale alipoachia Zainab kuchangia kwamba mabaraza yetu yanahudumiwa na Wizara tatu; Mabaraza ya Kata yapo chini ya TAMISEMI, Mabaraza ya Wilaya yapo chini ya Wizara ya Ardhi, lakini mwananchi anapokata rufaa anakwenda Wizara ya Sheria na Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Kurekebisha Sheria waliwahi kufanya kazi hii na walileta mapendekezo Serikalini, sasa Waziri atatuambia mapendekezo yalifanyiwa kazi? Mabaraza yetu ya Kata hawana mafunzo, hawana hata vitabu rejea yaani ukiwaambia warejee kwenye kesi ambayo iliwahi kutokea hawana pa kurejea. Kwa hiyo, wanafanya kazi kutokana na mazoea na akili ya mtu inavyomtuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani kuna haja ya Sheria namba tano kufanyiwa marekebisho makubwa. Pia hawa Wajumbe wa Baraza hata ukisema Mwenyekiti anapokwenda kwenye eneo la tukio la baraza hawana ulinzi hawa watu. Kwa hiyo, wananchi wanaweza wakawafanyia fujo na kuwapiga hata kuwafanyaje wanavyoweza kwa sababu hawana ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia Mahakama ya Ardhi wapangiwe muda wa kumaliza kesi. Mahakama ya Rufaa zingine wamepangiwa muda wa kumaliza kesi; kesi 200 kwa mwaka, lakini Mahakama ya Ardhi hatujui na hawajapangiwa muda wa kukamilisha kesi zao na kusikiliza kesi kwa sababu Mahakama ya Ardhi kuna kesi nyingi sana zinazosubiriwa kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa wa Ardhi na wa Mipango Miji; hapa ndiyo kuna majipu ya kutumbuliwa. Mheshimiwa Lukuvi hapa ndiyo kuna majipu yaliyoiva kwa sababu Maafisa Ardhi wanagawa ardhi eneo ambalo wanajua ni eneo la wazi, wanagawa ardhi eneo ambalo wanajua watajenga shule, wanagawa ardhi maeneo ambayo ni ya soko; lakini wanafanya makusudi na ndiyo maana watu wanavunjiwa bila sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu alievunjiwa analeta hati yake kuonesha kwamba anamiliki kihalali eneo hilo, lakini Maafisa Mipango Miji wapo, Maafisa Ardhi wapo. Nikimsikia Mheshimiwa Waziri amewatumbua hawa watu nitafurahi sana kwa sababu wapo ambao wanafanya makusudi na kuwapa wananchi hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hati ya umiliki wa ardhi ipo hata kwa Serikali zetu. Safari hii ripoti ya CAG, Halmashauri zetu walipata hati za mashaka kutokana na halmashauri zetu kutokuwa na hati miliki ya maeneo yao. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hili lifanyiwe kazi haraka sana ili halmashauri zetu wawe na hati za kumiliki mali hasa ya ardhi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Dodoma, Dodoma tuna suala la Mkungunero halikuhusu sana lakini linakuhusu kwa sababu wewe ndiye Waziri wa Ardhi. Mkungunero pale vita vilishawahi kutokea, watu wakapigana, watu watatu wakauawa. Wananchi wa Mkungunero walishaandika barua kwa Waziri Mkuu, Mawaziri waliopita kabla yake walikwenda Mkungunero, tulikwenda nao, lakini mgogoro wa Mkungunero haujakwisha mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro mkubwa kati ya Hifadhi ya Mkungunero na vijiji 17 vya Chemba na Kondoa. Sasa hivi wananchi wa Kondoa hawawaruhusu Maafisa Wanyamapori kufanya kitu pale. Kilomita 50 tu tuliomba ili wananchi waweze kulima, lakini imekuwa kazi miaka nenda rudi, miaka nenda rudi hili suala halijakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri suala la Mkungunero liishe sasa. Tumewaalika Mawaziri wa Maliasili, Waziri Mkuu alikwenda, yeye mwenyewe tunamwomba aende ili suala la Mkungunero na wananchi liishe Vijiji 17 wanagombea ardhi pale, wanaomba kilomita 50 tu waweze kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Dodoma Mjini, suala la CDA na Manispaa tumechoka nalo, wananchi wamechoka nalo. Inawezekana limetuchosha kwa sababu CDA hamuwapi fedha za kutosha, wanabomoa nyumba za watu bila fidia, wanachukua ardhi za watu bila fidia, wanalipa fidia kwa ardhi waliyotwaa kwa tathmini ya mwaka 2002, 2005 sio haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimsihi na nimwombe Mheshimiwa Lukuvi anajua sana suala la CDA na suala la ardhi ya manispaa, Mheshimiwa Rais alipokuja hapa wakati wa kampeni alisema CDA, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na halmashauri watakaa na kushughulikia suala la ardhi ya Manispaa ya Dodoma, nimsihi sana na Waziri wa TAMISEMI kama hayupo Naibu wake yupo na Mheshimiwa Jenista yupo, niwaombe sana washughulikieni suala la CDA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Dodoma wanaipenda sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi na ndiyo maana tunapata kura nyingi, lakini sasa hili la CDA halijashughulikiwa, namsihi sana Mheshimiwa Waziri ashughulikie hili suala la CDA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo la Kongwa, Kata ya Dabalo na Kata ya Segala wana ugomvi mkubwa sana na watu wa Kongwa mpaka kati ya Kata ya Dabalo na Segala na watu wa Kongwa, ni mgogoro wa muda mrefu. Wananchi wameacha kulima pale kwa ajili ya mgogoro ule unaoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mkoa mmoja lakini mgogoro ule umedumu kwa muda mrefu hakuna namna ya kumaliza mgogoro ule. Nakusihi ndugu kwa ndugu hawaongei, ndugu kwa ndugu wanatafutana, ndugu kwa ndugu wamekasirikiana kwa sababu ya mgogoro uliopo pale Kata ya Dabalo, Kata ya Segala na Wilaya ya Kongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiw;a Waziri ana uwezo huo,aumetatua migogoro mingi katika nchi yetu, huu mgogoro hautamshinda, nimwombe na ikiwezekana twende pamoja kwani kuna shida gani, twende pamoja mimi na yeye Mheshimiwa Lukuvi tukamalize suala hili, tukamalize mgogoro wa wananchi. Mimi nipo tayari, Mheshimiwa Lukuvi anajua kwamba nipo tayari kwenda pamoja naye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa suala la National Housing. National Housing wamefanya kazi kubwa na inayoonekana. Kabla ya mwaka 2007/2008 National Housing walikuwa wanapata ruzuku kutoka Serikalini, lakini baada ya kuingia Mkurugenzi Mchechu, National Housing imebadilika kwa kiasi kikubwa. Wanajenga nyumba mijini…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini wapunguzieni VAT ili tununue nyumba za National Housing.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nisamehe. Ni mdogo wangu, Mheshimiwa Dokta Ashatu Kijaji, Mbunge wa Kondoa Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yoyote haiwezi kuendelea bila kulipa kodi, kodi ndiyo msingi wa maendeleo. Kwa hiyo, kila mwananchi anatakiwa kulipa kodi kabla hajadai huduma lakini Watanzania tumezoea kudai huduma bila kulipa kodi. Tunadai hospitali, barabara, maji, umeme lakini ni wangapi wanaolipa kodi kwa uhakika? Wafanyakazi ni walipa kodi kwa uhakika kwa sababu pesa zao hawazikamati mkononi, wanakatwa kodi moja kwa moja. Ifike wakati sasa wananchi wa Tanzania tufurahie kulipa kodi ili maendeleo tunayoyataka tuyapate kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, sipingani na azma ya Serikali ya kuanzisha viwanda lakini tunapofikiria kuwa na viwanda tufikirie pia kuwa na malighafi. Tunasema mazao yanaoza; mazao gani yanayooza? Tunasema matunda yanaoza Muheza, Ukerewe na maeneo mengi lakini je matunda haya yapo mwaka mzima kiasi kwamba tukiwa na viwanda vitano vya kukamua juice watapata malighafi ya kutosha? Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mashamba makubwa kwa ajili ya malighafi kwa viwanda tunavyovipigia kelele? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Serikali iweke mkakati madhubuti wa kuwa na mashamba makubwa ambayo pia yatazalisha ajira. Kwa hiyo, tuwe na mashamba makubwa tukilenga viwanda ambavyo tunataka kuvianzisha lakini tukisema tunaanzisha viwanda ku-create ajira bila malighafi viwanda hivyo haviwezi kufanya kazi. Kwa hiyo, tulitazame suala hili kwa upana wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa mkulima ni nani anayejali mkulima huyu kalima nini? Je, katumia mbolea? Je, analimaje? Je, anatumia zana gani? Maafisa Ugani wetu hakuna anayejali na hawatoshi hasa katika maeneo yetu ya vijiji. Kwa hiyo, kuna haja Maafisa Ugani kuwaweka wakulima katika hali ya kujua kwamba sasa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu inatakiwa na wawaelekeze wakulima kulima kwa lengo la kupata mapato zaidi kwa ajili ya kuendeleza viwanda vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna suala la kupata mapato, tumesema tunataka kodi ili tuwe na fedha za maendeleo kwa ajili ya Taifa letu. Hata hivyo, kuna suala la ubia kwa maana ya Serikali kuingia ubia na mashirika mbalimbali na watu binafsi lakini utekelezaji wa suala hili ni mdogo sana. Suala la ubia tumeliongea kwa muda mrefu sana katika Bunge hili lakini ni makampuni mangapi yameingia ubia na Serikali? Je, ni mashirika mangapi yameingia ubia na Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mdogo tu, sisi tulipelekwa Malaysia mwaka 2008 ili Wamalay waje wajenge barabara ya Chalinze – Dar es Salaam wakishirikiana na NSSF mpaka leo hatujaambiwa tatizo ni nini? Tungepata pesa kwa sababu wale wange-charge kodi kidogo kwa ajili ya kuendesha ile barabara lakini mpaka leo suala la ubia linakwenda taratibu mno katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, NSSF walikubaliana na watu wa Malaysia kwamba watajenga magorofa 25 Ilala Mchikichini mpaka leo hakuna kinachoendelea. Hatuwezi kusema tunataka maendeleo, tunataka ubia wakati utekelezaji wa suala la ubia linaenda taratibu mno tatizo ni nini? Lazima tujue tatizo liko wapi? Hata tunaposema tunafufua viwanda, hawa watu wa viwanda wameulizwa mnakumbana na matatizo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujiulize walikumbana na vikwazo gani na tumeandaa akili zetu kupambana na changamoto tutakazokutana nazo katika masuala ya viwanda? Hili suala la PPP ni muhimu lazima kuliangalia. Tuwaulize NSSF kilichokwamisha ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze ni nini? Watuambie kilichokwamisha ujenzi wa nyumba zile ni nini? Tungepata mapato mengi kutokana na suala hili, naomba tuliangalie.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna haja ya kuangalia mashirika yasiyo na tija. Ngoja niwape mfano, tangu tuanzishe RUBADA wamesha-deliver nini kwa Serikali hii? Kuna watu waliomwambia Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba RUBADA tu inaweza kulisha Taifa hili lakini RUBADA iko wapi? Mpaka leo RUBADA wanapewa ruzuku. Mashirika yasiyo na tija yaondoke sasa kama kweli tunataka kupata maendeleo. Hakuna haja ya kuwapa ruzuku, wanalipwa mshahara, wanalipwa per diem za safari lakini hakuna tija, hili ni vizuri tukaliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa la fedha Tanzania shillings kutotumika katika mauzo au manunuzi, tatizo ni nini? Suala hili tumelisema mpaka tumechoka. Naomba Waziri wa Fedha hebu suala hili lifanyiwe kazi sasa, nchi nyingi zilizoendelea wanathamini pesa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tozo kwa watalii limeongelewa sana. Wabunge tujiulize kuna makampuni yalirudisha vitalu 13, kwa nini vilirudishwa? Lazima tujiulize kwa nini vilirudishwa ili tujue tanaanzia wapi kuliko kuanza na tozo wakati wenzetu Kenya wameondoa tozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme lingine, tumechoka sisi wa Dodoma kila siku tunaambiwa Makao Makuu ya Serikali ni Dodoma lakini hatuoni kinachoendelea. Mashirika ya Umma, Ofisi za Serikali, mnajenga majengo Dar es Salaam, hivi mna dhamira ya dhati ya kuhamia Dodoma? Mimi nilileta Hoja Binafsi ili mtuambie kwa nini hamtaki kuhamia Dodoma? Mnatupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, hatutaki! Mtuambie kwa nini hamtaki kuhamia Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hana hata ofisi, Manispaa tutakwenda kumfukuza pale alipo ili mumtafutie pa kufanyia kazi zake. Hamtaki kuhamia Dodoma na hamtaki kumjengea Mkuu wa Mkoa ofisi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mkungunero linatuumiza, Serikali hamtaki kulizungumza kwa nini? Wananchi waliomba heka chache sana kwa ajili ya kilimo, Maaskari wale wa Wanyamapori hawapiti kwa wananchi, hawapiti pale barabarani kwa sababu kuna uhasama mkubwa na Serikali haitaki kulishughulikia. Ninawasihi hebu suala la Mkungunero lifike mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake wa Mkoa wa Dodoma hawajatua ndoo vichwani na mvua inanyesha miezi miwili tu hapa Dodoma. Ukisema suala la maji, Waziri wa Maji anaturemba tu hatuelewi anachotusaidia. Tunaomba sasa, kama kweli Serikali ina dhamira ya kuhamia Dodoma tuanze kuwasaidia wananchi wa Dodoma, tumtue mwanamke wa Dodoma ndoo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake wanaamka saa tisa, ndiyo maana wanaume wa Dodoma wengine wameoa wanawake wanne, anafanyaje? Yeye ni Mkristo kila siku saa tisa mwanamke yuko barabarani kwenye maji, hatuwezi, jamani mtufikirie katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Dodoma kuna Wilaya zilizoanza; tuna Wilaya ya Chemba, Wilaya ya Bahi ilianza siku nyingi hakuna maji, hakuna umeme, Mheshimiwa Badwel ameomba mpaka amechoka, Mheshimiwa Nkamia ameomba mpaka amechoka, tatizo ni nini kwa Wilaya za Dodoma? Bahi pale maji ni ya chumvi, huwezi kuoga, huwezi kunywa hata mnyama hanywi, kila mwaka tunaomba maji Dodoma, tatizo ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini msisahau kumuongezea CAG…
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ya leo na ninakushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kabla sijasema lolote basi, niunge mkono hoja hii kabla sijasahau. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1973 Wabunge wenye akili timamu, wenye uwezo walikaa pale Karimjee wakaamua kwamba Makao Makuu ya nchi hii yaje Dodoma na tangu kipindi hicho Marais waliopita wamefanya kazi kubwa, Rais wa Awamu ya Kwanza amefanya kazi kubwa, Rais wa Awamu ya Pili amefanya kazi kubwa, Rais wa Awamu ya tatu amefanya kazi kubwa, Rais wa Awamu ya Nne amefanya kazi kubwa na Rais wa Awamu ya Tano ameamua kutekeleza yale ambayo yaliamuliwa mwaka 1973.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania kwa ujumla pamoja na sisi wananchi wa Dodoma tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa maamuzi haya. Wametekeleza dhamira ya wananchi kwa sababu ukitoka hapa Dodoma mpaka Kagera unafika siku hiyo, ukitoka hapa mpaka Songea unafika siku hiyo, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa dhamira hii ambayo wameamua kuhamia Dodoma kwa awamu na sisi tunawaunga mkono na mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao wana uwezo wa kujenga mahoteli, wana uwezo wa kujenga viwanda, wana uwezo wa kufanya miradi mbalimbali tunawakaribisha Dodoma. Kuna ardhi ya kutosha, barabara zinapitika, ukitaka kwenda Singida utakwenda kwa lami, Iringa utakwenda kwa lami, Arusha utakwenda kwa lami na Dar es Salaam utakwenda kwa lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nianzie hilo kwamba tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, lakini niombe kwa Serikali hii kwamba CDA waliopewa mamlaka ya kustawisha mji huu hawana fedha, wanatakiwa kujenga barabara, wanatakiwa kupima viwanja, wanatakiwa kuhakikisha kwamba squatter hakuna hapa, wanatakiwa kuhakikisha kwamba hakuna foleni kama Dar es Salaam lakini hawana fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu ambao umeletwa sikuona kama CDA wametengewa fedha yoyote kwa ajili ya kupanga Mji wa Dodoma. Nimeangalia katika kitabu chako ukurasa wa 51 kanda maalum ya kiuchumi sikuona kama Dodoma imewekwa katika kanda maalum kiuchumi. Kwa sababu watakaojenga viwanda katika Mkoa wa Dodoma watataka ardhi, lakini ardhi hii wanaipataje kama wenye ardhi hawatalipwa fidia, watapataje ardhi kama nyumba za wanakijiji hazitalipiwa fidia. Kwa hiyo, kuna haja ya kuweka Dodoma katika kanda maalum ya kiuchumi ili Serikali itakapoamua sasa kuhamia na wafanyabiashara mbalimbali watakapoamu kuijenga Dodoma basi iwepo fedha kwa ajili ya kutenga maeneo, iwepo fedha kwa ajili ya huduma mbalimbali, huduma ya maji taka, huduma ya maji, barabara, upimaji wa ardhi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie sasa Mpango ambao uko mbele yetu. Nimeona kwenye Mpango maeneo mbalimbali yameainishwa na nimeona mazao ambayo yameainishwa ambayo yamepewa kipaumbele, lakini naona haitioshi. Hata mipango iliyowekwa kwa ajili ya miwa, tumbaku, mpunga, lakini bado mazao kama mbaazi, chai, korosho, bado mazao mengi ambayo nilitegemea kwamba Serikali itaonesha mkazo maana asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima. Lakini kama asilimia kubwa hii ya Watanzania hawatawekewa mkakati maalum hakika hatutafaulu kwa haya ambayo tunayategemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahamasisha kujenga viwanda, lakini viwanda hivi ambavyo tunahamasisha kujenga tunategemea malighafi itoke ndani ya nchi yetu, lakini viwanda vingi ninavyoona vitakuwa vya mazao sio vya mazao ya mpunga tu au mazao ya chai au mazao ya korosho tu, lakini mazao yako mengi, lakini Tanzania wananchi walio wengi wanategemea mvua. Sasa katika karne hii ya tabia nchi inayobadilika kila siku ifike wakati kwamba tusitegemee mvua, lazima tuhakikishe kwamba kilimo cha umwagiliaji kinapewa kipaumbele katika mikoa yetu bila kujali mkoa huu una mvua au mkoa huu hauna mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea maeneo kama yale ya Rubada, maeneo ambayo Serikali ilitoa kwa ajili ya kilimo ili kuiwezesha nchi kuwa na mazao ya kutosha. Kule Kasulu kuna shamba kubwa karibu ya eka 10,000 au 5,000 wale wanaotoka Kasulu wanajua tungeweza kuendeleza yale mashamba na tukayagawa kwa wananchi au Serikali ikaona namna ya kuendeleza yale mashamba, ili tunaposema kwamba nchi iwe ya viwanda basi malighafi ipatikane nchini na Watanzania wafaidi kuwa na viwanda katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Kilimo haina mtaji wa kutosha kutoa pembejeo au kuwapa wananchi pembejeo, lakini wako wananchi wengi ambao wangependa kulima, wangependa kukopa pembejeo, wangependa kukopa matrekta, lakini benki haina fedha. Na benki ina kituo kimoja tu, kituo kiko Dar es Salaam, ukimwambia mkulima wa Kagera, atoke Kagera, Mara, Kigoma kwa ajili ya kwenda kutafuta mkopo Benki ya Kilimo Dar es Salaam, hakika ni kazi kubwa na anapokwenda Dar es Salaam hana hakika kama atapata huo mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sikivu iangalie namna ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, lakini ione namna ya kuwawezesha wakulima kusogeza huduma ya benki karibu nao. Nishauri pia kwamba