Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ignas Aloyce Malocha (35 total)

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi anavyomudu nafasi yake na anavyochanganua majibu mbalimbali. Hata hivyo, nataka kumshauri aiangalie sana ofisi yake inayotoa majibu ya maswali, ni jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ameelekeza taratibu tunazotakiwa kuzifuata na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilishazifuata, Mikutano ya Vijiji, Mikutano ya Madiwani, Mikutano ya DCC, Mikutano ya RCC na vigezo vipo na Bunge linajua hivyo na tulishaomba. Nataka aniambie ni lini wananchi wale watapata Wilaya mpya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, haoni kwamba kitendo cha kuunganisha Wilaya, Sumbawanga Mji na Sumbawanga Vijijini ambazo jiografia zake ni ngumu kunamfanya Mkuu wa Wilaya asiweze kumudu nafasi yake na hatimaye wananchi wa Wilaya wa Sumbawanga Vijijini kucheleweshwa kimaendeleo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu zetu za kitakwimu zinatuonesha Halmashauri ya Wilaya hii ambayo anazungumzia Mheshimiwa Mbunge, ukiiachia Sumbawanga Mjini kwa vigezo vya kijiografia kwa ukubwa wake ina square meter 1,300 ambapo kwa Wilaya inatakiwa iwe na square meter 5,000 lakini halmashauti iliyobakia ina square meter 8,000. Kwa hiyo, ukizi-combine maana yake hapa unapata equivalent ya Wilaya mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naomba nikiri wazi, Wabunge wengi sana wanasema wengine wamewasilisha taarifa, ndiyo maana wiki mbili zilizopita nimeagiza, baada ya Mheshimiwa Shangazi kuja ofisini kwangu kwa ajili ya Jimbo lake la Mlalo kuhusiana na suala hili, nikasema nimewaagiza wataalam wangu kuniletea orodha za halmashauri na wilaya zote ambazo zimeleta mapendekezo yao. Nia yangu ni tuweze kubaini ni wilaya ngapi zilipeleka maombi ili kama hazijakidhi vigezo vile tuweze kuwapa marejesho ni mambo gani wanatakiwa kuyarekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Malocha aniamini kwa sababu amesema wameshawasilisha haya yote, nitakwenda kufuatilia kwenye orodha ambayo nimeagiza. Tukiona kwamba kila kitu kiko sawa au kama kuna marekebisho ambayo yanatakiwa yafanyike tutawasiliana kwa sababu wananchi lengo lao kubwa ni kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini suala hili litatekelezwa. Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, tukishajua hatua iliyofikiwa, tutaona jinsi gani tutafanya kuhusiana na suala hili la Sumbawanga Mjini na Vijijini. Bahati nzuri ofisi yetu iko chini ya Mheshimiwa Rais mwenyewe, tutamshauri ipasavyo kwamba watu wa Sumbawanga kwa jiografia yao ilivyokuwa ngumu, Wabunge wanapata shida sana kutoa uwakilishi mzuri katika maeneo yao, basi Sumbawanga wapate maeneo ya kiutawala.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilishatuma maombi ya kugawa Halmashauri ambayo iliambatana na maombi ya Wilaya, Jimbo na kupitia vikao vyote kuanzia Vijiji, WDC, DCC, RCC na kuonekana kwamba, ina vigezo vyote na hata watawala ambao wametawala maeneo hayo wanaujua ukweli huo; kwa mfano Mheshimiwa Manyanya, Mheshimiwa Mkuchika, hata baadhi ya Wabunge ndani humu, hata Waziri Mkuu aliyepita alishashuhudia ndani ya Bunge. Je, ni lini wananchi hawa watapata haki yao ya kugawanya Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumbukumbu yangu Mheshimiwa Malocha ndiye alinisababisha mpaka nikaanda database ya kuona kwamba Halmashauri zilizoleta matakwa ya kugawanywa Halmashauri halikadhalika Mikoa. Nikiri wazi kwamba Mheshimiwa Malocha alikuja mpaka ofisini kwangu tukalijadili suala hili na ndio maana nikawatuma wataalam wangu waandae database hiyo ikiwemo pamoja na uanzishwaji wa mji mpya kwa kaka yangu hapa kukata maeneo ya Korogwe ilikuwa yote pamoja katika mchakato huo, Mheshimiwa Profesa Maji Marefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na lile ndio maana tumepata muongozo sasa hivi kama viongozi wapya katika eneo hilo. Tumewatuma wataalam wetu sasa hivi wanaandaa kikosi kazi kwa ajili ya kutembelea maeneo yote ya Tanzania ili kubainisha yale maombi yaliyokuja waliofikia vigezo, kama ndugu yangu Mheshimiwa Malocha anavyosema huko, waliofikia vigezo kwamba waweze kupata hizi halmashauri na Wilaya mpya au halikadhalika Mikoa mipya ambayo imependekezwa. Basi haya yakifanyika, naomba nikuahidi Mheshimiwa Malocha kwamba timu itafika kule site kufanya final finishing, kumalizia zoezi la mwisho la kuhakiki na nikijua kwamba, eneo lako kweli ni eneo kubwa na umekuwa ukililalamikia kwa muda mrefu. Kwa hiyo kikosi kazi kitafika kule site kama maelekezo tuliyopeana pale ofisini kwangu.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo ahadi nyingi zilizotolewa na viongozi kuanzia Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na sasa Awamu ya Tano. Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuandaa ahadi hizo kwa kutengeneza kitabu cha mpango wa utekelezaji na sisi Wabunge tukagawiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha kwa kifupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ushauri mzuri na Serikali tunaupokea.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Sera ya Serikali ni kuwa na chuo cha ufundi VETA kila Wilaya lakini hadi sasa ipo baadhi ya Mikoa haina hata chuo kimoja cha ufundi VETA kwa mfano Mkoa wa Rukwa.
Je, Serikali ina mpango gani, wa kiuwiano wa kuhakikisha Mikoa yote ambayo haina vyuo vya ufundi VETA inapewa kipaumbele kwanza?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba kila Wilaya inakuwa na VETA na kila Mkoa inakuwa na VETA bado uko palepale. Niseme tu kwamba kwa mfano Mkoa wa Rukwa aliyosema changamoto iko ndani ya Mkoa katika kutoa kiwanja, kwa hiyo tungeomba kwamba zile changamoto ambazo zinajitokeza za upatikanaji wa eneo Mkoa wakamilishe ili ahadi ya Serikali iendelee kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais ameipatia Wizara yangu, vyuo vya Folk Development College‟s Wizara kama nilivyosema kwenye majibu ya awali itafanya tathmini ya VETA, itafanya tathmini ya hizo Folk Development College‟s ambazo ni 53 tumekabidhiwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba tutatoa kipaumbele kwenye yale maeneo ambayo yalikuwa hayana vyuo vya ufundi ili kuhakikisha kwamba hii ahadi ya Serikali inatekelezwa kwa vitendo.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ya 2016/2017, miradi mingi ya umwagiliaji iliyokuwa imeanza katika hatua za awali katika Halmashauri zetu na kuombewa fedha haikupangiwa fedha; kwa mfano, katika Jimbo langu, mradi wa Nkwilo, mradi wa Uzia, mradi wa Nzogwe, mradi wa Mkanga na mradi wa Momba.
