Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Silvestry Fransis Koka (19 total)

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Waziri na Serikali kwa kuamua kurejesha takribani hekta 2963 kwa wananchi. Pamoja na kazi hiyo nzuri ya Serikali kwa wananchi ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika urejeshaji huo wa eneo hili kuna eneo dogo la takribani ekari 300 tu, ambalo lina zaidi ya kaya 250 ambalo halikufikiriwa katika mpango huu na ambapo limewafanya wananchi hawa wanaokaa katika eneo hili sasa wakae kwa mashaka na kujiona kwamba wao ni wanyonge kwa sababu hawakuwekwa katika mpango huu ambao uliwarejeshea maeneo wenzao.
Swali langu la kwanza, je, ni lini sasa Serikali itaamua kurejesha eneo hili dogo ili kuwatendea haki kama ilivyotenda haki kwa wananchi wengine na wananchi hawa wa Vingunguti waweze kujiona kwamba wametendewa haki kama hao wengine.
Swali la pili, kwa sababu Serikali imekuwa na nia njema na imechukua hatua mbalimbali, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri pengine akishirikiana na Waziri wa Wizara ya Mifugo atatembelea eneo hili la Pangani maarufu linaitwa Vingunguti, ili tuweze sasa kukaa na wananchi na kupata ufumbuzi wa kudumu kutokana na mgogoro au tatizo hili la wakazi wa eneo hilo?
himiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi tu kwamba Serikali haiwezi kuendelea kurudisha maeneo kwa wananchi, hasa katika hilo eneo ukizingatia kwamba eneo la awali lililokuwa na ukubwa wa hekta 4000 wananchi walipewa eneo la hekta 2963 sawa na asilimia 74 ya eneo lote. Hivyo kuendelea kulimega ni kufifisha pia azma ya Wizara ya Kilimo na Mifugo, katika kuendelea kuzalisha mitamba bora ambapo tunahitaji kuwapeleka wafugaji wetu katika maendeleo ya kuwa na ufugaji bora na endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili niseme tu kwamba, Wizara imekuwa na nia ya dhati kufika katika lile eneo na kukutana na wananchi na hasa kukutanisha pande zote mbili, ukizingatia mara ya mwisho tumekuwepo kule tarehe 4/3/2016, lakini kama hiyo haikutosha Wizara yangu iko tayari kuendelea kukutana nao ili muafaka uweze kufikiwa.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Wananchi wa Kata ya Tangini na Pangani ambapo ndiko barabara hii inapita, wamekuwa wakipata adha kubwa sana. Takriban zaidi ya miaka mitano iliyopita upembuzi yakinifu, usanifu pamoja na tathmini kwa maana ya evaluation ilishafanyika na wananchi hawa wanadai kiasi cha fidia ya shilingi
8,552,777,000/= na hadi leo hawajapata fidia hiyo na hawajui wataipata lini. Mbali na hili jitihada za…
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Yah. Jitihada za RCC kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii zimekwama kwa sababu ya fidia hii haijalipwa. Je, Serikali italipa lini fidia hii kupisha maendeleo ya barabara hii kwa wananchi hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa sasa barabara hii imezuiwa kupitisha magari zaidi ya tani 10: Je, TANROADS ina mpango gani wa kurekebisha barabara hii ili shughuli za kiuchumi za wananchi hawa ziweze kufanyika kwa kupitisha magari ambayo ni zaidi ya tani 10?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Koka kwamba mara tutakapopata hizo shilingi bilioni 8.65 tutazitoa na kuanza kulipa fidia. Lini? Kama nilivyosema katika jibu la msingi, tunazitafuta hizo fedha na mara tutakapopata tutazilipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kitu kimoja; anafahamu kwamba barabara hii ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 – 2020, nimhakikishie, tuliahidi na tutatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kuiwezesha barabara hii ibebe magari ya zaidi ya tani 10, nimelipokea, nitawasiliana na Meneja wa TANROADS Mkoa tuone nini kifanyike ili ombi la Mheshimiwa Mbunge, ambapo ni mahitaji ya wananchi wake hasa wa Kata za Tangini na Pangani waweze nao kupata unafuu kiuchumi. Namwomba tu, kama anaweza kuharakisha, kama hawa wananchi wanaweza wakasamehe hiyo shilingi bilioni nane, nimhakikishie mwezi ujao tutaanza kujenga.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya mradi huu mkubwa kwa takriban shilingi bilioni 90 ambao umekamilika. Pamoja na pongezi hizi, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Bado kuna tatizo la msukumo wa maji kutoka Ruvu Juu ili yaweze kuwa na pressure ya kutosha kuwafikia watejea, tatizo linalotokana na uhafifu wa umeme. Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha tatizo hili, ili mradi huu uweze kuwa na mafanikio makubwa zaidi hususan kwa wananchi wa Kibaha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pamoja na kazi