miradi ile ambayo ilikwishaanza sasa ndio ikamilishwe kabla hatujaanza miradi mipya, kwa sababu tunapojirundikia miradi mingi wakati fedha hatuna za kutosha tunajikuta miradi mingi imekwama. Kwa hiyo, kuna haja ya kumaliza miradi ile ambayo tulishaanza, lakini tukatoa vipaumbele kwa miradi ambayo tunaona inaweza ikaisaidia nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kwamba lazima tujue tunapotaka kuwa na viwanda umeme tunatoa wapi? Je, umeme upo wa kutosha nchini? Ifike sasa habari ya Mchuchuma na Liganga utoe megawatt 600 zile ambazo zimepangwa, lakini tunaweza tukapata wawekezaji wengi tusiwe na maji, tusiwe na umeme wa kutosha kwa hiyo, hata kuhamasisha kwamba, wajenge viwanda itakuwa ni kazi. Watajenga viwanda, lakini watakosa maji, watakosa umeme; kwa hiyo, mambo muhimu katika kuwawezesha hawa wawekezaji ni jambo muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini reli ya kati, ili kuhifadhi barabara zetu lazima tuwe na reli ya kati inayofanya kazi vizuri . (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema nimeshangazwa na maneno ambayo nimeyasikia kwa baadhi ya Wabunge. Kazi yetu Wabunge ni kuishauri Serikali, lakini Mbunge unaposimama na kusema matusi sidhani kama Waziri wa Fedha anaweza akaandika matusi hayo yanayosemwa. Unaposema maneno ya kejeli sidhani kama Waziri anaweza akaandika maneno ya kejeli katika kitabu chake cha Mpango. Kwa hiyo, kwa sababu kazi yetu ni kuishauri Serikali tusimame tuishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka kuanzia mwezi wa nne mpaka mwezi wa sita Bunge lilikaa hapa kujadili Bajeti ya Serikali, lakini wapo wengine ambao waliweka plaster kwenye midomo yao, waliishauri Serikali wakati gani? Leo watu wanasimama wanasema tulishauri Serikali kipindi cha bajeti! Tulishauri Serikali hawakusikia! Mimi sikuwaona walioishauri Serikali zaidi ya Wabunge wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba tukubaliane na haya ambayo yapo kwa sababu bajeti hii ilijadiliwa na upande mmoja na tukakubaliana kwamba, haya ni sawa. Na leo watu wanachangia baada ya kuona bajeti iliyopitishwa na Wabunge wa CCM ni sawa. Ninaomba kazi yetu Wabunge ni kuishauri Serikali, tuishauri Serikali, tuache lawama, tuishauri Serikali tuache matusi, tuache kubeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwamba watu wanajua na tumeona katika Majimbo yetu baada ya kusema kwamba elimu ni bure, maeneo mengine darasa la kwanza waliandikishwa watoto 100, maeneo mengine watoto 200. Kwa hiyo, huwezi kusimama ukadharau hili kwa sababu wako wananchi ambao hawakuweza kuandikisha watoto kwa sababu ya michango ya shule. Tunakotoka wananchi wanashukuru kwamba sasa watoto wanasoma kwa sababu wanalipiwa michango na Serikali. Na ninashangaa kwamba wengine walisema vyama vyao vilisema kwamba wangelipa ada mpaka university, sasa tunalipa mpaka form four wanabeza, akutukanaye hakuchagulii tusi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wako ambao hawaangalii mbele, wanaangalia nyuma siku zote. Zamani watu walibeza wakasema Mheshimiwa Kikwete anachekacheka, Mheshimiwa Kikwete hawezi, leo wanasimama wanamsifu Mheshimiwa Kikwete. Hakika nadhani tuyatafakari na kuchambua yale ambayo tunaona yatalisaidia Taifa letu, tuyaweke yatusaidie katika kuendeleza nchi hii. Tunajua hali ya kodi katika nchi yetu, tunajua Wabunge wamesema, Serikali imesikia, Mawaziri wamesikia, Waziri Mkuu tunaye kwenye Bunge letu amesikia.
Mheshimiwa Waziri…
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama katika Bunge lako Tukufu, lakini nikushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze Kamati zote mbili kwa kazi nzuri walizofanya. Wamefanya kazi nzuri kwa muda mfupi sana, lakini wamefanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopitisha bajeti hapa kila Wizara tunapitisha bajeti zake tukiamini kwamba fedha zitakwenda kwenye Wizara hizo kwa wakati muafaka. Lakini kwa Taarifa ya Kamati ya Maendeleo ya Jamii, nimesikitika jinsi mtiririko wa fedha ulivyo na hasa katika Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania milioni 45 tunategemea kuhudumiwa na Wizara ya Afya kuhusu huduma ya afya. Wazee wanaitegemea Wizara ya Afya, wanawake, watoto, vijana, kwa hiyo, milioni 45 fedha zinapopelekwa asilimia 21 kwa muda wa miezi sita ina maana Watanzania hawana pa kukimbilia na hasa wale ndugu zangu ambao wanaishi vijijini na hawana uwezo wa kujitibu na hawana bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kweli ninaposema hili kwa sababu tunapata matatizo tunapokwenda vijijini, unamkuta mtu anaumwa na anaumwa kweli kweli na hana fedha, na zahanati au kituo cha afya jirani yake hakuna dawa. Kwa hiyo, mzigo unakuwa kwa Mbunge ambaye amekwenda kutembelea pale au mzigo unakuwa kwa Diwani aliyeko eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana kwamba tunapopitisha bajeti hapa basi fedha ziende kwa wakati. Utakuta mwezi wa tano au wa sita ndipo Wizara ya Fedha inapeleka fedha katika Wizara mbalimbali na mwisho wa mwaka unapofika fedha zinarudi nyingi tu Wizara ya Fedha kwa sababu fedha zimepelekwa muda umekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna deni la MSD tangu Bunge lililopita; tangu mwaka wa jana wakati tunapitisha bajeti tuliomba sana kwamba deni la MSD lilipwe ili MSD wawe na uwezo wa kununua dawa na kuzisambaza mikoani, lakini hili deni linapungua kidogo kidogo mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri wa Fedha afya za watanzania ni muhimu kwa hiyo, deni la MSD lilipwe ili MSD wawe na uwezo wa kuagiza dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wazee fedha za maendeleo wamepelekewa asilimia 21, nimeshangaa kweli. Mwaka jana tulipitisha bajeti tukiomba fedha kwa ajili ya kukarabati Hospitali ya Rufaa ya Mirembe; wanaotibiwa pale wana ugonjwa wa afya ya akili, wameshawapiga manesi na madaktari wengi tu pale, lakini mpaka leo hospitali ile haijakarabatiwa. Hospitali ile ilijengwa tangu mwaka 1926, kwa hiyo, miundombinu ya hospitali ile imechakaa kweli; wauguzi na madaktari hawatoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kabla ya mwezi wa kumi na mbili Wizara itakuwa imepeleka watumishi wa kutosha, lakini mpaka leo watumishi ni wale wale, wauguzi wakiingia asubuhi ni mpaka jioni saa moja ndipo wabadilishane na posho za overtime hazilipwi kwa wakati. Na mimi simlaumu Mheshimiwa Ummy kwa sababu hana fedha. Posho za wauguzi hazilipwi, fedha za safari na za likizo hazilipwi kwasababu Wizara haina fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani tuwakumbuke Wizara ya Afya. Naona tunawatetea sana walimu lakini hata wauguzi na waganga hawana watetezi, watetezi wao ni sisi. Pamoja na walimu, wauguzi na waganga nao wanateseka; hawana nyumba, overtime na fedha za likizo hazilipwi kwa wakati, na wao watizamwe kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais John Pombe Magufuli alipomteua mdogo wangu Ummy Mwalimu kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee alijua umahiri wake katika kazi, na mimi nampenda kwa sababu anafanya kazi nzuri. Mheshimiwa Ummy nakupenda kwa sababu unafanya kazi nzuri, lakini nina tatizo moja, najua huna fedha lakini takwimu ambazo zimeoneshwa hivi karibuni zinaonesha kwamba kati ya wanawake wajawazito 100,000 wanawake 556 wanapoteza maisha.
Mheshimiwa Waziri ninajua una uwezo wa kuja na mkakati madhubuti kabisa kuhakikisha kwamba hivi vifo vinapungua. Tusiwafanye watoto wetu wasichana wakaogopa kuzaa kutokana na vifo. Ninaomba sasa leo ukijibu hoja za Wabunge useme mkakati ambao umeandaa kwa ajili ya kupunguza vifo vya wanawake na hata vifo vya watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahamia Dodoma lakini kwenye Taarifa ya Kamati inaonesha kwamba Hospitali za Rufaa tulizonazo hazina watumishi wa kutosha; Hospitali ya Benjamin Mkapa kati ya watumishi 751 wapo 51 tu. Kama uhakiki wa watumishi umekamilika basi waajiriwe; hao wanaotoka Dar es Salaam wanaiacha Muhimbili kule wanaacha Hospitali za Rufaa kule Dar es Salaam wanakuja dodoma, tuna hospitali moja tu hapa ya General. Lakini Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo ina vifaa vya kutosha vya kazi, hakuna watumishi, watumishi 700 wanahitajika pale na wale wanatibu wagonjwa wa ndani na wa nje; wagonjwa wa Dodoma na wa nje ya Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba kama uhakiki umeshamalizika basi waajiriwe wafanyakazi wa kutosha pale Benjamin Mkapa, Hospitali ya Mirembe na Hospitali yetu ya Mkoa ili kuhakikisha kwamba huduma inayoendelea kutolewa pale iwe ya kuridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niungane na msemaji, Mbunge aliyepita kuhusu ugonjwa wa kansa. Mimi kwa miaka mitatu nimepoteza ndugu watatu kwa ugonjwa wa kansa. Lakini hatujajua ugonjwa wa kansa unaambukizwaje, na tunatakiwa kujikinga vipi, na unasambaa au hausambai? Si mimi tu, wako wananchi wengi wa Tanzania ambao wanatamani kupata elimu kuhusu ugonjwa wa kansa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kusema habari ya viroba vilivyojaa madukani. Vijana wetu hasa waendesha bodaboda asubuhi anapiga viroba vitatu na ndio maana ajali za pikipiki haziishi, viroba sasa viuzwe kwenye bar, tuache kuviuza madukani. Kwa sababu wengine wataogopa kuingia kwenye bar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia kuhusu elimu. Sisi Kamati yetu ya PAC tulitembelea Chuo cha Ufundi Arusha; tuliona kazi kubwa ambayo inafanywa na kile chuo, wamebuni mambo mengi sana, wametengeneza mashine za kilimo cha kumwagilia, wamechukua kiwanda cha kuzalisha umeme kule Kikuletwa Wilaya ya Hai lakini hawana fedha. Pamoja na juhudi kubwa na kuwafundisha vijana namna ya kujitegemea, wavulana kwa wasichana wanajifunza mambo mengi sana pale lakini hawana fedha. Ninakuomba Waziri wa Elimu kiangalie kile chuo kwa jicho la huruma sana. Pamoja na kwamba tuna VETA lakini wanafunzi wanaweza wakatoka VETA wakaenda wakajifunza mambo makubwa sana pale Arusha Technical College.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna malalamiko kwamba wanafunzi ambao hawastahili kupata mikopo na wanapata mikopo wanaweza wakarudishwa majumbani. Ninaomba hili Waziri wa Elimu aliweke wazi kwa sababu wanafunzi wetu wapo wengi vyuoni, lakini hawajui hatima yao. Tumeambiwa uhakiki bado unaendelea, hatujui uhakiki utakamilika lini, na je, kama watapatikana ambao hawastahili kupata mikopo itakuwaje, watarudishwa majumbani au Serikali itaendelea kuwahurumia na wakaendelea na masomo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watoto wa maskini wengi tu,wengine walikuwa na wafadhili wakasoma shule ya sekondari private school lakini anapoanza chuo mfadhili anamuacha. Mwingine baba au mama alikuwa na uwezo kipindi hicho lakini amebaki yatima hawezi kulipa chuo kikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri aliangalie hilo kwa umakini na wanafunzi wasirudishwe kwa kuwa hawastahili kupata mikopo kwa kuwa wameshaanza kusoma. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kwa kutupa nafasi tena ya uhai katika maisha haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwamba sasa imetekeleza yale yaliyoamriwa tangu mwaka 1973 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhamia Dodoma. Nimeona kwa vitendo.
Mheshimiwa Rais alisema tarehe 25 mwezi wa Saba mwaka 2016, kwamba Waziri Mkuu atahamia Dodoma na Mawaziri na Makatibu Wakuu pamoja na Watendaji wengine. Jana katika uwanja wa mashujaa, Serikali ilisema mpaka sasa waliohamia Dodoma ni watumishi zaidi ya 2,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi huo. Tatizo nililonalo ni hili; wakati Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anajibu hoja za Wabunge katika Bajeti ya Waziri Mkuu alisema kwamba Muswada wa Sheria ya Serikali kuhamia Dodoma utaletwa Bungeni hivi karibuni, lakini hakusema muda. Utaletwa Bunge hili; Bunge lijalo au Muswada huo utaletwa mwaka 2020? Hakusema.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Dodoma wanataka time frame kwamba ni lini Muswada wa Sheria wa Serikali kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu utaletwa Bungeni na kujadiliwa na Bunge hili? Jambo hilo ni muhimu sana kwa sababu hata ilipoamuliwa mwaka 1973, hakuna
Sheria iliyotungwa na Bunge hili mwaka 1973 na kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi. Kwa sababu hatua imechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, sasa ni muhimu kupata time frame ya Muswada kuletwa Bungeni na kujadiliwa na Bunge hili na sasa iwe sheria kwamba Makao Makuu ya Serikali ni Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba Mji wa Dodoma kuwa Jiji. Hatua zote tumeshafanya, tumeshapitisha kwenye Baraza la Madiwani, tumeshapitisha DCC na vikao vya RCC, lakini mpaka leo agizo hilo au ombi letu halijatekelezwa.
Naiomba Serikali, vigezo vyote tumezingatia, kanuni zote tumezipitia, Serikali ione namna sasa ya kuifanya Dodoma kuwa Jiji na hasa ukizingatia ujio wa watu wengi na vigezo vyote vimetekelezwa kama agizo la Serikali lilivyosema. Sasa tunaisubiri Serikali itupe Jiji la Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi wanahamia Dodoma na wengi wangependa kujenga na wawekezaji wengi wangependa kujenga katika Mji huu na hata viunga vya Dodoma kwa mfano Bahi, Chamwino na maeneo mengine, lakini bado tuna changamoto ya miundombinu.
CDA ambao wamepewa kazi ya kuhakikisha kwamba wanapanga Mji, hawana fedha za kutosha kupanga mji huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Serikali sasa iangalie Mji wa Dodoma kwa macho ya huruma na kwa kuzingatia kwamba wengi wanahamia na wengi wangependa kujenga, lakini CDA ambao wamepewa mamlaka ya kupanga Mji, hawana fedha za kutosha. Kwa hiyo, CDA wapate fedha za kutosha, washirikiane na Manispaa ya Dodoma kupanga mji huu tusiwe na squatter kama miji mingine ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma katika Bajeti ya Waziri wa TAMISEMI, mdogo wangu Mheshimiwa Simbachawene. Nimeona jinsi alivyoonesha maabara yaliyojengwa nchi nzima na akasema kwamba katika ukurasa ule wa 27 na akaonesha kwamba mpaka sasa tumekamilisha asilimia 27% tu ya majengo ya maabara. Katika Mkoa wangu kuna maeneo mengi ambayo majengo ya maabara hayajakamilika. Naomba Serikali yangu sikivu kwamba majengo yale sasa, Serikali ione namna ya kuyakamilisha na Walimu wa Sayansi ambao wameajiriwa kwa sasa wapate kuwafundisha watoto kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba hata mikoa mingine maabara hazijakamilika kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, katika Wilaya na Halmashauri zetu kama hakuna vifaa vya maabara vya kutosha, hakika wanafunzi hawatajifunza kwa vitendo. Tunatamani wanafunzi
wanaosoma sayansi wajifunze kwa vitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shida katika Wilaya yetu ya Bahi. Mimi ni Mbunge wa Mkoa, kwa hiyo, Wilaya zote za Dodoma ni zangu. Tuna shida kubwa katika Wilaya ya Bahi na Wilaya ya Bahi tunategemea kwamba hata wawekezaji na hata ofisi nyingine za Serikali zinaweza
kujengwa katika maeneo ya Bahi, lakini pale hatuna Hospitali ya Wilaya. Kituo cha Afya kilichopo kinalaza wagonjwa nane tu. Tulileta maombi maalum kwa Serikali kwamba hospitali ile tena iko njiani, Kituo cha Afya kile kipewe huduma zinazostahili, tupewe theatre ndogo. Wanawake wanaotaka kujifungua, kama wana matatizo wanaletwa Dodoma Mjini, kilometa 65. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeleta maombi maalum kwa Serikali yetu. Naomba sasa kwa ajili ya wananchi wa Bahi; ni miaka kumi sasa tangu Wilaya ile itengwe lakini mpaka leo hawana hospitali ya Wilaya, lakini hata Kituo cha Afya kilichopo basi kiimarishwe ili kiweze kuwahudumia
wananchi wa Wilaya ya Bahi. Afya ya Mtanzania ni muhimu, afya ya mwanamke na mtoto ni muhimu, lakini hatuna hata theatre ndogo pale. Naiomba Serikali ilifikirie sana jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shida pale Bahi ya maji. Tumeleta maombi maalum kwa Serikali kwamba itusaidie maji. Maji ya pale Bahi hayastahili kwa matumizi ya mwanadamu. Naomba sana Serikali ikawasaidie wananchi wa Bahi, maji ya pale yana chumvi mno na Bahi kuna madini ya uranium. Kwa hiyo, naiomba Serikali iwasaidie wananchi wa Bahi kwa kuwaangalia kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kitabu cha bajeti ya Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ukurasa wa 39. Nimeona ajira ambazo zimetolewa kwa mwaka huu unaokwisha, ajira 9,721. Siyo mbaya, kwa sababu wamepewa Maaskari Polisi, Uhamiaji na kadhalika; lakini tuna shida kubwa ya wahudumu wa afya katika maeneo yetu. Wahudumu katika Vituo vya Afya na Zahanati zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Dodoma pamoja na wafanyakazi kuhamia kwa wingi, hospitali ya Ben Mkapa inapunguza, wagonjwa wanakwenda Hospitali ya Mkoa, lakini pale kuna wahudumu 51, kati ya wahudumu 751. Kuna upungufu mkubwa sana. Nilitegemea kwamba Waziri wa
utumishi angeliangalia hili kwa macho ya huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu wa Watendaji wa Mitaa. Tuliambiwa kwamba kada hii tunaweza kuwaajiri, lakini tunawaajiri vipi kama hatuna bajeti? Naisihi tena, Serikali yangu sikivu iweze kuwapa mamlaka Halmashauri zetu pamoja na fedha. Kuwapa mamlaka siyo neno, lakini fedha za kuwalipa hawa Watendaji wa Mitaa na Watendaji wa Kata watazitoa wapi? Naomba hili litazamwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya Madiwani imezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge. Linatuhusu kwa sababu na sisi ni Madiwani. Madiwani ndio wasimamizi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yetu. Posho yao ni ndogo mno. Madiwani wakumbukwe. Wao ndio wasaidizi wetu, wao ndio wanaosimamia miradi yote ya maendeleo; tukiwasahau hatuwatendei haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nichangie kuhusu Zahanati ya Hamai. Tuliomba fedha kwa ajili ya kituo hicho
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na pia nampongeza Mheshimiwa Ummy, Waziri wa Afya pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi ambazo tunaziona kwa macho pamoja na ukata wa fedha ambazo wanazipata kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kituo chetu cha afya kile kilichopo pale Chamwino - Ikulu, ni kituo ambacho kingeweza kuwa mfano kwa vituo vingi vya afya, lakini kile kituo hakina watendaji, hakina madaktari, hakina wauguzi, hakina vifaa tiba kituo ambacho kiko kwenye geti la Ikulu.

