Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa (15 total)

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa mipaka kati ya TANAPA na vijiji na vitongoji jirani vinavyowazunguka.Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza mgogoro huu kati ya TANAPA na vitongoji vya Kitame, Razaba, Gama-Makani katika Kata ya Makurunge?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro yote mitatu iliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge inahusiana na hifadhi ya Taifa Saadani iliyoanzishwa kisheria kwa Tangazo la Serikali Namba 281 la mwaka 2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro baina ya Kitongoji cha Kitame, Kijiji cha Makurunge na hifadhi umetokana na malalamiko kwamba wananchi hawakushirikishwa katika zoezi la uwekaji wa mipaka hivyo kusababisha yaliyokuwa maeneo yao kuingizwa ndani ya hifadhi bila ridhaa yao. Hata hivyo, kumbukumbu zinaonyesha kwamba kuwa wananchi walishikikishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mkutano wa kijiji mama cha Makurunge ambacho kitongoji hiki ni sehemu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro baina ya shamba la Razaba na hifadhi umetokana na utata wa takribani eneo la hekta 3,441 alilopewa mwekezaji Bagamoyo Eco-Energy kwa hati miliki namba 123097 ya terehe 9 Mei, 2013 ili amiliki na kuendesha shughuli za kilimo cha miwa katika eneno ambalo kiuhalisia limo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadani. Juhudi za kutatua mgogoro huu ziliendelea kufanyika kwa takribani miaka minne kwa kuhusisha ngazi za Vijiji, Wilaya, Mkoa na Wizara zinazohusika na hatimaye kutolewa maelekezo kupitia agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu agizo ambalo lilizingatia athari za mazingira zilizotishia uwepo wa hifadhi ya Saadani iwapo kilimo cha miwa kingeruhusiwa katika eneo linalozungumziwa.
Mgogoro baina ya Gama -Makani na hifadhi unatokana na malalamiko ya wananchi kuwa baadhi ya waliofidiwa wakati wa uanzishwaji wa hifadhi katika eneo hilo hawakuwa wamiliki wazawa wa maeneo hayo. Hata hivyo taarifa zinaonyesha kuwa mchakato wa malipo ya fidia ulifuata taratibu muhimu ikiwemo ushirikishwaji wa karibu wa uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo, Serikali za Kata na Serikali za Vijiji husika ambao ulizingatia ilivyohitaji la kuwalipa wananchi waliostahili na si vinginevyo. Pamoja na maelezo haya, Serikali imekwishaunda timu ya pamoja ya wataalam ambayo inaendelea na kazi ya kutafuta suluhisho la migogoro ya ardhi nchini ikishirikisha Wizara mbalimbali kama ilivyoahidiwa wakati wa Bunge la Bajeti lililoahirishwa mwezi Juni, 2016.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji safi na salama katika Mji Mkongwe wa Bagamoyo katika Kata za Magomeni na Dunda:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Mji Mkongwe Bagamoyo maji kwa kiwango cha kuridhisha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mji Mkongwe wa Bagamoyo katika Kata ya Magomeni na Dunda wanapata huduma ya maji ya mgao kutoka katika chanzo cha Ruvu Chini.
