Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Salome Wycliffe Makamba (23 total)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, majibu ya Mheshimiwa Waziri hayaridhishi. Anaongea habari ya gesi asili Shinyanga yaani mpaka gesi asili ije kufika hizi ni ndoto na kwa kweli tutaendelea kuumia na bei ya maji. EWURA hawajaenda kufanya consultation, hawajaenda kuongea na wananchi, wamepandisha bei ofisini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Maji ya Shinyanga na Kahama wametengeneza muungano wakaweka kitu kinaitwa SHUWASA na kazi ya SHUWASA ilikuwa ni kuboresha usambazaji wa huduma ya maji katika Wilaya hizi mbili. Badala yake SHUWASA sasa hivi wanauzia maji Mamlaka ya Kahama na ya Shinyanga ambapo watumiaji wa mwisho wanaumizwa na bei kubwa kwa sababu ya kuwepo na mtu wa katikati. Waziri ana mpango gani wa kujaribu ku-standardize suala la bei ya maji katika wilaya hizi mbili kwa sababu hali hii inawaumiza wadau na wawekezaji wanakimbia kwa sababu hakuna huduma? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nikimnukuu Mheshimiwa Rais Magufuli kwenye kampeni zake alisema atahakikisha akiingia madarakani nchi nzima tutapata maji na kama tukikosa maji atawageuza ninyi Mawaziri kuwa maji, lakini mpaka leo hamjawa maji. Shinyanga ni Kata nane tu za Wilaya ya Kahama Mjini ndiyo zina maji wakati Kata 12 zote mpaka leo hazijapata maji, watu wanahangaika wanatumia maji taka na inatishia kuleta milipuko ya magonjwa. Ni lini watatimiza mpango wa kutandaza mtandao wa maji katika Wilaya hizi mbili ili watu waepukane na magonjwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge pamoja na jazba aliyokuwa nayo wakati akiongea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimfahamishe kwamba masuala ya kupandisha bei yapo kisheria. Huyu mdhibiti ambaye anaitwa EWURA ipo procedure ambayo lazima aifuate. Kwa hiyo, procedure ya kupandisha bei ilifuatwa, hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Spika, pia naomba afahamu kwamba jurisdiction ya SHUWASA ni katika Mji wa Shinyanga kule Kahama wana mamlaka nyingine ambayo inashughulikia Kahama. Kwa hiyo, tunayo mamlaka ambayo inaleta maji SHUWASA kwa bulk halafu SHUWASA sasa ndo inafanya distribution.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hoja kubwa hapa ungesema tu kwamba unaona bei iliyowekwa ni kubwa, hilo ni jambo ambalo tunaweza tukazungumza. Ndiyo maana kwenye majibu tumesema kwamba nusu ya gharama za uendeshaji wa SHUWASA ni kulipa bili za umeme. Kwa hiyo, bili za umeme zikishushwa definitely na bili ya maji itashuka. Tukasema kwamba uzalishaji wa umeme kwa mfano kama tunatumia nishati ambayo inalazimisha bei ya umeme ishuke basi hata bei ya maji itashuka, ndiyo hoja ambayo ulikuwa umeuliza kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia ukielezea suala la kwamba mpaka sasa upatikanaji wa maji maeneo mengi hakuna, lakini ni lazima Mheshimiwa Mbunge afahamu tulipitisha bajeti mwaka huu na tumepanga fedha za kutekeleza miradi na kila Wilaya inaendelea kutekeleza. Sasa akilizungumza kwa ujumla inakuwa vigumu kuelewa swali lake tulijibu vipi. Nataka awe specific na swali kwamba ni Wilaya ipi na ni mradi upi ambao haujakamilika. Serikali inaendelea kukamilisha miradi kulingana na mpango ambao Wabunge mlipitisha.
