Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Ridhiwani Jakaya Kikwete (35 total)

MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itayachukua Mashamba Pori yasiyoendelezwa kwa Shughuli iliyokusudiwa yakiwepo Mashamba ya Aghakan, Lucy Estate na Gomba Estate na kuyagawa kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada waliyofanya wenzangu naomba kabla sijajibu swali nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunichagua mimi na mwenzangu Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula kuwa katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; ahadi yangu kwake na kwa viongozi wote wa juu yetu ni kwamba hatutowaangusha tutafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kwa ruhusa yako nijibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, hatua za ubatilishaji wa milki nchini hutekelezwa ikiwa mmiliki wa shamba au kiwanja amekiuka masharti ya umiliki yaliyoainishwa kisheria.

Mheshimiwa Spika, Shamba la Agakhan kwa sasa lipo ndani ya eneo la mpangomji ambalo limeingizwa kwenye Mpango Kabambe wa uendelezaji wa Jiji la Arusha. Kwa kuzingatia mpango huo, eneo la shamba hilo limepangwa kuendelezwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu, eneo la biashara na makazi. Mmiliki wa eneo hilo alipaswa kuendeleza kwa kuzingatia mpango huo. Kutokana na kubadilika kwa mpango wa matumizi ya eneo hilo, Serikali ipo katika mazungumzo na mmiliki ili kuona namna bora ya kutekeleza mpango huo.

