Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Aeshi Khalfan Hilaly (16 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naamini dakika tano kwangu zitanitosha, nitaongea haraka haraka tu.
La kwanza, nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako kwa hotuba nzuri uliyotutolea, lakini kuna mambo matatu ambayo ningeomba utusaidie wakati ukija kutujibu hoja zetu. La kwanza, nimesikia kwamba Serikali itanunua mahindi tani laki moja mwaka huu, lakini naomba kujua Mheshimiwa Waziri, tunanunua mahindi lakini hatujataja bei tutanunua mahindi haya kwa bei gani? Ni vizuri mkawaeleza wananchi wakajua mahindi haya tutayanunua kwa shilingi ngapi ili wawe wanajua wasije wakauza mahindi yao, wakalanguliwa na walanguzi wengine kwa bei ya chini. (Makofi)
Kwa hiyo, ni vizuri utakapokuja hapa, uwatangazie wananchi hawa tutanunua mahindi tani laki moja, japokuwa ni ndogo, hazitoshi, lakini muwaambie wananchi hawa na wakulima kwamba tutanunua mahindi kwa bei kadhaa kama ilivyokuwa ikitokea siku za nyuma ambazo mlikuwa mkitusomea bajeti. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri ukija hapa utujibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba kuchangia kwenye suala la mbolea. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake, lakini niseme kitu kidogo. Kuna mbolea aina ya Minjingu ambayo imekuwa ikipelekwa katika mikoa mbalimbali. Naomba, hebu lichukulie suala hili kwa umakini sana na kwa uzito. Naamini wataalam wako wanafahamu; kama kweli mbolea hii inafaa, basi naomba mlichukulie kwa uzito wa hali ya juu na kama haifai, njooni mtuambie hapa, hii mbolea haifai.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimkukumbushe tu Mheshimiwa Waziri, tulikuwa na mbolea ya aina nyingine ya DAP iliyokuwa inauzwa sh. 90,000/= mpaka sh.100,000/=, lakini kilipokuja Kiwanda cha Minjingu kuanza ku-supply mbolea hii, mbolea nyingine zote zikashuka bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, mbolea hii ya Minjingu, uende kiwandani, ukawatembelee, mje mtuambie kama mbolea hii inafaa. Kama inafaa, Serikali iongeze nguvu pale, kwa sababu hii ndiyo inaweza kusaidia kushusha mbolea nyingine zote ambazo zinatoka nje.
Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa kama kweli mbolea ya Minjingu inafaa na wataalam wako wanasema inafaa, basi tuipe kipaumbele sana tuweze kuwaangalia hawa na kuweza kuwasaidia kwa sababu kaulimbiu yetu ni ya viwanda na viwanda tulivyonavyo ni hivyo, tuanze navyo, tuweze kuvi-support. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba nikiri hapa, mwaka 2015 makampuni mengi ya mbolea yalikataa kuikopesha Serikali mbolea, lakini wapo mawakala wadogo wadogo walioamua kwenda kuchukua mikopo benki wakaenda kununua mbolea ku-supply kwa wananchi lakini mpaka leo hawajalipwa. Mheshimiwa Waziri hebu, lichukulie hili, hawa mawakala ni wadogo, wamekopa fedha za riba, lakini mpaka leo mwezi wa Saba huu mawakala hawa hawajaweza kulipwa fedha zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, hawa mawakala mara nyingi wanakuwa wakituokoa sana; hawa wakubwa wanapogoma, mawakala wadogo wanaweza wakatusaidia, nasi tuwaone!
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni suala la uvuvi. Naomba nizungumzie uvuvi kidogo kwa sababu nimebakiwa na dakika tatu. Mheshimiwa Waziri wavuvi hawa wanaumizwa sana. Leseni zimekuwa za kila aina! Ukimwangalia mwenye mtumbwi, anachajiwa leseni, mwenye wavu anachajiwa leseni, mvuvi mmojammoja anaachajiwa leseni, akivua tena dagaa hizo hizo leseni, akisafirisha Dar es Salaam leseni. Hebu angalieni hili Mheshimiwa Waziri mfute hizi leseni maana yake kodi zimekuwa nyingi mno kwa mtu mmoja. Kwa hiyo, tumekuwa tukiwaonea sana wavuvi bila kuangalia ni jinsi gani wanavyoteseka katika uvuvi kwa wanaokwenda huko kwenye shughuli za kujitafutia maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siongei mengi, nilitaka kukumbusha tu haya machache ambayo nimeona kwamba Mheshimiwa Waziri anapokuja kutujibu atuambie, suala la bei ya mahindi, atuambie mbolea ya Minjingu kama inafaa, lakini vilevile atuambie mawakala hawa wataweza kulipwa lini fedha zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, lakini vilevile kuipongeza Wizara yote ya Ujenzi.
Mimi ndani ya Jimbo langu la Sumbawanga Mjini kwa kweli, wananchi kupitia mimi, nitoe shukrani zangu nyingi sana za dhati, tumepata barabara zote kwa kiwango cha lami, zimejengwa na zimekamilika ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwa hoja moja tu ya uwanja wa ndege. Kwenye bajeti ya mwaka huu uwanja wa ndege ndani ya Jimbo la Sumbwanga Mjini unajengwa. Sasa wako baadhi ya Wabunge wametaka kupinga wakisema uwanja wa ndege ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini usijengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme ukweli, uwanja wa ndege wa Sumbawanga ukijengwa utarahisisha mambo mengi; na uwanja wa ndege unapojengwa eneo lolote lile ni maendeleo makubwa. Sasa nataka niseme, mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri bajeti hii iende kama ambavyo imepangwa na wananchi wa Sumbawanga walikusikia na wamefurahi sana na mimi kama Mbunge nasema hivi, ninaunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nilitaka niwashauri Wabunge, kila Mbunge amechaguliwa jimboni kwake na wananchi wake. Mimi nimehangaika miaka mitano kuhakikisha tunapata bajeti ya kujenga uwanja wa ndege na hatimaye tumefanikiwa, ninaomba kila Mbunge akalilie jimbo lake. Na Waheshimiwa wengine waliokuwa wanasema tusijenge uwanja wa ndege, basi kwao wakajenge reli hiyo siyo kwangu, mimi kwangu sihitaji reli, nahitaji uwanja wa ndege. Barabara ya lami ninayo, nataka sasa uwanja wa ndege ujengwe ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema hivi kwa sababu Wabunge hawa wanaopinga uwanja wa ndege ndiyo wanaosafiri kutoka Wilayani kwao wanapita Wilaya ya Jimbo la Sumbawanga Mjini wanakwenda Mbeya kufuata uwanja wa ndege. Sasa tunataka tuwarahisishie, uwanja ukijengwa Sumbawanga hawatasafiri kwa muda mrefu. Kwa hiyo, nataka niseme tu kuwa Mheshimiwa Waziri nakuunga mkono na nitatetea hoja hii, ilimradi kuanzia mwaka huu uwanja huo utajengwa na wananchi wa Sumbawanga watapanda ndege kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kutoka Sumbawanga kwenda Dar es Salaam tunapanda kwa shilingi 900,000, lakini uwanja utakapokuwa umekamilika tutapanda kwa shilingi 200,000, mtakuwa mmetusaidia mno.
Kwa hiyo, nasema kwa haya machache kwa dakika tano ulizonipa, nilitaka kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri kwamba, tunaomba sasa uwanja huu wa ndege ujengwe kama tulivyokuwa tumekusudia kwenye bajeti yako. Ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi njema na kazi nzuri anayoifanya kwa kuwatumikia wananchi ambapo mpaka sasa ninaamini kabisa kwamba Rais ndiyo mzalendo namba moja wa nchi yetu hii kwa kazi kubwa sana ambayo ameweza kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache sana ya kuchangia na Wabunge wenzangu wengi wamechangia, lakini nataka kuchangia suala la CAG kupewa fedha ndogo. Sioni dhamira ya dhati au dhamira njema ya Serikali yetu katika suala la kuhakikisha tunawamaliza kabisa mafisadi nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha tulizowapa CAG ni fedha ambayo itatosheleza tu kulipa mishahara na kuendesha ofisi pale, hatutoweza kwenda mbali zaidi kufuatilia fedha zetu ambazo leo hii Serikali yetu ya CCM imesema elimu bure mpaka shule ya msingi, mpaka shule ya sekondari na fedha tumepeleka, nani wa kuzifuatlia fedha zile? Sasa ninaona kuna shida, Waziri atuambie ana dhamira gani au ana chuki gani au Bunge mtuambie CAG ni adui wa Serikali? Na kama ni adui tujue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake mimi nijuavyo, CAG ndiyo anaetusaidia sisi kuona, CAG ndiye anayeweza kutuambia wapi kumeibiwa fedha Bunge likaenda kufuatilia. Kwa hiyo, ninavyojua CAG ndiye jicho la Serikali yetu na Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Leo Serikali yetu, Waziri wa Fedha unampa fedha ndogo sana ambazo ninaamini yeyote yule ambaye anataka kujua ufisadi upo wapi lazima tumtumie CAG, fedha hana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema leo kwamba akiwa amepungukiwa fedha aje agonge tena mlango, usipomfungulia mlango, aende wapi? Kwa hiyo, ninataka Waziri ukija utuambie CAG ni mtumishi wa Serikali? CAG ni adui wetu? CAG ni nani, ni shetani au ni mtu gani? Tujue. Maana yake tunakua tunamtenga, tukimchukia bila sababu yoyote ya msingi na leo hii unamwambia aje akuombe fedha tena, atakuwa akija kukuomba mara kwa mara mwisho wa siku atakuwa anakupigia magoti hatoweza kukuchunguza, hatoweza kukukagua na dhamira ya Serikali yetu na Rais wetu ni kuhakikisha mafisadi wote tunawateketeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunampa fedha kiasi kidogo, tunawezesha watu wengine, mfano tunaenda kumpa TAKUKURU shilingi bilioni 72. Ili TAKUKURU afanyekazi vizuri anamtegemea CAG avumbue maovu kule, leo tunampa fedha kiasi kidogo asiweze kufanya kazi. Hili naomba sana tulisimamie, Wabunge kama kweli Wabunge kazi yetu ni hiyo basi naomba tulisimamie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Waziri wa fedha, ninakumbuka kwenye party caucus ukija kujitambulisha kama Mbunge na Waziri, kuna kauli ulisema leo hii nataka kuiamini. Ulisema Wabunge tusitegemee kukupenda. Hili leo umekuja kusema Wabunge tukatwe kiinua mgongo chetu kodi, Mbunge peke yake tena unasema narudia ili wananchi watuchukie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani niseme hili Wabunge msikilize, katika hili wananchi hawataweza kutuchukia, wataendelea kutupenda kwa sababu nusu ya fedha hizi asilimia 60 zinakwenda kwao. Inawezekana Mheshimiwa labda hujui uchungu wa Jimbo. Sisi ndiyo tunaojua uchungu wa majimbo yetu. Kwa nini iwe ni kwa Mbunge peke yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema ukarudia tena, narudia tena, narudia tena ili wananchi wasikilize, Wabunge tukupigie makofi na mimi nasema Wapinzani walikuja hapa wakasema na wenyewe wanaunga mkono hoja, nilitaka kucheka sana.
Mimi nataka niseme mimi leo nasema hivi, kama atatokea Mbunge yeyote wa CHADEMA akaja akaandika hapa barua kwako, kwamba mimi naomba nikatwe kiinua mgongo na posho hizi kwa barua na mimi nitakuwa wa kwanza kukatwa. Mnikate! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hii Mheshimiwa Waziri uliitoa wapi, umekuja kuwapa ajenda isiyokuwepo hapa, hili sijui limetoka wapi? Maana yake hawa jamaa tulikuwa tumeshawaua, wanakuja wanasema na wenyewe wanaunga mkono hoja. Nataka niseme, waje hapa Wabunge wa CHADEMA hususani Mheshimiwa Silinde aandike barua kwa maandishi yake kwamba na mimi niwe wa kwanza kukatwa posho na mimi niwe wa kwanza kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo changu na mimi nitakuwa wa pili kutoka yeye.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Hamna, hatoweza kuja hapa. Sasa hii tusiwe tunawapa hapa kila siku sababu ya kusema. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri ukija hapa kodi zetu kwenye kiinua mgongo ifutwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kuongelea kuhusiana na suala la kilimo. Tumetoa kodi kwenye mazao mbalimbali, tunatoa kodi tukitegemea kwamba tutazalisha, lakini ninavyojua wafanyabiashara hawa mawakala wadogo wadogo walioamua kukopa mabenki na kwenda kuwakopesha wakulima pembejeo, mpaka leo fedha hizi hawajalipwa, mwaka wa pili unakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha hebu liangalie hili, wapeni fedha hawa Kilimo wawalipe hawa wakulima, wakawalipe hawa mawakala ili mwaka huu waweze kuagiza mbolea kutoka nje, waje huko wawakopeshe tena wakulima. Lakini mpaka leo fedha hizo hakuna. Sasa tutategemea nini? Mnasema kilimo uti wa mgongo, kilimo ndiyo tunakitegemea, nashindwa kuelewa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kabla muda haujakwisha ni suala la afya. Wizara ya Afya wamepewa fedha ndogo. Kutokana na kukosekana kwa fedha tumejikuta tuna majengo ambayo yalijengwa na Taasisi ya Benjamin William Mkapa, ndani ya Mkoa wa Rukwa mpaka leo hayajafunguliwa kwa kukosa fedha. Matokeo yake mwaka wa tatu sasa unakwenda, majengo yanaharibika na unajua majengo yasipotumika yanaenda yanashuka thamani siku hadi siku. Wapeni fedha wakafungue zahanati zile na majengo yale ili yaweze kufanya kazi. (Makofi)
Nheshimiwa Naibu Spika, mwisho najua bado dakika nyingi kengele ya kwanza hiyo! Kuhusu suala la kodi kwenye transit goods tumeingiza VAT, lakini ninavyojua anayetakiwa kulipa VAT ni yule mtumiaji wa mwisho! leo mzigo unatoka hapa unakwenda Zambia, wanalipia VAT. Mzigo unatoka hapa unakwenda Congo tunalipia VAT. Mwisho wa siku hawa wasafirishaji watatuhama watakwenda kwenye bandari nyingine. Hivi kwa nini hili hatulisikii? Kwa nini tunapowashauri Serikali hamtaki kusikia? Nataka niulize hii Kamati ya Bajeti ina kazi gani? Kama maoni yao yote hakuna hata moja iliyochukuliwa, futa Kamati ya Bajeti, eeh!(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana tumeweka Kamati ya Bajeti kuishauri Serikali lakini hakuna hata moja kwa kumsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, anasema mambo yote hayajaungwa mkono hata moja na Waziri. Toa chini wanatumia fedha nyingi, sasa hivi wako kwenye vikao wanakaa kule, hakuna lolote linaweza kuchukuliwa.
Mimi nasema kwa uchungu sana, nina nia njema na nchi yetu, lengo la Wabunge ni kuiongoza nchi yetu, tuwashauri Mawaziri, tuishauri Serikali ili tuweze kwenda kule tunakotaka kwenda na kule ambapo Rais wetu anataka kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ana dhamira njema sana lakini inawezekana tunampotosha, kuna baadhi ya mambo hatumwambii ukweli. Sasa hao wasafirishaji wakihama wakihamia Beira, wakahamia Mombasa, bandari yetu inakufa. Tulikuwa na nia ya kuongeza bandari ya pili kutokana na mizigo kuwa mingi leo hii ukienda bandarini mizigo inapungua. Itapungua leo, itapungua kesho, itapungua siku hadi siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kuna suala la kodi kwenye crude oil ambayo leo yamewekwa mwaka jana na mwaka juzi uliopita tuliondoa kodi hiyo kwasababu tuliona kama ni raw material anayekuja hapa ili viwanda viweze kutengeneza mafuta ya kula.

