Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mary Deo Muro (14 total)

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye majibu yake ya msingi amesema kwamba Mkoa wa Pwani ulikuwa na wananchi wachache, lakini kwa kuwa Mkoa wa Pwani sasa hivi una ongezeko kubwa la wananchi. Je, haoni kama ni wakati muafaka kwa Mkoa wa Pwani kuwa na Mamlaka yake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na majibu yote ya Mheshimiwa Waziri, haoni kwamba kunatakiwa kuwepo na mpango wa kati kabla ya mpango huu ambao anasema kuna upembuzi ili kuondoa maji machafu katika Mkoa wa Pwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nilisema kwamba wakati Mamlaka ya DAWASA inaanzishwa, Miji ya Bagamoyo na Kibaha haikuwa na watu wengi. Kwa sasa nakiri kabisa kwamba ni miji ambayo imekomaa ina watu wa kutosha.
Mheshimiwa Mbunge, kupitia Sera ya Maji na Sheria ya Maji Na.12 ya mwaka 2009 unaweza kumwomba Mheshimiwa Waziri mwenye mamlaka akaidhinisha uanzishwaji wa Mamlaka katika Mji wa Kibaha. Ijulikane kwamba au utambue kwamba Mamlaka zinazoanzishwa zinatakiwa kujitegemea. Kwa hali hiyo, italazimika ziwe na chanzo chake cha maji. Kwa hiyo, unapoleta hilo ombi ni vyema mkatafakari na kujiweka sawa.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu suala la huduma ya majitaka kwamba kuwe na mpango wa kati wakati tunaendelea kusanifu uondoaji wa majitaka kwa Miji ya Bagamoyo na Kibaha, mpango wa kati upo. Tunaweza tukajenga mfumo wa mtandao wa majitaka lakini mpango wa kati ni kujenga septic tanks kwa kila nyumba ambazo zinasaidia kuondoa majitaka kwa kipindi cha kati.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwenye majibu yake ya msingi amesema zimetumwa shilingi milioni 358; je, zimetumwa lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili uendelezaji unaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, shilingi milioni 358 zilitumwa miezi miwili iliyopita na tulipata fedha kutoka Serikali ya Japan bilioni 29.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba uendelezwaji unaanza lini. Katika hizo fedha sasa hivi kinachofanyika ni kuandaa mikataba, ni maeneo mengi ambayo yalikuwa bado mikataba haijaandaliwa. Ni kuandaa mikataba kwa sababu usanifu ulishafanyika ili kuweza kuingia sasa mikataba na wakandarasi na kazi hiyo iendelee kutekelezwa.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa matatizo yaliyoko sehemu nyingine ya Vyama vya Ushirika ni sawa na tatizo lililoko kwenye Mkoa wa Pwani kwa Coastal Region Cooperative Union - CORECU, majengo yake kutaka kuuzwa na kununuliwa na wajanja wachache. Je, Serikali ina kauli gani juu ya ku-rescue hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Chama Kikuu cha Ushirika cha Pwani - CORECU kimekuwa kikipita katika wakati mgumu pamoja na mambo mengine kwa sababu ya madeni makubwa ambayo yameendelea kutishia uhai wa chama hicho. Hivi tunapozungumza CRDB ambao wamekuwa wakikidai chama hicho fedha nyingi, tayari walishaenda mahakamani na taratibu zilianza za kutaka kuuza mali za CORECU. Ni suala ambalo limetokana na mchakato wa kimahakama lakini pamoja na hayo, Serikali na Wizara inaendelea kufanya majadiliano kuangalia namna gani ya kunusuru mali zile zisiuzwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kurejea kusema kwamba naomba Waheshimiwa Wabunge tutoe elimu kwa wanaushirika kwamba wao ndiyo hasa inatakiwa wawe watu wa kwanza kulinda mali za ushirika. Kwa sasabu wanapoingia kwenye mikataba ambayo inahatarisha mali zile, baadaye ni vigumu sana Serikali kusaidia kwa sababu inakuwa ni suala la kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali ilisaidia sana kujaribu kuondoa changamoto ya CORECU kwa sababu hata kwenye mkopo ambao wanadaiwa Serikali ilishasaidia kulipa baadhi ya fedha, nafikiri imelipwa zaidi ya shilingi bilioni moja. Hata hivyo, nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba jitihada zinaendelea kuangalia ni namna gani ya kunusuru mali za CORECU zisiuzwe.