Mheshimiwa Waziri, ninaiomba Serikali sasa kwamba kituo kile kitazamwe kwa macho ya huruma ili wananchi wa Wilaya ya Chamwino waweze kupata huduma nzuri karibu na geti la Ikulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kukamilisha majengo ya kituo cha afya Mima na Mbori. Vituo hivi vya afya vina zaidi ya miaka kumi havijakamilika. Kati ya wale wanawake 556 wanaokufa kwa mwaka, wanawake walio jirani na kituo cha afya Mima na Mbori ni kati ya hao wanawake 556.

Mheshimiwa Ummy nitafurahi sana ukiacha alama katika Wizara hii maana wewe ni mwanamke mwenzetu, wewe ni mwanamke kama wanawake wanaopata mimba na kupata matatizo makubwa. Nikusihi, ninajua bajeti yako siyo kubwa, una bajeti kidogo sana na niwasihi Waheshimiwa Wabunge tutakapokuja kujadili bajeti kubwa tuhakikishe kwamba Wizara hii inapata fedha za kutosha kwa sababu ndiyo Wizara inayoangalia afya za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, hata wanawake ambao wanatamani kupata huduma ya ugonjwa wa cancer, kujua afya zao hawapati kwa sababu vituo vyetu havina wataalam. Sasa ukitaka kupunguza wagonjwa katika hospitali zetu za rufaa lazima uimarishe vituo vya afya, lazima uimarishe zahanati zetu na unaziimarisha kwa huduma, kwa kuwa na watendaji wa kutosha.

Nikusihi na niisihi Serikali yangu sikivu, sasa kwamba sasa ifike wakati kwamba zahanati zetu zinaimarishwa, vituo vya afya vinakuwa na watendaji wa kutosha, vifaa tiba na wahudumu wa kutosha kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Taasisi ya Jakaya Kikwete imefanya kazi kubwa ya kukoa shilingi bilioni 3.75, lakini fedha walizopewa pamoja na kuomba shilingi bilioni nne wamepata shilingi milioni 500 tu. Hivi wanaweza wakafanya nini? Wamefanya kazi kubwa kwa Watanzania, wameokoa Watanzania walio wengi. Naomba Serikali yetu iiangalie taasisi hizi ambazo zinafanya kazi za kuwasaidia Watanzania katika kuimarisha afya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tusiwavunje moyo Madaktari Bingwa wetu, wasomi hawa tusiwavunje moyo, kama ni fedha wapelekewe ili ziwasaidie katika kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie dirisha la wazee. Hospitali zetu zina dirisha la wazee, lakini je, dirisha la wazee kuna dawa? Wazee ni asilimia sita tu ya Watanzania lakini je, wanapata dawa katika dirisha lao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliandika andiko maalum kwa ajili ya kituo cha afya Bahi, mpaka leo wanawake wanakufa kule Bahi kwa sababu ya kukosa huduma muhimu katika kituo cha afya Bahi tena kiko barabarani, kingesaidia na ajali zinazopatikana maeneo yale. Hawana x-ray, hawana huduma yoyote yaani ni kituo cha afya duni sana, lakini ni kituo cha afya cha Wilaya. Sasa hivi Wilaya ya Bahi ina zaidi ya mika kumi tangu ianzishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia wodi ya wazazi Hospitali ya Mkoa. Tulikuomba shilingi bilioni moja tu mwaka jana ulipotembelea ile hospitali, tukakuamini Dada Ummy kwamba utatufikiria na utatuombea hizo hela...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini pia namshukuru Mungu wangu kwa uzima na afya njema aliyonijalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Waheshimiwa Wabunge wote wanaosema kwamba bajeti ya Wizara ya Maji iongezwe, kwa sababu maji ni uhai. Nami kama mwanamke ambaye wenzangu wanahangaika usiku na mchana kutafuta maji, napata shida sana ninapowaona wenzangu hasa wa maeneo ya vijijini ninapofanya ziara; siku moja nililetewa maji ambayo sikujua kama ni majivu au ni maji, lakini yalikuwa maji ambayo wananchi wangu walikuwa wanayatumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kwamba katika Mikoa ya Kanda ya Kati, Mikoa ya Singida na Dodoma Serikali itutazame kwa jicho la huruma sana kwa sababu hatuna mvua. Nimemsikia Mbunge wa Mkinga akisema kwamba kwake mvua inanyesha na imepitiliza, lakini hata kwa Mkoa wa Dar es Salaam mvua zinanyesha sana, Mikoa ya Kanda ya Kusini mvua zinanyesha, lakini sisi tulishasahau mvua; na mvua zinazonyesha sasa hivi haziwezi hata kujaza dimbwi. Kwa hiyo, wanawake wa Mkoa wa Dodoma wanateseka mno kwa kutafuta maji.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nahisi maeneo ya vijijini watu wameacha mambo ya dini wakaoa wanawake wengi hasa Wakristo, kwa sababu ukioa wanawake wengi mmoja akiwahi kwenda kisimani mwingine atabaki kulinda mji. Kwa hiyo, wanapata shida. Asubuhi saa kumi ndiyo wanatoka kwenda kutafuta maji na wanarudi saa tano mwanamke akiwa na ndoo moja na asubuhi wanaondoka na majembe na ndoo kichwani na jioni anarudi na ndoo na jembe begani. Naomba ufike wakati sasa Serikali ione namna ya kuisaidia hasa Mikoa hii ya Kanda ya Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Dodoma na viunga vyake, unakua kwa kasi kubwa sana, lakini miundombinu ya maji ni ile ile. DUWASA bajeti yake ni ile ile, vijiji vinavyozunguka Mji wa Dodoma wanategemea DUWASA kupata maji, DUWASA haina uwezo wa kusambaza maji kwa vijiji ambavyo viko eneo la mji huu. Mji huu wameshakuja wafanyakazi 2,800 kwa taarifa nilizopata hivi karibuni, lakini miundombinu ya maji iko pale pale. Maji yanatoka Mzakwe Kijiji cha Veyula hakina maji; UDOM hapa Ng’ong’ona hawana maji, Mkonze karibu tu na Kilimani hapa, hawana maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Serikali iangalie kwa jicho la huruma Mji wa Dodoma kwa sababu unakua kwa kasi kubwa sana na miundombinu ya maji taka ndio hatuwezi kusema kwa sababu miundombinu ya majitaka DUWASA hawawezi peke yao bila mkono wa Serikali. Serikali iwasaidie DUWASA kuweka miundombinu ya maji taka lakini na maji ya kunywa kwa wananchi wa Dodoma Mjini pamoja na viunga vyake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali sasa, tumesema kuna maji, kuna mvua katika maeneo mengi, lakini shule zetu za sekondari na shule zetu za msingi hawana maji. Kwa nini Serikali isitafute namna ya kuvuna maji kwa shule zetu, Vituo vya Afya na Zahanati ili suala la maji katika Vituo vya Afya, Hospitali, Shule za Sekondari na Shule za Msingi sasa iwe ni hadithi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizingatia kwamba sasa hivi wazazi hawatakiwi kuchangia; hawachangii ada, lakini ukiwaambia wachangie kulipa bili ya maji hawakubali, lakini tukivuna maji hatutahangaika kuwaambia kwamba wachangie bili ya maji. Kwa hiyo, Serikali ione namna sasa ya Vituo vyetu vya Afya na Shule za Sekondari na ikiwezekana Shule za Msingi pia wapate maji kwa kuvuna maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa vijiji kumi haujafanikiwa katika Mkoa wetu, maeneo mengi mradi wa vijiji kumi kupata maji haujafanikiwa sana na haujafanikiwa sana kwa sababu waliokuwa wana-monitor ni Wizara. Kwa hiyo, Halmashauri zetu hazikuwa na nafasi ya kusimamia ipasavyo. Wakandarasi ambao wamefanya kazi zao vizuri, walipwe ili wakamilishe kazi zao.

Pia tuna suala la Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini viwanda, malighafi watapata wapi? Kwa sababu malighafi kwa sehemu kubwa ni mazao na mazao tunategemea mvua. Suala la umwagiliaji litiliwe mkazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna bwawa la Kongogo lina miaka minane halijakamilika. Miaka minane hata skimu yenyewe haijaandaliwa. Wananchi wameshasubiri mpaka wamechoka, ile skimu ya Kongogo haijafanya kazi. Contractor aliyekuwepo, mpaka ameondoka skimu haijafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji ya Maporomoko ya Ntomoko, tuliwahi kumpeleka Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu aliyepita, Mheshimiwa Pinda mwaka 2013/2014 na akatuahidi fedha na akapeleka, lakini hazikutosheleza na mradi ule una uwezo wa kusambaza maji vijiji kumi na nane. Sasa hivi nimeona vijiji vinane tu ambavyo vimewekwa kwenye bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana na suala la Farkwa. Farkwa litasaidia sana maji ya Mzakwe, Bahi, Chemba na Chamwino, lakini mradi ule tume….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, lakini suala la Farkwa Ntomoko na Dodoma Mjini…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe na timu yake kwa kazi nzuri ya usimamizi wa maliasili ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania walio wengi hawajui umuhimu wa uhifadhi, faida za uhifadhi na kuwa hakuna somo la uhifadhi katika mitaala yetu na hata kwetu sisi Wabunge ni wachache sana waliowahi kutembelea mbunga za wanyama, malikale na kadhalika. Nashauri somo la uhifadhi liingizwe kwenye mitaala ili mtoto wa Kitanzania akue akijua umuhimu wa uhifadhi, kutunza misitu, malikale na kadhalika. Vijana wakiwa mashuleni wajifunze kupanda miti, kufuga nyuki na wawapende wanyama, kwa jinsi hiyo tunaweza kupunguza malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utalii wa ndani kwa vijana wetu litiliwe mkazo. Kwa kufanya utalii wa ndani vijana watajifunza mengi na kuacha uadui na wanyamapori na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro ya ardhi na hasa mipaka ya vijiji na Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na kadhalika. Migogoro mingi huchangiwa na Serikali kutokuwa makini, wananchi hawalimi kwa siku moja ndani ya mapori, wanalima kwa miaka kisha wanajenga nyumba bora za kuishi, zahanati na shule bila Serikali kuchukua hatua yoyote. Ni vizuri Serikali ikachukua hatua mapema wananchi wanapovunja sheria za uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtazamo wangu sioni sababu ya kuwepo kwa TTB. TTB haina vyanzo vya mapato, kazi zinazofanywa na TTB zinafanywa na TANAPA na NCAA. Ni halali mashirika hayo kuichangia TTB? TTB haiwezi kufanya kazi ipasavyo. Hata hivyo, tulielezwa kwenye semina kuwa vivutio vya Tanzania havitangazwi ipasavyo hii ina maana kwamba TTB wameshindwa kazi. TTB ni hasara kwa Taifa, ivunjwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Balozi zetu katika nchi mbalimbali kuwepo na kitengo cha utalii kitakachofanya kazi ya kutangaza vivutio vya Tanzania. Kwa kuwa TTB hawawezi kwenda kila mahali kutangaza vivutio vya Tanzania, Kitengo cha Utalii kwenye Balozi zetu kinaweza kufanya kazi nzuri yenye manufaa kwa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wanyamapori wanafanya kazi kubwa na yenye hatari kubwa ya kupambana na majangili, lakini wanalipwa mishahara midogo sana sawa na askari wanaofanya kazi kwenye maeneo yasiyo hatarishi. Pamoja na hayo wanafanya kazi kwa masaa mengi kwa sababu ni wachache. Serikali ieleze ni lini askari wanyamapori wataajiriwa wa kutosha na kupewa motisha ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu ya Tanzania haina mwenyewe, mtu yeyote na kwa wakati wowote anaweza kufyeka miti atakavyo na asichukuliwe hatua yoyote. Nchi zingine duniani mtu haruhusiwi kukata miti bila kibali cha Serikali. Serikali inafanya nini kulinda misitu ya nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema aliyotujalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema jambo, nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa maamuzi mazito na makubwa aliyoyafanya kwa kwa sisi wakazi wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba ardhi ya Manispaa ya Dodoma iwe mikononi mwa wananchi na tumeomba Wabunge wamepita, Wabunge wamekuja wamepita, lakini mwisho wa siku Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Awamu ya Tano imetupa ardhi yetu ya Manispaa ya Dodoma. Sina lugha ya kusema, sina namna ya kushukuru kwa niaba ya wananchi wa Dodoma hasa Manispaa ya Dodoma. Tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho naiomba Serikali hii, iweke mipango mizuri kuhakikisha kwamba wananchi ambao walishalipia ardhi na hawajaoneshwa viwanja vyao, wakaoneshwe viwanja vyao sasa. Uwekwe utaratibu ambao wale ambao walikuwa wanalipia kidogo kidogo wamalizie kulipia na kupata viwanja vyao. Mpango uwekwe wakati mikakati inaendelea, basi liwepo dirisha kwa ajili ya kuhudumia watu ambao walikuwa wanalipia viwanja, hawajaoneshwa viwanja vyao na wale ambao wanalipia kidogo kidogo huduma ziendelee kama ilivyokuwa CDA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie bajeti hii ya Wizara ya Kilimo sasa, kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili, karibu asilimia 75 ya Watanzania wanategemea kilimo; na kilimo wanachotegemea ni kilimo cha kusubiri mvua, bila kujali tabianchi, bila kujali kwamba zipo mvua za kutosha. Asilimia 4.9 tu ya bajeti ya Serikali ndiyo imetengwa kwa ajili ya kilimo. Kwa hiyo, tunaona jinsi ambavyo kilimo hakijapewa msukumo mkubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea kwamba Benki ya Kilimo ingepata fedha za kutosha kwa ajili ya Watanzania ili waweze kukopa; wakulima wa kati, wakulima wadogo na hata wakulima wakubwa. Mabenki ya biashara yanashindwa kuwakopesha wakulima wa kati na wadogo kwa sababu ya riba kubwa na kwa sababu hawana dhamana, wanategemea mvua inayotoka kwa Mungu. Hakuna mabwawa makubwa kwa ajili ya kilimo, hakuna makinga maji kwa ajili ya kilimo. Kwa hiyo, wakulima tulio wengi tunategemea kilimo cha mvua. Kwa hiyo, naomba kwamba Serikali ione namna ya kuchimba mabwawa ya kutosha ili wananchi walime kwa kutegemea kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo la mbegu. Mbegu asilimia 65 inaagizwa nje ya nchi. Hatuwezi kutegemea mbegu kutoka nje ya nchi kwa asilimia 65, ASA wanafanya kazi gani? Kama ni fedha, wapewe wazalishe mbegu. Sasa hivi wakulima wanategemea mbegu kutoka sokoni. Mbegu ya sokoni iliyozalishwa miaka 20 iliyopita, haiwezi kumsaidia mkulima kujiinua kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Kambi za JKT, tuna Magereza; tungeweza kutumia Magereza na Kambi za JKT kuzalisha mazao ya kutosha kulisha nchi hii. Wana maeneo makubwa. Kama hawana maeneo makubwa, Serikali iwape maeneo JKT walime. Tunao vijana wengi, tunaweza kuanzisha mashamba darasa kwa ajili ya vijana na vijana wakalima na wakajitegemea na wakazalisha kiasi kikubwa sana kwa ajili ya nchi hii na tukauza na tukapata fedha nyingi sana za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupanga ni kuchagua. Tunaweza tukapanga kwamba kwa kuwa mikoa ya Kanda ya kati hatuna mvua za kutosha, basi tupate Maafisa Ugani watakaotusaidia kuwashauri wakulima juu ya kilimo cha alizeti, karanga, ufuta, mtama kutokana na hali ya tabianchi. Ukimwacha mkulima alime anavyojua, hawezi kujua mvua itanyesha lini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hapa Dodoma mvua inanyesha mwezi wa 12, mwezi wa Kwanza, wa Pili mvua inakatika. Mwaka huu mvua imenyesha mwezi wa Pili mwishoni na mwezi wa Tatu. Wakulima waliopanda mwezi wa 11 hawakuambulia kitu. Hivyo, kuna haja ya kuwa na Maafisa Ugani wa kutosha ili wawashauri wakulima namna ya kukabiliana na tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ununuzi wa pamoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa jambo hili la ununuzi wa pamoja, lakini hapo....

