Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omary Ahmad Badwel (6 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuwa miongoni mwa Wabunge watakao changia katika hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwa kuwa ndio mara yangu ya kwanza katika awamu yangu hii ya pili ya kuwa Mbunge wa Bahi kusimama hapa katika Bunge lako Tukufu naomba nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wananchi wenzangu wa Jimbo la Bahi, kwa kweli kwa kuniamini na kunichagua tena kuwa Mbunge wao na mimi ninawaahidi mbele yako, imani ile ile waliyokuwa nayo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita nitaendelea kupambana nihakikishe mwaka 2020 imani yao inakuwa bado ipo hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mawaziri wote ambao Mheshimiwa Rais amewachagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili leo hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitisha bajeti yake katika mwaka wa fedha unaokuja. Nimemsikiliza kwa makini sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na maeneo mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu ambayo ameyagusa hususan amegusa katika uboreshaji na kuleta mapinduzi ya kilimo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni muhimu na nadhani wote tunatambua namna ambavyo kwamba sehemu kubwa ya wananchi katika nchi yetu ya Tanzania wanategemea kilimo. Zipo juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa na Serikali zimewatoa walikuma walipokuwa wakilima kwa jembe la mkono kwa sehemu kubwa sasa wanalima kwa zana mbalimbali ambazo wanazitumia na wameongeza uzalishaji. Katika hili nataka nichukue nafasi kumpongeza sana Mheshimiwa Mwigulu, ameanza vizuri na mimi nataka nimtie moyo katika kazi yake ambayo amefanya, sisi tumekuwa tukimfuatilia, kama alikuwa nalala masaa kumi, sasa apunguze alale masaa matano kwa sababu kazi hii ni kubwa ya kupambana kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata mabadiliko makubwa ya kimapinduzi na waweze kuvuna kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo yanapata mvua nyingi wachukue hatua ya kuwaendeleza lakini yapo maeneo kama Dodoma ambapo pia hayapati mvua za kutosha na tunahitaji sana kilimo cha umwagiliaji. Katika Wilaya yangu ya Bahi sehemu ya umwagiliaji ni sehemu muhimu kwa sababu ni Wilaya ya ukame lakini tumeanza, miradi ile ni ya muda mrefu imechakaa nilikuwa naomba Wizara ipitie ione namna ambavyo itaboredha na kufufua miradi mbalimbali ya kilimo cha umwagiliaji katika Wilaya ya Bahi ili kuwapunguzia wananchi adha ya kuomba chakula kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nisisitize na niseme wakati tunaendelea kuwahamasisha wananchi kulima na kufanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha kwamba kilimo kinachukua nafasi kubwa katika nchi yetu lazima tuangalie na mambo mbalimbali ambayo yanaweza yakawakuta wakulima hasa wakati wanandelea na zoezi la kulima. Kwa mfano majanga mbalimbali, nilikuwa najaribu kuangalia pamoja na juhudi mbalimbali Serikali bado yapo maeneo inapaswa kujipanga upya. Kwa mfano, unapo himiza wakulima kulima wanakumbwa na majanga mbalimbali, wanakumbwa na ndege waharibifu wa mazao, wanakumbwa na wadudu, wanakumbwa na magonjwa lazima sasa pia tuwe na dhama ambazo zitaweza kupambana na mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wa Bahi wamekumbwa na ndege waharibifu, Mheshimiwa Mwigulu amehangaika sana lakini Tanzania nzima hatuna hata ndege moja yaani ni jambo la ajabu kabisa! Kwamba hakuna hata ndege moja katika nchi yetu ambayo inaweza kumwagilia dawa wakati kuna wadudu au kuna magonjwa au kuna ndege wamevamia mashamba. Tukipata matatizo kama haya tunakwenda kukodi ndege Nairobi, tunakwenda kukodi ndege nchi jirani, hivi maafa haya yakija kwa pamoja nchi zote hizi za Afrika Mashariki Tanzania tutakimbilia wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anajibu hoja hii atuambie katika Bajeti ijayo wahakikishe kwamba wanatenga fedha za kununua ndege kwa ajili ya dharura ya mambo mbalimbali yanayowakumba wakulima. Kwa kweli, hii ni aibu na ni jambo la hatari kwa sababu wakulima wamefanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi nimshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye kitengo chake cha maafa wakati zoezi linaendelea na Mheshimiwa Mwigulu anahangaika wale ndege wameshindikana alituma watu wa maafa kupitia Brigedia Msuya kwenda kuona namna ambavyo ndege wanashambulia na wenyewe wamejiaonea lakini hakuna kitu cha kufanya. Ndege imekodiwa, imekuja mpaka Dodoma haijafanya kazi unaambiwa ndege haina dawa ya kumwagilia. Sasa hata gharama ambazo ndege hiyo imekodiwa kuja kutoka Nairobi mpaka hapa halafu inafika hapa Tanzania haiwezi kufanya kazi iliyokusudiwa inasema hakuna dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue hivi katika awamu ijayo wanafanya nini kuhakikisha kwamba hata kama bado wanakodi ndege lakini dawa ipo na maandalizi mengine yamefanyika vizuri.
