Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Omary Ahmad Badwel (5 total)

MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:-
Wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye rasilimali mawe, mchanga na maji inapotokea wakandarasi wanachukua rasilimali hizo au mojawapo kwa ajili ya ujenzi huchukua bure au kwa malipo kidogo na hivyo kuwakosesha wananchi haki ya kunufaika na rasilimali hizo; hali hii ni tofauti na maeneo yenye madini ambapo wananchi hunufaika na uwepo wake:-
Je, Serikali haioni haja ya kuweka bei elekezi kwa wakandarasi wanaohitaji mawe, mchanga au maji ili wananchi wanaoishi maeneo yenye rasilimali hizo waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Ahmad Badwel, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake inamtaka kila mmiliki wa eneo la kuchimba madini amiliki leseni halali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, hata hivyo leseni katika maeneo ya uchimbaji wa madini ya viwanda na ujenzi yanatakiwa pia kupata leseni bila kuchimba kiholela. Wakandarasi wanaofanya kazi ya ujenzi hulazimika pia kupata leseni za kuchimba madini ya ujenzi na kulipa mrabaha pamoja na ada nyingine kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa wakandarasi wasiokuwa na leseni za uchimbaji hununua madini ya ujenzi kwa wananchi wanaochimba na pia kufanya shughuli za ujenzi, pamoja na hayo, Wizara kwa kushirikiana na Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMA) hutoa matangazo kwenye Ofisi za Madini za Kanda na Maafisa Madini Wakazi yakionesha bei ya soko ya ndani ya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wa madini ya ujenzi wanaweza kuwasiliana na ofisi ya madini kupata mwongozo wa bei ya soko kwa sasa ili kupata ufahamu wa bei halisi ya mazao hayo.
MHE. DANIEL E. MTUKA (K.n.y. OMARY A. BADWEL) aliuliza:- Rais wa Awamu ya Nne aliahidi barabara ya kijiji cha Nondwa - Sanza, Wilaya ya Bahi itachukuliwa na TANROADS Mkoa wa Dodoma, hata hivyo ahadi ya Mheshimiwa Rais haijatejelezwa mpaka sasa. Kwa kuwa kipande hicho kinahusisha TANROADS Dodoma na Singida. Je, Serikali ipo tayari kuiagiza TANROADS Dodoma na TANROADS Singida kukiingiza kipande hicho cha barabara katika mpango wa matengenezo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Badwel, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Chidilo - Zegere hadi Nondwa yenye urefu wa kilometa 31 ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Barabara hii inaungana na barabara ya Mkoa ya Igongo, ambapo ni mpakani mwa Dodoma na Singida kuelekea Chipanga - Chidilo hadi Bihawana Junction, yenye urefu wa kilometa 69 ambayo mwaka 2010 ilipandishwa hadhi kutoka barabara ya Wilaya na kuwa barabara ya Mkoa. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa hadi sasa maombi ya kupandisha hadhi barabara ya Chidilo - Zegere hadi Nondwa hayajawasilishwa rasmi Wizarani kwangu. Ili Wizara yangu iweze kuyafanyia kazi maombi ya kuipandisha hadhi barabara hii kuwa barabara ya Mkoa, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge afuate utaratibu uliobainishwa kwenye Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009 kwa kupitisha maombi hayo kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa.
MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:-
Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji; hata hivyo Wenyeviti hao wamekuwa wakifanya kazi kwa kujitolea bila kulipwa posho za kujikimu na Serikali imekuwa ikiahidi kuangalia uwezekano wa kuwalipa posho za kujikimu viongozi hao:-
Je, ni lini sasa Serikali itaacha kuendelea kuahidi juu ya malipo hayo na kuanza utekelezaji kwa kuanza kuwalipa viongozi hao posho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Ahmed Badwel, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inathamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na viongozi wa vijiji na mitaa katika kusimamia shughuli za maendeleo katika ngazi ya msingi ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka utaratibu ambapo posho za viongozi wa Serikali za vijiji na vitongoji zinalipwa na Halmashauri kupitia asilimia 20 iliyotengwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na kurejeshwa kwenye vijiji. Napenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge tushirikiane katika kuzisimamia Halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinatengwa na kulipwa posho stahiki. Hata hivyo, kutokana na baadhi ya halmashauri kushindwa kutekeleza suala hili kikamilifu, suala la kutenga asilimia 20 litawekwa katika sheria kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ambayo inatarajiwa kuletwa Bungeni ili kurekebisha kasoro zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kuendelea kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ili kujenga uwezo mkubwa zaidi wa kulipa posho hizo.
MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:-

