Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rhoda Edward Kunchela (57 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijaanza kuchangia, naomba nitoe shukranI zangu mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kufika hapa. Pia napenda kushukuru chama changu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kunifikisha hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Mpango huu kuna mambo mawili au matatu ambayo nahitaji kuchangia. Jambo la kwanza ni kuhusiana na uvuvi haramu pamoja na uwindaji haramu ambao unaendelea katika nchi yetu. Sasa katika Mpango huu ambao nimeupitia sijaona kama kuna mkakati wa kuweza kuzuia hao majangili ambao wanaendelea kuua watu wetu na kuiba wanyama. Pia kuna wawindaji ambao wanapewa vibali halali, ningeomba Serikali sasa kupitia huu Mpango iweke mkakati wa kuhakikisha kwamba pamoja na kupewa vibali lakini ijulikane ndani ya hizo National Park wanafanya shughuli gani. Nikitoa mfano kwenye Mkoa wangu wa Katavi kuna Wapakistan zaidi ya 40 ndani ya lile pori, lakini ukiulizia ni shughuli gani wanafanya siyo za kiuwekezaji. Nimewahi kutembelea pale, unakuta wengi wao ni madereva lakini wengine wanapika, ndiyo wanaohudumia kwenye hoteli pale ndani. Kama Serikali tuangalie hawa wawindaji ambao wana vibali kabisa vya kuwinda katika mbuga zetu wanafanya shughuli gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mbuga pia kuna viwanja vya ndege, sasa hatuwezi kuelewa hawa wawindaji wanasafirisha vitu gani. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tusiendelee kulalamika kwamba ndovu wanaibiwa inabidi kuchukua hatua. Nitoe masikitiko yangu kwa rubani ambaye alitunguliwa na hawa majangili katika mbuga ya Meatu. Kama Serikali au TANAPA wameshindwa kuweka usalama kwa hawa mapolisi ambao wanalinda wanyama wetu pamoja na mbuga zetu basi ni bora tukajua ni jinsi gani tunawalinda hawa wanyama wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mchango wangu wa pili unajikita katika viwanda. Mapinduzi ya viwanda yanatakiwa yaendane na uzalishaji wa umeme yaani huwezi ukazungumzia viwanda bila kueleza unaongezaje nguvu ya umeme katika viwanda vyetu. Mpaka sasa Tanzania tunazalisha umeme megawatts 1,247 lakini Mpango Mkakati wa Miaka Mitano uliopita Serikali iliweka mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawatts zaidi ya 2,780 lakini hatukufikia malengo. Tunapozungumzia mapinduzi ya viwanda basi tuhakikishe kwamba nguvu kubwa tutaongeza kwenye uzalishaji wa umeme kwa sababu hatuwezi tukazungumzia viwanda bila umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme hatuzungumzii kwenye viwanda tu pia tunauzungumzia kwenye matumizi ya kawaida ya wananchi wetu nikitoa mfano wa Mkoa wangu wa Katavi. Mkoa wa Katavi mpaka sasa tunatumia umeme wa generator hata kama tuna viwanda vidogo vidogo kwenye mkoa wetu basi hatuwezi kuzalisha product ya aina yoyote kwa sababu umeme siyo wa uhakika. Kuna kipindi inafikia wiki nzima wananchi wa Mpanda au Mkoa wa Katavi wanakosa umeme. Kwa hiyo, mapendekezo yangu katika suala la umeme Serikali iangalie sasa ni jinsi gani tunakwenda kuweka mikakati mizuri katika kuweka nguvu ya kuzalisha umeme hasa kwenye kipimo cha megawatts. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu unajikita zaidi kwenye afya. Kama Serikali tunahitaji kufikia malengo, maana nimesoma Mpango huu una mipango mizuri kabisa ambayo inatakiwa tuifikie kwa ajili ya ku-achieve hizo goals ambazo mmeziweka. Kitu ambacho nakiona kinafeli zaidi katika Mipango yote ni kwamba tuna mipango mizuri lakini lazima kuwe na implementation na monitoring lakini Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali tatizo hakuna ufuatiliaji. Kwa hiyo, naomba Serikali hata kama mnajikita kwenye sekta binafsi, sekta za afya, pamoja na elimu, inapopangiwa bajeti fulani basi implementation iongezwe kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilohilo la afya, Mkoa wangu wa Katavi ni almost kama miaka saba iliyopita mpaka leo tumepata Manispaa Serikali ilitoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na kuna eneo kubwa karibuni heka mia tatu lilishanunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ambayo inaonesha hospitali itajengwa lini. Pia wale wananchi ambao walikuwa wanakaa kwenye eneo ambalo Serikali ililinunua mpaka sasa wengi wao hawajalipwa. Naomba Serikali katika mpango wenu mhakikishe ujenzi wa hospitali katika mikoa au manispaa mbalimbali unafanyika lakini pia bajeti yake ipangwe na kuonyeshwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nilitaka kuzungumzia kuhusiana na ukusanyaji wa mapato. Tunapozungumzia ukusanyaji wa mapato kama Serikali ya CCM miaka yote tunalalamika lakini mchawi ni nani? Kuna watu ambao hawalipi kodi lakini Serikali imekaa kimya, miradi inashindwa kutekelezwa, tuna mipango mizuri lakini kodi tunapata wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge katika Bunge lililopita 2010, kulikuwa kuna kashfa ya sukari, kuna watu ambao walihusika na kutoa vibali vya Serikali na wengine wakaenda kununua sukari nchini Brazil kuleta Tanzania. Hasara tuliyopata kwenye kashfa ile ya sukari ni zaidi ya shilingi bilioni 300. Wengi wao wengine tunawafahamu kwa majina akiwepo Mheshimiwa Mohamed Dewji. Kwa hiyo, naomba kabisa ile ripoti ya Kamati ya Bunge iletwe hawa watu washughulikiwe na walipe kodi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa kama hizi zinapotea kumbe tungeweza kufanya maendeleo kutokana na kodi hiyo. Kuna watu tunawaachia wanarandaranda na wanatumia pesa za wananchi. Kwa hiyo, naomba Serikali tuwe strict kuangalia ni mianya gani inayosababisha tunapoteza pato la Serilkali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaposema tunahitaji kuwekeza katika elimu basi tuwakumbuke Walimu wetu kwa kuwalipa mishahara yao lakini pia tutengeneze mazingira mazuri katika shule zetu. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, nahitaji kuchangia katika maeneo machache kutokana na udhaifu na nini kifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu matatizo ya elimu duni nchini na kufeli kwa wananfunzi hasa katika Mikoa inayofanya vibaya kama Mikoa ya Tanga, Tabora na Mikoa ya Kusini. Hii inasababishwa na Walimu kukosa makazi mazuri kwa ujumla na hivyo Walimu kukosa moyo wa kufundisha katika shule walizopangiwa hasa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukosefu wa miundombinu hiyo na umbali mrefu kufika mjini. Mfano, Mkoa wa Katavi inamchukua Mwalimu muda mrefu kufika mjini kufuatilia madai yake kutoka kijijini mpaka mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya Walimu, hili limekuwa ni tatizo kwa nchi nzima. Walimu wanachukua muda mrefu kulipwa madai yao, madeni ya nyuma na kadhalika. Hii imesababisha Walimu kupoteza muda mwingi wakiwa mijini kufuatilia madai yao na hivyo kushindwa kufundisha na muda wa kufundisha wanafunzi unapotea bila sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Naomba sasa Wizara iweke mipango kwa namna ya kusaidia Walimu hawa wasipoteze muda mrefu mijini kufuatilia madai yao na hivyo wajikite zaidi kufundisha wanafunzi hawa ambao wanasoma katika mazingira magumu. Uchache wa Walimu na Walimu kuishi katika mazingira magumu, hivyo Serikali sasa ihakikishe utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za Walimu kwa wakati ili kuondoa usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la baadhi ya shule hasa vijijini kuendelea kuwanyanyapaa wanafunzi ambao wanakuwa wamepata mimba kwa bahati mbaya (mimba za utotoni) kutokana na mazingira ambayo wanafunzi hao wanatoka. Nini kifanyike? Serikali itoe agizo sasa ili wanafunzi hawa waliojifungua mashuleni, warudishwe waendelee na masomo na wasinyanyapaliwe. Pia Serikali iweke mpango mkakati wa kuhakikisha wanafunzi hao wanaonyonyesha wawe na darasa lao maalum ili wawe huru na wale wasionyonyesha wasije kuharibika kisaikolojia kutokana na kuchangamana nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi umekuwa ukisuasua na kusababisha wanafunzi kukosa huduma nzuri za malazi na hivyo wanafunzi kutokana na umbali kushindwa kuingia darasani (utoro) na kusababisha wanafunzi kufeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali iwape nguvu wananchi katika baadhi ya maeneo ambao tayari wananchi wamechangishana pesa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na hivyo wameshindwa kumaliza. Sasa Serikali ione umuhimu sasa wa kuwasaidia wananchi maana wamebeba majukumu ya Serikali, isiwapuuze wananchi, imalizie majengo hayo (Mabweni) ili kunusuru wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya shule za binafsi zimekuwa zikitoza ada kubwa na kuwaumiza wananchi. Hivyo Serikali iangalie upya ada hizi katika shule binafsi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabla ya kuanza kuchangia napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai ambao amenipatia. Napenda niunge mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa asilimia mia moja. Kwa nini naunga mkono asilimia mia moja, kwa sababu hotuba ya Upinzani imeeleza uhalisia wa maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika document zilizopita kila siku Wizara hii inapunguziwa bajeti. Abuja Declaration ambayo mlisaini mwaka 2001 lengo lake hasa ili kuwa ni ku-improve afya ya Watanzania. Ukisoma kwenye vitabu vyenu kuanzia TAMISEMI mpaka hii hotuba yenu ambayo mmei-present leo inaonyesha dhahiri kabisa kwamba hamjajipanga kwa sababu pesa mlizotenga ni ndogo.
Pia ukiangalia kwenye hii bajeti ya TAMISEMI inasema kwamba mlitenga shilingi bilioni 277 lakini kuna shilingi bilioni 518, jumla inakuwa ni shilingi bilioni 796. Sasa ukipiga kwa asilimia 100 ya shilingi trilioni 22 ambazo zimetengwa unapata ni asilimia 4.5. Shirika la Afya Duniani linasema kwamba mnatakiwa mfikishe asilimia 15. Sasa hii inaonyesha ni kiasi gani mme-fail kutekeleza hii Abuja Declaration, ingekuwa haina maana msingesaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nataka nichangie kidogo kuhusiana na Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi. Siwezi kuunga mkono hoja kwa sababu ni aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuendelea kupunguza bajeti, lakini wananchi wetu wanaendelea kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali hii Mheshimiwa Waziri hakuna vitendea kazi lakini aibu nyingine inayoikumba Serikali ya Chama cha Mpinduzi ni kwamba hospitali nzima hakuna BP machine wala thermometer na oxygen machine ipo moja na inatumika kwa wodi sita, sasa hii ni aibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusiana na masuala ya wazee. Wazee ni watu ambao wanateseka kwenye nchi hii lakini ukisoma kwenye hii hotuba ya Waziri haijaonyesha specifically mmetenga kiasi gani kwa ajili ya kutunza hawa wazee, mme-generalize tu yaani inaonekana kama hampo serious na hawa wazee. Naendelea kuwashangaa wazee kwa nini wanaendelea kukipa kura Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kwa sababu Halmashauri zetu zimeshindwa kukusanya mapato haya basi sasa zingeachiwa Manispaa kukusanya mapato. Inaonekana kabisa kwamba Wizara ya Afya mmeshindwa kuchukua jukumu lenu la kuwahudumia wazee ingawa mnasema kwamba Sera ya Wazee ni kuwahudumia bure kitu ambacho mnawadanganya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Sera ya Afya. Ukisoma hotuba ya Waziri katika kata 3,990 kwa Tanzania nzima kata 484 ndizo ambazo zina vituo vya afya. Huu ni utani mnaoufanya kwa Watanzania wetu kwa sababu haiwezekani kuna difference ya kata 3,506 hazina vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye sera hii ya afya inasema vijiji kuwa na zahanati katika vijiji. Tuna vijiji zaidi ya 12,245, ukisoma kitabu cha Waziri wanasema tuna zahanati kwenye vijiji 4,502 tuna difference ya vijiji 8,043 hatuna zahanati na moja ikiwa ni Wilaya ya Mpanda pamoja na vijiji na kata zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la afya ni kwamba tukidumisha afya za wananchi wataweza kufanya kazi, watajenga uchumi wao lakini siyo kuendelea kutupa porojo hizi ambazo mnatupa kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi imekuwa ni wimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisoma kitabu cha bajeti hapa mmesema kwamba mmetenga shilingi bilioni 1.8 lakini ni second time, mara ya kwanza Serikali ilitenga pesa wajanja wakapiga ile pesa wakaila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni Serikali gani ambayo haipo serious zinatengwa pesa kwa ajili ya wananchi kujengewa hospitali yao lakini watu wachache wanachukua pesa wanakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui kama hizi pesa zipo theoretically au mnaingia sasa kwenye utekelezaji kwa ajili ya kuwajengea Hospitali ya Mkoa wananchi wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe masikitiko yangu na hii inawezekana tukaendelea kupiga kelele kumbe Serikali ya Chama cha Mapinduzi sasa imelemewa na mzigo. Ni Serikali gani ambayo kila kitu ninyi mna-set kwamba ni priorities kwenu? Afya, elimu, katiba, viwanda yaani kila kitu, lakini hatuoni utekelezaji. Mna documents nyingi sana mmeandika, ni theoretically! Sasa ingewezekana basi ingekuwa vizuri mka-set kitu kimoja baada ya kingine, kwamba tunaweka afya na mipango yetu ni moja, mbili, tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ajitahidi basi akatembelee hata Zimbabwe; kuna hospitali inaitwa Palalanyatu, ni hospitali iko Harare pale, ni kama Muhimbili. Huwezi kukuta hata takataka, huwezi kukuta inzi, lakini leo wanapoka magazeti, media, wanasema Muhimbili ina vitanda, huduma zimeboreshwa. Ni uongo na unafiki mtupu! Wakatembelee waangalie Zimbabwe wanafanya nini? Wakaangalie wenzao wanafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza, labda niseme, kutokana na upungufu wa vitendea kazi kwenye hospitali zetu hasa Mkoa wa Katavi, maana imefikia kipindi sasa hata wauguzi wetu ni wachache katika zahanati zetu katika hospitali. Nitoe masikitiko yangu kwamba wiki moja iliyopita nilipigiwa simu na ma-nurse kwamba vifaa baadhi ya hospitali vipo lakini wauguzi wetu hawana ule ujuzi wa kuweza kutumia vile vifaa. Sasa unashangaa vifaa vipo lakini mama mjamzito anapelekwa wodini ma-nurse wanashindwa kutumia vifaa vile. Wanakwambia tumtangulize mama wodini wakati tunamsubiri Daktari ili kuja kumtibu huyo mgonjwa. Sasa ni vitu ambavyo vinatia hasira. Kama mko serious... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la nyimbo na muziki wa Tanzania linazidi kukua kwa kasi kwa sababu Watanzania wanapenda burudani, sanaa na kujifunza kupitia nyimbo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tatizo la wasanii wa Tanzania kutofanikiwa kiuchumi; wasanii wananyonywa sana, wasanii wanapata faida kidogo huku hawa wasambazaji wakineemeka kupitia wasanii wetu. Lakini pia gharama za kurekodi kazi za wasanii wetu, muziki wa audio na video kurekodi gharama ziko juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali kusimamia hasa kwa wasanii wetu wapunguziwe gharama za kurekodi na kuzalisha kazi zao. Kuna wasanii wengi wanashindwa kuzalisha kazi zao kwa sababu kipato chao ni cha chini sana. Nini kifanyike? Kuanzisha studio ya Serikali ili kuendelea kuwainua wasanii wachanga wenye uwezo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wizi wa kazi za wasanii, Mheshimiwa Waziri Serikali ina uwezo kabisa kuzuia wizi wa kazi za wasanii hasa kuweka password katika nyimbo zao, CD, DVD ili hawa wasambazaji wakose mwanya wa kuiba kazi za wasanii ambao wanazalisha kazi zao katika mazingira magumu sana. Mheshimiwa Waziri, leo kuna baadhi ya studio ziko hapa nchini kurekodi video moja mpaka shilingi milioni saba, Je, Serikali haioni haja ya kudhibiti gharama hizi na wasanii wetu wakaweza kustahimili hizi gharama na nini kifanyike? Serikali idhibiti, soko la muziki hasa kwa hawa wamiliki wa studio mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la usajili wa haki miliki ya msanii, mzunguko wa kupata haki miliki ya msanii umekuwa ni mrefu sana, pia mzunguko wa kupata sticker ili kazi itambulike na usajili wa TRA. Hivyo basi, ninaomba Serikali kupunguza mlolongo wa usajili na pia kuweka ofisi za usajili kila Mkoa ili kupunguza mzunguko wa kupata hizo sticker za TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwako Mheshimiwa Waziri ni kuwashauri pia wasanii hawa wafanye kazi kwa ushirikiano. Nyimbo zifuate utamaduni wa Kitanzania, wasanii wasijiingize kufanya kazi za kisanii na siasa hii inashusha muziki wetu awe CCM, CHADEMA au ACT, wasanii wetu kujiingiza katika siasa kunashusha soko la Tanzania hususani muziki. Mfano wa nchi ambazo wasanii walishuka hasa kwa kuchanganya siasa na kazi za sanaa ni Zimbabwe na Congo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu rushwa katika mchezo wa mpira wa miguu na netball, Mheshimiwa Waziri chunguza kwa makini suala hili ili timu zetu zifanikiwe bila dalili za rushwa. Ngoma za jadi na ngoma za asili zisisahaulike kwa mustakabali kwa kutunza, kuendelea na kukuza utamaduni wetu na siyo kuendelea kukuza muziki wa kizazi kipya pekee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Wizara ya Utalii ambayo imesheheni mipango mizuri ya utalii nchini ili kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi halali na wawindaji nchini, kuhusiana na wavuvi ambao wapo katika maeneo yenye mito, maziwa, mabwawa na bahari, naomba hawa wavuvi leseni zao zichunguzwe upya maana kumekuwa na malalamiko mengi kwa wageni kuingia nchini kwa lengo la utalii na kumbe baadhi yao wanavuka mipaka ya kilichowapeleka katika maeneo ya utalii, hawana vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matatizo mengi sana ya ujangili katika mbuga zetu. Serikali imejipangaje kuhusiana na kudhibiti hawa wawindaji halali wanaoingia kama watalii katika mbuga zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike, Serikali ichunguze ni namna gani ya kudhibiti hawa watalii na siyo kuwaacha peke yao mbugani. Wanafanya nini hasa maana tumeona ujangili mwingi umekuwa ukifanyika na wanaokamatwa wengi ni wageni. Hivyo, Serikali iongeze vitendea kazi kama magari kwa ajili ya kufanya patrol ndani ya mbuga zetu, kuwapa silaha zenye uwezo askari wa wanyamapori. Pia Serikali iboreshe maslahi ya askari wa wanyamapori ili wafanye kazi kwa moyo na kuwazuia kufanya biashara haramu (pembe za ndovu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwekezaji ndani na mbuga, kumekuwa na malalamiko mengi kwa baadhi ya mbuga kwamba wawekezaji hawa wanaajiri watu wengi ambao ni wageni kutoka nchi jirani na maeneo kama Pakstani, Wahindi na Wazungu. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kuwapa uhuru hawa wawekezaji kuajiri wageni zaidi kuliko wazawa ambao wapo wenye uwezo na elimu kuweza kuhudumia mfano hoteli zilizopo mbungani, customer services na madereva. Shughuli hizo wangeweza kufanya wazawa kwa wingi kuliko wageni wanaoletwa kuchukua fursa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbuga ya Katavi ichungwe zaidi. Je, ni jinsi gani wawekezaji hawa wanasaidia wakazi wa vijiji vya jirani kwa huduma kama maji, zahanati, barabara na madawati? Wawekezaji hawa wanaingiza vipato vikubwa hivyo wanapaswa pia kusaidia jamii inayowazunguka katika mbuga hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanja vya ndege, kutokana na uhaba, ukosefu wa vifaa vya kisasa kama kamera katika viwanja vya ndege inachangia kutoroshwa kwa rasilimali zetu mfano ndovu, vyura na kadhalika. Hivyo, Serikali ihakikishe inawezesha upatikanaji wa vitendea kazi bora kama kamera, mashine za ukaguzi, x-ray na screening machine. Nini kifanyike? Ulinzi uongezwe zaidi hasa katika viwanja vya ndege ambavyo viko ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia kwa waathirika wa Operesheni Tokomeza Serikali iangalie namna gani ya kufidia watu walioumizwa, kuibiwa na kupigwa. Mfano katika Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Mpanda Vijijini, Kata za Isengule na Kapalamsenga, askari polisi walijeruhi watu ambao hata hawahusiki. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia suala hili?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Diplomasia ya Uchumi. Mheshimiwa Waziri pamoja na kusoma hotuba ya Wizara kuna mipango mingi mizuri hasa ya namna gani tunaweza kukuza uchumi wetu kupitia balozi zetu za nje ya nchi. Najielekeza katika balozi zetu hasa uendeshaji wa balozi zetu, Majengo (Pango), wafanyakazi katika Balozi, biashara zinazoweza kuingiza kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa Balozi; kumekuwa na gharama kubwa za uendeshaji katika balozi zetu kutokana na Balozi nyingi kupanga majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pango la ofisi; kutokana na kukosa majengo ya ofisi, Balozi zimekuwa zikipanga, kitu ambacho ni gharama kubwa ukizingatia Balozi nyingi hawapati bajeti ya kutosha ya uendeshaji na hivyo pesa nyingi zinaishia kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Ni muda sasa wa Serikali kujikita katika kuhakikisha Balozi zinapewa bajeti ya kutosha ili wamiliki majengo kama ofisi na hivyo kuondoa aibu wanayoipata sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kushindwa kulipa kodi Zimbabwe. Licha ya Balozi kwa sasa kumiliki nyumba kama ofisi lakini pia inamiliki baadhi ya biashara kama Tanzania Club. Watanzania hupangishwa au mtu mwenye vigezo kuweza kuendesha lakini sasa Serikali ihakikishe inasimamia miradi hiyo kwa sababu kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa mali za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za ajira nje ya nchi; pamoja na Tanzania kuwa na fursa za kiuchumi tumeona tatizo la wageni kupewa fursa kirahisi rahisi tu, kitu ambacho ukienda nje ya Tanzania si rahisi kupata fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Work Permit; Serikali sasa ihakikishe inaweka sheria ambazo zitawabana wageni kutimiza vigezo vya uwekezaji na si kupata fursa za ajira kirahisi rahisi kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wamekuwa wakipoteza fursa za ajira huku wageni wakipewa kazi hizo. Zimbabwe si rahisi kupata work permit. Imefikia hatua Watanzania wamekaa kule zaidi ya miaka 10 lakini kupata work permit si kazi rahisi na hivyo Zimbabwe ni moja ya nchi ambayo inajipatia pesa kupitia wageni, hivyo Serikali ya Tanzania iwe mfano mzuri ili tukuze uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya mahusiano ya Kimataifa sasa yawe na msaada kwa ajira mbalimbali za maana, si zao wageni wakija Tanzania wanapewa fursa nzuri na kazi za ngazi ya juu huku Watanzania wakiajiriwa nje ya nchi wanapata kazi zisizo na msingi kama viwandani, kusafisha viwanja vya mipira, kulea wazee na kuwasafisha wazee. Ifike sehemu sasa Watanzania waheshimiwe kwa sababu wageni wakija Tanzania wanaheshimika na kupewa fursa zenye maslahi mazuri kwao na si kunyanyasika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, balozi zitafute fursa mbalimbali za kiuchumi kwa kufungua miradi mbalimbali kama vile maduka ya vitu vya asili ya Tanzania vitakavyouzwa katika balozi zetu na zisibweteke na kukosa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Tanzania imekuwa kimya sana, Watanzania wanateswa na wananyanyaswa na kuuliwa lakini Serikali imekuwa ya upole bila kutoa matamko makali kama nchi. Mbona wageni wakija Tanzania wanaishi kwa usalama na Serikali inalinda diplomasia ya nje ya Tanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadhi ya balozi zetu ni mbaya katika maeneo yafuatayo:-
Mishahara ya wafanyakazi katika balozi zetu, ukarabati wa ofisi zetu, majengo mengi hayana hadhi ya Balozi za Tanzania na ukizingatia majengo ya balozi baadhi unakuta yako nje ya miji mbali na mjini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
Ombi kwa Serikali kuzuia mbegu feki mipakani. Iangalie mipaka yote ya Tanzania kuna mbegu feki zinapita na hivyo kuathiri kilimo kwenye mpaka wa Tunduma na Namanga wananchi wanaingiliana katika shughuli na hivyo kuleta upenyo wa kupitisha mbegu feki kutoka nchi za jirani
kama Zambia, Malawi na Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mapato TRA. Serikali iangalie kwa jicho la tofauti kwa wafanyabiashara wanapokadiriwa na TRA katika maeneo yao ili kulipa kodi, kuna malalamiko biashara zao ndogo na wanakadiriwa kulipa kodi kubwa hivyo kuwafanya washindwe kulipa kodi
na kufunga biashara zao na ukizingatia jiografia ya kupata bidhaa kutoka nje ya Katavi na mikoa ambayo iko pembezoni iangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Serikali iboreshe huduma za Wizara Afya na Elimu bure kuhusu VVU katika maeneo yenye watu wengi hususani migodini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo na Mifugo naomba Serikali iendelee kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa tatizo na hii inaendelea kuleta upungufu wa chakula kutokana na migogoro hii. Wakulima kuchomewa mashamba, mifugo kuuawa au kupigwa risasi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi; pamoja na juhudi za Serikali katika kulinda mazingira hususan pembezoni mwa fukwe za bahari na pembezoni mwa maziwa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto katika Ziwa Tanganyika; naomba Serikali iangalie upya ujenzi wa hoteli na nyumba za kuishi pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, je, wanafuata taratibu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi; kuna baadhi ya wavuvi ambao sio wazalendo ambao wanatumia baruti na nguvu ambazo hazifai katika vyanzo vya maji mpaka sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti za gesi zinazoendelea baharini, ni jambo jema Serikali kuendelea kuruhusu uchunguzi au tafiti zinazoendelea kufanywa na wawekezaji katika Bahari ya Hindi ili wagundue ni wapi na gesi ipo kiasi gani katika bahari. Wawekezaji wana vifaa vyao na sio Watanzania/uzalendo kuhusika? Je, Serikali ina uhakika gani tafiti zinazofanywa katika bahari juu ya uvumbuzi wa gesi kwamba haiathiri mazingira chini ya bahari? Je, Serikali ina mkakati gani ili inunue vifaa vya uchunguzi kujua wawekezaji hao hawaathiri mazingira baharini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko ya wananchi wanaotoa taarifa kwa polisi kuhusu viwanda feki vinavyotuhumiwa kuharibu mazingira, mifuko ya plastiki, ukataji wa miti ya asili kiholela, wino – viwanda, viwanda vya viroba kiholela, uvuvi haramu. Wananchi ni wazalendo na mazingira yao lakini wanapoisaidia Serikali kuwataarifu, Serikali na hawa wanaoharibu mazingira wamekuwa wakitajwa, je, Wizara yako inatoa tamko gani? Wananchi wakiwa kimya bila kutoa taarifa kuhusu uharibifu huu mazingira mnategemea nini kama sio jangwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina wanaojenga barabara waharibifu wa vyanzo vya maji Mkoa wa Katavi; Mto Kuchoma Wilayani Mpanda umekauka kutokana na matumizi makubwa ya maji yanayotumiwa na mkandarasi huyu. Serikali inatoa tamko gani ili kunusuru mto huu kwa matumizi ya wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Katuma pamoja na banio za umwagiliaji; pamoja na Serikali kusimamisha ujenzi wa vibanio kiholela katika Mkoa wa Katavi ambao kwa sasa wakulima wanapata maji, urasimu wa kupata vibali ili kujenga vibao vya kisasa na vinavyofuata utaratibu wa kulinda vyanzo vya maji mkoa mzima kuna vibanio sio zaidi ya vitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itapunguza urasimu huu wa kupata vibali halali vya mabanio unaofanywa na baadhi ya watendaji au ni utaratibu unaofanywa na Wizara husika? Hii inaleta usumbufu mkubwa, Serikali inasema nini katika hili, waathirika wakubwa wakiwa wakulima hususan Mkoa wa Katavi. Jambo hili liangaliwe upya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami nataka kuchangia kidogo kuhusiana na miundombinu katika Mkoa wa Katavi. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai. Pia naunga mkono asilimia 100 hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nataka nijikite zaidi katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Kwanza kabla sijaenda mbali zaidi, ukisoma katika ukurasa wa 22 na 19, nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri; barabara ya kutoka Mpanda
- Stalike, barabara ile imekwisha, lakini ukisoma kwenye hotuba ya Waziri ametenga shilingi bilioni 4.1. Sasa pesa hizi ametenga kwa ajili ya ujenzi wa kitu gani? Ukisoma, mradi umekamilika. Nadhani atakapokuja kuhitimisha anieleze hii shilingi bilioni 4.1 ni ya nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna madaraja mengi katika Mkoa wa Katavi ambayo yamekuwa yanasuasua kwisha na watu wa Katavi wanaendelea kupata shida, hawana mawasiliano kutoka kwenye Wilaya moja kwenda kwenye Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna daraja la Iteka ambalo liko katika Halmashauri ya Nsimbo, daraja hili karibu kila mwaka limekuwa likiua watu, magari yanakwama, watu wanalala njiani, lakini katika bajeti hii sijaona popote daraja hili limetajwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya kutoka Kibaoni – Mpanda; barabara hii imechukua muda mrefu sana. Watu wa Katavi wanahangaika, lakini muda mwingine wanasafiri zaidi ya masaa 12 kutoka Mpanda mpaka Sumbawanga, lakini katika bajeti hii sijaona kokote ambako Mheshimiwa Waziri ametenga bajeti kwa ajili ya kumaliza hizi barabara. Sasa sielewi ni nini mkakati wa Serikali; ni aidha kuendelea kuwatesa na kuwanyanyasa watu wa Katavi? Kwa sababu ukiangalia kwenye mikoa mingine, kwa mfano, Mkoa wa Bukoba pamoja na Pwani wametengewa zaidi ya
shilingi bilioni mbili kwa ajili ya matengenezo tu ya kawaida; lakini Mkoa wa Katavi leo hii tunaongea mnatutengea shilingi milioni 27! Za nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nijikite katika suala la mawasiliano. Wakazi wa Katavi ni watu ambao wanatangatanga, wanapata shida. Mawasiliano ni ya hovyo, barabara ni mbovu, sasa Mheshimiwa Waziri, kuna wakazi wa Kata ya Ilunde iko katika Jimbo la Mheshimiwa Engineer Waziri wa Maji; Kata ile watu wanasafiri kilometa 10 mpaka 15 kwenda kutafuta network ili awasiliane na mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Serikali gani hii ambayo mpaka leo mtu anasafiri, anatembea kilometa 10, anatembea kilometa 15 kwenda kutafuta network na network yenyewe inakuwa ni mbovu, mtu mpaka apande kwenye mti ndiyo awasiliane! Hatutakubali watu wa Katavi. Kwanza nashangaa kwa nini watu wa Katavi bado wanaendelea kuwa na imani na Chama cha Mapinduzi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya kutoka Tabora - Sikonge kwenda mpaka Katavi. Barabara hii imechukua muda mrefu sana, mpaka sasa Wakandarasi haijulikani, kila siku wanaweka tu changarawe, wanarekebisha na ma-grader, ukipita, watu wanalala njiani lakini pia kuna Mto Koga ambao miaka mwili iliyopita kuna zaidi ya watu 30 walikufa katika mto ule, lakini ile barabara mnayotuletea ni marekebisho tu. Kimsingi, hamko serious na Mkoa wa Katavi. Naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri, ni kwa nini hawakutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa Mkoa wa Katavi? Wanayotuletea ni marekebisho tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la kushangaza, ukisoma kwenye ukurasa wa 285 anasema; barabara hizi zitatumia kwa ajili ya marekebisho shilingi milioni 846 kwa kilometa 695.5. Ukigawanya shilingi milioni 846 kwa kilometa 695.5, katika hizi barabara zaidi ya saba zilizotengewa kwa ajili ya marekebisho, kila barabara yenye urefu wa kilometa 112, barabara ya kutoka Mamba – Kasansa; barabara ya kutoka Mpanda – Ugala; barabara ya kutoka Mnyamasu kwenda Ugala; zina zaidi ya kilometa 111; na nyingine, hii barabara ya kutoka Kagwira kwenda mpaka Karema ni kilometa 250.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu nadhani ni utani, unawezaje kufanya marekebisho kwa barabara yenye urefu wa kilometa 250 kwa shilingi milioni moja? Huu ni utani na hatuwezi kukubali kwa sababu kuna mikoa ambayo inapewa vipaumbele na Mkoa wa Katavi ukiendelea kuwekwa nyuma wakati ndiyo mkoa ambao unaoongoza kwa kuzalisha mazao ya chakula ambayo Waheshimiwa humu ndani wanatumia vyakula hivyo. Sasa hatuwezi kuendelea kukaa kimya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie pia kidogo kuhusiana na ujenzi wa uwanja wa ndege. Mwaka 2010, Serikali ilitenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege katika Mkoa wa Katavi, katika Manispaa ya Mpanda, lakini mpaka hivi tunavyoongea, wakazi wale hawajalipwa na wengine wakati wanalipwa zile pesa kwa jili ya kupisha ujenzi wa ule uwanja, watu walilipwa sh. 75,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu ambaye alikuwa ana nyumba, ana kiwanja unaenda kumlipa sh. 75,000/=! Mpaka leo ninavyoongea kuna wananchi ambao wanalala kwenye mahema na wako mjini katika Kata ya Ilembo; pia kuna Kata ya Airtel ambayo wakazi wake wengi walitolewa kwenye lile eneo ambalo uwanja ulijengwa. Sasa watu hawa hawawezi kuendelea kusubiri huruma ya Serikali. Viwanja vilikuwa ni vya kwao na walikuwa wamejenga nyumba, sasa waliamua tu kupisha ujenzi huo.
MHeshimiwa Naibu Spika, pia wakazi wa Mpanda hawakuwa tayari kwa ajili ya matumizi ya Uwanja wa Ndege, kwa sababu majority ya watu wa Katavi wanatumia usafiri wa reli ambapo usafiri wa reli wenyewe ni wa hovyo, barabara ni mbovu, mnaenda kuwapelekea Uwanja wa Ndege ambao mpaka sasa wanapanda watu wawili, watatu kwenye vindege vile vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kufahamu, hii TTCL ina faida gani? Sioni faida ya TTCL kwa sababu ukiangalia Hallotel wamekuja juzi tu, lakini leo wanafanya vizuri. Sasa labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha, atueleze faida ya TTCL ni nini? Kuna haja gani ya kuendelea kuitengea bajeti TTCL?
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu sasa, Wizara ina mkakati gani wa kuongeza pesa katika Mfuko wa Barabara kwa Mkoa wa Katavi? Kwa sababu hakuna kitu chochote kinachoendelea hapa. Ukisoma kwenye ukurasa wa 287, hakuna bajeti yoyote iliyotengwa kwa ajili ya Mkoa wa Katavi. Sasa wakazi wa Katavi wataendelea kusubiri miradi ambayo haikamiliki kwa wakati, lakini ni miradi ambayo inawafanya watu wa Katavi waendelee kudanganywa kwamba mtaletewa barabara, mtatengenezewa standard gauge kwa ajili ya watu ambao wanasafiri kwa njia ya reli, hakuna chochote! Mtaendelea kuwadanganya mpaka lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitaji majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri ni lini sasa wakazi wa Mkoa wa Katavi wataacha kusafiri siku mbili mpaka tatu kulala njiani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kufahamu, ni kigezo gani ambacho kinatumika kwa ajili ya kuwapata wakandarasi… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ni kigezo kimojawapo cha kuongeza uchumi au kudhoofisha uchumi kwa ujumla katika Tanzania yetu. Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa ambayo imeendelea kudumaa kiuchumi na moja ya sababu ni kukosa barabara zenye uhakika na kusuasua kwa kuchelewa kujenga barabara na kutengewa fedha ndogo zinazochelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mpanda - Koga yenye urefu wa kilomita 1.0 na Mpanda - Uvinza zimesubiriwa na wananchi kwa muda mrefu waondokane na kero hii ya kulala barabarani kunakosababishwa na barabara mbovu na madaraja kukatika. Nini hatua ya dharura inachukuliwa kuwakomboa wananchi ili waondoke katika kero hii? Kuchelewa kwa bidhaa katika maeneo ya biashara, mazao kuoza yakiwa njiani, je, Serikali haioni kwamba kupitia barabara hizi mbovu zinaendelea kuwafanya wananchi hawa wa Katavi kuendelea kuwa maskini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii iliyopangwa kwa mikoa hii inayoungana mitatu Tabora-Kigoma na Katavi, tulitegemea itengwe bajeti ya kueleweka ili imalize hizi barabara. Mfano barabara ya Kibaoni - Mpanda ikamilike kwa wakati lakini mpaka sasa haijulikani nini kinasababisha barabara hizi zisikamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zilizotengwa kufanyiwa marekebisho ya changarawe na udongo, Wizara ingeangalia maeneo ambayo hayapitiki kabisa yarekebishwe yote. Kwa jiografia ya Mkoa wa Katavi hakuna barabara za kuchepuka hivyo daraja linapovunjika/bomoka basi watu hawasafiri wala kuendelea na safari. Serikali hii sasa iwe na vipaumbele kutokana na mahitaji ya wananchi wake na wasifanye wanachotaka wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba changamoto hizi zifanyiwe kazi mapema:-
(i) Barabara zinazojengwa katika Manispaa ya Mpanda hazina viwango na hazina mitaro. Ni barabara mpya lakini zina viraka, je, ni kigezo gani kinatumika kila wakati kuendelea kuwapa kandarasi wakandarasi hawa?
(ii) Kucheleweshwa pesa kwa kandarasi hii inaleta shida na miradi kuchukua muda mrefu imekuwa ni kero sasa.
(iii) Usafiri wa reli Mpanda - Tabora – Dodoma, Serikali ihakikishe ujenzi wa reli ya kisasa sio siasa tu bali iingie katika utekelezaji.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zinaonesha kuwa ugharamiaji mdogo umedhoofisha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za BRN mwaka 2014 zinaonesha kuwa matumizi ya Serikali katika Afya ni asilimia 11.1 ya matumizi yote ya Serikali. Sekta hii ni muhimu kwa ustawi wa jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati nyingi katika Halmashauri zote za Katavi, Nsimbo, Mlele na Mpanda; asilimia 90 ya zahanati hizi za Katavi ziko nje ya mji. Kwa jiografia, ni ngumu kidogo. Wananchi wanateseka, wanasafiri kutoka Kata ya Kabage Jimbo la Tanganyika, umbali wa kilometa zaidi ya 40 kufuata zahanati katika Kata ya Isengule au Kapala, Msenga, anafika Zahanati ambayo haina dawa wala Wauguzi. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kila kata inapata huduma za afya bila kusafiri umbali mrefu kiasi hiki? Huu ni unyanyasaji kwa watu wa vijijini hususan Katani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa Fedha Serikali ilitenga shilingi 1.99 sawa na asilimia 9.2% ya bajeti yote ya Serikali. Bajeti ni ndogo sekta hii ni kubwa mno na Wizara ni pana, naomba iongezewe bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na jamii yenye uwezo kwa kuchangia katika ujenzi wa uchumi, hatuwezi kukwepa kuwekeza ipasavyo kwenye Sekta ya Afya. Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali ya Mkoa Katavi? Hospitali iliyopo ni ndogo na mahitaji ni makubwa mno. Oxygen Machine ni moja tu haikidhi mahitaji ya Wanakatavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 alifariki Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda. Inawezekana tungekuwa na mashine za oxygen mbili au tatu, Mkurugenzi angepona kwa sababu siku hiyo Mkurugenzi huyu anapata shida ya kupumua, mashine ilikuwa inatumiwa na mama mjamzito aliyekuwa hoi threatre. Je, hamwoni kwamba kwa uchache huu Serikali itaendelea kupoteza watu na viongozi bila sababu zisizo na msingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara iangalie Mkoa wa Katavi, iongeze bajeti, vifaa tiba, dawa na BP machine.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
HE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Habari na Michezo ni Wizara muhimu zaidi ikilenga kuinua michezo, burudani na kuelimisha jamii kupitia nyimbo na michezo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nahitaji kujua ni lini Serikali itakamilisha kuweka ofisi za usajili kila wilaya ofisi za COSOTA na BASATA ili kuondoa usumbufu kwa wasanii wakitaka kusajili kazi zao mpaka waje Dar es Salaam; huoni kama huo ni usumbufu kwa wadau wa sanaa. Je, hamuoni kama huu ni upotevu wa kodi kwa sababu msanii mchanga hawezi kujigharamia mpaka afike Dar es Salaam na pia kuna urasimu mkubwa katika ushuru wa stamp? Je, ni lini Serikali itaondoa kero hizi; itapunguza urasimu kupitia usajili COSOTA, BASATA na TRA, wasanii kuibiwa kazi zao, kujenga ofisi kila Wilaya, kuzingatia maadili katika kazi za sanaa za maigizo, michezo, nyimbo, vichekesho vinavyokiuka maadili ya Kitanzania? Ni lini Serikali kupitia COSOTA/BASATA itaacha ubaguzi kwa kuwafungia nyimbo/maigizo kazi za sanaa kwa baadhi ya watu na wengine hawachukuliwi hatua wanapotengeneza video zinazochefua jamii. Itawatafutia masoko wasanii. Kazi za sanaa zinalala ukizingatia nchi kama Kenya wako vizuri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Bunge kuonesha live. Ni lini Serikali italiachia Bunge kuoneshwa live. Je, hamuoni kwamba kuzima Bunge mnajichimbia kaburi nyie wenyewe. Mmeondoa uhuru wa Watanzania kuongea kwa uhuru, kuonya, kuelimisha na kuikumbusha Serikali kupitia Bunge live na Serikali yao.

