Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mgeni Jadi Kadika (16 total)

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri aliyonijibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni kesi ngapi zilizolipotiwa kwa kipindi hiki cha mwaka wa uchaguzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni kwa nini kesi zinacheleweshwa wale walemavu hawapi haki zao kwa haraka?
Na je, ni mikoa mingapi inayoongoza kwa mauaji ya maalbino? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu Mikoa ambayo inaongoza ni Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Shinyanga na Kigoma.
Swali lake la pili anauliza kwamba ni kesi ngapi, takwimu halisi zilizotokea baada ya kumalizika uchaguzi naomba nimpatie baadaye lakini ninachoweza kusema ni kwamba toka mauaji haya yameanza mwaka 2006 mpaka mwaka jana takribani watu wanakadiriwa kwenye 40 mpaka 43 wameweza kufariki, lakini watuhumiwa karibu 133 na kati ya hao watuhumiwa ambao wamehukumiwa kwa adhabu ya kifo ni 19 tayari ambao wameonekana wana hatia. Kwa hiyo, hizi takwimu za baada ya uchaguzi mpaka saa hivi, hizi naomba nikupatie baadaye. (Makofi)
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa Daktari amehakikisha kuwa chanzo cha ugonjwa huu hakijulikani, je, yuko tayari kutenga fedha ili uchunguzi uendelee? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa wanawake wengi hawajui ugonjwa huu, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa mafunzo au elimu hasa vijijini ili kujua dalili za ugonjwa huu pale unapojitokeza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali kutenga fedha, tayari Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kutoa huduma za afya nchini kwa magonjwa yote siyo tu ugonjwa huu wa leiomyomata uteri. Ugonjwa huu siyo hatarishi kiasi cha kusema utengewe programu maalum na bajeti maalum kwa sababu kuna vipaumbele vingine vya magonjwa mengine hatari zaidi kuliko huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu kutoa elimu kwa akinamama hususan wa vijijini, hili ni jambo ambalo Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa ikilitekeleza kwa kasi zaidi kuliko Serikali zilizopita kutokana na uwepo wa Mpango Maalum wa kuajiri Wahudumu wa Afya Vijijini (Community Health Workers) ambao watakuwa wakitoa elimu kwenye kaya na kwenye jamii kila siku. Zamani walikuwepo wahudumu hawa lakini walikuwa wakitoa huduma hiyo kwa kujitolea (voluntary) lakini sasa Serikali ya Awamu ya Tano imeanzisha mpango wa kuwaajiri kabisa na tunawafundisha kwa wingi sana katika kipindi hiki.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara ya Tanga daraja la Wami ni jembamba mno, magari mawili hayawezi yakapishana kwa wakati mmoja; hata juzi tu gari la maiti liliwahi kutumbukia: Je, Serikali ina mpango gani wa kulipanua daraja hilo?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Mheshimiwa Mbunge atakumbuka, tulipokuwa tunaongelea bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kati ya miradi tuliyoongelea ni upanuzi wa daraja la Wami. Kwa hiyo, naomba kumhakikishia, kwa kuwa mmetupa fedha, tutatekeleza kile ambacho kipo katika bajeti yetu.
