Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Susanne Peter Maselle (10 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUZANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuwasemea Wanamwanza. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nami nitoe shukrani kwa chama changu ambacho kimeniteua kusimamia Mkoa wa Mwanza kwa sababu wamejua kwamba naweza na nitakitendea haki. Nawashukuru pia akinamama wa CHADEMA wa Mwanza kwa kuniteua mimi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuniamini na kunituma ili nishughulikie kero zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wanamwanza hasa wavuvi, wafugaji na wakulima wamenituma niwasemee yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa wanathamini sana habari na taarifa ndiyo maana Wavuvi wakiwa katika uvuvi huwa wanasikiliza redio, wanakuwa na redio. Wafugaji wanapokwenda kuchunga wanakuwa na redio na wakulima vile vile na ndiyo maana kuna redio zinaitwa redio za wakulima. Wamenituma nije niseme kwamba kwa Serikali kukatiza kuonesha live Bunge ni kuwanyima haki yao ambayo inatokana na kukatwa kodi zao. Kwa hiyo, wameniambia kwamba nilisemee hilo na nimelisemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzetu wamekuwa wakiunga mkono kwa sababu wanajua ni nini wanakuja kukifanya. Wamefanya hili Bunge ni kama resting house. Wanalala, tunawaona kwenye magazeti wamesinzia na ndiyo maana wanaleta hoja ya kwamba Bunge lisioneshwe live kwa sababu wanajua adhabu itakayowapata na kuna wengine ambao adhabu hiyo imeshawapata, hawakurudi Bungeni hapa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kuwasemea wavuvi. Wavuvi wamekuwa wakinyang‟anywa nyavu zao na kuchomewa moto; lakini sitaki nionekane na-support ila swali langu ni kwamba je, hawa watu wanaouza hivi vitu na viwanda vinavyotengeneza si wanajulikana? Kwa nini Serikali inaendelea kuchukua kodi kwao na kuwanyamazia? Hii ni double standard! Ndiyo maana Mkoa wa Mwanza ulipotangazwa kwamba ni mkoa unaoongoza kwa watumishi hewa, matokeo yake Mkuu wa Mkoa alihamishwa na kupelekwa sehemu nyingine wakati yeye ndiye aliyekuwa anasimamia mkoa huu na anasimamia watumishi hao. Hilo lilikuwa ni jipu ambalo lilitakiwa kutumbuliwa mapema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uvamizi wa wavuvi na kunyang‟anya vifaa vyao vya uvuvi ambavyo wamevinunua kwa shida na kwa kujinyima. Naomba Serikali idhibiti hao wanaowanyang‟anya kwa sababu ulinzi umekuwa ukiwekwa kipindi tu ambacho sikukuu zinakaribia, lakini wanyang‟anyi hao wamekuwepo kila wakati. Kwa hiyo, naomba Serikali iimarishe ulinzi katika Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu vifaa vya uvuvi. Wavuvi wamekuwa wakiuziwa vifaa vya uvuvi kwa bei ghali sana. Kwa mfano, kama engine ya Boti imekuwa ikiuzwa shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni nne na nusu. Kwa mwananchi wa kawaida wa kipato cha chini hawezi ku-afford kununua engine ya shilingi milioni nne, kwa maana hiyo basi, tunaomba Serikali iwe inakopesha vifaa hivyo kwa wananchi wetu ambao wana kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu kilimo. Mawakala wamekuwa wakiwauzia wakulima mbegu ambazo zimeoza, ambazo hazisaidii kwa kilimo. Kwa mfano, tarehe 22 Februari, 2016, wakulima wa Pamba wa Magu walikuwa wakiilalamikia Serikali kuhusu mawakala kuwauzia mbegu ambazo zimeoza na hii ilisababisha kero kubwa sana, lakini sikuona Serikali kuchukua hatua yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inavunja nguvu wakulima wetu kwa sababu wanapotoa malalamiko kwa Serikali na Serikali kunyamaza kimya, inaonekana kama vile wamedharaulika. Tukizingatia kwamba tunaenda kuingia kwenye uchumi wa viwanda na hatuko serious na hiki kilimo, sijui hivyo viwanda tutaviendesha vipi. Naomba Serikali na Wizara iwe inasikiliza maoni ya wananchi ili tuweze kusonga mbele na tusiwavunje moyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Kiwanda cha Mwatex. Kiwanda hiki kimekuwa kikifanya kazi kwa kusuasua; na hii ni kwa sababu ya tatizo la umeme. Umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara. Kwa maana hiyo basi, kama tunakwenda kuwa na uchumi wa viwanda, tunaomba kwanza tuanze na hivi viwanda vyetu ambavyo vilikuwepo vilivyokuwa vinatoa ajira kwa mama zetu, wakipeleka pamba; ilikuwa inawasaidia hata kuendesha maisha yao. Leo hii tunasema kwamba tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda huku viwanda vilivyokuwepo hamjavishughulikia. Tutakuwa kama vile tutacheza makida makida. Naiomba Serikali sasa iamue kwanza kukarabati viwanda ambavyo vilikuwepo Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumizie kuhusu ufugaji. Tanzania tuna mifugo mingi sana, lakini wafugaji wetu hawana elimu. Naomba Wizara husika itoe elimu kwa wafugaji hawa. Tunashindwa kuuza ngozi zetu katika masoko ya Kimataifa kwa sababu ngozi zetu hazina kiwango. Ng‟ombe anawekewa alama mwili mzima, sasa unapopeleka ngozi ya aina hiyo, huwezi kupata soko zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, naiomba Wizara husika itoe elimu kwa wafugaji wetu jinsi ya kutunza hizi ngozi. Kuna sehemu ya mwili wa ng‟ombe ambapo unaweza ukaweka alama na isiathiri ngozi. Kwa hiyo, waende mpaka kijijini wakatoe elimu hiyo ili tuweze kupata masoko mazuri katika masoko ya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kiwanda ambacho kipo Mwanza, Ilemela, sehemu ya Saba Saba. Kile kiwanda kimekuwa godown. Sasa unashangaa