Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Deo Kasenyenda Sanga (66 total)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Pamoja na hayo, Serikali imekiri kwamba ni kweli jambo hili limechukua muda mrefu. Zaidi ya miaka 18 watu hawa wanaishi katika mazingira magumu; na baadhi ya wananchi pale sasa vibanda vyao walivyojenga kwa sababu hawaruhusiwi kuongeza, familia zao wamekwenda kuwekeza kwa ndugu zao; wanaishi tofauti na familia zao.
Mheshimiwa Spika, swali; Serikali itakuwa tayari kuwaonea huruma watu hawa na kuwalipa fidia haraka ili waweze kuishi jirani na familia zao?
Mheshimiwa Spika, la pili. Kwa kuwa wananchi hawa wamejichagua na wawakilishi wao watatu, leo wanakuja hapa, yuko tayari sasa kukutana na mimi, Waziri na Waziri Mkuu na Waziri wa Ardhi, ili tukae pamoja tuwape majibu hawa wawakilishi wa wananchi ambao wanakuja? Nakushukuru?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nimekiri kwamba ndiyo, suala limechukua muda mrefu. Ukweli ni kwamba Soko la Makambako lilionekana kwamba ni soko la Mji wa Makambako, kimsingi ni Soko la Kimataifa. Kwa hiyo, pesa zinazotakiwa ku-compensate Halmashauri ya Makambako isingeweza kuzilipa na ikaendelea vizuri na shughuli zake. Zinahitajika Shilingi bilioni 3,400 kuweza kulipa fidia watu 272.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo maana nikafanya maamuzi, nikalichukua hilo kulileta katika Wizara yangu. Nimeiomba Hazina inipe pesa hizo niweke kwenye bajeti. Ningewaachia ninyi Makambako, msingelimudu. hili ni Soko la Kimataifa, ni Soko la Tanzania. Mtakachofaidi nyie ni ushuru na kodi kutokana na soko lile. Kwa hiyo, hili ni suala la haraka na nilizungumze na lenyewe liko kwenye score card yangu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Wawakilishi watatu, Mheshimiwa Sanga, hili suala nalimudu, usiende kwa mkuu wangu wa kazi! Mheshimiwa Waziri Mkuu hahusiki, uliache nilishughulikie mimi. Una uzoefu wa kufanya kazi nami. Usisahau ule wimbo wa “Nyumba ya upanga!” Kwa hiyo, naweza kulimudu, uwalete kwangu na nitawahakikishia; ni watu 272 wanadai Shilingi bilioni 3,400 na nimeshaomba kwa Hazina kusudi pesa zilipwe.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, niishukuru Serikali kwa mpango mzuri ambao sasa unatupa matumaini. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa, suala hili limechukua muda mrefu wa mradi huu wa REA na wa Songea na wa Makambako kwenda Songea ambao ulikuwa unaunganisha Kijiji cha Lyamkena na Kiumba. Je, ili kuwapa matumaini wananchi wangu kwa sababu suala hili kama nilivyosema limechukua muda mrefu, Waziri sasa atakuwa tayari baada ya kwisha Bunge tuende tukafanye mkutano atuambie kwamba alivyosema Machi mradi unaanza?
Swali la pili, kutoka ofisi ya TANESCO pale Makambako, kuna mita kama 400 hivi 500 kwenda kwenye Kijiji au Mtaa wa Kivavi na Mtaa wa Kibagange. Tunashukuru Serikali mlishatupa transfoma na nguzo zilianza kujengwa ni muda mrefu sasa zimesimama tumekwama nguzo za kumalizia na wire. Serikali itakuwa tayari sasa kutupa wire na nguzo ili tumalizie mradi huu wananchi waweze kufaidika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa nakubaliana na yeye na kwa ridhaa yako, baada ya Mkutano huu tutafuatana mimi na yeye kwenda kwenye maeneo yake kuhakikisha kwamba maeneo yake yanapata umeme uhakika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, vijiji alivyovitaja kwa kweli vina urefu siyo mrefu sana kutoka umeme unapoishia na kwa kweli kuna transfoma ya zamani pamoja na nguzo zilizooza, kwa sasa tunafanya mabadiliko ya kubadilisha transfoma kwenye maeneo yake. Mabadiliko haya yatajumuisha pia vijiji vya Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, kadhalika Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba katika ziara yangu kwenye swali lako la nyongeza la kwanza. Napenda niunganishe na vijiji vyako hivyo viwili nitavitembelea ili kuona kama hizo transfoma zilizopo zinafaa au hazifahi ili tufanye marekebisho.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na mimi kupata nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kijiji cha Ikelu kinafanana kabisa na swali la Korogwe; kuna mradi wa kutoka Tove kuja Mtwango mpaka Ilunda, bomba la maji limepita lakini kijiji cha Ikelu ni kilometa mbili tu hakina maji. Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea maji wananchi hawa hasa ikizingatiwa kuwa wako kilometa mbili tu toka bomba lilipo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna mradi wa Tove-Mtwango ambao unapita karibu na kijiji hicho anachokisema. Awamu ya kwanza hatukuwa tumefikiria kijiji hicho kupata maji lakini sasa kwa jinsi tunavyotanua mtandao wananchi wale walioko umbali wa kilometa mbili toka bomba lilipopita tutaweza kuwaunganishia ili wapate maji.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, vilevile niishukuru kauli ya Serikali kwa kunipa matumaini kwamba sasa wananchi wangu wangu wa Makambako watapona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Makambako ni la muda mrefu takribani zaidi ya miaka 30 na kitu, mradi ambao tunao pale ulikuwa unahudumia watu 15,000 na sasa tumeshaongezeka na tumefikia zaidi ya watu 160,000. Je, Serikali imejipangaje kuona sasa tatizo hili linatatuliwa mapema na kama Rais alivyokuja alituahidi kwamba tatizo hili atalitatua?
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Waziri mwenye dhamana alikuwepo siku ile wakati Rais anazungumza kwamba, atakapomteua Waziri aanzie Makambako leo unawaambiaje watu wa Makambako?
La pili…
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotoa maelezo ya nyongeza kwa muuliza swali la msingi niseme tu kwamba, nitakachofanya sasa baada ya Bunge hili mimi nitatembelea Makambako, tutakwenda kuongea na wananchi ili tuwape mpango ambao tunao wa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru majibu mazuri ya Waziri ya kutununulia baadhi ya vifaa vya upasuaji ili tupate huduma hii. Kama nilivyosema vifaa hivi vimekaa tu haviwezi kufanya kazi, ni sawa na mifugo umechukua majike umeyaweka hujapeleka madume hakuna kitu ambacho kitaendelea pale. Serikali haioni sasa uko umuhimu wa kupeleka kwa mfano hizi dawa za usingizi ili shughuli za upasuaji ziweze kuanza? (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Rais alipopita pale aliahidi kuwaondolea kero wananchi wa Makambako ili wasiende kufanyiwa upasuaji Njombe na Kibena kama nilivyouliza kwenye swali la msingi. Hawaoni sasa iko haja ya kuchukua fedha za dharura kununua vifaa hivi pamoja na vile vilivyopelekwa ili shughuli za upasuaji zianze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deo Sanga kama ifuatavyo:-
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
13
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikiri nilifika pale Makambako na nikaenda mpaka Hospitali ya Kibena wakati nilipotembelea Makambako mpaka Njombe. Kihistoria ni kwamba watu wa Makambako walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Kibena na ni kweli Hospitali hii inakabiliwa na changamoto kubwa sana na nimshukuru Mbunge kwa kweli lazima niweke wazi, ni miongoni mwa Wabunge ambao kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana na nilitembelea mpaka miundombinu ambayo yeye mwenyewe alishirikiana na halmashauri yake kuiweka sambamba na miundombinu ya elimu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tunakupongeza kwa hilo kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba vifaa viko pale havifanyi kazi ni kweli na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema vifaa vile havifanyi kazi. Pia hata lile jengo nadhani ukarabati ulianza kufanyika na hata mfumo wa maji zile koki zenyewe zilikuwa hazifanyi kazi vizuri. Kulikuwa kunatakiwa koki maalum ambazo unagonga kwa mkono inafunguka badala ya kushika ku-avoid contamination. Zoezi hilo limeenda vizuri ikiwa ni pamoja na urekebishaji wa mitaro, lakini changamoto kubwa pale imekuwa ni fedha. Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha ile bajeti iliyotengwa iweze kufika angalau lile jengo lifanye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia amesema wazi Mheshimiwa Rais alipita kule wakati wa kampeni na aliahidi kushughulikia hospitali ile ya Makambako ili ifanye kazi vizuri. Kuhusu kutenga pesa za dharura, mimi nasema jukumu letu kubwa katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha tunaoenda nao ile bajeti ambayo ilielekezwa kwenda pale ambayo kwa bahati mbaya haijafika vizuri basi tutawasiliana ndani ya Serikali yetu ili iweze kwenda. Sasa hivi tumesema tumeongeza sana ukusanyaji wa mapato tutahakikisha yale mapato yanayokusanywa kwa zile bajeti zilizopangwa ambazo pesa hazijapelekwa ziweze kupelekwa ili miradi iweze kutekelezeka na wananchi wapate huduma.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mzee Deo Sanga naomba nikiri kwamba tutakuwa pamoja kuhakikisha kwamba wananchi wa Makambako hasa tukijua ni center kubwa sana kwa watu wa Mbeya na Songea, tutasaidia eneo lile liweze kupata huduma bora za afya.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba niulize swali la nyongeza ambalo linalingana kabisa na lile la Morogoro Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za kutoka Njombe – Mdandu - Iyayi na kutoka Njombe - Lupembe -Madeke, zilishafanyiwa upembuzi na usanifu miaka miwili, mitatu iliyopita:-
Je, ni lini sasa barabara hizi zitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Sanga kama ilivyo kwa Mheshimiwa Prosper Mbena pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kikwembe ni wafuatiliaji sana wa masuala haya ya barabara na fidia katika maeneo yao. Nawapongeza sana kwa hilo na nawaomba waendelee na juhudi hizo kwa sababu kwa kufanya hivyo wanatuunga mkono sisi tulio katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo dhamira yetu pekee ni kuwajengea wananchi miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo ameziongelea Mheshimiwa Sanga katika bajeti ambayo wameshaipitisha kuna mafungu ambayo yametengwa kwa ajili ya kuanza kujengwa kwa lami. Namhakikishia Mheshimiwa Sanga kwamba katika zile fedha zilizotengwa katika barabara hizo mbili, ikiwa na ile ya kwenda Madeke na hii ya kwenda Iyayi tutazisimamia kuhakikisha zinaanza kutumika kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami kama ambavyo viongozi wetu wa kitaifa waliahidi.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Makete ndipo ambapo kituo kinachozalisha mitamba katika wilaya hiyo na wananchi wa Wilaya ya Makete ndiyo wamekuwa miongoni mwa wanaofaidi na mikoa mingine jirani kama alivyosema:-
Swali, hivi sasa Serikali imejipangaje kuona sasa Halmashauri jirani za Mkoa wa Njombe hususan Wilaya ya Wanging‟ombe, Njombe, Ludewa, Halmashauri ya Mji wa Makambako na Lupembe zinafaidika kupata mikopo ya kuwakopesha mitamba hii ili iweze kuzalisha katika halmashauri hizi wananchi waweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Makete walitoa eneo kubwa sana kwa kituo hiki na eneo hilo bado kubwa halitumiki, Serikali imejipangaje kuona wananchi wa Wilaya ya Makete wanakopeshwa mitamba hii ili waweze kupata eneo ambalo limekaa tu halitumiki waweze kunufaika nalo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni namna gani Serikali imejipanga kutoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri ambazo zimepakana na shamba ili kujipatia mikopo kwa ajili ya kuweza kujiendeleza katika ufugaji; Wizara ipo tayari kushirikiana na Halmashauri hizo ili waweze kuona fursa zilizopo katika Benki ya Kilimo, lakini vilevile katika Benki ya TIB na NMB ili waweze kupata fursa ya kupata mikopo na kuwekeza katika ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kama Wizara ina mpango wa kugawa ardhi kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo; napenda kusema kwamba pamoja na Serikali kutambua umuhimu wa Sekta Binafsi na wananchi mmoja mmoja kujihusisha katika ufugaji; kwa sasa Serikali inaona kwamba ni vizuri shamba hilo likaendelea kubakia mikononi mwa Wizara ili liweze kutumika kwa ajili ya watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wizara inatambua kwamba huko nyuma jitihada za kubinafsisha ardhi pamoja na mali nyingine za Wizara, hazijazaa matunda makubwa sana; na mpaka leo hii viwanda vya nyama ambavyo tumebinafsisha pamoja na viwanda vya ngozi, lakini vilevile blocks za ranchi za Taifa, uzoefu umetuonesha kwamba hatujapata mafanikio makubwa sana katika kuendeleza Sekta ya Mifugo kwa utaratibu huo.
Kwa hiyo, Serikali na Wizara inalenga kuwekeza zaidi katika mashamba hayo na katika sekta kwa kusimamia yenyewe badala ya kubinafsisha mashamba hayo.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, niulize swali la nyongeza linalolingana na Wilaya ya Uyui. Katika mji wa Makambako kipolisi ni Wilaya ya Kipolisi, pamoja na maelezo ambayo Serikali imetoa mazuri. Je, Serikali ina mpango gani hasa hususani kituo cha Makambako ambacho ndicho kiko barabarani yaani kiko njia panda ya kwenda Mbeya, Songea na askari hawa hawana nyumba kabisa hata moja ya kuishi?
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzijenga nyumba katika kituo cha Polisi cha Makambako na wakati eneo la kujenga nyumba lipo? Nakushukuru
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu swali ambalo liliulizwa la nyongeza la Mheshimiwa Ntimizi, ni kwamba tuna ujenzi wa nyumba za askari kwa awamu mbili. Kwa hiyo, hoja yake kwamba eneo la Makambako limo katika utaratibu huo ama halimo?
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani cha kufanya anipatie muda nipitie kwenye orodha ya zile Wilaya maana kujua Wilaya zote kwa Mikoa ni rahisi sana, lakini kujua Wilaya zote na maeneo yote nchi nzima exactly ni wapi nyumba hizi zitajengwa hasa ukiangalia kwamba inawezekana baadhi ya Wilaya mgao haujafanyika. Inahitaji nipitie kwa hiyo baada kupitia nitamjulisha, ikiwa haimo katika awamu ya kwanza basi tutazingatia katika awamu ya pili.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini naomba niulize maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali langu la msingi nimeelezea namna ambavyo wananchi wa Kata ya Saja, Kijiji cha Nyigo na Mtewele namna wanavyopata tabu kwani huduma zote zinapatikana Makambako na kwenda kwenye Halmashauri yao kutoka Saja kwenda Wanging‘ombe ni kilometa 88 na kwenda Makambako ni kilometa 20 na kutoka Mtewele ni kilometa tano na Waziri amekiri ni kweli katika suala la upatikanaji wa huduma ni mbali. Kwa nini Waziri asiagize shughuli hii ya vikao ianze kufanyika? Siku za nyuma vilishafanyika na kupelekwa kwenye vikao vinavyohusika vya mkoa na hivi juzi tu tulikaa kwenye kikao na mkoa tayari walianza kushughulikia. Niombe Waziri sasa ashughulikie suala hili na kuagiza kwamba waweze kukaa vikao ili wananchi hawa wapate huduma jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Kijiji cha Nyigo, GN ambayo iko katika Halmashauri ya Makambako inaonyesha Kijiji cha Ngigo mpaka wake mwisho ni barabara ya zamani ya Mgololo. Hata hivyo, uongozi wa Iringa umewahi kwenda pale na kutaka kupotosha ukweli. Niombe sasa Waziri asimamie na afuatane na mimi ili tukaone ile GN ambayo tulipewa Halmashauri ya Mji wa Makambako ili wananchi wale waweze kupata huduma jirani na Mji wa Makambako. Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna suala zito kama linalohusu mipaka. Mimi namuelewa sana Mheshimiwa Sanga katika concern yake hiyo, wananchi wanahitaji kweli kwenda eneo hilo lakini kwa sababu maeneo ya mipaka yameshaainishwa itakuwa ni vigumu leo niagize kufanya jambo fulani. Isipokuwa nifanye jambo moja, endapo haya mahitaji yanaonekana ni ya msingi, kama nilivyosema katika jibu langu la awali, Mheshimiwa Deo Sanga najua una ushawishi mzuri sana katika maeneo yale na ukizingatia kwamba ulikuwa Mwenyekiti wa Chama wa Mkoa kwa hiyo kauli yako inasikika vizuri sana, nadhani mchakato ukianza kama nilivyoeleza katika vikao vyetu vya vijiji vya WDC, DCC na RCC jambo hili litaisha vizuri. Jambo hili linaenda hadi kubadilisha zile coordinates katika GN, ndiyo maana nasema lazima liwe shirikishi, watu wa maeneo hayo wakubaliane kwa pamoja ni jinsi gani tutafanya kama tunataka kubadilisha mipaka. Kwa mujibu wa Sheria Sura 287, kifungu cha 10 mpaka 11 vimempa mamlaka Waziri mwenye dhamana kubadilisha mipaka lakini ni endapo itaonekana ninyi mmemaliza mchakato huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Kijiji cha Nyigo kwamba GN zimebadilishwa yaani haziko sawasawa, naomba niseme kwamba katika hilo niko radhi kutembelea kijiji hicho. Katika safari zangu za Nyanda ya Juu Kusini nitamshirikisha na nitamuomba tushirikiane kama tulivyoshirikiana katika ziara yangu iliyopita lengo kubwa likiwa ni kuleta mtengamano mzuri katika maeneo yetu.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, suala la Monduli linafanana na suala la Makambako.