Nakushukuru sana Mheshimiwa Jenista pia kuagiza sasa waende wakafanye tathmini katika vijiji vyangu vya Bahi ambavyo vimeathirika, vijiji 15 wananchi wale wamerudi kabisa nyumbani mashamba yameliwa ndege wamewashinda kwa hiyo nakushukuru sana na ni matumaini yangu kwamba tathmini hiyo itafanyika mapema kwa sababu wale wananchi chakula walishamaliza toka mwaka uliopita walikuwa wanatarajiwa wavune sasa wapate hicho chakula hawana chakula, siyo kwamba mnakwenda kuwafidia lakini waende wakasaidiwe na Serikali kuhakikisha kwamba wanarudisha maisha yao ya kawaida kupitia janga hili la ndege ambalo wamelipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa habari ya umeme tumetoka REA two tunakwenda REA three. Lakini mtakumbuka bahati nzuri baadhi ya Wabunge tuliokuwa hapa, mimi ni miongoni mwa Wabunge waliolalamika sana katika awamu iliyopita kusahauliwa kwa habari ya umeme katika vijiji vyake. Mimi nadhani ndiyo Wilaya pekee katika nchi nzima, ambayo wakati tunahangaika habari ya umeme ndiyo haikupata umeme hata kijiji kimoja cha REA. Hili halikuwa jambo nzuri ilikuwa ni uonevu kwa Wilaya ya Bahi, wakati Kondoa wanaipa vijiji 56, Mpwapwa vijiji 40, Kongwa vijiji 30, Mkoa huu huu Bahi hauipi hata kijiji kimoja. Namshukuru sana Mheshimiwa Simbachawene baada ya kuona malalamiko yangu hapa yeye akiwa Waziri akafanya kila jitihada ambayo inatakiwa nikapatiwa vijiji vitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vijiji ilikuwa ni kama zima moto ya uchaguzi, kweli wale Wataalamu walikwenda, mkandarasi alipewa ile kazi mpaka ilipofika mwezi wa kumi wakati tunapiga kura vile vijiji vimesimama vyote, hakuna hata mashimo yamechimbwa, nguzo zimewekwa leo tunahesabu miezi minane, mradi ule umesimama.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nilikuwa naingoja hii siku ya leo ili nije hapa kwako, kwa sababu mimi nimeenda kushukuru vijiji, sijaenda kushukuru hivyo vijiji vitano nimefanya hivyo kwa maksudi. Sijaenda kushukuru kwa sababu nataka yule uliyemwambia au Serikali iliyomwambia afute vile vijiji vitano tuende naye tukashukuru naye pamoja ili kama tutazomewa azomewe yeye na mimi, kwa sababu kwa kufanya hivi kwa kweli ni kutokuwatendea haki watu wa Bahi mmewanyima vijiji kabisa asilimia mia moja, halafu mmewapa vijiji vitano wameanza kazi ya kuchimba mashimo na kuchomeka nguzo mmekwenda kufuta hivyo vijiji vitano!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwa kweli siyo sawa mimi naomba maelezo Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwa nini vijiji vimefutwa na lini vijiji hivi vitarudishwa kabla ya REA III, naambiwa sasa vimepelekwa kwenye REA III kitu ambacho siyo sawa. Nataka virudi kwenye REA II wakati inamalizika mwezi wa saba kwa kweli na hivi vijiji viwe vimewaka umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji; kama nilivyosema Mkoa wa Dodoma ni kame na sisi kama Wilaya ya Bahi tuna shida kubwa sana ya maji, tumehangaika sana, Bahi ni Makao Makuu, ni Wilaya mpya na mji mpya ambao sasa ilikuwa kijiji tume- promote kile kijiji kimekuwa Mji uhamiaji umekuwa mkubwa ofisi za Serikali zote zimeamia pale…..
MWONGOZO WA SPIKA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mwongozo wa Mwenyekiti.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu mbalimbali wamehamia pale kwa hiyo panahitaji maji. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana nisisitize Mheshimiwa Waziri Mkuu Mji huu wa Bahi utizamwe kwa jicho la umakini.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa!
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Badwel naomba uketi....
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, siikubali taarifa nadhani hajui cheo cha Waziri Mkuu ni nani.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiye Mkuu wa Mawaziri wote, kwa hiyo, hata ninapomueleza hapa atatoa maelekezo kwa Wizara husika kufanya kazi ambayo mimi naisema hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hasa ukizingatia nafasi zetu hapa ni ndogo, unapopata fursa kama hii ni vizuri kuwasemea wananchi. Inawezekana nimechangia hapa nisipate fursa ya kuchangia mahali pengine na mimi ni Mbunge kama yeye na Jimbo na yeye ana Jimbo aniache nifanye kazi walionileta wananchi wa Bahi. Simuingilii kwenye Jimbo lake kama hana cha kusema arudi nyumbani kwake Jimboni akafanyae kazi za Jimbo kule asikae hapa Bungeni lakini sisi tunayo mambo ya kusema nitaendelea kuyasema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya maji Mheshimiwa Waziri Mkuu, Bahi hakuna maji najua unanisikiliza na kwa kauli hii ya Mbunge ambaye hataki wewe uambiwe juu ya maji, utapeleka maji Bahi ili wananchi wajue kazi niliyoifanya hapa ilikuwa na tija na sikuja kufanya mchezo hapa. (Makofi)
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ilikuwa ni habari ya sheria mbalimbali. Wizara yako Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo inasimamia Tume ya Kurekebisha Sheria, zipo sheria nyingi sana zimepitwa na wakati, ni vizuri Serikali ikatafuta utaratibu mzuri wa kuziangalia sheria hizi mbalimbali ili ziweze kufanyiwa marekebisho ziweze kutoa tija iliyokusudiwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitia kwenye Kamati zetu hususan Kamati ya Katiba na Sheria, tumeona namna ambavyo Tume ya Sheria inapitia sheria moja kwa miaka mitatu, inafanya uchunguzi wa mapitio ya sheria moja kwa miaka mitatu! Mimi nadhani huu ni muda mrefu sana, unatenga fedha mwaka huu milioni 800 kuipa Tume ya Kurekebisha Sheria kuangalia sheria tatu tofauti, mwakani haijamaliza unatenga tena milioni 800, mwaka unaofuata milioni 800, utakuta zaidi ya bilioni mbili zinatumika lakini yale makusudio ya kurekebisha ile sheria bado hayajafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani mkae muangalie namna nzuri ambapo itaweza kufanya hii Tume ya kurekebisha sheria nyingi kwa wakati mmoja ili ziweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia unasimamia Tume ya Haki za Binadamu. Hii Tume ya Haki za Binadamu imesahauliwa kabisa na Serikali. Ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu, Tume hii imepewa pesa ya pango tu kwamba pale wanapokaa waweze kulipia ofisi, sidhani kama hiyo ndiyo kazi ya Tume ya Haki za Binadamu. Tume ya Haki za Binadamu ina kazi nyingi, kama Serikali ipo serious kuhakikisha kwamba haki za wananchi zinapatikana waiangalie hii Tume ya Haki za Binadamu, waipe fedha za kutosha ili iweze kufanya ufuatiliaji mbalimbali wa mambo yanayohusu haki za binadamu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nizungumzie habari ya fedha milioni 50 ambazo tunatarajia kwenda kuzipata katika vijiji vyetu, tunaomba kwa kweli utaratibu uandaliwe vizuri na pengine sisi Wabunge tushirikishwe kuletewa utaratibu huo ili tuweze kujua fedha hizi zinakwenda kugawiwa vipi na zitumikeje katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka yalikuwepo mabilioni ya Kikwete yalikuja hivi tu kwa matamko, lakini baadaye fedha zile zilitoweka hatukujua zimekwenda wapi, tunatamani sana kuona fedha hizi safari hii zinakwenda kila kijiji zinawekewa utaratibu mzuri na Wabunge ambao tunakaa kule tunajua vikundi vyetu tunajua wananchi wetu uchumi wao, tushirikishwe vizuri ili na sisi Wabunge tuweze kutoa ushauri kusaidia yale madhumuni ya milioni hamsini kupelekwa katika kila kijiji yaweze kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kunipa nafasi na niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali kwa mwaka unaokuja wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya toka amechaguliwa mwaka 2015 na sisi Wabunge tunamuunga mkono na tunaahidi kwamba tutaendelea kumuunga mkono ndani ya majimbo yetu lakini pia kama viongozi wa kitaifa ndani ya nchi yetu yote ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali pia kwa ujumla kwa masuala ya umeme ambayo sasa inaonekana REA III inakwenda vizuri na mimi Mbunge wa Bahi nilikuwa nikilalamika hapa kila wakati juu ya kukosa umeme, lakini naona mambo yangu safari hii shwari, kwa hiyo nashukuru sana Serikali kwa kuitambua na kuona Wilaya ya Bahi nayo inaweza kupata umeme tena kwa maana ya vijiji vyote Wilaya nzima, ahsante sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake wa kupunguza kodi mbalimbali na hususan zile ambazo zinawalenga wananchi wa chini ambao wamekuwa wakifanyia biashara mbalimbali hususani mazao, tunaipongeza sana Serikali na
hivi karibuni niliuliza swali pamoja na mazao mengine lakini pia nilizungumzia sana habari ya ubuyu na ukwaju, nilikuwa naomba pia Serikali itoe ufafanuzi sasa kwa sababu haya yanaonekana kama mazao ya misitu hivi huwenda yasiwe yanajumuishwa katika hili zoezi la upunguzaji wa ushuru mpaka tani moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi Bahi kule ukwaju na ubuyu ni sehemu ya mazao muhimu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kina mama na vijana ambao wamekuwa wakitafuta maisha. Kwa hiyo, ni vizuri ubuyu na ukwaju ukatangazwa hapa rasmi kwamba nao utaanzia tani moja kutozwa ushuru ili wale wananchi wenzetu wanaofanya kazi hii Bahi na ukizingatia Bahi ni Wilaya ya ukame ina vitu vichache sana hivyo ambavyo wananchi wanaweza kuvitumia kwa ajili ya maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa kuondoa hii tozo ya kodi ya magari kwa maana ya kodi za barabarani na kuamua kuipeleka kodi hiyo kwenye mafuta, uzuri wa jambo hili tu kwamba ingawa tutatozwa lakini we don’t feel kwamba kuna kitu tunachangia tofauti na wakati ule ukiambiwa kwamba lipia shilingi 300,000/400,000 unaguswa kuzikusanya hizo fedha lakini sasa kwa mtindo huu tumekuwa tulikipa pole pole bila kufikiri kwamba unalipa na hiyo tunaendeleza kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bahi ni eneo la ukamae na Wabunge wenzangu ni mashahidi safari hii ukitokea Morogoro tu ukifika pale Gairo ukianza tu, Mkoa wa Dodoma unaanza kukutana na ukame mkali, tofauti kabisa na wenzetu katika Wilaya zingine na mikoa mingine. Kwa hiyo, nilidhani kwamba kuna haja kubwa ya kuangalia Mkoa wa Dodoma huu katika suala la miundombinu ya umwagiliaji hususani Wilaya yangu ya Bahi. Wilaya ya Bahi ni ndiyo Wilaya kame zaidi kuliko zote katika Mkoa huu wa Dodoma, lakini Mungu ameijalia Wilaya Bahi ina ardhi kubwa ina mabonde mazuri, lakini tunakosa fursa ya miundombinu sahihi ya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bahi tuna skimu za umwagiliaji kumi, kati ya skimu hizi kumi kama zimekuwa zimeendelezwa vizuri na zinafanya kazi vizuri zingechangia kwanza wananchi wenyewe kupata chakula cha kutosha katika eneo la Wilaya ya Bahi. Lakini pia kwakuwa hapa Dodoma sasa ni Makao Makuu na watu wengi wanahamia tungeweza pia kupata vyakula mbalimbali hapa jirani kuliko kutoa vyakula mbali kutokana na hali halisi ya ukame wa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwahiyo naiomba sana Serikali embu ipitie upya ile miradi kumi ya umwagiliaji iliyopo Bahi, maana mingine ama imechakaa na ni ya muda mrefu, lakini mingine ilijengwa ikaishia nusu haikukamilika, haifanyi kazi, mingine ilianza hata robo haijafika na fedha nyingi zimepotea na zile fedha hazifanyi kazi yoyote, nilikuwa naomba sana Wizara husika waje Bahi wapitie miradi yetu yote hii kumi waone namna ambavyo watawasaidia wananchi wa Bahi kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili hali ile ya sisi kuomba chakula kila mwaka ipungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo na tathimini ifanyike ili wananchi wa Bahi waweze kupatiwa chakula hata kama ni cha bei nafuu kwa sababu hali kwa kweli ni mbaya sana sio sisi tu kama wananchi, lakini hata mifugo kwa sababu mvua haikunyesha vizuri pia hata hali yetu ya mifugo itakuwa ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la viwanda Mheshimiwa Waziri sisi Bahi ndiyo Wilaya tunaongoza kwakuwa na ng’ombe nyingi katika mkoa huu wa Dodoma, lakini hatuna hata viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa nyama ambavyo vingesaidia sana wananchi wale mifugo yao ambayo wanaifuga ingeweza kuleta tija zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri huwa nakusihi hapa namna unavyo waahidi Wabunge viwanda na mimi Bahi nahitaji kiwanda cha usindikaji nyama, ninakuomba sana tushirikiane tuweze kupata kiwanda hicho ili wananchi waweze kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji, Bahi kama nilivyosema ni Wilaya kame na mji wa Bahi ule ulikuwa ni kijiji tume u-promote mpaka umekuwa mji kwa sababu ile ni Wilaya mpya lakini tumekuwa na shida ya muda mrefu sana ya maji katika mji wa Bahi. Nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri miradi ambayo tumeomba ya Bahi kwa miaka saba sasa wa maji pale Bahi mjini hatujapatiwa fedha, kwahiyo siku moja na sisi bajeti ioneshe kwamba Bahi mji ule unakwenda kupewa maji ya kutosha ili wananchi waweze kujenga kitu ambacho kimewashinda sasa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia miradi hii ya maji imekuwa na gharama kubwa mno, nataka niishauri Serikali inawezekana ninao ushahidi kwamba miradi hii ya maji imekuwa ikiongezewa fedha nyingi sana na wataalam wetu sio waaminifu, wamekuwa wakiongeza fedha hizi za miradi ya maji na inakuwa fedha nyingi kiasi kwamba tunashindwa kutekeleza miradi mingi katika vijiji vyetu na nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu iangaliwe kama tunauwezo leo wa kusema barabara ya kilometa moja inatengenezwa kwa bilioni 1.2, tunauweza kusema leo umeme ukisambazwa katika kijiji kilometa kumi utalipwa kiasi fulani, lakini pia tunaweza kufika mahali tukasema kwamba maji yakisambazwa katika kijiji kwa kilometa tatu au nne yatakuwa na gharama kiasi fulani hata kama mazingira yatakuwa tofauti kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa hali hii ambayo tunakwenda nayo siyo rahisi sana kutekeleza hii miradi ya maji, unaambiwa kila mradi ukigusa unaambiwa ule ili ukamilike unataka milioni 700; ili ukamilike