Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lucy Simon Magereli (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti nipo. Naomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa kuchangia. Niwie radhi kuwa nimeisikia sauti yako kuwa ningekuwa next, lakini ni suala jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mapaji mengi, lakini kwa kujaaliwa fursa ya kuwepo hapa leo ili na mimi nitoe mchango wangu katika Wizara iliyoko mbele yetu.
Naomba kabla sijaendelea niungane na nimpongeze sana Mheshimiwa Mama Janet Mbene, kwa kweli mchango wako nimekusikia wakati wote uliposimama, uliiongelea ajenda ambayo na mimi ningetamani sana tuendelee kuiangalia kwa nguvu. Niulize tu kwa Mawaziri wahusika, Wizara ya TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora kwamba where is the woman?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Koffi Annan aliwahi kusema “There is no tool for development more effective than empowerment of a woman.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, there is no tool for development more effective than empowerment for a woman. Sasa nimezitazama hotuba, nimekwenda mbele, nimerudi nyuma, nimesikitishwa na namna ambavyo tunapewa empty promises. Mnafahamu population ya wanawake Tanzania ni kubwa, lakini kwenye elimu mmetuambia ni bure, lakini katika uhalisia hiyo elimu bure haina mkakati. Sasa tunapita around the bush kutafuta means and ways ya kui-subsidize hiyo elimu bure katika utaratibu ambao tulikuwa hatujajipanga; lakini bado katika hilo suala la elimu hata nilikopitia, swali langu lilibakia lile lile, where is a woman? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kwenye afya, nikatamani niwaulize, kwenye bajeti ambayo imekuja mbele yetu kimsingi imekuwa ya jumla na kwa jinsi hiyo inaendelea kuniacha niendelee kuuliza, where is the woman? Afya ya mwanamke, afya ya uzazi kwenye ripoti ya mpango nimeona mnasema vifo vya akina mama eti vimepungua kutoka 450 na kitu kuwa 410, kwa kuvipunguza vifo hivyo kwa idadi tu ya akina mama 30 hivi kutoka kwa akina mama 100,000 wanaojifungua, siyo jambo la kujisifia hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika mmelitoa with pride kabisa ndani ya ripoti mnasema vifo vya akina mama wanaojifungua wakati wa uzazi vimepungua; lakini fikiria ni uchungu kiasi gani eti akina mama mia nne na kitu wanakufa kati ya akina mama 100,000 wanaoingia kujifungua, halafu tunataka kusema it is an achievement. It is not! Where is the woman? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaalam mmoja aliwahi kusema you need a sense of history to know how to handle the future. Kama historia tuliyoibeba katika maisha yetu haijaweza kutuelekeza namna gani future yetu inaweza kwenda, ni dhahiri kabisa kwamba kwa sababu leo niliamua ku-centre hapo niwaeleze ya kwamba akina mama wamelia kwa muda mrefu, wamelia katika labor rooms wakati wakijifungua, wamelia kule jikoni ambako wanapika na kuni mbichi, moshi unawaumiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wamelia sana wanaposafiri kilometa nyingi kwenda kutafuta maji, wanawaacha watoto wao wadogo nyumbani, wanarudi wanakuta wameunguzana moto wakati wakijaribu kupika uji kwa sababu mama amechukua muda mrefu kwenda kutafuta maji; akina mama wamelia sana wanapolima mazao yao halafu yanakosa masoko; yakipata masoko yanapata masoko ya ajabu ajabu, wanakopwa, wanaibiwa na wachuuzi huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wamelia sana vijana wao walipomaliza shule wakakosa ajira ya uhakika, wakarudi mitaani wakawa vibaka, wamechomwa moto kwa sababu Serikali haijaandaa mpango maalum wa kuwasaidia vijana. Imewaacha akina mama wakilia na kulia. Akina mama wamelia sana wanaume zao walipoondoka vijijini wakawaacha peke yao na watoto, wakaenda mjini kuhangaika kutafuta ajira kwa sababu kilimo hakilipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema 80% ya Watanzania ni wakulima, lakini mmeshindwa kabisa kulitazama suala hilo katika mkakati ambao ni mahsusi. Mimi sitaki kwenda huko, nataka kuwauliza, where is the woman? Bei ya bidhaa inapopanda; jana niliongea na mama yangu ananiambia mwanangu sasa sukari hapa kwetu ni shilingi 2,500, nikamwambia mama vumilia. Eeh, 2020 bei itashuka, hamna matatizo. Akina mama wamelia sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora wanisaidie kulia na akina mama hawa kwa sababu maisha yao hata wakienda kujifungua wanakokotwa na mikokoteni ya ng‟ombe, wanapelekwa katika zahanati ambazo hazina huduma za kutosha; wakijifungua watoto wao wanafariki kwa sababu ya upungufu wa huduma; nilimsikia Mheshimiwa Malapo asubuhi anasema zahanati haina maji. Imagine mwanamke anayekwenda labor ward halafu hakuna maji, halafu utamwambia kufariki mtoto wako ni bahati mbaya. Bahati mbaya kwao tu, akina mama tu au na kwa wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kwenye janga kubwa la madawa ya kulevya, our youths are frustrated. We have a lot of miserable children around the streets na hili lote linatokea kwa sababu mipango ya Serikali haijamtazama mwanamke kama mwanamke. Nataka kuuliza tena katika bajeti zenu na katika mipango yenu, where is the woman?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaalam mmoja kutoka Singapore aliwahi pia kusema naomba nirejee, when women thrive, all the society benefits and succeeding generation are given a better start in life. You guys have gone through the same process. Ninyi wote mko na akina mama zenu, mlizaliwa.
Sasa naomba ukiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ukiwa Waziri wa TAMISEMI, Afya na kadhalika usifikiri ya kwamba hakuna mama yako, shangazi yako, dada yako kijijini ukafikiri mipango hii tu inaweza kwenda bila kumtazama mwanamke katika jicho lenye uhakika, halafu ukadhani unakwenda kufanikiwa. When women thrive all the society benefits and succeeding generation are given a better start in life. What are we doing to give our succeeding generation a better start in life? Where is the woman? Where is the woman katika haya tunayoyafanya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakosea sana kama Taifa kuwaacha nyuma wanawake. Viwanda vidogo vidogo ni suala ambalo kwa kweli mnapokwenda kwenye mkakati wa viwanda lingekuwa limewatazama wanawake, ndiyo watu wenye commitment, ndiyo watu ambao wangezalisha malighafi ambazo zingesaidia viwanda vikubwa; lakini mmeyaweka in general. Kwa hiyo, naomba Mawaziri wanaohusika kwenye hili, tukienda kwenye hitimisho mnisaidie. Naomba mjibu hili swali, kwa sababu nobody can ever stay here and say he never recognize a woman in his life or in her life.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuambieni kwamba suala la umeme wa REA, mlipoona ni kazi nyepesi sana kufikiri ya kwamba ni mradi ambao mnatakiwa kubeza baada ya zile fedha za MCC kukatwa, mkadhani ni sawa sawa; akina mama wanapika gizani, akina mama wanaungua na mkaa na moshi. Hilo ndiyo jambo ambalo mngetakiwa kuliweka mbele ili hatimaye mwanamke apate ahueni. Aki-smile, you guys all smile. Make a woman smile. There is no life without a woman in this world man. Tukubaliane hivyo. Where is the woman? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani sana neno langu liwe sheria halafu niwalazimishe kufanya ninayotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa sababu naona muda wangu umekwisha, lakini naomba Waheshimiwa Mawaziri wanijibu, where is the woman in your plans?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia jioni ya leo katika Wizara ya Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano.
Kabla sijaenda mbele nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kuwepo ndani ya jengo hili, ninamshukuru amejibu ndoto zangu, ingawa ninachokiona haki ya Mungu ninastaajabu. Sikuwahi kufikiri kile chombo kinachoitwa Serikali ambacho tuliamini ni supreme haya ndiyo kinayoyafanya na kwa kweli ninasikitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea nimpongeze na nimtaje kwa heshima kabisa kiongozi wangu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, kamanda, kuwa mpinzani kwa miaka zaidi ya 20 siyo mchezo. Kazi uliyoifanya tumeiona, leo Bunge hili lina watu mahiri sana ndani yake ambao wataisaidia sana Serikali hii na si Bunge hili tu hata Bunge lililopita ndiyo kati ya Mabunge ambayo yaliwaamsha Watanzania wakajua ni nini kinachoendelea kwenye nchi yao na hatimae tuko hapa tulipo na tunafanya tunachokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye suala la daraja la Kigamboni. Nilimsikia Mheshimiwa Tizeba akichangia akisema, eti kwenye bajeti ya Wizara wameweka kivuko kingine cha Kigamboni; sawa sawa kabisa na mkiweke kwa sababu lile daraja mmetengeneza photo point, watu wakapige picha, siyo kwamba mmetengeneza liwasaidie chochote watu wa Kigamboni. Tulikuwa tunahangaika na vivuko vibovu…
…habari ndiyo hiyo, tulieni sasa mpate habari zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunahangaika na vile vivuko vibovu despite the fact kwamba viko tu kilometa sifuri kutoka Ikulu, lakini huduma tuliyokuwa tunapata pale ni mbovu kabisa na leo Serikali ikaja ikatuahidi ya kwamba tunajenga daraja halafu maisha yetu yatabadilika, hayajabadilika chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lile daraja linaendelea kuchajiwa, Watanzania wa Kigamboni wanalipia lile daraja, tena eti mnasema mnaweza kumtenganisha Mtanzania wa Kigamboni na baiskeli na pikipiki na bajaji na hiace na gari la mzigo. Hivi mmemtenganishaje huyo Mtanzania wa Kigamboni? Mmempa ahueni gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za kivuko ndizo hizo hizo zilizohamishiwa kwenye gharama za daraja la Kigamboni, Mmempa ahueni gani mama ntilie? Mmempa ahueni gani yule Mtanzania anayesubiri kununua kifaa cha ujenzi akafanyie shughuli zake za ujenzi? Mmempa ahueni gani ikiwa lile guta tu ambalo linachukua bidhaa Buguruni na Kariakoo kupeleka Kigamboni linachajiwa gharama ile ile sawa na iliyokuwa inachajiwa kwenye gharama za kivuko? Hakuna mabadiliko, hakuna ahueni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kivuko mlituambia mnatuchaji kwa sababu kuna gharama za uendeshaji, well and good. Mmeleta daraja tunachajiwa gharama zile zile, eti mnasema anayekwenda kwa mguu tu ndiye amepata ahueni, amepata ahueni gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi niko Dar es Salaam nimekwenda mjini kwa shughuli za kikazi nikapigiwa simu nyumbani, mtoto anaumwa. Nimekwenda asubuhi nimelipa shilingi 2,000, nikarudi Kigamboni kumchukua mtoto nikalipa shilingi 2,000, nikarudi hospitali nikalipa shilingi 2,000, baada ya mtoto kutibiwa nikarudi nyumbani nikalipa shilingi 2,000, ni lazima nirudi kumalizia lile jukumu langu mjini nikalipa shilingi 2,000, jioni nilirejea nyumbani nimelipa shilingi 2,000, umenisaidia nini? And that not only me, Watanzania wengi wa Kigamboni wanapitia katika hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifikirie upya kuhusu habari ya tozo za daraja la Kigamboni; mmetumia pesa za Watanzania, lazima ziwarejee.
Lazima pesa za Watanzaia zilizotumika kujenga daraja la Kigamboni, mmejenga Malagarasi, mmejenga la Mkapa, mbona lile hamku-charge? Hawa Watanzania wa Kigamboni na wao wanalipa road licence kama ninyi. Zile gharama za barabara tunazokatwa kwenye lita moja ya mafuta na wao wanalipa, mbona mnawa-double charge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukubaliane ya kwamba mmewaonea sana watu wa Kigamboni, mmewanyanyasa sana, mmewanyonya mno kwa tukio hilo la kuamua kuwa-charge kwenye lile daraja, lakini tukubaliane pia kwamba, hamjawatendea haki hata kidogo. Utabaki kuwa msimamo wangu na Mheshimiwa Waziri naomba ulichukue hilo ulifanyie kazi utupe majibu, hutaki tutakuachia lile daraja sasa upigie picha tuendelee kupita kwenye Kivuko kwa sababu tunachajiwa kitu kile kile, adha yetu ni ile ile, lakini shukrani kutuongezea kingine basi, ili walau tuendelee kuteseka kwa sababu, sioni kama umekuja na mkakati wa maana sana juu ya kusaidia hatma ya Kigamboni na maendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lile eneo la Kigamboni ukishaondoka tu pale darajani, pana njia nyembamba kama mrija wa biki. Kwa hiyo, mlipanda pale juu mkafanya kazi ya kisiasa, mka-celebrate mkaondoka, hamkujua watu wakishaondoka mjini basi kule mliko-cross mkasema cross overs sawa, baada ya kuondoka darajani unarudi Kigamboni, barabara pale iko wapi? Usanifu wa kina mnaoita, sijui na upembuzi yakinifu ulishafanyika, wale matajiri wanaomiliki matenki ya mafuta maeneo yale barabara iliyopangwa kutoka daraja la Kigamboni ilipaswa ipite maeneo yale, leo sijui mmekaa meza gani, mmejadiliana namna gani, wananchi wangu wananiambia mmebadilisha msimamo, eti mmeamua kwenda kupitisha daraja tena eneo la makazi ya wananchi ambao hawakufanyiwa tathmini, mnaendelea kutunyonya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye suala lingine, suala la Serikali kukopa holela; Serikali yetu eti imepata kimbilio la kwenda kukopa fedha China na wao wamejua kabisa ya kwamba wana ajenda yao. Na mkigonga tu hodi wanasema yes, what do you want men? Mmepewa dola milioni 500 kwa ajili ya fedha za maendeleo…
MHE. LUCY S. MAGERELI: ...hizo pesa zikapotea. zikayeyuka.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakandarasi wanaofanya miradi ya maendeleo hapa Tanzania, wakandarasi wa Kichina, wamedai fedha zao mlishakula! Mkatumia mwanya mwingine kwa sababu mnajua kukopa kiholela mmerudi Uchina, mmeomba dola milioni 500 zingine. Mlikataa msaada wa Marekani wa MCC mkidai ya kwamba eti hamtaki pesa zenye masharti! Mchina alipowapa dola milioni 500 akawaambia sharti la kwanza lazima wakandarasi wa Kichina wote walipwe, ambao wanaidai Tanzania siyo chini ya dola milioni 365. Mmekataa masharti yapi na mmepokea yapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tukubaliane kabisa ya kwamba, kwenye hili lazima muwe waangalifu kwa sababu kwanza mnakopa fedha nyingi sana kutoka source moja! Hatari hata kwa ustawi wa Taifa, hatari hata kwa usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie suala la mizigo bandarini. Naomba nieleze kwa masikitiko kabisa ya kwamba bandari ya Dar es Salaam ina hali mbaya na inekoelekea sijui inakwenda kufa sina hakika, kwa sababu kwa mwezi wa kwanza na wa pili tu kwa takwimu, naomba nirejee, mizigo iliyokuwa inapita kwenye bandari ya Dar es Salaam kutoka Zambia imepungua kwa 42%, container kwa 28%, magari kwa 55%. Mizigo iliyokuwa inakwenda Congo imepungua kwa 9%, container 31%, magari 50%. Mizigo iliyokuwa inakwenda Burundi imepungua kwa 27%, mizigo iliyokuwa inakwenda Malawi imepungua kwa 35.6%, container kwa 11%, lakini mizigo ya Uganda imepungua kwa 77%. Nchi nyingine zikiwa na bandari ndiyo zinazojivunia kwa sababu, ni moja ya mlango wa uchumi... Imeisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa ya kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Nje. Kwa utangulizi tu, nianze kwa kuonesha masikitiko yangu juu ya ukandamizwaji wa demokrasia unaofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili Bunge sasa limegeuka kuwa mwiba mkali sana kwa ustawi wa demokrasia ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono jitihada zote zilizofanyika siku ya jana kuhakikisha kwamba tunaleta attention ya kuwasaidia vijana wetu ambao hawakutendewa sawa. Whether mliikubali au mliikataa lakini ulimwengu unajua ya kwamba hapo mmekosea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Msigwa umefanya kazi yako vizuri, hongera sana. Naomba pia kuunga mkono hotuba ya Kamati ya Mambo ya Nje, mmefanya kazi nzuri, mmetendea haki mlichokiona na huo ndiyo ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ku-declare kwamba ni mjumbe wa Kamati hii na katika kutekeleza majukumu yetu ya Kamati, nieleze tu masikitiko yangu kwamba hii ndiyo Wizara ambayo tulikuta hata cha kuzungumzia hakipo, kila unakogusa tabu, shida, karaha, fadhaha. Ukizungumzia shughuli za utendaji wa watendaji katika Wizara ya Mambo ya Nje yaliyoko kule fadhaha, ukitazama Balozi zetu zilizoko nchi za nje fadhaha, bajeti ya maendeleo waliyotengewa hawakupata hata senti moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika kwa kweli kuona hotuba hii ambayo nimeisoma mwanzo mwisho, sijajua Waziri anaogopa, ana hofu au ana mashaka, lakini nilitarajia aje na hotuba ambayo ni ya kitaalam, ina mikakati na ina mipango lakini Mheshimiwa Waziri amekuja na hotuba ya kisiasa. Nikajiuliza yale tuliyoyaona wakati wa Kamati, japo sawa Waziri mpya kwa this time, nikajua atayaona na kwenye hotuba yake ndiko atakakokuja na yale ambayo aliyaona ni upungufu na ataonesha mikakati yake na way forward lakini Mheshimiwa Waziri ameandika siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye hotuba yake ukurasa wa 111, amesema malengo ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017, nimeyasoma yote ni siasa. Nisome mawili ya mwanzo tu, la kwanza kutangaza nchi yetu kama moja ya nchi duniani zenye mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa, kwa kufanyaje?
Lla pili, anasema kuongeza uwakilishi wetu nchi za nje kwa kufungua Balozi mpya ofisi za Kikonseli na kuimarisha rasilimali watu na fedha wakati haya ndiyo ambayo kwenye Kamati tumezunguka tukiyatazama, hizo Balozi tulizonazo tu ziko hohehahe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia Mheshimiwa Mbunge, mama wa CUF anasema alikwenda Msumbiji akakuta katika Ofisi ya Balozi mama ntilie anaingia anauza chai, hakuna hadhi. Mimi iko Balozi tulifika tukakutana na mende, panya na popo. Sasa akituambia tu kwa maneno mepesi kama alivyosema katika lengo lake la pili kwamba anataka kufungua Ofisi za Balozi wakati viwanja tulivyonunua havijajengwa, viwanja vilivyotolewa havijajengwa, nyumba tulizopewa kwa ajili ya Ubalozi ziko hoi, ndiyo hizo zenye popo na mende, sasa anafunguaje Balozi nyingine mpya wakati zilizopo hii ndiyo hali yake? Basi fine, tulitegemea aseme at least kwa details kwamba tutafanya moja, mbili, tatu, tutakarabati lakini tutaongeza na hili yaani tulitaka hata kuona nyingi ngapi? Ndiyo maana nasema hii ni siasa kwamba tutafungua Balozi mpya, ngapi, wapi na kwa gharama ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni huduma za kibalozi. Watendaji wetu katika Balozi zetu mbalimbali wana hali mbaya, huduma ni shida lakini hata vipindi vyao vya kuhudumia vinapokwisha fedha ya kuwarejesha nyumbani ni tatizo. Badala yake, kama alivyosema Mheshimiwa Msigwa, uteuzi wa nafasi za Balozi katika nyakati fulani zimeonekana ni adhabu kwa wale watu ambao wanaonekana ni threat kwa wanasiasa fulani. Kilicho kibaya ni kwamba unapigwa jina Ubalozi halafu unaachwa hapo. Kwa hiyo, pale Foreign Affairs kuna watu wenye titles za Ubalozi wengi tu, wakiona unakerakera kwa kuweko hapa basi wanakutafutia mahali wanakwenda kukuficha pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakaporejea ningetamani haya ninayoyazungumzia atuoneshe kimkakati hasa kwamba anakwenda kuchukua hatua gani na atupe na time frame. Kwa sababu hata suala la Sera ya Mambo ya Nje, hii ambayo imetumikiwa kwa miaka kadhaa sasa ya Economic Diplomacy, hakuna tulicho-achieve. Kwa sababu kingekuwepo angekuja nacho akatuonesha kwamba kwa kipindi kilichopita tumefanya yafuatayo lakini hotuba yake imeongea siasa mwanzo mwisho na hakuna ambacho kiukweli amemudu kutupatia kama takwimu za kuonyesha achievement na if so, what is next? Je, tunakuja na sera nyingine au bado tunaendelea kutumikia hiyohiyo iliyoshindwa? Mchangiaji mmoja amesema tumeleta wawekezaji wa kutosha. Sawa, walipotosha wakafanya nini? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utangazaji wa vivutio na fursa za uwekezaji Tanzania, kama alivyosema Mheshimiwa Mwanjelwa, natamani sana labda tungeweka sasa goals na kila Afisa wa Balozi aliyeko Ubalozini ambaye ana wajibu wa kutekeleza haya mwisho wa bajeti ya mwaka mmoja atuambie ame-achieve nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hawauwezi kumdai ame-achieve nini kwa sababu hawawa-finance, hawawa-facilitate wale watu, kwa hiyo hawa-perform. Wamekaa kule wanaendelea ku-enjoy diplomatic securities lakini kiukweli najua hawawezi kukubali ku-set goals na kuanza kufanya assessment ya performance kwa sababu hawajawa-facilitate maafisa wetu walioko maeneo ya Balozi ili waweze kutekeleza wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiombe Serikali itusaidie katika Wizara ya Mambo ya Nje, bajeti wanayopewa haikidhi haja hasa kwenye miradi ya maendeleo. Ile ndiyo sura ya Tanzania katika maeneo ambayo tuna uwakilishi lakini kama kweli tuna Balozi ambazo mapaa yanavuja na umekaa sitting room mende anapita, kiukweli hata kama tungetaka wafanye nini isingewezekana kwa sura ile. Mwaka jana wametengewa bajeti ya shilingi bilioni nane lakini hawakupata hata senti moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Diplomasia. Kama kweli majukumu tuliyokipatia Chuo cha Diplomasia ndiyo tunayotaka kitekeleze, basi Serikali inatakiwa kuja na kauli ituambie kwamba hicho chuo kweli ni Chuo cha Diplomasia au wameshabadilisha ajenda. Kile chuo kwa miaka mitatu mfululizo hawajapata senti moja ya pesa za maendeleo halafu tunasema wawafundishe Mabalozi wetu, wake wa Marais na kadhalika, hiyo haiwezekani unless tuwe na mkakati mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi leo nichangie katika hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na mimi nitajielekeza eneo moja mahsusi kabisa la ukuaji wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ukurasa wa 10, kuna quotation pale alitoa iko kwa lugha ya Kiingereza lakini ilitolewa pia tafsiri isiyo rasmi ambayo na mimi ningependa pia niirejee, nayo inasema hivi; “Ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo. Unatokea katika maeneo ambayo watu maskini wanaishi, kwa mfano, maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali. Unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu maskini wanazo, kwa mfano, nguvu kazi isiyo ya kitaalamu na unapunguza bei za bidhaa ambazo watu maskini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo.” Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye kati ya maeneo aliyoyazungumzia kwamba yamefanya vizuri sana ni eneo hili la ukuaji wa uchumi. Maoni yangu mimi binafsi ni kwamba ukuaji wa uchumi hauwezi kuja kama katika uchumi wa leo hatuwezi kuishirikisha sekta binafsi. Sekta binafsi imetengwa kabisa na kwa bahati mbaya kuna baadhi ya kauli ambazo
zimekuwa zikitolewa na Kiongozi Mkuu wa nchi ambazo kwa kweli ukizitafakari kwa undani unaona kabisa kwamba kuna a missing link somewhere ambayo inatupelekea sisi kwenda kudumaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuombe Mheshimiwa Rais, lakini na Serikali kwa ujumla kwamba ile kampeni yake aliyoianzisha ya malaika waishi kama mashetani, sasa umefika wakati muafaka kwamba kauli hiyo ifutwe kwa sababu ugomvi huo wa kuwataka wale malaika
sasa warudi kuishi kama mashetani umegeuka kiama kwa wale wenyewe mnaowaita mashetani kwa maana ya Watanzania wa hali ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inaposhindikana sekta binafsi au wawekezaji walioko ndani ya nchi hii kuendesha na kukuza mitaji yao lakini kutoa michango yao katika uchumi wa nchi, mwisho wa siku anayeathirika siyo yule ambaye ni mwenye kipato hicho cha juu ambaye kwa reference ya Mheshimiwa Rais ni malaika lakini anayeathirika ni yule ambaye anaitwa shetani. Sasa na mimi kwa sababu niko kwenye kundi hilo la mashetani, naomba nilete ujumbe wangu maalum nikisema tunaomba waacheni malaika waendelee kuwa malaika, waacheni waendelee kufanya zile karamu zao kwa sababu zile karamu, yale makombo yanayodondoka kwenye zile meza za malaika kwetu sisi ndiyo riziki, ndiyo neema. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotaka malaika wageuke mashetani, shida kubwa iko kwa Watanzania wa chini. Sasa nastaajabu tunapoona hotuba zinazosema kwamba kuna ukuaji wa uchumi. Tuwaache malaika wanaoshughulika na sekta ya ujenzi waendelee lakini tuwasaidie waweze kuendelea kwa ustawi kwa sababu wanapofanya kazi zao za ujenzi sisi mashetani tunaokotaokota makombo kwa kupata kazi za ajira za ujenzi lakini wakiagiza bidhaa in bulk kwa maana ya bidhaa nyingi basi na sisi tunapata ahueni kwa sababu zinapokuwa nyingi sokoni na sisi tunapata kuzipata katika bei ya ambayo ni ya ahueni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitolee mfano wa mzalishaji na mwekezaji mmoja Bakhressa ambaye katika kibano ambacho amekipata kwa muda mfupi wa Serikali ya Awamu ya Tano, amebadilisha kabisa mkakati wake wa uwekezaji na kwa kiasi kikubwa mtaji wake sasa anauhamishia maeneo mengine ya Afrika kwa maana ya nchi nyingine za Afrika. Hatua hiyo tu inaleta ujumbe straight kwamba kuna ajira ambazo zimeathirika. Kuna hao mashetani sasa ambao kwa yule malaika Bakhressa kuadhibiwa na kupangiwa kodi ambazo haziko realistic na masharti mengine ambayo hayatekelezeki kibiashara, amepunguza wafanyakazi lakini zingatieni ndiye anayezalisha mpaka maziwa na maji ya shilingi 500 na sisi mashetani tunapata ahueni ya kunywa maji ya chupa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo kama la Breweries, tuache malaika hawa wa Breweries wazalishe kwa sababu wakizalisha sisi mashetani wa kule mashambani, mazao yetu ya ngano na shairi yanapata soko la uhakika. Pia wale wanaojishughulisha na shughuli za usafirishaji na sisi vijana wetu wako kwenye kuwa madereva wa hayo magari lakini wako katika kuwa utingo wa hayo magari na kutoka hapo na sisi tunapa riziki na vijana wetu wanakwenda shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo kwa mfano la bandari. Wakati bandari ina-operate katika kiwango chake ilitusaidia sana sisi tunaoitwa mashetani kupata kiasi kikubwa cha ajira na vijana wetu kutumika katika eneo la bandari ambapo kwa sasa kutokana na kiwango cha uingizaji na utoaji wa mizigo kushuka, vijana wengi sana wamepoteza ajira bandarini. Vilevile yale magari yaliyokuwa yanaondoa mizigo bandarini na kupeleka mikoani na nchi za jirani napo palikuwa kuna kundi kubwa la Watanzania ambao walikuwa wanahudumia kama madereva, utingo lakini mama ntilie katika maeneo tofauti walikuwa wanapata riziki zao kutokana na eneo hilo. Naamini sasa nimeeleweka ninapojaribu kusema ya kwamba tuwaache malaika waendelee kuwa malaika kwa sababu sisi mashetani tunapotea kwenye karamu za meza zao, wanapodondosha
na sisi ndiyo tunaishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata taarifa juzi kupitia vyombo vya habari kwamba Private Sector Foundation wanakuja Dodoma kwa ajili ya kuonana na Serikali, naamini taarifa hiyo mnayo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu, hao ndiyo watu ambao unatakiwa kuwapokea na mimi sijui niombe kama Mheshimiwa mwingine aliyesema, muache Waziri Mkuu atusikilize. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba hawa watu wa private sector wanapokuja Dodoma kuja kuonana na Serikali wapewe fursa, wapewe usikivu…
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimaanisha kumueleza Waziri Mkuu nilisikia kupitia vyombo vya habari kwamba The Private Sector Foundation wanakuja Dodoma kuja kuonana na Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba uwapokee hao watu na uwasikilize kwa sababu kama nilivyosema awali makombo ya kwenye meza za karamu zao kwetu sisi ni neema. Hebu acheni private sector sasa ishamiri, itoe ajira kwa Watanzania, izalishe bidhaa nyingi ili bidhaa zishuke bei lakini muwape na access ya ku-import ili bidhaa ziwe nyingi kwenye masoko na kwenye mzunguko ili na sisi tunaokuwa referred kama mashetani, naupenda sana huo msemo sana kwa sababu ni fahari kweli kuitwa na Rais wako kwamba wale wote ambao tuna kipato cha chini basi sisi ni mashetani na sisi tupate kuneemeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nataka niende kwenye suala moja la msingi ambalo nimeliona na niombe attention. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, kuna suala limejitokeza ambalo naendelea kulistaajabiwa. Jambo hili ni kwamba, Mheshimiwa Rais ametoa kibali kwa mwekezaji mmoja wa hapa Tanzania, Dangote, achukue mgodi wetu wa makaa ya mawe, achimbe mwenyewe, asafirishe mwenyewe, atumie mwenyewe, huu ni utaratibu gani? Huu ni wizi wa namna gani wa wazi na hadharani? Sasa leo tunahangaika na mchanga wa ACACIA bandarini nimeona mpaka leo Tume imeundwa wakati kuna mahali tumemfungia fisi buchani halafu tutamuuliza umekula kilo ngapi? Hivi uwezekano huo kweli upo? Mheshmiwa Naibu Spika, kati ya mambo sasa ambayo Bunge hili linatakiwa liisimamie Serikali na kulitazama upya ni hili suala la Mgodi wa Makaa ya Mawe. Haya ni kati ya makosa makubwa kabisa ambayo tumeyafanya hata kama lengo ni kumbembeleza mwekezaji basi hapa tumekwenda kinyume kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo lingine la wawekezaji na mitaji yao. Kauli za Mheshimiwa Rais zimeendelea kuwa tata kila mara na kusababisha wawekezaji wengi kupata mashaka kuhusu mitaji yao wanayoiwekeza ndani ya nchi hii lakini na wanaotaka kuja sasa na wao wanaongeza mashaka ya kwamba wawekeze ama la.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru ingawa naona muda umekuwa mfupi, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, na kushukuru sana kwa kunipa fursa nichangie na mimi Bajeti ya hii Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na nianze kwa kueleza na kukubaliana kwamba ninaunga mkono hoja zote katika ripoti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja ya suala la Daraja la Kigamboni. Hili mimi nitaendelea tu kulisemea tu sana kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa. Tozo katika Daraja la Kigamboni zimekuwa kero kuliko msaada, gharama zinazotozwa pale kwenye lile daraja ni kubwa kuliko hali halisi ya wananchi wa Kigamboni. Tulitarajia kama ambavyo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati anazindua lile daraja alivyosema, kwamba daraja lile lifungue fursa za kuwasaidia Watanzania, wananchi wakazi wa Kigamboni kubadili mfumo wa maisha yao lakini pia kujipatia fursa za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wakazi wa Kigamboni bado ni aina ya wananchi ambao wanawaza watoto wao watakula nini, watapata wapi ada ya shule, lakini pia wanawaza hata namna ya kugharamia mavazi ukilinganisha na hali halisi ya uchumi ilivyo leo na ukiangalia hali halisi ya uchumi wa Tanzania, mimi nafikiri bado hatujafikia mahali pa kulipia tozo za huduma muhimu na nyeti kama barabara na madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili naomba kabisa Mheshimiwa Waziri litazamwe upya, ikiwezekana kama iko lazima sana kwa sababu daraja hili limejengwa kwa ubia wa NSSF na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania basi lile eneo la NSSF lifanyiwe utaratibu fedha zile ambazo zilitolewa kama mchango wa NSSF kwenye ujenzi wa lile daraja zilipwe, kwa sababu daraja hili kulingana na jinsi ambavyo nimesoma kwenye hotuba yako itakuwa ni connection ya interchange ile barabara ya haraka ya Chalinze, sasa kama ndivyo je, ni eneo lile tu la kuvuka pale kwenye daraja litakuwa linalipiwa ama na barabara zote za interchange zitakazo unganisha na daraja la Kigamboni zitakuwa zitalipiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama zote zitalipiwa bado tufahamu kabisa kwamba ni changamoto kubwa kwa Watanzania wa sasa hivi na hali ya uchumi ilivyo jamani hatujafika huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie baadhi ya vipaumbele ambavyo vimeoneshwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu eneo la Kigamboni nikianzia na barabara ya Kongowe – Mjimwema – Kivukoni ambayo kulingana na taarifa zilizopo katika kitabu cha Waziri ni ya kilomita 25 na imepangiwa shilingi bilioni 1.290. Mheshimiwa Waziri niombe sana kwamba barabara hii ni muhimu sana kwetu na tangu mwaka jana ilikuwa katika bajeti yako, lakini kwa bahati mbaya nadhani ilipata fedha kidogo mno ambapo utaratibu wa upanuzi ulianzia tu eneo la pale kwa Mwingira mpaka kufika Mji Mwema na imeishia hapo.