Mheshimiwa Spika, naomba nitambue Mheshimiwa Masele ndiye aliyeuliza swali kwa Mheshimiwa Rais kuhusu bei za maji.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Waziri umetuaminisha kwamba mmetupatia shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga barabara na pia mmetupa shilingi milioni 320 kwa ajili ya kukarabati barabara hizi. Mheshimiwa Waziri barabara ya Phantom-Majengo, ni barabara ya muhimu kweli na barabara hii inachangia pato la Halmashauri kwa asilimia 25. Barabara hii ina urefu wa mita tano na tunasema tunataka tufanye Serikali ya viwanda, kule kuna viwanda vidogo vidogo vya mazao ya mpunga na mahindi.
Mheshimiwa Waziri, hauoni kama kuna umuhimu wa kuingiza barabara hii katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili tuweze kutekeleza mpango huu wa Tanzania ya viwanda kwa kuendelea kuzalisha na magari yaweze kupita? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Waziri mmetenga shilingi milioni 181 tu kwa ajili ya barabara na tena ni kwa ajili ya ukarabati tu wa barabara, lakini nikufahamishe kwamba kule hakuna barabara hata moja ya lami, barabara zote ni za vumbi na fedha mliyotenga ni kidogo na ile ni Halmashauri mpya. Unawaambia nini Watanzania wa Ushetu, watawezaje kupata barabara nzuri za lami ilihali mmewatengea fedha kidogo namna hii, nini mpango wa Serikali kwa Halmashauri hii mpya?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimaanisha kilometa tano.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Mji wa Kahama kimkakati tunafahamu na ndio maana hata ninyi katika Mji wa Kahama mlikuwa mnapeleka maombi kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi kwamba Mji ule sasa uwe Manispaa kwa kadri unavyokua. Ukiangalia barabara ya Phantom - Majengo ina kilometa 5.2 ni barabara ya kimkakati ina jukumu kubwa sana, ndiyo maana tumesema mwaka huu tumeanza kutenga fedha hizo. Hata hivyo, unafahamu Mji wa Kahama siyo barabara hii tu ndiyo tunaanza kujenga, kuna miundombinu ya barabara za lami pale zilikuwa zinaendelea na mimi nilifika pale miezi michache iliyopita kuja kukagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kubwa tunajua kwamba eneo hili ni eneo la mkakati, kama Serikali tutafanya kila liwezekanalo, lakini siyo Mji huu peke yake. Serikali tumejipanga kuna ahadi za Mheshimiwa Rais katika maeneo mbalimbali, hivi sasa ukiangalia katika Halmashauri mbalimbali, juzi Mheshimiwa Rais alikuwa kwa ndugu yangu pale Mheshimiwa Mbowe, alikuwa akiangalia miundombinu ya barabara. Pia nchi nzima hata kwa Mzee Lubeleje kule Mpwapwa kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunachotaka kufanya ni kwamba ndani ya miaka mitano tufanye mabadiliko makubwa sana katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika ujenzi wa barabara za lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge, siyo kwa Mji wa Kahama peke yake isipokuwa katika miji mbalimbali katika Halmashauri zetu hizi tutahakikisha ujenzi wa barabara za lami hasa kutumia fedha za World Bank ambayo Serikali imechukua commitment ya kutosha kubadilisha miji yake yote iweze kubadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi ni mashahidi mnafahamu sasa hivi, Halmashauri za Miji nyingi sasa hivi na Manispaa zimebadilika katika suala la ujenzi wa barabara za lami TAMISEMI imeamua kufanya hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo la Ushetu