Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Risala Said Kabongo (25 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na shule za ufundi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Shule ya Ufundi Moshi (Moshi Technical School), shule hii ya ufundi ilikuwa ikitoa elimu ya ufundi kwa wanafunzi kutoka mikoa mingi Tanzania na baada ya masomo ya elimu ya sekondari wanafunzi hawa walijiunga na Vyuo vya Arusha Technical na Dar Technical pamoja na Ifunda Tech. Kwa sasa shule hizi za ufundi zina hali mbaya sana hasa Shule ya Ufundi Moshi; majengo yamechakaa sana vifaa vya ufundi vingi vimekufa na hivyo umuhimu wa shule hii kama ya ufundi, inaendelea kushusha taaluma za ufundi katika nchi yetu na hasa kipindi hiki ambacho tunakwenda kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda ambao unategemea nguvukazi kubwa ya vijana waliopitia taaluma ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri anapohitimisha aniambie ametenga bajeti kiasi gani kwa ajili ya kuimarisha shule za ufundi Tanzania. Hii itasaidia sana vijana wetu ambao wamekuwa wakikosa ajira baada ya kumaliza shule na kujiunga kwenye vitendo visivyo na tija kwa Taifa ambapo wangekuwa na utaalam wa ufundi mbalimbali wangeweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakaguzi wa shule. Kumekuwa na changamoto kubwa kwa wakaguzi wa shule ambao wengine wamepewa magari ya kuzungukia na kukagua shule, lakini tatizo la magari hayo wakati mwingine yanakosa bajeti za mafuta ya kuwawezesha wakaguzi kufanya kazi zao kwa ufanisi. Naomba kujua kuwa Waziri amejipanga vipi kuhusiana na changamoto hii na atalitatuaje kupitia bajeti yake ya 2016/2017 ili kuhakikisha wakaguzi wanapata fursa ya kufikia kwenye shule zote nchini na kufanya ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa shule. Uboreshaji wa shule za msingi na sekondari uangaliwe kwa karibu ili kuongeza tija, shule zetu ni chakavu sana, huduma za madarasa, vyoo havifai kwenye shule zetu, hakuna viwanja vya michezo, madawati, nyumba za Walimu. Pamoja na changamoto zote hizo, tatizo la vitabu ni kubwa sana, naomba Waziri anapohitimisha atuambie amejipangaje kwa bajeti yake ili kuweka sera za kusaidia huduma shuleni kupunguza gharama kubwa kwa wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mishahara ya Walimu. Mishahara ya Walimu ni midogo sana ukilinganisha na kazi kubwa anayoifanya Mwalimu. Naomba Waziri aangalie ni namna gani anaweza kuangalia upya suala la mishahara ili kuwapa motisha Walimu wetu. Hali ya maisha imepanda sana, hivyo kupelekea Walimu kushindwa kujikita katika ufundishaji na kujiingiza katika biashara ndogondogo baada ya vipindi vya darasani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia suala la elimu kwa watumishi waliopo kazini. Kumekuwa na wafanyakazi ambao wamekuwa wakifanyia kazi idara mbalimbali kwa muda mrefu na baadaye kutaka kujiendeleza kutokana na uzoefu wao wa kazi wanazozifanya. Wanapotaka kujiendeleza wanaambiwa cheti cha form four, ambacho pengine wakati huo hakikuwa kizuri ila amekuwa mzoefu wa kazi hata kwa miaka zaidi ya 10. Naomba Waziri anapohitimisha atuambie ni namna gani anaweza kutengeneza mfumo wa elimu ya juu kwa watumishi wa umma wanaohitaji kujiendeleza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara ya Nishati na Madini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la ukataji wa miti na kuvamia mapori kwa ajili ya uchomaji wa mkaa baada ya ujangili wa wanyama sasa ni ujangili wa misitu. Namtaka Waziri atoe majibu ni namna gani Serikali hii kupitia Wizara hii imejipanga kuzuia au kupunguza matumizi ya mkaa hasa mijini ambako kuna nishati mbadala ya gesi na soko kubwa la mkaa limeelekezwa huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukataji wa miti kwenye mapori umeendelea kusababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha mafuriko sehemu kubwa nchini. Mafuriko haya yanatokana na ukataji wa miti ambayo huzuia kingo za mito na hivyo kusababisha mafuriko makubwa. Namtaka Waziri atoe majibu ya kina ni namna gani amejipanga kuokoa misitu kwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, namtaka Waziri atoe majibu ni kwa namna gani Serikali imeweka mkakati wa kudhibiti wachakachuaji wa mafuta ya magari ili kuondokana na adha ya uharibifu wa magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashuhudia matumizi ya solar kama umeme mbadala maeneo mengi nchini na hasa mijini. Namtaka Waziri anipe majibu ni kwa namna gani zinaweza kusaidia wananchi wa vijijini ili watumie nishati hii kwa wingi kwa kuuza solar kwa bei nafuu kwenye maduka ya Serikali ili wananchi wengi wafaidike na nishati hii. Naomba Waziri anipatie majibu haya kwa faida ya wananchi wetu wa vijijini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia hoja iliyopo mezani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya ujenzi wa nyumba, mfano Shirika la Nyumba (NHC) nyumba zao ni gharama kubwa sana kuanzia shilingi milioni 50 mpaka milioni 270 na kuendelea. Nyumba hizi kimsingi hazimnufaishi Mtanzania wa kawaida mwenye kipato cha chini. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapunguza gharama hizi ambazo kimsingi zinatokana na Serikali kutokuchangia gharama za miundombinu kama barabara, maji na umeme, gharama ambazo sasa zinatolewa na NHC kupitia mikopo ya ujenzi wa nyumba hizi, hali inayosababisha gharama ya ujenzi kuwa kubwa sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na miundombinu hii kumekuwa na suala la VAT ya asilimia 18 katika kununua nyumba hizi ambazo kimsingi VAT zimelipwa kwenye vifaa vya ujenzi. Ninaitaka Serikali itoe tamko kupitia Wizara hii ni lini itatoa VAT hizi kwa nyumba zote za Shirika la Nyumba ambalo ndilo mkombozi wa Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo mikopo ya magari, ningeshauri Serikali itoe mikopo ya nyumba za NHC kwa watumishi ili waweze kukatwa fedha kiasi. Hii itaondoa hali ngumu za wastaafu wetu ambazo wanapata baada ya kustaafu katika utumishi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Ardhi imekuwa ikifanya kazi bila kuwa na bajeti. Tatizo la Tume hii inafanya kazi ya kuangalia eneo baada ya shughuli kubwa ya upimaji. Ningeshauri kama Tume hii itaendelea kuwepo ipewe bajeti ya kutosha na itoe ushauri kabla ya eneo kupimwa. Ninaitaka Serikali itoe majibu ya kina kuhusiana na Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, ninaitaka Serikali itoe tamko kuhusu wananchi wanaovamia vyanzo vya maji (waliopo ndani ya mita 60) ambazo wanatakiwa kuondoka. Mfano mzuri ni vyanzo vya maji vilivyopo Mkoa wa Arusha ambako kuna tatizo kubwa la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya maziko hasa ya mijini yamekuwa na changamoto kubwa sana. Ninamtaka Waziri anipe majibu kuwa Wizara yake imejipangaje kukabiliana na tatizo hili la maziko katika maeneo ya miji kama Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Kilimanjaro ambazo ardhi ni changamoto kubwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bomoa bomoa ninamtaka Waziri aniambie Serikali imejipangaje katika kulipa fidia kwa wananchi hawa ambao wanaendelea kubomolewa nyumba zao na fidia zinazotolewa haziendani na hali halisi ya gharama za ujenzi wa nyumba? Ni kwa namna gani wananchi hawa watafidiwa kulingana na hali halisi ya maisha ya leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ambayo inachangia Pato kubwa la Taifa. Kwanza kabisa nipende kuipongeza hotuba nzuri ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchango wangu mimi nitajikita kwenye suala zima la utalii. Tunapozungumzia utalii nitazungumzia mambo matatu muhimu ili tuwe na utalii endelevu. Ili tuwe na utalii endelevu tunahitaji vivutio vya utalii, ili tuwe na utalii endelevu tunahitaji namna ya kufikia vivutio hivyo, tunahitaji malazi ya kuwalaza wageni wetu wanapofika kwenye vivutio vya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala la vivutio vya utalii. Nchi yetu ya Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na vivutio vyenye ubora wa hali ya juu ukilinganisha baada ya nchi ya Brazil. Lakini cha kusikitisha sana pamoja na kwamba Wizara hii inachangia asilimia kubwa kwenye Pato la Taifa, kwa mfano nikiangalia asilimia 17.5 inachangia Pato la Taifa kupitia Utalii, lakini asilimia 4.8 inatoka kwenye misitu, asilimia 25 ya Pato la Taifa kupitia fedha za kigeni zinatoka kwenye suala zima la utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nashangaa sana tunaona kitakwimu mapato haya ni makubwa lakini ukilinganisha na vivutio tulivyonavyo bado tunahitaji kuwekeza nguvu kubwa sana kwenye suala la kuboresha utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vivutio tulivyonavyo bado tunapata mapato kidogo sana, lakini tunapata watalii wachache sana ambao wanatembelea vivutio vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imejaa mambo mengi imejaa mipango mingi; lakini niseme ukweli tusiporekebisha changamoto za miundombinu, hasa miundombinu ya barabara bado suala la utalii tutakuwa tunaimba kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu na barabara ni changamoto kubwa hasa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Magharibi na Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ukitaka kuwekeza katika Mikoa ya Kusini, Mikoa ya Magharibi na Mikoa ya Kanda ya Ziwa utakumbana na suala zima la changamoto ya barabara. Gharama zinakuwa ni kubwa sana kwa wageni wetu wanaotembelea hifadhi zetu na maeneo yetu ya utalii hii ni kwa sababu ya changamoto za barabara. Wawekezaji wengi wanashindwa kuwekeza katika sekta ya utalii ni kwa sababu ya changamoto ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto nyingine kubwa ni ya viwanja vya ndege. Tuna viwanja vya ndege vya kimataifa vya Kilimanjaro, Dar es Salaam, lakini sasa tuna uwanja wa ndege wa Songwe. Uwanja wa ndege wa Songwe ambao tunategemea ndio utakuza utalii wa Kusini hauwezi kufanya kazi peke yake usiposhirikiana na viwanja vidogo kwa mfano kiwanja a Iringa, kiwanja cha Katavi ambacho a ndege zinazokwenda kwenye hifadhi ile ya Katavi zinaweza kutua kule; hatuwezi kukuza utalii wa mikoa hii kama hatuwezi kuimarisha hivi viwanja vya ndege. Nikisema hapa leo gharama ya kutoka Dar es Salaam mpaka kwenye hifadhi ya Ruaha na kurudi ni karibu dola 700, (shilingi 1,400,000).