Tangu tarehe 23 Machi, 2016 Serikali ilikamilisha upanuzi wa chanzo hicho na ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini hadi matanki yaliyoko Makongo eneo la Chuo cha Ardhi, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kuwezesha wananchi hao kupata huduma ya maji kwa uhakika, Serikali tayari imemwajiri Mkandarasi anayejulikana kwa jina la Jain Irrigation System kwa kazi ya kujenga tanki kubwa Bagamoyo Mjini. Ataweka mabomba ya kutoa maji kutoka bomba kuu na kuyaleta kwenye Tanki na atalaza Mabomba ya kusambaza maji kwa wananchi katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na Kata ya Magomeni na Dunda. Kazi hii imeanza mwezi Machi, 2016 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2017.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa, huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya Bagamoyo zimekuwa dhaifu sana kutokana na upungufu mkubwa wa miundombinu, vitendea kazi, uhaba wa watumishi na ukosefu wa dawa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma
za afya katika Hospitali hiyo kwa kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu bora, vitendea kazi, kuiongezea watumishi na dawa za kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi 1.4 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambapo itahusisha kuboresha miundombinu ya Hospitali na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile zimetengwa shilingi 185,000,000/= kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kutokana na ruzuku ya maendeleo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya vituo vya kutolea huduma za afya, shilingi 59,790,600/= kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya upanuzi wa wodi ya wazazi, ukarabati wa kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD) na eneo la kuhudumia wagonjwa wa dharura pamoja na kumaliza ukarabati wa wodi ya wanaume. Aidha, Serikali imetoa kibali cha kuajiri Madaktari na watumishi wengine wa afya ambapo Halmashauri hiyo pia itapewa kipaumbele. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Katika Mradi wa REA II, Jimbo la Bagamoyo lilipewa vijiji 10 tu na bado utekelezaji wake unasuasua na uko nyuma ya ratiba:-
Je, ni lini miradi ya umeme kwa Vijiji vya Kongo, Kondo na nyongeza ya Matimbwa itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ilikamilisha kupeleka umeme vijijini kupitia Mradi wa REA Awamu ya Pili ikiwemo Wilaya ya Bagamoyo mwezi Desemba, 2016. Kazi ya mradi huo katika Wilaya ya Bagamoyo ilijumuisha ujenzi wa njia kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 80.13, ujenzi wa njia kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 106.67 pamoja na ufungaji wa transfoma 41, kazi nyingine ilikuwa kuwaunganisha wateja wa awali 2,066 na gharama za utekelezaji wa mradi zilikuwa shilingi bilioni 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Kijiji cha Matimbwa iliyobaki kupatiwa umeme pamoja na vijiji vingine ikiwemo Kondo vitafikishiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu iliyoanza mwezi Juni, 2017 utakaokamilika mwaka 2020/2021.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Wananchi wapatao 1,025 wa Vijiji vya Kiromo, Zinga, Pande, Mlingotini na Kondo walifanyiwa uthamini wa mali zao tangu mwaka 2008 ili kupisha mradi wa EPZA Bagamoyo lakini hadi sasa hawajalipwa fidia:- Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi hao fidia stahiki?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la ukanda maalum la kiuchumi la Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone) ni moja ya miradi ya kimkakati ya kitaifa. Awamu ya kwanza ya mradi huu inahusisha ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa, eneo la viwanda kando ya bahari ambapo kwa kuanzia viwanda 190 vitajengwa na ujenzi wa miundombinu wezeshi na saidizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 mpaka mwaka 2010 Serikali ilifanya uthamini wa eneo lengwa lililokuwa na wananchi 2,273 na kubaini mahitaji ya fidia ya shilingi bilioni 58.771. Katika kipindi cha kati ya Agosti, 2012 na Februari, 2015 Serikali iliwalipa wananchi 1,155 jumla ya shilingi 26.66 kama fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kasi ndogo ya upatikanaji wa fedha ya fidia kutoka Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2017, Septemba, Serikali iliamua kubadilisha chanzo cha fedha za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya utaratibu mpya wabia katika mradi wa Bagamoyo (China Merchant na State Reserve Fund SGRF) ya Oman watatoa fedha za fidia kwa makubaliano maalum na mbia mwenzao (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwahakikishia wananchi wa vijiji vya Pande, Zinga, Kiromo, Mlingotini na Kondo kupitia kwa Mheshimiwa Mbunge wao, kuwa pindi majadiliano ya hawa wabia watatu yanayoendelea sasa yatakapokamilika watalipwa pesa zao mara moja.
