Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Ridhiwani Jakaya Kikwete (90 total)

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kulikuwa na wananchi wa Kata za Oldonyo Sambu, Mlangarini, Bwanani na Nengung’u ambapo Jeshi limechukua maeneo yao na Serikali ikaahidi kwamba ingewafidia.

Je, ni nini sasa kauli ya Serikali kuchukua maeneo ya mashamba haya ya Tanzania Plantation na Nuru Farm ili wale wananchi waweze kufidiwa kama Serikali ilivyowaahidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Shamba la Aghakan lililokuwa chini ya Manyara Estate lilikuwa linaajiri zaidi ya watu 2000 kama ajira; na sasa Aghakan imelichukua shamba hilo tangu mwaka 2006 ikisema itajenga Chuo Kikuu: Sasa ni miaka 16 imepita bila kujenga Chuo Kikuu wala kuajiri wananchi hao.

Je, nini kauli ya Serikali kuhusu shamba hilo kukaa miaka 16 bila kuendelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na fidia ya Jeshi, ni kwamba nitawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Ulinzi ili waweze kutujulisha vizuri juu yah atua ambazo wameshafikia. Tutakapokuwa tumeshapata taarifa za kina, nitakutana na Mheshimiwa Mbunge ili niweze kumpa mrejesho huo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na shamba la Aghakan; mwaka 2017, Mheshimiwa Rais aliagiza Wizara nne zikutane ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje, Ardhi, Fedha na Elimu kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo za Taasisi. Hivyo inalazimika kusubiria utekelezaji wa mpango wa uendelezaji uliokusudiwa kutokana na mazungumzo yanayoendelea kati ya taasisi hiyo na Serikali, mazungumzo hayo kwa upande mwingine yanaratibiwa na Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumepata mrejesho au hatua ya mwisho ya mazungumzo hayo, tutamjulisha na hatua stahiki zitafuata. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kutokana na ongezeko kubwa la wananchi ndani ya Jimbo la Momba kwa baadhi ya vitongoji na vijiji: -

Je, ni lini Serikali kwa kupitia Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili watakaa kwa pamoja ili kugawa baadhi ya maeneo ambayo ni ya hifadhi ili kuwapatia wananchi wa vitongoji vya Mbao, Ntungwa, Twentela pamoja na Kaonga ili wapate sehemu ya kulima kwa sababu wamekuwa kama wakimbizi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Condester, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama mnavyojua kwamba nchi yetu inaongozwa na utaratibu wa sheria, ugawaji wa maeneo yote ni jambo linalofuata kisheria. Nami nimwagize tu au nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huu uanze kwao ili watuletee tuweze kupeleka kwa mtu aliyekabidhiwa mamlaka kugawa vipande vya ardhi katika nchi hii, yaani Mheshimiwa Rais, ili sasa utaratibu mwingine uweze kufanyika. Nashukuru. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Moshi imekuwa ikileta orodha ya viwanja ambavyo wamiliki wake hawajaviendeleza kwa muda mrefu:-

Je, ni lini Wizara itaridhia na kufuta viwanja hivyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Priscus Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi, utwaaji wa ardhi yoyote ni jambo la mchakato na utaratibu huo unaanza katika vikao vyenu kule chini katika Halmashauri yenu.

Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge, waanzishe mchakato huo, walete katika level ya Wizara, tumpelekee Mheshimiwa Rais kwa hatua nyingine zinazotakiwa kufanyika. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto iliyoko Arumeru ya mashamba ambayo hayajaendelezwa iko pia katika Wilaya ya Karatu kwa baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo kutokuyaendeleza na hivyo kufanya mapori ambayo yanahifadhi Wanyama ambao wanajeruhi Watoto na wananchi kwa ujumla.

Je, ni lini Wizara itasimamia hili ili mashamba ambayo hayajaendelezwa yaweze kutwaliwa kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa utoaji wa maeneo umeelekezwa kisheria katika Sheria ya Ardhi Na. 4 na Na. 5 na Kanuni zake nyinginezo. Nataka nimwelekeze Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili kama nilivyoeleza katika majibu mengine ya msingi kwamba hili ni jambo la mchakato, anzisheni mchakato katika maeneo yenu na hatua za kufuatwa juu ya maeneo hayo zitafanyika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza; swali la kwanza kwa kuwa watuhumiwa wengi wanakaa muda mrefu mahabusu na kesi zao zinachelewa kwa sababu ya upelelezi. Ni lini Serikali italeta sheria Bungeni kuweka ukomo wa makosa ya jinai?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa makosa mengi ambayo watu wanakaa muda mrefu kwenye mahabusu hayana dhamana; ni lini Serikali italeta Bungeni sheria ili kuruhusu makosa yote kuwa na dhamana?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Bunge lako limekuwa linafanya marekebisho ya mara kwa mara ya sheria zetu hasa zile zinazohusu Penal Laws na Criminal Procedure Act ambayo kwa kumbukumbu nzuri Mheshimiwa Mbunge katika Bunge la mwezi Februari moja ya sheria inayohusu upelelezi ililetwa hapa katika mabadiliko madogo ya sheria na yako mabadiliko tuliyoyafanya ikiwemo kuruhusu sasa upeleleze ukamilike kwanza kabla kesi hazijapelekwa mahakamani.

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 13 katika issue za presumption of innocence nayo pia imesisitiza juu ya kuwepo kwa haki jinai ambazo zinataka mtu asiukumiwe kwanza isipokuwa kila mtu mbele ya sheria aonekane si mkosefu mpaka pale mahakama itakapodhibitisha jambo hilo.

Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na kuhakikishia Bunge lako lote kwamba Serikali chini ya uongozi wa Rais wetu mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya mabadiliko ya sheria ili kukidhi haki ya jinai kama ambavyo umetaka ifanyiwe marekebisho.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na Mwanasheria Mkuu natambua kwamba mwaka jana tulibadilisha sheria ya kuzuia ukamataji kabla ya kukamilisha upelelezi, lakini jambo hili bado halitekelezeki na ndiyo maana hata hivi karibuni Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amelisemea na amelitolea maelekezo; kwa mantiki hiyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali haioni umuhimu wa kurekebisha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) ili kuweka ukomo wa upelelezi kama ambavyo wenzetu wa upande wa Zanzibar wamefanya na nchi jirani za Kenya, Uganda, Malawi na kadhalika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka masharti nafuu ya dhamana kwa watu ambao hawana mali kwa sababu hivi sasa masharti ya dhamana ni makubwa kuliko makosa hivyo ni kana kwamba tunakomoa wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Neema Lugangira swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu ya msingi wakati najibu swali la Mheshimiwa Enosy Swalle nilieleza hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa inaendelea kuzifanya kuboresha ili dhana nzima ya haki jinai na pia nimeeleza katika Bunge lako kwamba katika moja ya hatua kubwa ambayo imefanyika ni mashirikiano na taasisi mbalimbali zisizo za Kiserikali, Asasi za Kiraia na Taasisi za Dini na Vyuo vinavyotoa elimu ya sheria juu ya andiko lililotolewa kutafuta maoni ya watalaam hawa ili tuweze kufikia sehemu ya kujadili mambo yote ya msingi yanayoambatana na issue za haki jinai.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zetu zipo wazi kabisa juu ya masuala ya haki jinai na katika eneo hilo la haki jinai ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tuna pande mbili kuna wanaotenda jinai na wanaotendewa jinai. Sasa kama mpango mzima utakuwa ni kuwatetea waliotenda jinai uelewe upande wa pili kuna waliotendewa jinai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tulikuwa tuna tatizo la panya road, sasa inasemwa hapa kama vile polisi wasikamate mpaka upelelezi upatikane na ndiyo maana tulipotunga hii sheria mwaka huu nafikiri tuliweka wazi kwamba kwa baadhi ya makosa ya kawaida ambayo hauoni sababu ya haraka ya kwenda kumkamata mtu kama upelelezi haujakamilika tunaweza tukasema yawe hivyo, lakini kwa kweli ni lazima tujue kwamba watu wanaotendewa makosa ndiyo wanaotakiwa kuonewa huruma zaidi na kusaidiwa kuliko wanaotenda makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niombe rai kwamba twende hivyo kwasababu kwa kufanya hivyo ndiyo maana nchi ipo salama hata leo hii. Vinginevyo tukibadilisha jurisprudence hapa tunaweza tukaharibu kabisa haki jinai ikawa ni tatizo, lakini haki jinai inapande mbili. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo inadaiwa viwanja takribani 1,000 na pia hao wananchi wa Makurunge hawana sehemu ya kukaa ambayo ipo sahihi.

Je, ni lini Serikali au Wizara itawapatia Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mashamba mawili ambayo ni Greenwood na Jeneta ambayo umiliki wake ni wa utata ili kuweza kuwasidia wananchi hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri ni lini anaweza akaja Bagamoyo ili kuja kuyaangalia yale mashamba ya Greenwood na Jeneta ili atoe tamko la Serikali kuhusu umiliki wake yale mashamba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, juu ya shamba la Greenwood na Jeneta nadhani taratibu za kisheria zinaeleza na wananchi wa Bagamoyo wanatakiwa wafuate hizo taratibu kama kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo ili kama Serikali itajiridhisha juu ya maombi yao na kama ninavyosema kwamba kutakuwa na utata wowote basi tutaangalia kuona jinsi gani tunaweza kuliamua.

Mheshimiwa Spika, juu ya suala la pili, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie tutakamaliza Bunge hili katika kipindi nitakachokuwa kwenye ziara katika Jimbo langu litakuja Bagamoyo ili tuweze kushughulikia kero hiyo. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; baadhi ya wananchi waliovunjiwa nyumba hizi tayari walikuwa na hati ambazo zilikuwa zimetolewa na Serikali. Sasa je, Serikali haioni imefanya maonezi makubwa kwa kuwavunjia wananchi ambao tayari walikuwa na hati zilitolewa na Serikali yenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili nataka kujua sasa ni lini Serikali itatoa viwanja mbadala kwa wananchi hao ili kutokuwaumiza kama walivyofanya sasa? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la hati miliki pia kuhusiana na suala la pili la viwanja mbadala kwa kuwa jambo au shauri hili liko mahakamani, ningeomba tuwe na subira na tutakapopata mwongozo wa mahakama tutakuja kueleza hatua zinazofuatia.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kutokana na mabadiliko ya tabianchi mipaka mingi ya asili baina ya mikoa na mikoa, wilaya na wilaya, kata kwa kata, vijiji kwa vijiji, vitongoji kwa vitongoji imebadilika sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kubadilisha sasa Mipaka hiyo ili iwe sawasawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali letu la pili. Je, ni nili huo mradi wa Korea utaanza?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Ritta Kabati kwa niaba ya Mheshimiwa Angelina Malembeka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusiana na jambo la tabianchi, ni kweli ipo baadhi ya mito ya asili ambayo imekauka hivyo kusababisha migogoro katika baadhi ya maeneo. Hata hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na kulihakikishia Bunge lako kwamba Serikali imeshafanya zoezi la kutambua na kuchora ramani za mikoa hiyo, hivyo suala hilo litakapokuwa limetokea zipo hatua ambazo zimeshachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, juu ya ni lini mradi utaanza, nataka kulihakikishia Bunge lako kuwa, pale tutakapokuwa tumeshaandaa taratibu zote, ikiwemo kuweka ofisi na kupata wataalam wakaosimamia zoezi hilo, zoezi hilo litaanza.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwa kweli vijiji hivi kama majibu ya msingi yanavyosema; ni kweli upimaji huu ulifanywa lakini walio wengi wanaolalamika ni kwamba upimaji haukuwa shirikishi. Kwa mfano, kuna mgogoro wa Mkutano na Kikunyungu, Kipelele, Nangumbu au Ngongowele na Ngunja. Wanachozungumza pale ni kwamba yale mawe wakati wanabeba kuna mahali walichoka wakayatunza mahali. Matokeo yake hawakurudi pale, kwa hiyo, yule aliyekuja kuchukua a-coordinate majira ya nukta akachukulia pale. Kwa hiyo, hicho ndiyo chanzo cha migogo mingi kwenye hivi vijiji ambavyo nimevitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna mgogoro kati ya Wilaya ya Kilwa na Wilaya ya Liwale kwenye Vijiji vya Nanjilinji na Milui. Mgogoro wake scenario yake inafanana na hiyo hiyo, kwamba wakati wanapima wakazi wa wilaya hizi mbili zote hawakushirikishwa. Sasa Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kufuatana nami baada ya Bunge hili twende Liwale akatatue migogoro hii?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya changamoto iliyotokea ni kweli yako baadhi ya maeneo ambayo yana changamoto hizo. Nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge tutapanga ziara twende tukakutane na wananchi wake ili kumaliza kero katika maeneo yake. Ahsante.
MHE. EMMANUEL KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ina vijiji 62; na katika mpango wa Land Tenure Support Programme, vijiji 30 tu vilifanyiwa kazi: Je, ni lini Serikali inakwenda kukamilisha kazi hii ya vijiji 32 vilivyobaki?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari mara baada ya Bunge hili kuambatana nami kwenda kufanya ziara ndani ya Jimbo langu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Kunambi maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza naomba kukiri mbele ya Bunge lako kwamba kweli ule mkakati ulipofanyika mara ya kwanza, yaani ile programme ya LSTP ulipita katika vijiji 32 ndani ya Halmashauri ya Mlimba ambayo ina vijiji 62. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumeshatenga fedha, basi tutakwenda kwa ajili ya kumalizia vijiji hivyo vilivyobakia kwa sababu programme hii ili kuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, la pili nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge kwisha tutakwenda pamoja katika Halmashauri yake ili Kwenda kujadili siyo tu matatizo haya ya mipango ya matumizi bora ya ardhi, lakini pia na kutatua kero nyingine zinazoendelea katika maeneo ya matumizi ya ardhi. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Ni ukweli usiopingika kwamba migogoro ya ardhi imekuwa ikileta changamoto kubwa ikiwemo maafa na pia udumavu wa uchumi wa Taifa letu: Je, Serikali haioni sasa ni wakati umefika wa kuipanga ardhi kuitambua kwamba hii ni ardhi ya kilimo, hii ni ardhi ya mifugo na matumizi mengine kwa Taifa letu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Kunti Majala, swali lake la nyongeza juu ya utaratibu wa kutambua ardhi za Tanzania. Naomba kwanza nimrudishe Mheshimiwa Mbunge katika Sheria zetu zinazoongoza usimamizi yaani Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5 ambazo zinatambua uwepo wa mgawanyo huu ambao yeye ameusema.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, pia Wizara imeendelea kufanya semina mbalimbali na elimu mbalimbali kwa wananchi ili kuweza kuwatambulisha. Pia ziko hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na ufahamu juu ya mgawanyiko wa maeneo ya ardhi ikiwemo kufanya hatua kubwa za kuelewesha Umma wetu kwa jumla yake. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa ni ukweli pamekuwa na migogoro mingi sana kwenye Jimbo la Kibamba kuhusiana na kutokamilika kwa urasimishaji, sasa je, Serikali ina mkakati gani kumaliza kabisa migogoro hii inayohusiana na urasilimishaji kwenye Jimbo la Kimbamba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mtemvu kwamba kama ambavyo nimeeleza katika swali la msingi kutoka kwa Mbunge Kunambi, hatua hizo ambazo zimechukuliwa kule Mlimba ndiyo ambazo pia zinaendelea kuchukuliwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kama nilivyoeleza; kuendelea kutoa elimu na kuendelea kuhakikisha Halmashauri zetu zinaendelea kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwemo mipango iliyowekwa na kushirikisha wananchi katika kuweka taratibu za ardhi katika maeneo yao.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini Wizara yake itaridhia upanuzi wa Mji wa Moshi kufikia kilometa za mraba 142 ukizingatia sasa hivi tuna kilometa za mraba 58 na maombi yako ofisini kwao; na hata damp tumenunua Moshi Vijijini na makaburi yanajaa, tutahitajika tena kununua pia?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Priscus Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli maombi ya Mheshimiwa Priscus yalifika katika Ofisi zetu, lakini kama inavyofahamika mwenye mamlaka ya kuongeza maeneo ya kiutawala ni Mheshimiwa Rais. Hivyo, maombi yake tuliyapeleka katika ngazi husika na majibu yatakapokuwa yametolewa tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa jicho lako kuniona. Naomba katika Halmashauri yangu ya Mkalama, Kata ya Matongo Kijiji cha Mnung’una yuko mwananchi mmoja ambaye amechukua ardhi ya wananchi karibu ekari 400; na hata baada ya matumizi bora ya ardhi ameendelea kukaidi: Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kama yuko tayari kufuatana nami ili kwenda kuondoa tatizo hili ambalo ni kubwa sana kwa wananchi wangu wa Matongo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Francis kwamba niko tayari kuongozana naye kwenda kuzungumza juu ya mgogoro huu ambao unakabili vijiji vyake katika eneo hilo la Kata ya Matongo.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi unaohusu wananchi wa Kata ya Malula na Majengo walioko katika eneo linalozunguka uwanja wa KIA?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Pallangyo, Mbunge wa Arumeru, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tutakapokuwa tumemaliza Bunge hili, nitaomba kuongozana pia na Mheshimiwa Pallangyo ili twende tukazungumze na wananchi wale tuweze kujua undani wa tatizo lenyewe na baada ya hapo tuweze kutafuta suluhu ya pamoja katika kuleta maendeleo katika maeneo yetu ya Arumeru. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza niikumbushe Serikali kwamba, kuna eneo la Soga kwenye shamba la Mohamed Enterprise tayari kulishakuwa na maelekezo ya ekari 500 kurudi Serikalini. Kwa kuwa, kuna changamoto mbalimbali zinazoendelea kusababisha kutokutekelezwa kwa agizo hilo.

