Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rose Kamili Sukum (12 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Naomba na mimi niwe mmojawapo wa kujadili hotuba na mpango wa bajeti wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Tawala za Mikoa na Utawala Bora, kinachonisikitisha ni kwamba kabla sijajadili kwanza habari ya bajeti, suala la utawala bora haupo kabisa kwa TAMISEMI. Upo kwa maandishi tu kusema kwamba wanaridhika na kuhakikisha kwamba kwa wakati muafaka wananchi wanapata taarifa zao kwa ubora zaidi na pia kusimamia vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, simlaumu sana Waziri wa TAMISEMI, bali namwambia kwamba watendaji wako au Maafisa Masuuli katika Halmashauri mbalimbali hawako vizuri. Wao hawatekelezi ipasavyo suala la utawala bora. Wananchi katika Halmashauri mbalimbali hawana taarifa kabisa hata ya miradi yao ya maendeleo; hawana taarifa ya fedha ambazo zinafikishwa huko, je, utawala bora hapo uko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pia kwenye suala la utawala bora inatugusa sisi Wabunge wote wa Viti Maalum. Ninashindwa kuelewa huo waraka uliotolewa na Waziri wa wakati huo ambao siujui kwamba Wabunge wa Viti Maalum hawaruhusiwi kuingia kwenye Kamati ya Fedha ndani ya Halmashauri zao ambazo wanahudhuria. Hii inawagusa Wabunge wote, sio mimi peke yangu. Ni kwa nini hatuhudhurii hizo Kamati za Fedha? Naomba kutambua hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kairuki uko hapo, wewe ni mwanamke na ni Viti Maalum, umeteuliwa kuwa Waziri, kwanini sisi kama Wabunge hatuhudhurii kwenye Kamati za Fedha ambazo ziko kwenye Halmashauri zetu? Napenda kujua kwanini msibadilishe utaratibu huo ambao haufuati utawala bora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesababisha katika Halmashauri nyingi, saa nyingine Waheshimiwa Wabunge hawaingii. Mbunge wa Viti Maalum angekuwepo maeneo hayo, ni wazi kabisa angekuwa mdhibiti wa fedha na mali ya Halmashauri yetu husika au mali ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la utawala bora pia naomba sana TAMISEMI kubadilisha taratibu kuhusu Wenyeviti wa Vijiji na Serikali yao kuweza kupewa posho au angalau hata msharaha kidogo ili waweze kufanya kazi vizuri kusimamia miradi ya maendeleo kwenye vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye suala la Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhusu kuomba tuidhinishe makadirio ya shilingi trilioni 6.023 kwa ajili ya mpango wa maendeleo na makadirio ya fedha kwa mwaka huu wa 2016/2017. Mishahara tu pamoja na matumizi mengineyo imekwenda kiasi cha shilingi trilioni 4.4 lakini fedha za maendeleo ni shilingi trilioni 1.6 tu! Ukigawanya hizi fedha za maendeleo kwa Mikoa 26, kwa Wilaya 139, kwa Tarafa 562, kwa Kata 3,963, kwa Mitaa 4,037 kwa vijiji 12,545 na Vitongoji 64,677 maana yake wastani wake kwa ujumla, kila timu itapata shilingi 18,663,609.95 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu mwangalie kwenye suala la maendeleo kama hizi fedha zinakidhi haja. Kwenye taarifa yao ya fedha wameonesha kwamba wamepewa mikoa kadhaa, wamepewa vijiji kadhaa au wamepewa Wilaya kadhaa. Ina maana fedha za maendeleo hazitoshi hata kidogo! Mimi nadhani ifikie mahali sasa kwamba sisi kama Wabunge waangalie TAMISEMI waweze kupata fedha za kutosha. Ili waweze kukidhi haja ya wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali kidogo kuhakikisha kwamba hebu hata hizi fedha za maendeleo zimekwendaje? Nikachambua programu za maendeleo kadhaa. Nikaenda kwenye programu ya maendeleo ya barabara vijijini, kasma ya 4,170. Unakuta kwamba wameomba fedha shilingi bilioni 224.7, hizi hela ukiangalia kazi yake ni kuratibu na kutekeleza mpango, kufungua barabara za vijijini ambazo hazipitiki ambayo hela yake sasa ukiangalia kwenye mchanguo huoni ni vijiji gani ambavyo wanastahili kufungua hizo barabara na ni hela kiasi gani haikuoneshwa?
Pia kwenye matengenezo ya barabara maeneo ambayo ni korofi kwenye barabara za Halmashuri, haioneshi ni barabara za Halmashauri gani, ni barabara ya wapi ni ya kijiji gani, haioneshwi kabisa. Sasa sisi kama Wabunge tunaidhinisha nini? Tunatakiwa tujue, tuidhinishe kitu ambacho tunajua, kama inaenda kwenye Wilaya ile au kama inaenda kwenye Halmashauri fulani, basi ifahamike kwamba ni Halmashauri kadhaa safari hii wamepata, labda ninyi mkapate mwaka 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuangalie kwa undani. Pia nilienda moja kwa moja kwenye programu nyingine ambayo ni kasma ya 3,280, programu ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiit, fedha zimeombwa kuidhinishwa, ni shilingi milioni 412 tu! Hatuna maji, hatuna fedha za kutosha kwenye Halmashauri zetu, hatuna visima. Leo ni shilingi milioni 412, ni kufanya ufuatiliaji wa miradi, tathmini, kuratibu shughuli na kuratibu vikao vya kitaalam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunahitaji vikao vya kitaalam au tunataka visima vya maji? Sasa tunapitisha nini? Naomba mkarekebishe hapa! Tena fedha zenyewe zinatoka nje, fedha za ndani hazipo. Tunafanyaje? Miradi itaendeleaje? Ina maana kwamba Watanzania bado wataendelea kukosa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Hanang. Wana-Hanang tuna upungufu mkubwa sana wa maji. Hata fedha ulizozipeleka Mheshimiwa Waziri safari iliyopita, hakuna maji. Unaenda Gehandu, hakuna maji; sijui Galangala, hakuna maji na fedha nyingi zimeenda; unaenda Garoji, hakuna maji. Hata Mjini Katesh yale maji ambayo yametengenezwa na Mfuko wa Rais nayo hayapo saa hizi. Visima vipo tu kama sanamu. Kwa hiyo, watu wanaenda kuabudu sanamu, hakuna maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri lazima hilo mliangalie pia kwa upande wa TAMISEMI, mtafanya nini kuhusu masuala ya maji na fedha hizi tunazoziidhinisha sasa hivi, shilingi milioni 412, kweli ni za kufuatilia au tunahitaji visima vya kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitishwa na suala la elimu. Ukiangalia, tunasema kwamba tunapata elimu bure, kupunguza tu ile ada, lakini michango ni mikubwa sana. Nafikiri ifikie mahali sasa TAMISEMI tuangalie suala la michango ile ya ziada ambayo itawasaidia wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge amesema watu walikuwa wanakwenda na maakuli, chakula cha nyumbani. Kipindi hiki magonjwa yako mengi, mwanafunzi hawezi kwenda na chakula kutoka nyumbani kwao. Kitakuwepo kipindupindu, sijui na ugonjwa gani sijui na kitu gani; inatakiwa wanafunzi wale mahali pamoja. Mimi nadhani sasa Serikali ifikie mahali kwamba muangalie suala la chakula shuleni, itolewe na Serikali. Hiyo ndiyo kupunguza adha kwa wazazi kwa ajili ya wanafunzi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kikubwa zaidi ni hela za MMES. Huu mpango wa hela za MMES na MMEM, tunaomba mwangalie utaratibu wa hela za MMEM na MMES. Siyo kupitia tena kwa Wakurugenzi, halafu eti Mtendaji wa Kata ndio anasimamia hizo hela. Ziende moja kwa moja kwenye shule. Sasa zinavyoacha kwenda kwenye shule, wengine wanaanza kumega kidogo kidogo ambapo ukifika, hazipo shuleni tena kwa walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la afya. Hospitali zetu hazina dawa, uchakachuaji umekuwa mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutumbua majipu, lakini nashindwa kuelewa, mnasema kwamba tusimtaje Mheshimiwa Rais hapa, huyu Mheshimiwa Rais anachelewa kutumbua Wakurugenzi kwenye Halmashauri zetu na wengine wanaokula fedha. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya mipaka na shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi za wanyamapori, sababu za mifugo kuingia kwenye hifadhi husababishwa na viongozi na watumishi wa maliasili kwa kuwanyang‟anya maeneo yao kuwa maeneo ya hifadhi bila kuwafidia maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzisha mapori tengefu, mapori ya akiba na ushoroba maeneo hayo yote ni vijiji vilivyopimwa kwa ajili ya wananchi wanaopakana na hifadhi. Bila kuwa na utaratibu unaoeleweka kwa Wizara ya Ardhi, Maliasili, Kilimo na Mifugo, TAMISEMI na Wizara ya Maji kamwe hamtapata suluhisho la wafugaji na wakulima wanaozunguka hifadhi. Nashauri kuwa na kikao cha pamoja kutafuta suluhisho la kupatikana kwa ardhi ni kuwa na mpango wa kupatikana maeneo ya wafugaji na wakulima siyo kazi ya kuwakamata na kuwaua wao na mifugo yao. Tupeni mpango wa kumaliza tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sheria Namba Tano ya mwaka 2009 (Sura 283), Sheria hii inazungumzia upande mmoja wa hifadhi. Je, maeneo mliyoongeza kwa kuwaghilibu viongozi wa vijiji kwa kutumia viongozi wa Wilaya na Mkoa, inawagusa wapi?