Mheshimiwa Spika, shamba la Gomba Estate ni miongoni mwa mashamba ambayo wamiliki walichukua mikopo na kushindwa kurejesha kwa hiyo shamba hilo kwa sasa lipo chini ya uangalizi wa taasisi ya benki ya Standard Chartered na Shirika la NSSSF. Ili kutatua changamoto ya urejeshaji wa mkopo, Serikali kwa kushirikiana na wamiliki na taasisi tajwa imeanza zoezi la kupanga, kupima ardhi husika ili kupata viwanja vitakavyouzwa ili mkakati wa kurejesha mkopo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu shamba la Lucy Estate, miliki ya shamba husika ilibatilishwa mwaka 1999 kutokana na kukiukwa kwa masharti ya umiliki. Hata hivyo, mmiliki wa shamba hakukubaliana na hatua hiyo na hivyo alifungua shauri Na. 50/2015 katika Mahakama Kuu ya Arusha dhidi ya Serikali kupinga ufutaji huo. Baada ya majadiliano ya kisheria, ilikubaliwa kwamba aliyekuwa mmiliki alipwe fidia ya maendelezo yaliyokuwepo. Hivyo, Serikali inaandaa mpango wa matumizi wa shamba hilo kwa ajili ya matumizi mbalimbali na sehemu ya shamba husika itatumika kupata fedha kwa ajili ya fidia.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Kata ya Makurunge watapatiwa eneo la makazi la Razaba baada ya maeneo yao kuchukuliwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 147 la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati eneo hili linachukuliwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji wananchi waliokuwa wakazi wa eneo hilo walilipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria. Aidha, tunatambua uwepo wa wananchi 16 ambao wamekuwa wakidai kulipwa fidia zao, Serikali inaendelea kushughulikia madai hayo na yatakapokuwa tayari tutawapa taarifa.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wa Kata ya Majengo Tunduma waliovunjiwa nyumba zao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 133 lililoulizwa na Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kabla sijajibu swali nitoe maelezo machache ya utangulizi. Kikao cha Makatibu Wakuu wa Nchi za Tanzania na Zambia kilichofanyika mwezi Oktoba, 2013, pamoja na mambo mengine kiliazimia kwamba alama za katikati ya mpaka (Intermediate Boundary Pillars) kwa sehemu ya mpaka yenye urefu wa kilomita 50 ziongezwe ili kuzuia ongezeko la shughuli za kibinadamu na pia eneo la hifadhi ya mpaka lipunguzwe kutoka mita 100 kila upande zilizokuwa zinatambulika hapo awali hadi mita 50 kila upande. Hata hivyo, pamoja na maazimio hayo kutekelezwa, baadhi ya wananchi waliendelea kuvamia eneo la hifadhi ya mipaka kwa kujenga makazi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017, Serikali ilitoa tamko la kuvunja nyumba zote zilizojengwa katika eneo la hifadhi ya mpaka suala ambalo lilipingwa na wananchi 134 kwa kufungua Shauri Na. 195/2017 katika Mahakama Kuu, Mbeya. Shauri hilo lilifutwa mwaka 2019 na hatimaye jumla ya nyumba 193 zilizokuwa ndani ya eneo la mita 50 za hifadhi ya mpaka zilibomolewa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hiyo, wananchi 35 walifungua tena shauri Na. 12/2019 katika Mahakama Kuu Mbeya kudai fidia kutokana na kubomolewa kwa nyumba zao. Baada ya mazungumzo nje ya Mahakama (mediation) yenye lengo la kuwapatia viwanja mbadala, wananchi hao kushindikana, shauri hilo limepangwa kuendelea kusikilizwa tarehe 5 Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua shauri hilo na kauli yetu ni kwamba tusubiri mwongozo au maamuzi ya mahakama ili tujue hatua zinazofuatia.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kurekebisha ramani ya nchi yetu baada ya baadhi ya maeneo kujazwa mchanga kuongeza ukubwa wa ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali namba 80 la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali la msingi la Mheshimiwa Mbunge, napenda kutoa maelezo mafupi kuwa, ukubwa wa eneo na mipaka ya nchi unajulikana na ipo bayana. Hivyo kujazwa mchanga kwenye baadhi ya maeneo hakuongezi wala kupunguza ukubwa wa eneo la nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ramani ya nchi inaonesha sura ya nchi huandaliwa ili kuonyesha hali halisi iliyopo ardhini ikijumuisha taarifa za kijiografia za asili ambazo ni pamoja na mito, maziwa, milima na bahari; na zile zisizo za asili ambazo zinazojumuisha barabara, reli, mabwawa na miji. Moja ya sababu ya kuhuisha ramani ni kuonesha uhalisia wa sura ya nchi na kuhakikisha kuwa mabadiliko yanayotokea katika ardhi yanaoneshwa kwenye ramani mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ina mpango wa kuandaa ramani mpya nchi nzima zinazoonesha sura ya nchi Tanzania Bara. Ramani hizo zitaandaliwa kupita mipaka kupitia Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Upimaji na Ramani (Project for Improvement of National Land Data Infrastructure) utakaotekelezwa kwa mkopo utakaotolewa na Serikali ya Korea kwa muda wa miaka minne (2022/23 -2025/2026).
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali ipo tayari kufanya mapitio ya upimaji wa vijiji nchini kwa kuwa migogoro mingi imesababishwa na upimaji usio shirikishi wa mwaka 1970?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kabla ya kujibu swali lake la msingi kuwa kilichofanyika katika miaka ya 1970 haikuwa upimaji wa vijiji bali ilikuwa ni Operesheni Maalum ya Serikali ya kuanzisha Vijiji vya Ujamaa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 2000 Serikali ilitekeleza Programu ya upimaji wa vijiji kwa lengo la kuvifanya vijiji kuwa mamlaka kamili za usimamzi wa ardhi za vijiji. Mathalani, katika Mkoa wa Lindi jumla ya vijijii 401 kati ya vijiji 523 vikiwemo Vijiji vya Wilaya ya Liwale vilipimwa kwa njia shirikishi na kuwekewa alama za mipaka.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya wakulima na wafugaji katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazosabisha migogoro ya matumizi ya ardhi ikiwemo hiyo ya wakulima na wafugaji. Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha migogoro ya matumizi ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro hususan Wilaya ya Kilombero inatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kumilikisha ardhi kupitia Mradi wa Kuwezesha Umilikishaji wa Ardhi (LTSP) ambapo jumla ya vijiji 58 viliandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na Hakimiliki za Kimila 150,006 zilisajiliwa. Kati ya vijiji hivyo 58, vijiji 32 vipo katika Halmashauri ya Mlimba ambapo jumla ya Hakimiliki za Kimila 41,797 zimesajiliwa na 30,699 zimechukuliwa na wananchi.

