Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Desderius John Mipata (40 total)

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, katika Bunge la Kumi nilitumia muda mwingi sana kufuatilia na kuuliza maswali juu ya upelekaji wa huduma hii kwenye Kata hizi za mwambao na sababu kubwa ni kwamba Kata hizi ni za mpakani, zina changamoto myingi zikiwepo changamoto za kiusalama pamoja na usafiri, barabara zake hazipitiki vizuri. Majibu yaliyokuwa yanatolewa na Serikali hayana tofauti na haya, na sasa hivi Serikali kama imejichanganya kidogo. Mara ya mwisho walikuwa wanasema Halotel ndiyo wangeweza kupeleka mawasiliano kule, sasa wanakuja na msimamo wa Vodacom jambo ambalo litawachanganya wananchi kikamilifu, na nilikuwa juzi Kata ya Ninde ambako wanasema utekelezaji umekwishaanza, hakuna dalili zozote zaidi ya kwenda kuonyeshwa site basi. Vilevile Wampembe hakuna kitu kinachoendelea, kwa hiyo nina mashaka majibu yamekuwa ni yale yale, ninaiomba Serikali ihakikishe kwamba inapeleka mawasiliano haya kama inavyoahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasizoee kuahidi wanieleze leo ni miujiza gani wataifanya iwe tofauti na ahadi walizokuwa wanazitoa wakati ule?
Swali la pili, katika Jimbo langu pia hasa Kata ya Isale. Kwanza niishukuru Serikali kwa kupeleka mawasaliano Kata ya Kate, kuongeza usikivu na hatua nyingine inayoendelea kwenye Kata ya Sintali. Kata ya Isale yenye vijiji vya Msilihofu, Ntuchi na Ifundwa, usikivu siyo mzuri, na nilipata kuuliza hapa pia nikaelezwa kuna hatua na kampuni imepewa kazi ya kuboresha mawasiliano katika eneo hilo, nataka kujua ni lini kazi hiyo itakamilika? Asante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba ajue hii ni Serikali ya awamu ya Tano, ni Serikali ya kasi, ni Serikali ya hapa kazi tu. Ahadi tuliyokupa imezingatia commitment iliyotolewa na mfuko huo tunaoongelea UCSAF. Kwa hiyo ninakuahidi, kama ulivyosisitiza mwenyewe na mimi narudia kwamba ifikapo mwezi Juni 2016, Kata hizo tatu mawasiliano yatakuwa yamefikishwa na atakayefikisha ni Vodacom Tanzania. (Makofi)
Kuhusu swali lako la pili, kama unavyoniona huwa napenda kusema kitu ambacho kina takwimu. Swali hili ni jipya kwangu na nakuhakikishia baada ya saa tisa alasiri tuonane nitakuwa nimewasiliana na watu wa UCSAF nikupe majibu sahihi. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nina maswali mawili ya nyongeza. Barabara ya Nkana – Kala mwishoni mwa mwaka jana ilijifunga na ikalazimika kutafuta fedha za dharura zaidi ya milioni 400 ambazo Serikali iliipatia na tukapeleka ndiyo ikafunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi imefanyika vizuri, naishukuru sana Serikali. Hata hivyo, lipo tatizo kwamba tusipopeleka pesa kwa sasa hivi kwa jiografia ya barabara zile ambazo zinaenda mwambao mwa Ziwa Tanganyika kwenye miporomoko, juhudi kubwa iliyofanyika na Serikali mwaka huu, haiwezi kulindwa na fedha kidogo iliyotengwa na Halmashauri ndiyo maana tuliomba fedha pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiuliza Serikali, je, inakubaliana na ushauri wangu kwamba ili kulinda fedha zilizotumika mwaka jana inatakiwa ipeleke pesa nyingine zaidi kwa barabara hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, iko barabara ya Kasu – Katani – Chonga – Chalatila – Myula na ile ya Kisula - Milundikwa na Malongwe. Barabara hizi ni za Halmshauri, zimekuwa zikijifunga kila wakati na sababu kubwa ni hiyo hiyo ya Halmashauri kuwa na pesa kidogo. Ni lini Serikali itaongeza pesa kwa Halmashauri ili ziweze kumudu kutengeneza barabara katika viwango vinavyohitajika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika swali langu la msingi, hizi barabara na mazingira ya mvua tunayokuwa nayo katika misimu ya mvua siyo rahisi kuahidi kwamba, barabara hii pekee tupeleke fedha kiasi hiki. Tatizo linapotokea Serikali inashughulikia chini ya Mfuko wa Dharura ambao upo katika kila TANROAD Mkoa. Naomba tuvumiliane kwa mazingira tuliyonayo, Serikali itaendelea kuongeza juhudi, kuhakikisha inatekeleza wajibu wake wa kuhakikisha mawasiliano sehemu zote za nchi yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, naomba hizi barabara tukaziangalie upya na ziletewe maombi kama ambavyo hizi zingine zililetewa ili Wizara yetu iweze kuzitathmini na kuangalia vigezo vile kama vinakidhi kupandisha hadhi au kuviongezea fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnafahamu kwamba fedha zilizoko ni zile ambazo zinapangwa hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge uwezo tunaopewa ni ule ambao Bunge linaidhinisha na kiwango kile tunachopata kupitia Road Board ndicho kinachogawiwa kwa nchi nzima.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Tunaposukuma uanzishwaji wa mamlaka hizi, tunataka kuharakisha maendeleo kwa wananchi. Mji wa Namanyere umekuwa na maombi haya muda mrefu na majibu yamekuwa ya namna hii hii, tangu Bunge lililopita majibu yamekuwa ni haya ya kusema kuna timu ya wataalam watakwenda kuhakiki ili majibu ya kuanzisha yapatikane. Nataka kujua kama Serikali inaweza ikatoa hasa tarehe maalum au time frame ili wananchi wajue hasa ni lini zoezi hili litakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miji midogo mingi hapa nchini inaendelea kukuwa ikiwepo ile ya Chala, Kate ambako ni Makao Makuu ya Jimbo, Wampembe, Kipande na kwingineko, lakini mpangilio wake umekuwa si mzuri sana kutokana na Halmashauri kukosa fedha za kufanya utaratibu wa mipango ya uendelezaji wa miji hiyo. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ukuaji huu wa miji usioridhisha hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mipata, anataka time frame ya lini jambo hili litakamilika. Mheshimiwa Mipata amekuja ofisini kwangu si chini ya mara mbili katika jambo hili na siyo Mipata peke yake na wadau mbalimbali wengine kutoka Lushoto, wengine kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya jambo hili. Ndiyo maana nilisema hapa siku zilizopita kwamba, jambo hili kwa sababu limekuwa ni kilio cha Wabunge wengi, mpaka Waziri wangu akaagiza kwamba tulete database ya status ya kila maombi haya yamefikia wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleze, naweza nika-table hii status ya database mpaka kwa kaka yangu pale Ilula, mpaka kwa kaka yangu Profesa Majimarefu wote maombi yao yapo katika hili na hii chati yote iko hapa wataalam wetu tumewaagiza sasa jinsi gani watakwenda kufanya assessment.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili naomba niseme, hapa katikati tumepata matatizo, kuna Halmashauri zingine zinaanzishwa kwa presha hata zile GN namba zinapotajwa zile code zinakosewa, zinapokosewa maana yake unaingilia katika mipaka ya Halmashauri nyingine. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mipata avute subira, sitaki kusema ni lini inaanza, lakini lengo letu kubwa ni kwamba, ndani ya kipindi hiki cha mwaka huu wa fedha tunapoanza, imani yangu kwamba, hii kazi itakwenda kwa kasi kwa sababu hata mimi sipendi kila siku kusimama hapa kujibu swali hilo hilo. Kwa hiyo, imani yangu ni kwamba, jambo hili tutafikia mwisho, wenye kukidhi vigezo watakidhi na wale ambao watakuwa na upungufu wataambiwa wapi warekebishe ili mradi wapate mamlaka. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mipata avute subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine alizungumzia suala zima la mipangilio mibaya ya miji. Ni kweli sasa hivi ukiangalia hasa miji mingi inayokua, maeneo mbalimbali yanajengwa kiholela sana. Hata hii miji midogo, kwa mfano, ukienda hata pale Kibaigwa, eneo la karibu tu hapa, ukienda kuna ujenzi kama unatengeneza kachumbari vile, kitunguu, nyanya kila kitu yaani miji imekuwa hovyo hovyo kabisa. Ndiyo maana tunapopita katika Halmashauri zetu tumewaelekeza Maafisa wa Mipango Miji na Maafisa Ardhi, jukumu lao kubwa sio kuchukua mshahara wa Serikali tu na kukaa ofisini, japokuwa resource ni ndogo lakini wakitumia taaluma zao, tutafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani Afisa Mipango Miji au Afisa Ardhi yuko ofisini pale, nje ya Halmashauri palepale, lakini watu wanaendelea kujenga kiholela katika maeneo yasiyokuwa sawasawa. Tumetoa maelekezo kwamba Maafisa Mipango Miji na Maafisa Ardhi watumie own source zilizokuwepo, kuona jinsi gani watatumia taaluma yao kufanya mipango rafiki ya kijamii, angalau wananchi wetu waishi katika mipango bora. Kwa sababu ukitegemea kwamba utapata bilioni mbili (2) kwa wakati mmoja kupanga mipango miji, inawezekana itakuwa changamoto kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimwambie Mheshimiwa Mipata kwamba, tumeliona hili na tumeendelea kutoa maelekezo na kwa kutumia platform hii ya leo naomba niwaagize Maafisa Mipango Miji wote na nilishawaagiza Afisa Mipango Miji wa Bahi na Magu nilikopita kwamba, wahakikishe maeneo yao yote wanapokuwa Ofisini, yanakuwa maeneo rafiki yaliyopangwa vizuri kwa kutumia taaluma zao.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Nakusukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya ujenzi wa barabara kutoka Kitosi kwenda Wampembe na barabara kutoka Nkana kwenda Kala na alitoa ahadi kwamba barabara hizi zitapandishwa hadhi ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka, na kwa bahati mbaya sana katika mwaka huu barabara hizi bado hazi bado hazikutengewa fedha za kutosha na Halmashauri haina uwezo wa kutosha kuzihudumia.
Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha kwamba ahadi ya Rais huyu inabaki na heshima na fedha ziweze kupatikana?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mpatakama ifuatavyo:-
Ni kweli kuna barabara nyingi Tanzania ambazo zinahitajika kupandishwa hadhina tuna barabara pale ofisini, karibu 150 ambazo zinatakiwa kupandishwa hadhi. Barabara hizi ukizipandisha hadhi maana yake ni kutafuta fedha ili uweze kuweka katika viwango vya barabara za TANROADS.
Lakini nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, wakati tutakapoanza mchakato wa kuzipandisha hadhi barabara hizo na barabara zako tutaziangalia kwa sababu tunaamini kwamba barabara zako ni muhimu sana kwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wako.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizoko wenye Mji Mdogo wa Mbalizi unafanana kabisa na changamoto zinazopatika kwenye Mji Mdogo wa Namanyere ambao pia ni Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi. Mamlaka hii ya Mji Mdogo wa Namanyere inahudumiwa na Mamlaka Ndogo ya Mji wa Namanyere. Mamlaka hii imeshindwa kuhudumia Mji huu kutokana na kupanuka zaidi kwa Mji wenyewe. Na kwa kuliangalia hilo Halmashauri imeshapitisha katika vikao vyake maombi ya kupata mamlaka ya Mji wa Namanyere. Je, ni lini Serikali itazingatia maombi haya ili kukidhi huduma zinazohitajika sana kwenye Mji huu wa Namanyere? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia ombi hili. Mheshimiwa Mbunge alifika ofisini kwangu na walinisaidia sana kuandaa database ya kuangalia maombi yote ya Miji Midogo katika Halmashauri zote za Miji mipya na Halmashauri ya Mkoa. Tunachokifanya hivi sasa ni kwamba wataalam katika Ofisi ya Rais - TAMISEMI wataenda katika maeneo mbalimbali; na nilishasema mara kadhaa; baada ya kupata ile database, kujua nani wamefikia hatua gani, waliokidhi vigezo, na ambao hawajakidhi vigezo. Hivi tutavipata hasa baada ya wataalamu kufika site.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mipata, naomba nikuhakikishie kwamba, watu wetu watafika Namanyere, watafika maeneo ya yote Sumbawanga na maeneo yale yote ambako kuna matatizo haya ya wananchi kutaka maeneo yao aidha yawe Miji Midogo, kupata Halmashauri mpya, au kupata Wilaya mpya. Wataalam wakishakamilisha lile zoezi tutakavyoangalia, pale vigezo vitakapokuwa vimefikiwa naamini Ofisi ya Rais - TAMISEMI haitosita kuipa mamlaka hii kuwa Mji Mdogo rasmi.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyere ni moja ya mamlaka iliyotembelewa na timu ya uhakiki kutoka Serikali za Mitaa na kwa taarifa tulizozipokea ni kwamba mamlaka hiyo ilikuwa imetimiza vigezo vyote na kwamba kulikuwa na dosari ndogo ndogo ambazo kwa kweli wataalam wetu wameshaleta ripoti na kukamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua ni lini hasa wananchi wa Namanyere wategemee kupata hicho walichokiomba kuwa Mamlaka ya Mji kamili wa Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka katika Bunge lilipita nilijibu swali la Mheshimiwa Mipata na kaka yangu Mheshimiwa Malocha pale, walipokuwa wanazungumza suala zima la Namanyere na sehemu ya Sumbawanga. Ndiyo maana kati ya tarehe 14 na 15, nilikuwa Rukwa na Katavi na niliweza kufika mpaka Namanyere. Hata hivyo, timu yetu ya wataalam ilifika Namanyere kufanya uhakiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kwamba zoezi hili sasa litakuwa lipo katika stage ambayo ni muafaka sana, mambo yatakapokamilika.
Naomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na hofu, ni kwamba yale maamuzi sahihi yatafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sio yeye peke yake, hata akina Profesa Maji Marefu hapa, mpaka Mzee wangu hapa wa Mpwapwa, wote wana masuala hayo hayo. Kwa hiyo, tuondoe hofu, ofisi yetu inafanya kazi, tutapata mrejesho muda siyo mrefu sana. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Serikali ya Awamu ya Tano katika matendo yake imeonekana inasimamia haki. Nataka kujua kama pato la kodi hii Serikalini kwa magari yaliyosimama kwa muda mrefu kwa sababu za msingi, lina tofauti yoyote na pato analolipata mwananchi au mtumishi hewa kutoka Serikalini?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni ushauri. Kwa kuwa magari yanayotozwa kodi hii hutumia mafuta na kwa kuwa kodi hii imekuwa na adha katika ukusanyaji wake na ni kero pia kwa wananchi: Je, Serikali inapokea ushauri kwamba, kodi hii ihamishiwe kwenye mafuta ili kurahisisha ukusanyaji wake na kuondoa kero kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kodi hizi hutozwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge letu Tukufu. Kwa hiyo, kuifananisha na watumishi hewa siyo sahihi kabisa na ndiyo maana nimesema Serikali ina nia na imeanza maboresho ya sheria hii ili kuweza kuondokana na adha hii wanayoipata watumishi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuifananisha kwa sababu ni ngumu kwa sababu ya jiografia ya nchi yetu. Huwezi tu kusema gari hii imesimama bila kujiridhisha kweli imesimama. Kama ilitolewa mjini na ikapelekwa Vijiji ambavyo hatuwezi kuvifikia, inakuwa ni tatizo kusema gari hili limesimama. Ndiyo maana nasema, naomba tuvute subira, tutakapoleta Finance Bill ya mwaka huu 2016/2017 anachokipendekeza Mheshimiwa Mbunge kitaonekana na adha hii itaondoka kabisa wala haitakuwepo tena kwa wananchi wetu.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Katika Jimbo la Nkasi Kusini kuna Mbuga ya Wanyama inaitwa Rwamfi Game Reserve. Pamekuwepo na migogoro baina ya mipaka yake na Vijiji vya Ng’undwe, Mlambo, King’ombe Kasapa na vinginevyo. Katika michango mingi nimekuwa nikiuliza maswali lakini pia katika mchango wa Wizara hii niliweza kuorodhesha vijiji hivi kwamba vina mgogoro. Je, Waziri anafahamu kwamba mgogoro upo na ni miongoni mwa orodha iliyokwishamfikia kwa ajili ya kusuluhisha migogoro hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme tu kwa ujumla kwamba katika migogoro ya ardhi ambayo Serikali imekwishaorodhesha, yote kwa ujumla ni migogoro takribani 289. Miongoni mwao ambayo inahusiana na masuala ya uhifadhi ni migogoro 35, ukifanya hesabu ya haraka pale ni kama asilimia kumi na mbili na nusu ya migogoro yote ya ardhi nchi nzima inahusu uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro alioutaja kwenye eneo lile jirani kabisa na Katavi kule ni miongoni mwa migogoro ambayo imeorodheshwa kwenye orodha ya migogoro ya hifadhi ambayo tunakwenda kuishughulikia. Naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki tuonane ili kwanza nimthibitishie kwamba migogoro hiyo ni miongoni mwa ile iliyoorodheshwa halafu asubiri hatua ambazo Serikali inachukua kushughulikia migogoro yote inayohusiana na masuala ya uhifadhi.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, nina swali moja la nyongeza. Kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ameonyesha kwamba wako mbioni kujenga ghala mjini Sumbawanga lakini ameonyesha na sehemu mbalimbali ambazo ni centre, ni sehemu za mijini mijini. Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba kwa upande wa Sumbawanga ambako barabara sasa inaimarika an kutokana na hali ya hewa nzuri, maeneo ya uzalishaji zaidi yako Wilayani. Je Serikali haioni kwamba iweke mkazo katika kujenga maghala katika maeneo ya uzalishaji kama vile Nkasi, Sumbawanga Vijijini, Kalambo, Matei kule maana yake kuna barabara za lami ili iweze kupunguza pia hasara ya kwenda kuyafuata mazao hayo na kuleta Sumbawanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba mara nyingine kumekuwa na changamoto ya kuweka huduma ya maghala kwenye maeneo ambayo hakuna uzalishaji, lakini kwa sasa kwa sababu bado hatuna maghala mengi, Wizara inaweka maghala kwenye maeneo ambayo yako katikati katika maeneo ambayo ni rahisi kuweza kupata mazao kutoka kwenye Wilaya mbalimbali. Lakini kadri uwezo utakavyoongezeka, nia ni kujenga katika Wilaya zote tuwe na maghala ya kuweza kuhifadhi chakula.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza:-