Je, Serikali ina mpango gani mbadala wa kuifanya miradi hii iweze kuondelea ili wananchi waweze kuondokana na tatizo la njaa na kukuza uchumi wao na Taifa zima kwa ujumla?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mipata kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi mingi haikupangiwa fedha kwa mwaka huu na tulifanya hivyo kwa sababu ndiyo kwanza tumeanzisha hii Tume ya Umwagiliaji.
Tukasema kwanza tumalize miradi ambayo tayari ilikuwa inaendelea. Katika mwaka utakaofuata, miradi hiyo yote tutakwenda kuiangalia na kuipangia fedha ili iweze kumalizika. Kwa hiyo, lazima twende kwa hatua, lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti tulianza kwanza na miradi ambayo ilikuwa inaendelea, lakini nikuahidi kwamba katika mwaka utakaofuata tutakwenda kuikamilisha miradi iliyobakia.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kumekuwa na taarifa zilizotapakaa katika mitandao ya kijamii zinazoeleza ugunduzi wa gesi aina ya helium. Je, Serikali inaweza kutueleza nini juu ya taarifa hizo, ni za kweli au ni za uongo?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba, utafiti umefanywa na vyuo ambavyo vinatambulika duniani kimojawapo ni Oxford na Durham na wamepiga mahesabu kutokana na utafiti wa Jiofizikia uliofanywa miaka ya 80 na 90 wakafikia kiwango cha gesi ya helium.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tofauti hapa ya hizi gesi, helium inapatikana kwenye kina kifupi lakini hii gesi nyingine methane inapatikana kwenye kina kirefu na duniani ambaye ana helium nyingi ni Marekani. Kwa hiyo, gesi kule Marekani inaanza kupungua ndiyo maana na sisi tunaitafuta kwa udi na uvumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichogundulika ni kutokana na mahesabu ya huko nyuma na kinachofuata kwa miezi michache inayokuja Helium One ikishirikiana na watalaam wengine watafanya drilling ya huko Ziwa Rukwa. Hapo ni upande wa Ziwa Rukwa ndiyo imepatikana kiasi hicho estimate ya kwanza 54.2 billion metric cubic feet. Hata hivyo, watachimba kule Lake Rukwa, wataenda Eyasi, wataenda Natron nadhani baada ya kama mwaka mmoja hivi tutajua kwamba tunaweza kuanza kuuza helium duniani. Kwa hiyo, hizo ni taarifa za uhakika zinatoka chuo cha uhakika cha Oxford.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanzishwa kwa pori hilo mwaka 1959 hadi sasa ni miaka 57; je, Serikali inaweza kusema kwa kipindi hicho, imepata faida gani zaidi ya Askari Wanyamapori kukodishia wafugaji na wakulima wasio na uwezo kuruhusiwa kulima halafu baadae wanagawana mazao?
Swali la pili, kwa majibu yaliyotolewa ninapata imani kuwa, Mheshimiwa Waziri anadanganywa na wataalam wa chini yake. Je, yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kwenye Mbuga hiyo, ili akajionee changamoto zilizopo na baadae asiweze kudanganywa na watumishi wake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza pori lina faida gani na zaidi ya miaka 50 iliyopita anataka kujua kuna faida gani imepatikana kutokana na uhifadhi huo?
Kwanza niseme tu kwamba faida za uhifadhi ziko zile ambazo unaweza ukazitazama kwa macho au ukazikamata mkononi ambazo ni za kifedha na pengine ni za kiuchumi moja kwa moja. Lakini uhifadhi hasa wa mapori wakati mwingine faida zake unaweza usizione kwa macho au ukakamata kwa mikono kwa sababu faida zake ni za kiikolojia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, faida zake zinakwenda kuambukiza hata uwekezaji, hata shughuli zingine za kiuchumi, lakini pia hata uwepo wa dunia tunayoishi na nchi tunayoishi yakiwemo masuala ya hali ya hewa, upatikanaji wa maji, na mambo mengine ya namna kama hiyo. Kwa hiyo, faida zipo na ni nyingi, lakini kama alikuwa anakusudia za kiuchumi zinazohusiana na fedha, hilo ni suala la takwimu na kwa hiyo basi anaweza kutafuta fursa tukaonana na kwa kutumia wataalam ambao na wenyewe nitawasemea kwenye swali la pili basi tunaweza tukapata takwimu, kujibu vizuri zaidi kuhusiana na suala la faida za kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la kuongozana, kwanza niweke sawa juu ya suala hili ambalo linajirudia mara nyingi sana la kwamba kuna kupata taarifa ambazo ni za uongo au za kudanganywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna jambo niko makini nalo ni hilo na naomba Waheshimiwa Wabunge mnisaidie ili kwa upande wangu lakini nafikiri kwa Serikali nzima; ikiwa kuna majibu ambayo yanakuwa yanatia mashaka na pengine ni ya uongo; kwa sababu majibu ya uongo ni kama vile yamedhamiliwa. Kama kunajitokeza mazingira kama hayo, basi tuanze sasa kukataa namna hiyo ya kufanya kazi, kwa sababu hiyo ni namna ambayo haifai.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa upande wangu anayetoa jibu ninamfahamu, na anapotoa jibu namuambia anaweka saini kabisa kwenye jibu hilo analonipatia. Sasa baada ya hili kwa sababu tayari umeishanipa hiyo indication baada ya hapa, mimi na yeye tutakwenda kutafuta jibu sahihi ni lipi kulinganisha na hili ili yule aliyelitoa sasa kama kweli amedanganya, kwa sababu kudanganya ni dhamira, basi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni na taratibu, lakini kwa kawaida kila mmoja kila mtumishi wa Serikali, anao wajibu wa kutenda kazi zake sawa sawa na anao wajibu kwenye masuala ya kujibu maswali, anao wajibu wa kujibu maswali kwa niaba ya Serikali na kwa hiyo, anawajibika kutoa majibu ambayo ni sahihi.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ina vituo vya afya vitano ambavyo havina magari ambavyo ni Laela, Kayengeza, Msanadamungano, Mpuwi na Milepa, na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imejitahidi sana katika kuweka bajeti kwa mwaka 2013/2014, 2014/2015 ili kukabiliana na adha hii lakini Serikali haijatoa fedha ili halmashauri iweze kununua magari hayo. Sasa Serikali inaithibitishiaje halmashauri kwamba ikitenga fedha inaweza kuipatia ili iweze kununua magari kukabiliana na tatizo hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia tatizo la msongamano wa wingi wa wagonjwa katika Kituo cha Afya Laela, na amezungumzia utatuzi wa tatizo hilo kwa mpango wa muda mrefu, wakati kwa sasa tatizo hilo ndiyo lipo na ni kubwa sana kutokana na wingi wa watu na kupanuka kwa mji mdogo. Nataka Serikali inieleze, kwa sasa inafanyaje mpango wa dharura ili kuokoa wananchi wanaosongamana katika kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mchakato wa bajeti unaokuja, naomba ninyi anzeni tu ule mchakato wa awali wa kuhakikisha kwamba mnatenga ile bajeti halafu sisi tutasimamia jinsi gani katika Bajeti ya mwaka 2017/2018 hilo gari liweze kupatikana, yaliyopita si ndweli tugange yajayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msongamano wa sasa tulionao katika hospitali, nakumbuka Mheshimiwa Mbunge tulikuwa pamoja pale katika eneo lako. Kwanza wasiofahamu jimbo la Mheshimiwa Malocha, liko kama mbalamwezi hivi ambao mwezi mchanga, ambayo kuna watu wengine wanatoka maeneo ya Pembe mbali sana kuja katika Hospitali ya Sumbawanga. Kwa hiyo, mwenyewe nime-verify lile tatizo, ni tatizo la msingi na hili naomba nimwelekeze RAS wetu wa Mkoa wa Rukwa kwamba aangalie jinsi gani kwanza kama mpango wa haraka kuhakikisha eneo hili linapata angalau huduma katika sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni kweli, wananchi wa Mheshimiwa Malocha pale wakitoka kule Pembe mpaka kufika hapa kama mgonjwa anaweza akafariki. Kwa hiyo, naomba nikwambie ofisi yetu itawasiliana na ofisi ya mkoa pale tuangalie mipango mikakati ya haraka kuwasaidia wananchi wa eneo lako ilimradi waweze kupata huduma ya afya kama ilivyokusudiwa na Watanzania wengine.