Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sophia Hebron Mwakagenda (64 total)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda Waziri atuambie, kwa migodi kama ya Kiwira ambayo tayari inazalisha, je, tunapata kiasi gani kama Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nifanye masahisho kidogo, Mgodi wa Kiwira haujaanza kazi rasmi, uko katika kukamilisha detailed design na hatua za kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi. Hata hivyo, mgodi huo utakapoanza, Halmashauri zote zinazohusika zitanufaika na mambo yafuatayo. La kwanza, Halmashauri zitakuwa na uwezo wa kukusanya service levy ambayo ni asilimia 0.3. Kadhalika zitaweza kupata mrabaha ambao utaingia Serikali kuu. Pia, mradi wa Kiwira unakadiriwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 utakapoanza kufanya kazi. Kwa hiyo, wananchi wa Mbeya na Watanzania wengine wataendelea kunufaika na kupata ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika mradi huo utakuwa sasa na kipengele kinachowalazimisha wakandarasi na wamiliki wa migodi kuanza kuwashirikisha Watanzania kwa kununua bidhaa zao pamoja na huduma za jamii ili huduma za jamii zianzie maeneo yanayozunguka mgodi huo. Kwa hiyo, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge Mradi wa Kiwira utakuwa na manufaa makubwa sana kwa Taifa lakini pia kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Kwa kuwa Waziri amekiri kwamba bajeti iliyopita walitenga milioni 870, lakini ni milioni 157 tu ndiyo zimepelekwa. Je, haoni umuhimu wa kuhakikisha pesa iliyobaki inapelekwa.
Swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Rungwe imepata mafuriko na uharibifu wa barabara umekuwa mkubwa sana, naomba Wizara hii itutumie pesa za haraka kwa ajili ya emergency kwa ajili ya vijiji kama tisa zaidi ya kilometa 40; kama Kijiji cha Kyobo, Ikuti na sehemu za Lupepo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka pesa hizo haraka kwa ajili ya kusaidia barabara na madaraja yaliyoharibika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika majibu yangu ya msingi nilisema bajeti ilikuwa ya shilingi milioni 870, zilizopelekwa mpaka sasa ni shilingi milioni 157, jibu hili nimekuwa nikilitoa kila mahali katika vipindi mbalimbali. Nilisema wazi, ukiachia changamoto ya ujenzi wa barabara, lakini kuna miradi mingi kipindi kilichopita ilikuwa haiendi vizuri. Nilitolea mifano miradi ya maji na miradi mingineyo kwamba upelekaji wa pesa ulikuwa ni tatizo kubwa sana, lakini kulikuwa na sababu zake za msingi. Katika mwaka uliopita pesa nyingi sana zilienda katika matukio makubwa ambayo yalikuwa yamejitokeza kama suala la uandikishaji na uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchakato wa hivi sasa, Serikali imejielekeza zaidi katika ukusanyaji wa mapato, ndiyo maana hivi sasa hata ukiangalia kwa mara ya kwanza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imevunja rekodi katika ukusanyaji wake wa mapato. Nilisema kwamba hata miradi iliyokuwepo mwanzo imesimama, lakini hivi karibuni miradi hiyo inapelekewa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia yetu ni kwamba, katika kipindi hiki cha bajeti kilichobakia nina imani Serikali itajitahidi kupeleka fedha katika miradi yote iliyosimama nikijua wazi katika maeneo hayo mengine wakandarasi ambao ni wa ndani na wengine wa nje wanaendelea kudai. Kwa hiyo, suala hili tunaweka kipaumbele siyo kwa ajili ya maeneo hayo tu isipokuwa kwa Tanzania nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mafuriko na kuharibu miundombinu ya barabara, hili nilisema ni kweli. mwaka huu ukiangalia maeneo mbalimbali tumekuwa na changamoto ya mvua kubwa iliyonyesha. Nimetolea mfano kule Rungwe, ukienda Kyela, ukienda Kilosa na maeneo mbalimbali, yote yameathirika kwa ajili ya mvua na ndiyo maana tulipeleka utaratibu kwamba kila Halmashauri ianishe uharibifu wa miundombinu mara baada ya mvua ile kunyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu letu kubwa ni kuangalia sasa kile ambacho tunaweza kusaidia kwa kipindi cha sasa. Kwa hiyo, baada ya uharibifu huo, Serikali itachukua jukumu la kusaidia siyo maeneo ya Rungwe peke yake, isipokuwa maeneo mbalimbali ambayo yameathirika na nafahamu hata maeneo ya Morogoro hali ilikuwa mbaya sana na maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la Muheza liko sawa na sisi watu wa Rungwe Magharibi, katika Hospitali ya Makandana tuna shida ya watumishi wa afya, vile vile na usafiri kwa ajili ya wagonjwa hususan wanawake. Je, ni lini Serikali itawatazama wananchi hawa kuweza kutuletea wataalam ikiwa pamoja na gari jipya la wagonjwa kama mlivyofanya kwa watu wa Muheza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anavyosema Mheshimiwa Mbunge, siku ya Jumatatu nilikuwa katika Hospitali ya Makandana pale katika Wilaya ya Rungwe, nilitembelea Hospitali na nilibaini miongoni mwa changamoto mbalimbali katika Hospitali ile na kwa pamoja tukaangalia jinsi gani tutafanya kama Serikali kuweza kutatua changamoto zile. Ndiyo maana hata katika maagizo yangu niliwaeleza kwamba hospitali ile licha kwanza suala la madawa lakini suala la gari la wagonjwa na hata suala la ukusanyaji wa mapato katika hospitali ile haliko sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuta pale wanatumia mifumo ya analog, kutumia risiti ambayo kwa kiasi kikubwa inapoteza fedha nyingi za Serikali, ndiyo maana nimeagiza mwisho wa mwezi huu lazima wahakikishe wanatumia mifumo ya electronic. Kwa hivyo, haiwezekani hospitali kubwa kama ile wanakusanya sh. 3,000,000 kwa mwezi wakati kituo cha afya cha Kaloleni kinakusanya sh. 40,000,000 kwa mwezi!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunalifanyia kazi kwa upana wake. Kuhusu suala zima la miundombinu tumetembelea miundombinu, nina hakika maelekezo tuliyopeana siku ya Jumatatu tutaendelea vizuri na mwisho wa siku tutapata gari la wagonjwa ili hospitali yetu iwe katika mazingira mazuri na wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma bora ya afya.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Sophia Mwakagenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nataka kujua commitment ya Serikali juu ya benki hii ya wanawake ni lini itaiongezea ruzuku ili hiyo riba ambayo imekuwa ni kubwa iweze kuwa ndogo kuweza kusaidia kuwakopesha wanawake hasa wa vijijini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, commitment ya Serikali inajionesha wazi kwa Serikali kutenga bajeti ya shilingi bilioni moja kwenye mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuiwezesha benki hii kufungua dirisha maalum kwa ajili ya mikopo kwa wanawake. Hiyo ndio commitment yetu tunasubiri utekelezaji tu.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri katika suala, hili ninapenda kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vifaa hivyo anavyovizungumzia ambavyo vinasambazwa katika maeneo yetu ya zahanati, kwa Wilaya yetu ya Sumbawanga, Wilaya ya Nkasi, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini pamoja na Kalambo vifaa hivi havipo. Kama vinasambazwa vinasambazwa lini? Na je, Serikali itachukua mpango upi mkakati wa kuweza kufuatilia na kuhakikisha kwamba vifaa hivi vimesambazwa katika maeneo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba Mkoa wa Rukwa ni Mkoa uliopo pembezoni; ni Mkoa ambao hauna Hospitali za Wilaya. Hata juzi Mheshimiwa Malocha alizungumzia suala la Hospitali ya Wilaya, kwa maana ya kituo cha Rahela kipasishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado Mkoa wa Rukwa hauna Hospitali ya Wilaya, kwa hiyo ndio maana hospitali yetu ya Rufaa ya Rukwa inakuwa na msongamano wa wagonjwa wengi katika eneo lile.
Sasa ni lini Serikali itahakikisha zahanati zetu, vituo vyetu vya afya vinakuwa katika ukamilifu wake na vifaa tiba vyake ili kuondoa msongamano katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwamba vifaa vitasambazwa lini? Mpaka sasa tunavyozunguza, hatujaanza kuvisambaza vifaa hivi kwa sababu vifaa hivi 500,000 vinatokana na tamko alilolitoa Mheshimiwa Waziri wa Afya wakati wa bajeti kama mpango maalum. Bajeti imeanza kutekelezwa mwezi Julai na bado hatujapokea fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango huu mzuri ambao Waziri wa Afya ameuanzisha kwa majaribio mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa ambavyo vinapaswa kuja kwa utaratibu wa kawaida vimeendelea kupelekwa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini na hivi 500,000 ni kwa ajili tu ya kufanya majaribio ya kuona kama tukiwapa delivery packs akinamama wanaoenda kujifungua, pengine inaweza ikasaidia kupunguza changamoto mbalimbali zilizopo kwenye mfumo. Kwa hiyo, huu ni mpango mpya na maalum na bado haujaanza kutekelezwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu Vituo vya Afya na Zahanati kuweza kutoa huduma kwenye Mkoa wa Rukwa; kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge hili, ziara yangu ya kwanza ni Mkoa wa Rukwa. Mwezi uliopita kabla ya bajeti hii ya Bunge hili nilifika kwenye Mkoa wa Katavi. Baada ya Bunge hili nitafika kwenye Mkoa wa Rukwa kuona ni namna gani tunaweza tukashirikiana nao kuwawezesha kuanzisha huduma za upasuaji na huduma za maabara kwenye vituo vyote vya afya vilivyopo kwenye mkoa huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Hospitali za Wilaya, yeye kama Mbunge akishirikiana na Wabunge wa Majimbo, wanapaswa kukaa kwenye vikao vyao vya Halmashauri na kupanga mpango kabambe wa kujenga hospitali hizi na Serikali Kuu itawasaidia pale ambapo watakuwa wamekwama. Napenda watambue kwamba jukumu hili ni lao kama Halmashauri kuanzisha miradi ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya na sisi Serikali Kuu tunawajengea uwezo tu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa tatizo la Mara la vifaa tiba pamoja na gari la wagonjwa, ni kama la Rungwe. Napenda kujua commitment ya Serikali kwa Hospitali ya Makandana katika Wilaya ya Rungwe, ni lini watatuletea gari na kutuongezea vifaa tiba kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wa Wilaya ya Rungwe katika Hospitali ya Makandana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikupongeze na niwashukuru sana kwa dua zenu njema. Nakumbuka siku ile nilivyotoka kule baada ya kutoa maagizo kwamba mfumo wa kielectroniki ufanye kazi pale, baada ya muda fulani nikapata ajali, watu wakasema, watu wa huko wamekushughulikia? Nikasema hapana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana. Agizo langu nililotoa ndani ya mwezi mmoja lilitekelezeka katika hospitali ile na nilipata mrejesho kwamba makusanyo yamebadilika sana katika hospitali ile ya Makandana. Kwa hiyo, naomba niseme kwamba kweli nilitembelea pale nikakuta gari za wagonjwa hali yake sio nzuri sana. Tulibadilishana mawazo na bahati nzuri wana Mkuu wa Wilaya mzuri sana katika eneo lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nilichukue hili kwa sababu kuna vitu vingine tumeshaanza kuvizungumza kuona ni jinsi gani tutafanya kuboresha hospitali ile, tutajadili kwa pamoja ili hospitali hii iweze kupata huduma nzuri, kwa sababu kuna network nzuri ya Waheshimiwa Wabunge katika eneo hilo, mnaofanya kazi kwa pamoja kwa agenda kubwa ya hospitali yenu, basi naamini jambo hili tutalitatua kwa pamoja, kama mawazo shirikishi kuhusu tufanye nini katika mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa jibu la msingi la Mheshimiwa anasema Benki Kuu haiwezi kuingilia kutoa bei elekezi, tunawezaje kusaidia Benki ya Wanawake iweze kutoa riba ndogo kwa kupata ushauri kutoka kwenye Wizara yake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo, kwa mujibu wa sheria Benki Kuu haiwezi kutoa hiyo riba elekezi na napenda niseme kwamba riba hizi zilizopo ni kwa mujibu wa Sera ya Riba ya mwaka 1992. Kwa hiyo, lazima tuendane na sera tuliyoipitisha humu Bungeni ili kuweza kuhakikisha kwamba sekta ya fedha inafanya vizuri ndani ya uchumi wetu na kwa Benki ya Wanawake naamini Mheshimiwa Waziri wa Afya anaweza kulisimamia hili na kuweza kutoa riba ambayo ni nzuri, lakini hawezi kukiuka misingi ile iliyowekwa na Sera ya Riba ya mwaka 1992.
MHE. SOFIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tuliku-miss hekima zako.Kwa kuwa tatizo la wana Ngara linafanana kabisa na tatizo la watu wa Rungwe. Rungwe kuna vyanzo vingi sana vya maji, lakini tuna shida ya maji katika Vijiji vya Mpandapanda, Ikuti na sehemu nyinginezo. Je, Mheshimiwa Waziri anatusaidiaje tuweze kupata maji ukizingatia tunavyo vyanzo lakini watu bado wanahangaika kupata maji salama? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nimesimama kwa kutoa majibu ya ujumla kwa wale wengine ambao pengine watauliza swali linalofanana na la Mheshimiwa Sofia.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka huu, kama alivyosema Naibu Waziri kwamba kila Halmashauri tumepanga fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa miradi ya maji. Sasa katika Halmashauri yako, ninyi ndio mlipanga vipaumbele kwamba kwa mwaka huu mtapeleka maji kwenye Vijiji vipi?
Mheshimiwa Spika, tumetoa mwongozo kwamba kama mmeshapanga vipaumbele, tangazeni tenda ili tupate Mkandarasi aweze kufanya. Waziri wa Maji anafanya kazi ya uratibu, mtekelezaji ni Mkurugenzi wa Halmashauri ambayo wewe unatoka kule. Naomba tusaidiane kusimamia hawa Wakurugenzi kwenye Sekta ya Maji ili waweze kufanya kazi inayotakiwa wananchi wetu wapate maji.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, jibu la Mheshimiwa Waziri halijaniridhisha. Bodi ya Chai Rungwe imeweka wanunuzi wa chai wa aina mbili, wako WATCO na Mohamed Enterprises. Mohamed Enterprises amekuwa akinunua chai ya wakulima kwa bei nzuri na
WATCO ikawa inanunua chai kwa bei ya chini, lakini cha kushangaza Serikali ikaamua kumwambia Mohamed Enterprises aombe kibali upya, mpaka sasa tunaongea Mohamed Enterprises hana kibali cha kununua chai ya
wakulima na hii inapelekea wakulima kuuza kwa bei inayotaka Serikali ambayo ni ya chini.
Swali langu la kwanza, Serikali iko tayari kuvunja Bodi hiyo ili tuweze kupata watu tunaowaamini watakaotetea
wakulima wa chai wa Rungwe? (Makofi)
Swali langu la pili; Serikali iko tayari na Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kuonana na wakulima wa chai na kusikiliza kero za wakulima wa chai wanavyoteseka kwa muda mrefu? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na hilo la pili, nitakuwa tayari kuandamana naye muda wowote kuanzia sasa kwenda kusikiliza kero za wakulima wa chai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la nyongeza la kwanza, kama nilivyoeleza bei ya chai hupangwa kwenye mkutano wa wadau ambayo kawaida inakuwa ni bei ambayo tunasema ni bei dira. Maana yake ni bei ambayo hairuhusiwi mtu yeyote kumlipa mkulima chini ya hapo, lakini
Kanuni za zao la chai zinaruhusu majadiliano yafanyike kati ya mkulima na mnunuzi, maana yake wanaweza wakakubaliana bei kuwa juu ilimradi isije ikawa chini ya kile ambacho kimewekwa kama bei dira. Kwa hiyo, tofauti anayoiona Mheshimiwa Mbunge kuhusu wanachotoa WATCO na Mohamed Enterprises
inatokana na majadiliano yale ya ziada ambayo kanuni inaruhusu.
Mheshimiwa Spika, vilevile ningependa kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tofauti ya bei hutokana na ukweli kwamba kunakuwa na tofauti ya ubora wa chai moja kutoka mkulima mmoja hadi mwingine, kwa hiyo mara nyingine kuna makampuni yanaamua kulipa kitu tunachoita bonus au malipo ya ziada kutokana na ubora wa chai, ndiyo maana tunaendelea kuwashauri wakulima wetu wajaribu kulima chai kwa viwango vinavyotakiwa ili kuwa na ubora ambao utawafanya wapate bei nzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuvunja Bodi ya Chai kwa sababu hiyo, katika hali kama hii inakuwa ni vigumu kusema kwamba wao wanahusika moja kwa moja, kama nilivyosema kama Mheshimiwa Mbunge haridhiki na majibu ambayo nimeyatoa niko tayari kukutana naye ili niendelee kumuelewesha zaidi, pia kuandamana naye kwenda kwa wakulima wa chai.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, Halmashauri mara nyingi tatizo la fedha ni shida kubwa sana. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutuambia ni jinsi gani atahakikisha Ofisi yake inatimiza yale malengo ya fedha iliyoahidi kwenda kwenye Halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusu usimamizi, aseme
kwa kina atazisimamiaje Halmashauri zake zisifanye ufisadi kwa kuwa, imekuwa ikijirudia mara kwa mara na kutuletea matatizo katika Halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunazungumzia suala zima la fedha na fedha hizi zinatafutwa kwa gharama kubwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
Naomba nimhakikishie, nilikuwa nikifanya ziara katika Halmashauri zote na nashukuru Mungu sasa nimebakiza chini ya Halmashauri 10 kuzipitia Tanzania nzima. Ajenda yetu ya kwanza ni suala la uadilifu katika usimamizi wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaambia na nimetoa maelekezo katika maeneo yote kwamba Wakurugenzi na Waweka Hazina sasa lazima wanapokwenda katika Kikao cha Kamati ya Fedha ambapo Madiwani na Wabunge ni Wajumbe hapo, lazima watoe taarifa ya transactions katika Halmashauri zao, fedha zilizopokelewa na matumizi yake yalikuwaje. Siyo kupokea lile kabrasha la mapato na matumizi ambapo Mbunge au Diwani anashindwa kujua ndani kilichokuwemo. Kwa hiyo, tumetoa maelekezo haya vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge ambao sisi ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha kwamba tukiingia katika vikao vyetu, tuweze kuzisaidia Halmshauri hizi kwa sababu sisi ndio wafanya maamuzi ambao tunawawakilisha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasihi Wabunge wote kwamba kwa moyo mkunjufu na moyo wa dhati tuzisimamie Halmashauri zetu, compliance iwepo na wananchi wetu wapate huduma na maendeleo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa takribani miaka miwili iliyopita kumekuwa kuna uhitaji mkubwa sana wa mafunzo ya ujasiriamali, lakini kumekuwa kuna walimu wanaofundisha chini ya kiwango. Serikali inasema nini kuwadhibiti walimu hao kwa kupunguza bei lakini pia kufundisha katika viwango ambavyo vinaweza kusaidia walaji ambao wengi ni wanawake?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, somo la ujasiriamali ni somo ambalo linaweza likafundishwa katika ngazi mbalimbali kama ambavyo wengi tunafahamu, ujasiriamali upo katika sura mbalimbali. Kuna ule ambao unakuwa informal ndio wajasiriamali hawa wadogo wadogo wanaanza, lakini kuna ule ambao unakuwa katika ngazi kubwa zaidi. Kwa hiyo kunaile kupata mafunzo ya awali na kupata mafunzo makubwa zaidi. Jambo kubwa ambalo ningependa leo Waheshimiwa Wabunge mlifahamu ni kwamba katika suala zima la ujasiriamali wengi tunafikiria ni ile kufanya biashara, kuuzauza labda vitu au maduka na vitu kama hivyo. Lakini ujasiriamali tunachotamani hasa watu wakifahamu, ni ile namna gani mtu anafanya shughuli zake kwa njia tofauti ili kuongeza thamani, kiasi kwamba hata Waheshimiwa Wabunge kufanya Ubunge pia ni ujasiriamali wa aina yake. Kwa hiyo, naomba tulizingatie katika sura hiyo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa nchi za Uturuki, Ujerumani na Italy wanakunywa sana chai ya Tanzania. Je, ni lini Serikali itapeleka Kiwanda katika Wilaya ya Rungwe kwa ajili ya wakulima wa chai ili waweze kuuza chai yao ambayo ni nyingi ikaweza kusaidia katika hizo nchi nyingine?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilonalo ni nguvu ya soko. Mheshimiwa Sophia tumeshazungumza kwenda kwenye maonesho ya Kimataifa kwenda kutafuta hayo masoko. Leta hizo order zako kusudi demand pool iwashawishi watu wachakate chai. Kuna watu wana chai hawana soko, sasa wewe nimeshakuruhusu uende kwenye maonesho. Nenda basi ulete hizo order. (Kicheko/Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Natambua katika Mkoa wa Mbeya tayari REA Awamu ya Tatu imeishazinduliwa, lakini kuna changamoto kubwa sana katika Wilaya ya Rungwe katika vijiji vya Lupoto, Katabe na Ibungu mpaka sasa hawajapata umeme na hatujajua ni lini watapata. Naomba majibu ya Serikali tuweze kujua ni lini Wilaya hizi zitapata umeme wa REA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nakushukuru ulivyouliza, hapa tunapoongea katika kijiji cha Lugota wakandarasi wanaendelea na kazi, kwa hiyo wanaendelea kupata umeme, lakini vijiji vya jirani pia tutavitembelea ambavyo bado lakini vijiji vyote ulivyotaja kwenye eneo lako vitapata umeme wa REA na umeanza mwezi wa tatu na kwako wewe utakamilika mwakani mwezi wa saba.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Swali la kwanza, kwa kuwa jibu la msingi la Serikali inakiri kwamba shamba hili lilipata hati kuanzia mwaka 1978 mpaka mwaka 1981.
Je, ni kwa nini Serikali haikuwa na hati ambayo leo hii mwekezaji huyu amekuwa akiwaonea wananchi wa vijiji hivyo tajwa alivyovitaja Mheshimiwa Waziri?
Swali la pili, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali akiwemo na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali binafsi siwaamini katika utekelezaji wao wa kazi zao. Je, Mheshimwa Waziri huoni umuhimu wa mimi na wewe kuongozana na kwenda kuwasikilisha wananchi na wanakijiji wa Nyelegete waliokataa kusikiliza mahusiano yao, mimi na wewe tukaenda kwa pamoja. Ni lini na utakuwa tayari tukaongozana kwenda kusimamia hili?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema ni kwa nini Serikali haikuwa na hati. Si kweli kwamba Serikali haikuwa na hati kama anavyosema, maeneo yote yanayomilikiwa na Serikali yanafahamika toka awali, na wanakijiji wanaozunguka eneo lile walitambua kwamba lile lilikuwa ni eneo la Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kumuuzia mmiliki mwingine tofauti na Serikali ili aweze kuishi vizuri na wanakijiji wanaomzunguka ni lazima ule uhakiki wa mipaka ufanyike kwa kuhusisha pande zote ambazo zinahusika katika mgogoro huo, kwa sababu huwezi ukampa tu wakati huo huo na wananchi pia nao walikuwa wanalitazama shamba lile.
Mheshimiwa Spika, lazima kufanya ule uhakiki wa mipaka ili kumfanya huyu mwekezaji ambaye yupo aweze kutambua mipaka yake vizuri. Kwa vyovyote unavyouza kwa mtu lazima umkabidhi eneo lako na kuhusisha kwamba ni wapi ambapo mipaka yako inaishia. Kwa hiyo, suala hilo nadhani linaeleweka kwa staili hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema habari ya kwenda Mbarali, nakumbuka mwezi Machi nilikwenda katika Mkoa wa Mbeya na Mbarali nilifika na suala hili lilizungumzwa, lakini kama bado halijatatuliwa na mgogoro bado upo, nadhani tutaangalia ratiba itakavyokuwa imekaa ili tuweze kuongozana na kusikiliza wale wananchi jinsi wanavyolalamika lakini najua chini ya mikono salama ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi masuala hayo yatatatuliwa. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa SIDO ndio wanaohusika kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo lakini imeonekana wanachaji pesa kubwa sana hasa mafunzo ya vifungashio. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie ni jinsi gani SIDO itapunguza bei na kusaidia hao wajasiriamali wadogo waweze kufanikiwa katika biashara zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kimsingi bei iliyokuwa inakuwa-charged ilikuwa inategemeana na gharama halisi za upatikanaji wa vifungashio hivyo. Jambo ambalo tunaweza tukafanya ni kuendelea kuangalia uwezekano wa kuipatia SIDO ruzuku ya kutosha lakini pia kuwakaribisha watu binafsi katika kutengeneza vifungashio hivyo kwa kadri itakavyowezekana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kutokana na jibu la msingi alilojibu Mheshimiwa Waziri ni kwamba ranchi ile imepewa wawekezaji wazawa, ni kweli; lakini wao wazawa wanawakodisha wananchi kulima na si kama vile mkataba unavyosema. Hiyo ni moja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkataba ni mkataba unaweza ukavunjwa kama unakiukwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuvunja huo mkataba na kuwapatia wananchi wafugaji wa Mbarali waweze kufuga kwani hawana nafasi za kufuga kutokana na maeneo tengefu kuzuiwa na Serikali? Naomba Serikali iwapatie wananchi waweze kufuga mifugo yao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni juu ya wawekezaji wanavunja mkataba kwa kuwakodisha wananchi. Jambo hili tumelisikia na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeweka mkakati kwanza kabisa tunathaminisha Ranchi zetu zote katika Taifa letu kwa kuangalia ile mikataba yote ambayo tuliwakodisha wawekezaji ambao hawakukidhi mahitaji yetu sawa na mikataba; tutavunja kwa kutangaza upya na kuwakaribisha wafugaji wote wenye uwezo wa kuweza kufuga kulingana na matakwa ya mkataba.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Mwakagenda anauliza kama tutawapa wananchi. Lengo letu sisi ni kuona kwamba ranchi hizi zinatumika kwa malengo mahususi; mosi ya kuhakikisha pia hata ranchi hizi zitusaidie katika kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima; lakini mbili, ranchi hizi ambazo zimetapakaa nzima, ziwe ni sababu kubwa ya kuongeza kipato katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, huu mkakati utakapokamilika na tutakapokuja nao; tunaomba Wabunge wote nchi nzima watupe ushirikiano ili tuweze kufanikisha ajenda hii ya kusukuma mbele tasnia ya ufugaji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri bado kuna shida katika ujenzi unaoendelea pale Ipinda, nilikuwa nataka kujua Serikali imefuatilia gharama ya pesa ilizotoa na uhalisia wa majengo yanayojengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ujenzi wa zahanati ni kitu kingine, lakini utendaji wa wafanyakazi ikiwemo madaktari ni shida hasa Zahanati ya Ikuti Rungwe na hapo Ipinda hakuna watendaji wa kazi. Ni lini Serikali itatoa wafanyakazi ikiwemo madaktari na hasa Madaktari Bingwa wa wanawake kusaidia wanawake wa Wilaya ya zahanati ya Ipinda lakini pia Zahanati ya Ikuti Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo:-
Katika swali lake la kwanza anauliza iwapo Serikali imefuatalia kujua gharama iliyotumika na majengo ambayo yamejengwa. Majengo ambayo yanajengwa ni kwa mujibu wa ramani ambayo imetolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na ni na suala ambalo matarajio yangu makubwa na Mheshimiwa Mbunge akiwa ni sehemu ya wananchi wa Halmashauri ile ni vizuri akatuambia ni sehemu ipi ambayo anadhani kwamba haridhiki, lakini mpaka sasa hivi ninavyoongea hata Mbunge wa Jimbo hajaleta malalamiko yoyote kwamba labda kuna ubadhilifu katika ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaongelea juu ya suala zima la upatikanaji wa wataalam, suala la kujenga majengo jambo moja na suala la wataalam jambo la pili, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni nia ya Serikali kuhakikisha pale tunapomaliza ujenzi na wataalam wapatikane kwa mujibu wa Ikama na jinsi mahitaji yanavyopatikana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sambamba na ufutwaji wa kodi wa vifaa vya watu wenye ulemavu, je, ni lini Serikali itawagawia bure walemavu kwenye kaya maskini vifaa vya uhafifu hauoni kwa watu wenye ulemavu wa macho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kadri vinavyokuwa vinapatikana, kwa hiyo, hili ambalo ameliuliza dada yangu Sophia nimhakikishie tu kwamba Serikali itaendelea kutoa vifaa hivi. Hata hapa, muda mfupi uliopita kama wiki mbili/ tatu/mwezi mmoja uliopita tumekuwa na hilo zoezi la kugawa vifaa hivi saidizi. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya hivyo kupitia bajeti zake lakini pia kupitia wadau mbalimbali wanajitokeza kusaidia kundi hili la watu wenye ulemavu (Makofi).
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, pamoja na majibu yasiyoridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, atakubaliana nami kwamba imekuwa ni kawaida kwa Serikali kutokuwalipa waathirika wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo Wilaya hii ya Kyela? Barabara hii toka imejengwa hakuna aliyelipwa mpaka sasa na ndiyo maana wananchi wamefungua kesi Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, imekuwa ni kawaida ya Serikali kutokulipa wananchi wengi katika Taifa hili wanapowabomolea kwa kigezo cha ujenzi wa barabara, wakati huohuo mmewawekea umeme na maji. Kama mlijua wameingia kwenye hifadhi ya barabara kwa nini mlitoa huduma hizo za kijamii? Nataka majibu ya Serikali ni kwa nini wanafanya hivyo, wananchi hawapati haki zao wakati wamekaa kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 50 katika eneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza, namuomba sana Mheshimiwa Mbunge aridhike tu kwa hatua ambayo Serikali inachukua. Kwa sababu hivi navyozungumza shilingi bilioni 1.008 zililipwa kwa wananchi ambao walikuwa wanaathirika na ujenzi wa barabara. Hao wachache waliobakia kwa sababu wamepeleka kesi Mahakamani, ni haki yao wasikilizwe na Mahakama ili waweze kupata haki zao.
Mheshimiwa Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba sisi kama viongozi tunalo jukumu kubwa sana la ku-influence wananchi wetu. Kwa hiyo, labda nikuombe tu kwa sababu hii kesi iko Mahakamani tuonane ili angalau nikupe mbinu za kushawishi wananchi hawa ili waweze kuondoa kesi yao na ikiwezekana huduma ya barabara iweze kupita kwa sababu ni muhimu sana katika ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba zimekwenda huduma kwa wananchi sehemu ambazo tunatekeleza miradi, inaweza kuwa kweli kwamba pale ambapo wakati mwingine ujenzi wa barabara haujaanza au hata kabla ya kuwa na mradi wa barabara, yaweza kuwa kulikuwa na huduma, lakini wakati sasa mradi wa ujenzi wa barabara unakuja ndipo sasa pale tunalazimika kufanya zoezi hili la kuweza kuwaondoa wananchi lakini na kuwapa haki zao kwa mujibu wa sheria.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nafikiri ukiliangalia kwa ukaribu unaweza ukagundua kwamba ni wakati gani huduma ilikwenda na wakati gani mradi huu wa barabara umekuja. Ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na shida ya walimu wa alama kwa ajili ya wanafunzi viziwi. Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha tunapata walimu zaidi kuweza kuwasaidia watu wanaotumia alama katika kujifunza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi hawa walimu ambao wanatumia alama nayo ni elimu maalum. Kwa hiyo, sisi tunalitazama kwa mapana yake yote na ndiyo maana nimesema kwamba katika hao walimu watakaoajiriwa, naamini na hao wanaotumia alama ni miongoni mwa hao wenye uhitaji maalum na watachukuliwa ili kuweza kuhudumia wanafunzi wanaohitaji walimu wenye kutumia alama.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itazuia wagombea Urais kutoa ahadi ambazo zinachukua muda mrefu kutekelezeka ikiwepo suala la zahanati na barabara? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, wagombea nafasi za Urais wanaenda kuuza sera kwa wananchi ili kwa sera hizo waweze kuchaguliwa. CCM ambao ndiyo tulichaguliwa na wananchi baada ya kuuza sera na ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais na katika kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais mkataba wake na wananchi waliompa kura ni miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shuhuda, tumekuwa tukipata fursa ya kujibu maswali juu ya maeneo mbalimbali ambayo ahadi za Mheshimiwa Rais zilishatekelezwa. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kuzuia ahadi hizo kwa sababu zimekuwa zikitekelezwa. (Makofi/Kicheko)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali langu linamuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, je, ni lini Bunge pamoja na Wizara ya Fedha wataleta Muswada mpya wa kuweza kuidhibiti Serikali kukopa madeni kwa maana imeonekana tuna madeni makubwa na Serikali inakopa bila ya sisi Wabunge kufahamu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ya Awamu ya Tano, kama ambavyo nimekuwa nikiliambia Bunge lako Tukufu tunafuata sheria, Katiba na taratibu zote za Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu ukopaji Serikali yetu imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134. Hakuna hata siku moja ambapo Serikali yetu imekopa bila Bunge lako Tukufu kujulishwa na kupitisha. Huwa tunaleta tunavyoleta bajeti ya Serikali tunataraji kukopa kiasi gani, Bunge lako linaturuhusu na tunakwenda kukopa kile tulichoruhusiwa na Bunge lako Tukufu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Ahsante, kwa kuwa jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri, suala la tafiti katika vyuo hivi ni kutokana na ucheleweshwaji wa pesa za maendeleo na ndio maana ardhi inabaki kubwa kwa muda mrefu bila kutumika. Je, Serikali imejipanga vipi katika bajeti hii kupeleka pesa katika Wizara hii hasa eneo la Uyole kwenye hicho Kijiji cha Nkena, lakini na Uyole Mbeya Mjini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majibu yangu ya msingi nimejibu, lakini vilevile wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kafumu kuhusu Igunga nimesema hapa kwamba sisi kama Wizara ya Kilimo tumeboresha kuhakikisha kwamba ile directorate yetu ya utafiti sasa hivi itakuwa ni taasisi inayojitegemea kwa maana ya TARI. Pia nimetoa maagizo kwamba TARI ama vituo vyetu vya utafiti vyote visitegemee tu pesa za Serikali, lakini pia vijiongeze kuhakikisha vinaandika maandiko (proposals) ili waweze kupata pesa za ziada kwa ajili ya kuhakikisha tafiti zetu zinaboreshwa na zinatendewa haki. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa mgodi wa Kiwira, umesimama kwa muda mrefu, je Serikali ina mpango gani ya kutafuta Wawekezaji ambao wanaweza kufufua mgodi ule ambao miundombinu yake inakufa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, Mgodi wa Kiwira sisi kama Serikali tumejipanga kuangalia ni namna gani ya kuwezesha mgodi huo uweze kufanya kazi. Niseme tu kwamba tunashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuangalia namna sasa ya kuzuia au kuangalia namna ya kuweza kuondoa zile changamoto zilizopo katika mradi wa Kiwira, ili uchimbaji ule wa Makaa uweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wengi wameonesha nia ya kutaka kushiriki katika kuchimba Mgodi huo wa Kiwira. Sisi kama Wizara, kwa kweli hatuna shida yoyote, tunahakikisha kwamba ikiwezekana mwaka huu, mgodi huo upate fedha na watu waweze kuchimba na vile vile tutafute wawekezaji wengine ambao wanaonesha nia ya kuwekeza pale, tushirikiane nao kuhakikisha kwamba Mgodi wa Kiwira unaanza kufanya kazi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama ilivyo kwa wananchi wa Newala, Wilaya ya Kyela ina zao la kokoa. Je, ni lini Serikali itatusaidia kupata wafanyabiashara wengi zaidi kuweza kusaidia kununua zao la kokoa kwa wananchi wa Wilaya ya Kyela? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kama ilivyo kwa mazao mengine, Wizara yetu inalo jukumu kupia TANTRADE, kuhakikisha kwamba tunashirikiana na Wizara ya Kilimo kutafuta masoko ya uhakika na wawekezaji ili kuweza kuendeleza mazao yote. Kwa hiyo zao la kokoa ni mojawapo ya mazao ya kimkakati na linapendwa duniani na hivyo nalo ni sehemu mojawapo ambayo linashughulikiwa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama ilivyo kwa Wilaya ya Chunya, Wilaya ya Kyela haina mahabusu ya wanawake hivyo kupelekea kupelekwa Wilaya ya Rungwe. Je, ni lini Serikali itajenga mahabusu ndogo ya wanawake kwa Wilaya ya Kyela?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimezungumza kwamba changamoto inayosababisha tusiwe na ujenzi wa magereza yetu ambao siyo wa kasi kubwa sana ni kutokana na ufinyu wa bajeti. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Gereza la Wanawake Kyela ni miongoni mwa maeneo ambayo tunayaangalia kwa jicho la kipaumbele sana. Kwa hiyo, pale ambapo bajeti itakaa vizuri Gereza la Wanawake Kyela litakuwa ni jambo la kipaumbele.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa zao la tumbaku na pamba, ni lini Serikali itaongeza bei kwenye zao la chai katika Wilaya ya Rungwe na cocoa katika Wilaya ya Kyela? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bei linakuwa determined na soko lakini moja ya mkakati wa Serikali kwenye zao la chai ni kuanzisha mnada hapa hapa nchini badala ya kutegemea mnada wa Mombasa. Kuhusu cocoa tunaendelea kuwasiliana na wanunuzi wa cocoa duniani ili kuona kama wanaweza wakanunua cocoa ya Tanzania. Kwa hiyo, mikakati ya Serikali ni mizuri kwa upande wa chai na cocoa na mkakati wa kuwa na mnada wa hapa hapa nchini utasaidia kuwapatia wakulima wa chai bei nzuri. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo kwa wananchi wa Ludewa ni lini Serikali itaweka na kuharakisha utekelezaji wa kuwalipa fidia wale wananchi wa Wilaya ya Kyela waliopisha mradi wa Boarder Post? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Magufuli alipokuwa ziara Kyela ametoa maelekezo ili tuweze kuwalipa mara moja wananchi katika eneo hili, nimwarifu tu Mheshimiwa Mbunge, nami nimeongea na wananchi hawa baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais na tunalifanyia kazi suala hili ili tuweze kuwalipa wananchi hawa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mwakagenda avute subira, sisi tumejipanga kama Serikali na kwa sababu Mheshimiwa Rais pia amekuwa na concern hiyo, wananchi watapata haki zao mara moja.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa na madeni mengi hasa kwenye Balozi za nje ambazo Mabalozi wetu wanaishi na ni tabia ambayo inatuletea image mbaya kama taifa. Je, ni lini Serikali italipa hayo madeni ya pango za nyumba za Mabalozi wetu katika nchi mbalimbali za dunia hii tuliyopo sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili katika bajeti zake za miaka ya hivi karibuni limekuwa likitenga fedha mara kwa mara kwa ajili ya kulipa madeni hayo. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli madeni yapo na kila wakati madeni ni sehemu ya maisha lakini Serikali itaendelea kulipa kadiri uwezo unavyopatikana. Hata hivyo, mkakati mkubwa wa Serikali sasa ni kuzuia madeni mengine kutokea kwa kulipa madeni kwa wakati. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba suala hili litafanyiwa kazi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika kutokana na jibu la msingi la Wizara nataka kujua kwanza, je, Serikali haioni kwamba inapoteza muda katika utekelezaji wa miradi mbalimbali hususan miradi ya barabara kwa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, barabara hii ni barabara muhimu sana katika uchumi wa Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe. Je, hawaoni kuna umuhimu wa kuongeza muda wa kufanya kazi kwa haraka ili hii barabara iweze kukamilika na wananchi wa mikoa hii miwili waweze kufaidika katika ujenzi wa kiuchumi katika Taifa hili la Tanzania?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu, usanifu wa kina utaratibu wa manunuzi na ujenzi ni utaratibu wa kimataifa na maana yake ni kuhakikisha kwamba hiyo kitu inaitwa value for money inapatikana vizuri kwa sababu msipofanya taratibu mkaainisha mahitaji yote, matokeo yake ndio kufanya upembuzi ambao ni pungufu na mkiingia tenda mnaweza msipate value for money.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, hoja yake ya kwenda haraka Serikali inaenda haraka ili kuhakikisha na sehemu kubwa ni msongamano wa pale Mbeya Mjini, ndio maana tunataka kuchepusha ili tutajenga mchepuo kwa ajili ya malori, lakini pale katikati kwa ajili ya kupanua ili msongamano usiwe mkubwa pale mjini Mbeya.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TCRA imeruhusu TBC kama TV ya Taifa kuonekana kwenye ving’amuzi vyote, lakini TCRA inaisimamia vipi TBC kuweza kuonyesha habari kwa uhakika na bila upendeleo kwa vyama vyote na wananchi wote? Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana

Mheshimiwa Naibu Waziri Mhandisi kwa majibu mazuri sana aliyotoa kwa maswali aiyoulizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa swali la nyongeza napenda niseme tu kwamba TBC kama vituo vyote vya kitaifa duniani vina hadhi ya must carry ambayo kila kisimbusi lazima kibebe, kwa hiyo, siyo kitu cha Tanzania tu, kipo duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, hili ni suala la maudhui; suala la maudhui upande wa TBC ni wazi, kama una maudhui yako tafadhali peleka TBC. Hakuna upendeleo wowote unaofanyika, wewe kama unaamini ni upendeleo ni shauri yako, lakini leta maudhui yako yaoneshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nikusisitizie, kama kuna mtu hapa ana wasiwasi maana wengi wanaongea hawajawahi hata kupeleka maudhui, nileteeni mimi kama hayo maudhui hayataoneshwa. Ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo katika Jimbo la Simanjiro vivyo hivyo Jimbo la Rungwe kuna shida ya mawasiliano hasa katika Kata za Ilima, Swaya, Bujera pamoja na Ikuti. Je, ni lini Serikali itasaidia wananchi wa maeneo haya waweze kupata mawasiliano mazuri hususan katika mitandao yote wana shida ya mawasiliano? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna maeneo katika Jimbo la Rungwe ambayo yana changamoto ya mawasiliano. Ni kweli pia kwamba hata Mbunge wa Jimbo la Rungwe, Mheshimiwa S. H. Amon amekwishafika ofisini lakini pia bahati nzuri ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu ambako ndiyo tunashughulikia masuala hayo, tumekwishaongea, amekwishaleta barua kwa maandishi na tayari zabuni ya Awamu ya Tano maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Sophia ambayo hata Mbunge anayafahamu yatajumuishwa kwa ajili ya kupelekewa mawasilinao. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. WAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekubali na kukiri kwamba toka mwaka 1972 wazee wa CCM wamekuwa kwenye Baraza za Mahakama: Je, ni lini Serikali italeta sheria tuweze kubadilisha wazee hawa watoke kwa wananchi na siyo kwenye vyama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba wazee hawa wanatoka kwenye Chama cha Mapinduzi, haoni wanakwamisha juhudi za Mahakimu kwa kutoa haki kwa mahabusu wanaotoka Upinzani? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza lazima tutoe heshima kwa wazee wetu kwa busara zao. Kama wanatoka Chama hiki au chama kile, lakini wazee wetu ni wazalendo, wazee wetu ni walezi, wazee wetu ni kioo cha jamii, tuwape heshima wanayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, tuko katika mchakato wa kubadilisha mfumo mzima wa Mahakama na hasa katika makosa ya jinai. Sheria hii ilipitishwa mwaka 1972 na ndiyo maana tumeona umuhimu huo na mchakato huo unaendelea na pale utakapokamilika tutawajulisheni. Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, samahani, nakurudisha hapa. Katika swali la msingi anasema kwamba umekiri wazee wa CCM ndio wazee wa Baraza. Ni kweli umefanya hivyo? Maana kwenye jibu lako mimi sijaona hilo. Ndiyo swali lake hasa! Unaweza kuchukua dakika moja kulijibu.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kufafanua hilo. Sijakiri hivyo, lakini nilichosema katika maelezo yangu ni kwamba wazee wazee wetu tulionao katika jamii zetu, tuwape heshima na tutambue busara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nimesema kwamba kama sheria hii ilipitishwa mwaka 1972, Mahakama iko katika mchakato wa kutazama umuhimu wa kurekebisha taratibu hizo za Kimahakama na hasa kwa matumizi na uchaguzi wa wazee ambao watakuwa wanasaidia Mahakama zetu za mwanzo na za juu. Nadhani hiyo ndio ufafanuzi nilioutoa. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Chakula pia ni moja ya utamaduni. Je, Serikali inasema nini juu ya vyakula vinayotoka nje ya nchi ambavyo ni kinyume na utamaduni wetu wa chakula cha asili ambacho tulikuwa tunakitumia? Nataka kujua tunatoa tamko gani kuzuia vyakula ambavyo siyo vya utamaduni wetu na vinaathiri afya za Watanzania?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya maswali yaliyotangulia. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali alilouliza ni mtambuka linalohusu biashara ya nje na sekta mbalimbali ambapo Wizara yangu haiwezi kulitolea tamko hapa kwamba kuanzia sasa vyakula ambavyo siyo vya utamaduni visiingie nchini. Hili ni suala pana ambalo hata Bunge lako Tukufu lina mamlaka ya kuweza kulijadili kwa upana zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na jibu la msingi la Serikali, Serikali inao wajibu wa kuwekeza kwenye michezo yote ndipo wafadhili wanafuatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mchezo wa ngumi kama navyoutetea hauna ufadhili wa Serikali ili kupata timu nzuri itakayotuwakilisha kimataifa. Ni lini Serikali itaandaa maeneo ya wanamichezo hawa kufanya mazoezi ili waweze kuwa vizuri na kuweza kushinda katika timu za kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Wizara husika, hasa kwenye ngumi, ameonesha jitihada za kusaidia wachezaji wa ngumi kwa sasa. Serikali kwa wachezaji wa ngumi wanaume tayari wameonesha jitihada ni lini sasa watafanya hivyo kwa wachezaji wa ngumi wa kike ambao bado wako nyuma kwenye vifaa vya kufanya mazoezi ili waweze kushinda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ni miongoni mwa mapromota wanawake wachache kabisa ambao tunao nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikianza na swali lake la kwanza ambapo amesema kwamba Serikali ina wajibu wa kuwekeza katika michezo yote. Ni kweli kwamba sisi kama Serikali tuna wajibu wa kusimamia lakini kazi kubwa ya Serikali ni kuandaa miundombinu na kuweka mazingira wezeshi ya kisera pamoja na sheria. Suala la ufadhili wa michezo yote nchini Tanzania ni la vyama pamoja na mashirikisho ambayo ndiyo yanasimamia michezo hiyo vilevile kwa kushirikiana na wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sisi kama Serikali tunao mpango wa kuhakikisha kwamba tunafanya uwekezaji mkubwa zaidi katika michezo. Ndiyo maana umeona katika kipindi cha hivi karibuni nchi yetu imepata fursa ya kuweza kushiriki kwenye mashindano mbalimbali na sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kwamba tunafanya ufadhili katika michezo mbalimbali ukiwepo mchezo wa ngumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye swali lake la pili pia ametaka kujua ni lini sasa Serikali itaanza kuweka mkakati kuhakikisha kwamba tunakuza mchezo huu wa ngumi. Kama ambavyo amezungumza ni kweli sisi kama Wizara ya Michezo kwa kipindi cha hivi karibuni tumefanya jitihada kubwa sana ya kuhakikisha kwanza tunaboresha mchezo huu wa ngumi na jambo la msingi ambalo tumelifanya ni kuhakikisha kwamba tunaunda Kamisheni ya mchezo huu wa ngumi. Lengo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba mchezo huu wa ngumi unapata mafanikio makubwa kitaifa na kama ambavyo tumeshuhudia kwamba ni mchezo ambao tunaamini kabisa kama uwekezaji ukifanyika vizuri utakuwa na mafanikio makubwa

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kwa upande wa Serikali tayari tulishaanza kuweka mikakati na matunda yameanza kuonekana ndiyo maana jana tulishuhudia wanamasumbwi watatu wamekuja hapa na mikanda ya kutosha kabisa. Kwa hiyo, kama Serikali tunatambua umuhimu wa mchezo huu na tunaahidi kwamba tutaendelea kufanya uwekezaji mkubwa vilevile kwa kushirikiana na wadau. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kutokana na jibu la msingi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, tunaomba Serikali iweze kufuatilia majibu ya chuo hiki kwa sababu ni muhimu kwa wana-Mpanda kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo kwa wana- Mpanda, Shirika la la Utafiti la Uyole lina kituo pale Kijiji cha Nkana katika Wilaya ya Chunya, wameanzisha utafiti kwa muda mrefu, lakini mpaka sasa Wizara ya Elimu haijaweza kuwezesha utafiti ule kuendelea kwa ukosefu wa fedha. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha katika utafiti ule ili watu wa Nkana na Uyole, Mbeya, waweze kuendeleza shughuli za kilimo na kuweza kuwasaidia Watanzania? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mhesimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunchela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu ombi lake la sisi tufuatilie kuhusu chuo hicho, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufuatilia, lakini majibu ambayo tumetoa sasa ni kwamba sisi tumeomba taarifa kutoka kwa Halmashauri ya Mji wa Mpanda lakini mpaka sasa hatujapata taarifa. Kwa sababu yeye anatokea kule, nafikiri itatusaidia sana kama angeweza kusukuma kwa kushirikiana na Halmashauri yake ili tuweze kupata taaarifa hiyo ili tujue hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na utafiti huo ambao anauzungumzia wa Uyole, naomba nifuatilie kwa sababu hajasema ni utafiti gani ili niweze kujua ni nini hasa ambacho kinampa changamoto Mheshimiwa Mbunge.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali haioni kwamba imewavuruga Walimu wa sekondari ambao wamesomea kufundisha watu wa rika ya sekondari na kuwapeleka katika elimu ya msingi, haioni kwamba imewachanganya na imeshusha morari ya utendaji kazi zao? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali haioni umuhimu wa kuajiri Walimu ambao wako mtaani hawajaajiriwa kwa kukosa ajira kwa muda mrefu, kwa nini wasiwaajiri Walimu hawa wakaenda kufundisha shule za msingi katika ngazi ambayo wao wameisomea? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza anazungumza kwamba tunashusha morari, siyo ya kweli, hayo yalikuwa ni mapokeo tu, sisi wengine Walimu tunafahamu kwanza mzigo wa kufundisha sekondari na shule ya msingi unatofautiana, ni heavy duty sekondari kuliko shule ya msingi, ile inawaelekeza kwamba watu walipopelekwa pale hatukuwa na maandalizi mazuri, watu wakapokea tofauti, lakini waliopokea vizuri wameendelea kufundisha na hakukuwa na shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kupanga Mwalimu afundishe shule ya msingi au shule ya sekondari siyo kushusha morari yake, hili tu nimesema kulikuwa na upungufu mkubwa, kama Serikali, kama una watu zaidi ya 11,000 wako wanafundisha vipindi vichache sana kwa siku na kuna Walimu katika shule ya msingi wanafundisha vipindi vingi, ilikuwa ni busara kutumika kuwapeleka kule kufundisha, lakini tumeshachukua hatua, tuliwaelekeza Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri zetu, wakakaa wakazungumza nao wanaendelea kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ajira, ni kweli kwamba tuna upungufu mkubwa wa Walimu katika shule za msingi na sekondari, lakini juzi hapa tumeajiri Walimu 4,500, tumeomba kibali cha Walimu 22,000 hasa masomo ya shule za msingi, masomo ya fizikia na hisabati katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kadri Serikali itakapopata uwezo ndivyo inaweza kuajiri, huwezi kuajiri tu kwamba kuna Walimu mtaani, hapana, lazima uajiri Walimu lakini wapate stahiki zao na uwezo wa kuwalipa kila mwisho wa mwezi pamoja na mahitaji mengine. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni muhimu wa kuwakumbuka wazee hawa ambao wamelipigania Taifa hili kama zawadi kwao kufuta jasho kwa kile walichokifanya bila ya kuwasahau wazee waliopigana vita ya pili ya dunia?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze na nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa majibu mazuri ambayo yanatokana na historia ya Taifa letu na wazee wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 11(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeshaweka utaratibu wa mamlaka ya nchi kuweka mifumo na sera ambazo zitawajali Watanzania waliokwishakutumikia Taifa hili katika nyanja mbalimbali na kulifanya Taifa lifike mahali lilipofika kwa kuwahifadhi kutumia sheria na sera mbalimbali. Kwa muktadha wa wazee wote nchini na Watanzania wote ambao wamehudumu katika Taifa hili kwa namna moja ama nyingine, Katiba imeshatuwekea utaratibu na ndiyo maana tunazo sera na sheria nyingi tu ambazo zinashughulikia masuala ya ustawi wa wazee kwa ujumla wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha msingi cha kufanya ni sisi kama Wawakilishi wa Watanzania kuendelea kushauriana na Serikali katika kuboresha eneo moja ama lingine ili kuwahifadhi wazee wote ndani ya Taifa letu kwa kuzingatia mchango wao kwenye Taifa hili katika maeneo mbalimbali na maeneo tofauti.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwea kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri zao la kahawa jinisi ambavyo bei yake iko chini zao la chai pia, bei yake iko chini kwa muda mrefu. Je, Serikali ina mkakati gani kuongeza bei ili kuweza kuwasaidia wakulima wa chai kupata kipato kiweze kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kama alivyosema zao la chai bei yake inaendelea kushuka. Ni kutokana na yaleyale ni over supply katika soko la dunia, lakini wanywaji wanabaki ni walewale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu uzalishaji unaweza kuongezeka ndani ya miaka mitano, lakini wanywaji wa chai na watu wenye uwezo wa kununua hiyo chai kuongezeka kwake mpaka afikishe zaidi ya miaka 18 na kuendelea. Mkakati mmoja wa Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunakuwa na mnada kama walivyokuwa wenzetu wa Kenya hapa nchini, ili kuuza chai yetu kwenye mnada hapa nchini, lakini mkakati wa pili tunaendelea kwenye mazungumzo na wenzetu wa China, ili kupata bilateral agreement tuuze moja kwa moja chai yetu kwenye ma-super market ya China badala ya kuuza kwa kutumia…

MWENYEKITI: Asante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kama ilivyo katika mikoa mingine, Wilaya ya Rungwe tunayo shida kubwa sana ya mashine za kuchomea taka na kuzivunjavunja ikiwemo pamoja na ukosefu wa vifaatiba ambavyo vinatakiwa kupatikana katika hospitali ile. Je, Serikali inajipangaje kutusaidia wananchi wa Wilaya ya Rungwe tuweze kupata mashine hiyo ikiwepo na mashine za X-ray za kusaidia wanawake katika Wilaya ya Rungwe, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mbeya na nimpongeze kwa swali lake hilo ambalo ameuliza kuhusiana na masuala ya kuchomea taka na upatikanaji wa huduma za X-ray. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za uchomaji taka katika hospitali mbalimbali na sisi kama Wizara tumetoa mwongozo huo katika vituo vyetu vyote vya kutolea huduma za afya na tunaendelea kufanya tafiti za teknolojia rahisi ambazo zinaweza zikatumika katika kutengeneza vichomea taka kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niiombe tu Hospitali ya Wilaya ya Rungwe kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI na hata kupitia kwetu Wizara ya Afya tupo tayari kushirikiana nao kuwapa ushauri na huo utaalam ili sasa waweze kujenga hicho kichomea taka kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa huduma ya X-ray, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tumeendelea kufanya tathmini ya uhitaji wa huduma za X-ray katika hospitali mbalimbali za Wilaya ndani ya nchi na tumetengeneza orodha ya Hospitali zote za Wilaya ambazo zinahitaji huduma hii na tumeshaanza mkakati wa uagizaji wa mashine mpya za kisasa za digital X-ray. Nimhakikishie kwamba pindi X-ray hizo zitakapofika basi na Wilaya ya Rungwe nayo tutaifikiria. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimimiwa Spika, ahsante, kwanza nipongeze nchi za Scandinavia zilikuwa zikisaidia sana Serikali yetu kupeleka Walimu wa mahitaji maalum kwa muda wa miaka mingi, swali langu la kwanza.

Je, ni lini Serikali itaongeza nguvu ya kipesa kuweza kuwadahili wanafunzi wengi zaidi watakaosomea mafunzo ya alama?

Mheshimimiwa Spika, swali la pili katika Wilaya ya Rungwe kuna shule ya watu wenye ulemavu ya Katumba ambayo ina miundombinu iliyochakaa kwa muda mrefu na ina Walimu wachache wa lugha za alama pamoja na lugha za watu wenye ulemavu, Serikali itatia jitihada gani kuweza kusaidia shule hii ya Katumba kupata mahitaji hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimimiwa Spika, ni kwamba suala la watu Wenye Ulemavu ni muhimu sana na Serikali inatambua na kulipa
kipaumbele. Katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na wanafunzi wengi wanaoweza kujifunza lugha ya alama kwa sababu haitoshi tu kila mtu kuongea anavyoelewa ni vizuri kukawa na lugha ambayo kwa yoyote utakayemkuta anaongea lugha ya alama itakuwa ni hiyo hiyo. Wizara tayari ilishashughulikia na kuna vitabu ambavyo vimeshatayarishwa ambavyo vinaweza kuwafundisha watu wengi tukiacha wanafunzi hawa wazazi waweze kuifahamu lugha ya alama.

Mheshimimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwezeshwa suala hilo. Na kwa upande wa shule ambayo imezungumzwa ya Katumba niseme tu kwamba kwa suala la Watu Wenye Ulemavu hilo ni suala muhimu kwa sababu Tanzania inahitaji kuona kwamba wananchi wote wanafaidika na elimu, iwe mlemavu, iwe asiye mlemavu. Kwa misingi hiyo nikuombe tu Mheshimiwa nitaona kwamba kuna umuhimu wa kutembelea shule hiyo ili iweze kusaidiwa inavyotakiwa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ninasikitika sana kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, tulipoomba Serikali itoe kodi na ikakubali ilikuwa ni furaha kwa Wanawake wengi wa Nchi hii ya Tanzania. Jana ilikuwa ni siku ya hedhi salama kwa wanawake duniani. Tumeonana na wadau wanaoshughulikia pads, hakuna lalamiko walilolitoa juu ya uendeshaji zaidi ya kodi ambayo Serikali imetoa kwa wanao- import na kuwaacha watengenezaji waliko hapa nchini.

Swali langu; ni nini Serikali itafanya kuweza kusaidia wawekezaji wa ndani wanaotengeneza taulo hizi ikiwemo Jessy, HQ na wengineo ili kuweza kupunguza gharama ya taulo za kike?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali itakubali kuweka ulazima wa wauzaji wanaouza taulo hizi kuweka gharama ya bei katika taulo hizo ili kufanya bei zote zifanane kama ilivyo kwa mazao kama ya Coca cola na Pepsi nchi nzima ina bei moja. Serikali itachukua wazo letu la kuona wkamba ni lazima iandikwe bei katika taulo hizo ili kukwepa kwa wale wanaoweza kuongeza hasa wasafirishaji na wauzaji na bei hii iweze kupungua.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kusahihisha alichokisema kwamba wazalishaji wa ndani bado wanalipa kodi ya ongezeko la thamani kwenye bei ya bidhaa hizi, hapana. Tumeondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa hii kwa bidhaa zinazotoka nje ya Nchi na zile zinazozalishwa ndani ya Nchi ndiyo maana nikasisitiza kwenye jibu langu la msingi, majibu ambayo Serikali iliyatoa kwa swali namba 2938 ambalo liliulizwa na Mheshimiwa Stella Ikupa Allex na kwa mwongozo wako naomba kulisoma swali lake liliuliza hivi:-

“Kutokana na umuhimu wa taulo za kike Nchini, Je, Serikali inaonaje ikiondoa kodi kwenye taulo hizi?”

Mheshimiwa Spika, Serikali ilisema kwenye swali hili kwamba ukiondoa kodi haiwezi kuleta atahari moja kwa moja kwenye bei ya bidhaa husika kwa sababu bidhaa husika inategemea mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, tukienda Nchini Botswana, tukaenda Nchini Kenya ambako waliwahi kuondoa kodi kwenye bidhaa hizi hakuna athari yoyote iliyoonekana kwenye taulo hizi za kike. Kama tunataka kweli kumsaidia mtoto wa kike kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kumsaidia mtoto wa kike, naomba tuisikilize Serikali inasema nini; Serikali siku zote imekuwa ikisisitiza kwamba, sisi kama Serikali tuna mpango na tayari tumeanza kufanya mchakato wa kuona ni jinsi gani ya kutoa bidhaa hii bure kwa watoto wa kike na siyo kuondoa kodi jambo ambalo halina athari yoyote zaidi ya kupunguza mapato ya Serikali. Jambo hili lilipelekwa kisiasa zaidi na mimi nawaomba kwenye mambo ya msingi yanayogusa Watanzania tusiingize siasa, hilo ndiyo suala ambalo nataka kuliweka hivyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili baada ya majibu yangu haya ya swali lake la kwanza, hakuna ulazima wowote wa kuandika bei kwenye bidhaa hizi kwa sababu tuko kwenye soko huria na Serikali yetu hatutaki kuingilia jambo hili, tunachohitaji ni kuja na mpango wa kibajeti wa ku-deal na jambo hili ili tuwasaidie watoto wetu wa kike.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika mchezo wa ngumi, asilimia 99 ya wachezaji wanapata maumivu. Je, ni lini Serikali italazimisha ma- promoter kuwakatia bima hasa mabondoa wanawake hapa nchini Tanzania? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza kwa sababu Mheshimiwa Sophia Mwakagenda ni promoter pekee mwanamke ambaye anashiriki kwenye michezo ya ngumi. Nikija kwenye swali lake la msingi ambalo ametaka kujua kwamba ni lini sasa Serikali tutasimamia hawa wanaocheza michezo ya ngumi kuweza kukatiwa bima; nikiri kwamba imekuwa ni changamoto ya muda mrefu kwamba wachezaji wengi ambao wanacheza michezo ya ngumi wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu ikiwepo kutokuwa na Bima za Afya.

Mheshimiwa Spika, kwenye hivi vyama ambavyo vinashiriki mchezo huu ndondi kumekuwa kuna migogoro ya muda mrefu sana na ndiyo maana wachezaji hawa wakawa hawapati ile haki yao ya kuweza kupata Bima ya Afya. Kwa sasa hivi kama Wizara, tumeshaunda shirikisho la kuweza kusimamia mchezo huu wa ngumi nchini Tanzania. Lengo mojawapo kwenye vile vipengele ambavyo tumeviweka, ni kuhakikisha kwamba ni lazima kwa Ma- promoter kuwakatia Bima za Afya wachezaji wao.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kama ilivyo kwa Kiwanda cha SONAMCU kilichopo Songea Mjini. Je, ni lini Serikali itatusaidia sisi wananchi wa Wilaya ya Rungwe kwa Kiwanda cha Chai cha Katumba ili kuongeza kiwanda kingine na kuleta ufanisi wa utengenezaji wa chai na kuleta bei bora kwa wakulima kwa sababu kutakuwa kuna ushindani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kujua Serikali itaruhusu lini kiwanda kingine kijengwe kuweza kusaidia wakulima wa chai? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi sisi tungetamani kuona viwanda vingi vinajengwa na vinaweza kuchakata mazao ya wananchi na kwa tija. Kwa hiyo, kadri viwanda vinavyojengwa, sisi ndiyo tunavyofurahi, kwa hiyo, hatujazuia kiwanda kingine kujengwa Katumba na kilichopo tungependa kiweze kufanya kaz vizuri zaidi. Kwa hiyo, kama kuna kikwazo chochote ambacho kinawakabili hawa Wana Katumba, ni vema tufahamishwe ili tuweze kushirikiana nao katika kuondoa vikwazo hivyo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, report ya UNESCO ya mwaka 2018 inaeleza kwamba huwezi kuwa na viwanda kama huna nishati ya kutosha na maji ya kutosha. Je, Serikali inajua suala hilo? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; suala la viwanda 100 kila Mkoa ni suala lililotamkwa kisiasa. Serikali inaweza ikatuambia ni viwanda vingapi vilivyotengenezwa tayari katika Taifa hili la Tanzania ikiwepo Mkoa wa Mbeya kuna viwanda vingapi vimeshajengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kama Serikali inatambua umuhimu wa nishati ya umeme wa kutosha ili kuendesha viwanda hivi. Jibu ni kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Awamu ya Tano inatambua sana na ndiyo maana imeanzisha mikakati mbalimbali ya kuboresha na kuongeza umeme, kuna umeme wa gesi unazalishwa, lakini pia mpango mkakakti mkubwa sana ambao namuomba Mheshimiwa Sophia auunge mkono, ule wa kupata umeme kutoka Bonde la Mto Rufiji ili tupate umeme wa kutosha kwenye viwanda lakini pia matumizi ya majumbani. Lakini hata na wananchi wa kawaida hawajasahaulika ndiyo maana kuna umeme wa REA unalipwa kwa gharama ndogo sana ya shilingi 27,000 kwa kila Mtanzania na kila Kijiji, na nyumbani kwao watapata umeme wa kutosha sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua idadi ya viwanda ambavyo vimepatikana katika kila Mkoa na anasema ni tamko la kisiasa. Kwanza naomba nimwambie Mhehsimiwa Mbunge kwamba hili ni tamko mahususi la mpango mkakati wa Chama cha Mapinduzi, siyo tamko la kisiasa linatekelezeka, tumeshazindua, tumetuma mwongozo nchi nzima, Wakuu wa Mikoa wameitwa hapa Dodoma, Wakuu wa Wilaya wameelekezwa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa imetenga maeneo mbalimbali ya kuanzisha viwanda, imeshiriki Mbeya, tumeenda Lindi na maeneo mengine. Tumeshapata viwanda vipya zaidi ya 3000 katika nchi nzima na nitawasiliana na viongozi wa Mkoa kupata idadi haliis ya Mkoa wa Mbeya ambao anatoka yeye kupata hivyo. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba nimuombe Mheshimiwa Sophia ashiriukiane na Serikali ya Chama cha Mapinduzi na ikiwezekana na mwenyewe awezeshe, awe na kiwanda ili akina mama kama yeye waweze kupata uchumi jumuishi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, kuna shida kubwa sana kwa waletaji wa pembejeo kwenye majimbo yetu. Jimbo la Rungwe linalima sana mazao ya viazi, lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa pembejeo. Tunaomba kujua Serikali inafanya mbinu gani ya kuhakikisha wanaoagiza pembejeo wanaleta pembejeo kwa wakati kwa wakulima?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wawekezaji na hasa hao wabia ambao mnawapa kazi hiyo ya kusambaza pembejeo wanaleta pembejeo nyingine hazina viwango na hivyo kusababisha kupata mazao hafifu kwa kuwa pembejeo iliyoletwa si sahihi kwa wakulima wetu. Je, ni hatua gani itachukuliwa kuhusiana na suala hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza utaratibu wa kuagiza pambejeo tunatumia mfumo wa bulk procurement. Utaratibu huu tender hutangazwa ambapo waagizaji wote wa mbolea wanakuwa wamesajiliwa na wanashindanishwa na kupewa time limit ya uagizaji na ku-deliver katika kila mkoa.

Mheshimiwa Spika, mfano kwa mwaka huu mahitaji yetu ya mbolea kwa nchi nzima ni jumla ya tani 700,000 na ambazo zinatakiwa ziwe delivered kuanzia mwezi wa 11 na jambo hilo limeendelea na mpaka sasa hatujapata tukio lolote la ukosefu wa pambejeo katika mikoa yetu. Kwa hiyo, kama kuna case inahusu maeneo ya Rungwe, nitamuomba Mheshimiwa Mbunge anipe hiyo specific case li tuweze kuifuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ubora, Wizara ya Kilimo kupitia mamlaka yetu iliyokuwa ikiitwa TPRI ama kwa sasa inajulikana kwa mujibu wa sheria tuliyopitisha katika Bunge lililopita TAFA, tunafanya ukaguzi katika maduka yote yanayouza pembejeo. Pale ambapo tutakutana na pembejeo fake tunachukua hatua za kuwapeleka Mahakamani. Mpaka sasa kuna zaidi ya kesi tano za wasambazaji ambao walikutwa wana pembejeo fake.

Mheshimiwa Spika, ili kulitatua tatizo hili sasa hivi kwa sababu biashara ya pembejeo inafanyika katika wilaya, Wizara ya Kilimo sasa hivi tuko katika hatua za mwisho za kuanzisha kitu tunaita Customer Service Centre ambapo mkulima popote alipo katika nchi hii ataweza kupiga simu bure pale ambapo aidha kakutana na pembejeo fake ama kapata tatizo lolote la kiuatilifu ama tatizo la ugonjwa katika eneo lake na sisi kuweza kumhudumia kwa wakati. Tunachukua hatua hii ili kupunguza tatizo la gap ya muda kati ya athari inapotokea mpaka pale huduma inapoenda kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachosisitiza unapoenda kununua pembejeo popote hakikisha umepata risiti ya muuzaji ya EFD ili tutakapokuta kuna tatizo tuweze kumchulia hatua. Hili la Rungwe, kama kuna special case, karibu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, kuna shida kubwa sana kwa waletaji wa pembejeo kwenye majimbo yetu. Jimbo la Rungwe linalima sana mazao ya viazi, lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa pembejeo. Tunaomba kujua Serikali inafanya mbinu gani ya kuhakikisha wanaoagiza pembejeo wanaleta pembejeo kwa wakati kwa wakulima?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wawekezaji na hasa hao wabia ambao mnawapa kazi hiyo ya kusambaza pembejeo wanaleta pembejeo nyingine hazina viwango na hivyo kusababisha kupata mazao hafifu kwa kuwa pembejeo iliyoletwa si sahihi kwa wakulima wetu. Je, ni hatua gani itachukuliwa kuhusiana na suala hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza utaratibu wa kuagiza pambejeo tunatumia mfumo wa bulk procurement. Utaratibu huu tender hutangazwa ambapo waagizaji wote wa mbolea wanakuwa wamesajiliwa na wanashindanishwa na kupewa time limit ya uagizaji na ku-deliver katika kila mkoa.

Mheshimiwa Spika, mfano kwa mwaka huu mahitaji yetu ya mbolea kwa nchi nzima ni jumla ya tani 700,000 na ambazo zinatakiwa ziwe delivered kuanzia mwezi wa 11 na jambo hilo limeendelea na mpaka sasa hatujapata tukio lolote la ukosefu wa pambejeo katika mikoa yetu. Kwa hiyo, kama kuna case inahusu maeneo ya Rungwe, nitamuomba Mheshimiwa Mbunge anipe hiyo specific case li tuweze kuifuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ubora, Wizara ya Kilimo kupitia mamlaka yetu iliyokuwa ikiitwa TPRI ama kwa sasa inajulikana kwa mujibu wa sheria tuliyopitisha katika Bunge lililopita TAFA, tunafanya ukaguzi katika maduka yote yanayouza pembejeo. Pale ambapo tutakutana na pembejeo fake tunachukua hatua za kuwapeleka Mahakamani. Mpaka sasa kuna zaidi ya kesi tano za wasambazaji ambao walikutwa wana pembejeo fake.

Mheshimiwa Spika, ili kulitatua tatizo hili sasa hivi kwa sababu biashara ya pembejeo inafanyika katika wilaya, Wizara ya Kilimo sasa hivi tuko katika hatua za mwisho za kuanzisha kitu tunaita Customer Service Centre ambapo mkulima popote alipo katika nchi hii ataweza kupiga simu bure pale ambapo aidha kakutana na pembejeo fake ama kapata tatizo lolote la kiuatilifu ama tatizo la ugonjwa katika eneo lake na sisi kuweza kumhudumia kwa wakati. Tunachukua hatua hii ili kupunguza tatizo la gap ya muda kati ya athari inapotokea mpaka pale huduma inapoenda kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachosisitiza unapoenda kununua pembejeo popote hakikisha umepata risiti ya muuzaji ya EFD ili tutakapokuta kuna tatizo tuweze kumchulia hatua. Hili la Rungwe, kama kuna special case, karibu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama ilivyo kwa wananchi wa Kilolo, ni lini Serikali itakiamuru Kiwanda cha Chai cha Katumba kuongeza bei ya chai kwa wakulima wadogo wadogo katika Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya chai katika soko la dunia hivi karibuni iliyumba kidogo. Kwa hiyo, kampuni nyingi za chai zimekuwa na changamoto ya soko katika kuuza chai zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bei kwa wakulima wadogo wadogo naamini baada ya kutengemaa kwa soko la chai duniani sasa hivi ni dhahiri shairi kwamba kampuni nyingi za chai ikiwemo hiyo ya Katumba, Mbeya na nyingine zitaweza kuwaongezea bei wakulima kwa sababu sasa kuna uhakika wa soko katika soko la dunia.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jibu la Mheshimiwa Waziri, je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa Vyama vya Ushirika ili waweze kuwalipa wakulima wa kokoa Wilaya ya Rungwe na Wilaya ya Kyela kwa wakati kwa maana mpaka sasa wanadai madeni yao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inatambua kwamba kokoa ya Kyela na Rungwe ni kokoa bora baada ya kokoa ya Ghana.

Ni nini Serikali itafanya kuwawezesha wakulima hawa na kuwasimamia bei yao iongezeke maana hiyo uliyosema Mheshimiwa Waziri ya shilingi 5,000 bado ni ndogo, haitoshi kwa wakulima maana wao ndiyo wawekezaji wakubwa na wenye kazi kubwa katika ukulima wao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mwakagenda maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kulipa wakulima kwa wakati, kwa utaratibu na mwongozo ambao Wizara ya Kilimo imeutoa, baada ya mnada, mkulima anatakiwa awe amepata fedha zake ndani ya saa 72. Huu ndiyo utaratibu ambao tumeuweka. Kwenye minada ya kokoa tumejenga utaratibu ambapo mkulima anapewa malipo ya awali kabla ya mnada na baada ya mnada hupewa fedha ambayo ni difference kati ya fedha ya awali na fedha ambayo mnada umefikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatua tunazochukua sasa hivi ni kuviwezesha Vyama vya Ushirika kupitia Tanzania Agricultural Development Bank kupata fedha kwa gharama nafuu ili waweze kuwa na uwezo wa kukusanya mazao kwa wakati na kuyapeleka mnadani na pale ambapo mnada unakuwa bei yake haivutii, wakulima waweze kusubiri mnada uweze kuwa na bei nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Vyama vya Ushirika vya Kokoa vilivyoko katika Mkoa wa Mbeya sasa hivi vina maongezi na Tanzania Agricultural Development Bank na sisi Wizara ni sehemu ya majadiliano hayo. Bado hatujaruhusu wachukue fedha kwa sababu riba ambayo iko mezani ni kubwa kwa kiwango cha asilimia 9. Kwa hiyo, tunaendelea na majadiliano na hili tutalirekebisha. Tumhakikishie tu kwamba tutaendelea kuboresha mfumo wa stakabadhi ghalani ili kupunguza gap kati ya mnada na fedha kumfikia mkulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ubora, ni kweli na ndiyo maana bei ya kokoa ya Tanzania imepanda kutoka Sh.3,000 mwaka 2017 na sasa imefika wastani wa Sh.5,000 kwa kilo. Bado sisi kama Wizara tunaamini kwamba kokoa yetu ni bora. Sasa hivi hatua tunazochukua, tumeanza utaratibu wa certification ili kuweza ku-meet International Standard ili na sisi tuwe na zile competitive advantage ambazo zinakubalika katika soko la dunia. Ni lazima bidhaa ile ithibitike kupitia kitu kinaitwa Global Gap Certification kwamba bidhaa hii ni organic.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hizi ndiyo hatua tunachukua na mwaka jana tulipitisha sheria ya TAFA hapa na sasa TAFA wanaanza kazi ya ku-certify mashamba ili yaweze kupata hiyo hadhi. Kwa hiyo, tunaomba mtupe muda tuko kwenye hatua nzuri tunaamini tunafika, Inshaallah.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa hospitali ya Makandana wilaya ya Rungwe imeshajengewa wodi ya wanawake. Serikali ina mpango gani wa kutuongezea madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUNGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeboresha miundombinu katika hospitali ya Wilaya ya Rungwe, hospitali ya Makandana kwa kujenga wodi ya wanawake ili kuendelea kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika Halmashauri ya Rungwe. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba bado Serikali ina mipango ya kuendelea kuboresha miundombinu hiyo ikiwemo kuongeza vifaatiba lakini pia kuongeza madaktari.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimhakikishie kwamba kwa sera na miongozo kwa sasa hospitali zetu za Halmashauri bado hazijawa na mwongozo wa moja kwa moja wa kuwa na waganga mabingwa, kwa maana ya madaktari bingwa katika hospitali hizo, kwa sababu kwa ngazi ile madaktari wa ngazi wanaopatikana bado wana uwezo mzuri wa kutibu na tuna mfumo mzuri wa rufaa pale ambapo kuna kesi ambazo zinashindikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kwamba Serikali itaendelea kuboresha ikama ya madaktari katika hospitali ya Makandana ili waendelee kuhudumia vizuri wananchi wetu wakiwepo wanawake katika wodi hizo na kwenda kuboresha huduma za afya kadri ya matarajio ya wananchi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuwa Serikali imekiri kuleta Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2009 Bungeni, je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta mabadiliko ya sheria ambayo inawafanya makosa ya jinai kwa wafungwa waliokaa mahabusu kwa muda mrefu iletwe ili iweze kupunguzwa muda wa kukaa muda mrefu kwa mfano wale wafungwa Masheikh wa Uamsho?

Swali la pili, Serikali haioni umuhimu sasa badala ya kuwekeza kujenga mahabusu mpya nyingi iwekeze kwa kumsaidia DPP kujenga uwezo wa kusimamia kesi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa mahakamani, ushirikishwaji na ujibuji wa maswali yao wakienda mahakamani inakuwa bado upelelezi unaendelea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khatib Said Haji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza lilikuwa linasema je, hatuoni haja sasa ya kuweza kufanya baadhi au mabadiliko katika hii Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba akipata muda akiipitia sheria hii atagundua kwamba tayari kuna baadhi ya maeneo yalishafanyiwa marekebisho kitu ambacho sasa kimeelekea katika kupunguza kwa asilimia kubwa huu mrundikano. Kwa mfano, ukiangalia katika kifungu cha 170; ukiangalia kifungu cha 225 na ukiangalia katika maeneo ya 163 na hayo na baadhi ya mengine ni maeneo tuliyoyafanyia marekebisho ili kuona tunapunguza hii changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tunapotaka kufanya marekebisho ikiwa addendum ama amendment ya sheria kuna mambo ya msingi tunakuwa tunayaangalia. Kwanza tunaangalia applicability ya ile sheria, je, ipo applicable? Ikiwa kama sheria ina tatizo katika utekelezaji wake pale tunasema sasa tuna haja ya kufanya mabadiliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hilo halitoshi tunakuwa tunaangalia na mahitaji ya jamii kwa wakati ule, sasa kikubwa mimi niseme tu kama wanahisi au Mheshimiwa Mbunge anahisi kwamba kuna haja basi tutakwenda kukaa tuipitie tena tuone, pamoja na mabadiliko tuliyokwisha kuyafanya tutakwenda kukaa ili tuone kwasababu lengo na madhumuni ni kuhakikisha kwamba changamoto za mrundikano wa majalada na mrundikano wa mahabusu katika mahakama na wafungwa inapungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hilo halitoshi swali la pili Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba tuone namna ya kuwapa uwezo au kwa nini tusifanye maarifa DPP tukampa kazi ya kuweza kufanya upelelezi ili mambo yakaenda. Kazi ya kufanya upelelezi kwa mujibu wa taratibu kuna vyombo maalum vinavyohusika kufanya upelelezi. Wenye kufanya upelelezi ni polisi na siyo polisi wote kuna vitengo maalum vya kufanya upelelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenye kufanya upelelezi labda ni watu wa TAKUKURU, wenye kufanya upelelezi labda watu wenye kazi maalum tukisema leo DPP tunampa kazi ya kufanya upelelezi tunamuongezea jukumu lingine na usije ukashangaa akasema na kamshahara nako kapande. Mimi niseme tu kwamba kwa kuwa haya mashauri yametolewa tunayachukua tunakwenda kuyafanyia kazi nakushukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA, Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa majibu yaliyotolewa na Serikali, nilikuwa ninamuomba Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na mimi pamoja na Madiwani wa Wilaya ya Rungwe aweze kufuatilia uhalali wa majibu waliyompatia, hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kijiji cha Mpuguso Itula, Lukoba kinapata maji kutoka chanzo cha Kasyeto lakini, Kasyeto yenyewe ambayo inatoa chanzo cha maji wanakijiji wake hawapati maji. Je, ni lini Serikali itahakikisha watu hawa wa Kasyeto pamoja na Mpumbuli wanapata maji, maana wao ndiyo wanaotoa chanzo cha maji nao si wanufaika wa maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa majibu ambayo Serikali imeweza kutoa hapa ni majibu yenye uhakika. Hata hivyo tutatuma timu yetu kwenda kufanya uhakiki wa kuona uhalali wa maelezo ya Mheshimiwa Mbunge. Vilevile kwa vijiji vya Mpuguso na vijiji jirani, na vile vijiji ambavyo chanzo cha maji kinatokea kama ilivyo ada ya Wizara ya Maji vijiji ambavyo vinatoa chanzo cha maji huwa ndio wanufaika namba moja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ninaendelea kutoa maelekezo kwa watendaji wote wa Wizara ya Maji na RUWASA, pamoja na Mamlaka kuhakikisha maeneo yote ambayo yanatoa vyanzo vya maji lazima wawe wanufaika namba moja.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wilaya ya Rungwe Mahakama yake ya Wilaya ni jengo la siku nyingi sana. Ni lini Serikali itatusaidia kujenga jengo jipya ambalo litakidhi vigezo vya kuweka wafanyakazi na kuwa na nafasi nzuri ili waweze kufanyakazi kwa weledi na kwa ufasaha zaidi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda ambalo anataka kujua lini Serikali itajenga Mahakama katika Wilaya ya Rungwe.

Mheshimiwa Spika, Mahakama iko kwenye mpango ambao ni wa kipindi hiki tulichonacho cha mwaka wa fedha kuanzia mwaka 2021 mpaka 2025. Katika kipindi hicho tutahakikisha maeneo yote ambayo hayana Mahakama za Wilaya majengo mapya yanaenda kujengwa kwenye maeneo yote ambayo hayana Mahakama za Wilaya.

Kwa sasa hivi kwenye eneo hilo la ujenzi ni matarajio yangu kwamba ifikapo mwaka 2025 eneo hili la Mahakama tutakuwa tumeshamaliza kabisa shughuli za ujenzi. Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kwamba, tunakwenda kukujengea hii Mahakama katika kipindi cha awamu hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kipekee nimshukuru Mkuu wa Wilaya mpya aliyekuja katika Wilaya ya Rungwe, jana ameweza kuwaita wadau wanaonunua zao la maziwa na kuhakikisha wanapatikana wengi na wala siyo mmoja tena.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; Serikali haioni kuna haja ya kuleta Sheria Namba 3 ya mwaka 1977 ambayo ilikuwa inataka wakulima wote wanakaa katika mfumo wa kijiji. Sasa inawafanya Bodi ya Chai ambao ndiyo watoaji wa leseni hawawapi wakulima mmoja, mmoja kwa maana mkulima wa chai aweze kwenda kukopa benki, aweze kujua ni chai yake amuuzie nani na amkatae nani, sheria hii inawabana. Sasa kwa nini Serikali isilete marekebisho ya Sheria hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mrajisi wa Ushirika Wilaya ya Rungwe na sijui wilaya zingine alianzisha ushirika mpya na kuondoa ushirika wa kwanza bila kuwahusisha wakulima. Serikali inasemaje kwa hilo japokuwa jibu la msingi amesema ameweka, anasimamia na anafuatilia. Serikali ifuatilie kwa kina juu ya wakulima hawa ambao wao wanajua wapo RSTGA, lakini leo kuna kitu kinaitwa RUBUTUKOJE, wakulima wameachwa njia panda. Naomba Serikali ifuatilie kwa ukaribu suala hili. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana dada yangu kwa ufuatiliaji wa karibu kuhusiana na maendeleo ya wakulima wa chai na maziwa katika Wilaya ya Rungwe.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema kama kuna maendeleo ambayo anayaona kupitia Mkuu wa Wilaya kama tulivyosema tayari tumeshaanza kulishughulikia hili, ili kupata taarifa maalum kama nivyosema kwenye jibu la msingi kupitia Tume yetu ya Ushindani (FCC). Kwa hiyo hilo analolisema kuhusiana na Sheria Na.3 ya mwaka 1977, basi tutaangalia hilo pia, lakini tukipata taarifa maalum kulingana na ambavyo tumeomba kwa maana ya utaratibu wa ununuzi, namna bei zinavyopangwa katika soko, lakini pia na majina ya wanunuzi ambao wanashiriki katika ununuzi wa chai na maziwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mrajisi katika Vyama vya Ushirika, naomba nalo tulichukue kama Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, tutafuatilia ili tuone ni namna gani tutatatua changamoto ambayo inawakabili wakulima wa chai na maziwa katika Wilaya ya Rungwe. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kama ilivyo kwa Chama cha TFF kwenye eneo la ngumi kumekuwa na ubabaishaji mwingi sana kwa kitu kinachoitwa Rais wa ngumi.

Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia uongozi huu unaokaa kwa muda mrefu bila kufuata katiba kama inavyosema? Ahsante kwa kunipa hiyo nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara kupitia BMT lakini kupitia kwa Msajili, tunaendelea kufuatilia hizi katiba ambazo wamechomeka vipengele ambavyo vinawafanya watu kuendelea kukaa madarakani. Mheshimiwa Mwakagenda suala lako tunalipokea na pia nitafanya ziara katika maeneo hayo na tutapitia katiba yao pia kwa upya tuone ni wapi wameweka vipengele hivyo. Nikuhakikishie kupitia msajili tutaangalia na tutashauri lakini pia wanachama, mtushauri pale ambako mnaona hizi katiba zinakandamiza uhuru wenu katika vyombo hivyo ambavyo mnashiriki vya kimichezo. Tuko tayari kupokea ushauri wenu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Serikali kwa kukubali kuitengeneza barabara hiyo ya Bujela – Masukulu - Matwebe.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni lini Serikali itaisaidia Sekondari ya Lake Ngozi iliyopo Kata ya Swaya ambapo ni ngumu kufikika majira ya mvua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inajipangaje kuhusiana na barabara zote na madaraja ambayo yanaunganisha kati ya barabara na shule ambapo imewafanya wasichana wengi washindwe kwenda shuleni kutokana na mvua nyingi zinazonyesha zaidi ya miezi nane katika Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu ni lini Serikali tutasaidia kujenga barabara inayoelekea Sekondari ya Lake Ngozi kuhakikisha inapitika ili kusaidia wanafunzi ambao wanatumia barabara hiyo ili iweze kupitika kwa kipindi chote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi kwamba Serikali tunaendelea kutenga fedha kuhakikisha barabara hizo zinapitika kwa wakati wote na tunazingatia maombi maalum kama haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu barabara na madaraja yote ni ajenda yetu sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA kuhakikisha safari hii tunayashughulikia. Ndiyo maana katika bajeti ambayo mlitupitishia hapa, moja ya malengo yetu makubwa na ya msingi sasa hivi ni kuhakikisha tunakwenda kujenga madaraja hususan katika yale maeneo korofi, kujenga mifereji pamoja na zile barabara ambazo hazipiti ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ya barabara muda wote. Kwa hiyo, nimwambie tu kwamba akae mkao wa kutulia Serikali ipo kazini. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa swali la nyongeza.

Kama ulivyosimamia hospitali ya Makandana na kupata wodi ya wanawake bado tunashida ya x-ray wananchi wanaambiwa waende hospitali ya Igogwe. Ni lini Serikali itatupatia x-ray mpya katika hospitali ya Makandana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hospitali ya Halmashauri ya Rungwe maarufu kama Makandana ina tatizo la x-ray pamoja na juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu mingine, kipaumbele pia ni kupeleka vifaa tiba zikiwemo x-ray. Na katika mipango ya fedha ya miaka ijayo tutahakikisha pia hasa mwaka ujao katika mgao wa x-ray lakini na vifaa tiba vingine tunaipa kipaumbele Halmashauri ya Rungwe kwa maana ya Hospitali ya Makandana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni kweli kwamba, katika halmashauri zetu kunatengwa fedha asilimia 10 kwa maana ya mbili, nne na nne kwa wanawake, lakini ufuatiliaji wa mkopo huu baada ya kupewa hivyo vikundi unakuwa ni mgumu sana kurudisha fedha kwenye halmashauri. Serikali ina mkakati gani wa kudai madeni hayo ili fedha zirudi zikopeshe wanawake wengine kwa wakati unaofuata? Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa, swali linahusu wanaume nao watapataje access ya hizo fedha?

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, wanaume tunaomba wapate, lakini wanapokwenda kukopa huwa hawaelezi wake zao kama wamekwishakopa mkopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA – (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mpango huu wa kukopesha asilimia kumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Serikali imeboresha utaratibu kupitia Sheria Na. 12 ya Mikopo kwa maana ya fedha za Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kuhakikisha sasa siku za nyuma hatukuwa na asilimia kwa ajili ya ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo hii. Kwa hivyo, ilikuwa ni ngumu kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kufuatilia vikundi ambavyo vimekopeshwa kwa ajili ya kurejesha mikopo ile ili vikundi vingine vinufaike zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini kuanzia mwaka wa fedha ujao tumeweka kifungu cha ufuatiliaji katika vikundi hivyo kuwawezesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kufuatilia vikundi vile pamoja na kuviwezesha kuhakikisha marejesho yanafanyika ipasavyo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mradi wa REA-I na REA- II katika Wilaya ya Kyela Vijiji vya Lupaso Ndondwa na Mabuga mpaka sasa hawajapata umeme.

Je, nini jitihada za Serikali kuhakikisha tunapata umeme maeneo hayo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yapo baadhi ya maeneo ambayo REA I na REA II ilikuwa haijakamillisha, kulikuwa na changamoto mbalimbali ambazo sasa tumezitafutia mkakati maalum wa kuzimaliza na tunahakikisha kwamba inapoelekea 2022 tunapomaliza REA III round II na vile viporo vyote vya nyuma tutakuwa tumevimaliza, yalikuwepo matatizo ya Wakandarasi kushindwa kumalizia kazi kwa sababu ya changamoto mbalimbali lakini sasa tatizo hilo tumelitibu na tutahakikisha kwamba kila mwananchi anapata umeme katika maeneo yote ambayo yamepitiwa na mradi kulingana na scope ilivyokuwa kufikia 2022 kama ambavyo tumesema.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaikumbuka Barabara ya Bujera – Masukulu mpaka Matwebe katika Wilaya ya Rungwe kuweza kutujengea? Mheshimiwa Waziri naomba jibu la Serikali.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mkoa wa Mbeya, wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Rungwe mimi nimefika, na maeneo ya Mbeya kwa ujumla wake; na tumekubaliana kwamba tunapotaka kujenga barabara za eneo hili usanifu wa kina lazima ufanyike kwa sababu ya miundombinu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mbheshimiwa Sophia kwamba, pesa ikipatikana wakati wowote, barabara hii itajengwa kiwango uliyoitaja muhimu sana kwa watu wa Rungwe cha lami. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; nataka kujua pesa hizo za vitambulisho ambavyo wajasiriamali wanavitoa huwa zinaingia akaunti gani na mahesabu yake ni yapi, swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wanaonaje wakaweka utaratibu hasa wafanyabiashara wa mbogamboga na mama ntilie ambao mitaji yao ni midogo wakahakikisha kwamba chaji yao inakuwa moja kwa nchi nzima badala ya bei inakuwa juu zaidi kwa sababu wengi mitaji yao ni midogo, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKLI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ametaka kujua tu fedha za wajasiriamali wadogowadogo zinaingia katika mfuko gani, ni kwamba zinaingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, huko ndiko ambako fedha zinakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili alikuwa tu anataka kujua ukomo. Nieleze tu kwamba wakati Serikali inapanga ukomo wa shilingi 20,000 ilikuwa imezingatia vipato vya wananchi wetu na ndio maana awali hawa wakina mama ntilie, wafanyabiashara wadogowadogo walikuwa wanalipa fedha nyingi zaidi kwa kuchangia kidogokidogo kila siku lakini ilipowekwa shilingi 20,000 maana yake tulikuwa tumewasaidia kupunguza hiko kiwango. Kwa hiyo, hiki kiwango ambacho kipo kwa sasa bado kinazingatia hali halisi iliyopo lakini sisi tutalipokea ombi lako na tutaendelea kulizingatia kwa kadri ya mahitaji ya wafanyabiashara wetu, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Wilaya ya Rungwe katika Kijiji cha Masukulu kumekuwa na shida sana ya maji japokuwa Serikali ilipeleka fedha. Je, hamuoni kuna haja ya kutuongezea fedha ili maji yaweze kuenea katika vijiji vinavyozunguka Kata ya Masukulu?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, lakini kubwa ambalo nataka nimuhakikishie, Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, dhamira yake kumtoa mwana mama ndoo kichwani, kwa hiyo sisi tupo tayari kutoa fedha kuhakikisha wananchi wako wa Masukulu wanapata huduma ya maji sasa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa njia pekee ya kuisadia TAZARA ni kubadilisha hiyo sheria iliyoanzisha TAZARA, Serikali inatoa tamko gani la haraka kuhakikisha sheria hiyo inabadilishwa ili Tanzania iwekeze zaidi kuliko wenzetu wa Zambia wanaosuasua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spik, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sheria hii imekuwa ni kikwazo kwa upande wa Tanzania kuwekeza katika reli hii kwa sababu kama nilivyosema, hisa ni asilimia 50 kwa 50. Kila ukiwekeza upande wa Tanzania haiongezi hisa katika upande wetu, lakini nia ya Serikali ni kwamba ingewezekana hata leo sheria hii ingeweza kubadilishwa tuwekeze katika upande wetu kuweza kutoa huduma kwa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kwamba sheria hii hatuwezi kuibadilisha upande wa Tanzania mpaka tukutane na watu wa Zambia. Wenzetu walikuwa na uchaguzi wameshamaliza, wamefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, tumeshawaandikia barua tunasubiri wakijibu tukikutana jambo hili nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge litafanyiwa kazi haraka sana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naiuliza Serikali, Mgodi wa Kiwira kwa muda mrefu sana umesimama, je, ni lini Serikali itaamua kuleta wawekezaji au Serikali kuweka nguvu ili kusudi Mgodi huu wa Kiwira uweze kutoa ajira, lakini pia kuipatia pato Serikali yetu ya Tanzania. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Kiwira ni kweli tunatamani kwamba ndani ya Serikali uweze kuanza na wakati wa nyuma tumekuwa tunatamani kwamba taasisi zetu mbili TANESCO pamoja na STAMICO waweze kukaa pamoja na kukubaliana, kwa sababu mgodi ule pamoja na kwamba unatoa tu makaa ya mawe, lakini pia kinatarajia kuwa chanjo kingine cha kutoa nishati na kwa jinsi hiyo inahusisha taasisi zetu mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema tu kwamba mwezi Julai, TANESCO pamoja na STAMICO waliwekeana makubaliano ya kufanya kazi kwa pamoja na hivi ninavyoongea Shirika letu la STAMICO lipo katika harakati za ku-mobilize mwekezaji ili mgodi ule uweze kuanza. Nakushukuru sana.