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni mtalii gani au mwekezaji gani anaweza kuwekeza kwenye utalii kwa gharama zote hizi? Ni mtalii gani wa ndani ambaye anaweza akatoka mfano Mkoa wa Iringa kwenda Hifadhi ya Ruaha kwa kulipa 800,000 kwa usafiri wa gari? Tutakuwa tunaimba utalii wa ndani, tutakuwa tunaimba uwekezaji lakini hatutoweza kuwekeza kama miundombinu hii haitafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala zima la malazi. Suala la malazi ni changamoto kubwa, niwapongeze wawekezaji wa Mkoa wa Arusha ambao wao wameweza kuwekeza zaidi pia kwenye masuala ya hoteli. Hoteli nyingi zilizopo katika Mkoa wa Arusha zina hadhi za hoteli ya kitalii. Lakini hoteli hizi zinazidiwa wakati wa high season watalii wanalazimika kwenda kulala nchi jirani, wanalala Nairobi ni kwa sababu hoteli hizi hazitoshi, lakini pia hoteli zetu zilizojengwa kwenye mikoa yetu ya Nyanda za Juu Kusini mfano Mikoa ya Iringa, Mbeya, Mikoa ya Magharibi, Mikoa ya Kanda ya Ziwa bado ni changamoto kubwa kwa wageni wanaotembelea maeneo hayo. Kwanza huduma zinazotolewa kwenye hoteli zile ni huduma duni ambazo haziendani na hadhi ya huduma ambazo wageni wetu wanatarajia. (Makofi)
Vilevile ningependa kutoa ushauri kwa Serikali, watoe masharti nafuu kwa wawekezaji hawa mnaotaka kuwekeza katika sekta ya utalii, kuwekeza kwenye tour operators. Kwa mfano mwekezaji anataka kuwekeza Kusini unatofautishaje mwekezaji wa Kusini na mwekezaji wa Kaskazini, kwanza mwekezaji wa Kusini ana changamoto ambazo nimezitaja, vivutio vile viko mbalimbali, barabara ni mbovu, lakini pia mwekezaji huyu hajavutiwa. Wizara haijampa mwekezzaji huyu ya yeye kuwekeza katika mikoa hii ya Kusini. Kwa mfano ukiwekeza katika suala zima la utalii, la tour operator unatakiwa kulipa dola 2,000 na sijui kwa nini ni dola kwa Mtanzania mimi nilitegemea labda watalipa Tanzania shillings lakini analipa dola, dola 2000 kuwekeza tour operator.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu tour operator anahitaji kulipa TRA, anahitaji kulipa SUMATRA malipo yamekuwa ni mengi. Lakini huyu tour operator nitamtofautishaje na tour operator anayekuja kuwekeza Kusini? Wanaokuja kuwekeza Kusini, Mikoa ya Magharibi na Mikoa ya Kanda ya Ziwa wapunguziwe angalau ifike hata dola 1000 ili waweze kuvutiwa kuja kuwekeza katika mikoa ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiboresha maeneo haya ya uwekezaji, mahoteli yetu, tour operator, tunaweza pia tukatoa ajira nyingi sana kwa wazawa ambao wengi wamemaliza vyuo. Kwa mfano Chuo cha Taifa cha Utalii kimetoa wanafunzi wengi wa certificate pamoja na diploma tangu mwaka 2006, lakini wanafunzi hawa hawajaajiriwa, hawana ajira hata kwenye Wizara.
Kwa hiyo, ningeomba pia Waziri anapokuja kuhitimisha hapa atuambie pia ni ajira ngapi zimetoka kwa wanafunzi hawa waliomaliza katika chuo hiki kama ilivyo Mweka na Pasiansi?. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningependa kuongelea suala pia la Maafisa Utalii katika mikoa yetu. Ninaomba Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na TAMISEMI iangalie namna ambavyo itaweza kuajiri Maafisa Utalii kwenye mikoa yetu, wilaya zetu, lakini pia kwenye halmashauri. Hii itasaidia sana kuibua vivutio mbalimbali vilivyoko kwenye mikoa yetu kwa kushirikiana na wataalam. Vilevile itasaidia kuondoa umaskini kwa wananchi wanaozunguka katika maeneo yanayozunguka hifadhi zetu au maeneo yetu ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanaoishi kwenye maeneo hayo wamekuwa ni maskini kwa sababu hawana namna ya kutumia vile vituo vyao bila miongozo ya hawa maafisa utalii. Ukiangalia suala zima la utalii wa kitamaduni, utalii huu sasa hivi umepotea hauthaminiwi, lakini ukiangalia nchi nyingi zimekuwa zikitumia utalii wa kitamaduni kuweza kunufaisha wananchi wanaozunguka karibu na maeneo ya hifadhi, wamekuwa wakitumia tamaduni zao, wamekuwa wakitumia taaluma zao kwa mfano wengine wamekuwa ni wachoraji na wameweza kufaidika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siungi…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nichangie Wizara hii ya Mambo ya Nje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua Serikali inawatumiaje Mabalozi waliopo nje ya nchi katika kutangaza nchi yetu kwa maana ya ushiriki katika majukwaa ya kiuchumi. Mfano sekta ya utalii inachangia pato la Taifa kutokana na fedha za kigeni takribani asilimia 25. Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha naomba aniambie wana mpango gani wa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza Tanzania ili kuendana na kasi ya kukua kwa uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya Mabalozi hawajui vizuri nchi na vivutio vilivyopo. Ofisi za Mabalozi hazina wataalam wa utalii ambao wanaweza kuitangaza nchi yetu kupitia Balozi zetu. Naomba Mheshimiwa Waziri anipe majibu wana mpango gani kuwa na Maafisa wa Utalii katika Balozi zetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu ni namna gani wanafunzi wanaosoma nje ya nchi wanapata misaada kupitia Balozi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2017/2018 ni uhuishwaji wa viwanda nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda haviwezi kuwa endelevu kama hakutakuwa na malighafi ambazo kimsingi zinatokana na kilimo. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba bila kuwa na mapinduzi ya kilimo ndoto ya Tanzania ya viwanda haitafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu kilimo chetu bado ni duni sana kuweza kuzalisha malighafi za kulisha viwanda hivyo vinavyokusudiwa. Hivi karibuni nimetembelea Mkoa wa Songwe, wakulima wanapata shida sana kutokana na ukosefu wa pembejeo za kilimo na zile chache zinazotolewa kwa mfumo wa vocha na mawakala zinakuwa za urasimu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kwa mapendekezo ya Mpango huu wa 2017/2018 iweke bajeti ya kufanya tathmini ya idadi ya wakulima ili pembejeo zinazotolewa ziendane na idadi ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ya mazao ya wakulima hayaeleweki, naomba Waziri atuambie kwa mpango huu wa 2017/2018 Serikali imejipangaje kufungua masoko ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika. Kumekuwa na changamoto nyingi sana kwenye suala la afya nchini, kwa mfano Hospitali ya Wilaya ya Vwawa inayotegemewa na Mkoa mzima wa Songwe ina upungufu mkubwa wa madawa, Madaktari na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya ziara kuangalia huduma ya mama na mtoto, wanawake 14,695, sawa na wanawake 15 – 20 kwa siku wanajifungulia hapo. Wagonjwa 150 – 200 wanahudumiwa kama outpatient kila siku katika hospitali ya Wilaya. Huku idadi ya Madaktari wakiwa watatu na uhitaji ni Madaktari 23. Sambamba na watumishi 507 na uhitaji ni watumishi 1,112. Watoto wa umri wa miaka 0 – 28 wanafariki kwa siku na kupelekea idadi yao kuwa 180 kwa takwimu za 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri anahitimisha aniambie kwa mpango huu wa 2017/2018 wana mkakati gani wa kupandisha hadhi hospitali ya Wilaya ya Vwawa kuwa hospitali ya mkoa ili kuwa na bajeti ya kutosha kukabiliana na changamoto katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako majengo yaliyoachwa na wakandarasi waliojenga barabara ya Sumbawanga – Tunduma ambayo yapo kilomita tatu kutoka Tunduma Mjini eneo la Chipaka na Serikali ilitoa commitment ya kufanya majengo yale kuwa hospitali ya Wilaya naomba commitment hiyo iwekwe kwenye mpango ili kusaidia kupunguza tatizo la huduma za afya, ukizingatia kwamba Tunduma ni mpakani na watu wanaohitaji huduma ya afya ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la Black market. Soko hili lipo ndani ya mpaka wa Zambia na wafanyabiashara wengi, zaidi ya 1000, wa upande wa Tanzania wanafanya biashara zao katika mpaka huo; hii inasababisha ukosefu wa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kufahamu je, katika mpango huu wa 2017/2018, Serikali imeweka utaratibu gani wa kuwarudisha wafanyakazi katika eneo la Tanzania ili kuongeza mapato katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Binafsi nitoe pole kwa misiba iliyolipata Bunge letu kwa kipindi cha mwaka huu. Kipekee nikushukuru kwa upendo wako kwa Wabunge hata tunapokuwa na matatizo unakuwa mstari wa mbele kutusaidia. Naomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu mahali pema peponi. Mheshimiwa Sitta, Mheshimiwa Hafidh na Mheshimiwa Dr. Elly Macha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuungana na Wabunge wenzangu katika kuangalia changamoto mbalimbali za miundombinu ya maeneo mbalimbali katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na Mkoa wangu wa Songwe ambao ni mkoa mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto za barabara katika Mkoa wa Songwe, mfano, barabara inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Momba inayoanzia Chapwa, kupitia Vijiji vya Nanole, Chiwezi, Msambatu, Chindi, Msagao hadi Chitete. Naomba Waziri anapohitimisha aniambie ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya barabara hii ili kusaidia maendeleo ya Mkoa mpya wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imepitiwa na barabara kuu ya Tanzania kwenda Zambia kwa takribani urefu wa kilometa 50 kati ya eneo la Doma na Mikumi na kwamba barabara hii ilianzishwa kabla ya mwaka 1964 kabla Hifadhi ya Taifa ya Mikumi haijatangazwa. Wakati barabara hii haijawekwa lami, magari yalikuwa machache na yalipita kwa mwendo mdogo. Baada ya barabara kuwekwa lami magari yaliongezeka sambamba na mwendokasi hivyo kusababisha ajali na vifo vingi vya binadamu na wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto hizo, TANAPA mwaka 1999 waliainisha na kujenga matuta maeneo yenye mapito ya wanyama. Jumla ya matuta 12 yalijengwa na alama za barabarani kuwekwa katika kilometa 50 zilizo za hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizokusanywa na TANROAD mwaka 2012 katika kituo cha Doma zilionesha kuwa kulikuwa na magari 1,750 kwa siku yanayopita katika barabara hii ambayo asilimia 60 yalikuwa ni magari ya mizigo na mabasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina hii ya magari ndiyo inayosababisha ajali za kuwagonga wanyama. Hifadhi kwa kushirikiana na TAWIRI mwaka 2014 walihesabu na kubaini idadi ya magari imeongezeka na kuwa 1,991 kwa siku. Matokeo ya utafiti 2014 yanaonesha ifikapo 2025 gari
zinazopita hifadhi zitakuwa 4,699 kwa siku. Idadi hiyo ya magari ni kubwa sana kuweza kuimudu kwa siku hivyo, ni lazima tuchukue hatua madhubuti kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua mikakati ya Serikali kwa bajeti hii ya 2017/2018 kuhusu ujenzi wa barabara mbadala ya Melela – Kilosa – Mikumi yenye urefu wa kilometa 141.78 ili kupunguza idadi ya magari yanayopita katika hifadhi na kuokoa uwepo wa Hifadhi ya Mikumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Afya ni kigezo kimojawapo katika maisha ya mwanadamu. Hivyo basi, sekta ya afya ni muhimu sana katika mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa UKIMWI kwa akina mama ambao wamejifungua salama, kumekuwa na uhaba wa dawa kwa akina mama wajawazito na waliojifungua salama. Mfano, mama mjamzito anachukua dawa hospitali ya Vwawa na anaishi Usangu. Baada ya kupata mtoto na mtoto kufikisha miaka miwili mama anatakiwa kurudi kituo chake cha kwanza ili kuendelea na dawa. Ikifika wakati wa kurudi hospitali ya awali mama anaacha kwenda kuchukua dawa kwa sababu mbalimbali. Kwa mfano, umbali wa vituo vya afya vya kuchukulia dawa, gharama za usafiri, majukumu ya malezi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya msingi kwa Wizara ni kwa nini Wizara isiweke mpango wa kutoa dawa kwenye ngazi ya zahanati zilizoko karibu na wananchi ili kuendelea kuokoa nguvukazi hii ya Taifa letu. Mfano, mtu anatoka Ichesa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Vwawa kilometa 45 hadi 50, barabara ya vumbi na usafiri wa bodaboda. Hii inasabishia watumiaji wa dawa kuacha dawa na kuendelea kuwa na madhara yatokanayo na magonjwa nyemelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto za vifaa tiba kwenye hospitali zetu, bado wajawazito wanatakiwa kuwa na vifaa vya kujifungulia. Mfano gloves, code tie inayotumika kufunga kitovu cha mtoto anapozaliwa, pamba na gauze. Je, Waziri anatusaidiaje kwenye suala la vifaa hivi kwa wanawake wanaojifungua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa aina ya folic acid kwa wajawazito bado zimekuwa adimu sana kwenye hospitali zetu, badala ya kutolewa bure mama mjamzito analazimika kununua kwenye maduka ya dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie kuhusiano na upungufu wa Madaktari Bingwa kwenye hospitali zetu za rufaa sambamba na wakalimani wanaotumia lugha za alama kwa walemavu wanaokwenda kutibiwa katika hospitali zetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Nitaanza na suala la utamaduni katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, lugha ya Kiswahili inapewa kipaumbele cha juu katika nchi yetu, ni jambo jema. Ila napenda kuonesha hisia zangu katika Wizara hii kwa mustakabali wa Taifa hili kwa kuwa lugha ya Kiingereza imekuwa ikitumika maeneo mengi katika Serikali yetu, mfano interviews za kuomba kazi hufanywa kwa lugha ya Kiingereza, hotuba na mawasiliano mengi hufanywa kwa lugha ya Kiingereza, ukienda kwenye suala la biashara za kimataifa kati ya nchi na nchi kwa wafanyabiashara wetu na wa nje hufanywa kwa lugha ya Kiingereza.

Mheshimiwa Spika, kwa ushauri wangu ningeomba pamoja na kutumia Kiswahili, bado nchi yetu haijaweza kujitegemea kama nchi za Kichina wanavyoweza kutumia lugha yao ya ndani. Hivyo basi, kwa kuwa bado tunategemeana na nchi nyingine kiuchumi, bado tunahitaji kufundisha lugha za Kiswahili na Kiingereza katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, michezo; kwa kutambua umuhimu wa michezo katika Taifa letu, kuwa michezo ni afya, ajira, mahusiano na pia kutangaza Taifa letu kitalii, bado tuko nyuma sana kwa kutumia michezo yetu kwa manufaa ya Taifa hili. Nashauri Wizara kuwa na Sports Academy kila kanda kwa nchi yetu ili kuweza kuinua vipaji vya vijana wetu mpaka kwenye ngazi za chini.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze wadau mbalimbali kwa kutumia michezo kupeleka ujumbe wa jamii, lakini kama Wizara, tunaomba michezo itumike vizuri katika kuitangaza nchi yetu lakini pia kupinga vitendo mbalimbali vya kurudisha nyuma maendeleo ya nchi, mfano, kupinga ujangili wa tembo kupitia michezo, kupinga utumiaji wa dawa za kulevya na kupinga ndoa za utotoni na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, michezo kupitia utalii. Michezo ni kiunganishi kikubwa cha nchi na nchi kupitia vivutio vya utalii wetu. Nasema hivyo kwa sababu leo ukitaja Timu ya Arsenal unataja nchi ya Uingereza. Kwa Taifa letu bado hatujafika kuwa na Timu ya Taifa ambayo inaweza kuitangaza nchi yetu kiutalii. Hata Serengeti Boys ambayo inabeba jina kubwa la Hifadhi ya Serengeti, haijaweza kutangaza hifadhi yetu hata kwa hadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, naomba kushauri Wizara kuwasaidia vijana wenye vipaji vya michezo ili kuitangaza nchi yetu. Limekuwa ni jambo la kawaida kuona mchezaji amejitahidi na kufika kiwango kikubwa ndiyo Wizara inamtambua. Nashauri vipaji vya vijana wetu vianzie shule za msingi ili waweze kusaidiwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni nimehudhuria Kilimanjaro Marathon, Mkoa wa Kilimanjaro na nilikimbia mbio za kilometa tano, kilichoniumiza ni kuona washindi waliopatikana ni kutoka nchi ya jirani ya Kenya. Hii inanipa tabu sana hata kutangaza Mlima Kilimanjaro kupitia mashindano hayo muhimu.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali kupitia Wizara ijifunze kuanzisha mashindano kama haya ambayo kwa sasa yanafanywa na wadau ili kuweza kuandaa vijana wetu mapema, hasa kutumia Jeshi letu ambalo pia lina nidhamu na vijana wengi. Vilevile, kama tunavyojua michezo ni ajira, tunaweza kuajiri vijana wengi kupitia michezo. Hii itarudisha nidhamu ya michezo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, taasisi nyingi za Serikali ziliajiri wanamichezo wengi kuwa watumishi, mfano mzuri ni TANAPA, iliajiri watumishi wengi wanamichezo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu katika nchi yetu. Kwanza, niipongeze hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo imetolewa na Waziri Kivuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitazungumzia Hifadhi ya Mikumi ambayo imepitiwa na barabara kuu ya Tanzania – Zambia yenye urefu wa kilomita 50 ambayo ilianzishwa mwaka 1964 kabla ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Barabara hii imekuwa na ongezeko la magari mwaka hadi mwaka. Kwa takwimu za mwaka 2012 idadi ya magari yalikuwa yanapita katika hifadhi ni 1,750 sawa na asilimia 60 ambayo yalikuwa yakipita kwenye kilomita 50 ndani ya hifadhi. Mwaka 2014 magari yaliongezeka hadi kufikia 1,991 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili ni kubwa na maoteo yanaonesha ifikapo mwaka 2025 magari yanayopita katika Hifadhi ya Mikumi yanaweza kufika 4,699 kitu ambacho ni hatari sana kwa kukua kwa Hifadhi ya Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madhara ya kiikolojia ambayo yanaweza kutokea kwa magari hayo kupita ndani ya hifadhi. Pamoja na madhara hayo ya kiikolojia kuna ajali nyingi zinatokea ikiwa ni pamoja na vifo vya wanyama na binadamu. Kumekuwa na ajali nyingi, nina takwimu kidogo hapa za mwaka 2011 - 2015. Nikiangalia katika takwimu zangu zinaonesha mwaka 2011 idadi ya vifo vya wanyama ilikuwa 125 katika Hifadhi ya Mikumi lakini 2012 idadi ya wanyama waliogongwa ni 111, mwaka 2013 ni wanyama 132, mwaka 2014 ni wanyama 354 na mwaka 2015 ni wanyama 237.