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa majibu mazuri na ufafanuzi wa swali langu la msingi umeeleweka lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Jimbo la Kwela? Nauliza hivyo kwa vile Ukanda wa Ziwa Rukwa haujaguswa kabisa karibu Kata 13 na Kata saba za Ukanda wa Juu na zenyewe hazijaguswa kabisa, jumla Kata 20 hazijaguswa hata kijiji kimoja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itamalizia kupeleka umeme katika REA III katika vijiji 68 ambavyo havijapelekewa umeme katika Kata za Mpwapwa, Jangwani, Mpuhi, Likozi, Kalambanzite, Lusaka, Lahela na Sandurula?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Malocha kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya umeme kwa wananchi wa Jimbo lake. Mheshimiwa hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ni lini Serikali itapeleka
umeme katika Kata zake 20 ambazo zimebaki, kwanza kabisa tunakubaliana na Mheshimiwa Malocha kati ya Kata 27 zilizopata umeme ni Kata mbili ziko katika Jimbo lake. Kwa hiyo, Kata 25 zilizobaki kama ambavyo ameeleza ikijumlishwa pia Kata zake za Kipeta, Kilangawani, Kigamadutu pamoja na Malegesya na shule za sekondari
alizozitaja zitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA ambao umeanza kutekelezwa nchi nzima mwezi huu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimpe uhakika
Mheshimiwa Malocha kwamba Kata zake zote 27 na zile mbili ambazo zimepata bado Vitongoji vyake navyo vitapelekewa umeme kuanzia mwezi huu hadi miaka minne ijayo. Kwa hiyo, tuna uhakika Kata zako 27 Mheshimiwa Malocha zitakuwa zimepata umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vijiji 68, ni kweli
kabisa vipo vijiji 68 katika Jimbo la Mheshimiwa lakini na vitongoji 237. Tunapopeleka umeme katika vijiji 68 katika Jimbo la Kwela tunapeleka pia katika vijiji 237 ambapo vitongoji vyake vyote havijapata umeme.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa
Malocha vitongoji vyake vyote ambavyo havijapata umeme vile vya Mpwapwa, Muze, Halula na Mwandui vyote vitapata umeme. Ahsante sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana; lipo tatizo kubwa kati ya Uwanda Game Reserve na vijiji vya Kilangawana, Maleza, Legeza, Mpande, Ilambo, Mkusi, Iweliamvula na Ngomeni. Kwa watu wa TFS
kuhamisha mipaka inayotambulika toka enzi za nyuma na kusogeza katikati ya vijiji. Tatizo hili ni kubwa sana na mimi nilishaenda mara kadhaa kumwambia Waziri kwamba naomba afike asikilize pande zote mbili kwa sababu ninachokiona hawa askari wa TFS ni kama wanagandamiza wananchi wakati jambo lipo wazi. Je, ni lini Serikali itatuma uongozi wa kwenda kuangalia haki juu ya wananchi wale?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, anazungumzia juu ya suala la Uwanda Game Reserve na ujirani wake na vijiji vilivyopo jirani na eneo hili la hifadhi. Na hoja yake inafanana na zile hoja zilizotangulia
pale mbele kwamba mipaka iliyowekwa na TFS katika miaka ya karibuni au katika siku za karibuni imeingia ndani ya maeneo ya vijiji.
Kama nilivyosema hapo awali kwamba sio vema
kwenda moja kwa moja na kutoa kauli ambayo inaonekana kama ni ya uthibitisho au ni ya ukweli kwamba mipaka ya hifadhi ndiyo iliyoingia kwenye maeneo ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niweze kusema jambo moja tu hapa kwamba tuelewane kitu kimoja kwamba mipaka tunayoizungumzia ya miaka mingi haikuwa na alama; kwa hiyo, kuna suala la kuweka mpaka kuwepo lakini kuna suala pia la mpaka kuwekewa alama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka ya karibuni kilichofanyika au kinachoendelea kufanyika ni kuweka alama za kudumu hizo beacons au maboya au unaweza kutafuta
lugha nyingine yoyote ya Kiswahili, lakini ni alama
zinazoonekana. Sasa wakati wa kuweka alama
zinazoonekana Serikali inafuata mipaka ambayo ipo kwa mujibu wa maandishi kwa kutumia GPS coordinates kwenye ramani ambayo haikuwa imewekewa alama. Sasa kwa kuwa wananchi hawakuiona ile mipaka kwa alama zinazoonekana
licha ya kwamba kwa mujibu wa sheria zipo kwenye ramani, sasa hivi wananchi wanadhani kwamba alama hizo zimehama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba alama hizo zinawekwa mahali pale ambapo ndipo kwa mujibu wa sheria alama hizo ndipo zilipo na kwa hiyo sasa ni vema tukasubiri utaratibu unaofanyika na Serikali wa kwenda kuweka alama kwenye maeneo hayo kwa sabau kuweka alama sio maana yake tayari hatua za mwisho zimeshafanyika za kuweza kuwahamisha wananchi; tunaweka kwanza alama kutambua maeneo hayo halafu baada ya pale tunaweza kuendelea na kuelimishana kwamba kwa nini mpaka upo hapa na sio pale.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara hii nimekuwa nikiulizia mara kwa mara na hii ni kutokana na umuhimu wake. Katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 ukurasa wa 62 inaeleza kuwa itafanyiwa upembuzi yakinifu na hivi sasa ni miaka miwili sioni dalili ya kutenga pesa kwa ajili ya kufanya usanifu katika barabara hiyo. Je, ni lini sasa Serikali itatenga pesa kwa kuanza kazi hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mawaziri wote wawili ni wapya, yawezekana hawajatambua vyema umuhimu wa barabara hii. Naomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara ya kutembelea barabara hii toka Mlowo hadi Kibaoni ili ajionee fursa zilizopo katika barabara hiyo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu sana umuhimu wa barabara hii na pengine hukupata fursa ya kufahamu Waziri wangu alishapita katika sehemu ya kipande cha hiyo barabara; nami nilikusudia kupita lakini kwa bahati mbaya kulikuwa na dharura. Nimhakikishie sasa hivi baada ya Bunge nitapita katika barabara hiyo na nitaanzia Tunduma. Kwanza kuanzia Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe kuanzia Vwawa, Tunduma na nitafuata hii barabara mpaka inakoishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuahidi nitafuata hiyo na tumempa commitment na fedha zimetengwa, tunaanza na ujenzi wa Daraja la Momba na mara tutakapomaliza Daraja la Momba tutatenga fedha ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza katika swali la msingi umuhimu wa ujenzi wa daraja la Mto Momba kwamba ni kiungo muhimu katika kuunganisha mikoa mitatu. Kwa kuwa Sera ya Serikali katika ujenzi wa barabara za lami inazingatia barabara zinazounganisha mikoa. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii muhimu kwa kiwango cha lami inayounganisha mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Ignas Malocha kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufuatilia ujenzi wa barabara hii.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Malocha amekuja ofisini kwetu mara nyingi na tumeongea sana kuhusu barabara hii na tumemwambia mara tutakapokamilisha ujenzi wa daraja la Momba hatua itakayofuata ni kuhakikisha tunaanza na kazi ya feasibility study and detail design kwa ajili ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Tumeongea hayo ofisini na mimi nimwombe yale ambayo tulikubaliana ofisi tutayatekeleza kwa manufaa ya wananchi wa mikoa hii mitatu.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Serikali imejenga mradi wa maji katika Mji Mdogo wa Laela ulioanza mwaka 2014 na umetumia takribani shilingi bilioni moja na milioni mia nne; na mradi huu unaonekana umekwisha, lakini cha ajabu hautoi maji, jambo ambalo limeleta taharuki kubwa sana kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Laela. Je, ni lini Serikali itahakikisha maji yanatoka katika mradi huo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, huu Mradi wa Mji wa Laela ambao Mheshimiwa anauzungumzia nimeutembelea na nimeona umefikia hatua za mwisho, walikuwa katika ufungaji wa zile solar panels. Sasa katika ufungaji wa solar panels kukatokea kwamba ile mota ambayo iliwekwa haiendani na ukubwa wa zile panels. Kwa hiyo nimetuma wataalam waende kule wakaangalie namna ya kutatua tatizo hilo. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha mradi ule ambao umetumia fedha nyingi za Serikali unafanya kazi kwa manufaa ya wananchi.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mahakama ya Mwanzo Mtowisa ni mahakama iliyojengwa toka enzi za mkoloni na kutokana na hali hiyo imechakaa na inahatarisha maisha ya wananchi. Ndiyo maana Serikali katika bajeti ya mwaka 2015/2016 ni miongoni mwa mahakama iliyopangwa kujengwa upya. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuipa kipaumbele cha pekee kunusuru hali inayoweza kutokea kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa vile vikwazo ulivyovieleza vya upatikanaji wa kiwanja na hati miliki vyote vilishakamilika na uongozi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga ulishathibitisha. Je, ni lini sasa Mahakama hiyo itaanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU - KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi kwamba katika mipango ambayo Wizara tumejiwekea ni kuhakikisha tunatimiza ukarabati wa ujenzi wa Mahakama kadri ya upatikanaji wa fedha za maendeleo. Hivyo kwa sababu katika mwaka huu wa 2017/2018, Mahakama ya Mwanzo Mtowisa ni kati ya Mahakama za Mwanzo ambazo zimewekwa katika mkakati huu, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi fedha zitakapopatikana jambo hili litatekelezeka.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kwa sasa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Ujenzi la Taifa, baada ya utafiti kufanyika kupitia teknolojia mpya ya ujenzi wa Mahakama kupitia Moladi ambapo imeokoa takribani asilimia 50 ya gharama za kawaida naamini kabisa fedha hizi zikipatikana Mahakama ya Mwanzo wa Mtowisa na yenyewe itaguswa pia.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kushika nafasi hiyo mpya na kwa kweli ameanza kuifanya vizuri Mwenyezi Mungu aendelee kumuongoza aendelee kuifanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza sisi sote tunafahamu wazi kwamba maeneo yaliyo na madini yanatoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri kwa machimbo madogo madogo kwa kujipatia kipato na vilevile Serikali kukusanya kodi. Tunafahamu kwamba Serikali ilishafanya utafiti katika maeneo mengi, lakini utafiti huo uko ndani ya vitabu mpaka uende maktaba jambo ambalo sio rahisi wananchi wa kawaida vijijini kutambua wapi kuna madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa nini Serikali isiainishe maeneo yote yenye madini kwa uwazi ili wananchi waweze kuyatambua na kufanya kazi ya uchimbaji mdogo mdogo?
La pili umesema kwamba wananchi wanaweza kutumia ofisi za kanda za Magharibi zilizopo Mpanda na Dodoma, jambo ambalo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida hasa wa vijijini kuzitumia ofisi hizo kutokana na umbali uliopo. Kwa nini Serikali isiweke branch katika mikoa yote ili kurahisisha wananchi kuzishilikia ofisi hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ijulikane tu kwamba matumizi ya ofisi zetu za Wakala wa Jiolojia ni matumizi ambayo yanawahusu Watanzania wote. Ni bahati mbaya tu kwamba wageni wanaotoka nje kuja kutafuta madini hapa nchini wao wanazitumia zaidi ofisi hizi kuliko sisi Watanzania.
Naomba nitoe wito sasa kwa Watanzania wote tuzitumie Ofisi zetu hizi za Wakala wa Jiolojia ili ziweze kutusaidia katika sekta hii ya madini.
Lakini la pili kwa nini Serikali sasa isiweke branch kwa kila Wilaya na kila maeneo. Naomba nimuombe Mheshimiwa Malocha, na kwasababu amekuwa mdau mkubwa sana wa kufuatilia jambo hili kwaajili ya wananchi wake; sisi ni watumishi wa wananchi, sisi hatukai ofisisni Mheshimiwa Malocha ukiwahitaji wataalamu wetu wa Jiolojia kuja kwenye eneo lako wakati wowote watakuja, na hata kama utamuhitaji Waziri mwenyewe atakuja kwasababu sisi ni watumishi wa wananchi.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru Serikali kwa jitihada zake za ku-support ujenzi wa vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu la Kwela tunavyo vituo vya afya ambavyo vimeanza kujengwa toka mwaka 2004 na wananchi wamejenga mpaka jengo la OPD kukamilika, lakini vituo hivyo mpaka sasa vimesimama kwa sababu havijapata fedha tena. Vituo hivyo ni Kituo cha Ilemba, Kahoze na Muze.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha ku-support wananchi juhudi zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anauliza ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya ambavyo vimeanzishwa na wananchi muda mrefu.