TAARIFA.....

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sina kampuni, kampuni ya baba ile, siyo ya kwangu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongelea kuhusu crude oil, mafuta yetu ya kupikia. Tumeongeza kodi kwenye viwanda vyetu vinavyotengeneza mafuta na sasa hivi tumeweka kodi ya raw material inayotoka nje ili iweze kuzalishwa wananchi wetu hawa waweze kupata mafuta kwa bei nafuu, sasa tumembana kote kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumembana kwa wakulima hawa wanaozalisha alizeti, anapoenda kuuza kiwandani yale mafuta yanapotoka pale yanakuwa na kodi, lakini vilevile tumewabana sasa hawa waagizaji mafuta ya crude oil inayotoka nje na yenyewe imewekwa kodi. Lengo letu ni kuinua viwanda, dhamira ya dhati ya Rais ni kujenga viwanda na hawa wawekezaji wanasema walitaka kuomba waongezewe angalau mwaka mmoja mbele ili viwanda vya hapa nchini viwe vimekamilika waweze kuzalisha hapa crude oil. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi lakini nimuombe Waziri pale ambapo tunakuwa tunawashauri basi haya tunayowashauri wayachukue kwa sababu sisi tunawawakilisha wananchi na haya tunayoyaongelea hapa ni mawazo ya wananchi ili muweze kuyafanyia kazi na tuendelee pale ambapo Rais anapotaka tufike. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa kunipa nafasi tena kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini.
Jambo la pili naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, ninaamini Watanzania wote tuko nyuma yake kumwombea Mungu ili aendelee na kazi hii nzuri aliyokuwa ameianza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la tatu, nawapongeza Mawaziri wote walioteuliwa. Naomba niwakumbushe tu wengi wenu tulikuwa huku nyuma, tunakaa pamoja, lakini mmetuacha, mmetangulia, naomba mtumtendee haki kwa sababu na sisi ipo siku tutakuja kukaa huko mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie masuala matatu, lakini katika masuala hayo yapo ambayo inawezekana kwa njia moja au nyingine isiwaguse Mawaziri waliopo mbele yetu hapo; Mheshimiwa Simbachawene, Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Angellah Kairuki, ni kutokana na majukumu niliyonayo. Inawezekana wakati huo wa kuchangia muda mwingine nisiwepo, Mawaziri waliokuwepo waya-note, wayachukue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la kwanza ni kuhusiana na uwanja wa ndege. Sumbawanga tumejaliwa kuwa na mambo mengi, lakini yapo mengi ambayo tumeyatekeleza kwa mwaka 2010/2015, lakini yapo machache ambayo tulikuwa hatujayakamilisha, ni pamoja na uwanja wa ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeiona bajeti hii ambayo ninaamini tumepata fedha za kujenga uwanja wa ndege, lakini kuna shida moja naomba ichukuliwe kwa sababu wakati tunafanya tathmini ya yale majengo ambayo wananchi wanatakiwa walipwe fidia, tathmini ile imechukua miaka saba sasa. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwenye bajeti hii tumetenga fedha za uwanja ndege, lakini tumetenga fedha kwa tathmini ya miaka sita iliyopoita. Kwa hiyo, naomba sasa tathmini ile ifanywe upya ili wananchi wapate haki yao na waweze kujenga kutokana na gharama zilizopo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ambalo ni kero kwa wananchi; na kwa hili naomba nichukue nafasi kumpongeza Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi, kwa kazi kubwa aliyoifanya mpaka hapa tulipo leo. Isipokuwa shamba lile la Malonje limekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi na Mheshimiwa Waziri alisema atakuwa ni mtu wa mwisho kuongelea shamba lile. Sasa nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, alifanyie kazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimpe nguvu tu Mheshimiwa Waziri, kwa sababu shamba hili linahusiana na watu wa TAMISEMI na Mheshimiwa Waziri unanisikia, basi naomba tulifanyie kazi ili wananchi waweze kupata shamba lile lililokuwa ni kero kubwa na sisi tunazingatia kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo, lakini naamini kabisa kilimo ni ajira. Tukiwapa ardhi wale wananchi, wanaweza wakalima na wakapata mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Rais, mgombea wetu alipokuja Sumbawanga kwenye kampeni aliniahidi, akasema endapo mtamchagua Aeshi, chochote atakachoniomba nitampa. Mimi naomba nimwambie Mheshimiwa Rais, sihitaji Uwaziri, wala Unaibu Waziri, naomba anisaidie shamba lile liweze kurudi kwa wananchi. Ninaamini uwezo huo anao na anaweza akatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, ni maji. Mheshimiwa Waziri tuna mradi mkubwa sana wa maji wa shilingi bilioni 32, mradi ambao tumeweza kujenga miundombinu yote, lakini shida imekuja kila tukichimba kisima hakina maji. Sasa nataka niseme maji ya kutoka Lake Tanganyika tungeweza kuyapata kwa sababu kutoka Lake Tanganyika – Kasanga kuja Sumbawanga ni kilometa 90. Ninaamini kabisa endapo tukipata fedha, tukajenga mradi ule wa maji wa kutoka Lake Tanganyika - Kasanga ukapita Matai na Sumbawanga vijiji vyote vitaweza kufanikiwa kupata maji. Kwa hiyo, nataka niseme tu, jambo hili tuliangalie kwa umakini, endapo tutapata fedha, basi tujaribu kutafuta njia moja ama nyingine ya kuweza kutoa maji Lake Tanganyika ambayo yataweza kuwanufaisha watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni kuhusiana na umeme. Tumepeleka vijiji vingi sana lakini bado vijiji vichache ili tuweze kufanikisha Jimbo lote la Sumbawanga mjini kuwa na umeme. Kwa hiyo, Waziri anayehusika na dhamana ya umeme, naomba naye alichukue kwa sababu kwa upande wa CCM kwa sababu tupo wengi, inakuwa ni vigumu sana kupata nafasi ya kuchangia mara ya pili.
Mwisho kabisa ni kuhusiana na meli MV. Liemba. Tumeona kwenye bajeti kwamba MV. Liemba itafanyiwa marekebisho, nasikitika sana! Meli ile mara ya mwisho nilipanda nikaona kuna jenereta imewekwa juu kabisa kule, ipo nje na ni hatari kubwa. Vilevile meli ile imekuwa ni ya muda mrefu sana, ina umri zaidi ya miaka 120, wananchi bado wanaendelea kuitumia meli ile, ni hatari kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama tumeweza kununua meli Ziwa Victoria, basi ni vizuri sasa na Lake Tanganyika tukakumbukwa angalau kwa meli moja ya kuanzia. Baada ya kusema hayo machache, naomba haya machache niliyoongea, naamini ni ya muhimu ndani ya Jimbo langu la Sumbawanga Mjini, mengi nimeyafanya kama Mbunge, mengi nimeyakamilisha, haya machache ukiyakamilisha mwaka 2020 napita bila kupingwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Mpango wa Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza awali ya yote nataka niliweke Bunge sawa. Wabunge tulioko humu ndani tunatoka maeneo tofauti tofauti. Wako ambao wanatoka maeneo ambapo wanachi wanalima mahindi, karafuu, pamba au korosho. Ni wajibu wa kila Mbunge kuhakikisha anatetea maeneo anakotoka, lakini vilevile kuhakikisha anaitetea Tanzania nzima kwa ujumla kwa jambo analoliona haliko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilisikia hotuba ya Mbunge mmoja akiponda Wabunge wengine wanaotetea maslahi ya wananchi wao. Imetokea na desturi mbaya sana ndani ya Bunge hili, wako watu wanaojifanya wao ni wema sana kuliko wengine, wako watu wanaojifanya wao wako karibu sana na viongozi wa juu kuliko watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya jana ya Mheshimiwa Musukuma kutupinga sisi Wabunge tunaotetea suala la wakulima wa mahindi lilitukera sana sana. Ukilala na mgonjwa utajua matatizo ya mgonjwa, inawezekana Mheshimiwa Musukuma anakotoka hakuna wakulima. Sisi tuna wakulima ambao tunatakiwa tuwatetee kwa nguvu zote, hili limetukera sana. Niwaombe tu Wabunge kama unachangia, changia yale unayoweza wewe kuyasema ndani ya Bunge usiwakere wenzako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye hoja sasa, nimepitia taarifa ya Mheshimiwa Mpango. Katika kurasa zake zote hakuna sehemu aliyomkumbuka mkulima na wenzangu wote wamechangia kuhusiana na kilimo lakini hawa wote waliotoka hapa, wale wote waliochangia suala kubwa linahusiana na kilimo na kilimo ndiyo uti wa mgongo. Asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo yanakera sana, Serikali haieleweki nini inafanya. Hili nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimamie. Serikali inapiga marufuku mazao yetu tusiende kuuza nje lakini haina uwezo wa kuyanunua mahindi yale. Sasa ifike wakati mkulima huyo ambaye anatupa kura nyingi sana sisi, mkulima huyo ambaye anahangaika sana kuhakikisha Taifa hili halipati njaa, basi tumkumbuke na kuhakikisha kama tunazuia mazao yasiende nje, basi tuyanunue, lakini kununua hatununui, kuwaruhusu kuuza nje hatuwaruhusu, matokeo yake tunataka kuzuia mfumuko wa bei kwa kumuumiza mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa kilo tano za mbegu ni Sh.12,500/= lakini leo gunia la mahindi ni Sh.25,000/ = mpaka Sh.30,000/= na mbolea ni Sh.65,000 mpaka Sh.70,000/=. Mkulima ili apate mbegu na mbolea ya heka moja anahitaji auze gunia zaidi ya 10, tunamwonea sana mkulima. Leo hii Mbunge mwenzangu alikuja na hoja akaomba mwongozo lakini kwa bahati mbaya alikosea Kanuni, kesho tutajipanga tena upya ili tuliamshe dude humu ndani, Wabunge tusimame kwa umoja kuhakikisha tunawatetea wakulima na Serikali ije na kauli kwamba kama imeshindwa kununua, basi iwaruhusu kuuza yale mazao yao. Kama tunaongelea Mpango wa Maendeleo na uchumi wa nchi ni lazima tuhakikishe tunamtetea na kumsaidia mkulima ili kilimo kile kiwe na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuja na kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, wananchi wakafurahi sana, wakaunga mkono kauli mbiu hiyo, lakini leo tumekuja na kauli mbiu nyingine mpya ya viwanda. Hata hivyo, bila kilimo viwanda havipo, sasa sijui tunakwenda wapi. Kila nikipitia hii hotuba yote ya Mheshimiwa Mpango inahusiana na kodi tu, tunakusanya kodi, tutakusanya kodi, hao tunaowatoza kodi kila siku wamechoka sasa hivi hawana kiasi chochote cha kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atusaidie, wako baadhi ya watu wanaoidai Serikali, wako wakandarasi wanaoidai Serikali lakini na Serikali inawadai kodi. Kuna tabia imejitokeza, huyo mfanyabiashara anayedaiwa kodi anazuiliwa biashara zake, anauziwa vitu vyake wakati na yeye upande wa pili anaidai Serikali kwa nini wasikae chini wakapiga hesabu zao na mwisho wa siku kama anaidai Serikali imkate deni moja kwa moja kuliko kumfungia biashara yake na mwisho wa siku anapoteza dira. Sasa kama tunataka uchumi mzuri, basi tuhakikishe na hawa wanaotudai tunawalipa ili waweze kuendelea na biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea uvuvi, katika mtu anayeteseka ni pamoja na mvuvi wa Lake Tanganyika. Mvuvi mmoja ana leseni zaidi ya 10 au 20, mvuvi huyo huyo akitoka Kirando akihamia wilaya nyingine anatakiwa akate leseni mpya, boti hilo hilo moja la uvuvi lina wavuvi 12 kila mvuvi ana leseni na kila mvuvi anailipia. Sasa wavuvi wanahama wanatoka Wilaya ya Nkasi wataenda Wilaya ya Tanganyika, wakitoka Wilaya ya Tanganyika watakwenda Lagosi, kote kule mvuvi analipia leseni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza ukamkuta mvuvi ana leseni zaidi ya 100, hivi tunakwenda wapi? Kwa nini tusiweke utaratibu wa mvuvi mmoja kuwa na leseni moja kwa sababu ziwa lile ni letu wote, ziwa ni moja hakuna maziwa mengine pale Lake Tanganyika lakini huyu mvuvi tunamwonea siku hadi siku. Ifike wakati kama tunataka kuinua uchumi wa nchi hii basi na huyu mvuvi aangaliwe kwa jicho lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hivi Mheshimiwa Waziri amesomeshwa na mtu gani? Ni mvuvi, mkulima, mfanyabiashara au mtoza kodi? Nataka akija hapa aje anijibu kama alisomeshwa na mkulima lazima awe na uchungu na wakulima, kama alisomeshwa na wavuvi atakuwa na uchungu na uvuvi na hatimaye kwenye Mpango wake humu angewaweka watu hawa akawapa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi inawezekana labda alisomeshwa na mtoza kodi maana humu ndani ni kodi, kodi; atakamua ng’ombe maziwa na hatimaye atakamua damu. Naomba sana akija kujibu hapa atusaidie, kwanza atuambie kama Serikali haina uwezo wa kununua mahindi iruhusu twende tukauze kokote tunakotaka. Huyu mkulima wanamwonea mno kila wakiamka wao ni kumbana tu lakini siyo wajibu wa mkulima kuhakikisha mwananchi hafi na njaa, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake hawafi na njaa, sasa sisi leo ni kumbana tu ooh bwana chakula kimepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeshindwa na Zambia, mahindi yanatoka Zambia yanakwenda Kenya on transit hapa, sisi tumebaki tunatazama tu tunasema kuna njaa, kuna njaa, kuna njaa. Naomba Waziri akija atuambie kama ana uwezo wa kununua mahindi atuambie atanunua mahindi, kama uwezo wa fedha hatuna turuhusu mahindi yaende yakauzwe nje kwa sababu nakumbuka kauli ya Mheshimiwa Rais ambaye sisi wote tunampenda na tunampigania alisema kwamba, mkulima auze mahindi kwa bei yoyote anayotaka, akiuza Sh.100,000/= au Sh.200,000/= sawa ni kama vile mvuvi au mfugaji ambaye hatumuingilii chochote kile kwenye mifugo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina uchungu sana na mkulima. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alitudanganya hapa, Waziri huyu ni jeuri sana kwa sababu amesema ameanza kununua mahindi na sasa hivi wametenga shilingi bilioni 40 kuhakikisha mahindi yananunuliwa. Jamani mbona wanasema uongo kila siku? Hakuna hata chembe ya gunia moja lililonunuliwa kutoka Rukwa, Katavi na Mbeya halafu wanakuja kutuambia wametoa fedha za kununua mahindi, hivi kuna Mbunge asiyejua kinachoendelea ndani ya Jimbo lake? Nani? Kila kukicha ukiamka asubuhi meseji unazo kwa hiyo unajua kila kitu kinachoendelea ndani ya Jimbo lako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo Waziri wa Kilimo anadanganya kwamba ametoa fedha za kwenda kununua mazao, hakuna fedha yoyote iliyotoka kwenda kununua mazao isipokuwa wamekopa shilingi bilioni mbili kutoka CRDB na hatimaye wamezipeleka Njombe na Songea, sasa kule Sumbawanga ni Tanzania au ni Tanganyika? Kule Katavi ni Tanzania au Zambia? Kwa nini wanakuwa na ubaguzi wa hali ya juu at least wangegawa kidogo kidogo lakini hatimaye mahindi hawanunui, wanawadanganya wananchi, wanakaa wanawabeza wakulima.