Mheshimiwa Spika, Sheria kandamizi za mitandao. Hamuoni kwamba Watanzania pamoja na Sheria hii mpya ya habari hawajajifunza na kutambua vizuri matokeo yake. Mnawafungulia mashtaka Wapinzani tu CHADEMA, CUF wao CCM hawavunji Sheria? Acheni tabia ya kunyanyasa watu. Roma Mkatoliki mlimteka kwa sababu tu kaongea ukweli kaisema Serikali, Je, uhuru wa habari uko wapi?

Mheshimiwa Spika, habari Bunge; leo hata waandishi wa habari wanaoingia Bungeni hawapati taarifa kamili ili ziruke kwa Watanzania mpaka ziwe zimekuwa edited (filter) kitu ambacho kinapunguza ukweli wa habari. Wizara iangalie hili ili kuweka uhuru wa waandishi wa habari kupata taarifa kutoka Bunge.

Mheshimiwa Spika, kuchunga hotuba za Kambi Rasmi ya Upinzani. Hii ni kero na hailisaidii Taifa. Kambi ya Upinzani ni mbadala wa Serikali tawala katika kuisaidia Serikali kibajeti katika vipaumbele ili Wizara zisonge mbele. Sasa hotuba zinapofanyiwa editing, je, hamuoni kama mnapoteza lengo la Upinzani kuisaidia Serikali. Tunajenga nyumba moja na Taifa moja, ubaguzi usifanyike kwa Upinzani tu bali angalieni haki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa sababu imeonyesha mwelekeo wa wapi Serikali inatakiwa itekeleze katika vipaumbele vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji wa nyuki, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kukuza ufugaji wa nyuki lakini bado Watanzania hawana elimu ya kutosha ili wayatumie mapori yetu kupata asali kwa ajili ya biashara. Serikali itoe elimu kwa Watanzania waweze kufuga nyuki kisasa na wayatumie mapori yetu vizuri ili wapate kipato. Wizara iwasaidie vijana, wafugaji kwa kuwapa elimu, mikopo na vifaa vya kufugia nyuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwindaji haramu; pamoja na Serikali kuendelea kupinga biashara hii haramu, ujangili na mauaji ndani ya mbuga zetu, nahitaji kufahamu mambo haya na nisipopata majibu nitashika shilingi.

(i) Kuna Mchina alikamatwa na lori la meno ya tembo katika mbuga ya wanyama Katavi. Mchina yule akaachiwa eti alikuwa hajui Kiswahili. Je, hamuoni kwamba kuwaachia maharamia hawa ni Serikali imeshindwa kusimamia uharamia huu? Naomba majibu Mchina alifanywa nini na kesi ikoje?

(ii) Kuna taarifa kuhusu majangili kutoka nchi jirani za Rwanda, Kongo na Burundi wanaingiza makundi ya ng’ombe mbugani wanajifanya wanachunga au wamepotea njia na kuingia hifadhini. Je, Usalama wa Taifa kuhakikisha upotevu na uharamia huu haufanyiki uko wapi kuyasemea haya? Je, hamuoni ujirani huu tusipokuwa makini tutapoteza rasilimali zetu? Mkakati wa Serikali kuhakikisha mnazuia hawa maharamia wafugaji kuingia na kuvuna pembe za ndovu ukoje?

(iii) Rushwa kwa wawekezaji katika mbuga zetu. Serikali imeweza kudhibiti rushwa hizi na kulinda uwindaji haramu, waliokamatwa na pembe za ndovu kuachiwa Wizara ya Maliasili imeshindwa kusimamia hili.