Kwanza naomba nimtaarifu kwamba nia njema ya Serikali ya kuhakikisha kwamba huduma ya afya inafika kila mahali ikiwa ni pamoja na Wilaya yake, katika hospitali 67 ambazo zinaenda kujengwa za Wilaya na Wilaya yake ni miongoni mwa hospitali ambazo zitaenda kujengwa. Hiyo ni nia njema ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma inapelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hivyo vituo vyake kama nilivyojibu kwenye swali la msingi pale pesa inapopatikana hakika naomba nimhakikishie na hii itakuwa miongoni mwa vituo vya afya ambavyo vitaboreshwa ili viweze kutoa huduma tunayoitarajia.(Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru Serikali kutambua umuhimu wa barabara hiyo kiuchumi. Barabara hiyo ipo toka enzi ya mkoloni na kutokana na milima na miinuko iliyopo katika barabara hiyo, kipindi cha masika husababisha ajali nyingi sana, jambo ambalo huwatia hasara wananchi, pia Serikali kwa matengenezo ya mara kwa mara. Kwa nini Serikali isikubali kutengeneza hiyo barabara kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maeneo ya mlimani ni kilometa nane, barabara hiyo ni finyu sana, ikitokea lori limekwama, hakuna gari yoyote inayopita na husababisha adha kubwa kwa wananchi, kwa nini eneo hilo lisipanuliwe na kuwekewa kingo mlimani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu hili eneo la barabara hii ambalo linapita kwenye milima mikali amekuwa akilifuatilia sana mara nyingi, na mimi binafsi tumezungumza naye sana juu ya eneo hili na nilimwahidi pia kwamba baada ya Bunge hili nitatembelea eneo hili ili tuone namna bora zaidi ya kuweza kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua hii sehemu ambayo ina milima ndiyo maana kwa upande wa Serikali tunajenga barabara hii kwa kutumia zege na ninaamini kabisa tutakapokuja kufanya uamuzi wa kuweka lami katika barabara hii hatutarudia kufanya matengenezo kwenye sehemu hii ambayo tumeweka zege kwa sababu barabara iliyotengenezwa kwa zege ya cement inadumu kwa muda mrefu na inakuwa imara. Kwa maana hiyo ni kwamba matengenezo yanayoendelea ni sehemu ya mkakati wa kupunguza na kukamilisha matengenezo ya barabara katika sehemu hii korofi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wananchi wa Kwela kwamba tutalitazama vizuri eneo hili na ninatambua kwamba eneo hili la milima mikali na kule chini kuna utelezi mkali ambapo tunaweka changarawe. Kwa hiyo, tutaliangalia kwa macho mawili ili tuone namna bora ya kuboresha eneo hili. Barabara hii kama ulivyosema ni muhimu, tutajipanga kama Serikali tuweze kuiangalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge na wananchi wavute subira, wakati tunaendelea na michakato mbalimbali ya kukamilisha barabara katika maeneo mbalimbali, eneo hili tutalitazama kwa makini. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika majibu ya msingi ya Serikali imeeleza kwamba tani 62,000 za mahindi zilinunuliwa mwaka 2016/2017 na tani 26,000 zilinunuliwa mwaka 2017/2018. Unaona kwamba kiwango kinapungua badala ya kuongezeka wakati uzalishaji umeongezeka maradufu na wakulima wanaozesha mazao kwenye maghala. Ni zipi sababu zinafanya kiwango hiki kishuke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jinsi alivyozungumza ni kweli imekuwa ikishuka, mazao yetu yamekuwa yakishuka, lakini naomba niseme tu kwa kipindi cha mwaka wa fedha uliopita bajeti ilikuwa ndogo na tunategemea mwaka huu bajeti itaongezeka na hivyo tatizo zima hilo litakuwa limeshakamilika, ahsante. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA. Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri na Waziri wake kwa utendaji wa kazi, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, mradi huu wa Muze Group unategemewa kupeleka maji katika vijiji 10 vyenye wakazi 40,000 ambavyo ni Kijiji cha Kalumbaleza A, B, Muze, Mbwilo, Mlia, Mnazi mmoja Asilia, Ilanga Kalakala, Izia na Isangwa. Maeneo haya hukumbwa na kipindupindu kila mwaka kutokanana na shida ya maji, mwaka huu wananchi wapatao 605 waliugua kipindupindu, katika hao wananchi 15 walikufa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa mradi huu ili kunusuru vifo kwa wananchi?
Swali la pili, kwa vile Mtaalam Mshauri wa mradi huu alishaanza kazi na amesha- raise certificate Wizara ya Maji; Je, ni lini watamlipa fedha zake haraka ili mradi huu uweze kuanza mapema? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee anavyowatetea wananchi wake. Nataka niwahakikishie kwamba maji ni uhai, Wizara ya Maji hatutakuwa sehemu ya kupoteza uhai wa wananchi wake. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutakuwa sehemu ya kusimamia mradi huu ili uweze kutekelezeka kwa wakati wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge cha saa saba tukutane ili twende kuhakikisha Mkandarasi huyu analipwa kwa wakati ili mradi usikwame na wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuteuliwa lakini vilevile nimpongeze kwa ufafanuzi mzuri. Pamoja na ufafanuzi, ninayo maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Swali la kwanza, maeneo yenye rasilimali muhimu kama hayo ya Ziwa Rukwa pamoja na maelekezo mazuri ya Serikali yanahitaji ufuatiliaji na usimamizi wa karibu. Je, toka Serikali imetoa maelekezo hayo umefanyika ufuatiliaji kujiridhisha kama mazingira hayo hayaharibiwi tena?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, rasilimali muhimu ya gesi ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia inaweza kuinua uchumi wa Tanzania na kukuza uchumi wa Taifa letu kwa ujumla. Je, Serikali ina mkakati gani kuanza kuchimba gesi hiyo ili Taifa linufaike kabla gesi hiyo haijaanza kuchimbwa mahala pengine duniani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Malocha pia kwa ufuatiliaji wake mzuri na nimshukuru kwamba sasa kwenye eneo hili la Ziwa Rukwa tunaweza kuelekeza nguvu kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linahusu ufuatiliaji. Kwa kweli tuna kila sababu ya kushirikiana naye kwa ajili ya kufuatilia hili kwa kushirikiana na wananchi na viongozi walioko kule. Mheshimiwa Malocha nadhani baada ya Bunge hili tutakuwa pamoja kwa ajili ya kwenda kufuatilia kuona yale maagizo ambayo ameyatoa Mheshimiwa Waziri yametekelezeka kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye eneo la gesi, ni kweli kabisa imegundulika gesi hii ya helium ambayo ni maalum kabisa katika nchi yetu na sisi kwenye eneo letu la mazingira tayari imeshafanyika Tathimini ya Athari ya Mazingira kwa awamu ya kwanza kwa ajili exploration. Atakapopatikana mwekezaji kwa awamu ya pili tutakuwa tayari kuja kufanya tena Tathmini ya Athari ya Mazingira ili kuhakikisha kwamba gesi hiyo inapatikana na kuweza kutumika. Ahsante sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Barabara aliyoulizia Mheshimiwa Haonga ina umuhimu wa kipekee kwani inaunganisha mikoa mitatu, Mkoa wa Songwe, Rukwa na Katavi na ni barabara yenye umuhimu wa kiuchumi kwa mikoa ile mitatu hata kwa Taifa zima kwa ujumla. Katika Ilani ya CCM mwaka 2010, ukurasa wa 62, barabara hiyo iliingizwa kufanyiwa upembuzi yakinifu. Sasa hivi tumebakiza miaka miwili na nusu sioni dalili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu, ni lini Serikali itaanza kazi katika barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge tumezungumza sana kuhusu maeneo yake na maeneo haya ambayo anazungumza ya Kwera yana structure special. Nimhakikishie yeye na wananchi kwamba eneo hili tunaendelea kulitazama vizuri.