La kwanza; kwa kuwa wapo watu wanaokopesha
kienyeji na hutoza riba kubwa inayofikia asilimia 30 kwa mwezi na inapotokea mkopaji akakosa kulipa maana yake mwezi unaohusika gharama hiyo hupanda kwa maana ya compound interest kwamba mtaji pamoja na asilimia iliyopaswa kutozwa hufuata kwa mwezi mwingine na hali
hii huacha wananchi katika hali ngumu sana. Je, Serikali inawajua vizuri hawa watu na ina mpango gani wa kutafuta njia ya kuimaliza kadhia hii? (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa watumishi ndiyo walengwa
wakuu katika jambo hili pamoja na wastaafu ambao wako karibu kustaafu na kadhia hii huwafanya wapoteze hata ufanisi kazini; je, Serikali haioni umuhimu wa kulichukulia hili
jambo kama vita ya madawa ya kulevya kwa sababu watumishi wengi wanastaafu wakiwa hawana kitu chochote na familia zao zinasambaratika?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, ni kweli kabisa riba hizi kwa hawa wakopeshaji wa mitaani ni mzigo mkubwa kwa wale wanaolazimika kwenda kukopa huko
na ndiyo maana Serikali imekuwa inasisitiza kwamba kadri inavyowezekana wasiende huko, lakini jibu langu la msingi ni kwamba; sasa hivi Serikali tunafanya jitihada kubwa na tayari tumeshaandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri ili jambo hili baada ya kulifanyia kazi kwa mapana yake liweze kushughulikiwa kwa ukamilifu na maagizo maalum ya Serikali baada ya kuwa waraka huu umepitiwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lile la kusema kwamba
tuichukulie kama vita nafikiri tusiende huko kwa sasa kwa sababu waraka umeandaliwa, ni vizuri tupate nafasi ya kulichukulia maamuzi tukiwa tumetulia. Ahsante.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, walemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi sana na mara nyingi changamoto
hizi hubaki zinawakabili wanafamilia, ikitokea bahati mbaya familia ikawa na uwezo mdogo sana, shida huwa kubwa. Je, Serikali iko tayari kuwapa walemavu wote nchini msamaha wa matibabu kama ilivyo kwa wazee, wakiwemo watu wenye ulemavu wa ngozi ambao
matibabu yao huhitaji utaalamu wa kibingwa zaidi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mijibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2002 inatambua makundi ambayo yanatakiwa kupata msamaha wa matibabu, ikiwemo watu wenye ulemavu wasio na uwezo, maana siyo
kila mtu mwenye ulemavu hana uwezo. Watu wenye ulemavu wasio na uwezo hao wanaweza wakapata huduma za matibabu bila malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba kwa wazee siyo wazee wote hawana uwezo, tunao wazee humu ni Wabunge wana uwezo. Kwa hiyo, sera inasema wazee wasio na uwezo, naomba hili lieleweke wazi kwa watoa huduma wote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Mwaka 2016 Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara Mkoani Rukwa na alipata nafasi ya kuonana na Wakala wa Mkoa wa Rukwa. Kama tunavyojua, Mkoa wa Rukwa ni mchangiaji mkubwa sana wa uzalishaji wa chakula hapa nchini. Mpaka sasa hakuna kilichopatikana katika madai haya na Wizara imekuwa ikitoa majibu ya namna hii hii kila siku; haioni kama inadidimiza kilimo katika nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawakala wamekata tamaa na ndiyo walikuwa wanatusaidia mkoani kwetu na sasa chakula kitapungua Mkoa wa Rukwa kwa sababu ahadi ya Waziri Mkuu ambaye aliongea na Mawakala, haijatimizwa kwa sababu ya majibu ya kila siku kama haya.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba majibu yamekuwa ni kama haya kwa sababu huo ndiyo ukweli, kwamba ni vigumu sana sisi kukimbilia kulipa madeni ambayo tunafahamu kuna wizi ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi tunachofanya ni kuhakikisha kwamba tunaondokana na mfumo ambao unarahisisha wizi na ndiyo maana mfumo wa kununua mbolea kwa mkupuo hatutakuwa tena na tatizo la kuanza kuwa na madeni kwa sababu mbolea itakuwa inanunuliwa dukani kama Coca Cola. Kwa hiyo, tunachosema, watuvumilie tu, hatuwezi tukalipa fedha ambazo ni wazi ni za wizi. Tuna ushahidi.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Mji wa Namanyere ambao unakua pia kwa kasi na unapangwa vizuri, tumeshaomba uweze kupandishwa hadhi na kupata Mamlaka ya Mji wa Namanyere kwa maana ya Halmashauri ya Mji. Kamati ya Kitaifa ilishakuja ikaangalia na ikaona kwamba tuna vigezo vingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua na wananchi wa Namanyere wajue, ni lini Serikali itapandisha hadhi Mji wa Namanyere ili tuweze kunufaika na miundombinu inayopaswa watu wa mjini, wanufaike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mwaka 2016 nilikuwa na Wabunge, Mheshimiwa Mipata na Mheshimiwa Keissy pale tulipokuwa tunatembelea katika eneo lile na tumezunguka na ndiyo maana tukaamua kutuma timu. Waziri wangu akatuma ile timu ya haraka kupitia maeneo yote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba niwaambie kwamba timu ile sasa wataalam ndiyo walikuwa wanahakiki kupitia vigezo mbalimbali baadaye mchakato utakavyoenda, utakapofika, basi utaambiwa kwamba Mji wetu wa Namanyere umefikia katika hatua gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie kwamba lile jambo liko katika ofisi yetu linafanyiwa kazi baada ya ile timu yetu ya uhakiki kwenda kufanya kazi. Kwa hiyo, naomba tuvute subira tu kusubiri mchakato huo ukamilike halafu tutapata mrejesho kwa mustakabali wa Mji wa Namanyere.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais alitembelea Namanyere na akatoa ahadi kwamba akipita tutapata kilometa tano za barabara ya lami. Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo amekuwa akilisema mara kwa mara lakini mpaka sasa halijatekelezwa.
Nataka kujua Serikali ina mpango gani kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na hata nilipotembelea Namanyere Mheshimiwa Keissy alizungumza katika mkutano nilipokuwa ninaongea na Watumishi kuhusu ahadi hiyo sambamba na ahadi ya maji ambapo bwawa lilikuwa linaendelea kujengwa.
