Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Juma Selemani Nkamia (20 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala, kwa kutujalia afya njema leo. Nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, amefanya kazi nzuri sana kwa muda mfupi sana na naomba aendelee na moto huohuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri unayoifanya na Waheshimiwa Mawaziri wote. Kwa kweli sasa tunaamini kabisa kwamba Serikali iko kazini. Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Spika na Katibu wake Dkt. Kashillilah pamoja na Naibu Spika kwa kufanikisha Bunge kuwa na studio yake. Duniani hakuna ambapo Bunge linaoneshwa toka asubuhi mpaka jioni na vyombo vya habari, jambo hili ni zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilishangaa kusikia mtu anasema matangazo kutooneshwa ni kuvunja demokrasia. Hao waliotuletea hiyo demokrasia wenyewe hawaoneshi Bunge toka asubuhi mpaka jioni. Sisi tumechaguliwa na wananchi baada ya kwenda kuwaona na kuwaomba kura, siamini kama tulikaa kwenye televisheni na kuwaambia wananchi tuchagueni, turudi huko tukawatumikie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa niipongeze sana Timu ya Yanga Afrika wamefanya vizuri sana. Mimi ni mwanachama wa Simba na-declare interest lakini katika mechi yao ya juzi kule Cairo walicheza mpira mzuri sana, walikuwa wanawakilisha Tanzania. Naomba nimpongeze sana Rais wa Yanga Bwana Yussuf Manji kwa kazi nzuri ya kusajili wachezaji wazuri. Huwezi kuwa na wachezaji wabovu halafu unalalamika tunafungwa…
MHE. JUMA S. NKAMIA: Kama hali ilivyo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimpongeze sana Bwana Manji kwa kazi nzuri aliyofanya na aendelee kuisaidia Yanga Afrika. Naamini katika mchezo wao na Angola wanaweza kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye hoja zangu chache, kwanza nianze na suala la kilimo. Sisi Wilaya ya Chemba tuna mgogoro kidogo, si mgogoro in such, bali ni tamaa za watu wachache na wenzetu wa Kiteto. Tunaishi vizuri sana na watu wa Kiteto lakini wapo baadhi ya watu wanatuvuruga sana. Ni wazi kwamba Tanzania unaweza kwenda mahali popote bila kubaguliwa ili mradi tu ufuate sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wakulima wetu wa Wilaya ya Chemba wanaokwenda Kiteto wengi wamefukuzwa na juzi juzi wakati mimi na Mheshimiwa Ndugai, bahati mbaya hana nafasi ya kusema humu, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto kule akasema mimi na Mheshimiwa Ndugai tutamkoma kwa sababu tunatetea haki za wapiga kura wetu. Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu liangalie jambo hili vizuri ili wananchi hawa waweze kuishi kwa amani, walime na waweze kufanya kazi zao bila tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kushauri ni suala la mfumo wetu wa uendeshaji wa Serikali. Tulipokuja kwenye ule mfumo wa D-by-D nashauri turudi tukaangalie upya tena. Huu ugatuaji wa madaraka umefanya baadhi ya mambo hayaendi vizuri kwangu mimi ninavyoona, kwenye elimu na afya ndiko kwenye matatizo makubwa. Leo Waziri wa Elimu hana mamlaka na shule ya kata, Waziri wa Afya akienda Hospitali ya Wilaya hana mamlaka nayo na Waziri wa Habari akienda kule Sumbawanga akawaambia wawe na Maafisa Habari kila Halmashauri hana mamlaka nayo. Kwa hiyo, naomba jambo hili tuliangalie vizuri kwa kufanya marekebisho kidogo ili tupunguze kidogo nguvu ya TAMISEMI iende kwenye Wizara nyingine kazi ziweze kwenda haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri kidogo kuhusu usafiri Dar-es-Salaam. Njia ya kupunguza tatizo la msongamano ni pamoja na Serikali kuhamia Dodoma. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Wewe unaweza kusema aah wewe kwa sababu inawezekana fikra zako zinaishia hapa karibu, huoni mbali. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la msongamano wa magari Dar-es-Salaam na hata huu utaratibu wa DART tunaoanza nao siyo suluhisho. Hakuna miji mikubwa duniani kwa watu waliojipanga vizuri hata London, hakuna foleni kubwa pale mjini kwa sababu wametengeneza utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuhamia Dodoma imeshindikana basi tuanzishe utaratibu kwamba mtu anayetoka Gongo la Mboto akifika Airport kutengenezwe parking mahali aache gari aingie kwenye public transport. Vivyo hivyo kwa njia ya kutoka Bagamoyo, Mbagala, Tabata, tutapunguza tatizo la msongamano wa magari pale Dar-es-Salaam. Naamini jambo hili likifanyika litakuwa limetusaidia kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hata mfumo wa mabasi ule ambao mmeutengeneza pale Dar-es-Salaam, njia za mabasi zile ziko katikati. Unapotengeneza bus lane katikati pale halafu ni njia moja basi likiharibika katikati pale ya nyuma yatakwenda wapi kwa sababu iko line moja tu! Hebu angalieni vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kushauri kidogo, amezungumza hapa Mheshimiwa Kessy kwamba wafute hata michezo watu wasiende nje, hapana, mimi napingana naye kidogo. Kwa mfano, Timu ya Bunge kwenda kucheza kwenye michezo ile ya EALA ndiyo ushirikiano wenyewe wa Afrika Mashariki. Nimwombe Mheshimiwa Keissy aje tufanye mazoezi akifanya vizuri na aende kwenye timu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Malocha amezungumzia suala la watu wengi kutopiga kura katika uchaguzi uliopita. Mimi nikupe tu mfano, Wilaya ya Chemba kijiografia ndiyo wilaya kubwa kuliko wilaya nyingine katika Mkoa wa Dodoma, kutoka Kata moja ya Mpendo mpaka kufika Makao Makuu ya Tarafa ni kilometa 64, kutoka mpakani na Kiteto mpaka kufika mpakani na Singida kilometa 275. Nilishangaa kuna wilaya nyingine zilikuwa na Kata nane (8) ama 12 zimegawanywa yakawa majimbo mawili, hata hiyo population yake siyo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Malocha, tazameni namna gani baadhi ya Wilaya kama Chemba igawanywe yawe majimbo mawili, tuna kata 26, eneo lake ni kubwa kweli. Kuna wilaya sitaki kuzitaja, lilikuwa na Mbunge mmoja sasa hivi kuna majimbo matatu, ndani ya Tanzania Bara, hebu tuliangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa nataka kushauri kwenye suala la maji, tuongeze nguvu kwenye mabwawa. Sisi tumehangaika na mradi wa maji wa Ntomoko kule, sasa hivi mradi ule hauwezi kufika vijiji vyote 17, tuangalie utaratibu mwingine lakini tuongeze nguvu kwenye kujenga mabwawa. Mfano, Bwawa la Farkwa pale, Mlongia na Itolo pale katikati likitengenezwa bwawa wananchi hawa wataondokana na matatizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana wewe binafsi na nirudie kusema Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli chapa kazi. Wenzetu sasa ndiyo basi tena kwa sababu hata mgonjwa akiwa mahtuti unajua huyu kesho sijui kama atafika. Sasa baada ya kuisoma namba hata namba sasa hivi kuisoma inakuwa ni shida. Wakati mwingine tulieni, binadamu mzuri hapigi kelele hovyo. Utalalamika sana, kuonekana kwenye TV si hoja, kwani unatafuta mchumba? Wewe unataka uonekane kwenye TV unatafuta mchumba? Unataka wakuone ili iweje, nenda Jimboni! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anakuja mtu mzima analalamika hapa ndani ya Bunge, TV hazionekani, wewe unataka ya nini?
MHE. JUMA S. NKAMIA: Ndiyo, mbona zamani hazikuwepo TV hizi ulikuwa wapi wewe? Unakuja humu ndani mtu mzima kabisa, tunakuheshimu sana, unasema TV hizi, sasa hivi watu hawaonekani, waonekane ili iweje, nenda kafanye kazi. Mimi nawashangaa tu, kumbe watu walikuwa hawafanyi kazi wanategemea TV, tuonekane hapa ili iweje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia, naomba kazi hiyo iendelee. Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Katibu wa Bunge kwa kazi nzuri mliyofanya. Sisi wengine ndiyo tulioanzisha mawazo hayo, yamefanya kazi vizuri hongereni sana. Hawa wanaosubiri televisheni waende. Kwa nini usiende kuomba kazi ya utangazaji kama unataka kuonekana kwenye televisheni? Nenda, nafasi zipo tu, TV ziko nyingi tu utaonekana, utapaka poda usoni, tutakuona.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo makubwa matano. Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kumpongeza yeye binafsi na Naibu wake mtani wangu pale Mheshimiwa Ole-Nasha na wataalam wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwashukuru sana wakulima wote wa Wilaya ya Chemba na Mkoa mzima wa Dodoma kwa juhudi wanazozifanya kujikwamua pale walipo na kusonga mbele. Tuna migogoro kidogo ya ardhi kwa wakulima wetu. Kuna mgogoro ambao sasa umedumu kwa takribani miaka 11 kati ya Kiteto, Kondoa na Chemba. Mheshimiwa Waziri nikuombe tu kama umeweza kwenda kukutana na wafugaji kutana pia na wakulima na siyo kukutana nao tu bila kuwa na strategic plans za kuondoa matatizo hayo. Ningeomba sana jambo hili ulizingatie kwa kina sana. Tumekuwa na matatizo haya siyo kule Kiteto tu hata kule Lahoda ambako ni jirani sana na anapotoka Mheshimiwa Waziri, hebu tushughulikie matatizo haya yaishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni masoko ya wakulima. Mwaka 2011 Benki ya CRDB ilitaka sana kuwainua wakulima wa alizeti katika Mkoa wa Dodoma, Iringa, Manyara na Singida. Ilifanikiwa hata kutoa mikopo kwa baadhi ya watu ili waweze kupandisha bei ya alizeti. Kutokana na mfumo wa Serikali kuruhusu mafuta ghafi kutoka nje yaingie Tanzania bei ya alizeti ikashuka, hata hao wakulima wa alizeti wakapoteza mwelekeo na hata wale ambao walikuwa wanafanya biashara hii ya kuwanyanyua wakulima na wao wakaingia hasara ikiwa ni pamoja na benki na wale waliokopa na wafanyabiashara wengi wameingia kwenye madeni bila sababu ya msingi na yote haya yamesababishwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rwanda pale na Uganda, wameongeza kodi ya mafuta ghafi kutoka nje kwa lengo la ku-boost kilimo cha mazao yao ambayo yanazalisha mafuta. Let us be serious, tufanye jambo hili kwa nia njema ya kuwasaidia wakulima wetu. Mheshimiwa Waziri bahati nzuri unatoka Singida, wazalishaji wakubwa sana wa alizeti ni Dodoma, Iringa, Manyara, Arusha na kwingineko lakini bado Serikali imeruhusu uagizaji wa mafuta kutoka nje tena kwa watu wachache ambao leo ndiyo wanasababisha matatizo makubwa kwa wakulima wetu halafu tunakaa tunalalamika. Nilidhani hili jambo lazima tuwe serious sana, sisi tunashauri tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo, Dar es Salaam imejaa watu sana lakini tumefikia hatua sasa na mifugo nayo angalau iende ikaangalie Jiji kabla ya kupelekwa kwenye machinjio. Magazeti yanaweza kufika Mbeya au Mwanza saa 12 asubuhi nyama inashindwaje kufika Dar es Salaam tunapeleka ng‟ombe mzima? Kama gazeti linachapishwa Dar es Salaam saa 12 unalisoma Mbeya, unashindwaje kupata figo ya ng‟ombe iliyochinjwa Shinyanga ikapatikana Dar es Salaam asubuhi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nashangaa, Wizara ya Kilimo inakuaje na Makao Makuu yake Dar es Salaam, hameni, mnakaa pale kufanya nini? Hameni tu, nendeni Arusha, nendeni Shinyanga, nendeni Mwanza hata Dodoma.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Hata Geita nendeni, hata Bukene sawa, hata Chemba njooni.
Kwa hiyo, mimi nadhani upo umuhimu wa Serikali kuwa serious na jambo hili. Tafuteni utaratibu wa kuwa na viwanda vya nyama katika mikoa ambayo ina wanyama wengi hasa ng‟ombe. Ukipita barabara hii magari yanayosafirisha ng‟ombe kwenda Dar es Salaam masaa 12/13 what is that? Mimi sijaona duniani ng‟ombe na wao wanakwenda kuangalia Jiji ni Tanzania peke yake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nizungumzie kidogo Maafisa Ugani. Maafisa Ugani wengi waliopelekwa na Serikali vijijini wameajiriwa kwa ajili ya kupata kazi lakini hawafanyi kazi yao. Mbunge leo anaweza kufanya ziara kwenye kijiji fulani anaambatana na Afisa Ugani wananchi hawamjui, anafanya nini? Kwa Kiswahili rahisi ni kwamba hapa mtu kapata kazi siyo kazi imepata mtu. Hebu waangalieni hawa, zaidi ya kwenda kupima nyama asubuhi anachukua figo anaenda nyumbani hana kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka kuzungumzia Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI mwezi wa tatu mwishoni mwishoni hivi wakati mvua zinaishaisha ilisaidia Mkoa wa Dodoma hela kidogo kama shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununua mbegu za mihogo na mbegu za ule mtama mfupi. Hivi mlitaka wakulima hawa wapande mihogo ile ife au ule mtama usifike ili keshokutwa mseme mmepata njaa hatuwezi kuwaletea chakula kwa sababu tuliwapa mbegu? Unawezaje kupeleka mbegu wakati msimu umeisha? Hebu niambie kule Chemba unawapelekea mbegu mvua imeisha, kule Mvumi kwa Lusinde umewapelekea mbegu mvua imeisha, watafanya nini? Let us be serious! Mtu anakaa ofisini Dar es Salaam hajui hata mvua inaisha lini Dodoma anasema pelekeni milioni 10 hizi wakanunue mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Mwigulu, mimi nakujua wewe ni mchapakazi mzuri sana na mimi nakupenda tu kama rafiki yangu na ndugu yangu, pamoja na juhudi zote unazofanya za kukutana na wakulima na wafugaji, kukutana nao peke yake siyo solution. Mnaweza mkakutana mkapiga soga, mkamaliza na wakafurahi sana kwamba atatekeleza, ukipeleka kwa wataalam wako hawashughulikii jambo hili. Kesho na keshokutwa atakayepoteza umaarufu ni wewe na siyo wale wataalam wako. Pamoja na kukutana nao chukua hatua, shirikiana vizuri sana na TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya kwanza hapa nilisema tuna-problem kidogo katika mfumo wetu, huu mfumo wa kugatua madaraka. Leo huyu Afisa Ugani aliyeko kule huna mamlaka naye yuko chini ya TAMISEMI, chini ya Mkurugenzi, Mkurugenzi huna mamlaka naye wewe. So let’s get somewhere the government should sit down and see hivi mfumo wa ugatuaji wa madaraka huu kweli umetusaidia? Lazima tuu-review, nchi zingine zinafanya hivyo kwani ku-review kuna dhambi gani? Tu-review ili tuone umuhimu wake, kama tunaona kuna mahali pamekwenda ndivyo sivyo turekebishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni bei za mazao ya wakulima. Mwaka jana wakulima wa Mkoa wa Dodoma waliouza mahindi NFRA wengi walikopwa na walichelewa sana kulipwa. Naomba mwaka huu Serikali iwasaidie wakulima hawa, alhamdulilah wamebahatisha mahindi na alizeti kidogo basi tukichukua mazao yao tuwalipe kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nakupongeza pia kwa kwenda Kondoa kule japo Chemba ulipita tu kwenda kuangalia ndege iliyokuwa inamwagia ndege dawa, ahsante sana. Nakushukuru sana kwa sababu hata Chemba wale ndege japo waliendelea kutuumiza kidogo lakini wengine waliohamia Kondoa walikufa, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe hasa kwenye alizeti hebu kuwa very serious, tafuteni altenative ya kujenga viwanda iwe Singida hata Dodoma sisi hatuna tatizo. Tukiwa na kiwanda hapa naamini alizeti inayozalishwa central corridor hii inaweza kusaidia sana nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya na mimi naunga mkono hoja, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema leo na nawashukuru Wabunge wenzangu wote mlionipa pole wakati nimepata maradhi juzi; nashukuru sasa niko salama na nimejiunga na ninyi. Pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Mheshimiwa Engineer Manyanya kuwa Mawaziri katika Wizara hii, lakini pia nimpe pole sana dada yangu, Mheshimiwa Engineer Manyanya kwa msiba uliompata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima ya kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Bashe kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa ya Kamati yetu. Hata dada yangu, Mheshimiwa Susan naye leo kapendeza na anayafahamu kidogo mambo ya elimu kwa sababu alikuwa warden pale Chuo Kikuu akigawa vyumba kwa wanafunzi kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na jambo la kwanza, nataka kuzungumzia hili suala la ada elekezi, nasikia kwamba Serikali ina mpango wa kuja na mfumo huo. Nadhani suala la ada elekezi lazima Serikali ikae iliangalie kwa kina sana, kwa sababu hakuna mtu anayelazimishwa kumpeleka mtoto shule ya kulipia. Suala lililopo hapa ni kwa Serikali kusimamia na kuhakikisha shule zote za Serikali zinakuwa bora, lakini leo kumwambia mzazi, ama kumwambia mwenye shule, kwanza kuendesha shule ni gharama kubwa, hata yale mabasi tu wanalazimishwa kupiga rangi. Kwa kweli upo umuhimu mkubwa wa Serikali kuliangalia jambo hili na sidhani kama ni jambo la busara sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka niseme tu kwamba, kuhusu hiki Chuo Kikuu cha Saint Joseph, mimi ni mmoja kati ya watu walioathirika kwa sababu mtoto wa marehemu kaka yangu alikuwa anasoma kule Arusha. Chuo hiki kimefungwa, waliofanya makosa ni TCU, wamekifunga chuo hiki na wenyewe ndiyo waliotoa kibali cha kuanzishwa kwake. Mheshimiwa Waziri leo amesema amevunja Bodi, hivi watoto hawa walioathirika, nani atawalipa? Pia kukipa chuo kibali cha kuendesha elimu ya chuo kikuu kuna hatua zinafuatwa na hata kukifungia kuna hatua zinafuatwa. Wanafunzi wale wamepelekwa Moshi pale, wengine wamepelekwa Morogoro, leo wanaambiwa wale ambao walikuwa wanapata mikopo hawatapewa tena mikopo kwa sababu wameongezewa semester moja. Ni kosa la wanafunzi hawa au kosa la Serikali? Kwa hiyo, naomba Serikali mliangalie vizuri sana jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Waziri hebu chunguza watu wako; hivi walikifunga chuo hiki kwa halali ama kulikuwa na mbinu nyingine? Kwa hiyo, nikuombe sana, kwa sababu tulioathirika ni sisi wazazi.
Wanafunzi wanahamishwa, wengine wamekuja UDOM hapa wanaambiwa kwa sababu kule sijui walichelewa, waongezewe semester moja, waliokuwa wanapewa mikopo hawatapewa tena mikopo. Nani sasa atakayelipia hiyo gharama wakati ninyi ndiyo mlifanya kosa? Angalieni kwa kina sana; namwomba Mheshimiwa Waziri alichunguze sana jambo hili. Pamoja na hatua nzuri aliyochukua hebu awachunguze vizuri watu wake wa TCU, walitenda haki kwenye kukifunga chuo hiki ama kulikuwa na mbinu za chini kwa chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba nizungumzie kidogo suala la shule ambazo zinapewa hadhi ya kwenda A Level, hasa katika shule hizi za Kata. Shule nyingi hizi zina miundombinu duni na nimshukuru Mheshimiwa Waziri, ameniahidi kwamba atanisaidia kupata fedha ya kuchimba kisima cha maji katika Shule ya Sekondari ya Farkwa na Shule ya Sekondari ya Msakwalo. Shule hizi zina miundombinu duni sana, wakati mwingine sisi Waheshimiwa Wabunge tumekuwa sasa ndiyo kama walezi wa shule hizi, kila jambo lazima sisi tusimame kidete, wakati mwingine magodoro hakuna, Wabunge wanatoa, hiki hakuna, Wabunge wanatoa. Niiombe Serikali iziangalie vizuri shule hizi, mnapopandisha hadhi ya shule mjiridhishe kwanza, kwamba, je, inakidhi! Hili ni jambo ambalo nadhani mkiliangalis vizuri linaweza kutusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nataka kuzungumzia huu mfumo wetu wa D by D, kwenye Kamati wamesema, lakini na mimi tena nichangie. Hebu uangalieni vizuri huu mfumo, nimesema kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, nimesema kwenye Wizara nyingine, angalieni, fanyeni kwanza review, unatusaidia kiasi gani! Leo Waziri wa Elimu naweza kusema mwisho wake hapa Dodoma ni Dodoma Sekondari na Msalato, akifika kule, Waziri anayeshughulika na shule zile Mheshimiwa Simbachawene. Waziri akifika huyu kule mgeni kabisa, halafu akienda kwenye Halmashauri Waziri wa Elimu anasimamia tu kile kitengo cha ukaguzi, lakini Maafisa wengine wote wapo chini ya TAMISEMI. Nadhani kuna tatizo hapa, hebu kaeni chini muangalie namna gani, sisi kazi yetu ni kushauri tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, na mimi naomba leo niseme kidogo jamani. Uchaguzi uliopita umepita na mshindi kajulikana; mshindi CCM. Mpira hauwezi kwisha, tena unataka kuja kulalamika nje, uchaguzi umekwisha. Leo mtu anasimama hapa anasema oh, tuliibiwa kura, ninyi mlikuwa wapi wakati mnaibiwa! Acheni kutafuta sababu, tafuteni chanzo cha kwa nini mlishindwa. Ninyi mnajua kabisa kwamba timu ya mpira yenye wachezaji 11, mchezaji mmoja anapoumia anaingia wa timu ile ile, ninyi ilikuwaje mkachukua mchezaji wa upinzani mkamuweka! Mchezaji wa Simba kaumia, mmechukua wa Yanga mkaweka pale, amefungisha leo mnakuja kulalamika hapa! Kabisa tu, eeh, lazima tuseme tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunakaa kimya humu sio kwamba hatuna uwezo wa kusema, tuna uwezo wa kusema. Mchawi mwenyewe, unaanza kutafuta mchawi, mchawi utatoa wapi wakati mchawi ni wewe. Kwa hiyo, niwaombe tu, muwe mnatafakari kwanza! Wewe nyoosha mdomo, fanya nini, lakini that‟s the truth, utaongea sana, utapiga kelele sana, ukweli ndiyo huo na umekuingia vizuri. Eeh! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kelele wala hainisumbui. Nataka niwaambie, nataka niwashauri in future kama mnataka kuwa chama kizuri cha Upinzani, miaka minne ijayo na miaka 20 ijayo, anzeni kutafuta wachezaji wenu.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tusikilizane. Mheshimiwa Magereli, Mheshimiwa Matiko tusikilizane. Mheshimiwa Nkamia malizia! (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Ninyi tukaneni lakini ukweli ndiyo huo. Wenye akili wanajua, wapiga kelele wanajua na najua imewaingia vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwanza naunga mkono hoja…
MHE. JUMA S. NKAMIA: Nataka niwambie tu. Kuna baadhi yenu humu…
MHE. JUMA S. NKAMIA: Ahsante, namalizia. Nataka niwape mfano mmoja. Benard Tapie aliwahi kusema kwamba, kuna baadhi ya watu wakiamka asubuhi wakijiangalia kwenye vioo, wana sura mbaya wanatamani kutapika. Sasa ninyi mnaoshangilia humu, mna sura mbaya mnatamani kutapika.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataalah kwa kuniamsha salama na mimi nitoe mchango wangu katika bajeti hii ya Wizara ya Habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kwangu mimi binafsi ni mwalimu wangu wa darasani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana mama yangu Makamu wa Rais, nimpongeze Waziri Mkuu na hali kadhalika nimpongeze rafiki yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye na Naibu Waziri wake, Dada yangu Wambura kwa kazi nzuri mliyoanza nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utakuwa kwenye ushauri zaidi. Kwanza ni TBC, mimi nimekulia pale. Ametoa mchango mzuri sana Mheshimiwa Zitto Kabwe, lazima tufike wakati tufanye maamuzi! BBC inaendeshwa kwa tv license, kila mwenye televisheni analipa paundi 100 kama sikosei ilikuwa wakati naishi kule, kwa ajili ya kuendesha BBC. Zaidi ya wafanyakazi 4,000 wa BBC katika channel zote – wana lugha karibu 143, wanaendesha kwa kutumia tv license! Fanyeni maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, msiogope kwamba leo tuki introduce tv license wananchi watakasirika – wanataka kuona matangazo! They have to pay! Tutaondoa hii lawama, tv haionekani, haifanyi nini! Hilo lilikuwa wazo langu la kwanza. Mheshimiwa Zitto amezungumza pale, eh kabisa, anzisheni tu. Ninaamini Wabunge mkijenga hoja vizuri, TBC watapata fedha, wana hali mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mwaka wa sita kwangu hapa Bungeni, TBC hawana hela, mwaka nenda mwaka rudi, decide sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni michezo. Nasikia magari ya TFF yamekamatwa leo wanadaiwa TRA hawajalipa, wanadaiwa karibu shilingi bilioni 1.16. Kodi iliyotokana na mchezo kati ya Taifa Stars na Brazil. Ninavyofahamu Serikali ilikopa fedha shilingi bilioni tatu kutoka NMB kusimamia mchezo ule. TFF wameshalipa ama hela yao iliyochukuliwa na TRA karibu shilingi milioni 407. Waziri Nape nikuombe kaka yangu, kaa na TFF, kaa na TRA kodi hii wala haiwahusu TFF. Fedha yao inachukuliwa bila sababu hapa, TFF hawana hela wale, kaa nao, kila kitu kinajulikana. Kulikuwa na Kamati Maalum ambayo ilikuwa inasimamia mchezo ule kati ya Tanzania na Brazil uliofanyika uwanja wa Taifa wakati wa maandalizi ya Fainali za Kombe ya Dunia nchini Afrika ya Kusini, TFF ilikuwa ni umbrella tu lakini hawakuhusika na kitu chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumza kuinua michezo, Utainuaje michezo wakati ngazi za chini msimamizi mwingine, ngazi za juu msimamizi mwingine! Ndiyo mimi nasema mfumo wetu D by D we have to sit down tuutafakari kwa kina umetusaidia?
Leo Waziri wa TAMISEMI ndiye anasimamia UMISETA, anasimamia UMITASHUMTA, hana wataalam wa michezo, wewe ndiyo una wataalam, utakwendaje? Kaeni chini, sisi kazi yetu ni kushauri tu. Kaeni chini muangalie, hivi TAMISEMI wakisimamia UMISETA are they capable? Wana wataalam? UMITASHUMTA huko ambako mnazalisha wachezaji, nani anasimamia na wataalam wapo? Pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Baraza la Michezo chini ya Mzee wangu Dionis Malinzi, nampongeza sana, lakini hatuwezi kufikia malengo bila kufanya mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo nilitaka nilisemee kidogo, angalieni leo kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Ndugu Charles Boniface Mkwasa “Master” anadai mshahara! Mwaka jana hapa tulipitisha bajeti ya mshahara wa makocha wa timu za Taifa, kwa nini msimlipe? Kwani mkimlipa hizo fedha dola 12,000 alizokuwa analipwa mzungu kuna dhambi gani na anafundisha national team? Ameonesha kwamba anaweza kufanya kazi yake vizuri na mimi naamini kwa dola 12,000 zile mkampa Mkwasa mkampa na wasaidizi wake, wanaweza kufanya wonders kwa ajili ya Taifa letu. Kwa nini mmezuia? Mlipeni tu eeh. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni vyama vya michezo. Vyama vingi vya michezo havina ofisi. Uwanja wa Taifa nilikuona Mheshimiwa Nape siku moja wale Wachina pale wanatengeneza kiwanda cha mbao, kwa nini msiwape vyama vya michezo ofisi mle? Uwanja ule ni mkubwa na watawasaidia zaidi hata kwenye ulinzi na kuboresha uwanja ule, wapeni. Leo Chama cha Darts kinatembelea kwenye begi la mtu ambaye ni Mwenyekiti, ndiyo ofisi yake. Wawekeni mle tatizo liko wapi? Mnawakata hela kidogo, kwani shida iko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kuhusu vyombo vya habari. Nitakuwa sijatenda haki sana bila kuwazungumzia waandishi wa habari wenzangu. Waandishi wengi wa habari wa Tanzania hawana mikataba ya kudumu ya kazi. Wengi wanalipwa per piece, hawana bima na hawajui mustakabali wa maisha yao ya baadaye. Leteni sheria hapa ndani ya Bunge tuunde sheria, ama Bunge litengeneze sheria, vyombo vya habari viwe na wajibu wa kuhakikisha waandishi wao wa habari wana mikataba ya kazi, wana bima na wanakuwa na mustakabali wa maisha yao ya baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waandishi wa habari wengi wanalalamika sana hakuna mikataba, hakuna nini. Wanatembea kwenye vumbi. Wanalipwa kutokana na piece yake aliyokwenda kutafuta. Tukileta sheria hapa, Bunge likatunga sheria, nina imani kabisa kutaundwa bodi maalum ya waandishi wenyewe, kwa hiyo Serikali itakuwa ni ku-monitor tu. Lakini mkiunda bodi maalum ya kusimamia kama zilivyo NBAA kwa ajili ya wahasibu, madaktari wana bodi zao, kwani waandishi wa habari wana dhambi gani? Leteni sheria hapa tufanye kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa lakini siyo kwa umuhimu, niwapongeze sana wasanii wa Tanzania, wanafanya kazi nzuri sana. Wanastahili kweli jasho linalowatoka? Leo kwenye simu humu ukipiga mlio unasikia Diamond, ukipiga hivi unasikia fulani, ukipiga hivi unasikia nani. Je, nani anawajibika kulipa, wanapata kweli haki yao au makampuni ya simu haya yanawatumia tu kama kigezo cha kupata umaarufu? Tufike mahala tuone jambo hili. Wengi wameshauri hapa, ni kweli.
