Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Selemani Said Jafo (21 total)

Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kuleta Azimio hili hapa Bungeni, kwa sababu najua jambo hili ni jambo lenye manufaa makubwa sana kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa Kiongozi mwenye dhamana katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Azimio hili kwetu tunalipokea kwa mikono miwili, nikijua wazi kwamba vijana wetu wanaosoma shule za msingi na sekondari, hivi sasa tunapojielekeza katika suala zima la michezo mashuleni, sasa Azimio hili linatupa nafasi nzuri sana ya kuwaandaa vijana wetu katika michezo bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia kuhusu vijana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na timu yake. Juzi tuliwashuhudia vijana wetu wa Serengeti Boys kule India wakifanya maajabu makubwa sana. Mheshimiwa Naibu Waziri, ikikupendeza sana vijana wale inapaswa tuwalete hapa Bungeni tuwatie moyo, walifanya kazi kubwa kwa kushiriki michezo ile, katika michezo yote hakuna mchezo waliofungwa, walifanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana vilevile nilishuhudia katika vyombo vya habari, timu yetu ya Azam ya Vijana, walipokuwa wakishirikisha timu za Uganda, Kenya na hapa Tanzania, katika timu yao ni kwamba michezo yote wameweza kufanikisha, wameshinda michezo yote na kupata kombe lile, imeleta heshima kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ina jukumu la michezo ya UMISETA ambayo inaendelea hivi sasa, naomba tulipokee Azimio hili kwa moyo mkunjufu, nikijua kwamba katika michezo yetu hii, sisi kama Serikali tunaoasisi michezo mashuleni, vijana wetu hawa tukiwaandaa vizuri katika Azimio hili sasa, maana yake tutaweza kupata vijana bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siku za usoni tujue vijana hawa ndiyo tunatakiwa sasa tuwalee vizuri katika suala zima la taaluma, huko baadaye tukapate Madaktari na Professors. Kama tusipokuwa na usimamizi mzuri katika eneo hili maana yake vijana leo hii wanaposhiriki michezo wataweza kutumia madawa haya, mwisho wa siku wanapofika sasa katika kutumia akili yao katika taaluma inawezekana tukawa na vijana wengi ambao watashindwa kufanya vizuri kimasomo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nampongeza sana, Azimio hili limekuja katika muda muafaka. Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba nimhakikishie wazi, kwa sababu tuna mtandao mpana wa vijana katika shule zote, tutahakikisha tunashirikiana na Wizara ya Habari na Michezo kuhakikisha kwamba jambo hili linatelekezwa vizuri katika shule zetu zote ili vijana wetu wanapokwenda kushiriki katika michezo, kwanza iwe ni ajenda ya kudumu katika michezo yote; kwamba wafahamu utumiaji wa dawa hizi siyo sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kwamba, kutoa maelekezo ya kutosha kwamba wao wawe Mabalozi wazuri kuhakikisha kwamba tunalea kizazi cha vijana ambao watakuwa wazuri wa kuelewa jambo hili la utumiaji wa madawa ya kuongeza nguvu katika michezo siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, langu lilikuwa ni commitment katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwamba tutashirikiana vema kuhakikisha kwamba Serikali yetu inakuwa ni Serikali ya mfano, kwa suala la utumiaji wa dawa katika kuongeza nguvu katika michezo halitoruhusiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia zote mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mola)aliyetuwezesha, ambapo ilikuwa siku ya kwanza, ilikuwa asubuhi, ilikuwa jioni, tukakamilisha siku ya kwanza. Tukaenda hivyo mpaka leo tumefika ilikuwa asubuhi na itakuwa jioni siku ya sita na tutakamilisha jukumu letu tulilopewa katika Wizara hii kuwasilisha hoja hii mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati ya moyo wangu sana naomba nimshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, aliyenipa dhamana kubwa sana ya kusimamia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo ina watumishi takribani 388,000 sawa na watumishi asilimia 74.02 ya watumishi wote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Spika, nikushukuru wewe kwa kazi kubwa na Wenyeviti wa Kamati, pia niwashukuru sana viongozi wote wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI, ikiongozwa na mkubwa wangu Mheshimiwa Jasson Rweikiza na Mheshimiwa Mama Mwanne Mchemba, lakini wapiganaji wote wa Kamati hii walikuwa wametoa maelekezo ya kutosha mpaka na sisi tukapata umahiri wa kuweza kuwasilisha hoja hii hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa dhati ya moyo wangu niwashukuru Wabunge wote. Michango ilikuwa mizuri sana yenye afya ambayo kwa namna moja au nyingine inatuwezesha kama Wizara tuone nini tunapaswa kufanya katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru familia yangu kwa msaada mkubwa. Mkiona ninapendeza maana yake nyuma kuna watu wanafanya shughuli hiyo, lakini niwashukuru watoto wangu wote, najua wengine saa hizi wako masomoni, Mungu awafanyie wepesi masomo yao yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana, baba yangu amefariki, nimshukuru sana mama yangu mzazi kwa malezi mazuri. Siku zote amekuwa mama mlezi kwa kipindi chote, namshukuru sana mama yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe. Mjadala huu unavyoendelea walikuwa wakiufuatilia japokuwa katika vipindi vya vipande vipande, wengine wakati mwingine wanakaa mpaka saa sita usiku, saa tano usiku, kuona mjadala jinsi gani unaendelea katika ofisi abayo nimepewa dhamana Mbunge wao kuweza kuisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii ilikuwa ni hoja nzito, Wabunge waliochangia kwa kweli wamepatikana takribani
123. Kati ya hao Wabunge 71 walichangia kwa kuzungumza hapa Bungeni na Wabunge takribani 52, wengine walikuwa wanaongezeka saa hizi kwa maandishi, hawa wamechangia kwa maandishi. Najua kwa mujibu wa mwongozo wa kanuni zako na suala zima la muda, naomba Wabunge wote mliochangia mridhie kwamba kumbukumbu yenu itaonekana katika Hansard za Bunge za Taarifa yetu hii ya Wabunge waliochangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema ukweli hoja zimekuwa nyingi, lakini hoja hizi zote nazichukulia kwamba ni hoja zilizolenga kujenga mwenendo na utendaji mkubwa wa Wizara yetu. Hoja ya kwanza ambayo Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Rweikiza, mkubwa wangu na ninaomba Wabunge wengine wote mridhie, sitaki kuwataja Wabunge hapa kwa majina inawezekana mtu mwingine nikamuacha ikaja kuwa nongwa, kwa nini nimesema, lakini sijatajwa. Naomba wote tuliozungumza tubebwe na Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI. Akitajwa yeye basi, chukulia na mimi nimetajwa katika hoja hiyo kwa sababu nilichangia Bungeni. Maana naweza nikasema dada yangu Mheshimiwa Zainab Mndolwa hapo, wengine wakasema kwa nini umemtaja yule peke yake na mama Kauthar yupo hapa jukwaani ikawa nongwa hapa shughuli ikaanza kwa nini umemtaja yule peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja ambayo ilionekana Wabunge wengi wamechangia, Mwenyekiti wa Kamati alizungumzia ni suala zima la mapokezi ya fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hoja hii ukiiangalia imetamalaki mahala mbalimbali, hata katika hoja za CAG katika vipindi tofauti ilikuwa ikielekeza jinsi gani fedha hazifiki katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kamati yetu ya Utawala Mheshimiwa Rweikiza amezungumza hapa kwamba ndiyo hoja ambayo hata katika Kamati walizungumza sana. Naomba nikiri wazi kwamba hoja hii ni ya kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ni-appreciate juhudi kubwa za Serikali kwa sababu kwa ujumla wake kutoka Hazina kwa kipindi hiki cha sasa hivi katika mwaka wa fedha 2017/2018 mpaka tunapofika mwezi Februari tumeweza tumepokea takribani shilingi bilioni 231.33 sawa na asilimia 50 ya fedha za mengineyo. Hata hivyo, katika suala zima la maendeleo tulipokea jumla ya shilingi bilioni
914.39 sawa na asilimia 50 ya bajeti iliyokuwa approved ya mwaka wa fedha 2017/2018. Hata hivyo, ruzuku ya maendeleo inatolewa kulingana na ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika imani yangu kubwa kwamba kwa sababu bajeti iliyotolewa mpaka mwezi Februari mwaka huu tumefika asilimia 50, lakini hapa katikati tunatarajia kupokea pesa za ile miradi viporo ambayo ninyi Wabunge tuliwaita, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi na Maafisa Mipango. Hazina inafanya harakati nadhani kabla ya mwezi Juni tutapata baadhi ya fund ya fedha imani yangu kubwa mwaka huu wa fedha kiwango cha fedha kilichopokelewa kitazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili naomba sana niwahimize wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninachoamini ni kwamba fedha zote zinatoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali, tunapaswa katika ile ajenda ya pamoja kama Taifa, kuhamasishana suala zima la watu waweze kulipa kodi ambapo naamini kodi ikilipwa Mfuko Mkuu wa Serikali hautaona aibu kupeleka pesa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 tumetenga miradi mikakati. Ajenda yetu ni nini? Licha ya Halmashauri kutegemea fedha zile kutoka Serikali Kuu lakini miradi ya Halmashauri ibuni miradi ambayo itasaidia kuchagiza upatikanaji wa fedha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Katika hili niwasihi Wabunge wote katika Kamati zetu za Fedha kule katika Halmashauri zetu tusiwaonee aibu Maafisa Mipango, badala ya kubuni mipango wao wanakaa tu Maafisa Mipango haiwezekani. Haiwezekani leo hii kuna Halmashauri zimepeleka miradi mikakati mpaka leo hii lakini kuna Maafisa Mipango wengine wamelala msikubali Waheshimiwa Wabunge katika Halmashauri zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha imetengwa kwa lengo kubwa kuhakikisha kwamba tunapata watu mahiri kwa ajili kuhakikisha wanafanya resource mobilization tupate fedha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, jambo hili nina imani kwamba kama Taifa kwa pamoja tutaweza kufika mahala pazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa ni suala zima la TARURA bahati nzuri msaidizi wangu Mheshimiwa Kakunda amelizungumza hapa kwa kina, lakini kama tunavyofahamu ni kwamba hii ni taasisi mpya ambapo mtandao wa barabara kama nilivyosema awali tuna mtandao wa barabara takribani kilometa 145,000, lakini kilometa karibuni 108,000 zote zinasimamiwa na TARURA maana yake changamoto ni kubwa, lakini ukiangalia mgao wa bajeti ambayo tunaitegemea ni ile asilimia 30 kutoka Road Fund. Wabunge mlisema hapa kwamba ikiwezekana formula iweze kurekebishwa. Waziri Mkuu wakati anazindua TARURA mwezi Julai, 2017 alilizungumzia hili kwamba Serikali ikae na jambo hili tunalifanyia kazi kama Serikali kwa pamoja kuona namna gani bora vipi baadaye, TARURA kiwe chombo kinachoweza kusimama kipate fedha kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaozalisha uchumi, kule maeneo ya vijijini ambao mazao na mifugo inakotoka waweze kusafirisha malighafi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Serikali tunaenda kulifanyia mpango mpana zaidi tuangalie ikiwezekana vyanzo vingine vya mapato, maana yake hata tukiitegemea mgawanyo huu hatutoweza kujibu shida za mitandao ya barabara ya kilometa 108,000.9. Ni lazima kama Wabunge wote endapo Serikali itakuja na mpango mkakati wa kutafuta fedha, kuhakikisha fedha hizi zinakuwa ring fenced kuenda kujibu matatizo ya barabara vijijini, naomba Wabunge wote tuungane na Serikali katika ajenda hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengine, nimesikia akina Mheshimiwa Lusinde walisema barabara zetu, madaraja yetu, kule Nzega kuna daraja kule la ndugu yangu Mheshimiwa Bashe maeneo yote ya nchi hii, ndugu yangu Mheshimiwa Lubeleje alizungumza barabara zake za Mtanana, tunayafahamu haya Wabunge wote naomba niwaambie. Ajenda yetu kubwa ni kuhakikisha tutabaini barabara zote, lakini tutaisimamia TARURA iweke legacy katika nchi hii ni taasisi inayofanya vizuri kuboresha miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha ajenda ya TARURA, jambo lingine lililojitokeza ni suala zima la uwekezaji wa elimu msingi bila malipo. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kila mwezi kuanzia mwezi Disemba, 2015, Serikali ilikuwa ikitoa bajeti ya fedha takribani shilingi bilioni 23 kwa ajili ya ku-service suala zima la programu ya elimu bure. Hata hivyo mwaka jana tulikwama, Wabunge wengine ninyi mlisema humu ndani kwamba fedha zile hazitoshi. Tulimuomba Mheshimiwa Rais akasema tusubiri mwaka wa fedha umefika sasa, bahati nzuri mwaka huu tumepata additional fedha karibuni 3.6 bilioni ambayo inaongezeka katika suala zima la elimu msingi bila malipo. Jambo hili litatupa nguvu kuhakikisha programu hii inaenda vizuri, kwa sababu nikijua wazi kwamba kuna wanafunzi ama watoto walioongezeka wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naomba nikiri kwamba jambo hili Watanzania naomba niwasihi Wabunge tuache kubeza mambo mengine ambayo yana maslahi mapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Wabunge wamesema mpango huu hauna maana yoyote, ndugu zangu naomba niseme kuna watoto wa maskini ambao walikuwa wanashindwa kabisa kupata elimu, tuone kwa nini mwaka 2016 Januari mara baada ya suala zima la elimu msingi bila malipo, kwa nini tuliweza kuwapokea mpaka watoto wenye umri wa miaka kumi wanataka kuja kuanza darasa la kwanza. (Makofi)

Kuna wakati mama mjane, baba amepotea, ana mtoto wake anataka kumpeleka shule lakini anaambiwa lete uniform, lete dawati, mchango wa shule wanashindwa, lakini baada ya elimu msingi bila malipo tumeona watu wengi wakiwatoa watoto waliowaficha, waliokuwa wakiwatwisha vikapu vya vitumbua na karanga, sasa wamepelekwa shule. Kwa hiyo, jambo hili ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nafahamu jambo lolote lenye mafanikio lina changamoto yake, changamoto ndio suala zima la ujenzi wa madarasa, madarasa yanakuwa pungufu, madawati na hali kadhalika walimu. Hata hivyo, naomba niwaambie Serikali haikulala, Serikali katika mwaka huu wa fedha tumeamua kuwekeza vya kutosha. Inawezekana kuna bajeti zingine msizione katika vitabu hivi lakini naamini mtaviona katika mpango wa Serikali katika maeneo mbalimbali hasa vilevile katika suala zima la Wizara ya Elimu, ndiyo maana mwaka huu mnaweza mkaona tutakuwa tunafanya arrangement ya ndani ya Wizara kati yetu na Wizara ya Elimu, inawezekana watu wengine wanahoji kwanini fedha nyingi za miundombinu hatuzioni TAMISEMI wakati ninyi ndiyo mnaojenga madarasa na vyoo vya shule za msingi Kamati ilisema, hili tunalifanyia kazi mtaona ujenzi wa madarasa, ujenzi wa vyoo, ujenzi wa nyumba za walimu jinsi gani Serikali imejipanga kwenda kujibu matatizo katika sekta ya elimu katika nchi yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ambayo ndugu yangu Mheshimiwa Bashe alizungumza hapa kwanini TAMISEMI inaonekana bajeti zake zote zimeenda katika recurrent expenditure. Kama nilivyosema, TAMISEMI ukiiangalia bajeti ya mishahara recurrent expenditure yote ni ya nchi nzima mwaka huu ni trilioni 7.4; lakini bilioni 4.1 yote ni mishahara kwa watumishi waliopo chini ya ofisi ya Rais, TAMISEMI, hata katika bajeti process obvious utaona gharama hizi zinaongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu bajeti peke yake katika ofisi hii inachukua asilimia 56 ya bajeti ya mishahara ya nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata leo Wabunge mkisema kwamba walimu waongezewe mishahara, wauguzi waongezewe mishahara maana yake unaongeza recurrent expenditure kwa ajili ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni jambo jema, kwa hiyo msishangae ndugu zangu kwamba bajeti peke yake ni trilioni 1.8 ya development budget out of trilioni 6.58 ni kwa sababu ni kwamba watumishi wengi na transaction nyingi za kiutumishi ziko katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mambo ambayo yalitamalaki sana ni suala zima la ujenzi wa miundombinu ya afya. Tumetoka mbali na hapa nilisema siku nilipo-table hotuba bajeti yangu, Tanzania tumetoka mbali ukiangalia hospitali za wilaya, vituo vya afya, zahanati changamoto ni kubwa, nilisema wazi tutafika kipindi ambacho nchi hii imeweka historia, Mheshimiwa Dkt. John Pombe ameweka historia, ataweka historia kubwa ndani ya miaka hii mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii katika vituo vya afya, nenda Hospitali ya Amana, nenda Muhimbili, nenda kokote, nenda hata hospitali ya Tabora pale mtani wangu siku ile juzi alivyokuwa anachangia hapa Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, idadi ya watu wamejazana ni kwa sababu hatuna back up strategy kule katika ngazi zetu za kata, hatuna vituo vya afya vyenye kufanya upasuaji ndiyo maana mama kama hitaji la upasuaji ni lazima aende katika Referral Hospital.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo maana ajenda ya kwanza tumeanza kujenga vituo vya afya 208 kwa mara ya kwanza. Vituo hivi ni historia ambayo haijawahi kuwekwa kipindi chochote cha nchi hii kuweza kuweka miundombinu, tena niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge nilisema tutapeleka fedha hizi kwa kutumia force account na Wabunge kweli mmesimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika watu wanaostahili heshima kubwa ni Wabunge ninyi mmeweka historia kusimamia fedha zile kwa force account. Shilingi milioni 500 kwa mwanzo ukizipeleka katika Halmashauri wakatumia Wakandarasi tu hakuna kitu, lakini tulielezana, tulikubaliana, mkaenda kusimamia, sasa mafanikio makubwa yamepatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hiyo tu mwaka huu katika bajeti tumeamua kujielekeza katika suala zima la ujenzi wa hospitali za Wilaya. Hili lilikuwa ni tatizo kubwa sana Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama siku moja amekuja ofisini kwangu ametoka “jicho nyanya” anaomba Hospitali ya Wilaya kwake, anasema mimi Waziri mzima sina Hospitali ya Wilaya, sasa kawape salamu wale watani zangu wa Songea kwamba kule unaenda kujenga Hospitali ya Wilaya ya kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa faida ya nchi hii naomba nizitaje Hospitali ya Wilaya hizo kila mtu aweze kujifahamu. Tutajenga Hospitali za Wilaya 67 mwaka huu kwa maelekezo maalum na ramani maalum, wataalam wangu nimewatuma kazi hiyo, wakishirikiana na watu wa Wizara
ya Afya, Mkoa wa Arusha tukianza tunajenga Hospitali ya Wilaya ya Longido na Ngorongoro, katika Mkoa wa Dodoma tunajenga Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, Bahi na Chemba, katika Mkoa wa Dar es Salaam tunajenga Wilaya ya Kigamboni na Wilaya ya Ilala kwa rafiki yangu pale Mheshimiwa Mwita Waitara pale Kivule tutaenda kujenga, katika Mkoa wa Geita tutaenda kuweka Geita DC na Nyang’hwale; Katika Mkoa wa Iringa tutajenga Mufindi, Kilolo pamoja na Iringa; katika Mkoa wa Kagera tunaenda kujenga Kagera DC, Karagwe na Kyerwa, Mkoa wa Kigoma tutaenda kujenga Uvinza, Buhigwe na Kasulu; Mkoa wa Katavi tutaenda kujenga Mlele, Mpimbwe na Mpanda; Mkoa wa Kilimanjaro tutaenda kujenga Siha na Rombo. Siha tunaenda kumalizia pale na Rombo kwa Mheshimiwa Joseph Selasini tunaenda kujenga; Mkoa wa Lindi tunaenda kujenga Ruangwa na Lindi DC kwa rafiki zangu hawa akina Mheshimiwa Bobali na mwenzake Mheshimiwa Dismas Bwanausi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Manyara tunaenda kujenga katika Wilaya ya Mbulu DC na Wilaya ya Simanjiro; Mkoa wa Mara tunaenda kujenga Bunda DC, Musoma na Rorya; Mkoa wa Mbeya tunaenda kujenga Busokelo, Mbeya DC na Mbarali; Mkoa wa Morogoro tunaenda kujenga Gairo, Morogoro na Malinyi; Mkoa wa Mtwara tunaenda kujenga Mtwara DC, Nanyamba pamoja na Masasi; Mkoa wa Mwanza tunaenda kujenga Buchosa pamoja na Ilemela; Mkoa wa Njombe tunaenda kujenga Wanging’ombe, Njombe DC pamoja na Makambako; Mkoa wa Pwani tunaenda kujenga Kibiti, Kibaha DC pamoja na Kibaha TC; katika Mkoa wa Rukwa tunaenda kujenga Nkasi, Sumbawanga na Kalambo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Ruvuma tunaenda kujenga Nyasa, Songea DC pamoja na Namtumbo, Shinyanga tunaenda kujenga Shinyanga DC, Ushetu pamoja na Bariadi; Mkoa wa Simiyu tunaenda kujenga Itilima pamoja na Busega; Mkoa wa Singida tunaenda kujenga Singida DC tena tunaipeleka kule Ilong’ero ambapo watu walikuwa wanalilia sana muda wote pamoja na Mkalama DC; Mkoa wa Songwe tunaenda kujenga Ileje DC pamoja na Songwe DC; Mkoa wa Tabora tunaenda kujenga Uyui pamoja na Sikonge. Mkoa wa Tanga tunaenda kujenga Korogwe, Tanga DC pamoja na Muheza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tunaenda kutafuta fursa zingine katika baadhi ya maeneo kuhakikisha jinsi gani tutafanya tupate fedha zingine kama tulivyofanya katika vituo vya afya kuhakikisha tunaenda kuongeza Hospitali za Wilaya kwa kadri itakavyowezekana katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili najua ndugu zangu wa Tanga pale Korogwe walikuwa wamepanga hospitali ile ijengwe Korogwe TC, lakini katika suala zima la proper resource allocation Hospitali ya Korogwe iko pale Mjini Korogwe DC, ikaonekana siyo vema twende tena tukawapelekee Korogwe TC pale pale. Kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya maamuzi hospitali tunaenda kujenga kwa Maji Marefu, wale wa Korogwe DC hospitali yao wataipeleka Korogwe TC kwa ajili ya wananchi waweze kupata huduma vizuri. Haya ndiyo mambo ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mambo mengine ni suala zima ni ajenda ya viwanda. Niwashukuru sana Wabunge kuna siku ambayo tumethubutu hapa. Mheshimiwa Rais ajenda yake ni kwamba jinsi gani tutafanya uwekezaji wa viwanda katika nchi yetu na ndiyo maana katika ofisi yetu tukaona kwamba tuna Wakuu wa Mikoa, tuna Wakuu wa Wilaya na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa. Tutafanya vipi tuunge mkono ajenda hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliamua kutoa maelekezo kuwa Mikoa yote ijenge viwanda 100 katika kila Mkoa kwa mwaka mmoja. Bahati nzuri tarehe 20 Machi, Wakuu wa Mikoa tulikutana hapa Dodoma kufanya tathmini ya kwanza ndani ya miezi mitatu tumefanikiwa vipi katika jambo hili. Bahati nzuri ndani ya miezi mitatu tumejenga viwanda vidogo 1,285, ujenzi wa viwanda hivi ni sawa sawa na asilimia
49.4 ya utekelezaji wa lengo. Mimi naomba niwapongeze Wabunge wote katika maeneo yenu, lakini niwapongeze Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Maafisa Maendeleo ya Jamii tuliwaita hapa kwa ajili ya kuwapa terms of reference, nini wanapaswa kufanya katika suala zima la ujenzi wa viwanda, tumeanza kupata mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi viwanda vidogo ndugu zangu ndivyo vinavyoajiri watu wetu kati ya wanne, watano mpaka 10. Viwanda 1,285 hata kiwanda kimoja kikiwa na wastani wa kiwango cha chini watu watano, unazungumza takribani watu karibuni 6,000 wamepata ajira ndani ya miezi hii mitatu. Haya ni mafanikio makubwa ambayo naomba Waheshimiwa Wabunge tuungane kwa pamoja katika suala zima la ajenda hii tutafanya vipi zaidi kuongeza ajira kwa vijana wetu na mwisho wa siku tutaenda kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika ofisi hii mambo ni mengi na jambo lingine ambalo lilijitokeza ni suala zima ambalo Mheshimiwa Dunstan Kitandula alilizungumza hapa, kwamba ameona hotuba yote mwanzo mpaka mwisho haina habari ya mambo ya lishe. Tena anasema Mheshimiwa Selemani Jafo ulikuwa miongoni mwa wapiganaji wa lishe! Naomba niwaambie budget speech maana yake inatoa summary ya baadhi ya mambo mengi huwezi uka-capture yote, lakini kuna majedwali, kuna vitabu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 katika bajeti ya mwaka huu tumetenga takribani shilingi bilioni 15 tumetoka shilingi bilioni 11 tumeenda shilingi bilioni 15 ambapo hii maana yake tunaenda kujibu, hata hivyo siyo kutenga fedha kwa mara ya kwanza kutokana na agizo la Makamu wa Rais tuliamua kuwasainisha mikataba Wakuu wa Mikoa wote nini wanapaswa kufanya katika suala zima la afya haswa suala la lishe, tunajua wazi leo hii hatuwezi kupata watoto ambao wanasoma vizuri kama lishe yao itakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema suala la udumavu, mtoto akipata udumavu katika siku 1,000 za kwanza, mtoto huyo hata akiwa mkubwa anakuwa poyoyo hawezi kuelewa hata mwalimu akimfundisha. Mwalimu akimwambia Juma sema ‘a’ na yeye anasema Juma sema ‘a’ haelewi lolote! Lazima tuwekeze katika suala zima la lishe. Hivyo, Mheshimiwa Kitandula na Wabunge wote naomba niwaeleze kwamba mwaka huu tumechanga sekta ya lishe shilingi bilioni 15 ili kuhakikisha kwamba tunatengeneza kizazi kilicho imara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watu wote wanaenda vizuri katika suala zima la lishe na kupambana na udumavu.

Jambo lingine lilikuwa suala zima la mifumo ya elektroniki, naomba nishukuru sana, mwanzo ukusanyaji wetu wa mapato ulikuwa na changamoto kubwa na ripoti ya CAG ilikuwa inazungumza wazi jinsi gani uvujifu wa mapato umekuwa ukiendelea kila siku, lakini hata hivyo tumejitahidi sana hivi sasa makusanyo ya mapato yote sasa tunatumia mifumo ya elektroniki, hata hivyo hatutegemei tena huko tunakokwenda baadaye watu kutumia vitabu vya risiti ya kawaida, lengo letu ni kuzisaidia hizi Halmashauri ziweze kukusanya mapato ya kutosha kwa lengo kubwa ni kwamba Halmashauri zetu zikiwa na nguvu kubwa ya kiuchumi zitaweza kufanya mambo sahihi mengi sana katika suala zima la kuendeleza maendeleo katika Wilaya zetu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa suala zima la posho ya Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Jambo hili tumelichukua kama Serikali, ninafahamu wazi tulipokuwa katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere pale Dar es Salaam Madiwani wote kupitia kwa Wenyeviti wao wa Halmashauri na Mameya walileta hoja hii na Mheshimiwa Rais alisema tumeichukua hoja hii, tunaweka vizuri mfumo wa kiuchumi wetu pale utakapokuwa vizuri basi tutaangalia jinsi gani jambo hili tuweze kulitendea wema kwa kadri itakavyofaa.

