Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa (31 total)

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyokuwa kwa Nzega Mjini, Mheshimiwa Rais wetu alipokuwa kwenye kampeni katika Jimbo la Bagamoyo aliwaahidi wananchi kuikabidhi kambi ya mkandarasi iliyopo Daraja la Makofia kwa wananchi wa Bagamoyo ili waweze kuanzisha shule ya msingi. Naomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri taratibu zimefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilimjibu Mheshimiwa Bashe, dhamira ya Serikali ya kuhakikisha majengo yanayojengwa na wakandarasi yanatumika baada ya mkandarasi kukamilisha kazi zake katika shughuli zingine za kijamii iko pale pale, lakini utaratibu wa kuyapata hayo majengo ndiyo tunaobishania. Namhakikishia Mheshimiwa Dkt. Kawambwa ombi lake maadam lilifika kwa utaratibu uliotakiwa, tutaendelea kulifanyia kazi kwa utaratibu huu ambao nimemweleza Mheshimiwa Bashe kwa lile eneo la Nzega na tutatumia njia ile ile tuliyotumia kwa shule ile ya Bulunde.
MHE. DKT. SHUKURU KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ingawa ni majibu ambayo mimi na wananchi wangu wa Bagamoyo yanatupa matatizo. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kama atakubali kuielekeza timu hii ya pamoja iliyoundwa ili iweze kukutana na wawakilishi wa wananchi hawa akiwemo Mbunge na Waheshimiwa Madiwani wa jimbo la Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, TANAPA inawatoza fedha wananchi wa Makurunge na Matipwili wanapovuka daraja eneo la Gama katika Mto wa Wami wanapokuwa wanafanya shughuli zao, mtu Shilingi 5,000 na gari Shilingi 25,000, je, nini kauli ya Serikali kuhusu uhalali wa tozo hiyo?
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dokta Shukuru Kawambwa Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ushauri alioutoa nitaufikisha mbele ya Kamati hii maalum. Kwamba pamoja na utaratibu waliojiwekea wa kuweza kutimiza malengo yao kwa mujibu wa kazi walizopewa na hadidu za rejea.Ni jambo jema na ni wazo zuri na litaweza kuboresha matokeo ya kazi wanayoifanya kwa kuwashirikisha pia Mheshimiwa Mbunge pamoja ma Madiwani wanaohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili linlohusiana na TANAPA kuwatoza wananchi ada hizi; kwanza nalisikia kwa mara ya kwanza na kwa kuwa ni suala jipya kujua mantiki yake na sababu zake kwanini liko hivyo nahitaji muda kidogo, lakini kwa wakati huu nikiwa nimesimama hapa naliona lina ukakasi wa namna Fulani. Kwa hiyo namuomba Mheshimiwa Mbunge anipe nafasi, nalishughulikia mara moja katika kipindi hiki hiki cha Bunge na pengine kwasababu ya uzito wake kuwa mkubwa, mchana huu nikutane naye, nitakuwa nimeshafanya mawasiliano angalau ya awali kujua likoje halafu tuweze kutafuta suluhisho lake.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa changamoto za Jimbo la Busega zinafanana na zile za Jimbo langu la Bagamoyo, vijiji viwili, Kijiji cha Kongo na Kijiji cha Kondo ambavyo vilikuwa ndani ya mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya II ambapo mpaka hivi sasa havijaanza kuwekewa umeme. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie kuna mkakati gani wa kuwezesha vijiji hivi kuwekewa umeme kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Mheshimiwa Kawambwa kuna vijiji 12 vimebaki ambavyo nataka tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote 12 vilivyobaki tumeviingiza kwenye REA Awamu ya III.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Kondo pamoja na maeneo ya jirani ambayo ameyataja ni maeneo ambayo yataanza kuwashiwa baada ya Julai. Mwezi wa Septemba na Oktoba kati ya vijiji ambavyo vitawashiwa umeme kwenye Jimbo la Bagamoyo ni pamoja na Kijiji cha Kondo ambacho amekitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Kawambwa ameendelea kufuatilia sana mahitaji ya wananchi wa Bagamoyo kuhakikisha kwamba vijiji vyote na kwa vile viko karibu na Dar es Salaam vinapata umeme wa uhakika.
Nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kawambwa umeme atakaoupata kwenye Vijiji vya Kondo na maeneo ya jirani utakuwa ni umeme ambao utaunganishwa na kilovoti 400 ambao utakuwa haukatiki mara kwa mara.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa vile tatizo la maji katika Mji Mkongwe wa Tukuyu linafanana sana na tatizo la upatikanaji wa maji katika Mji Mkongwe zaidi Bagamoyo, ambapo huduma ya maji iko chini, maeneo mengi hayapati maji hasa eneo la Mji Mkongwe upatikanaji wake wa maji ni mdogo hata Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo iko katika ratiba ya mgao wa maji ambapo inasababisha huduma kuwa nzito katika Hospitali hiyo na maeneo mengine kama Kisutu na Nia Njema hakuna hata mtandao wa maji. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuboresha upatikanaji maji katika Mji wa Bagamoyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba tumekamilisha ukarabati wa mradi wa Ruvu Chini ambao kwa sasa unatoa lita milioni 270 kwa siku, bomba linalosafirisha maji kutoka Ruvu Chini linapita Bagamoyo hadi Dar es Salaam. Sasa hivi tayari Serikali kupitia Wizara ya Maji imeshasaini mkataba kwa ajili ya kuweka mabomba kusambaza maji maeneo ambayo yalikuwa hayana mtandao wa mabomba na sasa hivi tumeanzia maeneo ya Kiluvya na tuna mkataba mwingine ambao Mhandisi Mshauri anatambua maeneo ya kupitisha mabomba ambayo watakwenda mpaka katika Mji wa Bagamoyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza maji tayari tunayo, kilichobaki ni kusambaza. Kwa hiyo, shughuli hiyo itafanyika wakati wowote. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Moja, kwa vile Waziri amekiri kwamba maji yanapatikana kwa mgao: Je, Waziri atakuwa tayari kuiagiza DAWASCO ili iiondoe hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo katika utaratibu wa mgao ili kuweza kuboresha huduma ya afya katika hospitali hii ya Wilaya?
Swali la pili; je, mradi huo wa usambazaji mabomba utajumuisha kata zote tisa za Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bagamoyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shukuru Kawambwa nikuhakikishie, baada ya mradi huu kukamilika mwezi Juni, 2017 Hospitali ya Bagamoyo haitakuwa na matatizo ya maji tena. Katika Mkataba unaoendelea, suala hili limeainishwa kuhakikisha kwamba Hospitali ya Bagamoyo isiwe na matatizo ya maji tena.