Mheshimiwa Spika, kama kungekuwa na uwezo wa kutoka na shilingi hapa ningetoka nayo, lakini kwa Mpango huu kesho tutakuja na ajenda nyingine hapa, tutakuja na Kanuni nyingine mpya ili kuhakikisha kesho Bunge linasimama pamoja kuhakikisha Serikali inatoa kauli ya kununua mazao yale au kuyaruhusu yaweze kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba nisubiri majibu ya Mheshimiwa Waziri na baadaye naweza nikaunga mkono hoja au nisiunge mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia Mheshimiwa Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurudi salama na kuja kuwatumikia wananchi wa Jamhuri wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii tena kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kuwatumikia wananchi hawa. Nisiwe mchoyo wa fadhila kutoa shukrani kwa Wabunge wote walio humu ndani kwa heshima kubwa waliyonayo mbele ya Waziri Mkuu ndiyo maana unaona Bunge letu hili sasa hivi liko salama salmini. Laiti isingekuwa mahusiano mazuri na Waziri Mkuu leo hii Mawaziri wengine tungeshikana mashati humu ndani ngumi zingeruka, lakini haijawahi tokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongee mambo machache sana lakini yanayohusiana na Mkoa wangu wa Rukwa. Kama inavyojulikana sisi tunatoka Nyanda za Juu Kusini lakini zao letu kubwa ni mahindi. Nimeiona bajeti NFRA waliomba shilingi bilioni 86 lakini Wizara ya Fedha imetenga shilingi bilioni 15. Ni nini dhamira ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhusiana na hawa wakulima wanaolima zao la mahindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa wakiongelea mambo mengi, nimeona wakiongelea kilimo cha pamba, korosho, katani, tumbaku lakini bila kulima mahindi hawa wanaolima tumbaku watakula nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli NFRA wametengewa shilingi bilioni 15 na naamini shilingi bilioni 15 zinatosha tu kwenye Wilaya moja tena Wilaya ya Sumbawanga Mjini kwa mahindi ambayo tunalima kwa wingi. Sasa ombi langu ni kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ananisikiliza, endapo Serikali haitakuwa na uwezo wa kununua mahindi haya ambayo wakulima wameyalima basi Serikali isifunge mipaka, iache mahindi yawe huru kila mtu akauze anapotaka kwa sababu mwaka jana mlifunga mipaka mlikuja kufungua mipaka dakika za mwisho kwa masharti makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilimfuata Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na kumweleza kuna wakulima au wafanyabiashara wadogo wadogo wenye gunia 10 au 15 wanataka kuvuka kwenda Congo, Kigoma leo hii mwambao wa Lake Tanganyika imekuwa ni rushwa kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ananisikiliza; kama hawana uwezo wa kununua mahindi wawaachie wakulima wakauze mahindi wanapotaka. Watakuja hapa kama alivyosema Mheshimiwa Bashe mwaka huu, watazuia tena mahindi tusipeleke nje ili waweze kusingizia kwamba, hakuna mfumuko wa bei, wanawaumiza wakulima, hawana soko la kuuza mahindi yao, matokeo yake wamemweka mkulima ndiyo ngao ya kuhakikisha wananchi wa Tanzania hawafi na njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii si kazi ya mkulima, ni kazi ya Serikali kuhakikisha mkulima au mwananchi wa Tanzania hawezi kufa na njaa, mkulima mnambania kila eneo, kila sehemu na vikwazo juu ya vikwazo. Nimwombe tu Mheshimiwa Waziri kwa kweli mwaka huu kama itatokea wanafunga mipaka mimi nitakuwa wa kwanza kushikana mashati humu ndani ya Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sambamba na kilimo kuna mateso mengine yanawapata wavuvi wa Ziwa Tanganyika. Hawa Mawaziri mimi sijui Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Ulega tulimtegemea sana kama Mbunge kijana na Naibu Waziri kwamba atakuwa kimbilio la wavuvi; matokeo yake amekwenda kule amekutana na Waziri mwingine kazi yao imekuwa kuwaadhibu tu wavuvi, choma nyavu na mitumbwi, nyanga’anya huyu, piga faini huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu niambie huyu mkulima anateseka, mvuvi anateseka nani kimbilio letu sisi wakati wa uchaguzi? Semeni tu maana imekuwa ni matamko tu, nafikiri kuna kasoro au tatizo ndani ya Wizara zetu na nafikiri labda kuna baadhi ya Mawaziri wanataka kumhujumu Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ana dhamira njema sana lakini kila kukicha nyavu zimechomwa, maboti yamechomwa, faini kubwa, mkulima hana pa kuuza mahindi, Mheshimiwa Tizeba ameinuka mbolea hakuna, yaani tabu juu ya tabu, vitu vinapandana siku hadi siku hakuna unafuu wowote kwenye hizi Wizara mbili, ni mateso juu ya mateso mpaka hata ngo’mbe wenyewe wanateswa sasa hivi wanapigwa mihuri siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Tizeba na Waziri wa Mifugo, hebu watupe afueni kidogo, tupumue sisi huko tunakotoka, matokeo yake sisi ndiyo tunaotakiwa kuwatetea, sasa tunakuwa tukiongea siku hadi siku na hawatusikilizi, matokeo yake tunakuwa kama tunaimba nyimbo bila sababu yoyote ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee barabara ya kutoka Sumbawanga – Tunduma, haijawahi tokea, ina kilometa 234 lakini ina matuta 240, matuta ni mengi kuliko kilomita tulizokuwa nazo kutoka Tunduma - Sumbawanga. Nataka nitoe mfano tu, Mheshimiwa Mipata alitoka India kufanyiwa operesheni ya mgongo ametua na ndege pale Airport Songwe kapanda gari kufika Sumbawanga mgongo umemrudia tena kutokana na matuta yalivyokuwa mengi kupita kiasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu ananisikiliza, Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu sijui ananisikia au wanaongea, sijajua; matuta yamekuwa mengi, tumwombe sana Mheshimiwa Waziri wajaribu kupunguza matuta haya, ni kero kubwa kuliko ambavyo tulitegemea kupata barabara ya lami yenye manufaa na wananchi. Sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hilo alichukue na alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni kuhusiana na meli, Lake Tanganyika. Kila nikisikia hapa nasikia Mwanza meli mpya, tishali jipya, hivi Lake Tanganyika tumerogwa? Tuna meli toka uhuru mpaka leo hatuna meli nyingine yoyote ile. Wananchi hawa wanateseka mno na ukiangalia ile meli kwa kweli hata ng’ombe hatakiwi kupanda kwenye ile meli lakini leo kila kitu kinaachwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu afanye ziara siku moja aende akaitembelee ile meli aone athari zake na uchakavu wake ulivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kiwanja cha ndege. Tumekuwa na mvutano wa muda mrefu sana lakini uwanja wetu wa ndege naamini ukikamilika utaleta tija kubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa hususan Jimbo la Sumbawanga Mjini. Tunapokuwa na kiwanja cha ndege na ndege zetu ambazo sasa hivi zimepatikana zikifika Sumbawanga tutarahisisha hata wawekezaji kufika ndani ya mikoa yetu na hata watalii kuja kwenye mikoa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka juzi tumepitisha bajeti ya kujenga uwanja, bajeti ya mwaka jana tumepitisha tutajenga uwanja, bajeti ya mwaka huu nimeona tunajenga uwanja, sasa sijajua labda ni uwanja mkubwa sana kuliko wa Dar es Salaam au ni uwanja mkubwa kuliko Dodoma kwa sababu kila mwaka tunapitisha bajeti, ifike wakati iwe mwisho. Kama bajeti ya mwaka huu itapita watuambie sasa wananchi wetu wasubirie uwanja wa ndege kama utajengwa au hautajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa kubwa tunalolililia sisi, wale wananchi wanaozunguka uwanja wa ndege toka wamefanyiwa tathmini ya malipo huu ni mwaka wa kumi wakati huo bei ilikuwa iko chini leo hii vifaa vya ujenzi vimepanda, viwanja vimepanda, sasa sijui fidia hii tutawalipa kiasi gani. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ifike mahali wananchi hawa ni wa kwetu sisi na sisi ndiyo tunaowatetea. Tuwe na moyo wa imani jamani, Mungu ametufundisha tuwe na upendo, tusali, tuombe Mungu, tuwasaidie na wale wasiokuwa na uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya wanapokuwa Mawaziri wanajisahau na bahati mbaya sana wakiwa huko sijui huwa kuna kitu gani kinapita, huwa wanajisahau kabisa kama na nyie ni Wabunge kama sisi. Wakirudi nyuma huku ndiyo wanaanza kuomba miongozo na kadhalika, lakini wakiwa huko wanajisahau kabisa, Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aangalie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nitawazungumzia watumishi hawa wa darasa la saba kama walivyosema Waheshimiwa Waunge wenzangu. Sumbawanga tuna dereva anaitwa Mapugilo ambaye alishawahi kumwendesha Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Injinia Stella Manyanya, kamwendesha vizuri, kaendesha Mawaziri wengine vizuri, kamwendesha Mkuu wa Mkoa, Waziri Mkuu Mstaafu, akija Sumbawanga gari la Mkuu wa Mkoa analotumia anayemwendesha ni Mapugilo, darasa la saba, lakini leo wameenda kuwatumbua, leo hii wamefukuza madereva wengi wa darasa la saba ambapo naamini kabisa udereva sio elimu, udereva ni ujuzi. Dereva anaweza kukuendesha hata kama hajui kuandika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, naamini kwa hili wanalisikiliza, warudisheni watu hawa. Warudisheni Watendaji wa Vijiji ambao wenyewe tuliwaajiri kwa cheo cha darasa la saba. Jamani tuwe na imani, hawa tunaowaonea ni binadamu kama sisi, inawezekana kwa njia moja au nyingine hatujui au hatuna ndugu ambao wanateseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukimwangalia Mapugilo hana nyuma hana mbele, kafanya kazi leo mwaka wa 50 bado miaka mitano astaafu leo hii tunamfukuza, hivi kweli utu uko wapi? Wakulima shida, wafanyabiashara shida, madereva wa darasa la saba shida…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayoifanya na hatimaye wananchi wote watanzania wote kwa ujumla wameridhika na mwendo kasi anaokwenda nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu kwamba tumuombe Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema aendelee kututumikia sisi wananchi ambao kwa sasa tunaimani kubwa sana kwa yale yote ambayo ameanza nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya hapa ndani ya Bunge, lakini vilevile amekuwa ni mwepesi pale anaposikia kuna tatizo basi anakwenda haraka sana na kwenda kulitatua tatizo lile ambalo sisi kama Wabunge huwa tunatoa miongozo humu ndani na mwisho wa siku inawezekana taarifa ikawa ya uwongo au ya kweli lakini alikuwa mtu mwepesi wa kwenda kulishugulikia tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tatu naomba niwapongeze sana mawaziri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu namfahamu vizuri sana ni mchapakazi na mzalendo lakini Mheshimiwa Engineer Masauni ambaye ni kijana mwezangu tumekuwa tukifahamiana kwa kweli ni wazalendo wawili ambao wamekidhi kushika nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja tatu lakini moja nimekuwa nikilia ndani ya Bunge Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumekuwa tukipitisha bajeti kila mwaka kuhusiana na uwanja wa ndege wa Sumbawanga Mjini, uwanja ule una faida kubwa sana kwetu lakini mwaka juzi nilipiga makofi hapa nikapiga kelele na hatimaye nikaahidiwa kujengewa uwanja wa ndege na bajeti ikapita, mwaka jana vivyohivyo na mwaka huu Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu ameisema, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameitaja tena kaitaja mara mbili uwanja wa ndege wa Sumbawanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu nipate uhakika tu kutoka kwake wakati anakuja kutujibu mwaka huu ni kweli tutafanikiwa kujengewa uwanja wa ndege hilo nataka nilipate kwa sababu juzi tumeenda kumzika mzee wetu Mheshimiwa Marehemu Mzee Mzindakaya tulikuwa na Mheshimiwa Spika tumepata shida sana kutua katika uwanja ule. Na yeye mwenyewe Mheshimiwa Spika akaridhika na akaahidi ndani kwa wananchi pale kwamba kwa mwaka huu wa fedha atajitahidi kupambana kuhakikisha kwamba uwanja wa ndege ule unajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikuombe sana kama una viwanja kumi unataka kujenga mwaka huu kiwanja namba moja kiwe kiwanja cha Sumbawanga Mjini ni aibu kubwa tunaposafiri sisi kutoka hapa mpaka Mpanda wakati Mpanda imezaliwa kutoka Mkoa wa Rukwa wana uwanja wa ndege wa lami Sumbawanga hatuna uwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Songwe wameweza kupata uwanja wa ndege kabla ya Sumbawanga kwa hiyo utaangalia kero tunayoipata sisi Wabunge, lakini na wananchi pamoja na Mheshimiwa Rais mwenyewe wakati anasafiri kuja kwenye kampeni kero kubwa…

