Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ignas Aloyce Malocha (14 total)

MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Sumbawanga ina Wilaya mbili ambazo ni Sumbawanga Mjini na Sumbawanga Vijijini:-
Je, kwa nini ina Mkuu wa Wilaya mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa Halmashauri mbili unatokana na Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sura 287 (Mamlaka za Wilaya) na Sura 288 (Mamlaka ya Miji) ambapo lengo ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Sheria hizi zinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kuanzisha Halmashauri katika Wilaya moja zenye hadhi ya Wilaya, Mji, Manispaa na Jiji. Aidha, Wilaya ni sehemu ya Serikali Kuu ambayo uanzishwaji wake unazingatia Sheria ya Uanzishwaji wa Maeneo Mapya kwa maana ya Mikoa na Wilaya, Sura 297 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili Wilaya mpya iweze kuanzishwa vipo vigezo na taratibu mbalimbali ambazo vinapaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na mapendekezo hayo kujadiliwa katika Mikutano ya Vijiji, Baraza la Madiwani, Kamati za Ushauri za Wilaya na Mikoa. Hivyo, endapo halmashauri hizo mbili zikikidhi vigezo na kuwa na Wilaya kiutawala na hivyo kuwa na Mkuu wa Wilaya, nashauri mapendekezo hayo yapitishwe katika vikao vya kisheria ili yaweze kujadiliwa na hatimaye yawasilishwe kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa hatua zaidi kwa mujibu wa sheria.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Mbuga ya Akiba ya Uwanda katika Wilaya ya Sumbawanga Vijijini ilitengwa miaka ya nyuma wakati idadi ya watu ikiwa ndogo sana ikilinganishwa na sasa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kulipunguza pori hilo ili kunusuru shida inayowapata wananchi wanaozunguka eneo hilo ya kukosa maeneo ya kilimo na ufugaji?
(b) Je, kwa nini wananchi wa maeneo hayo wanapigwa na Askari wa Wanyamapori na kunyang’anywa mali zao, wakati hakuna alama yoyote inayoonyesha mpaka katika mbuga hiyo?
(c) Je, wananchi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo wamenufaika na nini zaidi ya vipigo wanavyovipata?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba Uwanda lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5,000 lilianzishwa mwaka 1959 na kutangazwa upya kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba 12 ya mwaka 1974, kwa tangazo la Serikali namba 275 la tarehe 8 Novemba, 1974. Kati ya mwaka 1974 na 2013 pori hilo lilikuwa chini ya usimamizi ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambapo lilikabidhiwa rasmi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii tarehe 20 Januari, 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, pori hili linazungukwa na jumla ya vijiji tisa ambapo asilimia kubwa ya wakazi wake wanajihusisha na shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji. Umuhimu wa pori hili umejikita katika uhifadhi wa rasilimali wanyamapori, mimea na mazalia ya samaki katika Ziwa Rukwa ambayo ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo. Pamoja na umuhimu huo, Pori la Akiba Uwanda kama yalivyo maeneo mengine ya hifadhi, linakabiliwa na changamoto ya ongezeko la shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, eneo kubwa la pori hili ni sehemu ya Ziwa Rukwa, na sehemu iliyobaki yenye eneo la kilometa za mraba 400 ni nchi kavu. Kutokana na umuhimu huo Wizara yangu inaona ni mapema kupunguza ukubwa wa pori hilo kwa sababu uamuzi huo utaathiri sababu na malengo ya kuanzishwa kwake. Hata hivyo, Serikali kwa upana wake itajumuisha eneo hili la Pori la Akiba la Uwanda, kuwa miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kushughulikiwa kimkakati zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu haikubaliani na vitendo vya baadhi ya watumishi wake, wakiwemo Askari Wanyamapori kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga, kuwanyang’anya mali, kuwatoza faini kinyume cha utaratibu, kuwachomea moto nyumba zao, na kuwanyanyasa kwa namna yoyote ile, kwa kisingizio cha kutekeleza matakwa ya sheria. Wizara yangu inasisiza msimamo wa Serikali wa kuendelea kusimamia utawala wa sheria, na hivyo kujipanga zaidi, ili kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi watakaodhibitika kukiuka, kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaombwa, kutoa