Swali la pili; mpango huu ukikamilika Mheshimiwa Kawambwa ni kwamba Kata zote tisa za Jimbo lako Bagamoyo zitapata huduma ya maji kutokana na mradi huu.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, isipokuwa nina maswali mawili ya nyongeza ya kuuliza. Moja, Mheshimiwa Waziri katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, tulitengewa fedha jumla ya sh.82,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa wodi kwenye Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, lakini mpaka hapa tunapoongea fedha hizi hazijapelekwa katika Halmashauri. Je, Mheshimiwa Waziri atatuhakikishia Bagamoyo kwamba fedha hizi zitaweza kutolewa kabla ya mwaka huu kumalizika ili tuweze kuboresha huduma katika hospitali hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri amenijibu kuhusu ujenzi wa OPD kwa kutumia fedha za (own source) za kwetu wenyewe, lakini OPD hii ni mbovu sana; haina uwezo wa kuhudumia wagonjwa kwa kadri ambavyo ingeweza kutoa huduma ile ambayo wanasema inafaa kwa wananchi wale wa Bagamoyo. Inahitaji ujenzi mpya kabisa. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari ku-commit kiasi cha fedha ili angalau tuweze kuijenga upya OPD hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la commitment ya Serikali katika bajeti ambayo mwaka huu tunaondoka nayo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba bado tuna mwezi mpaka tufike mwezi wa Sita. Lengo letu Serikali ni ile wodi iweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la OPD, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwanza Bagamoyo tumeingiza katika program maalum ya RBF na hivi sasa tumewapelekea takriban shilingi milioni 150 kutokana na kuwepo kwa zahanati zao 15. Mpango huu utaenda takriban miaka mitatu kwa sababu tume-site kama ni sehemu ya mfano kuanzia na hiyo program.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati tunaenda na hizi intervention, kwa sababu lengo letu ni kupandisha vituo vyetu viwe na star. Bahati nzuri Jimbo lake ni miongoni mwa maeneo yaliyofanya vema. Katika vituo 15, vituo 11 vilipata star.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wetu ni nini? Ni kwamba tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo, nami naifahamu OPD yaou pale Bagamoyo jinsi ilivyo, tutashirikiana kwa pamoja nini kifanyike tuhakikishe tunafanya marekebisho makubwa katika OPD ile, kwa sababu wagonjwa wengi sana ukiangalia katika jiografia ya pale wanatibiwa pale. Kwa hiyo, Serikali tutafanya kila liwezekano ili mradi tuweze kuweka mazingira yawe mazuri.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Bagamoyo, vijiji vya Kondo na Kongo vilikuwa kwenye REA Awamu ya Pili lakini miradi hii haikutekelezwa na katika REA Awamu ya Tatu miradi ya vijiji hivi haimo. Nilishamsikia Mheshimiwa Naibu Waziri akitamka hapa Bungeni kwamba miradi yote ile ambayo haikutekelezwa kwenye Awamu ya Pili ndiyo itapata kipaumbele katika Awamu ya Tatu.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambiaje wananchi wa vijiji vya Kongo na Kondo waliokwemo kwenye Awamu ya Pili lakini wamefutwa kwenye Awamu ya Tatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nipende kusema viko vijiji kwa nchi mzima ambavyo havikutekelezwa katika scope ya REA Awamu ya Pili lakini vilikuwa ndani ya mradi. Vijiji vyote ambavyo vilikuwa chini ya REA Awamu ya Pili vitaendelea kutekelezwa katika Awamu ya Tatu ya REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwamba vile vijiji vyake vya Kondo na Kongo na vingine, viko kama vijiji vinane hivi viko katika mradi wa REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kawambwa aamini tu kwamba vijiji hivyo vitapatiwa umeme katika mradi wa REA Awamu ya Tatu ambao umeshaanza na tayari katika Mkoa wake wa Pwani tumefanya uzinduzi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Shukuru Kawambwa kama kuna shida tutakaa lakini tumhakikishie vijiji vyake vitapata umeme kupitia mradi wa REA.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yenye kutia moyo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza; nilijulishwa na uongozi wa REA kwamba Vijiji vya Kongo na Kondo ambavyo havikutekelezewa miradi yake katika awamu ya pili vimeingizwa kwenye orodha ya miradi ya nyongeza kwenye REA-III ambayo imeombewa kibali kwa ajili ya utekelezaji. Sasa swali; je, lini kibali hicho kitaweza kutolewa ili miradi hiyo itekelezwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kufuatana na orodha ya miradi ya REA Awamu ya Tatu kwenye Jimbo la Bagamoyo, vijiji vingi katika Kata za Fukayosi, Makurunge, Mapinga, Kerege na Zinga havitopata umeme. Je, Serikali ina mkakati gani kuweza kuvipatia umeme vitongoji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwa juhudi zake anavyofuatilia mahitaji ya umeme kwa wananchi wa Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyotaja, Vijiji vya Kondo, Kongo, Matimba pamoja na Fukayosi kimsingi vilishapata approval na viko kwenye REA awamu ya tatu hii inayoanza sasa hivi. Naomba nimhakikishie kwamba katika shule yake ya sekondari aliyojenga Fukayosi kwa wafadhili, tayari wiki ijayo wanafanya survey ili ianze kupelekewa umeme katika awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyobaki ambavyo amevitaja; Mapinga, Kerenge pamoja na maeneo ya Zinga ambavyo ni vijiji 22, navyo vitaanza kupelekewa umeme kuanzia mwezi Machi, 2019 na kufikia mwaka 2020 vyote vitakuwa vimeshapata umeme.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Bagamoyo imepata hadhi ya Mamlaka ya Mji Mdogo mwaka 2005 na miaka 10 baadaye mwaka 2015 baada ya kujitathimini na kuona tumetimiza vigezo tumeomba kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji. Je, Serikali inatupa jibu gani kuhusu Bagamoyo kupandishwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tulipokea maombi ya Mji wa Bagamoyo kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji sawa sawa na ambavyo tumepokea maombi mengi ya aina hiyo. Kwa sababu kupandisha hadhi Mji kuwa Halmashauri ya Mji kunaweza kusababisha ongezeko la mahitaji mengi ya kiutawala, bado maombi hayo yako kwenye mchakato na tutayafikiria muda utakapofika na kuzingatia na uwezo wa Serikali.