yule aliyeuziwa alitoa nini kwa Serikali mpaka anashindwa kufuatiliwa? Kiwanda kimekuwa godown ya vyuma chakavu na Serikali inaangalia tu, mpaka najifikiria kwamba kulikuwa kuna nini hapo? Labda aliyeuziwa alikuwa ametoa kitu ambacho kinafanya Serikali inyamaze kimya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba viwanda hivyo vifuatiliwe kwa sababu ni aibu na ni dharau kwa Serikali. Mwekezaji anapewa kiwanda na anashindwa kukiendeleza na Serikali inanyamaza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba sisi Wasukuma sio wavuta bangi. Hapo nyuma kuna Mbunge alisema kwamba Wasukuma bangi huwa inatusaidia kupata nguvu za kwenda kulima. Mimi nimezaliwa Mwanza na ni Msukuma; ninachofahamu ni kwamba sisi huwa asubuhi tunakula ugali na maziwa, tunakwenda kulima na ndiyo maana hata miili yetu ukiiangalia unaiona imepanda; hakuna Msukuma ambaye ni legelege. Nina wasiwasi sana na huyu Mbunge inawezekana siyo Msukuma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu athari za upungufu mkubwa wa dawa na chanjo kwa akinamama na watoto. Itakumbukwa kuwa mwishoni mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu na sina uhakika kama tatizo hilo limekwisha hadi tunapozungumza hapa ndani sasa kwenye Mkutano wa Bajeti, nchi yetu ilikumbwa na ukosefu au upungufu mkubwa wa dawa pamoja na chanjo za magonjwa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilikuwa mbaya kiasi cha Serikali kujichanganya katika kauli zake za kujitetea na kutaka kuonesha kuwa lilikuwa suala dogo lakini ukweli ni kwamba halikuwa suala dogo ndiyo maana Makamu wa Rais alisema kauli nyingine Wizara wakasema kauli nyingine. Wakati Waziri mhusika, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akisema kuwa hakuna tatizo la ukosefu wa dawa na kwamba hizo ni habari za kwenye mitandao tu, kesho yake bosi wake, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu akiwa pale Mwananyamala Hospitali akakiri kuwa nchi ina tatizo la upungufu mkubwa wa dawa na chanjo lakini eti halitakuwa la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukiri kule, kauli ile ya Serikali ilikuwa ni ya ajabu na ilikuwa na ukakasi mkubwa sana masikioni mwa Watanzania ni kama vile walikuwa wanaambiwa wavumilie hali hiyo kwa sababu haitakuwa ya muda mrefu. Hivi kuna mahali mnaweza kucheza na maisha ya Watanzania kama kwenye afya na matibabu (uhai)? Hivi mnawezaje kusema ukosefu wa dawa halitakuwa tatizo la muda mrefu bali mfupi tu huku mnajua kuwa wakati huo kuna wagonjwa hospitalini wanahitaji dawa na wanakufa kwa kukosa dawa? Mnawezaje kusema kuwa tatizo hilo halitakuwa la muda mrefu wakati kuna akinamama wajawazito hospitalini wanasubiri matibabu na wengine wamejifungua wanahitaji matibabu na watoto wao wanahitaji chanjo? Huku ni kucheza na maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata taarifa ya Serikali na wananchi wangu wa Mwanza wanataka kusikia Serikali ikisema hapa Bungeni, je, akina mama wangapi hususan wajawazito na wale waliojifungua na watoto waliozaliwa wameathirika na ukosefu huo wa dawa na chanjo hospitalini? Tumefikia hatua nchi inakosa dawa na vifaa tiba na chanjo za kifua kikuu, polio, surua, lubele, kichaa cha mbwa, manjano na magonjwa mengine hatari kwa afya ya mama na mtoto. Kwa hiyo, Watanzania na kipekee wananchi wa Mwanza wangependa kusikia Serikali ikiliambia Bunge hili athari ambazo Taifa hili limepata na litazipata miaka mingi ijayo kwa kitendo cha akinamama wajawazito kukosa dawa na chanjo, akinamama waliojifungua na watoto wao kukosa dawa na chanjo, nini athari zake kwa jamii yetu ambayo bado inapambana na utapiamlo, udumavu na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ujenzi wa vituo vitatu kila Halmashauri kuboresha huduma na uchunguzi na matibabu ya mapema ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa kina mama. Hivi karibuni wakati akizindua kampeni ya bure ya uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa akinamama iliyofanyika mjini Mwanza, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu alisema kuwa Serikali ina mpango wa kujenga vituo vitatu kwa kila Halmashauri nchini kwa ajili ya kuboresha huduma na uchunguzi na matibabu ya mapema ya magonjwa hayo ili kuwanusuru akinamama. Ilisemwa kuwa zimetengwa shilingi bilioni saba na Serikali hii na Benki ya Dunia itasaidia shilingi bilioni tano katika kufanikisha suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimepitia taarifa ya bajeti ya Wizara hii kuangalia utekelezaji wa kauli hiyo ya Serikali sijaona mahali ambapo fedha hizo zimetengwa. Wananchi wa Halmashauri za Mwanza wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji huo ambao utaweza kuokoa karibu wanawake asilimia 60 walioko katika hatari ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo huku wakiacha nyuma watoto wanaohitaji malezi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Serikali ituambie hapa imefikia wapi katika kusogeza huduma za magonjwa hayo katika hospitali za Bugando na KCMC kama alivyosema Makamu wa Rais ili kupunguza mahitaji ambayo hospitali ya Ocean Road inakabiliana nayo kwa sasa. Pia naomba kujua maendeleo ya kampeni hiyo ya bure hususan kwa Mkoa wa Mwanza ambayo ingepaswa kwenda sambamba na utoaji wa elimu au kujikinga au kuzuia magonjwa hayo kwa akinamama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kampeni ya malaria na ugawaji wa taulo za usafi wa mwili kwa mabinti kwenye shule zetu. Hivi