MHE. MGENI J. KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya nyongeza, ninayo maswali mawili. Kwa kuwa Serikali inaitisha zabuni mwezi wa Februari kama ilivyosema na imetenga shilingi bilioni tatu kwa mwaka wa fedha 2016/2017: Je, Serikali haioni kuwa ni muda mfupi unaobakia mpaka kumalizika bajeti? Je, daraja hilo kweli litajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili: Je, Serikali haioni kuchelewesha kujenga daraja hilo ni kuzorotesha maendeleo na kuongezeka kwa ajali na hicho ndiyo kilio cha watu wa Tanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumhakikishia Mheshimiwa Jadi Kadika kwamba huo muda unatosha sana. Taratibu ni lazima zifuatwe kabla ujenzi haujaanza. Kwa hiyo, hatua za kwanza zilikuwa ni kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimaye kuandaa nyaraka za zabuni, kazi hiyo tumeikamilisha. Sasa mwezi wa Pili, tunaitisha tenda na mambo yakikamilika tukampata mkandarasi, hiyo shilingi bilioni tatu itatoka na kazi ya ujenzi itaanza.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa kuunda Tume ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya na kuongeza vituo vya tiba. (Makofi)
Swali langu la kwanza, Serikali baada ya kupiga marufuku uingizaji wa biashara za viroba na kuteketeza mashamba ya bangi, je, adhabu gani iliyowekwa kwa wale watakaoingiza viroba na wale watakaopanda mbegu za bangi katika mashamba yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, ni Mkoa gani unaoongoza kwa idadi ya vijana walioathirika zaidi kwa dawa za kulevya? Na Serikali inawaangaliaje vijana hao baada ya kupona? Watawapa msaada gani ili waweze kujiendeleza na maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, adhabu gani watapata; adhabu zimeainishwa kwenye sheria zetu, tuna sheria inayozuia matumizi ya vilevi, hususan dawa za kulevya (The Narcotic and Drug Abuse Act) kwa hivyo, ndani mle imeainishwa adhabu ya mtu anayetumia na mtu anayeingiza na mtu anayesaidia kuwezesha mambo hayo. Kwa hiyo, adhabu itatolewa kwa mujibu wa sheria hizo, sikumbuki ni adhabu yenye ukubwa kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili, ni Mkoa gani ambao unaongoza; Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi kuliko mikoa yote, ukifuatiwa na majiji mengine na sasa Serikali inachukua hatua gani kuwasaidia watu ambao wameathirika na dawa za kulevya. Mikakati tuliyonayo ni kama hii ya kuanzisha kliniki za kutoa dawa ya methadone. Hii dawa ya methadone inasaidia sana kwa wagonjwa kuacha kutumia hizi opioids kwa sababu methadone na yenyewe ni katika group hilo hilo la opioids, lakini uzuri wa methadone haisababishi utegemezi kama zile dawa nyingine. Kwa sababu dawa hizo nyingine kama heroin na cocaine zinasababisha utegemezi ambapo utegemezi ule unaweza ukaondolewa na dawa nyingine ambayo inafanya replacement ya dawa zile, kwa hiyo, mtu anaweza akaacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ni la kwanza, lakini la pili, ni kuwasaidia kwenye shughuli mbalimbali za kurudi kwenye jamii, kama kushiriki kwenye ufundi na kuwapa mafunzo mbalimbali, ili waweze kuwa intergrated kwenye jamii.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeondosha kodi ya vifaa hivyo lakini utafiti wa mitandaoni unaonesha watu wenye Ualbino katika nchi yetu hawapungui 17,000 na waliofanyiwa uhakiki ni 7,000 tu na vifaa vilivyopelekwa MSD ni boksi 100 na miwani 50. Je, Serikali haioni vifaa hivi bado havijatosha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, baada ya kugawa vifaa hivi, je, Serikali inachukua hatua gani kwa wafanyabiashara wale wanaouza mafuta haya kwa bei ya juu ili kulikomesha kabisa tatizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya watu wenye ulemavu hapa nchini na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba mahitaji haya yanapatiwa ufumbuzi. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kadiri ambavyo bajeti itakuwa inaongezeka basi mahitaji ya watu wenye ulemavu yataendelea kupatiwa mwarobaini wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ambalo amesema kwamba kuna watu ambao wanauza kwa bei ya juu hizi lotion za watu wenye ualbino; niseme kwamba Serikali itaendelea kufuatilia suala hili kwa maana si sahihi kwamba kama vitu vinaingizwa bila kodi halafu mtu auze kwa bei ya juu. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili litafanyiwa kazi na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia wajawazito wanaofika kliniki na kugundulika kuwa wameathirika na maradhi haya ya UKIMWI, je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwapatia dawa pamoja na lishe bora ili waweze kupata afya bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, dawa zote za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI kwa makundi yote wakiwemo wa akina mama wajawazito zinatolewa bure kwa gharama za Serikali. Dawa za kuongeza virutubisho mwilini wakati mwingine zinaweza zikawa hazipatikani lakini zikipatikana pia kwa akina mama wajawazito zinakuwa ni bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwapa lishe, hatujaanza utaratibu wa kutoa lishe kwa kundi hili la akina mama wajawazito wala kwa kundi lolote lile kwa sababu tunaamini hilo ni jukumu la kawaida tu la kila siku la kifamilia. Kuna miradi kutoka katika NGOs mbalimbali ambazo zinafanya kazi kwa ukaribu na Wizara yetu, wanafanya hivyo kwa baadhi ya maeneo nchini lakini sisi kama Serikali hatujaanza kutekeleza mpango wa kutoa chakula kwa akina mama wajawazito ambao wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ilitoa elimu na tamko kuwa wanaume ambao hawajafanyiwa tohara wana maambukizo zaidi. Je, ni Mkoa upi ulioelimika na wanaume wengi kufanya tohara kwa hiari zao ili kuzuia kuambukiza maradhi ya UKIMWI?