Kwa hiyo, hoja hii ni hoja ya msingi tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge, tumeipokea tutaendelea kuweka miundombinu vizuri ya ukusanyaji wa mapato na kuangalia pale tutakapokuwa na hali nzuri tutaliwekea utaratibu mzuri wa wananchi na hasa Madiwani wetu ambao wanafanya kazi kubwa sana. Naomba nikiri wanafanya kazi kubwa iliyopitiliza tuweze kuangalia ile posho yao iweze kuongezeka ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni suala zima la maeneo mapya ya utawala. Hoja hii imechangiwa na Wabunge wengi, tumesikia kwamba mtaa mmoja una watu karibu 20,000, kule Mondole na Msongola tumesikia hilo akina Mheshimiwa Malembeka wakilalamika, naomba tulichukue jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uwezeshaji wa mamlaka mpya na hasa katika sehemu zile za wilaya; kwa mfano kaka yangu Mheshimiwa Malocha alizungumzia sana jimbo lake, maana Jimbo lake lipo kama mbalamwezi, ana changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuseme tumeyachukua haya, lakini tutaangalia utaratibu wa kufanya, kwa sababu lengo letu kubwa kama Serikali kwa sasa ni kujikita katika maeneo mapya tuliyoanzisha lazima kwanza tuyaboreshe, hili ndilo jambo la kwanza. Kama kuna zile special cases kiserikali tutaangalia nini cha kufanya ili kuweza kujibu matatizo ya wananchi. Lakini kipaumbele cha kwanza sasa tulichokiweka ni suala la kutatua matatizo ya zile Halmashauri na wilaya mpya kama kule Tanganyika, tulizozianzisha; lazima zisimame vizuri kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa linahusu utawala bora. Watu walizungumza kwamba kuna wakati mwingine watu wanatumia vibaya madaraka yao. Sheria ipo ndiyo , ya kumuweka mtu kizuizini, lakini viongozi wanatumia madaraka yao vibaya. Kama nilivyosema, ni kwamba sisi tumeendelea kutoa mafunzo awamu kwa awamu. Hivi sasa nilisema wazi kwamba yale ni mafunzo ya utawala tuliyoyamaliza kwa Wakurugenzi pamoja na Wakuu wa Wilaya; na hapa katikati tutatoa tena mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ninyi Waheshimiwa Wabunge mnafahamu; hata humu ndani ya Bunge kwamba tabia hatufanani hata siku moja, ndio tabia ya binadamu. Kwa hiyo, kuna vitu vingine vinaweza vikarekebishika lakini vingine ni mambo ya kibinadamu. Hata hivyo jukumu kubwa la ofisi yetu ni kuhakikisha kwamba tunasimamia utaratibu. Tumesikia Waheshimiwa Wabunge, tutalisimimamia jambo hili na hasa maeneo mbalimbali yenye changamoto kubwa tutayaweka sawa ili yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine hata wiki hii iliyopita nimeweza kuyatolea maelekezo, kwamba kuna baadhi ya mambo yalikuwa yamesimama, nimetoa maelekezo yale mambo ndani ya siku 14 yaanze kufanya kazi zake ili kwamba tuhakikishe utawala bora unafanya kazi yake. Nilitoa maelekezo kule Tunduma kwa Mkuu wetu wa Mkoa, na nina imani mambo yale yatakwenda vizuri na muda si mrefu ile migogoro yetu itakuwa imeisha na tutahakikisha tunawatumikia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kuna hoja nyingine ilikuwa inahusu miradi ya TSP, ULGSP, kwamba kwa nini miradi 18 peke yake, kwa nini miji minane peke yake, naona pale kaka yangu wa Kasulu, Mheshimiwa Nsanzugwanko juzi amenitumia ki-note anasema namuona Mheshimiwa Zitto mwenzangu barabara zake zinajengwa, mimi kwangu choka mbaya kwa nini na mimi ni halmashauri ya mji. Ni kwamba tulianza na miji 18 ile ambayo nimesema kuna Arusha, Tanga, Mbeya, Mwanza na miji mingineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeamua, kama nilivyosema tumetengeneza barabara za kisasa na tunaendelea kutengeneza na mwaka 2020 tutamaliza miradi hii. Miradi ya halmashauri ya miji pamoja na Manispaa zipatazo 18 ujenzi ndio unaendelea hivi sasa. Hata hivyo hii kazi inafanyika kwa awamu. Kuna miji ambayo imesahaulika ambayo imeingizwa katika programu hii inayokuja kuna Mji wa Nzega, Mbulu TC na Kasulu, wataalam wetu wako mbioni wanaifanyia taratibu, itakapoiva tu jambo lile litakuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kwamba halmashauri za miji zote ziwe katika ubora ule tunaoukusudia. Hata hivyo, kuna jambo lingine mahususi ambalo hata leo hii asubuhi watu wamelitolea mwongozo suala la eneo la Jangwani. Nimezungumza katika Mradi wa DMDP ajenda yake kubwa miongoni mwa yakufanya ni kwamba licha ya ujenzi wa barabara za kisasa, ujenzi wa masoko na sehemu za kupumzikia lakini ajenda yetu kubwa tumetenga takribani dola milioni 20 kwa ajili ya kuhakikisha tunalishughulikia Bonde la Msimbazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ndugu zangu mambo haya ya majanga huwezi kuyazuia. Mheshimiwa Naibu Spika, hata nchi zilizoendelea, angalieni leo kule Marekani wakati mwingine California utakuta maji yamefurika mitaani, hali ni mbaya na wananchi wako katika hali mbaya. Hili jambo si Tanzania peke yake, inapoteokea matatizo haya ya majanga wakati mwingine hayajalishi ukubwa wala uchumi wa nchi, hayachagui. Jana tulikuwa tunaangalia kule Arusha hali ilikuwa mbaya kweli kweli katika baadhi ya maeneo, maeneo mengine yanasombwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuseme, kwamba kama Serikali kwa bahati nzuri tumeliweka kwenye mkakati, tumejipanga kutumia dola milioni 20. Pia kwa bahati nzuri hapa na Mheshimiwa Zungu kaka yangu vilevile ameniletea andiko la mpango mkakati ili kama ikiwezekana Serikali tuangalie option; nini tufanye katika Bonde la Msimbazi na eneo la Kariakoo. Jambo hili pia lote tunalichukua kwa pamoja. Nia yetu kama Serikali ni kuangalia ile njia sahihi na nzuri ili hatimaye tuweze kujibu matatizo ya Watanzania katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba niseme kwamba kuna suala ambalo limezungumzwa na manaibu wangu wamelitolea ufafanuzi, suala la walimu wa kuhamishwa kutoka sekondari kwenda shule ya msingi; limeleta mkanganyiko mwingi sana. Nafahamu jambo lolote likiwa geni/jipya lina changamoto yake kubwa. Hata hivyo tufahamu kwamba lengo la Serikali ni kuwapa huduma wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, kuna baadhi ya wilaya leo hii zilikuwa na walimu wa sanaa na walimu wa arts, mwalimu wa arts tunatarajia kwamba mwalimu awe na vipindi visivyopungua 20 kwa wiki, lakini imefika wakati mwingine kuna mwalimu mwingine wa kiingereza au kiswahili wiki nzima ana kipindi kimoja tu. Akiingia saa nne asubuhi leo Jumatatu mpaka wiki ijayo saa nne asubuhi ndio anaingia darasani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia miongoni mwa maeneo ambayo tuna changamoto kubwa ni suala la masomo ya kiingereza. Leo hii nenda katika shule zetu mtafute mwalimu wa kiingereza mwambie akupigie ung’eng’e wake wa kiingereza, msikilize vizuri. Tuna walimu wengi lugha vilevile wako huku sekondari ambao hawakuwa na vipindi. Jambo la kuwachukua na kuwapeleka katika shule za msingi si baya. Hata hivyo Waheshimiwa Wabunge hoja yenu mliyozungumza, suala la induction course, hili ni jambo mahususi na zuri, tunaomba tulichukue kwa ajili ya kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafahamu walimu hao kweli kwa sarakasi tulizokuwa tunapiga huko sekondari na huku unajua kuna elimu, kunaitwa “mlamwa luwaza” kuna mambo ya uchopekaji, kuna lugha nyingi zinatumika. Kwa hiyo huyu mwalimu wa sekondari lazima akajifunze kuchopeka huku shule ya msingi anachopeka vipi. Jamani kuchopeka inaita intergration katika lugha nyingine. Sasa kuna lugha inafundisha uchopekaji wa masomo, kwa hiyo, lazima hawa walimu, mlivyosema hoja yenu kwamba ikiwezekana wapate induction course, jambo hili kama Serikali tunalichukua kwa ajili ya uboreshaji kwa sababu tunajua ufanisi wao wa kazi utatokana na suala zima lilivyo.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la malipo, tumepeleka sasa hivi takribani bilioni arobaini. Katika bilioni 40; asilimia 20 ni kwa ajili ya kuwagawanya walimu; asilimia 20 maana yake tunazungumza wastani wa shilingi bilioni nane. Bilioni nane, imani yangu kubwa, Waheshimiwa Wabunge nimewasikia. Kuna wale walimu ambao tumewahamisha na wanastahili kulipwa. Ninaamini katika Halmashauri nyingine hakuna tatizo, ila kuna baadhi ya Halmashauri kweli ninakiri inawezekana matatizo yapo. Tutaweza kushughulikia case by case kutokana na halmashauri ambazo hazikufanya vizuri. Lakini nina amini Halmashauri zingine watu wamefanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tutawaangalia wale wakurugenzi ambao tumepeleka fedha katika halmashauri yake kwa ajili ya walimu wale wanapohamishwa, kwa nini amezizuia, hazikuweza kufanya kazi hiyo; tutashughulika nao. Kwa sababu haiwezekani, tumetoa maelekezo watu wapo maofisini wanashindwa kutekeleza maeleo haya. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge jambo hili kama Serikali sisi tumelichukua kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaboresha katika maeneo mbalimbali ya utendaji wetu wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya TAMISEMI yapo mengi na ndiyo maana nikiangalia hapa kila jambo ninalolitazama naona tamu, linataka ulitolee maelekezo, lakini hatuwezi kuyamaliza yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi naomba niseme wazi kwamba kuna miradi mingi sana imetengwa katika mamlaka ya Serikali za Mitaa na jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kwamba bajeti hii ambayo mimi nitaomba Wabunge wote mridhie ipite na ipite kwa sababu ndiyo bajeti ya mishahara ya watu wetu wote. Walimu takribani 300,000 na watumishi wengine 388,000; asilimia 74.6 leo unashika shilingi unataka kuondoa shilingi, unataka kumnyima mwalimu mshahara wake? Kwa hiyo mimi nina amini wote tutakuwa katika agenda moja ya kuhakikisha hii bajeti inapita vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nikiri kwamba hoja zote za Waheshimiwa Wabunge sisi tumezipokea na zingine zitakuja kwa ufafanuzi mbalimbali wa kimaandishi na hoja hizi lengo letu kubwa si kuzisikia na kutoa maandishi, ni kwa ajili ya kwenda kujipanga kuyatekeleza. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kupitia timu yangu mahiri iliyopo hapa kuna Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege tutahakikisha mwaka 2018/2019 tunakuja kuwatumikia katika majimbo na mikao yenu yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaongeza kasi yetu ya utendaji wa kazi na tutakuja kubainisha changamoto mbalimbali zinazobainika katika maeneo yetu, lengo letu kubwa ni kwamba lazima tuwatumikie wananchi katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, mnajua kuna baadhi kuna mapungufu baadhi mengine yapo, hayo vilevile tutayasimamia kwa karibu zaidi. Ajenda kubwa ni kuhakikisha kwamba kila mtu katika eneo lake anaweza kutimiza wajibu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba niwasihi wahehsimiwa Wabunge, naomba tupendane sote kwa pamoja; tukipendana tukiwa na upendo bila kujalisha mipaka ya aina yoyote tutaweza kupata mafanikio makubwa kwa sababu bajeti tunayojadili leo ni bajeti inayohusu mustakabali wa nchi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa zote. Kwa hiyo, nawasihi sana upendo kwetu ndio litakuwa jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ridhaa yako, kabla sijahitimisha hoja yangum naomba kutoa hoja maalum, kwamba katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imetengewa shilingi bilioni
2.3 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Halmashauri. Kwa kuwa Halmashauri ya Handeni inapaswa kuhama na kujenga Ofisi katika Kata ya Kabuku, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaliomba Bunge lako tukufu liridhie mabadiliko ya bajeti yaliyotengwa kwa ajili ya kujenga Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Handeni ihamishwe kwa ajili ya kujengea Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Halmashauri ya Mji wa Handeni itachukua majengo ya Ofisi zitakazoachwa na Halmashauri ya Handeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo yote, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza binafsi napenda kuchukua fursa hii kukupongeza wewe kwa kutuongoza. Pia nishukuru Kamati zote kwa kazi kubwa waliyofanya na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni michache sana, kubwa zaidi kwanza naomba nishukuru kwa mchango wa Kamati ya Bunge ya LAAC kwa kazi kubwa tunayoendelea kuifanya kwa pamoja. Nikiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, niishukuru sana Kamati hii toka tulipoanza kufanya kazi pamoja, mimi mwenyewe binafsi nashuhudia mapinduzi makubwa sana katika usimamizi hasa wa rasilimali fedha, kwa upande wangu naishukuru sana Kamati. Kwa kweli kwa upande sisi hata utapoona leo hii kuna mabadiliko makubwa sana ya jinsi gani rasilimali fedha na upatikanaji wa hati safi mpaka zimefikia asilimia 90, hili si jambo haba ni Kamati imefanya na Serikali tumetekeleza katika baadhi ya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue mapendekezo ya Kamati yalivyotoka kwa ajili ya kwenda kuyafanyia kazi kwa sababu lengo kubwa ni kwa ajili ya kuboresha utendaji wa Serikali katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao, kwa sababu wamechangia mambo mbalimbali na naamini lengo lao ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali fedha. Ndiyo maana tunaona hata ripoti ya CAG inavyotoka na hata Kamati inavyotushauri tumeamua kuchukua hatua mbalimbali katika vipindi tofauti, takribani toka ripoti zilivyotolewa tumechukua hatua kwa watumishi takribani 343. Hili siyo jambo dogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie hakuna jambo kubwa katika maisha kama kuchukua hatua kwa watu ambao wamefanya makosa na tunajua kwamba watu hawa wana familia zao, lakini kama viongozi lazima tufanye maamuzi na hili niseme tumechukua hatua mbalimbali; kuna watu wengine wamefukuzwa kazi kabisa, kuna watu wengine wamepewa onyo na kuna wengine wamepelekwa Mahakamani hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakumbuka hata ripoti ya CAG ilivyotoka siku ile ile unakumbuka, kwamba maelekezo yalitoka na karibu Wakurugenzi watatu siku ile ile walipoteza kazi, tukiangalia Halmashauri ya Ujiji, Halmashauri ya Kigoma na hali kadhalika Halmashauri ya Pangani. Hata hivyo, sisi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza maelekezo ya Kamati, kama Kamati ilivyosema kwamba pale tumeanzisha Kitengo ambacho kinaitwa Follow up and Investigation Unit, kitengo ambacho kimetusaidia kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakumbuka hata juzi juzi kulikuwa na tukio kule Ulanga ambapo unaona kwamba ni maamuzi na mwelekeo sahihi ya kitengo hiki. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba, tunaboresha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa na mwisho wa siku tuhakikishe kwamba zile rasilimali fedha zinaenda kusimamiwa vizuri katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuhakikishe kwamba Ofisi yangu itaendelea kutekeleza maelekezo ya Kamati kwa kadri iwezekanavyo, lengo kubwa ni kwamba rasilimali fedha zielekezwe katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ziende zikajibu matatizo ya wananchi. Katika kipindi hiki cha karibuni tumeweza kuchukua maamuzi mbalimbali, kwa mfano, ukiangalia kule Nyang’wale, Nkasi na Tunduru na maeneo mengine mbalimbali. Haya yote tumeyafanya tukiwa na lengo kwamba, basi zile hoja mbalimbali zinazotolewa ziweze kufanyiwa kazi kwa ajili ya mustakabali na Serikali yetu iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ilijitokeza katika suala zima la Mfuko wa Vijana hasa upande wa kanuni na ni kweli tulitunga sheria hapa. Bahati nzuri sheria yetu iko very straight forward, kwamba sheria yetu inatekelezeka moja kwa moja. Hata hivyo, ofisi yangu mchakato wa kanuni sasa hivi uko hatua za mwisho, wadau mbalimbali wameshashiriki, tuko katika stage ya mwisho kabisa ambayo nina imani na kupitia ofisi yangu pale tunatarajia huenda mwishoni mwa mwezi huu mchakato huu utakuwa umekamilika. Kwa hiyo jambo hili litakuwa tayari utekelezaji mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana hasa niwashukuru wenzetu wa Wizara ya Fedha. Zamani kwa vipindi tofauti tumeona tatizo la upelekekaji wa fedha lilikuwa kubwa sana, lakini hivi sasa nadhani kutokana na maelekezo yanayotolewa na Kamati ya LAAC, leo hii ninavyozungumza zaidi ya kati ya shilingi 1.3 trillion ambayo ni development budget iliyopaswa kwenda katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa zaidi ya shilingi bilioni 640 zimeshafika, ni wastani wa asilimia 48.8, mpaka hivi sasa ndani ya kipindi hiki mpaka mwezi Desemba. Naona trend hii mpaka tukapofika mwezi wa Sita hali itakuwa ni shwari sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika jambo hili Waheshimiwa Wabunge naomba niwaambie katika suala zima la utekelezaji wa ripoti ya CAG, lakini halikadhalika maelekezo ya Kamati, jambo hili sasa nina imani linaenda vizuri zaidi. Maana yake leo hii ukizungumza zaidi ya shilingi bilioni 640, ambayo katika kipindi cha nyuma inawezekana hiyo ndiyo fedha ya mwaka nzima, leo hii Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wanashuhudia katika Wilaya zetu jinsi gani zaidi ya shilingi bilioni 105 zinaenda kujenga hospitali 67, haijawahi kutokea ndani ya muda mfupi zaidi ya shilingi bilioni 105 inatoka. Pia zaidi ya shilingi bilioni 23 inaenda kuhakikisha tunajenga majengo ya halmashauri katika halmashauri zetu, lengo kubwa Watendaji wapate ofisi rafiki, hii haijawahi kutokea. Zaidi ya shilingi bilioni 1.4 watu ambao wako kandokando ya ziwa na bahari, ambao ilionekana kwamba tatizo kubwa lilikuwa ni boti, fedha hizo zote zimeshatoka kwa asilimia 100. Hii ni fahari kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba, Serikali kwa upande wake hasa katika upelekaji wa fedha na nikiangalia trend hivi sasa mabadiliko yamekuwa makubwa sana. Hata hivyo, juzi juzi tumepeleka zaidi ya bilioni 54 kwa ajili ya Sekta ya Elimu, tukiboresha miundombinu ya elimu, hii ni kazi kubwa sana ambayo nina imani jambo hili zamani halikuwepo. Kwa hiyo tukiri wazi kwamba ,Serikali imendelea kutekeleza maelekezo ya CAG, halikadhalika maelekezo ya Kamati yetu ya Bunge ambayo inatushauri vyema katika kipindi chote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine kuhusu ripoti ya ukaguzi maalum uliofanyika kule Kaliua. Naomba niwaambie kwamba, ofisi yangu iliamua hivyo kwa sababu ukiangalia idadi ya watumishi ni wengi zaidi ya watumishi 60; watumishi 60 siyo jambo dogo na halitaki maamuzi ya nanihi. Naishukuru sana Kamati imetuelekeza vizuri na hata hivyo tuliunda timu maalum ambayo ilienda kule site na Jumapili, ina maana keshokutwa hapa itatolewa ripoti ya watumishi wale 60 jinsi gani kwa kadri iwezekanavyo hatua kwa wale kuhusu labda suala zima la kinidhamu, mtu apelekwe wapi, kama mtu ana mambo ya kijinai. Mambo hayo yote yako katika utekelezaji, hata hivyo Kamati ilielekeza wale watumishi mbalimbali wengine waweze kurudishwa na hivi sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeanza kulitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie wewe na Wajumbe wa Kamati, jukumu letu sisi kubwa ni kuhakikisha kwamba ripoti ya CAG lakini maelekezo ya Kamati tutaendelea kuyatekeleza kwa kadri tutakavyoona inafaa. Lengo kubwa ni kuonyesha jinsi gani nchi yetu tunakwenda kujibu matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali yao hivi sasa, Serikali hii ambayo kwa sasa ukiangalia trend ya utendaji wake wa kazi tumebadilisha utaratibu wetu wa kazi, tunakwenda kujibu matatizo ya wanachi kwa kubaini changamoto na kuzitafutia majawabu. Hili ndiyo jambo la kushukuru. Hali hii zamani haikuwepo hivi lakini sasa hivi tunaona jinsi gani uwajibikaji umekuwa mkubwa sana, nidhamu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa sasa imebadilika tofauti na mwanzo watu walikuwa wanafanya kazi kwa mazoea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru Kamati imetushauri jinsi gani tuongeze kada ya watumishi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha tunapata watumishi wa kuweza kutenda vyema katika maeneo yetu. Ndiyo maana hapa karibuni tumeajiri zaidi ya watumishi 21,000 katika sekta mbili tu ya afya ambayo tumeajiri zaidi ya watumishi 8,800 hali kadhalika sekta ya elimu zaidi ya watumishi 13,000. Najua kwamba bado matatizo yapo na ndiyo maana Serikali inajieleza kuhakikisha katika kila eneo tunatatua matatizo haya kwa kadri iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeona changamoto ya idadi ya Wakaguzi wa Ndani na kuweka mifumo. Hili jambo tumelipokea lakini naomba niseme, Ofisi ya TAMISEMI sasa hivi imejiimarisha katika mifumo ya TEHAMA na sasa hivi kuna mifumo ya GoT-HoMIS na mifumo mingine ya ukusanyaji wa mapato. Katika vituo vyetu vya afya vyote fedha zinakwenda moja kwa moja na eneo hili tumeajiri zaidi ya watumishi 530, hawa ni wahasibu. Lengo kubwa ni kuhakikisha fedha zote zinazofika katika kituo cha afya ziweze kusimamiwa vyema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wajumbe wameshauri, inawezekana technicalities za watumishi wetu uwezo bado mdogo. Ndiyo maana jambo hili tumeendelea kutoa maelekezo na hivi sasa wataalam wangu wengine wako Morogoro pale kwa ajili ya kutoa mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, nikushukuru sana lakini niseme kwamba Ofisi yangu itaendelea kufanya kila iwezekanavyo kwa mustakabali mzuri wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwa upande wangu kwanza, nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha leo hii tunajadili hoja muhimu sana za Kamati, lakini kubwa zaidi nipende kuzipongeza Kamati zote mbili.
Kamati hizi mbili zote zilizowasilisha hotuba zake hapa zimetuonesha kwamba, ni jukumu gani tunatakiwa tulifanye katika kipindi hiki cha sasa baada ya kupata ripoti hizi zilizofanyika mwaka 2014 na 2015. Tukiwa mwaka 2016 sasa, kama Wabunge na kwa ujumla kama Serikali tujue tutafanyaje ili wananchi waweze kupata huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze katika Kamati ya LAAC. Naomba nimpongeze Mwenyekiti na timu yao yote ambayo katika njia moja au nyingine, wao wanatusimamia zaidi kwa karibu katika ofisi yetu. Naomba nikiri wazi kwamba, maelekezo waliyoyatoa kwetu sisi na kaka yangu Boniface Simbachawene tumepata viongozi ambao wanatushauri ili kazi yetu iweze kufanyika vizuri katika kipindi cha sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja mbalimbali lakini zote zina mashiko. Hoja ya kwanza ilikuwa ni suala zima la Sheria ya Manunuzi na kweli ukifuatilia ripoti ya Mkaguzi na hali kadhalika Kamati ilivyofanya uchambuzi mbalimbali ilibainika kwamba kuna changamoto kubwa sana na kutoa maelekezo nini tukifanye. Katika hili, ofisi yetu imeshaanza kuyafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza tumetoa maelekezo katika Halmashauri zote; kwa vile tuna watendaji katika ngazi mbalimbali wengine wakiwa wapya, wahakikishe katika utiifu wa utendaji wa kazi zao, jambo la kwanza wanazingatia Sheria ya Manunuzi ili kuleta tija katika Halmashauri zetu. Hata hivyo, ukifuatilia ile ripoti imeonesha maeneo mbalimbali ambayo watu walifanya mambo ya hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie na nilijulishe Bunge lako kwamba, katika eneo hili tumechukua hatua mbalimbali. Katika Halmashauri mbalimbali baadhi ya Wakurugenzi wamepoteza nafasi zao, lakini baadhi ya Wakuu wa Idara waliobainika, wameweza kuchukuliwa hatua mbalimbali na hivi sasa wengine wamepelekwa mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili katika ofisi yetu hatutavumilia kabisa, wale wote ambao wameonekana ni kikwazo ambao kwa njia moja au nyingine wamehujumu fedha za Serikali na sisi tukiwa tumepewa dhamana katika eneo hilo; naomba tulihakikishie Bunge lako kwamba, ofisi yetu imejipanga hivi sasa tutafanya marekebisho makubwa sana na ndiyo maana nimesema kwamba, Kamati imeibua jambo hili ambalo ni jema, ni maelekezo na sisi tunakwenda kulifanyia kazi.
Suala lingine ni Udhaifu Katika Usimamizi na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Ni kweli, Kamati ilibaini kulikuwa na udhaifu mkubwa sana katika maeneo mbalimbali, lakini katika eneo hili kulikuwa na marekebisho ya kimuundo kidogo baada ya kupitia hizi hoja mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ofisi yetu hivi sasa kuna Kitengo Maalum cha Ufuatiliaji ambacho kinafuatilia maeneo mbalimbali katika jitihada za kuhakikisha kwamba miradi hii iweze kutekelezeka vizuri, hasa kwa fedha zilizotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, jukumu lake kubwa vilevile ni kuhakikisha kwamba inatoa ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya CAG na Kamati ya LAAC. Ndiyo maana katika kipindi chote cha mijadala baadhi ya wawakilishi wa kitengo hiki walikuwepo katika mijadala hii kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa jinsi ya kufanya katika maeneo mbalimbali ili yaweze kuleta tija katika eneo letu la kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana katika suala zima la ufuatiliaji, Waziri wangu hapa alitoa maelekezo mbalimbali hata kule Kigoma na Kasulu na baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali walichukuliwa hatua za kinidhamu mara baada ya kubainika kwamba baadhi yao walishindwa kutimiza wajibu wao wa kikazi waliopewa. Katika taarifa mbalimbali hivi sasa, ukisoma racket news, ukiangalia kule Kinondoni, Kondoa, Kahama, Kigoma-Ujiji na maeneo mengine mbalimbali baadhi ya watu wamechukuliwa hatua. Hii ni kwa sababu tunatekeleza lile ambalo limeonekana kwamba lilikuwa ni changamoto kubwa sana katika ofisi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kila sababu kulinda rasilimali hizi za wananchi ili ziweze kuleta tija katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja inayohusu uzembe katika kusimamia Mifumo ya Makusanyo ya Mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika hilo na ndiyo maana tumefanya kazi kubwa sana. Wakati tunaingia pale na kaka yangu Boniface Simbachawene Halmashauri zilizokuwa zinakusanya kwa kutumia mifumo ya kielekitroniki zilikuwa chini ya asilimia 30; leo hii tumefikisha karibuni asilimia 92. Hata hivyo, tumetoa maelekezo mbalimbali katika zile Halmashauri mpya ambazo hazina network hasa za umeme na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunafikia lengo la asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini, maelekezo haya ya Kamati tuna kazi kubwa tunayoifanya katika ofisi yetu hapa na tutafika mahali pazuri na ndiyo maana leo hii Halmashauri mbalimbali zimeweza kukusanya karibuni mara mbili ya ukusanyaji wa mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikushukuru sana, na kwa vile nina ufinyu wa muda, nipende kushukuru. Kubwa zaidi ni Kamati iliyotusaidia na naomba tukiri katika Kamati hii kwamba, ofisi yetu itajitahidi kutekeleza maelekezo yote kwa mustakabali wa nchi yetu ambao tunajua ndiyo tija wanayoitarajia wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Nchi ambayo ametuwezesha katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuweza kupata fursa kuwasilisha hoja yetu hapa na Wabunge wamechangia, lakini pia napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa imani yake kwangu amenipa fursa ya kuhudumu katika Ofisi hii ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kipindi chote hiki. Kwa kweli Mheshimiwa Rais, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwa uongozi wake. Sambamba na hilo pia napenda kumshukuru Waziri wetu Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa kwa fursa kubwa anayotupa sisi wasaidizi wake tukiwa humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru kipekee, Waziri wangu mwenye dhamana, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene kwa maelekezo mazuri, lakini umekuwa sio Waziri peke yake isipokuwa umekuwa kama kaka kwangu, pia ni kocha unayenipa fursa ya kuweza kutimiza majukumu yetu katika ofisi hii kubwa ambayo inawakilisha wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Namshukuru sana Waziri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge na viongozi wote wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda sana kumshukuru Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Serikali za Mitaa na Utawala, ndugu yetu Mheshimiwa Rweikiza pamoja na Kamati yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii ndiyo Kamati pekee ambayo ukija kuiangalia inajadili mafungu yapatayo
28. Kwa kweli tunawashukuru sana na timu yako kwa msaada mkubwa katika ofisi yetu. Hatuna cha kuwalipa, mmekuwa Walimu, mmekuwa waelekezaji wazuri mpaka leo hii tunapohitimisha hoja yetu hii ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nitoe shukrani zangu za dhati kwa watumishi wote wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ushirikiano wao mzuri, kwa upendo wao, wametusaidia sana na kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene kuhakikisha kwamba tunatekeleza majukumu yetu katika kipindi hiki cha mwaka huu na mpaka leo hii tunakuja kuomba sasa Bajeti nyingine ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru familia yangu; namshukuru mama yangu mzazi kwa malezi mazuri.

Kwa kweli nawakumbuka sana na ninajua mmeni-miss sana, lakini yote hii ni kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa msaada na dua zao njema siku zote wanaoniombea ninapotimiza majukumu yangu nikiwa hapa Bungeni, nikiwa Jimboni halikadhalika, nikiwa maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba dhamana aliyotupa Mheshimiwa Rais tunaitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Wajumbe tukiwasilisha hoja yetu, Waziri wangu mwenye dhamana akiwasilisha hoja hii, tulipata fursa ya kubaini michango mbalimbali ikitoka kwa Waheshimiwa Wabunge, nami niliyojifunza katika haya ni jambo moja kubwa. Lengo kubwa la Wabunge ni kuona Ofisi hii inaweza kufanya kazi yake vizuri na Wabunge wengi sana walijielekeza katika suala zima la sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukija kuangalia, nami nimepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali. Nilipotembelea kweli katika nchi yetu hii, ukienda maeneo mbalimbali utakuja kubaini kwamba sekta ya afya ina changamoto kubwa. Ndiyo maana kiongozi wangu akinituma nipite sehemu mbalimbali, tumeweza kuzibaini na ndiyo maana humu tunapangia mipango ya pamoja, nini tufanye ili mradi twende mbele zaidi na tunajua wazi kwamba, nchi yetu ambayo tulikuwa tunataka katika Sera yetu ya Afya kuwe na ujenzi wa zahanati takriban kila kijiji, tulipaswa kujenga zahanati 12,545, lakini mpaka sasa hivi tumefikia zahanati 4,470. Halikadhalika katika vituo vya afya, tulikuwa na sababu ya kuweza kujenga vituo vya afya 4,420, lakini mpaka leo hii tumejenga vituo vya afya 507. Kwa hiyo, tuna kazi kubwa sana ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali zetu za Wilaya, kati ya Wilaya zetu ambapo Wilaya zetu 139, hivi sasa sehemu zenye huduma tunapata Hospitali 119 peke yake.