Mheshimiwa Spika, nasisitiza Serikali za Halmashauri kuhakikisha zinasimamia mipango ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa ili kupunguza uwezekano wa kuibuka au kuendelea kwa migogoro baina ya watumiaji wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kudhibiti na kuimarisha mbinu za utatuzi wa migogoro kwa kutoa elimu kupitia mikutano ya wananchi kuhusu mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa kwa pamoja, kutungwa kwa Kanuni za Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi na kuhimiza matumizi ya ardhi yenye tija.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta zitaendelea kudhibiti na kushughulikia migogoro na kuitafutia ufumbuzi iliyopo ili kuimarisha ustawi wa jamii baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kutatua migogoro ya ardhi kati ya Wananchi na Wawekezaji wenye mashamba makubwa Kibaha Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendelo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 17 la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua jitihada za kutatua migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika maeneo mbalimbali hususan katika Jimbo la Kibaha Vijijini. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufanya ukaguzi wa ardhi iliyomikishwa kwa wawekezaji ili kubaini iwapo masharti ya umiliki yanazingatiwa.

Pili, kuchukua hatua za ubatilisho kwa wawekezaji waliobainika kukiuka masharti ya uwezekezaji; na Tatu, kupanga upya ardhi iliyobatilishwa kwa kushirikiana na Mamlaka za Upangaji kulingana na mahitaji halisi ya sasa hususan hazina ya ardhi, huduma za kijamii na makazi. Aidha, Wizara inaendelea kutoa elimu kwa jamii na wawekezaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na miongozo ya sekta ya ardhi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani juu ya mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji na hayatumiki kuzalisha mali na ajira nchini?
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa yapo mashamba makubwa nchini ambayo yamegawiwa kwa wawekezaji ambapo baadhi ya mashamba hayo yanatumika kwa uzalishaji mali na ajira na mengine hayatumiki kama ilivyokusudiwa. Wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine imeanza kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji kwa kufanya ukaguzi na kuainisha changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni kufanya majadiliano na wawekezaji waliobainika kuwa na changamoto ili kuzipatia ufumbuzi kwa pamoja kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji. Kwa mashamba ambayo yametelekezwa, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wamiliki walioshindwa kutekeleza masharti ya uwekezaji ikiwemo kuyarudisha na kuyapangia matumizi upya kwa manufaa ya umma.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya Wafugaji na Wakulima katika Wilaya za Liwale, Nachingwea na Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa Niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kumjibu swali lake Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Mkoa wa Lindi Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya ardhi katika Wilaya zote zilizotajwa ikiwemo Liwale, Nachingwea na Kilwa, lakini pia ni pamoja na maeneo ya Lindi Vijijini. Migogoro hii inatokana na kuongezeka kwa mifugo katika maeneo hayo, changamoto ya tafsiri ya mipaka ya ardhi katika vijiji hivyo, usimamizi mbovu wa mipango ya matumizi ya ardhi. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo kimsingi ndiyo suluhisho la migogoro ya mwingiliano baina ya watumiaji wa ardhi. Hadi sasa jumla ya vijiji 114 katika Wilaya ya Kilwa, Nachingwea na Liwale vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2204, Serikali imepanga kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 40 ikiwemo Liwale (17), Nachingwea (12) na Kilwa (11) katika Mkoani wa Lindi, ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali kuhusu majengo yaliyopo maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 45 lililoulizwa na Mheshimiwa Tarimba Abbas Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba majengo yote yaliyosimama yaendelezwe kwa kikamilifu kama ilivyoainishwa kwenye milki zao na vibali vya ujenzi ili majengo hayo yasitumike kwa matumizi yasiyofaa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, Serikali ina kauli gani juu ya maeneo ya ardhi yanayotumika na Serikali au Taasisi zaidi ya miaka 12 yakiwa hayana hatimiliki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 62 lililoulizwa na Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa maeneo mengi yanayomilikiwa na Taasisi za Umma yana hatimiliki. Hata hivyo, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa maelekezo kwa Taasisi na Idara za Umma kuhakikisha maeneo yao yanapangwa, kupimwa na kupatiwa hatimiliki.