Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Faida Mohammed Bakar (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja hii ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutufikisha hadi leo tukiwa katika hali ya uzima na usalama.
Pia napenda sana kuwashukuru wanawake wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Kusini Pemba kwa kunichagua kwa kura za kishindo na kuniwezesha kuwa Mbunge wao, nawaahidi sitowaangusha kama kawaida yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nianze kwa kuipinga ripoti ama hotuba ya Kambi ya Upinzani, ambayo ameisoma Mheshimiwa Ally Saleh, kusema kwamba Zanzibar uchaguzi ulikuwa mbaya, wananyanyaswa, ushindi hawakupata CCM, wao ndiyo waliopata ushindi, wamenyang‟anywa ushindi, mimi niwaulize ushindi huo waliupata wapi? Kupata ushindi siyo bure, kupata ushindi ni kazi, kwa hiyo, naomba tu tustahimiliane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kwenda moja kwa moja katika bajeti. Kwanza napenda kuipongeza Wizara hii na Mawaziri wetu wa Wizara hii Mheshimiwa January Makamba na Mheshimiwa Mpina, Mwenyekiti wangu wa Wilaya, alikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya, nilipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Vijana. Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya kwa ushirikiano mzuri, nawatakia kila lenye kheri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuupongeza uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015, kwa ushindi wa kishindo ambao tumepata Chama cha Mapinduzi, tukawa tunaongoza Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. Pombe Magufuli. Uchaguzi wetu Mkuu ambao ulifanyika kwa kule Pemba CUF walipata huo ushindi, lakini nashangaa wanasema nini na wao wamo humu ndani? Mnasema hamuukubali Uchaguzi Mkuu mbona ninyi mmo humu ndani hamtoki, au mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu? Kwa sababu kama hamuutambui uchaguzi ule, mngetoka mkaenda majumbani mwenu, mmo humu, mnachukua posho, mnafanya kila kitu hapa, lakini hamuukubali uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mama Samia Suluhu Hassan, wanawake tunaweza. Mama huyu ni fighter, anafanya kazi usiku na mchana katika Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunakupongeza Mama Samia. Pia napenda kumpongeza Waziri wetu Mkuu Majaliwa mtu wa watu, mtu wa vitendo, jembe hongereni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda sana kuupongeza uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, Uchaguzi ambao umekuwa wa demokrasia, uchaguzi ambao Vyama vya Upinzani ambavyo vimeshiriki uchaguzi huu wa marudio, wa tarehe 20/3/2016, Chama cha ADC, chama cha TADEA, Chama cha Wakulima, vilishiriki uchaguzi huu wa marudio, CUF wao na chama cha CHADEMA wakapingana na uchaguzi huu wa marudio na lazima waukatae Uchaguzi huu, kwa sababu uchaguzi wa Oktoba, 2015 waliiba kura.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wamezoea bobo hawa, bobo kama hulijui nitakwambia. Napenda kuupongeza uchaguzi huu wa marudio chini ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliyoongozwa na Mheshimiwa Jecha.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Jecha hongera popote ulipo, kwa kusimamia Uchaguzi wa Zanzibar kwa amani na utulivu na usalama. Jecha hoyee!
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, uchaguzi huu uliompatia ushindi Mheshimiwa Rais wetu Mtukufu, Ali Mohamed Shein, Rais jasiri, Rais mstahimilivu na kama Rais siyo mstahimilivu basi angekwishakufa kwa hawa Wapinzani, lakini Mheshimiwa Dkt. Shein ni Rais jasiri, ameiweka Zanzibar katika amani na utulivu. Vile vile tunavishukuru Vyombo vya Usalama wa Taifa, vyombo vya Muungano.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Ally Saleh kaa kitako nikueleze, ninyi mlipokuwa mnasema nilinyamaza, sasa na mimi nasema ni bosi wenu wa Chama cha Mapinduzi nasema nataka mnyamaze!
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilindie muda wangu tafadhali, nina mambo mengi ya kusema hapa leo. Pia nampongeza Balozi wetu Seif Idd, ni Kiongozi bora.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Ninyi hamumtaki kwa sababu anawatia adabu, Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, Oyee!!!!
