Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hamida Mohamedi Abdallah (37 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia. Nianze kwa kumpa pole Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ndugu yetu Engineer Stella Manyanya kwa msiba ambao ameupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nichangie hotuba hii ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii ni nzuri, ina mikakati mizuri, yenye utekelezaji wake kwa kipindi hiki tunachokitarajia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mambo mengi, mafanikio mengi katika upande huu wa elimu. Tumejenga shule nyingi za msingi, shule za Sekondari, shule za ufundi VETA, Vyuo vikuu lakini uwepo wa vyuo vikuu huria katika Mikoa yetu. Vyuo vikuu hivi vilivyopo katika mikoa yetu kwa kiasi kikubwa vimeweza kuwasaidia vijana wengi, watumishi wengi, kuingia katika kujiendeleza na elimu hii ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio haya tuliyoyapata, lakini kuna changamoto mbalimbali katika miundombinu ya elimu. Waheshimiwa Wabunge wengi sana jana wamechangia katika changamoto mbalimbali zilizopo katika eneo hili la elimu. Pamoja na kutokuwepo kwa Walimu wa kutosha lakini vitendea kazi tumeona ni changamoto kubwa. Tumefanya jitihada kubwa sana katika kuhakikisha shule zetu za sekondari zinakuwa na maabara katika kila eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule hizi zilijengwa kwa changamoto kubwa sana na kwa agizo la Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu iliyopita. Hata hivyo, tumeona maabara hizi zimeendelea kubaki hivi hivi, hazina hata samani ndani ya vyumba vile, matokeo yake vyumba vile vimeendelea kukaa hivi hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu kubwa ni watoto wetu wapate masomo kwa nadharia, lakini kwa vitendo pia. Kwa hiyo, ningependa Mheshimiwa Waziri atakavyofanya majumuisho yake hapa leo, atuambie ni mkakati gani ambao ameuandaa katika kuhakikisha maabara zetu tulizozijenga zinafanya kazi kama ambavyo tumetarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani kubwa sana na Serikali ya Awamu ya Tano yenye kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu. Tumeona jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais wetu anavyotekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuanza kutoa elimu bure kuanzia shule ya awali, shule ya msingi na shule ya sekondari. Vile vile tumeona jitihada kubwa anayofanya katika kutatua kero hii ya madawati na madawati haya yatakuja katika Majimbo yetu. Tunamwombea kila la heri Mheshimiwa Rais wetu, aendelee na jitihada ambazo anazifanya lakini aendelee kutuongoza Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona katika shule hizi za ufundi, shule za VETA. Sera ya Elimu ilisema kujengwa shule za VETA katika kila Wilaya. Nashukuru katika Mkoa wetu wa Lindi, Lindi Manispaa tunayo shule hii ya VETA, lakini kutokana na sera hii ya ujenzi wa shule hizi za VETA kila Wilaya hatujafanikiwa kwa kiwango ambacho tumekitarajia. Wilaya nyingi zimekosa kuwa na vyuo hivi vya VETA. Kwa hiyo, hii inawafanya vijana wetu wengi wanaomaliza darasa la saba, wanaomaliza form four ambao wamefeli kushindwa kuendelea na shule hizi za ufundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa na shule za ufundi katika shule zetu za msingi hasa pale kwetu katika Mkoa wa Lindi, tulikuwa na shule za msingi ambazo zina shule za ufundi, lakini baada ya sera hii ya kujenga vyuo katika kila Wilaya. shule zile za ufundi zilifungwa. Tunapata shida sana kwa sababu shule hizi za VETA hazipo katika kila Wilaya, matokeo yake vijana wetu wanaofeli darasa la sababu, wanashindwa kujiendeleza. Shule zile zilikuwa zinasaidia sana katika kuwafanya vijana wetu wanapata fani mbalimbali na hatimaye wanaweza kujiajiri wenyewe.
Mheshimwa Naibu Spika, napenda kumwomba Mheshimiwa Waziri kwamba, shule zile ambazo zilikuwa na shule za ufundi, basi ziweze kuendelea na shule hizo za ufundi ili watoto wetu watakapomaliza darasa la saba na kufeli, basi waendelee kupata elimu hii ya ufundi na hatimaye waweze kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Lindi na Mtwara kielimu kwa muda mrefu tuko nyuma sana. Hii imechangiwa na mambo mbalimbali nitasema jambo moja tu ambalo lilisababisha kuwa nyuma kielimu katika Mikoa hii miwili ya Lindi na Mtwara. Katika harakati za ukombozi wa nchi za Afrika, maeneo ya Mkoa wa Lindi na Mtwara, yalikuwa ni maeneo ya mafunzo ya kivita kwa ajili ya maandalizi ya ukombozi huu wa nchi za Afrika. Kulikuwa na makambi ya South Afrika ya Nelson Mandela, kulikuwa na makambi ya Msumbiji ya Samora Mashelu, lakini kulikuwa na makambi ya nchi za Zimbabwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mikoa hii ya Lindi na Mtwara lilikuwa ni eneo linaloitwa danger zone, kwa hiyo, kwa kweli Serikali haikuweza kujenga shule kama ambavyo tulitarajia na kufanya watoto wa mikoa hii miwili waweze kuwa nyuma kielimu. Kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na jitihada hizi kubwa tulizozifanya za kujenga shule za sekondari kila Kata, lakini tuna changamoto kubwa sana ya ukosefu wa Walimu katika shule zetu. Suala la Walimu kila Mbunge aliyesimama amelizungumzia, pamoja na kuwa na maslahi duni, lakini tumekuwa na ukosefu mkubwa sana wa Walimu hasa Walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Lindi, mahitaji ya Walimu wa sayansi yalikuwa 726, lakini waliopo ni 262 na pungufu ni 464. Upungufu huu ni mkubwa sana, maana hata nusu ya mahitaji yetu kwa walimu hatukupata. Kwa kweli Serikali haijatutendea haki maana tutaendelea kuwa nyuma mwaka hadi mwaka kwa kiwango hiki cha Walimu tuliowapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu atutazame kwa jicho la huruma sana katika Mkoa wa Lindi kuhakikisha tunaongezewa idadi ya Walimu hii hasa wa sayansi ili watoto wetu waendelee kupata elimu iliyo bora kwa kipindi hiki tunachokitarajia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la maslahi ya walimu limeongelewa karibu na Wabunge wote waliozungumza tangu jana hadi leo, lakini mafao ya Walimu wastaafu pia yamekuwa ni tatizo, kwa hiyo naiomba Serikali yangu sikivu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwaangalia Walimu hao wastaafu…
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na timu yake kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo yenye kuleta tija na kuboresha suala zima la elimu. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha taarifa yake ya mapato na matumizi katika kipindi hiki cha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa kuwasilisha taarifa yao nzuri, taarifa ambayo imetoa maelezo mbalimbali ya kuishauri Serikali lakini wameona changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika kipindi hiki ambacho tunamaliza cha 2017/2018. Kwa hiyo, imeturahisishia sana kwa sababu kila Mbunge aliyesimama amezungumzia mambo ambayo tayari Kamati wameshayaona, imekuwa ni rahisi kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpetia taarifa hii ya Waziri, nimeona namna ambavyo Serikali imepiga hatua kwa namna mbalimbali kwa lengo la kutaka kuleta tija katika suala zima la kuleta mabadiliko makubwa sana upande huu wa elimu, lakini kuwafanya vijana wetu waingie katika mfumo huu wa sekta ya viwanda. Katika kipindi hiki cha bajeti tunayoimaliza, Wizara ilijitahidi sana katika kuboresha vyuo vikongwe na mimi kama Mbunge wa Mkoa wa Lindi nilizungumzia sana Chuo cha Ualimu Nachingwea (TTC Nachingwea) kwa sababu chuo kile ni kikongwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Elimu alisikia kilio chetu na napenda kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu, dada yangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, kwa kweli amesikiliza kilio chetu na kwa bahati njema aliweza kututengea fedha, ametupatia shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa Chuo cha Ualimu Nachingwea.

Kwa hiyo, hizo ni jitihada kubwa sana ambazo Serikali yetu inazifanya za kutaka kukiimarisha Chuo cha Ualimu cha Nachingwea ili kiendelee kuleta tija na kuzalisha walimu kwa sababu bado changamoto kubwa ya walimu tunayo katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyeki, lakini nimeona ambavyo Serikali inaweza kuboresha elimu kwa upande sekondari. Labda nizungumzie katika Mkoa wangu wa Lindi ambapo tuna Shule ya Lindi Sekondari, shule hii ni kongwe, ilijengwa na wakoloni toka mwaka 1959 lakini ilikabidhiwa Serikalini mwaka 1963.

T A A R I F A. . .

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyeki, namwomba Mheshimiwa Mwambe asinipotezee muda wangu na hiyo taarifa yake ni ya kwake mwenyewe, sina time nayo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba Shule ya Lindi Sekondari ni kongwe na naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ili shule hii iingizwe katika mpango wa ukarabati wa shule kongwe kwa sababu ni shule ya muda mrefu, tumeirithi kutoka mikononi mwa wakoloni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwaka 2016 shule hi imepata ajali ya moto kutokana na hitalafu ya umeme na imeathirika vibaya mno. Katika madarasa 28, 18 yameathirika vibaya sana lakini bado kuna matundu ya vyoo 24 nayo yameathika na shule hii ina wanafunzi zaidi ya 900. Kwa hiyo, kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo ameungana na wananchi wa Mkoa wa Lindi katika kufanya harambee na kuhakikisha shule hii inajengwa. Pamoja na jitihada hizo kubwa tulizozifanya bado tuko nyuma kabisa katika kufanikisha ujenzi wa shule hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali kwa sababu shule hii ina four one, form four, form five na form six na watoto wanaosoma form five na form six ni watoto wa Tanzania nzima na si watoto wa Lindi peke yake na hii shule ni ya Serikali. Kwa hiyo, naomba kabisa Serikali kutia mkono wake kuhakisha wanatuunga mkono ili shule hii iweze kujengwa na watoto warudi katika mazingira safi na salama ili waweze kupata elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Mawaziri ambao wametembelea mkoani kwetu Lindi na kila Waziri aliyepita alikuja kutoa pole katika eneo la shule ile. Lakini cha kusikitisha, wageni hao wote waliokuja wametoa pole ya mdomo tu na kutuahidi kwamba tutasimamia suala hili na shule itajengwa. Kwa kweli mimi nasikitika sana imekuwa kama ni sehemu ya utalii wageni kuja kutembelea pale, lakini bado katika ujenzi wameendelea kutuachia wananchi wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali iweze kusimamia na kuweza kutuunga mkono katika kuhakikisha shule hii inajengwa kwa sababu ilikuwa ni shule tu ya kawaida lakini sasa hivi baada ya kuungua moto viongozi walishauri kwamba tujenge shule ya jengo la ghorofa. Mahitaji ya ghorofa ni shilingi 2,200,000,000; lakini pamoja na kuwa tumefanya harambee tumepata shilingi 700,000,000 tu. Sasa shilingi 700,000,000 kujenga jengo la shilingi 2,200,000,000 kwa kutumia harambee tutafika miaka 15 jengo lile halijakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba kwa dhati kabisa Serikali yangu itutazame kwa jicho la huruma, itusaidie kutuunga mkono kuhakikisha Shule ya Lindi Sekondari inajengwa ili watoto wapate mahali pazuri pa kukaa na kupata masomo. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali na natumaini kabisa Mheshimiwa Profesa Ndalichako atasikiliza kilio chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu katika Mkoa wetu wa Lindi tunafanya vibaya sana. Katika shule ambayo inakuwa ya mwisho Mkoa wa Lindi tunaongoza, tunaweza kuwa wa pili mwishoni, wa kwanza mwishoni lakini kuna mambo mbalimbali yanachangia elimu kushuka katika Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Lindi tuna shule za sekondari za Serikali 113 lakini asilimia 60 ya shule hizi hazina walimu wa hesabu wala masomo ya sayansi. Sasa ukitulinganisha sisi na shule zingine ambazo zimekamilika, zina maabara za kutosha na vifaa vya kutosha, zina walimu wa hesabu na sayansi, hivi kweli sisi tutakuwa wa kwanza au wa pili au hata kumi bora tutaingia, hata 20 hatuwezi, hata tukaishi kwa miaka 100 kwa style hii hatuwezi kufika.

Kwa hiyo, bado tunaendelea kuleta kilio chetu kwa Serikali kuhakikisha mnatupatia walimu wa hesabu na sayansi ili watoto wetu wa Mikoa hii ya Kusini ya Lindi na Mtwara waweze kupata masomo haya ya hesabu na sayansi ili tuweze kulingana na wanafunzi wa maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Mkoa wa Lindi ni mkoa ambao umesahaulika, tunaitwa mikoa ambayo imesahaulika, ni mikoa maskini, mikoa ambayo iko pembezoni. Kwa hiyo, Mkoa wa Lindi ni mojawapo ya mikoa hiyo lakini Serikali ilituambia kwamba bajeti hizi zitazingatia mikoa ile ambayo iko pembezoni mwa mji. Tunaiomba Serikali iutazame Mkoa wa Lindi ukizingatia kwamba ni mkoa ambao umesahaulika. Kwa hiyo, tuna matumaini makubwa sana kuona kwamba Serikali inatubeba kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia ukurasa wa 26, umeelezea masuala mazima ya elimu na ufundi stadi. Mimi naipongeza sana Serikali kwa sababu sasa imeonesha kwamba inataka kuendeleza ujenzi wa Vyuo hivi vya Ufundi Stadi katika Mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu pamoja na maeneo mengine Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Lindi tumebahatika kupata Chuo cha VETA na kipindi kilichopita nilizungumzia chuo hiki kwamba kina changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya majitaka, lakini bado mpaka leo tatizo hili lipo linaendelea. Pia Chuo kile cha VETA hakina mabweni na tunategemea wanafunzi kutoka Wilaya za Mkoa wa Lindi wapate mafunzo pale wale ambao hawakubahatika kuendelea na masomo, lakini wazazi wanashindwa kwa sababu mazingira ya kuishi mzazi anapanga nyumba. Leo mzazi ampangie nyumba mtoto wa kike, hivi kweli tunamtakia kheri mtoto huyu wa kike akae kwenye nyumba ya kupanga peke yake, hana mtu wa kumtazama na gharama za chakula mzazi agharamie? Kwa hiyo, inakuwa ni mzigo mzito na kusababisha baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Lindi wanashindwa kumudu kuwaleta watoto wao pale...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja mbalimbali za Kamati ambazo zimewasilishwa ndani ya Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wetu wa Kamati ambao wamewasilisha Taarifa nzuri, pia Kamati zimefanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kutoa maoni na kuishauri Serikali katika maeneo ambayo tumeona kuna changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhangaika kule na kule kutafuta fedha kwa ajili ya Uwekezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Nchi yetu. Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais, wetu kwa kuridhia fedha za export levy asilimia Hamsini kurudi katika Mfuko wa Maendeleo ya Korosho. Fedha hizi tulikuwa tumezikosa kwa kipindi cha muda karibia wa miaka Minne, mitano pia tulipata changamoto mbalimbli katika kuhakikisha kwamba zao la korosho linaendelezwa kama ambavyo tumelikusudia. Kwa hiyo, niishukuru sana Serikiali kwa kutoa uamuzi huu wa kuhakikisha kwamba asilimia 50 inarudi katika Mfuko wa Maendeleo ya Korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ninaomba sana Bodi ya Korosho kuhakikisha kwamba fedha hizi zinasimamiwa ipasavyo katika matumizi ya Mfuko wa Maendeleo ya Korosho. Tunajua kwamba Wakulima wetu walipata changamoto mbalimbali lakini hata Bodi ilipata changamoto katika kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao za kuhakikisha kwamba zao hili la korosho linaendelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la Shirika letu la Maendeleo Tanzania (NDC). Tumekuwa na mradi huu wa Mchuchuma na Liganga wa muda mrefu lakini tunashindwa kutekeleza kutokana na changanoto mbalimbali ziliyopo, ninaiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba inamaliza mazungumzo na Mwekezaji huyu GNT kuhakikisha kwamba NDC sasa wapewe fursa ya kuendeleza mradi huu wa Mchuchuma na Liganga. Ni mradi mkubwa, mradi ambao utatuletea fedha nyingi na utatuingizia mapato ya kutosha pia tutakuwa na ajira nyingi za kutosha katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nizungumzie suala la Shirika la TPA kwa maana ya Mamlaka ya Bandari Tanzania. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu amewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha kwamba Babdari ya Dar- es-Salaam inapanuliwa, Bandari ya Tanga, Bandari ya Mtwara katika kuhakikisha kwamba tunaendelea kutoa huduma mbalimbali lakini kuongeza Mapato ya nchi yetu na kuhakikisha kwamba uchumi wetu unaendelea kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Rais amewekeza katika mradi mkubwa wa SGR. Sasa ninaomba ndugu zangu wa bandari wachangamkie fursa hii, kuhakikisha kwamba wanajipanga vizuri kuona namna ya kutumia usafirisahaji wa mizigo kutoka bandarini kwa kutumia njia hii ya reli kupitia mradi wetu wa SGR ili kusafirisaha mizigo mbalimbali ambayo inatoka bandarini.

Mheshimiwa Spika, SGR inauwezo wa kusafirisha tani 10 kwa safari moja, kwa hiyo tutakuwa tumenusuru na tumesafirisha mzigo mkubwa kwa haraka, pia tutakuwa tumeongeza mapato na ajira na wadau mbalimbali wataendelea kufurahia huduma ya bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Rais pia, amewekeza katika mradi mkubwa wa SGR. Sasa ninaomba ndugu zangu wa bandari wachangamkie fursa hii, kuhakikisha kwamba wanajipanga vizuri kuona namna ya kutumia usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwa kutumia njia hii ya reli kupitia mradi wetu wa SGR ili kusafirisha mizigo mbalimbali ambayo inatoka bandarini. SGR ina uwezo wa kusafirisha tani 10 kwa safari moja. Kwa hiyo tutakuwa tumenusuru na tumesafirisha mzigo mkubwa kwa haraka, lakini pia tutakuwa tumeongeza mapato na ajira na wadau mbalimbali wataendelea kufurahia huduma ya bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ningeomba ndugu zetu wa TICTS wanaosafirisha ma-container kutoka bandarini; uwezo wa bandari yetu ni mkubwa sana. Kamati yetu imetembelea katika Bandari yetu ya Dar-es-Salaam na tumeona huduma ambazo zinatolewa katika bandari ile. Hata hivyo, tuna changamoto kubwa kwa ndugu zetu wa TICTS hawa katika terminal gate number 8, 9, 10 na 11, na juzi madereva wamefanya mgomo kwa sababu ya huduma mbovu inayotolewa na ndugu zetu hawa wa TICTS, wanasababisha wanaotumia Bandari yetu ya Dar- es-Salaam kuona kwamba kuna changamoto na hatimaye tunaweza tukapoteza sifa ya Bandari yetu ya Dar-es-Salaam; na Bandari yetu ndio roho ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe ndugu zetu wa Bandari kuhakikisha kwamba wanaendelea kufanya mazungumzo ya kimkataba na ndugu zetu hawa wa TICTS ili waendelee kutoa huduma nzuri na bandari yetu iwe na sifa ya kuendelea kutumika katika nchi yetu. Niwaombe pia ndugu zetu wa Bandari kuhakikisha ujenzi wa magati mapya ya namba 12, 13, 14 na 15; kuhakikisha kwamba upanuzi huu unaendelea kufanyika na bandari yetu iendelee kuwa na sifa ya wadau na wawekezaji mbalimbali waweze kutumia.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, sasahivi Serikali inabidi tujipange kuhakikisha kwamba tunapanua bandari kwa kujenga Bandari ya Bagamoyo. Kwa sababu sasahivi ukiangalia Bandari ya Dar-es-Salaam imeshasheheni. Na ukiangalia baada ya miaka 10 Bandari ile itakuwa imeelemewa. Kwa hiyo ni wakati muafaka sasa wa kuhakikisha kwamba, Serikali inajipanga vema kuhakikisha kwamba tunajenga Bandari yetu ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna jambo ambalo tulishaondokananalo, lakini sasahivi linaanza kunyemelea katika Bandari yetu ya Dar-es-Salaam. Wanaopokea mizigo yao kuna kasoro ndogondogo za wizi wa vitu vidogovidogo. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, niwaombe ndugu zetu wa Bandari kuhakikisha kwamba wanaendelea kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha kwamba wanaosafirisha na kupokea mizigo yao basi iwe salama.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hayo ni mambo muhimu sana katika mashirika yetu kuhakikisha kwamba wanaendelea kusimamia huduma zetu vizuri na wananchi mbalimbali waendelee kutumia Bandari yetu ya Dar-es-Salaam.