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa wale wanyama tu ambao wanaonekana barabarani lakini wanyama wengine wanagongwa wanaenda kufia ndani ya hifadhi. Kwa idadi hiyo kubwa ni lazima hatua zichukuliwe. Barabara hii imekuwa ni changamoto kubwa na hatua zisipochukuliwa basi tunaweza kupoteza uhai wa Hifadhi ya Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa Wizara. Wizara ya Maliasili na Utalii wanaweza kukaa na Wizara ya Miundombinu ili waangalie namna gani ya kuboresha barabara ya Melela – Kilosa - Mikumi yenye urefu wa kilomita 141.75 kwa kiwango cha lami ili tuweze kupunguza idadi ya magari ambayo yanapita ndani ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kitu kingine ninachoweza kuishauri Wizara ni kufanya utafiti kwa nchi nyingine ambazo barabara zinapita ndani ya hifadhi na tunaweza kuona namna gani wao wanafanya na tuweze ku-implement kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kwa TANAPA kama wanaweza kutoa tozo za magari yanayopita hifadhini yaani kutoza magari badala ya abiria ili tuweze kupata mapato yanayotokana na magari yanayopita hifadhini wakati tukiendelea kufanya tafiti mbalimbali kwenye nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato yanayopotea kutokana na magari kupita kwenye barabara ya Mikumi ni makubwa sana. Tafiti za mwaka 2012 zinaonyesha hifadhi inapoteza shilingi bilioni 4.7 kwa tozo za abiria lakini Serikali inapoteza shilingi bilioni 1.4 kwa tozo kwa ajili ya magari. Kwa hiyo, ukiangalia ni fedha nyingi sana kama Wizara tungeweza kuzingatia kutoza hizi tozo basi tungeweza kupata mapato mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke kwenye barabara ya Mikumi, niingie kwenye kimondo ambacho kipo Wilaya ya Mbozi katika Mkoa wa Songwe. Katika Mkoa wangu wa Songwe kuna kitu kinaitwa kimondo, sidhani kama Wabunge wengi wanakifahamu labda kwa kukisikia lakini ni kivutio pekee sana kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Kivutio hicho kina changamoto nyingi sana na kinasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Ukiangalia miundombinu katika kivutio kile hairidhishi, majengo ya Ofisi ni chakavu sana, kimondo kile hakina uzio ili kusaidia ukusanyaji wa mapato lakini pia vyoo haviridhishi hivyo kusababisha wageni wengi kutofika katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka katika mchango wangu uliopita nilisema kwamba eneo lile liboreshwe hata tuweze kuweka camp site ambazo wasafiri wanaokwenda nchi za Malawi na Zambia wanaweza kufanya camping katika eneo lile na tukaweza kuongeza mapato. Kwa hiyo, nashauri Wizara itenge fedha kwa ajili ya miundombinu ya eneo la kimondo ili kuweza kuvutia wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono hoja ya kupunguza tozo kwenye biashara za utalii. Tozo zimekuwa nyingi sana kwenye Wizara hii na wafanyabiashara wengi wanakwama kutokana na tozo. Vilevile pamoja na tozo hizi hakuna one stop center ya kulipia hizi tozo ili wafanyabishara waweze kufanya biashara zao kwa urahisi. Hii inasababisha hata uwekezaji wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupungua sana na kusababisha wawekezaji kushindwa kuja kuwekeza katika mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo utalii wa utamaduni na utalii wa fukwe. Utalii wa utamaduni umekuwa ni kivutio kikubwa sana kwa wageni wanaotembelea kwenye maeneo yetu ya uhifadhi. Unapotoka kwenye maeneo ya hifadhi, wageni wengi wamekuwa wakilazimika kwenda kwenye maeneo ya vijiji ili kuona utalii wa kitamaduni lakini utalii huu haujaboreshwa vizuri, hivyo huwafanya wageni wengi kutofurahia aina hii ya utalii wa utamaduni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna utalii wa fukwe, fukwe zetu nyingi bado hazijaboreshwa, sio nzuri, hazivutii. Kwa hiyo, tumekuwa tuna tatizo kubwa la wageni kutumia fukwe zetu, ni chafu, takataka ni nyingi, zinanuka na hazina huduma nzuri. Kwa hiyo, nadhani Wizara ijikite katika utalii huu ambao pia wageni wengi sasa wanapochoka kuangalia wanyama wanapenda kuona utalii wa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia hili suala la hawa wanaokwenda kufanya field kwenye hoteli za kitalii. Kumekuwa na changamoto kubwa sana ya vijana wetu kwenda kufanya field, imekuwa sasa ni mtindo wa kawaida kwa watu wenye hoteli kuwatumia vijana hawa kwa idadi kubwa kuwafanyia kazi na baadaye kutokuwapa ajira. Imekuwa kama ni kawaida kwa wao kupewa kazi za field wanapomaliza wanachukua watu wengine lakini ukiangalia idadi ya watu wanaofanya field na idadi ya waajiriwa ni ndogo na kuwafanya vijana hawa kukata tamaa, kulipwa fedha kidogo na wengine hawalipwi wanaambiwa ni field. Kwa hiyo, vijana wetu hawa wamekuwa wakitumika sana kwenye hoteli hizi za kitalii.

Mheshimiwa Mwenyekti, kwa hiyo, naomba Wizara ije na sera au mpango wa kuona ni namna gani hawa vijana wanapomaliza vyuo wanapokwenda kwenye field, wangapi wanaajiriwa na wangapi wanaondoka. Kwa sababu inakuwa kama ni mtindo sasa wao kutumika tu kuwapatia faida wale ambao wana hoteli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani na nashauri muichukue na kuifanyia kazi. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara hii ya Afya. Kwanza kabisa natambua jitihada za Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kusimamia afya ya mama na mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwa akinamama ambao wana matatizo ya kupata ujauzito. Tatizo hili ni kubwa sana hapa nchini na linasababisha unyanyapaa pamoja na ndoa nyingi kuvunjika. Waathirika wakubwa wa tatizo hili ni wanaume na wanawake lakini inakuja kutokea kwamba wanawake ndiyo wanakuwa wanabeba tatizo hili. Kwa hiyo, namwomba Waziri aendelee kusimamia jambo hili ili wanawake wapunguziwe suala hili la unyanyapaa unaotokana na matatizo unaotokana na matatizo ya kupata ujauzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Dar IVF clinic ambayo ni clinic inayotoa matibabu kwa akinamama hawa wanaoshindwa kupata ujauzito; hospitali hii imekuwa ikisaidia sana wanawake wanaoshindwa kupata ujauzito na wanawake wawili mpaka watatu wanahudumiwa kwa siku. Tunaweza kusema kwamba wanawake zaidi ya 50 wanahudumiwa matatizo haya ya kupata ujauzito kwa maana ya kupandikizwa watoto au kusaidiwa njia mbalimbali za kupata uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za matibabu ni kubwa sana kwenye suala hili. Mwanamke au familia inaingia kwenye gharama ya dola 7,000 au 8,000 hadi dola 10,000 kwa mwanamke kupata matibabau haya. Familia nyingi zinauza rasilimali lakini pia zinaingia katika mikopo kuingia katika kusaidia wanawake hawa kupata ujauzito. Ushauri wangu kwa Serikali ili kupunguza gharama hizi kwa familia dawa zinazotoka nje ili kusaidia wanawake hawa kupata ujauzito zina gharama kubwa, lakini pia nataka kuishauri Serikali pamoja na Wizara hii kuondoa kodi kwenye dawa hizi ili ziweze kupatikana kwa urahisi, lakini pia kuondoa vizuizi vingi vinavyoambatana na uingizwaji wa dawa hizi ili tuweze kusaidia wanawake hawa na kuondoa urasimu pia ambao unapelekea dawa hizi kuchelewa kuingia nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kushauri Wizara ya Afya kusaidia dawa hizi kama zinaweza zipatikana kwenye MSD ili tuweze kuzipata kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuishauri Wizara ni Madaktari Wataalam, kama ilivyofanywa kwenye Taasisi ya Moyo kupandikiza Figo tunaomba Wizara itafute hawa wataalam ambao wanaweza kusaidia zoezi hili kwenye hospitali zetu za rufaa ili tuweze kusaidia wanawake hawa kupata ujauzito kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mhesimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu, nataka pia Wizara ione namna gani tunaweza kutoa elimu kwa jamii ili kuona tatizo hili siyo la wanawake pake yao bali na wanaume pia wanahusika. Hii litasaidia sana kuondoa unyanyapaa kwa wanawake ambao wanashindwa kupata ujauzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie pia kwa kumpongeza Waziri wa Afya na Naibu wake tena kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, lakini niwaombe kwenye zile zahanati zetu kwenye maeneo ambayo tunatoka kwenye Majimbo yetu, kwenye Mikoa yetu ziboreshwe kuna tatizo kubwa sana la maji kwenye zahanati zetu. Tunaomba namna ambavyo tunakarabati zahanati zetu tuweke gata ili kuweza kuvuna maji ya mvua na itasaidia sana kuweza kupata maji katika zahanati zetu na watu waweze kujifungua kwa usalama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa dakika tano hizi ningependa kujikita kwenye makundi matatu yanayotoa huduma katika Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, kuna makundi matatu yanayotoa huduma katika Mlima Kilimanjaro, kuna waongoza watalii, wapagazi na wapishi. Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ni hifadhi maarufu duniani lakini hifadhi hii ni moja ya maajabu saba ya dunia. Ni hifadhi yenye urefu wa mita 5,895. Vilevile hifadhi hii ina wageni wengi wanaotembelea kuliko Watanzania. Nikiangalia nina takwimu hapa mwaka 2013/2014 wageni wa nje walikuwa 35,682 na wa ndani walikuwa 2,021 lakini mwaka 2016/2017 walifika wageni 45,818 na wageni wa ndani walikuwa 2,723 tunaona tofauti ilivyo kubwa.

