Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Omary Ahmad Badwel (16 total)

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu lake la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba vikundi 39 vya vijana na akina mama wamepata shilingi 23,800,000. Nataka kujua je, fedha hizi ni kwa muda wa fedha wa miaka mingapi?
Swali la pili; fedha hizi shilingi 23,800,000 zimekwenda katika Vijiji vipi na vikundi vipi katika Halmashauri ya Morogoro vijijini? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linasema pesa hizi zimeenda kwa vikundi vingapi. Ninaomba nifanye mrejeo swali hili nadhani nilijibu katika Bunge lililopita. Niliainisha vikundi hivi na nilikiri wazi nikasema kwamba pesa hizi zilizotengwa kwa Halmashauri ya Morogoro Kusini ni chache sana ukilinganisha na mahitaji halisi yaliyotakiwa kupelekwa. Nikatoa msisitizo hata katika wind up ya bajeti yetu ya Wizara ya TAMISEMI, nikasema ndugu zangu hizi pesa own source Wabunge ndiyo wenye jukumu ya kwenda kuzisimamia. Kwa sababu pesa hizi haziendi kwa Waziri wa Fedha wala haziji TAMISEMI, pesa hizi zinabakia katika Halmashauri na vikao vya Kamati ya Fedha za Halmashauri ndiyo vinavyopanga maamuzi ya mgawanyo wa pesa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana katika bajeti yetu ya mwaka huu tukasema Halmashauri yoyote haiwezi ikapitishwa bajeti yake lazima kuonyesha mchanganuo kwa sababu hata hizi zilizopelekwa ni chache hazitoshelezi. Kipindi kilichopita nimesema hata Mkaguzi wa Hesabu za Serikali outstanding payment ambayo wapeleke karibu shilingi bilioni 39 hazijakwenda kwa wanawake na vijana. Mwaka huu peke yake tunatarajia kwamba kutokana na bajeti ya mwaka huu tumepisha shilingi bilioni 64.12 zinatakiwa ziende katika mgawanyiko huo. Lengo langu ni nini? Ni kwamba kila mwananchi, kila Mbunge atahakikisha kwamba hizo bilioni 64 tukija kujihakiki mwaka unapita katika Jimbo lake amesimamia katika vikao vyake pesa hizo zimewafikia wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni vikundi vingapi kwamba nivitaje kwa jina naomba niseme kwamba kwa takwimu nitampatia ile orodha ya mchanganuo wote wa vikundi vyote katika Jimbo la Morogoro Kusini.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakandarasi hawa wakati wanaendelea kujenga barabara hizi katika maeneo yetu mbalimbali wamekuwa wakitumia bidhaa mbalimbali ikiwemo mawe, mchanga, maji, vibarua na vifusi; na kwa kuwa Serikali katika mikataba yao inakuwa kwenye BOQ imeweka bei maalum ambayo inawalipa wakandarasi hawa lakini wengi wakandarasi hawa wamekuwa wakichukua bidhaa hizo katika vijiji vyetu bure au kwa bei ndogo sana na hivyo kuwakosesha wananchi wa maeneo hayo kunufaika na bidhaa hizo. Je, ni lini Serikali sasa itatoa angalau bei elekezi kwa wakandarasi wote wanaofanya kazi za kujenga barabara waweze kununua mawe na bidhaa nyingine ili wananchi nao wafaidike kama watu wa madini na maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omary, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba wanaojenga hizo barabara ni sisi wenyewe, ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kodi zetu. Kwa kweli masuala haya lazima tukubaliane tunaya-balance vipi kati ya upatikanaji wa material ya kujengea barabara pamoja na upatikanaji wa fedha za kujenga barabara yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Omary kwamba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo ndiyo yenye dhamana ya kutoa bei ya fidia kwa maeneo ambayo yanatwaliwa na Serikali italifanyia kazi suala hili lakini siyo rahisi kutoa bei elekezi kwa sababu nchi ni kubwa na kila mahali pana thamani yake tofauti sana. Vinginevyo itakuwa ni kitabu kikubwa sana ambacho kitaorodhesha kila mahali na thamani ilivyo kwa nchi nzima, itakuwa ni ngumu. Nadhani njia inayotumika ambayo kwa kawaida ni mazungumzo kati ya halmashauri na wale ambao wanahusika na eneo linalotwaliwa pamoja na mkandarasi ni nzuri zaidi kufikia muafaka wa bei ya kutumika katika kununua eneo linalotumika kwa ajili ya upatikanaji wa hayo material ya kujengea barabara.