unataka milioni 600, lakini wanakuwa watu binafsi wanachimba visima wanasambaza maji wanauza ukimuuliza umetumia milioni ngapi wanasema nimetumia milioni 30, lakini Serikali hakuna milioni 30 ni milioni 200; milioni 300; milioni 400 kitu ambacho kimekuwa ni kikwazo kikubwa. Nadhani kuna haja ya kuipia wataalam wetu hawa waelekezwe vizuri na kupitia kuona gharama za miradi ya maji zinakuwa kwenye standard kama miradi ya barabara. miradi ya umeme na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeiacha miradi ya maji wanabuni wenyewe tu kutokana na hali halisi kwahiyo katika ubunifu huo wako wataalamu ambao wamekuwa sio waaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Dodoma tunao punda, tulinde hawa punda kule vijijini wananchi wengi hawana uwezo wa kusafirisha mazao kwenye magari, pikipiki na na kadhalika wanatumia punda leo tukimaanisha kiwanda hapa kila siku punda wanakwenda na punda ndio wanyama nadhani hapa Dodoma wanaozaliana kwa uchache sana, lakini wanyama wenye msaada mkubwa sana, nadhani Serikali iangalie namna ya kuwalinda hawa punda kwa sababu la sivyo hawa punda watapotea latika Mkoa wa Dodoma, Mkoa wa Singida na maeneo ya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli unafika pale mpaka punda wale unawaonea huruma, kwa sababu punda ni rafiki zetu wazuri, wamekuwa wakitusaidia miaka mingi kwenye mashamba yetu mizigo yetu mbalimbali, lakini leo tunaagalia na wengi tunapita hapo tunaona na nimesikia kile kiwanda kimefungwa sina hakika. Nilikuwa naomba jambo hili liwekewe mkazo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba punda wanalindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie tu kwa kuunga mkono hoja hii, namtakia kila la heri Mheshimiwa Waziri hotuba yake hii ipite salama na baadaye kazi ya maendeleo iweze kuendelea kwenye nchi, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara hizi mbili ambazo ziko mbele yetu. Kwanza naomba niwapongeze Mawaziri wote wawili kwa kazi nzuri pamoja na Naibu Mawaziri wao na wasaidizi wao mbalimbali ambao wamekuwa wakishirikiana nao katika kufanya kazi mbalimbali za maendeleo za nchi yetu kupitia Wizara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza watumishi ambao serikali baada ya kuwaondoa katika utumishi na baadaye imekubali kuwarudisha. Kwa kweli nawapongeza sana, lakini pia nawapa pole kwa madhira waliyoyapata katika kipindi kila cha miezi mitatu ambao hawakuwepo kazini. Kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali kwa kusikia ushauri wa Wabunge na kuwarudisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri maamuzi magumu na yanayolenga maisha ya watu kama hivi wakati mwingine kwa kweli Serikali itafakari kwa kina kabla haijachukua maamuzi magumu kama haya. Pengine sisi Wabunge wakati mwingine isitoshe tu kuishauri Serikali kufanya maamuzi tofauti na waliyoyafanya awali, lakini pia wakati mwingine tuelekeze pia kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini viongozi waliohusika walishauriwa pia na watendaji ambao hawakuwashauri vizuri mpaka wakachukua maamuzi haya. Nao wawajibike wakati mwingine waone uchungu wa kutoka kazini na namna ambavyo walikuwa wakitegemewa na watu mbalimbali na dhoruba ambayo wanaipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nashukuru mpango amaboa umeletwa na Wizara juu ya fedha za CDG kutumika katika miradi michache ambayo itaweza kukamilika kwa wakati na kuweza kutoa huduma tofauti na miradi ambayo tulikuwa tunafanya kidogo kidogo. Huo ni mpango mzuri na sisi Bahi tumeiga hata kwenye bajeti hii ambayo tumependekeza sasa kuwa na miradi michache lakini ambayo itaweza kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachokiomba Serikali izileta hzi fedha. Ukiangalia fedha hizi za CDG kwa mfano Wilaya ya Bahi tumepangiwa bilioni moja na milioni mia mbili, na sasa imebaki miezi mitatu muda wa mwaka kwisha, lakini hakuna hata senti tano ambayo imekuja. Kwa hiyo ni vizuri sasa hizo fedha zikaletwa, tukiwa bado tupo Bungeni hizi fedha tuzione zimekwenda kwenye Wilaya zianze kufanya kazi ambayo kwa kweli tulikuwa tumekusudia na kuipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tunakubali miradi mingine ya Kitaifa inakwenda. Ukiangalia kila mahali miradi ambayo inasimamiwa kitaifa inakwenda, lakini miradi ya halmashauri haiendi halmashauri hazina fedha. Tuna watumishi wengi kule mpaka unafika mahali nasema tunawalipa mishahara bure kwa sababu hakuna fedha ambazo wanaweza kuzisimamia kuleta maendeleo kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kweli imeweka watumishi wengi na ni wataalam na wana sifa mbalimbali na wakipewa fedha wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo wakishirikiana na wananchi; basi fedha ziende pia kwenye halmashauri zetu. Isiwe baba tu sasa anaonekana Serikali Kuu anafanya kazi lakini halmashauri ambayo sasa inachukuliwa kama watoto hawafanyi kazi. Hata sisi wazazi tunakwenda kazini na watoto tunawapeleka shule, kwa hiyo pia wazazi na watoto wapewe haki sawa katika kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za bajeti katika maendeleo mbalimbali ukiacha hizi fedha za CDG nazo pia zinapashwa kwenda katika halmashauri zetu ili ziweze kufanya kazi ambayo imekusudiwa. Kuna miradi mingi ya wananchi ambayo wameifanya kule ya kujenga zahanati, nyumba za Walimu, madarasa na tuliwaaambia wajenge mpaka hatua fulani halafu Serikali itakwenda kuwasaidia. Tunasubiri fedha hizo wazipate ili waweze kufanya hiyo kaiz ya kumalizia majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboma haya yamekaa muda mrefu, mahali pengine hata sisi viongozi kama Wabunge tunaona hata aibu kwenda katika baadhi ya vijiji. Umewahaidi wananchi mwaka huu kwamba tutatenga fedha, tunatenga kweli halmashauri lakini fedha zile haziendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mifano mimi kwangu kule Bahi kuna kujiji cha Mayamaya wamejenga zahanati mpaka wamefika hatua ya visusi huu mwaka wa tano. Kuna kijiji cha chonde wamejenga zahanati wamefika hatua ya visusi huu ni mwaka wa tano na Mbunge unakwenda kila mara unafanya mikutano unabaki na hadithi ile ile, mwaka huu tumewatengea fedha milioni arobaini, unakwenda mwakani tumewatengea fedha milioni arobaini. Mwisho wanatuona na sisi ni watu ambao tunawadanganya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Serikali ifanye tathimini, iwatake Wakurugenzi kufanya tathimini ya miradi yote ya wananchi ambayo imekwama kwa muda mrefu. Uandaliwe mpango kabambe wa kwenda kumalizia haya magofu, yatatuletea shida wakati tunakwenda kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, lakini pia itatuletea shida kwenye uchaguzi tunaokwenda wa mwaka 2020. Ni vizuri Serikali ikachukua hatua madhubuti kama ambavyo inachukua ili kukamilisha hii miradi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Bahi imegawanywa miaka 10 iliyopita, lakini watumishi waliotoka hapa Dodoma wakati huo tunakaa hapa