Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Deo Kasenyenda Sanga (27 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi hii kuungana na wenzangu kuunga mkono bajeti ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mjadala ambao ulikuwa unaendelea humu ndani wako watu waliosema hakuna utawala bora, Rais anaingilia mihimili mingine, mimi niseme, hivi wewe ndiyo baba mwenye nyumba, mke uliyemuoa ana watoto amekuja nao...
MHE. DEO K. SANGA: ...amezaa na mtu mwingine na mtu mwingine, wewe ndiyo wa tatu…
MHE. DEO K. SANGA: Unasimamia watoto wa kwako na hawa, hivi hawa wengine wakiwa wezi huwezi kuwaambia acheni wizi?
MHE. DEO K. SANGA: Utaambiwa unaingilia? Ndugu zangu, kwa nini tunadhoofisha nguvu zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano?
Rais anafanya kazi nzuri sisi sote ni lazima tukubaliane kwamba Rais anafanya kazi nzuri. Mawaziri wake wanafanya kazi nzuri ni lazima tuwaunge mkono, tumeona kwa macho yetu wenyewe. Halafu tunakuja hapa tunasema anaingilia mhimili mwingine. Hivi mtu unakuwa mwizi asiseme kwamba jamani acheni wizi? Hawa Ofisi yako Waziri Mkuu na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli lazima waangaliwe vizuri watumbuliwe na wenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM…
MHE DEO K. SANGA: Kila wakati mmesema Serikali hii hakuna chochote, hakuna kitu, sasa imeleta bajeti tangu mimi nimekuwa Mbunge hakuna bajeti nzuri na yenye mwelekeo mzuri kama hii, hii sasa imebaki ni ukombozi kwa Watanzania. Tuseme kweli jamani, tuwe wapenzi wa Mungu bajeti hii ina mwelekeo mzuri, inaonesha dira kwamba sasa angalau wananchi wetu matatizo mbalimbali yatapungua au yatakwisha kabisa katika miaka mitano, lazima tuipongeze Serikali ya CCM.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sasa Jimbo langu la Makambako. Rais alipotembelea katika mji wetu wa Makambako aliahidi ahadi sita na moja kutatua tatizo la maji katika mji wa Makambako.
Pili ilikuwa ni lami kilometa sita katika mji wa Makambako; tatu ilikuwa ni fidia ya soko la kimataifa kulipwa kwa wananchi wa mji wa Makambako na nne ilikuwa ni vifaa vya upasuaji katika hospitali ya mji wa Makambako.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mji wa Makambako tumepata madaktari wazuri, tatizo kubwa tunalolipata gari letu la kubebea wagonjwa kila siku linapeleka mara tano, mara sita Wilayani Njombe kwa ajili ya upasuaji. Tuombe sana Serikali itupe vifaa vya upasuaji ili kupunguza gharama za kupeleka watu kule Njombe kila wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tano, ni kuimarisha uwanja wetu wa michezo na sita ilikuwa ni umeme vijijini. Ahadi hizi zote za Rais nimewapelekea Mawaziri wote wanaohusiana na Wizara hizi. Ombi langu wahakikishe wanazifanyia kazi ili ziendane na kasi ya Rais wa Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, pale Makambako upande wa Polisi ni Wilaya inayojitegemea Kipolisi, yupo OCD na kadhalika. Tuna eneo kubwa sana la kujenga nyumba za polisi hata nyumba moja ya polisi pale haijajengwa. Ombi langu tuhakikishe tunajipanga vizuri ili tuweze kuwajengea nyumba nzuri za kuishi hawa askari wetu wa polisi pale Makambako.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jambo lingine upande huo huo wa polisi, katika kituo chetu pale ni centre kubwa sana ya kwenda Mbeya, Songea, Liganga na kadhalika. Gari la polisi linalotumika ni la siku nyingi na wakati fulani RPC amekuwa akitoa gari kutoka Njombe. Niombe sana tuhakikishe pale tunapewa gari na wakati fulani gari lingine limechukuliwa kutoka Ludewa na ndiyo lipo pale Makambako. Kwa hiyo, niombe sana katika bajeti hii kuhakikisha tunapata gari letu la polisi ili gari la Ludewa liweze kurudi Ludewa mahali ambapo walikuwa wameliazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu inaelezea kujenga VETA kila Wilaya. Naomba tuhakikishe tunajenga VETA katika Wlaya yetu ya Njombe ili vijana hawa wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne waweze kwenda kujifunza ujuzi mbalimbali katika eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Waziri wa Ujenzi, tulikuwa tumeleta maombi kupitia kikao chetu cha RCC cha Mkoa kupandisha hadhi za barabara inayotoka Makambako – Mlowa - Kifumbe - Kitandililo na barabara nyingine ya TANROAD ambayo inatoka Ikelu - Ilengititu – Kifumbe. Niombe sana kwa sababu Halmashauri haina uwezo wa kuweza kutengeneza barabara hizi tuombe zipandishwe hadhi ili kusudi ziwe zinapitika wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua bajeti hii hata kuchangia ni wajibu wa kuchangia lakini kama nilivyosema ni nzuri, ni lazima tuiunge mkono ili Serikali iende ikafanye kazi.
kwa sababu ya Serikali ya Awamu ya Tano na watu wanaomsaidia Rais Waheshimiwa Mawaziri, songeni mbele msisikilize maneno ya watu hawa, wanataka kuchelewesha shughuli za maendeleo. Hawa wamejipanga kuchelewesha shughuli za maendeleo ili 2020 tukwame, songeni mbele na watakwama wao. (Makofi)
Sasa umekuja hapa hutaki kuchangia na watu wamekutuma hapa uje kuchangia maana yake nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu nimalizie kwa kusema naunga mkono bajeti hii naitaka Serikali kuhakikisha tunapotoka hapa inakwenda kufanya kazi zilizopangwa katika maeneo yetu, CCM!
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie angalau kwa dakika tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri, Watendaji wote wa Wizara hii ya Elimu, wanafanya kazi nzuri, mwelekeo tumeshauona nadhani tumeuanza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Walimu wa Sayansi ambao Wabunge wenzangu wamelizungumzia sana. Sasa tatizo ambalo naliona, bila kuona namna gani tutalitaua, tutaendelea kuwa na tatizo na Walimu hawa wa Sayansi. Kwa mfano, Walimu hawa kila mwaka wanaopatikana ni wachache; na tatizo kubwa ambalo linajitokeza ni kwamba baadhi ya sisi wazazi; Walimu wenyewe tunawajengea mazingira watoto kwamba somo hili ni gumu. Hili ndiyo tatizo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu tuone namna gani tunaanza kujenga misingi huku chini kutoka Shule za Msingi mpaka Sekondari kuona watoto wanapenda somo hili. Tukitengeneza vizuri watoto walipende somo hili, tutamaliza tatizo la Walimu wa Sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia suala la shule binafsi. Shule za watu binafsi, naweza kusema ni sawa na hospitali za watu binafsi ambazo zinahudumia na Serikali inapeleka ruzuku pale. Hata Mwalimu Nyerere wakati ameanza kuambia Taasisi mbalimbali… (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mwalimu Nyerere wakati anaanzisha shule za watu binafsi, Taasisi za kidini na kadhalika, ilikuwa ni kuisaidia Serikali. Kwa hiyo, nadhani sasa muda umefika, tuone namna ya kusaidia shule hizi kwa sababu na zenyewe zinatoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi Shule za Sekondari ambazo tumezianzisha katika Kata mbalimbali, Serikali imefanya kazi nzuri; tusimamie, ziboreshwe zilingane na hizi na baadaye hizi zitajifuta pole pole zenyewe. Hii ya kuelekeza kwamba kuwe na ada elekezi, sioni kama tutakuwa tunafanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linguine ni suala la Walimu. Kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Makambako, nilikuwa nadhani TAMISEMI Wizara hii ya Elimu, hebu tuone namna hii ya kuhakiki madeni haya haraka ili Waalimu hawa waweze kupewa stahiki zao. Wenzangu wengi wamesema hapa, Walimu wanafanya kazi nzuri sana; sasa tuone namna ya kuhakiki madeni haya ili waweze kulipwa stahiki zao haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya, nirudie tena, shule za watu binafsi zinafanya kazi nzuri, Serikali, isaidie kabisa. Zinafanya kazi nzuri sana. Tuwatie moyo! Mwaka 2015 shule hizi za watu binafsi zimefanya kazi vizuri, zimetoa watoto waliofaulu sayansi vizuri. Sasa kwanini tusiziunge mkono? Kwa nini tusiwasaidie?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii ya Waziri wa Elimu asilimia mia moja kwa mia moja, baada ya kuona haya marekebisho ya ada elekezi yaondolewe. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru na mimi kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana Wizara hii, watendaji wote na Waziri na Naibu Waziri, wamefanya kazi nzuri na bajeti hii ina muelekeo mzuri; wapate fedha, sisi tunasubiri maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja alikuwa anachangia jana hapa, anasema daraja la Kigamboni halina faida, hivi kweli halina faida daraja la Kigamboni, kweli? Ila amesema amekwenda mara nane, mara ngapi, anakwenda na kurudi, si ndio faida yenyewe. Kama daraja halipo angekwendaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ni kwa ajili ya watu wa chini. Na watu wa chini kule, hivi tunakwenda kuwaambia leo mambo hayo watu wa Kigamboni kweli? Eeh, wanatembea kwa mguu, si ndio wana faidi daraja hili. Songa mbele Waziri, usirudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumzia habari ya kuuza zile nyumba. Nyumba ziliuzwa Waziri Mkuu alikuwa Mheshimiwa Sumaye. Mheshimiwa Sumaye ndiye aliesimamia mambo hayo, ndiye alieuza zile nyumba, lakini na nyumba zile na nyumba…
MHE. DEO K. SANGA: …mnanijua, wee!
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nyumba zile…
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nyumba zile walionunua ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni Mheshimiwa Sumaye, si athibitishe!
Mheshimiwa Mwenyekiti, walinunua nyumba zile ni Watanzania, ndio walionunua zile nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri mwenye dhamana, pale mjini…
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Waziri katika bajeti aone namna ya kutafuta fedha hata kilometa moja na nusu Makambako Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, katika kupandisha daraja barabara za Halmashauri kwenda TANROADS, kuna barabara ya kutoka Makambako - Kifumbe, kutoka Usetule kwenda Kitandililo, tafadhali sana. Lakini vinginevyo Rais wa Awamu ya Tano…
MWENYEKITI: Ahsante! Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wachangiaji wenzangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu; Waziri Mkuu; Makamu wa Rais; Mawaziri na Waziri mwenye dhamana hii ya afya, pamoja na Naibu na Watendaji wake wote, kwa namna ambavyo wameonesha vizuri mwelekeo wa bajeti hii kwa mwaka wa 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli. Unajua wakati fulani vijembe hivi! Hivi kweli pale Muhimbili hakuna mabadiliko! Muhimbili ukienda sasa hivi pana mabadiliko makubwa kabisa. Duka la MSD Mheshimiwa Rais alisema litakuwa pale, Waziri mwenye dhamana amesimamia liko pale. Vitu vingine, kuna mabadiliko makubwa! Kwa kweli tuwatie moyo kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kuna mchangiaji mmoja alizungumzia lugha fulani iliyokuwa inagusa akinamama. Akinamama wametuzaa; kalipuka! Ni mama zetu hawa, wametuzaa, lakini mmoja vile vile siku ya nyuma yake pia naye alidhalilisha akinamama hawa hawa! Alitamka kwamba alipokwenda huko wakapigwa, wakakatiwa shanga zao. Hivi ndiyo vya kuzungumza hapa vitu nyeti kama hivyo? Eeh! Sasa niseme, kama Mwenyekiti wa CCM mwenzangu kwa yule kijana ambaye Mbunge alizungumzia lugha ambayo CCM hatukumtuma, mimi namwombea radhi kama Mwenyekiti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tuliopo hapa, kila mmoja ana akili; na wakati fulani tuliopo hapa wote ni vichaa, lakini vichaa vinatofautiana. Ukienda upande wa elimu na ndiyo maana sekondari, shule za msingi na kadhalika huwa kunakuwa na shule za watu wenye vipaji maalum. Maana yake hawa wana akili kuwazidi wenzao. Sasa baadhi ya Wabunge hapa walizungumzia habari ya viti kumi ambavyo Mheshimiwa Rais anawateua kwa kazi maalum, kwa vipaji maalum. Ndiyo maana alimteua Mheshimiwa Tulia, Naibu Spika kwa kazi maalum. Kwa hiyo, tusimwingilie Mheshimiwa Rais, kazi ambazo anawateua watu, zile nafasi kumi amemteua Waziri wa Fedha, ameteua na wengine, tusimwingilie nafasi zile kumi. Hata Mheshimiwa Mbatia amewahi kuteuliwa kupitia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie habari ya Jimbo la Makambako. Nilimwandikia Mheshimiwa Waziri ile ahadi ya Mheshimiwa Rais. Ndugu zangu, naishukuru Serikali, miaka miwili, mitatu iliyopita mmepandisha hadhi Kituo cha Makambako kuwa hospitali na mmetuletea Madaktari wa kutosha, tunao. Tatizo kubwa nimekuwa nikisema hapa na niliseme tena kwa Mheshimiwa Waziri, tuna jengo la upasuaji, tulichokikosa ni vifaa vya upasuaji. Gari letu la wagonjwa limekuwa likipeleka watu Njombe kila siku, mara saba, mara tano mpaka mara nane. Ni gharama kubwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha na nilimltea, akaniambia Daktari anipe orodha ni vitu gani vidogo vidogo ambavyo vimekosekana. Nilimpa! Atakapohitimisha aniambie wamejipangaje kuona sasa tunapeleka vifaa vya upasuaji pale Makambako ili kuwaokoa akinamama na watoto, gari lisiwe linakimbia kwenda Njombe na Ilembula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo hospitali yetu ya Makambako tuna wodi ya akinamama na watoto. Wodi nzuri iliyojengwa zaidi ya miaka miwili, vimebakia vitu fulani fulani havijakwisha; miaka miwili tume-invest pale hela ya Serikali. Nawaomba Wizara waone uwezekano wa kuona tunamalizia jengo hili ili liweze kufanya kazi iliyokusudiwa. Chonde chonde, ili kuokoa hela ya Serikali ambayo imeendelea kukaa kwenye majengo hayo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kufungua maduka ya MSD katika hospitali zetu za mikoa na wilaya, naomba sana, Mkoa wetu wa Njombe ni mpya. Mkoa huu ndiyo Mkoa ambao sasa una kitega uchumi kikubwa ambacho kitaanzishwa, Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, naomba sana tuhakikishe tunapeleka Duka la MSD la Madawa pale Mkoani Njombe ili kuwasaidia wananchi wetu wa Wilaya na Mkoa wa Njombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Mji wa Makambako tumejenga zahanati tisa katika vijiji tisa; na karibu zahanati saba tumeshazipaua. Naomba Serikali ione upo umuhimu sasa wa kutenga bajeti ya kumalizia kuwaongezea nguvu wananchi hawa wa Mji wa Makambako. Hili linawezekana na ni kwa nchi nzima. Yako majengo ambayo yamejengwa hayajamalizika, tunaomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kumalizia haya majengo ambayo yalishajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna Kituo cha Afya ambacho kilijengwa katika Kata ya Lyamkena. Kituo hiki cha Afya kina zaidi ya miaka miwili. Kilishapauliwa na kadhalika, bado hakijamaliziwa, kimeendelea kukaa pale. Jengo hili la kituo cha afya, inawezekana kabisa na majimbo mengine vituo vya afya kama cha Makambako, vipo! Tutenge fedha kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya ili kazi iliyokusudiwa iweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwa kasi anayokwenda nayo ambapo yuko nyuma ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imani yangu na imani ya Wabunge hawa, atatufikisha salama. Nampongeza sana kwa dhati pamoja na Watendaji wake. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema, atakapokuwa anahitimisha, basi ni vizuri atueleze kwa ujumla wake ili tuweze kuwa kitu kimoja na CCM ahadi ambazo iliahidi, tunamtegemea yeye kupitia Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya, nisiwachukulie muda wenzangu, niseme tu naunga mkono hoja ya Waziri wa Afya kwa asilimia mia moja. Nawashukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Wanasema ukiona watu wanasema wewe una tatizo, wewe songa mbele, wewe ni jembe unafaa kutumikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea bajeti nzuri yenye mwelekeo na kwa kumteua Waziri Mpango pamoja na Naibu Waziri. Naipongeza Wizara ya Fedha na Watendaji wote kwa kutupa bajeti yenye mwelekeo mzuri kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mategemeo yetu Watanzania ni kwamba matatizo ya maji, elimu, afya, barabara, umeme yatapungua. Hii ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ahadi alizozitoa Mheshimiwa Rais kwa Watanzania ikiwemo Mji wa Makambako ambapo aliahidi maji, vifaa tiba, lami kilomita sita, umeme na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu bajeti hii hata waliotoka humu ndani nao wanahitaji maendeleo kwenye Majimbo yao. Rais wetu alishasema maendeleo hayana chama, peleka maendeleo hata huko katika Majimbo waliyotoka utakuwa unawatendea haki Watanzania. Ingawa wenzangu watasema, aah, aah, ndugu zangu tunawapelekea maendeleo Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala hili ambalo limeleta mkanganyiko mkubwa juu ya mageti ambayo yalishatangazwa kwamba yanaondolewa kwenye Halmashauri zetu yanayohusiana na ushuru. Waziri atakapokuwa anahitimisha hapa atuambie jambo hili limekaaje maana tayari linaleta mkanganyiko kuhusiana na kuondoa mageti haya ya ushuru wakati Halmashauri zilishaweka bajeti na wananchi wameshapata kauli ya kwamba ushuru sasa umeondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri kwa kuondoa tozo mbalimbali kwa wakulima. Jambo hili limeleta faraja kubwa sana kwa Watanzania na wakulima wetu. Nirudie tena kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kumteua Waziri huyu Mheshimiwa Dkt. Mpango sasa tunaona mipango itakwenda vizuri, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napingana na hawa watu ambao wametoka hapa na wamekuwa wakipinga kwamba hii bajeti haina mwelekeo na kadhalika, ndugu zangu uchaguzi ulishakwisha, Rais sasa ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu, Waziri Mkuu ni Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa pamoja na Mawaziri wote walioteuliwa, naomba chapeni kazi ya maendeleo kwani watu wanasubiri maendeleo katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wamezungumzia sana suala la kiinua mgongo. Mimi niseme tu kwamba suala la kiinua mgongo linagusa Watanzania wote hasa watumishi. Watumishi pamoja na Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukikatwa kodi mbalimbali lakini kodi hii ya kiinua mgongo kwa watumishi nadhani iangaliwe upya. Kwa sababu watumishi hawa wametumikia nchi na wamekatwa kodi mbalimbali. Kwa hiyo, naomba suala la kiinua mgongo kwa watumishi wote kwa ujumla liangaliwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali imesikia kilio cha Wabunge ambao wamezungumzia sana suala la manunuzi kwamba lilikuwa ni tatizo kubwa katika Halmashauri zetu na wenzangu wengi wamesema hapa. Suala hili la manunuzi ilikuwa hela zikipelekwa kwenye Halmashauri zinaliwa tu na baadhi ya watendaji ambao siyo waaminifu. Naishukuru sana Serikali, Waziri alisema hapa unaletwa Muswada wa kubadilisha Sheria ya Manunuzi na mimi naafiki kwamba utaratibu huu ukibadilishwa utaleta tija na maendeleo katika Halmashauri zetu na hizi fedha zote zinazojadiliwa hapa sasa zitakwenda kutumika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wetu wa Makambako sasa tunazungumzia suala la kujenga viwanda, watu wanahitaji kuwekeza viwanda katika mji wetu lakini tatizo kubwa ni upatikanaji wa maji. Niipongeze sana Wizara ya Maji ambayo tayari imetenga fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la maji katika Mji wa Makambako. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ya Fedha ipeleke haraka fedha hizi ili ziweze kuleta maji ili wawekezaji waweze kuanzisha viwanda katika Mji wetu wa Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, hili nimelisema mara nyingi sana, naomba nirudie, Serikali imewekeza fedha kwenye hospitali yetu pale kwa miaka zaidi ya minne sasa, tumejenga wodi mbili kubwa za akina mama na watoto imebaki tu kumalizia, miaka minne imebaki magofu. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu liangalie suala hili zinahitajika hela kidogo sana ili wodi hizi ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwani fedha ya Serikali imekaa pale kwa muda mrefu. Namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha aone ni namna gani atatatua tatizo hili la kumalizia wodi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba hospitali ile ya Mji wa Makambako imeshapandishwa hadhi na kuwa hospitali kamili na kwa miaka mitatu tunakwenda vizuri. Tatizo ambalo lipo katika Mji wetu wa Makambako, nilimueleza hata Waziri wa Afya na Waziri wa TAMISEMI, tayari tuna jengo pale la upasuaji ambalo limeshakamilika lakini tunakosa tu vifaa tiba vya upasuaji. Tuna gari letu la ambulance kwa siku mara saba linapelekea wagonjwa Njombe kwa ajili ya upasuaji. Fedha inayohitajika ni kidogo sana hata shilingi milioni 30 hazifiki ili tuweze kununua vifaa vya upasuaji vilivyobakia ili shughuli za upasuaji ziweze kuendelea. Mmetuletea Madaktari wazuri wako pale wamekaa tu hawawezi kufanya kazi kwa sababu shughuli za upasuaji hakuna. Namuomba Waziri wa Fedha atakapokuwa anahitimisha aone namna ya kutatua tatizo la kununua vifaa vya upasuaji ili kuweza kutatua tatizo la Makambako. Vifaa vinavyohitajika ni kifaa cha kuchanganyia dawa ya usingizi na vitu vidogo vidogo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Waziri Dkt. Mpango chapa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mpango huu ambao umeletwa mbele yetu. Mpango huu ni mzuri sana, una mwelekeo mzuri na dira nzuri ya kuhakikisha shughuli zote ambazo zimepangwa hapa zinakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua hata vitabu vitakatifu vinasema unapotaka kwenda peponi au mbinguni ni lazima ukeshe ukiomba. Sasa kazi ya kukesha na kuomba si ndogo, ni kubwa sana, kazi ya kukesha na kuomba na ukishakesha na kuomba ndio unaweza kufika peponi au mbinguni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano kazi kubwa ambayo ilikuwa ikiifanya ni kuturudisha kwenye mfumo, kuachana na ule utaratibu tuliouzoea kwa hiyo, ilikuwa inaturudisha kwenye mfumo. Turudi tujenge nidhamu katika Serikali na kazi hiyo imefanywa na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, amefanya kazi nzuri sana. Hata wakati anawaambia Watanzania anaomba ridhaa aliyasema haya kwamba, nipeni nitafanya moja, mbili, tatu; leo anayafanya haya tunasema aahhaa, anafanya vibaya! Lakini mtu mmoja amewahi kusema ukiona mtu anakusifia jiangalie mara mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayofanywa na Serikali kupitia Mawaziri waliopo na huyu ambaye ameleta mpango huu ni kazi nzuri sana. Sasa kwamba Serikali imeturudisha kwenye mfumo, imedhibiti mambo ya pesa, Mheshimiwa Mpango baada ya kudhibiti sasa peleka kwenye Halmashauri ili zikafanye kazi, maana kwanza alikuwa anaturidisha kwenye mfumo na sasa tumerudi kwenye mfumo, kwa hiyo fedha sasa zianze kwenda kwenye Halmashauri ili zikafanye kazi iliyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu waliozungumzia habari ya Liganga na Mchuchuma. Na mimi napata ukakasi, hivi kuna tatizo gani linalofanya shughuli ya Liganga na Mchuchuma ikwame? Kwenye mpango imekaa vizuri, tunaomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana suala la Liganga na Mchuchuma hebu sasa liweze kusonga mbele kadri ambavyo lilikuwa limepangwa ili liweze kusaidia Tanzania, tuweze kupata ajira nyingi kwa vijana wetu wa Tanzania kama ambavyo mpango upo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua napata taabu kitu kimoja kidogo sana! Mambo mengi amenimalizia yuko pale, ambayo nilikuwa nimeyaweka hapa kwa sababu...! Sasa naomba niseme! Eeh, ndio mwenyewe! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani wote ni Wabunge sawa, kila mmoja ana hadhi yake ameingia hapa, tunahitaji kuheshimiana. Tunapomnyooshea mtu, Mbunge mwenzako kwamba eti wewe huoni uchungu kwa sababu uliteuliwa, tena huyu ndiye anaheshima kubwa sana kuliko wewe, kwa sababu kama alivyosema Mbunge mwenzangu pale kwamba kila mmoja amepata kura kwa idadi tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nani aliyepata humu ndani kura nyingi kama za Mheshimiwa Magufuli, nani? Sasa zile zote si ndio amepewa yule kwa heshima ya Watanzania? Ndugu zangu tuheshimiane, aliyeteuliwa, ambaye hakuteuliwa wote ni Wabunge. Wakati fulani ninyi wenyewe ndio mnatoka huko mnakwenda pale, Waziri eeh, moja, mbili, tatu! Ni Waziri huyu, apewe heshima yake kama ambavyo Wabunge wengine tuko hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kudhibiti mambo yote sasa peleka fedha Halmashauri zikalipe na fidia zile pamoja na Makambako ikiwemo. Kuna fidia kule wananchi wangu wanadai kule ili zikaweze kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla mpango huu nauunga mkono vizuri, ni mpango mzuri ambao sasa peleka fedha zikaanze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sina la ziada. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza kwa kazi nzuri sana zinazofanyika katika nchi hii ya Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli pamoja na Waziri na Naibu Waziri na watendaji wa Wizara. Ombi, pamoja na bajeti nzuri ikiwemo barabara za Mji wa Makambako kilometa sita za lami; naomba kujua mradi wa kujenga One Stop Center lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, utaanza pale Idofi maana watu hawa wamekuwa wakisubiri muda barabara kutoka Ilunda – Igongolo urefu wa kilometa tisa ni ya TANROADS mbele inaendelea Kifumbe - Mahongole mpaka Makambako urefu wa kilometa 19. Ombi, iunganishwe iwe kuanzia Igongolo kuwa TANROADS.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano Lyemukena – Majengo - Kifumbe, Kitandilo-Mahongole hakuna mawasiliano, tunaomba mawasiliano
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. DEO K. SANGA:Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naipongeza sana Serikali kwa kuleta muswada huu ambao Wabunge wameelezea kwa muda mrefu sana ili kuleta tija na mabadiliko makubwa ambayo huko nyuma lilikuwa ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kupitia Waziri wa Fedha, Naibu na watendaji wote wa Wizara hii ya Fedha ikiongozwa na Mheshimiwa Mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli lilikuwa tatizo kubwa sana tulifika mahala unakuta bati moja lilikuwa linaweza kununuliwa kwa shilingi 35,000; simenti shilingi 22,000; mimi ninasema hivyo iko haja ya kipindi kilichopita mimi kama Mbunge, Mfuko wa Jimbo tulinunua simenti kwa shilingi 22,000 na bati la geji 28 kwa shilingi 35,000; ukiuliza wanasema Sheria ya Ununuzi. Jamani mbona huko madukani wanauza bei chini? Sheria ya Ununuzi. Kwa hiyo nadhani sasa imeletwa wakati muafaka kabisa kwamba sasa tutaangalia soko linasema nini. Kwa hiyo mimi nadhani tutawatendea haki watanzania walipakodi na kadhalika.
Lakini pamoja na marekebisho hayo, nivizuri marekebisho hayo bado Serikali iendelee kuangalia mapungufu madogo madogo ambayo yataendelea kujitokeza ili waendelee kukaa na kuona namna ambavyo waweze kurekebisha uendelee mpango mzuri zaidi kadri ambavyo itakavyokuwa inakwenda. (Mkofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu Kamati ya Mipango na Fedha za Halmashauri, mimi nishauri na niombe sana, sijaona kama wameleta amendment hapa; lakini ni vizuri Kamati hizi hasa Kamati ya Mipango na Fedha ya Halmashari iendelee kama ilivyokuwa ni lazima angalu ipitie kwa sababu Kamati hizi zinakaa kila mwezi mara moja ili kuona kwenye Halmashauri yao ni kitu gani ambacho kimejadiliwa kwenye Bodi ya Zabuni. Sasa tukiondoa kabisa Kamati hii ya Mipango na Fedha na wao ndio wenye fedha za Halmashauri na bajeti hii ambayo tumeendelea kuijadili na kuimalizia sasa Serikali imetenga fedha nyingi kwenda huko, haki ya Mungu zitakwenda kuliwa, tutakuwa tulichokifanya hakipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana kwamba waone uwezekano kabisa wa Kamati hii ya Mipango na Fedha kama alivyo Mpango mwenyewe Waziri wetu aone uwezekano wa kwamba Kamati hii ni vizuri ikapitia, itakuwa tumeitendea haki kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiuangalia muswada huu umelenga pia kuwa hudumia walemavu, jamii mbalimbali, akina mama, watoto na kadhalika, tumeutendea haki kabisa muswada huu nadhani umefika mahala pake ambapo sasa maelekeo ni mazuri.
Mimi niombe tu Waziri Mpango tunakuamini sana, Bunge hili linakuamini sana, wewe, Naibu wako pamoja na Wizara nzima, tuombe sana, Kamati ya Mipango na Fedha, niombe sana ishiriki kwenye mambo hayo ambayo wao watakuwa wamepitisha kule hawa wanapitia kuangalia kilichomo kwenye Halmashauri yao tutakuwa tumeitendea haki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vinginevyo naunga mkono hoja, ahsante sana, nakushukuru.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwanza nizungumzie suala linalohusiana na maji. Kwenye bajeti ya kipindi kilichopita kuna miradi mikubwa ambayo tuliipitisha hapa. Kwa mfano, kuna miradi mikubwa ya maji ya miji ya Makambako, Njombe na Wanging’ombe ambapo ilionyesha fedha zinatoka Serikali ya India. Kwa hiyo, ni vizuri Waziri atakapokuwa anasimama atuambie Serikali imejipangaje juu ya kutatua tatizo la maji kwa mradi mkubwa huu wa Makambako, Njombe na Wanging’ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la pembejeo hizi za ruzuku ambapo Mkoani kwetu Njombe zinachelewa sana. Sisi tunaanza kupanda kuanzia mwezi wa 11 na kuendelea. Kwa hiyo, Serikali ijipange vizuri msimu huu tunaokwenda sasa kuona kwamba pembejeo hizi zinafika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, kuna hawa wasambazaji ambao mpaka sasa wanaidai Serikali na mpaka sasa wako watu ambao wamefilisika, wako watu wanauziwa nyumba zao. Ni lini Serikali italipa deni hili ambalo wananchi hawa walisambaza pembejeo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne, ni suala la lumbesa kwa wakulima, nadhani Serikali ijipange vizuri suala hili lipigwe marufuku kwa nchi nzima ili kusudi isiwaumize wakulima.
