Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka (14 total)

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa madaraja haya jinsi yalivyojengwa, kipindi cha mvua huwa ni kero kubwa kiasi kwamba mawasiliano yanakatika kabisa pamoja na kwamba madaraja yapo watu wanashindwa kuja mjini, wanashindwa kwenda vijijini; na kwa kuwa tunafahamu kwamba uchumi unategemea sana barabara na barabara zinaunganishwa na madaraja; na kwa kuwa maeneo hayo ya Jimbo ndiyo maeneo yenye uchumi mzuri kwa maana yanapata mvua za kutosha na mazao yake ni ya kuaminika.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuyajenga madaraja haya katika kiwango cha kuyafanya yapitike hata wakati wa mvua ili Wilaya iweze kupata mapato na uchumi kipindi chote na watu kuondolewa kero za kusafiri wakati wa mvua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Makanyaga kwa namna alivyoitikia wito wetu wa kuingia kwa umakini kuhusiana na matatizo haya ya madaraja mawili. Kwa taarifa tulizonazo kupitia TANROADS Mkoa, madaraja haya yanapitika isipokuwa kwa mwaka huu, mvua ilikuwa nyingi sana na siltation iliziba, maji yakawa yanapita juu ya daraja. Tunaamini hali ya mvua ya mwaka huu ambayo haikuwa ya kawaida pengine miaka ijayo hali haitakuwa hivyo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tutahakikisha TANROADS Mkoa wanaendelea kuyaangalia haya madaraja na wakiona kuna umuhimu wa kuyapandisha, kuyaondoa, kuyapanua na kuyageuza ili tulete daraja tofauti na zaidi ya hii vented drift kupitia Road Board ya Mkoa, mapendekezo hayo yatapitiwa na hatimaye Serikali itaangalia namna ya kuyashughulikia. Kwa taarifa ya Road Board Mkoa pamoja na TANROADS Mkoa, mazingira ya madaraja hayo ambayo tumeyatengeneza mwaka jana tu na mwaka juzi yanatosheleza kwa mazingira ya kiuchumi yalivyo sasa katika hilo eneo.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na naamini kwamba haya yaliyozungumzwa yote yataenda kutekelezwa. Naomba kuongeza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa, Vijiji vingi vya Jimbo langu ni vikubwa sana na kwa kuwa, umeme huu wa REA umekuwa ukifikishwa kwenye maeneo ya kati ya vijiji tu. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuusogeza umeme huu sasa kwenye vitongoji vilivyo mbali na maeneo ya kati ya vijiji ili wananchi hao katika vitongoji hivyo nao waweze kunufaika na umeme huu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, namshukuru sana Mheshimiwa Makanyaga kwanza kwa kuuliza swali hili.
Kwa kuwakumbusha tu, ni kweli kabisa kwa awamu ya II tumepeleka kwenye vituo, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Chilonwa kwamba awamu ya III inapeleka sasa kwenye vitongoji na kwenye vijiji vyote na kwenye mashine na kwenye taasisi za jamii ikiwemo shule. Nimhakikishie hata Kijiji chake Mheshimiwa Chilonwa cha Chalinze sasa kitapata umeme, Kijiji chake cha Kawawa kitapata umeme, Kijiji cha Malichela kitapata umeme, Kijiji cha Membe kitapata umeme, Kijiji cha Bwawani nacho kitapata umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie kuwa vijiji vyote vitapata umeme.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini niweke wazi tu kwamba vijiji vilivyofaidika mpaka sasa ni vijiji vitatu ambavyo ukilinganisha na jumla ya vijiji 47 vya Jimbo langu ni sawa na asilimia 6.4. Kuna vijiji kama 12 hivi vilikuwa na huduma hii ya maji kabla, vinakuwa vijiji 15 vinavyofaidika ambavyo ni sawa sawa na asilimia 31.9.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Tanzania tunakimbilia kwenye Tanzania ya Viwanda. Tanzania inayotaka wananchi wafanye kazi kwa bidii, kwa nguvu bila maji, tukijua kwamba, maji ni muhimu katika maisha ya binadamu, tusipopata maji safi na salama uwezekano wa kuwa na magonjwa ya hapa na pale yatakayotufanya tushindwe kufanya kazi inayostahili na kwa hiyo, tushindwe kuipeleka Tanzania katika Tanzania ya Viwanda.