kama ulivyosema ni kwamba tunafahamu Ushetu ni Halmashauri mpya na ndiyo maana, ndugu yangu hapa Mheshimiwa Elias Kwandikwa kila siku anapambana na Jimbo lake la Ushetu, kama unavyopambana Mheshimiwa Mbunge hapa. Naomba kuahidi kwamba kwa kutumia Mfuko wa Barabara, nikuahidi tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo tutahakikisha maeneo ya Ushetu na maeneo mengine tutaweka nguvu za kutosha na hasa hizi Halmashauri mpya tutaweza kuzifungua ili wananchi kule waweze kupata huduma wajisikie huru kama wananchi wenzao wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi takribani wiki mbili inakwenda ya tatu sasa Shinyanga, Kahama maji hayatoki. Wale watu wanatumia maji ya kununua hakuna maji kabisa. Tatizo inasemekana kwamba hamjalipa bili ya umeme kama Mheshimiwa Rais alivyoagiza. Mheshimiwa Waziri wale watu wanapata shida, hivi ni lini mtarudisha yale maji ili watu waendelee ku-enjoy tunu za Taifa hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wiki mbili zilizopita Mamlaka nyingi za maji zimekumbwa na tatizo la kukatiwa umeme hivyo kufanya mitambo ya kuzalisha maji isifanye kazi, hii ni kwa Shinyanga pamoja na maeneo mengine pia. Kutokana na tatizo hilo, tarehe 8 Wizara ya Maji, Hazina na Mkurugenzi wa TANESCO walikaa kikao na kuna makubaliano ambayo yamefikiwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya muda mfupi suala hili litatuliwa ili liwe na ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napenda Mheshimiwa Mbunge ajue kwamba ni kweli kabisa kwamba Mamlaka zimekuwa hazilipi bili za umeme na kama Mamlaka hazilipi bili za umeme TANESCO itakufa. Kwa hiyo, tumeweka utaratibu kwamba tuhakikishe tunalipa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa na nia nzuri kabisa ya kuwatetea wananchi wao, wengine wanasema kwamba bili ni kubwa na kadhalika lakini bila kuweka bili ya kiwango ambacho kitawezesha hizi Mamlaka ziweze kujiendesha wenyewe tatizo hili tutaendelea kuwa nalo. Kwa hiyo, naomba sana EWURA wanapopita kufanya hesabu za maji tuwe waangalifu tunapojaribu kuziingilia zile kwa sababu zinatusababisha tufike kwenye hii hali ambayo tumefika.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na ningependa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Kahama nyumba za Polisi zina hali mbaya kweli, na nimewahi kuuliza hapa na kumuomba Mheshimiwa Waziri akaniahidi kwamba watatusaidia kukarabatai zile nyumba. Kwanza hazitoshi na zina hali mbaya.
Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kutusaidia kuweza kukarabati nyumba zile ili anglau polisi nao waweze kuishi katika mazingira mazuri? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Salome kwa kuleta jambo hili. Nilishazungukia Wilaya ya Kahama. Kama tunavyojua Kahama ni moja ya eneo potential sana katika nchi yetu, hata kimakusanyo; kwa hiyo hata vijana wetu wanaokaa kule na wanapokabiliana na changamoto za eneo husika wanatakiwa wawe katika mazingira mazuri. Tunalitambua jambo hilo na kwa sababu limekuwa likiletwa mara kwa mara. Niseme tu kwamba tutalipa kipaumbele, tutalipa uzito ili hadhi za nyumba za askari wetu ziweze kulingana na eneo husika.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Kahama, Kata ya Mwendakulima kuna mgogoro wa muda mrefu sana kati ya Kanisa la Katoliki na Kijiji cha Mwendakulima na sasa ni mtaa juu ya ardhi ambayo Kanisa hili limemiliki.
