Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mbaraka Kitwana Dau (66 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie Mpango uliowasilishwa na Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia sote hapa tumeamka salama na tunaendelea na shughuli zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika namna ya kipekee kabisa niwashukuru wapiga kura wa Mafia kwa kuniwezesha kuwa Mbunge kwa kura nyingi sana na leo nimesimama kwa mara ya kwanza katika Bunge lako Tukufu nikichangia Mpango huu. Ninachotaka kuwaambia wananchi wa Mafia, imani huzaaa imani. Wamenipa imani na mimi nitawarejeshea imani. Ahadi yangu kwao, nitawapa utumishi uliotukuka uliopakwa na weledi wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wenyewe watakuwa mashahidi, wameshaanza kuona baadhi ya ahadi ambazo niliziweka kwao zimeanza kutekelezeka. Wananchi wa vijiji vya Juwani na Chole wa visiwa vidogo ambavyo hawakuwa na maji kwa muda mrefu, maji yameshaanza kutoka kule. Wananchi wa visiwa vidogo vya Bwejuu na Jibondo maji wataanza kupata baada ya wiki mbili kutoka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali makini na Serikali sikivu ya CCM kwa kuanza na sisi wananchi wa Mafia. Nimeongea na Waziri makini kabisa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi tukiomba watupatie meli ya MV Dar es Salaam ili kuondoa kero ya usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati. Kimsingi Waziri amekubaliana na hilo na naomba niwafahamishe watu wa Mafia kwamba Serikali imekubali kutuletea meli ya MV Dar es Salaam. Hivi sasa mchakato wa masuala ya kitaalam na ya kiutawala unaendelea na meli hiyo itakuwa Mafia ndani ya muda mfupi kutoka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee vilevile kuipongeza Serikali, tuliomba gati na niliongea na Waziri, Mheshimiwa Mbarawa, bahati mbaya hayupo, lakini ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani upo nakuona hapo, tuliomba gati lifanyiwe maboresho kwa kuletewa tishari kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kuwafahamisha wananchi wa Mafia na Bunge lako Tukufu kwamba tishari lile limefika Mafia juzi, taratibu za kuli-position kwenye gati lile zinaanza na usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni utaboreka zaidi.
Naomba ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani unifikishie salamu kwa Mheshimiwa Waziri, bado tuna matatizo upande wa pili wa Nyamisati, kule maboresho bado hayajafanyika. Tunatambua kwamba Mamlaka ya Bandari ilishatenga bajeti kwa ajili ya kufanya maboresho upande wa Nyamisati. Meli hii itakayokuja kama upande wa Nyamisati hakutafanyiwa maboresho itakuwa haina maana yoyote.
Kwa hiyo, nakuomba kwa namna ya kipekee ndugu yangu Mheshimiwa Ngonyani na nikimaliza kuchangia nitakuja hapo kwako nikuelezee in details. Maboresho ya Bandari ya Nyamisati ni muhimu sana katika kuhakikisha meli ile ya MV Dar es Salaam inafanya kazi zake baina na Kilindoni na Nyamisati bila ya matatizo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee pia nikushukuru ndugu yangu, mzee wangu Mheshimiwa Profesa Muhongo. Nilikuletea concern yetu watu wa Mafia kuhusiana na kusuasua kwa mradi wa REA. Ukachukua hatua na ninayo furaha kukufahamisha kwamba nimeongea na watu wa TANESCO na tumekubaliana kwamba mradi ule utakabidhiwa baada ya mwezi Machi, hivyo basi nakushukuru sana. Pia tulinong‟ona mimi na wewe kuhusu suala la submarine cable kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, submarine ndiyo solution …
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau, naomba sana tuendelee kutumia lugha ya Kibunge.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nilikuomba Mheshimiwa Muhongo kwamba ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme Mafia ni kuzamisha submarine cable kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni.
Kimsingi ukaniambia niendelee kukukumbusha. Mimi kwa kuwa wewe ni jirani yangu hapa kila nikifika asubuhi shikamoo yangu ya kwanza ni submarine cables…
MWENYEKITI: Kwa mujibu wa Kanuni ya 60, elekeza maongezi yako kwa Mwenyekiti.
MHE. MBARAKA K. DAU: Submarine cable itakuwa ndiyo salamu yangu ya kwanza ya asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nianze sasa kuchangia Mpango. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Ashatu wameleta Mpango mzuri sana. Mimi naamini madaktari hawa wawili watatuvusha, tuwape ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye ugharamiaji (financing) wa Mpango huu. Mpango uliopita ulipata matatizo makubwa sana kutokana na ukosefu wa fedha. Naamini kwa ari na kasi iliyoanza nayo Serikali ya Awamu ya Tano ambapo ukusanyaji wa mapato umekuwa mkubwa sana sambamba na kubana matumizi ya Serikali, financing ya Mpango huu wa sasa haitakuwa tatizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, concern yangu ipo kwenye sehemu ya pili ya financing ya Mpango huu ambayo ni sekta binafsi. Sekta binafsi wanakuja kuwekeza lazima sisi wenyewe tuweke mazingira wezeshi kama mlivyosema katika Mpango wenu, kwamba ili watu waje kuwekeza hapa lazima mazingira yawe mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, ninachotaka kusema ni kwamba tuwe waangalifu na hawa wawekezaji wanaokuja. Nitatolea mfano kule Mafia na Mzee wangu Mheshimiwa Lukuvi naomba unisikilize vizuri sana hapa, tuna Kisiwa kinaitwa Shungimbili. Mafia imezungukwa na visiwa vingi tu lakini kimoja kinaitwa Shungimbili. Kisiwa hiki cha Shungimbili kimebinafsishwa au sijui niseme kimeuzwa au sijui niseme kimekodishwa bila ya Serikali ya Wilaya kuwa na habari. Namuuliza Mkurugenzi anasema hana taarifa, namuuliza DC wangu anasema hana taarifa, naomba sana…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na usalama na leo tumekutana hapa tukiwa na afya njema ili kuweza kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Mtukufu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyoiendesha nchi yetu mpaka sasa, kwa ukusanyaji mzuri na uongozi mzuri katika kipindi kifupi alichokua madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu pia nizielekeze kwa ndugu yangu, Komredi, Mheshimiwa Waziri Mwigulu pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Olenasha, kwa kazi nzuri na hotuba nzuri waliyoiwasilisha leo asubuhi hapa. Combination yao ni nzuri sana na tunawategemea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niendelee kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo langu la Mafia kwa kunichagua na kuendelea kuniamini niweze kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kwa kusisitiza hili, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba ile x-ray machine na ultrasound machine ambazo niliziahidi katika kampeni yangu, zimeshatoka bandarini na zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii, zitakuwa Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nukta hii, namshukuru sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kuweza kutusaidia kupata vibali muhimu vya TFDA na leo x-ray machine na ultra sound, tayari zinaelekea Mafia mwisho wa wiki hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia Taasisi ya MIDEF ambayo ndiyo iliyo-donate mashine hizi kwa Jimbo la Mafia. Na mimi mwenyewe pia nijipongeze kwa ushindi mkubwa nilioupata kwenye uchaguzi na kwenye kesi iliyofunguliwa na mgombea wa chama cha CUF. Nimeshinda, akakata rufaa na nimeshinda tena. (Makofi)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia hotuba ya Waziri wa Kilimo.
Kwa upande wa Jimbo la Mafia, uchumi wa Jimbo la Mafia umebebwa na uvuvi na utalii. Kwa masikitiko makubwa sana kuna taasisi ya Serikali maarufu kama Marine Park, badala ya kuwa msaada kwa wananchi wa Mafia imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Mafia. Taasisi hii ya Marine Park, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, naomba sana na utakapohitimisha nitahitaji kusikia kauli kutoka kwako kuhusiana na Marine Park.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wanatudhulumu watu wa Mafia kwenye mgao unaotokana na mapato ya watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 wanachukua Marine Park na asilimia 30 ambapo 10 zinakwenda kwenye Halmashauri na asilimia 20 inakwenda kwa vijiji husika ambavyo watalii wale wanakwenda. Mgao huu siyo sawa ukizingatia maeneo mengine kama Hifadhi ya Wanyamapori ambapo wananchi wa maeneo husika wanapata asilimia 60 na Serikali Kuu inapata asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapokuja kwenye Marine Park, wamekuwa wakitudhulumu wananchi wa Mafia. Tumelisema sana hili! Kila ukiongea nao wanakwambia kwamba hii ni sheria, hii ongea na watu wa Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda sana wakati unahitimisha hotuba yako Mheshimiwa, ndugu yangu rafiki yangu Komredi Mwigulu ulitolee maelezo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea suala la Marine Park, watu wa Marine Park wametoka katika kazi yao ya msingi ya uhifadhi na hivi sasa wamekuwa madalali, wanauza ardhi. Visiwa vitatu vya Mafia vidogo vidogo sasa vimeshauzwa na Marine Park. Visiwa hivyo ni Nyororo, Mbarakuni pamoja na Kisiwa cha Shungimbili. Huu mchakato wa kuuza pengine siyo tatizo kubwa sana, tatizo kubwa sana kwa nini hawataki kufuata taratibu? Huwezi ukauza ardhi au kuibinafsisha bila kuwashirikisha wananchi husika wa vijiji vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, kwa masikitiko makubwa sana, watu wa Marine Park wamevibinafsisha visiwa hivi kwa kutengeneza mihtasari fake kuthibisha kwamba wananchi wameshirikishwa. Ukweli ni kwamba wananchi hawajashirikishwa na nyaraka walizo-forge ninazo hapa, nitakuletea kwako hapo ili uzione na uweze kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mgao usio sawia wa maduhuli yanayotokana na watalii, vilevile pesa zinazotolewa pale kwa mujibu wa maelezo yao wenyewe Marine Park wanasema kwamba Marine Park ya Mafia ndiyo inaendesha Marine Park zote Tanzania. Mapato yanayotoka kule, sehemu kubwa yanaendesha Marine Park nyingine za nchi yote. Kisiwa kama Mafia kidogo chenye uchumi mdogo kwenda kukitwisha mzigo wa kuendesha Marine Park zote zilizopo Tanzania, kwa kweli hili siyo sawa. Hata huu mgao wa asilimia 70 wanautoa baada ya kutoa gharama zote, kwa maana ya gharama za uendeshaji. Hii tunaiona pia siyo sawa. Namwomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, hili nalo aliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tukirudi kwenye suala la uhifadhi wenyewe, Marine Park kazi yao ya uhifadhi yenyewe imewashinda ukianzia Moa, Pwani ya Tanzania mpaka Msimbati kule, mabomu yanapigwa usiku na mchana. Pale Dar es Salaam kuanzia Magogoni pale Ikulu kwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli mpaka Pemba Mnazi, mchana na usiku ni mabomu yanapigwa kama nchi iko kwenye vita. Tunashangaa uhifadhi gani wanaoufanya hawa wa Marine Park. Mheshimiwa Waziri Marine Park ni jipu na ninaomba sana ulitumbue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, mkononi mwangu hapa ninao waraka uliotolewa na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kilimo na Mifugo wakati ule Mheshimiwa John Pombe Magufuli, waraka wa tarehe 12 Agosti, 2008, ukitoa ruhusa kwa wavuvi ambao wamezuiwa wasitumie mitungi ya gesi migongoni mwao wanapokwenda kuvua katika kina kikubwa cha maji. Kina cha mita 50 mtu hawezi kuzamia kwa kuziba pua, ni lazima aende na mtungi wa gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Marine Park wanawakataza wananchi na wanaendelea kuwakamata. Hivi ninavyozungumza, wapigakura wangu zaidi ya 20 wameswekwa rumande kwa sababu wamevua kwa ya kutumia mitungi ya gesi. Mitungi ya gesi Mheshimiwa Waziri, haiharibu mazingira, inamsaidia mvuvi aweze kwenda kina kikubwa zaidi kwenda kutoa nyavu zake zilizonasa. Haina uhusiano wowote na uharibifu wa mazingira, hata ndugu yangu Makamba anaweza akathibitisha hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo cha mwani, Marine Park...
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sera ya kuwekeza kwenye viwanda, nashauri tujikite zaidi kwenye viwanda vidogo vidogo vyenye kuongeza thamani ya mazao yetu badala ya viwanda vya kuzalisha bidhaa kamili kama hatuna “comparative advantage” ya bidhaa za aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali itafute mwekezaji wa Kiwanda cha kusindika samaki katika Kisiwa cha Mafia sambamba na kupata meli za uvuvi zenye zana za kisasa zenye uwezo wa kuvua katika bahari ya kina kirefu. Mafia ipo karibu na mkondo wenye kina kirefu kunapopatikana samaki wengi na wakubwa wa aina mbalimbali kama Jodari (Tuna) nguva (King fish) samsuri (Marley) na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa viwanda vya sukari umekuwa mdogo na hautoshelezi kulisha soko la nchi nzima. Ipo hoja na haja ya kuvutia mwekezaji kuwekeza katika bonde la Mto Rufiji ili kuondokana na tatizo la kuagiza sukari kila mwaka. Naishauri Serikali pia katika kipindi hiki kuelekea kujitosheleza kama uzalishaji wa ndani wa sukari, Serikali itoe vibali kwa kuagiza sukari kwa viwanda vyenyewe, mfano, Mtibwa, Kagera na kahalika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kuwa hapa wote tukiwa salama na afya na kuweza kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa nimshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ndugu yangu Mheshimiwa Makame Mbarawa na Naibu wake rafiki yangu Mheshimiwa Ngonyani kwa hotuba nzuri sana ambayo kwa kiasi kikubwa sana imejikita katika kuondoa matatizo na kero mbalimbali za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye uchangiaji. Kuna dhana hii ambayo ilikuwa ikizungumzwa sana ya maeneo ya pembezoni, maeneo yaliyosahaulika. Kwa bahati mbaya sana, kila inapojadiliwa maeneo ya pembezoni na yaliyosahaulika kisiwa cha Mafia kinasahaulika. Wananchi wa Kisiwa cha Mafia wana kila aina ya sababu na sifa zote za kuitwa watu ambao ni wa maeneo ya pembezoni na waliosahaulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo mtu akisafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza kuanzia saa 12 asubuhi akifika saa 3 au 4 lakini mwingine akaondoka na boti Dar es Salaam pale akielekea Mafia basi yule wa Mwanza atafika wa Mafia hajafika. Nayasema haya kwa sababu adha ya kusafiri kwa boti kutoka Dar es Salaam mpaka unafika Mafia inaweza ikachukua siku moja mpaka mbili na ndiyo maana kwa makusudi kabisa tukaamua wananchi wa Mafia wanapotaka kusafiri wanakwenda Kusini kidogo kwa kutumia barabara ya Kilwa mpaka maeneo ya Mkuranga, wengine wanakata kushoto wanakwenda Kisiju. Sasa matatizo yanaanza pale, barabara ya Kisiju - Mkuranga kilometa kama 46 ni ya vumbi, ni mbaya sana na imekuwa ikipigiwa kelele sana lakini bado haijashughulikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bandari ya Kisiju ni kama economic hub ya Kisiwa cha Mafia kwani mazao yote ya nazi na yanayotokana na bahari yanapitia bandari ya Kisiju lakini tatizo la uharibifu wa barabara ile ya Mkuranga – Kisiju ni kubwa. Nimeangalia kwenye Kitabu cha Mheshimiwa, nikakisoma mara mbili mpaka tatu sikuiona barabara ya Mkuranga - Kisiju ambayo ni kilometa 46. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha basi alitolee maelezo suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namna ya pili ambayo abiria wengi wanaitumia kufika kisiwa cha Mafia ni kwenda mpaka Bungu, Rufiji wanakata kushoto wanakwenda mpaka kwenye bandari ya Nyamisati. Baina ya Bungu na Nyamisati ni kama kilometa 41, pale napo pia barabara ni kama hakuna. Ina mashimo na kipindi kama hiki cha mvua inakuwa kama imekatika. Wananchi wa Mafia wanaposafiri na boti kutoka Kilindoni wakafika Nyamisati wana kazi nyingine pale ya kudandia magari mbalimbali na wengine bodaboda ili wafike Bungu na hatimaye kuja Dar es Salaam. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha ulielezee hilo pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Kisiwani Kwenyewe Mafia, kuna barabara kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi kilometa 55. Mkononi kwangu hapa nina Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo tuliyoinadi kwa wananchi, ndani ya Ilani hii inasema wazi kabisa, Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo tutajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi (Bweni). Hata hivyo, nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuiona barabara hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana atakapokuja ku-wind up alitolee maelezo na hilo nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mafia kuna barabara inaitwa Airport Access Road kilometa 14 inatoka Kilindoni inakwenda mpaka Utende ambayo imetengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa masikitiko makubwa sana, barabara ile haijakabidhiwa huu unafika mwaka mmoja toka imekamilika. Naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri, itakapofika wakati mkandarasi anataka kuikabidhi barabara ile Serikali msikubali kuipokea kwani ina mashimo mwanzo mpaka mwisho na mpaka leo haijazinduliwa. Barabara ina matatizo, kuna jokes zinaendelea kule Mafia wanasema kama gari ikipata pancha ukipiga jeki badala ya ile gari kwenda juu basi jeki ndiyo inatitia chini kama vile umepiga jeki kwenye matope. Kubwa zaidi wenyewe wanaiita barabara ya Big G maana yake ina mashimo mashimo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nizungumzie kuhusu Bandari ya Nyamisati ambayo na yenyewe pia imo katika kitabu hiki cha Ilani ya CCM. Jana kwa bahati nilipata fursa ya kuongea na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) akanithibitishia kwamba bandari ile itajengwa lakini pesa zilizotengwa zilikuwa ni kidogo na walipoenda kufungua zabuni wakakuta ame-quote shilingi bilioni nane na wao Mamlaka ya Bandari hawana uwezo wa kulipia fedha hizo. Akanihakikishia Mkurugenzi Mkuu kwamba wamenunua dredger (mashine la kuchimbia na kuongeza kina kwenye bandari), kwa hiyo wamesema kazi hiyo wataifanya wao wenyewe.
Mheshimiwa Waziri naomba wakati utakapokuja ku-wind up uniambie na uwaambie wananchi wa Mafia ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya Bandari ya Nyamisati kazi ambayo wataifanya wenyewe Mamlaka ya Bandari? Vinginevyo kwa mara ya kwanza mimi sijawahi kutoa shilingi hapa lakini leo kama nisiposikia habari ya Bandari ya Nyamisati kiasi gani kimetengwa na mimi nitaingia kwenye record hapa ya kuzuia shilingi au pengine hata noti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mafia. Sasa hivi tuna kilometa 1.5 ili ndege kubwa ziweze kutua tunahitaji runway yenye angalau kilometa 2.5 ili watalii waweze kuja moja kwa moja katika Kisiwa cha Mafia. Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri iliyobaki pale ni kilometa moja tu, naomba sana mtupatie hiyo kilometa moja ili watalii waweze kuja Mafia na tuweze kunufaika na biashara ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MV Dar es Salaam…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, shukurani kwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wa Wizara kwa hotuba nzuri yenye kuleta matuamini kwa Watanzania. Mradi wa umeme wa REA kwa Kisiwa cha Mafia umebakiza vijiji na maeneo 10 kukamilika, navyo ni vijiji vya Gonge, Jojo, Mariam, Bani, Jibondu, Juani, Chole, Dongo na Maeneo ya Tumbuju, Bwejuu na Tongani. Ombi langu kwa Wizara ni vijiji na maeneo husika viingizwe kwenye mradi wa REA Phase III.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uzalishaji wa umeme kwa sababu umeme Mafia unatokana na chanzo cha mafuta yanayoendesha majenereta yaliyopo. Kutokana na gharama kubwa ya ununuzi wa mafuta na matatizo ya usafiri wa mafuta hayo kwa njia ya bahari, ombi letu wananchi wa Mafia ni kwamba, Serikali sasa iunganishe na umeme wa SONGAS kupitia kupitishwa kwa submarine cable kutokea Nyamisati kwenda Kilindini takriban kilomita 50 ili kuondokana na adha ya kusafirisha mafuta mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utafiti wa mafuta na gesi, katika Kisiwa cha Mafia ni jambo linalofanywa mara kwa mara. Kwa habati mbaya sana wananchi wa Mafia wamekuwa hawapewi taarifa tunaomba Wizara na Waziri wakati atakapokuwa anajibu awaeleze wananchi wa Mafia kama mafuta au gesi vimegundulika Mafia au hapana ili kuondoa hali ya sintofahamu kwa wananchi wa Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kwenye ugunduzi wa gesi hasa maeneo ya kina kirefu cha bahari yaani off share maeneo ya Kusini mwa Tanzania. Mpakani mwa Wilaya ya Kilwa na Mafia, katikati ya bahari kuna visima viwili ambavyo kimpaka kimo katika Wilaya ya Mafia, lakini kutokana na matatizo ya usafiri shughuli za uchimbaji na utafiti zimekuwa zikifanyika kutokea Wilaya ya Kilwa.
Swali je, wananchi wa Mafia wananufaika vipi na visima hivi ambavyo kimipaka vipo Mafia lakini shughuli za uchimbaji zinafanyika Kilwa?
Suala lingine ni bomba jipya la gesi kutoka Kusini kuja Dar es Salaam, ujenzi umekamilika kwa asilimia 100. Swali, je, ni lini bomba litaanza kusafirisha gesi kutoka Kusini kwa matumizi ya kibiashara? Swali lingine, ni lini umeme ghafi utachakatwa na kuweza kutumika kwa matumizi ya majumbani?
Mheshimiwa Naibu Spika, natanguliza shukurani na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba hizi mbili alizozileta Waziri wa Fedha na Mipango, Hali ya Uchumi na Bajeti ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na salama, leo tumekutana hapa kujadili mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru sana Dkt. Phillip Mpango, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kutuletea bajeti ambayo nimeiita ni bajeti ya kihistoria. Haijapata kutokea katika historia ya nchi yetu Bajeti ya Maendeleo ikawa asilimia 40 ya bajeti yote ya Taifa. Kwa kweli pongezi nyingi sana zimwendee Mtukufu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa dhamira hii ya dhati ya kuwaondoa wananchi wa Tanzania katika lindi la umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata faraja kubwa sana, nilikuwa najaribu kufanya tathmini ndogo hapa, nikagundua miundombinu peke yake imetengewa asilimia 25.4, elimu asilimia 22 na bajeti ya afya ni asilimia 9.2. Hapa kwenye bajeti ya Wizara ya Afya, Abuja Declaration inatutaka tutenge bajeti ya asilimia15. Wanasema Rome haikujengwa siku moja, kidogo kidogo ndani ya bajeti mbili, tatu zijazo tunamwomba sana Dkt. Mpango Azimio hili la Abuja la asilimia 15 katika bajeti ya Wizara ya Afya lifikiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze moja kwa moja kwenye kuchangia bajeti. Ushiriki wa sekta binafsi na sekta ya umma katika miradi ya pamoja kimekuwa ni kilio cha siku nyingi sana, tumelizungumza sana hili na ninayo furaha na nahisi faraja kubwa sana, kupitia kwenye bajeti hii nimeuona ushiriki huu wa sekta binafsi na sekta ya umma kwa maana ya PPP, tatizo langu ni dogo tu!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha basi atuletee na mchanganuo, kwa sababu tumeona tu humu miradi, mimi naiona kama ni blanket imewekwa humu, miradi kama ya barabara ile ya Chalinze – Dar es Salaam express way, mradi wa Reli ya Kati, miradi hii ya umeme ya phase III kule Kinyerezi ipo tu kwa ujumla ujumla!
Mheshimiwa Naibu Spika, tungeomba sana hebu watupatie break down na frame work, timeline kwamba miradi hii tunafanya labda tutaanza na mradi wa reli ya kati standard gauge, labda tarehe fulani mpaka itakapofikia mwaka wa fedha miaka miwili, mitatu, mbele mradi huu utakuwa umekwisha; labda mradi wa bandari ya Bagamoyo utaanza tarehe fulani mwaka wa fedha fulani na utakwisha hivi, ili tupate kwa ujumla wake haya mambo yanakwendaje; lakini kutujazia tu miradi ya jumla bila ya kutupa timeline inatusumbua sana, kwa sababu tunajenga matumaini, lakini ndani yake hatujui miradi hii itakuja lini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye suala la utalii. Nilizungumza hapa kwenye Wizara ya Maliasili na Utaii ilipoleta bajeti yake na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri namwona pale na namwomba Mheshimiwa Waziri anitegee sikio. Takwimu zinatuambia kwa miaka miwili kati ya mwaka wa fedha uliopita na mwingine wa nyuma yake, utalii wetu umeshuka kwa karibu watalii laki moja, sasa sitaki kujielekeza kwenye sababu gani zimepelekea watalii kupungua. Nataka nijielekeze kwenye namna ambavyo tunaweza tukatangaza utalii wetu ili tupate watalii wengi na kuhakikisha kwamba tunapata mapato katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumza utalii mara nyingi tunajikita kwenye vitu viwili tu, Mlima Kilimanjaro na Mbuga, wakati Tanzania na Naibu Waziri wakati anajibu swali hapa juzi alisema wazi kwamba Tanzania ni ya pili duniani kwa vivutio vya kitalii, sasa hivi vivutio vingine vitatangazwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Kisiwa cha Mafia na nilizungumza hapa wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwamba kule Mafia tuna samaki anaitwa ‗Papa Potwe‘, huyu samaki ni samaki wa ajabu, anatabia kama za dolphin, ni samaki rafiki, watalii wanapenda sana kuja kuogelea naye. Je, ni wangapi wanajua habari za samaki huyu ‗Papa Potwe‘?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunaomba sana mtengeneze package ya vivutio vyote ili muweze kwenda kuviuza huko nje, kwa sababu Halmashauri hatuna uwezo wa kumtangaza ‗Papa Potwe‘! Ni lazima tusaidiwe na nguvu ya Serikali. Kwa hiyo naomba sana tutanue wigo katika utalii wetu katika kuutangaza na kuhakikisha kwamba tunapata mapato mengi ili kuendeleza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mpango, hili nililizungumza kwako kama mara moja au mara mbili hivi, masikitiko yangu makubwa kuona kwamba Kisiwa cha Mafia hakikuingizwa katika zile flagship project kwa ajili ya Mpango wa Pili wa Maendeleo, kwa maksudi kabisa! Mimi nilikuwa naiona Mafia kama ndiyo Zanzibar mpya! Tuifungue kiutalii Mafia ili watalii waje.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale tuna matatizo mengi na tunahitaji investment ndogo sana kuifungua Mafia. Barabara inayotoka Kilindoni mpaka Rasimkumbi kilometa 55 ikitengenezwa hiyo ikitiwa lami pamoja na bandari yetu na ndugu yangu Ngonyani pale ananisikia, kuhusu bandari ya Nyamisati, Mamlaka ya Bandari imetenga nafahamu kwamba bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ile, ikikamilishwa sambamba na bandari ya Kilindoni na kuongezwa kwa runway, airport ya Mafia…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Maliasili na Utalii. Mheshimiwa Waziri nianze kwa kuunga mkono hoja yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili suala la utalii ni suala ambalo lipo interconnected, tunazungumzia utalii ambao uko under utilized. Utalii ili uwe utalii, utalii ili uweze kufanya kazi sawasawa ni lazima sekta nyingine saidizi ziweze kusukuma twenda sambamba, kwa mfano, suala la miundombinu kuanzia barabara na maeneo mengine ya usafiri, hata huduma za viwanja vya ndege. Matatizo yetu ya usafiri na utalii yanaanzia pale airport ya Dar es Salaam na Kilimanjaro. Mtalii anakuja anakutana na mazingira ambayo ni very unfriendly, hawezi kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtalii anakaa anasubiri wale wanaochukua visa on arrival anakaa masaa matatu, mwingine anakaa kwenye foleni pale airport yenyewe, kuna joto, air condition hazifanyi kazi anaanza ku-experience matatizo akiwa pale kiwanja cha ndege. Sasa tunapozungumzia kukuza utalii tuangalie na aspect kama hizi tuhakikishe kwamba vituo vyetu vya airport na maeneo mengine ambayo watalii wanakuja wanaanza ku-experience mambo mazuri, pamoja na vitanda kule kwenye hoteli zetu ziwe za kutosha na miundombinu mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii dhana ya utalii tumejikita zaidi kuangalia mbuga pamoja na Mlima Kilimanjaro na vivutio kama hivyo. Lakini dhana ya utalii ni pana zaidi ya Mlima wa Kilimanjaro na mbuga. Kwa mfano, mimi natokea kisiwani Mafia, Kisiwa cha Mafia ni kisiwa tajiri sana kwa utalii, lakini mazingira ili uingie Mafia ni magumu kweli kuanzia usafiri kwa maana usafiri wa bahari na usafiri wa ndege. Lakini kubwa zaidi ni namna gani Serikali inatangaza utalii katika maeneo mbalimbali ya vivutio hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia tuna samaki anaitwa a whale shark au kwa jina lingine la Kiswahili anaitwa Potwe, samaki huyu ana tabia kama za dolphin, ni samaki friendly anaweza akaogelea na watalii, hana matatizo. Lakini dunia nzima samaki huyu anapatikana Australia na Mafia tu. Ni wangapi miongoni mwa Watanzania tunalijua hilo kwa utalii wa ndani peke yake ikilinganishwa na utalii wa nje? Kwa hiyo tunahitaji kwanza kutangaza na kuwekeza katika miundombinu ili vitu hivi vinapokuwa connected pamoja, basi utalii wetu utasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia kuna vivutio mbalimbali kama scuba diving, sport fishing na utalii wa kwenda kuangalia papa Potwe, lakini bado Serikali haijatia mkazo kuweza kutusaidia kutangaza utalii huu. Kikubwa zaidi Mheshimiwa Waziri pale kisiwani Mafia hatuna hata Afisa wa Utalii utawezaje kukuza utalii kwenye destination muhimu kama ya Mafia bila ya kuwa na Afisa wa Utalii wa Wilaya? Tumelizungumza hili sana, tumeandika barua lakini mpaka leo hatujapata Afisa wa Utalii.
MWENYEKITI: Ahsante muda wako ulikuwa ni dakika tano tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuanza kwa kuunga mkono hoja. Pili, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri Profesa Jumanne Maghembe na Naibu wake Engineer Ramo Makani kwa hotuba nzuri na yenye kuleta matumaini kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali sikivu ya CCM kutanua wigo wa vivutio vya utalii kwa muda mrefu kumejengeka dhana kuwa utalii maana yake ni mbuga za wanyama na maeneo ya fukwe peke yake. Dhana hii si sahihi, kwani utalii una wigo mpana zaidi. Kwa mfano katika jimbo langu la Mafia (Kisiwa) kuna samaki aina ya papa mkubwa sana anaitwa Mhaleshark (Potwe) ni one of the species of shark, papa huyu ni adimu sana duniani, kwa sasa anapatikana Australia na Mafia tu dunia nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Australia ni ghrama kubwa kwa mtalii kwenda kumuona samaki huyo na moja ya sifa za whaleshark ni papa rafiki ana tabia zinazofanana na dolphin (pombuwe) mtalii anaweza kuogolea naye bila ya kupata madhara yoyote ile. Hivyo mtalii Australia anatumia gharama kubwa ikiwa ni pamoja na kukodi helikopta kwenda maeneo ya mbali sana kuogolea na papa. Lakini kwa upande wa Mafia papa huyu anaonekana umbali usiozidi mita 300 kutoka bandari kuu ya Kilindini Mafia. Ombi letu wana Mafia Serikali kupitia Bodi ya Utalii itusaidie kuutangazia ulimwengu upatikanaji na papa huyo ili kuongeza watalii wengi Mafia sambamba na maboresho ya hoteli zetu za kitalii na miundombinu ya kuingia na kutoka Mafia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uvunaji wa mikoko katika Kisiwa cha Mafia mwekezaji Tanspesca amewekeza kiwanda cha kamba katika kijiji cha Jimbo na kupewa kibali na Wizara ya Utalii kukata baadhi ya mikoko. Tunaiomba Wizara sehemu ya mapato yatokanayo na kukatwe kwa mikoko hiyo ibaki katika Halmashauri ili kuweza kusaidia shughuli za uhifadhi katika Kisiwa cha Mafia ikiwemo kupanda mikoko mingine kufidia ile iliyokatawa.
Suala lingine ni kukosekana kwa Afisa Utalii katika Wilaya ya Mafia. Pamoja na potential kubwa ya utalii katika Wilaya ya Mafia bado mpaka sasa hatuna Afisa wa Utalii wa kuratibu shughuli za utalii kisiwani Mafia, tunaomba Wizara kulifanyia kazi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine nawashukuru Waziri na timu yake yote na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mahiga, Naibu wake na timu nzima ya Wasaidizi wao katika Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia hoja kwa kuelezea masikitiko yangu ya utoaji wa Visa katika Balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia tunataraji Serikali sasa imefika wakati tuanzishe utaratibu wa kutoa Visa online, utaratibu huu sasa wa watu kutakiwa waende wenyewe moja kwa moja ni wenye usumbufu na umepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Wizara ione umuhimu pia wa kufungua ofisi za ubalozi wa Tanzania Korea ya Kusini, kule kuna potential kubwa ya kunufaika na fursa za teknolojia na watalii kutembelea nchi yetu. Pia Balozi zetu kutumika vizuri kwa kutangaza Tanzania kiutalii na fursa nyingine za kibiashara ili nchi yetu inufaike na uwepo wa Balozi hizo badala ya utaratibu wa sasa wa kutoa Visa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia ione umuhimu wa kuongeza kasi ya kujenga au kununua majengo kwa ajili ya Balozi zetu wenyewe, baada ya miaka 55 ya uhuru badala ya kuendelea kupanga wakati nchi nyingine ndogo kama Eritrea zimejenga nyumba zao wenyewe. Umefika wakati sasa Serikali iongeze kasi ya ujenzi au ununuzi wa majengo yetu wenyewe kwenye Balozi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii ili nami nipate kuchangia Hotuba za Bajeti mbili hizi, Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na afya njema. Nielekeze pongezi zangu kwa Mheshimiwa Waziri, George Simbachawene pamoja na dada yangu, Mheshimwa Waziri, Angella Kairuki kwa hotuba nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, teknolojia inakuwa kwa kasi sana siku hizi. Leo tumeshuhudia maelezo hapa mtu anamaliza semester mbili ndani ya miezi minne, habari kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo nimefunga, nimefunga kwa maana nina swaumu au nimejizuia kula. Nimefanya hivyo kwa makusudi tu ili nimwombe Mwenyezi Mungu aniongoze katika haya nitakayoyazungumza leo niseme iliyo kweli, basi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu ambacho nakiamini cha Quran, Sura ya 33, Aya ya 70 baada ya audhubillah mina shaitwan rajim, Mwenyezi Mungu anasema Bismillah Rahman Rahim; ya ayuha ladhiina aamanuh, takkullah wakulu kaulan sadida. Hii ni Aya ya Mwenyezi
Mungu. Tafsiri yake; Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu, muabuduni Mwenyezi Mungu na semeni kauli zilizo za kweli’”
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mwenyezi Mungu aniongeze niseme ile iliyo ya kweli. Wilaya ya Mafia, Hospitali ya Wilaya ya Mafia ambayo mimi ni Mbunge wao haina huduma ya X-ray takribani miaka minne sasa. Nilipokuwa najinadi niliwaahidi wananchi wa Mafia kwamba
nikipata fursa hii nitajitahidi kushirikiana na watu mbalimbali Hospitali ya Mafia iwe na X-ray mpya kabisa. Nimetimiza, true to my words, nimetimiza ahadi hiyo, mwezi wa Nne mwaka wa jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa masikitiko makubwa sana huu ni mwezi wa Nne mwaka 2017. Mwezi wa Nne mwaka 2016, X-ray machine ile mpya imefika Mafia na katika nukta hii kwa namna ya kipekee kabisa ningeomba nitambue msaada mkubwa sana aliyeutoa mama yetu kipenzi, Mheshimiwa Salma Kikwete alipokuja Mafia. Sina uhakika kama kanuni zinaruhusu Mbunge anayeongea ampigie makofi Mbunge aliyekaa, lakini naomba Bunge tumpe makofi makubwa sana Mheshimiwa mama Salma.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya X-ray ile kufika Mafia zikaanza figisufigisu. Mtu wa kwanza; na bahati mbaya simwoni hapa; Mheshimiwa Waziri wa Afya; akatuambia kwamba hamruhusiwi kuifunga kwa sababu tuna mkataba na Kampuni inaitwa Philips na kampuni hii ndiyo pekee
inayoruhusiwa kufanya ukarabati na matengenezo ya ile Xray ya zamani. X-ray ya zamani ni chakavu, ni ya teknolojia ya miaka ya 1970, ukiitengeneza inaharibika. Sasa leo wanasema kuna mkataba na Philips, mpaka leo umefika sasa mwaka mmoja X-ray ile bado ipo kwenye stoo, nawauliza wahusika wanatuambia mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mafia ni kisiwa, huna namna kusema kwamba labda mgonjwa utamhamishia hospitali ya jirani, sasa wagonjwa wetu sisi referral hospital yetu lazima umpandishe kwenye boti kwa masaa tano kwenda, referral hospital Temeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa huko wakati wa Pasaka, tumepeleka wagonjwa wawili Hospitali ya Temeke, tunafika Temeke na kwenyewe nako tunaambiwa X-ray ni mbovu kwa zaidi ya mwezi mmoja, haohao Philips. Tunawauliza wahusika wanasema mkataba na Philips umekwisha toka mwaka wa jana. Mafia tunazuiwa tusifunge kwa sababu kuna mkataba na Philips, Temeke wanasema X-ray mbovu Philips mkataba umekwisha, tushike lipi? Hili la Temeke watalizungumza wenyewe akina Mheshimiwa Mangungu na Mheshimiwa Mariam Kisangi na ndugu yangu
Mheshimiwa Mtolea lakini mimi najikita kwenye Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika…
T A A R I F A...
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba naipokea Taarifa ya Mheshimiwa Waziri kwa tahadhari kubwa sana. Kwanza hajanipa time frame, kwa sababu hili jambo limekuwa likienda kwa danadana kwa muda mrefu sana. Hicho chumba ambacho wamekitoa mwanzo walisema sisi wenyewe tujenge halafu tuhamishie ile mashine mpya kule. Midhali yeye amesema leo kwamba
wametupatia chumba hicho; mimi nafahamu kule hatuna chumba cha ziada; lakini kama ataweza kutupatia kingine cha kujenga haraka kwa hizo milioni 50, tutashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niliache hili suala kwa sababu nilikuwa nilielezee kwa upana zaidi. Niingie kwenye suala la pili. Kwenye ukurasa wa 11 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia migogoro ya mipaka baina ya wilaya, mikoa, vijiji na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule Mafia mipaka yetu ni bahari, hakuna namna nyingine ya kupakana na kijiji cha karibu, tunaopakana nao karibu ni ndugu yangu Bwege kule upande wa Kilwa. Tungeomba sana mipaka ya bahari ije iwekwe, kwa sababu kule mafia kuna exploration za mafuta zinafanyika, kwa kiasi kikubwa sana zimo ndani ya eneo la Mafia lakini kutokana na logistics yale makampuni yanafanya
wakitokea Kilwa. Sasa matokeo yake chochote kinachopatikana kinaonekana ni sehemu ya Kilwa wakati kimipaka, kihalisia ile ni sehemu ya Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba sana wataalam watakapokuja, sijui wanatumia vitu gani vya kisayansi ili kutofautisha mipaka kwenye bahari lakini waje watuoneshe. Kuna kisiwa kimoja kinaitwa Kisiwa cha Ukuza, kisiwa hiki ni sehemu ya Mafia, lakini shughuli zote za kijamii zinafanyika kutokea Kilwa, tungeomba sana Mheshimiwa Waziri hilo nalo atusaidie kutupatia ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati; tumeomba zahanati…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dau, naambiwa muda wako umekwisha.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongeza nyingi kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, Mheshimiwa January Yusuf Makamba na Naibu wake Mheshimiwa Luhaga Mpina
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuelezea ari kubwa ya kimazingira inayokikabili Kisiwa cha Mafia na visiwa vidogo vidogo vinavyoizunguka Mafia. Mabadiliko ya tabia nchi kwa kiasi kikubwa vinatishia kuviondoa kabisa kwenye uso wa dunia visiwa vya Bwejuu, Jibondo, Chole na Juani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la kina cha bahari limepelekea kiasi kikubwa cha ardhi ya visiwa hivyo kumeguka. Kwa Muktadhi huu natarajia Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja yake aje atueleze wananchi wa Mafia hatua ambazo Serikali inachukua katika kuokoa visiwa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia ni Kisiwa chenye vyanzo vichache vya maji lakini kutokana na kukua kwa shughuli za kijamii vyanzo hivi vimeanza kuvamiwa na mvuto hali hii inatishia upatikanaji wa maji safi na salama, nichukue fursa hii kwa namna ya kipekee kumwomba Mheshimiwa Waziri au Naibu wake kuja kutembelea Mafia ili kujionea hali ilivyo kimazingira .
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchafu unaotupwa katika Bahari yetu ya Hindi kwa kiasi unatokana na mifuko ya Plastic (maarufu kama mifuko ya rambo). Kwa namna ya kipekee kabisa napenda kuomba Serikali yangu Tukufu kupiga marufuku matumizi ya mfuko na vifungashio vya plastic
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusoma Jarida moja la uchunguzi la Kimataifa, likitoa Matokeo ya Uchunguzi ya kuonyesha kuwa kama hali ya utupaji taka baharini ilivyo sasa ikiendelea vivi hivi ifikapo mwaka 2050 ndani ya bahari kutakuwa na takataka nyingi (hususan) mifuko ya plastic kuliko idadi ya samaki. Hivyo, ipo haja sasa ya kupiga marufuku mifuko ya plastic.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji miti kwa madhumuni ya kuchoma mkaa, sasa ni janga la Kitaifa. Naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kupiga marufuku uchomaji na usafirishaji wa mkaa. Niiombe Serikali kupunguza bei ya gesi ili wananchi wengi waweze kuhama kwenye kutumia mkaa na kutumia gesi asilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niwatakie Watanzania wote kwa kusherehekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Sheria na Katiba Palamagamba Kabudi. Nianze na hali za Mahakama zetu nchini hususan Mahakama za Mwanzo. Hali za majengo, watumishi na vitendea kazi ni mbaya sana. Katika Wilaya ya Mafia tuna Mahakama ya Mwanzo moja tu na imechakaa na haina watumishi wa kutosha. Wananchi wa Mafia wanalazimika kusafiri masafa marefu kwenda kufuata huduma za Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuiomba Serikali ituongezee Mahakama za Mwanzo angalau mbili katika maeneo ya Utende na Vunjanazi sambamba na kuimarisha vitendea kazi na kuongeza watumishi wa Mahakama ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haki ya dhamana kuu mahabusu kwenye rumande zetu kuna mahabusu wengi wanashikiliwa katika mahabusu zetu wakati wapo wenye kukidhi vigezo vya kumchukulia dhamana. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja alitolee ufafanuzi hili jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo umuhimu wa Serikali kuongeza bajeti ya Wizara hii ili kuhakikisha suala la utoaji wa haki nchini linafanyika kwa weledi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakukushuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpa pongezi kubwa sana mtoa hoja, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na timu yake yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielekeze pia pongeze zangu kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zake thabiti na za dhati katika kuhakikisha kwamba analifufua Shirika letu la Simu la TTCL, imewekwa pale management ya vijana, management nzuri kabisa. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, muasaidie sana hawa katika kuwaongezea mtaji ili waweze ku-compete vizuri katika soko hili ambalo lina ushindani mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nianze kujielekeza katika katika kuchangia hotuba hii. Katika hiki kitabu, ukurasa wa 49 na 50 unazungumzia ujenzi na ukarabati wa vivuko mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mafia, sisi kule hatuna namna yoyote, lazima tupate boti au meli ya aina yoyote ili kututoa kwenye kisiwa kikubwa na kutuleta huku sehemu ya bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mwaka 2016 wakati nachangia hotuba hii, nilimuomba Mheshimiwa Waziri, naye anakumbuka kwamba sisi watu wa Mafia tuna matatizo sana ya usafiri wa kuingia na kutoka Mafia. Akatuahidi kwamba ile iliyokuwa MV Dar es Salaam, ambayo ilikuwa imeegeshwa pale, haina shughuli yoyote, tulipoiomba akatukubalia, lakini akasema ina matatizo kidogo ya kimkataba na ya kiutaalam; wakishayamaliza watatuletea Mafia iweze kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumesikia tangazo, mwenye mamlaka ameichukua ile meli, amewapelekea watu wa Jeshi, hatuna tatizo na hilo. Tatizo letu ni kwamba je, Mheshimiwa Waziri baada ya kutuondolea ile MV Dar es Salaam, katika hotuba yako, nimeisoma na kuirudia hapa kwenye maeneo ya vivuko hivi na ferry mbalimbali, hakuna mkakati wowote wa kuondoa tatizo la usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni katika kisiwa cha Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwa sababu naye anatokea kisiwani vilevile, baadhi ya maeneo mengine yamepangiwa kwa alternative route, wengine wanaona kama vile kuzunguka; mnawajengea vivuko wafupishe safari zao, lakini sisi hatuna namna, lazima tupande boti. Sasa hatusemi kwamba maeneo mengine wasipelekewe vivuko, lakini haya maeneo ambayo yana alternative route japokuwa ya kuzunguka, yasubiri kwanza mtupe kipaumbele sisi ambao hatuna namna yoyote, lazima tuvuke maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa majibu ya kusema kwamba jaribuni kuwashawishi private sector waje wasaidie, tumefanya sana na Mheshimiwa Waziri ni shahidi, tumeongea na Bakhresa, tumeongea na Zacharia, bado wanasitasita kuleta usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati. Sasa hili moja kwa moja ni jukumu la Serikali sasa, mtuletee huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye kiti chako hapo, uniandike jina langu kabisa, nitazuia shilingi mpaka nipate majibu, ni lini Serikali itakuja na mkakati thabiti kabisa kuhakikisha kwamba inapatikana meli au boti ya kisasa ili kuondoa tatizo la usafiri baina ya Nyamisati na Kilindoni Mafia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gati la Nyamisati. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, walituahidi mwaka 2016 hapa wametenga shilingi bilioni 2.5 na kweli zimekuja tumeona mkakati unaanza pale, wataalamu wapo, utafiti wa udongo umeshaanza na ujenzi na tenda imetangazwa wiki iliyopita na ujenzi utaanza hivi karibuni. Tunaipongeza sana Serikali na tunashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa gati lile utachukua mwaka mmoja kukamilika. Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, wananchi bado wanapata matatizo. Bandari ya Nyamisati haina sehemu ya abiria, kuna banda tu bovu bovu pale, hakuna vyoo, hakuna maji, hakuna hata ngazi ambayo inaweza ikarahisisha abiria kupanda kwenye boti na kushuka. Tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri kupitia Mamlaka ya Bandari, naamini wapo, watusaidie pale. Na mimi binafsi nimefanya juhudi, nimeandika barua kwa Katibu Mkuu wa Ujenzi na nimemsikia asubuhi hapa akitambulishwa, Ndugu Nyamuhanga kwamba tunaiomba ile ngazi iliyokuwa pale inatumika kwa ajili ya MV Dar es Salaam ambayo haifanyi kazi kwa sasa, mtuletee Nyamisati kwa kipindi hiki cha muda wa mwaka mmoja wakati ujenzi unaendelea, isaidie. Sijajibiwa ile barua, wala sina taarifa zozote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, ninaamini Serikali ni sikivu na Mheshimiwa Waziri sasa nalileta kwako rasmi, tunaomba sana mtupatie ile ngazi angalau kwa muda huo wa mwaka mmoja tuweze kuondoa tatizo la kupanda na kushuka katika gati la Nyamisati.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi, kilometa 55 ilikuwa ni ahadi ya Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alipokuja kuomba kura Mafia mwaka 2005 na 2010 tena na kwenye Ilani ya Uchaguzi, 2015 - 2020 imo, kwamba barabara ile itafanyiwa upembuzi yakinifu. Nimekiangalia hiki kitabu kuna mahali nimeona kuna shilingi bilioni 1.5. Tafsiri yake sijaipata, lakini naomba utakapokuja kuleta majumuisho hapa, uniambie labda hiyo ndiyo kwa ajili ya usanifu na uchambuzi wa kina kuhusu barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, hususan Mheshimiwa Naibu Waziri yeye alikuja Mafia na tukamwambia kwamba Mafia ni kisiwa, kuna tatizo la udongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kuikarabati ile barabara, wataalamu wanasema udongo uliobaki utafaa kwa miaka miwili tu, baada ya hapo utakuwa umekwisha na mkitaka kujenga barabara ya lami itabidi udongo muutoe Dar es Salaam gharama itakuwa ni kubwa sana.
Kwa hiyo, naomba sana mtuharakishie ujenzi ule wa barabara ya lami Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi kilometa 55 tu ili tusije tukakumbwa na tatizo la ukosefu wa udongo ambao unakwisha kutokana na matengenezo ya kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu alifanya ziara Mafia Septemba, 2016, tukamwambia kilio chetu, ATCL ije Mafia, usafiri ni taabu, ni gharama kubwa sana usafiri wa ndege Mafia. Round moja tu ya kwenda one way ni shilingi 160,000; kwenda na kurudi inakwenda shilingi 300,000 mpaka shilingi 320,000. Tumeona ATCL wameanza route ya kwenda Mtwara, tunaomba sana ile ya kwenda Mtwara ipitie Mafia
– Mtwara; ikitoka Mtwara – Mafia – Dar es Salaam; itatusaidia sana kutuondolea tatizo hili la gharama kubwa ya usafiri wa ndege. Tukifika sisi Magharibi pale, jua likizama Mafia, huna namna ya kutoka. Akipatikana mgonjwa huna namna ya kutoka kwa sababu ndege zinazokuja pale ni ndogo na usiku uwanja ule hauna taa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nukta hiyo labda nizungumzie tena huu Uwanja wa Ndege. Tunaishukuru Serikali iliutanua, lakini bado kuna hilo tatizo la taa. Uwanja hauna taa na ikifika usiku, akitokea mgonjwa amepata dharura, basi mjue huyo mgonjwa chance za kupoteza maisha ni kubwa zaidi kwa sababu hakuna namna ya kutoka ndani ya Mafia ila ni kupitia bahari na ukiingia kwenye boti ni safari ya saa tano mpaka sita.
Kwa hiyo, tunaomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Mafia, tukakwambia hili jambo, ukasema utalitilia kipaumbele. Nimejaribu kuangalia kwenye kitabu hiki, sijaona uwekaji wa taa na utanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia. Naomba sana wakati unakuja kuhitimisha hoja yako utuelezee mikakati ya kuhakikisha kwamba Uwanja wa Ndege wa Mafia unawekwa taa na unaongezwa ukubwa ili kuongeza fursa za kitalii pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki mbili zilizopita nilileta swali hapa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza mtoa hoja, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na timu yote iliyofanikisha mchakato wa Makadirio ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Mwenyekiti, barabara ya Airport Access Road - Kilindoni mpaka Utende Wilayani Mafia yenye urefu wa kilometa 14 pamoja na kukamilika kwake, lakini kwa masikitiko makubwa imejengwa chini ya kiwango. Ni matumaini yangu Mkandarasi atalazimishwa kuirudia barabara ile na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa kuitia hasara Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia kutokana na jiografia yake kuwa ni kisiwa, tunategemea sana Uwanja wa Ndege. Ikitokea dharura hususan nyakati za usiku, ndege haziwezi kuruka kwa kuwa uwanja hauna taa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea dharura ya mgonjwa kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, anaweza kupoteza maisha, kwani ili afike Dar es Salaam, atahitaji kusafiri kwa boti kwa takriban masaa nane hadi kumi ili afike katika Hospitali ya Rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, boti ya uokoaji katika Bandari za Kilindoni na Nyamisati ndiyo usafiri wa wengi katika Kisiwa cha Mafia. Ila hatari kubwa iliyo mbele ni kwamba hatuna huduma za uokoaji, yaani Coast guard kutokana na idadi kubwa ya wasafiri kati ya bandari hizi mbili. Tunaiomba sana Serikali iweke Kituo cha Coast guard ili likitokea jambo la dharura waweze kutoa msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu boti ya abiria kati ya bandari ya Nyamisati na Kilindoni Mafia. Wananchi wa Mafia tupo katika wakati mgumu kwenye usafiri wa kuingia na kutoka Mafia. Tumejaribu kushawishi wafanyabiashara waje wawekeze kwenye usafiri wa baharini, lakini mwitikio mpaka sasa umekuwa ni hasi mno. Hivyo tunaiomba Serikali ichukue jukumu la kutuletea kivuko cha kisasa baina ya bandari hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 2.5 na tender ya ujenzi imeshatangazwa na ujenzi utaanza muda siyo mrefu. Kwa kuwa ujenzi utachukua zaidi ya mwaka, mazingira ya sasa ya bandari ile siyo mazuri kabisa. Hakuna vyoo, hakuna jengo la abiria na ngazi ya kupanda na kushukia abiria. Niliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Ujenzi kuomba ngazi iliyokuwa ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa haitumiki ili itusaidie pale Nyamisati. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wakati wa kujibu hoja, nipate ufafanuzi juu ya ombi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kutoka Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi yenye urefu wa kilometa 55, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi; na imo katika Ilani ya CCM 2015 -2020. Nimeangalia kwenye kitabu hiki sijaona fedha zozote zilizotengwa kwa ujenzi wa barabara hii. Naomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu wananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kutoa pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mafia inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa ni ukosefu wa huduma ya x-ray.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia ni kisiwa na kutokana na changamoto ya usafiri hospitali hii wananchi wanapata taabu sana kuwasafirisha kufuata huduma ya x-ray Wilayani Temeke, Dar es Salaam. Mimi binafsi kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali nimefanikiwa kupata x-ray mpya na ya kisasa na tayari ipo Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa x- ray imefika Mafia toka mwezi Aprili, 2016 mpaka leo hii bado ipo store, haijafungwa. Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja Katibu Mkuu wanafahamu suala hili, ukweli nashindwa kuelewa ni kwa nini hamtaki kutoa ruhusa x-ray ili ifungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga chumba kipya kwa ajili ya x-ray mpya siyo wazo baya ila ombi letu ni x-ray mpya ifungwe katika chumba cha x-ray ya zamani na ile ya zamani chumba kipya kitakapokuwa tayari ifungwe. Hii itasaidia sana kwani kwa sasa wananchi wanapata usumbufu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hopitali ya Mafia pia haina jokofu la kuhifadhia maiti. Suala hili ni muhimu sana kutokana na kukua kwa sekta ya utalii na shughuli za kijamii kuongezeka, inapotokea dharura ya mtu au watu kufariki ambao siyo wenyeji kwa Mafia usumbufu mkubwa unajitokeza kama ilivyotokea kuanguka ndege ya Comoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuipandisha hadhi zahanati ya Kironywe kuwa kituo cha afya; Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mafia yenye jumla ya vijiji 23 na kata nane haina kituo cha afya hata kimoja. Tayari hatua za awali tumeshazikamilisha tunaomba Wizara sasa iharakishe mchakato huu ili Wilaya tuwe na kituo kimoja cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati za Bwejuu, Mlongo, Gonje na Jimbo zilitengewa fedha ili kumalizia mabomba, lakini mpaka sasa tumekapokea robo tu ya fedha hizo. Kwa namna ya kipekee zahanati ya Bwejuu ambayo ipo katika kisiwa kidogo cha Bwejuu ambapo hakuna huduma yoyote ile ya kitabibu, hakuna hata sanduku la msaada wa kwanza (first aid kit) tunaomba Serikali iharakishe upatikanaji wa fedha hizo ili wananchi wapatoa 1,000 wa kisiwa cha Bwejuu wapate huduma hii muhimu.

