Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Josephat Sinkamba Kandege (36 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru kwa fursa nyingine tena, naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao walipata fursa ya kuchangia kwa kuongea walikuwa jumla ya Wajumbe 19 na waliochangia kwa kuandika walikuwa jumla 17, jumla yake ilikuwa ni 36.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyoanza kusema asubuhi, umuhimu wa hoja hii nzito, naamini na wewe mwenyewe ni shahidi leo siku ya Jumamosi nisingependa kupoteza muda mwingi wa Waheshimiwa Wabunge, lakini wewe mwenyewe unaona jinsi ambavyo wametoa msukumo wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla naomba nikumbushe, wewe ni shahidi jinsi ambavyo kulikuwa na kazi kubwa ya uanzishaji wa Kamati ya Bajeti na uanzishwaji wa Sheria ya Bajeti na misingi ambayo ilikuwa imewekwa ili tuondokane na ile hali ambayo Bunge lilikuwa linafanya kama rubber stamping waliita watu hivyo. Tukasema tuondoke hapo, tufike mahali ambapo Bunge litashiriki katika mchakato mzima wa kuandaa bajeti na utekelezaji wake. Ombi ambalo ni vizuri na Serikali bahati nzuri wanasikia, isingependeza tukarudi nyuma tulikokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa ni vizuri kwanza tukajengea uwezo Ofisi ya Bajeti na sitarajii, maana hili limeanza kujitokeza pale ambapo Bunge linataka kuwa na uwezo wake mzuri sasa kumekuwa na tabia hata ule uwezo mzuri, wale watumishi wazuri ambao wanapikwa na Bunge wanaanza kuhamishwa wanapelekwa upande wa Serikali, haitapendeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukawa na uwezo mkubwa, twende na wengine ambao Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shahidi ukienda nchi kama Uganda, Kenya inafika mahali ambapo Kamati ya Bajeti, inakuja na bajeti mbadala ili kulinganisha na ile bajeti ambayo inaletwa na Serikali, huko ndiko ambako tunatarajia kwenda. Kwa hiyo, itakuwa si vizuri kama Serikali watatumia fursa ya kuanza kuchukua vile vichwa vizuri ambavyo vinatengenezwa wakapeleka upande wa kwao. Hilo lilikuwa la jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo na baada ya kutambua Wajumbe waliochangia, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, naomba kwa uchache nishukuru Serikali kwa sababu iko hapa wamesikia na mengi kimsingi na wao wamekiri kwamba ni ya kwenda kuyafanyia kazi, nitaje machache na kwa ujumla Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa kuongea kama watapenda niwataje majina lakini kwa kuokoa muda, naomba nisitaje hata wale ambao walichangia kwa kuandika naomba nisitaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya masuala ambayo yamesemwa kwa kiasi kikubwa ni vizuri nikasema. Kimsingi wajumbe wengi wamesisitiza juu ya suala zima la kulipa deni la TANESCO. Sisi sote ni mashahidi, uko umuhimu sana wa kuhakikisha kwamba deni hili linalipwa maana tunaamini Tanzania ya viwanda bila kuwa na uhakika wa umeme hatuwezi kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na suala zima la ushiriki wa private sector (PPP). Si rahisi kwamba masuala yote ya maendeleo tutaiachia Serikali kwa maana ya ile miradi mikubwa. Kwa hiyo, ni vizuri kama ambavyo Waheshimiwa wengi wamechangia kwamba fursa iwepo na itumike kuhakikisha kwamba private sector inashiriki kama injini ya kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, tumekuwa tukiongea muda mrefu tangu ukiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, mapendekezo ambayo yaliletwa Serikalini juu ya kuanza ujenzi wa barabara, kutoka Dar es Salaam kufika Morogoro na kwa kuanzia Chalinze zile njia tatu. Taarifa ambazo zilikuwepo ni kwamba private sector walikuwa wako tayari. Sasa hadithi imekuwa ya muda mrefu ni vizuri sasa Serikali ikaenda kwanza kutenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, katika Wajumbe wengi waliochangia yamesemwa maneno kwamba kuna hizi kauli za kutoka kwa Mheshimiwa Rais, anatamka pesa inapatikana. Niombe Waheshimiwa pamoja na nia njema ni vizuri tukaenda kutazama budget frame kwa ujumla wake, hiki ambacho kinatamkwa na Mheshimiwa Rais ukienda kwenye bajeti utakuta kipo. Siyo kwamba anaamka tu anatamka halafu pesa inapatikana. Mifumo ya bajeti iko sahihi. Kwa hiyo, ni vizuri kwa nia njema kwa sababu haya ambayo yanafanywa ni kwa ajili ya Watanzania ni vizuri tukafuatilia utaratibu wa bajeti twende kwenye vitabu, turejee tujue hayo ambayo yanatamkwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wameongelea kuhusiana na suala zima la kilimo ambalo na Kamati ya Bajeti kimsingi tumesisitiza kwamba ili twende kwenye Tanzania ya viwanda ni vizuri uwekezaji ukawekwa wa kutosha kuhusiana na suala zima la kilimo. Bahati nzuri Serikali imesikia, hii habari ya kwamba mvua zisiponyesha mara moja tu tunaanza kuwa na wasiwasi hatuwezi kwenda tukasema ni Taifa la kwenda kwenye uchumi wa kipato cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ziko nyingi, kama mtu hakuchangia hoja asitarajie kusikia hoja yake ikijibiwa, hayo ambayo nayajibu ni yale ambayo yamechangiwa kwa ujumla na yakapewa uzito na bahati nzuri, hiki ninachokisema nimekisomea. Kwa hiyo, sikukiokota mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto za kibajeti, Wajumbe wengi wamechangia. Wabunge wameainisha kuwa katika taarifa ya Kamati hali ya uchumi kwa mujibu wa taarifa ya kutoka Benki Kuu na mwenendo wa mfumuko wa bei, Serikali inashauriwa kuhakikisha kwamba inakaa chini na kutathmini mwelekeo uliokuwa umetolewa awali na hali ya sasa. Ni vizuri tukaanisha ili tukapata namna ambavyo tunaenenda kama tuko kwenye right track. Hili niombe Serikali kujisahihisha si vibaya, tutazame wapi tuna-miss point ili isije ikafika mpaka dakika ya mwisho ndio tukajikuta tume-miss kile ambacho tulikitarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kuhusiana na mafunzo kwa Bunge zima. Imechangiwa na Wabunge wengi ni hoja ya msingi ni vizuri Serikali mkajipanga maana exposure ni jambo la msingi sana. Pamoja na ufinyu wa bajeti lakini ni lazima tuhakikishe kwamba Wabunge wanajengewa uwezo ili wafanye kazi yao ya kikatiba ya kuhakikisha kwamba wanaisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeongelewa hoja kuhusiana na Serikali kukopa ndani na sisi Kamati tumeliona, tukaishauri Serikali. Serikali ina muscles za kutosha ina uwezo mkubwa wa kwenda kutafuta mikopo nje, ni vizuri hii mikopo ya ndani tukaiachia sekta binafsi ili wahangaike na hizi fedha ambazo watazipata kwa urahisi. Tumeiomba Serikali iharakishe zoezi la kufanya sovereign rate ili waende kutafuta mitaji huko nje kwa sababu inapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la shilingi milioni 50 ya kila kijiji, wewe ni shuhuda ulishiriki wakati tunajadili na tukakubaliana kwamba pesa hizi zinazotolewa si pesa ya ruzuku, ni pesa ambayo ni ya mkopo na pesa ya mkopo lazima ujihakikishie kwamba huyu unayemkopesha anaenda kuzirejesha vipi kwa sababu pesa hii ni revolving fund. Tunaiomba Serikali iharakishe mchakato ili pesa hizi zikitolewa zikifika kwa wananchi ziweze kurejeshwa ili wananchi walio wengi, Watanzania wengi waweze kupata fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda hautoshi naomba sasa nijikite katika maazimio ambayo tunaomba Bunge lako liiitake Serikali kwenda kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako Tukufu lipokee maoni na mapendekezo ya Kamati kuwa Azimio la Bunge kwa utekelezaji wa Serikali ili taarifa hiyo ije iletwe namna ambavyo Serikali imetekeleza na kwa kuzingatia ushauri mzuri ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia pande zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa na Kamati zote mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika mbili nyingi sana kwangu kwa sababu nategemea kutoa ufafanuzi kwenye eneo moja tu nalo liko ukurasa wa 38 ni kuhusiana na ubovu wa barabara za mipakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo sisi kama Taifa tumekuwa tukiweka vipaumbele kwa barabara ambazo zinaunganisha Mikoa, lakini pia kuna umuhimu mkubwa sana kwa barabara za mipakani na hasa barabara yetu ya kwenda Uganda kule kwa kupitia chombo chetu cha TARURA tutahakikisha kama Serikali ukarabati unafanyika ili barabara hii iwe nzuri iweze kusaidia katika shughuli nzima za kulinda mipaka yetu, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Naibu Spika, awali ya yote kwa sababu ndiyo mara ya kwanza nikihudumu katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba unipatie fursa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia kusimama leo kuchangia na kutoa baadhi ya ufafanuzi katika hoja zilizoletwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba uniruhusu kipekee nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Joseph John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa kwangu kuniteua nihudumu katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Tatu, naomba niishukuru familia yangu, mke wangu na watoto wangu kwa namna ambavyo wamekuwa wakiniwezesha kuweza kuhudumu katika nafasi hii. Nafasi ya nne, si kwa umuhimu ni kwa Chama changu cha Mapinduzi, wapiga kura wangu wa Jimbo la Kalambo kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakishirikiana nami katika kuhakikisha kwamba tunaweza kuhudumu katika nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa muda naomba uniruhusu niwatambue Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri ikiongozwa na Kamati yetu chini ya uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Jasson Rweikiza na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Mwanne Mchemba, kwa maelekezo na ushauri ambao wamekuwa wakitoa katika Wizara yetu, hakika ni hazina kubwa sana kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kufafanua baadhi ya hoja kabla Mheshimiwa Waziri hajaja kufafanua hoja zitakazokuwa zimebaki. Katika michango ambayo imetoka kwa Waheshimiwa Wabunge ukianzia na Kamati kuna suala zima la ushiriki wa Waheshimiwa Wabunge katika vikao kwa maana ya DCC, Mabaraza pia na kikao cha RCC.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba pale ambapo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakipata fursa ya kushiriki katika vikao hivi, michango yao imekuwa ya muhimu sana, imekuwa ikileta tija, tunahitaji sana uwepo wa Waheshimiwa Wabunge kushiriki katika vikao hivi. Ndiyo maana Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetoa waraka ikiwaelekeza Makatibu Tawala na Wakurugenzi kuhakikisha kwamba ratiba zao ambazo wanazipanga ni zile ambazo zitazingatia ratiba za Waheshimiwa Wabunge kuweza kushiriki katika vikao hivi ili michango yao ya maana ambayo tunahitaji iweze kuchukuliwa, kwa sababu wao ndiyo wawakilishi wa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi ni pamoja na suala zima ambalo liliongelewa kwenye Kamati, hapa Bungeni halikutokea sana, lakini ni ukweli usiopingika kwamba Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakihitaji na jambo ambalo ni la muhimu kuhakikisha kwamba hata ziara za viongozi wa Kitaifa wanapata taarifa ili washiriki, maana wao ndiyo wawakilishi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Nabu Spika, kuna hoja iliyojitokeza kuhusiana na suala zima la asilimia 10 ya mapato ya ndani kutengwa kwa ajili ya kwenda kwa akina mama pamoja na vijana. Waheshimiwa Wabunge, pia kwa wakati fulani waliongelea juu ya kuanzisha asilimia mbili kwa ajili ya kwenda kwenye kundi la watu wenye uhitaji maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa hivi ambayo haioneshi dhahiri, umeandaliwa utaratibu wa kuhakikisha kwamba kwa kupitia Finance Bill ya mwaka 2018/2019 kipengele hicho ambacho kinampa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kuingiza katika sheria hiyo kipengele ambacho kitazitaka Halmashauri zote kuhikisha kwamba wanatenga na wasipotenga Wakurugenzi wachukuliwe sheria safari hii kitaweza kwenda kuwekwa humu. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba pesa hizi zinakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia juu ya suala zima la kuwawezesha akina mama na vijana kupata elimu ya ujasiriamali. Ni ukweli usiopingika kwamba ukienda kukisaidia kikundi bila kuwa na elimu ya ujasiriamali ni sawa na unapeleka fedha ambayo una uhakika kwamba haitatumika na kuleta mapinduzi makubwa ambayo tunatarajia yapatikane kwa vikundi hivi kwa maana ya akina mama, vijana lakini pia na kundi maalum la hawa watu wenye uhitaji maalum. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba jambo hili linaenda kutekelezwa na ninaamini Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha jambo hili pia atalifafanua kwa uzuri zaidi ili nia njema ambayo imekusudiwa na Serikali iweze kutimizwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa suala zima ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na uanzishwaji wa TARURA. Tunashukuru kwa pongezi ambazo zimetolewa kwa maeneo ambayo TARURA imeanza kufanya kazi vizuri matunda yake dhahiri yanaonekana. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba chombo hiki ambacho kimeanzishwa kinaenda kufanya kazi ambayo tunatarajia ili yale maombi ambayo Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakitoa/wakiomba baadhi ya barabara zao za kwenye halmashauri zao zipandishwe hadhi yanaenda kusita kwa sababu watakuwa wanaridhika juu ya utendaji wa chombo hiki cha TARURA ambacho kimeanzishwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kukiamini chombo hiki, chombo hiki bado ni kipya. Tunahitaji kukiunda vizuri na Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda kwamba wakati TARURA inaanzishwa tumelazimika kuchukua watumishi waliokuwa kwenye Halmashauri ndiyo hao ambao wakaajiriwa. Lakini naomba niwahakikishie, vetting inaendelea kufanyika ili tuhakikishe kwamba wale tu ambao wana sifa na weledi ndiyo ambao watabaki kuendelea kutumika katika chombo hiki. Ni azma yetu kuhakikisha kwamba wale tu ambao wana ufanisi ndiyo ambao wataendelea kufanyakai TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ambayo imesemwa na juu ya suala zima la kuongezea pesa TARURA. Tunakubaliana na hoja hizi ambazo zimetolewa na Serikali katika kipindi ambacho Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati fulani akiwa anatoa ufafanuzi, alisema ni vizuri tukatazama ndani ya Serikali namna bora ya kuweza kuhakikisha kwamba tunakiwezesha chombo hiki, lakini pia tukiwa na uhakika kwamba chombo hiki kinaenda kufanyakazi iliyokusudiwa na Waheshimiwa Wabunge na siyo suala tu la kuwa na bajeti kubwa ambayo haiendi kufanya kazi iliyokusudiwa. Kwa hiyo, tunaomba tukipatie fursa chombo hiki, tukijenge, tukiimarishe maana mwaka mmoja si umri mrefu. Naamini kadri siku zinavyokwenda chombo hiki kitasimama vizuri na tumepata pongezi kutoka maeneo mbalimbali ambapo TARURA imeanza kufanya kazi nzuri. Naomba nipongeze sehemu zote ambazo wamefanya kazi vizuri na wale wengine ambao wanaenda kwa kusuasua wajirekebishe, wahakikishe kwamba kile ambacho tumekusudia ndani ya Serikali kinaenda kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima ambalo limejitokeza kuhusiana na ujenzi na ukamilishaji wa zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali za wilaya. Ni ukweli usiopingika kwamba Watanzania wana kiu kuhusiana na suala zima la kupata huduma iliyo bora ya afya, kutokana na Ilani yetu ya CCM tumeliweka hili kwamba ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba kila kijiji inaenda kujengwa zahanati kwa kushirikisha wananchi lakini pamoja na kushirikisha Serikali, kila Kata tunakuwa na kituo cha afya na pale ambapo hamna hospitali ya wilaya, hospitali ya wilaya inaenda kujengwa.

Naomba niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba azma hii ya Serikali ni thabiti na ninatambua kabisa kwamba kila Mheshimiwa Mbunge sehemu ambayo hakuna kituo cha afya au hakuna hospitali ya wilaya angetamani hata leo au jana iwe imejengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, safari ni hatua, ni vizuri tukakubaliana kwamba nia njema ya Serikali ambayo imeanzishwa ya kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vya afya, zahanati tunaenda kuifanya. Katika nafasi hii nikiwa nahudumu nimepata fursa ya kutembelea maeneo mengi, muitikio wa wananchi kuhusiana na suala zima la ujenzi wa vituo vya afya haitiliwi mashaka, muitikio ni mkubwa sana, naomba niendelee kuwaomba wananchi kuendelea kushiriki katika kutoa nguvukazi yao na kusimamia kuhakikisha kwamba kila shilingi ambayo inatolewa inaenda kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kufafanua hayo machache, naomba kipekee nimshukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Selemani Jafo, Naibu Waziri mwenzangu Mheshimiwa George Kakunda kwa ushirikiano na maelekezo ambayo nimekuwa nikipata katika kazi yangu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu spika, Wenyeviti wote wa Kamati na Wabunge kwa ujumla kwa ushirikiano ambao kwa kweli hata siku moja sijapungukiwa. Hakika Mwenyezi Mungu atasimama pamoja na ninyi kwa sababu dhamira ya kuwatumikia Watanzania iko dhahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja iliyotolewa yako mengi ambayo yamesemwa. Lakini kwa ajili muda nitaomba nijikite katika maeneo mawili ambayo Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ambalo naomba nianze ni suala zima la TARURA. Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamechangia wengine wakiounga mkono TARURA uwanzishwaji walio wengi wameounga mkono uanzishwaji. Lakini ambalo limejirudia mara nyingi sana kwa kila Mbunge ambaye alipata fursa ya kuchangia kuhusiana na chombo hiki ni suala la mgawanyo asilimia 30 kwa 70.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitoa ufafanuzi wakati tunahitimisha hoja ya bajeti ya kwetu lakini kwa sababu chombo hiki kinaingiliana na TANROADS ndiyo maana na leo imekuwa likijirudia mawazo ambayo yanatolewa na Waheshimiwa Wabunge inaonesha jinsi ambavyo tuna kiu ya maendeleo kuhakikisha kwamba barabara zetu na hasa zile za vijijini zinapitika vipindi vyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tunakiri, lakini pia si busara sana tukasema tunagawana umaskini kwa sababu mtandao wa barabara ambazo zinahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami ni nyingi na kila Mbunge ambaye amepata nafasi ya kusimama hapa aliomba barabara kiwango cha lami na hata kwako nimesikia upande wa kule wakati Mheshimiwa Frank Mwakibete anasema amesema na yeye anaomba barabara ya lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la kujenga barabara zetu kwa kiwango cha lami bado uhitaji ni mkubwa sana ni vizuri mkatupa fursa tukalichukua wazo jema kama hili ili tuje na namna ambayo itasaidia kuhakikisha kwamba hatuendi kufifisha kazi nzuri ambayo imeanzishwa juu ya suala zima la kujenga barabara zetu kuziunganisha zile za Mikoa na zile za mipakani kwa kiwango cha lami eti tu kwa sababu tunataka kuongezea asilimia nyingi kwenda TARURA. Ni vizuri na tukaanza kufikiria sisi Wabunge kwa ujumla wetu namna mzuri ya kupata chanzo kingine ilikuwa ni kusema kwamba sasa tunaenda kubadilisha formula kutoka asilimia 30 na 70.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ambayo imesemwa kwa urefu sana na ikawa inavuta hisia za Waheshimiwa Wabunge na hasa Wabunge wa kutoka Mkoa wa Morogoro na hoja hii iliibuliwa ikasemwa kwa uzuri sana na Mheshimiwa Devotha Minja. Sisi kama Serikali jambo hili tunalijua, lakini ni vuzri pia tukaelezana unaposema unajenga barabara kiwango cha lami tukubaliane hiyo barabara inajengwa kwa utaratibu upi na ni lami ipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko aina nyingi za lami hasa katika mradi ambao umeendeshwa na unaendela tunategemea kwamba utakamilika ndani ya mwezi huu, Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa ambayo kwa maana ya mji wa Morogoro ni mioungoni mwa miji ambayo imepata miradi huu mradi unaitwa ULGSP ambao unajengwa kwa jumla ya shilingi bilioni 12 ambao Waheshimiwa Wabunge hasa wa Morogoro walikuwa wanasema kwamba ni gharama sana kujenga barabara hii inafika mpaka bilioni tatu haijapata kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli haijapata kutokea, lakini hiyo barabara inajengwaje ndiyo suala ambalo lazima tuulizane. Barabara inapojengwa kuna hii inaitwa surface dressing, lakini ile ambayo tunajenga Morogoro inaitwa asphalt concrete ni miongoni mwa ujenzi wa barabara za lami ambazo zina gharama kubwa lakini ni vizuri pia tukaambizana ni kazi zipi ambazo zinafanyika. Barabara zile za Morogoro zinahusisha kilomita 4.6 na kazi ambazo zinafanyika naomba kwa ruhusa yako nizitaje. Kuna kutengeneza barabara ya Tubuyu - Nanenane Maelewano yenye urefu wa kilometa 4.6 na kazi zifuatazo zinafanyika:-

(i) Kutayarisha road bed, kuandaa matabaka ya barabara ambayo ni G3, G7, G15 na C1 kwa maana ya cement stabilizer layer; na