Dodoma kama Makao Makuu ya Wilaya ikiwa Dodoma Vijijini mpaka leo huu mwaka wa 10 wamehamia Bahi hawajalipwa mafao yao ya uhamisho. Kwa kweli ni kitu cha ajabu sana. Watu wanasubiri miaka 10, wako waliostaafu, wako waliokufa, wako waliohama kwenda wilaya nyingine, wako waliobaki pale Bahi mpaka leo hawajalipwa fedha zao za uhamisho, miaka 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na wakati wa kushika shilingi nitashika mshahara wa Mheshimiwa Waziri mpaka aniambaie ni lini atawalipa hawa watumishi wa Bahi milioni mia nane sabini wanazodai kwa kipindi cha miaka 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA. Tunaipongeza Serikali na sisi Wabunge wenyewe ndio tumetunga sheria ile ya TARURA hapa, lakini upo upungufu katika ufanyaji kazi wa TARURA. Ukiangalia katika mchango wa Waheshimiwa Wabunge hapa wako Waheshimiwa Wabunge ambao wameshukuru sana namna ambavyo unashirikiana vizuri na TARURA, lakini wako Waheshimiwa Wabunge wameonesha tu kasoro katika namna ambavyo TARURA inashirikiaa na halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahali pengine wako Mameneja wa TARURA wamejisifu wanasema sisi ni chombo pekee, sisi ni chombo maalum, lazima Mheshimiwa Waziri kauli hii waiondoe waelekeze kwamba wao ni wakala na mimi najua wakala yeyote anafanya kazi kwa niaba ya mtu fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawa kama ni wakala ina maana wanafanya kazi kwa niaba ya halmashauri na ndio wenye barabara wanapashwa kuripoti, wanapashwa kushirikiana na Mkurugenzi, wanapashwa kuhudhuria vikao mbalimbali vya halmashauri ili Madiwani ambao ndio wenye hizo barabara, ndio wanatekeleza ilani, ndio waliowaahidi wananchi kutengeneza barabara nao waweze kutoa ushauri katika utengenezaji wa barabara na kusimamia katika utengenezaji wa barabara zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa mara ya kwanza kututengea fedha katika bajeti hii za hospitali ya wilaya, jambo hilo tunalishukuru sana. Hata hivyo, nashauri, kama ambavyo tumetumia force account kwenye miradi ya vituo vya afya ambavyo pia wametupatia pesa na tumeona ufanisi mkubwa katika kutumia force account kwenye ujengaji wa vituo vya afya. Hizi fedha Wizara ielekeze nazo pia zitumike kwa mtindo wa force account. Hizi bilioni moja na nusu zinaweza kufanya kazi kubwa na kama upungufu unaweza kuwa kidogo tu kabla ya kukamilisha hizi hospitali za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI wamekuwa wakitupangia watumishi na wamekuwa wakituletea watumishi, tunaomba waache kutupangia vituo, watuletee watumishi kwenye halmashauri, Mkurugenzi ndiye apange vituo vya hawa watumishi. Leo wanaleta Walimu 20 halafu wanawaandikia na majina ya shule wakati pengine shule ile wanayompelekea haina upungufu kama ambavyo shule ambayo hawakuitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri katika maeneo ya watumishi Walimu, watumishi wa hospitali na watumishi wa kada zingine wamletee Mkurugenzi, wamwambieni hawa ni wataalam fulani, yeye atawapangia vituo vya kazi kulingana na yeye anavyoona wapi pana mahitaji muhimu, kuliko kutupangia moja kwa moja kutoka Wizarani. Kwa kweli wamekuwa hawatutendei haki na mara nyingine wanakwenda kurundika watumishi mahali ambapo tayari walikuwepo na shule ya pili au ya tatu inakuwa haina watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza kwa kuondoa riba ya asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya akinamama na vijana, lakini wahakikishe inafika. Kuondoa riba tu peke yake bila fedha hizi kutengwa haiwezi kusaidia kwa sababu wako Wakurugenzi katika kutenga hizi fedha wanaamua wanavyotaka, akijisikia kutenga anatenga.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana mheshimia Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri ambao kwa kweli, wametoa ushirikiano mzuri sana kwangu katika kipindi chote ambacho wamekuwa Mawaziri. Wamefika kwangu Bahi kwa nyakati tofauti na Mheshimiwa Waziri hivi ameniahidi Jumamosi ijayo tena anakuja Bahi. Kwa hiyo, kwa kweli nina kila sababu ya kuwashukuru na matokeo ya ujio wao pia yameonekana kwa sababu pale Mji wa Bahi tumekuwa na shida ya maji kwa muda mrefu sana, lakini Mheshimiwa Waziri aliruhusu pesa shilingi milioni 400 katika bajeti hii ambayo tunakwendanayo na kwa kweli, watu wa Bahi wameanza kupata maji angalau kwa kiwango kidogo, lakini maji yameanza kutoka na kwa mara ya kwanza watu wa Bahi wameyaona maji ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika bajeti hii nimeona wametuongezea shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Maji wa Bahi, ingawaje fedha hizo hazitoshi, na Mheshimiwa Waziri kwa kuwa unakuja basi utaona namna ambavyo tutakuomba kule Bahi. Ninaamini utashirikiana na sisi kama ambavyo umeshirikiana kukamilisha kabisa ule Mradi wa Maji wa Bahi, mji ambao unakua kwa kasi ili watu waweze kuyatumia maji kwa shughuli mbalimbali za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Wizara ilitupa fedha ya kuchimba visima vitano katika mwaka huu wa fedha ambao tunakwendanao na tayari tumechimba visima vitatu katika vijiji vya Ilindi, Bahi Makulu na Mpamata. Sasa tunakwenda kuchimba katika Kijiji cha Ikungulu na Lamaiti. Katika bajeti ambayo tunakuja sasa kwa kuwa mlitupa fedha za kuchimba visima katika vijiji vitano bila pump, lakini naona mmetuwekea sasa katika hivi vijiji vitano, safari hii mmetuwekea fedha shilingi milioni 100 kwa kijiji kimoja cha Ilindi. Sasa nilikuwa nataka nijue Mheshimiwa Waziri umetupa mwaka jana fedha za kuchimba visima vitano, tumeshachimba vitatu na tunakwenda kuchimba viwili vingine na vitakuwa vitano ambavyo havina pump, lakini kwenye bajeti hii unatoa tu kisima kimoja kama tukafunge pump kwa maana ya kisima cha Kijiji cha Ilindi. Nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Waziri kama umesahau vijiji viko vitano, basi niongezee hivyo vijiji vinne pia navyo tupate fedha kwa ajili ya kufunga pump ili wananchi wameona visima vimechimbwa wawee kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia, viko vijiji kadhaa ambavyo navyo vina shida kubwa katika Wilaya ya Bahi na hususan kwa sababu Wilaya ya Bahi ile ni Wilaya ya ukame, ningeomba pia katika vijiji baadaye utakaapopanga bajeti zako vijiji vya Chikola, Chonde, Ikumbulu, Chifutuka, Chaliigongo, Chikopelo, Chalisanga na Mkola navyo kwa kweli uweze kuvipata fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha hotuba yake katika ukurasa wa 273 ziko taarifa ambazo mimi nataka nimwambie taarifa zile si sahihi. Nimeona kwamba katika mradi ule wa visima vilivyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) imeonesha pale kwenye ukurasa wa 273 kwamba kwenye Wilaya yangu ya Bahi viko vijiji vya Mzogole ambapo kuna kisima namba 278 kwa kupitia Mkandarasi Godwin Mwasombwa na kijiji cha Zejele namba 279 kupitia Mkandarasi Emmanuel Nyaumba kwamba vijiji hivyo vimkechimbiwa visima na kwa bahati mbaya visima vimekutwa havina maji.