Mheshmiwa Mwenyekiti, jambo la tano ni mifugo. Suala la mifugo limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wafugaji na wakulima na watu wanapoteza maisha. Aidha, Kamati au ninyi Serikali muone namna ambavyo nchi ya Sudan wana mifugo mingi kuliko sisi lakini hakuna tatizo la wakulima na wafugaji, waende kule wakajifunze wenzetu kule wanafanyeje mpaka hakuna migogoro ambayo ipo kama huku kwetu kila wakati mara watu wameuawa na kadhalika. Kwa hiyo, nadhani Serikali ijipange kuona namna ya kuondoa tatizo hili la mifugo na wakulima kwa sababu limekuwa ni kubwa sana, siyo kitu kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sita, hapa kuna watu wamezungumzia Wizara hii ya Kilimo. Mimi niseme ndugu zangu, Waziri huyu Tizeba na Naibu wake wakati fulani tunawalaumu bure tu, sasa watachukua wapi fedha kama hawana fedha? Nadhani sisi tuungane kwa pamoja kuona namna ambavyo tunaiambia Serikali ili bajeti ya msimu huu tunaokwenda iwe nzuri kuliko bajeti iliyokwisha ambapo ilitengwa shilingi bilioni 20 tu ambazo hazijatosha kitu chochote.
Kwa hiyo, nilikuwa nadhani sasa badala ya kumlaumu Waziri na Naibu wake na Wizara kwa ujumla, tuone namna ambavyo sasa Serikali inajipanga kuona msimu huu tunakuwa na bajeti ya kutosha kwa sababu ndiyo uti wa mgongo kwa wakulima wetu. Nadhani tukifanya hivyo, Serikali ikiongeza bajeti tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi lakini kwa sababu na mimi nipo kwenye Kamati hii nirudie tena kuzungumzia hili suala la maji, Waziri utakaposimama uwaambie wananchi wa Makambako wataondokana lini na tatizo kubwa hili la maji na uwaambie fedha za kutoka nje wananchi wale wa Njombe, Wanging’ombe wanazipataje na mpango huu sasa unaendeleaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake kwenye busara wa kuhamisha Wizara zote kuja Makao Makuu Dodoma. Pili, vile vile nimpongeze Waziri mwenye dhamana ndugu yetu Jenister Mhagama kwa kusimamia vizuri wizara hizi; zinaturahisishia sisi kama Wabunge kuweza kupita katika maofisi ambayo yako jirani, kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze na Wizara ya Afya; niiombe sana Serikali ione namna ya kuboresha maboma mbalimbali ambayo tumejenga huko kwenye majimbo yetu hasa zahanati na vituo vya afya ili yaweze kumalizika na kufanya kazi kama ambavyo sera inaelekeza
kuwa kila Kijiji na Mtaa kuwa na zahanati na kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na kwenye Jimbo langu; mimi na Waheshimiwa madiwani wenzangu na Serikali tumeweza kujenga zahanati 13 na kituo cha afya kimoja kizuri sana ambacho kimesimamiwa na diwani mmoja anaitwa Mlumbe kutoka pale Yamkeno. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ione namna ya kuboresha vituo hivi ili kusudio lile la kuwa na zahanati na Kituo cha Afya Kilonani iweze kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niishukuru sana Serikali kwa eneo langu la Makambako kwa kutupa vifaa vya upasuaji; naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo imetupa vifaa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maji. Naomba nipate majibu juu ya miradi ile mikubwa ya Miji 17 kwa Wizara hii ya Maji, fedha ambazo zinatoka India, katika miradi hii 17 mikubwa, mmojawapo upo katika Jimbo langu la Makambako. Kwa hiyo, naomba nipate majibu kutoka kwa Serikali, kwamba ni lini sasa fedha hizi zitakuja ili wananchi wa Makambako wawe na matumaini kwamba watapata mradi huu wa maji kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba Waziri mwenye dhamana atakayemteua ataanza kuja Makambako na nashukuru sana Waziri alikuja kama
ambavyo Rais alisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo. Niiombe Serikali ione namna ya kuboresha Wizara hii ya Kilimo hasa pembejeo hizi za ruzuku kwa sababu Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi juu ya pembejeo za ruzuku. Nadhani Serikali ione namna ya kupunguza tozo na kodi mbalimbali hasa kwa pembejeo hizi za mbolea ili kusudi kila maduka yauze na mkulima aende kununua kwa bei ambayo ni ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile Serikali ione namna ya kuboresha mbegu. Wako watu ambao wamekuwa wakifanya kazi ya kuchakachua hizi mbegu; wakulima wetu wanapopanda mbegu hizi zimekuwa hazioti. Niiombe sana Wizara kwamba ifufue maeneo ambayo
walikuwa wanapanda mbegu kama pale Uyole, Njombe tulikuwa na pale NDC, tuna maghala pale na mashamba walikuwa nayo, wafufue suala hili la pembejeo ili wananchi wetu waweze kupata. Kwa hiyo, suala la mbolea nimeshalizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu; niombe sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, pamoja na kazi nzuri anayoifanya, ingawa wapo watu wengine hata ungefanya kazi watasema hakuna kinachofanyika; unajua mtoto wa kambo hata ungemlea namna gani atasema hakuna kazi
zinazofanyika; Waziri unafanya kazi nzuri kupitia Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwamba katika ahadi zile za rais za kilometa sita za kujenga lami katika Mji wa Makambako, nikuombe sana na ile kilometa moja ambayo ulisema ingeanza mwaka huu wa 2016/2017 na muda
uliobaki ni mfupi, nimwombe sana Waziri ahakikishe kwamba, kilometa sita zile ambazo Rais alisema, mwaka wa 2017/2018 zinajengwa, ile ahadi itekelezwe ili wananchi wangu wa Makambako waweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme. Nikupongeze sana Mheshimiwa Profesa Muhongo, Naibu Waziri wako pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo tunaiona mnaifanya, hongereni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme, kwenye jimbo langu, maana kipindi kilichopita ilikuwa nipate awamu ile ya pili ya REA; lakini yule mkandarasi ambaye mlinipa, Lucky Export na baadaye mkamwondoa, kwamba hakuwa anakidhi vigezo, sasa mmeniambia mnaniletea mwingine kutokana na majibu ambayo nilimuuliza hapa Naibu Waziri. Niombe sana ahakikishe safari hii mkandarasi huyo anakuwa site kule Makambako katika vijiji vile nilivyovitaja ili shughuli hii ya umeme wananchi wangu waweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fidia. Waziri wa Viwanda yuko hapa na Waziri wa Fedha yuko hapa, Waziri Mkuu alipokuja Makambako aliwaona wale wananchi, yaani mimi Mbunge wao silali. Chonde chonde, niwaombe sana kuhakikisha kwamba tunawapa fidia wananchi hawa kwasababu wameteseka zaidi ya miaka 18. Nikuombe sana, fedha hizi kwa Serikali ni hela ndogo, ili tuhakikishe sasa; kwa sababu na kwenye Bajeti ya Mwaka 2016/2017 walishawekwa; nimwombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Mpango tuhakikishe kwamba fedha hizi zinatolewa ili
wananchi wangu wa Makambako waweze kupata kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliwaahidi kwamba jamani suala la fidia tutakwenda kulimaliza. Nimwombe sana na mimi namwamini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, michezo. Ndugu yangu Mheshimiwa Mwakyembe uko hapa, Rais alituahidi kutuboreshea uwanja wetu wa michezo, nimwombe katika Mpango wake wa Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ahakikishe anaweka bajeti kwa ajili ya kuanza kutengeneza uwanja wetu wa michezo pale Makambako.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu. Niipongeze sana Serikali, tangu ilipokuwa inatoa fedha kwa ajili ya elimu bure watoto wameweza kuongezeka na kadhalika, lazima tuipongeze Serikali kwa kazi nzuri. Tumwombe Waziri mwenye dhamana kuhakikisha mnapeleka vifaa vya maabara ili watoto wetu waweze kupata elimu yenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la fedha; tuhakikishe zinakwenda kwa wakati katika halmashauri zetu ili na sisi kama Madiwani tukiwa huko tuweze kusimamia zifanye shughuli za maendeleo kama ambavyo zimepangwa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini liko jambo hapa lazima niliseme, nisipolisema hapa nitasema wapi. Wapo Wabunge wenzangu wamesema, hivi iko sheria gani inayosema wewe Mbunge kwa sababu una kinga ukiitukana Serikali usikamatwe, sheria ya wapi? Kama umeitukana Serikali ni lazima ukamatwe upelekwe kwenye vyombo husika ukahojiwe kwa nini umeitukana Serikali. Kwa hiyo tusiweke kama kinga kwa sababu tuna kinga basi tuitukane tu Serikali halafu tusikamatwe, mimi sikubaliani kabisa, lazima tukamatwe, chombo kinachohusika kitufikishe mahali panapohusika. Unajua wako watu walizoea Serikali iliyopita kazi yao ni kuitukana Serikali, lazima tukubaliane na mabadiliko! Wewe unaitukana Serikali wakuache tu, unapita unaitukana Serikali wakuache, haiwezekani! Haiwezekani! Serikali inafanya kazi nzuri, tunaona (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe wa kwanza kuchangia katika hotuba hii ya Viwanda na Biashara. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri wote na watendaji wa Wizara mbalimbali kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kutekeleza Ilani ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hapa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, ukurasa wa 24. Hivi Mkuu wa Nchi ndiye baba, Rais, amepita mahali wananchi wamelalamika akatoa jibu kwamba atawasaidia, sasa hapa wanasema kwa nini alitoa majibu ya papo kwa papo kule wapi na nini, walitaka afanye nini? Watu wamemlalamikia Mheshimiwa Rais, si lazima ndio awape majibu wanasubiri na kwenye Ilani ya CCM tulisema tutatekeleza tutatoa majibu ya kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo vile vile Bunge lako hili tumesema kwamba kuna baadhi ya mikataba hasa ya madini sio mizuri tulisema hapa, sasa imetekelezwa tena tunalalamika tunasema kwa nini michanga na kadhalika, aaa. Serikali imeunda Kamati ya kushughulikia, tuiache Serikali ifanye kazi yake. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie juu ya Wizara hii, juu ya fidia iliyoko katika Soko Kuu la Kimataifa katika Mji wetu wa Makambako. Kitabu cha bajeti, kilichopita cha 2016/2017, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wa Makambako na Mheshimiwa Rais alipopita pale aliwaambia fidia hii mtalipwa; na alipokuja Waziri Mkuu alisema majibu nitarudi nayo mimi ya kuwalipa fidia wananchi wa Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabisa Serikali ione maana kwenye kitabu hiki cha bajeti ambacho kiko hapa, cha 2017/2018 haipo tena, hazijawekwa. Kwa hiyo niiombe Serikali itekeleze na mwisho ni mwezi huu Juni, niiombe sana Serikali ihakikishe inalipa fidia za wananchi wa Makambako, vinginevyo mimi kama Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa leo nitashika shilingi kama nitakuwa sijapata majibu maana kwenye bajeti ya 2017/2018 hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali ihakikishe inalipa fidia ya wananchi katika maeneo ya Makambako. Wananchi hao wamekaa kwa muda mrefu, hawawezi kufanya kitu chochote wala kuendeleza wala kufanya kitu chochote katika maeneo yale na Serikali ilisema italipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri uko hapa na nilikutana na Waziri wa fedha akanihakikishia tutalipa fidia, nikuombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya viwanda uko hapa nimwombe ahakikishe wanasimamia kulipa fidia katika eneo hili la Makambako. Vile vile katika fidia, wako hawa watu wa ujenzi, kuna mradi unaojengwa pale, one stop center ambao unajengwa katika eneo letu la Makambako, vile vile nao wanahitaji kulipwa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kupitia hili nimwombe sana wahakikishe wanawasiliana pia katika Wizara hii nyingine ambayo kuna fidia mbili hapo, kuhakikisha tunalipa fidia ya Mji wetu wa Makambako ili wananchi wa mji ule waendelee sasa kuwekeza viwanda na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, limezungumzwa kwa uchungu sana suala Liganga na Mchuchuma. Suala hili limezungumzwa kwa miaka mingi, mpaka tunajiuliza kuna tatizo gani sisi watu wa Kusini kule? Kuna tatizo gani na ni uchumi mkubwa katika Mkoa wa Njombe na Kitaifa kwa ujumla, lakini mpaka sasa hatujaona hapa nini ambacho kinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, alipokuja Waziri Mkuu tumekwenda pale Liganga mwaka huu, wale wawekezaji wametenga hela za kulipa fidia, wale wawekezaji wako tayari na Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema Kamati maalum itaundwa ya kuona je, zile fedha zilizotengwa, bilioni kumi na tatu, zinaendana na fidia ile?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri, mpaka sasa wamefikia wapi juu ya kulipa fidia ya Liganga na Mchuchuma ili mwekezaji yule aweze kuendelea na shughuli ile kwa sababu fedha zipo? Ni uchumi mkubwa sisi tunaoutegemea sana katika Liganga na Mchuchuma na mwekezaji yule tunamkatisha tamaa maana sasa hatuelewi nini kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali ihakikishe kwamba inalipa fidia kwa sababu fedha zipo mwekezaji anazo yeye mwenyewe na kuhakikisha wawekezaji wale wanaanza na walikuwa tayari kuanza. Bajeti iliyopita mlituambia mwaka huu wa 2016/2017 mwekezaji ilitakiwa aanze, nini kimechelewesha? Tupate majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, leo katika Wizara hii kwa kweli inafanya kazi nzuri ya kuhakikisha viwanda vinajengwa katika nchi yetu na ndio uchumi. Tukiwekeza kwenye viwanda tutapata ajira na kadhalika. Nakubaliana kabisa Mheshimiwa Mwijage anafanya kazi nzuri pamoja na watendaji wake na Naibu Waziri, lakini nirudie tena, nasema kwa uchungu kabisa, wale watu wa Makambako hivi sasa wako njiani wanakuja, kwa hiyo jioni Mheshimiwa Mwijage anao na Mheshimiwa Waziri Mkuu jioni atatakiwa akutane nao, kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema majibu nitarudi nayo mimi, sasa wanakuja. Nimwombe jioni ahakikishe anakutana na hao watu wa kutoka Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linanipa tabu, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu nitakaposhika shilingi juu ya kulipa fidia ya watu hawa mniunge mkono, kabisa, yaani Mbunge mwenzenu napata tabu juu ya watu hawa kulipwa fidia. Kwa sababu kwenye bajeti humu ya mwaka huu hazimo sasa maana yake mpaka mwezi Juni hii zilitakiwa ziwe zimeshalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage sijui nisemeje, wale watu wananipa tabu kwa kweli. Yaani nakosa raha juu ya kulipa fidia hizi, niiombe sana Serikali yangu. Mheshimiwa Rais alishasema fidia ilipwe sasa nini? Yamechukuliwa makaratasi yote yanayotakiwa ya wale watu, wako 274 yako kwenu Hazina na Mheshimiwa Mwijage anayo.