Kwa sasa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi yetu na kwa sababu hiyo idadi ya watu pamoja na mahitaji ya huduma mbalimbali ikiwemo chakula vitaongezeka. Wilaya ya Bahi ambayo ni miongoni mwa Wilaya za Dodoma ina fursa muhimu za uzalishaji mchele kutokana na jiografia yake lakini inakwamishwa na miundombinu chakavu na isiyokamilika katika skimu zake za umwagiliaji wa zao la mpunga:-

Je, Serikali imejiandaa kuchukua hatua gani kutoa fedha za ukarabati na umaliziaji wa miradi hiyo ya umwagiliaji ili Wilaya ya Bahi ipate fursa ya uzalishaji mchele kwa wingi na kukidhi mahitaji ya chakula katika Mji wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Ahmad Badwel, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kukamilisha na kukarabati miundombimu ya umwagiliaji chakavu iliyopo Wilaya ya Bahi, Serikali itafanya tathmini ya miradi hiyo kabla ya mwezi Desemba, 2019 na utekelezaji wake utahusisha wadau mbalimbali wa miradi ya umwagiliaji wakiwemo washirika wa maendeleo, wawekezaji binafsi na ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Lengo ni kuhakikisha kuwa, kilimo cha umwagiliaji kinakuwa cha uhakika na kuongeza upatikanaji wa chakula nchini.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi pamoja na vyama vya wamwagiliaji wa maeneo hayo kuandaa maandiko kuomba mikopo kutoka taasisi za kifedha kama vile Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa lengo la kukamilisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji ili wananchi wa maeneo haya waweze kuwa na uhakika wa chakula cha kutosheleza kwenye maeneo yao.
MHE. OMARY A. BADWEL aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa baadhi ya wananchi wamekuwa wakinufaika na mradi wa TASAF ambao kwa kiasi umekuwa ukifanya vizuri, aidha mradi huu umefika vijiji vichache tu na vijiji vingine bado havijafikiwa na Serikali iliahidi kuwa vijiji vyote vitanufaika na mradi huu.

(a) Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya mradi wa TASAF kufikia vijiji vyote nchi nzima?

(b) Kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya viongozi kukata fedha za walengwa wa TASAF moja kwa moja kwa kuwakatia bima, michango mbali mbali ya vijiji na kadhalika bila ridhaa yao. Je, Serikali inatoa kauli gani katika jambo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Ahmad Badwel Mbunge wa Bahi lenye maswali mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulipoanza mwaka 2013 uwezo wa fedha uliokuwepo ulitosheleza kufikia Vijiji/Mtaa/Shehia 9,986 ikiwa ni asilimia 70 ya Vijiji/Mitaa/Shehia zote nchini. Vijiji/Mitaa/Shehia ambavyo havijafikiwa ni 6,858.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshakamilisha hatua zote za maandalizi ya Kipindi cha Pili cha Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini ambacho kinatarajia kuanza utekelezaji mwishoni mwa mwaka huu 2019 baada ya Serikali kupata fedha. Kipindi cha Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kitatekelezwa kwenye Halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar katika Vijiji/Mitaa na Shehia zote ikiwa ni pamoja na kufika kwenye Vijiji/Mitaa/ Shehia 6,858 ambavyo bado havijafikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ufafanuzi kuhusu matumizi ya fedha za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. Fedha hizi ambazo ni ruzuku zinatolewa ili kaya iweze kugharamia mahitaji ya msingi kama chakula, gharama za elimu na afya na kuwekeza kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kuongeza kipato. Hivyo, ni maamuzi ya kaya husika kupanga matumizi ya fedha hizi ili mradi haziendi kwenye matumizi ambayo hayaisaidii kaya kujikwamua na umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika baadhi ya maeneo, viongozi wa vijiji wanalazimisha kukatwa kwa ruzuku za walengwa ili kukatiwa bima ya afya au kulipia michango mbalimbali. Hii si sawa na haikubaliki. Napenda kusisitiza, lakini vilevile niagize, kwamba walengwa wasikatwe fedha zao moja kwa moja bali walipwe stahiki zao na iwapo kuna michango inayotakiwa kama ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya kijiji basi michango hii itozwe kwa wananchi wote wa kijiji husika na siyo kukata moja kwa moja kutoka fedha za walengwa wa TASAF peke yao. Nimalizie kwa kusisitiza kwamba viongozi wote waliokuwa wanatoa amri ya kukata fedha za walengwa wa TASAF moja kwa moja bila ridhaa ya walengwa hao, waache kufanya hivyo mara moja, kwa kuwa huu siyo utaratibu na wala siyo sahihi na vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba, baadhi ya halamshauri zilishawahi kufanya hivyo na Wakurugenzi waliagizwa warudishe fedha hizo na tayari wamesharudisha. Ahsante.