(iv) Wafanyabisahara (wa China) wa meno ya tembo kuendelea kuisaidia Serikali kutoa misaada ni kujificha nyuma ya pazia.
(v) Usimamizi wa ukataji miti hovyo Kibaoni, Nkasi leo hii ni jangwa kabisa. Serikali ione namna ya kuzuia uharibifu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha mbuga za Mikoa wa Kusini; Lindi/Mtwara (Selous), Katavi (Katavi), Rukwa (Rukwati), kuna kigugumizi gani kuzitangaza mbuga hizi? Mnaitangaza Serengeti kila leo wakati kuna mbuga kubwa hamzitangazi kuna nini hapo? Katavi kuna twiga mweupe na tembo wakubwa lakini Serikali haina mkakati kabisa wa kuzitangaza mbuga hizi kuna nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miundombinu, Serikali iboreshe viwanja vya ndege Katavi, Kigoma na Mwanza ili watalii wasipande ndege zaidi ya mbili kufika Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua ni namna gani Serikali itaitangaza Katavi angalau tupate watalii kutoka Zambia? Kwa nini Mikoa ya Kusini hamuitangazi mnaendelea kuzitangaza mbuga ambazo zimetosha kutangazwa kama Serengeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa operation tokomeza ujangili, ni lini mtawafidia wananchi waliochomewa nyumba zao, biashara zao, wakabakwa, wakateswa nje ya utaratibu wa kutafuta majangili? Ni lini mtawalipa hawa wananchi fidia zao kwa mateso waliyopewa; na huku Askari Wanyamapori wapo wanaishi kwa furaha huku wananchi hawa wakiishi katika mazingira magumu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvunaji wa misitu, magogo na mbao, kuna uharibifu wa misitu unafanyika katika mapori yafuatayo:-

(i) Ipole – Tabora;
(ii) Inyonga – Mpanda;
(iii) Lyamgoloka – Mpanda Vijijini; na
(iv) Jimbo la Nsimbo – Kata nyingi zinafanya biashara hizi na watendaji wa Kata kuuza magogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuwawajibisha hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhifadhi wa viboko katika Mbuga ya Katavi unahatarisha uhai wa viboko kutokana na kukithiri kwa vizibo vya umwagiliaji na viboko kukosa maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nilitaka nichangie machache kuhusiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwanza nataka niunge hoja asilimia 100 hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kutokana na hotuba hii kuonesha mwelekeo wa namna gani Wizara inaweza kutatua kero ambazo zinalikabili Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la usalama wa nchi kama wapinzani lakini pia kama Watanzania ambao tuna haki ya kuzungumza na kuikosoa Serikali hatuna maana mbaya, tunathamini kabisa michango ya Jeshi, tunaelewa kabisa kazi ambazo zinafanywa na Jeshi letu, kwa hiyo, si kwamba tunapinga kila kitu. Tunachotaka ni kuikosoa Serikali katika yale mapungufu ambayo tunaona kabisa kupitia Jeshi hili basi linaweza likafanya marekebisho katika baadhi ya sehemu ili tukaenda sawa na wananchi wakawa na amani hiyo ambayo mnaisema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nizungumzie kidogo kuhusiana na migogoro ya ardhi kati ya wananchi na Jeshi. Kumekuwa na changamoto kubwa kwenye maeneo mengi ya Jeshi ambayo sasa wananchi wamekuwa wanayalalamikia, kwamba Jeshi limeingilia kwenye makazi ya watu, lakini unakuta tena Jeshi hilo hilo linasema wananachi wamevamia maeneo ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aeleze ni mkakati gani ambao sasa Wizara au Serikali hii imepanga ili kutatua migogoro hii ya ardhi ambayo imesababishwa na Jeshi, aidha, wananchi kuvamia maeneo ya Jeshi au Jeshi kuvamia maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka niseme kidogo, katika Mkoa wangu wa Katavi kuna kata ya Misunkumilo pamoja na Kata ya Mpanda Hoteli. Katika maeneo haya kuna wananchi wako pale wamejenga wana miaka zaidi ya 60 mpaka leo. Vilevile kuna viwanda pale na pia kuna wananchi wana mashamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wamezuiliwa kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yale, wameshindwa kulima, wananchi wanakufa na njaa katika kata zile. Eneo lile lina mgogoro lakini Serikali mpaka sasa haijawahi kusema ni lini sasa mgogoro huu utakwisha ili hawa wananchi sasa waache kupigwa, waache kunyanyaswa na Serikali ambayo mnasema ni Serikali ya amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la malipo ya wanajeshi. Hivi tunavyoongea kuna wanajeshi zaidi ya 250 ambao wamehamishwa kutoka Makao Makuu kuja Dodoma hapa katika Mji wa Dodoma, hawajalipwa na wengine wako humu ndani. Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa hawa wanajeshi? Mmewahamisha, mmewaleta hapa watu wameacha familia zao. Tunaomba sasa katika bajeti hii itengwe fedha kwa ajili ya kuwalipa hawa wanajeshi, wanateseka na familia zao zinateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee pia suala la mwisho linalohusu utawala bora. Tunathamini kabisa kazi zinazofanywa na Jeshi, lakini tunaomba hawa wanajeshi bajeti hii sasa ilenge maana ya kuwajengea nyumba ili watoke katika makazi ya watu, maana imekuwa ni kero; wananchi wanakuwa wanaogopa, lakini na Jeshi nalo zile kambi zake zinashindwa kufanya yale majukumu kama Jeshi kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na migogoro mingi. Ni kweli, wanajeshi wana haki kabisa endapo mwananchi anakuwa amekosea, lakini kero nyingine inapokuja kuna makosa madogo madogo, unakuta mwananchi amemuudhi huyu mwanajeshi basi hicho kipigo atakachokipata, wengine ni vilema. Ukiangalia katika fukwe zetu unakuta mwanajeshi anamlazimisha mwananchi kula samaki mbichi, leo hii tumefikia hapa! Wananchi wetu wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaliomba Jeshi, ni kweli wananchi wanakosea, sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RHODA E. KUMCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwanza nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu pia nitoe pole kwa familia ya Mheshimiwa Tundu Lissu huko aliko Mungu amponye kwa haraka ili arudi katika majukumu yake ya Kitaifa. Pia nitoe shukurani kwa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Taifa Mheshimiwa Mbowe kwa kazi ya kujenga Taifa hili, pia namna anavyotetea na kujenga demokrasia katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia maendeleo ya uchumi wa Taifa hatuwezi kuacha kuongelea demokrasia ya nchi hii. Hatuwezi kuzungumzia uchumi wa Taifa hili bila kuzungumzia demokrasia na maendeleo katika Taifa hili, haiwezekani leo hii wafanyabiashara wakubwa,
wachumi mbalimbali wanatoa takwimu namna gani wanatoa taarifa ili Taifa hili liweze kwenda mbele, wanatoa taarifa na kuisaidia Serikali, wanatoa taarifa ambazo kimsingi zingeweza kulisogeza Taifa hili mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii watu wakipambana, wakitoa taarifa, wakikosoa Serikali, wanakwenda kupata shida na misukosuko mingi katika biashara zao na wengine wamefukuzwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa kwenye hoja za msingi. Nataka nizungumzie kidogo namna gani ya kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato pamoja na kuzuia matumizi mabaya ya fedha katika taasisi za Umma. Tumekuwa tukipitia taarifa nyingi katika mashirika mablimbali ikiwepo TPA pamoja na Bandari; mifumo ya ukusanyaji wa kodi, mifumo ya namna gani wanatunza taarifa za fedha imekuwa ni kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimwambie tu mwalimu wangu Mheshimiwa Dkt. Ashantu Kijaji, kwamba tukishindwa kuboresha mifumo hii ya ukusanyaji wa fedha, namna gani ya kusimamia matumizi ya fedha katika taasisi hizi. Tunakwenda kupoteza fedha nyingi na leo hii tukiendelea kutoa taarifa hizi tutaonekana wabaya, tutaonekana tunaongea sana lakini lengo hasa ni kuhakikisha tunatoa taarifa ambazo zitaisaidia Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia taarifa kuhusiana na masuala ya matumizi ya EFD mashine. Imekuwa ni kero, unakuta mfanyabiashara wa mahindi anatoka Mkoa wa Katavi anakuja kuuza mahindi yake Dar es Salaam mpaka afike Dar es Salaam ameshakutana na vizuizi vingi, lakini upatikanaji wa hizi mashine hizi electronic mashine imekuwa ni mtihani . Mfanyabiashara anatoka Wilaya ya Mlela anakuja mpaka Mpanda kutafuta tu hiyo risiti ili aweze kusafirisha mzigo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningemwomba Mheshimiwa Waziri katika suala zima la kuboresha hii mifumo ya namna gani ya ukusanyaji kodi, tuachane na mfumo wa kutumia manually kwa sababu watumishi wengi bila kuwasimamia vizuri unakuta tunapoteza mapato katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba tu kupitia mpango huu ambao kimsingi sijaona kwamba kuna sehemu imeandikwa kwamba mtakwenda kuhakikisha kila maeneo kila point ambayo itakuwa na ukusanyaji wa mapato mwongeze hizo mashine lakini kumekuwa na kero kubwa kwa hawa matrafiki. Sisi ambao tunasafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Katavi unakutana na trafiki anakwambia umetembea over speed, ume-overtake lakini ukimwambia sasa okay nilipe Sh.30,000/= niendelee na safari yangu anakwambia sina mashine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini anakwandikia karatasi fekifeki tu unapita haijulikani hizo pesa zinakwenda wapi, leo tunapiga kelele watu wanakufa na njaa, watu wana shida ya maji, leo hii mngeweka mifumo hii mizuri na hizi mashine zikawepo za kutosha, pia kusimamia hii mifumo ya EFD kwamba kila center wanaposimama hawa matrafiki basi kuwe kuna hizi mashine ili kuondokana na huu udanganyifu ambao upo katika taasisi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya procurement entity, kumekuwa na udanganyifu mkubwa, tumekuwa tukipitia taarifa katika taasisi mbalimbali unakuta masuala ya documentation imekuwa ni issue imekuwa ni tatizo, unamuuliza procurement officer kwamba ni kwa nini kwenye masuala ya procurement masuala ya uingizaji wa bidhaa na utoaji wa bidhaa unakuta hakuna document ambayo inaonesha kwamba amepokea bidhaa kiasi gani na ametoa bidhaa kiasi gani, lakini unauliza unaambiwa kwamba mimi sina utaalam, tunakwenda kutengeneza Taifa gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu katika maeneo ambayo nafahamu kwamba tunapoteza vifaa vingi, tunapoteza pesa nyingi ni katika masuala ya procurement entity especially katika ofisi zetu ambao kuna Department za Procurement. Kwa kuwa kuna shida nyingine unakuta katika taasisi katika ofisi unakuta hakuna kitengo cha procurement ni mtu tu hata kama ni mhasibu anaamua tu kwamba leo sasa na-issue, natoa, nanunua, naagiza vitu natengeneza tenda, hatuwezi kwenda hivi bila kuboresha mifumo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia watendaji wetu katika hii procurement entity wanatakiwa wasimamie, pia uhifadhi wa documentation katika hizo strong room wanatakiwa wapewe, ili leo tunapotaka kumwajibisha mtu tujue kabisa tunaanzia wapi. Watumishi wengi wamekuwa wanashughulikiwa wengine wanafukuzwa kazi kwa kosa hili tu, kutokuwa na documents za kimsingi ambazo wangeweza kuonesha na akajitetea, pia kumekuwa na shida katika masuala yaku-handleover ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamuuliza Procurement Officer katika hizi taasisi zetu unamuuliza kwamba inakuwaje umepokea documents za ofisi bila kuoneshwa kwenye hiyo store umeacha vitu gani. Unamuuliza Procurement Officer anakwambia kwamba mimi nimepokea tu na kukabidhiwa ofisi, haiwezekani na ukiomba taarifa ya vifaa ambavyo vinakuwepo katika store hizi unakuta kwamba hakuna taarifa za ukweli. Sasa leo hii tunakwenda kusimamia vifaa, mali za umma pamoja na pesa za wananchi tunakosa taarifa kupitia kwenye masuala ya procurement, tutaendelea kupata shida, tutaendelea kupiga kelele huku wananchi wetu wakipata shida huku wachache wakijinufaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la viwanda. Mkoa wa Katavi katika bajeti iliyopita na pia katika mpango huu sijaona mkakati wa kuhakikisha mnatuongezea viwanda katika mkoa wa katavi. Hii ni tatizo, bajeti iliyopita wanatuambia kwamba tunaletewa viwanda zaidi ya nane, viwanda zaidi ya nane vitatusaidia nini Mkoa wa Katavi. Watanzania walioko kule wanahitaji viwanda zaidi ya hivi ambavyo wametupatia, kwa sababu na ukisoma kwa taarifa wanakwambia tumepewa viwanda nane na kiwanda kimoja kina uwezo wa kuajiri watu watatu, sasa hizo ajira ndio hivyo viwanda vya matamko ambavyo mnavisema , hatuwezi kuendeleza viwanda katika nchi hii bila kuwa na takwimu za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mapinduzi ya viwanda hayawezi kwenda tofauti na upatikanaji wa maji ya kutosha pamoja na umeme. Mkoa wa Katavi tuna visima vya maji zaidi 1000, leo hii watu wa Katavi wanakosa maji safi na salama kwenye mpango huu naona tu mikoa tofauti na Katavi sijaona kwamba kuna mkakati wa kuhakikisha Katavi tunapata maji. Hivi viwanda vya miujiza mnavyovisema kwamba tunahitaji kuingia kwenye mapinduzi ya viwanda ni vipi? Kwa sababu ninavyoelewa tunaposema mapinduzi ya viwanda lazima kuwe kuna upatikanaji wa maji wa kutosha pamoja na umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo katika masuala ya umeme wanatuletea majenereta mawili, tena majenereta mawili ambayo yamechoka. Nilitegemea kwamba kwa kuwa Serikali hii ni sikivu basi wangeongeza hata miundominu ya umeme kama masuala ya umeme wa REA lakini wametuletea umeme wa REA katika Wilaya ya Mlele, kitu ambacho hata watu wa Wilaya ya Mlele wameshindwa kulipia gharama, gharama zimekuwa kubwa lakini leo tungejikita kuhakikisha tunaweka miundominu katika mabonde yetu ambayo tuko nayo Mkoa wa Katavi leo hii tusingekuwa tunalalamika masuala ya umeme. Watu wa Mkoa wa Katavi, watu wa Wilaya ya Mpanda wanakaa wiki nzima hawapati maji, lakini bili zinakuja wananchi wanalipa, wanaletewa bili watu wana maisha magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia taarifa za TANESCO zimekuwa kizungumkuti. Umeme unakuja wanawasha, wanazima, watu wanaunguziwa vifaa vyao kwenye ofisi zao, hatuwezi kuendelea kulea uozo huu ambao unaendelea kwenye Mkoa wa Katavi bila kusema namna gani wanaitenga Katavi lakini namna gani wamekuwa wakitenga bajeti ambayo haijitoshelezi hususani katika masuala ya miundominu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala pia ya umeme leo wametutengea zaidi ya bilioni mbili katika mradi wa maji ambao unatoka Kanoge mpaka kuja katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda. Ukisoma kwenye taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya Mkoa wa Katavi, wanasema kwamba umefika kwenye hatua ya ulazaji wa mabomba, sasa kwa muda wote huo kweli, watu wanakosa maji, watu wanakunywa maji ya kwenye mito, wanapata hata homa za maini, wanapata typhoid kupitia maji machafu ambayo wanakunywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani ungefika Mkoa wa Katavi ukaona namna gani watu wa Katavi wanapata shida, lakini leo hii wamekuwa wanaitelekeza Katavi,watu wanakunywa maji machafu hawaleti pesa kwa wakati. Pia hii yote ni kutokana na kwamba wananchi wengi wamekuwa na uwoga wanashindwa kuhoji wakihofia hawa watu wasiojulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie masuala ya mikopo kwa wanafunzi. Waliahidi kwamba watatoa ajira Rais alipokuwa Moshi tarehe moja hiyo siku ya Meimosi aliahidi kwamba ataajiri watumishi wapya lakini matokeo yake wamefanya replacement. Watu wengi walioonewa katika masuala ya vyeti feki au mwingiliano wa vyeti mara mbili, mfano katika shule ambayo ipo katika Wilaya ya Mpanda kuna Walimu ambao walihamishwa kutoka halmashauri moja kutoka Halmashauri ya Nsimbo kuja katika Halmashauri ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa katika mfumo wakajikuta kwamba majina yao yame-appear mara mbili leo mpaka hivi ninavyoongea hawajapata mishahara yao, lakini Serikali imekaa kimya, tumepiga kelele za kutosha na Waziri pia nimeshamweleza kuhusiana na tatizo hili lakini leo Serikali imekaa kimya. Sasa ni halali kweli kwa watu ambao wamesoma na wana vyeti mnawasulubu na kuwapa mateso makubwa haya, huku mkimwacha Bashite akila good time pale Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusiana na suala la maliasili pamoja na hifadhi. Imekuwa pia ni tabia kwenye hii Serikali ya CCM kuendelea kutumia askari wa wanyamapori hususani katika Wilaya ya Mpanda, Jimbo la Mpanda vijijini Kata ya Isengule Paparamsenga, ni kwa nini Serikali hii ya CCM inashindwa kutenga maeneo au inashindwa kupima maeneo kwa wakati? Leo hii kwa kufeli kwa Serikali hii kwamba wameshindwa kupima maeneo hayo kwa wakati pia kuonesha mipaka ya hifadhi ni ipi na makazi ya wananchi ni yapi, matokeo yake wamekuwa wanawaacha wananchi wanachomewa nyumba zao, wanauliwa na askari wa wanyamapori lakini inafikia wakati mpaka wananchi wanabakwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni Serikali gani ambayo inawaagiza wananchi badala ya kwenda kuwaondoa na kuwapa elimu wananchi kuhusiana na suala la mipaka leo wanakwenda kuwabaka, wanawachomea nyumba zao ni Serikali gani hii ya CCM?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti ya Waziri Mkuu. Kwanza nataka niseme tu mwanzo kwamba nahitaji kumpa pole Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, lakini pia pamoja na Wabunge wote wa Upinzani ambao kwa muda mfupi wiki mbili zilizopita wamepata matatizo na kashkash kutokana na Jeshi la Polisi kutumia nguvu, lakini pia viongozi wetu kuendelea kupata shida kwa sababu wanapigania haki katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji kujikita kwenye mambo machache tu na ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize kwa makini kwa sababu katika Mkoa wa Katavi tuna changamoto nyingi ambazo tangu mwaka 2008 mpaka sasa tumekuwa tukipigania mambo haya lakini Serikali ya Chama cha Mapinduzi inashindwa kutoa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 halmashauri ilitenga fedha kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu, lakini pia kuna fedha ilitengwa kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa hospitali ya mkoa katika Mkoa wetu wa Katavi. Hata hivyo, lakini projects hizi zimefeli, pesa zimepigwa, halmashauri iko kimya na sisi kama Wabunge tumekuwa tukipata hoja kutoka kwa wananchi kwamba ni kwa nini mambo haya, Mkurugenzi pamoja na Baraza la Madiwani 2010 mpaka 2015 walipitisha maazimio haya na fedha hizi zikawa zimetumika ndivyo sivyo, lakini tukihoji kwamba ni kwa nini michakato hii imeishia hewani, wananchi wanapiga kelele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo haya, kwa sababu ujenzi wa hospitali ya mkoa, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo katika Mkoa wa Katavi yalikuwa yametengwa katika eneo moja kwa maana ya Kata ya Kawajense. Kuna zaidi ya ekari mia tano lakini mpaka sasa wananchi wako pale, wamechukuliwa maeneo yao hawajalipwa fidia, wakienda kufuatilia kwa Mkurugenzi pamoja na Meya Serikali iko kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini tamko la Serikali ili tujue kwamba wananchi hawa ni kweli wameporwa maeneo haya na ni kwa nini Serikali iko kimya kufuatilia michakato hii? Kwa sababu maswali ya msingi nimekuwa nikiyauliza sana kuhusiana na wizi huu uliofanyika katika Manispaa ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Waziri Mkuu atakapokuja kuhitimisha, naomba kabisa kupitia jambo hili, kwa sababu ndiyo imekuwa kero ya wakazi wa Mkoa wa Katavi. Sasa kama Serikali ni sikivu na imekuwa ikitumbua majipu. naomba katika Manispaa hii ikasimamie jambo hili. Wizi uliofanyika katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo katika Mkoa wa Katavi, lakini pia wizi uliofanyika katika suala zima la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; nataka niongelee tu kidogo kuhusiana na ununuzi wa gari la taka. Baraza la Madiwani 2010 - 2015 lilipitisha fedha zaidi ya milioni mia moja kwa ajili ya ununuzi wa gari la kisasa la taka, lakini mpaka hivi tunavyoongea gari halijanunuliwa, matokeo yake Baraza la Madiwani linakuja kupitisha fedha nyingine kununua gari lingine jipya. Maana yake yule Mr. Kisira ambaye alipewa tenda kwa ajili ya ununuzi wa hilo gari la taka mpaka sasa hajarudisha hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zimepigwa, matokeo yake Baraza la Madiwani kazi yake ni kupitisha tu kwamba tunanunua gari lingine wakati tukiendelea kufanya mchakato huyu Mr. Kisira ambaye ndiye alikuwa mzabuni wa ununuzi wa hilo gari la taka alishindwa na hakuwa na vigezo vya kununua hilo gari la taka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nifahamu tu, kwamba kama Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu inashindwaje kwenda kutatua mgogoro huu ambao umekuwa ni kero kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi, lakini mpaka hivi tunavyoongea wananchi wa Mkoa wa Katavi Manispaa ya Mpanda wanachangishwa shilingi elfu mbili kila kaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takataka zinazagaa kwenye maeneo yao, Manispaa iko kimya, ukimuuliza Mkurugenzi hana majibu, Meya hana majibu. Sasa tutaendelea kupongeza mambo kama haya ikiwa manispaa ni chafu? Mnatumbua maeneo mengine Manispaa ya Mpanda mnaiacha na wananchi wanachangishwa fedha. Sasa mtueleze tu kwamba gari hili la taka, mimi kama Mbunge nimeshindwa kupata majibu ya msingi niende nikawaeleze nini wananchi wa Manispaa ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niongelee kidogo kuhusiana na masuala ya viwanda. Bado tuna changamoto za viwanda katika Mkoa wa Katavi na hazikidhi na ukizingatia Mkoa wa Katavi tunalima sana, kwa maana ya mazao ya biashara pamoja na mazao ya chakula. Sasa tunavyoongea ni kwamba hatuna viwanda ambavyo vinaweza kukidhi kuzalisha ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda cha alizeti ambacho kiko katika Kata ya Makanyagio, Kiwanda cha Mpadeku. Kiwanda hiki kiko dormant, tunalima alizeti lakini hawazalishi hata zaidi ya tani moja, matokeo yake tumekuwa tunatumia gharama kubwa za uzalishaji, kitu ambacho kinasababisha sasa tunatumia gharama kubwa ya uzalishaji lakini hatupati masoko, lakini pia hatupati faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba tu, kwa sababu mnajinasibu ya kwamba ni Serikali ya Viwanda, basi ningeomba tu sasa mtuongezee viwanda kwenye Mkoa wa Katavi kwa sababu viwanda vingi ambavyo viko kule tukitegemea vingeweza kuzalisha mazao mbalimbali tungeweza kusindika mazao hayo kwenye viwanda vidogo vidogo lakini imekuwa ni tofauti, kwamba wananchi hawaoni matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika changamoto hizo za viwanda, Manispaa ya Mpanda imetenga eneo la Kata ya Misunkumilo, eneo hili wamechukua wajasiriamali wadogo wadogo ambao wamewatoa katika maeneo mbalimbali kwenye Manispaa ya Mpanda. Wamewafukuza kwenye maeneo ambayo wanafanya kazi wakiwepo wanaokata mbao maana ya viwanda vya mbao kwenye Manispaa, lakini wakiwepo wakata vyuma, wale mafundi welding.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe tu wajasiriamali hawa wadogo wadogo wamepelekwa katika eneo la Misunkumilo, Manispaa wametenga eneo hili, lakini wamepelekwa kule, hakuna umeme, hakuna maji lakini pia miundombinu yake ni mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Serikali hii ni sikivu ningeomba ingeweza kuwasaidia wananchi hawa kwa sababu wanapigwa, wanafukuzwa kwenye manispaa wanapelekwa kwenye eneo ambalo hakuna miundombinu, sasa niombe tu kama mko tayari kweli kuwasaidia wananchi kwa ujumla na wakazi wa Mkoa wa Katavi mpeleke kwanza miundombinu ya maji pamoja na umeme na si kukurupuka tu kuwafukuza wananchi kuwapeleka kwenye maeneo ambayo hakuna miundombinu ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tu suala la mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake, wazee pamoja na walemavu katika Mkoa wetu wa Katavi. Mikopo inayotolewa katika manispaa ninayotoka mimi, Manispaa ya Mpanda Mjini, leo hii tunavyoongea vijana wamekopeshwa fedha, baadhi yao kwa maana ya kwamba sasa hawa Maafisa Maendeleo na watendaji ambao wanahusika na masuala mazima ya kutoa mikopo hii, kuna baadhi ya vikundi vinatoa malalamiko kwamba pesa hizi zinatolewa kwa ubaguzi kwa maana ya kuangalia itikadi zao za vyama na mambo mengine. Kwa hiyo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie kidogo kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka niseme kwamba, bajeti ya dawa kwenye Wizara hii imechukua sehemu kubwa ya bajeti nzima. Kwa hiyo inaonesha kabisa kwamba kwa kuchukua bajeti hii kubwa ya dawa, kwamba Serikali hii imejipanga kutibu zaidi watu kuliko kuwapa kinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niongelee kidogo kuhusiana na Mkoa wangu wa Katavi. Mkoa wa Katavi sasa hivi sisi ni vinara kwa watoto wadogo wa kike wanapata mimba za utotoni kwa zaidi ya asilimia 36.8. Kwa hiyo ningeomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze kwamba, kama Wizara na Serikali kwa ujumla wana mkakati gani wa kuhakikisha hawa vijana au watoto wadogo wa kike wanapata elimu ya uzazi wa mpango, ili tupunguze hili janga katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu tu, watoto wa kike wsichana 624 ambao wako chini ya umri wa miaka 18 kwa mwaka wanajifungua katika hospitali zile zile zilizopo katika Mkoa wetu wa Katavi, hatuna hospitali ya mkoa, tuna hospitali ya wilaya na hizi zahanati ndogo ndogo. Hata hivyo pia zahanati hizi pamoja na hospitali ya wilaya zimekuwa zikibeba mzigo mkubwa. Upungufu wa watumishi unasababisha watumishi hawa kufanya kazi wana-over late, wanafanya kazi na malipo yao pia, bado wanawacheleweshea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kuangalia uzito wa jambo hili, mimba za watoto katika Mkoa wetu wa Katavi limekuwa ni tatizo kubwa na watumishi pamoja na Madaktari, Wauguzi, pamoja na Manesi wanafanya kazi kubwa sana. Hakuna wodi za kutosha; akinamama wanalala wawili wawili kwenye vitanda. Kwa kupitia hii Serikali ya viwanda sasa wajipange na si kupeleka tu pesa kwenye mambo yasiyo na msingi, waangalie vipaumbele vya Watanzania kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujenzi wa hospitali ya mkoa. Kama nilivyosema na nimekuwa nikiongelea sana jambo hili. Pesa ilitengwa zaidi ya bilioni moja, lakini mpaka sasa hivi haieleweki zile pesa ziko wapi. Kwa hiyo, tunaomba kupitia Wizara jambo hili hebu likae wazi, pesa hizi zirudishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi huyu, Mchina aliyehusika kupiga hizi pesa pamoja na Baraza la Madiwani lililopita waeleze pesa hizi ziko wapi, kwa sababu wanawapa mzigo watu wa Mkoa wa Katavi wanasafiri kutoka Mpanda kwenda Mbeya kufuata huduma kwenye hospitali za rufaa. Kwa hiyo, watu hawa wasiendelee kuwapa matatizo watu wa Mkoa wa Katavi, watu wanatumia gharama kubwa, wanasafiri siku nyingi kufuata huduma za rufaa katika Mkoa wa Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue tu Serikali wamejipangaje, kwa sababu takwimu zinaonesha kwamba afya ya akili kupitia Hospitali yetu ya Milembe, wagonjwa wanaongezeka kwenye hospitali hiyo. Sasa kama Serikali wamefanya utafiti gani kuona kwamba kwa nini Watanzania wengi kupitia haya magonjwa ya akili wanaongezeka katika Hospitali ya Milembe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Tanzania pia, ni nchi ya tatu ambayo inaongoza kwa udumavu na ni nchi ya 10 inayoongoza kwa udumavu uliokithiri. Sasa ningeomba tu, kwamba kwa takwimu hizi tukielekea kwenye Serikali ya viwanda na tunategemea kwamba hawa ni watoto, maana yake watakwenda shuleni tunakwenda kuzalisha watoto ambao watakuwa na utapiamlo, watoto ambao watakuwa na udumavu wa akili, hawatapata elimu ya kutosha. Sasa hiyo Serikali ya Viwanda bila kuwekeza kwenye elimu kupitia hawa watoto kupata lishe bora tunakwenda kutengeneza Taifa la namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuna changamoto nyingi, lakini ningeomba haya machache Serikali iyashughulikie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi lipewe hati za Kambi na maeneo yao kwani mpaka sasa wananchi wanaendelea kuwa na migogoro na jeshi na migogoro hii ni ya muda mrefu. Je, Serikali kupitia Wizara hii ni lini itaondoa unyanyasaji huu unaoendelea kufanyika kwa wananchi kuzuia kufanya shughuli za kiuchumi na wakati maeneo hayo bado yana migogoro? Je, Wizara haioni kuwa kuendelea kushindwa kutatua kero hizi ni kuwaongeza umaskini wananchi? Wananchi wanapigwa na wanajeshi wanapata vilema kwa sababu ya kuingia kwenye maeneo hayo ambayo mpaka sasa hatma yao haijulikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Misunkumilo, Jimbo la Mpanda Mjini, Katavi mpaka sasa wananchi pale hawajalipwa fidia zao kwa sababu jeshi ndiyo lililoingilia mipaka ya wananchi. Je, Wizara inawafikiriaje wananchi hawa kwa kuwalipa fidia zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa ziada wa utumishi hauko katika sheria za utumishi. Wanajeshi wanaingia saa 12.00 asubuhi wanatoka saa 12.00 jioni. Ni sheria gani inawafanya wanajeshi kufanya kazi saa nyingi tofauti na watumishi wa umma? Sheria inasemaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za askari ni chache na zimechoka. Tangu kipindi cha Mwalimu Nyerere mpaka sasa nyumba zilizojengwa ni chache mno na hii imepelekea wanajeshi kuishi pamoja na wananchi kitu ambacho kinaondoa dhima ya jeshi. Serikali wanaona jambo hili ni sahihi kama siyo sahihi kupitia bajeti hii wamejipangaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko ya uonevu kutoka kwa wananchi kuwa baadhi ya wanajeshi wasio na maadili ya kazi wamekua wakionea wananchi kwa kuwapiga bila sababu kwa sababu tu ya vyeo vyao. Je, Serikali haioni kukaa kimya kwa matendo haya ambayo hayaendi na maadili ya kazi na vitendo hivi vinavyoendelea vinalichafua jeshi?
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami niweze kuchangia kidogo Mpango. Nitachangia katika maeneo mawili au matatu, lakini jambo la kwanza nilitaka kuzungumzia kupitia hiki kitabu cha Mpango; ukisoma ukurasa wa 10 wameelezea maendeleo ya miundombinu katika Taifa letu. Nami niseme, Mheshimiwa Waziri ameainishaa baadhi ya mikoa ambayo mpaka sasa hakuna muunganiko wa lami kwa maana ya mikoa, hasa ukiangalia Mkoa wa Tabora, Ruvuma, Lindi, Mtwara pamoja na Tabora, Katavi, Kigoma na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kupitia huu Mpango, kwa sababu katika mikoa hii bado kuna changamoto ya miunganiko hii ya barabara; na jambo hili la suala la miundombinu katika hii mikoa ambayo imebaki nyuma, inaleta ukakasi na inaendelea kuwatesa wananchi kwa maana ya kwamba wanashindwa kufanya biashara na ukizingatia katika kanda hizi, asilimia kubwa ni wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali kupitia Mpango huu, kwa sababu umeainisha kabisa kwamba katika mikoa hii imebaki nyuma ili sasa wakazi hawa wa mikoa hii nao wapate ahueni ya maisha kupitia masuala ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia masuala ya fidia, miundombinu ya barabara nilitamani sana iendane na masuala ya kufungamanisha uchumi wao na wananchi, kwa maana tunaposema maendeleo ya vitu, iendane sambamba na maendeleo ya uchumi wa wananchi, kwa maana ya personal development.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika maeneo mengi ambayo yanahusiana na masuala ya fidia kwa maana ya wananchi ambao walikumbwa na bomoa bomoa katika mikoa mbalimbali, kwa mfano Mkoa wa Mwanza, Dar es Salaam, Katavi na mikoa mingine ambayo bomoa bomoa imepita; ni kweli wananchi wanazihitaji barabara lakini katika mikoa ambayo bomoa bomoa imepita wananchi wengi wamebaki ni masikini. Sasa lengo la Serikali ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu uchumi mnaosema umekua kwa asilimia 7.0 ni uchumi wa aina gani? Tunahitaji kuona mafanikio au uchumi wa wananchi unakwenda moja kwa moja kwa wananchi kwa maana ya kwamba msivunjie nyumba wananchi ambao wamejenga kwa gharama kubwa, leo wanaishi katika nyumba za kupanga. Katika jambo hili mnapokuwa mnafanya tathmini na hata wananchi ambao wanakuwa wameachwa, wameshindwa kufanyiwa tathimini, mweze kuwalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo suala la uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Jambo hili limekuwa ni changamoto na mpaka sasa kuna taharuki kwa wananchi ambao waliingia kwenye mchakato huo. Kwa hiyo, naiomba Serikali, kwa sbabu mnatangaza amani ambapo mnatumia nguvu kubwa kuwaaminisha watu kwamba katika uchaguzi huu kila kitu kiko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makovu na majeraha ya watu ambao wameumia kwenye uchaguzi huu especially katika Mkoa wangu wa Katavi, tarehe 5 Novemba, 2019 Mtendaji aliagiza watu wakawavamie vijana wa CHADEMA; na mpaka sasa kuna kijana ambaye anaitwa Dominic Bazilio Mwila alipigwa na Mgambo mpaka akafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme katika hayo marekebisho mnayoyatoa, kwamba tunahitaji kufanya maridhiano ya pamoja, naomba kabisa, kama kweli mnahitaji kuwa na maridhiano ya pamoja na kuwe na amani katika Taifa hili, mwache kuumiza watu na majeraha ambayo wanayapata. Leo hii tutarudi kwenye uchaguzi, lakini watu wana majeraha, watu wameumizwa, watu wako ndani na siyo katika Mkoa wa Katavi tu peke yake…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rhoda, mtu alipigwa na mgambo huko kwa mambo yao huko. Sasa ukituambia au ukiwaambia waache, sasa kweli unaamini hawa wamemtuma huyo mgambo amuue huyo ndugu yetu! Endelea tu kuchangia.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaendana sambamba kabisa na masuala ya uchaguzi, ndiyo maana nikasema, kama mnahitaji amani mnayoitangaza, wasimamizi na wahusika waliotumia mamlaka yao kufanya majanga haya kwenye maeneo mbalimbali, siyo mkoa wa Katavi peke yake, mpaka na mikoa mingine, naomba kabisa katika masuala ya maridhiano kwenye mambo haya ya suala la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tupunguze majeraha na kutumia nguvu ambayo Serikali inatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika maeneo ambayo kuna upungufu, hawa Watendaji au Makatibu Tarafa, Wasimamizi Uchaguzi...