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Pwani, tangu alama ya X zilivyowekwa Serikali haijarudi kutoa mrejesho kwamba kitu gani kinaendelea na wananchi wale kujua tathmini hiyo watalipwa kiasi gani. Je, ni lini watarejesha mrejesho kwa wananchi ili waweze kujua malipo yao yatakuwa kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali iliweka alama za X mwaka 2015 na sasa hivi tunaelekea 2018. Wananchi wanauliza watalipwa kwa tathmini ile au uthamini utafanywa mwingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameuliza ni lini Serikali itapeleka mrejesho, naomba nimtaarifu muda si mrefu Serikali itapeleka mrejesho wa namna ambavyo malipo haya ya bilioni 21.6 kwa wakazi wa maeneo haya inakojengwa msongo huu wa kilovoti 400. Kwa kuwa mimi na yeye ni Wabunge tunaotoka Mkoa wa Pwani na niwataarifu pia Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Koka na Mheshimiwa Ridhiwani maana nao wamekuwa wakifuatilia, kwa hiyo muda si mrefu tutawapelekea mrejesho na taarifa wataipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza kwamba kwa kuwa tathmini ilifanyika mwaka 2015 na tunaelekea mwaka 2018, naomba tu nimtaarifu kwamba malipo ya fidia yatalipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa miradi yote iliyojengwa katika Wilaya ya Kibaha Mjini iko chini ya viwango na imetokana na kwamba Wilaya ya Kibaha haina Mhandisi wa Maji anayetumika pale ni Mhandishi wa Mazingira. Je, ni lini Kibaha italetewa mtaalamu wa maji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ametaja kwamba Pangani iko miongoni mwa kata zitakazopata maji, lakini Pangani ina mradi ambao umegharimu shilingi milioni 531 ambao umejengwa chini ya kiwango kwa mabomba kuunganishwa na moto badala ya connector. Je, yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kujionea ubadhirifu uliofanyika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa kuelezea mafanikio ya mtambo wa Ruvu Juu maana ndio lilikuwa swali la msingi, kuona kwamba maeneo yale ambayo mtambo ule umepitisha maji yanapata maji kwa sasa baada ya kuwa umekamilika. Haya maswali mawili anayoongezea ni tofauti na lile swali la msingi. Maswali anayoyauliza ni miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Kibaha.
Mheshimiwa Spika, hii ni sehemu nyingine lakini hata hivyo tutakupa majibu kwamba kama miradi ya Kibaha Mjini anasema yote imetekelezwa chini ya kiwango, hii ni kazi ambayo inabidi twende tukaiangalie, hatuwezi kuwa na jibu hapa, maana yake hatuelewi hilo. Mimi taarifa niliyonayo kwamba kazi zimefanyika lakini kama ni kweli iko chini ya kiwango tutakwenda kuliangalia.
Mheshimiwa Spika, pia huo mradi wa Pangani anaousema ana wasiwasi wa utekelezaji wake, nao naomba pia tupewe nafasi tutakwenda kuangalia na kama kuna tatizo tutachukua hatua kulingana na taratibu zetu za kusimamia miradi ya maji.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hekta 270 za shamba hilo kuongezwa haziwezi kukidhi mahitaji ya wananchi wa Mkoa wa Pwani pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wanaotumia majani hayo, je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza zaidi ya hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hei imekuwa bei aghali, je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza bei ili kuvutia wananchi wengi kutumia majani hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anataka kujua kwamba hizi ekari 270 ni ndogo kuweza kukidhi haja ya mahitaji ya chakula cha mifugo kwa Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Dar es Salaam, je, Serikali tumejipangaje? Jibu la swali hili ni kwamba Serikali tumejipanga vizuri na ndiyo maana tumehakikisha kwamba maeneo yetu ambayo ni ya mifugo likiwemo hili la Vikuge na mengineyo yale ya Holding Grounds na hata maeneo yetu ya NARCO pale Ruvu tunawekeza sana sasa hivi katika kuhakikisha kwamba tunapata maliso ya kutosha ili kuweza kuwa-supply wafugaji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na swali la pili ni juu ya bei; ni kweli, bado bei za hei na mbegu za malisho ziko juu. Hivi sasa tupo katika hatua ya mwisho kama Serikali ya ku-certify mbegu za malisho ili nazo ziweze kuuzwa kama zinavyouzwa mbegu za mahindi, mpunga na mazao mengine ili kuwawezesha wafugaji wetu waweze kupata mbegu hizo kwa bei nafuu. Hivi sasa bei ya kilo moja ya mbegu za malisho ni takribani shilingi 17,000. Mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba zinashuka ili ziweze kuwasaidia wafugaji walio wengi.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kwenye jibu lake la msingi amekiri kwamba tathmini ilifanyika 2012/2013; swali sasa watu hawa wamekatazwa wasiendeleze na nyumba zao zimebomoka na tathmini hairudiwi na anasema kwamba mkandarasi anaanza ujenzi; je, anaanzaje ujenzi wakati wananchi hawa hawajalipwa fidia yao?