Mimi bahati nzuri nimefanya kazi kwenye nchi nyingine, siyo rahisi ukute Marekani wanapiga wimbo wa Sugu. Kwanza hawamjui na hawana interest naye. Siyo rahisi wimbo wa Koffi Charles Olomide uusikie BBC unless amehojiwa, kwetu tumeiga mambo ya ajabu sana. Stick on that, mimi naamini kabisa tutafika mahali tutarudisha heshima ya Taifa letu na wasanii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya naunga mkono hoja. Ahsanteni sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kunijalia afya njema siku ya leo ili na mimi niweze kuchangia katika hoja hii iliyo mbele yetu ya Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitakuwa ni mwizi wa fadhila nisipoungana na wenzangu kwenye jambo hili la kiinua mgongo cha Wabunge. Wengi wamesema sana, wametoa na mifano kwamba pengine Mheshimiwa Waziri kwa sababu hana jimbo, hajui adha za Wabunge na mimi nimuombe tu ili ajue taabu wanayopata Wabunge ajaribu mwaka unaokuja wa 2020 aone adha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunazungumza bajeti ya 2016/2017, sijaona impact yoyote ya kuwa na haya makato ya Wabunge katika bajeti ya mwaka huu. Ukikaa ukijiuliza kwamba kwa nini ameileta sasa, ni swali ambalo bado linaleta ukakasi kupata majawabu yake. Ukipita mitaani kuna hearsay kwamba unajua ameagiza Mheshimiwa Rais, nadhani watu wamefika wakati wanashindwa kuweka mambo yao wanataka kumchonganisha Rais na watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amekuwa Mbunge kwa miaka 20 na anajua matatizo ya Wabunge. Kwa hiyo, kila kitu kusingizia kwamba ni Rais kaagiza naamini si kweli. Mheshimiwa Rais ni mtu makini sana, lakini sasa hivi kila anayetaka kufanya maamuzi ameagiza Rais nadhani tunakosea, tufanye kazi zetu kwa mujibu wa kazi tulizokabidhiwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri, ni rafiki yangu alitazame vizuri sana hili, kazi hii ngumu baba, ondoa hicho kitu. Mimi nampenda ni rafiki yangu, amefanya kazi na marehemu kaka yangu, lakini kwenye hili hatuko pamoja. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili napenda kuzungumzia hili suala la VAT kwa utalii. Mimi nimeiona bajeti ya Kenya ambapo kwenye ukurasa wa 29, Waziri wa Kenya amefuta VAT. Hoja yake ya msingi Kenya wanasema baada ya kuweka VAT watalii wamepungua sana kwenda Kenya. Kwa hiyo, wameamua kuiondoa sasa ili ku-motivate watalii waingie na naamini mapato yao yataongezeka zaidi. Sasa kama ulikaa nao kama ulivyodokeza awali hiyo wamekutia changa la macho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kidogo suala la ule Mfuko wa Maji na Mafuta, jambo hili umelizungumzia lakini kwa kweli hatujalizungumza sana humu ndani, maji ni tatizo kubwa zaidi katika nchi yetu. Mheshimiwa Dkt. Kafumu amezungumza pale, lakini tusipokuwa na fedha katika Mfuko huu wa Maji ndoto ya kuondoa tatizo la maji bado itaendelea kutusumbua Watanzania. Kwa hiyo, naomba tuliangalie jambo hili kwa kina sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mara ya kwanza kwa kugundua kwamba crude oil kutoka nje yanashusha bei ya alizeti ambayo tunaizalisha Tanzania na inaweza kuongeza bei yake. Naomba kwa hili kwa kweli nimpongeze sana na Mungu aendelee kumbariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la TRL na RAHCO, ni-declare interest, mke wangu ni mtumishi wa TRL, kuna haja gani ya kuwa na makampuni mawili ndani ya nyumba moja? Unganisheni iwe kampuni ya TRL ifanye kazi ya kuwatumikia Watanzania. Kama lengo ni kuwa na utitiri wa viongozi tu watafutieni mahali pengine, lakini kwa kweli suala hili ni muhimu sana, hebu angalieni muone namna gani mtafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye makusanyo ya fedha kwenye Halmashauri na Majiji, mimi naomba sana TRA wakusanye na ni nchi hii tu duniani sijawahi kuona labda Somalia kwa sababu sijawahi kufika, mtu anaweza kujenga ghorofa 25 haulizwi fedha katoa wapi, ni Tanzania tu. Huwezi kujenga nyumba Uingereza au Marekani usiulizwe fedha umetoa wapi, lakini ni nchi hii tu ambako mtu anaweza kwenda Magomeni akaporomosha ghorofa 25 haulizwi umetoa wapi fedha.
Kwa hiyo, naamini kama kodi itakusanywa na TRA, kwanza kutakuwa na nidhamu lakini tunaomba sasa mrudishe zile fedha kule kwenye halmashauri ili zikatumike vizuri. Naomba Serikali muwe makini kwenye jambo hili. Kama siyo fedha haramu, ni halali kwa nini msiwe mnahoji? How come leo kama mfano Mheshimiwa Keissy umkute anajenga ghorofa 25 pale Kariakoo, fedha anatoa wapi halafu Serikali mnamuacha tu. Waulize hawa watu fedha inatoka wapi ni halali au ni haramu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nilitaka kuzungumzia suala la vifaa vya michezo kwa Tanzania. Michezo ni afya, hujenga urafiki, hujenga undugu lakini nchi nyingi duniani zimetambulika kutokana na michezo. Leo watu wanakesha tukiwemo Wabunge humu kuangalia Euro 2016, ondoeni kodi ya vifaa vya michezo. Vifaa vya michezo ni ghali sana na wanaoendesha michezo nchi hii wengi ni Wabunge. Hakuna Mbunge anayemaliza kipindi cha Bunge akaenda jimboni kwake bila kwenda na jezi, mipira na vitu vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mashindano ya UMISETA analetewa barua, mkoa sijui timu ya netball inakwenda wapi Mbunge, punguzeni ama ondoeni kabisa kodi ya vifaa vya michezo angalau kwa miaka miwili, mitatu tuweze kuondoka hapa tulipo twende tunapotaka kwenda. Nadhani tukifanya hivi tutakuwa tumefanya jambo la maana sana kwani tutaboresha michezo yetu kuanzia primary school, secondary school hadi katika vyuo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuwashukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, dada yangu hapo Dkt. Ashatu, niendelee kuwaombea ila nimkumbushe tu gratuity aachane nayo, atafute vyanzo vingine. Kwenye simu kuna hela, anzisha TV license, madini, fedha iko nyingi huko. Hii ya Wabunge wenyewe nilikuwa napiga hesabu haifiki hata shilingi bilioni nne, kwa nini tugombane kwa kitu kidogo hiki? Tuachie kwani hiyo fedha ndiyo inatujengea msingi mzuri. Kama nilivyomuomba mwaka 2020 ajaribu kugombea aone adha yake na kama hata hii gratuity huna sijui kama tutamuona hapa tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi namhakikishia kabisa, hii miaka mitano namuombea amalize aende jimboni tuone kama atarudi hapa kama ataondoa hii graduity. Kura za maoni tu saa nne misa ya kwanza pengine hayupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe hii atusaidie sana ibaki tuendelee na sisi kwenda kujenga Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi hii nichangie kidogo kwenye taarifa hii, lakini nitajikita zaidi kwenye taarifa ya Kamati ya Viwanda na Biashara. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu na nimpongeze sana Mwenyekiti na Kamati yake hiyo, niseme Kamati zote mbili kwa kazi nzuri walioifanya ya kutuchambulia yale ambayo Kamati hizi zinatakiwa kufanya kwa mujibu wa kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema Sera hii ya Viwanda ni jambo zuri sana kinadharia lakini utekelezaji wake ndio changamoto kubwa sana. Nadhani hata Mheshimiwa Rais mwenyewe anapata shida pia kwenye utekelezaji wake kwa sababu kaikuta tu kwenye ilani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ambalo siku zote najiuliza na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda yupo hapa ni vizuri akasikiliza. Tunapozungumza uchumi wa viwanda leo, hivi tulikuwa na viwanda vingapi; tumejiuliza kwa nini viwanda vile vilikufa? Kwa nini viwanda vile vilikufa this is the basic question ambayo lazima tujiulize na tuje na concrete research; kutoka pale tunaweza kuanza kufikiria kujenga viwanda vipya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Lakini tukisema tu nakuletea kiwanda leo, kesho, keshokutwa hatuwezi kwenda hivyo. Sidhani hata nchi zilizoendelea kiviwanda zinaenda katika style hiyo; tulikuwa na viwanda vingi MWATEX, MOTEX, lakini viwanda vimekufa; bila kujua aliyeua viwanda hivi tutaimba wimbo huu wa kuwa na Taifa la viwanda leo, kesho na hata milele. Leo tunazungumza kiwanda cha General Tyre utakifufuaje mpira huna? Uta-import mpira kutoka nje utatengeneza gurudumu utamuuzia nani na kwa bei gani? Haya ni maswali ambayo lazima tufike mahali tukae chini tujiulize, tuje na majibu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sera yetu tunasema tunajenga viwanda; nani anajenga Serikali au watu binafsi? Mfumo wa uchumi duniani sasa hivi, mimi sio mchumi lakini mfumo wa uchumi duniani sasa hivi unazilazimisha third world countries kupiga makofi kwa yale yanayoamuliwa na wakubwa. Leo tunasema watu wafanye investment Tanzania ya viwanda; tuna viwanda karibu 30 vya pamba lakini raw material zinazoingia kwenye viwanda vile hazitoshi. Tuna-import karibu asilimia 51 ya mafuta ya kula kutoka nje, viwanda vya mbegu za pamba ambavyo vingeweza kutoa mafuta havipati material ya kutosha kwa sababu uzalishaji wa pamba wenyewe umeshuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kwenye mawese na alizeti; viwanda vipo vya kutosha, nadhani tuanze sasa pengine tuimarishe viwanda vilivyopo sasa badala ya kuanza kufikiria kujenga vingine. Kwa sababu wasiwasi wangu tukiendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda kwa kiwango kikubwa hata hivi ambavyo vipo tena navyo vitakufa. Kwa sababu mfumo wa soko duniani sasa hivi ni competitive lakini how can you compete with a giant katika uchumi. Hayo ni mambo ambayo lazima tuyaangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikiliza siku moja rafiki yangu, Mjomba wangu, Waziri wa Viwanda anasema amepata soko la mihogo china; sasa nikasema tunahamasisha kujenga viwanda halafu tena tunataka tuuze raw material nje, hivi viwanda vitafanyaje? Ni jambo la kukaa sisi kama Taifa tufanye maamuzi kwa lengo la kuitoa nchi yetu hapa ilipo iende mahali. Nimetoa angalizo tu kwamba mfumo wa globalization duniani leo kwa third world country kama ya kwetu na tukawaomba hawa hawa wakubwa njooni mjenge viwanda, lazima tuwe very careful. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu njooni na concrete research kwamba kwa nini viwanda hivi vilikufa; mkija nayo mkakaa mezani mka-brainstorm vya kutosha mtakuja na policy nzuri sana ya kuleta viwanda ambavyo kweli tunavihitaji. Leo ukimuuliza Mwijage hata ukikutana nae hapo mlangoni anakwambia nakuletea kiwanda, ukikutana nae canteen pale anakwambia nakuletea kiwanda; sasa hata bajeti yenyewe hivi viwanda anasema anakuletea hana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hapa imetuambia leo kwamba fedha iliyotengwa kwa ajili ya hili zoezi haijatoka; lakini Waziri wa Viwanda yupo tayari kukuletea kiwanda. Sasa I have been asking kwamba hivi viwanda mnavyo kwenye mifuko ya makoti? Tusipowaambia ukweli tutakuwa tunadanganyana na sisi bila kusema ukweli hatuwezi kusaidia nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unaweza kulalamikiwa hivi kwamba ukaonekana huyu jamaa mbona anasema sema vibaya, no lazima tuseme ukweli kwa lengo la kusaidia Taifa letu, lakini tukisema tu kwa sababu ya kufurahishana tutakuwa hatuendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu Ilani ya uchaguzi ya Chama chetu imeweka mambo mengi sana nafikiri, samahani kwa siku zijazo hata vyama vya siasa ni vizuri mgombea Urais akapatikana kabla ilani hazijaandikwa. Kwa sababu matokeo yake hata Rais huyu amekuta ilani ina ahadi 148; hata ule utekelezaji ule wa milioni 50 kila Kijiji mpaka wakati mwingine namuonea huruma Rais; kwa sababu unakuta umeandikiwa vitu walioandika watu wengine wewe unaambiwa nenda katekeleze. Nadhani tufike mahali tuseme ukweli kwa lengo la kulisaidia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la viwanda tunawashukuru sana Kamati mmefanya kazi nzuri sana lakini pia tuache siasa kwenye viwanda. Ukianza kusema nakuletea kiwanda huna kiwanda mfukoni, don’t do that; mtapiga sound hapa wee 20 years inakaribia kuisha, kesho tutasema jiulizeni tu. Niombe Mheshimiwa Mwijage wewe baba mkwe sijui nani sielewi vizuri lakini tusaidie tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanye stadi nzuri ya mfumo wa uchumi duniani ulivyo sasa. Mkifanya utafiti wa kutosha kwamba mfumo wa uchumi duniani ukoje then unaweza kuja na hii concrete idea ukafika mahali ukasema tunachofanya hiki, ni hiki na hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho tu kwa mfano, viwanda vya kuchambua pamba, tuviimarishe vile ili mafuta haya yazalishwe hapa nchini, lakini pia tuwasaidie wakulima bila kuboresha kilimo tutaimba wimbo wa viwanda leo, kesho na kesho kutwa. Kila Kijiji leo tuna extension officers lakini wanasaidia wananchi wetu kwenye kilimo vipi? Bado wananchi wanamwaga mbegu na hawa ni waajiriwa wa Serikali na wanalipwa; kila mwisho wa mwezi kuna extension officer anapata mshahara, ana kazi gani zaidi ya kupima ng‟ombe na anachukua maini, they have nothing to do.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuboresha kilimo mfumo huu tunaouzungumza wa viwanda utatusumbua sana wazee wangu. Tukae chini tutafakari nchi yetu iweze kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na nawashukuru kwa mara nyingine tena niwapongeze sana Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys kwa kufuzu kwa michezo ya under seventeen ya Afrika, hongera sana Mheshimiwa Nape na timu yako yote; sasa tujipange basi kuiandaa timu yetu kwa sababu hiyo nayo pia ni sehemu ya viwanda. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nawapongeza sana wachezaji wa Simba, jana kidogo watulaze na viatu, lakini kwa kweli kazi waliyoifanya ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu, la kwanza nachukua nafasi hii kwa dhati kabisa ya moyo wangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuleta maendeleo ya Taifa letu. Wakati mwingine maneno haya ni kwa sababu mnafanya
kazi nzuri. Ukiona mtu anakushambulia hivi, ujue unafanya kazi nzuri sana. Na mimi niwatie shime kwamba endeleeni na kazi hiyo ili Taifa letu liweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa, nawapongeza watu wa TAMISEMI vilevile na Wizara ya Afya kwa kutupatia fedha kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Hamai ambacho kwa leo ndiyo tunakitumia kama Hospitali ya Wilaya ya Chemba. Nawashukuruni sana na ninaomba kazi hiyo ya kujenga wodi, nyumba za waganga iweze kufanyika kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumzie maji. Tuna Mradi wa Maji wa Ntomoko, alisimama Mbunge mmoja hapa akasema ufutwe, lakini mimi nasema ashindwe tu, kwa jina la Yesu. Ni kama amedandia gari katikati, kwa sababu hajui chanzo chake na hajui mwisho wake. Mradi huu una changamoto zake ndogo ndogo, lakini mimi namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kukubali kwenda, kama Mungu akijaalia wiki ijayo ili na wewe ujionee kwa namna moja
ama nyingine changamoto zilizopo kwenye mradi huu ili ziweze kutatuliwa na watu wapate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni suala la kuhamia Dodoma. Kwa namna ya kipekee kabisa sisi Wabunge wa Dodoma tulikuwa na mkakati kabla ya tamko la Mheshimiwa Rais kuleta muswada binafsi hapa Bungeni ili Serikali ihamie Dodoma, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuamua kwa dhati ya moyo wake kuhamia Dodoma, lakini suala hili halipo kisheria. Naiomba Serikali sasa ilete muswada Bungeni hapa ili iwe sheria. Anaweza kuja mtu mwingine kesho akasema Makao Makuu ya nchi anayapeleka kwingine. Kwa hiyo, niwakumbushe hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile pamoja na kuhamia Dodoma, harakisheni ujenzi wa mradi wa maji wa bwawa la Farkwa ambao pia utaongeza maji Dodoma, Chemba, Chamwino na Bahi. Leo tathmini imeanza kule Farkwa, Mombose na Bubutole, vile vijiji vinahama basi wale watu
walipwe fidia zao mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, Serikali lazima iwe active, lakini siyo kuwa active kwa kukosea. Nitoe mfano, samahani sana, jana nilikuwa naangalia mkutano wa waandishi wa habari (press conference) na yule Bwana anaitwa sijui nani yule…Roma Mkatoliki. Hivi Waziri
wa Habari alikwenda kufanya nini? Unajua wakati mwingine unaweza kuambiwa ukweli ukachukia, lakini ni afadhali uambiwe ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Habari amekwenda kwenye mkutano wa Roma Mkatoliki,
anampisha na kiti, anayeongoza press conference ile ni Zamaradi Kawawa, Afisa wa Serikali. Hivi kesho, mtu akikwambia wewe ndio ulimteka Roma, utakataaje? Ni vizuri uchukue ukweli hata kama unauma, lakini take it. At the end of the day unaweza ukafanya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine mnamgombanisha Mheshimiwa Rais na wananchi bila sababu ya msingi. Mimi sikuona logic kabisa. Mimi siyo mwanasheria, nimesoma uandishi wa habari na nimesoma uhusiano wa kimataifa, lakini this is wrong. Is not applicable! Kwa hiyo, Serikali wakati mwingine mnaingia kwenye mtego wenyewe bila kujua. Hebu liangalieni hili, ilitokea wapi mpaka Mheshimiwa Waziri anakosa kiti, anahama, halafu huyu mtu binafsi anafanya press conference, wewe unakwenda kufanya nini? What were you doing there? Halafu leo akina Nkamia wakisema ukweli humu, kuna watu wanasema, aah, unajua labda kwa sababu alikosa Uwaziri. No, we have to tell you the reality! This is a principle!
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu suala la kuongeza maeneo ya utawala. Hapo nyuma tumeongeza sana maeneo ya utawala lakini bado tunashindwa kuhudumia yale maeneo tuliyoyaongeza. Hebu angalieni, malizeni kwanza tatizo la yale maeneo mliyoyaongeza ya
utawala ndiyo muanze kuongeza maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Jimbo ulipoletwa, idadi ya watu ilikuwa tofauti na sasa. Fanyeni review, Chemba ilikuwa na watu 160,000, leo tuko watu 250,000, lakini bado
kiwango cha Mfuko wa Jimbo kinachotolewa ni kile kile cha wakati ule na wakati mwingine kinapunguzwa, amesema Ngeleja hapa. Hebu angalieni namna gani mnaweza kuongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo. Jana amesema hapa Mbunge wa Kiteto, kuna tatizo kubwa kati ya Wilaya ya Chemba, Kiteto, Kongwa na Gairo. Watu wa Kiteto wanafikiri kama ni Jamhuri ya Wamasai hivi ndani ya Tanzania. Baadhi ya viongozi wanaopelekwa katika maeneo
haya, nao ni shida. Hebu tusaidieni, mtaniwia radhi. RAS wa Manyara, DC wa Kiteto, DC wa Chemba, kabila moja na wanawasiliana vizuri sana. Matokeo yake kumekuwa na crisis katika Wilaya hizi kwa sababu Wagogo, Wakaguru, Warangi hawatakiwi Kiteto. Amekaa miaka 30 anaambiwa ondoka leo. Hivi leo na sisi tukaamua Mrijo tukafunga mpaka, hakuna Mmasai kuingia Chemba… Taarifa...
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ni ushauri, wala siyo taarifa tu. Kwanza hawa niliowasema, ni watani zangu wote, hawa Wakurya wote watani zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema, tunazungumza leadership credibility. Wapo watu wanapewa vitu vidogo vidogo kuwaumiza baadhi ya watu. Mtu amekaa miaka 30, unamwambia ondoka leo, acha nyumba yako, wewe ni Mrangi nenda Chemba. Wewe ni Mgogo toka, nenda Kongwa, wewe ni Mkaguru toka nenda Gairo. Tukae kimya! This is a problem. Ni ndani ya Tanzania hii kaka yangu anayoisema pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tufike wakati sasa tuwe serious ili tuendelee kuishi kwa umoja na amani yetu. Namshukuru kaka yangu pale, namheshimu sana kwa ushauri wake, nimeupokea, lakini pia kwa wakati mwingine nanyi upande wa pili muwe mnaangalia maneno ya kutumia, isiwe upande mmoja tu. Kisu kikate kote kote. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie la mwisho, mimi ni mwana michezo. Naomba sisi Wabunge tuiunge mkono timu ya Serengeti Boys kwa nia njema kabisa na Serikali nayo iweke mkono wake ili timu yetu ikafanye vizuri, badala ya kulaumu tu wachezaji, na sisi tuoneshe moyo wa upendo kwa timu zetu ili tupate vijana walete heshima kwa Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie kwa uchache tu, kuhusu Wizara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhana wataala kwa kunipa afya njema na kusimama leo mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia machache kwa lengo la kuisaidia Serikali kuboresha pale ambapo naamini inaweza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Mimi simpongezi tu Mheshimiwa Rais hivi hivi bali nampongeza kwa kuzingatia vigezo vitatu vya leadership. Kwanza ujasiri, pili, uthubutu na tatu kujiamini kwake. Katika falsafa za kiongozi bora akiwa na misingi hii mitatu, anakuwa kiongozi bora. Ndivyo ambavyo Mheshimiwa Rais anafanya, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wake pamoja na Serikali yote kwa ujumla. Nampongeza sana Mheshimiwa Harrison Mwakyembe, Naibu wake na Watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kweli Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 18 na hata Sera ya habari ya 1993 inazungumza juu ya kwamba kila mtu ana haki ya kupata habari. Sina haja ya kwenda mbali sana, lakini haki ya kupata habari pamoja na wajibu wa kupata habari vyote hivi vinategemeana. Haki bila wajibu haiwezi kwenda. Si kwa sababu tu Katiba inatamka na Tanzania imeridhia matamko ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, watu wavunje sheria tu kwa makusudi kwa sababu Katiba imetaka hivyo. Sidhani kama hiyo ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti Waadishi wa habari wa nchi hii wanafanyakazi kubwa sana. Vyombo vya habari vinavyafanya kazi kubwa sana, lakini kuna kitu kimoja ambacho sisi waandishi tunasahau. Mwandishi wa habari ni sub-soldier, hili lazima ulielewe. Hakuna nchi yoyote duniani, mimi siamini na sijawahi kuona kwamba vyombo vya habari vinaweza vikaamka tu magazeti yanatunaka tu watu wakaa kimya. Ndiyo maana ya kuwa na state. State maana yake ni ku- protect citizen wake katika Taifa lile. Ndivyo ambavyo kazi inafanya. Nawashukuruni sana Mheshimiwa Waziri endeleana na moyo huo huo, chapa kazi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumzie kidogo kuhusu michezo. Mpira wa miguu ndio mchezo unaopendwa kuliko yote duniani kwa sasa hivi. Naipongeza sana timu yetu ya Serengeti boys na viongozi wa TFF. Hata hivyo, timu za vijana hazijengwi na TFF, zinajengwa na vilabu. Hili lazima TFF; na nashukuru rais wa TFF, Rais anayemaliza muda wake yuko hapa; ninachosema lazima Vilabu viakikishiwe kwamba kweli vina wachezaji wa timu za vijana. Tusijidanganye tukasema TFF ama Serikali inaweza kuwa na academy yake kuwatengeneza wachezaji, hiyo haijatokea duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti ni imani yangu kwamba Mheshimiwa Waziri na bahati nzuri sasa kwamba FIFA imetoa room kwa Serikali ku-interfere pale ambapo wanaona mashirikisho ya mpira na michezo mingine hayafanyi vizuri tofauti na ilivyokuwa wakati wa Blatter. Kwa hiyo Mheshimiwa Mwakyembe you have the room, ukiona hapaendi vizuri FIFA imetoa hiyo. Jitahidi sana, lazima tuhakikishe vilabu hivi vinakuwa na timu za vijana zilizo imara ili tupate national timu inayoweza kwenda kushindana. Otherwise tutapiga kelele miaka nenda, miaka rudi, hatuwezi kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nidhamu pia kwa wachezaji, wachezaji wasipokuwa na nidhamu; hata hapa ndani ya Bunge ndiyo maana tunatunga hizi kanuni ili tuwe na nidhamu. Kama hawana nidhamu hatuwezi kufanya vizuri katika michezo, hili lazima tuliangalie. Sitaki kuzungumzia rafiki zangu hapa wananiambia point za Kagera nasema hizo nawachia TFF watajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo kuhusu Shirika la Utangazaji Tanzania. Mimi kwa maono yangu na kwa mtazamo wangu na kwa analysis nzuri tu kwamba uanzishwaji wa Redio Tanzania kubadilishwa kuwa Shirika la TBC lazima kuna makosa yalifanyika. Hili shirika ni shirika la habari, lakini halina tofauti kimuundo na TANESCO, halina tofauti kimuundo na bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo TBC pale kuna Wakurugenzi zaidi ya 10, mameneja 14 wakati pale wanahitajika viongozi wanne tu. Mkurugenzi Mkuu, Mkuu wa vipindi, CP, Meneja wa Ufundi, umemaliza. Mheshimiwa Waziri angalieni Muundo wa lile Shirika ndiyo maana leo wanapata tabu sana. Lile ni broadcasting house siyo Shirika la Uzalishaji, hapo ndipo tatizo linapotokea. Leo Ryoba anapata tabu sana pale kwa sababu anashindwa kuendesha lile shirika limekuwa ni kama shirika la uzalishaji na si broadcasting house. Angalieni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna matatizo ya vifaa, hata ile studio ambayo ilitengenezwa wakati ule wa TVT ndiyo studio inahusika kuzalisha matangazo yaende huko nje. Usikivu umekuwa duni. Leo ukienda huko Pangani wapi unasikia KBC Kenya. Hapa Chemba ukienda kwa Mtoro ndiyo hatusikiki kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko Mlalo ndio kabisa wanasikia Kenya. Ukienda huko Tanganyika huko wanasikiliza Kongo. Lazima tufanye investment ya kutosha. Hata live coverage ni aibu kabisa kwa Shirika kubwa kama lile kwenda kuazima chombo cha kurushia matangazo kutoka kwa mtu binafsi. Kabisa! Ni aibu! Juzi Rais anakwenda Mtwara wameazima chombo kwa mtu binafsi Benjamin, pale wanalipa sijui dola mia sita sijui ngapi ni aibu. Msaidieni Ryoba yule, vinginevyo atashindwa. (Makafi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hii tunayotumia hapa Bunge imetengenezwa tu amplifier lakini pia zile flyways zina life Span. Nunueni vingine na nimefurahi kusikia Mheshimiwa Waziri kwamba mwezi wa sita vitakuja vingine. Wazee sisi wengine tumekulia pale kama siyo TBC tusingekuwa hapa. Mimi mtoto wa mfinyanga vyungu naingia Bungeni, kama si TBC tusingekuwa hapa leo. Kwa hiyo, isaidieni sana TBC hasa kwenye vifaa lakini na muundo wake. Mheshimiwa Mwakyembe nakujua fanyakazi yako angalia ile shirika vizuri badilisha style irudi kuwa broadcasting house na siyo shirika la uzalishaji. Weka viongozi wanne tu Mkurugenzi Mkuu, wa Ufundi, Control programs umemaliza unasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JUMA S.NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kunipa nafasi hii, ili na niweze kuchangia kwenye Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhana Wataala kwa kunijaalia kuwa na afya njema wa Bunge wote katika Bunge hili la Jamhuri ya Mauungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Dkt. Mpango na dada yangu Dkt. Ashatu kwa bajeti nzuri sana, bajeti ambayo inaonekana dhahiri kwamba ikitekelezeka nchi yetu itafikia hatua nzuri sana ya maendeleo. Bajeti ambayo inamgusa kila Mtanzania kwa nafasi yake, mkulima, mfanyakazi, mwanafunzi na Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, bajeti hii sasa iende kwenye maeneo yaliyodhamiriwa. Watanzania wengi tatizo kubwa maji, nashangaa leo Mbunge wa Pangani, Mto wa Pangani umepita katikati ya Mji wa Pangani lakini wananchi wanalia maji. Chemba kule tuna matatizo makubwa ya maji, fedha ziende kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji. Tukimaliza hili, twende kwenye tatizo la nishati ya umeme; wananchi wakiona mambo haya yanafanyika naamini kabisa kwamba nchi yetu itaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, ninasikitika kwamba kuna Mbunge mmoja hapa, nisingependa kumtaja jina, alisema barabara ya lami ya kutoka Dodoma kupita Chemba, Kondoa kwenda Arusha haina manufaa kwa wananchi wa Chemba.