ushirikiano katika kuwabaini watumishi wa aina hii, na pia wachukue hatua stahiki kabla, wakati na baada ya matukio ya aina hiyo ili kuirahisishia Serikali kuchukua hatua sahihi kwa wakati sahihi. Hata hivyo Wizara yangu inasisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopakana na hifadhi, wazingatie na kutii sheria bila shuruti. Ili hifadhi hizo ziendelee kuleta manufaa kwa taifa wakiwemo wananchi hao kwa tija zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba ni kipindi kifupi tu, takribani miaka miwili na nusu tangu usimamizi wa Pori la Akiba Uwanda, ukabidhiwe kwa Wizara yangu. Tayari tumeanza mkakati wa kuwekeza kwa kuboresha miundombinu na vivutio ili kuhakikisha kwamba pori hilo linarudi kwenye hadhi yake ya awali. Kabla ya kufanyika kwa shughuli za utalii zitakazoiwezesha Serikali kushughulikia ipasavyo changamoto za maendeleo ya wananchi. Azma hii inaendana na mipango ya Serikali ya muda mrefu ya kuboresha shughuli za utalii Ukanda wa Kusini.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Kituo cha afya kilichopo Laela kinategemewa na Kata za Lusaka, Kasanzama, Laela, Mnokola, Miangalua na Kaoze; kutokana na kupanuka kwa kasi kwa mji huo na ongezeko la watu wanaohudumiwa katika kituo hicho, kimesababisha upungufu wa dawa, wataalamu na vifaa tiba.
(a) Je, ni lini Serikali itakipa kituo hicho hadhi ya Hospitali ya Wilaya?
(b) Je, ni lini kituo hicho kitapatiwa gari la wagonjwa?
(c) Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam wa kutosha, vifaa tiba na dawa za kutosha katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Kituo cha Afya Laela hakina miundombinu inayokidhi sifa za kuwa hospitali, kazi inayofanyika kwa sasa ni upanuzi wa miundombinu ya kituo hicho ambapo tayari jengo la upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito limekamilika pamoja na wodi ya mama wajawazito na wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji. Aidha, mpango wa muda mrefu katika eneo hilo ni kujenga Hospitali ya Wilaya kukidhi mahitaji ya matibabu kwa wagonjwa wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za rufaa kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika kituo hicho kwa sasa zinatolewa kupitia magari ya kawaida ya Halmashauri kutokana na ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa. Ni matarajio ya Wizara kwamba Halmashauri itaweka kipaumbele katika kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi wa gari la wagonjwa.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa watumishi katika Kituo cha Afya Laela ni tisa kati ya 45 wanaohitajika. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imepewa kibali cha kuajiri watumishi wapya wapatao 42 ambapo baadhi yao watapelekwa kituoni hapo. Kuhusu dawa na vifaa tiba, kituo kimetengewa bajeti ya shilingi bilioni 9.3 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Serikali ilituthibitishia kuwa gesi aina ya Helium iligundulika katika Ziwa Rukwa na kwamba gesi hiyo ina thamani kubwa na ni adimu sana duniani:-
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kuchimba gesi hiyo ili Watanzania waanze kunufaika na gesi hiyo kabla haijagunduliwa au kuchimbwa mahali pengine duniani?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kampuni ya Helium One Limited imefanya utafiti wa gesi ya Helium katika Bonde la Ziwa Rukwa. Taarifa za awali zinaonesha uwezekano wa kuwepo kwa gesi ya Helium kiasi cha futi za ujazo bilioni 54 katika maeneo ya Ziwa Rukwa. Matokeo haya yanatokana na uchunguzi wa sampuli tano za mavujia ya gesi ya Helium katika maeneo hayo, kiasi ambacho kinakadiriwa kuwa kikubwa zaidi ya mara sita ya mahitaji ya dunia kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Helium One Limited imefanya utafiti huo kupitia kampuni zake tanzu za Gogota (TZ) Limited, Njozi (TZ) Limited na Stahamili (TZ) Limited zinazomiliki leseni za utafutaji wa gesi ya Helium katika Ziwa Rukwa. Kampuni hizi zilipewa leseni za utafutaji wa Helium katika maeneo mbalimbali kuanzia mwaka 2015. Shughuli za utafutaji wa kina wa gesi ya Helium unaendelea kwa kukusanya taarifa zaidi za kijiolojia, kijiokemia, kijiofizikia na 2D ili zitumike kwa ajili ya uchorongaji wa visima vya utafiti wa gesi asilia kilichopo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, uchimbaji wa gesi ya Helium utaanza mara baada ya kazi ya utafiti wa kina, upembuzi yakinifu na tathimini ya athari za mazingira kukamilika. Baada ya utaratibu kukamilika, uchorongaji katika maeneo ya Ziwa Rukwa unatarajiwa kuanza mwaka 2018.