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Rhoda, kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Mheshimiwa Rhoda taarifa kwamba kwanza tuwe wakweli kwenye Bunge hili, suala la kusema kwamba watu wanauawa, kulikuwa hakuna uchaguzi sehemu yoyote unaofanyika, kulikuwa kilichofanyika ni ujazaji wa fomu sasa huyo mtu aliyeenda kuuawa kwa kujaza fomu, kulikuwa kumetokea nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine hapa jamani tuwe tunasema ukweli. Haya mambo, vitu vinaenda kwenye nchi za watu. Tanzania inachafuka kwa mambo ya uongo. Hakuna uchaguzi uliofanyika, ni ujazaji wa fomu. Huyu mtu aliuawa wapi? (Makofi)

MWENYEKITI: inawezekana walikuwa wanagombea mpango kando au nini, ndiyo anachosema Mheshimiwa Rhoda. Malizia, bado dakika moja tu.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu. Ninachokiongelea hapa, kifo cha mtu huyu kinahusishwa na masuala ya uchaguzi kwa sababu kama nilivyosema mwamzo, Katibu Tarafa pamoja na Watendaji walitoa magizo kwenda kuwashughulikia wagombea CHADEMA. Kwa hiyo, kesi ipo, Ndiyo maana nasema katika maridhiano haya, katika mipango ya Serikali kuhakikisha mnatuliza uchafuzi uliotokea, naomba kabisa m-deal katika maeneo ambayo kweli hali siyo shwari na Serikali ione haja ya kuweza kutatua migogoro ambayao ipo na inaendelea. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Nakushukuru sana.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi niweze kuchangia mawazo kidogo kwenye Wizara ya Kilimo, Maliasili pamoja na Maji. Nadhani hii ni karibuni mara ya kumi nimekuwa nikizungumza jambo moja katika Mkoa wangu wa Katavi asilimia 90 ya wananchi wa Mkoa wa Katavi wengi ni wafugaji pamoja na wakulima lakini ukisoma hotuba ya Kamati zote mbili hususan kilimo pamoja na Maliasili hizi ni Kamati ambazo zinaingiliana kwa baadhi ya mambo. Changamoto kubwa walioieleza Kamati ni pamoja na migogoro na manyanyaso yanayoendelea kwa wakulima pamoja na wafugaji katika taifa hili. Sasa kwa ujumla wake manyanyaso hayo pamoja na uonevu umekuwa ukifanyika katika mikoa ambayo ina wafugaji wengi na wakulima wengi.

Mheshimiwa Spika, lakini wiki mbili zilizopita jambo la aibu Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika pamoja na Mkurugenzi wa Tanganyika walipokea pesa ya rushwa shilingi milioni 60 walimchaji mfugaji mmoja alikuwa na ngombe zaidi ya 600 wakawa wanamtoza milioni moja kwa ng‟ombe mmoja.

Sasa sheria inasemaje; mambo haya tukiwa tunalalamika watu wanaona kwamba tunalalaika kila siku lakini tunachokisema katika Taifa hili katika Mkoa wa Katavi naweza nikasema katika Wilaya ya Tanganyika inaongoza kwa rushwa chini ya huyu Mkurugenzi anaitwa Lumuli pamoja na Mhando, huu ni mwaka wa nne nazungumzia mambo haya.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, wizi, rushwa zimekidhiri katika Wilaya ya Katavi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, tunapokuwa tunazungumzia mambo haya...

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Rhoda kuna taarifa nilimsikia Mheshimiwa Msongozi

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nimemsikia mchangiaji anayeendelea kuchangia akizunguza suala la Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwamba wamepokea rushwa ya shilingi milioni 60. Kwa hiyo, nataka mchangiaji atueleze anaweza kutoa ushahidi kwa jambo hili analolizungumza?

SPIKA: Mheshimiwa Rhoda.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee na mchango wangu kwa sababu hata Mheshimiwa Jacqueline anayoongea haishi Mkoa wa Katavi wala haelewi kinachoendelea katika Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niongelee uonevu na unyanyasaji unaofanyika na Mkuu wa Wialaya huyu huu ni mwaka wan ne na si hayo tu, Mheshimiwa Waziri alikuwepo juzi wiki tatu zilizopita anaelewa wizi wa pesa zilizopigwa na huyu Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi anaelewa. Sasa Serikali imechukua hatua gani kuwawajibisha huyu Mkuu wa Wilaya ambaye kwetu kule ni mzigo watu hawamtaki kwa sababu amekuwa ni chanzo cha migogoro sio solution. Badala ya kumsaidia Mheshimiwa Rais amekuwa ni tatizo na anatamba kule yeye ndio Mfalme sasa kule yaani ndio Mungu mtu wa Wilaya ya Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu hawamuhitaji kutokana na kwamba amekuwa ni chanzo cha migogoro na sio solution kwenye Wilaya ya Tanganyika. Nataka Waziri akija atueleze ni sheria ipi ilitumika kuchaji ng‟ombe mmoja milioni moja na sheria inasema ni shilingi 30,000 kama ni ng‟ombe akiingizwa kwenye eneo la hifadhi. Sasa Mamlaka haya ya halmashauri ya Tanganyika wameyatoa wapi na wamechukuliwa hatua gani, Mheshimiwa Waziri akija atueleze wizi huu wa pesa zilizopigwa na huyu Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, solution yake ni nini.

SPIKA: Mheshimiwa Rhoda unasema ni wamechaji milioni moja kwa ngombe mmoja?

MHE. RHODA E. KUMCHELA: Mheshimiwa Spika, ndio ng’ombe mmoja

SPIKA: Yesu na Maria na huyo Mkuu wa Wilaya ni nani?

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, Mkuu wa Wilaya anaitwa Muhando na Mkurugenzi anaitwa Rojazi Lomoli.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie vijiji 920 Mheshimiwa Lukuvi alikuwepo kwenye ziara ya Rais iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana lakini tulitangaziwa kwamba kuna vijiji 920 vilivyorasimishwa kutoka kwenye maeneo ya hifadhi wananchi wapewe kwa maana ya uhaba wa maeneo ya malisho.

Mheshimiwa Spika, sasa mpaka hivi tunavyoongea si Mkoa waKatavi peke yake mpaka na maeneo mengine baada ya kauli hizi ambazo Mheshimiwa Rais alitamka kwamba haitaji kuona wafugaji wanateseka katika Taifa lakini imekuwa ni vice versa. Wafugaji wamekuwa wakipigwa ukienda kwenye Kata ya Stalike watu wanapigwa lakini Rais alitoa kibali watu waendelee kuishi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Asante sana Mheshimiwa Rhoda dakika tano zimeisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu pia naunga hoja maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Spika, Tanzania tuna mifugo ya takribani zaidi ya milioni 30.5 kwa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Uvuvi na Mifugo kwa mwaka 2017/2018; na Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na mifugo mingi katika Bara la Afrika.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa takwimu hizi hazioneshi uhalisia wa Watanzania kunufaika na wingi wa mifugo. Kwa hiyo changamoto zilizopo kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi; nadhani sasa Waheshimiwa Wabunge wameeza kwa upana wake; changamoto tulizonazo ziko wazi. Tunakosa viwanda kwa ajili uzalishaji; Waheshimiwa Wabunge wameongelea masuala ya uzalishaji wa nyama, maziwa, pia viwanda vya ngozi. Tuna changamoto za kukosa sera na kanuni ambazo zingeweza ku-support tukapata ubora wa bidhaa, tukaweza kuuza ndani ya nchi na kupata masoko nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapata changamoto kwa kutokupata sera na kanuni ambazo zingewezesha wawekezaji kwenye Sekta Binafsi, wangeweza kuwekeza na tukapata viwanda na tukapata bidhaa ambazo zingeweza kulinufaisha taifa.

Mheshimiwa Spika, niongelee kwa kifupi, Mkoa wa Katavi tuna changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi, na tangu mwaka 1961 tulikuwa na hifadhi moja tu; lakini kwa sasa tunahifadhi za kitaifa zaidi ya tano. Sasa unaona tatizo la migogoro ya ardhi, kwa maana ya wafugaji kukosa maeneo ya malisho ni kutokana na Serikali kuendelea kuchukua maeneo tengefu, pia kuendelea kuchukua maeneo kwa ajili ya kutenga maeneo ya hifadhi. Kwa hiyo kama Serikali ikiendeela kutenga maeneo haya, kuchukua maeneo ya wananchi ambao kwa sehemu kubwa walikuwa ni wafugaji wakaweka hizo hifadhi, sasa hawa wafugaji wetu wanakwenda wapi? Ndiyo maana unaona wanasambaa kwenye mikoa mbalimbali, wanaenda kuvamia maeneo ambayo mengine ni maeneo ya wakulima, makazi na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo Serikali, kwa sababu tuna eneo kubwa la misitu ione namna ya kuweza kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji, ili kuondoa migogoro hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee kidogo kuhusiana na Mkoa wangu wa Katavi. Kumekuwa na mauaji ya kipuuzi kabisa yanayoendelea; na ni nimseme tu kwa kifupi Mkuu wa Wilaya ambaye anajiita ni Muhando katika Wilaya ya Mpanda Vijiji, kwa maana ya Tanganyika, amekuwa anatumia ubabe ambao kimsingi ni unyanyasaji ambao unaendelea kwenye taifa na watu hawana sehemu ya kusemea.

Mheshimiwa Spika, ukihitaji nikupe CD ya mauaji ambayo yametokea katika Kijiji cha Lyamgoloka, ni hii hapa. Wananchi wamepigwa risasi, watu wanachomewa nyumba, mifugo inapigwa risasi, watu wanapigwa hawaelewi hatima yao ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa taifa hili mnalosema ni la wanyonge ni kwa nini Serikali hii ya Awamu ya Tano inakaa kimya? Ni kwa nini mnashindw ku-solve migogoro ambayo inaendelea katika Jimbo la Mpanda Vijijini? Na hawa askari wa wanyamapori ambao wengine wamekuwa si waaminifu wanapora ng’ombe, ng’ombe wanapigwa risasi. Ni kwa nini Serikali hii inashindwa kutatua migogo hii?

Mheshimiwa Spika, na huyu Mkuu wa Wilaya amekuwa sasa ana kashfa nyingi na wananchi wa Mpanda Vijiji hawamtaki kutokana na kero na matatizo ambayo yanaendelea kwenye hili. Vijiji ambavyo vimeathirika kutokana na Mkuu huyu wa Wilaya ambaye sasa anajifanya ni Mungu mtu kuna Kaseganyama, Mnyamasi, Karema, Ikole, Isengule, Kapalamsenga pamoja na Vijiji vya Iseganyama.

Mheshimiwa Spika, watu wanaishi kama wako porini, ni kwa nini Mkuu wa Wilaya anafanya matendo ya kinyama, anaamlisha Askari wa wanyamapori pamoja na Polisi kwenda kuwapiga wananchi; leo watu wanaishi kwenye mahema, watu hawaelewi hatima yao ni nini. Hivi leo wafugaji wamekuwa wanaishi katika mazingira ambayo hawaelewi hatima yao ni nini halafu mnasema nchi ni ya amani?

Mheshimiwa Spika, ninaomba Waziri atakapokuja kuhitimisha aeleze ni namna gani atatatua mgogoro na huyu Mkuu wa Wilaya Muhando sisi hatumtaki, wananchi wa Jimbo la Tanganyika hawamtaki kwa sababu tangu ameingia katika Mkoa wa Katavi amekuwa ni kero na hana suluhisho katika migogoro ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, niongele masuala ya tozo; bado iko pale pale. Halmashauri ilitenga kwamba wafugaji wanapoingiza mifugo kwenye maeneo ambalo si sahihi, kwa maana ya hifadhi watozwe shilingi 50,000 kwa mara ya kwanza, kwa pili wanatozwa shilingi 100,000 na kuendelea. Sasa fedha hizi watu wamekuwa wanatozwa zaidi ya 100,000. Ng’ombe mmoja akiingia kwenye chanzo cha maji wanalipishwa mpaka milioni moja; sasa hizi pesa zinakwenda wapi?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Rhoda tunakushukuru sana.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa ili niweze kuchangia Wizara hii pia naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Spika, katika Taifa letu asilimia 53 ya ardhi yetu ni misitu, pia asilimia 15.4 ni eneo ambalo linafaa kwa ajili ya kilimo, malisho na maeneo mengine. Sasa inashangaza kama bado tuna eneo kubwa kiasi hiki na Wizara hii ya Makazi inashindwa kutenga maeneo kwa maana ya kutenga maeneo ya makazi kwa wananchi wakapata hati zao na tukaepuka migogoro ambayo inaendelea. Hilo ni jambo la kwanza. Pia Serikali hii ikatenga maeneo kwa ajili ya malisho ili kuepuka migogoro kati ya hifadhi na Serikali.

Mheshimiwa Spika, pia kuna migogoro mingi ambayo inaendelea kwenye nchi hii inasababishwa na Wizara hii kushindwa kutatua migogoro ya ardhi, kuna masuala ya Taasisi za Serikali kukosa Hatimiliki, wananchi wanapewa hati kwa mfano kwenye Manispaa ya Mpanda kwenye Kata ya Misunkumilo, ukija Mpanda Hoteli, Milala na maeneo mengine wananchi wale wamepewa hati na wamepelekewa huduma za kijamii kwa maana ya masanduku ya kupiga kura, umeme, maji pamoja na barabara .(Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa watu hawa wanakwenda kuwaondoa, ni Serikali hii moja ya Awamu ya Tano, imepeleka huduma hizo, pia Jeshi liko pale pia nao hawana hati. Sasa mazingira haya yanapelekea wananchi wetu kupata shida, wananchi wanajenga nyumba katika mazingira magumu sana na wananchi wetu wengi ni maskini. Kwa hiyo Wizara hii ione namna ya kuharakisha jambo hili la kutoa hati kwa wananchi haraka iwezekanavyo hususani katika maeneo ambayo wananchi wanajenga katika makazi mapya.