Wananchi wameniambia nimsihi tu kwamba, kama yeye hapendi kupita kwenye barabara apite porini. Eeh! Lakini Wabunge wa Arusha, Manyara na kwingine kote, wanaunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukitoka Arusha, Dodoma masaa manne, lakini mtu anabeza juhusi za Serikali katika kuhakikisha kwamba barabara hii imejengwa kwa kiwango cha lami. Mwenyekiti wewe ni shahidi ulipotoka Moshi kupita hapa, ulipokuja hapa ukasema hivi ile ni barabara ama kiwanja cha ndege. Vijiji vilivyoko karibu na barabara hii maisha yao yameanza kubadilika kwa wale wanaojishughulisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mtu hajishughulishi anasubiri barabara ile iende mpaka chumbani kwake, haiwezekani. (Makofi)

Kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba ni vizuri tuunge mkono juhudi za Serikali zinazofanywa bila kujali tofauti yetu. Maslahi ya Taifa hayana mgawanyiko, maslahi ya Taifa lolote hayana mgawanyiko, ningeomba pia bajeti hii ijielekeze zaidi kwenye elimu. Pia ni vizuri mkafanya analysis kidogo kuhusu fedha zinazo kwenda kwenye shule hizi za msingi huko vijijini, zinafanya kazi iliyokusudiwa? Nina wasiwasi kwamba inawezekana fedha nyingine zina kwenda huko kwenye hili suala la elimu bure bado fedha zile hazifanyi kazi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri niliwahi kusema nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza hapa hebu lete kwenye financial bill ile tozo ya ving’amuzi ili TBC iweze kuendelea. Muache kutoa fedha kutoka Hazina kupeleka TBC ichukuliwe fedha ya ving’amuzi ambayo itakwenda kuendesha shirika la umma lile. Na mimi nitakuwa mwizi wa fadhila nisipompongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye hili suala la makinikia. Nitoe rai kwa Wabunge wenzangu kwa wana CCM wenzangu wote tunakadi za kijani hakuna mwenye kadi ya kijani zaidi ya mwingine, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wapinzani maslahi ya Taifa hayagawanyiki, tuungane sote, Mheshimiwa Rais ameonyesha jambo jema baada ya kuunda tume zile mbili.

