Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge (28 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote naomba niwashukuru wananchi wa Wanging‟ombe kwa kunipa kura nyingi sana nikawa Mbunge wa Bunge hili. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Naomba niwaahidi Watanzania pamoja na Mheshimiwa Rais kwamba nitaifanya kazi hii kwa bidii zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi kila aliyesimama hapa amezungumza tatizo la maji kwenye eneo lake. Sitaweza kuyajibu yote, lakini nitatoa bango kitita cha kuelezea utekelezaji wa awamu ya kwanza ya programu ya maji ambayo imegusa kila Halmashauri, kila Wilaya, kila Mkoa, mji Mkuu wa Mkoa, Mji wa Wilaya; ni miradi mingi sana.
Katika awamu ya kwanza tumekuwa na miradi 1,888 na miradi 1,200 imekamilika, bado miradi 700 na kitu inaendelea na iko kwenye hatua mbali mbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru Wabunge. Bunge lililopita mliidhinisha tuanzishe Mfuko wa Maji ambapo tuliamua kabisa kwamba tuanze kwa shilingi 50 ya lita ya mafuta, tukapata shilingi bilioni 90. Sasa naomba sana, tutakapoingia kwenye Phase II ya programu ambapo tumeainisha miradi mingi yenye thamani ya bilioni 3.3 US Dollar ambayo ni sawa sawa na trilioni sita, ndani ya miaka mitano, tutatimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoiongelea kwenye hotuba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo pia ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ambapo tunasema kwamba sasa imefika mahali tufikishe upatikanaji wa maji vijijini asilimia 85 na mijini asilimia 95. Katika miaka kumi ijayo tunataka tuseme asilimia 100 kwa vijijini na mjini lazima wapate maji, kulingana na programu ambayo tumeiandaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapofika kwenye bajeti tunaomba sana Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono ili fedha za ndani ziweze kutekeleza jambo hili. Wafadhili wameshaahidi zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kwamba watachangia kwenye hiyo shilingi bilioni 3.3 Us Dollar. Nusu tayari wameshaahidi. Kwa hiyo, ina maana kwamba Serikali lazima tutafute nusu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili kila mtu apate huo mradi wake, tunahitaji tupate mapato mengi ya ndani ili tuweze kutekeleza miradi hii. Kwa hiyo, naomba sana tutakapofikia mahali hapo, Waheshimiwa Wabunge, mtuunge mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme machache katika miradi ambayo inaendelea hivi sasa. Kwanza kulikuwa na mradi wa kutoa maji katika bomba la Kashwasa kupeleka Tabora - Igunga na Nzega pamoja na vijiji 89 vitakavyonufaika. Tumeshapata fedha kutoka Serikali ya India, sasa hivi tunatafuta mkandarasi, tunafanya kitu kinaitwa pre-qualification. Wataanza kuleta tender zao. Tunategemea ikifika Julai, Mkandarasi atakuwa ameanza kazi ya kujenga mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kilio cha wananchi wengi wanaoishi kando kando ya Ziwa ya Victoria kwamba maji yale yaweze kupatikana. Tayari tumeshaanza miradi mingi ya kutoa maji ndani ya Ziwa Victoria kupeleka kwenye miji yote inayozunguka Ziwa Victoria. Kwa hiyo, mradi unaendelea na kazi nyingi zitaanza kuanzia mwezi wa saba mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi pia wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara na Mikindani. Tumeshakamilisha usanifu, bomba kubwa litajengwa kilometa 60 na vijiji karibu zaidi ya 29 ambavyo viko kando ya bomba lile vitapatiwa maji. Tunakamilisha mazungumzo na Serikali ya China kwa ajili ya kuweza kupata ufadhili pamoja na Serikali ili tuweze kukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna mradi mwingine ambao utaongeza upatikanaji wa maji katika Mji wa Dar es Salaam. Tumekuwa na kilio na ahadi kwa muda mrefu. Sasa tumefika mahali kwamba mradi ule wa upanuzi wa Ruvu Chini utakamilika mwezi wa pili; na upanuzi wa mradi wa Ruvu Juu utakamilika mwezi wa tatu. Kwa hiyo, tukifika mwezi wa tatu matanki yote ya maji ambayo tuliyajenga kwa muda mrefu, yatakuwa yameshajaa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi tunayoendeleanayo sasa ni kusambaza maji yawafikie wananchi, kwa sababu kwenye sera ya maji tunasema upatikanaji wa maji uwe mita 400 hasa kwa wananchi walioko vijijini. Kwa wale wanaokaa mijini, tunataka tuwaunganishie maji kwenye nyumba zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi hii inaendelea na kwenye programu hii nina hakika kabisa tutaanza na maeneo kama ya Kimara, Kibamba, Kiluvya, kwenda mpaka Mlandizi, maeneo yale yote tutayasambazia maji baada ya kupatika wingi wa maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa eneo hili la Temeke na maeneo mengine ya upande huu pili kama Mkuranga, tuna uchimbaji wa visima Kimbiji na Mpera. Tumeshakamilisha visima nane na sasa hivi tutaingia kwenye awamu ya pili ya kujenga miundombinu ili tuhakikishe kwamba tunapata maji ya kutosha kwa wananchi wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda; na kwa sababu nimesema nitaleta bango kitita kwa utekelezaji wa mambo yote haya, naomba tukubaliane kwa leo kwamba mtapata report na mtatusaidia katika kujenga hoja katika kufanya miradi maeneo mengine ambayo yamebaki. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri ambapo kila Mbunge aliposimama amezungumzia angalau tatizo alilonalo kwenye eneo lake kuhusu upatikanaji wa maji. Kumekuwa na mabishano kuhusu asilimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba tutaendelea kuyapeleka maji, kwa maana kwamba kutokana na ilani ya Chama cha Mapinduzi, tumesema vjijini tutapeleka kwa 85% ifikapo mwaka 2020 na mijini tutapeleka kwa 95%. Tunafanya hivi kwa kufuata programu ya maji ambayo tulianza nayo mwaka 2007. Kuna miradi ambayo tulianza kuitekeleza, kwanza tutakamilisha miradi ambayo haijakamilika, halafu tutaingia awamu ya pili ambayo tumeanza sasa hivi, kuweza kuainisha ni miradi ipi na maeneo yapi tunakwenda kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge watakaporudi kwenye Majimbo yao, kwenye Halmashauri zao wakaangalie vipaumbele ambavyo wangetaka tuanze navyo. Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ameelekeza maeneo 65 nchi nzima ndiyo kipaumbele na sisi katika kufanya kazi tutafuata hilo. Sasa ninyi Waheshimiwa Wabunge mtusaidie ni wapi ungetaka tuanze napo, kwa maana kwamba tuweze kufikisha hizi asilimia tunazosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa, mwaka 2025, lengo la Serikali ni kwamba tutapeleka maji kwa kiwango cha 100% vijijini na mijini. Changamoto tunayoipata katika maeneo ya mijini sasa ukishaongeza upatikanaji wa maji unaongeza pia maji taka. Sasa tunataka katika hii phase ya pili, tuingie katika namna ya kuweza kuongeza jinsi tutakavyoondoa maji taka katika miji yetu ili pia tuweze kuondoa changamoto za maradhi kama kipindupindu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hilo tutaliweka kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametoa mwelekeo na sasa kila sekta tutakwenda kuangalia ni miradi ipi kulingana na ceiling ya bajeti. Pia nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tulishaweka Mfuko wa Maji toka mwaka jana na Mfuko wa Maji huu kutokana na tozo ya mafuta ambayo tuna uhakika, zile shilingi 50 kwa kila lita tutapata kama shilingi bilioni 90 mpaka ikifika Juni. Fedha hizi zitasaidia kulipa wakandarasi ambao sehemu kubwa wamesimama na fedha hiyo imeanza kutoka na tayari tumeanza kupeleka kwenye Halmashauri.
Naomba sana Wakurugenzi wetu fedha zile ambazo tunapeleka specifically kwa mradi, walipe miradi ile ambayo tumeamua kuimaliza kwanza. Miradi mingi ipo kwenye 90% na 95%. Tukiweza kuwalipa tuna uhakika wananchi wetu wataanza kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana fedha hizi zisiende kufanya kazi nyingine, tutakuwa wakali na tutachukua hatua kwa Mkurugenzi ambaye ataamua kuzitumia fedha hizi anavyotaka yeye. Fedha hizo ni moto, kwa hiyo, tumepeleka tuhakikishe kabisa wanakwenda kulipa Wakandarasi wamalize miradi ili wananchi wetu waanze kupata maji. (Makofi)
Kwa upande wa Da es Salaam naomba niseme tu kwamba ikifika mwezi Machi, tutakuwa tumepata maji yanayotosha mahitaji, kwa maana ya kiujumla wake ya wananchi. Kazi kubwa ambayo tutakuwa tunakwenda kufanya sasa ni ule usambazaji. Kule Kimbiji na Mpera tumeshachimba visima tayari saba kati ya visima 12 kwa ajili ya maeneo mengine ya Kigamboni, Mkuranga ili tuweze kukamilisha na kuhakikisha wananchi wa maeneo yale wanapata maji. Kwa hiyo, naomba sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tutachukua haya mawazo yenu yote na tutayaweka kwenye Mpango ili tuhakikishe kwamba tunakwenda kutekeleza kama tulivyopanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi wengi ambao wanaishi kandokando ya Ziwa Victoria nimetoa ahadi na Rais ameahidi kwamba tutachukua maji ya Ziwa Victoria kuweza kusambaza katika miji yote mikuu ya mikoa inayozunguka Ziwa Victoria pamoja na Makao Makuu ya Wilaya. Hii miradi tumeshaanza, mingine kwa kutumia wafadhili mbalimbali, lakini mengine tutakwenda kufanya kwa kutumia fedha zetu za ndani. Sasa tutakapofika kwenye bajeti, basi Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono ili tuweze kutekeleza miradi kama ilivyokuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Nashukuru kwa nafasi, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI W A MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali yote nakushukuru wewe mwenyewe binafsi, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote mbili kwa michango ambayo wametupa. Nataka nitoe ahadi kwamba michango yote mlioyoitoa kwa kuongea humu ndani na mliyoleta kwa maandishi, tutaijibu na tutawapa bango kitita cha maelezo yote kwa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwape imani kwamba ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, Wizara hii inaongozwa na wahandisi; kuanzia Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, wote ni wahandisi waliosajiliwa. Nina hakika kabisa haya mawazo yote mliyotoa Waheshimiwa Wabunge, tutakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kwamba nchi yetu matatizo ya maji tunakwenda kuyafikisha mahali ambapo ni salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Serikali yoyote ambayo inapenda kutawala, halafu wananchi wake hawana maji. Kwa hiyo, kwa Serikali ya Awamu ya Tano, maji ni kipaumbele kimojawapo. Mheshimiwa Rais wetu kila mahali alipokwenda kuomba kura, aliahidi kwamba suala la maji nakwenda kulishughulikia kwa nguvu zote. (Makofi)
Ndugu zangu, tuna miezi sita tangu tumeingia madarakani na toka Mheshimiwa Rais, Magufuli ameingia madarakani, sasa fedha zimeanza kupatikana na tumeanza kuzipeleka kwenda kwenye Halmashauri zote. Kwenye Mfuko wa Maji zilikuwa zimetengwa shilingi bilioni 90, lakini mpaka leo tumeshapeleka zaidi ya shilingi bilioni 107 kwenye Halmashauri. Hii inaonesha kabisa kwamba kuna nia ya dhati na ya kweli kwamba tunakwenda kumaliza matatizo ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu tunasema ikifika mwaka 2020 lazima tuhakikishe wananchi wetu wote wanaoishi vijijini, wanapata maji kwa kiwango cha asilimia 85 na wanaokaa mijini wanapata kwa kiwango cha asilimia 90. Kwa hiyo, kazi tumeshaianza. Naomba ndugu zangu mtuamini, tutakwenda kutekeleza jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi ya Upinzani na Kamati ya Bunge wote wameshauri kwamba tuongeze uwezo wa Wizara hii kufanya miradi zaidi. Katika kuongeza uwezo, kimojawapo ni lazima tuongeze rasilimali fedha. Kwa hiyo, mapendekezo yaliyotolewa kwa kambi zote mbili kwamba tupanue wigo wa Mfuko wa Maji; kama tunaweza kukubaliana kwamba tu-ring fence Mfuko wa Maji, tuna hakika kabisa tutafanya miradi mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Naibu Waziri, Programu ya Awamu ya Kwanza ya WSDP, tulikuwa na miradi 1,800; mpaka sasa tumekamilisha miradi 1,200. Kwa maana kwamba WSDP tumekuwa na mafaniko ya asilimia 62, hiyo ndiyo iliyofikisha kupata asilimia 65 ya wananchi wanaokaa vijijini. Tumepata asilimia 68 kwa maana ya wastani wa programu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la data, mtu unaweza ukasema kwanini unasema 68 wakati eneo lingine wako 40? Ni kweli data hizi tumechukua wastani kinchi; na data ina-base kwa population siyo kwa namba ya vijiji. Maana mmoja anasema mimi nina vijiji kumi vimepata maji, lakini vijiji 90 havina maji, kwa maana havikupata maji kwa programu hii ya WSDP; lakini kuna mipango mingine ambayo ilikuwa inaendelea sambamba na mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na miradi ya Water AID, watu wa UNICEF miradi mingi imekuwa inaendelea ambao hawakuwa wameingia kwenye programu. Kwa hiyo, tunaposema mafanikio haya, tuna base na population.
Kwa hiyo, inaweza kuwa ni vijiji vitatu, lakini ndiyo vyenye watu wengi zaidi. Data hizi zimetoka huko kwenye Halmashauri, sisi tumefanya compilation. Huu mradi unatekelezwa na watekelezaji zaidi ya 100 kwa sababu Halmashauri zetu sasa hivi ziko 181, Halmashauri tu peke yake! Bado kuna taasisi nyingine ambazo zinaendelea kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, kila Wilaya katika mwaka huu tumezingatia na kuhakikisha kila Halmashauri ya Wilaya tunaipa fedha za kutekeleza programu.
Mheshimiwa Naibu Spika, waliosema wanataka kutekeleza vijiji gani, imetoka huko kwenye Halmashauri, ndiyo walioleta vipaumbele Wizarani tukachuja. Kulingana na ceiling tukasema basi anza na vijiji hivi; lakini tukipanua wigo, tutaendelea na vijiji vingine. Kwa hiyo, naomba msiwe na shaka kwamba mbona nimepewa hela kidogo? Hapana, tumepewa fedha za kutosha. Hata mimi nasema fedha tulizopewa na tulizotengewa zinatosha. Lazima tuoneshe kwamba katika hizi tulizopata tunaweza kufanya kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme kwa kifupi kuhusu hii programu. Sasa hivi kuanzia Januari, tumeanza kutekeleza programu ya awamu ya pili. Washirika wa maendeleo wakiwepo Benki ya Dunia, African Development Bank, KfW na wengine wameahidi kwamba kwenye programu ya pili watatoa dola bilioni 3.3 ambazo ni karibu trilioni saba kwenye programu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunauhakika kabisa katika miaka mitano ijayo tutafikisha hizi asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini, kwa sababu tayari wapo Washirika wa Maendeleo pamoja na Serikali. Kwa hiyo, duty yetu ni kuwahamasisha wananchi kweli tuweze kupata makusanyo ya kutosha, fedha hizi ziweze kuingia kwenye mfuko wa maji ili tuweze kutekeleza miradi mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafadhili pia wameanza kuwa wazito, wanapoona Serikali hatuchangii kwa kiwango kikubwa, basi na wao vilevile wanakuwa wazito kuchangia. Kwa hiyo, kama Serikali tutaonesha kabisa direction kwamba lazima tuweke fedha ambazo zimetengwa ziende kwenye maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ushauri kambi zote mbili kwamba tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini (Rural Water Agency). (Makofi)
Sasa hili kwenye suala la sustainability au uendelevu; tumesema miradi ya maji ili iweze kuwa endelevu, tumekuwa tunawatumia hawa water users, wale watumia maji. Serikali ikishajenga mradi, tumekuwa tunakabidhi kwa watumia maji kuendesha mradi ule ili kusudi mradi uwe endelevu na uweze kutoa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi tumefanikiwa, lakini yapo maeneo ambayo bado kuna matatizo ya hizi Water Users Associations. Tumeendelea kutoa mafunzo, lakini pale tukianzisha Rural Water Agency nina hakika uendelevu wake utakuwa unafanana kutoka Wilaya moja kwenda Wilaya nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hili tunalipokea, ni zuri. Wizara yangu itaanza kuandaa cabinet paper, tutapeleka kwenye Baraza la Mawaziri, tutaangalia namna gani tunaweza kuanzisha hii Rural Water Agency ili itusaidie kufanya miradi yote hii iwe endelevu. Kwa sababu itakuwa haina maana unajenga mradi, baada ya siku mbili mradi ule unakuwa hautoi maji; na inawezekana hautoi maji kwa sababu ya kitu kidogo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi ya maji, tofauti na kujenga barabara; unaweza kuwa na mradi wa barabara wa kilometa 100 ukajenga kilometa 50, unaweza kuendelea kutumia kilometa 50; lakini mradi wa maji ni lazima umalize mpaka mita ya mwisho. Lazima maji yafike kwenye tanki ndiyo yanaweza kutoka. Kwa hiyo, miradi ya maji ni lazima ikamilike kwa namna inavyotakiwa. Huwezi kusema partial completion. Kwa hiyo, ndiyo tofauti ya miradi ya maji na barabara au ya kujenga nyumba au na vitu vingine. Kwa hiyo, tutazingatia na nina hakika tukiwa na Rural Water Agency, miradi yetu itakuwa endelevu kwa sababu tutakuwa na norms ambazo zinafanana kutoka mradi mmoja mpaka mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la Mfuko wa Maji, bajeti iliyotangulia ya 2015/2016 tulikuwa tumetengewa shilingi bilioni 90. Performance yake imekuwa nzuri kwa sababu hizi fedha ni ring fenced, Wizara ya Fedha imeweza kutupa zaidi ya hizi shilingi bilioni 90 kwa sababu ndivyo walivyokusanya. Kwa hiyo, naamini kabisa tukipanua wigo zikapatikana zaidi ya shilingi bilioni 90 tutafanya miradi mingi zaidi kama nilivyosema toka awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kidogo kuhusu miradi mikubwa ambayo tunayo. Kwanza kuna maombi mengi ya watu kutaka kupata maji ya Ziwa Victoria. Sasa miradi mikubwa ya Ziwa Victoria ambayo tunayo ni kama sita; tuna mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Tabora, Nzega, Uyui, Sikonge, Igunga na vijiji 89 ambavyo vipo kando kando ya zile kilometa 12.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Munde ametaka kujua action plan. Ni kweli mradi huu tumeuzungumza muda mrefu, lakini Serikali imeshapata mafanikio; tumeshapata fedha kiasi cha shilingi bilioni 536 kutoka Exim Bank ya India. Mkataba wa fedha hii umeshasainiwa na tayari pre-qualification tumeshaikamilisha. Ni kwamba sasa kazi haiwezi kuanza mpaka wenzetu kwa utaratibu wa mfadhili aseme, ndiyo endelea (no objection), ndicho kinachosubiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kazi zote tumefanya. Atakaposema no objection endelea, tunaanza kusaini mkataba na makandarasi, wanajaza zile tender, tunaendelea kufanya kazi. Kwa hiyo, ninaamini kabisa Serikali ya India itakwenda kutoa no objection kwa namna tulivyokuwa tumekubaliana. Na mimi nitafuatilia kuhakikisha kwamba kazi hii ambayo tumewaahidi Watanzania kwa muda mrefu hasa wa Kanda ya Tabora, Nzega, Igunga na Uyui kwamba huu mradi sasa unakwenda kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine ambao wameusema kwa maandishi na kwa nguvu sana ni Mradi wa Lake Victoria kwenda Sumve, Malya, Malampaka, Kwimba, unaweza kuipata kwenye ukurasa 126. Mradi huu tumewapa fedha ya kuanza kufanya usanifu maana huwezi ukajenga mradi kama hujafanya usanifu. Kwa hiyo, tumeshaweka fedha, ina maana Serikali imeshakubali kuutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine wa Ziwa Victoria ni unaokwenda Busega, Bariadi, Langabilili, Mwanhunzi. Mradi huu tumeutengea shilingi bilioni tano. Kwa hiyo, tayari kuna commitment ya kuanza kutekeleza mradi huu. Kuna mradi mwingine wa kupeleka maji kwenda Isaka, Tinde na Kagongwa, nao tumeshautengea fedha na kwenye randama mtauona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mwingine kutoka Ziwa Victoria kwenda Mwanza, Bukoba, Misungwi na Magu. Tayari tumepata mkopo kutoka European Investment Bank na sasa hivi tupo kwenye tendering stage ili kuweza kupata makandarasi na tuweze kuanza kujenga mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi mingi kwa ajili ya Mradi wa Makonde, Mheshimiwa Mkuchika amesema kwa uchungu sana. Kama Senior Member of Parliament naomba nikuhakikishie mradi huu tunakwenda kuukarabati. Ni mradi wa siku nyingi, ni mradi muhimu, ninaamini kabisa kwa mpango ambao tumeuweka, ukiangalia kwenye randama tumewaka kwenye miji 17 ambayo tayari tumeahidiwa na Serikali ya India kupata dola milioni 500 ambazo ni karibu trilioni moja. Sasa tumeona huu mradi kwa sababu utahitaji fedha nyingi tumeuwekea katika hii miji 17 pamoja na miradi mitatu ya Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo mradi huu umewekwa kwenye mpango mzuri, Mheshimiwa Mkuchika, naomba kabisa waambie wapiga kura wako kwamba Serikali inakwenda kutekeleza mradi huu. Angalizo lako kwamba wale waendeshaji wa mradi wanapeleka maji kwa watu wanaofanya biashara, nimeshawaambia kuanzia sasa hiyo biashara waache. Kwa hiyo, hawataendelea kufanya kazi hiyo, vinginevyo nakwenda kuwakamua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza katika Mradi wa WSDP kuna suala la kuchagua tutumie teknolojia gani? Pale mwanzo tulipoanza, sehemu kubwa ya miradi hii walichagua kutumia visima kwa sababu visima ilikuwa ni technolojia rahisi na namna ya kuiendesha imekuwa rahisi. Kwa hiyo, michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi, wameacha kutaka kuwa na teknolojia ya visima. Kwa hiyo, kila mahali kama kuna mto, wanataka tuchukue maji Tabora kutoka Mto Malagarasi; Bukoba wanataka tuchukue maji kutoka Mto Kagera, likewise wa Lake Victoria, likewise wa Ziwa Nyasa wote wangetaka tuchukue miradi kutoka kwenye maeneo kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua mradi kwa mfano huu wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Kahama na Shinyanga, mradi huu umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 250, huu ni mradi mmoja. Sasa ukichukulia bajeti ambayo inatolewa kwa mwaka ya shilingi bilioni labda 400, sasa ukipeleka mradi mmoja ina maana utakuwa umefanya kazi moja. Ndiyo maana tulifikiria tuanze kwanza na kutatua hili suala la kutumia visima ili tuwe na miradi midogo midogo ambayo tunaweza tukai-spread kwenye nchi. Sasa baada ya kufanya vile na kuona maeneo mengine kwa sababu ya tabia nchi, suala la visima imeonekana havipo sustainable, yaani havina uendelevu. Baada ya miaka miwili, mitatu unakuta kisima kile kilikuwa kinatoa maji, maji yanapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumeona tutaanza kufanya usanifu, kubadilisha yale maeneo ambayo angalau kuna mabwawa na sasa hivi nahimiza kwamba Serikali itaanza kujenga mabwawa makubwa ili iwe ndiyo source ya kutawanya maji kwa watu wengi kwa muda mfupi na kwa nguvu ya Serikali ya Awamu ya Tano jinsi tunavyokwenda, naamini kabisa jambo hili tunaweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana tushirikiane Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa tuanze kuangalia uwezekano wa kuvuna maji ya mvua, tuongeze reservers, tuongeze upatikanaji wa maji kwa kuwa na mabwawa mengi zaidi. Haya mabwawa yanaweza yakawa ni kwa watu kutumia maji lakini pia yanaweza kutumika kwa mifugo na pia tunaweza tukatumia kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, ni kitu ambacho ni endelevu. Tukifanya kwa muda wa miaka mitano ijayo tutakuwa kabisa tuna uhakika na chakula cha kutosha na tutakuwa hatuna njaa. Hata yale maeneo ambayo ni kame, wakishakuwa na mabwawa haya, nina hakika tutakuwa hatuna tatizo la chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeshashauri na kuelekeza Halmashauri watunge sheria ndogo ndogo hasa kwenye shule, kwenye zahanati, lazima tu-design kuvuna maji ya mvua ili tupunguze magonjwa yanayoambukiza kwenye shule zetu zote. Tukiwa na matenki na tukavuna maji, watoto watafundishwa kunawa mikono; nina hakika tutapunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa yanayoambikizwa kama kuhara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Zitto kwamba kuna mradi wa umwagiliaji maeneo ya Lwiche na kwamba alikuwa halioni kwenye randama. Naomba nimwambie kwamba jambo hilo lipo na kwenye randama ipo, Serikali inakwenda kufanya kwanza feasibility study na usanifu wa mradi, ndiyo condition ya wafadhili ambao ni Kuwait Fund. Wanazo fedha US Dollar milioni 15, lakini wanasema Serikali ifanye na Serikali tumeweka fedha za kufanya usanifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia alikuwa na hoja kuhusu mradi wa Kigoma kwamba tunachukua hatua gani? Ni kweli mradi wa Kigoma umechelewa kukamilika, lakini mpaka sasa tumechukua hatua ya kumkata tozo kwenye mkataba ule. Mkataba ulikuwa uishe Machi, 2015 kwa hiyo, umeshachelewa; lakini kulingana na mkataba jinsi tulivyokubaliana, mkandarasi akichelewesha mradi, kuna kitu kinaitwa liquidated damages, maana yake ni tozo kwa kuchelewesha. Uzuri wa mradi ule ni kwamba vifaa vyote vinavyohitajika na Mkandarasi vipo Kigoma. Kazi ina progress karibu asilimia 60. Kwa sababu kila kitu kipo, tumeshambana mkandarasi kwamba ikifika mwezi wa kumi atakuwa amekabidhi mradi. Kwa hiyo, mradi utakamilika mwezi wa kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kusimamisha mkataba utake kutafuta mkandarasi mwingine, kwanza tutapata matatizo mawili. Huu mradi ni wa mfadhili, ukisha-terminate contract, mfadhili anajitoa. Kwa hiyo, itabidi tutafute hela. Sasa kama hatukuweka fedha kwenye bajeti, ina maana mradi utazidi kuchelewa. Kwa hiyo, ni vizuri aendelee kukatwa liquidated damages lakini akamilishe mradi, na sisi tutaendelea kumbana na kuweza kusimamia kuhakikisha anamaliza kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na hoja za baadhi ya Waheshimiwa kuhusu miradi ya maji Dar es Salaam. Kama nilivyosema sasa hivi Dar es Salaam tumeshakuwa na maji yanayozalishwa kutoka kwenye mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu yanatosheleza kwa mahitaji ya sasa. Tatizo tulilokuwanalo ni ule mtawanyiko (distribution) na sasa hivi Dar es Salaam watu wamepanua sana kuliko ilivyokuwa mwanzo. Kwa hiyo, watu wapo maeneo mengi ambayo hayana mtandao. Serikali tumeshaanza kushughulikia suala la mtandao wa mabomba ili maji haya ambayo tayari yanazalishwa yaweze kuwafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam hapo nyuma kulikuwa hakuna maji, lakini leo maji yapo na mabomba yanapasuka. Tatizo letu ni kwamba miundombinu ni ya siku nyingi sana, kwa hiyo, tunaikarabati na tunajenga miundombinu mipya ili maeneo yote ambayo hayana maji tuweze kuhakiksha kwamba yanapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wameongelea suala la maji machafu, ni kweli. Tulisema ngoja kwanza tuweke nguvu kwenye upatikanaji wa maji safi na salama. Haya maji ninavyozungumza yanawekewa dawa, yanachujwa. Ndiyo tumeweka nguvu na yamepatikana. Ukizalisha maji mengi zaidi lazima utazalisha pia maji machafu. Tunao mpango wa kuboresha huduma ya maji machafu kutoka asilimia 10 mpaka asilimia 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Korea Kusini wameshatuahidi kutupatia dola milioni 89 kwa ajili ya kuanza kutengeneza mitambo ya kuchuja maji machafu. Kwa sasa tumekuwa tunapeeleka maji baharini lakini hii siyo sawasawa. Inatakiwa maji machafu yaingizwe kwenye mtambo yaweze kusafishwa. Maji haya pia tutayatumia kwa baadhi ya kilimo na baadhi ya viwanda kwenye cooling, kwa mfano, Kinyerezi tunatumia maji ambayo yameshapitiwa au wanaita recycling; umeshayazungusha kutoka uchafu na kuja kwenye maji safi; lakini yatatumika kwa ajili ya viwanda. Yale maji yanayotoka Ruvu yatatumia watu kwa ajili ya kunywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maeneo ambayo hayana mtandao, kwa mfano, wengi wamezungumza habari ya maji kutoka Mto Rufiji, Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea vizuri. Jambo hili ni kweli, tungeweza kupata maji yale yangeweza kufika kwa watu wengi zaidi. Kilichotukwamisha mwanzoni ilikuwa ni makubaliano ya teknolojia ya kutumia na vilevile fedha ambazo zingehitajika kwa miradi kama hii, inakuwa ni nyingi. Kwa hiyo, tutaendelea kulishughulikia, kama nilivyosema tutafanya usanifu na kuweza kuongeza. Tukichukua maji ya Rufiji na maji ya Kimbiji na maji ya Ruvu, tunahakikisha kabisa hata hili suala la kuwa na viwanda, kwa sababu kweli huwezi kuwa na viwanda endelevu kama huna maji. Kwa hiyo, lazima tutahakikisha kwamba maji yanapatikana kwa ajili ya kuhakikisha nchi yetu inakuwa na viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, watafiti wanasema ukiwekaza dola moja kwenye maji ina maana inazalisha dola tano kwenye uchumi. Kwa hiyo, ni jambo la msingi sana, tutahakikisha kwamba tunawekeza kwa nguvu zote kwenye suala hili la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi mwingine wameulizia kuhusu mradi wa Manispaa ya Lindi. Ni kweli tumekuwa na mradi ambao pia umecheleweshwa, ni katika miji ile saba ambayo imefadhiliwa na Benki ya Ulaya. Huu mradi utakamilika ikifika mwezi wa nane mwaka huu. Naye mkandarasi pia tumeanza kumkata tozo kwa kuchelewesha. Kwa hiyo, inakuwa kwa mkandarasi ni hasara kama ataendelea kuchelewa zaidi, kwa sababu ataendelea kukatwa. Mpaka sasa tumeshamkata zaidi ya shilingi bilioni 3.6 kwa kuchelewesha mradi ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa pia kuhusu mradi wa Sumbawanga na mradi huu pia nao umecheleweshwa, lakini tumembana Mkandarasi na mradi utakamilika utakapofika mwezi wa sita. Naye pia tumemkata karibu shilingi bilioni 4.2 kwa kuchelewesha mradi ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri 181 kila mmoja hapa angesimama angesema tu vijiji ambavyo havina maji; hiyo ni obvious wala mimi sitaki kupingana naye; yeyote atakayesimama. Hata Mheshimiwa Lukuvi angesimama angesema vijiji vyake ambavyo havina maji. Ndiyo maana tumeweka mpango huu kabambe wa WSDP kuhakikisha vijiji vyote vinapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwamoto amezungumza kwa nguvu sana kuhusu maji Ilula. Tumepata watu wa kutusaidia Serikali ya Australia, ule mradi unakwenda kujengwa; na tupo kwenye hatua nzuri ya kuweza kufika muafaka. Kwa hiyo, zipo hoja nyingi sana na niseme tu, hoja zote ambazo Waheshimiwa Wabunge mmetupa kwa kuongea humu ndani kwa maandishi tutawapatia majibu. Labda nipitie baadhi ya hoja ambazo ninazo hapa.(Makofi)
Mheshimiwa Kiula alizungumza habari kwamba katika Halmashauri yake maeneo mengi ni kame na alikuwa anasema hawana mito; na alikuwa anafikiria, je, kwa nini maji yale ya Igunga yasifike mpaka Singida?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi namwambia tu jambo hili itabidi tulifanyie usanifu kwanza (feasibility study) tuone possibility kama maji yale bado yatakwenda kwa njia ya mtiritiko. Ukisema utaweka pampu maana yake unaongeza gharama za uendeshaji mradi. Halafu tunasema maji ni lazima yalipiwe kwa sababu ili Serikali iweze kufanya miradi mingi na kuiendesha miradi hii ni lazima walipie. Kwa hiyo, unaweza kukuta gharama ya wananchi kulipa maji yale ambayo yametengenezwa kwa fedha nyingi inaweza ikawa siyo sustainable au endelevu. Kwa hiyo, mambo yote hayo tunayaangalia kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha tumeweka fedha kwa ajili ya kufanya usanifu kwenye mabwawa mapya ya Nduguti pamoja na bwawa la Mlanchi. Kwa hiyo, tutayafanyia usanifu.
Mheshimiwa Mboni Mhita amezungumza habari ya mabwawa yake ya Manga, Mkata na Kwa Ndungwa. Mwaka huu wa fedha Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga miradi zaidi ya shilingi bilioni 1.129 imetengwa kwa ajili ya kuanza kujenga miradi ya vijiji kumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Mheshimiwa Victor Mwambalaswa amezungumzia habari ya Bwawa la Matwiga; bwawa hili lilishakamilika, limefikia asilimia 85; tumewakabidhi Wakala wa Visima na Mabwawa kukamilisha hiyo sehemu iliyobaki. Kwa hiyo, bwawa hilo Mheshimiwa linakwenda kukamilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bwanausi, umetoa ushauri kwamba Serikali ijipange upya ili kusimamia fedha za miradi zinazopelekwa kwenye Halmashauri; ungetaka kiundwe Kitengo cha Ufuatiliaji. Mimi nafikiri solution ya usimamizi wa miradi ni hiyo kuwa na Wakala wa Maji Vijijini. Tutakuwa na mfumo endelevu wa kusimamia miradi ya maji. Kwa hiyo, ushauri wako ni mzuri na tunaupokea.
Mheshimiwa Savelina Mwijage alisema Mkoa wa Kagera una vyanzo vingi vya maji lakini havitumiki ipasavyo, ni pamoja na kutaka kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria. Mkoa wa Kagera tunayo miradi ambayo inachukua maji kutoka Ziwa Victoria ikiwepo na Manispaa ya pale Bukoba maana ipo ndani ya Mkoa na pia Karagwe kuna ziwa ambalo lipo. Tunaanza na usanifu, kuchukua maji kwenye ziwa ambalo lipo jirani na Karagwe kupeleka mji wa Karagwe. Kwa hiyo, ushauri wako ni mzuri, tutaendelea kuangalia na vyanzo vingine ambavyo vipo karibu na wananchi.
Mheshimiwa Mgimwa alikuwa anashauri Rural Water Agency pamoja na kuongeza tozo ya shilingi 100. Ushauri wako unapokelewa na nimeshaelezea. Mheshimiwa Mary Nagu pia amezungumzia suala la kuimarisha Mfuko wa Maji pamoja na uanzishwaji wa Rural Water Agency. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Anna Tibaijuka amezungumza kwa kirefu kuhusu ushirikishaji wa sekta binafsi. Ni kweli tukisema miradi yote hii itafanywa na Serikali na kwa kulingana na uhitaji jinsi ulivyokuwa mkubwa, tutakuwa na safari ndefu. Sasa wazo lako ni zuri na ndiyo maana tumeanza utaratibu wa PPP, lakini kwa mfumo kwamba unatafuta mfadhili anayejenga ana-finance lakini Serikali inafanya operation.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, anajenga, anamaliza kujenga, anakabidhi Serikali inaendesha. Kwa hiyo, sisi ndiyo tutakuwa na wajibu kuhakikisha ule mradi unaendelea kuwa endelevu. Kwa namna nyingine unakuwa umeshirikisha Serikali pamoja na sekta binafsi kwa utaratibu wa PPP, kwa maana ya building and finance. Kwa hiyo, ushauri wako ni mzuri, tutaendelea kuhamasisha wananchi ambao wanaweza kujitoa katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu unaweza ukaja tukazungumza kwamba wewe unazalisha maji, sasa namna gani tutakubaliana fedha yako itarudi, namna ya kuendesha mradi ule, basi tunakaa na Serikali imesharuhusu kwenye Sheria ya Manunuzi kwamba tunaweza tukatumia sekta binafsi kwenye miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lolesia Bukwimba amezungumza habari ya Jimbo la Busanda kwamba lina kero kubwa ya maji na hasa katika Kata ya Nyakagomba na Nyamigota. Katika mwaka wa fedha tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 3.280 kwa ajili ya Halmashauri yako ya Busanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa fedha hizi zitakwenda kujenga miradi ambayo Halmashauri yako imeweka ndiyo kipaumbele. Kama bado kutakuwa na miradi ambayo fedha hizo hazijatosha, basi ni mpango, mwaka utakaofata tutaendelea na kuweza kujenga miradi ambayo itakuwa bado haijashughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa William Ngeleja alisema mradi wa maji wa Katungulu ulianza kutekelezwa miaka minne, hadi sasa haujakamilika. Tulikuwa na matatizo kwa miaka mitatu mfululizo, fedha ambazo zilikuwa zinatengwa kwa ajili ya maji hatujawahi kupata zaidi ya asilimia 40 ya allocation.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza kuona kwamba kwa miaka mitatu yote mtiririko wake wa fedha haukuwa unaoridhisha na ndiyo maana unakuta miradi mingi tumeibua kama alivyosema Naibu Waziri, sasa tuna miradi zaidi ya 374 ambayo tayari mikataba imesainiwa na inaendelea. Kwa hiyo, jukumu letu sasa ni kuhakikisha kwanza tunakamilisha hiyo miradi ambayo tayari tulishaiibua kwa muda mrefu. Tunamaliza hiyo kwanza halafu tunaibua miradi mipya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameongelea suala la kwamba, miradi mingi huko nyuma inachukua maji kutoka Ihelela unapeleka Kahama, lakini wananchi wa Ihelela hawana maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya miradi yote ambayo tunaiibua sasa, lazima watu wanaokaa kwenye chanzo wafikirie kwanza kupewa maji ili wawe ni sehemu ya kulinda miradi hii. Kwa hiyo, tunabadilisha mfumo na ndiyo maana unasema miradi yote na kwenye bomba kubwa, wote wanaokaa kilometa 12, ni lazima wapewe maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, miradi iliyokuwa imeshajengwa tunaanza kwanza kuanzia kutoka mwanzo mpaka mwisho, kwa sababu kwanza, hawa watatunza chanzo ili chanzo chetu kiwe endelevu, kiweze kutumika kwa miaka mingi ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda wangu ni mdogo na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge naamini kabisa wamenielewa nilivyosema kwamba tusiwe na shaka na timu hii tuliyokuwa nayo, tutakwenda kufuatilia miradi na kuhakikisha inatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna wengine wamezungumza habari ya miradi inajengwa chini ya kiwango. Sasa kwa kweli nitakuwa mkali katika wahandisi wote kwenye sekta hii ambao watafanya miradi chini ya kiwango. Tutahakikisha tunafuatilia ili miradi yetu iwe endelevu. Kwa sababu kuanzia usanifu, ujenzi, matengenezo, yote lazima tufuate specification za kihandisi ili miradi yetu iwe endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakushukuru kwa nafasi hii. Naomba kwa heshima kubwa Waheshimiwa Wabunge mniunge mkono. Naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi uliyonipa. Nianze kwanza kwa kuishukuru Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa uongozi wake mzuri ambao umesaidia sana Wizara yangu katika kutekeleza majukumu ya kuwapatia Watanzania maji safi pamoja na kilimo cha umwagiliaji. Pia niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, wamezungumzia kwa uchungu kabisa matatizo ya wananchi wetu wanaokosa huduma ya maji hasa katika maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba hatujafikia malengo, ukiangalia Azimio Namba Sita la Umoja wa Mataifa linasema kwamba nchi wanachama wote wahahakikishe wananchi wao wanapata maji kwa asilimia 100 ikifika mwaka 2030. Sasa Tanzania ni mwanachama lakini sisi kwa nchi za Afrika tuliamua kwamba jambo hili la kuhakikisha kwamba tunawapatia wananchi maji safi na salama kwa haraka zaidi kuunda Umoja wa Mawaziri wa Maji katika Afrika ambao unajulikana kwa jina la AMCOW na Tanzania imepewa heshima ya kuwa Mwenyekiti kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2016 mpaka 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba Rais wetu ndiyo atakayekuwa anazungumzia suala la maji kwenye vikao vya Umoja wa Nchi za Afrika kwamba mmefanya nini. Mnajua jambo hili la kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji ni lazima tuwe na nguvu ya pamoja. Kama tulivyobuni katika Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwamba haitawezekana Serikali peke yake kuweza kufikisha huduma ya maji kwa wananchi wote ni lazima tuwe na nguvu ya pamoja ya Serikali, wananchi pamoja na washirika wa maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mwaka 2007/2008 mpaka Juni 2016 tulianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ya awamu ya kwanza. Washirika wa maendeleo pamoja na Serikali waliweza kuweka fedha kwenye mfuko kiasi cha bilioni 1.6 ni karibu trilioni 3.2, hizi ni fedha nyingi na tumeweza kujenga miradi mingi zaidi ya miradi 1,800 ili kuondoa hali ilivyokuwa huko mwanzo na sasa tumefikia mahali ambapo angalau wastani wa maji vijijini, wananchi wanapata kwa asilimia 72. Hii haina maana kwamba kila kijiji kina asilimia 72, viko vijiji vingine vina asilimia 30 na vingine vina asilimia 80. Sasa ukichukua wastani kwa kuangalia idadi ya watu wanaopata maji kwenye vituo ambavyo vimejengwa imefikia asilimia 72.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ambalo tunalipata ni kwamba Serikali imejenga miradi mingi lakini miradi mingi haifanyi kazi kama Waheshimiwa Wabunge mnavyosema. Serikali pia imeanza kubuni mradi mwingine wa kuhakikisha hii miradi iliyojengwa kwa fedha nyingi za Serikali iinakuwa endelevu na inafanya kazi. Tumefanya tathmini wastani wa asilimia 30 ya miradi mingi iliyojengwa haifanyi kazi. Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la DFID tumeanzisha mpango mwingine wa kuhakikisha miradi hii inakuwa endelevu, imetoa kama Euro milioni 80, bilioni 214 kwa kila kituo cha maji kitakachotengenezwa na Halmashauri wanapewa fedha zaidi ya paundi 1500. Mpango huu tumeshaupeleka nchi nzima kwa Halmashauri 185.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge tuzihamasishe Halmashauri zetu ziiingie kwenye mfumo huu ili miradi yote ambayo tayari tulishaijenga na tumetumia fedha nyingi iweze kufanya kazi na wananchi wetu waweze kupata maji. Ni Halmashauri 57 ndiyo zimeitikia wito huu, naomba Halmashauri zilizobaki pia ziingie kwenye mpango wa kujenga vituo vya maji. Ukishajenga kituo kimoja unaongezewa fedha na DFID ili kusudi uweze kujenga vituo vingi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika programu ambayo tumeanza Julai, 2016 awamu ya pili ya programu tayari washirika wa maendeleo wameweza ku-pledge kiasi cha dola bilioni 1.6 ambazo zitaingia kwenye utekelezaji wa miradi, katika vile vijiji ambavyo vilikuwa havijapata miradi tutaviingiza kwenye hii program. Tayari nimetayarisha mwongozo toka mwezi wa Julai, nitawapa nakala Waheshimiwa Wabunge kabla hamjaondoka muondoke na huu mwongozo wa kuhakikisha kwamba Halmashauri zetu kwanza zinakamilisha miradi iliyokuwa inaendelea na pia zinaanzisha miradi mipya ili kusudi tufikie hii mipango ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepita kwenye Halmashauri unakuta wanasema kwamba tunasubiri fedha, fedha haziwezi kuja kwa sababu hata zikija huna kitu cha kufanya. Unatakiwa uanze maandalizi, uweze kufanya manunuzi baada ya pale hela itakuja kwa certificate. Mfumo huu umetusaidia toka Januari mpaka Desemba tumepeleka shilingi bilioni 177 kwenye Halmashauri zetu kwa ajili yamaji vijijini na miradi mingi imekamilika sasa hivi wananchi wanapata maji. Tumeshafika zaidi ya asilimia 76 kwa sababu miradi inakamilika na wananchi wanaendelea kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana ndugu zangu tusibaki tunasema fedha haziji, fedha zinakuja kwa kazi maalum, haziwezi kuja zikakaa tu. Tumekuta baadhi ya Halmashauri wanazo fedha kwenye akaunti lakini hakuna wanachokifanya. Sasa nasema tuache ufanyaji kazi wa kimazoea, lazima kila wakati watu twende kwenye mfumo wa kutoa matokeo. Tukija kwenye mfumo wa kutoa matokeo nina hakika wananchi watapata maji kulingana na malengo ambayo Serikali imeweza kuweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema maji ni uhai, maji ni uchumi na maji pia ni utu. Hautaweza kujenga viwanda kama maji hakuna. Hivi vitu vyote lazima tufanye kwa pamoja. Najua kabisa Serikali inaweka bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuweza kuandaa miradi mikubwa. Kila mmoja alikuwa anasimama hapa anataka maji ya Ziwa Victoria, anataka maji ya mito mikubwa, tutakwenda kufanya vile jinsi tunavyojenga uwezo wa nchi. Hata hivyo, kwa kuanzia tulisema tuanze na miradi ambayo uendeshaji wake unaweza kufanywa na vijiji lakini jinsi tunavyoendelea…
Lazima Serikali tutaingia kwenye miradi mikubwa. Nitasema miradi michache ambayo kwa mwaka huu wa kwanza tumeweza kufanya.