Je, Waziri atakuwa yupo tayari kuambatana nami mara baada ya Bunge kwenda kusaidia kuondoa hizo changamoto zinazosababisha utekelezaji wa agizo hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, pale Kata ya Kikongo kuna mwekezaji anaitwa Trans-continental na shamba moja la UFC ambalo lipo mikononi mwa Serikali, kuna wananchi ambao wapo pale muda mrefu, wana miaka mingi, karibu 15 mpaka 20, na wawekezaji hao hawajaendelea.

Je, Serikali inatoa tamko gani kuwaruhusu wawekezaji hao kuendelea na shughuli zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na suala la Soga kwenye shamba la Mohamed Enterprise naafikiana nawe Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kutatua kero hizi maana tunaambiwa yanayoendelea huko siyo mazuri sana.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kuhusiana na jambo la trans- continental kule Kikongo na Waya mifugo, Mheshimiwa Mbunge nataka nikuhakikishie utayari wa Serikali, kwenda kushirikiana nawe kutatua kero hizi. Pili, katika Shamba la Waya, tutashirikiana na Wizara ya Mifugo kuhakikisha kwamba hatua zinazostahiki kufuatwa ili kukabidhiwa shamba hilo kama ambavyo Serikali iliamua nazo pia zinafuatwa. (Makofi)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Namshukuru Mheshimiwa naibu kwa Majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, naomba kutaka kujua, kwa kuwa watu wa Aga Khan kwa maana ya Taasisi ya Aga Khan wanasema kwamba ninyi Wizara ya Ardhi pamoja na Wizara nyingine Tano ikiwemo Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, mnazuia wao wasiendeleze shamba hilo kwa kuwa kuna jambo ambalo hamkulifanya ili waweze kuendeleza shamba hilo. Nini kauli ya Serikali kuhusu taasisi hiyo?

Swali la pili, ni lini utatembelea shamba hilo ili kujua wazi dhahiri shahiri kwamba kuna nini juu ya jambo hilo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO
YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nitoe taarifa kuhusu shamba hili la Aga Khan. Shamba hili wakati linaombwa mwanzo liliombwa kwa ajili ya kilimo, lakini kutokana na maendeleo ya ukuaji wa Mji wa Arumeru Magharibi ikalazimika matumizi ya shamba lile yabadilike na kuwa eneo la kupanga Mji kwa maendeleo ya maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo kumetokea changamoto baina ya maeneo ambayo yanaendelezwa na hii Taasisi ya Aga Khan na Serikali, hivyo ndivyo mgogoro anaouzungumza Mheshimiwa Mbunge ulipoibuka. Maelekezo ya Serikali ni kwamba, punde tutakapo maliza mazungumzo hayo taratibu nyingine kwa ajili ya uendelezaji zitaendelea.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, swali lake la pili ulikuwa umeshalijibu?

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ombi la kwenda kuona shamba hilo ili kuona maendeleo mengineyo. Natoa ahadi kwamba niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge ili kuona na kufuatilia yanayoendelea katika shamba hilo.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.

Kwa kuwa, ripoti ya sensa ya sasa ya mwaka 2022 imeonesha wazi kwamba ongezeko la watu ni zaidi ya Milioni 16 katika kipindi cha miaka Kumi, hii imeshabihiana sana na wananchi wengi wasio na ardhi kuvamia mapori yasiyo endelezwa kwa miaka mingi.

Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kufanya tathmini upya ili yale maeneo ambayo hayajaendelezwa na wananchi wako mle wamejenga waweze kurasimishwa rasmi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwangu mimi na upande wa Serikali ninaamini ushauri uliotolewa na Mheshimiwa Mtemvu Mbunge ni jambo nzuri na ni jambo la kufanyiakazi nasi ndani ya Wizara nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tumekwishapokea taarifa ile ya sensa na ndani yake yako mambo mengi sana ikiwemo kuangalia jinsi gani Serikali sasa inaenda kuondokana na maeneo ambayo hayajapangwa vizuri lakini pia kurasimisha maeneo ambayo yameiva kwa ajili ya urasimishaji.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa zaidi ya miaka Sita wananchi wa Korogwe wanalia na shamba la Mwakinyumbi lililotelekezwa na Serikali imekuwa ikituahidi lakini hakuna matokeo. Mheshimiwa Waziri ni nini sababu inayoifanya Serikali ishindwe kulifuta shamba la Mwakinyumbi na kuwarudishia wananchi wafanye shughuli za uzalishaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mnzava Mbunge wa Korogwe swali lake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli juu ya shamba hilo ambalo limetajwa na Mheshimiwa Mbunge taarifa zimeshafika Wizarani na taratibu za kiutawala kwa ajili ya kulitwaa shamba hilo na kulirudisha kwa wananchi zinaendelea na tutakapo kuwa tayari tutakupa taarifa za kina juu ya jibu la maombi ya wananchi wa Korogwe.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante; je, Serikali ina mikakati gani endelevu ambayo itakuwa imejiwekea ili kuepusha migogoro hii ambayo inapelekea wananchi wetu kuuana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni hatua gani zinachukuliwa na Serikali kwa wale wanaobainika kusababisha migogoro hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kufanya jitihada mbali mbali za kuhakikisha kwamba ina suluhisha migogoro hiyo ikiwemo kuendelea na programu za kupanga, kupima na kumilikisha lakini pia kuendelea kupanga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha mipango yote inaendelea kupangwa katika maeneo hayo.

Pia, kushirikiana na mamlaka za upangaji, tumeendelea kuelimishana na kupanga bajeti kuhakikisha kwamba maeneo yote vijiji yanaendelea kupimwa na kupangwa ili kuondoa malalamiko ya wananchi ikiwemo migogoro hii inayoendelea katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali la pili lililoulizwa na Mheshimiwa Maimuna Pathan, juu ya hatua gani zinazofanyika kwa wale ambao wanaendelea kufanya fujo, jeshi letu la polisi limejidhibiti katika kuhakikisha kwamba watu wote wanaofanya matatizo au kuendeleza fujo katika maeneo yetu wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea majibu ya Serikali lakini sheria ilivyo sasa inaelekeza kwamba ujenzi au uendelezaji uanze ndani ya miaka mitatu lakini sheria hiyo haitoi ukomo ni lini majengo hayo yamalizike kujengwa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuleta sheria ambayo itaweka ukomo katika uendelezaji wa majengo na wale ambao watakaidi waweze kupata adhabu kwa kuchelewesha ujenzi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pil, ni nini kauli ya Serikali hasa katika uendelezaji wa majengo ya miradi ya taasisi za umma kama vile NSSF, PSSSF na National Housing ikiwemo suala la majengo yale ambayo yametelekezwa kama vile Hotel Embassy, Motel Ajib kule Dar es Salaam na mengineyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba Abbas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na sheria inazungumza vipi juu ya yale majengo ambayo hayajaendelezwa; kwanza nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya sheria ya Ardhi inayohusu uendelezaji, inamtaka muendelezaji au mtu anayepewa milki aendeleze ndani ya miaka mitatu, ni kweli lakini wako baadhi ya watu wamekuwa wanafanya kazi ya kuanzisha ujenzi ndani ya miaka mitatu na kwa sababu sheria hiyo imetoa ombwe katika lini anatakiwa amalize.

Mheshimiwa Spika, ushauri wako ulioutoa tunauchukua Mheshimiwa Mbunge na ndani ya Wizara tumeendelea kufanyia kazi na itakapofika punde tutakuja kuwasilisha mbele ya Bunge lako ili Waheshimiwa Wabunge, wapate kujua sasa ni kipande gani au mwaka gani mtu anatakiwa kumaliza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, juu ya Serikali inaendelezaje majengo yaliyosimama, maelekezo ya Serikali ni kwamba majengo yote ambayo hayajaendelezwa yaendelezwe ili yaweze kukamilika yasije yakatumika kwa matumizi yasiyofaa. Juu ya Shirika la National Housing, hasa in particular, Serikali imekwishaelekeza juu ya shirika hilo liweze kukopa na mwanzo lilikopa shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya uendelezaji na sasa tupo katika mazungumzo na wenzetu wa Hazina ili tuweze kukopa katika kipande kilichobakia ili tuweze kumalizia sehemu iliyobakia katika majengo mengine.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, napenda kupata ufafanuzi, mwaka 1974 mpaka 1980 kulikuwa na program ya Serikali kupitia Wizara ya Mifugo ya kuwasaidia wanakijiji wa Kijiji cha Mekomariro kunenepesha mifugo yao, na baada ya miaka hiyo Serikali ikaacha maeneo hayo. Ni miaka 43 sasa maeneo hayo yanatumiwa na wanakijiji, na eneo lililokuwa linatumiwa na Wizara ya Mifugo halina hati wala halina GN. Ni kwa nini sasa wananchi wenye maeneo hayo bado wanasumbuliwa na Serikali kwamba eneo hilo ni la Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna maeneo ya migogoro ya Mekomariro, Sirorisimba na Lemololi Mahanga, Ng’oroli na Mahanga, ni lini Serikali itaenda kuwasaidia maeneo hayo kuyapima na kuyapa hati za kimila? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili yaliyoulizwa na Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la shamba la kule Mekomariro ambalo linaonekana halina hati, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo halina ukweli wowote kwa sababu shamba lile tunavyofahamu Serikali, linayo hati. Ila tunatambua ukweli kwamba upo mgogoro baina ya shamba hilo na wananchi katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili juu ya lini sasa Serikali itaenda kumaliza jambo hilo? Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kumaliza kujibu maswali hapa, tutakaa mimi na yeye sasa tukubaliane ni lini twende katika eneo hilo ili kumaliza yale ambayo yanaendelea kuleta mgogoro katika eneo hilo.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwulize Naibu Waziri wa Ardhi, Serikali inapeleka lini fedha za upimaji wa ardhi katika Halmashauri ya Ushetu hasa katika kata zinazokua kwa kasi; Kata ya Igwamanoni, Kata ya Idahina, Nyankende pamoja na Burungwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maombi ya wananchi wa Ushetu juu ya kupimiwa eneo lao yalishawalishwa kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, tutakapokuwa tumeshapata fedha hizo, tutaleta fedha Ushetu ili sasa maeneo yale yaweze kupimwa, kupangwa na kumilikisha wananchi wetu ili maendeleo yaweze kupatikana kama ambavyo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka pengine nitoe ufafanuzi kuhusiana na hizi pesa ambazo halmashauri zinaomba kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha. Naomba watambue, fedha aliyotoa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ile Shilingi bilioni 50 inakwenda kwenye Halmashauri kulingana na maandiko wanayotoa. Fedha ile inakwenda kusaidia kwenye Halmashauri ambazo ndiyo zenye mamlaka ya Upangaji. Kwa hiyo, tunategemea ile pesa isihesabike kama ndiyo fedha inayokwenda kukamilisha kazi, isipokuwa Halmashauri zinatakiwa kutenga fedha ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya ardhi. Kwa hiyo ile isihesabiwe kama ndiyo fedha ambayo inategemewa sana katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mamlaka za Upangaji, sisi tuna-support kuongeza kile ambacho ninyi mmetenga kwa ajili ya maendeleo ya Ardhi na siyo kwamba tunatoa bajeti kwa ajili ya ku-fulfill mpango mzima wa kupanga katika maeneo yenu.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Kwa kuwa Mvomero ni miongoni mwa Wiliya ambazo bado zina changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji: Je, Serikali inamkakati gani wa kuendelea kuyafuta mashambapori yaliyopo Mvomero ili muweze kuwagawia wananchi na kupunguza tatizo hili la migogoro ya wakulima na wafugaji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Mvomero bado tuna migogoro ya ardhi pamoja na kwamba imepungua.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami baada ya Bunge hili kwenda kutatua migogoro hii Mvomero? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Zeeland Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na jambo la mashamba, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilishakagua mashamba 75 na katika hayo, mashamba 15 yalishatolewa ilani ya kuendelea kufuatiliwa katika maana ya kufutwa au kuona utaratibu mwingine wowote, utakaofanyika. Katika hatua hizo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale tutakapokuwa tumekamilisha taratibu nyingine zote tutamjulisha kwa niaba ya wananchi wake ili aweze kujua hatua Serikali ilizochukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kuongozana mimi naye kwenda Jimboni kwa ajili ya kutatua migogoro hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari baada ya hapa, kwa sababu ni njia ya kwenda Jimboni kwangu, nami nitasimama Mvomero pale tuweze kutengeneza mambo mazuri ili kuweka hali ya usalama na watu wetu wakae vizuri.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, ila napenda kufahamu kwamba: Je, Mheshimiwa Waziri haoni sasa ni muda muafaka wa kufanya ziara Ludewa kwenda kutembelea hizo kazi na kugawa hati zile za mwanzo kwa wananchi ili kuongeza hamasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mbunge kwamba umuhimu huo tunauona ndani ya Wizara na niko tayari sasa kuongozana naye baada ya Bunge kwenda kukabidhi ardhi zilizogaiwa ili kutengeneza hamasa kwa wengine waweze kujitokeza kwa wingi.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu na ni kero kubwa kwa wananchi wa Ng’ang’ange; je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kufanya ziara katika kijiji hicho ili kuweza kutatua hiyo kero kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza linaloulizwa kwa niaba ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mbunge kwamba kwa kuwa tumepanga ziara ya Mkoa wa Iringa, ambayo tutataka tutembelee majimbo yote na Halmashauri zote za Iringa, niko tayari pia kufika Halmashauri ya Kilolo ili kwenda kukutana na wananchi tuzungumze na kumaliza mgogoro huu. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali ina mpango gani wa kuwarudishia mashamba wananchi waliodhulimiwa na taasisi ya EFATHA Kijiji cha Moro, Msandamungano na Mpwapwa, vilivyopo Wilaya ya Sumbawanga Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mgogoro uliopo baina ya vijiji hivo vilivyotajwa na Shirika la Efatha Ministry ambapo katika kuhangaika nalo, tunatambua kwamba zipo kesi zinazoendelea na nyingine ambazo zimeshaamuliwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tunafanya ziara ya Nyanda za Juu Kusini, tutafika na eneo la Rukwa ili kuzungumza na wananchi na kutatua mgogoro uliopo.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri, lakini pia nimshukuru kwa kutupa milioni 2008. Kama unavyojua Wilaya ya Lushoto ni kubwa sana. Kwa hiyo, milioni 208 ni fedha chache sana. Swali la kwanza, je, Serikali haiona sasa kwamba kuna haja ya kuongeza fedha zile angalau zifike hata bilioni moja ili kumaliza upimaji katika Wilaya ya Lushoto?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; takwimu za nchi nzima zinaonesha kwamba ni asilimia 25 tu ya sehemu ya ardhi ndiyo iliyopimwa katika nchi hii ya Tanzania. Je, haioni Serikali kwamba inasuasua sana kwa suala hili la kupima na kuleta migogoro ndani ya nchi hii. Sasa Serikali ina mpango gani au ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha kwamba inatenga bajeti ya kutosha na kupima ardhi hii nchi nzima ili kuondoa migogoro ndani ya nchi hii ya Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu maswali ya nyongeza Mheshimiwa Shekilindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali imeendelea ku-support hatua mbalimbali zanazofanywa na halmashauri zetu kuhakikisha kwamba miradi au maeneo yetu yanapimwa. Katika kufanya hivyo Serikali imepata mkopo wa dola milioni 150 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umilikishaji wa ardhi ambapo katika moja ya mambo makubwa yanayoenda kufanyika ni kuendelea kupima na kupanga ardhi ya Tanzania. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kwamba anaona fedha hizi hazitoshi lakini mipango kwa ajili ya kupima Tanzania nayo pia inaendelea.