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli nakubaliana na yeye kwamba kumekuwa kuna makabila mengi nchini ambayo traditionally hawapendi kufanya tohara ya kukata, wana tohara nyingine ambazo wanafanya za elimu na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua hilo na ndiyo maana tumeweka msisitizo sana katika suala hili. Kwenye Country Operational Plan ya mwaka huu tumepewa takribani milioni 526 za Kimarekani na Mfuko wa UKIMWI wa Rais wa Marekani (PEPFAR). Hizo pesa ndani yake pamoja na kuongeza watu 360,000 kwa ajili ya kuwapa dawa za ART lakini pia tutahamasisha na kuimarisha mkakati wetu wa kuwafanyia tohara wanaume katika mikoa ambayo predominantly hawapendi kufanya tohara ya kukata.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninayo maswali mawili tu ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, na Serikali ina nia nzuri tu ya kuwasaidia vijana na kuwapatia ajira, lakini kuna baadhi ya waajiri bado wanateswa wafanyakazi hao na wananyang’anywa simu wanapofika, passport, wanafungiwa ndani, hawajui waende wapi. Je, Serikali, ina mkakati gani wa kuifuatilia na kulikomesha tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali inatuambia nini? Ni ubalozi upi ambao umefanikiwa kupambana na matatizo haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA NCHI NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema kuna baadhi ya waajiriwa huwa wakifika wananyang’anywa simu, passport, na kadhalika na kwamba Serikali ina mkakati gani juu ya kushughulikia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Balozi inapokuwa inapata taarifa za namna hiyo inachukua hatua na ninachokiomba tu kwa waajiriwa wote walioko katika nchi hizi za kiarabu, linapotokea tatizo kama hilo wataarifu Balozi, ndio maana tunasema wanapewa mikataba na mikataba ile inalinda haki zao, lakini pia inalinda wajibu wa mwajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, kuhusu Ubalozi upi umefanikiwa kufanya hayo, balozi zote zinafanya kazi hizo. Cha muhimu ni kujua tu kama kuna changamoto au kuna kadhia yoyote wale waajiriwa wanatakiwa kutoa taarifa kwa Balozi husika. Wao wanafanya kazi na sisi tunaendelea kufuatilia kwamba, wanatekeleza kzi yao ipasavyo.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza bado sijaridhika na majibu aliyotoa kwa sababu hayo ni majibu ya kila siku. Baada ya hapo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa miundombinu ya Kituo cha Konde ni mibaya sana hasa wakati wa mvua mpaka askari avue viatu ndiyo aweze kuingia kwenye kituo kutokana na maji yanayopita mbele ya kituo. Je, hili nalo linahitaji fedha za bajeti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Kituo hicho cha Konde pamoja na nyumba za askari ni mbovu kabisa hazikaliki. Waziri amenijibu kuwa anasubiri fedha ni mwaka gani huo, mwaka huu au miaka kumi ijayo? Nataka kupata jibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba arejee swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza halijasikika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu kwa pamoja maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgeni Kadika, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo hicho cha Konde ni kweli kinahitaji marekebisho na sisi tuna mpango wa kurekebisha pale ambapo tutakapopata fedha na azma hii ipo palepale. Hata hivyo, Mheshimiwa Mbunge pia ana nafasi kwa yale mambo ambayo yanaonekana kwamba ni ya dharura, ni mambo madogo madogo ambayo Mbunge hayamshindi kama mabati, anaweza akachangia jitihada hizo kurekebisha mambo hayo lakini sisi kwa upande wetu kama Serikali tuna mambo mengi tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala lake la pili kuhusiana na changamoto za nyumba za askari, nadhani Mkoa wa Kaskazini Pemba ni miongoni mwa mikoa ambayo inafaidika na ujenzi wa nyumba za askari takribani nyumba 12 na Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nyingine 400 vilevile Mkoa wa Kaskazini Pemba tutajenga. Kwa hiyo, hiyo ni katika jitihada ambazo Serikali tunafanya na vilevile tunapokea msaada kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge au wadau wowote katika kusaidia jitihada za Serikali kupunguza changamoto hii kubwa ya vituo vya polisi pamoja na makazi ya askari hapa nchini.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa swali la nyongeza.