T A A R I F A . . .

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, unajua tungekuwa tunaelewa kwamba Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani tunatekeleza Ilani ya CCM tusingesema hivyo. Wote hapa tunatekeleza Ilani ya CCM ndiyo tuliyopata ridhaa, ndiyo maana naiambia Serikali yangu ya CCM itekeleze Ilani ambayo tulishaiambia. Kwa hiyo wote humu tunatekeleza Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, nadhani ameelewa humu ndani wote tunatekeleza Ilani ya CCM, ndiyo inayosimamiwa na ndiyo maana tunaiambia Serikali sasa yale mambo ambayo iliahidi iweze kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimalizie tu kwa kusema Mheshimiwa Mwijage na watendaji wake, wamenielewa nilichokisema, niombe sana kuhakikisha mpaka Juni, angalau wale watu tuwalipe fidia zao kama ambavyo tulikuwa tumeahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya nikushukuru sana, niishukuru Serikali, nimshukuru Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza naunga mkono ushauri wa Kamati ya Kilimo na Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, pamoja na Mawaziri, Waziri wa Maji, Naibu Waziri pamoja na wataalam wa Wizara hii ya Maji pamoja na Mawaziri wote wa Wizara zote kwa kazi nzuri wanazozifanya za kutekeleza Ilani ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kama mchumi. Imezungumziwa hapa kwamba fedha zilizotengwa kutoka mwaka jana, shilingi bilioni 900 ya 2016/2017 na sasa zimetengwa fedha pungufu utofauti na nani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naipongeza sana Wizara kupitia wataalam, wametenga kitu ambacho ndio uhalisia ambao fedha zitakwenda kwenye miradi. Kwa sababu fedha zilizotengwa mwaka jana hatukuzifikia na ndiyo maana wameonesha hapa tumefikia asilimia 19. Kwa hiyo, nawapongeza sana wataalam wa Wizara hii kwa maana wametenga sasa fedha ambazo zinakwenda kutekeleza uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wenzangu ambao wamesema iongezwe tozo ya shilingi 50. Naungana nao kabisa kwamba angalau itaongeza fedha katika huu Mfuko wa Maji. Kamati ya Bajeti watakwenda kukaa kuona namna ambavyo hii tozo yashilingi 50; nadhani tutakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate maelezo mazuri Mheshimiwa Waziri atakaposimama, katika miradi ile iliyopata fedha kutoka Serikali ya India ambapo kuna miradi 17 katika Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo na Makambako; watueleze kwa sababu tayari hapa baadhi ya Wabunge tumekuwa na wasiwasi kwamba fedha hizi ambazo zimekuwa zikitoka nje tumekuwa hatuzipati. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama atueleze kwa kina uhakika wa kupata fedha hizi ili wananchi wangu wa Makambako wajue fedha hizi zitakwenda kutekeleza mradi ambao Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba shughuli ya maji Makambako itatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna Mradi wa Bwawani wa Bwawa la Makambako ambao ni tofauti na mradi huu mkubwa. Mradi huu ulishatangazwa na Mamlaka ya Maji Iringa (IRUWASA) wanaosimamia. Na ilivyotangazwa suala hili liko Wizarani. Nataka nipate majibu nini sasa kinaendelea ili wananchi wa Makambako wajue mradi huu sasa umefikia hatua gani kwa sababu umetangazwa na una muda mrefu tangu watangaze, zaidi ya miezi miwili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, niwaombe Wizara, fedha kwa mfano zilizotengwa mwaka jana mpaka sasa mtusaidie wenzetu ma-engineer walioko huko, wataalam wa maji, mpaka sasa kuna baadhi ya miradi haijatangazwa. Sijajua kuna kigugumizi gani? Mtusaidie Wizara wanaohusiana na mambo ya Mkoa kule na kadhalika ambapo fedha hizi zilizotengwa katika eneo langu zingeweza kusaidia kupata maji katika vijiji vifuatavyo; vijiji vya Mbugani, Mawande, Mtulingala, Mahongole, Usetule na Ibatu wangepata maji. Lakini vilevile Mheshimiwa Waziri nisaidie kuna mradi mkubwa ule wa Tove ambao unahudumia vijiji kadhaa, vimeishia pale Ilunda. Ilunda pale kuja kwenye kijiji cha Ikelu ni kilometa mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi unasimamiwa na nani? Nani ambaye anazuwia wananchi pale Ikelu wasipate maji? Naomba utakaposimama hapa Waziri uniambie kwa sababu maji pale yako mengi na kadhalika, hawapati maji pale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niwe mtu wa kwanza kuanza kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanazozifanya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la elimu. Naishukuru tena Serikali kwa namna ambavyo imeanzisha mpango wa elimu bure, hivi sasa wanafunzi wamekuwa ni wengi sana katika mashule yetu. Kuna shule kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Makambako; Shule ya Ikwete, Shule ya Mashujaa na Shule za Juhudi. Shule hizi ni za siku nyingi, zimechakaa sana majengo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa namna ya kipekee kabisa ikishirikiana na wananchi nami Mbunge wao pamoja na Waheshimiwa Madiwani, tuone namna gani tunajiimarisha kuweza kujenga shule hizi ili zifanane na shule nyingine ambazo zipo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la pili la afya. Naipongeza sana Serikali kwa dhati kabisa kwa kazi nzuri inayofanya katika maeneo yetu kwa kutenga fedha nyingi kupeleka katika Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali. Kazi hiyo ni nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, katika Halmashauri ya Mji wangu wa Makambako tuna Kituo cha Afya kimoja, kinachoitwa Lyamkena. Tunaomba na sisi pia tupewe fedha kama ambavyo zimepewa Halmashauri nyingine ili nasi Kituo cha Afya hiki kiweze kufanya kazi za upasuaji na kama ambavyo vituo vingine vinafanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha ambazo wamenipa kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Mji wa Makambako. Naishukuru sana. Pia katika Hospitali ya Mji wa Makambako niiombe Wizara au Serikali, Kituo cha Afya kilipandishwa hadhi tangu mwaka 2013 na kuwa hospitali, lakini mgao wa dawa bado tunapata kama Kituo cha Afya wakati ni hospitali. Naiomba sana Serikali itupe mgao wa dawa kama hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni maji. Naipongeza Serikali kwa dhati kwa namna ambavyo imenipa fedha za miradi katika Kijiji cha Ibatu, Usetule, Mtulingala, Mahongole na Mbugani - Nyamande, Kiumba na Ikelu. Hivi sasa shughuli za maji kule zinaendelea. Naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo inataka kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Serikali, kuna mradi mkubwa ule wa fedha za kutoka India ambazo zilitengwa kwenye bajeti. Mradi ule wa miradi 17, Tanzania Bara miradi 16 na Zanzibar mradi mmoja (1). Katika miradi hiyo na Makambako ipo na Njombe Mjini ipo na Wanging’ombe ipo. Naomba kujua, ni kitu gani kinakwamisha mradi huu usianzishwe? Kwa sababu tulipata taarifa wakati fulani, alikuja Waziri wa India pale Ikulu, alisaini mkataba huu. Tatizo ni nini? Kimekwamisha kitu gani mradi huu hauanzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ione namna ambavyo itaanzisha mradi huu wa fedha za kutoka India ili kutatua tatizo la Mji wa Makambako katika suala hili la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu ujenzi. Alipokuja Mgombea ambaye ni Rais sasa, katika Mji wa Makambako, alituahidi kutupa kilomita sita za lami katika Mji wa Makambako. Mpaka sasa hata kilomita moja haijaanza. Kila nikiongea na Mheshimiwa Waziri, amekuwa akiniambia kwamba safari hii ilitengwa kilomita mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali angalau wangeanza kwa kilomita mbili hizi, angalau katika Mji wetu wa Makambako, ungekuwa ni mji unaopendeza kupitia barabara zake za lami. Siyo hivyo tu, naiomba pia TARURA, katika Mji wa Makambako kuna barabara ya kutoka pale Makambako kwenda Maguvani. Maguvani ni eneo la sekondari, pana korongo kubwa katikati. Naiomba Serikali itupe fedha za dharura kwa sababu hivi sasa wanafunzi wanaotoka ng’ambo kwenda katika shule hii ya Sekondari ya Maguvani wanazunguka Mjini Makambako ambako ni kilomita 10 wakati pale ni kilomita moja na nusu tu. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ione namna ya kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TARURA vile vile, tuna stendi ya Mji wa Makambako. Stendi ile ndiyo stendi kubwa lakini maji yote yanapotiririka yanakwenda kwenye majumba ya watu na nyumba kadhaa zimeanguka. Naiomba Serikali ituwekee makalavati ambayo yatanusuru nyumba hizi za wananchi katika stendi kuu ya Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alipokuja Rais katika Mji wa Makambako alituahidi kutujengea uwanja wa mpira. Tumeshaandaa uwanja na mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Naiomba sana Serikali kuona namna ya kutimiza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais kwa wananchi. Kila wakati tumekuwa tukiwaambia kwamba muda bado, tunaiomba sasa Serikali ichukue jukumu la kuhakikisha uwanja huu unajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwenye suala la umeme kwa nchi nzima na hususan katika Halmashauri yangu. Vijiji vingi sasa Mkandarasi yuko site anaendelea kuweka nguzo. Naipongeza sana Serikali kuona sasa katika vijiji vyote vya Halmashauri ya Mji wa Makambako vitapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, katika Kijiji cha Kifumbe kwenda Kijiji cha Mtanga ni kilomita tano mpaka sita. Shughuli hii Mkandarasi anayoendelea nayo, kijiji kitakachobaki katika ukanda huo ni hicho peke yake. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, ione namna ya kuona kijiji hicho nacho kinaunganishwa katika awamu hii inayoendelea hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ione namna ya kuanzisha mashamba kwa ajili ya mbegu mbalimbali za kilimo hasa mahindi katika ukanda wetu. Tatizo la mbegu limekuwa ni kubwa sana. Utaona wakati fulani baadhi ya watu wamekuwa wakichakachua mbegu, ni kwa sababu mbegu hizi ni chache. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ione namna ya kuanzisha mashamba kwa ajili ya mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Mawakala waliosambaza pembejeo. Hivi sasa ni zaidi ya miaka mitatu, hawajalipwa. Naiomba Serikali kama kuna baadhi ambao walifanya kazi nzuri katika kufuatilia na katika kuhakiki, basi walipwe. Wale ambao walichakachua wakafanya udanganyifu waambiwe kwamba ninyi hamlipwi kwa sababu mmefanya udanganyifu, lakini wale waliofanya vizuri walipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu fidia kwa soko la Kimataifa, Makambako. Wale watu sasa imekuwa ni tatizo kubwa. Naiomba Serikali, wakati fulani wameandamana, wamejaa kwenye mafuso kwenda Dar es Salaam na wakasema watashuka pale Ikulu, kama kuuawa wauawe. Nilimwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nilimwambia, nikawasihi. Naiomba sana Serikali, chonde chonde tuone namna ya kuwalipa fidia hawa watu. Zaidi ya miaka 21 sasa hawajalipwa fidia, kwa hiyo, imekuwa ni tatizo kubwa sana. Naomba sana walipwe fidia watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wakati nachangia suala la Mambo ya Ndani, naomba niseme kama ifuatavyo: Makambako ndiyo center. Unapozungumzia kwenda Mbeya, Makambako ndiyo center; unapozungumzia kwenda Songea, Makambako ndiyo center; unapokwenda Iringa, Makambako ndiyo center. Ni center wakati fulani baadhi ya wahalifu ndiyo wanakimbilia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hata wale waliokuwa wanafanya uhalifu kule Kibiti walipatikana baadhi ya wawili, watatu pale Makambako. Nikaenda mimi pale Polisi wakaniambia Mheshimiwa Mbunge njoo uwaone watu hao. Walikimbia kumbe wakaenda Songea. Walipoona Songea msako mkali, wakakimbilia Makambako. Kwa hiyo, naomba sana, tuone katika magari yatakayokuja ambayo Mheshimiwa Waziri jana alisema, katika mgao tuone… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza niungane na wenzangu kuipongeza Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Mawaziri wote pamoja na Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Afya na watendaji wake wote, Makatibu Wakuu na kadhalika. Kazi ambayo inafanywa na Serikali hii hakuna mfano, ni kazi nzuri sana ukienda kwenye idara na wizara mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie hii moja tu ya afya. Katika halmashauri yangu ya Mji wa Makambako tumepewa fedha shilingi bilioni moja milioni mia tano kwa ajili ya kujenga hospitali yetu ya Mji wa Makambako. Tumepewa shilingi milioni mia saba kwa ajili ya kuboresha kituo chetu cha afya katika Kata ya Lyamkena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, naomba sana katika hospitali au kituo kilichopo Makambako pale; pale ni centre. Dawa tunazopata hazikidhi, tunahitaji tuongezewe dawa ili ziweze kuhudumia watu wetu; na ndiyo maana na mimi nimeunga mkono jitihada za Serikali zinazofanywa na nimejenga vyumba viwili vya Madaktari pale vitafunguliwa mwishoni mwa mwezi huu, vyumba viwili vya kutolea huduma vya Madaktari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanazungumza; Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi amewahi kusema kwamba Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa aliyofanya kwa miaka miwili katika sekta mbalimbali ni sawa na miaka 10, hakuna mfano. Sasa kwa kazi hizo ambazo anazifanya; ukienda kule China Rais wa China amepewa kuwa ni Rais wa maisha kutokana na kazi anazofanya, kwa nini Magufuli asiwe Rais wa maisha kutokana na kazi anazofanya? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka miwili tu kazi ambayo amezifanya ni nzuri na kubwa. Kwa kweli lazima tumuombee kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu hapa kazi yao ni kubeza. Nilikuwa namsikia mtu mmoja akisema hizi hela ambazo zimewekwa hapa kwenye bajeti kama hazitaenda hizo hela basi nipeni mimi. Wako watu hapa wanabeza, jamani hii ni bajeti, ni mwelekeo wa bajeti, lazima tuishukuru Serikali kwa kazi inazofanya. Mnasema kama hizi hela zimewekwa tu, kama haziwezi kwenda; amesema mwenzangu mmoja kule kwa hata unapoamka unasema Mungu wangu tunakuomba na kadhalika; lakini yako mambo unamshukuru na kumwomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu tamka unanijua? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kweli kwa kazi nzuri ambazo zinafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie, pamoja na dakika chache hizi niiombe sana Serikali; tumejenga zahanati 10, tumeshaezeka, tumepiga lipu, tuko hatua za mwisho. Tuiombe Serikali mtutengee fedha kwa ajili ya kumalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, mimi pamoja na Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Njombe, tunaipongeza Serikali kwa kutujengea Hospitali ya Mkoa wa Njombe. Jengo la OPD limeisha, ombi langu kuwa fedha zilizotengwa hapa tuone namna ya kumalizia hospitali ile ili ianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na Mungu akubariki sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anaozifanya pamoja na Mawaziri wote; Waziri Mkuu, Waziri mwenye dhamana na Naibu Mawaziri wa Wizara hii ambayo tunachangia pamoja na Makatibu wake na wote wanaomsaidia katika Wizara hii. Kazi zinazofanyika tunaziona, ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye Jimbo langu la Halmashauri ya Mji wa Makambako. Pale Makambako kuna eneo fulani panaitwa Idofi ambapo Wizara walikuwa wamesema tuandae kwa ajili ya kujenga One Stop Centre na eneo hili kazi iliyofanyika kuwaomba wananchi wale ni kazi kubwa, ngumu na ambayo mpaka sasa hatuelewi nini kinachoendelea na kwa sababu bado hawajalipwa fidia na kwenye kitabu nilikuwa naangalia sioni mahali ambapo panaonyesha utayari wa kujenga one stop center kwa ajili ya manufaa ya watu wa Makambako, ombi langu niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapo atueleze One Stop Center ipo au haipo. Na kwa sababu pana msongamano sana wa magari na nini pale, wenyewe mnaona mnapokwenda Songea, Mbeya, pana msongamano mkubwa sana wa jam ya magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; niishukuru tena Serikali kwa namna ambavyo imetenga bajeti kwa ajili ya kutengeneza kilometa sita za Mji wa Makambako ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi na sasa naziona hapa, nawapongeza sana na shughuli hiyo nimeiona pale sasa imeshaanza kwa mita 150, najua kwamba sasa wakati mkandarasi anaendelea na bajeti hii itakuwa imeshafika muda wake mtaendelea kuikamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara ambayo ni ya TANROADS, unapokwenda Songea road pana Kijiji kinaitwa Ilunda, kutoka Ilunda kwenda Igongolo pana kilometa tisa ambazo ni za TANROADS, ukiendelea mbele barabara hii mbele inaendelea inakwenda Ilengititu, inakwenda Kifumbe, Mahongole inakuja kutokea Makambako na utaona sasa barabara hii kwa kilometa tisa ambazo zimetengenezwa pale barabara mbele inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kwamba barabara hii sasa iingizwe kwa TANROADS ili kusudi kwa mzunguko huu pale ni kilometa 19, ili mzunguko wa barabara kwenda kutokea Makambako uweze kuwa mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima niipongeze tena Serikali kwa barabara ya kutoka Nyigu kwenda Igawa ambayo inapita pale kwangu Makambako, kazi inayofanyika ni nzuri sana. Ombi langu ni kwamba zile barabara za pembeni na zenyewe, naona wanaendelea, basi nina imani kwamba mtakamilisha vizuri kama ambavyo iko ile waliyokamilisha pale Mafinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze tena barabara ya kutoka Makambako kwenda Songea ambayo nimeiona iko kwenye bajeti. Ombi langu kwa Wizara, barabara hii kwenda Songea ukitoka Makambako kwenda Njombe vichepu vya basi kipo kimoja tu kiko pale Mtwango, utaona hakuna mahali ambako mabasi yanaweza kusimama na nyumba zimejaa kutoka Makambako mpaka Njombe. Ombi, muone namna ya kupanua mabega ili kuwe na vituo vya basi kwa ajili ya barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mawasiliano, katika mawasiliano kutoka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja tu, kuna jambo muhimu. Nije kwenye suala ambalo Rais analifanya, Mheshimiwa Rais wetu amekaa hapa ndani kwa miaka 20 akisikiliza hoja mbalimbali ambazo zilikuwa zinasemwa pande zote mbili. Hoja hizo sasa ndiyo zinatekelezwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuwapa fidia wananchi wangu wa Jimbo la Makambako. Nawashukuru sana, kwa dhati kabisa kwa sakafu ya moyo wangu, nawashukuru sana, wamefanya kazi nzuri. Kwa sababu fedha hizi wamezidai kwa muda mrefu, lakini kupitia ahadi ya Mheshimiwa Rais imetekelezwa. Narudia tena kuwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaposhukuru, kuna ombi tena kuhusu fidia nyingine. Pale Makambako kupitia Wizara ya Ujenzi, wana eneo ambalo waliomba, tuwaombe wananchi kwa ajili ya kujenga One Stop Centre katika Kijiji cha Idofili, kilometa tano tu kuingia Mjini Makambako ukitokea barabara ya Iringa. Katika eneo hilo, vile vile kunatakiwa kulipwa fidia ili waanze kujenga One Stop Centre. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika hitimisho lake, basi aseme neno ili roho za wananchi wangu wa Jimbo la Makambako waweze kupona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tuna Liganga na Mchuchuma. Imezungumzwa kwa muda mrefu sana kuhusu uchumi wa Liganga na Mchuchuma. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Fedha, atuambie ni nini kinachokwamisha Liganga na Mchuchuma isitekelezwe au isianze? Kwa hiyo kwenye hitimisho pia nitaomba nipate majibu, tatizo ni kitu gani ambacho kinafanya isianze? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tumejenga zahanati nyingi sana katika nchi yetu ambayo magofu haya ni mengi ikiwepo Jimbo la Makambako. Makambako tuna zahanati ya vijiji zaidi ya 13 ambazo wananchi, Waheshimiwa Madiwani, Serikali, Mfuko wa Jimbo pamoja na mimi Mbunge wao tumejenga zahanati hizi. Ombi langu kwa Wizara ya Fedha, tuone sasa ni namna gani kwa nchi nzima na kupitia hata Halmashauri yangu ya Makambako tuzimalize zahanati hizi ili zianze kufanya kazi kusogeza huduma kwa wananchi wetu na hasa akinamama na watoto.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine napenda sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha, nipate majibu hasa ya miradi ya maji 17 nchini ikiwepo na Makambako kwa fedha za kutoka Serikali ya India kwa mkopo nafuu. Maana mpaka sasa hatuelewi kazi hii inaanza lini. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri pia katika miradi hii 17, mmojawapo upo Njombe, Makambako, Wanging’ombe na mahali pengine Zanzibar kule kuna mradi mmoja nadhani. Basi ni vizuri Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini miradi hii itaanza ili wananchi waweze kupata huduma hii ya maji kama ilivyokusudiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, katika Wizara mbalimbali ambazo tumekuwa tukichangia hapa ndani, Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema, nami naomba niseme Mheshimiwa Waziri. Namwomba Waziri wa Fedha, fedha hizi za miradi mbalimbali basi ziende kwa wakati ili shughuli zilizopangwa kule kwenye Halmashauri yetu ziweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Waziri, kupanga ni kuchagua. Kuna watu walizungumzia habari ya kununua ndege, habari ya reli, habari ya huo umeme kwamba huo umeme wa kutoka Bonde la Rufiji hauna manufaa na reli haina manufaa. Niseme kwamba Bunge lililopita la mwaka 2010 - 2015, Waheshimiwa Wabunge walisema hapa, ni nchi ya ajabu hii kutokuwa na ndege zake yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Serikali imetii kupitia Mheshimiwa Rais wetu, maana alikuwepo Bungeni hapa wakati ule akiwa Waziri, leo ametii, amenunua ndege katika nchi yetu, tunasema kwa nini amenunua ndege, hazina manufaa. Tukiwa hapa Bunge la mwaka 2010/2015 tulizungumzia hapa, ni nchi gani haina reli? Reli hii ya kati ni reli ambayo imepitwa na wakati, tunataka standard gauge. Mheshimiwa Rais ametii, amekubali, sasa ametafuta fedha tunajenga reli ya standard gauge. Kupanga ni kuchagua ndugu zangu, ni lazima tusiwe vigeugeu, tuiunge mkono Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulizungumzia hapa kwamba wawekezaji wanashindwa kuja ni kwa sababu umeme hautoshi. Leo ufumbuzi umeme kutoka Bonde la Rufiji, tunasema ule mradi haufai. Sasa tunajikatisha tamaa wenyewe kwa wawekezaji wanaokuja kwamba kumbe umeme kule haupo. Tuunge mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano juu ya mipango mizuri ambayo ipo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mpango na Wizara yake na Watendaji wake, achape kazi asonge mbele. Mipango ni mizuri sana. Kwa hiyo, sisi tuko nyuma yako, tunamuunga mkono kupitia bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamesema hapa, Mheshimiwa Waziri amekuwa muwazi, ameeleza kila jambo; hili liko hapa, hili bado hivi, hili liko hivi. Tunamuunga mkono, achape kazi, asonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niungane na wenzangu kujadili Mpango huu wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii ya kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, pamoja na Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri ambayo leo tunaijadili hapa ya Dkt. Mpango, kwa kupitisha bajeti ile ambayo tulikuwa tunakaa hapa na ndio sasa tunayaona yaliyokuwa yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mpango tunakupongeza sana na timu yako na wataalam wako na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo ipo mbele yetu, kwa kweli lazima tuwe wakweli, nianze na Wizara ya Afya, Mheshimiwa Mpango imezungumzwa hapa kuna baadhi ya watu wanasema bajeti iliyoongezeka zaidi ya bilioni mia mbili na kitu bado hawaoni maana yake, mimi nimebaki nashangaa Waheshimiwa Wabunge. Hivi bajeti ile si baadhi ya vituo, zahanati na vituo vya afya ambavyo vimejengwa si lazima fedha ziongezeke? Kazi nzuri imefanywa sana na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ikiwepo kwenye jimbo langu vituo afya viwili vimeongezeka na hospitali ya Wilaya ya Halmshauri, lazima tuipongeze Serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanywa hivi sasa kituo cha afya kwenye jimbo langu mwezi wa pili kinafunguliwa kwa fedha ambazo Serikali ya Awamu ya Tano kama walivyosema wenzangu vituo zaidi ya 300 na kila Jimbo nadhani vituo hivyo vipo. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali hata mwenzangu jirani ananiambia hata Tarime vipo, eeh kwa hiyo lazima tuipongeze sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile tukija kwenye upande wa maji, mwenye macho haambiwi tizama maji katika nchi nzima asilimia kubwa imepungua hata kwenye jimbo langu tu suala la maji ipo miradi inaendelea pale iko miradi mingi katika jimbo langu, ni fedha tu kwa hiyo Mheshimiwa Mpango tunakupongeza. Ipo miradi ile 26 ya maji katika nchi, katika miradi 26 mradi mmoja upo kwenye jimbo langu katika mpango huu wa wewe Mheshimiwa Mpango. Sasa tunaipongeza sasa Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija miundo mbinu ya barabara za kuunganisha mikoa kwa mikoa, leo mtu anatoka kule Mbinga kwa Mheshimiwa Mapuda, anatoka Mbinga asubuhi ikifika usiku anakuwa Mwanza, barabara zimetengezwa ni fedha hizi za Awamu ya Tano. Kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija barabara pale kwangu pia kwenye jimbo langu barabara za lami zinatengenezwa, ukitoka pale iko barabara ambayo barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam - Zambia sasa hivi kwenye jimbo langu pale Makambako barabara na viunga vyake vinapendeza sana, kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia hapa reli wenzetu wa kanda ya ziwa wamekuwa wakipata taabu sana juu ya reli hii ya kati, Serikali imechukua jukumu ya kuishughulikia reli hii, watu wanasema aaa mpango sio reli; kupanga ni kuchangua. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Mpango kwa namna ambavyo umeelezea hapa kwamba reli hii lazima inakamilika songa mbele kama alivyosema mwenzangu Mheshimiwa Ndassa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukija upande wa ndege, nimewahi kusema hapa Bunge la mwaka 2013 hapa na baadhi watu walikuwa wanazungumizia hapa duniani kokote kule hamuwezi kuwa mkawa hamna ndege za nchini kwenu, Rais amechukua jukumu la kununua ndege katika nchi yetu, tunaipondeza sana kwa taarifa hii ambayo kuna ndege zingine zinakuja mwakani mwezi Novemba, tunakupongeza Dkt. Mpango na Serikali ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri ambapo ndege hizi zitapunguza kero mbalimbali ambazo watu walikuwa wanapata tabu kusafiri lakini zitaongeza utalii wa ndani, Mheshimiwa Mpango songa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofanya ziara kwenye Jimbo langu mikutano 65 nimefanya kila siku nilifanya mikutano mitatu hakuna mwananchi hata mmoja aliporuhusiwa kuuliza maswali aliyezungumzia Katiba hayupo hata mmoja hayupo! Hata mmoja hayupo, watu walikuwa wanaauliza habari ya maji, barabara, pembejeo na kadhalika hakuna. Sasa leo tuanze kupoteza fedha kwa ajili ya Katiba, niombe sana Serikali na Rais na Waziri Mkuu upo hapa msijadili habari Katiba wananchi sio tatizo Katiba. Tatizo ni maendeleo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kazi iliyofanya Serikali ya Awamu ya Tano, tumuombe Mheshimiwa Spika na Wabunge wote baada ya kumaliza Bunge hili sijajua linaisha lini tufanye party ndogo ya kuipongea Serikali kwa kazi nzuri iliyofanywa, kwa hiyo, nikuombe Mwenyekiti jambo hili lipewe kipaumbele tufanye party ndogo ya kuipongeza Serikali kwa namna ambavyo inafanya kazi na leo narudia, kwa kazi iliyofanywa kwa miaka mitatu unadhani ni kazi ya miaka 20 huo ndio ukweli. (Makofi)