Mheshimiwa Spika, pili, katika ardhi ya Tanzania, takribani asilimia 20 ya maeneo ya Tanzania yamepimwa ambapo viwanja zaidi ya 2,800 na mashamba zaidi ya 28,000 yamekwisha tambulika. Hivyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi linaendelea kufanyika na ni mipango na maelekezo ya Serikali kuhakikisha kwamba ardhi yote ya Tanzania inapimwa. Ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza; la kwanza, je, Serikali inatambua kwamba tabia hii inafanyika katika jimbo langu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Je, Serikali sasa iko tayari kulifanyia kazi hii ili kuondokana na tatizo hili kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali inatambua juu ya tabia za baadhi ya viongozi au wananchi wanaoshiriki katika kuhakikisha kwamba wanawanyima watu haki zao. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba kwa kutambua hilo Serikali imejidhatiti kuhakikishi kwamba inachukua hatua zote husika na pale inapotokea wananchi wanashindwa kwenda kushtaki basi na sisi pia kama wawakilishi wa wananchi tunaruhusiwa kufikisha vilio katika ofisi hizo mbili ikiwemo mkurugenzi na ofisi ya makamu wa pili wa Rais kama nilivyoeleza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba haki za watu wote wanaostahiki kuingia katika mfuko wa TASAF zinapatikana.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, zoezi la TASAF, kwa maana ya kukwamua familia maskini ni zoezi zuri. Huko nyuma lilikuwa liko kwenye package ya kuwalipa tu kwa ajili ya kuwasaidia kwenye mambo mbalimbali; sasa kumeongezwa package ya kuwapa hadhi halafu wanalipwa. Lakini maeneo mengi tumeanza kuona wazee wetu…

SPIKA: Swali lako Mheshimiwa Mtaturu.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, tumekuwa wazee wetu wakitumikishwa wanafanya zaidi ya miaka 60 kitu ambacho sio kizuri katika maeneo yetu; je, Serikali inasemaje kuhusu jambo hili?

SPIKA: Ngoja kabla sijaiambia Serikali nataka nikuelewe wewe kwa hiyo ni jambo bayo kufanya kazi na kulipwa? Yaani uliza swali lako vizuri ili Serikali ijue inakujibuje, ni jambo bayo wale maskini kuambiwa wafanye kazi halafu walipwe?

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, si maskini watu wazee zaidi ya miaka 70 wanafanya kazi ya kuchimba mitaro, kutengeneza barabara, ambayo package hiyo ilikuwa inalenga kwa ajili ya vijana ambao wanatoka kwenye familia maskini swali langu ndio hilo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Mtaturu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika baadhi ya maeneo malalamiko haya yamekuwepo. Sisi kama Serikali tumekwishatoa mwongozo na huo ndio mwongozo unaoongoza shughuli za TASAF; kwamba wazee wote walio juu ya miaka 60 na akina mama wajawazito pamoja na watoto wadogo hawaruhusiwi kufanya kazi katika mazingira hayo ambayo yeye anayasema. Isipokuwa Serikali, na sheria vinaelekeza kwamba vijana wenye nguvu watafanya kazi kwa niaba ya wazee hao. Na kama itatokea kwamba mzee amelazimishwa basi sheria itafuata mkondo wake katika kuchukua hatua za msingi. (Makofi)

SPIKA: Sasa hayo maelezo ni ya jumla najaribu kuwaza mzee kama anao uwezo wa kufanya hiyo kazi halafu anyimwe; nadhani pengine huo mwongozo wa Serikali utazame. Kuna wazee kweli hawawezi kufanya kazi lakini wapo wazee wanaweza kufanya kazi na kama ameenda yeye kuomba hiyo kazi hoja ya kulazimisha ndiyo shida. Kama yeye ndio alienda kuomba kazi ni kwamba hiyo kazi angeweza kuifanya sehemu nyingine. Na hata humo ndani kuna wazee ambao wanaweza ubunge, wako wazee wanapewa mikataba hata Serikalini, sasa tukiweka kwa jumla namna hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri hii inakaaje?

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Serikali naomba nitoe maelezo mafupi juu ya jambo hili.

Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Serikali unataka wazee walio juu ya umri wa miaka 60 wasipewe kazi hizo kwa sababu ya ugumu wake; lakini inapotokea kwamba mazingira hayo yapo mwongozo unawaongoza kwamba wachukuliwe vijana ambao ndani ya kaya ile anayetoka huyo mzee ili wafanye kazi kwa niaba ya yule mzee. Sasa kumekuwa na incidence ambazo vijana wanakataa kwenda kufanya kazi au wakati mwingine wanawakatalia wazee wao kufanya kazi, kwa hiyo mzee kwa kutambua kwamba kuna hela ataikosa anaamua mwenyewe aende kufanya kazi hiyo. Sasa haya ni mazingira yaliyopo, lakini sisi kama Serikali tumeweka sheria na miongozo ambayo iko very strict, kwamba mzee aliyezidi miaka 60, mama mjamzito, mtoto chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kufanya kazi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, swali langu linataka kufahamu kimsingi kwamba taasisi kubwa za nchi yetu, kwa maana ya Mahakama, Bunge na executive ya president, wale viongozi wakuu na wenza wao wanapokuwa madarakani wanaanzisha taasisi ambazo zinafanya makubwa katika nchi yetu. Taasisi hizo zinaaminika duniani zinapata fedha nyingi katika nchi yetu. Wanavyoondoka madarakani hakuna mfumo mzuri wa kiserikali wa kuziendeleza taasisi hizi. Kwa mfano Mkapa Foundation, WAMA, Tulia Trust leo inafanya makubwa lakini ukiondoka inapotea, Mama Magufuli alikuwa na taasisi ya wazee hatumwoni Mama Magufuli akiendeleza taasisi ya wazee.

Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali viongozi hawa wanapotoka madarakani kuna utaratibu gani wa kuendelea kusaidia taasisi hizi kubwa kama nchi zilizoendelea, tunavyoona Jimmy Carter leo inaweza kuwa January Makamba. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, swali alilouliza Mheshimiwa Abubakari Asenga Mbunge ni swali zuri; lakini kwa kuwa hadi hapa tunapozungumza sasa hakuna sheria wala mwongozo wowote unaotutaka sisi kufanya kazi au kupeleka kibajeti juu ya hizo taasisi za wenza wa viongozi naweza kusema kwa namna moja au nyingine kwamba hatuna la kufanya kwa sasa hivi. Hata hivyo, kama mawazo yako yatakuwa mazuri tutaangalia, lakini kuchukua fedha za umma kupeleka kwenye taasisi za watu binafsi hili jambo halijakaa sawa.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini katika Mkoa wetu wa Katavi changamoto bado ni kubwa sana. Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika vituo vya afya pamoja na Hospitali za Wilaya, lakini hospitali hizo zinashindwa kufanya kazi kama hadhi ya Hospitali ya Wilaya na badala yake kufanya kazi kama zahanati kutokana na upungufu mkubwa sana wa watumishi katika hospitali zetu za Wilaya za Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nijue, zipi hatua za haraka za Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaweza kupata watumishi ili waweze kupata huduma zilizo bora? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Katavi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatambua upungufu uliopo katika hospitali ndani ya Mkoa wa Katavi, lakini katika kupitia utaratibu ambao Serikali imeuweka kupitia mifumo ambayo tumeianzisha ndani ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, ambapo mojawapo ni pamoja na HR Assessment System, tumeweza kugundua hilo tatizo. Pia kwa kupitia mifumo ya upangaji wafanyakazi, tumeshaliona jambo hilo na ndiyo tumeahidi kupitia bajeti hii inayokuja ambayo tutawasilisha mbele ya Bunge lako hapa, kwamba hilo jambo la upungufu wa watumishi katika Mkoa wa Katavi nalo pia ni moja kati ya jambo tunalokwenda kulishughulikia.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa watumishi wengi wanaojitolea wamefanya kazi ya ziada, na kila mara ajira zinapotoka hawa wanaojitolea huwa hawapewi nafasi ya kupewa ajira: Je, Serikali mna mpango gani wa kuwasaidia wale wanaojitolea katika nafasi za Ualimu na Unesi waweze kupewa nafasi hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge wa Tanganyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anayoyasema kwamba kumekuwa na watu wanaojitolea lakini wakati mwingine inapotokea ajira zimefunguliwa wanapata matatizo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwongozo wa ajira katika nchi yetu unataka ajira zote ziwe katika ushindani. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama watafuata taratibu zilizowekwa, hatuna tatizo katika jambo hilo.

Mheshimwia Mwenyekiti, ni kweli kwamba tatizo la upungufu wa walimu na kada nyinginezo katika utumishi wa umma ni jambo ambalo tunalijua na Serikali imeendelea kulishughulikia jambo hilo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufanya hivyo kama ambavyo tumeahidi na katika bajeti yetu tunakuja kusoma hapa hivi karibuni ya mwaka 2023/2024, majibu yote atayapata.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Katika Halmashauri ya Lushoto yenye shule za msingi 180, ina uhaba wa walimu takribani 1,400, hali inayosababisha sasa angalau wastani wa shule moja kuwa na walimu wanne tu: Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuhakikisha kwamba inakwenda kuboresha ikama katika Halmashauri ya Lushoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upungufu upo kama nilivyokiri katika jibu la msingi, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo la ikama la mahitaji ya walimu au madaktari au kada zozote katika maeneo yetu linaanza kwenye mchakato ndani ya Halmashauri zetu. Kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Halmashauri yake ya Lushoto ilete mahitaji hayo, nasi kama Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, tutalichukua jambo hili na kwenda kulifanyia kazi na tutakapopata kibali cha ajira, basi tutahakikisha kwamba tunampelekea wafanyakazi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anahitaji.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Samahani sana, naona hata majibu yaliyotolewa hayana uhalisia kabisa. Nafasi tano kwa wapishi nchi nzima na nafasi 200 za makatibu muhtasi kwa ajili ya shule ya sekondari. Katika maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema pia eneo hili la ajira kwa halmashauri zimepewa nafasi. Hakuna Halmashauri hata moja nchini inaajiri kada hizo.

Mheshimiwa Spika, maswali yangu madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa wazazi wengi nchini wamebeba mzigo mkubwa wa kulipa michango kupitia watumishi hawa ambao wanalipwa kwa michango ya wananchi; na kwa kuwa katika shule zetu familia moja inaweza kuwa na watoto wawili, watatu mpaka wanne, Serikali haioni kuwa ni wakati muhimu na muafaka wa kuweza kuongeza ikama ya ajira hii kwa ajili ya watumishi hawa ili kupunguza mzigo kwa wazazi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika kibali cha ajira kilichotolewa juzi Serikali haikutoa kipaumbele kwa ajili ya Walimu wa kada ya kilimo…

SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, je, ni kwa nini Serikali haiweki kipaumbele kutoa kibali kwa Walimu wa mchepuo wa kilimo ili vijana wetu waweze kupata stadi za klimo kutoka shule za sekondari nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu tulizotoa ni takwimu sahihi na usahihi wake unakuja kutokana na ukweli kwamba, Mheshimiwa Mbunge ajira hizi zinatokea kwenye halmashauri zetu. Halmashauri ndizo zinazoomba na sisi kama Ofisi ya Rais, Utumishi, tunapokwenda kuomba Kibali tunaomba kwa ikama iliyoombwa tukiangalia na Bajeti ambayo imepitishwa na Bunge lako. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwanza apate kufahamu kwamba kilichoelezwa hapa ni kutokana na taarifa zilizoombwa kutoka katika maeneo yetu ya halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, pia pamoja na hilo tunakubaliana kiukweli kwamba hitajio la kuongeza ikama kwa ajili ya ajira hizi ambazo zimeelezwa ni jambo la msingi na sisi kama Serikali tumelisikia. Pia nimwombe tena Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako, tunapokwenda kutaja vipaumbele vya maeneo yetu ya kiutawala kwa maana ya halmashauri, basi tuangalie kwamba hii ni sehemu moja wapo ya eneo muhimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili, juu ya walimu wa mchepuo wa kilimo. Ameeleza hapa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, wakati anatoa taarifa juu ya idadi ya nafasi za ajira zilizotolewa, iko nafasi ya ajira za Walimu, ziko nafasi za eneo la afya. Katika eneo hili la elimu naamini kabisa kama kipaumbele ndani ya halmashauri zetu kitaainishwa wazi, kwamba tunahitaji Walimu watakaokwenda kusaidia kusimamia eneo la kilimo, basi sisi kama Serikali sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tuko tayari kwenda kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba malengo ya kuhudumia wananchi wetu yanakamilika. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Tuna walinzi katika shule zetu za msingi, sekondari, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya lakini hakuna…

SPIKA: Swali.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, je, kada hizi zinalipwa na Mamlaka ipi hasa kwa sababu kuna mkanganyiko mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, juu ya ajira hizi za walinzi na kada mbalimbali kama ulivozitaja walipaji ni halmashauri kutokana na ikama ambayo wamejipangia.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itaweka kipaumbele kuajiri Maafisa Mipango na Maendeleo ya Jamii ili kupanga na kuchechemua maendeleo katika halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri Maafisa Mipango na kada mbalimbali katika Serikali kama ambavyo imekuwa inaombwa vibali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Vile vile, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa vibali 30,000 vya kuajiri kada mbalimbali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama eneo hilo alilolieleza na uhitaji ambao tunaufahamu, nataka nimhakikishie kabla ya mwisho wa mwaka jambo hilo tutalifanyia kazi tuweze kuhakikisha kwamba hiyo kada imeenea kama ambavyo imeombwa. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza;

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zoezi hili la upandishaji wa madaraja kwa maeneo mengine ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza inaonekana kwa mara ya mwisho ni tangu mwaka 2020/2021, na idadi ya watumishi walio kasimiwa kupandisha madaraja hailingani na waliopandishwa mpaka sasa;

Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala la pili, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa likizo kwa watumishi hasa kada ya Walimu;

Je, Wizara ina mpango ngani kuhakikisha kwamba Wizara ya Fedha sasa haitapunguza ile ceiling ya fedha za likizo zilizopo na badala yake waongeze zaidi?