Mheshimiwa Spika, lakini ninajua ya kwamba, Serikali imewekeza fedha nyingi ili kupanua Bandari ya Tanga, pamoja na upanuzi wa Bandari ya Mtwara. Tuhakikishe kwamba tunaendelea kusimamia huduma zile muhimu ambazo zinahitajika katika maeneo ya bandari hizi ambazo nimezitaja ili ziendelee kufanya kazi vizuri. Tunaona kwamba Serikali imefanya kazi kubwa na imesogeza huduma karibu kwa wananchi, lakini pia imepunguza msongamano mkubwa ambao ulikuwa unajitokeza pale Dar-es-Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la TARURA. Tunayo changamoto katika eneo hili la TARURA. Tunaona kwamba Serikali imewekeza sana fedha nyingi, lakini tunaona uwezo wa TARURA kuna upungufu mkubwa wa ma-engineers katika maeneo ya Halmashauri zetu, tumeona pia kuna changamoto ya uwepo wa Ofisi za TARURA pamoja na changamoto kubwa ya uwepo wa magari. Kwa hiyo ndugu zetu hawa wanashindwa kusimamia kwa sababu ya ukosefu wa vifaa hivi. Ninaiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba tunakamilisha kuwa na ofisi za TARURA, lakini kuwa na vitendea kazi vya kuwarahisishia kufuatilia ujenzi mbalimbali ambao unaendelea katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru sana lakini pia niunge mkono ushauri uliotolewa na Kamati ya PIC pamoja na hoja ambazo ziko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na wewe nakutakia kila la heri, Mwenyezi Mungu aendelee kukubariki. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa hotuba yake nzuri yenye kulenga kukuza uchumi wa viwanda vidogo vidogo na kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hii ya uwekezaji wa viwanda iliyoainishwa katika utekelezaji wake wa Mpango huu wa mwaka 2016/2017, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea maeneo mbalimbali ya Majimbo yao juu ya uendelezaji wa upandishaji wa thamani ya mazao yao wanayolima, lakini juu ya vijana na wanawake kuwezeshwa kushiriki katika uchumi huu wa viwanda vidogo vidogo ili kukuza ajira na kuleta ustawi wa vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO ni mkombozi mkubwa wa wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini ni mkombozi mkubwa kwa vijana na wanawake katika kuyafanya makundi haya yaweze kushiriki katika uchumi huu wa viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kusaidia SIDO Mkoa wa Lindi fedha za kutosha ili kusaidia kundi kubwa la vijana na wanawake kupata elimu ya kutosha kupandisha thamani ya mazao yanayolimwa Mkoani Lindi. Naishukuru Serikali, imetenga bajeti ya shilingi bilioni sita katika Mikoa minne tu. Naomba Mkoa wa Lindi ufikiriwe kuwezesha SIDO iweze kusaidia Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi ya uwekezaji EPZ, Lindi Manispaa ni wafaidika wa mradi huu. Eneo lilishatengwa lakini hatuoni chochote kinachoendelea juu ya mradi huu. Tunaomba Serikali itupe majibu juu ya mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza sera endelevu ya viwanda ya mwaka 1996 Mkoa wa Lindi ulikuwa na viwanda. Kwa mfano, Kiwanda cha Usindikaji wa Mafuta ya Karanga na Ufuta (Nachingwea); na Kiwanda cha Ubanguaji Korosho, Lindi Vijijini na Lindi Manispaa. Viwanda hivi havikuwahi kufanya kazi hata siku moja, Mheshimiwa Waziri analijua hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yake ya swali namba 19 la Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Viwanda 1996/2020 Mheshimiwa Waziri alisema, juhudi zinafanyika ili viwanda vilivyosimama vifanye kazi. Mheshimiwa Waziri anieleze, juhudi hizi zipo katika hatua gani za utekelezaji? Mheshimiwa Rais aliwapa matumaini Wana-Lindi na kuwaambia atahakikisha viwanda vinafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nangependa Mheshimiwa Waziri anieleze, Maafisa Biashara wana kazi gani katika Halmashauri zetu? Hatuoni chochote wanachofanya zaidi ya kusimamia ukataji wa leseni za biashara; kingine ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini kwa hotuba yake nzuri yenye kuleta matumaini makubwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Kuna tatizo kubwa la umiliki wa maeneo yenye udongo unaoashiria kuwa na madini. Maeneo hayo yapo chini ya Serikali za Vijiji na Halmashauri. Hawa watu wanaopewa leseni za umiliki wa maeneo haya bila hata Serikali ya Kijiji wala Halmashauri kujua ni kutengeneza migogoro na wenye maeneo yao na kuiona Serikali yao haiwatendei haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri aniambie ni utaratibu upi unatumika wa utoaji wa leseni hizi za umiliki wa maeneo haya yenye udongo wa madini? Leseni zinazotolewa zinadumu kwa kipindi gani? Katika tozo zinazotozwa mwenye eneo lake anafaidikaje? Halmashauri husika inapata nini kutokana na uharibifu mkubwa unaofanyika?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anipe majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza kwa dhati Wizara katika mikakati yake ya utekelezaji wake wa bajeti ya mwaka 2016/2017. Lengo kubwa la kutaka Serikali kuendeleza ardhi ni kwamba ardhi ni muhimu sana ndiyo inayokuza uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa MWenyekiti, Lindi Manispaa eneo la Mkwaya kuna ardhi kubwa inayomilikiwa na Mhindi mmoja. Ni shamba kubwa haliendelezwi, wananchi wa kijiji cha Mkwaya wanakosa eneo la kulima na mmiliki huyo hafanyi chochote. Ninaiomba Serikali kuona kwa namna gani wananchi wa kijiji cha Mkwaya watasaidiwa kupata ardhi hii ambayo haitumiki waweze kutumia kwa ajili ya kilimo cha mpunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya utalii vipo Kaskazini mwa nchi yetu. Nashauri Serikali ianzishe kituo kingine cha utalii Kusini mwa nchi yetu. Utalii siyo kuona wanyama pori tu, hata bahari yetu ya Lindi na ngoma za utamaduni. Ujenzi pia wa hoteli kubwa upande wa Kusini zinaweza kufanya watu wengi kutembelea Kusini na kuja kuona mambo mbalimbali na kuliongezea Taifa letu uchumi na mapato. Pia tunayo Selous ya Liwale. Naomba iboreshwe ili watu wengi waje Liwale kwa ajili ya kuona wanyama na uwindaji halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua atakapokuja kufanya hitimisho, Mheshimiwa Waziri atueleze tunaye mjusi yule mkubwa aliyepo Ujerumani (dinosaur) anayeingiza mapato kule Ujerumani. Mjusi huyu aliyetoka mkoani Lindi, kijiji cha Mipingo. Sisi Tanzania tunapata nini katika mapato yale yanayoingia Ujerumani kupitia mjusi huyu? Kijiji hiki cha Mipingo kinafaidikaje na mjusi huyu? Napenda kupata taarifa ya maswali haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukupongeza wewe binafsi kwa kushika nafasi hiyo ya uwenyekiti na kuweza kuliongoza Bunge letu, na Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza na kukubariki. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2023/2024. Taarifa ni nzuri, imesheheni mambo mbalimbali ya maendeleo yaliyotekelezwa na miradi mikubwa ya kimkakati. Vile vile imegusa maeneo mengi katika kuboresha sekta mbalimbali kama vile sekta za elimu, afya, barabara, kilimo na mambo mbalimbali.

Mheshimwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo ana maono makubwa pamoja na kuwa na mapenzi makubwa kwa Watanzania, mpenda maendeleo, mzalendo na mwanamapinduzi wa kweli mwenye huruma ya kipekee kabisa, na hatuna mfano wa kumfananisha. Tuendelee kumtakia kila la kheri na kumuombea maisha mema ili Mwenyezi Mungu aendelee kumuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nizungumzie suala la kilimo. Niipongeze Serikali kwa kuendelea kuiimarisha sekta ya kilimo. Tumeona namna mbalimbali ambavyo inaendelea kuimarisha kwa kuifanya Benki ya Kilimo kuendelea kukua na kuendelea kuwahudumia wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona namna ambavyo Serikali inaendelea kutoa ruzuku. Si hivyo tu, bado tumeendelea kuona namna ambavyo wanapata mafunzo mbalimbali ya kufanya kilimo chetu kiwe kilimo cha biashara na kuendelea kupata masoko kupitia mitandao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo bado tuna changamoto katika eneo la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mikoa yetu ya Kusini, sisi wana Kusini zao letu kubwa ni zao la korosho, na ni zao la biashara, ni zao ambalo linatufanya wananchi tuweze kuishi na tuweze kumudu kuendesha maisha yetu. Kwa hiyo panapotokea changamoto ya kutetereka zao la korosho hata kidogo tunapata shida kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo tumeona kwamba bei ya korosho inazidi kuporomoka. Hii ni changamoto kubwa sana kwa wakulima ukizingatia kwamba zao hili unapozalisha, unapolihudumia mpaka kufikia hatua ya kupeleka sokoni pana njia ndefu na mchakato ni mrefu sana. Sasa, mkulima anategemea anapopeleka sokoni anaweza kupata bei nzuri ya kuweza kurudisha gharama ambazo ameweka katika kuhakikisha kwamba anazalisha korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali ilitazame suala hili la bei ya korosho na tuhakikishe kwamba tunawatia nguvu wakulima ili waendelee kuwa na moyo wa kulisimamia zao hili la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pembejeo Kanda ya Kusini tuna msimu wa kalenda ya upuliziaji (Sulphur) kwenye mikorosho. Sasa, kanda ya kusini hatulingani na kanda nyingine. Tunaiomba Serikali kutuletea pembejeo kuendana na kalenda yetu ya kilimo cha korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile bado tuna hoja ya usajiri wa wakulima wetu. Tunajua kwamba Serikali inaendelea kusimamia usajiri wa wakulima ili kuwabaini wakulima wa korosho waweze kupata huduma nzuri kutoka Serikalini na kuwabaini na kujua idadi ya mikorosho ambayo ipo katika maeneo ambayo tunalima korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mohamed Bashe, Waziri wa Kilimo kwa kuja na Mpango wa Jenga Kesho Ijayo Iliyo Bora. Mpango huu wa kuwashirikisha vijana kuingia katika sekta ya kilimo, kuwafanya vijana waweze kupata mafunzo na kupata mitaji ili kuingia katika uzalishaji wa shughuli za kilimo ni mpango mzuri. Si hivyo tu, pia kuwafanya vijana hawa kuwasimamia na kupata masoko ya mazao ambayo wanayalima.

