Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ally Seif Ungando (16 total)

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji kwenye Jimbo la Kibiti kwenye maeneo ya Delta kama Nyamisati, Mchinga, Mfisini, Kiomboi, Masala, Kiongoroni, Naparoni na Mbunchi.
Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Delta yanakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 25,780; ambapo wakazi wapatao 12,942 sawa na asilimia 50.2 wanapata huduma ya maji kwa sasa. Hivyo ninakubalianana ipo changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua changamoto hiyo Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 iliidhinisha shilingi milioni 403 na tayari zimepokelewa shilingi milioni 272.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji kumi. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri imetenga shilingi milioni 83.2 kwaajili ya ujenzi wa mfumo wa maji ya bomba katika kijiji cha Nyamisati.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo yaliyobaki kadri rasilimali fedha zitakavyo patikana.
MHE. ZAINAB M. VULU (K.n.y MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:-
Kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais kutaka kumaliza kabisa urasimu wa upatikanaji wa hati za kimila na hati za ardhi mpaka sasa bado ni tatizo kwa Wilaya ya Rufiji:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Afisa Ardhi Mteule?
(b) Je, Serikali haioni kwamba ina kila sababu ya kupeleka vifaa vya kisasa vya kupima viwanja na mashamba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida, Afisa Mteule na ni Mwajiriwa katika halmashauri husika. Kabla ya kuteuliwa kuwa Afisa Ardhi Mteule, mapendekezo ya uteuzi huanzia katika halmashauri husika kutoa pendekezo ambalo linawasilishwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa husika ambaye na yeye ataliwasilisha pendekezo hilo kwa Kamishna wa Ardhi. Pendekezo litakapowasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi, Kamishna atafanya uteuzi wa Afisa Mteule Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji afuate utaratibu huo nilioueleza hapo awali ili halmashauri yake iweze kupata Afisa Mteule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inatambua umuhimu wa kupima viwanja na mashamba hapa nchini. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imekuwa ikiziagiza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji. Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa vifaa hivyo, Wizara kupitia Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kununua vifaa vya upimaji ambavyo vitasambazwa katika Kanda nane za Wizara yangu ili halmashauri zote zilizopo ndani ya kanda hizo ziweze kunufaika.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Eneo lote la Vijiji vya Delta na Mto Rufiji lina wakazi zaidi ya 30,000 na halina usikivu wa simu za mkononi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti na hatimaye kuweka minara ya simu katika Vijiji vya Ruma na Mbwera, Msala, Kiomboni, Kicheru na Kiasi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Mbwera, Msala na Kiasi vimeshapatiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa Kampuni ya Simu ya Viettel (Halotel).
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa mawasiliano katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Vijiji vya Ruma, Kiomboni na Kicheru vimeingizwa katika mpango wa pili wa mradi wa Kampuni ya Simu ya Hallotel ambao unategemea kuanza wakati wowote.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kwa changarawe barabara ya Kibiti – Nyamisati. (a) Je, ni sababu zipi zilizochelewesha kukamilika kwa ahadi hiyo? (b) Je, ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za kuchelewa kwa matengenezo ya barabara ya Kibiti – Nyamisati kwa kiwango cha changarawe ni upatikanaji wa fedha. Tathmini iliyofanyika imebainisha kwamba barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 40.8 inahitaji shilingi bilioni 1.2 ili kufanyiwa matengenezo kwa kiwango cha changarawe. Hata hivyo, ili kuifanya barabara hiyo angalau iweze kupitika Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 iliitengea barabara hiyo shilingi milioni 45.79 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya kilometa 38.31 na katika mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 24 zilitumika kwa marekebisho ya sehemu korofi yenye urefu wa kilometa mbili na matengenezo ya kawaida ya kilometa 15. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matengenezo ya barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Serikali itajitahidi kutenga fedha za matengenezo kwa awamu ndani ya kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipande cha kilometa 32.8 kilichobaki baada ya hapo awali kufanyika matengenezo ya kilometa nane kwa kiwango cha changarawe kutoka Kibiti mpaka Ruaruke yaliyofanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Wananchi wa wa Kibiti wanaishukuru Serikali kwa kupata Mji Mdogo Kibiti na kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti na viongozi.