Kwa hiyo, nikuombe sana katika bajeti yako ya utusaidie kutengwa fedha za upanuzi wa hiyo barabara kwa sababu ndicho kiunganishi kikubwa cha kutoka eneo la Kivukoni mpaka kwenda kuunganisha na Kongowe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimeona Mheshimiwa Waziri amelitaja daraja la Mzinga, nikuombe sana lile daraja msimu wa mvua tunapata matatizo makubwa sana, na mwaka juzi daraja lile lilikatika kabisa tuliishi kwa msaada wa ujenzi uliofanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo, nimeona umetenga fedha pia kwa ajili ya daraja hilo, tunaomba pesa hizo zipatikane na hilo daraja lijengwe ili kuweze kuwa na connection baina ya wakazi wa Kigamboni na eneo la Temeke; lakini ukizingatia na hiyo express way ambayo nimeona mnaijenga, nimeona inakwenda mpaka eneo la Mbagala ambayo na amini ile barabara ya Kongowe itakuwa ni feeder road kwenda kwenye hiyo interchange ambayo umeizumzumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye barabara ya Tungi – Kisiwani – Kibada. Mheshimiwa Waziri wakati wa hotuba yako wakati wa uzinduzi wa daraja la Kigamboni kwa maneno yako mwenyewe kabisa ulisema umejipanga na utakwenda kumalizia lile eneo la kilomita 1.5 lililobaki baada ya daraja kwenda mpaka pale kwa Msomali, na ulisema fedha zipo na ujenzi ungekamilika mapema iwezekanavyo. Hata hivyo lile eneo limebaki na sura kama alivyosema Mheshimiwa Shabiby jana, kwamba umevaa koti zuri safi na tai lakini chini umevaa kaptula na makobazi.