(ii) Kujenga njia za chini za ardhi kupitisha huduma kwa maana ya service dacks.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa mashuhuda, inapotokea barabara imejengwa mtu anataka kupitisha mabomba anakwenda kuomba kibali eti aje aanze kukata barabara, sasa kwa barabara inayojengwa Morogoro jambo hilo halitatokea kwa sababu hiyo service imeshakuwa provided. Lakini kama hiyo haitoshi, kuna kuondoa tabaka la udongo pale Morogoro ilibidi kuondoa milimita 600 kwa sababu kuna ule udongo mweusi. Kwa ujumla naomba kwa ajili ya muda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hakuna senti tano ambayo imeliwa na Tume zimeundwa, TAKUKURU wameenda wamechunguza ukiitazama unaweza ukadhani kwamba pesa imeliwa lakini kwa sababu ni kitu ambacho ni technical, naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba ni thamani ya pesa imetumika Mheshimiwa Mbunge asiwe na shaka juu ya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa muda.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi jioni ya leo ili kuchangia. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam kwa ujumla, mengi nimechangia kupitia Kamati ya Bajeti. Kwa leo kuna machache ambayo nadhani iko haja ya kuongezea ili kumtengeneza ng‟ombe vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza wachangiaji wengi ni kama vile dhana haieleweki kwamba Serikali inataka na sisi tujazie ya kwetu, badala yake watu wanakuja wanalalamika kama vile essence ya kuwepo wao kuchangia haina maana. Tungewasikia wapi kama fursa hii isingepatikana, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge ni fursa ya kuchangia ili tuwe na mpango mzuri kwa ajili ya kulivusha Taifa hili, Taifa ni la kwetu sote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma maoni ya Kambi ya Upinzani wanachokisema ni kama vile wana nchi ya kwao kiasi kwamba hata boti hili likienda vibaya wao wana option ya pili, haitujengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo ambayo nimeyatoa kwa utangulizi naomba nichangie kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee ukurasa wa saba wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri ambayo katika matazamio yake anatarajia kwamba bei ya mafuta itaendelea kuwa nzuri. Naomba tukumbushane OPEC walishakubaliana kwamba watapunguza uzalishaji wa mafuta, tafsiri yake ni nini? Kama uzalishaji wa mafuta utapungua maana yake bei itapanda, sasa katika mipango yetu lazima tulijue hili na tukishalijua sasa tujiandae tunafanyaje kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwombe Mheshimiwa Waziri, ni manufaa yapi ambayo tulipata kama Taifa baada ya bei kushuka? Kwa sababu haiwezekani tuache liende kama linavyoenda bei ikishuka hakuna ambacho Serikali inafanya, bei ikipanda hakuna ambacho Serikali inafanya. Ni vizuri tukawa na mkakati maalum kwamba pale ambapo inatokea bei kushuka tuone faida moja kwa moja ambayo inapatikana kutokana na anguko la bei ya mafuta. Lakini ingependeza sana kama ungeanzishwa Mfuko Maalum ili kuweza ku-stabilize pale ambapo bei zikipanda sana basi kuwe na namna ya kuweza ku-absolve shock ambazo zinajitokeza wakati bei za mafuta zimepanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote ni mashuhuda kwamba pale ambapo bei ikipanda hata siku moja tayari siku inayofuata tunaambiwa nauli zinapanda na kila kitu kinapanda. Sasa ni vizuri katika mipango yetu tukajiandaa tunaitumiaje fursa kama hiyo pale inapotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mpango wa maandalizi ya bajeti kuna prediction kwamba hali ya chakula itakuwa nzuri. Naomba nipingane na hili kwasababu kwa taarifa tulizonazo ni kwamba kuna ukame unatarajiwa kuwepo. Kwahiyo, hatuwezi tukasema hali ya chakula itakuwa nzuri, sio sahihi. Kwa hiyo, kwenye mipango yetu lazima factor hiyo tuiweke na tuseme sasa hiki kinachotokea tunafanyaje ili hali ya uchumi wetu isije ikaharibika kwa kiasi kikubwa. Ni vizuri katika mipango ambayo inawekwa tukaweka hiyo factor kwa sababu ipo; kama jambo una uhakika litatokea ukajifanya kwamba hulijui utakuwa husaidii Taifa. Ni vizuri tukalijua, tukajiandaa kwamba tunafanyaje kama Taifa ili tusije tukapata tabu kutokana na upungufu wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza wenzangu kuhusiana na kupungua kwa mizigo bandarini. Ni kweli, lakini ambacho ningeomba kiingie na kionekane vizuri kwenye mipango yetu, sisi sote ni mashuhuda kwamba bandari ya Dar es Salaam haina uwezo wa kupokea meli kubwa za kuanzia 3G, 4G uwezo huo hatuna, nini kifanyike? Tumekuwa tukisikia muda mrefu kwamba bandari ambayo itajengwa Bagamoyo itakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kupokea meli za ukubwa wa fourth generation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipata fursa ya kutembelea bandari ya Mombasa ukaona uwekezaji uliofanywa na wenzetu na hawakuishia kwenye Bandari ya Mombasa wameenda sasa Bandari ya kule Lamu, kiasi kwamba tusitarajie. Hata kama tutafanya upanuzi wa geti namba 13, 14 bila kuanza seriously ujenzi wa bandari ya Bagamoyo hakika tunajiandaa kwenda kushindwa kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri katika mipango yetu tukajielekeza katika hilo kwamba hata ungepanua vipi Bandari ya Dar es Salaam imeshafika mwisho. Kwahiyo, ni vizuri katika mipango yetu tukajielekeza katika kuanza kujenga bandari ya kisasa ambayo itakuwa na uwezo wa kupokea meli za kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia taarifa na hii pia tulikutana nayo hata wakati tumekutana na Wizara ya Fedha. Kuna fikra ndani ya Serikali kwamba mpango unaokuja sasa hivi juu ya currency yetu ni kuhama kutoka utaratibu wa fluctuation floating twende kwenye fixed na fikra iliyopo Serikalini ni kwamba tu-peg shilingi yetu kuibadilisha na dola kwa shilingi 2,193 kama sijakosea, ni jambo jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tafsiri yake ni nini? Ni kwamba tayari tunajiandaa kwamba shilingi yetu inakwenda kuanguka, faida ya ku-devalue shilingi inakuwa ni rahisi kwa mtu ambaye anakuja kuwekeza kwetu kwa ile direct foreign investment lakini disadvantage ambayo tunakuwa nayo ni kwamba itakuwa ni gharama sana kwa mtu ambaye anataka kupeleka mizigo nje kutoka Tanzania akija kubadilisha na pesa yetu atakuta anapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri hii hali ya kuacha soko ndio liamue na tutafute namna nzuri ambayo itahakikisha kwamba shilingi yetu haiyumbi sana, ndiyo namna iliyokuwa nzuri kulikoni habari ya kwamba unasema fixed, ukishafanya fixed ikija kutokea kipindi uchumi umeanguka maana yake tutalazimika ku-devalue shilingi yetu kwa kiasi kikubwa sana. Ni vizuri ikafanyika tathmini na utafiti wa kutosha kabla hatujafikia hatua hiyo, tujue madhara ambayo tumekuwa nayo kwa kuachia bei ya soko ni yapi na hicho ambacho tunatarajia kukifanya faida yake ni ipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapendeza sana tukiwa na makampuni ya Kitaifa kwa ajili ya Watanzania, sioni katika mpango unaokuja nia thabiti ya kuhakikisha kwamba TPDC inawezeshwa kwa niaba ya Watanzania ili kuweza kushiriki katika upstream na downstream katika suala zima la mafuta na gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikataba iliyopo mizuri kabisa inaonesha kwamba, wakiweka mtaji basi ushiriki wao na share ambayo watakuwa wanapata ni kubwa, lakini pale ambapo hawezeshwi kwa maana ya capital, kitabaki kugawanywa kile kidogo ambacho kimebaki. Sasa kwa Taifa ambalo tungependa kampuni ya Taifa kama zilivyo State Oil, Petrolbras ni kwamba Serikali zao ziliwekeza ndiyo maana makampuni haya yakawa na uwezo mkubwa. Ni vizuri na sisi tukahakikisha kwamba TPDC inawezeshwa kwa ajili ya Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la uvuvi wa bahari kuu. Silioni hili likijitokeza dhahiri lakini limekuwa likisemwa siku nyingi. Nakumbuka katika bajeti iliyotangulia ya 2015/2016 ilikuja Wizara ya Uvuvi wakisema kwamba wanahitaji pesa kwa ajili ya kununua meli ya doria. Ikatengwa nadhani kama shilingi milioni 500 wakapewa, hadithi ya hiyo pesa imetumikaje mpaka leo haijulikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, haiwezekani kile ambacho tunapata kwenye bahari kinazidiwa na maziwa ya Victoria na Tanganyika. Maana yake kuna tatizo kubwa ambalo hatujafanya kiasi kwamba wanakuja Wakorea kuvua samaki wengi sana wanatajirika kutoka katika maji ya kwetu lakini sisi kama Taifa tunapata nini? Ni vizuri sasa likajitokeza waziwazi kwamba kama Taifa tunafaidika vipi na bahari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusiana na General Tyre; sisi sote ni mashahidi, Wabunge wote tunatumia magari, kwa hiyo hatuna jinsi lazima tununue matairi kwa ajili ya magari, kwa hiyo soko lipo wazi hata kama mngekuwa na uhakika wa ku-service gari za Wabunge tu una uhakika wa kupata tairi ambazo zina ubora lakini soko lipo la kutosha nchi zote hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kasi ya kufufua General Tyre ni vizuri ikaonekana dhahiri; haipendezi tukaendelea kutazama tu kwenye makaratasi, inatosha tunataka utekelezaji. Kama imeshindikana tuambizane kwamba idea hii imeshindikana, labda tuanze thinking nyingine, lakini ukirejea kama miaka minne, mitano General Tyre inatajwa, Mchuchuma na Liganga inatajwa, kule Natron inatajwa, itoshe kutajwa tunataka kwenda kutenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini katika Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo tunataka maneno kidogo vitendo viwe vingi, vitendo vikiwa vingi huna haja ya kusema sana wenzako watakuwa wanatafuta namna gani ya kukosoa. Lakini pale unapotenda kama ambavyo tumetenda kuhusiana na suala zima la ndege, kuna wengi walibeza wengine wakasema ni ndege chakavu, lakini ukija hata asiyekuwa na macho atapapasa, atajua kwamba hii siyo ndege chakavu, ni ndege mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Naibu Spika, nashukuru na mimi kupata fursa ili niweze kuchangia machache. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja na nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika maeneo mawili matatu ambayo yalipata kuchangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni vizuri likatolewa ufafanuzi. Iliafikia hatua wengine wakasema kwamba Serikali hii haina mipango ndiyo maana Msimbazi maji yanaingia na hawaelewi nini ambacho kinaendelea, ni vizuri sana nikachukua fursa hii kuweza kutoa taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Dar es Salaam ya miaka hiyo wakati tunapata uhuru na leo kuna tofauti kubwa sana, ongezeko la watu ni kubwa. Lakini Serikali inayoongezwa na Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ina azma ya kuhakikisha kwamba, Jiji la Dar es Salaam linakuwa mahali salama kwa kuishi na hasa naomba niongelee Bonde la Msimbazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, DFID kwa kushirikiana na Benki ya Dunia hivi sasa ninavyoongea kimetengwa kiasi cha dola milioni 20 na tayari wameshapatikana watalaam waelekezi, kampuni kubwa mbili za kimataifa ambalo moja kazi yake ni kuweza kufanya tathmini kujua athari za mafuriko ndani ya Bonde la Msimbazi hasa Msimbazi ya Chini, na kushauri nini kifanyike, ujenzi upi ufanyike ili athari hii ambayo tunaipata; sisi sote ni mashuhuda inayptokana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo kati ya dola milioni 20 ni package kutoka katika paundi milioni 49 ambayo ina kazi nzima ya kuhakikisha kwamba kwa kupitia utaratibu wa Tanzania Urban Resilience Programme tutakabiliana na tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mshauri huyu anaitwa COWI Tanzania Limited ameshamaliza kazi yake na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuko kwenye hatua za mwisho kwa kuweza kupata mshauri mwelekezi ili feasibility study ifanyike na ujenzi uweze kuanza kufanyika. Pia katika lile Bonde la Msimbazi kuna awamu ya pili ambapo tayari package nayo imeshatolewa ambayo tunataka kuanzia Bonde la Msimbazi mto unakoanzia kule juu kabisa, kutakuwa na kazi ya kuhakikisha kwamba kuna wale watu ambao wanatakiwa wahamishwe. Vilevile ujenzi ufanyike ili eneo lile ambalo tukipata leo unaona ni sehemu isiyofaa patengenezwe namna nzuri ni ile ambayo itakuwa ni recreation areas kwa ajili ya kuvutia. Pia kuwe na shughuli za kila siku ambazo zitafanyika tukiwa tunahakikisha pia hatuwi na tatizo la mafuriko kama ambavyo tumekuwa tukikubwa na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi, kuna mradi wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo kasi awamu ya pili, jumla ya kilometa 20.3 kuanzia Kariakoo kwenda mpaka Mbagala. Mpaka sasa hivi kandarasi imeshatangazwa na itafunguliwa tarehe 20 Mei, 2018. Kwa hiyo, akipita Mbunge anasema kwamba Serikali hii haina mipango, inawezekana labda mtu hana taarifa nini ambacho kinaendelea. Ni vizuri tukaelezana ili mkajua, kwamba tuko makini tumejipanga na tutahakikisha tunakonga nyoyo za Watanzania waliochagua Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya machache naomba nimpishe mwenzangu naye achangie katika yaliyojitokeza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa mbele yetu. Aidha, baada ya kuunga mkono hoja naomba nichangie baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine ikiwa ni mara yangu ya nne kuongelea suala zima la maporomoko ya Kalambo pamoja na Hifadhi ya Msitu wa Kalambo kuwa chini ya TANAPA nimekuwa nikileta ombi hili na nitaendelea kurudia nikiamini ipo siku Serikali itanielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maporomoko ya Kalambo yako mpakani mwa nchi ya Tanzania na Zambia. Pamoja na maanguko ya maji kuwa mazuri sana upande wa Tanzania kuliko upande wa Zambia lakini kwa upande wa Zambia wameyatangaza maporomoko haya kwamba ni maporomoko ya pili Afrika baada ya yale ya Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linashindikana kutokana na uwezo mdogo wa Halmashauri ya Kalambo kwa maana ya uwezo mdogo wa kifedha na weledi katika tasnia ya utalii. Hivi ninavyoongea tembo wanaokadiriwa 17 mpaka 25 wapo ndani ya msitu wa Kalambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara kwa mara nyingine maporomoko ya Kalambo na Msitu wa Hifadhi ya Kalambo viwe chini ya TANAPA ili wahifadhi na kutangaza vivutio hivi vya utalii.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge waliopata fursa ya kuchangia, kwanza kwa kuzipongeza Kamati zote tatu kwa taarifa ambazo wamezitoa, ni taarifa nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nipongeze Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, ikiongozwa na Dkt. Jasson Rweikiza na Makamu wake na wajumbe wote kwa ujumla. Naomba nitoe takwimu chache, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, jumla tulipata bajeti tuliyopitishiwa na Bunge lako Tukufu Sh.1,803,400,959,500 na katika hizo, naomba niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais, tumeweza kupata pesa kwa ajili ya shughuli za maendeleo jumla ya Sh.856,560,441,937. Hii ni sawasawa na asilimia 47.5, hiyo si haba na fedha zote hizo zimeenda kwa ajili ya shughuli za maendelo.

Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa fedha hizo, jumla ya Sh.141,605,849,192 zimepokelewa ofisi kuu kwa maana ya Wizarani na kati ya fedha ambazo ilikuwa jumla ya Sh.345,113,541,000, lakini bilioni 40 zimepokelewa kwenda kwenye Serikali za Tawala za Mikoa; kati ya bajeti ya Sh.93,184,414,000, jumla ya Sh.694,643,380,250 zimepokelewa kwenye Halmashauri za Serikali za Mitaa, kati ya jumla ya Sh. 1,365,107,004,500 zilizoidhinishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, tunakushukuru sana, tunashukuru Wizara ya Fedha, hizi fedha zote zimeenda kufanya kazi za maendeleo. Kati ya fedha hizo, iko jumla ya bilioni mia moja nukta tano ambazo ni za kujenga hospitali 67 katika Halmashauri zetu. Tumepanga katika bajeti inayokuja tunaenda kuongeza hospitali 27 katika zile 67, kwa hiyo ukijumlisha utaona namna kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali ya CCM chini ya Uongozi wa Rais wetu, mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi zimeenda shilingi bilioni 23 kwa ajili ya kujenga Ofisi zetu za Halmashauri; lakini pia zimeenda shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kununua boti; zimeenda shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya Jimbo, Waheshimiwa Wabunge ni wanufaika na naamini fedha hizo zitakuwa zimetumika kwenda kuchochea kwenye shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambazo zimeibuka ambazo ni vizuri tukatolea ufafanuzi. Hoja ya kwanza inahusu suala zima la TARURA, tunaomba tupokee pongezi ambazo Waheshimiwa Wabunge wote waliopata fursa ya kuchangia wamepongeza kazi nzuri ambayo inafanywa na TARURA, lakini kuna upungufu ambao wanataka uboreshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa fedha, asilimia 70 kwa 30 kwa mujibu wa Sheria iliyopo na TARURA tangu imeanzishwa ndio ina miaka miwili, kuna mapitio ambayo yanafanyika ili tupate formula itakayokuwa nzuri, baada ya kujua mtandao mzima wa barabara na kiasi cha fedha ambacho kinatolewa, tujue namna gani ambayo tutawezesha chombo hiki kizuri ambacho kina upungufu mchache lakini Waheshimiwa Wabunge wengi wamesifia juu ya utendaji kazi wa TARURA. Kwa hiyo, tunaomba tuendelee kukiunga mkono.

Mheshimiwa Spika, hapa Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusiana na suala la kuripoti; ni kweli, azma ya kuanzishwa kwa TARURA wengi tunajua, wakati ule, ilikuwa kila Mbunge ambaye sasa akirudi kule, Diwani anataka angalau wapate hata kilometa mbili, kwa hiyo, value for money kwa ujumla wake, ilikuwa haionekani, tunaamini kabisa, iko haja ya Waheshimiwa kushiriki katika kutoa mapendekezo, TARURA waende kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, yako mengi na dakika tano ni chache, hivyo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe mmojawapo ambao wamepata fursa ya kuchangia hoja na kupata fursa ya kujibu baadhi ya hoja ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kipekee nianze kwa kushukuru kamati yetu ya Utawala na TAMISEMI kwa maelekezo ambayo wamekuwa wakitupatia lakini pia Waheshimiwa Wabunge katika michango yao yote ya kujenga. Kama kuna Wizara ambazo zimetendewa haki ni pamoja na Wizara yetu. Kwa ujumla nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya kuhusiana na TARURA ambayo imeongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi kuanzia kamati yetu, lakini pia Kambi Rasmi ya Upinzani imeongelea juu ya suala zima la TARURA kuongezewa fedha, lakini kama siyo kuongezewa fedha, pia wameongelea suala zima la kutaka mgawanyo wa fedha utazamwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika na Waheshimiwa Wabunge wote ni mashuhuda, hali tuliyoanza nayo kuhusiana na suala zima…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Hawanisikilizi eeh!