nzuri hii, lakini bado maeneo ya Kidenge, Muheza, Kidagulo, Kikalabaka, Mikongeni na Mbwawa hawajakamilishiwa mradi wa usambazaji wa maji ili waweze kufaidi mradi huu. Je, kupitia bajeti hii tunayokwenda nayo Mheshimiwa Waziri yupo tayari kushughulikia na kuhakikisha miradi hii inakamilika ili wananchi waweze kupata huduma hii nzuri kwa mradi huu ulio bora ambao umeshakamilika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Koka kwa jinsi ambayo anawapenda wananchi wake wa Kibaha Mjini. Kwa sababu mara zote anafuatilia kwa kupiga simu kwa kuja Ofisini moja kwa moja, kumwona Mheshimiwa Waziri pamoja na mimi kuhusiana na tatizo la maji la Mji wa Kibaha, kwa sababu Mji wa Kibaha kwa sasa unapanuka sana. Swali la kwanza, pressure ni kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji tuligundua kwamba hakukuwa na umeme wa kutosha ili kuweza kuendesha mtambo ule kwa sababu ni mkubwa. Kwa sababu hiyo, tulitenga fedha na tayari sasa kazi inafanyika na imeanza kukamilika ili kuwa na umeme wa kutosha ambao utaweza kuendesha mtambo uliojengwa ambao ni mtambo mkubwa. Kwa hiyo, hili suala Mheshimiwa Koka ni kwamba tunalimaliza muda wote wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama nilivyozungumza katika swali letu la msingi kwamba kupitia awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, tunatenga fedha kuhakikisha kwamba maeneo yote ya Kibaha na maeneo yote yanayopitiwa na bomba kuu la kutoka Ruvu kwenda Dar es Salaam tutahakikisha kwamba tunaweka miundombinu ya kutosha ili wananchi waweze kupata maji, umbali wa kilomita 12 kutoka eneo la bomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba programu hiyo tunayo ambayo imeanza kutekelezwa kwenye mwaka wa fedha.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Nabu Spika, nakushukuru na namshukuru Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa jitihada kubwa ya kusambaza umeme. Pamoja na hayo nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, toka mradi huu ulipoanza na wananchi kufanyiwa tathmini ni takribani miaka mitatu na wananchi hawa wameacha shughuli zao za maendeleo na hawana fedha kwa ajili ya kuanzisha shughuli nyingine ya maendeleo. Ni lini sasa Serikali itaanza kulipa fidia hii ili wananchi wajiandae kwa ajili ya kuwa na shughuli za maendeleo mbadala katika maeneo mengine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika mradi wa umeme REA III, Vijiji vya Jimbo la Kibaha Mjini ikiwa ni pamoja na Mkombozi, Lumumba, Kalabaka, Saeni, Jonuga, Mbwawa, Miomboni, Madina, Mbwate, Visiga, Viziwaziwa, Mtakuja, Maili 35 na Kumba vimeondolewa katika utaratibu mzima wa REA III na katika kufuatilia kwangu hatujapata majibu ni utaratibu gani utatumika kuipatia Mitaa hii umeme kama ilivyokuwa imepangwa na wananchi wana mtafaruku mkubwa. Je, Serikali sasa ina mpango gani mbadala kuhakikisha mitaa hii yote inaendelea kupata umeme kama tunavyojua umeme ni uchumi na maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Koka hongera sana katika kufuatilia masuala ya fidia. Mmefika hatua nzuri kwa sababu ya jitihada zako.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika maeneo yaliyofanyiwa tathmini kama nilivyoeleza kwenye swali langu na jibu langu la msingi kwamba taratibu zimeshakamilika na ni matarajio yetu mwisho wa Desemba na mwanzo wa Januari mwakani, malipo yatakuwa yameshaanza kutoka. Kwa hiyo, wananchi wa maeneo yale wategemee fidia katika kipindi hicho, lakini kama nilivyosema, taratibu za uhakiki zimeshakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili; nitumie nafasi hii kusema kwamba yako maeneo ambayo kwa kweli ni mitaa ingawa katika hali ya kawaida inaonekana kama vijiji. Maeneo haya ambayo yako mjini kwa sababu miradi ya REA inakwenda vijijini, uko mradi unaoitwa urban ratification ambao katika Wilaya ya Kibaha hasa Mjini na maeneo ya jirani yatapelekewa umeme kupitia mradi huu. Mheshimiwa Koka kwa bahati nzuri sana, katika maeneo ya Lumumba, Mtakuja na Viziwaziwa ziko transformer 11 zimetengwa kwa ajili yakupelekewa umeme katika maeneo hayo.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwa niaba ya wananchi wa Kibaha nishukuru kwa kutupatia hiyo 1.4 bilioni katika upanuzi wa hospitali hii, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ya Tumbi inapokea takribani asilimia nane hadi 10 ya majeruhi wote Tanzania. Licha ya miundombinu hafifu katika chumba cha kupokelea majeruhi hospitali hii imekuwa ikijitahidi kupokea majeruhi na kuwatibia na kwa mujibu wa taratibu majeruhi hutibiwa bila kutozwa chochote na hatimaye Serikali inapaswa kurejesha fedha hizi kwa hospitali ikiwa pamoja na Hospitali ya Tumbi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takribani miaka mitano fedha hizi hazijarejeshwa katika hospitali hii, jambo ambalo limepelekea huduma kuwa hafifu na za kubabaisha. Je, Serikali sasa itarejesha lini fedha hizi ikiwa ni pamoja na special package kulingana na idadi kubwa ya majeruhi yanayokwenda katika hospitali hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kituo cha afya mkoani ambacho kinahudumia takribani wakazi 150,000 wa Mji wa Kibaha kina miundombinu hafifu, wagonjwa wanalala chini jambo ambalo linapelekea hata wagonjwa wengine kupewa rufaa pasipostahili kwa ajili ya kukosa miundombinu ya kutolea huduma.
Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kupandisha hadhi kituo hiki ikiwa ni pamoja na kukipatia miundombinu na vifaa tiba ili kiweze kukabili na kuwahudumia wananchi wa kibaha ambao ni mji unaokua kwa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maswali yake Mheshimiwa Koka ni maswali ya msingi. Hospitali ya Kibaha ni hospitali ambayo iko pembeni mwa Barabara Kuu ya Morogoro, na karibuni katika kipindi kirefu sana tumeshuhudia ajali nyingi zikijitokeza katika maeneo haya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge unalolizungumza ni jambo la kweli kabisa. Katika swali lako la kwanza Serikali tutafanya analysis ili kuisaidia hospitali hii iweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la special package ya kusaidia hospitali hii, nadhani Serikali nayo itafanya kwa kina ili jambo hili liweze kwenda vizuri ili Hospitali hii ya Tumbi iweze kutoa huduma kwa wananchi kama inavyokusudiwa. Naamini si wananchi wa Mkoa wa Pwani au wa Kibaha peke yake, hapana, ni wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wengi wao wakipata ajali hospitali hiyo ndiyo limekuwa kimbilio la karibu zaidi kabla mtu mgonjwa hajafikishwa katika Hospitali ya Muhimbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, juu ya kituo cha afya cha mkoani; ni kweli na mimi niliweza kufika kituo kile mwaka jana mwanzoni. Sasa hivi mgonjwa yeyote hataruhusiwa kwenda Hospitali ya Tumbi mara baada ya Hospitali hii kupandishwa. Kila mgonjwa wa Kibaha Vijijini lazima atibiwe katika kituo hiki ndipo apewe referral na yule wa Kibaha Mjini atibiwe kituoni pale ndipo apewe referral; lakini kituo kile cha afya kina changamoto kubwa sana. Bahati nzuri watu kutoka Wizara ya Afya walikuja pale kufanya analysis kuangalia ni jinsi gani kinaweza kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya pale awali ilionekana ina upungufu mkubwa, ikiwepo wodi ya wazazi, lakini Mbunge nikushukuru sana kwa juhudi kubwa uliyofanya na wananchi wako na viongozi wako, wodi ya wazazi sasa hivi pale imejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, licha ya kujengwa ile wodi ya wazazi, lakini mmetenga karibu 700,000,000. Katika milioni 700 karibu milioni mia mbili arobaini na, ni kwa ajili ya ukarabati, mtajenga theatre ambapo kabla hospitali hii haijapandishwa kuwa hospitali ya Wilaya lazima kuwe na theatre room na bajeti ya mwaka huu pia mmetenga bajeti hiyo, lakini mmetenga bajeti ya kununua standby generator.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme kwamba katika bajeti ya mwaka huu naamini kwamba tutasukuma kwa kadri iwezekanavyo ili pesa hizi ziweze kupatikana ili miundombinu ile ikamilike ili Kituo cha Afya cha Mkoani kiwe na hadhi ya Hospitali ya Wilaya ili wananchi wa Kibaha waweze kupata huduma bora katika maeneo haya. Ahsante sana.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Ikumbukwe kuwa Mji huo wa Kibaha ndio Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani wenye Wilaya sita na yenye idadi ya watu zaidi ya 1,100,000, Mji huu wa Kibaha umekuwa unaongoza katika ujenzi wa viwanda ukiwa na viwanda vikubwa sita, vya kati 16, vidogo 78, vinavyoendelezwa kujengwa vitatu na ambavyo vipo katika taratibu za ujenzi kwenye makaratasi 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukipata kikwazo kikubwa hasa kwa wawekezaji hasa wanapotaka kuendeleza viwanda wanapobaini kwamba huu ni mji tu na wala hauna hadhi ya Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo basi na tukizingatia kwamba Sera Kuu ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwenda katika uchumi wa kati ni viwanda na inatekelezwa vizuri na kipekee na kwa kuongoza kwa mji wa kibaha, ni kwa nini sasa Serikali isitoe upendeleo wa pekee na kuupatia mji huu hadhi ya manispaa ili tuweze kwenda kwa kasi kulingana na sera ya Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wa Kibaha kwa utiifu na unyenyekevu kabisa wanaomba ombi lao hili lipewe uzito wa kipekee. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nimsifu Mheshimiwa Silvestry Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kwa jinsi anavyopangilia hoja zake kwa niaba ya wananchi wa Kibaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa na mwongozo wa Serikali wa mwaka 2014 bado tunahimiza kwamba Halmashauri ya Mji wa Kibaha ifanye kila linalowezekana ili kuweza kutimiza vigezo hivi nilivyovitaja mwanzoni kwenye jibu la msingi ili waweze kufikia hadhi ya kupandishwa kuwa Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kwa kweli tunaungana nao wakazi wa Kibaha. Ni mji wa muda mrefu na sisi tunashangaa kwa nini hawajaweza kuwavutia watu wengi waongezeke kwenye Mji. Hii idadi ya watu wote waliotaja inafanana na idadi ya wakazi wa Mkoa mzima wa Pwani. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka 2012, Mji wenyewe wa kibaha ambao ndio uko kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha ulikuwa na wakazi 128,488, hizo ndizo taarifa tulizonazo. Kwa hiyo pamoja na kutilia uzito ombi lake bado tunahimiza kwamba Mji wa Kibaha wajitahidi kutimiza vigezo vilivyowekwa. Ahsante sana.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea ikiwa ni pamoja na hii ya umeme, pia Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi kubwa wanayofanya kufuatilia miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kulipa fidia ni kuwawezesha wananchi wanaoathirika na miradi hii mikubwa ya maendeleo ili waweze kupata fedha za kuweza kufanya shughuli nyingine mbadala za kiuchumi wanapopisha maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia zimekuwa zikichelewa sana, wakati mwingine takribani mpaka miaka mitano huku wananchi hawa wakitaabika bila kuweza kufanya shughuli mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza. nafahamu uhakiki wa tathmini na hususan katika maeneo ya Kibaha Mjini, Vijijini na mpaka Chalinze ulikwishakamilika toka 2017.

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Je, ni lini sasa kwa uhakika wananchi hawa watalipwa fedha zao?