Mheshimiwa Spika, Makambako kuna eneo linaloitwa Kipagamo ambalo miaka ya huko nyuma wananchi waliipa Jeshi kwa ajili ya matumizi ya shabaha. Maeneo hayo sasa tayari wananchi tumejenga shule na tayari kuna makazi ya watu na matumizi hayo sasa hayatumiki kama ambavyo yalivyokuwa yamekusudiwa huko nyuma kwa sababu pana shule na makazi ya watu.
Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuwarudishia wananchi eneo lile ili liendelee kutumika kwa shule na makazi ya watu na kwa sababu barua tulishaiandika kupitia Serikali ya Kijiji na nilimpa mwenyewe Waziri mkono kwa mkono, je, ni lini sasa Serikali itarudisha eneo hilo hilo liendelee kutumika kwa wananchi? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba barua hiyo Mheshimiwa Mbunge alinikabidhi na nimeipokea na mimi nilichofanya ni kuipeleka Makao Makuu ya Jeshi ili wanipe maoni juu ya suala hilo. Ikumbukwe tu kwamba maeneo yaliyotolewa kwa ajili ya Jeshi yalipangiwa kazi za Jeshi, kwa hiyo inawezekana kwamba eneo hili sasa hivi halitumiki tena kwa shabaha kutokana na ukaribu wake na makazi ya watu lakini huenda linashughuli nyingine za kijeshi.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa hapo wavute subira tupate maoni ya Jeshi kuhusu eneo hili, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na ni imani yangu kwamba maoni hayo nitayapata muda siyo mrefu. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupewa
nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu
mazuri ya Serikali nina maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kwa kuwa lengo la Serikali ilikuwa ni
kujenga VETA kila Wilaya ili vijana wetu waweze kupata mafunzo, vijana ambao
wanakuwa wameshindwa kuendelea na vyuo vikuu na kadhalika. Je, sasa
Serikali imejipangaje kuhakikisha inakamilisha azma yake iliyopanga ya kujenga
chuo cha VETA kila Wilaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na majibu mazuri kama
nilivyosema ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali kwa majibu yake imesema kule
Njombe tuna Chuo cha Ulembwe pale ambacho kinamilikiwa na Wilaya yetu ya
Njombe. Je, Serikali sasa kwa majibu haya imejipangaje kuhakikisha chuo hiki
kinaboreshwa kama walivyosema ili wananchi wa Wilaya ya Njombe hususan
pamoja na Jimbo la Makambako, vijana hawa waweze kwenda kusoma chuo
hiki cha VETA ambacho kiko pale Ulembwe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika,
ahsante sana. Serikali imeendelea na hiyo mikakati, lakini niseme tu kwamba
kujenga chuo kimoja cha VETA ni gharama. Kwa hiyo, kwa kutumia fursa hii
kwamba Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) navyo sasa hivi
vimerudishwa katika Wizara yetu. Tunaangalia katika Wilaya ile ambayo ina chuo
cha aina hiyo basi kiweze kuboreshwa na kiweze kuchukua nafasi ya mafunzo
ambayo yatakuwa yanatolewa yanayowahusu wale wananchi wote bila kujali
sifa zao ili mradi wana akili timamu lakini hali kadhalika kwa wale ambao
wanahitaji mafunzo yale yanayofanana na yanayotolewa katika VETA yaweze
kupatikana, tayari tumeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Mkoa wa Kagera, chuo cha
Gera tayari sasa hivi kimeshafanyiwa ukarabati, lakini pia Rubondo tumeshaanza
kufanya ukarabati, kuna Kibondo, Kasulu na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa upande wa Ulembwe tutahakikisha
kwamba chuo hicho kinaboreshwa. Niwafahamishe tu kwamba ili tusifanye kazi
ambazo hazina tija, tayari Wizara imeshapanga kukutana na Wakuu wa Vyuo
vyote vya FDC’s ili kuweza kukaa pamoja na kufahamu kwa undani changamoto
zilizowakabili kabla hatujatoa fedha za kwenda kukamilisha au kuanza uboreshaji
wa vyuo hivyo.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika,
nashukuru na mimi kunipa nafasi niulize nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inafanya kazi nzuri ya kuwapelekea umeme wananchi katika nchi yetu; na kwa kuwa kipindi kilichopita Serikali kwenye Jimbo la Makambako hususan vijiji vya Ikwete, Nyamande, Manga, Utengule, Mlowa, Mahongole, Kitandililo na Kifumbe iliahidi kutuletea umeme katika Awamu ya Pili na mkandarasi ambaye tulikuwa tumepewa alikuwa ni LAC Export na mkandarasi huyu baadae Serikali kupitia Bunge hili walisema
wamemuondoa kwa sababu alikuwa hakidhi vigezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali
itatupeleka katika vijiji hivi nilivyovitamka umeme Awamu hii ya Tatu ili wananchi hawa waweze kupata umeme kama ambavyo wanapata sehemu zingine? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nikubaliane na Mheshimiwa Sanga na nampongeza, kweli nilipomtembelea alinipa
ushirikiano mkubwa na inaonesha Mheshimiwa Sanga pamoja na kwamba wananchi wanakuoenda, lakini na sisi tunakupenda kwa kazi unayowafanyia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kweli kabisa vijiji saba katika eneo la Makambako ikiwemo pamoja na vijiji alivyovitaja vya Ikwete pamoja na Kifumbe ilikuwa vipatiwe umeme kupitia mpango huo. Na kama utakumbuka Mheshimiwa Sanga, uko mradi unaojenga usafirishaji wa umeme kutoka Makambako kupitia Madaba hadi Songea
na ndiyo vijiji vilitakiwa vipatiwe umeme kutoka utaratibu ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata vijiji vyote vile, saba pamoja na vitongoji vyako vyote imeingia katika mpango wa REA ulioanza kutekelezwa katika maeneo ya Makambako pamoja na Njombe kuanzia tarehe 15 Januari,
2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwamabia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu umeanza rasmi tangu tarehe 15 Januari, 2017 na tunachofanya sasa na wananchi na Wabunge ni kuzindua Mkoa hadi Mkoa ili kuwakabidhi wakandarasi Waheshimiwa Wabunge mliko ili na ninyi wote mkitusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Deo Sanga tumeshazinfua tangu tarehe 15 Januari na wananchi wako wa vijiji hivyo saba pamoja na kijiji cha Kifumbe wataanza kupata umeme kupitia mradi huu wa REA wa Awamu ya Tatu.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa suala la Lulindi linafanana kabisa na tatizo lililoko katika jimbo la Makambako. Makambako kuelekea usawa wa kwenda Mbeya ni kilometa mbili eneo moja linaitwa Majengo hakuna mawasiliano. Kilometa tano kuelekea usawa wa kwenda Njombe kijiji chenye eneo la Kyankena Kiumba hakuna mawasiiano; Kitandililo Mawandea hakuna mawasiliano. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka minara hii ilimawasiliano yaweze kupatikana katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea na Mheshimiwa Deo Sanga kutokana na matatizo hayo na matatizo hayo yanatokanana maeneo yenye mteremko kwa hiyo mawasiliano yaliyopo katika eneo hili kuna maeneo ambayo hayana mawasiliano kwa sababu yako chini. Kwa hiyo, tutahakikisha kwamba kwanza kama nilivyokuambia nitapenda nipite hayo maeneo barabara hiyo nikajionee halafu baada ya hapo tuwatake watu wa Mawasiliano kwa Wote wajaribu kurekebisha hayo maeneo ambayo ni ya mteremko tunawezaje kuyapelekea mawasiliano.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nami niulize swali fupi. Hospitali yetu ya Makambako ilipandishwa hadhi tangu 2013 na kuwa hospitali kutoka kituo cha afya, lakini mgao wa dawa mpaka sasa tunapata kama kituo cha afya. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kupeleka mgao kama ambavyo ilipandisha kuwa hospitali kwa sababu wataalam, Madaktari wapo na chumba cha kufanyia upasuaji kinaanza mwezi huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, nilipofika pale jimboni kwake nikiwa naye ni miongoni mwa watu ambao wame-invest pesa zao binafsi kuwasaidia wananchi wao. Mheshimiwa Mbunge hongera sana katika hilo. Changamoto ya mgao wa dawa, kwamba bado unapata kwa mfumo wa kituo cha afya; wakati huo huo ikiwa kwamba Makambako ni center kubwa sana ya watu kutoka katika hizi barabara mbili; ya kutoka Ruvuma na kutoka Mbeya; tunajua ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba eneo lile kwa bajeti ya mwaka huu tutaliangalia vizuri. Tutafanya kila liwezekanalo kumwongezea bajeti kwa sababu tunataka ile center ya upasuaji ifanye kazi vizuri. Hata hivyo, Serikali tutaangalia tufanyeje ili wananchi wa Makambako waweze kupata huduma vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba niseme kwamba Serikali imelisikia na itakwenda kulifanyia kazi jambo hili.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Naishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeonesha nia nzuri ya kutatua tatizo kubwa la maji lililoko katika Mji wa Makambako. Swali la kwanza, kwa sababu Serikali imetenga fedha hizo dola ambazo amezitaja hapo, dola milioni 38, nataka kujua ni lini sasa mradi huu utaanza ili wananchi wa Makambako waepukane na tatizo kubwa wanalopata Makambako na hata wawekezaji wa viwanda inashindikana kwa sababu maji hatuna?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu mradi huu mdogo ambao kama alivyosema tenda imetangazwa ambao ni kwa ajili ya bwawa dogo la Makambako, nilipofuatilia Mkoani wanasema tayari iko Wizarani lakini Wizara bado haijarudisha kule ili mkandarasi aanze kazi. Je, ni lini sasa mkandarasi huyu ataanza kazi kwa mradi huu kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anauliza ni lini huu mradi mkubwa wa dola milioni 38 unatarajiwa kuanza. Kwa faida ya Wabunge wengine ambao watafaidika na mradi huu wa dola milioni 500 za mkopo nafuu kutoka Serikali ya India, niseme kwa sasa hatua inayoendelea tayari Hazina imekamilisha taratibu za kusaini makubaliano ya fedha kwa maana ya financial agreement. Pia Wizara inaendelea sasa kufanya manunuzi ya ma-consultant watakaokamilisha usanifu na makabrasha ya zabuni kwa ajili ya mradi huu. Mheshimiwa Deo Sanga baada ya kukamilisha taratibu hizi basi tutaendelea na kutangaza tenda na kuhakikisha kwamba mradi huu unaanza kwenye mwaka wa fedha wa 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu tenda inayoendelea ambayo inafanywa na Halmashauri ya Mheshimiwa Deo Sanga, niseme kwamba kwa vile ametoa taarifa kwamba tayari wameshaleta hizo nyaraka Wizara ya Maji, naomba nifuatilie kama kweli zimeshaletwa na tusimamie ili waweze kurudisha haraka ili shughuli iendelee. Mheshimiwa Sanga naomba tuwasiliane kwa hili.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.
Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kupitia Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya wajasiriamali wakiwemo wa Makambako juu ya Soko la Kimataifa, nini kauli ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Serikali ilitoa kauli wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya Ulinzi na kuhusu wafanyabiashara wajasiriamali wa soko la Makambako naomba kumwambia Mheshimiwa Sanga kwamba Serikali sasa inafanya uhakiki wa mwisho, itakapokuwa imekamilisha kufanya uhakiki huo Serikali itaanza kuwalipa wajasiriamali na wananchi wote ambao wanastahili kulipwa fidia katika maeneo mbalimbali yaliyotwaliwa na Serikali.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Niulize maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, lakini kabla sijauliza niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuteuliwa kwake, vile vile kutokana na majibu mazuri ambayo yamelenga utekelezaji wa Ilani ya CCM kutatua kero za wananchi, kwa majibu haya nimefarijika sana, ni imani yangu kwamba tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu eneo hili bomba la mafuta linapita nyuma ya Hospitali yetu ya Mji wa Makambako na linapita eneo la polisi pale na linapita kwenye maeneo ya wananchi kama ambavyo swali la msingi limesema.
Je, sasa kutokana na kwamba amesema atawatuma watu wa TANROADS ili waweze kwenda kuona na kushughulikia. Ni lini sasa hao watu wa TANROADS waende mapema ili kusudi kabla ya mvua za Disemba hazijaanza kunyesha ili kutatua kero ambayo ipo kwa sababu wananchi wanashindwa kupita na magari katika maeneo haya ambayo nimeyataja?
Mheshimiwa Mweyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi baada ya kumalizika Bunge hili, ili akaone maeneo ambayo yametajwa katika maeneo hayo? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pongezi zake nazipokea, lakini pia eneo hili linalopita bomba lina changamoto ipo. Pamoja na kuleta shida kwa wananchi kupita katika eneo hili, lakini pia ni hatari ndio maana niseme tu kwamba, nimeagiza mara moja sehemu hii iangaliwe, ili pia tuweze kuepusha hatari kwa sababu kama bomba linapita maeneo ya makazi na huu Mji wa Makambako ni mji ambao unakua kwa haraka, shughuli za kibinadamu nazo zimeongezeka, ili waangalie pamoja na kuona kama kuna hatari yoyote inaweza ikatokea, kitaalam tuweze kulisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge. Nitatembelea Makambako ili pia nione hizi hatua za haraka zimechukuliwa na kwamba tatizo hili linaweza kumalizika. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mwaka jana tumepitisha kwenye bajeti miradi 17 mikubwa nchini Tanzania, ikiwemo 16 Tanzania Bara na mmoja Zanzibar, ikiwemo na Makambako, kutokea fedha za kutoka India. Je, Waziri anawaambia nini wananchi wa Makambako juu ya ule mradi mkubwa ambao utajengwa katika Mji wa Makambako, lini utaanza ili wananchi hawa waweze kuondokana na adha na tabu ya maji wanayoipata katika Mji wa Makambako?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tumepata mkopo wa dola milioni 500 kutoka Serikali ya India na sasa hivi Wizara ya Fedha inakamilisha taratibu, wakishamaliza tunasaini financial agreement na mimi niko tayari, nimeshaandaa. Baada ya hilo tukio tu nitapeleka Wahandisi wakasanifu haraka. Wakishamaliza usanifu, tukiingia mikataba, tutajua mkataba utaanza lini na utakamilika lini, kwa hiyo niwahakikishie wananchi wake wa Makambako kwamba huo mradi unakuja.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa sababu tatizo la Mpwapwa linalingana kabisa na tatizo kubwa la Makambako. Mji wa Makambako una wakazi wengi zaidi ya laki moja, na tatizo la maji ni kubwa sana. Wananchi wa Mji wa Makambako alipopita Mheshimiwa Dkt. Magufuli kipenzi chao na kipenzi cha watanzania, walimueleza tatizo la maji katika Mji wa Makambako, kuna mradi ambao ulishasanifiwa wenye gharama ya zaidi ya bilioni 57, na Waziri wa Maji ambaye yupo sasa alikuwepo siku hiyo wakati anaahidi.