Mheshimiwa Mipata kwa sababu nafahamu pale Namanyere ndiyo Makao yenu Makuu ya Mji kwa ahadi hii ya Serikali na sisi ametupa dhamana kuhudumu katika ofisi yake, tutafanya kila liwezekanalo katika kipindi hiki cha miaka mitano, ahadi ya Mheshimiwa Rais kupitia TARURA tutaitekeleza, tutakapofika mwaka 2020 tusiwe na changamoto nyingine yoyote katika suala la hiyo kilometa tano Mheshimiwa Rais alizoziahidi. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba wafanye kama walivyosema. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mapema mwaka huu Waziri wa Maji alitembelea Mkoa wa Rukwa na akatembea Wilaya ya Nkasi, pia alipata nafasi ya kutembelea Mradi wa Kawa. Mradi wa Kawa una umri wa miaka sita na umetumia zaidi/karibu shilingi bilioni tatu, lakini wananchi wa vijiji vya Shengelesha, Kundi na Kalundi hawajaanza kupata maji, licha ya miundombinu yote kuwa imeshajengwa ya kupeleka maji.
Je, Serikali inawaambia nini wananchi hawa juu ya kupata maji mapema iwezekanavyo?
Swali la pili, hivi karibuni Serikali iliifunga shule ya sekondari ya Milundikwa na kuihamishia Kasu. Kijiji cha Kasu hakina maji ya uhakika ya kuweza kusaidia wananchi pamoja na shule.
Je, Serikali ipo tayari kufanya utafiti ili kipatikane chanzo kizuri kitakachowezesha kusaidia shule na kijiji cha Kasu, Katani, Milundikwa na Kantawa kwa ajili ya huduma ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mipata.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Mipata kwamba utekelezaji wa mradi wa bwawa la Kawa umekamilika.
Mheshimiwa Spika, baada ya Mheshimiwa Waziri kutembelea pale Mheshimiwa Mipata ulimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba mradi ule sivyema uendeshwe kwa kutumia jenereta inayotumia mafuta ya diesel, ukamshauri kwamba ni vyema tutumie umeme wa jua. Kutokana na huo ushauri wako nikufahamishe kwamba sasa tumekamilisha usanifu na wakati wowote tutanunua umeme wa solar na kufunga pale ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, ninaahidi ya kuwa ni muda mfupi tu unaokuja wananchi watapata huduma ya maji, kwa sababau maji yapo na miundombinu yote imeshakamilika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ni kweli baada ya Serikali kuhamisha shule ya Milundikwa na kuipeleka Kasu kumejitokeza tatizo la maji pale, ikiwemo vijiji vya Kantamwa, Milundikwa na Katani.
Mheshimiwa Spika, ninamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri husika ashirikiane na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, kwa sasa mtaalam tunaye kule tayari ili tuweze kufanya usanifu tupate chanzo kitakachohudumia hii shule ya Kasu pamoja na vijiji vinavyozunguka ili wananchi wa maeneo hayo wasipate tatizo la huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja na ombi moja kwa Serikali. Naanza na swali, maeneo mengi nchini hususan maeneo haya niliyoyataja ya Kata ya Kala, Ninde, Wampembe na Kizumbi yanayoendeleza shughuli za kilimo wananchi wake wanaishi maisha duni. Pamoja na mkakati uliosemwa na Serikali juu ya uendelezaji wa shughuli hiyo ya uvuvi wa kisasa na ufugaji wa samaki lakini bado maeneo haya niliyotaja umaskini haupungui kwa kasi inayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, kwa vile na yeye mwenyewe ni mtaalam katika eneo hilo la ufugaji wa samaki, yuko tayari kututembelea katika Kata hizi nne ambazo ni maarufu sana kwa uvuvi ili kuhimiza ufugaji wa samaki na kunusuru wananchi kiuchumi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni ombi kwa Serikali. Takribani wananchi 1,000 wa Vijiji vya Kasu, Milundikwa, Kantala pamoja na Kisura wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa ardhi uliosababishwa na eneo lao kuchukuliwa na jeshi. Licha ya kwamba Serikali ilitoa eneo hili kwa wananchi kihalali lakini sasa hivi jeshi limetwaa eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itume mtu au kiongozi mahsusi akauangalie mgogoro huu ili wananchi wapate mahali pa kulima kwa sababu sasa hivi wana sintofahamu kubwa sana na mvua sasa zimeanza kunyesha. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi napenda nimpongeze Mheshimiwa Mipata lakini naomba pia nichukue fursa hii kumpongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu mpenzi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mkakati mkubwa kabisa wa Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo inatambua kwamba jamii ya wavuvi walio wengi katika nchi yetu ni jamii maskini ndiyo maana imeamua kuirejesha Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Huu umekuwa ndiyo mkakati mahsusi ili sasa tuweze kufika kwa wafugaji na wavuvi nchi nzima tukahamishe na kuwasimamia katika kuhakikisha kwamba wanapiga hatua ya kimaendeleo yao wenyewe kiuchumi lakini pia vilevile kupiga hatua kuwa katika mchango mahsusi kabisa wa pato la Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kwamba sisi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi tuko tayari, tutakwenda Nkasi na tutafika kote katika nchi hii walipo wafugaji na wavuvi. Kauli mbiu yetu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ufugaji ni maisha yetu, uvuvi ni maisha yetu na maisha yetu ni ufugaji na uvuvi kwa pamoja. Nakushukuru.
MHE. DESUDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na nichukue nafasi hii kutambua juhudi kubwa sana na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri waliyoifanya kwenye shule hii, lakini pia usimamizi mzuri uliotolewa na Mkuu wetu wa Wilaya na kwa hakika nimeridhika sana na majibu ya Serikali, lakini hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; shule hii ni ya bweni kwa kidato cha tano na cha sita. Haina nyumba ya matron wala haina uzio wa ulinzi wa wanafunzi. Naomba Serikali itoe hela zaidi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na huduma ya vijana hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Halmashauri ilijitahidi kuchimba kisima cha maji lakini kiko mbali kidogo na shule. Naomba Serikali itoe pesa zaidi kwa ajili ya kusogeza maji kwa ajili ya huduma ya wanafunzi hawa. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mipata na Mheshimiwa Keissy, wilaya yao ni miongoni mwa wilaya zinazoongoza katika ujenzi wa madarasa. Mwaka jana peke yake wamejenga madarasa 550 ambayo yanatakiwa kuezekwa sasa hivi. Kwa hiyo nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili hitaji la kwanza alilosema la nyumba ya matron, uzio; nilifika pale Milundikwa, nimeona kweli ni mahitaji halisi nayo tutayafikiri kadri ambavyo tunapata uwezo wa kifedha lakini kwa kushirikiana na halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu kisima, shule ya sekondari ya Milundikwa tumeiingiza kwenye orodha ya shule 100 ambazo zitapata ufadhili wa fedha kutoka kwa Sultan Qaboos wa Oman. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa kunipa nafasi. Wakazi wa Wilaya ya Nkasi karibu nusu wanakaa mwambao wa Ziwa Tanganyika ambapo wanajishughulisha na shughuli ya uvuvi. Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa imepiga marufuku kabisa shughuli za uvuvi kufanyika mchana na kufanyika kwa kutumia vifaa vyovyote vya kielektroniki kama vile tochi na taa za solar ambazo zinatoa mwanga mdogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa wavuvi wamekaa na wamechanganyikiwa hakuna kazi yeyote wanayoifanya na hawawezi kuendesha maisha yao kwa sasa hivi. Kwa hiyo, naiomba Serikali ione namna ambavyo wataiona changamoto hii kwa namna ya pekee kwa sababu wananchi hawana namna ya kujisaidia kwa sasa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba katika siku za karibuni kumetokea hali ya sintofahamu kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika kutokana na katazo ambalo limefanywa na Serikali. Wabunge wanaotoka katika ukanda huo wengi wamekuwa wakija ofisini kwetu kufuatilia akiwepo Mheshimiwa Keissy, yeye nimeongea naye sana kuhusu hili.