TAARIFA.....

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, angenipa nafasi ili kusudi niweze kumuelewesha aweze kuelewa. Nimesema tulishatoa mwongozo toka Julai tulivyoanza mwaka wa fedha ambao unaelezea kila kitu kuhusu miradi inayoendelea pamoja na miradi mipya. Na mimi nitampa nakala ya mwongozo huo aangalie ili akasimamie Halmashauri yake nini cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mnielewe na mnikubalie kwa sababu tukianza kubishana hapa ndiyo maana miradi haiendi, naomba sana. Wabunge wote nitawapa mwongozo, nitawapa na taarifa ya utekelezaji wa programu ya awamu ya kwanza. Kwa hiyo, tumepeleka kwa maandishi na pia tumewafanyia semina hawa Wakurugenzi na Wahandisi wa Maji kuhusu jambo hili, lakini unafika mahali mtu bado anashangaa shangaa, haelewi cha kufanya. Sasa hayo ni majipu itabidi tuanze kuyatumbua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niseme baadhi ya mafanikio ambayo tumeweza kupata. Mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Ruvu, Ruvu Chini na Ruvu Juu umekamilika. Hivi sasa tunaweza kuzalisha maji lita milioni 502 kati ya milioni 544 zinazohitajika kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam. Tatizo letu tulilonalo lilikuwa ni mtandao na sasa hivi Serikali tunaendelea na kujenga mtandao maeneo yote ambayo hayana mtandao ili kusudi waweze kupata maji. Kwa mwaka huu wa fedha Serikali itaweka fedha zaidi katika kujenga mtandao katika maeneo ambayo hayana maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Ziwa Viktoria kupeleka Tabora, Nzega na Igunga mpaka Sikonge. Tayari tumeshapata mkandarasi, tumepeleka Serikali ya India tupate no objection ili tusaini mkataba, mkadarasi yule aweze kuanza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi pia wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Magu, Misungwi, Lamadi na kupanua maeneo ya Ilemela katika Jiji la Mwanza. Tarehe 16 tunasaini mkataba, Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo nawakaribisha tuje tusaini mkataba na kazi ile inaanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa kutoa maji ya Ziwa Victoria kupeleka miji ya Kagongwa, Tinde na Isaka, tayari mkandarasi tumeshampata tuko kwenye maandalizi ya kuweza kusaini mkataba na kazi ile itaanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umezungumziwa mradi wa milioni 500 wa Serikali ya India wa Mheshimiwa Deo Sanga, Mji wa Makambako, Muheza pamoja na ile Miji 17 ikiwa ni pamoja na Zanzibar. Hatua tuliyofikia mpaka sasa tuko kwenye hatua ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya usanifu wa kina na kutengeneza makabrasha ya zabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu tunavyoanza mwaka wa fedha 2017/2018 tender zitatangazwa na kazi ile itakwenda kuanza kufanyika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Deo Sanga pamoja na wale wote wa miji ile 17 tunakwenda kuikamilisha kazi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii uliyonipa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Bunge lako kujadili hoja hii kwa huo muda wa siku tatu. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia Wizara hii. Wabunge wapatao 193, zaidi ya nusu ya Wabunge waliopo hapa wamechangia kwa kuandika na wengine wameongea hapa. Walioweza kuchangia kwa maandishi wako Wabunge 102 na walioweza kuongea hapa ni Wabunge 91. Nawashukuru sana. Ushauri wenu wote mlioutoa, Wizara yangu itauzingatia katika utekelezaji. Naomba niwahakikishie, haya maandishi na majibu tutayatoa kabla ya mwisho wa Bunge hili. Kwa hiyo, kila mmoja atakwenda Jimboni kwake akiwa na majibu ya hoja zake alizokuwa amezitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza habari ya kugawana maji yaliyopo. Kama nilivyosema kwenye hotuba yangu, rasilimali za maji tulizonazo nchini ni kilometa za ujazo
96.27 ambapo tukigawana sisi kwa population ya nchi kila mmoja anaweza akatumia maji ya ujazo 1,800, lakini tumefanya utafiti na kufuatilia, maji haya tunategemea zaidi mvua. Hali ya tabianchi kama mnavyoona imekuwa inapungua mwaka hadi mwaka, kwa hiyo, hata rasilimali za maji zinapungua. Sasa sisi kama Serikali ni lazima tuwe na mikakati ya kuhakikisha tunaongeza rasilimali za maji nchini kulingana na mahitaji ili tuweze kuwagawia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuchukue hatua mbalimbali. Pamoja na hatua hizo tunazozichukua, Serikali ina mpango maalum wa kutunza vyanzo vya maji; kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuhakikisha vyanzo vinabainishwa, vinawekewa mipaka; tunatengeneza ramani pamoja na kuandaa taratibu za fidia kwa sababu baadhi ya watu tutawaondoa maeneo yale ambayo yana vyanzo vya maji na maeneo oevu. Hili naomba sana Waheshimiwa Wabunge tukubaliane kwamba lazima tuchukue hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuwa na mipango hii, tunaomba tutoe wito kwa Watanzania wote, tusiendelee kulia kwamba maji hakuna na tuna miradi mingi ambayo imejengwa kwa fedha nyingi za Serikali, leo haifanyi kazi. Haifanyi kazi kwa sababu vyanzo vile vilivyoainishwa, leo havitoi maji. Kwa hiyo, sasa ni lazima sisi tuchukue hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetembelea Mkoa mmoja, naweza nikasema Mkoa wa Rukwa nikakuta kuna chanzo ambacho kilikuwa kinatoa maji kwa vijiji kama vinne, lakini chanzo kile kwa sababu watu wamekivamia, ndiyo eneo wameweka la ufugaji ng’ombe, kwa hiyo, maji hakuna. Leo hawapati maji! Inabidi tuanze kutafuta tena njia nyingine ambazo ni gharama zaidi kwa Taifa ili kuwapelekea wananchi wale maji wakati maji yalikuwepo. Kwa hiyo, ni lazima tuchukue hatua kwamba wananchi washiriki katika kutunza na kulinda vyanzo vya maji lakini pia tutoe elimu ya kutosha, wananchi waache kulima na kufuga katika maeneo ndani ya mita 60 ambayo tumeainisha ndiyo vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwahamasisha wananchi kutumia teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua, hiyo itaongeza rasilimali ya maji kama mlivyochangia Wabunge wengi. Tumekuwa tunapata mvua, lakini maji yote yanakwenda baharini. Sasa tunaanza kuchukua hatua kwa mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na kwenye Taasisi zetu, kwenye shule, zahanati; hakuna sababu ya kuwa huna maji ya kuwahudumia wagonjwa wakati tunaweza tukavuna maji ya mvua kwenye paa la zahanati. Tumetoa mwongozo kwa Halmashauri zetu zote nchini sasa tuanze kuchukua hatua. Ikibidi tutunge Sheria ndogo ndogo za kudhibiti watu ambao hawatataka kufanya suala hili la uvunaji wa maji ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za muda mrefu Serikali imepanga kujenga mabwawa ya kimkakati, likiwepo Bwawa la Farkwa, Ndembela na Kidunda ili kuweza kuongeza rasilimali za maji. Pia tumetoa mwongozo kwa Halmashauri zetu kwamba tuwe na mkakati kwa kutumia mapato ya ndani tujiwekee ratiba wa kujenga bwawa moja kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki ni kitu kinachowezekana kwa mabwawa madogo madogo; tutaondoa tatizo la wafugaji wetu kuwa wanazunguka nchi nzima tatizo kubwa wanatafuta maji kwa ajili ya mifugo. Tukiwajengea mabwawa kwenye maeneo yao, migogoro ya wafugaji na wakulima itapungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wabunge wengi wamezungumza habari ya mifumo endelevu ya kuweza kuendesha miradi yetu ya maji katika maeneo ya vijijini. Wizara inaendelea na uandaaji wa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji kwa kutumia ofisi zetu za mabonde kama ya Rufiji, Ziwa Rukwa, Ruvuma na Pwani ya Kusini; Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na bonde la kati. Sasa hivi tunaandaa taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuweza kuajiri wataalam watakaosaidia mabonde haya katika suala hili la mifumo endelevu ya kusimamia rasilimali za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto za uendelevu za huduma ya maji, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na upatikanaji wa takwimu. Sasa hivi tunazungumza habari ya wastani wa upatikanaji wa maji 72.15%, lakini Kambi ya Upinzani wao badala ya kusikiliza takwimu za Serikali wanakwenda TWAWEZA. Sasa unamwamini TWAWEZA kuliko Serikali!