Je, sasa tatizo hili la mradi mkubwa wa bilioni 57 litatatuliwa lini ili wananchi wa Makambako waendelee kupata maji.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Sanga kwa ufuatiliaji wake. Maana yake pamoja na kufuatilia miradi midogo midogo ya Halmashauri ya Makambako, lakini bado kumbe amesoma na nyaraka za mradi mkubwa unaolenga kutoa maji Mto Tagamenda, kuhakikisha kwamba maji yanapatikana katika Mji wa Makambako. Lakini nikufanyie marekebisho kidogo kwamba, mradi huo unatarajia kugharimu dola milioni 32.9 na Serikali yako Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo mwenyewe uliwashawishi wananchi wako wameichagua, ilipeleka andiko Serikali ya India, na nisema tu kwamba Mheshimiwa Sanga unawaisha shughuli, tunatarajia ifikapo tarehe 15 mwezi Julai, mwezi tunaouanza kesho kutwa mambo yanaweza yakaiva kutoka Serikali ya India na tayari tukaanza na taratibu ya kutekeleza huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nikuhakikishie pamoja wananchi wa Mji wa Makambako, na hasa kwa kuzingatia kwamba ndugu yangu Sanga wewe ni shemeji yangu, kwa hiyo maji utapata.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, kwanza nianze sana kwa kumpongeza Rais John Pombe Magufuli, Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji, pamoja na wataalam wa Wizara hii, kwa namna walivyotutengea bajeti ya Wizara ya Maji katika Halmashauri yetu ya Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu wametutengea fedha nzuri, hasa ukizingatia za mradi mkubwa ule wa Makambako ambao kwa muda mrefu wananchi wa Makambako wamekuwa wakipata tabu sana juu ya kupatikana kwa maji. Anawaambia nini wananchi wangu wa Halmashauri ya Makambako, kwamba baada ya kutenga bajeti ile mwaka wa fedha unaanza keshokutwa, ili fedha zile ziweze kwenda kujenga mradi ule mkubwa lakini ukiwepo pamoja na Kijiji cha Kiumba, Mutulingara yenyewe pamoja na Ikelu na vijiji vingine ambavyo vimekosa maji. Ni lini sasa fedha hizi tulizozitenga zitakwenda? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Makambako tuna Bodi ya Maji, kwa muda mrefu Halmashauri ilishapitisha majina ya kuja katika Wizara, mwaka mmoja na nusu sasa Bodi ya Makambako haijateuliwa katika vyombo vinavyohusika. Sijajua ni TAMISEMI au ni Wizara ya Maji. Je, ni lini sasa mtateua ili watu hawa waendelee kufanya kazi katika Bodi ya Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge Sanga, ameshukukuru kwamba tumemtengea milioni 992.8, lakini anasema sasa nini kinafuata. Kinachofuata ni utekelezaji wa hiyo bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia mafaili, mwaka 2013 Wizara ilitoa mwongozo na ikatoa kibali kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri kwamba, baada ya kupata bajeti wanatakiwa kufanya taratibu za manunuzi na kusaini mikataba, lakini nakala ya mikataba walete Halmashauri. Hapo katikati kulitokea tatizo kidogo, tayari nimeshamwagiza Katibu Mkuu, aweze kutoa mwongozo mwingine, tutashirikiana pamoja na Hazina ili sasa utekelezaji wa hii bajeti ambayo imepitishwa, Waheshimiwa Wabunge, Wakurugenzi wa Halmsahauri wapewe mwongozo jinsi ya kufanya. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba suala hili tunalifanyia kazi, kwa ajili ya kutoa mwongozo kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la la uteuzi wa Bodi, tunatumia sheria namba 12 ya mwaka 2009. Zipo Bodi ambazo zinateuliwa na Wizara ya Maji, lakini zipo Bodi ambazo zinateuliwa na TAMISEMI. Kwa hiyo, hili nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nitalifuatilia ili tuweze kujua sasa nini kinafanyika na tuweze kuona ni wapi pamekwama Bodi yake haijateuliwa.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Rais alipotembelea Mji wa Makambako aliwaahidi Wanamakambako kwamba atatoa fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la Mji wa Makambako kupatiwa maji; naishukuru Serikali kwamba na kwenye bajeti zilitengwa fedha za kutoka India: Mheshimiwa Waziri anawaambia nini Wanamakambako kuhusu fedha ambazo zimetengwa kutoka Serikali ya India kutatua tatizo la Mji wa Makambako kupata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni aliahidi kwamba tutaboresha upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako. Tayari Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya India imeweza kupata fedha za kuchangia uboreshaji wa huduma za maji katika Mji wa Makambako. Taratibu za kupata Mhandisi Mshauri atakayefanya usanifu wa kina ili kuweza kujua ni maeneo yapi na usambazaji wake ukafanyika zinaendelea kufanyika na hatua hizo zitakapokuwa tayari, tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa nia ya Serikali ni kumtua mama ndoo, kumsogezea huduma jirani ili kuweza kupata maji hasa vijijini na mijini; na kwa kuwa kuna miradi 17 mikubwa ya maji hasa fedha za kutoka India ambazo zilipitishwa kwenye bajeti hapa; na kwa kuwa Mji wa Makambako umekuwa ni miongoni mwa miji ya kupata mradi huu mkubwa wa maji katika miji ile 17.
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wangu wa Mji wa Makambako ili waweze kupata maji, ni lini miradi hii itaanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Deo Sanga kwa kufuatilia mradi huu wa mkopo wa dola milioni 500 kutoka Serikali ya India. Hata jana tulizungumza naye na alinituma niende kwa Waziri wa Fedha na majibu niliyopewa na Waziri wa Fedha ni haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu sasa zinakamilishwa ili tuweze kusaini mkataba wa fedha (financial agreement) na baada kukamilisha kusaini basi moja kwa moja Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaanza kutangaza tender kumalizia usanifu ili pamoja na hiyo miji 17 bwawa lako la Tagamenda litajengwa ili Mji wa Makambako upate huduma ya maji.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Kituo cha Polisi Makambako ni kituo cha kiwilaya na kwa sababu Makambako ndipo katikati ya kwenda Songea, Mbeya na Iringa; na kwa sababu, Waziri alituahidi kutupatia kitendea kazi cha gari. Je, ahadi yake ya kutupatia gari iko pale pale ili shughuli za kipolisi pale ziweze kufanyika kwa ufanisi mzuri?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pana uhitaji mkubwa wa gari katika Kituo cha Makambako. Niendelee kusema tu kwamba, Serikali inaendelea kuweka umuhimu mkubwa wa kukipatia gari kituo kilichopo hapo na punde magari yatakapopatikana tutaweka kipaumbele kile kama ambavyo tuliahidi.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Makambako ni mji unaokua kwa kasi na Serikali ilishatenga fedha kutoka Serikali ya India ili kutatua tatizo la maji Makambako ambalo kuanzia mwezi huu wa nane, wa tisa, wa kumi na kuendelea mpaka Desemba hali huwa inakuwa ni ngumu sana.
Je, Serikali ina mpango gani sasa kuwathibitishia wananchi wa Makambako juu ya fedha za India kwamba sasa watapata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepata dola milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika miji 16 Bara na mmoja Zanzibar ikiwemo pia na Mji wa Makambako. Sasa kinachoendelea kwa sasa hivi, Mheshimiwa Mbunge, tunasubiri financial agreement isainiwe kati ya Hazina na Serikali ya India, lakini Wizara ya Maji na Umwagiliaji tunajiandaa na kuwapata wahandisi washauri kwa ajili ya kukamilisha usanifu haraka na kutangaza tender. Kwa hiyo, nikuhakikishie wananchi wa Makambako baada ya muda watapata maji ya uhakika kutoka kwenye huo mradi mkubwa utakaotekelezwa na fedha za Serikali ya India.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Barabara ya kutoka Ilunda - Igongolo yenye kilometa tisa ni ya TANROADS na imetengenezwa lakini mbele inaendelea kwenda Kivitu – Kifumbe – Makambako urefu wa kilometa 19 na tuliomba ipandishwe hadhi. Ni lini Serikali itaipandisha hadhi barabara hii kuwa ya TANROADS ili itengenezwe iweze kuzunguka kama ambavyo imefanyika kwa zile kilometa 9?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, sisi sote ni mashuhuda tukiwa katika Bunge lako Tukufu Wabunge wengi walikuwa wakiomba barabara zao zipandishwe hadhi na zichukuliwe na TANROADS. Mawazo hayo Bunge lako Tukufu likachukua na kulifanyia kazi kwa nini Wabunge wengi tumekuwa tukiomba barabara zichukuliwe na TANROADS?
Mheshimiwa Spika, jibu ni jepesi kabisa kwamba kwa sababu barabara ambazo ziko chini ya TANROADS zimekuwa zikitengenezwa kwa kiwango kizuri. Ndiyo maana tukasema tuanzishe chombo ambacho kitakuwa kinafanya kazi nzuri kama TANROADS wanavyofanya na ndiyo essence ya kuanzishwa kwa TARURA.
Mheshimiwa Spika, naomba tutoe fursa kwa chombo hiki ambacho tumekianzisha ndani ya Bunge lako kifanye kazi. Naamini kinafanya kazi nzuri kwa sababu tumeanza kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya Wabunge, wengi wana- appreciate jinsi ambavyo TARURA imeanza kufanya kazi. Naamini hata Mheshimiwa Mbunge kilio chake si barabara kuchukuliwa na TANROADS bali barabara itengenezwe ipitike kwa vipindi vyote.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Mji wa Makambako ni Mji mkubwa na ni Mji ambao una tatizo kubwa sana la maji. Baadhi ya wananchi wanashindwa kujenga viwanda kwa sababu ya uhaba wa maji. Kuna miradi 17 ya fedha kutoka Serikali ya India. Serikali iniambie hapa je, ni lini sasa miradi hii ambayo mmojawapo ni ya Mji wa Makambako utaanza ili wananchi wa Makambako waweze kunufaika na wajipange kwa ajili ya kujenga viwanda?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbunge wa Makambako pamoja na Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Mheshimiwa Mbunge wa Makambako, kwanza kabisa tunaishukuru Serikali kwamba mkataba wa kifedha kati ya Serikali ya India na Tanzania umeshasainiwa tayari. Pili, kulingana na masharti ya mkataba huo, Serikali ya India imeshaleta Wahandisi Washauri tayari, wengi ambao sasa hivi tutafanya manunuzi kupitia kwenye hilo group.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba shughuli hii inakwenda kwa kasi sana na matarajio yake ni kwamba kabla ya mwaka huu tulionao 2018 haujafika Desemba, tunataka tuhakikishe kwamba Wakandarasi wako site na wanaanza utekelezaji wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa. Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe ni shahidi kwamba nilishaelekeza mamlaka yangu ya maji ya Iringa na wanaendelea kutekeleza miradi katika Jimbo lake na mwaka huu tumetenga fedha. Kwa hiyo, tutaendelea kutekeleza pamoja na pale Mjini ambapo mimi mwenyewe nilipatembelea, tutahakikisha kwamba tunawapatia maji safi na salama wananchi wake. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais, mgombea wakati ule 2015 aliahidi Makambako Mjini kutupatia kilometa sita za lami; na kwa kuwa Serikali tayari imeanza kutupatia mita 150 ambazo tayari zimeshajengwa na mkandarasi ameondoka; na tayari tena atakuja kujenga mita 150. Kwa nini sasa mkandarasi huyu amekuwa akija mita 150 gharama itakuwa ni kubwa, kwa nini asianze kujenga kilometa sita zote kwa pamoja ili kukwepesha gharama ya Serikali isiwe kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jah People (Mheshimiwa Deo Sanga), Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, ahadi ambazo zilitolewa na Mheshimiwa Rais wakati akiomba kura kwa Watanzania ziko nyingi, na ziko za aina tofautitofauti. Zile ambazo zinahitaji fedha nyingi zinaratibiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na zile nyingine ambazo ni idadi ndogo ya kilometa ambazo zinajengwa zinaratibiwa kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI na ndiyo kama hiyo ya Makambako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba kama ilikuwa ni kilometa sita na Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba tayari tulishajenga mita 150 na nyingine 150, naomba nimhakikishie kwamba kabla ya miaka mitano kukamilika ahadi ya Mheshimiwa Rais kwa kilometa sita tutakuwa tumekamilisha.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali juu ya kituo hiki. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kituo hiki kilijengwa siku nyingi tangu 1970; na kwa kuwa majengo mengi yamechakaa; na hivi karibuni, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano alipopita katika eneo hilo aliwaahidi Wanabunda wa kituo hiki kwamba kituo hiki kitakarabatiwa haraka; ni lini Serikali itakarabati kituo hiki ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Bunda?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Makambako tuna kituo cha afya ambacho kinahudumia wananchi wa Mji wa Makambako; na kwa kuwa mwaka 2017 Serikali ilitupa fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba, hasa vya upasuaji na kwa sababu sasa hivi kituo hakina x-ray, ultrasound na vifaa tiba. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ambazo iliahidi shilingi milioni 500, kwa ajili ya kununua vifaatiba na hela za kujengea wodi ili wananchi hawa wasipate adha ya kwenda kupimwa sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Ikizu ni miongoni mwa vituo bora kabisa katika Wilaya ya Bunda ambayo kinatoa huduma ya upasuaji. Pale wana mpaka ambulance na mortuary ya kisasa kabisa. Lakini pia naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ya kukarabati vituo vyetu vya afya vilivyochakaa bado iko pale pale. Kutegemeana na upatikanaji wa fedha, tutaendelea kufanya ukarabati na maboresho.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Sanga anataka kujua lini vifaa kama x-ray pamoja na ultrasound vitapelekwa katika kituo chake cha afya cha Makambako? Naomba nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepeleka fedha MSD kwa ajili ya kununulia x-ray pamoja na ultrasound. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya vinavyokarabatiwa vinatoa huduma ya upasuaji pamoja na vipimo kwa kutumia x-ray. Kwa hiyo, nawataka wananchi wa Makambako wahakikishe katika ujenzi unaofanyika, pia na jengo la x-ray liwepo. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kata ya Lyamkena, Kijiji cha Kiumba Makatani Kilabuni, Mheshimiwa Waziri anajua, walichomeka nguzo na baadaye wakaziondoa. Ni lini mtawarudisha nguzo zile ili wananchi waendelee kupata umeme? Nataka kauli ya Serikali. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nilifika Jimbo la Mheshimiwa Sanga na kwa kweli nilitembelea maeneo yale, eneo la Makatani, leo asubuhi kabla sijaja hapa wamepeleka nguzo nyingine 20. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakandarasi wako site wanaendelea na kwa vile amenikumbusha pia kesho nitamwagiza Meneja akafuatilie utekelezaji wa maeneo hayo ambayo ameyataja.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Mwaka 2015, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa Makamboko kulipa fidia kwa ajili ya eneo hili linalojengwa Kituo cha One Stop Centre yalikuwa maeneo mawili, tunaishukuru Serikali imelipa fidia kwa ajili ya kujenga soko la kimataifa na sasa bado hili la Idofi ambalo linajengwa kituo hiki. Nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alipotoka Njombe alifika eneo la Makambako na tukampeleka pale Idofi ambapo alikutana na wananchi na Mheshimiwa Diwani mhusika na wananchi wana imani kubwa na Serikali juu ya kulipa fidia zao. Je, ni lini sasa Serikali itawalipa fidia wananchi wa Idofi ili waweze kuendelea na shughuli mahali pengine watakapohamia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mwaka huu wa fedha wa 2019/2020, hivi sasa tutaanza kuandaa bajeti, naiomba Serikali, ni kwa nini kwenye bajeti hii ya 2019/2020 usiingizwe mpango huu ambao umeingizwa hapa? Nakushukuru.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Deo Sanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi, lakini aliahidi kujenga mradi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja sasa katika ujenzi wa kituo hicho kuna process kama ambavyo jibu la msingi limesema; kuna usanifu wa awali usanifu wa kina na hatuwezi kujenga mradi bila kulipa fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Deo pamoja na wananchi wa Jimbo lake Makambako ni kwamba mradi ni ujenzi wa kituo cha pamoja lakini katika mradi ndio kuna hizo hatua zingine, kwa hiyo nimhakikishie kwamba…