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA) aliuliza:-
Baadhi ya vituo vya Polisi na Magereza nchini vina majengo chakavu sana vikiwemo Kituo cha Polisi Bagamoyo na Gereza la Kigongoni Bagamoyo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kujenga nyumba za Polisi na Askari Magereza Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli baadhi ya Vituo vya Polisi na Magereza nchini vina majengo chakavu ambayo yalijengwa miaka mingi iliyopita na kituo cha Polisi na Magereza Bagamoyo kikiwa miongoni mwao.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga Kituo cha Polisi, Gereza na nyumba za kuishi za Askari katika Wilaya ya Bagamoyo na Wilaya nyingine nchini zisizo na majengo hayo, ujenzi huo utajengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha za bajeti. Sambamba na hilo, Wizara imeweka msisitizo katika matumizi ya rasilimali zilizopo kama vile ardhi ili kupunguza tatizo hili kwa kujenga vituo vya Polisi katika Wilaya 25 na Magereza katika Wialaya 52 kote nchini.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Mwezi Septemba 2015 Serikali ya Tanzania, China na Oman kwa pamoja zilisaini mkataba wa ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo:-
Je, ni lini ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utaanza rasmi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utaanza rasmi mara tu Timu ya Wataalam wa Serikali (Government Negotiation Team) kukamilisha majadiliano na wawekezaji ambao ni Kampuni ya China merchants port holdings company limited ya China na Oman State General Reserve Fund na Serikali kuridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 7 Desemba, 2016 Serikali ilifanya uamuzi kwamba mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utekelezwe kwa ubia na sekta binafsi ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo. Kufuatia uamuzi huo tarehe 31 Machi, 2017 Serikali ya Tanzania ilipokea andiko la mapendekezo ya uwekezaji lililowasilishwa kwa pamoja kati ya Kampuni ya China Merchants Port Holding Company Limited ya China na Oman State General Reserve Fund.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatarajiwa kuwa timu ya majadiliano ya Tanzania itakamilisha majadiliano hivi karibuni na ujenzi kuanza mara tu baada ya mkataba wa uwekezaji wa mradi kusainiwa kati ya Serikali na wawekezaji.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Upanuzi wa barabara kutoka mita 22.5 hadi 30 kutoka katikati ya barabara umesababisha baadhi ya wananchi katika Kitongoji cha Sanzale, Kata ya Magomeni kufuatwa na barabara na nyumba zao kuwekwa X:- Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Barabara ya mwaka 1932 ilifanyiwa mabadiliko mwaka 2007, ambapo eneo la hifadhi ya barabara lilibadilika kutoka mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande wa barabara kuu na barabara za Mikoa kuwa mita 30 na hivyo kufanya eneo la hifadhi ya barabara kuwa mita 60 badala ya mita 45 za awali.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko hayo, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ilifanya zoezi la kuainisha maeneo yote yaliyoathirika na Sheria mpya ya Barabara ya mwaka 2007 kwa nchi nzima. Aidha, wananchi wote wenye mali zao katika eneo la kuanzia mita
• hadi 30 kutoka katikati ya barabara kila upande ambao wamewekewa alama ya “X” ya kijani watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa pindi maeneo yatakapohitajika kwa ajili ya ujenzi au upanuzi wa barabara na hivyo mali zao kuathirika.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Kampuni ya Utafiti wa Gesi na Mafuta imeanza kazi kubwa ya utafiti wa mafuta na gesi katika eneo la Mng’ongo, Kijiji cha Fukayosi, Kata ya Fukayosi, Wilaya ya Bagamoyo:- Je, ni nini matokeo ya utafiti huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kampuni ya Gesi na Mafuta iitwayo Dodsal Hydrocarbons & Power (Tanzania) kutoka Falme za Kiarabu inaendelea na utafiti wa mafuta na gesi katika eneo la Mng’ongo katika Kijiji cha Fukayosi, Kata ya Fukayosi, Wilaya ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Spika, kupitia utafiti huo, Kampuni ya Dodsal Hydrocarbons & Power ilifanikisha kuchimba kisima cha utafiti chenye urefu wa mita 3,866 kiitwacho Mtini-1. Kisima hicho kilianza kuchimbwa tarehe 8 Mei, 2015 na kufungwa tarehe 20 Julai 2015. Matokeo ya utafiti katika kisima hiki ni kwamba haikugundulika gesi ya kutosha kukidhi matakwa ya kiuchumi ingawaje kuna viashiria vya gesi kidogo vilivyoonekana wakati wa uchimbaji katika mashapo ya miamba ya eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Vitongoji vingi katika Jimbo la Bagamoyo havijafikiwa na mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini nchini:-

Je, ni lini TASAF itaviingiza vitongoji hivyo katika mpango wake wa kunusuru kaya maskini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Manajimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Bagamoyo ulianza mwaka 2013 ambapo vijiji/mitaa 66 vilijumuishwa katika mpango huo. Hadi sasa jumla ya walengwa katika kaya 12,081 wamenufaika na mpango huo. Aidha, jumla ya fedha zilizotumika katika mpango huo ni kama ifuatavyo:-

(a) Uhaulishaji fedha kwa (conditional cash transfer) Sh.9,709,631,300.