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama na kuchangia Mpango wa Maendeleo uliopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo wameionesha kuhakikisha kwamba mpango huu unakuja mbele yetu nasi kama Wabunge tuchangie na kuongeza nyama pale ambapo tunaona panahitaji kuongezwa nyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi mgumu wa kuamua Serikali sasa ihamie Dodoma rasmi, watumishi wote wa Wizara zote zihamie Dodoma sasa, yeye mwenyewe, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwishahamia na tunawakaribisha wageni wote ambao mnakuja; Dodoma hakuna foleni, Dodoma ni salama, waje wafanye kazi ya ujenzi wa Taifa hili kwa umakini na kwa wepesi zaidi kwa sababu hakuna foleni katika Mji huu wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo yanatakiwa na yanahitaji utekelezaji wa haraka katika suala la kuhamia Dodoma. Mpaka sasa hakuna sheria inayotamka kwamba Dodoma ni Makao Makuu na nadhani kuna mambo yanaweza yakakwama kama hakuna sheria ambayo inatamka Dodoma ni Makao Makuu. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa Sheria iletwe Bungeni itakayotamka rasmi kwamba Dodoma ni Makao Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali ya Awamu ya Tano, kabla ya kazi zote zilizokuwa zinafanywa na CDA kukabidhiwa Manispaa, CDA walikuwa na bajeti yao ya takribani shilingi bilioni 47 kwa ajili ya kuendeleza Mji huu wa Dodoma. Kwa sababu hatuna sheria inayoiruhusu Manispaa kutumia au kutoza tozo kwa ajili ya uendelezaji wa Makao Makuu ya Dodoma, Manispaa ina bilioni tisa tu za fedha za maendeleo. Zile bilioni 947 ambazo zilitengwa kwa ajili ya CDA kuendeleza Mji huu bado hazijapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu shughuli za uendelezaji wa Manispaa ya Dodoma ni kubwa sana na hatutaki kuingia kwenye matatizo ya msongamano wa magari kama Dar es Salaam na Arusha na Miji mingine, tunataka Mji wetu upangwe vizuri na mji wetu usiwe na squatter, Mji wetu uwe na barabara za kutoka na kuingia zisizoruhusu msongamano. Manispaa hawawezi kufanya kama hatuna fedha za maendeleo za kutosha kwa ajili ya kuendeleza Mji huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda tuwe na wataalam pia wenye uwezo ambao watasaidia kupanga Mji wa Dodoma. Tunataka Mji wa Dodoma uwe tofauti na Miji Mikuu ya Barani Afrika kwa sababu mji huu unajengwa kwa wakati muafaka na kwa fedha ambazo naamini kabisa kwamba tutazipata. Tunataka barabara za mabasi yaendayo kasi, tunataka malori yasiingie mjini, hatuwezi kufanikiwa kama hatuna bajeti. Tutafanikiwa tu pale ambapo tutakuwa na bajeti, lakini la muhimu tuwe na sheria inayotamka Dodoma kama Makao Makuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani CDA walikuwa wanatoza tozo ya asilimia 35 kwa ajili ya kuendeleza Mji.

Mamlaka ya Manispaa hawana huo uwezo. Tunaomba sasa tukumbukwe katika hilo ili Mji wa Dodoma upendeze kwa barabara, kwa mipango ya mitaa kuwa maeneo ya masoko, stendi na kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema mengi pia niipongeze Serikali ya CCM kwa maamuzi makubwa ya kuangalia kwamba yale ambayo yalikuwa yamesimama sasa yanafanyiwa kazi. Sisi watu wa Dodoma tunashukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, reli inakuja mpaka Dodoma, sio reli iliyokuwa standard gauge inayoishia Morogoro, wameshapatikana Wakandarasi na wanaendelea na upembuzi yakinifu na taarifa ya Waziri imeonesha kwamba hawa watu wamekwishapatikana, wanafanya upembuzi na mwisho wa siku tutakuwa na reli ya mwendokasi mpaka Dodoma. Kutoka Dodoma mpaka Dar es Salaam itakuwa aidha saa moja au masaa mawili na wananchi watafaidika na reli ambayo inajengwa sasa kwa standard gauge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona kwamba ilikuwa kuja Dodoma lazima ukodi ndege yako, sasa hivi ndege ya Serikali inakuja Dodoma bila shida. Waheshimiwa Wabunge wengi nawaona mnapanda Bombadier bila kujali wewe ni wa Chama cha Mapinduzi au wewe ni wa Upinzani au wewe huna chama au wewe una chama. Kila Jumatatu asubuhi Bombadier ikitua hapo ina wananchi wengi wanaoshuka Dodoma, kwa hiyo, naishukuru sana Serikali ya CCM kwa kununua ndege na ndege sasa inawahudumia wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Spika na niwapongeze kwa kile walichokifanya. Mheshimiwa Spika, aliunda Kamati mbili zilizoshughulikia madini na ikatungwa sheria ya kushughulikia madini na sasa wizi tuliokuwa tunafanyiwa haupo tena, fedha zile ambazo tulikuwa tunaibiwa na wawekezaji hazitakuwepo tena! Naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa haya mambo makubwa ambayo tumeona wamefanya kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuhusu suala la kilimo. Asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima lakini hawapati mbegu bora kwa wakati. Pembejeo za kilimo ni ghali mno na hata viwanda tunavyotaka kuanzisha tunaanzisha malighafi tutapata shambani. Niishauri Serikali yangu, pembejeo zipatikane kwa wakati kwa wakulima lakini zipatikane kwa bei nafuu anayoweza kumudu mkulima. Wakulima wetu baadhi bado wanakwenda kununua mahindi sokoni, wanakwenda kupanda mahindi waliyonunua sokoni. Wananunua mtama sokoni, wanakwenda kupanda mtama walionunua sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali sasa wahakikishe kwamba pembejeo zinafika kwa wakati. Hata hivyo, bado hatujatilia mkazo suala la kilimo cha umwagiliaji. Kufuatana na tabia nchi kuharibika, sasa hivi mvua hazieleweki zitanyesha wakati gani, kwa hiyo ni vizuri pia tukakazania kilimo cha umwagiliaji, mabwawa yale ambayo yalichimbwa na mengine hayajafikia hatua za mwisho, basi Serikali ione namna ya kupeleka fedha. Sisi Dodoma tuna bwawa la Farkwa, lingetusaidia kwa kilimo cha umwagiliaji, lingetusaidia hata kwa masuala ya maji katika Wilaya zetu ambazo zinapakana na Mto Farkwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo, mifugo na uvuvi sijaona kama limetiliwa mkazo sana kuhusu suala la mifugo na uvuvi. Kuna ng’ombe wengi sana hapa nchini lakini hatuna viwanda vya nyama, hatuna viwanda vya ngozi, hatuna viwanda vya maziwa ya kutosha. Niiombe Serikali kama kuna uwezekano wa kuingia ubia na wananchi wawekezaji wakafungua viwanda vya nyama, migogoro ya wakulima na wafugaji itapungua, kwa sababu wafugaji watauza mifugo yao kwenye viwanda vya kuzalisha nyama, wakulima watakuwa na viwanda kwa ajili ya mazao yao. Pia suala la uvuvi tuna viwanda vichache sana vya samaki, Serikali iangalie suala hilo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake, lakini pia nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati, Kamati ya UKIMWI na Kamati ya Maendeleo ya Jamii na hasa nampongeza sana Mheshimiwa Serukamba kwa ripoti yake nzuri na hasa nimesoma katika ukurasa wa 41 kuhusu pads za watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili tuliliongea katika Kamati yetu ya Bunge Wanawake (TWPG) na tukaunda vikundi vidogo vidogo vinavyoshughulikia mambo ya jinsia, bajeti ya jinsia. Nakumbuka kikundi kinachoshughulikia taulo za wanawake ni kikundi cha ambacho Mwenyekiti ni Mheshimiwa Zaynabu Vulu na Katibu wake ni Mheshimiwa Catherine Ruge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili tumelishughulikia na Bunge la mwezi Novemba, 2017 tuliwaita Wakurugenzi kutoka Wizara mbalimbali tukakaa nao, tukajadili mambo mengi yaliyohusu jinsia na mambo yaliyohusu watoto wa kike na hasa taulo za kike na tukaiomba Serikali kwamba isipoweza kupunguza bei, basi watoe bure taulo hizo kwa sababu hata wanawake wa vijijini wanapata shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kabla ya Bunge la Bajeti kama tulivyowaagiza wale Wakurugenzi wapeleke taarifa ofisini kwa Mawaziri wao kwamba tukutane na Mawaziri, Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Afya watuambie kwamba habari ya taulo za kike kupunguzwa bei au kutolewa bure kwa wanafunzi limefikia wapi? Ninaamini Mawaziri watalishughulikia na kabla ya Bunge la Bajeti watatuletea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la uhaba wa watumishi au uhaba wa wauguzi katika Mkoa wangu. Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri ya kuhamishia Makao Makuu Dodoma na sasa watumishi wengi wamekuja Dodoma na watumishi hawa wanahudumiwa na wauguzi wachache na watumishi wachache wa hospitali wa hapa Dodoma. Hatujaongezewa wauguzi, hatujaongezewa madaktari na kama Kamati ya Maendeleo ya Jamii walivyosema kwamba Hospitali ya Benjamin Mkapa haitumiki vizuri, ni kweli haitumiki vizuri kwa sababu ina vifaa vingi, ina wataalam wachache na ina wauguzi wachache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa kwamba Waziri utalichukua hilo na utaongeza watumishi pale Benjamin Mkapa na vifaa tiba najua vipo vya kutosha, lakini hatuna wauguzi na watumishi wa kutosha wa kuweza kutumia vile vifaa ili kupunguza foleni kubwa iliyopo Hospitali ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia uhaba wa walimu katika Mkoa wangu. Siku moja tulikwenda na Waziri wa TAMISEMI hapa Iyumbu tu mjini na tukakuta wanafunzi wako 800 na walimu wako wanane. Hebu fikiria hao walimu wanavyofanya kazi ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule moja ya msingi Ntomoko, shule ya msingi Ntomoko, wanafunzi ni wengi lakini walimu wako watatu. Ninaamini Serikali itaona namna ya kuwaongeza walimu hasa katika shule zetu za msingi na hata shule zetu za sekondari pale ambapo kuna upungufu mkubwa wa walimu. Kwa sababu shule za vijijini, shule ambazo ni remote areas walimu ni wachache mno na hasa walimu wa sayansi, kiasi kwamba hawakidhi mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la capitation. Zamani fedha za capitation zilikuwa zinapelekwa shuleni na Walimu Wakuu ndio waliokuwa wanahusika kununua vitabu. Tangu suala la elimu bure, Serikali au Wizara imeamua kununua vitabu kuanzia vitabu vya wanafunzi wa darasa la nne hadi wanafunzi wa darasa la saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu mkubwa sana wa vitabu mashuleni. Siyo Dodoma tu, naamini hata mikoa mingine kuna upungufu mkubwa wa vitabu vya wanafunzi kuanzia darasa la tano hadi darasa la saba. Tunategemea kwamba hao wanafunzi wanapoanza darasa la tano, wanatarajia kufanya mitihani ya kuingia kidato cha kwanza. Kwa hiyo, kama hakuna vitabu, hawawezi kusoma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Dodoma takriban kitabu kimoja wanatumia watoto sita hadi nane. Kwa hiyo, naomba tu Serikali yetu sikivu ione umuhimu sasa wa kununua vitabu na kuvipeleka mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna upungufu mkubwa wa madarasa. Tangu Serikali itoe elimu bure mashuleni, sasa hivi kuna mfumuko mkubwa sana wa watoto wanaoanza darasa la kwanza. Kwa hiyo, madarasa hayatoshi na hakuna namna ya wananchi kuchangishwa au wazazi kuchangishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hakuna namna ya kuongeza madarasa. Kwa hiyo, naomba Serikali sasa itoe tamko, namna gani tunaweza kuongeza madarasa bila kuchangisha wazazi? La sivyo, Serikali ichukue jukumu la kujenga madarasa ili wanafunzi wanaoingia darasa la Kwanza na wale wanaoanza form one wapate namna ya kusoma na namna ya kusoma kwa uzuri zaidi, wasisome chini ya miti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza sana, tumetoka kuwa na semina na Taasisi ya Moyo kule Dar es Salaam. Niwapongeze sana kwa kazi nzuri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini namshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kunipa muda wa kusimama katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi nzuri pamoja na Watendaji wengine ambao wapo chini ya Wizara hii kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kila jambo chini ya jua lina makusudi; na sisi tumeletwa humu ndani kwa makusudi ya Mungu.

Hata kama ulitumia njia zako za giza, lakini Mungu amekubali uingie humu kwa makusudi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mungu kamweka kuwa Rais wa nchi hii kwa makusudi maalum.

Kwa anayoyafanya ni makusudi ya Mungu anayoyatekeleza. Kwa hiyo, nawaomba Watanzania tudumishe amani, tudumishe umoja tunapozungumza mambo ya Kitaifa.

Nawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, amwezeshe kuwa na hekima na maarifa ya kufanya kazi hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tu. Kazi anayofanya ni kubwa, hawezi kuwa na marafiki. Marafiki wasioitakia mema Tanzania hawawezi kumpenda. Kwa hiyo, lazima tumweke kwa Mwenyezi Mungu kila siku.

Nampongeza sana kwa kazi nzuri anayofanya ya kusimamia rasilimali za Taifa hili. Nimesoma kwenye Mtandao kwamba Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick kaingia Tanzania. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaingia kwa ndege yake binafsi, kaja kuongea na Rais wetu kuhakikisha kwamba rasilimali, fedha ambazo hawakulipa wanalipa. Jamani, ningekuwa na uwezo ningesema Watanzania wote tumwombee huyu baba, Mungu ampe maisha marefu, lakini pia aendelee kumpa maarifa ya kutawala katika nchi yetu. Asiyemtakia mema na sisi tunamlaani kwa sababu Mungu alishatupa uwezo; ukimlaani mtu ambaye hakutakii mema na amani, analaanika. Kwa hiyo, yule ambaye hamtakii mema Rais wetu, atalaanika tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefarijika baada ya kuona makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga sasa wataanza kuchimba na kiwanda kitajengwa pale na wananchi wanalipwa fidia. Tumelizungumza muda mrefu sana suala la Mchuchuma na Liganga na sasa imefika mwisho. Sasa tunaona matokeo ya Mchuchuma na Liganga. Nimeona kwenye bajeti kwamba na wananchi watalipwa fidia. Kwa hiyo, Tanzania chuma cha reli ambacho tunakitaka tutatoa Liganga kule ambako tutachimba chuma; lakini na vyuma, nondo kwa ajili ya ujenzi tutapata Liganga kwa sababu tutakuwa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watani zangu wale wa kutoka Bukoba, reli inajengwa, watakuwa wanafika baada ya siku moja tu badala ya siku mbili. Ndugu zangu wa Mwanza na Mara watakuwa wanasafiri kwa muda wa siku moja tu kwa sababu tunajenga reli ya standard gauge. Tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa juhudi kubwa na kazi kubwa anayoifanya ya kuwatetea Watanzania. Tulikuwa mvua ikinyesha tunalala Kilosa siku mbili, ukitoka Dar es Salaam unalala Kilosa siku mbili ndiyo ufike Dodoma. Kwa hiyo, hayo tena hatuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeze pia kwa ajili ya kuleta Makao Makuu Dodoma. Sitaacha kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu kwa suala la Serikali kuhamia Dodoma. Nawashauri Wawekezaji, Waheshimiwa Wabunge, Dodoma viwanja vipo, fursa za uwekezaji ni nyingi, karibuni mwekeze Dodoma. Dodoma patakuwa pazuri kuliko Dar es Salaam kwa sababu tunajenga kufuata plan ya Mji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme habari ya kilimo. Nilipozungumza katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu niliomba kwamba suala la kilimo litiliwe mkazo kwa sababu tunataka viwanda, nchi yetu iwe ya viwanda; lakini je, tuna malighafi? Malighafi ya viwanda vya kilimo iko wapi? Nikapendekeza kwamba tuwatumie JKT katika suala la kilimo cha umwagiliaji, tutapata mazao ya kulisha viwanda vyetu. Pia tunaweza tukatumia Magereza wakalima kilimo cha umwagiliaji na tukajitosheleza kwa mazao kwa ajili ya viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ranch zetu sioni kama zinaweza ku-feed viwanda vyetu vya nyama. Hata hivyo, wafugaji bado hawajafuga ufugaji wa kisasa kiasi kwamba tunaweza tukalisha viwanda vyetu ndani ya nchi. Kwa hiyo, lazima tuwe na mikakati katika masuala ya kilimo, kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa kisasa lakini hata vijana wetu tunaweza tukaanzisha Makambi ya vijana kwa ajili ya ufugaji, kilimo cha horticulture, kilimo cha kisasa na tukawa na malighafi ya kutosha katika nchi yetu; na tukawawezesha hasa hawa wanaoandaa mbegu. Wazalishaji wa mbegu ni asilimia 35 tu wanazalisha, tunaweza tukawawezesha lakini kama hawawezi pia watu binafsi wanaweza kupata mikopo kutoka mabenki yetu na wakazalisha mbegu za kisasa kwa ajili ya kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu vivutio vya utalii. Bado vivutio vyetu havijatangazwa. Tulipotangaza kidogo, Waisrael walikuja 600 kwenye utalii wa nchi yetu. Je, tukitangaza zaidi ya hapo tutapata pesa nyingi kutoka kwa watalii? Tuwafundishe watoto wetu utalii. Utalii ufundishwe mashuleni; vivutio vifundishwe mashuleni ili mtoto anapokua ajue kwamba kuna vivutio vizuri ndani ya nchi yetu. Hapa ukiwauliza Waheshimiwa Wabunge wangapi wametembela Serengeti, Selous na Mikumi, inawezekana wasifike hata 50. Kwa hiyo, hatujatangaza utalii vya kutosha. Tutangaze utalii vya kutosha tutaopata fedha za kutosha kuendesha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Sekta ya Uvuvi tuitangaze kwa kadri inavyowezekana ili hata doria zifanyike tuone kwamba Sekta ya Uvuvi inachangiaje pato la Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dodoma tuna uranium hapa Bahi, hatujaanza kuchimba. Tuna madini ya kutosha ndani ya nchi yetu; tuna nickel pale Itiso, Chamwino. Tukiweka sheria nzuri ambazo zitawabana wawekezaji kama Mheshimiwa Rais alivyoamua, tunaweza kuwa matajiri kiasi kwamba watoto wetu wakaishi maisha ambayo hawakuyatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiseme kwamba Tanzania ni nchi maskini, sisi sio maskini na wala tusikae tunalaumiana. Juzi juzi nilimsikia Mheshimiwa Mbunge mmoja anasema kwamba wawekezaji sio wezi, hawa wachimbaji wa madini sio wezi. Amesahau kwamba mwezi uliopita tu alisema kwamba wawekezaji ni wezi, kutokana na mikataba yetu. Tunataka kuijenga nchi yetu, tumetumwa na wananchi kuishauri Serikali. Tuishauri Serikali pamoja ili tusonge mbele katika mambo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dabalo tunajenga Kiwanda cha Miwa na tumeshampata Mwekezaji, lakini huyu Mwekezaji hajapa hati ya kumiliki ardhi. Naiomba Serikali, mpeni yule Mwekezaji hati miliki aweze kujenga kile kiwanda na wananchi wa Dabalo ambao amewapa mikopo kwa ajili ya kulima miwa waendelee na kile kilimo na viwanda viendelee kuwa vingi vya kutosha katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi ya leo na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama katika Bunge lako hili tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema Wabunge wengine na mimi niungane nao kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako kwa kazi nzuri anayofanya na alianza kufanya hata kabla hajawa Waziri, alikuwa mtumishi mwema kule alikokuwa NACTE na naamini anaendeleza utumishi huo, mimi sina la kukwambia zaidi ya kukuombea kwa Mwenyezi Mungu na kuwaombea watumishi wengine wa Wizara hii kwa Mwenyezi Mungu ili kazi yao iendelee kuwa njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kupongeza Serikali kwa progaramu ya lipa kulingana na matokeo (EP4R), kwa programu hii wamefanya kazi kubwa ya ukarabati wa shule kongwe nchini. Katika mkoa wangu wa Dodoma wamekarabati shule ya sekondari Mpwapwa, shule ya sekondari Dodoma, shule ya sekondari Bihawana na Shule ya sekondari ya Msalato pia. Wanafanya kazi nzuri, shule hizi zilikwishachakaa na siku moja tuliingia katika vyoo vinavyotumika katika shule hizi nilishangaa uwepo wa Mungu kwa wanafunzi, kwa sababu nilishangaa watoto hawapati fungus, shule ilikuwa yanatisha hasa vyoo na mabweni.