Sheria hii inawanyanyasa wafugaji kwa kuwanufaisha viongozi wa Wilaya na Kamati zao za usalama na mikoa kwa kulazimisha kutolewa rushwa au kukandamiza wafugaji kulipa faini. Hii mifano imefanyika Tarangire katika vijiji vya Ayamango, Galapo, Mkungunero, Sangasanga, Lulenge, Pori la Wamimbiki, Utengule huko Kilombero North Safari na kadhalika. Hii sheria ifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha za kuudhi, kauli aliyoitoa Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Jumanne Maghembe katika mahojiano yaliyofanyika katika vipindi vya ITV dakika 45 ni lugha ya maudhi na dharau kwa wafugaji.
(a) Mapato yatolewayo na Maliasili na Utalii ni asilimia 22.5 huwezi kufananisha na mifugo ambayo hutoa mapato ya kiasi cha asilimia 4.5 akifananisha kuwa ukiwa na shilingi nne na ukiwa na shilingi 22 utachukua shilingi ngapi? Hiyo ni dharau, je, ng‟ombe wanaochinjwa Tanzania haijachangia kutokuagiza nyama kutoka nje? Hiyo siyo dola?
(b) Wafugaji hukaa nyuma ya mikia ya ng‟ombe zao tu, je Waziri alitakaje? Kuna style nyingine za kufuga ng‟ombe?
(c) Ng‟ombe wote walioko mipakani mwa hifadhi wana magonjwa kama kimeta, homa ya mapafu na kadhalika, hivyo nyama zao hazifai kwa kuliwa. Je, Waziri anaweza kutoa ushahidi wa magonjwa hayo kwa mifugo yote inayochinjwa?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia Hotuba ya Waziri wa Maji kwa Wizara yetu hii muhimu ambayo ni nyeti sana kwa viumbe vyote ambavyo vimeumbwa duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kusema kwamba, maji ni uhai. Maji ni uhai kwa viumbe vyote vilivyoko hapa duniani. Maji ni uhai kwa maana ya kwamba, bila maji vifo vinaweza kutokea. Ukiugua kitu cha kwanza unapewa maji kwa drip, hayo ni maji. Bila maji mtakuwa na njaa kali sana nchini, ndiyo maana ya kusema ni uhai. Pia bila maji hutakuwa na viwanda vyovyote wala hutakuwa na maendeleo yoyote ya kutengeneza barabara wala hutakuwa na maendeleo ya aina yoyote endapo maji hayatatiliwa mkazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wetu Engineer anajua na nimeshamsumbua mara nyingi safari iliyopita kuhusu suala la maji, lakini kwa kweli, walikuwa wanajaribu kujitahidi, lakini nahisi kwamba, Waziri wewe kama Waziri hutaweza kuleta hizi hela za bajeti! Bajeti uliyotenga bilioni 915 haina kazi yoyote kwa sababu, hata bajeti iliyopita, safari iliyopita haikufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sasa ifike mahali Wizara ya Maji, Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, TAMISEMI kwa sababu nao wanapitishiwa fedha, nendeni kwa Rais mkaombe hela. Hatuna haja ya sisi kuzungumza habari ya bilioni mia tisa hapa kwa sababu, haitoshelezi! Sasa kama haitoshelezi tunaongelea nini? Nadhani tuache, nendeni kwanza mkafanye hiyo kazi, halafu mrejeshe hapa kwamba, hela tumeongezewa! Uchukuzi wanapewa trilioni mbili! Mahali ambako uhai tunautegemea, bilioni 900! Tunazungumza nini sasa hapo? Naona tunapoteza muda tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara haiwezi kutengenezwa bila maji, hakuna kiwanda kinatengenezwa hamna maji pale. Sasa kama barabara haiwezi kutengenezwa hawa wanapewa hela kubwa halafu maji wanapewa hela ndogo! Hii ni dharau kubwa kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kuhusu suala la uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini. Ukweli ni kwamba, wakala huyu atafanya kazi na wewe Wizara utakuwa na mahali pa kukamata; fedha zote zinazokwenda vijijini hutumika vibaya. Maafisa Masuuli wameona kwamba, fedha za maji sasa ndio duka lao! Ndiyo mahali pao pa kupata mitaji kwa sababu, kuna Wizara mbili! Wizara ya Maji inazungumza habari ya mradi wao kutoka Wizarani, TAMISEMI nayo ina mradi wa maji unakwenda pale kwenye Halmashauri D-by-D, lakini nao hawafuatilii. Kwa hiyo, imeonekana lile ndio duka lao ambalo wanafanya matumizi makubwa yasiyofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hivi kwa sababu, kwa Wilaya ya Hanang naomba kuzungumzia masuala ya Programu ya Usafi wa Maji na Mazingira. Mpaka sasa hivi ninapozungumza hapa zaidi ya 4,000,757,000/= zimekwenda pale, lakini ukiambiwa miradi ile ya vijiji 10, Mheshimiwa Waziri ambayo anasema ni asilimia 80 kwenye taarifa yao, ni vijiji saba tu ambavyo vimepata maji kati ya vijiji 96!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang ina vijiji 96, vijiji saba tu! Hiyo ni asilimia 70 kweli au mnawadanganya Watanzania kwa asilimia? Hakuna maji! Siyo kwamba, ile Wilaya haikuwa na Waziri, ilikuwa na Waziri! Mimi nina mashaka Mawaziri hamuwezi hilo! Twendeni kwa Rais atupe maji, ndiye anayeweza, hakuna mtu mwingine! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Kambi ya Upinzani kuhusu uanzishwaji wa Wakala kwa maana ya kwamba, fedha zetu zisimamiwe vizuri. Kwenye maandishi utaambiwa kwamba, wamechagua vijiji 15, lakini vijiji havina maji! Saa hizi ukiondoka Waziri nenda Hanang, utakuta hata pampu za maji hazipo hata hivyo vijiji saba! Mwananchi hana maji, pampu za maji mbovu! Ni hali mbaya kabisa. Kwa hiyo, ni lazima kuangalia ni jinsi gani tuweze kuokoa hela za Watanzania na hela zinazotokana na misaada mbalimbali kutoka nchi za wenzetu wanaotusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang, Ishponga ilipewa milioni 209 hawana maji ya kutosha! Ukiangalia value for money hakuna kilichofanyika! Waziri wa TAMISEMI msaidie Waziri wa Maji kwamba, hela kule zinaliwa bure. Garawja ilipewa bilioni moja na point moja ya kutengeneza mradi wa maji, hayo maji bado hayajakamilika mpaka leo! Kwenye vitabu vyao vimeonesha maji yamekamilika, kumbe bado, hela zote zimetumika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha nyingine Mogitu, mradi wa Kateshi na Mogitu ni mradi mmoja, lakini utakuta wanasema mradi wa Mogitu umetumia milioni 578,000/= halafu mradi wa Kateshi umetumia milioni 867; sasa mradi wa Kateshi na mradi wa Mogitu ni mmoja ambapo kuna hela za Rais pale pia, milioni 390! Huo mradi mpaka sasa hivi bado haujakamilika, watu wa Kateshi hawajapata haya maji ambayo yanatokea Mogitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaambiwa kupitisha kalavati tu, zimetumika milioni mia mbili sijui na kitu! Eti kuchimba barabara halafu kupitisha bomba chini, milioni mia mbili na kitu! Tunataka Mheshimiwa Waziri aende akahakikishe kwamba, hizi fedha pia, zinatumika vibaya ndiyo maana tunakosa maji; watu wa Hanang hawana maji, ni vijiji vichache tu vilivyopata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda, Basotu tunatumia maji ya ziwa, ni chanzo cha maji kizuri, lakini yale maji hayako salama. Hayako salama kwa sababu mashamba ya ngano yanayolimwa yanapigwa dawa ya kuua wadudu, maji yote yanaelekea kwenye hilo ziwa, wananchi wanatumia yale maji hayako kwa njia ya bomba. Ni Wizara ipi inayoweza kuwasaidia wale wananchi wa Basotu, Hanang waweze kupata maji safi na salama ambayo hawapati kansa kama inavyofanyika sasa hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la Hanang, suala la irrigation; scheme ya irrigation imepelekwa Hanang, iko kweli kwenye Kijiji cha Endagau, lakini fedha zake zote pia zimetumika! Milioni 410 zimetumika vibaya na tunahitaji irrigation kwa hali ya juu. Saa hizi ni kweli umetupitishia hela kuja kule, lakini nani msimamizi kama hakuna wakala? Ndiyo maana tunasema kuwe na wakala wa kusimamia miradi ya maji kwenye vijiji kwa sababu ya upotevu wa fedha nyingi sana za Serikali. Sasa sisi tutalia! Waziri analia! Kila mtu analia kwa ajili ya maji kumbe ni fedha zinatumika vibaya pia kwa asilimia100. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaomba hili aliangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la irrigation ukweli ni kwamba, fedha mlizotenga bilioni 35 ni ndogo sana. Mnategemea kutengeneza mradi wa irrigation wa hekta laki nne, hekta laki nne utazipataje kama hela ni hizi bilioni 35! Hazitatosha kwa ajili ya irrigation. Kwa hiyo, hatuna budi kuongeza kwa sababu, tuna mabonde mengi sana, ili kuondoa njaa nchi hii hatuna budi kutenga hela za kutosha kwa ajili ya irrigation ili kuondokana na njaa. Leo tunakosa sukari wakati kuna irrigation ya kutosha, tuna mabonde ya kutosha! Peleka hela ya kutosha wananchi walime miwa, ili waweze kutengeneza sukari yao, hakuna haja ya kuagiza nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabonde. Mabonde nchi hii yameelekezwa Kusini zaidi, lakini wamesahau pia Kaskazini zinahitajika sana fedha za kutosha. Tunaomba muelekeze kule pia, kwa ajili ya irrigation kuweza kupeleka hela za kutosha, sio lazima kupata hizi, naomba sana hili liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala hasa la upotevu wa fedha. Nimejaribu kwenda TAMISEMI mara nyingi, nimejaribu kwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri, lakini hakuna anayesaidia kuhusu upotevu wa hela za Hanang! Milioni 540 za maji mpaka sasa hivi hazionekani zimeelekea wapi! Atatusaidiaje Watanzania Wanahanang ili milioni 540 za maji zionekane zimeelekea wapi? Tunataka taarifa hizi anapo-wind up atwambie kwamba, tutapata wapi hizo hela zilizopotea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba sana kumwomba Mheshimiwa Waziri u…
