Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zubeda Hassan Sakuru (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu unalenga moja kwa moja katika changamoto ya masoko ya kilimo pamoja na bidhaa za kilimo. Wakulima wengi wanapata faida ndogo kutokana na ukosefu wa masoko na uhakika wa bei za mazao yao. Kushuka kwa shilingi mara kwa mara kumepelekea wanunuzi kununua mazao ya wakulima kwa bei ndogo sana na kumuacha mkulima akifanya kilimo cha hasara. Leo hii, ubovu wa miundombinu nchini unasababisha wakulima kukosa masoko ya uhakika na hivyo kupelekea kuuza mazao yao kwa hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto za kilimo, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulialika wataalam wa kilimo ili kuchambua na kutoa mapendekezo juu ya namna bora ya kutatua changamoto ya masoko ya wakulima. Tena kuna maabara ndogo ya siku tano iliandaliwa ili kutathmini mifumo ya masoko kwa mazao ya mahindi na mpunga. Je, programu hii ilitoka na matokeo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kupiga marufuku uingizaji wa sukari nchini bado ipo haja ya kuzuia pia uingizwaji wa bidhaa za mifugo nchini kama vile nyama, maziwa kwani wafugaji wengi wa Tanzania wanaendelea kuwa na mifugo mingi na uzalishaji hafifu. Leo pamoja na kuwa na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, Tanzania hainufaiki na fursa hizo hasa kwa bidhaa za maziwa na ndiyo maana leo katika maduka mengi ya rejareja bidhaa za nje za mifugo zimejaa na hazina ubora wala usalama kwa mtumiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya uvuvi hasa katika Bahari Kuu ya Hindi haujapewa kipaumbele kama mojawapo ya shughuli muhimu ya kiuchumi. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwezesha wavuvi wa Kitanzania kujishughulisha kwa manufaa na kuongeza pato la Taifa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti ya FAO ya mwaka 2014 inaonesha kuwa Uganda na Tanzania ziliongoza katika uvuvi wa maji baridi ambapo Tanzania ilishika nafasi ya nane. Changamoto kubwa ambayo ilitolewa kama tahadhari ni kupungua kwa samaki hasa katika maziwa makuu (Victoria ikiwa ndio mojawapo). Je, ni mkakati gani wa makusudi uliowekwa kuhakikisha uvuvi wa maji baridi unakuwa endelevu katika kuchangia uchumi wa Taifa?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia lakini kabla ya kuanza kuchangia ningependa kushukuru chama changu cha Demokrasia na Maendeleo kwa kunipa nafasi ya kuwa mwakilishi wa Mkoa wa Ruvuma kupitia Baraza la Wanawake wa CHADEMA.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kabla sijachangia ningependa kupongeza hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani ambayo imekuja na mawazo mbadala na naamini kwamba Waziri ukiwa makini utaweza kuyachukua mawazo yetu kwa sababu yanaelezea viini vya matatizo lakini pia yanaelezea ni wapi tunaweza kulipeleka Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya Tanzania iko rehani. Leo tunapozungumza, tunazungumza juu ya mtoto wa Kitanzania ambaye anashindwa kushindana katika soko la ajira katika dunia hii. Kwenye dunia ambayo tunaendana na kasi kubwa ya mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia, mtoto wa Tanzania leo anajifundisha kuhusu World War One lakini application yake katika maisha ya kawaida hatuyaoni. Sidhani kama Marekani, nchi zilizoendelea leo wanajifunza kuhusu Majimaji War na bado wana mapinduzi katika uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kuhusu mtoto wa Kitanzania katika ushindani wa soko la ajira, tunampeleka wapi mtoto wa Kitanzania ambaye leo atika mfumo wa elimu kuanzia primary education mpaka secondary education anasoma kitu kile kile lakini kwa replication ya utofauti wa lugha! Kuanzia darasa la tatu mpaka darasa la saba binti wa Kitanzania, kijana wa Kitanzania anasoma kuhusu sayansi kwa lugha ya kiswahili, akienda kusoma form one mpaka form four anaenda kusoma the same thing katika lugha ya kiingereza. Tunaenda mbele au tunarudi nyuma?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto kubwa ya kuweza kushindana na soko la ajira katika Afrika Mashariki, na nioneshe masikitiko yangu makubwa kwamba kati ya vitu ambavyo Tanzania imeviweka rehani kwa mfano tukizungumzia suala zima la elimu ni pamoja na kubadilishwa kwa mitaala kwa kauli za Mawaziri. (Makofi)