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Barabara ya kutoka Kibaoni – Kasansa – Muze – Ilemba – Kilyamatundu – Kamsamba hadi Mlowo Mkoani Songwe inaunganisha Mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe; wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa na maombi ya muda mrefu kutaka barabara hiyo itengenezwe kwa kiwango cha lami ili kuboresha maisha na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla:-
Je, ni lini barabara hiyo itatengenezwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibaoni –Kasansa ambayo ni kilometa 60.57 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Katavi. Barabara ya Kasansa – Kilyamatundu ambayo ina urefu wa kilomita 178.48 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Rukwa; na barabara ya Kamsamba – Mlowo ambayo ina urefu wa kilomita 130 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni kiungo sana kati ya mikoa hii mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe kwani inapita katika Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu sana kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Hali ya barabara hii ni nzuri kwa wastani ila inapitika kwa shida wakati wa masika katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kufahamu umuhimu huo itaanza ujenzi wa Daraja la Momba ambalo ni kiungo muhimu katika barabara hiyo na katika mwaka wa fedha 2016/2017 ndiyo tuaanza ujenzi huo wa barabara ya Momba. Kwa sasa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) upo katika hatua za mwisho za kupata mkandarasi wa kujenga daraja hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga sh. 2,935,000,000 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuanza ujenzi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa sh. 3,000,000,000 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Daraja la Momba kwenye barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kazi za kuifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo uanze na hatimaye ujenzi kwa kiwango cha lami ufanyike.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Katika bajeti ya 2016/2017 Serikali ilipanga kujenga baadhi ya Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini.
(a) Je, ni hatua ipi imefikiwa katika ujenzi wa Mahakama hizo?
(b) Kwa kuwa Mahakama ya Mwanzo Mtowisa katika Wilaya ya Sumbawanga Vijijini ni miongoni mwa Mahakama iliyopangiwa bajeti ya ujenzi kutokana na uchakavu mkubwa na hatarishi kwa wananchi, je, ni lini ujenzi utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU - KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijiibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Mahakama imepanga kujenga na kukarabati majengo yake katika maeneo mbalimbali nchini. Mahakama imejiwekea mpango wa kujenga na kukarabati majengo hayo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Utekelezaji wa mpango huu unaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Mahakama imepanga kujenga Mahakama Kuu Kigoma na Mara na kufanya ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama Kuu Sumbawanga. Aidha, kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, kipaumbele kimetolewa katika Mikoa ya Simiyu, Njombe, Katavi, Manyara, Lindi na Geita.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imepanga kujenga Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini. Mahakama ya Mwanzo Mtowisa ni moja ya maeneo yaliyopangwa kujengwa na ujenzi utaanza mara moja baada ya upatikanaji wa fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Mahakama wa kujenga majengo kwenye Mikoa mbalimbali, kikwazo kimekuwa ni upatikanaji wa viwanja pamoja na hati miliki za viwanja.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Katika ukanda wa Bonde la Ziwa Rukwa katika Jimbo la Kwela, kwenye ukingo wa Milima ya Lyamba Iyamfipa inayoambaa katika Kata za Mfinga, Mwadui, Kalumbaleza, Nankanga, Kapeta hadi Kaoze, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiokota madini mbalimbali bila kutambua ni madini ya aina gani.
(a) Je, Serikali imeshafanya utafiti wowote katika maeneo hayo?