Je, Serikali ina mpango gani kuongeza kasi ya
upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Jimbo la Chilonwa?
Swali la pili, je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu sasa siyo lazima kila kijiji kichimbiwe kisima chake au kiwe na chanzo chake, wakati mwingine chanzo kimoja kiweze kuhudumia hata vijiji viwili/vitatu. Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kufanya hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu concern ya Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana tukiangalia eneo la Wilaya ya Chamwino liko karibu katika Makao Makuu sasa ya nchi yetu. Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana unafahamu takribani zipatato wiki Nne nilikuwa katika mradi wa maji wa Wihunze ambao nimeona kwamba Mkandarasi anafanya kazi kwa kusuasua na kutoa maagizo ikifika tarehe Tatu mwezi huu tulioanza nao mradi huo uweze kukamilika na ninasikia hali kidogo inaenda vizuri. Hiyo yote ni juhudi ya Serikali kuangalia jinsi gani tutafanya miradi hiyo ipatikane.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hiyo, ndiyo
maana hapa nimezungumza katika majibu yangu ya awali kwamba, mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 1.058 kwa ajili ya kupeleka juhudi hii ya maji, hata hivyo naomba nikuhakikishie kwa sababu, eneo la Wilaya ya Chamwino hasa Jimbo lako ni eneo la kimkakati na Ikulu yetu ya Mheshimiwa Rais ndiyo inapojengwa pale. Naomba nikuhakikishie kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wananchi wa maeneo yale wanapata huduma ya maji kwa sababu, ndiyo sehemu ambayo ni pumulio la katikati la Jiji la Dodoma, lazima tuweke juhudi za kutosha. Naomba ondoa hofu, Serikali itakuwa na wewe daima kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa vizuri katika Jimbo lako.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, asante nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ni ombi namuomba sasa Mheshimiwa Waziri tuondoke naye mguu kwa mguu twende katika eneo hili la daraja ili tukalione kwa pamoja tuwe na uelewa wa pamoja wa namna gani nzuri zaidi ya kulishughulikia daraja lile, kwa sababu majibu haya maeneo fulani hayako sawa.
Swali la pili kwa kuwa daraja hili ni moja kati ya ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni za mwaka 2015 pia lipo daraja kati ya Msanga na Kawawa. Je, Serikali haioni kwamba kunaumuhimu sasa wa kuendelea kutekeleza ahadi za viongozi wakati ule wa kampeni mwaka 2015 walishughulikie daraja hilo pia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama hutajali Jumatatu baada ya Bunge saa saba mchana twende manaake hapa ni karibu, twende tukalione ili tuwe na uelewa wa pamoja kama ulivyopendekeza. (Makofi)
Katika swali la pili ni kweli kwamba dhamira yetu ni kuhakikisha ahadi zote za viongozi wetu wote kuanzia Awamu ya Nne na Awamu ya Tano tunazitekeleza kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo nimuhakikishie kwamba ahadi hii ya daraja hili alilolitaja tutalishughulikia kwa kadri tutakavyopata uwezo kifedha.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa sababu hiyo naomba niwe na swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, baada ya barabara hii sasa kutengenezwa na kuwa inapitika angalau kwa uzuri, magari makubwa na yanayobeba mzigo mzito sasa yanaitumia barabara hiyo kiasi kwamba eneo la kama kilometa moja limetengeneza tifutifu kubwa sana ambayo kama isiposhughulikiwa kipindi hiki, mvua itakaponyesha itakuwa shida sana kupitika. Mheshimiwa Naibu Waziri anasema nini kuhusu kuirekebisha sehemu hiyo kipindi hiki kabla mvua haijanyesha ili isije ikakosa kupitika tena? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, anachosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, bahati nzuri nimeenda kui- survey barabara ile na lile eneo moja kati ya Kijiji cha Msanga na Kawawa pale katikati hali imeharibika sana. Uharibifu ule ni kutokana na kwamba katika ujenzi wa Ikulu Ndogo ya Chamwino, malori ya TBA yanatumia barabara ile.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tumeongea na Mkurugenzi, bahati nzuri watu wa TBA wamekubali kufanya marekebisho katika barabara ile.
Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana TBA kwa sababu sasa hivi nao wanachonga barabara ya kilometa tano kutoka pale Kawawa kwenda maeneo ya Matelu ambayo ni mafanikio makubwa.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Ofisi yetu ya Chamwino chini ya Mkurugenzi tumeshafanya hiyo harakati na watu wa TBA wamekubali wataona jinsi gani ya kufanya ili mradi kurekebisha eneo lile liweze kupitika kwa wananchi wa Chamwino.

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Chilonwa, Vijiji vya Bwawani, Kata ya Kamanchali na Vijiji vya Mlebe, Kata ya Msamalo nguzo zilikuwa zimeshapelekwa kwa ajili ya kuweka umeme na mashimo yakachimbwa, lakini baadae nguzo hizi zikaja kuhamishwa.
Je, Serikali ina mpango gani sasa kuona umuhimu wa kuvipa vipaumbele vijiji hivi ambavyo vilikuwa vimeshapelekewa nguzo na kuondolewa ili katika awamu ya tatu visije vikawa vijiji vya mwisho tena? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Makanyaga, Mbunge wa Jimbo la Chilonwa kwa swali lake zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwamba ni kweli vipo baadhi ya vijiji ambavyo vilipelekewa miundombinu ya hizi nguzo, lakini baadae zikahamishwa kwa kuwa havikuwepo kwenye mpango wa utekelezaji wa kupeleka umeme vijijini REA Awamu ya Pili. Nimdhibitishie kwamba kwenye hii REA Awamu ya Tatu ambayo inaendelea kwa round hii ya kwanza, vile vijiji vyote ambavyo kwa bahati mbaya, kwamba vilipelekewa nguzo halafu zikaondolewa, miradi hiyo itatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba vijiji vyote nchi nzima vitapata miundombinu ya umeme kwa kipindi hiki ambacho kinaendelea. Ahsante sana.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na majibu hayo mazuri naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Buigiri ni eneo linalojulikana kwamba kuna Shule ya Watoto Wasiona kabisa na wengine wana uono hafifu. Je, Serikali haioni kwamba kuna kila sababu ya kulishughulikia suala hili la usalama barabarani katika eneo la Buigiri kwa umuhimu na haraka ili kuondokana na tatizo la ajali pale Buigiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna kituo kwa ajili ya wasioona sehemu za Buigiri kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge. Kiutaratibu tunategemea sehemu zenye mahitaji maalum kama hayo kuwe na watu ambao wanawaongoza wanaovuka barabara ili wasiweze kupata ajali. Lakini hata hivyo, nimshauri na kumueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tutaendelea kutafuta utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba watu wenye mahitaji maalum kama hao wanapokuwa wanavuka na kutumia barabara zetu wanasaidiwa ili wasiweze kupata madhara.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri yanayotia moyo wananchi wa Jimbo la Chilonwa. Lakini pamoja na majibu mazuri sana naomba niwe na swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya sababu zinazofanya badhi ya watumishi kukwepa kwenda kufanya vijiji vya ndani ndani ni ukosefu wa nyumba za kuishi.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kusaidia upatikanaji wa nyumba katika zahati zilizo vijiji vya ndani ndani sana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwaka, Mbunge wa Ikulu kuwa kwanza naomba niipongeze Halmashauri ya Chilonwa kwa jinsi ambavyo wameweza kukamilisha zahanati nne. Yeye katika swali lake anauliza namna Serikali kuwezesha kupatikana nyumba za watumishi. Kama ambavyo amefanya kazi nzuri kwa kushirikiana na Halmashauri yao kuhakikisha wanakamilisha zahanati hizo ni vizuri jitihada hizo ambazo zimefanyika wakaanzisha uanzishaji na ukamilishaji wa nyumba za watumishi kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba ukiwa na zahanati nzuri bila watumishi kuwa na sehemu iliyo salama ya kwenda kufanyia kazi.