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana nami kupata fursa hii ili niweze kuchangia taarifa ya Kamati kuhusu Hesabu Serikali za Mitaa pamoja na PAC. Kwanza kabisa niombe Wabunge wote tukubali kupokea maoni au mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ili kuweza kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya hii ya LAAC ina kazi ngumu sana. Wote tutambue kabisa kwamba Halmashauri zetu zote zinatakiwa zikaguliwe na Kamati ya LAAC. Kila Mbunge hapa ana Halmashauri yake, nadhani haya maoni yanamgusa kila mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumzia suala la ugumu na usugu wa matatizo ambayo yako kwenye Halmashauri na yote yanatokana na kwamba sasa hivi Serikali yetu ambayo haitaki kusikia imesema ina ufinyu wa bajeti. Kama kuna ufinyu wa bajeti, umebana hizo fedha ili uweze kufanya jambo, kama hawakaguliwi si ndiyo wizi unaongezeka? Kama unaongezeka, nani anaweza kuwabana kama Kamati ya LAAC au PAC haitapewa mafungu ya fedha ili kwenda kutembelea miradi yote ambayo inafanyiwa kazi na Halmashauri zetu au na Wizara mbalimbali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ucheleweshaji wa fedha katika Halmashauri zetu umesababisha baadhi ya miradi kutokamilika. Miradi hiyo haikamiliki kwa sababu fedha zinapochelewa kwa kuwa baadhi ya Maafisa Masuuli na Wakuu wa Idara waliopo kwa tamaa waliyonayo basi hutumia fedha zile halafu wanasubiri za mwaka unaofuata. Kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa ambalo lipo la Serikali kuchelewesha hizo fedha za maendeleo nao wanachangia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ifikie sasa mahali Serikali ikubali kwamba fedha zikitolewa zitolewe kwa wakati ili maendeleo ya watu yaweze kufanyika. Ndicho tulichokiona kwenye Kamati ya LAAC tulipokuwa tunaendelea kukagua kwamba ucheleweshaji ule unasababisha Maafisa Masuuli kula hizo fedha bila kutumia utaratibu unaofaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine maagizo kutoka ngazi ya juu yamesababisha ubadhirifu wa fedha au kutumia fedha ambazo haziko kwenye bajeti katika Halmashauri zetu. Utakuta Mkuu wa Mkoa anawaagiza wakatumie fedha kwenye mafungu ambayo yeye hausiki kupitisha hiyo bajeti, DC naye anaagiza, DAS anaagiza, RAS anaagiza na kuchukua fedha. Kwenye ukaguzi huo tumeona kwamba kuna RC alikuwa anaagiza fedha zitumike kwenye sehemu ambayo haipaswi kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huo ndiyo ubadhirifu mmojawapo ambao tumeugundua kwenye Kamati ya LAAC. Tunaomba haya maagizo yanayotoka juu basi wawe na mafungu yao ya fedha, mnataka kutengeneza madawati mtuambie fedha iko wapi ili wakatengeneze madawati. Siyo unaagiza watengeneze madawati halafu hakuna fedha kwenye bajeti, ni ngumu sana kufanya hiyo kazi kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, sisi Kamati ya LAAC mmepata taarifa kwamba tumekagua Halmashauri 66. Sababu ya kukagua Halmashauri 66 ni ukosefu wa fedha tumeshindwa kwenda kukagua hata miradi ya maendeleo. Kati ya Halmashauri 164, ni Halmashauri 66 tu ndiyo zimekaguliwa, je, ubadhirifu unaoendelea kufanyika kwenye zile Halmashauri zilizobaki ni kiasi gani? CAG pia amekosa hizo fedha, je, kama CAG hajaenda kukagua ile miradi ya maendeleo ubadhirifu unafanyika kwa kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke suala value money, wanasema fedha zimekwenda kuchimba kisima, visima ni hewa, zimeenda kujenga sekondari, sekondari ni hewa, zimeenda kutengeneza barabara, barabara ni hewa na hakuna anayekwenda kukagua. Waziri wa TAMISEMI unafahamu kabisa wewe peke yako hutoshi kwenda kukagua hizo Halmashauri zote, lazima tusaidiane. Leo mnabana hizo fedha, je, tunafanyaje sasa na fedha zimetumika vibaya na hakuna miradi ya maendeleo iliyofanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, udhaifu na udhibiti wa Mkaguzi wa Ndani. Mkaguzi wa Ndani yuko chini ya Internal Auditor General, lakini huyu Mkaguzi wa Ndani kwa masuala ya kiutawala yuko chini ya DED, hebu niambieni atawapeni taarifa iliyo sahihi kweli kama yuko chini ya DED? Matokeo yake yule Mkaguzi wa Ndani anashikwa anaambiwa ukitaka usafiri, ukitaka hela usitoe taarifa inabidi asizitoe. Je, tunafanya nini kuhusu huyu Mkaguzi wa Ndani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri katika Halmashauri zetu Mkaguzi wa Ndani asiwe chini ya Mkurugenzi au Afisa Masuuli kwa sababu taarifa hazitolewi mpaka wagombane, wakishagombana na Mkurugenzi ndiyo unapewa taarifa kwamba kuna fedha imeliwa au kuna kitu fulani kimefanyika. Nashauri kwamba Mkaguzi wa Ndani awe chini ya Internal Auditor General na taarifa zake ziende pale na utaratibu wa shughuli zake zote utoke kule au awe chini ya CAG kuliko kuwa chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulizingumzia, kazi ya ufuatiliaji na usimamizi ni ngumu sana na kubana matumizi pia inahitajika lakini Kamati zote kutotembelea miradi hatufanikiwa. Kamati ya PAC na LAAC kama hazitatembelea miradi hatutaweza kufanikiwa kwa jambo lolote. Tumeona wote tuliokuwepo kwenye hizo Kamati kwamba kama hatukwenda kutembelea tunaangalia taarifa ya kwenye makaratasi hatutafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Afisa Masuuli anaweza kuwa mjanja, suala la risiti zinaweza kuandikwa zikaletwa hapo na akawa na hati safi, lakini kumbe kule kwenye kazi hakuna kilichofanyika. Kwa hiyo, nadhani sasa suala la ufuatiliaji kama lipo tunatakiwa sisi kama Kamati ya LAAC, kama Kamati ya PAC au Wabunge wote kwa ujumla kutembelea miradi ili kuhakikisha kwamba miradi inafanywa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho kimeonekana zaidi ni kwamba wakati Bunge linaendelea na Halmashauri zinaendelea na vikao vyao. Hiyo imesababisha sehemu kubwa sana ya Wabunge kutokujua mapato na matumizi yanayofanyika kule. Hata Mfuko wa Jimbo imeonekana wazi kabisa Mbunge hajui fedha zake zimetumikaje na hata akiuliza anaambiwa hela zimeshatumika zimefanya kazi zingine. Kama Mfuko wa Jimbo unaweza kutumika, Wabunge mna kazi gani kama hamuwezi kudhibiti mapato na matumizi ya Halmashauri zetu au ya Serikali kwa ujumla? Kwa hiyo, tunatakiwa kupata hiyo fursa ili kuweza kufanya kazi ya usimamizi wa Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokigundua zaidi kwenye Halmashauri zetu pamoja na kwamba tuna manunuzi yasiyozingatia sheria lakini pia kuna watu ambao wanatumia nafasi zao kuingiza mikono yao pale. Mkuu wa Mkoa anakwambia umtumie mkandarasi huyu, mimi ndiyo nawaagiza na mkandarasi hajatimiza wajibu wake. Je, hamuoni kwamba tunatumia fedha za umma vibaya? Tunawalalamikia sana Maafisa Masuuli kutofanya kazi yao vizuri lakini sehemu kubwa ni maagizo yale yanayotoka kwa sababu ni mkubwa anamuagiza Mkurugenzi, haya yametokea maeneo mengi kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi suala la Wakurugenzi ambao hawaelewi utaratibu wa Halmashauri imekuwa ni tatizo kubwa. Uteuzi wa juzi tu umefanyika Julai lakini kilichotokea kwenye Halmashauri ya Hanang mfano kuna watumishi wamekula fedha shilingi bilioni 1.2 na uchunguzi umefanywa na Mkuu wa Mkoa na imebainika fedha hiyo kuliwa, lakini kwa kuwa Mkurugenzi haelewi, maskini ya Mungu ametoka TFDA hajui masuala ya Halmashauri akapewa ushauri na wale waliotumia ile fedha kwamba hawa watumishi waliokuwa hiyo fedha tunashauri warudi kazini wateremshwe vyeo siyo wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiona suala kama hilo ujue kwamba hawa Wakurugenzi wapya wanahitajika aidha wakapewe semina au waende shule ambayo itawasaidia kujua ni namna gani watakavyoweza kuendesha hizo Halmashauri. Kwa sababu kama unashauriwa na mtumishi wa chini yako uliyemkuta pale ambaye na yeye amehusika kwenye kutumia hizo fedha halafu na wewe unaishauri council kwamba hawa watumishi adhabu yao ni kuteremshwa cheo, wamekula shilingi bilioni 1.2. Hebu niambie kwa nini wale wa Kagera wameshtakiwa kwa Rais wakati yule wa Hanang aliyekula shilingi bilioni 1.2 anaambiwa aendelee na kazi? Kwa hiyo, kuna mambo ya kufanya ili kuweza kuisaidia Serikali hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Naomba pia iwe nafasi pekee ya kuwapa pole ndugu zangu wapendwa wa Arusha, Walimu na wazazi waliopotelewa na watoto wao. Mwenyezi Mungu awape faraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata hii fursa ya kuchangia bajeti ya Wizara hii ya maji ambayo naita kwamba iko ICU. Sababu ya kusema iko ICU, ukweli ni kwamba kama mwaka jana ilitolewa au iliidhinishwa bajeti ya bilioni 915.2 na haikutolewa yote na leo tena tunaidhinisha bajeti ya bilioni 632.6 ambayo hatuna uhakika wa kutolewa; na tena iko pungufu ya bilioni mia mbili themanini na moja ya bajeti iliyopita mwaka jana, maana yake Serikali yetu haifanyi kazi ya kukusanya mapato nchi hii.