Swali la pili, kwa kuwa tathmini ilifanyika 2012/2013 na sasa hivi ni miaka mitano imepita, je, Serikali ina jibu gani kuhusu kurudiwa kwa tathmini au malipo yao itakuwa vipi kwa sababu nyumba nyingine zimebomoka na nyingine zimeanguka. Ni mkakati gani ambao wataufanya ili wananchi wale waweze kupata malipo yao kwa tathmini mpya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, eneo hili la barabara ya kutoka TAMCO kwenda Mapinga ni barabara muhimu sana, hivi ninavyoongea tunaendelea na utaratibu wa kuhakikisha ujenzi unafanyika ili kuweza kukamilisha kilometa tano za eneo hili. Eneo hili ni muhimu sana kwa sababu barabara hii sehemu ambayo tunayoanza kujenga ndiyo maeneo ambayo ndiyo kitovu cha Mji wa Kibaha kwa maana ya kwamba maendeleo yanafanyika katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa eneo hili ujenzi unaanza, lakini kuhusu fidia ni kwamba kumbukumbu muhimu za fidia katika eneo hili zimeshachukuliwa na kumbukumbu muhimu zimekubaliwa na wananchi ambao wamepisha eneo la ujenzi, kwa sababu hiyo haitaathiri malipo yao wakati ujenzi unaendelea.
Kwa hiyo, kikubwa tu niwapongeze na kuwashukuru wananchi wa eneo hili kwa uzalendo na kwa kweli nao wanahitaji hii barabara iweze kuwepo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi tumeweka kumbukumbu vizuri na wananchi wameshasaini kukubali malipo ya kwao na pia upo utaratibu kama tukichelewa kulipa kuna viwango huwa vinabadilika kutokana na utaratibu uliopo.
Mheshimiwa Spika, pia kwa eneo hili ambalo ujenzi utaanza, utaratibu wa kuwalipa wananchi fidia upo mbioni, kwa hiyo niwatoe hofu wananchi kwamba wakati ujenzi unaendelea kufanyika na malipo yao yatafanyika hususani kwa kilometa hizo tano ambazo tumetathmini kwa sababu eneo lote hili la barabara wanastahili kulipwa kama shilingi bilioni 8.9 hivi. Kwa hawa wa kilomita tano, kama shilingi bilioni moja hivi itatumika kulipa fidia. Niwatoe wananchi wa maeneo haya watalipwa fedha zao kulingana na taratibu ili kupisha barabara hii muhimu kwa ajili ya maendeleo yao wao wenyewe.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Amekiri kwamba kuna matatizo lakini swali langu la kwanza linasema, kama hivyo ndivyo, wanafunzi wamemaliza wakiwa hawana ufundi wowote, kwa sababu kile chuo kilikuwa cha madarasa kwa ajili ya vijana wetu na kilikuwa kinafundisha udereva hamna magari, karakana hamna, madarasa mabovu na wameondoka wakiwa hawana ujuzi wowote na intake yao imekwisha. Je, Serikali ina mpango gani kwa ajili ya vijana hao, baada ya kurekebisha upungufu huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa hakuna vifaa vya kufundishia miundombinu hakuna na bado intake hii wanachukua wanafunzi, nini kauli ya Serikali katika hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba pamoja na upungufu uliopo katika Chuo cha FDC Kibaha, elimu iliyokuwa inatolewa inakidhi viwango stahiki vya ufundi ambao Chuo kile kimesajiliwa kwa ajili ya kutoa. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba wale vijana waliomaliza Serikali imejiridhisha kwamba wamekuwa wakipata mafunzo vinginevyo chuo kile kingeshafungwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba ni namna gani sasa tunarekebisha hiyo hali, nimeshamjibu kwenye jibu letu la msingi kwamba tayari tupo kazini, tunafanya tathmini ili kuweza kujua upungufu uliopo katika vyuo vyote 50 vya FDC ili sasa tuanze utaratibu wa kukarabati, na kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kuna nguvukazi ya kutosha ili elimu inayotolewa iweze kuwa bora kuliko sasa. Kwa hiyo, nimwambie tu asubiri tayari zoezi linaendelea.