Mheshimia Naibu Spika, ukubwa wa barabara inayotoka darajani ni kubwa mno ya njia tatu pande zote mbili lakini inakwenda kuingia katika barabara ndogo halafu mbaya na chafu sana, tena wakati huu wa mvua ukifika eneo lile hata kupita na gari ndogo ni shughuli kubwa na pevu. Kwa hiyo tunaomba kipande hicho cha kilometa 1.5 kimaliziwe kama ambavyo uliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hiyo hiyo ya Mheshimiwa Waziri ya siku ya uzinduzi wa daraja la Kigamboni alisema lile eneo la darajani, mpaka pale kwa Msomali kwa maana ya kuunganisha barabara ya Kivukoni kupitia Tungi, Vijibweni mpaka Kibada usanifu umeshakamilika na barabara ile ilipaswa kuanza, ujenzi ungeanza Mei 2016 lakini mpaka ninavyozungumza leo hakuna kinachoendelea eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sielewi kilichotokea yawezekana ni ufinyu wa bajeti lakini tunaomba sasa msimu huu kwa maana bajeti hii inayokuja mtusaidie eneo lile liweze kukamilika na barabara ile ikamilike kwa sababu ndio barabaara ambayo ina wasaidia wananchi wengi wa kazi ya maeneo ya Kisarawe II, kata za Kibada, Mji Mwema kupita kwa ajili ya kuja kukutana na eneo la daraja la kuvuka kuja mjini. Barabara ile ya sehemu ile ni mbaya sana na kisehemu cha lami kilichojengwa kuanzia Tungi mpaka Vijibweni karibu kuelekea hospitali eneo limeshaharibika kabisa lina hali mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia nizungumzie au ni muulize Mheshimiwa Waziri atusaidie. Katika bajeti iliyopita ulitupangia fedha kwa ajili ya barabara ya Kibada - Mwasonga kuelekea Tundwi Songani. Najua unaufahamu umuhimu wa barabara hii, ndiyo barabara ambayo magari makubwa sana ya yanayotoka Kimbiji kuelekea Kiwanda cha Saruji cha Nyati yanakopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile kwa kweli imepata uharibifu mkubwa sana kutokana na matumizi makubwa ya yale maroli na kwa hiyo wananchi wa kawaida na usafirishaji wa kawaida unashindwa kuendelea kabisa katika eneo lile kwa sababu mara nyingi yale magari yanapoharibika au yanapokwama katika barabara ile wakazi wanashindwa kuendelea na maisha yao ya kawaida. Kwa hiyo, sasa sielewi imekuaje kwamba barabara hii ya Kibada – Mwasonga – Tundwi kuelekea Kimbiji haijatengewa fedha msimu huu wala haujaizungumzia wakati 2016/2017 ilikuwepo kwenye bajeti yako Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia nizungumzia barabara ambayo nimeona umeizungumzia katika kitabu chako ukurasa wa 35, barabara ya bandari ambyayo ni ya kilomita 1.2 lakini barabara ya Mivinjeni kilometa moja na Dock Yard kilometa 0.7. Barabara ile Mheshimiwa Waziri nikusihi sana kwamba tungependa itengewe fedha lakini itanuliwe kiasi cha kutosha, kwa sababu msongamano wa yale maroli pale bandarini unatupashida shida sana.