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mwezi Septemba, 2015 Serikali iliwalipa fidia wananchi wanaopisha mradi wa bandari katika Vijiji vya Pande na Mlingotini. Miongoni mwao wananchi 687 walibainika kwamba walipunjwa fidia zao; kwa hivyo Serikali iliwafanyia uhakiki mwezi wa kwanza mwaka jana ili kubaini fidia stahiki za wananchi hao. Je, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia zao stahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tarehe 22 Mwezi wa sita mwaka jana wakati anazindua kiwanda cha Elvin katika Kata ya Mapinga, Mheshimiwa Rais aliwatangazia wananchi wanaopisha mradi wa EPZ Bagamoyo kwamba wale wote ambao hawajalipwa fidia zao wanaweza wakarudi sasa katika maeneo yao wayaendeleze maeneo yao. Je, ni lini EPZA na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo itawaruhusu wananchi hao kumiliki maeneo yao kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia suala hili; lakini na yeye amekiri kwamba uhakiki ulifanyika kufuatilia wale waliopunjwa. Hapa tatizo kama nilivyosema kwenye suala la msingi ni ukosefu wa pesa za kutosha kutoka kwenye Bajeti ya Serikali kufidia maeneo ya kiuwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu Serikali imeshapata njia hii ya pili ya wabia watatu kutafuta pesa, nimshauri Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kusudi tupate fedha za kuweza kuwafidia kila mtu aridhike kusudi mradi wetu uweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu tamko la Mheshimiwa Rais. Tamko la Mheshimiwa Rais ni maelekezo, watu wa EPZA, watu wa halmashauri na hapa kunapashwa kuingia wananchi, watakaa kusudi watekeleze tamko la Mheshimiwa Rais. Jambo ambalo ningependa Watanzania walielewe lile eneo limeamuliwa kwamba ni Export Processing Zone. Sasa kuna mchakato unapaswa ufanyike kusudi wewe ukawekeze vinginevyo; lakini kwa mamlaka niliyonayo EPZ na halmashauri na wananchi na wewe Mbunge tutakaa chini tuangalie namna ya kuwekeza kwa manufaa ya watu wote.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani za wananchi wa Bagamoyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa namna ambavyo amesimamia ujenzi wa tenki kubwa la maji Bagamoyo, swali langu ni kuwa, je, lini mradi wa usambazaji wa mabomba ya maji katika Mji wa Bagamoyo pamoja na kata zote za Bagamoyo utaanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Programu ya Maendeleo ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji katika Mkoa wa Dar es Salaam tunakaribia kuikamilisha. Baada ya kupata vyanzo vya maji tunayo maji ya kutosha, tuliweka makadirio ya dola milioni 100 kwa ajili ya usambazaji. Awamu ya kwanza tulipata dola milioni 32 na miradi hii inaendelea, ndiyo ambayo imejenga hilo tenki analolisema Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa hivi tumepata tena dola milioni 45 na mwezi huu tunatangaza tender ili tuweze kupata mkandarasi ili ahakikishe kwamba sasa tunaweka mabomba ya kusambaza maji katika maeneo yote likiwemo eneo la EPZ kule Bagamoyo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake kwamba huduma ya maji katika eneo lake tunakamilisha. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maijibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuzingatia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba GNT inatarajia kukamilisha majadiliano hivi karibuni. Sasa wananchi hawa watatakiwa bila shaka kuhama baada ya majadiliano kukamilika na ujenzi unaanza mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi 687 ambao walithibitika kuwa na mapunjo katika fidia zao na wakahakikiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Je, wananchi hawa lini watalipwa fidia zao ambazo tayari zimeshahakikiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa fidia ya wananchi haijakamilika katika eneo hilo la Bandari, moja katika bilioni 57.7 imelipwa mpaka sasa bilioni 45 peke yake, lakini pia kuna hawana wananchi ambao walikuwa wana mapunjo katika fidia zao na wao hawajalipwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu miundombinu ya Shule ya Msingi Pande, Shule ya Msingi Mlingotini na Zahanati Pande ambazo wananchi wanaendelea kuzitumia. Kwa vile watatakiwa kuondoka, nini kauli ya Serikali kuhusu kuihamisha miundombinu hiyo kuwapelekea mahali ambapo watakuja kuitumia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kawambwa kwamba anafuatilia sana upatikanaji au ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na anafahamu kabisa kwamba Bandari hii itakapojengwa ni fursa kwa wakazi wa Bagamoyo. Kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa kwa kutetea wananchi wake lakini pia amekuwa akifuatilia sana juu ya fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, kwamba Serikali inawajali wananchi ndiyo maana jumla ya shilingi bilioni 48 imelipwa kama fidia kati ya kiasi cha fedha cha bilioni 57 ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hawa. Eneo hili ni kubwa, lina ukubwa wa hekta 800 ni eneo kubwa sana, kwa hiyo changamoto zilikuwa nyingi, lakini Serikali imekamilisha kuwalipa wananchi. Wako wananchi wachache ambao walikuwa hawajalipwa pamoja na taasisi ikiwemo Taasisi hii ya Uvuvi Mbegani pamoja na hizi shule ambazo Mheshimiwa amezitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba, kwa sababu Serikali iko committed; ni kwamba wananchi ambao walipunjwa uhakiki umekamilika, kwa hiyo wakati wowote kama ilivyofanya kwenye malipo yao ya awali watalipwa hawa wananchi. Kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Bagamoyo kwamba utaratibu unakamilishwa ili sasa hizi fedha ambazo zimekuwa ni za nyongeza; ni kiasi kidogo tu kama, Serikali imelipa bilioni arobaini na nane na bilioni zingine nane zipo; ni kwamba tupo committed kulipa hizi fidia. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi wananchi hawa watalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anauliza juu ya hatima ya shule hii ya Pande. Ni dhahiri kwamba kati ya zile fedha bilioni nane zilizobaki ni hizi taasisi ambazo ziko chini ya Serikali ambazo ni pamoja na Shule ya Msingi ya Pande, Shule ya Msingi ya Mbegani, Zahanti ya Pande pamoja na Mbegani. Kwa hiyo hizi ndizo shilingi bilioni nane zilizobaki kwa ajili ya kulipa na kuhamisha hizi taasisi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi tumejipanga vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna uhakiki wa kuhamisha makaburi lakini pia tuliweza kupata thamani ya shilingi zaidi ya milioni mia tano ili kuweza kuhamisha makaburi pamoja na kuhamisha hizi shule. Kwa hiyo fedha zimeshapatikana na kibali kimeshatolewa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bagamoyo wasiwe na wasiwasi, fedha hizi zilizobaki bilioni nane pamoja na hii milioni mia tano zipo, tutahamisha hizo shule ili wananchi wapate huduma na ujenzi uweze kuanza mara moja.