MHE. ENG. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanayotia matumaini kwa wananchi wa Kata zote tano za Tarafa ya Itiso ambayo wanapata huduma pale pamoja na Wilaya ya jirani ya Chemba ambayo pia wanapata huduma katika Kituo cha Afya cha Haneti. Hata hivyo pamoja na majibu hayo mazuri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kituo hiki na chumba hiki kiweze kufanya kazi vizuri kunahitajika kuwe na vifaa tiba vinavyohudumia mle ndani. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba jengo linapoisha basi na vifaa tiba viweze kupatikana ili wananchi waweze kupata huduma?
Mheshimiwa Mwenyekitil, pili wataalam husika ni wachache sana. Hata katika Kituo cha Afya cha Haneti madaktari na wataalam wengine ni wachache. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba kituo na jengo hili litakapoikwisha la upasuaji wataalam pia wanakuwa wanapatikana wa kutosha wa kuweza kuwahudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya swali la kwanza uwepo wa vifaa vya upasuaji na vifaa vingine pale ambapo Kituo cha Afya cha Haneti kitakuwa kimekamilika ili viweze kuanza kufanya kazi, naomba nimhakikishie, kwanza, katika Kituo cha Afya cha Haneti tayari vifaa vya upasuaji vimeshanunuliwa vipo tayari. Kwa hiyo tunasubiri tu kikishakamilika na vifaa vingine vitaongezwa ili kianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anauliza kutaka kupata uhakika pale ambapo vituo vya afya vinakamilika wataalam/watumishi wawepo wa kutosha. Ni azma ya Serikali maana itakuwa hakuna sababu ya kumalizia majengo yakawa mazuri halafu tukakosa watu wakuweza kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba pale vituo vinavyokamilika na watumishi watapelekwa. Ndiyo maana hivi karibuni kuna nafasi ambazo zilishatangazwa kwa ajili ya watu wa afya waweze kuomba na waweze kuajiriwa.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nichukue nafasi hii kushukuru kwa jibu zuri, fupi, linaloeleweka la Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo, kwa maana ya uelewa wa pamoja nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri tuondoke pamoja twende tukatembelee hii barabara kutoka Zajilwa – Gongolo – Umoja hadi Izava, lakini pia na barabara kutoka Zajilwa hadi Itiso tuone, tushauriane tuone jinsi barabara ilivyo. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, ombi alilotoa Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga tutalitekeleza.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali ya kwamba katika Bajeti ya mwaka 2019/2020 mabwawa haya mawili sasa yatatengewa fedha kwa ajili ya ukarabati. Naamini kabisa hata wananchi huko waliko wanasikiliza, watakuwa wamefurahia sana haya majibu. Wako tayari kufuata maelekezo yoyote ya kiutaalamu yatakayotolewa na Serikali kuhakikisha kwamba mabwawa haya yatakapokuwa yametengenezwa na kukarabatiwa, yasije kupambana na tatizo hili tena.