Mheshimiwa Naibu Soika, kweli unafiri ni haraka sana kutoka Kigamboni kwa kuvukwa kwa daraja na kuondoka haraka kufika mjini lakini ukishaondoka darajani tu unakutana na hii barabara ya bandari imejaa foleni ndefu, unakutana na barabara ya Mandela imejaa foleni ndefu, kwa hiyo, shughuli ile inabaki kuendelea kuwa shughuli vilevile. Hata kama kungekuwa na nafuu barabara ya bandari bado utaratibu wa kuegesha magari yale makubwa ni mgumu mno na barabara hii inashindwa kupitika. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie utaratibu wa kutengeneza parking maalum ya yale magari ili barabara zibaki huru zitembee kwenda na kurudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana, nimeona umetenga bajeti yako pia ukurasa wa 214 umetenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa gati ya pale Kivukoni, Kigamboni. Eneo lile nalo ni shida kubwa sana, vivuko vile tunashukuru vinafanya kazi na vinatusaidia sana kwa sababu sisi kwa bahati mbaya tumejikuta na hilo janga la kujikuta barabara kwa maana ya daraja tunalipia na kivuko tunalipia, hewala kama ndivyo ilivyowapendeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikuombe basi mtusaidie sana Bajeti hii fedha za utanuzi wa gati pale zipatikane kwa sababu hata kama pantoni imefika imetia dock pale utaratibu wa utokaji wa magari unakuwa taratibu mno kwa sababu eneo ni finyu mno. Kwa hiyo, pantoni kupakia ruti nyingine iende inachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru kwa haya ya leo, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kuchangia ndani ya Bunge hili Tukufu katika hii hoja ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Ningetaka nianze na kuendelea hapo hapo alipoishia Mheshimiwa Kubenea kuhusu ATCL kwa sababu hili ni suala muhimu sana ambalo lazima tuendelee kukumbushana, lazima tuambiane ukweli, lazima tuwe wakweli juu ya nini tunataka kuhusu kuifufua ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiona ni kwamba nadhani wataalam wa Tanzania hawajapewa fursa kabisa na wala nadhani hawakushirikishwa wakati ulipokuja mjadala wa kutaka kuifufua ATCL. Naamini wangeshirikishwa maamuzi haya yaliyofanywa leo yasingefanywa. Hivi jamani ni nani aliyemshauri Mheshimiwa Rais kwamba anunue ndege? Kulikuwa kuna uwezekano mkubwa kabisa wa kuifufua ATCL kwa kutumia ndege za kukodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hatukuhitaji ndege kubwa Tanzania kwa wakati huu kwa sasa. Hivi tunatakaje kwenda kushindana na mashirika makubwa ya kimataifa ya ndege ambayo yameshajiimarisha kwa muda mrefu, ambayo pamoja na yenyewe yanafanya biashara ya hasara. Badala ya kufikiri ya kwamba tunahitaji kwanza kuimarisha mtandao wa ndani wa ndege kabla ya kuanza kushindana kimataifa.

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu kwa kusema suala siyo kuhitaji ndege. Ndege gani, kwa utaratibu upi, kwa malengo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri na ningeomba nisikilizwe kwa sababu hivi tunavyozungumza yaani hata viwanja vya ndani ya nchi vya ndege havifai kwa matumizi yetu. Mtalii leo akitua pale JK Nyerere anataka kwenda Ruaha, anataka kwenda Rubondo, anataka kwenda kisiwani Lake Victoria anapata tabu ya kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunadhani ukweli halisi ni kwamba Tanzania inao uwezo wa kununua ndege kubwa wakati network ya ndani bado haijakuwa imara? Ambacho kingefanywa sahihi ni kwamba tulihitaji kuimarisha network yetu ya ndani kwanza halafu baadaye tutapiga hatua hiyo kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize, hivi ni nani aliyemshauri Mheshimiwa Rais kwamba tununue ndege kutoka makampuni tofauti tofauti? Tunaongelea habari ya Bombardier, tunaongelea habari ya Boeing, tunaongelea habari ya Air bus. Haya yote ni mzigo kwa nchi hii. Ndege za Bombardier zitahitaji kuwa na service centre yake yenyewe, ndege za Boeing tutahitaji kuwa na service centre, ndege ya Air bus itahitaji service centre. Unatengeneza service centre Tanzania kwa ndege moja ya Air bus? Unatengeneza service centre kwa ndege moja, mbili za Boeing!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukubaliane kwamba kesho na keshokutwa Bunge hili litakaa tena tupeane taarifa, tulaumiane kwamba tumechezea kiasi kikubwa sana cha pesa za walipa kodi katika kuifufua ATCL ambayo mwisho wa siku imegeuka kuwa msiba kwa Taifa. Nawaambieni huu ndiyo ukweli, ATCL miaka mitano ijayo tutakaa ndani ya Bunge hili tutajadili jinsi ambavyo imekuwa tatizo kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwamba hili suala la ATCL warudi kwenye mikono ya wataalam, watafute menejimenti nzuri, washauriane, waone namna ambavyo ATCL itafufuliwa. Hizo ndege mnazozisubiria huko kwa sababu hebu kwa mfano tumetumia bilioni 130 ku- sort ile kesi ya Mahakama ya Bombardier zile bilioni 130 ni ndege nne zingine za Bombardier. Jamani mnataka mseme hata hapo mlifanya rational decision? Hizo pesa bilioni 130 ziliidhinishwa na Bunge gani? Nani aliyeidhinisha pesa zika- sort hiyo tatizo la Mahakama Canada? Hasara ambayo ATCL itatutengenezea ni kubwa na itaenda ku-bust. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye suala la Daraja la Kigamboni. Naomba nishukuru na nipongeze mchango wa Mheshimiwa Zainabu Mndolwa. Daraja la Kigamboni ni mzigo kwa Watanzania wa Kigamboni. Sisi tulikuwa tunatumia vivuko vya Magogoni, MV Kigamboni na Alhamdullaah wametuongezea kivuko kingine cha MV Kazi. Vile vivuko vyote tunalipia, awali nyuma kabla ya daraja tukaambiwa daraja litakuja kuwa suluhisho na kutupunguzia gharama kama optional way ya kupita kama huhitaji kulipia au huna huo uwezo wa kulipia. Lile daraja limefanywa la kulipia, tena basi tulifikiri ni kwa muda fulani specific lakini it’s a life time business. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, kwa hili kwa kweli wamewadanganya na wamewadhulumu wananchi wa Kigamboni. Walikuwa na sehemu yao ya kulipia kwenye ule mkataba na NSSF, Serikali wameingia mitini, wamegoma kulipia sehemu yao ya mkataba, badala yake wamewaangushia wananchi wa Kigamboni kulipia zile gharama na hata hawaja-specify kwamba ni kwa muda gani. Maana yake sasa sisi tumeshakuwa commodities of trade.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa Kigamboni ukitaka kuvuka kwenye daraja unalipa, kwenye kivuko unalipa na basi si gharama kidogo ni gharama kubwa sana. Gari ya daladala ambayo inatoka Mnazi Mmoja kuja Kigamboni kuvuka pale darajani inalipia Sh.7,500 kila inapopita.

Sasa fikiria kweli wananchi wa Kigamboni kama tulifikiri tukipata daraja basi tutapata na namna rahisi ambayo tutakuwa tunavuka kutoka Kigamboni kuja Dar es Salaam badala yake mpaka leo tuna…

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ningeweze kuafikiana nalo kama tungekuwa tuna mbadala mwingine, lakini sisi tunalipa kote kwenye kivuko unalipa na kwenye daraja unalipa. Kwa hiyo sikubaliani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hoja nyingine ya barabara ya Kibada - Mwasonga – Tundwi – Kimbiji. Nashukuru Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake ametaja barabara hii ambayo tangu bajeti ya mwaka wa 2016/2017, 2017/2018 imetajwa na imetengewa fedha. Ile barabara ni muhimu sana kwa eneo hilo la Kigamboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara inapita katika kata nne ambazo bahati nzuri tunashukuru ni katika kata ambazo zina maeneo mengi ya uwekezaji. Ile barabara hata leo hii ukipita hali yake ni mbaya mno na tumekuwa tunaitengea fedha inatajwa, inatengwa, inatajwa lakini haipewi fedha na wala haijawahi kufanyiwa kulingana ambavyo taarifa zimekuwa zimetolewa katika kitabu cha Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata taarifa zilizotolewa hapa kwenye kitabu ukurasa wa 34 sijaelewa kilichomaanishwa kwa sababu kwenye sehemu ya 21 inasema barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji kilometa 19 lakini sehemu ya 22 inasema barabara ya Kimbiji – Tundusongani kilometa 30.5 sijaelewa kwa sababu sidhani kama barabara hii inafika kilomita 49 point something nadhani kuna jambo hapa halikuwekwa sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ile barabara haipitiki hasa wakati wa mvua. Nimeona wanasema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaendelea, tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie hata itengenezwe kwa kiwango cha moram na ishindiliwe vizuri, iwekewe mitaro ya barabara kwa sababu yale malori ya cement yanapita kutoka Nyati Cement Kimbiji yanapata shida sana kupita kwenye ile njia na mara nyingi yanakwama na yakishakwama maisha yetu ya Watanzania wa eneo lile yanakuwa magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie pia mtandao wa barabara katika Manispaa ya Dodoma. Naamini tunakubaliana wote tuliokaa ndani ya nyumba hii kwamba uamuzi wa kuhamia Dodoma nadhani kuna step ilirukwa ya kuandaa miundombinu. Barabara za Dodoma sasa hivi mji huu asubuhi unasimama msongamano ni mkubwa sana na barabara ya Dodoma ni nyembamba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi barabara ya Dar es Salaam hii kwa maana ya kutokea maeneo ya Ilazo kuja Kisasa mpaka kufika eneo la Bunge asubuhi ni eneo lenye msongamano mkubwa sana. Nimeona orodha ya barabara zinatajwa hapa katika ukurasa wa 36 barabara ya Shabiby- Arusha-Dodoma road-round about, barabara ya Chimwaga- Chinyoya-Kikuyu, barabara ya Dar es Salaam-Nane nane na nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, hizi barabara waziangalie kwa jicho la wepesi tena kwa kipaumbele kabisa especially haya malori makubwa yanayoingia mjini ile barabara ambayo ilikuwa imeandaliwa inayotokea Ihumwa basi ile barabara ijengwe kwa uharaka ili tupunguze magari makubwa ambayo yanaingia ndani ya Mji wa Dodoma na kusababisha msongamano mkubwa sana na ikitokea kwa mfano hapa Dodoma barabara moja tu ikapata hitilafu mji wote unasimama. Kwa hiyo, wanaweza kuona namna ambavyo haiko networked sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie hoja yangu kwa kusema naomba tuwe wakweli, naomba tunaposema tunaishauri Serikali tuseme ukweli, naomba tunapopewa ushauri na wataalam hasa katika maeneo haya ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Yako mambo mengi sana katika Wizara hii ambayo yamekuwa kama wimbo wa kawaida hivi upembuzi yakinifu, sijui uchambuzi wa kina yaani kuna ucheleweshwaji mwingi tunashindwa kusema ukweli kwamba bajeti yetu haikidhi haja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa busara ya meza yako, na mimi nimepata fursa ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, ni bayana kabisa kwamba budget performance ya nchi hii inaendelea kuporomoka siku hadi siku. Haya huhitaji kutumia microscope kutafuta details. Ukipita vijijini unakutana na watoto ambao bado wanaugua utapiamlo. Bado suala la lishe tu ya Watanzania halijaweza kukidhi angalau tukawa na Watanzania wenye afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo ambayo ukiyatazama kwa undani unagundua kabisa kwamba performance yetu bado ni chini sana. Suala la makusanyo ya mapato kupitia TRA kila siku tunaambiwa makusanyo yanapaa kwa kasi ya ajabu, wakati biashara zinakufa. Hivi uhusiano huo uko wapi? Hayo mapato wanayokusanya, yanatokana na nini? Wamegeuka wanyang’anyi sasa TRA, wakikuta unajikakamua, unakazana na kabiashara kako, kila siku wanatamani kuingiza aina mpya ya mfumo wa kukubabaisha na kukusumbua na kukubambika ili mwisho wa siku wapate ile fahari wanayoitafuta ya kusema mapato ya nchi yanakua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alama nyingine ni upelekaji wa fedha za maendeleo/fedha za miradi. Mmeona katika Wizara nyingi sana zilizowasilishwa hapa na wakati tunafanya shughuli za Kamati, taasisi na Idara nyingi sana za Serikali fedha za maendeleo zimepata asilimia sifuri mpaka asilimia tano. Hicho ni kigezo cha kusema hatu-perform kama Serikali. Waheshimiwa Wabunge wa CCM wametupa ushahidi mzuri tu kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina mipango, ndiyo maana tunaendesha nchi kwa mfumo wa butua butua, yaani linalozuka mezani siku hiyo, ndiyo linalozungumzwa ndiyo linalofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la msingi sana ambalo tukilijadili kwa details unaweza kushangaa. Kuna miradi kama Bwawa la Kidunda. Kwa taarifa nilizopewa kwa waliokuwepo bwawa hili lipo kwenye Bajeti za Serikali tangu mwaka 1974, lakini mpaka leo bwawa hilo halijawahi kujengwa na bado linaitwa mradi wa kimkakati.