Mheshimiwa Mwenyekiti huu ni mpango mzuri kwa sababu unatuongezea ajira kubwa kwa vijana kwa sababu kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ajira nchini. kwa hiyo mpango huu ni mzuri, lakini pia utakuza uchumi wetu kupitia shughuli zakilimo kwa vijana wetu. Tumeanza vizuri ingawa zipo changamoto ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kwa kuwa mpango huu ndiyo unaanza, tuutakie kila la kheri, Mungu aubariki uende salama na vijana wetu waweze kufanikiwa. Mwaka kesho tutakapokuja basi tuhakikishe kwamba katika maeneo yetu walau tutoe uwiano wa vijana wanaotoka katika majimbo yetu. Kwa mfano mwaka huu katika jimbo langu ametoka kijana mmoja tu, lakini ukiangalia katika majimbo mengine utakuta kuna vijana sita hadi nane katika jimbo moja. Kwa hiyo mwakani tuhakikishe kwamba tunaingia katika uwiano ambao walau kidogo unafananafanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu nishati. Tunaishukuru Serikali, kwamba inaendelea kusimamia na kuimarisha sekta ya nishati. Zipo changamoto ndogondgo ambazo zinaendelea, lakini Serikali bado inaendelea kuzisimamia kuhakikisha kwamba Watanzania tunapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matumizi ya gesi nyumbani. Sisi pale Lindi Manispaa tulianza na mpango huu katika Kata ya Mnazi Mmoja, na Serikali imeweka miundombinu ya matumizi ya gesi nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tunatamani sasa kufanya matumizi ya gesi nyumbani na kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni, lakini bado tuna changamoto. Changamoto iliyopo ni kwamba vifaa vya matumizi, majiko, pasi na vifaa vingine ambavyo vinatumika nyumbani vimekuwa vya gharama kubwa. Niiombe sana Serikali kuhakikisha kwamba vinapunguza kodi ili Watanzania walio wengi waweze kumudu kununua majiko ya gesi na umeme ili tuondokane na matumizi ya kuni na mkaa. Hii itaweza kutusaidia katika kuhakikisha kwamba tunatunza mazingira yetu, lakini pia itatusaidia kuona kwamba wanawake ndio watumiaji wakubwa wa majiko haya. Tuta-solve muda mwingi wa kukaa jikono na badala yake tutakwenda kufanya shuhguli mbalimbali za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba tuhakikishe kwamba kodi inapungua katika vifaa hivi na kuwafanya watu wengi waweze kutumia gesi nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nuzungumzie suala la Mradi wa LNG. Tunashukuru kwa hatua mbalimbali ambazo tumeenda nazo, na tunamshukuru Mheshimiwa Rais alitoa idhini ya kusaini mkataba wa awamu ya kwanza, na walituambia kwamba mkataba wa pili utasainiwa mwezi wa 12, lakini leo tunapoongea ni mwezi wa nne. Hatujui kuna changamoto gani zilizojitokeza zilizosababisha mkataba huu uwe haujasainiwa awamu ya pili. Wana Lindi na Watanzania wanatamani kusikia changamoto ni nini na awamu ya pili ya kusaini mkataba huu itakuwa ni lini ili tuelekee kwenye utekelezaji wa mradi huu wa LNG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunayo changamoto kwa wazalishaji wa chumvi. Sisi tunaoishi ukanda wa bahari tunazalisha chumvi, lakini wazalishaji wetu wa chumvi wanapata changamoto ya masoko na bei kuporomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba tumefungua fursa za uwekezaji nchini, na tumetoa leseni kwa Mwekezaji mkubwa wa kuweka kiwanda cha chumvi nchini, kwa maana ya kwamba atusaidie kununua chumvi iliyopo ndani ya nchi yetu. Hata hivyo, matokeo yake mwekezaji yule ananunua chumvi nyingi kutoka nje na chumvi yetu ya Tanzania inaendelea kukaa. Kwa hiyo hii ni changamoto kubwa. Kama tatizo ni kwamba chuvi yetu haina ubora ule unaotakiwa ni vizuri mwekezaji akaja kutufundisha ni chumvi ya aina gani yeye anaitaka ili Watanzania waweze kuzalisha na kupata soko la chumvi. Hili ni jambo muhimu, tulisimamie na kulizingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa; wenyeviti hawa wanatufanyia kazi nzuri sana. Hata hivyo wenyeviti hawa hatuwapi nafasi yoyote ya kuwanunulia vifaa; vifaa wananunua wenyewe lakini kazi zetu wanatufanyia. Inafika wakati wenyeviti hawapati posho yao. Sasa tujue, kupata posho yao ni halali ama si halali? Na kwa nini hawapati posho zao. Tutafute namna ya kutatua changamoto hii tuliyonayo, hasa kule kwetu Lindi Manispaa, wenyeviti wana miezi 16 hawajapata posho zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya TACTIC, na sisi Lindi Manispaa tumeingia katika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, nakupa sekunde 30 umalizie.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Mambo mengine nitaandika kwa maandishi ili Serikali iweze kutusaidia mambo kadhaa ambayo tunayahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, magereza nyingi nchini miundombinu ni chakavu, ninaomba Serikali kuona namna yoyote ya kurekebisha jengo la Magereza Lindi, hakuna gari, TAKUKURU walio wengi wanatumia magari binafsi, wasaidiwe Lindi kupata magari, zimamoto vifaa hawana tunahitaji boti ya uokoaji. Lindi tunapata changamoto, Serikali itusaidie.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuungana na Waheshimiwa Wabunge katika kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwapongeza Wizara kwa uwasilishaji wa taarifa yao ya bajeti ambayo imepunguza maswali mengi ya Waheshimiwa Wabunge na imetupa matumaini makubwa kwamba bajeti hii sasa inakwenda kutekeleza miradi mingi katika nchi yetu na kuendelea kuleta mapinduzi makubwa ya nishati katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, January Makamba, kwa kuweka Wiki ya Nishati. Imetusaidia sana kwa sababu tumepata elimu tosha na imeweza kutupunguzia maswali mengi ambayo tungeweza kuyauliza ama kuchangia hoja katika Bunge letu hili. Kwa hiyo, nikupongeze lakini niendelee kukutakia heri katika mipango mizuri ya utekelezaji ambayo tunategemea 2023/2024 tunakwenda sasa kuleta mapinduzi ya ukweli katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa kuendeleza Gridi ya Taifa. Mkoa wa Lindi kwa maana ya Lindi tunategemea sana umeme kutoka Somanga, umeme kutoka Mtwara, pia Mtwara panapotokea changamoto ya mashine zao kufeli, maana yake Lindi tunapata umeme wa mgao kwa hiyo inakua ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafarijika kuona kwamba mradi wa Gridi ya Taifa unaotoka Makambako – Songea – Masasi – Maumbika kwenye power extension, maana yake tutakuwa sasa na umeme wa uhakika na sasa tutakaribisha uwekezaji katika Mkoa wetu wa Lindi kama ambavyo tumejipanga kuhakikisha kwamba fursa za uwekezaji Lindi ziko nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme huu wa Gridi ya Taifa ambao tunautegemea kutoka Makambako pia utakwenda kutoka Masasi kuelekea Nachingwea – Liwale, lakini kutoka Nachingwea kuelekea Ruangwa. Kwa hiyo, tunausubiri kwa hamu sana. Lakini tunaona kwamba mradi huu umechukua muda mrefu, ni mpango wa zaidi ya miaka mitatu, nikuombe kuhakikisha kwamba mradi huu unakwenda kwa haraka na sisi Wanalindi na Mtwara tuendelee kufaidika na Gridi ya Taifa ili uwekezaji wetu uweze kuwa rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na niwapongeze, Waheshimiwa Wabunge leo waliochangia mradi wa LNG maana kila mmoja amehamasika kuchangia mradi huo wa LNG nakuona sasa tunakwenda ukingoni katika utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa LNG ulianza karibia miaka saba iliyopita lakini tunashukuru kwamba Serikali yetu imekuwa Sikivu, imepitia hatua mbalimbali na hatimaye wananchi wetu wameweza kulipwa fidia katika eneo la mradi na hatua mbalimbali shirika la TPDC wameweza kuchukua. Katika eneo wameanzisha barabara za ndani kwa ndani tunashukuru vijana wa Lindi wameweza kupata ajira, lakini tulichokuwa tunategemea sasa katika eneo lile TPDC waje kufanya usafi wa mazingira pale kuhakikisha kwamba eneo linakuwa safi. Walianza kwa hatua nzuri lakini ghafla wakasimama hatuelewi sababu ya kusimama kwao ni nini lakini tunategemea kwamba eneo lile liwe safi kwa ajili ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huu wa LNG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi huu tumeendelea kupata fursa mbalimbali, tumewapokea EPZA wamekuja Lindi na tumewaonesha maeneo mbalimbali ya uwekezaji, kwa hiyo tunategemea sasa fursa nyingi kuja Lindi kuongeza mzunguko na uchumi mkubwa lakini kuongeza ajira katika Mikoa yetu ya Lindi na Mtwara na hatimae nchi nzima ya Tanzania. Kwa hiyo, sisi kwetu ni maendeleo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaipongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia uwekezaji wa ujenzi wa chuo cha masuala ya umeme pale Lindi katika eneo la Kata ya Mbanja, Kata ambayo unakwenda kutekelezwa mradi wa LNG na Mtaa wa Makasialeo ndipo ambapo Chuo hiki kitajengwa na hatua mbalimbali wameanza kutekeleza katika ujenzi wa chuo hiki. Sisi kwetu ni mapinduzi makubwa na ni faraja kubwa kwa sababu watakao faidika wa kwanza na mradi huu wa LNG ni sisi wana Lindi. Tunashukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba inakwenda mbio katika kuhakikisha mradi huu unakwenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la REA. Tunashukuru mradi wa REA umetekelezwa kwa kiwango kikubwa na sasa hivi tunaona kwamba vijiji vingi vinapata umeme, vijiji vilivyobakia ni hatua ndogo na Mungu akijalia mpaka 2024 itakuwa vijiji hivi vimeweza kukamilika na wananchi watanzania tutakuwa tumepata umeme kila kona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana nilikuletea kilio kutoka Lindi Manispaa, ipo mitaa ambayio ilikuwa haijapata umeme. Tunajua kwamba mradi wa Peri-urban ilibidi utufikie pale Lindi Manispaa lakini kutokana na changamoto mbalimbali maana yake mradi ule umechelewa na wala hatutegemei kuja Lindi kutekeleza mradi wa Peri-urban. Ninakushukuru sana umekuwa msikivu, tulipoleta maombi yetu ya mitaa kadhaa itekelezwe mradi huu wa REA ulitukubalia. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametutengea fedha bilioni tano katika kutekeleza mradi huu wa REA katika eneo la Lindi Manispaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utatekeleza kilomita 26.4 njia kubwa lakini njia ndogo ni kilomita 13.7, kwa hiyo ninategemea kwamba baada ya bajetii kukamilika Mkandarasi ataanza kazi kwa sababu mkandarasi tayari ameshakuja kuripoti na maeneo tayari yameshafanyiwa kazi, tunasubiri tu fedha itoke ili Mkandarasi aingie kazini aweze kutekeleza mradi huu wa REA. Watakao nufaika na mradi huu ni ndugu zetu wa Mtaa wa Jangwani, Nyange, Chikonjwi, Ruaha Mnazi Mmoja pamoja na maeneo mengine. Mheshimiwa Waziri kwa hiyo nakushukuru sana Mungu akubariki na tuendelee kukuombea ili Watanzania tuweze kupata huduma kutoka Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mradi wa matumizi ya gesi majumbani. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Nishati kwa kampeni hii mahsusi ya kumtua mama kuni kichwani, kwa kweli tunaiunga mkono Waheshimiwa Wabunge maana yake sasa tunakwenda kwenye kampeni maalum ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaondokana na matumizi ya kuni na mkaa lakini wanakwenda kutumia nishati iliyo safi. Hili ni jambo jema kwetu kwa sababu matumizi ya kuni na mkaa yana athiri afya ya mwanadamu na tunajua ya kwamba matumizi ya gesi yanarahisha katika matumizi ya kupika pamoja na mambo mengine badala ya kutumia muda mrefu unatumia muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Lindi Manispaa Mnazi Mmoja tuna power extension ya matumizi ya gesi majumbani, Serikali ilituahidi nyumba mia mbili mtatufungia lakini mpaka leo hatujaona utekelezaji wa nyumba mia mbili kufungiwa matumizi ya gesi majumbani. Mheshimiwa Waziri kwa hiyo ningeomba utakapokuja ku-wind up utuambie ni lini utakuja kutekeleza na kukamlisha mradi huu wa nyumba mia mbili kuweza kufungiwa gesi majumbani ili wananchi waendelee kutumia kadri wanavyoweza kutumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya gesi ni muhimu sana kwetu na mimi niendelee kuiomba Serikali kwa sababu wananchi wanapenda kutumia gesi, wanapenda kutumia umeme lakini vifaa vya matumizi hayo kwa mfano majiko ya umeme, majiko ya gesi yamekuwa ya gharama kubwa. Wananchi wetu hawawezi kumudu kununua majiko ya gesi na majiko ya umeme. Niombe sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha katika bajeti hii inayokuja kuona namna gani wanapunguza kodi ili Watanzania walio wengi waweze kumudu kununua majiko ya gesi ili tuendeleze kampeni hii ya kumtua mama kuni kichwani tuone tumefikia kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ni jambo jema litatuletea tija na Watanzania wengi wataondokana na matumizi ya kuni na mkaa majumbani kwa sababu tunaona uharibifu wa mazingira unaendelea kukua kwa kasi kubwa sana na tunaona hali ya mabadiliko ya tabianchi, joto limekuwa kali mvua hazipatikani kadri tunavyotumaini. Kwa hiyo, tuone namna bora ya kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanaondokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono kwa asilimia mia, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Kwa sababu nachangia kwa mara ya kwanza, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwake lakini kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwapa moyo Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kumpongeza Makamu wetu wa Rais Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu, kwa kuwa Makamu wa Rais, mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa nyadhifa kubwa katika nchi yetu na imeweza kutupa heshima kubwa wanawake wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu na Baraza lake Tukufu la Mawaziri kwa kuchaguliwa kwao lakini kwa kuthibitishwa kwake Waziri Mkuu katika Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nami naendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kumwongoza aweze kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ya kipekee kabisa niwashukuru wapiga kura wanawake wa Mkoa wa Lindi, UWT wa Chama cha Mapinduzi kwa kuniwezesha leo nikawa ndani ya Bunge lako Tukufu, nami nawaahidi kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nachukua nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa Hotuba yake nzuri aliyoitoa ambayo imeelekeza mipango ya utekelezaji wake kwa kipindi hiki kitakachoanzia 2016/2017, hotuba ambayo inatupa matumaini makubwa katika kuhakikisha afya za Watanzania zinaboreka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne katika kuboresha huduma ya afya nchini kwetu. Tunajua na tumeona mafanikio makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne, mafanikio hayo ndiyo ambayo yatazaa matunda mema katika kipindi hiki kinachokuja cha 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa tuliyoyaona, lakini bado tuna changamoto kubwa nyingi katika maeneo mbalimbali. Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea changamoto mbalimbali zilizopo katika Majimbo yao lakini zilizopo ndani ya mikoa yetu. Napenda kuongelea changamoto kubwa ambazo zimo katika Mkoa wetu wa Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo hospitali ya Mkoa wa Lindi Manispaa inayoitwa Sokoine Hospital. Hospitali hii ina changamoto kubwa sana, changamoto kubwa tunajua kwamba Hospitali ya Mkoa wateja wake wakubwa ni wagonjwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Wilaya mbalimbali zilizopo katika Mkoa wa Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Sokoine, ina wagonjwa wengi sana, lakini Madaktari waliokuwepo ni wachache, kwa hiyo, inasababisha wagonjwa kushindwa kupata huduma kwa wakati kwa sababu tu ya mlundikano wa wagonjwa wengi kwa kukosa Madaktari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunalo tatizo kubwa la Madaktari Bingwa wa Wanawake. Wanawake tunapata matatizo makubwa sana na wengi wanapoteza maisha kwa sababu tu ya kukosa huduma iliyokuwa stahiki. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri alitazame kwa jicho la huruma suala ili Mkoa wa Lindi tuweze kupata Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapokuwa na Daktari Bingwa katika Hospitali ya Mkoa itanusuru wanawake wengi kutoka wilaya mbalimbali. Kwa hiyo, tunaomba sana tuweze kupata Daktari Bingwa katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto nyingine kubwa ya kutokuwa na miundombinu iliyo kuwa mizuri ya majitaka na majisafi. Hospitali ile ya Mkoa wa Lindi tunajua ni hospitali kongwe, ni hospitali ya muda mrefu, miundombinu yake ya maji imekuwa michakavu sana na kusababisha katika wodi ya wazazi kukosa maji na Mheshimiwa Waziri ni mwanamke, anajua maji yalivyokuwa muhimu katika wodi ile ya wazazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba kwa dhati kabisa suala hili la kufanya ukarabati wa miundombinu katika hospitali yetu ya mkoa, Serikali itusaidie kuhakikisha miundombinu ile inabadilishwa na kuwekwa miundombinu mingine. Katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi naisemea sana ile kwa sababu ndiyo inabeba wagonjwa wengi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkoa wa Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mashine ya endoscopy, mashine ile inakosa mtaalam na kusababisha mashine ile kukaa muda mrefu bila kutumika lakini wagonjwa wanakosa tiba kwa kukosa mtaalam ambaye anaweza kutumia mashine ile. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri atutazame kwa jicho la huruma ili tuweze kupata mtaalam atakayeweza kuiendesha mashine ile ili wagonjwa wa magonjwa haya ya vidonda vya tumbo waweze kupata tiba kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya mbalimbali tumeona Wilaya nyingine zimekosa kuwa na Hospitali za Wilaya, ni pamoja na Lindi Manispaa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya hitimisho lake atueleze ni namna gani ataweza kuzisaidia Wilaya hizi ambazo hazina Hospitali za Wilaya ili Wilaya hizi ziweze kupata hospitali na wanawake na watoto waweze kupata huduma hizi za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo imeongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni ukosefu wa madawa katika hospitali zetu. Katika hospitali zetu za Mkoa wa Lindi zote zinakosa madawa. Tuna Wilaya sita katika Mkoa wa Lindi, ikiwepo Wilaya ya Liwale, Nachingwea, Lindi Vijijini, Kilwa, Lindi Manispaa pamoja na Ruangwa, tunakosa madawa ya kutosha na kufanya wagonjwa wakose madawa na hatimaye wengine kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba wananchi wetu wengi hawana uwezo wa kununua madawa katika maduka ya dawa. Wanapokosa dawa katika hospitali zetu za Serikali zinawafanya washindwe kupata tiba kwa wakati na kusababisha vifo vingi vya wanawake na watoto. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili la upatikanaji wa madawa katika hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mfuko huu wa Bima ya Afya. Nchi yetu sasa hivi tumeingia katika Mfuko huu wa Bima ya Afya na wananchi wetu tunawahamisha kuingia katika Mfuko huu wa Bima ya Afya. Suala hili Waheshimiwa Wabunge wengi wameliongelea, tunapata tatizo kubwa kwa sababu wanapokwenda hospitali wanapata maandishi tu na badala yake dawa wanakosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inawakatisha tamaa; na hata wale ambao wangependa kuingia katika mfumo huu wanapata hofu na kuacha kuingia katika mfumo huu wa Bima ya Afya. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye jitihada zaidi ya makusudi katika kuhakikisha hospitali zetu nchini kote zinakuwa na madawa ya kutosha na tutakapofanya kampeni hii ya kuingia katika Mfuko wa Bima ya Afya, wananchi wetu watakuwa na matumaini ya kupata dawa katika mahospitali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala lingine la Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake katika Halmashauri zetu. Katika Halmashauri zetu tunatenga asilimia kumi; tano ya vijana na tano ya wanawake, lakini tumeona katika Halmashauri zetu nyingi hazina mapato ya kutosha na kupelekea pesa inayopatikana kuonekana kwamba ni kidogo haitoshelezi. Katika Majimbo mengine yana Kata zaidi ya 30. Majimbo mengine yana Kata 33, mengine yana Kata 30, na mengine Kata 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa na mapato madogo, mathalan unapata shilingi milioni 10 ya vijana na shilingi milioni 10 ya wanawake…
MWENYEKITI: Ahsante. Muda wako ndiyo huo, tunakushukuru.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wake, dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama na ndugu yangu Mheshimiwa
Mavunde kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini kwa kuwasilisha hotuba yao nzuri yenye mwelekeo wa kazi kwa kipindi hiki cha mwaka 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana ndugu yangu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli amefanya kazi nzuri kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja, nasi wananchi wa Lindi tuna matumaini makubwa na yeye na tuko nyuma yake katika kuunga mkono jitihada kubwa anazozifanya katika kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchangia katika hotuba yake ambayo ameiwasilisha Mheshimiwa Waziri wetu. Naipongeza sana Serikali kwa jitihada kubwa inayoifanya ya kuongeza kukuza uchumi, lakini kupunguza umaskini wa wananchi wetu katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Mawasiliano, Ujenzi wa barabara, Bandari, reli, viwanja vya ndege na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia namna ambavyo Serikali inaendelea kuboresha miundombinu yetu hasa ya barabara na hasa tukiangalia Jiji la Dar es Salaam tumeshuhudia msongamano wa magari unavyoendelea kupungua. Hizi ni jitihada kubwa sana ambazo zinafanywa na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada hizi za kuunganisha barabara za mikoa na mikoa na kuendelea kukarabati barabara hizi, ni vizuri sana tukaangalia katika Mkoa wetu wa Lindi kutoka Dar es Salaam, barabara inayokwenda Lindi kuna maeneo ambayo sasa hivi yanasumbua sana. Ukitokea hoteli tatu kwenda Mbwemkuru kuna maeneo yana mashimo mengi sana kiasi kwamba magari hayawezi kupita vizuri. Hata Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania alipokuja katika ziara yake Mkoa wa Lindi aliona namna ambavyo barabara
ile imeharibika hata kama mashimo yale yalitiwa kifusi kidogo, lakini hali ilikuwa siyo shwari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba barabara hii waitazame kwa sababu kwa kweli tumehangaika katika kipindi kirefu sana tangu uhuru upatikane, lakini tunaishukuru Serikali yetu imejitahidi kuiwezesha barabara hii kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iendelee kuiangalia vizuri ili iendelee kutuhudumia wananchi wa Mikoa hii ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 30 ameongelea vivuko na usafiri majini. Napenda kuishukuru sana Serikali kwamba katika kipindi cha Bajeti hii ambayo tunaimalizia katika eneo la Lindi Manispaa, tulipata pesa shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kujenga kivuko cha Lindi – Kitunda, lakini hatuoni chochote kinachoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kitunda wanahangaika sana hasa wanawake, pindi anaposhindwa kujifungua na analazimika kuja katika hospitali kubwa ya Mkoa kufanyiwa operation namna ya kumsafirisha mtu huyu ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali ituangalie, itusaidie kwa nguvu zote ili tuweze kupata kivuko kiweze kutusaidia wananchi wa Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi huu wa LNG, uchakataji wa gesi katika eneo hili la Lindi Manispaa, Kata ya Mbanja, Kijiji cha Likong’o. Eneo hili lilishapimwa na lilishatolewa hatimiliki ya eneo lile na wananchi sasa hawana uhakika tena wa wao kuendelea kuishi pale, lakini wananchi wale hawajapewa fidia zao mpaka leo. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuharakisha kwa sababu eneo lile limekuwa siyo lao tena na limeshakuwa sasa ni miliki ya Serikali kupitia Shirika hili la Mafuta. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu kuwasaidia wananchi hawa ili waweze kupata fidia na wao waweze kujiendeleza katika maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa sana katika kuwawezesha vijana wetu kupata mafunzo ya stadi za kazi na ujuzi ili na wao waweze kushiriki katika uendelezaji au uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana katika Mkoa wetu wa Lindi tumebahatika kupata Chuo cha VETA na kipo katika eneo la Lindi Manispaa. Tunajua Sera ya Elimu ni kujenga vyuo kila Wilaya, lakini kutokana na uchumi tuliokuwa nao, itachukua muda mrefu sana kuweza kuwa na Chuo cha VETA kila Wilaya. Ombi langu kwa Serikali ni kwamba, chuo hiki kimekuwa kinatoa mafunzo mengi sana pale Lindi, lakini vijana wanaoshiriki ni wachache sana kwa sababu ya ukata wa maisha. Chuo kina changamoto zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hakina mabweni ya kulala wanafunzi, lakini nyumba za Walimu na miundombinu pia ya maji machafu imekuwa ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, tuna imani kubwa na Serikali hii. Tunaomba itusaidie sana katika kuhakikisha Chuo kile kinakuwa na mabweni ya kulala wanafunzi ili ndugu zetu wanaoishi katika Wilaya nyingine ikiwemo Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Kilwa, Lindi Vijijini nao waweze kushiriki katika kupata mafunzo katika chuo kile cha VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kubwa sana; wanafunzi wanaosoma pale wanaishi katika nyumba za watu binafsi wakilipa pango, kwa hiyo, imekuwa ni changamoto kubwa sana. Wanajilipia pango wenyewe, lakini hata gharama za maisha za kuishi ni za kwao
wenyewe. Kwa hiyo, imekuwa ni changamoto kubwa sana na wazazi wengi wanashindwa kuleta wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali itusaidie wakati mipango mingine; mipango ya muda mrefu inaendelea ya kutujengea mabweni, basi ihakikishe inatoa gharama ya chakula kuwapunguzia ukali wa maisha wanafunzi ambao wanasoma pale na nina imani mkitusaidia kutuchangia gharama za chakula, basi wanafunzi wa maeneo mengine ya Wilaya nyingine wataweza kushiriki katika kuja kusoma mafunzo ya ufundi stadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kushirikiana na Jumuiya ya Ulaya na Plan International, tunao mradi wa YEE. Mradi huu unafanya vizuri sana katika eneo letu la Lindi Manispaa na Lindi Vijijini. Kwa hiyo, tunawashukuru sana. Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na timu yake kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kipindi hiki cha 2016/2017 lakini kwa maandalizi ya utekelezaji wa mpango huu wa 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwa dhati kuishukuru Serikali kwa kufanya usanifu kilomita 91 za barabara za Masasi – Nachingwea - Nanganga kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, kwa barabara za mkoa ambazo zipo katika mpango wa mwaka 2017/2018 kilomita 537.9, naiomba Serikali kuiangalia barabara itokayo Nachingwea – Liwale kwani hali si shwari, kipindi cha masika barabara hiyo haipitiki kabisa. Naiomba Serikali kuingiza katika mpango wa bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Lindi ni mkongwe sana na ulitumika hata kipindi cha Ukoloni na ni kiwanja bora katika Afrika ulikuwa namba tatu. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kuhakikisha uwanja wa Lindi unapewa kipaumbele ukizingatia Lindi sasa tunategemea uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha LNG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali imeweza kutuunganisha Watanzania kupitia sekta ya mawasiliano.

Bado katika Mkoa wa Lindi tuna vijiji havina kabisa mawasiliano. Kwa mfano, Nachingwea (Kijiji na Mbondo); Ruangwa (Nangurugai na Nandandala); Kilwa (Mandete, Mandawa, Mavuji na Kandawale) na Liwale (Ngongowele, Mirui, Mlembwe na Mpigamiti). Naomba Serikali kupitia Mfuko wa UCSAF kuvisaidia vijiji hivi viweze kupata mawasilino.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy kwa uwasilishaji wa taarifa yake, iliyosheheni afya za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa jitihada kubwa inayofanya katika kuimarisha na kuboresha afya zetu Watanzania. Lakini niendelee kuipongeza Serikali kwa kutuunganisha Watanzania katika mfumo rasmi wa bima ya afya. Nimpongeze kwa dhati kabisa Mkeshimiwa Waziri Ummy na Naibu wake kwa jitihada kubwa sana waliyoifanya katika kampeni ya kuhamasisha mfuko huu wa bima ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwetu Lindi tunashukuru kwa dhati kabisa, Mheshimiwa Waziri Ummy aliandaa utaratibu wa kampeni rasmi, japokuwa yeye hakufika lakini wawakilishi wake walifanya kazi na jitihada kubwa ilionekana na tuliweza kuongeza idadi ya watu wanaotumia bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi kubwa zinazoonekana za kuimarisha na kuboresha afya za Watanzania, bado tuna changamoto kubwa sana. Katika upande huu wa bima ya afya inaonekana watumiaji wa bima ya afya ni wengi lakini upatikanaji wa dawa umekuwa ni duni kabisa. Kwa hiyo, naiomba Wizara kuimarisha katika eneo hili la upatikanaji wa dawa ili wananchi waweze kupata tiba vizuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali yetu ya Mkoa wa Lindi tuna changamoto mbalimbali. Tuna changamoto kubwa sana ya Madaktari Bingwa, kwa sababu Hospitali ya Sokoine Mkoa wa Lindi ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, wateja wake wakubwa ni wananchi kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Lindi, hivyo tunahitaji Madaktari Bingwa katika Hospitali yetu ya Sokoine.