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya Wakulima na Wafugaji Kata za Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mtibwa, Kanga, Mziha na Doma?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali Na. 63 la Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kata za Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mtibwa, Kanga, Mziha na Doma Wilayani Mvomero. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo hatua ya mwaka 2013 ya kutenga kwa kutumia fedha za ndani kwenda kutatua migogoro katika jumla ya vijiji 72 kati ya vijiji 130 vilivyomo katika Wilaya hiyo ambavyo vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kurasimisha, kupanga na kupima ardhi katika Miji Midogo ya Mawengi, Lugarawa, Luilo na Manda – Ludewa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 89 lililoulizwa na Mheshimiwa Joseph Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Wizara kupitia Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi iliikopesha Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kiasi cha shilingi milioni 405 kwa lengo la kupanga na kupima na kurasimisha miji midogo ya Mlangali, Mavanga, Ludewa na Mudindi ambapo jumla ya viwanja 7,911 vimepangwa na viwanja vingine 2,120 vimekamilika katika utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa maelekezo wataalamu wa ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kuanza kukusanya takwimu muhimu kwa ajili ya kupanga na kupima katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.
MHE. NANCY H. NYALUSI K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarudisha Shamba la Kijiji cha Ng’ang’ange kwa wananchi kufuatia mauziano kati ya EFATHA na Kijiji kutofuata sheria?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2003 Taasisi ya Efatha Ministry iliomba eneo lenye ukubwa wa ekari 200 katika Kijiji cha Ng'anga'nge kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi, Kilimo na Mifugo. Taratibu zote za utoaji eneo husika zilifuatwa ikiwemo Kikao cha Halmashauri ya Kijiji, Mkutano Mkuu wa Kijiji na Kamati ya kugawa ardhi ya Wilaya pamoja na fidia za mali zililipwa.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini maeneo mengi ya Mji wa Lushoto yatapimwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, halmashauri ni mamlaka ya upangaji kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, hivyo majukumu ya kisheria ya kutenga bajeti, kwa ajili ya kupanga na kupima yapo ndani yao. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetoa mkopo wenye thamani ya shilingi bilioni 55.6 kwa halmashauri 55, Vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro na Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam, kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa halmashauri zilizokopeshwa fedha hizo ambapo jumla ya shilingi milioni 208 zimetolewa kwa ajili ya kupima viwanja takriban 2,600 katika maeneo ya Lushoto Mjini, Mnazi, Mlola, Mlalo na Lukozi. Pamoja na jitihada hizi za Serikali, natoa rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Halmashuri zote nchini kuhakikisha kuwa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa viongozi wanaowanyima wananchi kwa makusudi haki yao ya kuwa wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali namba 18 lililoulizwa na Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji naomba kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini. Nataka nimwakikishie yeye na watanzania wote kwamba tutaendelea kufanya kazi na kazi itaendelea.

Mheshimiwa Spika, Sasa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, zoezi la utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni zoezi shirikishi na hujumuisha Wataalam kutoka Halmashauri, Maafisa wa TASAF, Wananchi wa maeneo husika yanayosimamiwa na viongozi wa vijiji/mitaa/shehia.

Mheshimiwa Spika, inapotokea kiongozi au viongozi wamewanyima haki wananchi kwa makusudi bila sababu yoyote ile hatua zifuatazo huchukuliwa dhidi yao: -

(a) Endapo uongozi wa vijiji/mitaa/shehia utashinikiza kuondoa majina ya kaya kwenye orodha ya utambuzi bila kuafikiwa na jamii, zoezi la utambuzi husitishwa na taarifa hupelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri/Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar) na nakala hupelekwa kwa Mkurugenzi wa TASAF.