Kwa mliosoma mambo ya negotiations, kuna aina mbili za negotiation baada ya jambo hili. Kwa kuwa sasa sisi kama Taifa tumekuwa na power kwenye negotiation itakayofuata kwenye compromise negotiation, nina amini kabisa tutafaidika na jambo hili. Jambo hili linahitaji umakini mkubwa sana, ni jambo linalohitaji akili ya kutosha Mheshimiwa Rais ameshaonyesha njia, nina wasiwasi kwamba inawezekana kabisa tusipate ile trilioni 1.08; kwa sababu ni suala la negotiations. Lakini tunapokuja kwenye mjadala huu automatically kwenye win win situation nchi yetu itafaidika. Ndio maana nikasema wapinzani, wana CCM tuungane pamoja tum-support Mheshimiwa Rais kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hawa wachimba madini wanakwenda kuweka mgodi mkubwa sana kule Chemba, endapo jambo hili litafanikiwa na tukawa na win win situation, automatically hata wananchi wa Chemba watapata mafanikio kwenye huo uwekezaji unaokuja kule Chemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni suala la kisheria, mimi sio mwanasheria, lakini kwa kuwa sio kuku na sitagi mayai lakini najua yai viza ni lipi? Tufike mahali, si rahisi na siamini hivyo kwamba mikataba ikusanywe na maroli iletwe hapa Bungeni siamini. Kinacholetwa Bungeni ni muswada wa sheria sisi Wabunge tusimame kuhakikisha kwamba tunabadilisha Muswada wa Sheria ili nchi yetu iweze kufaikika kutokana na madin haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine nashangaa kusikia Mbunge anasema leteni mikataba hapa Bungeni, maana yake unazungumza maroli mawili/matatu na hilo sio jukumu la Bunge, jukumu la Bunge ni kutunga sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba endapo sheria hii ikija wote tuungane pamoja wapo wanasheria humu watusaidie tuone ni namna gani nchi yetu inaweza kupata mafanikio kwenye suala hili la uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana nikasema Mheshimiwa Rais ameonyesha ujasili wa hali ya juu sana, lazima tumuunge mkono, lazima tushikamane wote wapinzani, wana CCM na ndio maana nikatoa mwanzoni nikasema sisi wote Wana-CCM hakuna mwenye kadi ya kijani zaidi kuliko mwingine lazima tuungane wote tu kwa sababu kadi zetu wote zinafanana. Niombe na wapinzani tuungane kwenye jambo hili na nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mbunge wa Iringa Mjini, Mheshimiwa Peter Msingwa aliposema suala la maslahi ya Taifa halina mgawanyiko mimi chama fulani, mimi chama fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bomba la mafuta kutoka Uganda linapita Singida, linapita Chemba linakwenda Tanga. Naomba ajira zitolewe kwa watu wa maeneo hayo, lakini pia wananchi waelezwe mapema litapita kwenye vijiji vipi? Sambamba na hilo ile barabara ya Handeni, Kiberashi, Kibaya, Chemba, Donsee, Lalta, Farkwa, Kinyamshindo hadi Misung’aa kule kwa Mheshimiwa Tundu Lissu ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami kazi ianze sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umekwisha.
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai mimi na sote tuliomo humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kabisa niishukuru na kuipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha mradi huu wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ni muhimu sana kwetu, na wote tunafahamu kwamba kulikuwa na kama mashindano hivi kati ya nchi hizi za Afrika Mashariki kuhusu bomba lipite hili wapi, lakini baada ya Serikali ya Tanzania kufanikiwa na mradi huu kuzinduliwa kule Tanga kwa kweli imekuwa ni faraja kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Chemba bomba hili linapita si chini ya kilometa 170 kutoka mpakani na Kiteto hadi mpakani na Singida. Linapita Mrijo, Chandama, Songolo, Goima, Paranga, Farqwa, Kwamtoro, Ovada hadi Kinyamshindo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, wananchi ni vizuri wakaelezwa mapema ili wasiendeleze baadhi ya maeneo yao kwamba bomba hili litapita wapi. Lakini pia itakuwa vyema sana kwa wale ambao wataguswa na eneo lao kuchukuliwa wakalipwa fidia yao stahiki kwa kipindi muafaka, litakuwa limewasaidia sana. Pia ni mradi mzuri kwasababu ukiangalia kwa siku, Mama Tibaijuka alikuwa anajaribu kupiga hesabu pale na mimi nimejaribu kupiga hesabu hapa kwamba kwa siku Tanzania tunapata dola 2,708,325, it’s a huge amount of money na hii hela itatusaidia sana.