MWENYEKITI: Waheshimiwa tunaomba utulivu ndani ya Bunge.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Kwa hiyo nimwahidi Mbunge na wananchi wa Makambako kwamba mradi utatekelezwa hatua zote pamoja na ulipaji wa fidia utafanyika.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 11 Aprili, 2019 kwa kuwa Waziri aliapa mbele ya wananchi wangu na mbele ya Rais alipokuja tarehe hiyo. Je, ni lini mradi huu utaanza na ni mwezi gani utaanza ili wananchi wangu waendelee kuwa na imani kutokana na kiapo alichokifanya siku ile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, siku ile kulikuwa na changamoto ya Mradi wa Ngamanga, kwa kuwa siku ile ilionekana ni lazima wataalam wabaki pale ili waweze kutatua tatizo hili; ni lini sasa hatua zilizochukuliwa ili kutatua mradi huu wa Ngamanga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Sanga kwa kazi kubwa sana anayoifanya katika Jimbo lake la Makambako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa Mheshimiwa Rais alivyofanya ziara na Mheshimiwa Waziri wetu alitoa commitment ya kuhakikisha mradi huu utatekelezeka haraka. Nataka nimtoe hofu kabisa sisi kama Wizara tumejipanga na tunatambua kabisa agizo la Mheshimiwa Rais kwamba tukishindwa kutekeleza mradi huu, tutatumbuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara ya Maji hatupo tayari kutumbuliwa, tutafanya kuusaini mkataba ule haraka ili utekelezaji wa miradi ya maji miji hii 28 utekelezwe kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa katika mradi ule wa Ngamanga, tulishatuma wataalam wetu na tumeshaangiza mabomba, kuna kazi inaendelea naamini ndani ya muda mfupi utakamilika na wananchi wake watapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa miradi mbalimbali: Ni lini ahadi za Mheshimiwa Rais zitatekelezwa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami katika Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa jirani yangu, tumezungumza mambo mengi ya Makambako. Niseme tu, ahadi za Viongozi Wakuu zikiwemo ahadi za Mheshimiwa Rais tunaendelea kuzitekeleza. Ziko ahadi ambazo tumemaliza kuzitekeleza, ziko ambazo ziko na asilimia kadhaa na zipo nyingine ambazo bado. Naahidi tu Bunge lako kwamba ahadi zote ambazo zimetolewa na viongozi, tutaendelea kuzitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi ambazo zilitolewa Makambako, ziko ahadi nyingi; iko ahadi ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami, tunaendelea na ujenzi, Mheshimiwa Mbunge anafahamu, tumeshaanza kidogo kidogo, tutajitahidi tuweze kuweka kiasi kikubwa ili tuendelee kwa Mji wa Makambako uweze kukaa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu pia kwamba pale barabara kubwa tumeitengeneza vizuri, kulikuwa na foleni nyingi pale kwenye mizani, tumeziondoa kabisa; Mji wa Makambako unawaka taa vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla, waende wajifunze waone namna nzuri tu kuweka taa katika Mji wa Makambako. Ukienda Makambako, hali ni nzuri kabisa. Tunajua tena tuna ujenzi wa One Stop Station pale Idofi; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na yenyewe ni sehemu ya ahadi, tuko kwenye mpango wa kufanya ujenzi pale. Kwa hiyo, tunaendelea na hatua nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu ahadi zote za viongozi tutaendelea kuzitekeleza na kwa ufundi mkubwa, Serikali imejipanga vizuri kuona ahadi hizi za viongozi wetu tunaweza kuzitekeleza.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili. La kwanza, pamoja na mradi huu kutoa maji katika Mji wa Makambako, bado haijakamilika ikiwepo pamoja na kujenga tenki la lita laki 5 ambalo lilikuwepo kwenye mradi, huo uzio wa eneo la chanzo cha maji pamoja na kukamilisha ofisi ya mamlaka ambayo ilikuwa ndani ya huo mradi. Je, ni lini sasa vitu vyote vitatu vitakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Serikali imetupatia fedha za mkopo nafuu kutoka India kwa ajili ya miradi ile 28 ikiwepo na Makambako, naishukuru sana Serikali, wataalam walishakuja katika Mji wa Makambako wakatembelea na mradi ule umelenga kuhudumia kata tisa ikiwepo Lyamkena na mwisho mpaka Mlowa. Je, ni lini sasa mradi huo utaanza ili wananchi wa Makambako waweze kunufaika na mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, kwanza nimpongeze sana Mbunge, mzee wangu Mheshimiwa Deo Sanga lakini ni Mbunge mfuatiliaji; siyo mara moja au mara mbili amekuwa akija katika ofisi yetu katika kuhakikisha wananchi wake wa Makambako wanapata huduma hii muhimu hasa ya maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi ule sasa hivi umefikia asilimia 60 ya utekelezaji, nasi tumekuwa wafuatiliaji wa karibu sana katika kuhakikisha Mji ule wa Makambako unapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie na tumwagize Mkandarasi aongeze nguvu, nasi kama Wizara hatutokuwa kikwazo katika kudai certificate na kumlipa kwa wakati katika kuhakikisha mradi ule haukwami na ukamilike kama ulivyopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la utekelezaji wa mradi wa miji 28, nitumie nafasi hii binafsi nimpongeze Mheshimiwa Waziri wangu lakini pia nimpongeze Katibu Mkuu na wataalam wetu kwa jitihada kubwa zilizofanyika katika kuhakikisha mradi huu unaanza mara moja kwa miji zaidi ya 28 Bara na mradi mmoja utakuwa Zanzibar katika kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la maji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ninalotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, wataalam washauri walishapita huko katika maeneo. Kikubwa katika mpango wetu ni kuhakikisha kwamba mnapofika mwezi wa Tisa Wakandarasi wawepo katika maeneo yote kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndani ya mwezi wa Tisa Wakandarasi watakuwa site na utekelezaji utakuwepo, ila la muhimu tunaomba ushirikiano katika kuhakikisha tunashirikiana ili tuweze kutatua tatizo hilo.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Suala la maji la Tukuyu linalingana kabisa na matatizo ya maji katika Jimbo la Makambako. Mambo ya upembuzi yakinifu yalishafanyika. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka maji au kutatua tatizo la maji katika Mji wa Makambako kwa sababu, tumekuwa tukiwaahidi watu kwa muda mrefu, ni lini sasa mradi ambao tumekuwa tukiwaambia wananchi utaanza kutekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Makambako ni moja ya miji 28 ambayo inakwenda kunufaika na mradi ule mkubwa ambao tumeshapata fedha kutoka Benki ya Exim. Hivyo, Serikali inakwenda kuanza kutekeleza miradi hii yote ndani ya miji 28 ifikapo mwezi Aprili. Mheshimiwa Deo Sanga mradi wa maji Makambako nao ni sehemu ya miradi ya miji 28 hivyo kufikia mwezi Aprili wataalam wetu pamoja na wakandarasi watafika site kuanza kazi.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Jeshi ni mali ya wananchi na wananchi ni sehemu yao. Sehemu ya Idofi Kihanga, eneo la pale Makambako kuna tatizo kati ya jeshi na wananchi na wananchi hawa wana eneo ambalo wanalima, wamepanda ulanzi, wanagema ulanzi kwenye eneo hilo. Sasa wana zaidi ya takribani miaka saba au nane wamekosa kupata kipato chao kupitia ulanzi. Je, Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi ili akaone mgogoro huu namna ambavyo tunaweza kuutatua, ili wananchi hawa waendelee kugema ulanzi wao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Sanga sababu hata kipindi nilipokuwa kule Ujenzi, niliwahi kutembelea eneo la Idofi kwa sababu ni sehemu ambapo kuna mradi wa Serikali pale. Niseme tu kwa ujumla wake iko migogoro kadhaa kwenye maeneo mbalimbali ambayo yanamilikiwa na majeshi yetu. Kama alivyosema Mheshimiwa Sanga ni kweli kwamba Jeshi ni la wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuwaomba tu Waheshimiwa Wabunge ikiwemo Mheshimiwa Sanga tuendelee kushirikiana na ameshauri nitembelee sehemu husika ili kutatatua mgogoro uliokuwepo. Nimhakikishie Mheshimiwa Sanga kwamba maeneo yote ambayo yana migogoro iko kamati maalum tuliiunda imetembelea maeneo yote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Sanga tunafahamu changamoto iliyokuwepo pale Idofi nimhakikishie tu tutaenda kuimaliza kwa sababu uko mkakati Wizara tumeutengeneza ili kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanamilikiwa na Jeshi ambayo yana changamoto tutaenda kuzimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali ya nyongeza mawili. Swali la kwanza; kwa kuwa kuna miradi inayoendelea katika Jimbo la Makambako, Mradi wa kwanza mkandarasi yupo Usetule-Mahongole; mkandarasi wa pili yuko Ibatu; na mkandarasi wa tatu yuko Mtulingana, Nyamande na Bugani. Je, ni, lini Serikali itawalipa wakandarasi hawa ili waweze kumalizia miradi hii kwa sababu wanakwenda kwa kususasua ili wananchi waendelee kupata maji yaliyokusudiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa mradi huu wa kutoka fedha Serikali ya India miji 28 ikiwemo na Mji wa Makambako. Miradi hii tangu yupo Waziri Profesa Maghembe inazungumzwa na kwa mara ya mwisho alipokuja Rais ambaye ni Marehemu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wananchi wa Makambako waliuliza ni lini mradi huu utaanza? Sasa nataka kujua kwa sababu kuna baadhi ya watu wanataka kuwekeza viwanda pale, wanakosa kuweka viwanda, tunakosa wawekezaji wengi ni kwa sababu mradi huu haujaanza. Sasa nataka Serikali iniambie hapa na iwaambie wananchi wa Makambako, ni lini mradi huu utaanza ili wananchi waendelee kuwekeza viwanda kama ambavyo wanahitaji pale Mji wa Makambako? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, lini wakandarasi watalipwa? Tayari wakandarasi mbalimbali wameanza kulipwa na Wizara inafanya jitihada kila tunapopata fedha kuendelea kupunguza list ya wakandarasi ambao wanadai Wizara. Kwa hiyo kadri tunavyoendelea kupata fedha, list itakapomfikia mkandarasi huyu na yeye pia atalipwa.