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba niongezee kwamba Serikali haiwezi ikaanza kununua udongo ama changarawe kwa sababu miradi hii tutashindwa kuijenga. Sasa hivi Serikali inatumia kila kilometa 1 kujenga barabara kwa takribani shilingi bilioni 1. Sasa kama tutaanza kununua udongo, changarawe tutashindwa kuwajengea wananchi wetu hawa barabara hizi. Serikali inalofanya tu ni kulipa fidia hasa kwenye structure kwa mfano majengo na maeneo mengine lakini hatuwezi kuanza kununua udongo, changarawe na vitu vingine tutatishindwa kujenga miundombinu kwa ajili ya Watanzania.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa, Wakandarasi wengi wanaotumia bidhaa hizi hawafuati taratibu hizi ambazo zimeelezwa na Mheshimiwa Waziri, ama kununua mawe na bidhaa nyingine kwa watu wenye leseni, mara nyingine wamekuwa wao wenyewe wakiamua kuchukua hizo bidhaa katika maeneo yetu na bila kulipa mrabaha katika Halmashauri au bila kuwanufaisha wananchi katika maeneo yetu ambako bidhaa hizo zinatoka;
Je, Serikali iko tayari sasa kuangalia utaratibu mzuri ambao utanufaisha hizi Halmashauri zetu pamoja na wananchi husika katika maeneo husika ambayo bidhaa hizi zinapatikana?
Swali la pili, kwa kuwa wakati wa zoezi hili la uchukuaji bidhaa mbalimbali za ujenzi pia hutokea uharibifu wa mazingira katika maeneo yetu ikiwepo uchimbaji wa mashimo makubwa na kuacha hayo mashimo katika maeneo yetu, pia afya za wananchi zinaathrika kwa mavumbi na kadhalika;
Je, Serikali inachukua hatua gani madhubuti kuhakikisha kwamba inadhibiti suala la uharibifu wa mazingira pamoja na afya za wananchi katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa wachimbaji wadogo hasa wanaojihusisha na uchimbaji wa madini ya ujenzi pamoja na viwandani kwa kiwango kikubwa sana hawalipi ada pamoja na malipo mengine Serikalini. Nichukue nafasi hii kuwataka rasmi wachimbaji wadogo wote popote walipo waanze sasa kufanya hivyo.
Hata hivyo, manufaa yanayoweza kupatikana kutokana na uchimbaji wa kokoto pamoja na mchanga ni pamoja na kutakiwa kama ambavyo sheria inawataka kulipa ushuru wa Halmashauri ambao ni asilimia 0.3, haya ni matakwa ya sheria, ni vizuri sana ninakushukuru Mheshimiwa Badwel, nichukue nafasi hii kuwahamasisha viongozi wa Halmashauri ili waanze kukusanya ushuru huo kutoka kwa wakandarasi wanaochimba kokoto pamoja na mchanga kote nchini. Kwa hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Badwel kwa kuwakumbusha wananchi ili wachukue hatua hiyo, ninawaagiza pia wakandarasi wote waanze kufanya hivyo mara moja.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, athari za mazingira, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Badwel kwamba uchimbaji wowote wa madini jambo la kwanza kabisa wanalotakiwa kufanya ni juu ya kutokuharibu mazingira. Huwezi kuchimba madini bila kuharibu mazingira, lakini wana jukumu kwa mujibu wa Sheria za Mazingira na kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, wana wajibu wa kisheria wa kutunza mazingira.