Mheshimiwa Waziri Ummy alituahidi kutupatia madaktari wanne, ningependa kujua madaktari hawa watakuja lini katika hospitali ya Mkoa wa Lindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Lindi ni hospitali kongwe iliyojengwa mwaka 1954, naishukuru sana Serikali kwa kuifanyia ukarabati wa kutosha na majengo yanaonekana ni mazuri, majengo nadhifu, yanapendeza lakini bado tuna changamoto kubwa ya miundombinu ya maji taka. Ninaiomba sana Serikali kusimamia katika eneo hili ili hospitali hii iweze kuwa na miundombinu ya maji machafu katika mfumo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upatikanaji wa maji safi pale Sokoine ni mdogo kabisa, tunajua hali ya mji wa Lindi hakuna kabisa maji, wananchi wa Lindi bado tunaendelea kupata shida, lakini bado tunaendelea kuiamini Serikali yetu na jitihada kubwa inayofanya ya kuimarisha upatikanaji wa maji katika Mji wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bado katika hospitali ya Sokoine kuna changamoto kubwa sana ya x-ray. X-ray iliyopo imeshapita muda wake wa matumizi, inashindwa kufanya kazi na wagonjwa wanashindwa kupata huduma hii ya x-ray. Ninamuomba kwa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri Ummy kuitazama Lindi Sokoine ili tuweze kupata x-ray mpya iweze kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri Ummy, hospitali ya Wilaya ya Kilwa katika eneo la mortuary hakuna majokofu ya kutunza maiti pale, ninaomba kwa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri Ummy tuitazame Wilaya ya Kilwa ili wahakikishe katika eneo lile la mortuary tunapatiwa majokofu ili tuweze kufanya kazi zetu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hospitali ya Wilaya ya Liwale, tunayo x-ray pale katika hospitali ya Wilaya lakini mtaalam wa ku-operate mashine hizi za x-ray hakuna, Mheshimiwa Waziri Ummy tunaomba utuangalie...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuishakwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAMIDA H. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Niendelee kumpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uwasilishaji wa bajeti ya utekelezaji wa mambo mbalimbali kuhusiana na masuala ya elimu kwa kipindi hiki cha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali kwa mafanikio makubwa ya kuhakikisha upande wa elimu unaendelea kuboreka. Hata hivyo, pamoja na mafanikio na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali yetu bado tuna changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali zinazowafanya watoto wetu washindwe kabisa kuendelea na elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona suala la ujauzito ni changamoto kubwa sana kwa watoto wetu wa kike. Vilevile bado tuna changamoto zingine kama vifo na utoro mashuleni umekithiri kwa kiasi kikubwa sana. Kwa hiyo, lazima tujipange katika kuhakikisha utoro mashuleni unaondoka kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado vifo vingi vinasababisha watoto wetu kushindwa kuendelea na masomo. Naiomba sana Serikali ijipange vizuri kuhakikisha kwamba maji salama yanapatikana katika maeneo yote kwa sababu maeneo mengi hatupati maji salama. Watoto wetu wanakunywa maji ambayo si salama na yanawasababishia matatizo ya kiafya na kwa sababu hospitali, zahanati ziko mbali sana, si vijiji vyote vina hospitali, kwa hiyo, mtoto anapopatwa na ugonjwa wa kuharisha asipopata tiba kwa haraka kwa kweli inamsababishia kifo. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali izingatie suala la upatikanaji wa maji katika maeneo yote ili kuhakikisha watoto wetu wanapata maji safi na salama na kuendelea kuimarisha afya zao ili waweze kumaliza elimu kama ambavyo wametarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali yetu kwa kukarabati vyuo vikongwe katika nchi hii. Katika mkoa wetu wa Lindi tuna TTC Nachingwea, chuo kile ni kikongwe kinahitaji kukarabatiwa kwani miundombinu yake ni mibovu na kimechakaa. Kama mimi ningekuwa Bwana Afya ningefunga kile chuo, kwa kweli kinasikitisha sana. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kukitazama chuo kile kwa jicho la huruma sana ili kiendelee kudumu kwa muda mrefu na kiweze kuzalisha Walimu kwa sababu mahitaji ya Walimu bado ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishukuru sana Serikali imeweza kukarabati Chuo cha Ufundi kilichopo Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Ruangwa. Tunashukuru sana chuo kile kimekarabatiwa na sasa kimeanza kupokea wanafunzi 28 na wameshaanza mwaka huu wa kwanza. Niiombe sana Serikali kuharakisha kujenga mabweni kwa sababu bado tunahitaji watoto wa kike na wao waweze kushiriki katika kupata mafunzo ya ufundi stadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wa kike anapolala kwenye nyumba ya kupanga tunamtengenezea nafasi ya kushindwa kuendelea na masomo. Kwa hiyo, bado tunahitaji mabweni yajengwe pale ili watoto wa kike waweze kukaa katika mabweni na waendelee na masomo na itasaidia Wilaya nyingine zilizopo Mkoa wa Lindi watoto kuja kushiriki kupata mafunzo katika Wilaya ya Ruangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna mategemeo makubwa sana na Chuo chetu cha VETA kilichopo Mkoa wa Lindi katika eneo la Lindi Manispaa na hili nalizungumzia kila mara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Bajeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Napongeza sana kwa namna ambavyo Jeshi letu linavyoendelea kuchapa kazi na kuendelea kuimarisha amani ya nchi yetu. Naliomba sana kuendelea kuyalinda maslahi ya Jeshi letu, lakini kujengewa mazingira mazuri ya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Mkoani Lindi, Wilayani Nachingwea, tunayo Kambi kubwa ya Jeshi maarufu kama Majimaji camp. Kambi hii ni kubwa ilijengwa na Baba wa Taifa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kutembelea na kujionea hali halisi ilivyo pale, nyumba za Askari wetu zimekuwa chakavu sana na majengo pia yamekuwa machakavu. Naiomba Serikali kuboresha nyumba zile na majengo yao ya kazi ili waishi katika mazingira safi na rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mwigulu L. Nchemba kwa kuwasilisha bajeti ya Wizara yake katika kipindi cha bajeti cha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze Wizara hii kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kuendelea kudhibiti vitendo vibaya, viovu vinavyofanyika katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Wajumbe wa Kamati kwa kufanya ziara katika Mkoa wa Lindi. Kwa kweli wamethibitisha uchakavu wa nyumba za maaskari wetu zilivyochakaa, inatia huruma sana. Naiomba sana Serikali katika nyumba hizi zitakazojengwa katika kipindi cha bajeti hii ya 2018/2019, tupate mgao wa nyumba kwa ajili ya Polisi wetu na Askari Magereza katika Wilaya za Lindi Manispaa na Wilaya ya Nachingwea; naiomba Serikali kusikia kilio chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuwapa pole wananchi wa Mkoa wa Lindi na wana CCM wote wa Mkoa wa Lindi kwa msiba mkubwa uliotupata wa Mzee wetu Alhaji Ally Mtopa. Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema peponi, amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi lakini nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anazozifanya za kuwatumikia Watanzania na kazi zake zinaonekana. Niwapongeze pia Waheshimiwa Naibu Mawaziri wake kwa kazi ambazo wanamsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo inaelezea mapitio na mwelekeo wa kazi katika kipindi cha 2018/2019. Vile vile niipongeze sana Serikali yangu kwa kazi kubwa inayoifanya katika kutekeleza mambo mbalimbali na mambo yote yaliyotekelezwa kwa kweli yameleta mafanikio makubwa katika nchi yetu na mambo yote yanaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika utekelezaji kwa kipindi hiki cha 2017/2018, bado tunazo changamoto mbalimbali. Nizungumzie upande wa barabara zetu. Katika bajeti hii ambayo tunategemea itaishia mwezi huu Juni, katika Mkoa wetu wa Lindi tulibahatika kupitisha bajeti ya ujenzi wa kiwango cha lami kutoka Nanganga – Luchelegwa – Nachingwea -Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri husika atakapofanya windup atueleze mpango huu wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami umefikia wapi maana hatuoni utekelezaji na kipindi cha mwaka huu kinakwisha bado robo moja tu tutamaliza mwaka. Pia ningependa kujua, tulitenga pia bajeti ya kufanya uthamini wa barabara inayotoka Nangurukuru - Liwale - Nachingwea nayo pia atueleze imefikia wapi katika utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Lindi kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza ahadi yake ya kutuletea kivuko pale Lindi. Tumepokea kivuko MV Kitunda, Mheshimiwa Rais aliahidi kutoa na ameweza kutekeleza. Kwa hiyo, tunashukuru sana na tunampongeza, tunamwombea dua njema ili aweze kutekeleza mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa ya barabara inayotoka Dar es Salam – Lindi – Mtwara. Barabara hii ni mkombozi sana wa wananchi wa Mikoa hii Kusini lakini bado kuna changamoto kubwa ya barabara kuwa na mashimo mengi lakini TANROADS wanashindwa kufanya ukarabati kwa kukosa fedha. Naiomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa barabara hizi. Barabara ya Kusini ni mkombozi wa watu wa Kusini na kutuletea maendeleo wananchi wa Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeona katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namna ambavyo kilimo sasa kimeleta tija kubwa katika nchi yetu lakini bado tunaona Serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha inaendeleza kilimo katika nchi yetu. Ukiangalia zao la korosho ambalo sasa hivi limeendelezwa katika mikoa mingi nchini Tanzania lakini bado tuna Sheria ya Korosho ambapo kabla haijasafirishwa inatozwa export levy ambapo mapato yake asilimia 65 yanaenda katika Bodi ya Korosho na asilimia 35 inabaki katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika fedha hizi Bodi ya Korosho inanunua pembejeo na kufika kwa wakati kwa wakulima lakini pia inanunua magunia, inazalisha mbegu bora ya korosho na inafanya mambo mbalimbali ya kuendeleza zao hili la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 shilingi bilioni 88 zilipatikana na mwaka 2017/2018 zaidi ya shilingi bilioni 133 ziliweza kupatikana lakini fedha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja lakini naiomba Serikali irudishe fedha hizi katika chombo chetu cha Bodi ya Korosho ili iweze kufanya kazi. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nianze na kuunga mkono hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa namna ambavyo imeimarisha mitandao ya kiuchumi katika ujenzi wa barabara, madaraja, gati, reli, viwanja vya ndege na bandari. Uwekezaji huu kwenye miundombinu itafanya wawekezaji/uwekezaji kukua kwa kasi na kuongeza mapato ya nchi.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali kufuatilia ukarabati wa barabara za lami unaondelea. Wahandisi wahakikishe wanawashauri wakandarasi kuweka viraka vya lami vinavyofanana na uhalisia wa lami ya zamani. Sasa hivi barabara zetu ziko kama zimechorwa rangi, viraka vyeusi na lami yenyewe nyeupe. Sura ya barabara inaonekana kama ni michoro ya rangi. Taifa letu ni kubwa, nchi yetu tuipe heshima na kuiweka katika sura nzuri inayopendeza.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake kwa kuwasilisha taarifa yao ya mapato na matumizi kwa kipindi hiki cha 2018/2019. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza Mawaziri hao kwa sababu wanafanya kazi kama timu na nimeshuhudia katika kipindi kifupi tu kazi ambazo zinafanyika za usimamizi wa rasilimali hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia rasilimali hii ya madini, kwa kweli anastahili pongezi zote. Kwa kila namna tuendelee kumuombea dua njema Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya nzuri, afya njema ili aweze kusimamia majukumu yake ambayo yanaleta faida katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia Wizara ya Madini kwa usimamizi, kwa muda mfupi wameweza kuongeza mapato kwa zaidi ya asilimia 120. Hii ni kazi nzuri na wameweza kusimamia vizuri na kwa mabadiliko haya ya sheria ambazo tumezipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Mkoa wa Lindi. Katika Mkoa wa Lindi tumebahatika kuwa na madini mbalimbali. Tunayo ruby, sapphire, graphite, gypsum, chokaa, chumvi na dhahabu lakini niseme Serikali bado haijafanya maamuzi ya kuweka mazingira wezeshi ya kusimamia rasilimali hizi za madini ambazo zipo katika Mkoa wa Lindi ili ziweze kunufaisha Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali wameweza kutoa leseni kwa wawekezaji hawa wa graphite ambao wako Ruangwa. Tunategemea sasa waanze mara moja uchimbaji huu wa madini ili wananchi wa Ruangwa waweze kupata ajira lakini uchumi wetu pia uweze kukua katika Mkoa wetu wa Lindi na hatimaye Serikali yetu iweze kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo gypsum ambayo ipo Kilwa katika eneo la Kiranjeranje, Hoteli Tatu na maeneo mengine. Hii gypsum ina ubora wa kidunia, ni suala la kujivunia kwamba tuna rasilimali ambayo ipo katika soko la dunia lakini bado Serikali haijatilia mkazo katika usimamizi wake na kuweka mazingira wezeshi kuifanya Serikali yetu iweze kupata mapato. Sasa hivi kuna uchimbaji tu ambao upo kiholela, kwa hiyo, tunapoteza mapato mengi sana kupitia madini haya ya gypsum. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali kusimamia uwekezaji huu wa gypsum ili Serikali iweze kupata mapato lakini pia wananchi wa Mkoa wa Lindi tuweze na sisi kukuza uchumi wetu kupitia hii gypsum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wazalishaji wengi wa chumvi nchini Tanzania lakini na kwetu Lindi tuna wazalishaji hao wa chumvi lakini tuna changamoto mbalimbali katika eneo hili la chumvi. Wadau hao wa chumvi mara nyingi wamekuja kuleta kilio chao kwa Serikali lakini bado hatujapata nafasi ya kuwasaidia. Naiomba sana Serikali kuwatazama kwa macho mawili ili wazalishaji wa chumvi nao waingie katika ushindani wa soko na tuweze kuwa na viwanda vya chumvi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa chumvi kuna tozo mbalimbali. Ziko tozo ambazo zinatozwa kupitia halmashauri kati ya asilimia 5 - 10 lakini bado utakuta wanunuzi wa chumvi wanaposafirisha njiani tena wanakumbana na tozo zingine mbalimbali. Pia kuna ushuru wa mikoko ambao unatozwa na Wizara hii ya Maliasili na Utalii lakini cha kusikitisha tozo hii inatozwa eneo lote la mikoko. Kwa hiyo, mimi naishauri Serikali tozo hii wangeelekeza katika eneo lile ambalo linazalisha chumvi kuliko kutoza katika eneo zima la mikoko. Tozo hii inatozwa katika kila ekari mbili na nusu Sh.130,000, kwa hiyo bado tunaona wazalishaji wa chumvi wana mzigo mkubwa ukiangalia mlolongo wote wa tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna tozo ya kuandikisha mashamba na inatozwa kila mwaka Sh.320,000 na kuna leseni wanalipia kila mwaka. Kwa hiyo, tunaona mzigo ambao upo kwa wazalishaji wa chumvi na kusababisha chumvi yetu ya Tanzania kuuzwa bei ya juu kuliko chumvi ile ambayo inaingizwa kutoka nje ya nchi. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali kuangalia baadhi ya tozo hizi ambazo zinaleta kero kwa wazalishaji wa chumvi na kufanya chumvi iwe bei ya juu basi tuweze kufanya mabadiliko ya sheria ili tuweze kuwasaidia wenzetu wazalishaji wa chumvi na tuweze kuwa na viwanda vya chumvi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao wachimbaji wa madini wanawake. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, siyo kwa kuwa yeye ni mwanamke tu lakini kuwatazama hawa wachimbaji wa madini wanawake ili Serikali sasa iwape mafunzo na iwawezeshe kwa kuwapa vitendea kazi na wao waweze kuingia katika fursa hii ambayo ipo ya madini na kupata leseni za kuwaruhusu kuingia katika uchimbaji huu wa madini. Kwa hiyo, hili ni suala muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine tunalo hili Shirika letu la STAMICO, hili shirika bado halina miguu. Naiomba Serikali kulisaidia shirika hili kama ambavyo tumeweza kuwasaidia ATC, Kampuni ya Simu, TANESCO, basi na hawa STAMICO tuone umuhimu wa kuwasaidia ili na wao waweze kupata miguu wasonge mbele. Wanayo mipango na mikakati mizuri lakini wanashindwa kutekeleza kwa sababu tu ya kukosa fedha. Kwa hiyo, hilo ni suala muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Spika wetu kwa kuteua Kamati Maalum iliyoenda kusimamia masuala mazima ya madini. Kwa kweli wamefanya kazi nzuri na tumeona mazao ya kazi ile. Bahati njema tumepata faida katika Kamati ile tumepata Mawaziri. Kwa hiyo, tuna imani kabisa na wao, nasi tunawaunga mkono katika shughuli zao mbalimbali katika kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, naiomba Wizara izingatie maoni na ushauri wa Kamati ya Madini. Tumeshauri mambo mengi sana na kwa bahati njema baadhi ya mambo wameyafanyia kazi, tumeyaona katika kitabu chao. Niwatakie kila la kheri katika bajeti hii, Serikali iweze kutoa fedha kwa sababu Wizara ni mpya inataka kujipanga vizuri katika kuhakikisha inasimamia rasilimali za nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia taarifa za Wizara hizo mbili, ambazo zipo mezani. Kwanza nianze kwa kuunga mkono taarifa hizo.

Mheshimiwa naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi ambazo anaendelea nazo za kukutana na makundi mbalimbali katika kuendelea kuimarisha ili nchi yetu iendelee kusonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa nzuri ambazo anazifanya za kuendelea kuimarisha katika kutoa huduma mbalimbali, lakini kwa dhamira njema ya kuhakikisha tunafikia malengo ya kuzalisha Megawatt 5000 katika kuhakikisha sasa Tanzania tunakwenda katika uchumi huo wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia ni mpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Dotto kwa kuteuliwa kwake na kuwa Waziri katika Wizara hii ya Madini. Ni Wizara mpya lakini ni Wizara ambayo inakwenda vizuri, tunafanya nayo kazi vizuri. Kwa kipindi kifupi tumeona jitihada kubwa sana wanazozifanya katika kukuza uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie upande wa REA ambao Waheshimiwa Wabunge wengi wameuzungumzia. Upande wa REA kwanza naipongeza nchi yetu kwani tumeweza kuwashawishi wawekezaji kuja kufungua viwanda vya uzalishaji wa nyaya, uzalishaji wa transformer, LUKU na vifaa mbalimbali pamoja na nguzo za umeme na kufanya kazi ya usambazaji wa umeme kuwa rahisi na kutumia muda mfupi katika utekelezaji wa usambazaji huu wa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitegemea kwamba Wakala wa Umeme Vijijini kwa kutumia fursa hii wa uwepo wa viwanda ndani ya nchi, wangeweza kufanya kazi kwa speed ambayo tuliitarajia ya kusambaza umeme katika vijiji vingi nchini Tanzania. Tunajua kwamba mradi huu wa REA ndiyo mkombozi kwa wanyonge kule vijijini. Tumeona maeneo ambayo tayari umeme huu umefika, namna ambavyo vijana wamefurahia na wanahangaika kujiajiri katika kuendesha shughuli mbalimbali zinazotumia umeme. Kwa hiyo, umeme wa REA umekuwa ni mkombozi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kwa sababu tumetenga fedha kwa ajili ya mradi wa REA, lakini ukiangalia kiwango cha mafuta tunachoagiza na kuingizwa nchini na kiasi cha mafuta kinachouzwa: Je, kinalingana na ile fedha ambayo REA wanaipokea? Kwa hiyo, tunayo changamoto ya upatikanaji wa fedha ya kusukuma miradi hii ya REA kuhakikisha Watanzania umeme unawafikia. Pia tungeongeza Wakandarasi ili kusukuma hizi kazi ziweze kwenda kila kona na kuhakikisha umeme unafika kwa wakati kwa wananchi kule vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kuwapongeza Baraza na Mawaziri na kuipongeza Serikali kwa namna ambavyo wameweza kuondoa VAT katika umeme kule Zanzibar, wamefanya jambo la kiungwana sana. Kwa kweli hoja hii ilikuwa ina manung’uniko mengi sana, hata sisi Wanakamati tulikuwa tunajiona kwamba hatuna amani. Kwa hiyo kwa uamuzi ambao Serikali imeufanya kwa kweli tumefarijika sana, kwa sababu tumeona tunaendelea kuimarisha Muungano wetu ili twende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie upande wa TANESCO, kwanza nilipongeze shirika kwamba linakwenda, totauti na pale zamani. Shirika hili sasa limeanza kulipa madeni kwa TPDC, kwa hiyo ni hatua nzuri sana kwa sababu sasa wanaweza kwenda. Shirika linaonesha sasa linajiimarisha. Rai yangu kwa Serikali, zile ofisi za Serikali ambazo zina madeni makubwa ziungane kwa pamoja kuhakikisha tunawaunga mkono TANESCO kwa kuwalipa madeni yao, ili sasa waweze kujiimarisha katika kuhakikisha wanatoa huduma iliyokuwa bora kwa wateja wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia kwa hatua mbalimbali ambazo wamezifikia, leo Watanzania tunanunua umeme kupitia simu zetu, wametupunguzia mzigo mkubwa tofauti na zamani, imeleta tija sana lakini pia imepunguza madeni, imeweza kufunga umeme wa LUKU, haya ni maeneo makubwa kwa Shirika hili la TANESCO.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo kubwa ambazo wanazifanya kulikuwa na wizi wa umeme lakini wamejitahidi katika kudhibiti wizi ule wa umeme ambao ulikuwa unatokea. Kwa hiyo wote kwa pamoja tuungane katika kuhakikisha tunaendelea kulilinda shirika hili kwa kuwasaidia panapotokea tunaona katika maeneo umeme unabiwa, basi tuweze kutoa taarifa ili mara moja watu hao washughulikiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nipongeze juhudi kubwa zinazofanya na Serikali kupitia Wizara hii, tumeweza Serikali kupanua bandari pale Dar es Salaam kupunguza msongamano lakini Bandari ya Tanga na kule Mtwara ili kuweza kusogeza huduma kwa wananchi, ni maendeleo makubwa sana, kwa sababu kama wananchi wa Mikoa ya Kusini wanapata mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kule Mtwara, kwa kweli ni faraja kubwa sana na ni maendeleo kwetu kwa sababu yanaweza kuongeza ajira katika sekta mbalimbali. Kwa hiyo nipongeze juhudi ambazo zinafanywa na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie upande wa LNG; tunajua yanayoendelea Serikalini ya kukamilisha mazungumzo mpaka hapo mwaka 2023/2024. Naiomba sana Serikali katika eneo lile ambao inakwenda kutekeleza mradi LNG wapo wananchi ambao wanaishi pale na kwa kipindi kirefu sasa karibu miaka mitano walishaambiwa kwamba wasiweze kujiendeleza pale, kwa maana tumewambia maendeleo yao yakae likizo kwa muda fulani, naiomba sana Serikali yangu kwa kipindi karibu cha miaka mitatu mfululizo fedha inatengwa kwa ajili ya kuwapa fidia hao wananchi lakini fedha hiyo haitoki. Sasa ningependa wakati Waziri ana wind up aniambie ni kwa nini fedha hii haitoki kwenda kupewa fidia wananchi wale wa Kata ya Mbanja, Kijiji cha likong’o.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie upande huu wa madini, nimshukuru sana Waziri wa Madini na Naibu wake, kwa kweli walitoa ushirikiano katika kuhakikisha tozo mbalimbali kwa wazalishaji wa chumvi hasa wale wa Lindi ambao walikuja hapa Dodoma tukakaa nao pamoja na kuona baadhi ya tozo ziondolewe ili kuwafanya wazalishaji wa chumvi waweze kuingia katika ushindani wa masoko, lakini tuweze kuwa na viwanda vya chumvi nchini Tanzania. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Waziri, Mheshimiwa Dotto pamoja na Naibu wake, lakini hata wakati ule dada yangu Mheshimiwa Angella Kairuki alifanya kazi kubwa ya kutusaidia na hatimaye wananchi wale wanaendelea vizuri katika uzalishaji wa chumvi, lakini kuna Halmashauri ambayo

