Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zubeda Hassan Sakuru (1 total)

MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, Januari mwaka 2016 Wizara ilitangaza kufanya msako mkali kwa ajili ya kukabiliana na wahamiaji haramu. Jambo la kusikitisha ni kwamba, wimbi la ongezeko la wahamiaji haramu limeendelea na mwezi Mei mwaka huu wa 2017 Mkoani Ruvuma, Wilaya ya Mbinga katika Kata ya Kigonsera, takriban wahamiaji haramu nane walikutwa miili yao imetupwa katika kijiji hicho. Nataka kujua kauli ya Serikali msako huu umeishia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kumekuwa na changamoto kubwa ya vitendea kazi hasa katika mikoa na ofisi ambazo ziko mipakani. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba mikoa hii ambayo iko mipakani inapewa vitendea kazi? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuileta hoja hiyo. Kwa kupitia swali hili niwaelezee tu Waheshimiwa Wabunge kwamba hapa kuna mambo mawili; kwanza, kuna wapitaji haramu na wahamiaji haramu.
Mheshimiwa Spika, hili la wapitaji haramu ndiyo ambalo tumekuwa tukikutana na adha kama hii aliyoisema kwa sababu wanabebwa kwenye malori. Wakishabebwa kwenye malori wana-suffocate, wanakosa hewa, wanakosa chakula na hata wanafikia hatua hiyo wengine kupoteza maisha na kutupwa.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi pamoja na Magereza wamehangaika sana kwa vigezo tu vya kiubinadamu, mara kwa mara wanawakuta wakiwa wameshatupwa wakiwa hawana nguvu, hata wanawatafutia huduma za kwanza ikiwepo hospitali na kuwapikia chakula.
Mheshimiwa Spika, kubwa tunalofanya, kama tulivyopitisha jana kwenye itifaki ile, tunahangaika namna ya kuanza kukabiliana na hawa watu kuanzia kwenye mipaka wanakotoka, hasa kwa hawa wa upande wa wapitaji haramu, lakini pia na kuwa na sheria zinazowiana.
Mheshimiwa Spika, jambo linalotusumbua kwa sasa ni kwamba sisi tunahangaika kukabiliana nao kwenye nchi yetu, lakini unakuta wameshasaidiwa kupita kuanzia wanakotoka katika hizo nchi nyingine walizopita ikiwemo majirani zetu wa Kenya.
Mheshimiwa Spika, pia baada ya kuwa wamemaliza Tanzania, kwingine wanakokwenda wanakuwa wanapita katika mazingira ambayo katika nchi hizo wanaruhusu. Kwa hiyo, hilo ni moja ya jambo ambalo tunapambana kuhakikisha tunaziba mianya hiyo kwa utaratibu wa kushirikiana, lakini pia na kisheria; sheria zinazowiana.
Mheshimiwa Spika, hili la wahamiaji haramu ambao wamekusudia kuja kwenye nchi yetu, tumetoa rai kwa wananchi wote pamoja na viongozi wa kuanzia ngazi za matawi na vijiji kuhakikisha kwamba wanatoa ushirikiano na wanafichua pale wahamiaji haramu walipo na muda wowote, siyo tu pale ambapo wanaona kuna maslahi yao yameguswa.
Mheshimiwa Spika, tunaongea na wenzetu wa TAMISEMI, tunataka kuangalia uwezekano, ule mfumo uliokuwa unatumika na Chama cha Mapinduzi wa kuwa na Balozi anayeshughulikia nyumba 10, ndiyo uwe utaratibu ambao viongozi wetu wa mitaa, wale wa Serikali za Vijiji wanaounda Serikali za Vijiji, wapatikane kwa kuwakilisha mitaa badala ya sasa hivi ambavyo wanachaguliwa, wanaweza wakatoka mtaa mmoja na wakawakilisha kijiji kizima.