Mheshimiwa Spika, hatua tunazochukua kwa wakandarasi na wamiliki wa leseni wasiotunza mazingira ni pamoja na kuwafutia leseni zao lakini pia kuwachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria hizo mbili.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Badwel pia natoa tamko rasmi, Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira huwa tunachukua hatua za kisheria kwa wale wasiotunza mazingira kwa mujibu wa sheria.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wengi wameitikia wito wa kusaidiana na Serikali katika kujenga Vituo vya Polisi hususani katika Wilaya yangu Bahi, wananchi wa Kijiji cha Chipanga A, kwa miaka mitano iliyopita wamejenga kituo cha kisasa, kikubwa na kwa asilimia 100 wamejenga wao wenyewe. Licha ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliyekuwepo Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa baadaye Mheshimiwa Silima kutembelea kituo kile na kumuomba kifunguliwe na wao wakaahidi kitapokelewa na Serikali na kufunguliwa lakini hadi sasa ni miaka mitano mpaka kituo kile kinachakaa hakijafunguliwa. Je, ni lini Serikali sasa itakipokea kituo hicho na kukifungua kabla hatujaamua kukitumia kwa matumizi mengine?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bahi, kwa jinsi ambayo wameweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa kituo hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nichukue fursa hii kuwaelekeza Jeshi la Polisi nitakapotoka hapa wanipatie taarifa ni kwa nini mpaka leo kituo hiki hakijafunguliwa. Baada ya kupata taarifa hiyo tutakaa na Mheshimiwa Mbunge tuone utaratibu wa kuweza kukifungua.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa yalikuwepo makubaliano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi miaka minne iliyopita ya kufungua Chuo cha VETA katika Wilaya ya Bahi, katika kijiji cha Kigwe na yako majengo yaliyokuwa ya Chuo cha Kilimo ya Halmashauri na Wizara iliomba ipewe majengo yale ili iweze kufungua chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kupitia kikao cha Madiwani miaka mnne iliyopia iliyakabidhi majengo yale kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Naibu Waziri wakati huo Mheshimiwa Mulugo alikwenda kutembelea majengo yale na akayakubali kwamba yanafaa kufunguliwa Chuo cha VETA. Lakini hadi sasa miaka mnne imepita majengo yale yamekaa bure, Wizara haijarudi tena.
Je, ni lini sasa Wizara itarudi pale kuendelea na mchakato wake wa kufungua chuo cha VETA katika Halmashauri ya Bahi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu kwa pamoja kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanaona kuna majengo yanayostahili kuweza kutumika kama sehemu za kuweza kutolea mafunzo ya ufundi, wanipe taarifa hizo ili tuweze kuyatathimini kwa pamoja na hivyo kuwezesha sisi kupanua wigo wa kuongeza vyuo vya kutolea mafunzo ya ufundi katika nchi yetu, ikizingatiwa kwamba hata hivyo uhitaji ni mkubwa lakini imekuwani ngumu kwetu kuweza kujenga VETA kwa Wilaya zote kwa wakati mmoja.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa tarafa ya Chipanga Wilaya ya Bahi, kwa takribani miaka 15 iliyopita waliamua kuchanga wao wenyewe na kujenga kituo cha polisi na wakakikamilisha kwa thamani ya wakati huo shilingi milioni 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimehangaika sana, nimempeleka Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo alikuwa Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha akakiona kituo akashangaa kwa nini hakifunguliwi, nikampeleka Mheshimiwa Naibu Waziri Silima wakati huo akakiona kituo akaona kwanini hakifunguliwi, lakini pia nimemuandikia sasa barua Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mheshimiwa Naibu Waziri lakini mpaka leo kituo kile hakijafunguliwa.
Sasa nilikuwa nataka kujua hapa leo ama Serikali inatoa kauli ya kufungua kituo cha polisi kile mara moja au itoe kauli ya kutokifungua sisi na wananchi wa tarafa ya Chipanga tukifanyie kazi nyingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Badwel pamoja na wananchi wake kwa jitihada hizo lakini nimhakikishie kwamba hili jambo aliwahi kulizungumza mimi sikuwa na hakika na taarifa kwamba mpaka leo bado kituo hicho hakijafunguliwa. Lakini Mheshimiwa Badwel nataka nikuahidi kwamba tukitoka hapa tukae, tufuatilie tuone lini tutafungua kituo hiki ili wananchi waendelee kupata moyo na wsivunjike moyo wa maeneo mengine na Jimbo lako kwa ujumla wake.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ni muda mrefu sasa Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wamekuwa wanadai fadha zao na hawajui ni lini watalipwa malimbikizo haya. Je, sasa Serikali iko tayari kuziagiza halmashauri kupitia Wakurugenzi kuandaa idadi ya fedha ambazo kila halmashauri inadaiwa na viongozi hawa ili Serikali baadaye itoe maelekezo ya namna ya kuwalipa viongozi hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sina hakika kama katika maelekezo haya ya kuwalipa Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa kama pako mahali panaeleza wanalipwa kiasi gani. Je, Serikali sasa iko tayari kutamka hapa kwamba hizo asilimia 20 ambazo zinapelekwa hao Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa watalipwa kiasi gani kila mmoja kwa mwezi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna halmashauri zingine zinafanya vizuri lakini kuna zingine ni changamoto kubwa. Ukipita huko kwenye halmashauri nyingine utaona kwamba zile asilimia 20 marejesho hayajarudi vijijini. Hata hivyo, tumetoa maelekezo mbalimbali, lakini naomba tutoe maelekezo tena na tutatoa maelekezo kwa waraka maalum kwamba jinsi gani sasa halmashauri hasa Wakurugenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokaa katika Kamati ya Fedha katika ajenda ya mapato na matumizi sisi tukiwa wajumbe lazima tuangalie ile compliance ya kurudisha zile fedha katika halmashauri zetu. Bahati mbaya sana katika sehemu nyingine utakuta Ma- DT wanakuwa kama Miungu watu, hawafanyi maelekezo ya Kamati zao za Fedha wanapofanya maamuzi. Kwa hiyo, jambo hili tutatoa maelekezo mengine ya ziada ili asilimia 20 ya fedha hizi ziwewe kurudi vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika suala zima la kupeleka hizi asilimia 20 mara nyingi zina-differ kutoka halmashauri kwa halmashauri, ndiyo maana tumesema kwamba tunafanya marekebisho ya Sheria ya Fedha ambayo humpa Waziri mwenye dhamana katika kifungu maalum, nadhani katika ibara namba 45, dhamana ya kutoa maelekezo maalum ya namna ya kufanya. Jambo hili lisiwe ni jambo la hiari isipokuwa liwe ni kwa mujibu wa sheria. Lengo kubwa ni kuwasaidia Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa na Vijiji. (Makofi)
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Bahi nayo ni miongoni mwa Wilaya hizo kadhaa ambazo hazina Hospitali ya Wilaya na kumekuwa na matatizo mengi sana, lakini pale Bahi tuna kituo cha afya ambacho hakijafikia level ya upasuaji.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuwaambia wananchi wa Bahi kwamba labda upo mpango wowote mzuri wa kusaidia kile Kituo cha Afya Bahi ili angalau hatua ya upasuaji hasa akina mama na huduma zingine muhimu ziwepo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimefika mara mbili kwenye Halmashauri ya Bahi na juzi juzi tulikuwa na Mheshimiwa Mbunge jimboni kwake takribani mwezi mmoja na nusu na bahati mbaya Bahi hawana Hospitali ya Wilaya wala vituo vya vya afya na kile kimoja kiko katika hali mbaya. Kutokana na maombi ya Mbunge tayari tumeshapeleka shilingi milioni 500 ndani ya wiki hii. Tunaenda kukiimarisha Kituo cha Afya cha Bahi, tunakijengea miundombinu ya upasuaji na maabara. Nia yetu ni kwamba Bahi pale huduma zote za msingi ziweze kupatikana kwa ukaribu zaidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, ombi lako limekubaliwa na Serikali na tunalifanyia kazi. Lengo letu ni kwamba wananchi wa Bahi wapate huduma nzuri kama wananchi wengine.
MHE. OMARY H. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utozaji huu wa ushuru na kodi mbalimbali kutoka Wizara hii ya Maliasili na Utalii katika maeneo mbalimbali mahali pengine umekuwa ama haukufikiria vizuri au umekuwa kero. Kwa mfano katika mazao ya ubuyu na ukwaju, mazao ambayo yana bei ndogo sana kwa maana ya shilingi 100 kwa kilo na katika masoko ya Dar es Salaam na maeneo mengine ya miji yanauza kwa shilingi 200. Mazao haya yamekuwa yakivunwa ama na kina mama wenye kipato cha chini au vijana na watu wengine ambao wanapambana na umaskini.
Hata hivyo, Wizara hii kupitia Maliasili wanatoza shilingi 350 kwa kilo na imewafanya sasa wafanyabiashara hawa washindwe kabisa kufanya hii biashara kwa sababu bei yenyewe ni ndogo na sasa inafikia shilingi 500 baada ya ushuru huu.