Sasa narudia kwa maneno haya niliwahi kusema Bungeni hapa, Rais wa China kwa kazi nzuri amekuwa akifanya na Marais wengine nchi mbalimbali wenzetu kule walisema awe Rais wa maisha. Narudia Rais huyu awe Rais wa maisha kutokana na kazi nzuri anayoifanya, lazima tuwe wa kweli, lazima tuwe wa kweli hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naunga mkono hoja, ya Mpango wa Dkt. Mpango kwa kazi nzuri, songa mbele na nakushuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nami niungane na wenzangu kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze na jambo ambalo limezungumzwa sana jana leo na tangu huko nyuma kuhusu udhaifu wa sisi Wabunge.

Mheshimiwa Spika, hawa wenzetu upande wa pili, katika bajeti ambazo tumekuwa tukipitisha hapa hawajawahi kusema ‘ndiyo’ hata mara moja. Kwa maana hiyo, wanataka kutuchelewesha kwa kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. Kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Waziri Mkuu na Mawaziri pamoja na wewe mwenyewe Spika ambaye unatusimamia kuisimamia Serikali, ni kazi nzuri sana. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo Waziri Mkuu amewakilisha hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, nianze kwa kuishukuru Serikali kwa namna ambavyo kwenye Jimbo langu la Makambaku, kwa namna ambavyo wananchi wangu wamekuwa wakilia juu ya kulipwa fidia kwa Soko la Kimataifa zaidi ya miaka 18; mwaka 2018 kupitia Ofisi hii inayosimamiwa na Mipango na Waziri, amelipa fidia zaidi ya shilingi bilioni tatu na kitu. Natoa shukrani sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba kuna baadhi ya watu kumi na kitu hawakuwepo wakati wa uhakiki, naomba sana watu hawa walipojitokeza watu wa uhakiki walikuwa wameondoka. Kwa hiyo, naomba waweze kuhakikiwa ili nao waingie kwenye kulipwa fidia.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili naiomba Serikali, kuna eneo pale pale Idofyu kuna mpango wa kujenga one stop center, sasa napo tunahitaji wananchi wale kulipwa fidia. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, kwenye mpango huu iweze kuwalipa fidia wananchi wangu wa Makambaku.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naishukuru Serikali kwa suala la umeme awamu ya tatu. Kwenye Jimbo langu natoa shukrani kubwa sana, najua na Watanzania wenzangu, Waheshimiwa Wabunge wenzangu ni hivyo hivyo. Napongeza sana kwa namna ambavyo wananchi, wameweza kupata umeme katika maeneo yote ya Jimbo langu la Makambaku.