Swali la pili, Serikali sasa haioni kwamba kuna haja ya kufanya maandalizi ya malipo haya mapema ili tathmini ikishafanyika wananchi waweze kupata malipo yao mapema bila kupata usumbufu na malalamiko makubwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, Koka. Kwanza napenda kumshukuru sana na kumpongeza kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia miradi yetu kwenye sekta ya nishati na hususan katika suala hili la fidia kwa mradi huu wa Kinyerezi hadi Arusha, pia tumepokea pongezi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo swali letu la msingi limesema kwamba fidia hii ya shilingi bilioni 21.56 zimetengwa kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018. Ni matarajio yetu kwa kuwa uhakiki wa fidia hii umekamilika na matarajio yetu kwamba mwisho wa mwaka huu wa fedha, pesa hizi zitalipwa na naomba niendelee kuwashukuru wananchi wa maeneo ya Kisarawe, Kinyerezi yenyewe, Kibaha, Chalinze kwa uvumilivu wao. Napenda niwathibitishie Serikali italipa fidia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; tunapokea huo ushauri na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kweli nia ni hiyo ya kuona kwamba maeneo wanayochukua kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa, wananchi wanawezeshwa. Ndiyo maana wakati wa bajeti tutaomba atuunge mkono. Tumetenga kabisa kiwango kikubwa tu cha fidia kwa miradi mikubwa ambayo inatarajiwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha huo 2018/2019 na kuendelea. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. SILYVESTRY F. KOKA: Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nia njema ya Serikali kurejesha baadhi ya maeneo ya shamba la mitamba la Kibaha kwa wananchi, kuna eneo dogo ambalo wananchi wanalikalia linaitwa maarufu Vingunguti. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari mimi na yeye kwenda kukutana na wananchi ili kuona muafaka kati yao na shamba hili la mitamba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa machinjio ya kisasa yaliyokuwa yanajengwa pale kwenye Ranchi ya Ruvu ina zaidi ya miaka minne haijaendelea na ujenzi na huku mahitaji ya nyama bora ni makubwa kwa Pwani na Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza ujenzi wa machinjio haya hata kwa ubia kati ya wananchi na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anataka kujua kama niko tayari kwenda Kibaha na nataka kumhakikishia niko tayari kwenda Kibaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, anataka kujua nini msimamo wa Serikali juu ya machinjio ya kisasa ya pale Ruvu. Ni kweli mradi huu umekawia, lakini kupitia mradi wa uendelezaji wa sekta ya kilimo, Serikali ya Korea imeonesha nia ya kutukopesha dola za Kimarekani takribani milioni 50 ambapo hivi sasa utaratibu Serikalini unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na moja ya miradi ambayo itakwenda kunufaika na pesa hizi ni pamoja na machinjio ya kisasa ya Ruvu ambayo haitaishia kaktiak kuwa machinjio tu, tutakuwa na Leather Complex ambayo itakwenda kutengeneza na uchakataji wa ngozi. Pia vilevile tutakuwa tayari kutengeneza bidhaa mbalimbali za ngozi kupitia mradi huu wa machinjio ya pale Ruvu. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ya ujenzi wa barabara inayofanya. Pamoja na pongezi hizo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa kero kubwa kwa wananchi wetu ni fidia. Barabara hii ya kilomita 23 ina jumla ya fidia ya bilioni 8.9; je, kwa nini Serikali sasa isilipe wananchi hawa fidia wakaweza kufanya shughuli zao za kiuchumi na ikaendelea na ujenzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna barabara ya Kwa Mathias mpaka Msangani ambako ndiyo Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi la Ardhini (Land Force). Barabara hii ina ahadi ya lami muda mrefu. Je, Serikali imefikia wapi kukamilisha au kujenga lami hii katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kulipa hizi fidia kwa wananchi. Nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara nyingi nimemsikia hapa ndani ya Bunge na hata tukizungumza kule nje amezungumza juu ya fidia hii ya wananchi wa maeneo haya. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba suala hili linaendelea kushughulikiwa na kwa mujibu wa taratibu na sheria wananchi watalipwa mapema sana fidia yao hii ambayo Mheshimiwa Mbunge anaitaja. Kwa hiyo, nimwondoe hofu pamoja na wananchi kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kuhusu barabara ya Kwa Mathias – Msangani ni ahadi ya Serikali. Katika mwaka huu wa fedha 2018/2019, Mheshimiwa Mbunge anatambua tumetenga fedha kwa ajili ya kuendelea kuboresha barabara hii ili hatimaye iweze kutengenezwa katika kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe hofu wananchi wote wa maeneo ya Kwa Mathias na maeneo ya Msangani na maeneo yote ya Kibaha kwa ujumla tu kwamba, Serikali imeitazama barabara hii na kuangalia umuhimu wa maeneo yenyewe tutaendelea kuiboresha ili barabara hii iweze kupitika vizuri zaidi na kutoa huduma kwa vikosi vyetu ya Jeshi vlivyopo katika maeneo haya.
MHE. SILYVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nichukue fursa hii kwa dhati kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kazi kubwa anayoifanya katika miradi ya umeme na hususan mradi mkubwa wa Stiegler’s gorge ambao unakwenda kutuondolea gharama kubwa ya umeme hakika ni neema. Nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri ameshatutembelea zaidi ya mara tatu katika Jimbo langu, anachapa kazi na kwa pamoja Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, pamoja na kuchukua muda mrefu katika fidia hii, lakini wananchi wa Kibaha wana taarifa kwamba wenzao wa Arusha na Singida walikwishakupata malipo, kama hivi ndivyo, je, wanapata malipo kwa ubaguzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika miradi ya ujazilishaji katika Mji wa Kibaha yaani densification Mitaa ya Muheza, Mbwate, Lumumba, Sagale, Mkombozi, Mbwawa Hekani, Kumba na Mtakuja miradi hii bado haijaanza utekelezaji kama ilivyokuwa imeahaidiwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha miradi hii ambayo wananchi wanaisubiri kwa hamu ili waweze kupata umeme na kukidhi mahitaji yao ya kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Silvestry Koka, ndugu yangu kutoka Jimbo la Kibaha Mjini kuwa kwanza tumepokea pongezi na nichukue fursa hii kumpongeza yeye binafsi Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzake wa Mkoa wa Pwani ambao wanapitiwa na mradi huu akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Kibaha Vijijini, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze pamoja na dada yangu Mheshimiwa Bonnah, Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa kazi ya kuwasemea wananchi wao na kufuatilia masuala ya fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema nimefanya ziara katika maeneo yao mbalimbali, lakini nataka niseme moja ya jambo ambalo limejitokeza baada tu ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuja na mapinduzi ya kutaka kutekeleza mradi wa Rufiji Hydro Power Stiegler’s, njia hii ya msongo wa kilovoti 400 ilikuwa inaitwa Kinyerezi – Chalinze - Tanga. Kwa hiyo baada ya kuja na ule mradi ilikuwa lazima sasa kuwe na line ya kilovoti 400 kutoka Rufiji mpaka Chalinze ambayo