Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ally Seif Ungando (19 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaitwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Wilaya ya Kibiti. Kwanza nikupe hongera kwamba umedhihirisha kwamba katika Bunge hili wewe kweli ni Mtemi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kuwashukuru wananchi wangu wa Kibiti, na niwaahidi kwamba nitawapa ushirikiano kwa kila linaloleta maendele kwani hiyo ndiyo kiu ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hoja ya Mheshimiwa Magufuli Rais wa nchi hii, ni kipenzi wa nchi hii, kama ifuatavyo na nitaanza na ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mizunguko yake Mheshimiwa Rais yamekuwepo malalamiko mengi katika ardhi. Ningeomba mamlaka husika katika eneo hili wachukue hatua stahiki kwa kutoa hati za ardhi kwa haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo nafahamu kumekuwa na migogoro mingi katika sekta hiyo na ninnaomba Waziri mwenye dhamana afanye kazi yake kuhakikisha Wilaya ya Rufiji hususan Kibiti, tunapata Afisa Ardhi Mteule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kuchangia kuhusu kilimo. Tunafahamu sasa kwamba wananchi imefika wakati walime kilimo chenye tija, walime kilimo chenye manufaa kwani hayo ndiyo mahitaji ya wananchi. Kumekuwa na kero nyingi katika upatikanaji wa pembejeo za ruzuku. Ningeomba kuishauri Serikali badala ya kupeleka vocha vijijini watoe kodi ambazo hazina ulazima ili pembejeo zipatikane kwa bei rahisi katika maeneo husika. Nafahamu kumekuwa na malalamiko mengi kwamba vocha zikifika vijijini wananchi hawazipati kwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika migogoro ya mifugo na wafugaji. Nafahamu katika Jimbo langu kuna migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kata ya Mtunda. Ningeomba sehemu ambayo inahusika wachukue hatua haraka iwezekanavyo. Pia ningeomba nishauri katika sehemu husika ya Kata hiyo kuundwe Kamati ya Kusuluhisha Migogoro hiyo. Tungetoa wakulima watano na wafugaji watano ili wakae kuangalia ni jinsi gani watatatua migogoro hiyo, pindi itakaposhindikana ndipo taarifa ziende kwa DC naye achukue hatua stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba wakulima na wafugaji wanatuletea kipato katika nchi hii, lakini wafugaji naona kama wamesahaulika. Kuna kila sababu ya kuandaa ranch katika Wilaya yetu ya Kibiti na huko kwenye ranch lazima zipelekwe huduma muhimu zikiwepo majosho, vikiwemo vituo vya minada ili sehemu husika wananchi nao waone kwamba wanafaidika na ufugaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine niende katika uuzaji wa korosho. Suala hili limekuwa na migogoro mikubwa kwamba mkulima anakatwa kodi nyingi na vyama vya msingi kiasi kwamba mkulima wa korosho anaona hana sababu ya kwenda kulima zao hilo. Ningeshauri kwamba baadhi ya kodi ambazo siyo za lazima zitolewe katika zao hilo la korosho.
Sehemu nyingine ambayo ningependa kuchangia ni katika huduma ya afya. Nafahamu kwamba Wizara husika imejipanga kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati katika vituo vya afya. Lakini si dawa tu wangeangalia na maslahi ya watumishi hao. Kweli nafahamu tuna migogoro mingi, tuna madai mengi ya watumishi ambayo hawajalipwa na kwamba tunaweza tukawapelekea dawa na wakashindwa kutuhudumia ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia sehemu nyingine ya kwenye viwanda. Ninafahamu Wilaya yangu ya Kibiti kuna kiwanda cha kusindika samaki, lakini kiwanda hicho kimetelekezwa, hakifanyi kazi. Kwa hiyo ningeomba pindi tutakapoamua kuunda viwanda vipya tukifufue na kiwanda hicho cha Misati. Kiwanda hicho kipo Nyamisati, umeme umekwenda lakini maji bado hayajafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika miundombinu ya barabara. Tunafahamu pindi tutakapopeleka viwanda hivyo sehemu husika tupeleke na mahitaji muhimu yakiwemo barabara, maji, umeme wenye uhakika ili mwekezaji atakapokuja kuwekeza sehemu husika basi ashawishike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni ajira kwa vijana. Tunafahamu nchi yetu ina tatizo kubwa la ajira kwa vijana, ninaomba mamlaka husika itoe mikopo yenye riba nafuu kwa vijana ili waweze kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningeomba vyuo vyetu vya VETA kijana anapohitimu apewe mtaji wa kuanzia maisha, badala ya kusubiria ajira ili ajiajiri mwenyewe hiyo itakuwa chachu ya kumletea kipato na familia yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ningependa kuchangia ni katika ukusanyaji wa mapato wa Halmashauri. Nafahamu kwamba sasa hivi Halmashauri nyingi zimefunga mfumo wa kimashine, ningeomba TAMISEMI wafutilie kwa karibu mno kuhakikisha kwamba mapato ya Halmashauri hayapotei. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika michezo. Nafahamu sasa hivi mpira ni ajira. Naamini katika Wilaya zetu tungetoa kipaumbele kwa kujenga viwanja vya kisasa, wananchi wanaweza wakajiajiri wenyewe kupitia sekta hiyo ya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika zao la korosho lipo tatizo kubwa sana kama ifuatavyo:-
(i) Upatikanaji wa pembejeo za sulphur. Hapa lipo tatizo kubwa kwani pembejeo hazipatikani kwa wakati;
(ii) Mfumo huu siyo rafiki kwa mkulima, haumletei tija mkulima, kumekuwa na udanganyifu sana katika mfumo huu wa pembejeo za ruzuku;
(iii) Naomba mfumo huu uboreshwe kwa kutoa kodi ambazo siyo za lazima ili pembejeo ziuzwe kama Coca-Cola katika maduka yote ya pembejeo;
(iii) Mfumo wa Stakabadhi Ghalani nao una changamoto kubwa, hasa katika Jimbo langu la Kibiti, kwani wakulima mpaka leo wanadai malipo yao ya mauzo ya korosho zao kama shilingi bilioni sita hivi msimu wa mwaka 2012/2013. Jamani kwa nini mkulima anakopwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za zao la korosho:-
(i) Maghala ya kuhifadhia;
(ii) Pembejeo za uhakika na wakati;
(iii) Wataalam;
(iv) Viwanda vya kubangulia korosho;
(v) Ukosefu wa soko la uhakika; na
(vi) Miche bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hizi zote zinaweza kutatuliwa kama kila mmoja atafuata wajibu wake kama Bodi ya Korosho. Bodi hii ya Korosho inakusanya pesa nyingi kwa kila msimu wa mauzo ya korosho, lakini cha kushangaza haimsaidii kabisa mkulima na zao la korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti kama vile Kibiti, Mtawanya, Bungu, Jaribu, wanalima sana mazao ya matunda kama mananasi, pasheni, embe, papai, machungwa, machenza, ndimu, limao na parachichi. Tatizo la kilimo hiki ni soko la uhakika, kwani mpaka sasa soko lipo moja tu, la Bakhresa, Azam. Soko hili halina tija kwa wakulima wa matunda kwani yupo peke yake, hata bei ya kununua mazao hayo hupanga yeye mwenyewe tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali yangu sikivu ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, ili kupata soko la mazao ya wakulima wa matunda ni kujenga viwanda vya kusindika matunda katika maeneo ambayo matunda yanalimwa kwa wingi, kama Jaribu, Kibiti, Mtawanya, Bungu na Mlanzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la minazi katika Jimbo langu linapotea kwa kiasi kikubwa kwani kumeibuka ugonjwa mbaya wa minazi ambapo hakuna anayejali. Hatujaona Extension Officers wanaojali kuhusu zao hili la biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Uvuvi ina umuhimu sana katika uzalishaji mali kwa vijana wetu ambao wanakumbwa na tatizo kubwa la ajira kwa vijana. Katika Jimbo langu la Kibiti, kuna maeneo ya Delta ambayo yamezunguka kando kando ya Bahari ya Hindi. Sekta hii ni muhimu sana kwa pato la Taifa letu la Tanzania kwani vipo vikundi vingi vya uvuvi katika maeneo hayo ambayo vinasimamiwa na BMU.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali yangu sikivu kuwapa vijana vifaa vya kisasa vya uvuvi kama vile boti za kisasa, nyavu ambavyo vinawezesha uvuvi bora na endelevu. Kuchimba mabwawa ya kufugia samaki badala ya kutegemea mabonde.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Kibiti mifugo ipo mingi na mpaka inaleta migogoro ya wakulima na wafugaji kama vile Muyuyu, Makima, Maporoni. Napenda kushauri Serikali yangu sikivu kutenga maeneo ya kulima na ufugaji ili kutoa au kukomesha kabisa migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri katika Wizara yenye dhamana, hasa ndugu yangu Mheshimiwa Mwiguli Lameck Nchemba, sasa ana kazi ya kufanya kuhakikisha tunashirikiana naye kwa pamoja, sisi sote kwa kuboresha mazingira ya wafugaji kwa kuwajengea miundombinu kama:-
Kujenga machinjio ya kisasa;
Kujenga majosho;
Kujenga malambo;
Kuwapelekea Afisa Mifugo kuwa karibu nao;
Kujenga vituo vya minada;
Kuunda Kamati ya watu 10 kila Sekta tano za wakulima na wafugaji ili kutatua migogoro hiyo kabla hawajapelekana mbele ya sheria;
Wafugaji wawe tayari kulipa ushuru wa minada. Hii inawafanya wakulima waone umuhimu wa ufugaji katika maeneo yao; na
Kujenga viwanda vya bidhaa ambazo zinatokana na mifugo kama maziwa, ngozi na nyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ng‟ombe kila kitu mali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda kumuuliza swali ndugu yangu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba; kwa nini mazao yote ambayo yameundiwa Bodi za Mazao, mazao hayo hayafanyi vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao yenye Bodi ni matatizo. Korosho hoi, pamba hoi, chai hoi, pareto hoi, kahawa hoi, tumbaku hoi. Hii inaonesha kwamba hizi bodi hazimsaidii mkulima na badala yake zinamnyonya mkulima kwa asilimia kubwa sana na kumwachia maumivu makali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao ambayo hayana bodi ni ufuta ambao uko hai, mbaazi hai, kunde hai, njugumawe hai, mihogo hai, mahindi hai, m punga hai. Mazao haya yanafanya vizuri katika Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kauli Mbiu, Ukitaka Mali Utaipata Shambani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya tele na kuweza kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti, nawaahidi sitowaangusha, naomba ushirikiano kutoka kwao, Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Kwanza nampongeza Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako pamoja na Watendaji wake wote wa Wizara husika kwa kazi yao nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala ya masomo haiendani na changamoto ya maisha ya kila siku. Napenda kuishauri Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kufikiria kurudisha mitaala kama ilivyokuwa zamani ya sayansi kilimona sayansi kimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake ya elimu Bure. Katika Jimbo langu la Kibiti wazazi wameitikia kauli hii kwa kupeleka watoto wengi kuandikishwa katika shule zangu za msingi. Japokuwa zipo changamoto, naamini huu ni mwanzo tu yote yataisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali yangu sikivu inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kulipa madeni yote ya Walimu, kuwapandisha madaraja kwa wakati, kuwalipa madai yao ya likizo, kuwalipa posho ya mazingira magumu kama kwenye Jimbo la maeneo ya Kibiti, Delta, Mfisini, Mbwera, Kiongoroni, Maparoni na kadhalika
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimba za utotoni. Napenda kumshauri Waziri wangu mchapakazi wa Wizara hii kuangalia suala hili kwa umakini. Moja, aboreshe mazingira ya shule na yawe karibu na makazi ya wananchi.
Pili, mtoto akipata ujauzito baada ya kujifungua apewe kipaumbele cha kurejeshwa tena shuleni. Tatu, kuhakikisha tunajega mabweni ya kutosha katika shule zetu za sekondari zote za kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuyapongeza mashirika ambayo si ya Kiserikali jinsi yanavyochangia sekta hii ya elimu. Nalishukuru shirika la CAMFED jinsi linavyotusaidia kwenye suala hili la elimu katika Jimbo langu la Kibiti na wananchi wote tunawaunga mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia katika mada hii ya viwanda. Kwanza, niwashukuru sana wananchi wangu wa Kibiti kwa kunipa kura nyingi sana na nawaahidi sitowaangusha. Pili, napenda kuwashukuru na kuwapongeza akinamama wote kwani tunafahamu bila ya mama tusingekuwa hapa duniani, kwa hiyo, hakuna mtu kama mama. Napenda pia kuunga mkono hoja hii mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakwenda kujielekeza katika mada hii ya viwanda. Mada hii ya viwanda ni muhimu sana kwani inagusa sana maisha ya mwanadamu hususani vijana katika soko la ajira. Angalizo langu ningeanza kwa kusema kwamba Waziri mwenye dhamana aangalie ni maeneo gani ya kuanzisha viwanda kutokana na malighafi zinavyotoka sehemu husika. Mfano katika Jimbo langu la Rufiji, tunalima sana mananasi, mpunga, mihogo na korosho. Kwa hiyo, tuna kila sababu lazima tupate viwanda sambamba na mazao hayo. Atakapotuletea viwanda hivyo naamini wakulima wetu sasa watapata soko lenye tija sasa hivi soko la mazao ya matunda ni moja tu kwa Bakharesa, wananchi wetu wakipeleka mazao yao wanakaa foleni kubwa matokeo yake mazao yao yanaharibika na mkulima anapata short. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rufiji tuna Kiwanda cha Kusindika Samaki Nyamisati, lakini kiwanda hiki hakifanyi kazi. Naomba Waziri mwenye dhamana tukutane naye ili tuangalie changamoto ni nini ili kiwanda hicho kianze kufanya kazi. Unapozungumzia prawns lazima utaigusa Rufiji kwani prawns wengi wanapatikana Nyamisati na kiwanda hiki kipo sehemu yenye kina kirefu cha maji. Unapozungumzia kiwanda huna budi urekebishe na uboreshe maeneo ya kufanyia kazi ikiwemo kupeleka maji, umeme na barabara ili mwekezaji anapokuja apate urahisi wa kuwekeza katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kutoa ushauri kwa Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kwamba hivi viwanda vinavyoagiza mitambo kutoka nje iangalie ni jinsi gani ya kupunguza kodi. Kwani kodi mkiweka kubwa, hawa jamaa watakaokuja kuwekeza katika viwanda hivi wataona kama mzigo mkubwa ambapo wataona haina tija kuwekeza katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rufiji tuna Bonde la Mto Rufiji lakini naliona kwamba halina tija yoyote. Sasa hivi tuna uhaba wa sukari, lakini katika bonde hili tungelima miwa na kuweka viwanda vya sukari hata hii shida ya sukari hapa nchini naamini ingeepukika kabisa au kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia viwanda lazima uboreshe mazingira ili yawe rafiki kwa watu watakaokuja kuwekeza katika maeneo husika. Angalizo langu ni kwamba wawekezaji wa nje wanapokuja ni lazima wananchi wa maeneo au wazawa wa maeneo yale wafaidike. Tunachoogopa wasije wawekezaji kutoka nje wakafikia mjini wakachukuliwa na master plan wale wananchi wanaozunguka maeneo yale wakawa hawafaidiki na sekta hii ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia mikopo katika taasisi za kibenki, naomba wazawa wapewe elimu ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri wao wenyewe. Katika elimu hii ni vema tukaboresha vyuo yetu vya VETA na viwanda vyetu vidogo vidogo (SIDO) ili wananchi wapate jinsi ya kujifunza ili waweze kujiajiri wenyewe na kujitegemea katika sekta hii ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nipende kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji wake wa kutumbua majipu. Wadengereko wote wa Rufiji wanasema wako pamoja naye na wanamuunga mkono kwamba aendelee kutumbua majipu ya nchi hii kwa sababu wananchi sasa wanahitaji maendeleo hawataki maneno. Wameona utendaji wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwamba unaleta tija kwa nchi hii. Nasi tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu apate afya njema aendelee kutumbua majipu ili kila mmoja afuate taratibu zinazotakiwa katika utendaji wake wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia viwanda lazima unagusa maisha ya watu wa hali ya chini. Kwa hiyo, bajeti hii naiunga mkono mia kwa mia, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nami kuchangia kwa maandishi katika mada hii ya miundombinu kwani ni muhimu sana katika Jimbo langu la Kibiti.
Katika Jimbo langu la Kibiti kuna changamoto kubwa katika miundombinu, hasa maeneo ya Delta hakuna mawasiliano kabisa; Mfisini, Kiomboni, Sanenga, Salale, Mbwera, Mbuchi, Kingongo, Mberambe, Msala, Mchinga, Maparoni, Mbuchi, Pombwe, Kechuru; katika maeneo haya mazingira si rafiki kwa mawasiliano na barabara zao pamoja na magati ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa gati la Nyamisati, napenda kuishauri Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanza haraka sana ujenzi wa gati la Nyamisati, kwani gati hili ni muhimu sana, litahudumia Wilaya mbili za Mafia na Kibiti kwa kuhudumia wananchi wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Bungu – Nyamisati; barabara hii nayo ni muhimu sana kwani inatumiwa na wananchi wa Mafia na wa Kibiti, tena barabara hii ijengwe kwa lami. Kibiti – Ruaruke – Nyamisati; barabara hii nayo iboreshwe kwa kiwango cha changarawe kwani ina mchango mkubwa wa kukuza uchumi wa wakulima. Kufungua barabara mpya kutoka Kipoka – Maparoni – Msala, jamani hii ni barabara muhimu sana kufunguliwa kwani italeta mchango mkubwa sana wa uzalishaji mali katika uchumi wetu wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kibiti – Makima – Kisarawe – Chole. Hii nayo ni barabara muhimu ya Chole Kati kuja Dar es Salaam. Kinyanya – Magogo – Matatu – Msoro, nayo ni barabara ya muhimu sana kwa kuja katika Makao Makuu ya Kata ya Mtawanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la minara; nashauri Serikali yangu sikivu ipelekwe maeneo husika ili nayo iwafaidishe wananchi wa sehemu husika kwa kuboresha huduma za jamii kama kujenga shule, zahanati, kuchimba visima, barabara na kadhalika. Katika Jimbo langu la Kibiti kuna maeneo mengi ambayo hayana mawasiliano, kama maeneo ya delta na nchi kavu kama Mng‟aru, Kimbugi, Miwaga, Ngulakula, Rungungu, Mangwi, Nyamwimbe, Ruaruke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibiti – Mchukwi; barabara hii ni muhimu sana kwenda Hospitali ya Mission ya Mchukwi. Barabara hii iwekewe lami kwani hospitali hii inawahudumia watu wengi sana kutoka ndani na nje ya Wilaya yangu ya Kibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ni muhimu sana, upewe kipaumbele katika bajeti hii. Bandari hii ikiisha itachangia mchango mkubwa katika Pato letu la Taifa, kupunguza msongamano wa foleni katika Jiji la Dar es Salaam na vijana wetu kuajiriwa kupitia bandari hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapambano dhidi ya UKIMWI; kila mmoja anawajibika kuhakikisha anapambana na suala zima la UKIMWI. Wahakikishe kutoa elimu wakati wa ujenzi wa barabara ili watu wapime kwa hiari na watambulike kisha wapewe elimu ya ushauri nasaha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa salama salimini. Napenda kukushukuru wewe kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia katika mada hii ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza Waziri mwenye dhamana, ndugu yetu Mheshimiwa Muhongo na Naibu wake kwa kufanya kazi kubwa katika Wizara hii. Kweli nia yake ya kuzima kibatari katika nyumba zetu na kwa wananchi kwa ujumla inaonekana. (Makofi)
Pili, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kunipa umeme katika vijiji vyangu 18, kikiwemo Kibiti, Nyamisati, Mchukwi, Bungu, umeme unawaka. Kwa hiyo, sina budi kuipongeza Wizara hii kwa kazi nzuri inayoifanya kwa kuwatumikia wananchi wa Jimbo langu la Kibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vijiji kadhaa ambavyo havina umeme katika Jimbo langu la Kibiti lakini uwekaji wa miundombinu unaendelea. Cha ajabu ni kwamba kasi hiyo haiendani na matakwa ya wananchi. Vijiji hivyo ambavyo wakandarasi wako site ni kama Nyamatanga, Lungungu, Lwaluke, Kikale, Mtunda na Muyuyu. Naomba sasa Waziri mwenye dhamana afike na kuona kwa nini wakandarasi hawa wanashindwa kukamilisha miradi hii kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni fidia katika mradi wa umeme wa Kinyerezi, watu 400, kwamba cha ajabu kuna baadhi ikiwemo Dar es Salaam fidia hizo wamelipwa lakini wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti mpaka leo hawajalipwa. Ukiangalia tathmini imepita muda mrefu, je, sasa Waziri huyu mwenye dhamana akija kuwalipa wananchi fidia hii watalipwa kwa bei ile ile au kwa tathmini nyingine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti lipo tatizo katika maeneo ya Delta....umeme. Eneo hili la Delta lina kata tano, vijiji 16, vitongoji 27 mpaka leo hakuna hata kitongoji kimoja kilichopata umeme. Naomba Mheshimiwa Profesa Muhongo atumie jitihada zake zote kuhakikisha vitongoji hivi vinapata umeme hata wa nguvu za jua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi anayofanya na sisi Wandengereko wote tuna imani naye katika kuhakikisha kwamba ataleta maendeleo katika wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti na kwa nchi nzima kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme katika matumizi ya gesi majumbani. Haya matumizi ya gesi majumbani wananchi wapewe elimu fasaha ili kwamba sasa watumie gesi waachane na kukata miti, mkaa na kuni. Umeme ndiyo njia ambayo itachangia kutunza mazingira. Katika nishati hii ya gesi kwamba watolewe vikwazo ambavyo siyo vya lazima kwamba gesi ipatikane kwe bei nafuu na kila mmoja aweze kuitumia majumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kibiti viko vijiji 40 ambavyo bado havijapata umeme. Naomba katika Phase III iangalie vijiji hivyo ikiwemo Inyamatanga, Lwaluke, Matima, Lungungu na Itawatambwe nayo iangaliwe na tuhakikishiwe tunapata umeme katika Phase III. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawapongeza wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti, na mimi nawaahidi kwamba sitawaangusha, nitawapa ushirikiano katika kuangalia tunaleta maendeleo katika Jimbo langu la Kibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme viko vijiji ambavyo mradi huu unaendelea, lakini bado ujenzi wake hauendi kwa kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo lingine niliseme ambalo ni changamoto ya Shirika letu la umeme (TANESCO) katika Wilaya yetu ya Kibiti, ni kwamba yako matatizo mengi ikiwemo usafiri, posho za ziada na maslahi yao ya kazi na elimu za fidia. Tunafahamu kwamba miradi hii ya REA haina fidia na inakuwa vigumu wananchi wanapokosa elimu, wanapokwenda kukatiwa miti yao inaweza ikaleta migongano baina ya wananchi na mtendaji husika katika maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia kwa mia kwamba sasa wananchi wanahitaji maendeleo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kumpongeza Profesa Sospeter Mwijarubi Muhongo na Naibu wake Waziri Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Kalemani na Katibu Mkuu wa Wizara Profesa James Pallangyo Justin William Ntalikwa kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanawapatia Watanzania umeme kwa kuzima kibatari majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kushukuru katika Jimbo langu la Kibiti vipo baadhi ya vijiji tumeshapata umeme kwenye phase I ambapo ni 18 kati ya 40. Vijiji hivyo ni Kibiti, Nyamisati, Mchukwi, Mlanzi, Mahenge, Bungu, Songa na vinginevyo lakini umeme wake bado unasumbua wakati wote. Naomba Serikali yangu sikivu ya Chama Tawala kuliangalia suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji ambavyo umeme umefika lakini bado haujawaka. Vijiji hivyo ni Mwangia, Mngaru, Kimbuga, Miwaga, Ngulakula, Uponda Uchembe na Jaribu Mpakani. Vijiji hivi miundombinu ya umeme imekamilika lakini bado kuwashwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji ambavyo havifanyi vizuri katika suala zima la ukandarasi na miundombinu yake haiendi kwa kasi. Wakandarasi katika maeneo haya kazi zao zimesimama kwa muda mrefu. Naomba wananchi wa Jimbo la Kibiti tuelezwe tatizo ni nini. Vijiji hivyo ni Nyamatanga, Rungungu, Ruaruke Kikale, Mtunda na Muyuyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, fidia ya mradi wa umeme wa kilowati 400 toka Somanga - Dar es Salaam – Kinyerezi. Lipo tatizo la fidia katika mradi huu kwani cha ajabu yapo maeneo wameshalipwa lakini katika Jimbo langu la Kibiti bado kabisa. Naomba majibu kutoka kwa Waziri mwenye dhamana fidia hii tutalipwa lini na tutalipwa kwa kiwango kile au tutafanyiwa tena valuation mpya kwani umeshapita muda mrefu. Maeneo ambayo wameshafanyiwa malipo ni Dar es Salaam, Kipunguni Kivule.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme maeneo ya delta. Maeneo haya yote ya delta ambayo yana Kata tano za Salale, Msala, Kiongoroni, Maparoni na Mbuchi. Kata hizi zipo kwenye mazingira magumu pembezoni mwa Bahari ya Hindi ambapo vipo jumla ya vijiji 16 sawa na vitongoji 67.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Kibiti vijiji ambavyo havina umeme vipo 40. Naomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi katika phase III Jimbo langu la Kibiti tupewe umeme. Vijiji hivyo ni Kinyanya, Mkupuka, Nyamwimbe, Bumba Msoro, Pagae, Makima Motomoto, Mjawa, Zumbwini na Tomoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya gesi majumbani ni muhimu sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu gesi iondolewe vikwazo kama vipo kwani nishati hii ina mchango mkubwa katika kutunza mazingira kwani itapunguza matumizi ya mkaa, kuni, umeme na mafuta ya taa katika matumizi ya siku majumbani na wananchi wapewe elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya gesi na faida zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika letu la Umeme TANESCO Rufiji lina changamoto kubwa kama ifuatavyo:-
(i) Vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi;
(ii) Usafiri;
(iii) Posho za saa za ziada;
(iv) Posho za likizo;
(v) Ukarabati na majengo ya ofisi na nyumba; na
(vi) Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu miradi ya REA kwamba haina fidia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia Wizara hii ya Ardhi katika Jimbo langu la Kibiti. Kwanza napenda kuipongeza Wizara hii kwa ujumla pamoja na Waziri mwenye dhamana baba yangu Mheshimiwa William Lukuvi kwa anavyochapa kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ni Wizara mtambuka kwani ardhi ni muhimu sana katika shughuli za kila siku za mwanadamu. Hatuwezi kujenga viwanda bila ya kutenga ardhi ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kibiti lina ardhi ya kutosha lakini naiomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kutoa msisitizo kwa watendaji wetu wa Halmashauri kuwajibika katika shughuli zao za kujenga Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Baraza la Ardhi na Mahakama ya Ardhi; Baraza la Ardhi katika maeneo yetu tunapoishi ni muhimu sana, kama Baraza la Ardhi la Kata. Napenda kuishauri Serikali yangu sikivu itoe semina elekezi ya Baraza hili la Ardhi ili liipe uwezo wa ufahamu katika shughuli zake za kutatua migogoro ya ardhi katika kata zetu. Mahakama ya Ardhi nayo iwe inatoa lakini kwa muda mfupi; hii itachangia kupunguza dhana potovu ya rushwa kwa wananchi wenye migogoro katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa hati za kimila katika Jimbo langu la Kibiti bado ni tatizo, naomba Wizara yenye dhamana ambayo inaongozwa na Waziri wetu mchapakazi na mwenye weledi mkubwa, Mheshimiwa Willium Lukuvi ahakikishe Jimbo langu la Kibiti sasa wananchi wanapata hati za kimila kama kauli yake Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi katika Jimbo la Kibiti ipo migogoro kadhaa ambayo inahitajika kupatiwa utatuzi kama kata ya Mlanzi na Mahenge. Maeneo mengine ni ya Kibiti na Bumba Msoro; mgogoro wa mpaka kati ya kijiji cha Msafiri, Nyambili, Uponda na maeneo mengine. Katika Jimbo langu pia ipo migogoro ya wakulima na wafugaji. Hii inatokana na kutopanga matumizi bora ya ardhi kama kutenga maeneo ya kilimo, ufugaji, benki ya ardhi pamoja na maeneo ya kujenga viwanda. Migogoro hiyo ipo kata ya Matunda na maeneo mengine. Hapa jimboni kwangu kuna watu wasiojulikana wamechukua maeneo ya Nyatanga, Nyale, Ngambuni, Kisima, Nananyumbani, wananyanyasa wananchi wangu wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumuuliza swali Waziri mwenye dhamana, kwa nini hadi leo Songa hawajapata kijiji ikiwa vigezo vyote vya kupata kijiji cha Songa umekamilika lakini hadi leo Serikali bado haijakitangaza kijiji hicho cha Songa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto katika Idara ya Ardhi Jimboni kwangu Kibiti ni kutokuwa na vitendea kazi vya kisasa ili kuhakikisha wanapima kwa haraka, usafiri wa uhakika, Afisa Ardhi Mteule, fedha ndogo inayotokana na kodi ni vizuri ingebaki asilimia 50 badala ya asilimia 30 ya sasa. Kuongeza watumishi, kwa sasa wapo wachache, kuwalipa posho za kujikimu kwa wakati, kuwalipa posho za masaa ya ziada na hili inatokana na upungufu wa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji tunawapenda na tunawahitaji katika Jimbo letu la Kibiti; lakini angalizo langu ni kwamba hawa wawekezaji wasipewe ardhi kwa kulipia fidia badala yake wafanye kama ifuatavyo:-
(i) Wanakijiji watoe ardhi na wawekezaji watoe mtaji ili pande zote mbili wawe wamiliki wa kiwanda hicho husika, hii itasaidia kutatua migogoro na dhana potovu ya mwekezaji kuwa kama mnyonyaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na taasisi za fedha, napenda kusema Waziri mwenye dhamana atoe tamko maalum juu ya kuzitaka taasisi za fedha zote hapa nchini kutambua hati miliki za kimila nazo ni dhamana ya wananchi kupata mikopo katika taasisi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja mia kwa mia, Hapa Kazi Tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi leo nichangie hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote itabidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ili nichangie hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja; sababu, hotuba hii imejali maslahi ya wananchi wa vipato vya aina zote. Pili, niweze kumshukuru kwa kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Baraza lake kwa ujumla. Hii kauli ya Hapa Kazi kwa
kweli inaonekana kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Kibiti takriban Mawaziri watano wamefika ndani ya mwezi mmoja. Hata wananchi wa Rufiji kwa ujumla wamesema kwa kweli Serikali hii ya Awamu ya Tano inakwenda na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa katika afya. Nashukuru kwamba Idara ya Afya imetugawia kila kituo shilingi milioni 10 ambazo tumekarabati, kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika Idara ya Afya. Kuna baadhi ya zahanati ina watumishi mmoja-mmoja ikiwemo Kiomboni, Kechuru, Msalale…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, hebu badilisha hiyo microphone nenda sehemu nyingine.
MWENYEKITI: Aah ok, basi endelea.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndivyo nilivyo. Nikupe taarifa tu nina kigugumizi, nina kilema ambacho amenipa Mwenyezi Mungu, hata hii mic ukiibadilisha hutaweza kunibadilisha, haya ni maumbile aliyonipa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongelee suala la kilimo. Wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti bado wanalima kilimo cha Nungu abile, yaani ina maana Mungu yupo, watu wanalima ili kusubiria mvua wakati sasa hali ya hewa imebadilika. Ninachoomba Waziri anayehusika atuletee miundombinu ya umwagiliaji Kibiti ili wananchi walime kilimo chenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unavyozungumzia kilimo chenye tija kwa sisi wananchi wa Kibiti lazima tuzungumzie masuala ya korosho. Korosho bado Chama Kikuu cha Msingi kina matatizo, kwa sababu wananchi wanalima korosho zao, wanapopeleka katika hayo masoko bado makato yao yanachukua muda mrefu katika kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala zima la elimu. Tunafahamu Serikali yetu imeweka mfumo wa elimu bure, lakini kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto, katika Wilaya yangu ya Kibiti kuna upungufu mkubwa hasa wa watumishi, majengo na nyumba za
walimu. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu huu ni upungufu iliangalie Kibiti kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Benki ya Maendeleo ya Akinamama; sote tunafahamu bila ya akinamama hatuwezi tukasonga mbele. Hawa akinamama lazima tuwaboreshee mazingira yao kwa sababu muda mwingi wa nyumbani akinamama ndio wanalea familia. Tuna kila sababu ya kuangalia kwa jicho la huruma ili katika vile vikundi vyao wapewe mikopo ya bei nafuu. Jambo la kushangaza ni kwamba benki hizi zimekaa mijini tu, je, kule vijijini watafika lini ili na kule akinamama wetu wa vijijini nao wakafaidike? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie na suala la miundombinu kwa sababu, barabara yetu ya Bungulu kwenda Nyamisati haipitiki. Tunaomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aiangalie barabara hii kwa sababu barabara hii inafaidisha wananchi wa Kibiti na wananchi
wa Mafia kwa ujumla. Mbali ya barabara upo ujenzi wa Gati – Nyamisati, ujenzi huo wa Gati Nyamisati likirekebishwa naamini kwamba wananchi wa Mafia na wananchi wa Kibiti watafaidika na gati hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kwamba, Wilaya ya Kibiti ina Kata 16, lakini ziko baadhi ya Kata ziko Delta. Kwa hiyo, Delta iangaliwe kwa jicho la huruma kwa sababu miundombinu ya Delta siyo rafiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga hoja asilimia mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza hotuba ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa imegusa maisha ya wananchi wa aina zote katika nchi hii yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Jenista Mhagama katika Wizara yake anafanya kazi kubwa na yenye tija kwa Taifa letu kwa ujumla na Naibu wake Mheshimiwa Antony Mavunde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu la Kibiti zipo changamoto nyingi katika suala zima la afya. Sina budi kushukru Serikali yangu inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kutuletea mradi wa BRF kwa kupata kila zahanati shilingi 10,000,000 kwa ajili ya kuboresha zahanati zetu na kununua baadhi ya vifaa vya tiba kama vitanda na vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kila penye mafanikio hapakosi changamoto, katika Jimbo la Kibiti changamoto kubwa katika idara ya afya ni moja ambayo ni upungufu wa watumishi, ikama ni 630 waliopo 152 upungufu ni 478; naomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi
watuangalie kwa jicho la huruma pamoja na upungufu wa watumishi lakini zipo changamoto zingine kama umaliziaji wa majengo, maboma yaliyoachwa kwa muda mrefu. Kituo cha Afya Kibiti kimezidiwa katika utoaji wake wa huduma, naomba iangaliwe kwa jicho la huruma kwani ndio inayobeba Kibiti kwa ujumla katika idara ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu ka Kibiti zipo changamoto nyingi katika sekta ya kilimo kama maafisa ugani wapo wachache, kwa hiyo husababisha wananchi wangu wa Jimbo la Kibiti kushindwa kulima kilimo chenye tija. Hata hao wachache waliopo nao wana
changamoto ya uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi kama magari na pikipiki, upatikanaji wa pembejeo kwa wakati nalo ni tatizo kubwa linalowakabili katika sekta hii ya kilimo katika jimbo langu la Kibiti, kwani pembejeo haziji kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi hizi pembejeo ambazo tunaletewa kwa ruzuku naomba mfumo huu ubadilishwe kwa kuondolewa kodi ambazo si lazima ili pembejeo hizi ziwe kama vocha na kwa bei nafuu. Kuhusu mashamba darasa njia hii ni nzuri sana kwa wakulima wangu wa jimbo la Kibiti kuwapa elimu ili waweze kulima kilimo chenye tija; aidha, stakabadhi ghalani ni mfumo ambao nao katika uuzaji wa mazoa ni mzuri lakini unachangamoto kubwa kama chama kikuu cha CORECO – Pwani kina matatizo makubwa na moja ni kufanya minada kiujanja, pili kuchelewesha malipo ya minada na vilevile vyanzo vya msingi navyo ni tatizo tuna kila sababu ya kupitia upya mfumo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, sina budi kuishukuru Serikali yangu kwa kuanzisha elimu bure. Lakini kila penye mafanikio hapakosi changamoto, moja upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa, vyumba vya walimu na baadhi ya maeneo watoto hutembea umbali mrefu
kwenda kwenye shule. Katika jimbo langu la Kibiti kuna maeneo ambayo yapo kwenye delta, walimu wanafanyakazi kwa hali ngumu kabisa. Naomba wafanyakazi hawa wa maeneo haya ya delta wapewe hata posho ya kujikimu ya mazingira magumu.
Mwisho namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu mama yetu Joyce Ndalichako kwa kufanya ziara katika jimbo langu la Kibiti hasa maeneo ya delta, maeneo ya Nyamisati, Salale, Mfisini na tunashukuru sana kwa kutuletea pesa za ujenzi wa mabweni shule ya sekondari Nyamisati shilingi 261,000,000 na Mtanga delta shilingi 256,084,461.25 tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika sekta hii ya miundombinu kama barabara ya Bungu - Nyamisati tunaomba barabara ijengwe kwa kiwango cha lami kwani kipindi cha mvua huwa inapitika kwa taabu sana ukizingatika barabara hii inatumika kwa majimbo
mawili, wananchi wa Kibiti na Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ujenzi wa gati la Nyamasati nalo ni muhimu sana kwa wananchi waishio maeneo ya delta. Kwa ujumla barabara ya kutoka Muhoro – Mbwera barabara hii nayo ni muhimu sana kwa wananchi waishio maeneo ya Mbuchi, Mbwera, Kipoka Maparoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwa maandishi katika hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakapoongelea maendeleo ya nchi hii huna budi kutilia mkazo masuala ya miundombinu, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, hii inaonesha jinsi gani Mheshimiwa Rais wetu alivyo mzalendo katika ufanyaji kazi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, sina budi kuwapongeza Mawaziri wenye dhamana, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, Mbunge na Naibu wake Mheshimiwa Injinia Edwin Amandus Ngonyani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kibiti zipo changamoto nyingi hasa barabara ya Bungu – Nyamisati. Barabara hii ina jumla ya kilometa 42. Naomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kuiangalia kwa jicho la huruma barabara hii. Tunaiomba Serikali yangu barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami kwani kufanya hivyo inaturahisishia kwa wananchi wa maeneo ya Delta kama Nyamisati, Salale, Kiomboni, Mchinga, Mfisini na ndugu zetu majirani zetu wa Wilaya ya Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Gati la Nyamisati; naiomba Serikali yangu sikivu suala hili lipewe kipaumbele kwani gati hili lina umuhimu sana kwa wananchi wa maeneo ya Delta na Mafia kwa ujumla. Katika Jimbo langu la Kibiti lina jumla ya Kata 16, kati ya hizo zipo tano ambazo zipo katika maeneo ya Delta, kati ya hizo ni Maparoni, Mbuchi, Salale, Msala, Kiongoroni. Katika Kata za Maparoni, Mbuchi, Salale, Msala, Kiongoroni katika Kata ya Maparoni, Mbuchi, Kiongoroni kuna barabara ya kutoka Ikwiriri – Kibiti, naomba njia hii ipewe kipaumbele kwani inatuunganisha Wilaya mbili, Kibiti na Rufiji na barabara hii ambayo inapita vijiji vingi sana ambavyo ni Mchukwi, Rungungu, Nyamatanga, Ruaruke, Kikale, Mtunda, Muyuyu, Umwe, ambapo barabara hii ina jumla ya kilometa 48. Ili kurekebisha barabara hii tuna kila wajibu wa kujenga Daraja la Ruhoi kwa box karavati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ya baadhi ya vijiji vyangu hakuna mawasiliano kama Makima, Mchukwi, Nyambunda, Ngulakula, Mngaru, Nyakinyo na maeneo mengine, tunaomba tupatiwe mawasiliano ili tuboreshe kupeana taarifa kwa njia nyepesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usiposhukuru kwa kidogo hata ukipata kikubwa huwezi kushukuru. Tunashukuru Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia Wilaya mpya ya Kibiti, lakini tuna ombi la barabara ya lami kutoka barabara kuu hadi tunapojenga Makao Makuu ya Wilaya na kwenda kwenye kituo chetu cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ruaruke kwenda Nyamisati. Barabara hii ina madaraja mawili ambayo ni Mkelele, Mkumbwa na Mkelele Mdogo ambayo yamesombwa na maji kwa hiyo hadi sasa barabara haipitiki kwenda Nyamisati – Ruaruke ambayo ni muhimu sana inatoka Muhoro hadi Mbwera. Barabara hii ina jumla ya kilometa 41. Awali ya yote sina budi kuishukuru Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutupatia wafadhili wa kujenga Daraja la Mto Mbuchi na Daraja dogo la Kipoka lakini yapo maeneo ya Mkelele mchakato wa kupata mzabuni, naomba ufanyike haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishakamilisha madaraja haya mawili tunawaomba tena wafadhili hawa wa DFIB, tunaomba barabara yetu ya kutoka Muhoro hadi Mbwera watujengee kwa kiwango cha tuta kubwa ili kulingana na hali halisi ya mazingira ya maeneo hayo, yanahitaji makalavati kila baada ya mita 200 kwani maeneo haya ni ya sehemu ya maji njia yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka njia panda ya Kingwera kuja Mchukwi hospitali ambayo ina urefu wa kilometa tano, naiomba Serikali yangu sikivu watuwekee lami kwa barabara hii, ni muhimu sana kwani inapitiwa na wagonjwa wengi ambao wanakwenda kupata matibabu katika hospitali hii ya Mchukwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano, maeneo ya Delta; katika Jimbo langu la Kibiti naomba maeneo ya Delta watuangalie kwa jicho la huruma kwani katika mazingira haya hatuna mawasiliano ya simu. Tunaomba tupatiwe mawasiliano ya simu kwani mtu akipata matatizo hakuna njia mbadala ya kupata msaada mwingine bila ya njia ya mawasiliano. Barabara ya maeneo ya Delta naomba Serikali yangu itujengee magati ya gharama nafuu na kujaza matuta katika barabara zetu za maeneo hayo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia Wizara hii ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi anayoifanya kwa Taifa hili. Pili, nampongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kibiti hakuna budi kuishukuru Serikali yetu sikivu kupitia Wizara yake ya Afya kwa kutupatia gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) aina ya Toyota Land Curiser kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kibiti. Hii itatusaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na pili, kupata vitanda 20 vya kulazia wagonjwa na vitanda vitano vya kujifungulia na magodoro pamoja na shuka zake. Sisi Wanakibiti kwa ujumla tunamwahidi tutavitunza vifaa hivi vyote pamoja na gari la wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila penye mafanikio hapakosi changamoto. Changamoto kubwa ni Ikama ya Watumishi katika Wilaya yangu ya Kibiti. Pia tuna upungufu mkubwa wa watumishi. Vile vile posho zao za masaa ya ziada ya kufanya kazi, madai ya fedha za likizo na motisha kwa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kibiti hadi sasa haina Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, inafanya Kituo cha Afya Kibiti kupokea wateja wengi kuliko uwezo wake. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara yako itupandishie kituo hiki kiwe Hospitali ya Wilaya. Katika kituo hiki hatuna Mochwari ya kuhifadhia maiti. Pia hakuna ukarabati wa kituo hiki kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kibiti kuna Kata tano, zipo maeneo ya Delta. Naomba Mheshimiwa Waziri atuangalie kwa jicho la huruma sana, kwani maeneo haya mtu akipata matatizo hakuna msaada wowote. Naomba tupatiwe ujenzi wa theatre ya upasuaji katika Kituo cha Afya Mbwera na kutupatia watumishi wa kutosha Ikama 149; waliopo ni tisa na pungufu ni 140. Naomba tusaidiwe. Kata hizo ni Maporini, Mbuchi, Msala, Kiongoroni na Salale.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie. Kwanza awali ya yote nishukuru vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hii kwa sababu sasa Kibiti tunalala usingizi. Hii ni kwa sababu Kibiti ilifikia muda hata mtu anayegonga mlango unamjua kipindi cha usiku unashindwa kwenda kufungua mlango, lakini nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimefanya kazi ipasavyo Kibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuiomba Serikali yangu Tukufu kwamba iangalie sasa jinsi gani ya kuboresha maslahi ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Hii ni kwa sababu hawana nyumba za kuishi, vitendea kazi vyao magari machache kwa hiyo, naomba kila jitihada wapatiwe vyombo vyao ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kwa kuunga mkono hoja kwa sababu hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa kweli imegusa maisha ya mtu wa hali ya chini kwa sababu ukiangalia katika sekta zote amezigusia kwa hiyo tuna kila sababu ya kumpongeza jinsi gani anavyofanya kazi na hii ndio kiu ya wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na afya, katika Wilaya ya Kibiti tunashukuru tumepata fedha ya kukarabati kituo kimoja cha afya Mbwela, lakini kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto bali tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta hii ya afya lakini tuna baadhi ya maboma wananchi walijitolea lakini bado hayajakamilika. Kwa hiyo, naomba mtuangalie kwa jicho la huruma wananchi wa Kibiti mtukamilishie maboma yetu ili yaweze kutoa huduma kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa wa madawa katika vituo vyetu vya afya kwa sababu ule Mfuko wa CHF unachangia, lakini moja ya sera ya afya kama mama mjamzito, mtoto chini ya umri wa miaka mitano na mzee zaidi ya miaka sitini matibabu bure. Anapokwenda kwenye kituo kile cha afya inabidi apewe dawa kwa yule mwananchi ambaye anachangia. Kwa hiyo, tuombe Serikali nayo iongeze fungu katika kupeleka dawa katika Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo ndugu zetu na jamaa zetu ambao wanaishi na VVU. Tunafahamu kwamba unapoanza kutumia dawa za VVU lazima upate lishe bora, lakini familia nyingi ambazo hazina uwezo wa kupata lishe hii bora. Kwa hiyo, ningeomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma watu hawa wenye makundi maalum, wapewe hata ruzuku ili waweze kupata lishe bora na wanapopata lishe bora wakati wa kutumia dawa hata ule uambukizi unapungua. Kwa hiyo, tusipofanya hivyo maana yake itakuwa maambukizi yanaendelea lakini tukiwapa lishe bora hata yale maambukizi yataweza kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Kibiti pato letu kubwa tunategemea kilimo na tuna kilimo cha aina mbili; tuna kilimo cha biashara na tuna kilimo cha mazao ya chakula. Mazao ya biashara tunategemea zao la korosho, sisi kule kwetu Kibiti korosho ndio dhahabu, ndio makinikia lakini zao hili la korosho linafanya vizuri lakini zipo baadhi ya changamoto ningeomba Wizara husika kwamba sasa watu wanasema kesi ya shamba inaishia shambani, tunaomba aje kule Kibiti yapo makandokando ili tumweleze makandokando hayo ili tuweze kuyamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tushukuru kwamba sasa hivi tumepata miche ya korosho bure na kweli wananchi wa Kibiti tumepanda mikorosho mingi ambayo itafanya Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na kipenzi chetu Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo zao la ufuta, ningeomba Waziri mwenye dhamana kwamba sasa aangalie jinsi gani zao hili nalo liuzwe kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu tumeona kwenye zao la korosho, stakabadhi ghalani kwamba mkulima anapata fedha nyingi zenye tija. Kwa hiyo, ningeomba basi na zao hili la ufuta nalo liuzwe kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mwananchi mkulima anaweza akafaidika na zao lake hilo la ufuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa wa Maafisa Ugani katika Wilaya yetu mpya ya Kibiti. Mbali na upungufu wa watumishi hao lakini tuna changamoto ya vifaa vya kutendea kazi vikiwemo pikipiki hata Ofisi zao hakuna ambapo sasa yule Afisa Ugani anashindwa kutimiza wajibu wake kwa kukosa vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu elimu, nashukuru Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwamba elimu bure, lakini kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Changamoto kubwa ambayo tuko nayo sisi wananchi wa Kibiti moja tuna upungufu wa Walimu, nyumba za Walimu, madawati na madarasa. Kwa hiyo, ningeomba sasa leo Serikali ituangalie kwa jicho la huruma sisi wananchi wa Kibiti basi ni kale kasungura kidogo na sio Kibiti mtupatie ili tuweze kufikisha lengo la wananchi wetu kupata elimu bure katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu, nafahamu kwamba tuna barabara yetu kubwa ambayo inatoka Bungu kwenda Nyamisati. Barabara hii inatumika na wananchi wa Wilaya mbili na ndugu/jirani yangu hapa Mheshimiwa Dau, Mbunge wa Mafia. Barabara hii kwa kweli ningeomba tuiangalie kwa jicho la huruma kwa sababu kipindi inaponyesha mvua inashindikana kupitika. Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, ningeomba sasa basi mtufikirie ili tuweze kupata barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami ili wananchi wa Mafia na Kibiti waweze kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ujenzi wa gati Nyamisati, nachelea kusema kwamba tatizo nini, kwa sababu tunaambiwa mkandarasi tayari ameshapatikana lakini mpaka leo ujenzi wa gati unashindwa kuendelezwa pale Nyamisati, wakati gati hii ya Nyamisati ikijengwa wananchi wa Mafia jirani zangu watafaidika, lakini na mie vilevile ambaye naishi katika Wilaya ya Kibiti (Nyamisati) nitafaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia gati lazima tupeleke kivuko cha kisasa kutoka Nyamisati kwenda Mafia kwamba usafiri unaotumika kwa kweli siku Mwenyezi Mungu anakileta mtihani wake nachelea kusema sijui kitatokea nini kwa sababu hali ya vivuko vyetu ambavyo wanavitumia sio salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo tuna matatizo ya maji katika Wilaya yetu ya Kibiti kwamba upatikanaji wa maji ni kama asilimia 38 tu na vijiji vingi havina maji lakini hata ile miradi ambayo tayari imekamilika bado inasua sua katika kutoa huduma yake kwa sababu tunafahamu maji sio biashara, maji ni huduma. Kwa hiyo niiombe Serikali itenge ruzuku kidogo ipeleke katika miradi ya maji ili iweze kukarabatiwa, ilipe gharama za bili za umeme na kuweza kulipa gharama za vibarua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo iko baadhi yake ni miradi mikongwe, ipo muda mrefu ambayo inatakiwa ifanyiwe ukarabati ili iweze kutoa huduma. Miradi hiyo ni kama wa Jaribu, Bungu, Nyamisati ambayo miradi hiyo yote ingefanyiwa ukarabati na miradi ya Lualuke, Mkenda na Muyuyu ingeweza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Waziri wa Nishati namshukuru sana sasa hivi Kibiti suala lile la umeme kukatikakatika limekuwa historia maana Kibiti tulikuwa umeme kama indicator ya gari, unazima unawaka lakini sasa hivi Kibiti tuna umeme wa uhakika ambao tumeunganishwa na Gridi ya Taifa, kwa hiyo sisi kama wananchi wa Kibiti tuna kila sababu sasa ya kutumikia umeme huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ombi kwa Waziri mwenye dhamana kwamba sasa Kibiti tunaomba tupate na Ofisi ya TANESCO, kwa sababu kutoka Kibiti kwenda Ikwiriri kuna takribani kilometa 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa leo salama salmini nachangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na barabara ya Bungu – Nyamisati. Waziri barabara hii ni muhimu sana na ukiangalia ni ahadi takribani ya Marais awamu mbili zilizopita walisema kwamba barabara hii tutajengewa kwa kiwango cha lami. Barabara hii ikijengwa itafaidisha Wilaya mbili, Wilaya ya Kibiti na Mafia. Mimi kila siku napokwenda kwenye mikutano yangu ya hadhara nashindwa kutoa jibu kuhusu barabara hii ya Nyamisati kwamba Serikali ina mpango gani kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna barabara ya kutoka Kibiti kwenda Mloka; barabara hii nayo ni muhimu sana ukizingatia sasa hivi kuna mkakati wa kufua umeme wa maji kule Mloka. Ningeomba sasa Serikali basi iangalie kwa jicho la huruma barabara hii ya Bungu - Nyamisati na Kibiti - Mloka na ukiangalia hivi karibuni Wilaya ya Kibiti tumekumbwa na janga la watu wasiojulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ziko barabara zetu za mitaa ambazo ni barabara za Kibiti, Bungu na Jaribu, TARURA haina kipato kikubwa cha kuweza kujenga barabara hizi kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ujenzi wa Gati Nyamisati ambapo tunaambiwa mkandarasi yuko site lakini leo asubuhi nimeongea na wananchi wangu wa Nyamisati bado kazi haijaanza ya ujenzi wa Gati Nyamisati. Tukijenga Gati Nyamisati watafaidika wananchi wa Kibiti, lakini hata wananchi wa Mafia watafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa la wananchi wanaokwenda Mafia kutoka Nyamisati hawana usafiri wa uhakika. Tunaiomba Serikali waangalie jinsi gani ya kutununulia meli ili tupeleke kule Nyamisati itoke Nyamisati na kwenda Mafia. Usafiri ambao unatumika sasa hivi ni usafiri ambao siyo salama, siku yoyote Mwenyezi Mungu akileta mtihani wake linaweza likatokea la kutokea. Kwa hiyo, tunaomba Kibiti na Mafia muiangalie kwa jicho la huruma, sababu tunajua ndiyo kasungura kenyewe ni kadogo lakini hiki hiki tugawane na siye wananchi wa Kibiti tufaidike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda katika mawasiliano, Kibiti kwenye baadhi ya maeneo yetu hatuna mawasiliano kwa maana ya minara ya simu. Iko minara miwili ambayo imejengwa maeneo ya Delta, kule Mbwera lakini mpaka leo haijafunguliwa. Uko mnara umejengwa Mbuchi lakini mpaka leo bado haujafunguliwa lakini viko karibu vijiji 20 hatuna mawasiliano ndiyo maana hata kule Delta tukivua samaki wetu tunashindwa kupiga simu sokoni kujua leo soko bei yake ikoje. Kama kungekuwa na mawasiliano tungepiga simu tukajua sokoni leo prawns bei imekuwa juu na sisi tupeleke samaki wetu ili tupate faida yenye tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa ndugu zetu hawa wa SUMATRA. SUMATRA wanafanya kazi lakini ninachoomba watoe ushirikiano na wadau. Hivi leo Kibiti wamezuia Noah zisipakie abiria kwenda kwenye barabara kuu, lakini wametoa zuio lile hawakuwashirikisha wadau. Kumekuwa na manung’uniko mengi inaonekana Serikali hii ya Awamu ya Tano siyo ya wanyonge kwa sababu wamefanya maamuzi pasipo kuwashirikisha wadau. Wangewashirikisha wadau wangejua mbadala wake ni nini kusingekuwa na manung’uniko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Wizara hii ya Ujenzi kwamba barabara nyingi zinazokwenda mikoani ziimarishwe na washirikiane na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa sababu nguvukazi nyingi zinatembea barabarani kwa muda mrefu mchana. Kwa mfano, mtu anapanda basi saa 12.00 Dar es Salaam anakuja Dodoma anafika saa 12.00 jioni, muda ule ukiuangalia ni kwamba watu hawakuweza kuzalisha mchana kutwa walikuwa wanatembea tu barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika takwimu takribani wananchi 12,000 kwa siku wanatembea barabarani kwa muda mfupi. Ningeomba sasa waangalie utaratibu kama nchi jirani ya Kenya wananchi wengi wanasafiri usiku ili mchana waweze kufanya kazi na shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, hili liangaliwe kwamba jinsi gani wataboresha ulinzi na usafiri wananchi wasafiri usiku ili mchana waweze kuzalisha mali na kuiletea tija Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niipongeze sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Chama cha Mapinduzi. Ndugu zanguni kila zama ina wakati wake. Tulianza na Mzee wetu hapa Baba wa Taifa (ujamaa na kujitegemea), akaja Mzee Mwinyi (ruksa), kweli tukaona ruksa, akaja Mzee Mkapa (utandawazi) kweli tukaona utandawazi, akaja Mzee Jakaya (maisha bora kwa kila Mtanzania) lakini sasa tumekuja Hapa Kazi Tu. Sasa nashangaa kazi inafanyika bado watu wana maneno maneno. Jamani tubadilike, sasa hivi hakuna maisha ya ujanja ujanja, sasa hivi ni maisha ya Hapa Kazi Tu. Pia inasemwa asiyefanya kazi asile, hata kwenye vitabu vya dini ipo. Kwa hiyo, ndugu zangu kama mlikuwa ni watu wenye ujanja msubiri mwaka 2025 muendelee na ujanja wenu, lakini awamu hii ni awamu ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado nipo katika Jimbo langu la Kibiti tunashukuru tumepata pesa ya kujenga daraja katika Daraja la Mbuchi, lakini barabara ya kutoka Muhoro kwenda Mbwera naomba nayo hii muiangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni kwa kunisikiliza, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi leo nichangie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitaanza na Mradi wa Maji Kibiti, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba sasa hali ya ulinzi Kibiti imeanza kuimarika, Kibiti shwari, sasa shida yetu maji, wale watu waliokuwa wanatuua tumewamaliza sasa hivi shida yetu imekuwa maji, tatizo Kibiti ni maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mradi wa maji Kibiti. Huu mradi wa maji wa Kibiti umekamilika na unatoa huduma, lakini bado unasuasua kwa sababu huu mradi ni mkubwa na haupatiwi fedha ya aina yoyote ya ruzuku ili kuweza kuendesha mradi ule. Tuna gharama kubwa ya kulipa bili ya umeme, vibarua, hata na baadhi ya vioski, tunaomba sasa Wizara iangalie kwa jicho la huruma mradi huu wa maji Kibiti ingeweza kuwapatia fedha kidogo ili kuweza kuendesha mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iko miradi saba ambayo haifanyi kazi kutokana na miradi hii kuchakaa. Miradi hiyo ni kama Kijiji cha Luaruke, Jaribu Mpakani, Mtawanya, Muyuyu, Mkenda na Kibiti. Wizara iangalie jinsi gani ya kuweza kupeleka fedha za ukarabati wa miradi hii ili iweze kutoa huduma, miradi hii ipo kwa muda mrefu imekosa fedha ya kufanyia ukarabati kwa hiyo, inashindwa kutoa huduma iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kule Jimboni kwangu nimechoka kusuluhisha ndoa kwa sababu muda mwingi wanandoa wanakwenda kutafuta maji visimani na baba anashindwa kuwa na imani mkewe kweli amekwenda kisimani au amekwenda kwenye mchepuko. Kwa sababu maji yanatoka mbali na huko kisimani ukienda maji yenyewe yanakuwa ya kulindia, kwa hiyo, baba anakosa imani kwa hiyo, tumekuwa na migogoro mikubwa ya wanandoa kule Jimboni kwangu Kibiti. Ningeomba Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi gani ataangalia Kibiti kwa jicho la huruma utupatie maji katika vijiji vyetu vya Kibiti vilivyobakia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mwaka jana tulipata fedha, zile fedha tumeziona kwenye makaratasi tu, lakini uhalisia maji yenyewe Kibiti hakuna. Sasa hapa Waziri hebu angalia ilionekana kama kuna mgomo baridi baina ya Wizara na Halmashauri zetu kwamba fedha zinakaa Wizarani lakini mradi unatekelezwa Wilayani, kule Wilayani hampeleki fedha kwa ajili ya ufuatiliaji, ukiangalia ni kama kuna mgomo baridi, mnasema ninyi huko Wilayani mtangaze tender halafu muandae certificate mlete huku Wizarani, kule Wilayani kwenyewe kazi hazifanyiki kwa wakati, sasa hilo nalo mliangalie kwamba mgomo baridi huu upo wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana kwamba watu sasa wameamua kugoma kuwaangalia ninyi Wizara mtafanikiwa au hamtafanikiwa. Kwa hiyo, ningeomba ili muangalie kama mnaweza mkafanya hii miradi ya maji kwa kutumia force account basi fanyeni kwamba hizi fedha ingizeni kwenye kijiji husika wao wenyewe wasimamie maana ndiyo wenye uchungu na ndiyo wenye shida ya maji, tunaweza tukafanikiwa kwa jitihada zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unavyoizungumzia Kibiti lazima uzungumzie maeneo ya Delta kwamba Kibiti zipi kata tano ambazo ni Delta ambayo ina vijiji 17, vitongoji 42, huko kote hatuna maji safi na salama. Unapokosa maji safi na salama hata shughuli za uzalishaji zinashindwa kufanyika kwa wakati. Maeneo hayo kama ya Nyamisati, Kiomboni, Saninga na Simbaulanga, kote huku hatuna maji ya uhakika, ningeomba Wizara angalieni jinsi gani ya kutufikishia maji katika maeneo hayo ya Delta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hivyo hatuna watumishi wa kutosha katika Idara hii ya Maji Wilayani kwetu Kibiti. Wilaya hii inaelekea tunaweza tukakosa ufanisi wa kazi wenye tija kutokana na upungufu wa watumishi na vitendeakazi. Mpaka leo Kibiti hatuna gari idara ya maji, unapokosa vietendeakazi utashindwa kufanya kazi yao kwa ufanisi. Kwa hiyo, ningeomba sana Wizara muiangalie kwa jicho la huruma Kibiti. Kwanza tumeathirika kwa yale mauaji tu Kibiti tumeathirika. Kwa hiyo, Wizara lazima uiangalie Kibiti kwa jicho la huruma mtusaidie Kibiti tumeathirika tatizo maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hiyo viko baadhi ya vijiji kama vile Makima, huu Mji unakua kwa kasi lakini pana tatizo la maji na ndiyo maana ukiangalia kila Mbunge humu akisimama analia na maji na ukiangalia mwaka 2015 katika ahadi zetu tulisema tunakabidhi maji kila kijiji, sasa leo usiku wa deni mfupi, Wandengereko kule tunasema hakuna shughuli ndogo kwamba mwaka 2020 tukifika tutaongea nini majukwaani? Maji yenyewe mpaka leo tumeishia kuyaona kwenye makaratasi tu? Ukiangalia kwenye makaratasi kweli maji unayaona, lakini ukienda uhalisia kule vijijini maji hakuna, sasa nashindwa kujua kwamba hawa wataalam wetu wanatufanyia mawele au wanatufanyia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tatizo la maji hili ni janga la kitaifa, muangalie jinsi gani ya kutusaidia katika Wilaya yangu mpya ya Kibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunisikiliza, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote sina budi kumshukuru Mungu kwa kunipa wasaa wa kuchangia kwa maandishi. Pia nampongeza sana Waziri, Mheshimiwa Mpina na Naibu Waziri Mheshimiwa Ulega.

Mheshimiwa Spika, Kibiti tuna ng’ombe wengi sana, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu wafanye mazingira ya wafugaji yawe rafiki kwa kuwajengea malambo, majosho, machinjio ya kisasa, vituo vya minada na vituo vya kukusanyia maziwa. Kwa kufanya hivyo itatatua mgogoro baina ya wakulima na wafugaji kwani wananchi watafaidi kwa Halmashauri kukusanya ushuru na kuongeza kipato chake cha ndani hivyo kukamilisha miradi yake ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Kibiti ni Jimbo ambalo lipo pembezoni mwa Bahari ya Hindi ambapo kata tano, vitongoji 42, vijiji 17 vipo maeneo ya Delta na hivyo shughuli kubwa ya kujipatia kipato ni shughuli za uvuvi. Kwa hiyo, naiomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Spika, uvuvi wa kamba mti, naomba yafuatayo yafanyike; kuongeza muda wa uvuvi (msimu); kubadilisha muda wa msimu, kwa sisi Wana Kibiti kamba mti wanapatikana kuanzia mwezi wa nane hadi wa 12; kupunguza wingi wa kodi; muda wa kuleta meli isiwe chini ya miaka 10, iwe zaidi ya miaka 20 na kuwasaidia wazawa kupata mikopo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ufugaji samaki, naomba Wizara ije na mpango mkakati wa kuanzisha uchimbaji wa mabwawa ya ufugaji wa samaki. Kwa kufanya hivyo, kutaongeza kipato, lishe bora, ajira kwa vijana na mapato ya Halmashauri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kwa maandishi. Kwanza naipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri ya kuhudumia wananchi wenye kipato cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Makamu wetu wa Rais mama yetu Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu kwa kazi nzuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi nzuri anayoifanya. Jimbo langu la Kibiti lina jumla ya Kata 16, Vijiji 58, Vitongoji 272, Shule za Msingi 74, Sekondari 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, katika Jimbo langu la Kibiti kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa kada hii ya afya kama 320 waliopo ni 120. Tunaomba Serikali yetu sikivu ituangalie kwa jicho la huruma. Pili kuna maeneo ya baadhi za kata zina wingi wa watu, lakini hadi leo hakuna vituo vya afya. Kata hizo ni kama Bungu, Ruaruke, Jaribu Mpakanina Mlanzi. Sambamba na hilo kituo cha afya Kibiti kinafanya kazi kubwa kuhudumia wananchi wa kata zaidi ya moja, naomba tufanyiwe ukarabati mkubwa ili kiweze kutoa huduma yenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Wilaya ya Kibiti haina gari la chanjo na wagonjwa, ina upungufu mkubwa wa magari, naomba Serikali yetu ituangalie kwa jicho la huruma. Wilayani Kibiti kuna baadhi za kata zipo Delta kwenye Bahari ya Hindi Visiwani kama Kata ya Mbuchi, Kiongoroni, Msala, Maparoni, Salale sawa na kata tano, vijiji 17, vitongoji 42, vipo Delta. Naomba watumishi wa maeneo haya Serikali iwaangalie kwa jicho la kipekee kutokana na kufanya kazi kwenye mazingira magumu, kama kupewa motisha na kutofanya kazi kwa muda mrefu kwenye kituo kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo hatuna kabisa mafriji ya kuwekea chanjo, boti kwa ajili ya kusafirisha pindi mama mjamzito atakapopata rufaa, upungufu mkubwa wa nyumba za watumishi. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kibiti, tunamshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutusaidia vituo vya afya viwili, ambavyo tunavifanyia ukarabati mkubwa na ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambavyo vyote ujenzi wake unaendelea kwa kasi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, moja ya Ilani ya Uchaguzi ya 2015 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni elimu bila malipo (elimu bure). Kwenye Jimbo langu la Kibiti mwitikio wake ni mkubwa sana. Lakini kila panapo mafanikio hapakosi kuwa na changamoto kama vile upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, nyumba za Walimu, vyoo bora vya kujisitiri Walimu na wanafunzi, upungufu wa Walimu na Walimu kukaa sehemu moja kwa muda mrefu mpaka Walimu sasa wanakuwa kama wanakijiji na baadhi ya Walimu kudai madai yao ya uhamisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo badhi ya shule kwenye visiwa jumla yake ni 17 ambazo Walimu wake mahitaji yao muhimu kama huduma za kibenki inawalazimu waje Kibiti. Naomba Serikali yangu sikivu ituangalie, hawa wapewe hata posho ya kujikimu kwa mazingira magumu kama motisha. Naomba kushukuru kwa kupata pesa za ujenzi wa mabweni, madarasa machache, pikipiki kwa ajili ya Maafisa Waratibu Elimu Kata na pesa za EPFR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji; hadi leo Kibiti hakuna hata mradi mmoja wa maji ambao unatekelezwa licha la kuchimba visima jumla 12 na kupata maji. Naomba Serikali yangu sikivu tuanze kujenga miundombinu ili zana ya kumtua mama ndoo kichwani iendani na kauli ya hapa kazi tu. Tuna miradi Kibiti takriban mitano inahitaji ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara; nashukuru Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kuunda chombo ambacho kinasimamia shughuli za kurekebisha miundombinu yetu katika majimbo yetu TARURA. Chombo hiki kinafanya kazi nzuri, kwa hiyo kuna kila sababu ya kuongezewa uwezo wa kifedha na watumishi ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Changamoto kubwa kwenye Jimbo langu la Kibiti, moja kuchonga barabara za mitaa za Kibiti, Bungu, Jaribu Mpakani, Nyamisati, pamoja na kujenga mifereji yake barabara ya Muhoro Mbuchi, iangaliwe kwa jicho la huruma kupata tuta la kifusi ili iweze kutoa huduma kipindi chote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kumalizia barabara ya kwenda Makao Makuu ya Wilaya, kilomita mbili zilizobakia kwani ujenzi wa Ofisi hii unakwenda kwa kasi kubwa. Wananchi wa maeneo ya DELTA wanapata shida kubwa kipindi wakiwa wanasafiri, tunaomba ujenzi wa magati katika bandari zetu ndogondogo kama Kiomboni, Mfisini, Mchinga, Salale, Simbaulanga, Ruma, Jafa, Mbwera, Kechuru, Maparoni, kujengewa barabara ya lami kutoka Bungu hadi Nyamisati kwani ujenzi wa gati karibu na unakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme; naomba Kibiti ituangalie kwa jicho la huruma katika maeneo ya DELTA visiwani, hadi leo hakuna hata kisiwa kimoja kimepata umeme wa aina yoyote kama Kata ya Salali, Msala, Mparoni, Kiongoroni, Mbuchi na Vitongoji vyake vyote. Hata kwenye maeneo haya ya nchi kavu kama kama Makima, Zimbwini, Mbumba, Msoro, Nyamwimbe, Manguri na maeneo mengine, tunashukuru kwa kupata Meneja wa TANESCO, kwa hiyo tunaomba sasa tujengewe Ofisi ya TANESCO kwenye Wilaya yetu ya Kibiti.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawawiliano.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nashukuru kwa ujenzi wa Gati la Nyamisati lililogharimu shilingi bilioni 14 na kazi inaenda vizuri sana. Nina kila sababu ya kujivunia Serikali yangu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi yake nzuri. Kweli huyu ni mzalendo namba moja kwa kujali wananchi wa hali ya chini, wanyonge, kwani gati hili likikamilika litatua changamoto za usafiri kwa wananchi wa Wilaya ya Mafia na Kibiti.

Mheshimiwa Spika, lakini kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Barabara yetu ya Bungu- Nyamisati, naomba ijengwe kwa kiwango cha lami kwani kipindi cha mvua huwa haipitiki kabisa kwa hiyo huwaletea usumbufu wananchi hasa wa Wilaya ya Mafia na Kibiti. Naiomba Serikali yangu sikivu ituangalie kwa jicho la huruma. Vilevile, barabara ya kutoka Muhoro - Mbwera nayo ifanyiwe ukarabati wa kiwango cha changarawe kwani ina manufaa makubwa ukizingatia sasa kuna ujenzi mkubwa wa Kituo cha Afya-Mbwera.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kibiti lina jumla ya kata 16, vijiji 58 na vitongoji 272. Kati ya hivyo, baadhi yake vipo kwenye visima/delta au pembezoni mwa Bahari ya Hindi ambavyo vina jumla ya kata 5, vijiji 17 na vitongoji 42. Moja ya changamoto ya maeneo hayo ni kutokufikika kwa urahisi, miundombinu yake ya barabara siyo mzuri kabisa kama maeneo ya Kata za Msala, Mbuchi, Kiongoroni, Salale na Maparoni. Naiomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ituangalie kwa jicho la pekee ili tupate magati madogo madogo sambamba na barabara zake ili kufikike kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jambo lenye manufaa kwa wananchi waishio vijijini kwa kuunda chombo ambacho kinakwenda kutatua kero za wananchi waishio vijijini cha TARURA. Naomba sasa chombo hiki kiongezewe nguvu za kifedha na ikama ya watumishi ili wakatekeleze wajibu wao bila ya kupata kikwazo cha aina yoyote sambamba na kuongezewa vitendea kazi kama magari na maboti ya kuendea site.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali yangu sikivu ituongezee fedha katika Jimbo langu la Kibiti ili tuweze kukamilisha baadhi ya barabara zetu za lami kama kutoka Kibiti kwenda Makao Makuu ya Wilaya. Kazi imeshaanza lakini inasuasua kutokana na uhaba wa fedha.

Mheshimiwa Spika, naomba barabara za mitaa zichongwe ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa mifereji. Mfano barabara ya Kibiti Mjini, Bungu Mjini, Jaribu Mpakani Mjini, Nyamisati Mjini, barabara hizi za mitaa miundombinu yake siyo rafiki kupitika wakati wote na ukizingatia miji hii inakua kwa kasi na ina wakazi wengi sana. Barabara ya kwenda Makima ambayo ina jumla ya kilomita 32 tayari kilomita 17 zimeshachongwa bado kilomita 15. Tunaomba chombo chetu cha TARURA kipewa fedha za kutosha ili kutatua changamoto hizo.

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo yenye mito ambayo kipindi cha mvua huwa hayapitiki kwa urahisi. Maeneo hayo ni kama Kibanga Hodi, Mkelele Mkumbwa, Kipoka, Nyafeda na Daraja la Mbwera Mjini. Naomba maeneo haya yaangaliwe kwa jicho la pekee.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Kibiti hadi leo kuna maeneo hayana mawasiliano ambapo ni jumla ya vijiji 24 kwenye maeneo ya nchi kavu. Vijiji hivyo ni Nyambunda, Nyambili, Majawa, Nyamatanga, Mchukwi A&B, Ngondae, Machepe, Nyamwimbe, Nyakinyo, Tomoni, Kingunguri, Mkenda, Kivinja A&B, Msindaji, Muyuyu, Ruaruke, Mbawa na Kilolatambwe. Kwenye visiwa (Delta – Rufiji) vijiji ambavyo havina mawasiliano ya simu ni Kiomboni, Mfisini, Salale, Mchinga, Ruma, Kiomboni, Pombwe, Jafa, Mbuchi, Mbwera Magharibi na Mbwera Mashariki, Maparoni, Kechulu, Msala, Tuwasalie na Kiasi. Upatikanaji wa mawasiliano utaongeza kipato kwa wanafamilia, kutoa taarifa kwa haraka pindi majanga yanapotokea kama ya wahalifu na mauaji ya watu wasiojulikana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Nishati kwa maandishi. Napenda kuwapongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wanazima vibatali nchi nzima na kuwasha umeme maeneo yote ya vijijini na mijini.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Kibiti tunashukuru sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo hadi leo vipo vijiji ambavyo havina umeme ambavyo nguzo na waya tayari kwa muda mrefu lakini cha kushangaza hadi leo umeme bado haujawaka kutokana na tatizo la transfomer. Vijiji hivyo ni Nyamatanga, Kikale na Ruaruke; naomba vijiji hivyo viangaliwe kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kibiti lina jumla ya Kata 16, vijiji 58 vitongoji 42 vipo katika visiwa vya Bahari ya Hindi kama Mfisini, Kivimbuni, Salale, Msala, Mbwera na maeneo mengine ambayo hadi leo havina umeme kabisa. Naomba Serikali yangu sikivu ituangalie kwa jicho la kipekee katika visiwa vyetu vya Kibiti.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hivyo, Wilaya ya Kibiti ina Mji Mdogo Kibiti ambapo ina jumla ya vitongoji 39 ambavyo baadhi ya vitongoji havina umeme kabisa; kama vile Makina, Zimwini, Nyambangala, Mroso, Bumba, Ugezi, Kikota, Penda Miwaga, Penda na Kimbuga.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.