(b) Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri/Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar) huchunguza tuhuma hizo na ikithibitisha tuhuma hizo mhusika husitishwa kujihusisha na shughuli zozote za Mpango wa TASAF. Aidha, baada ya kusimamishwa, mhusika huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kupewa karipio au kuondolewa kwenye nafasi yake.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzisaidia Kibajeti Taasisi za Wenza wa Viongozi Wakuu wa nchi ili ziweze kujiendesha na kupata ufadhili?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ta Utumishi wa Umma na Utawala Bora naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakar Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria za nchi, taasisi za wenza wa viongozi wakuu wa nchi zinasajiliwa na kuendeshwa kwa taratibu zinazotumika kusajili na kuendesha taasisi nyingine binafsi na zisizo za Kiserikali. Hadi sasa Serikali haina mwongozo wa kisheria au kikanuni unaoielekeza kutoa usaidizi wa kibajeti kwa taasisi za wenza wa viongozi wakuu wa nchi.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi wa Mkoa wa Katavi kila mwaka kwa kuendelea kutenga Ikama na Bajeti kama inavyopitishwa na Bunge lako. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali ilitenga nafasi 522 za kada mbalimbali kwa Mkoa wa Katavi na katika mwaka wa fedha ujao (2023/2024) tunakusudia kutenga Ikama ya ajira mpya 914 kwa Mkoa wa Katavi iwapo Bunge lako likiridhia na kuipitisha Bajeti ya Serikali iliyopendekezwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi wa kada ya ulinzi, upishi na makatibu muhtasi katika shule za sekondari za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali namba 82 lilliloulizwa na Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ajira kila mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga nafasi 201 za Makatibu Muhtasi na tano za Wapishi. Watumishi husika wataajiriwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. Aidha, kwa katika Kifungu cha 6(1) cha Sura ya 298 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Toleo la 2019, Waajiri mbalimbali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa hutenga bajeti kwa kuzingatia kada na maeneo yote ya vipaumbele ikiwemo Walinzi, Wapishi na Makatibu Muhtasi na kuwapanga katika maeneo yenye uhitaji ikiwemo shule za sekondari za kata nchini.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutimiza masharti ya ajira kwa Watumishi ikiwemo kuwapandisha madaraja na stahiki zingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza matakwa ya kisera, kisheria na miongozo mbalimbali ya kiutawala na kiutumishi inayolenga au inayoelekeza Serikali katika kumtimizia masharti na haki za mtumishi wake. Aidha katika kufanya hivyo Serikali imeendelea na Utaratibu wa kupandisha madaraja watumishi ikiwemo utaratibu wa mpandisho wa mserereko. Pamoja na hilo Serikali imeendelea pia kuongeza kima cha chini cha mshahara na pia kuongeza allowance katika kazi za ziada na posho za muda wa ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo pia mwaka 2021/2022, Serikali ililipa shilingi bilioni 124.3 kwa watumishi 75,007 ikiwa ni malimbikizo (arrears) ya mishahara. Vilevile, Serikali iliongeza umri wa watoto wa watumishi wa umma kunufaika na huduma ya bima kutoka miaka 18 hadi miaka 21 ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya watoto 65,353 wamesajiliwa.
MHE. AMINA DAUD HASSAN aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kufuatilia miradi ya TASAF iliyokamilika ili kuhakiki uendelevu wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daud Hassan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kuhakikisha kuwa miradi ya TASAF inakuwa endelevu, jamii huunda kamati ya matunzo na ukarabati ambayo jukumu lake ni kuweka sheria na taratibu za kusimamia matunzo na kuendeleza miradi hiyo. Mradi unapokamilika hubaki chini ya uangalizi wa wataalamu na TASAF wakishirikana na Halmashauri husika kwa kipindi cha miezi sita na baadaye mradi huo hukabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika ambayo huendelea na jukumu la usimamizi, uendeshaji na matengenezo kwa kushirikiana na idara au taasisi inayohusika na miradi hiyo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2019 Serikali ilifanya majaribio ya mfumo wa kieletroniki wa malipo kwa walengwa katika mamlaka za utekelezaji 19. Baada ya majaribio, mwaka 2020 mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki ulipitishwa rasmi na walengwa kuanza kutumia mfumo huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kutokea changamoto katika baadhi ya maeneo ya utekelezaji. Hivyo utaratibu wa malipo kwa sasa upo katika njia tatu; kwa njia ya simu, akaunti ya benki na njia ya malipo ya fedha taslimu.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu ni uchaguzi wa mnufaika mwenyewe atumie njia gani kadri ya mazingira yake. Aidha, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge tusaidiane kuelimisha walengwa juu ya njia hizi kuu tatu za malipo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafufua upya Tume ya Taifa ya Mipango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali namba 138 lililoulizwa na Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya Muswada wa Sheria kuanzisha Tume ya Mipango. Muswada huu unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni katika Mkutano huu wa Kumi na Moja wa Bunge lako unaoendelea sasa. Muswada wa Sheria ukipitishwa Bungeni, Tume ya Mipango inatarajiwa kuanza shughuli zake katika mwaka wa fedha 2023/2024 yaani tarehe 1 Julai, 2023.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wanaojitolea kutumikia katika kada mbalimbali za utumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu Swali Na. 239, lililoulizwa na Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iliweka mazingira ya kuwawezesha vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali kujitolea katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia sifa za ziada zitakazowawezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali za ajira zinapotangazwa. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kifungu Na. 2.1.2 cha Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la Mwaka 2008 na Kanuni D. 6 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 ikisomwa pamoja na Kanuni Namba 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, ajira kwa nafasi zilizo wazi katika Utumishi wa Umma hujazwa kwa ushindani na uwazi kwa kufanya usaili na kupata washindi katika nafasi husika.