Nimhakikishie tu kwamba kilichotokea ni mkanganyiko kidogo kuhusu kanuni ambayo hairuhusu uvuvi kwa kutumia jenereta na kwa kutumia solar ya zaidi ya wati 50; maelekezo sahihi tumeshayatoka kwa hiyo tunaamini katika siku chache hili litakuwa limeshakamilika na wavuvi wataendelea kuvua kama kawaida.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi usikivu kwa ujumla hasa mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Tarafa ya Wampembe, Kata ya Kala, Wampembe, Kizumbi pamoja na Ninde hazina kabisa usikivu wa Redio Tanzania, bahati mbaya sana maeneo haya hayana mawasiliano ya barabara ya uhakika. Viongozi ni mara chache wanatembelea maeneo haya ukiacha DC, Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Chama. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha usikivu katika eneo hili ili wananchi wa Ziwa Tanganyika mpakani kule wawe na usikivu wa kutosha kusikiliza matangazo mbalimbali ya nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kama nilivyotangulia kusema mwanzoni, tuna mpango wa kufanya suluhisho la kudumu ambalo tunaweza kukarabati ile mitambo michache ambayo inaweza ikafika eneo la nchi nzima. Kwa mfano, mtambo ule wa Mwanza unaweza ukaenda mpaka maeneo hayo na tayari tumeshaandika andiko kupeleka kwa mbia wetu wa maendeleo ambaye tayari amekubali kufanya ukarabati wa mitambo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa, kuliko kusubiri hizi fedha kidogo kidogo za kila mwaka ni bora tukaifufua ile mitambo ya AM ambayo haina matatizo kabisa na sifa zake ni kwamba inakwenda mbali sana na haipati pingamizi la milima.
Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili kusudi tuweze kupata majibu kutoka kwa mbia wetu wa maendeleo na kuweza kufufua mitambo yetu ambapo maeneo hayo aliyoyataja yatapata usikivu pamoja na nchi nzima.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Vijiji vya Kasu, Milundikwa, Katani, Kisula pamoja na Malongwe, Kata ya Kandanse wameamua kujenga Kituo chao cha Afya Kasu na wadau mbalimbali wameonesha kuwachangia ikiwepo Mfuko wa Jimbo. Je, Serikali ipo tayari kuwaunga mkono juu ya juhudi zao hizo za kupata Kituo cha Afya? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ninafahamu Mheshimiwa Mipata na mwenzake Mheshimiwa Keissy katika Wilaya yao kule wamefanya kazi kubwa sana ya kuhamasisha ajenda ya afya na ndiyo maana nilipofika pale nimeona jiografia ya Wilaya ya Nkasi ina changamoto kubwa sana. Hii ndiyo maana katika kipaumbele chetu, kwa kuunga mkono wananchi wa Kasu, tumehakikisha kwamba katika kipindi cha hivi karibuni tutawezesha Kituo cha Afya cha Kasu na Wampembe kuhakikisha kwamba vile vituo vya afya viwili vya maeneo hayo viweze kupata huduma ya upasuaji kwa lengo kubwa kwamba population iliyopo kule na wengine kutoka nchi jirani muweze kuhakikisha mnawa- manage vizuri katika sekta ya afya. Kwa hiyo, hilo tumeliangalia na tunalipa kipaumbele. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kijiji cha Kasapa wanakabiliwa na changamoto inayofanana na wananchi wa Kijiji cha Nyakanazi. Mwaka huu walikosa kabisa maeneo ya kulima baada ya wahifadhi wa msitu wa TFS Kalambo kuweka mipaka ya eneo lao na kuonekana kijiji na maeneo yote wanayolima, yako ndani ya hifadhi na kwa kuwa Halmashauri tayari imeanza mchakato wa kuliona hilo.
Je, Serikali iko tayari kuungana na mawazo ya Halmashauri pamoja na Ward DC ya Kijiji cha Sintali ili wananchi hawa waweze kupata eneo la kulima?(Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na napenda kujibu swali la Mbunge makini sana wa kule Nkasi Kusini, Mheshimiwa Desderius Mipata kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mipata ameleta tatizo hilo tayari kwenye Wizara yetu na nilimuahidi kwamba tutakwenda tuliangalie suala hilo katika site huko na tutafanya maamuzi baada ya hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ahadi yangu iko pale pale na Serikali itatekeleza kama ambavyo itaona inafaa. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi usikivu kwa ujumla hasa mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Tarafa ya Wampembe, Kata ya Kala, Wampembe, Kizumbi pamoja na Ninde hazina kabisa usikivu wa Redio Tanzania, bahati mbaya sana maeneo haya hayana mawasiliano ya barabara ya uhakika. Viongozi ni mara chache wanatembelea maeneo haya ukiacha DC, Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa Chama. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha usikivu katika eneo hili ili wananchi wa Ziwa Tanganyika mpakani kule wawe na usikivu wa kutosha kusikiliza matangazo mbalimbali ya nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kama nilivyotangulia kusema mwanzoni, tuna mpango wa kufanya suluhisho la kudumu ambalo tunaweza kukarabati ile mitambo michache ambayo inaweza ikafika eneo la nchi nzima. Kwa mfano, mtambo ule wa Mwanza unaweza ukaenda mpaka maeneo hayo na tayari tumeshaandika andiko kupeleka kwa mbia wetu wa maendeleo ambaye tayari amekubali kufanya ukarabati wa mitambo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa, kuliko kusubiri hizi fedha kidogo kidogo za kila mwaka ni bora tukaifufua ile mitambo ya AM ambayo haina matatizo kabisa na sifa zake ni kwamba inakwenda mbali sana na haipati pingamizi la milima.
Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili kusudi tuweze kupata majibu kutoka kwa mbia wetu wa maendeleo na kuweza kufufua mitambo yetu ambapo maeneo hayo aliyoyataja yatapata usikivu pamoja na nchi nzima.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Serikali inafanya juhudi kubwa sana ya kuupa Mji wa Namanyere maji, lakini mpaka sasa Mji wa Namanyere unapata chini ya asilimia 20 maji. Zipo juhudi zimefanyika na Serikali lakini tatizo kubwa ni ununuzi wa mashine ya kusukuma maji, mpaka sasa mashine hiyo haijanunuliwa. Naiomba Serikali itueleze ni lini wananchi wa Namanyere watapata mashine ili waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mipata akishirikiana na Mheshimiwa Ally Kessy walinifuata ofisini, wakaniomba wataalam ili waende wakajaribu kuangalia ni jinsi gani watanunua hiyo mashine. Wataalam niliowatuma, taarifa wamekamilisha, nimhakikishie Mheshimiwa Mipata kwamba, sasa hivi tunatuma hela ili mashine inunuliwe na wananchi wa Nkasi wapate huduma hiyo ya maji. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Bunge lililopita nilisimama hapa nikauliza juu ya support ya Serikali katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasu, nikajibiwa kwamba siyo muda mrefu pesa zitapelekwa zaidi ya shilingi milioni 500. Nataka kujua, ni lini Serikali sasa itapeleka pesa hizo maana nimetoka Jimboni bado hatujazipokea pesa hizo? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi ya Serikali kupeleka pesa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasu ni mara pesa itakapopatikana kwa sababu ni ahadi ambayo tumeiweka na tuko very firm katika hilo. Tutahakikisha katika mgao wa awamu inayofuata na kituo chake cha afya kinapata mgao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi, katika wilaya ambazo zinaenda kujengewa hospitali za wilaya ni pamoja na wilaya yake. Kwa hiyo, naamini adha ambayo wananchi wa Nkasi wamekuwa wakiipata kuhusiana na suala zima la matibabu litapungua muda siyo mrefu sana.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nakiri kwamba ni kweli Jeshi la Kujenta Taifa wametusaidia na wanaendelea kutusaidia hata katika kazi nyingine, lakini wakati shule hii inatwaaliwa ilikuwa na miundombinu mingi sana na sasa miundombinu bado haijarejeshwa yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shule hii sasa haina nyumba hata moja ya Mwalimu na ukizingatia kwamba ina Kidato cha Tano na Sita ambayo ni boarding ni wasichana wanakaa peke yako. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendelea kutupatia pesa zaidi na hasa pesa za kujenga nyumba za Walimu ambapo sasa hivi hakuna hata nyumba moja?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili wakati Serikali inatwaa eneo hili na kuipatia Jeshi limezuka suala lingine ambalo ni gumu zaidi. Wanajeshi walipokuja pale wamechukua eneo sasa la mashamba wanayolima wananchi na kufanya wananchi zaidi ya elfu tano wa Vijiji vya Kasu, Milundikwa, Kisula na Malongwe zaidi ya elfu nne kukosa mahali kabisa pa kulima. Naiomba Serikali je, iko tayari kufikiria upya na wakati mwingine ione uwezekano wa kuwagawia wananchi sehemu ya eneo ili waendelee kuendeleza maisha yao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Wizara yangu iko tayari kuendelea kusaidiana, kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya katika kutoa vifaa vya ujenzi ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kuifanya shule hii ipate miundombinu inayotakiwa. Bila shaka kutakuwa kuna bajeti za kawaida za kupitia Halmashauri nazo hizo wakizielekeza huko na sisi tutakuwa tayari kutoa mchango wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kutwaa eneo hili na kufanya watu wengi karibu elfu nne kukosa sehemu ya kulima nataka nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haijalitwaa eneo hili bali eneo hili lilikuwa ni mali ya Serikali mali ya JKT toka mwanzoni. Kama wakati wa JKT kurudi pale imetokea kwamba eneo lililochukuliwa ni zaidi ya lile la awali hilo naweza nikalingalia, lakini ukweli ni kwamba taarifa tulizokuwa nazo ni kwamba JKT wamekwenda kuchukua eneo lao la awali walilokuwa nalo kabla ya mwaka 1994 kusitisha shughuli za JKT.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge tukae ili tulijadili suala hili na ikiwezekana tufanye ziara pale tuone tunaweza kusaidia vipi. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi.