Sasa mimi ombi langu ni kwamba ni vizuri Waheshimiwa Wabunge pamoja na Madiwani wa maeneo husika. Kwa sababu nimeanza kuona kuna tatizo moja dogo tu na ningeomba kuishauri Serikali; kwamba wanawashirikisha sana Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Hawa ni watendaji wa Serikali, lakini wanaoulizwa maswali ni Wabunge na Madiwani. Mbunge ukienda mahali wananchi wanakuuliza hebu tuambie bomba likipita hapa sisi tutafaidika nini? Mbunge unashindwa kutoa majibu kwasababu aliyekwenda kuhudhuria hivi vikao vingi vingi hivi ni Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa na nashukuru sana baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambako bomba hili linapita walishirikishwa kule Tanga.

Ningetoa rai kwamba sasa tunapokwenda kwenye process hii ya ku-finalize hili suala Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani wa maeneo husika ni vizuri wakashirikishwa. Seriakli msi-ignore sisi ni wawakilishi wa wananchi tu lakini sisi ndiyo responsible kwenye maswali ya wananchi. Kwa nia njema tu, tushirikisheni ili na sisi twende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kiwango hiki cha fedha tutakachokipata ni kikubwa kidogo. Maeneo mengi bomba hili litakapopita vijiji vingi havina maji, na ndiyo maana mimi na Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Dodoma, Manyara na hata Tanga bomba lilikopita ndiko ilikopimwa barabara ya lami kutoka Handeni - Kiberashi - Kibaya - Mrijo, Chemba - Donsee - Farqwa - Porobanguma - Kwamtoro mpaka Singida. Kwa hiyo nadhani ni wakati muafaka saa Seriakli ijenge ile barabara kwa kiwango cha lami ili hata usimamizi na usalama wa bomba hili uwe mzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya nakushuru sana na ninaipongeza sana Serikali na naunga mkono. Jambo hili ni jambo jema sana kwentu, ni jambo jema kwa Watanzania wote tuungane ili tufike pale Mheshimiwa Rais wetu anataka tufike pamoja na chama chetu, chama tawala. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru sana wewe bunafsi, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia leo kuwa na afya njema. Kwa namna ya kipekee tena niongeze kukushukuru sana Profesa Dkt. Mtemi Chenge kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana na nimpe pongezi za dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, mwalimu wangu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu, Mawaziri wote na Makatibu Wakuu wote

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa uniruhusu nimpongeze sana ndugu yangu Jafo, anafanya kazi nzuri sana. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni; nami naamini kwa kazi hii anayoifanya Jafo huwezi kujua huko mbele ya safari, kikubwa endelea kumuomba Mwenyezi Mungu, Mungu ndiye anayepanga kila kitu. Nikupongeze sana kaka yangu Kakunda na Naibu Mawaziri wote wawili, Katibu Mkuu Mzee wangu Mzee Iyombe, dada yangu Chaula na Nzunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na suala la maji. Serikali kupitia TAMISEMI na hata Wizara ya Maji wanafanya kazi kubwa sana kwenye miradi mikubwa na miradi midogo, lakini msema ukweli ni mpenzi wa Mungu. Kama Mheshimiwa Rais ameweza kufanikiwa kupunguza ufisadi bado eneo la maji kuna ufisadi mkubwa sana kwenye miradi ya maji vijijini. Miradi mingi haikamiliki kwa wakati, miradi mingi fedha zinafujwa, miradi mingi haiko kwenye kiwango matokeo yake Serikali inaingiza fedha nyingi lakini miradi hii baada ya muda mfupi inakufa. Niombe sana jambo hili mliangalie kwa umakini na ikiwezekana Serikali undeni tume maalum kuchunguza miradi mikubwa na midogo ya maji nchi nzima kwa sababu kuna crisis kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo tu, kuna mradi mmoja wa maji uko kule kwenye kijiji kinachoitwa Lahoda, nilikwenda na Mheshimiwa Waziri Kakunda. Serikali imetoa shilingi milioni 551 lakini hata tone la maji hakuna, na Waziri kaenda pale aadanganywa kwamba baada ya mwezi mmoja tutarekebisha mradi huu, maji yataanza kutoka. Waziri Kakunda akaagiza apelekewe akiba ya fedha walimwambia kuna shilingi milioni 83, hakuna hata senti tano. Kesho wanamuona Mheshimiwa Rais hafai, kumbe ni kwa sababu ya watendaji wachache. Niiombe Serikali ichukue hatua juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kule Chemba tunavyozungumza hapa, Mondo, Daki, Hongai, Chandama; tumechimba maji muda mrefu lakini two years now hakuna kinachofanyika. Niiombe Serikali, inafanya kazi nzuri sana, lakini hebu hakiksheni huko chini tunakotoka sisi miradi mingi ni useless. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilikuwa nataka nizungumzie kidogo elimu. Nadhani kuna mahali tume-mess up. Hivi mwalimu alikuwa anakwenda darasani anakwenda anasema good morning folks, how are you? Leo unampeleka akafundishe chei chei shangazi. Si kwamba walimu hawatoshi, kuna tatizo kwenye upangaji wa walimu. Shule za mijini, hapa Dodoma Mjini kuna access ya walimu 371, shule ya sekondari ya Mpendo ina walimu wanne. Sasa hivi tatizo ni kukosekana kwa walimu au tatizo ni mpango wa walimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, hebu fanyeni tathmini kabla ya kufanya hilo zoezi. Mnatawanya walimu bila kujua; TAMISEMI, leo mzee Iyombe uko hapa baba yangu, kwanza shikamoo.

Nikuombe, leo TAMISEMI mnapanga Mwalimu Juma Nkamia anaenda shule ya msingi Msaada. Akifika pale halmashauri anamkabidhi barua nimepangiwa shule ya msingi msaada, wapelekeni walimu acheni Halmashauri ndizo zipange waende wapi, lakini ninyi mtapanga wataenda kujazana mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hivi katika shule za mjini walimu wengi wamejaa wanatoka wapi? Wengi wasichana wazuri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia, shule nyingi za mjini wasichana wengi, wazuri tu hivi, hivi hawa wanapangwa makusudi au wanakosea? Niwaombe tu, fanyeni utafiti muone. Hapa tuna vitu ambavyo hatuendi sawasawa na matokeo yake watu wanafikia hatua wanasema; “aah, unajua Serikali ya CCM haijafanya…” si kweli! Wapo watu ndani ya Serikali wanafanya makosa kinachotukanwa Chama cha Mapinduzi, chukueni hatua! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu hiyo hiyo, ajira za walimu. Ajirini walimu wa kutosha, lakini mhakikishe wanapangwa kule kwenye matatizo kweli si unaajiriwa vimemo kibao, acheni hii kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye issue ya watumishi, mimi sielewi tu. Watumishi kwenye halmashauri wengi hawatoshi, lakini nchi hii hapa katikati hapa kuna kitu tumefanya makosa makubwa sana, tumeongeza maeneo mengi ya utawala wakati hatuna resources. Hivi unaweza kuniambia uliigawaje Wilaya ya Siha na Wilaya ya Hai zikawa Wilaya mbili? Population ya pale ipoje? Hapa ni watu walitafutiwa vyeo. Tufike mahali tuangaie, kuna baadhi ya wilaya hazistahili kuwa Wilaya, vunja; Wilaya ina watu 70,000 ya nini? Ukisoma kwa sisi tuliosoma mambo ya International Relations kuna kipengele kinasema mtu anatafutiwa nafasi kwa sababu hana eneo lingine, anatafutiwa nafasi ili awe kiongozi mahali aje atafutiwe nafasi kubwa, this is wrong.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, zipo baadhi ya Wilaya vunja, kama wapo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, kazi ziko nyingi za kufanya, wapeni hata Wakuu wa Idara tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho TAMISEMI ninyi ndio mnashughulikia Mfuko wa Jimbo, unakuta baadhi ya maeneo Wabunge hawa ile fedha ya Mfuko wa Jimbo, fanyeni tathmini upya. Tangu sheria imetungwa mpaka leo kiasi kile kile, jimbo limeongezeka, Chemba sasa hivi tuna karibu watu laki tatu na ushee, ile ile, hatuwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na niishukuru sana Serikali kwa kweli, leo mimi nikitoka hapa kwenda Chemba dakika 45. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais, ongezeni fedha kwenye TARURA barabara zetu zijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Mheshimiwa Jafo nina vituo vya afya viwili, Hamai milioni 400, Kwa Mtoro milioni 500, naomba zile za Kwa Mtoro ziingie tutulie. Umenipa bilioni moja na milioni mia tano Hospitali ya Wilaya ya Chemba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru. Sana nitatoa ushauri tu kwa sababu na mimi nimeshawahi kukaa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hakuna nchi yoyote duniani inaweza kuendelea kimichezo bila kuwa na makocha wake wazawa. Ni aibu kubwa kwa Taifa la Tanzania leo kuchukua makocha kutoka Burundi kuja kufundisha timu zetu za Premier League. Kocha Msaidizi wa Simba anatoka Burundi, Mbeya City - Burundi, Mbao FC – Burundi. Katika FIFA ranking Tanzania iko juu kuliko Burundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani ni wakati wa Serikali sasa kuwekeza ku-train makocha. Hata kwenye michezo ya Commowealth juzi, mabondia wetu walikuwa wanasimamiwa na makocha kutoka Kenya kwa sababu makocha wetu hawana sifa za kukaa kwenye ring. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni viwanja vya michezo. Ni kweli viwanja vyetu katika mikoa yetu vingi, hivi vya mpira wa miguu vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi, lakini havipo kwenye hadhi nzuri. Ushauri wangu ni kwamba ili utoe product nzuri ya wachezaji lazima uwe na viwanja vizuri. Niiombe Serikali, wala siyo dhambi, kila mkoa Majimaji, Mbeya, hebu ikiwezekana wakae na Jeshi, JKT wanaweza ku-maintain hivi viwanja na vikawa katika ubora mzuri zaidi, wao wakawa wanachukua kamisheni kama Chama cha Mapinduzi. Viwanja hivi vitakuwa na ubora sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Misri, ukienda Port Said, ukienda Ismailia, viwanja vyote ni vizuri kwa sababu vinakuwa maintained na Jeshi. Badala ya JKT kushughulika na mikopo ya matrekta, huu ni wakati sasa wa ku-maintain viwanja hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa tatu. Leo tuna wachezaji wengi sana wa kigeni hapa Tanzania na tuna mokocha wengi wa kigeni hapa Tanzania. Kama kuna kosa ambalo mchezaji anayecheza kwenye nchi nyingine as an International Player or Profession anaweza kupata kosa kubwa sana kama atakwepa kodi. Lionel Messi alipata matatizo, Christiano Ronaldo alipata matatizo kwa sababu ya kukwepa kodi, Tanzania wachezaji wetu hawa wa kigeni hawalipi kodi na hata registration fee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchezaji anasajiliwa kwa milioni themanini lakini anachukua hiyo fedha anaondoka nayo kwenda nyumbani kwao, Serikali inakosa mapato. Niwaombe BMT hili jambo waliangalie. Kuna wachezaji wamesajiliwa hapa kutoka Zimbabwe, kutoka Uganda, kutoka Kenya, kutoka Ivory Coast, kutoka Benin na wengine hawana hata kiwango, lakini fedha anayolipwa kama registration fee haitozwi kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, leo hata ukimuuliza Mheshimiwa Waziri pale kwamba, hebu tuambie tu wachezaji wa kigeni kwenye registration fee walilipa kodi kiasi gani? Sidhani kama ana majawabu? Huu ndio ushauri wangu ambao nimependa niutoe leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nchi zilizoendelea kimichezo duniani fainali za FA zinafanyika Makao Makuu ya nchi ile husika, lazima tuwe na huo utamaduni kuliko mwaka jana tumecheza Dodoma, mwaka huu Arusha, keshokutwa utasikia Chemba, kutoka Chemba utaenda kucheza wapi, Mafia, eeh! Au kwa Mheshimiwa Kakoso kule. Tuwe na msimamo kwamba fainali ya FA inachezwa kwenye Makao Makuu ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhuhana – Wataala ametuamsha salama. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri mnayoifanya, Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nitazungumza kuhusu huu mradi wa Education Programme For Results (EP4R). Niwapongeze sana Wizara kwa kweli kwa sababu kwa kupitia programu hii tumeona mabadiliko makubwa sana kwenye shule za zamani au shule kongwe vilevile katika baadhi ya shule ambazo zilikuwa na hali mbaya, kwa hili kwa kweli nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yako yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukipita ukienda katika shule zilizokuwa zamani mfano Mpwapwa, Sengerema kule ambapo na mimi nilisoma ukienda Pugu, shule zimebadilika kutokana na kazi nzuri mnayoifanya. Hizi hela ni za wafadhili na mfadhili anatoa fedha anapoona unafanya vizuri lakini nasikia TAMISEMI wanataka sasa ziende kwao, Serikali ni moja tu mnagombea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara ya Elimu wanashughulika na elimu, wanatengeneza miundombinu bado TAMISEMI wanataka nao hizo fedha ziende kwao, mnataka nini? Wakati mwingine hata mfadhili anaweza tu aka-doubt kwamba kwa nini hizi fedha mnataka ziende kule TAMISEMI wakati huku pia zinasimamiwa vizuri, Serikali ni hiyo moja tu.