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Swali la kwanza, ni kwa nini Serikali haikufikiri kabla haijaanzisha mradi huo wa maroli kupaki pale Misugusugu mpaka ikafikia wananchi wa Misugusugu wanapata TB?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nini mkakati wa Serikali wa dharura kwa ajili ya kuokoa maisha ya wana Misugusugu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Deo Muro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kwa nini Serikali haikufikiri kabla, Serikali siku zote inafikiri, ilifikiri enzi hizo na sasa inaendelea kufikiri ili kuendelea kuboresha maisha ya wananchi wetu hasa hawa wa Misugusugu na ndio maana Wizara ya Ujenzi imeanza kuiboresha barabara ile ili kuondokana na changamoto hii ya vumbi pamoja na kwamba Serikali inatekeleza mradi huu wa Euro milioni 23 kuhakikisha sasa eneo lile la Misugusugu kituo kile kinaondoka na kinahamia vigwaza. Kuonesha kwamba Serikali inaendelea kufikiri na kutenda kwa ajili ya wananchi wake, haya tunayoyatenda Vigwaza yanakwenda kutendwa Manyoni na pia tunakwenda kutekeleza mradi wa aina hii kule Nyakanazi ili kuhakikisha huduma hizi zinafanyika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni mkakati wa dharura, ndio huu ambao nimeeleza kwamba Serikali inaboresha barabara il, lakini tunahakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati. Nitoe wito kwa Watanzania wote kwa ujumla maana ya kuwa na vituo hivi ni kuhakikisha mizigo ile yenye uhatarishi wa upotevu wa mapato tunaendelea kui-control hatua kwa hatua. Hata hivyo, pia wito wangu kwa Watanzania ni kuhakikisha kwamba wao wanakuwa wazalendo zaidi kwa Taifa lao ili mizigo hii ambayo wana- declare kwamba inaenda nchi jirani isiendelee kushushwa ndani ya Taifa letu. Unapoona gari linashusha mzigo ndani ya kijiji chako jiulize mara mbili kwa nini halikushusha mjini na lazima Watanzania wafahamu kwamba hakuna maendeleo bila kodi itakayolipwa na sisi Watanzania wenyewe na Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha mfano na tunatenda kwa vitendo kwamba kodi ya Watanzania sasa inapelekwa kwenye miradi inayowafikia wananchi moja kwa moja.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, swali la kwanza kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Pwani especially sehemu hizo zilizotajwa, walisitishiwa tangu 2014 wakati wa Awamu ya Nne, na anasema kwamba watalipa fidia kwa uthamini wa 2018 watu hawa walikuwa wanajenga wakaacha ujenzi na gharama zimepanda.

Je, Serikali iko tayari kulipa hasara ambayo maongezeko ya gharama za ujenzi watakapokuwa wanalipa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa Serikali imekaa kimya muda wote huu. Je Waziri yuko tayari kufuatana na mimi baada ya Bunge ili akaweze kuongea hayo ambayo ameyaeleza hapa wananchi waweze kumuelewa kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru kwa kufuatilia ili suala hili ni swali lake la pili, lakini pamoja naye niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Chalinze kwa kufuatilia hili swali kwa karibu.

Mheshimiwa Spika, lakini nataka nimueleze Mheshimiwa Mbunge na na wananchi wa Mkoa wa Pwani wakati wa mwaka 2014/2015 Serikali ilipo design mradi huu wa Kinyerezi, Chalinze, Segera Tanga ulikuwa kabla haujafanywa maamuzi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa Rufiji Hydro Power.