Katika Bunge lililopita niliweza kuorodhesha vijiji vya kata tatu ambavyo havina mawasiliano mazuri Kata ya Kala vijiji vyote; Kata ya Sintari kijiji kimoja na Kata ya Ninde vijiji viwili, nataka kujua, Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kwamba mawasiliano yanapatikana katika vijiji hivyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni nayo orodha ya vijiji vingi hapa. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuwasiliane ili tuweze kuona hivi vijiji katika hizi Kata tatu alizozijata pamoja na hii Kata ya Kala na Minde ili tuweze kuona kwa sababu tunaendelea kupeleka hii huduma ya minara. Kwa hiyo, nakuomba tu tuwasiliane ili uwe na uhakikika kwamba vijiji vyako na kata hizi zote ziko katika hiyo orodha. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Naomba niulize swali moja la nyongeza. Tarafa ya Wampembe yenye Kata nne za Kala, Wampembe, Kizumbi na Ninde iko kwenye mpango wa REA. Ninavyosema hivi, hakuna harakati zozote zinazoendelea katika kupeleka umeme katika maeneo haya. Je, ni lini Serikali itapelekea wananchi umeme katika maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mipata juu ya lini Serikali itapeleka umeme katika Tarafa ya Mwampembe; na ameainisha kwamba iko katika mpango wa REA. Napenda nimthibitishie kwamba Mkandarasi Nakuroi Investment yupo anafanya kazi katika Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwelekeze Mkandarasi na tumetoa maelekezo kwamba wasifanye kazi kujielekeza kwenye eneo moja. Kwa kuwa hakuna changamoto nyingine ya kuagiza vifaa, nawaomba Wakandarasi wote wa miradi ya REA wawe na magenge ya kutosha katika Majimbo yote na Wilaya zote ili kazi zitekelezeke kwa wakati na kwa speed ambayo tunaitarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo ni hilo, nitaongea na Wakandarasi wote nchi nzima. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kufuatia majibu ya Serikali tayari barabara hii imetumia zaidi ya milioni 439.8 katika jitihada ya kutaka kuifungua. hata hivyo, mwaka huu haijatengewa fedha na wanasema itaendelea kuitengea fedha kadri fedha itakavyozidi kupatikana. Je, Serikali haioni kwamba kwa kufanya hivi inachelewa na fedha ambazo tayari imesha-invest kwenye barabara hizi zitakosa thamani?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kufuatia mvua nyingi zilizonyesha katika Mkoa wa Rukwa kuna barabara katika Jimbo la Nkasi Kusini zimefunga kabisa. Barabara hizo ni pamoja na Kisula - Malongo Junction - Katongolo- Namasi- Ninde - Kanakala na tayari TARURA imeleta taarifa ya orodha ya barabara hii. Je, ni lini fedha sasa zitatolewa kwa ajili ya kwenda kurudisha miundombinu ili iweze kutumika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza uniruhusu kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Mipata barabara hii amekuwa akiipigania kwa nguvu zake zote na ndiyo maana Serikali imesikia kilio chake na hicho kiasi cha pesa kikaanza kutumika.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie kama ambavyo yeye mwenyewe amesema itakuwa si busara kwa Serikali kuweza pesa bila kupata matunda kwa sababu matunda yanayotarajiwa ni barabara kufunguka. Hata hivyo, naye atakubaliana nami kwamba barabara hii haikuwepo kabisa na kazi kubwa ambayo imekwishafanya kuhusiana na ujenzi wa madaraja pamoja na yale makalvati hakika pesa ikipatikana kipande ambacho kimebaki kitaweza kufunguliwa na wananchi waweze kupita kwenye hiyo barabara.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anaongelea baada ya mvua kunyesha kumekuwa na uharibifu katika barabara hizo ambazo amezitaja na bahati nzuri TARURA walishaleta makisio ya nini ambacho kinatakiwa kutumika. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pesa ambazo zilitengwa kwa ajili ya emergence almost zote zilishakwisha na theluthi mbili ya pesa hizo zilitumika katika kurudishia miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimhakikishie kwa sababu bajeti ilishapitishwa naamini muda siyo mrefu pesa ikianza kupatikana na eneo la kwake litaweza kufunguliwa hizo barabara.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Hivi karibuni katika kuboresha shughuli za afya nchini, Serikali ilitoa ahadi kwamba itatoa pesa kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya cha Wampembe pamoja na kile kinachojengwa na wananchi cha Kasu. Nataka kuuliza, ni lini pesa hizi zitatolewa ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mipata, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumesema wazi kwamba tunajenga, tunaboresha vituo vya afya kwa mara ya kwanza 208 na tutatumia takribani shilingi bilioni 156 pamoja na kuimarisha miundombinu mingine hasa ya wahasibu. Hata hivyo, naomba nikiri wazi, juzi juzi tumeweka katika ile batch ya mwisho ya vituo 25 na muda siyo mrefu hapa nilikuwa naongea na Mheshimiwa Nkamia kuhusu fedha hizo. Kwa hiyo, tuta-cross checks vizuri ili katika maeneo yote tuliyoyapa kipaumbele fedha ziweze kufika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika halmashauri ya Mheshimiwa Mbunge ambapo kulikuwa na changamoto ya ukosefu wa Hospitali ya Wilaya, katika mpango wetu wa Serikali wa kujenga hospitali 67 na wilaya yake tunakwenda kuipatia Hospitali ya Wilaya. Ni kwa imani yangu kubwa kwamba wananchi wa Nkasi kwa ujumla wake watapata huduma nzuri za afya katika maeneo yao.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa mawasiliano unazidi kupanda kwa huduma za jamii na kiuchumi. Wananchi wa Kata ya Ninde na Kata ya Kala katika Ziwa Tanganyika ndiyo pekee hawana mtandao wa simu. Nimechukua hatua kama Mbunge kuandika barua kuleta Wizarani na kumfuata Mheshimiwa Waziri kumueleza juu ya tatizo hili. Je, wananchi watapata lini huduma hii muhimu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mipata, kama ifuatavyo:-
Mheshimwia Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya maeneo machache ya nchi yetu huduma za mawasiliano ya simu ni duni. Kwanza nimpongeze kwa jinsi anavyofuatilia; ameshakuja mara nyingi sana ofisini kufuatilia huduma za mawasiliano kwa eneo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, tenda imetangazwa na hivi karibuni tutawapa watoa huduma ambao wataenda kuweka minara sehemu mbalimbali ambazo mpaka sasa hivi hazina huduma za mawasilinao. Baada ya kufanya hivyo, basi huduma hiyo itaanza kupatikana kama kawaida kwa wananchi wake. (Makofi) Ahsante. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi pamoja na majibu ya Serikali, naomba nieleze kwamba gari lililopo Kituo cha Afya Kala ni bovu sana na halifanyi kazi na Kala ipo umbali wa kilometa 150; hakuna mawasiliano yoyote ya simu wala barabara haifai. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye huduma za afya zinazotolewa kwenye vituo vyenye udau wa Serikali na wadau wengine, wananchi wa Kala wameamua kujenga kituo cha afya kwenye Kijiji cha King’ombe wao wenyewe, lakini vilevile wako wananchi wengine wameamua kujenga kutoka kwenye kata zao, Kata ya Ninde, Kata Kate na Kata ya Nkandasi. Je, Serikali iko tayari kuunga mkono juhudi hizi za wananchi?