Mheshimiwa Waziri, je, uko tayari kwenda na mimi katika Jimbo hili na Kata hii kuweza kutatua mgogoro huu maana umekuwa ni wa muda mrefu na unaleta hali ya kutoelewana kati ya Kanisa na wananchi wa Mwendakulima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimahakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kwenda naye katika eneo hilo na ikiwezekana kuwashirikisha wenzetu wa Wizara ya Ardhi tuone mgogoro huo namna ya kusuluhisha, lakini kwa kuanzia hata leo niko tayari tukutane mimi na yeye tujadiliane kuhusu hili.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri, tunafahamu kwamba sekta zisizo rasmi zinachangia sana Pato la Taifa na wengi wao wako kwenye hatari ya kupata ajali na magonjwa kama watu wa bodaboda. Serikali ina mpango gani wa kurasimisha na kuwaweka katika mpango wa bima ya afya sekta isiyo rasmi, hasa vijana wetu wa bodaboda? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunatambua kwamba sekta isiyo rasmi nayo ina mchango mkubwa sana katika ukuaji na kuchangia katika uchumi wa nchi yetu, lakini sisi kupitia bima ya NHIF na CHF tunatambua makundi haya na kwa kupitia vikundi vyao kuna mfumo wa bima ambao wanao ambao wanaweza kukata kwa kupitia vikundi vyao. Lakini hata hivyo, kwa mtu mmoja mmoja sasa hivi tunakuja na utaratibu wa CHF iliyoboreshwa ambayo nayo itakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutoa huduma kwa mtu mmojammoja ambaye atakuwa anahitaji.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya viwanda Tanzania ni gharama kubwa za uzalishaji katika viwanda hivi. Serikali ina mpango gani wa kuweka mazingira wezeshi ili kupunguza gharama kama kuboresha miundombinu na kutengeneza mazingira mazuri ya kilimo cha malighafi kama pamba kwa ajili ya uzalishaji wa viwanda hivi? Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira hayo ili wawekezaji hasa kwenye viwanda vya nguo waweze kupata gharama nafuu za uzalishaji zitakazopelekea wao kupata faida?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, viwanda vingi vimekuwa vikikwama kwa sababu ya kukosa mitaji. Je, Wizara ina mkakati gani wa kuzungumza na mabenki ambayo yanatoa mikopo kuweka riba nafuu kwenye viwanda ili waweze kupata pesa kwa ajili ya kufanya biashara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza hapo awali, Serikali kwa kutambua changamoto zilizopo ndiyo maana ilikuwa imeitisha kikao na wadau ili kujadili na kuweza kubaini changamoto hizo na hivyo ipo mbioni katika kuzifanyia kazi ikiwemo kuangalia mazingira ambayo yanafanya bidhaa hizo zisiwe na ushindani wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mitaji, ni kweli kwamba kuna baadhi ambao wanahitaji kuwekeza lakini suala la mitaji hasa katika uwekezaji binafsi ni jukumu la mwekezaji mwenyewe. Kwa upande wa Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaweza kulima pamba iliyo bora zaidi, lakini pia wanastahili wapate faida inayostahili kutokana na kilimo chao.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Uti wa mgongo wa nchi hii uko kwenye kilimo. Tunategemea kilimo ili tuweze kupata maendeleo kwenye nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali. Shinyanga na Kahama tunaongoza kwa kilimo cha mpunga na mahindi. Mpaka sasa ninapoongea ruzuku imepungua kwa zaidi ya 50%. Nini mpango wa Serikali kuongeza ruzuku ili tuweze ku-improve kwenye kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza amezungumzia kwenye zao la mpunga na mahindi na juu ya kuongeza ruzuku. Nilipokuwa najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli nimesema kabisa kwamba hatutakuwa na ruzuku kwa mwaka huu kwa sababu mazao yote yawe ya kimkakati, yawe yale ya nafaka, wote watakuwa wananunua isipokuwa kwa bei elekezi.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Mradi wa bomba la Ziwa Victoria umeshafika katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, lakini usambazaji katika Kata nyingi bado haujafanyika, Kata ya Mwenda kulima, Kagongwa, Iyenze, Isagee maji hayajafika. Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza maji ya Ziwa Victoria ili wananchi waweze kunufaika? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza tutambue jitahada kubwa zilizofanywa na Serikali, tunatambua kabisa tulikuwa na changamoto kubwa sana, katika Mji wa Kahama na Shinyanga na Serikali ikaona haja sasa ya kuyatoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya kutatua matatizo haya ya maji, kikubwa maji yale yamekwishafika lakini imebaki changamoto tu ya usambazaji. Hivyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge, wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani, sisi tumekwishawaita Wakurugenzi wote na tumekwishawaagiza katika mapato yao wanayoyakusanya watenge asilimia katika kuhakikisha wanasambaza maji kwa wananchi ili waweze kupata maji safi salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la msingi la ajali za barabarani kwa bodaboda na vyombo vingine vya usafiri. Tatizo hili ni Kitengo cha Usalama Barabarani kugeuza kitengo hiki kama chanzo cha mapato. Watu wanakwepa matrafiki, wanakimbia kwa sababu ukikamatwa hakuna onyo, ni faini. Bodaboda siku hizi wanakamatwa kwa kukimbizana na trafiki. Nadhani hii inasababishwa na uzee wa sheria hii ni ya mwaka 1973. Ni lini Serikali italeta mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani ili tufungue mjadala wa namna gani tutaiboresha ili kupunguza ajali za barabarani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDAIN YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Salome, Muswada huu uko njiani, muda wowote tutauleta tuje tuujadili tuone namna ambavyo tunaweza tukafanya mabadiliko ya baadhi ya sheria hizi. Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, tuko mbioni kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, Jimbo la Shinyanga Mjini katika Kata za pembeni, Kata ya Chibe, Mwalili, Old Shinyanga, Kizumbi na Mwawaza kuna shida kubwa sana ya maji, watu wanakunywa maji ya kwenye madimbwi.