(a) Je, kuna tatizo gani hadi leo Mamlaka ya Mji haijaanza kazi na kumpata Meya?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka Mkurugenzi wa Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya
Kibiti ni mpya na ilianzishwa rasmi Julai, 2016. Halmashauri hiyo ilipatikana baada ya kugawanywa kwa Halmashauri Mama ya Rufiji ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Sababu kubwa iliyochelewesha uundwaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibiti ni ufinyu wa bajeti. Hali hiyo imechangia Halmashauri kushindwa kuitisha uchaguzi mdogo kujaza nafasi zilizo wazi za Wenyeviti wa Vitongoji ili kuunda Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo pamoja na Mwenyekiti wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Halmashauri hiyo inajiendesha kwa kutumia mapato ya ndani ambayo yalianza kukusanywa Oktoba, 2016. Hivyo, hali ya kifedha itakapokuwa nzuri, Halmashauri itafanya uteuzi wa Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo pamoja na kukamilisha uchaguzi wa Mwenyekiti ili Wenyeviti hao waweze kumchagua Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo anayetakiwa kuchaguliwa miongoni mwa Wenyeviti hao wa vitongoji.
MHE. HAWA M. CHAKOMA (K.n.y. MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:-
Wananchi wa Mji wa Kibiti wamefanikiwa kupata mradi wa maji, ingawa una changamoto nyingi katika utendaji wake:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwa ajili ya kulipia umeme na kulipa vibarua?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza usambazaji maji na mtandao, hasa ikizingatiwa kuwa, Mji huo unaendelea kukua kwa kasi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimia Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafahamu juu ya gharama zinazohusika katika uendeshaji wa Mamlaka za Maji kuwa ni pamoja na kulipa umeme na wafanyakazi wanaohusika katika uendeshaji huo. Kwa mujibu wa Sheria Namba 12 ya Huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2009, Halmashauri za Wilaya zimepewa wajibu wa kusimamia uendeshaji wa mamlaka katika kutoa huduma ya maji safi kwa wananchi katika miji yao, hivyo ni matarajio ya Serikali kuwa, Halmashauri ya Mji wa Kibiti inatimiza wajibu wake huo kwa kuwezesha ugharamiaji kwa kupitia bajeti zake na makusanyo kutokana na matumizi ya maji katika Mji wa Kibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafahamu ongezeko kubwa la watu linalosababisha kupanuka pia kwa eneo la Mji wa Kibiti. Kwa ufahamu huo katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, jumla ya Sh.568,477,000/= zimetengwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya mji safi na usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Mji wa Kibiti. Fedha hizo zitatumika katika kuongeza mtandao wa mabomba wenye umbali wa kilometa tano pamoja na kufufua visima vilivyopo ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Kibiti, itaendelea na uwezeshaji katika ujenzi wa miradi ya maji kwa lengo la kuongeza na kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Mji wa Kibiti na Tanzania kwa ujumla.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Maeneo ya Kibiti, Bungu, Jaribu Mpakani na Nyamisati katika Jimbo la Kibiti yanakuwa kwa haraka sana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupanga mipango miji?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mitandao na kuchonga barabara za mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kwa mujibu wa Sheria Namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 imeandaa Mpango Kabambe (Master Plan) wa Mji Mdogo wa Kibiti ili kuwa dira ya upangaji na uendelezaji wa mji huo ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kibiti. Kazi hiyo imepangwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari, 2018 na kuwasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuidhinishwa na kusajiliwa. Michoro hiyo itakuwa na jumla ya viwanja 360 ambapo kati ya hivyo, viwanja vya matumizi ya makazi ni 205, makazi na biashara 82, viwanja vya matumizi ya umma 25, makazi maalum (housing estate) nane , viwanda vidogo 20 na maeneo ya wazi 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu zikiwemo barabara ndani ya Mji Mdogo wa Kibiti utaanza kutekelezwa baada ya kuidhinishwa kwa michoro ya mipango miji na Wizara yenye dhamana na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA (K.n.y MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:-
Asilimia 90 ya wakazi wa Delta ya Mto Rufiji katika Kata ya Salale, Maparoni, Mbuchi na Kiangoroni ni wavuvi ambao hutumia mitumbwi isiyo na mashine na ndilo eneo pekee katika mwambao wa Bahari ya Hindi kunapatikana samaki aina ya kamba (prawns) kwa wingi; na kwa kuwa Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 imeazimu kuwapatia wavuvi wadogo wataalam, vifaa vya kisasa vya uvuvi ili wajiendeleze na kuongeza Pato la Taifa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa maeneo hayo semina kuhusu uvuvi bora wa kisasa?