inaunganishwa na Dodoma na kimsingi kwa ajili pia ya kuwezesha treni yetu ya umeme ambayo kama maelezo yalitolewa inatarajia kuanza kazi Novemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi, nami mwenyewe pia ni muhanga kwa sababu nawakilisha wanawake wa Mkoa wa Pwani. Nataka niseme kwa kweli kwa kuwa mradi huu wa ujenzi wa njia hii ya msongo wa kilovoti 400unaanza kutekelezwa Januari, 2020, hatuwezi kuanza mradi huu bila kuwalipa wananchi fidia. Kwa hiyo kiwango kilichotajwa kwenye jibu langu la msingi cha bilioni 36 na kwamba ndio wakati wake muafaka sasa wa kulipa kwa sababu hata fidia inayolipwa maeneo ya Singida, maeneo ya Mkoa wa Manyara kwa ajili ya njia ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida mpaka Namanga ni kwa sababu mradi umeanza kutekelezwa na ndio maana lazima ulipe fidia maana yake ni moja ya masharti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa maeneo haya niliyoyataja, tunawashukuru na tunawaomba radhi kwamba wamechukua muda mrefu lakini wamekuwa na subira, waendelee na kwamba sasa kwa kweli mchakato wa malipo upo mbioni kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ametaja maeneo ya Muheza, Lumumba, Madina, Mtakuja, Mbwawa kote huku mimi na Mheshimiwa Mbunge tulifanya ziara pamoja, nataka niwathibitishie wananchi kwa kazi ambayo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anafanya kwamba maeneo haya tuliahidi kuyapelekea umeme kwa mradi wa Peri-urban na huo mradi wa Peri-urban pia unagusa Jimbo ya Ukonga kwa ndugu yangu Mheshimiwa Waitara pia kwa ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya maeneo ya Kigamboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa hatua iliyofikiwa, mradi huu unaanza mwezi wa Nne kwa sababu taratibu zote za manunuzi zimekamilika na kwa sasa wakandarasi wale au wale ambao wametenda ipo hatua ya post qualification. Kwa hiyo Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa maeneo ambayo yanakua kwa kasi kupelekea mradi wa Peri-urban. Naomba tu waendelee kuvumilia mwezi wa Nne mwishoni utaanza huu mradi. Ahsante sana.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kweli nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Kibaha kumpongeza sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa kazi nzuri ya ujenzi wa daraja lile la Ubungo, lakini vilevile barabara hii kubwa ambayo kwa sasa itaishia Kibaha na itaokoa gharama kubwa za msongamano wa magari kutoka Mjini Dar es Salaam kuja Pwani. Pamoja na pongezi hizo kubwa, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo ni kilometa 19.2 inaishia kidogo tu baada ya mizani ya zamani pale Kibaha. Maana yake ni kwamba ile trafic ya magari yote ambayo yatakuwa yanakwenda mikoani yatakuja kwa kasi na yataishia pale ambapo ni almost katikati ya mji wetu mdogo wa Kibaha. Kwa maana hiyo ni kwamba Mji wetu wa Kibaha magari yatakuwa mengi na hakika utakuwa umesimama wananchi wa Kibaha hawataweza kufanya shughuli zao za kiuchumi katika mji ule kwa sababu ni mdogo na magari yatakuwa mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikao chetu cha Regional Road Board tuliomba barabara hii angalau iongezewe mpaka pale Kwa Mathias ili sasa iweze kuhudumia Mji ule wa Kibaha na kuleta maana njema zaidi ya maendeleo katika mji wetu. Vilevile kama tutamwongezea mkandarasi huyu aliyepo kazini gharama zitapungua kwa maana hakutakuwa na mobilization hata process za tenda. Je, Serikali ina mpango gani sasa kukubaliana na ombi letu ili barabara hii iweze kuleta manufaa zaidi katika mji wetu wa Kibaha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili barabara Kwa Mathias hadi Msangani ambayo inakwenda mpaka Makao Makuu ya Land Force tumejenga mita 400 za lami na barabara ya TAMCO kwenda Mapinga inaendelea kujengwa kilometa 4 na wananchi hawajapata fidia. Je, Serikali ina mpango gani kukamilisha barabara hizi na kuhakikisha wananchi wanapata fidia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nizipokee pongezi nyingi alizotoa Mheshimiwa Koka lakini pia nimpongeze sana kwa juhudi anazofanya kwa kushirikiana na Mkoa wa Pwani kuhusu maendeleo mbalimbali ya Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anazungumzia juu ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii kutoka eneo ambalo tunaishia kwa maana ya Maili Moja kwenda mpaka Kwa Mathias. Kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kwamba ujenzi wa kilomita 19.2 ni awamu ya kwanza. Kwa hiyo, tutaendelea na awamu zingine kadri tunapopata pesa kwa maana ya kuendelea na ujenzi kwenye eneo hili kupita Picha ya Ndege - Kwa Mathias - Mlandizi – Chalinze. Kwa hiyo, nimtoe hofu tu tumejipanga vizuri na Serikali tunafahamu kwamba baada ya upanuzi huo wa barabara kwa kweli tutaleta magari mengi sana kwa upande wa Kibaha na maeneo haya Mlandizi kwa maana hiyo tutakuwa tumehamishia foleni kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri kwamba tutakuja na awamu zingine ili tuweze kutatua na kuendelea kufanya maboresho makubwa ya ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumzia barabara ile ya Kwa Mathias kwenda Msangani na barabara ya kutoka TAMCO kwenda Mapinga ambayo ni kilometa 24 na tumeshapata wakandarasi kuanza ujenzi katika maeneo haya. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la fidia tunalishughulikia kwa sababu ni utaratibu na kanuni kwamba kabla mkandarasi hajaanza kazi fidia zitakuwa zimelipwa. Tunafanya jitihada za kuwasiliana na wenzetu Wizara ya Fedha ili tuweze kulipa fidia. Pia niwahakikishie tu wananchi wa maeneo haya waondoe hofu tumejipanga kuwafanyia maboresho ya barabara zao lakini pia tutawalipa stahili zao za fidia kama ilivyo kulingana na taratibu zetu.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kuipongeza Serikali yetu kwanza katika suala la afya ambapo tayari ilitupatia milioni 500 kwa upanuzi wa Kituo chetu cha Afya Mkoani na imetekelezwa, lakini vilevile bilioni moja na laki tano kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mradi ambao unaendelea, sambamba na hilo nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ikama ya Watumishi wa Afya ni 360 na tulio nao ni 255 tunao upungufu wa Watumishi 105 katika Idara yetu ya Afya jambo ambalo linasababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wanapokwenda kupata huduma na tukizingatia kwamba sasa Hospitali ya Wilaya inakwenda kukamilika mapema; je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ajira kwa upungufu huu ili kusudio la kutoa huduma hii liweze kukamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vilevile ikama ya Watendaji wa Mitaa ni 73 na tunao 50 na tuna upungufu wa Watendaji 23 na tunapata malalamiko sana hasa tunapofanya ziara katika mitaa yetu kwa wananchi wetu na ikizingatia kwamba tunakwenda sasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa; je, ni lini sasa Serikali itajazia upungufu wa watumishi hawa ili huduma hii iweze kuwafikia wananchi na tusiwe na malalamiko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Silvestry Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunamshukuru sana kwa pongezi zake kwa kazi nzuri ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi Awamu ya Tano. Swali lake la kwanza ametaka kujua ni lini tutapata Watumishi kwenye Sekta ya Afya.