Maana yake tuna kazi kubwa ya kufanya. Katika hili nawashukuru Wabunge wote. Waziri wangu akija hapa kwa sababu atakuwa na muda mrefu wa kufafanua, atazungumza mambo haya kwa undani zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao katika njia moja au nyingine, nilivyokuja site kule tulishirikiana vizuri. Hili naomba nikiri wazi, mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango Malecela hapo ulizugumza kwa uchungu sana, hasa katika kituo chako cha Ndungu kule, na mimi bahati nzuri nilifika kule Same mama yangu. Kilio chako unasema kwamba Same ni kubwa na hapa ulitoa reference kwamba ni kilometa za mraba karibu 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wananchi wa pale na nilipofika pale, ndiyo kilio ambacho wewe ulikileta siku zote, nilipofika pale kweli nilikikuta. Nikuhakikishie kwamba mimi na kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, tulishirikiana na Wizara ya Afya ambapo wenzetu wapo katika upande wa sera, katika ile haja yako hasa ambayo umeipigia kelele kipindi chote na ukaacha maagizo kwa viongozi wako nilivyofika pale site, tutahakikisha mwaka huu huenda mwaka Mungu akijaalia, kabla ya mwezi wa saba kazi ya ujenzi wa theatre utaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafanya hivyo katika maeneo mbalimbali. Katika agenda yetu tulisema tutafanya ujenzi wa vituo vya afya vipatavyo 100. Lengo letu ni nini? Ni kuhakikisha sasa tunapeleka huduma kwa wananchi. Ndiyo maana wakati mwingine Hospitali zetu za Wilaya na zile za Rufaa zinahemewa kwa sababu huku chini vituo vya afya uwekezaji ulikuwa mdogo, ndiyo maana Serikali hii sasa imeamua kufanya maamuzi katika mpango wake hasa katika suala zima la ujenzi wa zahanati tumetenga takriban shilingi bilioni 22.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuhakikisha kwamba tunaenda kuendeleza ule ujenzi wa zahanati takriban 370 huku tukishirikiana na nguvu za wananchi; tutaenda kufanya suala zima la ukarabati wa vituo vya afya 144, sambamba na kuhakikisha tunajenga maboma mengine 100, kuyamalizia 539. Hili tutaenda kulifanya katika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika katika mpango mwingine mkakati tumetenga takriban shilingi bilioni 11.4. Katika eneo hilo, tutafanya? Lengo letu ni kwamba kuna vituo vya afya vinavyojengwa vipatavyo 94; tutaenda kuongeza nguvu hapo. Lengo ni kwamba tuweze kuvimalizia wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna vituo vyetu vingine 12 kama ni maboma yanataka umaliziaji, tutahakikisha tunashirikiana na wananchi ili hizi shilingi bilioni 11.4 na maeneo mengine twende tukawekeze katika suala zima la vituo vya afya tuweze kupata sasa mpango mkakati mzuri tuwasaidie wananchi Watanzania waweze kupata huduma nzuri. Mwisho wa siku ni kwamba wananchi waliipa ridhaa Serikali hii ya Awamu ya Tano, imani yao kubwa ni kwamba Serikali itaenda kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami na kaka yangu hapa naomba niwaambie kwamba tumejipanga kuhakikisha tunafanya mabadiliko makubwa katika sekta ya afya tukiwa sisi ni watekelezaji wa sera katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kipindi cha sasa mnafahamu zamani tulikuwa na changamoto sana ya dawa na ninyi Wabunge mara nyingi mmekuwa mkiuliza maswali hapa kuhusu suala zima la ukosefu wa dawa; na ndiyo maana katika mwaka huu ambao tunaenda nao, tulitenga takribani shilingi bilioni 106.3 na mpaka tunafika katika miezi ya katikati, mwezi wa tatu tulipeleka takribani shilingi bilioni 79.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyokuwepo hivi sasa ni kwamba wakati mwingine Serikali inapeleka fedha, lakini usimamizi wa fedha siyo mzuri. Katika hili naomba nimshukuru Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI anayeshughulikia suala la afya, katika kuzunguka kwake huko ametuibulia mambo mengi sana na ya msingi.

Ndiyo maana naomba mtuwie radhi ndugu zangu Wabunge, kwamba wakati mwingine tukifika kama mtaalam hasa aliyepewa dhamana ya uongozi kama DMO, huenda fedha zipo, zinashindwa kutumika kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, jambo hilo hatutalivumilia kwa maslahi mapana ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani hata kidogo! Tulipofika mwezi wa saba mwaka 2017 mwaka unaanza, takriban shilingi bilioni 20.5 zilikuwa hazijatumika ambapo wataalam wetu walitakiwa wazitumiwe kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba. Hili jambo haliwezekani hata kidogo. Katika utaratibu wa sasa tutaenda kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunasimamia vyema sekta yetu ya afya, wananchi waweze kupata fursa nzuri ya kuamini kwamba Serikali yao sasa iko vitani kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma nzuri ya afya. Nawapongeze sana wadau mbalimbali, Waheshimiwa Wabunge, katika maeneo mbalimbali mmetumia mifuko yenu ya Mfuko wa Jimbo kuhakikisha kwamba mnajenga kusaidia nguvu za wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, hongereni sana katika hilo. (Makofi)

Pia niwapongeze badhi ya Wakuu wa Wilaya, wamethubutu kwa kiwango kikubwa; kwa mfano, nilifika kule Tunduru, kuna Mkuu wa Wilaya ya Tunduru pale Bwana Homera, nimekuta amefanya harakati kubwa za ufyatuaji wa matofali. Nilipokuwa site juzi juzi nilimwuliza, akaniambia kuna takriban matofali milioni 14 yameshafyatuliwa. Lengo ni kuhakikisha anasaidia ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, halikadhalika na katika sekta ya elimu. Tunataka mfano kama huu. Tunataka mfano kama DC yule wa Korogwe aliyefanya kazi kubwa katika maeneo hayo. Tushikamane kwa pamoja, lengo letu twende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie suala zima la matumizi mifumo ya elektroniki; mkumbuke kwamba kama Ofisi ya TAMISEMI, tumefanya uwekezaji mkubwa sana katika suala zima la kimifumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tulikuwa tunatumia zile risiti za kawaida za karatasi, lakini sasa hivi Idara yetu ndiyo Idara ambayo ina miundombinu iliyojitosheleza, lengo kubwa ni tujielekeza katika mifumo ya elektroniki. Ndiyo maana mpaka mwezi Machi, tumeweza kukamilisha kuweka mifumo katika Halmashauri zetu zipatazo 177. Hii ni kazi kubwa! Tumebakiza Halmashauri nane tufikie Halmashauri
185. Lengo letu ni kwamba ikifika mwezi Juni, tuwe tumekamilisha zoezi katika zile Halmashauri chache ambazo zimebaki, ambazo zote ni Halmashauri mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba nikiri wazi, katika eneo hili tumepata mafanikio makubwa sana. Kwa mfano, ukiangalia na hata ukienda Mikindani kwa ndugu yangu pale Mheshimiwa Maftaha, tulikuwa tunakusanya takriban shilingi milioni 600 tu kwa mwaka, lakini baada ya mfumo wa sasa hivi, taarifa inaniambia kwamba karibuni shilingi bilioni 2.6 zimeshaanza kukusanywa. Hii ni kazi nzuri inayoendelea kufanyika. Hata kule Arusha tulikuwa tunakusanya takribani shilingi bilioni tano, leo hii tumefikia shilingi bilioni 10 point something.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata suala zima la vituo vya afya, kwa mfano nilitembelea kituo cha afya cha pale Kaloleni, Arusha, walikuwa wanakusanya shilingi milioni nne tu kwa mwezi; lakini baada ya kuwaambia wasimike mifumo, baada ya hapo wanakusanya kuanzia shilingi milioni 24. Haya ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jukumu letu sisi Wabunge ni kuhakikisha tunaenda katika Halmashauri zetu; Serikali inapoenda kujipanga tuhakikishe na sisi tunachukua nafasi yetu kusimamia mifumo iende ikasimikwe vizuri, siyo kusimika peke yake, lazima matumizi ya mifumo yaweze kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itatoa ushirikiano wa kutosha. Lengo letu ni kwamba own source zikusanywe vizuri ili mradi wananchi waweze kupata fursa ya maendeleo katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja katika suala zima la Mfuko wa Vijana na Akina Mama; na mkumbuke katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 ilikuwa imetengwa bajeti ya shilingi bilioni 56.8, lakini mpaka tunapozungumza hapa juzi juzi, ni shilingi bilioni 15.6 zimepelekwa.

Kwa hiyo, nawaombe ndugu zangu Wabunge, kwamba zile own source za asilimia tano za vijana na akina mama hazifiki kwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango; fedha zile zinaishia katika Halmashauri zetu. Niwasihi sana, tunaposimama katika vikao vyetu vya Kamati ya Fedha tuombe kuelekeza kwamba fedha itakayokusanywa lazima ipelekwe kwa vijana na kina mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie, sisi Ofisi ya TAMISEMI tutachukua jukumu hili kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba tunasimamia; lengo kubwa ni vijana na akina mama waweze kupata mikopo washiriki katika shughuli za uchumi wa nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata hoja ya msingi kutoka kwa Mheshimiwa Ikupa pale akisema walemavu wamesahaulika katika jambo hili. Naomba tuwaambie Mheshimiwa Ikupa na wenzako ni kwamba jambo hili tumelichukua na Mheshimiwa Waziri wangu ataliwekea utaratibu vizuri, tuone jinsi gani ya kufanya katika asilimia kumi angalau na walemavu waweze kukumbukwa, wananchi hawa waweze kushiriki vyema katika suala zima la uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ajenda kubwa ilizungumzwa hapa ya barabara. Katika ajenda hii ya barabara ukizungumzwa kila mtu anaguswa na ajenda ya barabara. Ndiyo maana ukikumbuka mwaka 2016 tulitengewa karibu shilingi bilioni 249.7 hapa na mpaka mwezi Machi, tulipelekewa karibun shilingi bilioni 142, lakini kuna kazi kubwa sana ilifanyika; tumejenga maboksi kalavati kama 23, tumejenga madaraja, tumejenga barabara ya kilometa 11,111.57. Hii ni kazi kubwa inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, leo hii ukitembea katika Miji mbalimbali kazi kubwa iliyofanya TAMISEMI inapimika kwa vigezo vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika hii Miji yetu Mikuu kupitia mradi ya TCSP Project, tumefanya kazi kubwa sana katika maeneo haya nane; lakini ukienda zile Halmashauri za Miji 18, zamani ukipita maeneo hayo utakuta barabara za vumbi, lakini leo hii, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeamua kuweka ujenzi wa barabara za lami katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie, katika bajeti ya mwaka huu ambayo imetengwa takribani shilingi milioni 247.7 tutaenda kufanya kazi kubwa ya kuondoa vikwazo hasa ujenzi wa madaraja na kuondoa vikwazo na ndugu yangu mmoja nimemsikia hapa jana alikuwa anazungumza kwamba sisi hatufikiki, hili ni jukumu la ofisi yetu. Nami bahati nzuri naomba niwaambie kwamba tumejipanga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu ni kuacha legacy kwamba tukiondoka na kaka yangu hapa, hata tukihama watu waseme hapa alikuwa Mheshimiwa Simbachawene na Jafo, walifanya hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini binadamu aliyekuwa sahihi lazima afanye kazi aache legacy katika maeneo yake. Na sisi naomba niwaambie, tutaenda kuacha legacy katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wazi kwamba Ofisi hii ni Ofisi ya wananchi, ndiyo bajeti ambayo inabajetiwa mwananchi kijijini, Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani na Waheshimiwa Wabunge na kila…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya kama ni bashrafu tu, naomba niseme sasa naunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)


Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa nguvu na uzima kwa kuweza kuhakikisha tunachangia mchango huu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa dhamana na kuniamini kuweza kuhudumu tena katika ofisi yake nikiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba sitamuangusha na nitazidi kumuomba Mwenyezi Mungu siku zote aweze kunipa nguvu na uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kumshukuru kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango na dada yangu, Naibu Waziri, kwanza kwa kazi kubwa wanayofanya. Leo hii tunajadili Mpango, lakini mimi katika ofisi ninayoiongoza naomba kutoa shukrani za dhati sana kwa Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa inayofanya na nishukuru kwa sababu imeendelea kuiwezesha ofisi yangu kwa kipindi chote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala huu wa Mpango wetu, kikubwa zaidi ni kuangalia jinsi gani tutamwezesha mwananchi wa kawaida kuweza kukuza uchumi wake. Mpango wetu wa Taifa unaeleza dhahiri kabisa kuhusu chombo ambacho kiko katika ofisi yangu, tumekianzisha mwaka huu kiitwacho TARURA. Malengo yetu ni kwamba ikifika mwaka 2020 tuwe na mabadiliko makubwa sana katika suala zima la miundombinu ambayo hiyo itawawezesha wananchi kukuza uchumi wao kupitia malighafi au mazao yanayozalishwa katika maeneo yao. Nishukuru ofisi hii kwa jinsi ilivyojipanga kwa sababu katika mwaka huu wa fedha peke yake takribani shilingi bilioni 573 tutazielekeza katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa bila kuwa na mipango mizuri, mambo hayo hayawezi yakafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa kiwango kikubwa, nikijielekeza katika sekta ya elimu ambayo nimesikitika sana kwa sababu nimeona baadhi ya Wabunge wenzetu humu ndani wengine wakibeza jambo hili kubwa sana lililoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano la kuwawezesha Watanzania masikini kwa kuwa na programu ya elimu ambayo inagharamiwa na Serikali, lakini wengine walikuwa wakisema maneno ya kebehi kabisa kama hakuna chochote kilichofanyika. Kwa kweli, kwa dhati kabisa naweza kusema hii si haki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika chain yetu hii tunavyozungumza hivi sasa, tujipime sisi tuko humu ndani ya mamlaka Mwenyezi Mungu ametupa fursa tumeingia humu Bungeni, lakini tuwaangalie Watanzania hao wadogo-wadogo ambao hali yao ni tete, ni taabani, hata ile gharama ya kulipia certificate ya form four wengine walikuwa wanashindwa. Leo hii programu ya elimu bure ambayo takribani shilingi bilioni 18.77 zimekuwa zinatoka, sasa hivi takribani shilingi bilioni 23 kila mwezi zinatoka, halafu kama Mbunge anasimama humu ndani anabeza kabisa kwamba hakuna lolote, nadhani tuna sababu ya kufanyiwa tathmini sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kazi kubwa iliyofanyika. Ninyi mnafahamu kipindi kirefu tumesema shule zetu za Serikali hazifanyi vizuri, leo hii Wizara ya Fedha na Wizara ya Elimu kwa ujumla wetu katika suala zima la uwekezaji mkubwa tunaofanya katika sekta ya elimu, shule kongwe takribani 89 zote tunaziboresha ziweze kutoa mazingira ya ushindani. Mpaka sasa tunaenda takribani shule 43 ambazo hali yake ilikuwa ni hoi bin taabani. Shule hizi tunabadilisha miundombinu yake lengo kubwa iwe ni miundombinu wezeshi. Katika Mpango huu unaokuja tunaangalia ni jinsi gani tunaenda kukamilisha shule hizi nyingine tupate shule 89 ambazo zitakuwa na level ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine tupate fursa tutembelee mazingira yetu kuangalia tulipoanzia na wapi tunakokwenda. Nendeni Mpwapwa, Msalato, Mzumbe kwenye hizi shule ambazo Serikali imefanya investiment kubwa ya fedha za Serikali karibu shilingi bilioni moja kila shule. Mimi nimewaambia wazi kwamba lengo letu ni kuhakikisha elimu yetu inarudi katika mstari unaokubalika na haiwezi kurudi bila kuweka mipango na mipango yenyewe ndiyo hii inayojadiliwa humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme bahati nzuri Mheshimiwa Mwenyekiti wewe unafahamu shule yetu ya Mpwapwa zamani ilikuwa imechoka kabisa, leo hii ukifika Mpwapwa unashangaa hii shule ya aina gani! Nenda Msalato hapa watoto walikuwa wakifika shuleni wiki moja mtoto anatamani aende nyumbani. Tumeenda na Kamati ya Bunge kutembelea tumekuta watoto 580 wamekataa kwenda likizo wote wame-register kwamba watabaki shuleni kwa sababu wanasema sasa hivi tumekaa shule kama tuko katika hoteli. Hii yote ni investiment kubwa inayofanywa na Serikali. Leo Mheshimiwa Mpango amekuja na Mpango wa jinsi ya kuboresha ili suala la elimu liende mbele zaidi. Naomba niseme wazi, tuwe wazalendo katika kuangalia jinsi gani tunafanya nchi yetu iende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimesikia na bahati nzuri dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alizungumza katika suala zima la sekta ya afya, kumbukeni huko tulikotoka na sasa hivi tukoje. Ukiachia bajeti ya dawa Mheshimiwa Ummy amezungumza, lakini ajenda ya miundombinu, ninyi wenyewe mnafahamu huko tulikotoka leo hii kupitia fedha za World Bank, fedha za ndani na fedha kutoka Canada tunafanya investment kubwa katika nchi hii kwa mara ya kwanza haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumepata karibu shilingi bilioni 10 fedha za ziada kutokana na mipango mizuri ya Serikali, mpaka donors countries wanaridhika na utendaji wa Serikali ya Tanzania. Hivi sasa tuna-scale up hiyo programu, tunaenda karibu vituo 216 kutoka 172, hii ni kazi kubwa inayofanyika, lakini kazi hii maana yake ni jinsi gani Serikali imejipanga kutekelza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mimi nimpongeze Mheshimiwa Mpango, ndugu yangu usikate tamaa. Wakati mwingine safari yoyote ukiona unapigiwa kelele ujue kwamba safari hiyo inaenda vizuri, chapa kazi kaka na sisi tuko nyuma yako tunaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie Watanzania, Mpango wetu katika suala zima la miundombinu, bahati nzuri juzi-juzi tulikuwa kule Mwanza World Bank wanatusaidia suala zima la uboreshaji wa miji hii Tanzania. Ukienda Mbeya, Tanga, Arusha na miji yote mikuu tumefanya mabadiliko makubwa, lakini Manispaa zetu tunafanya uwekezaji mkubwa wa kujenga barabara za lami, kuweka taa na kujenga madampo ya kisasa. Mpango huu unaokuja sasa hivi unaangalia ni jinsi gani tunaenda ku-scale up hiyo programu yetu ili kuhakikisha Miji, Halmashauri na maeneo mbalimbali yanaimarika katika miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo yote ni kutokana na sera nzuri ya Serikali inavyofanya resource mobilization na wadau wetu wanaridhika kwamba kazi zinakwenda. Juzi tukiwa Mwanza, World Bank imetoa extension ya mradi wetu wa UGLSP, badala ya kuishia mwaka 2018 sasa wame-extend mpaka 2020, hii ni faraja kubwa kwa Serikali ya Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, jukumu letu kubwa ni lazima tuwe wazalendo tuone tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Kweli, unaweza ukatoa mawazo lakini siyo kukashifu kwamba hakuna jambo linalofanyika. Ingekuwa nchi nyingine kama Wabunge tungesema wapi kuna gap kidogo turekebishe twende mbele zaidi, lakini sio kukashifu kama hakuna kinachopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimesikia Wabunge wengine walikuwa wakibeza hata suala zima la uchumi wa viwanda. Nimshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Mwijage amefanya kazi kubwa sana na mimi ni Wizara wezeshi ya kumwezesha kaka yangu Mheshimiwa Mwijage instrument yake ifanyike vizuri. Leo hii Mheshimiwa Mwijage na Rais anahangaika ili tuhakikishe tunajenga viwanda ili watoto waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mimi nikiwa mwenye mamlaka na Serikali za Mitaa, juzi juzi wakati tunawaapisha Wakuu wa Mikoa niliwapa target nikasema Mheshimiwa Mwijage anahangaika na viwanda, lazima kama Wakuu wa Mikoa, leo katika bajeti yetu ya mwaka wa fedha 2017/2018, bajeti ya own source ni karibu shilingi bilioni
61.5. A unit plants ya kiwanda cha kawaida cha kubangua korosho, ukienda Newala, Masasi, ukienda SIDO wanakupatia kiwanda cha shilingi milioni 10. Kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti hapa Singida, uliza zile mashine SIDO zinauzwa kiasi gani, average ni kati ya shilingi milioni mbili na nusu mpaka milioni sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, own source yangu ambayo ipo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, shilingi bilioni 61, hata kama unit plants ya kiwanda kidogo ukiweka shilingi milioni 10 ni sawasawa na viwanda 6,100, ni beyond expectation ya viwanda 2,600 kwa mwaka. Hivi vitu ni just calculation, is just about numbers. Kwa hiyo, sisi kama Wabunge wetu lengo letu kubwa ni jinsi gani tuna-play ile leadership position, katika mamlaka zetu jinsi gani tutafanya sasa kuhakikisha tunaweka uwekezaji mkubwa tunaboresha viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri wa Viwanda na Biashara, juzi wakati tunazindua operation ya viwanda 100, Naibu Waziri pale alitoa sera pana sana ya viwanda. Bahati nzuri mama mwenye Mifuko ya Uwezeshaji, dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, ana mifuko 17, tumetoa fursa jinsi gani tutafanya kama Watanzania kwa ajenda ya viwanda ambayo ipo, tukiungana kwa pamoja tunatoka. Tatizo kubwa kuna watu wengine hawataki hili jambo lifanikiwe kwa sababu watasema kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi imefanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niwaambie tunaenda kushinda ushindi mkubwa kwa mafanikio makubwa. Kikubwa zaidi kaka yangu Mheshimiwa Mpango chukua yale maoni mazuri ya Wajumbe humu, tuyaweke vizuri tuone jinsi gani tutasonga mbele Mpango wetu uive vizuri. Nikuhakikishie, kwa Mpango huu na juhudi ya Serikali inavyokwenda na naomba niwahakikishie Wizara zote ambapo Wizara yangu ndiyo inakumbatia mambo mengine yote, Wizara wezeshi, tutashirikiana kwa kadri iwezekananavyo Mpango huu na mambo mengine yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matamanio yangu makubwa wafike watu nchi jirani waje Tanzania kuja kujifunza kupitia kwetu. Kuna watu wengine wanaona kwamba eti kufanya ufahari kwamba lazima uende kwenye kujifunza, hapana tufike muda Tanzania lazima tuache legacy nchi yetu. Leo hii tumepata mfano katika mradi wetu wa DART unaoendelea Dar es Salaam tumeshinda katika majiji duniani. Mwezi wa pili tunaenda New York, Marekani kuchukua tuzo maalum ni Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoenda katika suala zima la utengenezaji wa barabara za mwendo kasi awamu sita tumemaliza awamu moja lakini awamu hizo zote ndizo ziko ndani ya Mpango ambao leo hii ndiyo Mheshimiwa Mpango anau-submit hapa. Si muda mrefu sana tunaenda kuhakikisha tunatekeleza mradi wa barabara ya Kilwa - Mbagala - Gongo la Mboto. Lengo ni kulifanya Jiji letu la Dar es Salaam na maeneo mengine yawe rafiki kwa ajili ya suala zima la kujenga uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Tanzania tumepata ufahari mkubwa, takribani nchi sita na wengine mpaka leo wanazidi kuomba kupitia kwetu TAMISEMI waje Tanzania kujifunza mipango mizuri ya utekelezaji wa miradi yetu. Haya yote yanataka sisi Wabunge ambao ni decision makers ambao tunawawakilisha wananchi hapa tufanye maamuzi mazuri, tushirikiane na Serikali, pale penye upungufu tuboreshe vizuri zaidi nini tufanye ili tuifikishe nchi yetu mahali salama ambapo Watanzania watajivunia kwamba wamepata viongozi ambao wako humu na wamekuja kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya yote naomba niseme wazi kwamba tunaenda vizuri. Kikubwa zaidi tutaboresha kwa michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge ndiyo maana ya Bunge lazima Wabunge watoe maoni, maoni yale yakikusanywa tunatengeneza Mpango mzuri lakini Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nikuhakikishie kwamba Tanzania ikifika mwaka 2020 kuna watu mpaka wengine wataogopa kugombea humu ndani. Wasipoogopa kugombea basi lazima wata-join na watu ambao wana uhakika wa kushinda, election is not a numbers. Kama
tunaenda katika utaratibu huu mzuri naomba niwaambie hakuna mashaka lazima tutafika mahali muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya niliyoyazungumza, naomba niseme wazi kwamba kama Wabunge tuungane kwa pamoja, tujenge uzalendo wa nchi yetu, tuhakikishe jinsi gani tunafanya na tuweke maslahi ya wananchi mbele. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, ubariki Mpango huu, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza awali ya yote napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha mwaka huu wa 2018 na hili ni Bunge letu Tukufu tumekutana Bunge la Wabunge wenyewe kwa sababu ndiyo Kamati za Bunge zinawasilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kupongeza Kamati zote mbili na nipende kuwapongeza kwa dhati ya moyo wangi Wenyeviti wa Kamati na Wajumbe wao wote. Mimi nashukuru sana Kamati ya LAAC tumekaa muda mrefu sana tukijadiliana, kwa kweli imetupa mwongozo mkubwa sana wa nini tunatakiwa tufanye katika kuhakikisha kwamba tunazisimamia vizuri Halmashauri zetu. (Makofi)

Mgheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika kamati ya LAAC nimekuta hoja hii ya fedha za ALAT ambazo zimetumika kinyume na taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli chombo kile huko nyuma kilikuwa hakiendi vizuri na ndiyo maana hivi sasa kuna timu imeundwa na leo hii Kamati Tendaji ya ALAT Taifa iko hapa Dodoma kwa ajili ya kupitia repoti ya ukaguzi maalum iliyofanywa. Lengo lake ni kwamba yale yatakayobainika hatua mbalimbali ziweze kuchukuliwa. Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kwamba inapopata repoti kuhakikisha inafanyakazi vya kutosha kuhakikisha kuondoa machafu yote. Sisi tumejipambanua, ajenda yetu ni kuhakikisha kwamba pale kwenye maovu ya aina yoyote tuweze kuyafanyia kazi kwa mustakabali mpana wa rasilimali za nchi yetu ziweze kukaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli taarifa ya Mkaguzi Mkuu imeeleza suala zima la manunuzi yasiyozingatia Sheria na utaratibu na kweli hili lilitokea huku nyuma. Kamati ilizibainisha wazi, na halmashauri mbalimbali zilizoitwa pale kuna maelekezo mengi yalitolewa. Hata hivyo jukumu letu sisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika hilo, tuliweza kuchukua hatua mbalimbali kwa wale wote ambao walikiuka taratibu. Tumechukua hatua takribani kwa watumishi wapatao 434, kati ya hao tisa wamefukuzwa kazi, 210 wamepewa maonyo mbalimbali, watumishi 15 wapo katika vyombo vya dola, lakini 28 wamesimamishwa kazi kwa ajili ya uchunguzi, wapatao 64 wako katika hatua ya uchunguzi mbalimbali za kiupelelezi, 13 wametakiwa kulipa fidia hasara waliyoisababisha katika maeneo yao hali kadhalika watumishi wanne wameshushwa vyeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kubwa la hili ni kutekeleza yale ambayo yamebainishwa katika repoti mbalimbali. Hili ni jukumu letu, lazoma tuweke nidhamu katika nchi yetu. Kwa sababu Halmashauri zetu; kwa mfano tukichukua bajeti ya mwaka huu ya trilioni 31.7 karibu trilioni 6.58, asilimia 20.7 ya total budget iko katika halmashauri zetu. Kwa hiyo tusiposimamia vyema tutaliangusha taifa hili. Kwahiyo naomba niwashukuru Wajumbe wa Kamati, na maagizo mbalimbali tunaendelea kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajenda nyingine ni kuhusu ukusanyaji wa mapayo. Ni kweli Halmashauri zetu huko nyuma tulikuwa tunakusanya watu wanasema kwa zile receipt za ngalawa. Sasa kuna maelekezo mbalimbali ya jinsi ya kutumia mifumo ya electronic katika Halmashauri zetu. Katika jambo hili tumefanya hatua mbalimbali na hasa kuzihimiza Halmashauri zijirekebishe katika ukusanyaji wa mapto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru tunapozungumza Halmashauri zote 184 zimeshaingia katika mifumo huo wa ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo hii ofisi yetu imehakikisha kwamba inetekeleza agizo hili, vilevile Kamati wanafaham. Katika hatua mbalimbali Kamati ya TAMISEMI na Kamati ya LAAC tumeendelea ku-report kwamba tumeweza kutekeleza katika yale ambayo maeneo hapo awali yalikuwa na mapungufu makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo naomba niwaombe Wabunge wenzangu, sisi tukiwa kama Madiwani katika Halmashauri zetu, hata hii mifumo ikiwepo bado kuna watu wengine wana-divert kutoka katika mifumo hii. Badala ya watu kuhakikisha tunasimamia lakini kuna watu wengine wanatumia mifumo mingine kwa sababu wameshazoea ubadhirifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana mifumo hii sasa ipo, tusisitize katika Halmashauri zetu na kuhakikisha wale ma-accounting officers katika Halmashauri zetu na wasimamizi wao wote wa chini wahakikishe fedha zinakusanywa, zinaingia katika mfuko ili hatimaye tuweze kupata mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nyinyi mnafahamu, hata katika sekta ya afya kwa kutumia mifumo leo hii tumepata faida kubwa sana. Hospitali zilikuwa zinakusanya wastani wa shilingi 150,000 mpaka 200,000 kwa siku lakini leo hii wanakusanya kuanzia milioni moja mpaka milioni 1.5 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna variationkubwa sana, ukiangalia hospitali nyingine kwa mwezi wanakusanya takriban wastani wa shilingi milioni nne sasa wanakusanya milioni ishirini na sita mpaka milioni arobaini. Kwa hiyo mfumo wa ukusanyaji wa mapato; na mimi niwashukuru sana Kamati zote, Kamati ya LAAC kwa ajili ya kubainisha hili na kutoa maelekezo na Kamati ya TAMISEMI inayotusimamia katika jambo hili. Tumepata mafankio makubwa; na mimi nina imani tutaendelea kuweka msingi mzuri wa ukusanyaji wa mapato katika maeneo mbalimbali