(b) Kwa kuwa mikopo hutolewa kwa vikund mbalimbali; je, Serikali itatoa mikopo kwa vikundi vya uvuvi vilivyopo kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitoa mafunzo ya uvuvi endelevu kwa wavuvi kupitia semina, warsha, vipeperushi, makala, redio na luninga kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau mbalimbali. Katika kusambaza teknolojia mbalimbali za uvuvi, katika mwaka 2016/2017, Wizara ilirusha hewani vipindi saba vya redio na kimoja cha luninga vilivyohusu Wakala wa Mafunzo (FETA). Ukuzaji viumbe kwenye maji, uzalishaji bora wa samaki, mbinu za kutambua magonjwa ya samaki na uvuvi endelevu. Aidha, vipindi 19 vilirushwa hewani kwa lengo la kuwaelimisha vijana na kuwajengea uwezo wa kuingia katika uvuvi. Pia Wizara imechapisha nakala 1,000 za mwongozo wa ugani katika Sekta ya Uvuvi kwa lengo la kutoa elimu kwa wavuvi na wakuzaji viumbe kwenye maji.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mpango wa kutoa ruzuku kwa wavuvi ambayo inalenga kuwasaidia wavuvi kupata zana bora na vifaa vya kuvulia zikiwepo injini za boti kwa utaratibu wa uchangiaji ambapo wavuvi watangaia asilimia 60 ya gharama na Serikali itatoa asilimia 40. Katika awamu ya kwanza jumla ya engine 73 zimenunuliwa na vikundi 27 kutoka Ukanda wa Pwani katika Halmashauri za Bagamoyo, Mafia, Lindi, Manispaa, Mtwara Mikindani, Temeke, Mkinga, Muheza na Tanga Jiji vimekidhi vigezo. Hivyo, napenda nitumie fursa hii kumuomba Mheshimiwa Mbunge ahimize wavuvi katika Halmashauri ya Kibiti kujiunga katika vyama vya Ushirika vya Msingi ili waweze kutumia fursa hii kwa kuwa mpaka sasa hakuna kikundi kutoka Wilaya ya Kibiti au hata jirani Wilaya ya Rufiji kilijitokeza kuomba zana za uvuvi za ruzuku.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la WWF pamoja na Halmashauri ya Rufiji imewezesha wavuvi kuanzisha VICOBA 36 vyenye jumla ya wavuvi 829 na kupewa mafunzo ya ujasiriamali. Pia, Wizara kupitia Mradi wa Usimamaizi wa Uvuvi na Maendelea Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) inaandaa Mpango kazi utakaokuwa na program za vipindi mbalimbali kuhusu usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi ambazo zitarushwa katika televisheni na radio mbalimbali. Wavuvi wa nchi nzima wakiwemo wa Kibiti watanufaika na elimu itakayotolewa kupitia mpango kazi huo.(Makofi)
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Ufunguzi wa Kituo cha Afya Mbwera ulifanyika tarehe 27/8/1994 na aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, wakati huo Dkt. John Samwel Malecela lakini hadi sasa kituo hicho hakina hadhi hiyo ya kuitwa Kituo cha Afya.