Mheshimiwa Spika, ombi kwa Serikali, kuna kijiji kinaitwa Mtanga ambako umeme umefika kule Kifumbe, pale ni kilometa tano, kimebaki peke yake; naiomba Serikali iwapatie umeme ili nao waweze kufaidi kama ambavyo wenzao wanafaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile niishukuru pia Serikali kwa namna ambavyo imeweza kutupa fedha katika vijiji kadhaa kwa ajili ya suala la maji. Kwa kweli naishukuru sana. Ombi, tunataka kujua, fedha hizi za mkopo nafuu kutoka India ni lini mradi huu utaanza ili wananchi wa Makambaku waweze kufaidika na mradi huu mkubwa ambao utatatua changamoto kubwa kabisa ya maji iliyopo katika mji wetu wa Makambaku na Kijiji cha Ikelu?

Mheshimiwa Spika, mimi nimekuwa Diwani kwa miaka 10. Mpango wa afya kwa namna ambavyo Serikali imetoa fedha nyingi kwenye Vituo vya Afya, nami ni mmojawapo nimepata. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali kwa dhati kabisa. Vile vile tumepata fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Rufaa ya Halmashauri ya Mji wetu wa Makambaku, shilingi 1,500,000,000/= na hivi tunakwenda vizuri, naishukuru sana Serikali kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi, tuna Kituo cha Afya ambacho tulikuwa tunakiita Hospitali ya Mji wa Makambaku, tupate X-Ray kwa ajili ya huduma mbalimbali katika mji wetu wa Makambaku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa TARURA tunakwenda vizuri. Tunaiomba Serikali iongezee fedha upande wa TARURA ili barabara zinazounganisha baadhi ya kijiji na kijiji ziweze kupitika vizuri. Naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anayehusika; Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Rais mgombea wakati ule 2015 tuliahidiwa kilomita sita za lami katika Mji wa Makambaku. Mpaka sasa zimetengenezwa mita 150. Ombi langu ni kwamba barabara hii ya kilomita sita iweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilimo. Amezungumza Mheshimiwa Vuai Nahodha hapa; suala la kilimo ni asilimia kubwa sana ya wakulima wetu na mbolea ambazo wanazipata ziko bei juu, haziwiani na mauzo ya mazao yanayozalishwa. Nini kifanyike?

Tunaiomba Serikali ione namna ya kusimamia bei ya pembejeo ili ziweze kupungua ziendane na uzalishaji wa kilimo, lakini vilevile tunaiomba Serikali ilete wawekezaji kwa ajili ya kujenga Kiwanda cha Mbolea ili mbolea hii iweze kuwa bei chini na izalishwe nchini kwetu hapa hapa.

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, jambo lingine, tuna maboma ya Zahanati kwa nchi nzima. Kwangu peke yake kuna maboma ya zahanati zaidi ya 13 katika vijiji. Tunaiomba Serikali, katika mwaka huu wa fedha wa 2019/ 2020 angalau ione namna ya kutoa fedha nyingi ili maboma haya yaweze kupungua. Kila Jimbo angalau maboma matano au mangapi, tukifika 2020/2021 tunaweka tena bajeti maboma haya tutakuwa tumeyamaliza. Kwa hiyo, ombi langu ni kwamba Serikali iongeze fedha kwenye maboma haya.

Mheshimiwa Spika, nilisema hapa kipindi kilichopita na leo naomba nirudie; mwenzangu amesema kwamba kiongozi wetu, Rais wetu ana maono makubwa sana, wote hapa tunakubaliana. Mipango hii mizuri iliyowekwa, nilisema hapa kwamba huyu anatakiwa aombewe awe Rais wa kudumu kutokana na mipango aliyoifanya. Sasa kama siyo hivyo, basi ili mipango hii iweze kukamilika vizuri, tuombe angalau aongezewe kipindi kimoja mpaka 2030 ili mipango yake aliyoipanga iweze kukamilika vizuri. Kama ni hivyo, mimi na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, 2021 tutatembea nchi nzima, mimi nitakuwa wa kwanza kuwaambia Watanzania tumwombee aongezewe kipindi kingine ili akamilishe mipango na ndoto zake nzuri za maendeleo kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe ni shahidi, hata kwenye Jimbo lako unaona namna ambavyo shughuli mbalimbali zinavyofanyika ikiwepo barabara, Vituo vya Afya, na kadhalika. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali na hasa Waheshimiwa Wabunge, tutakapofika 2021 tuanze kutembea kuwaambia Watanzania, kwamba tumwongezee kipindi kingine ili ndoto zake ziweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu hawa ambao sasa wametoka humu ndani, watakuja tena hapa, watapinga hii bajeti ambayo tunaijadili hapa, lakini kwenye Majimbo yao wanahitaji huduma mbalimbali. Kwa sababu Rais wetu alisema maendeleo hayana chama, basi wananchi wapelekewe maendeleo, lakini isingekuwa hivyo, hawa walitakiwa walambwe na viboko kabisa. Kwa sababu wamekuja hapa kuwakilisha kwenye Majimbo yao… (Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Sanga.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweza kuchangia. Kwanza naunga mkono hoja kwa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ikisimamiwa na Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wanafanya kazi nzuri sana ya kutulinda sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana nilikuwa nasikiliza wachangiaji wenzangu hasa upande fulani, hebu fikiria Jeshi la Polisi na Mahakama visiwepo angalau kwa siku moja nini kitatokea? Ni lazima tumpongeze Waziri kwa kazi nzuri ambayo anafanya kupitia Jeshi la Polisi la kutulinda sisi na mali zetu na nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Njombe tulipata tatizo la mauaji ya watoto. Jeshi la Polisi lilifanya kazi kubwa ya kuwakamata wahusika, hivi sasa wanajibu tuhuma walizozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nizungumzie kwenye Jimbo la Makambaku, mwaka 2016/2017 kulikuwa na mauaji vijana wengi walikuwa wananyang’anywa bodaboda zao na wanauwawa. Jeshi la Polisi limeweza kuwakamata wote waliokuwa wanafanya vitendo hivyo. Nampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama - Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya - Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama, RPC na OCD na wapelelezi wake wa Jimbo la Kiwilaya la Kipolisi pale Makambaku. Wamefanya kazi nzuri sana, walikamata mpaka magaidi pale Makambaku, wale ambao walikuwa wanafanya mauaji kule Kibiti wamekamatwa pale na Jeshi hili hili la Polisi. Kwa hiyo, ni lazima tulipongeze sana kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili niwapongeze kwa kujenga nyumba za askari wetu kwa nchi nzima na hususan kwenye Mji wetu wa Makambaku. Tangu tupate uhuru hatujawahi kupata nyumba za Jeshi la Polisi, safari hii tumejengewa nyumba na wanaendelea kujenga nyumba nzuri za kukaa Askari wetu. Hata mimi Mbunge wao nimeweza kuchangia kwa asilimia kubwa kufanikisha nyumba zile ambazo Serikali ya Magufuli imetupa fedha. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Makambaku ndiyo njia panda ya kwenda Songea, Mbeya, Iringa, tunaomba utupe gari ili Askari hawa waweze kufanikisha shughuli zao za kidoria kwenye Mji wetu wa Makambaku. Tunaomba sana tupate gari ambalo litasaidia kufanikisha shughuli za kiusalama katika Mji wetu wa Makambaku.

Mheshimiwa Spika, vilevile gereza liko Wilayani Njombe, kupitia Wizara hii ya Mambo ya Ndani tunaomba waone umuhimu wa kujenga gereza katika Halmashauri yetu ya Mji wa Makambaku. Sisi wa Makambaku tutawatafutia eneo la kujenga gereza kwa ajili ya wahalifu ambapo kwenda Njombe ni mbali. Kwa hiyo, eneo lipo, nikuombe sana Waziri mwenye dhamana uone namna ya kutenga fedha kwa kipindi kinachokuja ili kujenga gereza katika Mji wetu wa Makambaku.

Mheshimiwa Spika, nizungumze jambo la mwisho, pamoja na kazi nzuri si vizuri kuwataja hawa Askari lakini kupitia Bunge lako naomba niwataje kwa sababu ya kazi nzuri wanayofanya, akiwepo OCD wa Mji wa Makambaku, Mkuu wa Upelelezi pamoja na timu yake ya askari kadhaa wanaofanya kazi nzuri ambapo waliweza kufanikisha kukamata silaha mbalimbali katika mji wetu. Naomba muone namna ya kuwapandisha madaraja hawa askari kwa namna ambavyo wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo askari kadhaa ambao labda wakati fulani wanaweza kuwa si wazuri …

SPIKA: Mheshimiwa Sanga, unawapongeza askari wako wa Makambaku lakini hapa Dodoma Wabunge wote mnakaa kwa amani kabisa, salama kabisa lakini RPC wa Dodoma hamumpongezi, hii inakuwaje? (Kicheko/Makofi)

Eendelea Mheshimiwa Sanga.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, ni kweli na ndiyo nilikuwa nakuja huko kutokana na kazi nzuri wanazozifanya na hata sisi Wabunge hapa, sisi kule Iringa kuna msemo wanasema ‘tukikala kilega’, tukilegea ni kwa sababu ya usalama wa hawa wanaotulinda. Kwa hiyo na Dodoma hapa tunalindwa, tunakaa majumbani salama huko tunakokaa hakuna bughudha mitaani, tunatembea mpaka usiku wa manane ni kwa sababu ya Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho baada ya maelezo haya, Mheshimiwa Waziri na timu yako kaza buti, endelea kuchapa kazi, askari mmoja anayeharibu si jeshi zima bovu. Kwa hiyo, hawa askari ambao wanataka kulichafua Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wako Siro muendelee kuwadhibiti ili warudi kwenye mstari vinginevyo kazi ni nzuri na mnadhibiti vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hili suala la mikutano ambalo wenzangu wamelizungumzia hapa, kwenye mikutano watu walikuwa wanafanya kazi ya kuja kutukana si kufanya shughuli za maendeleo. Sasa hivi mikutano tunafanya kila watu kwenye maeneo yao, shughuli zinakwenda vizuri, Waziri kaza kamba. Nikutakie kila la kheri katika shughuli hizi ambazo ziko mbele yetu, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli pamoja na wanaomsaidia kazi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu yuko hapa ambaye kila wakati tunamweleza matatizo ya maeneo yetu na Mawaziri wote wanaotusaidia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Ummy pamoja na Naibu Waziri wake na Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI kwa maboresho waliyofanya ndani ya sekta ya afya. Wanafanya kazi nzuri nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na Jimbo langu la Makambako, nilipewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Lyamkena, shughuli ya ujenzi imeshakamilika tangu Desemba, 2018. Tunaomba sasa tupatiwe vifaa tiba na waganga ili kituo kile kiweze kuanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, tunaomba kituo mama ambacho kilikuwa kama ni hospitali ya mji wa Makambako ambacho ni Kituo cha Afya cha Makambako ambacho kinafanya kazi nzuri lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa X-ray na Utra Sound. Mheshimiwa Rais alivyokuja tulimueleza matatizo yetu na nashukuru aliwaagiza watendaji ikiwemo Wizara ya Afya na TAMISEMI na bahati nzuri nilipokutana na Waziri wa Afya ambaye ni Mheshimiwa Ummy Mwalimu nilikueleza juu ya jambo hili na uliniahidi kwamba utanipa X-ray. Nakushukuru kwa dhati kabisa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Makambako. Vilevile niombe sasa atakapotupa X-ray usisahau muwasiliane na wenzako wa TAMISEMI angalau tupate Utra Sound ili vifaa tiba hivi viweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaiomba Serikali angalau tupate fedha za kujenga wodi ya akina baba. Mlitupa fedha za kujengea wodi ya akina mama na watoto imeshakamilika na inafanya kazi katika Kituo hiki cha Afya Makambako bado wodi ya akina baba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tupate wodi ya akina baba kwa sababu jengo lililopo ambalo lilijengwa kwa ajili ya kuweka vifaa tiba vya X-ray na Utra Sound ndiyo vyumba kadhaa vimegawiwa vinafanya kazi kama wodi. Kwa hiyo, tunaomba tupate fedha kwa ajili ya kujenga wodi ya akina baba.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa kutupa fedha za kujenga hospitali ya halmashauri yetu shilingi bilioni moja na milioni mia tano. Kwa dhati nakushukuru sana kwamba sasa tunakwenda kupata ukombozi wa tiba kwa wananchi wetu wa Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna zahanati nyingi ambazo tumezijenga katika halmashauri yetu. Halmashauri yetu kwa kushirikiana na wananchi, mimi Mbunge, Waheshimiwa Madiwani na wadau wengine zimejengwa zahanati zaidi ya 13. Tulitegemea katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo angalau tungepata fedha kiasi ili zahanati kadha kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 ziweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefikia mahali pazuri, zimeshapigwa lipu na kadhalika. Zimeshakamilika vimebaki vitu vidogo tu. Tumeshaanza kujenga nyumba za waganga katika zahanati hizo. Naomba Serikali ione umuhimu wa kutupatia fedha mwaka huu wa 2019/2020 ili baadhi ya zahanati hizi ziweze kukamilika. Hata hivyo, naishukuru Serikali kwa kuongeza fedha kwa ajili ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nimwombe Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Kituo cha Afya mama cha Makambako kipo katika center kubwa ya Makambako, kwenda Njombe, Mbeya, Iringa na sehemu nyingine, mtuongezee dawa kwa sababu tunapata kwa kiwango kidogo sana wakati kituo hiki kilikuwa kama hospitali kabla ya kutupa fedha za kujenga hospitali. Nikuombe sana uone namna ya kutuongezea dawa ili kukidhi kuwahudumia wananchi wa Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza nianze sana kwa kuishukuru serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri inayofanya juu ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimshukuru Waziri Mpango na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wizara kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Nichukulie tu kwa mfano; kazi ambayo Mpango unafanya nichukulie tu kwenye Jimbo moja tu la Makambako acha nchi nzima ambako kazi inafanyika kubwa; mmeweza kutupa fedha nyingi ambazo hivi sasa wakandarasi wako site wanafanya shughuli za kusogeza huduma ya maji kwa Wananchi Ikelu, Ibatu, Nyamande, Mtulingala shughuli hizo zinaendelea vizuri, nakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mmetupa fedha ambazo tunajenga hospitali pale ya Halmashauri ya Mji wa Makambako. Mmetupa fedha, shilingi bilioni 1,500, juzi mmetuongezea tena shilingi milioni 500. Kwa hiyo, hospitali ile inakwenda vizuri. Pia mmetupa fedha tumejenga Kituo cha Afya pale Lyamkena. Kwa hiyo, napongeza sana na kazi mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyika katika Halmashauri yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukienda kwenye suala hili la uchaguzi, kwanini watu wamejitoa, wanasema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa amezungumzia kwamba watu wasijitokeze kwenye ofisi. Siyo kweli. Nizungumzie tu kwenye Jimbo langu; kuna Kata 12. Kata saba hakuna mtu aliyejitokeza hata mmoja. Kwa hiyo, hata kabla hawajasema hili, tulishinda tayari Kata saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa wameona mwelekeo wa nchi nzima. Hilo ni Jimbo moja. Muelekeo wa nchi nzima, wameshaona tayari ushindi haupo. Kwa hiyo, wakaona ni vizuri watangaze kwamba wanajitoa, hakuna jambo kama hiyo.