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajenda nyingine iliyobainishwa ni suala la mikataba. Kwamba kuna usimamizi mbovu wa mikataba; na ndiyo maana naomba niwaambie kwamba sisi ofisi yetu baada ya kuona hili sasa tumejikita katika kusimamia mikataba. Naomba niwaambie kwamba tumeshaanza kuchukua hatua mbalimbali na ninyi wenyewe nio mashahidi. Hata mwaka huu kama mlivyoona kwamba suala la mikataba inayokiuka utaratibu, hasa kule Nkasi tumemsimamisha Mkurugenzi kwa ajenda tu hii ya usimamaizi wa mikataba; pamoja na maeneo mbalimbali. Mmesikia maeneo hata Butiama juzi tumemsimamisha Mkurugenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo sasa hivi tunawafanyia vetting Wakurugenzi ambao wanashindwa commitment zao za kazi. Ndiyo maana hata ndugu yangu pale Nape ameshika shavu hapa ananisikiliza, niwaambie tu kwamba nafanya kazi kweli kweli tunahakikisha kwamba tutafanya vetting, na Mheshimiwa Rais ameteuwa hawa Wakurugenzi wana uwezo mkubwa. Hata hivyo lakini wale watakaobainika baada ya kuona kwamba mambo mengine hayaendi vizuri si jukumu la Serikali hii kuvumilia watu ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miradi ya maji. Ni kweli, na bahati nzuri kaka yangu Engineer Kamwelwe amelizungumza hapa; tutalisimamia. Waheshimiwa Wabunge mnafahamu huko tulikopita kuna maeneo mengine wakandarasi wengine tumewatoa katika miradi hii ya kazi. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunapata wakandarasi ambao wako competent. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na tatizo lingine la wasimamizi, wakandarasi na washauri. Wakati mwingine kulikuwa na negosiation inafanyika kuhusiana na miradi hii ndiyo maana ilikuwa inaenda vibaya. Mnakumbuka tulivyokuwa Korogwe kule nilimuomba Mheshimiwa Rais atupatie fursa ya ku-blacklist wakandarasi wote wa miradi ya maji, hali kadhalika miradi ya barabara ambao wanakwamisha. Naomba niwaambie hili zoezi sasa hivi linaendelea na si muda mrefu mtaona watu mbalimbali wakili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwasihi Wabunge. Kuna wakandarasi wengine ni marafiki zetu. Wakati tunawashughulikia naomba mtuache tuwashughulikie kwa nidhamu ya nchi hii, kwa sababu hatuwezi kukubali fedha ambazo zinaenda kwa wananchi kuna watu wengine wanazifanyia mambo ya hovyo ambayo hayakubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala zima la asilimia tano. Ni kweli kwamba historia ya huko tulikotoka hii asilimia tano ilikuwa haiendi vizuri. Wale walio katika Kamati ya TAMISEMI wanafahamu kwamba tuliitengeneza bajeti guideline, kwamba lazima kila Halmashauri itenge asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha uliopita takribani shilingi bilioni 19 kwa mara ya kwanza ziweze kufika katika Halmashauri zetu. Mwaka huu tuna zaidi ya shilingi bilioni sitini na moja kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto amezungumza hoja hapa, leo hii tuna Bodi yetu ya Serikali za Mitaa; nimewaambia wataalamu wetu, kwamba fedha hizi kwa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa tunaweza tukatengenezea utaratibu na tukaweka mfumo mzuri ili Halmashauri zetu zipeleke huko moja kwa moja kwa utaratibu mzuri ili watu waweze kukopa na hatimaye compliance ya ulipaji wa madeni iweze kuwa vizuri. Watu wanaona hizi fedha zinatolewa kama sadaka, hapana hizi fedha zimelengwa ni kwaajili ya kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nishukuru sana, katika mwaka huu wa fedha Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wamesimama hapa kushuhudia yaliyotokea leo hii katika Halmashauri nyingi. Hii ni tofauti na yaliyotokea nyuma ambayo ripoti hii leo tunaijadili. Kwa kiwango kikubwa maeneo mengi watu wameendelea kufanya vizuri. Katika hili niwasihi Waheshimiwa Wabunge fedha hizi siku zote nasema zinabaki katika Halmashauri zetu kule kule hazifiki kwa Dkt. Mpango, hizi ni Kamati ya Fedha kila mwezi tunakusanya mapato yetu. Naomba tusaidiane katika kuhakikisha kwamba tunasimamia fedha hizi ili vijana wetu na akina mama katika maeneo hayo waweze kupata fursa ya mikopo ambayo itawasaidia katika uwekezeji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana ile ajenda yangu ya kusema viwanda vidogo 100 katika kila mkoa; tena nilisema viwanda vidogo vidogo na maana yangu ni kwamba kiwanda kidogo unit price ya kiwanda kidogo kina range kati ya shillingi milioni tano mpaka milioni kumi. Ukija katika bajeti yetu ya takriban shilingi bilioni sitini plus. Ukizungumza unit price ya kiwanda cha wastani cha milioni 10 unazungumza viwanda takribani 6000 hata nusu ya pesa hiyo ikitoka karibuni bilioni 30 unazungumza karibuni viwanda 3000 tume- outstand expectation ya viwanda 2600 kwa mikoa yote. Kwa hiyo, nilizungumza target ile ili viongozi tuweke leadership ya kuhakikisha tunawahamasisha watu wetu, ambao wengine ni wadogo wadogo wanataka kusaidiwa. Hii ni sehemu ya employment kwake la kumuwezesha kufuka katika suala zima la kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuhakikisha maagizo ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali zinafuatiliwa, jambo hili tumelichukulia hatua kali sana. Tumewaagiza Wakurugenzi wote kwamba tutawapima kwa utekelezaji wa maagizo ya CAG. Jambo hili nimeripoti mpaka katika Kamati na tuko firm katika hili; na naomba niwaambie mtaona kundi kubwa la Wakurugenzi tutawaondoa katika nafasi zao, wale wataoshindwa ku-meet target ambayo tumewaelekeza; kwa sababu nikijua hapa hii ndiyo sehemu ambayo inaenda kujibu matatizo ya wananchi wetu ili hatimaye waone kwamba maeneo mbalimbali wananchi wanapata fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa hii, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuzipongeza Kamati zote kwa hoja iliyowasilishwa leo Bungeni hapa na ninaomba nikiri wazi hapa kwamba sisi hapa jukumu letu kubwa ni kupokea michango ya Wabunge kwa maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha Wizara yetu au Serikali kwa ujumla wake tuweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Kamati ya TAMISEMI na Kamati ya Sheria Ndogo. Mheshimiwa Mwenyekiti ninafahamu fika wewe ndiye mwenye dhamana ya Kamati ya Sheria Ndogo na maelekezo yako ya aina mbalimbali yameweza kutusasidia katika utekelezaji wa majukumu yetu. Hata hivyo tutaendelea kuboresha yale ambayo yamebainishwa hapa na Waheshimiwa Wabunge hasa katika suala zima la zoezi la kusaini sheria ndogo. Wataalam wanazipitia ili kuondoa makosa ambayo yamebainika na hatimaye tufanye maamuzi kwa ajili ya kuzisaini tupate sheria ndogo zenye kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni mbalimbali yametolewa hasa katika suala la ujenzi wa Strategic City Project. Kuhusiana na mradi huu niishukuru sana Kamati ya TAMISEMI, imefanya kazi kubwa sana katika maeneo mbalimbali. Wamekwenda maeneo Jiji la Tanga, wametembelea hapa Dodoma kwa ufupi, lakini na maeneo mengine na tumepata mchango wao kwa kadri iwezekavyo, kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachukua ushauri kuhusu ujenzi wa mifereji. Tukumbuke mradi huu sawa sawa na ile miradi mingine mitatu mikubwa tuliyo nayo. Mradi wa karibuni shilingi bilioni 840, ambapo tunajenga katika miji yetu hii. Tuna Mradi wa DMDP wa milioni 660 na Mradi wa UGSLP karibuni milioni 800 vilevile ambapo katika sehemu hii tunachukua maoni ya Kamati, kwamba kipaumbele kikubwa ni lazima tuhakikishe kwamba tunatengeneza mifereji katika maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie kwamba katika mradi huu jambo hili tunalichukulia kwa nguvu zote licha ya mifereji pia tunaweka taa za barabarani kwa ajili ya wakati wa usiku. Hali kadhalika katika maeneo mbalimbali tunajenga na madampo ya kisasa ili kuiwezesha miji yetu iwe miji rafiki sambamba na ununuaji wa mitambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja inayohusu huduma ya afya, naomba nishukuru sana na nishukuru Kamati kwa kiwango kikubwa. Katika mpango wetu wa kuboresha vituo vya afya 205 hivi sasa zoezi lile linaenda vizuri. Hata hivyo nafahamu kwamba changamoto ya afya hatuwezi kuimaliza kwa siku moja, lakini Serikali imeweka uwekezaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru mama yangu mama Kahigi aliipongeza Wizara hii kwa nguvu zote na kutoa changamoto katika Hospitali ya Bukoba Vijijini. Mchango wako mama Kahiji sambamba na Mzee wetu Mbunge wa Bukoba Vijijini; ndiyo maana kwa sababu mlikuwa hamna Hospitali ya Wilaya tumepeleka ujenzi vituo vya afya pale Katoro na Kashanje kwa lengo la kwamba huduma za upasuaji ziweze kufanyika katika eneo lile. Hata hivyo Halmashauri ya Bukoba Vijijini tumeiweka katika mpango wa ujenzi wa zile hospitali 64 katika Wilaya ambazo hazina hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hili sasa hivi lipo katika kipaumbele chetu; eneo hilo tutalipatia huduma ya afya kama tunavyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi kama nilivyosema kwamba Kamati ya TAMISEMI imefanya kazi kubwa sana hasa ushauri wa meneo mbalimbali; si wa Bunge tu lakini hata nje ya Bunge tukiwa katika vikao vya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri wazi kwamba walivyotembelea kule Kilolo waliona hospitali ya mfano ya Wilaya ya Kilolo, na mimi tu niseme kwamba nimetoa maelekezo na tutaendelea kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi nini afanye ili hospitali ile ya mfano iweze kukamilika ili sisi sote tujivunie tumefanya jambo kubwa la mfano katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja iliyohusu mabasi ya mwendo kasi, kwamba ratiba imebadilika. Naomba niwahakikishie kwamba ofisi yetu inafanya kazi kubwa sana; kwa sababu mradi huu leo hii katika Bara la Afrika ndani ya miaka 13 baada ya utoaji wa tuzo maalum Afrika sisi Watanzania tumekuwa watu wa kwanza katika miaka 13 tumeweza kushinda mwaka huu. Tarehe 9 JAnuari wa kwanza Tanzania imetunukiwa tuzo hii maalum kwa mradi wa mwendo kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mradi huu una changamoto yake kubwa kama mama Ruth Mollel alivyosema na ndiyo maana kila siku tunaendeleza uboreshaji na ndiyo maana sasa hivi kuna tender imetangazwa lengo kubwa ni kwamba tuweze ku-meet zile specification za World Bank ambazo katika agreement yatu tumekubaliana kwamba tuwe na service provider ambao mkataba wao tunadhani ndani ya mwezi wa tano inawezekana tukaenda mahala pazuri zaidi kuhakikisha kwamba tunapata service provider. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu hii ni awamu ya kwanza lakini tunajumuisha awamu zote sita; tutakuwa na watoa huduma vizuri zaidi kuondoa shida kubwa ya mabasi yaendayo kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la karakana pale Jangwani ni kweli na Wajumbe wa Kamati wanafahamu, mmelitembelea pale, changamoto ile ni kubwa. Ndiyo maana katika mpango wa muda mfupi kupitia Mradi wa DMDP tumepeleka fedha kwa ajili ya survey, na sasa hivi wataalam wanafanya survey kuondoa lile tope na bonde lote ili kulibadilisha Bonde la Msimbazi ili mvua inaponyesha maji yote yaelekee kwenda baharini.

Hata hivyo katika backup strategy nimetoa maelekezo kwa wenzetu wa DART kwamba mabasi yale yote yaache kulala pale eneo la Jangwani yaende kulala eneo la Gerezani ambako kuna eneo limetengwa ili kuepusha gharama nyingine ambazo zinaweza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu jambo jipya lolote lazima lina changamoto yake kubwa, lakini changamoto hii tunaendelea kujifunza na kufanya marekebisho makubwa hatimaye tuweze kupata fursa kubwa sana kuhakikisha nchi yetu inaenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Kamati ya TAMISEMI na ushauri wenu mmetoa mlipotembelea ukarabati mkubwa wa shule kongwe Tanzania, tunachofanya ni ukarabati wa kwanza kihistoria. Tunakarabati shule 89 tunatumia takribani shilingi bilioni 89 na kazi hii kubwa inafanyika na Kamati imeendelea kushauri japokuwa kuna baadhi ya wakandarasi walitukwamisha especially TBA.

Hata hivyo tumetoa maelekezo ili kwamba miradi hii yote ipate mafanikio makubwa na shule zetu kongwe zirudi katika ubora wake ule tunaokusudia. Hatimaye tupeleke elimu bora kwa vijana wetu na sisi kama Watanzania tujivunie kwamba katika mamlaka zetu za Serikali sasa shule zetu za Serikali zinatoa huduma bora kwa vile vijana wana mazingira rafiki ya kujifunzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna inayohusu TARURA. Nishukuru Kamati imetufundisha mambo mengi sana. TARURA ni chombo kipya na hivyo tunapaswa kukilea kuanzia sasa. Sasa hivi ndiyo kwanza kama mtoto anaanza kukaa chini, ana miezi sita. Wabunge mnafahamu eneo hili sasa ninyi mna ownership kubwa sana katika TARURA. Leo hii ukiwa Mbunge wewe ndiye msemaji mkubwa sana wa TARURA katika Wilaya yako. Yaani ndiyo maana ninasema kwa Wabunge kwamba kuanzishwa kwa TARURA inakuwa kama kipa katoka wewe Mbunge unadhamana kubwa ya kukielekeza chombo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba niseme, na ninyi mmeona changamoto kubwa ya kifedha, kwamba mgawanyo ni wa asilimia 30 naomba hili kwa sababu ni suala la Wabunge wote tutalijadili hapo baadae kwamba nini kifanyike ili kuufanya wakala huu uweze kusimama vizuri. Hata hivyo jukumu letu kubwa kupitia TARURA sasa tunataka tuhakikishe kwamba tunaimarisha miundombinu yetu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa kujali value for money na ubora wa kazi.

Mheshi,wa Mwenyekiti, ni imani yangu kubwa kwamba tutashirikiana kwa pamoja, wakala huu utaweza kutimiza wajibu wake kwa sababu mwisho wa siku jambo hili litaleta faraja kubwa kwa Watanzania. Hii ni kwa sababu huko chini ndiko mazao yanakozalishwa wananchi maskini wako huko. Nina imani miundombinu hii tutaiimarisha, na tutahakikisha kwamba katika maeneo mbalimbali wananchi wanapata huduma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepewa dakika tisa, japokuwa nina hoja nyingi sana za kujadili, niseme kwa ujumla na nikuhakikishie kwamba sisi ambao tuna jukumu kubwa sana la kuhakikisha katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tunafanya kazi kubwa ya kutosha tumejipanga. Kamati nawaombea sana ili Mungu asaidie muendelee kutushauri. Lengo kubwa ni kwamba Wizara hii iweze kufanya vizuri na wananchi wapate huduma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana ninaomba kuwasilisha, lakini naunga mkono hoja zote zilizowasilishwa hapa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika leo hii ambapo tunahitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa imani yake kubwa kwangu kwa kunipa nafasi ya kuhudumu katika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Napenda pia kutoa shukrani zangu kwa Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi bora. Shukrani za pekee ziende kwa Waziri wangu Mheshimiwa George Simbachawene ambaye alikuwa akinipa maelekezo ya mara kwa mara katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nachukua fursa hii kuwapongeza viongozi wote wa Bunge wakiongozwa na Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri uliowezesha Bunge hili Tukufu kujadili bajeti hii. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa uchambuzi wa kina ambao umesaidia sana kuboresha bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa kunipa fursa tena kwa nafasi hii kwa mara nyingine ya pili kuhudumu katika Bunge hili. Ndugu zangu wananchi wangu, nawapenda sana, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa umuhimu sana nipende kuishukuru familia yangu, wake zangu pamoja na watoto. Shukrani kubwa zaidi ziende kwa mama yangu mzazi aliyenizaa na kunilea vizuri pamoja na baba yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi sasa naomba nijielekeze katika kujibu baadhi ya hoja zilizochangiwa na Waheshimiwa Wabunge kwa njia ya maandishi na kwa kuzungumza. Majina ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia watatajwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI atakapokuwa akijibu hoja mbalimbali za Wabunge. Kutokana na muda, hoja ambazo hazitajibiwa hapa tutaziwasilisha kwa maandishi ili Waheshimiwa Wabunge wote waweze kuzipitia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi walichangia katika maeneo yafuatayo:-
(i) Usimamizi wa mapato katika Serikali za Mitaa;
(ii) Maeneo mapya ya utawala;
(iii) Migogoro ya ardhi;
(iv) Usimamizi wa watumishi katika mamlaka ya Serikali za Mitaa; na
(v) Kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji na mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukianza katika hoja zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ambazo kwa kiwango kikubwa zimeungwa mkono na Wajumbe wengi katika Bunge hili, lilikuwa suala zima la Halmashauri kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana. Ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Halmashauri zote zimeelekezwa kupitia mwongozo wa bajeti kutenga 10% kwa ajili ya mkopo wa vikundi vya wanawake na vijana. Aidha, katika uchambuzi wa bajeti agizo hili limezingatiwa na Halmashauri zote zimetenga 10% ya mapato ya ndani. Wakuu wa Mikoa wanaelekezwa kusimamia utekelezaji wa jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza hapa, sisi Wabunge wote ni Wajumbe wa Kamati za Fedha na Mabaraza ya Madiwani. Kwa sababu mwongozo wa bajeti umeshaeleza na Halmashauri zote zimeshatenga 10% katika bajeti zao za mapato ya ndani na ndiyo criteria iliyotumika kupitisha bajeti ya kila Halmashauri yake, tuna jukumu la kuhakikisha suala hili linatekelezwa. Kwa sababu hii 10% ni own source kwa maana kwamba ni mapato ya ndani yanayokusanywa katika Halmashauri husika, ina maana pesa zile zinaishia katika Halmashauri na kwamba Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani ndilo linafanya maamuzi hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia yangu ni kusema kwamba kila Mbunge akitoka hapa atahakikisha kitachokusanywa kinagawanywa kwa wananchi ili mradi vijana na akina mama waweze kupata mikopo hiyo. Nisisitize pia tutakapofanya hivyo lazima tuangalie ni jinsi gani tunawagusa walemavu ili mradi nao waweze kushiriki katika shughuli za ujasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kulikuwa na hoja ya ukusanyaji wa ushuru wa minara ya simu na mabango ambapo suala hili limekuwa ni changamoto kubwa. Ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba ushuru wa minara ya simu na mabango hutozwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali ya Mitaa, Sura Na. 290. Kuhusu malipo ya vijiji na watu binafsi, malipo haya hulipwa kwa mmiliki wa eneo ambalo minara huwekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, malipo haya hayahusiani na malipo ya ushuru ambayo Halmashauri inatakiwa iyapate. Hivi sasa Serikali inakusudia kuwasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Serikali za Mitaa ili kuweka mfumo mzuri wa malipo, ushuru wa minara na mabango kwa watu binafsi katika Serikali ya Vijiji ili mradi uwe sawasawa kwamba kila Halmashauri iweze kunufaika na mchakato huo tunavyoenda katika ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa suala zima la matumizi ya mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri. Jambo hili tumelielezea katika vipindi mbalimbali na Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele kulisimamia hili na kutoa maagizo. Katika bajeti ya mwaka huu tunasema itakapofika muda ulioagizwa katika hotuba ya mwaka wa fedha 2016/2017 tuliyoisoma hapa ambayo inajiainisha katika ukurasa namba 13 na 16, kwamba kuanzia Julai 1, 2016 kila Halmashauri zote zinatakiwa kukusanya mapato yake yote kwa mifumo ya kielektroniki. Baada ya mifumo hii kuanza hakuna Halmashauri itaruhusiwa kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge, sisi ni Wajumbe katika Mabaraza yetu, kila mtu akachukue nafasi yake kuhakikisha kwamba katika Halmashauri yake anakwenda kuweka misingi imara ili mwaka wa fedha 2016/2017 twende katika mfumo thabiti wa kuweza kukusanya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tumetoa maelezo sehemu tofauti kwamba tulipotumia mifumo hii mabadiliko ya ukusanyaji wa mapato yamekuwa makubwa sana. Sehemu ambayo walikuwa wanakusanya shilingi 200,000 mpaka shilingi 300,000 kwa siku, mara baada ya kuweka mfumo huu watu wanakusanya zaidi ya shilingi 3,000,000 mpaka shilingi 4,000,000. Ni jukumu la kila Mbunge kuhakikisha sasa anaenda kusimamia eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Ofisi ya Rais - TAMISEMI, tunatoa onyo kwa watendaji ambao wataenda ku-temper na mifumo hii. Naomba niwaeleze, watendaji wote ambao watathubutu kwa njia moja au nyingine kwenda kuhujumu mifumo hii, tutahakikisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaenda kuwashughulikia kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala zima la Halmashauri irejeshewe 70% ya kodi ya ardhi badala ya 30%. Majibu ya hoja hii ni kwamba utaratibu wa kugawanywa kodi ya ardhi ya asilimia 30 kwa Halmashauri na asilimia 70 kwa Wizara ya Ardhi umewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya sheria hii yanayopendekezwa pamoja na wazo la kuwezesha Halmashauri kubaki na mgao unaostahili kabla ya kuwasilisha Wizarani, mchakato huu sasa unaenda ambapo marekebisho haya ya sheria yatakapokamilika, jambo hili tutaliangalia sote kwa pamoja kuona ni jinsi gani tuliweke ili mradi Halmashauri ziweze kukidhi kupata mapato halisi katika suala zima la Kodi ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna hoja imejitokeza sana kuhusu suala zima la Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) juu ya uhamishaji wa Mfuko wa CHF. Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia na Mwenyekiti wa Kamati alilielezea hili katika taarifa yake. Kwa hiyo, ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoko sasa, imeweka utaratibu wa hiari kwa kila kaya kujiunga katika Mfuko huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa Wizara ya Afya inaandaa Muswada wa Sheria ya kufanya Mfuko wa Afya ya Jamii kuwa lazima. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Viongozi katika ngazi zote, wataendelea na jitahada mbalimbali za kuwaelimisha wananchi ili kuhakikisha kwamba wale wadau mbalimbali kama waendesha bodaboda, mamalishe, watu wa pikipiki, wafanyabiashara wadogo, basi wote mwisho wa siku waweze kujiunga katika Mfuko huu kwa ajili ya kuimarisha afya ya Taifa letu na wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lililojitokeza ni kwamba, Serikali itoe fedha za Halmashauri ili kulipa madeni ya Wazabuni na Wakandarasi, kuondoa usumbufu kwa Halmashauri kutoka kwa wadeni wao. Hoja hii imejadiliwa na Wabunge wengi. Kama nilivyosema, Waziri wangu wa Nchi akifika hapa atakuja kutoa ufafanuzi mbalimbali kwa Wabunge wote waliochangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya hoja hii ni kwamba Serikali inatambua madeni ya Wazabuni yaliyopo, waliotoa huduma mbalimbali katika Serikali kuu, Halmashauri na Taasisi zetu. Serikali itahakikisha kwamba madeni hayo yataendelea kulipwa kwa kadri fedha zitakavyopatikana. Aidha, Halmashauri zinaelekezwa kutoanzisha madeni mengine mapya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine iliyojitokeza kuhusu suala zima la ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Hii ilikuwa moja, lakini nilivyofuatilia nimeona ni watu wengi wamekuja na hoja hii kuhusu maeneo yao. Kwa hiyo, nijibu kwamba tuna Halmashauri zipatazo 44 ambazo ujenzi unaendelea na tumetenga kati ya Shilingi milioni 500 mpaka Shilingi milioni 850. Naomba nizitaje Halmashauri hizo kwa faida ya Bunge hili kwa sababu kila mtu atataka kujua katika eneo lake ni eneo gani limeguswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ambazo zimetengewa mgao huo kati ya Shilingi milioni 500 mpaka Shilingi milioni 850 ni Kalambo DC, Kyela DC, Bumbuli DC, Kaliua DC, Nkalama DC, Ikungi DC, Ushetu DC, Nyasa DC, Ilemela MC, Masasi DC, Gairo DC, Busokelo DC, Momba DC, Uvinza DC, Kakonko DC, Buhigwe DC, Mbogwe DC, Nyang’hwale DC, Njombe TC, Wanging’ombe DC, Makambako TC, Mlele DC, Msimbo DC, Mpanda DC, Simanjiro DC, Kiteto DC, Mkinga DC, Kilinda DC, Mpangani DC, Magu DC, Mtwara DC, Chamwino DC, Mafia DC, Kibaha DC, Msalala DC, Kahama TC, Butiama DC, Tarime DC, Chemba DC, Kibaha TC, Geita TC, Busega DC, Itirima DC na Bariadi TC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna Halmashauri mpya ambazo zimeanzishwa zipatazo 20 na ambazo zimetengewa Shilingi bilioni 2,140 ambazo ni Busocha DC, Bunda TC, Chalinze DC, Handeni DC, Ifakara TC, Itigi DC, Kasulu TC, Kibiti DC, Kondoa TC, Madaba DC, Mafinga TC, Malinyi DC, Mbinga TC, Mbulu TC, Mpindwa TC, Nanyamba TC, Newala TC, Nzega TC, Songwe DC na Tunduma TC. Hizi zimetengewa Shilingi bilioni 2,140 ambayo inaenda kuanza ujenzi katika harakati hizo. Nimeamua kuzitaja hizi kwa sababu kila Mbunge hapa alikuwa anazungumza suala zima la ujenzi wa Halmashauri mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maeneo ambayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa nafasi niliyopata kidogo naomba niendelee kufafanua. Vile vile kuna suala zima la Chemba ambapo Mheshimiwa Felister Bura alikuwa anazungumzia kuhusu ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Chemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi wa majibu yetu unasema, Halmashauri ya Chemba imetenga eneo la ekari nane kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, zimetengwa Shilingi milioni 20 kwa ajili ya kupima eneo ili maandalizi ya awali ya ujenzi wa hospitali hiyo yaanze.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala kwamba mradi wa umwagiliaji wa Gawaye, Manispaa ya Dodoma na Mradi wa Maji, Bahi ukamilishwe. Katika ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeendelea kukamilisha ujenzi wa mfumo wa umwagiliaji katika Kijiji cha Gawaye kwa gharama ya Shilingi milioni 631.68. Kazi hii ya uwekaji mifumo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2016, ambapo jumla ya eneo la ukubwa la ekari 97 umekamilika kati ya ekari 100. Inatarajiwa kuwekewa mifumo hiyo ya umwagiliaji na kuwezesha wananchi kulima zao la zabibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile watu wamechangia katika eneo la elimu hasa katika suala la elimu bure. Kulikuwa na mawazo ambayo wengine wanasema suala la elimu bure halikuleta tija. Kikubwa zaidi naomba niwashukuru Wabunge wote. Karibu asilimia 99, kila Mbunge aliyesimama hapa alikuwa ana-appreciate suala zima la elimu bure. (Makofi)
MheShimiwa Naibu Spika, ni lazima tukiri, kuna wenzetu ambao ni maskini kabisa, hali ilikuwa ni ngumu. Leo hii ndiyo maana hata tulipoanzisha suala hili, kuna watoto ambao tumewasajili mwaka huu wana miaka 10 mpaka 11. Nini maana yake? Maana yake watoto hawa walikuwa wanakosa fursa ya kwenda shule kutokana na hali ya maisha yao. Leo hii tumekumbwa na tatizo la madawati kwa sababu idadi kubwa ya watu waliokuwa wanakosa elimu, sasa wameenda shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo la kuishukuru sana Serikali na Chama cha Mapinduzi na mtazamo wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekubali kutenga Shilingi bilioni 16.77 kila mwezi kwa ajili ya ruzuku katika eneo hili. Kwa hiyo, tunashukuru sana. Naamini kwamba jambo lolote lina changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake kwa kazi kubwa waliyoifanya; na kwa sababu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni Wizara pacha na Wizara ya Afya lakini ukienda katika Wizara ya Elimu, Wizara ya Maji unaikuta TAMISEMI inazungumzwa muda wote; na ukiangalia michango mingi sana imejilenga katika suala zima la uboreshaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea mchango wa Kamati ambao maelekezo yake kwa kiwango kikubwa na michango ya baadhi ya Waheshimiwa Wajumbe wengi sana walipendekeza ikiwezekana mambo ya afya yote yabakie katika Wizara ya Afya, ambalo hili nimeona watu walikuwa wakipendekeza kwamba itoke TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nifanye rejea kidogo katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, nawaomba Waheshimiwa Wabunge ikiwezekana turejee katika Katiba, Ibara ya 145 na Ibara ya 146 yenye kuweka utaratibu wa Serikali za Mitaa, lakini vile vile Ibara 146 ikizungumza majukumu ya Serikali za Mitaa. Hili lina umuhimu mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hapa kuna ajenda moja ya msingi ambayo tunatakiwa kama Wabunge tuiangalie kwa pamoja, tuone jinsi gani tutafanya kuweza kupata fedha za kutosha kuhakikisha tunahudumia huduma za afya. Hili ndilo jambo la msingi. Kwa sababu hata ukichukua mambo yote ukipeleka Wizara ya Afya; leo hii tunapozungumza deni hata la MSD halipo TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sugu alikuwa anazungumzia suala zima Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwamba haiko TAMISEMI. Maana yake ni nini? Ni kama Taifa, kama Serikali sasa hivi inavyojipanga ya Awamu ya Tano kutafuta fedha kwa kadiri iwezekanavyo kutoa huduma za kijamii katika jamii yetu, hilo ni jambo la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme kwamba, kama Wabunge tujiandae vya kutosha tuone jinsi gani tutaimarisha Sekta ya Afya. Tutaimarisha Sekta ya Afya katika kuhakikisha tunafanya kila liwezekanalo kutafuta fedha nyingi za kutosha kuhudumia miradi ya afya. Hili tukilifanya vizuri, maana yake ni nini? Ukizungumza kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, walioajiriwa zamani wanafahamu. Leo hii mhudumu wa afya au nurse yuko Kigoma au yuko Kibondo, umwambie siku ya kupandishwa daraja lake, maana yake ni mpaka aende Makao Makuu ya Wizara. Ndugu zangu, tutazalisha matatizo makubwa kuliko tanayoyaona hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuseme, ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, naamini kila Mbunge alishiriki katika bajeti ya Halmashauri yake na kila Mbunge aliainisha vipaumbele vyake vya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na kila Mbunge aliweka kipaumbele chake cha ununuzi wa gari la wagonjwa, halikadhalika Hospitali ya Wilaya, lakini bajeti ni mchakato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaanza katika ngazi za Vijiji, unakuja katika ODC, inakuja katika Halmashauri, inaenda katika Wizara, lakini mara nyingi sana tunazungumza ukomo wa bajeti. Ukomo huu wa bajeti tusipoweka nguvu za kutosha za ukusanyaji wa kodi, maana yake hapo tutakwama. Kwa hiyo, nataka niwashawishi Waheshimiwa Wabunge, kwamba katika ile ajenda ya kufikiria kwanza saa nyingine tuiondoe yote, ina maana kwanza tunakuwa tumevunja Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara 145 na Ibara 146. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata watumishi tunaowahudumia ambao wako vijijini itakuwa ni changamoto kubwa, itakuwa ni mzigo mkubwa sana, tutakuja kumlaumu hapa Waziri wa Afya kwamba kuna watumishi wako, wako kule Kibondo, Mtwara au wapi, hawajapanda madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utaratibu utakuwa mzuri, kama fedha zitakuwa zinapatikana vizuri, naamini tuta-empower Mabaraza yetu ya Madiwani, yatafanya maamuzi sahihi zaidi katika kuweka vipaumbele vya kuhakikisha Sekta ya Afya inakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwashawishi Waheshimiwa Wabunge hapa, haya mambo kwa sababu naamini Wizara ya Afya kama ni regulator, yeye anasimamia sera na anasimamia hospitali za Serikali, halikadhalika katika sekta binafsi, jambo hili tukiliweka vizuri hasa katika kutafuta rasilimali fedha halafu kuzisukuma chini katika Halmashauri na kwa sababu kuna mfumo uliokamilika kwa…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kwanza kumpongeza Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi kwa hotuba nzuri na mtandao mzima wa barabara ambao wananchi wana imani kubwa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mambo mbalimbali kwa ajili ya sekta ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo nataka nichangie katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika baadhi ya maeneo ambayo Wabunge hasa Mheshimiwa Mary Muro, Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mheshimiwa Ester Bulaya na sasa hivi Mheshimiwa Julius Kalanga katika suala zima la upelekaji wa fedha za miundombinu ya barabara katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakati mbalimbali kwamba maeneo mengine yamekuwa na changamoto kubwa na ndiyo maana Serikali kwa kipindi kirefu sasa imeamua kubadilisha utaratibu wake wa upelekaji wa fedha kuelekeza fedha nyingi katika Halmashauri zetu. Japokuwa bado hazijatosheleza angalau hali si haba, ndiyo maana hata ukiangalia kitakwimu katika Bajeti yetu ya Mwaka 2010/2011 shilingi bilioni 84 tu ndiyo zilikuwa zimetengwa kwa bajeti ya barabara lakini bajeti yetu ambayo tumeipitisha juzi hapa tumetenga karibu shilingi bilioni 272. Lengo kubwa ni kuziwezesha Halmashauri mbalimbali japo tuweze kuzifungua barabara zile ziweze kupitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, najua kwamba changamoto ya mtandao wa barabara za Serikali za Mitaa ni mkubwa hizi fedha hazitoshi, lakini Serikali lazima tutaendelea kuangalia jinsi gani tunatafuta rasilimali fedha kuhakikisha kwamba tunaboresha. Ndiyo maana wakati mwingine tunashirikiana hasa kwa kutafuta funds kutoka hata kwa wenzetu wa World Bank ndiyo maana Halmashauri nyingi sana za Miji hivi sasa mitandao ya barabara imebadilika, ni kwa ajili ya juhudi hizo kubwa sana zinazofanyika, lengo kubwa ni kufungua barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upelekaji wa fedha, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa sababu mwaka wa fedha haujakwisha, kwa zile bajeti ambazo zimetengwa katika mwaka huu wa 2016/2017, Wizara ya Fedha itakuwa inafanya harakati za kutosha kuhakikisha kwamba barabara hizi tutaziwezesha ili kazi zetu za barabara ziweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Hussein Bashe ambayo ilikuwa ikizungumzia suala zima la Wakala wa Barabara ambao unaanzishwa sasa hivi vijijini, hoja yake ni kwamba changamoto kubwa ni fedha na jinsi gani tutaanzisha wakala ambapo sasa mgawanyo wa fedha hauko sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la kisheria, kwa sababu kwa sheria yetu tuliyonayo ni kwamba asilimia 30 ya fedha hizi zinaenda katika bajeti ya barabara za Halmashauri na asilimia 70 inaenda kwa ajili ya TANROADS, ndiyo maana tumekusudia kuanzisha Wakala lakini jambo hili liko katika hatua za mwisho, ilikuwa ni mapendekezo ya Wabunge humu ndani ya Bunge, basi kama kutakuwa na mawazo mengine tofauti tutatafakari. Lengo kubwa ni kwamba wananchi wetu katika maeneo yao barabara ziweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo haya kama michango ya Waheshimiwa Wabunge yote tunayachukua kwa pamoja, jukumu kubwa la Serikali inaangalia jinsi gani itafanya kuhakikisha kwamba barabara zetu zinapitika katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Ahmed Shabiby, alikuwa akizungumzia suala zima la barabara yake pale Mjini ambapo kulikuwa na ahadi ya kilometa tano na Mheshimiwa Shabiby anasema kweli na ndiyo maana siku ya Alhamisi Mheshimiwa Shabiby anakumbuka tulikuwa Jimboni kwake. Ahadi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara ile ya kilometa tano ujenzi unakamilika na ndiyo maana juzi nilivyofika pale Gairo ujenzi wa barabara ile sasa unaendelea. Ni imani yangu kwamba Serikali katika kipindi hiki cha miaka mitano, itafanya kila liwezekanalo ule mtandao ambao ni ahadi ya Serikali, ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa ya ujenzi wa kilometa tano uweze kukamilika katika eneo la Gairo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab alizungumzia suala zima la ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilometa tatu pale Mjini Muheza. Naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab kwamba ile ahadi ya Mheshimiwa Rais ndiyo hivi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa inachukua ahadi mbalimbali. Imani yangu ni ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano ahadi ile iweze kutekelezeka kwa sababu commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba ahadi zote hasa za ujenzi wa miundombinu ya barabara ndani ya kipindi cha miaka mitano hii tuweze kuzikamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mbunge, Mheshimiwa Vedasto Ngombale ambaye amechangia nadhani kwa maandishi, Mheshimiwa Bwege naye alizungumzia ile barabara ya kwenda Kilwa Kivinje na mwaka huu kulikuwa na commitment ya shilingi milioni 800 ambayo ipo katika bajeti ya mwaka huu wa 2016/2017. Kwa vile jua halijachwa bado ni imani yangu kwamba zile fedha zitapatikana kwa kipindi hiki kwa kuwa ipo katika mpango huu wa bajeti, bahati nzuri Mheshimiwa Bwege ni kwamba tayari tumeshaingizwa katika bajeti, hivi sasa naamini Wizara ya Fedha, fedha hii ikishatiririka basi tutatoa maelekezo Wakandarasi waingie site haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kipindi hiki cha mvua hali ni mbaya na nilipokuja kule kwenu nimeona kwamba hali ya barabara ile siyo nzuri zaidi ndiyo maana commitment ya Serikali mwaka huu ilitenga shilingi milioni 800 hizi tutahakikisha kwamba zikishapatikana basi ujenzi utekelezwe katika ubora unaokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya dada yangu, Mheshimiwa Bonnah, kuhusu suala la ujenzi wa barabara chini ya Mradi wa DMDP ambao hata wewe unakuhusu katika Jimbo lako la Ilala. Mradi huu utakuwa na takribani shilingi zisizopungua bilioni 600 na nusu na kuendelea, ambapo mchakato wake kweli ilibidi uanze tokea zamani lakini kuna mambo mbalimbali yalikuwa yamekwamisha. Hata hivyo, hivi sasa tupo katika hatua nzuri, Mbunge wa Temeke na Mbunge wa Mbagala, ni mashahidi, mwezi mmoja na nusu uliopita tumekwenda kuangalia ukaguzi wa ujenzi wa barabara hizi hasa utengenezaji wa daraja lile kubwa la Twangoma ambalo lina urefu wa karibu mita 800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mchakato huu katika maeneo mengine umekwama ni kwa sababu ya lile jedwali la tathmini. Imani yetu ni kwamba kulikuwa na mchakato hapa, inaonekana hali siyo nzuri sana katika ufanyaji wa tathmini. Jambo lile likikaa vizuri kwa sababu sasa hivi Wakandarasi wameshapatikana, ni imani yangu kwamba ujenzi wa barabara hii sasa utaanza mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie, katika Jimbo lako la Ilala nitasimamia kwa karibu zaidi na maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha barabara zile tunazijenga. Kwa sababu barabara zile ndiyo zitakuja kufungua Mji wa Dar es Salaam nyingine ni feeder roads zinaunganisha katika barabara kuu yetu ya DART, zingine ni barabara ambazo zinapita katika mitaa yetu ya Jiji la Dar es Salaam. Sasa hivi ukiangalia hata mvua ikinyesha mitaro yetu imekuwa ni tatizo, mradi ule unakwenda kutengeneza mitaro, unatengeneza barabara halafu unafanya settlement katika maeneo mengine. Kwa hiyo, naomba niseme kwamba Serikali imeweka commitment katika maeneo haya kuhakikisha mradi huu wa DMDP ambao Wabunge wa Jiji la Dar es Salaam lengo letu ni kuufungua mji ule vizuri, tutakwenda kulifanya hili kwa kadri iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi naomba niwahamasishe Waheshimiwa Wabunge hasa kwa fedha tunazozipeleka katika Halmashauri zetu, tuzisimamie vizuri, kwa sababu imani yangu kubwa katika maeneo mengine hali huwa inakuwa siyo shwari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Ahsante sana.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA ZA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kuunga mkono hoja iliyotolewa hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu, katika watu wanatuishi kwa upendo mkubwa sana sisi Waheshimiwa Wabunge ni ndugu zetu wa Dodoma. Kauli zetu zisiwafadhaishe wenyeji wa Dodoma. Hili ni jambo la kwanza, lazima tuliweke sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wWakati Mheshimiwa Rais anakusudia hili jambo jema ambalo lina maslahi mapana kwa nchi yetu, halafu na sisi viongozi tuliopewa dhamana tukionekana tunatoa mishipa kama vile jambo hili siyo jema, nadhani tunawanyong’onyeza sana kwa kiwango kikubwa wenyeji wetu wa Dodoma, hili ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kwa sababu Azimio hili lilikuwa ni suala zima la maelekezo ya kisheria ije Dodoma. Niseme kwamba Ofisi yangu ipo katika maandalizi ya mwisho kabisa ya hii sheria ya kuja Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika suala la miundombinu, Ofisi yangu ambayo ina mamlaka ya kufanya hivyo, mwaka huu hapa Dodoma tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa, stand ya kisasa pamoja na recreation area. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kupitia TARURA lengo letu ni kwamba tunataka tutengeneze barabara za pete za kutosha, nanyi sasa mnafahamu, hata ukitoka St. Gasper unakuta barabara nyingine zimefunguka. Lengo letu ni kwamba tuwe na ring road za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie ndugu zangu, Dodoma ndiyo itakuwa ndiyo Mji wa kwanza the best hapa Tanzania kwa upangaji mzuri. Ofisi yangu imeelekeza na hivi sasa tumekamilisha viwanja 15,000 eneo la Mtumba vimekamilika na hivi sasa watu wapo foleni kugombania hivyo viwanja kwa ajili ya mustakabali wa Dodoma. Kuna viwanja 21,000 tunavipima maeneo ya Ihumwa kule. Lengo letu ni kwamba tuhakikishe Mji wa Dodoma ndiyo Mji mzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, mnafahamu, hata ukiwa unashuka na ndege, ukiwa unashuka Dodoma ni tofauti kama unaposhuka maeneo ya miji mingine. Hili ni jambo la kujivunia kwetu sote. Kubwa zaidi katika hili, najua Mheshimiwa Rais amepewa kwa mujibu wa Sheria Sura Na. 288 katika kifungu cha (5)(3) katika suala zima la uanzishaji miji, tukipitia sheria tutajua haya mambo ni jinsi gani Mheshimiwa Rais hakukurupuka alifanya kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika kwa sababu Mheshimiwa Rais amepewa dhamana na Watanzania na dhamana aliyopewa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ilani imeainisha jinsi gani Serikali hii itahamia Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika agenda ya comparison, nadhani kuna kitu kidogo kilikuwa na sintofahamu kuona kwamba Mheshimiwa Rais kwa nini aliwabagua watu wa Moshi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie ndugu zangu, Moshi kilomita za mraba ni 58 peke yake. Naomba niwaambie, tukienda katika utaratibu wa vigezo, Wabunge wa kule wanafahamu. Ndiyo maana kulikuwa na suala zima la extension hata kuhakikisha kwamba kuna vikao vingine watu Hai watenge maeneo yao kwa ajili ya jiji la Moshi. (Makofi)