Ni nini mpango wa Serikali kupeleka mtandao wa maji kwenye Kata hizi kwa sababu hata sasa ukiwafuata Mamlaka ya Maji wanasema hawana fedha kwa ajili ya kupeleka maji safi na salama. Nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanapeleka fedha na kupeleka maji katika Kata hizo za pembezoni.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba, maeneo ya Shinyanga Mjini ni kweli imekuwa ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa changamoto ya maji, lakini Wizara hapa tulipo chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan siyo Wizara ya wananchi kunywa maji kwenye madimbwi.

Mheshimiwa Spika, hili tayari tumeendelea kulifanyia kazi na maeneo haya yote ambayo bado yana changamoto, Wizara tutaleta fedha, tutasimamia kuhakikisha kwamba Majimbo yote, maji yatapatikana ili kuona wananchi wanapata maji safi bombani na ya kutosha. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika Jimbo la Shinyanga mjini Kituo Kikuu cha Polisi kilikuwa na hali mbaya jambo ambalo uongozi wa Polisi waliamua kujenga kwa fedha zao za ndani, lakini kituo hicho kipya kilichojengwa bado hakijakamilika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha katika kituo hicho ili kiweze kukamilika? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu uchakavu wa Kituo cha Polisi Shinyanga Mjini kinachohitaji ukarabati, tutafanya tathmini ili kuona kiwango cha fedha zinazohitajika kuwezesha ukarabati huo kufanyika, tuingize kwenye mpango wa bajeti katika miaka inayofuata.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano ambayo Mheshimiwa Waziri anakiri watu wamekuwa wakinunua bando, kwa sababu ya kuingia na kutoka kwa internet mtu anajikuta bando lake lina-expire kabla wakati hajalitumia. Sasa, kwa sababu hiyo, Je, Serikali haioni ipo haja ya kutengeneza utaratibu bando liwe linachajiwa kwa matumizi kwamba linaisha kwa sababu umetumia badala ya kuchajiwa kwa sababu muda wa lile bando umekwisha?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salome Makamba Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kulikuwa na changamoto hiyo lakini Serikali ikalitambua hilo na njia pekee ya kutatua changamoto hiyo ni Serikali tulitoa maelekezo ya kuhakikisha miradi yote inayojengwa nchini sasa inajengwa ikiwa na uwezo wa kutoa huduma ya internet hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tulibadilisha kanuni zetu pale ambapo unaona kabisa kwamba muda wako unaelekea kuisha lakini bando lako bado linatosha inawezekana ulikuwa umesafiri ukaenda sehemu ambayo haina internet basi utapata fursa ya kuhamisha au kujiunga na kifurushi kingine lakini na ile balance uliyokuwa nayo unai- carry forward.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kupitia hizi njia ambazo Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba inaboresha huduma ya mawasiliano tunaamini kabisa kwamba kupitia njia hizi na mabadiliko ya kanuni zetu itawezesha wananchi kutumia bando lao na mpaka linaisha. Ahsante.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Kiutaratibu Mahakama inapokuwa imetoa maelekezo kwenye jambo hili la watoto wa kike kuolewa chini ya umri, Mahakama ilishatoa maamuzi kwamba Serikali ilete mabadiliko ya sheria Bungeni.