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ehe, Mheshimiwa Sanga, hebu subiri.

T A A R I F A

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nataka kumpatia taarifa mzungumzaji kwamba kwenye Kata zake 12 hawakujitokeza wagombea. Siyo kweli. Katika Kata zote walijitokeza Wagombea wa Chama cha CHADEMA. (Makofi)


MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Sanga, unaikubali Taarifa au unaikataa?

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua huyu ni dada yangu sasa…

MWENYEKITI: Unaikubali au unaikataa?

MHE. DEO K. SANGA: Naikataa, siyo kweli. Siyo kweli! Nitampa tu mfano. Pale Ngamanga ambako palikuwa panaongozwa na CHADEMA hawakujitokeza kwa sababu tumejenga zahanati na wao wamekiri na Mwenyekiti yule ameacha. Kwa hiyo, napongeza sana kwa kazi ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ndiyo maana nilisema wakati ule, kwa nini Rais huyu asiwe wa maisha? Narudia tena, sasa ili mipango ikamilike kwa shughuli ambazo zimeanza za reli, ndege na kadhalika, ni vizuri muda utakapofika 2025 aongezewe hata miaka mitano ili miradi iweze kukamilika vizuri.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Bungara.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Eeeh!

MWENYEKITI: Haya.

T A A R I F A

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa Taarifa kwamba naunga mkono kwamba Katiba ibadilishwe azidishiwe muda, pia na vyama vya upinzani navyo vifutwe…

MWENYEKITI: Mheshimiwa hebu kaa chini. Kaa chini! Mheshimiwa nitakutoa nje sasa hivi, kaa chini. Mheshimiwa Sanga, endelea.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyama hivyo vitajifuta vyenyewe kwa sababu hawaelewi wanakwenda mbele au wanarudi nyuma. Vitajifuta vyenyewe. (Makofi/Kigelegele/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa sababu sasa tumenunua ndege zaidi ya saba na tunataka angalau sasa viwanja vyote katika mikoa yetu viweze kuruhusu ndege kutua; kiwanja chetu cha Njombe ambacho hivi sasa mlituambia kwamba kiko kwenye mpango wa kutengeneza ili ndege zetu hizi ziweze kutua. Naomba tukamilishe kiwanja kile cha Njombe ili Wana-Njombe nao waweze kusafiri kwa ndege zao ambazo zimenunuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo liko kwenye mpango ni juu ya Liganga na Mchuchuma. Liganga na Mchuchuma ikianzishwa na ikakamilika, uchumi wa Mkoa wa Njombe na uchumi wa Taifa utaongezeka kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo, sisi tunaotoka Kusini tunategemea sana pembejeo aina ya mbolea ya DAPO na Urea, ndizo tunazozitumia sana katika mazao yetu; na mbolea hizi ziko katika bei ya juu. Pamoja na kwamba kuna bei elekezi, tunaomba tuwe na mpango shawishi kwa wawekezaji waweze kujenga viwanda vya mbolea katika nchi yetu, angalau vitapunguza bei za mbolea na kuwa chini hasa mbolea ya DAPO na Urea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia juu ya kukamilishwa kwa maboma, nami naunga mkono. Tuna maboma ambayo yamejengwa na wananchi, Waheshimiwa Madiwani na Waheshimiwa Wabunge, likiwepo Jimbo la Makambako. Tumejenga maboma mengi; tuone namna ya kutenga fedha kukamilisha maboma haya, mengine yameshaezekwa, yanasubiri tu kupigwa ripu na kukamilisha na kadhalika ili maboma haya yaweze kukamilika kwa muda muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna miradi mikubwa, mmojawapo ukiwa wa maji, ule wa mkopo nafuu wa fedha kutoka Serikali ya India ambao utakamilisha miji karibu 28. Katika miji hiyo 28 na Njombe, Wanging’ombe, pamoja na Makambako ipo; tunaomba miradi hii, wananchi wanaisubiri kwa hamu sana ili kuweza kutatua tatizo la maji katika Mji wetu wa Makambako na mahali pengine ambako miradi hii itapitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la ujumla ambalo nilitaka niseme, hili nalirudia tena; Mheshimiwa Dkt. Mpango, katika mipango ambayo umekuwa ukiipanga; ya miaka mitano na huu ambao tunaujadili hapa sasa, endelea, songa mbele. Kazi yako ni nzuri, unakwenda vizuri, Watanzania wanakutegemea. Wanategemea sana kwa mipango hii ambayo tunaijadili hapa. Mungu akubariki na akuongoze na amlinde Rais wetu ili kusudi tuweze kukamilisha miradi hii. Mawaziri wote ambao wanafanya kazi yako, wanafanya kazi nzuri na ndiyo maana shughuli zinakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kunipa nafasi name niwe miongoni mwa wachangiaji wa bajeti hii iliyoko mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru sana kwa dhati Serikali ya Awamu ya Tano kwa mwelekeo wa bajeti hii ambayo imegusa kila sekta, nampongeza sana Rais wetu. Vilevile nimpongeze kwa kumteua Dkt. Mpango na Naibu Waziri, lakini pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Pia niwapongeze watumishi wote Wizara ya Fedha kwa mwelekeo wa bajeti hii nzuri ambayo imegusa kila mahali, imegusa kila sekta, nampongeza sana Waziri kwa kazi nzuri ambazo mmekuwa mkizifanya hasa bajeti iliyoko mbele yetu. Hongera sana Mheshimiwa Mpango kwa kazi nzuri ambayo iko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nizungumzie hizi taulo za kike. Serikali iliondoa VAT kwenye bajeti iliyopita kwa ajili ya kuwasaidia mama zetu, dada zetu na watoto wetu kwa ajili ya taulo hizi za kike. Lakini baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwa sio waaminifu bei haikuweza kupungua. Sasa Serikali imeweka mkakati na mpango mzuri wa kuhakikisha viwanda vyetu vya ndani vinazalisha taulo hizi ili bei ziweze kupungua. Ombi langu kwa Serikali, tusimamie ili lisije likatokea tena kama ambavyo wafanyabiashara kadhaa hawakuweza kupunguza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la wafanyabiashara au wajasiriamali mbalimbali ambao Waziri wakati anawakilisha hapa alisema sasa Serikali haitafunga biashara, haitafunga maduka au biashara mbalimbali za wafanyabiashara hususan wilaya na mikoa kutumia makufuli haya ya TRA. Ombi langu makufuli haya ya TRA, sasa Serikali ihakikishe wilaya na mikoa yatupwe ili kuwapa imani wafanyabiashara, maana Waziri alisema hapa mwenye mamlaka wa kuagiza makufuli haya yafungwe ni Kamishna wa TRA. Sasa ili kuwapa imani wafanyabiashara basi wakufuli haya katika wilaya na mikoa yatupwe kabisa ili kusudi kuwapa imani wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la ukusanyaji kodi liko vizuri, lakini ukienda pale Kariakoo kuna maduka mengi sana. Serikali iangalie Kariakoo sasa imegeuza yale maduka kuna watu wanaweka bidhaa mbele ya milango ya wafanyabiashara, hawa machinga na ndiyo inasababisha sasa baadhi ya wafanyabiashara kufunga maduka nao waweke kama machinga, waweke mbele ya milango. Kwa hiyo, Serikali itakosa kodi kwa wafanyabiashara kwa sababu nao wanafunga sasa. Wanaweka mbele ya maduka. Serikali ifanye utafiti wa kutosha ili kuhakikisha hao wanaoweka mbele ya maduka watafutiwe eneo ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara vizuri na kulipa kodi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Serikali imeweka vizuri utaratibu wa magari haya yanayoagizwa kutoka nje. Ukiingia kwenye system unapata bei ili uweze kuagiza kutokana na kodi ambayo utailipa. Sasa kuna jambo ambalo mimi nashangaa tunaweka kwenye system. Mimi ni miongoni mwao, hivi karibuni mimi nimeagiza magari ambayo yameonesha magari haya kwa mwaka 2012 kodi yake ni hii. Wiki iliyopita magari yamefika, kodi ya gari la mwaka 2012, trekta unit IVECO lilikuwa shilingi 10,300,000 ukiacha kodi zingine, tayari limekwenda shilingi 13,000,000 kwa hiyo ongezeko la shilingi 3,000,000 tofauti na bei iliyoko kwenye system linaathiri sana wafanyabiashara. Ombi langu tuhakikishe bei tuliyoiweka kwenye system na ndiyo hiyo inakuja kulipiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho ni kuhusu Mkoa wa Njombe, tuna Liganga na Mchuchuma, ni uchumi mkubwa sana katika Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla. Tunashindwa kuelewa ni kwa nini haianzishwi, kama tunakuta mipango Serikali iliyoweka ni mizuri mingi, basi tuhakikishe angalau tuanze kwa kuchimba mkaa kwa sababu kuchimba mkaa kule Mchuchuma na Liganga kunahitaji vifaa viwili tu, caterpillar na dozer, tuanzishe kuchimba ili wananchi wa Mkoa wa Njombe na hususan Wilaya ya Ludewa wajue Serikali ina mpango wa kuhakikisha tunachimba mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho niiombe Serikali katika makusanyo sasa ambayo tunaendelea kukusanya katika bajeti hii tunapeleka kwenye halmashauri mapema ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa ambayo tumepitisha bajeti hapa ndani Bungeni. Kwa mfano kwenye Jimbo langu Serikali imetupa fedha, tumejenga Kituo cha Afya Lyamkena, niombe na kituo kile kimeisha tupatiwe fedha kwa ajili ya vifaa tiba ili Kituo cha Lyamkena kiweze kuwahudumia wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako. Ninaipongeza sana Serikali kwa mipango mizuri ambayo maji, afya na kadhaika, mmekuwa mkisaidia katika nchi hii na hususan Halmashauri yangu ya Mji wa Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana kupitia Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii ya Fedha. Hongera, chapa kazi na kaza mwendo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na Wabunge wenzangu kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayowafanyia Watanzania kwa miradi mbalimbali ambayo imefanywa katika nchi yetu. Kazi zilizofanywa na Serikali hususani katika nchi yetu ni nyingi na ndiyo maana baadhi ya Wabunge wamesema na mimi naungana nao Mheshimiwa Rais huyu kwa kazi alizozifanya ndani ya miaka minne na zaidi, nadhani kwa sababu tuna ugonjwa huu wa Corona, tuna tatizo pia ambalo limeingia katika nchi yetu hasa miundombinu kuharibiwa na mvua ambazo zimenyesha nyingi sana, imevuruga mipango ya Rais ambayo alikuwa ameipanga katika miaka mitano na katika miaka mitano tena iwe kumi, kwa sababu mipango itakuwa imeharibika kutokana na haya mawili niliyoyataja, nadhani Bunge linalokuja iletwe Katiba hapa aongezewe miaka mitano mingine mbele ili aweze kukamilisha ndoto za Watanzania ambazo amepanga ziweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija na ndugu yangu Mheshimiwa Jafo ambaye ndiye anasimamia Wizara hii, kwa kweli mdogo wangu Mheshimiwa Jafo amefanya kazi kubwa sana, pamoja na wanaokusaidia Naibu Mawaziri wawili, Katibu Mkuu na wataalam wote katika Wizara hii. Ukiangalia ukurasa wa 54 unasema tulikuwa na vituo 535 sasa tuna vituo 968 vikiwepo na vya Makambako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jafo amefanya kazi kubwa sana. Kwa sababu amewafanyia kazi Watanzania naye tunamwombea kwenye Jimbo lake kule asitokee mpinzani upite bila kupingwa pamoja na wanaokusaidia nao wapite bila kupingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wapo wasaidizi wa Rais akiwepo Waziri Mkuu, kazi kubwa anayowafanyia Watanzania kwa kuzunguka, jana tu tumemwona alikuwa Zanzibar, anawazungukia Watanzania kutekeleza shughuli ambazo Rais amezipanga. Naye Waziri Mkuu kule Ruangwa, mimi na Wabunge tunakuombea upite bila kupingwa. (Makofi/Vigelelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile na dada yangu Mheshimiwa Jenista kwa kazi anazozifanya namwombea kule Peramiho apite bila kupingwa ili aendelee kuwatumikia Watanzania. Pia Spika wetu Job Ndugai kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Bunge hili kuwatumikia Watanzania naye tunamuombea apite bila kupingwa. (Makofi/ Vigelegele)

MBUNGE FULANI: Naibu Spika kule Mbeya.

MHE. DEO K. SANGA: Lakini na wewe Naibu Spika mdogo wangu, Mheshimiwa Tulia tunakuombea kule Mbeya upite bila kupingwa ili uweze kuwatumikia Watanzania. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maombi haya, nirudi sasa kwenye Jimbo langu la Makambako.

MBUNGE FULANI: Na wewe upite bila kupingwa.

