Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Edward Franz Mwalongo (50 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nianze kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini kwa kunipa kura nyingi ili niwe mwakilishi wao. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, nitafanya kila linalowezekana niwawakilishe vema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sikupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais basi na mimi nichukue nafasi kumpongeza sana, hotuba yake ilikuwa nzuri na kweli imetoa mwongozo na mwanga jinsi nchi yetu inavyoweza kwenda.
Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wa Mawaziri, niwaombe wawe na amani, wafanye kazi kwa bidii wawatumikie Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijikita sasa kwenye Mpango, niseme mpango ni mzuri lakini nina mambo machache ya kusema. Watu wa Kanda ya Kati wanasema reli ya standard gauge lakini sisi wa Mkoa wa Njombe na Mbeya tuna reli tayari pale ya standard gauge ya TAZARA lakini malori bado yapo barabarani. Tukiacha hilo, kwenye Mpango tunasema kuna upembuzi yakinifu wa kujenga reli kutoka Mtwara - Mbamba Bay zaidi ya kilomita 800, sikatai, ni vizuri kwa maana ya kwamba ni kufungua mikoa iliyopo pembezoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kutoka Makambako - Liganga ni kilomita 200, hivi shida iko wapi? Hivi kipi ni rahisi, k ujenga reli kutoka Makambako - Liganga ambako chuma ndiko kipo au kuanza kufanya upembuzi wa kilomita 800 za reli mpya ya Mtwara – Mabamba Bay? Nashauri tufanye kile cha rahisi na pafupi chuma kitoke Liganga ili tufanye maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Njombe ndiyo unategemewa kuwa Mji Mkuu wa machimbo haya ya Kusini mwa Mkoa wa Njombe. Ndiyo mji utakaopokea wageni wengi, ndiyo mji ambao utatoa huduma lakini mji huu hauna maji. Kinachosikitisha zaidi katika Mji wa Njombe, mito miwili mikubwa imekatiza katikati ya mji. Niombe Serikali na nimuombe kaka yangu Mheshimiwa Lwenge, ameshaniahidi tutaenda Njombe tukaone ni namna gani sasa Mji wa Njombe utapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vyote vya Jimbo la Njombe Kusini au Mjini havina maji. Wananchi walichanga fedha wakiahidiwa kwamba kutakuwa na mradi wa Benki ya Dunia kusaidia ujenzi wa mradi wa maji. Fedha zao zimekaa huko Serikalini lakini maji hakuna. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameshaniahidi basi niamini hilo litaenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala la afya, tunakwenda kujenga uchumi wananchi hawana afya itasaidia nini? Pale Njombe sisi tuna hospitali ambayo mara inageuzwa Hospitali ya Mkoa, mara Hospitali ya Rufaa ya Mkoa lakini ukifika huwezi kujua kama umefika hospitali kwa jinsi ilivyochakaa. Utajiuliza hivi hapa ilitokea vita au kulitokea nini, lakini ukiingia ndani utaona watu wamelala, ni wodi. Hali ya hospitali ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali ione nini tufanye katika hospitali ile. Hospitali ile imerithiwa kutoka kwenye Kampuni ya TANWAT ikakabidhiwa Serikali kwa maana ya Halmashauri ya Wilaya, Halmashauri zimekuwa zikiongezeka mpaka sasa ziko tano bado zinatumia hospitali ile ile na sasa inakuwa Hospitali ya Mkoa bado ni ile ile, eneo lenyewe la hospitali halizidi heka mbili.
Kwa kuwa mkoa umeshapewa eneo katika kijiji cha Mkodechi kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Mkoa ambapo wameshafanya uthamini, wameshalipa fidia na wameshaweka mipaka, niombe Serikali itafute fedha tujenge hospitali hii. Tukijenga Hospitali ya Mkoa wa Njombe maana yake itasaidia sasa wananchi wa Njombe kwa maana ya mkoa pamoja na hao wawekezaji wanaokuja kwenye migodi hii kupata huduma ya afya na kuendelea na uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu. Niipongeze sana Serikali kwa hatua iliyochukua, changamoto zipo sikatai. Ni muhimu unapoanza jambo upambane na changamoto ili kusudi ujipange vizuri zaidi. Naomba sana Serikali ijitahidi changamoto hizi iziangalie kwa haraka. Wengi wamesema hapa lipo tatizo la walimu, maslahi yao yaangaliwe vizuri, wana madai, wamekwenda likizo hawalipwi, wanapandishwa vyeo nyongeza zao hawapewi, niombe sana suala hili lipewe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo ambalo kwangu naliona ni kubwa, tatizo la elimu kwa watoto wa kike. Tatizo hili ni la kitaalam kidogo na ni tatizo linalotokana na makuzi ya mtoto wa kike. Mtoto wa kike katika makuzi yake anafika mahali haudhurii shule kwa sababu ya kukosa zana za kujisitiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena tuna bahati sana Waziri wa Elimu ni mama, Naibu Waziri wa Elimu ni mama, Makamu wa Rais ni mama na Waziri wa Afya ni mama, naomba tulione hili. Watoto hawa wa kike hawahitaji hata zaidi ya shilingi 10,000 kwa mwaka ili wajisitiri. Hawawezi kuhudhuria shule kwa sababu hali zao siyo nzuri. Haudhurii shule kwa zaidi ya siku 30 ata-perform vipi vizuri, mbona haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona taasisi nyingi za kina mama hazizungumzii habari ya watoto wa kike tuwasitiri namna gani ili wahudhurie shule. Taasisi zote zinazunguka zunguka tu pembeni zinafanya vitu vingine visivyo vya msingi. Naomba sana suala hili liangaliwe, Serikali ione namna gani itafanya kusaidia watoto wa kike wahudhurie shule siku zote za masomo ili kusudi waweze kupata elimu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme. Nashukuru sana Profesa Muhongo amefika Jimboni kwangu na tumejaribu kuona vyanzo vya umeme na ameniahidi kwamba Jimbo langu litapata umeme. Tatizo ninaloliona kama nchi kwa suala la umeme ni nguzo. Sisi Njombe tunazalisha nguzo nyingi sana, Serikali ifike mahali ifanye maamuzi kwa kuwawezesha wafanyabiashara wa Njombe wawe na mitambo ya kusindika nguzo zile. Kwa sababu nguzo hizi na umeme tunaoenda kusambaza nchi nzima ni mwingi sana, tunahitaji nguzo nyingi sana na Njombe sisi tuna uwezo wa kutoa hizo nguzo zote zikapatikana, lakini nani awezeshe wale wananchi ili waweze kuwa na mitambo ya kusindika zile nguzo?