(a) Je, Mheshimiwa Waziri mwenyewe haoni haja ya kwenda Mbwera kuona hali halisi ya kituo hicho baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu wake kuona kama kimekamilika?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha kwani wanaotakiwa ni 39 na sasa waliopo ni wanne tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Kituo cha Afya Mbwera kilifunguliwa muda mrefu na kinakabiliwa na uchakavu wa miundombinu na uhaba mkubwa wa watumishi ikiwemo madaktari, tabibu na wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imepeleka jumla ya shilingi 560,000,000, kati ya fedha hizo shilingi 400,000,000 zimetolewa na Serikali kupitia wadau wa maendeleo wa Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Funds) na shilingi 160,000,000, zimetolewa na Serikali ya Watu wa Korea kwa lengo la kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kujenga chumba cha upasuaji, nyumba ya mtumishi, wodi ya wazazi (maternity ward), jengo la maabara, kurekebisha mfumo wa maji safi na maji taka, chumba cha kuhifadhia maiti (mortuary) na kichomea taka (incinerator).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa jengo la wodi ya wazazi na jengo la upasuaji yapo katika hatua ya msingi na ujenzi unaendelea kwa kutumia mfumo wa force account. Vilevile shilingi milioni 300 zimepelekwa bohari ya madawa (MSD) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Kituo cha Afya Mbwera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la watumishi wa afya Serikali inalitambua na mnamo mwezi Novemba, 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti ilipewa watumishi wapya 11 wa kada mbalimbali za afya. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imepanga kuajiri watumishi wapya wa kada mbalimbali za afya 199.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete alipokuwa kwenye harakati za Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 alikubali kuwa mlezi wa Shule ya Sekondari Mahenge na akaahidi kutatua tatizo sugu la maji katika shule hiyo.
Je, ni lini Serikali itaipatia shule hiyo maji safi na salama kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la maji safi na salama linalozikabili baadhi ya shule za sekondari hapa nchini, ikiwa ni pamoja na Shule ya Sekondari Mahenge iliyoko Wilayani Kibiti. Ili kukabilina na tatizo hilo katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 36 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya elimu sekondari wilayani humo. Kati ya hizo fedha shilingi milioni 10 zitatumika kwa ajili ya mradi wa maji safi na salama katika Shule ya Sekondari Mahenge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga na kutoa fedha za miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya shule.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa wananchi wa Nyamisati wamekuwa wakipata adha kubwa sana katika eneo la kivuko. Je, ni lini Serikali itajenga Gati la Nyamisati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Gati la Nyamisati umeanza tangu tarehe 16 Machi, 2018 baada ya mkandarasi M/s Alpha Logistics Tanzania Ltd. na M/s Southern Engineering Company Ltd. kukabidhiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) eneo la mradi toka tarehe 2 Machi, 2018. Kazi ya ujenzi wa gati hili zinatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi Machi, 2019 kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 14.435.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizofikiwa mpaka sasa hivi ni kufanya upimaji wa bahari (bathymetric survey), uchunguzi wa udongo (geotechnical investigation) katika sehemu ya kujenga gati na usafishaji wa eneo (site clearance). Pia mkandarasi anaendelea na maandalizi (mobilization) kwa ajili ya kuanza kazi rasmi baada ya kazi hizi za awali za upimaji kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya kazi hii kumekuwa na changamoto kadhaa kama vile mwingiliano wa vyombo vinavyotumia kivuko na vile vya mkandarasi. Mfano, vessel inayofanya kazi ya uchunguzi wa udongo inaingiliana na vyombo vya usafiri, changamoto hii inatatuliwa kwa kujenga gati la muda (temporary berth) kwa ajili ya kuhudumia wasafiri.