Mhesimiwa Naibu Spika, sisi Watanzania hapa tuna vitongoji 64,677, hivi vitongoji vyote vinahitaji maji, lakini ukiangalia wanasema wametoa miradi 1,333 ndani ya vitongoji 64,677, ndiyo maana nimesema wako ICU.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji tukubaliane ni uhai na kwa kuwa maji ni uhai, ni uchumi, ni msingi wa amani na ni haki za binadamu, nadhani sasa ifike mahali tuangalie ni jinsi gani tukomboe nchi hii kwa ajili ya maji. Mbinu pekee ya kuikomboa ni kuhakikisha kwamba, hii bajeti inarudiwa upya, hii bajeti ikarekebishwe upya tuijadili ili Watanzania waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maana kwamba, Mheshimiwa Rais mwenyewe alitoa Kauli Mbiu kwa wanawake kwamba, nitawatua ndoo za maji vichwani. Sasa hapo ni kutua ndoo za maji au ni kuwawekea ndoo za maji? Labda hatujui Kiswahili! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo napenda tulijue vizuri kwamba, kama ni kutua hizo ndoo basi nendeni kwenye sera ya maji ya mwaka 2002, kuhusu suala la miradi ya maji vijijini, kila mwananchi aweze kupata maji isizidi mita
400. Je, mpaka sasa hivi mna mita mia ngapi ambazo zimewafikia hao akinamama, kama mnataka kuendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ya kuokoa hii Wizara, nawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja hasa sisi wanawake, ili tuwakomboe wanawake wenzetu vijijini; mimi nina uhakika asilimia 99 tumetoka vijijini ndipo tukaenda mjini. Sasa mjue kabisa kwamba, akinamama wanachota maji kwa umbali mrefu sana, sio chini ya kilometa 20 wengine, wengine kilometa tano na kadhalika wanaamka saa 9.00 kwenda kuchota maji. Namna pekee ya kuwasaidia ili waweze kuleta maendeleo ni sisi kuhakikisha kwamba, tunaliomba Bunge hili kwamba hizi fedha ziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ya kuongeza kwenye huo mfuko, tunaomba kuuliza ile tozo ya sh. 100/= tuliyoiomba kwa nini mliikataa? Kama mnaweza kufanya maendeleo au mnaweza kutoa zile fedha za maendeleo, ni kwa nini mlikataa ile tozo ya Sh. 00/= tusiitoze kwenye mafuta, badala yake mkakaa kimya? Mngetueleza tena kwamba haiwezekani kwa sababu bei ya mafuta inapanda. Bora tupande bodaboda kuliko kukosa maji. Kama tungekosa maji humu ndani nyie wanaume mngekuwa na vikwapa na sisi wanawake ni uvundo mtupu; sasa kwa nini tusiangalie suala la maji kwa wenzetu na tuwaokoe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ya kuboresha huo Mfuko wa Maji, basi tutafute namna nyingine ya Mfuko wa Barabara ichangie Mfuko wetu wa Maji sh. 100 ile ipatikane ili maji yapatikane vijijini. Mfuko wa Umeme upatikane, kwa sababu barabara huwezi kujenga bila maji. Kwa hiyo nao wachangie kwenye ule Mfuko wetu wa Maji ili tuweze kuboresha hiyo miradi ya maendeleo kwenye vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kujua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipatia fursa hii niweze kuchangia Wizara hii ya Kilimo ambayo ni muhimu kwa jamii nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana kuona kwamba Serikali haitambui umuhimu wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kinachonisikitisha zaidi ni kwamba mhimili huu una maisha ya Watanzania wote. Ukiangalia kwa ndani kabisa karibu 98% wanategemea chakula kwenye Wizara hii ya Kilimo na pia 80% wanategemea ajira na 95% raw material. Ina maana kwamba hii Wizara ndiyo Wizara mama kwa sababu wategemezi wake ni wengi mno, lakini bado inaonekana kwamba hii Wizara haifai kwa kupewa 3% ya miradi ya maendeleo. Sababu ni nini, nashindwa kuelewa.