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Mwenyezi Mungu kutujalia Muungano huu, ulioasisiwa na Hayati Abeid Amani Karume na Hayati Julius Kambarage Nyerere, Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema Viongozi wetu shupavu.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano una maendeleo mengi sana, Wazanzibari tuko kila pembe ya Mikoa ya Bara, tunafanya biashara, tumeoana, tunashirikiana.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii kwa kazi nzuri azifanyazo akishirikiana na Naibu Waziri wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu miundombinu ya mitandao ya simu katika Kisiwa cha Pemba. Kwa kuwa Kisiwa cha Pemba mtandao unaopatikana kwa urahisi katika maeneo mengi na hasa vijijni hususani mtandao wa TiGO haupatikani vizuri. Naiomba Serikali kupitia Wizara hii iweze kulishughulikia suala hili la mtandao wa TiGO uweze kuenezwa sehemu zote katika kisiwa hiki kwa kuwa mitandao husaidia sana wananchi na hasa wafanyabiashara katika mawasiliano ya haraka na ya karibu. Naishauri Serikali kulishughulikia tatizo hili la mtandao wa simu katika Kisiwa cha Pemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee kuhusu viwanja vya ndege. Pamoja na Serikali kuviimarisha viwanja vya ndege katika nchi hii sambamba na Serikali kununua ndege za kisasa za kuhudumia wananchi wake, napenda kuomba Serikali iendelee kukifanyia ukarabati mkubwa Kiwanja cha Ndege cha Pemba na zaidi kukipanua ili kukidhi huduma ya kupokea ndege kubwa za kisasa pamoja na kuziwezesha ndege hizi kuruka na kutua muda wote wa mchana na usiku. Wananchi wa Pemba wanapendelea sana kutumia ndege kwa ajili ya safari za kijamii na kibiashara, naomba marekebisho yafanywe katika kiwanja hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na pumzi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kama ifuatavyo:-
Kwanza napenda kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini kurejesha jina langu kuwa mgombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na kwamba nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Chama cha Mapinduzi kwa kura zenu za kishindo. Nawashukuru sana na sitawaangusha, tutafanya kazi kwa pamoja kukiendeleza Chama chetu cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, mdogo wangu Mheshimiwa Ummy, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ushirikiano mkubwa na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa kweli hakika wanawake tunaweza, hasa tukisaidiana na wanaume. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja hii kwa kuongelea Zahanati yetu ya Bunge kwanza kwa sababu, wahenga walisema sadaka huanzia nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kukushukuru sana kwa jitihada za Bunge hili kutupatia Wabunge zahanati mpya ya kisasa yenye viyoyozi na kila kitu mle ndani. Zamani zahanati ilikuwa ni ndogo, chumba kimoja, tulikuwa tunawekewa yale mapazia, mtu akisema upande huu, upande huu ugonjwa wa mwenzake anaujua, lakini mkaona kwamba Wabunge ni watu pia wa kuhifadhiwa. Kwa hiyo, mkatupatia zahanati iliyopo pale mbele kwenye geti kubwa pale kwa mbele, nafikiri wengi labda watakuwa hawaijui, lakini naomba kushukuru Bunge kwamba zahanati hii ni nzuri sana sasa hivi. Sisi Wabunge tunasitirika vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwashukuru hawa Madaktari. Naomba kuwataja kwa sababu jamani hawa Madaktari wanatusaidia sana, Dkt. Chaula wa kwanza huyu, Bingwa wa Magonjwa ya Ndani (Physician). Dkt. Temba, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Dkt. Kiboko, Dkt. Solomon, Sister Sanya, Sister Disifa, Sister Solo, Sister Habiba huyu wa Maabara, Sister Jacquiline huyu Mfamasia. Jamani tunaomba kumshukuru Mwenyezi Mungu na kulishukuru Bunge kwa kitendo kile pale kuwekewa sisi Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ila tunaomba sana yawepo maboresho mbalimbali, naomba kwamba, ikubalike iwe ya saa 24 isiwe ya saa 12. Kwa nini nikaomba hivyo, naomba hata sisi Wabunge tutakapopata matatizo tuweze kulazwa pale yaani tupatiwe vitanda pale, tutakuwa tumesitirika zaidi na vilevile tutakuwa na usiri mkubwa. Vilevile kuwe na maboresho ya haraka ya vifaa tiba, nafikiri vifaa tiba vipo, lakini viongezwe na madaktari pia, waongezwe kama itakuwa ni ya saa 24. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huduma ya afya. Tunaishukuru Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kutujengea Hospitali kubwa ya Benjamin William Mkapa iliyopo hapa Dodoma. Hospitali hii inatibu magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya figo. Pia naomba kuishukuru Serikali kwa kuweka kile Kitengo cha Matatizo ya Moyo kule Muhimbili. Sasa ninachokiomba ni kwamba, matatizo haya ya figo yawe especially yanatibiwa hapa Dodoma kwa sababu, Dodoma pia ni Makao Makuu, yawe yanatibiwa hapa na kule Muhimbili ibakie tu matatizo ya moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mauaji ya wazee, wenzangu waliongea; kila siku nikisimama hapa naongea mauaji ya wazee, vikongwe. Wazee wetu ni vikongwe na wengine wale wenye matatizo ya ngozi (albino), wanauliwa sana katika nchi yetu hii, ingawa Serikali imefanya jitihada kubwa kuondoa tatizo hili, lakini inatokea kwa siku na siku huwa wazee wanauliwa. Mheshimiwa mmoja alizungumza hapa, ingawa wengine labda watakuwa na matatizo, lakini zisichukuliwe sheria mikononi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na mimi naungana na yeye, wazee wetu hawa ni wazee na sisi pia tutakuwa wazee. Inaniuma sana kuona wazee wanauliwa; kwa nini wazee wanauliwa? Wanauliwa kwa kuhusishwa tu na mambo ya kishirikina kwa sababu ana macho mekundu. Mheshimiwa Waziri hili, wewe ni mwanamke mwenzangu, uwe mbele na imara sana katika kuliimarisha hili na kuwachukulia hatua kubwa sana wauaji wa wazee wetu.
Mheshimiwa Spika, wazee ni wazee wetu, wametuzaa, wametuweka matumboni mwao miezi tisa mpaka kumi mpaka wametuzaa. Kama mzazi anataka kukuua, angekuua alipokuzaa pale kitandani, asingekuja kukuua wewe umeshakuwa mtu mzima. Jamani tuwahifadhi wazee. Wazee ni dua kubwa, tuwapende wazee. Mheshimiwa Waziri naomba hili alichukue sana na kulifuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vituo vya kulelea wazee. Tanzania tunaishukuru Serikali kwamba vituo vipo vingi vya kulelea wazee, lakini jamani aaa, hapana! Vituo vya kulelea wazee vingi vyao vibovu, vifaa hawana, vyakula hawana, hawana nguo, hali zao ni duni sana, utawahurumia! Vituo vipo, lakini tunaomba ipangwe bajeti maalum ya vituo vya kulelea wazee wetu jamani. Wazee ndiyo kila kitu katika maisha yetu, bila wazee sisi tusingefika hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukatili wa watu wenye ulemavu. Ukatili wa watu wenye ulemavu ndiyo sana, unajua ukatili siyo lazima mtu kumuua au kumpiga, lakini hata kama mtu mwenye ulemavu ana elimu yake nzuri, ni msomi mzuri, lakini akibisha hodi kwenye Ofisi, anadharaulika eti kwa sababu hana miguu, hana mikono, hana macho yaani inasikitisha sana.
Mheshimiwa Spika, watu wenye ulemavu ni watu wa kuwahifadhi sana kwa sababu na wewe hujijui. Leo wewe uko mzima una midomo, una miguu, una mikono, lakini kesho utakuwa na wewe mlemavu. Tusipende sana kuwadharau watu wenye ulemavu kwa sababu Mwenyezi Mungu atuepushie, lakini na sisi ni walemavu watarajiwa. Napenda sana kuwaomba wananchi wa Tanzania tusiwadharau watu wenye ulemavu kwa sababu watu wenye ulemavu na wao ni binadamu kama sisi, ni wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, naomba kuzungumzia kuhusiana na Benki ya Wanawake. Toka niingie Bunge hili, toka ianzishwe Benki ya Wanawake natetea Benki ya Wanawake Zanzibar mpaka leo. Kila siku jibu ninalolipata process zinaendelea, mchakato unaendelea. Mheshimiwa Kigwangalla karibuni tu alinijibu na nikamsifia sana bajeti iliyopita Mheshimiwa Samia ambaye alitoa ofisi yake pale Bwawani. Naomba tu kuulizia, hii Ofisi imefikia hatua gani au ni kitu gani kinachokwaza mpaka Benki ya Wanawake isianzishwe kule Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Zanzibar pia, kuna wanawake, kuna wazee kuna vijana. Pia nao kuna wafanyabiashara wadogo wadogo na wakubwa wanahitaji huduma hizi za Benki yao ya Wanawake.