Nashukuru Mheshimiwa Mwenyekiti.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jambo la watumishi kupandishwa madaraja nimeeleza katika jibu langu la swali la msingi; kwamba Serikali imeendelea kupandisha madaraja ikiwemo utaratibu wa mserereko, ambao ndio maarufu sasa hivi ambao unaingiza kundi kubwa la wafanyakazi katika kipindi kimoja ili kuweza kuwapandisha katika madaraja stahiki. Pamoja na hilo pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali haina mpango wa kupunguza fedha za wafanyakazi katika masuala yanayohusu likizo kama alivyoeleza katika swali lake la pili. Nashukuru sana.
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la nyongeza, ahsante Naibu Waziri kwa majibu ya Serikali mazuri na nina maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaongezea ruzuku wawezeshaji wakati wa malipo wakati wa masafa marefu ya kuwafikia walengwa?

Na swali la pili; shilingi 24,000 ni kidogo sana kwa wakati huu tulionao; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaongezea ruzuku wanufaika wa mfuko wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amina Daud Hassan kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la kwanza juu ya kuongeza ruzuku; nataka nimhakikishie Mheshimiwa Amina, kwamba Serikali iko katika mchakato ikijadiliana na wadau mbalimbali wakiwemo wahisani wetu juu ya maslahi na utaratibu mzima wa miradi hii ya TASAF, hivyo hii ni moja ya agenda ambayo inakwenda katika mjadala. Juu ya jambo la udogo wa pesa inayotolewa; niseme Serikali imesikia jambo hili na katika mjadala unaoendelea kama nilivyoeleza katika swala la kwanza la nyongeza, ni kwamba Serikali nao wanajadiliana kuona jinsi gani tunaweza kuangalia kuongezea ruzuku kidogo kwa wafaidika ili kuweka mazingira mazuri ya wao kufaidika na mradi huo; ahsante sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi kuuliza swali la nyongeza. Katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni tulitenga kujenga Zahanati katika Kijiji cha Udimaa ambacho hakina Zahanati kupitia mradi wa TASAF.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Zahanati ya Udimaa kwa kupitia mradi wa TASAF? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Chaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi inaibuliwa na wananchi, na sisi kama Wizara au Ofisi ya Rais inayosimamia miradi ya TASAF majukumu yetu ni kuchukua miradi hiyo na kuingiza kwenye mipango ya bajeti. Pale itakapopatikana bajeti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi wake huo tutakwenda kuufanyia kazi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimesikia majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza, lengo la kuwapelekea hizi fedha lilikuwa ni kuwasaidia tukiamini ni masikini, kwa hiyo hawana uwezo wa kununua simu. Kwenye simu kuna makato na benki kuna makato. Hatuoni kuweka hilo jambo ni kuondoa lile lengo la kuwasaidia hawa wanufaika ambao hawawezi hata kununua simu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mchakato wa kuwapata wanufaika uligubikwa na mambo mengi sana ikiwemo ubaguzi wa kivyama, kwa maana ya vyama vya siasa. Nini kauli ya Serikali kupitia upya tena mchakato huu ili tuwapate wenye sifa wanaostahili kuwa wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nirejee tena maelezo ambayo nimeyatoa katika swali la msingi.

Mheshimiwa Spika, malipo ya pesa hizi yako katika njia kuu tatu, ni choice ya mhusika mwenyewe njia gani aitumie. Kama akiona kwamba njia ya simu ni ngumu kwake kwa sababu hana simu hiyo inayopokea, anaweza kwenda katika njia nyingine ya benki. Kama akiona njia nyingine ya benki ni ngumu kwa sababu benki iko mbali, upo utaratibu wa kulipa fedha taslimu kupitia madirisha yetu. Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge option hizi zote zinawezekana katika maisha ya kawaida ya ubinadamu wetu na Watanzania wetu na mimi na Serikali tunaamini hivyo.

Mheshimiwa Spika, juu ya swali la pili la upatikanaji wa wanufaika. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba baadhi ya maeneo kumetokea changamoto juu ya utambuzi wa wanufaika katika miradi hii ya TASAF, Serikali imekwishayafanyia kazi katika baadhi ya maeneo na tunaendelea kutambua katika yale maeneo yenye changamoto, nataka nikuhakikishie katika Jimbo lako la Nkasi Kaskazini nako pia timu ya TASAF itafanya kazi, nasi tunategemea zaidi ushirikiano kutoka kwako Mheshimiwa Mbunge ili kuweka mambo ya wanufaika vizuri kwa sababu nia ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba wanufaika wote au walengwa wote wa TASAF wanafikiwa na kufikia malengo yao. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Wapo wanufaika waliowahi kunufaika na TASAF nazungumzia wazee, vikongwe ambao hawana wasaidizi walio katika Wilaya ya Korogwe, ambao wametemwa na mfumo wa TASAF.

Je, Serikali haioni kama imewaonea wazee wale kuwaondoa kwenye mfumo ingali bado hawawezi kujikimu maisha yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sekiboko, Mbunge wa Tanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni utambuzi shirikishi ambao unaanza ngazi za vijiji na ngazi hiyo tunaamini kabisa kwamba kila mmoja anamtambua na kumjua mwenzake. Utambuzi ndani ya level ya Serikali ni level ya uhakiki tu. Tunachokiangalia kama Serikali ni zile taarifa ambazo zinatoka katika kijiji ambacho wahusika hawa au wanufaika wanatokea. Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge siyo nia ya Serikali kuwadhulumu watu au kuwanyima wanufaika haki yao.

Mheshimiwa Spika, natoa angalizo sana kwa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Halmashauri zetu, kuhakikisha kwamba wanufaika wote wanaotakiwa kuingia kwenye mfumo wa TASAF wanaangaliwa na kutambuliwa ili Serikali iweze kufikia malengo yake ya kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji katika mfumo huu mzima wa kunyanyua maisha ya wale ambao wanaonekana wanahitaji kuingizwa katika mfumo wa TASAF ili kuwawezesha kiuchumi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafsi.

Mheshimiwa Spika, ninataka kujua kwamba, kwenye vijiji vyetu kuna watu ambao walipaswa kuwa na sifa kupata huduma ya TASAF na viongozi wengi wa vitongoji na vijiji wameweka watu ambao hawana sifa. Nini mpango wa Serikali kufanya auditing kuhakikisha kwamba watu wote ambao wanapaswa kuingizwa kwenye mfumo wanaingizwa na wale ambao hawapaswi kupata hiyo huduma watolewe katika huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika swali lililoulizwa na Mheshimiwa Sekiboko, naomba kurudia tena mbele yako na kulieleza Bunge lako na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, mfumo wa utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni mfumo shirikishi ambao unaanzia kwenye ngazi za vijiji vyetu, kwa hiyo ninachotegemea kutoka kwa wananchi ambao watashiriki mkutano wa utambuzi ni kuweza kuwatambua watu wote wanaotakiwa kushiriki katika mfumo huo.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe taarifa ndogo, tumewahi kufanya ziara katika baadhi ya Wilaya, tumekwenda pale tukakutana na kituko cha mwaka. Watu wanakataa watu walioingizwa kwenye mfumo wa TASAF ndiyo haya ambayo Mheshimiwa Waitara anayasema. Nataka nirudie tena mfumo huu ni mfumo shirikishi na nitoe wito kwa wananchi wote katika maeneo yote, mnapoitwa katika mikutano ya TASAF hebu jaribuni kushiriki ili kuondoa ubabaishaji wa baadhi ya watu ambao wanachomeka ndugu zao na watu wasio na sifa katika mfumo huu na kudhulumu wale watu wenye sifa, wanaostahili kuingia katika mfumo wa TASAF. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nashukuru majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini zoezi zima la utambuzi katika Jimbo la Mwibara lime – collapse.

Je, ni lini Serikali itafanya tena zoezi hilo upya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mwijage, Mbunge wa Mwibara, samahani kwa kukuchanganya majina nimekuita Mheshimiwa Mwijage badala ya Mheshimiwa Kajege. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika eneo lako la Mwibara nikiri kwamba mimi kama Naibu Waziri sijapata taarifa za kina juu ya wapi tatizo lilitokea na nini kilitokea mpaka zoezi zima likasimama, lakini ninaomba nilichukue hilo jambo na baada ya kumaliza session hii ya maswali na majibu tukutane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujadili kwa kina tuone nini kinafanyika na wapi walikosea ili tuende tukasahihishe tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza tena kwamba ni nia ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba wanufaika wote wa TASAF tunawafikia na kuwatendea haki katika kupata wanachostahili. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda Wilayani Nyang’hwale kuonana na akina mama wakongwe zaidi ya 80 ambao wameorodheshwa na zaidi ya miaka mitatu hawajapata stahiki yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nipo tayari na tutaongozana ili kwenda kuwatambua na tuzungumze kwa pamoja. Siyo tu utambuzi wa hawa, lakini pia suala zima la changamoto zilizopo katika eneo lake la utawala kuhusiana na mradi wetu huu wa TASAF. (Makofi)
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, moja, kwa vile wakati tunapitisha bajeti ya Wizara hii, Wabunge wengi ambao ni wawakilishi wa wananchi walionesha haja ya kuiomba Serikali kuwaangalia vijana mbalimbali wanaojitolea kwa jicho la tatu, hasa katika maombi ya kazi, na kwa vile Serikali yenyewe ndiyo imesema kwamba ilitengeneza mazingira haya ili kuwapa competitive advantage vijana hawa wanapotoa nafasi za kazi, swali la kwanza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuja na mabadiliko ya hizi sera, kanuni au sheria ili kuweka hii competitive advantage kwa hawa vijana pindi maombi ya kazi yanapopelekwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini sasa kauli au commitment ya Serikali kwa vijana mbalimbali waliopo katika vituo mbalimbali vya kazi sasa wakiwa wanajitolea kutoa huduma mbalimbali kwa Watanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA
UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ng'wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabla sijajibu maswali yake ya nyongeza, nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo hajawasahau vijana wake, na kwa kweli anafanya kazi nzuri, na Mwenyezi Mungu atakujalia dada yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maelezo ya ziada aliyoyatoa Mheshimiwa Ng’wasi Kamani ninaunaga naye moja kwa moja, ni kweli Bunge lako wakati linajadili Hotuba ya Bajeti hii ya Wizara yetu ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Wabunge wengi walizungumza sana juu ya jambo la vijana wanaojitolea. Na nataka nirudie tena kueleza kwa kifupi juu ya commitment ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikiri kupokea maoni ya Wabunge wote na kwamba tutakwenda kuyafanyia kazi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ninapozungumza leo saa nane kikao cha kwanza kwa ajili ya kujadili jinsi gani Serikali inakabiliana na tatizo la ajira tunakwenda kuanza chini ya uongozi wangu, kwa sababu Mheshimiwa Waziri amenikasimia mamlaka hayo niweze kulisukuma mbele jambo hili la ajira kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwenye swali lake la pili juu ya commitment ya Serikali; kwa maelezo niliyotangulia kutoa hapa, ni wazi kwamba Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejizatiti kuhakikisha kwamba inakabiliana na jambo hili, na tuko bega kwa bega naye Mheshimiwa Rais sisi kama watendaji wake, kuhakikisha kwamba tunakwenda kuli-address jambo hili na kulitafutia mwarobaini wake.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali; je, sasa kwenye Ajira Portal ni lini mtaongeza key ambayo itam-pick yule kijana ambaye amejitolea ikawa ni sifa ya nyongeza katika kuajiriwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA
UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kurejea tena kwenye maelezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wakati anafunga mjadala wa hoja ya Wizara yetu wakati wa bajeti. Alieleza na ninaomba ni- quote kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alieleza kuwa; Serikali imeyachukua maoni yote yaliyotolewa na Wabunge, na kwamba tunakwenda kuyafanyia kazi na utakapofika muda wa kuwashirikisha Wabunge kama wadau kwa kutoa maoni juu ya mfumo mzuri wa kutoa ajira kwa vijana wetu ambao mawazo mazuri kama haya anayoyatoa Mheshimiwa Mbunge yataingizwa ndani yake, tutakuja kulishirikisha Bunge lako na Wabunge watapata nafasi hiyo ya kueleza yale yote ambayo wanayataka yaingie katika mfumo.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini tunazungumzia maisha ya watu kwa idadi ya watu 863 ambao wameonekana hawana hatia ni asilimia 41.8 ni watu wengi sana katika utendaji wa umma na watu hawa wamepitia mateso, wamedhalilika katika jamii ambayo tunaishi ambapo tuhuma tayari ni uhalifu sasa swali. Serikali inachukua jitihada gani kuwasafisha watumishi ambao wamepelekwa Mahakamani kwa tuhuma za rushwa asilimia 41.8 wameoneka hawana hatia kutumia nguvu ile ile ya kuwatangaza ni wahalifu, wanatumia nguvu gani kuwasafisha watumishi hao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa madhara ni makubwa ya kisaikolojia, kijamii na haiba yao imechafuka kwenye macho ya umma. Kwa muda gani Serikali itaendelea kuvumilia kuwaona watumishi hawa wanaendelea kuhangaika na nini jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba wanarudi katika utumishi wakiwa wana haiba njema na safi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Dennis Londo utaratibu wa utumishi wa umma umeelezwa ndani ya sheria kama nilivyozitaja pamoja na sheria nyingine lakini pia utaratibu wa kuwarudisha watumishi kazini nao pia umeelezwa katika sheria hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Dennis Londo utaratibu wa kuwaandikia wale ambao wamekwisha safishwa na Mahakama na kuonekana kwamba hawana makosa utaendelea kufanyika. Pamoja na hilo pia Mheshimiwa Rais, ameelekeza na ndiyo tunayo yafanyia kazi kwamba lazima tuhakikishe kwamba hawa watu ambao wanakutwa hawana makosa tunawafanyia haki la kwanza, lakini pili wanarudishwa kazini mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo lote Mheshimiwa Rais ameendelea kuhakikisha kwamba kupitia Tume yake wa Utumishi wa Umma taratibu na haki zote wa watumishi hawa zinafuatwa na kusimamiwa. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na niwapongeze kwa juhudi mnazofanya za TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona sasa hivi kuna utaratibu wa viongozi wa aina moja au Maofisa wa aina moja kufungua group na kutumiana document za kiserikali ndani ya group. Je, hiyo sheria mliyoitunga imejua na hiyo kwamba imo huo au haimo?