Mheshimiwa Spika, waongoza watalii, wapishi na wapagazi wamekuwa ndiyo engine ya kupandisha wageni katika Mlima Kilimanjaro na wapagazi hawa wanapandisha Mlima kwa mwaka wakiwa na idadi ya zaidi ya 30,000 lakini kwa muda mrefu waongoza watalii hawa wamekuwa hawapati stahiki zao kama inavyopaswa. Watu hawa wamekuwa wakionekana kwamba hawana elimu wala hawana ujuzi wa kutosha, lakini ndiyo wanaofanya kazi kubwa sana, wakikosekana basi hakuna mgeni anayeweza kupanda Mlima Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo basi ninaiomba Serikali itambue kuwa waongoza watalii ni kazi ya kitaalamu na ya kitaaluma inayostahili kuheshimiwa, kuthaminiwa ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya kazi, pia watambulike kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitarejea barua moja hapa ya wakati Mama Shamsa Mwangunga alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, hii ni pamoja na utekelezaji wa changamoto zinazowakabili waongoza watalii, pamoja na wapishi na wapagazi. Ilikuwa ni barua tarehe 15 Desemba, 2015 na tarehe 8 Aprili, 2016. Kulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja ya namna ya kuwalipa wapagazi hawa, wapishi na watembeza watalii ambayo ilikuwa ni ya GN Na. 228 ya mwaka 2008. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kikao hicho walishiriki Tanzania Association of Tour Operators, Kilimanjaro Association of Tour Operators, Kilimanjaro Guard Association, Tanzania Tour Guard Association, Tanzania Porters Organization na kwa upande wa Serikali walishiriki Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Kwa masikitiko makubwa kuna zaidi ya makampuni 400 yanayofanya shughuli za kupandisha Mlima Kilimanjaro lakini ni Makampuni 20 yanayowalipa stahiki hawa wapanda mlima, wapagazi na wapishi. Wengi wao wanawalipa shilingi 5,000/shilingi 8,000 mpaka shilingi 10,000 inasikitisha sana. Kwa sababu wapagazi hawa na wapishi na watembeza wageni wanafanya kazi ngumu, wengine wanafia kule mlimani, wengine wana familia, wana majukumu makubwa, hawana makato yoyote yanayowafanya baada ya kumaliza muda wao wa kazi hizi waweze kufaidika na kazi hii lakini bado wanalipwa kipato cha chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kingine kikubwa Watumishi hawa kwa kuwa hawapati mikataba kutoka kwa waajiri wao kama Tour Operators wanapoteza mapato mengi sana ya Serikali, kwa mfano hizi withholding tax hawawezi kulipa kwa sababu hawana mikataba na waajiri wao.

Kwa hiyo, ninaomba Serikali iangalie sana suala hii kwa mfano, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya kazi hawawezi kukwepa kukaa pamoja kuweza kushughulikia tatizo hili. Wamekuwa na kilio cha muda mrefu na hakuna msemaji wameunda vikundi vyao vya kuwasemea, lakini wanapofika kwa mwajiri wanakuwa hawana mtetezi kwenye Wizara ya Kazi, wakati mwingine kwenye mikoa kunakuwa na mwakilishi mmoja tu wa Wizara ya Kazi ambaye anakuwa na mambo mengi hawezi kuwasemea watu hao. Lakini vilevile wamekuwa wakipata mafunzo katika Chuo cha Taifa cha Mweka, kumekuwa na mafunzo ambayo yanatolewa ya muda mfupi wiki tatu wanalipa shilingi 800,000 ili waweze kupata certificate. Lakini nilikuwa naiomba Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hii mada muhimu iliyoko mezani. Hoja ya kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika, Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa ndiyo hoja ambayo tumekuwa kukiijadili muda mrefu katika Kamati yetu ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiri tu kuwa mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo na kwamba nichukue fursa hii kipekee kumpongeza sana, Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa TANAPA, Ndugu Allan Kijazi pamoja na timu yake kwa kuendelea kusimamia maeneo ya Hifadhi za Taifa TANAPA, yenye hifadhi 16, mapori ya akiba 28, mapori tengefu 42 yanayosimamiwa na TAWA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mapori ya Akiba yanayopandishwa hadhi ni miongoni mwa mapori 42 yanayosimamiwa na TAWA. Kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kukabiliana na changamoto za ujangili wa mapori kwenye maeneo yanayopakana na mapori ya akiba. Maeneo mengine yanayokuwa na changamoto ni sehemu ya ujambazi ambao umekithiri maeneo ya mipakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni uvuvi haramu ambao umekuwa ukikabili mapori haya na uingizaji wa silaha za kivita ambazo pia zimekuwa zikiingizwa kupitia kwenye mipaka ya mapori haya. Kumekuwa na malengo mbalimbali ambayo yamesababisha kupandisha mapori haya kuwa hifadhi za Taifa. Malengo hayo ni pamoja na kuimarisha uhifadhi wa maliasili kama tulivyoona kwenye Kamati yetu, hususani pia wanyama pori, mimea adimu, mazalia ya samaki, viumbe wengine na ndege wa aina mbalimbali ikiwemo korongonyangu.

Mheshimiwa Spika, kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu imekuwa ni hoja muhimu pia ya kufanya maporo haya kupandishwa hadhi. Sambamba na hilo ni kuimarisha mifumo ya kisheria ambayo itakwenda kusimamiwa na hifadhi za Taifa TANAPA. Vilevile kuongeza pato la Taifa kupitai shughuli za utalii ambazo zitakwenda kuendeshwa katika ukanda wa hifadhi za Magharibi. Kwa kuwa shughuli za kijamii hazitaruhusiwa kuendeshwa katika mapori haya wakati eneo hili linapandishwa kuwa Hifadhi za Taifa, napenda kushauri masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii inaweza kupelekea kuendelea kuwa na migogoro mingi ambayo imekuwa ikitokea katika maeneo mengine kama haya, wananchi wa maeneo haya ambao ni wafugaji kulingana na Sheria za Hifadhi hawataruhusiwa kuendelea kufanya shughuli za kijamii kama kufuga, kuokota kumi na kuvua samaki. Hivyo, sambamba na kupandisha hifadhi hizi, mapori haya ningependa kushauri mambo yafuatayo ili Serikali iweze kuyatekeleza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa hii ni fursa ya miji ya jirani kama Geita, Biharamulo, Bukoba na Ukerewe, napenda kushauri kuweko na mikakati ya kuendeleza miji hii. Hivyo, viwango vya utoaji huduma viwe vinakidhi mahitaji ya soko la utalii ili kuwezesha wananchi wanaopakana na Mikoa ile kuweza kufaidika na hili suala la upandishaji hadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili ningependa kushauri Serikali ijenge mazingira kuiwezesha TANAPA kuyaendeleza mapori haya yatakayopandishwa hadhi. Suala la tatu, napenda kuishauri Serikali kusaidia miundombinu ya kufika hifadhi, iboreshwe. Suala la nne, naomba Serikali isaidie kuondokana na urasimu wa kutoa misamaha ya kodi kwa wafadhili wanaotoa pesa kusaidia maeneo hayo, hasa kwenye suala la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kushauri Serikali kuwe na bajeti ya kutosha kusaidia shughuli za uendeshaji kwa kuwa mpaka sasa kati ya Hifadhi 16 za Taifa ni hifadhi tano tu ambazo zinajiendesha zenyewe, hifadhi nyingine zote ni tegemezi. Kwa hiyo, kwa kuwa tunaenda kwenye kipindi cha bajeti, kuwe na bajeti ya kutosha kusaidia hifadhi hizi kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ione kuna haja sasa ya kufanya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa ni kipaumbele cha Taifa kwa kuwa Wizara hii sasa imekuwa ikichangia pato kubwa la Taifa na kwamba ni miongoni mwa Wizara zinazoingizia pato kubwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja hii ya kupandisha hifadhi hizi za Magharibi kuwa na hadhi ya TANAPA kwa kuwa kupandisha hadhi hifadhi hizi zitaisaidia sana wananchi wanaozunguka maeneo haya ya Magharibi kuendelea kiuchumi, lakini pia kusaidia mipaka yetu ambayo inayozunguka nchi jirani. Vile vile, kama tulivyoona, itasaidia ulinzi katika nchi yetu na kuzuia migogoro mingi ambayo inatokana na nchi zinazozunguka katika hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa Taifa lililoelimika ni Taifa bora kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ongezeko la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari; kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wa kike kupata mimba na hivyo kusababisha kukatisha masomo yao. Watoto hao wa kike wanapokatiza masomo yao wanakwenda kuwa walezi wa watoto hali ambayo inawafanya waingie kwenye umaskini na wengine kujiingiza kwenye ukahaba ili waweze kumudu kulea watoto wao. Hata hivyo, watoto hawa wanaweza kuingia kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU na hivyo kuacha familia zao zikiwa na huzuni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, visababishi vingi vya watoto kuingia kwenye kupata ujauzito nitavitaja vichache ikiwemo hali ya umaskini inayowakabili wanafunzi, hivyo, watoto wa kike hudanganyika kwa urahisi, umbali mrefu wa kutoka kwenye makazi yao kuelekea shuleni, shughuli zinazowazunguka watoto hawa wa kike mfano kuchota maji, kuokota kuni na kadhalika. Nashauri Wizara ilete muswada wa kubadilisha Sheria ya Mtoto ili mtoto wa kike akipata mimba aweze kuendelea na masomo ili kuwasaidia watoto hawa. Hii iende sambamba na adhabu kali kwa mtu yeyote anayempa mimba mtoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu ya elimu, kumekuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya elimu mfano vyumba vya madarasa, mabweni, matundu ya vyoo ambavyo haviendani na kasi ya ongezeko la idadi ya wanafunzi na miundombinu ya shule au elimu. Darasa moja wanafunzi zaidi ya 60 hii haileti afya ya elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uwiano katika wanafunzi na walimu, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana hasa shule za Serikali ukilinganisha na shule za binafsi. Naomba Serikali na Wizara ijifunze kutoka shule za binafsi itasaidia kuboresha shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tatizo la walimu wa kufundisha viziwi na walemavu kwa ujumla, kumekuwa na tatizo kubwa la walimu wa walemavu kwenye shule zetu hivyo kupelekea watu hawa kukosa huduma muhimu ya kupata elimu sambamba na shule za ufundi na VETA. Mfano, shule ya Moshi Technical ilikuwa ikipokea walemavu wengi na walisoma pamoja na kupata elimu ya ufundi jambo ambalo limewasaidia sana ambao hawakuweza kuendelea na elimu ya juu wameweza kujitegemea kwa kujiajiri.