Nashauri Serikali kwa kuwa ni moja, acheni Wizara ya Elimu wasimamie na wanafanya vizuri tu na isitoshe hata fedha zinapokwenda kwenye Halmashauri kwenye shule zetu bado maelekezo yanatoka TAMISEMI kwamba watumie force account, hizi fedha zisimamiwe vizuri na matunda yake tunayaona, ulikuwa ni ushauri wangu wa kwanza, msigombee fito mnajenga nyumba moja, nadhani Mheshimiwa Kakunda umenielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie hizi shule za private, amesema pale kaka yangu James Mbatia kwamba shule hizi zimetoa mchango mkubwa sana. Bahati mbaya tu mimi sikusoma private, lakini watoto wangu wanasoma private. Hawa watu wa private ni Watanzania na wanaosomeshwa ni Watanzania wenzetu, tusiwaone kama competitors, hawa ni partner wa elimu ya Tanzania. Hii ni kwa sababu hata ukiangalia kodi zao ni nyingi sana lakini kodi zinazotozwa kwenye private sector kwenye elimu wanaoumia ni wazazi ambao ni Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Mheshimiwa Waziri tafuteni muda muwe mnakaa na hawa private sector ya elimu mara kwa mara, ni vizuri kushauriana kwa sababu wanatoa mchango mkubwa sana kwa kweli. Wakati mwingine pia ni vizuri kumsikiliza tatizo lake na ukilisikia vizuri inawasaidia, kwa sababu utaona hata Mheshimiwa Rais anakutana na wafanyabiashara wanajadiliana, wanafikia muafaka na wakati mwingine maamuzi yanatoka palepale. Kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni jambo jema mkaliangalia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata ufunguaji wa shule, mimi nina mtoto wangu mdogo ana miaka 10 mtoto wa mwisho, anasoma private school lakini anaamka saa kumi basi linalomchukua yule mtoto linapita saa 11 alfajiri kwa sababu madarasa yanaanza saa mbili, lakini huwa najiuliza hivi hawa watoto wanaenda kusoma au wanaenda kulala?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu angalieni hata uwezekano, kwa sababu Kamishna wa Elimu anapotoa kwamba shule zifunguliwe tarehe fulani na zifungwe tarehe fulani, hii ni changamoto kubwa sana. Hivi kuna haja ya kuanza madarasa saa mbili? Hebu angalia kwa mfano Dar es Salaam ile, mtoto anachukuliwa Mbagala anaenda kusoma Masaki au Tegeta kwa mfano, anachukuliwa saa kumi alfajiri, akifika darasani analala tu huyu. Kwa hiyo, nilikuwa nadhani hata hii mihula muiangalie pia halafu kwani ni lazima shule zifunguliwe siku moja na zifungwe siku moja, kila mtu na utaratibu wake! Nilikuwa nadhani ni jambo ambalo Mheshimiwa Waziri mliangalie, kwa sababu hata hiyo private school ukiangalia asilimia 80 ya wanafunzi wanaokwenda katika university wanatoka kwenye private school, almost 80 percent. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye form four asilimia 80 ya wanafunzi wanaokwenda A - Level wanatoka private school. Tuwajengee mazingira hawa kwa sababu wanafanya vizuri na wakati huo huo Serikali tunafanya vizuri pia katika shule zetu. Nilikuwa nadhani nitoe ushauri kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho, shule hizi wakati mwingine michezo ni kivutio kikubwa sana kwa watoto wetu kusoma, lakini michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA tumeishusha sana hadhi na heshima yake. Leo akina Zamoyoni Mogella, Mkweche, Makumbi Juma na Abeid Mziba tuliwatoa huko kwenye UMISETA, lazima tuwekeze huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ishirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Michezo ili tuwatengeneze vijana wawe wazuri. Leo tusishangilie tu kwamba timu yetu imefanya vizuri vijana hawa, lakini baada ya pale hatuna tunachokifanya, watoto wanasambaratika, hatujengi Taifa bora. Mimi nadhani na bahati nzuri Mheshimiwa Kakunda wewe ni mtu wa michezo hebu tengenezeni mazingira ili vijana hawa wa shule zetu, UMISETA na UMITASHUMTA wafanye vizuri kwenye michezo na Taifa liweze kuwekeza zaidi, kwa sababu michezo ya UMISETA ndipo unapopata vijana watakaokwenda kucheza kwenye national teams zetu, iwe riadha, iwe football, huko ndiko tunakowapata, lakini tukisubiri kuokoteza mitaani bila kuweka msingi tutakuwa tunafanya makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais alipokuteua Mheshimiwa Kakunda kwenda Wizara hii nadhani pia aliona kwamba una uwezo mkubwa sana wa kushawishi namna gani michezo ya UMISETA iwe na tija na iwe na nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya ninashukuru sana na nirudie kusema Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana, endelea kusimamia huu Mradi wa EP4R.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa dakika tano kwa sisi wataalam wa habari dakika tano ni muhtasari tu wa habari. Kwa hiyo, nitaenda straight.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kupoteza muda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kaka yangu Kitila kwa kazi nzuri mnayofanya. Mwaka jana kwenye Bunge hili nilitoa maombi kwamba iundwe Tume Maalum ya kuchunguza miradi ya maji. Mwaka huu wakati wa Ofisi ya Waziri Mkuu nilitoa ombi hilo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji ni zaidi ya makinikia, naomba Bunge liunde Tume huru ya Bunge ichunguze miradi ya maji. Nimemsikia kaka yangu hapa akisema, Mheshimiwa Rais ameanza kuchukua hatua hakuna sababu, tusimwache Rais peke yake, Bunge lina nafasi yake kama muhimili, likachunguze miradi hii ya maji lakini wakati Bunge linaunda Tume hiyo na watu wa Mambo ya Ndani wajiandae kupanua Magereza. Miradi mingi ya maji kwa Wabunge tunaotoka vijijini imekuwa ni deal tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano mmoja mdogo sana, Chemba pale tuna miradi mitatu, kwa mfano Mradi wa Goima aliyepewa ukandarasi alikuwa Afisa wa TAKUKURU. Mimi nimemkuta site huyo Afisa wa TAKUKURU ndiye Mkandarasi aliyepewa mradi wa Maji wa Goima na sasa hivi amekimbia kabisa hata Kondoa hayupo. Kelema Kuu pale umechezewa tu, hela inachezewa tu hivi halafu tukisema humu ndani tunaonekana kama watu wa hovyo hivi, hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ninaomba hata ukizunguka kukagua miradi yote Tanzania bila kuchukua hatua na ukaunda tume ya kukusaidia wewe kesho na kesho kutwa utaonekana hujafanya kazi, utapanda kwenye matenki, huwezi kupanda kwenye matenki yote Tanzania nzima. Umri wako nao unakwenda, unafanya kazi nzuri sana, lakini mwisho utakuja kuanguka kwenye matenki bila sababu. Jambo la kwanza ni kuunda Tume huru ya Bunge ifanye uchunguzi nchi nzima, miradi mikubwa na midogo inapigwa. Pili, ninakuomba Mheshimiwa Waziri mmeshafanya tathmini Bwawa la Farkwa wananchi wanasubiri fidia wako tayari kupisha ujenzi wa mradi ule wa maji. Tatu, hizi COWSOs mnazosema ni sera ya Taifa ya maji wananchi hawana utaalamu wowote wa kusimamia miradi ya maji, mkishatumia shilingi milioni 500 mnakabidhi kijiji mradi wa maji baada ya miezi miwili ama mitatu mradi unakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sera inaweza ikabadilishwa, badilisheni hii Sera ya COWSOs tuangalie namna gani ya kusimamia miradi hii ambayo imekamilika lakini leo unatengeneza mradi baada ya miezi miwili unakufa, unawakabidhi mradi wanakijiji hawana utaalamu wowote unawaambia mtasimamia huu mradi, badilisheni hii sera. Wamewaletea wazungu ikifika wakati haifai badilisha, wananchi tunachotaka ni maji siyo sera nani asimamie mradi wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Mheshimiwa Waziri ninakuomba kwa dhati kabisa njia sahihi ni kujenga mabwawa. Chemba kule tunaomba hela ya mabwawa mawili kati ya Kinkima na Churuku, kati ya Itolo na Mlongia hatuna matatizo yoyote na kujenga Bwawa la Kisangaji kule Kondoa, lakini Kondoa mmetugharimu sana kwenye Mradi wa Maji wa Ntomoko, na leo watu karibu zaidi ya 18 wanahojiwa kule Kondoa, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuchukua hatua hiyo, tujengeni mabwawa tumalize hilo tatizo.

Pia Mheshimiwa Waziri nikuombe hivi hawa DCCA wameenda kutuibia kule, wamechimba kisima cha maji pale Ovada shule ya sekondari fedha ya Serikali wamelipa milioni 32 hicho kisima hakina hata maji, tumechimba kisima kingine what kind of this? Mpaka DCCA kampuni ya Serikali nayo wezi! Nilikuwa najiuliza hivi wanalipwaje hawa watu hakuna maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, ninakuomba pamoja na kuunga mkono hoja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kw amuda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nichangie machache kwenye kamati hizi tatu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhanahu-wataala kwa kutupa afya njema.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, niipongeze sana Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya afya vinavyosimamiwa na TAMISEMI na Wizara ya Afya, wamefanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Rais kwa hili hata uchaguzi ujao kama ni 2020 au 2022 anatereza tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri iliyofanywa ya ujenzi wa vituo vya afya, zipo kasoro ndogondogo kwenye maeneo yetu, zinaweza kurekebishwa. Rai yangu na ushauri wangu kwa Serikali ni kuandaa watumishi wa kutosha watakaofanya kazi kwenye vituo hivi vya afya. Leo tutajisifu tumetengeneza vituo vya afya vizuri, vifaa vitakavyowekwa kwenye vituo hivi ni vifaa vya kisasa, je, tumejiandaa vya kutosha kuwa na programu ya kupeleka watumishi huku? Hili ni jambo ambalo nadhani kwamba ipo haja sasa Wizara ya Afya, TAMISEMI na Utumishi kuanza kuchukua hatua za haraka kwa sababu MSD tayari wameshaanza maandalizi ya kununua vifaa, nani atakwenda kuvipokea kule na hao wataalam watakaopokea wana ujuzi huo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, nije kwenye elimu. Kwa mtazamo wangu mimi nafikiri tumepoteza plot somewhere. Elimu yetu ya sasa imekuwa ni ya biashara zaidi. Vyuo vikuu karibu vyote vinaandaa extension officers na tunawafundisha vijana kwa kuwafahamisha kabisa kwamba tunawaandaa kwa ajili ya ajira, ajira zenyewe hazipo.

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri, leo pale Chemba wanafanya mahojiano ya kupata Watendaji wa Vijiji nafasi sita lakini walioomba ni 870, walioitwa 220. Juzi Chamwino hapa, walikuwa na nafasi nne za Watendaji wa Vijiji lakini walioomba walikuwa 1,500. Jeshini nimeona siku moja wameenda kwenye uwanja wa mpira wanagombea nafasi nane. Kwa hiyo, elimu yetu inawajenga watu kwa ajili ya ajira badala ya kujiajiri. Nadhani tuangalie namna gani tunaweza kufanya kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye utawala bora, lakini naomba nizungumzie mwisho kwa sababu lina changamoto yake. Kwenye walimu, siamini kama kweli tuna matatizo makubwa ya walimu ila tuna tatizo la reallocation ya walimu. Mfano ni hapa Dodoma Mjini, kuna excess ya walimu 371 lakini shule za pembezoni huko Chemba, Kongwa, Mpwapwa zina matatizo ya walimu. Kwa hiyo, TAMISEMI wakae chini waangalie, hivi tatizo ni nini? Nadhani tatizo liko hapohapo TAMISEMI, wakae chini waangalie namna gani reallocation ya walimu ilivyo, walimu wanapelekwa lakini hawakai, wanarudi kwenye shule za mjini.