Aidha, wananchi waliokuwa wanatumia gati la zamani ambalo sasa linajengwa jipya katika eneo hilohilo walikuwa hawataki kuhama, hata hivyo, uongozi wa Wilaya umefanikisha wananchi hao kuhama lakini wanahitaji wajengewe choo katika eneo jipya la kufanyia biashara walilohamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TPA tayari wanaendelea na taratibu za kujenga choo hicho cha umma ambapo mpaka sasa wapo kwenye hatua za kumpata mkandarasi wa kujenga choo hicho.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika kampeni za uchaguzi tarehe 18 Novemba, 2005 aliwaahidi wananchi wa Kibiti kuwa Serikali yake itajenga barabara ya Kibiti-Kikale ili kupunguza adha kubwa ya usafiri wanayopata wananchi wa Vijiji vya Mchukwi, Rungungu, Nyamatanga na Kikale ambamo barabara hiyo inapita:-
a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
b) Je, ujenzi huo unaotarajiwa utakuwa ni wa kiwango gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibiti - Kilale ni sehemu ya barabara ya Kingwira – Ruaruke - Mtunda – Myuyu yenye urefu wa kilometa 66.2 ambapo kipande cha Kibiti - Kikale kipo kati ya barabara ya Ruaruke - Mtunda. Tangu kutolewa kwa ahadi na Mheshimiwa Rais mwaka 2005 barabara hiyo imefanyiwa matengenezo ya kilomita 56 na ukarabati wa daraja la Ruhoi lenye urefu wa mita 24 kwa gharama ya shilingi milioni 151.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, barabara hiyo imetengewa shilingi milioni 185.02 kupitia TARURA kwa ajili ya matengenezo ya kilomita 65.9 kwa kiwango cha changarawe ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-

Katika Jimbo la Kibiti kuna mifugo mingi kama ng’ombe, mbuzi na kondoo, hivyo kusababisha mtafaruku baina ya wakulima na wafugaji, kwani wafugaji hawajawekewa mazingira rafiki kwa mifugo yao:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira rafiki kwa mfugaji?

(b) Je, ni lini mazingira hayo yataboreshwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kibiti ni moja ya Wilaya nane zilizopo katika Mkoa wa Pwani. Wilaya hii ina mifugo takribani Ng’ombe 50,000, Mbuzi 8,852 na Kondoo 4,877. Serikali inao mkakati wa kuboresha mazingira rafiki kwa wafugaji wa Wilaya ya Kibiti kwa kufanya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 80 kwa ajili ya kuanzisha minada miwili ya awali ambapo wafugaji watapata mahali pa kuuzia mifugo yao, Shilingi milioni 18 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa machinjio; na jumla ya shilingi milioni sita zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa josho. Aidha, Wilaya ya Kibiti kupitia Serikali za Vijiji imetenga takribani hecta 22,000 kwa ajili ya wafugaji katika vijiji18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yaliyotengwa yatawezesha wafugaji kupata malisho na machunga. Wataalam wameendelea kuwahamasisha wafugaji kushiriki katika kuboresha maeneo yaliyotengwa na kusisitiza wakulima wasivamie maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji. Pia, mifugo ifugwe kulingana na ukubwa wa eneo na pale inapozidi, basi ivunwe ili kuendana na hali halisi ya ukubwa wa eneo.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa mikakati ya kuendeleza sekta ya mifugo nchini katika Wilaya ya Kibiti ikihusisha uboreshaji wa malisho, ujenzi wa majosho, minada ya awali, machinjio na miundombinu ya maji kwa mifugo na utekelezaji wake, unatarajiwa kuanza hivi karibuni kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ZAYNABU M. VULU (Kn.y. MHE. ALLY S. UNGANDO) aliuliza:-

Ukarabati wa Kituo cha Afya Mbwera yakiwemo majengo ya upasuaji, Wodi ya Wazazi na mengineyo unakwenda kwa kasi sana:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme kwenye Kituo cha Afya Mbwera?