Nashauri Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI ili kuona namna ya kuboresha shule ambazo zinatoa mchanganyiko wa elimu ya ufundi na kawaida ili kusaidia vijana wetu vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo ya elimu ya juu; suala la wanafunzi waliokopa kurudisha mkopo ni la muhimu sana. Wasiwasi wangu ni namna ya urudishaji wa mikopo kwa wale ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira. Naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha anipe ufafanuzi wa jinsi gani waliochukuwa mikopo ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira watarudisha mikopo hiyo ili kusaidia wahitaji wengine wa mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya Kiswalhili kwa kufundishia. Nakubaliana na matumizi ya lugha ya Kiswahili lakini wasiwasi wangu ni kama tunaweza kutumia Kiswahili. Kama hatutaweza kukitumia mpaka elimu ya juu itakuwa ni changamoto kubwa sana. Nasema hivi kwa sababu lugha tunayoitumia kwa elimu ya juu ni Kiingereza hivyo italeta mkanganyiko kwa watoto hasa lugha ya Kiingereza wanapofika elimu ya juu. Nashauri tutumie lugha zote mbili kwa manufaa ya kibiashara na uchumi wa nchi yetu na Afrika Mashariki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa nchi yetu. Kama ilivyo katika dira ya Taifa ya kulinda na kudumisha amani na usalama wa Taifa letu; pamoja kuendelea kulinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya maadui wa ndani na nje ya nchi yetu; usalama wa mipaka ya nchi, mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya nchi ya Tanzania na Malawi umekuwa wa muda mrefu hivyo kuendelea kuathiri ukuaji wa uchumi kwa nchi yetu hasa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huo unaendelea kuathiri shughuli za uwekezaji katika eneo la Ziwa Nyasa na hivyo kufanya mdororo wa kiuchumi kwa wananchi na kupoteza mapato katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aniambie mgogoro huu umefikia wapi ili kuweka mahusiano mazuri kati ya nchi ya Tanzania na Malawi na pia kuinua uchumi wa nchi yetu kupitia fursa zilizopo katika Ziwa Nyasa na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira kwa vijana waliopata mafunzo ya JKT; kumekuwa na changamoto kubwa ya ajira nchini na hii ni pamoja na vijana wanaomaliza mafunzo JKT na kupelekea vijana hawa kujiingiza katika vitendo vya uvunjaji wa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma taasisi za Kiserikali, kwa mfano TANAPA ilikuwa ikichukua vijana wengi waliomaliza JKT na kuwapatia ajira hali ambayo kwa sasa imepungua na kufanya nidhamu kupungua sana kwa taasisi zinazojihusisha na masuala ya ulinzi na usalama wa maliasili zetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002, nchi yetu ina eneo la hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mkoa wa Songwe una vyanzo vingi vya maji ambavyo vingeweza kutumika vizuri, vingeweza kusaidia huduma ya maji pamoja na kilimo cha umwagiliaji ambacho kinaweza kulisha nchi nzima. Ushauri wangu kwa Serikali, Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Kilimo vikae pamoja na kuona ni namna gani wanaweza kutumia vyanzo vya maji ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji kwa mkoa mpya wa Songwe

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango shirikishi wa maji shirikishi katika Mto Momba na Songwe unaweza kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na kutoa ajira kwa makundi ya vijana na akina mama ambao wengi wanategemea kilimo. Wizara ishirikiane na sekta binafsi kukamilisha miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uharibifu wa miundombinu ya maji na umwagiliaji; kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya maji hasa maeneo ya vijijini. Mfano, maeneo mengi ambayo yamewekwa mabomba ya maji ya kuchota kwa ujumla, wananchi wamekuwa wakiharibu mabomba hayo kwa kuwa hawana uchungu na miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri uwekwe utaratibu wa kuchangia miundombinu ya maji ili wananchi watambue thamani ya miundombinu ya maji na kuithamini. Hii itasaidia ukarabati wa miundombinu hiyo bila kutegemea ufadhili pindi miundombinu hiyo ikiharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la upotevu wa maji hasa kwenye mashamba makubwa ya mpunga na mfano mzuri ni Bonde la Usangu - Mbarali. Miundombinu ya umwagiliaji ni ya zamani tangu kukiwa na mashamba machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za haraka zisipochukuliwa kudhibiti kilimo holela cha umwagiliaji katika Bonde la Usangu kuna uwezekano mkubwa wa uzalishaji wa nishati ya umeme katika Bwawa la Mtera na Kidatu ukapotea kwa kiwango kikubwa kutokana na upotevu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia haki za binadamu ziheshimiwe, mfano; haki ya kupata elimu, afya, maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini bado ni changamoto kutokana na wananchi wengi kupata maji yasiyo salama. Uharibifu wa mazingira ni hatari sana kwa maisha ya binadamu kwa asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanatumia misitu kama malighafi kwa shughuli za uzalishaji na huduma pamoja na kuwa ni fursa ya ajira kwa watu wengi. Uharibifu wa mazingira ni chanzo cha mafuriko na ukame wa kutisha

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Wizara ya Mazingira na Wizara ya Kilimo kuhakikisha utoaji wa elimu juu ya utunzaji wa mazingira unapewa kipaumbele na ikiwezekana kuwepo na faini zinazotozwa kwa watumiaji wabaya wa maji na vyanzo vyake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maji ni afya, uhai na maendeleo, ninashauri Wizara ya Maji kwa kushirikina na Wizara zote ihakikishe kuwa majengo yote ya taasisi mbalimbali yawe na michoro itakayoonesha utunzaji wa maji ya mvua ili kusaidia wakati ambao kuna upungufu wa maji. Mfano katika shule, hospitali, ofisi, hoteli na shughuli zote za kilimo cha umwagiliaji kuwekewa mifumo ya kutumia maji kidogo na kuzuia upotevu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kushauri Wizara iendelee kutembelea na kutoa elimu kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji hasa kusisitiza suala la mita 60 kutoka vyanzo vya maji. Kuendelea kutumia mila na desturi zinazosaidia utunzaji wa maeneo yenye vyanzo vya maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii muhimu kwa utoaji huduma katika sekta ya Ardhi. Migogoro ya ardhi nchini ni mikubwa mno hivyo naomba kuendelea kuishauri Serikali, kupitia Wizara hii ya Ardhi kuweka mpango madhubuti, kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji ili kuepuka migongano hii ambayo haina tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Kumekuwa na changamoto kubwa ya kodi nyingi kwenye ujenzi wa nyumba za NHC, hivyo kupelekea nyumba hizi kuendelea kuuzwa bei ya juu. Kama Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii nimekuwa nikitoa maoni yangu kuhusu Wizara ya Miundombinu, Nishati na Madini,Maji na Umwagiliaji ili kuona ni namna gani ya kupunguza mzigo kwa NHC ambao imekuwa ikiubeba na kugharamia kila kitu na kufanya gharama hizi kwenda kwa mnunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa za upimaji wa ardhi; kumekuwa na malalamiko makubwa kwenye suala la upimaji wa ardhi na hivyo kupelekea wananchi wengi kutokupima ardhi zao. Ushauri, Wizara ya Ardhi ishirikishe sekta binafsi katika suala la upimaji. Maeneo mengi kwenye Halmashauri zetu hayajapimwa hivyo kufanya ugumu wa uwekezaji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Wizara ya Ardhi kujikita kwenye mikoa mipya na inayokuwa ili kuendelea kupanga mipango miji ambayo ni tatizo kubwa sana katika nchi yetu, sambamba na kujenga maeneo ya uwekezaji kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe ni mkoa mpya, nashauri Wizara itoe upendeleo wa kipekee kuendeleza Mkoa wa Songwe kwa kupima viwanja, kutenga maeneo ya uwekezaji ili kuvutia wadau mbalimbali kuendeleza mkoa, sambamba na ujenzi bora wa nyumba za kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kuchangia Wizara hii na kwa kunimheshimiwa mwenyekitipa pumzi ya kusimama hapa kwenye Bunge lako Tukufu leo. Nianze kwa kupongeza Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii kwa kupata fursa ya kufanya ziara za kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo muhimu ambayo kama mdau wa uhifadhi, ningependa kuyasisitiza ni Wizara hii kuwa na ubunifu. Kumekuwa na utalii wa aina moja miaka mingi, hivyo nashauri tuwe na aina nyingi za utalii ambazo zitafanya mtalii aache fedha zake, kuliko kutegemea fedha za lango kuu, wakati mgeni anaingia hifadhini. Mfano kivutio kilichopo Hifadhi ya Manyara ni mfano mzuri wa ubunifu. Nashauri maeneo mengine yafanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la vitalu vya uwindaji. Kumekuwa na sintofahamu kutokana na kauli mbalimbali za kuzuia na kuruhusu uendeshaji wa vitalu vya uwindaji. Kutokuwa na msimamo wa matamko katika Wizara hii kunaathiri shughuli nzima ya uwekezaji kwenye vitalu vya uwindaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu, biashara hii inauzwa au inafanyiwa masoko kabla ya mteja kutumia bidhaa. Hivyo, tunaweza kupoteza mapato mengi na kuwafanya wafanyabiashara ya utalii wa uwindaji kukata tamaa ya kuwekeza nchini. Mfano, leo tuna vitalu 61 havina wawekezaji, lazima tujiulize tumekosea wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mipaka. Kumekuwa na migogoro ya uhifadhi na wananchi wanaozunguka hifadhi zetu. Kama hatutaweza kuweka suluhisho la mipaka yetu ya hifadhi, tunakwenda kuwaumiza wananchi wetu kwa kuendelea kuwatoza faini kubwa na adhabu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri kwamba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Maliasili na Mifugo tuweze kukaa pamoja ili kuwa na mpango wa pamoja wa matumizi bora ya ardhi na kuweza kupunguza na kumaliza kabisa migogoro ya mipaka.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii ya kuchangia mfano wa utoaji wa huduma ya afya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la ukatili kwa watoto; kumekuwa na changamoto kubwa ya ukatili dhidi ya watoto hasa wa chini ya miaka mitano. Inapotokea mtoto huyu anapata jaribio la kutendewa ukatili au jaribio la kubakwa na anapotakiwa kutoa ushahidi Polisi inaonekana kuwa ushahidi hautoshelezi na hivyo watuhumiwa wengi kuachiwa huru, hali hii inaongeza sana matukio ya ubakaji