Mheshimiwa Spika, Miji 28 utekelezaji wake kama nilivyojibu kwenye swali lake la msingi, mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu 2021 utekelezaji wa miradi hii utaanza na itatekelezwa kwa miezi 24.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wananchi wale wamesubiri kulipwa fidia kwa muda mrefu; na kwa kuwa, hawawezi kuendeleza kufanya shughuli yoyote katika maeneo yaliyozuiliwa, wanapata shida katika nyumba zao, hawawezi kuongeza kitu: Je, sasa Serikali imejipangaje; ni lini itawalipa fedha zilizobakia ili waweze kupisha ujenzi wa mradi huu wa One Stop Centre? (Makofi)

Swali la pili; kwa sababu fedha za kujenga mradi huu zilishatengwa na zipo; nilipofuatilia fedha hizi zipo: sasa ni lini mradi huu ambao una manufaa makubwa kwa wananchi wa Makambako utaanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia fidia kwa wananchi wake wa Jimbo lake la Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mradi huu una maslahi makubwa na mapana kwa nchi yetu na kwa uchumi wa nchi yetu hasa kwa wasafirishaji upande wa SADC na East Africa Community, hata hivyo, fedha hizi ni za World Bank. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imelipa uzito, litafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo tulipe fidia kwa wananchi hawa ili wapishe kazi ya ujenzi ifanyike na huduma ya uchukuzi iweze kuboreshwa katika Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuniona kunipa swali la nyongeza.