Kwa hiyo, Wizara ya Nishati na Madini kwa namna itakavyowezekana iwawezeshe wananchi wenye nia ya kufanya shughuli hiyo ya kusindika nguzo ili wazalishe nguzo nyingi zaidi. Tunaagiza nguzo South Africa, Zimbabwe na Kenya, tena ni hadithi ya kusikitisha unaambiwa nguzo zimetoka Njombe zimepelekwa Kenya zimenunuliwa na mkandarasi zinarudishwa Mara na wakati Njombe sisi nguzo pale zimebaki hazina mnunuzi. Kwa hiyo, niombe sana suala hili lishughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni elimu ya ufundi, hivi tujiulize… (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako mzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, naona jina langu linakupa shida kidogo naitwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini. (Makofi)
Kwanza kabisa naomba nianze kwa kuwapongeza Mawaziri, Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini naomba nikiri mbele ya Bunge lako walinitunukia nishani ya mtetezi wa watoto wa kike na Waziri wa Afya alitangaza mbele ya Bunge lako na tarehe 8 Machi, 2016 waliniita Dar es Salaam, wakanitunukia nishani ile. Nashukuru sana na naomba Wabunge wote watambue kwamba nishani ile nimepewa na ninayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, umesema tusiongelee habari ya zahanati vijijini, ni ngumu sana kutenganisha. Ni ngumu kwa sababu mazingira tunayotoka yana mahitaji hayo, lakini wananchi wetu wanategemea tuliseme hili katika Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze na tatizo la watoto wenye uzito mdogo, japokuwa hali ni mbaya sana katika Halmashauri zetu na umesema tusiseme lakini tunaomba tuseme. Halmashauri ya Mji wa Njombe ilitegemewa kuwa na wanaojifungua 190, lakini kwa sababu mazingira yametokea kwamba Halmashauri ile imezaa Halmashauri zingine na idadi ya watu imeongozeka, hospitali ile sasa imekuwa ya mkoa, imekuwa na wanaojifungua sasa wanafika 4,580.
Mheshimiwa Spika, katika 4,580 wanaozaliwa kama watoto wenye uzito mdogo ni 202, lakini wanaofariki sasa inatia huruma. Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii alisema tupige hesabu ya coaster. Kwa hiyo, pale Halmashauri ya Mji wa Njombe, tuna kosta zaidi ya tatu wanakufa kila mwaka watoto 82, ni jambo la kusikitisha sana. Nimeona kuna mpango wa Wizara wa kusaidia namna gani ya kuokoa maisha ya watoto hawa. Naomba Waziri atapokuwa anapanga mambo yake, atukumbuke Njombe kwa ajili ya kuokoa watoto wanaozaliwa na uzito mdogo.
Mheshimiwa Spika, ukienda pale hospitali inasikitisha, kile chumba ambacho kinatumika kutunzia wale watoto hakijulikani kilikuwa ni store au kilikuwa ni nini na hali ya hewa ya Njombe ni baridi sana, vifaa vyenyewe ni duni na pamoja na wataalam nimesoma kwenye kitabu cha Waziri cha hotuba yake anasema Njombe kuna mtaalam mmoja. Mtaalam mmoja kwa kweli kuhudumia watoto 82 kwa mwaka, hiyo shughuli ni pevu kweli kweli. Kwa hiyo, naomba Wizara itakapokuwa inafanya majumuisho itoe angalau maneno ya imani na maneno ya kuwafanya Wananjombe waone kwamba, Serikali yao imewakumbuka.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nirudie tena masuala ya afya ya mtoto wa kike. Mtoto wa kike ndiye mama wa kesho, harakati nyingi sana zinamwangalia mama, kwamba mama akijifungua, mama anapata matatizo, lakini haziangalii mtoto wa kike kwa sababu mtoto wa kike akiwa na afya bora ndiyo mama wa kesho mwenye afya bora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mimi nimefarijika sana jinsi akinamama walivyoichukua ajenda ya kusaidia watoto wa kike kupata stahiki zao, kupata dhana za kujisitiri. Sasa cha msingi na kikubwa tuone tunafanyaje, sawa Serikali imeshapata taarifa na yenyewe inajitahidi, lakini baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameanza kushauri jinsi gani Serikali ifanye.
Mheshimiwa Spika, Mbunge mmoja jana alishauri kwenye vyuo kwamba mkopo unapokuwa ni mkopo kwa mtoto wa kike basi uongezewe. Gharama ya ile bidhaa wala sio kubwa kwa chini kabisa ni shilingi 20,000 kwa mwaka, kwa chini kabisa. Ni shilingi 1,500 kwa mwezi. Kwa hiyo, naungana na Mbunge yule kwamba kwenye mikopo ya shule, basi tuangalie kwamba watoto wale wa kike waweze kuongozewa hicho kiwango.
Mheshimiwa Spika, nimeangalia kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba Bima ya Afya wanataka kujitathmini na bima ya afya wana bima ya afya kwa watoto wa shule. Mtoto mmoja wa shule bima yake ya afya ni shilingi 50,400. Tuombe sasa basi watakapokuwa wanajitathmini bima ya afya, kwa mtoto wa kike mwanafunzi ihusishe bidhaa hiyo, hayo ndiyo matunda ya uhuru na hayo ndiyo matunda ya ustaarabu kwamba sasa tunaendelea, katika bima ya afya kuna package hii ya mtoto wa kike, lakini vilevile kama nilivyosema huko juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni tatizo la wauguzi. Kuna shida kubwa sana ya wauguzi hospitali nyingi hazina wahudumu wa kutosha, lakini Wizara inasema ina mpango wa kuboresha vyuo na kadhalika. Ningependa kushauri kwa ziada kwamba hebu tuone sasa, hebu tushuke chini, tunayo Bodi yetu ya Mikopo, Bodi ile imeng‟ang‟ana tu haifanyi hata utafiti, inakopesha tu watu wa university, kule university wanaosoma course nyingine hazina hata ajira.