Je, kama haimo na hairuhusiwi mnafanya nini ili sheria i-accommodate ili kuwaepusha wanaotumia huo mtandao wasije kupatwa na matatizo ya kuhukumiwa na hiyo Sheria ya kuwa na Nyaraka za Serikali kwa sehemu zisizo husika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria inayosimamia nyaraka za Serikali inaelekeza wazi kwamba mawasiliano ya Serikalini yafanyike kwa njia ya barua lakini haielekezi vinginevyo. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba haitokuwa sawa na ni marufuku ya Serikali kuwasilisha au kutumiana document za Kiserikali kupitia njia ya WhatsApp na njia nyingine zisizo rasmi isipokuwa kwa yale maelekezo ambayo yatakuwa yametolewa vinginevyo katika mamlaka.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza.

Kutokana na jibu la msingi ambalo Mheshimiwa Waziri umelitoa hauoni kwamba bado tutakuwa nyuma ya teknolojia kwa sababu mwisho wa siku tunahitaji kuweka mifumo ambayo itazilinda hizo document lakini ziende kwa haraka kwa sababu teknolojia inasaidia kufanya kazi kwa haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najibu swali la msingi nimeeleza mpaka sasa baada ya kupitishwa kwa Sheria Namba Kumi ya mwaka 2019 Serikali imekwisha tengeneza au kujenga mifumo ya TEHAMA zaidi ya 860 kwa ajili ya kusimamia utendaji wa Serikali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mwakagenda kwamba Serikali bado inaendelea kuitengeneza mifumo mbalimbali itakayosimamia ambayo italeta Serikali yote katika adabu ya kiutendaji.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii Wizara ndiyo inahusika na masuala ya TASAF watu wangu wa Jimbo la Bunda kumekuwa na matatizo makubwa sana ya malipo ya TASAF karibu nchi nzima, naomba Waziri atamke kwamba kuna nini kinachoendelea katika TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Getere, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Getere najua swali lake linatokana na ukweli kwamba yako baadhi ya matatizo au changamoto zilizojitokeza katika utendaji ndani ya Taasisi yetu inayosimamia Mfuko wa Kunusuru Kaya Maskini yaani TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yako maamuzi na maelekezo makubwa yaliyokwishafanyika ambayo sasa yale mapungufu yote yaliyojitokeza au mapungufu kwa asilimia kubwa yaliyojitokeza ndani ya TASAF tunaweka sawa. Nataka nimhakikishie kwamba yeye na Wabunge wote humu ndani wasiwe na wasiwasi Serikali iko kazini na kazi ya kurekebisha zile kasoro zote zinaendelea kufanyika, ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, Sheria ya Utumishi inaelekeza pia likizo ni haki ya mtumishi lakini likizo ile inatakiwa iambatane na stahiki zake za usafiri au nauli kwa mtumishi, lakini mpaka sasa kuna changamoto ya Walimu kupewa likizo lakini kutokupewa nauli ya kwenda makwao. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inapokea malalamiko ya watumishi juu ya baadhi ya madai au malimbikizo ya madai kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Mbunge lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeendelea kufanya hatua za malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe taarifa mbele ya Bunge lako kwamba hadi sasa tunapozungumza Serikali imekwishalipa zaidi ya wafanyakazi 126,924 ambao kwa gharama ya kifedha ni sawasawa na bilioni 216 kwenda kulipa madeni yote ambayo yanaendelea, ninachoweza kusema katika Bunge lako wale wafanyakazi wote ambao wana madeni ya malimbikizo wawasiliane na Ofisi zetu kupitia Wakurugenzi wa Halmashauri pia kupitia Ofisi ya Rais ili madeni yao yote au madai yao yote ya malimbikizo tuweze kuyaangalia mara mara moja.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi na nashukuru kwa majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza, kwa kuwa kila kazi inayotangazwa tunaambiwa tunataka uzoefu na hakuna mtu anatoka shuleni na uzoefu. Kwa hivyo, walimu wanaojitolea hicho ni kigezo kwamba kujitolea sasa imefika wakati hii sheria iwe ni kigezo namba mbili baada ya meritocracy.

Swali la pili, kwa kuwa Wizara nyingi sasa zimeshatengeneza miongozo ya kujitolea, nilikuwa nasoma moongozo wa Wizara ya Elimu wa kujitolea kwa Walimu wa June na Wizara ya Maendeleo ya Jamii wa 2021, kwa nini sasa ninyi ambao ni wa Utumishi, muendelee kupoteza muda badala ya kuleta mabadiliko ya sheria haraka sana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba iko miongozo mbalimbali ambayo inaongoza juu ya jambo zima la kujitolea, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba maagizo yalikwishatolewa na Bunge lako juu ya Serikali kuanza utaratibu wa kuja na sheria na miongozo juu ya jambo la kujitolea kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba, kumekuwa na miongozo mbalimbali lakini hakuna utaratibu maalum unaolenga kuelekeza juu ya jambo zima la kujitolea.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba maagizo uliyoyatoa tunayafanyia kazi, na ndani ya Ofisi ya Rais – Utumishi, tumekwishaanza michakato hiyo na sasa hivi tuko katika document na kama nilivyoeleza kwamba document zitakapokuwa tayari tutazileta mbele ya Bunge lako Mheshimiwa Spika ili Wabunge waweze kutoa mawazo yao, baada ya hapo sasa tuweze kuleta ije kuwa sheria.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba Serikali inayachukua mawazo yote mazuri yaliyotolewa na Wabunge, pamoja na michango yao katika kipindi cha Bunge la Bajeti na kwamba tunayafanyia kazi na kuyaleta mbele ya Bunge lako ikiwa kama miongozo ya Serikali.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, wako watanzania wengi ambao wana ujuzi na stadi mbalimbali na ziko nchi ambazo tunapakana nazo zina uhaba wa kada mbalimbali za utumishi.

Je, Wizara hii iko tayari kuketi na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuweza kuwasaidia Watanzania hawa waweze kupata ajira katika nchi hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, wazo lililotolewa na Mheshimiwa Mbunge la kuketi na Wizara ya Mambo ya Nje, sisi kama Serikali niseme tunalichukua na tutakaa na wenzetu na kutengeneze miongozo mizuri ya kuona ni jinsi gani tunauza ajira nje ya nchi yetu.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, Serikali haioni uko umuhimu sasa wa kuweka majina ndani ya data base waliojitolea na wanaoendelea kujitolea ili wawe wa kwanza kuajiriwa wakati huo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, hali ilivyo kwa sasa na miongozo iliyotolewa na Serikali inahifadhi majina ya watu wote wanaoshiriki michakato mbalimbali inayohusu ajira ndani ya database.

Mheshimiwa Spika, nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba database tuliyonayo sasa inaishi kwa mwaka mmoja, baada ya mwaka mmoja ili turuhusu watu wengine nao waweze kuingia, lakini wazo analolisema ni moja ya mabadiliko makubwa ambayo yanakuja kuletwa na huu mchakato ambao sasa unafanyika wa mabadiliko ya Sheria ya Utumishi, pia sera mbalimbali zilizopo ili kuweza kuweka mahitaji yote ya ajira katika chombo kimoja lakini mwongozo mmoja ambao utaweza kutoa nafasi kwa Watanzania wote. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika ahsante. Msingi wa kuanzishwa kwa mafunzo kwa vitendo kazini ni kuziba ombwe kati ya mafunzo waliyopata wahitimu vyuoni pamoja na soko la ajira. Sasa, kwa kutokuwa na kipaumbele cha kuajiri wale waliopata haya mafunzo kwa vitendo kazini kwanza, ni sawasawa na kupoteza lengo la kuanzishwa kwa mafunzo hayo. Sasa, kwa kutokuwa na kipaumbele cha kuajiri wale waliopata haya mafunzo kwa vitendo kazini kwanza, ni sawasawa na kupoteza lengo la kuanzishwa kwa mafunzo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba niruhusu kidogo na mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

SPIKA: Mheshimiwa Ridhiwani huko ni kupoka madaraka sasa, endelea (Kicheko)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nisamehe kwa sababu niliona kwamba niombe ruhusa kwako, nadhani ujumbe umeshafika. (Kicheko)

SPIKA: Subiri na wewe umeweka historia, kwa hiyo, nimekuruhusu toa salamu zako. (Kicheko)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba kuwa ni kweli anayoyasema Mheshimiwa Zainab Katimba na ndiyo maana nataka nikiri mbele ya Bunge lako, wakati wa mijadala mingi inayoendelea juu ya masuala mazima ya ajira na utumishi, jambo la mazoezi ya kujitolea au mafunzo ya vitendo limekuwa ni moja ya jambo la mjadala mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako limesema kwa sauti kubwa na Serikali imesikia. Ndiyo maana sasa tuko katika mchakato wa kufanya review ya Sheria yetu ya Utumishi wa Umma ili kuweza kuangalia mapungufu yote yaliyopo na kama nilivyosema kwenye ahadi yetu kwamba tutakapokuwa tayari tutaileta hapa na Bunge lako litapata nafasi ya kutoa mawazo na sisi kama Serikali tuweze sasa kutengeneza sheria ambayo itakuwa inabadilisha Sheria ya Utumishi wa Umma ili kuweza kutengeneza mustakabali mzima wa ajira na vipaumbele katika nchi yetu.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, tunakubaliana kwamba semina elekezi ni muhimu mara baada tu ya kuteuliwa. Nina swali moja tu la nyongeza.

Kwa kuwa ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyotolewa hivi karibuni, imezungumzia matumizi mabaya ya waliopewa mamlaka, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, namna wanavyotumia masaa 24 kuwaweka watu ndani bila kufuata taratibu.

Je, ni lini Serikali italeta Mswada hapa Bungeni ili tufanye marekebisho kuwaondolea hayo mamlaka wabaki kuwa wasimamizi wa shughuli za maendeleo na yabaki kwa Jeshi la Polisi pekeyake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni ukweli kuwa kwamba sasa Serikali imekwisha toa tayari taarifa ya kijinai, na kwamba taarifa hiyo imekwisha anza kufanyiwa kazi na wananchi wanashirikishwa katika maeneo mbalilmbali ili kuweza kutoa maoni yao na baada ya hapo taratibu nyingine za mabadiliko ya sheria ziweze kufuatwa.

Mheshimiwa Spika, namuomba mheshimiwa Mbunge na Bunge lako liwe na Subira wakati mchakato wa kuendelea kukusanya maoni ya watu yanaendelea kupatikana ili itakapokuwa tayari sasa tuweze kuleta; na kama kutakuwa na mapendekezo ya mabadiliko ya sheria na kama kutakuwa na miongozo yeyote ile sisi kama Serikali au nchi tuweze kuifanyia kazi, ahsante.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itarejesha utaratibu wa mafunzo elekezi ya uongozi, utawala bora na uadilifu kwa watumishi ambao wamefikia ngazi ya Afisa Mkuu ili wanapopata nafasi za uteuzi waweze kutumika ipasavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma na Sheria ya Utumishi wa Umma pia Ibara ya 4 hadi Ibara ya 8 inampa mamlaka Katibu Mkuu Kiongozi kuweza kuhakikisha kwamba utumishi wa umma unakuwa ulio bora na ambao unakwenda na weledi lakini pia ambao unaweza kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, nataka kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako, kwamba Serikali imeendelea kufanya utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watendaji wote au watumishi wote ambao wanakuwa katika ngazi za uteuzi ili kuweza kuwa katika viwango bora vya kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, nataka kumhakikishia kwamba hilo jambo au maombi ya Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuyafanyia kazi na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunakuwa na utumishi ulio bora kama ambavyo sheria inamtaka Katibu Mkuu Kiongozi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa, ni zaidi ya miaka mitano imepita tulikuwa hatuna ajira katika Taifa letu, tunaonaje kama tusibadilishe angalau utaratibu kwa sababu wale wa miaka mitano ambao hawajaajiriwa na mkawataka wa hivi karibu hatuoni kama tunawaacha nje kwenye mfumo wale ambao walimaliza kwa miaka hiyo mitano ya nyuma? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa JKT zamani ilikuwa ni mujibu wa sheria kila mwanafunzi akimaliza anaenda mwaka mmoja JKT lakini sasa hivi bajeti kwa kuwa ndogo wananchaguliwa wachache. Hatuoni kwamba tunawanyima nafasi wale wachache ambao hawajachaguliwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na gap hilo la miaka mitano kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia kulihakikishia Bunge lako kwamba ziko jitihada za maksudi zinazofanywa na Serikali kuhakikisha kwamba gap hilo tunalitoa.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI tumekwishaanza kufanya jitihada hizo na unayoyaona yanayotokea sasa ikiwemo kuongezeka kwa matangazo ya nafasi za ajira ni moja kati ya hatua hizo zinazofanyika.

Mheshimiwa Spika, juu ya jambo la pili, kuhusu vijana ambao wameachwa katika kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita ambao hawajajiunga na JKT, ambao Mheshimiwa Mwakagenda anasema ni group la wasomi. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia kulihakikishia Bunge lako kwamba Serikali katika utaratibu huo huo imeendelea kufanya juhudi za maksudi kuhakikisha kwamba gap hilo nalo tunalifunga ili vijana wengi wa Kitanzania waweze kupata fursa hiyo. Kwa kweli katika jambo hili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa vibali vingi sana vya ajira katika kipindi cha mwaka 2022/2023 ambapo vibali 20,000 vilitoka pia 2023/2024 ambapo vibali zaidi ya 30,000 navyo vimetolewa kwa ajira mbalimbali ikiwemo ikiwemo ajira hiyo ya vijana ambao wamekosa sifa za kuingia JKT.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa, umaskini unatofautiana kutokana na mahali kwa mahali. Maskini wa jamii ya wafugaji, makazi siyo kitu cha msingi kwake, lakini maskini wa mahali pengine makazi inawezekana ikawa ni kitu cha msingi kwake. Kwa hiyo, ni lini Serikali itaona haja ku-standardize hivi vigezo vya kuzipata kaya maskini ili jamii ile iepukane na migogoro? (Makofi)

Swali langu la pili, nitazungumzia vile vipengele vinne vya Miradi ya TASAF na nitazungumzia suala zima la Public Work Program kwamba, kwa kuwa miradi hii inapokamilika inakabidhiwa katika mitaa au vijiji. Ni lini sasa Serikali itaweka utaratibu maalum kuhakikisha kwamba wanashirikishwa wanakijiji wote au jamii yote ili miradi ile iwe vipaumbele kwa jamii husika badala ya zile kaya zilizolengwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza juu ya ku - standardize vigezo. Utaratibu wa kupata wahusika au wafaidikaji ni utaratibu kwanza shirikishi. Wananchi wanashirikishwa katika ngazi ya kijiji, wanajadili juu ya taratibu zao, wanajadili juu ya vigezo na kutambua wapi ambao wanatakiwa kufaidika katika mradi huo. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie, tunapokwenda hata kwenye jamii ya wafugaji, wafugaji wenyewe wanashirikishwa ili kuweza kutambua na kutanabaisha vipaumbele vyao. Hivyo pia tunapokwenda kwenye jamii za wakulima na jamii mbalimbali. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba taratibu ziko wazi, vikao vinayokaa ni shirikishi na wanavyohitaji wananchi ndivyo ambavyo mradi wetu wa TASAF unakwenda kusimamia.