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, Waheshimiwa Wabunge, takwimu za upatikanaji wa maji zinaendana na uwingi wa watu wanaopata maji, siyo kwa wingi wa vijiji. Maana mtu anasema nina vijiji 100; vinavyopata maji viko 30. Kwa hiyo, anasema wastani ni hivyo. Haiendani hivyo! Tunaangalia wingi wa watu wanaopata maji kulingana na Sera yetu ndani ya umbali wa mita 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila kituo cha kuchotea maji tumeweka wastani wa watu 250. Kwa hiyo, kwa namna hiyo ndiyo tumetengeza takwimu, lakini bado tunaweza tukaboresha zaidi suala hili la upatikanaji maji, lakini usitumie TWAWEZA, kwa sababu TWAWEZA anaweza akamwuliza mtu kwa kupiga simu. Huwezi kufanya utafiti kwa kupiga simu. Sisi tunazo data. Nakubali kweli kuna miradi mingi ambayo ilikuwa inafanya kazi, leo ina changamoto kwamba maji hayatoki, lakini ni jambo la kufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye hotuba yangu, tumeshatoa mpango sasa wa kukarabati miradi yote ambayo haitoi maji. Payment by result, Serikali ya Uingereza imeweka fedha zaidi ya shilingi bilioni 200 na kitu kwa miaka mitatu kusaidia Halmashauri zetu kufufua miradi yote ambayo imekufa (ambayo haifanyi kazi). Kwa hiyo, mpango huu ni mzuri na nina hakika kwamba tukifufua miradi yote ya zamani tutakwenda vizuri na tutakwenda kweye data hizi ambazo tunazizungumza leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaahidi wananchi wetu kwamba ndani ya miaka mitano, ikifika mwaka 2020 Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha upatikanaji wa maji unafika asilimia 85 vijijiini na asilimia 95 mijini. Ndugu zangu huu ni mwaka wa kwanza wa Bajeti, ndiyo tumemaliza. Tunaandaa sasa mwaka wa pili. Kwa hiyo, hatuwezi kufikia asilimia 85 katika bajeti ya mwaka mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa kwanza tulipanga bajeti ya shilingi bilioni 915 kwenye maendeleo, lakini sasa kuna hatua mbili; kwanza unafanya manunuzi halafu unakwenda kwenye utekelezaji…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kumekuwa na hoja watu wanasema kwamba pesa zilizopangwa mwaka huu ni kidogo. Mimi nasema siyo suala la kusema kidogo, suala kubwa ni fedha kupatikana. Kwa hiyo, bajeti yetu ya mwaka huu ya shilingi bilioni 913, sisi kama Wizara tumeshafanya manunuzi. Fedha zilizotolewa zaidi ya shilingi bilioni 10 ambazo ni asilimia 19, ni zile ambazo tayari tumelipa certificates kwamba fedha hii
inakwenda kulipa kazi iliyofanyika. Fedha ambazo tayari tumeajiri Wakandarasi na tumeshasaini mikataba zaidi ya fedha hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tunakwenda kwa utekelezaji wa hiyo shilingi bilioni 915 na Serikali kwa commitment hiyo ni kwamba mpaka ikifika Juni; kwa sababu hii status ilikuwa ni mwezi wa Tatu; kuna mwezi wa Nne, wa Tano na wa Sita. Kwa hiyo fedha itatolewa na Serikali kama ilivyokuwa imepanga. Kwa hiyo, hakuna haja ya kuwa na wasiwasi wa hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya hilo, kuna hizi dola milioni 500 za kutoka Serikali ya India. Katika utaratibu wa upangaji wa bajeti, wakati mnaandaa zile ceiling, mara nyingi huwezi ukaiweka kwenye vitabu vya Hazina fedha ambayo bado hujasaini ule mkataba wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ambayo naomba niitoe ambayo tayari Kamati ya Madeni na Mikopo imeshaidhinisha fedha hii, kwa hiyo, fedha hii itakuja kupatikana katika mwaka wa fedha huu wa 2017/2018. Kwa hiyo, fedha ya Bajeti ya Wizara ya Maji itaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikubwa ambacho naomba na ambacho ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge nimeona, kwa kweli kila mmoja amekuwa analia na Jimbo lake. Naomba sana, tatizo kubwa tulilokuwa nalo ni utekelezaji ndani ya Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepeleka fedha za Mfuko wa Maji katika Halmashauri mbalimbali lakini mpaka leo kuna Halmashauri fedha zipo lakini hakuna walichokifanya. Sasa ndiyo maana tunafikiria kwamba ili tuweze kujenga miradi hii ya maji, lazima tuanzishe Mfumo wa Wakala wa Maji Vijijini ili tuwe na standard inayofanana katika utekelezaji. Kwa sababu mpaka leo yuko Mkurugenzi hajafanya manunuzi, anasubiri apelekewe fedha na tumetoa mwongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, tumewapa nakala za mwongozo kwamba hatutapeleka fedha, bajeti yetu ni cash budget. Tunapeleka fedha mahali ambapo kuna utekelezaji na ndiyo maana kumekuwa na hata uwiano wa mgao. Tumepeleka fedha, unaweza ukakuta mahali pengine zimekwenda fedha nyingi kwa sababu wana mradi, lakini sehemu nyingine utapeleka fedha nyingi mradi hawana, hawataki kubadilika wanataka kufanya kazi kimazoea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane katika kusimamia Halmashauri zetu ili tuendane na kasi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Ningeweza kusema maji hoyee, lakini ndiyo hali halisi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kabisa kuondoa tatizo hili la maji kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Mkutano wa Kimataifa ambayo tunasema lengo la sita la maendeleo endelevu wanataka kwamba tukifika mwaka 2030 tuhakikishe wananchi wetu wanaoishi vijijini na wanaokaa mijini wanapata maji kwa asilimia 100. Nataka niwahakikishie Bunge hili kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano itahakikisha tunafikisha lengo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imetolewa hoja ya kuboresha Mfuko wa Maji na hoja hii imetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Maji na Mifugo. Ni hoja nzuri na ilishatolewa hata kipindi kilichotangulia, lakini kulingana na Kanuni zetu, hatuwezi tukaamua humu ndani. Tutaipeleka kwenye Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kile kipindi cha siku saba, tutafanya mashauriano na kuona namna gani pendekezo la Wabunge la Kamati ya Bunge pamoja na Wabunge wengi wameunga mkono. Tutaona namna gani jambo hili linaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la mchango wa Mheshimiwa Kitwanga. Amechangia hapa kwa hisia kubwa kuonesha kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi haijafanya chochote kwa Wilaya ya Misungwi. Sasa nataka nimwulize Mheshimiwa Kitwanga kama yupo, labda yale maneno anasema ni ya kwake au ya wananchi; kwa sababu wananchi nitawaambia nini kimefanyika Misungwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tumesaini mikataba, Mkurugenzi wake na Mwenyekiti wa Halmashauri alikuwepo, tunasaini mikataba hadharani ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria Wilaya ya Misungwi, kwa fedha nyingi, zaidi ya shilingi bilioni 38.5, zinakwenda Misungwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anaposema anakwenda kuhamasisha wananchi wakabomoe huo mtambo wa Ihelele, maana yake analeta uasi au anataka asithamini kazi iliyofanywa na chama chake? Basi ajitoe kwenye chama! Eeh!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali imepeleka fedha, sasa leo maendeleo ambayo yameshafanyika ni lazima tuwahamasishe wananchi wetu. Kitu cha kwanza tuwahamasishe wananchi wetu kutunza miundombinu ambayo tayari tumeshafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ukasema miundombinu ambayo tumefanikiwa tukabomoe. Ukichukulia umeme kwa mfano, unatoka kijiji kimoja unaruka vitatu unakwenda cha nne, sijasikia mahali wanang’oa nguzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimwambie Serikali inaendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Misungwi na Usagara. Kwa upande wa Usagara, watapata maji yatakayosukumwa kutoka eneo la Nyashishi hadi kilima cha Usagara ambapo watazalisha maji kiasi cha lita milioni tatu. Hadi sasa usanifu wa awali unaojumuisha Buswelu umefanyika. Kwa hiyo, kazi hii itafanywa kwenye mwaka huu wa fedha, tumeshaweka fedha. Sasa akisema haungi mkono maana yake hii fedha shilingi bilioni 4.46 tupeleke Wilaya nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mji wa Misungwi, Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza tayari imesaini mkataba na mkandarasi wenye thamani hiyo ya shilingi bilioni 38 kwa ajili ya kupeleka maji katika Mji wake wa Misungwi. Tumepata ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo ya Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo Ufaransa. Sasa leo ukisikia mtu wa Misungwi anasema kwamba kwa kweli haithamini kazi ya Serikali ni kitu kinachosikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Misungwi, awamu ya kwanza ya mradi Serikali itajenga miundombinu ya maji kutoka Kijiji cha Mbarika kwenda Misasi kupitia Vijiji vya Lutaletale, Bugisha, Naya, Ikula, Sumbungu, Makale, Kasororo, Misha na Nabwawa. Kwa hiyo, miundombinu hii tayari imekamilika kwa fedha ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Vilevile zaidi ya shilingi bilioni
3.5 imepangwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingine katika Wilaya ya Misungwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kwa hisia sana kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo yao. Naomba Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla wao waunge mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto za upatikanaji wa maji nchini. Katika maeneo mengi nchini, miradi ya maji na umwagiliaji imeendelea kutekelezwa na ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji kama ilivyoelezwa katika hotuba yangu. Miundombinu iliyokamilika kujengwa ni mojawapo ya mafanikio ya Serikali na inabidi tushirikiane kuhakikisha inatunzwa ili wananchi waendelee kupata huduma inayokusudiwa na kwa ubora unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema sikutarajia sana kauli hii itoke kwa Mheshimiwa Kitwanga, mtu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya mgawanyo wa fedha usiokuwa na uwiano sawa kwenye Halmashauri. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, ni kweli hatujagawa sawasawa kwa sababu ya kasi ya utekelezaji kutofautiana. Kwa hiyo, suala hili tunalifanyia kazi lakini tumetembelea kila Halmashauri na kuwaelekeza mahali ambapo kuna matatizo ya wataalam tunatumia Mamlaka za Mikoa au Kanda kusaidia kuwaelekeza namna ya kufanya manunuzi na kuweza kusimamia miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu fedha za USD milioni 503. Kama nilivyosema, wakati tunafanya ceiling fedha hii tunaitarajia kwamba itasainiwa kabla ya mwisho wa mwaka huu. Kwa hiyo, bajeti yetu ya maji itaruka toka shilingi bilioni 600 na itakwenda zaidi ya shilingi trilioni 1. Kwa sababu hii fedha ya USD milioni 503 tayari imeshaidhinishwa na Kamati ya Madeni na Mikopo. Tunatarajia mkataba utasainiwa kabla ya Juni kwa sababu Kamati ya Mikopo imeshaidhinisha na itakuja kuonekana kwenye bajeti ya 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee hoja moja ya Kambi ya Upinzani kuhusu tenda ya miradi ya Ziwa Victoria kwenda Tabora na Nzega. Mwasilishaji wa hoja hii ya Kambi ya Upinzani anasema kulikuwa na harufu ya rushwa. Nataka kwanza nimhakikishie harufu ya rushwa labda iko upande wake kwa sababu katika taratibu za manunuzi za tenda wakati mkiwa kwenye mchakato kuna stage fulani mkifika mnataka sasa kupata aliyeshinda huwa kunatolewa muda wa kutosha kwamba kuna mtu mwenye malalamiko anatakiwa apelekwe kwenye mamlaka za PPRA na PPA. Waziri wa Maji hawezi kuingilia kwenye mchakato ya tenda, hii hairuhusiwi na pia hairuhusiwi kwenda kwenye magazeti. Mchakato huu uliandikwa hata kwenye magazeti mtu analalamika anakwenda kwenye magazeti, sasa leo wanawatumia Wabunge kulalamika, hiki kitu hakikubaliki. Ni lazima twende kwenye kanuni na taratibu za manunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, manunuzi yamekwenda vizuri na tumepata wakandarasi wazuri na kila hatua tulioifanya tunawasiliana na mwenye fedha Exim Bank. Kama kuna kampuni imeonekana imetumia rushwa kule India haruhusiwi kupata kazi ile, kwa hiyo sisi tunapeleka kwake. Kama kungekuwa kuna jambo ambalo halikubaliki na Serikali ya India wangesema, Serikali ya India wametoa No Objection kwamba endeleeni. Sasa ndugu yangu wa Kambi ya Upinzani yeye hili analitoa wapi? Sasa mkandarasi ameshapatikana, tayari tumeshasaini mkataba na anakwenda kuanza kufanya kazi. Namshauri aunge mkono fedha zile zifanye kazi ili kuleta maendeleo kwa wananchi waliokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee kidogo kuhusu masuala ya azma ya Serikali kuboresha huduma ya maji safi kwa Jiji la Dar es Salaam. Kama tulivyosema tumeshaongeza uzalishaji kutoka lita milioni 300 kwa siku sasa tumefikia lita milioni 504 kwa siku. Mheshimiwa Mnyika maeneo mengi aliyosema ya mabomba ya Mchina leo yana maji. Ninayo taarifa ya leo kwamba maji yanatoka. Tatizo lililopo mabomba ya Mchina yamekaa muda mrefu hayakuwa na maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna watu sehemu zingine waliamua kutoboa na tatizo tulilonalo sasa ni umwagikaji ovyo wa maji katika mabomba haya lakini kazi hiyo ndiyo tunayoishughulikia ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu katika maeneo yale ambayo hayakuwa na mtandao. Kuna mkandarasi ameshaanza kufanya kazi Changanyikeni kwenda mpaka Bagamoyo kuongeza mtandao. Pia tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia nao watajenga mtandao maeneo mengine. Kwa hiyo, tunaendelea kutafuta fedha na kwenye bajeti hii tumeweka fedha za kujenga mitandao katika maeneo yale ambayo hayana mtandao. Kwa hiyo, maji yapo mengi na ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika maji yanayotokana na visima vya Kimbiji na Mpera tunategemea kupata lita milioni 260. Katika mwaka huu wa fedha tunategemea tujenge sasa mtandao wa bomba la kuleta maji maeneo ya Kigamboni na maeneo mengine yote ambayo hayana maji kwa upande ule. Kwa hiyo, Serikali inafanyia kazi suala hili na hayo matatizo madogo madogo ya kuvuja na kadhalika ndiyo kazi inabidi tuifanye. Ndiyo maana sasa hivi tunataka tuimarishe sana Shirika la DAWASCO kwa ajili ya kupeleka maji kwa wananchi. Kwa sababu DAWASCO kwa utaratibu uliokuwepo anakwenda kushughulikia kuwasha mitambo sisi hatutaki afanye kazi hiyo. Tunataka tufanye maboresho, yeye ashughulike na wateja moja kwa moja, aende kwa Mheshimiwa Mnyika ili tupeleke maji haya kwa wateja wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa, wananchi waliounganishiwa maji kwa Dar es Salaam hawazidi 300,000 tunataka sasa wafike 1,000,000 ili waweze kuchangia gharama za uendeshaji. Nimeshawaambia hiyo ndiyo kazi ya kufanya tupate wananchi wengi waliounganishwa na maji safi. Pia tuna miradi ya majitaka, mfumo wa majitaka kwa Dar es Salaam kwa muda mrefu ulishakuwa hakuna na wananchi chini ya asilimia 20 ndiyo ambao wameunganishwa na maji taka. Tumepata fedha toka Korea Kusini pamoja na Benki ya Dunia tunakwenda kujenga mitambo ya kisasa ya kusafisha maji taka kwa ajili ya Jiji letu la Dar es Salaam. Kwa hiyo, ndugu zangu tumeahidi na tunatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimwambie Mheshimiwa Mnyika na Wabunge wengine wa Dar es Salaam maeneo ambayo sasa maji yanapatika. Ukichukulia kwa mfano Temeke, maeneo ya Kurasini Beach, Baraza la Maaskofu, Mtoni, Sabasaba, Mtoni kwa Kabuma, Temeke Wiles, Temeke Quarter, Temeke Sokota, Temeke Veterinary, Temeke Sandali, Temeke Mwembe Yanga, St. Mary’s Mbagala, VETA na Rangi Tatu. Haya maeneo yalikuwa hayana maji lakini sasa yana maji. Ukija kwa Kimara, Stop Over kwa Koleza, Kimara Bakery, Kimara Polisi, Michungwani, Mbezi Igubilo, Kimara, TANESCO, Kimara B Bonyokwa, leo maeneo haya yanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija sehemu za Ilala, maeneo ya Buguruni Mnyamani, Buguruni Sokoni, Buguruni Rosana, Buguruni Y2K, Sharifu Shamba Bondeni, Kipata Kariakoo, Uhuru kuanzia round about to Lumumba, Illala Bungoni, Mtaa wa Mafuriko, Amani Kariakoo leo wanapata maji maeneo yote yalikuwa hayana maji. Ni kazi kubwa inafanyika ndugu yangu Mheshimiwa Mnyika. Eneo la Tabata Mbuyuni, Ogongombelwa, Kilumi Chang’ombe, Banebane, Vigunguti Darajani, Segerea, Tutundu, Makaburi Mwasaka, Vigunguti, Kwamnyamani, Maji Chumvi Kasukuru, Msamvu Street, Kibangu Ubungo, Segerea kwa Bibi, Kisukuru Chumba Kimoja na Kibangu Unovo leo wanapata maji. Kwa hiyo, kazi kubwa tumeshafanya kwa kuboresha huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam. Ni lazima tuthamini kazi ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa msukumo mkubwa anaoutoa kuondoa kero hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema maeneo yale mengine ya pembezoni haya sasa tunaendelea na utaratibu wa kuongeza mtandao. Naamini tutafanikisha kwa sababu maji yapo. Tuna tatizo la upotevu wa maji na ndiyo maana tunasema DAWASCO sasa tunataka a-concentrate na distribution pamoja na kudhibiti upotevu wa maji, tuachane naye na kwenda kuwasha mitambo kila siku kule Ruvu Chini, Ruvu Juu kazi hiyo itafanywa na watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna muda basi nafikiri naweza nikaongezea baadhi ya hoja, kuna Mradi wa maji Kishapu. Hii ilikuwa hoja ya Kamati ya Bunge, kazi ya usanifu wa miundombinu ya kusambaza maji katika Mji wa Kishapu imekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumziwa mambo mengi lakini kama nilivyosema tutajibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, habari ya umwagiliaji Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea kwa kirefu sana. Miradi hii ilikuwa inashughulikiwa katika Programu ya Maendeleo ya Kilimo. Sasa sisi Wizara ya Maji kazi yetu kubwa ni kushughulika na ujenzi wa miundombinu na miundombinu mingi iliyokuwa imejengwa ni kweli tumekuta ipo hovyo. Awamu hii inabidi tuanze pale walipoanzia wenzetu tuweze kurekebisha na tumeanza kuainisha maeneo ambayo yanatakiwa yarekebishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimepitia miradi mingi na Naibu Waziri amepitia miradi mingi. Kazi yetu mwaka huu wa fedha wa bajeti tulisema tuirekebishe miradi ile ambayo iko tayari inafanya kazi kabla ya kujenga miradi mipya lakini pia kufanya usanifu wa miradi mipya ambayo inaendana na ujenzi wa mabwawa. Hii ni kazi ambayo tutaendelea nayo katika bajeti hii na tumeweka maeneo mengi kwenye bajeti ukisoma hotuba utaona maeneo mengi tumeelezea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba hapa kwenye umwagiliaji tunahitaji uwekezaji zaidi kama Taifa. Mwaka wa kwanza hatukuweza kuweka uwekezaji wa kutosha, mwaka wa pili hatujaweza kuweka pia uwekezaji wa kutosha lakini nina imani mwaka utakaofuata tutaweka uwekezaji wa kutosha wa kujenga miundombinu ili tujiondoe kwenye tabu hii ya kuwa na njaa kila mwaka. Najua katika hizi hekta milioni 29 ambazo zinafaa kwa umwagiliaji tukiziendeleza hatutakuwa na tatizo la chakula. Pia tutaelekeza na aina ya mazao ya kulima ili kusudi kwa sababu wengi wanafikiri kuondoa njaa ni kulima mahindi tu na mpunga.
Lakini tunaweza kulima mahindi tukamwagilia. Kwa hiyo, nadhani sasa kama Taifa tuweke rasilimali na wanaoweza kuweka rasilimali ni Wabunge mnaoidhinisha bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza kwa kirefu sana masuala ya umwagiliaji. Nami nakubaliana naye kabisa na namuunga mkono amesema vizuri sisi Wabunge ndiyo tunaopanga bajeti sasa tuwekeze zaidi kwenye umwagiliaji kwa ajili ya kujiondoa katika tatizo la chakula maana ndiyo kitu cha msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihitimishe kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni yenu na mapendekezo mliyotoa. Niwahakikishie msiwe na wasiwasi, Wizara ya Maji ina bajeti ya kutosha ya kutekeleza miradi tuliyopanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba sasa nitoe hoja kwamba Bunge lako liingie kwenye Kamati ya Matumizi na kuweza kuidhinisha bajeti hii ili twende kutekeleza tuliyojipangia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Watanzania wetu wanapata maji safi na salama na pia wanaendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nitoe masikitiko yangu kwa Mbunge mwenzetu kushambuliwa na majambazi. Kwa kweli, tunampa pole sana na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kumsaidia apone haraka aje afanye kazi zake za Kibunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wenu kwa namna mlivyochangia, hakuna hata mmoja aliyepinga kwamba tusiianzishe hii Kamisheni ya kuendeleza Bonde la Mto Songwe. Nashukuru kwa sababu siyo kawaida, mara nyingi kuna wengine wanapinga tu hata mazuri, lakini kwa leo angalau kwa namna moja au nyingine wote wameunga mkono kwamba hii Kamisheni ni muhimu ianzishwe kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu walioko kwenye Wilaya tano. Katika Wilaya hizi tano vijiji 48 vitanufaika na miradi hii ambayo imeibuliwa kwa manufaa ya nchi zote mbili upande wa Tanzania na upande wa Malawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kwa maoni ambayo yametolewa na Kamati ya Bunge, yote haya katika mkataba huu ambao tumesaini kati ya Malawi na Tanzania, vifungu hivi vyote viko very flexible kwamba hakuna kifungu ambacho hakina namna ya kurekebisha. Madaraka yote ya kurekebisha vifungu hivi tumeipa lile Baraza la Mawaziri. Baraza la Mawaziri la pande zote mbili watakuwa na uwezo wa kuongeza jambo lolote jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba mambo mengi mazuri haya ambayo mmeyaleta Waheshimiwa Wabunge, tutaangalia namna ya kuyapeleka katika kuboresha mkataba wetu ili uweze kuleta manufaa zaidi ili tuweze kuendeleza bonde hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa sababu hawa wananchi wa vijiji 48 ambao ni zaidi ya 315,000, kwanza watapata umeme wa uhakika. Kwa awamu ya kwanza ambayo tunajenga Bwawa la Songwe Chini ambalo litaweza kutoa megawati 180 Tanzania tutaanza na mgawo wa Megawati 90 ambazo tutaziingiza kwenye gridi ya Taifa. Kwa sababu azma yetu ni kupeleka umeme vijijini kwa sehemu kubwa, hivi vijiji 48 nina hakika kwa mpango huu watapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hizi hekta 6,000 za kilimo cha umwagiliaji. Wakati madhara ya mto huu ulivyokuwa unafurika mara kwa mara, hata hiki kilimo cha umwagiliaji kilikuwa kinakuwa tatizo kwa sababu mashamba ya wananchi maeneo ya Kyela na Ileje, yalikuwa yanajaa maji kiasi ambacho iliathiri sana kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yale. Tukija kuboresha sasa tukajengea miundombinu ambayo imeboreshwa, nina hakika sasa kutakuwa na kilimo endelevu na tunainua uchumi kwa ajili ya wananchi wanaoishi maeneo haya. Kwa hiyo, ni kama wengine walivyosema, kwamba mkataba huu umechelewa, ungekuja mapema zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tujue kabisa kwamba tumeanza kuzungumza uanzishwaji wa kitu cha namna hii toka mwaka 1976, lakini tumekuwa tunapanda ngazi kidogo kidogo. Tulipofika mwaka 2001 ndiyo tukaanzisha ile Kamisheni ya Mpito au Interim Secretariat ambayo nayo imefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kujenga hii Ofisi ya Makao Makuu hapo Kyela. Kwa hiyo, ofisi tayari ipo imeshajengwa; na tutaanzia pale katika kusimamia sasa miradi hii iliyoibuliwa itakayoleta manufaa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lissu alikuwa na mashaka, alifikiri kwamba katika kusaini mkataba huu alienda Lwenge peke yake. Naomba nimtoe wasiwasi kwamba hakwenda Mheshimiwa Lwenge peke yake, ilikwenda kama Serikali ikiwa na wataalam wote waliobobea katika sheria, akiwepo Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, masuala ya sheria yote yamezingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Olenasha amefafanua vizuri namna ya kutekeleza miradi inayokuwa inashirikisha zaidi ya nchi moja, lakini katika kutatua migogoro, hili suala la kwenda kwenye SADC au UN, hiki ni kitu cha mwisho kabisa. Tumeweka hatua ya kwanza na kwa maelewano tuliyokuwanayo katika miaka yote hii hatufiki huko, kwa sababu kazi tunayoifanya ni ya manufaa kwa nchi zote mbili. Ndiyo maana nasema kwamba sasa tunaimarisha uhusiano wetu kwa nguvu zaidi kwa ku-develop miradi inayotunufaisha Malawi na Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata hili suala la mgogoro wa mpaka au mgogoro wa Ziwa Nyasa nina hakika tumeanza vizuri kwa sababu hiki kitakuwa ni kichocheo kimojawapo ambacho kimetuunganisha zaidi Malawi na Tanzania katika kufikia muafaka wa jambo hili ambalo linazungumzwa la matumizi au rasilimali za Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wetu una namna ya kutoka kama nchi moja ikionekana inakiuka makubaliano, tumesema kwenye Kifungu cha 18 kwamba nchi moja inaweza ikavunja mkataba inapoona mwenzie hatekelezi yale tuliyokubaliana kwa kutoa notice ya miezi sita kwa maandishi, kwa hiyo, kuna namna ya kutoka, lakini sitaki tukifike huko kwa sababu hatuwezi kutoka na kwa sababu pia, hii miradi ambayo imeibuliwa ya kujenga umeme na miradi mingine, tayari wafadhili wameshaonesha nia, kama nilivyowasilisha pale mwanzo. Wameshaonesha nia ya kutusaidia ili tuweze kuendeleza Bonde hili la Mto Songwe kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme tu kwamba maoni yote ambayo Waheshimiwa Wabunge mmetoa, tutaendelea kuyaboresha. Kwenye Council, katika zile Wizara sita, kuna Wizara ya Fedha pia ipo. Kuna mmoja alikuwa anataka kuhakikishiwa kama kuna wataalam wa fedha watakuwepo. Wizara ya Fedha ni mojawapo katika Wizara ambazo zinaingia kwenye Council, kuna Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na Wizara ya maji. Ila kwenye Mkataba wetu tumeweka nafasi ya ku-opt advisor yeyote au Wizara yoyote ambayo tunafikiri kwa muda ule tunapokuwa tunajadili tunaweza tukamwingiza kwenye Council ili kusudi aweze kusaidia, kutegemea ni jambo gani tunalolishughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkataba uko vizuri, uko flexible. Kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa namna mlivyochangia, niwashukuru tena kwa maana kwamba sasa tunakwenda kuanzisha hii Kamisheni ambayo itatusaidia kwa maendeleo ya wananchi wetu wa pande zote mbili. Pia, tutaondoa huu wasiwasi wa wananchi wetu ambapo mto kila mara ukifurika walikuwa mara wanakuwa Malawi, mara wanakuwa Tanzania; ili kusudi waweze kufanya maendeleo endelevu, sasa watakuwa na uhakika wako Tanzania na wameshaendelezwa, wameshapata mahitaji mengi ya kuwainua kiuchumi. Kwa hiyo, nina imani kabisa baada ya utekelezaji wa mradi huu, tutakuwa na jambo la kujivunia kwa kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Songwe kwa faida ya nchi zote mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, nirudie tena kukushukuru wewe kwa namna ulivyoendesha mjadala huu. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote mbili kwa namna walivyochangia; na nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wengine ambao pia wameweza kuchangia na kuunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, kwa heshima kubwa naomba kutoa hoja ili Kamisheni hii sasa iweze kuanzishwa, ya Ushirikiano Kati ya Malawi na Tanzania kwa ajili ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naunga mkono hoja kwa sababu naamini malalamiko ya wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe yaliyo na Pori la Akiba la Mpanga – Kipengere litafanyiwa kazi na Waziri.