(b) Je, ni lini kazi hiyo itaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali itapeleka umeme katika Vijiji vya Mbuchi, Mbwera Mashariki na Mbwera Magharibi kupitia utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) III unaoendelea. Kazi hiyo itaanza Mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021. Mradi huo unahusisha kupeleka umeme wa Gridi ya Taifa katika eneo la Mbwera kutoka Muhoro kwa kujenga njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 40; ujenzi wa njia ya kusambaza umeme yenye urefu wa kilomira 2.78; ufungaji wa transfoma moja (1) ya KVA 50; pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 48 ikiwemo Kituo cha Afya cha Mbwera. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 1.56. Ahsante.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-

Wananchi wanaoishi katika Jimbo la Kibiti hutumia nishati ya mkaa na kuni kwa matumizi ya nyumbani, shuleni, gerezani na kadhalika, hivyo kusababibisha uharibifu mkubwa wamazingira kwa kukata miti hovyo:-

(i) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka nishati mbadala?

(ii) Je, ni aina gani ya nishati itakayotumka badala ya kuni na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swal la Mheshimiwa Ally Seif Ungado, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 (The National Energy Policy, 2015) imetoa mwongozo wakuboresha maisha ya wananchi kwa matumizi bora ya nishati kupitia teknolojia ya kisasa badala ya kuni na mkaa. Aidha, Serikali imekuwa ikichukua jitihada za makusudi kuendeleza vyanzo mbalimbali vya nishati ili kuongeza mchango wa nishati mbadala katika upatikanaji wa nishati nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha muda wa kati kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, Serikali inatekeleza miradi ya kuzalisha umeme kupitia vyanzo vya gharama nafuu vya maji na gesi ikiwa ni mkakati ya kuwawezesha wananchi kumudu kutumia nishati vya umeme wa gharama nafuu kwa ajili ya kupika badala ya kuni na mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia katika Miji ya Mtwara, LIndi, Pwani na Dar es Salaam ikiwa ni nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa. Kwa kuwa sehemu ya kuni na mkaa unaotumika katika Jiji la Dar es Salaam huzalisha katika Wilaya ya Kibiti, hatua ya kuanza kutumia gesi asilia kwa kupikia itapunguza uharibifu mkubwa wa mazingira kupitia ukataji miti hovyo kwa matumizi ya kuni na mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine tarehe 18 Mei, 2018, Serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ilisaini kataba nakampuni ya Mihan Gas Limited kwa ajili ya kusambaza vifaa vya kupikia, mitungi ya gesi na majiko kwa kutumia liquidifies Petroleum Gas au gesi ya mitungi kwa watumishi wa umma na wananchi wengine. Mpango huo pia unalenga kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-

Jimbo la Kibiti lina Kata 5 na Vijiji 17, sawa na Vitongoji 72 ambavyo vipo kwenye maeneo ya Delta lakini havina umeme:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme kwenye Visiwa hivyo?

(b) Je, utapelekwa umeme wa aina gani?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwapatia huduma wananchi wake Serikali kupitia TANESCO ilifanya upembezi yakinifu kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijiji vya Pombwe, Kiongoroni, Mbuchi, Mbwera Mashariki, Mbwera Magharibi, Maporoni, Kiechuru, Msala, Kiasi, Kiomboni, Mchinga na Mfisini vilivyo katika Delta ya Mto Rufiji. Aidha, katika hatua hiyo imesaidia kupata mahitaji halisi na kubaini changamoto zilizopo katika kutekeleza mradi wa kufikisha umeme katika vijiji hivyo. Mradi wa kupeleka umeme katika maeneo hayo tajwa unatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Desemba, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya upembuzi yakinifu kufanyika vijiji vya Mbuchi, Mbwera Mashariki na Mbwera Magharibi vitaunganishiwa na umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Muhoro umbali wa kilomita 40. Ujenzi wa njia ya umeme itatumia nguzo za zege kwa kuwa maeneo mengi ni chepechepe na oevu. Vijiji vingine vilivyobaki vitapelekewa umeme wa solar kwa kuwa ujenzi wa laini ya umeme wa Gridi kupeleka katika vijiji hivyo umekuwa na changamoto kutokana na jiografia ya maeneo hayo, ahsante.