(b) Kama jibu ni hapana, je, ni lini utafiti utafanyika ili kujua eneo hilo lina madini gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia miaka ya 1950 Serikali imekuwa ikifanya utafiti mbalimbali wa awali wa madini kwenye maeneo ya Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa yakiwemo maeneo ya Jimbo la Kwela kwenye mwambao wa milima ya Lyamba Iyamfipa. Utafiti wa awali ulibaini uwepo wa madini mbalimbali yakiwemo madini ya vito kama vile Garnet, Kyanite, Zircon na Sapphire na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za uwepo wa madini katika Ukanda wa Bonde wa Ziwa Rukwa zinapatikana kwenye ofisi zetu za Wakala wa Jiolojia Tanzania. Hata hivyo nachukua nafasi hii kuwashauri sana ndugu zetu wote wakiwemo wa Jimbo la Kwela kutumia Ofisi zetu za Madini za Kanda ya Magharibi iliyoko Mpanda na taarifa zilizopo kwenye ofisi ya Wakala wa Jiolojia iliyoko Dodoma, ambapo wako wataalam watawasaidia kuyachambua madini hayo pamoja na kuwashauri namna ya kufaidika na rasilimali hiyo ya madini.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kujenga barabara ya Ntendo – Muze (kilometa 37.04) kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Barabara ya Ntendo – Muze yenye urefu wa kilometa 37.04 ina umuhimu wa kipekee kiuchumi kwa Bonde la Ziwa Rukwa, kwani ndiyo inayotumika kusafirisha mazao kutoka Bonde la Ziwa Rukwa kwenda kwenye masoko. Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara ya Ntendo – Muze imeendelea kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili ipitike bila matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii itaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali kwa kiwango cha changarawe na zege hususan sehemu korofi na miteremko mikali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Kwa sasa Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara zinazounganisha Makao Makuu ya Mikoa na nchi jirani na hatimaye barabara za Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi milioni 170 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa kiwango cha zege sehemu zenye miinuko na miteremko mikali maeneo ya Mlima Kizungu. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ili barabara hii iendelee kupata matengenezo yatakayoiwezesha kupitika majira yote ya mwaka. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Kutokana na tatizo kubwa la ukosefu wa maji katika Mji Mdogo wa Muze Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilipitisha mpango wake wa kuondokana na tatizo hilo kwa kuanzisha mradi mkubwa wa kuchukua maji toka Mto Kalumbaleza na kusambaza katika Vijiji vya Muze, Mlia, Mnazi Mmoja Asilia, Ilanga, Mbwilo Kalakala, Isangwa na Uzia:- Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili kutekeleza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha za utekelezaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji. Kwa sasa Mtaalam Mshauri anaendelea na kazi ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa maji wa Muze Group ili utekelezaji wake uweze kufanyika katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga kiasi cha Sh.500,000,000 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Muze Group.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Upo uharibifu mkubwa wa mazingira katika Ukanda wa Ziwa Rukwa unaotokana na ukataji miti ovyo, wingi wa mifugo na kilimo kisichozingatia utaalamu; shughuli hizi zinahatarisha kukauka kwa ziwa hilo kwa miaka ijayo:-
Je, Serikali ina mpango gani madhubuti na wa haraka kunusuru ziwa hilo, hasa ikizingatiwa kuwa imegundulika gesi ya helium katika ziwa hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo Oktoba, 2016 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alifanya ziara ya kutembelea Mkoa wa Rukwa na moja ya maeneo aliyotembelea ni Bonde la Ziwa Rukwa ambapo alitoa maelekezo ya kuanza mchakato wa kulitangaza Ziwa Rukwa kama eneo nyeti la mazingira kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kutangaza eneo hilo kuwa eneo nyeti unaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa kwa 2018. Eneo hilo litakapotangazwa rasmi kuwa eneo nyeti litakuwa chini ya usimamizi wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mzingira (NEMC) ambalo kwa kushirikiana na wadau litaandaa mpango wa matumizi ya eneo husika hivyo kuongeza nguvu ya usimamizi wa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Waziri alielekeza Halmashauri zote ambazo zina eneo katika Bonde la Ziwa Rukwa kuweka alama za kuonesha mwisho wa umbali wa mita 60 kutoka kwenye kingo za Ziwa Rukwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kuweka mabango ya kukataza shughuli zinazoharibu mazingira ndani ya umbali huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa eneo la Bonde la Ziwa Rukwa limebainika kuwepo kwa dalili ya gesi ya helium. Tathimini ya Athari ya Mazingira imefanyika katika hatua hii ya utafiti ili kuweza kubaini athari na madhara yoyote yanayoweza kutokea wakati wa zoezi hilo.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Ilemba katika Halmashauri ya Sumbawanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya saba kwa gharama ya shilingi bilioni 3.3 ikiwemo Kituo cha Afya Milepa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Vilevile Serikali imeweka kipaumbele cha kujenga hospitali tatu za Halmashauri katika Halmashauri tatu za Wilaya ambazo ni Sumbawanga, Nkasi na Kalambo kwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 kila moja na fedha hizo zimepelekwa kwenye Halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ina vituo vya kutolea huduma za afya saba, viwili vikiwa binafsi na vitano vya Serikali vinavyohudumia watu takribani 369,471. Ujenzi wa Kituo cha Afya Ilemba ulianza mwaka 2011 kwa kujenga Jengo la OPD na nyumba mbili za watumishi kwa kushirikisha wananchi. Mpaka sasa majengo hayo yamefikia hatua ya upauaji na kiasi cha Sh.82,805,611 ambapo ruzuku kutoka Serikali Kuu ni Sh.54,116,121 na nguvu za wananchi Sh.28,789,490 imetumika. Halmashauri inaelekezwa kuzingatia na kuweka kipaumbele kwenye bajeti kuhusu ukamilishaji wa mradi huo kabla ya kuanzisha miradi mipya.