Mheshimiwa Spika, jambo hili sio kweli Mheshimiwa Waziri. Kama nkuna watu walikupa taarifa hizi wamekudanganya kwa sababu mimi binafsi nimeshituka kuona hapa kwenye kitabu chako kwamba mmetuchimbia hivyo visima katika Vijiji vya Mzogole na Zejele lakini hakuna maji. Nikafanya utafiti, nimewasiliana na uongozi wa kijiji, nimewasiliana na Mheshimiwa Diwani, Mhandisi wa Maji wa Wilaya na Mkurugenzi, wote wamenijibu kuwa jambo hili halikufanyika. Kwa hiyo, nilikuwa naomba jambo hili wakati unajibu hoja mbalimbali za Wabunge na mimi unijibu kumetokea kitu gani zimeletwa taarifa hapa ambazo si sahihi. Kama ahawajachimba na fedha hizi zipo waende wakachimbe visima hivi na nina uhakika maeneo haya watapata maji.

Mheshimiwa Spika, lakini wakati tunaendelea na miradi hii ya maji ni vizuri pia tukaiangalia kwa jicho lingine miradi ya umwagiliaji. Kwa mfano sisi watu wa Dodoma kila mtu anajua namna ya ukame wa Dodoma, hata watu mwaka huu wameshangaa kuona mvua kubwa namna hii, ni baraka tu za Mwenyezi Mungu. Lakini kwa kweli tuna shida kubwa ya ukame na mkombozi pekee kwenye Wilaya hizi za Dodoma, hususan Wilaya yangu ya Bahi ni kuwa na kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, tunazo skimu kumi pale katika Wilaya yetu ya Bahi, lakini skimu hizi miongoni mwao zimechakaa, ni za muda mrefu, hazikutengenezwa kwa kiwango kizuri na skimu hizi zinazhitaji matengenezo makubwa. Katika bajeti iliyopita nilipata nafasi hapa ya kuchangia, nikaomba Wizara ije itume wataalam wake kuja kufanya tathmini ya kina kujua hii miradi ya umwagiliaji Bahi hasa mahitaji yake ni nini maana imepitwa na wakati. Miradi hiyo ni Bahi Sokoni, Nguvumali, Matajira, Mtazamo, Mtitaa, Uhelela, Chikopelo, Kongogo, Lubala na Uhelela. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri safari ile hukutuma hiyo timu, lakini safari hii naomba utume timu Bahi ije ione miradi hii inahitaji mahitaji gani ili iweze kuendelezwa na sisi wananchi ambao wilaya yetu ni ya ukame tuweze kuitumia kikamilifu kupata chakula na tuepukane na ombaomba ya chakula kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, uko Mradi wa Kongogo ambao umeniahidi Jumamosi ijayo unakuja kuutembelea. Huu ni mradi wa muda mrefu wa bwawa na sehemu nyingine inataka kwenda kumwagilia. Ni mradi ambao umekuwa ukilalamikiwa na wananchi muda mrefu, umetumia fedha nyingi na umeniahidi kwamba utafika siku ya Jumamosi. Mimi mwenzio nilipokwenda mara ya mwisho nilipokelewa na mabango juu ya namna ambavyo watu hawakuridhika na utengenezaji wa Mradi huu wa Kongogo. Sasa siwatumi hapa waje na mabango siku ya Jumamosi utakapokuja, lakini watakupa ujumbe wa namna ambayo wamesikitishwa na kuchelewa kukamilika na kutokuridhika kwa kiwango cha mradi huu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini gharama za miradi ya maji zimeelezwa na Waheshimiwa Wabunge hapa na mimi mwaka jana niliwahi kusema jambo hili kwa kweli gharama za miradi ya maji ni gharama kubwa mno. Wako baadhi ya wataalam wetu si waaminifu, wamekuwa wakishirikiana na wakandarasi kuhakikisha kuongeza kiasi cha fedha cha miradi hii na imekuwa ni vigumu sana. Mimi naamini kama miradi hii ingetafutiwa njia bora ya utekelezaji kwa miaka yote hii leo tusingekuwa na kilio hiki tunacholia hapa. Kilio hiki tunacholia kimesababishwa na sehemu ya wataalam wetu na wakandarasi ambao sio waaminifu, lakini pia na usimamizi hafifu na Wizara kutokujituma kutaka kubadilika na wakati kwamba, hivi kwa nini kila siku tunalia kilio hicho hicho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni vizuri na mimi nakubaliana, na umezungumza vizuri asubuhi kwamba miradi ya shilingi milioni 600, shilingi milioni 700 ni miradi ambayo imeumiza wananchi kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, umekuwa ukiunda tume hizi na zimekuwa zikifanya kazi nzuri sana, hebu tubadilike na kwenda kwenye tume ambayo itachunguza utekelezaji wa miradi ya maji. Uunde Tume hapa ya Kibunge iende ikaangalie namna ya kutengeneza miradi inavyotengenezwa, ifanye tathmini ya muda, gharama, kwa nini miradi ya umeme tunaambiwa ukienda kilometa kadhaa ni shilingi kadhaa, lakini miradi ya maji huwezi kukuta hiyo habari, kila mtu anajipangia vile anavyoona yeye inafaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima jambo hili kwa kweli liangaliwe kwa kina, kiki fedha zitumike chache, lakini zenye tija, vifaa bora na wananchi waweze kupata huduma hii ya maji kama ambavyo inasisitizwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nakuomba sana hebu uunda tume itakayochunguza miradi ya maji tuisaidie Serikali. Tume ile ya Wabunge itakuja na mapendekezo na hapa tunapofikiria kuunda huu Wakala wa Maji Vijijini uwe na kitu cha kuanzia kwamba inakwenda kusimamia kitu gani ambacho kimechunguzwa kikamilifu na kimetolewa maelekezo na kinaweza kutoa tija na ufanisi, ili wananchi wetu hawa wasiendelee kulia kilio cha kukosa maji.