Swali la pili juu ya vipaumbele ambavyo vipo katika maeneo yetu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyokuwa nimejibu katika swali la msingi na maelezo ya ziada katika swali lake la kwanza la ziada, kwa uhakika kabisa nataka nimuhakikishie yeye na kulihakikishia Bunge lako kwamba tunapokwenda katika vijiji mambo yote yanayotakiwa na wanayohitaji wananchi ndiyo kipaumbele cha mradi huo wa TASAF na siyo vinginevyo.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika,pamoja na jibu zuri la Serikali lenye kuleta matumaini lakini kwa kuwa hii Tarafa ya Mbwera ipo visiwani na changamoto kubwa ya upungufu wa nyumba za walimu zaidi ya 35, hasa katika maeneo ya Twasalie, Kiongoroni, Mbuchi na Saninga. Je, Serikali inatupa matumaini gani kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025?

Swali la pili kwa kuwa Tarafa hii ya Mbwera siku za nyuma huko ilijengewa sekondari moja tu kwa ajili ya Kata zote tano lakini kwa sasa Mheshimiwa Mbunge Twaha Mpembenwe na wananchi wa Tarafa hizi hasa Kata ya Mbuchi na Msala wamejenga sekondari imefikia ngazi ya lenta. Je, Serikali ina mpango gani wa kuchangia jitihada hizi za Mheshimiwa Mbunge na Madiwani na wananchi wa maeneo haya ili kukamilisha hizi sekondari? ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba upatikanaji wa bajeti ndiyo kigezo kikubwa kinachoweza kusaidia shule hizo kujengwa. Hivyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa Kata hizo za pembezoni hatutowaacha isipokuwa Serikali yao inaendelea kutafuta fedha na itaendelea kuweka fedha ili kujenga shule hizo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwanza nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo anashirikiana na Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Mpembenwe kwa jinsi anavyofuatilia maendeleo ya wananchi wetu. Nataka nimhakikishie kwamba pamoja na kujengwa kwa shule ambapo kumekwama katika Kata hizo za Mbuchi na kule alikosema nataka nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kutenga bajeti katika mwaka ujao wa bajeti kama ilivyofanya katika mwaka huu kwa kutenga bilioni 55.75 ili kuendelea kusaidiana na wananchi kuweza kufikia malengo makubwa ya kuwapelekea elimu wananchi wetu.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa kutokana na Waraka huo wa Serikali sina uhakika sana kama unazingatiwa kwa Wilaya ya Tunduru, kutokana na mwaka jana tulipata Walimu wa Shule za Msingi 56 na waliohama ni 57. Je, Serikali ina mpango gani wa kutufidia wale waliohama?

Swali la pili, je, Serikali haioni haja ya kutoa Waraka maalum kwa ajili ya Tunduru pekee kwa kuwa wale wote wanaohama labda inawezekana kutokana na mazingira waliotokea na wanayokwenda kuyakuta hawakubaliani nayo.

Je, Serikali haioni haja ya kutuletea ama kuajiri waajiriwa ambao wanaotokana na maeneo yale ili waendelee kubaki pale na kupunguza kero hiyo ya kuomba kuhama? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu kilio cha wananchi wa Tunduru kilishafikishwa katika Ofisi zetu mbili zote ikiwemo Ofisi ya Rais, Utumishi ili kuweza kuyashughulikia na hizo taratibu kufuatwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali, kwa maana ya kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi hilo jambo tumeshalichukua na tutakwenda kulifanyia kazi na Mheshimiwa Mbunge tutakapokuwa tayari tutakujulisha ili upate kujua hatua ambayo zimefikiwa katika jambo la kufidia hili gap lililopo katika upande wa walimu wako.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili nataka kumhakikishia Mbunge kwamba siyo taratibu za Serikali kutengeneza Waraka kwa ajili ya Halmashauri moja au Wilaya Moja. Waraka ni kwa ajili ya Tanzania nzima ili kuweza kukabiliana na changamoto iliyopo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imechukua kilio hicho na inakwenda kukifanyia kazi na itakapokuwa tayari tutakuja kumjulisha yeye pamoja na Bunge lako.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri naona umesimama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru juu ya eneo linalohusu watumishi kuwa wako kwenye harakati za kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine muda mwingi kuliko hata kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, wewe ni Mbunge unajua kinachotokea, jambo hili linapaswa kupatiwa majibu ya uhakika kwa sababu ni kweli kabisa kwamba watumishi wengi wanapangiwa mahala na wanakwenda kule kwa mipango ya harakati za kuanza kuondoka toka siku waliyofika. Ni ukweli kwamba huwezi ukazuia mobility ya watumishi wa umma kwa sababu wao ni binadamu kuna changamoto na mambo mbalimbali yanayowasibu pia.

Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya watumishi ambao wao ni wanandoa wanachangamoto kubwa unamkuta mume yupo Kigoma, mke yuko Mbeya familia hii inapata changamoto ya kutokuwa Pamoja, pia watumishi hawa hawatafanya kazi kwa ufanisi kwa sababu muda mwingi wanafikiria juu ya mwenza wake yuko mbali.

Mheshimiwa Spika, jambo hili wacha tulichukue tusijibu kwa haraka tukae na mamlaka za ajira na hasa TAMISEMI ili tuweze kutengeneza mfumo mzuri, tuangalie pengine inawezekana huko Tunduma ambako wanahama walipelekwa ambao hawapendi Tunduma lakini wako wengi wanaopenda kwenda Tunduma kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, tutajaribu kutengeneza utaratibu tuone tunaweza tukafanyeje bila kuvunja umoja na mshikamano wa Taifa letu kwa sababu pia kuwapangia watu kutoka sehemu aliyotoka huko huko itakuwa ni jambo, lakini wapo wanaoweza kuwa wanapenda kwa kiasi fulani, tunaweza tukafanya maamuzi hayo kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ni pikipiki 85 zilizotoka kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii zimetoka kwa Mikoa 21 na Mkoa wangu wa Tabora zimetoka pikipiki nne. Pikipiki mbili zimeenda Wilaya ya Urambo kwa Kata ya Kazaroho na Uyumbu na zingine zimeenda Kaliua. Sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha inatenga pikipiki nyingi za kutosha kwa ajili ya kuwezesha Afisa Maendeleo, kwa ajili ya kazi hizi za kufatilia mikopo?

Swali la pili, Kanuni ya utoaji mikopo Februari 2021 iliwaagiza Wakurugenzi kutenga pesa 500,000 hadi milioni 5,000, 000 kwa ajili ya ufuatiliaji wa mikopo lakini siyo kila Halmashauri ina uwezo wa kuwa na pesa za kutosha. Swali langu kwa Serikali, haioni kama na Serikali yenyewe ni chanzo cha mikopo hii chefuchefu ambayo tunashindwa kukusanya na kufuatilia vikundi hai na ambavyo siyo hai.

Je, ina mpango gani kuhakikisha sekta hii ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapata vitendea kazi vya kutosha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza la utengaji wa pikipiki hizi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utengaji au upatikanaji wa pikipiki hizi kigezo cha kwanza ni upatikanaji wa bajeti. Kwa hiyo, kama Serikali tutaendelea kutenga bajeti ili tuweze kuwafikia wananchi wote ikiwezekana Kata zote au Wilaya zote za Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kwamba Halmashauri nyingine hazina uwezo wa kutenga pesa kwa ajili ya kupeleka Maafisa wetu kwenda kuangalia au kufuatilia vikundi hivyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa haya pia ni maelekezo ya Serikali kwamba Wakurugenzi wote katika Halmashauri zote wahakikishe kwamba wanaendelea kutenga fedha kama ambavyo imeelekezwa na wale ambao watashindwa maelekezo yetu ni kwamba wawasiliane na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuona ni jinsi gani tunatatua tatizo hilo. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Licha ya majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kufuatana na swali la msingi, nilikuwa natanguliza tu, maombi yatakuja, tayari tumeshaongelea, kwa hiyo, yatakuja. Yakija naomba mtufikire.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza. Manispaa yetu ya Morogoro ina kata 29 lakini ina tarafa moja. Kata zake ni kubwa sana: Je, Serikali haioni kuwa inaweza angalau ikatupatia tarafa ya pili kusudi kuwe na tarafa mbili kwa sababu kata ni nyingi sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kwa sababu mkazo wa Serikali sasa hivi ni kuimarisha miundombinu pamoja na huduma za jamii; miundombinu ya Manispaa ya Morogoro bado siyo mizuri hasa kwa upande wa Barabara: Je, ni lini Serikali itaweza kuwapa fedha na kuwaongezea kusudi barabara zetu za Manispaa ya Morogoro ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuongezwa tarafa ya pili. Naomba kumshauri Mheshimiwa Mbunge na pia kuishauri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kufanya vikao kwa ajili ya maombi hayo kama ambavyo amesema juu ya maombi ya kuwa Halmashauri ya Jiji. Utaratibu uko wazi. Kikao cha kwanza ni cha Bodi ya Ushauri ya Wilaya (DCC), baada ya hapo maamuzi yenu yanapelekwa katika kikao cha Mkoa, yaani Bodi ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na baada ya hapo tunakwenda kumwasilishia Mheshimiwa Waziri ili sasa maamuzi ya kugawa Halmashauri yenu au Manispaa yenu ili mweze kupata tarafa ya pili na taratibu nyingine kwa ajili ya kuwa jiji ziweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, hilo ni jibu kwa swali la kwanza. Swali la pili, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali kupitia TARURA imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inaimarisha miundombinu katika majiji yetu, Manispaa zetu na Halmashauri zetu zote zilizopo ndani ya nchi yetu. Hivyo nataka nimhakikishie tena Mheshimiwa Mbunge kupitia Halmashauri yake, watengeneze bajeti yao, watengeneze vipaumbele vyao, watuletee Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tutakwenda kufanyia kazi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa baadhi ya watumiaji wenye mahitaji maalum baadhi huwa wanasota kwenda kupata huduma: Je, Serikali inaweza kuhakikisha kwamba vyuo na mashule vilivyojengwa hivi karibuni vimewekewa visaidizi maalum kwa watumiaji hawa kufika vyooni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Asha Abdullah Juma, almaarufu Bi. Mshua, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika taratibu za Serikali, katika kila Halmashauri wako watu wanaitwa Wakaguzi wa Ubora wa Shule zetu. Maelekezo yetu Serikali ni kwamba wakaguzi wote wa ubora wa shule, wapite katika kila shule iliyopo ndani ya Halmashauri zetu kuhakikisha kama hili hitaji au changamoto iliyoelezwa na Mheshimiwa Bi. Asha (Mshua), inafanyiwa kazi, kuhakikisha kwamba walemavu wote au wenye mahitaji maalum wote mahitaji yao yameangaliwa. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza nishukuru kwa majibu, lakini Serikali imesema itasimamia mikoa ili iweze kusimamia Halmashauri zisizo na utayari wa kuanza kutekeleza miradi.

Mheshimiwa Spika, lakini mikoa yenyewe imekuwa na chagamoto ya kuwa na fedha ambazo zinafanya ufatiliaji, tumekuwa tukiona tukienda ndio tunakwenda nao.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha kifedha Sekretarieti za Mikoa ili zitekeleze wajibu wao ipasavyo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; fedha hizi hutolewa chini ya masharti ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 1982; zipo Halmashauri zinapata fedha zaidi ya walichoomba na ziko Halmashauri zinapata pungufu ya walichoomba na zipo zinazocheleweshewa kabisa kupata kuanzia mwezi wa tano hadi wa sita, na Halmashauri zinazopata zaidi zinafanya ubadhirifu wa kutumia fedha zaidi nje ya matumizi ambayo walipanga na nyingine zinazopata kidogo hazitekelezi mikakati yao kikamilifu. (Makofi)

Je, Serikali ina mkakati gani na kauli gani tunaipata kutoka kwa Serikali kuhusu suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Victor Tendega kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na fedha zinazotakiwa kupelekwa katika mikoa nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, fedha zote zinazopelekwa katika maeneo yote kwa mujibu wa kanuni ambayo yeye mwenyewe amei–cite inayotoa miongozo ya fedha, inataka wahusika waombe fedha TAMISEMI ili wapelekewe na kama yako maeneo ambayo yametokea mapungufu hayo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutafatilia na tungeomba taarifa hizo utupe za kina ili tuweze kuzifatilia.

Pili juu ya upendeleo; nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali haifanyi upemndeleo na kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, miradi inayotekelezwa ndio ambayo inaielekeza Serikali ifanyeje, katika force account kinachofanyika ni kwamba Halmashauri husika inapokuwa tayari kutekeleza mradi inatoa taarifa kwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, na fedha zinapelekwa na katika ilani ambayo inasimamiwa na wakandarasi Serikali inachofanya ni kwamba baada ya mkandarasi ku-raise certificate basi Serikali inapeleka pesa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie na Bunge lako kwamba Serikali iko makini inaendelea kufanya kazi vizuri na kama yako mapungufu katika maeneo ambayo wewe Mheshimiwa Mbunge umewahi kupita, basi utupe taarifa tuweze kufatilia na kuyafanyia kazi. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nishukuru Serikali kwa majibu yake. Wilaya ya Kyerwa tunayo mapungufu ya watumishi kwenye sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya.

Je, lini Serikali itaongeza watumishi kwenye sekta hizo ambazo nimezitaja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuna watumishi 18 ambao wamestaafu mwaka 2018 wakiwemo watendaji wa kata, watumishi hawa mpaka sasa hivi bado hawajalipwa mafao yao. Nini tamko la Serikali juu ya watumishi hawa kulipwa mafao yao ili na wao waweze kufurahia utumishi ambao wametumikia Taifa hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba Serikali imeendelea kupandisha madaraja watumishi wake pia imeendelea kuajiri watumishi katika maeneo ambayo yanahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapungufu aliyoyaeleza Mheshimiwa Mbunge nataka nimwahidi kwamba Serikali imeendelea kuyashughulikia na kwa mfano katika bajeti iliyopita ya mwaka 2022/2023 vibali vya ajira 30,000 vilitolewa na watumishi wote hawa waliajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka unaofuta wa fedha ambao Bunge lako limetupitishia bajeti yetu tunatarajia kuajiri wafanyakazi au watumishi 45,000. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba Serikali itaendelea kukabiliana na upungufu wa watumishi katika sekta zote zilizomo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anataka kujua juu ya watumishi 18 ambao hawajalipwa mafao. Nataka nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwamba watumishi hao kama hawajaleta barua katika Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi basi barua zao zifike haraka na kama wameshazileta baada ya hapa naomba nipate taarifa zaidi ili niweze kuyafatilia.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Serikali mwaka jana ilipandisha vyeo au madaraja watumishi katika sekta ya umma baada ya kushindwa kupandishwa kwa takribani miaka mitano. Upandishwaji huu umesababisha changamoto ya walioajiriwa mwanzo na walioajiriwa baadaye wote kujikuta wapo katika kundi moja au daraja moja. Nini tamko la Serikali kutoa maelekezo kwa mamlaka za ajira nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili ifanye uchambuzi na hatimaye walioajiriwa wakiwa daraja moja waweze kuwekwa katika madaraja stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Kassinge Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba kuwapandisha vyeo watumishi ni sehemu ya kuwapa motisha ili waendelee kufanya kazi vizuri pia ni eneo la kuendelea kusimamia usimamizi wa watumishi wa umma katika nchi yetu. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hapo mapungufu yaliyojitokeza katika utumishi ambayo yanahitaji watu wapandishwe vyeo yote tunayafanyia kazi na tutaendelea kutoa taarifa kadiri tunavyoendelea kupata nafasi ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taarifa za watumishi wako zote ambao wana malalamiko kama hayo kupitia wewe tungependa tuzipate Serikali ili tuweze kuzifanyia kazi na kuweza kuwapatia haki yao wafanyakazi hao.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata fursa hii kuuliza swali la nyongeza. Katika Halmashauri ya Mji wa Bunda kuna walimu takribani 28 wamekuwa wakikwama kupandishwa madaraja na ili hali kuna wenzao wamekuwa wakipandishwa madaraja kila mwaka walioajiriwa kwa mwaka mmoja. Tumelifuatilia suala hili wanasema tatizo ni mfumo na mimi nimechukua hatua ya kumpigia Katibu Mkuu Utumishi. Ningependa kujua ni lini sasa tatizo hili litaisha kwa hawa walimu 28 wa Halmashauri ya Mji wa Bunda ili waweze kupata haki yao kama wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Serikali ni kwamba watumishi wote wanaostahili kupandishwa vyeo wapandishwe kwa mujibu wa taratibu kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi. Na hapa nakusudia na nimaelekezo ya Serikali, kwamba kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bunda Mji na viongozi wote katika Halmashauri nyingine zote Tanzania, maelekezo ya Serikali yako wazi na wayafate na kutotii maelekezo hayo ni kutotii uelekezo halali ya Mheshimiwa Rais, ambayo ameelekeza katika, alipokuwa anatoa maelekezo tarehe 19 Aprili, kwamba anataka wafanyakazi wote wanaostahili kupandishwa vyeo wapandishwe vyeo, wanatakiwa kufanyiwa recategorization wafanyiwe recategorization, lakini pia wale ambao kwa muda mrefu sana wamekuwa wanasubiri kuajiliwa nao pia wenye sifa za kuajiriwa, waajiriwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo maelekezo haya yote nataka nikuhakikishie Bunge sisi kama Wizara au Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunayasimamia hayo na ni maelekezo yetu kwamba tunataka halmashauri zote nazo zisimamie na kama kuna sehemu yeyote pamekwama basi wawasiliane na Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi ili kuweza kushughulikia changamoto zitakazokuwa zimejitokeza. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe kauli ya changamoto kubwa iliyopo ya mfanyakazi anapandishiwa mshahara vizuri kabisa lakini harekebishiwi mpaka anastaafu, na inampa matatizo ya kupata haki zake. Mheshimiwa hii ni changamoto kubwa naomba Serikali itoe kauli yake. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Sitta Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kwanza kulihakikishia Bunge lako lakini pia kumuhakikishia Mbunge ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunayo idara maalum inayohusika na masuala ya marupurupu, mishahara na nyongeza zote ambazo ni stahiki za mtumishi anatakiwa kupata. Sasa kama wapo watumishi ambao wanachangamoto katika hayo ofisi yetu iko wazi na ningeomba tupate taarifa hizo ili sasa tuweze kushughulikia na wafanyakazi wetu wote waweze kupata haki yao kama ambavyo imeelekezwa katika ratiba yetu. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa nafasi hii nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, sasa Serikali haioni kwamba kuna haja ya kubadilisha sheria iliyopo ambayo inawanyima haki watoto wale kwa sababu wanaachwa wakiwa wadogo sana, wachanga, kiasi kwamba inaweza ikawasababishia vifo kwa kukosa uangalizi wa karibu wa mama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba, Serikali sasa haini kwamba kwa kumnyima hizo haki mama yule ambaye amejifungua mtoto njiti wa siku zile za nyongeza kunaweza kukamsababishia matatizo ya afya ya akili ambayo itagharimu tena Serikali kumtibia matatizo ya afya ya akili ambayo yatamfanya asifanye kazi yake ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la kubadilsha sheria nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sheria zipo, miongozo ipo na taratibu zipo. Changamoto inayotokea labda ni ile ambayo naweza kusema kwamba kuna baadhi ya Waajiri ambao kwa roho mbaya tu wanaamua kuwanyima hawa wazazi wanaopata watoto njiti. Lakini kwa upande wa sheria na zote zimeelezwa wazi, na mimi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako, lakini pia kutoa maelekezo kwa waajiri wote kwamba inapotokea mama amepata mtoto njiti na mazingira yanafahamika, watoto wanatakiwa kulelewa katika kangaroo basi ni wito wangu kwamba waongozwe pia na ubinadamu katika yale mamlaka ambayo wamepewa ili waweze kuwapa nafasi wazazi wakalee watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili katika maeneo ambayo kinamama may be labda wanakumbwa na hili tatizo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliita kwamba tatizo la afya ya akili; nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali inayoongozwa na mwanamama Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali wakinamama Watanzania, inawajali watoto wa Tanzania lakini pia inatambua na kuheshimu na kulea afya za akili za Watanzania. Kwa hiyo nataka nikuhakikishie kwamba kama panapotokea matatizo hayo Mheshimiwa Rais ameishatoa maelekezo lakini pia na sisi tuwe chini yake tunamsadia, tumekwishapewa maelekezo na tunachotakiwa kufanya ni kuwaonea huruma wazazi hawa na kuwapa nafasi ili waende wakalee watoto wao ambao wamezaliwa katika mazinguru magumu kama hayo yaliyotajwa. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENNEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri yanayotolewa na Naibu Waziri, Ridhiwani Kikwete nimesimama kwa sababu ya uzito la suala la watoto njiti. Wazazi wao wanapotakiwa wakimaliza siku 84 katika likizo ya uzazi, na bila shaka wote tunakubaliana kwamba siku 84 kwa mtoto aliyezaliwa njiti anakuwa bado hajaimarika sawa sawa; na unjiti unatofautiana, wengine wanazaliwa na miezi sita, wengine wanazaliwa miezi saba, wengine wanazaliwa miezi nane wanakuwa hawajakamilika uumbaji unakuwa bado unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo chama/NGO inayohusiana na masuala ya kusaidia watoto njiti, wamekwishaleta malalamiko mengi sana Serikali. Sasa leo nataka nionyeshe mahala ambapo Waheshimiwa Wabunge tusaidiane katika kuona kama tunahitaji kweli kubadilisha sheria au sheria iliyopo inajitosheleza kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Kanuni za Utumishi wa Umma ya Mwaka 2009 Kanuni ya pili, H16 mnaweza mka-google hata nikimaliza kujibu swali mtapata maelezo yanayosema; “Except in cases of illness or other cases of emergence” yaani kwenye kesi hizi mtumishi ana haki ya kuomba extension of leave. Sasa tunajaribu kuona kama inatosha au haitoshi Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu kundi hili ni kweli mtu akizaliwa anapofariki inaumiza sana na wengi humu tumezaliwa tukiwa njiti. Hatujisemi tu humu lakini tusingeangaliwa kwa zaidi ya siku 84 tungekuwa hatupo leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuipitie hiyo Kanuni halafu Waheshimiwa Wabunge wale wenye maoni, watatuletea maoni kama inatosha au haitoshi? (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa likizo ya uzazi ambapo wanaume wanapata siku tatu;

Je, Serikali haioni umefikia wakati kuongeza walau mwezi mmoja kwa wale wenza ambao watakuwa wamezaa watoto njiti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Toufiq Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake linaweza kuwa limejibiwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri wakati anatoa maelezo ya ziada katika majibu yangu niliyompa Mheshimiwa Mtanda. Na mimi nadhani ili nalo tuliunganishe katika maombi aliyotoa Mheshimiwa Waziri la kutoa maoni ili kuona kama kuna sababu ya kurekebisha baadi ya vifungu vilivyomo katika sheria na kanuni inayoongozwa masuala yote ya likizo hasa pia kwa wanaume ambao Mheshimiwa Toufiq anawapigia debe waongezwe zifike siku 30. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na watoto njiti lakini pia kuna wanawake ambao wanajifungua watoto zaidi ya mmoja;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea siku akina mama hawa ili angalau waweze kuweza kuwalea vizuri hawa watoto mpaka wanapofikia umri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikiri mbele yako kwa kuwa mimi siyo mtalamu sana katika eneo hili analozungumza Mheshimiwa Mwaifunga, hasa anapofikia mama amezaa watoto zaidi ya mmoja au wawili au watatu kwa maana kwamba anahitaji kipindi gani ili aweze kupumzika. Lakini nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako, maelezo aliyotoa Mheshimiwa Waziri yatioshe kufungua ili boksi la mjadala wa hii sheria na kanuni ili tuweze kuona jinsi gani tunaweza tukarekebisha hasa tukiweka into consideration mawazo mazuri ya Mheshimiwa Mbunge Hawa Mwaifunga. (Makofi)
MHE DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Ni kwa nini sasa Serikali inapoita vijana kwa ajili ya usaili isiangalie hizo sifa na vigezo kuliko hivi sasa pengine nafasi ni ishirini wanaitwa watoto 3,000 mpaka 5,000? Wanasababisha vijana wengi kuteseka hapa Dodoma wakati wa kusubiri huo usaili. (Makofi)

Swali langu la pili, ni kwa nini vijana wengi wamekuwa wakijitolea au kupewa nafasi za mikataba lakini inapotokea ajira hawa vijana hawapati kipaumbele, wamekuwa wakijitolea miaka minne, mitano kiasi kwamba zikitoka ajira wanaajiriwa wapya. Hii kwa kweli inaumiza sana na inaliza sana kwa vijana wetu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali maswali mawili ya Mheshimiwa Ritta Kabati kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na nafasi chache wanaitwa wengi, katika maelezo ya msingi nilieleza kwamba nafasi za ajira kwa sasa kwa mujibu wa kanuni ambazo zimepitishwa na Bunge lako ni nafasi za kiushindani. Hivyo tunapotangaza matangazo matarajio yetu ni kwamba watajitokeza wengi ili waje kushindana kwa ajili ya kupata nafasi hizo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli nakiri mbele ya Bunge lako kwamba malalamiko juu ya wingi wa wanaoomba na dhidi ya nafasi kuwa chache umeendelea kujitokeza. Serikali yako imeendelea kufanya juhudi za dhati kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto hii. Lakini kupitia Bunge lako maelekezo yalishatolewa na Ofisi ya Rais inayoshughulikia Utumishi imeyachukua na inakwenda kuyafanyia kazi na tutapokuwa tayari tutaleta majibu mbele ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kuhusu wale wanaojitolea halafu baadaye wanakuja kukosa ajira. Wakati naeleza katika swali la msingi, ajira za Serikali zinazingatia sifa, taaluma, uwazi na usawa, na ni maelekezo ya Bunge lako kwamba katika uwazi huo na usawa huo, ulielekeza kwamba ajira zinapotolewa waitwe watu wadahiliwe kwa usawa na uwazi, sasa inapotokea kwamba mtu aliyepo kazini anakosa kazi hili tena linakuwa niseme ni jambo la kiufundi zaidi na siyo jambo la mtu kuonewa. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wanaofanya kazi waendelee kuhakikisha kwamba wanashindana vizuri ili waendelee kupata kazi kama ambavyo wengine wamekuja kwenye ushindani.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Waziri ametamka wazi kwamba nafasi hizi zinatolewa kwa ushindani, lakini kule vijijini ambako wanafunzi wengi ambao wanaomba hizi nafasi ndiko waliko, Magazeti hayafiki wala mtandao hakuna.

Je, huo ushindani wa haki unapatikanaje katika mazingira ya aina hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, vilio vinekuwepo hasa katika maeneo ya kule vijijini kabisa, na ni maelekezo yetu kama Wizara kuhakikisha kwamba matangazo yote yanayoletwa ya ajira yanakwenda kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri na kuhakikisha yanafika kwenye vijiji husika, yafike kwenye ofisi za vijiji, yafike kwenye ofisi za kata na maeneo yote yaliyo muhimu kwa ajili ya wananchi kupata taarifa, ili ajira hizi ziendelee kukimbiliwa na Watanzania wote kwa usawa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jambo la kuita watu wengi kwenye nafasi chache chache za usaili limekuwa ni jambo sugu na Serikali hamuwezi kulifanyia kazi; je, hamuoni sasa umefika wakati kuwapa posho angalau wale mnaowaita, ili waweze kujikimu wanapokuwa Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo analosema la kutoa posho kwa wanaoomba, hili ni jambo la kibajeti, lakini pia ni jambo la kisera. Kwa hiyo, tutakapokuwa tumejenga uwezo, Mheshimiwa Zuberi Kuchauka na Wabunge wote basi nalo pia litaangaliwa, lakini kwa sasa niseme jambo hilo ni gumu kidogo. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tunajua wanaotakiwa kuajiri Serikali Kuu ni Menejimenti hya Utumishi kupitia Sekretarieti ya Ajira; je, ni lini Serikali sasa itachukua hilo jukumu badala ya kuachia idara zinazojitegemea? Kuachia Wizara nyingine kuajiri watumishi wa Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly Ntate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali iliamua kugatua baadhi ya mamlaka yake na kupeleka kwenye Taasisi na Wizara mbalimbali ili kupunguza lile lundo la watu wote kuja katika sehemu moja, lakini pia tukizingatia professional katika uajiri, lakini mawazo anayotoa Mheshimiwa Mbunge ni mawazo ambayo hata sisi ndani ya Wizara tunayaangalia, lakini nataka nikuhakikishie kwamba mambo yote haya yanakwenda kisera, kimkakati, na baada ya kujiridhisha kwamba tutakapoyachukua kuyarudisha Wizarani au kuendelea kufanya katika njia nyingine yatakuwa na tija kwa ajili ya kusaidia Watanzania inapofika kwenye jambo zima la ajira.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mawazo yako ni mazuri, na sisi kama Wizara tuyachukue na kuendelea kuyafanyia kazi na tutakuja kujulishana vizuri baadae. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mfumo wa ajira ulioko sasa una manung’uniko mengi; Serikali haioni iko haja sasa ya kupitia mfumo wenyewe kwa ujumla ili uwe rafiki kwa vijana wetu walioko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amandus kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati tunawasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, hoja anayoeleza Mheshimiwa Mbunge ilitolewa pia katika kikao kile na yalikuwa ni makubaliano ya Bunge lako kwamba tutayachukua mawazo mazuri yale na kwenda kuyafanyia kazi, na haya yote yatakapokuwa yamekamilika basi yatakuja kuonekana katika sera na sheria ambazo baadae nafikiri zinaweza zikabadilika kutokana na mawazo mazuri ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maagizo ya Bunge yanaendelea kufanyiwa kazi, na tutakapokuwa tayari tutakuja kuleta taarifa katika utaratibu wa vile vikao vyetu.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kabisa ambayo yamekwenda shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa ya sensa ya mwaka 2012 nchi yetu ina jumla ya nyumba 11,873,1950; kati ya hizo, nyumba bora ni 3,444,519 sawasawa na asilimia 37.1 maana yake tuna nyumba 8,429,431 ambazo ni sawa na asilimia 62.9 nyumba hizi sio bora, lakini kati ya hizo nyumba 2,359,906 sawasawa na asilimia 25.4 ni nyumba zimeezekwa kwa nyasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu; nyumba ya kawaida ya vyumba viwili inahitaji shilingi 400,000 kwa maana ya kununua bundle mbili za mabati. Je, kwa nini Serikali isiweke pale shilingi 200,000 kwa mtu ili na yeye achangie shilingi 200,000 ili hatimaye Serikali itumie kama shilingi bilioni 432 kuondoa kabisa nyumba za nyasi katika nchi hii? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; ni kwa nini Serikali isiweke viwango vya nyumba bora, ili kila mwananchi awe anazingatia ujenzi wa nyumba bora? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Joseph George Kakunda, maswali yake mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumekamilisha sera ya nyumba na makazi jibu lako litakuwepo ndani yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali la pili; ni kwamba Wizara imeendelea kuandaa rasimu ya Taifa ya Nyumba ambayo pamoja na mambo mengine itatoa mwongozo wa viwango vya nyumba bora vinavyotakiwa kuzingatiwa na wadau wote. Aidha, sera hiyo itaweka uratibu rahisi wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi vya gharama nafuu, upatikanaji wa mikopo ya nyumba, mfumo wa uratibu wa wadau wa sekta ya nyumba na hivyo kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora kuwa za gharama nafuu, ahsante.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sababu kubwa ambayo inasababisha wananchi waweze kushindwa kujenga nyumba bora ni gharama kubwa ya vifaa vya ujenzi, lakini vifaa hivi ni suala ambalo haliko Wizara ya Ardhi, liko Wizara ya Viwanda na Biashara.