Tulizungumza mara kadhaa, turudie tu kwamba tumeshaangalia changamoto hii katika maeneo mbalimbali pamoja na Kibaha, lakini tumeshaomba Kibali Utumishi kupata Watumishi wa Sekta ya Afya 12,000. Kwa wakati huo tukipata kibali hiki na kuajiri tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba watumishi hawa watapelekwa katika eneo hilo wakatoe huduma kwa watu wetu ili waendelee kufurahia maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anasema kuna upungufu katika Watendaji wa Mitaa na Vijiji na kwa sababu kuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ni kweli kwamba kuna baadhi ya maeneo katika mitaa yetu na vijiji hatuna watendaji, lakini jambo hili la uchaguzi naomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na Watanzania wengine wote, hao hao wanaosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni Watumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kupata Watendaji wa kila siku kutoa huduma kwa watu wetu, lakini wakati wa uchaguzi kama itatokea kuna kijiji au mtaa ambao hauna Mtendaji wa Kijiji, basi wale Watumishi wa Umma waliopo pale watafanya kazi hiyo kwa niaba ya Serikali na tunahakikisha kwamba jambo hilo litaenda vizuri bila tatizo. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri na wananchi wa Kibaha Mjini wanaunga mkono jitihada za Serikali za maendeleo hususan katika sekta ya umeme.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kama unavyoona ni takribani miaka sita sasa na leo ni mara ya nne nauliza swali hili hapa Bungeni. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri atoe kauli thabiti kwamba malipo haya kwa wananchi wa Mnalugali, Boko, Sofu, Zegereni watalipwa lini fidia hii ili sasa na wenyewe waweze kushiriki na kufurahia miradi hii mikubwa ya umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, miradi ya umeme katika Mji wa Kibaha na hususan peri-urban na densification imekuwa ikisuasua na haijakamilika. Miradi hii imepita pembezoni mwa wananchi wengi na wanalalamika kwamba hawakuweza kufikiwa na miradi hii. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha sasa miradi hii inakamilika na wananchi wanapata umeme ili kufaidi maendeleo na matunda ya nchi yao?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Koka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli usanifu wa mradi huo ulianza miaka mingi toka miaka mwaka 2015 na 2016 lakini baadaye tulipoanza kutekeleza mradi mkubwa wa Julius Nyerere mwaka 2018, tulifanya usanifu upya ili kuhakikisha kwamba mradi huu unakuwa ni mpana na endelevu. Mradi huu ambao unahusisha fidia ya wananchi wa Kibaha utahusisha pia fidia ya wananchi wa kutoka Kinyerezi, Kiluvya, Chalinze, Kibaha mpaka kufika Dodoma na unaelekea mpaka Singida.

Mheshimiwa Spika, taratibu kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, tumeanza kufanya matayarisho ya malipo na sasa tumetenga shilingi bilioni 21.56 kwa ajili ya kuwalipa wananchi wote. Wananchi wa Kibaha peke yake ambao wanafika 432 wenye jumla ya shilingi milioni 932 malipo yao yameshaanza kutayarishwa. Malipo hayo yanakwenda sambamba na ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka mradi mkuu wa Julius Nyerere utakaofua megawatt 2,115 kutoka Rufiji-Chalinze, Chalinze- Dar es Salaam (kilometa 115) na pia Chalinze-Dodoma, ambapo tumetenga jumla ya shilingi milioni 32.82. Kwa kuwa ujenzi wa mradi wa huu utaanza kabla ya mwezi Juni, ni matumaini yetu na kwa maandalizi mazuri ya watu wa Wizara ya Fedha tutaanza kuwalipa wananchi kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusiana na suala la peri- urban na densification, tumeanza programu ya kupeleka umeme kwenye maeneo yote ya ujazilizi. Maeneo ya kutoka Dar es Salaam mpaka hapa Dodoma takriban vitongoji 12,822, utekelezaji umeanza katika maeneo Dar es Salaam hadi Kibaha kwa vitongoji 272 ambapo vitongoji vya Mheshimiwa Koka vimo. Pia tunapeleka umeme kwenye peri- urban anayoizungumza Mheshimiwa Koka kwa maeneo yanayofanana na vijiji ya Kibaha ambayo siyo vijiji kwa kwa gharama ya shilingi 27,000 na utekelezaji umebaki mitaa 12 kati ya mitaa 128. Mradi huu unakamilika mwezi Mei, mwaka huu.