(b) Miradi ya kutoa ajira za muda 277 yenye thamani ya Sh.3,560,991,100 imetekelezwa.

(c) Vikundi 536 vya kuweka akiba na kuwekeza vyenye jumla ya wanachama 7,591 vimewezeshwa na hadi sasa wanachama wa vikundi hivyo wameweza kuweka akiba ya Sh.27,277,100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Sehemu ya Pili ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Bagamoyo inatarajia kuanza kabla ya Juni, 2019 kwa maana ya mwaka huu ambapo jumla ya vijiji na mitaa 44 vitafikiwa. Hivyo, jumla ya vijiji na mitaa 110 katika Wilaya ya Bagamoyo vitakuwa vimenufaika na mpango huo.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Mji Mdogo wa Bagamoyo ulianzishwa tarehe 15/6/ 2005. Mwaka 2013/2014 Mamlaka hiyo iliiomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupewa hadhi ya Halmashauri ya Mji baada ya kujiridhisha kuwa na sifa stahili.
Je, ni lini Serikali itaipa Bagamoyo hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria za Serikali za Mitaa Sura 287 (Mamlaka za Wilaya) na Sura 288 (Mamlaka za Miji), pamoja na mwongozo wa Serikali kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Mwaka 2014, mapendekezo ya kupandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo kuwa Halmashauri ya Mji yanapaswa kujadiliwa kwanza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kabla ya kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa uamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maombi hayo yalijadiliwa katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo tarehe 28, Septemba, 2018 (mwaka huu), na Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) tarehe 06, Oktoba, 2018 na kwa kuwa hayajajadiliwa kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ambao wamepanga kikao hivi karibuni, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inamuomba Mheshimiwa Mbunge awaarifu wadau wa Mji wa Bagamoyo wawe na subira hadi taratibu hizo zitakapokamilika na uamuzi kufikiwa.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Ujenzi wa Barabara ya Makofia-Mlandizi-Vikumburu kwa lami ni ahadi ya Ilani ya CCM tangu mwaka 2010, na kwa sababu upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hiyo umekamilika:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Makofia-Mlandizi- Vikumburu ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia TANROADS Mkoa wa Pwani inayounganisha Wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe. Serikali imeanza mpango wa kuijenga barabara ya Makofia-Mlandizi- Vikumburu kwa kuanza na hatua ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni na uthamini wa mali zitakazoathiriwa na ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kazi ya usanifu ilikamilika Agosti, 2017 kwa kipande cha Makofia-Mlandizi na kipande cha Malandizi-Maneromango usanifu ulikamilika Novemba, 2018. Baada ya usanifu wa sehemu iliyobaki ya Maneromango- Vikumburu kukamilika na gharama ya barabara nzima kujulikana, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiedelea kutafuta fedha za ujenzi, barabara hii itaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali ili kuendelea kupitika kipindi chote cha mwaka. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, jumla ya Sh.753,381,515 zimetengwa kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Kufuatia majibu ya Swali langu Na. 17 lililojibiwa tarehe 07/11/2018 kuhusu Bagamoyo kupata hadhi ya Halmashauri ya Mji, Serikali ilielekeza kwamba tusubiri wasilisho la Kamati ya ushauri ya Mkoa wa Pwani (RCC) ili Ofisi ya Rais (TAMISEMI) iweze kulifanyia kazi ombi hilo; na suala hilo limeshajadiliwa na RCC na taarifa kuwasilishwa Ofisi ya Rais (TAMISEMI):-