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shuhuda jinsi ambavyo tulianza Waheshimiwa Wabunge wengi walikuwa wanalalamikia jinsi ambavyo utendaji kazi wetu wakati matengenezo ya barabara yalikuwa chini ya Halmashauri. Kila Mheshimiwa Diwani na Wabunge sisi tukirudi kule ni Madiwani, kila mmoja alikuwa anaomba kipande angalau kilometa moja kitengenezwe. Kwa hiyo, value for money ilikuwa haionekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tupokee pongezi ambazo tumepokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge juu ya utendaji bora wa TARURA. Wengi wamesifia juu ya chombo hiki, lakini ni ukweli usiopingika kwamba tuna safari ya kuhakikisha kwamba tunaimarisha TARURA ili ule upungufu ambao Waheshimiwa Wabunge wamesema uweze kurekebishika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni ukweli usiopingika kwamba kilometa ambazo zinahudumiwa na TARURA, chombo hiki ambacho tumekianzisha sisi wenyewe, takribani kilometa 108,000 ni nyingi. Pia wameomba ikiwezekana mgawanyo ubadilike kutoka asilimia 30 kwa 70. Zipo sababu za msingi kwa nini tulikwenda kwenye hiyo formula? Nasi Serikali tumesikiliza kwa Waheshimiwa Wabunge, imeundwa Tume ambayo inafanya tathmini kupitia upya ili pale ambapo tukija na majibu ya uhakika tushirikishe Bunge letu katika kuwa na formula ambayo itahakikisha kwamba TARURA inafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala zima la ukosefu wa vitendea kazi ikiwepo magari. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeliona hili na ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeanza kununua magari ili kuhakikisha maeneo yote ambayo hakuna gari ziweze kufikishwa. Tumeanza na gari 22 katika kipindi kilichopita na safari hii tunaenda kununua gari 22. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge maeneo yote ambayo yana uhitaji mkubwa wa magari tutayazingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya. Kipekee naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeweza kupata kiasi cha shilingi bilioni 100.5 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na hospitali. Tumeanza na hospitali 67 na Waheshimiwa Wabunge wote ni mashuhuda kwamba katika bajeti ambayo tutaomba baadaye watupitishie tunaenda kuongeza tena hospitali 27. Ni kazi kubwa na nzuri; ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba huduma ya afya inasogezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba waheshimiwa Wabunge tusaidiane tuhakikishe kwamba tunasimamia malengo ambayo tumeweka Ofisi ya Rais TAMISEMI kufika tarehe 30 mwezi Juni, yale majengo saba yawe yamekamilika na wananchi wa Tanzania waanze kupata huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, pia tunaenda kuongeza hospitali nyingine 27. Fedha imetengwa na ninaamini muda siyo mrefu Waheshimiwa Wabunge watapitisha ili tuweze kwenda kujibu kijibu kiu kubwa ya Watanzania kuhakikisha kwamba wanapata huduma ya afya umbali usiokuwa mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima ambalo napenda niongelee kidogo kuhusiana na usafiri wa mabasi ya mwendokasi kwa Dar es Salaam. Hili limechangiwa sana na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam. Naomba niwahakikishie azma ya Serikali ya kuhakikisha kwamba msongamano wa usafiri kwa Dar es Salaam unapungua, iko pale pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mchakato ambao tulikuwa tumeanzisha wa kumpata mwendeshaji wa mwanzo ambaye kwa mujibu wa mkataba interim operator ilikuwa a-oparate na mabasi 140, lakini ndani ya mwezi huu Aprili tutahakikisha kwamba kandarasi inatangazwa na ukifika mwezi wa nane Mwenyezi Mungu akijaalia tutakuwa tayari tumeshampata mkandarasi wa kuendesha mabasi hayo na yataongezeka kutoka mabasi 140 mpaka mabasi 305. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba niwahakikishie kwamba mchakato tutahakikisha unakwenda vizuri. Kama hiyo haitoshi, tunaenda kujenga barabara ya kuanzia katikati ya Mji wa Dar es Salaam kwenda Kilwa Road kwenda Gongolamboto kwenda Tegeta. Ni azma ya Serikali ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanapunguziwa adha ya usafiri kwa maana ya msongamato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kuna suala zima la DMDP, naomba niwahakikishie Wabunge na hasa Wabunge wanaotoka Dar es Salaam, tupo vizuri tumejipanga muda siyo mrefu wao wenyewe watajionea jinsi ambavyo mchakato unakamilika na barabara hizi zinaanza kutengenezwa ili kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inaendelea kuwa mahali salama pa kuishi na wananchi kufurahia matunda ya chama chao cha CCM.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima limeongelewa kuhusiana na asilimia 10 ambayo inatakiwa itolewe kwa ajili ya akinamama, vijana na watu wenye uhitaji maalum kwa maana ya watu wenye ulemavu. Wewe ni shuhuda kwamba tumepitisha sheria, kwa hiyo ni takwa la kisheria kwa Wakurugenzi wote kuhakikisha kwamba wanatenga asilimia 10 kutokana na mapato yao ya ndani. Tayari kanuni zilishakuwa tayari, muda wowote ndani ya mwezi huu kanuni zitakuwa zimetoka, kwa hiyo Mkurugenzi yeyote hatakuwa na kisingizio kwa nini hatengi hizo fedha na kuhakikisha kwamba fedha hizo zinakwenda kuwafikia Watanzania tuliowakusudia, ikiwa ni akinamama, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote, kila Mbunge ambaye alitoa hoja yake tutaijibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukru sana kwa muda wako. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kuunga mkono hoja. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao walipata fursa ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango imetolewa na Waheshikiwa Wabunge, mingi ikiwa ni ya kujenga. Nasi sote ni mashuhuda kwamba maji ni uhai, tuna uhitaji wa maji na tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba maji yanawafikia Watanzania wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambapo ukienda huko ndiyo unakutana na wananchi ambao wanahitaji maji, hakika tunaamini katika jitihada ambazo zimewekwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kwamba tunaenda kumtua ndoo mwanamama, ni ahadi ambayo tumeahidi kwa Ilani yetu, nasi tukiahidi huwa tunatekeleza. Kwa hiyo, naamini kwa siku ya leo tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunaunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, kuna maneno yamesemwa mengi kwamba kiasi cha fedha ambacho kinatolewa hakitoshi. Ni vizuri pia tukajiridhisha kwamba katika hicho ambacho kinatolewa kiende kikafanye kazi iliyokusudiwa. Kwa sababu haijalishi kiasi cha wingi wa fedha kama management yake isipokuwa nzuri; hakika hata kingekuwa kingi namna gani hakiwezi kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yetu na hasa katika utaratibu wa uanzishwaji wa mamlaka ya maji; hapa katikati na wewe ni shuhuda, wakati mwingine ilikuwa tunatupiana mpira, inaonekana hili liko TAMISEMI, hili liko Wizarani, kiasi kwamba sasa ukitaka kufuatilia kujua exactly ni nani ambaye amesababisha wananchi wetu wasipate maji wakati mwingine ilikuwa inatuwia ugumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu wetu huu wa kuanzisha mamlaka hii, nawe ni shuhuda, pale ambapo tumeanzisha agency kama TARURA inakuwa ni rahisi kujua exactly nani awe responsible na awe answerable na kila mtu abebe msalaba wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini na kwa bahati nzuri sisi kama TAMISEMI tuna utawala mpaka kijjini na kwa sababu Serikali hii ni Serikali moja, kinachofanyika ni kuhakikisha tu kwamba tuna-mainstream ili ijulikane nani anafanya nini, lakini kwa sababu lengo ni kumfikishia mwananchi wa kawaida huduma ya maji, naamini na fedha hizi ambazo zimepatikana na hii agency ndiyo imeanza hivi karibuni, naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla na Uongozi wa Wizara ya Maji ili tukasimamie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu naamini mbele ya safari baada ya hiki ambacho kitakuwa kimetolewa, kikionekana kimesimamiwa vizuri hakijatosha, sasa hoja itakuwa ina mashiko kwamba sasa tuongezee fedha zaidi kwa sababu tuna uhakika juu ya usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami na wewe mwenyewe ni shuhuda, hatuna wasiwasi juu ya uongozi na bahati nzuri kuna mamlaka za maji kila mji. Naamini hakika fedha hii ambayo itaenda kutolewa itaenda kukidhi haja ya kuhakikisha kwamba maji yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shuhuda, wakati fulani ilikuwa ukianza kutafuta fedha unaambiwa nyingine zimeenda Wizara ya Elimu, nyingine zimeenda TAMISEMI, kiasi kwamba unashindwa kuzi-trace kwa ujumla wake, lakini sasa hivi kwa utaratibu huu ambao umeanzishwa hakika Profesa atakuwa na uhakika wa kusimamia kila shilingi na itakuwa ni rahisi kwake yeye kuweza kuwawajibisha wale wote ambao watakuwa hawatimizi malengo ambayo yamekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba niendelee kuunga tena mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata fursa ya kuweza kuchangia hoja iliyowasilishwa na Wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja na kipekee naomba uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake na Katibu Mkuu na Watumishi wote kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitoa kwetu sisi Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kimsingi Watanzania wote ni mashuhuda. Kazi kubwa ambayo inafanywa katika kuboresha afya za Watanzania haitiliwi mashaka hata Mtanzania mmoja. Kwa hiyo, naamini kwa moto huu ambao umeanza hakika Watanzania watarajie mambo makubwa mazuri chini ya uongozi wa viongozi wetu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako Wabunge wengi ambao wamechangia na karibu wote walikuwa wakipongeza. Kama kuna mtu ambaye hakupongeza basi labda amepongeza kimoyo moyo lakini hata upande wa pili nao ni mashuhuda kwamba kazi nzuri inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna hoja ambazo zimeibuliwa na ambazo sisi kama TAMISEMI ni vizuri tukajibu kiasi. Katika hoja mojawapo ni pamoja na upungufu wa watumishi wa afya katika hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati. Tunakiri kabisa kwamba kuna upungufu, mpaka sasa hivi tunao watumishi wapatao 56,881 sawa sawa na asilimia 48, kwa hiyo tuna upungufu wa asilimia 52, lakini maelezo yapo ambayo yanajisheheni kwamba kwanini tunao upungufu kiasi hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote Watanzania ni mashuhuda kwamba kama kuna sehemu ambayo uwekezaji umefanyika ni katika Sekta ya afya, vituo vya afya vimeongezeka, zahanati zimeongezeka, kwa vyovyote vile lazima ionekane kwamba kuna gap, lakini pia kuna sababu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa mfano, katika wataalam ambao wanazalishwa tumekuwa na wataalam wachache sana hasa madaktari kuhusiana na masuala mazima ya meno, lakini hata kuhusiana na suala zima la mionzi lakini ziko jitihada ambazo zimechukuliwa na Serikali za makusudi kuhakikisha kwamba upungufu huu ambao unaonekana kwa sababu azma ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, afya ya Mtanzania ndiyo kipaumbele. Kuna jitihada za makusudi ambazo zinafanywa ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata huduma ya afya tena kwa umbali usiokuwa mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba na naamini kibali kitapatikana, tumeomba kuweza kuajiri watumishi 15,000. Lakini pia naomba nichukue fursa hii kupongeza Mfuko wa Benjamini Mkapa na wametusaidia wameajiri watumishi kama 300 kwa muda wa miaka miwili na sasa hivi wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi ambalo naomba nitoe maelekezo katika Mikoa yote, tuhakikishe maeneo yale na hasa ya pembezoni na vijijini ambako ndiyo kuna upungufu mkubwa, tuhakikishe kwamba wataalam hawa wanapelekwa kwa sababu kumekuwa na namna unakuta mijini wako watumishi wa afya wengi lakini ukienda vijijini unakuta wako wachache. Kwa hiyo, pale ambapo inatajwa upungufu, ukienda maeneo ya mjini hukuti upungufu kama ambavyo iko mijini. Nitoe maelekezo mahsusi tuhakikishe kwamba inafanyika redistribution ili maeneo yenye upungufu mkubwa yaweze kupelekwa hao wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe ni shuhuda, tukiwa hapa wakati Mheshimiwa Waziri wa Utumishi aliwasihi Wabunge kama kuna kituo chochote au zahanati yoyote ambayo inalazimika kufungwa kwa sababu eti hakuna mtumishi, aliwaomba Waheshimiwa Wabunge waandike barua ili tuweze kujaza pengo hilo na amini Waheshimiwa Wabunge walitenda haki katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja pia zimeibuliwa kuhusiana na Community Health Workers, hoja ya msingi tunaiunga mkono lakini ni vizuri tuka-balance hizi equation. Si rahisi pamoja na nia njema ya kuhakikisha kwamba tunawaajiri hawa, lakini itakuwa si busara pale ambapo tuna kituo cha afya au tuna zahanati ambayo tunashindwa kuifungua kwa sababu hakuna mhudumu wa afya tukaenda kuwaajiri hawa. Kwa hiyo, pamoja na nia njema ni vizuri tukatumia structure iliyopo, tunao Maafisa Ustawi wa Jamii ni rahisi kuweza kuwa-train na wakaweza kuwasaidia watu wetu lakini azma kwa siku za usoni tutahakikisha kwamba nao watu wanaweza kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamelisema vizuri kuhusiana na suala zima la lishe. Hakuna namna pekee ambayo unaweza ukawekeza kuhakikisha kwamba unawapata Watanzania wenye brain nzuri kama hatuwekezi katika siku 1,000 za mwanzo. Wataalam wanatuambia kwamba tunaanza kuhesabu tangu pale ambapo mimba inatungwa mpaka mtoto anapokuja kuzaliwa na miezi ile miwili ndiyo muhimu sana katika kuweza kuhakikisha tunawekeza katika hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumepokea, tunajua umuhimu wa jambo hili na ndiyo maana nina kila sababu ya kumshukuru Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumewekeana mikataba na Wakuu wa Mikoa wote Tanzania, Mikoa 26 kuhakikisha kwamba suala la udumavu linabaki historia na tumekuwa na utaratibu wa kupimana kila baada ya miezi sita na muelekeo ni mzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na sisi kwa nafasi zetu za uongozi ni mabalozi, tunapofanya mikutano yetu ni vizuri tukahakikisha kwamba elimu hii tunaifikisha kwa Watanzania wenzetu. Maana hakuna namna pekee ambayo unaweza uhakikisha kwamba watoto wetu wanakuja kushindana na mataifa mengine kama hatujawekeza katika umri wao wakiwa bado watoto wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwasihi Waheshimiwa Wabunge limesemwa juu ya kujihakikishia afya kwa kila Mtanzania. Namna pekee na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atakuja aliseme kwa kirefu ni kuhakikisha kwamba Watanzania mwelekeo ni kujiunga na Bima ya Afya. Bima ya afya ndiyo mkombozi wa kuhakikisha kila Mtanzania anaenda kupata tiba pale ambapo anapatwa ugonjwa tena tiba ambayo ya kisasa kabisa. Haipendezi pale ambapo inatokea Mtanzania anaenda wakati anaumwa, anashindwa kupata matibabu eti kwa sababu hana fedha au hajajiunga na bima ya afya. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge sisi ni viongozi ni vizuri tukatoa hamasa kwa Watanzania, mataifa yote duniani utaratibu ndiyo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Waheshimiwa Wabunge walichangia na alianza kusema Mheshimiwa Nachuma, akataja Mkoa wake wa Mtwara na hasa na maeneo yote ambayo ni mwambao mwa bahari. Kuna mazalia mengi sana ya mbu, akaomba ifanyike jitihada za makusudi. Sisi sote ni kwamba Tanzania tuna kiwanda chetu cha viuadudu ambacho kipo pale Mkoa wa Pwani na kipekee Mheshimiwa Rais naomba tumshukuru aliweza kuwekeza shilingi bilioni 1.3 na fedha hizo zikatumika katika kununua viuatilifu hivyo kwa ajili ya kusambaza halmashauri zote Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni wajibu wetu Wakurugenzi wote Tanzania tuhakikishe kwamba hicho ambacho kilianzishwa na Mheshimiwa Rais kiwe endelevu kwa kuhakikisha kwamba tunatenga kwenye bajeti zetu fedha kwa ajili ya kuanza kununua viuatilifu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapambana na mazalia ya mbu. Lakini pia ni vizuri hamasa ikatolewa kuhakikisha kwamba mazalia ya mbu tunatokomeza. Wenzetu Zanzibar wameweza Tanzania Bara pia tunaweza, ni suala la kuamua na tukishirikishana sisi sote inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe katika hayo ambayo sisi yamejitokeza tukaona tuyatolee ufafanuzi, naomba niendelee kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa fursa ili niweze kuchangia machache. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee nipongeze taarifa za kamati zote tatu. Kamati zimesheheni weledi wa kutosha na ushauri ambao sisi tumeupokea kama Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia katika taarifa za kamati mbili. Naomba nianze na Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali kipindi hiki tumefaidika sana na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na kamati hii, maana kuna maelekezo, na sisi kama Serikali tumefanyia kazi ndio maana zile sheria zote ndogo ambazo zilikuwa zikilalamikiwa hapa zamani sasahivi imebaki ni historia. Naomba niipongeze sana kamati ukianzia na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wote kwa ujumla wamekuwa na msaada mkubwa sana kwa Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Kamati ya Utawala na TAMISEMI. Kamati hii imekuwa ya msaada mkuba sana. Hata hivyo naomba nijikite katika suala zima ambalo sisi Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla wetu; mwanzo lilivyoanza lilikuwa kama lina ukakasi. Ni suala zima la vitambulisho kwa wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna ubunifu ambao Mheshimiwa Rais amefanya ni suala zima la kuwatambua wajasiriamali wadogo na kwamba, kupitia wajasiriamali wadogo tutaweza kuwapata mamilionea wengi wa kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa nikimuwakilisha Mheshimiwa Waziri nikaenda Halmashauri ya Kigamboni, kuna wajasiriamali wadogo ambao wamepewa vitambulisho na CRDB kwa kuwatambua imeanza kuwakopesha pasi na riba; hakika pongezi kwa Mheshimiwa Rais ni ubunifu wa hali ya juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninaomba nichukue fursa hii kwa Waheshimiwa Wabunge, kama ambavyo tumekuwa tukishauri mambo mazuri basi nitumie fursa hii huko kwetu kwenye majimbo na sisi tuhimize wajasiriamali wadogo waweze kutambuliwa. Na katika fedha ambazo zinapatikana katika hii asilimia 10 ambayo tumekubaliana naomba nipongeze kamati zote ni jitihada za kamati ndio zimesababisha asilimia 10 ikatengwa ambayo inakopeshwa bila riba. Sasa ni vizuri tukaanza kuwatambua wajasiariamali hawa wenye vitambulisho ndio wakawa kipaumbele katika kupatiwa mikopo ambayo haina riba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimetolewa hoja nyingi, katika hoja moja ni pamoja na suala zima la TARURA; tunashukuru kwa pongezi ambazo zimetolewa, lakini imesemwa hoja kwamba, kiasi cha fedha kwa maana ya asilimia 30 haitoshi. Ni kweli inawezekana ikaonekana haitoshi lakini ni vizuri tukakumbushana Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Waziri alivyokuja alitoa ufafanuzi kwamba, kuna mapitio ya formular ya namna ya ugawanyaji wa hiyo asilimia 30 kwa 70. Ninaomba niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa pale ambapo utafiti utakuwa umekamilika formular ikaja hakika tunajua kabisa uko uhitaji mkubwa wa kujenga barabara hasa ambazo ziko vijijini. Vilevile lakini tusije tukasahau pale ambapo TANROADS wanajenga ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami pia ni wa gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kwamba, mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge tunayazingatia na Serikali itafanyia kazi ili tuje na formular ambayo itakuwa inazingatia uhalisia na pesa ziweze kwenda kwa mgawanyo uliosahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa ongezi ambazo zimetolewa kuhusiana na suala zima la afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala zima la Afya Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusiana na Watumishi ambao wanatakiwa waende kwenye Vituo vya Afya na Hospitali zetu ambazo zimejengwa. Naomba tuendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, Serikali hii ya CCM ambayo sikio lake linasikia kila sauti ambayo inatoka na hivi karibuni ninyi nyote ni mashuhuda kwamba kuna nafasi ambazo zimetangazwa kwa ajili ya ajira ambazo deadline ni tarehe 7 mwezi huu hii yote ni katika kuhakikisha wanaajiriwa Watumishi wa kutosha ili haya majengo ambayo yanajengwa isije ikageuka kuwa white elephant.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la Shirika la Soko Kariakoo kuna michango ambayo imetoka naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na sisi Serikali tumeliona lakini pia kuna maboresho makubwa sana utendaji wa masoko Kariakoo umebadilika na hivi kwa mara ya kwanza wametoa gawio kwa Serikali jumla ya shilingi milioni kumi ni mwanzo mzuri nakushukuru kwa fursa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Spika, nakushukuru kwa fursa ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao wamepongeza hotuba nzuri sana ambayo imewasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa dakika tano na hoja ambazo zimeibuka kuhusiana na Wizara ya TAMISEMI sina uhakika nitagusa ngapi lakini kwa sababu tarehe 8/4/2020 Mheshimiwa Waziri wa Nchi atakuwa na fursa ya kuwasilisha hotuba yake, ufafanuzi tutautoa na tutakuwa na muda wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, sasa niruhusu nipitie machache katika kutoa ufafanuzi. Kuna hoja ambayo ilikuwa imeibuliwa na Mheshimiwa Engineer Chrisotpher Chiza ambayo ilikuwa inahusu ushauri katika majengo ya Serikali na hasa katika maeneo ambayo kuna matukio mengi ya radi, akashauri Serikali ianze kuweka vitega radi. Naamini katika maeneo ambayo yanapata tatizo kubwa ni pamoja na Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanatoka maeneo ambayo kuna usumbufu mkubwa wa radi, wazo hili sisi kama Serikali tumelichukua na tulishaanza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, katika majengo yote ya Taasisi za Umma ambayo yataendelea kujengwa tutahakikisha kwamba tunaweka vitega radi, kwa sababu pale ambapo radi inatokea athari zake zinakuwa kubwa. Ni vizuri pia hata wananchi sisi Waheshimiwa Wabunge tutumie fursa kuelimisha wananchi kwa sababu gharama yake wala sio kubwa sana katika kuweka vitega radi.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambayo ilikuwa imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kidogo akiwepo Mheshimiwa Vulu, Mheshimiwa Bobali Hassan, Mheshimiwa Christina Ishengoma, Mheshimiwa Livingstone Lusinde ikiwa inaongelea suala zima la TARURA pamoja na kazi nzuri ambayo inafanyika, lakini wameomba kwamba ikiwezekana bajeti ya TARURA itazamwe.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba maeneo mengi TARURA imekuwa ikifanya kazi vizuri ukiachilia mbali huo ufinyu wa bajeti, lakini pia ni vizuri pia tukakumbushana kwamba pamoja na kwamba TARURA inahudumia takribani kilometa 108,942, pia TANROAD nayo ambayo ina mzigo mkubwa kwa sababu barabara zake nyingi ambazo zinajengwa ni zile za kiwango cha lami ambayo gharama yake ni kubwa, lakini ni ukweli usiopingika na baada ya hili Serikali kulitambua tumeanza kupitia formula ambayo itasaidia.

Mheshimiwa Spika, pia ni ukweli usiopingika kwamba tukitegemea bajeti hii ambayo tunatenga kila mwaka kwa ajili ya kujenga Taasisi kubwa kama TARURA, fedha hii haitoshi. Ndiyo maana Serikali inatumia vyanzo vingine kuhakikisha kwamba tunaijengea uwezo TARURA kama ambavyo hata mwanzo TANROADS ilijengewa uwezo ikasisimama vizuri ili iweze kufanya kazi kama ambavyo inatarajiwa na Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 bajeti imekuwa ikiongezeka kwa kadri inavyopatikana. Tunaendelea kuijengea uwezo TARURA ili ifanye kazi nzuri kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wengi wamesifia kazi nzuri ambayo inafanywa na TARURA.

Mheshimiwa Spika, iko hoja ambayo iliibuliwa na Mheshimiwa Mohamed Omar Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji ambayo inahusu Jimbo lake ambako kumepatikana mafuriko makubwa sana, lakini kipekee akawa anaomba kwamba Kituo cha Afya kile ambacho hakiwezi kutumika hata baada ya kwamba mafuriko yameondoka, basi ni vizuri Serikali ikatazama uwezekano wa kujenga Kituo cha Afya kipya.

Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, avute subira kama ambavyo nimesema kwamba kuanzia tarehe 8, bajeti yetu itawasilishwa, atapata ufafanuzi ulio mzuri kuhusiana na nini ambacho tumepanga kufanya.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja pia ambayo imeibuka ambayo ni vizuri nikatumia fursa hii kutoa ufafanuzi; kuna Kampuni ambayo inajenga Stiegler’s Gorge kule ambapo kumekuwa na ubishano, service levy ilipwe wapi? Je, inatakiwa ilipwe sehemu ambayo Ofisi iko kwa maana ya Kinondoni au ilipwe sehemu ambayo mradi unatekelezwa?