Swali la pili Waziri wa Afya alipotembelea kwetu alituahidi kutupata shilingi milioni 400 kwenye Kituo cha Afya cha Wampembe na mpaka sasa sijaona fedha hiyo zimeonekana katika vitabu mbalimbali, lakini pia hatujazipokea; je, Serikali bado ina mpango huo wa kutupatia pesa katika Kituo hicho cha Wampembe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi kwa dhati kwa moyo wao wa kujitoa kuhakikisha kwamba vinajengwa vituo vya afya baada ya kuona kwamba changamoto ya kuwa katika hivi vya ubia inawakabili. Katika Serikali kuunga jitihada za wananchi naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika pesa ambayo inatarajiwa kupatikana muda si mrefu Kituo cha Afya Kasu nacho ni miongozi mwa vituo vya afya ambavyo vinaenda kupatiwa fedha ili viweze kujengwa na kuweza kutoa huduma ambazo wananchi wanatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ameniambia kwamba Mheshimiwa Waziri wa Afya alivyoenda baada ya kuona changamoto kwa wananchi wa Wampembe aliahidi kituo hicho kingeweza kupatiwa jumla ya shilingi milioni 400 ili kiweze kupanuliwa. Naomba nimhakikishie kwamba ahadi hiyo bado ni thabiti ni suala la tu la muda, pesa ikipatikana hatutasahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa ujumla wake naomba uniruhusu, unajua unapokuwa na Waheshimiwa Wabunge ambao wako kwenye Halmashauri moja na majimbo yako mawili ni sawa na ambavyo unapokuwa na watoto mapacha. Ni wajibu wako kuhakikisha kwamba unakuwa na balancing ambalo kama Serikali tunaenda kulifanya. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Nkasi hatuna kabisa zao la biashara, na kwa kuwa Wilaya ya Tanganyika inapakana na Wilaya ya Nkasi, naiomba Serikali, je, iko tayari kwenda kufanya utafiti ili wananchi wa Wilaya ya Nkasi wapate kuruhusiwa kulima zao la pamba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu la swali la nyongeza la Mheshimiwa Mulugo na katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Mipata, hayo maeneo yote yanapakana na Jimbo la Mpanda pamoja na lile la Katavi. Kama nilivyosema ni suala la utafiti katika Wizara yetu ya Kilimo ili tujiridhishe kwamba funza mwekundu bado yuko kwenye maeneo hayo au ameshaondoka? Kwa hiyo, tunaomba muda tumalize kufanya utafiti wa kina na wa haraka ili tuweze kuwapatia majibu ya msingi na ya uhakika. Ahsante.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mkoa wa Rukwa hauna chuo chochote cha ufundi cha VETA na Serikali hapa imetuahidi mara nyingi kwamba tutapata chuo hicho. Je, ni lini chuo hicho kitajegwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Chala kinaendesha shughuli zake kwenye majengo ya Kanisa Katoliki na kwa kuwa Kanisa Katoliki wanahitaji majengo yao na wananchi wameanza kuchukua hatua ya kujenga majengo mengine ili kuhamishia huko chuo, je, Serikali iko tayari badala ya kufanya ukarabati kwenye majengo yale yaliyokuwa ya mission wahamishie juhudi hizo kwenye wazo hili la wananchi ambapo wanajenga majengo kwa maana kuhamisha Chuo cha Chala?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mipata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Mkoa wa Rukwa kutokuwa na Chuo cha VETA, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali ni kujenga vyuo vya VETA katika mikoa na wilaya zote. Kwa hiyo, tuna mpango wa kujenga chuo katika Mkoa wa Rukwa kama tutakavyofanya katika mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kuangalia uwezekano wa kuwaunga mkono wananchi katika kujenga chuo wilayani kwake badala ya kutumia kile cha Chala, nafikiri walete maombi Wizarani na sisi tutakaa nao. Kimsingi Wizara tuko tayari kuwaunga mkono wananchi na wilaya ambazo zenyewe zinaanza kujenga na kuwasaidia hata kwenye miundombinu kadri hali ya fedha itakavyoruhusu.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo la Nkasi Kusini vipo vijiji kadhaa ambavyo havina mawasiliano ya simu na nimefanya juhudi sana kumtembelea Mheshimiwa Waziri, mara tatu hivi na kumuandikia barua, vipo Vijiji vya Kasapa, Msamba, Mlalambo, Ng’undwe na vinginevyo. Je, ni lini sasa vijiji hivi vitapata mawasiliano ya simu ambayo ni muhimu sana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba amekwishafika Ofisini kwangu mara tatu, kwa ajili ya kufuatilia changamoto ya mawasiliano katika Jimbo lake la Nkasi Kusini. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari orodha ya vijiji ulivyoniandikia kikiwemo Kasapa, Msamba na Mlalambo vimekwishaorodheshwa kwa ajili ya kutangaziwa tenda hivi karibuni kabla ya mwezi Mei ili viweze kuingizwa kwenye mpango wa kupewa minara ya mawasiliano.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu haya yaliyotolewa na Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mnamo mwezi wa pili mwaka huu wahifadhi wa Rwafi Game Reserve, walifyeka mazao ya wananchi wa kijiji cha King’ombe zaidi ya hekari 359 za mazao mbalimbali. Wakati wanafyeka agizo la Mheshimiwa Rais lilikuwa limekwishatolewa na sasa wananchi hawa hawana chakula. Je, Wizara ipo tayari kufidia chakula hicho walichofyeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili chakula ni uhai na moja kati ya hitaji la msingi la maisha kwanini Wizara inafikiria kwamba kufyeka ni kusuluhisha migogoro inayojitokeza badala ya kutafuta suluhisho lingine?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze kwa sababu amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa sana katika kutetea wananchi wanaoishi kando kando na maeneo ya hifadhi. Lakini taarifa kwamba mwezi wa pili mwaka 2019 askari wa Rwafi Game Reserve walifyeka mazao kwenye hekari 359, ndiyo nazisikia leo na iwapo ni kweli kwamba taarifa hizi zipo na zimefika katika Wizara yangu, basi Wizara itachukuwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge anataka kufahamu kwamba kufyeka mazao ndiyo suluhu ya migogoro hii lakini pia athari zake kubwa kwa wananchi ambao watakosa chakula. Mheshimiwa Rais alikwisha toa maelekezo na askari wetu wote wanajua katika hifadhi zetu zote za Taifa ni marufuku kufyeka mazao ya wakulima kwa sababu mazao mengi ni ya muda mfupi na iwapo hili linaendelea kutokea naomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane ili tuweze kuchukuwa hatua.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi. Vijiji vya Katani, Malongwe, Sintaling, Kana na vinginevyo viko katika Awamu ya III ya kupewa umeme mzunguko wa pili lakini mpaka sasa hatujapata. Je, ni lini mradi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu spika, nishukuru sana majibu yaliyotolewa upande wa Wizara ya Nishati lakini kwa kusisitiza kwa jinsi alivyouliza Mheshimiwa Atu sisi Wizara ya Madini kwa kushirikiana na TOL…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malizia kabisa jina lake kwa sababu kule ukikatisha kule kwao anaweza ikajulikana kuna Mbunge mpya humu ndani. Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu spika, ahsante sana Mheshimiwa Atupele Mwakibete. Ni kwamba Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Kampuni ya Oxygen Limited katika lile eneo ambalo linatoa ile hewa ya carbondioxide kampuni ya TOL wameweka sensa maalumu kwa ajili ya ku-detect hewa ile inapojitokeza kutambua mapema, na hewa hiyo inapojitokeza zile sensa zinatoa taarifa kwamba kuna hewa chafu inakuja na kwa kweli wanatoa taarifa katika maeneo yale kwa watu wanaozunguka maeneo yale kuweza kukaa mbali na lile eneo na kuhakikisha kwamba hapatokei tena vifo vinavyotokana na watu kupumua hewa hii ya ukaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna zile hatua za awali zimeshachukuliwa na kwa kweli Tanzania Oxygen kupitia leseni yao namba 139 ambayo imetolewa mwaka 2002 wako tayari sasa kuhakikisha kwamba wanakwenda katika uwekezaji na kuhakikisha kwamba wanakwenda kuitumia ile hewa ya carbon dioxide katika matumizi mbalimbali ambao yamepangwa ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge yako katika mpango wa pili wa utekelezaji wa mradi wa REA, na kwa kweli katika eneo la Katani na Malongwe imeshaingia kwenye mpango huo na utekelezaji wake unaanza Februari mwaka huu kuanzia tarehe 28. Lakini kuna suala moja ambalo Mheshimiwa hajauliza kule Wampembe umbali takribani wa kilometa 68 kutoka Mjini ni eneo ambalo ni tengefu sana, eneo hili lilikuwa nalo liingie kwenye mpango wa round ya pili lakini badala yake tumeanza kuitekeleza kuanzia wiki iliyopita. Nimeomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge ili awape taarifa wananchi wake wananchi wa Wampembe ambao wanahitaji umeme kwa haraka sana ahsante sana.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nishukuru sana majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza katika majibu ya Serikali nimeeleza kwamba kuna juhudi zinafanyika za kupata eneo ili jengo la Mahakama ya Wampembe lipatikane. Lakini niseme tu kwamba tatizo la kupata eneo si tatizo kupata eneo mimi na wananchi tunaahidi kutoa eneo kwa haraka. Tunaiomba Serikali kupitia na kwa vile sasa hivi tunaenda kwenye bajeti.