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa!

T A A R I F A

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimpe mzungumzaji taarifa kwamba ule Mkoa wa Songwe huko Mkoa wa Mbeya na sio Mkoa wa Songwe kwa hiyo hata sisi Mkoa wa Songwe tunahitaji bado kiwanja ahsante (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hilaly.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naipokea taarifa lakini nataka niseme ukitaka kujua kero hiyo waulize viongozi waliopita Mkoa wa Rukwa wanashuka Mbeya, kutoka Mbeya uwanja wa Songwe mpaka uikute Sumbawanga kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga kuna matuta zaidi ya mia 250 na hayo matuta kwa bahati mbaya sana Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi hayuko hapa, lakini Mheshimiwa Kamwele ambaye alikuwa Waziri pale aliahidi mbele ya marehemu Mheshimiwa Rais John Pombe Mafuguli kwamba ndani ya miezi mitatu atakuwa ameondoa yale matuta, yale matuta ni kero kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukuombe kama matuta hayawezekani kuondolewa uwanja wa ndege iwe kipaumbele cha kwanza mwaka huu tujengewe uwanja wandenge ili uweze kurahisisha usafiri wa kwenda maeneo yale. Maeneo ya Rukwa yana vivutio vingi sana vya utalii lakini hatuwezi kupata watalii kuja kule wakiangalia kero ya usafiri ya kutoka Dar es salaam mpaka uikute Sumbawanga kwa hiyo utakuta unachenji karibuni mara tatu mara nne kubadilisha usafiri ili uweze kufika Sumbawanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa uzalendo wenu kwa uchapakazi wenu, kwa urafiki wenu baina nyie na mimi mwaka huu ule uwanja utajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili hoja yangu ya pili ni kuhusiana na property tax, Serikali ina nia njema sana na naunga mkono zoezi hilo lakini linanipa changamoto kidogo nikasema nijaribu kuchangia bajeti hii ni nzuri lakini nikasema nichangie kwa sababu ya wasiwasi na wasiwasi ni akili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunachaji kupitia kwenye hizi LUKU za TANESCO lakini bahati mbaya kuna nyumba nyingine kiwanja kimoja zimejengwa nyumba nne na kila nyumba moja ina LUKU ya kwake sasa sijui kama tutakuwa tunalipa property tax au tutakuwa tunalipa kila mpangaji ana lipa ile kodi nilitaka nijue nifafanulie kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimejikuta Dar es Salaam pale kuna mtu ana apartments zaidi ya 20 au 30 na kila mtu ana LUKU yake. Sasa ile property tax maana yake ni nini? Ni kodi ya jengo au ni kodi ambayo kila mpangaji anatakiwa alipe? Hilo unatakiwa unipe ufafanuzi kidogo kwa sababu nimekaa nikiwaza sana sipati majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo haliniingii akilini. Nimekuwa nikilalamika hapa Bungeni na kwenye Kamati nilipokuwepo. Kuna hawa watu wanaotengeneza LUKU kuwauzia TANESCO. Nitatoa mfano wa Kampuni wanatengeneza LUKU wanawauzia TANESCO, baadaye wanakuja kutengeneza sub meter, inatengenezwa na huyo anawauzia wananchi ambao ni wawekezaji wanaojenga apartments hizi, wale wanafunga LUKU zao wenyewe, wananunua umeme kutoka TANESCO wanawauzia wananchi wale ambao ni wapangaji, wao wananunua kwa shilingi 380 kwa uniti lakini wao wanawauzia shilingi 500 kwa uniti moja, sasa ninataka nijue je, Serikali imeruhusu wafanyabiashara kuuza umeme ambao unazalishwa na TANESCO? Ninachokijua mimi ni kwamba mfanyabiashara au mwekezaji anaweza akazalisha umeme akawauzia TANESCO na TANESCO wajibu wake ni kuwauzia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zimeibuka kampuni nyingi na kwa bahati mbaya sana kampuni hiyohiyo inatengeneza tokens inauza bila Serikali kujua. Ile kodi anayouza kwa faida anamlipa nani? Mheshimiwa Waziri wa Fedha jambo hili liangaliwe sana. Watu wa TANESCO wanafahamu na hii ndiyo biashara yao baina ya TANESCO na hao ambao wanauza umeme kwa wapangaji wadogo wadogo.

Nitakutolea mfano, mtu ana jengo lenye kama apartments kumi, ananunua umeme wa TANESCO anafunga LUKU ya TANESCO moja halafu anachukua sub meter anafunga. Wale waliofungiwa sub meter wananunua tena token ambazo Serikali au TANESCO hawafaidiki na chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo kuna vitu viwili kwanza wanavunja sheria, lakini la pili, wanatengeneza faida. Je, ile faida tunawajibikaje sisi kama Serikali tunapata wapi kodi kutokana na hilo jambo? Mheshimiwa Waziri nikuombe, kama utapata nafasi mniite niwaeleze kwa sababu jambo hili nimekuwa nikilifuatilia sana ni wakwepaji wakubwa wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu lingine ni kwamba kwenye nyumba hizi nyingine kama National Housing, tunafungulia luku za TANESCO ambazo kila mwananchi aliyepanga atalipa moja kwa moja property tax kupitia luku. Je, hawa waliofungiwa sub meters wanamlipa nani hiyo kodi ya pango? Tunaijua? Hatuijui! Ipo kwenye mfumo? Haipo kwenye mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo nataka niseme liangalie hili, TANESCO wanafahamu tatizo hili na tumekuwa tukihoji sana, nani kawapa leseni ya kuuza hizo tokens? Na watengenezaji wapo. Wale wafuatilieni muone miaka mitano hii hiyo biashara waliyokuwa wanaifanya wamemlipa nani kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niipongeze Serikali imeweza kuangalia Madiwani wakasema wanaweza wakalipwa moja kwa moja kutoka Wizarani. Tumeangalia Makatibu Tarafa, tutawalipa laki moja kutoka Wizarani, lakini tumeacha changamoto moja ya Watendaji wa Kata ambao na wenyewe tumewaongezea posho shilingi laki moja, lakini umetoa maelekezo kwamba shilingi laki moja hizi zitalipwa moja kwa moja na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kutengeneza tatizo lingine. Watakopwa wale jamaa mpaka mwisho, na hakuna Mtendaji wa Kata atakwenda kumfuata Mkurugenzi wake akadai malimbikizo ya madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninataka niseme kwamba huu mfumo ambao tumeuanzisha mwanzo kwamba Madiwani watalipwa moja kwa moja kutoka Hazina na Makatibu Tarafa watalipwa posho ya shilingi laki moja, na Watendaji ambao tumewaongezea shilingi laki moja walipwe moja kwa moja kupitia Hazina. Tukiwaruhusu wapewe na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani hizo hela hawatazipata kamwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, hilo ninakuomba kwamba kama kuna uwezekano basi na hizi posho za Watendaji wa Kata zihamishiwe moja kwa moja Hazina ili waweze kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ulikuwa ni huo. Lakini kubwa ni suala la TANESCO na LUKU na hizi sub meters ambazo zinasambazwa kwenye apartments nani anawajibika katika hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote naomba niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa wenyeviti wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja mbili tu, kwanza nilitaka nilikumbushe Bunge siyo kila mtu anayechangia humu ndani kwa maslahi ya Taifa inaonekana kuna jambo limepita au kuna mtu amenunuliwa au kuna rushwa imefanyika ni lazima kama Wabunge tuko hapa kwa ajili ya kuwakilisha wananchi, lile ambalo tunaliona haliendi sawa tuna umuhimu wa kuja kulisema hapa na Serikali iweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile upande wa Waheshimiwa Mawaziri pale wanapoona kuna tatizo basi walisimamie hili jambo liweze kuisha kuliko kuwa na uwoga wa kutokulisimamia jambo ambalo tunaona haliendi sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilikuwa Makamu Menyekiti wa Hesabu za Serikali, tulikuwa na mgogoro wa uwekezaji kule Kigamboni katika mradi wa Dege ECO Village. Spika aliagiza na baada ya kuagiza Kamati ikakaa na baada ya Kamati kukaa, ikaunda Kamati ndogo kufuatilia jambo hili, majibu yakaja ndani ya Bunge, Bunge likapitisha Azimio lakini cha kushangaza baada ya Bunge kuvunjwa Mkurugenzi wa NSSF pamoja nafikiri na Waziri labda anaweza kuwa anahusika sina uhakika sana, ikachukuliwa maamuzi ya kumkamata Mwekezaji na kumuweka ndani siku 21 na kumnyang’anya kila kitu ambacho alikuwa amewekeza katika mradi ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi ni mkubwa sana, Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika mradi wa Dege Eco Village ambao uko Kigamboni. Sasa matokeo yake mradi ule umekuwa magofu haujulikani uko wapi, ukienda Serikalini kuuliza wanakwambia mradi huu tumeuchukua umeuchukua kwa njia gani, haijulikani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni kwamba tumemkamata Mwekezaji tukauchukua kwa kumlazimisha, leo Serikali imechukua ule mradi unatafuta Mwekezaji mwingine uweze kuuza, wasiwasi wangu na angalizo langu ni kwamba mwakani au baada ya muda mchache Mwekezaji anaweza kwenda Mahakamani na akashinda kesi ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaiomba Serikali ije na majibu mazuri. Kwanza ituambie ni njia ipi iliyotumia kuweza kumnyang’anya mwekezaji share zake. Pili, mradi ule ulikuwa na Wakandarasi wako site, wale Wakandarasi wanalipwa na nani? Mradi umechukuliwa lakini wale Wakandarasi wanadai fedha zao. Je, Serikali italipa au ndiyo wanadhulumiwa moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linasikitisha sana kulikuwa na Wakandarasi zaidi ya 20 pale, yuko Mkandarasi Mkuu wako ma-subcontract wengi sana walikuwa wamefanyakazi pale. Lakini mpaka leo hawajalipwa pesa na mradi umechukuliwa na Serikali sasa nani atakayelipwa ninamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu hii taasisi iko chini yake, aweze kutuletea majibu anapokuja kufanya majumuisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa zaidi ambalo nimeliona ni vizuri Serikali ikafahamu, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameongelea suala la SGR hapa kwamba ni mradi mzuri unakwenda vizuri tumeanza na loti namba moja tumekuja na loti namba mbili na sasa hivi tunaelekea loti namba tatu na tunaelekea kumaliza na loti namba nne mpaka namba tano na namba sita, naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa sana iliyoifanya. Lakini ninaona kuna changamoto na changamoto hiyo nisipoiongelea nitakuwa siyo mzalendo wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kujenga loti namba moja, tumejenga loti namba mbili tukaruka tukaenda kujenga loti namba tano. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, Wajumbe wa Kamati wenzangu wengine wako hapa, tulipoenda kukagua maeneo yote tumeridhika kabisa na maeneo namba moja na namba mbili tumeenda namba tano tumekuta hali si shwari, Mkandarasi wa pale amejenga kwa asilimia Nne tu mpaka sasa na ana muda wa mwaka mmoja na miezi minne lakini hakuna jambo lolote lililofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu inakuja tumetangaza tender nyingine loti namba sita ambayo inatoka Tabora kwenda Kigoma hapa kuna harufu mbaya sana ya rushwa, Waziri anatumia madaraka vibaya ya kutumia neno linaitwa single source kugawa kazi kwenye makampuni ambayo hayana sifa. Mkandarasi aliyeshinda nafasi hiyo ambayo amepewa tender ya kujenga barabara ya kutoka Tabora kwenda Kigoma, Mkandarasi huyu ndiye anayejenga loti Namba Five ambaye amejenga asilimia Nne, na sasa hivi wanampa kujenga loti Namba Sita kwa single source.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii single source nataka niijue inatumia vigezo gani ili kuweza kumpa Mkandarasi aweze kuendelea na mradi mwingine.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa anayezungumza sasa hivi Mheshimiwa Mbunge, kwamba wakati tunakagua mkandarasi huyu wa China katika loti hiyo ambayo anaisema ya Isaka Mwanza, tuligundua mapungufu makubwa sana mojawapo ikiwa ni matatizo ya kiusalama kwa wafanyakazi hata First Aid Kit hakuna, ambulance zinazotakiwa ziwepo hakuna, hata sasa hivi kama unavyosema muda aliopewa hadi sasa ni asilimia Nne tu. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba angekuwa na sifa ya kupewa hiyo single source ni yule aliye perform vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nataka nimpe hiyo taarifa.