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii inaunga Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi. Barabara hii ukiifuatilia kutoka Kamsamba inaenda kuungana kule Kibaoni. Kama nilivyosema nitapita kuangalia lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa kwamba zile ahadi zinaendelea kutekelezwa. Bado miaka miwili lakini naamini hapa mwishoni speed yetu itakuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za ujenzi zimeshaanza. Kwetu sisi kutambua mahitaji, kufanya usanifu na michoro ni hatua za ujenzi. Kwa hiyo, tutakwenda kwenye hatua nyingine ya mwisho kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi na nimwombe tuendelee kushirikiana na kupeana mrejesho ili hatimaye hii barabara tuweze kuiunga na mikoa hii mitatu iweze kuwa katika muunganiko mzuri.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali ina mpango gani wa kiuchumi wa kuimarisha barabara za vijijini katika mikoa ambayo haijapitiwa na lami ili kwenda sambamba kiuwiano kiuchumi tunapokwenda kwenye Serikali ya viwanda na uchumi wa kati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la ndugu yangu Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara za vijijini kikawaida unaratibiwa na TARURA. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea na michakato, lakini mapendekezo ya ujenzi wa barabara zote za vijijini kama nilivyozungumza huwa unaanzia kwenye Mabaraza ya Madiwani, inakwenda kwenye RCC kisha kama Wizara tunapatiwa. Kama linatuhusu Wizara ya Ujenzi, tunalishughulikia kama ipasavyo lakini kama inahusu TARURA, basi wenzetu wa Wizara ya TAMISEMI nao wanashughulikia kama inavyopaswa. Ahsante.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ziwa Rukwa linatoa ajira kwa wananchi wengi kutoka katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Vilevile ni ziwa ambalo imegundulika gesi aina helium lakini ziwa hilo hilo linatabiriwa kukauka kwa miaka ijayo. Nini mkakati wa Serikali katika kunusuru ziwa hilo lisikauke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Malocha, Mbunge wa Kwela, shemeji huyu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi sana, tayari Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa January Makamba alishatoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba wanawasilisha ofisini kwetu vyanzo vyote vya maji pamoja na changamoto zake. Ziwa Rukwa ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya maji ambavyo hata bila kutuletea jina hilo tayari kitaifa tunafahamu kwamba Ziwa Rukwa ni chanzo cha maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Malocha na Mheshimiwa Mulugo, baada ya mkutano huu mimi pamoja na wataalam tutakuja kwenye Ziwa Rukwa ili kujionea sisi wenyewe namna gani mazingira yalivyoharibiwa ili tuweze kuchukua hatua stahiki na za haraka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Malocha pale kwa shemeji yangu Movu pale wapelekee salamu waanze kufanya maandalizi ili wanipokee twende nao Ziwa Rukwa tuweze kufanya kazi hii ya Serikali. ahsante sana. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ujenzi wa miradi ya umeme awamu ya pili na awamu ya tatu bado utekelezaji wake hauendi kasi kama ilivyopangwa hasa katika Mkoa wa Rukwa, Jimbo la Kwela na tatizo kubwa ikiwa ni upatikanaji wa nguzo. Mkoa wa Rukwa unahitaji nguzo 13,000. Pamoja na jitihada zote, ni nguzo 350 tu zilizopatikana. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hilo ili miradi ya umeme iweze kutekelezwa haraka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na kweli nilitembelea eneo lake. Nimhakikishie tu kwamba kero ya nguzo kwa sasa kimsingi haipo. Mwanzoni mwa mwaka 2017 tulisitisha kuingiza nguzo kutoka nje ambapo ndiyo lilikuwa tatizo la Wizara kwa muda mrefu. Waagizaji wa nguzo walikuwa wanachukua miezi sita hadi nane kufikisha hapa nchini, hivi sasa nguzo zinapatikana. Mahitaji yetu ya nguzo kwa mwaka ni 200,800 wakati nguzo zinazopatikana kwa wazalishaji wa ndani ni nguzo 2,000,872. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge miradi hii itatekelezeka kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimetembelea Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na nampongeza sana anavyohangaikia maendeleo ya wananchi wake. Ni kweli mkandarasi anasuasua na jana tumemwelekeza, hivi sasa anaendelea katika Kijiji cha Maendeleo ili kusudi aanze kuwapatia wananchi umeme. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Mbunge lakini suala la nguzo hivi sasa siyo kero kubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Ni lini Serikali itatatua mgogoro wa muda mrefu wa mpaka kati ya Hifadhi ya Uwanda na Vijiji vya Ilambo, Mpande, Kilangawana, Legeza, Kapenta, Mkusi na Iwelamvua ili kuondoa manyanyaso ambayo wananchi wanapata kwa kunyang’anywa mazao, vifaa vyao vya kilimo na kuwapiga na mwaka juzi mtu mmoja aliuwawa? Ni lini Serikali itatatua mgogoro huu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Malocha, Mbunge machachari kweli kweli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kumekuwepo na changamoto ya mgogoro ambayo imekuwepo katika eneo lile. Hivi sasa tumejipanga katika kipindi hiki, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii atakwenda kuona eneo hilo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane ili kusudi apate ratiba kamili ni lini atakuja, mtatembelea maeneo ya vijiji vyote hivyo na kuona ni hatua gani zichukuliwe kuhakikisha kwamba hiyo migogoro ambayo imedumu muda mrefu basi yote inatatuliwa kwa kipindi hiki.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Ni lini Serikali itatatua mgogoro wa muda mrefu wa mpaka kati ya Hifadhi ya Uwanda na Vijiji vya Ilambo, Mpande, Kilangawana, Legeza, Kapenta, Mkusi na Iwelamvua ili kuondoa manyanyaso ambayo wananchi wanapata kwa kunyang’anywa mazao, vifaa vyao vya kilimo na kuwapiga na mwaka juzi mtu mmoja aliuwawa? Ni lini Serikali itatatua mgogoro huu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Malocha, Mbunge machachari kweli kweli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kumekuwepo na changamoto ya mgogoro ambayo imekuwepo katika eneo lile. Hivi sasa tumejipanga katika kipindi hiki, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii atakwenda kuona eneo hilo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane ili kusudi apate ratiba kamili ni lini atakuja, mtatembelea maeneo ya vijiji vyote hivyo na kuona ni hatua gani zichukuliwe kuhakikisha kwamba hiyo migogoro ambayo imedumu muda mrefu basi yote inatatuliwa kwa kipindi hiki.