Mheshimiwa Spika, tunayo Tume ya Umwagiliaji, kwa kweli imekuwa na watumishi wachache na yule bosi wao anakaimu leo mwaka wa tatu, sijui ni mwaka wa nne, inakuwaje mtu anaweza kukaimu miaka yote hiyo na mtu anafanya kazi vizuri, anachapa kazi vizuri, tunashirikiana naYe vizuri? Mpeni nafasi ya kuwa Mkurugenzi kamili, ili aweze kujiamini na kufanya kazi ile kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono tozo ya shilingi 50 iongezwe kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameshauri, ili iweze kuongeza kiwango cha fedha ambacho kitatusaidia sana katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. asante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, nampa hongera Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola kwa majukumu. Nachukua fursa hii kukumbusha juu ya wito wa Serikali kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Tarafa ya Chipanga, Wilayani Bahi waliamua kujenga Kituo cha Polisi cha Tarafa toka mwaka 2003 na kukikamilisha lakini hadi sasa hakijafunguliwa takribani miaka 16 sasa. Wananchi walichangia zaidi ya milioni 40 wakati huo, lakini wamekatishwa tamaa na Jeshi kutokukipokea kituo hicho na kukifungua. Kituo hicho kina umuhimu mkubwa kikifunguliwa kwa kulinda usalama wa mali na wananchi. Naomba sasa kifunguliwe. Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie japo kidogo katika Muswada huu wa kutambua rasmi kwamba Dodoma sasa ni Makao Makuu. Kwanza nichukue nafasi kama walivyotangulia Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuamua sasa kutekeleza rasmi jambo
letu ambalo limekuwa kwa miaka mingi halijatekelezwa na sasa Serikali yote imeshahamia rasmi hapa Dodoma na yeye mwenyewe ameahidi kuja hapa Dodoma hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza sana Wizara kwa kuleta Muswada huu mzuri ambao kwa kweli umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na hatimaye leo umeingia hapa Bungeni naamini baada ya hapa sasa Dodoma ni rasmi kwamba, ni Makao Makuu ya Nchi yetu na hakutokuwa na kitu tena cha kuyumbisha makao makuu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia ya kutoa ushauri kidogo kwa sababu napongeza hatua Dodoma sasa kuwa jiji na Mheshimiwa Rais ametangaza na sisi watu wa Dodoma tumepokea na tumefurahi sana. Hata hivyo, nataka nishauri tu kwamba, tukiangalia katika haya majiji liko Jiji la Dar es Salaam lina Manispaa tano sasa, nadhani kama hivyo, lakini kuna Jiji la Arusha lina Manispaa moja, Jiji la Tanga Manispaa moja, Mwanza Manispaa mbili, lakini Dodoma sasa inaonekana bado kuna manispaa moja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kupitia sheria hii ya Dodoma sasa kuwa makao makuu, tunataka kujua nini kitafuata? Tunaweza kuwa Halmashauri zaidi ya moja kwa maana ya Manispaa. Hii nadhani itasaidia sana kuleta maendeleo kwa haraka, kwa sababu leo ukienda pale ofisi ya ardhi Dodoma hata hospitali sidhani kama kuna watu wengi kama pale. Maana watu wameamka, watu wameamua kujenga hapa Dodoma lakini inaonekana ofisi zile zinalemewa lakini naamini kama tukiwa na Manispaa mbili zikagawanyika.

Mheshimiwa Spika, kwanza zitasaidia urasimu kupungua lakini hata usimamizi wa ujenzi wa miundombinu na mipango kwa upande mmoja utakuwa unapanga mipango yake na upande wa pili unapanga mipango yake, Dodoma itaendelea kwa kasi sana. Nadhani tuangalie pia mfumo huu wa Jiji moja na kuwa na Manispaa moja huko mbele tuone vizuri kama tunaweza kuwa na manispaa zaidi ya moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua tunapitia upya master plan yetu ya Mji wa Dodoma na ni vizuri kweli kuipitia kwa sababu jambo la miaka 45 iliyopita huwezi kulinganisha na leo. Nataka niseme tunashukuru sana kwamba jambo hili limechelewa, ukiangalia kama jambo hili tungekuwa tumelipitisha mwaka huo sabini na kitu leo tungekuwa na mbanano mkubwa wa Dodoma hapa lakini, kwa sababu wakati ule mwamko wa kimaendeleo watu wengi walikuwa bado hawajui nini kitatokea.

Mheshimiwa Spika, mfano, leo kuna barabara ya sita, barabara ya saba, ya nane, ya tisa mpaka barabara ya kumi na mbili tumeamua sasa zigeuzwe iwe barabara za njia moja, kwa sababu zilikuwa planned zamani na watu walikuwa hawafikiri kwamba labda kutakuwa na magari mengi kama sasa. Hata hivyo, leo hii kwa uelewa mkubwa tulionao na watalaam wetu wapo, najua wameiweka Dodoma sasa miaka 1000 ijayo, kwa maana kwamba watai-plan Dodoma sasa hata kama sisi tumeondoka miaka 50, miaka 100, miaka 200 watu wasitulaani sisi kwamba, hawa nao walio-plan wali- plan vibaya leo tumebanana.

