Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Susan Anselm Jerome Lyimo (28 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili niweze kuchangia katika Mpango huu. Niseme kwamba Serikali haijajipanga, kwa sababu kwa muda mrefu tunakuwa na Mipango lakini haitekelezwi na inachosikitisha ni kwamba Waziri Mpango kama jina lake lilivyo, ndiye aliyekuwa anatuletea Mipango ya siku za nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme, kwa kweli tatizo kubwa Tanzania inajulikana dunia nzima kwa mipango mizuri sana lakini haitekelezeki. Tulikuwa na mipango mpaka inachukuliwa na nchi nyingine inakwenda kutekelezeka lakini kwa kwetu ni tatizo. Vilevile tatizo kubwa ambalo naliona ni kwamba, hii Mipango haipimiki, haina viashiria ni jinsi gani inapimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwa mifano, ukiangalia kwenye suala la kilimo ni kwa kiasi gani wameweza kuoanisha Chuo cha Sokoine ambacho kinatoa wahitimu wa masomo mbalimbali ya kilimo na ni jinsi gani wamewahusisha na wakulima. Leo hii tukiulizwa takwimu za wakulima hapa Tanzania hatuzijui, wakulima wakubwa ni wangapi hatujui. Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya Serikali kuchimba zaidi na kuona ni jinsi gani wanapata data za kuweza kutusaidia mipango yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mipango mingine inachekesha. Tunajua Tanzania ni nchi ambayo geographical location yake yenyewe ni uchumi wa kutosha, bandari ya Dar es Salaam ingeweza ku-serve nchi zaidi ya sita ambazo ni land locked, lakini kwa jinsi gani tunatumia bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, leo tuna mpango wa kujenga Bandari ya Bagamoyo. Sasa unajiuliza hii ni mipango ya namna gani! Ukijenga Bandari ya Bagamoyo maana yake lazima ujenge na reli, kwa sababu huwezi kutoa mizigo bandarini kwa maroli, tunahitaji kuboresha bandari tulizonazo kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuboreshe Bandari ya Dar es Salaam, tuboreshe Bandari ya Mtwara na tuboreshe Bandari ya Tanga. Tukishaboresha hivi then kama tutapata pesa nyingi, ndiyo sasa tuanze mradi wa Bagamoyo. Kupanga ni kuchagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani Serikali ni lazima iweke vipaumbele vyake vizuri, kile kidogo tulichonacho tuhakikishe tunakitengeneza vizuri ili kuweza kuzalisha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye suala la elimu na nazungumza kama Mwalimu na mdau namba moja wa elimu. Kumekuwa na pongezi nyingi sana hapa ndani za elimu bure, lakini ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 - 2015 na ya mwaka 2015 – 2020, katika suala la elimu anasema sasa tutafanya elimu iwe bora, ubora wa elimu. Hapo hapo unazungumzia ubora wa elimu, lakini unaongeza wanafunzi kibao, mwalimu hawezi kufundisha, darasa lililokuwa na watoto 70, leo lina watoto 200, hakuna nafasi ya mwalimu kupita kuona watoto wanasoma kitu gani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema na siku zote nasema kwamba, suala la elimu bure ilikuwa ni kwenye Ilani ya CHADEMA. Tunashukuru mmechukua, lakini tatizo mme-copy na ku-paste, bila ya kutuuliza hivi ninyi mlikuwa mtekelezeje? Kwa hiyo, hili ndilo tatizo. Hivyo, nawaombeni sana mje CHADEMA au UKAWA muulize ilikuwaje, mlikuwa mmepangaje! Msirukie rukie mambo tu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania Education Authority (TEA), hili ni Shirika la Elimu ambalo kimsingi lingesaidia sana kuboresha elimu. Tulisema, pamoja na kwamba, tuna sheria ya kuunda hiyo taasisi ilikuwa itolewe 2% ya Bajeti ya Serikali ipewe hii Taasisi ili iweze kusaidia, lakini mpaka leo jambo hilo halijafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala zima la Mpango. Mimi kama mwanamke niseme mpango huu Mheshimiwa Naibu Waziri wewe ni mwanamke, Waziri simuoni. Huu Mpango haujagusia kabisa masuala ya kijinsia kwa upana wake. Hakuna kitu chochote kimegusa jinsia, wakati tunajua Tanzania na dunia kwa ujumla, wanawake ni wengi kuliko wanaume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuitake Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha kwamba masuala ya kijinsia yanaoanishwa katika huu Mpango. Jana alizungumza, sitaki kwenda kwa kina lakini niseme watoto wa kike wanashindwa kwenda shule. Kama kweli tunataka kuboresha elimu Mheshimiwa Waziri wa Elimu huko naye ni mwanamke anajua, watoto wa kike wanaanza wakiwa sawa au zaidi kwa idadi na watoto wa kiume wanapoanza darasa la kwanza, lakini unapofika sekondari watoto wa kike zaidi ya nusu hawapo shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatokana na sababu kwamba tumeshindwa kuwasitiri watoto hawa kwa kuwapatia towel zao kila mwezi bure. Kwa sababu wenzetu Wakenya wanafanya hivyo. Kwa hiyo, nadhani hili ni suala la msingi sana kama kweli tunataka huo usawa hawa watoto wamalize darasa la saba, wafaulu wafike sekondari na huko wafaulu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la afya. Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka wanawake zaidi ya 8,500 wanafariki, hii ni sawa na mwanamke mmoja anafariki kila saa. Kwa hiyo naomba sana, suala la afya ni la msingi na ndiyo sababu narudia pale pale kwenye suala langu la asubuhi, kama kweli hii nchi ina kipaumbele na inapenda wananchi wake, Serikali isingethubutu kuleta magari 777 kwa ajili ya uchaguzi, yale magari ya washawasha ambayo nimezungumza asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gari moja ni dola 250,000 mpaka 400,000 wakati mashine za CT-Scan na MRI bei yake ni hiyo hiyo na Hospitali ya Taifa kama Muhimbili haina, achilia mbali hospitali za mikoa. Sasa ni kwa nini hizo fedha hata kama ni mkopo zisingetumika kuleta CT-Scan katika hospitali zote za rufaa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndiyo nasema mipango yetu ndiyo hiyo mibovu namna hiyo. Saa nyingine unajiuliza hivi hawa watu wanafikiria kwa kutumia kitu gani! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iende ijipange vizuri, ituletee mipango yenye tija, mipango ambayo itahakikisha kwamba kweli inaleta maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la utawala bora na niombe niungane na wenzangu wote waliozungumzia suala la Zanzibar. Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, utakwenda kutumia shilingi bilioni tisa kama ambavyo tumeambiwa, sijui zinatoka Zanzibar, sijui zinatoka huku, whatever the case, kama kweli tunaka kuboresha elimu, watoto wetu wanakaa chini, dawati moja ni shilingi 100,000/=, ina maana tungeweza kununua madawati... (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naomba kuchangia Wizara hii muhimu sana kama ambavyo Mheshimiwa Zitto alivyosema, inachangia kwa zaidi ya one third.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nianze kwa kuzungumza masuala ya TCU na niseme kwa kweli uamuzi huo wa kuivunja umechelewa kwa sababu ni kwa muda mrefu sana nimeongelea suala la vyuo hivyo pamoja na Kampala, japo sijajua Kampala inaendeleaje. TCU, kwanza niilaumu sana kwa jinsi ambavyo imekuwa ikidahili vijana ambao wanajua kabisa hawana uwezo. Nilikuwa nataka Serikali ituambie nini hatma ya vijana hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa sababu kuna vijana 500 waliohamishwa kutoka kwenye Vyuo vya St. Joseph Songea na Arusha na hususani Arusha. Hapa nina barua ya TCU iliyoandikwa na Profesa Mgaya ikisema kwamba vijana wote waliokuwa kwenye vyuo hivyo, hii ikiwa ni pamoja na wale 500, watapelekwa kwenye vyuo vingine na vijana hao wamekwenda; na kifungu cha tano kinasema kwamba wanafunzi wote ambao ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itahamishiwa katika vyuo watakapokuwa wamehamishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza, vijana hawa wamehamia SUA toka tarehe 28 mwezi wa Tatu wengine wamehamia UDOM toka tarehe 9 mwezi wa Nne na wengine wamehamia Mkwawa. Hapa ninapozungumza, vijana hao hawajapewa hata shilingi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi kwamba wasichana wataathirika zaidi, lakini nazungumza kama mzazi. Watoto hawa kama kweli wamekaa miezi miwili plus hawajapata kitu chochote, tunategemea tunapa wanafunzi wa namna gani? Vilevile nalaumu sana vyuo hivyo, inawezekanaje Wakuu wa Vyuo hao hawawasiliani na Bodi ya Mikopo ili kujua kwamba hawa watoto wanaweza hata wakasababisha fujo katika vyuo hivyo kutokana na hali waliyonayo? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri unapokuja utuambie nini hatima ya vijana hawa kutokana na huu mwongozo uliotolewa na TCU?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba nizungumzie suala la Walimu, sitaenda kwa details kwa sababu kila mtu ameliongea. Ni wazi kwamba elimu bora lazima iletwe na Walimu lakini vilevile Walimu hao kinachofuatia ni vitabu na hasa vitabu vya kiada. Ni jambo la kusikitisha sana kuona kwamba ile change ya Rada ya shilingi bilioni 75 ambapo najua shilingi bilioni 55 zimeenda kwenye vitabu, lakini vitabu vilivyotengenezwa ni vitabu ambavyo haviwezi kabisa kusaidia watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbatia ametoa mifano nami sina sababu ya kuendelea kutoa mifano, lakini kama mtoto wa Darasa la Kwanza, la Pili na la Tatu hawa ndio watoto ambao kile anachoambiwa ndiyo hicho hicho ataendelea kukiamini maisha yake yote. Sasa kama kitabu nilichonacho hapa kimepigwa chapa mara saba lakini bado kina makosa makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimepigwa chapa mara ya kwanza 2000, 2004, 2006, 2007, 2009 mpaka leo ni mara saba, lakini bado ina makosa lukuki. Unaposema namba nzima ni moja mpaka 99 ni makosa makubwa sana, lakini ukiangalia humu ndani ni aibu. Unamwambia vitu 11 lakini unasema ni 10, kwa hiyo, mtoto yule ataendelea kujua ni kumi kumbe ni 11. Huyu mtoto atajuaje kuhesabu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haishii hapo tu, ndiyo sababu tunasema Wizara ya Elimu ina matatizo makubwa sana. Kwa kweli kwa kuwa Waziri Kivuli wa hii Wizara nimeelewa mambo makubwa mengi ya kipuuzi; inawezekanaje kitabu kitoe ithibati mwaka 2006, lakini kitabu kimepigwa chapa 2007, inawezekanaje? Unawezaje kutoa ithibati kabla ya kitabu? Kwa hiyo, haya ndiyo mambo tunayoyasema. Wizara ina matatizo makubwa sana. Hata ukiangalia hii Sera ya Elimu, ni matatizo makubwa, kwa sababu huwezi kusema mtaala au curriculum inafundishwa. Toka lini mtaala ukawa unafundishwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli tuna matatizo makubwa sana. Nami ninaamini hivi vitabu ambavyo vimepitishwa kote huko na kupata ithibati wakati vina matatizo maana yake ni kwamba wana makusudi kabisa ya kuua elimu ya Tanzania, kwa sababu vitabu ukitoka Mwalimu ndiyo kitabu. Kama vitabu vina matatizo, watoto wanapata nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la elimu kwenye shule zetu za msingi na Vyuo Vikuu, kuna tatizo kubwa sana katika elimu ya juu. Sasa hivi kuna watu wenye Masters na Ph.D Dar es Salaam na maeneo mengi, kazi yao ni kusaidia wanafunzi kufanya thesis.
Kwa hiyo, unakuta mwananfunzi anamaliza masters lakini has nothing in the brain. Wanafanya plagiarism ya hali ya juu. Naomba kujua kwa Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, hivi huyu bwana anayeitwa Msema Kweli alipotoa hiki kitabu cha orodha ya Mafisadi sugu wa elimu ambao wengine ni Mawaziri, Wabunge nakadhalika, hivi Wizara ilichukua hatua gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaona vitu vinatolewa hadharani halafu Wizara haichukui hatua, maana yake ni kwamba wanabariki watu waendelee kusoma bila kuingia darasani. Kwa hiyo, nataka Serikali ituambie, ni lini wanachukua hatua kwa watu ambao wanafanya masters na Ph.D? Yaani mtu anajiita Doctor, kumbe siyo Doctor, unaenda kwenye mikutano, aibu tupu! Haelewi chochote, hawezi language hawezi nini? Sisi wenyewe ndio tunaoharibu elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu hapa Tanzania ninavyojua mimi kama Mwalimu unaanza nursery kwa mwaka mmoja au miwili, unaenda shule ya msingi miaka saba, unaenda ordinary level kwa maana ya Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne, halafu unaenda advance level Kidato cha Tano na cha Sita then tertiary level, miaka mitatu mpaka mitano kutegemeana na na degree.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mfumo wetu wa elimu. Kinachonishangaza leo na Mheshimiwa Waziri aje atuambie, ni lini mfumo huu umebadilika kwamba mwanafunzi anamaliza Kidato cha Nne moja kwa moja anaenda Chuo Kikuu? Imeanza lini na kwa utaratibu upi? Kwa hiyo, nataka tuelezwe sasa mfumo wetu wa elimu nionavyo sasa hivi, tumeamua kwamba kutakuwa na elimu msingi ya Darasa la Kwanza mpaka Kidato cha Nne. Nataka kujua tu, kwa nini tuna wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Nne wanaenda moja kwa moja Chuo Kikuu kwa ajili ya degree? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumza ni suala la utafiti wamezungumza wengi lakini niseme kwamba tulishafikiria na kuamua kwamba angalau utafiti upewe one percent ya GDP ya pato ghafi. Kwa takwimu za pato ghafi la mwaka 2013/2014 ilikuwa ni shilingi trilioni 44, naambiwa sasa hivi limeongezeka sana kama shilingi trilioni 90. Kwa hiyo, niliamini kwamba utafiti na hapa nazungumzia COSTECH ambao ndiyo wana mwamvuli wa tafiti zote. Kwamba wangepata sawa na shilingi bilioni 440 kwa pato la Taifa la shilingi trilioni 44.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa wamepata ten billion sawa na 0.025 ya pato la Taifa. Sasa hawa watu watafanyaje utafiti kama hawapati fedha? Mbaya zaidi, vyuo vyetu vikuu; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa takriban miaka mitatu mfululizo hawajapata fedha za utafiti. Tunategemea kweli nchi hii itaendelea kuwa ya viwanda kama haiwekezi kwenye utafiti? (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, kwa hiyo nilikuwa nadhani tuna…
Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa
Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika hoja hii muhimu sana ya sekta ya afya, kwa kweli bila afya hatuwezi kuwa hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze sana hotuba ya Kambi ya Upinzani na ile ya Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii na Maendeleo kwa sababu ndiyo ukweli wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kuzungumzia statistics za Wizara na uhalisia wa mambo yanavyokwenda kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati hii.
Kabla ya kuanza kwa sababu Wizara hii pia inahusika na masuala ya maendeleo ya jinsia, nitoe masikitiko yangu kwa jinsi ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye anasema kwamba yeye ni balozi wa wanawake ameweza kukemea mambo yaliyotokea nje, lakini yaliyotokea humu ndani ameshindwa kukemea. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri kama kweli wewe ni balozi ungekuwa muwazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala zima la upungufu wa wataalam. Ni jambo la kusikitisha na nichukue fursa hii kuipongeza sana Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa jinsi ambavyo inafanya kazi kubwa ya kuboresha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha na nashangaa Serikali inakuwa wapi. Tumeambiwa na Benjamin Mkapa Foundation wametengeneza theatres tisa, wameshazikabidhi kwa Halmashauri, tena zile za mipakani Rukwa, Kishapu na nashangaa Mbunge wa Kishapu anayesema shapu lakini kwake upungufu wa wauguzi ni 86%. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, theatre hizi tisa zimekabidhiwa kwa Serikali ni tatu tu zinafanya kazi, sita zipo tu na kuna watumishi lakini hazifanyi kazi, sasa tunajiuliza hii Serikali ya namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni vibali, tuna wataalam wa afya 4,491 wame-graduate toka mwaka 2014 mpaka leo hawajapata ajira. Madaktari Wauguzi na wataalam wa maabara wako mitaani, lakini hapo hapo tunasema tuna ukosefu mkubwa wa watumishi, sasa tunajiuliza kuna tatizo gani? Vibali hivi vinaenda kumaliza muda wake tarehe 30 Juni, watu wako nje. Kwa hiyo, naomba tutembee kwenye maneno yetu, tufanye kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuje kwenye suala la dawa, hapa tunapoongea dawa muhimu yaani essential medicine tuna upungufu wa asilimia zaidi ya 87. MSD ambao wanaohitaji shilingi bilioni 21 kwa mwezi kununua dawa wanapewa shilingi bilioni mbili tu za dawa muhimu. Ina maana kwamba kwa mwaka wanatumia fedha za mwezi mmoja tu. Hii ina maana gani? Ina maana Watanzania zaidi ya asilimia 80 hawapati dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye suala la ukosefu wa watumishi na hapa nizungumzie lab technician. Tumetoka kwenye suala zima za symptom yaani mtu haangalii tu dalili zako kwa macho, inatakiwa upimwe majibu yatoke laboratory lakini tuna upungufu wa asilimia 100 kwenye maeneo mengi nchini hapa. Tunaambiwa mikoa ya pembezoni zahanati hazina wataalam hata mmoja. Kwa hiyo, muuguzi au daktari anaenda kwa kukuangalia tu unaeleza historia yako anakupa dawa, ina maana Watanzania wengi wanapata dawa ambazo labda siyo za magonjwa yanayowasumbua. Kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ambacho kinasikitisha zaidi ni data tulizopewa za wanawake wanaokufa kila siku. Haiwezekani whether ni za Serikali kwamba ni wanawake 24 au hizo ambazo zinatoka kwenye National Bureau of Statistics kwamba leo wanawake 42 wanakufa kwa siku maana yake ni wanawake 1,300 kwa mwezi, kwa mwaka ni wanawake 15,000 sawa na wapiga kura wa Jimbo moja kule Pemba au Zanzibar. Hatuwezi kama akina mama kukubali hali hii iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu nchi hii ina uwezo, kama tuliweza kununua magari ya washawasha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia, kama tuliweza kununua magari ya washawasha 777 na ni 50 tu yalitumika kwenye uchaguzi na gari moja nime-google kwa Alibaba ambao ndiyo wanaleta magari lina gharama ya shilingi milioni 150 mpaka 400 lakini tuchukue wastani wa dola 300,000 kwa moja ina maana kwa magari 700 ni dola 210 milioni. Ukizipeleka kwenye hela za Kitanzania ni bilioni 420…
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Shilingi bilioni 420 kwa kata 3,990 tulizonazo Tanzania nzima zingeweza kupata ambulance. Nime-google ambulance moja ambayo tena ni advance inaenda kwa shilingi milioni 105, ukigawanya ina maana kila kata hapa Tanzania ingepata ambulance. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunajiuliza priorities za nchi hii ni zipi, ni afya ya Mtanzania au ni kitu gani? Kwa sababu nimesema magari 77 ya washawasha yangeweza kubaki, tunazungumzia yale 700 yaliyobaki yaani yangetosha kununua ambulance kila kata hapa nchini. Kibaya zaidi hayo magari ya washawasha yametumika 50 according to data. Sasa tunajiuliza hivi huu utaratibu ukoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mbwembwe sana, tukaambiwa kwamba CT-Scan imenunuliwa, hela zilizokuwa zifanye sherehe ya Wabunge zimenunua vitanda. Tumeenda Muhimbili ile CT-Scan ilitoka UDOM. Sasa watueleze hivi Wagogo na watu wengine wanaoishi Dodoma hawahitaji kutibiwa? Vilevile tunaambiwa hata vitanda vilitoka sehemu nyingine havikununuliwa. Sasa tunataka kujua zile hela za sherehe ya Wabunge zilienda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la Benki ya Wanawake. Kumekuwa na mazungumzo mengi hapa Bungeni kwa nini hatufungui matawi mikoani. Serikali hii hii ambayo iliahidi kutoa shilingi bilioni mbili kila mwaka kwa ajili ya hii benki hawajatoa. Mwaka huu ukiangalia kwenye kitabu cha maendeleo wametoa shilingi milioni 900. Tuliwashauri Wizara, Wizara hii ina taasisi kubwa nyingi, ni kwa nini taasisi kama ya Bima ya Afya, MSD, NIMR na nyingine wasipitishe fedha zao kwenye benki hiyo ili benki hiyo iweze kukua na kwenda mikoani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitika sana Mheshimiwa Waziri alivyomgombeza sana Mkurugenzi wa Benki hii lakini kwa kweli ukiangalia haiwezi kutoa riba nafuu kwa sababu haina fedha. Kwa hiyo, naomba kutoa pendekezo kwa Mheshimiwa Waziri kwamba ni lazima ifike mahali kama Serikali haina fedha iweze sasa kuchukua hayo mashirika niliyoyazungumza waweze kuwekeza fedha zao kwenye benki hii. Vilevile na Wabunge wanawake tunaweza kufungua akaunti kwenye benki hiyo ili iweze kwenda mikoani kusaidia akina mama ambao wanateseka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie sasa na suala la wazee. Naomba ni-declare interest mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Wazee wa CHADEMA Taifa. Wazee nchi hii wanajulikana kwa idadi lakini kibaya zaidi Sera ya Wazee imetungwa toka mwaka 2003 mpaka leo tunavyoongea miaka 14 baadaye hakuna sheria, hakuna kanuni, hakuna mwongozo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wazee wameteseka sana katika nchi hii, wameuwawa kwa sababu ya macho mekundu lakini hakuna sheria. Leo Waziri anasema mwezi wa tisa wataleta Muswada, tunakushukuru lakini tuseme tu kwamba umechelewa. Tunashukuru kwa hatua hiyo lakini ni kweli umechelewa. Tunaamini sasa huo Muswada na Sheria ikipitishwa, kanuni nazo zitatungwa mara moja ili wazee hawa waweze kuona kwamba wanaishi katika nchi yao kwa amani lakini wajue mchango wao katika nchi hii unathaminika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii. Kwanza kwa niaba ya wanawake wote Tanzania, Afrika na dunia nichukue fursa hii kumpongeza sana Fatma Samba Diouf kwa kuwa Katibu Mkuu wa FIFA kwa hiyo, nampongeza sana. Hii ni hatua kubwa sana kwa Waheshimiwa wanawake duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka tu naomba niseme mambo machache; la kwanza kuhusiana na ferry ya Dar es Salaam. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri alituambia kwamba ile ferry ilinunuliwa kwa shilingi bilioni 7.9. Nilikuwa naomba kujua leo hii ferry hiyo iko wapi? Kwa sababu, taarifa nilizonazo hiyo ferry sasa hivi haipo kazini! Nilikuwa naomba kujua iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la bajeti. Nilikuwa naomba Waziri anapokuja kutoa maelezo hapo anapo-windup atuambie inawezekanaje, tulipitisha bajeti ya Wizara hii nyeti sana kwa nchi yetu kwa shilingi bilioni 191 fedha za ndani kutoka Mfuko Mkuu, lakini mpaka Aprili 30, wametumia shilingi bilioni 607 zaidi ya asilimia 68 Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba maelezo ya kina inawezekanaje Wizara hii ipate fedha hizo na imezipataje wakati tuna matatizo makubwa kwenye Wizara nyingi ambazo hata asilimia 50 hawajafika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nililokuwa naomba kulichangia ni suala zima za nyumba za Serikali, limeongelewa sana. Nilikuwa naomba kujua, lile Azimio la mwaka 2008 kutoka kwenye maelezo binafsi ya Mheshimiwa Kimario mpaka leo limefikia wapi? Na je, mna mpango gani wa kuendeleza nyumba hizo au kuzirejesha, ili tujue wahusika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nizungumzie barabara ya Kinondoni, kutoka Mwenge mpaka Morocco. Nimefuatilia vitabu vya bajeti kuanzia mwaka 2013 mpaka leo, fedha ambazo zimeshatolewa ni shilingi bilioni 126, lakini barabara ile bado. Sasa nilikuwa naomba ilikuwa ni kuanzia Morocco mpaka Tegeta, lakini kwa awamu mbili; nilitaka kujua hizi fedha zimefika wapi kwa sababu mpaka majuzi hapa tulisikia Mheshimiwa Rais akisema kwamba anatoa zile fedha zilizokuwa za sherehe za Uhuru kwenda kujenga hii barabara.
Sasa nilikuwa nataka tu kupata maelezo, hizi fedha ambazo zimeshatolewa kuanzia mwaka 2013 mpaka leo ziko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana. Awali ya yote, nimpongeze sana Mheshimiwa Msigwa kwa hotuba yake nzuri sana pamoja na kwamba wengine imewakwaza lakini kwetu ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo ambalo limezungumzwa sana na niseme kwamba last time nilikuwa kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, suala la Chuo cha Diplomasia ni la msingi sana, wamezungumza wengi lakini naomba niende kwa maswali tu. Chuo hiki kilikuwa kipanuliwe na eneo walikuwa wanafuatilia kule Bagamoyo. Nataka Waziri anapokuja kujumuisha atuambie suala hilo limeishia wapi maana silioni mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la diaspora, ni jambo la kusikitisha sana. Bahati nzuri nimeangalia hotuba ya mwaka juzi, ya mwaka jana, hotuba ya mwaka 2014 inaonesha kwamba walikuwa wanafanya utafiti kujua Watanzania wangapi wanaishi nchi za nje, two years ago. Leo Mheshimiwa Waziri anatuletea taarifa kwamba Watanzania waishio nchi za nje wanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja. Tulitaka kujua idadi kamili ni wangapi ili tujue ni kiasi gani wanaweza kuleta nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Nigeria leo inaingiza dola za kimarekani bilioni 21. Sawa Nigeria ina watu wengi lakini Kenya jirani zetu, bilioni 1.4 mwaka 2015, Tanzania wanaingiza kiasi gani, hatuna kiasi. Kwa hiyo, kama walivyosema wenzangu nadhani hii Wizara diplomasia iko kisiasa zaidi lakini haiko kiuchumi Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine na tulilizungumza sana ni suala la kuhakikisha kwamba Mabalozi wetu wote walioko nje ya nchi wanakuwa angalau na mkutano mmoja ili wajue huko kwingine kuna fursa kiasi gani wakae pamoja wapeane taarifa. Nina taarifa kwamba nchi nyingine wanafanya hivyo, nimekuwa Finland nimeona kila tarehe fulani Mabalozi wa nchi zote wa Finland wanarudi nyumbani ili kutoa feedback ya mambo gani au changamoto gani wanakutana nazo na fursa gani wanakutana nazo. Hapa Tanzania tuna utaratibu gani, ni mwaka gani Mabalozi wetu wote wamewahi kuitwa wakakutana ili angalau wazungumzie fursa na changamoto wanazozikabili ili tuone nchi yetu inaendelea kiuchumi zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha, nimepitia kitabu cha maendeleo, Wizara kubwa namna hii ina shilingi bilioni nane (8) tu fedha za maendeleo, unless kuna fedha nyingine. Ukiangalia hotuba ya Waziri anazungumzia suala la kupanua Balozi, kwa fedha zipi? Hizi ambazo tunazo tumeshindwa, ukienda kwenye Ubalozi wa Zambia ni matatizo, ukienda kwenye Balozi nyingine nyingi ni matatizo, bahati nzuri tumekwenda, ni matatizo makubwa, mpaka hata Ubalozi wetu Marekani ni shida. Kama mwenzetu Idd Amin aliweza kujenga jengo kubwa sana pale New York Tanzania tumeshindwa na alijenga miaka ile, ni jambo la kusikitisha, tunaendelea kupanga. Tulisema ni kwa nini makampuni kama NSSF, NHC wasiingie ubia na Serikali kupitia Wizara hii ili waweze kujenga nyumba huko nje lakini naona jambo hili nalo limekufa kifo cha kishujaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma akiwa Waziri Membe mwaka 2014 na huko nyuma tuliongelea sana suala la dual citizenship (uraia pacha) lakini leo halionekani mahali popote na ni kama vile limekufa. Mheshimiwa Waziri anajua watu kwenye Diaspora walilalamikia sana suala hili la uraia pacha na tukawa tumeambiwa na Mheshimiwa Membe kwamba jambo hili linafanyiwa utafiti, litaendelea kushughulikiwa na litaingizwa kwenye Katiba iliyokuwa inapendekezwa lakini leo hakuna kitu, sasa tuwaeleweje jamani? Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba tujue status ya uraia pacha ikoje sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumza ni kwenye masuala ya ndoa. Tunajua kwamba ukiwa mwanaume Mtanzania, ukioa raia wa nje automatically yule mama anakuwa raia wa Tanzania lakini mwanamke wa Kitanzania akiolewa na mzungu au mtu mwingine ni tatizo kubwa. Sasa tunaomba kujua hii double standard inakuwaje kwa sababu hawa akinamama wananyimwa haki yao ya msingi. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la mjusi (dinosaur). Wizara hii pamoja na mambo mengine inashughulikia pia masuala ya kiutalii, huduma za jamii, elimu na kila kitu. Tuliambiwa kwamba yule dinosaur akiletwa hapa kwenye hili jengo hataenea, hiyo siyo issue yetu wala siyo hoja. Hoja ya msingi tunataka kujua, toka huyu mjusi amepelekwa huko Ujerumani ameingiza kiasi gani na Wizara hii ikishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wana utaratibu gani kuhakikisha kwamba tunapata fedha? Suala kwamba hakuna jengo la kuweza kumweka halituhusu, ilitakiwa Serikali ihakikishe kwamba inatafuta sehemu ambapo huyo mjusi akija atawekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tupoteze fedha nyingi hivyo za kutoka nje, watu wanaenda pale maelfu kwa maelfu kumwangalia yule mjusi lakini Watanzania hatupati chochote. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri akishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wa-make sure kwamba wanatuletea utaratibu kidiplomasia ni jinsi gani huyo mjusi ama analetwa au Tanzania tunapata kiasi gani na hicho kiasi hakianzii leo, kinaanzia miaka hiyo waliyompeleka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilizungumzwa sana hapa Bungeni na Mheshimiwa Fatuma Mikidadi mpaka maskini na Ubunge hajapata. Kwa hiyo, ili kumuenzi mwenzetu hebu tuhakikishe hili jambo linafikia mwisho wake. Bahati nzuri ni Mbunge wa CCM kwa hiyo naamini suala hili litashughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee suala la itifaki. Siku za nyuma Bunge jipya linapozinduliwa tunakuwa na semina ya masuala ya itifaki ili Waheshimiwa Wabunge waelewe ni mambo gani yanatakiwa na yanakatazwa na tulikuwa tunaletea Chief of Protocol anatupa semina. Sasa hivi utaona mtu amevaa suti bado ina label anaingia Bungeni anaenda popote, utaona mtu ana begi lake bado lina nylon yuko nalo tu. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo kwa kweli kama Wabunge tunapaswa kuyajua siyo tu hapa na Wabunge wengi wanasafiri nje, wanaenda hivyo hivyo. Kwa hiyo, nadhani ni wakati muafaka watuhakikishie kwamba hilo jambo linafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni suala la mtangamano wa Afrika Mashariki. Nilikuwa naangalia hivi ni lini tutafikia huo mtangamano wa Shirikisho la Afrika Mashariki kama kila leo tunaongeza nchi. Mimi najua kuna wengine wakiulizwa ni nchi ngapi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watasema ni tatu, nne, tano na wengine watasema sita. Naomba kujua Sudan tayari imeshakuwa member au haijawa, maana yake mimi hata sijui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaangalia vigezo gani, maana nilikuwa nafikiri, pamoja na geographical location lakini vilevile masuala mazima ya tabia yaangaliwe. Kwa hiyo, nadhani imefika wakati sasa tuangalie mambo haya. Pia napenda kujua ni nani wanaotoa kibali cha nchi kuwa ndani ya shirikisho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kwanza ili niweze kuchangia hoja hizi tatu muhimu sana ambazo kimsingi zinahusiana na maisha ya Mtanzania. Kipekee nitajikita zaidi kwenye masuala ya elimu, lakini sitaacha kuzungumzia masuala ya UKIMWI, madawa ya kulevya pamoja na masuala ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na masuala ya madawa ya kulevya; hapa kwenye Bunge lako Tukufu mwaka 2005 tulipitisha Sheria ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na sheria ile ilianzisha Mamlaka ambayo pamoja na mambo mengine ni pamoja pia na kukamata (ku-arrest) pamoja na kushikilia mali zao. Hivi karibuni tunaona ni jinsi gani mamlaka hii inaingiliwa; Mkuu wa Mkoa anaamua tu kutaja majina ya watu bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuliambiwa Mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa na majina hayo na vile vile tukaambiwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Kitwanga amepewa majina hayo. Ni kwa nini tume hiyo au mamlaka hiyo isishughulikie majina hayo ili tupate uhakika wa nani anatumia madawa ya kulevya. Ni kweli kwamba janga hilo ni kubwa sana, lakini lazima utafiti wa kina ufanyike, kwa sababu mtu na brand yake na kujijengea jina ni kazi kubwa lakini kulifuta ni jambo la haraka sana. Kwa hiyo, naomba utaratibu wa kisheria ufuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu. Mambo mengi yameongelewa, lakini niseme tu, ni wazi kwamba elimu ndio msingi wa Taifa lolote; hakuna Taifa duniani hapa lililoendelea bila kuwekeza kwenye elimu. Hata hivyo, kwa muda mrefu nchi hii imekuwa ikichezea elimu sijui kama ndio sera ya Chama cha Mapinduzi lakini kwa kweli inasikitisha sana. Amezungumza Mwenyekiti wa Kamati kwamba, Tanzania mfumo wetu wa elimu ni matatizo makubwa sana; hakuna nchi duniani yenye mifumo zaidi ya miwili katika elimu; Tanzania ndio nchi pekee yenye mifumo miwili ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kuwe na shule za msingi ambazo medium of instruction (lugha ya kujifundishia na kujifunzia) ni Kiswahili wakati shule nyingine za level hiyo hiyo medium of instruction ni kiingereza. Pia tukiangalia tuna elimu za aina mbili; tuna elimu bure na elimu inayouzwa na matokeo tumeyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii shule iliyokuwa ya kwanza Tanzania Feza ambayo wanalipa takribani milioni tano wanafunzi wametoka na division one na division two; division one 56 na division two wanafunzi watano au sita tu, lakini shule ya mwisho haina division one, two wala three, ina divison four wachache na zero zaidi ya 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia unaona wazi kwamba tuna matatizo makubwa sana ya mfumo wetu wa elimu na ndio sababu nitakuja pia na mapendekezo ya kuona ni jinsi gani tutaboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni kutokana na fedha kutopelekwa kwa wakati na hata zinapopelekwa zinakuwa zimechelewa; na haya yanajitokeza zaidi kwenye miradi mikubwa; na matokeo yake ni nini! Tuna miradi mikubwa ya hospitali; Hospitali ya Bugando tulitegemea kwamba wataweza kusimika mashine kwa ajili ya uchunguzi wa saratani; tunatambua kuwa kanda ya ziwa ina population kubwa sana; lakini jambo hilo halijafanyika; leo watu kutoka kanda ya ziwa wanakuja ocean road ya Dar es salaam; wakati huo huo tumekuwa na utayari wa kujenga airport Chato ambayo iko kwenye kanda hiyo hiyo ya ziwa. Kwa hiyo ni lazima tuangalie priority zetu ziko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali kwenye maeneo mbalimbali, lakini juhudi hizo ni za watu binafsi, wamekuwa wabunifu. Kipekee nimsifie sana Profesa Mohamed Janabi, amejitahidi sana kwenye Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na juhudi hizi binafsi bado Serikali haioni kuwa kuna haja ya kupeleka fedha nyingi. Leo Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete imepewa Shilingi milioni 500 tu kati ya Shilingi bilioni nne ambazo wanazihitaji; wakati tunajua kwamba huduma zikiboreshwa kwenye ile hospitali ni rahisi sana watu wetu kutibiwa ndani na kwa maana hiyo Serikali itaweza kupata fedha nyingi sana za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu, nadhani labda ile hospitali ibadilishwe jina iitwe JPM, Rais aliye madarakani sasa badala ya Kikwete labda sasa fedha zitakuwa zinatoka kwa sababu atakuwa madarakani. Naamini labda alivyokuwa Kikwete iliwezekana, kwa hiyo nashauri kwamba labda tukibadili jina likawa la Rais itasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzngumzia ni madeni ya Walimu, hili suala ni kubwa sana. Na-declare interest mimi ni Mwalimu. Katika kuboresha elimu jambo la kwanza la kuliangalia ni Walimu na si madarasa wala vitabu. Walimu wa Taifa hili wamedharauliwa kiasi cha kutosha, wamenyanyaswa kiasi cha kutosha. Haiwezekani leo Walimu wadai hata kama ni trilioni 1.06 au milioni 800; ni kwa nini hawalipwi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuulizane, kada gani nyingine hapa Tanzania ambayo ina madeni makubwa kiasi hiki? Yaani leo Mwalimu anaweza kwenda kituoni asilipwe mshahara kwa zaidi ya mwezi mmoja; nani anayeweza kukubali jambo hilo? Kwa hiyo, upole wa Walimu usiendelee kuifanya Serikali iache kulipa madeni yao na kuwafanya kama watu wa mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi ni hili suala la uhakiki. Mimi sielewi definition yake kwa sababu haiwezekani Walimu waitwe kwenda kusimamia mitihani, wamalize kusimamia mitihani, leo ni takribani miaka miwili wanaambiwa wanafanyiwa uhakiki. Hivi una mhakiki mtu kabla ya kufanya kazi au baada ya kufanya kazi? Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo tunaona yanaleta mushkeli katika elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze, na bahati mbaya sana Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa kamati, kwenye mapendekezo mwishoni kuna mengi hakuyasema lakini niseme; kuna suala la wanafunzi walioondolewa Chuo Kikuu cha Dodoma. Naamini kabisa kwamba kuondolewa kwa wanafunzi wale haikuwa bahati mbaya ilikuwa ni makusudi kwamba majengo yale sasa yawe wizara za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini nasema hivyo? Nasema hivyo kwasababu ukiangalia mwaka 2014 uliletwa Muswada wa Mrekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo hapa ili tuweze kuwaingiza wanafunzi ambao wataenda kusoma special education kwa ajili ya masomo ya sayansi. Leo hakuna Mbunge humu ndani ataniambia kwamba kwenye Jimbo lake hakuna shida ya walimu wa sayansi; na Mheshimiwa Jenista wakati huo Naibu Waziri wa Elimu alilihangaikia sana hili jambo, lakini leo wanafunzi wale wameondolewa, tunapewa sababu za ajabu ajabu, tunaambiwa walikuwa vilaza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoambiwa jambo, wewe mwalimu unapoambiwa kuwa wewe ni kilaza; kilaza kwa wale wasiojua hii ni terminology, na watoto wa University of Dar es Salaam huko nyuma, ni watu ambao hawaelewi chochote yaani wajinga. Kwahiyo, unapowaambia walimu wajinga…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Umemaliza, ni ya pili hiyo. Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja muhimu sana ya afya za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri tu kwamba na mimi ni Mjumbe wa Kamati hii, kwa hiyo mambo mengi yanayozungumzwa kwa kweli yananifurahisha na niseme tu kwamba Wizara inajitahidi, lakini Serikali inashindwa kupeleka fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kwa Taifa kubwa kama Tanzania, lenye watu zaidi ya milioni 50, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hii ndiyo ambayo imeshika jamii nzima nazungumzia hasa Fungu namba 53.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha kwa mwaka unaoisha Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii nikiondoa Fungu lile la Afya wametengewa fedha za maendeleo mpaka sasa hivi zilizoenda ni asilimia 2.3. Hii ni aibu kubwa mno, hivi tuaacha kuwaona watoto wa mitaani, tuaacha kuwaona watoto wadogo wenye mimba changa?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni Wizara inayoshughulikia wazee, niseme tu labda ndiyo sababu mvua hazinyeshi na zikinyesha zinanyesha za mafuriko, kwa sababu nchi hii ni kwamba tumelaaniwa na wazee. (Makofi)