Waziri hebu atuambie, wamepigwa sindano gani ya ganzi hampati hata kufumuka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kwenda Wizara ya Viwanda kama hukutumia Wizara ya Kilimo. Juzi Waziri wa Mambo ya Ndani amesema kiatu chake kinang’ara kwa ajili ya ngozi, kwa hiyo, wanategemea mifugo, mimi sijui kwa nini hatuoni hali halisi ya Wizara hii. Tumeona kabisa mawazo yaliyotolewa na Kamati, mawazo yaliyotolewa na Kambi ya Upinzani Bungeni, yanawaelekeza ni nini cha kufanya. Naomba sana muiangalie sana Wizara hii kwa sababu ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo linanitia wasiwasi nalo ni uwekezaji usio na tija. Sijui kama ametembelea maeneo yote ya uwekezaji, Serikali hii hii ya Awamu ya Tatu ilibinafsisha mashamba mengi sana, ikiwemo Wilaya ya Hanang mashamba ya NAFCO, naomba niyatolee mfano, yalibinafsishwa na Serikali hii lakini hakuna tija. Mashamba ya ngano, leo tunazungumza habari ya ngano inaagizwa nje, wakati kuna mashamba ya NAFCO yalikuwepo kule wamepewa wawekezaji. Matokeo yake mwekezaji huyo amepewa shamba la Gidagamowd amelima ekari 4,000 kati ya ekari 16,300. Shamba la Setchet amepewa ekari 16,330 amelima ekari 3,800. Shamba la Murujanda amepewa ekari 12,455 amelima ekari 6,000. Maana yake ekari zaidi ya 30,585 hazijalimwa, nayo ni mgogoro kwa sababu maeneo ambayo hayajalimwa wananchi wanaingia kulima, wengine wanaingia kufuga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza hawa wawekezaji ambao hawana tija kwa nini msiondoe yale mashamba kutoka kwenye mikono yao mkayarejesha kwa wananchi? Kwa nini yabaki kwao yana faida gani? Wakati wewe ndiyo Waziri wa Kilimo kwa nini asitoe kauli hiyo ya kurudisha mashamba hayo kwa wananchi? Kwa nini Waziri hakutembelea muda wote haya mashamba ya Hanang kwa ajili ya kutoa kauli? Mimi napenda kujua hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni vibaya sana kama mashamba yanakuwepo pale, Halmashauri haina tija, haipati hela ya mapato ya ndani, lakini Serikali nayo haipati kitu chochote, mmebinafsisha kila kitu, hakuna chochote tunachopata. Yale mashamba yalikuwa ni maeneo ya wafugaji waliyonyang’anywa na Serikali hii hii. Naomba hili liangaliwe sana kwa undani na nataka majibu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na maliasili, hii ni kero kubwa. Mheshimiwa Waziri nafikiri pia naye yupo kwenye ufugaji kama sijakosea lakini Naibu Waziri alikuwa Mkurugenzi wa Pingos na mwanasheria wetu, alikuwa anatufundisha ni jinsi gani tutapata haki kwa wafugaji, mbona amejisahau au huko ndani kuna nini? Kama yeye ndiye alikuwa mwalimu wetu leo tena hakuna kinachofanyika wafugaji wanakufa, wakulima wanakufa kutokana na migogoro ya ardhi, ni nini mnachotakiwa kufanya? (Makofi)