Mheshimiwa Spika, hivi hili neno mkakati Serikali ya CCM mna tafsiri yake sahihi ama huwa mnalizungumza tu? Ukilifanyia tathmini hilo bwawa matokeo yake ambayo yangeipa nchi hii ni makubwa sana, umeme, umwagiliaji, miradi ya kilimo na kadhalika. Linaitwa mkakati, linatengewa fedha hewa, haziendi bado linaitwa mkakati na mwaka huu nimeliona lipo mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la performance ya Bunge, hili niombe tulitazame tena. Unajua siku hizi tunakimbizana sana humu ndani ya Bunge. Dakika za kuchangia tano, muda wa kukaa masaa mawili, tarehe za kuingia pungufu. Hivi hili suala tutakwendaje nalo mbele kwa utaratibu huu? (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napokea taarifa ya Mheshimiwa Waziri lakini nimeeleza, unaitwa mradi wa kimkakati tangu mwaka 1974. Je, tafsiri ya neno kimkakati tunaifahamu? Hiyo ndiyo hoja ya msingi. Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nami kupata fursa kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2018/2019. Nianze tu kwa maelezo ya awali ambayo ningetaka niyaweke katika utaratibu ambao tumeutumia wakati wote kama Wabunge wa Kambi ya Upinzani, kama Kamati za Bunge tunapokuwa tunatekeleza majukumu yetu ya kuishauri Serikali, kama wadau wa maendeleo ya nchi hii tunapotaka kutoa ushauri wetu kwa Serikali na pia kwa wananchi wetu ambao ndio picha halisi ya kazi ambayo inafanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Biblia, Kitabu cha Yeremia 33:3, neno linasema hivi:-

“Niite nami nitakuitikia na nitakuonesha mambo makuu, magumu usiyoyajua.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maelezo yangu ya awali kwamba kama Wabunge, kama Kamati, kama wadau wa maendeleo tumekuwa tukiishauri Serikali hii lakini bado imeendelea kutuletea mipango ambayo ni copy and paste, yenye mambo yale yale ambayo hayatekelezeki, basi nimefikiri labda we need God’s intervation. Labda tusali sasa, kwa sababu kwa maneno tu kwa kusema kwa kuandika, kwa kuhubiri tumesema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitamani nikuletee memo kwenye Kiti chako nikuombe labda leo Bunge hili tulibadilishe liwe nyumba ya Ibada halafu niongoze maombi, halafu na Wabunge wanijibu kwa kusema twakuomba utusikie. Kwa sababu sijaomba, basi naomba tu muwe wasikivu, mnisikilize niombe.

Mwenyezi Mungu nakuomba uwakumbushe Serikali ya CCM kwamba wananchi wanataka huduma za maji, afya, elimu bora na sio ndege ambazo hawatozipanda mpaka wanakufa. (Makofi)

Mwenyezi Mungu nakuomba uwakumbushe Serikali ya CCM waache kutuletea mipango ya maendeleo hewa. (Makofi)

Mwenyezi Mungu ninakuomba uwakubushe Serikali ya CCM kwamba wananchi wa Simanjiro walihitaji maji kwa sababu sasa hivi wanakunywa maji katika bwawa moja na ng’ombe, hawakutaka ukuta Mungu wakumbushe hilo.

Mwenyezi Mungu naomba uwasaidie kuwakumbusha Serikali ya CCM...

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Umbulla lakini mambo haya huwa ni maneno yanayosemwa tu, ni tarakimu zinazotajwa tu. Hata bajeti zimekuwa zikitajwa kwa tarakimu hivyo hivyo mwisho wa siku asilimia moja, mbili, kumi na moja, tunangoja kuona hilo la Simanjiro litachukua muda gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na maombi yangu. (Kicheko)

Mwenyezi Mungu nakuomba uwaambie Serikali ya CCM ya kwamba uchumi wanaouhubiri unakua kwa kasi wao peke yao ndiyo wanaouona, wananchi wetu hawauoni na sisi Wabunge pia hatuuoni. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naanza mchango wangu niliomba idhini ya Kiti, kwa hiyo, naamini na wewe unamwamini Mwenyezi Mungu na hili wala halikupi shida, naomba niendelee na mchango wangu.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa maelekezo yako. Naomba basi niwakumbushe mimi kwa sababu tayari Mungu ameshaona dhamira niliyonayo moyoni kwangu, basi atayajibu maombi hayo kwa ileile dhamira yangu kwamba …

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Kitwanga kwa taarifa yake, lakini mngewapa fursa Watanzania wakachagua nini wanataka, kati ya ndege au nini ambacho kitaleta madhara kwenye maisha yao, wangekuambieni wanataka X-Rays, CT-Scan, MRI kwa ajili ya afya zao kwa sababu mpaka sasa hivyo ni vitu ambavyo vinaonekana ni vya kupatikana Ulaya na si Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nimalizie kwanza kwenye ile hoja yangu ya sala, kwamba namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwa amejidhihirisha yupo na anatenda miujiza katika maisha ya Mheshimiwa Tundu Antiphas Mughwai Lissu. Yule ambaye mlimtesa, mkampiga

risasi 18, mkakataa kupeleleza nani alifanya hivyo, mkashindwa kumtibu, navyozungumza …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Magereli. . . .

HE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Waziri wa Maji, kwa kazi nzuri aliyoifanya, baada ya malalamiko ya wananchi na wakazi…

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na mchango wangu. Naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kazi nzuri aliyoifanya baada ya malalamiko ya sisi wadau na wakazi wa Kigamboni kuhusu mradi wa visima 20 vya maji vya Kimbiji na Mpera ambavyo hata juzi wakati nauliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Mwita Waitara nilieleza kwamba vile visima havijakamilika, kwa hiyo, Serikali inatudanganya kutuambia kwamba visima vimeshakamilika kinachofanyika ni kutafuta fedha kwa ajili ya usambazaji. Kwa taarifa rasmi zilizotolewa na Serikali juzi nimeona amevunja Bodi ya DUWASA na kuwawajibisha waliohusika wote kwa sababu ya ubadhirifu uliofanywa katika vile visima 20 na kwamba mpaka leo havijakamilika. Kwa hilo, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo na mimi nataka nilizungumzie kwa kina ambalo ni unyanyasaji na matendo yasiyo sawa kwa wafanyabiashara, watu wa sekta binafsi na wawekezaji. Ukitaka kuwekeza Tanzania, unaandamwa na ada, tozo, kodi, ushuru, leseni, na vibali visivyopungua 30. Tunasema tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, tunafikaje huko? Sisi tunaikimbia PPP, hatutaki kufanya miradi ya ushirikiano, wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini kwetu tunawaandama kwa milolongo ya kodi, ada na tozo zisizomithilika, tunafikaje Tanzania ya Viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuwekeza katika kiwanda au katika sekta ya kilimo kwa ujumla, unatakiwa kulipia kibali cha BRELA, TBS, TPRI, TOSC, NEMC, Fire, Bima, OSHA, Zimamoto, TIN/VRN, Leseni ya Biashara, Vibali vya Kusafirisha Mazao, Ushuru wa Kusafirisha Mazao, Usajili wa Mbegu, Mabango, Bodi ya Usajili na Mizani na Vipimo. Ukiwa mwekezaji ukafika nchini ukapewa orodha ya kwamba haya ndiyo matakwa unayotakiwa kukamilisha ndiyo hatimaye usajiliwe na kufanya biashara Tanzania, naamini hata kama ungekuwa ni wewe ungekimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie swali lingine la mipango inayoendelea ya kutaka kuuwa Serikali za Mitaa.

Mipango yote tuliyonayo sasa hivi kiukweli na ukitazama hali halisi ilivyo tunamaanisha tunataka kurudi kwenye Centralization na si Decentralization ambayo ndiyo mfumo ambao tumekuwa tunautumia wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naisu Spika, tumechukua vyanzo vya mapato vyote vya Serikali za Mitaa. Majukumu ambayo yalikuwa yakitekelezwa na Serikali za Mitaa mengi sasa naona yapigiwa upatu kwamba yarudishwe Serikali Kuu. Majukumu kama ya ujenzi wa barabara za vijijini tukaanzisha mamlaka inaitwa TARURA. Leo Serikali za Mitaa zinakwenda kukutana na aina ngumu kabisa ya mateso kwa sababu hata fedha za utekelezaji wa shughuli zake zitatakiwa kuombwa kutoka Serikali Kuu. Mmeshaona kwa miaka miwili hii iliyopita unaomba fedha inachukua muda mrefu sana hata kupatiwa hizo fedha kwa ajili ya matumizi mengineyo ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fahamuni kwamba katika Serikali za Mitaa ndiko kwenye umma mkubwa wa Watanzania na ndiko wanakopata huduma kwa maeneo ya karibu. Sasa tunapofikiri kwamba lazima tupange mlolongo mrefu kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu, nadhani hili ni kosa kubwa tunalolifanya na Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kulirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo nimeliona kwenye bajeti kwamba kuna mpango wa kulinda viwanda vya ndani kwa kuongeza import duty. Mimi nadhani ambacho tunapaswa kufanya si kuongeza import duty kwa bidhaa zinazotoka nje ni kuangalia mazingira yetu yanavyoweza kuwa rafiki ili tuboreshe kilimo chetu lakini tuzalishe kwa wingi tutosheleze soko letu na tuweze kuwahudumia Watanzania bila kufikiri kuwakandamiza watu wengine ambao wanatakiwa kutuhudumiwa ambapo kwa wakati huo hatujaweza kuzalisha hizo bidhaa toshelevu kiasi tunachotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha Kamati na kabla sijasoma maoni hayo niliyoya-quote kisehemu kidogo, niipongeze Kamati ya Bajeti wamefanya kazi nzuri, wamechambua vizuri na wamekuwa honest, wamekuja kwenye Bunge na wamesema ukweli kuhusu wanachokiona kuhusu mwenendo wa bajeti ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 30, Kamati wanasema kwamba, Kamati inajiuliza kuwa upungufu huu mkubwa wa mikopo na misaada kutoka nje unatokana na nini? Naomba nisaidie kuijibu Kamati kwamba upungufu wa misaada na mikopo kutoka nje inaletwa na ukanywagaji wa Katiba katika maeneo ya utawala wa sheria, utawala bora, uhuru wa kupata habari, uhuru wa kujieleza, uchaguzi wa Zanzibar na mauaji ya raia ambayo mpaka sasa hayachunguzwi na hatupati majibu yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kupata nafasi hii kuchangia hoja ya Wizara ya Maji, lakini kabla sijaendelea nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya uzima na uhai na kuwezesha kuwepo ndani ya Bunge hili leo kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, neno “Maji” lina herufi nne tu; (M), (A), (J), (I) lakini nadhani ndiyo Msamiati mgumu sana ndani ya Bunge hili tangu nimeingia mwaka 2015 mwishoni ndilo jambo ambalo limekuwa likileta mjadala mkubwa, mgumu na ambao hauna majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasikitika kueleza masikitiko yangu kwamba suala la maji tufike mahali labda Serikali iseme imeshindwa halafu tuwape private sector huenda tukapata jibu.

Mheshimiwa Spika, Serikali haina vipambele. Tunatekeleza miradi mingi, mikubwa kwa wakati mmoja wakati tunafahamu ya kwamba resources zetu ziko so limited, tunatekeleza miradi midogo midogo mingi sana wakati tunafahamu kabisa kwamba resources zetu ziko limited badala yake tumekuwa na vipande vingi sana vya miradi ya maji ambavyo havikamiliki, havitoi matokeo, visima vinachimbwa haina maji, pamekuwa na Misamiati tu mizuri ya usanifu wa kina, sijui Bodi, hakuna jibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 148 nimeona ametaja suala la mradi wa fedha za India ule wa Miji 29, tunashukuru. Bajeti iliyopita mradi huu ulizungumzwa na kiasi hiki cha fedha kilitajwa na kwamba kingeanza kufanya kazi tangu Bajeti ya 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, ni kwa bahati mbaya sana kwamba mpaka sasa bado fedha hizo hazijaanza kufanyakazi katika miradi ya hiyo Miji 29 iliyotajwa. Lakini naamini bado nia na dhamira ipo kwa sababu ni fedha za mkopo ambazo tutakwenda kuzilipa kwa kodi zetu. Niwasihi Serikali katika utekelezaji wa mradi huu wa Miji 29, naamini walifanya utafiti wa kina kabla ya kuamua ya kwamba ni Mji gani na Mji gani fedha hizi zielekezwe. Basi uwiano wa ugawanyaji wa fedha hizo upelekwe kwa utaratibu kadri ya utafiti ili hatimaye basi angalau kwa mara ya kwanza tupate Miji 29 ambayo inasema sisi sasa hatuna tatizo la maji, limekwisha ili watu wengine wafikiriwe baada ya kuwa mradi huu umekwishakukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mradi huu wa Miji 29 nashukuru nimeuona Mji wa Mugumu nao umetajwa kwa Mama yangu. Umetengwa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kutibu maji katika Bwawa la Manchira. Bwawa la Manchira Mheshimiwa Waziri ni changamoto ya muda mrefu, nimezaliwa pale nimelikuta, nalisikia watoto wanaishai kuogela tu lakini hatimaye miaka mitatu, minne nyuma likaanza kufanyakazi lakini halina ufanisi.