Mheshimiwa Spika, hivyo, nitumie nafasi hii kuwashauri na kuwahamasisha vijana wanaojitolea katika kada mbalimbali za utumishi wenye sifa stahiki, kuomba nafasi za kazi pindi zitakapotangazwa ili waweze kushindana na waombaji wengine wenye sifa stahiki.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ni watumishi wangapi wa umma wamefikishwa Mahakamani kwa rushwa, wangapi wameshinda kesi na kurejeshwa kazini kwa kipindi cha 2010 – 2020?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2010 mpaka 2020, jumla ya Watumishi 2,060 walifikishwa Mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali ya rushwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 ya Sheria za Tanzania. Kati ya watumishi hao 2,060 walioshtakiwa, watumishi 1,157 walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu mbalimbali kwa mujibu wa sheria, huku watumishi 863 wakishinda kesi na kuachiwa huru waendelee na kazi.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza: -

Je, lini Serikali itarekebisha Sheria za Utumishi zilizopitwa na wakati hasa kipindi hiki cha teknolojia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kuendelea kudumu katika Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora. Sasa naomba kujibi swali la Janejelly James Ntate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa maendeleo makubwa ya kiteknolojia ambayo yamekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa Umma. Ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, Serikali imeendelea kufanya mapitio ya Mfumo wa Kisheria unaosimamia Utumishi wa Umma ambapo mwaka 2019 Serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Serikali Mtandao Namba10 ya Mwaka 2019 ili kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitishwa kwa Sheria hiyo kumeisaidia Serikali kuboresha utendaji kazi wake kupitia matumizi ya teknolojia. Pamoja na mambo mengine Sheria hiyo imewezesha kusanifiwa na kujengwa kwa jumla ya mifumo zaidi ya 860 ya TEHAMA Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na hatua za kupitia na kufanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zinazosimamia Utumishi wa Umma na Kanuni zake ili kuhakikisha kwamba zinaendana na mabadiliko ya teknolojia.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Ajira ya Utumishi wa Umma kuongeza kigezo cha kujitolea ili kutoa fursa kwa wanaojitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisau, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inafanya mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura Na. 298, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la mwaka 2008, Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 na Miongozo inayohusu masuala mbalimbali likiwemo suala la ajira.