Leo Taifa letu linaendeshwa kutokana na kauli za Mawaziri au vision ya Waziri badala ya vision ya Kitaifa ya mtaala wa elimu! Akija mmoja leo akifikiria kwamba sayansi ni muhimu kwa watoto wa Kitanzania, basi wote tunasomeshwa sayansi, akija mwingine akiamini kwamba biashara ni muhimu kwa waototo wa Kitanzania wote tnasomeshwa biashara, tunaelekea wapi kama Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nabado tujue kwamba na nashukuru kwamba Waziri Mkuu katika hotuba yake aliyoitoa Aprili, 2016 alizungumzia kuhusu kutoajirika kwa kijana wa Kitanzania kwa kushindwa kupata elimu na ujuzi wa kuweza kujiajiri na kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja ya sisi kama Tanzania, set aside our political differences, kuwa na mpango wa Kitaifa utakaoweza ku-match gap kati ya mahitaji ya soko la ajira na kile tunachokizalisha. Leo hii ukimchukua mtotowa Kitanzania kwenda kushindana na mtoto Jumuiya tu ya Afrika Mashariki, mtoto wa Kenya, mtoto wa Kitanzania anakaa wapi? Mhitimu wa Kitanzania anakaa wapi? Tunacheza pata potea kwenye elimu na tumewaweka watoto wa maskini katika ombwe wasijue watafanya nini wanapohitimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nasikitika sana Serikali inapokuja na hoja ya kuwa na ada elekezi. Unawekaje ada elekezi pale ambapo umeshindwa kuboresha miundombinu ya shule za Serikali? Na niseme tu mimi ni tunda au uzao la shule za Serikali, nimesoma all government schools, lakini shule nilizosoma leo ukiangalia matokeo yake na quality of the output they put in the market is a mess, is a shame. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kuhusu masuala ya kutoa ada elekezi lazima tuji-reflect katika matendo yetu, miundombinu ambayo tumeiweka katika shule za Serikali ni rafiki? Leo mnazungumzia kuhusu mimba za viherehere na nashukuru sana baadhi ya Wabunge wa upande wa Kambi ya CCM wamezungumzia kuhusu mimba za utotoni, lakini Rais wa Awamu ya Nne aliyekuwa na dhamana alisema ni mimba za viherehere, ni kauli mbaya ambayo haijawahi kutolewa na Mkuu wa Nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa changamoto ya watoto wanaotoka vijijini imetokana na ubovu wa miundombinu, umbali wa shule, lakini pia kutokuwa na miundombinu rafiki kwao. Leo hii tuna wanafunzi ambao wamepewa mimba na walimu wa shule za msingi, how do we place them katika market? Nafikiri Waziri kwa sababu wewe ni mwanamke na tupo katika zama za kuweza ku-value mchango wa mtoto wa kike katika kujenga uchumi na kujitegemea, basi naamini kwamba leo utatoa agizo la kufuta the ban ya watoto wa shule wanaopata mimba kutorudi shuleni. (Makofi)
Kuna kitu ambacho kinanifurahisha sana. Wakati ukiwa Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani la Taifa, sorry! Mheshimiwa Waziri ulitoa picha mwanafunzi amechora zombie na akachekwa, lakini je, Tanzania tuna wachoraji wa kutosha kujivunia? Katika mitaala yetu, tuna mitaala ambayo inaweza ku-accomadate fine and performing arts? Au sisi tunachagua tu baadhi ya career? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo kijana aliyechora zombie kama angepewa elimu ya ziada ya kuweza kujifunza fine and performing arts, si ajabu alivyochora zombie angepata A. leo hii anawekewa failure kwa sababu ameshindwa ku-accommodate masomo. Na mimi Mheshimiwa Waziri nikuambie Mheshimiwa Mwenyekiti aniruhusu, ni kati ya wanafunzi ambao waliweka determination na kuacha kile ambacho niliambiwa nisome. Leo katika Tanzania watoto wengi wanasoma si vile ambavyo wao wanataka bali mfumo unachotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazalisha madaktari wengi, juzi katika hoja sikuchangia, lakini katika hoja ya Wizara ya Afya kuna wanafunzi wahitimu karibu 1,000 ambao wamesoma udaktari leo hawana kazi, mfumo umewatenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie tena kuhusu migogoro inayoendelea katika vyuo vyetu vikuu. Ni dhahiri, shahiri kuna matabaka ya ushiriki wa wanafunzi katika vyuo vikuu kutokana na matabaka ya utofauti wa itikadi zao. Pamoja na kwamba kuna Mbunge aliongea hapa akaelezea kwamba hakuna u-CHADEMA, hakuna u-CCM, tuna ushahidi wa mwanafunzi ambae alikuwa Vice President wa Chuo cha UDOM ambaye amesimamishwa masomo kwa sababu tu ya kushindwa kufanya kazi kama ambavyo management ya chuo ilitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi huyu Rose Machumu alienda mahakamani akafungua shauri na katika shauri lake mahakama iliona kwamba alikuwa na legal stand ya kuwa kiongozi, lakini akapinduliwa. Mapinduzi tu haya ya kawaida tu haya ya kwenye kura za kawaida huku mtaani mnahaha, kwenye vyuo vikuu mnashindwa kushughulikia kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niangalie kuna kitabu hiki cha Africa Development Bail Out