Kwa kuwa katika miradi 28 ambayo inatakiwa ipelekewe maji na Mji wa Makambako ni miongoni katika miji hiyo 28; ni lini mradi huo utaanza katika mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sanga Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, miradi yote ya miji 28 mpaka dakika hii taratibu zote zimeshakamilika hivyo wakati wowote ule miradi hii katika miji yote 28 tunakwenda kuanza kufanya kazi mara moja.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona; kwa kuwa Mkoa wa Njombe nao ni mkoa mpya na kwa kuwa uwanja wa ndege upo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwa kuwa Njombe tumekuwa tukilima sana maparachichi.

Swali, ni lini Serikali itaanza kutekeleza kuujenga uwanja wa ndege katika Mkoa wa Njombe na kwa sababu Mbunge amekuwa akiuliza mara nyingi sana Mbunge Mwanyika juu ya uwanja wa ndege? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge mzoefu na maarufu katika Bunge hili tukufu; ni kweli kwamba Mkoa huu ni mkoa mpya na ni maarufu kwa kilimo cha maparachichi ambayo pia sasa hivi yamepata soko nje ya nchi. Wanahitaji uwanja wa ndege ili maparachichi yale yatoke moja kwa moja Njombe yaende popote ambapo yanahitajika huko duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema ana bahati kwamba eneo lake hili usanifu umeshafanyika, gharama zimeshajulikana na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Mama Samia kwamba Watanzania walipe kodi bila shuruti, pamoja na vyanzo vingine tukipata fedha za kutosha hata kesho tutajenga uwanja huu. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza; pamoja na majibu mazuri ya Serikali yenye kutia matumaini, kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo, wananchi wa eneo la Kivavi na eneo la Majengo na kwa sababu, wamesubiri kwa muda mrefu sana zaidi ya miaka saba na huu sasa tunakwenda mwaka wa nane. Je, Serikali itakuwa tayari kusimamia kama ambavyo wamesema hapa, ndani ya mwaka 2021/2022 na kuhakikisha kwamba, wananchi hawa watalipwa kama ambavyo amesema kwenye jibu la msingi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali itasimamia namna ya kuwalipa fidia wakati wa kuwalipa utakapofika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za Serikali za kuhakikisha inaongeza wigo wa umeme, tunazalisha umeme kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji, mafuta na gesi ambayo imezoeleka. Hata hivyo, tunafanya vitu vinavyoitwa energy mix, ambavyo ni vile vyanzo jadidifu tunaviita renewables ambayo kuna upepo, jua na ile wanayoita joto ardhi. Sasa, kwenye eneo la Makambako imeonekana tunaweza tukapata pale, umeme kwa kutumia upepo katika hicho Kijiji cha Majengo tulichokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatarajia kupata kama megawati 1,179 kutoka kwenye hizo renewables. Sasa, tumewakaribisha wawekezaji binafsi ili waweze kuwekeza katika eneo hilo ili isaidiane na Serikali katika kupatikana kwa umeme huo. Huo mkataba nilioutaja unaelekeza kwamba, yule mwekezaji binafsi anayekuja kuwekeza katika eneo hilo, yeye ndiye ata-acquire ardhi na kuweza kulipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nipende kutoa commitment ya Serikali, Mheshimiwa Deo amefuatilia sana kwa muda mrefu madai haya na malipo haya, nimhakikishie kwamba, tumefikia mwisho wa makubaliano na kutafuta wawekezaji katika eneo hili na Serikali itasimamia kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kuhakikisha kwamba, mkataba unaingiwa katika kipindi hicho kilichotajwa. Pili, kuhakikisha kwamba, kila yule anayetakiwa kulipwa fidia analipwa fidia stahiki katika eneo lake, kulingana na hali halisi na sheria inavyoelekeza katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Deo kwamba, wananchi wa Makambako wamefanikiwa na naendelea kuwasimamia vyema na kile wanachokistahili kukipata, watakipata kwa wakati. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; kwa kuwa viongozi wa Kitaifa waliahidi pale Makambako kutengeneza barabara kilometa mbili za lami pale mjini. Ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya viongozi wa Kitaifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema sisi kama Wizara na Serikali kazi yetu kwakweli ni kuhakikisha kwamba zile ahadi zote zilizoahidiwa na viongozi wa chama na hasa ngazi ya kitaifa zinatekelezwa, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako ahadi hizo zitatekelezwa kulingana na fedha zitakapoendelea kupatikana na hasa katika kipindi hiki cha miaka mitano ambacho ndicho tumekianza, ahsante. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Makambako kuhusiana na masuala ya Polisi na TANESCO ni wilaya na taasisi zingine ni wilaya. Serikali haioni sasa ni muhimuMakambako tupewe wilaya kwenye Halmashauri ya Mji wa Makambako kwa sababu taasisi zingine zote zipo kiwilaya kasoro halmashauri kutamka kwamba ni Halmashauri ya Wilaya ya Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, kama ifuatavyo:
-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba Halmashauri ya Mji wa Makambako ambapo yeye ndiye Mbunge wa eneo hilo kwamba kipolisi ni wilaya. Nieleze tu kuna wilaya za kipolisi na wilaya za kiutawala ambapo sisi Ofisi ya Rais - TAMISEMI tunasimamia. Ndiyo maana unajikuta kuna maeneo mengine ni Mikoa ya Kipolisi, kwa mfano Ilala ni Mkoa, lakini ni wilaya, kulikuwa na Kinondoni wakati fulani zilikuwa Wilaya za Jiji la Dar es Salaam wakati ule lakini bado zilikuwa zinatambulika kama ni Mikoa ya Kipolisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huwezi kuniambia tu kwa sababu Kinondoni ni Mkoa wa Kipolisi basi tutamke leo kutakuwa na Mkoa wa Kinondoni. Niseme tu hizo ni taratibu za kiutendaji za kiserikali endapo wao wanaona wanahitaji kuwa na halmashauri basi wafuate taratibu kama ambavyo tumejibu katika swali la msingi. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali. Pamoja na majibu mazuri ya wananchi wa vijiji hivi ambavyo vimetajwa, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza: Pamoja na Naibu Waziri kutamka hapa kwamba vijiji hivi vitapata maji mwakani na kingine cha Ikelu kina asilimia 98: Tatizo ambalo lipo aniambie hapa, Wakandarasi hawa wamesimama, hawaendelei kwa sababu hawajalipwa fedha; ni lini watalipwa fedha ili waweze kukamilisha miradi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili: nazungumza kwa uchungu, Pamoja na kwamba Wizara ya Maji wanafanya kazi nzuri sana na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Awamu ya Sita, kazi yake ni nzuri sana. Kuna jambo ambalo nataka nizungumzie hapa unisaidie katika miji 28 ambayo ilikuwa ipate maji kupitia fedha za mkopo nafuu kutoka India, limezungumzwa kwa muda mrefu, mojawapo ni Makambako nayo ipo kwenye miradi hiyo… (Makofi)

SPIKA: Sasa swali Mheshimiwa.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, sasa swali. Katika Mji wa Makambako ambao unategemea mradi huu mkubwa, una Kata tisa. Unapitiwa na Kata tisa. Wananchi hawa tumekuwa tukiwaambia kwa muda mrefu: Ni lini Mkandarasi atakwenda kuanza kutengeneza mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Kasenyenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kusema Wakandarasi tayari malipo yanaendelea na malipo tunalipa kwa awamu kadri ambavyo tunapata fedha. Ninaamini hata Wakandarasi wa Makambako nao kwa mgao wa mwezi huu wa Kumi ambao tunaugawa mwezi huu wa Kumi na Moja, nao wataingizwa katika malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na miji 28, napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri wetu Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, amefatilia kwa karibu sana suala hili na tayari wakandarasi wapo; na wenzetu kutoka Benki ya Exim kutoka India wamefika Tanzania, hapa Dodoma juzi na jana pia tulikuwa na kikao nao. Hivi ninavyoongea kikao kinaendelea ndiyo maana Mheshimiwa Waziri hapa hayupo. Kwa hiyo, niseme tupo mwishoni kabisa kuona kwamba story za suala hili la miji 28 sasa linafikia ukingoni. Tumshukuru sana Mheshimiwa Rais ameweza kusimamia kwa karibu suala hili mpaka linaelekea ukingoni. Ahsante. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutupatia fedha za mradi wa maji katika cha Ibatu.