Mheshimiwa Spika, mkopeshaji mwingine yeyote kwa mfano mkopeshaji wa kawaida, anapomkopesha mtu anaangalia jinsi ya kulipa. Leo hii Bodi ya Mikopo inahangaika kudai madeni ya wanafunzi ambao walisoma siku za nyuma, hapa kuna watu wanasoma vyuo vya afya, ajira Serikalini ipo. Bodi ya Mikopo basi ishuke chini, kama ni sheria basi waielete humu ndani tuibadilishe. Ikopeshe basi kwa kuanzia tu wanaosoma vyuo vya afya ili kusudi vijana hawa wanaosoma vyuo vya afya, wasome vizuri, wasome haraka na Serikali iwaajiri waweze kulipa hiyo mikopo.
Mheshimiwa Spika, liko suala la Bima ya Afya, naomba nipate ufafanuzi kwamba jana hapa Bima ya Afya imeshambuliwa kweli kweli. Ninavyofahamu kazi ya bima ni kufidia gharama, bima sio kazi yake kununua dawa. Ina maana kwamba, katika ile hospitali anatakiwa awepo mtoa dawa ili kusudi bima ifidie ile gharama.
Mheshimiwa Spika, niwaombe sasa Bima ya Afya na wenyewe wawe watafiti. Wamekubali kimsingi kwamba usipopata dawa hospitali utapata dawa kwenye duka. Hebu maduka yale waliyoingia nayo makubaliano yawepo hospitali pale pale ili kusudi mtu asiondoke kutoka pale hospitali kwenda sehemu za mjini kutafuta dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii itawasaidia wahudumu wa afya wafanye kazi kwa amani na itawasaidia wateja wao waweze kupata huduma vizuri kwa sababu Bima ya Afya wenyewe wanaonekana kwamba, ndio wahalifu na ndio wanyang‟anya fedha za wananchi kwa sababu wamepokea fedha na huduma haikupatikana, lakini sasa kwa kuwa bima ya afya wana-package ya kukopesha vifaa vya afya, wana-package ya kukopesha ujenzi wa zahanati na nini, waone sasa kama inawezekana, wakopeshe hata Halmashauri sasa package ya dawa, ili kusudi sasa Halmashauri ziweze kutoa zile dawa ili wao kama bima wafanye kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, liko suala la Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Kwa mtazamo wangu naona kwamba vyuo hivi sasa kwa kweli sioni kama kuna ulazima wa kuendelea kuwa Wizara ya Afya, tuvipeleke VETA ili kusudi viweze kuhudumiwa vizuri zaidi. Vyuo vile vina hali mbaya, havina vifaa vya kazi, havina wataalam, pale Njombe tuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, nakumbuka Mkuu wa Chuo aliyestaafu alikuwa ni Mwalimu wa Kiswahili.
Mheshimiwa Spika, pia pale kwenye Halmashauri ya Wanging‟ombe kuna Chuo cha Wananchi Urembwe, Mkuu wa Chuo aliyepo pale ni Mwalimu wa Kifaransa. Mimi kama fundi sielewi kabisa kwamba inakuwaje watu hawa wanakuwa ndiyo wakuu wa vyuo vya taaluma kama hizo, lakini je kuna ulazima wa kuendelea kuwa na vyuo hivi katika Wizara ya Afya? Kama ni sheria basi wailete tuibadilishe, vihamie VETA na VETA isimamie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu wa kawaida vile vyuo ukivipeleka VETA, VETA hawataaka kuvipokea kwa sababu vina hali mbaya mno. Kwa hiyo niombe Wizara ilitathmini hilo na ione, isiendelee kubeba mzigo ambao haubebeki, tunayo VETA ambayo ni mamlaka inayoshughulika na mafunzo ya ufundi study, itaboresha vile vyuo na Serikali itasaidia kuboresha vile vyuo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia naomba nitoe darasa kidogo. Jana hapa kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja alisema yeye ni muhanga wa bima ya afya. Kiswahili ni sehemu ya bidhaa tuliyonayo kama Watanzania, neno muhanga linatumika kimakosa, muhanga ni kujitolea. Sasa wewe huwezi kujitolea ukawa muathirika wa bima ya afya na niwaombe hata waandishi wa habari wapo, wasaidie jamani neno muhanga ni kujitolea. Watu wengine wanakosea wanasema wahanga wa ajali, wahanga wa mafuriko; hakuna muhanga wa ajali, wala muhanga wa mafuriko. Hawa wote ni waathirika. Waathirika wa mafuriko, waathirika wa ajali na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niseme nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba niokoe muda.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika mjadala unaoendelea. Awali ya yote nakupongeza sana kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya. Tunaomba uendelee hivyo hivyo na hao wanaotoka kwa hiari yao waendelea kutoka, lakini najua sasa uko nje wameshaanza kung‟atana wenyewe kwa wenyewe. Uendelee na kazi vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze na suala la msamaha wa kodi kwa ajili ya Mashirika ya Kidini. Kwa kweli Waswahili wanasema akufaaye wakati wa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Sisi na Serikali yetu lazima tujiulize, Mashirika haya ya Dini yamekuwa yakitoa huduma nzuri sana. Leo hii tumejenga Zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga Zahanati za Umma, Zahanati za Mashirika ya Dini zinakufa. Mashirika ya Dini yamejenga hospitali, yanahudumia wananchi; na ukijaribu kuangalia utakuta kwamba kwa Mikoa ile ya Nyanda za Juu Kusini, Mashirika yale yana vifaa bora sana vya matibabu na vifaa vile wanaviomba kutoka kwa wafadhili. Wanapewa bure kabisa; na vifaa vile ni gharama sana. Leo unasema walipe kwanza kodi. Unapotaka walipe kodi, maana yake, hawana hata senti tano ya kununua vile vifaa. Wamepewa bure, halafu wewe unasema walipe kodi kwanza, halafu tukishahakikisha kwamba kifaa hicho kimefika hospitali ndiyo wadai; watadai vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuwe waungwana kama Serikali kwamba huduma wanayotoa ni kwa ajili ya wananchi wetu. Ningeomba Serikali yetu, wakati fulani tunasema Serikali yetu ina macho; iende pale Ikonda Makete, ikaangalie ile hospitali jinsi ilivyo bora na inavyohudumia idadi kubwa ya watu na inavyohudumia kwa bei ndogo. Iende Peramiho, iende Ilembula, wakaone zile hospitali jinsi zinavyohudumia wananchi. Waende pale Uwemba Mission wakaangalie jinsi wanavyohudumia wananchi; halafu unasema wakipata vifaa vya huduma, wakipata madawa walipe kodi kwanza halafu