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma kwa wajawazito; pamoja na Serikali kuonesha msisitizo wa huduma ya bure kwa wajawazito bado kumekuwa na changamoto kubwa ya vifaa vya kujifungulia hasa katika maeneo mengi ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati zetu zimechoka sana na maeneo mengine hata maji hakuna hii ni hatari sana wakati mama anakwenda kujifungua. Pia vitanda vya kujifungulia ni changamoto kubwa kwenye zahanati zetu, vingi vimechakaa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumze suala la msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za Mikoa na Wilaya; hili limekuwa tatizo kubwa kwa kuwa zahanati zetu hazijaboreshwa vya kutosha, hivyo wagonjwa wengi kukimbilia hospitali za mikoa na kusababisha msongamano mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa Madaktari Bingwa bado ni tatizo kubwa hasa kwa upande wa akinamama na watoto. Naomba Waziri anapokuja kuhitimisha aniambie na hizi ajira mpya 2018/2019 wamejipangaje kuongeza idadi ya Madaktari katika hospitali zetu ili kusaidia tatizo hili la msongamano wa wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la MRI- Scan kwenye hospitali zetu na hiyo kusababisha vifo visivyo na sababu kwa magonjwa yasiyoweza kugunduliwa kwa vipimo vya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lishe; kumekuwa na tatizo kubwa la lishe, hivyo kuendelea kupata magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, ongezeko la uzito kwa watoto wadogo na watu wazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri anapokuja kuhitimisha aniambie kama Wizara wana mkakati gani wa kutoa elimu ya afya ili kuokoa Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa fursa ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia suala la ajira kwa wenye kiwango cha darasa la saba. Kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa kuona ni lazima kiwango cha ajira kianzie kidato cha nne. Ni jambo jema kabisa ndiyo maana ya kuanzisha elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu kwenye eneo hili, naomba kuishauri Serikali ione kuna umuhimu wa kuwarudisha kazini watumishi wote waliokuwa wameajiriwa kwa kiwango hicho cha elimu huko nyuma ili wafikie kipindi chao cha kustaafu na kupunguza gharama kubwa ya kuwalipa watumishi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hao wengi wao walioajiriwa kwenye kada za udereva, uhudumu na huduma mbalimbali katika ofisi za Serikali, kada ambazo hazihitaji utaalam mkubwa kwa level yao ya elimu. Najua Serikali ina nia njema ila kwa kipindi hiki cha mpito baada ya suala la elimu bure tunaamini mwamko wa kujiendeleza utakuwa mkubwa na hivyo kada hii ya elimu ya msingi itajifuta yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hifadhi ya mazingira; napenda kuipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango wa usafi kwa ajili ya utunzaji wa mazingira. Pamoja na Serikali kuanzisha mpango huu na kuongeza idadi ya wakaguzi na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji endelevu wa viwanda unaozingatia utunzaji bora wa mazingira. Napenda kuishauri Serikali kuona ni namna gani ya kupiga marufuku

vifungashio vya plastic ili kuendelea kupunguza uharibifu mkubwa wa mazingira kupitia vifungashio vya plastic.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo. Nimekuwa nikifuatilia sana kwenye mikoa mbalimbali nchini ambayo imekuwa ni wazalishaji wakubwa wa chakula. Napenda kuishauri Serikali kuhusu suala la pembejeo ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa upande wa upatikanaji. Kwa kuwa, maeneo mengi yana Mawakala ambao wamekuwa na urasimu mkubwa kwa namna ya upatikanaji wa pembejeo. Ushauri wangu, ni kwa nini Serikali isione umefika wakati wa kusambaza pembejeo hizi kwenye maduka na kuhakikisha inatolewa bei elekezi ili kila mkulima apate pembejeo hizi kwa wakati kwa kuwa kumekuwa na upendeleo mkubwa wa upatikanaji wa pembejeo kwa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mazao ya biashara. Pamoja na Serikali kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao ya kahawa, korosho, pamba na tumbaku, kuna zao la apples katika Mkoa wa Njombe ambalo kama Serikali itaweka mkazo itasaidia upatikanaji wa apples kwa wingi katika nchi yetu na kuacha kuagiza apples Afrika ya Kusini ili kuongeza kipato kwa wakazi wa Mikoa ya Kusini na kuongeza mapato na uchumi wa Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Elimu, Sayansi na Technolojia. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ya kuanza kuboresha elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uboreshaji wa elimu kumekuwa na changamoto kubwa ya walimu kukosa ujuzi na mbinu za kufundishia, sambamba na walimu kutovutiwa na mazingira ya ufundishaji, jambo ambalo linawafanya kutofundisha kwa bidii na hivyo kusababisha kushuka kwa ubora wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizi zimepelekea kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya kuhitimu. Uchambuzi wa matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne mwaka 2017 unaonesha wastani wa asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mitihani hiyo walipata daraja la nne na sifuri. Nashauri Serikali ijikite katika kushughulika na changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa walimu, kwa mujibu wa takwimu za BEST za mwaka 2016 na 2017 idadi ya walimu kwa shule za msingi imeshuka kutoka walimu 191,772 mwaka 2016 hadi kufikia 179,291 mwaka 2017, ikiwa ni anguko la asilimia 6.5 na kufanya uwiano wa walimu na wanafunzi kuwa 1:50. Aidha, katika shule za awali, idadi iliyopungua ni walimu 1,948 na kufanya uwiano wa walimu na walimu na wanafunzi kuongezeka kutoka 1:135 mwaka 2016 hadi kufikia 1:159 mwaka 2017 badala ya 1:25 ambao ni uwiano unaokubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule za sekondari kuna uhaba mkubwa wa walimu kwa baadhi ya masomo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hisabati kuna upungufu wa walimu 7,291, bailojia kuna upungufu wa walimu 5,181, kemia kuna upungufu wa walimu 5,373 na fizikia kuna upungufu wa walimu 6,873; hii ni kwa mujibu wa takwimu za BEST za mwaka 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu za Elimu ya Msingi za Mikoa (BEST Reginal Data 2017) walimu 7,743 wanatarajiwa kustaafu kati ya mwaka 2018 na 2019. Aidha, takribani walimu zaidi ya 30,000 wana umri wa zaidi ya miaka 51 ya kuzaliwa, hivyo na wao wanatarajiwa kustaafu muda mfupi ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa hakuna elimu bila walimu Serikali inatoa majibu gani katika maswali yafuatayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitu gani kimesababisha upungufu wa walimu ukizingatia kwamba kuna idadi kubwa ya wahitimu wa fani ya ualimu katika vyuo vya ualimu vilivyopo nchini? Je, Serikali imeajiri walimu wangapi mpaka sasa ili kukabiliana na upungufu huo? Serikali ina mpango gani endelevu wa kuhakikisha kwamba tatizo la upungufu wa walimu linatoweka kabisa? Serikali imepanga kuajiri walimu wangapi katika mwaka wa fedha 2018/2019 kama sehemu ya mchakato wa kupunguza tatizo la upungufu wa walimu?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja hii ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda haviwezi kuwa endelevu kama hakutakuwa na malighafi ambazo kimsingi zinatokana na kilimo. Waziri atakubaliana na mimi kwamba bila kuwa na mapinduzi ya kilimo ndoto ya Tanzania ya viwanda haitafanikiwa. Nasema hivi kwa sababu kilimo chetu bado ni duni sana kuweza kuzalisha malighafi za kulisha viwanda hivyo vinavyokusudiwa kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zao la mbaazi, zao hili uzalishaji wake umeongezeka sana ambapo wakulima walizalisha tani milioni 2.3 za mbaazi mwaka 2016. Naiomba Serikali iendelee kuangalia kwa jicho la ukaribu soko la mbaazi ili wakulima hawa wasiendelee kupata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mafuta, ninaamini kuwa wananchi wengi wanaelewa kuhusu utumiaji wa mafuta ya mbegu. Ninashauri Serikali itoe mikopo kwa wakulima ili waweze kuzalisha kilimo cha mbegu za mafuta na mafuta yatosheleze nchi nzima, sambamba na upatikanaji wa mashine kwa bei nafuu za kukamulia mafuta ili wakulima waweze kuuza mafuta na kupata faida kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia Serikali iendelee ku-support zao la apples katika Mkoa wa Njombe. Mwaka jana nilizungumzia suala hili naomba nilisemee tena kwa kuwa tumekuwa tunatumia sana apples kutoka Afrika ya Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya kilimo iangaliwe kwa jicho la karibu ili kusaidia wakulima wetu hasa kuwafikia kutoa elimu ya mbegu bora na kilimo chenye tija.