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa maelekezo mahususi; Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeelekeza service levy inatakiwa ilipwe kule ambako mradi unatekelezwa na wanufaika ni Rufiji pamoja na Morogoro vijijini. Kwa hiyo, hoja ya kwamba Ofisi iko Kinondoni ndiyo eti service levy ikalipiwe Kinondoni, siyo sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami niweze kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ndiye anayeniwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kila sababu ya kuwashukuru wananchi wa Kalambo, tulikubaliana kwamba nuru mpya ya Kalambo, kwa pamoja tunaweza; na hakika wamenirejesha kwa kishindo, nawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ulioletwa unaleta matumaini makubwa sana. Tanzania ya viwanda inawezekana. Viwanda vipi ambavyo tunaenda kuvijenga? Ni hakika Serikali lazima ijenge viwanda vya kimkakati lakini, ni wajibu wa sekta binafsi kushiriki katika viwanda vidogo vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotaka kujenga kiwanda maana yake ni lazima rasilimali fedha iwepo ya kutosha. Bila mtaji wa kutosha hakuna viwanda ambavyo tunaweza kujenga. Serikali ikijenga viwanda vya kimkakati, tukaiachia Sekta binafsi, wanaenda kutoa pesa wapi Hawawezi kwenda kukopa katika mabenki ya kibiashara, kwa sababu unapowekeza katika kiwanda hutarajii return ya haraka. Lazima ni mtaji mkubwa ambao return yake utaipata kidogo kidogo.?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, haiwezekani tuka-plan kwenda kushindwa. Tunapokuwa na Benki ambayo hatujaipa mtaji, kwa maana ya TIB, hakika ni kwamba tume-plan kwenda kushindwa. Tusikubali kufanya kosa hili, tuhakikishe tunaiwezesha Benki yetu ya TIB ili itoe fursa kwa wananchi kwenda kukopa kwa riba ambayo ni rahisi kulipika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashuhuda kwamba asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima na hasa ambao wako vijijini. Sitafarijika hata kidogo na wala sitaki kuamini kwamba Serikali imesahau mpango mzima wa SAGCOT. Tumesema lazima tuwekeze katika kilimo, ikaja mipango mizuri, naamini na hili litakuja; ni kwa sababu inawezekana bado wanakumbuka, ikija detail report itaainisha masuala yote ya kuhakikisha kwamba tunajitosheleza katika kilimo na tena kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, kwa utaratibu wake na Mpango waliokuja nao wa kuhakikisha kwamba tunaenda kubana matumizi, kutumia pale tu ambapo itaongeza tija. Ni jambo jema. Serikali imeagiza kwamba kuanzia sasa pesa zake zote ambazo Taasisi zimekuwa zikiweka katika Benki za kibiashara, zipelekwe Benki Kuu maana zote ni mali ya Derikali. Sina ubishi! Ubishi wangu unakuja pale ambapo kama utaratibu tutakaoenda kuufanya utasababisha mashirika yetu ambayo yashaanza kufanya vizuri, tukaya-suffocate. Haitapendeza!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni suala la control, naomba niikumbushe Serikali irejee Sheria ya Bajeti Kifungu cha 17, inaeleza kabisa kazi ya Treasury Registrar kwamba mashirika yote ambayo yako chini ya TR watapeleka bajeti zao kule, ataidhinisha na hata kama kuna suala la kwenda kuwekeza, ni lazima wawe wamepata idhini kutoka kwake. Hiyo ni control ya kutosha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile ambavyo wananchi na Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tunapata wasiwasi, ni kwamba utaratibu wa kuhamisha pesa zote kupeleka Benki Kuu, inaweza kuziua Halmashauri zetu. Hakika pia inaweza ikaua mashirika yetu. Sisi ni mashahidi kwamba mwaka 2015 tulivyokuja hapa tulisema kwamba ni vizuri Taasisi zetu zikawezeshwa ikiwa ni pamoja na TPDC ili iweze kushiriki katika uchumi wa gesi na mafuta. Sasa kama utaratibu itakuwa hatuwezeshi wakawa na fungu la kutosha, wakaweza kuwekeza, hakika ushiriki wa Watanzania kwa kupitia shirika letu hautaweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nyie ndugu zangu nyote ni mashahidi kwa jinsi ambavyo Shirika letu la Nyumba la Taifa lilivyokuwa na hali mbovu, leo hii limekuwa ni miongini mwa mashirika machache ambayo yanapigiwa mfano kwa namna ambavyo wanawekeza na naamini na Kalambo watakuja. Sasa zile taratibu kwa wale watu wanaofanya kazi vizuri tusianze kuwa-frustrate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesoma katika Mpango kuna suala zima la kununua ndege. Ni jambo jema sana, lakini haitapendeza tunaposema tunataka kufufua Shirika letu la Ndege, zinanunuliwa ndege mbili, lakini kwa utaratibu ambao utakuwa umewekwa kwa makusudi, wakashindwa hata kununua mafuta kwa sababu OC haijawafikia. Itakuwa hatutendi haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala zima la Wakandarasi wa ndani. Wakandarasi wa ndani wamekuwa wakiidai Serikali kwa muda mrefu. Kutowalipa Wakandarasi tafsiri yake ni nini? Barabara zetu hazijengwi zikakamilika kwa kiwango kwa wakati unaotakiwa. Tafsiri yake ni kwamba, miradi mingi inajengwa kwa gharama kubwa, kwa sababu kwa kutowalipa, wanalazimika kuidai Serikali riba, lakini hali kadhalika wanashindwa kulipa kodi kwa sababu wao wanaidai Serikali na Serikali haijalipa. Nasi tunataka kuwe na mzunguko wa kutosha; walipwe na Serikali, walipe kodi, lakini pia waweze kutoa ajira kwa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee, Serikali ihakikishe kwamba miradi ile ya barabara ambayo imeshaanza, ikiwa ni pamoja na mradi wa barabara kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda; Mradi wa barabara kutoka Sumbawanga kwenda Kalambo Port, unakamilika kwa wakati ili tuhakikishe kwamba kasi ya Tanzania ya kwenda kuwa nchi ya kipato cha uchumi wa kati, inawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tukubaliane, kupanga ni kuchagua. Haiwezekani tukatekeleza yote, ndiyo maana tukubaliane kwamba bila kujenga reli kwa standard gauge, hakika uchumi ambao tunataka upae na kufika uchumi wa kipato cha kati hatutaweza. Niwasihi ndugu zangu wote bila kujali unatoka eneo gani la Tanzania, tukubaliane mkakati wa kuhakikisha kwamba reli inajengwa. Bahati nzuri nyie ni mashahidi, kuna fungu ambalo lilitengwa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwekeza lazima utarajie kupata kule ulikowekeza. Tujiulize, kutokana na bomba la gesi, ni kiasi gani kinapatikana kama return kwa Serikali na hicho ambacho kinapatikana kipo kwenye mfuko upi? Kama siyo hapo tu, mkongo wa Taifa, pesa nyingi sana imewekwa, tunataka tujue, baada ya kuwekeza return yake iko wapi? Iko mfuko upi kwa manufa ya Watanzania? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi jioni ya leo hii niwe miongoni mwa wachangiaji wako. Awali ya yote, nalazimika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama leo nikiwa na nguvu ya kutosha na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Kalambo, nuru mpya Kalambo ambayo tumeiahidi tutaitimiza na hasa kwa kasi hii kila mtu ana kila sababu ya kuunga mkono Serikali inayoongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Kubeza ni kama namna tu ambavyo mtu ambaye ameanza safari unamwambia ongeza speed. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu najielekeza katika suala zima la bajeti ya mikoa. Nashindwa kuelewa kama hili limekuwa likitokea kwa bahati mbaya au ni katika design ambayo imewekwa. Ukipitia katika budget allocation, ukienda Mkoa wa Katavi, kupitia TAMISEMI wametengewa shilingi bilioni 3.9, unaujumlisha na Mkoa wa Lindi shilingi bilioni 6.1, unakwenda Mtwara na ya Mtwara imeongezeka hivi karibuni na sababu zinaweza zikawa zinapatikana lakini ni shilingi 10.7, ukienda Mkoa wa Rukwa ni shilingi bilioni 6.7, inawezekana pia hawakujua na Shinyanga nayo imetengewa kidogo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kandege, ni kitabu kipi hicho unachotumia?
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki hapa.
MWENYEKITI: Sawa, ili wote tuwe pamoja.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Ndiyo, maana ndiyo bajeti, hii nyingine ni porojo, sisi tunataka twende kwenye facts. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shinyanga imetengewa shilingi bilioni 9.2 na Singida ni shilingi bilioni 9 ukijumlisha mikoa yote hiyo na ukija ukilinganisha na hii yote na ukajumlisha Mkoa wa Manyara ambao ulikuwa sehemu ya Mkoa wa Arusha, mikoa hii miwili wametengewa jumla ya shilingi bilioni 38.3. Jumlisha pesa ya mikoa yote hiyo niliyotangulia kuitaja haifikii pesa ambayo imetengwa kwa ajili ya mikoa miwili na mikoa ambayo ilikuwa mkoa mmoja. Hili nimekuwa nikilisema, ifike mahali ambapo sasa Serikali ituelewe, haiwezekani ile mikoa ambayo tunasema iko nyuma kiuchumi ambayo haijaendelea, hiyo ndiyo ambayo iendelee kutengewa bajeti ndogo, hatuwezi kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya hawa ambao wanapata 27, hebu katafute kura, katafute jinsi gani ambavyo wanaitambua Serikali iliyopo madarakani kaangalie wametoa kura kiasi gani? Inawezekana kuna wataalam ambao wametangulia wako huko waka-design formula ambayo watahakikisha daima wao ndiyo wanapata pesa nyingi katika mikoa yao. Jambo hili halikubaliki! Tunaomba Serikali ituambie ni utaratibu gani ambao wanautumia katika budget allocation. Haiwezekani ambaye yuko nyuma useme ataendelea kuwa nyuma daima dumu. Hii nchi ya kwetu sote, keki kama ndogo tugawane kwa usawa.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi imekuwa ikisikika kwa wale ambao imegawanywa mikoa na Wilaya, Wilaya zingine zinafanana na kata zangu mbili, ukiwaambia kwamba na sisi tunaomba tuongezewe mgao wanasema hapana, huu ni ulaji lakini ni kwa sababu tayari wao ukubwa wa Wilaya ni sawasawa na kata zangu mbili. Mtu kama huyu ukimwambia kwamba Serikali iendelee kugatua madaraka kupeleka huko chini hawezi kuelewa kwa sababu tayari yeye alishatosheka. Naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, nimetoa sample tu ya hiyo mikoa na iko kwenye kitabu hiki. Wakati unakuja kuhitimisha ni vizuri ukatuambia formula gani ambayo inatumika katika kugawanya keki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niseme jambo ambalo limekuwa likinitia simanzi. Katika mikoa yote Tanzania, ukiachia hii ambayo ndiyo imeanza hivi juzi, Mkoa wa Rukwa ndiyo mkoa pekee kwa taarifa nilizonazo ambao hauna Chuo cha Ufundi kwa maana ya VETA. Kwa hiyo, naomba Serikali hii ili sisi tusilazimike kukimbilia huko ambako kuna vyuo, kupitia Wizara zote kwa namna mtakavyoweza kujikusanya ujenzi wa VETA Rukwa iwe miongoni mwa vipaumbele. Kwa sisi Kalambo tayari tulishatenga eneo na tunafuata ramani ili tuanze ujenzi tukiamini kwamba Serikali nayo itatuunga mkono hivi karibuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi na kwa bajeti finyu kama hii ambayo umeiona kupitia TAMISEMI hali kadhalika hatuna Hospitali ya Wilaya. Niiombe Serikali, huko ambako mlishapeleka vinatosha, sasa hivi tuelekeze nguvu maeneo ambayo tunaita peripherals ili wananchi wakienda sehemu zote za Tanzania wasijione ukiwa kwamba ukifika maeneo fulani inakuwa kama vile haupo Tanzania. Niiombe Serikali, bado hatujachelewa, naona Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko pale ana-take note, Mikoa yote ambayo ni under privileged ipewe kipaumbele tuhakikishe kwamba inapata allocation ya fedha ya kutosha na wananchi wako tayari kuiunga Serikali yao mkono si tena kwa hila bali kwa upendo wa dhati kutoka moyoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niyaseme machache ili yachukuliwe kwa uzito niliotaka ufike, kimsingi naunga mkono bajeti. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ili nami nisije nikamaliza kama Mheshimiwa Mwambe bila kuunga mkono, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu, afya na uwezo wa kusimama jioni ya leo, niungane na Watanzania wenzangu na Wabunge wenzangu ili kuishauri Serikali katika kuhakikisha kwamba kasi ya maendeleo na hasa umeme inaenda kutendeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kushauri kwa kuisaidia Serikali na hasa nimesikia hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri, akiwa anaelezea jinsi ambavyo bajeti imeongezeka kwa kiasi cha asilimia 50. Naomba nimkumbushe, hiyo asilimia 50 atakuwa amesahau shilingi bilioni 79, kwa hiyo, inapaswa iongezeke kwa kiasi cha zaidi ya asilimia 50. Hiyo shilingi bilioni 79 iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma katika Sheria ya Bajeti na hasa katika uanzishaji wa Mfuko wa REA, fungu lile ni ring fenced. Maana yake ni nini? Pesa hiyo haiwezi kwenda kutumika kwa shughuli nyingine yoyote. Kwa mujibu wa sheria inatakiwa iende upande wa REA. Sasa nini kilichotokea? Serikali inawezekana walijikopesha kiasi cha shilingi bilioni 79 ambacho wana wajibu wa kuhakikisha kwamba kinarudi na kinaenda REA, kwa sababu lengo lake ni kupeleka umeme vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kile ambacho ametaja kwamba ni ongezeko la asilimia 50, ukichukua na hii bakaa unayovuka nayo, naomba urekebishe vitabu vyako visome kwamba kuna shilingi bilioni 79 ambayo inapaswa iongezeke katika bajeti yako. Najua Serikali wamejikopesha na muungwana akikopa ana kawaida ya kulipa na Serikali hii inayoongozwa na CCM italipa ili dhana ya kuhakikisha kwamba umeme unafika kila vijiji Tanzania inaenda kufikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo napenda kuchangia ni kuhusiana na suala zima la uzalishaji wa umeme. Ukimsikiliza Mheshimiwa Waziri, tunajipongeza tumezalisha umeme wa kutosha, lakini ukitazama projection tuliyokuwa nayo na nini ambacho tulitarajia kuzalisha, bado kasi yetu haitoshi. Tulisema kwamba tungezalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe pale Kiwira, ilikuwa tuzalishe umeme pale Mchuchuma, lakini haya yote hatujaweza kufanya. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri anapokuja kumalizia hotuba yake, atuambie baada ya miradi hii kutofanya kazi, tunajielekeza wapi kwenye vyanzo vingine vya uhakika ili kasi ya kupata umeme wa kutosha kwa ajili ya kutosheleza Watanzania na kuuza kwa nchi jirani tunakwenda kuifikia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimwongezee vyanzo vingine vya umeme, ukienda Mkoa wa Rukwa pale, kuna makaa ya mawe maeneo ya Namwere pale. Wachunguzi wanasema kwamba makaa yale yanafaa kwa kuzalisha umeme. Namwomba Mheshimiwa Waziri aelekeze nguvu kule. Kama haitoshi, maporomoko ya Kalambo, maporomoko ya pili Afrika baada ya Victoria Falls ambayo hayajatumika vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii, hebu tutumie chanzo hiki kwa ajili ya kuzalisha umeme na kazi ni ndogo tu. Kama imewezekana kuwa na mahusiano mazuri tukaanza kuzalisha umeme kule Rusumo, ni rahisi kabisa kwenda kwa majirani zetu Zambia kwa sababu yale maanguko yako mpakani mwa Tanzania na Zambia. Hebu tufanye utafiti, maanguko yale tutumie kwa ajili ya kuzalisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze upande wa REA. Tumeambiwa tunaenda REA Awamu ya Tatu, ni jambo jema. Hata hivyo, ni lazima tujitathmini; katika hii Awamu ya Pili tumenufaika sawa? Haiwezekani maeneo kama Wilaya ya Kalambo ilikuwa na umeme sifuri, halafu unaposema tunaenda Awamu ya Tatu bila kutazama huyu ambaye alikuwa na sifuri amepata nini? Naomba kuwe na exception katika mtazamo kabla hatujakwenda REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri na maeneo mengine ambayo umeme ulikuwa haujafika, barua nimepeleka ofisini kwake, kwa uchache tu nimtajie vijiji ambavyo vimetajwa kwenye barua niliyopeleka kwake, ni pamoja na Kijiji cha Mwazye ambako anazaliwa Muadhama Polycarp Pengo, hakuna umeme pale. Pia Kijiji cha Kazila, Kijiji cha Kamawe, Tatanda, Sopa, Ninga, Kanyezi, Musoma na vyote hivyo viko kwenye barua. Alikuja Makamu wa Rais Mstaafu, akawaahidi wananchi; amekuja Mheshimiwa Rais, akatoa ahadi, naomba aende kutekeleza kabla hatujaenda hiyo awamu ya tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la TPDC. Ukitaka kushiriki vizuri, lazima uwekeze ili katika mnyororo wa uzalishaji na utafutaji wa mafuta na gesi, Shirika letu la TPDC ambalo ni kwa ajili ya Watanzania wote liwe na nguvu, linatakiwa liwekeze kwa maana ya mtaji. Ukisoma ile sheria, imeeleza kabisa kwamba ili uweze kushiriki, lazima uwekeze kiasi cha pesa ambacho kinatakiwa. Naomba Mheshimiwa Waziri kwa kupitia Wizara yake tutazame kwa jicho la huruma, jicho la maslahi mapana kwa ajili ya Watanzania wote tuhakikishe kwamba tunawekeza vya kutosha TPDC. Hii itaondoa hii dhana ambayo watu wengine wamekuwa wakisema eti wagawane wao lakini Watanzania kwa ujumla wetu tusiwe na shirika letu ambalo ndiyo kwa ajili yetu sisi sote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itasaidia sana, itaondoa kelele ambayo imekuwa ikijengeka kwamba eti mzawa ni kumjali mmoja mmoja. Hebu tujaliwe kwa ujumla wetu tuwekeze katika kampuni yetu kama ambavyo Mataifa mengine wamefanya. Statoil, lile ni shirika la Kiserikali, Petrol Brass ni shirika ambalo part ni Serikali na watu binafsi. Kwa hiyo, ni vizuri tuhakikishe nguvu hii tunapelekea huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini haya machache ambayo nimeyaongea yamechukuliwa kwa uzito na yatafanyiwa kazi. Nakushukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukushukuru na kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama jioni ya leo ili niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na ripoti ya Kamati ya Bajeti maana mimi ni sehemu ya taarifa ile, hivyo naiunga mkono kwa asilimia mia moja. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yote kwa ujumla. Baada ya pongezi hizo naomba nitoe michango kidogo kwa sababu naamini mengi yameandikwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kuipongeza kwa moyo wa dhati kabisa TRA kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, hii achievements ambayo imeonekana ni ushirikiano miongoni mwao na wanaweza kufanya vizuri zaidi, naomba tuwatie moyo. Sisi Wabunge tuwe ni sehemu ya kuhimiza ulipaji wa kodi, bila kulipa kodi nchi hii haiwezi kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachia mbali Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mapato kwa maana ya Commissioner General, Wakuu wa Idara karibu wote ni Makaimu. Sasa haiwezekani, watu ambao wanafanya kazi nzuri na mpaka wanavuka malengo waendelee kukaimu hili halifai. Naiomba Serikali kwa kupitia Bodi husika hebu hawa watu ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu kama Makaimu muwa-confirm na kama hawatoshi, muwaondoe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la pili ambalo naomba kuchangia na hili limejitokeza bayana kwenye taarifa yetu, ni namna ya ushirikishwaji wa Bunge kwa kupitia Kamati ya Bajeti pale ambapo Mheshimiwa Waziri wa Fedha anakwenda kukutana na Mawaziri wenzake Arusha. Jambo hili halijaanza katika mwaka huu wa fedha, lilianza mwaka wa fedha 2015/2016 na ukisoma report yetu hatukuridhika na kile ambacho kilijitokeza na Waziri mwenye dhamana wa kipindi hicho, aliahidi kwamba halitajitokeza, lakini safari hii limejitokeza tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba, wenzetu tunavyokutana nao kwa maana ya Mawaziri wa Fedha wa nchi nyingine, wanakwenda wakiwa wamejiandaa, wamehusisha Mabunge ya kwao kwamba baadhi ya mambo wanakwenda nayo wakisema haya ni ya kufa na kupona. Wanakwenda kuyatetea, wanajenga hoja na wanahakikisha kwamba yanapita.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri, kuna msururu wa vitu vingi sana ambavyo vimepitishwa. Imekuja orodha ya nondo nyingi, unasema haya yametoka wapi? Alishauriana na akina nani? inachekesha mahali fulani unakuta kwamba, wanasema tuondoe kodi ili tuweze kulinda viwanda vya kutengeneza viberiti kwa sababu hatuna misitu ya kutosha!
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna viwanda, kiwanda chetu kilichokuwepo cha Moshi kimekufa, leo tunasema kwamba hatuna miti ya kutosha kwa ajili ya kukidhi viwanda vyetu, hivyo viwanda ni viwanda vipi? Ni kwa manufaa ya nani? Kwa faida ya nani? Naamini, mapendekezo ambayo yametolewa na Kamati ya Bajeti kwamba jambo hili litazamwe lisijirudie, hakika halitajirudia, maana Mheshimiwa Waziri ni msikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu yangu nyingine ni kuhusiana na suala zima la mradi wa maji na hasa maji vijijini pamoja na suala zima la ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. Tumependekeza kwamba iongezeke tozo ya sh. 50/= ili jumla iwe sh. 100/= kwenye tozo za mafuta kwa maana ya petrol na diesel. Hii itatuwezesha kutupatia kiasi cha shilingi bilioni 250 na tumependekeza kwamba mgawanyo wa pesa hizi bilioni 220 iende kutatua tatizo la maji vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Mbunge hata mmoja ambaye anaweza akaniambia kwamba kwenye Wilaya yake hawana tatizo la maji, hayupo! Kwa hiyo, ni vizuri tukatoka jasho jingi kulikoni tukasubiri kuja kuvuja damu nyingi. Naomba Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla mlisikilize. Pia tumependekeza kwamba bilioni 30 iende kusaidia kumalizia ujenzi wa zahanati. Ni nani asiyejua kwamba ukirudi kwenye vijiji vyetu, wananchi wameitikia kwa moyo wa dhati wakajenga Zahanati zikafika usawa wa lenta, leo ukienda unamwambia mwananchi ashiriki kwenye shughuli nyingine ya maendeleo wakati maboma anayatazama hapati huduma ya afya, hawatuelewi. Kwa hiyo naomba hii shilingi bilioni 30 iende kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, karibia mwisho, nimesikia Serikali wana mapendekezo kwamba safari hii wanaenda kufanya adjustment kwa inflation rate ya five per cent, ni jambo jema! Lakini jambo hili haliwezi likaenda in a blanket form, lazima kuwe na exceptions, ukiongeza kwenye bia haina tatizo kwa sababu wauzaji wa bia wameongeza bei tangu mwezi Februari, bia zimeongezeka kutoka sh. 2,300/= mpaka 2,500/=. Kwa hiyo hiki ambacho mnafanya adjustment is ok! Wala haitaathiri chochote, kwa sababu walishaanza ku-enjoy!
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo langu nalipata kwenye suala zima la vinywaji baridi na hasa soda na juisi. Hivi leo hii tunasema kwamba tunaweka excise duty ya asilimia tano kwenye soda na wakati huo Serikali hiyo inasema kwamba tunataka Mtanzania mnyonge ambaye ndiyo mnywa soda, leo hii ndiyo tunaenda kumwwekea five percent! Ukitazama kipindi hiki ndiyo kipindi ambacho wenzetu waliojaaliwa kufunga wanafunga, anataka wakati anapata futari yake apate na juisi, apate na soda. Ndiyo kipindi kweli Serikali mnataka mkaongeze hiyo? Bei ya soda haijapanda kwa ujumla kama miaka mitano, leo hii mnataka itoke sh. 500/=, iwe sh. 600/=, halikubaliki hili! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vyanzo vingi, let‟s think outside the box.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipatia fursa nami niweze kuchangia katika hotuba iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri. Naomba niungane na Wabunge wenzangu waliotangulia kumpongeza kwa kazi nzuri ambayo inafanyika, haihitaji ushahidi, kila mtu anaona kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika Jimbo langu. Kipekee nashukuru kwamba Serikali ina ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Sumbawanga kwenda Kasanga Port na nimeona imetengwa jumla ya shilingi bilioni 74. Naiomba Serikali ihakikishe kwamba barabara hii inajengwa na ikamilike kwa wakati. Ni ukweli usiopingika kwamba mradi ukishachukua muda mrefu gharama yake inakuwa kubwa, lakini kama haitoshi kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeona kuna ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Matai kwenda Kaseshe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni shahidi alikuja akatembelea barabara hii na akaahidi kwamba Kandarasi atapatikana na kazi hii itatolewa. Sasa naomba katika bajeti iliyotangulia ilikuwa imetengwa bilioni 11, safari hii imetengwa bilioni 4.9. Tafsiri yake nimesoma na kukuta kwamba Mkandarasi atapatikana muda wowote, kwa hiyo kiasi cha pesa tofauti ya bilioni 11 iliyokuwa imetengwa wakati ule na sasa hivi naamini itakuwa imetolewa na ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nimeliona ni vizuri nikampongeza Mheshimiwa Waziri, kwa mara ya kwanza kivuko cha Mto Kalambo kimetengewa pesa za kutosha milioni 100 kwa ajili ya usanifu. Naamini haitaishia katika usanifu, kazi ya kujenga kivuko kile itaanza kwani ni ahadi ya Mheshimiwa Rais alipokuja kuomba kura Kalambo na akaahidi kwamba yeyote ambaye hatahakikisha kivuko hiki kinajengwa basi ajiandae kupisha nafasi hiyo. Naamini Mheshimiwa Waziri bado anakumbuka, hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo haitakiwi kupingwa na mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema kuhusu Jimbo langu, naomba niseme Kitaifa. Majuzi nilipata fursa ya kuuliza swali kuhusiana na suala la UDA Dar es Salaam na katika majibu ambayo nilipatiwa naomba nikwambie katika miradi ya kutolea mfano Kusini mwa Jangwa la Sahara yenye mafanikio ni pamoja na usafiri wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam, lakini pamoja na treni ya umeme Lagos. Kwa Watanzania wengi tunadhani kwamba mradi huu ni mradi mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie ukienda duniani miongoni mwa miradi ambayo inasifiwa ni pamoja na usafiri wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam. Ninachoomba ni vizuri Serikali ikahakikisha kwamba fursa hii inatolewa kwa Watanzania walio wengi ili hisa zile ambazo zinamilikiwa na Serikali zikaja kuuzwa kwa Watanzania walio wengi ili tukashiriki kumiliki uchumi huu kwa ajili ya Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi umekuwa ukipigia kelele kuhusiana na TTCL, naomba nikuhakikishie kama elimu ya kutosha haitolewi kwa Watanzania juu ya kununua hisa, basi hata hili ambalo umekuwa ukilipigia kelele kwamba Watanzania washirikishwe katika kumiliki halitawezekana. Mfano tunao, hisa ambazo zimetolewa kwa ajili ya kuuza za Vodacom imefikia tarehe 19 ambayo ilikuwa tarehe ya mwisho bado hisa hazijaweza kununuliwa. Naomba Wizara ya Fedha ichukue jukumu la kuhakikisha kwamba elimu kuhusiana na uwekezaji kwa maana ya kununua hisa inatolewa kwa Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Kenya walivyokuwa wamepeleka hisa zao sokoni za Safaricom walikuwa wametoa kwa muda wa mwezi mzima lakini ndani ya siku kumi zile hisa zilikuwa zimeshanunuliwa kiasi kwamba wakalazimika wasitishe. Sasa kwa Watanzania imekuwa ni hadithi tofauti na kwa bahati mbaya sana unakuta wakati mwingine hata Wabunge pia hatuna elimu juu ya umiliki wa hisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa makusudi Serikali lazima ihakikishe kwamba inatoa elimu maana taarifa ambazo tunapata kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ni kwamba…