ndiyo warudishiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali ifikirie upya jambo hilo na ione kwamba jambo hili ni la msingi sana kuhakikisha kwamba Mashirika haya yanaendelea kutoa huduma kwa ajili ya wananchi wetu. Vinginevyo tutasababisha hali ya afya kwa wananchi kuwa mbaya sana. Zipo Zahanati zimefungwa baada ya sisi kuanzisha Zahanati zetu, japokuwa Zahanati zetu za Serikali hazijasimama, lakini katika Jimbo la Njombe Mjini najua kuna Zahanati ya Kifanya imefungwa, kuna Zahanati ya Rugenge imefungwa, kwa sababu tu Serikali imeanzisha Zahanati. Ni vizuri basi tunapoanzisha Zahanati za Umma, tuangalie hawa waliotufaa kwa miaka mingi, tunafanya nao nini kuliko kuwaacha tu solemba namna ile, inakuwa haipendezi na wala haifurahishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la elimu. Katika mfumo wetu wa elimu tunao vijana ambao huwa tunawachagua kuingia kwenye ufundi. Wengine wanakwenda sekondari lakini wengine wanachaguliwa kwenda kwenye ufundi. Vijana wale wanachaguliwa kabisa kwenye chaguo la Serikali kwenda kujiunga na zile shule za ufundi, lakini kwenye mpango huu wa elimu bure hawamo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasoma katika madarasa yale ya Elimu ya Ufundi hayana vifaa kabisa, hawana bajeti, hawana vifaa vya kutendea kazi wala hawana Walimu. Kama tunaona mpango huu ni mzuri, uendelee kuwepo; kama siyo mzuri, ufutwe kwa sababu watoto wale tumewapoteza pale. Tunawapotezea muda wao, lakini vile vile tunawanyanyasa, kwa sababu hatuwapi vifaa vya kufanyia kazi, hawana bajeti na wala hawana Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika suala la elimu, naomba sasa tufike mahali tufanye tathmini; tunao mtihani unaoitwa Mtihani wa Kidato cha Pili. Hebu Serikali sasa iangalie, hivi mtihani ule tija yake ni nini? Kwa sababu zamani tulivyoanza na ule mtihani wa Kidato cha Pili, shule zilikuwa chache, leo shule zinafika 4,000 tunaendesha mtihani wa Kidato cha Pili, mtihani ambao wastani wa kufaulu uko chini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Serikali iangalie ifanye tathmini; unaweza ukakuta pale tunapoteza fedha nyingi bila sababu na wala ule mtihani hauna tija. Vinginevyo, naishauri Serikali sasa itumie utaratibu wa wastani. Ni kweli utalalamikiwa na wengi, lakini ifanyike pilot study zichaguliwe shule kama 100 zianze na utaratibu wa wastani.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa wastani utakuwa na gharama ndogo kuliko utaratibu wa sasa ambao unatumia fedha nyingi kwa ajili ya mtihani wa kidato cha pili na mtihani wenyewe sioni kama una tija yoyote kwa sasa. Ni vizuri Serikali ikaliangalia hilo, ikafanya utafiti na kuona kwamba huu mtihani je, uendelee kuwepo ama ufutwe kabisa, tutumie utaratibu wa wastani ili kuboresha elimu yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni VETA. Waheshimiwa Wabunge wengi wanaomba sana VETA zijengwe, hata mimi kwangu naomba VETA ijengwe, lakini tunajenga VETA za kitu gani? Hii ni hoja ya msingi sana kujiuliza. Unapojenga Chuo cha VETA kama kile cha Makete, Makete umejenga Chuo cha VETA unatoa ufundi wa magari. Hivi Makete kuna magari mangapi? Halafu una zana ngapi za kufundishia magari?
Mheshimiwa Naibu Spika, naona tunajenga vyuo ambavyo kazi yake kubwa ni kuhamisha vijana vijijini kupeleka mjini. Kwa sababu ukifundisha ufundi wa magari Makete, maana yake unataka Wanamakete wasome ufundi wa magari halafu wahame Makete waende kuishi mjini, kwa sababu idadi yao ni kubwa na haiwezi kuhudumia kama mafundi ndani ya Makete. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iangalie, chuo kinachofaa kwa Makete ni Chuo cha Useremala; lakini ni useremala wa aina gani? Ni lazima tujikite kwenye useremala wa kisasa. Uko mfumo ambao sasa namwomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda atusaidie kuona, tutapata wapi teknolojia inayoitwa knock down system kwenye mbao? Kwamba unaunda furniture halafu unaitenganisha unaifunga kwenye box halafu unaisafirisha; ukifikisha unakofikisha unaenda unaiuganisha tena. Tukianzisha vyuo kama hivi kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini likiwemo Jimbo la Njombe Mjini, vitakuwa na manufaa zaidi kwa sababu mbao zipo na vijana wapo, kuliko mnatuletea vyuo vya teknolojia ambayo hatuwezi tukaitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunaomba VETA hizi zifundishe kilimo, kwa sababu kilimo ndiyo kinaajiri vijana wengi zaidi. Zifundishe kilimo cha kisasa, lakini zifundishe usindikaji wa mazao. Liko Shirika letu la SIDO. SIDO inafanya kazi nzuri, lakini imejikita kwenye vyuma sana. Vijijini huko tunaomba SIDO ijikite kwenye kilimo. Wataalam wa SIDO wafanye kazi za kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunakwenda kwenye hoja ya viwanda; nafahamu kwamba unapohitaji viwanda unahitaji uwe na ardhi, uwe na miundombinu, uwe na nguvu kazi yenye taaluma, unahitaji malighafi, mtaji, soko na teknolojia. Hivi ndiyo vitu vya msingi. Sasa hivi tunazungumza viwanda, lakini ardhi tunayo, je, hali ya miundombinu ikoje? Kiwanda kinahitaji maji, kinahitaji umeme. Hali ya nguvu kazi yetu ikoje?