Naomba sana Mheshimiwa, sana sana, leo nafikiri nitakuja kushika shilingi hapa, lakini mpaka nijibiwe hii Benki ya Wanawake isiwe tu ni mdomo mdomo. Kila siku mdomo mdomo tu hapa. Naomba sana Benki ya Wanawake leo nijibiwe inaanza lini kule Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hoja hii ya bajeti yetu kuu. Naunga mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kupeleka pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri. Mimi namwita Mheshimiwa Waziri wa Mipango; huyu jina lake Mpango, kwa hiyo ana mipango mingi. Mheshimiwa Naibu Waziri, dada yangu au mdogo wangu, huyu ana jina gumu sana huyu! Ashatu, sijui jina la Kichina hili au la wapi, sielewi lakini Ashatu ni jina zuri sana, nafikiri la kihindi. Napenda kumpongeza kwa ushirikiano mzuri wa kazi. Wanashirikiana, wanafanya kazi na inaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda moja kwa moja kwenye hoja. Suala la maji limezungumzwa sana na kweli Serikali yetu inajitahidi sana katika kusaidia huduma za maji mijini na vijijini; lakini tukiangalia sana vijijini maji yanayotegemewa sana ni ya visima. Sasa maji yaliyoko vijijini hasa ya visima, visima vingi vinakuwa havitoi maji. Tunaomba sana, watu hawa wa vijijini hususan wanawake, sisi wanawake ambao tunahangaika sana, tunatoka usiku wa manane kwenda kutafuta maji masafa marefu na inafikia wengine hata kuachwa na waume zao kutokana na matatizo haya ya maji. Hebu tuwaondolee matatizo haya ya maji wanawake hasa wa vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza ilani yake ya 2015 hadi 2020 inatekeleza vizuri sana kujenga zahanati vijijini na mijini, lakini ukiangalia zahanati nyingi hazina vifaa. Akinamama wengi ambao wanakwenda kujifungua wanaambiwa wabebe ndoo, kanga, nyuzi, mikasi na viwembe. Huu ni udhalilishaji wa wanawake. Naomba sana Serikali ilione hilo na ilipe kipaumbele mambo ya zahanati na vifaa, siyo iwe zahanati tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zile zahanati ambazo zimejengwa na ambazo hazijamalizwa, zimalizike, siyo kutenga tena bajeti mpya ya kujenga zahanati nyingine ambapo zile za zamani zilizokuwa zimejengwa hazijamalizwa na vile vile vifaa hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunaishukuru Serikali yetu kutenga shilingi milioni 50 za vijijini, mitaa na kule Zanzibar tunaita shehia. Fedha hizi kwa kifupi ni nyingi sana. Serikali yetu imetenga fedha nyingi sana, lakini je, tujiulize, matumizi yake yatakwenda sawia? Sisi ni mashahidi kuona kwamba fedha za Mheshimiwa Jakaya Kikwete vilivyoteketea na fedha za TASAF zinavyoteketea. Je, hizi fedha shilingi milioni 50 za vijiji, shehia ya mitaa zitakwenda kutekeleza majukumu ya kuondolea wananchi umaskini zinatumika vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iangalie sana suala hili ili wanaohusika walisimamie vizuri tukiwemo na sisi Wabunge, maana na sisi tusijitoe, tumo katika utekelezaji wa majukumu ya shilingi milioni 50. Asilimia tano hizi za kwenda Halmashauri za vijana na wanawake ni siku nyingi tu, ni miaka mingi zinatengwa na zinaonekana katika makaratasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati ya PAC na zamani nilikuwa LAAC, tulikuwa tunaziona, lakini fedha hizi hazitumiki vizuri kule. Fedha watu wanatumia vibaya, sijui wanazifanyia nini kusema ukweli. Ukitazama hesabu, haziendani na wanawake hawa na vijana huwa hawapatiwi fedha hizi. Naishukuru sana Serikali kutenga hilo lakini tunaomba sana Serikali yetu iwe simamizi sana ya fedha hizi za asilimia tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wameongelea watoto wetu wa kike. Watoto wetu wa kike ni watoto ambao wanataka hifadhi kubwa sana; hivi ni kwa nini hizi pad siziwe free? Hizi taulo za watoto wa kike! Mtoto wa kike siku zake zikifika anaomba dunia ipasuke aingie; mtoto mama yake maskini, baba yake maskini, fedha ya kununulia taulo hana. Mtoto anabakia haendi shule siku saba au siku nane. Hii hatuioni kama ni muafaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, tuko chini ya miguu yenu Serikali, mwondoe VAT ili watoto hawa wapate kusitirika. Watoto wetu wa kike wanapata shida sana; wakati mwingine wanafeli madarasani kutokana na tatizo hili. Tatizo hili katujalia Mwenyezi Mungu, hatukulitaka wenyewe; watoto wetu hawakulitaka wenyewe. Wanaume hawana hili. Kwa hiyo, tunaomba na Waheshimiwa Wabunge wanaume wakichangia hapa watetee hili ili watoto wetu waweze kuhifadhika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pia naomba kuchangia hoja katika vipengele vifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, waandishi wa habari; kwa kuwa waandishi wa habari ni watu muhimu sana katika jamii kwa kuwa ndio wanaofanya kazi kuielimisha jamii katika Taifa letu, naiomba Serikali iweze kuwalinda na kuwapatia haki zao wanazowajibika kuzipata kama kuongezewa posho zao katika kazi wanazozifanya, kuwapatia vifaa vya kisasa na heshima yao ilindwe na wasidharauliwe. Kwa upande wa makazi na kadhalika, Serikali inatakiwa wawaongezee waandishi hao hasa wale wanaoonekana katika televisheni mbalimbali, waandishi wanatakiwa wapatiwe posho ya mavazi ili waweze kuonekana katika muonekano mzuri. Hili liangaliwe hasa kwa watangazaji wa TV ya Taifa TBC.

Mheshimiwa Spika, wasanii wa filamu waweze kupata haki zao ipasavyo kwa sababu wasanii wa Tanzania wanadharaulika sana na jamii inapendelea kuangalia au kununua kanda za filamu za nje. Naishauri Serikali kufuatilia ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara wanaoingiza kanda za filamu kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, nidhamu katika kazi za muziki; ni mara nyingi tunaona wasanii wakiimba nyimbo zisizo na maadili na kuvaa mavazi yasiyo na maadili na hasa kwa wasanii wa kike. Naishauri Serikali isimamie vema maadili ya wasanii, hasa wa muziki katika nchi hii, vinginevyo tutafika pabaya. Nashauri wasanii wetu wasiige tabia za nje bali waangalie mila na desturi za Kitanzania.

Meshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia pumzi hadi kufikia siku ya leo na tunawaombea maghufira ambao wametangulia mbele ya haki, Inshallah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi sana kwa Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na chama changu kitukufu Chama cha Mapinduzi. Na pia, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Shein, na vilevile kumpongeza Rais wangu Magufuli kwa jitihada kubwa ambazo anazichukua katika nchi hii, na kwamba ametujali sisi wanawake kwa kumteuwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza jembe! Huyu ni jembe kabisa! Huyu ni Mheshimiwa dada yangu Ummy, napenda kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kushirikiana na Naibu wake Dkt. Kigwangalla. Hawa ni viongozi bora sana na wanaiweza Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda kuongelea Benki ya Wanawake. Hii Benki ya Wanawake kila ninaposimama ninaitetea. Kwanza naipongeza kwa sababu imefanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Waziri ameongea kwamba shilingi 12,000,000,000 zimetolewa kwa wajasiriamali mbalimbali 9,650 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Dodoma, Ruvuma, Pwani na Mwanza, lakini kila nikisimama najiuliza, napata wivu sana mimi nasema kwa nini hii Benki ya Wanawake na Zanzibar isiwepo? Hii Benki ni ya Wanawake wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii benki si ya Dar es Salaam wala si ya Mwanza wala si ya Songea wala si ya sehemu moja tu, hii ni Benki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba Mheshimiwa Ummy uniambie leo, kila nikikuuliza unaniambai sijui hazijatolewa pesa milioni ngapi, kwani hii kazi ya kutoa hii pesa ni ya nani? Si iko katika bajeti ya Wizara yako? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba mshirikiane na Serikali na Wizara ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kule, mshirikiane Mheshimiwa Ummy, mimi sitapenda kusimama hapa tena kuiongelea Benki hii ya Wanawake wa Zanzibar.