Mheshimiwa Spika, maji yanayotoka pale yanafanana na ile aina ya Togwa tunayokunywa inayoitwa Obhosara. Huwezi kufananisha ya kwamba haya ni maji au hii no Togwa. Kwa hiyo nikushukuru na nitajisikia vizuri ikiwa hizi milioni 200 zitapelekwa na utaratibu wa kutibu maji yale ukafanyika.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la mradi wa maji wa Kimbiji na Mpera; suala hili nimelifuatilia kwa karibu sana kwa kipindi kirefu, nimezungumza na Waziri, nashukuru amekuwa akinipa mrejesho kila nilipofika kuzungumza naye. Leo sikupanga kulizungumzia lakini nilipokwenda kwenye hotuba ya Waziri nikakuta ametaja ya kwamba pale Kimbiji kwenye visima 20, tayari wamekamilisha visima 19 kwenye ukurasa wa 80, hili linanifanya niongee.

Mheshimiwa Spika, katika mradi wa Kimbiji na Mpera, visima vilivyokamilika ni tisa tu. Waziri anaposema kumekamilika visima 19 kwenye hotuba yake anamaanisha kutoa Ujumbe gani? Bajeti ya 2016/2017 tulijadili suala hili, 2017/2018, 2018/2019 na leo ni 2019/2020 bado hoja ya visima vya Kimbiji na Mpera iko kwneye hotuba ya Waziri. Mradi huu umekuwa ukitengewa fedha lakini ufanisi wake umekuwa mdogo na umekwenda pole pole sana sijafahamu ambacho kimetokea.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nakumbuka Mwaka 2017 wakati huo Waziri wa Maji akiwa Mheshimiwa Eng. Lwenge alikuja mpaka pale kwenye mradi wetu wa Kimbiji na deadline ya mradi huu mkataba ulikuwa unakwisa Oktoba, 2017. Mradi haukwisha wakapewa extension mpaka Disemba na wakaambiwa baada ya hapo watalipa penalty za kuchelewesha mradi lakini ninapozungumza mpaka Disemba, 2017 ule mradi haukwisha leo tunazungumza ni Mei, 2019 bado mradi wa maji wa Kimbiji na Mpera haujatupa hata kilometa moja ya mtandao wa maji. (Makofi)

Mhshimiwa Spika, mwaka jana niliuliza swali hili hili wakati huo ni Mheshimiwa Eng. Kamwele nadhani ndiyo alikuwa Waziri. Na yeye alijibu ya kwamba tayari utaratibu wa distribution unaanza lakini bado hata distribution yenyewe haijaanza na kwa maelezo ya Waziri anasema ndiyo kwanza wametangaza tenda za ujenzi wa Matenki kwa ajili ya kuanza distribution. Kwa hiyo mradi huu umemeza fedha nyingi, umechukua muda mrefu kama ilivyo miradi mingine mingi nchi hii ambayo unajikuta kwamba mkataba umetajwa miezi 36, miezi 48 lakini mikata mingi inakwenda ina-extend mpaka miezi 60 mpka 90.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la gharama za juu za uchimbaji wa visima; sijafahamu serikali ina mpango gani baada sasa ya kusuasua kwa uwezo wake wa kuwapatia wananchi maji kuwezesha watu binafsi wanaotaka kuchimba viisma vyao kwa maana ya ku-subsidies aidha ile mitambo au hao watoa huduma wapewe aina fulani ya leave kusaidia kushusha gharama za uchimbaji visima ili watu binafsi nao ambao hawawezi kufikiwa na hii huduma ya Serikali waweze kujipatia huduma za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano halisi ni Mji wa Kigamboni; Mji wa Kigamboni tangu ulipoumbwa haujawahi kuapata mtandao hata wa mita 600 za maji kwa maana ya maji ya Serikali maji ya DUWASA ama nyingine yoyote. Tumeishi miaka yote tukichimba visima wenyewe virefu na vifupi lakini kwenye mkakati ambao niliusikia kwenye ile Sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji namba 11 ya Mwaka 2009 ambayo tulikuwa tumeomba irudishwe Bungeni kwa ajili ya mapitio kwa sababu ina mkanganyiko wa kiutekelezaji ndipo ambapo kuna ile hoja iliyoletwa ya kwamba tutatakiwa kuja kilipia gharama za kumiliki visima binafsi ikiwa tumefanya initiatives ya sisi wenyewe kuchimba vile visima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana mnapokuja kutekeleza suala hili, Mji wa Kigamboni muuangalie kwa sura ya peke yake. Mwenye kisima chake kama mtataka kuanza kum-charge tozo yoyote ya kulipia basi uanze leo usim-charge gharama za nyuma kwa sababau ndiye aliyefanya ubunifu wa kuhakikisha kwamba anajipatia huduma ya maji ambayo Serikali haikuweza kumpa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ucheleweshwaji wa kukamilika kwa miradi ya maji; ni kwa bahari mbaya sana miradi mingi imekuwa na extensions za utekelezaji wa mikataba kwa hiyo hata thamani za miradi zinakuwa zinabadilika badilika kila mara wakati ambapo fedha za Wananchi zinaendelea kutumika kwa wingi na matokeo hayaonekani.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la usanifu unafanyika kabla ya kupata fedha; miradi mingi ya maji imekuwa ikifanyiwa usanifu sijui na upembuzi n.k wakati Serikali bado haina fedha. Kwa hiyo jukumu lile la usanifu linakamilika halafu Serikali haina fedha, badala yake inapofika ule muda sasa kwamba Serikali imepata fedha, ule mradi unakuwa hauna thamani ile ile na kwa jinsi hiyo kukuta kama miradi inakuwa inafanyiwa mipango ambayo inashindwa kutekelezeka kwa utaratibu ambao unakubalika kwa sababu ya kuwa muda umekwishakupita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la Taasisi za Serikali ambazo hazilipi ankara za maji. Sifahamu tatafanya nini, kwa sababu kama Serikali kama Wizara ya Maji inasimama leo Bungeni inalalamika katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba kuna taasisi za Serikali; siyo kuna, mimi nahisi taasisi za Serikali zote hazilipi ankara za maji. Kama ndivyo, je, kuna haja ya kuleta hoja Bungeni ya kwamba taasisi hizi zifutiwe kabisa basi utaratibu wa kulipa ankara za maji ili tujue kwamba sio wadeni, hata tunapopanga bajeti zetu, tusifikirie zile fedha za ankara zinazotokana na Taasisi za Serikali?

Mheshimiwa Spika, naomba kwa utaratibu maalum, kama Serikali ingeweza kuangalia shule zetu, wakahakikisha shule zote zinapatiwa huduma ya maji, ingekuwa vizuri. Kwa sababu fikiria watoto wa kike wanapotumia vyoo vya kawaida vya shimo katika mazingira ambayo hakuna maji wala hakuna toilet paper, suala la hygiene yao limebaki kuwa kitendawili. Labda hawa wangeweza kupewa maji na wakawa exempted, tungeweza kuliunga mkono vizuri suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la mabwawa ya kimkakati. Nasikitika kuona kwamba Bwawa la Kidunda Morogoro limetajwa tena leo na likiitwa bwawa la kimkakati. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Magereli, muda hauko upande wako.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, one minutes. Dakika moja ya kwako Mheshimiwa.

SPIKA: Unga mkono hoja. (Kicheko)

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muda huu. Mungu akubariki. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuchangia. Naomba nianze kwa kueleza tatizo la kwanza kabisa la nchi hii kwamba ni matatizo yanayohusiana na sera na mipango. Tuna changamoto ya kupanga nini tunataka, tuna changamoto ya kuamua nini tutekeleze na tunapoamua kutekeleza basi ni kwa manufaa ya nani na kwa kipindi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali tuwe waangalifu sana nini tunapanga, nini tunatekeleza, kwa wakati gani na kwa maslahi ya nani. Tuangalie mipango yetu ya maendeleo na vipaumbele tuvipange kadri tunavyoweza kutekeleza. Tumekuwa na vipaumbele vingi kuliko uwezo wetu wa kutekeleza, badala yake tunakuwa na orodha ndefu sana ya miradi ambayo hatuwezi kui-fund, tunatumia mikopo kutoka nje, pesa zinaingia kwenye miradi mikubwa, hiyo miradi haikamiliki, haiondoki ilipo wala haitunufaishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri ni huu wa Bandari ya Bagamoyo ambayo watu wengi wameizungumzia, ukurasa wa 99. Ziko kazi nyingi sana ambazo zimeshafanyika pale na pesa nyingi sana za walipa kodi zimeingia pale, leo yanakuja maelezo mepesi kweli kweli yanayosema eti wameshindwa kuelewana majadiliano na wawekezaji, ukurasa wa 99, naomba ninukuu inasema:

“Mradi umeshindwa kwa sababu wawekezaji hao kuweka masharti yasiyokuwa na maslahi kwa Taifa, masharti hayo ni pamoja na wawekezaji hao kudai kuachiwa jukumu la kupanga viwango vya tozo na kutoruhusu wawekezaji wengine katika eneo la kati ya Bagamoyo na Tanga.”

Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ambayo yangeweza kujadiliwa, haya ni maelezo ya kitoto kabisa kwamba eti tumeahirisha utekelezaji wa mradi wa Bagamoyo kwa sababu eti wawekezaji wameweka masharti, hatuna wataalam wa kujadili mambo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nishangae pia kwamba sasa Serikali inarudi kushika hatamu za huduma za kimiundombinu wakati ni kati ya eneo ambalo lingeweza kuvutia wawekezaji na ni miradi ambayo ingeweza kutekelezwa kwa mfumo kama alivyosema Mheshimiwa Turky hapa aidha wa hisa ama kupata wadau na wachangiaji wengine katika maeneo hayo ili kuboresha huduma zetu za kimiundombinu ili moja, tuweze kutanuka, lakini pili, tutoe huduma, tatu, tuweze kutoa ajira. Kwa nini Serikali sasa ndiyo mmiliki wa SGR, ndege za Serikali, Serikali ndiye sasa hivi mjenga Stiegler’s Gorge, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye danadana za ATCL. Mwaka jana nilisimama nikashauri, nikasema miaka michache ijayo of course nilitaja mitano, nafurahi kwamba hata hatufiki mitano tunakaa tena hapa leo kujadiliana namna ambavyo ATCL haisaidii nchi hii, haipigi hatua na imeshindwa kabisa ku-perform. Nilishauri kwamba tuanze kwanza na kuimarisha mtandao wa ndani wa ndege, mpaka sasa hivi hatua zilizochukuliwa ni dhaifu mno. Tunang’ang’ana kufikiria kwenda Uchina kuchukua abiria katika mipango ambayo siyo ya kudumu, si endelevu na wala haitaisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndege ambazo tumezinunua tulizinunua kwa maana ya lengo la kufufua ATCL, lakini kwa bahati mbaya hizo ndege zilipewa Wakala wa Serikali na sasa hivi tunavyozungumza kwa bahati mbaya nyingine tena, ndege hizo zimehamishiwa Ikulu. Sasa sielewi kwamba Ikulu imedhamiria kufanya biashara na bahati mbaya nyingine zaidi ni kwamba bado suala la ndege za Serikali tunazipa fedha kupitia bajeti ya Vote 62 lakini zinakwenda kuhudumiwa na Vote 20; pana kizungumkuti hapo tunaomba Waziri mhusika atatusaidia kuchambua jambo hilo ni kitu gani.

Mheshimiwa Spika, nirudi Dar es Salaam; suala la msongamano wa Dar es Salaam ni mkubwa, imekuwa shida na tabu. Sasa hivi Dar es Salaam mvua inanyesha ninyi nyote ni mashahidi, ule mji hautembei. Mradi wa mwendokasi tuliofikiria kwamba ungetupa suluhisho nao umekuwa shida, umekuwa tatizo sugu; mwendokasi hau-perform, lakini kibaya kuliko vyote kumekuwa na changamoto ya ununuzi na uuzaji wa tiketi. Scanner za pale hazifanyi kazi kwa hiyo, pesa zinatolewa na kuhifadhiwa kiholela na sijui zinakuwa reported namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine kibaya kuliko vyote, sasa hivi pale kwenye mradi wa mwendokasi hakuna chenji, ukidai chenji ya 200, 150 hupati. Kwa hiyo, kuna makusanyo mengine ya mapato yamezaliwa pale katika mradi wa mwendokasi na kuwanyang’anya wananchi na abiria wa Dar es Salaam fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ujenzi wa gati na maegesho eneo la abiria Ferry ya Kigamboni. Mwaka 2016/ 2017 na mwaka 2017/2018 tuliizungumza, tukalipangia fedha na 2018/2019 vilevile, lakini mpaka ninavyozungumza hadi leo pale Ferry ya Kigamboni hakuna kinachoendelea, abiria wetu bado wanarundikana kama mizigo, utaratibu wa huduma kama vyoo na huduma nyingine pale bado haujakamilika, utaratibu wa utoaji magari ndani ya vivuko na kuondosha eneo la ferry na kuingia bado ni changamoto.