Kuhusu Mfuko wa Bima ya Afya tunaomba Serikali iboreshe CHF ili iweze kutumika mpaka ngazi ya Mkoa na pia huduma za upasuaji zijumuishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mgao wa vitanda na mashuka kipaumbele tupewe Wilaya za pembezoni kama Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri Dkt. Harrison Mwakyembe na timu nzima waliofanikisha hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, niipongeze timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa mafanikio na heshima kubwa inayoiletea Tanzania. Niiombe Serikali bila kujali matokeo ya mashindano yatakayofanyika Gabon baada ya mwezi huu, Serikali isiwatupe vijana hawa, kwani wameonesha uwezo na vipaji vya hali ya juu, kutokana na umri wao kuwa mdogo tuwekeze zaidi kwao na naona akina Samatta wengi kutoka kwa vijana hawa.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF); ni ukweli usio na shaka hali katika shirikisho hili sio nzuri, migogoro na malalamiko ambayo kwa kiasi kikubwa tulishaanza kuisahau wakati wa uongozi uliopita chini ya Rais Leodgar Chills Tenga kwa sasa imerudi kwa kasi sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri asimamie vizuri shirikisho hili na kwa kuwa watafanya uchaguzi mwaka huu wapate viongozi wazuri ambao wataipeleka Tanzania mbali kupitia mchezo huu wa soka.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Natambua Wizara hii inawajibika kwenye Wizara hii kupitia maudhui na usajili wa vyombo vya habari. Tumeshuhudia magazeti na vipindi vya runinga vinavyoenda nje ya maadili, tumeshuhudia magazeti yakiandika habari za uongo na uzushi dhidi ya viongozi, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ni muathirika wa jambo hili. Ushauri wangu, Serikali ichukue hatua kali ikiwa ni pamoja na kufungia maisha magazeti au Televisheni zinazothibitika kufanya vitendo hivi vya kuchafua majina ya watu.

Mheshimiwa Spika, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC); usikivu wa TBC Redio upo chini ya asilimia 25 kwa nchi nzima, niiombe Serikali iongeze bajeti ya TBC ili iweze kuwekeza katika mitambo na kuongeza usikivu hadi vijijini ambapo ndipo wananchi walipo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba yao nzuri ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukanda wa Kusini (Southern Circuit) upo nyuma sana kiutalii pamoja na ukweli kwamba kuna vivutio vingi vya kitalii. Kwa mfano, Kisiwa cha Mafia katika Mkoa wa Pwani kimejaaliwa kuwa na vivutio vifuatavyo:-

Kwanza kuna whale shark, samaki huyu aina ya papa (potwe) wamebaki wachache sana na katika nchi chache duniani. Moja ya sifa nyingi za samaki huyu ni rafiki kwa mwanadamu kama livyo pomboke (dolphin) na watalii wanapenda sana kucheza na kuogelea naye. Kwa sasa samaki huyu anapatikana Australia, Philippines na nchi chache za Bara la Amerika ya Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na umuhimu wake na mvuto wake kwa watalii hakuna juhudi zozote kutoka upande wa Serikali katika kumtangaza samaki huyu. Juhudi pekee ni zile zinazofanywa na mmiliki wa hoteli na mtalii mwenyewe. Tunaiomba Serikali sasa itangaze kivutio hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuna scuba diving, hiki ni kivutio kingine kinachopatikana kisiwani Mafia. Mandhari ya chini ya bahari ya Mafia imesheheni samaki wa aina mbalimbali ambazo zinawavutia watalii kuja na kufanya uzamiaji wa bahari. Tunaiomba Serikali sasa itangaze kivutio hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni sports fishing ambapo ni uvuvi wa mchezo maarufu kama catch and release ambapo watalii wanavua samaki na kupiga nao picha halafu huwarejesha baharini akiwa hai. Ni kutokana na vivutio hivi pamoja na vivutio vingine vya Kusini vya Mji wa Kilwa na magofu yake, mbuga ya Selous na hot spring Utete Rufiji; Serikali sasa ije na mpango mkakati wa kutangaza vivutio hivi vya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu. Ni ukweli usio na shaka kumekuwa na ongezeko la utalii nchini. Lakini kuna utata mkubwa namna ambavyo takwimu hizi zinakokotolewa. Nimeomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kujibu atupe ufafanuzi juu ya kadhia hii. Je, watalii hesabu inachukuliwa kwenye mipaka yetu au viwanja vya ndege na mipaka ya bandari na bandari zetu au wakati wanaingia kwenye vivutio vyetu? Je, watalii wanaoingia Zanzibar moja kwa moja na kuondokea huko huko hawa wamo katika idadi ya watalii milioni 1.2 walioingia Tanzania mwaka wa jana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa mtoa hoja, Waziri Dkt. Hussein Mwinyi kwa kutuletea hotuba nzuri sana yenye kuleta matumaini kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Kisiwa cha Mafia ambacho kipo mpakani kabisa na Comoro kule. Takribani miezi miwili, mitatu iliyopita tulipata bahati ya kutembelewa na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Mwamunyange, katika juhudi za kuhakikisha kwamba wanafungua kikosi pale cha Jeshi katika Kisiwa cha Mafia ili kuhakikisha kwamba suala la ulinzi na usalama linaimarika pale kisiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo jema sana na sisi watu wa Mafia tumelipokea kwa mikono miwili. Lakini kuna mambo mawili hapa ni vizuri niyaweke kwa attention ya Mheshimiwa Waziri ayaangalie yaweze kutusaidia ili hili jambo liwe jema zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza; site ambayo wameichagua pale sisi na wenzetu pale Wilayani tumeiona kwamba sio site nzuri kwa sababu ni katikati ya Mji wa Kilindoni pale. Lakini kuna site ambayo iko maeneo ya Jimbo takribani kilometa 30 kutoka Mjini Kilindoni pale; tulikuwa tunapendelea na tungefurahi sana kama jeshi lingekwenda kule ili kukataa hizi crush na wananchi kwa sababu kule kidogo kumejitenga na watu wapo wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini angalizo la pili tungependa pia Kikosi cha Maji kiwepo pale kwa sababu sisi tunapakana na bahari kuu na kule kuna maharamia wale wa Kisomali na pia kuna meli za uvuvi ambazo zinakuja kuvua kule bila ya kibali cha mamlaka husika. Kwa hiyo, tungependa sana kije kikosi cha maji pale ili waweze ku-patrol ile bahari na kuhakikisha kwamba hakuna aina yoyote ya uvuvi wa kuvamia wa meli kubwa zinazokuja kuvua pale Kisiwani Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ningependa nijielekeze sasa kwenye suala la vijana wanaoingia kwenye JKT. Mimi kwa ufahamu wangu kila wilaya imetengewa sehemu yake ya vijana watakaokwenda JKT kila mwaka, lakini kwa bahati mbaya na masikitiko
makubwa sana Mheshimiwa Waziri, inapofika Wilaya ya Mafia wale washauri wa mgambo sijui wanatoka wapi, sijui wapo chini yenu au wako chini ya nani, Mshauri wa Mgambo wa Mafia siku zote lazima ataandikisha vijana kutoka nje ya Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, hili tunaomba sana mwaka huu lisijirudie, na kama litajirudia basi kuna hatari ya kuvunjika kwa amani katika Kisiwa cha Mafia, kwa sababu vijana wenye qualification wapo, lakini Mshauri wa Mgambo analazimisha kuwaleta vijana kutoka nje ya Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapowachukua wale huku nyuma tunaanza kuulizwa na wazazi, vijana wamemaliza shule za kata hizi, form four wanakosa nafasi, kwa nini nafasi hizi wanakwenda kuzichukua watu wanaotoka nje ya Mafia? Serikali imefanya hivi kwa makusudi kwa sababu ya kuleta uwiano ili Jeshi letu liwe na uwakilishi mzuri, kwamba kijana kutoka kila wilaya ya Tanzania anakuwepo katika Jeshi. Sasa zinapokuja nafasi zetu sisi mshauri wako wa mgambo Mheshimiwa Waziri anatuletea watu kutoka nje ya Mafia, inatukera. kwa hiyo kwa mwaka huu sasa tunasisitiza, hili jambo lisijirudie, kama ni kuvumilia tumevumilia kwa miaka ya nyuma huko inatosha sasa, enough is enough. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima. Nielekeze shukrani zangu kwa mtoa hoja Mheshimiwa Waziri Dkt. Charles Tizeba na Msaidizi wake ndugu yangu, Mheshimiwa William Olenasha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ilibahatika kuwa na wataalam wenye kuijua Sekta yao. Nampongeza sana pia Katibu Mkuu upande wa Uvuvi, ndugu yangu Dkt. Yohana Budeba ambaye kiasili naye ni mvuvi kama mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa huzuni kidogo kwa sababu haya nitakayoyazungumza leo, kwa kiasi kikubwa sana ndiyo kilio cha wananchi wa Mafia. Kuna Taasisi ya Serikali inaitwa Hifadhi ya Bahari na naamini wapo hapa. Taasisi hii imekuwa ni kero kwa wananchi wa Mafia. Lazima nianze kusema mapema kabisa, hakuna mtu wa Mafia yoyote anayepinga uhifadhi, wote tunaunga mkono uhifadhi; lakini aina ya uhifadhi unaoendelea Mafia na hii Taasisi ya Hifadhi ya Bahari, maarufu kama HIBAMA siyo uhifadhi bali ni uporaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi kama jina lake lilivyo, wanatakiwa wahifadhi, lakini badala yake hifadhi ya bahari wamekuwa ni waporaji na wauzaji wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nimuulize ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, hawa amewatuma waje kuuza ardhi au waje kuhifadhi maeneo ya mazalia ya samaki? Tunataka aje na majibu mazuri kabisa, kwa sababu hivi sasa, hivi ninavyozungumza, hifadhi wameshauza visiwa viwili. Kisiwa cha Shungimbili kimeuzwa, sasa hivi wako katika mchakato wa kuuza Kisiwa cha Mbarakumi na baadaye wanakwenda Nyororo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Hifadhi inasema wakati wanawaondoa hawa wavuvi katika hivi visiwa sheria inasema haya ni maeneo tengefu; na maeneo tengefu hayatakiwi kuwa na makaazi ya kudumu. Wanachofanya hifadhi, wanawaondoa wavuvi, vile visiwa wanaviuza kwa wawekezaji. Sasa inapingana na dhana nzima ya maeneo tengefu. Pale Shungimbili wameuza, imejengwa hoteli ya nyota tano; usiku mmoja dola 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie, toka imeuzwa kisiwa kile, Halmashauri ya Mafia haijapata hata senti tano, hatuujui mkataba uko wapi? Tuna sababu gani sisi tena ya kuipenda Hifadhi ya Bahari?