Nimepita hapo nje kuna bango la Wizara ya Afya linasema “Mzee Kwanza,” na linasema “Mzee alikuwa kama wewe na wewe utakuwa kama huyo mzee.” Ajabu ukiangalia hotuba nzima ya Waziri ameongelea kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi hapa nina hotuba ya Waziri ya mwaka jana alizungumza na alisema mwaka huu wa wataleta Sheria ya Wazee. Mwaka huu hakuna chochote kinachozungumzwa kuhusu Sheria ya Wazee. Wakati Sera ya Wazee inapita toka mwaka 2003 leo ni mwaka wa 14, hakuna Sheria ya Wazee na ndiyo sababu leo wazee wanauawa kwa sababu hakuna sheria inayowasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa kuwa Mheshimiwa Waziri mwaka jana alisema na siyo mara moja, amekuwa akijibu maswali hapa kwamba sheria italetwa, leo kwenye kitabu chake chote hakuna jambo lolote linalozungumzia kuhusu sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wazee wa Taifa hili wamelitumikia Taifa hili wametusaida kuleta uhuru, lakini wazee hawa wametelekezwa. Makazi yao hayaeleweki, chakula wanachokula ni taabu, kubwa zaidi naomba Serikali sasa ituambie ni lini inaleta Sheria ya Wazee, ili wazee wa nchi hii waweze kujua haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Wizara ya Afya. Wizara ya Afya, afya ndiyo jambo la msingi, afya ndiyo utajiri kama ambavyo Mahatma Gandhi amesema. Utajiri namba moja ni afya zetu wananchi. Unapokuwa na afya njema ndiyo unaweze kujenga Taifa. Afya za Watanzania ziko mashakani na ninasema hivi kwa sababu fedha hazijaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali kama ya Muhimbili ni hospitali ya Taifa, ilikuwa inaomba shilingi bilioni tano kwa ajili ya vifaa tiba hawajapewa hata senti tano. Hospitali ya KCMC imeomba shilingi bilioni nne hawajapewa hata senti tano. Hospitali ya Bugando kwa ajili ya mashine ya Kansa haijapewa fedha, tunategemea nini? Kubwa zaidi Hospitali ya Jakaya Kikwete ambayo inafanya kazi kubwa sana ya kutibu wagonjwa wa moyo, ambayo inasaidia sana kupunguza gharama za kwenda nje, lakini taasisi ile haijapewa fedha. Pamoja na kwamba Mawaziri inawezekana wanajitahidi sana, lakini fedha hakuna. Tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kama mwaka jana tulitoa shilingi trilioni 28 zimeshindwa kwenda japo asilimia 50 za fedha za maendeleo, leo tunaongeza tunasema shilingi trilioni 33 hizo hela zinatoka wapi. Kwa hiyo, jambo ambalo linashangaza hata zile fedha zetu za ndani bado haziendi tatizo liko wapi? Au mnatudanganya kwamba mnakusanya sana lakini fedha hazipo. Hili jambo kwa kweli linatutia wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ninapenda kuzungumza ni suala la madaktari walioajiriwa juzi. Hapa nina barua mbili kutoka TAMISEMI kwa ajili ya hawa madaktari. In fact, walikuwa waje Dodoma Chuo cha Mipango kwa ajili ya semina elekezi na wafike kabla ya tarehe nane, baadaye kuna barua nyingine inasema waende moja kwa moja. Hii imetoka juzi tarehe Mosi, waende moja kwa moja kwenye vituo, jana tena Dkt. Chaula ameandika barua nyingine waende moja kwa moja kwenye Halmashauri, huko kwenye Halmashauri watafutiwe sehemu za makazi na fedha. Hivi najiuliza hizo Halmashauri tayari zimetengewa hizo fedha au mnataka hawa madaktari waende huko kama ambavyo walimu wanateseka, wanafika wanaolewa na Wenyeviti wa Mitaa au viongozi wa kata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana tunahitaji kweli madaktari, kama ambavyo Kambi ya Upinzani imesema, sielewi inawezekanaje Rais tu ndiyo aseme baada ya hao madaktari kushindwa kupokelewa kule Kenya, leo anatoa kibali kwa hawa madaktari 258. Je, hawa 3,000 walioko mitaani wanakwenda wapi? Ndiyo sababu Kambi ya Upinzani inasema je, huu siyo ubaguzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawa wasingekuwa wamejiandikisha kwenda Kenya ina maana leo wasingeajiriwa, kwa hiyo kuna haja ya Serikali kuwa na mipango thabiti ya ajira ya watu wake na siyo kusubiri watu waende mahali fulani, wanatakiwa kwenda nchi fulani wakikosa ndiyo Serikali inawapa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba hawa madaktari wamesomeshwa kwa gharama kubwa sana, kwa maana hiyo, ni lazima kama wanapelekwa mahali kwenda kufanya kazi maandalizi ya kina yawe yamefanyika ili wasije kuwa frustrated. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie nadhani hiyo ni bado dakika tano. Pamoja na kwamba nia njema haikuwepo ya kupeleka madaktari hawa, kwa sababu wote tunajua Kenya ina madaktari wengi kuliko Tanzania, World Health Organization inasema kwamba daktari mmoja Kenya anahudumia wagonjwa 16,000 wakati Tanzania daktari mmoja anahudumu watu 20,000. Kwa hiyo, hainiingii akilini ni sawa na mgonjwa yuko ICU halafu na mwingine ana nafuu unasema daktari ampe dawa yule mwenye nafuu amwache yule ambaye amezidiwa. Kwa hiyo, hili jambo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongelee suala la ndoa za utotoni. Pamoja na kwamba sheria yetu inakinzana lakini hatuwezi kuvumilia watoto wa kike wakiendelea kupata mimba za utotoni, maana yake ni kwamba Serikali inaruhusu mimba za utotoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunajua kuna watoto wengi wako mitaani, rai yangu ni kwamba lazima tulete sheria hiyo, tuipitishe na nina hakika Mheshimiwa Ummy ulikuwa mstari wa mbele katika hili naomba usirudi nyuma. Suala la imani kweli lipo, lakini tuangalie madhara makubwa ambayo wanayapata watoto wa kike na yameshazungumzwa mengi na wewe unayafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa kweli Serikali kupitia Wizara hii na Wizara ya Sheria na Katiba walete sheria hiyo ili tuibadilishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni kuhusu Benki ya Wanawake. Ukiangalia katika randama benki hii ilikuwa inatakiwa kila mwaka ipewe shilingi bilioni moja, bado Serikali imetoa kwa mwaka huu shilingi milioni 69.

Jamani hivi kweli tunataka kuwawezesha wanawake mdogo wangu Mheshimiwa Ummy? Kama hii benki kwanza moja ipo Dar es Salaam na sehemu chache sana, tunataka benki hii iende maeneo yote. Wanawake ni wengi sana nchi hii na wanaume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani pamoja na Kamati yangu ya Maendeleo ya Jamii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili na mimi niweze kuchangia katika hoja muhimu sana ya elimu kwa sababu naamini wote humu ndani tunatekeleza majukumu yetu kwa sababu ya elimu. Hakuna Mbunge ambaye hajaingia darasa la kwanza awe yumo humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimesikitishwa sana, sana, sana na maneno aliyosema Mheshimiwa Salma Kikwete, ni mwanamke mwenzangu, lakini sishangai kwa sababu hata mume wake aliwahi kusema kwamba watoto wa shule wanaopata mimba ni viherehere vyao. Nimesikitishwa zaidi kwa sababu Waheshimiwa Mawaziri wote wawili ambao ni wanawake nao pia walikuwa wanapiga makofi. Jambo hili linasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo sababu naamini kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri alivyokuwa anajibu swali la Mheshimiwa Mama Sitta hapa Bungeni ilikuwa ni kiini macho tu, kwa sababu alisema by March angeleta mwongozo huo na hii ni Mei hajaleta na leo anampigia makofi Mheshimiwa Mama Salma Kikwete. Hii inaonesha ni jinsi gani humu ndani watu ni wanafiki, hawaishi/hawatembei katika maneno yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa hapa Tanzania tunataka tuwe na elimu jumuishi au elimu shirikishi kwamba kila mtoto asome.

TAARIFA...

MHE. SUSAN A. J LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sipokei taarifa yake kwa sababu nilikuwa nam-refer Naibu Waziri aliyetoa majibu humu ndani na leo anamshabikia Mheshimiwa Mama Salma Kikwete ambaye anaenda kinyume na kitu ambacho alikisema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la vitabu, nililianza juzi na bahati mbaya sikuwa na muda lakini nashukuru sana Mheshimiwa Doto Biteko ameliongea. Niseme ni wazi kwamba hapa ndani au katika Bunge lako baadhi ya Mawaziri wanaleta utani. Suala la vitabu ni zito sana. Wote tunatambua kwamba nchi hii ina ukosefu mkubwa wa Walimu na kwa maana hiyo vitabu vingekuwa vimetengenezwa vizuri watoto wangeweza kuvisoma na kuvielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo ambalo linasikitisha Mheshimiwa Waziri anasema watawachukulia hatua, tunataka kujua toka mwaka jana wakati tumekuwa na tatizo hili, amewachukulia hatua watu kiasi gani? Jambo hili linasikitisha kwa sababu leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ndiye aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu. Kwa hiyo, ina maana hivi vitabu vibovu vimetengenezwa chini yake lakini leo amekuwa elevated kuwa Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea suala la Kiingereza nchi hii, tunajua watoto wadogo ni tabula rasa kile wanachokipata mwanzoni ndio kina-stick katika ubongo wao. Leo ukichukua kitabu hiki cha Kiingereza kwanza title yenyewe, ‘I learn English language’, this is not English. Hata hivyo, ukienda katikati ukurasa wa 127 kinasema, look at this insects lakini ua (flower) limewekwa kama ni insect (mdudu).

Sasa mtoto wa darasa la tatu unamwambia leo kwamba ua ni mdudu anakuwa anajua kwamba ua ni mdudu. Kuna huyu mtu anaitwa Dkt. Elia Y. Kibga ambaye ndiye Acting Director amesaini, ajue kwamba Mungu anamwona watoto wake hawasomi vitabu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya msingi ni kwamba hivi vitabu sio tu vina matatizo ya kimaudhui bali pia vina matatizo makubwa ya kimantiki. Tunaomba vitabu hivi viondolewe mashuleni lakini kubwa zaidi tunaomba Tume au Kamati Maalum iundwe ipitie vitabu vyote kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita kuona makosa makubwa yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo vitabu hivi vimeshasambazwa takribani nakala milioni 16. Kama kila nakala ni Sh.5,000 bado usambazaji maana yake tuna zaidi ya shilingi bilioni 100 tumezipoteza, hela hizi zingeweza kabisa kujenga zaidi ya madarasa 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba tunaomba kabisa Bunge lako Tukufu liunde Kamati/ Tume Maalum iende ikachunguze uchapishaji wa vitabu hivi. Pia isiruhusu Taasisi ya Elimu kuwa ndiyo inayotunga vitabu bali kuwe na chombo ambacho kitasimamia kuhakikisha kwamba vitabu hivi vinakuwa vizuri kwa ajili ya watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye suala la vitabu nije kwenye suala la ripoti ya CAG. Wote tunajua kwamba Mlimani City, nadhani kila Mbunge amepita pale, mkataba wa Mlimani City ni mbovu haijapata kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya CAG ya 2005 inaonesha wazi kwamba ilikuwa inatakiwa pale Mlimani City pawe na hoteli ya three stars lakini mpaka leo hii tunaongea baada ya miaka 14 hakuna hoteli imejengwa pale. Mbaya zaidi mkataba huo unasema kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinapaswa kupata 10% ya gross profit, lakini cha ajabu mpaka leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinapata 10% ya net profit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaleta hasara kubwa na ndiyo sababu leo tunazungumzia miundombinu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa mfano, Bweni Namba Mbili (Hall Two) limefungwa toka mwaka jana hakuna mwanafunzi yeyote anayekaa pale kwa sababu ya uchakavu. Hizi fedha zingeweza kusaidia kufanya ukarabati wa jengo lile. Kwa hiyo, tunaomba sana hii ripoti ya CAG ifanyiwe kazi ili mapato ambayo yanaenda kwa mmiliki wa Mlimani City yawe yanaenda 10% ya gross profit na sio ya net profit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo nataka Wizara itusaidie na hii pia inatokana na CAG ripoti. CAG ripoti inasema 94% ya shule zilizoanzishwa nchini zinatoa huduma bila ya kusajiliwa. Hata hivyo, ni Wizara hiyo hiyo inapoenda kusimamia shule za private hata kama umeongeza darasani mwanafunzi mmoja tu shule inafungiwa. Mtuambie ni kwa nini 94% ya shule hazijafanyiwa usajili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo sasa nije kwenye suala zima la ukaguzi, limezungumzwa sana na hata leo tumesema kwamba bila ukaguzi elimu yetu haiendi. Hata hivyo, fedha zinazotengwa kwa ajili ya ukaguzi ni kidogo sana..

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam maarufu kama Magufuli Hosteli. Pamoja na kwamba Waziri hajaeleza gharama halisi lakini inajulikana kwamba gharama za hostel zile ni shilingi billioni kumi, that means kila jengo moja ni shilingi milioni 500. Haiwezekani na haingii akilini na nimejaribu kuongea na wahandisi, haiwezekani jengo linachukua takribani wanafunzi 390 liwe lina gharama ya shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba CAG akafanye special audit kuona ni kiasi gani kimetumika na kama ni kweli ni shilingi milioni 500 mimi niko tayari nitatoa shilingi milioni zangu 500 Serikali inijengee jengo kama hilo ili tuweze kuwaweka vijana wengine, kabisa. La sivyo labda naweza nikasema pia naweza nikaachia Ubunge kama kweli jengo moja la ghorofa tatu limejengwa kwa shilingi milioni 500. Mimi naamini hii ilikuwa ni siasa na kama ni hivyo basi tunaomba hata hizi hela za vitabu zijenge hosteli nyingine katika vyuo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mloganzila, mimi niseme kwa mara ya kwanza Tanzania imejenga hospitali kubwa ya Kimataifa na imekamilika toka mwaka jana mwishoni lakini mpaka leo haijafunguliwa rasmi kwa sababu tu haina watumishi. Naiomba Serikali na namwomba Mheshimiwa Rais, kama alivyotoa vibali kwa wale madaktari walioshindwa kwenda kuajiriwa Kenya, atoe vibali ili hospitali ile iweze kufanya kazi. Kwa sababu hospitali ile ni kubwa sana, ina vifaa vingi sana na wewe Mheshimiwa Mwenyekiti kama Mjumbe wa Kamati umeenda umeiona lakini imekaa pale kama white elephant.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana hospitali ile ifanye kazi kwa sababu itaingizia Taifa kipato kikubwa kwa sababu wagonjwa wengi watatoka nje ya Tanzania watakuja kutibiwa pale, kwa hiyo vipatikane vibali kwa ajili hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ualimu. Najua mengi yamezungumzwa kutokana na matatizo ya walimu na mimi niseme kama mwalimu. Elimu ni mwalimu. Mwalimu akipata mazingira bora ataweza kufanya kazi yake vizuri lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipatia fursa hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye hoja muhimu sana ya bajeti kwa sababu bajeti ni suala la kisera na ndiyo sababu huwa tunakuja kuitungia Sheria ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba bajeti hii kwa kweli kama ambavyo wamesema ni ya kihistoria, kihistoria kwa maana gani? Wote tunajua kwamba Wabunge ni wawakilishi wa wananchi lakini jambo linalosikitisha wananchi hao wameachwa holela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa misingi ifuatayo. Nimeona Wabunge wa CCM wakishangilia sana bajeti hii na kubwa wanalozungumzia ni suala la kuondolewa kwa kodi ya barabarani yaani motor vehicle. Hata hivyo, ukiangalia kimsingi motor vehicle ni vyombo vinavyotumia moto lakini leo mwananchi wa kawaida anayetumia mafuta ya taa, kibatari kijijini anatakiwa akatwe shilingi 40 kila anaponunua mafuta. Kuna Mheshimiwa mmoja hapa amezungumza akasema sasa hivi tunataka kuondokana na air pollution kwamba leo wazazi wetu waliotulea kwa vibatari kijijini tunawaona hawafai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme Serikali basi ingeondoa kwanza mafuta ya taa wahakikishe kwamba wananchi wanajengewa nyumba bora na wapinzani tumekuwa tukiongea muda mrefu kwamba vifaa vya ujenzi vipunguzwe ushuru ili wananchi wengi waweze kujenga nyumba bora na nyumba hizo ziweze sasa kuwekewa umeme, ziweze kuwekewa gesi. Leo mwananchi wa kawaida hata nyumba ya tembe anaenda kukatwa kodi. Inaelekea labda wengine tunatoka maeneo mengine tofauti kwamba hatujui wapiga kura wetu ni wa namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Ndassa ambaye najua ni very senior Mbunge humu ndani, anatuambia kwamba Mheshimiwa Shabiby amesema nauli hazitapanda, sasa najiuliza hivi Mheshimiwa Shabiby yeye ndiye mpangaji wa nauli au ni soko huru? Soko ndiyo lina determine kama nauli itapanda au siyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, simple arithmetic, basi lilikuwa linalipa shilingi 300,000 kwa mwaka hiyo motor vehicle leo basi linalotumia lita 400 kutoka let say Mara mpaka Dar es Salaam ina maana lita hizo 400 akiongeza shilingi 40 kwa kila lita atalipa shilingi 16,000. Ina maana kwa mwezi mmoja tu ni shilingi 480,000, kwa mwaka gari linaloenda na kurudi ni zaidi ya shilingi milioni tano. Ndiyo sababu Serikali imeonyesha wazi kwamba watapata faida. Kwa hiyo, hili suala kwamba wenye magari mabovu watayaleta barabarani siyo hoja kwa sababu haiwezekani watu wote wenye magari mimi naamini wana uwezo hatuwezi ku-justify sisi wenye magari kuongeza shilingi 40 kwa kuwatesa wale ambao hawana magari na hawategemei hata siku moja kununua gari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeambiwa na Mheshimiwa Ndassa sijui kama yupo amesema kwamba tusome

TAARIFA......

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siipokei na kwamba ananipotezea muda tu. Mimi nazungumzia suala la kupanda sijazungumzia suala la kushuka, kwa hiyo, aendelee na Umakamu wake kama ameshindwa kuweka bajeti yake vizuri atulie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hoja yangu ya pili, Mheshimiwa Ndassa amezungumza hapa suala la kwamba wapinzani hatusomi vizuri, hatusomi between lines nikategemea anatuletea facts ni mambo gani ambayo ameona katika bajeti yetu hatujazingatia. Nataka kuwaambia tu kwamba pamoja na kwamba Serikali ina wataalam wa kutosha, sisi wapinzani tumegundua kwamba vitabu vyao vyote vina makosa. Pamoja na kuwa na wataalam wengi wenye Ph.D tunaona vitabu Volume I, II, III and IV ukija ku-totalize ni trilioni 23, ukija kwenye matumizi ni trilioni 26.9, ukija kwenye bajeti ya Waziri ni shilingi trilioni 31, sasa tunajiuliza kama mna wataalam wa kutosha kwa nini kuna hizi variance kubwa namna hii?

Kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri utakapokuja utuambie inakuaje mapato na matumizi yanatofautiana lakini vilevile bajeti yako kuu uliyotusomea nayo ina tofauti kubwa ya trilioni tatu, mtuambie hizi ziko wapi, mmezitoa wapi. Kwa hiyo, nadhani mtusifu kwamba sisi wapinzani tumesoma kwa kina, tukachambua kwa kina na tukaja na facts. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la property tax ambalo umelizungumza Mwenyekiti umesema kwamba TRA sasa wanazikusanya, lakini nataka niwaambie, naomba nitoe mfano wa Kinondoni Municipality ambayo mimi natoka. Mwaka 2015/2016 tulikuwa tumepanga kukusanya shilingi bilioni kumi na tukaweza kukusanya shilingi bilioni 7.5. Sasa hivi TRA wametuambia watatuletea shilingi bilioni mbili kwa mwaka huu unaoisha, lakini hawajaleta. Kwa hiyo, suala la own source ni la muhimu sana na tunasema kwamba own source ile five percent ya vijana na wanawake inatakiwa itoke mule sasa kama tunakausha hivi vyanzo vya mapato hawa wanawake na vijana wanapata wapi fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, tunaongelea suala la D by D, kama tunagatua madaraka, tunataka Serikali za Mitaa nazo ziweze kufanya kazi sawasawa na kule ndiko kuna wananchi, leo tunakausha vyanzo vyao tunategemea nini? Nataka nijiulize, nadhani labda Serikali tuelewane, kuna Decentralization by Concentration na Decentralization by Devolution, sasa tunaomba tujue sisi Tanzania ni D by D ipi tunayoitumia? Kwa sababu mimi ninayoiona tunafanya Decentralization by Concentration yaani tumeamua kupeleka mambo yote kule lakini hatupeleki fedha, tunanyang’anya tena kile kidogo ambacho walikuwa wanakipata, maana yake ni nini? Ndiyo sababu tunasema ni kweli hii bajeti ni ya ajabu, ni ya kihistoria sijui ni ya kijiografia nadhani tuongeze pia na ya jiografia siyo kihistoria tu kwa sababu inatisha yaani ni tishio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumekuwa na hoja ya kujisifia sana kwa suala la standard gauge. Nasema mimi kama Mtanzania ni kweli ningependa sana tuwe na standard gauge nchi nzima lakini naomba nije kwenye mahesabu maana yake twende kwa mahesabu. Hii standard gauge wakati tumefunga mkataba na Wachina ilikuwa watujengee kilometa 2,190 kwa dola za Kimarekani bilioni 7.6. Hii ina maana kila kilometa moja ingekuwa ni sawa na dola za Kimarekani milioni 3.4. Leo mkataba ule haupo, tumeenda kwenye mkataba na Waturuki na Wareno kwamba Wareno hawa na Waturuki ambao wanatujengea hiyo kilometa 205 kwa dola za Kimarekani bilioni 1.2 maana yake ni nini? Maana yake ukigawanya, simple mathematics ni kwamba kila kilometa moja itagharimu dola za Marekani milioni 6. (Makofi)

TAARIFA.....

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa iko kwenye maandishi, labda anazungumzia Serikali ya Awamu ya Tano, lakini nazungumzia Serikali iliwahi, hii taarifa niliyonayo labda nitaileta baadaye lakini natambua kwamba tayari kulikuwa na mkataba huo wa Wachina. Nilichotaka kuzungumza ni kwamba tulikuwa na mkataba zamani sasa hivi tunao huu wa Waturuki, hoja ya msingi, kama ilikuwa ni bilioni 3.4 leo ni bilioni sita maana yake ni kwamba tuna-save au tunapoteza? Hiyo ndiyo ilikuwa hoja yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, nchi hii ni ya wakulima na wafanyakazi. Nimeangalia Kitabu cha Hali ya Uchumi ni jambo la kusikitisha. Ukiangalia suala la kilimo tumesema kwamba kilimo ndicho ambacho kinaweza kusaidia viwanda lakini leo hii ukisoma kitabu hiki cha Serikali yaani mazao ya biashara karibia yote isipokuwa kahawa na mkonge tu ndivyo ambavyo havijashuka kwa asilimia ya uzalishaji. Sasa kama mazao yetu yameshuka kwa kiwango kikubwa namna hiyo, tunategemea viwanda vyetu vitapata wapi malighafi kwa ajili ya viwanda hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wanasema kabisa bila hata aibu kwamba Tanzania eneo lake la umwagiliaji hatujafikia hata asilimia kumi ya umwagiliaji na wanatoa sababu kwamba kwa nini kilimo kimeshuka, wanasema ni kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi.

Mimi nilikuwa naomba niulize Serikali mabadiliko ya tabianchi yapo siku zote, ukame upo siku zote lakini Tanzania ni nchi ambayo ina vyanzo vikubwa vya maji. Leo nchi ya Misri inategemea maji kutoka katika Ziwa letu Victoria inakuwaje tunashindwa kutumia maji yetu wenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tuna vyanzo vingi mno vya mito lakini hatuvitumii. Leo kuna mvua kunakuwa na mafuriko kila mahali lakini tunashindwa ku- tap yale maji ili yaweze kusaidia kwenye kilimo chetu halafu tunasema asilimia zaidi ya 80 ya wanawake wa Tanzania ni
wakulima, wanalimaje kama hakuna maji? Halafu hii ni nchi wanasema ni ya viwanda, hivyo viwanda ni vya namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yote wanatuambia kwenye kilimo wameweza kupeleka asilimia tatu tu ya bajeti halafu tunategemea nini katika nchi hii? Kwa hiyo, kwa kweli bado nasema hii bajeti ni ya kihistoria kwa sababu imeacha kabisa wananchi wake, imeacha kabisa kilimo, imeacha kabisa masuala ambayo yanawagusa wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la elimu. Ukiangalia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, mara zote wamesema huu ni wakati wa kuboresha elimu yetu lakini ukiangalia hakuna uboreshaji wa aina yoyote. Huwezi kuwa na elimu bora kama huna ukaguzi. Wenyewe wamekiri katika kitabu hiki, ukurasa wa 260 kwamba katika shule zao hakuna ngazi hata moja wameweza kufikia asilimia 50. Kwa maana hiyo bado elimu yetu itaendelea kuporomoka wakati tunajua kipaumbele cha Tanzania ni elimu na bila elimu bora hatuwezi kufika mahali popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nataka kuzungumza ni suala la hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Sijaona limezungumzwa popote na nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje atuambie, tunataka kujua mabweni yanayoitwa Magufuli Hostel ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yamejengwa kwa gharama za kiasi gani kwa sababu taarifa alizozitoa Mheshimiwa Waziri wa Elimu alisema ni shilingi milioni 500 kwa jengo la ghorofa nne jambo ambalo mimi binafsi sikubaliani nalo. Nilisema kama ni kweli ni shilingi milioni 500 niko tayari kutoa shilingi milioni tano…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi hoja hii mkono.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Kipekee naipongeza sana Kamati yangu ambayo inaitwa Guantanamo kwa kuwa ina vichwa vikali sana. Pia napongeza kwa taarifa nzuri, lakini vilevile Taarifa ya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza zaidi kwenye elimu kwa sababu mimi ni mwalimu, lakini vilevile nitagusia mambo ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi yeyote au jamii yoyote hapa duniani ambayo imeendelea bila kuwekeza kwenye elimu, lakini sekta ya elimu hapa nchini inakumbwa na changamoto nyingi sana. Changamoto ya kwanza hatuwezi kuwa na elimu bora kama walimu hawajapewa mahitaji yao. Kumekuwa na kilio kikubwa sana cha walimu na hapa Bungeni kila siku tumekuwa tukizungumza na hata leo maswali mengi huwa yanaelekezwa kutetea maslahi ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea, walimu walioajiriwa Januari hadi leo hawajapata mishahara wala fedha za kujimu. Hawa ni vijana wadogo wanaomaliza vyuo. Tunategemea vijana hao, hasa watoto wa kike waolewe na Wenyeviti wa Mitaa au waolowe na Wenyeviti wa Vitongoji? Kwa hiyo, hayo ni matatizo makubwa. Tunaomba Serikali ituambie, ni kwa nini wanaajiri watu halafu hawawapi mishahara wala posho za kujikimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa walimu ni kuhusu masuala ya madaraja. Niliuliza swali kwa Waziri Mkuu hapa kwamba watumishi...

T A A R I F A . . .

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wanaweza, lakini hiyo watakuwa wanaolewa bila ya ridhaa yao kutokana na matatizo hayo ambayo wanayapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu suala la madajara. Baada ya zoezi la kuhakiki, ndani ya mwaka mzima, baadhi ya watumishi pamoja na walimu hawakulipwa nyongeza hizo. Na sisi tunajua kabisa watumishi ni endelevu, kwa hiyo, hilo zoezi la uhakiki limewaathiri sana watumishi wa umma wakiwemo walimu. Tunaomba pia Serikali ituambie ni kwa nini katika zoezi hilo wamehakikisha kwamba mwaka mzima watu hawa hawajapata maslahi yao au nyongeza zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa sababu nimesema kwenye elimu bora, ni walimu, vitabu na mazingira bora ya kufundishia, utakumbuka kwamba wakati wa bajeti ya mwaka 2017 tulizungumza suala la vitabu vibovu, ikapelekea Kamishna wa Elimu pamoja na baadhi ya watumishi kusimamishwa kazi lakini mpaka leo tunavyozungumza na Waziri alisema itaundwa Tume, lakini mpaka leo kama ambavyo imeandikwa kwenye Kamati yetu, bado hatujapata report, lakini kubwa ambalo nataka kuzungumza, mpaka leo wanafunzi hawana vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleweke kwamba life span ya vitabu ni miaka miwili mpaka mitatu kwa darasa la kwanza mpaka la nne kutokana na matumizi, lakini vitabu vya mwisho vimekuwa published mwaka 2013. Leo ni mwaka wa tano bado hatuna vitabu na tunategemea wanafunzi hawa wafaulu. Wanafaulu vipi kama walimu hawana morale, lakini na vitabu navyo havipo ambavyo ndio sehemu kubwa kabisa ambayo watoto wangeweza kusoma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kuwe na Tume kabisa au Kamati ya Bunge ambayo itapita kwenye shule kuona kweli tatizo hili ni kubwa kiasi gani ili Wizara iwajibike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna suala kubwa tulizungumza na limezungumzwa kidogo, suala la re-entry policy. Naomba nirudie, tulizungumza, nikategemea Kamati inapotoa ushauri, maana yake wameona mambo mengi, lakini Serikali ikalipiga chini. Leo limekuja kwa mlango mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme hivi, Serikali hii ilitoa guidelines kwa jinsi gani wanafunzi hawa wanaweza kurudi shuleni. Hata hivyo lilikuwa diluted ikaonekana kwamba watoto wanaopata ujauzito ni wachache sana. Sasa najiuliza, kama ni wachache sana kwa nini wasirudi shuleni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mazingira mengi ambayo yanasababisha matatizo hayo. Kuna mazingira magumu sana yanayosababisha matatizo hayo ambapo Serikali nayo inayajua. Mazingira hayo ni pamoja na kubakwa, vilevile tunajua kwamba shule ziko mbali, watoto wanakienda shule wanapita maeneo magumu, wazazi ni masikini, lakini hayo yote hayajazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba tunaomba sasa ni kwa nini kama Kamati imetoa maelekezo yake au ushauri, mtu mmoja tu anaweza kuja akabadilisha the whole thing. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona mgongano mkubwa uliopo, pamoja na kwamba maombi ya re-entry, yaani warudishwe shuleni yamekataliwa, lakini hapo hapo, AG tayari Mahakama ilishatoa hukumu yake mwaka juzi (2016), kwamba ile Sheria ya Ndoa, kifungu namba 13 na 17 hukumu ikawa in favour, lakini AG hapa Bungeni akatuambia kwamba Serikali imekata rufaa na wakati kweli ilikuwa haijakata.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Serikali pamoja na kugundua kwamba AG amekata rufaa Septemba, 2017 yaani mwaka mmoja na miezi miwili baada ya hukumu; tulikuwa tunaomba AG atasaidie, hivi ni muda gani au ni time frame gani baada ya hukumu mtu anaweza kukata rufaa? Kwa sababu hii ni mwaka mmoja na miezi miwili, ndiyo AG ameenda kukata rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtuambie, kwenye Katiba inaonesha kwamba kazi za AG ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye anaishauri Serikali. Sasa naomba mje mtueleze, hivi kweli AG anatoa ushauri kwamba mtoto wa chini ya miaka 18 anaweza akaolewa at the same time mnasema mtoto asipate ujauzito. Mtoto aliyepata ujauzito, asirudi shuleni! Kwa hiyo, hii contradiction na tutaomba hii contradiction mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka kuzungumzia ni suala la mabweni yanayojulikana kama Magufuli Hostel kwa suala la expansion joint. Niliongea kwa muda mrefu, yale mabweni mlituambia yamegharimu shilingi bilioni 10, lakini wengine wanasema shilingi bilioni 53, lakini madhara yake tumeyaona. Mnatuambia expansion joint; mimi navyojua joint ni pale kwenye maungano. Sasa kama zimepasuka mpaka maeneo mengine kwenye makabati na wapi, joints hapo ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba kabisa CAG afanye utafiti na ukaguzi wa kina, aje atuletee ripoti, hayo mabweni yamegharimu shilingi ngapi? Kwa nini kumekuwa na huo mpasuko? Kwa nini aliyeripoti akapelekwa Polisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitaka kuzungumzia ni kuhusu matokeo ya mitihani ya kidato cha nne. Tumekuwa tukizungumza mara zote na kwa historia, nashukuru kwamba Kamati imeleta summary kwamba kwa miaka mitano na hata hiyo mingine, ufaulu haujawahi kuzidi asilimia thelathini kwa maana ya division one mpaka division three. Naamini ina maana division four na zero, hiyo ni sawa na zero tu.

Hawaendi popote. Kwa hiyo, ina maana asilimia 70 ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne kwa miaka yote, hawaendi popote. Halafu tunazungumzia ubora wa elimu. Ukiangalia, hiyo asilimia 30, asilimia zaidi ya 80 wanatoka shule binafsi. Halafu Serikali hii inawaambia watu wenye shule binafsi, ni marufuku watoto kukariri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishangaa hii Serikali, tumesema siku zote, haiwezekani Serikali ambayo ina shule zake, yenyewe iwe refa, iwe mchezaji, iwe kocha; haiwezekani. Tukasema ni lazima kuwe na chombo maalum kitakachosimamia hizi shule; na ndiyo sababu kumekuwa na ubaguzi mkubwa kwenye suala la ukaguzi katika shule za private. Wanalipa shilingi 5,000 kwa kila mwanafunzi, lakini kwenye shule za Serikali ni bure na ndiyo sababu hakuna ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni muhimu sana Serikali iangalie kwamba kuna umuhimu wa kuwa na chombo ili kudhibiti ubora wa elimu hapa nchini, na sio wao wenyewe wanasimamia, shule nyingine zinakuwa hazina hata vyoo, hazifungwi, zinaendelea, zinasajiliwa, lakini za private hazifanyiwi hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la afya. Kwenye suala la afya napongeza juhudi zote, lakini niseme tuna tatizo kubwa la watumishi wa Wizara ya Afya na wamekiri wenyewe kwenye kitabu chao kwamba wana upungufu wa asilimia 48. Sasa hivi wana asilimia 52 tu. Kwa hiyo, jambo ambalo linanishangaza, nadhani linawashangaza Wabunge wote, kwamba tuna ma- graduate kibao wako mitaani, tunahamasishwa tufungue Vituo vya Afya na Hospitali, lakini Hospitali hizo na Vituo vya Afya vinafungwa kwa sababu hakuna watumishi. What a contradiction? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nilikuwa nadhani Serikali ituambie, tatizo ni kwamba hawana fedha za kuwalipa? Kwa sababu madaktari wapo, lakini hawaajiriwi, watu wanaendela kufa, akina mama wanajifungua wanakufa, watoto wanakufa na watu wazima wanakufa. Kwa hiyo, nilikuwa nadhani mtuondelee hiki kitendawili kwamba kama Serikali inakusanya kodi kama ambavyo mnatamba, kwa nini mkose fedha za kuwalipa wataalam ambao watakuja kusaidia maisha ya wananchi wetu kwa sababu naamini hakuna Taifa lolote linaloendelea kama wananchi wake wana afya mbovu. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tuna kila sababu ya kuishawishi, kuiomba au kuishauri Serikali, ikahakikishe kwamba Watumishi wa Wizara ya Afya wanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la Mloganzila. Niseme tu kwamba ile hospitali ni ya kufundishia (Training Hospital). Tunaomba sana ibaki kwenye lengo lile lile, maana yake kulikuwa kuna maneno kwamba Hospitali ya Muhimbili ihamie kule na nini. Nadhani sisi kama Watanzania, ni lazima tu-think globally but acting locally.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vyuo vikuu vyote duniani vikubwa, vinakuwa na hospitali zake ambazo zina specialty. Hii yetu ya Mloganzila ina specialty yake ya moyo.

Hii ilikuwa ni kwa East Africa kwamba wagonjwa wa moyo wa kutoka Kenya, Rwanda na Uganda watibiwe hapa. Leo nasikia tayari kuna baadhi ya wagonjwa wa Mwaisela wameshahamishwa wamepelekwa kule, hali ambayo inafanya Madaktari wa Muhimbili watoke Muhimbili waende kutibu kule Mlonganzila, jambo ambalo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani lengo lile la awali libaki pale pale ili ile Hospitali hii ya Chuo Kikuu cha Muhimbili ibaki na malengo yaliyokusudiwa. Maana yake tutaonekana watu wa ajabu kwamba Uganda wao wanaendelea, sisi Tanzania ibadilike iwe hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati yangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hoja hii muhimu sana ya Wizara ya Afya, kwa sababu wote tunaamini kwamba hakuna Taifa lolote linaweza kuendelea bila afya na hata viwanda tunavyotaka kwenda kuvijenga kama Watanzania watakuwa na afya mgogoro ni matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Wabunge kazi yetu kubwa ni kuishauri Serikali, lakini jambo ambalo linasikitisha sana kazi kubwa pia ya kwetu ni kupitisha bajeti/ kuidhinisha bajeti, tukiamini kwamba bajeti tunayoipitisha inaenda kufanya kazi yake vizuri. Lakini ni jambo la kusikitisha sana kama tunaweza kupitisha bajeti ya maendeleo mwaka jana tulipitisha shilingi bilioni 785 lakini cha ajabu fedha za ndani ukiangalia ni asilimia 17 tu zimeweza kwenda. Kati ya hizo ni shilingi bilioni 64 tu ndani zimeweza kwenda sawa na asilimia 17.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo tunawezaje kusema kweli afya zetu zitaboreka. Katika hilo tunawezaje kwenda kusema kwamba hospitali zetu zinaboreshwa, vifaatiba vinanunuliwa, haiwezekani na wala haiingii akilini. Kwa hiyo, naona saa nyingine kwamba hakuna hata sababu ya kupitisha bajeti kama bajeti tunazozipitisha hazitoki hela zinakuwa kwenye makaratasi, lakini uhalisia hakuna, yet Bunge linatumia fedha nyingi Wabunge wake kwenda kukagua miradi, miradi ambayo hakuna hata shilingi moja tumeweka, nadhani hata hao watendaji wanatuona sisi ni watu wa ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitakuja kuomba mwongozo kuna sababu gani kweli ya Wabunge kukaa hapa miezi mitatu, tunapisha bajeti ambayo kiuhalisia haiendi kufanya hiyo kazi wala hela hazitoki, hizi hela huwa zinakwenda wapi? Kwa sababu kama TRA wanakusanya..., tunajua kwamba tunatumia recurrent bajeti, lakini haiwezekani hela za ndani ziende asilimia 17.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala nzima la afya ya mama na jana Mheshimiwa Kangi Lugola alisema kwamba tuwe na Ilani za CCM, nimejaribu kwenda kusoma Ilani ya CCM. Moja ya mambo ni kupunguza vifo vya watoto soma Ibara ya 85, lakini tunashangaa kama Ilani inasema ni kupunguza vifo na vifo vinaendelea vya akina mama maana yake hatuna sababu ya kusoma Ilani ya CCM labda tusome ya Vyama vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija pia kwenye fedha zilizotengwa mwaka jana zilitengwa shilingi bilioni kumi na mbili na milioni mia moja, mwaka huu wameongeza shilingi milioni mia moja lakini hawajatuambia zile shilingi bilioni kumi na mbili za mwaka jana zilienda chache sana. Ukiendelea kuangalia haya mambo najua Mawaziri wanajitahidi sana lakini wanafanyaje kazi kama hakuna pesa. Kwa hiyo, haya mambo kwa kweli ni kuyaangalia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaongelea wanawake wengi wanavyofariki, lakini sijajua nchi hii tumerogwa na nani, mimi naamini aliyetuloga ameshakufa na huko alikozikwa hatujui twende tukafanye matambiko. Leo Tanzania asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima lakini tunaambiwa kila dakika 12 mtoto mmoja anafariki kwa sababu ya lishe. Nimepiga mahesabu kama mtoto mmoja anakufa ndani ya dakika 12 ina maana kwa sasa moja wanakufa watoto watano, kwa mwezi mmoja watoto 3,600, kwa mwaka watoto 43,000 kwa uhai wa Bunge miaka mitano ni watoto 219,000. Hili ni janga la Taifa na ninadhani lazima kuwe na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba watoto wanawekewa lishe. (Makofi)

Mimi nina dakika kumi. Mheshimiwa Naibu Spika, twende kwenye suala la Wazee najua halijazungumzwa kwa sababu Wizara hii ni kubwa. Mimi nina declare interest kwamba ni Makamu Mwenyekiti wa Wazee Taifa wa Chama changu, kwa maana hiyo nina kila sababu ya kuzungumzia matatizo makubwa ya wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Serikali ituambie mwaka 2003 walipitisha Sera ya Wazee, kila nikisimama kuhusiana na masuala ya wazee nazungumzia huwezi kuwa na sera kama hatuna sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017 walikuwa na mkakati wa kufuatilia mauaji ya wazee, kama tungekuwa na Sheria ya Wazee maana yake ni kwamba haya mambo yangekuwa yamewekwa na vifo vya wazee vingepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua kwamba ni wazee watarajiwa, lakini wazee wa Taifa hili wameendelea kuishi kwa matatizo makubwa. Mlizungumzia kwenye ilani yenu kwamba wazee watapatiwa bima na kwamba watakuwa wanatibiwa bure kwenye vituo vya afya. Ninaisoma, Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 85(h) inasema; “Kuimarisha huduma za matibabu ya wazee nchini kwa kuwapatia vitambulisho na kuwatungia sheria matibabu yao ya bure ili waweze kutibiwa bure katika vituo vyote bila usumbufu wowote.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa kiasi gani mmetekeleza hili? Wazee wanapata matatizo makubwa sana, wazee wanadharaulika hawana hata hivyo vitambulisho, kama wanavyo ni wachache sana. Hii ndiyo Ilani yenu ya 2010/2015 hamjaitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, walisema kwenye ilani yao kwamba watanunua magari 10 kwa vituo 10 vya wazee; mtuambie ni vituo vingapi vya wazee hapa nchini vimepata magari?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizungumzie kuhusu suala la matatizo ya afya ya akili (Generalize Anxiety Disorders). Kwa Jiji la Dar es salaam mwaka jana watu 150 mpaka 200 walikuwa wana-report kwenye vituo kwamba wana matatizo ya afya ya akili, hiyo ni kwa Dar es Salaam, ina maana tatizo hili linaendelea kukua kutokana na hali ngumu ya maisha, kutokana na wasiwasi, hawajui kesho yao itakuaje. Hata hivyo hatuna wataalam wanaoshughulika na afya ya akili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba tuna hospitali kubwa ya Mirembe, tumewahi kwenda kutembelea pamoja na Kamati yangu matatizo ni makubwa sana, watalaam ni wachache sana. Hata hivyo pamoja na kwamba watalaam hawa wachache bado Serikali haijaona umuhimu na ndiyo sababu tumeona kwamba tuna tatizo kubwa la watalaam wa afya mabingwa. Tuna upungufu wa takribani mabingwa 500, na hatujaona mkakati wowote wa Serikali kuhakikisha kwamba tulikuwa na mabingwa hawa ili waweze kusaidia watu wetu. Leo tunapita barabarani tunaona watu wanatembea hawajielewi, Serikali ina mkakati gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la kwenda kutibiwa nje, na kwenda kutibiwa nje kuna process ndefu kama ambavyo hata Mheshimiwa Spika amesema hata wengine tumewahi kwenda nje. Hainiingii akilini, juzi nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Afya akizungumza na nitaomba baadae atupe majibu wkaati aki-wind up; anasema kwamba lazima uhakiki ufanyike, mimi nakubaliana naye. Hata hivyo anaposema yawezekana watu wengine wamekwenda tu kufanya plastic surgery; kubadili maumbile au kuongeza maumbile au kufanya vyovyote vile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata shida sana, kwamba inawezekana hawa wanaokwenda kufanya hivyo hawakupita katika utaraibu wa kawaida, ni vigogo. Mimi ninaamini wananchi wa Tanzania mpaka upate kibali cha kwenda nje ni hassle kubwa sana, lazima jopo la madaktari likae, waangalie, wajue ni ugonjwa gani. Sasa mimi ninaposikia Waziri anasema wengine wamekwenda kufanya mambo mengine ambayo ni kinyume mimi nashindwa kuelewa, na nitaomba aje atuambie ni kwa sababu gani na wizara yake imefanya nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia. Ni jambo la kusikitisha kwamba Fungu 53 ambalo ndilo la maendeleo ya jamii limepewa shilingi bilioni 4.9 tu; na mimi nadhani huku ndiko kwenye maafisa ustawi wa jamii nashani na ndiyo sababu hawa maafisa ustawi wa jamii imeshindikana sasa kazi hizo wapelekwe kwa Makonda kule Dar es Salaam na matokeo yake ndiyo haya. Kwamba wizara imeshindwa kufanyakazi yake vizuri inamkabidhi kazi hiyo Makonda na Makonda hana watalaam. Kwa hiyo, ninaomba sana Wizara hii fungu namba 53 lipewe fedha ili watoto wetu waweze kuthaminiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ya awali ili na mimi niweze kuchangia katika hoja hii muhimu ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba Wizara hii ukiangalia kwenye fedha za maendeleo ndiyo Wizara ambayo inapata fedha nyingi kuliko Wizara zote. Kwa sababu katika shilingi trilioni 12 za maendeleo Wizara hii ambayo najua ni Wizara kama tatu zina takribani shilingi trilioni 4.1 sawa na asilimia 33. Pamoja na kupata fedha nyingi kiasi hiki tunaona ni jinsi gani barabara zetu zinavyojengwa chini ya viwango na fedha zinaibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitajikita zaidi kwenye suala ambalo lililetwa na Mheshimiwa Kiwanga akisema kwamba Mkoa wa Morogoro hawakuwa na Road Board wala RCC na Mheshimiwa Zitto alitaka kusimama kuomba Mwongozo, lakini haikuwezekana. Huu ni mwendelezo wa jinsi gani Serikali inayosema ni Serikali ya wanyonge lakini kama kilometa nne zinaweza kujengwa kwa shilingi bilioni 13 wakati katika hali ya kawaida kilometa moja ni kuanzia shilingi milioni 700 mpaka shilingi bilioni moja leo tunazungumzia shilingi bilioni 13 na zaidi kwa kilometa nne, hii inamaanisha kwamba kilometa moja imejengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni tatu. Jambo hili tunaliona ni wizi mkubwa na najua Mheshimiwa Magufuli amekuwa akisema anapambana na rushwa.

Sasa tunaitaka Serikali na Waziri atakapokuja kutoa majumuisho jioni atuambie fedha hizi zimekwenda wapi na wahusika wamechukuliwa hatua gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni upanuzi wa barabara ya Morogoro. Haya masuala ya ubaguzi yakiendelea katika nchi hii tunaenda pabaya. Haiwezekani katika eneo moja la barabara, mimi ninavyojua barabara inapaswa iwe imenyooka na iwe na upana wa kufanana. Barabara ya Morogoro inapoanzia kule bandarini upana wake ni kama mita 35 mpaka 40; lakini inapofika Ubungo hasa maeneo ya Kimara barabara ile upana kwa pande zote mbili ni mita 121. Kwa hiyo, naomba kufahamu hivi barabara siku hizi inakuwa sawa na chatu aliyemeza mtu au barabara inapaswa iwe imenyooka? Tunaomba maelezo najua Mheshimiwa Naibu Spika na wewe unakaa kule na umeona ni jinsi gani watu wamebomolewa halafu zinapokuja kauli kwamba hawa wabomelewe au hawa wasibomelewe kwa sababu wamenipa kura, haya mambo hatuwezi kuyakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nije kwenye suala zima la hapa Dodoma. Inajulikana kwamba Wabunge wengi, Mawaziri pamoja na wewe mwenyewe tunakaa maeneo ya Area D. Ilikuwa kuja Bungeni tunatumia takribani dakika tatu au nne, ilikuwa ni kama kilometa moja na nusu lakini sasa hivi tunakwenda mwendo wa kilometa sita na tunazunguka kwenye maeneo hatarishi sana. Wengine ukifika kwenye ile shule na tunashukuru Mungu kwamba kuna ile shule pale ambayo tunaweza kupita kwenye miti mvua zikinyesha tunahamia pengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi najua kuna teknolojia ya kila aina, hivi ni kwa nini Mheshimiwa Waziri na niliongea naye wasichimbe barabara ya chini hapa airport ili magari yaweze kupita chini? Najua Mheshimiwa Waziri umetembea nchi nyingi haya tunayajua. Jana kuna mmoja alisema kwamba magari ya Wabunge yawe yanapita, lakini tujue kuna emergency landing ya ndege jambo ambalo ni hatarishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hapo ni nusu kilometa tu kujenga barabara ya chini ili magari yaweze kupita na hasa ukizingatia kwamba hata yale maeneo pale biashara zimekufa kabisa. Kwa hiyo, naomba sana jambo hilo lifanyike kwa sababu tunaona barabara nyingine ya kwenda kwa Waziri Mkuu kule inajengwa tulidhani hii ya hapa ambayo inapitisha watu wengi ingekuwa rahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la nyumba za TBA, nimesoma kwenye kitabu hiki, mimi nimekaa kwenye nyumba ya TBA huu ni mwaka wangu wa 11, haijawahi kukarabatiwa wala kufanywa chochote hasa ukizingatia miundombinu ya maji ni ile ya zamani sana na kwa maana hiyo tunahitaji wabadilishe miundombinu hiyo ili iwe ya plastiki. Mimi nashangaa kama wameshindwa kuzi-maintain hizi nyumba ni bora wawauzie Wabunge au watu wanaozihitaji waweze kuzi-maintain. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa kwamba TBA wanapewa vibali vya kujenga nyumba mbalimbali including zile hosteli za Magufuli ambazo zimekuwa na expansion joint ni kwamba hawana uwezo, lakini huku wanaendelea kupewa matumizi makubwa ya kwenda kujenga nyumba mbalimbali. Kwa hiyo, mimi niseme kwa kweli haya mambo haya tukiendelea kunyamaza kama wenyewe wanashindwa ku-maintain za kwao wanawezaje kwenda kujenga na huko kwenye kujenga tayari wameharibu. Kwa hiyo, nadhani TBA kuna tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie barabara ya kutoka Bahama Mama kwenda Chuo Kikuu. Barabara ile kwa kweli imesaidia sana lakini bado haijakamilika. Kwa hiyo, tunaomba kujua hii barabara ya Goba - Makongo mpaka Chuo cha Ardhi inaisha lini? Vilevile ile ya Msewe ambayo kwa kiasi kikubwa imeharibu sana mazingira ya Chuo Kikuu. Barabara za chuo kikuu zimekufa kabisa kwani zimekuwa na mashimo makubwa, tunaomba sana mmalize ili watu waweze kupita kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii muhimu na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu sana ya elimu hasa kipindi ambapo kumekuwa na changamoto nyingi sana. Nishukuru sana kwamba Wabunge wote nadhani tunakubaliana kwamba suala la elimu sasa hivi ni janga la Taifa kwa sababu tunashuhudia mambo mengi yanayotokea na kubwa niseme kwamba katika elimu siku zote nimesema mwalimu ndio kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwa masikitiko makubwa sana Serikali bado haijaliona hilo. Leo walimu wana matatizo lukuki, yamesemwa na wengi. Kuna suala la kupandishwa madaraja, haiwezekani mwalimu alitakiwa apandishwe daraja toka mwaka 2003 mpaka leo yuko pale pale ameenda kusoma bado hajapandishwa daraja na hawa ni wengi na ndiyo sababu takwimu zinaonesha kwamba takribani asilimia 70 hawana morale wa kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi mishahara yao bado lakini niseme tu kwamba lingine kubwa katika elimu ni vitabu na mitaala. Huwezi kuwa na vitabu mizuri kama huna mitaala mizuri. Mwaka jana kipindi kama hiki niliongea na watu na wengine walichangia kuhusiana na ubovu wa vitabu katika nchi hii, jambo ambalo linafanya watoto wetu washindwe kusoma vizuri. Kwa sababu tayari walimu hawana morale, kwa hiyo the only alternative tungekuwa na vitabu vizuri wanafunzi hawa wangeweza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kitabu kinachoitwa kitabu cha uraia na maadili bendera ya Tanzania, kitabu cha darasa la tatu, ile rangi ya manjano zinaonekana mbili kule wameweka nyeusi yaani leo bendera ya Tanzania mtoto mdogo ambaye ubongo wake ni tete na kila anachoambiwa kina stick bendera ya Tanzania imebadilishwa, nembo ya Tanzania haina zile alama za shoka hazipo. Bendera iliyopo na nitaomba mtuambie hii ni bendera ya nchi gani. Bendera yenye rangi za kijani mbili chini na juu hamna rangi ya blue na katikati rangi nyeusi na hizo njano naomba mtuambie hii ni bendera ya nchi gani? Ukija kutujibu utuambie Mheshimiwa Waziri na Naibu wako, mmewahi kukaa mkapitia hivi vitabu baada ya kuambiwa bilioni zaidi ya mia moja zilitumika mwaka jana na baada ya kuongea sana na aliyekuwa kamishina akaondolewa kazini; ninaomba kujua mmefanya mambo gani au utaratibu gani kama Waziri ni kweli umeona hivi vitabu wewe mwenyewe kama profesa umeviona hivi vitabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu cha kuandika darasa la kwanza mtoto ambaye katika elimu yake ya awali hajasoma kitabu hakuna kitabu chochote cha shule ya awali, hakuna, anaenda kuanza darasa la kwanza kuandika kitabu cha page 117 lakini mbaya zaidi anaingia la pili kitabu cha page 40; what a contradiction? Yaani wa darasa la kwanza ambaye ndio anaanza page mia moja na zaidi, wa darasa la pili page 40. Darasa la kwanza kuandika anaenda siku ya kwanza kuandika anaandika hii; hii anaandika kitu gani? Hili ni somo la kuandika au ni sanaa?

Mheshikmiwa Mwenyekiti, haya mambo haya ndio sababu tunasema hatuwezi kukuabaliana na hili jambo, Nataka Waziri aniambie, tulikuwa na kitu kinaitwa Educational Material Committee (EMAC) ambao hawa ndio ambao walikuwa wanahariri vitabu na committee ikavunjwa kutokana na mambo fulani, mimi naomba kujua baada ya Kamati hii kuvunjwa ni nani wame-replace na ni nani wanahariri hivi vitabu katika hali hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo sababu ninasema, na watu wamesema; na ninaomba Wabunge wote waende wasome andiko la Profesa Kasmili Lubagumya waone ni jinsi gani elimu yetu ni mbovu kuanzia huku chini na mimi sishangai university level wakishindwa kuandika barua, aidha ya kiswahili au ya kiingereza kwa sababu huku chini hawakufanya chochote. Huwezi ukaamini wanafunzi wa UDOM anaulizwa jina la Makamu wa Rais hajui. Sasa unajiuliza kama mwanafunzi hajui Makamu wa Rais wa nchi hii, mtoto wa darasa la kwanza la pili hatajua sisi tulivyosoma ilikuwa tunajua yaani kila kitu kilikuwa hapa. Sasa katika hali hii ninaamini Waziri mmeamua sasa kuchukua kwamba nchi hii tunaendeshwa na machivelian principle kwamba inaendelea kuzungumza kuhusu elimu bure. Naomba tusijitoe ufahamu, maana ya bure ni nini? Wakaanza ni bure tulivyopiga kelele wakasema bila malipo, lakini ukisoma kamusi bure maana yake ni kitu kinachotolewa bila malipo yoyote. Ukisoma hotuba ya Waziri Mkuu inasema hivi; “wataendelea kuchangia kwa hiari maendeleo ya elimu kupitia ofisi ya Wakurugenzi” na kwa wale watu wenye miaka yangu na nyuma tunajua Mheshimiwa Chenge ulisoma enzi hizo kwamba tulivyokuwa elimu bure ilikuwa hata kalamu hununui, daftari hununui ilikuwa sana sana ni uniform.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo mnapotuambia ni bure wakati michango inaendele haiwezekani na niseme tu kwamba ndiyo sababu shule za private zinafanya vizuri; na Mheshimiwa Waziri nilkuambia na ni rafiki yangu. Kinachofanyika wana kitu kinaitwa Teachers Parent Association yaani huwa utatu huo ndio unaosaidia mnakutana wazazi, walimu na wanafunzi, kama mwanafunzi ana tatizo linaelezwa lakini kwenye shule za Serikali sana ni le bodi ambayo inasubiria shilingi 500 jinsi gani inaenda kugawanywa shuleni, ni vurugu tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nadhani hili suala la elimu bure bado halijakaa vizuri na limeleta mkanganyiko mkubwa hivyo inaweza kwa kweli kurudisha maendeleo ya elimu nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala kubwa hili la mjadala. Sasa niseme, katika hizo changamoto zote nionaomba sasa, kwa heshima kabisa kwamba tumesema report zangu zote au speech zangu zote tumekuwa tukiongelea suala la anguko la elimu na sasa mnaliona. Mnamshukuru mzee Mkapa, pamoja na maneno yote aliyokuwa amesema dhidi yetu kwamba sisi malofa lakini leo ameona kwamba elimu yetu iko vibaya na kwamba tunaenda sasa kufanya kazi; na naomba muongoze huo mjadala ili tuhakikishe kwamba elimu yetu inaboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho nililotaka nilizungumze ni suala la TETRA. Sisi tumeongea kwenye hotuba zetu hiki chombo huru cha kusimamia elimu, haiwezekani, tumezungumza mara nyingi tukasema lazima tuwe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, unga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii japo fupi. Nitaanza moja kwa moja na TAMISEMI nami kama Mwalimu nitazungumza zaidi masuala ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ungeniuliza kipaumbele namba moja, mbili na namba tatu vyote ningesema elimu, lakini kwa masikitiko makubwa bado Serikali hii haijawekeza ipasavyo kwenye elimu. Ukiangalia takwimu sekta ya elimu mwaka jana bajeti inaisha kwa ujumla wake ilipata trilioni 4.7, lakini trilioni tatu zimeenda TAMISEMI kwenye sekta ya elimu, katika fedha hizo asilimia saba tu ndiyo inakwenda kwenye fedha za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba miundombinu ya elimu ambayo wote tunaipigania including nyumba za Walimu hazijengwi. Hii ndiyo sababu ukiangalia kwenye hii hotuba hawajaeleza upungufu wa nyumba za Walimu ni ngapi, wamesema tu nyumba za Walimu kwa mwaka huu zimejengwa 290.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya World Bank inaonesha kwamba tuna upungufu wa nyumba 186,000. Kama tuna upungufu wa nyumba 186,000 na kwa mwaka mmoja wameweza kutengeneza nyumba 290 maana yake tunahitaji miaka 500 kukamilisha kujenga nyumba za walimu hapa nchini. Hili ni jambo la aibu na halipendezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa mwaka huu ukiangalia, bajeti ya mwaka huu trilioni sita kwa Wizara hii, only one trillion ndiyo inaenda kwenye maendeleo, maana yake ni kwamba only 27% ndiyo inakwenda kwenye maendeleo, yet tunategemea shule, nyumba za Walimu na vyoo vijengwe na kadhalika. Hatuwezi kuwa na elimu bora kama fedha haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanazungumzia suala la eti kumekuwa na ufaulu zaidi, nataka Serikali ituambie huo ufaulu unapatikanaje wakati Walimu 70% hawako motivated, huo ufaulu unaongezekaje wakati hakuna chochote kilichorekebishwa katika elimu. Naomba Serikali iangalie ni jinsi gani fedha za maendeleo zitakuwa angalau zinalingana na fedha za maendeleo katika Wizara hii inayo- deal na elimu na afya ili watu wetu wasiendelee kufa kwenye vituo vya afya na ili wanafunzi wetu waweze kusoma in a comfortable way. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala zima la Meya. Tunajua kwamba Mameya wote wanatakiwa wachaguliwe na Madiwani ambao wamechaguliwa. Leo Meya wa Manispaa ya Dodoma ameteuliwa na Waziri lakini ndiyo Meya wa Dodoma. Hivi kama tunatunga Sheria yetu ya Serikali za Mitaa, Kifungu Namba 20 kinaelekeza wazi Meya anapatikanaje, lakini inashangaza kuona kwamba mtu anayeteuliwa ndiyo anakuwa Meya wa Manispaa ya Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni kwa nini na hapo Naibu Waziri wa Wizara ya Jenista ni Diwani pale, sasa tunashangaa kwa nini tuna sheria zetu lakini tunazipuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumzia suala la Walimu wanaoondolewa kwenye shule za sekondari kwenda shule za msingi. Nakubaliana na wazo lakini ni kwa kiasi gani Walimu hawa watapewa mafunzo ili waendane na hali halisi ya kule wanakoenda kufundisha. Haiwezekani Mwalimu aliyekuwa anafundisha kidato cha tano au cha kidato cha nne anapelekwa kwenda kufundisha darasa la kwanza au darasa la pili, ni lazima wawe na mafunzo vilevile tunajua hawa wote hawajapewa fedha za kwenda kule wanakopelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Selemani Jafo akizungumza, naomba kujua hawa Walimu watawaondolea adha hii lini wapate fedha ili waweze kufanya kazi zao. Kwa taarifa nilizonazo Walimu karibu wote waliohamishiwa huko hawaendi na kama wanaenda basi wanaenda siku moja moja, kwa sababu maeneo waliyopo ni mbali na kule ambako wanatoka. Hivyo, naomba hilo pia lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kidogo japo limeshazungumzwa, kuhusu suala la Tunduma. Naomba sana Mheshimiwa Waziri alichukue kama special case kwa sababu haiwezekani Baraza la Madiwani ambao ndiyo wanapanga maendeleo tangu mwezi wa Agosti mpaka leo hawajakaa, limezungumzwa lakini naomba kusema kwamba sauti ya wengi ni sauti ya Mungu na Mheshimiwa Jafo najua yeye ni msikivu, naomba jambo hili alifanyie kazi haraka iwezekanavyo ili Madiwani wetu waweze kufanya kazi za maendeleo kama ambavyo miongozo yao inavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni suala la elimu ya msingi. Ni kweli wamesema kwamba asilimia 99 ya shule zetu za Serikali zina elimu ya awali, pamoja na uwepo wa shule ya awali Mheshimiwa Jafo hebu atuambie hizi shule… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika hoja hizi muhimu kimsingi ndiyo ambazo zinaleta maendeleo katika jamii zetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba kuna mtaalam mmoja ambaye alikuwa Rais wa Chuo Kikuu cha Harvard, alisema hivi: “if education is expensive, try ignorance”. Huyu siyo mwingine bali Derek Bok.

Mheshimiwa Spika, tuko hapa kwa sababu ya elimu, kama elimu yetu ni mbovu hatutapata wataalam na vyovyote vile hatutakuwa na maendeleo. Nimesikia kilio cha watu wengi na mimi siku zote nasema elimu ni mwalimu. Tumeshuhudia jinsi gani tumekuwa na upungufu wa walimu hususani walimu wa sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakubaliana nami kwamba bila sayansi hatuwezi kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Pamoja na kwamba tuna upungufu mkubwa wa walimu tukawa na lile zoezi la kupunguza walimu wa sekondari hasa wa masomo ya sanaa kwenda kwenye shule za msingi, nakubaliana nao kwamba elimu ya msingi ndiyo msingi kama pale hakuna mwalimu kabisa itakuwa matatizo lakini zoezi lile liligubikwa na matatizo makubwa na wengine wakarudishwa tena kwenye sekondari kutokana labda na fedha au sielewi ilikuwa nini?

Mheshimiwa Spika, nachotaka kuzungumza na hata ukiangalia Goal Na.4 la Sustainable Development linalozungumzia elimu bora, sawa na shirikishi kwa wote, unaona wazi kwamba lengo hili litakuwa vigumu sana Tanzania kulifikia kwa sababu ya tatizo kubwa la walimu, vilevile mazingira ya kufundishia. Hili linajionyesha kwa matokeo ya mitihani tuliyoyapata juzi.

Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba Tanzania tuna shule za vipaji maalum, shule za kata na shule za binafsi. Nitoe tu analysis kidogo kwa sample ya shule tatu, tatu; shule za Serikali kwa maana ya shule za kata na shule za binafsi. Wewe mwenyewe unajua kwamba wanaopata division four na division zero siyo rahisi kabisa kuendelea na elimu inayofuata.

Mheshimiwa Spika, nimechukua shule za tatu za binafsi ambazo zina jumla ya wanafunzi 236. Katika hizi shule tatu za binafsi waliopata division one ni 223 sawa na asilimia 95; waliopata division two ni 12 sawa na asilimia tano na waliopata division three ni mmoja sawa na asilimia 0.6, kwa hiyo, ukiangalia hawa wote wataendelea. Ukija kwenye shule za kata kwa hiyo sample niliyochukua, katika shule tatu zenye jumla ya wanafunzi 368 waliopata division zero na four ni 297, sawa na asilimia 80 na waliopata division one mpaka three ni wanafunzi 79 sawa na asilimia 20. Kwa hiyo, unakuta kwamba kundi hili linakuwa ni la wasindikizaji.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali nini cha kufanya. Ni kweli elimu bure imekuja na changamoto nyingi, wanafunzi wamekuwa wengi lakini sasa nini cha kufanya kwa sababu hatuwezi kuacha hali hii iendelee. Naishauri Serikali iendelee kuboresha miuondombinu kwa sababu unakuta shule hizo hizo za kata za Serikali ndiyo hizo hizi hazina walimu wa kutosha lakini kuna suala la chakula watoto hawa nao hawapati chakula shuleni. Kwa hiyo, unakuta nyumbani anatoka kwenye familia maskini hana chakula, anafika shule nako hamna chakula, ukilinganisha na wale wa binafsi unakuta tofauti ni kubwa sana. Kwa hiyo, naomba sana kwa sample hii na Mheshimiwa Waziri anajua tuone ni jinsi gani ya kuwasaidia watoto hawa wanaosoma kwenye shule za kata kwa sababu nao wanastahili kupata elimu kama wanayopata wengine. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukija hata kwenye shule zile ambazo tunaziita special schools, unakuta kwamba shule ya kwanza ya special schooI Ilboru imekuwa shule ya 36. Zile nyingine za Tabora na kadhalika unakuta ziko kati ya hizo 100 bora wala haziko kwenye 50 bora. Kwa hiyo, nadhani kuna haja pia kama hizi ni special schools na tunaamini wanaokwenda kule ni wale waliofaulu vizuri sana darasa la saba basi wawekewe mazingira ambayo kweli yanafanya wawe special kuliko wale wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudie tena kusema kwamba kwa kuwa elimu ni mwalimu naomba maslahi ya walimu yaboreshwe, wapandishwe madaraja, wapate mishahara yao kwa wakati lakini na yale maslahi yao mengine pia wayapate. Kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mwijage unaweza ukasomea chini ya mti au kwenye nyasi lakini kama una mwalimu bora, mwalimu mahiri utafaulu tu kuliko kusoma kwenye shule zenye AC lakini hakuna walimu au walimu waliopo hawafai. Kwa hiyo, naomba muwekeze zaidi kwa walimu ili tuweze kuboresha elimu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la Bodi ya Mikopo. Ni kweli kwamba Bodi ya Mikopo imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi lakini bado kuna tatizo kubwa la urejeshwaji. Pamoja na urejeshwaji naomba sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla inisikilize, kuna wanafunzi waliokuwa wanasoma kwenye vyuo ambavyo TCU iliwaondoa, wamepelekwa kwenye vyuo vingine, mpaka leo napozungumza hawajapata mikopo yao. Kuna waliokwenda SAUT zaidi ya wanafunzi 100 hawajapata kabisa na hawa ni wanafunzi ambao wanasomea ualimu. Pamoja na vyuo vingine lakini hiyo particularly nina majina ya wanafunzi, naomba sana Serikali ifuatilie ili wanafunzi hawa wapate mikopo yao. Haiwezekani kwa miezi minne, mitano kuanzia Novemba walipohamishwa mpaka leo hawajapata single cent na hawa wanastahili mikopo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kuoanisha suala la walimu wa sayansi na COSTECH. Nakumbuka kwamba tulikubaliana ndani ya Bunge hili au kwa sheria, sikumbuki vizuri lakini ilikuwa 1% ya GDP iende COSTECH ili kusaidia uvumbuzi na watoto wetu wanaosoma masomo ya sayansi. Cha ajabu hela hiyo haiendi na hata kile chanzo kingine walichokuwa wanakitegemea wamekuja kwenye Kamati wamesema nacho kimeondolewa. Kwa hiyo, leo tunapozungumza hata watoto wakiwa wabunifu namna gani kama COSTECH haina fedha maana yake tutakuwa tunacheza danadana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Profesa Maghembe alivyosema kwamba hisabati ni jambo la muhimu sana. Ndiyo sababu wanafunzi wanaosoma sayansi wakimaliza form six amepata labda ‘A’ zote inakuwa rahisi kwenda vyuo vikuu kusoma masomo yoyote hata ya Arts. Tuli-test Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1998, waliosoma PCM wakaja kusoma Law na wakafaulu vizuri sana lakini huwezi mtu wa Arts au tunaita Nguin ukasome sayansi, haiwezekani. Kwa hiyo, ni vyema tukawekeza kwenye sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inasikitisha, hili ni jambo la ajabu sana, tumeambiwa kwamba Bodi ya Mikopo asilimia 66 ya wanafunzi hawa ni Nguin per-se. Kwa hiyo, kama hiyo asilimia nyingine 30 inakwenda kwa wale accountant na mainjinia au natural sciences then tuna tatizo kubwa sana kwamba ni asilimia 30 tu na hiyo 30 sasa labda natural science inaweza ikawa asilimia 10 au 15 halafu tunategemea tutakuwa na Taifa la viwanda, haiwezekani. Nadhani ni muhimu sana kuwekeza kwa walimu wa sayansi. Hili ni tatizo kubwa kwa sababu hatujawekeza kwenye walimu wa sayansi lakini pia hatuna hata vitendeakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Sera ya Elimu inazungumzia masuala ya vitendeakazi, jambo la ajabu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, mimi ni dakika 10, hazijakwisha bado.

SPIKA: Hiyo ni kengele ya pili, malizia tu hiyo.

MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, jambo linaloshangaza, sasa hivi vitendeakazi (teaching aids) walimu wamekuwa wagunduzi kweli kweli, wanatumia miili yao kufundishia wanafunzi. Mimi nimeshangaa na hii itasababisha matatizo huko baadaye kwa sababu Mwalimu anamfundisha mtoto …

SPIKA: Mheshimiwa Susan inabidi uwe makini kidogo.

MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, kama unamfundisha mwanafunzi kuandika tano kwa kiuno watoto wa darasa la tatu, la pili, hili ni tatizo kubwa sana. Hii inaonyesha kwamba Serikali haina fedha ya kuwasaidia walimu kuwapa teaching aids. Naomba sana wasaidiwe kwa sababu utamuona mtoto wako anakuja nyumbani anatikisa kiuno unadhani ameshaanza mahusiano kumbe…

SPIKA: Hiyo tano inaandikwaje Mheshimiwa Mbunge. (Kicheko/Makofi)

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, ningekuwa nimevaa suruali ningekuonesha. (Kicheko)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, dakika zako zimekwisha.

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Leo nitachangia kwa masikitiko makubwa sana hasa nikikumbuka kwamba mwaka jana wakati kama huu nilikuwa na Naibu wangu Mheshimiwa Mwalimu Bilago, lakini leo hatunaye, kwa hiyo napenda tu niseme kwamba nina masikitiko makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kunukuu Mwanasayansi maarufu wa Kijerumani Bwana Albert Eisten, ambaye alisema:

“Dunia itaharibiwa sio na watenda mabaya bali kwa ukimya wa watu wema wakati maovu yanatendeka.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ina wasomi wengi kuliko Wizara zote Tanzania. Kwenye Kamati yetu ambayo mimi ni mjumbe imejaa Maprofesa ambao ndiyo ambao wanakaa kimya wakati wanaona mfumo wetu wa elimu unaharibika. Vilevile Maprofesa hao wanaongozwa na Profesa Ndalichako ambaye naamini ni msomi mzuri lakini hatuoni mfumo wa elimu ukibadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni kama kiwanda, hauwezi ukapeleka muwa kiwandani ukatoka muwa lazima utoke sukari. Leo hii wanafunzi wanaanza nursery mpaka anamaliza darasa la saba hajui kusoma wala kuandika, amepoteza miaka yote saba. Ndiyo sababu naunga mkono alichokisema mzee Kishimba pale kwamba sasa hivi elimu badala ya kuwa ufunguo wa maisha umekuwa kifungo cha maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunapoongelea elimu lazima tuongelee ubora wa elimu. Leo ambapo Sera ya Elimu ya mwaka 1995 ambayo ndiyo inatuongoza inatoa mitaala na vitabu tumeipigia kelele kwamba imepitwa na wakati lakini imekuja Sera ya mwaka 2014 ambayo hata miaka minne (4) haijaisha tayari inaanza kufanyiwa maboresho. Waziri anatumbia kwamba inafanyiwa maboresho kwa sababu haikupita kwa wadau, haiingii kichwani kwa sababu gani haikupitishwa kwa wadau?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunatumia sheria ya mwaka 1978 ambayo ilitumika kwenye Sera ya mwaka 1995 na inaendelea kutumika kwenye Sera ya 2014. Mimi binafsi najua kwamba huwezi kuwa na sheria bila kuwa na sera na kwa maana hiyo sera inapotengenezwa ndiyo unakuja kutengeneza sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya mwaka 2014 imesema bayana kwamba watoto watasoma mpaka darasa la sita halafu baada ya hapo wote wataenda sekondari, ndiyo tunaita elimu msingi lakini leo hawaitekelezi. Waziri ukimuuliza atakwambia kwa sababu sheria haijabadilika then tunauliza which come first sheria au policy? Kwa hiyo, wakubali kwamba walizembea na hayo mabilioni ya pesa yaliyotumika kutengeneza hiyo Sera ya 2014 watuambie kodi za wananchi kwa nini zinatumika bila wao kuwa na mkakati maalum wa kuhakikisha wanapotengeneza sera wanaenda kwanza kuijaribisha halafu baadaye ndiyo inakuwa sera kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia suala la ubora wa elimu, baada ya hiyo Sera sasa kuwa na matatizo, wamekuwa na miongozo na mambo mengi sana. Kwa mfano, ukisikiliza Waraka Na. 5 na wakati huo nadhani Kamishna wa Elimu alikuwa Profesa, nimesahau jina lake alikuwa Profesa Balalusesa. Unaposema mwanafunzi hawezi kufukuzwa shule mpaka amekuwa mtoro kwa siku 90 mfululizo siku za week days, hii ina maana miezi minne kamili kwa sababu kama ni mwezi mmoja una siku 22 za kwenda shule times 4 yaani miezi minne huyu mtoto akienda kwa mfano siku ya 86 bado hafukuzwi. Halafu Waraka huu uwe applicable pia kwenye shule za private, haiwezekani. Hakuna mwalimu mwenye shule yake ya private atakayeruhusu upuuzi wa namna hii. Haya mambo ndiyo sababu tunasema Tanzania mimi huwa sielewi tunaelekea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanasema kwamba mwanafunzi hawezi kufukuzwa mwaka anaofanya mtihani wa kumaliza shule. Ina maana kama uko darasa la saba, form four, form six huwezi kufukuzwa. Sasa na hii imepelekea kuporomoka kwa maadili kwa sababu mwanafunzi wa form four au form six akijua anafanya mitihani anaweza hata akaamua kumpiga mwalimu kwa sababu anajua hatafukuzwa mpaka Mahakama ithibitishe, hiyo Mahakama inathibitisha saa ngapi. Kwa hiyo, kuna mambo ambayo tunadhani hayajakaa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo nije sasa kwenye matatizo makubwa ya walimu. Hapa nina barua ya mmoja wa walimu hajapandishwa daraja toka mwaka 2003 amekuja kupandishwa juzi yaani mwezi huu wa nne ndiyo amekuja kulipwa mshahara wa kwanza kwa kupandishwa cheo toka 2003 anapokea Sh.140,000 mpaka juzi amekuja kupokea shilingi milioni moja sijui na laki ngapi, barua ziko hapa na ameendika several times. Sasa wako walimu wa namna hii wangapi? Kwa hiyo, nitampa Waziri husika atuambie ni kwa sababu gani wanawadhalilisha walimu kiasi hiki. Walimu ndiyo kila kitu kwa hiyo niombe sana Serikali iache kuwadhalilisha walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumzia ni suala zima la Bodi ya Mikopo ya Juu. Tumelizungumza jana kwenye hotuba na hata Kamati, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inapata fedha nyingi sana which is very good lakini fedha hizi takribani zaidi ya asilimia 52 kwa mwaka huu zinaenda kwenye Bodi ya Mikopo, ile miradi halisi ya maendeleo kuanzia shule za msingi mpaka elimu ya juu, ndiyo sababu unaona majengo mengi ya vyuo vya elimu ya juu pamoja na vyuo vya ualimu haitekelezwi kwa sababu fedha zinaenda kwenye Bodi ya Mikopo. Kwa hiyo, ni ombi langu kwamba vote ya Bodi ya Mikopo iwe peke yake ili irahisishe kwanza ufuatiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wala haiingii akilini kwa sababu gani Tume ya UNESCO ambayo iko chini ya Wizara hii ina vote yake na inapokea shilingi bilioni 2 tu lakini Bodi ya Mikopo inapokea takribani shilingi bilioni 500 kwa nini isiwe na vote yake. Kikubwa zaidi tunachozungumza hii Bodi ni lazima iwekewe vote yake peke yake ili irahisishe ufuatiliaji wa fedha zinazorejeshwa na ambazo zinatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba kuna miradi ya maendeleo mingi sana yaani kwa hiyo shilingi bilioni 863, shilingi bilioni takribani 400 ndiyo zinabaki. Jambo la kusikitisha miradi muhimu kama ya vyoo na usafi fedha za nje tu ndiyo zinahudumia. Kwa hiyo, leo tunahitaji wahisani watuchimbie vyoo, haiwezekani. Kwa hiyo, hili ni jambo muhimu sana lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni TET. Wengi wameongelea kuhusu vitabu, mtakuwa mnawafukuza tu Wakurugenzi lakini sawasawa, haiwezekani TET wawe ndiyo wachapishaji, editors, evaluators na wana approve, haiwezekani na haiko mahali popote. Kwa hiyo, ombi langu ni kwamba lazima kuwe na independent organ ambayo itakuwa inapitia vitabu hivyo. Pia editor atakayejulikana amehariri vibaya huyo ndiye achukuliwe hatua. Kwa mfano, haiwezekani SUMATRA yenyewe iwe inamiliki mabasi, kwa hiyo na huku haiwezekani hao TET watunge vitabu, wasambaze na ndiyo sababu tunapata matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho naomba sana Wizara sasa hivi wanataka kupeleka vitabu mpaka China wakati humu ndani hamjapeleka vitabu kwenye shule za private, mnaendaje China?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili niweze kuchangia na kipekee nipongeze sana hotuba ya kamati pamoja na hotuba ya Kambi ya Upinzani ambapo ni mwanakamati. Ninaomba sana Wizara itekeleze yale yote hasa maoni hayo ambayo kwa kweli ni ya msingi na ninaamini mkiyachukua tutaboresha sana sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa suala zima la bajeti. Wizara hii kama ambavyo wote tunajua ni Wizara muhimu sana kwa afya ya Taifa letu na hata hivyo tunavyosema kwamba Tanzania ya viwanda haitawezekana kama rasilimali watu wetu watakuwa wagonjwa na hawapati huduma bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kusikitisha sana kuona kwamba Wizara hii pamoja na kutengewa bajeti kubwa tulipitisha takriban shilingi trilioni moja lakini kwenye fedha za maendeleo tulipeleka bilioni 561 mpaka leo tunapozungumza imeenda shilingi bilioni 91 tu sawa na asilimia 16, hivi kweli asilimia 84 ya fedha tulizozipitisha ndani ya Bunge hili bado hazijapatikana na tunafikia mwisho wa mwaka tunaomba kujua ni kwa kiasi gani tunategemea ubora wa huduma za afya kama fedha ambazo tumekaa hapa ndani kwa kipindi cha miezi mitatu haziendi tunaiuliza Serikali tuna sababu gani ya kukaa hapa Bungeni tunapitisha fedha nyingi kiasi hicho ambacho tunaamini zinaenda kufanyakazi lakini fedha hazitoki huku tukiambiwa kwamba Serikali inakusanya fedha fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri atapokuja ku-windup atuambie hivi hiyo asilimia 84 inategemewa kwenda lini na hizo huduma zote ambazo zimekwama kwa huu muda ni kwa kiasi gani wananchi wame-suffer ni kwa kiasi gani watu wamefariki kwa sababu ya kukosa hizi fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo kutokana na uchache huu wa fedha naamini ndiyo sababu tunakuwa na matatizo mengi kwenye Wizara hii. Kwa mfano kuna watu wengi sana wanaenda kwenye hospitali wanafanyiwa vipimo lakini vipimo vinakuwa tofauti na ugonjwa alionao. nitatoa mifano hata Waziri akiita baadhi ya Wabunge ambao wamepata matatizo hayo ni wengi sana. Kwa mfano majuzi hapa niliangalia kwenye TV kuna binti mmoja amepimwa Muhimbili, amekutwa na matatizo ameambiwa ana matatizo ya ini, ini limeungua amekaa karibu anakufa amepelekwa India only to find ana matatizo ya moyo sasa watu wa namna hii wako wengi kiasi gani. Nilikuwa naomba Waziri atuambie tatizo ni uelewa wa madaktari wetu au technician au tatizo ni vifaa tulivyonavyo haifanyi kazi nilikuwa naomba hilo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la magonjwa yasiyoambukiza limekuwa kubwa sana na tatizo kubwa sasa hivi pamoja na diabetes ni pamoja na tatizo kubwa la kansa. Leo tunavyozungumza ni hospitali mbili tu za Serikali zina mashine ya mionzi yaani radiograph sasa na hii iko hospitali ya Ocean Road na hospitali ya Bugando lakini tuna hospitali zaidi ya mbili za rufaa tuna hospitali ya Kanda ya Mbeya, tuna hospitali ya Kanda ya Kilimanjaro kwa maana ya KCMC Kanda ya Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipo kwenye kamati ya maendeleo ya jamii kwa muda mrefu madaktari au wakuu wa hospitali hizi mbili kilio chao kikubwa kimekuwa ni fedha kwaajili ya kununua bunkers kwa ajili ya kuweka hizo bunkers ili waweze kuweka hizo mashine hospitali ya KCMC na hospitali ya Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sababu ya kupandisha hadhi au kuwa na hospitali za Kanda kama hatuna vifaa. Kwa hiyo, tatizo la Ocean Road kuwa na mrundikano litakuwa palepale kwa sababu wagonjwa katika Kanda kwa mfano Nyanda za juu kusini, wagonjwa katika Kanda ya Kusini, wagonjwa katika Kanda ya Kaskazini, wanapopata matatizo ya kansa wameshakuwa wameshatambulika wana kansa wanatakiwa wapate mionzi hawapati mionzi wanatakiwa tena waende Ocean Road kwa hiyo tunarudisha tatizo palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ukiangalia hata kitabu cha maendeleo cha mwaka huu hakuna fedha yeyote ya maendeleo iliyotolewa katika hospitali ya KCMC wala hospitali ya Mbeya. Kwa hiyo, wagonjwa wetu katika maeneo husika wataendelea kufariki kwa kukosa huduma za msingi kwa sababu tunaambiwa huduma kansa inaweza ikatibika kama imeweza kujulikana mapema lakini watu wamegundua lakini bado hawana access kwenye hizo hospitali, kwa hiyo. nilikuwa naomba hilo pia Waziri atusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala zima la watumishi ni wazi kwamba watumishi wa Wizara ya Afya, sekta ya afya kwa ujumla wake ni wachache sana na Waziri wanakiri ni karibu asilimia 50 lakini vijijini asilimia mpaka 74 hakuna wauguzi, hakuna wataalam wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa na tunaendelea pia kujenga vituo vya afya tunaendelea kujenga zahanati lakini suala la watumishi halijaonyeshwa. Inasikitishwa kuambiwa kwamba ni kwasababu ya kuondolewa kwa wale waliokuwa na vyeti feki, sijui waliokufa. Wewe unatambua kwamba kama ikama ipo tayari na fedha zao za mishahara zipo sasa kama hawa wameondolewa replacement ipo madaktari wapo kibao wana-graduate lakini vilevile wauguzi wanajaa sasa hoja ni nini hapa watuambie labda Serikali haina fedha lakini kutuambia wanaendelea na uhakiki na uhakiki wakati hawa watu walikuwa kwenye ikama na fedha zao zipo maana yake ukimuondoa, lazima umrudishe ambaye yupo na wapo mitaani ukipiga filimbi hapa madaktari ambao wako mitaani wapo kibao manesi wako kibao kwa sababu kila siku kila mwaka wana-graduate. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kweli tunaendelea kuweka afya za watu wetu rehani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nielezee kwamba ni makamu mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa chama changu na kwa maana hiyo sina budi kuongelea suala la wazee, toka nimeingia kwenye Bunge hili tumekuwa tukiambiwa tuna Sera ya wazee toka 2001 lakini mpaka ninavyozungumza sheria haijaja na ndiyo sababu wazee wanaendelea kudhalilika katika nchi hii. Wazee wanaendeshwa kwa sera kwa miongozo kwa taratibu lakini hakuna sheria nilikuwa naomba kila siku tunapigwa danadana tuwambia kwanini wanasema wanaendelea kuboresha, wanaendelea kufanya hivi lakini kwa nini msilete sheria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli hatuoni aibu kwamba wazee hawa ndiyo wametulea wazee hawa ndio wameleta uhuru katika nchi hii lakini wazee hawa leo mmesema mara mtawapa vitambulisho, mara sijui mtawapa nini lakini wazee hawa wananyanyasika kwelikweli na ninajua kwamba siyo wazee wote hawana uwezo lakini hata wale wasio na uwezo ikija sheria itawatambua kwa sababu hata leo nikimuuliza Waziri mwenye dhamana tuna wazee kiasi gani katika nchi hii sidhani kama wana-database. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana suala la wazee ni la muhimu lakini vilevile suala la pensheni ya wazee ni la muhimu siyo wazee tu waliokuwa wanafanyakazi, hata wasiokuwa na kazi walitakiwa walau wawe na posho ambayo itawasaidia kujikimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nije kwenye suala la ndoa za utotoni limeelezwa kwa kina lakini niseme ni jambo la aibu sana kuona kwamba sheria yetu ya mwaka 71 bado ndiyo tuliyonayo lakini kipekee niseme kwamba jambo hili lilipelekwa mahakamani na tayari limeshakuwa ruled out kwamba sheria hiyo ibadilike vile vifungu vilitakiwa vibadilishwe lakini kinachosikitisha Serikali kupitia AG wamekata rufaa. Sasa nashindwa kuelewa hivi ni kweli tunataka watoto wetu waolewe katika umri huo? Sheria ya mwaka 71 wakati tulikuwa hatuna shule leo tunasema kila mtoto aende shule yeye eti sheria bado ni ileile kwahiyo kuna confusion na ni lazima huo utata uweze kutatuliwa kwa sisi Wabunge kukaa pamoja na kuona umuhimu wa kubadili sheria hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo nilitaka kuzungumiza ni suala zima la huduma ya unasihi. Tuna matatizo makubwa sana Tanzania. Sasa hivi kuna suala stress na sonona (depression) na hii inatokana na changamoto za maisha ikiwa ni pamoja na kutopandishwa mishahara ikiwa ni pamoja na vyuma kukazwa na mambo mengi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hili linahitaji ushauri nasaha. Tuna vyuo vyetu vya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii, hasa cha Ustawi wa Jamii…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Susan kengele ya pili ilishagonga. Ahsante sana. Nilikuwa nasubiri umalizie hoja yako muhimu.

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwanza.

NAIBU SPIKA: Zimeshagonga mbili Mheshimiwa. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya awali ya kuweza kuchangia katika ripoti za kamati hizi mbili ambazo kwa bahati nzuri sana mimi ni Mjumbe wa kamati zote mbili. Niwapongeze sana Wenyeviti waliosoma, pia nipongeze na kukubaliana kabisa na maoni ya Kamati hizo kwa sababu hiyo ndio hali halisi. Nitaanza na Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo linajitokeza katika Wizara hii ya Afya ni tatizo kubwa sana la watumishi. Tatizo la watumishi katika Wizara ya Afya ni almost 50 percent. Ukiangalia lile lengo namba tatu la kuhakikisha kwamba tunakuwa na taifa lenye afya na watu wenye siha njema si rahisi kabisa kufikiwa kwa jinsi ambavyo tunaenda na trend ya bajeti. Pamoja na kwamba Mwenyekiti wangu amesema bajeti ya Wizara ya Afya imekuwa ikiongezeka, ni kweli inaongezeka kwa fedha lakini ukiangalia kwa percentage inapungua sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu takwimu mwaka 2014/2015 tulikuwa na asilimia 9, na that was the highest. Mwaka jana ilikuwa asilimi 5.5 ilhali sisi kama nchi tumesaini Abuja Declaration ambayo inapaswa Wizara ya Afya walau Sekta ya Afya itengewe asilimia 15, lakini jambo hilo hatujaweza kulifikia. Kwa maana hiyo, pamoja na juhudi zote za Waziri, Naibu na watendaji wote unakuta kwamba tatizo kubwa linakuwa ni bajeti. Kwa hiyo, ni ombi langu kwamba ni muhimu sana bajeti ya afya ikaongezeka kwa percentage na sio kwa figures.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilitaka kuzungumzia kwenye Wizara ya Afya na hili ni jambo kubwa sana, ni suala la bima ya afya. Waheshimiwa Wabunge mjue kwamba bima yetu ya afya inaisha Juni, kwa hiyo mjue kuanzia Julai mpaka Novemba hapo mtajijua wenyewe. Kwa hiyo, ni muhimu sana wakati tunajua sisi tuna bima, tuwaangalie wenzetu huko nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kamati imesema kwamba magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kwa kiasi kikubwa na magonjwa haya ni ya gharama kubwa sana. Jambo ambalo linasikitisha leo, wagonjwa wa figo ni wengi sana lakini dialysis ni very expensive. Ukiingia kwenye dialysis kipimo siku moja tu kusafishwa figo ni shilingi kuanzia 250,000 mpaka 350,000 lakini unatakiwa process hii ndani ya wiki moja mara tatu, kwa hiyo Mtanzania gani ataweza kujilipia kuanzia 750,000 mpaka 1,000,000 na? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachosikitisha naambiwa kuna ambao tayari walikuwa kwenye hiyo package, leo wameenda ku-renew bima zao wanaambiwa dialysis imeondolewa kwenye hiyo package. Kwa hiyo, kuna kilio kikubwa sana kwa wananchi ambao wana matatizo makubwa sana ya figo, lakini matatizo ya moyo na mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Serikali iangalie ni jinsi gani tumepiga kelele walete muswada ili kuhakikisha kwamba wananchi wote wanakuwa covered kwenye bima ya afya ili sasa gharama zipungue kwa wale ambao wanapata magonjwa haya makubwa, lakini jambo hilo bado hakijaweza kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la lishe; ni jambo la kusikitisha kuona kwamba kama nchi bado tuna watoto wenye udumavu wengi sana, takribani asilimia 32. Kinachosikitisha fedha iliyotolewa kwa ajili ya masuala haya ya lishe ilikuwa bilioni 289 lakini zilizopelekwa ni bilioni 123 sawa na asilimia 43 pekee. Kinachosikitisha zaidi, katika fedha hii asilimia 95 inatoka kwa wafadhili, yaani Tanzania kama nchi ni asilimia sita tu. Hivi kweli tunawategemea wafadhili hata kwenye lishe? Hili ni jambo ambalo halikubaliki. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo kama nchi
lazima tuone kwamba tunajikomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la elimu; imezungumzwa vyema kwamba msingi wa elimu ni elimu ya awali (nursery) lakini kwa takwimu zinatisha; kwamba tuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa nursery, tunao walimu 9000 kati ya watoto takribani 1,000,000. Kwa hiyo, unakuta uwiano ambao unatakiwa katika nursery iwe mwalimu 1 kwa watoto 25 sasa hivi wastani ni mwalimu 1 kwa watoto 146 lakini inatisha zaidi kwa Jimbo la Serengeti peke yake wastani mwalimu 1 wanafunzi 3,300. Hizi ni data tulizozipata kutoka MCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama mtoto ametoka nyumbani anaenda kuanza shule, wakati huo ubongo wake hauna chochote zaidi ya kile anachokiona hivi kweli mtoto anaenda kwenye darasa la watoto 200/300, atakuwa na mapenzi au na passion na shule? hawezi kuwa na hiyo passion. Kwa hiyo, ni muhimu sana tunahitaji takribani walimu 43,000 wa shule za awali ili tuweze kuhakikisha kwamba tatizo hilo linaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri uone umuhimu wa kupata walimu katika shule za awali lakini vilevile katika shule za msingi. Leo tunavyoelekea kwenye shule za msingi tunajua elimu bure imekuja na mambo yake mengi na changamoto nyingi. Je, Serikali mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba watoto wanaoenda kumaliza darasa la saba mwaka 2022 ambao watakuwa doubled; sasa hivi wanamaliza takribani 900,000 – 1,000,000 wataenda mpaka 1,500,000; je, mmejipagaje watoto hawa sekondari? Kwa sababu kila siku ikifika mwezi wa kwanza ndipo tunaanza kusema/Waziri Mkuu na Wakuu wa Mikoa wanatoa matamko ya kujenga shule. Hivi hamna utaratibu wa kutenga tengeo kwa sababu kama tunahitaji leo bilioni 700 na kwa ajili ya kujenga madarasa, kwa nini msiyaweke kwa awamu kila mwaka mkatenga walau nusu au robo kwa miaka mitano ili mhakikishe kwamba tatizo hili linapungua au kuisha kabisa? Hawana mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba kuna kila sababu ya kuwa na mpango mahsusi wa kuhakikisha kwamba mnatenga kila baada ya muda fulani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watoto wanafaulu wanaenda kusubiri madarasa bali madarasa yawasubiri wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile bajeti ya Wizara ya Elimu Sekta ya Elimu nayo inapungua, hela inaongezeka lakini ukiangalia asilimia inazidi kupungua. Tulianza na trilioni 4.7 mwaka 2016/2017 leo tupo trilioni 4.5; kwa maana ya kwamba bilioni 255 zimeshapungua. Je, tunapunguza fedha wakati tumekuwa na changamoto kubwa lakini wanafunzi wameendelea kuongezeka, walimu hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri kwamba walau kwenye total budget ya Wizara ya Afya na Elimu 0.05 mtoe kwa ajili ya kuajiri watumishi wa afya na watumishi wa Wizara ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye UKIMWI; suala la UKIMWI ni suala mtambuka na kwa maana hiyo suala la Mfuko wa UKIMWI ninaomba sana, mfuko huu about 90 percent unategemea nje, lakini wagonjwa ni wetu na wagonjwa wakishaanza dawa hizi hawawezi kuziacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana Mheshimiwa Jenista muhakikishe kwamba Mfuko wa UKIMWI sasa tunakua tunautegemeza wenyewe na hatutegemei watu wa nje kwa kiasi kikubwa, 90 percent leo wakikata maana yake wagonjwa wote waliopo kwenye dawa watakuwa hatarini kupoteza maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la UKIMWI kuna suala la VAT exemption. Kama Kamati tumekutana na wadau, hawa ambao ni development partners na hasa wale wanaotoka Mfuko wa Rais wa Marekani ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukisaidia sana masuala ya UKIMWI.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kumekuwa na mkinzano mkubwa sana wa kisheria kwa maana ya kwamba ile VAT exemption inasema kwamba NGO hazipata huo msamaha. Kikubwa ni kwamba tunaomba basi kuwe na utaratibu madhubuti ambao utawezesha hawa watu wapate VAT ili waweze kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, asante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na masikitiko yangu ni jinsi ambavyo hotuba yetu imekatwakatwa, lakini naamini kabisa watu wameelewa nini kinachoendelea na imekuwa bahati mbaya sana, mambo haya yanasemwa Mabalozi wetu wapo hapa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. Wizara hii ni muhimu sana na ndiyo kioo cha nchi kwenye dunia au kwenye ulimwengu wetu. Kwa hiyo chochote kinachofanyika ndani ya nchi, Wizara hii ipo responsible na ndiyo sababu umeona kwamba wameangalia Wizara zote kuanzia kilimo na nini na nini na ndiyo sababu hata Kambi ya Upinzani tumeongelea masuala hayo ya kilimo na mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kuna tatizo kubwa sana katika Wizara hii. Nizungumzie suala la watumishi, kumekuwa na tatizo kubwa sana la kupandishwa vyeo, pamoja na kwamba ni tatizo la kitaifa, lakini nilitegemea Wizara hii ingeweza kuwapandisha watumishi wake kwa takribani miaka 12 bado watumishi wa Wizara waliokuwa kwenye cheo fulani kwa mfano ile Foreign Service I mpaka leo kwa miaka 12 walitakiwa wawe Principal Officers lakini bado wako pale. kwa hiyo, naishauri Serikali wafanye kuwapandisha kwa mserereko ili waweze kupata hadhi yao na hivyo kuleta motisha katika kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia pia bajeti; bajeti na nashukuru hata Kamati imesema na Kambi. Ukiangalia mishahara, kwa mfano nimejaribu kuchukua, ukiangalia recurrent budget kwa mwaka jana na mwaka huu utaona kuna tofauti ya takribani shilingi bilioni 10, lakini kibaya zaidi angalia kwenye zile multilateral missions, unakuta kuna upungufu mkubwa sana wa mishahara. Kwa mfano, Balozi wetu wa London mwaka jana kwenye mishahara tu (basic salary) ilikuwa milioni 177, mwaka huu milioni 81. Ukija Lusaka ilikuwa milioni 93, mwaka huu milioni saba, ukienda Moscow ilikuwa milioni 116, mwaka huu milioni 77, ukienda Ottawa Canada ilikuwa milioni 107, mwaka huu milioni 49, ukija Rome ambako ni Multilateral tuna FAO na mambo mengine ilikuwa milioni 166, mwaka huu ni milioni 100, ukija Riyadh ilikuwa 110, mwaka huu ni milioni 81, ukija New York ambapo tuna Mashirika makubwa ya Kimataifa ilikuwa milioni 88, mwaka huu milioni 64.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ina-cut across kwenye Balozi zetu zote na hili ni tatizo kwa sababu tunajua kwamba toka mwaka 2016 walivyorudisha baadhi ya Maafisa wa Ubalozi, bado hawajafanya replacement. Nilikuwa Doha mwaka huu, pale wana watumishi wawili tu, Balozi na mtumishi mmoja au wawili, ukienda New York ni hivyo hivyo, nimetembea nchi nyingi kuna matatizo makubwa ya watumishi. Nataka kujua ni kwa sababu gani baada ya kurudisha baadhi ya watumishi, hawajawa-replace kwenye Balozi hizo kiasi kwamba hii inakuwa reflected kabisa kwenye hii mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na tatizo kubwa sana la utendaji na ndiyo maana tunasema sasa ni lazima Waziri anapokuja ku-wind up atuambie baada ya kupunguza Maafisa wa Balozi, ni kazi gani wamefanya kuhakikisha kwamba wanawa-replace ili kazi ziweze kwenda. Tunajua kwa mfano pale New York wameondoa watu wengi sana, kwa hiyo Kamati mbalimbali hazipati watu wa kufanya hizo kazi au mtu mmoja anafanya kazi ya watu watatu. Kwa hiyo, tunaomba na hilo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Bunge tuna passport za Kibalozi, lakini na wengine wengi. Siku za nyuma tulikuwa tuna utaratibu mzuri, Chief of Protocal alikuwa anakuja kutoa mafunzo ya etiquettes na ni jinsi gani mtu anaweza ku-appear. Leo hivi tunaona hata Mabalozi wetu hawajui hizo etiquettes; inawezekanaje Balozi wa nchi anafuta miwani kwa kutumia ulimi. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo tunaona hayafai kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana… (Makofi) (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii na nashukuru sana kwamba leo nasimama kuongelea suala la bajeti ya mwaka 2019/2020. Uzuri wa bajeti au ubaya wa bajeti tunaangalia utekelezaji wake na siyo uwasilishwaji wake wether umewasilishwa kwa mbwembwe namna gani, tunaangalia utekelezaji wake wa miaka iliyopita na hapa nina bajeti ya mwaka jana iliyosomwa na kaka yangu Dkt. Mpango na ukiangalia vipaumbele, tunaangalia vile vipaumbele je vilitekelezwa ama havijatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia kipaumbele cha kwanza kabisa mwaka jana ilikuwa ni kilimo na kilimo hicho kilikuwa ni kilimo cha umwagiliaji, ni wazi kwamba bado nchi yetu haijajikita kwenye kilimo cha umwagiliaji. Wote tunajua kwamba sasa hivi kwa kweli kilimo cha kutegemea mvua hakiwezekani kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Pamoja na kwamba wameendelea kujitahidi kiasi kidogo, tunategemea kabisa kwa kuwa nchi hii sasa ni ya viwanda ni lazima tufungamanishe bidhaa zinazotokana na kilimo ili sasa ziende zikachakatwe kwenye viwanda na hivyo kuweza kupata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni ukweli kwamba bado kilimo cha umwagiliaji hakijapewa kipaumbele na hata ukiangalia bajeti ya mwaka huu katika vipaumbele vya kilimo hicho kilimo cha umwagiliaji pia bado hakijawekwa kabisa. Kwa hiyo, nilikuwa natoa ushauri tu kwamba ni muhimu sana nchi yetu inarutuba nzuri na kila mahali kuna mazao tofauti, kwa hiyo nilikuwa naomba sana na ni ushauri sababu tumekuwa tukishauri mara kwa maralakini ushauri huwa haupokelewi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mpango nchi hii kama tunataka nchi hii tujiondoe hapa tulipo tuweze kujitegemea ni lazima tuwekeze vizuri sana kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa sababu tunajua kwamba Tanzania kama nchi zaidi ya asilimia 70 ni wakulima na kati ya hiyo asilimia 75 ya hiyo 70 ni wakinamama, kwa hiyo kama akinamama watakuwa kwenye lindi la umaskini, maana yake nchi hii haiwezi kuendelea kwasababu hakuna jamii iliyotelekeza wanawake ikaendelea. (Makofi)

Kwa hiyo, ninaomba sana sana suala la kilimo liendelee kupewa kipaumbele kwasababu kilimo na viwanda vinaenda pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili lilizungumziwa suala la wafanyabiashara, wote tumeona ni jinsi gani uwekezaji wafanyabiashara umekuwa mbovu katika mwaka huu unaoisha na ndiyo sababu sasa baada ya kuona na sisi tulivyopiga kelele nyingi kuhusiana na suala la kodi jinsi gani wafanyabiashara wanaondoka nchini, sasa naona hivi karibuni Mheshimiwa Rais aliita wafanyabiashara ninaamini sasa mnaanza kutuelewa na ushauri wetu mnaanza kuupokea kwa sababu nadhani tunaelekea kwenye mwaka wa uchaguzi, lakini hiyo itoshe kusema kwamba tutaendelea kutoa ushauri ambao ninaamini siku ambayo mtajisikia mtauchukua lakini tumekuwa kwenye hii mess kwa sababu ushauri mwingi ulikuwa haupokelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipaumbele kingine kilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na Madaktari Bingwa, tunakuwa na vitendanishi, lakini tumeshuhudia katika hili Bunge maswali mengi ya Wabunge yakiulizwa kuhusiana na suala na madaktari bingwa hawapo lakini vilevile Hospitali za Kanda pamoja na kwamba tumekuwa na hospitali za Kanda, hospitali hizo hazina vifaa muhimu sana. Tumesikia habari MRA, lakini vilevile nimekuwa nikizungumza na Wabunge wengine wakizungumza katika hizi Hospitali ya za Kanda hususan Hospitali ya Kanda ya Kaskazini na ile ya Mbeya kwamba kumekuwa na tatizo kubwa sana.

Kwamfano Kanda ya Kaskazini - KCMC lengo ilikuwa kuhakikisha kwamba kwa sababu tunajua magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa mengi hususan ugonjwa wa kansa na tukasema kwamba Hospitali ya Ocean Road ambayo ndiyo ilikuwa hospitali pekee inayoweza kutibu hasa kwa njia ya mionzi imelemewa, kwa hiyo Hospitali ya Bugando na Hospitali ya KCMC zikawa zimewekwa mahsusi kwa ajili ya kusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kusikitisha kwamba pamoja na juhudi hizo bado Hospitali ya KCMC ambayo tayari inaweza kupata hiyo mashine, lakini Serikali imeshindwa kujenga kile chumba kwa ajili ya kuhifadhi mashine hizo. Kwa hiyo nilikuwa naomba kwa kweli wananchi wengi wamekuwa wanakufa kwa kukosa huduma za hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa ukija kwenye bajeti ya mwaka huu kwa kweli mimi nasikitika sana kama mwanamke kuona kwamba bajeti hii Katiba yetu inasema kusiwe na ubaguzi wa aina yoyote, lakini kumekuwa na ubaguzi wa kijinsia na bajeti hii imekuwa gender insensitive. Kwa nini nasema hivyo suala la hedhi ni suala la kibaologia na sisi tulifurahi sana mwaka jana walipoondoa VAT kwenye pads (taulo za kike) na tumeenda hata nchi za nje kutangaza Tanzania ikaonekana kwamba imepiga hatua kuhakikisha kwamba na lengo kubwa lilikuwa ni kuhakikisha kwamba watoto wa kike wanakwenda shule ziku zote za masomo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi kwa sababu ni mwanamke kama mimi, watoto wa shule wa kike wanaotoka kwenye familia maskini wanakosa takriban siku 70 kwa mwaka kwa sababu ya masuala hayo niliyoyazungumza. Tulipiga vigelegele baada ya VAT kuondolewa, leo Mheshimiwa Waziri anasema wameifuta na sababu ya kuifuta wanasema kwa sababu lengo halijatimizwa. Hii ni Serikali, Serikali ina vyombo vyake vya dola ina vyombo vyake vya TRA ina kila kitu kuhakikisha kwamba kitu kikiisha pitishwa na Bunge kinaenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mifuko ya rambo ya plastiki imepigwa marufuku na tumeona utekelezaji wake kwa nini jambo kubwa kama hili linalohusu takriban nusu ya Watanzania lishindikane! Mimi naamini hata kama hao wauzaji au wasambazaji wamefanya hivyo Serikali bado ile VAT ambayo ni 18% wangeweza ku-ring fence kwa mfano mimi nachukulia mfano kuna wanawake kwa sababu watu katika umri huo ni kuanzia miaka 12 mpaka 50 sasa tukichukulia kama ni wanawake hawa au wasichana milioni 10 tuchukulie tu milioni 10 kwa mwaka yaani kwa maana ni kila mwezi kwahiyo hawa wanatumia labda pad moja ile I mean ile packet moja au wengine mbili, kwa hiyo tuchukulie wote ni moja kama wangechukua hiyo VAT ambayo ni 360 shilings kwa watu milioni 10 mara miezi 12, maana yake tungekuwa tumepata shilingi bilioni 43 kwahiyo Serikali ituambie hata kuzi-ring fence hiyo VAT wameshindwa? Kama kweli tatizo lilikuwa ni wasambazaji kwa nini wasinge-ring fence hiyo ili walau hizo fedha zinazopatikana basi ziwasaidie watoto wa shule ambao wataenda shuleni.