Je, Serikali itakuwa tayari kuweka au kutenga pesa ya ujenzi wa jengo hilo la Mahakama ya Wampembe kwa mwaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kupitia bajeti ya Serikali tumekuwa tukiahidiwa wananchi wa Nkasi kupata Mahakama ya Wilaya miaka mitatu mfululizo na leo kwenye kupitia majibu ya swali hili Serikali inatoa ahadi kwamba mwezi wa tani ujenzi huo utaanza. Je, zile sababu ambazo zipelekea tukashindwa kujenga na wananchi wakaanza kutuona Wabunge tunapoenda kuwaaambia tutapata jengo kwamba ni waongo? Je, zimeondoshwa? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ingawa hatutajenga Mahakama katika eneo hilo mwaka huu katika bajeti yetu lakini tutatoa kipaumbele katika bajeti itakayofuata mwaka kesho kama inaavyosema tufanye kazi kwa pamoja na tutajitahidi kutumia Mahakama ambayo sasa hivi iko katika hilo jengo ambalo tumeliazima lakini tunajitahidi tuingize katika bajeti ya mwaka kesho suala hili la ujenzi wa Mahakama haki. Tunatoa kipaumbele kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili tumejitahidi na mmjeitahidi na tunashukuru tumeondoa vikwazo vyote tumeingiza kwenye bajeti ya mwaka huu na mwezi Mei, nakuhakikishia ujenzi wa Mahakama hiyo utaanza bila wasiwasi ahsante sana.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru sana majibu mazuri ya Serikali, naomba tu utekelezaji uwe wa haraka kwa sababu msimu wa mvua karibu unafika. Katika operasheni zao mbalimbali, watu wa Maliasili wa Luafi Game Reserve wamekuwa wakiwafukuza wananchi usiku kwenye Vijiji vya King’ombe, Lundwe, Mlalambo, Kizumbi na Lupata: Je, utaratibu huo hauwezi kubadilika ili operesheni zao wafanye mchana ili sheria zifuate taratibu zake?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Kigwangalla alipofanya ziara Wilayani kwetu, aliahidi kutoa bati katika Kijiji China katika ujenzi wao wa zahanati: Je, bati hizi zitatolewa lini? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba nijibu hili la bati, la kwanza atajibu Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, naomba niwasiliane na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili kwisha ili tuweze kuona hatua stahiki za kuchukuliwa ili ahadi hiyo iweze kutekelezwa mara moja. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza nimuhakikishie kwamba kama kuna Askari wetu wa Wanyamapori badala ya kufanya operation mchana anakwenda usiku kufungua nyumba za watu anafanya makosa, maelekezo ambayo ninayatoa hapa ni kwamba operation hizo zifanyike mchana na zisifanyike usiku kwa mujibu wa sheria.(Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza vijiji nilivyovitaja vya Katani, Sintali, Nkana na Nkomachindo niseme na Malongwe pamoja na Wapembe nimeuliza kwenye swali la msingi ni lini hasa vitapata umeme? Hapa amesema viatapata kwenye mzunguko wa pili ambao utaisha mwaka 2021 na utaanza mwezi Julai mwaka huu. Sasa ni lini hasa nataka kujua kwa sababu wananchi wa maeneo haya wamezungukwa na maeneo ya umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili vijiji vya Kipande, Kundi kuna sekondari zetu lakini sekondari zote hazijaunganishwa na umeme, pia Kijiji cha Ntemba ambako kuna umeme unapelekwa safari hii hatua chache kama kilometa nne kuna Chuo cha Ufundi cha Mvima na kuna pia Kituo cha Afya cha Mvima. Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuja walitoa ombi la kuunganishiwa umeme na hadharani tulikubali kwamba tutawaunganishia umeme. Ni lini katika maeneo haya huduma za jamii yatapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifanya naye ziara katika Jimbo la Nkasi Kusini na maeneo aliyoyataja hayo tulitembea kwa pamoja. Lakini nataka niseme kwamba katika swali lake la msingi kwa vijiji alivyovitaja ikiwemo cha Wampembe anaulizia ni lini hasa umeme utawaka. Kama ambavyo tumejieleza katika jibu la msingi kwamba mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unatarajiwa kuanza tarehe 01 Julai, 2019 na kwa kuwa leo ni bajeti yetu nimwombe Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu liridhie bajeti hii ili tuanze kutekeleza mradi huu na kwa kuwa hatua za awali zimeshafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anaulizia umeme ambao unapelekwa katika Kijiji cha Ntemba ambako mita chache kuna Kituo cha Ufundi na Kituo cha Afya, ni kweli nilivyofanya ziara katika eneo lake jambo hili lilijitokeza na kwa kuwa ni sera ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba maeneo yote ya huduma za jamii ikiwemo vyuo, shule za sekondari na vituo vya afya vipatiwe umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kusisitiza ahadi hii ipo na kwamba eneo hili litapatiwa umeme na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri katika majibu ya nyongeza kwamba tumeelekeza TANESCO kufikisha umeme katika taasisi mbalimbali na kazi hiyo inaendelea. Ahsante.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa NaibU Spika, barabara mbili katika Jimbo la Nkasi Kusini zinazounganisha Makao Makuu ya Kata, Kata ya Kizumbi barabara ya Wampembe Junction - Kizumbi na barabara ya kwenda Makao Makuu ya Kata ya Ninde zote zimevunjika, madaraja yamevunjika na sasa hazipitiki kabisa na barabara ya Kizumbi tuliweza kumpeleka Mheshimiwa Waziri Jaffo alipotutembelea lakini bado mpaka sasa tunafuatilia sana hatujapata hizo pesa.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba barabara hizi zinafunguka na wananchi wa Kata hizi wanafikiwa kwa huduma mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu utaratibu wa matengenezo wa barabara zetu kupitia fedha ambazo zinatoka kwenye mfuko wa barabara ambao unapeleka fedha TANROADS na kupeleka fedha pia upande ule wa TARURA, utaratibu ni kwamba asilimia 90 ya fedha zote zinakwenda kwa ajili ya kurejeshea miundombinu hii kwa maana ya matengenezo na asilimia 10 ndiyo inakwenda kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mipata sijafahamu sawasawa labda baadae tuzungumze tuone kama hii barabara iko chini ya TARURA kwa sababu mmemtembeza Mheshimiwa Jaffo, lakini sisi kama Wizara ya Ujenzi tunashughulikia sera hii ya barabara, tunao wajibu wa kushirikiana na wenzetu upande wa TAMISEMI, kwa hiyo tuione, lakini kikubwa ni kwamba nimuombe tu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa aweze kuwasiliana na wenzake upande wa TARURA tuone kwamba eneo hili nani analishughulikia, lakini ni muhimu kwamba eneo hili lishughulikiwe mapema. Naelekeza kwamba lishughulikiwe mapema haya madaraja yatazamwe yarekebishwe ili wananchi wapate huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitatazama kwa makini eneo hili na saa nyingine utanipa details za kutosha ili tushughulikie eneo hili wananchi wako wasipate shida na najua wanayo hamu ya kupita katika maeneo haya kwa sababu maeneo haya yana uzalishaji mkubwa sana hasa mazao ya kilimo.