kimeandikwa na Profesa Norman A. S. King ambaye ni mwanachama wenu. Anaelezea na ame-rank reasons za kwa nini Tanzania hatuendelei. Mojawapo ya changamoto ambazo ni kwa nini Tanzania na mfumo wa elimu hauendelei ni pamoja na kutokuwa na match kati ya uhitaji wa walimu na wanafunzi kitu ambacho ni kweli, lakini kingine anasema poor quality of teachers in primary school yaani walimu wa shule za msingi hawakidhi viwango. Lakini pia anasema lack of housing for teachers, kukosekana kwa malazi kwa ajili ya walimu kumesababisha kuwa na matokeo mabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto nyingine nyingi ambazo shule zinakumbana nazo na leo hii mimi huwa nashangazwa sana, tunasemaje kwamba kuna upungufu wa madarasa, tunashangiliaje kuwa na ongezeko la madarasa nchini kama kiwango cha utoaji wa elimu kiko duni? Tunawezaje kushangilia ongezeko la wanafunzi wanaofaulu wakati kati ya hao wanaofaulu hawajui kusoma na kuandika? Tunawezaje leo kushangilia kuwa na ongezeko la maabara ambazo kimsingi hizo maabara hazitoweza kufanya kazi mpaka sijui bajeti ya mwaka gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongeleaje kuwa na maendeleo katika sekta ya elimu wakati mwalimu wa Kitanzania hana malipo stahiki wala yenye staha na kumuwezesha kumudu haki zake? Tunazungumzia kwamba kuna mambo mengi ya msingi ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi, kuna kitu ambacho kina-neglect na kuvunja moyo sana na kuvunja moyo sana katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanaitwa Tanzania One, wale vijana waofanya vizuri katika msomo yao, wakishakuja Bungeni, wakipigiwa makofi, wakishapewa zawadi laki moja, laki mbili hatma yao haijulikani. Kwanza nitoe pongezi zangu kwa mwanafunzi Gertrude Clement aliweza kuhutubia UN lakini pia…
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha mchango wangu kuhusu hoja ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la siasa vyuoni limeendelea kuwa mwiba kwa baadhi ya vyuo vikuu nchini. Menejimenti za vyuo zimekuwa zikiingilia Serikali za wanafunzi, lakini pia kuwanyima haki wanafunzi wanaoshiriki katika nafasi za uongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro mkubwa wa uongozi baina ya menejimenti ya Chuo cha Dodoma na Serikali iliyoondolewa madarakani kwa shinikizo la menejimenti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu si tu umechochewa na menejimenti ya chuo lakini pia umelenga kuwanyima wanafunzi waliochaguliwa kihalali na wanafunzi kuongoza Serikali ya wanafunzi pamoja na kuwasimamisha chuo kinyume na hukumu ya mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binti Rose Maruchu mwanafunzi wa mwaka wa tatu alichaguliwa na wanafunzi wa UDOM alisimamishwa chuo miezi miwili tu kabla ya kumaliza chuo lakini pia wakati kesi ikiwa mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi ilifunguliwa kabla ya tarehe 11/4/2016 lakini cha kushangaza kesi ikiwa mahakamani Bi, Maruchu alipokea barua ya zuio la kuendelea kuwa kiongozi na menejimenti ikaunda Serikali ya mpito kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata wakati kesi ya zuio inaendelea kusikilizwa mahakamani, wakili wa UDOM alitoa barua kuwa Maruchu amesimamishwa chuo tangu tarehe 11/4/2016. Waziri si tu kuwa menejimenti ilidharau mahakama lakini pia imelenga kumkomoa Rose ambaye alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa UDOSO kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote hukumu iliyotolewa dhidi ya Chuo cha Dodoma ilimpa ushindi Bi. Rose Maruchu na kuamuru chuo kimruhusu Rose kuendelea na masomo pamoja na majukumu yake, Rose hajarudishwa chuo huku akiwa amebakiza miezi miwili tu kumaliza chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haki iko wapi Mheshimiwa Waziri? Tunawapaje motisha wasichana waliopo vyuoni kugombea nafasi za uongozi wakati wakiwekewa mazuio na vikwazo vya maksudi? Menejimenti ya UDOM inapata wapi jeuri ya kukaidi amri ya mahakama? Kukaa kimya kwa Serikali ndiko kunakoinua malalamiko kuwa inashiriki kushinikiza menejimenti za vyuo kukandamiza na kuingilia Serikali za vyuo hasa zinazoongozwa na wanafunzi wenye mitazamo kinzani na menejimenti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naomba usimamie haki ya Rose Maruchu, kama Waziri mwenye dhamana lakini zaidi kama mama. Imagine unaona ndoto za mwanao zinazimwa kwa kutetea maslahi ya wenzake? Ni uchungu gani mzazi anaobeba kuona ada na jitihada zake kwa binti yake zinazimwa miezi miwili kabla ya kuhitimu miaka mitatu, cha uchungu wa gharama za kusomesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwako si tu kuitaka menejimenti kumrudisha Rose kama kiongozi, bali kutaka menejimenti ya UDOM kumrudisha chuo na kumwachia binti huyu haki zake kama mwanafunzi ikiwemo kufanya majaribio (tests), assignments zote na mitihani ili ahitimishe miaka yake mitatu. Nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi hii kujadili hotuba ya Waziri Mkuu katika kupitia mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka huu wa fedha wa 2017/2018. Pia nitoe pole kwa familia ya Mbunge mwenzetu Dkt. Elly Macha aliyefariki nchini Uingereza na naungana na wana CHADEMA wote kufikisha salamu hizi kwa familia yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuweka wazi kuwa naunga mkono kwa asilimia mia moja maoni ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe na naamini kwamba Serikali itaenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alipata kusema maneno yafuatayo naomba niyanukuu: “tunataka kuona katika Taifa hili vijana jeuri na wenye kujiamini siyo vijana waoga akina ndiyo Bwana Mkubwa, vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mfumo wa jamii isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya Kitanzania na tunataka kuona vijana waasi dhidi ya mfumo kandamizi, ubwana na ufisadi katika Taifa”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kijana nauliza swali ambalo vijana wenzangu wa Tanzania wanauliza where is Ben Saanane? Tunapozungumza leo hii kijana aliyezaliwa na mwanamke na Watanzania tunajua usemi wa Kiswahili unaosema “uchungu wa mwana aujuae mzazi” kijana wa watu Ben Saanane ana takribani miezi sita haonekani, hajulikani alipo, itakuwa ni kosa kubwa kama Bunge tukinyamaza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa mbalimbali zimeletwa mbele yetu, katika mijadala hii kunaonekana kwamba kulikuwa kuna namba 0768-797982 iliyosajiliwa kwa jina la Emmanuel Joseph, ndiyo iliyotuma ujumbe wa vitisho kwa Ben Saanane. Wasiwasi wangu kama kijana ambaye leo hii nipo katika siasa lakini siasa za upinzani na wasiwasi alionao Mama yangu Doris Harold Mboni alipo ni kwamba je, nini hatma yangu kesho?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza mwezi Oktoba, 2016 kulitokea uvumi wa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Nchini Devis Mwamunyange kwamba amelishwa sumu. Uvumi huu ulianza tarehe 2 Oktoba, 2016 lakini ukaja kufupishwa kwa kumpata kijana aliyetuma na kuanzisha
ujumbe huu kupitia TCRA na Jeshi la Polisi, tunachouliza ni kitu gani kifanyike, ni aina gani ya hasira na maumivu ya wazazi wa Ben Saanane waliyonayo wayafanye ili TCRA na Jeshi la Polisi liseme huyo aliyetuma ujumbe ni nani? yuko wapi na wamechukua hatua gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu wana CCM pamoja na wana CHADEMA na wana CUF hakuna dhambi kubwa duniani kama dhambi ya uoga, uoga huanza kumtafuna mmoja baada ya mwingine. Tumeimbiwa juzi hapa na kijana mwenzangu Diamond anasema tupige kimya, mimi kama tunda la aliloliacha Baba wa Taifa sitokaa kimya nikiwa kijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Waziri Mkuu kwa sababu tunapozungumzia hali ya kisiasa nchini ni lazima tuzungumzie tension iliyosambaa. Mimi kama Mbunge naweza nikajihakikishia usalama wangu lakini kwa wanaonipenda, familia yangu, jamaa zangu nawahakikishia nini? Tunapokaa hapa sasa hivi tunaongelea hali ya kisiasa kuwa nzuri nchini lakini kuna video zinatapakaa za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama akivamia kituo cha Television (Clouds Media) Waziri Mkuu hajazungumzia kitu chochote. Pamoja na kwamba hawa ni wateule wa Rais lakini ipo haja Waziri Mkuu kuzungumza haya kama Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali hapa Bungeni na tulitegemea kwamba hili litaonekana hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linasikitisha sana ni kuhusu pension ya Wazee ambayo iko chini ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mwaka 2010 hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kwa kuwa ilikuwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, wazee waliahidiwa pensheni, leo miaka 15 baadaye hakuna anayezungumzia pension ya wazee ambayo ilisemwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mwaka 2005 na 2010 ni dhahiri kuwa, waliokuwa wapigaji kura wakubwa walikuwa ni wazee, sasa leo tunawaachaje? Itakuwa dhambi kubwa sana kuhitimisha mjadala huu bila kuhakikisha Serikali inatekeleza ahadi yake ya kuhakikisha wazee wote nchini wanapata pension. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia kuhusu watu wenye ulemavu. Ni haki na wajibu wa walemavu kupata huduma zote za kijamii kama ambavyo tunapata sisi wengi lakini hali ikoje? Tukijiangalia na kufanya tathmini katika sekta mbalimbali za huduma za jamii, je, walemavu wamewekewa mazingira rafiki, kuwawezesha kupata haki zao za msingi kama tunavyopata wengine? Ukienda hospitalini, hakuna hata kitu kimoja kinachoonesha kwamba haya mazingira ni rafiki kwa walemavu, ukienda katika sekta ya elimu huwezi kukuta mazingira rafiki kwa ajili ya walemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mikakati imewekwa ambayo Serikali inasema kwamba imejaribu kuyajibu haya lakini kwa kiwango kikubwa mtu mlemavu anayezaliwa katika familia ya kimaskini anakuwa ameachwa kama alivyo. Sasa ni wajibu wetu kama Wabunge kuendelea kuikumbusha Serikali kuhakikisha inajenga mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira rafiki au mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara; tarehe 2 Februari, 2017, Waziri Mkuu alitoa katazo la uuzaji wa viroba. Hakuna asiyepinga matumizi ya viroba nchini, lakini je, hili katazo lilikuja kwa wakati na je, lilikuwa rafiki kwa wafanyabiashara?
Mfanyabiashara wa Dodoma tulioneshwa hapa amejipiga risasi shambani kwake kwa sababu alichukua mkopo. Tunasemaje kwamba tunajenga mazingira wezeshi wakati Serikali inatoa matamko bila kufikiria athari zake mbadala zinazojengwa kwa wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kwa ubaya gani kwa Waziri Mkuu kuzuia uzalishaji wa viroba nchini halafu wawape muda au grace period hawa wafanyabiashara warudishe viroba viwandani vifanyiwe packaging inayotakiwa ili kuhakikisha kwamba hawa watu wanaweza kurejesha mikopo yao. Leo hii mtu amejiua kwa hasara ya karibu bilioni mbili, bilioni tatu, Waziri Mkuu anasemaje kuhusu hicho kitu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu ambaye anapenda matumizi ya viroba hapa, kwa sababu mwisho wa siku hivi viroba mnavyokataza vinaenda kutengenezwa upya katika ujazo mwingine na mnasema kwamba matumizi yake wanatumia vijana, hapana. Leo ukienda kwenye
maduka ya reja reja mtoto wa miaka saba, nane anatumwa kwenda kununua sigara, kuna mtu anayezungumzia hiki kitu au kwa sababu sigara imeandikwa ni hatari kwa maisha yako? Ni lazima tuhakikishe kwamba, tunawawezesha wawekezaji na wafanyabiashara nchini kwetu mazingira ya kubadilisha maisha kwa kupitia matamko yatakayowajenga na siyo kuwabomoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumeona kwamba kuna baadhi ya makampuni nchini ambayo yanawafanyisha watu kazi bila ya kuwa na mikataba ya ajira. Je, Serikali inaliona hili? Kamati ya Miundombinu tulipita katika makampuni mengi ya simu na tukaona kwamba kuna
wafanyakazi ambao wanafanya kazi nchini lakini hawapewi mikataba ya ajira na hii mwisho wake inasababisha wao kushindwa kupata stahiki zao za kazi. Naamini kwamba Serikali inaweka mkakati wa kuhakikisha kwamba mikataba ya kazi katika sehemu za ajira inapewa kipaumbele na Watanzania hasa wazawa wanapata stahiki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije kwenye jambo moja la msingi; Tanzania ni yetu sote, Tanzania haitojengwa na CHADEMA peke yake, haitojengwa na CCM peke yake, ndiyo maana leo hii fedha za miradi ya maendeleo hazitoki Lumumba, mnakusanya kwa Watanzania waliowachagua na wasiowachagua, mnakusanya kutoka kwa wana CHADEMA na wasio wana CHADEMA, sasa tunapokuja tunajinasibu kwamba hii ni mikakati ya Serikali, hata TLP ingepewa dhamana ya Serikali, ingesimamia kwa sababu ni wajibu wa kila Chama kusimamia….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Sakuru.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Ruvuma wanakabiliana na changamoto nyingi katika utunzaji wa mazingira hasa misitu, hivyo kunahitajika jitihada za makusudi ili kukabiliana nazo. Kwa mfano, Wilaya ya Tunduru haipaswi kuwa maskini kutokana na utajiri wa misitu iliyonayo. Hata hivyo, mojawapo ya kero ni pamoja na mifugo kuvamia katika misitu, hivyo kuhatarisha uendelevu wa misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wilaya hii ina misitu ya Miombo inayokadiriwa kuwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 150,000, hivyo ni dhahiri kuwa uendelezaji wa misitu hii inahitaji uzalishaji mkubwa wa wananchi ili kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ipo haja ya Serikali kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi hasa uanzishwaji na uendeshaji wa viwanda unafanyika kwa umakini mkubwa.