Je, Mheshimiwa Waziri anafikiria nini juu ya kufuta ushuru huu ili kuwasaidia wale wafanyabiashara wadogo wadogo waweze kupambana na umaskini? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika tozo za mazao ya misitu na mazao katika sekta ya utalii zingine ni kero sana kwa wananchi. Moja ya tozo hizo ambazo ni kero kwa wananchi ni tozo ya matunda ya ubuyu na matunda mengine ya misituni ambayo wananchi wanakusanya na kupeleka kuuza. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tozo hizi ambazo ni kero zitafutwa pamoja na hii ya kutoza kodi ya ubuyu. (Makofi)
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa hawa walemavu ili waweze kupata hizi ajira na huduma zingine mbalimbali ni lazima wapiti shule, vyuo na taasisi zingine ili waweze kukubalika katika hili eneo la ajira. Sasa kwa kuwa wanapitia katika shule mbalimbali ambazo zina matatizo mengi na inawafanya wasiweze kupata elimu vizuri kwa mfano Shule ya Viziwi Kigwe ambayo hakuna maji kwa muda mrefu na shule ile ni ya kitaifa na inachukua wanafunzi wengi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea maji wanafunzi wa shule ya wasiosikia Kigwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali niseme kwamba hilo tumelichukua na kwa sababu ni suala mtambuka, tutafanya mawasiliano ndani ya Serikali kwa maana Wizara ya Maji ili tuweze kuona jinsi gani tunaweza tukapeleka maji katika Shule ya Kigwe, ahsante. (Makofi)
MHE. OMARY A BADWELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Tarafa ya Chipanga wameitikia wito wa kujenga kituo cha polisi miaka 13 iliyopita, kituo kikubwa kizuri na cha kisasa na wakati huo kilighalimu 40,000,000. Hata hivyo tangu nikiwa diwani mpaka nimekuwa Mbunge kipindi cha miaka 13 nimehangaika na Wizara ya Mambo ya Ndani wafungue wapokee na wafungue kituo kile cha polisi hawajafanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kumpeleka Mheshimiwa Shamsa Vuai Nahodha akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani akaagiza kifunguliwe hakikufunguliwa; nikampeleka Mheshimiwa Silima akaagiza kifunguliwe na akawahaidi wananchi wa pale ndani ya miezi sita kwamba kituo kile kitakuwa kimefunguliwa mpaka leo hakijafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, je, Serikali inajua kwamba miezi sita waliohaidi wananchi wa Kata ya Chipanga na Tarafa ya Chipanga kwamba imekwisha na hawajapokea kituo hicho cha polisi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama leo sikupata majibu ya uhakika ya kwamba wanakipokea na kuja kukifungua kituo kile cha polisi nawaambia Jumamosi ijayo nakwenda kuwakabidhi wananchi kituo chao cha polisi ili wafanyie shughuli zingine ikiwemo kukaa watumishi kama nyumba ambao na wenyewe wana matatizo makubwa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii si mara ya kwanza Mheshimiwa Badwel kuuliza swali hili Bungeni na binafsi nilipata fursa ya kuzungumza naye kuhusianana mchakato wa ufunguzi wa kituo hiki na nilikuwa nimemwambia kabisa niko tayari kwenda kufungua wakati wowote. Lakini Mheshimiwa Badwel tulikubaliana kwamba tuchukue hatua kwanza kuhakikisha kwamba RPC wa Mkoa wa Dodoma anakwenda kulikagua ili kuona maandalizi yote kabla ya ufunguzi yamekamilika. Makubaliano hayo baina yangu mimi na Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo nashangaa sana leo Mheshimiwa Badwel hazungumzii zile hatua ambazo tumepiga mimi na yeye binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu ambacho kilikwamisha ufunguzi ni changamoto ambayo imetokana na wananchi wenyewe pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa eneo lile. Tulichokubaliana na Mheshimiwa Badwel ni kwamba kutokana na hali ya kituo ilivyo inahitaji kiweze kuwekwa sawa vizuri. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa muda mrefu. Hiyo hiyo hatuwezi kuwa wezi wa fadhila tusipompongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa hali ya bajeti ilivyo mwaka huu wa fedha tumepanga takribani shilingi milioni 150 ambazo tutatoa kipaumbele katika kukamilisha vituo ambavyo vimefikia katika hatua kama ambavyo kituo hiki ambacho kiko katika Jimbo la Mheshimiwa Badwel kilipofikia.