T A A R I F A....
MWENYEKITI: Ahsante, ameshakaa. Mheshimiwa Kandege muda wako umekwisha. Hapana kengele ililia wakati wa taarifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja iliyo mbele yetu. Aidha, baada ya kuunga mkono hoja, naomba nichangie baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote ukianzia na Katibu Mkuu (Ujenzi) na Katibu Mkuu (Uchukuzi na Mawasiliano) pamoja na wataalam wote wa Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, naomba nichangie kwa kuanza na Jimboni kwangu. Niombe Serikali ihakikishe inajenga barabara ya kutoka Sumbawanga – Matai - Kasanga Port kwa kiwango cha lami. Ujenzi huu umechukua muda mrefu sana kutokana na upatikanaji wa fedha kutoka Wizara ya Ujenzi kwenda kwa mkandarasi na hivyo mradi kuwa na gharama kubwa kutokana na Serikali kulazimika kulipa fedha nyingi kutokana na mkataba. Kiasi cha fedha kilichotengwa ni cha kutosha, niiombe Serikali ihakikishe fedha zinatolewa ili mradi huu wa barabara uweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalopenda kuchangia ni juu ya ujenzi wa barabara ya kutoka Matai - Kasesya border, ambayo Mheshimiwa Waziri alipata nafasi ya kuitembelea na kuahidi kwamba mara mkandarasi atakapopatikana ujenzi utaanza. Katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017, Serikali iliweza kutenga kwenye bajeti

kiasi cha shilingi bilioni 11 na ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri imeonesha kwamba taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea. Ni imani yangu kubwa kwamba kiasi cha fedha kitaweza kutolewa kabla ya mwaka huu wa fedha haujamalizika. Katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/ 2018 barabara hii imeweza kutengewa kiasi cha shilingi bilioni 4.9 kutoka shilingi bilioni 11 kwa mwaka wa fedha 2016/2017, sitarajii gharama za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kupungua kwa zaidi ya nusu. Naiomba Serikali iharakishe utaratibu wa kumpata mkandarasi ili aanze ujenzi wa barabara hii muhimu sana kwani siamini kwamba nchi hii ina tatizo la upatikanaji wa wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu ujenzi wa Daraja la Mto Kalambo, ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa akiwa Waziri wa Ujenzi na akasisitiza siku alipokuja kuomba kura Kalambo akimtaka Mkurugenzi atangaze mara moja kazi ya ujenzi wa daraja hilo. Naomba niishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 100 japo kiasi hiki sidhani kama kinatosha kwa kuzingatia ukubwa wa daraja hili. Naiomba Serikali ihakikishe kwamba ujenzi wa daraja hili unaanza mapema na hasa kipindi cha kiangazi kwani mvua zikishaanza kunyesha siyo rahisi ujenzi kufanyika kwani mto hufurika kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ifike mahali Serikali itimize ahadi zake kwa vitendo kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga kwani ahadi hii ni ya muda mrefu sana. Umuhimu wa uwanja huu baada kukamilika kwa Uwanja wa Kimataifa wa Songwe na ule wa Mpanda Mkoani Katavi unajulikana na hakuna hata chembe ya ubishi. Naomba Serikali sasa itende haki kwani fedha za kutoka nje ni miaka zaidi ya mitatu zimekuwa zikioneshwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ngazi ya kitaifa naomba kuchangia kuhusiana na mradi wa usafirishaji wa DART. Ukienda kwenye mataifa ya nje miongoni mwa miradi inayopigiwa mfano Kusini mwa Jangwa la Sahara basi utakuta miradi miwili kama one success stories nayo ni treni ya umeme ya Lagos na Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ya Dar es Salaam. Ni jambo la busara kwa kuwa mradi huu kama moja ya miradi ya kitaifa na wenye mafanikio makubwa na hivyo kutouchukua kama mradi wa watu wa Dar es Salaam. Hivyo sote tuna jukumu la kuhakikisha kwamba mradi huu unapewa upendeleo wa pekee kwa maslahi ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile uwekezaji mkubwa unafanywa na Serikali kwa maana ya ujenzi wa miundombinu kwa awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na hata ya nne iko haja kubwa kwa Serikali kuhakikisha uwekezaji mkubwa unafanywa kwa Serikali kuuza baadhi ya hisa zake kwa Watanzania wengi na pia kuwa na maongezi ili mbia wa Serikali naye auze hisa zake kwa kuzipeleka DSE (Dar es Salaam Stock Exchange) ili umiliki uwe wa wananchi wengi na ili mtaji mkubwa uweze kupatikana utakaowezesha uwekezaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kuunganisha mabasi hapa nchini pamoja na uzalishaji wa matairi, hili litawezesha kauli ya Serikali yetu ya CCM ya Tanzania ya viwanda kutekelezeka kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mataifa ya wenzetu kama Ethiopia, Japan, Korea na kwingine wameweza kufanikiwa kwa kuweka mikakati maalum ya kuhakikisha kwamba kunakuwepo na upendeleo maalum kwa wazawa na makampuni ya wazawa wazalendo. Wakati umefika sasa kama Taifa tukafanya uamuzi huo bila ya kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa Waswahili unaosema ukiona vinaelea vimeundwa. Hayo makampuni yanayotamba duniani kama vile Samsung, Dangote, Hutchison Whampoa, DSM Port Operator - TICTS na kadhalika yametokana na maamuzi yaliyofanywa na Serikali zao mahususi kuyafanya yakue kabla ya kuyataka yaanze kushindana na nguvu za soko.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi jioni ya leo kupata nafasi hii kuchangia. Naomba kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa mbele yetu na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana. Naomba niungane na Wabunge wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake. Baada ya kupongeza naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Serikali inayoongozwa na CCM kwa nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba tunaanza kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kalambo, naomba kasi hii ambayo imeoneshwa tusije tukasita hata kidogo, tuhakikishe kwamba tunaenda kuimalizia kabisa na itumike ili kuwasaidia Watanzania walio Mkoa wa Rukwa na hususani Wilaya ya Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia wenzangu wakiwa wanamshukuru Mheshimiwa Waziri, wamepata ambulance ni jambo jema, naamini zamu nyingine na sisi Kalambo tutakumbukwa, ili kuunga jitihada za Mbunge huyu ambaye anaongea, maana ameweza kusababisha zikapatikana ambulance tatu. Ni wakati muafaka Serikali ikaniunga mkono ili tuokoe wananchi walioko Wilaya ya Kalambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matatizo ambayo tunayo makubwa wenzangu wamesema kuhusiana na suala zima la ukosefu wa watumishi pamoja na vifaa tiba na vitendanishi. Kama kuna maeneo ambayo yana tatizo kubwa ni pamoja na Wilaya ya Kalambo na ni kwa sababu kimsingi mikoa ya pembezoni imekuwa disadvantaged kwa kipindi kirefu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati wanapanga ikama ya safari hii naomba aitazame kwa jicho la huruma Wilaya ya Kalambo, tunahitaji kuziba pengo kubwa sana la upungufu wa watumishi katika kada hii ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema wenzangu nami nilirudie. Ni matarajio yetu kwamba tunapoongea na Serikali tunaongea nayo kwa ujumla wake na mpango mzima wa kubadilisha utaratibu wa circle ya bajeti ni ili kama kuna jambo ambalo halikupita katika Wizara husika tunapokuja kuhitimisha bajeti basi tuhakikishe jambo hilo linakuwa addressed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna hili suala zima la ujenzi wa vituo vya afya pamoja na kumalizia zahanati. Katika hali ya kawaida iko chini ya TAMISEMI lakini TAMISEMI na Wizara ya Afya ni Serikali moja na Serikali yenyewe inatokana na CCM, kwa hiyo tunaongea na Serikali ya CCM. Mlikuja kwenye Kamati ya Bajeti mkasema last time mnaenda kuleta bei halisia ili tukamalizie maboma na tuanze kujenga vituo vya afya. Sasa mwenzenu katika Wilaya ya Kalambo yenye kata 23 na vijiji 112 kuna vituo vya afya vitatu tu; mnaweza mkaona jinsi gani uhitaji ulivyokuwa mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejitolea wamejenga kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali hii kwamba wajenge kufika usawa wa lenta na baadaye Serikali i-take over na hakuna hata siku moja ambayo Serikali imekuja ikasema utaratibu ule umefutwa. Kwa hiyo, bado ni jukumu letu ni jukumu la Serikali kuhakikisha Wananchi ambao wamejitoa kwa moyo wao kazi nzuri hii iweze kumaliziwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mapendekezo, kwa namna iliyo nzuri tulipendekeza shilingi hamsini iwe kwenye tozo ili iende ku-address tatizo hili la ujenzi wa vituo vya afya pamoja na kumalizia zahanati ambazo wananchi wamejitoa kwa moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wasikie na watie uzito katika haya ambayo nnayasema naomba niishie hapo nashukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi leo kupata nafasi jioni hii ili kuweza kuchangia katika hotuba ya bajeti. Mengi yamesemwa na naomba niishukuru Serikali, nina kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa sababu mawazo mengi ambayo yalitolewa na Kamati ya Bajeti na kutolewa na Bunge yamezingatiwa.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyopata fursa ya kuongea ITV nilisema hivi, kwa nchi zetu zinazoendelea, bajeti kama hii iliyoandaliwa utategemea iandaliwe kipindi ambacho nchi inaenda kufanya uchaguzi mwaka unaofuata. Hata hivyo, kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli uchaguzi wala hatutarajii kwamba upo mwakani, kwa hiyo, ni bajeti ambayo inaenda kuwakomboa Watanzania kwa nia ya dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho mengi tumetoa na Serikali imezingatia, naomba nisitumie nguvu katika kuchangia kwa sababu naamini Serikali ni sikivu. Naomba niboreshe baadhi ya maeneo machache ambayo yapo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango ili waweze kuyatilia mkazo na marekebisho yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo naomba nijikite kwa kuanzia ni kuhusiana na VAT katika huduma uwindaji. Asilimia 18 inatozwa pale ambapo muwindaji anaenda kulipia block (block fee) eti nayo anatozwa VAT. La kushangaza zaidi hata pale anapolazimika kusafirisha trophy kupeleka nje ambayo amekatia leseni na ameruhusiwa awinde, wakati kwa mujibu wa sheria VAT on export hakuna kitu kama hicho, lakini kwa mwindaji tunataka atozwe asilimia 18, naomba Serikali mkatizame. Kama hiyo haitoshi hata pale ambapo ametozwa penalty lakini katika penalty hiyo nayo tunaweka na 18% VAT, sheria hiyo haipo. Kwa hiyo, naomba Serikali kwa ujumla wakalitizame kuanzia mwanzo mpaka mwisho ili marekebisho yafanyike twende kwa mujibu wa sheria inavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na taasisi na mashirika ya umma. Ni takwa la kisheria kwamba wanatakiwa kuchangia asilimia 15 ya growth revenue kwenda Serikali Kuu. Kinachoshangaza, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi kwa maana ya Income Tax, anapoandaa hesabu zake anatakiwa aoneshe kile kiasi ambacho alishatoa kupeleka Serikalini lakini jambo la ajabu ni kwamba akiandaa hesabu ikifika TRA wanasema hawatambui, kama vile Serikali haijapata hata senti tano, wanairudisha kama siuo allowable deduction, kwa hiyo, kunakuwa na double taxation. Naomba Serikali mkalitazame hili, halina tija kwa mashirika yetu, inaua mashirika yetu bila sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii hoja ya shilingi 40 ya tozo ambayo Kamati na naamini na Wabunge wote hata upande wa pili wanalitamani kimya kimya kwa sababu inakwenda kupunguza kero kubwa ya maji na hasa maji vijijini. Kwenye Kamati yetu ya Bajeti tumependekeza kwamba asilimia 70 ya pesa hizi ambazo zinakwenda kupatikana zikatibu kero ya maji vijijini na asilimia 30 ndiyo iende kutibu kero ya maji mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini hili halina mjadala, naamini hata upande wa pili wakiulizwa watapigia kura ya kuunga mkono suala hili. Kwa sababu hakuna hata mmoja, awe anatoka mjini, awe anatoka vijijini, tatizo la maji ni tatizo la kitaifa. Kwa hiyo, tukubaliane ndugu zangu kwamba ni vizuri katika hili tukaungana, hii tozo ambayo inapatikana ikatatue kero ya maji vijijini na mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niiombe Serikali, wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti yake amesema kwamba anaondoa road license lakini katika ile sticker ya road license kuna kiasi fulani cha fire extinguisher aje atuambie, nayo imeondolewa? Maana kama haijaondolewa itakuwa ni kero, kwa sababu ninyi wenzangu wote mashahidi, hakuna hata siku moja ambapo eti hiyo fire extinguisher imeweza kusaidia, sanasana ni stickers tu zinatolewa inakuwa ulaji. Naomba nayo iondolewe, ni kero kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hiyo haitoshi, kuna zile stickers za Wiki ya Nenda kwa Usalama. Lengo lilikuwa zuri kwamba tunataka magari ambayo yanatembea barabarani yawe ni yale magari ambayo ni road worthy, lakini sisi sote ni mashahidi, tumekuwa tukiuziwa stickers gari hazikaguliwi. Kwa hiyo, nayo ni vizuri iondoke, ni kero, haitusaidii chochote, inasaidia wachache ambao ni wajanja wajanja, ikiondoka hiyo itakuwa imetusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri anasema kwamba excise duty ya ngano inapungua kutoka asilimia 35 kwenda asilimia kumi. Naomba tuulizane Mheshimiwa Waziri, hali ya sasa ikoje, kwa sheria ilivyo leo hii asilimia 10 hiyo anatozwa yule ambaye anaagiza ngano anakuja kuisaga tukijua kwamba wananchi watanufaika. Sasa kwa kuondoa kwa hawa wengine brokers, huisaidii Serikali wala humsaidii mwananchi wa kawaida. Ni kama vile tunataka wawepo middlemen ambao watakuwa wanaagiza ngano halafu wanakuja wanawauzia wenye viwanda waende kusaga. Mheshimiwa Waziri, naomba ulitizame, ni bora hiyo ibaki vilevile iwe chanzo cha mapato ila wale ambao wanaagiza kwa ajili ya kuja kusaga tukijua kwamba bei ya mkate itakuwa imeshuka itatusaidia lakini hiki chanzo kiendelee kwa sababu kinasaidia katika kuongeza mapato kwa upande wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linalosemwa kuhusu suala la property tax, ni vizuri tukakumbushana Waheshimiwa Wabunge, sisi sote tulikuwa tunalalamika kwamba chanzo kisichotokana na kodi makusanyo yake yamekuwa hafifu, tukakubaliana kwamba ni vizuri kama TRA wanakusanya hawakusanyi pesa hiyo iende Mfuko Mkuu, ni wajibu wa TRA ikikusanya pesa hizo zizirudie Halmashauri maana ndiyo wenye hayo majengo, ndiyo msingi wake upo hapo, lakini si kwamba eti Serikali Kuu ichukue kama ni chanzo chake, la hasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukubaliane tangu mwanzo kwamba pesa hiyo ikikusanywa inatakiwa irudi kwenye Halmashauri husika ili yale majukumu ambayo Halmashauri inatakiwa iyafanye yaendelee kufanywa na Halmashauri. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili upigie mstari kabisa isije ikaonekana kwamba sasa tunanyang’anya vyanzo upande wa Serikali za Mitaa kwenda Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ushuru wa mazao, nimefarijika sana ilikuwa kutoka asilimia tano sasa inakwenda asilimia tatu. Naomba nisisitize, asilimia tatu hii iwe kwa mazao yote, isiwe kwamba eti kuna mazao ya biashara na mazao ya chakula maana itakuwa ni vigumu sana kuweza kujua ni wakati gani mahindi yanakuwa zao la biashara na wakati gani mahindi yanakuwa zao la chakula, hapo tutakuwa tunatengeneza mwanya wa rushwa bila sababu. Kwa hiyo, kimsingi ni vizuri hicho kiasi kikapungua lakini iwe sawa kwa ama mazao ya biashara au mazao ya chakula na tafsiri iko rahisi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waheshimiwa wengine wanasema kwamba tunaipunguzia Halmashauri uwezo wa kukusanya, lakini ukiipunguzia Halmashauri uwezo wa kukusanya hicho ambacho kingekusanywa na Halmashauri kikawa kwa mwananchi wa kawaida, mwananchi huyu wa kawaida maana yake disposable income inakuwa imeongezeka, atakwenda kufanya spending katika mambo mengine na kodi yetu tutaipata. Ni nani asiyependa wananchi wetu wakawa wana pesa mifukoni mwao? Kwa hiyo, ni wazo jema mimi naliunga mkono sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi kwamba hatukulala mpaka saa nane na naamini na mengine tutaendelea kushauriana na Serikali, yale ambayo hawakuyachukua wataendelea kuyachukua kwa sababu naamini Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla ni wasikivu na naamini na wenzetu wa upande wa pili hakuna sababu ya kuja na pages 200, tuje na pages chache…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ili niweze kuwa sehemu ya wachangiaji katika Rasimu ya Mpango. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya, maajabu ambayo nimetendewa kati ya Wabunge ambao 28 waliopita bila kupingwa ni pamoja na mimi, nina kila sababu ya kuwashukuru wannachi wa Jimbo la Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bajeti kwa hiyo nilitoa mchango wa kutosha. Hata hivyo, leo nitajielekeza katika masuala mawili; la kwanza itakuwa upande wa kilimo na la pili kama muda utatosha litakuwa upande wa local contents.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimekuwa sio cha kuvutia kwa sababu hakuna incentive ya kutosha ambayo imewekezwa ili mwananchi ambaye analima aone tija katika kilimo. Nawe ni shujaa unajua kabisa yaliyotokea miaka ya nyuma, leo nikipita nauliza hivi yako wapi mafuta yaliyokuwa yanatokana na karanga? Siyaoni, yako wapi mafuta ya kula yanayotokana na pamba? Siyaoni. Iko wapi Tanbond? Siioni, iko wapi Super Ghee siioni, iko wapi samli iliyoboreshwa, sioni. Yako wapi mafuta ambayo yanatokana na mahindi ambayo yamezalishwa Tanzania? Sioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufike wakati sasa ili wananchi wanaotoka Rukwa, Ruvuma, Iringa na maeneo mengine ambayo wanazalisha mahindi wasipate tabu ya kutafuta soko, wanafanya kazi kubwa sana katika kulima, si wajibu wao kutafuta soko. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba inaweka mazingira yaliyo bora ili mkulima kazi yake iwe ni kulima mbegu iliyokuwa bora na soko litafutwe na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tutafanyaje? Kwa kuhakikisha kwamba sio kwamba mahindi yatumike kwa ajili ya chakula cha binadamu peke yake, tu-extract kutoka kwenye mahindi tupate mafuta inasemekana kwamba ni mafuta yaliyo bora na tukienda supermarket unayakuta. Mafuta haya yanapatikana wapi? Kama iko mbegu mahsusi ni wajibu wa Serikali kwa kupitia research and development kutuletea mbegu hizi ili wakulima wetu waweze kufaidika na kilimo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mbali Zaidi, sasa hivi bei ya mafuta ya kula imepanda kweli kweli. Zaidi ya dola milioni 126 tunatumia kama nchi kwa ajili ya kuagiza mafuta. Tafsiri yake ni kwamba ajira tunawapelekea wengine na sisi tunabaki kuwa soko. Ifike wakati wa kuwekeza vya kutosha ili mafuta ya kula ambayo yanachukua mzigo mkubwa kwa Taifa tuweze kupeleka kwa watu wetu ili kilimo kiwe na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la local content. Ukitafuta namna gani tunamsaidia Mtanzania, mzalendo ili aone fahari ya kuzaliwa Tanzania tofauti na mwingine ambaye hakuzaliwa Tanzania, unatafuta kwa kurunzi ndiyo unaenda kuziona hizo fursa. Ifike wakati kwa makusudi mazima kama ambavyo wenzetu wamefanya kama Afrika ya Kusini, mwananchi wa Afrika Kusini anajua haki zake katika kuwekeza na fursa zipi ambazo anatakiwa kuzipata. Ni wakati muafaka tusione aibu ya kumpendelea Mtanzania ajivunie na fursa za kuwa Mtanzania na zionekane wazi. Hizi sheria ambazo zipo unaenda kwenye madini ndiyo unakutana nayo, sijui unaenda wapi zote zikusanywe kwa pamoja ili ionekane dhahiri kwa Mtanzania fursa alizonazo na upendeleo wa Dhahiri, tusione aibu kuwapendelea Watanzania. Wako wa nchi za jirani ambao wao wamekuwa na wivu na watu wao. Ni wakati muafaka, tusichelewe muda ndiyo sasa hivi, tuhakikishe kwamba tunawalinda Watanzania kwa kuweka vivutio vya wazi kabisa bila hata kuona aibu katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda upande wa ujenzi, kazi kubwa sana imefanyika katika ujenzi wa miundombinu, lakini ni watu gani ambao wamejenga hiyo miundombinu na hiyo fedha ambayo wamepata wameenda kuwekeza wapi, utakuta kwamba inaenda kwa wenzetu. Ni wakati muafaka kuhakikisha kwamba tunawasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kuwa mchangiaji wa kwanza kwa siku ya leo. Nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na sisi sote Wabunge ambao tumepata fursa ya kuwepo leo mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Bajeti. Kwa hiyo, nimepata fursa ya kutosha katika kuchangia mawazo ambayo yameboresha Mpango. Hata hivyo, naomba niendelee kujazia katika baadhi ya maeneo ambayo naamini Serikali itakuwa tayari kuendelea kuya-accommodate ili Mpango wetu uwe ni ambao utaleta tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuipongeza Serikali yetu, imefanya kazi kubwa na nzuri sana katika suala zima la miundombinu. Hata hivyo, tunapofanya kazi nzuri tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba kasi ileile tuliyokuwanayo ya kujenga miundombinu inaendelea na inaendelezwa kwa kasi kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuipongeza Serikali yetu imefanya kazi kubwa nzuri sana katika suala zima la Miundombinu; lakini tunapofanya kazi nzuri kuna wajibu wa kuhakikisha kwamba kasi ile ile tuliyokuwa nayo ya kujenga miundombinu inaendelea na inaendelezwa kwa kasi kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, tumeweza kuunganisha karibu mikao yote Tanzania, imebaki Mikoa michache, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba kasi ya kuunganisha miundombinu kwa maana ya barabara inaenea katika Mikoa yote, maeneo ambayo yamebaki na twende kuunganisha Wilaya zote.