Swali langu, Serikali imepata wapi nguvu ya kukiuka maamuzi ya Mahakama ya kuleta Muswada wa Sheria Bungeni na badala yake inakwenda kukusanya maoni ya wadau kuhusiana na sheria hii? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mahakama ya Rufani kutoa maamuzi ya mwisho kuhusiana na jambo hili, Serikali ilileta Muswada hapa Bungeni. Muswada huo ulipokelewa na kwa maelekezo ya Bunge lako tukufu tulielekezwa na Bunge tukakusanye maoni zaidi. Kwa hiyo ilichokifanya Serikali ni maelekezo ya Bunge, otherwise Serikali ilishaleta Muswada hapa. Tumetekeleza hayo maelekezo ya Bunge na tuko tayari kurudi tena kupokea maoni mengine ya Bunge itakavyoona inafaa. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Wabunge wote wa Viti Maalum na Wabunge wa Majimbo wako sawa kwa mujibu wa Katiba. Je, Serikali haioni haja ya kuleta sheria ambayo itaruhusu Wabunge wa Viti Maalum waweze kupewa mfuko wa jimbo ili na wao waweze kushiriki katika maendeleo ya halmashauri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, pale tutakapoanza kukusanya maoni ya wadau ambao ni ninyi Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya kuona namna gani tunaleta katika Bunge lako hili Tukufu Mabadiliko ya Sheria hii ya Mfuko wa Jimbo, tutazingatia pia hili suala la Wabunge wa Viti Maalum.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza juzi wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu swali linalofanana na hili alieleza bayana kwamba mahabusu wengi wanashindwa kutoka, kwa sababu ndugu zao au jamaa hawaendi kuwawekea dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu yapo makosa ambayo mtu anaweza akajidhamini mwenyewe na hili litapunguza msongamano mkubwa kwenye magereza. Nini kauli ya Serikali kwa Jeshi la Polisi na Magereza ambao mpaka sasa hivi wanaweka vikwazo kwa mtu kujidhamini mwenyewe na kuweza kutoka katika vizuizi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; bado katika magereza yetu njia zinazotumika kufanya ukaguzi kwa wafungwa hasa wanawake zinawadhalilisha wanawake na zinawaondolea utu wao na kuvunja haki zao. Kwa nini Serikali inashindwa kununua vifaa vya kisasa vya kufanya ukaguzi ili kuweza kutunza staha za wafungwa na maabusu hasa wanawake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba masuala ya dhamana yapo ya namna mbili moja inaweza kutolewa na polisi na nyingine inatolewa na Mahakama. Sasa pale ambapo kuna changamoto za polisi juzi nilieleza kwamba tunawahimiza RPC’S, OCD’S na Wakuu wa vituo wazingatie sheria kila inapotokea kosa inastahili dhamana watu waweze kutoa dhamana lakini pale inaposhindikana Mahakama ikitoa amri mtu apewe dhamana always tuta–comply ili dhamana iweze kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upekuzi unaodhalilisha tunatambua hilo na ndiyo maana kwenye bajeti yetu ijayo tumetenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kisasa vya kiteknolojia kuepusha ukaguzi unaodhalilisha siyo wanawake tu hata wanaume pia ili mtu akishapita pale anaonekana kama alivyo salama basi itakuwa imekamilika, ahsante.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi Kata ya Mamboya katika Jimbo la Kilosa maeneo mengi hakuna umeme. Nini mpango wa Serikali kuweka umeme katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumeeleza mara kwa mara hapa Bungeni ni azima ya Serikali wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba kabla kabla ya Desemba, 2023 vijiji vyote vimepata umeme. Naamini katika kata hiyo waliyoitaja vijiji vilivyomo ambavyo havijapata umeme vinakuwa vimepata umeme kabla ya mwezi Desemba kuisha mwaka huu.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kampeni za Rais wa Awamu ya Tano, aliahidi katika Mkoa wa Shinyanga atatujengea barabara kilometa 10, na juzi, mapema mwaka huu, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mpango, aliahidi wakati akizindua Hospitali ya Rufaa ya Mwawanza pale Shinyanga, kwamba atatujegea kilometa 10.