MHE. IGNAS A. MALOCHA (K.n. y. MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI) aliuliza:-

Tunaishukuru Serikali kwa kutujengea barabara ya lami kutoka Mpanda –Sumbawanga:-

Je, ni lini Serikali itamaliza kipande cha kilomita 86 eneo la Hifadhi ya Katavi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda yenye urefu wa km 245 ilifanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2009. Serikali kwa kutumia fedha za ndani imekamilisha ujenzi wa kilometa 188.5 kwa kiwango cha lami sehemu za Sumbawanga - Kanazi, (kilometa 75), Kanazi - Kizi - Kibaoni (kilometa 76.6) na Sitalike – Mpanda (kiolometa 36.9).

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi kwa barabara ya lami, hivyo ujenzi wa sehemu iliyobaki kati ya Kizi - Lyamba Lya Mfipa - Stalike (kilometa 86) utaanza mara moja kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya maandalizi ya awali ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuweka lami barabara muhimu ya Kibaoni-Kasansa-Muze- Kilyamatundu-Kamsamba kutokea Mlowo; ambayo inaunganisha mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibiwa swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutekeleza mipango ya ujenzi wa barabara ya Kibaoni- Majimoto- Kisansa-Muze-Kilyamatundu- Kamsamba hadi Mlowo yenye urefu wa kilometa 149 kwa kuanza na ujenzi wa daraja la Momba ambalo limekamilika hivi karibuni. Daraja hili limekuwa kikwazo kikubwa cha mawasiliano kati ya wananchi wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii katika mwaka wa fedha 2018/2019, jumla ya shilingi milioni 200 zilitengwa kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa barabara ya Kibaoni-Majimoto-Inyonga ikiwa ni sehemu ya barabara ya Kibaoni-Kasansa-Muze-Kilyamatundu- Kamsamba hadi Mlowo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020, fedha zimeombwa kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Ntendo-Muze- Kilyamatundu ikiwa pia ni sehemu ya barabara ya Kibaoni –Kasansa-Muze-Kilyamatundu-Kamsamba hadi Mlowo. Mara baada ya kukamilika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni za gharama ya ujenzi kujulikana Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hii.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga mradi wa umwagiliaji uliopo katika Kata ya Ilemba ambao ulijengwa na wananchi na ukabomolewa na mvua msimu wa 2018/2019?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini juhudi zilizofanywa na wananchi kwa kujenga Mradi wa Umwagiliaji Ilemba ambao umekuwa ukibomolewa mara kwa mara na mvua za msimu na kurudisha nyuma jitihada za wananchi kujiletea maendeleo. Aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa mradi huo kwa wananchi wa Jimbo la Kwela, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatuma wataalam kufanya tathmini ili kuona sababu zinazosababisha miundombinu kubomolewa na kutafuta njia za kuondoa tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itatafuta fedha na kuingiza katika mipango yake ya kibajeti baada ya taarifa ya tathmini ya wataalam hao kukamilika. Aidha, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ili kuandika maandiko mbalimbali ya kuomba fedha kutoka taasisi za fedha, wadau wa maendeleo na Benki za Maendeleo na Biashara kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kupitia utaratibu wa Jenga, Endesha na Kabidhi ili kuweza kupata fedha za kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Ilemba na hivyo kuwanufaisha wananchi wa Kata ya Ilemba na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla.