Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sabreena Hamza Sungura (11 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwa kuwa ni mchango wangu wa kwanza napenda kutoa shukurani za dhati kwa chama changu kwa kunirudisha Bungeni kwa awamu nyingine ya pili, ahsanteni sana ninawaahidi ukombozi mpaka pale nchi yetu kitakapoeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili; napenda kuchukua fursa hii kulaani vitendo vya kikatili na udhalilishaji vinavyofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi vya kupiga, kudhalilisha na kuburuza Wabunge ndani ya jengo takatifu, jengo linalotunga sheria, jengo linalofanya maamuzi katika nchi hii. Ni kitendo cha udhalili na ni laana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye suala zima la viwanda na biashara. Kinachoendelea humu ndani ni maigizo. Ni ndoto za alinacha kusema mtafanya mapinduzi ya viwanda na biashara ilhali zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawana umeme, hawana maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ni Mkoa wangu wa Kigoma, Mkoa ambao tunapata umeme kwa kutumia jenereta ambazo haziwezi ku-run heavy industry. Kwa hiyo tukisema tutaanzisha viwanda, alipita Mheshimiwa Rais Magufuli kwenye kampeni akasema kwamba atahakikisha Dangote anakuja kufungua kiwanda cha cement Mkoa wa Kigoma, swali langu ni kwamba kiwanda hicho kitafunguliwa kwa umeme upi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma hauna barabara za maana kwa maana ya barabara za kupitika. Leo hii naongea kuna wananchi walikwama zaidi ya saa 48 njiani kwa ubovu wa barabara. Mkoa hauna reli yenye standard gauge, mvua zikinyesha inakuwa ni shida. Mkoa hauna ndege za uhakika, Mkoa hauna boti ama meli za kisasa ambazo zitatusaidia kupeleka bidhaa mbalimbali katika nchi nne ambazo zinaungana na Mkoa wetu wa Kigoma. Ni viwanda gani hivyo mtakavyoleta kujenga, nchi imejaa urasimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikia Mheshimiwa Rais anasema kwamba kuna mishahara hewa, lakini nafikiri hajapewa information za kutosha, siyo tu mishahara hewa kuna fidia hewa nchi hii. Nimeshuhudia baadhi ya wananchi maeneo mbalimbali wakilipwa fidia hewa, mtu anahonga shilingi milioni 10 anapewa milioni 60. Sasa kama kuna fidia hewa hakuna kiwanda kitakachojengwa katika mazingira hayo, mnajidanganya na Serikali inajua kama fidia hewa zipo lakini kwa kuwa ni miradi yenu hamchukui hatua zozote za kudhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu mitaji. Ni wajibu wa Serikali kuwawezesha wananchi wake kupata mitaji ya kuendeleza viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa. Mheshimiwa aliyemaliza kuongea hapa, amezungumzia matusi ambayo amepata mwekezaji wa ndani, mzalendo ndugu yetu Mengi. Lakini juzi juzi tumesikia Bakhresa naye akiambiwa kwamba ni mkwepa kodi, unaweza kukuta uhuni ule umefanya na management ya watu wachache tu katika kiwanda kile. Sasa nasema ni wakati muafaka wa Serikali kuweza kuwapongeza na kuwashikilia wawekezaji wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu kama Ndugu Mengi, mtu kama Ndugu Bakhresa na familia zao, rasilimali walizonazo wakisema waweke kwenye fixed deposit kwa mwaka fedha, watakayopata matatizo yao na familia zao wanamaliza, lakini wanawekeza kwa niaba ya Watanzania. Please Watanzania wanaojitokeza kwenye uwekezaji, Serikali iwaunge mkono. Kwanza kwa kutoa ardhi, pili kwa kutoa sheria zozote ambazo ni kandamizi kwao, lakini tatu kwa kumaliza migogoro ya fidia kwa wananchi mbalimbali na nne kuhakikisha kwamba mnawapa ruzuku. Serikali isiwe kikwazo kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, napenda kuzungumzia zao la mchikichi. Mkoa wa Kigoma nilizungumzia hapa miaka 40 iliyopita tuliwapa mbegu nchi ya Malaysia, Malaysia sasa hivi inafanya vizuri kwenye zao hili kutokana na kuliendeleza. Ajabu na aibu ya Tanzania, zao hili halijafanyiwa utafiti, zao hili halina bodi wala Serikali hamna mpango madhubuti wa kuendeleza zao la mchikichi. Tunaiomba Serikali ituambie ni lini mtawekeza nguvu za kutosha kwenye zao hili kwa sababu zao hili linazalisha bidhaa zaidi ya 20 ndani ya zao moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache naweza nikataja mafuta ya mawese, naweza nikataja mafuta ya mise, zao hili linazalisha sabuni, zao hili linazalisha chelewa, zao hili linazalisha majani ambayo yanafunikia mapaa katika nyumba zetu, lakini zao hili linazalisha makafi ambayo tunatumia kama nishati ya kupikia. Serikali ya Chama cha Mapinduzi miaka 54 ya Uhuru haijaona umuhimu wa zao hili na kuweza kuliendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nilizungumzia kuhusu bandari. Kulikuwa kuna kelele za sukari, imefikia mpaka shilingi 3,000, shilingi 3,500, shilingi 4,000 mpaka shilingi 5,000 baadhi ya maeneo, lakini wakati Serikali imelala hapa Dodoma, sukari mbovu inapitishwa kwenye mwambao kuanzia Pangani mpaka maeneo ya Mbweni kule Dar es Salaam. Bandari bubu zimejaa, Serikali inajua, watu wanakusanya kodi, Jeshi la Polisi liko pale, Serikali haipati mapato. Hii ni Serikali inafanya kazi kwa utashi ama ni Serikali inafanya kazi kama panya road? Lazima muamke, lazima muwe makini, fedha za nchi zinapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Tanzania sasa hivi wengi ukienda hospitalini figo zinafeli kwa sababu ya kutumia sukari za KK.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wanaotengeneza juice na vijana na akina baba, kijiko kimoja cha sukari kinahudumia ndoo mbili za lita 20. Wananchi wanafeli figo na wakienda katika hospitali yetu ya Taifa Muhimbili hakuna matibabu wanayopata ya ziada. Napenda kusema kwa kusikitika niliwahi kukutana na mgonjwa mmoja ambaye figo zake zimefeli na sababu kubwa ikiwa ni hizi juice ambazo zinaungwa KK. Mgonjwa yule figo zimefeli kwa sababu ya sukari hizi lakini kilichotokea gharama za matibabu zimekuwa ni kubwa akawaomba wauguzi arudi nyumbani nikapumzike nisubiri kuonana na muumba wangu kwa sababu siwezi kukidhi gharama hizi za matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mnaweza mkaona kwamba sekta hii inaathiri vipi sekta nyingine. Mnaingiza sukari mbovu, Serikali mmelala, mnashindwa kuziba mipaka ya nchi, bidhaa mbovu zinaingizwa, Watanzania wanakufa, mnajiita Serikali ya hapa kazi tu. Mimi nawaita Serikali ya hapa kuchoka tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la uvuvi. Mkoa wa Kigoma tuna Ziwa Tanganyika na takwimu tu toka mwaka 2003 mpaka 2014 zaidi ya nyavu na mashine za bilioni sita zimeibiwa katika Ziwa Tanganyika. Lakini kama Serikali ingekuwa makini kudhibiti wizi huu basi ni imani yangu tungeweza kuvua samaki wa kutosha na tungeweza kutengenezewa viwanda vya kusindika samaki hivyo tungeweza kuuza samaki ndani na nje ya nchi. Sioni mkakati wowote wa viwanda vya kusindika samaki katika Ziwa Tanganyika. Tunaomba Waziri ukija kuhitimisha utuambie ni kwa kiasi gani utawekeza kwenye viwanda hivi ili vijana wa Mkoa wa Kigoma waweze kuajiriwa katika sekta hii ambayo ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna viwanda kama viwanda vya chumvi. Hivi ni viwanda ambavyo havijapewa kipaumbele kabisa. Ukiangalia Bagamoyo kuna chumvi inatengenezwa, ukiangalia Uvinza kule Kigoma kuna chumvi ambayo ilikuwa inatengenezwa, lakini Mtwara na kwenyewe walikuwa wanatengeneza chumvi, Serikali hatujaona hata siku moja mkitoa hata ruzuku ya madini joto kusaidia suala zima la chumvi. Kila mtu anayekuja hapa ni sukari, sukari, sukari, How about chumvi? Kwa nini mmesahau? Ama hamuoni kama Watanzania watakosa madini yenye chumvi yanaweza na yenyewe yakaathiri afya zao. Ningependa mtuambie mkakati gani wa kusaidia watu wanaosindika chumvi ili mambo yaweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ningependa kuzungumzia kuhusiana na suala zima la uwekezaji. Ukiangalia katika sekta ya uwekezaji maeneo mengi matumizi ya Taasisi na Mashirika ya Serikali, matumizi yamekuwa ni makubwa kuliko bajeti ya maendeleo. Huu ni udhaifu wa Serikali. Ukiangalia Taasisi nyingi hazina bodi, bodi zimeisha muda wake, TR ameikumbusha Serikali kwamba kunatakiwa kuundwe bodi mpya lakini Serikali bado imelala. Je, mna dhamira ya dhati ya hapa kazi tu ama mnaendelea kufanya mazingaombwe kwa Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba Mawaziri mnapokaa kwenye mabaraza yenu mumkumbushe Mheshimiwa Rais aunde bodi mbalimbali ziweze kusaidia kilimo katika nchi hii. Ninashukuru.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SABREEN H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
Kumekuwa na kero kubwa kuhusu ushuru wa vifaa vinavyopita bandarini hapa Dar es Salaam na bandari ya Zanzibar hali inayopelekea uwepo wa bandari bubu hasa Ukanda wa Pwani. Je, ni lini Serikali itaondoa hizi kodi za kero kwa wasafiri wa kawaida kabisa ambao si wafanyabiashara wanaotumia bandari hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kero ya mifereji mikubwa hasa maeneo ya mijini kujaa taka hususan wakati wa mvua hali ambayo inahatarisha maisha ya Watanzania. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzuia taka hizi ili zisilete magonjwa ya milipuko hasa maeneo ya mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na kero kubwa ya ukosefu wa maji hasa maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa mfano uwepo wa Kambi kama Bulombola na maeneo mengine Mkoani Kigoma. Ukosefu wa maji kwenye kambi hizo unapelekea uchafuzi wa maji kwa kuwa vijana wengi kwenye kambi hizo wanategemea Ziwa Tanganyika kwa shughuli za kuoga, kufua na kujisafisha. Je, ni lini Serikali itazuia uchafuzi huu wa mazingira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa dakika chache nilizopata, lakini namwomba Mwenyezi Mungu niweze kuzitendea vyema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu napenda kujielekeza kwenye suala zima la usafirishaji wa binadamu ambao ni Watanzania kwenda nchi za nje kufanya kazi na wengi wao wamekuwa wakiuawa na clips zinatumwa hapa nchini, zinazagaa kwenye mitandao ya kijamii, sisi kama Wabunge tunaona, Serikali imekaa kimya haisemi jambo lolote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ni hatari kwa sababu hawa wanaofanya biashara hii ya kusafirisha binadamu kwa maana ya human trafficking na kuwapeleka huko wanakwenda kuuawa kinyama, kwa nini Serikali haifanyi msako maalum wa kuhakikisha inawakamata? Vijana wetu tena vijana wa kike wanakwenda huko wanafanyiwa unyama lakini Serikali imekaa kimya. Tunataka tamko leo litoke, ni hatua gani zimechukuliwa kubainisha watu wanaosafirisha wasichana wa Kitanzania bila ridhaa ama kwa ridhaa lakini kwa udanganyifu. Wanakwenda kwa wazazi wanawahonga dola 200, 300 wanawaambia kijana wako anakwenda huko atafanya kazi nzuri supermarket, wapi, akifika kule anadhalilika anauawa, Serikali inasemaji juu ya hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni conflict of laws. Nchi yetu ina tabaka za watu mbalimbali, kuna mila na desturi mbalimbali. Sheria zetu zimeingia kwenye mgongano, tuna Sheria ya Mirathi lakini pia tuna Sheria ya Ndoa, tunayo Islamic Restatement Act lakini pia tunayo Sheria ya Kimila ambayo ni Customary Declaration Order ya mwaka 1963.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi sheria zinakinzana, kuna sheria ambayo inamtambua mtoto ni kuanzia umri wa miaka 21 lakini kuna sheria inayosema mtoto mwisho wake itakuwa ni miaka 18, lakini kuna sheria za Kiislamu zinazosema mtoto mwisho wake ni pale anapobalehe. Sasa linapokuja suala la mtoto aolewe ama aozeshwe kwenye umri gani ama aoe kwenye umri gani kuna mwingiliano wa mila, desturi, dini na sheria. Je, mambo haya tunakwenda nayo vipi? Ni lazima mijadala ya kina ifanyike ili kuhakikisha kwamba pande zote zinabaki bila dukuduku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siungi mkono ndoa za utotoni, naunga mkono wanaopendekeza watoto waolewe kuanzia umri wa miaka 18. Hata hivyo, kuna watoto ambao na wenyewe wanaingia kwenye mapenzi kabla ya umri suala ambalo linapelekea ubebaji wa mimba. Sasa mtoto yule alivyopata mimba kwenye umri wa miaka 13, 14 ni mzazi gani atakayekubali kuona mtoto wake mwenye umri huo mdogo anakaa nyumbani na anazalishwa, hapohapo sheria zetu haziwaruhusu watoto hao kuendelea na shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukubaliane, kama tutaamua mtoto aanzie umri wa miaka 18 aweze kuoa na kuolewa, je, mtoto anayepata ujauzito kabla ya miaka hiyo status yake itakuwaje? Kama tutakubaliana miaka 18 basi kuwe kuna exception, kama atapewa ujauzito kabla ya hapo aruhusiwe kuozeshwa kwa sababu kuna watu ambao mila zao kukaa na binti nyumbani mama yake mzazi anapata ujauzito na mtoto anapata ujauzito ni matusi. Naomba hili lifanyiwe kazi kwa namna ya kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia suala moja, tunayo Sheria ya Probate and Administration of Estate Act ya Tanzania ambayo inaunda Waqf Commission. Wenzetu wa Zanzibar tayari wana Waqf Commission na watu ambao wanataka mali zao zigawanywe kwa mtindo huo wanakwenda kwenye Waqf Commission wanapeleka mapendekezo yao na yanafanyiwa kazi. Kwa upande wetu wa Tanzania Bara tume hii ipo kwenye sheria lakini haijawahi kuundwa toka uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini Serikali itaunda Waqf Commission kwa upande wa Tanzania Bara ili wale ambao wanajisikia kupeleka mali zao pale ambazo zitakuja kusaidia vizazi vinavyokuja basi waweze kuzingatiwa na waweze kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa hili ni nini? BAKWATA imekuwa na malalamiko mengi sana, watu wengi hapa nchini hawana imani na BAKWATA hususan Waislam wengi hawana imani na BAKWATA. BAKWATA wanauza mali za Waislam, BAKWATA wanaingia kwenye migogoro wamewauzia akina Yussuf Manji mali za Waislam, kesi, vita, ngumi kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini sasa msitengeneze hii Waqf Commission ambayo itatoa sasa mali hizi ambazo zinawekwa kwenye mikono ya watu ambao kwa kiasi fulani hawaaminiki ziweze kuwa kwenye mfumo wa Serikali ili…
T A A R I F A....
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsikitikia sana Mbunge mwenzangu aliyesimama, kama ni Mtanzania ambaye anafuatilia vyombo vya habari na anafuatilia habari za kila siku katika nchi hii hawezi kuhoji BAKWATA kwamba haikubaliki na kundi kubwa la Waislam Tanzania. Kwa hiyo, hilo ni jibu ambalo linamtosha kama halijatosha aje nitampa research na mifano ya kesi ambazo BAKWATA wameuza mali za Waislam, kitu ambacho kinapelekea vita nchi hii.
Kwa hiyo, napendekeza kabisa kwamba Waqf Commission iundwe kama ilivyo Zanzibar ili hawa waporaji ambao wamejificha kwa mgongo wa BAKWATA suala hilo liweze kwisha na lipatiwe muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kugusia suala zima la migogoro ya kazi katika chombo chetu cha Commission of Mediation and Arbitration. Chombo kile tumekianzisha ili kiweze kupunguza mrundikano wa kesi za labour hususan katika mahakama zetu kuu. Hata hivyo, nasikitika kusema kwamba, majengo yake hayatoshi ku- accommodate wateja wanaokwenda pale. Ukienda pale unakuta makundi ya watu yamekaa kwenye vyumba vidogovidogo, kelele, hata wale wanaosikiliza mashauri hawawezi kuelewana, joto, giza, mrundikano wa watu, mpaka watu wengine wanafanya kupangiwa …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii adhimu ya kuweza kuchangia Wizara hii muhimu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inachukua asilimia 80 ya Watanzania yaani ukiangalia wakulima, wafugaji na wavuvi ni almost asilimia 80, asilimia 20 ndiyo ya Watanzania wanaofanya shughuli nyingine. Sekta hii isipoangaliwa kwa umakini wa hali ya juu ni dhahiri kabisa kwamba tunaweza tukaliingiza Taifa kwenye mgongano wa wenyewe kwa wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana, nchi hii imejaliwa maeneo mazuri, ardhi nzuri, mito, bahari, mabonde, milima na kila kitu na asilimia kubwa ya ardhi bado iko vijijini na wakulima na wafugaji wengi bado wapo vijijini, ni tatizo gani linalotushinda kama nchi kuweka sera nzuri zitakazohakikisha kwamba Taifa haliingii kwenye migogoro? Tuna Land Use Planning, tumejipanga kila kitu, kwa nini watu wanagombana, shida iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna sababu za kijiografia zinazopelekea watu wanahama na mifugo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kuna maeneo ambayo kwa mvua jinsi ilivyonyesha mwaka huu mifugo haiwezi ku-survive mafuriko lazima watahama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Tumeona nchi nzima mvua inanyesha lakini Dodoma hii kuna maeneo kabisa mvua haikufika automatically lazima wakazi wa maeneo hayo ama wafugaji wa maeneo hayo ku-shift kutoka hapa kwenda sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni wakati gani mfugaji huyu atakwenda kuomba kibali cha kuhakikisha kwamba anahama na mifugo yake na wakati mifugo wale wanatakiwa ile ili wasife na njaa? Kwa hiyo, tunapoweka sera, sheria na sheria ndogo lakini lazima tuhakikishe mabadiliko ya kijiografia ambayo yanaweza yakapelekea watu wetu waweze kuhama yanazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la uvuvi. Mkoa wa Kigoma tuna Ziwa Tanganyika na lina samaki wa aina nyingi sana lakini samaki wale kwa kweli hawavuliwi ipasavyo. Tuna dagaa wazuri ambao wanapelekwa Uingereza, Marekani, Malaysia na sehemu zingine lakini bado wanavunwa kwa kiasi kidogo sana. Tunaomba kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wetu na wavuvi wanaotoka Ziwa Tanganyika waweze kuvua uvuvi wenye tija na kulisha nchi lakini pia na kulisha nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida kwa wavuvi wetu katika Ziwa Tanganyika wanatekwa na maharamia kutoka Congo na wengine kutoka Burundi wakiingia kule wananyang’anywa nyavu zao, pesa, mashine na kadhalika. Hali hii inawarudisha vijana wengi nyuma na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuhofia usalama wao. Serikali inawa-guarantee vipi vijana hawa ambao wana-risk kwenda kutafuta maisha katika ziwa lenye kina kirefu kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuweza kuchangia uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia bado kodi kwa wavuvi ni kubwa. Nilikuwa na-discuss na Mheshimiwa hapa wa Ukerewe, wavuvi wanatozwa kodi kubwa sana za uvuvi, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza kodi hizi? Kwa sababu mvuvi anapokwenda kuvua kwanza kuna mawili, aidha, arudi salama ama asirudi salama. Kwa hiyo, pamoja na kuchukua risk yote hii kwa nini tunawatoza tozo kubwa na ni za kero? Mna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba tunapunguza kodi za kero kwa wavuvi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mkoa wa Kigoma tunalima, tuna zao la mchikichi. Kwa taarifa ya research zilizofanyika hivi karibuni, zao la mchikichi linatumika katika kuzalisha bidhaa mbalimbali katika nchi ya Europe kwa asilimia 80. Chocolate hizi zinazotengenezwa ili ziweze kuganda na ziweze ku-survive zinatumia zao la mchikichi, lakini hakuna utaratibu wowote unaowekwa kuhakikisha kwamba unafanyika utafiti wa kutosha na zao hili liweze kulimwa kwa umakini wa hali ya juu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika Bunge lako hili Tukufu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutupa afya na uhai na leo hii kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijielekeze kwenye mchango wangu kwenye mambo mbalimbali ambayo yameainishwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na ningeomba nianze na suala la kwanza kuanzia kwenye suala la Mahakama, lakini pia, mambo ya ndani, magereza na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa masikitiko yangu kwa kile ambacho nilikiona kimetokea Ijumaa iliyopita tukiwa Mahakamani Kisutu. Tulishuhudia kwamba, ile tunayoita miongoni mwa cardinal principle za Criminal Law kwamba, alignment to the Court kwa accused ama suspect inavunjwa waziwazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia kabisa kwamba, mtuhumiwa ana haki ya kufikishwa Mahakamani kwa wakati, lakini kulikuwa kuna sababu mbalimbali ambazo tunaambiwa kwamba, magari yameharibika hivyo, wale watuhumiwa hawawezi kuletwa mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunakuwa tunavunja ile misingi ambayo tumejiwekea kwenye sheria. Kwamba tunategemea Jeshi la Magereza liweze kujipanga vizuri na liwe linafanya kazi kwa wakati na tusiwe na visingizio vidogovidogo, itakuwa inatuharibia sura ya Wizara, lakini na pia sura ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwenda moja kwa moja sasa kwenye Mahakama ya Mafisadi, ile ambayo inaitwa The Corruption Economic and Organised Crime, High Court Division. Tulisema mafisadi papa na wale ambao ni mafisadi size ya kati kwa makosa yatakayoanzia bilioni moja wanatakiwa wapelekwe pale, lakini kumekuwa kuna upungufu wa watu wanaopelekwa kwenye Mahakama ile kwa sababu, kuna watu ambao hawafikii kile kigezo cha bilioni moja kwa hiyo, wanakuwa hawana sifa ya kwenda Mahakamani pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kama Mahakama ambayo tumeianzisha, tumeweka watendaji, tumeweka Majaji, tumeweka Maafisa wa Mahakama na maofisa wengine, inakuwa Mahakama ile tunaona kama haijiendeshi kwa makusudio ambayo yaliwekwa kwa sababu, watuhumiwa wanakuwa ni wachache sana. Hivyo, tungependa kuiomba Serikali iweze kupunguza kile kiwango kilichowekwa, ili watu wengi waweze kwenda kuchajiwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna changamoto. Changamoto ya kupata report za Mkemia Mkuu wa Serikali, zimekuwa zinacheleweshwa sana, kitu ambacho kinasababisha watuhumiwa wengi kuweza kucheleweshwa kesi zao. Hata ukiangalia katika hotuba ya Kitabu chetu cha Waziri Mkuu, ukurasa wa 62, ukiangalia idadi ya kesi ambazo zilipelekwa Mahakamani na idadi ya kesi ambazo ziliamuliwa kwa kweli, zinaonekana ni chache sana, hivyo, kunakuwa kuna shida hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili ambalo ningependa kuchangia ni suala la kufungiwa kwa mabenki yetu. Nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, tulishuhudia benki mbalimbali zikiwa zimefungiwa kwa kukosa mitaji. Hata hivyo, tunaangalia initial capital ya benki hizi ambazo wakati wanaanza ku-operate walianzisha kwa milioni 250, lakini wakapewa limit ndani ya miaka mitano waweze kufikia bilioni mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kilichotokea hapa ni kwamba, waendeshaji wa taasisi hizi za kibenki wameshindwa kufikia mitaji ile na kusababisha benki hizi kufungwa. Kwa hiyo, kwa akili ya harakaharaka hapa sisi tuko watu 360 humu ndani, hivi ni nani ambaye anaweza akapewa milioni 250 halafu akaambiwa azalishe mpaka bilioni mbili ndani ya miaka mitano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaweza tukaona hapa kwamba, kuna changamoto kubwa sana na waathirika wa suala hili wanakuwa ni Watanzania ambao ni wafanyabiashara wa kawaida kabisa ambao wanaambiwa walipwe 1,500,000/= halafu wasubiri process ya insolvence mpaka itakapokamilika. Ukiangalia hata katika sheria process hii ndefu na inachukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, tungejaribu kuyafikiria mabenki haya, ili pale tunapowawekea conditions za kujiendesha basi wawe na viwango ambavyo watafanya kazi na vitakuwa ni viwango stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kwenda kugusia suala la maji. Pale Kigoma Ujiji Manispaa kuna mradi mkubwa sana wa maji, lakini pia tuna changamoto ya umeme. Tuna pampu takribani 13, lakini mpaka sasa pampu zinazo-operate ni nne, pampu tisa zimekaa pembeni, changamoto kubwa ni umeme. Wakisema wa-operate pampu zote maana yake ni kwamba, shirika lile la maji litakuwa linajiendesha kihasara kwa sababu, utahitajika umeme ambao utakuwa ni 2.5 megawatt kwa mwezi, kiasi ambacho ni kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, the only solution ambayo tunaitegemea ni whether tuunganishwe na gridi ya taifa, ili ule mradi uweze ku-run ama Serikali iweze kutenga pesa kwa ajili ya kununua solar system, ili tuweze kupata maji safi na salama na watu waweze kupata maji kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, basi tungeomba Serikali ilifanyie mkazo suala hili kwa sababu, wananchi wetu wanaathirika sana, hususan wale wanaofanya ibada za asubuhi, mchana na usiku wanakuwa muda mwingi sana wanahitaji maji. Kwa hiyo, tukikosa maji kwa kweli, inakuwa ni kikwazo kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna changamoto ya maji katika Mji wetu wa Uvinza, kuna kituo cha afya kiko pale, mama mjamzito anapoenda kujifungua anatakiwa aende pale na dumu tano za maji, bila hivyo pale hupokelewi wala huzalishwi. Sasa kwenye mazingira kama haya tungeweza kuiomba Serikali, kwenye bajeti ya mwaka huu waweze kututengea kiasi kidogo cha pesa, ili angalau katika eneo lile la kituo cha afya kichimbwe kisima ambacho kitaondoa kero ya akinamama kuweza kwenda na madumu ya maji, ili waweze kupata huduma za kuzalishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ningependa kujikita kwenye dawa za kulevya. Kwa kiasi fulani ningependa kuipongeza Serikali kwamba, suala hili kwa kiasi fulani linapungua, lakini bado tuna changamoto, vijana wakati unga unazuiliwa vijana wengi wame-diverge, wanatoka kwenye unga wanaingia kwenye ugoro kwa maana ya tumbaku, lakini pia na mirungi. Kwa hiyo, Serikali sasa na yenyewe ijaribu kuangalia kwamba, huu ugoro ambao vijana wengi wanatumia una madhara gani na kuweza kutoa elimu kwa umma ili kuweza kuzuwia hujuma kama hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ningependa kuchangia kuhusiana na masuala mazima ya ardhi. Katika mradi unaoendelea wa upanuzi wa Airport ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ama ya Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, kumekuwa kuna wakazi ambao wanakaa maeneo yale karibu na airport ambao kuna ambao walipata upungufu wa fidia, lakini pia, kuna wale ambao hawakulipwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuja ikaahidi kwamba, itafanya malipo ya mwisho kwa wale ambao walipata fidia pungufu na wale ambao hawakulipwa kabisa wangekuwa included. Hata hivyo, mara baada ya malipo kubandikwa ilionekana waliopata fidia zile ni wale ambao walisahaulika na wale ambao walipata pungufu hawajaweza kupatiwa fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwenye Sheria zetu za Ardhi, yaani Sheria ya Land Acquisition Act, inataka pale Serikali ambapo inachukua ardhi ya wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa manufaa ya umma, basi fidia stahiki na ya haki iweze kutolewa kwa wakati, ili wananchi wale waweze kujipanga na maisha mengine yaendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali wakati tunaenda kwenye Bunge hili la bajeti, tunaenda kupitisha bajeti mbalimbali za Wizara; ningeomba waweze kuwaangalia wale wananchi wote ambao walipata fidia pungufu kutokana na ujenzi wa airport unaoendelea waweze kulipwa fedha zile na shughuli mbalimbali ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la ajira kwa vijana, kumekuwa kuna shida kubwa sana kwawenzetu wa bodaboda, lakini pia na Askari Polisi. Wiki tatu zilizopita nilishuhudia tukio ambalo ni la kusikitisha sana Dar-es-Salaam, maeneo ya Buguruni. Vijana wa bodaboda wakati wanaendesha bodaboda kwa jinsi ambavyo traffic wetu wamekuwa wakilenga kuwakamata na pale ambapo wanashindwa kufanikiwa kufikia vijana wale basi inafikia hata hatua traffic wanashika usukani ule wa mbele na kutaka kama kuugeuza hivi ili waweze kusimama wale vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni yule kijana alirushwa kutoka kwenye bodaboda kwenda mpaka barabarani na gari nyingine ikapita ikapitia kichwa moja kwa moja akapasuka na akafariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanasikitisha sana na vijana wengi nchi nzima wanalalamika, lazima tuwe na njia za staha ambazo zitatufanya tuweze kuwakamata hawa vijana hata pale wanapokosea lakini sio njia ambazo zinapelekea mpaka kwenye mauaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto na tungeomba wenzetu wa Mambo ya Ndani waweze kuona ni kwa jinsi gani wanaweza wakaongea na askari wetu polisi na kuwapa mafunzo kwamba lazima tufanye kazi kwenye njia ambayo itakuwa ni ya kibinadamu, lakini na njia ya staha ambayo haiwezi kupelekea vifo wala majeruhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye viwanda, nimeangalia mpango wa Serikali, nimeona kuna viwanda ambavyo vimeanzishwa na mashirika ya umma na taasisi nyingine takriban viwanda 110, lakini katika viwanda vyote hivyo vilivyoanzishwa kwenye mkoa wangu wa Kigoma sijaona kiwanda hata kimoja. Kwa hiyo ningependa kuishauri tena Serikali zipo sababu mbalimbali zinazopelekea mikoa ya pembezoni isiweze kupata viwanda uki-compare na Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Tanga. Sisi kwa sababu ya umbali tunapata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, napenda kumpongeza Rais mpya wa Tanganyika Law Society kwa ushindi huo mnono. Tuko pamoja naye sisi kama timu ya wanasheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa masikitiko yangu makubwa na kumpa pole Kamanda wetu na Waziri Kivuli wetu na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Tundu Lissu kwa madhila yaliyomkuta hapa Dodoma. Suala hili limeshakuwa komavu, ni suala ambalo katika jamii yetu ya Watanzania limekomaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kugusia Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Article 14 inazungumzia right to life. Kila Mtanzania ana haki ya kuishi na wajibu wa kutoa roho ni kazi ambayo inafanywa na Mwenyezi Mungu, lakini pale inapotokea mtu ameuawa, basi hata kwenye Islamic Sharia, mimi ni msomi wa Islamic Sharia, tunasema kuna option tatu; moja kisasi; mbili kusamehe; tatu, yule aliyemuua mwenzake abebe gharama za kuhudumia familia ya yule mtu aliyoiacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala la kutoa nafsi za Watanzania katika nchi yetu limekuwa ni common. Napenda niipongeze Serikali, mnajua kwamba kila mtu ana haki ya kuishi na ndiyo maana toka kipindi cha Mzee Mkapa, Mzee Kikwete na kuendelea, Serikali haijajaribu hata siku moja kuchukua jukumu la kunyonga, kwa sababu inajua kila mtu ana haki ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii tabia inayoendelea ya watu kunyongwa, watu kutupwa kwenye viroba, kupigwa risasi hadharani, inatutisha sana. Ni tabia ambayo sisi kama Taifa bila kuangalia vyama, sura na rangi lazima tuikemee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma uko pembezoni mwa nchi, lakini pia tuko karibu na nchi ambazo zimeingia kwenye vita. Tukiangalia sababu ambazo zilifanya watu wetu wengi wapigane huko nchi jirani ni mauaji ya kimya kimya ya watu wasiojulikana. (Makofi)

Kwa hiyo, kama nchini watu wataendelea kufa, kuumia, tusipochukua hatua, sisi tunakaa jirani kule, walikuwa wanakuja wakimbizi, tunawauliza sababu ya vita ni nini? Wanatuambia, tulikaa usiku baba akavamiwa akauawa. Watoto wakiamka asubuhi wanajua ni nyumba fulani ndiyo iliyovamia; kinachofuatia ni kisasi; vikaanza vita vya wao kwa wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kama Taifa, tuungane, tuhakikishe kwamba tunazuia aina yoyote ya Mtanzania asiweze kuuawa bila sababu. Mambo haya yamekomaa. Juzi juzi tulisikia Mtwara kule mtu kapigwa risasi kwenye kichogo, juzi juzi tumesikia Mwandishi wa Habari katekwa, kaumizwa; Ndugu yetu Alphonce Mawazo, Mwenyekiti wa Geita alipigwa kule hadharani akafariki; Ben Saanane kapotea mpaka leo haonekani. Mambo haya tukiyakalia kimya kama Taifa kwa kweli naamini tutaangamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Serikali ina moyo wa dhati ndiyo maana ikafuta adhabu ya kifo. Basi iendelee kusimamia haya mauaji ambayo yanafanywa na kuendelea kuchafua nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawakumbuka makamanda wetu waliopoteza maisha kule Kibiti. Ni dhahiri sasa, lazima Serikali isimame na Watanzania tusisikie tena vifo vinavyotokea bila sababu ya msingi ili kutii Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika Sheria yetu ya Ardhi, katika kifungu cha 167 kinachozungumzia uanzishaji wa Mabaraza ya Ardhi. Kaka yangu Mheshimiwa Cosato pale ameelezea vizuri sana kwamba Mabaraza haya yana upungufu, wengine wakapendekeza yaletwe yafutwe, wengine wakapendekeza hivi na hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza haya yameanzishwa kwa mujibu wa sheria. Ukiangalia kifungu cha 167(1) tunaona kabisa kwamba vyombo ambavyo vimepewa mamlaka ya kusimamia migogoro ya ardhi inaanza Court of Appeal inakuja High Court of Tanzania, inakuja District, Land and Housing Tribunal, inakuja Ward Tribunal na inakuja Village Land Council.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusikitika kwa kile kilichotokea kwa mwenzetu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Paul Makonda, miezi miwili iliyopita kuamua kufuta Mabaraza ya Ardhi kinyume kabisa na sheria za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo pekee chenye mamlaka ya kutunga sheria, chombo pekee chenye mamlaka ya kufuta sheria na chombo pekee chenye mamlaka ya kufanya amendment za sheria ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaomba Waziri wa Katiba na Sheria atueleze Mkuu wa Mkoa huyu mamlaka ya kufuta sheria za nchi hii anayatoa wapi? Mnataka nani aseme ili basi kila mtu…

T A A R I F A . . .

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limewahi kumwita Paul Makonda na kumwonya juu ya uvunjaji wa taratibu na sheria za nchi hii na aliomba msamaha akasema kwamba itakuwa ni mwanzo na mwisho, lakini mara baada ya hapo, tunaona Mabaraza ya Kata ya Mkoa mzima wa Dar es Salaam sasa hivi yamesitishwa na hakuna shughuli zinazoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kwamba ni mamlaka gani yanayompa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa huyu mamlaka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimewahi kuhoji kwenye Bunge hili kwamba ni nani kati yetu atapewa mtaji wa shilingi milioni 250 a-raise mpaka shilingi bilioni 2 ndani ya miaka mitano? Hoja yangu ni kwamba mabenki mengi yamefungiwa baada ya kukosa vigezo vya kutimiza mtaji wa shilingi bilioni 2. Athari yake ni nini kwa uchumi wa nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi walikuwa wamewekeza pesa kwenye mabenki hayo na wakati wakisubiri process za insolvency maana yake watachukua muda mrefu sana ili waweze kuletewa fedha zao. Waliahidiwa kwamba kwa awali watalipwa Sh.1,500,000 kila mmoja halafu watasubiri process ya mfilisi mpaka itakapofikia mwishoni ndiyo waweze kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sasa kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi iweze kuhakikisha kwamba inashusha riba ili watu wetu waweze kuwa na uwezo wa kurudisha mikopo katika mabenki yetu. Ukiangalia ripoti ya CAG inaonesha mikopo isiyolipika ilipanda kutoka shilingi bilioni 9.1 mpaka shilingi bilioni 2.5. Watu wengi kushindwa kulipa mikopo kwa sababu mbalimbali. Wapo ambao wanashindwa kulipa mikopo kwa sababu kodi za TRA zimezidi lakini wapo ambao wanashindwa kulipa mikopo kwa sababu sekta ya biashara na uchumi imezidi kudorora katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka napenda nizungumzie Special Economic Zone. Kuna suala zima la fidia ambalo limezungumziwa katika Ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia hata kwenye sheria zetu, mfano Sheria ya Land Acquisition Act, section 15 inaelezea kwamba maeneo ambayo yamefanyiwa tathmini kwa ajili ya kulipwa fidia ya Special Economic Zone (SEZ) na Export Processing Zone (EPZ) yaweze kulipwa takriban shilingi bilioni 60 kwa mwaka 2015/2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi fidia zile zimefikia shilingi bilioni 190. Hiyo ni kwa sababu kila mwaka kwa mtu ambaye alithaminiwa na alitakiwa alipwe fidia ukipita mwaka mmoja kuna 6% kama nyongeza ambayo anatakiwa aongezewe. Kwa hiyo, kwa wananchi wote wa maeneo ya Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Kigamboni kwa maana ya Kurasini (Tanzania-China Logistic Center), Mara, Ruvuma na maeneo mengine yote, fidia imeongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu Serikali imeshindwa kulipa fidia kwa wakati na hivyo kuliingizia Taifa hasara na mzigo mkubwa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka napenda kuitaka Wizara iwasaidie wawekezaji wetu kutoka nje. Kuna Tanzania Diaspora, tumeona hapa wenzetu Wachina na India, juzi hapa waliitishwa Wahindi wote waliopo duniani warudi India kwa ajili ya kwenda kufanya uwekezaji ambao utakaokuwa na tija. Wahindi waliopo Tanzania na wengine walitoka kwenye Bunge letu hili walienda India kuwekeza. Kwa nini Diaspora wetu ambao wapo nje ya nchi wenye uwezo mzuri, ambao wangeweza kuchangia uchumi wa nchi hii, hawawi included katika kuendeleza uchumi wa nchi hii?
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne iliweka Desk la Diaspora pale na walikuwa wameshaanza process hizi lakini mpaka sasa bado kimya. Ukiangalia katika Katiba pendekezwa ya Ndugu Warioba, Ibara ya 72, iliweka kipengele kwamba Watanzania ambao walibadili uraia kwa ajili ya kutafuta maisha wapewe special priority au hadhi maalum ili waweze kutambulika katika uchumi wa nchi yetu, waweze kumiliki ardhi, kuwekeza katika hisa na waweze kumiliki mali katika nchi yetu. Kwa hiyo, tunaomba tuweke desk maalum kwa ajili ya Diaspora ili waweze kujiunga vikundi kwa vikundi, waweze kuwekeza kwenye sekta za maji, kilimo, viwanda na kadhalika kwa sababu kuna Watanzania wenye fedha na wenye uwezo mzuri katika nchi za Arabuni, America na Ulaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni kabisa napenda nimalizie kwa kuzungumzia hali ya uchumi katika Mkoa wa Kigoma. Ukitaka kuhakikisha kwamba hali ya uchumi imekuwa mbaya, mwaka uliopita Mkoa wa Kigoma takriban miezi sita au mpaka saba wafanyakazi na wafanyabiashara wa maduka mbalimbali katika Mji wa Kigoma waligoma kufungua maduka kwa sababu walipandikiziwa tozo kutoka Sh.15,000 mpaka Sh.50,000 na Chama cha ACT Wazalendo. Hiyo inaonesha kabisa kwamba uchumi unayumba ndiyo maana watu waliamua kufunga maduka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Chama cha ACT Wazalendo walilikoroga akaja Ndugu Polepole akalinywa, alipoingia pale aliambia wananchi wanatakiwa wafungue maduka na kodi ile inashushwa. Kupandisha kodi ni mchakato wa sheria na ulifanywa kwa mujibu wa sheria na Baraza la Madiwani ndiyo lililopandisha na ikaenda Mkoani, TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri akaweka saini ikashuka, inakuwaje anakuja Mwenezi na kukataza kodi ile isilipwe?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika sekta muhimu katika nchi yetu, lakini pia na duniani kwa ujumla. Napenda kusema kwamba sekta ya kilimo ni sekta ambayo inazalisha mara 11 zaidi ya sekta nyingine katika nchi za Afrika hususani zilizopo katika Ukanda wa Jangwa la Sahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia vyama vya ushirika. Kumekuwa kuna migogoro mingi sana kwenye Vyama vya Ushirika. Vyama hivi vimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika ya Mwaka 2013 na mwenye mamlaka ya kushughulikia na kusimamia migogoro yoyote ndani ya Vyama vya Ushirika ni Ofisi ya Mrajisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wetu wa Mikoa na Wilaya na viongozi wengine wamekuwa wana-interfere sana sekta hii ya Vyama vya Ushirika na hivyo kusababisha matatizo. Wamekuwa wana-interfere katika suala zima la masoko, lakini pia katika suala zima la uchaguzi, kwamba nani awe kiongozi wa ushirika? Wamekuwa na interference kubwa sana, kitu ambacho kinatuletea migogoro na vyama vyetu vya ushirika vinashindwa kujiendesha kama vyama binafsi na hivyo vinaonekana kama ni vyama ambavyo vinaingiliwa na siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba wananchi wa Kasulu katika Pori la Kagera Nkanda katika ziara ya Mheshimiwa Rais aliwaruhusu wananchi wale wafanye shughuli za kilimo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya Mheshimiwa Rais kuondoka, wananchi walianza shughuli ile ya kilimo, lakini baadaye wananchi wale wamekuja kuingiliwa na kukatazwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya. Kwa hiyo, tunataka kujua kwamba nchi hii nani mwenye mamlaka ya kupinga amri ambayo imetolewa na Mheshimiwa Rais? Tunaomba wananchi wetu wa Kasulu wa Pori la Kagera Nkanda wapewe fursa ya kuendelea na kilimo kwa sababu ni haki yao ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kuchangia kuhusu suala zima la ardhi. Ardhi yetu imegawanyika katika maeneo mengi, hata ukiangalia kwenye sheria zake, kuna wenzetu hawa wa Land Use Planning, inaeleza kabisa kwamba tutakuwa na ardhi kwa ajili ya agriculture, tutakuwa na ardhi kwa ajili ya wafugaji, tutakuwa na ardhi kwa sababu ya reserve, tutakuwa na ardhi ya forest, tutakuwa na ardhi ambayo ni ya majanga hazard, lakini kwa nini ardhi ya wakulima mara nyingi inakuwa inaingiliwa na kusababisha migogoro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii migogoro imekuwa haiishi wala haipungui, kumekuwa kuna interference kubwa sana, sasa kama tumetenga vitengo vya ardhi ambavyo vime-categorize ardhi kutokana na sekta mbalimbali, kwa nini wakulima katika suala zima la ukulima wanaingiliwa na wanashindwa kufanya kilimo chao kwa nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni muhimu sana lingewasaidia wakulima wetu ni kuhusu kupata Hatimiliki ambazo ni za kisasa. Tunadanganywa hapa Bungeni kila siku kwamba Hatimiliki za Kimila na Hatimiliki za Kiserikali zina hadhi sawa katika mabenki yetu. Hili suala siyo kweli! Wakulima wanaoenda na Hatimiliki za Kimila katika mabenki hawapewi mikopo, mtu anaenda na Hatimiki ya Kiserikali anaonekana ana hadhi kuliko anayeenda na Hatimiliki ya Kimila. Wakulima wetu huko vijijini wanaenda kubalidishana mazao yao na chumvi, wanabasdilishana mazao yao na bodaboda, wanabadilishana mazao yao na nguo, wanabadilishana mazao yao na yeboyebo. Kwa nini Serikali isiweke mpango kabambe wa ardhi wa kuhakikisha kwamba hata ardhi za vijijini sina pata granted right of occupancy ili na wao waweze kuwa na hadhi sawa na watu wengine ambao wanapata mikopo na wasiendelee kubadilishana mazao zao na kuku na vitu vingine vinavyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwenye zao la mchikichi Mkoa wa Kigoma. Miaka ya 1970 Mkoa wa Kigoma tuliwapa zao hili mbegu nchi ya Malaysia na Malaysia sasa hivi inafanya vizuri kwenye zao hili kuliko kitu chochote, kwa nini Serikali sasa isiunde Kituo cha Utafiti ili waweze kutafiti zao hili na kuweza kutusaidia wakazi wa Kigoma. Wenzetu Burundi ukifika mpakani pale mwa Kigoma ukianza Burundi mpaka unafika Makao Makuu ya Mji wa Burundi nchi yote imepandwa michikichi, kwa nini mnashinda kuendeleza zao la mchikichi katika Mkoa wa Kigoma? Ningependa kupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wilaya yetu ya Kakonko tuna mazao ambayo tunalima, tuna mahindi, mihogo, mpunga, karanga lakini mazao ya biashara tuna tumbaku, kahawa na pamba. Serikali ina mkakati gani wa kuhakiksha kwamba mazao haya yanapatiwa ufanisi ili yaweze kusaidia katika sekta nzima ya Ardhi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta nzima ya kilimo inahusisha sekta nzima ya maji, huwezi kufanya kilimo bila kuwa na maji. Kwa hiyo basi, kwa sababu katika Wilaya yetu na Kakonko na maeneo mengine tumekuwa tukipokea Wakimbizi na kuna makambi mbalimbali ya wakimbizi hali ambayo inapelekea wakimbizi wale wakihitaji sekta ya nishati…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika bajeti iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuchukua fursa hii kuwapa pole viongozi wangu tukiongozwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa kufungwa takribani miezi minne wakiwa mahabusu na kukosa dhamana hali iliyopelekea kwa kweli Kambi yetu kuyumba na wanachama kuhuzunika takribani nchi nzima kwa kitendo kama hicho. Nawapa pole sana nawaombea Mwenyezi Mungu aweze kuwapa subira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchukua fursa hii kukishukuru Kiti chako, nikianza na Mheshimiwa Spika lakini na wewe mwenyewe na Mawaziri na Wabunge mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine walipata kunijulia hali pale nilipopata hitilafu ya kiafya. Nawashukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye mchango wangu. Wananchi wa Mkoa wa Kigoma wamenituma na wanahoji kwamba katika Mpango wa Maendeleo kulikuwa na suala zima la ununuzi wa meli ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika lakini wameshangaa miaka inaenda meli hii bado haijaweza kununuliwa wakati ni kitu ambacho kipo kwenye mpango. Kwa hiyo, wanaomba kwenye bajeti ya mwaka huu basi meli hii iweze kupatikana ili sasa wananchi waweze kupata fursa mbalimbali kutokana na suala zima la uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo napenda kuzungumzia na napenda kutoa shukrani kwani kwenye ziara ya Waziri Mkuu alivyokuja Kigoma kwa kuendeleza zao letu la mchikichi na kuanzisha Kituo cha Utafiti katika Mji Mdogo pale Kihinga na kuwezesha kupandikiza miti takribani 4,000 ikiwa na lengo la kwenda mpaka miche 5,000,00. Tunaomba Serikali isiishie hapo iweze kutusaidia kutafuta wawekezaji ili waweze kuwekeza hususani katika Bonde la Mto Luiche kwa kuwa watu wengi sana wana nia ya kuendeleza kilimo hicho lakini issue ni masuala ya kifedha. Pia watusaidie kwa Benki yetu ya Kilimo iwawezeshe wananchi kwa masharti nafuu kabisa waweze kupata mikopo na waweze kuitumia fursa hii adhimu ambayo imeletwa katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tungeomba wawekezaji wa zao la mhogo. Nimesikia China ni wanunuzi wazuri sana wa zao mihogo na Mkoa wa Kigoma tumekuwa tukilima sana zao hili. Tunaomba Serikali itusaidie na sisi kupata wawekezaji na wanunuzi kwenye zao hili ili angalau wananchi wetu waweze kuendeleza kilimo hiki ambacho kitakuja kuwa na tija kwa mkoa na kwa taifa kwa jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla wamekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na masuala mazima ya biashara. Wanasema biashara imekuwa na mlolongo mrefu. Ili mtu aweze kufungua biashara yake na ku-establish na ikakaa kwenye mstari mlolongo wa vitu vingi sana vinahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mtu anataka kutoa ajira kwa vijana, anataka kufungua ofisi, anahitajika alipe Pay As You Earn, Income Tax, OSHA, kwenye Manispaa katika Halmashauri zetu, Workers Compensation Fund, bado kuna mifuko mingi, NSSF na kadhalika atoe michango na Withholding Tax. Kwa hiyo, kumekuwa kuna mlolongo wa vitu vingi, mambo ya fire na kadhalika, ambapo ni mtu anajitahidi kutengeneza ajira mambo yote haya anatakiwa alipie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili kwa namna moja ama nyingine ni kikwazo kwa wafanyabiashara wetu. Kwa wale wanaotoka nje pia, wanatakiwa wa-obtain Certificate of Incentive kupitia pale TIC, tumekuwa na mlolongo wa vitu vingi. Nashauri Watanzania wa kawaida na wenyewe wasaidiwe, kama ilivyowekwa One Stop Center basi na Watanzania wa kawaida wanapotaka kuanzisha biashara zao mazingira yawe rahisi mtu akienda sehemu moja aweze kupata vitu vyote kwa wakati na aweze kufanya biashara zake ili aweze kupata kitu ambacho kitasaidia Taifa na yeye mwenyewe na familia yake kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia suala zima la dhamana lakini pia na mlundikano wa mahabusu katika magereza yetu. Tumekuwa na mlundikano wa mahabusu wengi kwenye magereza zetu bila sababu za msingi. Police bail imekuwa ni shida katika nchi hii na kumekuwa kuna mchezo watu hawapewi dhamana kwa makusudi tu wakisingizia kwamba haya ni maagizo kutoka juu lakini wakati mwingine hakuna maagizo yoyote kutoka juu, huko juu ni wapi, ni mbinguni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, urasimu tu unafanyika huku chini mtu anaamua kusema kwamba ni maagizo kutoka juu. Mimi siamini kama kuna sehemu yoyote ambayo ni juu kuna watu wapo kwa ajili ya kuwakandamiza watu wengine. Nashauri Serikali iweze kuingilia kati ili haki za dhamana ziweze kupatikana na mahabusu waweze kupungua katika magereza zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza kushangaa mtu kama Kiongozi wa Upinzani Bungeni ni Mbunge ana dhamana ya wananchi, ana familia, ana mali, amewekeza katika nchi hii, unamnyima dhamana mtu huyu akikimbia atakwenda wapi? Kwa hiyo, tuwawezeshe watu wetu basi ili Watanzania angalau na wenyewe wawe miongoni mwa watu wanaoishi katika nchi za watu wenye furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu Wakuu wetu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, hii amri ya kuwafunga watu saa 24 mpaka 48 ni mbaya na inaingilia mamlaka ya vyombo vingine ambavyo vimewekwa kwa mujibu wa Katiba. Unaweza kukuta baadhi ya maeneo Daktari amefanya tu jambo la kawaida ambalo lingeweza kuzungumzwa ama hatua zikachukuliwa kwa mujibu wa sheria lakini unakuta kosa limefanyika na Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anatoa amri ya kumfunga Daktari ndani saa 48 lakini kumbe kule theater kulikuwa na wagonjwa hata 5, 6, 7, 8 ambao wanatakiwa wafanyiwe upasuaji. Kwa hiyo, unakuta ni administrative decision ndogo imefanyika lakini ukienda kuangalia huko ndani zaidi inaathiri watu wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika hapa alisema, Serikali haiwezi kuwa kama nyumba ya kambale kila mtu awe na sharubu, kwamba kila mtu awe na haki ya kamata, funga, fanya hivi fanya hivi. Kama tumepeana maeneo ya kusimamia, wewe simamia haki, simamia kufungwa, simamia ulinzi, simamia hiki; basi kila mtu afanye kazi ambayo inamhusu. Kwa kweli hili suala la kuwapa mamlaka wenzetu kufunga watu saa 24 - 48, nafikiri siyo sahihi na ikiwezekana Serikali iweze kuleta sheria hapa tufanye amendment ili kuondoa hiki kipengele kwa sababu wananchi wamekuwa wakikilamikia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni posho za Madiwani. Halmashauri yangu ya Buhigwe wamekuwa wakilalamika takribani zaidi ya mwaka hawalipwi posho zao. Sisi hapa ni Wabunge hata tukifanya semina tu mtu akakosa kulipwa nafsi inahaha kama vile sijui amekosa kitu gani katika ulimwengu. Sasa tuwaangalie wenzetu hawa ambao mtu anafanya kazi miezi sita, mwaka mzima, ni Diwani na hawana shughuli za maana za kufanya huko lakini wanakosa hela ndogo ambayo ingewasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sishangai hii hama hama ya watu kutoka chama kimoja kwenda chama kingine ni kwa sababu ya ukata. Hakuna shujaa wa njaa, mtu yeyote akipata njaa ikamzidia lazima atasalimu amri. Kwa hiyo, unaweza kukuta kuna wimbi la watu kuhama kumbe njaa na yenyewe imekuwa ni sababu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iweze kuwasaidia basi Madiwani wetu ambao sehemu mbalimbali nchini wanadai waweze kupatiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara, muda wake ulikuwa umeisha tayari, utapata fursa ya kujibu. (Makofi/ Kicheko)

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sabreena, muda wako ulikuwa umekwisha, kengele ilishagonga, kwa hiyo, umeshamaliza muda wako. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia muswada huu ambao toka nchi imepata uhuru ulikuwa haujaletwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa Watanzania na wapenda mabadiliko kwa ujumla. Ukiangalia muswada huu una lengo zuri, lakini una matatizo makubwa kwenye uteuzi wa Mthamini Mkuu wa kufanya uthamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia hapa tumesema miaka yote kwamba, Mheshimiwa Rais amekuwa akilundikiwa vyeo kila mara, lakini katika Muswada huu bado tunasema kwamba, mthamnini huyu uteuzi wake utafanyika na mamlaka ile ile, hapa kuna tatizo. Mthamini Mkuu ni lazima angepatikana kwa sifa, watu mbalimbali waliopo Serikalini na walioko nje ya Serikali wapeleke sifa zao ili ziweze kuangaliwa, wachujwe, wafanyiwe interview na hivyo apatikane Mthamini Mkuu ambaye atakuwa na tija na hatakuwa na upendeleo kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi! Mthamini Mkuu anapochaguliwa na mamlaka ambayo iko Serikalini, kesho anaambiwa akafanye uthamini katika mali za Serikali, lazima huyu mtu atakuwa biased, lakini kama atateuliwa na mamlaka nyingine tofauti na Serikali ileile ambayo anaenda kuifanyia kazi, ataweza kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na hivyo hatakuwa na conflict of interest.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia suala zima la Muswada huu, ukija kwenye majukumu ya Mthamini Mkuu wa Serikali, tumeona hapa kifungu cha 6(1)(a), atakuwa na kazi ya kuishauri Serikali kwenye masuala yanayohusu shughuli za uthamini ikiwemo uuzwaji wa mali za Serikali na ununuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kupendekeza kwa kuwa, kumekuwa na tabia ya wanasiasa akiwemo Mheshimiwa Rais, Mawaziri na viongozi wengine Serikalini kwenda katika Halmashauri mbalimbali nchini na kuwahamisha wananchi wa maeneo hayo kwa sababu za kisiasa bila kupata ripoti ya tathmini ya awali kwamba nani atalipa gharama za fidia ya wananchi hao, ningependa muswada huu uwaonye na uwakanye wanasiasa wenye tabia hizo kwa sababu mmekuwa mnasababisha sintofahamu kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano namba moja; alikuja Mheshimiwa Rais wa Awamu iliyopita katika Manispaa ya Kigoma Ujiji akawazuwia wananchi wanaoishi katika maeneo ya mlima unao-face railway station kwamba wanatakiwa wahame kutokana na sababu za kijiografia. Ni zaidi ya miaka kumi mpaka leo hii anatafutwa mtu wa kulipa fidia hapatikani. Halmashauri wanaulizwa, wanasema fidia ile imekuwa ni kiwango kikubwa zaidi ya bilioni moja, hawana uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hamuoni kwamba tabia hizi za wanasiasa kwenda kutamka matamshi ambayo wanajua Serikali haiwezi kutekeleza ni kuwapa usumbufu wananchi wetu? Kwa hiyo, sheria hii i-declare kwamba wanasiasa na viongozi wengine wa Serikalini msiwe na mamlaka ya kwenda