Mheshimiwa Naibu Spika, hoteli ile ya nyota tano iliyojengwa pale, wale wanaoitwa wawekezaji wamebadilisha mpaka jina. Mheshimiwa Simbachawene nimemwona hapa, labda watusaidie wenzetu waliopo Serikalini, mamlaka ya kubadilisha majina ya maeneo, ni mamlaka ya nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, inayoitwa Thanda Hoteli, wala si majungu unaweza uka-google ukaiona, Thanda –‘T’ for tangle, ‘h’ for hotel, ‘a’ for alpha, ‘n’ for November, ‘d’ for delta and ‘a’ for alpha. Thanda hoteli utaiona pale ukiisha- google tu, unaona Thanda Hoteli Mafia. Thanda Ireland Hoteli Mafia. Hakuna kitu kama hicho Mafia. Mafia kuna Kisiwa kinaitwa Shungimbili, hakuna kisiwa kinaitwa Thanda Ireland. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie mamlaka haya ya kubadilisha mpaka jina la kisiwa wameyapata wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, wamejenga pale hawana hata building permit. Building permit anatoa Mkurugenzi wangu wa Halmashauri, yeye mwenyewe anashangaa anasema mimi naona majengo yanaota tu pale kama uyoga. Sasa tunataka kujiuliza wakati wanavichukua visiwa hivi kuvifanya maeneo tengefu, hoja ilikuwa kwamba kuna kiumbe kinaitwa kasa. Kasa anakwenda kupanda pale kutaga mayai.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo mmeshawauzia hawa wawekezaji, wameweka miamvuli pale Wazungu wanapunga hewa muda wote; huyo kasa atapanda juu kwenda kutaga mayai saa ngapi katika mazingira kama hayo? Kuna mambo ya ajabu sana yanaendelea pale Mafia. Kuna aina ya uporaji unaoendelea pale. Sasa tunawauliza ninyi mmekuja kuhifadhi, mmekuja kuuza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema wala sitatoa shilingi, lakini nitakachofanya, tutamwandikia Mheshimiwa Rais tumwambie kwamba Mafia inauzwa. Visiwa viwili vilishauzwa, watauza cha tatu, watauza na kisiwa kikubwa, mtatuhamishia sehemu nyingine kwa sababu tumewaambia miaka miwili, hamtaki kusikia. Kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana. Hata wananchi kuulizwa basi juu ya ule uwekezaji! Sheria zinasema, hawa watu wa hifadhi wamekuwa na kiburi na ni wababe sana. Wao wanaamini hiyo inayoitwa Sheria ya Hifadhi ina supersede sheria zote za nchi; Local Government Act mpaka Katiba ya nchi haimo. Wanakwambia hii hifadhi imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge, kwa hiyo sheria nyingine zote hazifai, inayofaa ni Sheria ya Hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana yule bwana anakuja pale anajenga hoteli, hahitaji building permit, hawataki kuwashirikisha wananchi, wananchi hawakuulizwa na hakuna mihtasari. Leo hapa nina hii document; nilipowauliza mbona wananchi hamkuwauliza? Wanasema wananchi tumewauliza, wakaenda kukaa na watu wanane pale Kirongwe baadaye ndiyo wanasema wananchi tumewauliza sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana nimwulize ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, kaka yangu, tena rafiki yangu sana; mambo haya yangefanyika kule Buchosa, yeye angekubali? Yeye ana visiwa kule; vingeuzwa visiwa vya Buchosa angekubali? Kwa sababu kila siku namwambia kitu hiki hiki kimoja hataki kusikia, kwa nini? Tunataka aje na majibu thabiti kabisa, kwa nini hifadhi ya bahari wanaendelea kuuza visiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo unaoitwa uhifadhi. Nenda pale Kigamboni Dar es Salaam kule Kijiji Beach, South Beach kule maeneo yale kaa kuanzia asubuhi mpaka jioni, yanapigwa mabomu utafikiri nchi iko kwenye vita na Ikulu iko pale pale. Hawa watu wa hifadhi wanaacha kwenda kukamata wapiga mabomu pale, wanakwenda kuuza visiwa kule Mafia, hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wanahamisha wananchi wa Nyororo, wavuvi wa pale, wamekaa karibuni miaka 15 wanawaondoa wanataka kuweka hoteli nyingine ya Nyota tano. Kisa nini? Wanasema sasa haya ni maeneo ya tengefu. Tunasema maeneo tengefu kusiwe na makazi ya kudumu. Kwa nini mnawatoa wavuvi halafu mnajenga hoteli? Hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jibondo, kisiwa kingine hiki; ndugu yangu Kwandikwa anafahamu sana haya. Wananchi wa Jibondo hivi sasa wako siege hawawezi kwenda kufanya shughuli zozote, wamezuiwa na watu wa hifadhi wasivue. Sasa tunawauliza, mmekuja kuwasaidia wananchi kuwahifadhi au kuwamaliza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuona kwamba uvuvi umeshindikana, wakaamua kulima kilimo cha mwani baharini. Wakalima wakapata mwani mwingi sana, wakaweka katika ma-godown yao. Imekuja meli kupakia ule mwani na kupeleka sokoni. Hifadhi ya bahari wanasema ile meli inavunja matumbawe, inaharibu mazingira. Kwa hiyo, hairuhusiwi kuingia, ule mzigo umeozea ndani. Nataka tuwaulize tu ndugu zangu, hivi ninyi hamna huruma? Hawa watu wa hifadhi hamna huruma? Watu mzigo umejaa ndani, hawaruhusiwi kwenda kuuza...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kuunga mkono itifaki ya Azimio hili na kwa namna ya kipekee kabisa niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuunge mkono hili jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Mafia, kwa kiasi kikubwa sana maisha ya watu wa Mafia ambayo ni kisiwa maisha yetu ni bahari na bahari ndio watu wa Mafia. Chochote kile ambacho kinaelekea katika kulinda na kuhifadhi bahari kwa maana nyingine hicho ni chenye kutoa manufaa na nafuu kwa watu wa Mafia. Hali ya mazingira ya bahari kwa sasa ni mbaya sana, kwa maana ya kwamba kuna baadhi ya visiwa, Mafia ni kisiwa lakini ndani yake kuna visiwa vidogo vidogo. Vile visiwa vidogo vidogo vingine vimeshaanzwa kumezwa na bahari kutokana na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya masuala ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa wadogo kule Mafia tulikuwa tunakwenda kuvua katika maji usawa wa magoti, lakini sasa hivi unaweza ukaenda maji ya kina kikubwa kabisa na vyombo na ukarudi ukiwa na kikapu kimoja au pengine ukarudi mikono mitupu. Kwa hiyo, ipo haja ya makusudi kabisa sisi Wabunge tukubaliane na tuliunge mkono Azimio hili ambalo lina nia njema na nchi yetu na mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha ifikapo mwaka 2030 ndani ya bahari na hususan Bahari ya Hindi kutakuwa na takataka nyingi zaidi kwa maana ya mifuko hii ya “rambo” na mifuko mingine ya plastiki kuliko samaki wenyewe. Kwa hiyo, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ilipotokea ile ndege ya Malaysia ikapotea na ikasemekana imeangukia baharini ndipo wataalam wakaenda kugundua mambo makubwa zaidi yaliyokuwepo chini ya bahari kutokana na uchafuzi wa mazingira, wakakuta kuna takataka nyingi mno. Tuna kila aina ya sababu kuhakikisha kwamba tunaunga mkono Azimio hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafia kuna taasisi maalum inayohusiana na masuala ya uhifadhi wa bahari maarufu kama Marine Park. Ningeomba sana na sina uhakika kama Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo yupo hapa, lakini ningeomba sana watusaidie wenzetu wa Serikali kuhakikisha kwamba ile Taasisi ya Hifadhi ya Bahari inajikita na kujiingiza zaidi katika suala la uhifadhi. Kwa sasa hivi wamekuwa wana mambo mengi zaidi kuliko uhifadhi wenyewe. Wamejiingiza katika masuala ya ukusanyaji wa maduhuli, wamejiingiza katika masuala ya ujenzi, masuala ya uwekezaji na uuzaji wa visiwa, wanajikuta mpaka kwenye the core business yao wamekuwa diverted na sasa wanashughulika zaidi na mambo ambayo hayawahusu na hayahusiani zaidi na uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kama Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi yupo hapa ahakikishe kwamba, anawaelekeza watu wa hifadhi ya bahari Mafia wajikite kwenye uhifadhi, hiyo ndiyo shughuli yao ya msingi waachane na habari ya kuuza visiwa, kuuza maeneo, mambo ya ujenzi, uwekezaji, ukusanyaji wa maduhuri hilo ni suala la TRA na Halmashauri ya Mafia tunaweza tukayafanya sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo suala la mbadala. Ndugu yangu Mheshimiwa Kitandula amekuwa akizungumza sana hapa, suala la ufugaji wa samaki. Baharini samaki wa bahari pia wanafugwa. Sasa kutokana na hali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii ili nami nichangie hotuba hii muhimu ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mwaka jana wakati nachangia hotuba hii ya bajeti nilisema hawa Madaktari wawili wa Uchumi, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Ashatu, kama tutawapa support watatufikisha mbali

sana, wengi hawakunielewa, lakini kutokana na uwasilishaji huu wa hii bajeti ambayo wengi wanaiita bajeti ya karne nadhani yale niliyoyasema mwaka jana yamethibitika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana wakati Mtemi Chenge anaahirisha Bunge, alitoa maangalizo mazuri sana, kwamba jamani hii bajeti haya ni mapendekezo, sisi tunatakiwa tutie nyama, tutoe maoni yetu. Sasa mimi nina machache ya kujazia kwenye bajeti hii nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Spika, vyanzo vya mapato, mimi natokea Mafia, kule Mafia tunavyo vyanzo vya mapato na ukusanyaji wa mapato ambao kwa mitazamo yetu tuliopo Mafia kule tunaona kwamba Serikali inapoteza mapato mengi sana. Tuna taasisi kule, inaitwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari hawa kazi yao kubwa ni uhifadhi wa bahari, lakini wamejiingiza katika masuala ya ukusanyaji wa tozo.

Mheshimiwa Spika, tungeomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango na kupitia Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wakichukue hiki chanzo, wawaagize TRA Mafia waanze kukusanya ile entry fees ya watalii wanaoingia katika maeneo ya hifadhi, tunawabebesha mzigo watu wa hifadhi ya bahari ambao si wao, kwa sababu wao wanatakiwa washughulike na hifadhi. Haya mambo ya kukusanya mapato yana wataalam na wataalam wa TRA wapo pale, Ofisi ya TRA ipo pale Mafia.

Mheshimiwa Spika, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri achukue haya maoni na amwagize Kamishina wa TRA amwaagize Meneja wa TRA pale Mafia, waanze kukusanya mapato yale kutokana na watalii. Hawa watu yale mapato wanashindwa hawana capacity, hawana uzoefu, hawana wataalam, matokeo yake pale tunakadiria kupata karibuni bilioni mbili kwa mwaka lakini wao wanakuja kutuambia kwamba tumepata milioni 700 milioni 600.

Mheshimiwa Spika, kinachoshangaza sana wanayatumia vibaya, wanarundika mle gharama za uendeshaji nyingi sana, likizo yao yamo humo, safari zao zimo humo, makongamano yamo humo na mambo chungu nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi haya mapato mwisho wa siku Halmashauri ya Mafia inatakiwa ipate asilimia 10. Sasa wenzetu wanavyorundika haya matumizi wanasema kwamba asilimia 10 hiyo baada ya kutoa gharama zote. Sasa gharama wanarundika mambo chungu mzima. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie aagize Mamlaka ya Mapato waanze kufanya kazi hiyo ya kukusanya mapato katika entry fees ya watalii kule Mafia.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linaweza likatusaidia sana kwa mapato limesemwa hapa asubuhi na Mheshimiwa Zaynab Vulu umefika wakati sasa tufungue hii Southern Circuit ya utalii kwani kuna fursa kubwa sana za utalii. Kama nilivyotangulia kusema mimi natokea Mafia, Mafia kuna fursa kubwa sana za kiutalii ikiwemo yule samaki anayeitwa potwe ambaye ni samaki maarufu sana duniani na anapatikana Mafia na Australia tu, lakini kwa bahati mbaya sana hatujaanza kumtangaza vizuri na watalii wengi wanakuja pale. Naomba sana Serikali ituangalie, tutangaze vivutio hivi, lakini sio tu kutangaza vilevile kuna tatizo la accessibility ya kuingia Mafia. Hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, usafiri wa kuingia Mafia ni mgumu, sasa hawa watalii watapita wapi, hatuwezi kila mtalii apande ndege afike Mafia, lazima wapite njia ya bahari, lakini njia ya bahari kwa bahati mbaya sana kuna matatizo, hakuna boti za kisasa, kuna magogo yale. Kwa hiyo tungeomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Waziri wa Ujenzi watusaidie sana pale Mafia kutupatia boti ya kisasa ambayo watalii wanaweza kuja, bahati nzuri Naibu Waziri wa Ujenzi Mzee Ngonyani nimemwona hapa, watupatie boti ya kisasa ili tuweze kufungua ile fursa ili watalii waje kwa wingi na wasafiri vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hilo kwa kuwa Mheshimiwa Ngonyani nimemwona suala la Gati la Nyamisati, Gati ya Nyamisati mwaka jana zilitengwa pesa hapa na nilitoa angalizo jamani hizi pesa ziende zikafanye hiyo kazi, tumebakiwa na wiki hazizidi mbili mwaka wa fedha unakwisha pesa zilitengwa, gati halijaanza kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana ndugu zetu wa Wizara ya Ujenzi...

TAARIFA ....

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, kuna tofauti kati ya Potwe whale-sharks na dolphins, kama yeye anazungumzia dolphins wanapatikana maeneo hayo aliyoyasema. Mimi namzungumzia whale-shark - potwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa watufungulie njia ya usafiri kwa upande wa Mafia, gati lile pesa zilitengwa, lakini mwaka unakwisha ujenzi haujaanza, tunaingia mwaka mwingine. Naomba sana Mheshimiwa

Waziri zile pesa zisiwe kama tena zimepotea, tutakapoingia mwaka mwingine wa fedha ule mchakato wa kujenga lile Gati la Nyamisati na kufungua fursa za utalii pale, ziweze kufikiriwa.

Mheshimiwa Spika, lingine suala la utalii kwa upande wa Mafia tulikuwa na Hoteli pale na ndugu yangu Mheshimiwa Maghembe anaifahamu. Hoteli ile ya Chole Mjini, ilifungwa kutokana na matatizo ya uendeshaji wa yule mmiliki pale. Kwa kiasi kikubwa sana yale matatizo yameshakwisha, pale ni chanzo kikubwa sana cha mapato. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI wakishirikiana kwa pamoja watufanyie utaratibu hoteli ile ifunguliwe ili Serikali isiendelee kukosa mapato.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji watalii na utalii wa Mafia zaidi ni wa scuba diving, sport fishing na vitu kama hivyo. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho hapa, aligusie hilo na kwa kushirikiana na Wizara hizi nilizozitaja ili tuweze kufungua fursa za utalii pale Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utalii pia unakwenda sambamba na miundombinu iliyo bora, barabara ya kutoka Kilindoni kwenda Rasi Mkumbi kilometa 55 na Mheshimiwa Waziri alizungumza kwa uchungu sana tunakwenda kubana matumizi, bajeti hii ni ya kubana matumizi. Nilizungumza wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mbarawa kwamba kule Mafia kuna tatizo, kile ni kisiwa kuna udongo ambao unakwisha...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na uhai kwa siku ya leo. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa wasilisho lake zuri. Mimi kwa haraka haraka nitaanza na hili ambalo Senator Ndassa jana alilizungumza kwa undani sana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda wa siku nne hapa tumekuwa tukijadili huu Mpango wetu, lakini wengi waliojikita katika kujadili hili wamezungumza suala la ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma. Sasa mimi sitaki kurudia kwenye mjadala huo kwa sababu mengi yameshasemwa. Huu Mpango na Waziri mwenyewe anakiri kwamba katika hili hatukufanikiwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nimuombe tu Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hoja yake pengine Bunge hili linasubiri sana kusikia kauli yake moja tu akisema kwamba anakivunja kile Kitengo cha Sekta Binafsi pale Wizarani. Aweke timu mpya pale, tuanze upya na hata kama ikiwezekana tumtafute mtaalam wa nje aongoze kile kitengo na hili wala sio jambo geni. Tulipoanzisha TANROADS lilikuwa ni jambo jipya, lilikuwa jambo gumu, tukamuweka raia wa Ghana pale akaanzisha kile kitengo na sasa wenyewe tumeweza kukiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa namuomba sana Mheshimiwa Waziri, vunja Kitengo cha Sekta Binafsi pale kwenye Wizara yako, tafuta wataalam hata kama ikibidi kutoka nje, tuanze upya, haiwezekani huu mwaka wa tano tunaimba tu sekta binafsi, sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hali ya kawaida hata wewe mwenyewe unatakiwa uwe embarrassed katika situation inavyokwenda sasa hivi. Kila siku tukisoma makabrasha hapa UDART! Hivi UDART ile kweli unaweza sema kwamba ni mfano mzuri wa ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi? Mheshimiwa Waziri kama ninakuuliza pale, hiyo sekta binafsi mle kwenye UDART imeingiza kiasi gani unaweza ukanijibu? Katika hali ya kawaida zile pesa ni za World Bank na yule aliyeingia pale sijui Simon nani sijui ndiyo sekta binafsi pale ni ubabaishaji mtupu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku mimi toka niko Chuo Kikuu nasikia habari ya Chalinze - Dar es Salaam Road Toll mpaka leo iko kwenye makaratasi. Sasa anzisha kitengo kile upya, wape malengo walau kwa mwaka basi hata tukipata mradi mmoja mkubwa mimi naamini tutasonga mbele sana. Haiwezekani Chalinze - Dar es Salaam miaka sijui sita, hiyo UDART mimi kwangu wala siihesabu kama ni mfano mzuri wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na sekta ya umma. Lakini katika hali ya kawaida hata hiyo habari inayoitwa kiwanda sijui ya madawa katika hali ya kawaida hicho nacho pia hakiwezi kuwa ndiyo mfano mzuri. Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana utakapokuja hapa uanze na kuvunja kile kitengo tuanze upya, wape malengo wakishindwa toa weka wengine mpaka tutafanikiwa, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimeangalia huu Mpango, kuna eneo umesema eneo la kuimarisha utalii, biashara na masoko, ujenzi na ukarabati wa kutengeneza miundombinu na kutangaza vivutio vya utalii hususan kile kinachoitwa Southern Circuit, kwa maana ya kwamba utalii wa maeneo ya Kusini. Mimi nitagusia sehemu ndogo tu. Najua eneo la Kusini ni pana sana, nitagusia Kisiwa cha Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Mafia ni maarufu sana kwa utalii, tuna samaki pale anaitwa potwe (whale shark), ni samaki ambaye ni wa ajabu na ni mkubwa kuliko samaki wote ukiondoa nyangumi ambaye si samaki na samaki huyu hajatangazwa. Lakini hata kama mkitangaza bado kuna suala la miundombinu. Kwa masikitiko makubwa sana Bandari ya Nyamisati huu sasa ni mwaka wa pili bajeti ya mwaka 2015/2016 zimetengwa shilingi bilioni 2.5 mpaka mwaka umekwisha bandari haijajengwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba hii nzuri leo asubuhi, nielekeze pia na pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais kwa namna anavyokitendea haki Kiti chake nasi Watanzania tunampa pongezi nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu Septemba, 2016, alifanya ziara katika Kisiwa cha Mafia, ziara yake kwa kweli imetuletea faraja kubwa sana na changamoto nyingi sana ambazo zilikuwa zinatukabili katika kisiwa chetu aliweza kuzifanyia kazi na kuzitatua. Hata hivyo, alipoondoka aliacha viporo kama vitatu, vinne hivi na tukakubaliana kwamba atatuita Ikulu twende tukaongee kuyamaliza haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nianze kwa kumkumbushia Mheshimiwa Waziri Mkuu viporo hivyo. Suala la kwanza leo asubuhi lilizungumzwa hapa. Suala la tatizo la X-Ray la Kisiwa cha Mafia unaingia sasa mwaka wa sita Mafia hakuna X-Ray na unaingia sasa mwaka wa pili toka Mbunge wa Mafia anayeongea sasa hivi alete X-Ray yake mwenyewe mpya ambayo haijafungwa mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri asubuhi hapa ameliambia Bunge lako kwamba Kampuni ya Philips italeta mashine za X-Ray kwa ajili ya hospitali za mikoa mwezi Juni na wao ndiyo wanawajibika katika kuzi-maintain kwa maana ya kufanyia matengenezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingetaka kwenda mbali sana, namwomba sana Mheshimiwa Waziri badala ya kusubiri hizo X-Ray za ku-import kutoka nje awaambie Philips kwanza wakatengeneze X-Ray ya Mafia mwaka wa sita huu haijatengenezwa. Hili halihitaji kusubiri Juni kama wao wapo hapa basi waende wakaitengeneze X-Ray ya Mafia, kwa sababu imekuwa haifanyi kazi kwa miaka sita na mimi leo ndiyo mara yangu ya mwisho kulisema hili jambo ndani ya Bunge hili, nitakachokifanya baada ya hapa nakijua mimi mwenyewe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu tulimfikishia kilio chetu ni tatizo la mgogoro baina ya hifadhi ya bahari ya Mafia na Halmashauri ya Mafia. Ningeomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Ulega nilimwona Mheshimiwa Waziri Mpina ametoka, lakini Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Abdallah Ulega namwona naomba anisikilize vizuri kwa sababu alikuja Mafia ameliona hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mafia ni Halmashauri ndogo sana na maskini, ina vyanzo vya mapato vichache sana, kuna Taasisi inaitwa Hifadhi ya Bahari. Ni taasisi ambayo staffing yake haizidi hata watu 15 lakini wanakusanya mapato kwa maana ya maduhuli kutokana na watalii wanaokuja kutembelea Kisiwa cha Mafia zaidi ya milioni 700 kwa mwaka na Halmashauri ya Mafia tunapewa asilimia 10. Halmashauri ya Mafia yenyewe kwenye vyanzo vyake vingine vyote inakusanya shilingi milioni 600. Utaona pana tatizo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi ndogo tu ambayo staffing yake haizidi hata watu 15 inakusanya shilingi milioni 700 lakini Serikali kwa maana ya Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ambayo ndiyo inawajibika na shule, inawajibika na Zahanati, inawajibika na Hospitali na wakati ule barabara na mambo mengine maji na vitu kama hivyo tunakusanya shilingi milioni 600. Eneo la utawala la Mafia limepunguzwa na Taasisi ya Hifadhi ya Bahari ya Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachokitaka na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja tuliliongea hili na akaahidi kwamba tutakutana Ikulu pale tuliongee tulimalize pamoja na Mawaziri wanaohusika. Ningeomba kwa namna ya kipekee sana hatuombi jambo kubwa, tunachoomba kwamba ule mgao basi angalau uwe wenye kufanana. Sisi ambao tuna mambo makubwa ya kuendesha tupate mgao mkubwa tupate asilimia 60 na hii hifadhi ya bahari ipate asilimia 40, kwa sababu kuna hatari Halmashauri ya Mafia ikapelekwa kule kwa Mheshimiwa Ungando, Kibiti kwa sababu hatuwezi kufikia malengo ya kukusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa zote zinakwenda kwenye Taasisi ya Hifadhi ya Bahari ambao hawawajibiki na jambo lingine lolote la maendeleo ya Mafia zaidi ya uhifadhi na Halmashauri nayo pia inafanya kazi ya uhifadhi. Ningeomba kwa namna ya kipekee sana kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu suala hili la kikao kile, tukutane ili tuliweke sawa na suala la kanuni wala siyo suala la sheria ni Waziri mwenye dhamana ya uvuvi na mifugo abadilishe kanuni tuanze kupata sasa Halmashauri asilimia 60 na Hifadhi ya Bahari asilimia 40. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine, tulilalamika kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu Hifadhi ya Bahari wanaacha kazi yao msingi ya uhifadhi na wameiingia katika masuala ya kuuza na kumiliki maeneo na wameuza visiwa. Kisiwa cha Shungimbili kimeuzwa na sasa pale kuna hoteli ya nyota saba kwa usiku mmoja ni dola elfu kumi (10,000). Kwa taarifa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Halmashauri ya Mafia haipati hata single cent kwenye mapato haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ambayo tungependa tukae na Mheshimiwa Waziri Mkuu tuyaongee, haiwezekani wao kazi yao kuhifadhi badala ya kuhifadhi wanauza maeneo na wanapouza maeneo hata huo mrabaha sijui kitu gani ambacho pengine Halmashauri tungestahili kupata hatupati hata kitu kimoja. Huu sasa unafika mwaka wa pili toka uwekezaji ule ufanywe pale na Halmashauri ya Mafia hatujapata hata senti tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa kilio chetu cha usafiri Mafia kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na naamini Waziri Mbarawa sijamwona lakini nimemuona Mheshimiwa Injinia Nditiye hapa. Nilikwenda kwake, tuna dhiki ya usafiri katika kisiwa cha Mafia, maeneo mengine tunaona watu wanajengewa vivuko na Serikali, tumejitahidi sana kuishawishi private sector watuletee boti zao binafsi hawajavutika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali kwa namna ya kipekee kabisa ichukue nafasi yake watutengenezee chombo, kule tuna sege tuko kama kwenye cage hatuwezi kutoka lazima tuvuke bahari. Hata hivyo, wanawajengea vivuko watu wengine sitaki kuwataja hapa wanajenga vivuko maeneo mengine ambayo yanapitika kwa barabara, sisi hatuna namna ya kutoka au kuingia Mafia lazima tupite kwenye kivuko, kivuko ambacho kinagharimu bilioni mbili mpaka tatu, hawataki!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mbarawa ameniahidi kwamba kwenye bajeti hii ataingiza hilo. Sasa nataka atakapokuja kujibu hotuba hii aniambie na Mheshimiwa Nditiye nimemwona watuambie watajenga kivuko mara hii au hawajengi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha atusaidie katika hilo kwa sababu imeshafika wakati sasa ni wakati wowote kule ni kama timing bomb, yale magogo tunayosafiria yale ambayo siyo salama wakati wowote yatazama na watu watapoteza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifikia hapo tunasema Mheshimiwa Nditiye, Mheshimiwa Mbarawa, Waziri wa Fedha mtakuwa masuulu, masuulu ni neno la Kiarabu, maana yake mtakuwa responsible na hiyo dhambi, kwa sababu wanawapandisha watu katika magogo, pesa wanatenga katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kupata vivuko vya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine pale, Mafia ni eneo dogo sana, kuna viboko wametoka kwa Mheshimiwa Ungando wamekuja Mafia pale, wameshafikia 40 sasa hivi. Kilio hiki tumekisema toka alipokuwa Waziri Mheshimiwa Maghembe, wanakula mipunga ya watu, wanakula mazao ya watu na kilio tumekileta Wizarani.(Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi wiki mbili zilizopita, Mwenyekiti wangu wa Kata wa CCM, Kata ya Ndagoni ameuawa na kiboko. Tumetoa taarifa mpaka leo wataalam wamekwenda pale badala ya kuwafanya utaratibu wa kuwavuna au kuwafanyia relocation wale kwa sababu Mafia eneo ni dogo hawawezi kukaa. Wapigeni sindano walale muwahamishe muwapeleke huko Rufiji, ndiko kwenye origin yao, pale sisi nafasi yetu ni ndogo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa wamekuja wataalam pale wameishia kupiga picha, je, nami namwuliza Mheshimiwa Hasunga anasubiri mpaka watu wangapi wafe na viboko ndiyo watakuja kuwaondoa wale viboko pale Mafia. Hili nalo pia na yeye pia utakuwa masuulu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme na nashukuru nyuma yangu yupo Profesa hapa. Suala la umeme vijijini, Profesa alituahidi lakini leo hayupo, naamini Serikali ni moja. Walituahidi kwamba visiwa vidogodogo vyote vitapata umeme unaotumia nguvu ya jua kwa maana ya solar. Kisiwa cha Jibondo, Kisiwa cha Bwejuu, Kisiwa cha Juani na Kisiwa cha Chole. Mheshimiwa Dkt. Kalemani ahadi hii naye alinihakikishia kwamba tutapata umeme mpaka sasa sijaona dalili zozote, naye pia atakuwa masuulu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara, Kisiwa cha Mafia siyo kidogo hivyo, kuna barabara ambayo ina urefu zaidi ya kilometa sitini pale…..