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Waziri ukurasa 69 imeelezwa kuwa Wizara inaweka beacons upya kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI na wananchi.

Mheshimiwa Spika, ushirikishwaji wa kazi hiyo haupo kwenye Pori la Akiba la Mpanga – Kipengere na taarifa hii nimemwambia Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii lakini hakuna hatua iliyochukuliwa TANAPA, bado TANAPA wameendelea kuweka beacons ndani ya vijiji vilivyoandikishwa kisheria. Jambo hili limeleta adha kubwa kwa wananchi hasa vijiji vya Iyayi, Igandu Hanganani, Ludwega, Mpanga, Malangali, Wangamiho, Masage na kadhalika. Naomba zoezi hili lisimamishwe ili ushirikishwaji wa kutambua mipaka ya awali iweze kutambuliwa ili kuondoa hofu kwa wananchi kwenye Serikali yao.

Mheshimiwa Spika, iliwahi kutolewa kauli ya Serikali katika kuondoa migogoro ya mipaka kuwa kuna Kamati ya Wizara ya Ardhi, Maliasili na TAMISEMI inayopitia kila hifadhi au Pori la Akiba zote nchini ili kutatua matatizo ya mipaka na vijiji vilivyoandikishwa na kuwekewa GN. Kazi hiyo sasa ni miaka mitatu sijawaona wakipita katika pori hili la Mpunga – Kipengere na hivyo kusababisha mgogoro huu kuwa mkubwa zaidi na kufanya wananchi wa jimbo langu kurudi nyuma katika kufanya kazi za maendeleo kwenye maeneo yao kwa kujenga mashule, zahanati na kilimo.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara hii iangalie upya haja ya kuwa na Mapori ya Akiba kwenye maeneo wananchi wameongezeka sana na itafika muda wananchi watakosa ardhi ya kuishi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii kwa hotuba yake nzuri na naunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Wanging‟ombe haina shule kidato cha tano na sita pamoja na shule za Mount Kipegere, Makoga, Wamihe na Wanging‟ombe kukidhi vigezo vyote vya kuanza masomo ya high level. Naomba Waziri alitolee maamuzi yanayostahili. Pia shule za Philip Mangula, Maria Nyerere, Mt. Kipegere, Makinga, Wanike, Wanging‟ombe, Igachunya, Luduga, Saji, zinayo mabweni na hivyo zipandishwe hadhi ya kuwa shule za bweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Wanging‟ombe ina upungufu mkubwa wa Walimu katika shule za msingi na sekondari. Kwa upande wa elimu ya sekondari hatuna Walimu wa hisabati na masomo ya sayansi. Naomba Wizara hii ituangalie kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujengewa Chuo cha Ufundi cha VETA eneo la Soliwaya - Wanging‟ombe kwani hatuna hata chuo kimoja kwenye Wilaya hii ya Wanging‟ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya awali kwa shule nyingi imekosa Walimu wa kufundisha kutokana na upungufu wa Walimu. Tatizo hili limetokana na hivi sasa wazazi kuacha kuchangia kuwalipa Walimu hawa kwa hiyo, Serikali ione maana ya kuelimisha kuhusu uchangiaji kwa maeneo yenye mahitaji kama hili la upungufu wa Walimu na hasa elimu ya awali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii ili Wizara hii itekeleze miradi iliyopanga pamoja na kujibu hoja zangu ambazo naziwasilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Muhongo na timu yake yote ya Wizara kwa utendaji uliotukuka kwenye utekelezaji wa REA Phase II. Wilaya ya Wanging‟ombe kuna vijiji vinahitaji transformer tu na LV line ya kilomita moja mpaka mbili ili wananchi wapate huduma ya umeme. Niliwahi kumwandikia Waziri lakini hadi leo hakuna utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji hivyo ni Lusisi, Ihanja, Idindilimunyo, Luduga sekondari, Igelehedza, Mpuhilu, Igelango na Ipunda. Majibu niliyopewa toka REA ni kuwa quantities za mkataba wa REA phase II zimekwisha. Sasa swali langu, je, mradi mlioanzisha REA kutoa umeme kupeleka Kijiji cha Itengelo ambacho hakikuwepo kwenye mpango wa REA II zimetoka wapi na kwa nini REA wanaanzisha miradi bila kuhusisha uongozi wa Serikali ya Wilaya pamoja na Bunge?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atekeleze ombi hili la wananchi wa Wilaya ya Wanging‟ombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nashauri ni kwamba, TANESCO wasipokee mradi huu mpaka wajiridhishe pasipo shaka kuwa umekamilika kufuatana na mkataba. Yapo maeneo mengi kama Imalinyi, Kanani, Ludinga nguzo zimewekwa lakini hakuna waya. Pia yapo maeneo zilifungwa transformer za size 50 ambazo zimekuwa zikiungua mara kabla ya kutumika. Zaidi ya transformer 40 kwa Mkoa wa Njombe zimebadilishwa baada ya kuungua. Specifications ziangaliwe upya kama ndizo sahihi kwani zimekuwa zinaungua hasa wakati wa mvua na radi. Sasa hivi ni kiangazi tatizo hili halipo, lakini mvua zitakaporudi linaweza kujirudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Wanging‟ombe ina vijiji 106. Katika mpango wa REA phase II na phase I ni vijiji 42 tu ndivyo vina umeme. Naomba mpango wa REA phase III Serikali ipeleke umeme kwenye vijiji vilivyobaki ambavyo ni takribani vijiji 64.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naunga mkono hoja hii na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hoja mengi yana dira nzuri kwa maana ya msimamizi wa sheria. Tatizo langu ni namna watendaji na hasa wanaosimamia hifadhi ya maeneo wanapochukua sheria mikononi na kupigana, kushambulia wananchi. Wanahisiwa kuingia ndani ya maeneo hayo, Jimbo langu lina mgogoro katika maeneo mawili yaani Hifadhi ya Kipengere na Mpanga Game Reserve, vijiji vinavyopakana na maeneo haya vya Moronga, Kipengere, Masage, Wangana, Ikunga na Imalilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawana amani na maeneo yao, pamoja na kuwa vijiji hivi vimeidhinishwa na vina ramani ya mpaka jinsi wanavyonyanyaswa na Kipengere Forest Reserve.
Aidha, vijiji vya Malagali, Mpaga, Ludunga, Mambegu, Hamjarami, Igando, Iyayi, Mayole na Mpanga Game Reserve wananchi walihamishwa wakalipwa fidia kidogo na kuhamishwa wengi hata fidia hawakulipwa. Naomba sana viongozi walioko hifadhi hii ya Mpaga waondolewe kwani wameshindwa kabisa kufanya kazi na viongozi wa Wilaya, Serikali na Vijiji na Mbunge wa Wilaya ya Wapingale kwa namna wanavyochukua sheria mkononi kwa kuwapiga wananchi, kufyeka mazao na kuwanyang‟anya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wanachukua rushwa, tumewakemea na Waziri nilikueleza, lakini mpaka leo hakuna hatua iliyochukuliwa. Naomba na wakati hilo halijafanyika wape maelezo viongozi wa hifadhi hizi, waache mara moja kuwashambulia raia kwenye nchi yao ili tulishughulikie tatizo la mpaka. Ili kuondoa migogoro hii pamoja na sheria lazima ziwe na manufaa kwa binadamu na uhifadhi ili sheria iwe endelevu. Sheria ilitungwa na Mipaka iliwekwa miaka mingi baada ya uhuru, wakati idadi ya watu ilikuwa ndogo tofauti na sasa, lazima wananchi wetu waongezewe eneo na hasa haya maeneo ya akiba ambayo hata wanyama hawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 51 nimesoma kuwa Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori umesaidia miradi ya kijamii kwenye Wilaya ya Wanging‟ombe kwa kujenga Ofisi ya Kata ya Wanging‟ombe, kuchimba kisima Mayale, na kununua vitanda 91 vya shule ya bweni sekondari Ilembula. Kwanza nashukuru kama kweli limefanyika, naomba kujua kiasi cha fedha zilizopelekwa au thamani ya vifaa kwa kila mradi.
Pili, utekelezaji wa msaada huu hufanyika vipi kwani mimi kama Mbunge ndiyo kwanza napata taarifa hii kwenye kitabu cha hotuba, sijawahi kushirikishwa wala kwenye Halmashauri ya Wanging‟ombe hatujawahi kushirikishwa. Sasa hii kama fedha ya umma kwa nini ifanywe siri kwa ajenda gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate maelezo ya kina.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wafanyakazi wote wa Wizara hii kwa kazi wanayoifanya na kuliletea Taifa letu sifa kubwa. Hotuba ni nzuri na naunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Wanging’ombe ina changamoto kwenye eneo la barabara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza barabara ya Njombe – Mironga – Makete (kilomita 109). Hii ni ahadi ya Ilani ya Chama Tawala. Mheshimiwa Rais aliwaahidi wapiga kura wangu kwamba wakimpa kura na akaingia Ikulu itakuwa ni barabara ya kwanza kuanza kuijenga. Ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa yuko Ikulu na barabara hii haijaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Njombe (Ramadhani) – Iyayi (kilomita 74). Barabara hii ni ya muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Njombe na hususan Wilaya ya Wanging’ombe. Barabara hii ilifanyiwa usanifu tangu Mwaka 2014 lakini sijaona kwenye Randama ya 2017/2018 kutengewa fedha za kujenga. Ni lini barabara hii itatengewa fedha za kujenga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Halali – Ilembula – Igwachanya - Itulahumba (kilometa 35). Barabara hii ni ya wilaya na nimemwomba Mheshimiwa Waziri kwamba ipandishwe daraja au ihamishiwe kwa Wakala wa Barabara (TANROADS). Barabara hii ni kiungo cha hospitali ya Ilembula (DDH) na Makao Makuu ya Wilaya (Igwachanya). Barabara hii ilifunguliwa na TANROADS kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara tangu mwaka 2013 kwa maombi maalum. Sasa barabara hii kwa takriban miaka minne haijapata routine maintenance. Naomba sana Mheshimiwa Waziri ombi langu lifikiriwe kwani sijaona kwenye Randama kutengewa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Wizara hii eneo la Makao Makuu ya Wilaya ya Wanging’ombe hayana mawasiliano ya uhakika ya simu. Mnara wa Vodacom umewekwa lakini hauna nguvu kabisa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijachangia, naomba nimtangulize Mungu mbele kwa kumshukuru sana kwa kunipa afya na hekima. Kwa kuwa natambua kwamba maandiko yanasema katika mambo yote tutangulize dua na sala na Bunge lako huwa tunaanza na dua na sala na mahali popote unapomtaja Mungu tunasema lazima umtaje katika roho na kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mbunge unapotoa mchango wako ni lazima umtangulize Mungu ili akupe hekima uweze kuchangia vitu ambavyo vitatupeleka mbele. Kwa hiyo, naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wake kwa namna walivyoleta hoja hii. Hoja imeandikwa vizuri sana, inatoa matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua kwamba ili tuweze kufikia uchumi wa kati lazima tuweke nguvu yote kwenye uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, ni jambo moja zuri, lazima tumuunge sana mkono Rais wetu ili tufikie azma hiyo ya uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme tu kwamba katika viwanda ambavyo tunavizungumza, kweli vipo vingi; nimejaribu kuangalia karibu nusu ya kitabu ina orodha ya viwanda lakini unaweza ukaona uhalisia wa uchumi wa viwanda na uchumi wa kipato cha mtu mmoja mmoja. Tanzania wananchi walio wengi ni wakulima na tunaweza tukawasogeza mbele kama tutawekeza viwanda ambavyo vitasaidia sana wao kuuza mazao yao ili waweze kuwaongeza kipato walichonacho. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Mwijage katika orodha kubwa aliyokuwa nayo hapa, ajaribu kuangalia na kuweza kulea viwanda vile ambavyo vinasaidia sana wakulima wetu kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Wanging’ombe asilimia 90 ni wakulima wa mahindi na viazi mviringo. Wakulima hawa hawana soko la kuuza mazao haya ya viazi. Katika viazi kuna tatizo sana la vipimo. Kuna Wakala wa Vipimo, nimesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wanasema wanashughulikia namna ya kusimamia vifungashio. Wakati wa mwanzo walikuwa na vifungashio vikubwa ambavyo wanajaza vile viroba vikubwa vya lumbesa ambapo ukipima kwenye kilo ni zaidi ya kilo 100 ambayo ipo kwenye sheria. Hata hivyo, usimamizi wake ni mgumu sana kwa sababu wafanyabiashara wanatanguliza mawakala ambao wanakwenda kuwarubuni wakulima kule mashambani. Naomba hii Wakala itafute mbinu za kusimamia jambo hili, kusiwepo na kurubuni wakulima katika kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchezo mwingine ambao wanafanya wanasema wewe Wanging’ombe usipouza viazi wanakwenda kununua Mporoto au Arusha ambapo wanaweza kuuza kwa vipimo hivi vya lumbesa. Nafikiri kwa sababu huu Wakala upo basi uwajibike ili wakulima wetu wauze viazi kwa kilo siyo kwa vipimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wameleta viroba vidogo ambavyo vinaweza kujaza debe tano. Sasa ili gunia litimie unajaza viroba viwili na lumbesa yake. Kwa hiyo, unakuta kwa wastani kunakuwa na debe kumi ambazo wanasema hizi sasa ndiyo kilo 100 kwa vipimo. Kwa hiyo, tukiweza kwenda kwa kipimo cha kilo, tutafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingine ambavyo nafikiri navyo tungevifanyia kazi ni viwanda vya mazao ya pamba, korosho, chai, kahawa, pareto, mahindi, mpunga na alizeti. Kwenye Jimbo langu tuna viwanda viwili; kimoja kinazalisha sembe, kinaitwa Mbomole Investment Company. Kile kiwanda hakizalishi kwa kiwango kikubwa kwa sababu tu TANESCO wameshindwa kutoa transformer ya KVA 200 kwa zaidi ya mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda kingine kimewekezwa pale cha kukamua mafuta ya alizeti kinaitwa Wende Investment Company. Hiki nacho kimeisha mwaka mzima lakini TANESCO wameshindwa kutoa transformer ya KVA 200. Sasa inawezekana mifano ya namna hii iko maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri kama anavyokimbia hivi, nilifikiri ni vizuri viwanda hivi ambavyo vimeshaanzishwa visaidiwe. Wananchi wetu tumewahasisha wananchi wetu walime sana alizeti kwa sababu kiwanda kipo, najua watapata mahali pa kuuza lakini kama kinakuwa white elephant kwa sababu ya transformer tu, basi Serikali ni moja, uweze kuona namna ya kuwasiliana na Mheshimiwa Dkt. Kalemani tupate transformer, wananchi wangu wapate mahali pa kuuza hiyo alizeti na transformer nyingine kwa ajili ya wananchi wangu kuuza mahindi ili waweze kuinua kipato chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uuzaji wa mahindi imeoneka ni ngumu sana kwa sababu kipindi fulani Serikali ilikuwa imefunga mipaka lakini nashukuru sasa mmefungua. Hata hivyo, kuna urasimu sana katika kuuza mahindi nje ya nchi au maeneo mengine. Tuwasaidie kwa viwanda hivi ambavyo vinaanza kuibuka kwa kuwezesha mambo kama ya umeme na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nichangie pia suala la kuinua uchumi. Nchi nyingi ambazo zimeendelea zilianza na viwanda vinavyohusiana na chuma. Tanzania tumezungumza habari ya Liganga na Mchuchuma kwa karne, kuanzia awamu ya kwanza ya Serikali zetu hizi lakini hakuna kinachoendelea. Unajua ukisema umtegemee Mchina, naye anataka kuinua uchumi wa nchi yake hataweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka uamuzi wa Rais uje kama wa Stiegler’s Gorge kwamba sasa tunaamua kujenga Stiegler’s Gorge, basi tuamue na kujenga Mchuchuma kwa namna yoyote inavyowezekana. Nina uhakika tutakuwa hatulii umaskini kwamba hatuna maji na vitu vingine, tunaweza kujitegemea wenyewe kama tulivyoanza kujenga reli. Nilifikiri kwamba nishauri na ndiyo maana naunga mkono hoja hii ili unisikie vizuri na ukalifanyie kazi kusudi Tanzania kweli ifike azma ya kuwa na uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambalo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kwamba hapa Dodoma kuna mwekezaji mmoja alianzisha kiwanda cha kutengeneza hizi ceiling boards kwa kutumia gypsum na malighafi yake inatoka Dodoma hapa hapa, kipo hapo Kizota na Mheshimiwa Waziri nilishawahi kumwambia. Mwekezaji yule ameshindwa kukiendeleza kile kiwanda kwa sababu ya ushindani wa soko. Tatizo lipo kwa wafanyabiashara ambao wanaleta semi-finished goods, wanasema hii ni gypsum ghafi lakini kumbe ni finished goods ambazo sasa wao hawalipii kodi. Sasa hiki kiwanda kimefungwa na huyu mtu ameamua kuondoka. Aliwekeza fedha na wananchi wa Dodoma walikuwa wamepata ajira na Serikali inakosa kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie suala hili ili kusudi mwekezaji yule akifungue hiki kiwanda cha Dodoma na kama kuna kodi ambazo zipo kwa mujibu sheria, basi yeye anasema hana tatizo kulipa kodi, lakini kwa nini watu wengine wanasamehewa kodi kwa finished products, wanadanganya kwamba wanaleta malighafi ya gypsum? Tutakuwa tumeendeleza sana Mkoa wetu wa Dodoma ambao sasa ni makao mapya ya Serikali. Kwa hiyo, naomba kumshauri Mheshimiwa Waziri walifanyie kazi jambo hili kiwanda kile kifufuliwe ili kiweze kuleta ajira kwa wananchi wetu na Serikali pia itapata kodi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, nashukuru sana kwa nafasi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu na pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, naomba nitoe pole kwa wananchi wangu wa Wanging’ombe kwa kufiwa na watu mashuhuri, makada wa Chama cha Mapinduzi. Tumefiwa na Diwani na Katibu Kata wa Kata ya Igima. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu hawa mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu. Waziri na Katibu Mkuu wote ni ma-engineer, nategemea kabisa ma-engineer hawatatuangusha katika kulifikisha Taifa hili kwenye uchumi wa kati. Tutafanikiwa kufikia uchumi wa kati kama Wizara hii imekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba hii, kwa kweli sijaridhika nayo. Kwa jinsi sekta hii ilivyo kubwa lakini hoja iliyoletwa ni kidogo sana na mambo mengi ya msingi yameachwa. Tukumbuke tulio wengi hapa ni watoto wa wakulima na kama Wabunge wote tulioko humu hatujawazungumzia wakulima inavyotakiwa kuhusu matatizo wanayopata kuanzia kupanda mbegu, hawana mbegu bora na hawapati kwa wakati; ukija kwenye kukuza mmea hawapati huduma ya ugani na viuatilifu; ukija kwenye soko ndiyo kabisa. Kwa hiyo, unakuta maeneo yote haya ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia mazao ambayo Mheshimiwa Waziri amewasilisha hapa, sijaona mkakati wowote wa kusaidia wakulima wa mahindi na kuna mikoa karibu kumi inayolima mahindi. Kama alivyosema mwenzangu aliyetangulia kwamba sasa hivi hatusemi mambo ya subsistence farming, yaani kilimo cha mahindi siyo kwa chakula tu, ni pamoja na biashara. Tunategemea Serikali imuwezeshe mkulima wa mahindi ambaye hana zao lingine aweze kujikomboa kwenye uchumi. Kama kuanzia kulima hajasaidiwa, inapofika kuuza ndiyo Serikali inasema tunataka food security, unazuia asiuze mahindi yake, tutakuwa tumemsaidia vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana NFRA iliweza kununua mahindi Mkoa wa Njombe lakini mwaka huu hawakuonekana kabisa. Wananchi wanauza debe moja Sh.2,000 mpaka Sh.3,000, kiasi ambacho hataweza kununua mbolea na kupeleka mtoto shule yaani maisha ni magumu kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Serikali hii ni ya wananchi lazima tuweke kipaumbele katika kuwasaidia wananchi hawa waweze kujikomboa na kuona faida ya kuwa na Serikali yao ambayo inasikia. Naamini kabisa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imesikia hili na najua tutafanya marekebisho. Mheshimiwa Waziri wakati atakapohitimisha bajeti yake alete kitu ili wakulima wa mahindi wampigie makofi. Mambo ya kuzuia mpakani watu wasiuze mahindi, hii haitusaidii, hatuwezi kutoka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua Waziri ni mkulima na mwaka jana nilimfuata kulima mtama, tumelima mtama pamoja nawe lakini mpaka leo hatujauza. Hapa nimeona kuna mkakati wa kuongeza zao la mtama, hivi tutalima mtama halafu iwe nini kama hatuwezi kuuza, magunia yamekaa yanaharibiwa na wadudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwenye eneo hili, pamoja na kwamba wewe ni rafiki yangu lakini tusifanye ngonjera, tunasema tunazalisha mtama kutoka tani 2,000 mpaka 3,000 halafu zitafanya kitu gani? Wanasema watahamasisha sekta binafsi waje wawekeze viwanda, lakini jambo hili ni long process, huwezi kulifanya katika msimu wa mwaka mmoja, kwa sababu watu tayari wamelima. Kwa hiyo, nafikiri tuwe na mkakati fulani ambao unamsaidia mkulima kuanzia ku-plan alime zao gani na asaidiwe vipi. Kama alivyosema mwenzangu pale, mnaleta mikorosho Dodoma inakauka, hivi kwa nini Serikali tusiwe na strategy kama tunawasaidia wakulima wa Mtwara na Lindi basi tungeweka nguvu yetu kule, huku kwingine tuweke nguvu kwenye mahindi, sehemu nyingine tuweke nguvu kwenye mpunga, nadhani kwa namna hiyo tutaweza kuwatoa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Wanging’ombe tunalima sana viazi na tunaanza kupanda Julai, mbolea inaanza kufika Oktoba wakati wameshamaliza kupanda, sasa mkulima umemsaidia hapo? Halafu tuna tatizo kubwa la ugonjwa wa ukungu wa viazi, kuna dawa ambazo zinaletwa kule hazijatatua tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hawa Maafisa Ugani wanafanya kazi gani? Sehemu nyingi nimeona Maafisa Ugani hawafiki kwa wakulima. Mimi ni mkulima lakini sijawahi kumuona Bwana Shamba anakuja kunitembelea kwenye shamba langu na nafanya hivyo kwa sababu nataka shamba langu liwe shamba darasa, wakulima waone Mbunge wao naye analima anavuna kiasi gani kwa heka, sasa huyu Afisa Ugani hafiki na mnaendelea kuwaajiri. Mimi nafikiri hawa watu kwa kweli kama ndiyo ufanyaji kazi wa namna hiyo, nimeona sehemu nyingi hawa Maafisa Ugani wanashughulika na mashamba yao, hawafiki kwa wakulima, kwa hiyo hatuwezi kutoka hapa tulipo. Tuna miaka zaidi ya 50 ya uhuru, tunataka tuone kilimo kinakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hili Shirika la NFRA, nimeona kwenye kitabu kwamba mwaka huu mna mpango wa kuongeza ununuzi wa mahindi kutoka tani 18,000 mpaka tani 26,000, lakini hamjaonesha hivi mahindi yaliyopo nchini ni kiasi gani ili tuweze kupima ufanisi wa NFRA. Mimi nachojua ni kwamba bajeti mnayoweka ya ununuzi wa mahindi ni kidogo na ndiyo maana umeweka tani kidogo lakini umetuficha kujua hivi nchi nzima tunazalisha mahindi kiasi gani, ndiyo tungejua ufanisi wa mpango wa hii NFRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeona kwamba kuna mpango wa kuongeza uzalishaji wa pareto. Kwa miaka ya 60 Mkoa wa Njombe tulikuwa tunaongoza kwa ulimaji wa pareto lakini wananchi wale wameacha kulima kwa sababu hakuna soko. Sasa nani atalima pareto kama hakuna soko na hivi tutapataje foreign exchange kama hatulimi pareto? Pareto ni zao moja ambalo linaingiza sana mapato ya fedha za kigeni. Kwa hiyo, mngeonesha mkakati namna gani tutawahamasisha wananchi warudi kulima pareto ili tuweze kuongeza pato la nchi. Kwenye kitabu hiki ambacho nimesema hakina maelezo ya kutosha, hakielezei kabisa mkakati wowote wa kukuza mazao haya ili tuweze kuongeza uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wetu wa Njombe wenyewe tunajiongeza, tunalima kilimo cha parachichi.