kuhamisha ama kusitisha shughuli za wananchi, shughuli za maendeleo pale ambapo Wathamini ambao mnawatungua sheria leo hii hawajafanya thamani halisi ya eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba vijana wetu ambao wana uwezo mzuri watashindwa kupata ajira kwa sababu tu watashindwa ku-meet hii condition ya umri. Hivyo basi, ili liendane sambamba na lile suala zima la miaka mitatu, tunasema kwamba tutakuwa na wasajili wa mpito na wasajili wa muda pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasajili hawa tunawaambia wawe na experience ya miaka mitatu, lakini tujaribu kuangalia taasisi nyingine, kwa sababu siyo kwamba Wathamini hawa ndio wawekewe miaka mitatu lakini tunao Wahandisi ambao wanawekewa experience ya one year, wakitoka hapo wanapewa certificate waananza ku-practice. Tunao wanasheria ambao wanapewa elimu ya mafunzo kwa kipindi cha miezi nane mpaka mwaka mmoja; wakimaliza hapo wanapewa muhuri wanakwenda kufanya kazi. Kwa nini kwa Wathamini mweke kikomo cha miaka mitatu? Hii siyo fair, tupunguze kikomo hiki tuweze kupata muda ambao ni wa mwaka mmoja wafanye mafunzo ya vitendo na hivyo wataweza kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napendekeza makampuni na biashara ziwe zinafanya uthamini kila mwaka kama zinavyofanya Halmashauri zetu na Manispaa zetu mbalimbali. Tumeona mwaka 2015 Manispaa ambazo hazikufanya uthamini wa mali zake walipatiwa hati chafu, basi ni vyema makampuni na mashirika na taasisi zilizo za Umma ziweze kuwa zinafanyiwa tathmini kila mwaka ili tuweze kupanua wigo wa mapato katika nchi yetu na kuhakikisha kwamba miradi inayopangwa na Serikali inafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika muswada huu sijaona mkazo ukitiliwa kwa wazawa. Tumeona kuna hawa Wathamini wa mpito na wa muda mfupi wakiwemo na wageni. Kwa nini tunakumbatia wageni kwa condition ambazo ni rahisi sana? Tunapoingiza watu wengi waweze kusajiliwa hapa nchini kupitia Bodi yetu ya Wathamini inamaanisha kwamba kuna ajira nyingine Wathamini wetu wa Serikali ama binafsi ambao ni wazawa watazikosa na nafasi hizi zitakwenda kwa wageni. Lazima tuweke utaratibu ambao utawabana wageni waweze kuachia nafasi hizi kwa wazawa na kazi hii iweze kufanyika kwa viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutengeneza soko la ajira, ni vyema basi mabenki yetu na taasisi za fedha ziwe na wathamini wenye sifa kwa ajili ya kuangalia thamani ya wakopaji na isiwe ni suala la short time pale ambapo mkopaji anaenda benki ndiyo mthamini anatafutwa kufanya thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema katika sheria hii basi tuweke kifungu ambacho kitasababisha taasisi zote za fedha, mabenki na mashirika mengine ya Kiserikali yawe na utaratibu wa kuwa na wathamini wao binafsi pale ambapo wateja mbalimbali watahitaji kwenda kukopa. Pia kuna Mashirika kama ya Bima, wenyewe wana loss assessors. Napendekeza kwamba hawa loss assessors wa Mashirika ya Bima basi nao wangekuwa wathamini ili pale inapotokea loss thamani halisi ya fidia ijulikane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia kwenye muswada huu ni kuhakikisha kwamba ili kufanya uthamini uliokuwa na tija hususan Serikalini, tumeona hapa awamu iliyopita ya Mheshimiwa Mzee Mkapa, nyumba za Serikali ziliuzwa kwa bei ya chini sana na Taifa likapata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti kuna nyumba ambazo ziliuzwa mpaka shilingi milioni mbili, mpaka shilingi milioni 10; lakini ukiangalia hali halisi, nyumba hizi zilitakiwa ziuzwe kwa gharama ya juu zaidi. Je, ni vipi sasa sheria yetu hii tunayoitunga leo itawadhibiti watu ambao wataliingizia Taifa hili hasara kama iliyotokea miaka michache huko nyuma na kufanya wafanyakazi wetu wa mashirika mbalimbali na wafanyakazi wetu wa Serikalini kukaa mbali na miji kwa sababu tu nyumba za Serikali ziliuzwa tena kwa bei ya kutupa ama bei ya bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema basi sheria hii iweke msisitizo na iweke mkazo wa kuhakikisha ni jinsi gani basi Wathamini wa Serikali watatenda kazi kutokana na hali halisi ya soko na siyo kulitilia Taifa hasara kama ilivyokuwa ikifanyika siku za nyuma.
Pia napenda niseme kwamba lazima tuwe na appellate jurisdiction. Mthamini Mkuu wa Serikali amefanya uthamini, labda mtu aliyefanyiwa uthamini, aidha, wananchi ama shirika ama taasisi yoyote haikuridhika na uthamini uliofanywa na Mthamini Mkuu wa Serikali, taasisi hiyo au mtu huyo ama wananchi hao wanakwenda ku-appeal wapi juu ya maamuzi yaliyofanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumwambia Mheshimiwa Waziri hapa mwaka 2015 katika uchangiaji wangu, nilimwambia kwamba kuna maeneo ambayo watu walifanyiwa uthamini. Mtu alihitaji kulipwa shilingi milioni 20, 30 mpaka 40 lakini alilipwa shilingi milioni mbili, tatu, nne, mpaka tano na kuna watu ambao walitumia fursa hiyo kuwahonga Wathamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ambaye alitakiwa alipwe fidia ya shilingi milioni 10 aliweza kulipwa mpaka shilingi milioni 60. Je, ni hatua gani za makusudi mnazoziweka kuhakikisha kwamba udanganyifu katika uthamini mnaudhibiti hivyo fidia ya haki stahiki iweze kulipwa kwa wananchi wetu na isiwe longolongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtu ambaye atakayesababisha mtu kupata fidia chini ya kiwango hatua kali ziweze kuchukuliwa chini ya sheria hii, aidha, iwe kufungwa miaka 10 mpaka miaka 20 kwa sababu watu hawa wanaliletea Taifa hasara na wanawatia umaskini Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 6) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata bahati ya kuchangia Muswada huu ambao umeletwa kwa Hati ya Dharura lakini pia tungependa kuikumbusha Serikali kwamba Miswada hii inayokuja kwa Hati ya Dharura mara nyingi tunakosa maoni mengi ya wadau. Kwa hiyo, wajitahidi Miswada iwe inakuja kwa njia ya kawaida kuliko Hati ya Dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi napenda nikushukuru wewe mwenyewe kwa kuleta Muswada huu kwenye Kamati yetu na hivyo kama Kamati kupata experience ya kupitia Miswada ya mabadiliko mbalimbali ya sheria za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nichangie kwenye Ibara ya 6 ya Muswada ambayo inafanya marekebisho na kuongeza kifungu kipya cha 42A(1)(2)(3) na (4). Kwenye mabadiliko haya ya sheria, tunaambiwa kwamba Mkurugenzi Mkuu atakuwa na mamlaka ambayo amepewa ya kufifilisha makosa lakini tunaona kwamba ni vyema basi mamlaka hayo asingeachiwa yeye peke yake, angeweza kufanya pamoja na Bodi ya EWURA ili kupanua wigo na kuondoa autonomy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine ni kwamba pale ambapo kosa litakuwa limefifilishwa na baadaye yule mtu hajakubaliana na suala lile akaamua kwenda mahakamani, hapa tunaona kabisa kwamba kutakuwa kuna offence moja ambayo inakuwa charged twice. Kwa hiyo, ni vyema basi mtu angeweza kuhukumiwa kwa mara moja kuliko kuwa na repetition ya kesi katika mahakama zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala la tatu pia ni pale ambapo mtu aliyefifilishiwa kosa atashindwa kulipa lile deni kwa wakati. Mapendekezo yalitoka kwamba kutakuwa kuna interest. Naona hapa kuna changamoto kwa sababu kuna mwingine anashindwa kulipa labda kwa sababu tu alikuwa ni mgonjwa kwa maana alikuwa na matatizo ya kiafya ambayo yamepelekea mpaka akashindwa kuilipa hiyo fedha kwa wakati. Kwa hiyo, tunapomwambia kwamba atachajiwa na interest, inamaanisha kwamba hapo hatujaangalia ule utu na uhalisia wa ubinadamu kwa sababu kila mtu ana sababu zake, kuna mwingine ni mkaidi tu ameshindwa kulipa lakini kuna mwingine amepata matatizo.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, hapa busara itumike kuhakikisha kwamba hiki kipengele cha kuongeza riba tukiondoe, hata kama kweli Serikali inataka mapato, lakini kiwe na sababu maalumu na kesi maalumu, kesi na kesi, siyo kwamba tu tuwachaji kwamba mtu aweke riba hata kwa mtu ambaye alikuwa na matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ambayo napenda kuchangia ni Sheria za Vivuko. Ibara ya 18 ya Muswada, kifungu cha 12(2) kinasema: “A person shall not carry any activities within the prescribed distance of public ferry which are likely to interfere with the ferry services operations or pollute public ferry environment”. Kifungu cha 12(3), kinasema: “Any person who contravenes the provision of this section commits an offence and upon conviction shall be liable to a fine not less than fifty thousand shillings but not exceeding five hundred thousand shilling shillings”.