Kwa hiyo, mambo haya yalikuwa katika mchakato zaidi. Kama Moshi yenyewe, kilomita za mraba pale ni 58, naomba tuelezane ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja kwanza, nawaeleza fact, kwa nini kila jambo linaenda kwa mujibu wa sheria? Ukianzia hilo sasa, ndiyo maana hata Moshi yenyewe naomba niwaambie, wewe Mhehimiwa Komu, subiri… (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais jambo lolote anashauriwa kwa wema. Naomba niwaambie, hakuna jambo lolote unaweza ukashauri kwa hasira. Kila kitu busara inatawala kufanya mambo yaweze kukamilika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Naibu wake, lakini kwa Wizara yote kwa ujumla wake kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Nami nasema hivyo nikijua wazi kwamba suala la kulinda amani ni jambo lenye changamoto kubwa. Ni Wizara ambayo kwa kweli niwapongeze wamefanya kazi kubwa sana na wanaendelea kufanya kazi kubwa. Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa nguvu ya kutosha kuhakikisha kwamba suala la amani ni jambo la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika nafahamu kwamba hakuna mbadala wa amani. Kwa hiyo, suala la usalama wa watu ni jambo la msingi sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwigulu na timu yake nawapongeza sana kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nita-reserve muda kwa wenzangu wengine, nitaongea kwa ufupi sana. Kulikuwa na hoja ambayo ilikuwa ikijitokeza hapa kuhusu suala zima la Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwa utaratibu ambao imeonekana kuna kesi mbalimbali zimejitokeza kuwaweka watu katika ule utaratibu wa masaa 48.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1997, Wakuu wa Mikoa wamepewa mamlaka mbalimbali katika kifungu cha (7) na Wakuu wa Wilaya ni kifungu cha 15, kwamba pale ambapo saa nyingine wanaenda katika tukio, au kuna jambo limeonekana kwamba kuna uvunjifu wa amani na suala la kijinai, basi Wakuu wa Mikoa au Wakuu wa Wilaya inawapa nafasi. Lengo kubwa ni kumweka yule mtu chini ya usimamizi fulani kwa ajili ya kuepusha madhara hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa michango ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali hapa, inaonekana sheria ile inatumika visivyo. Hata hivyo, jambo hili limejitokeza katika maeneo mbalimbali ndiyo maana ofisi yetu iliamua kuchukua jukumu maalum kwa ajili ya kutoa maelekezo maalum hasa kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwamba sheria ile iendelee kutumika kwa kadri maudhui yake yalivyokusudiwaa, lakini tusi-over do kinyume cha taratibu. Tuliweza kutoa maelekezo hayo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, lakini hata hivyo tumeamua kuanzisha zile session maalum kwa ajili ya mafunzo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hata humu Bungeni, sote sisi ni Wabunge, lakini wote hatu-act kwa kufanana. Kuna style mbalimbali za utendaji wetu wa kazi, ndiyo maana kati ya Wabunge tuliokuwepo humu kila mtu ana sarakasi zake za utendaji wake wa kazi. Kwa hiyo, katika njia moja au nyingine, wakati mwingine kuna upungufu wa kibinadamu kwa baadhi ya viongozi inawezekana, lakini siyo kwamba ndiyo jambo la kila kiongozi afanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jambo hili najua sheria ipo, lakini tumeendelea kutoa maelekezo mbalimbali hasa pale tunapoona kwamba kuna taratibu kidogo za kisheria zinakiukwa tunatoa maelekezo haya. Kwa kuwa sasa hivi tuko katika mchakato wa kumaliza mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa ambapo tumemaliza kwa Wakuu wa Wilaya hapa katikati na tunaenda katika session kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, ni imani yangu kwamba utafika muda katika haya mambo ambayo tunaona kipindi kirefu wakati mwingine kuna utaratibu kidogo umekiukwa, naamini wote tutakuwa katika mstari mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, napenda kuwasihi hasa Watanzania wote kwa ujumla wetu kwamba mara nyingi sana tutii utaratibu wa sheria ambapo naamini haya yote tukiyafanya kwa umoja wetu, tutaweza kuepuka migogoro mingi sana ambayo inatokea katika jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo tu, kuweza kutoa ufafanuzi katika maeneo hayo. Kubwa kama nilivyosema mwanzo ni kwamba niwasihi sana hasa Wabunge wenzangu na viongozi wengine, kwamba mara nyingi sana katika utendaji wetu wa uongozi na maisha yetu tuweke suala zima la ustaarabu na maisha ya kawaida na kuheshimiana. Naamini kama viongozi wa Kitaifa na watu wa aina mbalimbali kila mtu akijua mipaka ya kanuni ile ambayo nasema siku zote STK - Sheria, Taratibu na Kanuni itakuwa imetuwezesha sana kuishi katika Taifa letu tukiwa katika hali ya usalama na amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Niseme kwamba naunga mkono hoja hii asilimia zote mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nikupongeze wewe Spika wetu, kwa kutuongoza vizuri, lakini pia nizipongeze Kamati zote za Bunge zilizowasilisha taarifa zao nzuri sana. Vile vile niwapongeze Manaibu wangu wawili ambao kwa kweli wametoa ufafanuzi mpana, japo kwa muda mfupi sana.

Mheshimiwa Spika, yangu ni machache tu kwa ajili ya kuelezea kwa ujumla. Kwanza naomba nikuhakikishie wazi kwamba, Kamati ya TAMISEMI ambayo tunafanya nayo sisi Ofisini kwetu, imekuwa msaada mkubwa sana kutupa maelekezo muhimu kwa ajili ya Taifa letu. Nataka tuweke hizi rekodi vizuri kwa sababu leo hii unaona ni mashahidi karibuni wajumbe wote hapa wakisimama, wanazungumzia vituo vya afya, wanazungumzia hospitali za Wilaya, wanazungumzia barabara na wanazungumzia elimu. Hii yote japo inawezekana kuna upungufu wa hapa na pale, lakini ukifanya tathmini ya huko tulikotoka na tulipo hivi sasa ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo naishukuru sana Kamati kwa ushauri wake, mkubwa sana. Kamati hii kwa kweli imeweza kufanya mambo makubwa sana na ripoti yao tunaishukuru sana na naomba niseme wazi kwamba wametusaidia sana kuhakikisha Wizara hii inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mbalimbali ya kiujumla, ambayo sisi kwa upande wetu tunaomba tuyachukue kwa ajili ya kwenda kuyaboresha zaidi na hasa katika suala zima la bajeti, japokuwa tunafahamu mgao kama Naibu wangu alivyosema hapa, mgao ni kiduchu na napenda Wabunge wafahamu kwamba mtandao wa barabara ambao TARURA inahudumia ni wastani wa kilomita 127,000, kwa hiyo ni changamoto kubwa. Hata hivyo, sisi kama Serikali tutaendelea kuangalia jinsi gani tutafanya na hasa team yangu sasa hivi, kupitia Mtendaji Mkuu wa TARURA, niliwalekeza kwamba waone jinsi gani watafanya licha ya hizi fedha tunazopata katika Mfuko wa Barabara lakini wafanya resource mobilization kutoka maeneo mengine. Hivi sasa tuko katika negotiation na wenzetu wa World Bank kuangalia jinsi gani tutafanya kuiwezesha TARURA iweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ni kwa ujumla, tumesikia changamoto mbalimbali kwamba wakati mwingine fedha kutoka maeneo mengine zinakuwa na upungufu hasa katika kuimarisha sekta ya afya na hasa katika miundombinu. Naomba niseme kwamba tumelichukua hili na ndio maana katika maelekezo yetu, tunaenda kuangalia jinsi gani tutafanya, lengo kubwa ni kwamba miundombinu iendelee kujengwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba niwashukuru sana Wabunge; katika haya mapinduzi makubwa, Wabunge wamefanya kazi kubwa sana katika maeneo mbalimbali. Katika ujenzi wa vituo vya afya, tunaona jinsi gani Wabunge wameamua kujipambanua wenyewe kushiriki vya kutosha, hili lazima hansard iweze kunukuu vizuri, kwamba Wabunge wa Bunge hili, wameweza kudiriki kufanya kazi kubwa sana. Nina imani katika ujenzi wa hospitali za wilaya ambao tumeuanza na tunaendelea nao hivi sasa, hospitali 67, lakini mwaka huu wa fedha tena tunaendelea na hospitali 27 kama Naibu wangu alivyosema, naamini tutafika vizuri.