Swali, kwa kuwa mkandarasi aliyopewa mradi huu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Ibatu mpaka sasa ameingia mitini, hakuna shughuli zinazoendelea. Nini mpango wa Serikali na kwa nini Serikali isiweke mkandarasi mwingi au ikafanya kazi wizara yenyewe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga kuhusiana na mradi wa Ibatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumefuatilia huyu mkandarasi Farbank Company na tayari tumewaagiza mameneja ambao wako pale Njombe wanafanyia kazi. Kwa sasa hivi mkandarasi amerejea kazini siku hizi mbili, lakini tumempa muda wa maangalizo kwa wiki mbili na baada ya hapo basi sheria itafuata mkondo wake.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri ambayo imeifanya na hasa kwa barabara hizi kilomita sita na kilometa 3.5 kama alivyosema kwenye jibu la msingi zimejengwa. Kabla sijakwenda kwenda kwenye swali, nimshukuru Waziri wa TAMISEMI, Ndugu yetu Bashungwa alipopita kwenye kazi zake katika Mkoa wetu wa Njombe alikuta tuna maafa pale katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, akatoa fedha zake mfukoni kuwasaidia wahanga wale, namshukuru sana sana na wananchi wanakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, kwa kuwa kazi ni nzuri na kwa kuwa kilometa zilizobaki ni kilometa 2.5. Ni lini wataanza kuzijenga ili wananchi wa Makambako wawe na imani kubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini katika kilomita hizo zilizobaki zitamaliziwa kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa moja ya jitihada kubwa ambayo Mheshimiwa Mbunge anaifanya ni kuhakikisha hii ahadi ya Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kilomita sita inakamilika na kilomita zilizobaki ni 2.5 ambazo sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tunapaswa kuzitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishazungumza na Mheshimiwa Mbunge, tulishazungumza na TARURA Mkoa wa Njombe kuwaambia kwamba barabara hizi ziwekwe katika mpango wa kila mwaka wa fedha ili hizi kilometa 2.5 tuzimalize kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025. Kwa hiyo, matarajio yetu kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 barabara hizi kilometa 2.5 zitakuwa zimeshakamika. Ahsante sana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa barabara ya kutoka Nyigu kwenda Mgololo ambako ndiko kuna kiwanda kikubwa cha karatasi ambao ni uwekezaji mkubwa sana; na ni barabara ya uchumi ambayo imekuwa ikiwasaidia sana wananchi wa eneo hilo: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ni muhimu sana na mbao nyingi tunazoziona zinapita kwenye hii barabara. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili amekuja ofisini kama yeye kuliongelea.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi ni barabara za kimkakati. Kwa hiyo, namwomba yeye pamoja na wananchi wavute subira kwamba, kulingana na umuhimu wake na jinsi inavyoliingizia Taifa fedha nyingi, basi itakuwepo kwenye mpango ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Kata ya Mlowa, Kijiji cha Mkolango, wananchi wa Mkolango wamejenga zahanati pamoja na Diwani na Mbunge; na Rais alipokuja tulimweleza jambo hili na aliahidi kwamba sasa atakwenda kumalizia kwa sababu imekwisha, wameshaezeka na kila kitu; na Naibu Waziri na Waziri walikuwepo na ndiyo mlisikia: Sasa je, ni lini mtatuletea fedha ili wananchi wa Mkolango muweze kuwaunga mkono zahanati hii imaliziwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi wa Kata ya Mlowa, Kijiji hiki cha Mukolango kwa kutoa nguvu zao kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuanza ujenzi wa zahanati. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika bajeti ya Serikali ya mwaka huu wa fedha, fedha zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya zahanati na tutatoa kipaumbele katika zahanati hii ambayo Mheshimiwa Mbunge amesema. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi. Tuna Barabara ya kutoka Makambako – Mlowa – Kifumbe ambako inakwenda kutokezea kule Ilunda. Barabara hii tumekuwa tukiiomba ipandishwe hadhi na kuwa ya TANROADS na kwa kuwa kule mbele inakotokezea barabara hii tayari ni ya TANROADS. Je, kwa nini sasa barabara hii inakoanzia isiwe ya TANROADS ikaunga na kule mbele ambako inatokea kwai le iliyo ndani ya TANRAODS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotoa maelekezo katika swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Busega, niielekeze vilevile Halmashauri ya Makambako na Mkoa wa Njombe, kuhakikisha wanaanza na wao mchakato rasmi sasa ili barabara hii na yenyewe watu wa TANROADS, wakishapitisha vile vigezo vyao na wakaona inakidhi, iweze kupandishwa hadhi na kuwa barabara ya Mkoa ili iweze kusaidia wananchi wa eneo hilo.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali swali lina maelezo madogo.

Kwa kuwa, fedha nyingi zinapelekwa za maendeleo katika Halmashauri zetu nchini zikiwepo za afya, barabara, maji, elimu. Na kwa kuwa hivi karibuni Rais wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha nyingi za kujenga madarasa katika sekondari zetu Mabilioni kwa Mabilioni. Sasa Madiwani hawa hawasimamii kwenye force account hawamo, na hawa ndiyo wanaowaeleza wananchi tumepata fedha kiasi gani.

Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka Madiwani hawa wawemo ili kusudi maana ndiyo wanaowaambia wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vilevile kama nilivyosema ndiyo wanaosimamia na Serikali posho za mwezi tulizungumza kwenye bajeti hapa tunaomba waongezewe. Je, Madiwani wote nchini, bajeti ya 2023/2024 Serikali imejipangaje kuwaongezea posho za mwezi madiwani hawa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hospitali ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi sana katika Halmashauri zetu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Lakini nimhakikishie kwamba kwa mfumo wa force account, kwa kuwa Waheshimiwa Madiwani ni viongozi wasimamizi wa miradi hiyo, mwongozo wa haukuwaweka Madiwani kuwa sehemu ya Kamati zile kwa sababu wanahitaji kuhoji zile Kamati. Kwa hiyo, kama Diwani atakuwa sehemu ya Kamati ile atashindwa kujihoji mwenyewe lakini atashindwa kusimamia wananchi katika maeneo yale katika kutekeleza miradi ile.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninamuombe Mheshimiwa Mbunge aamini kwamba dhamira ya Serikali ni nzuri kwamba Waheshimiwa Madiwani wabaki na nguvu zao za kusimamia na kuhoji Kamati ili miradi iweze kutekelezwa kwa ubora zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na posho za Waheshimiwa Madiwani, kwanza niwahakikishie kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anathamini na anajali sana kazi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani na ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha amechukua jukumu la Serikali Kuu kulipa posho za Madiwani kama Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba Serikali inafanya tathmini ya kuona uwezekano na uwezo wa Serikali kuongeza posho hizo ili muda ukifika posho hizo ziongezeke kwa ajili ya Waheshimiwa Madiwani. Ahsante. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona; barabara ya kutoka Kibena kwenda Madeke barabara hii ipo kwenye Ilani na Mheshimiwa Rais, juzi alisema barabara hii itajengwa kwa lami na Mbunge wa Lupembe amekuwa akizungumza mara kwa mara. Nini kauli ya Serikali juu ya barabara ya Kibena - Madeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna maelekezo ambayo tumeyapata kwamba barabara hii ya Kibena junction - Madeke hadi Mlimba, Ifakara ijengwe kwa kiwango cha lami. Upande wa Morogoro ambako inakwenda tayari tumeshatangaza zabuni na upande wa Kibena kwenda Madeke ipo kwenye usanifu chini ya African Development Bank, lakini pia tunategemea tuanze kuijenga kwa kilometa chache kuanzia mwaka huu wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi nzuri ya kutuletea fedha za kujenga vituo vya afya na hospitali za Halmashauri: Je, katika Kituo cha Afya cha Lyamkena na Hospitali iliyoko Mlowa katika Mji wa Makambako, inafanya kazi na inahudumia wagonjwa asubuhi mpaka jioni; ni lini Serikali italeta watumishi ili kiweze kuhudumia masaa 24? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ameomba tu ni watumishi na katika jibu la msingi nililolijibu awali ni kwamba Serikali inatarajia kuajiri na tangazo la ajira litatolewa na Waziri wa Nchi na nafikiri inawezekana ikawa kabla ya wiki ijayo. Mara atakapolitoa, ajira zitakavyoombwa, sehemu ya watumishi tutakaowaajiri, baadhi tutawapeleka katika eneo hilo ili kuweza kusaidia. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa wananchi wa Makambako wana mategemeo makubwa sana katika eneo la Idofi ambako Serikali imekuwa ikiahidi kwa muda mrefu, je, ni lini watajenga one stop center na kumalizia fidia ambayo ilibaki kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Forodha cha Idofi ni kati ya vituo vingi vya Tanzania ambavyo tunategemea kuvijenga na tayari vilishaainishwa. Sasa hivi tunachofanya ni kupata fedha na kwanza kuwalipa fidia wale ambao wanapisha ujenzi na baada ya hapo tunaanza kujenga Kituo hiki cha Forodha pale idofi katika Jimbo la Makambako. Ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali imejenga vituo vingi ikiwepo katika Jimbo la Makambako, Kituo cha Ikelu, Kitangililo na Lyamkena.