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaenda kuanzisha Mchuchuma na Liganga kwa nguvu zote. Vijana wetu kule wana elimu gani juu ya nini kinaenda kufanyika kule? Pia liko suala la mitaji; mitaji tunaitoa wapi? Vijana kwanza hawana dhamana hiyo; moja, lakini vile vile riba ni juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Benki yetu ya Kilimo ina fedha kidogo mno; tuangalie sana katika huu utaratibu wa viwanda, tunapohamasisha viwanda, tunaweza tukajikuta hii nchi tunaigawa bure kwa wawekezaji na vijana wetu wanakuja mahali sasa wanakuwa watumwa ndani ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la bodaboda. Vijana wengi ndiyo wanaendesha bodaboda na wamejiajiri kwenye bodaboda, leo hii wanaongezewa hii kodi. Vijana hawa ukiacha hii kodi ya usajili, lakini vile vile wana kodi za Halmashauri, vijana hawa wana kodi ya SUMATRA, wanalipa bima. Bima ya pikipiki moja ni sh. 60,000/=, unajiuliza mara mbili mbili, hivi ni kweli tumedhamiria kuwasaidia hawa vijana? Ukiangalia mpango wa Serikali sasa ni kwamba vijana wamiliki bodaboda zao. Ina maana tumewageuza vijana hawa kama kitega uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri jambo hili liangaliwe upya, vijana hawa sasa wapewe pikipiki hizi kama tunavyosema, ama waendeshe hizi pikipiki, lakini kodi nyingi zihamishiwe kwenye mafuta. Labda tuone, Serikali ije ituambie, hivi tukihamishia hizi kodi kwenye mafuta, kutatokea nini? Kwa sababu malalamiko haya yako mengi ya kodi ya SUMATRA, kodi za road licence, yako mengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji vijana wafanye kazi kwa utulivu na tukiwawezesha vijana hawa wakalipa kupitia mafuta na wote wanatumia vyombo vya moto, tutaepuka usumbufu wa kukimbizana na askari, tutaepuka watu wa makampuni ya minada kuajiriwa na TRA, kukamata wasiolipa road licence.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ugumu gani hapa kufanya hii iingie kwenye mafuta? Kwa sababu tutasaidia vile vile magari mabovu; hatutalalamikiwa, kwa sababu mtu anasimamisha gari miaka miwili, akiingiza barabarani anaanza kudaiwa road licence. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie ili kodi hizi ziingie kwenye mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sula la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie upya utaratibu wa pembejeo za ruzuku kama (wanufaika) walengwa hawanufaiki na mfumo wa sasa ambao mawakala wanawauzia wakulima mbolea kwa bei ya juu kuliko bei ya soko kwa maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la viazi mviringo ni zao la kiuchumi kwa wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini na Mkoa mzima wa Njombe katika msimu wa Machi mwaka huu. Viazi vimeathirika na ugonjwa ambao hadi leo haujafahamika vizuri. Sasa niiombe Serikali ifanye utafiti na kuwaelimisha wananchi ili waweze kujizatiti na msimu mwingine. Pia Serikali iangalie jinsi inavyoweza kusaidia mbegu mpya ya viazi kwa wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini ili kuwasaidia wakulima kwanza katika uzalishaji wa viazi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Kilimo; naipongeza Serikali kwa kuanzisha Benki ya Kilimo, benki hii iongezewe mtaji ili iweze kukopesha wakulima wengi zaidi. Benki hii ianzishe dirisha la mikopo kwa wakulima wa kati ili kusaidia kasi ya kilimo na kuongeza ajira kwa haraka, kuliko sasa inapojihusisha zaidi na wakulima waliopo kwenye vikundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki hii ifungue tawi Njombe kwani ipo katikati ya Mikoa ya Iringa, Ruvuma na Mbeya na Mikoa hii shughuli kubwa ya wananchi ni kilimo cha mazao ya chakula, hivyo itakuwa imejiweka katika mazingira ambayo yatawezesha huduma kwa wakulima wengi zaidi na kuwapunguzia gharama ya kusafiri hadi Dar es Salaam. Pia hata benki yenyewe itakuwa rahisi kuwatembelea wakulima. Haya yote mwisho wa siku yanaongeza tija na kupunguza gharama kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Elimu. Kwanza kabisa, naomba ni-declare interest kwamba na mimi ni mmiliki wa shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makubwa niliyonayo hapa ni ushauri. Kwa sababu muda wenyewe ni kidogo sana, nikimbie na mwendo wa ushauri. Kwanza kabisa, namshauri Mheshimiwa Waziri, pale Wizarani liko tatizo la watu kujifanyia kutoa maamuzi. Wanatoa maamuzi hata bila kuangalia maamuzi haya yana madhara gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa hivi tunajadili suala la ada elekezi. Ada elekezi ukijaribu kufanya utafiti, hayuko hata mtu mmoja anayelalamika, lakini watu wa Wizara wameamua tu kuandika elekezi, wanachanganya vichwa vya watu, Watanzania wanababaika na kuona kwamba kuna hoja ya ada elekezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili la ada elekezi Mheshimiwa Waziri alitolee ufafanuzi, Watanzania wajue kwamba ada elekezi unataka kumwelekeza nani? Aliyekwambia umpeleke mtoto shule huko ni nani? Kwani shule ya Serikali iko wapi? Shule ya Umma ipo, mtoto apelekwe akasome. Kama ukipeleka shule ya private maana yake umehiari mwenyewe. Utakayokutana nayo huko, acha yakukute. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uko mtazamo pale Wizarani kwamba watu wanaamua tu mambo. Kwa hiyo, naomba usimamie utaratibu. Wewe mama nakufahamu, ni mtaalam, unajua jinsi ya kusimamia mambo. Simamia utaratibu watu wafuate utaratibu wa kuandika na kutoa maelekezo ili kusudi tuonekane kabisa kwamba private sector inayotoa elimu ni wadau wa Serikali na Serikali iwe tayari kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ufaulu hafifu katika shule za Umma. Naomba Serikali ijitahidi kwa sababu leo hii tunaswaga hawa watoto wanaendelea kusoma, lakini tukumbuke, Mheshimiwa Waziri wewe ni mtaalam unafahamu, asubuhi umesema kabisa kwamba unasimama ukijiamini kwamba wewe ni msomi na umesoma katika elimu iliyo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa watoto tunaowaswaga leo waende wamalize Kidato cha Nne kwa kuongeza idadi tu, tukumbuke kwamba itafika siku hawa watakuwa watawala. Watoto hawa ndio watakaokuwa Mawaziri, Marais na Wabunge. Hebu tujiulize, Taifa hili litakuwaje? Tutaanza kulalamika huduma hospitalini ni mbovu, huduma kila mahali ni mbovu kwa sababu tu watoto ambao tunawaswaga waende ili tujaze madarasa na wamalize Form Four watakuwa hawajapata elimu iliyo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la VETA. Kwenye hotuba nimejaribu kupitia na