Kwa hiyo niombe sana Serikali waendelee na programu hii na Mheshimiwa Waziri nikuombe Dodoma sasa ni Makao Makuu na hatuna majengo shule ya mfano na hasa ya wasichana katika Mkoa wa Dodoma, kama kuna uwezekeno programu hii itusaidie kujenga shule kubwa ya kitaifa, shule ya wasichana ambapo wasichana watajengewa mabweni, walimu watakuwa wa kutosha na iwe shule ya sayansi, tunawataka wasichana ambao watasoma sayansi kusaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru pia kwamba tumeona Waraka Na. 2 wa mwaka 2016 unayozungumzia kiwango cha ufaulu kwamba mwanafunzi wa form two akipata “D” mbili anaruhusiwa kuendelea na elimu, anaruhusiwa kusonga mbele darasa lingine, lakini hao wanafunzi wanaoruhusiwa kwa “D” mbili kwenda form three au kidato cha tatu ndiyo hao tunaowategemea kwenda vyuo vikuu, tunawaruhusu kwa ufaulu mdogo mno.

Mheshimiwa Waziri wewe ni Profesa, unajua ulivyo- fight kupata uprofesa wako, hukwenda na “D” mbili kidato cha tatu, kuna haja ya kubadilisha ufaulu kwa watoto wa sekondari tunawandaa wanafunzi kuwa maprofesa, tunataka watoto wetu wawe maprofesa kama wewe, tunataka wawe madaktari ufaulu wa chini wa “D” mbili haufai na umepitwa na wakati Mheshimiwa Waziri, niombe Serikali sasa na ukimwambia mtoto “D” mbili anakwenda kidato cha tatu hajishughulishi na kusoma na hata walimu hawaongezi bidiii katika kufundisha kwa sababu anajua mtoto akipata “D” mbili anaingia kidato kingine. Kwa hiyo, niombe sasa kuwepo na ushindani ili wanafunzi wajishughulishe na walimu wajishughulishe kuwaandaa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne hawapati nafasi ya kuingia kidato cha tano na wale wanaomaliza kidato cha sita wanashindwa kupata nafasi ya kuendelea na vyuo vikuu. Wanafunzi hawa wanarudi mitaani, lakini wanaporudi mitaani hawana kazi za kufanya, tunasema Serikali iwape asilimia tano ya mapato ya Halmashauri zetu ili wajiandae kuwa wajasiriamali, hawana elimu ya ujasiriamali pamoja na elimu wanayopata kwa muda mfupi kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii lakini haiwasaidii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikiimarisha VETA, ikaimarisha JKT na ikapeleka vifaa kwa ajili ya kujifunzia, watoto wetu wanaomaliza kidato cha nne wakaenda VETA wale wanaomaliza kidato cha sita wakashindwa kuendelea na masomo wakaenda VETA wakitoka kule watakuwa na stadi ya kuwatosha kujitegemea na hata Serikali unapotoa mkopo kwa ajili ya ujasiliamali wanapopewa mikopo ya kutoka Halmashauri zetu watakuwa na uwezo wa kujitegemea. Tunapowapa mikopo na elimu hiyo wanayotoka nayo ya nadharia sidhani kama elimu hiyo inawasaidia na matokeo yake asilimia 40 tu ya mikopo ya vijana inarudishwa asilimia 60 wanashindwa kurudisha kwa sababu hawana elimu ujasiliamali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tafiti zinazofanywa na vyuo vikuu na hasa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA). Tunategemea SUA iwasaidie wakulima wetu tafiti wanazozifanya za mazao, tabianchi, itusaidie katika kukuza kilimo, lakini tafiti hizi haziwafikii wakulima. Tafiti hizi zinaishia kwenye makaratasi na sana wanafaidi aidha wanaokaa Morogoro na wale ambao wanajuhudi za kufuatilia tafiti hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SUA imeanzishwa kutusaidia ninaomba sasa tafiti za mazao zinazofanywa na SUA ziwafikie wakulima na ziwasaidie wakulima, mbegu wanazozifanyia tafiti zifike kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida sana na walimu, nyumba za walimu, upungufu wa walimu wa sayansi, hili limezungumzwa na litaendelea kuzungumzwa na Wabunge, Serikali ione namna sasa, elimu bure wanafunzi wengi wanasoma, lakini madarasa ni yale yale, madawati ni yale, walimu wameongezeka kidogo, lakini wa sayansi hatuna hilo Serikali ione namna ya kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumzia pia ubunifu kwamba wanawajenga wanafunzi, wanawajenga watu katika ubunifu, lakini tusipoanza katika elimu ya sekondari hatutapata wabunifu wazuri hata katika mambo ya uchoraji, engineering na michezo kama hatutawajenga wanafunzi vizuri hatutawapata.

Pia kuhusu elimu ya TEHAMA, katika shule za sekondari hakuna elimu ya TEHAMA kama ipo ni shule za private, lakini shule za Serikali kama wanafundishwa ni nadharia, basi tuone namna wanapotoka sekondari wanaokwenda vyuo vikuu wanatamani kuwa wasomee masomo ya TEHAMA lakini anapoanzia kule kwanza lugha yenyewe ya kubabaisha ya kiingereza, lakini la pili hajawahi kuiona hiyo computer alipokuwa shule ya msingi wanayoiona computer ni wale ambao wanasoma shule za private. Serikali ijenge uwezo kwa Walimu na kujenga miundombinu katika shule zetu za sekondari za Serikali kwamba TEHAMA wanaianzia sekondari na anaanza akiwa na vifaa vya kutosha kusomea, miundombinu ianzie sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi uliyonipa ya kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema aliyonipatia, Muumbaji wa Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kumteua Mfugaji Mheshimiwa Mpina kuwa Waziri wa Wizara hii na kwa kumteua Mheshimiwa Naibu wake ambaye pia ni Mvuvi. Amewateua kwa makusudi maalum akijua kwamba wanajua changamoto za wakulima, wafugaji na wavuvi. Kwa hiyo wavuvi na wafugaji wana matumaini makubwa sana na Mheshimiwa Waziri aliyepo na Naibu wake kwa sababu wanaijua sekta hii vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwa haraka sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri na jinsi sekta ya mifugo ilivyochangia Pato la Taifa na nimefadhaika na kuhuzunika nilivyosoma taarifa hii jinsi sekta ya mifugo ambayo imetufanya kuwa nchi ya tatu Afrika kwa wingi wa mifugo lakini ikachangia kiasi kidogo sana katika Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana hatuko makini, inawezekana hatujajali sana sekta hii ya mifugo na uvuvi, kiasi kwamba tungekuwa serious katika sekta hii tungefanya vizuri na sekta ya mifugo ingechangia kama sekta ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Waziri ukusara wa 25 amesema Wizara ilikusanya bilioni 10.5 tu na kutochangia ipasavyo katika pato la Taifa na wakaorodhesha sababu huku, wakasema zaidi ya asilimia 20 ya maziwa yanaagizwa kutoka nje. Wakasema usafirishaji holela wa ngozi ndani na nje ya nchi, uingizaji mkubwa wa bidhaa za ngozi kutoka nje, kuwepo dawa bandia. Naamini tuna watalaam na naamini wataalam wetu kazi yao ni kusimamia sekta waliyoisomea na waliyopewa kuidhibiti. Nilikuwa na matumaini kwamba wasingeruhusu haya yote yakatokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, napata kigugumizi kuona kwamba sekta ya mifugo inachangia kiasi kidogo namna hiyo. Siyo mwaka huu tu, miaka yote ya nyuma sekta ya mifugo inachangia kidogo sana pato la Taifa. Tumepoteza bilioni 263.95 kwa sababu ya kutosimamia/kutodhibiti sekta ya mifugo na hii iko katika ukurasa wa 28 wa hotuba ya Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipita vijijini akinamama na vijana wanatembeza maziwa, hawana pa kupeleka kwa sababu hatuna viwanda vya maziwa; viwanda vya maziwa ni vinne tu nchi hii yenye ng’ombe wengi. Havitoshelezi kununua maziwa ya nchi nzima, lakini kama hatuwezi, hatuna viwanda vya kutosheleza tutafute namna ya kusindika haya maziwa yakauzwa nje ya nchi kuliko kutumia Lactogen (maziwa ya kopo) kwa watoto wetu, maofisini na hata mahotelini wakati tuna ng’ombe zaidi ya milioni 20, hatufaidiki na ufugaji tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafugaji waliopo hawafaidiki na ufugaji kwa sababu hawana namna ya kuuza ng’ombe, hawana namna ya kusafirisha ng’ombe nje ya nchi na hata utaratibu wa dawa za mifugo haueleweki. Wafugaji wananunua hawajui kwamba je, hii ni dawa halisi au dawa hii siyo dawa halisi, mradi kaikuta dukani kama ina jina bandia hajui kwa sababu hata Maafisa Ugani tulionao hawatoshelezi. Hatuna Maafisa Ugani wanaotosheleza mahitaji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, usafirishaji wa ngozi, hatuna viwanda vya ngozi ndiyo maana tunanunua viatu kutoka China na Kenya, nje ya nchi hatuna viwanda vya ngozi. Viwanda vya ngozi hatuna, viwanda vya maziwa vinne tu, viwanda vya nyama sijui ni vingapi hata ile cha Shinyanga nadhani imeshasimama, Tanganyika Packers ndiyo tulishasahau; kuna nini katika kuanzisha viwanda vya mifugo hapa nchini?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashindwa kuelewa/ nashindwa kujua tatizo lipo wapi. Mwaka huu au mwaka wa fedha unaoisha Wizara ya Mifugo walipiga chapa ng’ombe wakapata bilioni 14; kazi ndogo kweli lakini walipata bilioni 14. Hizi bilioni 14 hawajarudisha kwa wafugaji, hawajachimba malambo, wafugaji wanahangaika kipindi cha kiangazi, lakini kwa chapa tu wamepata bilioni 14. Wafugaji hawana malambo wakati wa kiangazi wanahama huku na kule, Wizara iwasaidie wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chuo chetu cha LITI kipo Mpwapwa, kile chuo kilishasahaulika siku nyingi, mabweni yamechakaa, hakuna vifaa vya maabara, mabweni yamechakaa, madarasa yamechakaa, bajeti ni finyu lakini wanafunzi Tanzania nzima wanakwenda pale kujifunza. Nimwombe Mheshimiwa Waziri akikumbuke Chuo cha LITI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme jambo moja tena, wavuvi wameonewa sana katika nchi hii. Nyavu inchi nne na inchi tano ni haramu, timba na kokoro ni haramu, nyavu inchi sita na saba kama ina macho 78 ni haramu, lakini kama ina macho 26 ni halali. Wavuvi wamechomewa nyavu zao waliokopa wengine wamekufa; wamekufa kwa sababu wanatozwa faini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unashikwa na samaki, samaki hao wakati wavuvi wanakwenda ziwani/baharini, Afisa Uvuvi amekagua nyavu lakini wanapotoka kuvua samaki wanakamatwa, nyavu zinachomwa na faini anatozwa milioni 25 au milioni 50 alipe ndani ya masaa 24. hivi ni nani nayeweza kuwa na milioni 50 kwa siku, akiweka pesa yake tayari tu kwa ajili ya kulipa faini kwa sababu ya nyavu ambazo Afisa Uvuvi amezikagua na Mkurugenzi wa Uvuvi alipitisha lakini bado nyavu zikachomwa. Watu wamekufa; Kanda ya Ziwa, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa watu wamekufa, Rukwa watu wamekufa kwa mambo ambayo Serikali ingeweza ikakaa na wavuvi na wakaelewana na wavuvi wakapata elimu hiyo na wasirudie makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako waliochomewa kimakosa, hawa waliowachomea kimakosa wanawafanyaje? Nyumba zao zimeuzwa walikopa benki, wanawafanyaje? Tunaambiwa nyama ina cholesterol tule samaki, Dodoma sasa hivi unaweza kutafuta samaki mabucha 20 usipate samaki kwa sababu ya matatizo yaliyopo kwenye maziwa na bahari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mwanza kuna mtu mmoja tu anaitwa Naipich ndiye ameruhusiwa kutengeneza nyavu, hivi yeye peke yake anaweza kutengeneza nyavu za Tanzania nzima? Hivi dagaa anavuliwa kwenye nyavu ya aina gani, kule Ziwa Viktoria kuna samaki wanaitwa Furu, Furu hakui hata ukimfuga miaka 20 yupo vilevile anavuliwa kwenye nyavu za aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusiwafanye wavuvi wakajiona kwamba wao sio Watanzania, tusiwafanye wavuvi wakatuchukia.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Ranchi zetu pia hazijatumika vizuri.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu wangu kwa neema yake ya siku ya leo ya kuzungumza katika Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kwamba Serikali inafanya kazi kubwa na Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla pamoja na Mheshimiwa Hasunga mmezunguka nchi nzima kuangalia changamoto ambazo zinaelezwa na Waheshimiwa Wabunge. Najua utakaposimama kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge mtazungumzia changamoto hizo kwa sababu mnazijua. Pia najua kwamba mmezikabidhi changamoto na kero hizi kwa wataalam wenu ili wazishughulikie na tunaamini sasa zitafanyiwa kazi. Tunakuamini Waziri na hukuzunguka bure na wataalam wako pia tayari kukusaidia na pale ambapo unaona hupati msaada najua utachukua hatua zinazostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitaka mmea wako uzae matunda lazima uutunze, lakini lazima uweke mbolea na maji na upige dawa. Ukitaka mifugo yako upate mazao mazuri lazima uilishe, wapate chanjo na wapate maji na malisho mazuri. Wizara hii ya Maliasili na Utalii inafanya kazi kubwa, inachangia asilimia 17.6 ya pato la Taifa. Wizara hii ndiyo Wizara inayoingiza fedha nyingi za kigeni, Wizara hii ndiyo inayoingiza asilimia 25 ya fedha zote za kigeni na Wizara hii ndiyo inayoingiza fedha za kigeni dola bilioni 2.3 kwa mwaka. Kwa hiyo, lazima Wizara hii ipate fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia bajeti tunayomaliza Wizara hii ilipata asilimia 33.5 tu fedha za maendeleo, fedha ambazo haziwezi kuimarisha Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunalalamika kwamba watalii hawaji kama wanavyokwenda katika nchi jirani, hawawezi kuja kwa sababu fedha za maendeleo hatuna, hatuwezi kuimarisha barabara zetu, huduma zetu haziwezi kupendeza kama fedha hazipo za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Utalii inafanya biashara na watu binafsi na bajeti iliyopita walisimamisha biashara ya wanyama hai kusafirishwa nje ya nchi. Serikali ikaahidi kabisa kwamba hawa watu watalipwa fidia na tulitegemea kwamba mpaka leo bajeti nyingine imeingia, Wizara au Serikali itakuwa imekwishalipa fidia. Hawa watu walikopa fedha kwenye benki, hawa watu walitumia fedha zao lakini mpaka leo Serikali haijalipa fidia kwa watu hawa.

Mheshimiwa Spika, nategemea Waziri utakaposimama utasema kitu kwamba hawa watu watalipwa fidia kipindi gani kwa sababu interest inaendelea kukua kule benki, lakini Serikali haijawalipa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nirudi nyumbani, kule kwetu Mkungunero - Kondoa tumeshawapeleka zaidi ya Mawaziri watano. Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ulikwenda, Mheshimiwa Hasunga alikwenda, tukaitisha mkutano mkubwa, ukawahutubia wananchi, ukaenda na Mbunge wa pale Mheshimiwa Dkt. Ashatu, wananchi wakapata matumaini, lakini mpaka leo hakuna kinachoendelea kati ya wananchi wa vijiji vya kule na hifadhi ya Mkungunero.

Mheshimiwa Spika, askari watatu waliwahi kuuawa kule, wananchi wanalima kule mazao yao yanafyekwa, ng’ombe wakiingia eneo lile la eka 50 tu wanachukuliwa, harudishwi kwa wenyewe na wenyewe wanatozwa faini, na ni mgogoro wa muda mrefu sana. Mheshimiwa Waziri ulipokwenda ulitoa ahadi nzuri na wananchi wakapata imani na wewe, kijana ulipokwenda na morale walikupigia makofi, wakapata imani kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasikitika, natamani kulia kwa sababu kila ninaposimama katika Wizara hili nalizungumza suala la Mkungunero. Mheshimiwa Rais alipompa Mheshimiwa Dkt. Ashatu nafasi ya Naibu Waziri, wananchi wa eneo lile la Mkungunero vijiji vile 12 walipata amani, kwamba sasa suala lao litaisha, lakini mpaka leo mwaka wa tatu sasa tumeanza, suala la Mkungunero bado liko pale pale. Ninakusihi hebu fanya kitu, ninakusihi wale wananchi shida yao sasa ikashughulikiwe.

Mheshimiwa Spika, lakini tena tuna suala la pori la Swagaswaga. Mpaka wa pori la Swagaswaga na Vijiji vya Handa na Lahoda ni tatizo kubwa. Mpaka upo lakini maafisa wako Mheshimiwa Waziri hawataki kufuata mpaka uliopo pale. Ninakusihi sasa ukashughulikie mipaka kwa sababu kila Mbunge anayesimama anazungumza suala la mipaka. Sisi Dodoma hatutaki migogoro na Serikali yetu, lakini kama migogoro haitatuliwi mapema wananchi hawawezi wakakubali, kama migogoro haishughulikiwi kwa wakati wananchi wataendelea kulalamika, Mheshimiwa Waziri naomba sasa suala hili likashughulikiwe haraka inavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie tena suala la tozo inayotozwa kwa TANAPA na Ngorogoro. Mashirika haya yanafanya kazi nzuri sana na hata fedha tunazopata yanatokana na mashirika haya. Na masharika haya nikubaliane na kamati kwamba wanatoa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa Mfuko Mkuu wa Serikali. Halafu wanatoa asilimia tatu kwenda Mfuko wa Uendelezaji wa Utalii, na fedha hizi zinakwenda Serikalini.

Mheshimiwa Spika, lakini bado wanatakiwa kulipa VAT, na bado wanalipa kodi. Ninadhani tozo hizi na gharama hizo ambazo mashirika haya yanaingia ndio maana unakuta gharama zetu ni kubwa kuliko nchi ya Kenya, gharama zetu ni kubwa kuliko nchi za jirani. Serikali inaona nini? Masharika haya ni Serikali, fedha zao hawatii mfukoni, fedha zao zinaingia Serikalini na fedha hizi ndizo zinazowasaidia kutengeneza miundombinu na watalii wanapokuja wanakuta kwamba kuna miundombinu mizuri. Ninaomba sasa Serikali ione namna kuacha VAT kwa fedha hizi ambazo kwa hakika zinakwenda Serikalini.