Lakini kipindi hiki ambapo bado fedha hazijapatikana, ikiwa kuna uwezekano wa kuendelea kukamilisha yale marekebisho madogo madogo ili kiweze kufikia viwango vya kuweza kufunguliwa rasmi waweze kufanya hivyo, vinginevyo tusubiri bajeti itakapokuwa imekamilika ili tuweze kukikamilisha na kuweza kukizindua. Wakati wowote hayo yatakapofanyika nitakuwa tayari kwenda kukizindua ili wananchi waweze kukitumia.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kuwa Serikali imeunda chombo kinaitwa TARURA na wakati huo kabla ya kuunda TARURA barabara zilizokuwa zinahudumiwa na Halmashauri ikaonekana utekelezaji wake si bora. Kwa kuwa tayari Serikali imeunda chombo hiki TARURA na lengo lake lilikuwa ni kuzifanya hizi barabara za mijini na vijijini kufikia hadhi kama hii ambayo tunaiomba kupandishwa hadhi kwa barabara. Je, nataka kujua bado kuna haja ya kuendelea kuomba kupandishwa hadhi barabara zetu au TARARU ielekezwe kuchukua nafasi ya kutengeneza barabara hizi vizuri kama ilivyokuwa inatengeneza TANROADS? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeunda chombo hiki kwa ajili ya kuboresha hizi barabara lakini bado kuna tofauti ya TARURA na TANROADS kwa maana ya asilimia ya fedha wanazopewa na Serikali ambapo TANROADS wanapata asilimia 70 na TARURA wanapata asilimia 30. Je, ni lini sasa Serikali itazigawia sawa kwa sawa taasisi hizi mbili kwa maana ya TARURA wapate asilimia 50 na TANROADS wapate asilimia 50 ili utengenezaji wa barabara hizi uwe katika kiwango kinachokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Badwel, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na kilio cha Waheshimiwa Wabunge kutaka barabara zao zipandishwe hadhi ili ziweze kuhudumiwa na TANROAD. Pia ni ukweli usiopingika kwamba tangu tumeanzisha chombo hiki cha TARURA ambacho kimsingi kinafanya kazi nzuri, kuna umuhimu wa kutathmini kama iko haja ya kutaka kupandishwa tena barabara hizi. Naamini kinachotakiwa ni kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa kwa viwango ili zilingane na zile ambazo zinazojengwa na TANROADS.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusu mgawanyo, iko haja lakini ni vizuri pia tukazingatia kwamba barabara nyingi ambazo zinajengwa na TANROADS zinajengwa kwa kiwango cha lami na barabara ambazo zinazojengwa kwa kiwango cha lami zinauhitaji mkubwa wa fedha ukilinganishwa na ambazo nyingi zinajengwa kwa changarawe na udongo. Kwa hiyo, ukifika wakati ambapo haja ikawepo kwamba tugawanye 50 kwa 50, naamini kwa mujibu wa taratibu zitakazofuatwa na Bunge lako likiidhinisha kwa mujibu wa sheria tutafika huko kwa siku za usoni.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maelekezo ya Serikali sasa ni kujenga zahanati katika kila kijiji na bahati nzuri wananchi katika maeneo mbalimbali wameitikia ujenzi wa zahanati hizo na wako katika hatua mbalimbali. Hata hivyo kwa bahati mbaya sana zaidi ya miaka minne, mitano baadhi ya vijiji wamejenga hizo zahanati na wamefika hatua mbalimbali hakuna fedha ya Serikali ambayo imekwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Serikali ilitoa maelekezo kwa Wakurugenzi kupitia upya bajeti ya fedha za CBG ili kupata miradi michache ambayo itakuwa na matokeo ya haraka na baadhi ya sehemu hizo katika Wilaya ya Bahi kwa mfano Kijiji cha Chonde tumezitengea fedha hizo lakini mpaka sasa fedha hizo hazijaja na mwaka unakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inawaambia nini Watanzania na Bunge hili kwamba ni lini sasa fedha hizi za CBG ambazo zimefanyiwa marekebisho zitakuja kwenye Halmashauri zetu na kuweza kufanya kazi ambayo imekusudiwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwanza niwapongeze Wabunge wengi wametumia mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kusaidia kwa kuungana na wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, hii ni pongezi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tunafahamu kwamba ni kweli, tulikuwa na kikao maalum ambacho