Mheshimiwa Spika, endapo itabainika bayana kigezo cha kujitolea kitatakiwa kuingizwa katika marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Serikali italeta Marekebisho ya Muswada wa Sheria Bungeni kwako. Kwa sasa Serikali imeandaa mwongozo unaoweka mazingira wezeshi kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali kujitolea katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia uzoefu utakaomuwezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali zitakapotangazwa.

Mheshimiwa Spika, mwongozo huu unalenga kuziba ombwe lililopo kutokana na kutokuwa na utaratibu mmoja ndani ya Taasisi za Umma kuhusu kujitolea.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa semina elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya mara kwa mara kuhusu utawala bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kutoa semina elekezi kwa viongozi wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Katika kipindi cha mwezi Februari hadi Agosti, 2023, Serikali ilitoa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya ambapo agenda moja wapo ilikuwa ni ya utawala bora.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali inaajiri kwa kigezo cha mwaka wa kumaliza chuo na kupitia mafunzo ya jeshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kutoa ajira kwa kada mbalimbali zinazohitajika katika Utumishi wa Umma, Serikali imekuwa ikizingatia Sera ya Menejimenti ya Ajira na Utumishi wa Umma Toleo la 2 la mwaka 2008 aya ya 4.2 ambayo inataka zoezi la ajira katika Utumishi wa Umma liendeshwe kwa wazi na ushindani ili kuwezesha Serikali kupata watumishi wenye utaalam na sifa stahiki kwa kuzingatia uwezo, weledi na umahiri wa waombaji fursa za ajira.

Mheshimiwa Spika, ili kuleta ushindani katika soko la ajira, vigezo mbalimbali hutumika kuzingatia mazingira maalum au mazingira mahsusi ya waajiri. Katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi zilizoingia katika mfumo wa Jeshi USU kutokana masharti ya kazi hizo na mahitaji maalum au mahsusi ya vyombo husika, ajira zinazotolewa kwa kigezo cha ukomo wa umri na kigezo cha kupitia Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, kada nyingine katika Taasisi za Umma nje ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi zenye mfumo wa Jeshi USU kigezo cha Kupitia Mafunzo ya Jeshi hakitumiki. Hata hivyo, waombaji wa fursa za Ajira Serikalini kwa masharti ya kudumu Serikali wanatakiwa kuzingatia Kanuni ya D. 39 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 ambayo inawataka wasiwe na umri usiopungua miaka 18 na wasiozidi umri wa miaka 45 kwa lengo la kuwawezesha kuchangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii walau kwa miaka 15 ili kustahili kulipwa pensheni.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaweka wazi vigezo vya kubaini kaya maskini zinazostahili kupokea msaada wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kumjibu Mheshimiwa Injinia Mwanaisha Ng’azi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, vigezo vya utambuzi wa kaya za walengwa viko wazi na vinatambulika. Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo ili kuweka record sawa katika Bunge lako:-

(i) Kaya ambazo hazina uwezo wa kupata kwa uhakika angalau milo miwili kwa siku;

(ii) Kaya isiyo na kipato cha uhakika na inayo wategemezi wengi wakiwemo watoto wanaokosa huduma za elimu na afya;

(iii) Kaya zinazoishi kwenye makazi duni yanayohatarisha usalama wa kaya;

(iv) Wazee wasio na msaada wowote;

(v) Watoto wanaoishi wenyewe bila wazazi au walezi.