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nami nianze pale alipoishia Chifu Kadutu kwanza kumpongeza mtoa hoja wetu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yake yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu mapema tu kwamba Wizara hii imepata bahati ya kupata Mawaziri ambao ni wapole, lakini watendaji sana kuliko kuongea. Naamini wanaitendea haki nafasi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wenyewe ni mfupi, nitakwenda kwa haraka kidogo, nianze na ujenzi wa gati la Nyamisati. Tunashukuru kwenye kitabu tumeiona humu na mkandarasi ameshafika pale na kama alivyosema kwenye hotuba yake Mheshimiwa Waziri kwamba kazi itaanza mwezi ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wasiwasi wangu ni mdogo tu kwamba anaonekana mkandarasi huyu katika kuji-mobilize pale ameanza kwa kusuasua, anakuja na magari na vifaa vichache sana. Ningeomba aongeze spidi kwa sababu hali ya bandari ya Nyamisati ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni shukurani vilevile tena kwa Serikali angalau kwenye kitabu tumeona kwamba meli ya Nyamisati - Kilindoni sasa inaelekea kujengwa. Tunaishukuru sana Serikali wametenga shilingi bilioni tatu ingawa tunaambiwa itagharimu shilingi bilioni saba, tutamalizia mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mdogo tu kwenye hili. Mheshimiwa Waziri hali ya usafiri baina ya Kilindoni na Nyamisati ni mbaya sana. Tunafahamu nia ya dhati na nia nzuri ya Serikali katika kujenga kivuko hiki kipya lakini kitachukua zaidi ya mwaka mmoja kuwa tayari. Katika kipindi hiki cha mpito, tunaiomba kwa namna ya kipekee kabisa Serikali iangalie namna gani tunaweza tukaishi ndani ya mwaka mmoja na nusu huu tukisubiri kivuko ambacho kinatengenezwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanaweza wakatupatia hata vivuko vya jeshi au sehemu zozote ambazo tayari wana vivuko vya ziada watuletee Mafia angalau tuanze kwa kipindi hiki ambacho kivuko chetu kinatengenezwa tuweze kutumia mpaka hapo kivuko chetu kitakapokuwa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi ya TEMESA anayoiongoza Mheshimiwa Waziri nashangaa sana, nia yake ya dhati na nia ya Serikali tunaiona lakini inaonekana limekuwa kama ni jeshi la watu watatu katika Wizara hii. Hawa TEMESA ni watu wa aina gani mbona hatuwajui? Jambo hili la kujenga meli kwa ajili ya Mafia tulitarajia watakuja Mafia wakae na wadau tuwaambie aina gani ya chombo ambacho kitatufaa watu wa Mafia kwa sababu kuna changamoto tofauti ya kutoka kwenye bahari na kuingia kwenye mto, kina kinaweza kikawa kinapungua, aina ya cargo, aina gani ya meli itakayotengenezwa, itabeba abiria wangapi, itabeba mizigo tani ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kama Waziri anapambana peke yake lakini taasisi yake ya TEMESA haimuungi mkono, hawajafika Mafia, kwa DC, kwa Mbunge wala kwa DED, hatujui hii meli mtaitengeneza katika specification zipi bila ya kuwashirika watu wa Mafia wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata mashaka sana na TEMESA kama kweli wana nia ya dhati ya kusaidia katika jambo hili. Kwa taarifa katika magari yanayotengenezwa pale Wilayani Mafia yamepelekwa TEMESA huu mwaka sasa wa nne, magari yale yako kule, hayajatengenezwa, yalikwenda kule kwa matatizo ya kama Sh.10,000,000 sasa hivi tunaambiwa yanagharimu zaidi ya Sh.40,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magari yale yametushinda yako TEMESA, vifaa vimeibiwa, spare parts zimenyofolewa, tunaambiwa chukueni gari lenu, lipieni gharama za ku- maintain ile gari pale mkatengeneze wenyewe. Kwa hiyo, nina wasiwasi sana na utendaji wa kazi wa hii taasisi ya TEMESA, Mheshimiwa Waziri atupie macho hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu taasisi hii ya SUMATRA. Mafia nadhani ndiyo itakuwa ni Wilaya pekee au eneo pekee katika nchi hii ambapo ukitaka kusafiri kwa boti lazima ufanye booking wiki moja kabla. Kwa sababu wameweka masharti pale ya kupakia mwisho abiria 50 na katika population ya watu karibu 70,000 kusafiri watu 50 kwa siku moja ni changamoto kubwa, watu wako foleni wanasubiri kusafiri zaidi ya wiki. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nami pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na afya kuweza kukutana leo. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri leo asubuhi, lakini nilikuwa nataka nianze tu na ushauri mdogo tu kwake. Hii Wizara haitakiwi kuendeshwa kwa operations. Naomba sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watendaji, wafahamu kabisa kwamba Wizara hii haitakiwi kuendeshwa kwa operesheni kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, operesheni zipo katika vikosi vya jeshi na kwenye theater za mahospitali. Kule ndiyo kuna operesheni. Wamefanya operesheni ya kwanza na ya pili, inatosha. Watoe elimu sasa, wasijikite kwenye operesheni kila siku, itakuwa kila siku kazi yao wanaifanya kama fire brigade sasa. Kazi yao ni kuzima moto tu. Waende wakatoe elimu. Nitatoa mfano mdogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la mitungi ya gesi limezungumzwa sana hapa. Mimi natokea Mafia, mwaka huu peke yake nimeshapoteza wavuvi zaidi ya watatu, wamekufa. Wamepiga marufuku kokoro, wameruhusu ring net ambapo watu wanakwenda katika kina kirefu cha mita 50, wakati huo unatarajia mvuvi aende aka-dive mita 50 chini bila ya kutumia mtungi wa gesi. Maana yake una-condemn to death, hakuna tafsiri nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa upande mwingine wanasababisha vifo kwa hawa wavuvi wetu. Sasa wanapokuja na hoja kama hizi za kusema kwamba wavuvi wasitumie mitungi ya gesi, mita 50 sijui wenzetu waliokuwa kwenye comfort zone, kwenye viti vyenu vya kuzunguka huko na Watendaji Maofisini sijui kama hawa wataalam wanakwenda kwa wavuvi na kuongea nao. Bahati nzuri kuna Chama cha Wavuvi na Wawakilishi wao, wapo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwa Mheshimiwa Waziri hebu wapate nafasi waende wakaongee na hao wavuvi wawaambie anayekwenda kuchukua majongoo kule chini ni nani na anayekwenda kuvua ni nani? Haiwezekani kosa la mmoja wakawahukumu wavuvi wote. Siyo sawa kabisa. Kama kuna dereva ameendesha gari akiwa amelewa, huwezi kufungia leseni za madereva wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inashangaza sana kama kuna wavuvi wanatumia mitungi ya gesi, wanafanya diving, wakifika chini kule wanachukua yale majongoo bahari, wa-deal na hao tu, wasiwazuie wote. Matokeo yake sasa tunapoteza watu na wavuvi wanafariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la hifadhi ya bahari nimekuwa nikilizungumza sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, ameanza vizuri sana, ametuletea mtendaji mpya pale, nami natarajia kwamba tutakwenda vizuri, lakini lazima zile changamoto ambazo amezikuta pale azifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri yetu ya Mafia na Mheshimiwa Ulega anafahamu, alikuja Mafia. Tunasisitiza siku zote, kanuni zao zinatuumiza kule Mafia. Leo Mafia, Halmashauri yangu inakufa. Hifadhi ya bahari, taasisi yenye staff wasiozidi 15 wanakusanya zaidi ya shilingi bilioni moja kutokana na maduhuli. Sisi Halmashauri ya Mafia ambao ndiyo Serikali, tunakusanya shilingi milioni 600. Ile Halmashauri inakufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumewaambia siku zote, wabadilishe ile kanuni, sisi tunataka asilimia 10 tu ya maduhuli yale. Nami naamini amekuja mtendaji mpya na pia Waziri mpya pale, wakae wabadilishe hii kanuni. Haiwezekani sisi Halmashauri ambao tunaendesha mambo mengi tupate asilimia 10 tu halafu Hifadhi ya Bahari ambayo staffing yake haizidi watu 15, wanachukua pesa chungu nzima. Kwa hiyo natarajia Mheshimiwa Waziri angalau mara hii kilio hiki watakisikia, wakabadilishe kanuni. Suala ni kanuni tu, wala siyo sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka jana naongea na Mkurugenzi wangu ananiambia mapato ya Halmashauri ya Mafia mwaka wa fedha unaisha mwezi ujao yako chini ya asilimia 47 na Waziri Mkuu bahati mbaya leo hayupo, lakini alishasema Halmashauri yoyote yenye kukusanya chini ya asilimia 80 inafutwa. Kwa hiyo, Halmashauri ya Mafia inakwenda kufutwa kwa sababu tu Hifadhi ya Bahari imechukua vyanzo vyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami katika kuongezea hili, nataka nisisitize, bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha yupo hapa, yale maduhuli yakusanywe na TRA inakuwaje sisi pale tuko watu wawili; kuna Hifadhi ya Bahari na kuna Halmashauri ya Mafia, lakini Hifadhi ya Bahari ndiyo wanakusanya halafu wanatoa gharama. Kwenye gharama mle sijui wanaweka night, safari, wanaweka maposho makali makali, halafu wakija wakitoa sasa wanasema tumepata shilingi milioni 700.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka chanzo hiki Mheshimiwa Waziri wa Fedha akichukue, TRA waende wakasimamie makusanyo ya maduhuli yanatokana na watalii kule Mafia. Hapo ndiyo itakuwa salama. Vinginevyo, tunaibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri leo asubuhi alikuwa akijibu swali hapa akawa anapata taabu kidogo katika kuelezea hawa samaki. Mimi sifahamu sana kuhusu samaki wa maziwani huko; furu, sijui nembe na gogo; sifahamu sana kuhusu hawa samaki. Ila kule baharini kuna misusa, ngawala na kuna samaki wadogo wadogo. Sasa tunaomba watupe tafsiri, tunawavua kwa nyavu zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali asubuhi alisema hapa kwamba hawa samaki wengi; nembe, sijui gogo ni samaki wapya waliokuja ziwani. Kwa hiyo, sheria ilianza halafu baadaye samaki ndiyo wakaja wakahamia. Sasa kama samaki walikutwa na sheria, kwa nini wameanza operesheni wakati wakijua hawa samaki walikuja baada ya sheria?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nami nianze kwa kuwapongeza sana watoa hoja, Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla na wasaidizi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natambua sana kwamba Mawaziri wa Serikali ya CCM ni wasikivu sana. Kwa bahati mbaya sana Mawaziri wa Wizara hii, Waziri na Naibu wake nashindwa kuelewa sijui kwa nini hawataki kunisikiliza mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la viboko waharibifu katika kisiwa cha Mafia nimeshalisema kwa Mawaziri wote wawili zaidi ya mara tano. Humu ndani pia nimeshalizungumza zaidi ya mara mbili lakini majibu ninayopata ni ya kusikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali katika Kisiwa cha Mafia ni mbaya sana. Nilisema kwamba Mafia; na wala siyo suala la kusema ni suala ambalo linafahamika; Mafia ni kisiwa eneo ni dogo viboko wamezaliana wameshafika zaidi ya 40 sasa, viboko wameshaua mpaka wananchi licha ya kuharibu mazao. Wanakwenda wataalam wanapiga picha, wanaangalia, wana-camp siku mbili, siku tatu wanarudi. Hali bado ni mbaya sana, shughuli za maendeleo zimesimama, wananchi hawafanyi kazi, wanafunzi hawaendi mashuleni; viboko imekuwa ni hatari kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho wamekwenda kiasi cha wiki mbili zilizopita wakaua kiboko mdogo, ni kama ndama wa kiboko. Sasa hii siyo rocket science, eneo dogo, viboko wengi; kuna options mbili tu; tuwavune ama muwakamate muwahamishie katika maeneo ambayo wanaweza waka-arrange vizuri bila matatizo yoyote. Sasa tusisubiri, nilisema hapa tena kwa uchungu kabisa, jamani mnahitaji watu wangapi wafe ndipo mwende mkawaondoe wale viboko pale Mafia? Hali sio nzuri. Mheshimiwa Waziri leo hii mimi mara yangu ya mwisho kulisema humu ndani hili jambo, siku akifa mtu mimi nachukua familia yote nakuletea wewe Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 61 wa kitabu hiki cha Mheshimiwa Waziri limezungumziwa suala la miradi ya kusimamia maliasili na kuendeleza utalii wa Kanda ya Kusini unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Nilikuwa na maoni na ushauri kwenye hili. Natambua kwamba sasa hivi wako katika mchakato wa usanifu, basi kuwe na kipengele cha utalii wa maeneo ya fukwe ambayo katika hili huna namna ukakiacha Kisiwa cha Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Mafia kimejaliwa kuwa na vivutio vingi sana vya utalii akiwemo samaki anayeitwa papa (whale shark) kwa kizungu. Ni samaki ambaye anapatikana maeneo machache sana duniani. Pamoja na sifa za papa kuwa ni mkali lakini aina hii ya papa ni mpole sana, ana tabia kama za dolphin, anacheza na watalii, anaogelea nao na wala hana madhara nao, wanapatikana Mafia peke yake lakini nani anayejua kuhusu papa (whale shark)? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu muangalie namna gani mnaweza mka-promote hivi vivutio vinavyopatikana katika Kisiwa cha Mafia. Vivutio hivi viko vingi, kuna sport fishing, kuna maeneo mazuri sana ya diving, kuna fukwe nzuri, kuna magofu ya kale, kuna mji unaitwa wa Kisimani Mafia, mji maarufu sana ambao umezama ndani ya bahari, uko chini ya bahari mpaka leo majengo yapo lakini sijui Mheshimiwa Waziri na timu yako mnajua kisi gani kuhusiana na hazina hii inayopatikana katika Kisiwa cha Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kwa Wizara nne kwa pamoja, Wizara ya Habari, Wizara hii ya Utalii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, hii package ambayo najua inafadhiliwa na Benki ya Dunia, kwenye ku-promote utalii katika Kisiwa cha Mafia lazima tuweke miundombinu sawa. Tatizo la Mafia sasa hivi ni accessibility, hakuingiliki, usafiri ni mbaya sana, hakuna boti, hakuna gati na hakuna miundombinu ambayo inaweza ika-support watalii wakaja kwa wingi. Kwa hiyo, mimi ningependa sana Mheshimiwa Waziri na timu yako mliangalie hili ni namna gani mnaweza mkaboresha kwa kushirikiana na Wizara nyingine, ikiwemo Wizara ya Ujenzi, namna gani mnaweza mkaboresha miundombinu ya gati pamoja na meli ili Mafia iweze kuwa na meli ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu hapa niliongea na Waziri wa Ujenzi, ipo meli pale ameitoa Bakhresa inaitwa Seabus, ile meli imetolewa bure kwa Serikali na wamepewa Wizara ya Ujenzi wamepewa ile taasisi inaitwa DMI ya mabaharia pale Dar es Salaam, hawana kazi nayo, ni meli kubwa ambayo inabeba takribani abiria 400. Tungeomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Waziri mwenzio wa Ujenzi angalieni namna gani mnaweza mkawashawishi DMI wakatupatia ile meli ikafanya kazi baina ya Nyamisati na Kilindoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika kuhakikisha kwamba utalii katika Kisiwa cha Mafia unatiliwa mkazo, ukurasa wa tisa wa kitabu hiki Mheshimiwa Waziri amesema vizuri tu kwamba katika kuunga mkono juhudi za kukuza utalii wa ndani Mheshimiwa Rais amejikita katika kuhakikisha analifufua Shirika la Ndege la ATCL. Pale Mafia tuna uwanja mzuri na wa kisasa kabisa, umekarabatiwa kwa Mfuko wa Millennium Challenge. Runway yetu ni kubwa na ni ya kutosha na abiria wapo. Tulikuwa tunaomba sana muangalie namna gani bombardier sasa inaweza ikaja Mafia hata kama kwa kuiunganisha na maeneo ya Mtwara, kwa maana itoke Dar es Salaam inatua Mafia inakwenda Mtwara halafu inarudi the same route.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Mafia tulimpa hili ombi akasema kwa sasa tuna bombardier mbili itakapokuja ya tatu, tutaangalia uwezekano wa kuifungua route hii ya Mafia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nalileta hili kwako na wewe uangalie namna gani mnaweza mkatusaidia ili Mafia tuweze kuwa na usafiri wa bombardier kwa sababu itakapokuja pale itanyanyua sana sekta ya utalii sambamba na kufanya marekebisho madogo katika terminal building yetu ya Kiwanja chetu cha Mafia ambapo imechoka kidogo lakini runway iko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kodi, tozo, ada, zimekuwa nyingi sana kwenye tasnia hii ya utalii, nyingi mno kiasi kwamba inafikia wakati mpaka inaanza kuwapa mzigo watalii na watalii wengine wanasema utalii wa kwenda Tanzania ni very expensive kwa sababu kumekuwa na hizo multiple za kodi kila mahali. Kwa mfano, Mafia pale Mheshimiwa Waziri pengine kwa kushirikiana na Waziri mwenzio wa Uvuvi kuangalia namna gani mnaweza mkapunguza ile kodi ambayo kila mtalii anayeingia Mafia katika maeneo ya hifadhi ya bahari anatakiwa alipe dola 24 bila kujali gharama za hoteli, chakula au kitu kingine. Kitendo cha yeye kuingia eneo la hifadhi anatakiwa alipe dola 24 kila siku na hizo unazizidisha mara siku atakazokaa. Kwa kweli ni pesa nyingi sana na watalii wengi wanashindwa kuja wanaona kwenda Zanzibar ni bora zaidi kwa sababu hakuna hii tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kuungana na wale wote ambao wamepeleka pongezi zao kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Pia nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa kutuletea bajeti ambayo kwa kweli kwa kiasi kikubwa sana inaakisi yale mawazo yetu tuliyoyatoa na Mheshimiwa Waziri ameya- accommodate mengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi Wabunge tumekuwa tukiambiwa sana kwamba tumekuwa Wabunge wa kutumia, kila siku tunadai hospitali, shule, barabara na kadhalika hatuji na mawazo mbadala namna gani Serikali inaweza ikapata mapato. Katika mchango wangu wa leo najikita zaidi kutoa namna mbadala ambapo Serikali inaweza ikapata mapato mengi sana na ndiyo utakuwa mchango wangu kwa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kule nyumbani. Mheshimiwa Waziri tuliteta siku moja lakini naomba leo niliweke hapa hadharani na naomba sana alifanyie kazi. Kule Mafia tuna Taasisi ya Hifadhi ya Bahari inakusanya maduhuli, si wajibu wao, wanaifanya kazi ile siyo kwa ufanisi mkubwa. Niliomba maduhuli yale kutokana na watalii wanaoingia Kisiwani Mafia yachukuliwe na TRA maana ndiyo wataalam wa kukusanya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Taasisi ya Hifadhi ya Bahari tunaitwika kazi nyingi. Kazi yake iwe ni kuhakikisha kwamba wanahifadhi mazalia ya samaki na shughuli nyingine za mambo tengefu yale. Mambo ya mapato wangechukua TRA, kuna kama shilingi bilioni mbili mpaka shilingi bilioni tatu kwa mwaka, kama mtatuletea TRA tutapata mapato mengi. Ofisi ya TRA ipo pale Mafia, wanaweza kukusanya yale mapato na Serikali ikapata pesa nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nimemuona hapa Waziri wa Nishati. Pale Mafia tuna kisima cha gesi kilichimbwa takriban miaka 10 au 15 iliyopita na Kampuni inaitwa M&P - Maurel and Prom, mwanzo waligundua kuna gesi nyingi sana pale lakini baadaye kukawa na technical problems hawakuweza kuendelea na kazi ile. Walipokuwa tayari sasa kwa ajili ya kuanza kuchimba na kuipata ile rasilimali ya gesi iliyopo Kisiwani Mafia, leseni yao ikawa imekwisha. Mpaka leo hii wanahangaika TPDC, Wizarani na kila mahali ili waweze ku-renew ile license yao waweze kuendelea na uchimbaji wa gesi ambayo imeonekana ipo nyingi sana katika Kisiwa cha Mafia. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati namwona hapa wahakikishe kwamba wanaharakisha huu mchakato wa hii kampuni ya M&P wapate hii license waje wamalizie kazi ambayo tayari walishaianza pale Kisiwani Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka niishauri Serikali namna bora ya kupata mapato ni eneo la uvuvi hususan katika bahari kuu. Nilipata bahati na heshima kubwa ya Mheshimiwa Spika kuwemo katika Kamati ile ya masuala ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Tumeona mambo mengi lakini kwa ufupi tu ningeomba kumshauri Waziri wa Fedha muende mkaitafute ripoti ile, siwezi ku-summarize yale yote kwa muda huu wa dakika hizi chache nilioupata hapa lakini kuna habari nzuri sana mle ambazo zinaweza zikaisaidia Serikali yetu kupata mapato mengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa ufupi tu kuna suala la bandari ya uvuvi na hili limezungumzwa sana. Mwaka wa Fedha 2014/2015 zilitolewa shilingi milioni 350 na Wizara ya Fedha kwenda Wizara ya Uvuvi ili kuanza masuala ya usanifu ili kuhakikisha kwamba bandari ile inajengwa lakini zile pesa sijui zilipotea wapi. Mwaka jana hii bajeti tunayoimaliza kesho kutwa zimetengwa shilingi milioni 500, hazikuwahi kutoka kutokana na makusanyo madogo. Bajeti hii zimetengwa shilingi milioni 500 nyingine kwa ajili ya usanifu wa kujenga bandari ya uvuvi lakini mpaka sasa bado haijaamuliwa site itakuwa wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuishauri Serikali kwa kuwa tayari tuna mradi wa kujenga Bandari ya Bagamoyo, kwa nini msiunganishe Bandari ile ya Bagamoyo kukawa na section ya bandari ya uvuvi? Tunakosa mapato mengi sana katika uvuvi ule wa bahari kuu kwa sababu tu hatuna bandari ya uvuvi. Bandari ya uvuvi multiplier effect yake ni kwamba value chain yake ni kubwa sana inaweza ikatusaidia sana kupata mapato mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulizungumza habari hapa ya kuwa na meli ya uvuvi, sikuliona suala hili katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sijui wazo lile limefia wapi. Tuwe na meli zetu wenyewe ambazo zitakwenda mpaka kwenye maji ya kina kirefu kwa ajili ya
kupata mazao mengi ya uvuvi. Tumewaachia makampuni ya nje, yanakuja yanachuma, yanaondoka na bahati mbaya sana na katika eneo hili Mheshimiwa Naibu Waziri nimemuona, wahakikishe wanawaambia TRA basi walau waweke mechanism nzuri ambayo itatoza kodi katika hizi meli kubwa ambazo zinatoka nje, zinakuja hapa kwetu, zinavuna rasilimali lakini TRA hawakusanyi hata senti tano. Kwa hiyo, ni eneo ambalo tunaweza tukasema ni oevu, mnaweza kuangalia namna gani mnaweza mkaongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi kulikuwa na sakata hapa la kupima samaki kwa rula. Mimi natokea Mafia, sisi ni wavuvi, kimsingi bajeti hii kwenye uvuvi wametusahau, hakuna kitu, kuna asilimia 0.01ya pesa zimewekwa pale kwa ajili ya mambo ya maendeleo kwenye tasnia hii ya uvuvi, kwa hiyo, tuna tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi navyozungumza na bahati nzuri nimemwona Waziri wa Uvuvi kule Mafia kimsingi tuna kiwanda kikubwa sana cha kuchakata samaki pale cha wale Tanpesca na Alpha Logistics, kinakaribia kufungwa. Walikuwa kila mwezi wanaondoa pale tani 20 mpaka tani 25 za samaki lakini kutokana na haya matamko yaliyokuja sasa hivi kiwanda kile kinashindwa kutoa samaki kwa sababu kuna samaki aina kama ya misusa, ngalala, hao ukubwa wao hakuna namna wanaweza wakaongezeka zaidi ya hizo sentimeta mnazozitaka ninyi. Kwa hiyo, wale ndugu zetu wa Tanpesca wamekataa kununua samaki kutoka kwa wavuvi wadogo kwa kuhofia kwamba huenda wakakamatwa. Hawa samaki niliowataja Mheshimiwa Waziri akae na wataalam wake waruhusiwe kuvuliwa kwa sababu hao samaki hakuna namna wanaweza wakaongezeka ukubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ile ilikuwa kila mwezi wanaleta tani 20 mpaka tani 25 sasa hivi huu mwezi wa tatu meli haijaja kwa sababu samaki wote wanaokwenda kule wanakuwa ni reject. Siyo wanakuwa reject kwa sababu labda umri haujafika, hapana! Hawa samaki kwa maumbile yao hawawezi kufika hizo size ambazo Wizara imeziweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kuwa Serikali ina nia njema ya kuhakikisha kwamba tunapamba na uvuvi haramu, naomba Waziri au wataalam wake waende Mafia, wakae na wavuvi, waangalie ni aina gani ya samaki wanakua kiasi gani. Kwa sababu mnatoa matamko au sheria lakini msiangalie kwamba samaki duniani au hapa Tanzania wapo kwenye maziwa tu kwenye bahari kuna species mbalimbali za samaki na zinakuwa na ukubwa tofauti ambao hauwezi kufikia pengine hivyo viwangowanavyovizungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la utalii. Sisi Mafia kule pamoja na uvuvi, kitu kingine kikubwa kule ni utalii lakini accessibility ya Mafia ni kama haipo, kwa sababu usafiri una matatizo. Nashangaa sana, bahati mbaya watu wa Uchukuzi hapa hawapo, lakini Bakhresa ameipa Serikali meli ile (sea bus) ije Mafia. Meli ile ina matatizo madogo tu ya kurekebishwa lakini mpaka leo Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi bado wanaendelea na taratibu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Mafia wanateseka, hakuna usafiri, wanapanda boat mbovu ambazo siyo salama, wanahatarisha maisha yao, lakini Serikali imeshapewa boat kinachotakiwa ni logistics za kumaliza ili kuhakikisha kwamba ile meli inakuja Mafia na inaanza kazi. Kwa bahati mbaya sana ndugu zetu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wanasuasua. Kwa nini hawataki kuiruhusu ile meli ikaja kuanza kazi Mafia hata kesho kutwa, kwa sababu tumepewa bure tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana mtoa hoja Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kutuletea mpango huu mzuri sana ambao kwa kiasi kikubwa sana unahitaji maoni yetu sisi Wabunge kuweza kuuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mezani kwangu hapa nina nyaraka kama tatu hivi ambazo zote zinahitaji sisi Waheshimiwa Wabunge tuzipitie ili tutoe maoni ili na Mheshimiwa Dkt. Mpango ayazingatie atakapokuja mwezi Machi hapa kutuletea mpango wenyewe. Nitakuwa na maoni katika maeneo kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni ugharamiaji wa mpango. Nitazungumzia namna gani mpango utagharamiwa kwa kupitia miradi ya PPP. Sijaona hasa, bahati nzuri tulirekebisha Sheria ya PPP Bunge lililopita ili tuone namna gani tunaweza tukavutia miradi mingi ya PPP ili kupunguza mzigo wa Serikali katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa sana, bado sijaona hasa namna gani miradi ya PPP inaweza ikatupunguzia mzigo. Kama tatizo ni sheria, basi hiyo sheria ileteni tena tuibadilishe ili tupate kuvutia wawekezaji wengi. Miradi niliyoiona humu ndani, kwa heshima sana, miradi sijui ya kujenga Hostel za CBE, miradi ya kujenga VETA na MSD, kwangu ni miradi mizuri, lakini naiona ni miradi midogo. Tunahitaji kuvutia miradi mikubwa zaidi ili miradi hii ya PPP ipunguze mzigo kwa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, imezungumzwa sana hapa. Nami nilipata bahati wiki mbili zilizopita, tulikuwa na ziara ya Makamu wa Rais, tumeona pale hali inakwenda vizuri lakini tunaiihitaji bandari hii sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Bagamoyo pamoja na mradi wa Standard Gauge ni miradi miwili pacha. Tunahitaji meli kubwa ziende pale. Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kwamba tunaiboresha hivi sasa lakini hizi meli zinakwenda kwa generations. Bandari ya Dar es Salaam inaweza ika-host pale meli ambayo ni za third generation basi na sasa hivi dunia inakwenda mpaka kwenye tenth generation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahitaji tupate Bandari ya kisasa ya Bagamoyo ambayo itaweza kubeba mizigo mikubwa, meli kubwa zenye kubeba mpaka container 10,000 ndiyo SGR itakuwa na maana zaidi. Kwa sababu ile SGR inahitaji iwe feeded na mizigo mizito. Kama meli haziwezi kufunga katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na ufinyu wa magati pale, tutarajie kwamba Bandari ya Bagamoyo itakapokuwa kubwa ndiyo itaweza kuifanya SGR kuwa na manufaa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa suala la Bandari ya Uvuvi. Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami, tulipokuja kwenye Kamati tulizungumza hili suala la Bandari ya Uvuvi, tunahitaji kuwa na bandari hii pengine sambamba na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, pale pale tuweke na section ya Bandari ya Uvuvi ili tupate kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwa sababu tunaona suala la ujenzi wa Bandari ya Uvuvi limekuwa likisuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ni shahidi, tulitenga pesa mwaka 2013/2014 shilingi milioni 500 kwa ajili ya feasibility study. Feasibility study imefanyika lakini hakuna kinachoendelea. Bajeti hii tuna shilingi milioni 300 kwa ajili ya feasibility study ya hiyo hiyo Bandari ya Uvuvi na bado hatujajua hata location Bandari ya Uvuvi itakuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba sana Bandari ya Uvuvi iunganishwe na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ili tumalize hili tatizo. Hili suala ambalo amelizungumza ndugu yangu Mheshimiwa Rehani vizuri kabisa la kuwa na meli zetu wenyewe kwa ajili ya uvuvi katika Bahari Kuu ni muhimu sana pamoja na kufufua lile Shirika letu la Uvivu la TAFICO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu leo yupo hapa. Kwenye masuala haya ya usafiri wa bahari, nilikwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, tukakaa pale Speaker’s Lounge na Mheshimiwa Waziri Mbarawa kuhusiana na tatizo la usafiri katika Kisiwa cha Mafia na meli ile ambayo Bakhresa ameipa Serikali bure kabisa ili ije itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Isack Kamwele hataki kuipeleka meli ile Mafia. Ameniambia point-blank kwamba hatupeleki meli hii Mafia kwa sababu hakuna abiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wa Mafia wako katika kadhia kubwa sana ya usafiri hivi sasa. Tunasafiri na magogo ambayo wakati wowote yanaweza yakapata madhila yakazama. Leo Serikali imepewa meli bure na Bakhresa, iko pale DMI, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Nditiye amenipa ushirikiano mkubwa sana kwenye hili, lakini Waziri Kamwele amenitamkia. Namwambia mbona kuna maagizo hapa tuliongea na Mheshimiwa Waziri Mkuu na wakati ule Waziri Mbarawa, tukakaa pale Speaker’s Lounge, Mheshimiwa Waziri Mkuu akatoa maagizo? Yeye anasema, hayo mambo ya siasa, achana nayo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashangaa, hivi maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mambo ya siasa? Mheshimiwa Waziri Kamwelwe anakataa kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu anayaita maagizo ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, nimeongea na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Mheshimiwa Hawa Mchafu anisaidie kufikisha huu ujumbe. Mheshimiwa Hawa Mchafu anakwenda kuongea na Mheshimiwa Waziri Kamwele anamwambia siwezi kupeleka meli Mafia itabidi nitoze nauli labda Sh.100,000, hailipi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri Mkuu anieleze, je, ile habari ya kupeleka meli Mafia ni habari ya kisiasa? Labda Waziri atakapokuja kujibu atuambie, kwa sababu meli tumepewa bure, haihitaji usanifu, haihitaji bajeti, haihitaji sijui upembuzi yakinifu, inatakiwa kauli tu kwamba meli peleka Mafia. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza pale Nyamisati kuna watu 150 wanalala pale wamekosa boti na wanasafiria boti za mbao. Boti ya kisasa ipo lakini wakubwa hawataki kuipeleka Mafia kwa makusudi tu. Sasa mnaipeleka wapi basi? At least mtuambie mnaipeleka wapi kwa sababu kule Zanzibar boti za Bakhresa ziko nyingi tu. Huwezi kupeleka sehemu nyingine yoyote isipokuwa labda ni Mafia. Mheshimiwa Waziri anasema achana nayo hiyo. Kwenye bajeti hii tunashukuru sana…

K U H U S U U T A R A T I B U . . .