karibuni taarifa kutokana na tafiti zilizofanyika zilionesha kuwa wasichana walioko shule au walio na umri mdogo wanapata athari kubwa sana kutokana na ugumu wa kupata mahitaji ya taulo za usafi wanapokuwa katika mzunguko wao wa kila mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari hizo ni mimba za utotoni kwa sababu ya kudanganywa ili wapate fedha za kununua taulo; wanashindwa kuhudhuria shuleni na kukosa masomo kwa siku tano hadi saba kila mwezi; kupunguza uwezo wao wa kufaulu kwa kukosa masomo na kuwa katika uwezekano wa kupatwa na magonjwa mbalimbali kutokana na kutumia vifaa visivyo sahihi na visivyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kumekuwepo na kampeni kubwa dhidi ya malaria ambayo nasikia imefika hadi kwetu Buchosa kwa ajili ya kupulizia dawa ndani na kwenye kuta za nyumba, ni wakati muafaka sasa Serikali ikalivalia njuga na kulipatia uzito mkubwa suala la kuwasaidia hawa watoto na mabinti zetu walioko shuleni wapate taulo hizo ili wabakie shuleni wasome, waepuke mimba za utotoni na magonjwa hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara walione hili na walichukue kwa uzito mkubwa sana. Inaweza hata kwa kuanzia kushirikiana na watu au mashirika ambayo tayari yameanza kampeni hii kama walivyokuwa wakifanya watu wa East Africa Television na East Africa Radio ambao walifanya kampeni kubwa kuhamasisha watu kusaidia mabinti hawa walioko shuleni wanaoteseka kwa sababu ya kukosa taulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, matibabu ya bure kwa wazee, kambi ya wazee wa Bukumbi na kambi ya walemavu Misungwi. Wazee wangu wa Mwanza, maeneo ya Buchosa, Sengerema, Ilemela, Nyamagana, Magu, Sumve, Ukerewe, Kwimba na Misungwi bado wanasubiri lini Serikali itatekeleza kwa dhati huu mpango badala ya kuwa kwenye makaratasi na maneno ya hapa Bungeni na kwenye mikutano au semina au warsha na makongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati lilifanyika zoezi la kutoa vitambulisho kwa wazee wanaotakiwa kutibiwa bure, naomba Serikali kupitia Bunge lako iwaambie Watanzania zoezi hili limefikia wapi na wazee wangapi wamepata hivyo vitambulisho hususan kwa Mkoa wetu wa Mwanza ambako wazee wetu waliotumikia Taifa letu wakiwa wakulima, wafugaji, wafanyakazi Serikalini sasa wamestaafu wanahangaika sana kupata matibabu. Tunaomba mtuambie kama mtaweza kuitekeleza kwa vitendo sera hiyo ambayo tunajua haikuwa ya kwenu. Kama imewashinda tuwaambie wazee wetu na watu wengine ambao tu wazee watarajiwa kuwa hilo litawezekana tu pale ambapo Serikali ya UKAWA itaingia madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mwanza wanapata shaka sana iwapo Serikali itaweza kutekeleza kwa vitendo sera hiyo wanapoangalia kambi ya wazee wasiojiweza ya Kigongo, pale Misungwi namna ambavyo wazee wale wametelekezwa na Serikali, hawana dawa, wanasumbuliwa na magonjwa na hawawezi kutibiwa, wanapangiwa bajeti isiyotosheleza kwa chakula wala matibabu. Hali hiyo mbaya ya kituo cha wazee cha Misungwi ambayo hata Mama Janeth Magufuli aliishuhudia mwenyewe haijaishia hapo pekee, kuna kilio kikubwa pale shule maalum ya walemavu wa ngozi ya Mitindo iliyoko Misungwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii ambayo inashirikiana na Wizara zingine kuhakikisha watoto wale wanapata stahili za kulinda afya zao. Vinginevyo iko siku tutaona machozi mengine humu Bungeni kuwalilia watoto wale kama ambavyo Waziri Mkuu aliyepita alitoa machozi kwa ajili ya albino.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SUSANNE P. MASELLE: nakushukuru Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijaanza kuchangia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuilinda familia yangu, hasa baba yangu ambaye alikuwa anaumwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nipongeze hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo imesheheni vitu vingi sana na vya muhimu ambapo Serikali kama itavichukua na kuvifanyia kazi, basi sekta hii itafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu uvuvi. Kanda ya Ziwa katika sekta hii ina umuhimu sana hususan Mkoa wa Mwanza, maeneo ya Buchosa, Magu, Kwimba na Ilemela wanategemea sana uvuvi, lakini Serikali naona kama haitilii umuhimu sana hii sekta. Kwa sababu gani nasema hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wamekuwa wakinyanyaswa sana kwa kunyang’anywa nyavu zao. Siyo kwamba nabariki watumie nyavu ambazo hazifai, la hasha! Mwaka 2016 nilizungumza nilivyokuwa nachangia kwamba Serikali inatakiwa itoe elimu jinsi ya kutumia hizi nyavu, ni nyavu gani wavuvi wanatakiwa watumie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza na Waheshimiwa Wabunge wengi sana walizungumza kwamba ni kwa nini maduka bado yapo ambayo yanauza; na viwanda vinatengeneza nyavu hizo? Wavuvi hawa wamekuwa wakinunua kwa kutumia pesa, matokeo yake, wananyang’anywa, zinachomwa na wanajikuta wanaingia katika umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Februari kulikuwa na mgomo wa wavuvi na Serikali ikasema kabisa kwamba inaunga mkono mgomo huo. Sasa mimi nikashangaa ni kwa nini Serikali iunge mkono badala ya kutatua tatizo? Maana yake ni kwamba inaunga mkono tuwe na watu ambao hawana kipato na mtu asipokuwa na kipato matokeo yake anakuwa anafikiria mawazo mabaya ambayo yanapelekea hata kujiingiza katika vitendo vibaya ambavyo siyo vizuri kwa jamii. Kwa mfano, tunaweza tukatengeneza watu ambao ni vibaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetaka tu Serikali na Mheshimiwa Waziri anapokuja atuambie ni mkakati gani walionao wa kuweza kutatua hili tatizo ili wananchi wetu waweze kufanya hii shughuli wakiwa na amani na kusiwe na ile tabia ya Serikali na wavuvi kuviziana. N kama vile wanaviziana kwamba wakitumia hizo nyavu na wenyewe wanakuja kuwanyang’anya ni kama kuviziana. Sasa tukitoa elimu, tutakuwa tumewasaidia sana watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kilimo, Mkoa wa Mwanza una eneo kubwa, takribani asilimia 53 ambalo limzungukwa na Ziwa Victoria. Hii inatoa nafasi kubwa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini mpaka sasa sijaona hatua yoyote ambayo imechukuliwa ili tuwe na kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa Mwanza. Wakulima wengi wamekuwa wakitegemea kilimo ambacho ni cha majira, lakini majira yakibadilika, wanashindwa kulima. Kama kwa sasa, kumekuwa na ukame, tungekuwa na kilimo cha umwagiliaji wananchi wetu wangeweza kulima bila kutegemea majira ambayo yanakuwa yanawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona chakula kimekosekana na wananchi wanapolalamika, kwa mfano Mheshimiwa Rais alikuja, nafikiri ilikuwa ni Shinyanga, watu wakamwabia kwamba wana njaa na akawaambia hawezi kuwapikia. Wanaposema kwamba wana njaa, siyo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii. Kabla sijaanza kuchangia napenda kutoa pole kwa wananchi wa Mwanza kwa tetemeko ambalo limetokea jana na pia nitoe pole nyingi kwa askari wetu Joyce ambaye alifariki kwa kupata mshituko na majeruhi wengine ambao wamepelekwa hospitali, natoa pole sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ulikuja Mwanza najua ulifanya mambo mazuri sana kama alivyoongea Mbunge wa Nyamagana, lakini kuna migogoro ambayo hukuipitia, kuna migogoro ambayo iko Ilemela. mwaka 2009 Jeshi la Wananchi lilifanya utambuzi wa maeneo yake na iligundulika eneo la Mlima wa Nyagungulu Kata ya Ilemela ilikuwa inafaa kwa makazi ya Jeshi. Sasa utambuzi huu baada ya kufanyika ilionekana kuna kaya 448 ambazo zilikuwa na makazi ya kudumu na tarehe 04 Novemba, 2014 ilifanyika tathmini ambapo Serikali ya Mkoa pamoja na Jeshi la Wananchi waliona kwamba wananchi hao wanapaswa kulipwa, na waliamua kwamba baada ya tathmini hiyo walisema kwamba ndani ya miezi sita wananchi hao wangekuwa wameshalipwa, lakini mpaka sasa bado hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyumba zingine ambazo ni za udogo mpaka zimeanza kuanguka hawawezi kufanya marekebisho yoyote au kuzikarabati kwa sababu wanaogopa eneo hilo linachukuliwa na Jeshi. Sasa Mheshimiwa Waziri ninaomba umalize huu mgogoro kwa sababu hawa wananchi wanateseka na wananchi wengi wamekuwa wakilalamika, wameandika barua nyingi sana. Wameandika barua kwa Mkuu wa Mkoa, barua hizi hapa nitakuletea, wameandika kwa Mbunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hii Wizara ya Elimu. Nitaenda moja kwa moja kwenye hoja zangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu mikopo ya elimu ya juu. Kumekuwa na malalamiko mengi sana ya vijana wetu kutopata mikopo na hata kama wakipata mikopo hiyo kwa mwaka wa kwanza, mwaka unaofuata wanakosa sifa kutokana na kwamba masharti yamekuwa yakibadilika kila wakati. Kila mwaka Serikali imekuwa ikija na masharti mapya. Hali hii inamfanya kijana anashindwa kusoma na ku-concentrate katika masomo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali, naomba masharti haya kabla hawajayatoa wayalete hapa Bungeni ili tuweze kuyajadili maana yamekuwa yakibagua wanafunzi wetu. Mwanafunzi anakuwa na uhakika wa kusoma mwaka mmoja, mwaka wa pili anajikuta anakosa sifa kutokana na masharti ambayo yanabadilika kila wakati na yanamfanya anashindwa kuendelea, anabaki kutangatanga. Matokeo yake sisi Wabunge ndiyo tunakuwa kama msaada wa hao wanafunzi maana wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu sifa zimemwondoa moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu asilimia 20 ya bajeti ya Serikali. Iliamuliwa kwamba asilimia 20 ya bajeti ya Serikali iwe inaenda Wizara ya Elimu, lakini mpaka leo hakuna pesa ambayo inatolewa kwenye hiyo bajeti. Bajeti ya mwisho kabisa ambayo ilitoa hiyo asilimia 20 ilikuwa ni bajeti ya mwaka 2008/2009 kipindi cha JK. Sasa sasa hivi mnajigamba kwamba mnakusanya pesa nyingi, lakini hatuoni hizo pesa zikienda huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri akija hapa atuambie hizo pesa zitakwenda lini kwa sababu pesa hizi kwa mfano zingeenda kila mwaka zingesaidia sana changamoto hizi ambazo zinawapata walimu, kununua vitabu, kujenga maabara na kutengeneza mazingira mazuri ya wanafunzi. Lakini tumekuwa tukipiga tu mark time tunakwepa hili jukumu letu. Waziri anapokuja hapa naomba atuambie hiyo hela itaanza kwenda lini kwa sababu tunaenda kupitisha bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu madai ya walimu. Wengi wameongea hapa, mwaka jana tulipitisha bajeti lakini bado walimu hawajaanza kulipwa na wana malalamiko mengi sana. Sasa hivi tunaenda kupitisha bajeti, naomba Waziri akashughulikie madai haya kwa sababu walimu wetu wamekuwa wakihangaika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alishakuwa mwalimu anajua kabisa changamoto zinazowakuta walimu. Sidhani kama na yeye alipata matatizo haya. Inawezekana labda alipata matatizo haya ndiyo maana analipiza kisasi labda niseme hivyo kwa sababu ni kwa nini sasa tunapitisha bajeti