kilihusisha Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Mipango, watu wa manunuzi especially na baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri wazi kwamba takribani wiki mbili zilizopita niliwasiliana na wenzangu, nilikuwa na kikao cha watu watatu, mimi hapa, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Waziri wa Fedha kuhusu upatikanaji wa hizo fedha kwa ajili ya kwenda kumalizia hiyo miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo imani yangu kubwa ni kwamba kabla hatujafunga mwaka huu; kwa sababu pesa zile tunaenda kujenga kwa kutumia force account jambo hili litakamilika vizuri. Lengo kubwa miundombinu hii twende tukalimalize katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa lengo la Serikali kutoa fedha hizi katika shule za msingi ni kusaidia uboreshaji wa elimu hiyo na sasa ni takribani zaidi ya miaka miwili fedha hizi zimekuwa zikienda katika shule zetu za msingi na sekondari. Je, sasa Serikali katika utekelezaji wa jukumu hili imepata changamoto gani za matumizi sahihi na kuondoa ubadhirifu katika fedha hizi? Kama zipo changamoto hizo wamechukua hatua gani kutatua na kupunguza changamoto hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omary Badwel, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba sasa hivi tuna uzoefu wa miaka miwili katika kugharamia elimu msingi bila malipo. Napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Waziri wangu na Serikali kuwasifu sana wasimamizi wote wa elimu kuanzia Maafisa Elimu katika ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri na Wakaguzi wa Ubora na wasimamizi wa elimu katika ngazi ya kata, Maafisa Elimu wa Kata na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi wamejitahidi sana kusimamia vizuri fedha hizi kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali. Maeneo machache sana ambayo yamekuwa na matatizo hatua zimechukuliwa na wengine wameshtakiwa kupitia Tume ya Utumishi wa Walimu na wachache sana ambao wameweza kuchukuliwa hatua. Siwezi kuwataja hapa kwa sababu idadi kamili sina lakini ni wachache sana ambao wamechukuliwa hatua. Kwa ujumla kazi ambayo sasa hivi inaendelea nchi nzima ni nzuri sana na wasimamizi wote wa sekta ya elimu wanastahili pongezi.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, lakini pia nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza habari ya tathmini na mimi nashukuru kwa kuniahidi kwamba kabla ya Desemba tathimini hizo zitakuwa zimefanyika ili waweze kujua fedha ngapi zinahitajika ili kumalizia na kukarabati miradi hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa tayari tuna miradi ambayo fedha zake zinajulikana kwamba zikipatikana miradi hiyo inaweza kukamilika kwa mfano Mradi wa Umwagiliaji katika Kijiji cha Kongogo ambao umekuwa ni wa muda mrefu. Swali la kwanza, je, Serikali sasa iko tayari kupeleka fedha kabla ya hiyo tathmini kwa sababu tayari tathmini yake inajulikana ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amehusisha kwamba wako washirika mbalimbali ambao wanaweza kutusaidia katika suala zima la miradi yetu ya umwagiliaji na sisi Bahi tayari tunao wafadhili ambao wanatusaidia hususan Shirika la LIC ambalo nataka nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa namna ambavyo wamesaidiana na kushirikiana vizuri na wananchi wa Bahi katika miradi hii ya umwagiliaji. Tayari wameshatuandikia andiko na michoro mizuri kabisa ya utengenezaji wa bwawa katika Kijiji cha Chikopelo lakini bado hatujapata fedha. Je, Serikali sasa itakuwa tayari kupokea andiko hili kutoka wenzetu hawa Shirika la LIC ili kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri waweze kututafutia fedha katika mashirika haya mbalimbali ya wadau wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omary Ahmed Badwel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kama Serikali iko tayari kwa ajili ya kupeleka fedha kwa mradi huu wa skimu ya Kongogo ambayo ni ya muda mrefu. Kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Badwel