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ingekuwa taarifa, basi nasema nimeipokea na naomba iwe sehemu ya mchango wangu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nasisitiza, sitaki niwe mbashiri mbaya, likitokea tatizo pale kwenye kivuko kile cha kutoka Nyamisati kwenda Mafia, halafu watu wakapoteza maisha, tunachokuomba Mheshimiwa Waziri Kamwelwe usije Mafia kuendesha zoezi la rambirambi pale. Maana yake inaonekana wewe ni fundi sana wa kukusanya rambirambi na masuala ya uokozi, sisi hatuko tayari kwa hilo. Kama unataka kutusaidia, utusaidie sasa hivi, usitusaidie wakati wa majanga kwa sababu meli ya kisasa kabisa ipo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu jana kwa namna nzuri sana aliyowasilisha makadirio ya Wizara yake kwa uweledi mkubwa sana. Jana mama yangu Mheshimiwa Anna Kilango alizungumza suala la uwekezaji na nashukuru kwa kuwa suala la uwekezaji hivi sasa lipo katika Ofisi ya Waziri Mkuu na tuna Waziri pale wa Nchi, nami katika mchango wangu nitajikita kwenye maeneo hayo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utalii, kuna kitu kinaitwa uwekezaji wa utalii wa katika eneo linaloitwa Southern Circuit, eneo la Ukanda wa Kusini. Nimeipitia ile document, sina uhakika sana kama Mheshimiwa Waziri wa Utalii yupo lakini kwa kiasi kikubwa sana hakuna maeneo yoyote yanayozungumzia ama kujadili utalii katika fukwe za pwani. Utalii kwa Kanda ya Kusini kuanzia Tanga mpaka Mtwara kule Msimbati, tuna fukwe nzuri sana kwa ajili ya utalii lakini hii document inayohusiana na Southern Circuit hakuna sehemu yoyote inazungumzia utalii wa fukwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia utalii wa fukwe huwezi kukiacha kukizungumzia Kisiwa cha Mafia. Kisiwa hiki ni miongoni mwa visiwa vizuri sana katika pwani ya Afrika Mashariki. Kina maeneo ya fukwe mazuri kabisa, kuna scuba diving, sport fishing, ni maeneo mazuri sana kwa uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sana Kisiwa cha Mafia ambacho sisi wenyewe tunaita ni New Zanzibar, kina offer mambo mazuri yote ambayo Zanzibar ina offer na pengine hata mimi naonekana ni Mbunge ninayetokea Zanzibar kwa sababu Kisiwa cha Mafia kinanasibishwa sana na mambo yanayoendelea kule Zanzibar. Tunatakiwa tuwekeze ili tuifungue Mafia kwani haitambuliki. Pamoja na vivutio vyote vizuri, Mafia inapata watalii wasiozidi 6,000 kwa mwaka wakati Zanzibar inapata watalii kwa malaki, sina takwimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini kifanyike? Pengine huo ndiyo ushauri wangu ambao Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu ningeomba unisikilize. Tunahitaji kufungua Kisiwa cha Mafia lakini unafikaje Mafia wakatu usafiri ni shida? Tuna kiwanja cha ndege pale kina urefu wa ran way ya kilomita 1.6 ambayo katika hali ya kawaida ndege kubwa haziwezi kutua. Ningeomba sana Waheshimiwa na nimekuona Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi pale Kwandikwa, kwa nini msiangalie uwezekano wa kuongeza ran way ya Uwanja wa Ndege wa Mafia kutoka kilometa 1.6 kwenda mpaka kilometa 3 na kuruhusu ndege kubwa ziweze kutua pale na kuweza kukifungua kisiwa cha Mafia kwa utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar inapata watalii wengi kwa sababu hiyo. Watalii wanakuja na ndege moja kwa moja kutoka nchi za Magharibi na kutua pale Zanzibar lakini ili ufike Mafia lazima utue Dar es Salaam halafu tena uingie kwenye ndege ndogo ndogo na kuja Mafia ambapo watalii wengi hawapendi kadhia ya aina hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri sana katika namna nzuri na bora ya kufungua Kisiwa cha Mafia ule uwanja wa ndege uangaliwe. Kuna terminal building ndogo sana, runway yetu pale ni ndogo sana Mheshimiwa Naibu Waziri uweze kuangalia ni namna gani mnaweza mkaongeza runway ili Kisiwa cha Mafia kiweze kufikika kwa urahisi na ndege kubwa ziweze kutua sambamba hata na ndege yetu ya bombardier. Kwa urefu tuliokuwa nao sasa hivi, ndege ya bombardier inaweza ikatua pale lakini bado hawajaanza hizo safari.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni accessibility kupitia kwenye bahari. Tuna ugomvi wa gati pale wa muda mrefu kidogo, gati la Nyamisati. Tunaishukuru sana Serikali imetutengea fedha na ujenzi umeshaanza pale na tunatarajia ujenzi ule utakamilika ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo lakini kukamilika kwa gati la Nyamisati kutakuwa hakuna maana yoyote iwapo Serikali haitatupatia boti ya kisasa ili watu sasa waweze kulitumia gati la Nyamisati sambamba na gati la Kilindoni ili kuunganisha maeneo haya mawili na wananchi waweze kusafiri bila matatizo yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni barabara. Ndani ya Kisiwa cha Mafia kuna barabara yenye urefu wa kilometa 55, inaitwa Kilindoni kwenda Rasi Mkumbi. Usanifu na upembuzi wa kina umeshakamilika. Naishukuru sana Serikali mambo haya yamekamilika kama miezi miwili, mitatu iliyopita. Sasa kilichobaki ni kutengewa fedha kwa ajili ya kuwekewa lami. Hii nimelisema sana, tatizo linakuja pale kwamba periodical maintenance ya barabara ile inakuwa ni gharama kubwa sana kwa sababu kile ni kisiwa, kuweza kupata udongo, udongo unakaribia kwisha. Itafika wakati sasa ili kufanyia periodical maintenance, inabidi udongo uutoe Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Kwandikwa nimemwona, waangalie uwezekano wa kuiwekea lami barabara hii ili haraka sana tuweze kuondokana na kadhia hii ya kuwa na wasiwasi labda huenda huko mbele udongo ukaisha tukashindwa kufanya periodical maintenance. (Makofi)

Lingine ni suala la Uwekezaji katika bahari kuu. Namshukuru sana Mheshimiwa Spika katika ile Kamati yake ya kuangalia namna gani nchi inaweza ikanufaika na rasilimali yetu ya bahari kuu; mimi nilikuwa ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ile. Tumeyaona mambo mengi sana na nimekuona ndugu yangu Mheshimiwa Ulega. Tulizungumza sana na wewe mwenyewe unalifahamu sana hili suala la blue economic. Kwanini Serikali sasa tusinunue meli ya uvuvi yetu wenyewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, meli ya uvuvi gharama yake haitazidi sana, ni baina ya dola milioni moja mpaka dola milioni sita, hapa katikati kulingana na uwezo wetu wa kibajeti. Ninaamini kwa Serikali yetu hii hatushindwi kununua walau meli mbili ama tatu. Suala la uwekezaji katika Bahari Kuu ni zuri sana. Kule huhitajiki kulima kama vile unavyoandaa shamba. Mwenyezi Mungu ameshalima, wewe unakwenda na kapu lako kuvuna tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga. (Makofi)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu kwa hotuba nzuri sana aliyoitoa leo asubuhi na yenye kuleta matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, natoa pongezi nyingi sana kwa chama chetu Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna ambavyo wameweza kutekeleza Ilani katika Jimbo langu la Mafia. Kwa uchache tu nimeangalia kwenye kitabu humu, Mheshimiwa Waziri anasema gati la Nyamisati limekamilika kwa asilimia 32, lakini nilikuwa pale wiki iliyopita, lile gati limeshakamilika kwa asilimia zaidi ya 90 na naamini mwezi ujao atalifungua. Kwa hiyo, napongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Jemedari Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kile kivuko ambacho tuliahidiwa mwaka jana hapa, kivuko cha kati ya Nyamisati na Kilindoni; nimekiona kwenye kitabu humu pamoja na matengenezo ya maegesho ya Nyamisati na Kilindoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja ambalo nililizungumza mwaka jana kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara hii. Mwaka jana hapa zilitengwa shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kivuko cha Nyamisati – Kilindoni bilioni tatu na bilioni nne kwa ajili ya maegesho upande wa Nyamisati na milioni 400 maegesho upande wa Kilindoni. Nilisema mwaka jana hapa, alikuwa Waziri Mheshimiwa Mbarawa, nikamwambia Mheshimiwa Waziri wanaokuangusha ni watu wako wa TEMESA, kuna tatizo TEMESA. Mwaka jana zimetengwa bilioni 3.8, leo tunamaliza bajeti hii hazijatumika kwa sababu sijui michakato imefanyaje, sijui mkandarasi kafanya vipi, imekwenda huko tenda imekosewa, imefutwa tumeanza upya. Labda hilo inaweza tukawa tumeelewa, vipi kuhusu maegesho milioni 400 Nyamisati na milioni 400 Kilindoni na yenyewe nayo tatizo ni nini mpaka mwaka umekwisha fedha zinatengwa tena kwa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa mwakani turudi tena hapa tukute wanatenga pesa nyingine kwa ajili ya kivuko na maegesho ya Nyamisati na Kilindoni. Mheshimiwa Waziri nikasema tatizo naliona lipo TEMESA, nimewaona wameandika humu kwamba wanashughulikia maegesho hayo, maegesho ya milioni 400 Kilindoni, maegesho ya milioni 400 Nyamisati, mwaka mzima? Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri, watu wake waTEMESA wanamwangusha na nilisema kwenye hotuba kama hii mwaka jana. Sasa nisingependa turudi mwakani tuzungumzie habari hii tena ya kivuko na maegesho ya Nyamisati na Kilindoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kivuko hiki ambacho kinatengenezwa pale na TEMESA. Kila tukiendelea kufuatilia pale unaambiwa sijui mkataba upo kwa Mwanasheria Mkuu, mara unaambiwa sijui tenda ile ilifutwa, mara unaambiwa subiri kuna vifaa vimeagizwa kutoka nje vinahitaji exemption, tatizo lipo kwa Waziri wa Fedha. Sasa ningependa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hotuba yake atuambie na atuhakikishie watu wa Mafia kivuko hiki kinatengenezwa na kipo katika hatua gani, maana yake hii habari ya kusema ya kwamba tunasubiri exemption kutoka kwa Waziri wa Fedha, ukimuuliza Waziri wa Fedha anasema jambo hilo halijui. Ukienda ukizungumzia baadaye unakuja unaambiwa aah kuna tatizo kwenye procurement kule wamefuta tenda yenyewe; sasa tushike lipi? Sasa ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie pale na watu wa TEMESA. I wish watu wa TEMESA wangejua tabu, dhiki, mashaka na adhabu wanayoipata watu wa Mafia kusafiri kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza kuna watu zaidi ya wiki nzima wako pale, vyombo vile vya mbao vimechoka havina uwezo wa kubeba watu wengi, watu wamekaa pale stranded wiki nzima, halafu mtu anatoa majibu mepesi tu kwamba sijui tenda imefanya hivi, mkataba sijui upo kwa Mwanasheria Mkuu, sijui Wizara ya Fedha haijatoa exemption; ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up atuambie kwa mapana yake kivuko hiki sasa kitakuwa tayari lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni barabara; barabara ya Rasimkumbi mpaka Kilindoni kilometa 45. Tulinong’ona asubuhi akaniambia kwamba hiyo hukuiona humo lakini msiwe na wasiwasi. Naomba sana na nilizungumza zaidi ya mara tatu hapa, ile barabara tatizo kubwa Mafia ni kisiwa periodical maintenance inabidi utafute udongo, udongo kule umekwisha, sasa wasipoitia lami ile barabara watakuja kujikuta kwamba wanaitengeneza kwa gharama kubwa sana. Ningeomba zile kilometa tano alizoniahidi basi azitekeleze Mheshimiwa Waziri namwamini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Uwanja wa Ndege wa Mafia, nimeona humu kwenye kitabu viwanja vyote vya ndege humu vinafanyiwa ukarabati lakini Uwanja wa Ndege wa Mafia una matatizo makubwa manne. Tatizo la kwanza runway ile ni fupi, hairuhusu ndege ndefu, tunaomba iongezwe. Tatizo la pili, terminal building lile ni kama hakuna, limechoka, linavuja na Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuja aliona. Tatizo la tatu, hakuna taa pale; sisi ile ndiyo escaping route yetu, ikifika usiku upo Mafia imetokea dharura ya mgonjwa, huna namna ya kum-evacuate kuja Dar es Salaam lazima aende na ndege na kama ndege yenyewe uwanja hauna taa, ina maana kwamba huyo mtu anaweza akapoteza maisha pale akisubiri evacuation siku ya pili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwetu sisi kutuwekea taa uwanja wa ndege wa Mafia siyo luxury wala siyo kwamba ni kitu cha anasa, ni necessity kwetu sisi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie basi hatima ya Uwanja wa Ndege wa Mafia na kuwekewa taa sambamba na kuongeza eneo lile la kupaki ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ATCL; tulizungumza hapa Mafia ni kisiwa cha kitalii, kwa siku kuna flight pale zaidi ya nne zinakwenda ndogo ndogo na zote zipo full. Nashangaa kwa nini bombardier haiji Mafia, abiria wapo wa kutosha, lakini watu wa ATCL bado wanasuasua kutuletea usafiri wa ndege kubwa pale kwa ajili ya Kisiwa cha Mafia. Nataka niwahakikishie kwamba watakapoleta bombardier pale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia malizia

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kusisitiza kuhusu suala la kutuletea bombardier kwa ajili ya kupunguza tatizo la usafiri Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia uzima na afya ili leo tuweze kujadiliana masuala yanayohusu nchi nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana mtoa hoja Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa namna walivyoutendea haki Mpango huu ulio mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu pia ziende kwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi kabla sijaanza kuujadili Mpango wetu huu. Namshukuru sana Waziri mwenye dhamana ya ujenzi, kivuko chetu kile cha Nyamisati kimeshaanza kujengwa na tumeahidiwa mwezi wa pili kitakuwa tayari. Kwa hiyo, nina kila aina ya sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na watu wote pale Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, sasa nianze kuchangia Mpango. Umekuwa ukisisitiza mara kwa mara hapa kuhusu suala la namna gani sisi Wabunge tunaweza tukaingiza input zetu ili huu Mpango uwe bora zaidi. Waheshimiwa Wabunge mara nyingi wamekuwa wakizungumza upande wa matumizi zaidi, kila mtu anakuja barabara sijui gati kuliko namna gani tunaweza kuboresha Mpango wetu ukawa na mapato zaidi ili kuweza kufidia hii miradi ambayo sote hapa kila mmoja anavuta mradi unaomhusu kwenye Jimbo lake. Mimi nitakuja na mapendekezo ya namna bora ambavyo tunaweza tukauboresha Mpango huu ili Serikali ipate mapato zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kwenye eneo la uvuvi wa bahari kuu. Amezungumza kwa muhtasari sana ndugu yangu Mheshimiwa Ally Keissy pale. Kwanza nianze kukushukuru wewe binafsi, ulinifanya mmoja wa wajumbe katika ile Kamati inayochunguza namna gani Serikali inaweza ikanufaika na uvuvi wa bahari kuu, tumekutana na mambo mengi sana na ningeomba sana ile taarifa kama itawezekana tuifanye public kwa sababu kuna mambo mazuri mengi sana mle. Hata mimi mwenyewe pamoja na kuwa ni mjumbe basi huwa naihitaji hata kuipitia na kuidurusu lakini inakuwa ni shida kidogo kwa sababu bado haijawa public.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa kwenye Mpango kwa nukta chache sana, nadhani nukta tatu ama nne kuhusu uvuvi wa bahari kuu. Jambo la kwanza Serikali inaangalia uwezekano wa kujenga bandari ya uvuvi. Jambo la pili kufufua shirika letu lile la meli la TAFICO. Jambo la tatu ni namna gani tunaweza tukapata vifaranga vya samaki na namna za kuvifuga kwenye vizimba. Haya yote ni mambo mazuri lakini naomba tuangalie namna gani tunaweza tuka-prioritize mambo haya. Tukiyachukua yote kwa ujumla wake inawezekana pengine gharama zikawa ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kwanza tu-focus kwenye bandari ya uvuvi peke yake, tupate bandari ya uvuvi. Watu wengine walisema kwa nini Bandari ya Dar es Salaam msiweke magati mawili au matatu na kule Zanzibar nako kuwe na gati maalum kwa ajili ya meli za uvuvi, haiendi hivyo. Typical bandari ya uvuvi ni fully fledge bandari, inakuwa na logistics center zake nyuma kule. Samaki huwezi ukawachanganya na bandari ya cargo, huku kuna mbolea, huku unashusha sijui chemical gani halafu kuna gati lingine tena unashusha bidhaa ya samaki, hatutopata accreditation ile ya European Union kupeleka vyakula nje kwa sababu kutakuwa na contamination kutokana na mazingira ya bandari ya mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapozungumzia bandari ya uvuvi tunazungumzia kitu kikubwa sana, very complex na tungeomba Waziri alijue hilo. Kwa bahati mbaya sana mpaka leo hii Serikali bado haijajua hata site bandari itajengwa wapi. Tumeshatenga fedha katika bajeti kama tatu zilizopita kwa ajili ya upembuzi yakinifu, walau kupata kujua bandari tunaenda kuijenga wapi, Kilwa, Dar es Salaam, Bagamoyo, Mafia au wapi? Mpaka leo hilo tu halijaamuliwa. Bajeti hii tunayoitekeleza tayari kuna fedha za upembuzi yakinifu nadhani shilingi milioni 300 au shilingi 500, I stand to be corrected, za namna ambavyo mshauri atapatikana ili aweze kutushauri bandari inajengwa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa dakika chache sana tuiangalie overview ya ile biashara yenyewe ya uvuvi wa bahari kuu. Eneo letu linaloitwa EEZ (Exclusive Economic Zone) la Tanzania ni zaidi ya kilomita za mraba 300,000 yaani hiyo ni nchi ndogo 10/15, hilo eneo lote ni la kwetu sisi. Kwa masikitiko makubwa eneo hilo lime-lay idle, hakuna kinachoendelea kule kwenye EEZ yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amelizungumza Mheshimiwa Ally Saleh pale kwa muhtasari kwamba Serikali na nashukuru Waziri mwenye dhamana yupo hapa, Serikali mwaka 2016 waliweka kitu kinaitwa royalty ya 0.4 kwa kila samaki. Samaki wanaovuliwa ni aina ya jodari (tuna) basi, soko la dunia halitaki samaki mwingine yoyote asiyekuwa jodari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa walipo-introduce royalty ya 0.4 wale wenye meli kubwa ambao ili aje kuvua kwenye pwani yetu (EEZ) walikuwa wanalipa leseni moja ni mpaka Dola za Kimarekani 36,000 na kwa wakati mmoja kwenye EEZ yetu zinaweza zikawepo kule meli zaidi ya 100, unaweza ukazidisha dola 36,000 mara meli 100, hiyo ni kwa ajili ya leseni tu na tulikuwa tunapata hizo. Hata hivyo, hapa katikati mwaka 2016 tukaweka 0.4 kwa maana katika kila kilo ya jodari 0.4 inabidi iende Serikalini pamoja na yale malipo ya leseni, wale mabwana wakakasirika wakaondoka. Kwa hiyo huu ni mwaka nadhani wa pili au wa tatu, hakuna kinachoendelea kule kwenye EEZ yetu na samaki kama wanavyosema watu wengine siyo bidhaa ambayo ni kama dhahabu, ukichimba itaisha, samaki ni wanapita (gyratory), usimpovua wewe atakwenda Somalia atavuliwa, kwa hiyo, sisi tunakosa kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niliuliza jambo hili kwenye Kamati na Mheshimiwa Mpango atakumbuka nikaambiwa 0.4 imeshafutwa bwana Dau hujui, toka mwezi wa Nne imefutwa, nikawaambia haiwezekani Bunge la Bajeti tumezungumza 0.4 hapa na Waziri mwenye dhamana akasema tunaangalia uwezekano wa kuifuta hapa katikati, nadhani jana, majuzi nikaambiwa kuna maendeleo yanaendelea huko 0.4 imefutwa. Sasa naomba jioni tutakapokuja, Mawaziri watakapoanza ku-react na hizi taarifa basi watuhakikishie 0.4 imefutwa au haijafutwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watuhakikishie ili tujue kwa sababu tunachopoteza ni kingi na tusipotoza haina maana kwamba, maana yake afadhali ile kauli unayosema Mwalimu Nyerere alisema hii dhahabu kama hatuna ufundi wa kuichimba ikae tu watakuja kuichimba vizazi vijavyo, lakini kwenye samaki hakuko hivyo, usipomvuna wewe ataenda kuvunwa Namibia. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa basi atusaidie namna gani ya kuona 0.4 inaondolewa na bandari ya uvuvi mchakato wake unaanza mara moja. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hizi tozo kwa ujumla wake naomba Waziri wa Fedha na Mipango aziangalie, hizi Sectoral Ministries kila mmoja anakuja na tozo yake, inakuwa ni vurugu! Kwenye utalii kule, sijui TANAPA Waziri wa Maliasili na Utalii naye anaweka tozo zake, huku Waziri Mifugo na Uvuvi anaweka tozo huku, sijui Waziri gani naye akiona kidogo tu mambo yanakwenda vibaya anaweka tozo. Kunakuwa na utitiri wa tozo, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ndiyo waratibu hizi tozo, hizi tozo kadri zinavyozidi kuongezeka...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau naambiwa eti ni kengele ya pili, lakini malizia nakupa dakika mbili umalizie.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi la mwisho kwa dakika moja tu, nilishaongea na Mheshimiwa Waziri Mpango, hii leo naongea mara ya nne na nilimwambia kwenye Kamati sitaongea tena kuhusu suala hili. Kuna chanzo cha mapato kipo Mafia pale ambacho watalii wanatozwa kuingia katika maeneo ya hifadhi ya bahari, kila mtalii analipa dola 24. Tunamwomba achukue yeye kile chanzo, tunampa sisi chanzo kile aongeze mapato ya Serikali, awaambie TRA waende wakakusanye wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti,, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)

MWENYEKITI: Hebu hilo la mwisho yaani wakusanye badala ya TANAPA au?

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana badala kuna Taasisi inaitwa Hifadhi ya Bahari (MPRU) ambao kimsingi wao kazi yao ni kuhifadhi maeneo na mazalia ya samaki, sasa tunapowapa kazi…

MWENYEKITI: Badala ya kule kwa Luhaga Mpina enhe?

MHE. MBARAKA K. DAU: Ndiyo, sawasawa.

MWENYEKITI: Aaa, sawasawa. (Kicheko)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa badala ya wao kuendelea kukusanya mapato, tunaona ile kazi ya mapato ni kazi ya TRA, wafanye TRA, halafu sisi tushughulike na uhifadhi.

MWENYEKITI: Nimekusikia Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa fursa hii, ili niweze kuchangia kwenye Azimio hili, awali ya yote ninaunga mkono Bunge letu kuridhia Itifaki hii ya kuzuia Uvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiokuwa na shaka katika eneo letu la exclusive economic zone (EEZ).

SPIKA: Waheshimiwa katika kuchangia mnaruhusiwa kuchangia ama mojawapo ya Azimio hili ama Maazimio yote katika uchangiaji wako. Lakini pia niwakumbushe Kamati ya Uongozi tukitoka saa saba by saa saba na nusu tuwe pale kwenye Ukumbi wa Spika, Kamati ya Uongozi tukutane Ukumbi wa Spika kuna kikao kidogo, Mheshimiwa Mbaraka Dau endelea.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa ufafanuzi huo, nitachangia kwenye Azimio la Itifaki ya Uvuvi haramu, ni ukweli usiokuwa na shaka katika eneo letu la exclusive economic zone EEZ kumekuwa na vurugu nyingi sana ya meli za kigeni zinazoingia kwenda kuvua kule bila ya na vibali na ruhusa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa haina uwezo, ilikuwa haina uwezo wa aina mbili, haina uwezo wa Vyombo vya kwenda kuwazuia kule kwa sababu ni mbali na bahari ni kali sana, lakini la pili tulikuwa hatuna uwezo kwa sababu Mikataba kama hii ya Kimataifa haikuwepo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Itifaki hii inakwenda kujibu swali hilo gumu kwamba sasa tunao uwezo, wale ambao wataingia katika eneo letu la EEZ na tukaweza kuwaona kwenye ile VMS Versa Monitoring System yetu pale DSFA. Tunao uwezo sasa wa kwenda kuwafatilia watakapokwenda kuweka nanga meli zao katika nchi Wanachama hizi sitini, tunaweza kwenda kufatilia kule na kujua kwamba meli kadhaa iliingia katika EEZ ya Tanzania bila ya kibali ikavua na sasa Serikali inachukua hatua.

Mheshimiwa Spika, sasa faida kubwa inayopatikana ni hiyo, na mimi katika faida hiyo nilikuwa na maombi au nyongeza au ushauri kwa Waziri mwenye dhamana wa aina tatu, ushauri wa kwanza, twende tukafanye overall ya regulation zetu, Kanuni zetu za ile Taasisi yetu ya Uvuvi wa Bahari Kuu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu gani? Kwa sababu sasa tunayo nyenzo ya kujua kwamba kuna meli iliingia kwenye EEZ yetu haina kibali ikaenda kutia nanga labda Seychelles tunatumia Mikataba ya Kimataifa kuikamata kule, Je, tumeshaikamata sasa tunafanya nini? Kwa sababu Sheria inataka ile meli au meli zile zije zihukumiwe kwa mujibu wa Sheria za Tanzania. Sasa ipo haja sasa ya kwenda kufanyia overall zile Kanuni zetu kwamba sasa je, meli ya aina hii inayokamatwa itaingia kwenye kosa lipi? Tunaitaifisha, tunapiga faini, tunafanyaje?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba wenzetu wa, na nimemsikia Mkurugenzi Mkuu hapa wa Mamlaka ya Bahari Kuu yupo wenzetu wa Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ile waende wakaanze kufanyia kazi hizo regulation sasa ili tuweze kunufaika na hii Itifaki.

Mheshimiwa Spika, ombi au ushauri wa pili, Bandari ya Uvuvi limesemwa hapa na Kamati, limesemwa na Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani, bila ya kuwa na Bandari ya Uvuvi na nilizungumza hapa nadhani wiki iliyopita, bila ya kuwa na Bandari ya Uvuvi faida hizi zinatutoka kwa sababu hii EEZ yetu kwa wakati mmoja inaweza ika-accommodate meli zaidi ya mia moja, zinavua wakishavua wanakwenda kwa wenye Bandari za Uvuvi Seychelles, Mauritius, Mordait na maeneo mengine huko.

Mheshimiwa Spika, sasa sisi tunakosa haya manufaa tukiwa na Bandari yetu ya Uvuvi zile zile meli zile tutazishawishi zije huku kwenye Bandari yetu zianze kushusha ule mzigo wafanye processing halafu baadaye na biashara yenyewe itaanza ku-boom kama vile ambavyo tulishuhudia biashara ya minofu ya samaki kule Mwanza kipindi kile Ndege zinakuja kuchukua mzigo na kuondoka.

Mheshimiwa Spika, nafasi ile bado tunayo kwa kupitia Itifaki hii na kuweza kufufua au kujenga Bandari yetu ya Uvuvi ambayo itasaidia sana katika kuwavutia sasa hawa wenye meli, tunaweka regulations kwa mfano sasa hivi tuna regulation zinazowataka wale wanaovua katika Bahari Kuu waje katika Bandari zetu, lakini wanashindwa kuja kwenye Bandari zetu kwa sababu hatuna Bandari za Uvuvi, tuna Bandari za Mizigo na Sheria za Kimataifa zinakataa kushusha mzigo wa chakula kwenye Bandari ya Mizigo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naendelea kusisitiza na kumuomba Mheshimiwa Waziri ule mchakato wa kujenga Bandari ya Uvuvi hata hii ya kununua meli inaweza ikasubiri tuanze na Bandari ya Uvuvi, ikijengwa Bandari ya Uvuvi multiply effect yake ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kutakuwa na ajira kwa vijana wetu kwa sababu inakuja na logistics centers zile, kutakuwa na ajira, biashara ita-boom kwa maana ya kwamba sasa mizigo itakuwa inakwenda ama kupitia Uwanja wa Ndege au kupitia kwenye Bandari zetu kwenda sokoni na maeneo mengine ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, pia nina ombi jingine dogo kwa Mheshimiwa Waziri, tumeona kwamba moja ya faida tutakazozipata hapa ni kunufaika na misaada mbalimbali inayotolewa na FAO kwa Tanzania. Kule Mafia eneo la Kitutia ndiyo nursery, ndiyo labour ya samaki zaidi ya asilimia 70 wanaozaliwa katika Bahari ya Hindi, lakini eneo lenyewe la Mafia limechoka, eneo lenyewe halitunzwi, eneo lenyewe wananchi wale ambao wanaitunza ile rasirimali hawanufaiki na chochote.