Napenda kujua na wewe Mwenyekiti ulikuwepo Bunge la Kumi, mwezi Novemba ilitolewa hoja Bungeni Kamati ikaundwa wakaleta taarifa yao Februari, 2015 ya kwamba kuna migogoro na inatakiwa itatuliwe. Kwenye taarifa aliyoitoa Mheshimiwa Waziri nzuri sana kwamba tayari wameunda timu inafanya kazi, sasa hiyo timu tangu 2015 na 2016 haijafanya kazi halafu imetengeneza sera itawasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri, itawasilishwa lini. Kama mwaka jana haikufanyiwa kazi na mgogoro uko watu wanakufa, hivi hiyo timu yenu ya wataalam au wanatoka nje kwamba hawakufika ndiyo wamefanya kazi sasa hivi.

Mimi naomba tuelewe, kama ni wataalam wa Tanzania muda wote huo kwa nini hawakufanya hiyo kazi na watu wanaendelea kufa. Huu mgogoro ni mkubwa sana na mnasaobabisha ni nyie Serikali kwa kweli kwa sababu watu wengine wanauawa na polisi, watu wengine wanauwawa na askari wa wanyamapori, ni mateso makubwa sana. Tunataka ardhi tengefu iwepo haraka iwezekanavyo kuondoa migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ardhi hii inatakiwa nini? Mnasema kwamba Halmshauri wakatenge watatenga wapi? Wilaya ya Hanang mmechukua heka zaidi ya laki moja, watatenga sehemu gani ili wafugaji wao wabaki pale, ni ngumu sana. Kwa hiyo, lazima muangalie ninyi wenyewe na Waziri tembea, hebu kaangalieni ninyi wenyewe siyo kutuma wataalam pekee yao, wafanye kazi kwenye eneo husika siyo kufanya kazi ya mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni taarifa inayotolewa hapa Bungeni kuhusu idadi ya mifugo waliopo Tanzania. Naomba kujua hii sensa ilifanyika lini? Mimi ni mfugaji ukiniambia ng’ombe milioni 28.4 ndiyo wako Tanzania ni kweli yaani unakubaliana na hilo? Mbuzi milioni 16, kondoo milioni tano, kuku wa asili milioni 37, hii ni taarifa ya hapa Dodoma au ni ya Tanzania nzima? Mimi sielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe sijaona sensa imefanyika nyumbani kwangu. Mimi ni mfugaji, sijaona aliyekuja nyumbani kwangu kufanya sensa ya ng’ombe. Sasa mtuambie hii taarifa yenu mliitoa wapi au mnaongezaongeza tu kama vile asilimia ya kuzaliwa na kadhalika, mimi nashangaa sana. Nina uhakika ng’ombe wako wengi, kondoo wako wengi, hata hao kuku ni wengi mno. Nafikiri hizi ni taarifa za mjini lakini siyo za kule ambako tunafuga mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tutakubaliana na Wizara hii maana yake sisi kila wakati tunasema jamani tuongeze bajeti halafu tukimaliza kuongea na kulalamika tukitoweka hapa ndani mkirudi mnasema hii bajeti ipite. Naomba kujua kuna matatizo gani, ni kwa nini tunashindwa kuelewana? Mawaziri ninyi mkishaacha Uwaziri mkija huku nanyi mnalia, sasa tunashindwa kuelewa, mtuambie kuna nini huko ili tusaidiane tuweze kupata manufaa kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya kusifiana, mimi leo nitamsifia sana Mheshimiwa Rais Magufuli. Mheshimiwa Rais Magufuli alipokuwa Shinyanga akasema kwamba afadhali mazao yapande bei ili wakulima tufaidike na sasa yamepanda bei mnalia nini? Wakulima tunafaidika nunueni debe kwa shilingi 30,000 ndiyo kazi hiyo maana yake yeye ndiyo kasema. Sasa tusipomsifia na yeye kwa kutupandisha sisi bei tutamsifia nani? Sasa na ninyi mnaanza kulalamika leteni mahindi bei ishuke, ishuke kwenda wapi? Mlikuwa mnatuumiza wakulima bei ya mahindi shilingi 5,000 kwa debe na shilingi 20,000 gunia sasa hivi tunapata shilingi 150,000, si raha yetu tumepata faida kuliko wafanyabiashara peke yao. Kwa hiyo, tunataka hiyo bei iendelee ili tuweze kupata manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi fursa ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Maji. Na mimi pia niungane na wenzangu kusema kwamba maji ni uhai, maji ni uchumi wa viwanda na hasa kilimo pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninachosikitika ni kwamba ndugu zetu wanasifia, wanasifia halafu wanadai, wanalia. Mimi napenda kuwaeleza Mheshimiwa Waziri kazi yako unaifahamu kama Wizara, jukumu lako ni kutafuta fedha, kuandaa miongozo ya utekelezaji na kutoa ushauri wa kitaalam. Mikoa kazi yao ni kusimamia na kutoa ushauri wa kiufundi na Halmashauri zetu kazi zake ni kutekeleza miradi ya maji vijijini. Kinachoshindikana kwetu ni wewe Waziri kushindwa kutekeleza wajibu wako. Umeshindwa kututafutia fedha, kwa nini umeshindwa kutafuta fedha? Kila Mbunge anakulilia kuhusu maji. Angalia bajeti yetu tuliyoipitisha ni kwamba tulipitisha shilingi bilioni 623.6 lakini ukashindwa kutafuta hizo fedha umetupatia shilingi bilioni 135, asilimia 22; ni wajibu wako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni wajibu wako kwa nini hukwenda kumlilia mwenzio, Waziri wa Fedha yupo hapa, mko naye kila kila siku, mpo nao kwenye Baraza lenu la Mawaziri mmeshindwa kututafutia hizo fedha, kuna nini au kuna mtu mwingine ameshikilia hii hela kwa sababu wapitishaji na waidhinishaji ni Bunge na Bunge likipitisha maana yake ni fedha na kodi za wananchi, siyo hela ya mtu binafsi. Kwa nini hizi hela zimeshindikana kuja kwenye mradi wa maji, kosa lipo kwako, tutakulaumu. Watu wanasema wewe ni mgeni, wewe sio mgeni kwenye Baraza hili la Mawaziri, ulikuwa Naibu Waziri wa Maji, kwa hiyo, wewe sio mgeni na Wizara, hakuna ugeni kwenye Wizara, wewe sio mgeni unafahamu kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo muhimu ya kuzungumza ni kwamba, je, maji ndiyo kipaumbele au bombardier ndiyo kipaumbele au standard gauge ndiyo kipaumbele. Waziri alipokuwa anatoa hotuba hapa, glass ya maji iko karibu yake, ya nini? Maana yake anataka kutengeneza uhai wake. Mlipokuwa kwenye Tulia Marathon nimewaona kabisa mmebeba maji, ya nini kama sio muhimu? Mimi nadhani maji ni muhimu na tuangalie suala la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda kuzungumzia suala la fedha zilivyotafutwa ambapo ameshindwa Waziri na tunakulaumu wewe Waziri kwa kweli kushindwa kutafuta hizi fedha. Kulikuwa na BRN ya kutekeleza miradi ya vijijini na hiyo BRN ilienda wapi? Zile shilingi trilioni 1.45 zipo wapi, za miaka mitatu iliyopita? Ina maana kwamba fedha zile zilipatikana, zilipokwenda vijijini hazikufanya kazi halafu wewe ukienda vijijini kule kutembelea miradi unapokelewa na Mkuu wa Mkoa/Mkuu wa Wilaya unaenda kupelekwa kwenye mradi mmoja tu kumbe miradi mingine yote ni mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Kamati ya LAAC, CAG anatuelekeza kabisa kusema kwamba miradi ni mibovu na kweli tukienda kukagua miradi yote ni mibovu haijatekelezeka halafu kwenye kitabu chako huku umeandika miradi yote imetekelezeka, haikutekelezeka. Ndiyo maana tunaomba kuunda Tume ambayo itaenda kuangalia haya masuala na ni watumishi wako wanaofanya hiyo kazi na wewe hukwenda kuwasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi ya Same – Korogwe ambayo imetolewa taarifa yake. Tangu mwaka 2014 ilitolewa fedha dola milioni 41.36, ni kutengeneza mradi huo ambao mmeuweka tena mwaka huu, sijui wa kuweka dawa, kutandika bomba, sijui wa kitu gani, haukutekelezeka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia kidogo kwa hizi dakika tano na nitazitumia vizuri. Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ina ubora wake, lakini pia kuna matatizo mengine madogo ambayo yapo, kwa hiyo naomba nichangie kwenye matatizo madogo ambayo yapo.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuna matatizo ambayo yako kwenye Wizara hii. Sisi Wilaya ya Hanang tulihitaji ardhi ile ambayo imerejeshwa kwa wananchi shamba la Gawal na shamba la Wareet kufuta hatimiliki ya awali ili wananchi waweze kugawiwa maeneo yao waweze kupata hatimiliki, lakini ofisini kwa Mheshimiwa Waziri naona kuna ugumu sana wa kuweza kufuta hiyo hatimiiki na tunaomba alifanyie kazi hilo kwa sababu ni muhimu sana, wananchi wanahitaji hatimiliki lakini hawawezi kupata mikopo kutokana na ugumu uliotokana na Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine la pili, napenda kuzungumzia suala la migogoro; sisi Wilaya ya Hanang tuna mashamba ya NAFCO ambayo kwao yamebinafsishwa kwa wawekezaji na tuna mgogoro sana na mwekezaji mmoja ambaye ni Ngano Limited au kwa jina lingine analitumia Rai Group, yeye ni wa Kenya, alibinafsishiwa mashamba matatu. Cha kushangaza huyu mwekezaji analima asilimia 30 tu tangu amepewa yale mashamba. Sasa Mheshimiwa Waziri nimesikia akinyang’anya mashamba ya watu wengine ambao hawajayaendeleza, sasa huku Hanang kwa nini ameshindwa kufika na wakati anafika hata Babati.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri afike Hanang akatembelee hayo mashamba ambayo yanaitwa Ngano Limited ayaone yakoje, lakini kwa taarifa fupi napenda kumweleza kwamba Halmashauri ya Hanang inategemea cess kutokana na mazao. Sasa hivi tumekosa hiyo cess kwenye mashamba hayo matatu, tulikuwa matajiri kutokana na kupata hiyo cess, lakini mashamba hayalimwi hata kidogo na wao wenzetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimweleze kwa kifupi Mheshimiwa Waziri aelewe kwamba shamba la Gidagamowd lina hekari 16,330 ambazo amebinafsishiwa huyo Ngano Limited. Yeye analima hekari 5000 tu, hekari 11,330 hajalima, hii ni miaka yote tangu amepewa hayo mashamba, yanakaa hivi hivi ni mgogoro.