Mheshimiwa Spika, kibaya kingine sawa kama ilivyo kwenye mwendokasi na zile scanner za tiketi pale ferry nazo hazifanyi kazi, kwa hiyo, sasa hivi tiketi unanunua inapita bure ikiwezekana yule anayekusanya akaamua kuzirudisha tena kule zikauzwa upya, zinauzwa upya; hicho ni chanzo kingine cha wizi wa fedha za Watanzania kupitia ule mradi wa malipo ya ferry pale Kigamboni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Mwaka 2016/2017 tuliwapa jumla ya asilimia 40.3 ya fedha zote za maendeleo sawa na shilingi trilioni 11.8, mwaka 2017/2018 tumewapa asilimia 40.8, mwaka 2018/2019 tumewapa asilimia 34.8, lakini bado unaweza kuona kabisa kwamba Wizara hii haijaleta matokeo tarajiwa ukilinganisha na kiasi cha bajeti kubwa ya maendeleo tunayowapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante ingawa nilikuwa na dakika kumi, umenipa pungufu ya hapo. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba nianze mchango wangu kwa kuipongeza Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, lakini sana sana Mwenyekiti wetu kwa uwasilishaji alioufanya leo ambapo ameleta kitu cha pekee kabisa, ameeleza na mafanikio na shughuli zilizofanywa na Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nisaidie kushangaa na katika kushangaa kwangu mnisaidie na ninyi kushangaa; na tukishashangaa, Maazimio ya Kamati yetu yaweze kuchukuliwa na kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, nina swali la kuuliza, hivi ni kwa nini kilimo au Wizara ya Kilimo isiwe Wizara kipaumbele? Ni kwa nini bajeti ya Wizara ya Kilimo inatolewa kwa shida sana? Kwa nini mpaka leo pembejeo ni shida sana? Kwa nini mpaka leo hatuwezi hata kujitosheleza kwa mbegu tu kwa ajili ya uzalishaji wa kilimo? Kila siku tunazungumza tunasema, kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa, kilimo kinaajiri Watanzani wengi, lakini tunayoyafanya kwenye kilimo haya- reflect huo ukweli tunaoujadili kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo ambayo inabidi tu tufike mahali tuyachukulie very serious. Bajeti ya kilimo mpaka leo, kuanzia baada ya yale niliyowaambia mnisaidie kushangaa halafu tuchukue hatua pamoja; Bajeti ya kilimo sasa itengwe ya kutosha halafu wapewe fedha yote kama ilivyoidhinishwa na Bunge. Tuepushe mambo ya mazao yetu kuozea shambani, tuepushe maziwa ya akina mama kuozea huko mashambani wanakoyakamua, twende na mkakati madhubuti wa kuandaa utaratibu ambao mazao ya kilimo yatakuwa processed, moja kwa ajili ya soko la ndani lakini ikiwezekana iwe na kwa ajili ya soko la nje.

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea Wizarani, kwa sasa kuna mapitio ya Sera ya Kilimo. Naomba nilete mapendekezo yangu. Kuna suala la kilimo hai, kilimo mseto na kilimo hifadhi. Hili Mheshimiwa Mama Ishengoma amelizungumzia vizuri kwa upana, dakika zangu ni tano tu. Naomba lipokelewe, liingizwe katika sera na litajwe kwenye Sera ya Kilimo kwa kuwa asilimia 96 ya wakulima wa nchi hii ni wakulima wadogo. Kilimo hai, mseto na hifadhi ni kilimo ambacho tukiki-adopt kwa hao wakulima wadogo (peasants) tutamudu kuzalisha zaidi, kutunza ardhi yetu, kuhifadhi rutuba na kulinda mazingira.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la mazao ya kilimo na mboga mboga. Unaweza kuona mwenyewe; sasa hivi mazao yetu ya biashara, korosho, kahawa, chai, pamba, yote tunazidi kuserereka kuelekea negative. Basi wakati tukiangalia nini kimetukuta huko, naomba tuhamie kwenye suala la kilimo cha matunda, mboga mboga na maua. Bahati nzuri hiki ni kati ya kilimo ambacho kinaweza kulimwa pia katika ule mfumo wa kilimo hai, hifadhi na mseto, kwa sababu mazao organic yanayozalishwa katika mfumo huo yanapata soko zuri sana kwa nchi za Ulaya kwa maana yanapokuwa exported.

Mheshimiwa Spika, sasa wakati tunajadili kwa nini korosho inatusumbua, kwa nini pamba imeshindwa kununuliwa msimu huu; na bahati nzuri kilimo cha matunda na mboga mboga ni watu private wanafanya; Serikali haijawekeza huko wala hakuna ambacho kimeshafanyika kwa niaba ya Serikai kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, sasa kati ya mambo ambayo ni kikwazo kikubwa sana kwenye suala la kilimo cha matunda na mboga mboga ni hizi kodi na tozo. Nina orodha ukurasa wa 11 wa Ripoti ya Kamati mnaweza kuona. Pana tozo na kodi zaidi ya 45. Nilitamani niwasomee, lakini dakika zangu ni tano. Kwakweli katika mazingira haya, maana yake tunawavunja moyo na tuna-discourage aina hii ya kilimo ambacho ni muhimu sana kwa ajili ya maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye suala la mifugo, kwa maana ya Wizara ya Mifugo. Tulipata bahati kama Kamati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika tano zimekwishapita. Ahsante sana kwa mchango wako Mheshimiwa Lucy.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nianze kwa kumshukuru mwenyezi mMungu muumba wa Mbingu na ardhi aliyetujaalia uzima wa kuwepo ndani ya nyumba hii, kujaribu kusema kwa niaba ya Watanzania, kushauri na kuwasaidia wenzetu wa Serikali kuona pale ambapo macho yao hayajaweza kufika au kuona yale ambayo wameyatazama katika namna ambayo Watanzania wengi hawayatazami.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamechangia na bahati nzuri leo tunakaribia mwisho wa bajeti ya Serikali, wamezungumza mambo mengi kuhusu sekta ambazo zinaajiri Watanzania wengi na namna ambavyo hazijatazamwa. Hata hivyo mimi leo nataka nianze kwa kuwazungumzia ndugu zangu wengine ambao wanachangia sana ustawi wa nchi hii lakini hawapewi kipaumbele, watu hao ni waandishi wa habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninyi ni mashahidi wote kwamba bila waandishi wa habari nchi hii ingelikuwa iko gizani. Ninyi kama watu wa Serikali mnajua kabisa namna ambavyo mnaongozana nao masaa 24 ili yale mnayoyatekeleza yawafikie wananchi, lakini mpaka leo maslahi ya waandishi wa habari ambao wanasaidia na kuchangia maendeleo na upashanaji wa habari mikataba yao ya ajira na maslahi bado ni duni sana. Bahati mbaya Waziri wa Habari hayupo lakini Naibu Waziri yupo, hebu rudini Wizarani mkaangalie namna ambavyo mnaweza mkasaidia tasnia ya habari muwasaidie ndugu zetu wanaotoa mchango wao nao wafaidi na wajisikie Watanzania ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la usiri ambao unalinyonya Taifa. Mwaka 2017 tulipitisha sheria ya ulinzi wa rasilimali za nchi. Sheria hiyo ililetwa Bungeni kwa mbwembwe, tena ikajadiliwa ndani ya muda mfupi, ikapitishwa, ikaungwa mkono kwa nguvu. Hata hivyo hatimaye mpaka leo ninavyozungumza bado kuna usiri mkubwa sana katika mambo yanayohusu leseni, mikataba na malipo ya Serikali yanayotokana na madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulijua ya kwamba sheria ile ilipopitishwa basi ilikuwa ndio mwarobaini na chanzo cha ulinzi wa rasilimali zetu, na ya kwamba katika katika kifungu cha 12 cha Sheria ya Milki ya Kudumu ya Utajiri na Rasilimali za Asili ya mwaka 2017; katika kifungu kile kinaruhusu ya kwamba mikataba yote inayohusu maliasili na madini na utajiri wa nchi hii kuletwa na kujadiliwa Bungeni lakini mpaka tunavyozungumza leo mikataba hiyo haijawahi kuja na hata hakuna dalili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri wetu, hiki ndicho kati ya vyanzo vya uhakika kabisa vya mapato, lakini hatujapata fursa ya kujadili na kuona ya kwamba Serikali inapata kiasi gani katika mirahaba na mambo mengine yanayohusiana na maliasili na utajiri wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la viwanda. Katika ukurasa wa 31 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ameelezea vizuri mipango yake. Nilipoanza nilisema nitakusaidia kuona pale ambako haujaona. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hatuwezi kujenga viwanda wala hatuwezi kushindana na nchi zinazochipukia kiuchumi kwa mkakati huu tulionao. Tumekiacha kilimo nyuma sana, lakini hata viwanda vyenyewe bajeti kiduchu tunayowapatia haiwezi kuwasaidia kutoka walipo.

Mheshimiwa Mwenyekti, mfano halisi ni bajeti ya mwaka 2018/2019 ambapo waliidhinishiwa shilingi 90 bilioni lakini wakapewa shilingi bilioni 5.4 tu ambayo ni asilimia sita. Mnazungumza habari ya uchumi wa viwanda wa nchi hii utokee wapi kwa asilimia sita ya fedha ya maendeleo unaotolewa? Namwelewa sana Mheshimiwa Mwijage na kilichomkuta, kwa sababu kwa asilimia sita unafanya nini? Bora utumbuliwe ukae benchi kama alivyo leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kuuliza swali; tunazungumzia Tanzania ya viwanda na uchumi wa viwanda; hivi ni nani katika nchi hii leo anayehangaika na kuangalia manpower, labour force, aina ya ajira na kazi tunazozizalisha kwenye vyuo vyetu ambavyo hatimaye vitakwenda kuchangia kuwa rasilimali watu katika Tanzania ya viwanda? Hatushughuliki na hilo kabisa. Vyuo vya VETA vinasuasua, havina fedha havina utaratibu, hata na mitaala yao nayo ni ya kuungaunga wanafundisha mapishi, wanafundisha vitu ambavyo kwa kweli tukizungumza Tanzania ya Viwanda bado mkakati wetu hauwezi kutufikisha tunapotaka kwenda

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala lingine la miradi mikubwa ambayo inasifiwa sana hapa ndani, ya Stiegler’s Gorge, SGR na vinginevyo. Kuna namna ambavyo hii miradi inakwenda kuifilisi nchi na tunakwenda kuibiwa mno kupitia hii miradi mikubwa. Nimesema leo nitawaambia yale ambayo hamja yaona. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Miundombinu hawa wawekezaji ni wajanja sana, wanatuletea BOQ ambazo zina specification za vifaa ambavyo hapa kwetu havipatikani. Nasi kwa sababu tunaharakia tunatafuta 10 percent tunasaini mikataba haraka wanachukua kazi. Mnajua kabisa ya kwamba sisi hatuwezi kujenga na hiyo Stiegler’s Gorge. Reli yetu tukijenga pesa zinakwenda nje, Stiegler’s Gorge pesa zinakwenda nje, upanuzi wa viwanja vya ndege pesa zote zinakwenda nje, ndege tunazonunua pesa zinakwenda nje. Kwa hiyo hii miradi mnaposimama na kuisifia fikirini ya kwamba Tanzania yenyewe inanufaika namna gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, na bahati mbaya sana hii ni miradi ambayo haina ile inaitwa high rate of return siyo miradi ambayo inakwenda kurudisha ile fedha yetu haraka ni miradi ambayo itachukua muda mrefu sana, na pesa zote zinakwenda nje. On top of that fedha tunayojengea hiyo miradi tunakopa kutoka nje na hatima yake hata tukianza kuzalisha au kutokana na kuwakamua wananchi wetu tutawalipa tena watu wale wale ambao waliojenga ile miradi. Kwa hiyo mimi naiita miradi ambayo inaiibia taifa na kututia hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la ujasusi wa kiuchumi. Unajua kuna jambo ambalo tukijaribu kuliangalia nashangaa sisi hatuwezi kuyaona kama ambavyo wanayaona wengine. Matajiri katika maeneo mengine wanapewa fursa za kuwa matajiri zaidi ili walipe kodi na wazalishe ajira lakini huku kwetu sisi tunataka wawe mashetani. Jama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa maelezo mafupi juu ya masuala mawili ambayo ni kero katika utendaji wa watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Moja ni hili la Wizara kuongeza maeneo ya hifadhi kwa kutwaa ardhi ya wananchi bila kufuata utaratibu. Binafsi suala hili naliona ni suala la kiuonevu sana kwa wananchi wa vijijini. Inasikitisha sana kuona sasa wanyamapori wanapewa kipaumbele na thamani kubwa kuliko wanadamu/raia wa nchi hii.

Mheshiwiwa Spika, suala la pili, ni mahusiano mabaya baina ya wahifadhi, wananchi na wafugaji wanaoishi jirani na mbuga. Sote ni mashahidi kuwa hali ya malisho ya mifugo ni changamoto kubwa kwa wafugaji wa Tanzania na Wizara ya Mifugo haijafanya jitihada kidhi kusaidia wafugaji kuzalisha malisho ya kutosha.