Mheshimiwa Spika, ningeomba kupitia Itifaki hii na Mheshimiwa Waziri tumeambiwa kwamba kutakuwa na aina hiyo ya misaada mbalimbali, basi tuangalie namna gani lile eneo litakavyoweza kutunzwa vizuri na kuweza kuleta manufaa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii, na ninaridhia Bunge letu liliridhie Itifaki hii ya Uvuvi haramu katika Bahari Kuu, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hii ya uhai na pumzi na leo tumeweza kukutana hapa kuweza kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru kwa namna ya kipekee sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jemedari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalazimika kuyasema haya mapema kwa sababu kwa namna ya kipekee sisi wananchi tunaotokea Mafia Kisiwani tumepata Ghati la Nyamisati ambalo limeshakamilika na Serikali hivi sasa inakamilisha Kivuko kwa ajili ya wananchi wa Mafia ambacho kitakuwa tayari nadhani kama siyo mwezi ujao basi utakuwa ni mwezi wa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nije kwenye mada husika, nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa namna ambavyo wamewasilisha taarifa zao hapa za mwaka. Nitajadili zote kwa pamoja, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma pamoja na Kamati ambayo pia ninaihudumu Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati ya Bajeti inasema TRA wamefanya vizuri sana katika ukusanyaji wa mapato na tunawapongeza sana na uwepo wa Kamishna Jenerari Mpya pale naamini umekuwa ni chachu wa kila siku tunayoiona TRA inavunja rekodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika sasa mpaka trilioni 1.5 kwa kweli ni mafanikio makubwa sana. Nasahihishwa hapa trilioni 1.9 ni mafanikio makubwa sana kwa kweli na tunawashukuru sana tunampongeza sana Kamishna Jenerari na tunaamini kwamba wataendelea kuvunje rekodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini taarifa inasema mapato yanayotokana na vyanzo ambavyo si vya kikodi hayajafanya vizuri sana. Sasa eneo hilo nafikiri ipo haja ya kuhakikishwa kwamba tuna improve, mwaka jana hapa tulipitisha Sheria hapa kuhusu masuala ya Bandari kwa sababu maeneo ambayo vyanzo vingi sana maeneo ambayo kule mapato yanakopotea sana ni kwenye hizi zinaitwa bandari bubu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipitisha Sheria hapa ambayo tumempa Mamlaka Waziri Mwenye dhamana ya masuala ya Bandari aweze kurasimisha Bandari ambazo anaona inafaa. Sasa nafikiri labda kama wenyewe wapo hapa watakapokuja na wao kuchangia watuambie watu wa Bandari, wanaohusika na dhamana ya Bandari, hivi mpaka sasa wamerasimisha Bandari ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano sisi tunaotoka kule kwetu kule Bandari zimekuwa nyingi sana na mapato ndiko yanakovuja vuja kule ili twende vizuri, lakini eneo jingine ni eneo ambalo ya mapato ambayo pia si ya kodi, mwaka jana na mwaka huu pia nilizungumza hapa kuhusu namna gani sasa kwa sababu tunaiona TRA inaweza kukusanya kwa asilimia nyingi sana na wako vizuri, lakini sasa inaonekana kwamba tunamkamua yule ng’ombe sasa anakaribia kumaliza maziwa yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ipo haja ya kuongeza tax base na kuangalia maeneo mengine ambapo Serikali sasa inaweza ikapata mapato ambayo pia mengine wala si mapato ya Kikodi na tulizungumza hapa mwaka jana na ninashukuru sana nimemuona Waziri Mwenye dhamana ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba yapo maeneo ambayo Serikali ikiwekeza kwa mfano kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, kwenye Uvuvi wa Bahari kuu, bado hatujafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imebahatika kuwa na Mawaziri ambao ni very aggressive na mimi ninawashukuru na ninawapongeza sana, wanafanya kazi nzuri sana. Lakini tunahitaji tuongeze nguvu zaidi kwa sababu mapato haya ambayo ninaamini tunayakosa kule kwenye uvuvi wa Bahari Kuu ni mapato makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeiangalia taarifa hii, pia tulitenga na fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi sijui tunakwenda vipi? Na nimeona pia kwamba Serikali ina Mpango wa kununua meli yake yenyewe ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nitoe angalizo kidogo hapa, isije ikawa ile hadithi ya Kuku na yai, kipi kianze, unaweza ukawa na Bandari ya Uvuvi pamoja ukanunua na Meli lakini kinachotakiwa kuanza hapa tuanze kwanza na ujenzi Bandari halafu meli ije, kwa sababu tutakuwa tunanunua kutokana na gharama kubwa za ununuzi wa Meli hizi za Uvuvi ambayo gharama zake ni kubwa naona. Serikali tungewekeza kwanza kwenye Miundombinu ya Kibandari ambayo multiply effect yake ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi kutakuwa na Viwanda mule vya kuchakata mazao mbalimbali ya samaki, ambayo yatafanya biashara ya minofu kama ile ambayo iliyokuwa ina-boom miaka ile ya 90 kule Mwanza na sisi tukaweza kuitumia Bahari Kuu yetu iweze kutu-feed na minofu ya samaki aina ya tuner ambao wanapatikana zaidi sana katika Pwani yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nashauri na Mheshimiwa Waziri unanisikia ni vizuri sana tukaharakisha mchakato ule wa kuwa na Bandari na Uvuvi tukishakuwa na Bandari ya Uvuvi baadaye meli, hata meli za wageni sasa tukazikaribisha zikaja alimradi kwamba wanapovuna mazao yetu kule Bahari Kuu wasiende nayo nje yarudi ndani ili yaweze kutoa ajira pamoja na mapato mengine zaidi ya Kiserikali ambayo yatasaidia katika kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala tulilizungumza kwenye Kamati suala la namna gani TRA inaweza ikakusanya Kodi ya Majengo, Kodi ya Majengo ni ushauri ambao ulitolewa na sikuiona kwenye taarifa lakini naomba niusisitize hapo, kwamba Kamati ilishauri katika mjadala badala ya kuanza kuhangaika na Wafanyakazi wa TRA wakaingia mitaani kwa wingi kwenda kufuata nyumba hadi nyumba. Inawezekana workforce hiyo tukawa hatuna na moja ya principle nzuri za ukusanyaji wa kodi, lazima Kodi iwe convenient, lazima kodi iwe economical huwezi ukatumia gharama nyingi sana kukusanya Kodi ambayo mwisho wake ile Kodi inakuwa ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, likaja wazo na naomba sana wenzetu wa Wizara ya Fedha na Mipango waliangalie pamoja na TRA likaja wazo kwamba hii kodi ya majengo kwa nini isiingizwe katika bili ya luku? Bili ya luku halafu ikawa spread kwa muda wa miezi kumi na mbili ili mtu anaponunua luku basi anakuwa ameshalipa Kodi yake ya Majengo, lakini na kubwa zaidi ni kwa sababu sasa hivi umeme umesambaa karibu nchi nzima, na kwa taarifa tulizo nazo kutoka kwa Wizara husika ni kwamba mpaka kufikia Juni mwakani 2021 tutakuwa tumefikia vijiji vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninaamini kwa kutumia utaratibu huu Serikali inaweza ikakusanya Kodi yake ya Majengo TRA bila ya bughudha bila ya kukimbizana na watu, au kuongeza workforce kubwa zaidi kuanza kuingia ingia kwenye address mbalimbali najua kuna changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine ya kibiashara labda nyumba moja inaweza ikawa na fremu za maduka labda thelathini, arobaini na kila fremu ina mashine yake ya luku lakini haya ni mambo ambayo administratively wanaweza wakaripoti baadaye wataalam au Watendaji wa TRA wakaenda maeneo kama hayo waka-harmonize hayo mambo na Serikali ikaweza ikanufaika zaidi na mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine tumeona ufanisi mzuri wa ile ETS ile stamp ya Kodi kwenye bidhaa ilivyoanza inafanya vizuri na kwa kuwa taarifa zinaonekana kwamba tunakwenda vizuri, nilikuwa nashauri tu na Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Bajeti ambaye ndiye mtoa hoja kama mtaona inafaa basi twende kuishauri Serikali sasa twende ku-extend zaidi bidhaa za aina nyingi zaidi ziingie kwenye utaratibu huu wa ETS kwa sababu umeonekana kwamba ni wenye manufaa makubwa sana na unaleta mapato mengi ya Kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nizungumzie jambo moja dogo kuhusiana na TRA, TRA wanatoa certificate kwa hizi Taasisi NGO‟s ambazo zinakuwa wanapata kama exemption ya kulipa kodi, na kule kwetu sisi tuna shida kidogo, tuna shida, kuna wawekezaji wamewekeza pale wanataka kuja kutupatia sisi kitu kinachoitwa CSR ile Cooperate and Social Responsibility kwa ajili ya kurudisha kwa jamii ya Mafia. Lakini hawa Wawekezaji wanatuambia kwamba wataipatia Halmashauri ya Mafia msaada wa bilioni mbili, lakini ule msaada wa bilioni mbili ukija ukiuchanganua na ninaamini wenzangu wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija ukiuchanganua ni kwamba ni mafunzo, ni semina ni tiketi za ndege za Wawezeshaji kutoka Ulaya kulala katika five star hotel na mambo mengine, lakini kinachokwenda kwa wananchi wa Mafia wenyewe ni almost sifuri kwa sababu wanakuja wao na ma-translators wao kwa ajili ya kutafsiri kwa watoto eti wanasema wanawafundisha namna ya ujasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo limetuletea matatizo sana na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Waziri Jafo kama upo nililileta kwako na ukasema kwamba utachukua hatua, kuna tatizo pale tunarundikiwa jambo, tunaambiwa CSR ya bilion mbili lakini ukweli hasa hakuna kitu kule on the ground na hii nimelisema hapa kwa makusudi, nimelisema hapa kwa makusudi kwa sababu lina tax implication kwa ajili ya TRA tuangalie Taasisi hizi sasa ambazo zinakuja kwa wananchi wetu na inaweza likaja likawa swali kwamba inakuwaje kwamba hayo mambo si mgeweza tu kuyamaliza huko kwenye Baraza lako la Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uendeshaji wa haya mambo kuna kitu kinaitwa technical no how na kuna kitu kinaitwa technical no who, sasa kwenye technical no how, nimejaribu kujenga hoja sana ili jambo liishe kule lakini wenzangu wamenizidi kwenye kitu kinaitwa technical no who, na ninaamini Waziri Mwenye dhamana wa hiyo unanielewa nina maana gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo, leo tumeweza kukutana hapa kujadili masuala yanayohusu nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa taarifa nzuri kabisa ambazo zimesheheni ushauri na maazimio mazuri sana. Naamini kama tutayafanyia kazi basi tutaona nchi yetu hii ikisonga mbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia Kamati zote mbili kwa pamoja. Kwanza nitaanza na Kamati ya Miundombinu; umefika wakati sasa namna ambavyo tunaendea ujenzi wa miundombinu yetu ya nchi iwe zaidi ya kimkakati na kwa nini ninasema hivyo?

Nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya miundombinu ambayo ukienda kuijenga sio miundombinu ambayo inakuwa ni mzigo sana kwa Serikali bali in the long run miundombinu ile inakuwa na tija na yenye kuleta fedha nyingi na mapato mengi kwa Taifa na nitatolea mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea katika Kisiwa cha Mafia, kisiwa hiki kinapata wastani wa watalii kama 6,000 hivi mpaka 7,000 kwa mwaka mzima, lakini Kisiwa cha Zanzibar kwa maana ya Unguja na Pemba kwa umoja wao wanapata watalii mpaka 600,000 kwa mwaka, utaona tofauti hizo. Sasa sizungumzi kwa maana ya ku-compete, nazungumza kwa maana ya ku-complement each other. Kwa nini Mafia inakuwa na watalii wachache, ni kwa sababu miundombinu yake haiingiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndiyo hicho ninachokisema kwamba kama ujenzi wa miundombinu utakwenda kimkakati zaidi kwa maana ya kufungua fursa zaidi za kiutalii kwa maeneo kama haya ya Mafia na maeneo mengine tunaamini kabisa badala ya kuwa ni mzigo kwa Serikali in the long run kutakuwa na mapato mengi sana kwa Serikali na vitu vyenyewe nitavielezea kwa muhtasari tu kwa sababu muda sio rafiki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni namna ya accessibility ya kuingia Mafia. Kwa sasa namna pekee salama na ya uhakika ni usafiri wa ndege ambao gharama yake ni kubwa sana, flight ya nusu saa inagharimu Sh.167,000. Kwa mwananchi wa kawaida ambaye uwezo wake ni mdogo, huo ni mzigo mkubwa sana. Sasa alternative yake ni kupita baharini ambako sasa kule baharini hali ya miundombinu sio nzuri. Vyombo vya usafiri ni vya magogo, havipo salama na kipindi kama hiki cha upepo mkali ambao upepo unaitwa upepo wa kaskazi inakuwa ni shida, inabidi wazuiwe abiria wasisafiri kwa muda wa wiki, wanakaa wanarundikana na inaleta shida kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Mafia tumepatiwa gati pale, Gati la Nyamisati, gati la kisasa kabisa, zuri kabisa, kwamba walau sasa hata kama chombo cha usafiri cha kisasa kitakapokuja kinao uwezo sasa wa ku-dock mahali na kupakia na kushusha abiria pamoja na mizigo yao kwa salama kuliko ilivyokuwa kabla ya hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukamilifu wa Gati lile la Nyamisati utakuwa hauna maana sana kama hatutakuwa na usafiri wa boti ya kisasa baina ya Nyamisati na Kilindoni Mafia. Kwa nukta hii pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais; kwenye bajeti ya mwaka huu tumewekewa shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya kujenga boti ya kisasa ambayo itakamilika ndani ya muda mfupi ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukichanganya haya, ule mzigo ambao pengine wasafiri walikuwa wanaubeba mkubwa sana wa ndege na watalii wengi kwao wao kupanda boti ni sehemu kama ya adventure ya kwenda mahali, tunaamini sana utafungua sasa fursa nyingi zaidi kwa maana ya kwamba watalii watakuja wengi sana kwenda kutembelea Kisiwa cha Mafia baadaye na Serikali nayo itapata mapato mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo hilo, miundombinu ya uwanja wa ndege; pale Mafia kuna uwanja wa ndege ambao runway yake ni urefu wa kilometa 1.6. Kwa urefu wa kilometa 1.6, ndege ambazo zinaweza zikatua na kuruka pale ni aina ya Fokker pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa tunataka utalii na baadhi ya watalii wanapenda zaidi wawe na direct flight kutoka wanakotoka, sasa ndege kubwa kama hizi za Boeing 737 na nyingine haziwezi kuja kutua moja kwa moja mpaka Mafia kwa sababu uwanja wa ndege una urefu wa kilometa 1.6 na unahitaji uwanja wa ndege wenye urefu wa angalau kilometa tatu na kuendelea ili kuweza ku-accommodate ndege kubwa zinazokuja moja kwa moja kutoka nchi za magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ombi langu na ni ushauri kwa Mwenyekiti makini kabisa na ni miongoni mwa the finest brains za Wenyeviti wa Kamati, Mheshimiwa Kakoso; atusaidie pale Mafia sasa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iweze ku-extend ile runway kutoka kilometa 1.6 kwenda kilometa 3.0 ili kuweza kuruhusu ndege kubwa kutua pale na kuruka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo litakwenda sambamba na ujenzi wa terminal building; tuna ka-terminal building pale kadogo sana ambako hata ndege aina hizi za caravan ambazo zinachukua abiria 12 na 13 zikitua mbili tu mnakuwa mmesharundikana pale passenger’s lounge. Kwa hiyo tunaomba sana upanuzi wa uwanja wa ndege huu uende sambamba na ongezeko la ujenzi wa terminal building.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisiwa cha Mafia kama nilivyotangulia kusema ni Kisiwa cha kitalii na utalii kwa sasa, kwa sababu kisiwa kimegawanyika katika maeneo makubwa mawili; eneo la kaskazini na eneo la kusini. Hili eneo la kusini ambapo ndipo kiwanja cha ndege kipo na shughuli za kiutawala kwa maana ya halmashauri na ofisi nyingine za Kiserikali zipo, pale miundombinu iko sawa kwa sababu watalii wakitua wanakwenda kwenye mahoteli moja kwa moja. Hata hivyo, kutoka pale Makao Makuu ya Wilaya kwenda moja kwa moja mpaka kaskazini kule kwenye light house ni kama kilometa 55 na ndiyo kabarabara kenyewe kamoja hakohako tu kama roho. Mheshimiwa Waziri Kwandikwa, mjukuu wangu, hebu kwanza watusaidie pale Mafia watumalizie hizi kilometa 55, sisi tena tunakuwa tumeshaagana na wao, tukiomba tutaomba mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kwa namna ya kipekee sana, tukimaliza ujenzi wa barabara hii ya kilometa 55, tutafungua na fursa za kiutalii upande wa kaskazini mwa Mafia ambapo nako pia kuna fukwe nzuri na kuna maeneo mengi sana ambapo mahoteli na ma-lodge yanaweza yakajengwa na kuweza kupata watalii wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la mawasiliano; namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Engineer Nditiye, alishafika pale Mafia na akaona changamoto zetu. Sisi kule zao letu kubwa ni zao la nazi, kwa hiyo minara ya simu inapata kidogo obstacles kwenye kurusha signals zake kwa sababu kunahitaji minara mingi zaidi kutokana na uwepo wa minazi mingi. Sasa maeneo mengi ya vijiji vya Mafia yanakosa mawasiliano ya simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Mawasiliano tuangalie kwa sababu eneo linapokuwa tena la kitalii na watalii siku hizi dunia imekuwa ndogo, imekuwa kijiji, wanataka zaidi kufanya mawasiliano ya intaneti, ya simu na vitu vingine, ingependeza zaidi tukawa na mawasiliano ya uhakika zaidi. Najua hilo lipo katika mikono salama kwa sababu watu wa Mfuko ule wa Mawasiliano kwa Wote na Mheshimiwa Naibu Waziri alinihakikishia kwamba watalifanyia kazi hilo ili kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri pale Kisiwani Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa harakaharaka tu nizungumzie kidogo na Wizara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau kwa mchango wako mzuri sana na ushauri, kwa hiyo muda wetu ndiyo huo, tunakushukuru sana.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nami nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wawili kwa mawasilisho mazuri. Nitakwenda kwa haraka kutokana na tatizo la muda.

Mheshimiwa Spika, nianze pale alipoishia Mheshimiwa Rehani, kuipongeza sana Serikali, Mawaziri wote wawili wa uvuvi upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara kwa kuondoa 0.4. Tumeanza kuyaona matunda. Pia nawe binafsi tunakushukuru kwa sababu mara ya mwisho tulipolizungumza hili jambo ulitia maneno yako na ninaamini Mawaziri wameyafanyia kazi na sasa tayari meli zimeshaanza kuja na tunapata mapato kama alivyosema Mheshimiwa Rehani.

Mheshimiwa Spika, nataka niendelee mbele kidogo kwamba Mawaziri wanasema wamesitisha kwa muda. Sasa ni muda muafaka sasa wakakaa wakaamua kama wanaifuta kabisa ama wanapunguza kiwango ama wanafanyaje ili hili jambo tulimaliza once and for all.

Mheshimiwa Spika, la pili, nilitaka nizungumze kidogo kuhusu suala la mkanganyiko wa matundu yale ya nyavu. Kuna sheria mbili hususan kule Mafia. Tuna sheria ya Hifadhi ya Bahari na tuna Sheria ya Uvuvi. Sheria hizi mbili zina mkanganyiko. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, alikuja Mafia ametusaidia kwenye eneo la dagaa. Tayari mgogoro kule umekwisha, lakini kwa sasa bado tuna mgogoro kwenye eneo la samaki. Sheria hizi mbili bado zinaendelea kugongana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi ili tumalize na hili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi atakubaliana nami, maeneo ya kuvua samaki wengi unatakiwa uende kidogo maeneo yenye kina kirefu. Sasa kwa bahati mbaya Wizara inazuia matumizi ya cylinder gas ya kuweza kuzamia chini kwa ajili ya ma- divers kwa sababu wanasema kwamba wanaenda kuchukua majongoo bahari. Sasa watu wanapokwenda kuvua kwenye kina kirefu cha maji bila kutumia msaada wa gas cylinder tunawa-condemn to death. Tunaomba sana mliangalie hili, mlifanyie kazi ili kuruhusu wananchi hawa waweze kuvua kwa kutumia gas cylinder. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la viboko. Mheshimiwa Waziri wa Utalii naomba anisikilize. Mwaka 2019 alituambia viboko wa Mafia watakwenda kupigwa mnada. Sasa hivi wameshafika 40 na wameshaanza kuingia mjini.

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii mje muwaondoe wale viboko Mafia kabla madhara makubwa hayajaendelea kufanyika. Mpaka sasa mtu mmoja ameshafariki, ng‟ombe kadhaa wameshauawa na mazao yamekuwa yakiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni Channel ya Utalii. Mheshimiwa Kanyasu mwaka jana hapa ulijibu swali langu kuhusiana na Channel ya Utalii kuja kutangaza vivutio vya utalii kule Mafia vya samaki aina ya Potwe na vitu vingine ambavyo vinavutia kule Mafia lakini mpaka leo hili jambo halijatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, Mafia ni sehemu ambayo ni ya kimkakati kabisa kiutalii, tungeomba sana Channel yetu ya utalii, ile ambayo inaoneshwa kwenye TBC waje kule wafanye shooting vivutio vile viweze kuonekana. Huyu samaki aina ya potwe tunamzungumza sisi tu humu ndani, watu wengi hawamjui, pengine hata Watanzania wengi nao pia hawamjui. Kupitia Channel yetu ile tunaamini kabisa mkitangaza tunaweza samaki yule akajulikana na vivutio vingine vinavyopatikana pale Mafia vikajulikana, ikatusaidia sana katika kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Kilimo cha Mwani; Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi mwani Mafia unalimwa na kina mama kule baharini. Tunaomba sana, wakulima wa mwami hawana vifaa, utaalam, hajawahi kuja mtaalam yoyote kutoka Wizara ya Uvuvi kuja kuwapa semina au maelezo yoyote kuhusiana na kilimo cha mwani kule Mafia.

Mheshimiwa Spika, amezungumza hapa Bobali kuhusu zao la nazi na kwamba zao la nazi linapendezesha sana chakula kwa watu wa Pwani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Dau dakika tano zimeisha…

MHE. MBARAKA K. DAU: …lakini…

SPIKA: Dakika 5 zimeisha Mheshimiwa Dau.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya kamati, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Ninaze kwa kumpongeza sana mtoa hoja leo asubuhi Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako yote ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Katibu Mkuu na timu yote pale Wizarani. Nitaanza na ukurasa wa 77 wa kitabu cha leo. Mheshimiwa Waziri pale anasema zimetengwa shilingi milioni 153 kwa ajili ya mgao wa maduhuli katika vijiji ambavyo vipo katika hifadhi ya bahari katika Kisiwa cha Mafia. Matatizo yangu yanaanzia pale, nina mambo mawili pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, hizi milioni 153 zimeandikwa pale kwamba zinakwenda kwenye vijiji 17 na Mheshimiwa Waziri alikuja Mafia tukasomewa taarifa kule Jibondo, Hifadhi ya Bahari ipo katika vijiji 12 tu na vitongoji vitano, hiki kitabu leo kinasema hifadhi ya bahari iko katika vijiji 17, imenishtua sana, hizi takwimu Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku- wind up naomba sana atupe maelezo, pengine inawezekana ikawa ni typing error, lakini kama sio typing error, basi kuna tatizo kubwa sana, kwa sababu moja ya kilio cha watu wa Mafia ni kwamba hifadhi ya bahari imekuwa ikiongeza mipaka kila uchao. Vilianza vijiji vitatu, vikaja saba sasa vipo 12, leo kitabu kinatuambia vijiji 17. Sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie, hivi vilivyoongezeka ni typing error au tayari himaya ya hifadhi ya bahari sasa imeongezeka tena kwa vijiji vingine. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna mgao hapa, kuna taarifa njema ambayo nashukuru sana Mheshimiwa Waziri amesema kuna shilingi milioni 43 zitaendelea kwa ajili ya kutolewa mikopo kwa wanavijiji ambao wamo ndani ya hifadhi ya bahari, ni jambo jema nashukuru sana kwa niaba yao. Hata hivyo, nataka nitoe tahadhari namna ya mikopo hii itakavyotolewa, uwepo utaratibu mzuri sana. Huko nyuma mikopo ilitolewa nje ya utaratibu, matokeo yake fedha nyingi sana hazikwenda kwa walengwa. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, watu wa hifadhi ya bahari, bahati nzuri naamini wapo hapa, wajue mambo yatakapokwenda uwepo utaratibu mzuri ili kusiwe na matatizo yaliyotokea kabla ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake leo asubuhi hapa ukurasa wa 62, wameeleza vizuri sana na nampongeza sana, kwamba wanafanya mapitio ya Sheria ya Uvuvi, Namba 22, ni jambo jema sana na katika moja ya mambo ambayo alipokuja Mafia Mheshimiwa Waziri tulimlalamikia kwamba kuna mgongano baina ya Sheria ya Uvuvi Namba 22 na Sheria ya Hifadhi ya Bahari. Sasa kwa kilio hiki sasa kuna mambo matatu ningeomba sana Mheshimiwa Waziri ayatilie maanani katika mchakato wake wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, suala la ukubwa wa nyavu wametuambia samaki watavuliwa kwa nyavu za nchi tatu. Mheshimiwa Waziri alipokuja Jibondo pale alipotamka neno kwamba samaki watavuliwa kwa nyavu ya nchi tatu wananchi walianza kugunaguna kwa sababu kule kwetu kwenye bahari kuna samaki wengine kwa asili ya maumbile yao hawakui zaidi ya ukubwa wa nchi moja na nusu, samaki aina ya ngalala, tili, mbono, samaki wadogo ambao kimaumbile hata ukiwaacha miaka 50 hawawezi kukua.

Sasa wametuletea sheria na sisi tumetoa maoni katika hii sheria mpya wanapoweka nchi tatu kuna baadhi ya samaki kama hawa niliowataja ngalala, misusa, tili, mbono hawatovuliwa maisha kwa sababu tundu la nchi tatu atapita tu huyo samaki, kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri waliangalie na hao wataalam, namshukuru sana alipokuja Jibondo akatuachia wataalam waje kutoa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako watalaam wale wavuvi waliwaambia tunashukuru sana mmekuja kutupa elimu, lakini mara ijayo mtakapokuja mje na wataalam wenyewe hasa wa kwenda kuvua baharini, tutachukua nyavu ya nchi tatu, tutakwenda baharini pamoja halafu na sheria kwamba nyavu hairuhusiwi kufungwa mawe chini isiburuze chini ili hao wataalam waende wakaoneshe namna gani ya kumvua samaki, nyavu chini isiguse na nyavu hiyo ni ya nchi tatu, kama utampata samaki hata mmoja. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri kama utaalam upo wa kuvua samaki wa nchi tatu kwa kutumia nyavu bila nyavu kugusa chini, basi tunaomba sana atuletee wataalam hao kwa ajili ya shughuli hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nyavu za milimita…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau malizia.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nyavu za milimita nane za kuvulia dagaa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, ametaja kwenye kitabu chake watabadilisha kutoka kwenye milimita 10 kuja kwenye milimita nane, ni jambo jema na tunashukuru sana. Tunaomba sana taarifa hizi ziende kule chini kwa sababu bado kule wataalam watekelezaji wa sheria wanaendelea kuwasumbua wavuvi. Mheshimiwa Waziri dakika moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Uvuvi; hili ni jambo ambalo limezungumzwa sana humu. Namna pekee ya kuleta ukombozi katika uvuvi na kuongeza mapato ya Serikali tuwe na bandari yetu ya uvuvi na nashukuru kwenye kitabu hiki nimeiona bandari ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni lile alilolisema Mheshimiwa Tizeba, Mheshimiwa Waziri akaiangalie ile kanuni ya 0.4 kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu imewakimbiza wakubwa wote wale hawaji sasa hivi, kwa hiyo naomba sana kama watai- relax ile ili meli zile zije zivue kwa sababu ile DSFIA inakufa na inakufa kwa sababu hakuna mapato yoyote anayekuja kukata leseni kwenda kuvua katika bahari kuu kwa sababu gharama ile ya loyalty ya 0.4 wanaiona ni kubwa, iliwekwa kwa nia njema lakini bahati mbaya sana wenzetu hawa hawajakubali kutuletea meli. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dau, muda umepita kwa kweli.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii na mimi nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndugu yangu Dkt. Mpango kwa kutuletea bajeti hii ambayo kwa kiasi kikubwa sana inaakisi matarajio na matazamio ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda wa takribani miezi minne, tupo hapa Dodoma tukianzia kwenye Kamati kuangalia ni namna gani tunaweza tukaishauri Serikali katika kuhakikisha kwamba tunaboresha bajeti mbalimbali za Wizara. Lakini kumekuwa na maneno kwamba wengi hapa muda mwingi sana tunautumia masuala ya matumizi; maji, umeme, barabara, hospitali, shule na vitu kama hivyo na muda mchache/mfupi sana tunautumia katika namna ya kuishauri Serikali itakavyoweza kuongeza wigo na uwezo wa kupata mapato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi mchango wangu utajikita zaidi namna gani ya kuishauri Serikali itakavyoweza kuongeza mapato ili sasa yale matumizi yaweze kwenda sambamba na mapato yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninakushukuru sana Mheshimiwa Mpango, nimesoma kitabu chako cha hotuba hususan katika eneo la mifugo na uvuvi, tozo na ada nyingi sana zimefutwa, tunaishukuru Serikali.Lakini tozo na ada nyingi zilizofutwa ni zile tozo zinazohusu masuala ya mifugo zaidi kuliko masuala ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali tuangalie sasa namna gani tunaweza tukaenda tukapitia zile tozo na ada mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uvuvi. Mvuvi bado ana mzigo mkubwa na mrundikano mkubwa sana wa ada na tozo mbalimbali. Kuna leseni kwanza ya chombo, leseni ya mvuvi mwenyewe, usajili wa chombo, ada/leseni ya kuvua kwa sisi tunaotoka Pwani kule kuvua pweza, samaki, kamba na vitu kama hivyo, kuna utitiri mwingi sana wa ada na tozo kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba sana Mheshimiwa Mpango utakapokuja basi utuangalie na sisi katika eneo la uvuvi. Hivi ninavyozungumza, pale mpakani Tunduma kuna mizigo na tani kadhaa za dagaa wanaotoka hususan kule Mafia wapo pale wamezuiwa kutokana na ile ada ya dola 1.5, hii imekuwa ni mwiba mkubwa sana kwa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hawa wafanyabiashara wanaouza dagaa wengi wanatokea maeneo ya Congo, wanakuja kule kwa mfano kule ninapotokea mimi Mafia wanakuja kununua dagaa, lakini wanakutana na tozo na ada nyingi sana. Mimi nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Mpango, tunashukuru kwa upande wa mifugo kule mambo yamekwenda vizuri na sisi wavuvi tunaomba pia mtukumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye eneo hilo hilo la uvuvi lakini sasa katika eneo la uvuvi wa bahari kuu. Tulizungumza hapa na mimi nimeshachangia mara nyingi sana kwamba namna gani Taifa hili linaweza likanufaika kutokana na uvuvi na mapato yanayotokana na uvuvi wa bahari kuu. Mimi nashukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, juhudi tunaziona; kwanza juhudi zile za kufufua lile Shirika letu la Uvuvi la TAFICO, ni juhudi za kupongezwa na kuungwa mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia juhudi tumeona kwamba kwenye bajeti imetengwa fedha kwa ajili ya kununua meli, lakini mimi bado ninaamini zile meli ambazo tutazinunua, uwezo wake hautokuwa mkubwa sana kulinganisha na meli zile ambazo za kigeni zinazovua katika ule ukanda wa kiuchumi wa bahari wa EEZ ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa sasa mimi ningeomba sana na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi simuoni hapa lakini nadhani Naibu atakuwepo. Tatizo lililokuwepo ambalo naomba sana tulianyie kazi, ni ilea da ya dola 0.4 ambayo inatozwa kwa kila kilo moja ya samaki aina ya jodari au maarufu tuna anayevuliwa katika EEZ yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya sana, wale wenye meli kubwa ada hii hawajakubaliana nayo na toka imewekwa wamesusa, hawaji. Sasa bahati mbaya tuliyokuwa nayo, ile mamlaka yetu ya uvuvi wa bahari kuu DSFA, ile inategemea mapato yake yote kutokana na leseni zitakazokatwa na wale wenye meli kubwa wanaokuja kuvua katika EEZ yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa kutokana na hii ada ya dola 0.4 wameona kwao ni mzigo mkubwa, wamehama wanakwenda katika nchi jirani wanakata leseni, nini hasara yake? Hasara yake samaki siyo kama madini labda ya dhahabu ukasema yapo pale Buzwagi au Bulyanhulu, hayatoki mwaka wowote tunaweza tukachimba, samaki wanatembea…

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. MBARAKA K. DAU: ...samaki, Mheshimiwa…

MHE. MATTAR ALI SALUM: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dau kuna taarifa. Mheshimiwa Mattar.