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hamida kengele ya pili imeshagonga, ahsante sana.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami niendelee kuungana na Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi katika kuhakikisha kwamba tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu wake na timu nzima ya Wizara hii ya Afya katika kuhakikisha kwamba wanaendelea kuchapa kazi na kazi zao zinaonekana. Mheshimiwa mmoja amesema aliye na macho haambiwi tazama, kwa sababu kazi hizi zinaonekana, tunaendelea kuboresha afya za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kufanya ziara katika Mkoa wetu wa Lindi. Imeleta tija sana na faida kubwa kwetu, lakini ameweza kujionea changamoto mbalimbali ambazo zipo katika Mkoa wetu wa Lindi katika eneo hili la vituo vya afya ambavyo vinaendelea kujengwa. Vipo ambavyo vimekamilika na vipo ambavyo havijakamilika lakini vinaendelea viko katika hatua nzuri sana, tunaendelea kuvisimamia kuhakikisha kwamba vituo hivi vinakamilika na vianze mara moja kutoa huduma. Vile vile vipo vituo vya afya ambavyo vimekamilika; Kituo cha Mnazi Mmoja pale Lindi Manispaa, lakini kituo kimoja pale Lindi Vijijini, kule Nyangamala, tunasubiri tu ufunguzi ufanyike vituo hivi vianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alifanya uzinduzi wa upimaji wa Saratani ya Shingo ya Kizazi pale Sokoine, Lindi Manispaa, huduma hii imeweza kusaidia kuwafikia wanawake wengi wameweza kujitokeza katika kuhakikisha kwamba wamekwenda kupima tatizo hili la Saratani ya Shingo ya Kizazi. Niendelee kuipongeza Serikali na niishauri Serikali kuendelea kutoa huduma hii ya mobile katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha kwamba wanawake wengi wanajitokeza kuendelea kupima tatizo hili ambalo linaonekana sasa linakua kwa kasi kubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kufanya kampeni ya utoaji wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa watoto wetu wa kike kuanzia umri wa miaka 14 japokuwa tunapata changamoto ya kwamba wazazi wa watoto hawa hawawaruhusu kupata hii chanjo. Naomba tuendelee kutoa elimu kwa wazazi hawa na watoto wetu ili waweze kupata kinga hii ambayo inatolewa na Serikali kwa sababu tatizo hili mbele ya safari linasababisha wanawake kunyanyapaliwa na waume zao kutokana na tatizo hili la kansa ya shingo ya kizazi na wanawake wengi wanapoteza maisha kutokana na tatizo hili kubwa ambalo linaendelea kukua katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulishirikiana na Mheshimiwa Ummy Mwalimu katika kuhakikisha kwamba tunahamasisha wananchi kujiunga na NHIF katika Mkoa wetu wa Lindi. Tatizo lililopo ni kwamba wananchi wengi hawana elimu ya kutosha ya upatikanaji wa kadi hizi za bima ya afya. Nashuhudia pale Ruangwa alitoa elimu na wananchi palepale hospitali walidiriki kukata na kujiunga na NHIF. Kwa hiyo, suala kubwa ni tuendelee na kampeni kuwahamasisha wananchi wetu kujiunga na NHIF ili waweze kupata huduma ya matibabu pale wanapopatwa na matatizo na inasaidia pale wanapokuwa hawana fedha, basi kupata matibabu bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, la msingi ni kuendelea kuimarisha vituo vyetu vya afya vyote viwe na dawa za kutosha ili wananchi wale wenye bima za afya wasikate tamaa na itakuwa ni njia nzuri ya kuwafanya hao wenye bima ya afya kuendelea kuhamasisha watu wengine ili waweze kujiunga na wao katika mpango huu wa bima ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika ujenzi wa vituo hivi vya afya, bado tunazo changamoto mbalimbali. Ukiangalia katika Mkoa wetu wa Lindi eneo hili la watumishi tuna changamoto kubwa sana na Mheshimiwa Waziri Ummy alipokuja alipata taarifa ya mahitaji ya watumishi katika Mkoa wa Lindi. Mahitaji yalikuwa ni watumishi 4,898 lakini watumishi waliopo ni 1,784, sawa na asilimia 36 na pungufu ilikuwa ni 3,114 sawa na asilimia 64. Kwa hiyo upungufu huu wa watumishi katika eneo hili la afya katika Mkoa wa Lindi ni kubwa sana na ni changamoto kwa sababu wananchi wengi wanakosa kupata huduma hii kwa kukosa Madaktari na watumishi mbalimbali katika maeneo haya ya vituo vyetu vya afya, zahanati na hospitali ambazo zipo. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Ummy Mwalimu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na timu nzima ya Wizara yake kwa uwasilishaji wa bajeti katika kipindi hiki kinachokuja cha 2019/ 2020, lakini kwa namna ambavyo wamejipanga katika kuhakikisha kwamba wanaendelea kuleta mapinduzi makubwa ya umeme katika nchi yetu na kuhakikisha kwamba tunajipanga kwa ajili ya uwekezaji na kukuza uchumi lakini kukuza ajira katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali kwasababu iko miradi mbalimbali ambayo inaendelea kutekelezwa, lakini mingine iko katika mpango wa utekelezaji na hii yote ina dhamira njema ya kuzalisha umeme katika nchi yetu kwa sababu bado tunahitaji matumizi makubwa ya umeme katika nchi yetu katika kuhakikisha kwamba tunaendelea kujipanga vizuri katika kuleta mapinduzi haya ambayo tunayategemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema kwamba katika mradi huu wa REA ambao Waheshimiwa Wabunge wengi wameusemea. Nimebahatika kupita katika maeneo mbalimbali tukiwa katika ziara ya Kamati katika kukagua miradi mbalimbali ambayo inaendelea na tumeendelea kuwasha umeme katika vijiji vingi nchini Tanzania. Kwa hiyo bado hali si mbaya sana ya umeme katika maeneo ya vijiji umeme unaendelea kuwekwa, lakini tunaamini kwamba vijiji vinaendelea kukua siku hadi siku, miji pia inatanuka au inaendelea kukua, kwa hiyo mahitaji ya umeme bado ni makubwa. Kwa hiyo niishauri tu Serikali kwamba katika eneo la REA basi ni vyema tukaongeza wakandarasi ili kazi zikaenda kwa spidi ambayo tunaitarajia kwa sababu kila mmoja wetu hapa anahitaji katika eneo lake basi vijiji vyote viwe vimefikiwa umeme kwa wakati mmoja jambo si rahisi sana kwetu, lakini tukijipanga vizuri basi angalau mwaka 2020 basi maeneo mengi yatakuwa yameweza kufikiwa na huu umeme wa REA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake; walikuja kupitia shirika la TPDC katika Mkoa wetu wa Lindi na walikuja kutuelimisha na kutoa elimu mbalimbali. Tumejionea mambo mbalimbali kupitia mkutano ambao tumeufanya katika Mkoa wetu wa Lindi. Kaimu Mkuu wa Mkoa alimshauri Waziri kwamba makandarasi yule anaonekana hayuko tayari kufanya kazi katika Mkoa wa Lindi. Sasa tuliomba tubadilishiwe mkandarasi yule aweze kuwekwa mkandarasi mwingine ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala mradi wa LNG, kama alivyotangulia kusema mdogo wangu Mheshimiwa Bobali pale, ni mradi mkubwa ambao tunautegemea katika mkoa wetu wa Lindi tuweze kuupokea ingawa tumeupokea tangu mwaka 2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kila mwaka tunatenga fedha za kuwalipa fidia wapisha mradi wa LNG katika eneo la Likong’o. Miaka minne mfululizo bajeti inakuwa inatengwa lakini fedha haitoki kwa ajili kuwawezesha ndugu zetu ambao wanapisha mradi katika eneo hili la likong’o. Sasa nilikuwa naiomba sana Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja na ninampongeza Waziri Mkuu kwa namna ambavyo anachapa kazi yeye na wasaidizi wake wote katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kibajeti ya maendeleo katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mvua zilizonyesha zimeathiri kwa kiasi kikubwa na uharibifu mkubwa wa barabara nyingi,mashamba na mifugo.

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali kuona namna ya kusaidia kwa haraka sana kuhakikisha wananchi wanapata chakula. Kupimiwa viwanja bure, kuwafanya wananchi kuwa na makazi na kujenga maeneo salama.

Mheshimiwa Spika, Serikali iongeze fedha upande wa ujenzi, barabara zimeathiriwa sana, sasa shughuli za usafiri na usafirishaji zimekuwa ngumu sana.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini nikishukuru Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Jimbo la Lindi Mjini kuniwezesha kurudi tena katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kutuletea Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa. Pamoja na hayo, amefanya kazi nzuri kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita katika kuhakikisha kwamba tunakuza uchumi wa taifa letu. Hakuna asiyejua, kila mmoja anajua kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano. Mpango huu umeweka kipaumbele katika kukuza uchumi wa bahari pamoja na uvuvi. Mwenyezi Mungu ametujaalia nchi yetu tuna bahari na maziwa. Eneo la bahari tuna kilomita za mraba 64,500 lakini upande wa maziwa tuna kilomita za mraba 62. Katika maeneo haya ndiko kunapatikana samaki na ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani, uzalishaji wa madini ya chumvi, gesi na mafuta, utalii wa fukwe za bahari pamoja na michezo mbalimbali ya bahari. Katika uwekezaji huu wa blue economy, eneo hili La bahari ni la Muungano, naomba kuishauri Serikali kuhakikisha kwamba tunazipitia sheria pamoja na miongozo na kanuni ili tuweze kufanya kazi vizuri katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kutekeleza miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kuhakikisha kwamba tunakwenda kusimamia uchumi huu wa bahari. Tunahitaji kuwa na wataalamu wenye kujua na wenye uzoefu ili tuweze kukuza uchumi huu wa bahari. Niishauri Serikali kupeleka wataalam wetu nje ya nchi kwenda kusoma ili waweze kupata ujuzi mzuri tuweze kuja kutekeleza haya ambayo tunayakusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo, tunahitaji pia uendelezaji wa sekta hii ya bahari uende sambamba na uwekezaji wa miundombinu yake. Tunahitaji kujenga bandari kwa ajili ya shughuli za usafirishaji na uvuvi. Hatuwezi kutumia bandari ya Dar es Salaam, leo inashusha mzigo wa sulphur halafu kesho inashusha samaki, hapana haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba Serikali yetu inaendelea kujenga bandari zitakazotumika kwa shughuli za uchumi huu wa bahari. Tunaweza kupanua na kujenga bandari kule Bagamoyo lakini tukajenga bandari kule Mkoani Lindi. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumepanua huduma hii ya bandari na kuendelea na uwekezaji huu wa uchumi wa bahari. Pia tunahitaji meli zinunuliwe ambazo zitakwenda kufanya kazi katika kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tungeweza kujenga chuo ambacho kitakwenda kusimamia masuala mazima ya uchumi wa bahari pamoja na uvuvi. Pale Lindi tuna maeneo mengi ya ardhi na tuko tayari kutoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki. Kwa hiyo, naishauri Serikali kujipanga vizuri katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kusimamia uchumi huu kwa ajili ya kuongeza kipato cha nchi yetu ili tuweze kuwahudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali ya bahari tunayo na rasilimali watu tunayo na Watanzania tuna afya nzuri ya kufanya kazi. Ni sisi Serikali sasa kujipanga katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kukuza uchumi huu wa bahari pamoja na uwekezaji kwenye eneo la uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona Waziri anapokuja kutoa taarifa yake ya kazi ya kipindi cha mwaka mmoja na kuonyesha kwamba mapato ya Wizara yake yameongezeka kwa kutoza faini, hii siyo sahihi. Tunategemea Mawaziri wasimamie tuone mapato yanaongezeka kupitia miradi ya kimkakati katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa katika kuhakikisha kwamba Serikali yetu inaendelea kufanya kazi za maendeleo na kuendelea kukuza uchumi kwa Taifa letu lakini kuendelea kukuza ajira na kuboresha maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pole kwa Watanzania kwa msiba mzito ambao umetupata pamoja na Waheshimiwa Wabunge nawapa pole sana kwa sababu tulizoea kufanya kazi na ndugu yetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Tumeona namna ambavyo ameweza kusimamia na kuendesha Serikali yetu kwa kipindi cha miaka mitano na ameweza kusimamia maendeleo makubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza Mama yetu Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu kwa uteuzi wake. Nina hakika kwamba ana uwezo mkubwa wa kusimamia Taifa letu na kuendesha yale mazuri yote ambayo alianza kufanya kazi na Mheshimiwa ndugu yetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba naanza kwa kuunga mkono hoja. Ukiangalia Mpango wetu hata ukiangalia mipango yote iliyopita tumeona kwamba kuna hoja ya Miradi ya Magadi Soda Engaruka, Mchuchuma na Liganga na LNG. Miradi hii mikubwa kila mwaka tunaiona ipo katika Mpango wetu wa Maendeleo wa Taifa lakini naona kwamba Serikali haijawa tayari kusimamia miradi hii kuhakikisha kwamba tunakwenda sasa kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Mradi wa Mchuchuma na Liganga soko la makaa ya mawe yapo ndani ya nchi na nje ya nchi lakini Serikali hatujakuwa tayari kuwekeza ili kuhakikisha kwamba uzalishaji huu unaendelea kuleta tija na manufaa kwa Taifa letu. Kwa hiyo, naiomba Serikali kusimamia ili kuhakikisha kwamba mradi huu unakwenda vizuri na unaleta tija na unaongeza mapato kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna Mradi huu wa LNG, kwanza niishukuru Serikali kwa hatua ambayo imefikia kuhakikisha kwamba imetoa fedha ya kulipa fidia kwa wanaopisha mradi pale Lindi katika eneo la Likongo. Hata hivyo, naiomba Serikali kuharakisha mradi huu ili sasa utekelezaji uweze kuanza na kuhakikisha kwamba tunakwenda nao vizuri kwa sababu mradi huu utatuletea manufaa makubwa na utaingiza mapato makubwa katika Taifa letu. Si kwamba tutakaofaidika ni wana Lindi lakini Tanzania nzima tutafaidika na mradi huu wa LNG. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali sasa kuharakisha mazungumzo ya mwisho yaliyobaki kuhakikisha kwamba sasa mradi huu tunakwenda katika utekelezaji. Nina hakika kwamba Mama yetu Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu atausimamia vizuri kuhakikisha kwamba tunakwenda kwenye utekelezaji. Pia naomba wafidiwa waliobaki kulipwa fidia zao basi Serikali iharakishe kutoa malipo ili wananchi wale tuweze kuwaondoa na waweze kupisha mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la afya. Katika Sera ya Afya tumeweza kutekeleza vizuri na Mpango wa Taifa wa Pili uliwekeza sana katika kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya na hospitali za rufaa. Tunaishukuru sana Serikali kwa kusimamia Mpango huo vizuri. Changamoto kubwa iliyopo na naomba Mpango huu wa Tatu uweze kusimamia ni kuhakikisha kwamba vituo vya afya vilivyojengwa vinakamilishwa kwa kuweka vifaa tiba na kuongeza wauguzi na waganga ili wananchi waendelee kupata huduma kama ambavyo tulivyotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano iliwekeza katika kuboresha sekta ya elimu na ilitumia trilioni 3.15. Ilifanya kazi kubwa katika kuhakikisha kwamba imewekeza katika sekta ya elimu. Naomba Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa kwa maono ya Mheshimiwa aliyekuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana kila Mkoa kwa mchepuo wa sayansi uzingatie kuhakikisha kwamba tunakwenda kuendeleza maono haya ili watoto wetu wa kike waendelee kupata elimu ya masomo ya sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunazo shule kongwe, najua mpango wa Serikali wa kujenga na kukarabati shule kongwe unaendelea kwa shule za sekondari pamoja na vyuo lakini bado hatujaangalia katika shule zetu za msingi. Kuna shule za msingi ambazo ni chakavu mno, ukiangalia kwa macho hazipendezi na hazikaliki madarasani na hazipo rafiki kabisa wanafunzi kukaa madarasani. Kwa hiyo, naomba Serikali sasa kupitia Mpango huu wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa uziangalie zile shule za msingi kongwe ziendelee kuingizwa katika Mpango maalum na Serikali iweze kuzikarabati ili tuwe na shule bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sera ya barabara, tunazo barabara kuu za kiuchumi zinazounganisha mkoa na bandari lakini zinazounganisha bandari na nchi Jirani. Tuna barabara inayotoka Dar es Salaam – Pwani - Lindi – Mtwara; tuna barabara inayotoka Dar es Salaam – Morogoro - Dodoma - Mwanza, lakini tuna barabara zinazokwenda nchi za jirani maana yake zinaunganisha uchumi wa nchi yetu na uchumi wa nchi Jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zetu zimekuwa dhaifu sana hata kama tunazikarabati utakuta barabara imekarabatiwa imetumika miezi sita tu tayari imeingia kwenye uchakavu. Kwa hiyo, Serikali yetu inaendelea kutumia fedha nyingi kukarabati kila mara barabara hizi lakini bado zinaonekana zipo chini ya kiwango. Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa kuhakikisha kwamba sera yake inakuwa wazi namna bora ya kuzikarabati na kuzijenga barabara hizi kwenye kiwango cha hali ya juu ili ziendelee kutumika katika kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala zima la TARURA. TARURA wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana lakini ukiangalia hata ofisi hawana, baadhi ya maeneo ofisi za TARURA hazipo tunatumia majengo ya kukodi lakini majengo yenyewe ni madogo hayana nafasi kubwa, pia bado hawana vifaa na magari na kuna upungufu mkubwa wa watumishi. Kwa hiyo, naomba sasa Serikali kuangalia namna bora ya kuwaboresha hawa ndugu zetu TARURA ili tuende nao vizuri na waweze kufanya kazi zao vizuri na sisi tuweze kufaidika na TARURA katika kuhakikisha kwamba wanaendelea kufanya kazi katika mazingira rafiki na tunategemea kwamba waweze kusimamia barabara zetu za kule kwenye Halmashauri zetu ziweze kuboreka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Mpango wa Tatu wa Taifa katika uwekezaji wa uchumi wa bahari. Nimeona kwamba sasa tunakwenda kuwekeza katika sekta hii ya uvuvi na kuhakikisha kwamba Serikali yetu sasa inaingia katika uwekezaji huu wa bahari. Ni jambo jema sana lakini nafahamu kwamba sekta hii ya uvuvi inatoa ajira za kudumu zaidi ya laki mbili, lakini inatoa ajira za muda mfupi zaidi ya milioni 4. Kwa hiyo, ni jambo jema sasa kuingia katika uwekezaji huu na sisi tutaendelea kufaidika na Serikali yetu itaendelea kuingiza mapato ya kutosha. Nashauri tu tuwekeze katika rasilimali watu kwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na wataalamu wenye ujuzi mkubwa wa kusimamia sekta hii ya uwekezaji huu wa uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Tatu wa Taifa pia umeonesha namna bora ya kusaidia ndugu zetu wa SIDO. SIDO wanafanyakazi nzuri sana na tukiwatumia ndugu zetu wa SIDO…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili Mheshimiwa.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, tuwekeze kuwasaidia na kuwapa nguvu ndugu zetu wa SIDO ili watusaidie kutoa elimu ya mafunzo stadi lakini tutakuwa na uwekezaji mkubwa wa viwanda vidogo vidogo kwa sababu wao wanasimamia shughuli hizi. Kwa hiyo, naomba tuwaunge mkono ndugu zetu wa SIDO ili kuharakisha maendeleo ya wajasiriamali wadogo wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa kwa kunipa nafasi nichangie hoja ambayo hiko mbele yetu. Katika halmashauri ambayo inakusanya mapato mapato madogo ni Halmashauri ya Manispaa ya Lindi. Jana nilikuwa nasikia Mheshimiwa Zungu kwake anakusanya bilioni 60 lakini ukiangalia kwenye halmashauri yetu tunakusanya bilioni moja na milioni mia tatu tu Lindi Manispaa ina majimbo mawili na majimbo hayo yana changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, ningeiomba Serikali kutusaidia kwasababu tayari tumeshaandika andiko mradi kwa ajili ya miradi ya kimkakati ya ujenzi wa soko kuu lakini ujenzi wa stendi kuu ya mabasi.