Mheshimiwa Spika, lingine ninalotaka kushauri ni kwenye michezo. Niombe sana Serikali lazima tuwe na programu ya walimu wa michezo. Kwenye mpira wa mguu Taifa hili ni kubwa sana, ni aibu sana kuwa na walimu wa mpira wa mguu qualified kutoka Burundi wanakuja kufundisha mpira wa miguu Tanzania. Ni aibu kwa sababu hatuna programu ya kuwa-train wachezaji wetu wanaostaafu mpira na wenye uelewa ili waje wafundishe vilabu vyetu, kutwa kucha timu zetu za Taifa hazitafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, angalia hata ligi ya wanawake leo inachezwa nyumbani na ugenini. Timu imetoka Njombe inakwenda kucheza Mwanza hawana mahali hata pa kulala halafu mnasema waende home and away akina dada wale. Leo asubuhi Timu ya Majimaji ya Songea imekwama Dar es Salaam inashindwa kwenda Tanga, kocha wao anasema vijana wamekula jana, usiku hawajala tunategemea msaada ili tuweze kwenda Tanga, hatuwezi kuendesha mpira hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kakoso ananiambia Yanga imetoka Tanga ika-draw ikaja Singida ika-draw, ndiyo matatizo hayo.

SPIKA: Mheshimiwa Nkamia, siyo timu za akina dada peke yake zinazotembeza bakuli, zipo na timu zingine mnatembeza mabakuli tu. (Makofi/Kicheko)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli. Sikutaka kuitaja timu hiyo kwa sababu rafiki yangu Mheshimiwa Mwigulu yeye ni mfadhili wa timu zote mbili. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la utawala bora. Utawala bora siyo uchaguzi na hili naomba niliseme kwa dhati sana na wewe juzi ulitania hapa. Naomba niiseme kwa dhati sana utawala bora siyo uchaguzi kwamba tukifanya uchaguzi kila baada ya miaka miwili, mitatu ndiyo utawala bora, siamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina elimu ya kutisha sana lakini ni philosopher na sifanyi mambo bila kufanya utafiti. Nchi zote zilizoendelea duniani hazikuendelea kwa sababu ya kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitatu. Wajerumani wale leo ndiyo the leading country katika uchumi Ulaya, Angela Merkel yule mama pale amekaa miaka 16. Rwanda tunayoipigia mfano hapa ndani, tunasema inafanya vizuri sana kwenye uchumi, Kagame amekaa miaka mingapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Lionel Messi huwezi kumuweka nje eti kwa sababu amecheza mechi kumi. Tupo kwenye siasa za ushindani, ukiwa na mchezaji mzuri acha aende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sisi kama Taifa lazima tufanye maamuzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Nkamia, nakuongeza dakika tatu uhitimishe vizuri. (Makofi)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hata hao Wazungu tunaokimbilia kwao, tunakwenda kulalamika unajua hivi na hivi na wao pia wameendelea nchi zao kwa kufanya utafiti. Ukiniruhusu nipo tayari kuleta hoja yangu hapa ndani ya Bunge. (Makofi)

MWONGOZO WA SPIKA

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, mmoja kati ya watu ninaowaheshimu sana ni Mheshimiwa Mchungaji na mmoja kati ya watu wanaonisumbua sana nilete ile hoja ya miaka saba ndani ya Bunge ni pamoja na yeye. Katika kudhihirisha hilo, hata yeye mwenyewe amekosea amesema nchi yetu inaongozwa kwa vipindi vitatu wakati siyo kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba unilindie muda wangu, nilichokuwa nataka kusema ni kwamba sisi kama Taifa hata tukifanya amendment ya Katiba si tunakwenda kwa wananchi. Leo Baba Mtakatifu yuko Uarabuni, anafanya study Uarabuni kwamba hii hali ya dunia inavyokwenda sasa ikoje? Wakatoliki wengi wanahama sasa kwenda kwenye Ulokole, lazima tutafute njia nyingine ya kujua kwa nini wanahama.

Mheshimiwa Spika, mimi hoja yangu haina maana kwamba Rais Dkt. Magufuli aendelee miaka saba, hoja yangu ilikuwa na maana ukomo wa Bunge ambaye Rais ni sehemu ya Bunge. Kwa hiyo, hata waandishi wengi na ninyi wengine mliokuwa mnalalamika hapa ndani baadhi yenu, hakuna mahali nilikotaja Rais Dkt. Magufuli akae miaka saba ila ukomo wa Bunge uwe miaka saba.

MBUNGE FULANI: Rais ni sehemu ya Bunge.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mchungaji Msigwa hiyo ndiyo anaipenda sana. Nikuhakikishie hoja hii ukiiruhusu ikaja hapa ndani ya Bunge…

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Zipigwe kura za siri (anonymous)…

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Hata dakika mbili hapa kila mmoja ataomba karatasi. Naomba mniruhusu nilete.

Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapa kwa leo, nimalizie kwa kusema nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Na Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Mawaziri chapeni kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniamsha salama leo, lakini pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli, pamoja na wasaidizi wake Mheshimiwa Jafo pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianzie pale alipomalizia pale Mheshimiwa Bura kwenye suala la Madiwani. Madiwani tusiwaone ni wa maana tu pale tunapokwenda kwenye uchaguzi. Nazungumza hili kwa nini? Nataka nitoe na mifano. Madiwani wengi Tanzania, kwenye Halmashauri nyingi hata posho zao za kisheria hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, visingizio vingi vimekuwa ni mifumo ime-bust, lakini kumbe Halmashauri nyingi ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba wameshindwa kupeleka fedha za maendeleo, wamejikuta expenditure imekuwa kubwa na matokeo yake Madiwani toka mwezi wa Kumi mpaka tunavyozungumza, hata posho za vikao vyao vya kawaida wanakopwa. Mheshimiwa Waziri Jafo anajua, Mkuu wa Mkoa anajua na RAS wa Dodoma anajua. Kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba ipo haja ya kuangalia hili suala kwa kina sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Waziri, nitumie fursa hii kuwapongeza sana. Leo Chemba tuna Vituo vya Afya vitatu; viwili Alhamdulillah vimejengwa vizuri; kimoja ndiyo hivyo, tia maji tia maji, lakini tunashukuru. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri tulikwenda naye pale Hamai, na akakuta ile hali ya pale na hakuchukua hatua yoyote, japo kauli yake pale alisema hajaridhishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, nimekuwa nikiona Waheshimiwa Mawaziri wanatembea sana Tanzania hii kwenda kutatua kero za wananchi, lakini juzi nilipokuwa Kanda ya Kusini kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais, nimeona yeye ndiyo anatatua matatizo hata yale ambayo ninyi mngeweza kuyatatua. Sasa mnazunguka kufanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni vizuri mkachukua hatua pale mnapoona kuna kasoro. Kwa mfano, pale kwa Mtoro, mtu amepewa tenda ya kutengeneza milango akalipwa shilingi milioni 15 zote hajapeleka hata frame moja. Watu wa Chemba wanajua, Ofisi ya TAMISEMI inajua na Mungu anajua. Chukueni hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tukisema hapa na ninyi pale TAMISEMI kuna majungu yanaletwa sana kule, kwamba ooh, unajua Mbunge wa Chemba, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mwenyekiti wa CCM wanataka posho tu. Posho za nini? Watu wenu pale TAMISEMI wakishasikia hivyo, sisi tunaomba Mheshimiwa Waziri aunde tume ikachunguze matatizo ya Chemba, hatutaki kumwonea mtu. Chemba imekuwa shamba la bibi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri achukue hatua. Tuliomba aunde tume apeleke pale ikachunguze. Tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Chemba tunaomba tupatiwe pesa mwaka huu. Pia hata tukipewa hizo pesa, hata zile 1.4 billion mlizotupatia, yule Boya ameshajenga lile jengo anadai fedha zake shilingi milioni 150, Halmashauri haina hizo fedha. Zimeenda wapi? Hata mkitupa leo, mimi sioni faida yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya. Dakika 20 zilizopita alinipigia engineer mmoja ambaye anajenga Hospitali ya Wilaya pale Chemba, wameingia mkataba toka mwezi wa Pili, leo walikuwa wanataka kugoma kuendelea kujenga, hawajalipwa hata senti tano na fedha mmeleta. Sasa tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, chukua hatua, hii inakusaidia kukujenga pia kwa siku zijazo. Ya Mungu mengi, huwezi kujua. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana kaka yangu, chukua hatua. Leo wanataka kugoma kujenga Hospitali ya Wilaya kwa sababu hawajalipwa, fedha mmeshaleta. Kuna tatizo gani? Mkataba toka mwezi wa Pili. Au mpaka wasikie Mheshimiwa Rais anakuja? Kwa hiyo, naomba mtusaidie juu ya hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye vitambulisho vya Mheshimiwa Rais. Hili ni wazo zuri sana sana sana, lakini huko Wilayani operesheni yake inakwenda tofauti. Baadhi ya watu wanamchukia Mheshimiwa Rais kutokana na baadhi ya Watendaji walioko huko Wilayani kulifanya hili kama vita. Wewe unawezaje kugawa vitambulisho hivi vya wajasiriamali chini ya ulinzi wa Polisi? Nani atakuja kuchukua? Hivi wewe kiongozi unaanza kukurupushana na akina mama unabeba masufuria ya pilau, unawalazimisha wanunue vitambulisho, nani atachukua? Chukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuzuia Polisi wa Chemba wasiende kugawa vitambulisho vya Rais. Sasa hivi vitambulisho vinauzika sana. Yule Mkuu wangu wa Wilaya alisema, mimi na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya tunazuia. Ashindwe kwa Jina la Yesu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda mimi na Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Kakunda wakati ule, mradi wa maji wa Lahoda uliojengwa na Mkandarasi Mrimi Construction akalipwa shilingi milioni 451, hautoi hata tone moja na maji. Hata tone hakuna, wala kisima hakikuchimbwa na mtu kalipwa fedha zote. Tukisema sisi, kesho wanakuja watu TAMISEMI pale, aah, unajua Mbunge anataka rushwa. Nendeni mkachunguze ili mjue kuna rushwa kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapakaziana tu! Mtu anaandika taarifa huko, unajua Mbunge anataka rushwa, unaitwa TAKUKURU. Nenda kachunguze, kama kuna tone la maji, kama sio mimi na Mwenyekiti wangu kwenda kuwaomba watu wa RIC watusaidie pale, lakini Mrimi Construction amelipwa milioni 450…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Keissy, usinijaribu.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa Mheshimiwa Nkamia, mzungumzaji, kwamba kule kwangu Wakandarasi walimfuata Mheshimiwa Nkamia ili tuonane nao wanipe rushwa. Nikawaambia siwezi hilo jambo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nkamia, taarifa hiyo.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, kuna watu walinifuata hapa wanasema, bwana tusaidie kwa Mheshimiwa Keissy. Nikamtafuta Mheshimiwa Keissy mwenyewe, nikajua ndio hao hao. Nimeipokea kwa mikono 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba Mheshimiwa Waziri aunde Tume Maalum ichunguze matatizo yaliyoko Wilaya ya Chemba. Nashukuru Mheshimiwa Mkuchika upo wewe ni mtu mzima, naomba mtusaidie. Matatizo ya Chemba yanaweza kutuletea matatizo mengine makubwa. Haiwezekani Mkuu wa Wilaya anasimama saa sita barabarani anasimamisha magari kama traffic, yuko peke yake. Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Mkurugenzi wa Halmashauri anajenga kwa miezi miwili na anataka kuchimba kisima cha kuuza maji pale Chemba wakati watu wanakunywa maji kwenye kisima nilichochimba mimi. Where do you get money? Halafu anakwenda TAMISEMI pale, aah unajua Mbunge anataka rushwa, unajua Mwenyekiti wa Halmashauri anataka rushwa. Rushwa gani mimi? I have got my own investment bwana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwaambieni ninyi, hamtaki kuchukua hatua. Mnasubiri mpaka Mheshimiwa Rais aje? Eeh, mnapokea majungu mnayaona ya maana. Tunayowaambieni, mimi nimesema, undeni Tume ikachunguze ili mjue nani mwongo? Unapiga chapa ng’ombe milioni 290 senti tano haipo. Unatuambia mfumo ume-bust, benki una shilingi milioni 40 tu, zimeenda wapi hela? Halafu Mbunge akisema hapa, aah, unajua wale wana majungu sana wale, wale wana majungu sana wale! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda mahali wako, ukaone. Mnatuambia aah, mnajua wale ni wanasiasa tu, wanasiasa tu wale. Hata hao wote wawili pale kwangu waligombea Ubunge wakashindwa; wote ni wanasiasa. Ooh, unajua tutahakikisha Nkamia uchaguzi ujao jina lake halirudi. Kwani lisiporudi, kwa Mungu haliendi? (Kicheko/Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Nkamia.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuamsha sote salama. Mimi nitachangia mambo matatu. Kwanza, nitazungumzia kwa ufupi sana maandalizi ya Timu ya Taifa, TBC na FIFA, ZDFA na TFF na muda ukiruhusu nitazungumzia kwa ufupi sana suala la uhuru wa habari.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu wake na watendaji wote wa Wizara. Kwa namna ya pekee nimpongeze sana Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu, dada yangu Fisoo na niwapongeze pia wasanii wote wa Tanzania, wanafanya kazi nzuri na wanafanya kazi kubwa kwa sababu kazi ya usanii ni ngumu sana na inahitaji ubunifu wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ni Shirika la Umma lakini bila kuwezeshwa kuwa ni mitambo ya kisasa usikivu wake hauko vizuri sana. Mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati, nashukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa siku za karibuni imeonesha kujali Shirika hili lakini yapo maeneo haisikiki vizuri. Hata kwako kule Kongwa yapo baadhi ya maeneo haisikiki vizuri, hata kule Chemba lakini pengine nadhani Serikali ikihakikisha kwamba fedha zilizotengwa zinakwenda itasaidia zaidi TBC kusikika na kuonekana vizuri. Hata hapa Dodoma ule mtambo hauko vizuri, kwa hiyo, hata maeneo ya kwetu kule Chemba, Kondoa, Singida wakati mwingine ni tabu kusikika. Kwa hiyo, nadhani ni vizuri jambo hili Serikali ikalitilia mkazo na kuangalia pia maslahi ya wafanyakazi wa TBC, nadhani baada ya siku Shirika hili litasimama kwa miguu yake yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, naomba nizungumzie maandalizi ya Timu zetu za Taifa. Ni aibu sana na lazima tukubali kama Taifa kwamba huwezi kuandaa mashindano halafu ukashika nafasi ya mwisho. Huwa inatokea mara chache sana, hata Korea walipoandaa Kombe la Dunia waliishia robo fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kama kuna vitu ambavyo vilinishangaza ni kuona Kamati inasema vijana wale wakichukua ubingwa wanawapa magari na shilingi milioni 20. Ni sawasawa na mtoto wako wa miaka 8 ana birthday unamwambia nitakununulia gari. Kwa hiyo, kuna mahali tulipwaya kidogo na pia hatukuiandaa timu hii vizuri kwa sababu hata mashindano iliyokuwa inakwenda kwa trials ilikuwa ni bonanza. Wamekwenda Rwanda kwenye bonanza, wakaenda wapi sijui kule kwenye bonanza hatukuwaandaa vizuri. Kwa hiyo, nadhani ni vizuri sasa tuangalie in future tunawaandaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tuwaangalie wachezaji hawa wanapatikana vipi kwa sababu nikiangalia ile timu ilikuwa ina wachezaji nane (8) wanatoka timu moja ya Alliance ambayo inashika karibu nafasi ya sita (6) kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kwa hiyo, kuna tatizo hilo, nafikiri tuangalie namna gani tunaweza kuwapata vizuri.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Timu yetu ya Taifa ya Taifa Stars inakwenda kwenye michezo ya AFCON Cairo na michezo hii imesogezwa mbele tu kupisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao unatarajiwa kuanza tarehe 5. Mwezi ukiisha maana yake ni kwamba tunaenda kwenye mashindano, lazima tujiandae vizuri sasa. Tusipojiandaa vizuri tunaweza kwenda kushika mkia kwenye lile kundi, Mungu pisha mbali lakini kwa kweli lazima tujiandae vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo limekuwa likijitokeza sana ndani ya Bunge mwaka nenda miaka rudi, tangu mimi nimeingia ndani ya Bunge hapa 2010 linazungumzwa nalo ni suala la Zanzibar kuwa mwanachama wa FIFA. Kwa mujibu wa United Nation Resolution No.25, Zanzibar is not a sovereign state. FIFA inatambua sovereign state except Wales, Scotland, England na Ireland ambazo ni founder wa FIFA.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Zipo nyingi.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nenda karejee kesi iliyoamuliwa katika Mahakama ya Rufaa ya Khamis Machano. Nadhani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikae na Serikali ya Zanzibar kwa sababu nayo hii isiwe kama kero ya Muungano, Tanzania Olympic (TOC) ina mwakilishi kutoka Zanzibar ambaye kwa sasa ndiye Rais wa TOC.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ipo haja kwenye nafasi za Makamu wa Rais wa TFF mmoja akatoka Zanzibar ili kuondoa hii hali ambayo kila siku inatokea humu lakini Zanzibar kuwa mwanachama wa FIFA ni jambo gumu. (Makofi)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, tarehe 16 Juni, 2011, Timu Maalum ya Zanzibar iliyokwenda FIFA iliandikiwa barua na aliyekuwa Katibu Mkuu wakati ule Bwana Volker kwamba Zanzibar is not a sovereign state, kwa hiyo haiwezi kuwa mwanachama wa FIFA, ni suala la busara tu.