Je, ni lini sasa Serikali itatupelekea waganga ili kusudi wananchi waendelee kupata matibabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Deo Kasinyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imejenga Vituo vya Afya vya Ikelu, Kitandililo na Lyamkena na nimpongeze sana Mheshimimiwa Deo Sanga, kwa namna ambavyo anawapigania wananchi wa Jimbo la Makambako na huduma za afya zimeendelea kuboreshwa. Nimhakikishie kwamba Waganga watapelekwa katika vituo hivi ili waanze kutoa huduma za awali za msingi wakati Serikali inaendelea kuajiri watumishi wengine kwa ajili ya kuwapeleka katika vituo hivi, ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; hata hivyo, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu ni mazuri na kwa kuwa wananchi wa Makambako eneo la kiutawala kama alivyojibu kwenye swali la msingi. Ni lini sasa Serikali pamoja na Tume hiyo Tukishiikiana mimi na Serikali tutakwenda kwenye Tume ili jambo hili liweze kutekelezwa haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Kesenyenda Sanga Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia majibu yangu niliyoyatoa katika swali la msingi, nimesema kwamba tunaendelea na maandalizi. Na niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sasa tuko katika maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura. Kwa hiyo kipindi kitakapofika Tume itatangaza na Mheshimiwa Deo ataweza kushirikiana na wananchi wenzake katika wilaya na mkoa ili kuleta mapendekezo ambayo wanaona yanafaa kwa ajili ya jambo hilo analoliomba, asante. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kuna boma la Mji mwema, Mkalanga pamoja na Kata ya Kivavi, ni lini Serikali itamalizia maboma ambayo wananchi wameshayajenga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, boma hili la Mji mwema lakini na Mkalanga ni maboma ambayo tayari tulishayaingiza kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kutekeleza ukamilishaji wa maboma hayo mwaka ujao wa fedha.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

(a) Kwa kuwa, Serikali inakubaliana na mawazo ambayo wananchi wa Kijiji cha Mtewele na ndiyo wanahitaji kupata huduma Makambako kwa sababu kutoka Makambako kwenda kwenye Kijiji hicho ni kilometa nne tu na kutoka kwenye Kijiji kwenda kwenye Halmashauri yao ni kilometa 72. Je, Serikali inatuagiza nini ili tuweze kufanikisha wananchi hawa kwa sababu wako tayari kurudi Makambako?

(b) Swali la pili. Kwa kuwa Kata ya Kivavi ni kata kubwa sana na kwa sababu Serikali inania ya kuwahudumia wananchi jirani na maeneo wanakokaa. Je, Serikali itakuwa tayari tuanzishe mpango wa kugawa Kata hiyo ya Kivavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu Kijiji hiki cha Mtewele kuwa kilometa Nne bado utaratibu ni uleule. Ni wao wenyewe kuanzisha mchakato sasa hapa inahusisha Halmashauri Mbili, kwa maana ya Wanging’ombe wakae kuridhia hili kwenye vikao vyao kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi na vilevile Halmashauri ya Mji wa Makambako nao waweze kupitia katika vikao vyao na waweze kuleta katika Ofisi ya Rais TAMISEMI ili mchakato huo uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili nalo vilevile linafanana. Kata hii ya Kivavi kuigawa lakini nataka niongeze tu kidogo hapo. Kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuendeleza maeneo yale ambayo yaligawiwa hivi karibuni na tumeona jitihada kubwa ya Serikali ninyi Wabunge ni mashahidi. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi sana kuhakikisha tunakamilisha majengo ya halmashauri, tunajenga nyumba za watumishi, tunajenga ofisi za Wakuu wa Wilaya. Kwa hiyo, kwa sasa kwanza kipaumbele kikubwa cha Serikali ni kuhakikisha tunaimarisha miundombinu kwenye maeneo ambayo yapo kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Kituo cha Makambako kimewakuta wananchi na wananchi walitoa eneo hilo kwa roho nyeupe;

Je, ni lini sasa Wananchi hao watalipwa ela zao kwa sababu mwaka jana Rais alipopita mwezi wa nane aliahidi na Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri alikuwepo, ni lini watalipwa wananchi hao ili wasiteseke fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kweli kwamba kituo cha Makambako kimekuta wananchi na uthamini ulishafanywa, na kuna takriban shilingi milioni 240 kwa ajiri ya kuwalipa fidia na kwa maagizo ambayo yameshatolewa na Mheshimiwa Rais wetu. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni ahadi ambayo lazima itekelezwe. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafatilia Wizara ya Fedha ili kupata fecha hizo za kulipa fidia ili wananchi hawa waweze kupata haki yao wapishe ujenzi wa kituo hiki, nakushukuru sana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga barabara ya Ramadhani – Iyai, Mkoani Njombe ambayo iko kwenye Ilani ya CCM kwa zaidi ya miaka 15?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli hii barabara ya Ramadhani
– Iyai tumeshaanza kuijenga kwa awamu. Mwaka huu nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeitengea pia fedha kwa ajili ya kuendelea kuijenga. Matazamio ya Serikali ni kuikamilisha barabara yote hii kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe, barabara ya kutoka Kibena – Lupembe – Madeke hadi Taveta, Mheshimiwa Swalle, Mbunge huyu, amekuwa akiizungumza sana barabara hii. Ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa kwa lami ili wananchi wa Lupembe wapate imani na Serikali yao?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii inaunganisha Mikoa ya Njombe, Iringa na inakwenda mpaka Morogoro, na katika mwaka wa fedha huu ambao tutaanza, ni miongoni mwa barabara ambazo tumezitengea fedha, ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Swali langu ni katika miji ile 45 na Makambako ipo; je, ni lini Serikali itaanza kujenga stendi na soko kwa Mji wa Makambako?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa TACTIC katika Halmashauri ya Mji wa Makambako. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nafahamu Makambako ipo awamu ya pili au ya tatu. Tunakwenda kusukuma kuhakikisha ujenzi wa stendi na soko katika Mji wa Makambako unaanza mapema iwezekanavyo. Najua taratibu za usanifu zimeshafanyika na zinaendelea kukamilishwa.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona: -

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Makambako inahudumia Halmashauri mbili, yaani Jimbo la Lupembe…

SPIKA: Swali lako Mheshimiwa? Nenda moja kwa moja kwenye swali, unataka Serikali ikujibu nini?

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nimekuelewa. Nataka Serikali, katika Jimbo la Makambako tarafa moja ina majimbo mawili, kila tarafa iwe na jimbo lake ili Serikali inapopanga mipango ya kuhudumia tarafa tuweze kuhudumiwa vizuri kwenye Tarafa yetu ya Makambako. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tunalipokea hilo na tutaangalia katika bajeti zilizotengwa tuone tupeleke kituo cha afya.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambayo Wizara hii ndiyo Wizara pekee iliyotengewa bajeti ya zaidi ya shilingi trilioni tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa majibu ya Serikali ni mazuri vipo baadhi ya Vijiji – Miji vinavyofanana na hivi alivyovitaja ikiwemo Ibumila na maeneo mengine. Je, Serikali iko tayari sasa kuwapatia wananchi umeme kwa bei ya vijiji kama alivyotaja vikiwepo Vikwete, Mkolango na Malombwe?

Swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Makambako wa Kata ya Kivavi na Kata ya Majengo wameathirika kwa muda mrefu wakisubiri umeme wa upepe na kulipwa fidia zaidi ya miaka 20. Je, Serikali inawapa majibu gani wananchi hawa ili kama haiwezekani wananchi waendelee na shughuli zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la kwanza la swali la Mheshimiwa Sanga, Serikali inayo nia ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba wananchi wanaunganishiwa umeme kwa gharama nafuu ambazo wanazimudu. Kama tulivyosema juzi kwenye bajeti yetu, tunaendelea kufanya tathmini na upembuzi yakinifu kubaini ni maeneo gani yanaweza yakawa yanakidhi gharama hizo za shilingi 27,000 pia kutafuta chanzo kizuri na cha uhakika cha kuweka ruzuku katika eneo hilo, kwa sababu ni kweli gharama za kuunganisha umeme ni kubwa. Pale ambapo tunatakiwa kuunganisha kwa shilingi 27,000 basi inabidi kuwekwa ruzuku kubwa na tunapounganisha kwa 320,000 basi tunaweka ruzuku kama nusu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Sanga na wengine wote kwamba jambo hili Serikali imeshalichukua na inalifanyia kazi tunaamini litakamilika siku chache zijazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la pili, ni kweli kwamba wananchi wa maeneo ya Makambako wameahidiwa kupewa umeme wa kutumia upepo na maeneo yao yalainishwa kwamba yatalipiwa fidia kwa muda mrefu. Tumechukua muda mrefu kwenye mazungumzo na wale waliotaka kuwekeza ninapenda kusema kwamba tumefikia hatua ya mwisho ya mazungumzo hayo, ambapo TANESCO tayari wamekwishatengeneza mkataba wa makubaliano na wanaupitisha kwenye taasisi yao na baadae utakuja Wizarani ili utolewe sasa kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Makambako kabla ya mwezi wa Tisa shughuli zitaanza site kwa kulipa fidia na kuanza kutekeleza mradi utakaotuongezea umeme wa upepo kwenye gridi yetu ya Taifa.(Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Mahongole wana kituo cha afya;

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa kituo cha Afya Kata ya Mahongole?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itamalizia Kituo cha Afya cha Mahongore kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ongezeko ni kubwa sana la uhalifu katika Mji wa Makambako na kwa sababu Makambako kipolisi ni Wilaya na tunakituo kimoja. Ni lini Serikali sasa itaondoa adha hii kwa kujenga kituo kingine pale Majengo, pale Idofi, pale Maguvani ili kuwaondolea adha wananchi waishi kwa amani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Sanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Mji wa Makambako umekuwa kwa kasi, kuna ongezeko kubwa la watu na shughuli za kiuchumi ambako ni kivutio kwa wahalifu pia. Nimuahidi tu kama kituo kilichopo kwa sasa hakikidhi haja, tutafanya tathmini kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya na kuona namna gani tutahitaji kufanya kwa maana ya kupanua huduma za polisi katika eneo lake. (Makofi)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona; kwa sababu Halmashauri yetu ya Mji wa Makambako ina maeneo ambayo ni vijiji na vitongoji. Je, Wizara haioni sasa ni muda wa kuwapelekea wananchi wa Makambako ambao wanalipa bei za kama mjini wakati mazingira ni vijijini yaliyo mengi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, na Mheshimiwa Mbunge kama mtakumbuka wakati tunawasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka ujao wa fedha tulieleza kwamba tumepokea kilio cha wananchi wengi na Waheshimiwa Wabunge kwamba ni kweli yapo maeneo ambayo yapo katika maeneo ya mijini, lakini yana sifa ya maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, tumeamua tuunde timu ya wataalam kutoka REA, TANESCO na Wizara ambapo itazunguka kwenye majimbo yote na kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kukusanya taarifa za maeneo yenye sifa hizo. Baada ya hapo na kwa kweli hatutangoja miezi sita iishe, basi maeneo haya wananchi watalipia gharama za kuunganisha umeme kama wananchi wa vijijini. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Njombe stendi ya Mkoa iko Njombe na kwa sababu Njombe ni pembezoni mwa mji, unapozungumzia mji ni Makambako ambako ndiyo highway ya kwenda Malawi kwenda Songea, kwenda Mbeya na kadhalika. Ni lini sasa stendi ya mabasi ya Mji wa Makambako itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga almaarufu Jah People, Mwenyekiti wetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, stendi ya Mkoa wa Njombe ni kweli iko katika mji wa Njombe, lakini naomba tukubaliane kwamba tunaichukua hoja hii ya Mheshimiwa Deo Sanga, nafahamu Makambako pale tuna stendi, lakini ni stendi ya mji inayohitaji maboresho kwa hiyo tutakaa mimi na Mheshimiwa Sanga tukubaliane tuone Wizara inaweza ikafanya nini kuboresha stendi pale Makambako Mjini. Ahsante.