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Kama alivyokiri Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mgonjwa wa kisukari ili aweze kuishi ni lazima apate dawa za kisukari kila siku. Sasa kule Jimboni Bagamoyo kwenye Hospitali ya Wilaya kuna tatizo kubwa sana la upatikanaji wa dawa hizi kwa wagonjwa wa kisukari. Pia hata vipimia vya kiwango cha sukari navyo havipatikani hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba dawa hizi na vipimo vinapatikana kwa urahisi ili wananchi wetu wa Tanzania waweze kuendelea kuishi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na vilevile majibu ya nyongeza ni kwamba tunatambua sasa hivi ongezeko kubwa sana la wagonwja wa kisukari, na sisi kama Serikali tumeelekeza nguvu zetu katika bajeti ambayo tumeitenga ya fedha kwa ajili ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi, bajeti ya ugonjwa wa kisukari nayo imo ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuongeza wigo wa utoaji wa huduma hii kwa kushirikiana na wadau, kusambaza vifaa vya upimaji, vilevile kusambaza dawa za insulin pamoja na vidonge vyake na katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kununua matumizi ya insulin.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba hili suala la Bagamoyo tutajaribu kulifuatilia kuhakikisha kwamba sasa huduma hizo za dawa pamoja na vipimo vinapatikana.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, pamoja na shukrani kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo ambayo amenipa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, eneo lile la Kitongoji cha Sanzale ni Bagamoyo Mjini na wananchi hawa wamewekewa alama za “X” miaka nane imepita, hawawezi kukarabati nyumba zao, hawawezi kujenga upya, hawawezi kufanya chochote na majibu ni kwamba watafidiwa pale maeneo yatakapohitajika. Je, ni lini maeneo hayo yatahitajika kwa sababu wananchi hawa psychologically wameendelea kupata matatizo makubwa sana? Wafanye nini maana wanaishi na watoto wao katika nyumba ambazo zimewekewa “X” lakini hawajui lini watalipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika barabara ya Makofia - Mlandizi ambayo imo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 pia katika Ilani ya mwaka 2015 kujengwa kwa kiwango cha lami. Wananchi hawa wanapenda kujua fidia zao zitalipwa lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASLIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kawambwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwa kufuatilia sana maendeleo ya Bagamoyo kwa ujumla wake. Natambua kwamba kutakuwa na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na hivyo hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge anazitaja ni muhimu kweli. Yeye mwenyewe anatambua kwamba zipo harakati za awali ambazo zimefanyika ili kuhakikisha kwamba fidia kwa wananchi wake zinalipwa mapema.
Mheshimiwa Spika, swali lake anasema ni lini sasa tutalipa fidia hiyo. Niseme kwamba harakati za ujenzi wa barabara ya lami kwa barabara ambazo zinaingia Bagamoyo zinaendelea na hatua za tathmini zimeshafanyika na kwa vile zina hatua mbalimbali, kwa upande wa TANROADS tumeshafanya jukumu letu na tunaendelea kuwasiliana ili kuweza kupata fedha ili wakati wowote tuweze kuwalipa wananchi hawa.
Mheshimiwa Spika, najua kwa eneo hili amelitaja mahsusi Mheshimiwa Mbunge, wapo wakazi wasiozidi 20 ambao wanahitaji kufanyiwa malipo ya compensation. Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Mbunge na Ndugu zangu wananchi wa Bagamoyo eneo hili wavute subira wakati wowote tutafanya zoezi la kuweza kuwalipa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anauliza juu ya compesation kwenye barabara hii inayotoka maeneo ya Mlandizi kuja Bagamoyo. Kama nilivyosema barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuja kutoa huduma katika Bandari ya Bagamoyo itakapojengwa hii ikiwa ni pamoja na eneo lingine kuja Bagamoyo ukitokea Kibaha, maeneo ya Vikawe kuja Mapinga na kwenyewe harakati zinaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, natambua Ilani ya mwaka 2010 ya Chama cha Mapinduzi na Ilani ya mwaka 2015 imetaja kupanua barabara hii. Kwa hatua ambazo tumefikia wananchi wameshapata valuation form wazijaze, wazirudishe halafu Serikali tutasimamia kwa haraka ili wananchi hawa pia waweze kulipwa kulingana na sheria inavyotaka.
MHE.DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Barabara ya Bagamoyo hadi Mlandizi ni barabara wezeshi kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba, Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami na wananchi wake kuweza kulipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imekwishafanya upembuzi yakinifu wa barabara aliyoitaja kutoka Bagamoyo mpaka Mlandizi, na sasa hivi hatua za usanifu wa kina zinaendelea ili kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami. Lakini mpaka sasa hivi kuna pesa ambayo imetengwa kwa ajili ya kui-mantain barabara hiyo iweze kupitika mwaka mzima. Kwa hiyo, usanifu wa kina utakapokamilika barabara hiyo itaanza kutafutiwa pesa kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Serikali imetenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Pangani - Tanga. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kama yuko tayari ujenzi huo kutumia wakandarasi wawili ili mmoja aanze Tanga mwingine aanze Bagamoyo kwa madhumuni ya kuharakisha ujenzi lakini kuwapa faraja pia wananchi wa pande hizo mbili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anatambua kabisa hatua nzuri za ujenzi wa barabara hii upande wa Serikali tulipofikia kwa vile anaendelea kufuatilia vizuri. Nichukue tu wazo lake kama ushauri ili wakati sasa wa kuanza ujenzi tutaona namna nzuri ya kufanya lot ili tuone kama hilo analolisema tunaweza tukalifanya tutaweza kulitekeleza.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya ambayo ametupa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mhshimiwa Spika, kwanza, katika kipindi hichohicho kampuni ya Dodsal imefanya utafiti wa gesi na mafuta katika Kata ya Vigwaza, Wilaya ya Bagamoyo. Napenda kujua nini matokeo ya utafiti huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, napenda kujua ni maeneo gani katika Mkoa wa Pwani ambapo gesi imegundulika kwa kiwango cha kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Jumanne Shukuru Kawambwa. Namshukuru sana ameuliza swali katika Kata yetu ya Fukayosi.