MWENYEKITI; Ahsante, na muda wako ndiyo kama hivyo Mheshimiwa Aeshi.

MHE. AESHI. K. HILALY: Hapana!

MWENYEKITI: Basi hitimisha hoja yako kwa dakika moja Mheshimiwa.

MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ngoja niendelee, nimeipokea taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa nitapunguza taarifa kwa sababu muda upo mwishoni halafu wachangiaji lazima wamalizie wale wawili, malizia Mheshimiwa Aeshi kwa dakika moja.

MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa, lakini la msingi hapo ninataka kusisitiza ni kwamba Mkandarasi huyu ambaye ameshindwa ku-perform amepewa tena tender ya kujenga kutoka Tabora kwenda Kigoma. Hoja ya single source ni pale Mkandarasi anapo-perform vizuri, anapofanyakazi vizuri ndiyo apewe kazi nyingine. Sasa mtu ambaye amejenga kwa asilimia Nne, hatujajua anajenga kwa kiwango gani tunamuongezea kazi nyingine ambayo hii hata asilimia 10 hajafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo ni kwamba kuna vitu havifanyiki sawa, nasi Wabunge hatutakiwi kukaa kimya.

MWENYEKITI: Ahsante. hata hivyo muda wako umekwisha.

MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza kusababisha watu kutaka kutoa rushwa, hatuwezi kukubali. Ninaiomba Serikali ije sasa na majibu mengine au iangalie upya utaratibu uliofanyika hauko sawa. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua mchango anaosema Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Aeshi nilitaka nitoe taarifa kwamba loti Namba Tano tangu ianze ilikuwa haijawahi kupata financing, fedha iliyokuwa inatoka ilikuwa ni fedha ambayo ilikuwa inawekwa akiba toka Serikalini. Hivi ninavyoongea ndiyo tunamalizia evaluation ya financing ya loti yote kuanzia Namba Three, Namba Four na Namba Five. Kwa hiyo, kwa sababu financing yake haikuwepo ni dhahiri kwamba kusinge kuwepo na kasi kubwa sana ya loti Namba Tano kwa sababu hakukuwahi kuwa na financing ambazo ziko attached na loti hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hili ambalo amelisema nadhani ni michakato ndiyo inaanza hamna mtu ameshapewa kazi nadhani ni michakato ambayo inaendelea.

Michakato ikiwa inaendelea hatuwezi tuka-conclude kwamba kuna tatizo kwamba kuna mtu amepewa.

MHE. AESHI K. HILALY: Taarifa ya Mheshimiwa Mwigulu siipokei, kwa sababu haiingii akilini mtu ambaye amejenga kwa asilimia Nne hata kama fedha haijapatikana, halafu mtu huyo huyo mnaanza mazungumzo naye tena ya awali ya kumpa kazi nyingine ambapo kazi ya kwanza hajaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya ukandarasi lazima awe na uwezo, kama uwezo anao angeanza kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka hili uliweke sawa, kuna jambo hapa haliko sawa kabisa. Mheshimiwa Waziri anataka kuhalalisha jambo ambalo halipo, bado dakika moja nilikuwa nahesabu hapa.