Kwa hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani na kuamua kutekeleza mradi huu kwa nia ya kufanya nchi iwe na umeme wa kutosha ilibidi ifanye utaratibu wa kuuisha upembuzi yakinifu kwa sababu mradi huu sasa wa Rufuji Hydro Power kuna njia mpya ambayo itajengwa ya KV 400 kutoka Rufiji, Chalinze ambayo inaelekea Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo suala ambalo limepelekea fidia hii kuchelewa kwa sababu lazima iuishwe, lakini tunatambua fidia inalipwa kwa mujibu Sheria na Kanuni. Kwa hiyo, malipo ya fidia hii kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani yatazingatia Sheria na Kanuni za nchi ambazo zinapeleka malipo haya ya fidia.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili amesema je, nipo tayari?, nataka nimualifu Mheshimwa Mbunge na mimi pia ni mdau ni Mbunge wa Mkoa wa Pwani hivi karibuni tu nilifanya ziara Kata ya Pera Jimbo la Chalinze na niliongea na wananchi suala hili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namkubalia kwamba baada ya Bunge hili au wakati wowote tunaweza tukafanya ziara katika maeneo ya Kibaha, maeneo ya Jimbo la Segerea, maeneo ya Kibaha Vijijini, maeneo ya Chalinze kuzungumza na wananchi na kwamba kwa kweli kama nilivyosema wakati wa bajeti yetu wataona tumedhamilia kabisa kulipa hii fidia kwa sababu mradi huu unaanza mapema Julai, 2020 na kukamilika Desemba, 2022, ahsante sana.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa shirika lilishajenga nyumba tayari na zimekosa wanunuaji, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba zile nyumba zinanunuliwa, itapunguza bei au itafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kujenga nyumba nyingi vile bila kuangalia mahitaji ya soko, je, Serikali haioni kama inapoteza hela za wavuja jasho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muro kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimthibitishie kwamba hakuna nyumba zilizokosa soko mpaka muda huu. Nyumba zote ambazo zilijengwa kwa ajili ya kuuzwa baada ya kuona watu hawawezi kununua kwa kiasi kile ambacho tulitarajia, nyumba zote zile zimepangishwa na kama zipo ambazo hazijapangishwa ni chini ya asilimia mbili. Hiyo imetokana tu na namna ambavyo mahitaji yalivyokuwa yakiombwa awali kwa sababu maeneo mengi ambapo nyumba zilijengwa awali yalikuwa ni mahitaji ya halmashauri husika, waliomba kujengewa, lakini baadaye hawakuchukua. Kwa hiyo shirika limeamua kuzipangisha nyumba zile na sasa hivi zote zimepangishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lake la pili anazungumzia habari ya mahitaji ya soko. Mahitaji ya soko ya nyumba bado ni makubwa sana. Kwanza tukiangalia tunahitaji kuwa na nyumba walau milioni tatu ambazo tunatakiwa tujenge walau nyumba 200,000 kila mwaka, hatujaweza kufikia idadi hiyo. Kwa hiyo, bado mahitaji ni makubwa zaidi kuliko ambavyo tunatarajia na ndiyo maana sasa kuna nyumba za gharama nafuu zitaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali tukianza na hapa Makao Makuu ya nchi.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa ni miaka 19 tangu mgogoro uanze na wananchi wale hawafanyi mwendelezo wowote, walijenga majengo yao wakasimamishwa. Je, Serikali ipo tayari kuwalipa fidia ya hasara ambayo wameipata kwa muda wote huo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Mary Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni muda mrefu na kwenye taarifa yangu hapa nimesema. Hata hivyo, kila kitu lazima kina win-win situation na ndiyo maana nimesema kwamba kuna mkakati unaendelea. Kikubwa zaidi nimuelekeze Mkurugenzi wetu wa Halmashauri ya Kibaha aende akakae na wananchi wakubaliane nini kifanyike kwa ajili ya eneo hilo ili kuondoa mgogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu lakini mwisho wa siku kila mwananchi awe na furaha.