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa umaarufu huo wa mabonde katika Ziwa Rukwa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilishaomba miradi ya umwagiliaji yapata sasa miaka mitano haijapata fedha ambayo ni Maleza, Ilemba, Msiya, Uzia, Kwilo na Milepa. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili miradi hiyo iweze kujengwa kwa manufaa ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana. Kikubwa niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge sisi kama Wizara ya Maji kama nilivyoeleza tunaendelea kutokana na changamoto zilizopo katika kilimo cha umwagiliaji ama uwekezaji wa umwagiliaji, tunazo skimu nyingi lakini hazijakamilika, Waziri wangu akaona haja sasa ya kupitia mpango huu kabambe ili tuwe na skimu chache ambazo zitakuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya mapitio haya katika maeneo ambayo ameyaelekeza tutawekeza fedha katika maeneo yake ili wananchi wanaweza kulima kilimo cha umwagiliaji.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, naipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya, vilevile upanuzi wa vituo vya afya, tunapongeza sana jitihada hizo za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na majibu hayo ninayo maswali mawili ya nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni kweli imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ilemba lakini katika bajeti zake mfululizo imekuwa ikitenga fedha kwa maana ya kumalizia jengo hilo lakini mfululizo wa miaka karibu minne Serikali haijatoa fedha. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba eneo hilo lina mwingiliano mkubwa sana wa watu kutokana na biashara ya mpunga na samaki na kunakuwa na milipuko mingi ya magonjwa, wananchi wanakufa, wanapata taabu sana. Naomba Serikali sasa itambue kilio hicho iweze kutupatia fedha kumalizia kituo hicho cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa Kituo cha Afya Ilemba, vipo vituo vingine vilishaanza kujengwa katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Vituo vya Afya vya Muze, Kaoze, Kiteta, Kalambanzite pia zahanati 12 na hii yote inatokana na sera ya kila kata kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kuwa na zahanati, jambo ambalo Serikali yenyewe imepanga na tumewahamasisha wananchi. Ni nini kauli ya Serikali katika kukamilisha majengo haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu, naomba uniruhusu kipekee nimpongeze Mheshimiwa Malocha na wananchi wake wa Jimbo la Kwela kwa jinsi ambavyo wameitikia wito mkubwa wa kuhakikisha kwamba ujenzi unafanyika. Kipekee, naomba nimpongeze hata Mkuu wa Mkoa, nilimuona akishiriki yeye mwenyewe katika kuchimba msingi katika ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwanza tunathamini sana jitihada ambazo zinafanywa na yeye binafsi na wananchi wake. Kwa kadri bajeti ya Serikali
inavyoruhusu, maeneo yote ambayo ameyataja, pia hajataja Kituo cha Afya Mpui, naomba nimhakikishie, kwa kadri bajeti itakavyoruhusu hatuwezi tukaacha nguvu za wananchi zikapotea bure. Iko kwenye Ilani yetu ya CCM, tumeahidi, tutatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Eneo hilo la kilometa 86 ni eneo korofi na liko katikati ya mbuga ya wanyama, wakati mwingine kama gari zinasafiri inafika gari inakwama katikati ya mbuga, jambo ambalo ni hatari kwa raia ambao watakuwa wamepanda basi hilo. Je, Serikali ituambie imetilia umuhimu gani kuliko kusema kwamba itakapopata fedha kwa sababu jambo hili ni muhimu mno kuliko, naomba majibu ya Serikali katika suala hilo, ni lini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nashukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja la Mto Momba ambalo linaunganisha mikoa mitatu. Nataka kuuliza baada ya ujenzi wa daraja hilo ni lini sasa Serikali itatenga pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu, kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, barabara inayounganisha mikoa mitatu, Mkoa wa Songwe, Rukwa na Katavi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ambayo nimetoka kujibu swali lake kwa sababu utagundua kwamba asilimia 65 ya barabara hii baada ya usanifu tulifanya ujenzi na ujenzi ulizingatia maeneo korofi zaidi. Nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba sehemu hii iliyobaki bado ina maeneo changamoto wakati fulani. Sisi kama Serikali tumeendelea kutenga fedha ili kushungulikia maeneo haya korofi. Hata katika mwaka huu wa fedha unaoendelea tumekuwa na fedha za kutosha kuhakikisha maeneo korofi wakati wowote tunayapa umuhimu wa kuyafanyia matengenezo.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa eneo hili watakuwa mashuhuda wa kuona kwamba wakati wote tunahakikisha kwamba barabara hii inapitika wakati tunajiandaa kwa ajili ya kuitengeneza katika kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira kwa vile sehemu kubwa ya barabara tumeitengeneza hii sehemu ndogo iliyobaki tutakwenda kuitengeneza kwa kiwango cha lami. Tumeweka mapendekezo katika bajeti hii inayokuja kama Bunge lako litatupitishia na Serikali ikapata fedha tutakwenda na hatua ya mwisho kuikamilisha barabara hii.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu barabara hii inayopita katika Daraja la Mto Momba, Mheshimiwa Mbunge anafahamu na nimetembelea eneo hili, ujenzi wa daraja umekamilika kwa sehemu kubwa na sasa tunaweza kupita mto huu. Mheshimiwa Mbunge anafahamu barabara hii ni ndefu sana ukitoka Momba mpaka uje Majimoto na mimi nimeliipita. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeiweka kwenye mpango wetu mkakati kwa maana ya sasa kufanya usanifu baada ya kukamilisha sehemu ya Mto Momba ambayo ni korofi ili sasa tuweze kuitazama kwa ajili ya kuitengeneza katika kiwango cha lami. Kwa hiyo, tuvute subira Serikali ikipata fedha tutakamilisha barabara hii.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa daraja, imekuwa ni faraja kubwa kwa kweli kwa wananchi, tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu hayo, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa barabara hiyo na imekubali kuanza kutenga fedha kwa ajili ya usanifu kwa maana ya kuweka lami lakini bado katika barabara hiyo yapo maeneo korofi ambayo yanasababisha magari kukwama wakati wa masika. Je, kwa nini Serikali isitenge fedha za kutosha kutatua tatizo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kipande cha barabara ya Ntendo - Muze chenye kilometa 37.07 ni barabara inayotegemewa na wananchi wa Bonde la Ziwa Rukwa katika kupeleka mazao Mji wa Sumbawanga; na kwa kuwa barabara hiyo ina changamoto nyingi sana ya kukwamisha magari.