Mheshimiwa Spika, iko haja ya kwenda kutazama barabara za kimkakati na hasa zile barabara ambazo zinaunganisha nchi yetu na nchi Jirani. Kwa mfano barabara iliyoko katika Jimbo langu la Kalambo kutoka Matai kwenda Katesha Boda ni miongoni mwa Barabara muhimu sana, ni vizuri Serikali ikatilia maanani ujenzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara ambayo inaunganisha nchi yetu na nchi ya Mozambique iko Ruvuma kule maarufu kwa jina la Likuyufusi Mkenda, ni vizuri kabisa Serikali ikahakikisha katika mpango barabara hii ikawekwa ili fursa ya kiuchumi kama nchi tuweze kuipata kwa majirani zetu wa Mozambique.

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi kwenye suala la barabara kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali katika ujenzi wa Reli yetu, tena ya Standard Gage, ni kazi ya kutiliwa mfano ya kupigiwa mfano, ni kazi ambayo imeanzwa, si vizuri tukaishia katika maeneo hayo; ni vizuri sasa tukaanza kufikiria networking kwa Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, tunayo Reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Zambia Kapiri Mposhi, lakini reli ile imejengwa kwa kiwango cha Standard Gauge.

Mheshimiwa Spika, tutumie fursa ya ujenzi ambao tumeianza kwenda mpaka Mwanza na Kigoma. Tutumie fursa ya Reli ya TAZARA. Kwanza tuondoe makandokando yaliyopo katika uendeshaji, kwa maana ya Management, lakini ni vizuri pia tukaendelea kuongea na wenzetu wa Zambia. Sisi tuna eneo kubwa, na hili eneo ambalo tunalo sasa tuanze kutazama uwezekano wa kuanzisha vipande vingine kutoka Tunduma pale kwenda mpaka Kasanga Port ili tuweze kutumia fursa ya kuunganisha na DRC kwa ajili ya mizigo yetu; wanahitaji sana mizigo kutoka kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Lakini kama hiyo haitoshi, hata ukitazama kuna hii habari ya Mtwara Corridor suala limeongelewa muda mrefu sana. Ifike mahali katika mpango wetu tujue kwamba tunataka network kwa nchi yetu ili kusiwe na sehemu hata moja katika nchi hii ambayo inakuwa disadvantage. Ni vizuri na ni wakati muafaka kwa Serikali kuhakikisha kwamba eneo hilo nalo reli inajengwa ili tuweze kutumia fursa ya kuunganisha na Lake Nyasa pale.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna mradi wetu ambao umeongelewa muda mrefu kuhusu Liganga na Mchuchuma tukiwa na uhakika wa usafiri wa uhakika kwenda kufika kule hakika nchi yetu tutakuwa tumefungua kila eneo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri ukatilia maanani masuala haya ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kuhusiana na suala zima la Afya. Naipongeza Serikali imefanya kazi nzuri sana katika kujenga vituo vya afya vingi vya kutosha. Sasa tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba sasa wataalamu na vifaa vinakuwepo vya kutosha ili hicho ambacho kimekusudiwa kiweze kutoa matunda kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wewe ni shuhuda, umekuwa ukilisema mara nyingi kwamba tusipokuwa na Bima kwa watanzania hawa hakika juu ya Mwananchi kupata matibabu kuanzia Januari mpaka Disemba itakuwa kwenye mashaka.

Mheshimiwa Spika, ni wakati muafaka sasa wa kuja na mpango na ukamilike haraka juu ya universal health coverage kwa watanzania hawa, ndio namna ambayo itatuhakikishia afya kwa watu wetu bila kujali kwamba mtu ana kipato au hana. Kwa sababu katika hali ya kawaida ugonjwa hauna muda, kwamba mtu atajiandaa na kuwa fedha ambayo ameitenga kwamba nikiugua nitakwenda kuitumia hii. Window pekee ambayo itatusaidia ni universal health coverage kwa Watanzania, tuanze sasa. Mheshimiwa Waziri wa Afya unasikia, ndicho kipimo chako katika kuhakikisha kwamba Watanzania wote watakukumbuka kwa kazi nzuri ambayo utakuwa umewafanyia kwa kuwaanzishia mfuko na ukamilike.

Mheshimiwa Spika, alianza Waziri aliyetangulia na eneo alilofika sasa ni wajibu wako kuhakikisha kwa maana wewe unaenda kumalizia kipande ambacho kilianzishwa na mwenzako.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichangie kuhusiana na suala zima upande wa Kilimo. Safari hii tumepata wake- up call, kwamba uhitaji wa mafuta ya kula ni jambo ambalo halibishaniwi, kila mtu atahitaji mafuta ya kula kinachotofautia ni kiasi gani na wingi ndicho mtu atatumia lakini hakuna mtu ambaye atasema hata tumia mafuta ya kula. Na sisi kama Taifa tumekuwa tukitumia fedha nyingi sana za kigeni kuagiza mafuta kutoka nje ambayo wakati mwingine hatuna hata uhakika na juu ya ubora wake.

Mheshimiwa Spika, nilishawahi kulisema hata siku moja hapa; kama kuna mambo ambayo enzi zile yalifanywa vizuri na the so called SIDO ilikuwa ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda kwa ajili ya kukamua mafuta ya alizeti na mafuta ya karanga. Hivyo viwanda na mawazo hayo ni wakati muafaka kwa kutoa hamasa kwa watu wetu kuhakikisha kwamba mbegu zilizo bora ambazo zitakuwa zinatoa mafuta ya kutosha (extraction rate) iliyo nzuri ebu tuhimize kila kaya; kama ambavyo ilitokea kipindi Fulani. Kwamba ilikuwa kila familia ijitosheleze katika chakula. Sasa ifike pahali ambapo hamasa itolewe kila familia walau kila mwananchi akawa na hata nusu heka akalima alizeti, ama karanga, kulingana na hali ya mahali Fulani. Ifike pahali ambapo tujitosheleze kwa mafuta ambayo tunazalisha sisi wenyewe. Kwanza tuna uhakika na ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilishawahi kusema siku nyingine hapa, hivi ile super G ambayo tulikuwa tunaiona imeenda wapi? Nini ambacho kilitokea Tanbond imeenda wapi? Nini ambacho kimetokea? Yale mafuta ambayo tunayapata kutokana na mbegu za pamba yameenda wapi? Nini kimetokea? Kama Taifa tuna kila sababu ya kujifanyia tathmini sehemu ambazo tumekosea turudi katika mstari ili wananchi wetu wawe na uhakika wa mafuta yaliyo bora, lakini pia ni chanzo kizuri cha mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe, kwa ujumla wake kazi ambayo imefanyika ni nzuri. Ni wajibu wetu sisi Watanzania tukahakikisha kwamba tunakuwa na spirit ya kupenda kufanya kazi; na ubunifu tukiupata kwa mtu tuulee, si kwamba inakuwa kama vile anafanya mtu kwa ajili ya manufaa ya Taifa lakini hatumuungi mkono kwasababu kama vile hatunufaiki wote.

Mheshimiwa spika, nakushukuru na Mungu akubariki sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo niweze kutoa mchango katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wote kwa hotuba nzuri ambayo hakika inaonyesha matumaini makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali kwa ku-respond timely kuhusiana na suala zima la Bima ya Afya kwa Watanzania wote. Walikuwa wamekusudia kwamba wangeweza kuleta Muswada mwezi Septemba lakini wamekiri kwamba kutokana na unyeti wa suala hili, basi ndani ya Bunge hili la bajeti wataweza kuleta Muswada huo ambao hakika sisi kama Wabunge tutakuwa na nafasi ya kufanya maboresho ili kile ambacho tunakikusudia kwa ajili ya Watanzania kiweze kufikiwa. Naomba Serikali isiishie hapo, tumeanza vizuri hivyo ni vema mlango huu tukautumia ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo nitachangia maeneo mawili nikipata nafasi na eneo la tatu. Eneo la kwanza ambalo naomba nishauri ni kuhusiana na hifadhi ya jamii kwa ujumla wake. Kama tumeanza kutambua umuhimu wa afya za watu wetu ni vizuri sasa in a holistic manner tukatizana ustawi wa Watanzania kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo mfuko unasoma ni hifadhi ya jamii lakini ukienda kufuatilia ndani unakuta kwamba hiyo hifadhi ya jamii zaidi inawalenga watu ambao wameajiriwa Serikalini na zile sekta za kuajiriwa ambazo zinajulikana. Hata hivyo, sekta ya Watanzania walio wengi, zaidi ya 65% ambayo inaajiri wakulima, wavuvi na wafugaji huoni dirisha ambalo limewekwa ili baada ya kuwa wamefanyakazi nzuri ya kujenga uchumi katika taifa hili waweze kuhudumiwa. Kila mtu ni mzee mtarajiwa watu hawa tunawasaidiaje ili baada ya kwamba wamefanyakazi nzuri waweze kuishi maisha ambayo ni decent, ambayo kila mtu anatamani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunakuwa tuna-refer Biblia ambavyo siyo sahihi kwamba kwa mwanadamu ambaye amezaliwa na mwanamke miaka yake ya kuishi si mingi akiwa na nguvu 70 au 80 lakini mbona tukitizama wenzetu wanafika miaka 99 wao Biblia yao ikoje? Ukija kutizama kwa ujumla unakuta ni namna ambavyo maandalizi yanafanywa ili mtu huyu baada ya kwamba amefanyakazi kubwa ya kujenga uchumi aishi maisha ambayo ni decent. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunasingizia kwamba unajua kwa culture yetu sisi Waafrika isingependeza mtu akishakuwa mzee atunzwe sehemu ambayo siyo pale alipozaliwa. Hii dhana nadhani imepitwa na wakati. Sisi ni mashuhuda pale ambapo tunakuwa na wazazi wetu na sisi tuko kwenye shughuli zingine jinsi wanavyopata taabu. Ni vizuri ifike wakati muafaka hawa watu ambao wamefanya kazi nzuri na kwa bahati nzuri kuna makundi ambayo vipato vyao viko tofauti tofauti, kuna wakulima ambapo kuna misimu ambayo wanapata fedha wanaweza wakachangia kwa utaratibu ambao utakuwa umewekwa, wavuvi wanaweza wakachangia katika utaratibu ambao utakuwa umewekwa na wafugaji halikadhalika ili pale ambapo umri ukishafika pale anapohitaji kutunzwa awe na option yake kwamba katika kile ambacho amekuwa akichangia apate pesa au a-opt kwamba naomba niende katika maeneo ambayo yametunzwa maalum kwa ajili ya kutunza wazee. Maeneo hayo kutakuwa na madaktari na huduma zote ambazo ni muhimu ili wengine waonekane kwamba kazi waliyoifanya hawakupoteza juhudi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali watutafutie fomula itakuwa ni sahihi ili kuwasaidia Watanzania hawa wengine ambao hawako kwenye kada ya utumishi Serikalini ili nao wafaidike ili tupate Watanzania ambao wanaishi miaka 99. Kama huko kwingine inawezekana kwa nini sisi isiwezekane? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo naomba kuchangia kwa siku ya leo ni kuhusiana na maendeleo kutofautiana kati ya mkoa na mkoa na halmashauri na halmashauri. Yapo mengine ni kwa sababu ya kihistoria hatuna wa kumlaumu imetokea hivyo na maeneo mengine yana uchumi mzuri kutokana na rasilimali zinazopatikana katika maeneo hayo. Sasa wengine wamefanyaje? Ili Taifa kwa ujumla wake kila eneo katika nchi hii liwe ni sehemu salama na ya kuvutia kuishi ni vizuri tukaja na Development Equalization Fund ambayo wale ambao wanazalisha in excess na wale ambao watakuwa willing na mtu yoyote yule aweze kuchangia ili sasa kama Taifa tutizame maeneo ambayo yanahitaji kusaidiwa kutokana na mfuko huo wasaidiwe ili kila sehemu ya Tanzania iwe sehemu salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu ulivyo sasa hivi ukamchukua Mkurugenzi ambaye yuko kwenye Jiji ambalo lina vyanzo vingi vya mapato ataonekana anafanya vizuri sana lakini ukampeleka katika halmashauri ambavyo vyanzo vyake ni kidogo huyo huyo ambaye alikuwa anaonekana anafanya vizuri sana mtaishi kumfukuza kwa sababu inaonekana kwamba ha-perform. Lazima tuje na fomula ya kusaidia wale ambao wanahitaji kusaidiwa ili tunyanyuke kwa ujumla kama Taifa. Mwananchi ambaye anaishi Newala atamani kuendelea kuishi Newala kulikoni kutamani kwenda Dar es Salaam kwa sababu inaonekana iko vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niwe miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia katika bajeti ya Wizara hii ambayo ni Wizara muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri. Baada ya kumaliza kuwapongeza niendelee kuwapa pole, nawapa pole kwa sababu gani? Kilimo ni suala la kuwekeza kwa maana ya bajeti uone kwamba inaongezeka kwenda kwenye kilimo lakini kwa takwimu nilizonazo kwa mwaka 2018/2019, 0.5% ya bajeti ndiyo ilienda kwenye kilimo; mwaka 2019/2020 asilimia 0.63 pekee ndiyo ilienda kwenye kilimo; mwaka 2020/ 2021 ni asilimia 0.58 ya bajeti ndiyo ilienda kwenye kilimo na mwaka huu wa 2021/2022 ni asilimia 0.8 chini ya asilimia moja ndiyo inaenda kwenye kilimo. Tafsiri yake ni nini? Kama zaidi ya 65% ya Watanzania na 70% wakiwepo wanawake wanajishughulisha na shughuli za kilimo, lakini katika kutenga bajeti unaweka asilimia 0.8 tafsiri yake ni kwamba we are not serious. Kama tunataka kufanya transformation kuhakikisha kwamba Watanzania walio wengi wanaondoka katika lindi la umaskini ni kuweka fedha za kutosha kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu umefanya utaratibu mzuri naomba Waheshimiwa Wabunge katika hili tusimame pamoja. Kama tunataka yafanyike mapinduzi ya uhakika ni kuhakikisha kwamba Wizara ya Kilimo inaenda kuongezewa bajeti. Na katika utaratibu ambao umeuweka kwa makusudi hizi Wizara zingine pamoja na kwamba bajeti zao zimepita, tuungane Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba Wizara ya Kilimo inaenda kuongezewa pesa ili tuweze kufanya mapinduzi na kuwasaidia Watanzania. Kwa hiyo, haijalishi bajeti ipi imepita kwa sababu bajeti ya mwisho ni bajeti kuu na sisi kama Wabunge tuna uwezo kabisa wa kuhakikisha Wizara hii inaongezewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo linazidi kushangaza na kusikitisha, sisi Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikao mitano ambayo ni big five katika uzalishaji lakini kichekesho chake kinakujaje, katika ambao wapo miongoni mwa big five, ndiyo mkoa ambao unaongoza katika lindi la umaskini. Tafsiri yake ni kwamba hiki ambacho mwananchi anazalisha kinakosa thamani, unazalisha mahindi lakini kama huwezi kuyauza maana yake huna uwezo wa kwenda ku-transact na kuweza kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwa ujumla wake katika hali hii ambayo wananchi wapo kwenye lindi la umaskini na huku wamezalisha wanatizama hicho ambacho umetoa jasho na damu yao hakina thamani, Serikali ije na majibu. Wanaenda kuchukua hatua gani ya makusudi kuhakikisha kwamba wananchi hawa ambao wanafanyakazi kwa bidii lakini wanaendelea kuwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimuombe Mheshimiwa Waziri na timu yake, tumelima mahindi miaka nenda rudi lakini tunazidi kuwa maskini. Naomba Serikali itujie na mazao mbadala, sasa hivi Serikali tulipata kota kwa ajili ya kupeleka soya beans China lakini niambieni wapi soya inapatikana na sisi kwa Mkoa wa Rukwa ardhi hiyo inafaa kabisa kwa kilimo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni vizuri Waziri ukatujia na majibu, unaenda kusaidiaje ili tuachane na habari ya kilimo cha mahindi ambacho kinatupa umaskini twende kwenye mazao ya soya, tukalime ngano ili na sisi tuondoke katika kundi la maskini na hiyo itakuwa imetusaidia. Vinginevyo tutakuwa tunalima, tunafanya kazi lakini tija haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka ya nyuma kidogo nchi ya Zambia ilikuwa kila mwaka wanategemea tulishe sisi Watanzania tuwalishe Wazambia lakini leo imebadilika yield per acre Wazambia kwa mahindi wanazalisha gunia 35, sisi Watanzania gunia 8 au 10, hatuwezi kufika. Pamoja na kuzalisha hizo 8 na 10 hata soko mwananchi hana la uhakika. Kama tunakubaliana sisi sote kwamba zaidi ya asilimia 65 au 70 wakiwemo wanawake lazima Wizara hii kwanza tuhakikishe kwamba bajeti inaongezeka ambayo ita-reflect uhalisia. Hii bajeti ambayo inakuwa chini ya asilimia moja hakika tutakuwa hatuwezi kufanya transformation ambayo inatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa sababu naamini Wizara watakuja na majawabu ya uhakika badala ya majibu, naomba niunge mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa na mimi siku ya leo niwe miongoni mwa wachangiaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na changamoto ambazo zinajitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mchangiaji wa kwanza alivyoanza kuchangia kuhusiana na tatizo la tembo, nami ni miongoni mwa waathirika wakubwa sana katika Wilaya ya Kalambo imekuwa ni historia ambayo hatujui imetoka wapi kwa sababu tunaambiwa zaidi ya miaka 100 tembo walikuwa hawapo katika eneo letu la Kalambo, lakini kwa sasa hivi imekuwa kama ni mifugo ambayo inaongezeka kwa kasi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri analijua hili na nimekuwa nikiwasiliana naye na wananchi wanatuambia kwamba enzi za mkoloni walikuwepo Maafisa Wanyamapori ambao walikuwa stationed pale. Sasa hivi ninachoomba wahakikishe kwamba wanakuwepo ili kutoa utaalam, lakini pia kuwaswaga tembo hao ili wasiendelee kuharibu mazao ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo naomba kwa leo nichangie; wamechangia wachangiaji waliotangulia kuhusiana na circuit ku-promote upande wa Nyanda za Juu Kusini ikiwemo pamoja na Katavi lakini na Kalambo Falls. Kalambo Falls ndio maporomoko ya pili ya Afrika baada ya Victoria Falls; hili nalisema kwa mara nyingine nikiamini sasa hivi Serikali inaenda kuweka nguvu yake kubwa kufanya promotion katika maporomoko ya Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Scenery nzuri ipo upande wa Tanzania lakini wenzetu wa Zambia wamekuwa wakitangaza as if scenery nzuri ipo upande wa kwao. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri pamoja na watalaam wake na Katibu Mkuu yupo, akiwa TANAPA tuliomba kwamba sisi Halmashauri ya Kalambo hatuna uwezo wa kutangaza, tuliwaomba wachukue maporomoko ya Kalambo kuyatangaza, lakini nini ambacho kimetokea, TFS ambao wana Hifadhi ya Msitu wa Kalambo wamechukua pamoja na maporomoko ambayo hawana uwezo wa kutangaza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachoomba, TANAPA ndiyo wachukue maporomoko, ule msitu ubaki na TFS lakini isiwe TFS ndiyo wachukue na Maporomoko ya Kalambo kwa sababu hawana uwezo wa kutangaza. It’s high time kwamba tutangaze Kusini Nyanda za Juu ikiwemo pamoja na Maporomoko ya Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namsihi sana Mheshimiwa Waziri, najua ana changamoto ya kibajeti, lakini kwa namna ambayo tunaweza kuchachusha, utalii ni pamoja na kuhakikisha kwamba maeneo yale ambayo hayajatangazwa, yanatangazwa na yanakuwa kivutio, sio kila wakati iende kaskazini, kaskazini imeshakuwa saturated, it’s high time kwamba sasa hivi tutangaze kuelekea huko ambako kuna mambo mazuri sana kwa ujumla yakitangazwa Taifa letu litanufaika wakati tunaendelea na changamoto za huko kwingine ambako watu hawapendi tena kwa sababu tumekuwa tukizidiwa na wenzetu wa upande wa Kenya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afike, kila Waziri ambaye amehudumu katika Wizara hii akifika Kalambo anakuja na picha, ndio inakuwa kwenye budget speech yake. Akawaulize Mheshimiwa Maige, Profesa Maghembe, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla mpaka kuna point wakati anateremka aka-faint pale tunaita Kigwangalla Point na yeye aende, hakika hatojutia kwenda kuona Maporomoko ya Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huu, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi jioni hii ili nichangie mchango kidogo. Mimi ni Mjumbe kwenye Kamati ya Bajeti, nimepata fursa ya kuchangia mengi kuishauri Serikali, lakini kwa jioni ya leo naomba niongelee maeneo mawili.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea suala la TRA, kwanza naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote na Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake.

Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Wajumbe wengine ambao wamepata fursa ya kuchangia wakiomba TRA iwezeshwe kwa maana ya kuwa na watumishi wa kutosha. Tutakubaliana kwamba suala la kutoza kodi ni suala la kitaaluma, linahitaji mtu ambaye amebobea amesomea na yupo vizuri ili anayetozwa kodi awe comfortable kwamba natoa kodi katika mikono salama. Sasa kama tunataka kuongeza mapato ya kutosha ni vizuri tukahakikisha kwamba TRA inakuwa na watumishi wa kutosha wenye weledi ambao wamewezeshwa kibajeti ili wafanye kazi zao vile inavyotakiwa. Haiwezekani tukiwa tunataka ng’ombe atoe maziwa, lakini ng’ombe huyu tunasahau kumlisha. Ni wakati muafaka tuhakikishe kwamba TRA inakuwa na staff wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Benki kuu kwa maana BOT wamefanya kazi nzuri sana. Kila Mtanzania anajua jinsi ambavyo shilingi yetu imekuwa imara kwa kipindi kirefu. Kwa hiyo juhudi ambazo zimefanywa na BOT pamoja na Wizara ya Fedha katika kuhakikisha kwamba shilingi yetu ni imara ni jambo la kupongeza. Kuna baadhi ya jitihada ambazo zimefanyika zikaonekana kama vile zinaumiza, lakini malengo yake ni mazuri ilikuwa na uhimilivu katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunamaliza kwenye Kamati ya Wizara ya Kilimo, ulisema kwamba kama Bunge hili ili likumbukwe kama ambavyo Bunge la Kumi na Moja litakumbukwa kwa kufanya kazi nzuri kuhusiana na suala zima la Madini, Bunge la Kumi na Mbili lina wajibu wa kufanya mapinduzi katika suala zima la kilimo ambalo hakika linaajiri Watanzania wengi.