T A A R I F A

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimpe taarifa kaka yangu kwamba hii dola 0.4 ikiondoshwa leo, wapo wawekezaji wenye meli zaidi ya 50 wapo tayari kuja kuvua kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, hii dola 0.4 ni tatizo kubwa katika nchi yetu katika uwekezaji wa bahari kuu, asante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbaraka Dau unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu kwamba naipokea taarifa hiyo pia naomba iwe sehemu ya mchango wangu kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema samaki hususan, maana yake samaki wanaozungumzwa hapa ni jodari tu (tuna) wale, wale wenye meli kubwa wakija kuvua wao habari ya samaki wengine wanaitwa by catch wale wanaovuliwa kwa bahati mbaya wale hawawahitaji, wao wanahitaji tuna tu. Sasa hawa samaki tuna ni samaki wa makundi, wanatembea, leo wapo katika pwani ya Tanzania, kesho wapo katika pwani ya Somalia na baadaye wapo kwenye pwani nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wewe unapozuia kwa maana ya kuweka masharti magumu kama hii royalty ya 0.4 hawa samaki haina maana kwamba watabaki hapa hapa Tanzania tu, samaki hawa wanahama na wanahama kutokana na texture ile ya bahari inapobadilika kwa sababu kuna hizi pepo za kaskazi, pepo za kusi, kuna nyakati bahari inakuwa na motomoto na kuna wakati bahari inakuwa baridi, kwa hiyo hawa samaki wanahama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tusipotoa ruhusa hii na mimi sisemi ifutwe kabisa, hata kama tukianza na labda 0.1 ili kwanza tuwavute hawa watu na ile Mamlaka yetu DSFA basi ianze kufufuka, tuweze kwenda vizuri na faida zinazotokana na uvuvi wa bahari kuu ni pamoja na vijana wetu kupata ajira kwenye zile meli kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za DSFA ni kwamba meli zinapokuja kuvua, watanzania wanapata fursa ya kuwa mabaharia ndani ya zile meli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini faida nyingine, kanuni zinasema na Mheshimiwa Ulega utakuwa unazifahamu, kanuni zinasema wale samaki (by catch) ambao siyo walengwa labda umevua papa, nguru, changu na samaki wa aina hiyo, hawa inabidi uje uwalete katika Bandari aidha ya Zanzibar au Bandari ya Dar es Salaam na inakuwa ni mali ya United Republic of Tanzania.Kwa hiyo, hizi faida zote sisi tunazikosa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeomba sana, najua kuna mchakato wa kisheria katika kupunguza, kufuta au kufanya hivi, basi tuuanzishe huu mchakato ili tuhakikishe kwamba tunanufaika na uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuna kitu kinaitwa uendelezaji wa utalii katika kanda ya kusini (southern circuit). Unapoizungumzia southern circuit, mimi nasikitika sana na nimemuona ndugu yangu Mheshimiwa Kanyasu hapa. huu utalii wa kanda ya kusini mbona utalii wa fukwe haupo? Sisi tunaotoka Mafia, Mafia na yenyewe ni sehemu ya kanda ya kusini; sasa hatuoni mikakati yoyote ya kuendeleza utalii katika fukwe ambapo Mafia ni sehemu kubwa sana ambayo watalii wanatakiwa waje pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna faida nyingi sana za kukifungua Kisiwa cha Mafia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mwijage, kwa hotuba nzuri ya bajeti yenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuweka mbele mapinduzi ya viwanda. Juhudi hizi tumeanza kuona matunda chanya na Tanzania ya viwanda sasa inaonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kisiwa cha Mafia wamehamasika katika kilimo cha miwa na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kupata mazao mengi, lakini tatizo limekuwa ni kutokuwepo na kiwanda cha kuchakata miwa ili kupunguza ukubwa wa mzigo na kujirahisishia usafirishaji wa mazao. Namwomba tu Mheshimiwa Waziri kupitia Shirika la SIDO, aangalie uwezekano wa Mtaalam kuja na kiwanda rahisi kusaidia wakulima wa miwa wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisiwa cha Mafia pia ni maarufu kwa ulimaji wa zao la nazi. Kwa kuwa zao la nazi linatoa mafuta na tui kwa matumizi ya mwanadamu, nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano wa kutupatia kiwanda kitakachochakata mazao yatokanayo na nazi ili kusaidia kukuza kipato cha mwananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais mwaka anazindua Bunge hili la Kumi na Moja alionesha masikitiko yake ya kukosekana kiwanda cha kusindika samaki kwa ukanda mzima wa Pwani kuanzia Mkoa wa Tanga mpaka Msimbati Mtwara. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa ukaribu suala hili la kiwanda cha kusindika samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijadili suala Kitaifa la viwanda. Niiombe tu Serikali yangu kwenye kuelekea viwanda, mkazo uwekwe kwenye kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi badala ya Serikali kujenga viwanda vyake yenyewe. Serikali haifanyi biashara, Serikali isubiri kutoza kodi na kupata fursa ya kutoa ajira kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, naomba Serikali ianzishe vyuo aina ya VETA katika makambi yetu ya Jeshi la Kujenga Taifa. Aina ya viwanda inayokuja sasa, lazima tuandae vijana wetu kwenye kada za kuendesha mashine (Machines Operators). Hii itasaidia kwao kupata ajira kwenye viwanda hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuoanisha uanzishaji wa viwanda na kilimo chetu. Sisi mazao yetu mengi ya matunda yanaoza mashambani kwa kukosa kiwanda cha kusindika matunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukweli kwamba tuna kiwanda cha Azam pale Mkuranga, lakini kiasi kikubwa wanaagiza matunda concentrate kutoka nje ya nchi. Hii inatokana na ukweli kwamba matunda yetu hayalimwi kitaalam na kupelekea shamba moja kutoa matunda yenye ladha tofauti na kushindwa kutengenezwa juice. Kilimo cha kisasa ndiyo namna pekee ya kuoanisha ladha ya mazao haya ya matunda ili yaweze kutumika kutengeneza juice.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ya kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini. Naipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kufuta kodi zenye kero kwa wakulima na wavuvi wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kero kubwa ya taasisi ya Serikali ya Hifadhi ya Bahari Mafia (HIBAMA) kwenye mgao wa maduhuli yatokanayo na watalii wanaoingia katika maeneo ya hifadhi, Halmashauri ya Mafia inapata asilimia 10 ya pato halisi, yaani baada ya kutoa gharama za uendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza asilimia 10 ni kiwango kidogo sana ukizingatia mzigo unaobebeshwa na Halmashauri kwenye kuendesha shughuli za afya, elimu na miundombinu. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri yeye ndiye mwenye kutengeneza kanuni, kwa kipekee tunamwomba sasa aridhie ombi letu la kubadili kanuni ili kiwango hiki kiongezwe kutoka asilimia 10 mpaka kufikia asilimia 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni hili la pato halisi (net income), baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji za hifadhi ya bahari zikiwemo semina, safari, likizo na malipo ya ziada, baada ya saa za kazi ibaki zile gharama za kukusanya mapato tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uwekezaji unaofanywa na hifadhi ya bahari katika visiwa vya Shungimbili, Mbarakuni na Nyororo. Kimsingi sisi watu wa Mafia hatupingi mwekezaji, bali namna ya uwekezaji na mchakato mzima ndiyo unaacha maswali mengi bila majibu. Kitendo cha kutowashirikisha wananchi hakikubaliki hata kidogo. Ni ushauri wetu kwamba suala la mwekezaji liachwe kwenye ngazi ya Halmashauri kutoka hifadhi ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ongezeko la vijiji vya eneo la hifadhi ya bahari. Hifadhi ilianza na vijiji vinne tu, lakini leo imeongezeka mpaka kufikia vijiji 13 na Wilaya ya Mafia ina jumla ya vijiji 23. Ukweli huo zaidi ya nusu ya vijiji ipo chini ya himaya ya hifadhi ya bahari na sasa wananchi wanakatazwa hata kulima mbali ya kuvua. Kilio chetu ni kwa nini mchakato wa kuongeza vijiji vya eneo la hifadhi haikushirikisha wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubinafsishaji wa kisiwa cha Nyororo na Mbarakuni usitishwe mara moja kwa maslahi ya Taifa hili ili kasa waweze kupata maeneo ya kutagia mayai yao, kuokoa kiumbe huyo asipotee katika sura ya nchi yetu.

Mheshimiwa Waziri, Meneja Mkuu wa Hifadhi ya Bahari awajibishwe kwa kosa la kuuza kisiwa cha Shungimbili kinyume na utaartibu wa kushirikisha wananchi na mwekezaji kujenga bila ya kuwa na kibali cha ujenzi (building permit). Vilevile huyu Meneja Mkuu alimwongopea Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara ya kiserikali Mafia kuwa Halmashauri ya Mafia haidai hifadhi fedha za maduhuli, lakini baada ya Waziri Mkuu kuondoka, Hifadhi ya Bahari walilipa Halmashauri shilingi milioni 44. Kitendo hiki cha kumdanganya kiongozi mkubwa huyu mbele ya Mkuu wa Wilaya ni kitendo cha utovu wa nidhamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa bajeti yenye matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mafia ni kisiwa na kutokana na jiografia yake hiyo hakuna mito yenye kutiririka mwaka mzima. Ukweli kuwa chanzo kikuu cha maji kisiwani Mafia ni uchimbaji wa visima virefu na vifupi. Kwa masikitiko makubwa miradi ya maji iliyoletwa Kisiwani Mafia ni michache sana hivyo kisiwa cha Mafia kina shida kubwa ya maji. Kupitia Bunge lako Tukufu kwa namna ya kipekee, tunaiomba Serikali ituongezee miradi ya maji kutokana na mazingira magumu ya upatikanaji wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kuvusha maji kutoka Kisiwa Kikuu cha Mafia eneo la Kiegeani kwenda Kisiwa kidogo cha Jibondo takriban kilometa tisa umekuwa kwenye hatua mbalimbali za michakato kwa takribani miaka mitano sasa. Kupitia Bunge lako hili Tukufu tunaomba Serikali iharakishe mchakato huu kwani Kisiwa cha Jibondo kwa asili na ardhi yake ni mawe matupu na hakuna namna yoyote hivyo kulazimisha kuchimbwa kisima kilometa tisa nje ya Kisiwa Kikuu cha Mafia na kupitisha mabomba chini ya maji mpaka Kisiwa cha Jibondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kwa kuwa mradi huo haupo wananchi wanalazimika kukodi mashua za uvuvi kuja Kisiwa Kikuu na madumu ya maji na kuchota maji na kuvuka nayo. Nyakati za pepo kali za kusi na kaskazi zoezi hili linakuwa gumu na wananchi wanatumia maji ya chumvi ambayo ni hatari kwa usalama wao. Hivyo, tunaiomba Serikali kuharakisha mradi huu ili kuondoa adha hii kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Philipo Mpango, kwa hotuba yenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa bajeti ya 2016/2017, taarifa inasema kati ya fedha za maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 18.89 kilikuwa kimetumika ambacho ni asilimia mbili tu ya fedha iliyoidhinishwa. Ni dhahiri hiki ni kiwango kidogo sana katika utekelezaji wa bajeti hii. Nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango utekelezaji wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2017/2018 uwe wa uhalisia zaidi kuliko kwenye makaratasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Ofisi hii ndiyo jicho letu sisi Bunge katika kuisimamia Serikali. Cha kusikitisha, ofisi hii imekuwa ombaomba kwa Serikali. Hili linatia shaka na doa kwenye uhuru wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kuwa utendaji wake unatakiwa uwe huru bila ya kuingiliwa na yeyote. Uhuru huo unakuwa na mashaka kama iwapo Mkaguzi anaenda kwa mkaguliwa kuomba fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu kwa mwaka 2016/2017, iliidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 44.6 lakini mpaka kufikia mwezi Machi 2017, Ofisi ilikuwa imepokea shilingi bilioni 32.6 ikiwa ni sawa na asilimia 73.05 ya bajeti ya matumizi ya kawaida. Ni dhahiri Ofisi hii itapata shida kama tulivyoshuhudia imeshindwa kufanya kaguzi kwenye baadhi ya Balozi na ofisi nyingine nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ya bajeti. Nianze na mgogoro wa shamba la Tumaini lenye ukubwa wa ekari 4,000 ambalo Mheshimiwa Waziri, kwa uzalendo wa hali ya juu wa kuthubutu alifuta hati miliki ya shamba lile. Hicho ni kitendo cha kijasiri kabisa na chenye kuendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kuwa suala hili lipo mahakamani, lakini wananchi wa Mafia wanaunga mkono uamuzi wa Mheshimiwa Waziri wa kuifuta hati na kulirejesha shamba miliki kwa wananchi. Ombi letu ni mara baada ya shauri lililopo Mahakamani kumalizika tunaomba mgao wa shamba hili ufanywe na Halmashauri yetu ya Mafia kulingana na vipaumbele vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumwomba Mheshimiwa Waziri alifute shamba la ng’ombe ambalo limebaki pori kubwa na ongezeko la watu limepelekea ongezeko kubwa la mahitaji ya ardhi kisiwani Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC); Halmashauri ya Mafia tumetenga eneo kubwa la kutosha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kupitia Shirika hili. Nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri, aagize uongozi wa Shirika hili kuanza mradi huu haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa hotuba yake nzuri na yenye kuleta matumaini. Tatizo la x-ray na Hospitali ya Wilaya ya Mafia limeingia katika hatua nzuri kuelekea kumalizika baada ya Serikali kutupatia mtaalamu wa mionzi (Radiology) na kufuatia mazungumzo yangu na Naibu Waziri Mheshimiwa Faustine Ndugulile tumekubaliana kuuwa tarehe 23 Aprili ataleta mtaalam sambamba na mtaalam wa kampuni iliyoleta x-ray hiyo ambao mimi Mbunge nawajibika kuwalipia gharama za safari zao kutoka India mpaka Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu mara ya kwanza mwaka 2016 niliingia gharama ya kuwaleta wataalam hao kwa gharama kubwa kuwafikisha Mafia na Wizara yako Mheshimiwa Waziri iliweka katazo la kufanya x- ray ya zamani iliyotolewa na kampuni ya Philips ambayo ndio yenye mkataba na Wizara kutengeneza mashine za x-ray. Mheshimiwa Waziri wataalam wale walikaa Mafia kwa wiki tatu huku mimi binafsi nikishughulikia vibali vya kufunga mashine bila ya mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo furaha kukufahamisha kuwa baada ya mjadala mrefu uliopelekea kujengwa kwa chumba kipya cha x-ray sasa Wizara imeridhia kufungwa kwa x-ray Mafia na Naibu Waziri amenihakikishia atatuma mtaalam wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo ninalotaka kulitoa hapa ni mnaingia gharama kwa mara ya pili kuwaleta wataalam kutoka India kuja kufunga x-ray ile. Ninaomba Wizara itekeleze ahadi yao hii ya kutoa ushirikiano ili x-ray ile ifungwe Mafia. Ni ukweli usio na shaka ikishindikana kufungwa mara hii sitapata na sitakuwa na uwezo wa kugharamia gharama hizi ambazo kwa kweli ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia gari la wagonjwa (ambulance)ni kuukuu na hufanya kazi kwa taabu sana na linaharibika mara kwa mara. Hivyo tunaiomba Wizara itufikirie kupata ambulance mpya. Sambamba na hilo Kisiwa cha Mafia kimezungukwa na visiwa vidogo vidogo vinne yaani Jibondo, Bwejuu, Chile na Juani. Kwa namna ya kipekee tunaiomba Wizara itusaidie kupata ambulance boats ili kusaidia dharura zinapotokea iwe rahisi kuwa wagonjwa kukimbizwa Hospitali ya Wilaya.

Mwisho tunaishukuru Serikali kwa ahadi ya shilingi milioni 500 za kujenga Kituo cha Afya Kirongwe. Tunaomba tuharakishiwe kupata fedha hizo ili ujenzi uanze mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kuunga mkono hoja. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Makame Mbarawa kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mafia ambayo kijiografia ni kisiwa ina tatizo kubwa la usafiri wa bahari kutoka na kuingia Mafia kupitia Bandari ya Nyamisati iliyopo Wilaya ya Kibiti. Tunaishukuru Serikali katika bajeti hii tumeona zimetengwa shilingi bilioni tatu kuanza ujenzi wa meli ya kisasa. Kwa kuwa mchakato wa kujenga meli hii utachukua muda wa miaka takribani miwili tunaiomba Serikali itupatie kivuko/meli ya muda wakati tunasubiri mchakato wa kujenga kivuko chetu ukiendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tunaiomba Serikali iagize SUMATRA waje kuangalia upya katazo waliloliweka la kupakia abiria 50 tu kwa boti zinazofanya kazi sasa hivi ambazo uwezo wake wa kupakia abiria ni mkubwa sana mpaka kufikia abiria 200. Kwa hali ilivyo sasa wananchi wanalazimika kusubiri mpaka wiki nzima, jambo ambalo linaleta usumbufu hususani kwa wagonjwa na wenye dharura mbalimbali. Tunaiomba SUMATRA waje Mafia na kuliangalia suala hili kwa kushirikiana na wadau wa Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wa ndege wa Mafia ni muhimu sana katika kukuza utalii nchini, Wilaya ya Mafia inapokea watalii zaidi ya 10,000 kila mwaka na wote hao wanatumia uwanja huu wa ndege. Mafia imejaliwa vivutio vingi vya utalii ikiwemo maeneo ya scuba diving, sports fishing, fukwe nzuri na samaki wa ajabu aina ya potwe (whaleshark) ambaye anapatikana katika nchi chache duniani lakini hali ya uwanja wa ndege wa Mafia ni mbaya sana, hakuna jengo la abiria (terminal building),barabara ya kutua na kurukia (runway) ni fupi yenye urefu kiasi cha mita 800 hali ambayo hairuhusu ndege kubwa aina ya Boeing kutua na kusababisha kukosekana kwa safari za moja kwa moja kutoka nchi za ughaibuni kuja Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kilindoni mpaka Ras Mkumbi kilometa 55 ipo katika Ilani ya CCM 2010 – 2015 na ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete. Hali ya barabara hii ni mbaya sana na nyakati za masika inakatika na kuvunja mawasiliano baina ya Tarafa ya Kaskazini na Tarafa ya Kusini. Vilevile udongo unaotumika katika kufanya matengenezo ya kawaida (periodical maintenance) unapatikana kwenye vijiji viwili tu vya Bweni na Jimbo, udongo huo unakaribia kuisha na wahandisi wanasema umebaki udongo wa kutumika kwa miaka mitatu tu, baada ya hapo tutalazimika kutoa udongo kutoka Rufiji. Njia nyepesi ni barabara hii kuwekwa lami ili kuepusha gharama kubwa ya matengenezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mwakyembe kwa hotuba nzuri na yenye kutia matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchezo wa mpira wa miguu bila shaka ndiyo mchezo unaopendwa na Watanzania wengi kuliko mchezo mwingine wowote hapa nchini. Ni ukweli usio na shaka shirikisho linalosimamia mchezo huu TFF, lina changamoto nyingi zinazohitaji kurekebishwa ili kuleta faraja na furaha kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto hizo ni Katiba ya TFF ina mapungufu mengi sana, mojawapo likiwa ni hili la uchaguzi wa kumpata Rais wa TFF. Ushiriki wa wadau ni mdogo sana na vigumu kuamini Rais wa TFF Taifa anapigiwa kura na Wajumbe 128 tu nchi nzima. Kuminywa huku kwa demokrasia kunasababisha kupata viongozi wabovu. Tatizo hili linaanzia kwenye ngazi ya chini kabisa mpaka Taifa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya Katiba ya TFF kufanyiwa marekebisho makubwa ili kuongeza ushiriki mkubwa wa wadau kwenye chaguzi za ngazi zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuanzishwa kwa kituo kikubwa na cha kisasa kwa wanariadha Wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara ni jambo muhimu katika kukuza vipaji vya wanariadha wetu. Nchi yetu miaka ya 1970 na 1980 ilikuwa haikosi kwenye orodha ya nchi zinazopata medali kwenye michuano ya Kimataifa na kwa kiasi kikubwa wanariadha hao walikuwa wanatoka maeneo ya Mkoa wa Manyara, hivyo ni muhimu Waziri ukalifanyia kazi wazo hili ili tuwe na chuo ama kituo cha kisasa cha michezo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzorota kwa michezo katika Majeshi yetu ni jambo ambalo Mheshimiwa Waziri alitupie macho vilevile. Zile zama za kina Willy Isangura, Nassoro, Michael, Kingu na kadhalika zimeyeyuka na tumekuwa wasindikizaji kwenye michezo ya Kimataifa. Ipo haja ya kuliangalia jambo hili kwa undani kujua chanzo chake na kupata ufumbuzi ili turudi kwenye zama zile mchezo wa ndondi na mingine iliyokuwa inatuletea sifa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.

Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kushukuru kwa nafasi hii. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako kwa hotuba nzuri na yenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mafia kwa kushirikiana na Mbunge wao wamefanikisha kujenga Chuo cha Ufundi, VETA. Majengo na miundombinu ya chuo hicho yameshakamilika na wanafunzi wameshaandikishwa na wameanza masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyonayo sasa ni usajili wa chuo. Tumeshafanya taratibu zote na Wakaguzi wa Kanda, wamekuja Mafia na kukikagua chuo na wameonesha kuridhika kwao na majengo, miundombinu na wana taaluma na wakufunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Wizara itusaidie kuharakisha usajili huu kwani Mafia ni miongoni mwa maeneo ya pembezoni na kuwavusha wananchi waje Dar es Salaam. Ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la shule binafsi kudahili wanafunzi na kisha kuwachekecha kwa mtihani migumu ili kupata wanafunzi best na kupata viwango bora, ni jambo ambalo Wizara lazima ilitupie macho, kwani linawanyima haki vijana wetu kwa uroho wa wamiliki wa shule ili kupata viwango bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la nazi linapotea kwa kasi kubwa na nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona mikakati yoyote ya kufufua zao hili ambalo ni muhimu sana maeneo ya mwambao wa Pwani hususan Kisiwa cha Mafia, mkoani Pwani. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hoja anieleze mipango kupitia utafiti ili kunusuru zao hili la nazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha utafiti wa kilimo kilichopo Mikocheni kina hali mbaya sana kifedha na Wizara bado haipeleki fedha ambazo kwa kiasi kikubwa itaokoa zao la nazi ambalo linazidi kupotea kutokana na minazi ya zamani kuanza kuzeeka na hakuna mipango mbadala ya kupanda miche ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha mwani kinacholimwa zaidi Kisiwani Mafia hakijapewa kipaumbele chochote katika bajeti hii. Miongoni mwa changamoto za kilimo hiki ni soko, mpaka sasa wananchi wa Mafia wamezalisha mwani mwingi na umerundikana katika maghala, changamoto nyingine ni vifaa duni wanavyotumia wananchi. Nimuombe Mheshimiwa Waziri awape zana za kisasa wananchi wa Mafia, hususani Kisiwa cha Jibondo ambao uchumi wao umeporomoka sana kutokana na katazo la kuvua wanategemea kilimo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto ya taaluma ya kisasa, tunaomba Serikali itupatie wataalam wa kuendesha mafunzo ya ukulima wa kisasa wa mwani. Ninashukuru na ninaunga mono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa fursa hii na nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa mabadiliko makubwa aliyoyafanya kwenye uongozi wa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari (MPRU) kwa kuteua mtendaji mpya na kuvunja bodi ya taasisi. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aharakishe kuunda bodi kwani pesa za maduhuli kwa Halmashauri ya Mafia zimekwama kutolewa kwa sababu MPRU haina bodi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni uwekezaji uliofanywa na MPRU kwenye Kisiwa cha Shungimbili na Hoteli ya Thanda. Mwekezaji anatakiwa alipe service levy ya 0.3 kwenye Halmashauri ya Mafia lakini wawekezaji hawa wamegoma kulipa ada hii kwa maelezo kuwa wanalipa moja kwa moja kwenye MPRU. Hii ni kinyume na sheria kwani ada hii ni haki ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, vilevile mwekezaji huyu Thanda Hotel mwaka jana wakati nachangia nilimuomba Waziri awaagize wafute jina la Thanda Island kwani Kisiwa kile kinaitwa Shungimbili na siyo Kisiwa cha Thanda. Waziri aliahidi kuwa maelekezo yameshatolewa kwa mwekezaji kufuta jina la Thanda Island lakini mpaka hivi sasa tovuti rasmi ya hoteli hiyo inasomeka kwa jina hilohilo la Thanda Island. Nimuombe Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi jambo hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mipaka ya Hifadhi ya Bahari katika Kisiwa cha Mafia, ,mwaka 1994 wakati Hifadhi ya Bahari inaanza ilianza na vijiji vitatu tu yaani Jibondu, Chule na Juani, hivi sasa hifadhi ipo katika vijiji 13. Cha kushangaza zaidi uongezaji wa vijiji vya hifadhi umefanyika kinyume na matakwa ya kisheria na wananchi wa vijiji husika hawakushirikishwa na wameingizwa kwenye hifadhi bila ya kupewa fursa ya kuulizwa na wao kutoa ridhaa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni maduhuli yatokanayo na watalii kuingia katika maeneo ya hifadhi. Kanuni ya Hifadhi inayopanga mgao wa asilimia 70 kwa Hifadhi, asilimia 10 Halmashauri na asilimia 20 vijiji husika haipo sawa hasa kwa kuzingatia Halmashauri ya Mafia ina majukumu makubwa katika jamii kama elimu, afya, barabara na maji. Tunaomba Mheshimiwa Waziri abadilishe kanuni na mgao uwe 50/50 baina ya Halmashauri na MPRU.

Mheshimiwa Spika, suala la ubinafsishaji wa Visiwa vya Nyororo na Mbarakuni, namuomba sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe MPRU inashirikisha Halmashauri kwenye uwekezaji wowote katika Kisiwa cha Mafia.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mafia kijiografia ni kusini na inahudumiwa na kituo kimoja cha Polisi cha Wilaya. Mapema mwezi wa Nne mwaka huu, gari pekee linalohudumia kituo hicho aina ya Land Cruiser (Pick Up) lilipata ajali ya kutumbukia baharini kwenye Bandari ya Kilindoni, Mafia. Kwa kuwa kina cha maji kilikuwa ni kikubwa, gari lile limeharibika sana kiasi cha kutoweza kutengenezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hali hii, Wilaya ya Mafia haina gari la Polisi; na kutokana na jiografia yake, hatuwezi hata kuazima gari kutoka Wilaya jirani. Mbaya zaidi, wahalifu wamechukua fursa ya kufanya uhalifu. Namwomba Mheshimiwa Waziri atupatie gari lingine, kwani hali inazidi kuwa mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri atupatie Kituo kidogo cha Polisi katika Tarafa ya Kivungwe, Kata ya Kivungwe. Hii inatokana na ukweli kwamba umbali kutoka kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ni mkubwa, wananchi wanalazimika kusafiri masafa marefu kufuata huduma hii ya Kipolisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mashehe wa Uamsho linaingia mwaka wa tano sasa bila ya kujulikana hatma yao. Mashehe hawa wamekaa rumande kwa muda mrefu na mmoja wa wake wa Mashehe hao amejiua kutokana na kushindwa hali ya maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, wapiga kura wangu watatu kutoka Wilaya ya Mafia wanashikiliwa rumande mwaka wa pili huu sasa kwa tuhuma za ugaidi. Tunaomba haki itendeke kwa mujibu wa sheria za nchi. Kama hawana hatia, basi waachiwe huru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Wilaya ya Mafia ipo katika hali mbaya sana. Kutokana na jiografia yake Wilaya ya Mafia hadhi yake inatakiwa iwe katika kiwango cha hospitali ya mkoa. Hii ni kwa sababu mazingira ya Kisiwa chenye changamoto kubwa ya usafiri, ukosefu wa huduma ya x-ray, vifaa vya maabara, Madaktari na Wauguzi kinapelekea uwepo wa adha kubwa kwa wananchi. Hivyo nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa namna ya kipekee atupie jicho hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mafia haina kituo cha afya hata kimoja. Naishukuru Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kirongwe, kutokana na sisi kuwa na maeneo ya pembezoni nilitarajia Mafia ingekuwa katika awamu ya mwanzo ya kupatiwa fedha hizi za ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunaomba sana Serikali itekeleze ahadi hii kwani wananchi hususan wakazi wa Tarafa ya Kaskazini wanalazimika kusafiri masafa marefu kufuata huduma ya afya. Wananchi hawa wamefarijika sana na taarifa za ujenzi wa kituo cha hiki cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo hospitali ya Wilaya ambulance iliyopo ni kuukuu na inaharibika mara kwa mara. Kwa mazingira ya Mafia tunahitaji kuwa na ambulance mpya na ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni pamoja na Mafia kuwa Kisiwa ndani yake kuna visiwa vingine vidogo ambavyo wanaishi watu; Visiwa hivyo ni kama Juani, Jibondo, Chole na Bwejuu ambapo kuna zahanati za Serikali. Kwenye visiwa hivyo, kuna changamoto kubwa ya kuvifikia na kuna wagonjwa wanaopata rufaa ya kuja katika hospitali ya wilaya, hakuna ambulance boat ya kuwaleta na kuwapeleka akinamama wajawazito, kupanda mitumbwi na vyombo vingine ambavyo si salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ametoa boats kwenye maeneo mengine ambayo yanaweza kufikika kwa barabara lakini kumepewa boat. Hivyo kwa namna ya kipekee, naomba kuwasilisha ombi la wananchi wa Mafia kutoka katika Visiwa vidogo vya Juani, Kibondo, Chole na Bwejuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu pia ni changamoto katika Kisiwa cha Mafia. Tunaishukuru Serikali tumepata shule za kata, lakini uhaba wa Walimu hususani Walimu wa sayansi limekuwa ni tatizo, tunaomba Serikali ituongezee Walimu wa sayansi ili kiwango cha ufaulu kiongezeke. Sambamba na hili ujenzi wa mabweni hususani kwa wanafunzi wasichana, kwa mfano Kata ya Kirongwe yenye shule ya sekondari Kirongwe wanafunzi kutoka Kijiji cha Jiji na Banja wanalazimika kusafiri masafa marefu karibu kilometa 10-15 kila siku jambo ambalo si salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utendaji wa TARURA Wilaya ya Mafia linatakiwa kutupiwa macho. Mpaka sasa barabara na madaraja katika Wilaya ya Mafia hakuna kilichofanyika, kwa mfano, barabara ya kunganisha Kijiji cha Banja na Jiji inapitika kwa tabu hasa kipindi hiki cha mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii na naanza kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru na kumpongeza mtoa hoja Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri. Nianze kuchangia hotuba hii kwa kurejea kitabu cha hotuba ukurasa wa 50 juu ya mkataba wa Nairobi kuhusu hifadhi, usimamizi na uendelezaji wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi. Mkataba huu unataka kuhakikisha tunalinda na kupambana na uchafuzi wa mazingira ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zinaonesha ifikapo mwaka 2035 eneo la pwani ya bahari ya Tanzania litakuwa na mifuko mingi ya plastiki na takataka nyingine kuliko samaki baharini. Nashukuru sana tamko la Mheshimiwa Waziri Mkuu na leo Mheshimiwa Waziri wa Mazingira kwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. Hatua hii imekuja wakati muafaka kwani hali ya mazingira ya pwani yetu ni mbaya na inaathiri wananchi hususani sisi tunaoishi kwenye visiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni matumizi ya mkaa, kama lilivyoelezwa kwa uzuri kwenye kitabu cha hotuba ukurasa wa 29, kasi ya ukataji miti kwa uchomaji wa mkaa imekuwa ikiongezeka siku hata siku. Nashauri bei ya gesi ipungue ili wananchi waweze kuacha matumizi ya mkaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upandaji wa miti kama lilivyojadiliwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 37 ni jambo jema. Naishauri Serikali yangu iongeze fedha kwenye kampeni za upandaji miti. Ni ukweli usio na shaka kasi ya ukataji miti imekuwa kubwa sana hivyo ipo haja ya kuongeza fedha kwa ajili ya kampeni za upandaji miti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuharibika kwa ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu kama lilivyoelezwa kwenye kitabu cha hotuba ukurasa wa 50. Ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu ndiyo inayotiririsha maji kwenye Mto Rufiji na hatimaye maji hayo ndiyo tegemeo kwenye uzalishaji wa umeme kwenye mradi wa Rufiji Hydro Project. Kwa msingi huu, ni muhimu ikolojia hii kutunzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri na hotuba yenye kusheheni mambo mazuri kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa uamuzi wake mzuri wa kujenga Mahakama Kuu katika Mikoa ya Mara na Kigoma. Uamuzi huu kwa busara unaenda kutatua kero ya muda mrefu iliyopelekea wananchi wa mikoa hii kusafiri masafa marefu ili kupata huduma hii muhimu. Ombi langu kwa Serikali ni kuziwezesha Mahakama hizi kuwa na bajeti ya kutosha ili kuziwezesha kufanya kazi zake kwa ubora na ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mafia yenye vijiji 23 ina mahakama moja tu ya mwanzo, hali hii inapelekea utoaji wa huduma za kisheria kuwa mbali na wananchi. Ombi langu kwa Serikali ni kwamba, itujengee Mahakama moja ya mwanzo katika Tarafa ya Kusini kwani wananchi katika maeneo haya wengi wanatoka katika Visiwa Vidogo Vidogo vya Juani, Chole na Jibondo, wanasafiri masafa marefu na wanatumia gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapitio ya adhabu na faini mbalimbali nyingi zimepitwa na wakati kulingana na mazingira ya sasa, hivyo niiombe Serikali yangu sikivu kufanya mapitio upya ya viwango vya faini na adhabu zilizopitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa nyumba ya Jaji Mkuu katika Jiji la Dodoma umekuwa ni ahadi ya siku nyingi, kiongozi wa mhimili ni vema akawa na makazi yenye hadhi sawa na wadhifa wake. Nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii na nampongeza sana mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na wasilisho lililojaa weledi wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Timu yetu ya Taifa kwa kuweka historia ya kufuzu Mashindano ya Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON yatakayofanyika nchini Misri Juni, 2019. Ni matumaini yangu na Watanzania baada ya kusubiri kwa miaka 39, TTF watajipanga vilivyo katika kuandaa timu yetu ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Mheshimiwa Spika, usimamizi wa viwanja vyetu hususan vya kuchezea soka uangaliwe kwa karibu na mamlaka husika. Kwa mfano, kwenye mashindano ya ligi kuu viwanja vingi hususan vya mikoani vipo katika hali mbaya kiasi kiasi cha kuhatarisha usalama wa wachezaji wenyewe. Naomba wasimamizi wa mpira nchini (TFF) waweke utaratibu madhubuti timu zinazocheza katika ligi kuu viwanja vyao vikaguliwe na wasiokidhi viwango walazimishwe kucheza kwenye viwanja vya jirani vyenye ubora.

Mheshimiwa Spika, Tanzania ilikuwa inasifika duniani kwenye mchezo wa riadha. Siyo siri wanariadha hawa wengi chimbuko lao lilikuwa Wilayani Mbulu, Mkoani Manyara. Umefika wakati sasa Wizara ikaona haja na hoja ya kujenga Chuo cha Michezo Wilayani Mbulu ili kulea vipaji vya vijana ili wengi wapate fursa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri na hotuba yenye kuleta matumaini kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mafia inakabiliwa na ukosefu wa gari la doria baada ya gari lililokuwepo kutumbukia baharini na kuharibika vibaya. Wilaya ya Mafia ni kisiwa kilichopo pembezoni mwa nchi Kusini Mashariki na kinapakana na nchi ya Comoro. Kutokana na ukweli huo, kuna umuhimu mkubwa suala la ulinzi na usalama kuimarishwa sambasamba na kupatiwa boti ya kisasa ya doria ili kuweza kukabiliana na matishio hususani ya ugaidi kutoka nchi za jirani.