Mheshimiwa Spika, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli Kampuni hii ilifanya utafiti pia katika maeneo ya Vigwaza, Kwala na Ruvu. Kazi inayoendelea sasa hivi ni kukusanya data na kuzichakata zile takwimu za mitetemo ambazo zinaitwa 3D. Kwa hiyo, kazi hiyo inaendelea ili kubaini kiwango cha gesi asilia kilichopo katika mashapo ambayo gesi imegundulika katika maeneno hayo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza ni maeneo gani katika Mkoa wa Pwani mpaka sasa gesi imegundulia. Kwa kweli ni maeneo hayo kama ambavyo nimesema katika jibu hili la nyongeza, ni Kwala, Ruvu na Vigwaza ambapo utafiti unaendelea. Sasa hivi data ambazo wanazikusanya za mitetemo hiyo ya 3D wanaendelea kuzifanyia michakato ili kubaini kiwango cha gesi na kuweza kutathmini kama kinafaa katika vigezo mbalimbali vya kiuchumi. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Jimbo la Bagamoyo kata zake zote isipokuwa moja tu ndiyo ina kituo cha afya ambacho ni kipya. Je, ni nini mpango wa Serikali kuweza kutupatia angalau kituo kimoja au viwili zaidi kwa Jimbo zima la Bagamoyo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Bagamoyo ina changamoto kubwa na hivi sasa tuliimarisha katika Kituo cha Afya cha Kerege. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadri iwezekanavyo na tukijua kwamba jiografia ya Bagamoyo na mahitaji yake yalivyo, nadhani kabla hatujafika mwezi wa saba, hapa katikati, tutafanya jambo katika kituo kimoja cha afya ambacho yatapendekeza kutoka Wilaya ya Bagamoyo. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Pamoja na shukrani za wananchi wa Bagamoyo kwa Mheshimiwa Waziri kwa kutujengea tanki kubwa la lita milioni sita Bagamoyo Mjini. Naomba kuuliza swali moja kwamba ni lini sasa Wizara itaanza mradi wa kusambaza mtandao wa mabomba ya maji ili maji hayo sasa yaweze kuwafikia wananchi katika Mji wa Bagamoyo na Kata zote katika Jimbo la Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri na nia njema ya kuhakikisha wananchi wake wa Bagamoyo wanapata maji safi, salama ya yenye kuwatosheleza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa suala hili la maji ni la uhitaji mkubwa sana tutalifanya kwa haraka ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Makofia - Mlandizi ni muhimu sana ambayo inaunganisha wananchi wa Halmashauri ya Bagamoyo na Kibaha Vijijini. Barabara hiyo sasa hivi ina matatizo sana ya kupitika hasa baada ya mvua hizi nyingi zilizopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2005, 2010 na 2015 kujengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini fidia italipwa kwa ajili ya barabara hiyo na lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kawambwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Kawambwa ni shahidi kwamba tumezungumza muda mwingi sana juu ya barabara hii. Barabara itakuwa na urefu wa kilometa zaidi ya 30 kuja Mlandizi. Kuhusu fidia tulishafanya tathmini tayari, tutaendelea kuwasiliana na wenzetu Wizara ya Fedha hizi fedha zipatikane ili wananchi hawa walipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi watalipwa kwa sababu tulikuwa na fidia nyingi nchi nzima katika maeneo mbalimbali, lakini tumefika hatua nzuri, maeneo mengi tumeshalipa fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kawambwa asiwe na wasiwasi. Nafikiri baadaye tuzungumze na tuongee na wataalam tuone hatua hii imefika wapi ili tuweze kulipa mara moja hii fidia ya wananchi wake.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika juhudi za kuboresha huduma za afya katika Jimbo la Bagamoyo, wananchi katika Kata mbalimbali zikiwemo Nianjema, Fukayosi na Mapinga wameanza ujenzi wa zahanati katika vijiji vyao. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu kuwaunga mkono kumalizia ujenzi wa zahanati hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu naomba kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa maana katika vituo vya afya vilivyojengwa vya kupigiwa mfano ni pamoja na Kituo chake cha Afya cha Bagamoyo. Naomba na wengine wa mikoa ya jirani ambao vituo vya afya vinaendelea kujengwa wakatazame mfano mzuri jinsi ambavyo walivyosimamia na value for money ikaonekana katika Kituo cha Afya cha Bagamoyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo Serikali imekuwa ikiwaunga mkono maeneo mengine katika Jimbo lake, tukimaliza hatua hii, kama ilivyo kwenye Ilani ya CCM kwamba tunahakikisha tunajenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata, naomba tuvute subira hicho ndicho ambacho ni ahadi yetu sisi kwa wananchi, tutaenda kutekeleza.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pia nichukue fursa hii kumpa pongezi sana kwa namna anavyowajibika tangu amepata nafasi hii, anamsaidia vizuri Mheshimiwa Mkuchika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja la nyongeza, kwa kutambua kwamba Awamu ya Pili itakapoanza mwezi Juni, 2019 na Wilaya ya Bagamoyo ina majimbo mawili, Chalinze na Bagamoyo, haitoweza kuzifikia kaya zote maskini katika Wilaya ya Bagamoyo kwani ni zaidi ya vijiji na mitaa hii 110. Je, nini tamko la Serikali kuhusu kaya maskini zile ambazo zitakuwa zimeachwa wakati Awamu ya Pili inaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana wananchi wa Jimbo lake la Bagamoyo hususani wale ambao wanaishi katika kaya maskini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilieleze Bunge Tukufu kwamba Mpango wetu huu au Mradi wetu huu wa TASAF unahudumia na umezingatia sana Muungano kwa maana unahudumia Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi mpaka dakika hii katika Jimbo la Bagamoyo au Wilaya ya Bagamoyo tumeshafikia zaidi ya vijiji 66 awamu ya kwanza na vijiji 44 vitafikiwa katika awamu ya pili hivyo kufanya jumla ya vijiji 110.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema tena kwenye jibu langu la awali kwamba mpaka dakika hii tumeshafikisha asilimia 70 kwa kaya maskini zote nchini tumebakiza asilimia 30. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wote kwamba katika Sehemu ya Pili ya Mpango wetu ule wa TASAF tumehakikisha kwamba tunauboresha zaidi kwa kutumia njia za kielektroniki kwa maana ya GPS ili kuweza kuboresha yale madodoso ili kuhakikisha kwamba tunaepuka zile kaya hewa. Vilevile tutafanya uhakiki kuhakikisha kwamba yale madodoso ambayo tumeyaboresha kweli yanafikiwa katika kaya zile maskini ili kila Mtanzania ambaye anaitwa yuko kwenye kaya masikini aweze kunufaika na mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba katika asilimia 30 iliyobaki kwa mpango na mradi wetu wa TASAF tutahudumia kaya maskini zote Tanzania na tutarudia tena kuhudumia zile kaya zingine za mpango wa kwanza ambazo zilikuwa ni asilimia 70. Kwa hiyo, naomba Watanzania wote wafahamu kwamba tumeboresha Mpango huu na kuanzisha mfumo wa kielektroniki ili tuweze kuhakikisha tunafikia malengo na wale wote wanaoitwa wako kwenye kaya maskini waweze kunufaika. Ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na nitahamasisha wadau kuvuta subira. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaendelea na mchakato wa kupata Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, je, ni lini Serikali itawaagiza Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwalipa Wenyeviti wa Vitongoji malimbikizo yao ya posho ambayo hayajalipwa kwa mda mrefu sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile Bagamoyo siyo Halmashauri ya Mji kwa hiyo hatuna fursa ya mafungu makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara. Sasa naomba kujua ni nini kauli ya Waziri kuhusu kutusaidia Bagamoyo mafungu ambayo yatatuwezesha kujenga miundombinu ya barabara na mifereji ambayo iko katika hali mbaya sana katika Mji wa Bagamoyo na Vijiji vya Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze na kumshukuru kwa kukubaliana na majibu kwenye swali la msingi na hili la kuwaomba wananchi wawe na subira wakati mchakato unaendelea, namshukuru sana kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza amesema kwamba Wenyeviti wa Vitongoji hawajalipwa kwa muda mrefu na mimi napenda kumhimiza Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya ya Bagamoyo kutekeleza maagizo ya Serikali ambayo yanamtaka arejeshe asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye kata husika ili yatumike, pamoja na kazi zingine, kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kwenye maeneo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amesema Mji wa Bagamoyo kweli una mahitaji ya miundombinu kama barabara na mifereji na amesema kwa usahihi kabisa kwamba itakapokuwa ni Halmashauri ya Mji ambayo inatakiwa iwe na sifa fulani kwa upande wa miundombinu sasa tuanze kupeleka mafungu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo. Mimi namuomba sana Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane hata baada ya Kikao hiki cha Bunge ili tuone ni namna gani mwakani tunaingiza kwenye bajeti ya TARURA huu ujenzi wa miundombinu ambao anaipendekeza.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na shukrani nyingi za wananchi wa Bagamoyo kwa Serikali kwa kuwajengea tanki kubwa la maji lita milioni sita Bagamoyo Mjini, naomba kuuliza swali la nyongeza kwamba, sasa ni lini shughuli ya mradi wa kusambaza au kulaza mabomba, mtandao huu mpya wa mabomba ya maji katika Mji wa Bagamoyo na Kata zinazozunguka Mji wa Bagamoyo utaanza kwa sababu tanki lile sasa hivi halileti tija ya kutosha kwa wananchi wa Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua changamoto kubwa sana ya maji katika eneo la Dar es Salaam pamoja na Pwani kwa maana ya Bagamoyo, Serikali imewekeza zaidi ya dola milioni 32 katika kuhakikisha wananchi wa maeneo haya wanapata maji. Nimhakikishie, hii ni hatua ya kwanza na tunamwagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Salama Dar es Salaam kuhakikisha mradi huu unaanza haraka ili wananchi wa Bagamoyo waweze kupata maji safi na salama.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kutambua kwamba hii ni ahadi ya chama chetu ya muda mrefu tangu Ilani ya mwaka 2010, huu ni mwaka wa tisa na sasa usanifu umekamilika, je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kwamba ni muafaka sasa kwa kipande kile cha Makofia hadi Mlandizi ambacho usanifu wake umekamilika kuanza taratibu za ujenzi mapema iwezekanavyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu hivi sasa usanifu umekamilika na wananchi hawa walikuwa wanasubiri fidia ya maeneo yao tangu kipindi ambapo barabara hii ilitangazwa kujengwa kwa maana ya takribani imefika miaka tisa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuwalipa fidia wananchi hawa kutoka Makofia hadi Mlandizi mpaka Vikumburu ili waweze kupisha ujenzi wa muundombinu huu muhimu kwa furaha?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shukuru Jumanne Kawambwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwa sababu nafahamu amekuwa akifuatilia sana barabara nyingi za Mji wa Bagamoyo, ikiwemo barabara hii ya Makofia-Mlandizi lakini pamoja na barabara nyingine ambazo zinaunganisha Mji wa Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, ni kweli kwamba barabara hizi alizozitaja, ukiichukua kutoka Bagamoyo - Mlandizi - Kisarawe ziko kilometa 100, lakini kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba kazi kubwa imeshafanyika na sasa tunakamilisha kufanya mapitio ya compensation (fidia) kwa wananchi ambao watapisha mradi huu. Kama ilivyo kanuni, tukishawalipa wananchi hawa sasa tutakuwa na haki ya kuanza kuenga kipande hiki cha barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu tu Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwamba kipande cha barabara hiyo kutoka Makofia mpaka Mlandizi kilometa 36.7 sasa tunakamilisha. Tathmini ya awali ilionyesha kama fidia ya shilingi bilioni 11 au 12, hivi sasa Mtathmini anafanya review ili tuweze kuwa na uhakika wa kiasi gani wananchi hawa wanastahili ili tuwalipe tuanze kujenga kipande hiki.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba kwa sababu barabara hii inaunganisha vipande viwili, kile cha kutoka Kisarawe - Mlandizi, kile kipande cha kutoka Kisarawe - Maneromango kama kilometa 10, hivi sasa ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, niseme tu kwa ujumla wake kwa wananchi wa Bagamoyo na Pwani kwa ujumla kwamba barabara hii yote kwa ujumla wake ujenzi tumeshaanza na tukilipa fidia pia kipande cha kutoka Mlandizi - Bagamoyo tutaanza kukijenga ili wananchi waweze kunufaika na matokeo makubwa ya kazi nzuri ya Serikali yao.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Nitangulize kutoa shukrani za wananchi wa Bagamoyo kwa juhudi kubwa ya Serikali katika kuboresha huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Bagamoyo kwa muda mrefu sana wamehangaika na ujenzi wa zahanati katika Vijiji viwili, kimoja cha Buma Kata ya Kilomo, kingine Kitame katika Kata ya Makurunge. Hivi sasa zahanati ya Makurunge imekamilika na Buma wakati wowote tutamaliza, tunamalizia ujenzi wa choo. Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, je, ni lini tutaweza kupatiwa watumishi na vifaa tiba katika zahanati hizi kwa kuzingatia kwamba, kwa muda mrefu wananchi hawa hawajapata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaomba kibali maalum kwenye Ofisi, Wizara ya Utumishi cha kuajiri Madaktari, Waganga na Wauguzi. Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, maeneo yote ambayo zahanati zimekamilika na vituo vya afya ambavyo vinajengwa nchi nzima na hospitali za wilaya na pale palipo na upungufu mkubwa tutazingatia maeneo hayo ikiwepo na eneo lake la Bagamoyo na zahanati mbili ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa fursa hii ya kuuliza swali moja la nyongeza na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kutambua kwamba tangu mwaka 2005 miaka 14 sasa wakati ambapo Bagamoyo ilipewa hadhi ya mamlaka ya Mji Mdogo uongozi na wananchi wa Bagamoyo wameendelea kupambana kutekeleza vigezo 12 vya kupandisha hadhi mji ule kuwa halmashauri ya mji. Mpaka hivi sasa imebaki vipengele hivyo viwili kimoja cha master plan kingine cha upimaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutaendelea kupambana na hiki cha master plan lakini upimaji wa ardhi ni suala ambalo linahitaji gharama kubwa. Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo haina vitendea kazi vya upimaji wa ardhi hivi sasa havina vyombo kwa ajili ya upimaji wa ardhi. Je, Serikali ina kauli gani kuweza kuisaidia halmashauri hii ambayo imepambana miaka 15 sasa kwa ajili ya kuweza kupata hadhi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Dkt. Jumanne Shukuru Kawambwa yeye na viongozi wake na wenzake na Mwenyekiti wa Halmashauri waliweza kufika ofisini mara kadhaa katika jambo hilo. Tunafahamu kwamba juhudi kubwa inafanyika na ni azma yetu kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yana kipaumbele tuweze kuyafanyia kazi. Katika jambo hili naomba niseme wazi kweli tumekuwa na changamoto katika suala zima la upatikanaji wa vifaa lakini hata hivyo niwashukuru sana wenzetu wa Wizara ya Ardhi kwa ushirikiano mkubwa tunaoendelea kuufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa halmashauri mbalimbali zitaweza kupata vifaa hivi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hivi vifaa vya upimaji vinaweza vikapatikana na tukumbuke wazi hata katika bajeti ya Wizara ya Ardhi jambo hili waliainisha wazi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Jumanne Shukuru Kawambwa kwamba Serikali inalichukua hili kwa uzito mkubwa sana kuhakikisha halmashauri zetu zinawezeshwa kuhakikisha zinapima maeneo yao kwa urahisi zaidi ahsante.
MHE. DKT SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Barabara ya Makurunge - Saadani - Pangani mpaka Tanga ni barabara ambayo inaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga kwa njia ya mkato.

Pia barabara hii ni kichocheo kikubwa sana cha utalii hasa kwa hifadhi yetu maalum ya Saadani ambayo kwa sasa haipati watalii wa kutosha kwa sababu barabara hiyo ipo katika hali mbaya. Barabara hii pia imeahidiwa; au iko katika mipango ya Serikali kwa ujenzi wa kiwango cha lami kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali: Ni nini mkakati wa Serikali kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ikitokea Tanga – Pangani – Makurunge – Sadani, inakuja mpaka Bagamoyo, ni barabara ambayo iko kwenye mpango wa ujenzi wa lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tumeshaanza ujenzi, tumeshapata mkandarasi ambaye anajenga barabara hii kutoka Tanga kwenda Pangani. Pia tuko kwenye mpango wa kujenga daraja katika Mto Pangani. Tunaamini kwamba baada ya ujenzi wa daraja hili katika Mto Pangani, italeta sasa mantiki ya kumalizia ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kuja Bagamoyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla kwamba ni mpango wa Serikali kuikamilisha barabara hii kwenye kiwango cha lami na ujenzi umeshaanza, tuvute subira, tutakuja kumalizia kipande hiki kinachobaki kwa maana ya kutoka Bagamoyo kwenda Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuko kwenye mpango na itafupisha barabara hii ukitokea Tanga kwa sababu itakuwa na kama kilomitaa 240 hivi tu kutoka Tanga kuja bagamoyo. Kwa maana hiyo, pia itatusaidia sana kufanya watalii waende maeneo ya Sadani kwa maana ya kutuingizia fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza na Naibu Waziri wa Maliasili kwamba tutaitembelea barabara hii kwa maeneo ambayo ni korofi kwa kipindi hiki baada ya mvua kupungua, tuhakikishe kwanza inapitika, inatupa huduma lakini wakati ule ule tutaendelea na utaratibu wa kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji imejenga tanki kubwa la maji mjini Bagamoyo lenye takriban uwezo wa lita 6,000,000 lakini kwanza tunaishukuru sana Serikali kwa kutukumbuka kwa jambo hilo adhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo ni kwamba faida ya tanki hili bado haijaweza kupatikana na kata nzima ya Kisutu, Kata ya Nianjema, Kata ya Magomeni na hata Kata ya Dunda zote kata hizi zinaendelea kupata tatizo la uhaba au kukosekana kwa maji safi na salama kwa sababu hakuna mtandao wa mabomba ya kusambazia maji hayo safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, ni lini sasa Serikali kupitia Wizara ya Maji itaweka mtandao wa mabomba ya kusambaza maji katika kata zote hizi Mjini Bagamoyo. Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, amekuwa mfuatiliaji katika kuhakikisha anawasemea wananchi wake wa Bagamoyo ili waweze kupata huduma hii muhimu sana ya maji na nataka nimhakikishie sisi kama viongozi wa Wizara hatutakuwa tayari kupoteza uhai wa wana Bagamoyo katika kuhakikisha wanapata huduma hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Usafi na Usafi wa Mazingira DAWASA tumeona haja kabisa ya kukabiliana na kutatua tatizo la maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mkoa wa Pwani. Lakini tumejenga matenki makubwa sana ya maji ikiwemo Bagamoyo zaidi ya milioni sita yote ni kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la maji. Lakini hii ni Awamu ya I ya ujenzi wa matenki, Awamu ya II ni suala zima za usambazaji. Tupo katika hatua ya kupata kibali katika kuhakikisha tunaanzisha sasa mtandao huu wa maeneo ambayo hayana maji, yanapatiwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunalifanya hili kwa haraka kibali kipatikane ili wananchi wa maeneo ya Kisutu na maeneo mengine waweze kupata maji safi na salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu haya mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nichukue nafasi hii kuwapa pongezi wawekezaji wa ndani, wazawa kwa kujenga viwanda hivi ambavyo vimepunguza tatizo la soko. Lakini pamoja na uwepo wa viwadna hivi viwili tatizo la soko bado ni kubwa sana na msimu uliopita mananasi yaliozea shambani na tatizo linaongezeka kwa utaratibu uliopo sasa hivi wa ununuzi wa mananasi haya ambao utaratibu huu unahushisha madalali kusababisha usumbufu mkubwa na wakati mwingine kupoteza mapato kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali iko tayari kuwahamasisha wawekezaji hawa ili waweke utaratibu rafiki utakaowawezesha wakulima kuuza zao lao la nanasi kwa urahisi zaidi na kwa kuwapatia kipato? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile zao hili ni zao la kibiashara na linafanya vizuri, linaipatia kipato Serikali pamoja na wakulima, sasa swali langu, je, Serikali iko tayari..., samahani pamoja na kufanya hivyo vizuri mkulima inabidi apambane yeye mwenyewe kwa hatua zote kuanzia kuandaa shamba, kupanda, kupalilia mpaka kuvuna na kadhalika na kubeba gharama zote.