Parachichi imeonekana ni zao moja ambalo kwa kweli soko linakuja, watu wanatoka Kenya nakuja kununua parachichi. Kwa hiyo, tunaomba Wizara iji-zero in kwenye zao hili la parachichi, mtusaidie masuala ya viuatilifu na namna ya kusindika zao hili. Naamini Mikoa ya Njombe na Mbeya itatusaidia kutoka hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda tunaweza tukafanikiwa tu kama utakuwa-based zaidi na mazao ya wakulima. Kama tunajenga viwanda vile ambavyo vitakuwa vina-process mazao ya wakulima, nina uhakika kwamba hata soko litajiongeza. Kama hatujaweka mkakati wa kuwasaidia wakulima katika mazao ambayo ni specific, yana watu ambao wanawekeza kwenye viwanda, ndiyo tunaweza tukawasaidia. Kwa hiyo, naomba utakapokuwa unahitimisha hoja yako ulizungumzie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia masuala ya kukuza kilimo, hatuwezi kuendelea kukuza kilimo kwa kutegemea hili jembe la mkono. Ni lazima tuanze na mashamba makubwa (commercial farming). Sijaona katika kitabu hiki akiongelea kwa ufanisi commercial farming, hatuwezi kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia machache kwenye mwongozo wa mpango wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimwia Waziri, Naibu Waziri pamoja na wataalam kwa kutuletea mapendekezo ya mpango. Tunapata nafasi ya kuchangia kwa sababu kuna kitu kilicholetwa. Kwa hiyo, nawapongeza, mmeleta maeneo mengi ambayo manafikiria kwamba tukiyatekeleza haya yatakwenda kujibu haja ya wakulima na wafanyabiashara wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango mzuri ni ule ambao hautaleta manung’uniko kwa wananchi. Tunasema kwamba uchumi unakua na pia wananchi wetu wameweza kuzalisha chakula cha kutosha ndiyo maana nchi inakuwa na amani, kama kuna njaa nchi haiwezi kuwa na amani. Pamoja na kuwa na hali hiyo ni vizuri tuangalie hawa wakulima ambao wametufikisha katika hali ya kuwa na utulivu, maana wanalima, hasa wakulima wa mahindi, wamelima miaka miwili mfululizo lakini hakuna anayewasemea wapi watauza mahindi yale na ndio maana kuna hii ziada. Kwa hiyo, mpango huu tunaoutengeneza ni lazima uende kujibu kwamba sasa mazao yao yatanunuliwa kama tunavyozungumzia mazao mengine ya biashara, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mapendekezo ambayo nafikiria ni kwamba ili mpango huu uweze kutekelezwa ni lazima tuone ni namna gani tutaongeza ukusanyaji wa mapato. Katika mapendekezo yaliyoletwa ni kwamba mwakani tunatarajia tukusanye shilingi bilioni 23, kwa maana ya TRA pamoja na Halmashauri zetu, sasa hii mradi ambayo tumeshaweka mikataba ni lazima tuhakikishe kwamba mikataba ambayo imeshasainiwa tunaitafutia fedha zake tuweze kutekeleza. Sehemu kubwa ya fedha hizi, kama alivyosema, zinatokana na mapato ya ndani. Kama hatuna mikakati mizuri ya kupata fedha hizi tutakuwa tunaingia mikataba halafu tunashindwa kulipa mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi tumeingia mkataba kwa mfano miradi ya umeme kupeleka vijiji 555, ni jambo zuri lakini haiendi kwa kasi kwa sababu wakandarasi wale hawalipwi ama hawalipwi kwa wakati. Tumeingia miradi mingi kwenye upande wa maji wakandarasi wengi kwenye miradi mingi hawalipwi certificate zao. Kama tunakuwa na mpango mzuri lakini hatuwezi kuwa tunawalipa wakandarasi mwisho wake inakuwa kwamba hatujibu haja ya wale wananchi kwamba wanapata maji na huduma nyingine ambazo zinatarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba katika miradi ya kipaumbele ambayo ameielezea kwenye ukurasa wa 34, iko kama 14 lakini nafikiri tuibadilishe. Mawazo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni mengi, tuwe na namna ya kuweza kubadilisha vipaumbele vilivyowekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kipaumbele cha kwanza ambacho wananchi wetu wanategemea sana ni ile miradi ambayo tuliwahamasisha wananchi wachangie nguvu zao kujenga zahanati, madarasa na maabara, ni miaka saba Serikali haijapeleka fedha. Nadhani hiki ndiyo kiwe kipaumbele cha kwanza ili wananchi hawa waone kweli tunatengeneza mpango ambao wananchi wanaukubali pamoja na kulipa madai ya kazi ambazo zimeshafanyika hasa za wakandarasi na yale madeni ya ndani, hiki kingekuwa kipaumbele cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha pili, katika miradi ile 14 nafikiri mradi wa kwanza ungekuwa wa kujenga Liganga na Mchuchuma, kingekuwa ndiyo kipaumbele chetu katika fedha tutakazokuwa tumezipata. Tumeuzungumza mradi zaidi ya miaka mitano lakini hatuoni hatua zinazoelezeka kwa wananchi kwamba Serikali inafanya nini. Tunazungumza miaka yote, hivi kuna tatizo gani mradi wa Liganga na Mchuchuma hauwezi kutekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunataka Tanzania ya Viwanda, hatuwezi kuwa na viwanda bila kuwa na chuma chetu. Kwa hiyo, nafikiri mradi huu uchukue nafasi ya kwanza katika ile miradi mingine ya kielelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, miradi ile ambayo tayari Serikali imeshaweka mkataba, tunaipongeza sana Serikali kwa ujenzi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma tayari mikataba imesainiwa, fedha zake zile lazima tuzitenge. Isifike mahali wale wakandarasi wanasimama kwa sababu hawalipwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Mradi wa Stigler’s Gorge, mkataba umeshawekwa fedha yake iwepo katika mpango huu. Pia na miradi ya REA nayo ni muhimu fedha zake ziwepo tuwe na uhakika. Ile mikataba ambayo imeshasainiwa fedha ziwepo. Viwanda vinavyohusiana na kilimo vipewe kipaumbele cha kwanza kwa sababu hizo ndizo shughuli ambazo wananchi wengi wanajihusisha na kutakuwa na mzunguko wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeamua Dodoma kuwa Makao Makuu, sasa Dodoma iwekewe kipaumbele katika miradi ya kuondoa msongamano. Imetajwa Dar es Salaam na Mwanza lakini tuanze na Dodoma maana tusipotengeneza sasa hizo Flyover na barabara za mchepuko tutakuja kuwa na tatizo hapo baadaye. Kwa hiyo, nilifikiri hilo jambo liwekwe kwenye vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu namna ya kupata fedha, ndiyo TRA inajitahidi lakini peke yake haitaweza kukusanya mapato tunayohitaji kuweza kutekeleza miradi hii. Kodi za nyumba (property tax) mmeamua TRA wakusanye lakini kwa ukiritimba wao hawataweza kukusanya kodi hii. Nafikiri Halmashauri zetu za Wilaya zikusanye hii property tax. Mheshimiwa Rais, alisema kila nyumba Sh.10,000, ni kitu rahisi kwa wale wa Tawala za Mikoa kukusanya fedha hizi kuliko TRA. TRA wanakwenda kufanya valuations kiasi kwamba mtu hawezi kulipa kodi zile. Kama alivyosema Mheshimiwa Rais nyumba za kawaida shilingi 10,000 na ghorofa shilingi 50,000, tukikusanya fedha hizi tuna mahali pa kuanzia. Kwa hiyo, nafikiri kwamba Halmashauri wakusanye kwa niaba ya TRA ili tuweze kuongeza mapato na kuweza kutekeleza mipango hii tuliyojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, pamoja na kwamba umeleta mpango mzuri lakini mawazo ya Waheshimiwa Wabunge uyaweke na utakapoleta majumuisho tuone ni jambo lipi ulilolipokea. Maana haya yanayoongelewa miaka yote huwa yanaongelewa lakini tujue ni lipi umelipokea na tuone maboresho ya mpango huu ili uweze kutekelezwa na kukidhi haja ya Watanzania wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Nianze kwa kutoa masikitiko yangu makubwa; kwanza nitoe pole nyingi sana kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa mauaji ya kikatili ya watoto ambayo yametokea. Kihistoria kabisa kwa Mkoa wa Njombe, Mkoa wa Njombe unajulikana ni mkoa wa amani na kwa miaka mingi hatujawahi kusikia vitu kama hivyo. Kwa kweli naomba sana, kutokana na kauli ya Mheshimiwa Waziri, kwamba wamejipanga vizuri kuweza kukomesha jambo hili. Naomba nitoe wito kwa wananchi watoe ushirikiano wa kutosha, kufikia watu wote ambao walikuwa na mipango ya kutaka kuchafua Mkoa wetu wa Njombe, mkoa ambao ni wa amani, ambapo tunawakaribisha wawekezaji waje kuendeleza mkoa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Kamati ya Ulinzi, Mambo ya nje na Usalama; niseme tu naiunga mkono kwa sababu mimi ni mjumbe pia na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, hasa wa Mambo ya Ndani kwa namna alivyotoka kwenye uninja na kwenda kuwa kamanda. Waziri Kangi Lugola, anafanya kazi nzuri na Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri na vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Tuviunge mkono, tuweze kushirikiana nao ili kusudi wafanye kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwa upande wa Nishati, niipongeze sana taarifa ya Kamati. Katika ukurasa wa 11 wamezungumzia maoni ya aina tatu; kuna suala la upelekaji wa fedha za mradi, kuna suala la vijiji vinavyorukwa na tatu kuna suala la kufungwa mashine umba zile transformer ambazo hazikidhi viwango. Kwa kweli Waziri wa Nishati na Naibu wake wanafanya kazi nzuri sana na pia ni wasikivu. Hata hivyo, nataka kusema pamoja na hiyo Wabunge tunapotoa ushauri tunataka wafanye vizuri zaidi ili ikifika mwaka 2020 basi tuwe na vijiji hivi vilivyolengwa kupatiwa umeme viwe vimepata; maana ukikuta mpinzani anakusifia, basi wala ujue kabisa huyu anakukebehi, lakini ukikuta, wa CCM anakusifia basi ana maana kweli umefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana, katika changamoto ambazo zimeelezwa na Kamati, kitu kikubwa watumishi wa REA wanapokwenda vijijini, hawapiti kwa viongozi wa vijiji. Kwa hiyo unakuta wanaleta orodha ya vijiji lakini unakuta vijiji vinaandikwa ni vijiji lakini halisi ni vitongoji. Sasa vitu kama hivi ni kwa sababu hawafiki pale; halafu pili wananchi wanashindwa kujua taarifa ya ratiba ya mradi. Kwa mfano, ukichukulia Wilaya ya Wanging’ombe; nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri amefika, ameona kabisa kasi ya utekelezaji wa mradi ule si nzuri. Tuna miaka miwili lakini ni vijiji saba tu na vitongoji ndivyo vimewashwa umeme, kati ya vijiji 38 vilivyolengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kushauri kwamba zile changamoto ambazo zinafanya utekelezaji uwe hauendani na kasi Wizara izichukue na kuzifanyia kazi na pia hii changamoto ya vijiji na vitongoji kuwa kuchanganywa ni kwa sababu tu hawaendi kwa viongozi wa vijiji, basi naomba jambo hili lirekebishwe ili kusudi tutakapokuja kwenye REA phase III, awamu ya pili, turekebishe yale maeneo ambayo yamerukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika REA Phase III unakuta vijiji vile ambavyo vilikuwa na umeme tangu awamu ya kwanza hawajanufaika na hii ya kulipa Sh.27,000. Kwa hiyo ili wanufaike na Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi naomba kwamba katika mzunguko wa pili hata vile vijiji ambavyo vilikuwa vimepata umeme kidogo, basi nao waingizwe kwenye mradi wa REA ili nao wanufaike na hii tozo ya Sh.27,000; kwa sababu hayo ndiyo niliyoona kuwa ni malalamiko ya wananchi wengi kule vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nikubaliane na hoja za Kamati. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na kuweza kufanya mambo ya kuwasaidia Watanzania katika kujiletea maendeleo. Awali ya yote nitoe pole nyingi kwa msiba wa Dkt. Reginald Mengi, ni kweli kwamba maandiko yanasema hakuna mji udumuo na kwamba kila nafsi itaonja mauti. Basi naomba kifo cha Dkt. Mengi kiwe ni fundisho kwa sisi tulio baki kwam ba iko siku yetu na kila mmoja ataulizwa nini amefanya kwa ajili ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza sana Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na viongozi wote kwa namna wanavyoiongoza Wizara hii. Wilaya ya Wanging’ombe haina hospitali ya wilaya, nishukuru katiak bajeti ya mwaka huu fedha zimetolewa, tumeanza kujenga hospitali ya Wilaya na nafikiri kufika mwezi wa Saba tutakuwa tumemaliza. Lakini pia nishukuru kwa uboreshaji wa vituo vya afya viwili, kituo cha Wa nging’ombe pamoja na Parangawani. Wananchi wale walikuwa wameanza kujenga kwa nguvu zao na Serikali imewaunga mkono. Basi naomba kwa sababu wameshamaliza, vifaa tiba na vifaa vinavyohitajika pamoja na wahudumu wa hospitali zile waweze kuleta m apema ili huduma ya afya iweze kufanyika.

Mheshimwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2018/19 na kwa sababu Serikali ni moja, na nimemuona Mheshimiwa Dkt. Mpango yuko hapa, kulikuwa na ahadi ya kutolewa karibu billioni moja kwa kila halmashauri ili kukamilisha maboma ya vituo vya afya pamoja na shule za msingi. Fedha ile haikutolewa mpaka leo na sisi tulikuwa tumewahamasisha wananchi wamejenga maboma kwa wingi kweli kweli. Wilaya ya Wanging’ombe tunavyo vituo vya afya saba, zahanati 13, wodi za wazazi mbili, nyumba za waganga tatu ambazo kukamilisha kwao kunahitaji karibu bilioni 2.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wale walikuwa wanategemea sana fedha ile itoke. Naomba sana kabla ya Bunge hili sisi ili tusionekane tunawadanganya wananchi. Tujitahidi Serikali iweze kuleta fedha hizi ili kwa juhudi hizi ambazo wananchi wanaendelea kuunga mkono kazi nzuri anayofanya Dkt. John Pombe Magufuli, basi fedha zile zitoke tuweze kukamilisha majengo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Awamu ya Nne, Rais Dkt. Kikwete aliahidi gari la wagonjwa katika kituo cha afya cha Makoga. Sasa ni miaka sita gari lile halijapatikana. Najua Serikali yangu ni sikivu, basi naomba sana gari la wagonjwa lililoahidiwa na Rais liweze kutolewa kwa kituo cha afya cha Makoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie pia katika hoja ya Waziri, kwanza pia nimpongeze nimeona pamoja na kwamba yeye ni Waziri wa Afya, amekuwa anashiriki katika ujenzi wa bweni la watoto wa kike katika sekondari ya Kilale katika Jiji la Tanga. Basi nimtakie kila la kheri hiyo azma aliyonayo katika wananchi wa Tanga. Lakini nikukaribishe pia kule Wilaya ya Wanging’ombe tuna shule ya wasichana ya Maria Nyerere na tuna tatizo la bwalo, basi naomba pia ukiweza kuja kuhamasisha wananchi tutafurahi sana ukitembelea wilaya ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia Bima ya Afya kwa wote, ni kweli katika eneo hili nafikiri tufanye kazi ya ziada zaidi. Hizi bima za afya ambazo zinatolewa katika kiwango cha kaya inakuwa haikidhi kupata matibabu wakienda kwenye hospitali zingine. Sasa nilifikiri huu mpango wa kuleta hii sheria tuwe na Bima ya Afya kwa wote. Kwa kweli naiunga mkono na ningeomba jambo hili lifanywe haraka. Lisichukue muda mrefu ili kusudi wananchi wote wapate huduma za afya mahali popote watakapoweza kwenda katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za afya zinazotolewa na Bima ya Afya kwenye hotuba amesema ni asilimia 8 tu ya Watanzania wote na hii nyingine ni asilimia 25 tu. Kwa hiyo, inakuwa haitoshi, kwa hiyo wananchi wengi wanapata shida katika kuweza kupata huduma kwa kutumia Bima za Afya. Pia kuna ahadi kwamba wazee wanaokuwa na zaidi ya miaka 60 watapata matibabu bure. Mipango ya kutoa hivi vitambulisho inakwenda polepole sielewi kwanini kwa sababu katika wilaya yangu hakuna hata mzee mmoja aliyepewa kitambulisho cha kupata matibabu bure na inawezekana na wilaya zingine hali kama hiii na tumeisema kwa muda mrefu. Kwa hiyo naomba sana mharakishe katika mpango huu kuhakikisha wazee wetu kweli wanapata tiba.

Mheshimiwa Mwenyekti, pia nipongeze utaratibu kwamba mna makazi ya wazee wasiojiweza 17. Basi naomba sana yaboreshwe makazi haya na wapate huduma zote ambazo ni za msingi wazee wetu ambao wameta mchango mkubwa sana kwa ujenzi wa Taifa hili. Tusiwaache wanakuwa ombaomba na Serikali yetu sikivu na ina uwezo wa kufanya mambo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba sana suala hili la wazee ulipe umuhimu wa pekee. Pia kwenye hizo hospitali ni kweli liwepo dirisha maalum, wazee wakifika pale wasikilizwe kwanza kabla ya watu wengine. Hili ni jambo ambalo litakuwa jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja hii na ninakubaliana na mawazo yote ya Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara hii kwa kweli imepata wanaoweza kuleta ufanisi mkubwa. Waziri na Naibu kwa kweli mnafanya kazi nzuri. Mnajibu maswali mazuri, kila mtu huwa anaridhika katika majibu yenu. Nashukuru kwa kupata nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa hotuba yake nzuri na kwa kuwasilisha Mpango mzuri ambao ni sehemu wa miaka mitano ambao tulipitisha Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo nampongeza sana. Pia naomba nipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo kila moja anaona. Kwabhiyo hata kama yupo anayebeza, anabeza kwa sababu zake, lakini vitu vinavyofanyika vinaonekana wazi wazi. Kwa hiyo niwapongezeni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitajikita zaidi kwenye suala la miundombinu. Katika Mpango ambao umewasilishwa, vipaumbele vimewekwa lakini katika hivi vipaumbele kuna eneo la ujenzi wa barabara za lami na nchi nzima tumeona barabara za lami zinajengwa, barabara za mkoa na barabara kuu zinazounganisha kati ya mkoa na mkoa. Naomba sana kwamba ili kusudi barabara hizi ziweze kudumu ni lazima tuweke mkakati mzuri wa matengenezo yake, tuongeze bajeti ya matengenezo ya barabara hizi ili isiwe barabara inajengwa baada ya miaka miwili inafumuliwa tena inajengwa nyingine. Ili tuweze kufikia maeneo yote ya nch, tuwe na mkakati mzuri wa matengenezo. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iongeze fedha kwenye fuel levy kwa ajili ya kupeleka Wakala wa TANROADS na TARURA ili barabara zetu ziweze kujengwa. Tumeanzisha TARURA tukiamini kwamba TANROADS ilifanya kazi nzuri, lakini ilifanya kazi nzuri kwa sababu tuliweka fedha ya kutosha ya matengenezo, kwa hiyo tuweke nguvu sana kwenye matengenezo ya barabara zetu hizi ili ziwe sustained.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba Mkoa wetu wa Njombe ukumbukwe kwenye barabara kuu ambazo ni muhimu ambazo hazijawekwa kujengwa kwa lami, kwa mfano, kwa barabara inayotoka Njombe Makete ifike mpaka Mbeya na barabara kutoka pale Ramadhani ifike mpaka Lyai iunganishe na barabara kuu ya Tazam highway.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba sana katika mpango huu tumeona kwamba kuna usambazaji wa umeme vijijini na kazi nzuri sana inafanyika. Mwaka jana nimechangia, nilisema katika usambazaji wa umeme maeneo mengi ambayo hata yameshajengewa miundombinu yamekuwa siyo sustained kwa sababu kwa muda mfupi unakuta nguzo zimeanguka au transform zimeungua, lakini sababu kubwa kwamba hatuweki bajeti kubwa ya matengeneo. Kwa hiyo naomba sana tuweke bajeti kubwa ya matengenezo katika miundombinu ya umeme ili kwamba hivi vijiji vyote zaidi ya 8,000 vimepata umeme, basi tufurahie kwamba tumeshapata maendeleo unajua mambo ya miundombinu ni kama mishipa ya damu ndiyo uhai wa mwili wa mwanadamu, basi miundombinu hiyo tuliyoijenga kwenye Taifa letu ni lazima iwe imewezeshwa sana hasa kwenye eneo hili la matengenezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nichangie ni suala la Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mwaka jana pia wengi wamechangia, mradi huu tumeuzungumza miaka mingi toka mwaka wa kwanza wa Mpango huu tumezungumza Mradi wa Liganga na Mchuchuma lakini mpaka leo hakuoneshi progress naamini katika hii sehemu ya mwisho ya mpango huu tutaweka nguvu kubwa, kama ni mradi wa kielelezo, kama ni mradi wa kipaumbele tuone utekelezaji wake tusiishie kusikia bado hatujalipwa hata fidia, sasa huu mradi kama kweli tumeamua kuujenga tuweke nguvu. Taifa lolote haliwezi kuendelea kama hakuna chuma, chuma ndiyo malighafi mama ya viwanda na sisi ndiyo tunasema tunajenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo lazima tuweke nguvu katika kutekeleza Mradi huu wa Liganga na mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie, ni sekta ya afya. Ni kweli Rais wetu ameamua kwa nguvu kubwa kujenga vituo vya afya 352 na hospitali za wilaya 69, ni jambo jema mimi nampongeza sana. Naamini kabisa Taifa lolote lazima na watu wenye afya uwe na mpango mzuri kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania wanapata tiba iliyoboreka, kwa hiyo naomba sana awamu hii katika Mpango huu pia tuweke nguvu kujenga vituo vingi zaidi. Wananchi wetu katika maeneo mengi tuliwahamasisha, wamejenga zahanati kila kijiji na maeneo mengi kila kata wamejenga vituo vya afya, lakini wamefika mahali wamekwama, yale maboma yamebaki mpaka leo miaka mitano, miaka sita, basi katika mpango huu naomba sana Serikali iangalie namna ya kukamilisha hata angalau hizo zahanati wananchi wamechangia waendelee kuwa na imani na Serikali ili angalau kila kijiji wawe wanaweza kupata huduma ya msingi katika hili suala la afya. Pia huu mpango wa bima ya afya kwa wote, naomba uletwe haraka, ni jambo moja nzuri litakalowasaidia Watanzania kupata afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuongelea, ni suala la kujenga uwezo wa makandarasi wetu ndani najua miradi mingi inatekelezwa na makandarasi na miradi mikubwa mingi tunatoa kandarasi kwa makandarasi kutoka nje. Tulianzisha Bodi ya Usajili wa Makandarasi ili tuweze kuinua uwezo wa wakandarasi wetu. Ile bodi ina kazi ya kusajili pia na kufuta, kama kuna wakandarasi hawaendi sawasawa na maadili ya ukandarasi ile bodi ina uwezo wa kufuta, kwa hiyo tusiogope kuwawezesha wakandarasi wetu kupata kazi. Suala kubwa ni kwamba kwa sababu naamini kabisa wapo wakandarasi ambao wapo daraja la kwanza, kwa maana kwamba kazi yoyote ile inaweza hata ile Stiegler’s gorge lingeweza kujengwa kujengwa na wakandarasi wetu wa daraja la kwanza, kinachohitajika ni kuwasimamia na kwamba pale ambapo wakandarasi wamefanya kazi, wawe wanalipwa kwa wakati. Wengi wameshindwa kuendelea na kazi ya ukandarasi ni kwa sababu Serikali imekuwa inachelewa kuwalipa kwa kazi ambazo wamekuwa wamefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama anakaa miaka miwili, miaka mitatu hajalipwa baadaye tunaanza kusema yule mkandarasi ni mwizi kumbe hajalipwa, kwa hiyo naomba Serikali jambo hili ijaribu kuangalia ili wakandarasi wetu na kwa kweli tutafurahi sana kama kila kazi itafanywa na wakandarasi wetu wa ndani. Nadhani hata ukienda China sehemu kubwa ya wakandarasi wanaofanya kazi kwao kule ni wao wenyewe wa China, hakuna Watanzania wanafanya kazi kule China. Sasa na sisi Taifa letu la uchumi wa viwanda lazima tufike mahali kazi zote zifanywe na wakandarasi wetu wa wazalendo ili tuwezeshe Mfuko huu utoke kutoka Serikalini uende kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni suala la kilimo. Ni kweli tunajenga uchumi wa viwanda, lakini uchumi wa viwanda kama hatujainua kilimo, hautakuwa na manufaa kwa sababu tunajenga reli sawa, lakini mazao ya kupitisha pale yatatoka wapi. Kwa hiyo ni lazima tuwe na mkakati wa kutosha kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinakua. Tuwe na pamba ya kutosha ya kuitoa Mwanza kuleta bandarini na tukauza nje, tuwe na chai ya kutosha na mazao mengine ambayo tumeweka ni ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri jambo lingine la kuangalia ni katika kuwezesha wakulima wetu wapate mbolea kwa wakati, lakini mbolea kwa bei elekezi ambayo Serikali imeshaianzisha, naipongeza mpaka sasa wanakwenda vizuri lakini nafikiri tufanye vizuri zaidi, tuangalie yale maeneo ambayo yalikuwa ni matatizo basi sasa hivi tuweze kuyaboresha ili wananchi wetu wapate mbolea kwa wakati na mbegu ili kilimo hiki kiweze kukua. Pia tusaidie wakulima hawa kupata soko kama wenzangu walivyosema, soko limekuwa ni tatizo, mwaka juzi mahindi yalikuwa yanauzwa kwa Sh.20,000 kwa gunia leo yanauzwa kwa Sh.80,000 kwa gunia, napongeza sana hali hiyo. Hii inatokana na masuala ya tabia nchi, kwamba mikoa mingi haikuweza kupata mavuno ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuweke nguvu katika kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, hatutaweza kukuza kilimo kwa kutegemea mvua na miaka hii nimeona mvua inapungua mwaka hadi mwaka. Kwa hiyo, niombe Serikali katika Mpango huu tuweke fedha za kutosha kwenye kilimo cha umwagiliaji, tumekuwa tunaweka fedha lakini hazitoki, naomba awamu hii ya mwisho wa Mpango huu zitoke fedha za kutosha, tuone utekelezaji wa kilimo cha umwagiliaji, naamini kabisa ndiyo mkombozi mkubwa wa kutufikisha katika uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. Ninapongeza kwa mambo makubwa manne, kwanza kwa kuweza kuzalisha umeme na tukawa na ziada ya megawatt 300, kwa maana kwamba sasa hatuna mgao wa umeme. Jambo lingine ninalokupongeza ni kuanzisha ujenzi wa mradi wa Rufiji hydropower ambao tutapata megawatt zaidi ya 2115. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la usambazaji wa umeme kwa mradi huu kabambe wa REA ambao tunategema kwamba vijiji vyote ikiwezekana vijiji zaidi ya 2,012 vitapata umeme. La mwisho pia nakupongeza kwa kuamua kwamba uunganishaji wa umeme maeneo yote vijijini itakuwa ni 27,000 japokuwa hili lina changamoto hasa pale ambapo wanapaswa wananchi kununua nguzo kwa shilingi 319, kwa mfano kama Mkoa wa Njombe, kwakweli naona kama hii bei ya nguzo kwa mwananchi kuweza kuunganisha umeme ni kubwa. Halafu akiunganisha yeye ile nguzo inakuwa ni mali ya TANESCO wale wengine wanakuwa wanaunganishwa kwa 27,000. Mheshimiwa Waziri, mimi naomba jambo hili uliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika huu mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini mwaka jana nilichangia, kwamba kweli ni kazi kubwa tunapeleka miundombinu katika vijiji 12,000 lakini kujenga miundombinu yake na kufanya matengenezo kuwa na uendelevu wa ile miradi lazima tuwe na mfumo wa taasisi kwa ajili ya matengenezo (Maintenance) kama hakuna mfumo mzuri wa maintenance miradi hii ita-collapse.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikichukuliwa mfano kwa Wilaya ya Wanging’ombe, mwaka jana nilisema, kulikuwa na transformer 30 zimeungua sasa kama huna mfumo wa kibajeti wa kuweza kumsaidia huyu mtu wa TANESCO ina maana kwamba wananchi wataendelea kuwa gizani pamoja na kwamba kazi kubwa mmeifanya. Kwa hiyo naomba sana muangalie mfumo wa kitaasisi wa maintenance. Ukichukulia mfano kwenye TANROADS tumeweka Mfuko wa Barabara katika Mfuko wa Barabara asilimia 90 zinaenda kwenye matengenezo na ndiyo maana barabara zinakuwa nzuri muda wote lakini kwenye kitabu hiki sijaona mfumo wowote wa maintenance wa hii Programu Kabambe ya Usambazaji wa Umeme Vijijini. Naomba jambo hili uliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye Wilaya yangu ya Wanging’ombe, hivi leo ninavyoongea kuna vijiji 54 havina umeme kabisa. Katika programu hiyo inayoendelea kuna vijiji 38 vina matumaini ya kupata umeme. Mkandarasi aliyepo wa Mkoa wa Njombe anaitwa Mufindi Power joint venture na Hagie kwakweli kasi yake ni mbovu na sidhani kama ataweza kumaliza hiyo December ambayo ndiyo mwisho wa mkataba wake kwa sababu mpaka sasa kwenye wilaya yangu ameweza kuwasha vijiji vinne tu na vitongoji vitano. Kati ya viji na vitongoji 48 sasa kwenye miezi sita nina wasiwasi kwamba sidhani kama anaweza kumaliza. Naomba Mheshimiwa Waziri uangalie namna gani mikataba hii ilivyoingiwa na namna inavyosimamiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimeona kuna udhaifu wa usimamizi. Meneja wangu wa TANESCO hana hata gari ya supervision anafikaje kwenda kuona huyo mkandaras anavyofanya? Maeneo mengi nguzo zimewekwa wanasema hawana waya na sehemu nyingine wanasema nguzo ndogo hakuna. Sasa kwa mkoa kama Njombe ambapo tunazalisha nguzo ninashangaa kwanini hili linatokea? Kwenye mikataba najua kuna kipengele kwamba ndani ya siku 30 mtu akileta certificate lazima Seriakli ilipe...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Kengele imeshagonga, ahsante sana.

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Ni hotuba nzuri, inatoa dira wapi tunaelekea katika kuinua kiwango cha elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, aiangalie sana Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe. Wilaya hii kitaalam ndiyo inayoongoza katika Mkoa huu na iko katika nafasi nzuri sana kitaifa kwa miaka mitatu. Nakuomba uidhinishe tuanze kidato cha tano na sita kwenye shule tatu za Makoga, Wanike na Wanging’ombe na nitakushukuru sana zingeanza mwaka huu. Tayari madarasa na mabweni kwenye shule za Makoga, Wanike na Wanging’ombe yamekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wilaya ya Wanging’ombe ijengewe Chuo cha VETA. Lipo eneo Soliwaya limeshaandaliwa kwa ajili ya kujenga Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Wizara kwa msaada wa kuboresha miundombinu ya shule ya sekondari ya Usuka na shule za msingi za Dalami na Ilembule. Naomba mpango huu uendelezwe mwaka huu katika shule ya sekondari ya Igosi na shule za msingi za Wanging’ombe, Palangawamu, Mtapa na Saja. Majengo hayo yamechoka sana kupita maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena kuwapongeza na kuwatakia kila heri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja hii nzuri iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri pia naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri sana katika kuendeleza ujenzi, uchukuzi na mawasiliano. Naishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka Njombe - Moronga kilometa 53 iliyoko jimboni kwangu, nimeona zimetengwa shilingi bilioni 12 ambayo imeweza kujengwa takribani kilometa 12 tu kwa mwaka 2018/2019, ninatarajia utaliangalia ili kasi ya ujenzi iongezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Njombe - Ramadhani - Iyaji kilometa 74 imefanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina toka mwaka 2013 yapata miaka mitano sasa kazi ya ujenzi kwa kiwango cha lami haijauza. Nimefuatilia hotuba hii sijaona mahali wala fedha kutengwa ili kuanza kazi ya ujenzi kulingana na upembuzi huo uliofanyika. Je, ni lini kazi ya ujenzi itaanza? Je, wananchi waliowekewa alama za “X” za kijani ni lini watalipwa fidia ili kuruhusu kazi za ujenzi kuanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Halali - Ilembule - Itulahumla nashukuru imetengewa fedha za matengenezo ya kawaida, lakini sijaona matengenezo ya Daraja la Halali ambalo limeathiriwa sana na mvua za mwaka huu. Naomba Serikali ifikirie kulijenga daraja jipya kwani ni jembamba sana na halijajengwa vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Makao Makuu ya Wilaya yapo Igwichemya, mawasiliano ya simu yana kilometa mbili tu kwani ulienda zaidi ya kilometa tatu toka Igwachenya kwa mtandao ya Vodacom, Airtel, Tigo hakuna mawasiliano. Naomba Serikali irekebishe hali hii. Katika kuboresha viwanja vya ndege vya Milua, sijaona mpango wa kuboresha kiwanja cha ndege cha Njombe ili kiweze kuhudumia ndege kubwa. Katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tuliahidiwa kuwa uwanja huu utaendelezwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha hotuba hii niambie unasema nini kuihusu barabara ya Njombe (Ramadhani) Iyayi kujengwa kwa kiwango cha lami.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa kuisimamia vizuri kuwa kiwango cha elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii ikiangalie Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Ulembwe. Chuo hiki kiko katika hali mbaya sana. Kwa kuwa miundombinu ni chakavu sana, naomba majengo yale yaboreshwe na kuezekwa kulingana na hali ya sasa. Wilaya ya Wanging’ombe haina Chuo cha VETA. Nimeomba majengo ya mhandisi mshauri yaliyopo pale Wanging’ombe yakubaliwe kutumike kwa kutoa elimu ya mafunzo ya ufundi VETA. Wizara ya ujenzi imeonesha nia ya kulikubali ombi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza tena Mheshimiwa Waziri kwa kunikubalia kukarabati shule mbili, moja ni shule ya msingi ya Dulamu na nyingine shule ya sekondari ya Usuka. Shule hizi miundombinu yake imekuwa modal kwa Wilaya yangu. Naomba mpango huo uendelezwe katika mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mpango mzuri wa kuendeleza elimu ya ualimu nchini. Tatizo lililopo hivi sasa ni upungufu mkubwa sana wa walimu na hasa shule ya msingi vijijini. Ziko shule zina walimu wawili tu kwa wanafunzi wa madarasa saba, hili ni janga. Ni vyema Wizara ijue namna ya kutatua janga hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeomba mfululizo kwa miaka mitano sasa kuanza kwa kidato cha tano na sita kwa shule za sekondari za Makoga na ile ya Wanike. Naomba majengo yaboreshwe na kukarabatiwa. Naomba sana zikubaliwe kupokea wanafunzi kwa mwaka huu 2018/2019.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naunga mkono hoja hii na nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa Wizara hii kwa namna wanavyojituma katika kutatua tatizo la maji nchini. Naomba yafuatayo yazingatiwe:-

(i) Uendelevu wa huduma ya kutoa maji lazima baadhi ya mifumo ya uendeshaji ifanyiwe utafiti.