Mheshimiwa Spika, vile vile niongele suala la Shirika la Nyumba la Taifa, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, tumeweza kuzungukia maeneo mbalimbali kwa maana ya miradi ambayo iko chini ya shirika hili ikiwepo na mradi wa Dege Eco ambao uko Kigamboni, TBA na maeneo mengine. Ukiangalia nyumba hizi kuna maeneo mengine kweli shirika wamejitahidi, lakini tunaona namna ambavyo Serikali inatumia gharama kubwa kwa kutumia pesa za Serikali kujenga nyumba hizi na tukiangalia outcome yake ni ndogo, outcome yake ni ndogo kwa sababu watumishi wengi wanashindwa ku-afford kununua na kupangisha kwa sababu gharama ziko juu. Kwa hiyo kupitia Wizara hii niombe pia Mheshimiwa Waziri kuona namna ya kuweza kupunguza gharama za upangishaji pia gharama za ununuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija changamoto nyingine ni kwa nini nyumba hizi zinakosa wateja. Unakuta nyumba zimejengwa kwenye maeneo ambayo hata miundombinu hakuna, barabara nyumba inajengwa porini, sasa unategemea mtumishi gani anaweza kwenda kupanga au kwenda kununua eneo hilo. Kwa hiyo Serikali ione namna ya kuweza kuboresha miundombinu ya maji, umeme, barabara na huduma za afya na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee jambo la mwisho kuhusiana na suala la mipaka; narudi palepale kwamba migogoro mingi na Mheshimiwa Waziri amesema Mkoa wetu wa Katavi pia umekuwa wa mwisho kwa kukusanya hayo makusanyo ya mapato kwenye hilo eneo. Ni kweli lazima tushindwe kwa sababu hata ukiangalia halmashauri yetu bado haina uwezo, leo tutawalazimisha watu wapime na hakuna ushirikishwaji wa moja kwa moja na hizi Taasisi Binafsi bei imekuwa iko juu sana, watu wanashindwa kulipia tozo hizi zimekuwa ziko juu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali ione namna ya moja kwa moja kuweza kushirikisha hizo kampuni binafsi, halmashauri zetu na Serikali kwa ujumla wake kwa sababu wananchi wanashindwa kupima maeneo kwa sababu gharama ziko juu na leo tutaendelea kuweka uzembe kwenye eneo hili matokeo yake tuje kuwabomolea wananchi na ndiyo masuala ya bomoabomoa Serikali hii inashindwa kulipa pia masuala yao ya fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, masuala ya uwekaji wa hizi beacon; kumekuwa na migogoro hii ya muda mrefu ambayo Mheshimiwa Waziri amesema na Mheshimiwa Rais ametamka kwamba kwenye eneo ambalo linahusisha mgogoro kati ya hifadhi na wananchi maana yake wananchi wapewe kipaumbele. Sasa katika maeneo hayo ninayozungumzia katika Kata ya Sitalike ambayo iko katika Jimbo la Nsimbo Lyamgoloka, Kasekese na maeneo mengine ambayo yana migogoro hii, ni kwamba Serikali hii imeshindwa kuwashirikisha wananchi moja kwa moja kwa maana ya kuonesha hiyo mipaka. Sasa ni lengo la Serikali hii kuhakikisha linatatua migogoro hii…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, kwa kuweka mipaka. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hotuba ya Kamati kwa kutoa maelekezo ya mahitaji ya elimu kitaifa pamoja na kuonesha utatuzi wa changamoto za elimu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii; ukimuelimisha mwanamke utaokoa jamii. Hivyo basi, hatua za haraka zichukuliwe katika kuongeza bajeti ya miundombinu katika shule za bweni za wanawake; kuboresha upatikanaji wa maji ili yawe ya uhakika; usalama kwa mabweni yasio na fence; huduma za afya katika mabweni ya kike na uboreshaji wa chakula kwa mabweni ya wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda mrefu sasa wananchi wa Katavi wamekuwa wakisubiri ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo. Tunataka majibu ya Serikali, ujenzi utaanza lini na tufahamishwe kama fedha zimetumika nje ya utaratibu au zimeliwa au chuo kilihamisha? Tatizo hili kuendelea kukaliwa kimya na Serikali na Halmashauri ambapo zaidi ya shilingi bilioni moja zimeliwa na chuo hakipo, inamaanisha kwamba Serikali ya CCM inalinda wezi au imehusika moja kwa moja kudhulumu Chuo cha Kilimo kwa Wana-Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kuwa na Chuo cha Kilimo Katavi ni kwamba kundi kubwa la wananchi wa Katavi ni wakulima na wafugaji hivyo kupitia chuo hiki wangepata elimu bila kutakiwa kusafiri kwenda mikoa ya mbali na kupunguza gharama hususani kuleta mapinduzi ya kilimo cha kisasa mkoani Katavi, uwekezaji, ajira na uchumi wa viwanda kupitia chuo chetu kilichoyeyuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchache wa vitabu Katavi, tunaomba viongezwe pamoja na shule za sekondari na shule za msingi. Pamoja na juhudi za walimu Mkoa wa Katavi kufundisha wanafunzi katika mazingira magumu lakini ufaulu wa wanafunzi shule za msingi tumekuwa na matokeo mazuri kimsingi. Naomba vitabu viongezwe kwani hali ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wasioona katika Wilaya ya Mlele mmetenga vitabu 6014, vitendea kazi kwa wanafunzi wasioona ni vichache mno viongezwe ili kuleta motisha.Fedha zilizotolewa kama motisha kwa Halmashauri P4R, shilingi 78,777,349 Mpanda, Nsimbo shilingi 102,473,308 na Mlele shilingi 80,688,319. Bado kuna uhitaji mkubwa, mbona mikoa mingine mmepeleka kiasi kikubwa cha fedha? Je, mmetumia kigezo gani katika mgawanyo huu kama sio ubaguzi huu wa keki ya Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa vitabu vya sayansi na biology. Mkoa wa Katavi (mgawanyo Kiwilaya, Mpimbwe - 0, Mpanda - 0), nini kimetokea mpaka Wilaya za Katavi kukosa vitabu vya kidato cha tano na sita katika mchepuo wa sayansi? Hamuoni kwamba mnapunguza molari ya wanafunzi kusoma mchepuo ya sayansi vitabu? Kidato cha kwanza, jumla ya vitabu 6,030 Mkoa mzima na kidato cha tatu jumla ya vitabu 3,780. Ukiangalia wingi wa shule na uwiano wa vitabu hivyo inaonyesha kabisa hakuna dhamira ya dhati ya kusaidia ufaulu kwa wanafunzi wa sekondari zetu za Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za sekondari ya wanawake za Mpanda Girls na Milala sekodari. Shule hizi hazina wigo (fence) kwa ajili ya usalama wa wanafunzi hawa. Je, ni lini Serikali itatenga bajeti itakayotekelezeka ili kunusuru wanafunzi wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba majibu ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Katavi, ni lini utaanza na kama fedha zilitumika hovyo Serikali inawachukulia hatua gani wahusika? Vilevile naomba michango kwa wanafunzi ipunguzwe kwani ni changamoto kubwa kwa wazazi wenye hali duni kiuchumi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa kazi yake kuu ni kulinda usalama wa Taifa, wananchi na mipaka yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majukumu makubwa ya Wizara hii bajeti hii bado haitoshi ili tuendelee kuwa na amani na utulivu tulionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya mipaka na Jeshi, Jeshi likiwa imara na wananchi wanakuwa salama katika Taifa. Ni lini Serikali kupitia Wizara hii itatatua mgogoro uliopo katika Kata ya Misunkumilo Manispaa ya Mpanda na Jeshi kuchukua eneo ambalo wananchi wamejenga? Ni lini Serikali itatatua mgogoro huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi liliwakuta wananchi likaazima eneo hili, leo hii linadai eneo ni la Jeshi na wananchi wamekatazwa kujenga na kulima katika eneo hili.

Je, Serikali haioni kwamba Jeshi linataka kuwapora wananchi maeneo yao na mashamba, nani atawalipa fidia wananchi hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kiusalama kuweka vifaa vya usalama vya kijeshi karibu na makazi ya watu yaliyopo katika Kata ya Mpanda Hoteli, Misunkumilo, Milala na Makanyagio; je, hamuoni huku ni kuhatarisha usalama kama ulivyotokea mlipuko wa mabomu Mbagala? Naomba majibu kuhusiana na suluhisho hili ili wananchi waondokane na unyanyasaji huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wanajeshi kuboreshewa maslahi yao kama mshahara, pensheni na nyumba zao; kuchelewesha maslahi yao haya kunapelekea baadhi yao kujihusisha na matukio ya ujambazi na uhalifu katika Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya uhalifu wa watu kuuawa, mauaji ya Kibiti, nini tamko la Serikali ili kuondoa na kumaliza uhalifu huu unaofanywa na baadhi ya wastaafu wanajeshi ambao siyo waaminifu. Ni aibu kuona nguo/vazi la Jeshi kutumika katika matukio ya aibu, Watanzania wana imani na Jeshi hili lakini kwa baadhi ya matukio ya kijinga yanayofanywa na baadhi ya watu yanalichafua Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Paulo Makonda, alipoenda kuvamia Clouds Radio alikuwa na watu au wanajeshi wawili waliovaa vazi la Jeshi kwa hili lililotokea hamuoni kwamba imelichafua Jeshi hili, nini tamko la Wizara na Serikali ili kumwajibisha huyu Bashite katika tukio hili, hamuoni kwa Jeshi kukaa kimya linaonesha Jeshi linahusika kufanya haya matukio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi wa mipaka na wananchi katika maeneo yanayopakana na nchi jirani je, mkakati gani unatumika pamoja na kuwashirikisha wananchi elimu kwa raia namna ya kutoa taarifa kuhusu ulinzi na usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Jeshi hili lijikite zaidi katika kulinda usalama wa Taifa na lisitumiwe na watu wenye nia mbaya kwa raia. Maonyesho ya makomando hadharani hamuoni kwamba inawapa mwanya watu waovu kujua ubora na udhaifu wa Jeshi letu. Mazoezi ya Jeshi hadharani yenye tija na sio ya kutisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho Jeshi la Kujenga Taifa lisitumike vibaya na utawala wa CCM kwa maslahi ya Chama Tawala, bali Jeshi hili liangalie maslahi mapana ya Taifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ubadhirifu wa shamba zaidi ya heka 1000 kwa ajili ya uwekezaji katika Kata ya Kakese, Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi. Shamba hili la kulima mpunga lipo katika Kata ya Kakese, Kijiji cha Mbungani na linamilikiwa na Charles Dofu na Lucas Busanda. Lilimilikiwa 1985, mwaka 1987 walianza kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kuchukua eneo hili ilikuwa ni kwa ajili ya uwekezaji ambapo awali lilikuwa la wananchi. Wawekezaji hawa wanachukua mikopo benki na kuilipa kwa kuwachangisha wananchi, wanajipatia fedha kwa kupitia kundi kubwa la zaidi ya wananchi 5000.

Mheshimiwa Naibu Spika, je ni kwa nini Serikali imemuacha mwekezaji huyu fake kuendelea kuwalaghai wananchi na kujipatia mikopo mikubwa ikiwepo NBC na wanaposhindwa kulipa mkopo wanataka wananchi walipe mkopo huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanalipishwa gharama kubwa wanapokodi mashamba. Kwa heka wanakodishwa kwa zaidi ya Sh.500,000/= kwa sababu ni eneo lenye udongo mzuri. Wananchi wanapiga kelele shamba lirudi kwa wananchi na Serikali ya Kijiji ili walime kwa bei ya chini na hivyo wajikwamue kiuchumi. Wananchi hawa wanatishia kuchoma moto shamba hili ambalo lina zaidi ya wakazi 8000. Hatua ya dharura inahitajika kuchukuliwa ili kuvunja Mkataba wa kujipatia maeneo kupitia kuwalaghai wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanataka kuandamana mpaka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri husika; kuna hali ya tafrani katika eneo hili. Ili kunusuru vurugu zisitokee naomba Serikali itatue huu mgogoro mkubwa katika Kata hii ya Kakese. Serikali imekuwa ikitatua kero nyingi katika nchi hii kwa maslahi ya Taifa na amani; mimi nimewazuia wananchi kuja Dodoma kwa maandamano nikiamini kwamba Serikali italifanyia kazi tatizo hili kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walifunguliwa kesi na hawa wamiliki wakatumia rushwa kuhonga polisi. Wananchi wakapigwa ili kuondoka ilihali lilipatikana kutoka kwa wananchi. Je hamuoni kwamba Serikali inaibiwa kupitia wawekezaji hawa wahuni kwa umma? Tunahitaji majibu kuhusu shamba hili; lirudi kwa wananchi, hali ni mbaya, ni mwizi huyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niipongeze hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kutoa mwelekeo wa bajeti mbadala kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya CCM haina mapenzi mema na wananchi wake katika kuwasaidia vijana kupata ajira kupitia viwanda vidogo vidogo. Tuna wimbi kubwa la vijana waliokosa kazi vijijini kwa takwimu hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Uanzishwaji wa Mradi wa Viwanda Vidogo Vidogo Vijijini 2016/2017. Serikali imeanzisha viwanda vipya 161 vidogo vijijini Tanzania nzima na kufanikiwa kuajiri vijana 1,098. Ajira hizi ni chache ukizingatia vijana wengi wako vijijini na hawana elimu. Tulitegemea vijana hawa wangewekewa mkakati wa kuwapatia ajira na si kuwadidimiza kiuchumi vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuboresha mazingira ya uwekezaji ni jukumu la Serikali ili kuhakikisha sheria kanuni na utendaji wa sekta ya umma unakuwa rafiki kwa wawekezaji ili kutoa ajira, kuwalipa vijana kwa wakati, kuacha unyanyasaji kwa vijana wanaofanya kazi migodini katika Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa Isulamilomo (Nsimbo Katavi), kuna mwekezaji mchimbaji yuko pale na hana leseni; amepora eneo kubwa na vijana wamebaki hawana maeneo. Huyu bwana (Mbogo) Simon Mdandila anazua tafrani na uvunjifu wa amani kwa kuwanyima fursa vijana kupitia kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana zaidi ya 450 wanashindwa kuchimba katika maeneo yao kwa rushwa iliyofanywa na huyu bwana Mbogo. Je Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inawazuia wawekezaji wa aina hii wanaotumia rushwa kuhodhi maeneo katika eneo la uchimbaji na huku vijana wakihangaika kupata ajira? Uwekezaji huu wa aina hii wenye lengo la kuwatesa wananchi pamoja na hali ngumu waliyo nayo usimamiwe ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ubadhirifu wa Kiwanda cha Kukoboa na Kusaga. Mashine hii ilinunuliwa na Halmashauri ikayeyuka, ilikuwa na thamani ya milioni mia moja lakini leo hii wananchi wakihoji hawapati majibu ya wizi huu wa wazi kabisa. Je Serikali hii kwa kuendelea kuwalea wezi wanaokula fedha za viwanda vya uwekezaji katika Manispaa ya Mpanda kwa kutochukua hatua yoyote hamuoni kwamba mnapoteza fursa za vijana kwa kuwalea wabadhirifu hawa bila kuwachukulia hatua?

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa viwanda uendane sambamba na ukuaji wa sekta ya nishati na umeme. Je ni mkakati gani wa haraka wa kuuhakikishia uchumi wa viwanda upatikanaji wa umeme unaoenda sambamba na mazingira ya uwekezaji sawia nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM bado haijajipanga pia kujiendeleza kiuchumi kupitia viwanda. Bajeti yenye asilimia 0.36 ya pato hili, je, Wizara hii imejipanga kweli kuwasaidia wananchi au utani?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa sababu imeonesha namna gani ya kuboresha na kutatua kero zilizopo katika Wizara hii hususan wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji ni migogoro inayosababishwa na Serikali kwa wafugaji. Naomba Serikali itatue kero na mapigano yanayoendelea katika makundi haya mawili. Serikali ina uwezo kabisa wa kutatua migogoro hii? Nini kifanyike? Serikali itenge maeneo maalum kwa wafugaji na wawe wanalipia maeneo hayo. Wakulima wapewe maeneo rasmi ili kuondoa vita hii kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isifanye siasa na makundi haya mawili. Tutabaki na Tanzania ambayo ni jangwa, wakati huo huo njaa kwa sababu kila eneo wakulima/wafugaji watafanya shughuli zao bila kujali utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Serikali isifanye siasa kwa kuongea tu bila utekelezaji. Ihakiki maeneo ili wafugaji wasiingilie mashamba na kuharibu mazao ya wakulima lakini pia wakulima nao Serikali ikipanga eneo la malisho basi wakulima wasilime kila eneo ili kutatua hii migogoro ya mapigano na vita kati ya makundi mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi – Wilaya ya Tanganyika na Mlele ni moja ya maeneo yaliyopita katika migogoro mingi na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Operation tokomeza ujangili, operation kuondoa wavamizi wa maeneo ya wakulima na wafugaji. Kata ya Kabage Wilaya ya Tanganyika, Mwampuli, Chemalendi, Mgimoto, wafugaji waliondolewa na Serikali kwa kupigwa, akinamama kubakwa na Askari wa Wanyamapori, wakaibiwa pesa zao, kuibiwa mali zao madukani. Je, hili lilikuwa lengo la Serikali kuwanyanyasa wananchi katika Kata ya Isengule, maeneo ya Lyamgoloka kuchomewa nyumba na Askari hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Serikali haijawahi kuwafidia wananchi waliokumbwa na kadhia hii. Walipwe fidia, Askari waliohusika kufanya vitendo hivi wapo na wanatembea kifua mbele huku wafugaji wakifilisika katika Taifa lao. Wananchi wakielezwa mipaka yao nadhani migogoro itapungua kuhusu utunzaji mazingira, kuhusu mipaka yao katika kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vya wafugaji, wafugaji wanapigwa risasi, ng’ombe wanaibiwa na hawa Askari. Je, Serikali ina lengo la kuwamaliza wafugaji, kwani ni dhambi mtu kuwa na mifugo mingi, Serikali iweke mkakati wa viwanda ili kupunguza migogoro hii wafugaji, visindike nyama na masoko yapatikane wananchi/wafugaji wakipata faida katika masoko kelele zitapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katavi na Vyama vya Ushirika. Katika hotuba hii nimeona Katavi kuna vyama vya msingi vya ushirika 14, wakati Mikoa mingine viko zaidi ya elfu moja. Je, hamuoni Katavi hamuwatendei haki? Katika vyama vya msingi ushirika vilivyopo pia kuna wizi wa waziwazi kwa wakulima wa tumbaku, zaidi ya milioni 600 zimeliwa na Viongozi Nsimbo- Katavi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa sababu imeonesha namna gani ya kuboresha na kutatua kero zilizopo katika Wizara hii hususan wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji ni migogoro inayosababishwa na Serikali kwa wafugaji. Naomba Serikali itatue kero na mapigano yanayoendelea katika makundi haya mawili. Serikali ina uwezo kabisa wa kutatua migogoro hii? Nini kifanyike? Serikali itenge maeneo maalum kwa wafugaji na wawe wanalipia maeneo hayo. Wakulima wapewe maeneo rasmi ili kuondoa vita hii kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isifanye siasa na makundi haya mawili. Tutabaki na Tanzania ambayo ni jangwa, wakati huo huo njaa kwa sababu kila eneo wakulima/wafugaji watafanya shughuli zao bila kujali utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Serikali isifanye siasa kwa kuongea tu bila utekelezaji. Ihakiki maeneo ili wafugaji wasiingilie mashamba na kuharibu mazao ya wakulima lakini pia wakulima nao Serikali ikipanga eneo la malisho basi wakulima wasilime kila eneo ili kutatua hii migogoro ya mapigano na vita kati ya makundi mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi – Wilaya ya Tanganyika na Mlele ni moja ya maeneo yaliyopita katika migogoro mingi na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Operation tokomeza ujangili, operation kuondoa wavamizi wa maeneo ya wakulima na wafugaji. Kata ya Kabage Wilaya ya Tanganyika, Mwampuli, Chemalendi, Mgimoto, wafugaji waliondolewa na Serikali kwa kupigwa, akinamama kubakwa na Askari wa Wanyamapori, wakaibiwa pesa zao, kuibiwa mali zao madukani. Je, hili lilikuwa lengo la Serikali kuwanyanyasa wananchi katika Kata ya Isengule, maeneo ya Lyamgoloka kuchomewa nyumba na Askari hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Serikali haijawahi kuwafidia wananchi waliokumbwa na kadhia hii. Walipwe fidia, Askari waliohusika kufanya vitendo hivi wapo na wanatembea kifua mbele huku wafugaji wakifilisika katika Taifa lao. Wananchi wakielezwa mipaka yao nadhani migogoro itapungua kuhusu utunzaji mazingira, kuhusu mipaka yao katika kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vya wafugaji, wafugaji wanapigwa risasi, ng’ombe wanaibiwa na hawa Askari. Je, Serikali ina lengo la kuwamaliza wafugaji, kwani ni dhambi mtu kuwa na mifugo mingi, Serikali iweke mkakati wa viwanda ili kupunguza migogoro hii wafugaji, visindike nyama na masoko yapatikane wananchi/wafugaji wakipata faida katika masoko kelele zitapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katavi na Vyama vya Ushirika. Katika hotuba hii nimeona Katavi kuna vyama vya msingi vya ushirika 14, wakati Mikoa mingine viko zaidi ya elfu moja. Je, hamuoni Katavi hamuwatendei haki? Katika vyama vya msingi ushirika vilivyopo pia kuna wizi wa waziwazi kwa wakulima wa tumbaku, zaidi ya milioni 600 zimeliwa na Viongozi Nsimbo- Katavi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maji ni uhai na kichocheo kikuu cha uchumi wa Taifa. Watu wanapokosa maji safi na salama ni tatizo katika Taifa. Wanafunzi wanapokosa maji kwa wakati wanaathirika kwa uchafu katika mazingira yao na husababisha kufeli kwa sababu katika mabweni wanafuata maji mbali sana. Kata ya Misunkumilo wanafunzi wa Mpanda Girls wanapokosa maji wanasafiri karibuni kilometa tano kufuata maji katika shule ya Milala Sekondari au Bwawani, usalama mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji kuchelewa kwisha. Hili ni tatizo kabisa. Miradi Katavi inachukua muda mrefu kwisha, je, ni utaratibu gani unatumika ili kuokoa hela hizi za wananchi na huku miradi inaharibika? Kwa mfano, Mradi wa Maji Kata ya Mwamapuli Wilaya ya Mlele – Katavi na Mradi wa Maji na Umwagiliaji Kata ya Ugala.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha namna gani Serikali haikujipanga katika miradi hii, mmetumia pesa nyingi lakini mpaka sasa miradi haifanyi kazi. Je, ni lini mtakamilisha miradi hii kwa wakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Ikonongo katika Manispaa ya Mpanda; ni lini mradi huu utakamilika? Wizara waache maneno mengi waseme ni lini watakamilisha mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu UDOM. Mfumo wa maji taka na mabweni uko karibu lakini pia mradi huu umekwama, mabweni hayapati maji wakati Serikali imewekeza pesa nyingi sana. Je, nini mkakati wa dharura kukinusuru Chuo Kikuu UDOM?