Mheshimiwa Spika, makazi kwa Askari Polisi na Magereza, Wilaya ya Mafia ni kero ya muda mrefu sana. Tunaiomba Serikali ijenge nyumba za askari wetu hawa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kuunga mkono hoja hii sambamba na kumpongeza mtoa hoja kwa wasilisho zuri lenye kuleta matumaini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Wilaya ya Mafia kwa kushirikiana na Mbunge wao, Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau wamefanikiwa kujenga Chuo cha Ufundi (VETA) na ujenzi wa Chuo hicho umekamilika takribani miaka minne iliyopita. Chuo hiki hadi sasa hakijapata usajili kutoka mamlaka husika kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa. Moja ya hoja iliyotolewa ilikuwa ni kukosekana kwa umeme katika Chuo hicho. Ninayo furaha kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa suala la umeme limeshatatulika baada ya wakala wa umeme vijijini kufikisha umeme katika chuo hicho na unawaka hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mafia ina shule sita za Kata. Kati ya shule hizo, zote zina tatizo la hostel za wanafunzi ukiondoa shule moja tu, shule ya sekondari ya Kitomondo. Tunatambua changamoto ya ufinyu wa bajeti. Tunaiomba Serikali itusaidie Mabweni ya wanafunzi kwa shule za Kirongwe, Baleni na Micheni. Shule hizi zina dahili wanafunzi kutoka maeneo ya mbali hususani maeneo ya pembezoni kwenye visiwa vidogo vidogo vya Juani, Chole na Jibondo. Inawawia tabu kupanda vyombo vya Mashua na Boti kwenda na kurudi majumbani ukizingatia nyakati za pepo kali za Kusini na Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja sambamba na kupompongeza Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho lake zuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuzuia miili ya marehemu (maiti) kama sababu ya deni la matibabu hususani katika Hospitali za Muhimbili na Mloganzila ni kero kubwa sana na ni jambo ambalo limekuwa likiigombanisha Serikali yetu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iliangalie suala hili na ilifanyie uamuzi wa kulifuta haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni mapambano dhidi ya malaria. Tuna kiwanda chetu pale Kibaha cha kutengeneza dawa ya kuulia vimelea vya vidudu vya malaria. Kiwanda kile kinakabiliwa na changamoto ya soko. Lile agizo la Mheshimiwa Rais kuwa kila Halmashauri ikanunue dawa pale halijatekelezwa sawasawa. Niiombe Serikali yangu sikivu kukiokoa kiwanda kile kwa kukipatia soko la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Kamwelwe, Manaibu Waziri Mheshimiwa Kwandikwa na Mheshimiwa Nditiye. Naishukuru Serikali kwa utekelezaji wa ujenzi wa Gati la Nyamisati. Gati hili ujenzi wake unakaribia kwisha na matarajio ni kufikia mwezi Juni mwaka huu. Tunashukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Spika, pia naishukuru Serikali kwa kutenga fedha za kujenga kivuko kipya kati ya Nyamisati na Kilindoni pamoja na ukweli kuwa kivuko hiki kilishatengewa fedha katika mwaka wa fedha 2018/2019 na mchakato wa kumpata mkandarasi ukaanza, lakini kwa masikitiko, kandarasi hii imefutwa kutokana na matatizo ya kisheria. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atupie macho utendaji wa Wakala wa Ufundi Umeme na Mitambo (TEMESA), wahakikishe mchakato wa ujenzi wa kivuko hiki cha Nyamisati na Kilindoni.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kivuko cha muda tulichopewa na Serikali kivuko kinachomilikiwa na Chuo cha Mabaharia (DMI), mpaka ninapoandika hapa bado hakijaanza kazi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri atie msukumo wa kuhakikisha boti hii inaanza kazi mara moja na hasa ukizingatia Gati la Nyamisati linakaribia kumalizika.

Mheshimiwa Spika, Gati la Kilindoni lipo katika hali mbaya sana, mbao zimechoka na ngazi ya kupanda na kushuka inakatikakatika mara kwa mara na kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) walishaahidi kufanya matengenezo makubwa ya gati hili. Kukamilika kwa Gati la Nyamisati itakuwa hakuna maana kama Gati la Kilindoni litakuwa bado bovu.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilindoni mpaka Rasi Mkumbi kilomita 45 ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na imo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020. Mpaka sasa upembuzi wa kina na usanifu umeshakamilika, bado kutengewa fedha za ujenzi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri chonde chonde ujenzi wa matengenezo ya muda wa (periodical) maintenance) unakuwa mgumu kwani udongo wa kufanyia matengenezo unakaribia kwisha. Hivyo ni bora barabara hii ikajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, Uwanja wa Ndege wa Mafia; tunaomba uongezwe urefu sambamba na kuwekwa taa ili kuwezesha ndege kubwa za Kimataifa kutua moja kwa moja na kukuza utalii sambamba na ujenzi wa jengo la abiria (Terminal building)

Mheshimiwa Spika, suala la mawasiliano katika Kisiwa cha Mafia bado ni changamoto katika Vijiji vya Miburani, Banja, Kitohi na Chemchemi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mtoa Hoja Mheshimiwa Waziri Joseph Kakunda kwa wasilisho zuri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisiwa cha Mafia kimejaaliwa hazina kubwa ya rasilimali za bahari na aina mbalimbali ya samaki. Kwa sasa kuna kiwanda kimoja tu cha kusindika samaki, naishauri Serikali yangu makini kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanda kikubwa cha kusindika samaki katika Wilaya ya Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kiwanda cha kusindika nazi; Tanzania inaongoza katika Afrika katika kulima nazi na inashika nafasi za juu katika dunia. Kisiwa cha Mafia kinalima zao hili kwa wingi lakini hadi sasa hakuna kiwanda hata kimoja cha kusindika nazi na mazao yanayotokana na nazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni utendaji kazi wa Shirika la Viwango (TBS);ni ukweli usio na shaka TBS inakabiliwa na changamoto kubwa ya vifaa vya kupima ubora ili iendane na kasi ya ukuaji wa viwanda nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni mfumo wa malipo ya ushuru wa bidhaa kwa kielektroniki yaani ETS; ni ukweli usio na shaka mfumo huu umesaidia kuongeza mapato ya Serikali, ni ushauri wangu sasa Serikali iongeze wigo wa bidhaa zinazotumia mfumo huu katika vinywaji na sigara kwenda kwenye bidhaa nyingine kama cement, nondo na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana mtoa hoja kwa wasilisho zuri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 10 anazungumzia kuhusu mpaka wa Mashariki ya Tanzania ambapo tunapakana na Bahari ya Hindi. Ukanda huu wa Pwani wenye urefu wa kilometa 1,424 ndipo Kisiwa cha Mafia kinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali tete ya usalama katika eneo hili ikiwemo tishio la magaidi kutoka nchi jirani, naleta ombi maalum kwa Serikali pawepo na kikosi cha wanamaji katika Kisiwa cha Mafia ili kujikinga na matishio hayo kwa sasa hapo kikosi kidogo (detach) ambacho kina vifaa duni na hawawezi kwenda maeneo ya bahari kuu ambapo uharamia unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 21 wa kitabu unazungumzia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana. Jeshi limeweka utaratibu mzuri na kila Wilaya kupewa nafasi kwa vijana kujiunga na Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Mafia kila mwaka kumekuwa na tatizo la vijana kutoka nje ya Mafia wanaoletwa kuchukua nafasi hizo. Nia nzuri ya Serikali ni kuhakikisha Jeshi letu linakuwa na sura ya kitaifa lenye uwakilishi wa kila kona ya Tanzania. Hili sio suala la ubaguzi, ni jitihada za makusudi za Serikali kwa maeneo ya pembezoni kama Wilaya ya Mafia vijana wake mnapata fursa ya kujiunga na Jeshi. Ni matarajio yangu Mheshimiwa Waziri ataweka miongozo kukabiliana na hali hii inayoharibu taswira ya Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Japhet Hasunga kwa wasilisho zuri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa saba wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri, kinaelezea kuhusu Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Wananchi wa Wilaya ya Mafia wameitikia wito wa kuanzisha Vyama vya Ushirika na Akiba na Mikopo lakini kwa masikitiko makubwa maombi ya Msajili wa SACCOS Haiba SACCOS yamepokelewa na Afisa Ushirika tokea tarehe 18 Machi, 2019 na hadi naandika hapa, Afisa Ushirika Mkoa wa Pwani hajatoa usajili kwa kisingizio cha kuwa anafanya uhakiki wa wanachama.

Mheshimiwa Spika, sheria inamtaka afisa kutoa usajili au kukataa ndani ya siku 60 na muda huo unamalizika kesho, Jumamosi, huku hakuna matumaini yoyote kwa SACCOS hii kusajiliwa. Naomba nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aingilie kati mchakato huu kurahisisha usajili.

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 11 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri unazungumzia upatikanaji wa mbegu bora za mazao. Nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti tulibahatika kutembelea Kiwanda cha Kusindika Mafuta ya Alizeti cha Mount Meru kilichopo Mkoani Singida. Moja ya changamoto kubwa inayokikabili kiwanda hiki ni upatikanaji wa alizeti kutoka kwa wakulima. Uzalishaji wa alizeti hautoshelezi kulisha kiwanda hiki kutokana na wakulima kutumia mbegu duni za kizamani ambazo zinatoa alizeti kidogo kwa ekari moja.

Mheshimiwa Spika, nilete ombi kwa Serikali kuagiza mbegu bora za kisasa kutoka India zenye tija kubwa kwa ekari. Mbegu hizi bora zitasaidia kulisha viwanda vyetu vya ndani na kuondokana na tatizo la kuingiza mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mafia inalima zao la nazi kwa wingi sana. Naomba kuishauri Serikali yangu kutuletea mtaalam wa kilimo na mbegu bora ili zao hili liweze kuwa na manufaa kwa wananchi wa Mafia na nchi nzima kwa ujumla. Nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri na lenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Spika, suala la bandari ya uvuvi limekuwa linasuasua kwa muda mrefu sana. Mwaka wa fedha 2013/ 2014 zilitengwa fedha kwa ajili ya pre-feasibility study na kiasi cha shilingi milioni 500 na mshauri elekezi alilipwa na kazi ilifanyika na mpaka sasa hatujui matokeo ya kazi ile. Baadaye fedha zimekuwa zikitengwa kila mwaka kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, hata bajeti hii tunayoitekeleza 2018/2019 zimetengwa fedha kwa ajili ya bandari hiyo ya uvuvi lakini hatuoni matokeo yeyote; na mpaka sasa hata eneo la kujenga bandari hiyo bado halijapatikana. Kwenye bajeti ijayo kupitia kitabu chake Mheshimiwa Waziri anaomba aidhinishiwe shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kazi ileile ya ushauri elekezi.

Mheshimiwa Spika, faida za bandari ya uvuvi ni nyingi ikiwemo utoaji wa ajira kwa vijana wetu nimuombe Mheshimiwa Waziri kuwa sasa fedha hizi bilioni 1.4 ziende na kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, uvuvi katika bahari ni fursa ambayo nchi inatakiwa iitumie vema. Kwa sasa uvuvi katika Bahari Kuu umedumaa na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Deep Sea Fishing Authority (DSFA) kwa sasa ipo katika hali mbaya sana. Mamlaka hii haipati bajeti yeyote kutoka Serikalini na inaendeshwa kwa mapato ya meli za uvuvi za kimataifa zinapokata leseni ya kuja kuvua katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilianzisha tozo ya dola 0.4 kwa kilo ya samaki itakayovuliwa. Baada ya kuanzishwa kwa tozo hii nchini wamegoma kuleta meli zao katika eneo letu hili la EEZ (Exclusive Economic Zone). Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri na Serikali Kuu kwa ujumla waifute tozo hii ili kuokoa mamlaka yetu hii.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikifuta tozo hiyo Serikali ianze kujipanga kwa kununua meli zake zenyewe za uvuvi wa Bahari Kuu sambamba na ujenzi wa bandari ya uvuvi kama nilivyoandika hapo awali. Nimeona kwenye hotuba kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) pamoja na mipango ya kununua meli mbili za uvuvi; hili ni jambo jema. Niiombe Serikali sasa iongeze kasi ya kutekeleza malengo haya.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni Kuhusu Hifadhi ya Bahari Mafia (MPRU) Taasisi hii imepewa Mamlaka ya kuwekeza katika visiwa vidogo vya uvuvi. Mwekezaji huyu amekumbwa na changamoto za kutoshirikisha Mamlaka za Halmashauri ya Wilaya kwenye kutoa vibali stahiki kama vibali vya ujenzi. Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mamlaka hii ya MPRU ampe maagizo ya kufuata sheria za nchi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni hili linalohusu vifaa vinavyotumia FAD’S (Fishing Aggregating Devices); tunaomba viletwe Mafia kwani kwa sasa wavuvi wanatumia njia za kutosa magari mabovu baharini na kuchafua mazingira.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri asubuhi ya leo. Katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 16 amezungumzia juu ya mpango wa ukuzaji wa utalii Kanda ya Kusini (REGROW) ambao unaenda kukuza utalii katika ukanda huo. Mpango huu bado hausemi chochote juu ya utalii katika fukwe za Pwani ya Kusini hususan Kisiwa cha Mafia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisiwa cha Mafia kina vivutio vingi vya utalii ikiwemo scuba diving, whale shark, sports, fishing, snorkeling na fukwe nzuri. Kupitia Mpango huu wa Kuendeleza Fukwe katika Kanda ya Kusini tunaiomba Wizara iingize ujenzi wa miundombinu katika Kusini cha Mafia kama ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kilindi mpaka Ras Mkumbi kilometa 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo la Ras Mkumbi Kaskazini mwa Kisiwa cha Mafia kina fukwe nzuri kwa ujenzi wa hoteli za kitalii sambamba na utanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mafia. Kwa kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kuruka (runway) kutoka urefu kama kilometa 1.6 ya sasa mpaka kufikia kilometa 3.0 ili kuwezesha ndege kubwa kutoka nchi za nje kutua Mafia moja kwa moja. Upanuzi wa uwanja ulenge kwenye kujenga jengo kubwa la abiria na eneo la maegesho ya ndege (apron).

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wanyama waharibifu akiwemo boko bado ni tatizo. Katika Kisiwa cha Mafia tunashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Kanyasu alifanya ziara na kusaidia upatikanaji wa fidia ya aliyepoteza maisha kwa kushambuliwa na boko na wale walioharibiwa mazao yao. Hata hivyo bado tatizo halijakwisha na viboko wameendelea kuingia mashambani na kula mazao na kutishia maisha ya wananchi. Niendelee kuiomba Serikali itupatie kibali cha kuvuna viboko hao kwani idadi yao imeongezeka maradufu. Vile vile Serikali iangalie uwezekano wa kujenga uzio kuzunguka maeneo ya mabwawa wanamoishi viboko hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni Channel ya TV ya utalii haioneshi vivutio vya Kisiwa cha Mafia. Tunaomba wahusika waje Mafia kurekodi katika channel hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru kwa fursa hii, sambamba na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa uamuzi wake wa busara wa kujenga ukuta wa Mererani; na matunda ya kazi hiyo tumeanza kuyaona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 13 na 14. Kwa mujibu wa hotuba hii mapato yameongezeka kutoka milioni 71,861,970 mwaka 2016 mpaka kufikia shilingi 1,436,427,228. Haya ni mafanikio makubbwa sana na ya kuendelezwa ili taifa liendelee kunufaika na rasilimali zake.

Mheshimiwa Spika, kama hotuba ya Mheshimiwa ilivyoonyesha ukurasa wa 15 na 16 kuhusu mkakati wa kuongeza thamani ya madini yetu kwa kualika kampuni tisa zenye nia ya kujenga viwanda vya uongezaji wa thamani ya madini ni jambo jema. Niombe Wizara iharakishe mchakato huu wenye manufaa makubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Matumizi Holela ya Baruti za Kulipulia Miamba. Suala hili limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wanaoishi maeneo jirani na migodi mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usio na shaka matumizi haya ya baruti yameleta madhara ya kiafya. Ushauri wangu ni kuwa wananchi wanaoishi jirani na machimbo haya walipwe fidia stahiki na wahame, wakaishi maeneo ya mbali na machimbo.

Mheshimiwa Spika, jambo linguine ni kwamba baruti hizi zimekuwa zikitumika nje ya matumizi ya migodi, hususan kwenye uvuvi haramu, jambo hili liangaliwe na udhibiti ufanyike.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutimiza ndoto ya Hayati Mwalimu Nyerere ya kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuzalisha umeme na Rufiji Hydro Power, maarufu Stiegler’s Gorge. Ushauri wangu, miundombinu wezeshi kuelekea eneo la mradi husuan barabara ya kutoka Kibiti kwenda Mloka iwekwe lami kurahisisha usafiri kati ya meneo hayo.

Mheshimiwa Spika, mradi wa REA katika Wilaya ya Mafia unaendelea vizuri na tunaishukuru sana Wizara na Serikali. Hata hivyo mradi wa kupeleka umeme wa jua (solar) katika visiwa vidogo vya Jibondo, Chole Jauni na Bwejuu ulikuwa uanze tangu Mwezi Septemba, 2018 lakini mpaka sasa hakuna dalili ya kuanza kwa mradi huo. Nichukue fursa hii kumuomba Mheshimiwa Waziri atuharakishie kuanza mradi huo na wananchi tulishaahidi na wamekuwa wakiulizia sana.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mafia inapata umeme unaoalishwa kwa kutumia mafuta ya diesel na ni miongoni mwa wilaya chache ambazo bado hazijafungamanishwa na grid ya taifa. Natambua juhudi za Serikali katika kutuletea nishati mbadala kama umeme wa jua na umeme wa upepo. Ningependa kuishauri Serikali, kutokana kukua kwa shughuli za uzalishaji wa viwanda mahitaji ya umeme katika Kisiwa cha Mafia yanakaribia kufika megawatt 5. Namna bora kwa sasa ni kutuletea umeme kutoka nje ya Kisiwa cha Mafia kupitia uzamishaji wa nyaya chini ya bahari (sub-marine cables) katika umeme unazalishwa kwa vyanzo vya gesi kutoka Somanga Fungu.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ujazilizi (Densification) kwa Vijiji vya Wilaya ya Mafia. Nilete ombi rasmi kwa Vijiji vya Bweni, Kanga, Jimbo, Banja, Juju, Kiwenje, Balemi, Kifinge, Kunjwi, Kibada, Gonge, Ndagoni, Marimbani, Kiegeani, Chemchem, Mlongo, Mibulani na Dongo. Vijiji hivi vimepitiwa tu na mradi wa REA katika awamu hii.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mafia imebahatika kuwa na kisiwa cha gesi eneo la Ndagoni kilichochimbwa na kampuni ya (M and P). Kwa bahati mbaya kwa awamu ya kwanza walikosa gesi baada ya kuwekeza fedha nyingi ilipokuja sheria mpya ya gesi (M and P) wanalazimika sasa kuomba upya leseni ya uchimbaji. Ushauri wangu kwa Serikali ni kuangalia namna ya kuleta amendments ya sheria kutoa mwanya kwa makampuni kama haya kuendelea na kazi za uchimbaji wa gesi katika Kisiwa cha Mafia.

Mheshimiwa Spika, (M and P) wamelazimika kutumia zaidi ya dola milioni moja kufukia kisima kule. La mwisho ni bei ya gesi asilia kwa viwanda kama Coca-Cola, Goodwill, Dangote n.k. ni kubwa, ipunguzwe.

Mheshimiwa Spika, nasukuru naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie Muswada huu muhimu uliopo mbele yetu.

Mhshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana mtoa hoja Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwa kutuletea Muswada huu ambao kwangu mimi nauona kama umekuwa ndiyo overdue, tulikuwa tukiusubiri kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Profesa hapa amesema tunalirudisha shirika hili kwenye miliki ya umma kwa sababu kubwa tatu kama zilivyoelezwa hapa; sababu za kiuchumi, kiusalama na kijamii. Napenda nianze mjadala wangu kwa ku-combine yote matatu kwa pamoja. Ni kweli na nianze kwa kusema mapema tu kwamba naunga mkono hoja hii kwa umuhimu wake na kutokana na hizi nukta tatu muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la usalama, uchumi na kijamii kwa Shirika kama la TTCL ambalo mwanzo lilikuwa ndani ya Serikali baadaye likatiwa katika mipango ya kubinafsishwa na sasa linarudi Serikalini ni muhimu sana. Hata hivyo, nina some reservations kwenye mpango huu. Kwangu mimi hili ni shirika la kimkakati lakini naona kama mazingira ambayo tunaanza nayo pengine yanaweza yakawa ni mazingira ya kulifanya hili shirika lisifanikiwe kama lilivyoshindwa huko mwanzo. Sasa ni muhimu haya mambo tukayangalia kama nilivyosema nitayazungumza yote kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, brand kubwa za TTCL ni Mkongo wa Taifa, Data Center pamoja na huduma hizi za mawasiliano. Kwa masikitiko makubwa sana Serikali tuliwekeza pesa nyingi sana kwenye Mkongo ule wa Taifa na
ukasambaa karibu nchi nzima lakini kwa bahati mbaya sana tukaruhusu tena na watu binafsi nao wakajenga mikongo yao parallel na Mkongo wa Taifa. Halotel wana network kubwa sana ya mkongo. Haya mashirika mengine wanajiita consortium; Vodacom, Tigo pamoja na Airtel na wenyewe nao pia wana mikongo yao ambayo ni kama missing link inajazia kwenye ule Mkongo wa Taifa. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba hizi infrastructures na hili suala la usalama hapa ndipo linapokuja mahali pake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani na naomba Mheshimiwa Waziri achukue ushauri huu kwamba hizi infrastructures hususani huu Mkongo wa Taifa lazima wote urudi Serikalini, hatusemi kwamba tunabinafsisha mashirika, tunabinafsisha zile infrastructures. Ukisharudi Serikalini, TTCL atakuwa na miguu ya kufanya kazi lakini tumewekeza kwenye mkongo na kwa bahati mbaya sana tukaruhusu na watu binafsi nao wamewekeza kwenye mkono, huu mkongo wa TTCL unakuwa redundant, matumizi yake ni madogo na mapato kutokana na matumizi ya huu mkongo yatazidi kushuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kama itawezekana tuangalie namna gani Kampuni kama za Halotel na ile mikongo ya ule ushirika wa Tigo, Vodacom pamoja na Airtel na yenyewe nayo pia tufanye utaratibu irudishwe Serikalini. Kwa kufanya hivyo tutaanza vizuri na TTCL. Kwa sababu katika hali ya kawaida, mkongo ni product kama vile unavyoona viwanja vya ndege, huwezi ukawa na kiwanja cha ndege cha private sector. Ni vizuri sana mikongo yote pamoja na extension zake zitakazofanyika zije kwenye umiliki wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu Data Center, hii ni another product ya TTCL. Nakumbuka kulikuwa na agizo la Mheshimiwa Rais hapa kwamba makampuni yote ya simu yaanze kutumia ile International Data Center yetu ambayo inamilikiwa na TTCL…

....Ilikuwa tarehe 1 Juni, nakumbushwa, lakini mpaka leo sijui labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuja kujibu hapo atuambie ni makampuni mangapi yame-comply na hii kitu sambamba na hilo na mabenki nayo pia wanatumia hii data center kwa sababu tumewekeza pesa nyingi sana pale. Haiwezekani ikawa tunaruhusu tena na watu wengine wanajenga na vi-data center vyao vingine parallel na ile data center ambayo Serikali tumeijenga kwa gharama kubwa sana na lilikuwa ni agizo la Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nitoe tu ushauri wa ziada wa namna ya kuifanya TTCL isimame kwa miguu yake. Ni muhimu sana kama ambavyo tulivyojadili katika Bunge la bajeti hapa, TTCL iongezewe mtaji. Nina wasiwasi mkubwa sana isije ikawa unamchukua mtu ambaye hajui kuogelea ukampeleka katika kina kikubwa cha maji ukamtosa, halafu ukamwambia tukutane juu anaweza akafia njiani. TTCL ni mtoto wa Mheshimiwa Waziri, wahakikisheni kwamba ile commitment ya Serikali ya kuongeza mtaji pale ili aweze kushindana na makampuni mengine ni muhimu sana sambamba na lile ambalo walilolisema wenzangu la kuuza hisa katika soko la hisa ili kuutunisha mtaji wa TTCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hili ambalo wazungumzaji wengi wamelizungumza la composition ya Board ya Directors pale. Hata mimi pia naunga mkono ile part ya Zanzibar kama ile Board itakuwa na watu watano basi wawili watoke Zanzibar na watatu watoke Tanzania Bara ili kuleta sura nzuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni uendeshaji wa shirika kwa maana ya Mkurugenzi Mkuu pamoja na Bodi yake tuwape uhuru. Mengi yamesemwa hapa sina haja ya kuyarudia, kama tunataka kulifufua hili shirika tuwaachie Mkurugenzi Mkuu na bahati nzuri tuna Mkurugenzi Mkuu mzuri sana, apewe mamlaka pamoja na Bodi yake waweze kufanya kazi bila ya kuingiliwa ili kuhakikisha kwamba Shirika letu hili linasonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo nimalizie kwa kusema naunga mkono hoja na nashukuru sana kwa fursa hii, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie muswada huu muhimu uliopo mbele yetu. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana mtoa hoja Waziri wetu, Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Philip Mpango kwa kutuletea marekebisho haya ya sheria ambayo kwa kisi kikubwa tumeyasubiri kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sheria hii ilikuja na ikapitishwa Bungeni mwaka 2010 kwa mara ya kwanza, baadae ikaja tena mwaka 2014 kwa ajili ya marekebisho na mabadiliko, leo ipo ndani tena humu Bungeni kwa mara nyingine tena tunaifanyia marekebisho, kwa hiyo, takribani sasa itakuwa ni kama miaka minane hivi. Mheshimiwa Waziri wakati unasoma hotuba yako uligusia mambo machache/ miradi michache ambayo inaonekana kwamba inaweza ikaitwa labda ni miradi ya PPP ukiwemo ule mradi wa Dar es Salaam wa mwendo kasi na mingine inaonekana ipo katika work in progress.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo haya tu utaona kwamba tulikuwa na sheria pengine ambayo haitoshelezi kwa kipindi cha miaka minane, ndiyo maana mpaka leo tukiulizwa mfano wa mradi wa PPP tunabaki kwenye magari ya mwendokasi ya Dar es Salaam ambayo kimsingi na yenyewe nayo kwa asilimia kubwa ni uwekezaji wa Serikali kupitia mkopo ule wa Benki ya Dunia na baadae ile component ya kununua mabasi ndiyo ambayo private sector imeingia, ukiangalia sana unaona pengine labda siyo PPP per se.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo pengine baada ya miaka minane ni kitu gani kimepelekea mpaka tunakuwa na miradi michache? Mabadiliko haya nafikiri kwa kiasi kikubwa sana yanajibu hilo swali, tumeona nakushukuru na kukupongeza sana, mmepunguza milolongo, mmepunguza zile sheria ambazo zilikuwa zinaonekana zinawakwaza wawekezaji na sasa tupo tayari kwa ajili ya kuangalia namna gani tunaweza tuka-implement hii sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na ushauri wa aina mbili katika kuboresha hii sheria, ushauri wa kwanza utakuwa ni wa kiujumla, lakini mwengine utakuwa ni wa kifungu. Ushauri wa kiujumla kwanza, kwanza huko Serikalini kwenye zile Inter Ministerial Communication inabidi ziwe improved, muweze kuongea, kwa sababu kuna tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati alikuja kuna wakati Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akasema kwamba inaonekana miradi ya PPP pengine siyo miradi ya kuitegemea sana na siyo miradi mizuri. Baadae siku nyingine wakaja wataalam wa Wizara hiyo wakasema kwamba mradi kama ule wa Dar es Salaam - Chalinze kwa sasa siyo priority tena sasa tunajenga reli ya standard gauge, kwa hiyo ule mradi kwa sasa hatuuangalii sana kwenye PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Kamati tulishtuka sana kwa sababu katika moja ya miradi ambayo tunaiangalia kwa jicho la huruma sana kuona kwamba ni namna gani PPP inaweza kwa Tanzania ikaanza ku-take place hasa kwenye masuala ya transport, barabara ya Dar es Salaam - Ubungo mpaka Chalinze, lakini inaonekana kulikuwa na hali fulani ya sintofahamu na mwisho wiki iliyopita tu na ndiyo maana nasisitiza ushauri wa kwanza ni mawasiliano Wizara ninyi muongee huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita tu nilikuwa naangalia television nikamuona Mtendaji Mkuu wa TANROADS anasema kwamba wanajenga barabara ile ya kutoka Ubungo mpaka Kibaha kwa barabara sita, hali kama hiyo unakuta kwamba tayari hiyo mipango ya PPP kwa barabara ya Chalinze - Dar es Salaam express way tayari imeshakuwa frustrated, kwa sababu kipande ambacho kingine ungetarajia kingemvutia zaidi mwekezaji ni kipande cha kutoka Ubungo mpaka pengine Kibaha, Mlandizi mpaka kufika Chalinze, ambako ndiko kuna foleni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inaonekana Serikali inajitwisha tena mzigo ya kutaka kufanya wenyewe wakati huku tayari tuna sheria nzuri ambayo tumeshairekebisha ile. Sasa mimi napata taabu kidogo kwa maana ya kwamba utauuzaje tena huu mradi kwa mwekezaji kutoka kuanzia Kibaha sasa ambako inaonekana Serikali inafanya marekebisho inajenga barabara yenyewe mpaka Kibaha, kuanzia Kibaha sasa ndiyo uanze kuelekea Chalinze sidhani kama unaweza ukampata mtu ambaye atakuwa tayari kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nashauri kwanza wenyewe huko Serikalini mkae, muangalie kipi kinatakiwa kianze, inaonekana Wizara ya Ujenzi inavuta kwake, labda pengine Wizara ya Fedha na ninyi mnavuta kwenu, kama vile hamko katika nyumba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika ushauri wangu ni kuweka benchmark. Tumeona kwenye vifungu humu Waziri sasa umepewa rungu, Waziri umepewa mamlaka makubwa sana kwa ajili ya utekelezaji wa hii miradi, utakuwa unakuja kuripoti kila baada ya miezi sita. Nilikuwa nafikiria pengine wewe mwenyewe ujiwekee benchmark hata kwenye kanuni hizo, kwamba ikifika baada ya miezi sita basi walau utuletee hata mradi mkubwa mmoja kwa maana ya ngazi hiyo ya Kitaifa. Haiwezekani tumekuwa na sheria kuanzia mwaka 2000 mpaka 2018 sasa hatuna miradi, na sasa hivi tunafikiri tumeirekebisha sheria yetu imeshakuwa nzuri zaidi, bado baada ya miezi sita au mwaka mmoja down the line Waziri kama hujaweza kushawishi kuleta miradi mikubwa naanza na hii miradi mikubwa kwanza, kwa sababu utakuwa umeipunguzia mzigo mkubwa sana Serikali, kwa maana ya uwekezaji kwenye reli, kwa maana ya uwekezaji kwenye mafuta, kwa maana ya uwekezaji kwenye viwanda vya kuchataka gesi, kwa maana ya ujenzi wa miundombinu kama barabara, bandari na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya miezi sita, ndani ya miezi 12, pengine miezi 18 kama unakuja tu unatupiga blaa blaa tu hakuna aina yoyote ya uwekezaji ambao umekuja mkubwa ina maana kwamba sheria yako hii ime- fail na pengine na wewe mwenyewe hukujipanga vizuri labda uwe muangalifu kwenye hilo. Hilo la kwanza kwenye kuweka hizo benchmarks katika level kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona sheria hii inakwenda kusaidia Halmashauri zetu, kuna miradi mingi sana kule kwenye Halmashauri, Halmashauri zina struggle, nazo pia tuziwekee benchmark kwa maana ya hao DCs, hao RCs, DEDs kwamba na wao pia watapimwa kutokana na namna gani wameweza ku-attrack hizi PPP na uwekezaji kuja ili kuipunguzia Serikali mzigo, kwa maana ya kwamba Serikali sasa itakuwa imepumua katika uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.