kwa ufuatiliaji wa karibu sana na ushirikiano anaowapa watu wake wa Bahi. Sisi kama Serikali kwanza tuko tayari kwenda kupeleka fedha na ndiyo maana kwenye bajeti ya mwaka huu, mwaka 2019/2020 tumetenga zaidi ya shilingi milioni 217 kwa ajili ya kufanya tathmini ya miradi hiyo ukiwemo huu wa Kongogo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anataka kujua pia kama Serikali tuko tayari kuchukua andiko walilofadhiliwa na wadau hao wa maendeleo. Serikali iko tayari na sisi binafsi tulishaanza lakini baada ya Bunge hili kwisha tunaomba atupe hilo andiko tulifanyie kazi. Kama tulivyosema hela tulishatenga tutafanya kila liwezekanavyo ili na hili andiko tulitekeleze haraka iwezekanavyo.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja namajibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na ninampongeza kwa kazi nzuri, nilikuwa na maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa katika miradi ya TASAF Awamu ya I na TASAF Awamu ya II, ulikowepo pia utekelezaji wa miradi ya miundombinu kama ujenzi wa barabara, ujenzi wa madarasa, miundombinu ya maji, utoaji wa fedha kwa ajili ya VIKOBA na miradi mingine mbalimbali, zikiwemo zahanati. Lakini baadaye katika TASAF three, TASAF Awamu ya II miradi hiyo kwa kiwango kikubwa iliondolewa, ama ilikuwepo kwa kiasi kidogo au haikuwepo kabisa.

Sasa je, katika huu mpango wa awamu ya pili wa TASAF inayofuata sasa miradi hii itahusika katika utekelezaji katika vijiji vyetua mbapo ilikuwa imetoa faida kubwa sana katika sekta mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa Awamu hii ya III ya ugawaji wa fedha kwa walengwa walikuwa wanakwenda kugawa fedha moja kwa moja kwa walengwa kwa maana hizi kaya maskini, lakini ilijitokeza pia uwepo wa kaya hewa, jambo ambalo lilisababisha fedha hizi za Serikali kwenda mahali ambapo kwa watu hawakuwa waaminifu na hivyo kutokufikia malengo yaliyokusudiwa.

Je, katika awamu hii ya pili ya ugawaji wa mradi huu wa fedha za TASAF Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba hakutokei tena walengwa hewa ili fedha hizi ambazo zimepangwa na Serikali kupelekwa huko ziweze kupelekwa huko ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na yeye ninampongeza akiwa mmoja wapo wa watu ma-champion mahiri katika kufuatilia walengwa wetu wa kaya maskini kupitia mpango wetu wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kabisa kwamba, mpango wa kunusuru kaya maskini, ni kweli awamu ya kwanza ulihusisha sana miundombinu, na ninaomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba, katika awamu yetu hii ya tatu kipindi cha kwanza, ambacho kinaisha mwezi huu na kipindi cha pili ambacho kinaanza mwezi ujao wa 12 mwaka 2019, tutaendelea na mpango wa miundombinu lakini tutajikita zaidi katika public works, kwa maana ya kwamba, zile ajira kwa muda, kwa wale walengwa ambao wanatokana na kaya maskini sana ili waweze kufanya kazi, waweze kupata ujira na ajira katika kuwawezesha maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, anasema Serikali tumejipangaje katika awamu ya tatu, Awamu ya II niliambie Bunge lako Tukufu kwamba tumejipanga, Serikali ya awamu ya tano, kuhakikisha kwamba walengwa wote kuanzia sasa hivi tutakuwa tunawaendea kwa kutumia njia za kidijitali kwa maana ya GPS, tutakuwa tunapiga picha kwenye kaya husika, lakini tayari tumeshafanya pilot project areas katika Mtwara DC, katika Halmashauri ya Nanyamba, lakini hata kule Siha na changamoto tulizozipata kule, ndizo ambazo zitatufanya tuboreshe katika maeneo mengine ambayo tutafika katika sehemu yetu hii ya pili inayoanza mwezi ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba pia tutakuwa tunawalipa walengwa kwa njia za kielektroniki, vilevile VIKOBA na tayari tumeshaweka mpango mkakati mwingine, kuhakikisha kwamba tutakuwa na wale wanaofuzu, kwa maana ya graduation, tutakuwa tunawapatia mafunzo na tunawaunganisha na taasisi za kifedha na hii yote ili kuweza kuwa na multiply effects. Ahsante.