Mheshimiwa Naibu Spika, Ufisadi katika Miradi ya Maji; kwa kuendelea kuona miradi ikisimama na bado wananchi hawapati maji na wananchi kukosa majibu ya maswali yao kuhusu ukosefu wa maji inaonesha ni namna gani hawa wakandarasi wameamua kuwatesa wananchi. Serikali itoe majibu ili wananchi wajue mbaya wao ni nani kati ya Serikali au mkandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vyanzo vya Maji Kuharibiwa Vizibo. Naishukuru Serikali kwa kuchukua hatua ya kuvunja vizibo ambavyo havijafuata utaratibu wa kupata leseni na kufuata utaalam katika ujenzi katika Mkoa wa Katavi. Sasa nini kifanyike? Kuvunja vizibo hivi kusiwe na ubaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ni Ndogo, iongezwe. Uhitaji wa maji ni muhimu kuliko kitu chochote. Ukosefu wa maji safi na salama umeleta usumbufu, magonjwa na vifo kwa watoto wachanga kuharisha kwa kunywa maji machafu, homa ya matumbo, kuugua typhoid na kufariki kwa rasilimali watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, nini hatua ya dharura Wizara ikishirikiana na mamlaka husika za maji katika mikoa ili kunusuru maisha ya Watanzania huku mkishirikiana na Wizara ya Afya ili tuondoe kero hii kwa wananchi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Upotevu wa Mapato ya Serikali: Waziri wa Fedha akichukua mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naamini tutapiga hatua. Upotevu wa mapato ya Serikali upo wa kutosha katika vyanzo vyetu. Mfumo wa machine za EFD lengo lake ni zuri kabisa lakini bado kuna upotevu mkubwa japo machine hizo chache zilizopo pia baadhi ya wafanyabiashara huidanganya Serikali. Ni lini mtaongeza machine za EFD kila Wilaya nchini ziwepo za kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha inasimamia wafanyabiashara ambao wanafanya udanganyifu katika biashara zao? Unakuta mfanyabiashara tayari ana risiti za bidhaa ambazo zinakuwa na bei ya chini. Je, kupitia hili ni wafanyabiashara wangapi wanakwepa kuandika katika machine bei ya halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukadiriaji wa kodi kwa wafanyabiashara ni kero na jambo hili linafanyika siyo kwa maslahi ya kuwasaidia wananchi, bali inawaumiza. Unawezaje kumlipisha kodi mfanyabiashara kabla ya biashara yake haijasimama? Je, hamwoni kuwa ule mkakati wa kupunguza umaskini kupitia kupungua makato makali ya kodi umefeli? Je, mpango wa kupunguza umaskini umefeli? Shilingi milioni 50 kila kijiji nadhani sasa ni muda muafaka wananchi wapewe fedha walizowaahidi katika Ilani ya CCM, watekeleze ili Watanzania wapate ahueni ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya Taasisi za Fedha zimekuwa zinakwepa kodi na kumekuwa na ufinyu wa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika Taasisi za Serikali; TBI, TANAPA, TANESCO, DAWASCO: Je, nani anafuatilia hili na kutoa taarifa kwamba matumizi ni sawa na kinachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwenye Taasisi zisizo za Serikali baadhi zimekuwa zikipunguza gharama, hivyo hazisemi ukweli na hivyo Serikali inashindwa kupata kodi ambazo ni halisi. Nini mkakati kuelekea Bajeti Kuu ili kusimamia taasisi hizi ili zilipe kodi halali na siyo kuiibia Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Jamii ya PSPF na NSSF ilikuwa na lengo zuri sana lakini katika kuwasaidia watumishi na wastaafu, changamoto ni moja kubwa katika mifuko hii ya jamii. Unakuta mtumishi amestaafu na anaishi mkoani na ni kijijini; ili apate mafao yake inampasa afuatilie mafao yake na inamlazimu kufika Makao Makuu na ukizingatia mifuko hii mingi iko mikoani. Kupitia bajeti hii, huu usumbufu utakwisha lini ili wananchi wapate huduma hizi kwa wakati, lakini pia wasisafiri umbali mrefu kufuata haki zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu ubadhirifu wa mapato na matumizi katika Halmashauri (Mpanda). Kulikuwa na ununuzi wa gari la taka zaidi ya shilingi milioni 100, gari halipo;Kumekuwa na ununuzi wa mashine ya kusaga na kukoboa zaidi ya shilingi milioni 90, haipo; vile vile kuna matumizi mabaya ya ardhi nje ya makubaliano na mikataba (shamba la Benki NBC – Kakese (Mpanda).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la ajira za nje na ushirikiano wa kimataifa kwa Afrika na Afrika Mashariki ni kubwa nchini lakini kuna tatizo katika ushirikiano huu, nafasi za ajira zimekuwa zinatangazwa muda mwingine kwa kufichwa, wananchi wanakuja kushtuka watoto wa wakubwa ndiyo wameajiriwa kimataifa huku watoto wa maskini hawapati fursa hizi. Je, kupitia tatizo hili ni ubaguzi huu kati ya watoto wa maskini na matajiri, Serikali imejipanga vipi kuondoa ubaguzi na urasimu wa ajira za kimataifa? Usawa uko wapi, ni lini watoto wa maskini watafarijika katika Taifa lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uchakavu wa Balozi Nje ya nchi, Balozi zina hali mbaya, tunapoteza fursa za uwekezaji, Balozi zinadaiwa mapango ya nyumba za ofisi na nyumba za watumishi ziko hovyo. Kwa bajeti hii moja kwa moja haioneshi kwamba inaweza kumaliza changamoto hizi katika Balozi zetu za Zimbabwe, Mozambique, Botswana na South Africa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa Serikali kusaidia wanafunzi waliopo masomoni katika nchi korofi, hivi karibuni yamejitokeza matatizo kwa wanafunzi wanaosoma nchi za nje, huko waliko kuna ubaguzi, vita, mitafaruku na wafanyakazi wa ndani kuuwawa nchi za nje, kutokana na matatizo hayo Serikali hii ya CCM haijawahi kusaidia moja kwa moja. Mfano tatizo la unyanyasaji na usafirishaji wa wafanyakazi wa ndani nchi za nje. Je, nini mkakati wa Serikali kupitia bajeti hii ihakikishe inasimamia waajiri wanaonyanyasa Watanzania wenzetu inaonekana nchi haiko katika mstari wa kusaidia/kuondoa tatizo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali/utawala huu utaacha ukandamizaji wa demokrasia nchini ili sasa hawa wawekezaji na ushirikiano wa nchi jirani na nchi za Ulaya ili waone kwamba kama watawekeza basi watakuwa katika nchi salama, lakini kadri siku zinavyoenda wawekezaji wanapungua? Je, hamuoni kuwa tunapoteza uchumi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mikakati mingi mizuri ya Wizara ya Ardhi, bado kuna changamoto nyingi katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii ungewekwa mkakati wa dharura wa kuhakikisha inawapimia mapema kabla hawajajenga wawe na hati ili kuondoa migogoro ya fidia kupunjwa na kunyanyasa wanaopisha ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi Manispaa ya Mpanda; Kata nyingi za Manispaa ya Mpanda hawajapimiwa je, ni lini sasa Wizara kupitia Ofisi za Kanda itaharakisha kupima maeneo haya ili wananchi wapate hati ambazo zinaweza kuwasaidia kukopa fedha katika benki. Kata ya Ilembo, Misunkumilo, Kata ya Kakese, Kata ya Mwamkulu na Kata ya Kashamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara isisubiri watu wajenge nyumba zao nzuri halafu inakuja kubomoa na kuwalipa fidia ndogo na za kucheleweshwa. Katika Bajeti hii Mheshimiwa Waziri ameonesha wazi kuwa na dhamira ya kutatua kero ya fidia kwa kuanzisha Bodi ya Fidia hii ikasimamiwa vizuri itasaidia vizuri na kuondoa kero za malalamiko nchini, hii nadhani ipangiwe mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi na wananchi wa Kata za Mpanda hotel na Misunkumilo; naomba bajeti hii ione namna ya kutatua mgogoro huu ni wa muda mrefu sana .

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupunguza gharama za uuzaji nyumba za NHC Manispaa ya Mpanda; mpaka sasa hakuna faida iliyopatikana kutokana na uuzaji wa nyumba hizi, je hamwoni kuendelea kuziacha nyumba, kama gharama haziwezi kupungua basi zipangishwe kwa watumishi wa Serikali kwa sababu kuna uhaba wa nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu katika nyumba hizo bado haitoshi, barabara, hospitali, shule, masoko. Hivyo kwa kuzingatia ukosefu wa miundombinu hii ndio inasababisha watu kushindwa kuhamia kule.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kutolipa madeni kwa wakati katika Mashirika ya Umma. Ukipitia Taarifa ya CAG kwa ujumla katika maeneo mengi CAG ameshindwa kutembelea baadhi ya maeneo kwa sababu ya ukosefu wa pesa katika Ofisi yake. Ninaomba Serikali ilipe madeni ili tupate taarifa za kimahesabu kutoka katika Ofisi ya Ukaguzi na Serikali ijikite kulipa madeni ili tuendeshe kazi za wananchi waliowalipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipe madeni ya DAWASCO, Jeshi, TANESCO na maeneo mengine ambayo Serikali hii imeshindwa kuyalipa kwa wakati na kusababisha taasisi za Serikali kushindwa kujiendesha zenyewe na matokeo yake taasisi hizi zimekuwa zikijiendesha kwa hasara na mikopo pia. Ni kwa nini Serikali inashindwa kulipa madeni hayo kwa wakati na huku mwananchi wa kawaida, mfano anadaiwa na Idara ya Maji 5,000/= tu anakatiwa maji. Je, hamuoni kwamba, Serikali inashinwa kujisimamia yenyewe kupitia taasisi zake? Ni lini sasa Serikali itaanza kulipa madeni haya makubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Katika mfumo wa manunuzi nimeangalia mambo makuu mawili ambayo kwa upana wake Serikali iangalie namna ya kuboresha au kurekebisha sheria. Sheria hizi za manunuzi zinasababisha mchakato wa manunuzi kununua mali za Serikali kuchukua muda mrefu, mchakato wa kutangaza tenda unakuwa mrefu sana, lengo ni kupata (Supplier) mwenye vigezo, lakini Serikali ione namna ya kuziangalia sheria hizi kimfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya muda; Miradi kusimama kwa sababu tu vifaa vimechelewa kutokana na manunuzi kuchukua muda mrefu. Changamoto ya gharama, masuala ya manunuzi yanasababisha pia, Serikali kununua bidhaa kwa gharama kubwa na kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu wamekuwa wakipata 10 percent na huku wakiibia Serikali kupitia mfumo huu wa manunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziara za Ukaguzi wa CAG na Bunge. Kwa ujumla malalamiko yaliyopo ni CAG kushindwa kufanya ukaguzi katika baadhi ya maeneo nchini na Bunge kupitia Kamati zake pia, zimeshindwa kukagua miradi. Dhamira ya uwazi wa pesa ya umma iko wapi? Au Serikali inafanya maksudi kunyima ofisi ya CAG pesa?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wachimbaji wadogo wadogo; taarifa ya Kamati, imejikita na kuonesha faida na hasara zilizojitokeza wakati pesa za ruzuku zinatolewa kwa hawa vijana na vikundi vyao. Bado naona kuna haja ya Serikali kuhakikisha inazisimamia pesa hizi za ruzuku kwa wanufaika wa ruzuku hizi na kuwapa semina za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano tu Mkoa wa Katavi leo baadhi ya vijana (vikundi vya wachimbaji wadogo wadogo) katika machimbo ya Isula, Milomo, Kapanda, Ibindi, Mtisi, Kampuni na Stalika, vijana hawa hawajapata mafunzo na hivyo mikopo au ruzuku chache zilizopatikana walizitumia kwa matumizi yao binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchache wa pesa ya ruzuku kwa wachimbaji wadogo wadogo, Kamati imeshauri iongezwe kwa usimamizi maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira na manyanyaso kwa vibarua wa wachimbaji wadogo wadogo; hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana bila waajiri wao kuwapatia vitendea kazi vyenye usalama katika mazingira magumu. Je, Serikali ina wachukulia hatua gani wachimbaji hawa wanaoajiri hawa vibarua hususan katika machimbo ya Ibindi, Kapanda, Mtisi na maeneo mengine kama Isulamilomo?

Mheshimiwa Naibu Spika, vibarua hawa wananyanyaswa na kunyimwa mishahara yao na wakihoji kuhusu maslahi yao wanafukuzwa kazi kwa sababu wamehoji. Je, Serikali hii ya CCM imeshindwa kusimamia unyanyasaji huu kwa vibarua wa wachimbaji wadogo wadogo?

Mheshimiwa Naibu Spika, uchache wa utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo wadogo, usumbufu wanaopata wachimbaji hawa wanapofuatilia leseni zao kuna urasimu mkubwa sana kupitia Maafisa Madini wa Wilaya na Mikoa pamoja na Kamishna wa Kanda wa Madini, ni kwa nini leseni hizi zinatolewa kwa usumbufu mkubwa na kusababisha wachimbaji hawa kushindwa kufanya kazi zao na kupelekea kuporwa machimbo yao kumbe wanacheleweshwa ili wanyang’anywe machimbo yao. Je, Serikali hamwoni kwamba jambo hili linakwamisha uchumi, nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inaongeza watumishi wa madini ili kuondoa usumbufu huu wa gharama wachimbaji kusafiri kutoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine, mkoa kwa mkoa, kufuatilia leseni zao. Maoni ya Kamati yazingatiwe pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme wa REA Vijijini, changamoto za umeme vijijini ni kubwa na kama Kamati ilivyoshauri Serikali ihakikishe inasimamia uwekaji wa umeme katika vijiji vyenye vipaumbele si kubagua vijiji na kuviruka baadhi ya vijiji hili jambo si sawa. Serikali iliangalie jambo hili kwa sababu upatikanaji wa umeme vizuri unapelekea uchumi kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa umeme katika Mikoa na Miji mfano, Dar es Salaam; mpaka sasa umeme Mkoa wa Dar es Salaam bado ni tatizo na Mikoa mingine kama Katavi, Mbeya na Rukwa bado tatizo ni kubwa. Je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha Taifa linapata umeme wa uhakika, maji ya kutosha halafu ndio mjipange kwa ajili ya mabadiliko ya uchumi wa viwanda, Je, Serikali haioni kuwa mnafanya kiini macho kuelekea uchumi wa viwanda?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu umuhimu wa Sekta ya Kilimo ambapo zaidi asilimia 57 ya wananchi wa Tanzania wanalima na kufuga na pia katika suala la ukuaji wa uchumi kwa mazao ya biashara na chakula, mfano zao la korosho ambalo leo Tanzania ni wanufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wa kilimo katika Taifa hili kwa zaidi ya asilimia 28 katika pato la Taifa, lakini leo wakulima bado hawapati faida na mazao yao na hivyo wanufaika wakubwa wamekuwa wafanyabiashara wa mazao zaidi ya wakulima maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaweka mifumo mizuri ili wakulima nao wafaidike na mazao yao nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Serikali kusambaza mbolea mikoani, lakini bado imeshindwa kwa asilimia kubwa kusambaza kwa wakati. Kwanza mbolea inasambazwa kwa kuchelewa na ikifika, wakulima wanapata mbolea wakati tayari kipindi cha kuweka mbolea kwenye mazao kimepita? Je, Serikali haioni kwamba kila mwaka inashindwa kusambaza mbolea? Nini mkakati wa kusaidia jambo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mbolea zinafika chache kwa wakulima. Tatu, bei ya mbolea ni kubwa sana, wananchi maskini ambao ni wakulima wa mikoani (vijijini) wanashindwa kununua mbolea hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, natumizi na elimu kuhusu mbolea hizi zinazotolewa, lakini ni lini wakulima watapatiwa elimu ya kutosha ili wapate mazao mengi na faida? Lingine ni mfumo wa ugawaji mbolea, pia una urasimu mkubwa; lini utakwisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa iliyopakana na nchi jirani kuna hili tatizo la mbolea fake. Mfano Mikoa ya Mbeya, Katavi na Kigoma. Ni lini Serikali itasimamia mbolea fake inayopita mipakani ili kusaidia wakulima ambao wengi wao wananunua mbolea fake hizi ambazo ni bei rahisi? Nini Tamko la Serikali katika jambo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi Jimbo la Nsimbo, Mpanda Mjini na Tanganyika ni maeneo ambayo tumbaku inalimwa, lakini bei ya tumbaku kwa wakulima hawa ni ya dhuluma. Walanguzi wamekuwa wakipanga bei wao na kuacha wakulima maskini hawapati faida. Nini tamko la Serikali kuhusiana na wizi huu wa bei ya zao la tumbaku unaofanywa na walanguzi wasio waaminifu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini; ni kwa nini Serikali inashindwa kutenga maeneo ya malisho nchini ili kupunguza kesi katika Mahakama kwa migogoro hii mikubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia maoni ya ushauri wa Kamati, nashauri Serikali itenge maeneo ya malisho ili kuondoa malalamiko ya wafugaji; ng’ombe zao kupigwa risasi zikiingia kimakosa hifadhini, mfano, Kata ya Majimoto, Luhafwe na Ikuba. Je, ni kwa nini Askari wa Wanyamapori wanapiga risasi ng’ombe kwa maelekezo ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya? Ni lini Serikali itaacha uonevu huu kwa kushindwa kutatua matatizo haya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ziwa Tanganyika zoezi la kudhibiti uvuvi haramu katika ziwa hili, limesababisha uonevu mkubwa kwa wananchi. Ni kwa nini hamwoni haja ya Serikali kuwapatia nyavu zenye bei rahisi kwa mikopo katika vikundi vyao na kuwasimamia ili kudhibiti uvuvi haramu na siyo kufanya zoezi la kudhibiti uvuvi haramu huku wavuvi hawajiwezi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo hakiwezi kutegemea mvua tu. Naomba Serikali ipitie bajeti yake kwa upya na kuhakikisha inaharakisha kumaliza miradi ya maji kwa muda muafaka. Vile vile nashauri Serikali iendelee kutekeleza miradi hii kwani Serikali inapata hasara na wakulima hawapati faida.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na mapitio ya hoja za Kamati za Sheria Ndogo zinazopitishwa na Halmashauri zetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko changamoto chache ambazo kimsingi zinasumbua walipa kodi na kupitia TAMISEMI, kwanza ni ushuru wa maegesho za Halmashauri ya Mji lengo ni kutoza faini kwa maegesho holela na wamiliki wa vyombo vya moto wamekuwa wakitozwa faini hizo shilingi 50,000 na mmiliki akishindwa kulipa anapelekwa mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faini hizi kupitia sheria hizi ndogo usimamizi wa pesa hizi TAMISEMI (kupitia Wizara ya Katiba na Sheria). Je, Serikali haioni kuwa sheria hii ni kandamizi kwa sababu Halmashauri nyingi hazijatenga maeneo ya kutosha ya maegesho hayo hususani mijini? Na je, wananchi wana uelewa kiasi gani kuhusu faini hizi na je, hamuoni kwamba ni Serikali yenyewe ilitakiwa itengeneze mazingira ya maegesho makubwa ili uonevu huu usiendelee?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zilizopitishwa na Halmashauri zetu kupitia makanyagio ya ng’ombe katika minada yetu nchini ushuru huu kwa wafugaji unawakandamiza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfugaji anasafiri kutoka Tarafa moja kwenda nyingine umbali wa kilometa 40 mfano kutoka Karema mpaka Mpanda Ndogo mfugaji anaende mnadani, anapoingia getini analipa ushuru auze/asiuze analipa ushuru na ng’ombe wanaposafirishwa kutoka katika minada katika mageti wanalipa tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii haiko sawasawa maana kuna ushuru mwingi kwa wafugaji na inawaumiza wafugaji. Serikali ilione hili ili angalau wafugaji hawa wawekewe mfumo wa kulipia mifugo yao kwa mara moja na sio ushuru wenye usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushuru wa kutupa taka, sheria mama na sheria ndogo zote zinalenga kuisaidia jamii kuzifuata sheria hizi kupitia mamlaka zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nasisitiza kupitia sheria hii ni nzuri kwa maana ya kutunza mazingira kwa katika hali ya usafi. Je, Serikali imeweka mazingira gani kabla ya kutunga sheria hizi? Serikali ione haja ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha na kupatiwa vifaa vya usafi halafu utekelezaji wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia sheria hizi ndogo Serikali iangalie upya mazingira ya afya kwa shule za msingi ambazo hazijakidhi vigezo. Mfano sheria inasemaje kwa shule za msingi ambazo watoto wanatumia tundu moja la choo na ni shule za msingi za Serikali, ni kwa nini mazingira haya magumu yako wazi Halmashauri ipo? Sheria inasemaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwazi wa sheria na semina kwa Madiwani katika Halmashauri nchini, kwa kuwa Madiwani wengi hawana elimu ya kisheria na wao ndio watunga sheria katika Manispaa na hivyo kupitia kukosa weledi wa kisheria inapelekea Madiwani kutunga sheria kandamizi. Je, Serikali inasimamia vipi kuhusu semina kwa Madiwani wetu kuhusu masuala ya sheria?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE.RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi ambazo Serikali inafanya kuhakikisha inapunguza magonjwa yanayoambatana na Ugonjwa wa UKIMWI kama TB na Magonjwa ya Zinaa, pamoja na majukwaa maalum ya Elimu zinazofanyika, bado maambukizi katika jamii yapo hususani katika eneo la vijana linaloambatana na matumizi ya madawa ya kulevya, je Serikali, haioni iko haja ya kuhakikisha vijana wanapata ajira ili kupunguza tatizo hili la chakula/lishe na UKIMWI.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkakati wa Serikali katika eneo hili pamoja na kuhakikisha jamii inapata aina ya vyakula vinakua na lishe, hivyo iko haja ya Serikali kuhakikisha mfumo wa viwanda hivi tunavyovijenga sasa pia vizingatie suala la kutengeneza nafaka zenye lishe bora na pia kuna wagonjwa Watanzania maskini wanatumia dawa hizi wanashindwa kupata vyakula vyenye lishe bora ili kuwasaidia kupata afya wanapokua wanatumia dawa hizi za kupunguza makali ya UKIMWI. Je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha inawapatia vyakula vyenye lishe bora waathirika hawa maskini pindi wanapofika katika dirisha la dawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukatili na Unyanyasaji wa Jinsia kwa Waathirika; kwa kuzingatia maoni ya Kamati, naomba Serikali iweke mkazo mkubwa kupitia madawati haya ya unyanyasaji wa kijinsia kutatua kero hii, kesi hizi zimekuwa zikichukua muda mrefu na hivyo kupelekea vitendo hivi kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la ajira limekua kiini kikubwa cha tatizo la baadhi ya mikoa kuendelea kusambaa kwa magonjwa haya hususani Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Morogoro, mikoa ambayo kuna wimbi kubwa la starehe na biashara ya Madawa ya Kulevya imeshamiri na pia wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao inaendelea. Hii yote inatokana na ukosefu wa ajira zisizoeleweka. Je, Serikali haioni kwamba ukosefu huu wa Ajira unapelekea maambukizi ya UKIMWI na matumizi ya Madawa ya Kulevya kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU; baadhi ya maeneo vijijini bado ni changamoto hususani waathirika wanaotoka vijijini na hii hupelekea mgonjwa kushindwa kufika hospitali kufuata dawa na hivyo Serikali ione haja ya kuongeza madirisha ya ugawaji dawa. Serikali kusimamia Halmashauri kupitia fedha zinazotengwa kwa ajili ya UKIMWI.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi Halmashauri hazitumii pesa hizi kwa mlengwa kuisaidia jamii hii, hivyo Serikali ione haja ya kusimamia katika Halmashauri hizi ili pesa zifike kwa walengwa, kupitia elimu kuhusu masuala ya UKIMWI, Warsha, makongamano na misaada kwa walengwa isiishie tu kulipanalipana posho huku wahusika haziwafikii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Magereza/ Mahabusu, mfano wa Gereza la Kalila, Nkulunkulu na Mahabusu zilizopo katika Manispaa ya Mpanda hali ni mbaya. Hii sio Mkoa wa Katavi pekee bali ni katika Magereza mbali mbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mlundikano wa wafungwa unapelekea utoaji wa huduma za afya bora kushindwa na wanazidiwa uwezo kuna wafungwa na mahabusu 39,312 na uwezo wa magereza ni kuhifadhi mahabusu 29,552. Je, Serikali ina mkakati gani kutatua changamoto hii katika Taifa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ya mwanamke na uchumi; kwa kuzingatia maoni ya Kamati mazuri yakifanyiwa kazi katika nyanja mbalimbali nadhani kutamsaidia mwanamke ambaye kimsingi anabeba majukumu makubwa na magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekua ikitenga fedha kwa ajili ya mikopo kwa wanawake yenye riba nafuu kupitia Halmashauri na Taasisi za kifedha, je, Serikali haioni kupita mikopo hii kuwa haiwasaidii wanawake maskini na badala yake wanaonufaika ni wale wanaojiweza kiuchumi, Serikali inaondoaje ubaguzi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa watumishi wa afya nchini; Mkoa wa Katavi una upungufu mkubwa wa watumishi wa afya, Madaktari Bingwa hakuna, lakini pia Manesi hawatoshi katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda na hii inapelekea kuleta msongamano mkubwa wa wagonjwa katika zahanati na katika madirisha ya dawa na kuna kipindi msongamano mkubwa hupelekea wagonjwa kuzidiwa wakiwa katika foleni wakisubiri huduma na wengine kupoteza maisha wakisubiri huduma kwa madaktari. Je, ni kwa nini Serikali mpaka sasa haijaajiri watu wa kada ya afya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali inapata changamoto hizi kila siku lakini, bado hazifanyiwi kazi? Je, Serikali hii haioni na haitaki kufanyia kazi ni kwa nini inaacha walipa kodi wanateseka na huku pesa zinapelekwa katika mambo yasiyo vipaumbele kwa wananchi maskini, mfano, Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Chato, E-passport mpya na ununuzi wa ndege ambao kimsingi haujazingatia mchakato wa manunuzi? Ni kwa nini Serikali inazitelekeza huduma za jamii nchini na kujikita zaidi kwa wananchi wasio maskini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 45, Kamati imeshauri Serikali kuja na mkakati wa kudhibiti tatizo la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika jamii hii wanaoathirika ni watoto na wanawake zaidi na jamii imekuwa ikipeleka taarifa katika Madawati ya Jinsia, Polisi na Mahakama, je, ni kwa nini Serikali inashindwa kusimamia kesi hizi na malalamiko kwa jamii kuhusu suala la kesi kuchukua muda mrefu na hivyo jambo hili kuendelea kufanyika kwa sababu watuhumiwa wanaendelea kutoka wanaposhutumiwa? Je, Serikali haioni kuendelea kukaa kimya na hizi kesi inajenga mazingira ya watuhumiwa kuishi kwa hofu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Afya ya Akili, Mirembe Dodoma; hospitali hii ina changamoto ya nafasi na huku inachukua wagonjwa 317 Wodini kila siku na inahudumia wagonjwa wa akili 43 kwa siku na kuhudumia wagonjwa 119. Kwa uwiano huu hospitali hii ambayo ndiyo kubwa nchini bado hospitali hii haitoshi na majengo yake ni chakavu pamoja na upungufu wa watumishi wa afya. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inaboresha huduma katika hospitali hii katika Mji wa Dodoma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la wagonjwa wa akili bado lipo katika Mkoa wa Katavi na kwa kuwa Serikali haifanyi utafiti katika mikoa kuona ni kwa nini ongezeko hili linatokea na nini kifanyike kusaidia jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kashato, Shule ya Msingi Nyerere na Shule ya Azimio, Jimbo la Mpanda Mjini ina watoto wenye matatizo ya akili wengi tu, lakini wana tatizo la kupata madarasa, huduma za vyakula pamoja na Walimu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia maoni ya Kamati yakizingatiwa na Serikali ikayafanyia kazi, kutokana na changamoto zilizopo kupitia zoezi zima la vitambulisho vya Taifa pamoja na Serikali kutumia pesa kwa ajili ya kutengeneza vitambulisho hivi (NIDA).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara kuiwezesha NIDA au kuharakisha kuipatia fedha NIDA ili wananchi ambao hawajapata vitambulisho mpaka sasa waondokane na usumbufu huu tukielekea kwenye electronic system kuhusu usajili wa wageni katika mfumo ili kujua kama wanaishi kihalali nchini. Katika zoezi hili Serikali isimamie kwa umakini usajili huu ili kuondoa malalamiko ya wageni kupata vitambulisho vya Taifa na passport kabla ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika zoezi hili la usajili wa vitambulisho hususan wananchi wa mikoani inaleta usumbufu kusafiri kufuata mikoa yenye huduma hii kama Dar es Salaam na kuwaongezea gharama wananchi. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuweka ofisi kila wilaya ili huduma za vitambulisho ifanyike kila wilaya nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu kubwa la Serikali kuangalia masuala yote yanayohusiana na siasa kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.