MHE. DEO K. SANGA: Watanzania wakiwepo wa Jimbo la Makambako nawapenda sana, wanajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye Jimbo la Makambako. Miradi iliyotekelezwa kwenye jimbo langu ni mingi sana. Ombi langu ni dogo tu kwa Watanzania hususani Jimbo la Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, tuna mradi mkubwa ule wa fedha za kutoka Serikali ya India kwa mkopo nafuu. Mradi ule tumewaambia wananchi mara nyingi sana na kwa muda mrefu kwamba mradi utatekelezwa. Kwa sababu Wizara inayohusika wako hapa, naomba waone namna ya mradi ule kuweza kuanza katika mji wetu wa Makambako. Tunashukuru kwamba kuna miradi ipo inayoendelea ikiwepo pale Mawande, Lingala, Nyamande na pale Ikeru. Miradi hii inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Vituo vya Afya, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, pale kituo chetu kipya cha Lyamkena kimeshafikia asilimia 99. Tunaomba vifaa tiba pamoja na wataalam ili kituo hiki kianze kufanya kazi iliyokusudiwa ikiwepo pia na hospitali ya Halmashauri yetu ambayo imejengwa pale Mlowa na imefikia asilimia karibu 100. Tunaomba kupata vifaa tiba ili ianze iweze kuhudumia Wanamakambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile upande wa Kituo cha Afya cha Makambako cha zamani, nimemwambia Mheshimiwa Jafo mara nyingi kwamba hatuna wodi ya wanaume; na wanaume wanaugua. Kwa hiyo, ombi langu tuone namna ya kupata fedha tuwapelekee tuweze kujengewa wodi ya wanaume.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija upande wa umeme wa REA, Waziri mwenye dhamana, haki ya Mungu nitoe neno la shukrani kabisa. Kwenye Halmashauri yangu kimebaki kijiji kimoja tu kupata umeme. Naomba kwa sababu nacho ni kimoja, kiweze kumalizwa. Nacho ni Mtanga. Vijiji vingine vyote tumeshapata umeme. Kwa hiyo, kilichobakia ni maeneo madogo madogo ya Vitongoji kuwapelekea. Kwa hiyo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yako kwa namna ambavyo mnatujali kupitia Rais wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni watu wa NIDA, Waziri mwenye dhamana yuko hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, basi baada ya maelezo haya, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nakushukuru sana, ahsante sana.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa wachangiaji. Katika kuchangia kwanza nianze kwa kuunga mkono hotuba zote mbili; wakati wa kufunga Bunge na wakati wa Ufunguzi wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Bunge linaahirishwa au likihitimishwa, ndiyo kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, jemadari na ndiyo iliyofanya Wabunge wengi turudi hapa ndani, kazi hii! (Makofi)

Katika ufunguzi, mwelekeo huu wa miaka mitano, naomba nichangie na nianze na elimu. Tunapozungumzia elimu bila malipo na ndiyo imefanya watoto wetu wengi wapatikane katika maeneo yetu, ambapo wazazi wao walikuwa hawawezi kuwapeleka shule. Elimu bila malipo kwenye sekondari tunasema, msingi na sekondari, ombi langu kwa bajeti inayokuja na Rais wetu mpendwa, isiwe elimu bila malipo kidato cha kwanza mpaka cha Nne. Inatupa taabu hata sisi Wabunge kule Majimboni wakati fulani kusema. Tunaomba iwe mpaka kidato cha sita yaani kuanzia kiadto cha kwanza mpaka cha sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunadhani hili linaweza kuwa ni zuri. Tunamwomba Waziri mwenye dhamana katika bajeti ambayo inakuja, hebu tujipange vizuri, tuishauri Serikali kupitia Rais wetu kwamba elimu bila malipo iendelee mpaka mpaka kidato cha Sita, yaani cha Kwanza mpaka cha Sita.Tutakuwa tumekwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia hapa juu ya mikopo, nilikuwa nafuatilia jana. Kwenye mikopo hii kuna baadhi ya watu ambao watoto wetu hawa wanafadhiliwa na taasisi mbalimbali na baadhi ya watu. Inapofika mahali yule mtu aidha ameshindwa kuendelea kumfadhili na kadhalika; unakuta mtoto amefaulu vizuri Kidato cha Sita na kuendelea anashindwa mkopo na baadaye anakuwa hana mahali pa kwenda kwa sababu wafadhili wake wameshindwa na kadhalika. Nami nina mifano hai mingi, watu mbalimbali na wananchi wanavyokuja kwangu, najua hii iko pia kwa Wabunge wenzangu.Ombi langu, jamani wapewe bila masharti, bila kujua amesoma wapi na kadhalika. Maadamu ana vigezo vya kupata mkopo, apewe bila masharti ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la umeme, ndugu zangu Waziri mhusika yuko hapa, Mheshimiwa Kalemani. Unajua penye kazi nzuri ambayo mtu amefanya lazima tumpongeze. Amefanya kazi nzuri sana. Ombi langu sasa kwenye jimbo langu, najua na kwa wenzangu, asubuhi tumetoka kuongea, Kijiji cha Mutanga kule, walianza kupeleka nguzo, lakini wamesimama. Ombi kwa Mheshimiwa Waziri, wananchi hawa wapewe umeme wa kule Mtanga na Ingangidung, utakuwa umetusaidia na baadhi ya maeneo, nitawasiliana na Waheshimiwa Madiwani, baadhi ya vitongoji ambavyo leo amezungumzia kwamba ni lazima na vyenyewe sasa tulete ili waweze kupata umeme. Kwa hiyo, nitawasiliana na Madiwani, mwishoni mwa wiki hii nitamkukabidhi maeneo ambayo bado hayajapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya, kazi iliyofanyika ni nzuri sana ya kujenga vituo, zahanati na kadhalika. Ombi langu, kwenye Jimbo langu la Makambako wananchi wanaonipenda sana, nami nawapenda sana kwa dhati kabisa kabisa; na Rais wao wanampenda sana; ombi langu tumekuwa tukizungumzia habari ya X-Ray na Ultrasound. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana yuko hapa, hivi kweli Mji wa Makambako ambako ndiyo corridor ya kwenda Songea, Mbeya na wapi, ndiyo Jiji kubwa, hivi hatuna X-Ray. Chumba cha X-Ray tulishakijenga, kipo tayari. Tunaomba katika bajeti tunayokwenda nayo tupate X-Ray, Mheshimiwa Waziri atakuwa ametutendea haki katika Mji wetu wa Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji; Mheshimiwa Aweso yuko hapa, ambaye ni Waziri wa Maji. Naomba ndugu yangu Waziri; Mawaziri wote wanafanya kazi nzuri, wanaendana na kasi ya mwenyewe, wote! Sasa Mji wa Makambako ndiyo mji mkubwa katika miji yote kwa ukanda. Ndiyo corridor pale jamani; kwenda wapi na wapi kama nilivyosema. Ule mradi mkubwa ambao tunapata mkopo nafuu kutoka Serikali ya India, ni vizuri sasa katika Miji 26 ile na Mji wa Makambako upo, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa amesimama hapa atuambie ni lini mradi huo wa maji Makambako utaanza ili nikawaambie wananchi wangu wa Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba leo asubuhi Mheshimiwa Waziri amenijibu kuhusu maji, sasa aseme hapa kwamba maji hayo ni ya mwakani au ni ya mwaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara, naishukuru Serikali kwa Mji wangu wa Makambako, tumepata fedha za lami kilometa 3.5 Mjini pale, tunaishukuru sana Serikali. Hata hivyo, wenzangu wameongelea chombo cha TARURA. Naomba kwenye bajeti hii tutakayoanza, naomba tuongezewe fedha ili barabara zetu ziweze kupitika msimu wote. Kwa hiyo, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu hapa kuna maboma mbalimbali ambayo yamejengwa; madarasa, zahanati na kadhalika. Ombi langu, Wizara hasa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, ahakikishe maboma haya ambayo wananchi wamejenga pamoja na Waheshimiwa Madiwani pamoja na Wabunge tuliomo humu ndani, yanaisha kwa kipindi hiki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, siyo kwa umuhimu…

NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wameongelea hapa juu ya Rais wetu kumwongezea aidha muda. Kuna watu wengine ni kama dhambi hivi kumwongezea. Ndugu zangu, mtu huyu amefanya kazi kubwa kwa miaka mitano iliyoisha na mipango ya miaka hii mitano, ombi langu hapa ndani, atake asitake tumwongezee muda ili aweze kufanya kazi na kukamilisha mipango yake vizuri katika nchi hii. Kabisa! Ili aweze kufanya kazi yake vizuri ili mipango aliyoipanga iweze kukamilika. Atake asitake, tumlazimishe! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, nilisema hapa kama mnakumbuka kipindi fulani kwamba China wamefanya hivyo na mahali pengine wamefanya hivyo, siyo dhambi kwa mtu anayefanya vizuri. Hata ninyi Wabunge mliorudi maana yake mlifanya vizuri, ndiyo maana watu walisema tena mrudi, kwa hiyo, siyo dhambi tena kumwongezea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na wenzangu kuipongeza Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuleta Miswada hii ya Dharura ambayo ndiyo tulikuwa tunaitaka sasa Serikali imetimiza, tunaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini unajua mtoto wa kambo hata ungemlisha, ukampa nyama za aina gani atalalamika kwamba hatunzwi. Kwa hiyo, hii sio kitu kigeni, ni kitu cha kawaida tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Miswada hii kwa kweli ni mizuri sana. Sheria hizi ambazo zitapitishwa Bungeni hapa, sheria zinatoa nafasi kurekebisha hata baada ya kuanza utekelezaji wa mikataba hii. Kwa hiyo, nadhani hili ni jambo jema sana ambalo tumelizungumza sana siku za nyuma. Bunge lililopita tumezungumza juu ya mikataba hii kwamba tunaibiwa, Rais amegundua ametuletea sasa tunataka nini, si ndiyo sasa tuipitishe hapa. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sheria inawapa wananchi kunufaika moja kwa moja na ajira na bima. Pia Halmashauri zetu zitazungumza na mwekezaji kuhusu mahitaji yao, sasa tunataka nini? Kwa kweli jambo hili ni jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile udhibiti wa maliasili inayopatikana, nia ya Rais wetu kufanya marekebisho kuja haraka inasaidia sana na ndiyo maana leo imeletwa hapa Bungeni. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, pia Miswada hii juzi na jana wadau mbalimbali tumekaa nao pale kwenye ukumbi wa Pius Msekwa. Idadi kubwa ya wadau wameunga mkono sana jitihada za Serikali. Sasa watu wanasema imeletwa kwa dharura lakini imeungwa mkono na wadau mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe tu, Miswada ya Habari imezungumzwa zaidi ya miaka 15 na ndiyo juzi juzi tumepitisha hapa, sasa tunataka na hii iwe hivyo? Mimi naunga mkono kabisa Muswada huu ambao umeletwa kwa sababu utaleta manufaa kwa wananchi na kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine hapa wanasema Serikali ya CCM 2019/2020 wataingia wengine thubutu, thubutu. Wananchi jambo hili wamelipokea kwa mikono miwili. Kila unapopita, kwanza wanaona tunachelwa. Wananchi wamelipokea jambo hili vizuri na sisi kama Wabunge tuungane ili jambo hili liweze kuanza kwa sababu liko vizuri. Kwanza tunategemea hata zile fedha za makinikia tutapata maji, barabara na kadhalika, kwa hiyo, tumuunge mkono Rais na Wizara kwa ujumla, tusiwakatishe tamaa, sisi tuwe nyuma yao kuhakikisha tunaunga mkono jitihada za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi hapa, unajua wakati fulani huwa nashindwa niseme nini maana Serikali ikileta jambo jema tunasema hapana, sasa tunataka Serikali ifanye nini?

Kuna usemi mmoja unasema shukrani ya nini, sitaki niseme huko, tuiunge mkono Serikali kwa jitihada inazozifanya ili kuhakikisha tunawaletea maendeleo Watanzania. Ili tuhakikishe reli inajengwa, bandari jana tumeona na kadhalika, tunataka tutoke hapo ili tupate uchumi wa kati na mkubwa kwa nchi yetu, kwa hiyo, ni lazima tuiunge mkono Serikali. Kwanza, tunampongeza sana Waziri, Mheshimiwa Profesa Kabudi kwa kuleta Muswada huu na sisi tupo nyuma yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza imezungumzwa katika sheria hii kwamba itafanya pesa zisipotee kiholela. Vilevile benki za hapa nchini zitatumika kulinda uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa asilimia 400.
Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na wenzangu kuipongeza Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuleta Miswada hii ya Dharura ambayo ndiyo tulikuwa tunaitaka sasa Serikali imetimiza, tunaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini unajua mtoto wa kambo hata ungemlisha, ukampa nyama za aina gani atalalamika kwamba hatunzwi. Kwa hiyo, hii sio kitu kigeni, ni kitu cha kawaida tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Miswada hii kwa kweli ni mizuri sana. Sheria hizi ambazo zitapitishwa Bungeni hapa, sheria zinatoa nafasi kurekebisha hata baada ya kuanza utekelezaji wa mikataba hii. Kwa hiyo, nadhani hili ni jambo jema sana ambalo tumelizungumza sana siku za nyuma. Bunge lililopita tumezungumza juu ya mikataba hii kwamba tunaibiwa, Rais amegundua ametuletea sasa tunataka nini, si ndiyo sasa tuipitishe hapa. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sheria inawapa wananchi kunufaika moja kwa moja na ajira na bima. Pia Halmashauri zetu zitazungumza na mwekezaji kuhusu mahitaji yao, sasa tunataka nini? Kwa kweli jambo hili ni jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile udhibiti wa maliasili inayopatikana, nia ya Rais wetu kufanya marekebisho kuja haraka inasaidia sana na ndiyo maana leo imeletwa hapa Bungeni. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, pia Miswada hii juzi na jana wadau mbalimbali tumekaa nao pale kwenye ukumbi wa Pius Msekwa. Idadi kubwa ya wadau wameunga mkono sana jitihada za Serikali. Sasa watu wanasema imeletwa kwa dharura lakini imeungwa mkono na wadau mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe tu, Miswada ya Habari imezungumzwa zaidi ya miaka 15 na ndiyo juzi juzi tumepitisha hapa, sasa tunataka na hii iwe hivyo? Mimi naunga mkono kabisa Muswada huu ambao umeletwa kwa sababu utaleta manufaa kwa wananchi na kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine hapa wanasema Serikali ya CCM 2019/2020 wataingia wengine thubutu, thubutu. Wananchi jambo hili wamelipokea kwa mikono miwili. Kila unapopita, kwanza wanaona tunachelwa. Wananchi wamelipokea jambo hili vizuri na sisi kama Wabunge tuungane ili jambo hili liweze kuanza kwa sababu liko vizuri. Kwanza tunategemea hata zile fedha za makinikia tutapata maji, barabara na kadhalika, kwa hiyo, tumuunge mkono Rais na Wizara kwa ujumla, tusiwakatishe tamaa, sisi tuwe nyuma yao kuhakikisha tunaunga mkono jitihada za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi hapa, unajua wakati fulani huwa nashindwa niseme nini maana Serikali ikileta jambo jema tunasema hapana, sasa tunataka Serikali ifanye nini?

Kuna usemi mmoja unasema shukrani ya nini, sitaki niseme huko, tuiunge mkono Serikali kwa jitihada inazozifanya ili kuhakikisha tunawaletea maendeleo Watanzania. Ili tuhakikishe reli inajengwa, bandari jana tumeona na kadhalika, tunataka tutoke hapo ili tupate uchumi wa kati na mkubwa kwa nchi yetu, kwa hiyo, ni lazima tuiunge mkono Serikali. Kwanza, tunampongeza sana Waziri, Mheshimiwa Profesa Kabudi kwa kuleta Muswada huu na sisi tupo nyuma yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza imezungumzwa katika sheria hii kwamba itafanya pesa zisipotee kiholela. Vilevile benki za hapa nchini zitatumika kulinda uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa asilimia 400.