Mheshimiwa Spika, soko ambalo linatumika sasa lilijengwa tangia mwaka 1950 ni muda mrefu sana soko limekuwa chakavu mno, hata mapato yanayoingia kutoka katika soko lile ni mapato madogo sana tunakila namna ya kuona Serikali ni kwa namna gani mnaweza mkatusaidia halmashauri ya Manispaa ya Lindi kuhakikisha kwamba tunapata fedha za kuwekeza katika miradi hii ya kimkakati ili kuongeza mapato yetu ya halmashuri ili tuweze kuhudumia wananchi wa halmashauri.

Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa barabara Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea suala zima la TARURA ninajua kwamba Serikali inaendelea kuboresha majiji miji pamoja na manispaa. Bahati mbaya sana miaka miwili mfululizo katika Manispaa ya Lindi hatujabahatika kupata fedha za kujenga barabara zetu.

Kwa hiyo, ninaiyomba Serikali itusaidie kuhakikisha kwamba kipindi hiki cha fedha tunapata fedha kwa ajili ya kuboresha Manispaa yetu ya Lindi na ukizingatia kwamba tuna changamoto kubwa za barabara na mvua zilizonyesha miaka miwili mfululizo ni mvua kubwa sana uharibifu mkubwa sana wa barabara upo katika maeneo yetu na barabara hizi kushindwa kutumika. kwa hiyo ninaiyomba Serikali iangalie katika hoja hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee swala la Watendaji wetu wa Kata, watendaji hawa ndio wasimamizi wa shughuli za maendeleo katika kata zetu lakini ndio wanaosimamia kukusanya mapato yetu katika kata zetu. Kuna changamoto kubwa sana katika eneo hili, ninaiomba Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha ofisi zao za kata na ofisi hizi zilizokuwepo ambazo wanadandiadandia tu hata vifaa vya kufanyia kazi hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba sana Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha ofisi za Watendaji wa Kata lakini kuboresha vifaa vya kufanyia kazi ikiwemo pikipiki na vifaa vingine vya ofisi ili iwe rahisi wao kupita katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha kwamba wanaendelea kukusanya mapato na Serikali tuendelee kupata mapato yetu ili tuweze kumudu kuwahudumia wananchi wetu katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninajua muda mdogo naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi/ Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuendelea na mjadala ambao uko Mezani wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako, pamoja na timu yake nzima ya Wizara yake kwa kazi nzuri ambayo wameifanya kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Tumeona mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, lakini bado katika mpango wa bajeti ya Wizara hii katika utekelezaji wa kipindi hiki cha 2021/2022 tumeona bajeti namna ambavyo inakwenda kuendelea kuboresha sekta ya elimu katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo. Hauwezi kwenda chuo ama chuo kikuu bila kuanza shule ya msingi. Tumeona namna ambavyo shule zetu za msingi, hasa zile zilizojengwa tangia miaka ya 1960, 1970, shule ambazo mpaka sasa hivi zinatumika lakini ni shule ambazo zimekuwa chakavu mno. Mabati yameshaoza. Wakati wa mvua watoto wanashindwa kukaa madarasani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba katika mpango wa kuboresha shule kongwe ambao ulitekelezwa kwa kipindi kilichopita ambao Mheshimiwa Prof. Ndalichako alianza nao, tunaomba tuendelee kuboresha shule zetu za msingi ziweze kuwa katika hali nzuri na tuendelee kuzitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waswahili wanasema usipojenga ufa utajenga ukuta, kwa hiyo, kuna kila sababu sasa ya Serikali kuona namna gani tunakwenda kuboresha shule za msingi. Na nina hakika maeneo mengi Waheshimiwa Wabunge wanayalalamikia katika shule hizi za msingi kuona kwamba zina uchakavu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Lindi Manispaa tunazo shule karibia 12, shule ambazo ni chakavu mno kupitiliza. Lakini unajua kwamba Mji wa Lindi ni mji mkongwe sana ambao walianza kukaa wakoloni huko. Kwa hiyo tuna kila sababu sasa ya kutusaidia Lindi kwa sababu maeneo mengi tumerithi kutoka kwa wakoloni kwa hiyo majengo yamekuwa machakavu mno. Ninaiomba sasa Serikali kuangalia namna gani wanaweza kutusadia kuhakikisha kwamba shule hizi za msingi zinaendelea kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru Serikali kupitia fedha za EP4R; zimekuwa ni msaada mkubwa na zimesaidia kwa kiasi kikubwa sana kumaliza maboma ambayo wananchi wamejitolea. Na pale Lindi tumefaidika na fedha hizi, zaidi ya milioni 200 zimekuja na zinafanya kazi ya kuendelea kukamilisha madarasa haya ili yawe katika sura nzuri na watoto wetu waendelee kupata masomo yao.

Mheshimiwa Spika, zipo changamoto za jumla upande wa shule za msingi na sekondari. Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukizungumzia karibia wiki nzima, kuna upungufu mkubwa sana wa walimu katika maeneo haya, na Mheshimiwa Rais ameshatoa katika hotuba yake kuajiri watu 600. Ninaomba tuzingatie katika sekta ya elimu kupeleka walimu wa kutosha ili watoto wetu waendelee kusoma vizuri lakini tuweze kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo ya walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa kuna changamoto ya wlaimu wanaostaafu kutopewa malipo yao kwa wakati. Hizi ni hoja za jumla ambazo zimezungumziwa, pamoja na kupandisha madaraja lakini nina hakika kwamba wahusika wataendelea kusimamia kuhakikisha kwamba changamoto hizi zinaondoka.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mwaka hadi mwaka kuhakikisha kwamba inatenga fedha kwa ajili ya kwenda kuwekeza katika vyuo vya VETA ambavyo vinawasaidia watoto wetu wanaomaliza darasa la saba wakashindwa kuendelea, pamoja na form four wanaoshindwa kuendelea na masomo ya juu. Kwa hiyo, vimekuwa vikisaidia sana kuwapa mafunzo mbalimbali vijana wetu ili waweze kupata ufundi stadi na waweze kutengeneza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Lindi Manispaa tumebahatika kuwa na Chuo hiki cha VETA na kimejengwa muda mrefu. Kuna changamoto; vifaa vya kufundishia vimeendelea kuwa chakavu lakini hata magari yameendelea kuwa chakavu kwasababu kuna masomo pia ya udereva katika vyuo hivi vya VETA.

Mheshimiwa Spika, vijana hawa wanaokwenda kupata mafunzo katika vyuo vya VETA ninaishauri Serikali kuwa na mahusiano kati ya chuo cha VETA, wanafunzi na halmashauri kwasababu wanavyokwenda kusoma VETA wanapata mafunzo mbalimbali, wanaporudi kwao baada ya kumaliza masomo wanashindwa kujiendeleza kwasababu wanakuwa hawana fedha za kuendelea kuzalisha na kukuza uchumi pamoja na kwenda kuwekeza kwenye viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kwasababu halmashauri tuna asilimia kumi ya mapato, ingeweza kutumika kwenda kuwaboresha vijana hawa ambao tayari wanapata mafunzo kutoka VETA ili sasa kuwawezesha vijana kuendeleza yale mafunzo waliyopata ili kuendelea kukuza uchumi na kuendelea kumudu kuendesha maisha yao. Nafikiri tukifanya hivyo tutakuwa tumepunguza mzigo mkubwa kwa Serikali, lakini tutakuwa tumewawezesha vijana hawa kujiendeleza kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Lindi Manispaa tumetoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vikuu, kampasi ya Lindi. Chuo Kikuu kampasi ya Kilimo tumetoa zaidi ya ekari 120 lakini mpaka leo ujenzi haujaanza. Lakini pia tumetoa ekari 150 kwa ajili ya Chuo Kikuu cha masuala ya Uvuvi na Usafirishaji Baharini.

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali sasa kutoa fedha ili kuendeleza ujenzi huu, kuhakikisha kwamba vyuo vikuu hivi kampasi ya Lindi vinaendelea kujengwa, lakini watakaofaidika na vyuo vikuu hivyo siyo Wanalindi peke yake, Kanda nzima ya Kusini watapata elimu pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba tunaendelea kuvisimamia vyuo vikuu hivi ili viweze kukamilika katika ujenzi wake hata kama si kwa asilimia 100 lakini kila mwaka tungeweza kutenga fedha na hatimaye tungeweza kumaliza kuhakikisha kwamba ujenzi huo unakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna chombo kinachoitwa SIDO; SIDO inatoa mafunzo ya ufundi stadi lakini inasimamia masuala mbalimbali ya wajasiriamali pamoja na wanaoingia katika uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo. Ninaiomba Serikali kuendelea kutumia SIDO katika maeneo yetu, maeneo ambayo chombo hiki kipo ili kuwezesha fedha za kutosha na kuendelea kuwawezesha vijana wengi kuingia katika maeneo haya ya ufundi stadi na uwekezaji wa viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Wake na timu yake ya wizara yake kwa namna ambavyo wanachapa kazi, lakini kwa namna ambavyo wamejiandaa na bajeti hii ya 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, bajeti hii imegusa kila eneo na imezingatia changamoto mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge tulikua tunampelekea Mheshimiwa Waziri hoja mbalimbali. Kwa hiyo, nimshukuru sana lakini nimtakie kila kheri katika utekelezaji wa kipindi hiki cha mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, yako mambo mbalimbali ambayo yako ndani ya mpango huu wa bajeti ambayo itatekelezwa katika kipindi hiki. Naomba nishauri tunamuomba Waziri wa Fedha ajitahidi sana kutoa fedha kwa wizara hii iweze kutekeleza mipango yake ambayo himo katika mpango huu wa mwaka 2021/2022 kwasababu kuna mambo mazuri yanayokwenda kupunguza kero mbalimbali ya changamoto hii ya maji, sasa utekelezaji huu utazingatia upatikanaji wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha kutoa fedha kwa wakati kuhakikisha kwamba Wizara ya Maji inapata fedha na inakwenda kuteleza miradi hii ya maji. Niishukuru Serikali kwasababu Lindi tulikuwa na changamoto kubwa ya maji katika eneo Kata ya Rasibula Mtwero, lakini tayari tuko katika mpango huo wa utekelezaji kikubwa ni upatikanaji wa fedha tukatekeleze huu mradi wa maji kuhakikisha kwamba Mitwero, Kikwetu na Mchinga changamoto ya maji inaondoka.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyopo Lindi Manispaa ni uwepo wa gari maji taka, lakini nimshukuru sana Waziri lakini niishukuru Serikali kwamba tayari tupo katika mpango wa utekelezaji wa ununuzi wa gari la maji taka ili kuhakikisha kwamba Lindi Mjini tunakuwa na gari la maji taka na kufanya utekelezaji wa maji taka ili kuweka mji wetu kuwa salama na wananchi wetu waendelee kuwa salama.

Mheshimiwa Spika, tunaamini kwamba uwepo wa maji duniani ni jambo kubwa ni jambo jema kwasababu mtu unaweza ukose umeme lakini usikose maji, unaweza ukose barabara lakini usikose maji, kwa hiyo, tunajua kwamba katika matumizi makubwa ya binadamu na shughuli za binadamu zinategemea sana uwepo wa maji. kwa hiyo, niitakia kila kheri Serikali yetu kuhakikisha kwamba inapata fedha za kutosha na kuweza kwenda kutekeleza miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na miradi ya maji ambayo ndugu zetu hawa la LUWASA walitekeleza kuweka viura katika mitaa, lakini ninajua kwamba Serikali ina nia njema ya kumtaka kila mwananchi aweze kuvuta laini ya maji nyumbani kwake ili afanye matumizi yake mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo ni kwamba maeneo ambayo yamepita mainline za maji inakuwa na umbali mkubwa kiasi kwamba mwananchi anashindwa kugharamia kuvuta maji kutoka kwenye connection mpaka nyumbani kwake gharama zinakuwa kubwa mno, lakini ukiangalia mabomba ambayo yanatoa huduma na wenyewe LUWASA nayenyewe yanakuwa na gharama kubwa ukilinganisha na bei ya madukani kwa hiyo tuangalie katika eneo hili ili tuhakikishe kwamba wananchi wetu wanaweza kumudu kuvuta line za maji manyumbani kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali kwenda kuhakikisha kwamba hasa Waziri na Naibu wake na timu yake katika utoawaji wa majisafi na salama ambayo tunapata huduma kutoka kwenye viwanda mbalimbali, maji mengine yanakua na chloride nyingi sana kiasi kwamba ukunywa yanakuwa chungu, kwa hiyo, ninamuomba Mheshimiwa Waziri aende akakaguwe ili kuangalia viwango vya ubora wa maji haya na kuweka hali za wananchi wetu ziendelee kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niendelee kuishukuru sana Serikali lakini niendelee kuwatakia kila kheri ili mipango yetu iliyomo katika bajeti hii tuweze kutekeleza kwa kipindi hiki cha 2020/2021. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana ahsante sana. (Makofi)


Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo mezani ya Wizara ya Uvuvi na Mifugo. Kwanza nianze kumpongeza Waziri pamoja na Naibu wake na timu nzima ya Wizara yake kwa kuwasilisha bajeti yao ya kipindi hiki cha mwaka 2021/2022 katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kutuunganisha Wabunge wote wa mikoa hii ambayo tunatoka maeneo ya ukanda wa bahari na kuweza kufanya kikao cha pamoja na kuchambua changamoto mbalimbali zinazowakumba wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Bashiru, aliyekuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi Taifa kwa kusimamia vizuri uandishi wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Ilani yetu imeeleza vizuri katika eneo hili la sekta ya mifugo na uvuvi kwa lengo la kutaka kuleta mapinduzi makubwa na kuzifanya sekta hizi ziweze kukuza uchumi, kukuza ajira, kuendelea kuwekeza kwenye viwanda vidogo vidogo na kuendelea kuleta ustawi wa wananchi wetu ambao wamejiajiri katika sekta hizo na hatimaye kuongeza kipato na kuleta mapato makubwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri na timu yake kwa sababu mengi wameyazingatia, lakini nina mashaka makubwa sana katika utekelezaji wake. Kwa sababu fedha ya maendeleo inayoletwa katika sekta hizi ni ndogo sana. Pamoja na kwamba kuna mipango mizuri ya utekelezaji wa kipindi hiki cha 2021/2022, kama fedha hazikuja kama ambavyo tunatarajia, maana yake yale yote mazuri ambayo tunayategemea katika kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hizi itakuwa ni kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Fedha, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya utolewaji wa fedha katika sekta mbalimbali. Namwomba sana Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mwigulu Mchemba aangalie namna gani atahakikisha anasimamia Sheria ya Fedha kupeleka fedha kwa wakati ili Wizara hizi ziweze kusimamia utekelezaji wa mambo ambayo tunayapanga na kuhakikisha kwamba tunaleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba Mpango wa Tatu wa Taifa umeelekeza nguvu kubwa sana katika uwekezaji wa uvuvi wa bahari. Naipongeza Serikali kwa sababu wameanza kwa kasi nzuri ya kuwekeza Bandari ya Mbegani na kwa kununua meli ya kuanza kufanya kazi katika sekta hii ya uvuvi. Hata hivyo, tukumbuke tuna wavuvi wadogo wadogo katika maeneo yetu; na sekta hii watu wengi wamejiajiri kwa sababu, sisi wazaliwa wa maeneo ya Pwani tangu wazee wetu, kazi kubwa ilikuwa ni shughuli ya uvuvi. Kwa hiyo, vijana wetu, watoto wetu, baba zetu, wamerithi kutoka kwa mababu zetu kufanya shughuli hii kuweza kujipatia kipato na kuweza kuendelea kumudu maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo iliyopita, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya kupata manyanyaso makubwa kwa wavuvi wetu. Hatutegemei kutokea yaliyotokea. Ndugu yangu Naibu Waziri, Mheshimiwa Ullega alikuwepo anayajua na ndugu zake wa Mkuranga, Lindi, Pwani na maeneo mengine Dar es Salaam anajua changamoto ambazo zimewakumba wavuvi wetu. Tunaiomba sana Serikali kuzingatia kwa sababu, wavuvi wetu wengi wamepoteza Maisha, wavuvi wengi wame-paralyze kwa kupata pressure, wavuvi wengi ndoa zao zimeharibika kwa sababu ya maisha yao kutoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvuvi mdogo ni mtu masikini sana, anapoingia baharini anapata samaki wa kumwezesha yeye kupata kipato na kuweza kumudu kuendesha maisha yake. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba tunasimamia kwenye eneo hili ili wavuvi wetu wasibughudhiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotunga sheria na kanuni tuzingatie katika maeneo husika. Unapomtaka mvuvi mdogo akavue mita 50 kwenda chini ya bahari na boti yake aliyokuwa nayo ni dhaifu, hana vifaa vya kisasa, hivi unategemea huyu unamtakia maisha mema kweli! Naiomba Serikali kutazama namna bora ya kuhakikisha kwamba tunawasaidia wavuvi wetu wadogo wadogo ili kutengeneza ajira na waweze kumudu maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba tunawaweka sawa wavuvi wetu wadogo kwa kuwapa elimu, lakini kuwawezesha kupata mikopo waweze kununua vifaa vya kisasa na waweze kuingia baharini kuweza kufanya shughuli zao. Huwezi kuanza jambo kubwa kama hujaboresha katika jambo dogo. Kwa hiyo, naiomba Serikali kusimamia katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mara nilikuwa namfuata Waziri karibia miezi mitano sasa, kila tukikutana ajenda inakuwa moja ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Masuala ya Uvuvi na Usafirishaji Majini. Sisi pale Lindi Manispaa tumetoa tayari ekari 150. Kwa hiyo, naiomba Serikali, Waziri atakapokuja ku-wind-up atuambie ni lini wataanza kujenga chuo hiki ili tuwekeze katika rasilimaliwatu kuhakikisha kwamba baadaye tutapata wataalam watakaokuja kusimamia sekta hii ya uvuvi na usafirishaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Lindi tumebahatika kupokea wafugaji. Wafugaji hawa mmetuletea lakini hamjawatengenezea mazingira ya wao kuweza kuishi vizuri. Imekuwa mwenye nyumba anaombwa na mtu mmoja kwamba nina familia ya watu 20, naomba niwalete kwako. Unapowaleta unawaacha, huwahudumii, huwatengenezei mazingira yoyote. Wafugaji hao wanahangaika, hawana maeneo ya kulisha mifugo yao na badala yake wanavamia mashamba ya watu na kusababisha migogoro mbalimbali. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba wafugaji waliokuja katika Mkoa wetu wa Lindi, watengenezewe mazingira mazuri ya kuishi ili waweze kufanya shughuli zao za ufugaji. Pale Lindi hatuna shughuli za ufugaji, sisi tumezoea kuishi kwa kuvua, tunakula samaki, lakini bado tunahitaji kula nyama ili tuendelee kuboresha afya zetu. Kwa hiyo, Serikali ifanye kila namna ya kuona namna gani wanaweza kuboresha wafugaji waliowaleta kwetu Lindi. Wana familia zao, wanahitaji kuishi vizuri, watoto wao wanahitaji kusoma, kwa sababu maisha yao hayaeleweki, hawana uhakika wa kuishi; mara leo wako hapa, kesho pale, kesho kutwa kule. Kwa hiyo, hali siyo shwari. Naomba Serikali isimamie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa. Nimekuachia kidogo umalizie, muda wako ulikuwa umeisha. (Makofi)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nianze kwa kufanya marekebisho ya jina langu mimi ni Hamida Mohamed Abdallah, ukisema Hamidu ni mwanaume na sio mwanamke. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya marekebisho hayo, nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Kalemani, Waziri wa Nishati pamoja na timu yake ya Wizara kwa kazi ambayo wanaifanya na wamefanya kazi nzuri sana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Bahati njema nilikuwa kwenye Kamati hiyo ya Nishati na Madini najua nini kilichokuwa kinaendelea katika utekelezaji wa masuala mazima ya maendeleo na kuleta mapinduzi makubwa ya umeme nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kipaumbele, kama ambavyo taarifa imeelezea katika kasi ya kuongeza uzalishaji wa umeme lakini pia utekelezaji wa mradi mkubwa wa LNG ambao tunategemea tutakwenda kuutekeleza. Nipongeze sana ndugu zetu wa TANESCO kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuendelea kutupatia huduma ya umeme katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana katika maeneo yetu ya Lindi Manispaa hatukuguswa na mradi wa REA. Kwa hiyo, bado tuna changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali kutofikiwa na umeme. Ndugu zetu wa TANESCO hawana uwezo mkubwa wa kuweka miundombinu katika maeneo yote ya Mji wetu wa Lindi Manispaa, kwa hiyo, bado tuna changamoto.