Kwa hiyo, mimi nadhani hilo ndiyo lingekuwa sasa wameifuta halafu mbadala wake ni mimi? Kwa sababu mimi nina hakika kuna watu tumewaona ambao wanatengeneza tayari walishusha, kwa hiyo wanatuambia tatizo ni wale wasambazaji. Kwa hiyo wasambazaji hao Serikali kama imeshindwa basi wa-ring fence hiyo hela halafu hiyo hela iende ikanunue hizo pad bure wagawe bure kama ambavyo wanafanya wenzetu wa Rwanda wenzetu wa South Africa na wenzetu wa Kenya, kwa hiyo huo ni ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuzungumzia hilo suala la ubaguzi, tunaangalia tunaona kwamba this time wamekuja Serikali inasema wanakusanya inaenda kukusanya kwenye wigs. Wigs ni bidhaa kwa ajili ya wanawake mawigi kwa Kiswahili. Lakini kuna watu natural hawana nywele, kwa hiyo lazima wavae hizo na unaona humu ndani mwangalie Esther Matiko, Susan Kiwanga umeona jinsi wamependeza, kwa hiyo kuna wengine hawana nywele natural wana vipilipili, kwa hiyo hizi zimeletwa kwa ajili hiyo. Kwa hiyo naendelea kusema kuwa kwa nini hawajachagua bidhaa ya wanaume waiwekee kodi wanachagua bidhaa za wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nadhani kwa kweli kuna kila sababu ya kuwambia Waziri kwamba hii bajeti imekuwa very gender insensitive na hatuwezi kukubaliana nayo, nilitegemea Wabunge wanawake tuandamane kupinga hili jambo, siyo hilo moja tu hasa hilo la pad. Lakini nimeanza kwa kauli ya kusema kwamba uzuri wa bajeti ni utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalia Wizara hizi mwaka jana kwa mfano Wizara ya Kilimo kama nilivyosema ambayo ndiyo inayoongoza kwa ajira ilikuwa imetengewa shilingi bilioni 48 lakini mpaka mwisho imepata only asilimia 42, ukija kwenye upande wa Viwanda na Biashara is even worse ilikuwa imepangiwa shilingi bilioni 90...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mosi, nitoe pole kwa Mheshimiwa Spika na kumshukuru Mungu kwa ajili yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kutoa pole nyingi sana kwa viongozi wangu Wakuu wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu na Manaibu Makatibu Wakuu na wajumbe wa Kamati Kuu waliopata misukosuko mingi wakati wakitetea demokrasia ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze na kumtia moyo Mheshimiwa Sugu (Osmond Mbilinyi), Mbunge wa Mbeya Mjini anayetumikia kifungo katika Gereza la Mbeya. Naamini haya yote yatapita kama upepo uvumapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma zaidi ya mara mbili hotuba ya Waziri Mkuu kuna maeneo mengi hayana ukweli na hayana uhalisia wa yanayotokea hapa nchini. Nikianza na mafanikio ya Awamu ya Tano kujenga ari ya uzalendo, kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Jambo hili limenishangaza kwa kuwa uzalendo msingi wake mkuu ni upendo na uelewano na ndiyo maana uzalendo haujengwi kwa kampeni bali kwa mahusiano mema na hivyo huja automatically. Vilevile hatuwezi kuwa na mshikamano au umoja kama kuna chuki, ubabe, matumizi mabaya ya dola kama ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na kuwa ulinzi na usalama dhidi ya upinzani umeimarishwa sana na ndiyo sababu kila leo ni wapinzani kukamatwa na polisi au kuripoti polisi na mahakamani. Mbaya zaidi hata walipopata dhamana ile siku ya Alhamisi Kuu eti gari za magereza zikawa mabovu wakati Kisutu Mahakamani magari mengi yalikuwepo bila kazi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ilipelekea viongozi hawa kuendelea kusota Segerea gerezani. Pia hata wafungwa na mahabusu waliokuwa wapelekwe Mahakama Kuu na nyinginezo walikosa kufika. Hii ni kinyume kabisa na huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu na haki za mfungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii imerejewa tena ukurasa wa 10 pale anapozungumzia masuala ya siasa baada ya miaka 26 ya Vyama Vingi nchini kuwa ni jukumu la kila chama kunadi sera zake. Najiuliza unanadi vipi sera wakati mikutano ya hadhara imezuiwa? Huku chama tawala kikifanya kupita Mwenyekiti wake wa Chama kwa kofia ya Urais huku wengine kina Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Mbatia, Mheshimiwa Zitto, Mheshimiwa Cheyo na kadhalika ambao ni Wenyeviti wa Vyama Taifa wakikosa fursa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua Wabunge na Madiwani kuruhusiwa kufanya mkutano ndani ya maeneo yao lakini ni wazi lengo la uanzishwaji wa vyama vingi na kazi ya vyama ni mikutano kwa ajili ya kupata wanachama. Hivyo ni ombi na rai yangu kuwa zuio hili liondolewe na kufuata Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992 iko wazi kwamba vyama vya siasa vitanadi sera zake sasa vitanadi vipi wakati Mheshimiwa Rais ameweka zuio?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unahamasishaje ujenzi wa demokrasia kwa wananchi wote kukiwa na ubaguzi ulio wazi? Ni jambo la ajabu sana kwamba katika awamu hii ubaguzi wa wazi wazi umetamalaki kinyume kabisa na tunu muhimu tulizoachiwa na Baba yetu wa Taifa. Tumemsikia Mheshimiwa Rais akisema hawa wamenipa kura msiwabomolee hata kama wamejenga ndani ya eneo la barabara au sehemu za vyuo na taasisi za Serikali huku wengine wakibomolewa tukiamini hawakumpa kura. Imani yangu ni kuwa unaposhinda wewe ni kiongozi wa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mshikamano kama nilivyosema unafanywa kwenye misingi ya upendo na umoja na ndiyo tunu muhimu kwa Taifa lolote vinginevyo tutakuwa tunajidanganya tukisema kuna mshikamano na amani. Niliposikia Wajumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara wakitaka kwenda kumtembelea mjumbe mwenzao Mheshimiwa Godbless Lema gerezani Arusha na zoezi hilo likakwama na baadaye Mwenyekiti na Makamu wake kuachia nafasi zao kutokana na sababu hiyo sikuamini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila sasa naamini kwa kuwa Kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii tulipokwenda kutembelea miradi ya maendeleo tulipofika Mbeya na kufika kwa RC na kwa kuwa ilikuwa weekend tulidhani ni busara kwenda kumtembelea Mheshimiwa Sugu, lakini cha ajabu hakuna Mbunge hata mmoja wa CCM aliyeambatana nasi jambo lililonithibitishia kuwa haiyumkini lililotokea Kamati ya Viwanda na Biashara ni kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kama kweli tungekuwa na mshikamano tuliouzoea Mheshimiwa Lissu angetembelewa na Wabunge wote bila kujali itikadi katika kipindi kirefu alipolazwa Nairobi Hospital. Katika hali hii ni wazi hatuwezi kusema tuna mshikamano kama viongozi. Ni ushauri wangu kuwa ni muhimu kutembea kwenye maneno yetu bado hatujachelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa Ofisi ya Msajili ambayo kimsingi ndiye mlezi wa vyama vyote vya siasa, imekuwa ama kwa makusudi ama kwa kujua na hasa ukizingatia Jaji ni msomi na ameapa kulinda Katiba yetu, cha ajabu anakubaliana na zuio la mikutano huku chama tawala kikifanya mikutano inayoongozwa na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Nilitegemea Mheshimiwa Jaji Mutungi angekemea hili lakini amekuwa akiandika barua vyama vya upinzani kujieleza pale ambapo wanatimiza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwezeshwaji wa wananchi, ni ushauri wangu kuwa elimu kuhusu mikopo itolewa kwa wakopaji ili wasije kunadiwa mali zao kwa kushindwa kurejesha. Vilevile kuna tuhuma nyingi kuwa mikopo hii inatolewa kiitikadi na hivyo wasio wanachama wa chama tawala wanatengwa. Naomba kama ni kweli jambo hili liachwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, UKIMWI bado ni tishio na hivyo ni muhimu sana sisi kama Taifa tuwe na vyanzo maalum vya fedha kwa ajili ya UKIMWI kwa kuwa bado fedha/dawa kwa asilimia mia moja tunategemea wafadhili wa nje. Ni muda muafaka sasa ule mfuko ulioimbwa muda mrefu utaanza basi uanze.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti,Wizara hii ndiyo yenye kusimamia haki na utawala wa sheria zilizowekwa na vyombo mbalimbali vya maamuzi. Katiba ndiyo Sheria Mama na hivyo ni muhimu mno Wizara hii kutekeleza majukumu yake kwa weledi na bila ubaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi katika kipindi hiki tunashuhudia jinsi Katiba yetu na sheria halali zinavyokiukwa. Mfano, tumeona na kusikia matamko yasiyofuata kabisa Katiba, Sheria na Kanuni yakitolewa hadharani tena bila woga, kama vile zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa wakati Sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu nakutokulipa watumishi wa Serikali annual increments na ama nyongeza ya mishahara iliyo kisheria eti kwa kigezo fedha zinaenda kwenye miradi mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo vya ukiukwaji washeria siyo tu vinakomoa wapinzani bali kutia doa nchi yetu ambayo ilionekana kama nchi yenye amani na utulivu na nchi ya kipekee (unique).Ieleweke kwamba bila haki hakuna amani wala upendo. Hivyo basi, tuna kila sababu ya kusimamia haki, Katiba nasheria ili nchi yetu iwe na amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matukio mbalimbali yanayoashiria Ofisi ya Taifa ya Mashtaka haifanyi kazi zake vizuri ama kwa makusudi ama kwa hofu. Baadhi ya mambo tunayoyalalamikia ni pamoja na kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji, kupotea kwa Ben Saanane, Azory, kupigwa risasi kwa Mbunge Mheshimiwa Tundu Lissu na kupotea kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo na kadhalika. Pamoja na matukio haya na mengine mengi Ofisi hii ya Mashtaka na Mkurugenzi wake amekuwa kimya kwa kutochukua hatua licha ya malalamiko mengi ya ndugu, jamaa na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa hakuna anayeweza kutengua uteuzi wa Mheshimiwa Rais ila yeye mwenyewe, hasa tukijua ni suala la kikatiba lakini pale inapoonekana waziwazi kuwa kuna mazingira yanayoonesha teuzi zinakuwa fadhila kwa jambo lililofanyika, tuna kila sababu ya kushauri. Wote tunajua Viongozi wa Kambi ya Upinzani akiwemo Mheshimiwa Mbowe wako kwenye Shauri Na.112 la 2018. Shauri hili linadhaminika lakini Hakimu wa Mahakama ya Kisutu aliwanyang’anya dhamana na kupelekwa mahabusu Segerea kwa siku 104 (zaidi ya miezi mitatu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichonishangaza ni Hakimu huyu kupandishwa cheo na kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Hata kama alikuwa amefikia kupandishwa cheo mtu yeyote ataamini ni fadhila kwa kuwa muda ulikuwa mfupi mno. Hata hivyo, rufaa ya Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu ilidhihirisha kuwa Hakimu huyo alikiuka utaratibu na hivyo dhamana ikawa wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haki kucheleweshwa ni haki kunyimwa. Wote tunajua wananchi wengi hawajui sheria lakini pia kesi nyingi zinachukua muda mrefu huku mahabusu wakiendelea kusota rumande. Mfano, kuna watu wamekaa rumande kwa miaka hadi sita bila kuhukumiwa na kwa sheria zetu hata mtuhumiwa akihukumiwa, ule muda aliokaa rumande hauhesabiki. Huu ni unyama na ukatili. Tunaishauri Serikali iliangalie suala hili ili watuhumiwa wasikae mahabusu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naiomba Serikali ijenge Mahakama za Mwanzo na za Wilaya ili haki ziweze kupatikana kwa wakati na kuwaondolea wananchi usumbufu wa kwenda mbali kutafuta haki zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, afya ni nguvu kazi ya Taifa lolote. Kamwe Tanzania ya Viwanda haitawezekana kama wananchi wake hawana huduma bora za afya. Pamoja na unyeti na umuhimu wa afya bado Wizara hii imetengewa fedha kidogo sana. Pamoja na Bunge lako Tukufu kupitisha zaidi ya trilioni moja, lakini zilizoenda za maendeleo ni 16% tu. Hii haiendani kabisa na ubora wa afya kwani, miradi mingi imekwama, lakini pamoja na upungufu huo bado fedha zinapungua hadi bilioni 866.2. Hali hii haina ishara njema kwa afya zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na watumishi wachache na kufanya kazi kwenye mazingira magumu bado viongozi wa kisiasa na Kiserikali wasio na taaluma hii wamekuwa wakiwadhalilisha kwa ama kuwasimamisha kazi au kutaka kujieleza mbele ya wananchi. Hivyo, ni muhimu tabia hii mbaya ya kuwa-demorolise madaktari wetu wanaopatikana kwa gharama kubwa sana iachwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, UKIMWI una uhusiano mkubwa sana na TB. Ni kama vile suala la TB halishughulikiwi sana. Hii ni hatari kubwa kwa kuwa, mgonjwa wa TB mmoja asiyetibiwa anaweza kuambukiza watu 10 – 20 kwa mwaka, lakini mbaya zaidi 40% ya wagonjwa wa UKIMWI pia, wana TB. Hivyo magonjwa haya yana mahusiano makubwa basi uzito unaopewa UKIMWI pia, uwekwe kwenye TB.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri nasaha ni muhimu sana hasa ikizingatiwa binadamu lazima akumbane na changamoto za maisha. Hivyo, ni muhimu kitengo hiki kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kujipanga kimkakati kuona ni jinsi gani watakavyotoa huduma hii hata ikibidi kwa gharama kwa kuwa, kuna wanasihi binafsi (wachache) wanaotoa fedha. Pia, vijana (wanafunzi) wawe wanapewa mafunzo kwa vitendo ili wamalizapo waende kusaidia wananchi wenye sonona na misongo ya akili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndoa za utotoni ni tatizo kubwa sana. Sheria hii ibadilishwe ili iendane na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, afya kwa wote haina mjadala ni muhimu sana, lakini Mtanzania awe na bima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuondolewa kwa tozo ya VAT katika pads bado ni kizungumkuti. Pamoja na Serikali kuondoa VAT bado fedha ni zilezile 2,000/= per pct na zaidi suala la je, kwa nini mpaka leo bado gharama ni ileile au zaidi?

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Wazee toka 2001 hadi leo haina sheria. Ni lini Muswada wa Sheria utaletwa ili wazee hawa wapate ahueni?

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imesaini mkataba (Abuja Declaration) ambapo kila nchi husika zilikubali kutenga asilimia 15 ya bajeti kuu ya Serikali kugharamia sekta binafsi. Ni jambo la ajabu kwamba, sasa inaonekana Serikali haioni umuhimu huo kwa kuwa, hivi majuzi Waziri wa Fedha alikiri haiwezekani kila mkataba tuutekeleze kama tulivyosaini kwa kuwa, sekta nyingine hazitapata kitu, nazo ni muhimu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, Wizara hii ina umuhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu. Hakuna nchi iliyoendelea duniani bila uwepo wa mawasiliano ya barabara, reli, anga na majini. Katika nchi inayoendelea kama Tanzania ambayo uchumi wake unategemea kilimo kwa asilimia 75 ni muhimu sana usafiri wa reli na barabara ukawepo ili kufikisha mazao sokoni.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ujenzi unaondelea ni muhimu sana barabara zijengwe kwa kiwango kinachostahili. Ikumbukwe kuwa zaidi ya 40% ya fedha za miradi yote imewekezwa kwa Wizara hii, hivyo, ni muhimu sana fedha hizi zikatumika ipasavyo. Kibaya zaidi fedha hizi zinanunua malighafi za ujenzi kutoka nje huku tukiwa na malighafi hizi kutoka nchini kama vile chuma cha Liganga ambacho kingesaidia mataruma ya reli na pia makaa ya mawe na madini mengineyo.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la ajabu kuona kuwa ATCL haina sera madhubuti na mpango mkakati, jambo linalosababisha shirika kuendelea kupata hasara kubwa. Pamoja na mpango wa biashara bado tumeshindwa kushika soko la utalii kutoka nchi mbalimbali kutokana na kutokuwa na uwanja wa ndege maeneo ya karibu na mbuga kama Serengeti hivyo, watalii hao kwenda Kenya na baadaye kusafirishwa na magari hadi mbugani, jambo linalotukosesha mapato mengi. Nashauri uwanja wa ndege wa Seronera ukarabatiwe ili watalii watue hapo na iwe rahisi kwenda kutalii.

Mheshimiwa Spika, kuna kilio kikubwa cha wananchi wa Dar es Salaam, hasa Ubungo - Kibamba, waliovunjiwa nyumba na cha ajabu tunaelezwa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze (Express Way), haitajengwa kwa sasa. Jambo hili limetonesha vidonda kwa wale waliovunjiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Uwanja wa Ndege wa Msalato umekuwa ukizungumziwa lakini cha ajabu pamoja na Makao Makuu kuhamia Dodoma uwanja umekuwa ni huu ulio katikati ya Jiji na ni mdogo. Mwanzoni tuliambiwa ni wa muda tu lakini tumeshuhudia ukiendelea kupanuliwa na watu wakivunjiwa nyumba zao. Hivyo, nataka kujua ile ahadi ya Uwanja wa Msalato ni lini itatimia?

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Hali ya Hewa nayo imekuwa na shida kubwa sana. Sielewi ni vifaa vya kizamani au ni utaalam hafifu. Inashangaza tunapopewa forecasts ambazo haziendani na uhalisia. Mfano kile Kimbunga Keneth kilivyotangazwa na hali ilikuwa sivyo kabisa, matokeo yake madhara yakawa mikoani na si kule Mtwara. Ni aibu kubwa sana katika ulimwengu huu wa digitali bado forecasts zinakuwa hazieleweki. Iko siku tutaambiwa kutakuwa na jua kali ghafla mnapata mvua za mafuriko, hivyo inakuwa janga kubwa na vifo.

Mheshimiwa Spika, kule Marangu kuna barabara kutoka Mtoni – Kirua, ujenzi ni kama umesimama lakini cha ajabu hata zile sehemu ambapo ujenzi umekamilika madaraja hayajajengwa. Hali hii ni hatari sana kwa kuwa barabara ni pana lakini kwenye madaraja ni nyembamba kuweza kupitisha gari moja tu, hivyo kwa madereva wageni kuna hatari ya kupata ajali. Mfano Mto Ghona/Wona, Mto Makoa, kwa kifupi mito yote toka Marangu Mtoni mpaka Kilema madaraja yake ni tishio kwa watumiaji.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa Dar es Salaam ni jiji kubwa kuliko majiji yote na lenye kuiingizia nchi pato kubwa sana. Hali ya msongamano Dar-es-Salaam inapoteza kwa kiasi kikubwa pato hilo. Haiwezekani gari kutoka Ubungo hadi Kibaha kilometa 30 litumie saa 2 – 3 wakati kwa hali ya kawaida ni dakika 30 – 45. Hali hii imekuwa mbaya zaidi kutokana na ujenzi wa barabara unaoendelea. Hivyo basi, ni muhimu sana malori ambayo ndiyo chanzo kikubwa cha foleni kutokana na ama kuharibika na ukubwa wake yatafutiwe njia mbadala au dry port eneo la Mlandizi au Ruvu kupunguza adha hii kubwa ili kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, suala la mawasiliano ya simu ni muhimu sana. Hivyo ni muhimu miundombinu ya minara iboreshwe ili kupata usikivu mzuri. Imekuwa ni kilio kikubwa kwa tatizo la usikivu wa simu kutoka eneo moja kwenda lingine.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, umeme ni nishati muhimu sana na bila umeme wa uhakika tusitarajie Tanzania ya Viwanda wala maendeleo ya kasi. Kwa bahati nzuri sana Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi sana ikiwemo upepo, makaa ya mawe, gesi asilia na maji. Tunatambua kuwa umeme wa maji ndio ulio na bei rahisi zaidi, ila angalizo la chanzo cha maji ni mabadiliko ya tabianchi.

Inashangaza sana kuona tumeshadadia mradi wa Stiegler’s Gorge bila kuchambua kwa kina uwezo wake (sustainability). Ni lazima tujiulize maswali yafuatayo; je, baada ya miaka mitano na kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi tutakuwa na maji toshelezi? Hasa ikizingatiwa mvua ndicho chanzo kikuu? Swali la pili, je, athari za kimazingira zimezingatiwaje, hasa kuzingatia ukatwaji mkubwa wa miti?

Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua mbalimbai zilizofikiwa kwa mradi huu na kwa kuwa kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa, naomba kwa heshima kabisa Serikali ibadili msimamo wake na kuacha kabisa mradi huu ambao athari zake ni kubwa kuliko faida.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu nimehoji sababu ya wateja wa umeme kulipia nguzo wakati nguzo hizo zinakuwa mali ya TANESCO? Kwa nini wakati tuna simu za Tanzania Postal & Telecommunications hatukulipia nguzo? Sasa ni sababu zipi zinafanya aliyewahi na kununua nguzo 10 wale wateja wapya watakaotumia nguzo zangu wasinilipe fidia? Wao watalipa service charges tu?

Mheshimiwa Spika, umeme wa REA ni muhimu sana hivyo, tunaomba REA III iongezwe kasi ili vijiji navyo viweze kuendelea na kupunguza kasi ya vijana kuhamia mijini.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hi ili niweze kuchangia hoja hizi mbili muhimu, miswada hii miwili muhimu sana, kwa afya za Watanzania lakini vile vile kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuanza kwanza nitoe pongezi kubwa kwa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, lakini vilevile kwa Kamati ambayo kwa kweli mimi ni Mjumbe na imefanyakazi kubwa sana ndio sababu kamati hii inaitwa Gwantanamo kwa hiyo nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niwapongeze Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara kwa kuweza kufikisha miswada hii miwili hapa mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba kama ambavyo Waziri amezungumza na kama ambavyo wengine wamezungumza miswada hii inakuja wakati ambapo imechelewa lakini ni wakati muafaka vilevile kwa sababu kwa kweli ukiangalia ni lazima kuwe na sheria inayojitegemea kuhakikisha kwamba masuala ya maabara na masuala ya taaluma ya kemia inafanya kazi yake sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba pamoja na kwamba tayari kuna marekebisho mbalimbali bado nitakuwa na marekebisho yangu lakini nianze na muswada wa kwanza ambao unahusu Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya mwaka 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba maabara ina mchango mkubwa sana kwa Watanzania na kwa jamii nzima ya Watanzania. Lakini muswada huu unakuja kutusaidia sana katika kuhakikisha kwamba maabara zetu zinafanya kazi vizuri, lakini vilevile sheria inaonyesha ni jinsi gani Mkemia Mkuu anaweza kusimamia maabara mbalimbali hasa ikizingatiwa kwamba kuna maabara nyingine zilikuwa hazifanyi kazi zake vizuri kwa kufuata utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba kwa kweli maabara hii imekuwa na mchango mkubwa sana na ina-cut across kwa mfano utagundua kwamba inafanya katika Wizara zote kwa mfano Wizara ya Waziri Mkuu utaona kwamba masuala ya madawa ya kulevya ni jinsi gani maabara hii basi inaweza kuchunguza. Lakini ukija kwenye Wizara ya Afya unaona ni jinsi gani maabara zimeweza kusaidia sana sana watu kutambua nani baba mzazi wa mtoto hasa ikizingatia kwamba sasa hivi kuna matatizo mengi, familia nyingi zimeonekana kwamba watu wanadanganya lakini inapofikia lazima mtoto ajulikane baba yake basi itakuwa ni rahisi. Lakini ile kwa ajili ya masuala mazima ya DNA.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna watu wengine wameweza kupoteza maisha yao kwa mfano unakuta mzazi anazaa mtoto mwenye jinsi mbili, kwa hiyo, anaona labda huu ni kizuka au nini. Kwa hiyo, maabara zinaweza sasa kutatua kuona ni jinsi gani ambayo ina nguvu akabaki ni mwanamke au ni mwanaume kwa hiyo haya mambo yatakuwa yameweka uwazi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija sasa kwenye muswada wenyewe kuna mambo ambayo nadhani tuyaangalie pamoja najua kwamba kutakuwa amendments mbalimbali ambazo zijaziona, lakini ukiangalia kifungu cha 4(4) naamini kabisa kwamba hii mamlaka uanzishwaji wake kile kipengele cha 4(3)(a),(b),(c),(d) na (e) vinajitosheleza kabisa. Nilikuwa napendekeza kifungu 4(4),(5) na (6) havina sababu ya Attorney General kuingia pale kwa sababu tayari ukiangalia zile kazi za juu zinaonesha kabisa mamlaka yenyewe inajitosheleza. Kwa hiyo, kama kuna mtu atakuwa na tatizo lolote aende akadai sehemu nyingine lakini nilikuwa nadhani ikiishia pale namba 4(3) inatosha mpaka (e) ile (4),(5) na (6) iondolewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina marekebisho kifungu cha 7 nadhani kwamba kutakuwa marekebisho wengine wataleta au mimi nitaleta kwamba hakuna sababu ya chairperson au chairman kwa sababu nikisema chairman it means also mwanamke kwamba ni lazima hiki kitu ni cha kitaalam zaidi na kitaaluma kwa hiyo kuleta mtu ambaye ana managerial experience bila kutuambia huyu mtu ni lazima awe amebobea katika masuala mazima ya sayansi hatuwezi kwa mfano kumpeleka lawyer akawe Mwenyekiti wa kusimamia watu ambao wana taaluma zao.
Kwa hiyo, nilikuwa napendekeza kwamba ni lazima huyu Mwenyekiti vilevile wa Bodi au ni mbobezi katika masuala ya kiataalam ya kikemia au ya maabara ili wale wataalam wanaposema naye aweze kusema. Kwa sababu anaweza vilevile naye akadanganywa kama hayuko kwenye hiyo taaluma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri pia ni lazima kuwe na balance ya upande wa private sector, lakini naona pale vyote katika kifungu hicho cha 7 ukiangalia composition ya board members sioni kama kuna upande wa private sector ambao umeshirikishwa na siku zote tunaongea PPP; kwa hiyo, nadhani kuna haja vilevile ya kuongeza sekta binafsi ili kuweka uwiano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoka kwenye muswada huu sasa nielekee kwenye muswada mwingine ambao nitajielekeza kwenye huu muswada wa taaluma. Kuna mambo ambayo nadhani yanahitaji pia ufafanuzi. Tunaongelea suala la taaluma yaani Chemist Professional Act. Kama ni taaluma ya kemia nilikuwa naomba maelezo kutoka Serikalini kwenye kifungu cha 4(7)(h)na (i); tunahitaji board member au council member ambao sioni wanasaidiaje hii taaluma ya kemia, kwa mfano unaposema u-representative au senior officer or above representing public service management huyu mtu wa utumishi anasaidia nini katika hii council hili baraza la kitaalamu .
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kifungu cha (i) kuna mtu anaitwa a police officer of rank of Inspector or above representing the Inspector General of Police swali la kujiuliza hivi kwenye hili baraza wanaenda kujifunza kutengeneza bunduki, wanaenda kufundishwa jinsi ya kutumia mabomu au kitu gani, kwa hiyo, nilikuwa nadhani watuambie tu huyu polisi kwenye Baraza la Wanataaluma anaingia kufanya nini. Kwa hiyo, nikipata hayo maelezo nitafurahi sana (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba Waziri ni tu ambaye yuko gender sensitive pamoja na kwamba hawajeleza kama kutakuwa na representation ya wanawake nilikuwa napendekeza kwamba kuwa kuwe kabisa na kipengele cha asilimia ngapi labda kama hawa members ni tisa basi walao wanawake wanne kwa sababu naamini kabisa kuna wanawake wengi sana wasomi sasa hivi kwenye fani ya sayansi miaka nenda rudi kuna Maprofesa wengi tu.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba kipengele kabisa cha gender kiwepo ili isije hii board member ikawana mwanamke mmoja au hamna kabisa kwa sababu tumezoea mfumo dume, lakini namwamini Mheshimiwa Waziri ananielewa ndio sababu anafurahi kwa hiyo watakiweka hicho kipengele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilitaka kuzungumza ni kipengele ambacho nacho nilisikia kimesharekebishwa sina haja kurejea. Kimezungumzwa na upande wa upinzani vilevile kuhusiana na kipengele cha 9(1) nadhani tayari wamekipata lakini ilikuwa kwamba at least masters ili walau hata mwenye Ph.D aweze kugombea hiyo nafasi.
Pia kulikuwa na suala moja ambalo nataka kulizungumza ambalo linahusu kipengele cha 18 nilikuwa nadhani kuna haja kabisa kwamba nchi hii the right to be heard is very important kwa hiyo nilikuwa nadhani huyu mtu ni lazima kama kuna tatizo lolote au hataridhika na maamuzi basi awe na haki ya kuweza kujitetea, asikilizwe na aweze kujitetea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ya mwisho ni kipengele cha 30 ambacho kinazungumzia procedure for inquiry nilikuwa napendekeza kwa sababu tayari tumeona kwenye clause ya 8(2) inaongelea kuhusu Kamati za Baraza na moja ya Kamati hiyo ni kamati ya nidhamu yaani disciplinary committee nilikuwa napendekeza kwenye 30(2); the council shall give opportunity for a chemist professional against whom misconduct is alleged, to appear before the disciplinary committee na sio before the council kwa sababu ninaamini kwenye disciplinary committee ndio masuala mazima ya nidhamu, jinsi gani mtu anaenenda, anaweza akaenda kule halafu badaye ndio kama itashindikana aende kwenye council, lakini kwenda moja kwa moja kwenye council naona ni kuipa kazi kubwa sana Baraza.
Kwa hiyo, nilikuwa nategemea hizi kamati tatu ambazo zimeorodheshwa kwenye 8(2) zingepewa majukumu, na jukumu moja la hii disciplinary committee ingekuwa pia kusikiliza watu wenye matatizo ya kitaaluma ambayo kwa vyovyote vile hii disciplinary committee pia ina watu ambao ni wana taaluma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni ambalo limezungumzwa na mimi pia nataka nizungumzie kuhusu mamlaka makubwa sana aliyopewa Mheshimiwa Waziri kwenye kifungu cha 34.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nadhani kuna haja na nimeangalia marekebisho ya Wizara bado sijaona kabisa kama kipengele hicho kimeguswa na ni vyema hii taaluma au hii professional ikapata independence ya kutosha na wanasiasa wasiingilie sana kazi hizo kwa sababu mara nyingi sisi wanasiasa tunataka tusikie kile ambacho tunataka kusikia au kuambiwa kile ambacho tunachotaka kusikia, kwa hiyo, ni vyema sana na ninaamini sana Wizara hii na niamini kwamba watawapa uhuru wa kutosha hivi vyombo viwili viweze kufanya kazi zao vizuri na kwa maana hiyo hizi bodi ziwe kweli za wanataaluma na zisiingiliwe sana na wanasiasa, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nyingine siku ya leo kuweza kuchangia katika Muswada huu muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote najiuliza hivi huwa tunatunga sheria ili nini? Naamini tunatunga sheria ili kutibu jambo fulani na tunatunga sheria tukiamini kwamba walengwa wanakubaliana na mambo mengi kwa sababu ndiyo yanayokwenda kuwa-affect. Katika hili walengwa wakuu ni walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na tumechambua Muswada huu kwa kina, tumekuwa na wadau mbalimbali na wadau hawa wengi hawakukubaliana kabisa na Muswada huu. Sababu kubwa ni ile ambayo Waheshimiwa wengi wanaiongelea nalo ni suala la chombo kimoja cha kuwasimamia walimu lakini tumeendelea kuwafanya walimu hawa kama kuku wa kienyeji yaani wana vyombo vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee walichokisema. Walimu wamekuwa na vyombo vingi kiasi kwamba wanajifananisha na wafungwa. Kwa mfano, wanasema, hata wafungwa wa mauaji hulindwa gerezani na askari wa aina moja tu ambaye ni Askari Magereza. Hatujawahi kuona vikosi vyote vya majeshi vikipelekwa gerezani kuwalinda wafungwa. Hata kwenye hitimisho lao wanasema kwamba wanaomba sana hili jambo au huu Muswada ungesubiri. Ukienda kwenye maoni ya Chama cha Walimu nao wanasema hivyo hivyo, hiki ni chama cha kuteteta haki za walimu na wanadai wao ndiyo walimu walioko madarasani. Nadhani tuna kila sababu, sawa tutapitisha kwa wingi wetu lakini kimsingi bado huu Muswada ulikuwa haujaiva kwa sababu una makosa mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa mfano, kumekuwa na hoja kwamba hii Bodi ya Kitaaluma ukiangalia kuna taaluma nyingine nazo zinasimamiwa na Bodi na mifano inakuwa kwa mfano Doctor’s Board, Engineers Board, lakini tuwaulize, hivi hizo Bodi mnazozi-refer zenyewe zina Tume? Hazina! Kwa nini ni walimu tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia hoja ya kwamba walimu wanasimamiwa na vyombo zaidi ya vitano na leo tunaongeza cha sita ni kweli na nadhani siyo sawasawa. Ukiangalia huu Muswada mzima kama ambavyo
wengine wamesema seriously ni kuwadhibiti walimu. Ukiangalia toka mwanzo mpaka mwisho hata hii hotuba ya Waziri hivyo hivyo, ni kuwadhibiti zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TSC sawa najua ile ni Kamisheni ya Utumishi na hii ni kwa public. Tukasema kulikuwa kuna shida gani hawa walimu ambao sasa wanakuwa included na wale wa private school kwa nini nao wasiingizwe huko tukafanya maboresho. Hivi ni rahisi kuwa na sheria mpya au ni rahisi kufanyia amendment sheria ambayo tunayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata Chama cha Walimu Tanzania wanasema hivyo hivyo kwamba wanakubaliana na TSC iboreshwe ili tu wawaingize kwa sababu TSC iko mpaka kwenye Wilaya. Yalikuwa ni mawazo ambayo nadhani yangeungwa mkono lakini Serikali ikishaamua jambo lake inakuwa hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Muswada nasema ulikuwa haujaiva, kwa sababu tumejitahidi kwenye Kamati kuufanyia maboresho, vilevile tulikuwa na Wizara kama kawaida, Ofisi ya AG lakini ukiangalia suala hili la Mwenyekiti wa Bodi ateuliwe na Rais lilizungumzwa na wadau wameweka mapendekezo na sisi tukauliza. Wameleta majibu yao, haya hapa wakasema hata kwenye Bodi nyingine Wenyeviti na wajumbe wanateuliwa na Waziri. Kwa hiyo, masuala kama haya yanatia aibu na ndiyo sababu nilimuuliza AG hii ni sawasawa na akanijibu akasema siyo sawa. Sasa unajiuliza kama AG Office ilikuwa kwenye Kamati hili hawakuliona na wamekuja wakatuambia ni sawa? Kwa hiyo, nadhani kuna tatizo. (Makofi)

Mheshimia Mwenyekiti, sasa niende kwenye Muswada, hiyo ilikuwa ni preamble. Katika Muswada huu naanza na section 5. Pamoja na kwamba nitakuwa na amendments zangu kesho lakini niseme tu kwamba hii composition ya Bodi haijakaa vizuri kabisa, nimelisema ndani ya Kamati na nalisema ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongeza kitu kipya kabisa kwa sababu tunaingiza private sector kwenye Bodi hii na private sector tunaweza kusema ni about 20 percent ya walimu wote. If that is the case, ni lazima kuwe na representation ya private sector. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia na AG atusaidie, kile kifungu cha 5(1)(iv), mimi najua members wa Bodi wanafanana kwa maana ya kwamba haendi pale kama sekretarieti au mtumishi. Ukisoma Kifungu cha 5(1)(iv) kinasema, two members appointed by the Minister from amongst persons with requisite qualifications to assist the Board in the discharging of its functions. Sasa najiuliza hii ni kazi ya member wa Bodi au ni ya sekretarieti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani kwa sababu kuna kifungu cha 12 ambacho kinazungumzia sekretarieti, hawa watu waende kule. Hapa tunahitaji members ambao wanakutana mara chache na hawa hawawezi kuwa na function ya kumsaidia Registrar. Hawa wanakuja kwa ajili ya maamuzi au mambo maalum. Kwa hiyo, hicho kifungu kiondoke lakini kiwe replaced na walimu wawili kutoka kwenye private sector. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema na narudia kusema, kama alivyosema Mheshimiwa Anatropia asubuhi, utaona Waziri ana jukumu kubwa kweli la ku-appoint, appoint, appoint. Mimi nadhani kwa sababu hapa Tanzania tuna vyombo vikubwa ambavyo ni umbrella vya walimu, kuna Chama cha Walimu Tanzania au Tanzania Teachers Union – TTU, vilevile kwenye upande wa private tuna TAPIE, tuna cha CHAKAMWATA ambacho mimi nilikuwa sikijui vizuri, kwa hiyo, kuna kila sababu ya hizi organisation zi-nominate watu wake halafu waingie kwenye Bodi na siyo Waziri kwa sababu hakutakuwa na hiki kitu tunaita carrot and stick. Kwa hiyo, nadhani kuna hiyo haja ya kuona kwamba hizi organisations kubwa namna hii zi-nominate watu wake waingie kwenye Bodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda section 7 anasema kwamba kazi ya Bodi ni pamoja na ku-suspend, lakini hawa walimu tayari wameajiriwa. Sasa nilikuwa naomba kujua kwa mfano wale wa Serikalini (public), je, Wizara ya Utumishi itakuwa consulted? Nani ana mandate? Ndiyo mambo kama haya tunasema inabidi yaangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mwalimu kwa mfano amekosea amelewa, kama amelewa ameshindwa kufundisha maana yake taaluma imeathirika, lakini vilevile kiutumishi amefanya makosa. Naomba majibu kutoka Serikalini, huyu mwalimu atachukuliwa hatua na Bodi, TSC au Wizara ya Utumishi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya ndiyo mambo ambayo tunaona kwamba kulikuwa kuna kila sababu ya kusubiri ili tu-harmonise halafu tuone tunaendaje mbele. Hakuna sababu ya kutunga sheria ambayo kimsingi haitaweza kufanya kazi kwa sababu TSC atasema mimi hili ndio jukumu langu, amelewa kwa hiyo, ni suala la kiutumishi, huyu wa Bodi atasema ameathiri taaluma wanafunzi hawajafundishwa vizuri. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo naona yanakinzana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye suala hilohilo la Waziri kuteuwa, ukienda hiyo section 14, wale watu wawili wa mkoani ambao anawaita supervisory officer, ambao nadhani pia wawe ni Assistant Registrar kwa sababu wanaenda kufanya kazi hiyo, hawaendi ku-supervise chochote. Nadhani kazi hii ni competitive kwa nchi nzima. Mimi nilikuwa nadhani iwekwe kwenye gazeti watu wa-apply halafu Bodi ndiyo itasimamia wakati wanafanya hiyo kama ni interview, whatever, then wale watakaopatikana ndiyo waletwe Waziri awapeleke huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru hili la criteria za registration walau Serikali imekubali, sijaona ammendments zao kwa hiyo sijui, lakini ukiangalia zile criteria za registration mambo yalikuwa mazito kwelikweli, nadhani kesho nitaona. Maana ammendment yangu imeletwa lakini ya Serikali sijaiona isije ikawa na-repeat na sijajua ni kwa sababu gani hazijaletwa? Sijajua kama wanavizia waone kwanza zetu halafu ndiyo waende wakabadili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kuhusu renewal ya leseni. Tulikuwa tunahoji kuhusu license, license ndiyo inapaswa kuwa renewed na sio registration.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muswada ukiangalia ile Part IV kwa kweli Mheshimiwa AG naomba usome section 41(3)(b) utuambie hiyo sentensi ina maana gani? If the employer of a person is identifiable from the details of the compliant, the employer. Ndiyo sababu nasema haya mambo yanatia kidogo kashkash, kwa hiyo, nadhani kuna kila sababu ya kwenda kupitia na kuona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba hawa watu wanapokuwa registered wanakuwa gazzeted, lakini wakifanya makosa wakiwa de-registered mnataka wapelekwe kwenye magazeti yote nchi nzima tena ambayo yana circulation ya haraka. Hii nia ni ovu, mnataka kuwadhalilisha walimu. Kwa nini na katika hilo msiwaweke kwenye gazeti, mnataka kuwaweka kwenye local news paper ili kila mtu aseme aah, mwalimu yule alifanya vile amefukuzwa. Kwa hiyo, nadhani hiyo siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba sisi CHADEMA kumbe tulikuwa far ahead kwa Serikali kwa sababu kwenye policy yetu hii hapa, kwenye masuala ya taaluma ya walimu tuna sera yetu na tunasema kwamba, CHADEMA itaanzisha Sera ya Maendeleo ya Walimu ambayo lengo lake litakuwa ni kuweka miongozo ya vigezo vya chini vya mahitaji ya mafunzo kwa walimu, kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi na mitaala. Sera hiyo, itaweka utaratibu kwa ajili ya kumuendeleza mwalimu kitaaluma kila wakati ili kuboresha utendaji kazi wa mwalimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaona ni jinsi gani sisi kwenye masuala ya walimu tumewapa walimu kipaumbele kwamba, lazima waendelezwe. Hii ya kwenu niseme tu mnawadhibiti, mmeanzisha ile Tume mkasema mtawapandisha madaraja, mtawaongeza mshahara, this is the third year hamjafanya hivyo. Leo mnasema kwamba mtaimarisha utaalamu wa walimu, mtawapa mafunzo, hamna hata fedha, mtawezaje kuwaendeleza kitaaluma? Hata hizo sehemu za kuwaendeleza hakuna.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ya awali na mimi niweze kuchangia katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali kama yalivyowasilishwa na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza la ujumla ambalo nataka kulizungumzia ni suala zima la mabadiliko haya ambayo tumekuwa tukiyapata mara kwa mara. Mimi nadhani ni muda sasa umefika kwa Serikali kuwa na mpango maalumu wa kurekebisha sheria zote kwa pamoja yaani kufanya mabadiliko makubwa kwa sababu kuanzia nimeingia kwenye Bunge mwaka 2005 tunaona marekebisho madogo madogo lakini kwa kipindi hiki cha kipindi Awamu ya Tano yamekuwa mengi kweli kweli na ukiangalia sanasana ni kuongeza adhabu na mambo mengine. Nadhani kuna kila sababu ya kuwa na mpango maalum wa Serikali hasa kwa kutumia Law Reform Commission ili kufanya marekebisho makubwa au kutunga sheria hizi upya ili wananchi wawe na amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Sheria ya Ustawi wa Wanyama, Sura ya 150. Tunaona marekebisho ya kifungu cha 59 cha Sheria mama kwa kuongeza adhabu kwa mfugaji anayefuga mifugo. Kama ambavyo ameongea Msemaji wa Kambi ni vigumu sana kujua mfugo au mnyama wako ana uoga, huo uoga unaupimaje? Kwa hiyo, nadhani tunavyotunga sheria na Mheshimiwa AG nashukuru umerudi tutunge sheria ambazo zinatekelezeka. Kwa sababu lengo la sheria yoyote ni kuhakikisha inaenda kutekelezeka lakini sheria kama hii kwa mfano ng’ombe hivi Mmasai anafuga ng’ombe mia moja na kuendelea atajuwaje ng’ombe huyu ana woga/wasiwasi na kwamba atachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka kujua sheria hii inagusa wale wanyama ambao tunawafuga ndani kwa mfano sisi kule Uchagani tunafuga ng’ombe na mbuzi ndani, nani atakuja kuhakikisha kwamba ng’ombe huyo ana woga, njaa au vyovyote vile. Kwa hiyo, nadhani kuna kila sababu ya kuangalia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo kubwa lililopo hapa ni malisho na tunajua kwamba Serikali ilitwaa malisho mengi na kubadilisha maeneo hayo kuwa ama hifadhi za Serikali au mapori tengefu. Kwa hiyo, nadhani wakati umefika sasa tuhakikishe kwamba pamoja na kutunga sheria hii lakini hatuwaadhibu wale wanaofuga mifugo kwa sababu Serikali yenyewe imeshindwa kuwapa maeneo ya kufugia mifugo yao lakini vilevile sehemu za kunywa maji, kwa hiyo, wanyama hao wanakufa. Tumeshuhudia wanyama wengi wanakufa kwa sababu ya kukosa maeneo ya kufugia. Vilevile tumeshuhudia matatizo makubwa au migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji ambayo imepelekea sehemu nyingine wanyama wamekuwa wakiuwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani kwanza Serikali itimize wajibu wake kuhakikisha kwamba mnapoleta hii sheria mmeweka mazingira wezeshi hii mifugo isife njaa kwa sababu hakuna mfugaji atakayekuwa anafuga mifugo ambayo anaamini huo ndiyo urithi wake kwa watoto, hicho ndicho chakula chake cha kila siku halafu mnyama huyo afe kwa makusudi. Kwa hiyo, nadhani ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba wanakuwa na maeneo maalumu ili wafugaji wetu waweze kufuga mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwenye sheria nyingine ambayo ni National Leaders Funeral Act, Sura
419. Najua kwamba sheria mama ilitungwa mwaka 2006 na ni bahati nzuri na nashukuru Mungu kwamba hakuna mpaka leo Kiongozi wa Kitaifa ambaye amefariki katika kipindi hicho. Wote tunajua kwamba kwa mila na desturi zetu hakuna mtu anayeweza kuachia ndugu yake kwa kuwa labda ni Rais, Makamu wa Rais au ni Waziri Mkuu aende akazikwe kwenye hilo eneo ambalo limetengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani kuna kila sababu ya kuirejea sheria hii na kuona kama tunaondoka kwenye hizo mila na kama ni hivyo basi tuambiwe hilo eneo lililotengwa liko wapi na kweli tunaamini kwamba wakifa hao viongozi kwa sababu wote hapa ni wasafiri tutakufa tu itakuwa ni lazima kuzikwa katika eneo hilo. Kwa hiyo, mnatulazimisha kutoka kwenye mila na desturi zetu kwa sababu huyo ameshakuwa ni kiongozi then abandon mila zetu tunampeleka huyu mtu kumzika katika eneo maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani tuangalie uhalisia wa mambo haya tusitunge tu sheria kwa sababu ni sheria au tumeichukua kwa watu lakini tuangalie katika mazingira tunayoishi hivi kweli nani atakayekubali ndugu yake anatoka labda kule Songea aende akazikwe kama ni Dodoma hayo makaburi yatakuwepo au ni Dar es Salaam siyo rahisi sana. Kwa hiyo, nadhani tuangalie ni jinsi gani tutalifanya jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye sheria ambayo inananihusu sana Sheria ya Virusi na UKIMWI. Nimesikiliza kwa makini na nimepitia vifungu kwa vifungu nikaona kwamba jambo ambalo linagombaniwa sana, kwanza niipongeze Serikali na kuishukuru kwa kuleta mabadiliko haya ya umri kwa sababu natoka kwenye Kamati ya Huduma za Jamii na jambo hili tumelisisitiza sana kwamba kutoka umri wa miaka 18 waruhusiwe kujipima wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu ndizo ambazo zinatuongoza na tunajua matukio yanayotokea, watoto wa chini ya miaka 15 ni wengi sana ambao wanapata maambukizi. Nazungumza hilo kama mshauri maana nimekuwa nikishauri baadgi ya wazazi na watoto. Kwa mfano, kwa Mkoa wa Shinyanga zaidi ya asilimia 50 ya watoto wa kike wanapata ujauzito chini ya miaka 18 na wote tunajua kwamba Virusi vya UKIMWI vinatokana na tendo la kujamiana na tendo hilohilo ndilo linapelekea mtu kupata mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeshuhudia watoto wa miaka 12 wanapata ujauzito ina maana nao wamefanya vitendo hivi. Pia kuna wale wengine ambao hawajavunja ungo kwa sababu wote tunajua huwezi kupata mimba kabla hujavunja ungo na watoto wanaovunja ungo ni kuanzia miaka hiyo 11 na kuendelea, kwa hiyo, tunaamini kwamba watoto hawa wengi wana virusi vya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunapozungumzia miaka 12 tunajua kwamba kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wanawalawiti na kuwabaka watoto wao na wazazi hao wengine wanaweza wakawa na virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo, itakuwa vigumu sana mzazi ambaye ana virusi vya UKIMWI kuruhusu mtoto wake kwenda kupima au kwenda kumuelezea apimwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani mtoto wa miaka 12 ni mkubwa tu kwa mazingira ya kawaida na ana uelewa wa kutosha. Katika shule zetu za msingi kuanzia darasa la pili ambapo ni mtoto mwenye miaka sita, saba na nane wanaanza kufundishwa elimu ya virusi UKIMWI na UKIMWI.

Kwa hiyo, suala la kwamba sisi sijui Tanzania mila na desturi, hizi mila na desturi zetu ni tofauti na za Kenya, Uganda, Malawi au Rwanda? Hakuna tofauti. Hata kama zingekuwa tofauti sisi tunaamini kwamba hawa watoto wakijitambua wataweza kujipima na kutambua hali zao za kiafya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza na nimepeleka Jedwali la Mabadiliko nadhani litakuja kwamba umri uwe miaka 12. Sitaki kurudia yale yaliyosemwa na Msemaji wetu wa Kambi kwani ameeleza waziwazi kwamba tunavyopunguza umri wa kwenda kupima maana yake tunapata watu wengi zaidi ambao watapima virusi vya UKIMWI na kujua afya zao. Naamini kabisa Tanzania kama nchi tunapaswa kuwa mstari wa mbele kwa sababu hatuwezi kufikia ile 90, 90, 90…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ya pili hiyo.

MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo ya kwanza?

MWENYEKITI: Ya pili.