Je, ni lini sasa Serikali itaipa Bagamoyo hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA C. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo ya kupandisha hadhi Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji yaliwasilishwa kwenye barua yenye kumbu Na. CAB.51/222/01/56 ya terehe 23 Januari, 2019 kutokq kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, maombi hayo yalichambuliwa kulingana na mwongozo wa kuanzisha maeneo ya utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Wilaya ya Bagamoyo ilikosa vigezo viwili muhimu ili kuiwezesha kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji. Vigezo vilivyokosekana ni kukosekana kwa mpango kabambe wa uendeshaji wa Mji (Master Plan) na eneo lake lililopimwa kuwa na chini ya asilimia 75. Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani amejulishwa kwa barua yenye kumbu Na. CCB.132/394/01B/30 ya tarehe 14 Machi, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi na wananchi wa Mkoa wa Pwani wakati wote na jitihada zao ili kukamilisha vigezo ili kuiwezesha Bagamoyo kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Wananchi wengi katika Kata za Fukayosi na Kiwangwa Bagamoyo wanalima mananasi kwa wingi sana.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhusu kuwajengea viwanda vya kuchakata zao hilo ili kuboresha kipato cha wakulima hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa Wilaya ya Bagamoyo ni moja kati ya Wilaya zinazolima mananasi kwa wingi Mkoani Pwani. Kwa kutambua uwepo wa malighafi hiyo kwa wingi, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kusindika matunda ikiwa ni pamoja na mananasi yanayolimwa katika Wilaya ya Bagamoyo. Hii inaendana na matashi ya dira yetu ya Taifa ambayo inatambua kuwa sekta binafsi ndiyo engine ya ukuzaji uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za Serikali za kuhamasisha uwekezaji viwandani zimezaa matunda ambapo kwa sasa kuna viwanda viwili vikubwa vya kusindika matunda katika Wilaya ya Bagamoyo vya Elven Agri Co. Ltd. na Sayona Fruits Co. Ltd. vyenye uwezo wa kusindika tani 28 za matunda kwa siku na kuajiri jumla ya wafanyakazi 755.

Aidha, ili kuwa na uhakika wa malighafi za kutosha kwa mwaka mzima, tunashauri Mheshimiwa Mbunge kuendelea kushirikiana na Serikali kuhamasisha uzalishaji wa aina nyingine za matunda yatakayotumika baada ya msimu wa mananasi kupita ili kuwezesha viwanda kuzalisha kwa kipindi kirefu kwa mwaka. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Kasi ya utekelezaji wa miradi ya REA III Jimboni Bagamoro ni ndogo:-

Je, ni lini miradi hiyo itakamilishwa katika Jimbo la Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa usambazaji wa umeme katika Mkoa wa Pwani ambapo Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya zinazonufaika na mradi unaoendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya vijiji 10 vya Jimbo la Bagamoyo vimejumuishwa katika utekelezaji wa mradi wa REA III, mzunguko wa kwanza unaoendelea. Hadi kufikia tarehe 25 Juni, 2019, vijiji vyote 10 ambavyo ni Kongo, Kimarang’ombe, Kitopeni, Kiharaka (Kiembeni na Minazi Minane), Matimbwa (Ugongomoni na Kibahengwa), Udindivu KKKT, Fukayosi, Kimele A&B, Mto wa Nyanza na Migude vimepatiwa umeme na wateja wa awali 927 wameunganishiwa umeme. Kazi inayoendelea kwa sasa ni kuunganisha wateja katika vijiji vyote vilivyotajwa kadri wanavyolipia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo imejumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 9.84; njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 37.14; ufungaji wa transfoma 21 za KVA 50 na 100 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,154. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 2.05. Kazi ya kusambaza umeme katika mradi huu utakamilika ifikapo mwezi Juni 2020.