Mheshimiwa Spika, mashirika haya yamefanya vizuri kipindi chote, na hata tunapoongea asilimia 17.6 ya Pato la Taifa mashirika haya yanahusika. Hata utalii wa picha kwenye mapori yetu yanahusika, lakini bado wanatozwa kodi hiyo.

Mheshimiwa Spika, sasa nizungumze suala la ushikaji wa wanyama au ng’ombe au mifugo katika mapori yetu. Serikali inaweza ikaongea na hao wafugaji, wakaweka utaratibu, kwamba wanaposhika ng’ombe wakaandikishane kijijini na wenye mifugo na Serikali iwe na RB kwamba nimeshika ng’ombe wa Mama Bura 400 na sasa kesi iendelee mahakamani ili huyu mtu aendelee kulima na aendeleze kufanya mambo ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mifugo umechukua, halafu unakuja kumtoza faini shilingi milioni 50, anatoa wapi? Serikali yetu ni Serikali ya wanyonge, mkulima akishikiwa mifugo yake waandikishane kwa Mwenyekiti wa Kijiji exhibit itabaki kwa mwenye mifugo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, inasikitisha na kuhuzunisha, lakini niishauri Serikali yangu, watafute utaratibu mzuri ila haya malalamiko yanayotokea kwa wafugaji yatoke, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu, lakini nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Jafo pamoja na wasaidizi wake. Mheshimiwa Jafo anafanya kazi kubwa mno na sijui kama familia yake anakaa nayo saa ngapi kwa sababu kila wakati tunamwona kwenye vyombo vya habari akiwa kwenye shughuli za Kitaifa. Nawaomba Wabunge wenzangu tuwaombee Mungu hawa Mawaziri kwa sababu wanatumia vyombo vilivyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Wakati wowote wanaweza wakapata hatari za barabarani na tulishuhudia juzi juzi tu Mheshimiwa Kakunda alipata ajali mbaya, tunamshukuru Mungu kwamba hakuumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuuliza swali moja ambalo limenisumbua, nimesikia baadhi ya Wabunge wa upande wa Upinzani wakisema kwamba hawaruhusiwi kufanya mikutano. Mimi ninavyojua ni kwamba kila Mbunge anaruhusiwa kufanya mkutano katika jimbo lake. Sasa sijui pengine tuje tupate ufafanuzi kwamba ni mikutano ipi wanayoilalamikia kwa sababu hata sisi tunaruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo yetu. Kama wewe siyo Mbunge wa Dodoma Mjini unataka uje ufanye mkutano katika Jimbo la Dodoma Mjini unataka nini Dodoma Mjini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokijua ni kwamba Mbunge anaruhusiwa kufanya mikutano kwenye eneo lake. Kama lipo jambo lingine Mheshimiwa Waziri naomba Serikali ije itoe ufafanuzi, lakini ndivyo ninavyojua. Pengine lisiwe kwa ajili ya kuwapotosha wananchi kwamba wamekatazwa kufanya mikutano iwe dhahiri kwamba Mbunge yeyote anaruhusiwa kufanya mkutano katika eneo lake la kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, neno la Mungu linasema aombaye hupewa, atafutaje huona na abishaye hufunguliwa. Sisi watu wa Dodoma tumeomba sana, tuliomba sana Serikali ihamie Dodoma na namshukuru Mheshimiwa Rais na Serikali yake ya Awamu ya Tano ametimiza lengo lile, yale maombi yetu tuliyoomba siku nyingi ameyatimiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi mvua za masika zikinyesha watu wanaotoka Kilosa kwa njia ya reli kuja Dodoma wanaweza wakalala wiki nzima njiani hawajafika Dodoma kwa sababu ya mafuriko. Sasa hivi reli inatengenezwa Standard Gauge kitu ambacho sisi Watanzania hatukutegemea kwamba tungepata kwa muda mfupi hivi. Naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wa kujenga standard gauge tena kwa fedha zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani ukitaka kuja Dodoma lazima ukodi ndege yako au ndege za kukodi, sasa hivi Air Tanzania inakuja Dodoma mara tatu kwa wiki, hatukulitegemea kwa haraka hivyo. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa mafanikio tunayoyapata Mkoa wa Dodoma. Sasa hivi mikutano mikubwa inafanyika Dodoma na hivi sasa tuna Bunge la Afrika Mashariki hapa hapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata Maafisa Mipango Miji wazuri na naamini Mji wa Dodoma utakuwa mji mzuri katika Afrika nzuri kama tutafuata utaratibu na ujenzi ambao tunaelekezwa na maafisa wetu ambao tumepata kutoka kwa Mheshimiwa Lukuvi. Kitu ambacho nakiomba ni kwamba kama kuna changamoto zozote kwa mfano ulipaji wa fidia kwa wananchi uende kwa wakati ili wananchi wapishe na makao makuu yaendelezwe kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kitu kimoja pia kwa Serikali yetu sikivu, Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali imeamua Makao Makuu yaje Dodoma, lakini bila sheria itakayoweka msingi kwamba Makao Makuu ya nchi hii ni Dodoma itaweza kuwa shida baadaye. Sijui mbele ya safari baada ya Mheshimiwa Magufuli kumaliza muda wake, atakayekuja simjui, lakini anaweza kuja mtu ambaye hapapendi Dodoma, kama hakuna sheria inayotamka kwamba Dodoma ni Makao Makuu kunaweza kukatokea mtafaruku mbele ya safari. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwamba walete basi Muswada wa Sheria hapa Bungeni na tuufanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ujio wa watu au ujio wa Makao Makuu nimeanza kuona changamoto kama upungufu wa maji, hasa maeneo ya UDOM kule, maji hayatoshi na kule kuna wanafunzi wengi wanaosoma kule. Niombe DUWASA wapate fedha za kutosha kwa ajili ya maji ili wageni wanaokuja basi wasiwazie tena Dar-es-Salaam wajue kwamba wamekuja mkoa wa asali na maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkoa wetu kabla ya ugeni huu haujaja tulikuwa na mahitaji ya Walimu wa sayansi 373, waliopo ni 258. Niiombe Serikali watuletee Walimu wa sayansi. Tuna maboma 116, tuna mahitaji ya maabara 116, yaliyopo ni 11 tu. Niiombe Serikali kukamilisha maboma ya maabara yaliyopo ili wanafunzi wapate elimu kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwa kukarabati na kujenga Kituo cha Afya Makole. Kituo kile kinahudumia zaidi ya wagonjwa 300, wauguzi hawatoshi, waganga hawatoshi, naomba tufikiriwe katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile jengo la Halmashauri ya Chamwino lina zaidi ya miaka 10 halijakamilika. Sasa hivi tunajitahidi kukamilisha ground floor lakini haitawatosha wafanyakazi wa Halmashauri ya Chamwino. Naomba fedha zitolewe kwa ajili ya kukamilisha jengo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Chemba wanaomba magari mawili tu ili yawasaidie kutoa huduma ya afya na elimu kwa sababu magari waliyonayo ni machakavu. Mkitusaidia katika hilo tutashukuru sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa neema yake iliyonipa nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako tukufu.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Athuman Kihamia, nachukua nafasi hii kumpongeza Athuman Kihamia aliyekuwa Mkurugenzi wa Kaliua, alipofika Kaliua yeye ndiye aliyetoa taarifa Serikali juu ya ubadhirifu mtu kama huyu anastahili kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashangaa mtu aliyesema juu ya ubadhirifu analaumiwa leo, sasa je, angenyamaza taarifa hizi zingepatikana wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni Mjumbe wa PAC na nitasema kweli yale ambayo tuliyazungumza Kamati ya PAC, Vote 20 haikujadiliwa PAC na hatukuwahi kuijadili na mtu anaposimama na kusema kwamba vote 20 ni kichaka anamkosea yule anayetumia vote 20. Huwezi kusema kwamba vote 20 ni kichaka, wakati vote 20 haikuwahi kujadiliwa na PAC na mimi nakwambia mimi ni Mjumbe…(Makofi)

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura kuna taarifa, Mheshimiwa Catherine Ruge.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, wala siwezi kupokea taarifa ya mtu ambaye sio Mjumbe wa Kamati, siwezi kupokea taarifa ya mtu ambaye sio Mjumbe wa Kamati.

WABUNGE FULANI: Buuuuu!

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika naendelea, Kamati yetu, Kamati ya PAC, upande wa pili sijui wamepatwa ugonjwa gani wa kelele!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu shilingi trilioni 1.5, tumezungumza sana, vizuri sana Kamati yetu imezungumza vizuri sana na taarifa tumeandika kuanzia ukurasa wa 15 hadi ukurasa wa 31 na tumefafanua kila jambo, kila kipengele hata yule ambaye hajui mahesabu anaweza akasoma na akaelewa kwamba tumeeleza nini kuhusu pesa trilioni 1.5 na naomba nisome ukurasa wa 35 inasema hivi na taarifa hii amesoma Mwenyekiti wa PAC; “Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha suala la tofauti ya shilingi trilioni 1.5 kati ya mapato ya Serikali na makusanyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 naomba kuweka kumbukumbu sahihi katika Bunge lako tukufu kuwa tofauti hiyo haikuwepo baada ya marekebisho ya hesabu kufanyika.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunajadili taarifa hii tulikuwa Wabunge mchanganyiko chama cha CCM Wajumbe walikuwepo, vyama vya upinzani Wajumbe wake walikuwepo, na waliuliza maswali na walisikia jinsi CAG alivyoeleza na walisikia TRA walikuwepo, BOT walikuwepo, Wizara ya Fedha walikuwepo walisema waziwazi wala hawakuficha jambo lolote, leo mtu anakuja anauliza trilioni
1.5 iko wapi?

MBUNGE FULANI: Wazushi hao

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, sema humu, utapata taarifa zote.

MBUNGE FULANI: Wazushi hao

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, soma taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waliodhani kwamba Tanzania bado itakuwa shamba la bibi, watapata taabu sana.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu yuko makini na anafanya kazi kwa umakini.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura, Mheshimiwa John Heche.

MBUNGE FULANI: Sikiliza.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei taarifa hiyo, unajua naomba unajua kupe aking’ang’ania kwenye ngozi hata kama anachomwa moto, ile ngozi inachomwa moto hawezi kujua, kwa hiyo, ameng’ang’ania jambo moja ambalo limefafanuliwa mbele kwenye taarifa hataki kusoma, asome taarifa yetu mpaka ukurasa wa 37 ataona maelezo, sasa aking’ang’ania ukurasa wa 15; atang’ang’ania na sisi tunasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano, inapiga vita ufisadi na wale watendaji waliodhani kwamba…

MHE. JAMES K. MILLYA: Taarifa.

MHE. FELISTER A. BURA: …ukifanya ufisadi, ndio namna ya kufanya kazi...

MHE. JAMES K. MILLYA: Taarifa.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika hawatafika mbali.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura kuna taarifa nyingine, Mheshimiwa James Millya.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee, na niseme kwamba…

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. FELISTER A. BURA:… kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano, haina muda kabisa na wale wabadhirifu wa mali ya umma.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura, kuna taarifa. Mheshimiwa Mwambe.

T A A R I F A

MHE: FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuwa macho na kuwarudisha Waheshimiwa Wabunge kwenye mstari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mwanzo Serikali ya Awamu ya Tano, haina mchezo, na wabadhirifu wa mali ya umma, haina mchezo na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alipoingia madarakani aliona mambo yaliyofanywa na baadhi ya mashirika ya umma na akawatoa wale, haraka ilivyowezekana. Nitoe mfano, kuna uwekezaji usio tija ambao Serikali iliona na baadhi ya watendaji kwa mfano NSSF Wakurugenzi wote, walifukuzwa kazi, kwa miradi isiyokuwa na tija. (Makofi)

Sasa niombe Serikali yangu…

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ya Awamu ya Tano, kusimamia miradi yote…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura kuna taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei taarifa kwa sababu Mheshimiwa Mbunge hataki kusoma taarifa yote, hataki kusoma kuanzia ukurasa wa 15 hadi ukurasa wa 37, asome apate mantiki yote ya maelezo ya CAG, Ofisi ya Hazina, BOT na Mamlaka ya Mapato Tanzania, kwa hiyo taarifa yake sipokei.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba nchi yetu, Serikali ya Awamu ya Tano, ambaye anafanya kazi…

MHE. JAMES K. MILLYA: Taarifa! Taarifa!

MBUNGE FULANI: Endelea, hiyo hiyo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa James Millya.

T A A R I F A

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa ndugu yangu kwenye ukurasa wa 37 kwamba ripoti ya PAC pale mwisho inasema hivi naomba ninukuu; “Kwa hiyo kitu tulichokuwa tunashughulikia nacho hapa, je, tofauti hii, imeletwa na nini? Tutapata maelezo ya kutosha kuhusu tofauti hii na ukiisoma ripoti yetu, utaona ile table, inaonesha kwamba tumepata reconciliation.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu ni CAG, kwa hiyo hilo linajibu hilo swali, naomba kuwasilisha. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Millya kwa kunisaidia na kuwasaidia wengine wasiotaka kusoma, wasome hii taarifa, kwa nini hawataki kuisoma!