Je, mpaka sasa ni viwanda vingapi vimepewa adhabu/faini kwa uchafuzi wa mazingira mpaka Machi mwaka huu na je, ni hatua gani madhubuti zinafanyika kuzuia uchafuzi wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ipo hoja ya kufanya tathimini ya kitaifa juu ya athari za mazingira hasa katika sekta ya uzalishaji wa viwanda na madini. Napenda kujua ni mkakati gani ambao Serikali imeweka ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira hasa katika miradi ya madini na kuangalia jinsi ambavyo migodi hiyo inakidhi matakwa ya kisheria juu ya utumiaji na usimamimzi wa mazingira migodini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utiririshaji wa maji taka nje ya mfumo rasmi wa majitaka hasa kipindi cha mvua umeendelea kuhatarisha mazingira hasa afya za watumiaji wa miundombinu katika miji. Ni dhahiri kuwa, pamoja na kuwa na changamoto za kimazingira na miundombinu, pia ipo haja ya kufanya tathmini ya mfumo kwa utiririshaji majitaka na athari zake kwa mazingira ikiwemo binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha mchango wangu katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia za ujenzi wa barabara; ili kupitisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami hasa barabara ya Tunduru – Mangaka - Matemanga, wananchi na wakazi wa vijiji vilivyopo kwenye Tarafa ya Nakapanya, baadhi ya wakazi hawajalipwa fidia mpaka sasa licha ya kukidhi vigezo vya kulipwa fidia zao. Vilevile wahanga wa Vijiji vya Songambele, Namakambale, Nakapanya, Pacha ya Mindu, Mtonya, Misufini, Namiungo, Mnazi mmoja na Majimaji nao wanadai fidia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na malalamiko mengi juu ya utoaji wa fidia kwa wahanga, bado wakazi wa Vijiji vya Muhuwesi, Chingulungulu, Msagula, Sevuyanke, Temeke, Sisi kwa Sisi, Mkapunda, Ngalinje, Mchangani, Kalonga, Lambai na Tunduru Mjini nao wanadai fidia kutokana na ujenzi wa barabara. Je Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo wanalipwa fidia kwa wakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, upanuzi wa uwanja wa ndege Dodoma; pamoja na mahitaji makubwa ya upanuzi wa uwanja wa ndege Dodoma, bado haitoleta tija katika mipango miji na usalama wa wakazi wa maeneo ya karibu kutokana na uwanja huu kuwa karibu sana na makazi ya watu. Mpaka sasa, bado wananchi wanaendelea kubomolewa nyumba na wengine bado kulipwa fidia wakati uwanja wa ndege wa Msalato ndiyo uliostahili kupewa kipaumbele na kuleta tija kwa matumizi sahihi ya viwanja vya ndege. Je, Serikali imetumia vigezo gani na kuzingatia nini katika ujenzi wa kiwanja hiki karibu na makazi ya watu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano; kuna changamoto kubwa ya mawasiliano hasa ya redio na simu katika Kata ya Nalasi Wilayani Tunduru. Upatikanaji wa taarifa umekuwa ni changamoto kubwa na kusababisha wananchi kukosa mawasiliano na taarifa. Je, ni lini Serikali itaboresha huduma ya mawasiliano hasa masafa ya redio?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubovu wa barabara; akiwa Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya Serikali kujenga barabara kwa kiwango cha lami kuunganisha Wilaya ya Mbinga hadi Mbamba Bay Mkoani Ruvuma, Wilaya ya Nyasa yenye kilometa 67, wakati Rais wa Awamu ya Nne akizindua madaraja pacha ya Ruhetei A, B na C. Hali halisi ya barabara ya Mbinga hadi Mbamba Bay sasa ni mbaya, hasa ukizingatia ni kipindi cha masika. Barabara hii haipitiki na wananchi wanakwama sana. Pamoja na Serikali kila mara kueleza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupata Mkandarasi, ahadi hii ya barabara inaendelea kuchukua muda kutekelezwa na kusababisha hasara kubwa za kiuchumi na kijamii. Je, Serikali inatoa kauli gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha mchango wangu katika mjadala wa Maliasili na Utalii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru ni mojawapo ya Wilaya kongwe nchini ambazo zimekuwa na matukio ya muingiliano wa shughuli za binadamu na wanyamapori hasa tembo. Baadhi ya matukio yamepelekea kuwepo na mauaji ya tembo hao na kisha wananchi kuwaondoa pembe na kugawana nyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni zaidi ya tembo 20 walivamia vijiji vya Wenje vilivyo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji wakitokea Msumbiji (Aprili, 2017) na wananchi waliwaua na kisha kuondoa meno yao na kugawana nyama. Vilevile wengine walivamia kijiji cha Jakika wakitokea Pori la Akiba la Selous na kuharibu zaidi ya ekari 50 za mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tukio hilo, zaidi ya watu watano walikamatwa. Pamoja na kuwa kuna muingiliano wa vijiji zaidi ya vitano na Pori la Selous na tembo hao wamekuwa wakisumbua zaidi, ipo haja kuweka mikakati madhubuti itakayoweza kuwadhibiti tembo kuingia katika vijiji hivyo na pia kuwashirikisha kwa karibu wananchi ili kupunguza mauaji ya tembo pale wanapoingilia maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shehena ya meno ya tembo; Tanzania inaonekana mbele ya Jumuiya ya Kimataifa kama Taifa ambalo halitambui kwamba kushamiri kwa vitendo vya ujangili ni pamoja na kutaka kuuza shehena ya meno ya tembo. Ikumbukwe kuwa kadri siku zinavyoenda idadi ya tembo nchini inapungua huku ikichochewa pia na kutokuwa na mbinu na mikakati madhubuti ya kukomesha vitendo vya ujangili. Mkoa wa Ruvuma ni moja ya mikoa inayoongoza kwa matukio ya kukamatwa kwa shehena za meno ya tembo na nyara za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali ya Tanzania bado imeshikwa na kigugumizi licha ya kuwa na idadi kubwa ya matukio 11,000 ya mauaji ya tembo kila mwaka, kutekeleza ahadi yake ya kuteketeza tani zipatazo 90 za shehena ya meno yaliyohifadhiwa katika maghala yake baada ya kuzikamata. CITES iliweka msimamo wa nchi zenye shehena kuteketeza shehena pamoja na kulifunga soko la China ili ku-discourage ujangili. Kwa masikitiko makubwa, Tanzania bado inashikilia kuuzwa shehena hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete aliwahi kusema katika kongamano nchini Uingereza kuwa imesitisha na kufuta msimamo wake wa kuuza shehena ya meno ya tembo. Muda mrefu sasa umepita tangu ahadi hiyo itolewe. Je, Serikali inatueleza ni lini itateketeza shehena hiyo kama walivyofanya majirani zetu Kenya? Pamoja na hayo, ipo haja ya Serikali pia kupinga kwa vitendo uuzaji wa meno na pembe za ndovu waliokufa naturally ili kuua kabisa soko la ndovu duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa utangazaji wa vivutio vya utalii; Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii lakini havijatangazwa vya kutosha ili kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi. Nimeona msanii wa kike Vanessa Mdee ni mmoja wa wasanii ambao wametumiwa na Afrika Kusini kutangaza vivutio vya nchi hiyo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwatumia wasanii maarufu/mashuhuri na Watanzania kama mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii nchini? Pia ni lazima kuhakikisha Balozi zetu katika mataifa mbalimbali zinaandaa utaratibu wa economic diplomacy ili kuhuisha sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza ajira kupitia sekta ya maliasili na utalii; vijana wengi hawana ajira nchini na hii imetokana na mwenendo wa dunia katika ajira lakini hii isisababishe Tanzania kupoteza lengo la kukuza ajira hasa kupitia sekta hii muhimu. Leo sekta ya utalii inakua lakini ajira zinazopatikana katika sekta hii ni chache sana. Hata vyuo vinavyotoa kozi za utalii nchini havikidhi hitaji kubwa la watu kwenye sekta ya utalii. Ipo haja ya kuwa na integration of national plans katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa utunzaji wa mali kale katika kukuza utalii; ipo haja ya Serikali kuwekeza ipasavyo katika kutunza mali kale ili kukuza sekta ya utalii. Mji Mkongwe Zanzibar, Isimani, Bagamoyo na maeneo mengine ni mojawapo ya maeneo yenye malikale lakini havijatunzwa na ku-maintain status zake (hadhi zake) ili kuvutia watalii wengi zaidi kutokana na historia za maeneo hayo. Miji hiyo ni ya kihistoria, Wizara ishirikiane na Wizara ya Utamaduni ili kuhakikisha maeneo hayo yanatunzwa ili kuongeza Pato la Taifa kutokana na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu biashara ya vinyago na utalii; ipo haja ya Wizara kuhakikisha kuwa wachongaji na wasanii wa vinyago hasa katika maeneo ya utalii wananufaika na kazi zao. Ni namna gani Wizara hii inahakikisha kuwa vinyago vinavyochongwa nchini vinanufaisha wachongaji wake na pia Serikali inanufaikaje na uuzaji wa vinyago hivyo? Iwapo Serikali itawekeza vya kutosha kuwasaidia wachongaji hawa itaweza kukusanya kodi na kuongeza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ni sekta ya muhimu sana katika ukuaji wa uchumi hasa katika mapinduzi ya viwanda. Ni ajabu sana kuona kuwa hakuna msisitizo mkubwa kwa sekta ya kilimo hasa ukizingatia kuwa hata mapinduzi makubwa ya viwanda duniani yaliyotanguliwa kwanza na mapinduzi ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ni sekta muhimu, siyo katika uzalishaji wa malighafi, bali pia katika kutoa ajira hasa ukizingatia kuwa vijana ni wengi kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ambayo imeweka wazi kuwa zaidi ya asilimia 52 ya idadi ya watu ni vijana. Hivyo Serikali ilitakiwa kutenga bajeti yake siyo tu kutekeleza sera yake ya viwanda, bali pia kuweka mkazo katika sekta ambayo inatatua changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado zipo changamoto kubwa ambazo zina athari kubwa na za moja kwa moja kwa sekta ya kilimo na ukuaji wake hasa miundombinu. Nchi yetu ina changamoto ya kijiografia. Kwa mfano, Mkoa wa Ruvuma una changamoto kubwa ya miundombinu hasa kwa Wilaya ya Mbinga, Nyasa, Namtumbo, Tunduru na hivyo kuleta changamoto ya masoko hasa kipindi cha masika. Hivyo Wizara hii inatakiwa kuweka mkakati wa pamoja na sekta ya miundombinu ili kuwezesha ukuaji wake na kuendeleza wananchi kiuchumi. Je, ukakasi wa kuweka miradi ya pamoja kukuza sekta hii muhimu unatoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa Mkoa wa Ruvuma ni mojawapo ya mikoa yenye kuzalisha kwa wingi mazao ya kibiashara na chakula. Hivyo tulitegemea iwe mojawapo ya mikoa yenye ukuaji mzuri wa kiuchumi, lakini hali ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kutoa majibu kuwa mbaazi ni nzuri kwa chakula, leo mwananchi wa Tunduru aliyewekeza kwenye mbaazi akitegemea soko la dunia, anadhihakiwa vipi kwa soko la mbaazi kushushwa na kauli za kisiasa? Ipo haja ya Wizara ya Kilimo kuwanasua wakulima hasa wanaotegemea jembe la mkono kwa kuwaunganisha na masoko na siyo kuwafanyia dhihaka pale wanapozalisha ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona kuwa Wana Ruvuma wanazalisha mazao ya kibishara na chakula lakini hawanufaiki na kilimo. Upo usemi unaosema kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe. Je, nguvu kiasi gani itumike ili Mtanzania aweze kunufaika na kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo linatakiwa kutazamwa kwa jicho la ziada ili kunusuru wakulima, nalo ni soko la mahindi. Nia njema ya Serikali iko wapi ikiwa NFRA haipewi fedha za kutosha na hivyo kupelekea kununua sehemu ndogo tu ya mahindi yaliyozalishwa nchi nzima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Ruvuma ambao kwa sehemu kubwa wakulima wamelima mahindi kiasi cha kuwa na ziada lakini kutokana na uwezo mdogo wa NFRA, leo mkulima anabaki na ziada ikumuozea shambani bila kuwa na uhakika wa soko. Hata kama Serikali inasema itajenga maghala kuhifadhi ziada (surplus), bado bei ya soko la mahindi haiwezi kumpa mkulima wa mahindi uwezo wa kurejesha gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa NFRA imeshindwa kununua mahindi, kuna ugumu gani wa Serikali kutoa kibali kwa wananchi kuuza mahindi kwa kuwa NFRA inanunua inachoweza kuhifadhi (ikiwemo kuwauzia WFP na private traders) lakini bado kiasi cha mahindi yaliyovunwa inabaki mikononi mwa mkulima na kuleta hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mkulima wa mahindi anufaike, ni aidha Serikali iongeze bajeti ya NFRA iweze kununua mahindi kwa bei nzuri ama/na kuamua kutoa uhuru kwa mkulima aliyezalisha ziada auze kwa bei ya soko la nje ambalo kwake ni nguvu yake mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. Siungi mkono hoja.