Mheshimiwa Spika, tunajua tuko kwenye mpango wa Mradi wa Peri-Urban, lakini kwa namna ambavyo mradi huu unatekelezwa unaenda taratibu mno na sisi tuna hamu kubwa ya maeneo yetu yote kufikiwa na umeme kwa sababu tunajua kwamba uwekezaji wowote unahitaji uwepo wa umeme. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba Mradi huu wa Peri-Urban kwa namna yoyote unakwenda kwa kasi kubwa na sisi wana Lindi tunahitaji kupata mradi huu.

Mheshimiwa Spika, sisi Lindi Manispaa tuna Majimbo mawili na Majimbo haya yana changamoto kubwa kwa sababu tuna maeneo ya pembezoni mwa mji na maeneo hayo sasa kuna uwekezaji mkubwa wa kilimo. Pia tunajua kwamba sasa wananchi wanakwenda kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ambacho kinahitaji uwepo wa umeme. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba mradi wa Peri-Urban unaharakishwa ili sisi wananchi wa Lindi tuweze kufaidika na mradi huu ambao utakuwa na gharama nafuu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado ndugu zetu wa TANESCO wamekuwa na changamoto kubwa sana kwa sababu wananchi wanahitaji umeme lakini gharama za ulipaji wa umeme wa TANESCO ni shilingi 300,000. Hizi ni gharama kubwa sana mwananchi wa kawaida hawezi kumudu kulipa shilingi 300,000 ili apate umeme, kwa hiyo, kuna changamoto hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wanasema hawawezi kutekeleza kwa kulipa shilingi 27,000 kwa sababu hawana waraka wowote kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Dkt. Kalemani nilikuwa na wewe kipindi kirefu na kila unapokwenda kwenye eneo la mkutano ulikutana na hoja hii na uliweka wazi kwamba kila mwananchi atapata umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 bila kulipia nguzo. Hata hivyo, suala hili bado linaendelea na wananchi wetu wanashindwa kumudu kuweka umeme.

Mheshimiwa Spika, pia TANESCO wana changamoto ya nguzo kwa sababu wananchi wengi sana wamelipia ili waweze kufungiwa umeme pale Lindi Mjini lakini TANESCO hawana nguzo hivyo wananchi wanashindwa kupata umeme. Hili ni suala la kushangaza watu wako katikati ya mji wanakosaje umeme?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kutokuwepo kwa nguzo ni changamoto kubwa, tunaomba Serikali isimamie suala hili kuhakikisha kwamba changamoto hii inaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao mradi wa matumizi ya gesi majumbani pamoja na magari. Bahati njema sana mwaka uliopita tumezindua mradi huu katika Kata ya Mnazi Mmoja eneo la Lindi Mjini. Tumefarijika sana na wananchi wana hamu kubwa ya kuona umeme huu sasa wanaendelea kufungiwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa offer kwa wananchi wa Lindi nyumba 300 kufungiwa umeme kupitia mradi huu wa matumizi ya gesi majumbani. Hata hivyo, tangia mradi huu umezinduliwa mpaka leo hakuna chochote kinachoendelea. Tunahitaji Mheshimiwa Dkt. Kalemani utuambie ni lini sasa mradi huu unakwenda kutekelezwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nianze kwa kukupongeza kwa kuwa Msaidizi wa Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja zote za Kamati mbili ambazo zimewasilishwa. Pia nawapongeza Wenyeviti wote wawili kwa namna ambavyo wameweza kuwasilisha taarifa ya kazi ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la EPZ ambalo mwanangu pale Mheshimiwa Ester Bulaya amelizungumzia, nami naomba niunge mkono hoja hiyo. Nizungumzie upande wa muundo wa Bodi ya EPZ. Ukiangalia muundo wa bodi namna ambavyo upo utaona kwamba, Kamati nzima ya bodi ina watu ambao ni wazoefu, wamebobea katika taasisi mbalimbali. Utaona ya kwamba wameshindwa kuisaidia EPZ iweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwasomee Waheshimiwa Wabunge waweze kujua. Mwenyekiti wa Bodi ni Waziri wa Viwanda na Biashara. Wajumbe wa Bodi; kuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Katibu Mkuu TAMISEMI, Katibu Mkuu Nishati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Kamishna wa TRA, Kamishna wa Ardhi, Kamishna wa TPSF na Rais wa TCCIA.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa utaona namna ambavyo hawa ndugu zetu wanashindwa kuisimamia EPZ. Tunaamini kwamba, watu hawa Serikali iliwateua kwa kuwaona kwamba wangekuwa msaada mkubwa katika mamlaka hii ya EPZ, lakini tunaona namna ambavyo EPZ inashindwa kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, EPZ ina miaka mitatu mfululizo haijapata fedha kutika Serikali kuu ya matumizi mengineyo. Sasa tunashindwa kuelewa chombo hiki Serikali imedhamiria kuwekeza viwanda mbalimbali ambapo vitazalisha bidhaa ambazo zingeweza kuingia katika ushindani wa masoko ndani ya nchi na nje ya nchi, lakini tunaona kwamba ajira kubwa kwa vijana ingeweza kuwepo katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, EPZ wanashindwa kufanya kazi kwa sababu hawana fedha za kuwekeza katika zones ambazo tayari walishajipanga nazo. Kwa hiyo, naiomba Serikali kuhakikisha kwamba, wanautazama upya muundo wa bodi, waone namna gani wataisaidia EPZ iweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie katika suala la viwanda vidogo vidogo (SIDO). SIDO imekuwa msaada mkubwa sana kwetu na tumeona namna ambavyo imewezesha wajasiriamali wengi kuingia katika uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo. Mwanzoni tumeona kwamba SIDO ilikuwa inafanya vizuri sana, lakini tunakokwenda SIDO inaonesha sasa maendeleo yake kushuka kwa sababu wanakosa fedha, vyanzo vyao vya mapato ni makusanyo yale ya ndani. Kutoka Serikali Kuu, kinachokwedna ni mishahara tu ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaona kuna kila namna sasa Serikali iitazame kwa macho mawili SIDO, kuhakikisha kwamba wanapewa fedha za kutosha ili waende kutoa mafunzo mbalimbali kwa wajasiriamali ili wananchi wetu waweze kuwekeza kwenye viwanda vidogo vidogo. Pia tumeona uchakavu mkubwa katika maeneo ya majengo yao ambayo wanayakodisha. Kwa hiyo, tunaona sasa Serikali ina umuhimu wa kuwasaidia ndugu zetu wa SIDO ili waweze kwenda vizuri na waendelee kutusaidia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongea sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo ametutafutia fedha nyingi. Nami Jimboni kwangu nimepata fedha karibia shilingi bilioni 18 kutekeleza miradi ya maji, madarasa kwa maana ya sekta ya elimu, sekta ya afya na sekta ya barabara. Kwa hiyo, tuendelee kumuunga mkono na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kumuimarisha ili aweze kutekeleza mipango yake ya kazi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza Bunge letu Tukufu lakini kwa kuaminiwa na Waheshimiwa Wabunge tuliomo ndani ya Bunge hili na kuweza kukaa kwenye Kiti ambacho umekaa hapo mbele. Na tunafarijika ukiwa hapo unatuongoza ndani ya Bunge letu Tukufu, Mungu akubariki sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutuletea bajeti ambayo sasa hivi tunaizungumza na tunaijadili katika Bunge hili lakini kutuletea matumaini katika uwekezaji wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, nitumie kwa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anachapa kazi lakini kwa namna ambavyo ametupatia fedha nyingi katika Majimbo yetu kutekeleza miradi mbalimbali. Tumeshuhudia miradi ya ujenzi wa madarasa katika sekta ya elimu katika madarasa ya shule ya msingi sekondari na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na hata Hospitali za Mikoa pamoja na Hospitali za Rufaa. Pia tumeona namna ambavyo barabara zetu zimeendelea kuimarishwa kuboreshwa kupitia TARURA pamoja na mambo mengine. Pamoja na hayo yote mazuri ambayo yameendelea kufanyika katika Majimbo yetu, lakini bado tunazo changamoto mbalimbali na sasa tunaomba Serikali isimamie katika kuhakikisha kwamba changamoto hizi zinapungua ama zinaondoka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la elimu tuna changamoto upande wa shule zetu za sekondari kukosa nyumba za Walimu, hii imekuwa ni changamoto kubwa sana na hasa kule vijijini Mwalimu anapokaa kwenye nyumba ambayo haina hata umeme namna ya kuandaa masomo yake ambayo anategemea siku ya pili aende akayafundishe darasani inakuwa ni changamoto. Ningeiomba Serikali kuhakikisha kwamba tunaboresha kuhakikisha Walimu wanapata nyumba bora za kuishi na kuwatia moyo kuendelea kusimamia masomo yao madarasani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunayo changomoto upande wa barabara. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ametupatia fedha nyingi katika kuboresha barabara zetu lakini bado tunayo changamoto kubwa hasa katika eneo la Lindi mjini. Zipo barabara hizi zina miinuko na mabonde kwa hiyo, uwekekaji wa kifusi katika barabara zile upo tofauti na barabara tambarale. Kwa hiyo, gharama kubwa inahitajika ya fedha katika kuhakikisha kwamba wanaimarisha barabara zile ziweze kupitika wakati wote wa kifuku na kiangazi.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaiomba Serikali kuwaongezea bajeti ndugu zetu wa TARURA waweze kusimamia kuboresha barabara zetu na ziweze kutumika vizuri lakini tujipange katika uwekezaji ambao wananchi wetu wanategemea kuwekeza katika maeneo yao. Tusipoimarisha barabara zetu uwekezaji utakuwa ni mgumu sana.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna sekta ya nishati. Katika eneo la Lindi Manispaa tumepitiwa na bomba la gesi linalotoka Mtwara kwenda Kinyerezi kule Dar es Salaam na walinzi wakubwa wa miundombinu ile ni wananchi katika maeneo husika ambayo bomba hili limepita. Lakini tunayo changamoto wananchi wetu wa Lindi Manispaa, Lindi Mjini na Jimbo la Mchinga unaposema upo Manispaa halafu unakosa umeme, mwananchi hakuelewi. Kwa hiyo, tunayo changamoto kubwa katika maeneo yetu ya baadhi ya maeneo kukosa miundombinu ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumejaribu kuongea sana na Serikali inatuambia kwamba tuna mradi wa peri-urban unaokuja, sasa mwaka wa tatu hatujaona mradi wa peri- urban. Sasa ninaomba Waziri atuambie ni lini mradi wa peri- urban utakuja Lindi Manispaa kuhakikisha kwamba wananchi wa eneo la Lindi Manispaa wanapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa katika vijiji ambavyo vimepitiwa na bomba la gesi, wananchi wale waliahidiwa kwamba asilimia ya mapato yatarudi kuja kuwekeza katika shughuli za maendeleo katika maeneo husika, lakini tangia bomba lile limepita wananchi tunaendelea kulinda hatujaona hata Shilingi Moja inakuja kwetu Lindi Manispaa kuwekeza katika miradi ya maendeleo, nalo watuambie ni lini watatuletea fedha hii ije kutekeleza miradi ya maendeleo Lindi Manispaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tuna mradi wa LNG ambao tunatarajia kwamba Lindi katika Kata ya Mbanja kule Likong’o utakuja kutekelezwa, lakini wananchi wanashangazwa vikao vyote vinafanyika Arusha why visifanyike Lindi Mjini? kuna tatizo gani wananchi wanakiu kubwa ya kuona vikao vinavyojadili suala la mradi wa LNG vinafanyika katika eneo la Lindi Mjini, Lindi Manispaa. Kwa hiyo, ni matarajio yetu ya kwamba vikao hivyo vinavyoendelea Arusha sasa virudi vigeuke kuja Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hayo tu tunataka mashirika haya ambayo yanakuja kuwekeza yaweke ofisi zao pale Lindi Mjini, tuone shughuli sasa zinaendelea lakini hata Shirika la TPDC waweke Ofisi pale Lindi Manispaa, ile kusafiri kila wiki wako Dar es Salaam wako Lindi sisi hatufurahishwi tungependa kuona kwamba Shirika la TPDC linaweka Ofisi Lindi majengo yapo, maeneo ya kujenga Ofisi yapo, tunawakaribisha waje Lindi kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la Kilimo. Nimefurahishwa sana na hotuba mbalimbali zinazoendelea hivi punde nimetoka katika kikao pale cha Bodi ya Korosho namna ambavyo Mheshimiwa Bashe anatutia moyo katika kuleta mapinduzi makubwa katika mazao yetu ya biashara hasa katika zao hili la korosho. Kwa hiyo, nishukuru sana lakini niendelee kumpongeza nimtakia kheri katika mapinduzi yale makubwa ambayo tunatarajia kuyapata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imezungumzia suala la Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Sasa kushuka kwa wakulima wadogo wadogo tumeona ya kwamba benki hii imewawezesha wakulima wakubwa, sasa tunahitaji wakulima wadogo wafikiwe na benki hii. Tusipomuwezesha mkulima kupata fedha ya kuwekeza kwenye mashamba yake, kilimo chao kitakuwa hakina tija miaka nenda rudi, tunajua ya kwamba Serikali inatupatia Sulphur, pembejeo bure lakini pembejeo ile wasipokuwa na fedha ya kuendelea kwenda kuwekeza katika mashamba tutakuwa bado hatujawasaidia.

Mheshimiwa Spika, Wakulima wetu hawakopesheki kwa sababu hawana Hati Miliki ya mashamba yao kwa hiyo, ninaiomba Serikali kuhakikisha kwamba sasa tuwarathimishe wakulima wetu waweze kupata Hati Miliki na waweze kuingia kwenye vyombo vya fedha waweze kupata fedha na waweze kuendelea kuwekeza katika shughuli za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la miradi ya kimkakati, muda mrefu sasa yapata miaka minne tumeomba fedha kutoka Serikali Kuu kutuwezesha kujenga soko jipya, soko la kisasa lakini kujenga stendi mpya ya mabasi ya kisasa. Katika Manispaa pekee haina stendi ya kisasa ni ya Lindi Manispaa. Inasikitisha sana mwaka wa Nne sasa tunafuatilia hakuna kinachopatikana, ninaomba wakati wa ku-windup Waziri husika atuambie kuna tatizo gani la kutotupatia fedha kwa ajili ya uwekezaji wa ujenzi wa soko jipya la kisasa lakini pia ujenzi wa stendi kuu ya mabasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa, Wenyeviti hawa wanafanya kazi kubwa sana na wanatusaidia sana katika kuimarisha ulinzi na usalama, lakini haijatokea hata siku moja tukawanunulia vitendea kazi. Kila kazi wanafanya kwa pesa yao lakini mapato wanayoyapata ni madogo sana. Ninaiomba sana Serikali kuangalia kwa jicho la huruma Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba Posho yao wanaongezewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaomba kuunga mkono asilimiamia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya maji.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu kwa namna ambavyo wanachapa kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuhakikisha kwamba huduma ya maji inawafikia Watanzania. Tunawapongeza sana na Mungu aendelee kuwabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri kwa kuwasilisha bajeti yake ya utekelezaji ya mwaka 2022/2023, bajeti ambayo inakwenda kupunguza changamoto kubwa ya maji katika nchi yetu ya Tanzania na kuhakikisha kwamba maji salama yanaendelea kupatikana.

Mheshimiwa Spika, nimebahatika kupita katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania katika shughuli za Kamati ya PIC. Nimekwenda katika Majiji ya Mwanza, Arusha, Dar es Saalaam na kuangalia miundombinu ya maji na shughuli mbalimbali za usambazaji wa maji na huduma za maji kwa wananchi; maji safi pamoja na maji taka; tumeona shughuli kubwa ambayo Serikali inafanya na tunawapongeza sana katika Mkoa wa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza kwa namna ambavyo wanasimamia utekelezaji katika kuwahudumia wananchi kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, ningependa kule kwetu Lindi kukawa na mabadiliko makubwa kama yaliyopo Dar es Salaam. Kuna siku nimeshawahi kukueleza Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso kwamba ningeomba Eng. Juma Meneja wetu wa Lindi aje kuja Dar es Salaam na timu yake kuja kujifunza namna ambavyo wanatoa huduma ya maji safi na maji taka ili kuhakikisha kwamba wananchi wa lindi wanaunganishiwa maji na kila mwananchi anapata huduma hiyo ya maji na kuweza kuchangia Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu. Katika Mji wetu wa Lindi tumepata fedha nyingi tangu mwaka 2021/2022 na utekelezaji wa miradi mingi unaendelea, miradi mingine imekamilika. Kwa mfano kama pale Ng’apa, Teleweni, Tandangongoro mradi wa Shilingi bilioni 2.8 umekamilika, na wananchi wanapata maji safi na salama. Pale Mingoyo pia tuna mradi wa tenki lenye ujazo wa lita 100,000 umekamilika na wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji. Fedha za COVID 19 kwa ajili Mradi wa ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 100,000 pale Kiduni zimetolewa na mradi unaendelea kujengwa; na hatimaye muda si mrefu utakamilika na wananchi wataendelea kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao mradi mkubwa sana pale Mitwero uliogharimu shilingi bilioni 3.5 ambao umekamilika kwa asilimia 80. Bado mradi ule unaendelea kusambaza mabomba kutoka Mitwero kwenda Mbanja na Jimbo la Mchinga ambako mama yangu amezungumzia hapa. Kwa hiyo ninaamini mradi utakapokamilika utakuwa umetoa huduma nzuri katika majimbo haya mawili na wananchi wataendelea kupata maji safi na salama.

Kwa hiyo ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu kwa kazi hii na upendo mkubwa wa wananchi wake wa kuhakikisha kwamba wataendelea kupata huduma ya maji safi na maji salama kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwalinda wananchi wetu ili waendelee kuwa na afya nzuri na kupunguza gharama kubwa ya matibabu inayosababishwa na wananchi kunywa maji ambayo si salama. Kwa hiyo pamoja na mambo hayo mazuri ambayo yamefanywa katika jimbo la Lindi mjini bado tunazo changamoto mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kila mwananchi anavuta maji nyumbani kwake. Kwa sasa tunayo changamoto mabomba yale makubwa ambayo wananchi wanataka kuvuta maji, lakini mabomba yamepita umbali mrefu na hivyo wananchi wanashindwa kuunganisha kwasababu gharama ni kubwa. Yawezekana mwananchi mwingine akaambiwa kutoka kwenye bomba kubwa mpaka nyumbani kwake analazimika kununua mita 300 au mita 400; sasa gharama ya kuvuta maji mpaka nyumbani kwake inakuwa kubwa. Kwa hiyo wananchi wengi wanashindwa kumudu kuhakikisha kwamba wanavuta maji nyumbani kwao.

Mheshimiwa Spika, na suala hili tulishalizungumza na Mheshimiwa Waziri na nilishakueleza na ulisema kwamba miradi ikishakamilika basi utatuongezea mtandao wa maji kuhakikisha kwamba wananchi wa Lindi wanaendelea kupata unafuu wa kuvuta maji nyumbani kwao.