Zanzibar kuna wanawake kama sehemu nyingine yoyote, Zanzibar kuna wanawake ambao ni wafanyabiashara kama sehemu nyingine yoyote, Zanzibar ni wapiga kura wakubwa wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo iwe mwisho, Mheshimiwa Ummy, naomba leo iwe mwisho wewe ni mwanamke mwenzangu naomba unisikie. Nasema mwisho iwe leo, la kama mimi sitajibiwa leo hapa kama Benki ya Wanawake itaanza shughuli zake Zanzibar, mimi na wewe tutakuwa hatuelewani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukatili dhidi ya watoto wa kike na wa kiume. Wote hapa ni mashahidi juu ya mambo yanayotokea katika dunia yetu hii, si hapa tu dunia nzima wanawake, na watoto wanadhalilishwa, wengi wa watoto wanadhalilika; wengi wa watoto jamani ni mashahidi kwenye whatsApp siku hizi mengi. Utaona mtoto kakatwa mkono, sijui kakatwa mguu, kakatwa kichwa; wanadhalilika watoto; kwa nini watoto wanadhalilika Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu kwa nini watoto wadhalilike? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kama Wizara yako inajitahidi katika kuwatetea watoto wa kike na wa kiume, lakini bado. Tunaomba watoto wa nchi wasidhalilishwe kwa sababu watoto ndio Taifa letu la kesho. Mheshimiwa Ummy Ally nakuomba sana maafisa wako wafuatilie sana habari kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo linajitokeza jamani, mimi naomba kusema tu ukweli, unanua sipendi kufichaficha. Watoto wanadhalilishwa kijinsia jamani ninyi hamjui wenzangu ninyi? Watoto wanadhalilishwa kijinsia, mimi nimekwenda kufanya ziara Mkoa wa Kusini Pemba, kila ninapokwenda wananiambia Mheshimiwa Mbunge tunalalamika watoto wetu washaharibika, watoto wameshaharibiwa, kwa nini baba mtu mzima uende kumharibu mtoto mchanga? Mtoto mdogo anayesoma shule, wa kike na wa kiume, kwa nini jamani? Nililia watoto wanadhalilishwa, wanaharibiwa maumbile yao jamani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwa Mwenyezi Mungu binadamu, akina baba nawaomba hii si nzuri. Mheshimiwa nasema kwa uchungu kwa sababu mimi ni mzazi Mheshimiwa Ummy, watoto wanabakwa na wanadhalilishwa. Sitaki niseme mengi leo, nikisema nitalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Kusini Pemba walinililia wakasema watoto wetu wanadhalilishwa mpaka shule kule, na kuna baadhi ya walimu wanawadhalilisha watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani inakuwa hivi? Watoto wetu tunawazaa wenyewe watoto, mtu babu eti anakwenda kumfanyia ushenzi mjukuu wake! Eeh! Baba aliyemzaa mtoto anamgeuka, kwa nini? Turudi kwa Mwenyezi Mungu sisi binadamu, si nzuri, inatisha. Tanzania hii inatakiwa iwe ya amani na utulivu na upendo, kwa nini tunabadilika? Tumeacha dini sasa hivi tunahururika na dunia tunafanya mambo ya ajabu binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimba za utotoni. Baba mtu mzima anakwenda kumjaza mimba mtoto; Sheria ya Ndoa irekebishwe, iletwe Bungeni tuirekebishe sheria hii, haikubaliki, watoto wanadhalilika wanapigwa mimba na watu wazima walio na madevu yao mengi tu, wanawadhalilisha watoto. Hii haikubaliki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wengine wanawaozesha watoto umri mdogo kwa sababu ya visenti, kwa sababu ya ng’ombe. Kwa nini tunafanya hivi binadamu? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto tuwajali na tuwatunze. Watoto ndio watakaokuja kutusaidia sisi, tusijione vijana kesho kutwa sisi tutakapozeeka na tutakapokuwa hatujiwezi wao watatusaidia; kwa nini tunafanya hivi?