Mheshimiwa Spika, na hata hivyo nafahamu kuna hospitali zipo, lakini hali yake ni mbaya, kwa sababu hata hapa nikisimama nikisema pale Kongwa kwa Spika wangu, hospitali yake ya Wilaya bado tia maji, tia maji. Kwa hiyo ni maeneo ambayo niseme kwamba, japokuwa wengine wanazo hospitali za wilaya, lazima twende tukaziangalie jinsi gani tutazifanya ziweze kutoa huduma vizuri zaidi. Hili ndiyo jambo ambalo tunaenda kufanya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikutoe mashaka kwamba, kuna maeneo mbalimbali tutayapa kipaumbele kwa lengo kubwa la kuona jinsi gani wananchi wetu, wanapata huduma vizuri.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na hoja ya Mbunge wangu, Mbunge wa Tanga nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo lile tumeshalifanyia kazi na barua imeshakwenda kwake kupitia kwa Mkurugenzi, lakini tumemkopi, kama hajaipata, basi tutawasiliana baadaye, lakini kila kitu kiko sawsawa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni, aondoe hofu katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba niseme kwamba naunga mkono hoja za Kamati hizi zote ambazo zimewasilishwa vizuri sana na Wenyeviti wa Kamati. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba mbingu na ardhi kwa kuniwezesha kutoa hoja yangu hapa Bungeni ya hotuba ya Bajeti Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kukupongeza wewe Naibu Spika lakini kumpongeza Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai kwa kazi kubwa mnayofanya. Pia niwashukuru sana Wenyeviti wote wa Kamati za Bunge kwa weledi, ufanisi na kwa kazi kubwa waliyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi kwa nafsi ya moyo wangu napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa kwangu kunipa Wizara hii kubwa ambayo bajeti yake ni zaidi ya asilimia 18 ya bajeti yote ya nchi, Mheshimiwa Rais nakushukuru sana. Nimshukuru Makamu wa Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan, halikadhalika nimshukuru Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa uongozi wake mahiri sana ambao unatuwezesha kufanya kazi zetu kama Mawaziri ambapo yeye anatengeneza timu hiyo kama kiongozi wetu hapa hapa Bungeni na Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru sana Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kwa uongozi wake mahiri akisaidiwa na Mheshimiwa mama Mwanne Mchemba, Makamu Mwenyekiti, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tabora kwa watani wangu Wanyamwezi, nawashukuru sana. Pia naishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na TAMISEMI kwa kazi kubwa waliyofanya katika kipindi hiki chote wakati tunaendelea na mchakato huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Capt. Mkuchika, Waziri pacha mwenzangu katika Ofisi ya Rais, kwa ushirikiano mkubwa aliotupatia. Vilevile niwashukuru Naibu Mawaziri wangu; Mheshimiwa Joseph Kandege na Mheshimiwa Mwita Waitara kwa ushirikiano mkubwa walionipatia. Pia nimshukuru Katibu Mkuu wangu Engineer Nyamhanga na Naibu Makatibu Wakuu wote Tixson Nzunda na dada yangu Dorothy Gwajima. Niwashukuru sana watendaji wote wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ushirikiano mkubwa na dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango lakini Ndugu yangu Dotto James kwa ushirikiano mkubwa sana waliotupatia katika utekelezaji ya bajeti ya mwaka 2018/2019 na katika mpango wetu wa bajeti ya mwaka 2019/2020. Kwa hakika sisi tumejivunia, kwa kweli kazi imeenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jedwali tulilowasilisha hapa, napenda kufanya marekebisho kidogo katika kiambatanisho katika ukurasa 158 hadi 159 kinachohusu ujenzi wa vituo vya afya 52 katika mwaka wa fedha 2019/2020 kama ifuatavyo: Kituo cha Mapera katika Halmashauri ya Mbinga kihamishiwe katika Kituo cha Afya Nangirikiri na Kituo cha Afya cha Kabwe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kihamishiwe kwenda Kituo cha Afya cha Ninde katika Halmashauri hiyohiyo ya Nkasi. Halikadhalika katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Kituo cha Afya cha Ikuna kihamishiwe kwenda Kituo cha Afya cha Kichiwa na katika Halmashauri ya Kasulu TC, Kituo cha Afya Kigadye kiende Heri Juu katika Halmshauri ya Kasulu Mji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Fungu 56 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI limeongezewa shilingi bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambayo inaenda TARURA. Baada ya kusikiliza kilio cha Wabunge humu ndani, Serikali imeona vyema iongeze takribani shilingi bilioni 33 ambayo kwa kiwango kikubwa inaenda kutatua matatizo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hali hiyo, kuna baadhi ya mafungu katika Fungu 56 yatakuwa na mabadiliko. Kwa mfano, kutasomeka shilingi 496,563,123,910 katika Fungu la Maendeleo badala ya shilingi 463,563,123,910. Hivyo, kufanya Fungu 56 katika Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya Kawaida kuwa na shilingi 550,200,093,910. Kwa maana hiyo, bajeti nzima ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI itakuwa na jumla ya shilingi 6,240,992,779,769. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya marekebisho hayo, sasa naomba kuwatambua Waheshimiwa Wabunge 130 waliochangia bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI; wakiwemo Wabunge 86 waliochangia kwa kuzungumza na Wabunge 44 walichangia kwa maandishi. Naomba niwashukuru sana kwamba hoja yangu imechangiwa na Wabunge wengi na hii inanipa ishara kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni eneo ambalo tunapata huduma kwa ujumla wake. Kutokana na maelezo yetu ya kikanuni, naomba majina hayo nisiyasome ila naomba yote yatambuliwe katika Hansard za Bunge kama Waheshimiwa Wabunge walivyochangia kuhakikisha kwamba Ofisi hii inatekeleza vizuri wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika Ofisi yetu ilikumbana na hoja nyingi lakini hoja hizo zimegawanyika katika maeneo yafuatayo: Posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji; kujenga uwezo wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; uchaguzi wa Serikali za Mitaa; mgawanyo wa fedha wa Mfuko wa Barabara zilizotengwa kwenda kwenye Halmashauri (TARURA); ushiriki wa wadau; utekelezaji wa Mradi ya Mabasi yaendayo Haraka lakini ujenzi na ukarabati wa hospitali za halmashauri pamoja na vituo vya afya na zahanati; ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali zetu na vituo vya afya; miundombinu ya elimu; ajira za walimu wetu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; vyanzo vya mapato vya Halmashauri na maeneo mengine kadhaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nishukuru sana michango katika maeneo hayo yote lakini niwashukuru sana Naibu Mawaziri wangu asubuhi waliweza kujibu baadhi ya hoja na wamezitendea haki sana. Niwashukuru sana wapiganaji hawa mahiri sana hasa ndugu yangu Mheshimiwa Waitara na Ndugu yangu Mheshimiwa Kandege, kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, mimi nitaenda kimuktadha, kwa upana mkubwa tu wa Ofisi hii jinsi gani inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo limezungumzwa ni suala la vitambulisho vya wajasiriamali, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa nia yake njema kwa wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwa wakitaabika ambapo sehemu nyingine walikuwa wanakamatwa na Mgambo, wanapigwa virungu na kunyang’anywa vyakula vyao, hali yao ilikuwa ni taabani. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake ya kuwajali Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nimesikia hoja za Wabunge mbalimbali wakisema kwamba inawezekana nia ikawa ni njema lakini utaratibu uliotumika siyo sawasawa. Kwa upande wangu kazi yetu ni kuchukua maoni ya Wabunge baadaye kwenda kuyafanyia kazi jambo ambalo halijakaa vizuri. Lengo ni kwenda kulirekebisha na hasa kuangalia vitambulisho hivi vinatolewa kwa akina nani. Lengo ni kwa wale ambao hawako katika sehemu rasmi sasa wanarasimishwa ili nao waweze kushiriki katika uchumi na mwisho wa siku waweze kupata kipato chao kwa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme eneo hilo inawezekana kweli kuna upungufu lakini hili jambo linatofautiana kutoka eneo moja na lingine. Kwa mfano, ukiangalia maeneo ya Dar es Salaam na maeneo ya miji mara nyingi sana hata kama kuna changamoto siyo kubwa sana. Hata hivyo, tumechukua maoni na ushauri wote wa Waheshimiwa Wabunge ili tukaangalie jinsi ya kuboresha jambo hili ambalo nia yake ni njema lakini lifanyike kwa uzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Naomba nikiri kwamba Wabunge wengi walichangia hapa na Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Bunge na Kamati yake walianza kuchangia kuanzia kwenye Kamati na hapa Bungeni. Vilevile Wabunge mbalimbali walichangia hoja, nawashukuru sana. Hoja hii ilipata michango mingi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Niseme wazi kwamba jambo hili inaonekana lina interest kwa Wabunge wote kuona ni jinsi gani tutaangalia suala za posho za Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi kwamba Madiwani wanafanya kazi kubwa sana, tunapopeleka fedha kule Madiwani kwa kweli wanasimamia kwa karibu zaidi. Hata posho yao kama nilivyosema iliongezwa awali lakini Wabunge wamesema kuna haja ya ku-review hizi posho. Kwa hali ya sasa kwa sababu tunaangalia muktadha wote nini kifanyike, kwa ujumla niseme kwamba tumelichukua wazo hili kwenda kulitafakari zaidi ni jinsi gani tutafanya hawa Waheshimiwa Madiwani kwa siku za usoni angalau kile kipato chao kiweze kuongezeka kwa sababu wanafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo limeonekana ni tete nalo ni la mwongozo wa utoaji wa posho imeonekana kwamba umekuwa ni changamoto kubwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Ofisi yangu imejipanga tutaenda ku-review tena ule mwongozo vizuri na haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni tuweze kubainisha wapi Diwani anatoka kwa mfano ukienda Jimbo la Mbinga kule Diwani mwingine anatoka kama mwezi anakwenda kwene mkutano atafanyaje na maudhui ya kazi wanayofanya. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba jambo hili mimi na wataalam wangu tutali-review vizuri ili Madiwani wetu wasiwe na kinyongo katika utendaji wao wa kazi ili kazi ziweze kufanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kama mnavyofahamu mwaka huu tunatarajia kwenda kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi huu unaongozwa na Katiba yetu, Ibara 144 na 146 imezipa mamlaka Serikali za Mitaa lakini zikatungwa sheria zetu, Sura Na. 287 na 288 ambapo huko tumeenda kuhakikisha uchaguzi huo unasimamiwa katika mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uchaguzi huu unaandaliwa na kanuni, tumeanza kuandaa kanuni,wataalam waliandaa zile kanuni kwa kina na umahiri wa hali ya juu. Pia tuliweza kuwashirikisha wadau mbalimbali kama Wakurugenzi wote wa Halmashauri; Wakuu wa Wilaya; Maafisa; Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Mikoa. Pia tukapanua goli zaidi ikaenda kwa wadau wa kisiasa, tukaenda kufanya mkutano wa siku mbili, tarehe 1 mpaka tarehe 2 kuhakikisha kwamba vyama vya siasa vyenye usajili vinashiriki kutoa maoni yao katika rasimu hii ya kanuni. Naomba nikuhakikishie, mkutano wetu na vyama vya siasa ulikuwa mzuri sana na wadau walishiriki vizuri sana katika kuhakikisha kanuni hizi wanaziboresha na kutoa mapendekezo. Sasa jambo hili lipo katika hatua ya mwisho ya ku-accommodate yale maoni ili kuhakikisha kanuni hizi zinafanya na baadaye kwenda kuzitangaza katika Gazeti la Serikali. Tunatarajia mwishoni mwa mwaka huu tutaenda kufanya uchaguzi wetu, matarajio yetu ni Novemba 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala nzima la utoaji wa mikopo. Nishukuru Naibu Mawaziri wangu wamelizungumzia, ni kweli utoaji wa mikopo umekuwa na changamoto kubwa sana hasa mikopo ya asilimia 10 ya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu. Nilishukuru Bunge hili, katika Finance Bill iliyopita wajumbe hawa walifanya marekebisho ya sheria na ilielekeza mikopo hiyo sasa itolewe kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwamba hapa mwanzoni mikopo ilikuwa inasuasua sana lakini naomba nisiwe mchoyo wa fadhila niishukuru sana Kamati ya Bunge la TAMISEMI na Utawala Bora ilivyokutana na mikoa yote kupitisha bajeti ilikuwa ni hoja mahsusi sana na ilijadiliwa kwa kina zaidi. Naomba nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge ndani ya siku hizi chache za wiki mbili baada ya maelekezo yenu, mwanzo zilikuwa zimetoka karibu shilingi bilioni 13 peke yake leo hii napozungumza mpaka tarehe 30 Machi, zimetoka takribani shilingi bilioni 20.7, haijawahi kutokea ndani ya kipindi kifupi ambayo ni utekelezaji wa lengo takribani asilimia 38.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikujulishe wazi kwamba tulipaswa Ofisi yetu itoe kanuni na kanuni hizo zimeshatoka na zimetoa maelekezo na zimeshatangazwa katika Gazeti la Serikali, hivi sasa ni kwamba ma-accounting officer ambapo Wakurugenzi wetu wa Halmashauri wanawajibu wa ku-comply na kanuni zilizotoka. Waliokuwa wanafuatialia vyombo vya habari siku ya Ijumaa asubuhi nilitoa taarifa kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri wahakikishe ile mikopo yote itakapofika tarehe 28 Juni, takribani asilimia 83.3 ya mikopo ya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu lazima yote iweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini asilimia 83? Ni kwa sababu mwezi Juni wanakuwa bado hawajafunga mahesabu na ndiyo maana nimesema ikifika tarehe 20 Julai, bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 mikopo hiyo inatakiwa itoke kwa asilimia 100. Kanuni ambazo tumezitoa zimewabana ma-Accounting Officer wale watakaoshindwa kupeleka mikopo hiyo kuna utaratibu wa kisheria ambao utaenda kuchukuliwa dhidi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naamini si rahisi kwamba kuna Mkurugenzi ambaye anataka kuingia kikaangoni kwa makusudi kwa kushindwa kutoa mikopo hii ya asilimia 10 ambayo ipo kwa mujibu wa sheria. Naomba nikuhakikishie katika jambo hili tutakuwa wakali sana, hatuna masihara kwa sababu hii ni haki ya vijana ambao wengi wao wamemaliza vyuo vikuu na wamekosa ajira, huu ni mlango mwingine mbadala wa vijana kujiingiza katika suala zima la ajira kuhakikisha wanaenda kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa sana humu ndani na nishukuru sana karibuni Wabunge wote walizungumza ni suala zima la elimu. Tunambiwa kwamba nchi zimegawanyika, kuna nchi zenye rasilimali mbalimbali na nyingine ni masikini zaidi lakini kuna nchi zimewekeza katika elimu. Ndiyo maana leo kuna mifano ya dhahiri kabisa, kuna nchi duniani mfano Switzerland na Nordic Countries ukiangalia rasilimali walizonazo ni chache lakini sasa hivi ndiyo watu ambao wanatawala dunia kiuchumi, ni kwa sababu wamewekeza katika maarifa ya watu. Ndiyo maana binafsi na Ofisi yangu inamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa programu ya Elimu bila Malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi hiki tokea Serikali ya Awamu ya Tano na Mheshimiwa Rais kuelekeza sasa wananchi wa Tanzania wapate elimu bila malipo, upande wa elimu ya msingi peke yake zaidi ya shilingi bilioni 374.3 zimetoka kusaidia elimu msingi bila malipo. Kwa upande wa sekondari zaidi ya shilingi bilioni 479.9 zimetoka kwa ajili ys elimu bila malipo. Jumla kuu ni zaidi ya shilingi bilioni 854.3 ambapo ni fedha nyingi haijawahi kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tukiri wazi watoto wa maskini na voiceless people wamepata msaada mkubwa sana. Tunaona shule zingine zinafurika ni kwa sababu watoto hawa wa maskini zamani walikuwa wanakosa elimu leo dirisha limefunguliwa, kipa katoka, sasa watu wanapata fursa ya kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie miaka ijayo dirisha la kuhakikisha tunajenga uchumi kwa pamoja itakuwa siyo kwa watu wenye uwezo peke yake bali na watoto wa maskini waliofunguliwa dirisha hili sasa tunasema tutajuwana mbele ya safari. Mheshimiwa Rais amenipa wajibu wa kulisimamia eneo hili, kwa kweli tunamshukuru sana kwa programu ya elimu bila malipo ameitendea haki nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la ajira ambalo limezungumziwa na wajumbe mbalimbali. Naomba niseme, Serikali ya Awamu ya Tano kwa lengo la kuangalia changamoto iliyojitokeza mpaka sasa zaidi ya walimu 13,632 waliajiriwa na kuripoti katika shule zetu za msingi na sekondari lakini si muda mrefu tutatoa ajira zingine zaidi ya 4,549 ambazo ziko katika hatua ya mwisho kabisa ambapo tumeshatangaza na watu wameshaomba ambapo jumla ya walimu watakaoingia katika soko la ajira watakuwa ni 18,181. Hii inaonyesha commitment Serikali iliyonayo katika suala hili la ajira na lengo ni kuongeza idadi ya walimu. Naomba nikiri wazi kwamba tutaendelea kuongeza idadi ya walimu ili watoto wetu katika shule zetu waweze kupata elimu bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, hapa juzi juzi aliweza kutoa takriban shilingi bilioni 29.9 kwa lengo la kwenda kumalizia maboma. Waheshimiwa Wabunge hawa ni mashahidi, maboma zaidi ya 3,200 yote yameenda kumaliziwa ukarabati. Siyo hivyo tu, mwezi wa Pili Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya shilingi bilioni 56 hapa. Serikali imetoa fedha hizo, ambapo ukija kuangalia lengo lake ni kwenda kujenga madarasa mapya 934 kwa ajili ya kuongeza madarasa. Vile vile kujenga mabweni mapya 210 ili kuhakikisha kwamba watoto wakiingia Kidato cha Tano waweze kupata mazingira mazuri ya kusomea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaenda kujenga matundu ya vyoo yapatayo 2,141. Hiki ni kipindi tunatarajia kabla ya mwezi wa Sita kazi zote ziwe zimekamilika. Vile vile tutajenga nyumba za walimu, hali kadhalika tunajenga mabwalo yapatayo 76 katika shule zetu. Hii yote ni kazi kubwa kwa lengo kubwa la kuhakikisha kwamba elimu inasonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikujulishe, tayari zimeshatoka shilingi bilioni 16 kwa ajili ya kununua vifaa vya zaidi ya maabara 1,280. Hii ni kazi kubwa. Lengo letu kubwa ni kwamba maabara hizi nazo ziweze kufanya vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, suala la ununuzi wa magari, takribani magari 26 kwa Maafisa Elimu Mikoa, manunuzi yameshafanyika na wiki tatu zilizopita nilitoa siku tisini nataka nione mikoa yote imeshapata magari. Lengo kubwa ni Maafisa wetu wa Elimu waweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika hotuba yangu nilizungumza wazi kwamba investment kubwa inaenda kufanyika hivi sasa katika suala zima la ujenzi wa miundombinu. Kwa mfano, kupitia mpango wa EP4R zaidi ya madarasa 1,200 tunaenda kuyajenga, zaidi ya matundu ya vyoo 3,000 yatajengwa na zaidi ya mabweni mengine ya ziada 300 yatajengwa, zaidi ya vyumba vya madarasa vingine vipatavyo 1,500 vingine mbadala, halikadhalika tutajenga nyumba za walimu na mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imejipanga kuhakikisha kwamba tunaenda kushughulikia changamoto ya kielimu na lengo letu kubwa ni kwamba Serikali inavyojielekeza kwenda katika uchumi wa kati lazima tujiwekeze vizuri katika suala zima la elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali haijalala, inafanya kazi usiku na mchana. Hata hivyo niwahakikishie, mmeona jinsi gani tumefanya mabadiliko makubwa katika ujenzi wa miundombinu katika shule zetu kongwe. Tumemaliza awamu ya kwanza shule 48 ambapo sasa hivi tunaendelea na shule 25 na bajeti ya sasa hivi ina shule 15. Lengo kubwa ni nini? Shule zetu sasa zirudi katika hadhi yake ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge hawa ni mashahidi, hata walipokuja hapa kuapishwa, wakati Mheshimiwa Rais alipokuja kuzindua Bunge hili, shule hata ya Dodoma Sekondari haikuwa hivi. Nenda hapo Dodoma, nenda Bihawana, Kondoa, Mpwapwa, Moshi Tech, Mtwara Tech kokote unakokwenda miundombinu imeboreka kwa kiwango kikubwa. Hii ni ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano. Lengo kubwa, shule zote kongwe zirudi katika ubora wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema shule hizi leo hii naomba na Waheshimiwa Wabunge tembeleeni maeneo yenu mkaone maajabu. Hata wale wa Dar es Salaam, nendeni Pugu Sekondari pale, nendeni Jangwani Sekondari pale, mtakuta maajabu makubwa yamefanywa ndani ya Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimesema bajeti hii ya kwangu sasa hivi ambayo nime-present hapa tunaenda kuboresha shule nyingine 15. Imani yetu ni nini? Tunataka shule zote ambazo zamani zilikuwa maarufu, lazima zirudi katika utaratibu wake ule ili Watanzania waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ajenda nyingine ambayo kwa kiwango kikubwa imejadiliwa hapa, ni suala zima la ujenzi wa miundombinu ya afya. Namshukuru sana Naibu wangu, amezungumza kwa kina katika eneo hili la afya.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa dhati ya moyo wangu, naomba sana nilishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sana tu. Waheshimiwa Wabunge ninyi mnaingia katika historia ya mpya. Nchi yetu ilikuwa na changamoto kubwa sana katika Sekta ya Afya. Siku zote huwa nazungumza, toka Uhuru mpaka Serikali ya Awamu ya Tano tulikuwa na Hospitali za Wilaya 77 peke yake. Vituo vya afya vilivyokuwa na uwezo wa kufanya huduma ya upasuaji, vilikuwa 118 peke yake. Ninyi Waheshimiwa Wabunge mmeingia katika historia, ndani ya kipindi kifupi, vituo vya afya 352 vimeboreshwa, haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi mmemwona Mheshimiwa Rais alivyokuwa Mikoa ya Mtwara na Ruvuma alituzindulia vituo vya afya kule; vya Mbonde, pale Masasi na Kituo cha Afya cha pale Madaba. Hii ni kazi kubwa, haijawahi kutokea. Naomba nirudishe heshima hii kwa Waheshimiwa Wabunge, msingekubali bajeti, vituo hivi visingepita. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika watu nchi hii wataingia katika historia ni Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Kumi na Moja, litaingia katika historia. Pia hamkuwa watu wenye hiana, mwaka 2018 nilileta bajeti hapa kuomba tujenge hospitali mpya 67, ninyi Wabunge mliridhia ikapita shilingi bilioni 100.5 na ujenzi unaendelea huko makwenu. Hii haijawahi kutokea na ujenzi huo unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewapa deadline, yale majengo saba, tarehe 30 mwezi Juni, nataka nione majengo yote yamesimama vizuri. Nilisema mwaka 2018, majengo yale ni kingiambago tu, yaani ni kianzio. Mwaka huu ndiyo maana katika majengo yale yale, Serikali imetenga fedha nyingine kwa ajili ya kuendelea kujenga majengo hayo. Vijana wa Tandale wanasema kampa, kampa tena. Mwanzo mmepata na mwaka huu mmepata tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, Bunge hili limekuja na vituo vingine vya afya na hospitali nyingine za Wilaya 27. Kwa interest ya Bunge hili naomba nivitaje; tunaenda kujenga Hospitali ya Wilaya ya Chalinze, Hospitali ya Wilaya ya Kondoa, tunaenda kuimarisha Hospitali ya Wilaya pale Kongwa, Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe, Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, Hospitali ya Wilaya ya Msimbo, Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, Hospitali ya Wilaya ya Liwale, Hospitali ya Wilaya ya Babati DC, Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa watani wangu Wasukuma, Hospitali ya Wilaya ya Mbeya, Hospitali ya Wilaya ya Kilombero, Hospitali ya Wilaya ya Newala, Hospitali ya Wilaya Kwimba, Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Sumbawanga. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, tunaenda kujenga Hospitali ya Wilaya ya Madaba, Hospitali ya Wilaya ya Msalala, Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Hospitali ya Wilaya ya Tunduma, Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Tabora, Kaliua, Handeni, Mkinga; jamani mnataka nini? (Vigelegele/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana rafiki yangu Mheshimiwa Mwakajoka siku ile alipokuwa anachangia nikasema, Mwakajoka shukuru basi.

NAIBU SPIKA: Nadhani atakuwa ana ndiyo yako leo huyu. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, haitoshi. Lengo letu ni kuhakikisha tunaboresha mazingira haya. Ndugu zangu, sisi tumepewa dhamana kama viongozi. Tutakuja kuulizwa kwa hizi dhamana tulizopewa. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, hata hao wanaosema hapana, siyo mbaya, kwa sababu tunakubali wote bajeti hii kwa pamoja. Hii ni bajeti ya kwenda kuwasaidia wananchi wetu siyo jambo lingine. Bajeti ya watu wasiokuwa na sauti (a voiceless people) bajeti yao ndiyo hii hapa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na jambo la ajenda hapa ya suala zima la ujenzi wa miundombinu. Naishukuru sana Kamati ya Bunge ya TAMISEMI na Utawala Bora, lakini nawashukuru Wabunge, kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wanavyosimamia miradi kule site. TAMISEMI sisi tunasimamia miradi katika maeneo makubwa manne; kuna miradi hii ya TARURA kwa ujumla wake, lakini kuna miradi inayoboresha Jiji la Dar es Salaam, DMDP ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 660.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna miradi ya TSP ambayo ukienda Mbeya unaikuta, Arusha utaikuta, Mwanza utaikuta, Ilemela, ukija Dodoma hapa unaikuta, ukienda Mikindani unaikuta na ukienda hata kwa ndugu yangu Mheshimiwa Zitto Kabwe pale Kigoma Ujiji utaikuta. Lengo la miradi hii ni kuimarisha miundombinu ya barabara. Tunajenga barabara za lami kuweka taa na madampo ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi katika Halmashauri zote za Miji, ndiyo maana leo mnamwona Mheshimiwa Mwanri anasema, ukifika Tabora ni kama umefika Toronto. Hii ni kazi kubwa iliyofanyika. Tunaimarisha Halmashauri zote za Miji na Manispaa. Ndiyo maana leo ukienda Bariadi, mji ni tofauti, Musoma, Tabora, Morogoro, Iringa, Sumbawanga, Mpanda, Korogwe, Moshi, miji ni tofauti. Hii ni kazi inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mwaka huu tutaendelea tena kujenga ujenzi wa madaraja katika maeneo mbalimbali. Nashukuru sana, baada ya kilio cha Waheshimiwa Wabunge tena, zaidi ya shilingi bilioni 33 imeongezeka; hii ni faraja kubwa sana. Nina imani jambo hili linaenda kutatua changamoto zetu katika mamlaka ya Serikali katika Serikali za Mitaa, katika ujenzi wa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie zaidi ya madaraja 113 mwaka huu ambayo tunatarajia kuyajenga chini ya TARURA. Pia kuna makalavati makubwa zaidi ya 273 tutayajenga; na makaravati madogo zaidi ya 2,403 yote tunaenda kuyajenga. Hiyo ni ukiachia mifereji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa inaenda kufanyika katika Jiji la Dar es Salaam. Niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya TAMISEMI walivyoenda kutembelea miradi ya DMDP pale Dar es Salaam, waliona maajabu makubwa katika maeneo ambayo mwanzo yalikuwa yamejishika. Mpaka kaka yangu Mheshimiwa Selasini alipofika pale eneo la Tuangoma alishangaa kuona hawa watu wa Mbagala Kuu na Kijichi walivyounganishwa na watu wa Kibada kwa barabara ya mfano haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nenda Kijichi pale, tembelea hali ni tofauti, nenda Mbagala Kuu, hali tofauti; maeneo ya Makumbusho hali ni tofauti, maeneo ya viwandani hali ni tofauti. Hii kazi lengo lake ni kwenda kubabilisha Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Ndugu zangu, naomba niwaambie, tutaendelea kuimarisha ujenzi wa vituo vya mabasi. Najua tulimaliza kule Korogwe, tumemaliza pale Songea, juzi juzi tumepita Songea lakini tunaimarisha kutokea Songea na maeneo mengine. Lengo letu ni kwamba madampo ya kisasa, magari ya kuzolea taka, lakini kila eneo lazima tuliimarishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine tunaloenda kulifanyia kazi, ni suala zima la ujenzi wa masoko. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, mwaka 2018 niliomba bajeti hapa; ujenzi wa Stendi ya Dodoma, halikadhalika ujenzi wa Soko Kubwa la Dodoma. Wengine walikuwa wananiambia, hii Jafo Power Point Presentation ni kanyaboya? Nikawambia mtaona vitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mnapoenda pale Nane Nane mnakuta stendi ya kisasa na soko la Kisasa linajengwa. Jukumu letu kubwa ni nini? Ni kuhakikisha tunabadilisha miundombinu yetu yote, wananchi wapate faraja kwa utendaji wa umakini wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya Serikali ya Awamu ya Tano. Katika hili mimi sina hiana, ninafahamu wazi Waheshimiwa Wabunge tutaendelea kushirikiana vya kutosha kuhakikisha miradi hii yote inaenda kufanyika kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachia na mambo mengine yote kwa ujumla wake na hasa niwaombe Waheshimiwa Wabunge, ofisi yangu ina watu wengi, kuna suala zima la mahusiano, mkubwa wangu Mheshimiwa Mkuchika hapa atakuja na suala zima la utawala bora; hata hivyo, tunaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa viongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nanyi mnafahamu hali tuliyotoka mwanzo na sasa hivi ni tofauti sana. Mwanzo tulikotoka hali ilikuwa siyo shwari sana, lakini baada ya mafunzo mbalimbali ambayo kupitia Chuo cha Uongozi, mnaona kidogo kwa kiwango kikubwa kama tuna changamoto ambazo tunaweza tukazitaja eneo kwa eneo, lakini kwa kiwango kikubwa sasa hivi kazi inaenda vizuri. Hata hivyo, tutaendelea kuimarisha suala zima la mafunzo na program mbalimbali kwa lengo la kujengeana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tufahamu kwamba watu wengine hawa ni vijana zaidi, sawa eeh, kwa hiyo, lazima kidogo kuna vitu vingine lazima training, tuwe tunapeana mawazo ili kuhakikisha kwamba mambo yanaenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge jamani, msiwanyong’onyeshe watu wanaofanya kazi. Naomba niwaambie, katika ofisi ambayo hailali ni ofisi yangu. Hawa Manaibu wangu, mwangalie Mheshimiwa Waitara huyu, toka ateuliwe hajapumzika. Mwangalie Mheshimiwa Kandege, wanahangaika. Nimewaelekeza wafike kwenu wawasikilize waangalie changamoto. Sasa ikitokea Mbunge hapa anakuja anasema hakuna lolote, inawanyong’onyeza sana hata watendaji wetu. Tufikie wakati angalau tushukuru kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine sitaki kusema tu, kaka yangu hapa alisema sijui TAMISEMI nini, ovyo kabisa. Jamani! Kulikuwa hakuna hospitali ya Wilaya kule, vituo vya afya vitatu vimeenda. Acha ukarabati wa shule na vitu mbalimbali watu wanafanya wanahangaika. Kama kuna magomvi tunashughulikia magomvi kwa magomvi, lakini sio kama unawavunja nguvu watendaji. Afadhali mimi! Mimi nina moyo mgumu, sina shida. Ila mnawapa stress watendaji wangu, hawa wasaidizi wangu. Kusema hakuna kitu TAMISEMI, jamani hii kazi yote kubwa inayofanyika. Watu hawalali kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania. Tu- appreciate kidogo jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema, mimi nina moyo mgumu, sina shida, lakini Serikali inafanya kazi kweli kweli. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, naomba niwaambie, hii ni legacy anaiweka, itadumu kwa miaka mingi. Hata kama mtu hupendi lakini legacy ipo. Haya mambo yote kwa uchache niliyowaelezea, siyo haba, shughuli nzito imefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hii kazi, naomba sana nimshukuru Waziri Mkuu wetu. Waziri Mkuu wetu halali, hapumziki. Wanaopitia vyombo mbalimbali, kila siku Waziri Mkuu yuko katika assignment. Lengo kubwa ni kwamba imani waliyotoa Watanzania kwa Serikali yao ya Awamu ya Tano mambo yaende vizuri, Waziri Mkuu hapumziki. Ningekuwa katika mikutano ya kisiasa ningesema pigeni makofi kwa Waziri Mkuu kidogo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema mnyonge mnyongeni…

WABUNGE FULANI: Haki yake apewe.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inafanyika ndugu zangu, kazi inafanyika na hii inafanyika bila hiana, watu wanahangaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, namkushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kwa kuwa kiongozi mahiri, anatuongoza vizuri. Naomba niseme kwamba Bunge hili na Serikali inaenda kwa utendaji wako chini ya usimamizi wa Dkt. John Pombe Magufuli na mama Samia Suluhu Hassan. (Vigelegele/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu wa kanuni yetu, napenda kuwatambua wote, kwa sababu nikimtaja mmoja mmoja itakuja kuwa sokomoko. Waheshimiwa Wabunge hapa mmechangia vya kutosha katika hoja hii. Hakuna hata mtu mmoja; ndiyo maana nimesema wote kwa sababu utaratibu umewekwa kikanuni, niseme Wabunge wote mmechangia kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo, mmenipa nguvu.