(ii) Programu ya Maji (WSDP) inawatekelezaji wengi ambao wanatofautiana sana katika approach ya utendaji. Wizara imetengeneza sera lakini watekelezaji wake hawako chini ya Wizara kwa mfano Halmashauri za Wilaya na kadhalika. Nashauri katika suala la utekelezaji au ufungaji wa miradi wa maji vijijini na usimamiwe na Wizara.

(iii) Tuongeze juhudi za uvunaji wa maji ya mvua, tujenge mabwawa mengi ili kuongeza rasilimali za maji na hili lisimamiwe na Wizara. Katika hili Jimbo langu la Wanging’ombe katika bajeti 2017/2018 Wizara ilipanga kufanya upembuzi na usanifu wa kujenga Bwawa la Ulembwe na Igwadianya, nataka kujua hatua ya utekelezaji na naomba mabwawa hayo yajengwe.

(iv) Mradi wa Mbukwa ulijengwa na UNICEF miaka ya 1976 ni chakavu ijapokuwa inahudumia zaidi ya vijiji 50. Najua toka Awamu ya Nne Serikali iliahidiwa na Serikali ya India kuwa mradi huu utaboreshwa. Nimeona kwenye hotuba zimelengwa dola za kimarekani milioni 48.99 kwa ajili ya kukarabati mradi huu. Naomba kwanza kuishukuru Serikali kwa kufuatilia utekelezaji wa mradi ili wananchi hasa wa kata za Wanging’ombe, Saja, Kijumbe, Ludinga, Ilembula na Uhamhule wanashida sana ya maji na hasa kuanzia mwezi wa sita (wakati wa kiangazi).

(v) Mheshimiwa Waziri ulitembelea Jimbo langu na uliahidi visima viwili katika Kijiji cha Ihanjulwa na Itulahimba, wananchi wale walikuchezea ngoma kwa imani kuwa utawaondolea kero ya maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa pongezi za dhati kwa Waziri na Manaibu Mawaziri wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia eneo la huduma za afya, Wilaya ya Wanging’ombe imepata fedha za kukarabati Kituo cha Afya cha Wanging’ombe milioni 300 na Kituo cha Afya cha Palangawanu milioni 100. Naomba Serikali itoe fedha milioni 300 ili kukamilisha kazi ambayo kwa sehemu kubwa imefanywa na nguvu za wananchi. Jengo la kituo cha afya na maabara vimeezekwa, jengo la mtumishi kuta zimekamilika, jengo la upasuaji limefikia usawa wa jamvi, jengo la wodi ya wazazi limefikia usawa wa jamvi na jengo la mortuary limefikia usawa wa kuezeka. Ni matumaini yangu Serikali haitaacha kazi hii kubwa bila kukamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya hii ina tatizo kubwa sana la huduma za afya. Viko vituo viwili tu vya afya vinavyofanya kazi, hatuna hospitali ya Wilaya ya Serikali. Kwa hiyo tukipata msaada wa kukamilisha Kituo cha Palagawanu kitapunguza tatizo hili. Wilaya inayo maboresho ya zahanati na vituo vya afya ambavyo tumeahidiwa fedha za miradi viporo ili kukamilisha Zahanati za Katenge, Ng’anda, Ivigo, Mtapa, Kanomelenge na Kituo cha Afya cha Igagala hakijaletewa fedha za kukamilisha zaidi ya miaka sita. Naomba pia Serikali itoe fedha za kujenga hospitali ya wilaya ambayo kwa miaka minne tumekuwa tumepangiwa fedha lakini fedha haziletwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la elimu, naomba Serikali isaidie kuboresha Shule ya Sekondari ya Makoga na Wanike ili zisajiliwe kuanza kwa kidato cha V na VI.Wilaya hii imeweza kujenga Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kutumia mkandarasi, lakini nyumba mbili zilizokabidhiwa TBA toka mwaka 2012 mpaka leo ziko hatua ya msingi na kazi imesimama. Nyumba hizo ni kwa ajili ya makazi ya Mkuu wa Wilaya na Afisa Tawala. Mkuu wa Wilaya anaishi nyumba ya kupanga toka Wilaya hii ilipoanzishwa 2011. Naomba Serikali itoe kibali kwa kutumia utaratibu wa kuajiri wakandarasi ili viongozi hawa waishi kwenye nyumba za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii na kutegemea maombi yangu kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe yatazingatiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ukurasa wa 25 wa hotuba, unatoa takwimu za miradi mipya ya uwekezaji mpaka Februari 2019 kuwa 145. Ningetaka kujua ni mingapi mpaka sasa imeanza kujengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea na baadhi ya wawekezaji ambao wamelalamikia mlolongo wa vikwazo au taratibu ambazo si rafiki kwa wawekezaji wanaokuja na mitaji yao. Kupata kibali au leseni inachukuliwa muda mrefu. Nashauri Serikali ipitie upya taratibu na hatua zilizopo ili tuvutie zaidi wawekezaji waje Tanzania badala ya kwenda kwa nchi za jirani. Kwa mfano, tunaweza tukaamua uwekezaji wa kujenga kiwanda, mlolongo wote wa hatua za kuchukuliwa zikamilike ndani ya Taasisi moja (one center) na kila hatua ipewe muda maalum (that is time factor) na uwepo ufuatiliaji wa kila hatua ili kujua sababu za mkwamo na hatua za kuchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji wa viwanda vinavyochakata mazao ya wakulima na wafugaji vipewe kipaumbele kwani hivi vitainua uchumi wa wananchi na kutoa ajira. Yupo Mwekezaji wa kujenga kiwanda cha kuchakata matunda ya maparachichi kinachotarajiwa kujengwa Wilayani Wanging’ombe (OLIVADO CO) amekuwa anazungushwa karibu amekata tamaa, nataka kujua ni lini atapewa leseni ili ajenge kiwanda hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na tatizo la soko la matunda ya parachichi kwa muda mrefu na baada ya mwekezaji huyu kuja tumehamasisha wananchi wetu kulima zao hili la parachichi, naomba sana Serikali itumie nguvu iliyokuwa nayo ili kiwanda hiki kijengwe mapema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naunga mkono hoja hii. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na uongozi wote wa Wizara hii kwa kuiongoza vyema Wizara hii na mengi yameonekana kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii iongezewe bajeti, hasa katika kuboresha miundombinu katika shule za msingi. Nyumba na madarasa yaliyojengwa kabla ya Taifa kupata uhuru yamechakaa sana na mengi kubomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Wanging’ombe pamoja na Mbunge tumehamasishana kujenga maboma ya madarasa na nyumba za walimu. Kwenye Ilani ya CCM 2015 - 2020 imeelekeza kushirikisha nguvu za wananchi na Serikali itapeleka mchango wake katika bajeti ya TAMISEMI na Wizara. Fedha zimekuwa zinatengwa lakini zimekuwa hazipelekwi kwenye Halmashauri husika. Naomba Wizara iliangalie jambo hili ambalo wananchi wametekeleza wajibu wao. Wilaya ya Wanging’ombe mpaka Oktoba, 2018 inahitaji shilingi bilioni moja kukamilisha maboma katika Sekta ya Elimu ikiwepo sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wameongelea suala la uhaba wa walimu, ninazo shule zaidi ya 20 zenye walimu chini ya watatu kwa shule zenye madarasa hadi darasa la saba. Naomba Serikali iajiri walimu na itoe mgawanyo sawa. Nimeona shule za mijini zina mlundikano wa walimu kwa kisingizio cha kuolewa, kukaa karibu na hospitali na kadhalika. Shule zilizo vijijini zimesahauliwa. Naomba jambo hili lirekebishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, alipofanya ziara Mkoa wa Njombe, Aprili, 2019, ametoa maelekezo kwamba majengo yaliyopo Kijiji cha Soliwaya, Wanging’ombe ambayo yalitumiwa na wasimamizi wa ukarabati wa barabara ya Nyigo – Makambako – Igawa yaanzishe Chuo cha VETA Wilaya ya Wanging’ombe. Halmashauri ya Wanging’ombe imemwandikia barua Mheshimiwa Waziri juu ya suala hili na nakala iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu, ninayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Wanging’ombe wanataka kujua, hili agizo la Mheshimiwa Rais litatekelezwa lini? Naomba Mheshimiwa Waziri wakati unaahirisha bajeti yake aseme kitu, wananchi wa Wanging’ombe wasikie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa namwita Mheshimiwa Waziri Comrade kwa jinsi alivyo sikivu kwa hoja za Wabunge na ninayo imani kuwa katika hili atalitengenezea utaratibu; ili litekelezwe wapewe, uwezekano. Tayari Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wameshaiandikia Halmashauri ya Wanging’ombe utayari wao wa kukabidhi majengo hayo kama tulivyoomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wameongelea kuhusu hoja ya kuboresha utaratibu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuo Vikuu ambao umeleta malalamiko na kiasi fulani kinawabagua wahitaji. Kwa kuwa fedha hizi ni mkopo na utatakiwa kurudishwa, kigezo cha kuangalia aina ya shule walizosoma hakina tija kwa sababu walio wanafunzi wanaopata ufadhili wengine wazazi wao wamekosa uwezo wa kuwapeleka vyuo vikuu. Naomba sana wanafunzi wote wapewe mikopo hata kama viwango vitatofautiana, lakini kuwakatalia kabisa kumesababisha watoto wengi kukosa elimu ya vyuo vikuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naunga mkono hoja ya Waziri na nampongeza sana Waziri, Naibu Mawaziri na vviongozi wote wa Wizara hii kwa hotuba yenye kuleta mabadiliko makubwa katika kujenga miundombinu itakayotufikisha kwenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizi, naomba Waziri arejee kwenye barabara ya Njombe (Ramadhani) – Igwachanya – Iyayi ambayo ni barabara muhimu kwani inaunganisha Makao Makuu ya Mkoa na Makao Makuu ya Wilaya ya Waging’ombe (Igwachanya). Pia inapita maeneo muhimu ya utalii ya msitu wa asili wa Nyumbanintu na Hifadhi ya Pori la Akiba la Mpanga/Kipangele pale Ludunga na kuunganisha na TANZAM Highway pale Igando. Barabara hii ilishafanyiwa upembuzi na usanifu wa kina toka mwaka 2014 ilipokamilika na ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015.

Mheshimiwa Spika, naomba pia Wizara ione uwezekano wa kuongeza kiwango cha lami pale Igwachanya ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya. Nimeona imepangwa kujengwa mita 100 tu kwa bajeti hii 2019/20. Kumleta mkandarasi kuja kujenga mita 100 itagharimu pesa kubwa kwani kuleta mitambo ya kujenga mita 100 haina tofauti na ile ya kujenga kilomita 5. Naomba tupate angalau kilomita 2.

Mheshimiwa Spika, sijaona mpango mahsusi na kuboresha Uwanja wa Ndege wa Njombe. Mkoa wa Njombe unahitaji kupata uwanja mkubwa wa ndege. Huu ulipo ni mdogo na pengine itakuwa vigumu kuupanua kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, nashauri toka bajeti ya 2018/2019 kuwa Wizara ijaribu kwenda pale Ilembula Hospitali tunao uwanja wa ndege na ardhi ya kutosha ambapo ingeweza kujenga uwanja mkubwa wa ndege kwa kiwango cha uwanja wa ndege wa mkoa. Hakutakuwa na gharama kubwa ya fidia kama kupanua ule Uwanja wa Njombe Mjini ambapo majengo mengi ya kudumu yamejengwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naunga mkono hoja hii na nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wa Wizara hii kwa kazi nzuri ya kusimamia majukumu ya Wizara hii. Mwaka jana wakati wa kuwasilisha hoja ya bajeti kwa Wizara hii nilichangia kuhusiana na kuwepo kwa Pori la Akiba la Mpanga/Kipengele lilianzishwa mwaka 1995; wananchi wa vijiji 14 vya Wilaya ya Wanging’ombe walihamishwa kupisha uanzishaji wa pori hili la akiba, walilipwa fidia na mipaka iliwekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hao wamejenga nyumba za kudumu, shule, majengo ya ibada na kadhalika. Hivi karibuni Mamlaka ya TANAPA wamekuja kuweka vigingi tofauti na mipaka ya awali bila kuwahusisha wananchi au viongozi wa wilaya. Jambo hili limeleta taharuki na hivyo kuzusha mgogoro mkubwa. Jambo hili nilimfikishia Mheshimiwa Waziri ili achukue hatua ili wananchi hawa waishi kwa amani na vilevile azma ya kuwepo hifadhi ya pori la akiba iwe endelevu. Nilitarajia ningeona lolote ndani ya hotuba hii, lakini sijaona mpango wowote uliopo kwa ajili ya pori hili la Mpanga Kipengere, kwa hiyo, lipolipo tu. Basi kama ni hivyo naomba ramani ya awali iheshimiwe na vijiji hivi vilivyosajiliwa viachwe viendeleze maeneo yao. Vijiji hivyo ni Moronga, Kipengele, Imalilo, Ikanga, Wangama, Masage, Malangali, Wagamiko, Mpanga, Luduga, Hanjawanu, Igando, Iyayi na Mayale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa tamko lake alilolitoa kwa vijiji vile vyenye migogoro na wananchi kwamba, Wizara iende kutatua migogoro ikihusisha wananchi, Serikali za Wilaya na ikikupendeza kumshirikisha Mbunge wa Jimbo. Nina imani agizo la Rais linahusisha pia mgogoro uliopo kati ya Hifadhi ya Pori la Akiba la Mpanga/ Kipengele na wananchi wa vijiji hivi 14 nilivyovitaja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Spika, pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu na Watendaji. Pongezi kwa kuzalisha umeme na kuwa na ziada ya MW 300 na hivyo kutokuwepo mgao wa umeme. Rufiji Hydro Power MW 2,115. Kuongezeka kwa kasi ya kuwaeleza umeme vjijini na kufikia vijiji 7,127 kati ya vijiji 12,268 na kufikia Juni 2020 vitafikia 10,268. Pongezi kwa uamuzi wa kutoza 27,000 kuunganisha umeme vijijini japo lina changamoto na linakwamisha wananchi hasa inapotakiwa kununua nguzo, maelekezo shilingi 27,000 ndani ya mita 30.

Mheshimiwa Spika, REA III, mzunguko wa kwanza, lengo vijiji 10,278 by June 2020, mzunguko wa pili lengo vijiji 1,990 kuanza Julai 2020.

Mheshimiwa Spika, Wanging’ombe vijiji 54 hivi sasa havina umeme kabisa, mzunguko wa kwanza vijiji na vitongoji 48, vijiji 38 na vitongoji 10 pogram todate vijiji vinne na vitongoji vitano. Mkataba unaisha Disemba, 2019. Swali, atakamilisha vijiji 39 ndani ya miezi sita? Mkataba umeonesha anasambaza line kubwa kilomita 95 wakati uhalisia kufikia vijiji 48 ni kilomita 150 mpaka leo addendum ya scope na muda haijasainiwa.

Mheshimiwa Spika, mkandarasi Mufindi power JV Hegy Engineering, utendaji wa kazi hauridhishi kabisa, bado maeneo ya vijiji 27 vilivyo kwenye mkataba aidha hajapeleka nguzo kubwa au hajatandaza wire au hajaanza hata kupeleka nguzo ndogo. Mkandarasi huyu hata hivyo vijiji vinne na vitongoji vitano inachukua zaidi ya miezi mitatu kuwasha umeme toka wateja wailipe TANESCO kwa madai kuwa mita zilifungwa bila kusajiliwa.

Mheshimiwa Spika, Meneja wa TANESCO Wilaya hana gari la kufuatilia utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Spika, kuunganisha umeme kwa wananchi 27,000 iwe ni ndani ya mradi au vinginevyo. Maelekezo ni kwamba, Sh.27,000 ni ndani ya mita 30; nguzo moja Sh.391,000, nguzo mbili Sh.450,000, halafu nguzo inakuwa mali ya TANESCO utakuta watakaofuata wanalipa Sh.27,000 tu. TANESCO wapewe bajeti ya kuweka nguzo.

Mheshimiwa Spika, hivi vijiji vimepewa scope ya wastani wa kilomita mbili, kwa hiyo eneo kubwa la kijiji na vitongoji havijapewa umeme. Sasa maeneo haya yaliyosalia pamoja na vijiji ambavyo havijafikiwa vimewekwa kwenye awamu ipi? Kwani kwenye hotuba page 61 Waziri ameongelea kuhusu idadi ya vijiji ambavyo havitafikiwa ifikapo Juni 2020, hajasema chochote kuhusu vijiji vilivyopewa scope kidogo, page 65 haielezei scope jazilizi na hakuna bajeti.

Mheshimiwa Spika, uendelevu wa mradi huu kabambe wa REA; mwaka jana nilishauri sambamba na kuwekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa mradi Serikali iwekeze fedha ya kutosha za matengenezo ili kuiwezesha TANESCO kuhimili mahitaji ya matengenezo, sijaona mpango huo kwenye bajeti hii. Mfano 90% Road Fund ni matengenezo; 7% Road Fund ni mwendeleo ujenzi mpya; 2% Road Fund ni utawala. Wilaya ya Wanging’ombe REA II transfoma 30. REA III transfoma tisa zimeungua wako gizani. Seven transformers are replaced but two not yet for more than six months.

Mheshimiwa Spika, mikataba; yapo majukumu (obligations) za mwajiri client na yapo majukumu (obligations) za mkandarasi. Mkandarasi lazima alipwe kwa wakati (30 days) baada ya kuidhinisha hati ya madai. Mkandarasi asipofikisha lengo la utekelezaji zipo hatua za kuchukua. Kila mwezi kuna Progress Site Meeting, hizi lazima zisimamiwe vizuri na Consultant na client. Tusisubiri mwisho wa muda ndio tuchukue hatua au zinaanza kuzuka hoja eti mkandarasi hana uwezo, swali alipataje kazi? Tathmini ya uwezo kikazi na kifedha ilifanyike (due diligence)?

Mheshimiwa Spika, orodha ya vijiji vilivyomo REA III round I navyo ni Ihanja, Lusisi, Mungate, Itambo, Udonja, Ujange, Kasagala, Lugoda, Ikwega, Matowo, Itowo, Ilulu, Gonelamefuta, Masage, Mapogoro, Ukomola, Saja, Igomba, Isimike, Mtewele, Ujindile, Uhambule, Msimbazi, Igelango, Mng’elenge, Ufwala, Katenge, Mbembe, Itandula, Mpululu, Igelehedza, Igula, Mayale, Ing’enyango, Ivigo, Luduga sekondari.

Mheshimiwa Spika, vijiji visivyokuwepo kwenye REA III round 1. Idunda, Masaulwa, Ikwavila, Uhenga, Mbembe, Ikulimambo, Idenyimembe, Igenge, Idindilimunyo, Iyayi, Igando, Hanjawanu, Mpanga, Malangali, Wangamiko, Litundu.