Mheshimiwa Spika, nashauri pia wenzetu kwenye hii Master Plan waipitie lakini wa-plan vizuri, hata kama hatuwezi kujenga barabara za njia sita kwa maana ya tatu huko, tatu huku lakini tuweke eneo ambalo linakubali huo ujenzi baadaye, hata kama leo tutajenga barabara moja, lakini kesho ikitakiwa mahitaji ya barabara mbili liwe eneo lile lile, barabara tatu eneo hilo hilo, kwa sababu itatusaidia sana kupunguza msongamano lakini pia kujenga mji wenye ramani ya kutosha wakati huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunatarajia Dodoma kuwa mji wa kisasa, mzuri utakaopendeza, kwa hiyo tunawapa kazi hiyo watalaam wetu kutembelea hata miji mbalimbali kujifunza kuona wenzetu wamefanya nini, walikumbana na changamoto gani, wamefanikiwa wapi ili haya yote mazuri wayalete hapa Dodoma na zile changamoto waweze kuziepuka mapema ili kwa kweli Jiji la Dodoma liwe zuri na liwe endelevu ambapo ukitaka kufanya jambo lolote
unaendeleza kutokea pale ulipokuwa, unasonga mbele kuliko kufikiri kuanza kulipa fidia na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nikiangalia hapa Dodoma leo tunaitangaza kuwa Makao Makuu lakini Ikulu iko Chamwino. Sasa nataka nipate pia maelezo kwa sababu Ikulu iko Wilaya ya Chamwino sasa Makao Makuu haya Ikulu iko pembeni labda tuambiwe na yenyewe, Chamwino kipande kile kinakuja huku Dodoma au kitabaki kule kule ili tuweze kujua sasa Mheshimiwa Rais tunakaa naye hapa Makao Makuu au tunakaa naye wapi?

Mheshimiwa Spika, vile vile nafikiri hata eneo la Mabalozi liko huko Dodoma, liko eneo la Dodoma lakini eneo la Ikulu liko Chamwino. Kwa hiyo, nadhani na hili nalo pia tupewe maelekezo yake kwamba, sasa Chamwino inabaki kuwa Ikulu kule kule Chamwino au Chamwino inarudi kuwa Dodoma kwa maana ya marekebisho ya mipaka kwa eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hapa sasa watakuja watu wengi sana kwa maana ya uwekezaji, lakini ukiangalia katika eneo la uwekezaji bado tuna urasimu mwingi sana. Tunakutana na wawekezaji wengi sana wanalalamika hapa, wanalalamika pale mambo yanachukua muda mrefu na wengi wanapenda kujenga Dodoma. Kwa mfano juzi tu tulikuwa tunakagua viwanda, wale wenye viwanda wengi wanasema sisi tunataka kuja kujenga Dodoma lakini bado tunasumbuliwa eneo, bado hatujapata.

Mheshimiwa Spika, tukashangaa sana kama tumeshatangaza Dodoma ni Makao Makuu na wako watu wanataka kuja kuwekeza Dodoma hususan viwanda na kadhalika lakini bado wanalalamika urasimu uliopo hapa. Nilidhani Serikali ingeliangalia hili jambo kwa upekee sana. Kama kweli tunataka Dodoma ikue haraka tutafute mbinu nzuri ya kuwafanya wawekezaji na watu wengine wanaotaka kuja kuwekeza Dodoma maeneo mbalimbali waweze kupata maeneo kwa urahisi, muda mfupi na kwa kweli tuwasaidie kuhakikisha wanafikia malengo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiwa na makao makuu ambayo hayana hata maeneo ya utalii, maeneo ya burudani itakuwa ni ajabu sana, kwa sababu mji huu sasa utapokea watu wa nchini mwetu, utapokea watu wa kimataifa, watapenda kuja kuona vitu mbalimbali. Sisi Wagogo tuna tamaduni zetu nadhani tutafute mahali ambapo pia tutaweka utamaduni wetu wa kabila la Wagogo ili watu waweze kuja kujifunza kwa sababu Dodoma ndio makao makuu. Hata kama hawa watani zetu wanatutaniatania lakini tunawaambia sisi tutabaki hapa hapa, hatupotei na tuweke utamaduni wetu hapa katikakati ya mji ili mtu akija aone kwamba, Dodoma Wagogo wapo na wanaendelea kufanya kazi zao kama Wagogo, najua hili utaniunga mkono vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo ya utalii pia, tuna mbuga zipo jirani jirani katika Wilaya ya Kondoa na Wilaya zingine hapa ziimarishwe hata kama zitakuwa ni mbuga za kutengenezwa kwa kuangalia hali ya hewa na kuhamishia wanyama ambao wako kwenye maeneo mengine ambayo wanaweza kukubali hali ya hewa hapa Dodoma, ni vizuri kwa kweli Serikali ikaone utaratibu wa kuhamishia hao wanyama. Kwa sababu tutakuwa na Mabalozi na wageni wa nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, nina hakika wageni hawa wote wangependa kuona wanyama wetu, wangependa kuona tamaduni zetu na Dodoma itapendeza kwa kweli ikiwa na vitu mbalimbali mchanganyiko, sio tu Makao Makuu ya Serikali na sisi kuhutubia, lakini pia kuwe na vitu ambavyo tukishawahutubia wanakwenda pia baadaye kuangalia mambo mbalimbali ambayo yatawaliwaza na yatawafanya waendelee kuipenda Dodoma.

Mheshimiwa Spika, lakini mahoteli vile vile makubwa na ya kisasa, tutafute namna ya kutenga maeneo mazuri na kuwashawishi wenzetu ambao wanaweza kujenga mahoteli mazuri, yuko mtu anaweza akaja Dodoma hapa akasema mimi hapa hata hotel moja silali. Anataka hoteli ya nyota tano, nyota ngapi, kwa hiyo lazima haya mambo yote tuyaangalie sana sasa ili tuweze kushawishi watu.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia mpango wa kujenga airport yetu. Sasa Mheshimiwa Rais akihamia hapa na Marais wengi watakuja, wengine wanakuja ndege zao kubwa hawawezi kutua hapa Dodoma, sasa sijui itatakiwa Mheshimiwa Rais akawapokee tena Dar es Salaam. Kwa hiyo, na hili jambo pia la uwanja nalo lipewe kipaumbele, ikiwezekana Mungu akipenda bajeti tunayokuja kupitisha mwakani kwa mwaka wa fedha unaokuja, tuone pia mipango ya ujenzi wa kiwanja kikubwa na cha kisasa cha ndege hapa Dodoma ili wageni wetu mbalimbali wanaokuja, mashirika mbalimbali ya kimataifa yaweze kuvutiwa pia kwamba sasa yanakwenda Dodoma lakini yatapata mahali pa kutua na sio waje Dar es Salaam wabadili ndege na mambo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja hii, naunga mkono Waheshimiwa Wabunge wote, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Mtuka Bahi ipo karibu zaidi kuliko Manyoni. Maana yake alipokuwa anasema hapa Bahi haijakaakaa vizuri, namwambia Bahi pamekaa kaa vizuri na Bahi ndio itakuwa sehemu ya kupumulia mji huu utapokuwa umejaa, kwa sababu Bahi na Mjini hapa ni karibu sana, kwa hiyo Mheshimiwa Mtuka angoje kwanza Bahi ikamilike halafu tutakuja Manyoni, lakini kwanza ukitaka kwenda Manyoni lazima upite Bahi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.