Mheshimia Naibu Spika, naomba niwaambie, ile speed yetu ya mwanzo tuliyokuwa tunafanya, kwa michango yenu, naomba niwaahidi inshaallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, speed ile itakuwa mara mbili zaidi kwa mwaka wa fedha unaokuja. Tunafanya hivi ili Wabunge mfurahi na mfurahi wote. Unajua Mbunge ukifurahi, unaondoa stress. Mambo yakienda huko hakuna shida, una uhakika mambo yako yanaenda yametulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwaambie, sisi jukumu letu ni kutengeneza mazingira. Tutawatengenezea mazingira kutekeleza miradi yote kwa wananchi. Ile inayowezekana yote tutaitekeleza kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Lile tutakaloshindwa kwa hali ya kibinadamu, basi hatuna namna, lakini kwa dhamira yetu inatuelekeza tufanye kila liwezekanalo kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi naomba nishukuru familia yangu kwa malezi mazuri sana; na watoto wangu na wake zangu. Siyo kwamba nina wake wanne, yule mtani wangu katania tu, kachomekea. Watoto wangu nawashukuru sana, ni watoto wasikivu sana, wanani- encourage baba yao kufanya kazi, napata spirit kubwa ya kufanya kazi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana mama yangu mzazi Khadija binti Mwalimu, namwombea sana mzazi wangu baba yangu Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema Peponi alipotangulia mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru wananchi wa Kisarawe, wapiga kura wa Kisarawe wamekuwa wakinivumilia hata wakati niko katika michaka michaka. Kwa kweli nawashukuru sana na wengine wapo humu ndani nawaona wapiga kura kule. Nawashukuru sana, wananipa nguvu. Naomba niwahakikishie kwamba commitment yangu kama kiongozi niliyepewa dhamana, ambapo Mheshimiwa Rais amenipa dhamana, lakini Mungu amenipa dhamana hii kuweza kuwatumikia wananchi, nitajitahidi kwa moyo wangu wote na nguvu zangu zote kutimiza wajibu wangu wote unaotakiwa, nikijua wazi mimi ni binadamu, nina maswali mawili; nina swali la duniani na nina swali siku nitakaporudi mbele ya mikono yake. Mungu anisaidie niendelee kutenda wema huo na kuhakikisha naweza kuwahudumia wananchi wote kwa moyo wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho zaidi nimshukuru Mheshimiwa Rais tena kwa mara nyingine kwa mapenzi yake, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, lakini niwashukuru Mawaziri wote wakiongozwa na Chief Whip wetu hapa dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kazi yao mahiri, dada yangu Mheshimiwa Mhagama halali, hapumziki anafanya kazi kubwa sana, huyu ndiye kiranja wa Mawaziri humu ndani, tunakushuuru sana dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama. Pia niwashukuru Wabunge wote, Wabunge wamekuwa wema kwangu wananipa moyo, hongera sana. Mungu awalipe sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote mbili pamoja na Wajumbe wa Kamati, hakika wamefanya kazi kubwa. Mimi nikiwa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa hakika naomba niipongeze Kamati ya LAAC ambayo binafsi nasema Wajumbe wa Kamati ya LAAC wamesaidia sana ofisi yangu kufanya kazi vizuri. Ushauri wote uliotolewa kwa kipindi chote umeendelea kuimarisha utendaji wa ofisi yangu lakini na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Tunajua kwamba hatuwezi kuwa correct a hundred percent katika muda mfupi, lakini tumejitahidi kwa kadri iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja mbalimbali zilijitokeza hasa katika upande wa suala zima la ukusanyaji wa mapato. Tukumbuke kwamba ukichukua historia tulikotoka nyuma hali ilikuwa mbaya sana na Kamati ya LAAC na Wajumbe huko tulikotoka hali yetu ya mwanzo ilikuwaje. Hata ukifanya reflection ya muda mfupi uliopita wa miaka michache collection yetu ilikuwa haifiki hata 80% kwa mwaka. Katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018, tulifikia 81%. Katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, tumefikia 90% na haya yote ni mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato. Hata hivyo, ushauri wa Kamati ya LAAC na Wajumbe kwa ujumla wake umesaidia, ndio maana katika utekelezaji huo ofisi yangu mwaka huu iliamua kununua PoS takribani 7,227 ambazo tumezigawa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya hivi kwa sababu halmashauri zingine uwezo wake ni mdogo wa kuweza kununua hizi PoS, kwa hiyo nishukuru sisi kama TAMISEMI tutaendelea kutekeleza maagizo yote yanayotolewa kwa lengo kubwa la kuboresha utendaji wa kazi wa Serikali na nia yetu ni kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika vizuri katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Hakika sasa hivi ukiipima Mamlaka ya Serikali za Mitaa ukusanyaji wa mapato umeongezeka na tutaendelea kuhakikisha kwamba ule upungufu wote uliojitokeza kama tulivyonunua PoS na kuweza kuzigawanya katika halmashauri. Pia tunaenda kuzisimamia kwa kuwa hali ya ukusanyaji wa mapato ilikuwa inasuasua, ili sasa tuweze kuliondoa tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lingine ni suala zima la matumizi ya force account. Niseme kwamba tulikotoka huko na sasa ni vitu viwili kidogo tofauti, japokuwa inawezekana kuna upungufu wa hapa na pale, lakini matumizi ya force account yamesaidia sana. Majengo yale tuliyokuwa tunajenga kwa wastani wa shilingi bilioni mbili leo hii kujenga kati ya shilingi milioni 400 mpaka milioni 500, ni mafanikio makubwa na katika hili niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu miradi hii haikujengwa hewani imejengwa katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa na timu yangu ya akina Mheshimiwa Waitara tulivyotembelea maeneo mbalimbali, miradi mingi kwa kweli kwa sababu kulikuwa na specification hata za ununuaji wa materials, bati iwe ya gauge namba ngapi, tofali, mfuko mmoja utoe tofali ngapi, kwa kweli kwa kiwango kikubwa pale wananchi na viongozi nyie mmefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kubeza hata kidogo mafanikio yaliyopatikana katika matumizi ya force account, kwa mfano unaenda mpaka kule ndani kabisa Nyasa utakuta hospitali ya Wilaya imejengwa nzuri kwa quality, lazima tuone kwamba tuna kila sababu ya kujisifu kwa matumizi ya force account. Hata hivyo, niishukuru sana Kamati ya PAC pamoja na Kamati ya LAAC, wote walipata fursa ya kutembelea miradi ya afya katika maeneo mbalimbali. Walijionea hali nzuri, japokuwa kunaonekana kuna upungufu wa hapa na pale na kazi ya Serikali yetu ni kuhakikisha kwamba pale kwenye upungufu tunaenda kuuboresha lakini kwa kiwango kikubwa matumizi ya force account yamesaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na Kamati za Fedha, tuhakikishe kwa pamoja licha ya kuwepo wataalam watakuwepo kule lakini sisi tuna jukumu kubwa sana kuhakikisha hii miradi tunaisimamia kwa karibu kwa kupitia Madiwani wetu kwa lengo kwamba tupate miradi iliyokuwa mizuri na naamini miradi mingi tumepata mafanikio makubwa sana kwa kutumia force account.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba Jiji la Dodoma halina barabara kabisa. Mimi nilikuwepo katika Bunge la Kumi na sasa hivi ni Bunge la Kumi na Moja. Nishukuru kwa hoja ya mama yangu inatusaidia kuhakikisha kwamba tuweze kuongeza juhudi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara. Naomba niwahakikishie kwamba Dodoma katika Miji ukifanya ulinganifu miaka mitano iliyopita na hali ya sasa ni tofauti sana, tunajitahidi kujenga miundombinu katika Jiji la Dodoma na hivi sasa tumekamilisha zaidi ya kilometa 168 ndani ya mtandao wa barabara za lami katika Jiji la Dodoma. Haya ni mafanikio makubwa sana ukilinganisha na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, sasa hivi tumeweka vifaa, tumeshasaini kandarasi ya ujenzi wa kilometa takribani 51 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya lami. Leo hii watu wa Ilazo, watu wa Kikuyu na watu wa maeneo mbalimbali mnafahamu maeneo mliyokuwa mnaishi mwanzo hali ilikuwa mbaya, hali ya mwanzo sio hali ya sasa lakini ushauri unachukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu kubwa yale mapungufu mengine lazima tutayafanyia kazi kwa sababu, hapa ndio makao makuu ya nchi yetu, lazima tuhakikishe tuna speed, tunaongeza juhudi kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa vizuri. Lakini hata hivyo niwahakikishie Jiji la Dodoma litakuwa ni jiji la pekee lenye miundombinu ya barabara za lami ukilinganisha na maeneo mengine hivi sasa kwa kadiri tunavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, agenda nyingine, kulikuwa na hoja, vituo vya afya vipo, lakini vifo vimeongezeka. Wajumbe naomba niwahakikishie, kwa sasa kwa takwimu zetu na wenzetu, Dada yangu hapa Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Wizara ya Afya. Kwa kweli vituo hivi vimesaidia sana kwa kiwango kikubwa, isipokuwa tutaendelea kufanya juhudi kubwa kuviboresha vituo hivi kwa juhudi ya Serikali tuliyofanya kwa ujenzi wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika kuhakikisha vyote vyenye mapungufu hasa ya vifaa tiba na kupeleka wataalam ndio maana hata sasa hivi ninapozungumza kuna watu wengine tayari tunawaajiri kipindi hiki kuhakikisha tunaongeza human resource kule katika maeneo yetu vituo hivi viweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wa wajumbe niseme tunaupokea, lakini hata hivyo Serikali imeshafanya juhudi kubwa na inaendelea kufanya. Lengo letu ni wananchi waendelee kupata huduma nzuri katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja suala zima la mfuko ule wa asilimia 10 ya vijana, akinamama pamoja na walemavu, huko tulikotoka hali ilikuwa mbaya na niishukuru sana Kamati ya LAAC ilipendekeza tufute yale madeni ya nyuma na kweli tulifuta. Na hata hivyo, naomba niwahakikishie kwamba sasa hivi kwa mujibu wa kanuni fedha hizi zinatoka vizuri sana. Kwa mara ya kwanza niliposoma ripoti yangu mwezi Septemba, 2019 zaidi ya shilingi bilioni 47 zilipekekwa katika vikundi hivi ambayo haijawahi kutokea ukilinganisha na miaka yote. Imani yetu ni kwamba, zile halmashauri zenye kulegalega na baadhi ya mapungufu mengine tutaenda kuyafanyia kazi kwa makundi haya yaweze kupata fursa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo, tunashukuru kwa maoni mazuri ya wadau na Wabunge pale wanapotoa maoni, inawezekana kwa mujibu wa kanuni zetu uboreshaje utakuwaje. Tutaendelea kuboresha kanuni ili mradi mifuko hii iweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, agenda ya madai ya Madiwani, wajumbe wa Kamati ya LAAC na Kamati ya TAMISEMI ni mashahidi, juzi nilivyokuwa natoa zile mashine za electronic nilitoa maagizo kwa halmashauri zote zenye madeni wakurugenzi walipe hayo madeni kabla ya Baraza la Madiwani halijavunjwa. Na hata jana nilipokuwa nikizindua Jengo la ALAT nikatoa agizo tena halmashauri zote, wakurugenzi wote wahakikishe madeni ya madiwani wanayodaiwa katika mabenki mbalimbali yaweze kulipwa. Na nimemuagiza Katibu Mkuu wangu TAMISEMI afanye mawasiliano kuona ni akina nani ambao ni changamoto kubwa na jana nilitoa mfano mmojawapo, halmashauri hiyo ni Halmashauri ya Gairo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaambie jukumu letu kubwa TAMISEMI tutaendelea kusimamia maeneo haya yote kuhakikisha Wananchi, hasa Madiwani wetu ambao wamefanya kazi kubwa na nzuri zaidi hakikisha siku ile ya kupata kiinua mgongo chao wasipate mashaka kwamba, fedha zao zinakatwa kwa ajili ya kupelekwa katika maeneo ya mabenki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini agenda ya ujenzi wa masoko, tumelipokea hili, lakini hata hivyo masoko yote tunayojenga hivi sasa tumetoa maelekezo wale wafanyabiashara wa mwanzo wote, hivi sasa nina orodha katika ofisi yangu kuanzia Soko lile la Kisutu, Soko la magomeni, Soko la Morogoro na masoko yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema wafanyabiashara walikuwepo mwanzo wote nipate orodha yao na hivi sasa orodha nimehifadhi pale TAMISEM. Kwamba, wale wafanyabiashara asilia lazima kila aliyetolewa pale soko linapokamilika aweze kupata nafasi ya kufanya biashara. Kwa hiyo, niwahakikishie kwamba, tume-consider mambo haya yote kwa maslahi mapana ya Wananchi wetu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kulikuwa na suala zima la ujenzi wa miundombinu ya barabara, hili naomba nimelichukua katika upande wa TARURA kwa ujumla wake, ushauri umetolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la michango kwamba, watumishi michango inaonekana deni limeongezeka, tumelichukua kwamba, kila linalotolewa kwa wajumbe hapa twende tukalifanyie kazi kwa maslahi mapana ya kuboresha Serikali yetu kwa maslahi mapana ya kuboresha suala zima la wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, binafsi nikiwa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya TAMISEMI niseme nimechukua maoni yote ya wajumbe na Wabunge wote kwenda kuboresha pale maeneo ambayo yanaonekana yana changamoto kubwa tuyafanye yaende vizuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja zote kwa jumla. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mola ambaye ameniwezesha kuweza kuwasilisha hotuba hii hapa. Lakini hali kadhalika kusikiliza hoja za Wabunge, lakini pia kunipa uhai na afya njema. Jambo hilo ni kubwa sana kwangu na hakika Mwenyezi Mungu ahsante sana Mwenyezi Mungu wangu.

Mheshimiwa Spika, ningelipenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kunipa dhamana ya kuhudumu katika Ofisi hii. Lakini nimshukuru Makamu wa Rais, Dkt. Isdor Mpango kwa maelekezo yake. Lakini kubwa zaidi naomba nimshukuru kwa dhati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa, kwa maelekezo yake, Mheshimiwa Majaliwa ni mwalimu, naomba niwaambie kazi yake professional yake ni mwalimu lakini ni mwalimu wa kufundisha kweli kweli, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikushukuru wewe kwa sababu umenipa fursa nimeweza kutoa hoja hapa lakini pia saa hizi kuweza kuhitimisha hoja yangu pamoja na Bunge lako Tukufu nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kupeleka shukrani za dhati kwa wazazi wangu, baba yangu mzee Saidi Ali Jafo Marehemu Mwenyezi Mungu ampatie pepo njema huko alipo lakini mama yangu mzazi Hadija Binti Mwalimu Madega kwa malezi mazuri sana ya kila siku na kuhakikisha kijana wao nafanya kazi kwa uadilifu. Ningelipenda kuchukua fursa hii kuishukuru sana familia yangu, Watoto wangu na Wake zangu wapenzi sana, nawapenda mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua wakati mwingine wananimisi sana...

SPIKA: Jamani makofi haya yawe ya nia njema hayo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA:…lakini kwa ajili ya majukumu ya Taifa letu ili liweze kusonga mbele.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, wangapi?

SPIKA: Na mmoja wa wake zake ni dada yangu, kwa hiyo shemeji yangu huyu bwana. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Naibu wangu Hamad Hassan Chande kwa kazi kubwa ya kushirikiana ambapo tumefanya kazi kubwa kwa pamoja katika kipindi hiki kifupi cha kuhakikisha hotuba hii inafika hapa. Lakini nimshukuru Katibu Mkuu wangu sana Mama yangu Mary Maganga kwa kazi kubwa, Naibu Katibu Mkuu Ndugu yangu Mohamed Abdul Hamis, lakini Professor Esnat ambaye yeye ndiyo Mwenyekiti wetu wa Bodi ya Wakurugenzi katika Baraza la Wahifadhi ya Mazingira, lakini Dkt. Samwel Mafungwa ambaye huyu ni Mtendaji Mkuu wa NEMC.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana watendaji wote katika Ofisi ya Makamu ya Rais kwa kazi kubwa wanayofanya, hakika mmefanya kazi kubwa sana ya kujituma kipindi chote. Nipende kuchukua fursa hii kuwashukuru Kamati zangu za Bunge zile mbili zilizofanya kazi kubwa sana, Kamati ya Sheria na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Lakini niwashukuru Wabunge wote waliochangia hapa ndani kwa michango yao mizuri sana. Wabunge wamekuwa mstari wa mbele kutusaidia sana kutuelekeza na kutushauri mambo mbalimbali hakika Wabunge tunawashukuru sana sana kwa michango yenu mizuri.

Mheshimiwa Spika, hoja yetu hii, nikushuru wewe kwasababu japo muda umekuwa mfupi lakini nimepata Wabunge wachangiaji kwa maneno takribani 26 na mmoja amechangia kwa maandishi. Hii inaonekana kwamba umetumia umahiri mkubwa sana kuhakikisha ndani ya muda mfupi wa Bunge wanapata fursa ya kuweza kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Naibu wangu, ameweza kutoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali hasa katika maeneo ya Muungano. Na hakika niseme kwamba kwa ujumla tumepokea maoni yote ya wajumbe na Wabunge wa Bunge hili. Lakini sisi jukumu letu kubwa sana ni kwenda kutekeleza kwa nguvu zote. Na bahati nzuri naomba niwahahakishie sisi wengine tutakuwa hatulali katika agenda hii.

Mheshimiwa Spika, tutahakikisha eneo la Muungano na Mazingira tunaenda kuweka legacy kama tulivyoweka huko nyuma katika maeneo mengine. Hili ni jukumu letu kubwa tunaenda kulifanya kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeweza kuona kwamba kulikuwa na suala zima la hoja kwamba Hospitali kuna suala zima la mikataba mingine inashindwa kusainiwa, tumeichukua hoja hii lakini naomba niwajulishe kwamba katika ule upande wa Hospitali ya Mnazi Mmoja na Ujenzi wa Barabara ya Chakechake mpaka Wete kule Pemba tayari jambo hili limeshafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwaambie Waheshimiwa Wabunge licha ya haya mawili tayari yameshafanyiwa kazi lakini yote yaliyokuwa pending tutahakikisha na ndio maana nimefanya ziara mara mbili kule Zanzibar tayari kuhakikisha mambo yote yapo pending tunayafanyia kazi. Naomba muwe na imani ya kutosha kwamba tutaenda kuwashughulikia, changamoto zote za Muungano ambazo tunajua kwamba hili jambo litaweza kutatua matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye suala zima la mfuko ule wa TASAF niwashukuru Wabunge wote wa Zanzibar, na juzi juzi nilikuwa natembelea miradi kule Zanzibar hasa miradi ya TASAF kwa kweli Miradi ya TASAF ya Zanzibar imefanya vizuri sana hasa katika upande wa majengo ya shule za sekondari na shule ya msingi. Lakini hali kadhalika vituo vya afya, na jukumu langu kubwa naomba niwahahakishie Wabunge mnaotoka upande wa Zanzibar katika upande wa miradi hii inayoelekea upande wa Zanzibar tutakuja kuisimamia kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Spika, na miongoni mwa ziara yangu nitakuja kuifanya ni kutembelea miradi yote ya Muungano sambamba na miradi yote ya Mifuko ya Jimbo ambayo fedha zimepelekewa kwa ajili mfuko wa Jimbo. Na hili nitaomba Wabunge tushirikiane kwa pamoja nitakapokuja kule nitawajulisha tuweze kukagua miradi yetu ya Mfuko wa Jimbo uliokuwapo upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana katika utekelezaji wa eneo hilo sasa hivi kiwango cha fedha kimeongezeka sasa kutoka shilingi bilioni 12 sasa Zanzibar katika kipindi kinachofuata kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye changamoto itapata takribani shilingi bilioni 36.7. Kwa hiyo, maeneo yote yenye changamoto tutahakikisha kwamba tunaenda kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, zile sheria ndugu yangu ulizozungumza zote kwa kadri iwezekanavyo tutaenda kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima la mfuko wa pamoja ni miongoni mwa kero au changamoto za muungano tutaenda kuzifanyia kazi, kwa hiyo ndugu zangu Wabunge naomba tuwe na subira tu katika maeneo hayo, yote tutaenda kuyafanyia kazi kwa kadri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, na katika upande wa Mazingira niwashukuru sana Wabunge wote mmejadili kwa kina agenda ya mazingira. Na hasa nikushukuru sana ulipozungumza suala zima ya ile mifuko mitatu ambayo ingeweza kutatua changamoto ya kimazingira, ni kweli mifuko hii ipo na bahati nzuri nchi mbalimbali wanatumia fursa hii ya mifuko hii. Wanatumia wanapata mafanikio makubwa sana na nikushukuru sana Mbunge mchango wako mkubwa sana, jambo hili tumelichukua kwa umoja wetu wote tutaenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hata hivyo, juhudi kubwa iliyofanyika mpaka hivi sasa kupitia NEMC na Wizarani hapa tumeshaanza kupata miradi mipya hivi sasa, takribani tumesha- source fedha zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni Ishirini na Sita, Laki Tisa Arobaini na Saba, Mia Sita Arobaini ya Sita ($26, 947,646) hii tayari ni kazi tayari imeshaanza kufanyika. Na nimetoa maelekezo kwa watendaji wangu pale nimewaambia sitaki watendaji wanaokaa bure bure nataka watendaji wanaofanya resource mobilization. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia yetu ni nini? Twende kupambana na suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na eneo hili tutaenda kulifanyia kazi kwa nguvu zote. Na hata hivyo nitaomba sana wenzangu Waziri Wizara ya Fedha kama ulivyosema tutashirikiana kwa karibu. Vile vikwazo vyote ambavyo vilikuwa ni changamoto kwa pamoja kama Serikali tutahakikisha suala zima la fedha zinazoingia basi ziweze kwenda kutekeleza miradi kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge aminini kwamba kipindi hiki tutahakikisha kwamba tunaenda kutekeleza utaratibu mzuri wa kwanza kupatikana fedha, la pili lakini kuhakikisha zile fedha zilizopatikana lazima ziende zikatekeleze Miradi ya Maendeleo. Hili ni jukumu letu kubwa tutaenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, katika suala zima la mabadiliko ya tabia ya nchi tuseme kwamba tumejipanga na hasa maeneo ya fukwe ambayo sehemu zingine zimekatika. Na ndio maana Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kazi pale Dar es Salaam, eneo la barabara ya Barack Obama. Lakini hata hivyo kuna kazi kubwa inayoendelea kufanyika kule Pangani Tanga na maeneo mbalimbali hasa upande wa Zanzibar, ambao tumezungumza wazi kwamba kuna maeneo mengine yanamomonyoka, kwa hiyo ni jukumu letu kubwa kwamba tunahakikisha tunafanya kila liwezekanalo maeneo hasa yenye changamoto ya kimazingira twende tukalishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna yale maeneo ambayo yalizungumzwa wazi kwamba kuna baadhi ya maeneo hasa maeneo ya visiwa, visiwa ambavyo vipo hatarini katika kuzama na hili hatulitarajii ila tunaomba Mwenyezi Mungu atuepushe katika hilo. Kiwango cha maji kimeongezeka kweli katika bahari lakini kupitia Ofisi yetu tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kupitia mifuko hii mitatu jinsi gani tunaweza kupata fedha za kusaidia maeneo yenye changamoto.

Mheshimiwa Spika, hili ndiyo jukumu letu kubwa tutaendelea kulifanya, na hii nipende kusema kwamba ushauri wa kamati kama ulivyoshauri kama kwa ujumla wake tulivyosema kwamba tutajitahidi sana katika kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi maeneo haya yote kwa ujumla wake. Lengo ni kwamba wananchi wa maeneo ya Tanzania yote waweze kupata fursa ya kuona Serikali yao imeweza kuwahudumia kwa kadri ilivyoweza.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna mambo mengi yamejitokeza na mambo haya imeonekana ni suala la elimu. Ni kweli elimu ni changamoto lakini katika maeneo yote mawili, upande wa Muungano kuelewa lakini upande wa Mazingira na ndiyo maana watu waliofuatilia jana tukio la jana tulifanya lile makusudi, lengo letu ni kwamba tuweze kutumia rasilimali chache katika upelekaji wa elimu. Tumeanza mwaka huu tumeweza kutoa elimu katika utaratibu wa makongamano lakini hata hivyo lengo letu kubwa ni kuhakikisha elimu hii tunaianza kuipandikiza kwa Watoto wetu wa shule za msingi na shule za sekondari.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimeelekeza katika Ofisi yetu suala zima la muungano tunaenda kuendesha mashindano ya insha kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari. Na hao wanafunzi watakaofanya vizuri lengo ni tuwape zawadi nzuri. Lengo ni kwamba kupitia insha itasaidia sana kuweka knowledge ya watoto kuelewa suala zima la muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima, mpango kabambe wa agenda ya kuhakikisha kwamba suala la mazingira, Wabunge wote mliojadili suala la mazingira ni kweli tatizo la mazingira ni kubwa mno, lakini jambo hili lazima awareness iwe ya kutosha. Lakini tuwe na jinsi gani mkakati wa kutosha kila mmoja wetu aweze kushiriki, ndiyo maana kupitia Ofisi yetu mwaka huu nimezungumza katika hotuba yangu mnamo tarehe 5 Juni, Tanzania tunaenda kufanya kitu cha kwanza ambacho hakijawahi kufanyika nchini mwetu,hili ni jambo gani? Tunaenda kuya-group yale mambo yote mliyozungumza humu katika jambo moja inaitwa kampeni kabambe ya kimazingira ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kampeni hiyo hatuachi mtu, kampeni hiyo tunaenda kuishindanisha mikoa kwa viashiria vyote tutakavyoviweka. Mifuko ya plastiki, upandaji wa miti, utengenezaji usafi. Kwa hiyo, mikoa yote itashindana. Tutashindanisha Halmashauri za Miji yote, Majiji yote, Halmashauri za Wilaya, tutashindanisha kata mpaka mitaa mpaka vijiji. Na tutataka tuwape Wabunge tuzo, Mbunge ambaye Kijiji chake kilikuwa cha kwanza Tanzania, hii ni kampeni kambambe ambayo tunaenda kuifanya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunaenda kuzishindanisha Wizara zote, Wizara ya Jenista Mhagama na Wizara ya Lukuvi yupi katika eneo lake alitunza mazingira mazuri. Kwa hiyo, Wizara zote zitashindana, Taasisi zote za Serikali zitashindana, Taasisi za, Private Sector zote zitashindana. Hii ni kampeni kambambe. Tunaenda kushindanisha hotel zote kuanzia One Star to Five Star mpaka Guest House ipi ilitunza mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaenda kushindanisha vyuo vikuu vyote Tanzania ni chuo gani kilikuwa the best ndani ya Tanzania katika utunzaji wa mazingvira. Tunaenda kushindanisha vyuo vya kati vyote vilivyoweza kutunza mazingira mazuri, tunaenda kushindanisha shule za Sekondari na Shule za Msingi. Hospitali za Rufaa za Mikoa, za Wilaya, vituo vya afya mpaka nani hii, katika upande huu wa elimu na upande wa afya watakaoshinda tunawapa special bonus.

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Wabunge zile shule za sekondari zitakazoshinda tumekusudia tuwape magari maalum ya shule, shule kumi bora tunaenda kuzitafuta.

Kwa hiyo, Wabunge kazi kwenu tunataka tuwashangilie Wabunge kumi ambao shule zao kumi zimepata magari hapa hapa Bungeni jambo hili tunataka tulifanye, hii ni kampeni kabambe. Lakini tunaenda kushindanisha migodi yote ipi inatililisha maji ya sumu kuharibu afya ya wananchi, kwa hiyo, tunaenda kushindanisha migodi yote na hali kadhalika tunaenda kushindanisha Hifadhi zetu zote. Tunataka tupate Hifadhi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba niwaambie maeneo hayo yote na tutapata zaidi ya washindi 152, washindi hao tutawapeleka kwa ajili ya Local Tourisms tutawafanya kuwapeleka katika hifadhi mojawapo ya kitalii wakiwapo Wabunge maeneo yao waliyoshinda hii yote itakuwa ni special kazi ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kampeni hii tutaenda kufanya jambo lingine kubwa katika kampeni kabambe. Suala zima la upandaji wa miti ya matunda katika taasisi zote tunaenda ku-add value katika agenda ya nutrition katika Taifa letu. Na nimesema hapa wazi kwamba katika zile shule zinazoshinda licha ya upatikanaji wa magari ya shule tutaenda kuwapa suala zima la madawati na vifaa vya kujifundishia katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yote waliyojadili Wabunge haya yapo katika Kampeni Kabambe ya Kimazingira ambayo Tanzania tutaiendesha mpaka 2025 kitaeleweka ndani ya Tanzania. Nini dhamira yetu? Tunataka tuone kwamba wageni wanapokuja waseme Barani Afrika miongoni mwa nchi iliyotunza mazingira ni Tanzania. Tunataka tuthubutu kufanya hivyo. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge haya yote mliojadili ndugu zangu naomba ni, naomba yapo. Na tarehe 5 Juni, tutawaalika Wabunge wote katika suala zima la uzinduzi wa hiyo Kampeni Kabambe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kampeni hii itakuwa na mabalozi maalum wakiwepo na Wabunge, tutawachagua Wabunge wawili, watakuwa mahiri, sijajua ni nani atakuwa, aidha Mheshimiwa Ester Bulaya ama ni nani sijajua ni nani. Hao Wabunge wawili na Mheshimiwa Kunambi pale anapiga debe kwa hiyo tutapata Wabunge wawili hao ni balozi. Lakini tutawachukua vijana wasanii wenye ushawishi mkubwa katika jamii kuwa mabalozi wetu katika suala zima la kampeni ya mazingira. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tutakuwa na watu ambao, watu ambao kutoka Private Sector ambao wanauwanda mpana wa kimazingira kushirikiana na Serikali katika agenda hii moja tunataka tuweke katika East Africa Community Tanzania tunataka tuwe ikiwezekana watu wa mfano tunaopigiwa mfano katika upande wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge hoja zote hizi zote tumezijaza. Mlisema mambo ya NEMC, ni kweli NEMC kidogo ilikuwa ni tatizo lakini nimeanza kazi nao.