Kwa kuwa viwanda vingi vimejengwa Nchini ili kuleta uchumi wa viwanda lakini viwanda vingi havifanyikazi kwa ukosefu wa malighafi.
Je, ni viwanda vingapi vilivyojengwa vya kuchakata ili kuondoa tatizo hili na kuipa Serikali mzigo kuagizia malighafi kutoka nje?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kimsingi ni swali la kitakwimu, lakini vilevile niseme tu kwamba kwa hali ya sasa, katika usindikaji wa mazao wananchi wenyewe wamekuwa msitari wa mbele katika kujifunza na kisindika mazao na kwa kutumia taasisi zetu kama SIDO wamekuwa wakipewa mafunzo ili kusindika mazao hayo.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo lililopo katika Mkoa wa Dodoma kama alivyouliza Mbunge aliyepita, nami tatizo hilo hilo katika Jimbo langu la Mgogoni. Jimbo hilo lina sekta muhimu sana kama Polisi na kadhalika, lakini bado mawasiliano ni tatizo:-

Je, ni lini, utajengwa mnara katika Jimbo hilo Kijiji cha Finya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo alilolitaja lina changamoto ya mawasiliano. Nakiri kwamba nimeshawahi kutembelea eneo lile na tumeshachukua coordinates kwa ajili ya kutangaza tenda ambazo zinatangazwa mapema mwezi wa tano kwa ajili ya kusambaza mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hilo litazingatiwa kwa sababu kuna taasisi za kijamii ambazo ziko maeneo ya pale. Itakapotangazwa tukapata mkandarasi kazi zitaanza na kumalizika mara moja. Ahsante.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yake lakini bado nina maswali mawili ya kumuuliza. Swali la kwanza; kwa kuwa vijana wengi au vijana wetu wadogo wanatumia mitandao kwa kutumia simu au ku-chart au kuangalia picha za ngono ambazo kuwa huleta hisia mbalimbali. Watoto hao ndiyo wale wanaobeba ujauzito wakiwa na umri mdogo kati ya darasa la sita mpaka darasa la tatu. Je, Serikali inaonaje suala hili?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ziko nhi za wenzetu wanazuia mitandao kurusha picha za chafu. Je, Serikali yetu inashindwa nini baada ya kukemea na kudhibiti ili kuzuia mambo haya yasiendelee na wale watakaofanya hivyo wachukuliwe hatua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ambayo yameulizwa na Mheshimiwa Mgeni:-

Mheshimiwa Spika, nikianza na swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kwamba kwa upande wa Serikali tunaonaje masuala haya ya utandawazi. Ni kweli tunatambua kwamba, changamoto imekuwa kubwa sana kwa suala zima la maadili na kwa kiasi kikubwa sana inchangiwa na hii mitandao ya kijamii. Ndiyo maana kwa kujua hilo sasa sisi kama Serikali tulikuja na Sheria mbalimbali na Wabunge wa Bunge hili ndiyo ambao walizipitisha hizo Sheria, lengo ni kuhakikisha kwamba, tunawazuia watoto wetu hususan vijana ambao wako chini ya umri wa miaka 18 kuweza kujihusisha na vitu ambavyo havifai kwa Taifa letu. Kwa hiyo, kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba jukumu hili siyo jukumu la Serikali peke yake ni jukumu letu sote.