Mheshimiwa Spika, vile vile ukasema ni vizuri tukasubiri katika bajeti inayokuja, lakini nikawa nafikiria kwa sauti kidogo, kwamba hivi hapa tulipofika hakuna ambacho kinaweza kikafanyika ili fedha zikapatikana kwa ajili ya kwenda kufanya mapinduzi kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikasema nilishauri Bunge, kwa kupitia Benki kuu kwa maelekezo ya kisera, ukawa na incentive kwa mabenki ya biashara; mosi, kuhakikisha kwamba interest rate kwa wale wanaokwenda kukopa kwa ajili ya shughuli za kilimo zinashushwa kwa makusudi mazima ili watu wawe na appetite ya kwenda kukopa kwa ajili ya shughuli za kilimo. Pia ili mtu umkopeshe kwenye kilimo sio suala la mwaka mmoja, kwa hiyo ndani ya Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu waweke utaratibu ambao kutakuwa na appetite ya kukopesha hawa watu wanaokwenda kufanya shughuli za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakumbuka kwamba Wizara ya Kilimo wamekuja wakasema kwamba, sasa hivi Watanzania tuna quota ya kuuza soya beans China kwa miaka mitatu. Sasa kama tukaacha na hiki kipindi kikapita, maana yake tutakua tumebakia na mwaka mmoja. Wataalam wa Wizara ya Fedha na BOT waje na utaratibu ambao utahakikisha mabenki yaamue, kwa hili kwa dhati kabisa twende tukakopeshe watu ili wa-engage kwenye kilimo ukijua kwamba hakika zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wako kwenye kilimo. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Taasisi zake wachukue kama changamoto waifanyie kazi ndani ya muda mfupi ili msimu wa mvua tuanze kuona fedha zina-flow kwenda kwenye shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa leo nilisema niseme hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa Wajumbe wanaochangia Mapendekezo ya Mpango ambao unaenda kuandaliwa na Serikali. Naomba nianze kipekee kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kunijaalia afya njema ili na mimi niwe miongoni mwa hao ambao wamejaaliwa kuchangia leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wajumbe waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana ambayo anafanya katika kuleta maendeleo kwa ajili ya Watanzania. Nami ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti, nimepata fursa ya kuchangia na kwa kiasi kikubwa sana naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake mengi ambayo tulichangia wameyapokea na katika kuja na mpango hakika hata yale ambayo yalikuwa yamesahaulika naamini wataenda kuyaingiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nitachangia katika maeneo machache. Eneo la kwanza litakuwa Bandari, Reli ya TAZARA, Reli ya Kati na SGR kwa ujumla wake na muunganiko wa kiuchumi. Kamati yetu tulipata fursa ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam maboresho makubwa sana yamefanyika, imefanyika kazi kubwa sana ya uwekezaji ambao baada ya muda mfupi tunatarajia kama Taifa tutaanza kupata matunda yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mahojiano ambayo tulifanya na Wachumi wakasema Tanzania kama tunataka kujihakikishia uchumi wa uhakika na biashara ya bandari iweze kufanya kazi ya uhakika ni mizigo ambayo inasafirishwa kwenda Kongo ya DRC na wala siyo Zambia na wala siyo Uganda, effort ambazo zinatumia kutafuta mzigo wa kwenda Uganda nusu yake inatosha kuweza ku-explore na kupata mzigo mkubwa wa kwenda Kongo DRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi kubwa nzuri sana ambayo inafanywa katika ujenzi wa reli Standard Gauge kwa maana ya SGR. Ni matumaini yetu sisi Watanzania kwamba reli hii hatujengi kwa ajili ya kusafirisha abiria, siamini hilo. Ili reli hii iwe na manufaa makubwa ni pale ambapo tutasafirisha shehena kubwa ya mzigo na mzigo ambao tunatarajia kupata kwenda bandari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilimsikia Mheshimiwa Naibu Waziri akiongelea habari ya Reli ya TAZARA na ubovu wake na manufaa ambayo tunategemea kupata kama nchi. Naomba niieleze Serikali na hili waliandike, kama tunatarajia kwamba mkataba huu utarekebishwa eti na Wazambia wana interest juu ya ufanyaji kazi bora wa TAZARA tunapoteza wakati na hili wanalifanya kwa makusudi. Naomba niikumbushe Serikali, hivi karibuni kuna malori karibu 300 ya Watanzania ambayo yalizuiliwa Zambia takribani mwezi mmoja mpaka miezi mitatu, hii wanafanya kwa makusudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niikumbushe Serikali ili katika mipango yao waweze kuweka mambo haya; mwaka juzi tulipata soko kama nchi wakati tulizalisha mahindi mengi sana kupeleka Kongo, lakini tulishindwa kupeleka kwa sababu ya kodi ambazo ziliwekwa na Wazambia, ikaonekana kwamba huwezi ukatoa gunia la mahindi Rukwa ukalifikisha Kongo likakulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najenga hoja hiyo, naomba niwaambie Serikali, ukitaka kufanya biashara ya uhakika kama Taifa na kuna matunda ambayo yako, hatuhitaji hata kutumia juhudi kubwa ya low-hanging fruits twende tukayachume haya matunda. Ukienda border ya Tunduma ambayo ndiyo border iliyo busy kuliko zote, mzigo ambao unatoka bandarini hauendi Kongo ya Moba wala Mlilo, unaenda Kongo ya Lubumbashi huko ndiko mizigo inakoenda. Kwa hiyo naomba katika mipango Serikali izingatie yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna border nne za kuweza kwenda Kongo; kuna Kongo kwa kupitia Kasesha border ambayo iko Jimboni kwangu, unapita Zambia kilometa 871 ndiyo unafika Kongo la Lubumbashi. Ukitaka kupita Kigoma, unaenda Moba kwenda mpaka Lubumbashi ni kilometa 750. Ukipita Tunduma ambayo ndiyo route ambayo inatumika zaidi ni kilometa 1,088.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa njia iliyokuwa fupi kuliko zote na naomba niipongeze Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana katika kuboresha bandari ikiwa ni pamoja na Bandari ya Kasanga na kwa bahati nzuri sana, tunavyoongea leo hii lami imefika mpaka Bandari ya Kasanga na katika bandari ya ambazo ni natural port ni pamoja na Kasanga ndiyo maana Wajerumani waliitaka Bandari ya Kasanga iweze kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini ambacho kinatakiwa kifanyike? Unajua katika kazi kubwa ambayo tunafanya ya kujenga reli ambayo itaanza kubeba mizigo, si suala la muda mfupi, itachukua muda mrefu kwa sababu heavy investment inatakiwa. Niiombe Serikali ukivuka kutoka Kasanga kwenda upande wa pili ni kilometa 480 tu ushafika Lubumbashi. Kwa hiyo kwa wale ambao walisoma hesabu kwa critical path analysis ndiyo shortest route, niiombe Serikali upande wa kule barabara ipo ambayo inatoka Moba kwenda Lubumbashi, kuna vipande vichache sana ambavyo vinahitaji kumaliziwa ili tutumie njia hii, tutakuwa tunapeleka mzigo Kongo bila kupita Zambia bila kukutana na vipingamizi ambavyo tumekuwa tukivipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, tuna mahusiano mazuri sana na Serikali ya Kongo, hiki kipande kifupi kwa sababu siyo kwamba kilometa 480 zote hazina barabara, barabara ipo ni maeneo machache sana haiwezi kuzidi kilometa 100. Tuanze kuvuna matunda haya ambayo hatuhitaji kutumia jitihada kubwa. Naamini kwa sababu Mheshimiwa Waziri anasikia, katika mpango ambao utakuja na bajeti ianze, kwanza ni bajeti ya maongezi tu, kinachotakiwa ni sisi tuwe na kivuko kutoka Kasanga kwenda upande wa pili ambacho kitaruhusu malori yapakiwe ndani. Ukifika kule ni barabara ya vumbi na kama kuna sehemu ambayo tutaweza kuwa na barabara ambayo PPP itafanya kazi ni kwa kipande hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuhitaji pesa nyingi, ni pesa ambayo ipo, hizi barrier zote ambazo tumekuwa tukikutana nazo za kiuchumi itakuwa ndiyo mwisho wake, tukitarajia kwamba eti tuna mahusiano mazuri na wenzetu wa Zambia wataturuhusu, tutachelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo na nimemwona Mheshimiwa Waziri akitikisa kichwa, naamini katika mpango ambao utakuja tutaliona hili likionekana vividly ili tuanze kuchukua hayo matunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami jioni ya leo niweze kuchangia. Naomba nipongeze taarifa zote za Waheshimiwa Wenyeviti, ni taarifa njema kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti, nimeshiriki katika kutoa michango na kwa siku ya leo nitaomba nitoe michango katika eneo moja tu. Ni ukweli usiopingika tumekuwa tukisema Bunge la Kumi na Mbili ni lazima liache legacy na litaacha legacy kwa kuhakikisha kwamba Serikali inasukumwa kwenda kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika pato la Taifa trilioni 163.88 sekta ya kilimo imekuwa ikichangia kwa trilioni 44.8 ambayo ni sawa na asilimia 26.9 ya pato la Taifa. Ni ukweli usiopingika kwamba Watanzania zaidi ya asilimia 66.3 nguvu yao yote iko kwenye kilimo. Kipekee naomba nipongeze Ubalozi wa Tanzania nchini China kwa kazi kubwa nzuri sana ambayo wamefanya katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na mkataba kati ya Tanzania na China wa kuuza zao la soya. Pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Balozi Kairuki, kazi njema sana anastahili kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi ya Tanzania mikoa ambayo zao la soya linastawi ni pamoja na Mikoa ya Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Tanga na Kagera hasa Karagwe. Matumizi ya zao la soya ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, soya inatoa product nzuri sana ya maziwa ya unga pia inatoa mafuta mazuri sana first class, pia inatoa zao wanaita soya nyama kwa wale vegetarian ambao hawataki kutumia nyama, pia inatoa chakula kizuri sana kwa ajili ya mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni kwamba kwa ku-concentrate katika zao hili ambalo tayari tuna soko la uhakika nchini China, tuna soko la uhakika India na Ulaya, ni wakati muafaka wa kuhakikisha kwamba Serikali yetu inaenda kuwekeza kwenye kilimo kwa sababu manufaa ya kulima zao hili; moja, katika eneo ambalo umelima soya kama ambavyo ipo kwenye mazao ya mikunde ni kwamba inarutubisha ardhi na hivyo kupunguza matumizi ya mbolea za kemikali kwa asilimia hamsini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, majirani zetu siku ile Spika alisema siyo vizuri kuzitaja nchi jirani lakini katika mifano mizuri naomba mniruhusu niseme. Pamoja na kwamba Tanzania ndiyo ambao tuna mkataba na China na tumefanya kazi nzuri ya kusafirisha China, lakini ni ukweli usiopingika kwamba soya nyingi imekuwa ikipatikana kutoka nchi ya Zambia na Malawi, wakati Tanzania ndiyo tuna mkataba na China kuuza zao hili. Ifike wakati Serikali kuhakikisha kwamba inawekeza katika kupata mbegu bora ili hiyo mikoa ambayo nimeitaja ambayo zao hili linastawi na uhitaji kwa Mataifa ni mkubwa sana tuhakikishe kwamba zao hili linakuwepo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba tumekuwa na tatizo kubwa sana la mafuta ya kula, tuki-concentrate katika zao moja tu la alizeti tukaachia soya tutakuwa hatufanyi vizuri. Naiomba Serikali na ni wakati muafaka, kwa fursa hii na mkataba ambao tumeingia na nchi ya China kwa miaka mitatu tuhakikishe kwamba dola nyingi zinaingia Tanzania kwa sababu tunauza tunapata forex, tunakuwa na soko la uhakika badala ya sisi kuendelea kuhangaika na zao la mahindi. Kama ambavyo nimesema inasaidia sana katika kurutubisha ardhi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba Serikali kuhakikisha kwamba inakuwepo mbegu bora ambayo wenzetu wanazo. Kwa mfano, kwa nchi kama Zambia wana aina saba za mbegu, wana mbegu aina ya spike, wanayo mbegu aina ya safari, wanayo mbegu aina ya dina, Tanzania hatuna mbegu hata moja. Naomba kipekee nipongeze Wabunge ambao wamekuwa vinara akiwepo Mheshimiwa Msongozi amehangaika sana kutafuta mbegu ili kuweza ku- supply katika maeneo yake na Wabunge wengi ambao walikuwa na nia ya kuweza kusaidia maeneo yao, lakini kwa sababu hatuna mbegu Tanzania na tumekuwa tukikumbana na vikwazo vingi tungeweza kusaidia Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ili na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji jioni ya leo. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, kwa hiyo mchango uliotolewa na kamati mimi ni miongoni mwa waliochangia. Hata hivyo kwa jioni ya leo nitaomba nichangie maeneo machache kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kujikita zaidi katika eneo linalohusu gharama za usafirishaji na jinsi ambavyo zinaongeza gharama kubwa katika ufanyaji wa biashara katika nchi yetu. Kipindi cha mwaka jana tukiwa hapa Bungeni sisi Waheshimiwa Wabunge tulipata fursa ya kugawiwa kitabu ambacho kimeandikwa na Mtanzania mwenzetu, Ndugu Erastus Mtui chenye jina la “Poverty Within Not on The Skin”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge tupate fursa ya kukipitia kitabu hiki, kina elimu ya kutosha na hasa kwa watunga sera ni kitabu cha lazima cha kukisoma. Nilikuta katika ambao wame-recommend kitabu hiki kisomwe ni pamoja na Prof. Kitila Mkumbo. Hakika kitabu hiki kinatoa elimu ya kutosha na kinatufaa Watanzania. Tanzania tuna watu wazuri ambao ni vizuri tukaunga mkono kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika ibara ya sita ya kitabu hiki unakutana na maongezi kati ya bilionea Aliko Dangote pamoja na Mo Ibrahim wakiwa wanaeleza jinsi ambavyo gharama ilivyokuwa kubwa kuchukua mzigo kutoka mpaka mmoja ndani ya Afrika kwenda upande wa pili wa Afrika. Ni wakati muafaka mpango wetu ujielekeze ni namna gani tunaenda kuboresha ufanyaji biashara. Maana ni ukweli usiopingika, ukishaweka gharama kubwa katika usafirishaji tafsiri yake ni kwamba gharama za mlaji lazima ziongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ambayo napenda niongelee kwa kirefu zaidi ni kuhusiana na mpaka wetu wa Tunduma. Wako Wabunge waliotangulia kuchangia, wanaeleza jinsi ambavyo kuna ugumu wa mpaka ule kufanya kazi vile ambavyo inatakiwa. Ni ukweli usiopingika inafika kipindi ambapo malori yanakaa mpaka siku nne mpaka siku tano bila kuvusha mzigo. Tafsiri yake ni kwamba tunaharibu uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee niipongeze Serikali imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa barabara. Ni wakati muafaka sasa tufungue corridor ya kupitia Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwenye lori anataka kusafiri kutoka Mwanza kwa kwenda mpaka Tunduma anaenda kilometa 1,400, mpaka kwenda kufika mpaka wa Tunduma na Nakonde; lakini huyohuyo aliyekuwa na mzigo kutoka Mwanza akipita Tabora – Sikonge – Mpanda mpaka kufika Sumbawanga na kufika Kalambo, Kasesha Border, ni kilometa 1,000 tu; maana yake anaokoa zaidi ya kilometa 400, kiuchumi tunaharibu uchumi kwa kupita umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama kuna mtu ambaye anasafirisha mzigo kutoka mpakani mwa Tanzania na Uganda kwa maana ya Mutukula mpaka kwenda kufika Tunduma ni kilometa 1,700; lakini akapita short cut, akapita Tabora – Mpanda – Sumbawanga na mpaka kufika Kalambo ni kilometa 1,080 tofauti ya kilometa 620. Kama hiyo haitoshi, gari limefika hapo likiwa na shehena ya mzigo, aidha inaenda upande wa pili au inakuja upande wa kwetu sisi, lori likikaa siku zaidi ya tatu mpaka siku nne ni gharama kubwa kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, katika mipango ya kuhakikisha kwamba, tunaboresha ufanyaji biashara na kupunguza gharama katika ufanyaji biashara ni kazi ndogo tu, mawasiliano kati ya Serikali yetu ya Tanzania ambayo naamini tuna mahusiano mazuri na Serikali upande wa pili wa Zambia, kufanya mpaka wa Kasesha ufanye kazi saa 24 kama ilivyo Tunduma. Tafsiri yake ni kwamba, badala ya malori kukaa muda mrefu Tunduma yataka mengine yataenda kupita Kasesha, na hivyo kufanya mzunguko wa kibiashara kuwa mkubwa. Ni kama ambavyo mwanzo kulikuwa na hofu kwamba kukiwa na Kasimuro Border ikiwa inafanya kazi itapunguza biashara Tunduma, lakini ukweli ni kwamba, frequency za kusafiri zitakuwa nyingi na kibiashara hakika uchumi utachehemka na itasaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa haina maana kujenga barabara za lami kwenda Tabora, Sikonge, kama barabara hizi zitakuwa unasubiri malori, ulione lori moja baada ya wiki. Na kimsingi naomba nipongeze wanaoenda Kigoma na Burundi wameanza kutumia hii route. Sasa ni wakati muafaka kwa Serikali kutoa hamasa; na hii itapunguza hata uharibu wa barabara ya kwenda Tunduma kwa hiyo, hata hiyo itakayokuwa inajengwa itakaa muda mrefu, tutahudumia magari mengi, shehena itakuwa kubwa na gharama ya ufanyaji biashara itakuwa ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kwamba, usafirishaji wa mizigo kwa nchi za Afrika Mashariki ni asilimia 30 gharama zaidi ukilinganisha na nchi za Kusini mwa Asia. Ukilinganisha na Marekani gharama zetu ziko kubwa zaidi kwa asilimia 60 mpaka 70. Sasa kwa vyovyote vile mlaji wa mwisho ndiye anaumia. Ni wakati muafaka mpango huu ukatafsiri kwa vitendo maana hakuna uwekezaji mkubwa ambao unahitajika, ni suala la kuhakikisha tu kwamba tunafungua hiyo corridor na inaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika muswada ulioletwa hapa Bungeni. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wote walioshiriki katika uandaaji wa muswada huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati najaribu kupitia taarifa ya Kamati ya sekta husika, kimsingi wameridhia pamoja na mapendekezo machache sana ukizingatia kwamba Muswada huu umefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa ndiyo maana naendelea kuwapongeza, hongereni sana kwa Muswada mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika maeneo machache kama ifuatavyo na la kwanza, ni ukweli usiopingika kuhusu umuhimu wa maabara ya Mkemia Mkuu lakini kwa kipindi kirefu sana kulikuwa na ufinyu mkubwa sana wa kibajeti kiasi kwamba zile kazi ambazo walitakiwa kuzifanya kwa ufanisi hawakuweza kuzifanya. Kwa kuletwa kwa Muswada huu na kuwa na subvote yake ambayo itasomwa kupitia Wizara husika, naamini Idara hii itatengewa pesa za kibajeti za kutosha. Tafsiri ya bajeti ni kwamba unaipa uwezo mkubwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuweza kutimiza wajibu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Ofisi hii ilikuwa na ufinyu mkubwa sana wa bajeti. Taarifa zinaonesha kwamba kuna kipindi walikuwa na uwezo wa kuwa na mapato ya shilingi bilioni mbili. Naomba niipongeze Wizara kwa kushirikiana na Mkemia Mkuu wa Serikali wamepandisha kiwango cha mapato kutoka shilingi bilioni mbili mpaka kufika shilingi bilioni 10. Ukitaja shilingi bilioni 10 inaweza ikaonekana kama ni pesa nyingi lakini ukilinganisha na majukumu yake na hasa kutokana na kuongezeka kwa kesi za kijinai ambazo zinahitaji uchunguzi ufanyike ili kesi ambazo zimerundikana ziweze kupatiwa ushahidi kiasi hiki cha pesa hakitoshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote ni mashuhuda kwamba wakati polisi wamekuwa wakikamata hayo yanayoitwa madawa ya kulevya lazima taarifa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ipatikane ambayo inathibitisha kwamba haya kweli ni dawa za kulevya au sivyo. Nitaomba niunganishe na wachangiaji wengine ambao wanasema kwamba ni vizuri kazi hii ikaachiwa polisi, mimi nasema hapana. Nasema hapana kwa sababu gani?
Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa mashuhuda tukipata taarifa kwamba kuna watu ambao wanabambikiziwa kesi kutokana na baadhi ya polisi kutokuwa waaminifu sasa kama tutampa na kazi yeye ndiyo a-prove kwamba sampuli hii ni madawa ya kulevya au la maana yake tunataka akamate yeye mwenyewe, afanye uchunguzi yeye mwenyewe, akatoe ushahidi yeye mwenyewe jambo hili halikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi itasaidia kwamba hata pale ambapo mahakamani unapelekwa ushahidi kutoka kwenye chombo ambacho ni independent ushahidi ule utaaminika na kila mtu atajua kwamba ametendewa haki. Sikubaliani hata kidogo pamoja na polisi kuwa na kitengo chao cha forensic, lakini wafanye kazi zile ambazo zitawasaidia katika kufanya uchunguzi wao ili kubaini matukio lakini siyo kupata uhakika kwamba ushahidi unaopelekwa mahakamani wao wawe ndiyo wameutengeneza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni mashuhuda kuna kipindi tuliambiwa zimekamatwa dawa za kulevya mara unaambiwa kwamba ilikuwa ni unga wa muhogo, sijui unga wa mahidi. Sasa tukienda kwa utaratibu huu sidhani kwamba tutakuwa tunatenda haki. Kwa kukitengea kitengo hiki bajeti ya kutosha tuna imani kabisa Ofisi za Kikanda zitaimarishwa na uchunguzi ambao unafanyika majibu yake yatapatikana kwa kipindi muafaka na hivyo huu mlundikano wa sampuli nyingi ambazo lazima zipelekwe Dar es Salaam itakuwa imepungua kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema kwamba muswada huu umetendewa haki na Kamati ya Kisekta niishie kwa kutoa huo mchango mdogo na kuunga mkono hoja. Nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nami kupata nafasi jioni ya leo ili niweze kuchangia machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi leo dakika tano ni nyingi, kwa sababu karibu yote ambayo tulichangia kama Kamati ya Bajeti Serikali imezingatia naipongeza sana. Ni vizuri tukakumbushana kwa sababu inawezekana wengine ni wapya kidogo, pia ni vizuri hata ukarejea msingi mpaka tunafika hapa hali ilikuwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama katika vyanzo vya mapato kwa maana ya vile vyanzo vya kodi na visivyo vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi vimekuwa vikikusanya kwa kiasi kidogo sana na Wabunge tumekuwa tukilalamika kwamba chanzo hiki hakifanyi vizuri, ndiyo maana tutakubaliana kwamba namna nzuri ni kuhakikisha kwamba TRA inaenda kukusanya pamoja na hiyo property tax ili tuje tuwapime katika performance. Kwa hiyo, nia ni njema naomba wenzetu siyo vizuri kupotosha katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niboreshe baadhi ya maeneo machache sana, ukianzia na nia njema ambayo unaiona Serikalini kwamba inavutia uwekezaji wa ndani ni jambo jema, lakini naomba niboreshe kuhusiana na suala zima la mazao ambayo yanazalishwa nchini na yakatumika nchini ili kuongeza thamani kuwe na tofauti katika ushuru ambao unatozwa ukilinganisha na mazao ambayo yanatoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema hivyo nalenga bia ambayo inazalishwa kwa kutumia barley ambayo inalimwa Tanzania, kimea kikatengenezwa Tanzania, kuwe na tofauti na ile barley ambayo inazalishwa kutoka nchi za nje ikaleta Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? ukiongea na TBL wana nia njema kabisa ya kuhakikisha kwamba wanafanya expansion katika uzalishaji na wana nia ya kuanzisha kiwanda kipya pale Iringa na tayari wameshafanya utafiti kwa kuwahusisha wananchi wa Njombe, Mbeya pamoja na Iringa na wameshafanya test kuonesha jinsi ambavyo udongo ule unaweza ukalima barley tukaacha kuagiza kutoka nje, tukazalisha hapa nchini, tukaongeza ajira kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanachoomba siyo kikubwa wanasema tunataka kuwe na tofauti ili tuvutiwe kuzalisha ndani, tukaongeza ajira kuwe na tofauti na kile ambacho kinaagizwa kutoka nje. Ukisoma katika hotuba pamoja na Muswada ambao Mheshimiwa Waziri ameleta hii hali njema tunaiona jinsi ambavyo zabibu ambayo itatumika kusindika mvinyo ambao unazalishwa Dodoma, treatment yake na ule mvinyo ambao unazalishwa kwa kuagizwa kutoka nje kuna tofauti. Kwa hiyo, Serikali wakalitazame waone namna ambavyo tutaweza kuwasaidia wananchi wetu wakazalisha barley wakaongeza ajira na kuongeza kipato kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kuboresha kidogo ni kuhusiana na uwekezaji jinsi ambavyo tunavutia, ni jambo jema. Viwanda vinajengwa vingi, lakini hebu tuulizane, viwanda vingi vinajengwa wapi na kwa nini vinajengwa maeneo fulani? Itakuwa vizuri Mheshimiwa Waziri wakati anafikiria katika siku za usoni, kuwe na kivutio maalum ili Mwekezaji ambaye alitaka ajenge kiwanda Dar es Salaam aseme badala ya kujenga Dar es Salaam naenda kujenga Kigoma kwa sababu kuna kivutio A, B, C, D. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo itasaidia badala ya viwanda kurundikana maeneo fulani, ni vizuri tukawa na maendeleo kwa Mikoa yote, ili vijana wetu wasije wakalazimika kukimbilia baadhi tu ya maeneo kwa sababu wawekezaji wana-concentrate eneo ambalo tayari miundombinu ipo. Kwa hiyo, namna pekee ya kuweza kuvutia ni kuhakikisha kwamba maeneo ambayo hayajaendelea na hayana vivutio vingine, basi vivutio vya kodi ndivyo ambavyo vinaweza vikawasukuma hawa Wawekezaji wakaenda kufungua viwanda katka maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusiana na asilimia 15 ya industrial sugar na hasa ambayo mara nyingi inatumika katika kuzalisha vinywaji baridi. Nia ya Serikali ni njema ya kuhakikisha kwamba hakuna abuse, kwamba sukari ambayo nia yake ni kutumika kwa ajili ya kuzalisha vinywaji baridi isije ikaingia mitaani ikauzwa kama sukari ya kawaida…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru kwa fursa ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania kwa mwaka 2018. Nina kila sababu ya kuishukuru Wizara kwa kuleta muswada huu ambao kimsingi umechelewa. Muswada huu ulitakiwa uwe umefika mapema. Ziko sababu za wazi kabisa kwa nini nasema muswada huu umechelewa katika kuletwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika composition ya wafanyakazi walio wengi Tanzania ni walimu. Kwa wingi wao huu walikuwa wanahitaji wawe na chombo ambacho kitawasemea, kita-regulate na kuhakikisha kwamba kazi ya ualimu inarudi hadhi yake kama ambavyo ilikuwa siku za nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna kazi ambazo zilikuwa zinaheshimika sana ilikuwa ni pamoja na kazi ya ualimu. Sasa hapa katikati imefika mahali ambapo kama vile mtu akikosa kazi ya kufanya, kazi ya mwisho ya kukimbilia ni ualimu. Sasa kwa muswada huu ambao naamini Bunge lako tukufu litaenda kupitisha na kuwa sheria, maana yake hadhi ya walimu Tanzania imeanza kurudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna michango ambayo imetolewa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakiwa wanataka kuoanisha suala la kuletwa kwa muswada huu na madai ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote ni mashuhuda jinsi ambavyo Serikali imekuwa ikihakikisha kwamba madai ya walimu yale yote ambayo yamehakikiwa yanalipwa. Kwa hiyo, hatuwezi tukasema kwamba eti kwa sababu walimu wana madai yao ndiyo tusianzishe chombo ambacho kitakuwa kinawasimamia na kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe ni shuhuda, katika professions nyingi ambazo zinaheshimiwa ni zile ambazo zina Bodi zake ambazo zina-regulate. Ukienda kwa upande wa sheria, kiko chombo ambacho kinaweka pamoja learned brothers and sisters na wamekuwa na taratibu namna ya kuweza kumtambua mwanasheria. Kuna sheria ambazo wanawekeana taratibu na huwa wanafanya kukutana kila mwaka wakijadili mambo yao. Naamini hii itakuwa ni fursa nzuri sana kwa walimu na wao kuweza ku- adress mambo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, utakuta hata kwa mfano Bodi ya Wahandisi ipo na sasa hivi wako Dar es Salaam wakifanya mkutano wao wa mwaka wakiadhimisha miaka 50 tangu wameanzisha. Kwa hiyo, suala la kuwepo kwa Bodi ya Walimu ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna madai kwamba tungeanza kuangalia habari ya miundombinu. Wewe na Waheshimiwa Wabunge wote ni mashuhuda. Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikihakikisha kwamba miundombinu inaendelezwa, inajengwa na vyumba vya madarasa vinaongezwa. Suala zima la nyumba za Walimu nalo linawekewa uzito unaostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, hivi karibuni tulishuhudia suala la kugawa pikipiki kwa kata zote Tanzania. Tafsiri yake ni nini? Tunataka hawa ambao wamegawiwa hivi vyombo vya usafiri iwarahisishie ili wakati tunadhibiti ubora wa elimu kusiwe na kisingizio na pale inapatikana posho ya shilingi 200,000 kwa ajili ya hivi vyombo kuhakikisha kwamba watu wetu kwa maana ya Waratibu Elimu wanapata fursa ya kwenda kuhakikisha kwamba elimu yetu inakuwa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna fursa ambayo Walimu wamekuwa wakikosa ni pale ambapo inatokea hata fursa ya kwenda kufundisha lugha yetu ya Kiswahili, Walimu wetu wako bora kabisa katika suala zima la kufundisha lugha ya Kiswahili. Ukilinganisha na nchi jirani kwa sababu hakuna chombo ambacho kinatoa udhibiti na kuweza ku-regulate na kiko specific kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mwalimu ambaye ameingia huko, isiwe kama vile ambavyo amekosa kazi zote, mtu kamaliza form six sasa anakusanya darasa anaanza kufundisha. Kwa hiyo, ni ngumu sana kuweza kuwa na professionalism na hili ndiyo kubwa zaidi kuliko mambo mengine yote. Tukiwa na hao watu ambao wanatambulika na professionals zao ni rahisi sasa hata kushughulikia matatizo yao na kuboresha hali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la capacity building, imesemwa hapa kwamba kwanza tuwajengee uwezo. Kwa Serikali ya Awamu ya Tano suala la kujengea walimu uwezo limekuwa ni kipaumbele na kwa kadri bajeti inavyoruhusu tutaendelea kuhakikisha kwamba tunawajengea uwezo ili walimu wetu wafanye kazi yao kwa weledi na kuhakikisha kwamba elimu bora tunayoitarajia kwa watoto wetu ndiyo inayotolewa. Hili linawezekana pale tu ambapo wao wenyewe kwa kuwa na Bodi ambayo na wao watashiriki katika kuhakikisha kwamba taratibu na kanuni ambazo zitaweza ku-identify wao kama walimu, itakuwa ni rahisi hata masuala ya kinidhamu wao wenyewe kuweza kuji- regulate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kabisa kwamba chombo hiki walipigana sana akina Mheshimiwa Mama Sitta kilitakiwa kiwe kimeshaanzishwa muda mrefu.