Napenda kumwambia Mheshimiwa Koka awape taarifa wananchi wa Kibaha kwamba peri-urban na densification katika eneo lao inakamilika mwezi Mei, mwaka huu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SIYLVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu haya ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, toka barabara ile ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha kukaribia kukamilika kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magari katika Mji wa Kibaha kiasi kwamba kutoka Kibaha Mjini mpaka pale Mlandizi kiasi cha kilometa 15 unaweza ukatumia hata masaa mawili na nusu wakati kuna barabara ya zamani kutoka pale Picha ya Ndege kupita Kongowe hadi Visiga ambayo ingelirekebishwa tu ingeweza kuondoa huu msongamano wakati mpango wa ujenzi unaendelea. (Makofi)

Swali la kwanza, je, ni lini sasa Serikali inakamilisha ujenzi/inajenga barabara ya njia nane kutoka Kibaha Mjini mpaka Mlandizi angalau kuondoa usumbufu huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara ya kuanzia pale TAMCO hadi Mapinga na kuanzia kwa Mathias hadi Msangani zinazojengwa kawa kiwango cha lami zinasuasua sana ujenzi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha na kukamilisha ujenzi huo ili matunda mazuri ya kazi ya Serikali yaweze kupatikana kwa wananchi wa Kibaha Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Koka Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nielekeze Meneja na TANROADS Mkoa wa Pwani ahakikishe kwamba anaondoa changamoto zote ambazo amepelekea barabara hii ujenzi wake unasuasua na kama kuna changamoto ambazo ameshindwa kuchukua hatua basi Wizara ipo tayari kutoa ushirikiano ili jambo hili na barabara ijengwe kwa wakati na kiwango kinachotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto ambazo ametoa hapa na msongamano wa magari tutauchukulia hatua, Serikali inafanya kazi hii na Mkandarasi yupo site Sasa kwa sababu tunaenda kwenye weekend hii naomba nimuhakikishe kwamba kabla ya Jumatatu atakuwa amepata majibu sahihi nini kinafanya barabara isuwesuwe iweze kurekebishwa mapema sana na hata jana nilipigiwa simu na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi ambao leo tuna kazi maalum wakikwama barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwelekeze Katibu Mkuu tunapojiandaa sasa muda mfupi ujao Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwenda kupiga kura za ndio za Mama Samia kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, changamoto hizo kwa wajumbe wanaporudi kwenda makwao hasa Dar es salaam hasa na maeneo jirani ziwe zimekomesha mara moja ahsante sana. (Makofi)
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, asante. naipongeza Serikali kupitia DAWASA kwa kazi nzuri iliyofanyika kule Mbwawa wananchi sasa wamepata maji kwa mradi kukamilika kwa asilimia 90. Pamoja na hayo nina maswali mawili madogo ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa matenki mawili ya maji katika Kata ya Pangani, kwa maana ya Mtaa wa Vikawe na Mtaa wa Pangani, unaodhaminiwa na Benki ya Dunia unajengwa kwa kusuasua. Tenki la Vikawe limefikia asilimia 50, lakini tenki la Pangani kwa ajili ya kuhakikisha sasa wananchi wa Kata ya Pangani wote wanapata maji bado halijaanza kujengwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhimiza sasa, ili hili tenki la pili liweze kuanza kujengwa?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, wananchi wa Kata ya Misugusugu na Visiga na hususan maeneo ya Zogoale, Jonuga pamoja na Saeni, kupitia Zegereni Viwandani, wana shida kubwa ya maji na wanahangaika kutumia maji ya visima na haya ni maeneo muhimu ya uchumi katika Jimbo letu la Kibaha Mjini. Ninafahamu kuna mradi wa takribani bilioni 3.3 unaotakiwa kujengwa.

Je, ni lini Serikali sasa inaanza kujenga mradu huu, ili kuwaondolea wananchi kero na kustawisha uchumi katika Mji wetu wa Kibaha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Silvestry Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mji wa Kibaha ni moja ya miji ambayo Serikali imeelekeza fedha nyingi kwa kuona kwamba, maji sasa yanakwenda kupatikana. Katika eneo la Pangani ni mradi mkubwa ambao tayari Serikali mpango ni kuelekeza zaidi ya bilioni tano na kazi zinatarajiwa kuanza mapema robo ya kwanza ya mwaka wa fedha ujao, kwa maana ya kuanzia mwezi wa tisa tunatarajia kazi itaenda kuanza katika mradi huu.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika maeneo ya viwandani, kama mwenyewe Mheshimiwa Mbunge alivyoongea, na nipende tu kumshukuru kwa kuweza kutoa pongezi zake kwa Serikali. Ni kweli Wizara bado imelekeza fedha za kutosha zaidi ya bilioni tatu na katika mwaka ujao wa fedha tunatarajia mradi huu uweze kutekelezwa na kasi ya mradi huu itategemea upatikanaji wa fedha katika Wizara, lakini lengo letu kubwa tunaelekea kwenye mageuzi makubwa. Miradi kama hii yote mikubwa tutahakikisha tunaisimamia kwa wakati.
MHE. SILYVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa sababu kwa kweli kwa kipindi kifupi imefanya kazi nzuri na hasa ilivyoondoa mkanganyo wa ulipaji wa kufungiwa umeme kwa wananchi ili tunalishukuru sana Serikali yetu imefanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kibaha bado tuna matatizo makubwa ya kusambaziwa umeme kwa wananchi na hususani katika mitaa ya Viziwaziwa kwa maana ya Sagale Magengeni, Sagale kambini lakini Muheza pamoja na maeneo mengine ya Misugusugu kwa maana ya Zogohale na Miomboni pia vilevile Madina hadi Kiembeni toka 2016 baadhi ya wananchi bado hawajapata umeme.

Je, ni lini sasa wananchi hawa watawekewa umeme ili waondokane na adha ya kukosa umeme katika Mji wa Kibaha?

Swali la pili, toka mwaka 2014 wananchi wengi wa Jimbo la Kibaha mjini walisimamishiwa maendeleo katika maeneo yao ambayo kunategemewa kupita mradi wa umeme wa msongo wa Kilowatt 400 kutoka Kinyerezi kuelekea Chalinze wasifanye lolote ingawa hadi leo bado wengine wanaendelea hata kutozwa kodi za ardhi.

Je, ni lini wananchi hawa watapata fidia zao ili waweze kufanya maendeleo maeneo mengine na kuondokana na adha hii?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Koka Mbunge wa Kibaha kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baadhi ya maeneo ya Mji wetu wa Kibaha hayajapata umeme lakini tayari Serikali imejitahidi kupeleka umeme katika hayo maeneo machache ambayo ni jitihada ya Mheshimiwa Mbunge katika kufanya ufuatiliaji wa kina kuhakikisha maeneo yote yanapata umeme. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote ya Kibaha yataendelea kupelekewa umeme kupitia mradi wetu wa Peri- Urban na tayari Mkandarasi huyo ameshaongezewa scope ya kazi kwa hiyo maeneo yote ya Ziwaziwa na mengine ambayo yametajwa na Mheshimiwa Mbunge yote yatafikiwa na umeme kadri tunavyozidi kuendelea mbele kwasababau ni jukumu la TANESCO na REA na Serikali kuendelea kupeleka umeme kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, ni kweli kwamba kuna maeneo ambayo yalitwaliwa na Serikali kwa nia ya kupitisha mradi wa Msongo wa kilovolti 400 kusafirisha umeme na sasa utakuwa unasafirishwa kutoka Chalinze kuelekea Kinyelezi kwa sababu uzalishaji mkubwa unafanyika katika maeneo ya Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imetoa fedha kwa TANESCO takribani Billioni 29.6 na kuanzia Julai, Mosi fidia zitaanza kulipwa kwa wananchi wa maeneo ya Chalinze, maeneo ya Kibaha na maeneo ya Kinyerezi kwa ajili ya kupisha mradi huo uanze kujengwa mara moja.