kuangalia, wamejaribu kulieleza, lakini najiuliza, hivi Waheshimiwa Wabunge, nani Mbunge yumo humu ndani mtoto wake anasoma VETA? Maana tunang‟ang‟ania ooh, tuanzishe VETA watu wakasome VETA! VETA tulizonazo hazina ubora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni fundi, nafahamu fika taaluma inayotolewa kule VETA, tunaamini kuna ufundi, lakini hakuna ufundi wowote wa maana unaotolewa. VETA hawana vifaa, hawana machines; kama wanazo ni za kizamani mno! Tumejenga Vyuo hatukarabati, sasa leo tunataka watoto waende VETA, wakawe mafundi wa nani? Wafanye kazi ya nani? Naomba sana Serikali iangalie kwamba tunahitaji VETA sawa, lakini ziwe ni VETA zenye ubora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza VETA, watoto hawa wapewe mitaji ya kuanzia ufundi wao huko mitaani. Vile vile lazima tutambue, unapokuwa na Chuo cha VETA, ni vizuri ukawa na kituo kinachoweza kuwa na mitambo kwa ajili ya kusaidia watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unamfundisha mtu kushona nguo, halafu unataka akate na mkasi wa mkono, ataendelea saa ngapi? Mafundi wangapi wameendelea mpaka leo? Tuwe tunafanya na utafiti! Kama tunataka watu wawe mafundi wa kushona, tuhakikishe kwamba tuna viwanda vikubwa vya ushonaji ambavyo kazi yake ni kukata nguo wale wachukue wakaunganishe. Sasa wewe unataka mtu akate nguo ile ashone, haiwezekani kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ada elekezi…
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika mijadala hii miwili iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC kwa hiyo, nitajielekeza zaidi na Kamati hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jambo kubwa sana wakati tukipitia hesabu za Serikali za Mitaa lililokuwa likijitokeza lilikuwa ni upungufu wa watumishi. Lakini nitajikita zaidi kwenye upungufu wa watumishi kwenye shule za sekondari, shule zetu za sekondari zina shida kubwa sana ya walimu wa sayansi. Katika Halmashauri zote ambazo tuliangalia vitabu vyake kila Halmashauri ilionyesha ina shida kubwa sana ya walimu wa sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke tumetumia nguvu nyingi sana kujenga maabara, lakini sasa lipo tatizo la walimu wa sayansi. Niiombe na niishauri Serikali kwa kadri nionavyo mimi na nguvu tunazozitumia kupata walimu wa sanyansi bado ni kidogo mno, hitaji la walimu wa sanyansi ni kubwa, walimu waliopo ni wachache sana na jitihada tunazoziweka ni ndogo mno ili kupata walimu wa sanyansi. Katika suala la walimu wa sanyansi tatizo kubwa ambalo limetufikisha hapa ni wana sanyansi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema wana sayansi wenyewe, ukichukua mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza hajui chemistry ni nini hajui biology ni nini hajui physics ni nini. Lakini mwalimu anayeingia darasani anaanza kumfundisha na kumwambia haya masomo ni magumu sana. Sasa kitendo hicho moja kwa moja kinapelekea mwanafunzi aanze kujenga hisia kwamba masomo haya ni magumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana sisi kama Wabunge, niiombe Serikali tutumie muda mwingi kuongea na wanasanyansi na waweze kuongea na wanafunzi kwamba sayansi sio ngumu na tangu hapo sayansi wala sio ngumu. Kwa sababu ugumu wa sayansi unakuja pale tu ambapo sayansi haina hadithi nyingi, ikiwa ni suala la formula ni formula, ikiwa ni Archimedes Principle ni Archimedes Principle, hakuna maelezo mengi wala nini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana tujitahidi sana na kama Serikali inaona inafaa ni bora ikaanzisha shule maalum za sayansi kwa maana ya kwamba tukianza na shule za sekondari specially school for science kwa hiyo pale tutajenga misingi mizuri, wanafunzi wale wataingia pale wakiwa wanajua kwamba wao ni wana sanyansi, huko mbele watatawanyika watapatikana madaktari, ma-engineer, walimu. Kwa hiyo tutakuwa tayari tumejenga msingi mzuri wa sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwendo tunaonenda nao sasa na upungufu wa walimu wa sayansi ambao upo, kwa kweli kuja kukamilisha na kuweza kumudu kuwa na walimu wa sayansi wa kutosha ni kama ni ndoto. Naomba sana Serikali ilione jambo hili ni gumu na ilione kwamba hili linatakiwa lifanyiwe kazi haraka sana ili tuweze kupata walimu wa kutosha wa sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye suala la maabara, tulipokuwa tukipitia hesabu hizi na wenzangu wameseme uchochoro mkubwa wa fedha za Halmashauri umekwenda kwenye maabara, kila Halmashauri ilifika pale ikaeleza kwamba fedha imepelekwa kwenye maabara lilikuwa ni agizo la Serikali. Agizo la Serikali ni muhimu, kiongozi mkuu wa Serikali lazima aagize, asipoagiza huyo atakuwa ni kiongozi wa namna gani? Hoja inakuja watendaji hawa wanajua miiko? Kwa sababu pamoja na hayo maagizo wenyewe wamekurupuka tu wametumia mpaka fedha za kununulia dawa, wamechukua mpaka fedha ambazo zilikuwa za miradi ya maendeleo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana, sasa tufanye zoezi la muhimu la kupitia maabara hizi tujiridhishe kwamba viwango vya fedha vilivyoenda kwenye hizo maabara ni sawa sawa na ubora uliopo kwenye hizo maabara? Kwa sababu fedha yote katika Halmashauri wanasema imeenda kwenye maabara, kwa hiyo, ni vizuri tukaangalia sasa thamani ya fedha kwenye ujenzi wa hizo maabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la uwezeshaji wa vijana na akina mama. Lipo tamko ambalo linasemwa kwamba ni asilimia tano kwa akina mama na asilimia tano kwa vijana kutoka Halmashauri zetu. Lakini kama kweli tunataka kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu na kuwapa akinamama mitaji ya kujiendeleza kibiashara, naona asilimia hizo tunazozitaja hazitoshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu moja, asilimia hiyo haipo kisheria, lakini pili