Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Josephat Sinkamba Kandege (7 total)

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo yaliyopo Matai kwenda Kasesya ni ahadi ya muda mrefu ya Serikali na Ilani ya CCM tangu mwaka 2010:-
(a) Je, Serikali itaanza lini kukamilisha ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga Port utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshmiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Matai hadi Kasesya yenye urefu wa Kilometa 50 ni sehemu ya Barabara Kuu inayounganisha nchi za Tanzania na Zambia katika mpaka wa Kasesya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ya Tanzania imekwishaanza kutekeleza mpango wa kuijenga kwa lami. Kazi ya usanifu wa kina na maandalizi ya zabuni ilianza mwezi Julai, 2014 na kukamilika Januari, 2015. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 11.614 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Matai – Kasesya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Kasanga Port yenye urefu wa Kilometa 112 imekamilika kwa takriban asilimia 53 ambapo kilometa 56 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 32.01 ili kukamilisha ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai hadi Kasanga Port ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2017.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafufua barabara ya Mkoa wa Mbeya kwenda Kasanga Port pamoja na kivuko cha Mto Kalambo ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara iliyokuwa inatumika zamani enzi za Wajerumani inayoanzia Wilayani Momba katika Mkoa wa Songwe hadi Kasanga Port. Barabara hiyo ilikuwa inapita katika Vijiji vya Kapele – Kakosi - Ilonga, ambapo jumla ni kilometa 55, ambayo kwa sasa ni sehemu ya barabara ya wilaya inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Momba. Aidha, katika Mkoa wa Rukwa barabara hiyo ilikuwa inapita katika Vijiji vya Mambwenkoswe – Kalepula - Mwimbi - Kasanga Port.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya maeneo katika barabara hiyo ya zamani, kati ya Mwimbi - Kasanga Port hayapitiki kabisa hasa wakati wa masika na katika maeneo mengine barabara inapitika kwa shida hususan katika eneo la Mto Kalambo kwa kuwa hakuna barabara rasmi. Serikali inawaasa wananchi wanaosafiri kutoka Momba na Mbeya kwenda Kasanga Port kutumia barabara ya lami ya Mbeya – Tunduma - Sumbawanga na kuunganisha katika barabara ya Sumbawanga - Matai - Kasanga Port inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumiaji barabara wanaweza pia kutumia barabara ya Wilaya ya Kapele – Kakosi - Ilonga Mkoani Mbeya, barabara ya Mkoa ya Mwambwenkoswe – Kalepula - Mwimbi - Matai na kuunganisha katika barabara kuu ya Sumbawanga – Matai - Kasanga Port Mkoani Rukwa.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Je, ni aina gani ya madini yanapatikana ndani ya Wilaya ya Kalambo kulingana na tafiti ambazo zimekwishafanywa na Serikali?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na tafiti za awali zilizofanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) pamoja na taarifa kutoka kwa wawekezaji wanaomiliki leseni katika maeneo ya Kalambo, madini yanayopatikana ni pamoja na madini ya chuma, dhahabu, galena kwa maana ya lead, shaba pamoja na madini ya ujenzi. Hata hivyo, GST wanaendelea kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Kalambo ili kubaini kama kuna madini mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wenye nia ya kupata taarifa kuhusu rasilimali za madini yaliyopo katika maeneo hayo, wafike katika ofisi zetu za madini pamoja na Wakala wake. Aidha, taarifa hizo zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara, tovuti ya GST pamoja na machapisho mbalimbali ambayo yapo katika Ofisi zetu za madini.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Serikali ilielekeza nguvu zake katika kutangaza vivutio vya utalii na wawekezaji kuja Kanda ya Kusini ili kupunguza msongamano wa utalii Kaskazini mwa Tanzania:-
(a) Je, ni kwa kiasi gani Serikali imeyatangaza maporomoko ya Kalambo ambayo ni ya pili Afrika baada ya yale ya Victoria kuwa kivutio cha utalii?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Hifadhi ya Msitu wa Kalambo pamoja na maporomoko haya yanakuwa chini yake kupitia Shirika lake la TANAPA?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Msitu wa Kalambo pamoja na maporomoko yake ipo chini ya Wizara yangu na inasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na.14 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Bodi ya Utalii nchini imekuwa ikitangaza utalii katika maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Tanzania ikiwemo maporomoko ya Kalambo kupitia Jarida Maalum la kutangaza maeneo ya utalii yenye changamoto ya kimiundombinu lijulikanalo kama Hard Venture Tourism, majarida mengine ya utalii, vipeperushi, tovuti mbalimbali ikiwemo the destination portal chini ya Bodi ya Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA ni shirika la umma chini ya Wizara yangu lililoanzishwa chini ya Sheria ya Hifadhi za Taifa kwa madhumuni mahsusi ya kuendesha na kusimamia matumizi endelevu ya maeneo yote yaliyopitishwa kisheria na Bunge kuwa Hifadhi za Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hifadhi ya Msitu wa Kalambo, maporomoko ya Kalambo yakiwa ni sehemu yake siyo Hifadhi ya Taifa, hivyo kusimamiwa chini ya Sheria ya Misitu. Kwa sasa Serikali itaendelea kusimamia msitu huu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na siyo TANAPA.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Serikali ilipata mkopo kutoka Benki ya Dunia na kujenga miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Jijini Dar es Salaam. Baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika Serikali ilitoa msamaha wa baadhi ya kodi wakati wa uingizaji nchini mabasi yanayotumika kusafirisha abiria katika mradi huo. Serikali inamiliki asilimia 49 ya hisa za mradi huo na mwekezaji asilimia 51.
(a) Wakati wa kukokotoa hisa kati ya Serikali na mwekezaji, je, sehemu ya msamaha imejumlishwa katika ukokotoaji wa hisa?
(b) Je, ni nini faida na hasara za msamaha huo wa kodi upande wa Serikali?
(c) Wakati wa kulipa mkopo huo, je, ni nini wajibu wa mwekezaji katika mkopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kimsingi mwekezaji hakupata msamaha wa kodi wakati wa kuingiza mabasi nchini bali alipewa punguzo la kodi hiyo (import duty) kutoka asilimia 25 inayotozwa hadi asilimia 10. Punguzo hilo lilitolewa kwa makubaliano na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(b) Mheshimiwa Spika, punguzo la kodi hiyo limesaidia kutoa unafuu wa nauli zinazotozwa kwa abiria wanaotumia mabasi ya UDART. Endapo punguzo hilo lisingekuwepo ni dhahiri kwamba gharama hizo zingejumuishwa katika viwango vya nauli kwa watumiaji.
(c) Mheshimiwa Spika, mwekezaji anawajibika kurejesha mkopo aliochukua kwa ajili ya kununulia mabasi pamoja na kulipa kodi Serikalini kwa mujibu wa sheria za nchi. Kwa upande wake, Serikali inawajibika kulipa mkopo Benki ya Dunia ambao ulitumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi
wa DART awamu ya kwanza kwa kuzingatia makubaliano (financing agreement).
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Ulumi kilichopo Kata ya Ulumi ambao ulianza kujengwa mwaka 2010 haujakamilika mpaka sasa.
(a) Je, ni sababu zipi zimefanya mradi huo kutokamilika mpaka sasa na ni lini utakamilika?
(b) Je, Serikali ilitenga kiasi gani cha fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 ili kukamilisha mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa ujenzi wa Mradi wa Umwagiliaji Ulumi ulianza kujengwa mwaka 2012 kwa kujenga banio lenye gharama ya shilingi milioni 213,279,000 kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Msaada wa Chakula baina ya Serikali ya Tanzania na Japan bila kuhusisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji mashambani ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.3 zinahitajika kukamilisha kazi zote. Aidha, Wizara yangu hivi sasa inafanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 kwa lengo la kuihuisha ili uendane na hali ya sasa. Kazi hii inatarajia kukamilika mwezi Septemba mwaka 2018 na kupitia mpango huu Mradi wa Ulumi ni miongoni mwa miradi iliyopewa kipaumbele kwa ajili ya uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji kwa manufaa ya wananchi wa Ulumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa mradi huu kwa wananchi wa Kalambo, Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2018/2019 itaingiza mradi huu katika bajeti kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili mradi huu uweze kuanza utekelezaji.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Jimbo la Kalambo lina kata 23 na vijiji 111; katika awamu ya kwanza na ya pili ya mradi wa REA ni vijiji vichache tu vilipata umeme.
Je, katika utekelezaji wa REA III ni vijiji vingapi vinategemea kupata umeme ili wananchi wa maeneo hayo waweze kujiandaa kujiendeleza kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza rasmi tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele mradi vitatu vya densification, grid extension pamoja na off- grid renewable vinavyolenga kuongeza wigo wa usambazaji katika vijiji vyote vilivyobaki nchi nzima, vitongoji vyote, taasisi za umma, na maeneo ya pembezoni ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme. Mradi wa REA Awamu ya Tatu katika jimbo la Kalambo utajumuisha vijiji 89 kupitia vipengele
- mradi vya densification grid extension, utaokamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya vijiji hivyo itajumuisha ujenzi wa njia ya msongo umeme wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 413.49; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 745; pamoja na ufungaji wa transfoma 149. Kazi nyingine itakuwa ni kuwaunganishia umeme wateja wa awali 9,816 kazi ya gharama hii ni shilingi bilioni 36.