na hashughulikii matatizo yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie wanafunzi wetu. Wanafunzi wengi hawana madawati kwa maana kwamba shule nyingi hazina madawati. Tunaomba hiki kilio kiishe maana malalamiko yamekuwa mengi sana, naomba hiki kilio kiishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu capitation grants. Mheshimiwa Tunza amezungumzia, lakini mimi ningeenda moja kwa moja kwenye Mkoa wangu. Nataka hii shilingi 4,000 ambayo ilikuwa inabaki kwenye Halmashauri kwa ajili ya kununua vitabu waniambie wameifanyia nini kwa sababu vitabu vyenyewe hawajanunua, sasa wameipeleka wapi. Nataka wananchi wangu wa Mkoa wa Mwanza hasa shule zangu za Mkoa wa Mwanza waambiwe kwa nini hiyo pesa haikununua vitabu na imeenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SUSAN P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hatukatai wala hatupingi Operation Uvuvi Haramu, lakini tunapinga operation hii inavyoendeshwa. Operation hii inaendeshwa bila kufuata weledi, wavuvi wetu wamekuwa wakiombwa rushwa kutokana na hii operation, utakuta mvuvi anaombwa rushwa ya mpaka milioni ishirini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu ni watu wa chini sana, unaenda unamwomba rushwa ya milioni ishirini, wakikataa wanakamata nyavu zao hata kama ni halali kwa uvuvi, wanaenda kuzichoma. Huu ni uonevu wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wetu wamekuwa wakionewa sana, wanalipishwa fine ambazo haziko kwenye Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 2003. Mtu analipishwa fine mpaka milioni hamsini. Huyu ni mvuvi wa hali ya chini, unategemea afanye nini? Matokeo yake wanaenda wanauza mpaka rasilimali zao, wanauza nyumba zao, wengine mpaka wamekufa kwa pressure kwa sababu ya hizi fine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua sheria hii inafanyiwa marekebisho na Wizara, lakini naomba sana Wizara inapofanya marekebisho haya iwahusishe wavuvi ambao ni wadau na ambao wataitumia hii sheria kuliko wao kukaa wenyewe na kufanya marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini Wizara inaogopa kukutana na hawa watu? Kuna shida gani? Ni vizuri Wizara ikawashirikisha; (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Wizara imetoa tangazo la hii operation ya kukamata nyavu ambazo si halali, lakini vile vile imezuia nyavu halali kuingia nchini. Kuna nyavu ambazo zimezuiliwa mipakani, sasa wanataka hawa watu watumie kitu gani? Hii sekta imeajiri zaidi ya watu milioni nne, sasa mnataka wafanye shughuli hii kwa kutuimia vifaa gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba wamezuia lakini sioni Wizara ikiweka mkakati wa kuweza kuwasaidia hawa wavuvi kwa kuwapatia vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuvua. Wamekuwa wakivua kwa kutumia nyavu zisizokuwa halali kwa sababu hawana vifaa na Serikali nimeona kwamba, haina makakati wowote wa kupeleka pesa kwenye hii Wizara kwa ajili ya kutatua haya matatizo ya wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hakuna elimu ambayo inatokewa kwa hawa wavuvi. Wavuvi wengi wamezaliwa wakakuta wazazi wao wanafanya shughuli hii ya uvuvi, kwa hiyo wakaingia tu kwenye hii shughuli na kuanza kuvua, hawajui hata sheria zipi ambazo zinatakuwa kuwaongoza, na Wizara imekaa tu, inatangaza operation bila hata kutoa elimu kwa hawa watu, ili waweze kujua ni nini wanatakiwa wafanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu viwanda. Hakuna viwanda vya kutosha vya kuchakata samaki. Tungeomba Wizara ije itueleze ina mkakati gani wa kuongeza viwanda kwa ajili ya kuchakata samaki kwa sababu, viwanda vilivyopo ni vichache na haviendani na mahitaji ya samaki wanaopatikana. Vile vile pia wametangaza Operation Number 3 ambayo wamesema kwamba kutakuwa na mahakama ambazo zinatembea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Mahakama itakuwa inafanya kazi gani, kwa sababu wamesema kwamba watakuwa wanaenda moja kwa moja kwa wavuvi wakiwakamata wanawahukumu hapo hapo; hawa wavuvi wataweza kujitetea wakati gani? Kwa sababu hawatakuwa na muda wa kuweza kutafuta watu wa kuwatetea. Wamesema kwamba, watakuwa wanaenda wanatoa hukumu hapo hapo, hiyo si sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba Bunge liunde tume ambayo itaweza kufuatilia hizi operation; kwa sababu kumekuwa na matamko. Tangu matamko yametoka watu wamefanya kama mradi wa kujipatia pesa, kila mmoja anakuja na la kwakwe mpaka wavuvi wamekuwa hawaishi kwa raha. Tukumbuke kwamba hawa ni watu wanyonge na wamesema kwamba Serikali yao inasimamia watu wanyonge. Watu wanyonge ndio hawa wavuvi wetu, sasa wanataka wasimamie watu gani? Naomba kwenye hilo tuweze kulisimamia kabisa kwa sababu hizi operation zinaumiza wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu mifugo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mwanza umezungukwa na Ziwa Victoria lakini maeneo mengi ya mkoa huu hayana maji. Maeneo kama ya Misungwi, Magu na Buchosa; maeneo haya yako karibu sana na Ziwa Victoria lakini hayana maji. Ni aibu sana kwa Taifa kama hili ambalo lina miaka 57 toka limepata uhuru halafu bado wananchi wana-share maji na viumbe.

Mheshimiwa Spika, ningeomba Waziri anapokuja ku- wind up atueleze wananchi wa Mwanza ni lini tutafaidika na hili ziwa kwa sababu haya maeneo sioni sababu kwanini mama zangu wa kule ninakotoka Misungwi wahangaike kuchota maji na ku-share na wanyama maji machafu wakati wako karibu kabisa na ziwa.