Mheshimiwa Mwwenyekiti, mwaka 2017/2018 Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kuweka lami kilometa 2 jambo ambalo linaweza likachukua miaka 18 kumaliza barabara hiyo. Kwa nini Serikali isiongeze fedha zaidi kuhakikisha barabara ile inakamilika ili kutoa huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya mwanzo nimeeleza tu kwamba kwenye mwaka huu wa fedha 2019/ 2020 tutakuja kuliomba Bunge lako Tukufu litupitishie bajeti yetu ili tuweze kutatua changamoto mbalimbali za barabara zetu hapa nchini ambazo zina mtandao mrefu sana na ambao kwa ujumla kabisa tayari upembuzi yakinifu ulishafanyika na tunaendelea na usanifu wa kina kwa maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, jibu lake la kwanza ni kweli kwamba mwaka huu tutatenga fedha nyingi kwa maeneo korofi ambayo yako kwenye barabara niliyoitaja hapo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwenye barabara ya Ntendo – Muze kwanza kuna milima mikali sana, na kwa kweli barabara ile ni mbovu na ina changamoto na ndiyo barabara ambayo tunategemea kupata mazao mengi kutoka maeneo hayo. Kuna fedha ambayo tumetenga kupitia TANROAD kwa ajili kwenda kurekebisha maeneo korofi ili barabara iweze kupitika mwaka mzima.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali katika REA awamu ya pili ilichukua umeme kutoka Mjini Sumbawanga na kupitisha katika jimbo langu kupeleka Mkoa wa Katavi maeneo ya Kibaoni bila kushusha umeme katika Vijiji vya Mbwilo, Mnazi, Kalumbaleza, Mpete, Mtapenda, Mfinga na Kizungu. Je, ni lini Serikali itashusha umeme katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze kwa kazi nzuri anayofanya kwenye jimbo lake na yeye mwenyewe anathibitisha tulishafanya ziara pia katika Mkoa wa Rukwa na Jimbo lake zaidi ya mara mbili. Nataka nimwarifu maeneo hayo ambayo ameyataja ambapo umeme ulipita wakati unaelekea Mkoa wa Katavi kwamba tumeshatoa maelekezo maeneo hayo yaingie kwenye REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili unaoanza Julai, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo Mkandarasi Nakuroi anaendelea na kazi katika Mkoa wa Rukwa na hususan katika jimbo lake na maeneo ambayo tulitembelea pamoja yanaendelea na kazi vizuri na yatawashwa umeme kwa kipindi kinachoendelea. Kwa hiyo kwa maeneo haya na kwa kuwa umeme ulipita na nafurahi leo ninaposimama hapa pia kama ambavyo mnafahamu Rais wa Benki wa Dunia ameshatoa fursa ya mradi wa kusafirisha umeme katika msongo wa KV 400 ambao unaelekea Sumbawanga, Mpanda, Nyakanazi, Kigoma, kwa hiyo kutakuwa na uhakika wa umeme katika maeneo aliyotaja Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Yapo mawasiliano hafifu katika Kijiji cha Kamnyazia, Kata ya Lusaka, Vitongiji vya Mpande. Halotel walishajenga foundation toka mwaka jana mwezi Agosti hawajaonekana. Ni lini sasa watakwenda kumalizia kazi ile ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameuliza maswali mengi sana kuonesha kwamba tunazo changamoto kubwa za minara katika maeneo yetu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge swali hili alilouliza kuhusu mnara wa Halotel nilichukue tu kama suala mahsusi ili tuweze kujua nini kilichotokea ili tuweze kuliondoa tatizo hilo na hatimaye mnara huu uweze kukamilishwa. Ahsante sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kabla sijaenda kwenye maswali, nami niungane na wewe kumpongeza Mheshimiwa Mzindakaya, nami ndio mrithi wake katika Jimbo, naomba wananchi waniunge mkono miaka 45 washuhudie maendeleo. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naenda kwenye swali. Namshukuru sana kwa majibu yenye ufanisi aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri, japo tatizo hili nimelisema hapa Bungeni mara nyingi sana, sasa ifike wakati Serikali iende kwenye utekelezaji iwasaidie wananchi hao ambao wanajisaidia wenyewe Serikali iwaunge mkono.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri afike kwenye eneo hili ili aone wananchi hawa wanavyohangaika kujinasua na umasikini. Waswahili wanasema kuona kunaongeza huruma kuliko kuambiwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha anataka kufahamu hatua za utekelezaji wa mradi huu umefikia wapi kwa sababu ameshasema mara nyingi. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, ni kwamba mradi huu umeibuliwa na nguvu wananchi na Serikali hii inawaunga mkono wananchi na ndiyo maana tumeanza kwanza kuboresha mfumo wa utendaji kazi wa Tume yetu ya Taifa ya Umwagiliaji. Kuanzia sasa tumeanza kujipanga Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ipo katika ngazi ya Wilaya, Mkoa, Kanda na Taifa.

Mheshimiwa Spika la pili, nachukua nafasi hii kuwaelekeza wataalam wa Taifa ya Umwagiliaji kwenda kwenye mradi huu haraka iwezekanavyo kufanya tathmini hiyo ili tuweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kufahamu ni lini nitaenda pale kuona? Baada ya Bunge hili nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, kuanzia tarehe 22 mwezi wa Tisa, nitakwenda huko kwenye Mikoa ya Rukwa na Katavi kwa ajili ya kufuatilia miradi hii. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nashukuru sana:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ile ya Awamu ya Pili ilipeleka umeme katika Mji Mdogo wa Laela, lakini haikushusha umeme katika sekondari ya Lusaka na Sekondari ya Kaengesa. Je, ni lini Serikali itashusha umeme katika sekondari hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Malocha amejielekeza kwenye utekelezaji wa REA II ambapo Mji wa Raela nao ulifikiwa, lakini ameeleza Sekondari za Kaengesa kwamba, hazijapatiwa umeme. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwanza nimpongeze kwa kazi nzuri, tuliambatana kwenye ziara katika jimbo lake mpaka Kilyamatundu, lakini tulitoa maelekezo kwamba, Mradi wa Ujazilizi Awamu ya II ambao unaanza tarehe 01Julai, 2019 na tuko hatua za mwisho za kuwapata wakandarasi maeneo ya Raela na hususan vitongoji ambavyo havijafikiwa na hizi sekondari.

Mheshimiwa Spika, namuagiza Meneja TANESCO wa Mkoa ahakikishe maeneo haya yanaingizwa kwenye Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili, ili waendelee kusambaziwa umeme na maeneo menginebya taasisi za umma katika Mkoa wa Rukwa kwa kuwa upo katika orodha ya mikoa 26 ambayo itafikiwa na Mradi wa Ujazilizi Awamu ya II. Ahsante sana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Upo mgogoro wa ardhi wa kimpaka kati ya vijiji vya Msandamuungano, Sikaungu na Gereza la Molo, je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo? Bahati nzuri na Waziri wa Mambo ya Ndani nilishamuona juu ya mgogoro huu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutoa hoja hii, lakini iko migogoro mingi kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi kwamba yako maeneo ambayo yana matatizo ya mipaka. Tumeshayapokea, tunayafanyia kazi na naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge, baada ya kumaliza kipindi cha maswali na majibu, tukutane ofisini kwa sababu akizungumza mpaka wa kijiji na kijiji hii inakuwa ni kazi ya TAMISEMI inahusiana na mambo ya GN. Ukizungumza habari ya magereza maana yake ni gereza kati ya wananchi lakini pia na Wizara yetu ya Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuonane, tuone kama maeneo haya ni miongoni mwa maeneo ambayo tumeyaainisha yenye malalamiko ili tuyafanyie kazi, mgogoro huu utaisha. Kama ni mipaka na mipaka na wenzetu wa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba maeneo yote ambayo yana migogoro yaishe mapema iwezekanavyo, kama kuna magereza iko pale inafanya kazi nzuri ya watu wetu, kama kuna vijiji ni kazi nzuri ya watu wetu ili malalamiko yasiwepo tuyamalize sisi kama viongozi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais. Ahsante.