Mheshimiwa Spika, pamoja na sheria kuwa na nia njema lakini bado tunaona kabisa ile kusema two miles kutoka kwenye public ferry yoyote kulia na kushoto mtu asifanye shughuli zozote, basi ni vyema Serikali ingeweza kuelezea kinagaubaga kwamba ni shughuli gani hizo ambazo zinazuiliwa kufanyika kwenye eneo husika. Kwa mfano, mtu anaweza kufanya shuguli ambazo zinazuiliwa kwenye eneo husika labda anafanya uvuvi wa kutumia mabomu lakini kuna watu wengine siku hizi tumeona hata wasanii wetu wanakwenda ku-shoot videos na vitu vingine kutokana na mambo ya sanaa kwenye maeneo kama hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaposema any activities maana yake ni kwamba kuna mwingine anaweza akafanya tu activities kwa nia njema lakini akajikuta ameingia kwenye huu mkumbo wa sheria. Ni vema Serikali ingeweza kusema ni shughuli gani ambazo zita-interfere hii public ferry na kusababisha madhara ndiyo hao waweze kuhusika na kifungu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Ibara ya 23 ya Muswada imeongeza baada ya section 9, section mpya ambayo inaelezea power of inspection, seizure and forfeiture. Hii ipo kwenye hizi legal gaming activities. Pia imewekwa kipengele ambacho Bodi itakuwa na mamlaka ya ku-destroy hizo gaming materials.

Mheshimiwa Spika, hapa mapendekezo yangu ambayo nayaona, ni vyema basi wangeweza ku-seizure, forfeiture na inspection na auditing lakini wasi-destroy kwa sababu unapo-destroy pale ambapo huu jamaa ataweza kwenda mahakamani na kuonekana kwamba hayo material yake hayakuwa illegal devices, itakuwa tena ni hasara kwake, kwa sababu tayari wameshaharibu mali yake. Kwa hiyo, kipengele hiki tungeweza kukitoa kwa sababu ni kibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuiomba Serikali iweze kuweka tahadhari. Pamoja na ku-promote hii michezo ya gaming na sport betting kwenye taifa lakini bado kuna vitu ambavyo vinaonekana moja kwa moja vinaathiri shughuli za wananchi na uchumi kwa taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kumekuwa kuna kundi kubwa la vijana na hata watoto, wanafunzi wa vyuo na sekondari, wamejiingiza kwenye michezo hii ya kubahatisha na sport betting wakiamini kwamba kuna fedha nyingi sana ambazo zinapatikana huko na ni kweli ikitokea mtu ameshinda anapata fedha nzuri. Hata hivyo, tuangalie fedha anayoipata mtu mmojammoja na hali ya vijana na nguvukazi ya vijana kila siku kupotea ni fedha nyingi sana. Pamoja na ku-promote michezo hii lakini pia Serikali iangalie ni kwa namna gani nyanja nyingine za kiuchumi zinaweza zikaathirika kutokana na michezo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna watu ambao wana uwezo mzuri wa kulima, kufanya kazi za mechanical, za magari, za kupaka rangi na kadhalika lakini mtu anaamua kuacha kazi zote hizo na kwenda kufanya sport betting kwa kutegemea kwamba iko siku ambayo atapata boom na atapata fedha ambayo itamkidhi mahitaji yake. Pia kwa wanafunzi, wamekuwa wakila ada wakienda kwenye michezo hii ya kubahatisha wakiamini kwamba watapata fedha nyingi zaidi watajikimu lakini pia wataweza kulipa na ada kutahamaki siku ya siku wanakuwa wamekosa vyote, amekosa ada lakini pia fedha za kijikimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hata ndoa za watu zimekuwa hatarini kwa sababu michezo hii haina muda maalumu ambao inachezwa. Kuna wanaocheza usiku, mchana, kina mama wengi wanakuwa hawaoni familia zao. Pia hata familia zimekuwa zikiathirika kwa sababu wababa wengi wamekuwa ni rahisi kuchukua fedha kuipeleka kwenye sport betting kuliko kuipeleka nyumbani familia iweze kula. Kwa hiyo, tuangalie, kama kweli Serikali ina nia ya kukusanya kodi kwenye eneo hili husika pia iangalie sekta nyingine za kijamii na za kiuchumi ni jinsi gani zinaathirika kutokana na michezo hii ya kubahatisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria nyingine ambayo napenda kuchangia ni mabadiliko ambayo yanafanywa kwenye Sheria ya Tafsiri ya Sheria, yaani Amendment of the Interpretation of Laws Act. Kifungu cha 38 cha Ibara ya Muswada huu kinapendekeza section mpya ya 54(a)(b)(2), ambayo inasema: “Where any written laws establishes a board and the board dully constituted, it shall lawfully for any prescribed operations requiring the decisions of the board to be performed by the Permanent Secretary of the Ministry responsible for the board until such time the board is dully constituted.”

Mheshimiwa Spika, kipengele hiki naona na chenyewe kina shida kwa upande mmoja ama mwingine kwa sababu Bodi imewekwa kwenye taasisi ama idara za Serikali kwa sababu tu ya ile check and balance kwamba hawa wanatenda na hawa wengine wanakuwa na maamuzi na ile kuondoa autonomy kwenye Wizara ama taasisi husika. Sasa tunaposema kwamba majukumu ambayo yatakuwa performed na Bodi pale ambapo Bodi haipo ama imevunjwa afanye Katibu Mkuu wa Wizara kwa niaba ya Bodi, naamini kabisa hii itaenda kutofautiana hata na sheria nyingine za nchi. Kwa sababu inaweza ikatokea Katibu Mkuu ama Waziri ana personal interest kwenye suala ambalo linakwenda kuamuliwa, kwa hiyo, tunaposema tulitoe kwenye Bodi tuliweke kwa mtu mmoja itakuwa ni shida. Kwa hiyo, kipengele hiki nacho kinaweza kikaathiri taasisi za kiserikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, lakini pia hata kama kuna ulazima Bodi imevunjwa na kuna maamuzi ya msingi yanataka kufanyika, basi itumike budget authority ambayo itakuwa na Katibu Mkuu wa Wizara lakini pia na Wakuu wa Idara, kwa umoja wao pamoja waweze kuamua hilo jambo kuliko kumuacha mtu mmoja ndiyo aamue kwa majukumu ya Bodi. Hii itakuwa inaharibu dhana nzima ya good governance. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ambacho napenda kuchangia ni Ibara ya 99 ya Muswada ambayo inatoa exemption ya value added tax kwa materials na mambo mengine yote ambayo yatazihusu government entities. Napenda kuiomba Serikali ingebadilisha msimamo na kuzitambua private sectors lakini pia hata Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni Mbunge mwenzetu, tumekuwa tukiona majimboni kuna Wabunge ambao wanaomba misaada kwa ajili tu ya kusaidia jamii husika, labda jamii imekutwa na mafuriko, ama jamii inaathirika, kwa mfano, sisi kina mama, vijana wengi wa kike wamekuwa hawana pedi za kuwasaidia. Kwa hiyo, kama tutawawekea exemption ya value added tax, hata kwa sekta binafsi ili mradi tu ni kwa public interest basi na wenyewe tuweze kuwa-include kwenye kipengele hiki badala ya kuacha iwe ni idara za Serikali peke yake. (Makofi)

Mweshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna mabadiliko ya kuivunja Social Security Regulatory Authority na kuwa na Social Security Act. Hiyo pia imeelezea majukumu mbalimbali ambayo yalikuwa yakifanywa na mamlaka hayo ambayo yanaenda kufutwa kwenye sheria hii na kuhahamishiwa kwenye Wizara mbalimbali lakini bado yakiwa yamebakia
kwenye Social Security Act. Hii italeta mkanganyiko kwenye utekelezaji wa majukumu kwa sababu tunaamini Wizara husika zimekuwa zikifanya kazi kutokana na instruments ambazo zipo kwenye Wiraza zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unapomwambia Waziri afanye kazi ambayo ipo kwenye chombo kingine na haipo kwenye instrument yake, ataitekeleza kwa bajeti ipi? Kwa hiyo, ni vyema tuliangalie pia suala hili ili majukumu ambayo yalikuwepo kwenye Social Security Regulatory Authority yaweze kupelekwa kwenye Wizara husika, kwa maana ya kisheria ili kusiwe kuna mkanganyiko katika kutekeleza kazi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi. (Makofi)