Mheshimiwa Spika, tunayo maombi mapya katika maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba mtandao wa maji unaendelea. Tuna eneo la Kitumbikwela upande wa pili wa Bahari. Tumeomba fedha Bilioni 1.95 ili kuwezesha kuweka mtandao huu kupitia Kijiji cha Mkundi, Mnengule, Iyato, Mtalala, Mwitingi Mwamoja na Nachingwea; tuhakikishe kwamba fedha hizi Mheshimiwa Waziri unatupatia ili kuhakikisha mtandao huu unakwenda kutekelezwa na wananchi wa upande wa pili wa bahari waweze kupata maji safi na salama. Tunajua kwamba maji yapo lakini bado hayajasambazwa kwenye mabomba katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna mradi mwingine wa usambazaji wa mabomba katika maeneo ya Mlandege, Muhimbili, Kipuri, Mmongo pamoja na Mnazi Mmoja; nayo tumeomba Bilioni 1.44. kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunategemea bajeti yetu itakapopita basi haraka uweze kutupatia fedha kwa ajili ya kwenda kuitekeleza hii miradi mipya kuhakikisha kwamba tunaweka wigo mpaka wa wananchi kufunga maji na kuweza kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna mradi mpya wa Angaza Sekondari ambao utagharimu Shilingi milioni 740, nayo ni maombi mapya kwako Mheshimiwa Waziri. Tunajua ya kwamba una kiu kubwa kuona kwamba Lindi kunakuwa na mabadiliko makubwa na mapinduzi makubwa ya kuhakikisha kwamba wananchi wa Lindi wanapata maji na sisi tuweze kuchangia mapato ya ndani katika Wizara hii ya Maji. Kwa hiyo bado yapo maeneo ambayo hayapo kwenye mpango. Tuna Kijiji cha Ruaha Mtaa wa Ruaha tuna kaya takriban 400 wanakosa maji safi na salama. Tunaiomba Serikali kuhakikisha kwamba wana Ruaha japo kwa kuwachimbia kisima.

Mheshimiwa Spika, lakini tuna eneo la Madingula…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 Mheshimiwa Hamida, malizia.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: … lakini bado tuna mtaa wa Mitonga kule Kata ya Mbanja ni mbali kutoka barabara kubwa, nao wanakosa maji. Tuhakikishe kwamba wananchi hawa tunawachimbia visima kwa haraka ili kunusuru maisha yao kwasababu wanatafuta maji umbali mrefu zaidi ya kilometa tatu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba wanatusaidia ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya hayo yote niendelee kumpongeza Jumaa Aweso kwa unyenyekevu mkubwa…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Juma Aweso, Waziri wa Maji kwa uwasilishaji wa Bajeti ya 2023/2024, bajeti ambayo ina mipango mikubwa ya kimaendeleo katika kuleta mapinduzi makubwa nchini Tanzania na kuhakikisha kwamba Watanzania tunaendelea kufurahia huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wanalindi mjini hatuna umasikini wa maji, tuna mradi mkubwa ambao umekamilika uligharimu Shilingi bilioni 33 pale Ng’apa. Mradi ule unazalisha maji kwa siku lita bilioni 7,500,000,000 na matumizi yetu ni bilioni 7,250,000,000. Katika miradi ambayo imekamilika ni mradi wa Tandangongoro, Ncheleweni Ng’apa uliogharimu shilingi 2,800,000,000 na mradi wa Mitoyo, shilingi 3,600,000,000, mradi wa Kiduni wa fedha za Covid-19 shilingi milioni 600, lakini na miradi mbalimbali ambayo bado inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu wanalindi ni mapinduzi makubwa sana katika kuhakikisha kwamba tunaendelea kutekeleza miradi hii ya maji na kuwafanya wanalindi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama. Hata hivyo, Lindi Mjini pamoja na fedha nyingi zilizotekeleza miradi ya kujenga matenki ya maji na usambazaji wa mabomba, bado tunayo changamoto. Wananchi wetu wanashindwa kuvuta maji majumbani kwao. Sisi wanalindi tunatamani kuichangia Serikali yetu kwa kulipa bili za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, na nimwombe ndugu yangu Juma Aweso, ninaamini kwamba anaumiza kichwa sana juu ya Manispaa ya Lindi kwa sababu hatujakamilisha kusogeza miundombinu ya maji kwenye mitaa yetu ili wananchi wetu waendelee kuvuta maji majumbani na watumie kadri wanavyoweza kutumia waweze kuchangia pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imechangia fedha nyingi sana, na tunatamani hizi fedha zirudi zikafanye kazi nyingine za kimaendeleo kuhakikisha kwamba tunaendeleza miradi hii ya maji. Hatuwezi kuchangia kama wananchi wetu hawataweza kuingia kwenye mpango wa kuvuta maji majumbani kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Jumaa Aweso kuitazama Lindi kwa jicho la huruma. Katika miradi mipya ambayo tunategemea kwamba inaendelea kutekelezwa, ni mradi wa Ngaza ambao unagharimu fedha shilingi 1,130,000,000. Pia tuna mradi wa Mkundi upande wa pili wa bahari wa shilingi milioni 800.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Jumaa Aweso, asubuhi hapa ametangaza kutuingizia advance ya fedha na tumeona zimesoma kwenye account za maji. shilingi milioni 100 imekuja Lindi Mjini kuhakikisha kwamba mradi huu Ngaza unaogharimu shilingi 1,130,000,000 unaendelea kutekelezwa. Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana kwa huruma yako na kwa mapenzi yako makubwa ya kuhakikisha kwamba sasa wanalindi tunapata mapinduzi makubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi mkubwa sasa hivi unaotoka Mitero kuelekea Jimbo jirani la Mchinga. Mradi huu unapita Kata ya Mbanja kwa maana ya Mtaa wa Mbanja, Mtaa wa Kipetu, unapita Masasi ya Leo, unapita Likong’o kwa maana ya Kata ya Mbanja, kata ambayo tunategemea kutekeleza mradi mkubwa wa LNG. Vile vile mradi huu unakwenda Jimbo jirani la Mchinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, tuhakikishe kwamba mitaa hii niliyoitaja inapata huduma ya maji, kwa sababu hawa ndio walinzi wa mitaro ile iliyopita bomba kubwa la maji lakini walishiriki kuchimba mitaro ya maji kuhakikisha kwamba mabomba yanalazwa na kuelekea katika Jimbo la Mchinga. Maeneo haya yana changamoto kubwa sana ya maji safi na salama. Nina uhakika na usikivu wake mkubwa Mheshimiwa Waziri atahakikisha wananchi hawa wanaendelea kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema kila Wilaya anatuletea fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya maji. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, ziko Wilaya zina majimbo zaidi ya mawili. Lindi tuna majimbo matatu; tuna Jimbo la Mtama, tuna Jimbo la Lindi Mjini, na tuna Jimbo la Mchinga kwenye Wilaya moja. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri azingatie majimbo haya ambayo kwenye Wilaya moja yana zaidi ya jimbo moja kuhakikisha kwamba fedha hizi anapeleka kila jimbo na siyo kila Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi mpya ambao tunauombea fedha kwa bajeti hii ambayo tunaipitisha hivi leo. Tuna mradi mkubwa wa maji kutoka Ruaha kwenda Mnazi Mmoja utakaogharimu shilingi 1,229,000,000. Ndugu zetu wa Ruaha wamekuwa na changamoto kubwa ya maji kwa muda mrefu. Hawajawahi kuona hata bomba la maji kule kwenye Mtaa wa Ruaha. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wetu Jumaa Aweso kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakuja na tunakwenda kuwatekelezea wananchi wa Ruaha Mnazi Mmoja ili waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna upanuzi wa mradi mkubwa ambao tunao kule Kitumbikwela, upande wa pili wa bahari, wananchi kule wanakosa maji safi na salama. Tunajua kwamba tumetengewa fedha za awali za kujenga matenki, Shilingi milioni 800, lakini tunahitaji kusambaza mabomba katika maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba wananchi wa kule Kitumbikwela, wanaendelea kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo ambayo tunatamani wawe na visima. Wananchi wanaendelea kutaabika kutopata maji safi na salama. Mheshimiwa Naibu Waziri katika safari yake Waziri wa Maji alitoa ahadi ya kutupatia visima vitano Lindi Mjini. Visima hivyo hakuna hata kimoja kilichochimbwa.

(Hapa kengele ililila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante, kengele ya pili hiyo.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono, nakushukuru sana, nikutakie kila la kheri katika mapinduzi makubwa tunayoyategemea katika Wizara hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi ya bajeti ya 2023/2024. Bajeti ambayo inatupa afueni wa kwenda kupunguza changamoto mbalimbali. Sina mashaka na bajeti hiyo na naunga mkono kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Kamati kwa taarifa yao, lakini kwa ushauri wao mzuri walioutoa na naomba Wizara kuzingatia ushauri wa Kamati ili waweze kuufanyia kazi na hatimaye ikiwezekana bajeti inayokuja, basi tuone mabadiliko ya changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vilevile Koplo Hamisi Masana kwa kukataa kupokea rushwa wakati anatekeleza kazi zake. Amekuwa ni mfano mzuri, lakini sio rahisi kwa watu wengine. Huyu ameonesha mfano mzuri na ni mzalendo wa kweli. Tuhakikishe basi wenzetu wengine wanafuata nyayo za Koplo Hamisi kwa kutopokea rushwa wakati wakiwa kazini ili tuweze kupunguza changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Polisi. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu kwa sababu nilikwenda kupeleka kilio cha Polisi. Lindi Manispaa tulikuwa hatuna Kituo cha Polisi, tulikuwa na Kituo cha Polisi lakini walikuwa wanatumia nyumba za kupanga. Ninamshukuru Waziri Masauni kwa wema wake wa kutupatia shilingi milioni 900 na tumeweza sasa kuendeleza ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja A, kituo hiki kitakuwa cha mfano Kanda nzima ya Kusini. Kwa hiyo, nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu kwa wema wako na kwa huruma ambayo umeionesha kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la Wilaya ya Lindi, Lindi ina Majimbo matatu na jiografia yake Mheshimiwa Waziri anaifahamu vizuri kwa sababu ameshawahi kuja na anajua mazingira yaliyopo. Changamoto tunayoipata ni vitendea kazi, ukiangalia ukubwa wa eneo tuna Jimbo la Mtama, Jimbo la Lindi Mjini na Jimbo la Mchinga, ukiangalia hayo maeneo hatuna magari ya kutosha. Panapotokea dharura yoyote Polisi wanashindwa namna ya kwenda kushughulikia changamoto ambazo zinajitokeza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana katika eneo hili ambalo umeagiza magari yaliyoingia nchini na magari ambayo tunategemea yatakuja, uitazame Lindi kwa jicho la huruma kuhakikisha kwamba, tunapata gari na Polisi waweze kufanya kazi yao vizuri kwa sababu kuna doria nyingine za usiku wanashindwa kufanyakazi kwa sababu ya kukosa vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi ile ya Polisi haina viti, haina fenicha, mazingira ya kazi ni magumu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana tutakapokamilisha ofisi mpya basi tupate vitendea kazi kuendana na hali ya ofisi na mazingira ya ofisi yatakavyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hiyo, niiombe Kamati ije kutembelea Lindi kuona mazingira ya nyumba za Polisi wanazoishi. Nyumba zile ni chakavu, nyumba zimepitwa na wakati, vijumba vidogo utafikiri mabanda ya kufugia Wanyama, ni huruma sana. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba, ziko fedha ambazo zimetengwa katika kujenga nyumba za Polisi, hebu rudi tazama Lindi, mazingira yaliyopo kuhakikisha kwamba, Polisi Lindi wanapata nyumba. Japokuwa tusiwezeshe nyumba za kukamilisha wafanyakazi wote, lakini kila mwaka tukipata kiasi cha kujenga nyumba za Polisi basi tuweze kupata nyumba za Polisi…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamida kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nilikuwa nataka nimpe Taarifa Mheshimiwa Hamida kwamba, uhaba wa nyumba kwa Askari Polisi na Magereza ni Tanzania nzima. Pale Tarime mvua ikinyesha Askari Magereza anafanya kuhamisha godoro kutoka sehemu moja kupeleka nyingine na ni vijumba ambavyo vimejengwa toka enzi za mkoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nampa taarifa hiyo ili Serikali ione ni kwa namna gani itenge bajeti ya kutosha kuboresha makazi ya Askari Polisi kwa maana ya Magereza na wengine wote. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Hamida taarifa unaipokea?

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Taarifa ninaipokea kwa sababu changamoto hiyo ni kubwa na ipo katika maeneo mbalimbali kama Mheshimiwa Mbunge alivyotolea taarifa, katika maeneo yote nchini Tanzania utakuta miundombinu mbalimbali imekuwa ni mibovu kwa hiyo, tunaomba Serikali kuhakikisha kwamba, kila mwaka wa fedha tunaendelea kupunguza changamoto ili hali ya ndugu zetu Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi na Usalama waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la uhamiaji. Ninajua kwamba, Serikali imeendelea kujenga majengo ya ofisi za Uhamiaji katika kuhakikisha kwamba, tunatoa huduma mbalimbali katika Mikoa mbalimbali, lakini nimshukuru pia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha na kuweza kujenga Ofisi ya Uhamiaji ya Mkoa wa Lindi. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kusimamia hilo, lakini changamoto iliyopo, bado vitendeakazi ni kizungumkuti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto kubwa ya kutokuwepo magari. Hawa ndugu zetu wa Uhamiaji wana doria za mchana na usiku, ukisema Ofisi ya Mkoa maana yake wanatembea Wilaya mbalimbali kuhakikisha kwamba, wanaangalia mambo yanavyokwenda, kuona wavamizi ambao siyo raia wa Tanzania wanaendelea kuingia bila kuwa na passport. Kwa hiyo, ni suala sasa la Serikali kuona namna gani wanasaidia, kama tumeboresha ofisi zetu, basi sasa vitendea kazi viboreshwe katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Lindi, tupatiwe magari ili waweze kufanya kazi usiku na mchana, lakini waweze kuhudumia wananchi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa huduma ya utoaji wa Passport, imekuwa ni suala zuri sana. Changamoto nyingi zimepungua, hakuna usumbufu kama ambavyo miaka ya nyuma ilikuwa inatokea, tuongezee kuwapa vitendea kazi vya kisasa, kutumia mifumo ya TEHAMA na kuharakisha huduma. Siyo Afisa Uhamiaji anakusanya hapa makaratasi ya maombi anapeleka Dar-es-Salaam, badala yake angeweza kutia kwenye computer na yakaweza kufika Dar-es-Salaam wananchi wakashughulikiwa na wakatapa passport kwa wakati. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Hamida. Muda wako umeisha.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali ambayo ipo ndani ya Bunge letu na sisi kama Wabunge tunaendelea kuichangia na kuiunga mkono asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba Waziri wa Fedha na timu yake nzima ya Wizara yake kwa namna ambavyo wamejipanga kuhakikisha kwamba wanaleta mapinduzi ya kweli katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa bajeti iliyokuja sina mashaka nayo na mimi nawatakia kila la kheri Mwenyezi Mungu aendelee kuwaongoza katika kuhakikisha kwamba trilioni 41 na zaidi iweze kupatikana ili mipango ya kimaendeleo katika nchi yetu iweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anachapa kazi lakini kwa namna ambavyo ametekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na ya kimaendeleo inayogusa jamii yetu. Sisi kama Wabunge kupitia majimbo yetu tumeshuhudia kuona miradi mbalimbali imetekelezwa na tumeendelea kupiga hatua kubwa. Mheshimiwa Rais wetu ni mzalendo wa kweli na kweli anataka kuleta mapinduzi ya kweli kuhakikisha kwamba anapunguza umaskini nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze ndugu zetu wa TRA kwa namna ambavyo wameendelea kuleta ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa miaka mitatu mfululizo kama taarifa ya Kamati ilivyotueleza. TRA wanatufanyia kazi nzuri, lakini kulipa kodi ni uzalendo. Wako wafanyabiashara ambao mteja anapoingia dukani kununua bidhaa na kumuuliza kwamba unataka bei ya risiti ama bei isiyokuwa ya risiti, huu si uungwana. Ninawaomba wafanyabiashara Watanzania tuwe wazalendo wa kweli tuhakikishe kwamba tunaiunga mkono Serikali kwa kutoa risiti. Watanzania wanapaswa wawe wazalendo kwa nchi yao kuhakikisha kwamba wanaponunua bidhaa basi waweze kudai risiti ili kwa pamoja tuungane kuhakikisha kwamba nchi yetu inasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Wizara ya Nishati; Wizara ya Nishati wanafanya kazi nzuri na sisi tunaiona, na mimi naendelea kuwabariki kwa sababu tunaendelea kunufaika na suala zima la nishati. Lakini wamekuja na mpango mahususi wa kumtua mama kuni kichwani. Mpango huu ni mzuri, Watanzania sasa tumechoka kutumia kuni na mkaa, na Watanzania walio wengi wanapenda kutumia umeme na gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Hasa sisi wanawake wa Mkoa wa Lindi na Mtwara tumechoka kutumia kuni na mkaa. Kwanza vinaathiri afya yetu ule moshi tunaovuta ukiingia ndani ya mapafu tunaathirika afya zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Waziri wetu wa Fedha kuhakikisha kwamba vifaa vya matumizi kama majiko ya gesi, majiko ya umeme, pasi na vinginevyo vinaondolewa ama vinapunguzwa kodi ili wananchi Watanzania waweze kumudu kununua majiko haya na waachane na matumizi ya mkaa na gesi. Wenzetu wameanza na kampeni nzuri na Wizara ya Fedha tuunge mkono kampeni hii inayofanywa na Wizara ya Nishati kwa kuhakikisha kwamba vifaa hivi vinapunguzwa bei ili Watanzania waweze kumudu kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Wizara ya Kilimo. Niwapongeze Wizara ya Kilimo kwa sababu wameongezewa bajeti ya milioni 900. Tuna mfumo wa ununuzi wa pembejeo, ninaomba Serikali waangalie kwa sababu mfumo huu hauendani na kalenda ya upuliziaji wa dawa ya mikorosho. Kwa hiyo ninaomba wabadilishe mfumo huu wa manunuzi wa pembejeo ili uendane na kalenda ile ambayo wakulima wanahitaji pembejeo kutumia katika zao hili la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia ndugu zetu wa TAWA pamoja na ASA aongezewe bajeti yao kuhakikisha kwamba wanaendelea kufanya utafiti wa kuzalisha mbegu bora ili wakulima waweze kupata mbegu yenye kuleta tija katika uzalishaji wa mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumzie suala la wazalishaji wa chumvi. Wazalishaji wa chumvi mpaka unapata kiroba cha kilo 25 gharama yake inafika takriban shilingi 4,500. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto mbalimbali, chumvi isiyotiwa madini joto maana yake haiwezi kutumika. Wizara ya Afya walitoa mafunzo na madini joto yalitolewa bure, lakini ikaenda madini joto kilo moja ikafika shilingi 30,000, na sasa hivi madini joto kilogram moja ni 150,000. Hii imekuwa ni changamoto na ni hatari tunaweza tukatumia chumvi ambayo haina madini joto kwa sababu ya gharama kubwa ambayo wanaifanya hawa wazalishaji wa chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kama ambavyo tunatoa pembejeo basi kwenye wazalishaji wa chumvi tutoe madini joto kwa ruzuku ya Serikali ili wazalishaji wa chumvi waweze kupata unafuu na urahisi wa kutumia madini joto na chumvi yetu iweze kutiwa madini joto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la ujenzi. Nipongeze Serikali kwa hatua mbalimbali tunazoendelea nazo za kuhakikisha kwamba njia ya kukua kiuchumi zinaboreshwa. Lakini tunayo changamoto, naomba tufanye mapitio tena ya sera na kuangalia sera ya barabara. Barabara hizi ambazo zinaunganisha Bandari na nchi jirani, barabara kuu za kiuchumi hazijengwi kwa ubora ule unao stahili, ama zikijengwa hazichukui hata mwaka tayari zimekufa. Pamoja na kwamba tunayo mizani ya kudhibiti uzito wa magari barabarani lakini bado barabara zetu zinaendelea kuwa mbovu na Serikali inatumia gharama kubwa sana kuhakikisha kwamba kila mwaka barabara zinafanyiwa ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Serikali kuhakikisha kwamba tunaweka mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba barabara hizi zinakuwa imara na zinaweza kudumu zaidi ya miaka miwili mitatu ili kuokoa fedha ya Serikali na iweze kwenda kufanya kazi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwazungumzie wakandarasi wa Tanzania hasa wale walioanzia class seven. Tunajua kwamba wao wanapata kazi ndogondogo lakini bado wana changamoto, kwanza wanapopata mradi wanakwenda kusajili mradi TRB, pia wanasajili mradi OSHA, na bado wanalipa madini, kokoto, mchanga na mawe wanalipa SBL kwa maana ya Levy kwa vibarua lakini bado wanalipa fire, wanalipa NEMC, bado wanalipa kodi ya TRA. Utakuta mlolongo wa tozo unakuwa mkubwa sana kwa hiyo wanatumia gharama kubwa lakini wakati mwingine viwango vinakuwa tofauti tofauti kila mara. Niombe Serikali kuhakikisha kwamba viwango basi viwe vinafanana kila wakati visiwe vinabadilika. Kwa hiyo niombe sana Serikali kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwatazama wakandarasi hawa ili nao wawe wakubwa ili waendelee kufanya kazi zetu na wasaidie watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu. Tumeona matunda mazuri katika maeneo yetu, tumefarijika sana. Miradi mikubwa ya maendeleo iko katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)