Mheshimiwa Spika, leo hii nimekutanisha wawekezaji wote waliokuwa na changamoto na ile inayoitwa TAM (Kibali cha Mazingira), watu wengine mpaka walikuwa wanalia pale wanasema wana miaka mitatu hawajapata kibali. Nimetoa maagizo nikasema haiwezekani shemeji yangu kwa mfano Ndugai anataka akaweke kituo cha mafuta pale Kongwa miezi sita hajapata kibali cha mazingira. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, watu wanapata frustration, watu wanataka kufanya uwekezaji lakini NEMC imekuwa kikwazo. Kwa hiyo, nimetoa maelekezo mahsusi, tumei-categorize miradi, group A na group B, hii yote tunataka tuibadilishe nchi yetu. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hapa halali mtu, ni mkikimkiki mpaka kieleweke. Nataka watu waisome Tanzania ya mfano kwanza upande wa Muungano lakini upande wa mazingira, tunataka tusonge mbele. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mwisho nimshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, mchakato huu wa bajeti katika Wizara hii aliuanza yeye. Naomba nimshukuru sana. Kipekee nimshukuru dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, huyu mama Ndugu zangu anapata taabu sana, kipindi hiki cha Bunge sisemi lakini kama ndiyo nyie wengine mngekuwa mnapiga dash kila siku, kazi yake ni kubwa yuko busy. Hata usiku hawezi kupumzika, naomba nizungumze ukweli. Huyu mama naomba niwaambie, kama kazi hii angepewa Ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma ndani ya siku hizi zote tunazokaa hapa naomba niwaambie katika yale mambo fulani asingeweza kabisa kwa kazi hii. Mheshimiwa Jenista Mwenyezi Mungu akulipe sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo yote, sasa naomba niseme naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha sisi sote kwa usalama na uweza wake kwanza kuturejesha katika Bunge hili tena kwa mara nyingine, lakini kwa kuweza kupitia mjadala huu tokea asubuhi mpaka saa hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa aliyoifanya na mpaka leo hii tumeleta Muswada huu Bungeni ili Waheshimiwa Wabunge waweze kujazia nyama na mwisho wa siku hii declaration iweze kupita rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu wazi kwamba nami nilidiriki katika Bunge la Kumi na hapa ilifika muda kwamba kila mtu alikuwa anasema, kwa nini Serikali mnasema Dodoma na kwa nini Dodoma hamfanyi uwe mji wa Vyuo Vikuu kwa sababu Serikali mmeshindwa kuhamia Dodoma? Leo hii nimeona katika Bunge hili la Kumi na Moja ilani imeelekeza, Mheshimiwa Rais anatekeleza ilani na Mheshimiwa Spika alikuwa akisherehesha hili. Leo hii tumeona kwamba Waheshimiwa Wabunge wote na Serikali kwa ujumla wetu tunapitia mjadala wa Muswada huu ambapo mwisho wa siku tutakuwa tunasema Dodoma ndiyo Makao Makuu yetu rasmi kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote, kwa kiwango kikubwa Muswada huu umechangiwa na Wabunge wengi. Hapa naona kwamba Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa kuongea wako 32 na wale waliochangia kwa maandishi wako watatu. Ukiona ndani ya muda mfupi tumepata sherehe kubwa sana ya Wabunge hivi, hii ni hekima kwamba kila mtu alikuwa na hamu ya jambo hili na mwisho wa siku Wabunge wote wameshiriki, nami nimefurahi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niseme wazi kwamba, nilipokuwa nikiwafuatilia Waheshimiwa Wabunge wote, nilichogundua ni kwamba katika Wabunge wote, kila mtu ana nia njema na Muswada huu na hii kuwa sheria isipokuwa ni maboresho tu ya uchangiaji, na ndiyo sarakasi zenyewe za Bunge, la sivyo Bunge halipendezi. Kwa hiyo, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge katika pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majina ya wachangiaji nitawasilisha kwa Hansard, yatakuwa yamerekodiwa. Niende moja kwa moja katika hoja lakini niwashukuru sana Waheshimiwa Naibu Mawaziri, kwanza walipokuwa wakichangia, pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya kutoa fafanuzi mbalimbali. Nami kazi yangu itakuwa ni ndogo sana kwa sababu mambo mengi sana kwa upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa ufafanuzi katika suala zima la Sheria ya Jiji, sitaki niende tena huko. Kwa upande wa Wabunge wengi sana walijadili hoja mbalimbali zenye kuweka muktadha wa kusaidia kuona jinsi gani sheria hii ina umuhimu sana kwetu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kuna hoja moja kubwa sana ambayo ili-surface ya suala zima la Zanzibar kwamba mbona haikushirikishwa katika hili? Naishukuru kwanza Kamati kwa sababu chini ya Mheshimiwa Rweikiza na Mheshimiwa Mama Mwanne Mchemba na Kamati yote ya Bunge kwa ujumla wake, Mheshimiwa Bobali na watu wote, wameshiriki vya kutosha na tulijaza nyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie kwamba consultation ya maelekezo yenu yote Kamati tuliweza kushirikisha maeneo yote ya Kiserikali, mambo yote yamekuwa mazuri. Kwa hiyo, naomba niwatoe shaka Waheshimiwa Wabunge katika eneo hilo kwamba jambo hili tunalojadili hapa lina baraka zote, wala msiwe na hofu. Hii ni kazi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Serikali ni kusikiliza maelekezo ya Wabunge na Kamati ya Bunge. Naishukuru sana Kamati ya Bunge, bahati nzuri ilifanya diversification ya huu Muswada mara nyingi sana ikashirikisha wadau mbalimbali na siyo maelekezo yao. Ni kweli niseme kwamba tulipata maelekezo nasi tukafanya ushirikishaji wa aina yote. Kwa hiyo, niwatoe shaka Waheshimiwa Wabunge wote kwamba jambo hili ushiriki wake umekwenda vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tupo katika mchakato mwingine wa sheria ya jinsi ya kuendesha Jiji la Dodoma. Sheria hii nadhani itasomwa tena kwa mara ya kwanza siyo muda mrefu sana, ndiyo maana hapa unaona timu ya Naibu wangu, Naibu Waziri wa Muungano vilevile na timu ya Wanasheria, leo hii wanakutana na wenzetu wa Zanzibar kwa upande mwingine wa sheria nyingine. Lengo kubwa ni kwamba jambo la Dodoma sasa liende vizuri wala lisiwe na mashaka ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi kama Watanzania na hasa Waheshimiwa Wabunge ninyi naomba niwaambie, katika watu ambao wataweka legacy ambayo haijawahi kufanywa na mtu yeyote ni ninyi Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili ambao mko humu ndani. Wenzetu wengine wengi walipita humu ndani, walijadili, hata akina Mheshimiwa Mzee Lubeleje walipokuwa katika Ukumbi wa Karimjee pale mwaka 2000 wamejadili jambo hili. Mpaka Mheshimiwa
Lubeleje amekuja hapa, lakini mara hii sasa sheria hii inakuja Bungeni kwa mara ya kwanza, ninyi Waheshimiwa Wabunge mna heshima kubwa sana katika nchi hii kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja mbalimbali zilijadiliwa na hasa kuhusu nini kifanyike katika Jiji la Dodoma. Watu wengine walizungumza wakasema kwa nini sasa tunaelekeza huku tunaacha miundombinu ya afya hakuna? Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, nchi yetu kwa kweli imejielekeza sana na ninyi mnafahamu, katika mambo ya kihistoria ambayo tunayafanya Tanzania kama nchi ni sasa hivi. Ukiangalia Waheshimiwa Wabunge wengine wanasema kwa nini tusijadili Sekta ya Afya? Dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu hapa ni shahidi, anafahamu naye ni custodian wa Sera ya mambo ya Afya; na siku zote tunasema kwamba hata kuhamia Dodoma, hatukuacha uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiiangalia hata Sekta ya Afya katika suala zima la dawa, tumeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mpaka shilingi bilioni 269. Hii maana yake Serikali inafanya kazi kubwa sana. Ujenzi wa miundombinu kihistoroia haijawahi kutokea ndani ya mwaka mmoja kujenga vituo karibu 210 na tunajenga vituo vingine. Hata hivyo, tunajenga hospitali nyingine za Wilaya 67 mpya. Hii ni investment Serikali inafanya, tunahamia Dodoma na tunafanya mambo mengine makubwa ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine walizungumza kwamba mbona miundombinu haiko sawasawa? Bahati nzuri Mheshimiwa Mavunde alizungumza, nami nilikuwa mgeni rasmi hapa, Waheshimiwa Wabunge wakumbuke siku ya tarehe 14 Mei, wakati na-table hapa bajeti yangu nilikuwa nazungumzia Jiji la Dodoma. Wakati natoka mlangoni hapa, mtu mmoja akaniambia Mheshimiwa Jafo, hii sasa nadhani ni comedy, hakuna kitu kama hicho kitakachofanyika. Nilimwambia tutajenga stendi, tutatengeneza soko na tutaweka ring road, Dodoma hii tutaifanya ibadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie, siyo muda mrefu sana, tumesaini mkataba wa shilingi bilioni 77.6, hilo ni eneo moja ambalo tunajenga soko la kisasa na Mheshimiwa Mavunde amesema haliko popote hapa nchini kwetu. Tunajenga stendi ya kisasa yenye ekari 84, hakuna hapa nchini kwetu. Juzi juzi tayari kazi ya ujenzi wa barabara mbalimbali tunazitengeneza. Hata sasa hivi kule Nala tunajenga stendi ya malori ambayo hakuna nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii watu wengine na Waheshimiwa Wabunge mnafahamu, hata hizi taa ambazo mnaona zinakwenda katika uwanja huu wa zamani wa airport tumezihamisha kwa sababu tumejenga pale barabara mpya kupitia TARURA. Kwa hiyo, tuna investment kupitia miradi ya TSP na tuna investment kupitia TARURA. Kwa hiyo, niwatoe shaka, katika Jiji ambalo litakuwa unique ndani ya Tanzania, ni Jiji la Dodoma, hakuna lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tumetoa maelekezo, ni marufuku kujenga kiholela Dodoma, kwa sababu tunataka jiji lenye sura tofauti kwa sababu ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu. Upimaji unaendelea; tumeshapima viwanja zaidi ya 20,000. Sasa hivi tuna mpango wa kupima viwanja vingine zaidi ya 20,000 maeneo ya Mkonze na maeneo mengine kule ndani ndani, maeneo ya Mtumba kule mbele. Tunafanya hivi ili Dodoma iweze kubadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie, hata ujenzi wa nyumba zetu, kwa ajili ya mustakabali wa kuwa na Jiji la Dodoma, tumetoa maelekezo, nanyi Waheshimiwa Wabunge naomba niwasihi, najua mmenunua viwanja. Tunajenga Dodoma kwa sura tofauti. Ukitaka kujenga uliza, bati yako ina rangi gani? Ukijenga kiholela maana yake utapata taabu tena kupiga rangi pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia yetu ni nini? Dodoma itakuwa na ladha tofauti. Kuna ukanda utakuwa na bati ya bluu, kuna ukanda utakuwa na bati nyekundu, kuna ukanda utakuwa na rangi nyingine. Hiyo ndiyo Dodoma mpya, ndiyo Makao Makuu ya Nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika suala zima la kufanya Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali imejipanga vizuri. Niwasihi sana, wakati mwingine kwa sababu najua tuko busy sana tukiwa hapa Dodoma, tutembee maeneo mbalimbali, hata ikiwezekana kuna maeneo mengine hayatembeleki lakini unaweza ukatembea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Waheshimiwa Wabunge, nendeni mkatembee hata dampo japokuwa siyo vizuri kutembelea dampo, lakini unaweza ukaenda dampo, ukawa na chipsi zako unakula. Hii ni unique structure ya Dodoma. Dampo la Dodoma huwezi ukakuta hata inzi mmoja kwa ajili ya maandalizi ya Makao Makuu ya Jiji la Dodoma. Hakuna kitu kama hicho maeneo mengine yoyote. Tunafanya investment ili Dodoma yetu iweze kuwa katika mazingira hayo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine, watu wanasema economic justification; na ndugu yangu hapa Mheshimiwa Bobali alizungumza. Hili linaelezeka. Naomba niwaambie jambo moja, watu tunasahau kuna sayansi ya kimaumbile. Ndiyo maana hata Mungu mara nyingi akituelekeza jambo, anatuambia jambo hili lina manufaa sana kwa watu wenye kutafakari. Sayansi ya maumbile inatuelekeza, jambo lolote linafanikiwa na linakuwa zuri sana endapo linaanzia katikati. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiliangalia yai ambalo kuku anataga, nenda ndani utaangalia utaona nuclear. Hata ukiangalia mboni ya jicho lako ambalo linakupa uwezo kuona ile lens haiwezi ikakaa pembezoni, hiyo ni sayansi ya kimaumbile, Mungu ameumba hivyo. Hata wewe mwanadamu, siku moja chukua tape measure jipime, katikati hapo utaona kumbe ndiyo kuna masuala ya utaratibu wa kibinadamu. Kwa hiyo, habari zozote za kufanya mambo
yabadilike kwa kasi ni sayansi ya maumbile. Naomba niwaaambie, inawezekana wanadamu hatujatafakari hilo kwa kina. Naombeni mkafanye hiyo research ya sayansi ya kimaumbile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linakupa nini? Maana yake linakujuza kwamba kumbe Dodoma kukiwa ndiyo Makao Makuu yetu ambayo tumeelekeza, kutasaidia uchumi chechefu katika maeneo mbalimbali. Leo hii utakuja kuona Miji kama Iringa, Tabora, Singida na mingine, watu kijiografia wataweza kutanuka katika ile multiplication ya uchumi. Ndiyo maana nawaambia ni sayansi ya kimaumbile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa dada yangu ananiwekea maji, nikidondosha tone hapa utakuta maji yanaanza kububujika yanakwenda pembezoni. Maana yake ni kwamba kitu chochote ukikiweka strategically katikati zaidi jambo hilo linapata manufaa mazuri zaidi. Kwa hiyo, naomba niwaambie, nendeni mkatafakari; ukifika usiku tandika kitanda fikiria sayansi ya kimaumbile, utakuja kuona hatujafanya makosa katika jambo hili la kuhakikisha kwamba Dodoma kunakuwa Makao Makuu yetu ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa zilikuwepo hoja mbalimbali lakini jambo kubwa ni kwamba leo hii tumwangalie mkazi wa Kakonko karibu na Burundi. Wakati mwingine anapotaka kupata huduma yoyote kwenda Dar es Salaam akili imwambie anapokuja Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria mkazi wa Mbamba Bay kule Nyasa kwa dada yangu, Mheshimiwa Eng. Manyanya, mwambie ama kwenda Dar es Salaam au kuja Dodoma. Mfikirie mkazi wa Tarime umbali apime kutoka Tarime kwenda Dar es Salaam na kutoka Tarime kuja Dodoma. Hii ndiyo maana nawaambia ni sayansi ya kimaumbile. Tukifanya hivi tutaitendea haki nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie kwamba jambo hili lilikuwa na tafakari ya muda mrefu isipokuwa ninyi Wabunge wa Bunge hili na Mheshimiwa Rais. Ilani ilielezea, sasa tunaenda kufanya maamuzi ya kisheria siyo ya kibabaishaji. Sasa tunatengeneza Sheria ya Makao Mkuu ya nchi yetu, Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niseme kwamba nimefurahi sana kwa sababu nami naingia miongoni mwa watu walioweka historia kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wanavyoweka historia humu. Hawa Waheshimiwa Wabunge watatajwa, Hansard zitasema Bunge la Kumi na Moja, hawa watu ndio pekee waliofanya maamuzi kuliko watu wengine wote kutengeneza sheria. Ni wangapi walipita lakini walishindwa kujadili sheria kama hii? Ni ninyi peke yenu, unique! Ninyi ni watu maalum sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapa ikiwezekana kila mmoja tupige picha pale nje kwa kumbukumbu. Maana mmetengeneza historia ambayo haijawahi kuwekwa na mtu mwingine yeyote, wengi wameshindwa. Rais ameamua, Waheshimiwa Wabunge tumefanya, tunajadili toka asubuhi kwa ajili ya kuhakikisha sasa tunapata Makao Makuu kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru sana. Hoja nyingi zimeshasemwa kuhusu suala zima la upimaji, uchumi na usalama. Ukiangalia usalama wetu Dodoma ikiwa Makao Makuu huwezi ukataka tena justification yoyote, iko wazi kabisa kwamba nchi yetu tunapoweka Makao Makuu hapa Dodoma hali ya kiusalama ikoje?

Kwa hiyo, hivyo viashiria vyote vilitusababisha kama nchi kwa pamoja kuamua, na leo hii sasa tunazungumza suala la kisheria kusema kwamba Dodoma tuiweke kwa mujibu wa sheria kuwa Makao Makuu yetu ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ni ya kiushauri. Niseme kwamba sisi kama Serikali tumeyachukua na hasa suala zima la uwekezaji mkubwa ili mji wetu uendelee kuwa unique wengine waweze kuja Tanzania kujifunza zaidi. Haya kweli yatatokea, kwa sababu tumeshaanza maandalizi yake na yanaenda vizuri. Hata mpango wa bajeti mwaka huu, nenda kasome kitabu changu kile cha Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhusu Dodoma, utaona mambo yote ya uwekezaji kwa ajili ya Dodoma kwamba sasa litakuwa jiji zuri la kisasa na Watanzania tutajivunia na watu wengine watakuja kujifunza kupitia Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi kama nilivyosema yameshajadiliwa, yameshachangiwa. Sasa kwa ufupi zaidi naomba niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu waridhie kwamba Muswada huu uweze kupita kuwa Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muktadha wa kwamba tujenge nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kuunga mkono hoja hii ambayo imeletwa na kaka yangu Mheshimiwa Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango. Kulikuwa na mambo kadhaa yamejitokeza yanayohusu Ofisi ya Rais, TAMISEMI na suala zima la bajeti kwa ujumla na hasa hoja kubwa iligusa suala la TARURA bajeti ni ndogo. Tulijadili hapa kwa kina na niseme wazi kwamba ni kweli, hata hivyo fedha nyingi zilizotengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu zaidi shilingi bilioni 284.7 ambayo kwa imani yangu ni kwamba kwa usimamizi wetu mzuri tutahakikisha tunafanya mabadiliko makubwa.

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara sasa hivi wanapitia ile formula ya 30% kwa 70% kwa lengo kubwa nini kifanyike kuhakikisha kwamba mtandao wa barabara wapo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao unahudumiwa na TARURA ambao takribani kilomita 127 ziweze kuwezeshwa vizuri, zikafanye kazi vizuri. Kwa hiyo naomba niwahakikishe Waheshimiwa Wabunge kwamba, Serikali inafanya kazi hii ndiyo maana mkiona sehemu mbalimbali kazi kubwa inaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa elimu katika bajeti yetu niliyowasilisha hapa ni zaidi ya shilingi bilioni 58.24. Hii ni program ya EP4R kwa ajili shule za sekondari ambayo naona kwamba huko tuna mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika pia Mradi wa Kuboresha Mpango wa Elimu ya Sekondari kupitia SEDP tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 48.99 katika bajeti ya mwaka huu. Hali kadhalika mpango wa EP4R kwa ajili ya shule za msingi tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 31.84 ambayo Waheshimiwa wataona ni kwa jinsi gani tunaenda kuitekeleza mipango hiyo katika mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa afya, naomba tuseme wazi kwamba tunaona juhudi kubwa ya Serikali, tumesikia hoja mbalimbali hapa lakini Serikali imefanya kazi kubwa sana. Ukiachia ujenzi wa hospitali 352 katika bajeti iliyopita, lakini mwaka huu tunaona kwamba tuna ujenzi wa vituo vya afya 352, lakini mwaka huu tuna vituo vya afya tena karibuni 52. Tunaendelea na ujenzi wa hospitali za wilaya 67, lakini hali kadhalika tuna hospitali mpya takribani 27. Kwa hiyo Waheshimiwa wataona katika mpango wa miaka miwili ujenzi wa hospitali 94 kwa mara ya kwanza ni outstanding performance kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo hili lazima tuna kila sababu ya kujisifu kama toka uhuru mpaka 2015 tulikuwa na hospitali 77 peke yake, lakini mpango wa miaka miwili, hospitali 94, tumevunja rekodi ambayo haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba nizungumze wazi, kwa mfano unaona kwamba kila mjumbe alikuwa anazungumza kwamba bajeti hii ilikuwa inajali vitu, mimi niseme kwamba bajeti hii inajali watu. Katika hospitali tulizozijenga kila moja ilikuwa inachukua takribani wataalam ambao wameajiriwa katika eneo siyo chini ya 20. Leo hii tunapozungumza hospitali hizi 97, vituo vya afya 52, ukizizidisha mara 20 unaona jinsi gani watu huko wanaenda kuguswa katika soko la ajira, lakini hata katika utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Spika, katika upande huu wa sekta ya elimu ambayo tuna miundombinu na tunatumia force account, unaona kwamba bajeti hii inaenda kuwagusa watu kwa kiwango kikubwa sana. Ndiyo maana nimesema kuwa bajeti hii ukisema ni ya vitu hapana, bajeti hii kwa ajili ya watu kwa sababu inaenda kutengeneza miundombinu, lakini hali kadhalika inawagusa watu katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba bajeti hii ambayo safari hii imekuja kujibu hasa matatizo ya Watanzania na imani yangu kubwa kwamba sisi Wabunge kwa umoja wetu tunaweka historia kwamba kutengeneza bajeti ya kihistoria ambayo haijawahi kutokea katika miaka hii ya karibuni, inawezekana. Lengo letu kubwa ni tuipe support bajeti hii, tuiunge mkono, halafu katika utekelezaji wa bajeti hii twende tukaisimamie vizuri kwa mustakabali mpana wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ajenda ya mwisho ilikuwa ni suala zima la vitambulisho vya wajasiriamali wadogo. Hili tumepokea changamoto mbalimbali hasa kero zinazotokea kule site, japokuwa maelekezo yalikuwa yamekuwa wazi kwamba lazima mfanyabiashara yule mdogo mauzo yake yasizidi milioni nne. Hata hivyo, katika utekelezaji wa jambo hili kila mtu alitafsiri kivyake, ndiyo maana unaona mikoa mingine imetulia, mikoa mingine ina changamoto. Jukumu letu ni kuangalia wapi kuna matatizo ili tuweze kuyarekebisha na lengo kubwa ni kwamba kila mfanyabiashara ambaye ni mdogo aweze kushiriki vizuri lakini hali kadhalika kutoa kadhia mbalimbali ambazo wananchi wetu zinawakabili.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache kwa sababu dakika zangu ni tano, naomba nikushukuru sana na naomba kuunga mkono bajeti hii kwa asilimia yote mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa mimi, nanyi kuturudisha salama na kutuingiza katika Bunge hili. Hakika Mungu ametufanyia mambo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimshukuru Mheshimiwa Rais kunipa dhamana tena kwa mara nyingine ya kuendelea kuhudumu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Pia niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe na familia yangu kwa ujumla kwa mapenzi makubwa ya kunirudisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge. Mchango wangu ambao nimepewa katika Wizara hii ya wananchi nitaendelea kushirikiana nanyi kutekeleza yale mambo yote mahususi yanayohusu katika maeneo yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 20 Novemba, 2015, Mheshiiwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa speech yake hapa Bungeni. Katika speech aliyotoa ukienda katika eneo la pili, maana baada ya kusema rushwa aliizungumza Ofisi moja inaitwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Katika speech yake alisema hafurahishwi na haridhishwi na mwenendo wa ofisi hii katika suala zima la usimamizi wa miradi isiyotekelezwa ndani ya muda, ukusanyaji wa mapato na mambo mengine ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yanamnyong’onyesha Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na niwashukuru Wabunge wote katika kutekeleza speech ya Bunge ile ya kuzindua Bunge la Kumi na Moja kipindi kile nikiwa nimepewa dhamana kuhakikisha kwamba, TAMISEMI inahusika na ujenzi wa zahanati, hospitali za wilaya na halikadhalika vituo vya afya. Kutekeleza hotuba ile tulitoka katika vituo 115 vyenye uwezo wa kufanya huduma ya upasuaji mpaka tumefika vituo 487, ni rekodi ya kwanza tumeiweka. tumetoka hospitali za wilaya 77, leo hii tunakamilisha hospitali 102 mpya ndani ya miaka mitano, lakini tumejenga zahanati zetu 1,198. Katika upande wa afya tunasema eneo tulilopewa Mamlaka ya Serikali za Mitaa tumejitahidi kutimiza wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya pili hii sasa ya ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili Mheshimiwa Rais alikazania tena katika suala zima la huduma ya afya, afya iweze kuimarika na hususan afya zetu za msingi. Katika eneo hili tumejipanga ndugu zangu. Kama tumeweka rekodi miaka mitano iliyopita Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tumeazimia kwenda kuvunja rekodi ya kwetu sisi wenyewe na Waheshimiwa Wabunge naomba niwahakikishie tutapambana kila liwezekanalo kuhakikisha tunamaliza changamoto za wananchi wetu katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nimewaita Wakurugenzi wote wa Halmashauri ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania upande wa Tanzania Bara na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya. Katika mwaka wa fedha unaokuja na niwaombe sana Wabunge ninyi mkiwa Wajumbe wa Baraza la Madiwani na Kamati za Fedha, tunaenda kuweka rekodi ya kwanza ya ujenzi wa vituo vya afya visivyopungua 185 ambavyo vituo hivi ni matumizi ya own source kabla hatujapata top up kutoka Serikali Kuu, hii inakuwa ni rekodi ya kwanza tunaenda kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwaambie Wabunge tumeshaazimia kikao cha leo na Wakurugenzi wote, kuna halmashauri zitajenga kituo cha afya kimoja, zenye bajeti ya kuanzia bilioni moja mpaka bilioni tano. Kuna halmashauri zitajenga vituo viwili kwa own source zenye bajeti kuanzia bilioni tano mpaka 12, lakini kuna halmashauri zitakazojenga zaidi ya vituo vitatu zenye bajeti kuanzia bilioni 12 na kuendelea. Tutapata zaidi ya vituo 185 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ambayo hizi ni fedha za mapato ya ndani kabla hatujaingia katika fedha za Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyozungumziwa ni kuhusu suala zima la TARURA hapa, tumelisikia sana. Mnafahamu tumefanya kazi kubwa miaka mitano japo resource zilikuwa chache, lakini Serikali tunaendelea kulifanyia kazi hili na nishukuru sana Bodi ya Mfuko wa Barabara, hivi sasa wanapitia ile formula kuangalia jinsi gani formula ikae vizuri kwa lengo la kuisaidia TARURA ifanye kazi vizuri. Ndugu zangu Wabunge, naomba tuwe na Subira timu inafanya kazi tutapata majawabu kabla mpango wa bajeti haujafika tutakuwa katika sura nzuri ya kuhakikisha jinsi gani TARURA inafanya kazi yake vizuri, lakini hiyo ikienda sambamba na kufanya resource mobilization, kutafuta vyanzo vingine vya kuisaidia TARURA ifanye kazi vizuri, hii ondoeni shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upande wa elimu ambayo tumepewa mamlaka ya kuhakikisha kwamba, elimu ya msingi tunaisimamia, tunaanza shule za awali mpaka kidato cha sita. Miaka mitano hii tulifanya kazi kubwa, ukiangalia shule kongwe kati ya shule 89 tumekamilisha shule 86 mpaka hivi sasa. Ninyi Wabunge ndio mashahidi, maeneo mlikotoka shule kongwe zilikuwa zimechakaa sana zimechoka, leo hii kazitazame tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 89 katika shule kongwe peke yake, lakini tunaenda kufanya kazi kubwa ya ujenzi wa miundombinu katika mpango wetu wa ujenzi wa shule za kata 1,000 ambao tunatumia zaidi ya shilingi trilioni 1.2 ndani ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda kujenga zile shule 26 za wasichana, lakini tutahakikisha kata zote 718 ambazo hazina sekondari za kata, Wabunge naomba niambieni, tunajenga sekondari kata zote ndani ya Tanzania. Tunaenda kusimamia program ya elimu bila malipo ambayo kila mwezi sasa inatumika hivi sasa shilingi bilioni 24. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda katika mradi mwingine unaitwa TACTIC katika suala zima la kuboresha miji yetu. umefanya vizuri ndani ya miaka mitano. Halmashauri zenu zote zenye manispaa na halmashauri za miji leo hii mkienda mnashangaa, tumejenga barabara nzuri, kuweka taa za barabarani, kujenga na madampo sehemu nyingine, miaka mitano inayokuja ni miaka ya funga kazi ndugu zangu Wabunge. Tunaenda kushughulika na mradi wa TACTICS katika miji 45, tunataka Watanzania walioondoka Tanzania 2010 wakirudi 2025 wapotee miji yao wasiweze kuifahamu.

Hii ndio kazi kubwa tunayoenda kuifanya. Katika eneo hilo ndugu zangu Wabunge naomba niwahakikishie hatutanii na hii miaka mitano ni miaka ya mchakamchaka miaka ya kazi. Naomba niwaambie Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Serikali kwa ujumla itatoa ushirikiano wa kutosha mambo yaende sawasawa bila kikwazo cha aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na issue ya suala zima la mikopo ya akinamama, vijana na wenye ulemavu. Tunaenda vizuri, tumenza awamu ya kwanza kutengeneza sheria na juzijuzi nimeshasaini mabadiliko ya kanuni kuhakikisha akinamama na wenye ulemavu waweze kupata fursa nzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda umeniishia, nilishukuru sana Bunge hili, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza sana mtoa hoja, AG wetu katika Muswada huu wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali. Pia yangu ni mafupi.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuunga mkono hoja hii iliyowasilishwa hapa. Pia ni wazi kwamba sheria hii inagusa sehemu ya Property Tax ambapo nami tuna eneo ambalo tunalisimamia. Kikubwa zaidi, napenda kumshukuru sana AG kwa hii kazi kubwa ambayo ameifanya kwa kuleta Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, pili, kwa sababu nasimamia Mamlaka ya Serikali ya Mitaa na ninajua kila jambo tunalofanya, lengo letu ni kwa ajili ya kuhakikisha tunaipeleka nchi yetu mbele. Kikubwa, naishukuru sana Wizara ya Fedha kwa ujumla. Katika kipindi hiki cha sasa ambacho mwanzo kidogo kulikuwa na changamoto kubwa sana katika Bunge letu kuhusu mambo ya Property Tax, ikionekana kwamba imeleta hali mbaya sana hasa katika sehemu za Miji.

Mheshimiwa Spika, kwa ushahidi wa karibu, kwanza naishukuru sana Serikali hasa Wizara ya Fedha, katika kipindi cha Awamu ya Kwanza mwezi Nne mwaka 2018 iliweza kutoa takribani shilingi bilioni 131.6 kwa ajili ya miradi mikakati ambayo imekuja katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Katika hizo, juzi nilikuwa naongea na wenzangu wa Manispaa ya Kinondoni na wengine kwamba Kinondoni mpaka hivi sasa wamepokea zaidi ya shilingi bilioni 32 katika miradi ya mikakati. Hata Property Tax wangekusanya, hailingani na fedha walizopewa wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Ilala, ukiangalia Machinjio ya Vingunguti, Soko la Kisutu linalojengwa pale hivi sasa imechukua zaidi ya shilingi bilioni 20. Jiji la Dar es Salaam wamepata takribani shilingi bilioni 50. Hizi zote ni kwa ajili ya miradi mikakati. Manispaa ya Moshi wamepata takribani shilingi bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya Moshi pale Mjini, ambayo hata ile Property Tax wangekusanya isingefika kiasi hicho. Juzi tulianza kwa ndugu yangu Mheshimiwa Mch. Msigwa pale, zaidi ya shilingi bilioni moja, sasa tutaenda kuimarisha machinjio ya pale Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa zaidi, ukiangalia trend ya kwanza, upatikanaji wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 131; safari hii, juzi tu, katika Mkutano wa juzi PST alikuwa na timu ya wataalam katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, imetoka zaidi ya shilingi bilioni 137. Hii ni trend nzuri.

Mheshimiwa Spika, kikubwa zaidi nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane kwa pamoja. Lengo letu ni kwamba sheria hizi zikipita, lakini kwa pamoja tukiwa na lengo moja la kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele; na hasa pale penye upungufu Waheshimiwa Wabunge wanaposhauri, tuchukue vizuri, itasaidia nchi yetu hii kuweza kusonga mbele.

Mheshimiwa Spika, kikubwa zaidi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuishauri Serikali kwa wema kwa kujua kwamba ushauri huu unaotolewa katika njia moja au nyingine, unaenda kuimarisha Mamlaka za Serikali zetu za Mitaa, kuimarisha Serikali yetu kwa ujumla na mwisho siku tuweze kupata mabadiliko makubwa kwa ajili ya nchi yetu hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache, kuna jambo moja ambalo Mheshimiwa Bobali alizungumza kuhusu Halmashauri zetu, nadhani hili limezungumzwa katika kifungu cha 10 ambacho ukiangalia amendment kimefafanuliwa vizuri na AG wetu hapa. Nadhani jambo hilo limekuwa addressed vizuri kuhusu wapi eneo katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya inaenda kukusanya.

Mheshimiwa Spika, otherwise, namshukuru sana AG na ninaomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)