Mheshimiwa Naibu Spika, askari wetu wanajeshi wamekuwa wakichukuliwa kwenda kutuliza ghasia katika nchi zenye vita na ghasia na askari wetu wamekuwa wakipelekwa kutuliza ghasia lakini wakipoteza maisha na kufa Serikali imekuwa ikichukua pesa kuzilipa familia kama rambirambi, lakini baada ya kumaliza msiba mnazitelekeza familia hizo na kuziacha zikiteseka. Je, Serikali ni kwa nini inashindwa kuendelea kuzisaidia familia zao ilihali walikufa vitani huku wakilinda mipaka yetu na kulinda mahusiano ya kidiplomasia? Serikali inalichukuliaje suala hilo ambalo linasababisha askari kuogopa kwenda kulinda amani nje ya Tanzania kwa sababu mnawatelekeza?

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la usajili wa vitambulisho (NIDA); hivi sasa wapo katika baadhi ya mikoa na zoezi hili linasababisha foleni na msongamano katika ofisi za usajili. Malalamiko ya wananchi ni kutozwa Sh.2,000 katika zoezi hili; je, Serikali haioni kuwatoza wananchi Sh.2,000 na wananchi ni maskini hawawezi kulipia gharama hizi katika mchakato wa kupata vitambulisho? Serikali inawasaidiaje wananchi maskini?

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji katika Balozi mbalimbali nchini; pamoja na juhudi za Serikali kupeleka Mabalozi na watumishi katika nchi wakilishi, kuna changamoto, kwa mfano, katika balozi Nchini China (Beijing), kuna watumishi wachache na bado malipo yao yanachelewa, uchakavu wa majengo na asilimia kubwa tumepanga, mfano, Balozi Zimbabwe na watumishi kujibana katika ofisi. Je, Serikali haioni iko haja kuwapatia fedha ili wafanye kazi pamoja na kuweza kutafuta fursa za kiuchumi?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia taarifa hii ya Kamati ambayo imetupa picha ya namna sisi kama Wabunge kujua wajibu na haki zetu na mchakato wa kutunga kanuni za maadili ndani ya Bunge. Muda ni finyu sana ambao umekuwa unatengwa tunapotunga sheria hizi na kupelekea Wabunge wasio na taaluma kupitisha kanuni ambazo baadaye huzilalamikia kanuni kuwaumiza hivyo muda uongezwe, hautoshi.

Kupitia kanuni hizi na lengo la Kamati hii katika suala la kutoa adhabu kwa Wabunge, kwa malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge ni kwamba Kamati hii iko haja ya kutoa muda kuwasikiliza Waheshimiwa Wabunge kwa undani kabla ya kutoa adhabu ambazo kimsingi ukisoma taarifa ya Kamati inalenga kwa asilimia kubwa kuwapa adhabu Wabunge wa Upinzani kuliko wa CCM.

Je, kupitia Kamati hii na malalamiko ya Wabunge, ni kwa nini kila siku adhabu zinatolewa kwa Wabunge haohao kila siku majina yanajirudia, hamuoni kuwa Kamati ya Maadili badala ya kuhakikisha Wabunge wanapata elimu ya maadili na msikimbilie kutoa adhabu ambayo inapelekea kuleta chuki na sio kufundisha kama lengo. Hivyo, Kamati ya Maadili ione namna ya kuongeza semina kwa Wabunge na Wajumbe wa Kamati pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upendeleo Bungeni, Kamati ione haja ya kuchunguza jambo hili ili likawe Bunge lililotukuka katika ujenzi wa Taifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kodi zinazokusanywa kupitia sanaa nchini bado Serikali hii ya Awamu ya Tano imeshindwa kuwasaidia wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kupata stika za TRA; ili kumwezesha msanii kuuza kazi yake kwa halali ni kwa nini Serikali inashindwa kuweka ofisi za usajili kila Wilaya na Mkoa ili kuondoa usumbufu kwa wasanii kwenda Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizi wa kazi za wasanii na hati miliki. Mpaka sasa Serikali imeshindwa kuwasaidia wasanii, wanafanya kazi katika mazingira magumu mpaka akamilishe kazi yake sokoni, lakini kazi hiyo inaibiwa, inampelekea msanii kutopata faida na kufaidisha wezi wa kazi hizi. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa wasanii pamoja na kulinda kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanja. Changamoto za viwanja vya michezo vingi vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi. Ni kwa nini Serikali inatumia kodi za wananchi hovyo kukarabati viwanja vya CCM ilihali viwanja hivi vingi nchini vina migogoro na kwa nini Serikali isichukue hatua ya kujenga viwanja vya michezo katika mikoa ili kuondoa ubaguzi huu na badala yake ijenge viwanja vya michezo katika mikoa na kuleta ajira, afya na michezo inawaweka watu pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Bunge Live; Serikali ya CCM imeshindwa kutetea hoja ya kwa nini Bunge halioneshwi na kupelekea wananchi kutoendelea kuiamini Serikali hii ya CCM kwa sababu inaficha mambo yake kupitia Bunge. Pia uminywaji wa demokrasia nchini kupitia vyombo vya habari kama radio, magazeti na kufungia nyimbo zinazokosoa Serikali, je, hawaoni kwa kufanya hivi ni kuonesha wamefeli.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongea kuhusu miundombinu. Miundombinu katika shule za Serikali ni mibovu na ndiyo inayosababisha wanafunzi kufanya vibaya katika shule za Serikali. Ziko changamoto nyingi katika elimu ya Tanzania. Elimu bure, mabweni, upungufu wa vitabu shuleni, walimu kupunguzwa na nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya elimu bure Serikali hii ya Awamu ya Tano imekurupuka vibaya na imesababisha matokeo mabaya. Ukiangalia gharama za kumnunulia uniform mwanafunzi, chakula, malazi, umbali na changamoto za familia hususan vijijini unakuta mtoto anasafiri umbali wa kilometa 20 kufuata shule na akifika shule kachoka, ana njaa na anawaza atarudije kwao baada ya masomo kwa umbali huo na huku usalama wake huo ni wa hofu kiasi hicho. Mnawafikiriaje wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kama hayo hususani vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri maslahi ya walimu yazingatiwe, nyumba za walimu wa shule za sekondari na msingi bado hali ni mbaya na usalama wao vijijini. Hii imesababisha walimu kukosa morale/motisha wa kufundisha kwa moyo kwa sababu ya changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule ya sekondari ya Wasichana Mpanda, shule hii ya wasichana haina uzio na ukizingatia eneo lililobaki kuzunguka shule ni pori na kuna wanyama aina ya viboko kipindi cha usiku huzunguka kwenye mabweni na husababisha wanafunzi kuishi kwa hofu hapo shuleni. Shule ya Mpanda Girls imezungukwa na wafanyabiashara, stand ya magari ya mizigo na biashara za wajasiriamali hivyo usalama wa wanafunzi hawa umekuwa mdogo na wa hofu. Waendesha magari makubwa kuweka stand hii pale imesababisha wanafunzi kupata mimba kutokana na mazingira yaliyopo, ni mabaya. Hivyo Serikali izingatie jambo hili la kuweka uzio ili usalama wa wanafunzi uimarike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu wanafunzi wenye ulemavu. Shule za Msingi Azimio, Kasahato na Nyerere zilizopo katika Manispaa ya Mpanda zimeelemewa mzigo wa wanafunzi walemavu na bado wana changamoto za madarasa ya kufundishia watoto hao, wanafundisha katika madarasa yasiyo na madirisha. Je, Serikali inawasaidiaje watoto hawa pamoja na walimu ambao kimsingi wanafundisha katika mazingira hayo magumu na vitendea kazi pia havitoshi? Serikali ina mkakati gani wa kumaliza matatizo haya ya wanafunzi walemavu na vifaa vyao husika?
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni muhimu sana endapo itazingatia ushauri wa Kamati, hususani katika suala la kutatua migogoro iliyopo kati ya wananchi na Hifadhi za Taifa (mipaka).

Mheshimiwa Spika, ni lini mtakuja Katavi kufuatilia na kutatua migogoro iliyowaathiri Wana Katavi hususani katika Kata za Isengule, Ikola, Kapala Msenga kijiji cha Lyamgoloka Jimbo la Mpanda Vijijini (Ikuba). Wananchi walipigwa na askari wa wanyamapori tangu 2004 mpaka sasa wananchi wanaishi kwa hofu, wanauawa kwa kupigwa risasi. Hivi karibuni kuna vijana wameuawa kwa kupigwa risasi.

Mheshimiwa Spika, akina mama wanabakwa, wananyang’anywa mali zao, je, Mheshimiwa Waziri ni sheria ipi inayoruhusu unyanyasaji huu kuendelea kutokea na Serikali hii inakaa kimya? Je, Serikali inasemaje kuhusu ukatili huu? Ni utaratibu gani unatumika kupima mipaka? Je, wananchi wanaingia ndani ya hifadhi au hifadhi inaongeza maeneo kwa kuwanyang’anya maeneo yao? Ni lini mtawalipa fidia kwa kuchukua maeneo yao bila utaratibu wa sheria?

Mheshimiwa Spika, mgogoro wa mpaka kati ya Stalike na hifadhi mpaka sasa wananchi hawa ni lini watarudishiwa maeneo yao? Wananchi wa kata hii wameshindwa kufanya shughuli za kiuchumi kulima na kutumia maji ya mito inayowazunguka. Je, ni lini jambo hili litaisha ili wananchi wafanye shughuli zao za kiuchumi?

Mheshimiwa Spika, kupigwa risasi ng’ombe/wafugaji; wafugaji wengi hawana elimu ya mipaka, makazi na hifadhi ni kwa nini elimu haitolewi kwa vijiji/vitongoji? Serikali ina kazi gani? Serikali kushindwa kuweka mipaka kumepelekea wafugaji kuendelea kunyanyasika katika Taifa lao.

Mheshimiwa Spika, sheria inasemaje kuhusu mauaji ya wafugaji na ng’ombe kupigwa risasi hovyo katika Kata za Ikuba, Majimoto, Luhagwe? Je, Serikali inasaidiaje tatizo hili la kitendo cha TANAPA kuvunja sheria kwa kuweka mipaka iliyo kinyume na GN.

Mheshimiwa Spika, suala la wafugaji kulipishwa faini na watendaji/askari wa wanyama pori ng’ombe mmoja inalipishwa shilingi milioni moja ikiingia hifadhi au mfugaji kupigwa risasi, Je, sheria ya haki za binadamu Wizara hii mbona iko kimya kuhusu unyama huu?

Mheshimiwa Spika, risiti fake wanazolipishwa wafugaji wetu je, Wizara inachukua hatua gani kuhusu tatizo hili? Ajira kupitia wawezeshaji hoteli zilizopo ndani ya hifadhi, Mkoa wa Katavi haunufaiki kwa wazawa kupata ajira mbugani, je, Serikali haioni ni tatizo?
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango bado haijakidhi kwenye hoja inayohusiana na utekelezaji, inajikita zaidi kupeleka fedha kwenye miradi mipya ambayo haikuwa kwenye mipango ya miaka mitano na badala yake Serikali hii ya Awamu ya Tano inajikita kupeleka fedha kwenye miradi mipya kama ununuzi wa ndege na ujenzi wa ukuta wa Mererani.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kiwanja cha ndege Chato na ujenzi wa Benki ya CRDB Chato, jengo kubwa la ghorofa Chato. Chato kuna vitega uchumi gani vikubwa vilivyosababisha kupeleka fedha haraka haraka na hii imepelekea malalamiko na baadhi ya miradi kupendelewa kama ya Chato. Usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mapato ya ndani kupitia Serikali za Mitaa mwaka 2017/2018 yalikuwa bilioni 437.6, asilimia 64 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, tunaomba ahadi mlizoahidi kupitia Ilani ya CCM mtekeleze kwa wakati na Waziri Mpango uje na majibu ya maswali ya wananchi wanayotuuliza kila siku kwenye mikoa yetu. Kwanza ni lini mtatoa laptop kwa kila mwalimu? Ni lini mtazipeleka shilingi milioni 50 za kila kijiji kwenye vijiji na matumizi na uwazi wa shilingi trilioni 1.5 ziko wapi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inabeba usalama wa Taifa. Kwa maana hiyo, kama Wizara hii ikiendelea kufanya vibaya kama ilivyo sasa, usalama wa Taifa utazidi kuwa hatarini. Ukizingatia kuwa usalama wa Taifa tunahitaji Serikali iangalie changamoto zifuatazo ili kunusuru Taifa; udhibiti wa uhalifu, mauaji, kubambikiziwa kesi, usalama mipakani, usalama wa wafungwa Magerezani, dawa za kulevya na matumizi ya nguvu kwa wananchi kupitia Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mauaji katika Taifa letu imekuwa ni changamoto kubwa ambayo kimsingi mpaka sasa wananchi wamebaki hawana majibu ya mauaji ambayo yameshatokea, lakini taarifa za matukio haya haya na ripoti inayoeleweka; tukio la Mheshimiwa Tundu Lissu kupigwa risasi mpaka sasa Serikali imeshindwa kutoa majibu ya tukio hili na kuwataja wahusika hasa wa shambulio hili. Je, ni lini Serikali itatoa taarifa ya jambo hili ili wananchi waondokane na hofu iliyopo kwamba Serikali inaficha wauaji hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu kupotea kwa Ben Saanane, kupotea kwa mwandishi wa habari Azory, maiti zinazookotwa bila taarifa kamili, kubambikiziwa kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri kupitia bajeti atuambie ana mkakati gani wa kuhakikisha Vituo vya Polisi na baadhi ya Polisi wanachukuliwa hatua kwa makosa ya kubambikizia kesi wananchi na wananchi wakitoa taarifa za matukio haya hawapati msaada kutoka Vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika ina malalamiko na kesi nyingi za wananchi kubambikiziwa kesi na badala yake watuhumiwa wanaombwa pesa na Askari ili wamalize kesi hizi. Je, Wizara ya Mambo ya Ndani hamwoni kwamba baadhi ya Polisi wasio waaminifu wanachafua Jeshi la Polisi? Mr. Said Anganisye ana kesi katika Kituo cha Polisi Kata ya Kabungu, Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mauaji ya bodaboda Mwakagana (Wilaya ya Mpanda) Polisi anashutumiwa kumpiga bodaboda mpaka kumuua na Polisi anajulikana kwa jina la Deus lakini mpaka sasa tunavyoongea wananchi hawana majibu ya vifo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya magereza yetu bado yana changamoto kubwa kwa maana ya kukosa vyumba vya kutosha pamoja na usafi; vyumba havina hewa na uchakavu wa magodoro yenye magonjwa. Wafungwa hawa pamoja na kwamba wanapewa adhabu, basi zisihusiane na kimazingira bali pia Wizara iangalie haki za binadamu. Kwa kuangalia utesaji na kazi ngumu sana wanazofanya wakiwa Gerezani, badala yake Serikali itumie wafungwa kufanya kazi za kimaendeleo zaidi na siyo mateso wanayopata ambayo hayana tija kwa Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchache wa vitendea kazi na sare za wafungwa ni aibu kwa Serikali kwa kushindwa kuwapa sare wafungwa na kupelekea Askari Magereza kuwapa nguo zao binafsi kama makoti na nguo za ndani. Mjitahidi kutatua jambo hili. Ni udhalilishaji kwa wafungwa kukosa hata nguo za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iongeze ulinzi mipakani na mikoa inayopakana na nchi jirani kama Katavi, hali ni mbaya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapa pole viongozi wa CHADEMA zaidi ya 15 wakiwemo Wabunge wa Upinzani ambao wana kesi katika Mahakama zetu, kesi za kisiasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe pole na Mungu amponye Mheshimiwa Lissu ili aweze kurudi aendelee na majukumu yake. Pamoja na kwamba mpaka sasa ripoti ya tukio la Mheshimiwa Lissu Bunge halijaleta ripoti hii na malalamiko mengi yaliyopo nchini. Mfano, kupotea Ben Saanane na Mwandishi Azroy, kifo cha Aquilina, vifo vya watoto Kibiti na Tundu Lissu kupigwa risasi. Ni kwa nini Serikali inatoa majibu tata na kuacha wananchi wakibaki na sintofahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Serikali kuendelea kukaa kimya inapelekea wananchi waamini kwamba Serikali hii ni Serikali isiyojali wanyonge na Serikali inayowaonea watu bila kuwasaidia wananchi na matatizo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara. Serikali ina hofu gani kuzuia mikutano ya siasa. Hii inaonesha kuwa katika Serikali hii ya Awamu ya Tano inaogopa kufichuliwa udhaifu uliopo ndio maana inaogopa ukweli.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuonesha kuwa uchumi unakuwa kwa 6.7 mwaka 2018 kutoka 6.2 kwa mwaka 2017, katika kukuza ajira na uboreshaji wa miundombinu na pia imefanikiwa kupunguza mfumuko wa bei katika jamii. Bidhaa na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu hizi bado hazina uhalisia na maisha ya wananchi ambapo bado maisha ni magumu na ajira bado Serikali imeshindwa kutatua kero hii ambayo ndiyo hoja kuu na changamoto kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya vijana na akinamama wajasiriamali wadogo bado ni magumu katika halmashauri zetu, japo Serikali imejikita katika kuwapa mikopo katika makundi haya, lakini bado marejesho katika vikundi hivi yameshindikana. Kwa hali iliyopo asa sioni kwamba mikopo hii inawasaidia moja kwa moja akinamama kwa sababu urejeshwaji wa mikopo hii kwao bila kuwasimamia, mafunzo, kuwatafutia masoko, miundombinu mibovu imepelekea vikundi hivi kushindwa kufanya biashara na ukosefu wa vifungashio ambavyo ni bora. Matatizo haya ya kimazingira na masoko ni kero kwa wajasiriamali, hivyo Serikali ije na mkakati thabiti kuokoa makundi haya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitambulisho vya wajasiriamali wadogo 670,000. Serikali hii pamoja na kuwatambua na kuwaondolea usumbufu wa maeneo ya biashara kupitia Serikali za Mitaa, bado kuna tatizo kwa sababu wajasiriamali wametoa Sh.20,000 lakini mpaka sasa hatuoni kwamba Serikali hii ina nia ya dhati kusaidia kundi hili kwa sababu kundi hili wanalipa kodi, ushuru na huku Serikali iko kimya. Je, ni lini watalimaliza hili kwa wakati?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna malalamiko ya wananchi kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masuala ya haki za wanawake, watoto na walemavu; nashauri Serikali ijipange kuyachunguza maeneo haya ili uvunjifu huu uishe. Wanawake wananyanyasika sana, hususan katika jamii na Magerezani. Ni kwa nini Serikali hii ya Awamu ya Tano imeshindwa kumaliza malalamiko haya ambayo kila siku yanaongezeka kupitia vituoni, Polisi na Mahakamani? Hii inasababisha kuteseka kwa wanawake na watoto ambao kimsingi ni kundi kubw. Hivyo Serikali iondoe malalamiko haya mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mlundikano wa mahabusu Magerezani na Vituo vya Polisi, mamlaka inayoshughulikia masuala haya imeshindwa kumaliza jambo hili. Gereza la Kalika, Nkulunkulu lililopo Mpanda mpaka leo mahabusu na wafungwa wanafanyiwa vitendo viovu na Askari Magereza na hawana sehemu ya kulalamika wakihofia maisha yao, kwa sababu hawa Askari wanaishi nao. Wanapoumwa hawashughulikiwi vya kutosha na kusababisha afya zao kuwa duni na ukizingatia wanalundikana katika Magereza hayo ambayo kiafya inakiuka haki za kimsingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, Serikali imeshindwa kutatua kwa sababu malalamiko bado yanaongezeka. Je, Serikali haioni kwa kushindwa mambo haya inafanya makusudi kupoteza nguvukazi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni vita dhidi ya rushwa. Matatizo ya kiuhalifu yataendelea kuongezeka kwa sababu baadhi ya Askari wasio waaminifu wamekuwa wakipokea rushwa na kuwaacha walalamikaji wakiishi katika maisha ya wasiwasi. Mahakama na Polisi ikishindwa kudhibiti mianya ya rushwa na tunaamini katika vyombo vya sheria ndiyo sehemu pekee inayoweza kutafsiri makosa, hii inaleta tafsiri mbaya katika jamii na wananchi wataamua kujichukulia hatua mkononi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ukarabati wa majengo ya Mahakama za Wilaya na Miko. Bado hali ni mbaya na hairidhishi katika Mahakama zetu. Uhifadhi wa mafaili ya kesi hupotea; hii inaleta picha mbaya kwamba na Mahakama zetu zinashindwa kulipa kipaumbele jambo hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, Baraza la Sanaa Taifa – BASATA; lengo la Baraza hili ni kuboresha ubunifu pamoja na kuibua vipaji mbalimbali pamoja na utafutaji wa masoko yenye ubora kwa wasanii.