Mheshimiwa Spika, ziwa hili limewasaidia watu wa Misri ambao wanatumia Mto Nile lakini wameweza kupata maji ambayo yanawasaidia hata katika viwanda kwa sababu wameweza ku-utilize hili ziwa vizuri. Sasa kwa nini sisi tunashindwa hata kupata maji ya kunywa tu ambapo ziwa kwa kiwango kikubwa liko katika nchi yetu?

Mheshimiwa Spika, nizungumzie miradi ambayo haijakamilika, Mradi wa Lumea Kalebezo. Mradi huu ulianza mwaka 2012 katika Halmashauri ya Buchosa na ulitakiwa kutumia miezi sita tu, lakini mpaka sasa hivi miaka sita mradi huu haujakamilika. Mradi huu ulikuwa wa kiwango cha shilingi bilioni 1.69 na mkandarasi ameshapewa shilingi bilioni 1.3 na maji hayajatoka. (Makofi)

Sasa Waziri nataka uje utuambie hii hela imeenda wapi, huu ni ubadhirifu wa hali ya juu sana. Hela za walipa kodi zinaliwa tu na tunaangalia tu. Nataka uje utuambie hawa watendaji waliyofanya haya mambo, waliolipa hela nyingi kwa mkandarasi wakati hajamaliza kazi watachukuliwa hatua gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu Taasisi za Serikali ambazo hazilipi bill. Kwa nini Serikali hawalipi bill katika taasisi zao matokeo yake wanakatiwa maji, wanakatiwa na umeme? Hii inasumbua watu wetu, mnawapa adhabu watu wetu ambao wanalipa bill kwa wakati. Tunaomba hili tatizo liishe; ni aibu sana kwa Serikali kukatiwa maji au umeme kwa sababu ya kutokulipa bill wakati ninyi mmekuwa mbele sana kuwakatia watu. Sasa tunaomba muoneshe mfano katika taasisi zenu.

Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa hospitali kukatiwa maji, yaani mnategemea sasa watu wetu wafanye nini, kama sisi wenyewe tunashindwa kujisimamia? Ninaomba unapokuja ku-wind up utuambie kwamba ni lini sasa mama zetu wataacha kubeba ndoo? Kwa sababu hili limezungumzwa sana na wabunge tumekuwa tukilisemea sana na tunaenda kupitisha bajeti kama kawaida. Tunaomba hii bajeti iende, pesa hizo ambazo tunazitenga naomba ziende kwenye hiyo miradi na miradi ikamilike.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo lililo wazi kabisa kwamba kutokana na maendeleo ya kasi ya teknolojia ambayo yameathiri nyanja mbalimbali za maisha, ikiwemo sekta ya mawasiliano na uchukuzi, mtazamo na tafsiri katika sekta hizi umechukua wigo mpana sana. Kwa sasa ukizungumzia mawasiliano na uchukuzi unazungumzia ulinzi na usalama, unazungumzia haki na uwezo wa kupata taarifa na maarifa (elimu na ulinzi) kwa haraka, unazungumzia mwingiliano wa maisha ya kila siku ya binadamu katika nyanja zote zinazojulikana kuanzia uchumi, siasa, jamii na kila kitu kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukweli huo, kupitia bajeti hii ya mwaka 2018/2019 ni vema Serikali ikalieleza Bunge ni kwa namna gani nchi yetu imejipanga katika sekta ya mawasiliano na uchukuzi katika zama hizi za mapinduzi makubwa, tumejipanga vipi kuyatekeleza hayo kwa vitendo?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupitia bajeti hii ya mwaka 2018/2019, sijaona mahali ambapo mipango na mikakati ya Serikali imeonesha kuwa Mkoa wa Mwanza unapaswa kuwa eneo la kimkakati katika nyanja za mawasiliano na uchukuzi hasa kwa eneo la Maziwa Makuu na kipekee kwa Afrika Mashariki. Nilitarajia Serikali hii ingetumia kadri inavyowezekana kimkakati ili Mwanza iwe kitovu cha usafiri kwa maana ya anga, maji na nchi kavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningetazamia katika nyakati hizi za ushindani mkubwa wa kibiashara na kiuchumi Serikali ingejikita katika kuimarisha na kuboresha miundombinu ya uchukuzi ili Mwanza kuwe kitovu cha usafiri kwa nchi za EAC, kwa maana ya kuunganika kwa njia ya barabara na nchi za Burundi, DRC, Uganda, Kenya, Rwanda na Sudani ya Kusini, na hii ni ahadi iliyowahi kutolewa na Rais Dkt. Magufuli mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwaambie wananchi wa Mkoa wa Mwanza ahadi hiyo imefikia wapi? Lakini wanataka kujua pia mikakati ya kuboresha na kurejesha reli yao, je, upo au ndiyo wasahau kabisa kama walishawahi kuwa na treni ambayo ndiyo usafiri rafiki kwa maendeleo ya kiuchumi duniani kote?