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Ally Saleh.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumwarifu kwamba kwa mujibu wa FIFA mbali ya zile nchi wanachama za awali alizozitaja lakini pia kuna nchi ambazo sio sovereign state kama Macau, Hong Kong na nyingine pia ni wanachama wa FIFA kwa sababu nyinginezo. Uanachama wa FIFA hauko-based or sovereign state tu.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ally, namheshimu sana, tumefanya naye kazi BBC na alikuwa anakaa kwangu. (Kicheko)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, pia ni rafiki yangu, kuna tofauti kubwa sana unapoizungumzia Macau…

SPIKA: Mheshimiwa Ally Saleh unabisha hilo? (Kicheko)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, sijawahi kukaa kwake. (Kicheko)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, Hong Kong, Macau siyo permanent member wa FIFA, kwa hiyo, asipotoshe Bunge. Taarifa yako nimeipokea lakini siyo sahihi na kwa sababu ni rafiki tunaheshimiana hakuna sababu ya kugombana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani hilo jambo ipo haja kwa Serikali kutumia busara.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, hata Mheshimiwa Ally Saleh anafahamu hakuna nchi isiyokuwa na sheria. Huwezi kusimama tu unasema mimi kwa sababu ni mwandishi wa habari nitukane kwa sababu kuna uhuru wa habari, hakuna. Hata huko kwa wakubwa Mheshimiwa Ally Saleh wewe shahidi hakuna mtu anaweza kuandika tu akatukana Serikali au akatukana Kiongozi yeyote kwa sababu tu kuna uhuru wa vyombo vya habari, uhuru una mipaka yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani. Leo ni kweli yapo baadhi ya magazeti yanaandika vitu vya ajabu sana and the Government is quiet. Sasa upande wa pili kule wanasema hili Gazeti la Tanzanite… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kama ni msumeno ukate kotekote. Hilo gazeti unalosema la Tanzania Daima nalo ni moja kati ya magazeti ya ovyo sana katika nchi hii na ninashangaa linaachwa. La ovyo sana na mmiliki wake yuko humu humu ndani, rafiki yangu. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Nani?

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, siwezi kumtaja, lakini yupo humu ndani na anasikia. kama hajasikia atapigiwa simu. Lazima tufike wakati kama Taifa, sheria za nchi ziheshimike. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili, Mheshimiwa Nkamia.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, jamaa alinikata pale.

SPIKA: Muda hauko upande wako.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Chemba, Wilaya ya Chemba, vipo visima kadhaa katika Kijiji cha Mondo, Daki, Chandama, Mapango, Machiga na Pangai ambavyo vimechimbwa huu ni mwaka wa pili Serikali haijatoa fedha kukamilisha miundombinu ili watu wapate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili mradi wa maji wa Ntomoko bado unasuasua na kuna dalili kwamba mradi huu hautakidhi haja ya vijiji 13 kama ilivyopangwa awali. Naiomba Serikali isimamishe kutoa shilingi milioni 800 zilizobaki kulipwa mkandarasi na zipelekwe Chemba ili zitumike kuchimba visima katika Vijiji vya Hamai, Chivuku, Kirikima, Songolo na Madaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naishauri Serikali sasa ijenge mabwawa mawili katika Vijiji vya Itolwa na Chivuku ambapo maji ya mvua yanapotea sana na hiyo itaondoa kabisa tatizo la maji katika eneo hili la Lower Irangi. Eneo hili limekuwa na shida kubwa ya maji lakini kama hatua hiyo itachukuliwa ni dhahiri tatizo hili litakuwa limekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Jumuiya ya Watumia Maji (COWSO) liangaliwe upya kwani sera hii imekuwa na tatizo kubwa na wananchi au Kamati za Maji hazina utaalam na matokeo yake miradi mingi inakufa. Nashauri Halmashauri za Wilaya zichukue jukumu la kusimamia mradi huu badala ya COWSO.

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya mradi wa maji ya bwawa la Farkwa imeanza. Naiomba Serikali ikamilishe malipo ya wananchi wa Mombose na Bubutole haraka ili kuepusha watu wanaoweza kufariki kabla ya kulipwa na matokeo yake watu wanashindwa wakawazike wapi kwa sababu tathmini ya makaburi inakuwa imeshafanywa. Naomba Serikali kabla ya kuleta maji Dodoma ianze na Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba ambapo tatizo la maji ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu hasa kwangu zaidi ni ushauri tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naiomba Serikali ichukue hatua ya kufuatilia miradi ya maji, kwa mtazamo wangu eneo hili lina ufisadi mkubwa sana. Miradi mingi inajengwa chini ya kiwango na wakati mwingine haikamiliki kwa wakati. Mfano, Mradi wa Maji Ntomoko, Wilayani Kondoa na Chemba ambapo licha ya Serikali kutoa trilioni mbili hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni ule wa Kijiji cha Laloda ambapo mkandarasi amelipwa zaidi ya milioni mia tano (Sh.500,000,000) na hakuna hata chembe ya maji inayotoka. Niiambie Serikali ikiwezekana kuunda Tume Maalum kuchunguza miradi mikubwa na midogo ya maji kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, naiomba Serikali iangalie kwa kina ukubwa wa Bunge letu, uwakilishi wake na dhana ya kubana matumizi. Nchi yetu ina Halmashauri mia moja themanini na tatu (183) na Wilaya zaidi ya 169, lakini idadi ya Wabunge ni 388. Zipo Halmashauri zina Wabunge zaidi ya mmoja na katika Wilaya yupo Mkuu wa Wilaya mmoja tu. Ushauri wangu ni kuiomba Serikali ipunguze utitiri wa majimbo na kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na Mbunge mmoja ili kupunguza gharama na kuhakikisha Bunge linakuwa active kuliko ilivyo sasa ambapo Bunge limekuwa kama mkutano wa hadhara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo pia nashauri hata utaratibu wa kuwapata Wabunge wa Viti Maalum utazamwe upya. Ushauri wangu ni kwamba kila mkoa uwe na Wabunge wawili wa Viti Maalum na hii itasaidia kupunguza idadi ya Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wabunge kutoka Zanzibar ipo hoja ya kubadilisha utaratibu uliopo sasa na kufanya kila Wilaya ya Zanzibar kuwa na Mbunge mmoja anayewakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia kuwaondoa Wabunge wanaowakilisha Baraza la Wawakilishi wanaohudumu pia Bunge la Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi sioni haja ya kuwa na Wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi kuhudhuria Mikutano ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi kwa wakati mmoja. Naamini kama ushauri huu utazingatiwa Serikali na Taifa litakuwa limepunguza gharama kubwa ya uendeshaji wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kuhusu viwanja vya michezo. Viwanja vingi vya michezo nchini vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM). Viwanja hivi vipo katika hali mbaya, nashauri Serikali ishauriane na CCM na ikiwezekana vikodishwe kwa majeshi kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo wanaweza kuviendeleza vikawa bora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru wewe, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniamsha salama na kupata nafasi hii ya kutoa mchango wangu kwenye Muswada huu ulio mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niunge mkono Muswada huu kwa nia njema tu kabisa, kwamba Muswada huu haujaanza leo na hata Bunge lililopita ilikuwa uletwe hapa kwa Hati ya Dharura. Nami ni mmoja kati ya watu waliotoa mchango mkubwa sana kwenye maandalizi ya Muswada huu. Kwa hiyo, nashangaa sana hata inapofika wakati Mheshimiwa Nape Nnauye anasingiziwa, Mheshimiwa Nape Nnauye amekuta kila kitu kimeshaiva, alichofanya yeye ni kusogeza mezani tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Habari kwa kuhakikisha Muswada huu umekuja sasa ndani ya Bunge letu. Lakini pia niishukuru sana Kamati yetu ikiongozwa na Mhesimiwa Peter Serukamba kwa kazi nzuri tuliyofanya kuhakikisha Muswada huu na sisi tunatoa mchango wetu na Serikali ikasikia na ikafanya mabadiliko kadhaa ambayo naamini yatakuwa na tija kubwa sana kwa Taifa letu na waandishi wa habari wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu ni muhimu kwa nini, kwanza kutakuwa na Bodi ya Ithibati, pili kutakuwa na Baraza huru la Habari. Niliwahi kusema hapa siku moja nikapambana sana na watu wa MCT niliposema kwamba, MCT ni NGO, lakini sasa inaundwa Bodi ambayo inatambulika kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashangaa sana baadhi ya waandishi wa habari ambao wanaupinga Muswada huu, nadhani si akili yao, kuna mtu kawatuma. Kuna mtu kawatuma, lakini wanajua kabisa kwamba, anawatuma ili jambo lao lenye manufaa kwao lisiweze kufanikiwa. Naamini huu ndio utakuwa muarobaini kwa tatizo la waandishi wa habari hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu jirani yangu pale Mheshimiwa Tundu Lissu amezungumzia suala la accreditation. Mimi nimefanya kazi maeneo mbalimbali duniani, huwezi kwenda nchi yoyote bila kuwa accredited kama mwandishi wa habari. Kazi hii si ya kuchoma mkaa, lazima uwe accredited ili watu wakujue wewe ni nani? Si kazi ya kuchoma mkaa, unaweza kuingia msituni ukakata mti tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilishangaa jana kuna mtu mmoja nasikia hapa ndani akasimama akasema Mheshimiwa Nkamia ni kanjanja! Mimi sifanyi kazi ya kuchunga mashamba ya chumvi ya Viongozi wa Chama Cha CUF kule Lindi. Mimi ni mwandishi wa Kimataifa, eeh! Kwa hiyo, kabla hujaja humu ndani kusema ingia hata kwenye google kwanza, google huyu mtu ni nani? Siyo unatumwa na wewe unakuja hivyo hivyo! Eeh, rafiki yangu Mheshimiwa Bobali, usibebe jeneza bila kujua kafa nani! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu kwa waandishi wa habari. Elimu kwa waandishi wa habari ni jambo la msingi sana, lakini pia wanasema journalism is an art. Bodi na Baraza waachiwe wafanye kazi ya kuhakikisha kwamba mwandishi wa habari huyu ni nani! Waziri anapotunga kanuni, ningemwomba sana kaka yangu Mheshimiwa Nape anapotunga kanuni awashirikishe pia na watu wachache waweze kumpa inputs za kutunga kanuni kwenye suala la elimu kwa mambo ya uandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Tido Mhando ambaye ni mwandishi anayepewa heshima kubwa, amemaliza form four tu, eeh! Ni form four leaver, lakini anaheshimika kwelikweli. Kwa hiyo, nilichokuwa nataka kusema hapa ni nini…
Subiri, usiwe na haraka. Ukitaka kula muhogo hakikisha una maji jirani, eeh!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema ni kwamba, sasa mnapotunga kanuni hakikisheni jambo hili mnaliangalia kwa makini sana. Sisi kwenye Kamati tumeliangalia na tumetoa ushauri wetu na nashukuru Serikali imelisikiliza vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Wamiliki wa Vyombo vya Habari. Jambo hili linaonekana si jema sana na watu wanajaribu kulizungumza sana huko nje kwamba, Muswada huu ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya, lakini naamini kwamba, Wamiliki wa Vyombo vya Habari inawezekana pia wenyewe hawajausoma bali wanafanya kazi kwa kusikia maneno ya uchochoroni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Muswada huu utawasaidia waandishi wa habari to the maximum na tutawaheshimu sana wandishi wa habari na wao pia wataheshimika kuliko ilivyo sasa. Mtu akimwona mwandishi wa habari anajua huyu ni mtu mwenye njaa tu na ndio maana wengi wanadharaulika, lakini Muswada huu utasaidia sana kujenga heshima ya waandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu tunakosea sana, mwandishi wa habari ni raia kama alivyo raia mwingine. Sasa mtu akija hapa ndani akisema mwandishi wa habari apewe ulinzi, Wabunge wenyewe hawana walinzi, mwandishi atapewaje ulinzi? Lazima mwandishi na yeye ajilinde mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuhusu wadau, tulipokutana kwenye Kamati wadau walipewa muda kwamba, walete mapendekezo, lakini kilichofuata walikuja wakakataa kuleta, kwa hiyo wamezira tu. Lakini mimi naamini kabisa kwamba wadau hawa wengi ni waajiriwa wa wamiliki wa vyombo vya habari kwa hiyo, inawezekana wengi wameogopa kuleta maoni yao wakiogopa mabosi wao! Ndio tatizo tatizo linapoanzia hapo tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naamini tuungane wote hapa sisi Wabunge wote; na ningeomba hata Kambi ya Upinzani hapa tulete hizi amendments tuweze kufanya marekebisho pale ambapo tunadhani panaweza kuwa na tija kwa waandishi wa habari badala ya kulalamikalalamika tu. Hata wenzetu Kambi ya Upinzani badala ya kuandikiwa hotuba na watu ambao wewe mwenyewe hujaijua vizuri unakuja kusoma hapa mbele, ni vizuri ukaandika mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini narudia tena, mimi ni mwandishi wa habari wa Kimataifa. Wale watu wanaolinda mashamba ya chumvi kule Lindi wanakuja hapa na elimu yao ya kuungaunga ya Ualimu wa UPE, wanakuja hapa wanasema Mheshimiwa Nkamia ni kanjanja waache, eeh! Kabisa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana na naunga mkono hoja.