Je, kwa kutambua umuhimu wa zao hili Serikali iko tayari sasa kuwaunga mkono wakulima hawa kwa kuwapa ruzuku katika pembejeo kama vile mbolea na pembeje zingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA):
Mheshimiwa Naibu Spika,ni dhamira ya Serikali kuhakikisha wakulima wa mananasi wa Bagamoyo wananufaika na kupata tija kupitia kilimo cha mananasi. Kumekuwepo na utaratibu wa katikati hapo kuingiza watu wa kati ambao mwisho wa siku wanawafanya wakulima hawa wasiweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali tutaendelea kuweka mipango madhubuti na miundombinu rafiki ili kumfanya mkulima huyu wa nana wa Bagamoyo apate soko la uhakika moja moja kupitia kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa na Mheshimiwa Mbunge ni shahidi yangu niliwahi kuzungumza naye pale Bagamoyo katika Kijiji cha Dutumi, Kata ya Dutumi tumeshazungumza tayari na muwekezaji Sayona Fruits Company Limited ambao wako tayari kushirikiana na Serikali na tumeanza kuwaandaa vijana na tayari ekari 50 imeshatengwa na tutachimba visima viwili na watu wa SUA wameshakwenda pale Dutumi, wameipima ardhi, wamejua mwekezaji anataka nini, baadae tutaanza utaratibu mzuri sasa kuhakikisha kwamba ile mbegu itakayokwenda kupandwa pale kwa matunda ambayo mwekezaji anahitaji atanunua moja kwa moja kutoka kwa wakulima Kijiji cha Dutumi na hivyo itakuwa soko kuwa la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili amezungumza kuhusu ruzuku na kuwawezesha wakulima. Niseme tu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu pia mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika hatua hii ya awali ningeshauri kwanza wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo kuitumia benki yetu ya kilimo ambayo pia ina fursa ya kuwawezesha kupata mikopo ambayo itaongeza tija katika uzalishaji wao ili baadae basi wasipate shida katika uzalishaji wao. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi nipende tu kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Mavunde Naibu Waziri. Lakini kwanza nipende kusema kwamba tumemsikia Mheshimiwa Kawambwa lakini pia na Wabunge wote ambao wamekuwa wakizalisha mazao ya matunda pamoja na mboga mboga, na nipende tu kusema kwamba kwa sasa tumeandaa kongamano maalum la uwekezaji katika nyanda za juu Kusini ambao tutalifanya Mbeya Jumatatu na Jumanne. Lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge Kawambwa tutafanya hivyo pia katika Mkoa wa Pwani tukitambua kwamba na wenyewe wana kilimo cha matunda na mboga mboga na tutaenda pia katika kanda zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili tunakusudia pia kuandaa kongamano maalum la kuvutia uwekezaji katika kilimo, mifugo na uvuvi na tutashirikiana na Benki ya Kilimo pamoja na Wizara husika, kwa hiyo tuombe tu Wabunge tushirikiane endapo kuna mahitaji mahusui basi tuweze kupata ili tuweze kushirikiana katika kuvutia uwekezaji huu, nakushukuru. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pia nichukue fursa hii kuwapa hongera sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa juhudi kubwa wanayoweka katika utekelezaji wa miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja la nyongeza. Kijiji cha Kondo katika Kata ya Zinga ambacho kilikuwa kwenye mradi wa REA II, mpaka kufikia Juni 2016 kijiji hicho hakikutekelezewa mradi wake na Mheshimiwa Waziri akaahidi vijiji vyote ambavyo havikutekelezewa miradi yao katika REA II basi vitapewa kipaumbele katika REA III. Huu ni mwaka 2019 kijiji hicho ambacho kiko katika Kata ya Zinga na humo ndani kuna Shule ya Msingi ya Kondo na jirani kuna Shule ya Sekondari ya Zinga, sehemu zote hizo hazina umeme mpaka hivi sasa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana kauli gani kuhusu kukipatia umeme Kijiji hiki cha Kondo na miundombinu ya Shule ya Sekondari Zinga na Shule ya Msingi Kondo mapema iwezekanavyo? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Mbunge. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Kawambwa kwa kazi nzuri anayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijajibu swali, Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake vijiji vyote sasa vimeshapata umeme kwa sababu ya kazi anayoifanya anavyofuatilia, kilichobaki ni vitongoji. Kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kati ya wilaya ambazo sasa hivi vijiji vyake ambavyo vimeshapata umeme ni pamoja na Jimbo la Bagamoyo, kwa hiyo Mheshimiwa hongera sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, alishughulika sana na Shule ya Sekondari ya Fukayosi mwaka jana, ilikuwa na changamoto ya umeme na imejengwa na Korea Kusini, tunampongeza sana ina umeme sasa hivi na inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitongoji 169 katika Jimbo la Mheshimwa Mbunge; vitongoji 161, vitongoji 100 vyote vina umeme bado vitongoji 69 na Kati ya vitongoji 69 ambavyo havina umeme ni pamoja na Kitongoji cha Kondo. Kwenye Kijiji cha Kondo kuna vitongoji vitatu; vitongoji viwili tayari vina umeme isipokuwa Kondo Kati anayozungumza Mheshimiwa Mbunge.

Kwa hiyo nimpe tu imani Mheshimiwa Mbunge kwamba nimeshawaelekeza wakandarasi kwa kushirikiana na TANESCO wameshaanza kupeleka umeme kwenye Kitongoji cha Kondo na watakamilisha tarehe 12 mwezi ujao. Wanapeleka kwenye Kitongoji cha Kondo pamoja na Shule ya Msingi ya Kondo, lakini pamoja na Shule ya Sekondari ya Zinga. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge wala asiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze kidogo kwa Jimbo la Bagamoyo na Chalinze, mkandarasi aliyeko kule anapeleka umeme kwenye vitongoji vyote na Peri urban inaanza tarehe Mosi mwezi ujao kujumuisha vitongoji vyote vya Bagamoyo pamoja na Chalinze. Chalinze kuna kijiji kirefu sana cha Msigi pamoja na Magurumatare cha kilomita 28 na chenyewe kinapelekewa umeme. Ahsante sana. (Makofi)