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema, tunaiomba Serikali yetu, sasa isimamie miradi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Haonga, kwa Mheshimiwa Felister Bura hiyo itakuwa ni taarifa ya mwisho, Mheshimiwa Haonga.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Bura, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa sipokei, kwa sababu wamefukuzwa kazi, Wakurugenzi wote waliokuwa NSSF kwa ajili ya ubadhirifu, Wakurugenzi kumi wamefukuzwa kazi. Kwa hiyo, hiyo taarifa siwezi kupokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali yangu, kwamba sasa, tuelekeze muda wetu, tuelekeze nguvu zetu katika kusimamia miradi yenye tija, maeneo yale, ambayo kwa mfano NSSF walikuwa wajenge Ofisi kule Nairobi, Wizara ya Mambo ya Nje wapo, kwa hiyo wawasiliane na NSSF huu mradi uendelee. Kuna mradi wa kuzalisha umeme Mkuranga, mradi huu uendelee kwa sababu Halmashauri ya Mkuranga ipo, NSSF wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna madeni ya SUMA JKT, Taasisi zilikopa watu binafsi walikopa, tuiombe Serikali wale waliokopa hawajaresha madeni, wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui ni kengele ya kwanza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai ambao ametupatia siku ya leo sisi Wabunge kwa ajili ya uwakilishi wa wananchi waliotuchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mambo makubwa anayowafanyia Watanzania. Kuna msemo unaosema Nabii hakubaliki kwako lakini kuna nchi wanazotamani Magufuli awe Rais wao kwa utendaji na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu tuwaombe viongozi wetu Mungu awape afya njema na waendelee kutawala kwa hekima na maarifa itokayo kwa Mungu. Wanafanya kazi nzuri, tuwa-support kwa jinsi wanavyofanya kazi nzuri. Sisi wananchi wa Dodoma tupo pamoja nao, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu lakini zaidi ya yote tunafanya kazi. Wabunge wa Dodoma tunafanya kazi kuonyesha kwamba tunamuunga mkono Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumefanyiwa mambo mengi sana na Serikali ya Awamu ya Tano. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana kwa Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo, tutamuunga mkono Rais wetu, treni ile iliyokuwa ya Mwakyembe Dar es Salaam utaikuta Dodoma, barabara za mizunguko utazikuta Dodoma, soko la kimataifa na standi ya kimataifa utavikuta Dodoma. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge usipojenga Dodoma utajutia maisha yako na familia yako itakulaani kwa nini hujajenga Dodoma kwa sababu Geneva ya Tanzania inakuja kuwa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza mji kuna mambo, kuna utwaaji wa ardhi na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazoendeleza. Wananchi wangu wa Dodoma wa Msalato pale ambapo uwanja wa Kimataifa unajengwa kuna wanaodai fidia. Niombe Serikali iwalipe wananchi wale fidia ili wakianza kujenga kusiwepo na malalamiko ya wananchi. Eneo la Ihumwa limechukuliwa kwa ajili ya bandari kavu, niiombe Serikali sasa wale wananchi walipwe fidia ili wasiendelee kuidai Serikali. Tunajua Serikali inafanya kazi kubwa lakini pia niombe kwamba malalamiko haya madogo sasa yasiwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ongezeko la watu Dodoma, shule sasa zimejaa sana watoto; shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeandikisha watoto shule za awali 15,000, watoto wa darasa la kwanza tumeandikisha 11,979, hawa si wachache. Tumejikita sana kwenye ujenzi wa shule za sekondari tukasahau kwamba watoto wa shule za msingi wanahitaji pia madarasa, wanavyoongezeka madarasa hayatoshi. Utafiti ufanyike kuona kwamba hawa watoto wanaoanza shule, kwa mfano hawa 15,000 shule ya msingi watakwenda wapi, madarasa hayatoshi. Tumekazania kujenga shule za sekondari lakini za msingi je? Madarasa ya shule za msingi hatujaongeza muda mrefu, Serikali iangalie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi Dodoma tulitoa ardhi kwa Serikali kwa ajili wa ujenzi wa shule nyingine, shule ya kitaifa badala ya Shule ya Sekondari ya Mazengo. Tulitoa ardhi na Waziri wa Elimu alipewa ile ardhi kwa ajili kujenga shule ya kifaifa badala ya Shule ya Mazengo iliyorudishwa kwa waliokuwa wamiliki wa Kanisa la Anglikana. Sasa eneo lile tulilolitoa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kitaifa mpaka sasa haijajengwa mwishowe wananchi watavamia lile eneo halafu tutaanza sasa suala la ulipaji fidia. Niombe sasa Wizara ikachukue eneo lile kwa sababu shule inayojengwa pale ni ya kitaifa itachukua wanafunzi Tanzania nzima basi waanze suala la ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lile tulilolitoa kwa ajili ya Shule ya Kitaifa halijajengwa mpaka sasa, mwisho wananchi watavamia lile eneo halafu tutaanza sasa suala la ulipaji fidia. Naomba Wizara ikachukue lile eneo kwa sababu shule inayojengwa pale ni ya Kitaifa, itachukua wanafunzi Tanzania nzima, basi waanze suala la ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Walimu 656 wa shule za msingi kwa shule za Dodoma za pembezoni. Dodoma Jiji kuna mahali ikama ni Walimu 10 lakini utakuwa Walimu wako watatu tu. Naiomba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, Serikali Sikivu, Serikali inayowajali wanyonge, Serikali iliyoamua kwamba kila mtoto apate elimu. Mtoto atapata elimu nzuri tu kama Walimu wako shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba maeneo yote na siyo Dodoma tu, naombe maeneo mengine ambayo Walimu hawatoshelezi tuletewe Walimu wa kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Serikali ya viwanda, yaani tunataka kujenga viwanda; hatuwezi kujenga viwanda kama hatuna wanasayansi na Walimu wa Sayansi ndio hawatoshi katika maeneo yetu. Naiomba Serikali yangu, wako Walimu waliomaliza Elimu ya Vyuo Vikuu na walisoma masomo ya sayansi, tuombe sasa katika ugawaji wa Walimu wa Shule za Sekondari, tupeni hao Walimu ili tuwapate watoto watakaotumika viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza suala la elimu, niombe sasa, katika Jiji letu tuna vijiji 34 ambavyo tunavihesabu kama ni mitaa. Wawekezaji wako wengi lakini hatuna umeme, vijiji hivyo vipate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Joel Mwaka amezungumzia suala la hospitali ya Uhuru na pesa za kujenga hospitali ya Uhuru ilitokana na maadhimisho ya Desemba 9, Mheshimiwa Rais akaamua hizo fedha zijenge Hospitali ya Uhuru Wilayani Chamwino. Mpaka leo fedha hizo hazijafika katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ili zijenge hiyo hospitali. Naiomba Serikali, katika bajeti hii hizo fedha zije na kama zilishatengwa na Mheshimiwa Rais alitamka, tupeni hizo fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ina miaka zaidi ya kumi wamehamia lakini wamehamia floor ya chini, lile jengo halijaisha. Tumeomba shilingi milioni 900 ili tujenge jengo lile la Halmashauri. Tunawashukuru kwamba mmetupa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hizo fedha zije sasa ili Mkuu wa Mkoa awe na ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Mariam amezungumzia suala la mabasi ya mwendokasi. Tunaishukuru Serikali na kuipongeza kwamba sasa hivi usafiri wa Dar es Salaam ni wa haraka, lakini mabasi yale mengi yameharibika, yatengenezwe sasa. Miundombinu ya mwendokasi imechukua pesa nyingi za Watanzania, Serikali ikubali kwamba yeyote mwenye uwezo wa kuendesha njia ya mwendokasi, basi waweke magari pale yaweze kuwahudumia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna maboma ambayo hayajakamilishwa au kuna maeneo ambayo vituo vya afya havijafika. Naomba Kata ya Kolo Wilayani Kondoa, wananchi wanatembea kilometa 30 kwenda kutafuta huduma ya afya. Naomba sana, Serikali itusaidie Kituo cha Afya pale Kondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Posho ya Madiwani; Madiwani ni watu muhimu katika Taifa hili, wanafanya kazi kubwa. Madiwani wafikiriwe, wanafanya kazi kubwa, lakini posho inayotolewa kwa Madiwani haitoshi, kidogo mno; na wakati mwingine wanakaa hata miezi mitatu hawajapata posho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu sikivu inayowajali wananchi wake, Posho za Madiwani zikafanyiwe ufumbuzi sasa ili Madiwani wafanye kazi kwa moyo mmoja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Felister.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na kwa neema yake aliyotupatia siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa shughuli za maendeleo zinazofanyika kwa mkoa wetu na nashukuru kwamba inawajali wananchi wake. Jiji la Dodoma linakua kwa kasi sana na watu wanaongezeka kwa wingi sana na kwa hiyo mahitaji ya maji ni makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya pembezoni kama Mpunguzi, Mtumba na maeneo mengine hawajapata maji kwa sababu mtandao unaohitajika kule unahitaji fedha nyingi. Sisi kama Jiji tumeomba shilingi milioni 800 kupitia Shirika letu la Maji la DUWASA ili waweze kuchimba visima vya maji katika maeneo ya pembezoni ili viwanda vitakavyojengwa maeneo hayo na ofisi zitakazofunguliwa wasipate shida ya maji. Kwa hiyo, tumeomba shilingi milioni 800 kwa ajili kuongeza visima kwa maeneo ya pembezoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miaka takribani nane au kumi na kila mwaka suala la Bwawa la Farkwa (bwawa la mkakati) linazungumzwa katika bajeti ya Waziri wa Maji na hatuoni jambo linaloendelea katika uchimbaji wa bwawa hili la mkakati. Bwawa hili kama alivyosema Waziri mwenyewe litawasaidia wakazi wa Jiji la Dodoma, Wilaya ya Chemba na Bahi na hasa wakazi wa Bahi ambao ni wakulima wazuri wa mpunga na wakulima hawa wanalisha Jiji la Dodoma na Mkoa wa Singida. Mwaka huu hatuna mchele kwa sababu mvua haikunyesha na bwawa lile halijachimbwa na kila mwaka tunaambiwa ni bwawa la mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa ifike wakati bwawa hili lichimbwe liweze kuwasaidia wananchi wa Chemba, Jiji la Dodoma na Bahi. Nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtua mama ndoo kichwani na wananchi ambao mradi huu utapita katika maeneo yao wanauhitaji mkubwa wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa mradi wa Ntomoko. Mradi huu ni wa miaka mingi sana na ni maporomoko ambayo yana maji ya kutosha. DUWASA ambao wamepewa kazi ya kutengeneza miundombinu na kufufua miundombinu iliyochakaa, wameomba shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuanza uchimbaji na kutengeneza mradi huu wa Ntomoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Ntomoko wamesubiri vya kutosha, wamesubiri miaka na mimi katika Ubunge wangu nimesimama katika Bunge hili mara nyingi nikiomba wananchi wa Ntomoko wapewe maji. Vile vijiji 12 vinavyozunguka mradi huu wa Ntomoko, maji hayajapatikana mpaka leo. Waliohujumu mradi huu na wako mahakamani, lakini kuwepo kwao mahakamani hakumfanyi mwananchi akapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Serikali yangu sikivu, wananchi wa pale wapewe maji, wananchi wa Ntomoko wanaona maji yanabubujika pale lakini hawajawahi kupata maji. Nashauri wachimbiwe kisima basi wapate maji kupitia kisima kwa sababu wao hawakula fedha za mradi, waliokula fedha za mradi wanajulikana, kwa nini wasipate maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 52 Serikali imesema kwamba vijiji 11 vinavyozunguka mradi huu watapata maji kupitia mradi mkubwa wa bwawa linalotarajiwa kuchimbwa, bwawa hili linachimbwa katika kata gani? Naomba Mheshimiwa Waziri ukija kujibu uniambie bwawa hili linachimbwa katika kata gani na kijiji gani ili hata Mbunge wa Chemba au mimi mwenyewe nitakapokwenda niwaambie wananchi kwamba vuteni subira, bwawa linakuja kuchimbwa hapa katika kijiji Fulani. Hata bajeti, anasema katika mwaka wa fedha 2019/2020, sijaona fedha zilizotengwa kwa ajili ya uchimbaji au usanifu wa bwawa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kule kwenye Bwawa la Farkwa kusema kwamba, hata wananchi wa kule Farkwa hawajalipwa fidia. Unasemaje kwamba mradi wa mkakati wakati wananchi hawajalipwa fidia? Niombe wananchi wa Mombosee na Bubutole walipwe fidia ili mradi utakapoanza basi kusiwepo na tatizo lolote la wananchi kudai fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi Ntomoko, naomba wananchi wale wakumbukwe walichimbiwe hata kisima. Wananchi wa Ntomoko, Fai na vile vijiji 11 kama nilivyosema Waziri atuambie kwamba bwawa hili linachimbwa katika kata ipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maji kule Kondoa. Kondoa tumepewa shilingi bilioni 4 kwa ajili ya visima, visima vimechimbwa, maji yako ardhini lakini hakuna miundombinu. Kwa hiyo, ukimwambia mwananchi kwamba kisima kimechimbwa inawezekana aliona gari likichimba kisima pale lakini, je, maji anayo? Mwananchi anachotaka ni maji, basi tuwajengee miundombinu wapate maji wale wananchi wa Kondoa Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hilo liko Chilonwa, Wilaya ya Chamwino, visima 12 vimechimbwa maji yapo tena virefu lakini hakuna miundombinu. Kwa hiyo, wanawake bado wanahangaika kilometa 10, 15 kwa ajili ya kutafuta maji. Tunajua Mkoa wa Dodoma ni kame, hakuna maji, maji lazima yatafutwe ardhini. Niombe sana Serikali yetu sikivu maeneo ambayo maji yamekwishachimbwa na yapo sasa miundombinu itengenezwe ili wananchi wapate maji, wanawake na watoto wafanye shughuli zingine waondokane na tatizo la kuamka saa kumi usiku na kuacha shughuli za nyumbani wakienda kutafuta maji. Vijiji vya Deti, Zajilwa, Itiso, Segala, Dabalo, Chilonwa, Nsamalo na Manchali visima vipo na viko visima nane vilivyochimbwa mwaka huu maji yapo lakini hakuna miundombinu na fedha tumeomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uvunaji wa maji limezungumzwa na Wabunge wengi, naomba sasa Serikali yetu kama hatuna uwezo wa kuchimba visima na kutoa maji maeneo ya mbali kwa ajili ya kuwasaidi wananchi wetu, basi Taasisi za Serikali, shule za msingi, shule za sekondari, zahanati, vituo vya afya, tujenge miundombinu ya kuvuna maji ya mvua. Inawezekana kabisa kero ya maji kwa wananchi wetu ikapungua. Naomba Serikali iweke mkakati huo na uvunaji wa maji hauchukui fedha nyingi na Mheshimiwa Waziri na Serikali inajua. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Bura kwa mchango wako.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. FELISTER A BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo na nikupongeze kwa kusimamia Bunge hili vizuri kwa siku ya leo. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake, mdogo wangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu kwa kazi nzuri sana wanayoifanya katika Wizara hii ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sina fadhila kama sitaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa mambo mazuri ambayo yanafanywa katika Mkoa wetu wa Dodoma baada ya Serikali kuhamia Dodoma. Tunaona sasa kuna mipango mikubwa ambayo imewekwa kwa ajili ya kuendeleza Mji wa Dodoma, mashirika mbalimbali yameanza kujengwa na watumishi wameshahamia Dodoma. Kwa hiyo niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, lakini zaidi ya yote niwapongeze kwa kuamua kutumia force account, kupunguza gharama kubwa ya ujenzi iliyokuwa inatumika siku za nyuma, majengo au vituo vya afya ambavyo vilikuwa vinajengwa takribani kwa Sh.1,000,000,000 sasa tunajenga kwa Sh.500,000,000. Ni jambo la kuipongeza sana Serikali na tunaona kwa kutumia force account tumeweza kujenga majengo mengi na tumeweza kujenga vituo vya afya vingi na niombe Serikali iendelee kutumia force account katika majengo yake, lakini hata kwa mambo mbalimbali ambayo kwa mipango mbalimbali ya ujenzi tunaona jinsi tulivyopunguza gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kwamba, kwa sasa Serikali imeagiza kwamba malipo yote yalipwe na kila biashara inayofanyika mwananchi au taasisi yoyote ipate risiti ya elektroniki, lakini naona Serikali inapata sana hasara kwa taasisi aidha za umma au za binafsi na hata baadhi ya maduka makubwa na hata wafanyabiashara, wengine bado wanafanya biashara pasipo na kutoa risiti ya elektroniki, kwa hiyo mapato mengi yanavuja kupitia njia hiyo. Nadhani udhibiti ukiwekwa madhubuti na bado kuna baadhi ya maduka au baadhi ya wafanyabiashara wanakuuliza unataka risiti ya eleketroniki na anakwambia ukitaka risiti ya elektroniki bei ni hii na ukitaka risiti iliyoandikwa kwa mkono bei ni hii na hata vituo vya mafuta usipoangalia risiti yako uliyopewa unaweza ukakuta risiti uliyopewa siyo ya mafuta uliyojaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi tunachukua risiti hizo bila kuangalia fedha uliyolipa, ni sawa na lita ulizopata, kwa hiyo bado kuna loophole sana katika matumizi ya risiti za elektroniki. Nimwombe Mheshimiwa Waziri au niombe sana Serikali yangu sikivu iangalie namna ya kusimamia matumizi ya risiti ya elektroniki. Nchi zingine ukienda huwezi kununua kitu bila kupata risiti iliyo sahihi, lakini Watanzania bado tunakwepa malipo kwa kutumia risiti za elektroniki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali kwa kuanzisha miradi ya mikakati reli ya kati, viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege na hata mitambo ya kufua umeme kule Julius Nyerere, kule Rufiji. Ni miradi mikubwa ambayo Watanzania hatukuwaza kuwa nayo leo, hatukuwaza hayo lakini Awamu ya Tano imeleta mambo makubwa hayo kwa Watanzania, itafika muda tukitoka Dar es Salaam tutafika Dodoma baada ya masaa mawili na reli hii itakuwa na faida zaidi kama itabeba mazao ya wakulima katika maeneo mbalimbali itakapopita reli hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwamba bandari kavu ipo Dodoma na mizigo mingi itachukuliwa Dodoma. Hata hivyo, mizigo hii reli itapata nafasi kama mazao ya wakulima yatakuwepo na iwe wakati sasa wa Benki ya Kilimo inafanya kazi Dar es Salaam na kama ina matawi sio nchi nzima lakini wakulima wamesambaa nchi nzima. Umesikia Waheshimiwa Wabunge wengi wanazungumza habari ya kilimo, kwa sababu wanaishi na wakulima na 65% karibu 70% ya Watanzania ni wakulima. Kwa hiyo tunaposema habari ya kilimo tuna maana na tunajua sababu ya kuzungumzia habari ya kilimo, kwa hiyo Benki ya Kilimo haijafanya kazi yake inavyotakiwa na kwa sababu ina matawi ambayo hayakusambaa nchi nzima bado ni vigumu kupata mikopo kupitia Benki ya Kilimo na wanaopata mikopo hiyo ni wale wanaoelewa na ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Benki ya Kilimo ukauliza ni wakulima wangapi wa Dodoma wameweza kukopa, ni wachache mno, sio kwamba hawataki wanataka, lakini kutoka hapa kwenda Dar es Salaam na kulala kwa ajili ya kutafuta mkopo ni kazi na kama tunalo tawi Dodoma, Singida hawana na kama tunalo tawi Dodoma Iringa hawana tawi, Babati hawana tawi, kwa hiyo tuone namna ya kuwaunganisha wakulima wa kati na wakulima wadogo kupata mikopo kupitia Benki ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tukipata mikopo tutaweza kununua pembejeo, tunatamani kulima kwa hali ya juu sana, lakini tunalimaje tunapata mikopo wapi, tunanunuaje pembejeo, ukisema ununue trekta sio chini ya 50,000,000. Kwa hiyo, sasa ni wakati wa Benki ya Kilimo kusambaa katika mikoa yetu na wakulima wakafaidi matunda ya kuwa na sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumzie Sekta ya Mifugo. Tumejaliwa kuwa mifugo Tanzania na Tanzania yetu ni nchi ya tatu Afrika kuwa na mifugo, lakini bado hatujaweza kuwa na viwanda vya kutosha kuchakata mazao ya mifugo. Nakumbuka Bunge lililopita niliuliza swali kuhusu viwanda vyetu vya kuchakata mazao ya mifugo na Mheshimiwa Waziri akaniambia kwamba wana utaratibu wa kuingia ubia na kiwanda kile kilichoko Pwani nadhani, kilichoko Ruvu, lakini michakato hii bado inaendelea. Kiwanda kimoja tu tusikitegemee pamoja na kwamba kuna viwanda vya watu binafsi, tungeweka utaratibu kwamba hata ranch zetu kama ni ranch moja au kama ni ranch mbili tuna ranch nyingi Tanzania, tukaweka ranch moja au mbili au tatu kama mfano, wakaanzisha viwanda au kiwanda kwa ajili ya kuchakata mazao ya mifugo ili Watanzania wapate masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachogomba hapa ni soko, hata ukirudi kwenye mazao watu wa korosho wanalia, watu wa pamba wanalia, tumbaku wanasema, kahawa wanasema, wakulima wa mbaazi wanatafuta soko, sisi wa zabibu ndio hatuna kabisa soko. Kwa hiyo tatizo lililopo ambalo naliona ni masoko, mazao tunayauza wapi, lakini hata mazao ya mifugo tunauza wapi, tuna ASASI Iringa, lakini tuna kiwanda kingine cha maziwa Tanga lakini hapa katikati Dodoma tuna kiwanda gani pamoja na kwamba tuna ranch, nyama tuuzie wapi. Nakumbuka walinifuata vijana wa UDOM hapa, wanataka kuuza nyama nje, lakini namna ya kusafirisha nyama hiyo ifike huko kwanza hawana mtaji, lakini la pili wanafanyaje. Kwa hiyo tungekuwa na kiwanda chetu Tanzania cha kuchakata ngozi nyama maziwa viwanda vya kutosha nafikiri wasingehangaika.

MWENYEKITI: Ahsante sana

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo kengele ya kwanza.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imelia Mheshimiwa Felister, ahsante sana nashukuru

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adimu ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya aliyonijalia siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano wa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma. Kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano tulikuwa tunaona kurasa ripoti ya PAC na ripoti ya LAAC zilikuwa na kurasa zaidi ya 100, lakini kwa sasa ukiangalia taarifa iliyoletwa na Kamati hizi mbili unaona jinsi matumizi yalivyodhibitiwa na Serikali na fedha za umma zinatumika ipasavyo. Ukitaka kushuhudia hali hiyo Bunge lako Tukufu lilitoa maazimio kwa Serikali na maazimio hayo yametekelezwa kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu mfano kwamba, Serikali imeboresha mfumo wa ulipaji kwa Mfuko Mkuu wa Serikali, lakini Serikali pia imeboresha mfumo wa ulipaji mishahara, kuondoa mishahara hewa, vile vile akaunti jumuishi Serikali imeboresha. Kamati yetu kipindi kilichopita tuliiomba Serikali kuona namna ya ukusanyaji wa madeni na hasa madeni ya SUMA JKT ambayo ilikopwa na watu binafsi. Tumeona mpaka mwezi wa sita mwaka 2018, Serikali imeweza kukusanya bilioni saba na milioni mia tisa. Pia tumeona madeni chechefu ya TIB
yameanza kukusanywa. Hii inaonesha jinsi Serikali ilivyo makini sasa kusimamia matumizi ya fedha za umma, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano. Serikali pia imehakikishia Kamati kwamba itaendelea kuzingatia Sheria ya Bajeti na kwa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo CAG ameona upungufu kwa mashirika aliyokagua kati ya mashirika 150 amekagua mashirika 122, lakini kati ya mashirika hayo aliyokagua ameona upungufu, kama walivyosema wenzangu lakini nianze na STAMICO.