Mheshimiwa Spika, nina ombi moja tu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tuongozane naye, tuambatane naye, twende tukayatembelee haya mabwawa mawili kwenye Kata hizi, ili kwa pamoja tuwe na uelewa wa pamoja nini hasa kinatakiwa kufanyika kwenye haya mabwawa. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru, nimekubali ombi lake. Nataka nimuahidi hapa kwa sababu Bunge lako tukufu litaahirishwa tarehe 8 Februari, basi tarehe 9 niko tayari kuambatana naye kufika Jimboni kwake, siyo kuangalia bwawa tu, ni pamoja na kuangalia kilimo cha zabibu.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali ambayo ameyatoa hapa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kwa umuhimu wa eneo lile niombe tu Mheshimiwa Naibu Waziri tupate nafasi twende sote kwa pamoja tutembee katika kijiji kile tuone jiografia ya pale na umuhimu wake ili Serikali iweze kuona inaisaidia vipi Halmashauri ya Chamwino katika kukamilisha zahanati ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Mbunge wa Chamwino Makao Makuu ya Ikulu ya Nchi kwa kukubali na kutupongeza, lakini mimi nipo tayari sana wakati wowote mwezi huu wa Tano twende katika Jimbo lake tukatembee. Ahsante.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa hivi punde, lakini pamoja na majibu hayo mazuri naomba niwe na maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali itapeleka wataalam kwa ajili ya kuyachunguza mabwawa hayo waone nini cha kufanya. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam hawa ili wakafanye kazi hiyo ikizingatiwa kwamba, mabwawa haya ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa jumla?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, baada ya bwawa la Izava kubomoka mwaka 2017/2018, inaonekana baada ya maji kupita kwa misimu miwili ule mchanga na tope lote lililokuwa limejaa pale chini limeondoka. Je, Serikali haioni pengine hii inaweza kuwa ni muarobaini kwa maana ya dawa ya kuyasafisha mabwawa yetu yaliyojaa tope wakafanya hivyo kwa mabwawa yote ambayo yana matatizo ya tope hapa nchini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joel Mwaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kwa umuhimu wa kilimo na umuhimu wa wananchi wa Chilonwa, Serikali kwamba, inachukua nafasi hii kuwaelekeza wataalam wa umwagiliaji Kanda ya Dodoma, hususan wa Halmashauri ya Chamwino waende kuanzia kesho kufanya tathmini na kuangalia uharibifu wa mabwawa hayo, ili kuishauri Serikali na kuanza haraka sana kuyaboresha mabwawa hayo ili kuimarisha kilimo cha uhakika katika wilaya hiyo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema kwamba, bwawa hili la Izava lilipobomoka maji kwa miaka hii mitatu yamesafisha tope lote. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kwa sababu tunapeleka wataalam hivi karibuni kuanzia kesho. Acha waende watathmini halafu watuletee majibu sahihi ya kitaalam, baada ya hapo Serikali itaona ni njia gani nzuri ya kufanya, kwa sababu hii njia ni kutokana na ajali ya mafuriko hatuwezi kusema ikawa ndio njia mbadala sasa ya kusafisha mabwawa yetu yote nchini.
MHE. JOEL M. MWAKANYAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu yanayotia moyo kwa wananchi wa Jimbo la Chilonwa. Pia nishukuru kwa ujumla wake jibu limekuwa la jumla mno kwa halmashauri lakini kwa jumla mno kwa Jimbo la Chilonwa, kwamba barabara nyingi zimetengezwa mwaka jana na nyingi zimepangwa kutengezwa mwaka huu. Sasa ombi langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa mwaka huu wa fedha 2019/2020 ambapo zimetengwa bilioni 1.366, naiomba Serikali ifanye kila linalowezekana kuhahikisha kwamba barabara hii ya kutoka bwawani kuja Ikowa angalau inatengenezwa na angalau iwe inatengenezwa kwa zile sehemu korofi ili iweze kupitika kipindi kizima cha mwaka. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS,TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Makanyaga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa majibu ya msingi kwamba uhitaji kwa ajili ya kukamilisha barabara hii ni shilingi milioni 668.2, ni kiasi kingi cha fedha na katika bajeti ambayo wametengewa ni bilioni 1.366 maana yake ukisema unamega kiasi chote barabara zingine ambazo nazo zina uhitaji maalum zitakosa kutengenezwa. Naomba Mheshimiwa Mbunge avute subra kama ambayo nimejibu kwamba Serikali inajitahidi kutafuta kiasi kingine cha fedha ili tuweze kutengeneza barabara hiyo iweze kupitika katika vipindi vyote. Katika mikoa ambayo sisi kama Taifa kipaumbele kwa barabara ni pamoja na Dodoma, ndio maana hata bajeti yake imetengwa nyingi ukilinganisha na mikoa mingine.