Nini mpango wa Serikali kuhakikisha inatekeleza ahadi hizo za viongozi wa Kitaifa, hasa katika mwaka huu wa fedha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salome Makamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi zote za viongozi wa Kitaifa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi katika bajeti ya mwaka huu tumezizingatia kwa kiwango kikubwa. Na kwa maana hiyo, hata barabara aliyoisema Mheshimiwa Salome Makamba ni miongoni mwa barabara ambazo tunakwenda kuzijenga, ahsante.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Serikali itapeleka lini fedha za kumalizia ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari ya mfano ya wasichana ambayo ipo katika Jimbo la Shinyanga Mjini?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali kwanza inamalizia miundombinu mingine, hii ni shule kama niliyosema mwanzo ya Singida ya shilingi bilioni tatu ambayo imejengwa pale Shinyanga Mjini.

Mheshimiwa Spika, Shinyanga Mjini walipata bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule hii ya wasichana ya Mkoa wa Shinyanga, na tayari kuna shilingi bilioni moja nyingine Serikali hii ya Awamu ya Sita imepeleka kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu iliyokuwa imesalia na baada ya hapo itafanyika tathmini nchi nzima kwa ajili ya mabwalo ambayo yanakuwa bado hayajakamilika ili Serikali iweze kutafuta fedha na kuipeleka kwenye ukamilishaji huo.
SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipanga kupeleka shilingi bilioni 195 ili kumaliza changamoto ya maji katika Mkoa wa Shinyanga. Nataka kujua Serikali imefikia wapi kutekeleza mpango huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salome Makamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuleta shilingi bilioni 195 katika eneo la Shinyanga ni miradi ya kimkakati ambayo Wizara tunaendelea kutafuta fedha. Mara tutakapopata fedha tutaendelea kuzileta kwa awamu ili kuhakikisha mradi huu unatekelezeka. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri; katika Jimbo la Shinyanga Mjini hususani Kata ya Kizumbi na Kitangia ambayo kimkakati ni maeneo ya viwanda, umeme haujafika katika maeneo mengi. Nini mkakati wa Serikali kupeleka umeme katika maeneo hayo? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba kuna baadhi ya maeneo siyo tu katika Jimbo la Shinyanga Mjini, lakini maeneo mbalimbali nchini ambapo kuna viwanda na ni maeneo ya uzalishaji na umeme haujafika. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeanzisha programu maalum ya kupeleka umeme katika maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi, viwanda na kilimo kwa sababu pia ni maeneo ambayo yanaweza kuipatia mapato Shirika letu la Umeme Tanzania na maeneo haya katika Wilaya ya Shinyanga Mjini pia yatazingatiwa katika mpango huu mahususi.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Kwanza kabisa niwapongeze Serikali kwa kutujengea Mahakama Kuu nzuri na ya kisasa katika Jimbo la Shinyanga Mjini. Swali langu Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Hakimu Mkazi imechakaa sana, actually ilijengwa tangu kipindi cha ukoloni. Nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Mahakama hizo zinakarabatiwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Makamba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika mpango wetu kwamba tumetenga fedha za kukarabati majengo yote chakavu nchini na kujenga mapya katika maeneo yale ambayo yana uhitaji huo. Ninakuahidi tu Mheshimiwa Mbunge uvute subira kidogo utaona kazi inaendelea kule kwa ajili ya ukarabati.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara iliyoko katika Jimbo la Shinyanga Mjini, Kata ya Ibadakuli, inayounganisha Kijiji cha Garamba ni mbovu sana kiasi kwamba ikifika wakati wa mvua watoto wanapata tabu hata ya kwenda shule. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba, inatengeneza barabara ile kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Garamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Salome Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachozungumza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, mipango ya Serikali ni kuhakikisha barabara zote ambazo zinasumbua zinatengenezwa kwa wakati. Kwa hiyo sasahivi jukumu letu ni, moja tumetenga katika vipaumbele, lakini la pili, tunatafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji. Kwa hiyo, tutatekeleza pia barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Ahsante.