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kumekuwepo na taarifa nyingi kuhusu dhamira ya kujengwa kwa daraja katika eneo la Kivuko cha Busisi – Kigongo. Ningependa kupata kauli ya Serikali suala hili limepewa uzito kiasi gani katika bajeti ya mwaka 2018/2019? Ili sasa isiwe tu maneno bali tuone utekelezaji, wananchi wa Mwanza hususani wanaotumia kivuko hiki kwa ajili ya kuingia na kutoka Jijini Mwanza kuelekea Sengerema, Buchosa au Mikoa ya jirani ya Geita, Kagera hadi nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda hadi DRC na kwingine wanataka kujua, je, ujenzi huu unaanza na kukamilika lini? Je, daraja litakalojengwa litakuwa la namna gani? Na sasa tuko katika hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mipango ya ujenzi wa meli, vivuko, kukarabati meli na vivuko vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria ikiwemo pamoja na baadhi ya maeneo ya visiwa 36 vilivyoko ziwani humo, nataka kusikia kutoka Serikalini, je, kwa mwaka huu unaoisha wamefanya ukaguzi wa vivuko au meli ngapi ili kupima uimara wake na ufanisi wake au tunasubiri kufanya ukaguzi pale tunapopata majanga? Je, mipango ya ujenzi wa meli na vivuko na ukarabati wa meli na vivuko unahusiana na vivuko vingapi na katika maeneo yapi hasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, katika vivuko hivyo Serikali ina mpango gani kukifanyia ukarabati mkubwa Kivuko cha Kome – Nyakalilo ambacho ni wazi kabisa kimeshaonesha dalili zote za kuchoka, kinaelemewa na abiria na mizigo hivyo kusababisha adha ya usafiri wa majini na usalama wa abiria na mali zao kutokuwa wa uhakika? Serikali inasubiri hadi maafa yatokee ndiyo iweze kukifanyia kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Kivuko cha Kome – Nyakalilo inavikabili vivuko vingi mathalani Kivuko cha Luchelele na mahali pengine, nasisitiza Serikali itoe takwimu ya jumla ya vivuko vinavyofanya kazi ndani ya Ziwa Victoria na viko katika hali gani kwa kila kimoja. Vivyo hivyo, takwimu za meli zinazofanya kazi Ziwa Victoria na hali zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ulitoa ruzuku kwa makampuni ya simu ili kufikisha na kuboresha huduma za mawasiliano vijijini na kwenye maeneo yasiyokuwa na wa kibiashara, kwa Kanda ya Ziwa Mikoa iliyobahatika ni Mwanza na Mara. Ningependa kujua mpango huo umekuwa na mafanikio kiasi gani? Ruzuku hiyo ilitolewa kwa namna gani na kwa utaratibu upi na ilikuwa kiasi gani na makampuni yapi yaliyopewa?

Mheshimiwa Naibu Spika, nauliza hivyo kwa sababu hali ya mawasiliano katika maeneo mengi ya vijijini bado siyo nzuri huku maeneo mengine yakiwa hayana mawasiliano kabisa, hasa maeneo ya visiwani ambayo yana vivutio vya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitekeleza au kukiboresha kilimo unagusa maisha ya mwananchi wa kawaida kabisa. Takwimu zinaonesha kuwa kilimo kinaajiri kati ya 70% hadi 75% ya Watanzania na kinachangia 20% hadi 28% ya pato la Taifa. Kwa nini sekta inayoajiri watu zaidi ya nusu ya ajira na inayochangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa inapuuzwa na kupangiwa bajeti ndogo ukilinganisha na umuhimu wake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije hapa ituambie kwa nini haitekelezi Azimio la Maputo kuhusu kilimo na usalama wa chakula ambapo ilitakiwa kutenga 10% ya bajeti ya Serikali kila mwaka kwa ajili ya kilimo. Pesa hii ingesaidia sana katika kutatua changamoto nyingi ambazo zinaikumba sekta hii ya kilimo na kukuza uchumi wa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa pamba wanazidi kukata tamaa kwa sababu pamoja na kazi kubwa wanayofanya wanaishia kupata hasara tu kuanzia maandalizi ya kilimo, kwenye mavuno na hadi kwenye mauzo. Wanakabiliwa na matatizo ya mbegu ambazo hazioti na wameuziwa na mawakala waliopitishwa na Bodi ya Pamba. Hivyo, inawalazimu kununua mbegu mara mbili na kuwafanya wapishane na misimu. Mbali na mbegu mbovu, wanakumbana na dawa ambazo haziui wadudu, wanunuzi wadanganyifu wanaochezea mizani ili kupata faida kubwa, pembejeo kuchelewa kufika na kupishana na msimu wa kilimo na kilimo cha kutegemea msimu huku kukiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa pamba wa Mwanza na maeneo mengine takribani mikoa 17 inayolima zao hili wanateseka sana na kuona zao hili kama halina faida kwao. Ni wakati sasa wa Serikali kutatua changamoto hizi ili wakulima hawa wafaidike na hili zao lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwafutie madeni wakulima wanaodaiwa kwa muda mrefu yanayohusu pembejeo na huduma za ugani hasa mbolea, viuatilifu na mbegu. Madeni haya ambayo yanaongezeka kila mwaka yanawafanya wanalima huku wakiwa na mzigo wa kulipa madeni kila mwaka, matokeo yake hawapati kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwapatie ruzuku wakulima kama mataifa makubwa duniani wanavyowapatia ruzuku wakulima wake. Kwa nini hapa tunaacha wakulima kuwa ni watu wa kuhangaika wenyewe? Tuanze na wakulima wa pamba, tuwasamehe madeni yao na wapewe ruzuku ili sasa turudishe hadhi ya maisha ya wakulima wa pamba ambao walitufanya tukasifika duniani na watu kuendesha maisha vizuri kabisa ikiwemo kujenga makazi bora na kusomesha watoto wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji kipindi hiki ni muhimu sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasumbua sana kutabiri misimu ya masika, vuli, kipupwe au ukame. Ni nini mikakati ya Serikali kibajeti hasa kwa maeneo ambayo wananchi wameshaonesha utayari kwa vyanzo au uwezo kidogo walionao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji kinaweza kabisa kuliokoa Taifa na mahitaji ya chakula, kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha ya wananchi. Nini mikakati ya Serikali hasa kulitumia Ziwa Victoria kama wafanyavyo wenzetu wa Misri ambao kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Mto Nile kutokana na