MWENYEKITI: Hitimisha hoja yako sasa.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninahitimisha. Ninaiomba Serikali iangalie upya utaratibu huu wanaotaka kuufanya, utaratibu huu wa single source unataka kutumika vibaya, unataka kuhalalisha vitu ambavyo hatutoweza kukubali wala kuvifumbia macho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona na kwa kunipa dakika tano zilizobaki na naomba kuchangia maeneo machache sana. Kubwa napenda kuchangia suala la kilimo na Wizara ya Kilimo kwa ujumla pale ambapo Serikali tumepoteza zaidi ya shilingi bilioni sita kwa mahindi yaliyoharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ilipitia taarifa hii, kimsingi tumesikitishwa sana na hatua zilizochukuliwa kwa Wakurugenzi wa Idara ile. Mwaka 2013/2014 Serikali ilitoa maagizo kwamba wananchi wasiuze mazao yao nje ya nchi na Serikali itanunua mahindi yote. Kwa bahati nzuri wananchi walilima mahindi mengi sana na kwa bahati nzuri Serikali ilianza kununua mahindi yale, lakini kwa bahati mbaya mahindi mengi yalirundikana Serikali ikawa haina uwezo wa kuyanunua. Ikafikia mwezi wa Novemba mvua zikaanza kunyesha, mahindi yakaharibika yakiwa nje hayajapokelewa na NFRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa Bungeni Serikali ilitoa tamko kwamba mahindi yote yaliyoko nje yanunuliwe na Serikali. Hapo ndipo kilipotokea kituko kwamba wananchi waliiuzia mahindi NFRA kwa mkopo, hatukuwa na uwezo wa kulipa mahindi yale. Mwaka 2014 kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sehemu nyingi tulipoteza nafasi zile kwa sababu wanachi walisema tumewakopa mahindi hatujawalipa. Cha kushangaza mahindi haya yalivyotunzwa yakiwa yameloana na mvua yaliharibika, lakini juzi miezi mitano iliyopita Serikali iliamua kuyauza mahindi yale mabovu. Tukapoteza takribani shilingi bilioni sita na pesa za ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nachangia jambo hili? Waziri wa Kilimo aliyekuwa wakati huo, Mheshimiwa Mwigulu Mchemba aliidhinisha mahindi yale mabovu yauzwe. Baadaye Waziri wa Kilimo akahamishwa akachaguliwa Waziri mwingine mpya, Mheshimiwa Tizeba, haikuchukua siku mbili akawafukuza kazi Wakurugenzi wote bila makosa. Sasa nataka aje Waziri atueleze ni njia ipi aliyotumia au ni utafiti upi aliofanya na kuwasimamisha kazi Wakurugenzi wale bila kosa lolote kwa sababu mahindi yale yaliharibika kutokana na idhini ya Serikali tununue mahindi yaliyoloana na mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inauma mtu ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu, mtu ambaye amelitumikia Taifa hili kwa uaminifu na kwa kazi ya kutukuka lakini anakuja mtu kumtumbua jipu bila kosa lolote. Nataka niseme tunamuomba Waziri wa Kilimo aje atutolee sababu ipi aliyotumia kuwasimamisha kazi Wakurugenzi wa Idara ile ya NFRA? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kubwa ambalo ni la kushangaza, tuna Meneja anatokea Mkoa wa Rukwa, amekaa Mkoa wa Rukwa takribani miaka 15, hana kosa lolote, kahamishwa kwenda Mkoa wa Songea ndani ya wiki mbili lakini kosa lile la kununua mahindi mabovu linamkuta yeye na yeye anasimamishwa kazi. Haki iko wapi? Mtu afanye nini ili alitumikie Taifa kwa uaminifu mkubwa? Kwa hiyo, sisi kama Kamati tunamuomba Mheshimiwa Waziri aje atujibu hatua zipi alichukua yeye kwenda kuwasimamisha kazi watu bila kuwa na kosa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kila mtu anataka aonekane anafanya kazi ndani ya Serikali. Kila mtu anataka aonekane anachukua jukumu lake kusimamia watu wengine, lakini hili sisi kama Kamati tunamtaka Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aje atujibu kwa nini aliwachukulia hatua wale bila kuwa na kosa lolote wakati kosa lilitokea tukiwa hapa Bungeni mwaka 2014. Tumuulize Waziri wa Kilimo aliyepita kwa nini aliruhusu mahindi yale yauzwe mabovu? Mbona yeye hakuwasimamisha kazi? Yeye hakuliona hili? Aliliona lakini wale walishindwa kwa sababu walikuwa wanasubiri ripoti…
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi ya kuongea kwa sababu muda wa dakika tano ni mfupi, naamini jioni nitakuja hapa kuongea tena dakika 15 zingine lakini namuomba Mheshimiwa Waziri aje atujibu katika hili. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi na uwajibikaji mzuri na kila Mbunge ndani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakuamini kwa asilimia mia kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia maeneo machache sana katika bajeti hii na kwanza, ni suala la maji.
Ndani ya Mji wa Sumbawanga Mjini tuna mradi mkubwa sana wa maji ambao napenda sana kwa niaba ya wananchi niwashukuruni sana kwa mradi ule. Sumbawanga sio mji peke yake pale mjini, Sumbawanga imezungukwa na vijiji vingi sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu mliangalie hili, mtusaidie kupata fedha za kuwezesha miradi ile midogo midogo ili wananchi wanaozunguka Mji wa Sumbawanga waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni la wafanyabiashara. Nataka kuongelea sana wafanyabiashara hususan wa Jimbo la Sumbawanga Mjini wengi ni wakandarasi na wengi wamefanya kazi ndani ya Seri kali, lakini ni muda mrefu sana hawajapata malipo yao. Hao watu
wanaumia sana kwa sababu wanadaiwa kodi, kwenye mabenki na kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linanishangaza Mheshimiwa Waziri Mkuu tumeunda kamati kila Mkoa ya kudai madeni ya wafanyabiashara ambao hawajalipa kodi. Kamati hiyo wameandika barua sehemu mbalimbali pamoja na kuzuia fedha ambazo wakandarasi
wamefanyia kazi Manispaa au taasisi nyingine, wakizuia fedha zile zote hawa watu wanakwama. Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu hili suala la kamati ambazo mmeziunda mikoani ziongozwe na watu wa TRA kwa sababu wao ni wataalam na wamesomea kazi hiyo. Nilikuwa nataka
nizungumzie hili ili mliangalie kwa uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo, wameongea Wabunge wengi na jana nimekusikiliza ukiongea na hawa mawakala wa pembejeo na umeahidi kwamba ifikapo tarehe 26 at least wachache watakuwa wameshaanza kulipwa wale ambao wamehakikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaumiza sana, watu hawa wamekopa kwenye mabenki na watu hawa kama mnakumbuka, nataka niweke kumbukumbu sawa wafanyabiashara au mawakala wakubwa walikataa kuikopesha Serikali. Wafanyabiashara wadogo wadogo hao
wakaenda kukopa fedha benki wakaenda ku-supply pembejeo na bahati nzuri tukapita kwenye uchaguzi vizuri sana, lakini baada ya uchaguzi kupita hawa watu hatujawakumbuka.
Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi wana imani kubwa sana na Serikali hii, liangalieni hili kwa jicho lingine watu wanaumia sana, watu wamekufa, watu wana presha na wengine wamejinyonga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni la kusikitisha, mwaka jana kwenye bajeti wakati tunapitisha hapa masuala ya pembejeo na kutoa ruzuku kwenye mbolea tukaichagua TFC iwe mwakilishi wetu. TFC ndiyo wamekuwa walanguzi wakubwa. Mheshimiwa Zitto amechangia hapa amesema umtume CAG, nikuombe kabla hujamtuma CAG msimamishe huyu Mkurugenzi wa TFC ana miaka 20 yupo pale, ana kampuni binafsi ya kwake. Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe sana kabla hujamtuma CAG kwenda kuhakiki au kuchunguza, kwanza huyu Mkurugenzi wa TFC mumsimamishe kazi. Jana mmemsimamisha mmoja, lakini huyu ni wa pili ili akae pembeni uchunguzi ufanyike. Nikuombe sana na naamini hili unalisikia ulichukulie kwa uzito wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni uwanja wa ndege. Uwanja wa ndege tumepata bajeti, tumeshatafuta mwekezaji, uwanja wa ndege utajengwa ndani ya Mji wa Sumbawanga Mjini, shida kubwa nayoiona ni wale wananchi wanaouzunguka uwanja wa ndege. Wale wananchi
wanaozunguka uwanja ule walifanyiwa tathmini miaka sita au saba iliyopita, gharama za ujenzi zimeongezeka na gharama za viwanja zimeongezeka. Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Simbachawene yuko hapa kwa sababu wanaotakiwa kuwalipa fidia sio Idara ya Ujenzi, hapana, wanotakiwa kuwalipa fidia wananchi ni sisi TAMISEMI kupitia Manispaa. Naomba tufanye tathmini upya kulingana
na wakati uliopo. Nafikiri hili Mheshimiwa utakuwa umelichukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni kuhusiana na umeme. Sumbawanga Mjini tumebahatika tuna umeme na hatuna mgao wowote lakini Sumbawanga imezungukwa na vijiji mbalimbali. Kwa bahati nzuri vijiji vingine vyote vimepata umeme tatizo kubwa ambalo naliona na nilishamwambia Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini na ameahidi kunisaidia ni vijiji ambavyo vinatoka nje ya barabara kilometa
tano kutoka barabarani, wale watu hawakubahatika kupata umeme. Hata hivyo, kwenye REA III nimeona baadhi ya vijiji vipo na niishukuru sana Serikali katika hilo. Niombe tu Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini naye aje azindue mradi huo wa REA III ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kuongelea kuhusiana na minara ya simu. Minara hii ya simu ni michache sana. Yapo baadhi ya maeneo hayana kabisa network.
Niwaombe Wizara inayohusika na jambo hili lichukulie kwa uangalifu mkubwa na kwa nguvu kubwa kuhakikisha sasa Tanzania nzima inafikika na Tanzania nzima mawasiliano yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika hili hili ni kuomba tu Serikali iwekeze TTCL, iache maeneo mengine iongeze nguvu TTCL ili na yenyewe iwe kama kampuni nyingine tulizonazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mengi ya kuongea lakini mengine nimeamua kuyaacha kwa sababu maalum. Nimalizie tu na suala la Bunge Sport Club.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ulikua kocha wetu. Kwenye bajeti ya mwaka huu tumeona mmetujali kidogo lakini ikumbukwe sisi tuna ugeni mwaka huu kwa sababu sisi ni wenyeji wa mashindano hayo.
Mheshimiwa Mwenyeki, nikuombe sana bajeti tuliyonayo japokuwa mmetuongeza haitutoshi kulingana na ugeni mkubwa ambao tutakuwa tumeupokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama taifa tusiingie aibu. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu uliangalie hili kwa sababu wewe ulikuwa kocha wetu.
Mashindano yakianza tutakuomba rasmi uombe likizo kidogo uwe kocha ili tuweze kuchukua kikombe kwa sababu kidogo tumeshuka kiwango baada ya wewe kutoka ndani ya mashindano haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwamba kuna mengine nimeyaacha lakini kuna kitu ambacho kinaniuma lazima nikiseme. Mimi ni miongoni mwa watu waliotishwa tena mimi sikutishwa kwa maneno nimemuona yeye mwenyewe, nimekutana naye uso kwa uso vis a vis,
akiniambia kwamba Wabunge mmezidi unafiki na baya zaidi maneno haya ameyatamka mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Alisema hivi; “Wabunge mmezidi unafiki na nitadeal na nyie nikianza na wewe.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo Dar es Salaam sikanyagi na naiogopa yaani nilikuwa nimei-miss mno lakini baada ya kutishwa nimeogopa inabidi nikae Dodoma na Sumbawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niliarifu Bunge na familia yangu ijue kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam miongoni mwa watu wanaowatisha watu ikiwa ni pamoja na nini. Mengine mabaya siyasemi wala mazuri yake siyasemi nasemea hili kwa usalama wa nafsi yangu.
Najua yapo mazuri aliyoyafanya na yapo mabaya
aliyoyafanya, lakini mimi naomba niseme hilo moja tu
kwamba ni bora tukaliangalia kwa makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo tayari kuhojiwa, nipo tayari kuja kusema na nitatoa ushahidi kwa sababu nilikuwa kwenye hoteli inaitwa Colosseum, niliitwa mbele ya Mkuu wa Wilaya na akanitisha. Sasa mimi sisemi mengi, naomba hili niseme kulitaarifu Bunge kwamba na mimi ni miongoni mwa watu ambao tunatafutwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
HE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante angalau kwa dakika tano. Nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mwisho, nimpongeze Waziri kufanya ziara kwa kuja kutembelea Mkoa wetu wa Rukwa na hatimaye kuliona Ziwa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziwa letu linakauka, ziwa ambalo ndiyo jina la Mkoa wetu wa Rukwa, lakini kwa sasa linaelekea kukauka. Nakuomba Waziri, Mheshimiwa January Makamba uendelee na nguvu hiyo na utenge fedha kwa ajili ya kusaidia Ziwa letu la Rukwa lisiweze kukauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umenipa dakika tano lakini naona zinataka kunichanganya ni chache sana. Niombe tu kwamba katika huu Mfuko wa Mazingira basi ianzishwe sheria kama ambavyo ilivyo sheria kwenye mifuko mingine. Hakuna maendeleo bila uwekezaji katika mazingira, hakuna maendeleo bila utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa ambalo nataka kuongelea leo ni suala la Serikali yetu kupiga marufuku viroba. Hili nataka kuliongelea kwa uchungu kidogo kwa sababu, sisi ndiyo Wawakilishi wa wananchi. Wananchi wanatakiwa sisi tuwatetee ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu ambaye anapinga uharibifu wa mazingira, lakini suala la kupiga marufuku viroba tungelipa nafasi kidogo. Kuna watu wamenunua viroba hivi, kuna watu wametumia fedha nyingi sana, kuna watu wamekopa fedha nyingi na hatimaye tumezuia biashara hii ambayo naamini kabisa biashara hii ilikuwa halali haikuwa haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimuulize Mheshimiwa Waziri kama biashara hii ilikuwa halali na leo hii tumepiga marufuku, wananchi hususan wafanyabiashara wa Mkoa wa Rukwa na Jimbo la Sumbawanga Mjini walinunua kwa wingi wakitegemea wakienda kuuza watapata faida, lakini tumevizuia. Niombe tu kauli ya Serikali kwa hawa ambao wamezuiliwa je, hatuna haki ya kuwalipa fidia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuliangalie hili kwa uchungu, kwa hisia kali. Leo hii mtu amekopa fedha benki, kachukua fedha zile kaenda kufanya biashara, amekopa viroba vyake akauze, leo hii tumevizuia, hebu niambie ni hisia gani anapata na uchungu gani mkubwa anaoupata. Kuna mtu amejiua Dodoma hapa, leo hii ukienda kwenye vituo vya Polisi kuna viroba vimejazana, matokeo yake wanachukua kimoja kimoja wananyonya. (Kicheko)
Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe sana, kwa sababu nahisi, najua uchungu wa mtu anavyofilisika. Kwa hiyo, hili liangalieni upya, litoleeni maelezo, ni bora tukazuia production, bora tukazuia kule ambako vinatengenezwa, tuwape muda wafanyabiashara hao waliovinunua wauze mpaka viishe, naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu kule kuna wafanyabiashara watano, mpaka leo wamekamatiwa mali zao, wamefilisika na nyumba zao zinauzwa. Nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri anapokuja kutujibu hoja yetu hapa, naomba hili alitolee ufafanuzi, ni lini hawa wafanyabiashara wataruhusiwa kuuza viroba vyao au Serikali itoe tamko iwalipe fidia ichukue viroba wakaviteketeze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa ilikuwa ni hiyo, kwa sababu sioni mantiki yoyote ya kile kitu ambacho ilikuwa ni halali, mtu akachukua fedha zake akaenda akanunua tena amenunua kiwandani, siyo haramu hiyo hapana, amenunua ili akauze apate faida, sisi tunazuia tunawanyang’anya tunakwenda kuvitunza kwenye maeneo mengine watu wanaumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge ndiyo wawakilishi wa wananchi, tunatakiwa tuwatetee wananchi, tusipowatetea humu ndani hakuna kwa kuwatetea kwingine. Naomba sana tuungane katika hili, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu aje atusaidie hili. Wananchi hawa ni wa kwetu sisi wote, ndiyo kazi yetu kuwawakilisha ndani ya Bunge, siyo kila kitu tunakiunga mkono hapana! Katika hili Mheshimiwa Waziri Mkuu nakuomba sana, binafsi kwa niaba ya wananchi nikuombe sana usaidie jambo hili waweze kuliruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri. Kwanza kabisa naomba nimpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa, kazi ya uzalendo, kazi ya kujitoa na kuhakikisha anatetea maslahi ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu kuwakumbusha Wabunge tukumbuke nyuma tulikotoka, Tanzania haikuwa kama hivi ilivyo leo. Wako watu walioumia, wako watu waliopoteza nafasi na wako watu waliopoteza muda wao kulitumikia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabisa naomba niwapongeze viongozi wote waliotangulia kwa kazi kubwa sana waliyoifanya. Ndiyo maana mpaka leo Chama cha Mapinduzi kiko madarakani kwa sababu naamini kila baada ya miaka kumi tunabadilisha uongozi na bahati nzuri Chama cha Mapinduzi kinashika nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake yote kwa ujumla inafanya kazi kubwa na ninaamini kabisa tunakwenda mpaka mwaka 2025 amalize muda wake yaani miaka kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuwa msikivu. Mwaka jana ni miongoni mwa watu niliochangia bajeti hii ya Wizara ya Fedha. Lakini kwa bahati mbaya wako baadhi ya Mawaziri waliniomba mwongozo kuhusiana na jambo la VAT on transit goods. Lakini leo nimeona wakishangilia. Hili nilitaka niliweke sawa tu kwamba ni vizuri na sisi ambao hatuna Ph.D tunapokuwa tunachangia, mnatusikiliza. Sisi wengine tunafanya biashara, sisi wengine tumezaliwa humo humo kwenye biashara, kwa hiyo, tuna baadhi ya mambo tunayajua muwe mnatusikiliza na tuna Ph.D za mitaani. Sasa Mheshimiwa Waziri nataka niombe sana pale ambapo sisi tunataka kuchangia basi yale mambo ya msingi muweze kuyachukua na kuweza kuyafanyia kazi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la VAT on transit goods tulilipigia kelele sana lakini mmelichukua mwaka huu mmeliondoa. Ninavyoona kwa bahati mbaya sana, mmeliondoa mmewekea kipengele cha wiki moja. Baada ya wiki moja mnawachaji tena VAT kwa mzigo unaokwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka turekebishe, turekebishe jumla! Nataka kushauri tu, Mheshimiwa Waziri, basi at least wekeni hata siku 30 kwa sababu kwa wiki moja kwa Bandari yetu ya Dar es Salaam na TRA yetu ya Dar es Salaam kila siku system iko down. Wiki moja itapita na matokeo yake tutawa-charge tena upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukuomba sana Mheshimiwa Waziri hili uliangalie, kesho unapokuja hapa basi uje utueleze nikuombe sana kama unataka kurekebisha jambo tulirekebishe moja kwa moja kwa sababu leo hii tumepoteza wateja wengi sana. Wateja wengi wamekimbilia Msumbiji kule Beira, wengine wamekimbilia nchi nyingine. Sasa tunapoanza utaratibu wa kutaka kuwarudisha wateja hawa basi tuhakikishe tunawawekea masuala yote ya msingi vizuri. Mfano, VAT tuiondoe, iwekeni mwezi mmoja, nafikiri kabisa hawa watu watarudi na biashara itaweza kuongoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutoa road license, kusamehe hii tozo ya road license, lakini tumechukua shilingi 40 tumeipeleka kwenye mafuta, naunga mkono hoja ya kuweka shilingi 40 katika kila lita, lengo letu ni maendeleo. Lakini toka uhuru tunalia suala la maji, ni wimbo wa Taifa kila siku maji, maji, maji. Kwa nini sasa shilingi 40 hizi tusizichukue tukaziwekea mfuko maalum wa maji vijijini. Tuitengee kabisa, tuiwekee kabisa ring fence pale kwamba hili hizi pesa tunazozipata ziende kwenye maji vijijini.

Mheshimiwa Waziri, kero ya maji bado ni kubwa na magonjwa yanayosababishwa na maji bado ni makubwa. Niombe sana suala hili tuliweke kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine siungi mkono kwa baadhi ya Wabunge wanaosema tuongeze shilingi 50 kwenye mafuta. Unajua ni rahisi kusema tuongeze na ninavyoona sasa itakuwa kila kitu unaongeza kwenye mafuta, tutafute vyanzo vingine ili tuweze kupata fedha za kuweza kutimiza bajeti yetu. Naunga mkono shilingi 40 lakini siungi mkono shilingi 50 kuongezwa kwenye mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yalikuwa mengi sana ambayo nilitaka kuongelea ni jambo hilo. Lakini la tatu nataka kuongelea uwanja wa ndege wa Sumbawanga. Kwenye bajeti ya mwaka jana tulipitisha bajeti ya uwanja wa ndege ujengwe wa kiwango cha lami, tumekuwa tukipigania sana. Lakini kubwa ambalo ninaliona sasa hivi ambalo nalipigania ni kwamba wale watu ambao wanatakiwa walipe fidia ambao wanazunguka uwanja wa ndege gharama za ujenzi zimezidi, ninaomba wafikiriwe upya ili waweze kufanyiwa uhakiki kwa gharama ya sasa. Na niipongeze kabisa bajeti yako, lakini nimpongeze kabisa kwa kujenga uwanja wa ndege sio uwanja wa ndege peke yake Sumbawanga lakini viwanja vingine vyote ambavyo vinajengwa kwa sababu ninaamini kila kwenye uwanja wa ndege maendeleo yatakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuliongelea, nataka niulize tu hivi shisha Mheshimiwa Waziri wa Fedha uko hapa na Waziri wa Mambo ya Ndani yuko hapa. Shisha hii ni haramu? Shisha hii ni madawa ya kulevya? Na kama ni madawa ya kulevya kwanini TRA mnakusanya kodi? Kwa nini ile tumbaku inapofika bandarini mnai-charge kodi? Na kama ni madawa ya kulevya, Waziri Ummy yuko hapa naye atujibu na kama ni madawa ya kulevya au shisha inatumika vibaya, hata sigara inatumika vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sigara watu wanaweka bangi mule, sigara unaweza ukaweka kitu chochote kile. Ni kazi ya polisi kuhakikisha ile shisha haitumiki vibaya lakini sasa leo tunaipiga marufuku, anatoka mtu tu huko sijui kagombana na mke wake au na mpenzi wake anakuja kusema shisha marufuku na hiyo marufuku ya shisha iko Dar es Salaam peke yake! Ukienda Arusha wanavuta shisha ukienda Dodoma hapa wanavuta shisha, ukienda sehemu nyingine wanavuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niombe Mheshimiwa Waziri kama shisha hii ni madawa ya kulevya tuipige marufuku leo na kwenye kodi tuiondoke maana kwenye kodi imo, ukiwauliza wale jamaa wa TFDA wanasema haina madhara. Ukimuuliza yule Mkemia Mkuu anakwambia haina madhara, lakini ukija huku wanakuambia hii inatumika na madawa ya kulevya. Ni wajibu wa polisi, ni wajibu wa kila raia akiona kama kuna mtu anatumia madawa yale au anatumia shisha vibaya akamatwe. Lakini ukienda nchi za kiarabu wanavuta, ukienda Uingereza wanavuta, ukienda dunia nzima kasoro Dar es Salaam. Nataka niseme, liangalieni tusiwaumize wananchi, wako watu wanalipia kodi Dar es Salaam lakini ikitoka inapigwa marufuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuongelea jambo la mwisho, ni suala la Bodi ya SELF. Bodi hii mwaka jana iliahidi kutoa mikopo ya shilingi bilioni 12 lakini hatimaye mwaka jana walitoa shilingi bilioni tisa. Mwaka huu walipanga shilingi bilioni saba kuweza kuwakopesha wafanyabiashara/taasisi kubwa. Lakini kwenye bajeti hii tumepanga shilingi bilioni 20 mwakani lakini bodi hii imevunjwa, haipo. Sasa hizi fedha zote tunazozipanga jamani tunangoja nini? Bodi hii imevunjwa leo ina mwaka mzima. Hebu jaribu kuangalia kama kuna jambo ambalo lingetakiwa kufanyika kwa haraka, lifanyike kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza mimi mkubwa kuliko Mheshimiwa Bashe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi angalau dakika tatu hizi, ili niweze kuchangia. Naenda moja kwa moja kumgusa mkulima ambaye asilimia 90 ya Wanarukwa ni wakulima wa zao la mahindi. Nimekuwa nikilalamika sana hapa kuhusiana na zao hili la mahindi kwamba sisi wakulima wa Rukwa asilimia kubwa tunalotegemea ni zao letu la mahindi kama zao la biashara. Nasikitika sana leo hii Sumbawanga kama alivyosema Mheshimiwa Malocha, gunia la mahindi ni shilingi 21,000 kwa mara ya kwanza kwa miaka 15 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niliwahi kulisema na Mheshimiwa Waziri hapa akatoa kauli kwamba tumefuta, sasa tunafungua milango ya kwenda kuuza mahindi kokote kule mkulima anapotaka. Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Waziri akaweka kikwazo kingine cha kutaka kibali. Hivi kuna mkulima gani anaweza kutoka Sumbawanga kuja kufuata kibali Dodoma? Hapo tulikuwa tunakaribisha rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inanisikitisha sana, huwezi kuruhusu mazao yaende nje halafu tuweke kikwazo kingine. Mkulima hawezi kuhimili vikwazo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha sana mbolea leo Sumbawanga hakuna; na ikiwepo ni mbolea ya magendo na leo hii toka jana kuna foleni kubwa sana ya kununua mbolea. Mbolea Urea leo hii imefika shilingi 65,000 mpaka shilingi 70,000. Huyu mkulima tunamweka katika fungu gani? Kwanza kabisa anabanwa kwenye mbolea, pili anabanwa kwenye kuuza. Sasa afanye biashara gani? Halafu kubwa ninachosikitika mimi sijui Mawaziri wetu wanafikiria nini? Bahati mbaya tunapochangia, wao wanacheka, mimi hii kitu huwa naumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu kwa nini havichukuliwi kuwa serious? Leo hii Mkenya anatoka hapa anakwenda kununua mahindi Zambia, anayapitisha kwenye barabara yetu, kwa magari yetu, anakwenda kuuza kwao, anatuacha sisi Tanzania tunakosa soko la kuuza mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, WFP badala ya kununua mahindi Tanzania na baada ya kukosa kibali cha kusafirisha mahindi kwenda nje, wameenda kununua mahindi Zambia, wameleta hapa, yako hapa Dodoma, yanasubiri kwenda maeneo mengine, sisi tumeshindwa kuwauzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, ifike wakati sasa Serikali ikae chini iliangalie jambo hili. Sisi tunao wajibu wa kuwawakilisha wakulima wetu, tuna wajibu wa kuwawakilisha wananchi wetu, lakini zao kubwa ambalo sisi tunalotegemea ni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima huyu anahitaji akivuna mazao yake auze ili aweze kununua bati, auze ili aweze kumsomesha mwanafunzi. Tumesema kila siku hapa lakini Serikali haitusikii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba leo Mheshimiwa Waziri, tunaanza kuvuna mazao mwezi wa tano na sita, lisije likatokea jambo lingine hapa ukatuambia unafunga tena mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hape kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi angalau dakika tano hizi niweze kuchangia kwa haraka haraka tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeamka tofauti kabisa, mara nyingi sana nilikuwa nafikiri Mheshimiwa Tizeba ni tatizo. Naomba nikiri leo ndani ya Bunge kwamba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo hana tatizo lolote. Tatizo ninaloliona hapa ni Waziri wetu wa Fedha ndiyo kikwazo kwa kila jambo tunaloliongelea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukilalamika sana kuhusiana na Wizara ya Kilimo, lakini leo naomba niseme kwamba kwa 18% iliyotengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kwenye kilimo tumefanya makosa makubwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri na Bunge lituunge mkono kwamba bajeti hii ikapitiwe upya ili tuje tuijadili kwa sababu muda bado tunao, lakini kwa asilimia 18 kwenye suala la maendeleo naomba niseme kimsingi tumeshindwa kutekeleza yale ambayo tulikuwa tumekubaliana toka mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa harakaharaka tu, nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutoa kikwazo cha vibali kusafirisha mahindi yetu kwenda nje. Nikuombe tusifanye tena makosa haya. Kosa hili limetugharimu sana hasa sisi wakulima wa mahindi na mpunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivyo kwa sababu, maeneo tunayotoka sisi ndiyo zao letu kubwa kama zao la chakula lakini ndiyo zao la biashara. Mnapofunga mipaka hii matokeo yake mnatufanya sisi tunaathirika zaidi. Sisi Wabunge wa maeneo hayo tuna kila sababu ya kuwatetea wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Sumbawanga gunia moja la mahindi ni shilingi 15,000 mpaka shilingi 20,000. Hebu niambie huyu mkulima leo hii unamwambia akalime tena mahindi ataweza kweli kulima? Kwa bahati mbaya mnambana kila kona na mkulima huyu hatumsaidii chochote. Narudia, hatumsaidii chochote. Nikuombe, kosa tumeshalifanya tusirudie tena kufanya kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vibali unavyovisema Mheshimiwa Waziri vitatoka mikoani unaenda kukaribisha rushwa kule, kwa nini msifute moja kwa moja? Uwezo wa kununua hatuna, uwezo wa kuwasaidia wakulima hatuna, waachieni wafanye wanavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la kusema mkulima ndiyo wajibu wake kuhakikisha mwananchi hafi na njaa, tunakosea. Kama hoja ni hiyo, basi hata sisi watumishi na Wabunge, ikitokea kuna suala la njaa tuwe tunakatwa na sisi mishahara yetu ili tukafidie kule ambako kuna tatizo la njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wakulima wetu hawa wanaonewa sana, ifike wakati sasa tuagalie jinsi gani ya kuwasaidia tuwaache wawe huru, walime wenyewe, wavune wenyewe na vilevile wakatafute masoko wakauze kokote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda haraka haraka, leo tuna mawakala wamekuja kututembelea hapa, mawakala hawa huu mwaka wa nne hawajawahi kulipwa hata senti moja. Tunaamini mmefanya uhakiki, mnaangalia madeni, mmechunguza, lakini Waziri wa Fedha aje atujibu hapa nini dhamira ya dhati ya hawa ambao walitusaidia wakati wa dhiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano, juzi kule kwetu kuna mfanyabiashara mmoja ambaye ni wakala alikuwa anaitwa Mohamed, kwa jina maarufu alikuwa anaitwa Mohamed Msomali, kauziwa nyumba yake kapata pressure amefariki. Basi kama mmehakiki madeni yale ambayo ni halali walipeni kwanza wapunguze machungu wakati mengine mnayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, najua tatizo haliko kwako, Waziri wa Fedha akija hapa aje atujibu, lile ambalo mmeona ninyi ndiyo halali yao wapeni mengine wataendelea kudai baadaye ili wakapunguze machungu waliyokuwanayo. Leo hii hapo walipo wana wiki moja wako hapa Bungeni, kulala kwa shida, kula kwa shida, matokeo yake wamekuwa ombaomba hapa ndani ya Bunge, nafikiri na leo wapo hapa. Hebu angalieni jinsi gani ya kuwasaidia, kuweni binadamu, Waziri wa Fedha liangalieni hili, walipeni hawa watu kwa sababu walitusaidia wakati wa shida, tena wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015. Kama hawadai, semeni hawadai ili wakaanzishe kazi nyingine waridhike kwamba sasa hivi hatudai, wasamehe hayo madeni. Mheshimiwa Waziri, hili sio la kwako, naomba Waziri wa Fedha aje atujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kuhusu mbolea. Kila Mbunge ana haki ya kuchangia lolote lile ndani ya Bunge hili. Kila Mbunge ana wajibu wa kuchangia na wengine wachangie, siyo tusipingane, tupingane kwa hoja, sisi siyo wataalam lakini wataalam wanatuambia mbolea ya Minjingu inafaa. Mimi naona kuna shida hapa, shida ni jina, brand ile, wangeongeza neno moja ‘s’ pale Minjingus ikawa la kizungu hapa tusingepiga kelele. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninavyojua kwa sababu kuna DAP, wameshazoea DAP kwa sababu ni la kiingereza. Leo hii hata shati…

T A A R I F A . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongelea kuhusu wataalam, sijui dada yangu kama ni mtaalam. Sasa hapa ndiyo kuna shida hapa, Mheshimiwa Waziri mje mtujibu wataalam wanasema nini, research yao inasema nini na kama inafaa watuambie inafaa na kama haifai tuambiwe haifai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka niseme ndani ya Bunge hili, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa mzalendo kwa kutaka kufufua viwanda vya nchi yetu lakini kuongeza viwanda...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu. La pili, naomba niwapongeze sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa wote kwa kazi kubwa wanayoifanya na hatimaye kuhakikisha Tanzania yetu inasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana pamoja na timu yako nzima kwa kazi kubwa uliyoifanya na hatimaye sasa tunakwenda mwaka wa tano ukituongoza kwa umahiri, kwa ujemedari mkubwa na hatimaye Bunge letu limefanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nina ajenda moja tu ambayo naomba unisikilize vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba alipe nafasi jambo hili. Nitaongelea suala la wavuvi.

Mheshimiwa Spika, tumelalamika sana kuhusiana na wakulima na hatimaye Serikali ikatusikiliza. Hata hivyo, kwa sababu Mkoa wa Rukwa umezungukwa na maziwa; Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika na Wanasumbawanga wengi ni wavuvi na wakulima leo nitaongelea kuhusu wavuvi. Kwa hiyo, kwenye sekta hii ya uvuvi nataka Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie kwa sababu ameongelea kwenye ukurasa namba 49.

Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi, naunga mkono kabisa hoja ya Serikali ya kupinga uvuvi haramu, sigombani nao katika hili. Wavuvi wa Lake Tanganyika wanakwenda kununua nyavu hizi madukani.

Mheshimiwa Spika, naomba nieleze kidogo kwamba kuna sheria imepitishwa kwamba nyavu ambazo zinatakiwa zivue ndani ya Lake Tanganyika ni milimita 8. Sasa hii milimita 8 inapitishwa na nani? Hii milimita 8 inapitishwa na watu wa TBS. Kwa hiyo, wale wenye maduka wanaagiza mzigo kutoka nje, unakuja TBS wanaukagua na TBS wanapitisha unakwenda madukani na madukani wananchi wale wanakwenda kununua kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli mbalimbali za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, inanisikitisha sana, kule Lake Tanganyika wale wavuvi wamekwenda madukani, wameuliza nyavu za milimita 8, wamenunua, wamekwenda kwa ajili ya uvuvi lakini kwa bahati mbaya sana Waziri wa Uvuvi pamoja na timu yake ikatuma na kipimo kingine kipya milimita 8 nyingine ambayo sijui wameitoa wapi. Wamekwenda tena kupima kule, wamekamata nyavu wakasema zile nyavu zipo chini ya kipimo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilimpigia simu Mheshimiwa Waziri Mkuu nikamueleza jambo hili, nilimpigia Waziri wa Uvuvi na Mifugo na Waziri wa Viwanda na Biashara, hapa kuna mchanganyiko, inasikitisha sana. Unakuta kuna raia au mtumishi amestaafu, amekwenda nyumbani kafika kule chini Lake Tanganyika amekuta kazi hakuna, wakamshauri kazi kubwa tuliyonayo huku ni uvuvi. Yule mtu anachukua kiinua mgongo chake anakwenda dukani kutaka nyavu halali, milimita 8 anaitaka, anapewa. Anafika kule anaunga nyavu zake anaanza uvuvi milioni 15 ameingiza katika uvuvi. Anakuja mtu mwingine wa uvuvi na kipimo chake kingine tofauti na cha TBS anapima anasema hii siyo milimita 8, anamkamata, anamtoza faini shilingi milioni tano lakini yule mzee anasema mimi nimenunua dukani; kwa nini hawa wanaouza nyavu wasikamatwe nikamatwe mimi ambaye sijui chochote? Mheshimiwa Waziri Mkuu watu hawa wanaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana Serikali ilifuatilia ikaunda Tume huru ikaenda kule; wamo watu wa TBS, Wizara ya Uvuvi na Usalama wa Taifa kupima zile nyavu zimeonekana ni halali. Sasa Waziri anatoa tamko kwamba anatoa miezi mitatu nyavu zile ambazo zipo chini ya kiwango cha kwao wao kuwa mwezi Juni wawe wameziondoa. Kwa hiyo, amewapa muda wa miezi mitatu waweze kuvua kwa muda ili waweze kufidia nyavu zile ambazo wamezinunua madukani.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kosa la Serikali, Serikali imekuja na vipimo viwili; TBS wana kipimo chao lakini Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wenyewe wana kipimo chao, mwananchi atajuaje kipimo halali ni kipi? Mwananchi huyu anayekwenda dukani kununua nyavu atajua vipi kuwa hii ndiyo TBS haitakiwi na hii ndiyo Wizara ya Uvuvi inatakiwa kwa sababu nyavu zipo madukani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana au kwa bahati nzuri sana, baada ya Serikali na Tume kugundua kwamba Serikali ndiyo yenye makosa, wakaruhusu kwamba nyavu hizo zitumike ndani ya miezi mitatu, lakini wameruhusu nyavu wakati sio wa uvuvi. Masika hii wavuvi wote wanasimamisha uvuvi kwa sababu wakivua dagaa wakizianika zinalowana. Wametoa miezi mitatu mwisho mwezi Juni lakini kosa sio lao. Kwa msingi huo ilitakiwa Serikali ilipe fidia kwa sababu makosa ni ya Serikali; makosa ni ya Wizara ya Uvuvi na Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilimpigia Waziri wa Viwanda na Biashara anajua na Mheshimiwa Waziri Mkuu, nikampigia Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi, wamekwenda wamechunguza imeonekana TBS wana makosa au Wizara ya Uvuvi ina makosa, kwa sababu wamekuja na vipimo viwili. Ushauri wangu tungewapa watu muda wa mwaka mzima. Shilingi milioni 15 kuirudisha ndani ya miezi mitatu kwa kosa la Serikali haitowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mvuvi huyu naye anaongeza mapato ndani ya Mfuko wetu wa Taifa, mvuvi huyu ni sawa na mkulima na mvugaji lakini anaonewa siku hadi siku. Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe sana muda aliotoa Mheshimiwa Waziri wa miezi mitatu ni mdogo kwa kosa la kwetu sisi wenyewe. Kama Serikali ingeweza kutusaidia basi huu muda ambao tumewapa wa miezi mitatu ambapo wavuvi wamesimamisha uvuvi kwa sababu kuna mvua, hawawezi kuvua wakati huu, uvuvi rasmi unaanza mwezi Juni, basi waruhusiwe kuanzia mwezi Juni, wapewe muda wa mwaka mmoja waweze kurudisha gharama zao ama Serikali ifidie gharama hizo iwarudishie fedha zao walizonunua nyavu madukani ambapo maduka hayo yanauza nyavu halali na leseni wanazo. Namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie wavuvi hawa wanahangaika sana na sisi ni wawakilishi wao tuna haki ya kuwatetea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya machache, naunga mkono hoja. Nikupongeze sana kwa kazi kubwa, nimpongeze na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya kuitumikia nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nipate nafasi ya kuchangia katika hii bajeti ya Wizara ya miundombinu, kwanza naomba niipongeze sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kazi kubwa sana inayoifanya lakini la pili naomba nikipongeze Chama changu kwa ushindi mkubwa kwa Majimbo mawili kule Mkoani Kigoma, ambako kama Mbunge na Wabunge wenzangu tuliteuliwa kwenda kupambana kuhakikisha kwamba Majimbo yale mawili yanarudi kwa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo kama matano hivi ambayo ningeomba sana Mheshimiwa Waziri akirudi ili niweze kupata majibu. Huu ni mwaka wangu wa nne nimekuwa hapa nikipitisha bajeti ya kujenga uwanja wa ndege napiga makofi ninawaambia wananchi kule Sumbawanga kwamba uwanja unajengwa na hatimaye mpaka leo uwanja wa ndege wa Sumbawanga haujawahi kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu spika, nimeona kwenye bajeti mwaka huu tena kwamba tutajenga uwanja wa ndege mjini Sumbawanga sasa nilikuwa nataka nikuulize sisi tumekuwa tukipitisha bajeti kila siku na tunarudi kwa wananchi kule kuwaeleza kwamba tutajenga uwanja wa ndege muda fulani, leo ni mwaka wa nne ukienda kwenye Hansard kule utakuta tumepitisha bajeti na uwanja wa ndege haujawahi kujengwa na mwisho wa siku tumeshalipa fidia Mkandarasi yupo site tunaingia gharama lakini uwanja haujengwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikajaribu kuuliza nini tatizo kwanini uwanja wa ndege haujengwi? Nilichokijua mimi ni jambo la kushangaza viwanja vya ndege vile vinne au vitano pamoja na kiwanja cha Kigoma nafikiri na Tabora na maeneo mengine imekwamishwa kwa sababu ndogo sana viwanja vya ndege vinasimamiwa na mamlaka ya ndege Tanzania TIA lakini viwanja vinajengwa na TANROADS shida iliyopo kule wafadhili wamegoma kutoa fedha kwa sababu vilitakiwa viwanja vile visimamiwe na TIA na sio TANROADS kujenga viwanja vya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni jambo dogo mno kwanini tunavutana kwanini tusirudishe mamlaka ya viwanja vya ndege iende kwenye viwanja vya ndege TANROADS wajenge barabara kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikuombe sana jambo hili limechukua miaka minne na nimuombe Waziri akija kutujibu hapa kabla sijapitisha bajeti yake nijue tunakwenda kujenga kweli moja kwa moja mwaka huu au na yenyewe itakuwa ni histori ya kupitisha bajeti kila siku kila siku na mwisho wa siku wananchi wanatuchoka, tumekuwa tukiwaambia tunajenga uwanja na hatuwezi kuujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili mimi Mjumbe wa Kamati ya miundombinu tumepata barabara ya Ntendo Muzye tulipata 0.9-kilometer hata kilometa moja haijafika kwenye bajeti hii nikamuuliza Waziri hivi kweli kumpata mkandarasi wa kuja kujenga 0.9 kilometa, hata kilometa moja haifiki utampata mkandarasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninaomba nishukuru baada ya mavutano kidogo Serikali imetusikiliza na hatimaye niipongeze Wizara imetupa kilometa 25. Lakini bado hoja yangu ipo pale pale barabara ya Ntendo-Muzye ndio barabara kubwa ambayo inailisha Mkoa wa Rukwa pamoja na Mbeya kule na Tanzania kwa ujumla. Kilometa kutoka Ntendo kwenda Muzye ni kilometa 35 lakini ukipeleka kilometa 25 tutakuja kwenye utata ule ule wa kilometa 10 nani atazimalizia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara na nimuombe Waziri wetu wa miundombinu atuongezee baada ya kutupa kilometa 25 atupe kilometa 35 ili tuweze kumaliza barabara ile barabara ile ni kero Mheshimiwa Rais anaijua, Mheshimiwa Waziri Mkuu anaijua na Mawaziri wote wanaopita pale kutoka Ntendo kwenda Muzye barabara ile haipitiki na watu wengi wanakufa. Lakini chakula chote kinatoka bondeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka niombe kwa sababu nimekaa na Mbunge mwenzangu anatoka Kwela lengo kubwa sisi Wabunge mtusaidie ili barabara ile iweze kujengwa kwa kiwango cha lami hizo kilometa 10 tuwaombe Wizara iweze kutuongezea ili tuweze kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo barabara ya kutoka Matai kwenda Kasesha ina kilometa 51 ukiwapa kilometa 35 tutabakia na kilometa 20 nyingine kwa hasara, na Sumbawanga ni mbali hivi barabara ndogo ndogo hizi au fupi fupi zinazoweza kujenga Dar es salaam ni rahisi zaidi kwasababu wakandarasi wapo karibu na maeneo ambayo wanayapata lakini ukitoa kilometa 25 kwa Sumbawanga kumpata mkandarasi kutoka maeneo mengine ni shinda kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri tunakuombe ili uweze kutusaidia, nazungumzia Bonde la Rukwa, bonde ambalo linakwenda mpaka Chunya mwisho wa siku linafika mpaka kule Mbeya barabara ile mbovu haipitiki, madaraja mabovu, nikuombe sana sisi tunaongea kama mkoa, mkoa wetu ulikuwa uko nyuma na sasa hivi umeanza kupiga hatua kubwa basi tunaomba Serikali na tumuombe Waziri aende akaangalie ile barabara ili iweze kupitika kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee standards gauge Wajumbe tulienda kutembelea reli ile iliyojengwa ya kisasa, nataka niseme nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali, Wabunge wote Wajumbe wote waliofika maeneo yale waliridhika kabisa na utendaji mkubwa wa Serikali wa inavyosimamia mradi ule. Kwa kweli ukiwa nje hawa wananchi ambao labda hawajatembea maeneo yale mkienda kutembelea Waheshimiwa Wabunge ni miujiza kwakweli reli imejengwa vizuri na sisi tuipongeze Serikali iweze kufanya sasa mambo mengine ili tuweze
kukamilisha barabara hii ya Reli iweze kufika Tabora, Kigoma, na kwenda Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nirudie tena kumuomba Waziri MV Liemba Lake Tanganyika ziwa kubwa lenye watu wengi lakini leo ni mwaka wa tano meli haitembei watu wanakufa kila siku watu wanaangamia lakini kila tukifika Bungeni tunaambiwa kuna bajeti mwaka huu tunajenga meli, mwaka huu tunatengeneza MV Liemba mwaka huu tunatengeneza MV Mwongozo hakuna meli hata moja iliyotengenezwa. Sasa mimi hoja yangu hapo ni kwamba tunapokuja kupitisha hizi bajeti na mwaka jana tumepitisha MV Liemba inajengwa mpaka leo haijaweza kukarabatiwa tufanye nini sisi Wabunge kwenda kuwaambia kule wananchi? Watupe majibu ili tukienda kule tuwaambie bwana hii meli tumeiondoa kwenye bajeti mpaka pale tutakapokuwa tumepata fedha ili tuweze kujenga meli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hatuna fedha tusiweze kutoa ahadi humu ndani kama tutajenga meli wakati fedha hatuna, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri mwaka huu, hiyo meli mpya sasa ikae pembeni tutengezeeni meli zetu zile ambazo tunazijua zianze kazi mpya itakuja baadaye. Lakini humu nimeona tuna Meli mpya mbili sijui tuna meli ya tani 3000 utapakia mzigo wa nani wa tani 300 Lake Tanganyika, kengele ya kwanza. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ya pili Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.