Kwa hiyo, Mheshimiwa mama Muro achukue maelekezo yangu haya kwamba namuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri yetu aende kukaa na wananchi pamoja na timu yote na ikiwezekana Kamati ya Fedha, on site meeting, wakubaliane nini kifanyike ili mradi kuondoa dukuduku za aina yoyote kwa wananchi wetu wa Kibaha Vijijini.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa tatizo la migogoro ya ardhi Mkoa wa Pwani inasababishwa na makundi makubwa ya mifugo inayotoka sehemu mbalimbali: Je, Serikali ina mpango gani kukaa Wizara ya Mifugo na Wizara ya Ardhi kupanga na kuzuia makundi hayo ya mifugo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, anasema ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, dawa siyo kuzuia. Tunashirikiana kama Serikali moja na Wizara zote zinazohusika na matumizi ya ardhi ambao ni wadau kupanga matumizi bora ya ardhi, kupanga maeneo ya malisho na kuweka miundombinu. Hiyo ndiyo dawa ya kuwawezesha wafugaji watulie, wafanye shughuli zao za ufugaji kwa tija zaidi. Dawa siyo kuwaondoa wala kuwafukuza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali kwa ujumla kwa pamoja tunafanya hiyo mikakati na katika kazi ambayo alitutuma Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, katika ile timu ya Mawaziri wanane tumeandaa utaratibu ambao tunapendekeza utakuwa ndiyo mwarobaini ambao utawezesha kuainisha maeneo, kuyatambua, kuyapanga na kupanga miundombinu katika maeneo hayo ili wafugaji na wakulima waweze kukaa mahali salama ili waweze kuzalisha na kuongeza tija katika nchi hii.

Kwa hiyo Serikali kwa ujumla kwa pamoja tunafanya hiyo mikakati na katika kazi ambayo alitutuma Dkt. John Pombe Magufuli, katika ile timu ya Mawaziri nane tumeandaa utaratibu ambao tunapendekeza utakuwa ndiyo muarobaini ambao utawawezesha kuainisha maeneo kuyatambua, kuyapanga na kupanga miundombinu katika maeneo hayo ili wafugaji nao na wakulima waweze kukaa mahali salama ili waweze kuzalisha na kuongeza tija katika nchi hii.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante nafikiri hata wewe umeshangaa ukiwa kwenye kiti hicho hicho mwaka jana nilisimama mbele yako nikiuliza kwa nini chuo hiki hakifanyiwi ukarabati na ilijibiwa na Wizara ya Elimu mpaka mwaka jana ilikuwa haijulikani kama chuo hiki kiko chini ya Wizara ya Elimu au TAMISEMI, walipeleka Wizara ya Elimu pesa ya chakula wakaenda kuwanyang’anya wakasema kwamba chuo hiki hakiko chini ya Wizara ya Elimu na mpaka tunavyoongea saa hizi watoto wa shule pale hawana chakula sasa hivi tunajibiwa na TAMISEMI ina maana mpaka sasa hivi ndiyo imejulikana kwamba chuo hiki kiko chini ya TAMISEMI.

Sasa swali je, ni lini chuo hiki kitapata ruzuku ya chakula kwa sababu makusanyo yao ni madogo sana?

La pili, ni lini majengo na miundombinu ya chuo hicho yatafanyiwa uboreshaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia suala hili na fedha zilipelekwa pale, hiki chuo kiko chini ya TAMISEMI, kwa hiyo ilipogundulika kwamba fedha zimepelekwa pale na Wizara ya Elimu, ikabidi zirudishwe zipelekwe kwa malengo yaliyokuwa yamekusudiwa. Lakini nimesema kwamba chuo hiki kimeshafanyiwa tathmini, tumepeleka fedha pale milioni 70 kwa mapato ya ndani kwa maana ya kupunguza shida iliyopo, lakini tunaendelea kutafuta fedha zikipatikana wakati wowote hata leo kitaanza kufanyiwa ukarabati huo mkubwa wala hamna shida.

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili anauliza habari ya chakula, hili naomba nilipokee tulifanyie kazi kwa sababu utaratibu ni kwamba wanafunzi wote ambao wapo maeneo yote nchi nzima wanaosoma lazima wapewe chakula na tunapeleka fedha ya chakula kulingana na idadi ya wanafunzi katika eneo hili na hawezi kukaa shuleni bila kuwa na chakula.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niahidi kwamba hili tutalifanyia kazi mapema iwezekanavyo liweze kufanyiwa kazi kama kweli ni tatizo katika eneo hilo.