Mheshimiwa Spika, vigezo hivi ndivyo vimewezesha Serikali kuweza kuhudumia kaya za walengwa 1,378,000 ambao wanaendelea kunufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF).
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-

Je, kwa nini viongozi wastaafu wa vitongoji na vijiji wenye sifa siyo wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uratibu wa awamu ya kwanza ya mpango wa kunusuru walengwa wa kaya maskini ulipoanza, taratibu zilibainisha kuondoa baadhi ya makundi wakiwemo watumishi wastaafu wanaopokea pensheni, watu walioajiriwa na kuwa na kipato cha uhakika, Viongozi wa Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Usimamizi za Jamii miongoni mwao ni Viongozi wa CCM katika ngazi za Kata na vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia maboresho ya taratibu za utambuzi na uandikishaji wa walengwa ya mwaka 2021, Kaya za Viongozi wa kisiasa wakiwemo Mabalozi wa Nyumba Kumi na Viongozi waliopo na wastaafu wa vijiji na vitongoji zinazokidhi vigezo zilipewa fursa ya kutambuliwa na kuandikishwa kwenye mpango huo wakati wa zoezi la utambuzi na uandikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa viongozi wastaafu wa vijiji na vitongoji ambao kipindi cha zoezi la utambuzi wa walengwa linafanyika walikubalika na jamii kuorodheshwa awali kuwa katika kaya maskini wajiandishe ili nao waweze kuingia katika mpango huo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kuwapandisha vyeo kwa mserereko kufikia daraja wanalostahili watumishi waliosubiri zaidi ya miaka 8 Kyerwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji vyeo kwa mserereko ni utaratibu unaotumika kuwapandisha vyeo watumishi ambao imethibitika kuwa walicheleweshwa kupandishwa vyeo kwa wakati kwa kuzingatia miongozo ya upandishaji vyeo iliyopo, uwepo wa nafasi iliyoidhinishwa katika Ikama na uwepo wa fedha za kugharamia upandishwaji vyeo kwenye bajeti, sifa za kielimu na kitaaluma na utendaji kazi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi wa maelezo hayo, Serikali itakuwa tayari kuwapandisha vyeo kwa mserereko watumishi waliotajwa na Mheshimiwa Mbunge endapo itathibitika kuwa wana sifa zilizoainishwa.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza siku za likizo kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa likizo ya uzazi kwa watumishi kwa mujibu wa Kanuni H12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2009 ambapo pamoja na Kanuni Pili ya Kanuni ya 12 inabainisha kuwa muda wa likizo ya uzazi kwa mtumishi mwanamke ni siku 84 ambazo hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuongeza siku za likizo pale mtumishi anapojifungua mtoto njiti, suala hili halijawekewa utaratibu wa kikanuni kutokana na taratibu wa uendeshaji wa shughuli za Serikali. Hivyo, Mtumishi (Mzazi) anaweza kuomba ruhusa ya kawaida kutoka kwa Mwajiri wake inapotokea changamoto kama hiyo.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, utaratibu gani unatumika kutangaza ajira nchini ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata haki ya kupata taarifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, swali namba 722, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti ya Ajira Toleo Na. 2 la mwaka 2008, Sura ya Nne, Aya ya 4(2) ikisomwa pamoja na ya Kanuni 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, nafasi za ajira katika Utumishi wa Umma ni za ushindani na zinazingatia sifa, taaluma, uwazi na usawa.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, matangazo ya ajira kwa ajili ya kujaza nafasi wazi ndani ya Utumishi wa Umma hutolewa kupitia tovuti za taasisi husika, mitandao ya jamii, magazeti na mbao za matangazo katika ofisi husika. Maombi ya nafasi hizi hudumu kwa muda wa siku kumi na nne 14 kwa kada za masharti ya kawaida na siku 21 kwa waombaji wa nafasi za Watendaji Wakuu na nafasi za Uongozi za Taasisi za Kimkakati.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, nyumba bora ya kuishi inatakiwa kuwa na sifa zipi na ni kwa nini Serikali haiweki ruzuku kwenye vifaa vya ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kumjibu Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge na Chifu wa Wakonongo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba ni mojawapo ya mahitaji muhimu ya mwanadamu. Nyumba bora ni ile yenye huduma bora kwa usalama na afya kwa wakazi wake. Jitihada za Serikali kuhakikisha nyumba bora zinajengwa kwa gharama nafuu ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya uanzishwaji wa viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi, kufanya utafiti na kuwezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kazi za ujenzi na kuhamasisha taasisi za fedha kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na ununuzi wa nyumba.