Mheshimiwa Spika, pia katika swali la pili, ametaka kujua kwamba nchi zingine zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuweza kudhibiti vijana wadogo ambao wako chini ya miaka 18 kuangalia vitu ambavyo havifai kwenye mitandao. Bado jibu langu liko pale pale kwamba ni wajibu wetu sote, upande wa Serikali na naweza nikasema kwamba kwa upande wa Serikali tumefanya kazi kubwa sana na ziko sheria ambazo tayari tumeshazipitisha ndani ya hili Bunge, lakini changamoto zimekuwa kubwa kwamba sheria hizi zinapopita Waheshimiwa Wabunge tumekuwa na ile tabia ya kuwa na mgawanyiko.

Mheshimiwa Spika, unakuta sheria tumepitisha kwa mfano, Sheria ya Cybercrime, lakini sasa unakuta wengine wanaanza kulalamika kwamba ile sheria inaminya uhuru na inakandamiza, kitu ambacho kinakuwa siyo cha kweli. Kwa hiyo nitoe wito ndani ya hili Bunge kwamba sheria kama hizi zinapopita katika Bunge ni vyema sisi kama viongozi tukawa wa kwanza kuzisimamia, lakini vilevile kwa yale maeneo ambayo sisi tunatoka, tuhamasishe jamii kuona kwamba namna gani ambapo suala zima la malezi siyo suala la Serikali peke yake ni suala la Serikali lakini pamoja na jamii kwa ujumla. Ahsante.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu yake ya kuridhisha, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenge wa Uhuru unaleta maendeleo ni sawa lakini kuna changamoto na kuna hasara kubwa, kwa sababu mkesha wa Mwenge unapolala unakuwa kishawishi na maambukizi makubwa mapya ya UKIMWI jambo ambalo linapelekea vijana wengi kuathirika. Je, kwa nini Serikali haiweki mfumo mwingine kwa kulaza Mwenge huu kwenye Vituo vya Polisi au Ofisi za Halmashauri ili kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI kwa vijana wetu? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mgeni, hilo la UKIMWI halina uthibitisho.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, watu wanalazimishwa wakalale kwenye mkesha wa Mwenge wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara. Je, hii ni kwa mujibu wa kanuni au sheria gani? Nataka kufahamu kuhusu suala hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niuambie umma wa Watanzania kwamba Mwenge una faida kubwa sana. Pia niuambie kwamba hakuna Taifa ambalo halina chimbuko lake. Mwenge ni chimbuko la Watanzania na ni utamaduni wetu. Hivyo, Mwenge utaendelea kuwa chombo muhimu na alama ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema kwamba mkesha wa Mwenge unasababisha maambukizi ya VVU, siyo kweli, kwa sababu kitu kimojawapo ambacho kinafanywa na Mbio za Mwenge ni kuelimisha mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya UKIMWI, Malaria pamoja na Kupambana na Dawa za Kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala haya ya UKIMWI, tunaelimisha nini kupitia Mwenge? Tunaelimisha kwamba ni lazima Watanzania wapime wafahamu afya zao, matumizi sahihi ya ARV’s na kuondoa unyanyapaa kwa waathirika wa magonjwa ya UKIMWI. Suala lingine ni mabadiliko ya tabia, Watanzania tunapaswa tubadilike tabia ili kuondokana na maambukizi mapya ya VVU. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Mwenge unasababisha maambukizi ya VVU kupitia hii mikesha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la nyongeza amesema kwamba watu wanalazimishwa kwenda kwenye hii mikesha, siyo kweli. Hakuna mtu anayelazimishwa, kila mtu kwa mapenzi yake anaenda kwenye mkesha wa Mwenge. Mimi mwenyewe nilikesha hakuna mtu ambaye aliniambia Ikupa njoo ukeshe kwenye Mwenge, nilienda nilikesha.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanafunzi mbalimbali wanakwenda kwenye mikesha hiyo kutokana na hamasa ambazo zinafanywa na mbio za Mwenge. Kwa hiyo, hamasa za mikesha hii ndiyo zinafanya watu wanajitokeza kwenda kukesha na kusikiliza ni nini kimefanywa na Serikali yao lakini pia kujua ni nini kinaendelea kutekelezwa na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu hayo, si ya kuridhisha kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge lililopita Abdallah Mabodi alishasema kuwa pesa zimeshatengwa kwa bandari hiyo lakini mpaka sasa hivi bado yaliyofanywa ni madogo tu. Je, ni lini itajengwa bandari hiyo kwa sababu ina umuhimu sana Bandari ya Wete?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Bandari iliyoko Zanzibar ni bandari kuu, ambayo huwa wafanyabiashara wote wanaitegema bandari hiyo na bandari hiyo ni ndogo inabeba meli moja tu kuteremsha mizigo na meli hiyo inapoteremsha mizigo inachukua kati ya wiki tatu mpaka nne na kusababisha meli kuondoka na kuteremsha mizigo Bandari ya Mombasa, nchi jirani na kuikosesha mapato Serikali ya Tanzania. Je, ni lini utafanyika upanuzi wa bandari hiyo ili tuondokane na matatizo. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba Serikali ilitazama mahitaji kwa maana yale mahitaji ambayo nimejibu katika jibu la msingi yamefanyika, huu upanuzi ambao nimeutaja hapa lengo ni kuhakikisha kwamba wakati hizi juhudi kubwa zinafanyika za kufanya maboresho makubwa, zile huduma muhimu zinaendelea kufanyika katika bandari hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nilikuwa najaribu kufanya rejea kwenye commitment nzima ya upanuzi wa bandari upande wa Zanzibar. Kiasi ambacho kilipitishwa na wakuu wa nchi kama level funding kwa ajili ya bandari za Zanzibar peke yake ni dola milioni 2.131. hii ni kuonesha kuwa wakuu wako committed kuonesha kwamba tunafanya maboresho makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo sasa utaratibu ule wa kutafuta fedha unaendelea kufanya upanuzi mkubwa ndiyo maana unaona juhudi zimefanyika na juhudi zinaendelea ili kuhakikisha tunafanya maboresho makubwa. Kwa hiyo, nikutoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba upanuzi utafanyika, hii ni commitment ya hali ya juu ambayo inasimamiwa na wakuu wa nchi, tutakwenda kufanya upanuzi wa bandari hii.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri lakini bado kundi hili ni kubwa mno. Ukienda masokoni watoto wanabeba mizigo, bandarini watoto wanapara samaki na wengine wanatumiwa kuuza madawa ya kulevya, kwa hiyo, bado Serikali inatakiwa kufanya kazi na ina mkakati gani wa makusudi kuliondosha kabisa tatizo hili ili watoto wetu warudi katika malezi mazuri na wapate elimu? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, vilevile kuna wanawake ambao wanajihusisha na udhalilishaji wa watoto, wanawatoa vijijini na kuwapeleka mjini na kuwafanyisha biashara ya ukahaba na ni kundi kubwa tu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuunda Kamati Maalum kuwafuatilia wanawake hawa na wanatakapopatikana wapewe adhabu ya kutosha ili iwe ni fundisho kwa wengine ili suala hili la kudhalilisha watoto liondoke kabisa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, ambaye naye amekuwa anafuatilia sana masuala ya ustawi na maendeleo ya watoto, nimpongeze sana kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, nianze kujibu maswali yake mawili. Tuna Sera ya Maendeleo ya Mtoto lakini tuna Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 ambazo zimeainisha haki za msingi za motto. Mtoto ana haki ya kutunzwa, kuendelezwa na kutofanyishwa kazi nzito. Kwa hiyo, hizi sheria zipo na ziko wazi na pale mzazi au mlezi anapokiuka basi hatua za kisheria zinachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe tu jamii na sisi kama Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuyasemea haya. Sisis kama Wizara tutaendelea kuchukua hatua pale tunapobaini na mashauri yale yanapofika katika ngazi ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hili ameongelea suala la watoto kufanyishwa kazi za kingono na baadhi ya walezi. Niseme tu katika Mpango Mkakati wa Serikali wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha mwaka 2021/2022, tumeelekeza kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto. Kamati hizi zimeanzishwa katika ngazi ya taifa mpaka katika ngazi ya kijiji na tunaendelea kuziimarisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pale tunapopata taarifa kwamba kuna matukio kama haya zile Kamati zina wajibu wa kuyafuatilia matukio hayo na sisi kama Serikali tunafuatilia na kuchukua hatua stahiki.