Suala la askari wanyamapori kukamata, kuswaga na kushikilia mifugo ya wafugaji katika hifadhi, kuwapiga risasi na kuwaua ng’ombe wanaowashikilia ni suala la kifedhuli na dhuluma. Askari wenu hufikia maamuzi hayo ya kukamata ng’ombe kwa misingi ya rushwa kuliko uhalisia. Mifugo ni maisha ya wafugaji. Unaposwaga na kushikilia mifugo ya wafugaji, kuiua na kuitelekeza bila huruma ni kuwafilisi na kuwatia umaskini wafugaji. Naomba Serikali itazame upya mambo haya ili kupunguza kero kwa wananchi na kuboresha mahusiano baina ya uhifadhi na wananchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za mifumo ya elimu ya Tanzania limekuwa tatizo sugu ambalo sasa ni bayana kwamba tunahitaji mbinu tofauti, nyenzo tofauti na mikakati tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali haijaamua kutafiti kwa kina kujua nini hasa hitaji la Watanzania kuhusu elimu itakayokidhi. Kipaumbele cha kibajeti kwenda Wizara ya Elimu na Taasisi ya Utafiti ya COSTECH kimekuwa dhaifu na kisichokidhi haja kwa miaka mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala yetu inabadilishwa kila siku/kila mara na hivyo kuondoa consistency ya mitaala kwa Walimu na wanafunzi. Hata hivyo, kutowashirikisha Walimu katika suala la uandaaji mitaala, inaondoa ownership na vionjo na mahitaji muhimu ya ufundishaji na kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016, Serikali ilifanya jitihada kubwa kuhakikisha shule zetu zote nchini zinapata madawati ya kutosha. Ni bahati mbaya sana kuwa kuna shule katika Jiji la Dar es Salaam, licha ya kuwa na msongamano wa wanafunzi madarasani, hazina kabisa madawati. Mfano halisi ni Shule ya Msingi Toangoma iliyoko Kigamboni ambayo ina watoto 540 ambao wanakaa chini. Hili ni jambo la aibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya elimu vinavyotolewa katika hatua mbalimbali za ukuaji kielimu. Watoto wetu katika shule za msingi wanaosoma katika mazingira dhaifu sana ikiwemo ukosefu wa vitabu vya ziada na kiada, ukosefu wa huduma za maji, umeme na madarasa ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wa hisabati na sayansi, bado ni changamoto. Idadi ya shule imeongezeka wakati hakuna maandalizi kidhi ya Walimu wa kutosha. Tunawaza kuwa Tanzania ya viwanda, lakini ikiwa hakuna Walimu wa kuandaa watoto wetu. Maslahi ya Walimu nayo bado ni kilio kikubwa kiasi kwamba Walimu waliopo kazini wamevunjika moyo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu kubwa, elimu yetu imekuwa ikitolewa kwa nadharia. Elimu muhimu ni elimu kwa vitendo. Tuboreshe maabara, vyuo vya ufundi viongezwe na mazoezi kwa vitendo yawe sehemu kubwa ya mtaala ili mambo yanayofundishwa yaweze kukaa na kudumu katika fikra za wanafunzi wetu kadri wanavyokua na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuhamisha Walimu wa Sekondari kurudi kuwa Walimu wa shule za msingi, halikuwa jambo la busara na tumewapeleka kama watu waliodharauliwa na kushushwa thamani na hivyo kutokuwa na moyo wa kufundisha. Kwa hiyo tujue hatujatatua tatizo, tumeliongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kupata fursa ya kuchangia hoja hii ya Muswada wa Maji. Kabla sijaendelea, naomba nipongeze kazi kubwa iliyofanywa na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa. Vile vile nashukuru sana ushirikiano mzuri tuliopewa na Serikali walipokuja katika majadiliano tulikuwa na vitu moto kweli kweli, lakini tunashukuru kwamba katika maeneo mengi tulifika mahali tukakubaliana. Hasa kitu ambacho kwangu kilikuwa kipaumbele kikubwa na ambacho nadhani nitakizungumzia leo ni suala la utunzaji wa mazingira kwa maana ya sanitation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sanitation limeachwa kabisa kwa maeneo mengi sana linapokuja suala la huduma za maji. Limekuwa kama ni kitu kinakuwa attached tu, yaani kinawekwa kiwepo, lakini unapokuja kwenye hoja za msingi na vifungu maalum kwenye kutazama especially kwenye funding, ukikuta wanapozungumzia habari ya kutoa huduma, yaani usambazaji wa maji, wanazungumzia usambazaji wa maji tu, hawazungumzii habari ya huduma za majitaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi, wengi mnakaa hapa Dodoma mnaona changamoto tunayoipata kwa mfano kuhusu majitaka. Yaani ni kitu kimekuwa taabu kweli kweli na mifumo kwa bahati haipo, mji unakua. Kwa hiyo, nawashukuru sana Wizara kwa kulitazama hili na kukubali kuliingiza katika Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri jambo la msingi kwamba tunahitaji sera inayojitegemea ya huduma za majitaka (sanitation). Tusipofanya suala hili, naamini kwamba litaendelea kubaki kuwa attached kwa sababu bahati mbaya suala lenyewe lina bahati mbaya kwamba lina-appear kwenye maeneo mengi. Lina-appear kwenye Wizara ya Afya, Wizara ya Mazingira, Wizara ya Maji na TAMISEMI. Kwa hiyo, limeonekana kama suala lisilokuwa na mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kwa kutoa maelezo mengine kwamba nilikuwa nafikiri haya ni maoni yangu binafsi na naomba niyatoe. Nafikiri suluhisho la shida ya maji vijijini siyo kuwa na RUWASA. Tumekuwa na mlundikano mkubwa wa mamlaka, taasisi, vyombo, bodi nyingi tu ambazo zote zinashughulika na maji. Tuna Wizara yenyewe, tuna hizo mamlaka za watumaji wadogo wa maji, tuna EWURA, tuna mamlaka za maji mijini, wote tunafanya suala lile lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri suala ni kusaidia namna ambavyo tungeweza kutumia mamlaka tulizonazo tukazi-equip lakini tukazipa fedha na man power na zikasimamiwa. Kwa sababu mnajua mpaka sasa hivi kuna miradi mingi sana ya maji inaendelea ambayo imekwama haijulikani mwanzo wala mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa naongea na Mheshimiwa Kitila nikamwambia mama yangu hana maji kule, tena anakaa mjini basi, hana maji kwa wiki mbili sasa. Mradi wa Bwawa la Manchira kilichotokea sijakifahamu mpaka kesho, lakini Mji wa Mugumu mpaka leo hauna maji. Nilipozungumza naye ananiambia iko program, ule mradi wa fedha za India. Kwa hiyo, unaona kabisa kuna mipango inakuwa inaendelea upande mwingine na tunatazama mipango mingine. Ukiangalia kwa mfano RUWASA haina its own source of funding, inategemea Serikali. Hivi vyombo vyote nilivyovitaja COWUSO, RUWA, EWURA, Mamlaka za Maji, DDCA, Mfuko wa Maji, vyote vinategemea Serikali. Sasa unaona kabisa inafikia mahali hata hiyo fedha inayotengwa na Serikali kwa ajili ya kutoa huduma za maji inakuwa haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri ambacho tungeweza kufanikiwa zaidi siyo kutengeneza RUWASA lakini kuviimarisha vile vyombo tulivyonavyo vitoe huduma zinazostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukienda kwenye majukumu ya DDCA yanafanana copyright na majukumu ya hii RUWASA tunayoiunda leo. Sasa je, zitakapoanza utekelezaji kwa sababu DDCA tayari ipo na mnajua kabisa kwamba ni kati ya vyombo ambavyo vinasuasua kabisa katika utekelezajiwa majukumu yake; je, tunataka kupata matokeo gani tofauti ambayo yameshindwa kufanyika na DDCA na sasa tunafikiri kwamba tutakapokuja na RUWASA mambo yatabadilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika kwamba kwenye Muswada huu pia haujazungumzia kabisa; nadhani umezungumzia au hujazungumzia, lakini suala la sekta binafsi lilikuwa ni suala ambalo tulihitaji kutazama kwa jicho la tatu. Tunao wadau wetu wengi sana katika maeneo yetu ambao wamefanya miradi ya maji na wapo ambao wapo interested kufanya miradi ya maji, lakini Muswada haujawatambua, wala haujatoa nafasi ya kuona namna ambavyo sekta binafsi inaweza kuchangia katika kusaidia wananchi wetu kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho nimesikitishwa nacho zaidi ni suala la penalties. Adhabu zilizowekwa kama walivyosema wenzangu ni kubwa, lakini nizungumzie maalum kwenye zile adhabu ambazo zimetolewa kwa mujibu wa section 66, kwamba mtu hata akikutwa ananawa miguu katika bomba la maji adhabu yake imepangwa kuwa shilingi 50,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza maji mpaka leo tunapozungumza maji ni adimu sana. Kwa jinsi hiyo maeneo mengi hayapati maji. Nilifikiri ambacho tungefanya ni kuzisaidia na kupeleka mamlaka kubwa kwenye zile mamlaka za watumiaji maji vijijini, wao ndio wajitengenezee regulations za namna ya kujisimamia na namna ya kupeana adhabu wao kwa mujibu wa sheria ambazo watajitungia kuliko kutengeneza sheria moja kwa mjoja na adhabu ambayo imekuwa specified kutokea huku, kitu ambacho kitakwenda kutoa adhabu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kweli kama mama anayefua nguo za mwanaye ametoka Clinic na kadhalika ukamwambia ametumia maji visivyo au amefua pembeni ya mto au pembeni ya bwawa ama namna nyingine ukampa adhabu hiyo, nadhani adhabu hizo ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwa mamlaka za watumia maji wajitengenezee utaratibu wao wenyewe, wana uwezo wa kujisimamia. Kwa sababu failure to that, kama tukitaka mamlaka haya yaje Serikali Kuu kama tunavyotengeneza kwenye Muswada huu, maana yake itabidi kuajiri Polisi na watu wengine wa kusimamia na kufanya usimamizi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kuzungumzia pia suala la The Water Resource Management Act ile ya 2009. Tulikuwa na mjadala huu kwenye Kamati yetu na tuliomba sana kwamba Serikali iangalie kwa makini suala hili iulete huu Muswada Bungeni tuujadili. Muswada huo na huu Muswada wa Water Supply and Sanitation Act, 2018 vinawiana na kuingiliana katika mambo mengi sana na kuna mambo mengine ambayo yana-contradict kwa sehemu kubwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana niwaombe Serikali, katika hatua inayofuata wakati wowote utakapoona inafaa, tunaomba Muswada wa Water Resources Management Act uletwe Bungeni tuujadili kwa sababu una issues nyingi sana zinazohusu vibali na tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hivyo vibali na utaratibu wenyewe wa kuvipata na namna ya tozo zilivyowekwa na adhabu zilizoambatana kwa kweli hatutafikia haya malengo tunayotaka ya kuwapa Watanzania maji ya kutosha mijini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muswada huo, unaozungumzia wa Sheria ya 2009 kwa mfano, nitolee mfano, Wilaya ya Kigamboni, sisi hatuna supply ya maji kabisa ya haya mabomba, watu wa Kigamboni wote tumejichimbia visima, tunatumia maji ya visima. Sasa kumetokea hili suala la kuanza kufuatilia habari za Sheria hiyo ya Water Resource Management ya 2009 ambapo kila mtu aliyejichimbia kisima anatakiwa kuwa na kibali lakini kuna fees ambazo unatakiwa kulipa. Serikali inapokuwa kuliangalia na inafanya utekelezaji wa suala hili, naomba itazame kwamba wako Wadau Binafsi ambao tayari kwa Serikali kushindwa kuwapa huduma ya maji, walishaamua na kutengeneza mifumo yao wenyewe ya kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuwe na leeway namna ya kuwapa relief fulani kwa sababu tayari wameshafanya initiative za kutafuta maji yao wenyewe ambao tulitarajia kwamba Serikali ingewa-subside badala ya kuwa-penalise lakini bahati mbaya naona kwamba mnawa-penalise.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho ni kwamba, naishauri Serikali ipokee na isikilize na ifanyie kazi maoni yote yaliyotolewa na Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa sababu tulikuwa na mjadala uliotoshelevu kabisa na tunategemea ya kwamba maoni ya Kamati yatakwenda kutoa mchango mzuri sana kwenye kuboresha Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote, nirudi kwenye jambo la akinamama; shida ya maji kama walivyozungumza wenzangu ni suala ambalo kwa sehemu kubwa sana, hasa vijijini, yanawalenga akinamama, sasa mimi leo, labda nitoe proposal yangu kwamba, hivi Mheshimiwa Rais anaonaje siku moja hapo mbele, Mheshimiwa Mbarawa, simaanishi kukitaka Kiti chake, lakini anaonaje siku moja amteue Waziri akiwa mwanamke na Naibu Waziri wake awe mwanamke na Katibu Mkuu awe mwanamke muone ambavyo Tanzania itapata maji ya kutosha kwa sababu wao wanaujua uchungu na maumivu ya kutafuta maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. (Makofi)