Je, Wizara hii iko tayari sasa kukaa na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuangalia zile sababu zote zinazofanya vifaa kuwa bei kubwa ikiwemo matamko ya viongozi, gharama kubwa za kodi na changamoto nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa mawazo yake mazuri, lakini nataka nimhakikishie tu kwamba yako maelekezo toka kwa Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kukaa na Wizara zote zinazohusika katika eneo hili la ujenzi wa nyumba ikiwemo Wizara ya Ujenzi, ili kuhakikisha kwamba gharama zinakuwa nafuu katika ujenzi, lakini pia katika vifaa na kuhakikisha mazingira yanakuwa mazuri ya upatikanaji wa nyumba zilizo bora na salama.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu ya Serikali. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali inawachukulia hatua gani waajiri wale ambao hawawapi safari hawa wanawake wanaonyonyesha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Serikali haioni imefikia wakati wa kuwa na takwimu sahihi ya wanawake wanaonyonyesha ili kupanga bajeti kuepukana na kisingizio cha ufinyu wa bajeti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hatua gani zimechukuliwa na Serikali, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba hatua zimeendelewa kuchukuliwa kwa waajiri wote ambao hawatekelezi majukumu kwa mujibu wa sheria tulizoziweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu takwimu, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu tumeendelea kuzichukua na kama zipo kesi zozote zile ambazo sisi kama Serikali hatuzifahamu au yeye kama Mbunge anazifahamu, basi ofisi yangu ipo wazi nakaribisha malalamiko hayo ili tuweze kuyashughulikia mara moja. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo linalowakuta wamama wanaonyonyesha limewakuta pia wamama waliopata watoto njiti. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu wamama hawa ambao wana nafasi ya kukaa muda mrefu na wale watoto, lakini mara nyingi waajiri wamekataa kuwalipa na kuwasaidia ili waweze kutekeleza wajibu wao wa kuwalea wanadamu hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wa Bunge lako, swali la pili lililoulizwa na Mheshimiwa Santiel ndiyo lipo katika eneo hilo. Sasa naogopa sana kujibu hapa halafu Mheshimiwa Santiel, tukamwambia kama tulivyojibu swali la nyongeza.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, amesema inategemea na busara; je, haoni kwamba Serikali inahitajika kuweka mkazo kwenye suala hili, kwa sababu siku 90 zile mama hazimtoshi kwa kipindi kile anapomlea mtoto njiti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, Serikali pia haioni haja ya kuweka mkazo kwa wanaume pia kuwasaidia wanawake kwa kuwaongezea likizo ya uzazi wanaume wanaopata watoto njiti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusu kuweka utaratibu, nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba maelekezo ya Bunge lako yalishatoka, lakini pia ni nia ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alituelekeza sisi aliotupa dhamana ya kusimamia Ofisi ya Rais, Utumishi, kuyaangalia mazingira yote yatakayomwezesha mtumishi wa Umma kufanya kazi yake akiwa yupo na furaha ya kutimiza hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo, Serikali imeandaa mwongozo wa ujumuishwaji wa jinsia katika Utumishi wa Umma mwaka 2023 ambao pamoja na masuala mengineyo tunazungumzia jambo la kutoa likizo kwa wazazi wanaopata watoto njiti likiwemo pia jambo hili la kuingiza wanaume katika sehemu ya watu watakaochukua likizo katika kipindi hicho cha kusaidiana kulea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo Serikali italeta mwongozo huu mbele ya Bunge lako, tutajadili kwa pamoja na tukubaliane kimsingi ni njia gani nzuri au ni kipindi gani kizuri cha kuwawekea wazazi hawa ili tuweze kufikia ulezi ulio bora usiochosha kwa mzazi mmoja au kwa mzazi mwingine, ahsante. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa vile mfumo wa TASAF katika Jimbo la Mwibara umekufa, matatizo ni mengi, malalamiko ni mengi; je, ni lini Serikali itafanya upya zoezi la kuwatambua wanufaika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumjulisha Mbunge na pia kulijulisha Bunge lako kwamba mfumo wa TASAF haujafa. Tunazo changamoto katika maeneo mbalimbali ambayo kweli yako matatizo hasa katika eneo la utambuzi na uandikishaji wa wanufaika hao.

Mheshimiwa Spika, nataka nirudie tena kuendelea kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako kwamba kama liko tatizo lolote, ofisi zetu zipo kwa ajili ya kusikiliza na kama taratibu zetu zinavyoeleza, kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri yeyote, basi rufaa zitapelekwa hapo na taratibu kwa ajili ya kutatua matatizo au changamoto zinazotokea yatafanyika.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali ya nyongeza;

(i) Je, nini kauli ya Serikali juu ya waajiri wa sekta binafsi ambao bado wanatumia kigezo hiki cha uzoefu kwenye kutangaza ajira?

(ii) Je, Serikali iko tayari kufufua ule utaratibu maalum uliokuwepo mwanzo na kuutengenezea sera ambao utawatambua na kuwapa kipaumbele wahitimu ambao wanajitolea kwenye ofisi mbalimbali za umma kwa ajili ya kupata uzoefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inafanya jitihada kubwa hasa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha kwamba wale waajiri wanazingatia vigezo ambavyo vinatakiwa katika ukuzaji au uenezaji au ule usimamizi wa soko la ajira. Mojawapo ni katika eneo la watu binafsi ambako nako mara kwa mara tunawaelekeza kwamba lazima vigezo vya kuingia viangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwenye sekta binafsi, pamoja na utaratibu ambao sisi kwenye soko la ajira tumeuzoea lakini ni kweli kwamba kwenye sekta binafsi kinachoangaliwa zaidi ni tija ili kuweza kusaidia mtu aweze kupata faida katika jambo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawazo yaliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge tunayachukua na tutaendelea kuyasimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo la pili; kwa wale wahitimu ambao wanaomba kazi, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inawatambua; na sasa tuko katika hatua za mwisho, kama nilivyowahi kueleza mwanzo, ya kukamilisha ule muundo mzima au taratibu nzima za jinsi wao pia tunawaingiza katika soko la ajira kwa kuzingatia vigezo. Vigezo hivyo ni pamoja na kigezo cha kuwajengea uwezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa maana ya lugha ya internship, lakini pia, kuweka vigezo vingine ambavyo vitawasaidia vijana waweze kuingia katika soko la ajira kirahisi, nashukuru.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nashukuru, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kuna Walimu waliajiriwa 2013 na kumekuwa na upandishwaji wa madaraja kwa makundi huku Walimu walio wengi wakiachwa nyuma bila kupandishwa madaraja kutoka 2013. Ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha Walimu hawa wanapandishwa madaraja?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa kuna kundi kubwa sana la Walimu wa Jimbo la Ngara ambao ni Walimu wa grade A ambao walitakiwa kuwa wamepandishwa mpaka kuwa grade G mpaka sasa hivi lakini wengi wameachwa nyuma na michakato hiyo. Ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha Walimu hawa wanapandishwa madaraja? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika majibu ya msingi, kwa kuwa vipo vigezo vinavyotumika kwa ajili ya kupandisha madaraja Walimu, nataka kulihakikishia Bunge lako kwamba ule uchambuzi wa uhakiki uliokuwa unafanyika umekwishakamilika kwa upande mmoja ambapo katika Mwaka huu wa Fedha unaokwisha 2023/2024, Serikali inatarajia kupandisha Walimu 52,551 wakiwemo Walimu 148 wa Halmashauri ya Ngara ambao wamekwishatimiza vigezo vinavyotakiwa. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba, Walimu hawa tutawapandisha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la Walimu ambao wamepandishwa katika grade nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Halmashauri ya Ngara kwamba, Serikali ilifanya uhakiki na uchambuzi wa walimu 283,193 wa halmashauri zote nchini. Katika uchambuzi huo tulibaini kwamba Walimu 54,242 wamekwishatimiza vigezo kwa wale ambao wanapandishwa madaraja na kati ya hao Walimu 540 wakiwemo wa Halmashauri ya Ngara na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Kagera, ambao walikumbwa na changamoto hizo wamethibitika kwamba wamepata vigezo hivyo, wote kwa pamoja nao tutaweka katika mserereko ili waweze kufika katika madaraja wanayotakiwa.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Utumishi, alipokuja Iringa alikutana na tatizo la Watendaji ambao walikuwa wamejitolea muda mrefu na hawakupata ajira na aliwaambia kwamba wawaajiri na mpaka leo hawajaajiriwa: Je, ni kwa nini baadhi ya Wakurugenzi hawatimizi matamko yale ambayo Mawaziri wanatoa?

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati alikuja Naibu Waziri wa Wizara gani?

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, alikuja Naibu Waziri wa Utumishi.

SPIKA: Mheshimiwa nani?

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nilipokuwa kwenye ziara Mkoa wa Iringa kwenye Manispaa ya Iringa nilikutana na changamoto ya vijana ambao walikuwa wamejitolea ambao walikuwa wamefanya kazi kwa takribani miaka miwili, lakini pamoja na kwamba walikuwa wamefanya hivyo ilipofika kwenye jambo la ajira, walipokwenda kufanyiwa usaili walionekana kwamba hawafai, lakini Serikali kupitia taratibu zake ilijiridhisha kwamba kulikuwa na sintofahamu katika mchakato huo.

Mheshimiwa Spika, tulielekeza kwamba mchakato ule urudiwe tena lakini pia wale vijana waliokuwa wanajitolea ambao walionekana kuonewa warudishwe kazini mara moja. Sasa juzi nilikuwa naongea na Mheshimiwa Mbunge akanihakikishia kwamba wale vijana bado hawajaajiriwa. Sisi kama Serikali tumeshatoa maelekezo kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi kulishughulikia jambo hilo mara moja. (Makofi)

SPIKA: Hebu kidogo hapo kwenye hawafai, hebu fafanua kidogo kwenye “hawafai.”

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa tulizopewa pale, vijana wale walionekana kwamba wamefeli katika mtihani, lakini kiukweli ni kwamba kulionekana kuna figisu zimefanyika katika kuhakikisha kwamba wamefikia hayo matokeo na ndipo Serikali ilipoelekeza mchakato huo uangaliwe tena upya. Ndiyo maana mpaka sasa hivi tunapozungumza hapa hakuna majibu ya wale ambao wameshaajiriwa kwa sababu ziko taratibu zinazofanyika. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimesikia majibu ya Naibu Waziri, niseme kwamba sijaridhishwa. Nataka kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba watumishi elfu mbili na kitu wame…..

SPIKA: Mheshimiwa Maganga subiri kidogo. Hujaridhishwa kwa maana ya kwamba jibu la Mheshimiwa Waziri halijajibu swali lako…

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ndio maana nataka niulize maswali mawili…

SPIKA: Maana kazi yangu ni kusimamia kanuni hapa mbele ili kama unaona swali lako halijajibiwa kikamilifu, huwezi kuuliza maswali ya msingi, maana yake jibu halipo.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, hapana, nipe nafasi niulize maswali mawili, labda nitapata majibu. (Kicheko)

SPIKA: Sasa inabidi uwe umeridhika na hayo majibu ndiyo uulize, kwamba haya majibu yaliyoko hapa, lakini bado una maswali ya nyongeza. Kwa hiyo, endelea Mheshimiwa, nimeelewa kwamba umeridhika na majibu sasa unataka kuuliza maswali yako ya msingi. (Makofi)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba pamoja na watumishi elfu mbili na kitu hao waliobainika, nataka kujua, wangapi ambao wamefungwa kwa ajili ya makosa ya kutuhujumu wananchi pamoja na Mheshimiwa Rais anatafuta pesa anapeleka kwenye miradi ya maendeleo? Nawe ni shahidi, umesema kwamba watu elfu mbili na kitu walibainika; wangapi walioko magerezani mpaka sasa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Serikali ya Awamu ya Tano ilitangaza kwamba itatengeneza Magereza ya Mafisadi ambao wanabainika ili wasiende moja kwa moja Mahakamani, wakae kwenye lockup za Mahakama ya mafisadi? Je, hamuoni sasa ni wakati muafaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge la kutaka kujua wangapi wapo magerezani; naomba nisiwe muongo mbele ya Bunge lako naomba nijiridhishe juu ya idadi kamili ili niweze kuja kumwambia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, swali la pili juu ya utekelezaji wa magereza maalum kwa ajili ya hawa wanaohujumu uchumi wetu, nadhani jambo hili linategemea zaidi upatikanaji wa fedha ili kuweza kutekeleza azma hiyo ya viongozi wetu kama ambavyo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa atatekeleza yale yote ya walitangulia kabla yake na ya kwake yeye ni kuandaa Tanzania anayoitaka, ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tunafahamu kwamba Baraza la Madiwani ni mamlaka ya nidhamu kwa watumishi ngazi ya halmashauri. Je, Mkurugenzi ana mamlaka ya kutengua maamuzi ya Baraza la Madiwani pale wanapobaini kwamba watumishi wamefanya makosa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, maamuzi ya Baraza la Madiwani hayapingwi na mtu yeyote na maamuzi hayo ni maamuzi yaliyokamilika ikiwa yamefuata taratibu na kama kuna mtu yeyote ambaye hatoridhika na maamuzi hayo, basi taratibu za kisheria zimewekwa wazi ili kuweza kutengua maamuzi hayo na siyo Mkurugenzi kujipa mamlaka juu ya maamuzi yanayofanya na Baraza la Madiwani. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Amina. Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni mpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini niongezee kwenye jibu alilolitoa kwa Mheshimiwa Genzabuke. Kamati ya Halmashauri inapojigeuza kuwa Kamati ya Nidhamu, Katibu wake ni Mkurugenzi na Wajumbe ni wale Madiwani. Sasa haiwezekani Katibu na ile Kamati wamefanya maamuzi halafu Katibu akaenda akageuza. Kama kulikuwa kuna mabadiliko hayo basi angepaswa kurudi tena kwenye Kamati ile ile ili aweze kugeuza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutajaribu kulichukua kwa kushirikiana na TAMISEMI, tulifuatilie tuone kilichotokea hasa ni kitu gani, ahsante sana. (Makofi)