Mheshimiwa Waziri nakuomba ulisimamie, na anayepatikana na hatia hii achukuliwe hatua kali, naona bado hatua hazijachukuliwa kali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee wetu, mzee wa mwenzako ni mzee wako, leo wewe mzee wa mwenzako unamdhalilisha. Kuna makabila mbalimbali wanawanyanyasa wazee kwa sababu ya kuona kwamba ni washirikina, wazee wakiwa na macho mekundu wanawaua; nashukuru Serikali siku hizi inajitahidi sana katika hili; na kuwaua ma-albino; nashukuru sana sasahivi Serikali imejitahidi, lakini tusichoke na tuone kwamba wadhalilishaji wa wazee wamo. Tuwalinde wazee, wapewe vituo vyao, nyumba zao ziwe safi, wapewe lishe kwenye vyakula vyao na vile vile walindwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzee wa mwenzako ni mzee wako tusijione leo vijana, sisi wenyewe tutakuwa wazee na tutataka kuhudumiwa. Ukiwaona saa nyingine unalia wazee nyumba wanazolala zile. Vituo vile Mheshimiwa Ummy jitahidi, vituo hata kama… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha leo tukiwa katika hali ya afya njema. Pia napenda kutoa pole kwa wazazi wenzetu ambao wamepoteza watoto wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda moja kwa moja kwenye makazi ya askari na vituo vya askari. Kama tunavyojua askari siyo vizuri kukaa uraiani kwa sababu askari hawa wana namna yao ya kuishi, wana siri zao na mambo yao ya kitaalam na ya kimaadili yao, siyo vizuri kuchanganyika yaani nyumba hiyo hiyo askari nyumba hiyo hiyo raia. Wao wanatakiwa watulinde sisi, wanatakiwa wawe na maeneo yao ya kuishi, lakini hawana nyumba. Kila nikisimama naongea kuhusu nyumba za askari hasa kule kwetu Pemba, hakuna nyumba za askari, wengi wanakaa uraiani na ni maili nyingi kutoka wanakokaa na kazini. Wanachelewa kufika kazini kutokana na usafiri, si vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuja Pemba, Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja Pemba, Pemba wanaijua, naomba nisiseme tena, naomba askari wajengewe nyumba na vituo vyao ni vibovu. Kituo cha Mkoani, Kengeja, Konde kote vituo ni vibovu vinavuja, mvua hizi zote zimo ndani kwenye vituo vile. Hivyo kweli jamani hatuwaonei huruma askari wetu, kwa nini tunawafanyia hivi askari? Naomba sana nisiseme tena kuhusu suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee hali ya amani na utulivu. Tunawashukuru sana wananchi wa Tanzania na Serikali yetu hasa kwetu Pemba kwa sababu zamani hatukuwa tunaishi vile, vyama vyote tulikuwa na matatizo kusema ule ukweli, huyu anampiga huyu, huyu anamuua huyu, huyu hamziki huyu, huyu haendi dukani kununua kwa huyu, lakini sasa hivi hali ya amani Pemba imetulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana wananchi wa Pemba na kwa kweli tujitahidi kuzidisha ushirikiano wetu ili tuweze kuishi kwa amani na utulivu katika Kisiwa chetu cha Pemba. Siasa tuiweke nyuma ili tuweze kuleta amani na utulivu na watoto wetu waishi vizuri katika Kisiwa chetu cha Pemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee ajira za vijana katika Kisiwa changu cha Pemba. Kule Pemba kuna vijana wazuri tena wasomi, unajua wasomi wazuri wanatoka Pemba, nyie mnajua hilo? (Makofi)

Wasomo wazuri wanatoka Pemba, vijana ni wasomi, wana maadili na ni wachapa kazi, lakini wakati wa ajira vijana wa Pemba wanaachwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.