Ziwa Victoria ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa hilo? Ni hatua gani Serikali inachukua pamoja na ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika kuwekeza katika shughuli za kilimo, uzalishaji na usindikaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanza ina rasilimali kubwa sana ya maji huku 53.25% ya eneo la mkoa likiwa katika Ziwa Victoria. Ni kwa mantiki hiyo kilimo cha umwagiliaji kinaweza kufanywa kutegemea maji ya ziwa hilo, pamoja na mabonde ya mito yanayopeleka maji katika ziwa hilo. Eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Mwanza ni takribani hekta 39,411 lakini mpaka sasa ni hekta 1,429 (sawa na 3.93%) ndizo zinazotumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Serikali iweke mikakati madhubuti kuongeza idadi za hekta ili wananchi wanufaike na hiki kilimo cha umwagiliaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na miradi ya maji ambayo imeshindwa kukamilika katika Mkoa wangu wa Mwanza, nitazungumzia mradi ulioko katika Halmashauri ya Buchosa Jimbo la Buchosa Wilaya ya Sengerema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Lumeya-Kalebezo Nyehunge wenye thamani ya shilingi bilioni 1.69; mradi huu ulianza Desemba, 2012 na ulitarajiwa kumalizika ndani ya miezi sita hadi leo ni miaka sita, mradi huo haujakamilika na mkandarasi alishalipwa bilioni 1.3 ambayo ni asilimia 90 ya fedha ya mradi mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ungekamilika kwa wakati ungesaidia kuondokana na matatizo ya maji kwa wakazi zaidi ya 16,000 katika halmashauri hiyo. Pamoja na mradi huo kutokamilika kwa wakati Serikali imekuwa ikitoa matamko ambayo mpaka sasa hayajasaidia mradi huo kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, terehe 30 Aprili, 2016, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema alisema Serikali imeunda Tume ya kuchunguza uzembe na madudu yaliyosababisha mradi huo kutokamilika huku mkandarasi akiwa ameshalipwa pesa karibu zote na maji hayatoki. Mwezi Juni, 2016, Mkuu huyo wa Wilaya akasema kuwa ripoti ya timu aliyoiunda imebaini u badhirifu mkubwa kwenye mradi huo na kuziomba mamlaka za juu kumchukulia hatua aliyekuwa handisi na Mkurugenzi wa Wilaya ya Sengerema kwa kumlipa mkandarasi pesa nyingi wakati kazi hajamaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, terehe 5 Aprili, 2017 aliyekuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI akijua kabisa muda wa kukamilika mradi huo umepita na pesa nyingi zimelipwa, akasema kuwa utakamilika na maji yatatoka ifikapo Juni, 2017, lakini mpaka sasa maji hakuna na watu wanahangaika.

Tarehe 15 Februari, 2018 Waziri wa Maji alitoa agizo akiwa hapa Dodoma akiwaagiza TAKUKURU kuchunguza mradi huo wa maji baada ya kuona Waziri Mkuu ambaye ni bosi wake akiwa Mwanza. Tarehe 15 Februari, 2018 Waziri Mkuu naye akaagiza TAKUKURU na Serikali ya Mkoa wa Mwanza walichunguze suala hilo na kuchukua hatua lakini mpaka leo hakuna majibu yaliyotolewa na maji hayatoki na wananchi wanazidi kuteseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wahusika wanapokuja kuhitimisha wawaeleze wananchi wa Buchosa ni lini mradi huo utakamilika na ni hatua gani zitachukuliwa kwa watu waliochelewesha mradi huo mpaka sasa wananchi wanateseka huku watu wengine wakitafuna kodi zao. Ni aibu kubwa kwa Halmashauri ya Buchosa iliyoko Nyehunge kilometa chache kutoka ziwani kukosa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miundombinu ya barabara ya Halmashauri ya Buchosa, wananchi wa maeneo haya walitaja mojawapo ya neema ambayo wangeipata kwa kuwa na halmashauri ni kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara. Barabara ya kutoka Nyamadoke ulipo mpaka wa Mwanza na Geita kuelekea Nyehunge Kalebezo, Bukokwa, Nyamazugo hadi Sengerema ni mbovu kwelikweli miaka yote na hata inapofanyiwa matengenezo au marekebisho yamekuwa yakifanyika kwa kiwango cha chini na kuifanya kutodumu kwa muda mrefu na kuwekewa molamu ngumu inayoweza kudumu hata zaidi ya mwaka haina mitaro ya kupitisha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imekuwa ikileta usumbufu kwa wafanyabiashara wa magari( vyombo vya usafiri) kwa magari kuharibika sana na hivyo kuongeza adha na shida ya usafiri hasa wagonjwa wanaokwenda kutafuta matibabu hospitali za Sengerema wakiwemo akinamama wajawazito. Pia wafanyabiashara na wakulima wa mananasi wanaotokea Nyamadoke, wavuvi wa kutoka Kahunda, Kafunzo, Kanyara, wasafishaji wa mazao ya misitu kutoka Bihindi, Bupandwa wanapata shida sana kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wahusika wanapokuja kuhitimisha wawaeleze wananchi wa Buchosa na Sengerema ni lini barabara hiyo itawekewa lami na kuwa barabara bora, pia wanataka kusikia ni lini barabara hiyo itaboreshwa kuanzia njia panda ya Nyamazugo- Sengerema ili wapite Katunguru wanapoelekea hadi Kamanga. Aidha, wananchi waelezwe ni kitu gani hasa kinasababisha barabara ya kuanzia Sengerema kuelekea Manga pamoja na umuhimu wake haijawahi kuwa katika hali inayostahili kwa shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nata kujua je, ni kwa sababu gani Serikali inagombania mapato ya vivuko na wale wawekezaji kule Kamanga kwa sababu Serikali nayo inamiliki vivuko Busisi, hivyo haitaki wananchi wavuke Kamanga hali inayowaathiri wananchi wa maeneo ya kuanzia Sengerema kuja Kasunganile, Lubondo hadi Kamanga kwa sababu hawawezi kwa vyovyote kwenda kurukia Busisi. Wanataka kusikia Serikali ina mipango thabiti kwa barabara hii badala ya kufanya ukarabati wa kuweka mchanga wa mfinyanzi, lini itaweka lami au molamu iliyo imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali sasa ituambie lini itaipandisha hadhi barabara hizi za Buchosa hadi Sengerema kutokana na matumizi muhimu na unyeti wake wa shughuli za kiuchumi na kijamiii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha