Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Suzana Chogisasi Mgonukulima (28 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Manispaa ya Iringa ina mradi wa machinjio ya kisasa ambao Kitaifa ni wa pili kwa ubora na una uwezo wa kuchinja ng‟ombe 100 na mbuzi 100 kwa siku, mradi huu umebaki kidogo kumalizika kutoka Serikali Kuu. Manispaa ya Iringa iliomba shilingi milioni 200/= ili kumalizia, gharama ya mradi ni bilioni moja. Hadi leo hii fedha hiyo haijatolewa hata senti na iliomba bajeti ya mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo ukimalizika, ajira zitaongezeka kwa vile machinjio hiyo ina uwezo wa kuajiri watu 200. Naomba Waziri anijibu: Je, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 mradi huo umeutengea fedha kama Manispaa ilivyokuwa imeomba?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutoa shukrani zangu za dhati na napenda nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijaalia uzima na afya njema ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Iringa kwa kunipa kura za kuweza kuwa mwakilishi wao. Pamoja na hilo sitakisahau Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kupokea kura za wanawake wa Iringa kwa kuwa wamenituma kuwa mwakilishi wao na kunipa go ahead. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, hii Wizara ni nyeti sana kwa muono wangu mimi na nilivyoiona. Hata hivyo, baada ya kuipitia hotuba hii kuna ugonjwa huu wa UKIMWI, ugonjwa huu una magonjwa nyemelezi kuna typhoid, homa za hapa na pale. Magonjwa haya yanapelekea hawa wenzetu ambao wana ugonjwa huu wa UKIMWI kuondoka haraka kwa sababu ya kukosa kutibiwa. Naiomba Wizara hii iweke Bima ya Afya kwa hawa wagonjwa ili wakiwa na magonjwa haya nyemelezi waweze kutibiwa. Hakutakuwa na sababu ya kupewa dawa za ARV wakati wakiugua magonjwa nyemelezi wanakosa dawa za kutibiwa typhoid ili waweze kupona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara hii ije na mpango mkakati juu ya elimu ya ulaji wa vyakula. Magonjwa sugu yasiyoambukiza kama moyo, saratani, sukari na mengine ambayo tunayafahamu, haya yanasababishwa na vyakula ambavyo Watanzania sasa hivi tunakula. Ni ukweli usiopingika tunapenda Watanzania wawe wajasiriamali ili wainue vipato vya maisha, lakini sambamba na hilo hawa wajasiriamali wanaolima mboga mboga, wanaofuga kuku ambao ndani ya siku 14 unakuwa ni mlo sahihi, hawa ndio wanaopelekea haya magonjwa kulipuka. Mkulima wa nyanya, mkulima wa mboga aina ya chinese dawa anamwagilia leo asubuhi, jioni wanachuma mboga wanakwenda kuuza. Sumu zote zinaingia kwenye mwili wa binadamu na kupelekea haya magonjwa yasiyoambukiza kukua kwa kasi katika Taifa letu
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi yetu ya Tanzania ni kubwa sana. Ina square mita za mraba 947,303. Mheshimiwa Waziri mwenye Wizara hiyo nina uhakika hataweza kufikia maeneo yote. Ushauri wangu naomba atumie vipindi vya redio na tv kuelimisha Watanzania kuhusu mlo bora. Tutafika pale ambapo tumekusudia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna hili shirika la MSD. Wizara kama haitajikita kuhakikisha inakuwa na mpango mkakati wa kuweza kulipa madeni yanayopelekea shirika hili kuidai Serikali, tutapiga makelele usiku na mchana dawa hazifiki kwenye Halmashauri, haitawezekana kwa sababu MSD inaidai Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni mambo ya fedheha pale inaposadikika kuwa nchi zinazoisaidia Tanzania kwenye magonjwa, maambukizi kuleta dawa kama dawa hizi za UKIMWI, zinapofika bandarini na shirika letu kushindwa kwenda kukomboa kwa sababu wanaidai Serikali, wale waliotusaidia wanatuona sisi ni wa ajabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichangie kuwa kwa sababu tayari zile hela za Wabunge, zilishaelekezwa kwenye madawati, zingekuwa bado, hizi ndiyo zilitakiwa ziende zikalipe kwenye shirika la MSD ili Serikali iweze kulipa, waweze kupata dawa zao na kuweza kupeleka kwenye Halmashauri zetu kama tulivyoazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya afya kwa kuipandisha hadhi hospitali ya Mkoa wa Iringa kuwa Hospitali ya Rufaa. Hospitali hii ilikuwa imeelemewa sana na wagonjwa waliokuwa wamejazana kwenye vitanda wawili wawili. Kwa wagonjwa wa kawaida unaona ni nafuu, lakini kwa akinamama wajawazito, tunafahamu akinamama wajawazito shape zao huwa zinabadilika. Sasa shape zile kulaza kitanda tunachokijua cha wastani wa Wizara ya Afya watu wawili si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya Wizara kuipandisha hospitali ya Mkoa kuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Iringa wameweza kujenga hospitali ya Wilaya. Jengo la utawala limekamilika, wodi ya wagonjwa wa nje limekamilika, wodi ya wazazi imekamilika. Baada ya kukamilika wodi ya Wazazi Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mheshimiwa Peter Simon Msigwa amepelekea vitanda 30 na magodoro yake kwa ajili ya kuwasaidia akinamama wajawazito hao. Kwa sababu hospitali ya Wilaya tumesema iko TAMISEMI, lakini TAMISEMI nafikiri wewe Waziri wa Afya ndiyo mwenye Mamlaka, naomba basi, kwa sababu hospitali hii imekosa vifaa tiba, kwenye bajeti yako ya mwaka 2016/2017 hebu waambie TAMISEMI watusaidie hivi vifaa vifike pale Hosptali ya Frelimo.
Mheshimiwa Spika, upande wa walemavu, Waziri nikisema hapa mimi kama mama mtu mzima, mwenye nusu karne, suala la kwenda kujifungua ni suala nyeti sana. Maeneo tunayoishi, tumeona wenzetu wenye ulemavu wa viungo wanapopata shida wakati wanapokwenda kujifungua. Kwanza kabisa mapokezi ya wale manesi yako tofauti na mtu ambaye yuko kama nilivyo mimi na pili, vitanda vile wanavyoenda kujifungulia si rafiki na wenyewe na maungo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namuomba Waziri mwenye dhamana kwa namna ya pekee, ndani ya mwaka huu wa bajeti hebu alipe kipaumble suala la wanawake walemavu wanapokwenda kujifungua. Nitaona umelitendea haki Taifa, nitaona umeweka tija sura ya mwanamke kwa mwanamke anapopata nafasi ya namna hiyo anakuwa na huruma ya pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo. Nakuja kwenye tatizo la meno na macho. Ni ukweli usiopingika karibu ya robo tatu ya Watanzania tunavaa miwani sasa hivi na tunaotoa meno ni takribani milioni 20. Naomba Wizara yenye dhamana iangalie mpango mkakati wa jinsi ya kutoa elimu ya vyakula vinavyoweza kupunguza watu tusiwe vipofu mapema na tusianze kutoa meno chini ya umri usiotakiwa. Masuala yote hayo yanasababishwa na hivi vyakula ambavyo tunakula, lakini kwenye mpango huu wa hotuba ya Waziri sijaona mahali ambako amewekea kipaumbele suala la macho na meno. Hivyo, nikaona ni wakati muafaka baada ya kuwa nimepata nafasi ya kuchangia, niweze kulisemea hilo.
Mheshimiwa Spika, mimi naishi Mkoa wa Iringa na nimezaliwa Iringa. Naiomba Wizara ya Afya kuhusu afya ya uzazi wa mpango ni hatari. Kwa nini nasema ni hatari? Napenda kama inawezekana sheria itungwe ndani ya Bunge hili inayokataza utengenezwaji wa viroba. Viroba ni pombe zinazonunulika kwa bei ndogo sana, kwa maana hiyo unakuta hawa watoto wa under eighteen wanaanza kulewa toka asubuhi na ndiyo inapelekea waanze kuzaa kabla ya umri wao, wakati akili ya kulea mtoto yenyewe haijakomaa. Dada na kaka kama yamkini wanaweza kuwa wameoana, je, kupata Taifa linaloongezeka kwa kasi, lisilokuwa na malezi ya kielimu, ya kiafya Taifa hili tunalipelekea wapi?
Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimetoa dondoo kuwa uzazi huu unasababishwa na ulevi wa pombe hizi zinazonunulika kwa bei ndogo ndogo. Tuliombe Bunge letu Tukufu, tutakapokuja kujadili, hebu tutunge sheria ya kutokutengeneza pombe hizi za viroba zinazouzika kwa shilingi mia tano, mia tano tuifute kabisa. Tanzania hii tunayokusudia itakwenda kwa kasi kwa sababu tutapata watu watakaozaa watoto ndani ya umri unaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba niunge hoja ya Kambi ya Upinzani kwa asilimia mia moja kwa maana ndiyo inayotoa mwongozo ili Serikali iweze kufanya vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa mkakati madhubuti (strategic plan) wa kutangaza rasilimali na vivutio vyetu kunasababisha nchi nyingine kunufaika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri mwenye Wizara husika wakati atakapokuja kuhitimisha hoja aje na mpango mkakati unaoelekeza kutoa fursa kwa taasisi au watu wenye uwezo ili waweze kutangaza vivutio na rasilimali zetu kimkakati zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwa ni vigumu sana kuona ujangili katika nchi yetu unakuwa kwa kasi wakati kuna watumishi walioajiriwa kwa kazi ya kulinda wanyama, hata pembe za ndovu zikikamatwa mwisho wake zinapopelekwa hakujulikani, hata mrejesho wowote katika Bunge hili Tukufu ili kupata taarifa yoyote endelevu juu ya kesi endapo watuhumiwa wameshinda kesi wananchi kinyemela. Hii ndiyo sababu kubwa inayokuza kazi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali isione vigumu kutoa taarifa muhimu kama hiyo katika Bunge lako Tukufu tena taarifa hizi zinapotolewa jina la mtuhumiwa litajwe kufanya hivyo hivyo ujangili utapungua.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni ya viwanda, napenda kushauri katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/2018, sekta ya kilimo ipewe kipaumbele cha kwanza ili kuwezesha pembejeo za kilimo kupatikana kwa wakati na itengwe bajeti ya kutosha. Kwa kufanya hivyo, wananchi watalima mashamba ya mazao ya biashara na chakula na kuwezesha viwanda vyetu kukua kwa kasi na kuinua uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maendeleo ili iweze kwenda na wakati ni lazima fedha za miradi zinazopitishwa na Bunge lako Tukufu zipelekwe kipindi husika. Angalia bajeti mwaka 2016/2017 hadi robo ya mwaka hata senti tano ya miradi ya maendeleo hazijapelekwa kwenye Majiji, Manispaa, Halmashauri na Miji Midogo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia jioni ya leo kwenye Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nianze na kundi la walemavu. Ninarudia tena kusema Mheshimiwa Ummy - Waziri wa Afya, matatizo wanayoyapata wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua bado yako pale pale. Niliongea mwaka wa jana katika Bunge hili lakini wakati nikiwa field huko kwenye majimbo nimekuta wauguzi wengi wanawanyanyapaa sana wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kwa dhamana ya nafasi yako, hili ulichukue na ulifanyie kazi, wale watakaobainika wanaendeleza vitendo vya kuwanyanyapaa wanawake wenye ulemavu wakati wa kujifungua wachukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 mpaka mwaka 2012 Hospitali ya Mkoa wa Iringa ilipata hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa. Tatizo ambalo linaikumba hospitali ile ni ukosefu wa madaktari bingwa. Hitaji la madaktari ni 24, hadi sasa hivi hospitali yetu ile ya rufaa ina madaktari watano, hivyo kusababisha kazi ya kiutendaji ya kuokoa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwa ngumu sana. Mheshimiwa Waziri, naomba hili ulichukue kwenye mgawo wako wa madaktari hao wanaopata ajira, basi Madaktari Bingwa uwapeleke kwenye Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja kwenye Mfuko wa Bima. Afya kwa wazee wetu wa Taifa hili imekuwa ni tatizo. Serikali imejikita kuwasaidia wazee hawa huduma ya magonjwa ya homa, tumbo, lakini si pale wanapopata magonjwa yale ya moyo, ini, figo, vipimo hivi lazima walipie. Sasa kama Serikali inataka kusaidia kundi la wazee; hivi vipimo nilivyovisema gharama yake ni kubwa; na Serikali haitaki kuwekeza mkono wake, hii huduma ambayo tunasema tunataka kuwasaidia wazee naona sio sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi Wizara ichukue jukumu hili kuhakikisha hawa wazee ambao Serikali imesema itawatibia bure, iwe bure ya magonjwa yote hata hayo niliyoyaainisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Hospitali ya Mkoa wa Iringa kupata hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Iringa tulijenga Hospitali ya Wilaya ambayo iko maeneo ya Frelimo na inaitwa Hospitali ya Frelimo. Hospitali hii ina wauguzi wakutosha, madaktari wakutosha, kinachokuja kuleta shida ni upungufu wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi ninapozungumza sasa hivi hospitali hiyo yenye wauguzi wa kutosha na madaktari wa kutosha haina vifaa vya uuguzi ambapo tumekosa kupata vipimo vya full blood picture, x-ray, ultra sound ambapo ingekuwa vipimo hivi viko pale, hospitali hii ingepokea msongamano wa wagonjwa ambao wanatakiwa kutibiwa pale ili wasiende kutibiwa kwenye hospitali ya rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ningependa nijikite kwenye unyanyasaji wa watoo wadogo wa kike. Sipo sambamba na wachangiaji waliosema, mtoto wa miaka chini ya miaka 18 kuozeshwa na kuwa mama wa nyumba ni makosa makubwa sana kiafya. Kwanza nyonga zake zenyewe hazijakomaa kuweza kuendeleza mambo ya mipango mingine ya kiutu uzima na hivyo tunawafanyia hayo matendo kiunyama kwa sababu tendo la ndoa kwa mtoto wa miaka chini ya 18 hana hisia nalo kwenye akili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Wizara hii kama sheria inakingana, kuwa haiwezekani kutungwa sheria hiyo, basi tutalazimisha Wizara ya Elimu iweke kiwango cha elimu ya mtoto wa kike ni Kidato cha 12, ili kama itaonekena kuna mzazi yeyote yule ana binti yake ameolewa chini ya miaka 18 aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tutakuwa tumewakwamua kundi la watoto wa kike ambao kwa tamaa za wazazi wao… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa Fungu 52 inaonesha kuwa hadi mwezi Machi, 2017 Wizara ilikuwa imepokea sh. 314,673,230.000.95 sawa na asilimia 43 ya bajeti ya Wizara, zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida pamoja na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuhusu fedha za maendeleo, randama zinaonesha kuwa hadi mwezi Machi, 2017 ni asilimia 34 tu ya fedha za ndani ndizo zilizotolewa na Hazina na kwa fedha za nje ni asilimia sita tu ya fedha hizo zilikuwa zimetolewa na Hazina kwa kipindi hicho. Hii ina maana kwamba bajeti ya maendeleo kwa fedha za ndani haijatekelezwa kwa asilimia 63 na kwa fedha za nje haijatekelezwa kwa asilimia 94. Kwa utekelezwaji huu duni wa bajeti ya maendeleo katika fungu hili, maoni yangu ni kwamba Serikali iwe makini kabisa na afya za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Fungu 53, kwa mwaka wa fedha 2016 - 2017 Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni
49.9. Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ilikuwa shilingi bilioni 41 na shilingi bilioni 8.848 zikiwa ni fedha za maendeleo. Hata hivyo, fedha za maendeleo hadi kufikia Machi, 2017 ni sh. 497,718,250/= sawa na asilimia 5.62 tu ya shilingi bilioni 8.8 zilizoidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni kwamba bajeti ya maendeleo katika fungu hili la Maendeleo ya Jamii haikutekelezwa takriban kwa asilimia 95. Fungu hili ndilo linalohusika na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii; na kwa maana hiyo, utekelezaji duni wa bajeti wa vyuo hivyo haviwezi kuwa na uwezo wa kujiendesha na kuzalisha wataalam wa kusaidia jamii zetu kujiletea maendeleo kwa kuweza kuibua fursa zilizo katika jamii zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo Wizara ya Maji. Maji ni uhai wa kila kitu, ikitokea jambo lolote hapa mtu mwingine ameanguka ghafla hapa Bungeni akifika pale hospitalini Madaktari wataanza kumwongeza drip la maji. Hivyo, tuone umuhimu wa maji unavyotakiwa katika maisha ya mwanadamu. Hata magari, meli, ndege vyote hivyo vinahitaji maji. Hata sasa hivi moto ukitokea jengo lolote utaona tunasema gari la zimamoto liko wapi, maji yaje ili waweze kuzima moto. Kama kweli maji ni uhai basi ifikie wakati muafaka wa kuona Serikali inaona jambo hili ni la umuhimu kitaifa na wazingatie kwamba kwa kukosa maji ni kukosa kuwa na maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu inasema tunataka kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani. Imeonekana suala la maji siyo tatizo la kifamilia ila ni tatizo la mwanamke ambapo si kweli. Tatizo la maji ni tatizo la kitaifa na hivyo tulijue kama ni tatizo la kifamilia ni janga la kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kutokana na kuwa mwaka jana tulikuwa tumeweka ongezeko la bei ya mafuta ya dizeli na petroli kwa ajili ya kuhakikisha maji yanafika vijijini lakini imeonekana ongezeko ya bei ya mafuta haya limetatua changamoto ya maji kwenye miji yetu. Changamoto ya maji kwenye miji si kubwa kama ilivyo kwenye vijiji. Hivyo basi katika bajeti hii naomba Wabunge wote tuombe tuwe na ongezeko tena la tozo kwenye mafuta tufikie Sh.100, basi asilimia 70 iende vijijini na asilimia 30 iende mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla suala la maji ameachiwa mwanamke utaona hata wakati wa uzinduzi, Waziri anakinga maji kwenye ndoo anamtwisha mwanamke kwa nini basi akikinga maji asimtwishe mwanaume wakati suala hili ni tatizo la kifamilia? Naomba tuelewe kwamba suala la maji siyo tatizo la mwanamke ni la kifamilia, hivyo basi, kama ni tatizo la kifamilia, isionekane ni kumtua ndoo mwanamke kichwani bali ni pamoja na waume zetu tuliokuwa nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niingie kuzungumzia Mkoa wangu wa Iringa, mkoa wenye neema na uliobarikiwa ambao una vyanzo vya maji, tuna Bwawa la Kihansi, Bwawa la Mtera, Mto Lukosi, Mto Mtitu na Mto mdogo Ruaha. Cha ajabu pamoja na kuwa tuna vyanzo vyote hivyo kuna vijiji vina shida ya kuliko mtu anavyoweza kufikiria. Vijiji hivyo ni Nyakavangalala, Lyamgungwe, Lupembelwasenga, Luhota, Mkalanga, Usolanga na vingine vingi katika mkoa huu pamoja na Mji Mdogo wetu wa Ilula ambapo chemchem ya Ibofye iko jirani sana na nafikiri ni kama mita za mraba zisizopungua arobani na tano. Tumeshindwa kuweka miundombinu ili watu wa Mji Mdogo Ilula waweze kupata maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi navyozungumza Mji Mdogo wa Ilula wanauziwa maji ndoo ya lita ishirini kwa Sh.500. Huo ni Mji Mdogo tena uko kwenye barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kuelekea Zambia. Naomba Mawaziri wenye Wizara hii washughulikie tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo hicho cha Ibofye kwanza kabisa kwenye bajeti ya mwaka 2000-2005, Bunge hili lilipitisha bajeti ili waende kufanya kazi ya miundombinu katika chanzo hicho, wakati huo akiwa Mheshimiwa Mbunge Mlawa. Hadi leo navyozungumza sielewi hata hizo fedha zilikoishia. Naomba Mawaziri wahusika walifuatilie suala hili iliwaelewe. Ndiyo maana tunasema tutakapoweka ongezeko kwenye bei ya mafuta kuwe na bodi maalum itakayofuatilia ongezeko la fedha hizi ili ziende kwenye miradi tuliokusudia wa kupunguza uhaba wa maji kwa wananchi katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Iringa ni kati ya mikoa ile minne inayozalisha sana chakula nchini Tanzania.

Nataka niseme njaa tunaitaka kwa makusudi kwa sababu ya kutokuwa na mbinu mbadala kwa wakati muafaka wakati nchi yetu ina wataalam waliosomea na kubobea. Tatizo letu ni kwamba wakati wa mvua hatuna mabwawa ya kutunza maji ya mvua ili wakati wote tuweze kuendelea na kilimo cha umwagiliaji. Kutokana na hilo, tuone ni wakati sasa wa kuhakikisha bajeti hii inayokuja kuombwa na Waziri mwenye dhamana imeongezeka ili tuweze kujenga mabwawa maeneo hayo ambayo nasema ni lazima tuwe na mabwawa yanayotunza maji ya mvua tuweze kuondokana na tatizo la maji. (Makofi)

Katika Mkoa wangu wa Iringa akinamama wengi wajasiriamali ni wakulima wa mazao ya mbogamboga. Hivyo kukosa mifereji ya umwagiliaji iliyo bora wanashindwa kumudu shughuli zao za kilimo na kuweza kujikwamua katika dimbwi la umasikini walilokuwa nalo ukizingatia kazi kubwa ya kulea familia ni ya mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri mwenye dhamana katika Mkoa wangu wa Iringa katika maeneo haya yote niliyoelekeza na vijiji ambavyo sikuorodhesha hapa kutokana na wanawake wale walivyo na juhudi kwenye kilimo ahakikishe amepeleka mradi wa maji ili waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo cha mbogamboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Kata yetu ya Mahenge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naunga mkono hoja ya Upinzani asilimia mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na pale nikikumbuka bajeti ya mwaka jana nilimwomba Waziri kuhusu hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa, ina upungufu wa Madaktari Bingwa sita. Kutokana na msongamano wa wagonjwa wanaopata ajali kutokana na njia kuu inayounganisha nchi yetu ya Tanzania na nchi jirani Zambia, Msumbiji, Malawi na Kusini. Hata hivyo, hadi tunafikia bajeti hii ya mwaka 2018/2019, sikuweza kusaidiwa hata kupata Daktari mmoja Bingwa wakati aliniahidi hapa. Naomba atakapokuja kuhitimisha aweze kunipa hilo jibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, imeonekana katika Taifa letu saratani ya shingo ya kizazi imekuwa ni tatizo kubwa sana.

Kwa taarifa ya yeye mwenyewe Waziri ameliambia Taifa kwamba katika wanawake wanaopimwa kwa mwaka wanawake 670 hupatikana na tatizo hilo. Hilo tatizo limeonekana ni kubwa na limeonekana kisababishi ni wanaume ambao hawajatahiriwa, lakini sikuona kwenye kitabu chake mkakati ambao ameuweka wa makusudi kutoa elimu kwa kundi la wanaume kutoruka njia mbili ili tatizo hili liweze kupungua kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waziri anapokuja kuhitimisha hoja hii aniambie Wizara imejipangaje kufanya utafiti wa kujua chanzo kikuu kabisa cha kusababisha hili tatizo likue kwa kasi katika Taifa letu kwa maana najua huwezi kutoa tiba kwenye tatizo ambalo chanzo chake hukijui. Ukilinganisha na taarifa ya wataalam hebu turudi miaka ya nyuma tulikuwa na wanaume wengi sana ambao hawajatahiriwa lakini hili tatizo halikuwa kwa kiasi kama ambaccho tunakiona kwa sasa. Hivyo, niiombe Serikali tatizo hili walilogundua ni sehemu moja ndogo tu, sehemu kuu ipo, hivyo Wizara ijipange kufanya utafiti wa kina ili tuweze kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuja kwenye mabadiliko ya tabianchi, sasa hivi katika Taifa letu kumekuwa na magojwa mengi sana ya mlipuko ambayo yanapelekea Taifa letu liweze kutafuta dawa katika nchi mbalimbali kuokoa maisha ya Watanzania. Hata hivyo, inasikitisha sana katika Taifa letu la Tanzania hadi sasa tunapozungumza asprin tunaagiza Kenya, nchi yetu ya Tanzania Wizara ya Afya asilimia 50 inatumia fedha hizi kuagiza dawa nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu hiki hakuna mkakati wa Wizara ya Afya ulioonesha kuwa tunakuja na mpango mbadala kutafuta wadau waweze kujenga kiwanda cha dawa katika nchi yetu ili kulipunguzia Taifa kutumia gharama kubwa sana kuagiza dawa nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana kwenye Wizara hii kuna 1.5 imepotea, sasa hili ni jambo la kushangaza sana na linasikitisha pale tunapokwenda kwenye hospitali zetu za rufaa kukosa vifaa wakati kuna hela zinazopotea bila kuelewa kitu chochote. Naomba Waziri mwenye dhamana wakati wa…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua za kwanza ndiyo za kupandia. Kwa masikitiko makubwa sana mvua za kwanza za kupandia mbolea na mbegu hazipatikani, hili limekuwa ni tatizo sugu sana katika Taifa letu. Tunaposema kilimo ni uti wa mgongo kwa Taifa letu la Tanzania ukizingatia asilimia 75 ni wakulima, kati yao asilimia 65 ni wanawake na wanawake ndiyo nguzo kuu katika familia zetu. Ni kwa nini basi Serikali kwa kutumia wataalam tulio nao wasiwe na mpango mkakati kuanzia sasa wajue ni wakati gani mbegu na mbolea zifike kwa wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tafiti imeonekana asilimia 25 ya wakulima hutumia mbegu bora. Katika kutumia mbegu bora asilimia 40 huchangia kupatikana kwa mavuno. Kwa maana hiyo, huyu mkulima atakavyokuwa amepewa mbegu bora mavuno yake yanapatikana kwa asilimia kubwa hivyo kipato chake kinamkwamua kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye kundi la kati. Kwa ujumla wake Watanzania tulio wengi watoto wetu tunawasomesha kwa njia ya kilimo, hii haipingiki. Naomba Waziri wa Kilimo anapokuja kuhitimisha hoja yake hii atuambie ni lini sasa Serikali imejipanga kuhakikisha mbegu na mbolea zinaenda kwa wakati muafaka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini inasikitisha, wamekiri kuwa asilimia 36 ndiyo sasa mbegu bora zinapatikana, asilimia 64 tunaagiza. Hebu fikiria, tuna vyuo vyetu vya kilimo, ni tatizo lipi linalotukumba sisi Watanzania tusitumie hivi vyuo vyetu kuweza kuwa na wataalam wanaoweza kuzalisha hizi mbegu bora zikapatikana Tanzania tukaepusha gharama ya kutumia kuagiza mbegu katika Taifa lingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukulia mfano Mkoa wa Iringa kuna Kiwanda cha Dash ambacho ni cha kusakata nyanya, hadi navyozungumza kimeshindwa kufanya kazi hiyo kutokana na kwamba wakulima wanaolima zao la nyanya hawatumii mbegu bora hivyo wameshindwa kuzalisha nyanya ambazo zinaweza zikaenda kwenye kiwanda hicho hatimaye na kiwanda kuendelea kufanya kazi. Tuna Maafisa Ugani katika nchi yetu wamebaki maofisini na ndiyo maana wakulima wanalima kwa kubahatisha hatimaye mazao hayapatikani ya kutosha, kama hili zao la nyanya nililotolea mfano la Kiwanda cha Dash. Naomba Serikali basi ifikie wakati wa hawa maafisa wetu kwenda kule kwenye vijiji wakashirikiane na wakulima wetu ili waweze kuwapa elimu ya kutumia mbegu bora na mbolea ili waweze kupata mazao yanayoendana na hitaji ambalo tunataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge jioni ya leo katika Wizara hii wanachangia Wizara hii kwa machungu makubwa sana hasa watani wetu wa jadi. Nachosikitika tutakapokuja kushika shilingi hiyo ya Waziri yatatoka maelekezo, tutaachia shilingi Wizara hii itabaki kama ilivyo. Nawashauri Waheshimiwa Wabunge kwa vile imeonekena wote tunataka katika Taifa letu la Tanzania kilimo kipewe kipaumbele hii shilingi ya Waziri wa Kilimo ishikiliwe mpaka mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia mustakabali wa nchi ya viwanda, viwanda hivi vinategemea mazao na mazao haya ndiyo tunayosema mbegu bora. Ukitaka mahindi mbegu bora na mbolea, ukitaka pamba mbegu na mbolea na dawa. Kama Wizara hii inakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kuwa bajeti inayotengwa na kupitishwa kwenye Bunge hili Serikali haitaki kutoa basi na wenyewe watuonyeshe kutuunga mkono kwamba Serikali imekaa kimya kwa kutokutoa fedha kwa wakati ili kilimo hiki tunachosema tunataka nchi ya viwanda kiweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitarudi kwenye zao la mahindi kwenye Mkoa wangu wa Iringa. Tunapozungumzia zao la mahindi Mkoa wa Iringa ndilo zao la …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa afya siku hii ya leo niweze kuchangia kwenye Wizara hii. Ninakushukuru Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Maji ukizigatia tunavyosema maji, maji ni kila kitu katika maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukizungumzia suala la maji kama ni uhai na ukiangalia kwa jinsi Serikali yetu haitaki kutekeleza ili sera hii ya kuwa maji ni uhai iweze kuwepo mimi nasikitika sana. Maji ni tatizo kwa nchi nzima hususan hata kwenye Mkoa wangu wa Iringa ukiangalia Nyakavangalala, Mkulula, Usolanga, Area Mgungwe, Luhota maji hatupati.

Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye kitabu cha Waziri ukurasa 267 hadi 279 visima ambavyo vimechimbwa kwenye Mkoa wa Katavi, jumla kulikuwa na visima 225 kwa nchi nzima lakini Mkoa wa Katavi peke yake ni visima 79.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko hayo ukitoa unaona ni visima 146 vinavyobaki kugawanya Mikoa 29 na ukigawa kwenye mikoa 29 unaona kila Mkoa utapata visima
7.7 ukifanya estimation ni visima nane lakini Mkoa mmoja tu visima 79. Haya ni masikitiko kwa sababu Mkoa wa Katavi ndiko anakotoka Waziri wa Maji. Tukisema sisi watu wa…

T A A R I F A . . .

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo siipokei kwa sababu Waziri wa Maji ndiye anayesimamia Mikoa yote ya Tanzania wapate maji, kwa msimamo huo yeye angelazimika kuhakikisha wataalam wanaenda kutoa elimu hiyo kwa Mikoa yote ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaona upinzani tukisema tunataka Mawaziri wasitokane na mfumo wa Vyama vya Siasa ni kwenye tija kama hii, maana wakipatikana Mawaziri wenye taaluma unapoingia kwenye miradi kama hii hutapendelea huko unakotaka upate kura wewe. Sisi wote Wabunge tunataka turudi humu ndani. Namuomba Waziri wa Maji anapohitimisha hoja yake hii hebu aniambie vijiji nilivyosema atapeleka wataalamu lini wakatoe elimu hiyo kamaaliyoifanya kwake Katavi hatimaye wakapata hivyo visima 79 badala ya kupata visima 7.7. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa hii miradi mikubwa ya maji ambapo Serikali inawekeza ukiangalia bajeti ya mwaka jana 2017/2018 Bunge hili lilipitisha bajeti ya bilioni moja kwa ajili ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Kahama, Shinyanga hatimaye Tabora. Hadi 30 Machi, 2018 hakuna hata senti tano iliyoenda. Sasa tumebakiwa na miezi mitatu ili bajeti ya mwaka 2017 ifungwe, ninaomba Waziri wa Fedha anataka kuniambia katika miezi mitatu iliyobakia hiyo trilioni moja tuliyoipitisha hapa ndivyo ataitekeleza kwa kipindi kifupi hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri ni vema tufikie wakati wa kupanga miradi yenye uwezo wa fedha ambazo tunazipata kwenye nchi yetu ili iweze kutekelezeka hatimaye Watanzania wote waweze kupata maji. Kwanza nina masikitiko makubwa ninapozungumza hapa katika Mkoa wa Iringa Wilaya ya Kilolo, Kijiji cha Nyanzu chenye wakazi wasiopungua 2,500 wenyewe kazi yao ni kilimo cha umwagiliaji ambapo takribani kama heka zisizopungua 2500 ni shamba la umwagiliaji. Hadi ninapozungumza hivi heka hizo zote vitunguu vimekauaka kwa sababu ya kukosa maji. Sasa mnaponiambia Mjumbe aliyepita anasema ni Halmashauri ambazo zinatakiwa zisimamie suala la maji wakati Waziri mwenye dhamana yupo, mwenye wataalam wake...

Mheshimiwa Spika, ninaomba maji watu wa Nyazwa wapate waweze kumwagilia mashamba yao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kunipa uzima kuwepo mahali hapa jioni ya leo niweze kuchangia Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya CAG ya 2017/18 inaonesha kuna ujenzi wa hospitali m bili za rufaa Mkoa huu mmoja na hospitali hizo zinazojengwa Chato imetengewa bilioni 9.9, Geita billioni 5.9 kwa mkoa mmoja tu ni bilioni 16. Hizo ni hospitali za rufaa kwenye mkoa mmoja. Ukizingatia huu mkoa wa Geita, wananchi wa mkoa huo wapo milioni 1.7. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukue Kanda ya Kusini yenye mikoa mitatu, Lindi, Mtwara, Ruvuma haina hata hospitali ya rufaa na tukichukua hii mikoa mitatu ina watu milioni 3.6. Ninashindwa kuelewa Wizara ina maana gani? Tunaposema tunataka kujenga hospitali za rufaa tunaangalia uwiano upi kwa wananchi wa maeneo husika? Nitamtaka Waziri anapokuja kuhitimisha hoja hii aje na majibu yanayotuambia mpango wa Wizara yake inaangalia eneo labda la kiongozi fulani lakini sio inaangalia tija kwa wananchi waliopo eneo husika kupeleka hospitali za rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri tunazungumzia upungufu wa watumishi Sekta ya Afya tena hawa watumishi wenye ujuzi wa kutoa huduma kwenye vituo. Tunapozungumzia hivi sasa hivi tuna upungufu wa asilimia 56, ni tatizo kubwa sana kwa Taifa. Nafikiri kwenye kitabu cha maendeleo sijaona mahali ambapo pameonesha kwamba katika mikoa ile niliyoitaja mitatu ya Kusini kwenye kitavbu cha maendeleo hakijatengewa hata bajeti. Hivi watu wa Kusini sisi tuna tatizo gani? Geita ni mkoa mpya kama Mkoa wa Njombe, Njombe ni ukweli usiopingika kuna matatizo yaliyozidi kuliko hata watu wa Geita lakini hakuna kinachoonekana kama Serikali inaangaliaje hivi vipaumbele katika hii mikoa mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nije na uwiano. Kwenye kitabu hiki nimejaribu kusoma vizuri sana, sikuona mahali panapoonyesha hospitali teule ya Kibong’oto iliyopo Mkoani Kilimanjaro kama imetengewa fedha ili waweze kuiboresha ukiangaliano uwiano wa ugonjwa huu wa kifua kikuu kuwa watu 10 wazima, watu 30 wanaohakikiwa wanakuwa na kifua kikuu. Ukiangalia kwenye uwiano wa Watanzania milioni 55 kwa sasa ukipiga mahesabu ina maana Taifa letu lina watu wenye ugonjwa wa Kifua kifuu milioni18, hili si jambo dogo! Milioni 18 ambapo ukiangalia asilimia 30 ya wenye…

T A A R I F A

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua yeye ndiye mwenye Wizara yake tunayoijadili, bado alikuwa na muda mkubwa wa kuja kujibu hii hoja kama nilivyomtaka wakati wa kujibu aje aseme.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suzan, kama unakosea haifai kwa sababu unakuwa unapotosha Umma na yeye ndiyo anaelewa…

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. Niachie niendelee. Nimesema katika watu 10,000 wazima, wapato 30 ambao wana hakikiwa, wana ugonjwa wa TB, tumefundishwa, NGO zinakuja hapa kutoa elimu na watu tunaandika ili tuje tuisaidie Serikali katika kuboresha kwenye bajeti. Sio kosa langu mimi, basi ni kosa la NGO zinazokuja kuelimisha kama wanatupotosha sio hoja yangu mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee. Basi sasa katika hilo kama alivyosema Waziri hata kwa idadi hiyo, hiyo hospitali niliyoitaja kwneye kitabu chako hiki hujaitengea bajeti ili uiboreshe vizuri. Naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilinde, umenipa muda mdogo nilikuwa na dakika 10 sasa dakika zangu nimepewa chache. Huduma ya lishe, nchi yetu ya Tanzania duniani ni ya 10, Afrika ni ya tatu, nchi ya Tanzania ilivyo, Mungu alivyoipendelea ina eneo kubwa, tunazalisha aina ya vyakula tatizo hapa ni elimu na elimu tunaipata wapi? Kwa Maafisa Maendeleo wa Jamii ambao katika Taifa letu wamekuwa ni wachache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa maafisa maendeleo wa jamii wanaishia ngazi ya kati, elimu hii ili itusaidie kuangalia watu wapate chakula, lishe bora ianzie kwenye vitongoji vyetu tunakoishi. Tuitake Serikali ianjiri maana vyuo vya maendeleo ya jamii vimepata wahitimu wengi ambao hawa na ajira, wamebaki mitaani. Hawa wangetoa elimu ya lishe nafikiri Taifa letu lisingefikia mahali hapa kulinganisha na neema ambazo Mungu nchi ya Tanzania aliipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia kwenye suala la tiba asilia. Tulikuwa na mafunzo Mkoa wetu wa Iringa mwezi uliopita ambapo kuna NGO iliendesha hayo mafunzo. Mkoa wa Iringa tu hili naomba Waziri ulichukulie kwa sababu waliomba Wizara iangalie upya jinsi ya kusajili waganga wa jadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa tu hadi sasa tunapozungumza umeshasajili waganga 878 na ambao hawajasajiliwa ni 900. Kwanini watu wameomba tulilete Bungeni? Imeonekana katika usajili huu nafikiri hakuna mpango mkakati ambao umeelekezwa hawa wanasajiliwa na afisa watendaji kwenye kata kiasi kwamba mtu anatoa hela anasajiliwa wanaanza kupotosha imani za watu ambao wanawadanganya kuwa akienda anasema kaleta kiungo cha albino…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa na muda umekwisha.

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa kuunga mkono hoja.

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Nimesema naunga mkono hoja hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau tuendelee.

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Siwezi kuunga hoja ya Dada Ummy.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania inataka iwe nchi ya viwanda, tuboreshe sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kwamba mikopo kwa wakulima inapatikana. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewawezesha wakulima kulima kilimo bora. Kilimo bora kinatokana na wakulima kuwa na mbegu bora na mbolea kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sera ya elimu bure, ni miaka miwili kama Taifa tumeona kuwa elimu bure inaathari kutokana na kuporomoka kwa ufaulu wa wanafunzi. Katika mpango huu uliopendekezwa na Waziri wa Fedha, je,kuna mkakati wa makusudi wa kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya elimu? Elimu ya kutosha inatakiwa kutolewa kwa wananchi wajue kuna baadhi ya shughuli za elimu kama wananchi wanapaswa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu uliopendekezwa kwa mwaka 2018/2019, hakuna sehemu iliyoonesha ukuzaji wa viwanda katika Mkoa wa Iringa ambavyo vilikuwepo katika Mkoa huo. Mkoa wa Iringa miaka ya nyuma ulikuwa na viwanda vya COTEX, Cocacola, IMAC, SIDO na Tyre,viwanda hivi viliwasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Iringa na maeneo mengine ndani ya nchi yetu kupata ajira, lakini katika mpango uliopendekezwa sijaona sehemu yoyote inayoonesha kwa mwaka 2018/2019 kuhakikisha viwanda hivyo vinaimarishwa ili kupatia ajira wananchi wa Mkoa wa Iringa na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili lipewe kipaumbele.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa letu la Tanzania sekta ya kilimo inaajiri wananchi asilimia 70 lakini bado Serikali haiwekezi kiasi ambacho kitakuwa na uwiano na hitaji la sekta hiyo.

(i) Pembejeo haziji kwa wakati na za kutosha mahitaji.

(ii) Wataalam wa sekta hiyo wapo wa kutosha katika Halmashauri.

(iii) Bei ya mbolea si rafiki kwa wakulima hasa kwa mwaka 2017 - 2018, bei ya mahindi iko chini sana kuliko bei ya mbolea. Gunia la mahindi ni Sh.30,000 wakati mfuko mmoja wa mbolea ya UREA ni Sh.56,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mifugo katika Taifa letu la Tanzania imekuwa tatizo kubwa kwa wafugaji kwa kukosa maeneo ya kufugia. Serikali iwe na mkakati wa makusudi kuhakikisha wakulima na wafugaji wametengewa maeneo kwa shughuli za kilimo na mifugo ili azma ya Tanzania ya viwanda iwezekane. Viwanda vinavyotakiwa kuwepo vinahitaji malighafi kutokana na kilimo na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvuvi, matatizo ya Sheria ya Uvuvi itazamwe kwa macho ya faida ya wavuvi na Taifa, siyo kuchoma nyavu za wavuvi bila kuhakikisha vyavu hii ni zile zinazotakiwa au la hasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali bajeti inayopitishwa na Bunge ifike kwa wakati kwenye Wizara husika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hotuba ya Waziri Mkuu inayohusiana na mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi yake na ya Bunge kwa mwaka 2018/2019, naomba nichangie kwenye huduma za jamii kipengele cha elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Waziri Mkuu imeonesha kuna mafanikio makubwa ya mpango wa utoaji elimu ya awali na msingi bila malipo. Katika maelezo yake imeonesha Serikali imekuwa inapeleka fedha zote za ruzuku moja kwa moja katika shule zetu. Sisi wawakilishi wa wananchi katika maeneo yetu tunayotoka fedha hizo hazifiki kwa wakati na pia hazitoshelezi mahitaji ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano hai wa Jimbo la Manispaa ya Iringa, kuna baadhi ya shule ambazo ruzuku hii haitoshelezi mahitaji yao. Mfano wameshindwa kumlipa mlinzi wa Shule ya Msingi Azimio kwa muda wa mwaka mmoja na miezi mitatu, pia maji yamekatwa wanafunzi wa shule ya awali hawapati uji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika ongezeko la kuandikisha watoto shule za msingi naona imeshuka kutoka 2,120,667 mwaka 2017 hadi kufikia 2,078,379 mwaka 2018. Je, hili ni ongezeko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tusiweke siasa katika elimu kwa sababu elimu ni ufunguo wa maisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya barabara Mkoani Iringa yamekithiri. Ninaomba Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ilichukue jambo hili kwa umakini ukizingatia mkoa huu unachangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri kwa Waziri wakati wa matengenezo ya barabara hasa kwa kutumia kifusi, kitumike kifusi ambacho hakina mawe yenye ncha kali, kama kifusi kilichowekwa barabara kutoka Tagamenda - Kitayawa - Ndiwili pamoja na Kidabaga; kifusi hicho kinasababisha uharibifu wa tairi za magari.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri kwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakati wa ujenzi wa barabara za lami kushirikisha Serikali za Vijiji kuwa walinzi wa alama za barabarani kwa kuwa wakati wa ziara iliyofanywa na Kamati ya Miundombinu tumekuta baadhi ya wananchi wanazitoa alama hizo na kusababisha ajali na upotevu wa hela za Serikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 Tanzania ilikuwa na viwanda 156. Viwanda hivi Serikali iliposhindwa kuviendesha ilivibinafsisha, lakini haviendelezwi. Kwenye hotuba ya Waziri hakuna mahali popote alipozungumzia chochote kuhusu waliobinafsishiwa viwanda na kutokuviendeleza. Tunaomba anapohitimisha hoja aje na majibu yanayoelekeza hatua zilizochukuliwa juu ya tukio hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imesemwa Tanzania ni nchi ya viwanda, je, ni viwanda vya kuchuja alizeti na kutengeneza pipi? Mbona sioni juhudi ya Serikali juu ya viwanda vya kutengeneza nguo ukizingatia tunahimiza zao la pamba lilimwe kwa wingi? Nafikiri ni wakati muafaka wa viwanda vyote vya nguo mfano Urafiki, Mwatex, Mutex na kadhalika vifufuliwe kwa kuwa tunahimiza Watanzania kulima pamba ili malighafi yetu itumike na hapa kwetu kwa wingi pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yote inayopitishwa kwenye Bunge lako juu ya viwanda haionekani utekelezaji wake. Je, Tanzania ya viwanda itakuja kihewahewa? Tunaomba majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Waheshimiwa Wabunge tunapoishauri Serikali hoja zote zichukuliwe, zifanyiwe kazi ili kuleta tija ya maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mbunge yeyote asiyetaka maendeleo katika Taifa lake, ndiyo maana wote huchangia hoja kwa hisia. Hivyo hoja zifanyiwe kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kutumia nafasi hii kuainisha upungufu unaofanywa na baadhi ya Jeshi la Polisi. Polisi kazi yao ni kulinda wananchi na mali zao, mipaka ya nchi na pia kuhakikisha amani inapatikana. Pia kudhibiti uhalifu wowote unaoweza kutokea ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sasa imekuwa ni kinyume na hayo, Jeshi letu la Polisi limepoteza uaminifu kwa wananchi wake kutokana na vitendo wanavyofanya. Kwa mfano, wananchi kubambikiwa kesi awapo kituoni. Unakuta mtu ana kesi ya kupiga mwenzake anaambiwa ameiba na kuvunja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia mikutano ya vyama vya siasa kinyume na taratibu ya Katiba ya nchi. Hivyo ningeomba Waziri mwenye dhamana aelekeze Jeshi la Polisi majukumu yao halisi na siyo vitendo vya uonevu wanavyovifanya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wanapenda rushwa na kuchelewesha kesi Mahakamani sababu wanachopewa hakiendani na kazi wanazofanya. Hivyo naomba waongezewe mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia na makazi ya baadhi ya askari nchini hayaridhishi na yanaenda kinyume na mila na desturi ya nchi yetu. Unakuta mtu anaishi kwenye chumba kimoja na ana familia, chumba kinatenganishwa na pazia au ma-box. Je, hayo ni maadili gani? Hao askari wanatembelewa na ndugu zao, uhuru hawaupati kabisa. Namwomba Waziri, Mheshimiwa Mwigulu jambo hili litazamwe kwa makini japo wakirudi majumbani kwao kupumzika wapumzike vizuri ili wakirudi kazini warudi na nguvu nzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ukurasa wa saba, tunaona ufafanuzi wa fedha iliyoidhinishwa kwa mwaka 2017/2018 ni trilioni 6.57 kwa ajili ya mishahara, matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hiyo tunaona mishahara ni trilioni 4.27 ila jumla ya fedha zilizopokelewa kufikia Februari, 2018 ni trilioni 3.33 sawa na asilimia 50.68 ya bajeti yote iliyoombwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, utoaji wa fedha iliyobakia utatolewa ndani ya kipindi hiki kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha, sababu tukiangalia muda uliotumika kutoa fedha iliyotolewa ni mwingi na fedha iliyotolewa inaonesha haitoweza kutosheleza hata bajeti ya mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira ni la muhimu katika Taifa, hasa tunaposema tunahitaji nchi ya viwanda, tutaendaje kupata product ya wataalam wa kuendeleza hivi viwanda siku za mbele endapo Walimu mashuleni hakuna, Walimu wa sayansi hakuna wa kutosha. Je,
tutapataje product yetu wenyewe ya kuendeleza viwanda vyetu endapo hatuajiri Walimu wa kutosha kutoka ngazi ya msingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifanye mikakati ya makusudi ya kuajiri walimu kuanzia ngazi ya msingi na pia kuwatengenezea mazingira mazuri Walimu sehemu wanazopangwa kwenda kufundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la utawala bora nchi yetu inatakiwa isimamie kwenye misingi ifuatayo:-

Kuzingatia utawala wa sheria, kuzingatia busara na kuzingatia heshima. Ila kwa mwenendo wa sasa unaoendelea wa kila mtu anasema anachokifikiria yeye italeta shida. Mfano tumeshuhudia Wakuu wa Wilaya wakiwaweka Wabunge ndani na kuwafukuzisha watu kazi bila kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Waziri mwenye dhamana, Wakuu wa Wilaya, Mikoa na Wakurugenzi wanaochukua hatua bila kujali taratibu wachukuliwe hatua za kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kama ifuatavyo:-

Suala la ajira ni la muhimu katika Taifa hasa tunaposema tunahitaji nchi ya viwanda tutaendeleaje kupata product ya wataalam wa kuendeleza hivi viwanda siku za mbele endapo Walimu mashuleni hakuna? Walimu wa sayansi hakuna wa kutosha, je, tutapataje product yetu wenyewe ya kuendeleza viwanda vyetu endapo hatuajiri Walimu wa kutosha kutokea ngazi ya msingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifanye mikakati ya makusudi ya kuajiri Walimu kuanzia ngazi ya msingi na pia kuwatengenezea mazingira mazuri Walimu sehemu wanazopangiwa kwenda kufundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la utawala bora nchi yetu inatakiwa isimamie kwenye misingi ifuatayo:-

Kuzingatia utawala wa sheria; kuzingatia busara na kuzingatia heshima. Kwa mwenendo wa sasa unaoendelea wa kila mtu anasema anachokifikiria yeye italeta shida. Mfano tumeshuhudia Wakuu wa Wilaya wakiwaweka Wabunge ndani na kufukuzisha watu kazi bila kufuata utaratibu. Nashauri Waziri mwenye dhamana, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wanaochukua hatua bila kujali taratibu za ajira wachukuliwe hatua za kisheria.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi ni suala mtambuka na siyo tu linaathiri sekta moja. Ili kukabiliana na suala hili, nguvu toka pande zote inatakiwa kutumika. Ofisi ya Waziri Mkuu, Fungu 37, miradi inayohusu kujiandaa kwa majanga na mabadiliko ya tabianchi haikupata hata senti moja. Kwa maana hii, nchi yetu ya Tanzania hatuoni kama hili ni tatizo na kama tunaona ni tatizo kwa nini basi tusione ni wakati kama Taifa kuyalinda mambo ya mazingira kwa kutumia fedha zetu ili kuondokana na tatizo la ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchafuzi wa mazingira kutokana na taka ngumu ni changamoto katika maeneo ya mijini kutokana na uwezo mdogo wa Mamlaka za Serikali za Mtaa na miundombinu hafifu ya usimamizi wa taka za aina hii hasa mifuko ya plastiki au rambo. Nchi yetu Tanzania ina Kiwanda cha Karatasi Nyororo Mkoani Iringa, Wilaya ya Mufindi, kinatoa karatasi za kiwango cha juu ambazo zinasafirishwa nchi jirani. Kwa nini Serikali isichukue maamuzi magumu kuwekeza katika utengenezaji wa mifuko ya kaki katika kiwanda hicho na kwa kufanya hivyo mapato ya Serikali yataongezeka, wakati huo matumizi ya mifuko ya plastiki itakoma na hali ya mazingira itakuwa salama. Ni mipango ambayo kama nchi hatupaswi kulialia, hapa ni uamuzi mgumu ambao unatakiwa kufanyika kulinusuru Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sheria ya utunzaji wa vyanzo vya maji ambayo inaelekeza shughuli za kibinadamu zisifanyike kandokando na mito, nashauri sheria hii isimamiwe kwa umakini kwani kuna maeneo mengine wanaambiwa wafanye shughuli zao ndani ya mita 60 na maeneo mengine mita 100. Nashauri watu wote waelekezwe umbali ufanane kama ni mita 60 au mita 100, kauli iwe moja tu kwa kuwa nchi ni moja na watu ni wamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukauka kwa Mto Ruaha Mkoani Iringa kunasababishwa na wakulima wa mpunga Mbarali ambao baada ya kumwagilia mashamba yao wanaacha maji yanatiririka ambapo kungekuwa na usiamamizi mkali wa kuhakikisha kila mwenye shamba baada ya kumaliza kumwagilia maji wanayarudisha kwenye mto. Kadri Mto Ruaha Mkuu unavyozidi kukauka wanyama wa Mbuga ya Ruaha, Mkoani Iringa watahama na mbuga hii ndiyo mbuga kubwa kuliko mbuga zote Tanzania. Nini kauli ya Serikali kuhusu hatma ya mbuga hiyo? Nataka kauli ya Serikali wakati wa kuhitimisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la haki za binadamu kwa nchi yetu ya Tanzania ni wimbo wa mdomo, lakini kiutekelezaji hakuna kabisa. Ni miaka 58 tangu nchi yetu ipate uhuru, lakini katika maeneo ya mahabusu, Vituo vya Polisi na Magereza nchi nzima haki za binadamu hakuna kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la haki za binadamu, tunagusa mambo mengi ikiwemo kusikilizwa, kutibiwa, malazi na sehemu ya kujisitiri kiafya. Hadi leo wanajisaidia mahali pa wazi huku wengine wanamwona. Isitoshe sehemu wanayojisaidia na chakula wanalia hapo hapo na kulala hapo hapo. Kutenda kosa kunamwondolea mtu kuwa siyo binadamu. Naomba Mheshimiwa Waziri anapohitimisha hoja hii atoe majibu, ni lini sasa suala hili litakoma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika kuwa hotuba ya Katiba na Sheria katika kipindi ambacho Taifa linapitia katika changamoto ya kutoheshimu utawala wa sheria, ni kipindi ambacho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria mbalimbali za nchi na kanuni zake hazifuatwi; ni kipindi ambacho matamko yasiyozingatia tena Katiba, sheria na kanuni yanatolewa hadharani kwenye majukwaa ya siasa na wakati mwingine hutolewa kwa waraka bila woga wowote; ni kipindi ambacho dira ya ofisi nyingi za Serikali imejielekeza inafanya nini ili mtu afurahi zaidi. Kwa maneno mengine, dira ni kumfurahisha mtu zaidi kuliko kuzingatia matakwa makuu ya katiba na sheria za nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nchi yetu inaingia kuwa Tanzania ya viwanda bado upande wa elimu bajeti inazidi kushuka, sijui Serikali inajipangaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukulie suala la Walimu, Walimu ni wachache sana hadi leo hii zipo shule zina Walimu wachache sana ukilinganisha na takwa la elimu. Walimu hao hao wachache hawana maandalizi mazuri ya kufundishia; miundombinu si rafiki, maeneo wanayoishi, madarasa yenyewe na hasa shule za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni ya Walimu wanayoidai Serikali, kupandishwa daraja, nauli za likizo na marupurupu mengine kwa kazi ngumu kama ya Mwalimu kumfundisha mwanafunzi aelewe kile anachojua yeye, halafu haki zake za msingi halipwi, atakuwa na moyo gani wa kufanya kazi hiyo. Naomba Waziri anapokuja kuhitimisha aniambie kwa mwaka wa bajeti 2019/2020 Wizara yake imejipangaje kumaliza madai ya Walimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua kwa kuwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaomaliza darasa la saba imefikia milioni moja kwa mwaka, wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni laki tatu tu, laki saba wanabaki , umri wao ni mdogo ni miaka 12 – 14, hawawezi kufanya kazi ya uzalishaji. Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kundi kubwa hili haliishii mitaani, kunakuwa na vyuo vya VETA kila wilaya ili kupunguza ongezeko la wahalifu nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Spika, miradi mbalimbali ya ujenzi wa viwanja vya ndege inaendelea katika Mikoa mbalimbali kama vile Msalato, Tabora, Kigoma, Mpanda, Mtwara, Shinyanga, Kilimanjaro, Sumbawanga, Arusha, Songwe na Mwanza. Kazi kubwa zinazofanyika katika miradi hiyo zinajumuisha ujenzi wa barabara za ndege, upanuzi na ukarabati wa maegesho ya ndege, ujenzi wa vituo vya waangalizi wa hali ya hewa, ujenzi wa barabara za kuingilia viwanja vya ndege, uboreshaji wa viwanja hivyo pamoja na ujenzi wa majengo ya abiria na mizigo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi zote hizo zinazoendelea bado kuna matatizo makubwa ya viwanja vingi kukosa uzio, tumeshuhudia Kiwanja cha Ndege cha Mwanza mtu aliyekatisha ndani ya kiwanja wakati ndege inaruka na kusababisha ajali. Lazima Serikali ihakikishe kila kiwanja cha ndege kinachojengwa na uzio unajengwa kuepusha madhara yanayoweza kutokea kwa wanyama na binadamu wanakatisha ndani ya kiwanja hata Kamati ilipotembelea Kiwanja cha Dodoma mbwa alikatisha.

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF ulianzishwa na Serikali kwa Sheria Na. 11 ya mwaka 2006 ukiwa na lengo la kupeleka huduma ya mawasiliano maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara. Mfuko huo umejitahidi kupeleka huduma hiyo lakini bado maeneo mengine yasiyo na mvuto wa kibiashara hayajapata huduma hiyo. Tunaiomba Serikali ifanye kama kusudio la sheria iliyoanzisha Mfuko huo lilivyo ili Watanzania wote huduma hiyo kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika,, Mradi wa Liganga ni miongoni mwa miradi ya kimkakati na ulianzishwa kwa lengo la kujenga kiwanda cha kufua chuma. Utekelezaji wa mradi huu umechukua muda mrefu, takribani miaka nane bado haujaanza. Kamati ilijulishwa na Wizara juu ya tathmini waliyoifanya katika bidhaa za chuma na kubaini kuwa vinakumbana na changamoto ya upatikanaji wa malighafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nia ya Serikali ya nchi yetu ya Tanzania ni kuwa nchi ya viwanda, kuna kila sababu kwa Serikali kuhakikisha inajipanga kukamilisha mradi huu wa Liganga ili chuma kinachopatikana iwe malighafi ya viwanda vyetu hapa nchini. Kwa kufanya hivyo, mapato yataongezeka na hivyo basi, tutakuza uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufikie malengo ya nchi yetu ya viwanda, Sekta ya Kilimo lazima iboreshwe. Hakuna viwanda bila kilimo. Hadi sasa Sekta ya Kilimo imesahaulika kabisa, pembejeo hazipunguzwi ruzuku ili wakulima wote wapate pembejeo na kwa kuwa asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali kwa utaratibu mpya, Serikali inapoteza mapato. Mjasiriamali ambaye alikuwa analipa ada/ushuru wa shilingi 500/= kwa siku kulingana na biashara yake, itamlazimu kwa mwezi kulipa shilingi 15/= ukizidisha kwa miezi 12 sawasawa na mwaka mmoja mjasiriamali huyu atalipa jumla ya shilingi 180,000/=. Kitambulisho hiki kinatozwa shilingi 20,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hesabu ya kawaida 180,000 – 20,000 = 160,000. Ukichukua wafanyabiashara wadogo wadogo, wapo wengi sana hivyo kwa kutumia njia hiyo Serikali inapoteza mapato makubwa sana. Serikali ijitathmini kuendelea na mpango huu au kubadilisha ili Serikali iendelee kupata mapato kutokana na tozo za mauzo ya ujasiriamali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzito wa Wizara ya Ulinzi, Serikali itoe fedha za maendeleo zilizoidhinishwa kwa ajili ya Fungu 38 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuhakikisha shughuli zote zilizopangwa na Wizara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amani tunayoiona hapa nchini ni kwa sababu mipaka yetu inalindwa vizuri, kwa kutotoa fedha za maendeleo kutasababisha Wizara hii isitimize wajibu wake kiurahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kulipa fidia kwa wananchi kwa maeneo yaliyochukuliwa na JWTZ na JKT na kutoa muda mrefu bila kulipa fidia jambo ambalo licha ya ucheleweshaji haki hadi wamiliki wameshafariki na hivyo kudhulumika. Ifike wakati Serikali isiwanyanyase wananchi kwa kiasi hicho. Kwa maeneo yote ambayo hadi leo fidia haijalipwa basi kwa bajeti ya mwaka 2019/2020 ilipe fidia zote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Spika, kuhusu mawakala wa pembejeo kwa msimu wa mwaka 2015/2016; Serikali haijawalipa fedha wasambazaji pembejeo na kila mwaka Wizara ya Kilimo inapitishiwa bajeti, ndani ya miaka minne bado Serikali imeendelea kuhakiki, kama siyo uonevu kwa mawakala hawa. Niombe wakati Waziri anakuja kuhitimisha nipate kauli ya Serikali kwa bajeti ya mwaka 2019/ 2020 italipa madai hayo.

Mheshimiwa Spika, kuchelewa kwa upatikanaji wa mbolea kwa wakati na isiyo bora; ni kwa muda mrefu sasa ndani ya nchi yetu mbolea inachelewa kupatikana kwa wakati ili mazao yaweze kupatikana. Azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda haiwezi kutimilika kama kilimo kitafanyiwa mzaha.

Mheshimiwa Spika, asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima, wanatakiwa wapate mazao ya kutosha ili waweze kusomesha, kujitibu na kadhalika, lakini wakulima hawa wanalima bila msaada wa Maafisa Ugani, Serikali haioni kuwa imewaacha wananchi walime kilimo cha mazoea kisicho na tija, kwa kufanya hivyo hatuwezi kushindana na nchi za Umoja wa Afrika Mashariki, ina maana Tanzania tutabaki nyuma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 tembo walishambulia mashamba ya wananchi ya Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Kilolo, Kijiji cha Mgowelo ambapo zoezi la kuhakiki lilifanyika lakini hadi leo hii hawajalipwa na uharibifu ulikuwa mkubwa, hakuna mwananchi aliyeambulia kitu chochote, wananchi hawa walipata shida kubwa sana ya chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ipo wazi shida ya kutowalipa watu hawa ni nini? Kwa kuwa ni haki yao kulipwa, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa mwenye dhamana wakati wa kuhitimisha hoja ya Wizara hii atoe majibu juu ya hatma ya wananchi hao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa Mamlaka ya TPDC bado inakabiliwa na changamoto za madeni na ukusanyaji usioridhisha na wadaiwa. Kwa taarifa ambazo zinaonesha kuwa hadi kufikia Juni 30, 2018, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania hasara ya shilingi bilioni sitini na nne na milioni mia tano arobaini na tatu (64,543,000,000) limepata.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo shirika haliwezi kujiendesha kibiashara. Nimwombe Mheshimiwa Waziri ni wakati wa kuwa na mpango mkakati wa kuhakikisha wanalisaidia shirika hili madeni yote yanalipwa ili liweze kujiendesha kibiashara kwa manufaa ya Taifa.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ukusanyaji duni wa mapato unavyoathiri utekelezaji wa bajeti ya Serikali unatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeonesha udhaifu na uwezo mdogo wa ukusanyaji mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitakiwa kukusanya shilingi trilioni 17.315 badala yake, ilikusanya shilingi trilioni 15.386 ikiwa ni pungufu ya shilingi trilioni 1.929.

Mheshimiwa Naibu Spika, natolea mfano wa ukusanyaji wa kodi za majengo, nikuombe Waziri jaribu kuandaa mfumo wa kushirikisha Serikali za Mitaa yaani maafisa wa TRA wawatumie watendaji wa mitaa kwa kuwa wlae watendaji wa mitaa kazi zao za kila siku wako mitaani nyumba kwa nyumba, zoezi hili litaleta mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mfumo wa kodi umekuwa ukilalamikiwa sana kwa miaka mingi na jamii ya wafanyabiashara ambao ndio walipa kodi si shirikishi wala si rafiki, jambo ambalo limesababisha kukwepa kodi na hivyo kupunguza wigo wa walipa na mapato ya Serikali, nikuombe Waziri wa Fedha maeneo ya muhimu unda Kamati Maalum ziangalie kama tatizo hili bado linakuwa ili litafutiwe uvumbuzi.