Ni matarajio kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao tuna nia njema na Serikali yetu na elimu yetu ambayo tunataka iweze kushindana, ni vizuri tukahakikisha kwamba tuna- support ili chombo hiki kiweze kuanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba nikushukuru kwa fursa. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa uliyonipatia ili niweze kuchangia hoja yetu ambayo ililetwa mezani kwako leo na ikapata wachangiaji wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha sisi sote kushiriki tukiwa na afya njema. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu naomba kipekee nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa busara ambao Watanzania walisubiri kwa muda mrefu na sasa ndoto ambayo ilikuwa ikiotwa na Watanzania ya Makao Makuu kuwa Dodoma imetimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Kamati yetu chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Jasson Rweikiza ambao kiuhakika wameutendea haki Muswada huu. Muswada ulikuwa unaonekana kama ni mfupi sana lakini umesheheni mambo mazito kweli kweli; na Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuchangia, hakuna mtu ambaye alitarajia kwamba wangeweza kuchangia kwa kiasi hiki kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ambalo tunakubaliana sote, hakuna hata Mbunge mmoja ambaye hakubaliani na Muswada ambao umeletwa na ndiyo maana hapo kwako huna hata addendum moja ambayo inapingana na hoja ambayo imeletwa na Wizara yetu. Naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatofautiana tu katika style ya kusema, lakini nia njema unaiona. Unaweza ukazunguka lakini mwisho wengine wanashindwa kuunga mkono, lakini kimoyomoyo wanakuwa wameunga mkono. Kama wasingeunga mkono ungeona addendum zipo hapo. Kwa hiyo, kipekee naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipitie baadhi ya maeneo ambayo yamechangiwa, tukianzia na Mheshimiwa Rweikiza ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati yetu ambayo inafanya kazi nzuri kabisa. Katika maeneo ambayo walipata wadau kuchangia, wadau waliomba kama inawezekana Muswada huu ukaunganisha na sheria nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupita kwa Muswada huu kuwa sheria, inafungua sheria nyingine ambazo zitakuja zitungwe ili kuwezesha Makao Makuu i-operate kwa namna ambavyo tunatarajia. Isingekuwa rahisi bila kuanza na Muswada huu kupita kuwa sheria ili kutangaza Dodoma kama Makao Makuu ya nchi rasmi ili vyovyote vile sheria nyingine zije kutungwa katika namna bora ya kuendesha Makao Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa hatutendi haki tukidhani kwamba kwa operation jinsi ilivyo, kwa muundo wa sasa, Makao Makuu yetu ambayo tunatamani yalingane na hadhi ya nchi yetu ya Tanzania, yanaweza kuwa vizuri kwa sheria hizi zilivyo. Kwa hiyo, ni vizuri tukubaliane kwamba tutavuka daraja tukifika wakati huo. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Miswada italetwa ili tuwe na namna bora ya kuenenda na kuhakikisha kwamba Jiji letu la Dodoma linakuwa katika hali ambayo sisi sote tunatamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ambayo ililetwa na Mheshimiwa Japhary ambaye ni Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara hii, akasema kwamba vikao vya kisheria havikufuatwa. Naomba nimtoe hofu kwamba hakuna hata moja ambalo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya bila kuwa cautious kuhakikisha kwamba taratibu na sheria zote zinafuatwa, vikao vyote vya kisheria vimefuatwa na mpaka kufikia hapa tupo salama salmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ally Saleh amesema kwamba Zanzibar haikuhusishwa. Naomba nimtoe wasiwasi, naamini kabisa alipo pale ni sauti ya Wazanzibari kwa sababu tusingeweza kuwajaza Wazanzibari wote wakaingia humu. Yeye ni mwakilishi na amekuwa akifanya kazi nzuri pamoja Wazanzibar wengine ambao wanasema kwa upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tukubaliane sisi sote kwamba ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo lina uwakilishi kutoka pande zote mbili na kwa namna ambavyo tunaenda vizuri, leo hii asubuhi Mheshimiwa Kakunda, Naibu Waziri, ameondoka kwenda Zanzibar kwenda kushirikisha Baraza la Mapinduzi Zanzibar jinsi ambavyo tunataka mambo haya yaende vizuri tukiwa tunashirikisha pande zote. Hii ni kwa sababu nia ya dhati njema iko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema ni kwamba ili tuwe na uelewa wa kufanana isije ikaonekana kwamba wengine hawalielewi hili ndiyo maana mwenzangu ameondoka kwenda Zanzibar kwenda kujadiliana na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuhusiana na tamko hili la uanzishwaji rasmi wa Makao Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Saleh amesema kwamba Watanzania hawajawahi kuhusishwa. Naomba nimkumbushe kwamba mwaka 1973 jumla ya matawi yaliyoulizwa yalikuwa 1,559 juu ya Makao Makuu ya nchi
kuhamia Dodoma. Jumla ya matawi 842 yalisema Makao Makuu yaendelee kubaki Dar es Salaam na jumla ya matawi 1,017 yalisema Makao Makuu ya nchi yahamie Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikiwasikiliza kwa ustaarabu kabisa. Ni vizuri nimalize, dakika kumi siyo nyingi sana Mheshimiwa Halima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Msigwa amesema kwamba tumekurupuka, vipaumbele ni vingi, lakini naomba nimhakikishie kwamba katika vipaumbele na sisi Wana-CCM ambao tulienda kujinadi kwa Wana-CCM na tukapewa ridhaa ni pamoja na kuweka bayana kwamba tunaenda kuhamia Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni jambo ambalo lilikuwa katika mpango wetu mahsusi siyo kwamba tumeamka nalo jana. Wakati tunaenda kuomba kura kwa wananchi 2015 tulilisema bayana na tukaaminiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wajumbe ambao wamesema kwamba master plan iliyokuwa imepangwa kwa wakati ule itakuwa imepitwa na wakati. Ni kweli, ndiyo maana ipo haja ya kuipitia kwa kadri ya wakati na sisi tupo flexible kuhakikisha kwamba Jiji letu la Dodoma linakuja kuakisi sura hasa ya Tanzania ambayo tunaitaka, Tanzania ambayo tulikuwa tunaiota, sasa tunakwenda kutekeleza. Maana sura ya kwanza ya Taifa lolote ni Makao Makuu ya Nchi na Dodoma ndipo ambapo tunakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa baada ya Muswada huu kuwa sheria, hakika tutakuwa tunahitaji bajeti special ya kuhakikisha kwamba Dodoma inajengeka ili iakisi taswira ya Tanzania ambayo tunaitamani. Maana siyo kwamba kila tukienda nchi za wenzetu, ukienda Afrika ya Kusini unaanza kutamani jinsi Pretoria na Johannesburg zilivyojengwa na wenzetu nao kuna baadhi ya vitu walivikosa wakasema tunataka kujenga miji yetu iwe ya kisasa na hiki ndicho tunaenda kufanya Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa heshima zote, kama nilivyotangulia kusema, hoja hii imeungwa mkono kwa pande zote na ndiyo maana hakuna addendum hata moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kunipa fursa kwa siku ya leo niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya na kuniwezesha kuwepo leo kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais. Hakika, naomba niungane na Wabunge wote ambao wamesema bajeti ya safari hii ni bajeti ya mfano, na hiki ambacho Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wamewasilisha, ndiyo maana hata Kamati ya Bajeti hatukupata kazi kubwa kwa sababu walikuwa flexible sana; nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika maeneo matatu. La kwanza; inawezekana hili tatizo limetokana na kanuni zetu na mfumo wetu, ifike wakati twende turekebishe kwa ajili ya manufaa makubwa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shuhuda; kila kipindi inapofika maandalizi ya bajeti tunapata wadau wengi kwenye public hearing. Lakini cha kusikitisha ni kodi zile za East African Customs ambazo maamuzi yake yanakwenda kufanyika huko na yanakuja kutekelezwa ambapo yanakuwa na athari kwa wafanyabiashara wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kama Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi tunakosa room ya kuwasaidia hawa Watanzania wafanyabiashara ambao wanakuja na mawazo mazuri. Lakini kwa sababu tayari maamuzi yanakuwa yalishafanyika East Africa pamoja na madhara ambayo wafanyabiashara wetu wanapata, tunakosa room kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasemea na kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali kama ni suala la kanuni tutazame room hii inapatikana wakati gani ili pale wanapokuja kuleta malalamiko yao kuhusiana na biashara wapi wanakwama, isije ikawa kama vile wanaleta tu hakuna utatuzi ambao unafanyika. Iko haja ya kulitazama kwa jicho la kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wewe una wafanyabiashara wengi sana kutoka katika jimbo lako. Wewe ni shuhuda jinsi ambavyo umekuwa ukipata malalamiko, lakini Bunge linafanya nini, tunashindwa kwa sababu ya utaratibu ulivyo. Ifike mahali tuone namna nzuri ya kuwasaidia wafanyabiashara kwa sababu wanakuja na cases ambazo ni genuine lakini tunashindwa kuwasaidia; la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla. Na Wabunge wote ambao wamepata nafasi ya kuchangia wamesema kwa nguvu kubwa kuhusiana na kuiwezesha TARURA. Na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri, wakati anahitimisha ametoa maelezo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna sehemu moja ambayo ni vizuri atazame kwa jicho la pekee. Amesema kwamba pamoja na hii pesa ambayo imeongezeka ambayo sisi sote tunajua kwamba inauma lakini inakwenda kutatua tatizo, na hasa changamoto kwa TARURA, lakini mgawanyo wake bado ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema hakuna haja ya kwenda kuanzisha mifuko mingine. Naomba unisikilize; uki-refer Sheria ya Roads and Fuel Tolls Act Sub Section Two inasema all moneys collected as roads and fuel tolls shall be deposited in the account of the Fund.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mfuko gani huu ambao unasemwa; huu ni Mfuko wa Road Fund ambao control yake haiko kwenye TARURA. Na wewe ni shuhuda; hivi karibuni TARURA wamekuwa wakihangaika katika kukusanya parking fees, lakini katika kukusanya hiyo parking fees hawaruhusiwi kutumia hata senti tano kwa sababu pesa hizo zinakwenda kwenye mfuko huo ambao wao hawana control. Sasa haitakuwa na maana kama tunasema inaongezeka shilingi 150 kwenda TARURA lakini hawana control.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri tu Mheshimiwa Waziri – na bahati nzuri ni msikivu sana – aende Section 4(a) kama ambavyo tulianzisha Mfuko wa Maji, sasa aongeze (c) iwe specifically kwa ajili ya kuanzisha Mfuko wa TARURA ili haya makubwa ambayo tunatarajia kama Taifa yaweze kutendeka. Lakini vinginevyo sisi sote ni mahuhuda, kwamba pesa zikiingia kwenye Mfuko Mkuu hazina rangi, kwamba hii ilikuwa meant specifically kwa ajili hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ili mambo yote yafanyike, ni kwa mujibu wa sheria. Sasa Mheshimiwa Waziri usije ukasema kwamba mtatengeneza utaratibu ambao hautakuwa umepitishwa na Bunge hili, utakuwa ni null and void. Kwa hiyo ni vizuri tukatoka kisheria tukajua sasa TARURA tunaiwezesha kama tulivyoiwezesha TANROADS, kusema kwao kote, nguvu yao yote, ni kwa sababu ni kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naomba nirudi sehemu nyingine ambayo hakika juu ya utendaji na ufuatiliaji wa fedha. Hapo zamani tulikuwa na utaratibu ambao Serikali ilikuwa inaleta taarifa yake kila quarter, lakini tukaja tukabadilisha, pamoja na digitali ilivyo, sasa Serikali inaleta baada ya nusu mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini; kama tumekosea tunasubiri mpaka mwisho tulishaingia chaka wote. Naomba Mheshimiwa Waziri ufikirie kwa mara nyingine utaratibu wa kuleta taarifa kila quarter ndiyo utumike ili kama kuna sehemu tunaona kwamba chanzo ambacho Mheshimiwa Waziri tumeanzisha, haki-perform vizuri, then kuwe na mid-year review ili tufanye marekebisho. Tusisubiri mpaka mwisho, tulishaenda kugonga pua halafu ndiyo tunasema tulikuwa tumepania hivi lakini katika makusanyo hatupati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nikiamini kwamba haya yamechukuli kwa uzito mkubwa. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi jioni ya leo ili niwe miongoni mwa waliopata nafasi ya kuchangia Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge waliompongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kuja na Muswada huu. Naomba pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mwanasheria Mkuu, hakika wamekuwa wasikivu na kama ambavyo umepata vionjo kwamba wasingekuwa wasikivu huu ungekuwa miongoni mwa miswada ambayo ingeonekana kwamba ni migumu sana. lakini hakika wanastahili pongezi kwa sababu mmetoa ufafanuzi wa kutosha na mpaka Kamati tukaridhika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechangia kwenye Kamati kwa hiyo leo nitakuwa na machache ya kuchangia. Zipo faida nyingi sana ambazo zinatokana na kupitishwa kwa Muswada huu na kuwa sheria na utekelezaji wake ukaanza. Naomba niikumbushe Serikali, tutumie faida ya kupitishwa kwa muswada huu ambao naamini utapitishwa kwa kura zote, hakutakuwa na hata kura moja ya kupinga kwa sababu ni jambo jema kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, manufaa ambayo tutayapata, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wa Fedha Kamati yetu imekuwa ikishauri mara nyingi sana kwamba iko haja ya kumalizia mchakato wa Taifa letu kuwa credit rated ili tuweze ku-access mikopo ya kibiashara ambayo ina interest kidogo. Sasa kwa kupitishwa kwa sheria hii tafsiri yake ni kwamba kwenye masuala ya kimataifa sisi tutaonekana kama ni nchi ambayo hakika transparency ipo, habari ya miamala shuku haipo kwa sababu tunatoa taarifa. Huo ndiyo uhalisia, ndivyo Taifa la Tanzania tulivyo. Kwa hiyo ni vizuri tutumie fursa hii tumalizie mchakato ule ili tuweze ku-access mikopo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ufafanuzi na mchango wangu kidogo kuhusiana na Sura 197 ambayo ni wajibu sasa wa kisheria kwa taasisi zote za kifedha kuhakikisha kwamba miamala shuku yote taarifa zake zinapelekwa Benki Kuu na ni wajibu wa Benki Kuu kuhakikisha kwamba ndiyo wanapeleka kwenye kitengo hiki. Hali kadhalika ni wajibu wa taasisi zote zinazojihusisha na bima kuhakikisha kwamba zinapeleka TIRA miamala yote ambayo ni shuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tafsiri ambayo inaweza ikawa siyo sahihi au haijaeleweka vizuri, kwamba kila muamala ambao ni shuku ukishapelekwa maana yake prosecution inakwenda kufanyika au inapelekwa PCCB. Kwa ufafanuzi ambao Serikali walituambia, miamala shuku inapopelekwa kazi ya kitengo hiki ni kufanya analysis na kujua kwamba je, kuna substance ya kuweza kuendelea na hiki ambacho kimeonekana kwamba ni shuku, kama siyo shuku inaishia hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Serikali wametueleza kwamba kwa utaratibu na matakwa ya sheria itakuwa ni vizuri kitengo hiki, FIU, kutoa taarifa kwa mtu ambaye alipeleka taarifa za muamala shuku ili vizuri pale ambapo umepeleka taarifa ujue imefanyiwa kazi, ili hata likija kutokea ambalo lingeweza kukuhusisha wewe kazi yako iwe kwamba ulitimiza wajibu wa kupeleka taarifa kwa kushuku, halafu wao ambao ndiyo wana wataalam wa kuweza ku- analyze na kuja na majibu watimize wajibu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia CMA tafsiri yake ni nini, kwa kuitaka na yenyewe ihusike. Hii itahakikisha, naamini itachangamsha hata soko letu la mitaji kwa sababu hata walioko huko Ughaibuni watajua Tanzania ni sehemu salama ambayo hata ukienda kuwekeza una uhakika hakuna namna yoyote ambayo miamala yako itakuja kuonekana kwamba imekuwa tainted.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi nzuri ambayo imefanya na Serikali, sina sababu ya kupoteza muda. Naomba Waheshimiwa Wabunge wote kwa umoja wetu tuunge mkono sheria hii ili ikatekelezwe tupate matunda yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)