MHE. SYLVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya TAMCO - Mapinga - Kibaha inayojengwa kiwango cha lami imekuwa inasuasua kwa muda mrefu, lakini pamoja na hilo wale wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hii hawajalipwa fidia hadi leo kwa maana ya wananchi wa kata ya Tangini na Pangani. Je, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia kama kwa mujibu wa sheria ulivyo?

Swali la pili barabara ya zamani kwa maana ya Dar es Salaam - Morogoro inayoanzia sasa Picha ya Ndege mpaka Mlandizi ni barabara ambayo ni kimbilio la wasafiri na wasafirishaji hasa barabara hii kubwa inapopata tatizo la ajali na kufunga barabara.

Sasa kwa umuhimu huo ni lini Serikali itaweka nguvu kurekebisha barabara hii ili iweze kupitika na kusaidia kutokuondoa msongamano wa barabara kubwa wakati kunapokuwa na ajali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Sylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara ya TAMCO - Mapinga kumekuwa na ujenzi wa kusuasua na pia baadhi ya watu hawakulipwa fidia. Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalifahamu jambo hili na inalifanyia kazi kuhakikisha kwamba hawa watu wanalipwa na ujenzi huu unakamilika kwa muda kwa hii barabara ya TAMCO - Mapinga ambayo ni barabara muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu barabara aliyosema ambayo itakuwa ni msaada mkubwa sana kwa ajili ya kusaidia panapotokea changamoto kwenye eneo hili la picha ya ndege naomba nichukue suala la Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kwa maana ya Wizara kupitia TANROADS tutalifanyia kazi kuhakikisha kwamba barabara hii inaboreshwa iwe ni msaada pale ambapo barabara kuu inapopata changamoto inatusaidia kuhakikisha kwamba hatupati changamoto kubwa kwa maana ya kukwama. Ahsante.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu hayo mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mali hizo zenye thamani ya takribani shilingi bilioni 37 ni mali ya Chama cha Wazee Waliopigana Vita ya Pili ya Dunia (TLC) ambazo wana haki nazo pamoja na watoto wao kwa mujibu wa katiba yao. Mali hizo zimekodishwa kwa muda mrefu na pesa zinakusanywa, mfano ni Upanga pamoja na kule Tarime, lakini fedha hizo hazijawafikia wale wazee ambao wanaishi kwa shida na wengine wanafariki hata kwa kukosa chakula: Je, ni lini Serikali itahakikisha fedha hizo zinawafikia wazee hao wafaidike nazo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kamati ya Serikali iliyokaa kwenye majadiliano mbalimbali haijawahusisha wazee hao wala watoto wao: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kupanga siku maalum ambayo atakutana na Kamati ya Wazee na Watoto hao ili washiriki kufikia maamuzi hayo ambayo Serikali imeyafikia?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa ku-declare kwamba baba yangu pia ni mmoja wa veteran waliopigana Vita ya Pili ya Dunia na sasa hivi ana miaka 103, ana akili timamu na anaulizia sana mali hizo.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, tathmini imeshafanyika na sasa tuko kwenye hatua ya kuhakikisha kwamba tunawafidia wazee hawa. Kwa hiyo, hili linaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tathmini ya kutowahusisha wazee waliopigana vita na watoto wao, tathmini hii ilikuwa pana na ilihusisha taasisi mbalimbali za Serikali. Bahati mbaya viongozi wa Chama cha TLC wote wamefariki, alikuwa amebaki mmoja wakati tathmini inaanza, lakini naye kwa sasa ameshafariki, hata hivyo tulihusisha baadhi ya familia ambazo tuliweza kuzifikia. Kwa hiyo, tathmini iliwahusisha wadau mbalimbali, nafikiri ikiwa nni pamoja na wewe Mheshimiwa Mbunge, tuliweza kupata mawazo yako kwa nyakati mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SYLVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Pwani ni mkoa mkongwe toka mwaka 1975 na maombi haya yalipelekwa Serikalini hadi kwa Katibu Mkuu Kiongozi toka mwaka 2016 tukiwa ni pamoja na Geita na Kahama.

Mheshimiwa Spika, hawa wenzetu walikwishapata Manispaa, vigezo alivyovizungumzia Mheshimiwa Naibu Waziri vinanipa utata, kwa sababu ukiangalia Manispaa ya Kigamboni wana kata nane, lakini wamepewa Manispaa na hadi sasa vigezo vyote alivyovizungumza hapo Mji wa Kibaha umekwishavitimiza. Sasa je, ni kwanini hatujapatiwa manispaa na ni lini tutapata Manispaa ya Mji wa Kibaha ili tuweze kufikia hadhi tunayostahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, sababu ambayo imechelewesha Halmashauri ya Mji wa Kibaha kupewa hadhi ya Manispaa ni kutokukidhi vigezo ambavyo tumeviainisha na Halmashauri inavifahamu. Kwa hiyo, ndiyo ilikuwa sababu kubwa ambayo imesababisha kuchelewa kwa Halmashauri hiyo.

Lakini lini itapewa hadhi ya Manispaa kwa sasa hivi kwanza Serikali tunajikita katika kuboresha maeneo yaliyopo na naamini kwamba mara baada ya Halmashauri ya Kibaha itakavyokuwa imekidhi vigezo na mamlaka husika kuona haja ya kuipandisha, tutafanya hivyo. Ahsante sana.