Mheshimiwa Spika, shamba lingine ni shamba la Murjanda alilobinafsishiwa huyo bwana ambalo lina ekari 13,400, kwa hiyo anayolima yeye ni ekari 6000, ekari 7,400 halimi.

Mheshimiwa Spika, angalia tena shamba lingine la tatu ambalo amepewa huyo mwekezaji ni shamba la Setchet, shamba hili lina hekari 16,300, analima hekari 3,500 tu, hekari 12,800 halimi. Mheshimiwa Waziri hebu aangalie kati ya hekari hizo zote hekari 34,000 mwekezaji huyo halimi, je angeyaachia yale mashamba kwa wananchi si yangelimwa yote na tungepata cess sisi Wilaya ya Hanang? Sasa hatupati cess, wewe pia kwenye Serikali hupati kodi yoyote kwa sababu ya tatizo alilonalo. Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa undani na kwa huruma kwamba Wanahanang sisi tunategemea kilimo, sasa kama halimi ya nini? Yarejeshwe kwa wananchi ili waendelee kuyalima, hatuna sababu ya kuwa na wawekezaji ambao hawafanya au hawatekelezi wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la tatu napenda kuzungumzia suala la kupima viwanja. Tuna tatizo la mpango wa upimaji shirikishi, kwa sababu matatizo haya yanatokea kwa Wilaya ya Hanang kutokana na kutokuwa na majalada na headed paper kwa sababu inabidi Wilaya ya Hanang wakachapishe kwenye government printers na ni ghali. Matokeo yake upimaji unakuwa wa gharama ya juu, tunaomba Wazri atusaidie tunafanyaje ili gharama ziwe chini na Wizara yake ndio inaweza hilo. Sasa kama hawataweza kuwawezesha Wataalam wetu walioko wilayani au wale ambao ni wataalam ambao sijui ni wa upimaji shirikishi uliopatikana siku hizi, basi wawawezeshe ili gharama ziwe za chini na wananchi waweze kumudu.