Mheshimiwa Naibu Spika, STAMICO CAG ameshindwa kutoa maoni yake kutokana na kasoro ambazo ni kubwa zilizoonekana katika shirika hili. Katika shirika hili la STAMICO shirika limepata hasara ya bilioni mbili na milioni 387 na hasara hii imetokana na nini, hasara hii imetokana na kutojumuishwa taarifa ya makampuni tanzu ya STAMICO. STAMI Gold Limited na Kyelwa Tin Company ambayo hesabu jumuishi ya mashirika haikujumuishwa kwenye taarifa ya hesabu ya STAMICO. Pia hali halisi ya madeni ya mashirika haya, lakini hali halisi ya madeni ya STAMICO, pia uwekezaji wa bilioni 33 ya uwekezaji STAMICO katika kampuni hizi sio wa uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, STAMICO haijafanya tathmini ya uwekezaji au ya makubaliano yake kati yake na Tanzania One Mining na kama ni uendeshaji wa pamoja au kama ni joint venture. Kwa hiyo haya yamefanya CAG asitoe maoni. Niiombe Serikali imeweza kudhibiti mambo mengi kwa mashirika ya umma imeweza kudhibiti matumizi mabaya kwa mashirika ya umma na hata kwa halmashauri zetu itupie jicho STAMICO na kusimamia haya ambayo CAG ameyaona kwa STAMICO. Pia STAMICO iliweka asilimia 10 ya uwekezaji kwa kampuni ya Itetemia, STAMICO haijawahi kupata faida stahiki. Kwa hiyo niiombe Serikali iangalie namna ya kuisaidia STAMICO.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tulikagua National Housing, National Housing kazi yake ni kujenga na kuuza majengo hapa nchini na imejenga majengo mengi katika halmashauri zetu, lakini kuna uwekezaji uliofanywa pale Kawe, uwekezaji wa nyumba 711 kwa site ya kwanza. Hata hivyo, mpaka sasa ule uwekezaji umesimama na umesimama kwa sababu Shirika la Nyumba la Taifa halina fedha za kuendesha ile miradi, lakini pia tumeona miradi ya pale eneo la Victoria pia kuna miradi mikubwa ambayo National Housing ilianza kujenga ni vitega uchumi lakini mpaka sasa miradi ile imesimama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina wasiwasi kwamba wale wakandarasi waliokuwa wanajenga zile nyumba watakuja kuleta hasara kwa National Housing kwa sababu watadai fedha. Wamesimama ujenzi sio kwamba wao wameshindwa kazi, wamesimama ujenzi kwa sababu hakuna fedha za kuendeleza ujenzi. Kwa hiyo wao wanahesabu kila siku faida, kila siku hasara wanayoipata kila siku wanachaji kwa National Housing na hizi fedha National Housing walizikopa sio kwamba ni za kwao na kule walikokopa kila siku riba inaingia.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali iamue kukwamua National Housing tusiache lile shirika letu zuri ambalo limefanya kazi nzuri kwa muda mrefu likapata hasara ambayo haitaweza kumudu kulipa na tumeona kama Serikali haitawasaidia bilioni 99 kwa ripoti ya CAG tuliyoipata watatakiwa kuwalipa wakandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze pia juu ya TPA au juu ya bandari tumeona hali halisi ya bandari ilivyo. Nawashukuru na kuwapongeza kwamba walitoa gawio Serikalini bilioni 168, walitoa Serikalini, nawapongeza sana, lakini kitu ambacho ni shida pale ni usimikaji wa mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa shughuli za bandari. Bandari ni shirika ambalo tunalitegemea kuisaidia Serikali katika mapato, lakini kama mifumo haieleweki na mifumo yenyewe imeshagharimu bilioni 57 lakini mpaka leo haijakamilika. Niiombe Serikali isaidie na kuisimamia bandari ili mifumo hii ikakamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la UDOM, UDOM waliingia mkataba na Bima ya Afya kwamba Bima ya Afya wajenge Hospitali ya Benjamini Mkapa na mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Dodoma naishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa hospitali ya Bima ya Afya, wengi wanapata huduma pale na huduma inayopatikana pale maeneo mengine inawezekana haipatikani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, BIMA waliambiwa na Serikali kwamba watapewa dhamana ya Serikali kufidia lile deni mpaka leo dhamana ya Serikali haijatoka. Mimi nilidhani ni kitu rahisi tu kwa Serikali kutoa dhamana ya kwake kwa mfuko wa Bima ya Afya. Kwa hiyo, niiombe Serikali, deni hili linazidi kukua kwa sababu ni muda mrefu sasa na mimi kama mkazi wa Dodoma naishukuru sana Serikali kupata hospitali ya Benjamin Mkapa. Lakini basi watoe dhamana kwa ule mfuko maana mfuko huu ni mfuko unaowatibu wenye uwezo na wasio na uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana. Naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha za umma na kwa kuchukua hatua za haraka pale ambapo inaonekana kwamba kuna ufujaji wa pesa. Naunga mkono ripoti za Kamati zote mbili. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ya siku ya leo kwa uhai na baraka tele katika maisha yetu. Nina mambo machache ya kuchangia; la kwanza, niipongeze Wizara kwa kazi nzuri ambayo tumesoma kwenye bajeti yao na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimshukuru kwamba sasa hivi wamekubali kukata vitalu kwa ajili ya wafugaji ambao wanazunguka maeneo ya ranch.

Mheshimiwa Spika, kwetu Dodoma tuna ranch ya Kongwa na wananchi wanakwenda pale kwenye vitalu vile kwa ajili ya ufugaji, lakini kitu ambacho naona ni kigumu kwa wananchi wangu ni kulipishwa ng’ombe mmoja Sh.10,000 kwa mwezi. Naona gharama hii ni kubwa sana, kwa sababu ranch wanapoingia hakuna majani ambayo yamepandwa na watumishi wa ranch, hakuna dawa ambayo wanapewa mifugo wanaoingia katika vitalu vile. Kwa hiyo ukisema kwamba mfugaji mmoja ana ng’ombe 50 tu na ng’ombe 50 kwa Dodoma ni ng’ombe wachache sana, ng’ombe 50 kwa mwezi akiingiza kwenye kitalu cha ranch ni Sh.500,000 kwa mwezi mmoja.

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara ione namna ya kupunguza bei hii ambayo ni kubwa katika vitalu vyetu ili kuwasaidia wafugaji. Hawana maeneo ya kuchunga ng’ombe, hawana maeneo kabisa na wanapomtoza mfugaji shilingi 10,000 kwa ng’ombe mmoja, akitoka pale hana pa kuuza maziwa, Dodoma hatuna kiwanda cha maziwa mpaka uende Arusha au mpaka mfugaji apeleke maziwa Iringa, kitu ambacho ni kigumu na ni gharama sana kwa mfugaji.

Mheshimiwa Spika, mbali ya hivyo wangetoa elimu wa wale ambao wanafuga katika vitalu vyao, hakuna elimu yoyote inayotolewa kwa wale wafugaji ambao wanafuga kwenye vitalu vya ranch na wanashindwa kununua mitamba ile, bora wangeruhusu mitamba ya ranch ikapanda ng’ombe za shilingi 1,600,000. Sasa mfugaji achunge ng’ombe kwenye kitalu Sh.10,000 kwa mwezi kwa kila ng’ombe, lakini akitaka mtamba anunue kwa Sh.1,600,000, sio haki. Naomba sasa Wizara iangalie namna ya kusaidia wafugaji wanaoingia kwenye ranch ambao wamekodi vitalu kwa bei ndogo, lakini wapate elimu na zaidi ya elimu wakubaliwe mitamba ya ranch iwapande ng’ombe wa wale ambao wako kwenye kitalu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni suala la chuo chetu cha TARILI cha Mpwapwa chuo hiki ni cha siku nyingi, ni chuo cha zamani, kinazalisha wataalam wazuri na kimepewa eneo kubwa sana na Serikali ya Wilaya ya Mpwapwa, lakini hawana vifaa, watumishi vibarua wa pale hawalipwi, waliokuwa wanashuhgulika mashambani kulima na kupanda majani kwa ajili ya ng’ombe walikwishaacha kazi, wala haki zao hawajalipwa. Hata hivyo, vibarua waliopo kuna vibarua 70 pale, nadhani wapo zaidi ya 70 hawajawahi kulipwa. Niombe kama kweli chuo kile ni cha thamani kwa Serikali yetu, kama chuo kile kina manufaa kwa nchi yetu, Serikali ione namna sasa ya kukisaidia kile chuo hata vifaa hawana, wanatakiwa kulima na kupanda mazao kwa ajili ya ng’ombe wale wanaowafuga pale na ng’ombe wa Mpwapwa ni wazuri mno ni wazuri sana hata kwa wafugaji wa mmoja mmoja, lakini hawana vifaa. Naomba Serikali sasa iwahudumie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tena juu ya Kiwanda cha SAAFI kilichopo Rukwa, na-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa PAC na tumekagua fedha ambazo zilitolewa na Serikali kwa ajili ya kiwanda hiki, ni zaidi ya miaka mitano Serikali haijafaidi kitu chochote na hiki kiwanda na Serikali ilisema inaingia ubia na yule mwekezaji na wakaingiza zaidi ya bilioni 10 kwa ajili ya kiwanda hiki, lakini hakuna manufaa yoyote ambayo Serikali inapata kupitia Kiwanda cha SAAFI. Naomba Serikali sasa leo watakapohitimisha watuambie ni nini ambacho kinaendelea juu ya kiwanda hiki maana fedha zile ambazo ziko pale zilizowekezwa ni mali ya umma, ni mali ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee pia machinjio ya Ruvu, Serikali imeweka fedha nyingi sana pale Ruvu fedha nyingi, tulijenga machinjio ya Ruvu kusaidia machinjio ya Dodoma, kusaidia machinjio ya Vingunguti lakini majengo yale yamekaa bure tu hayana kazi. Fedha za Serikali zimeingia mle lakini hakuna kinachoendelea. Tuliambiwa mashine zilishaletwa pale kwa ajili ya machinjio ya kisasa, hakuna kinachoendelea, je, tunaanzisha miradi ili tuache njiani kweli? Je, tunatumia fedha za umma ili zikae ziharibike bila matumizi, sidhani kama ndio lengo la Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuanzisha mradi na kuona kwamba mradi ule unawafaidisha Watanzania na wako wanaotafuta na wanachinja nyama hapa Dodoma ng’ombe, mbuzi, kondoo kusafirisha nchi za nje, machinjio ya Ruvu yangesaidia hata machinjio ya Dodoma, lakini majengo yale yamekaa pale hayana kazi. Naamini na vifaa vilishakuja lakini hakuna kinachoendelea na sijui kama vile vifaa viko Wizara ya Mifugo au vile vifaa vilishauzwa au bado viko bandarini mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara kwamba wameamua sasa kupitia Ranch ya Ruvu kwamba wameingia ubia na RIDP kwa ajili ya kujenga kiwanda kikubwa kwa ajili ya kuchinja, kwa ajili ya kupaki nyama na kwa ajili ya mambo kama haya yanayohusu mifugo. Ni jambo jema kabisa, lakini kwa nini tusitumie ranch zetu, ranch ya Kongwa ina mifugo mingi, nadhani kwamba ni vizuri ranch zetu zikasadia kuwa mfano na tukajenga viwanda vya maziwa, vya nyama katika ranch zetu kuliko kujenga maeneo ambayo hayana mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge hili na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema ambayo amenipatia.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana viongozi wa Kitaifa, Mheshimiwa Makamu wa Rais, dada yangu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuhamia Dodoma, nampongeza pia Waziri Mkuu kwa kuhamia Dodoma, lakini nawapongeza Mawaziri wote na Manaibu na Makatibu Wakuu na viongozi wote wa Serikali kwa kuhamia Dodoma. Dodoma ni salama, Dodoma ni kwema, Dodoma ni pazuri na wanafanya kazi katika hali ya hewa nzuri, vyakula fresh na hata ukiwaona afya zao zimebadilika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais, Hayati Baba wa Taifa alipotamka kwamba Dodoma ni Makao Makuu tangu mwaka 1973, tamko hili hakulifanya peke yake. Suala hili lilitoka Bungeni na Wabunge waliokuwepo kipindi hicho walikubaliana kwamba Makao Makuu yawe Dodoma na matokeo yake mwaka 1974 wakaanzisha Shirika la Uendelezaji Makao Makuu yaani CDA.

Mheshimiwa Spika, Marais wetu waliopita wa Awamu zote walifanya kazi ya kufanya maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma na ndiyo maana hata Awamu ya Nne wakajenga Ukumbi huu kwa maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma. Huwezi kusema kwamba kulikuwa hakuna mipango ya Serikali kuhamia Dodoma, kulikuwepo na mipango na ndiyo maana Serikali ikajenga ukumbi huu wa Bunge na kuhamishia shughuli zote za Bunge Mkoani Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sioni sababu ya kusema kwamba hakuna mipango iliyokuwepo ya Serikali ya Awamu zote kuhamia Dodoma. Mipango illikuwepo na ndiyo maana tukajenga na Ikulu-Chamwino Dodoma na ndiyo maana CDA ilikuwa inafanya kila linalowezekana kwa uendelezaji wa Makao Makuu Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kama kulikuwa na shida, tangu mwaka 1973 Watanzania walikuwepo angetokea mmoja akaleta Muswada binafsi kwamba hili la Dodoma sasa haliwezekani lakini Watanzania wote waliunga mkono ndiyo maana tangu mwaka 1973 Watanzania wanasubiri Serikali ihamie Dodoma. Serikali imehamia Dodoma tuwashukuru na kuwapongeza kwamba maamuzi yaliyosubiriwa kwa muda mrefu sasa yamefanyika.

Mheshimiwa Spika, tunao Wabunge ambao wana Awamu Nne humu ndani, wengine wana Awamu Tatu, wangeweza kuleta Muswada wa kupinga kwamba Makao Makuu imesubiriwa muda mrefu sasa hakuna haja ya kuja Dodoma, lakini wamefurahia ndiyo maana tunajumuika pamoja kushangilia.

Mheshimiwa Spika, niwape taarifa nzuri kwamba Dodoma itajengeka kwa mpangilio mzuri ajabu na wengi ambao wanaona siyo sawa, watakuja na najua nina orodha yao maana mimi ni Diwani. Wameomba viwanja kama hawataki kujenga Dodoma kwa nini wameomba viwanja? Nawakaribisha wajenge Dodoma na ambao wamekwishajenga nyumba zao ziko salama, mali zao ziko salama, kila walichonacho kiko salama.

Mheshimiwa Spika, Dodoma tuna master plan nzuri ambayo Dodoma utakuwa Mji mzuri Afrika Mashariki na kati na inawezekana Afrika nzima Mji wa Dodoma utakuwa ni mzuri. Master plan iliyokuwepo ikajengwa Abuja imetengenezwa upya na kila siku inafanyiwa marekebisho ili Mji wa Dodoma uwe Mji tofauti. Anayetaka kuwekeza kwa ajili ya viwanda aje tumetenga maeneo kwa ajili ya viwanda, anayetaka kujenga Chuo Kikuu aje, tuna maeneo tumetenga kwa ajili ya Vyuo vikuu, anayetaka kujenga hospitali nzuri za rufaa aje tuna nafasi tumemwekea. Kwa hiyo, msongamano huu wanauona ni wa muda tu, Mji wa Dodoma kutakuwa hakuna msongamano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru na naipongeza Serikali kwamba wazazi waliokuwa wanafanya kazi Dar es Salaam, wanaondoka saa 11 alfajiri wanarudi saa tano usiku watoto wameshalala, siku hizi familia zao zinawajua kwa sababu Dodoma hakuna foleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Dodoma tunajenga soko la Kimataifa…

T A A R I F A . . .

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mbunge aliyesema kwamba nyumba ambazo zipo na ambazo zimewahifadhi wageni waliofika robo tatu ni nyumba za Wagogo, kwa hiyo hatuna wasiwasi, tuko vizuri.

Mheshimiwa Spika, nimeshangaa na hotuba ya Kambi ya Upinzani ukurasa wa nane, wanasema; “Halmashauri ya Dodoma hakuna kikao cha Halmashauri ya Dodoma kilichokutana kuazimia kupandisha hadhi Manispaa ya Dodoma”

Mheshimiwa Spika, mimi ni Diwani wa Jiji hili na Baraza la Madiwani lililopita la Serikali ya Awamu ya Nne tuliomba Dodoma kuwa Jiji na ukitafuta taarifa hizo utazipata kwamba tulikwishakuomba na tukapitia hatua zote, tukaenda DCC na tukaenda RCC na tukapeleka ALAT Taifa na tukapeleka TAMISEMI kuomba Dodoma kuwa Jiji. Watu wetu siyo hivyo mnavyofikiria, tulikidhi vigezo vyote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wanaposema, waseme kitu ambacho wana uhakika nacho. Mimi ni Diwani wa Jiji hili, najua kilichosemwa na najua tulichokiomba sisi tuliokuwa Madiwani. Kwa hiyo, siyo kwamba Rais amekurupuka tu, lilikuwa ombi toka Awamu ya Nne kwamba Manispaa ya Dodoma tunaomba iwe Jiji.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, taarifa nyingine wanasema kwamba hatujitoshelezi kimapato; kwa taarifa, Rais mwenyewe alisema kwamba Dodoma ndiyo Jiji la kwanza kwa ukusanyaji wa mapato kwa mwaka huu wa fedha uliopita. Kama unabisha tafuta taarifa kwa vyombo vya habari utapata. Dodoma ndiyo Jiji la kwa makusanyo ya mapato, shangilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafanyta tunachokielewa na tuko tayari kupokea Jiji kwa kufanyakazi, siyo lele mama na niwaambie wananchi wa Dodoma sasa hivi wanafanya kazi kwa…

Mheshimiwa Spika, niwatoe hofu wanaohamia Dodoma, waje Makao Makuu kuna neema.

Mheshimiwa Spika, kuna neema na mwaka huu tunajenga barabara zaidi ya kilomita 100 ndani ya Jiji hili, unaboresha miundombinu, tunajenga Stendi kuu ya kuchukua mabasi 600 kwa mara moja.

T A A R I F A . . .

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, Mwakagenda asiniapishe kwa mambo ambayo hana uhakika nayo na nitamletea taarifa kwa sababu lilizungumzwa na Mkuu wa Nchi siyo leo, nitamwambia. Naomba niendelee kwa sabbau anachosema wala hana habari nacho.

Mheshimiwa Spika, nikwambie kwa Serikali kujiandaa vizuri kwamba tunapokea Makao Makuu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Niwaambie tu kwamba hatuna shida ya maji, tumejiandaa vizuri na niwaambie magari yote tunajenga ring roads ambazo magari hayataingia mjini kwa wale ambao hawataki kuingia mjini, kwa hiyo tumejiandaa vizuri na Serikali imejiandaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono kwamba Dodoma iwe Makao Makuu, tumesubiri kwa muda mrefu, miaka 45 siyo muda mfupi. Miaka 45 ni mtu mwenye watoto kama ni mtu wa kijijini ana wajukuu. Kwa hiyo, Serikali imetimiza yale ambayo Watanzania wote tulitamani yatimizwe. Zamani wanafunzi wakifanya mitihani wakiulizwa Makao Makuu ya Tanzania ni wapi? Wengine wanaandika Dar es Salaam, wengine aanandika Dodoma sasa hivi wataandika jibu sahihi, Makao Makuu ni Dodoma kwa sababu walikuwa hawajui, je, ni Dar es salaam au Dodoma? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo mengine kwamba Majengo hayatoshelezi, kwani Wizara wanafanya kazi chini ya mti? Wanafanya kazi kwenye majengo ya Serikali wala siyo ya kukodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwamba Muswada huu umekuja kwa wakati na unafaa na Watanzania wote wanafurahi sasa kwamba anapotoka Arusha anakwenda Mbeya ni siku moja kutoka Arusha kwenda Mbeya kwa sababu barabara zipo za lami na akipenda kulala Makao Makuu, saa nane waliotoka Mbeya wako Dodoma, waliotoka Mwanza saa nane yuko Dodoma na sasa hivi tunejengewa reli ya standard gauge watakuwa wanatembea masaa matatu, mawili wamefika Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono Muswada huu.