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kuniwezesha kuchangia hotuba iliyoko mezani. Nianze kwa kuzungumzia Mfuko wa Wanawake, Vijana na Walemavu ambao unatengwa kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kuwapongeza sana Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanazozifanya, nimpongeze Mheshimiwa Jafo na wasaidizi wake kwa kazi nzuri na zinazoonekana. Ninachotaka kushauri ni kwamba Mfuko huu utengewe akaunti yake maalum katika halmashauri zetu ili kufanya usimamizi mzuri wa fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo wa Serikali ni kila halmashauri kutenga fedha asilimia 10 kutokana na mapato ya ndani. Jambo hili ni jema sana iwapo litaratibiwa vizuri kwa kuwa litasaidia ajira kwa makundi haya hasa kwenye ujasiriamali. Naomba kuishauri Serikali ilete Muswada wa Sheria ya Kusimamia Mfuko wa Wanawake, Vijana na Walemavu. Mfuko wa Walemavu 2% utungiwe sheria inayozielekeza halmashauri kutenga kiasi hiki kwa ajili ya walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Ujenzi wa Barabara Vijijini (TARURA). Lengo ni kuhudumia barabara zote zilizokuwa zinahudumiwa na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji. Kumekuwa na changamoto mbalimbali katika TARURA kukubaliana na majanga kama mafuriko ambayo hupelekea uharibifu wa madaraja, makalavati na mashimo makubwa kwenye barabara vijijini, mijini na mitaa mingi nchini. TARURA inatekeleza majukumu yake kupitia fedha za Mfuko wa Barabara za mwaka wa fedha 2017/2018. Wakala waliidhinishiwa shilingi bilioni 230.8 kwa ajili ya matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita 34,024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Februari, 2018 TARURA imepokea bilioni 98.5 ambazo zimetumika kutengeneza barabara yenye urefu wa kilomita 4,183.3 tu. Naomba Waziri atakapohitimisha atuambie ni kwa nini fedha hizi hazitolewi kwa wakati ili kukamilisha barabara hizi kwa mwaka wa fedha unaoishia 2018. Kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri Mkuu ni kwamba barabara zilizopo chini ya TARURA ni kilomita 108,946.2. Mwaka huu wa fedha TARURA imesimamia matengenezo ya barabara ya kilomita 4,183.3 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za miradi ya maendeleo kutofika kwa wakati katika halmashauri zetu. Katika kujiletea maendeleo rasilimali fedha toka Serikali Kuu ni muhimu sana, lakini kuna tatizo la Serikali kushindwa kupeleka fedha kwa ukamilifu na kwa wakati kiasi kwamba utekelezaji wa miradi unashindikana na utaratibu wa manunuzi kutofanyika kwa wakati na kutofuata Sheria ya Manunuzi ambayo inahitaji kutimizwa kwa masharti hivyo kupelekea fedha kurudi Serikalini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimwa Mwenyekiti, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha ktupaa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora. Nipende kumpongeza sana Waziri wa Utumishi Kapteni George Huruma Mkuchika kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia Utumishi wa Umma. Nakiri kwa kusema nidhamu ya utumishi wa umma imerudi na uwajibikaji umeongezeka kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaulimbiu ya Awamu ya Tano ni uwekezaji katika viwanda unaochochea ukuaji wa nchi. Ili kuwekeza katika viwanda lazima tuwe na rasilimali watu tuliyoiandaa kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ndiyo inayoratibu na kusimamia utumishi wa umma nchini. Utumishi wa umma unatakiwa kuwa endelevu, unatunza historia na kumbukumbu za Serikali hali kadhalika utumishi wa umma unatakiwa kutekeleza kazi za Serikali iliyoko madarakani bila kujali inatokana na chama gani cha siasa ili kuondoa uwezekano wa mtumishi kutoa huduma kwa upendeleo au ubaguzi kutokana na itikadi za kisiasa. Kuingiza utumishi wa umma katika itikadi za vyama kutayumbisha utumishi wa umma ambao ndiyo injini ya utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii tena kumpongeza Waziri na viongozi wote kwa ujumla kwa maamuzi ya kurudisha kazini watumishi wa darasa la saba, walioondolewa kazini. Kwanza hii niseme inapunguza gharama kubwa kwa Serikali kuwalipa watumishi hawa. Sambamba na hilo hawa watajifuta wenyewe kwa kuwa baada ya elimu bure Watanzania wengi watatoka hapo na kufikia angalau kidato cha nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hawa wametumikia Serikali kwa muda mrefu kwenye fani ya udereva na uhudumu wa ofisi nyingi za Serikali yetu. Nimekuwa mtumishi katika Hifadhi za Taifa Tanzania na watumishi wengi walioko kwenye level ya darasa la saba ndiyo walinzi wakubwa wa rasilimali zetu, maliasili za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie upungufu wa watumishi, Wataalam kwenye Wizara ya Afya. Hili limekuwa na changamoto kubwa kwenye Idara ya Afya na hivyo kupelekea hospitali zetu za rufaa kubeba mzigo mkubwa. Nashauri eneo hili liangaliwe kwa jicho la pekee sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia kuhusiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). TFS imepewa dhamana ya kusimamia maeneo ya misitu 461 nchini. Maeneo haya yanahifadhiwa kwa malengo makuu matatu:-

(1) Ikolojia; hakuna anayefahamu umuhimu wa maji nchini, kwa binadamu, wanyama na mimea. Mfano, Jiji la Tanga wanategemea maji yake kutoka chanzo cha Msitu wa Amani Nature Reserve, Mkoa wa Kilimanjaro wanategemea maji kutoka chanzo cha Msitu wa Chome na Jiji la Dar es Salaam wanategemea maji kutoka Mto Ruvu – Msitu wa Uluguru ukiwa ndiyo chanzo chake.

(2) Lengo la pili ni kuhifadhi viumbe hai. Misitu hii inahifadhi viumbe adimu duniani. Mfano, vyura wa Kihansi na vinyonga wa pembe tatu.

(3) Lengo lingine ni kwa ajili ya utalii. Mfano Msitu wa Asili wa Amani, Chome, Maporomoko ya Kalambo na Msitu wa Rondo. Kwa siku za karibuni misitu hii imekuwa ikivutia watalii kutoka nchi za Asia kwa ajili ya utalii wa forest bathing kuondoa stress.

Mheshimiwa Naibu Spika, Utalii wa Kupiga Picha. Wasanii wa kizazi kipya wameonekana kuvutiwa sana na misitu yetu na wanakwenda kurekodi filamu katika misitu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Utalii wa Kuangalia Ndege wa Aina Mbalimbali Katika Msitu wa Rondo mkoani Lindi. Ndege hawa wanatoka mabara mbalimbali ya Ulaya na kuweka makazi yao katika Msitu wa Rondo. Msitu huu unashika nafasi ya 43 duniani kwa kuwa na ndege wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mazuri haya lakini misitu hii imekuwa na changamoto mbalimbali. Changamoto ya miundombinu ya barabara kabla na baada ya mvua. Mfano, Maporomoko ya Kalambo, barabara ya lami Sumbawanga kuelekea Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo kuelekea Bandari ya Kasanga mpaka wa Kongo na Tanzania kipande cha kilometa nane kuingia kwenye Maporomoko ya Kalambo, barabara ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia TARURA kuiangalia barabara hii ili kusaidia watalii wanaotembelea Maporomoko ya Kalambo pamoja na kuvutia wawekezaji wanaowekeza katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze TFS, Kamishna Prof. Silayo kwa kujenga ngazi zenye Urefu wa mita 270 kwa ajili ya kutembea kwenye maporomoko hayo na lengo ni kukamilisha ngazi zenye urefu wa mita 570 kwa mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imetembelea Amani N. Reserve – hali ya miundombinu ni mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu za idadi ya watalii wa misitu 2015/2016 ni 2,200, mwaka 2016/2017 walikuwa 3,000 na mwaka 2017/2018 walikuwa 3,500. Kwa takwimu hizi kama wangewekeza kwenye miundombinu tungepata watalii wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado mapato yanayotokana na misitu ni kidogo sana. Mwa 2015/2016 ni 245,000,000, mwaka 2016/2017 ni 310,000,000 na mwaka 2017/ 2018 ni 370,000,000. Pamoja na idadi kubwa ya maeneo ya misitu 461, ni maeneo 13 tu ndiyo yanayojiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mapato Ghafi kwa Serikali iangaliwe upya ili kusaidia hizi taasisi kujiendesha; asilimia 30 corporate tax, asilimia 18 VAT, asilimia 15 gawio la Serikali na asilimia 3 SDL; jumla ni asilimia 66. Mashirika haya hayawezi kumudu kujiendesha, tuwekeze kwenye miundombinu ili kuongeza wawekezaji na idadi ya watalii na mapato yataongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango wangu kwenye Wizara hii nichukue fursa hii kuwapongeza sana Wizara ya Maliasili na taasisi zake zilizochangia gawio kubwa Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto nilizozionesha kwenye mchango wangu Wizara hii imechangia kwa mwaka mmoja in order of priority, Tanzania Telecommunication Regulatory Authority, Tanzania National Park, Ngorongoro Area Conservation Authority, Tanzania Forestry Services. Taasisi tatu kati ya hizi ni Wizara ya Maliasili na Utalii, hii inaonesha umuhimu wa maliasili kwenye uchumi wa nchi, ni lazima tulinde maliasili zetu. Naomba kuwasilisha.