Mheshimiwa Spika, ya kwangu ni hayo, sina mengi ya kuongea zaidi ya kutaka Mheshimiwa Waziri afike Wilaya ya Hanang kutatua hiyo migogoro. Haya mashamba hata sisi tuna uwezo wa kulima. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea ukurasa wa kumi wa hotuba ya Waziri kuhusu ujenzi na ukarabati wa nyumba za polisi. Tunapenda kujua kati ya nyumba 400 zinazotarajiwa kujengwa kama Vituo yya Polisi Bassotu na Endasak vinahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama fedha zilizotolewa za maendeleo kiasi cha Sh.38,285,682,000/= zinahusiana na ujenzi na ukarabati wa nyumba za polisi. Kama ndivyo, je, Vituo vya Polisi katika Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara vina kiasi gani cha fedha za ujenzi na ukarabati? Wakati Mheshimiwa Waziri anajibu hoja, naomba kujua kama Vituo vya Polisi Bassotu na Endasaki vimetengewa fedha, kwani Kituo cha Bassotu Wilayani Hanang Mkoani Manyara, wamepewa barua ya kuondoka katika nyumba ambayo waliomba kuishi kwa muda kama kituo cha polisi. Je, lini kituo hicho kitajengwa na nyumba za polisi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni usafiri. Kutokana na kuwa na eneo kubwa la ulinzi kunatakiwa usafiri wa uhakika kwa polisi wetu wanaoishi kwenye vituo ambavyo vipo pembezoni na mbali na makao makuu ya Polisi Wilaya. Kwa hiyo, naomba kupatikane gari ambalo litawasaidia Polisi Bassotu ili waweze kulinda wananchi, raia na mali zao kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ajira. Naomba askari wa kutosha wa kike ili kuhifadhi hadhi ya wanawake kwani wanawake ni wengi sana kuliko wanaume.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Spika, Fungu 99 Sekta ya Mifugo. Changamoto kubwa ni migogoro inayowahusisha wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi pamoja na sheria kandamizi kwa wafugaji ambayo hutumiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, ng’ombe wakiingia kwenye hifadhi wanakamatwa na kutaifishwa, kutozwa fine kila ng’ombe mmoja Shs. 100,000; mchungaji hutozwa fine ya laki 300,000/= na mwenye ng’ombe kufungwa.

Mheshimiwa Spika, kwafano mfugaji Wambura wa Serengeti alipigwa fine ya shs. 5,000,000/=, kifungo miaka mitano na ng’ombe 294 kutaifishwa. Hiyo siyo halali kwa kuwa ukisha muadhibu si vema kutaifishiwa ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri naomba kuwe na mpango mkakati wa kuwasaidia wafugaji na kuwatembelea kwenye maeneo yao na kuwasikiliza.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Kero ya Usafirishaji wa Mifugo kwa Kutumia Malori. Kuna utozaji wa ushuru wa SUMATRA na TANROADS. Tunaomba ifuatilie kujua uhalali huo.

Mheshimiwa Spika, Ushindani Usio Sawa Hususan Bidhaa Mpya ya UHT. Sasa hivi ni viwanda vinne tu ndivyo vinazalisha maziwa kwa kutumia product ya ndani. Viwanda hivi vinanunua maziwa kwa wafugaji wetu na kutengeneza UHF. Cha kusikitisha hivi viwanda vinne vinavyonunua maziwa kwa wafugaji wa ndani hawakupewa punguzo la kodi. Ila Azam anayesindika maziwa ya unga kutoka nje ya nchi na kutengeneza UHT amepewa punguzo la kodi kwa asilimia 87.5

Mheshimiwa Spika, natoa ushauri kwa kuweza kulinda watu wetu wawekezaji wanaonunua maziwa kwa wafugaji kupewa punguzo.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Uvuvi. Mheshimiwa Waziri nachangia kuhusu maziwa madogo, kati na mabwawa. Ninatambua lengo la kuimarisha usimamizi, uendelezaji, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi na utunzaji wa mazingira.

1. Unyanyasaji, kwa wavuvi, wachuuzi na watumiaji wengine wa samaki.

2. Kufunga maziwa kwa muda wa miezi sita wakati huo mvuvi amelipa leseni ya mwaka moja.

3. Kufunga maziwa kunasababisha wachuuzi wanaotegemea mboga kukosa huduma hiyo kwa miezi sita.

4. Hawa wote kushindwa kujikimu kwa maisha yao kwa kuwa hawana pato lingine ni kuwatia umaskini.

Mheshimiwa Spika, nashauri maeneo yote ya mazalio ya samaki yasivuliwe kwa muda wote na mwaka mzima ili wavuvi nao wavue kwa muda wote kwa kuwa hiyo ndiyo sehemu ya kipato.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto na utatuzi wake; ukurasa wa 68–b-4-3 kutatua migogoro, Mheshimiwa Waziri napenda kujua ni jinsi gani utaweza kutatua migogoro ya Wafugaji na Watumishi wa TANAPA na wenye maeneo tengefu, kwani kumekuwa na sheria kandamizi kwa Wafugaji ambayo hutumika katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ng’ombe wakiingia kwenye hifadhi au game reserve, ng’ombe wanataifishwa, kutozwa faini kila ng’ombe Sh.50,000 hadi Sh.100,000, Mchungaji au mwenye Mifugo hutozwa Sh.300,000 au kifungo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, mfugaji aitwaye Wambura huko Serengeti alipigwa faini ya Sh.5,000,000, au kifungo cha miaka mitano (5) na kutaifishwa ng’ombe mia mbili tisini na nne (294).

Mheshimiwa Naibu Spika, Upande wa hifadhi ya Tarangire pia kupigwa faini wafugaji kila wakati na huo umekuwa ni utaratibu wa kila mara, Je, huo sio unyanyasaji kwa wananchi walio karibu na hifadhi hizo? Unyanyasaji huu umesababisha vifo kwa wafugaji kwa ajili ya kufilisiwa je, Mheshimiwa Waziri ataisaidiaje kupunguza adha kwa wafugaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyozunguka Hifadhi kurejeshwa kwa wananchi kama vile Vijiji vya vya Gedamar, Gijedabung na Ayamango vilivyopo Wilaya ya Babati Tarafa ya Galapo, kwani Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ina ukubwa wa kilomita za mraba 2,600 kwa Tangazo la Serikali la mwaka 1970, iweje mwaka 2010 kuwe na uwekaji wa beacon kwenye vijiji hivyo hapo juu? Ni vema kufanya uchunguzi wa hali ya juu kwa kuondoa huo uonevu kwa wananchi ambao wapo kwenye hivyo vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarangire National Park, Ruaha National Park, Rukwa Rwafi, Gurumeti Game Reserve, Ikorongo Game Reserve, Kijereshi Game Reserve na Maswa Game Reserve, baadhi ya Hifadhi za Taifa na maeneo tengefu yenye kunyanyasa wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, moja; ufunguzi wa masoko ya madini katika maeneo imejikita zaidi kufanya uzinduzi huu katika kila mkoa ambao kuna uchimbaji wa madini. Uzinduzi huu wa masoko ya madini uendane sambamba na utaratibu mzuri wenye kukidhi vigezo vyote vya usalama katika maeneo yote yenye machimbo husika nchini. Kwani maeneo mengi hayana wasimamizi au watumishi wa madini na askari ili kulinda madini hayo kwa ajili ya wachimbaji wengi kutokuwa waaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, utoaji wa elimu kwa wachimbaji mbalimbali juu ya umuhimu wa kutumia masoko ya madini yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, tozo za madini; watendaji wa mamlaka za kiserikali wanatoza kodi za tozo zilizofutwa. Inaaminika tozo hizi zote zinafanyika kwa maslahi binafsi ya wakusanya tozo hizo. Tozo hizo zinawalenga wachimbaji wadogo wadogo wa madini wenye uelewa mdogo wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini. Tozo mbalimbali zinazotozwa ni ushuru wa mawe, ushuru wa karasha, ushuru wa duara, ushuru wa mwalo na ushuru wa compressor. Tozo zinazotambulika na Serikali ni kama zifuatazo:-

Moja, royalty (mrabaha), ada ya ukaguzi (service and clearance) na service levy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa Serikali kusimamia sheria zilizotungwa ili kuwanufaisha pande zote za Sekta hii ya Madini hasa wachimbaji wadogo wadogo kukatwa tozo/kodi kwenye viroba vya mchanga au mawe.