Mheshimiwa Spika, COSOTA na BASATA; hivi vyombo viwili vinavyofanya kazi pamoja, lakini kuna changamoto kubwa kupitia mlolongo mrefu wa usajili kwa wasanii kupata (stamp) za TRA ili kazi ya msanii iingie sokoni na ukizingatia mikoani ofisi hizi zinalega na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna kanda hazina ofisi za Baraza hili COSOTA na BASATA na hii inapelekea kwa wasanii wachanga kushindwa kufuata hatua hizi na uchumi wao mpaka afike Dar es Salaam ndipo apate usajili. Je, hawaoni kwa kushindwa kupeleka huduma kila mkoa ni kuwaumiza wasanii ambazo wako tayari kusajili kazi zao na huku milolongo hii ikiwagharimu? Ni lini watajenga ofisi zao kila mkoa ili kuondoa usumbufu huu?

Mheshimiwa Spika, dhana ya kufungia vyombo vya habari; Sekta ya Habari tulitegemea lengo lake ni kuhabarisha kuelimisha kukosoa na kuburudisha, lakini dhana hii inabadilika kila siku kwa kufungia vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikifungiwa na kufunguliwa gazeti la Mawio Mwanahalisi, Raia Mwema, na baadhi ya redio. Ni kwa nini wanatoka katika dhana ya ukosoaji na wanataka kusifiwa tu?

Je, lengo la Wizara hii ni kwa nini linajikita zaidi katika masuala ya siasa na kuacha kufungia kazi za wasanii, filamu ambazo kimsingi ziko mtaani na zinaharibu jamii. Wana mpango gani katika suala hili kuchunguza kazi zinazosambaa katika jamii video, audio na picha chafu kwenye mitandao hawaoni kwamba wameshindwa?

Mheshimiwa Spika, Cyber Crimes Act na Sheria ya Takwimu. Makosa ya kimtandao ambayo kwa ujumla yanaminya uhuru wa kupata habari na kusambaza hili ni tatizo na limepelekea jambo hili kutumika zaidi kisiasa. Sheria hizi zinaminya uhuru wa kujieleza na kukiuka haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, ajira; malalamiko ya wasanii ni mengi katika tasnia hii hususan katika maslahi yao. Sanaa ni ajira, hivyo, tunaishauri Serikali kusimamia maslahi yao na mafao yao ili kuhakikisha wachezaji wasanii wanapata haki zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, niongelee kuhusu vifo vinavyotokana na ukatili wa Jeshi la Polisi. Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wananchi kunyanyaswa na baadhi ya Polisi na kuripotiwa katika maeneo mbalimbali. Mfano, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Vijijni (Tanganyika) amekuwa akitumia baadhi ya Askari kunyanyasa wananchi wa Tanganyika. Wananchi wanawekwa ndani (rumande) wanabambikiziwa kesi mbalimbali, wanachomewa nyumba kwa maelekezo ya Mhando.

Mheshimiwa Spika, mmoja kati ya wananchi waliopigwa risasi na Askari na kufa anaitwa Shinje, Aprili, mwaka 2018. Jambo hili na mengineyo yanayoendelea kutokea katika mkoa wetu, yanachafua Jeshi la Polisi, lakini pia Serikali kupitia Jeshi la Polisi inashindwa kulinda mali za raia wake na usalama wao. Hii inapelekea watu kutokuwa na imani na jeshi la polisi.

Mheshimiwa Spika, nataka Mheshimiwa Waziri akija hapa, ajibu ni kwa nini baadhi ya Askari wanafanya uovu na hawachukuliwi hatua; Wakuu wa Wilaya hawa Mheshimiwa Mhando wa Tanganyika na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda? Je, sheria za kutoa amri kwa Polisi kuwakamata raia wanatoa wapi wateuliwa hawa? Jambo hili linakera na lisipofanyiwa kazi linaenda kuleta athari kubwa.

Mheshimiwa Spika, kingine ni kuhusu upotevu wa mali za raia katika vituo, vifaa vya raia vinavyokamatwa na Polisi, pikipiki, TV, Redio vitu vingine. Hii imekuwa ni kero kwa sababu unakuta mtuhumiwa anakamatwa; ushahidi na kesi inaenda Mahakamani, lakini baada ya muda vitu vya ushahidi vinapotea, vinauzwa au unakuta mali za wananchi ziko mtaani. Mheshimiwa Waziri ajibu, hili linakera na kuchafua Jeshi hili ambalo linatumika vibaya na baadhi ya Polisi wasio waaminifu.

Mheshimiwa Spika, ni kwa nini RCO, Wakuu wa Vituo wanazuia Mikutano ya Hadhara na huku Polepole anaachwa akifanya mikutano ya ndani na nje? Intelijensia inapatikana kwa viongozi wa Upinzani tu ila kwa CCM hawapatikani na taarifa za intelijensia ambazo ni mbaya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba mkubwa wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari nchini, bado kuna changamoto katika Sekta ya Elimu hususani katika miundombinu na hii inapelekea kushuka kwa ufaulu na kusababisha walimu kuishi katika mazingira magumu na huku ni jukumu la Serikali kuhakikisha inatatua kero zao, hakuna Elimu bila walimu hivyo Serikali hii itatue kero ya nyumba bora kwa walimu wa Shule ya Msingi na Sekondari mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabweni, Shule ya Sekondari Mpanda Girls mpaka sasa haina uzio na shule inayotegemewa na wananchi kwa ufaulu wake, shule hii iko nje ya mji kidogo na imezungukwa na shughuli za kiuchumi stendi ya malori na mabasi makubwa soko na kilimo je? Hii shule ni ya wasichana kuzungukwa na shughuli hizi na pia shule haina uzio hamuoni kuwa Serikali inahatarisha usalama wa watoto na mimba kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viboko, shule hii, imezungukwa na bwawa na mito wakati wa usiku viboko wamekua wakizunguka kwenye maeneo ya mabweni na kuleta hofu kwa wanafunzi. Naiomba Serikali ione namna ya kutatua jambo hili kabla halijaleta madhara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia bajeti hii ambayo kimsingi imebeba dhana ya Serikali ya Viwanda, naomba kuikumbusha Serikali mchakato wa viwanda 100 kila mkoa. Mkoa wa Katavi kutokana na kuendelea kuwa na changamoto za maji na umeme pamoja na masoko kutokana na miundombinu ya barabara kuwa kero kwa usafirishaji, naomba utekelezaji kwa kutatua kero hizi ili viwanda vilivyoanzishwa na vikundi mbalimbali ikiwemo viwanda vya alizeti, Manispaa ya Mpanda; viwanda vya mazao, mpunga na mahindi; viwanda vya maziwa (makanyagio); viwanda vya nyama, ukizingatia Mkoa wa Katavi kuna ufugaji wa kutosha viweze kuendelea. Hivyo, ni rai yangu kuomba Serikali hii kufungamanisha sekta ya ufugaji na viwanda ili dhana ya viwanda ifanikiwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua majukumu makubwa ya Wizara hii katika ujenzi wa Taifa, usalama wa nchi kupitia mipaka ya nchi na usalama wa raia. Malalamiko ya wananchi kwa Jeshi hususani katika maeneo yaliyopakana na Jeshi kwa kigezo cha Jeshi kutokuwa na umiliki halali na wananchi kuingilia maeneo hayo kwa kupewa na Manispaa au Halmashauri na baadae kuleta migogoro ya wananchi kupigwa na wanajeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu Wizara ya Ardhi bado inashughulikia mipaka na maeneo hayo yaliyoingiliana na wananchi. Ni kwa nini Jeshi linachukua hatua ya kuwapiga, kuchoma nyumba, kubaka kina mama, kuwapa mateso yasiyoelezeka wananchi ambao kimsingi walipewa maeneo hayo kupitia Halmashauri? Ni kwa nini Jeshi linafanya unyama huu na huku Serikali ikiangalia unyama huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro uliopo katika Kata ya Misunkumilo kuhusu mpaka wa Jeshi jambo hili lipate ufumbuzi. Pia katika Jimbo la Kibamba ambalo Jeshi linaendelea na unyanyasaji kwa raia ni nini suluhisho?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. RHODA S. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo inachangia 29.1% ya Pato la Taifa endapo tutaongeza juhudi katika uzalishaji huenda Sekta ya Kilimo ndio ikaleta mageuzi makubwa nchini. Changamoto tuliyonayo ni kufeli kwa mipango ya Serikali yetu kufungamanisha miradi mikubwa ya kiuchumi na Sekta ya Kilimo sambamba na mikakati ya kuongeza thamani kwenye uzalishaji wa Sekta ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa takwimu za hifadhi ya chakula nchini tangu 2015 mpaka 2019 zinaonesha kiwango cha uzalishaji wa chakula kimeshuka kwa asilimia kubwa na inatisha. Nimeangalia takwimu zilizotumiwa na Benki Kuu Aprili, 2019 hifadhi ya chakula imeshuka kwa 82.7 kutoka mwezi Machi, 2019. Ukiangalia takwimu hizo utaona Machi, 2015 hifadhi ya chakula ilikuwa tani 452,054.0 lakini kufikia Machi, 2019 hifadhi ya chakula imeshuka mpaka 78,336.0.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya ardhi kuongeza uzalishaji. 53.3 ya ardhi yetu ni misitu na 15.4 iliyobaki ni ardhi yenye rutuba. Sehemu kubwa ya ardhi yetu hapa nchini inafaa kwa kilimo ila uzalishaji wetu umeendelea kushuka siku kwa siku. Kumekuwa hakuna utoshelevu wa kutosha wa chakula ili hali tuna ardhi yenye rutuba isipokuwa tuna maarifa duni ya kuongeza kiwango cha uzalishaji. Endapo tungekuwa na utoshelevu wa kutosha wa chakula basi hata ujenzi wa reli ya standard gauge unapaswa kutumika kusafirisha chakula Afrika Mashariki, DRC Congo, Burundi na Uganda na Rwanda.

Mheshimiwa Spika, takwimu za uagizaji chakula nje ya nchi na bei za vyakula; Bei zimeshuka na kuumiza wakulima. Uagizaji umeongezeka kutoka dola milioni 13.3 mwezi Machi, 2018 mpaka kufikia dola milioni 15 Machi, 2019.

Katika mazao sita makuu mazao manne bei zimeshuka, Machi, 2018 gunia la mchele 185.735.4 na sasa 168,520.5 kwa 9.3. Maharage ilikuwa 170,140 na zaidi imefika 165,3000 na zaidi kwa 2.8%. Uwele gunia kutoka 76,712.1 sasa ni 75.677.4 kwa 1.3%. Gunia la viazi 67033.8 imeshuka kwa 1.9 mpaka 68,302.9. Mtama 148.8371 mpaka 134,724.3 hatujafanya juhudi za kutosha kutumia sehemu ya ardhi yenye rutuba.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo yangu ni kama ifuatavyo:-

(a) Ifanyike juhudi ya kuongeza thamani ya mazao kama matunda kwa kufanya packaging na processing ya matunda juice.

(b) Kuweka mazingira bora ya kisheria na kisera kwa sekta binafsi kujenga viwanda na kuchakata korosho.

(c) Kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria kwa sekta binafsi ili kujenga viwanda vya kukamua mbegu za mazao kama alizeti.

(d) Kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria kwa sekta binafsi kujenga viwanda vya utengenezaji wa nguo textile industries pamba inayozalishwa nchini ni nyingi 20 peke huchakatwa nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, pamoja na Wizara hii kusheheni mipango bado tuna changamoto za kibajeti kuminywa na huku wafugaji wakiendelea kuteseka na kero za majosho, ukosefu wa viwanda vya kuchakata bidhaa za ngozi, changamoto za malisho, upungufu wa watumishi katika sekta hii, migogoro mikubwa na tozo holela kwa wafugaji.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo; nashauri kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria kwa Sekta Binafsi kujenga viwanda kwenye Sekta ndogo ya Ngozi na kuzalisha bidhaa za ngozi kwa wingi. Tanzania ina mifugo zaidi ya milioni 17.7 inayoweza kutoa bidhaa za ngozi isipokuwa bidhaa za ngozi zinazozalishwa ni milioni 2.6 kwa mwaka. Sehemu kubwa ya ngozi inauzwa nje bila kuchakatwa, ni 10% pekee ndiyo huchakatwa nchini. Napendekeza Serikali iweke mazingira bora ya kisera na kisheria kwa sekta binafsi kujenga viwanda vya nyama na maziwa.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 29.1 ya Pato la Taifa. Endapo tutaongeza juhudi katika uzalishaji huenda Sekta ya Kilimo ndiyo ikaleta mageuzi makubwa nchini. Changamoto tuliyonayo ni kufeli kwa mipango ya Serikali yetu, kufungamanisha miradi mikubwa ya kiuchumi na Sekta ya Kilimo sambamba na mikakati ya kuongeza thamani kwenye uzalishaji wa Sekta ya Kilimo. Mwenendo wa takwimu za hifadhi ya chakula nchini tangu 2015 mpaka 2019 zinaonesha kiwango cha uzalishaji wa chakula kimeshuka kwa asilimia kubwa.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia takwimu zilizotumiwa na Benki Kuu April 2019 – Hifadhi ya chakula imeshuka kwa 82.7 kutoka mwezi Machi, 2015 mpaka kufika 17.3 Machi, 2019. Ukiangalia takwimu hizo utaona Machi, 2015 hifadhi ya chakula ilikuwa tani 452,054.0, lakini kufika Machi 2019 hifadhi ya chakula imeshuka mpaka 78,336.0.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya ardhi kuongeza uzalishaji. 53.3 ya ardhi yetu ni misitu na 15.4 iliyobaki ni ardhi yenye rutuba. Sehemu kubwa ya ardhi yetu hapa nchini inafaa kwa kilimo ila uzalishaji wetu umeendelea kushuka siku kwa siku. Kumekuwa hakuna utoshelevu wa kutosha wa chakula ilhali tuna ardhi yenye rutuba isipokuwa tu na maarifa duni ya kuongeza kiwango cha uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, endapo tungekuwa na utoshelevu wa kutosha wa chakula basi hata ujenzi wa reli (standard gauge) unapaswa kutumika kusafirisha chakula Afrika Mashariki (Kongo DRC, Burundi, Uganda na Rwanda).

Mheshimiwa Spika, takwimu za uagizaji chakula nje ya nchi na bei za vyakula; bei zimeshuka na kuumiza wakulima, uagizaji umeongezeka kutoka dola milioni 13.3 mwezi Machi, 2018 mpaka kufikia dola milioni 15 Machi, 2019. Katika mazao sita makuu bei zimeshuka Machi, 2018 gunia la mchele 185.735.4 na sasa 168,520.5 kwa 9.3. Maharage ilikuwa 170,140 na zaidi, sasa imefikia 165,300 na zaidi kwa 2.81. Uwele gunia kutoka 76,712.1, sasa ni 75,677.4 kwa asilimia 1.3. Gunia la viazi 69,033.8 imeshuka kwa 1.0 mpaka 68,302.9. Mtama 148,8371 mpaka sasa ni 134,724.3. Hatujafanya juhudi za kutosha kutumia sehemu ya ardhi yenye rutuba.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo yangu; ifanyike juhudi ya kuongeza thamani ya mazao kama matunda kwa kufanya (packaging) na processing ya matunda (juice) kuweka mazingira bora ya kisheria na kisera kwa Sekta Binafsi kujenga viwanda na kuchakata korosho. Kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria kwa Sekta Binafsi ili kujenga viwanda vya kukamua mbegu za mazao kama alizeti. Kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria kwa Sekta Binafsi kujenga viwanda vya utengenezaji wa nguo (textile industries) pamba inayozalishwa nchini ni nyingi (20) pekee huchakatwa nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RHODA S. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, uchambuzi na utekelezaji wa bajeti; makato ya mshahara zaidi ya shilingi bilioni 168 kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo hayakupelekwa katika taasisi husika (CAG Ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu 2017/2018 ukurasa 189).

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ambazo hazina mpango wa matengenzo na kumbukumbu za matengenezo ya mali za kudumu (Maliasili na Utalii) ukurasa wa 287. Kwa mujibu wa CAG mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara ya Maliasili ina kesi Mahakamani baina yake na kampuni na watu binafsi ikidaiwa Sh.23,399,564,809 ukurasa wa 238. Kuna hatari ya kulipa fedha hizo kutoka kwenye bajeti endapo Wizara ya Maliasili na utalii itashindwa katika kesi hizo zilizoko Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ni muhimu kwa ustawi wa utalii nchini katika taasisi za Serikali. Wizara hii ni kinara kwenye madeni makubwa kuliko taasisi yoyote, kiasi hicho ni zaidi ya fedha za bajeti ya maendeleo. Wizara hii imefanya matumizi ya Sh.3,559,102,398 na hajalipwa. Waziri akija kuhitimisha ajibu jambo hili likoje?

Mheshimiwa Naibu Spika, safari za ATCL kutochochea ukuaji wa utalii nchini. Uamuzi wa kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ulipaswa kwenda sambamba na soko la utalii nchini. Kwa sababu Sekta ya Utalii ndiyo sekta kinara wa ongezeko la mapato ya kigeni na takwimu zinaonesha Kenya ndiyo inaongoza kuleta utalii nchini baada ya Marekani na tatu Burundi. Sasa jambo la kushangaza ATCL imetangaza kwa itaanza kufanya safari mara nne kwa wiki kutoka Dar es Salaam – Afrika Kusini. Ukiangalia masoko 15 yanayoongoza kuleta idadi kubwa ya watalii nchi ya Afrika Kusini ni ya nane. Sasa naomba Waziri akija kujibu anijibu yafuatayo:-

Je, kama hatuwezi kuitumia ATCL kuchochea soko la utalii tutaitumia kwa ajili ya kukuza sekta ipi? Napenda pia kujua uamuzi wa kupeleka ATCL Afrika Kusini baada ya kuanza na safari ambazo kuna soko kubwa la utalii, uamuzi huo unatokana na nini? Pia ni kwa namna gani ndege mpya ya ATCL mfano Dreamliner zinavyotumika kuchochea Sekta ya Utalii nchini? Napenda kujua kama upo mkakati kabambe wa kuyafuata masoko hayo ya utalii?

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya hifadhi na wananchi Mkoa wa Katavi; kuna migogoro inayoendelea katika Jimbo la Mpanda Vijijini, Kata za Vijiji vya Lyamgoloka, Iseganyanya, Isengule, Chamalendi, Ihefu, Kapalamsenga, Ikola, Karema. Wananchi hawa wanateswa na Askari wa Maliasili kwa maagizo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Mhando, wanapigwa risasi, wanachomewa nyumba na mifugo yao inatozwa faini kubwa. Sasa nataka kufahamu ni sheria gani inatumika kuwanyanyasa hawa raia wakati lengo la Serikali ni kutatua na si vinginevyo?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, masuala nyeti ya uwazi kwenye tasnia ya uziduaji yanayohitaji majibu ya Serikali; mchango wangu wa hotuba hii ya Wizara ya Madini mimi ni mdau wa madini natoka katika maeneo yenye machimbo, hivyo mchango wangu unajikita katika hatua kadhaa zinazochukuliwa katika utekelezaji wa Sheria ya Uwazi katika Tasnia ya Uziduaji ya mwaka 2015. Uwazi unasaidia kuzuia makandokando ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha haramu na utoroshwaji haramu wa fedha kutoka kwenye Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi. Hivyo, nitazungumzia mambo manne muhimu kuhusu uwazi katika tasnia ya uziduaji (madini, mafuta na gesi asilia).

Mheshimiwa Spika, nitaeleza athari za uwazi kuhusu kampuni 23 za uziduaji kutoorodheshwa katika Soko la Hisa Dar-es-Salaam. Katika mchango wangu nitaomba Serikali ituambie hatua za utekelezaji wa kanuni za mwaka 2019 zilizotungwa ili kuweka wazi majina ya watu watatu ambao ni wanufaika wa umiliki wa makampuni ya uziduaji.

Mheshimiwa Spika, nitawataja wanasiasa na wenye maslahi yenye kutia shaka katika kampuni za uziduaji (political exposed personalities). Sheria hizi za makampuni zinaiweka Tanzania katika nchi zilizo hatarini kutumiwa na wahuni kuficha mali za wizi kwenye tasnia ya madini, mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, Kampuni 23 za Uziduaji Kutoorodheshwa katika Soko la Hisa Dar-es-Salaam. Kati ya kampuni 54 za tasnia ya uziduaji ni kampuni nne tu ndio zilizoorodheshwa katika soko la hisa la Dar-es-Salaam (Dar e s Salaam Stock Exchange). Establishment Maurel et Prom Swala Oil & Gas (Tanzania) Public Limited Company. The Tanzania Cement Company Limited na TOL Gases Limited.

Mheshimiwa Spika, kampuni 23 za uziduaji kutoorodheshwa soko la hisa. Kampuni 23 kati ya 54 ni kampuni zinazomilikiwa na umma huku kampuni zao kuu zikiwa zimesajiliwa nchi za Canada, Kenya, Norway, South Africa na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia leo kwenye soko la hisa (Dar es Salaam) ni kampuni 28 za sekta mbalimbali zinazouza hisa zake katika soko hilo huku Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi zikiwa kampuni nne pekee. Endapo kampuni hizi za gesi na madini zikiorodheshwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam fursa ya uwazi itafunguliwa kutokana na kanuni za uendeshaji wa soko hilo zilivyo, wamiliki halisi wa kampuni watakuwa wazi hivyo kuondoa dhana ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na utakatishaji wa fedha haramu.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri akija hapa kuhitimisha hoja yake aseme ni kwa nini wasilete marekebisho ya Sheria ya Uwazi katika Tasnia ya Uziduaji ili kiwepo kipengele kinachowalazimisha kampuni zote za uziduaji kuorodheshwa katika Soko la Hisa Dar-es-Salaam. Waziri Biteko alitunga sheria Februari, 2019 kuhusu uwazi na uwajibikaji kwenye tasnia ya uziduaji, hivyo zielekezwe.

Mheshimiwa Spika, tungeweza kuwabaini hawa wanasiasa na watumishi wenye maslahi katika madini, lakini tunashindwa kubaini kwa sababu Sheria ya Maadili inazuia kuweka wazi. Hapa hakuna uwazi. Majibu nahitaji?

Mheshimiwa Spika, Waziri akija hapa kuhitimisha aseme ni kwa nini Serikali isilete sheria ya makampuni au sheria ya uwazi katika tasnia ya uziduaji, ili kuzuia uhuni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni muhimu kuelekea Serikali ya viwanda nchini, hivyo, kupitia hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeishauri Serikali kwa sababu Wizara hii imeelemewa na inahitaji uzalishaji mkubwa na usambazaji wa kutosha kwa walipakodi, hivyo iko haja sekta ya uzalishaji na usambazaji vikajitegemea ili ifanye kazi kwa ufanisi na wananchi na wananchi wafikiwe na umeme kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika, uunganishaji wa huduma za umeme; bado kuna tatizo gharama ziko juu, usumbufu kwa wananchi ambao tayari wameshaunganishwa na waliokamilisha mchakato lakini bado hawapati umeme, mijini na vijijini bado kuna tatizo. Tanzania ni nchi ya 83, kati ya 190 duniani kushindwa kuunganisha umeme kwa viwango, hivyo naishauri Serikali, iongeze juhudi katika kuwekeza kwenye ujenzi wa mabwawa na umeme wa upepo ili kupunguza pia gharama za umeme.

Mheshimiwa Spika, ukilinganisha gharama za umeme na Mataifa mengine Marekani 0.12, Ethiopia senti 2.4, Afrika Kusini 7.4, Misri 4.6, China na Korea senti 8.0 na Tanzania inalipa zaidi ya senti 10.7 dola kwa unit. Hiki ni kiasi kikubwa tofauti na nchi nyingine na hii inapelekea gharama za uzalishaji kuwa juu, production costs na hivyo kupelekea bidhaa kuwa juu nadhani Serikali ya Viwanda haitafikia malengo kama haitaweza kupunguza gharama hii.