makusanyo ni kidogo sana. Jambo lingine Halmashauri zina majukumu mengi kweli kweli ambayo yanawabana hawa wanashindwa kuyatekeleza, sasa kuja kumpa kijana ambaye yupo mtaani kumuita kumwambia kuna asilimia tano yako hapa na wewe kama Halmashauri una shida ya fedha inakuwa ngumu sana. Ndio maana tunaona Halmashauri zote hakuna Halmashauri hata moja ambayo imemudu kutoa hizo fedha kwa asilimia 100 kwa miaka yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali iangalie utaratibu huu ikiwezekana ubadilishwe, uwekwe utaratibu mwingine ambao utaenda kwa uwiano mzuri na tutahakikisha kwamba vijana wetu na akina mama wanapata hizi fedha kwa utaratibu mzuri, vinginenyo tutakuwa tunatumia nguvu nyingi sana kuelekeza kwamba ni asilimia tano kwa akina mama na asilimia tano kwa vijana wakati kumbe uwezo wa Halmashauri ni chini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu shughuli za Halmashauri ni nyingi sana sisi kama Wabunge tukija hapa Bungeni tukitoa maombi kwa Serikali kwamba kwenye Halmashauri yangu kuna shida hii, kuna shida hii Serikali inatujibu kwamba lazima iwe kwenye bajeti. Ukienda kwenye bajeti kuongea na watendaji pale Halmashauri jamani tuliingize hili na wao wanakujibu wanakuambia ukomo wa bajeti. Sasa hebu angalia mkanganyiko huu jinsi ulivyokaa ndio ufikie mahali useme kwamba asilimia kumi ikatolewe kwa vijana na akina mama haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana sasa Serikali ione hilo na ijaribu kuangalia kwamba tunafanya nini ili tuwe na utaratibu unaofanana kwa nchi nzima unaowezesha kutoa fedha kwa ajili ya vijana na kwa ajili ya akina mama, lakini hizi asilimia imeonyesha ni zoezi lililoshindikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni suala la asilimia 30 ya makusanyo ya ardhi ambayo Halmashauri mbalimbali zimekuwa zikikusanya na zinapeleka Wizara ya Ardhi. Wizara ya Ardhi hairudishi zile fedha kule Halmashauri na hairudishi kwa sababu inasema hawajaomba. Hivi jamani kuna sababu ya kuomba kwanini tunaweka bureucracy katika hili, wewe mwenyewe Wizara ya Ardhi ume-declare kwamba 30 percent itarudi council warudishie wape na maelekezo fedha yenu hii nataka mfanye hiki na hiki, kama kuna utaratibu wa kukagua kakague. Wizara ya Ardhi imerundika fedha zote kwake, hairudishi Halmashauri inasema hawajaomba na tunataka fedha hizi zikirudi zirudi kwenye maendeleo ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Wizara ipo serious na inataka fedha zirudi kwenye maendeleo ya ardhi kwa nini isirudishe fedha na ikatoa na maelekezo halafu ikayasimamia maelekezo yake Halmashauri zikapata fedha. Kwa hiyo, unakuja kuona kwamba Halmashauri zinakusanya hii fedha na wakati mwingine Wakurugenzi wanajitoa, wanatoa mpaka matangazo lipia kiwanja chako kwa gharama za Halmashauri tukitegemea kwamba 30 percent itarudi lakini ardhi hairudishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali irekebishe utaratibu huo badala ya kukusanya na kurudisha ibakize ile asilimia 30 kule kwenye Halmashauri ili zibakiwe na ile fedha kwa ajili ya maendeleo ya ardhi. Kama kuna maelekezo wanataka watu wa ardhi wayafanye wayatoe, wawape watu wa Halmashauri ili kusudi watekeleze huo mpango ambao Wizara inaona unatakiwa utekelezwe na Halmashauri kutokana na hilo fungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la East African Meat. Katika Jiji la Dar es Salaam walianzisha mradi wa kiwanda cha nyama pale Ukonga, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba Halmashauri ya Kinondoni, Ilala na Temeke walichanga fedha pamoja na Jiji lenyewe kwa ajili ya kuanzisha huu mradi ya East African Meat, wakaweka na utaratibu wakaajiri na wataalam mchango ule kama mtaji walianza kulipana mishahara siku ile fedha ilipoisha na kampuni iliishia pale pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli huu ni utaratibu mbaya sana kwa watumishi wa umma kwamba Halmashauri zimechanga fedha, halafu mmeanzisha kampuni, fedha mliyoichanga kama mtaji mmelipana mshahara na maduhuli, safari na vikao vya bodi na nini halafu fedha imeisha kampuni imeishia pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Serikali iangalie suala hili, moja katika suala hili la East African Meat kuna suala la kiwanja kilichopo pale Gongo la Mboto. Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam inaanza kuonyesha kwamba kile kiwanja ni mali yake. Ninaishauri Serikali kile kiwanja sio mali ya Jiji kile kiwanja ni cha manispaa zote za Dar es Salaam. Kwa hiyo, Serikali ione na iweze kusaidia kuhakikisha kwamba katika mali kidogo iliyobaki ambayo ni kiwanja kilichopo Gongo la Mboto Halmashauri zote za Dar es Salaam zinanufaika nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi tena kwenye suala la elimu naomba niseme jambo moja. Sasa hivi tumehangaika na maabara na madawati, lakini katika nchi yetu kuna kitu kigumu sana kinakuja kinaitwa elimu msingi na hii tumeshaanza kuitekeleza. Elimu msingi hii italeta ugumu zaidi kuliko wa maabara, kuliko wa madawati, kwa sababu itakapofika mwaka 2021 vijana walioko darasa la pili sasa watakuwa wamefikia kuingia kidato cha kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wataingia kidato cha kwanza wakiwa darasa la sita, watamaliza darasa la sita wataingia kidato cha kwanza. Kwa hiyo na hawa walioko darasa la tatu sasa na wenyewe watakuwa wanaingia kidato cha kwanza. Imani tunayojipa kama nchi ni kwamba tumefikisha zaidi ya asilimia 75 watoto wetu wanaenda sekondari. Lakini tukumbuke kwamba wapo asilimia 75 lakini wana uwezo kiasi gani? Wanatembea umbali gani? Sasa tunataka tupeleke asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali hebu tuunde Kamati za Wilaya za kulisimamia zoezi hili kusudi kila Wilaya iwe na mtazamo wa kuona jambo hili tutalikabili vipi litakapofika kuna shida kubwa ya madarasa, itatokea shida ya nyumba za walimu, itatokea shida ya mahali pa kuishi wanafunzi kwa hiyo lazima tuone. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke watoto hawa ni wa Watanzania wote unapomfikisha mwanangu darasa la sita halafu unamwambia anaenda form one umenielimisha kiasi gani mimi kama mwananchi? Ni vizuri elimu kwa wananchi ikaenda ya kutosha ili kusudi wajue kabisa kwamba vijana walioko darasa la pili sasa wataishia darasa la sita baada ya hapo wataingia kidato cha kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo maelezo haya yaende sambamba hata kwenye taasisi zisizo za Serikali zinazotoa elimu, matokeo yake tutakaa kimya itafika siku ya siku wale vijana wameshatekeleza huo mtaala mpya wa elimu wanaingia kidato cha kwanza kila mtu anashangaa. Wote tutakuwa tunashangaa kama vile tulivyokuwa tunashangaa kwamba kwanini shule zetu hazina madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hili tunalifahamu na watu wote sisi ni waelewa hebu tulifanyie kazi likae vizuri kusudi fanya maandalizi ya kutosha tukijua kabisa kwamba sasa ifikapo mwaka 2021 vijana wote walioko shule ya msingi watakwenda sekondari, lakini watakuwa wanaingia sekondari wakiwa wamekomea darasa la sita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niseme nashukuru sana kunipa nafasi na naunga mkono hoja asante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Awali ya yote niwapongeze sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili jinsi walivyowasilisha taarifa zao kwa umahiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sana na Taarifa ya Tawala za Mikoa (TAMISEMI). Kwanza kabisa liko tatizo kubwa sana ambalo nafikiri ni vizuri tukaishauri Serikali ikaona jinsi ya kufanya. Tunalo tatizo kubwa sana la watendaji katika vijiji na watendaji katika kata. Maeneo mengi watendaji hawa ndiyo wanasimamia maendeleo, watendaji hawa ndio wanaosimamia usalama wa wananchi kule vijijini, lakini hakuna watendaji kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine utakuta mwanakijiji mmoja wamemteua pale ndiye angalau awe anasaidia kazi za utendaji halafu wanakijiji wale ndiyo wanachanga angalau kumsaidia hela ya sabuni yule mtendaji wanayemsaidia. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Njombe Mjini, Kijiji cha Idunda, ni kijana wa pale kijijini ndiyo amekuwa kama Mtendaji na ni muda mrefu kijiji hakina Mtendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo linalojitokeza ni nini? Wananchi wachange kwa ajili ya maendeleo yao, lakini wachange tena kwa ajili ya kumwezesha Mtendaji waliyemweka kwa muda sasa, vitu hivi vinaleta shida sana. Pamoja na ufinyu wa bajeti ambao Serikali inakuwa ikilalamika mara kwa mara, huu ni wajibu wake kuhakikisha kwamba Watendaji wanapatikana na Watendaji hawa ndio watakaosaidia kusimamia maendeleo kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji wa Kata hakuna, kila Kijiji, kila Kata utaona Mtendaji anakaimu, anakaimu, anakaimu. Wanakaimu kwa miaka na Mtendaji akishakuwa Kaimu anakuwa ni Mtendaji anayekaimu Kata na wakati huo huo ni Mtendaji wa Kijiji fulani. Kwa hiyo, unaona kabisa pale kwenye Kata panakuwa hakuna Mtendaji ambaye anasimamia maendeleo katika ile kata. Hivyo naiomba Serikali iangalie kwa namna gani; pamoja na ugumu wote wa tatizo kubwa la ajira na tatizo la ufinyu wa bajeti; wapatikane watendaji; watendaji ni muhimu sana katika vijiji vyetu; ili kusudi waweze kusimamia maendeleo kwenye vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba ku-declare, mimi ni mmiliki wa shule na katika suala la elimu kwanza kabisa nipongeze sana Mkoa wa Njombe na Halmashauri yangu ya Mji wa Njombe Mjini kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ziko changamoto nyingi kwenye sekta ya elimu ambayo sasa ni vizuri sana TAMISEMI wakajipanga vizuri na wakaangalia namna gani watasaidia. Wananchi wanajitahidi, wanajenga madarasa, wanaandaa thamani za madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko tatizo la Walimu, na kinachofanyika kule mashuleni ni kwamba, kwa kuwa Walimu ni wachache, yako madarasa ya awali katika kila shule ya msingi. Utaona utawala wa shule unaiambia Kamati ya Shule kwamba darasa hili la awali halina Mwalimu, kwa hiyo Kamati ya Shule inafanya utaratibu wa kuratibu ni kwa namna gani itapata Mwalimu; hivyo Kamati ya Shule inaajiri Mwalimu kwa ajili ya darasa la awali; wakati mwongozo unasema hakuna Mwalimu wa darasa la awali na kwamba Walimu wote wataajiriwa na Serikali na watalipwa na Serikali. Matokeo yake sasa hali hiyo inatia dosari nia nzuri ya Serikali ya kutoa elimu bila malipo pale ambapo sasa wazazi wanaanza kuchangia kwa ajili ya Mwalimu wa darasa la awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, Serikali iangalie hilo na kama kunahitaji maelekezo, basi itoe maelekezo kwamba Mwalimu wa darasa la awali awe ni Mwalimu mwenye cheti na aliyeajiriwa na Serikali. Kama Kamati ya Shule itaona kuna umuhimu wa kuajiri Mwalimu basi iajiri Mwalimu kwa ajili ya madarasa mengine lakini si kwa darasa la awali; kwa sababu darasa lile sasa linaonekana kwamba ni darasa hafifu au darasa la hali ya chini sana ndiyo maana wanaajiri yeyote tu kule kijijini aendelee kufundisha darasa la awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika madarasa haya ya awali, liko tatizo lingine ambalo sasa linaanza kujitokeza. Mwongozo unasema kwenye sera kwamba watoto wakifika miaka minne na kuendelea wakasome madarasa ya awali katika maeneo ambako shule za msingi zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta kwamba Shule nyingine ziko zaidi ya kilometa sita kutoka Makazi ya wananchi na wananchi wa vitongoji hivyo wamejenga madarasa mazuri sana yanasimamiwa na Serikali zao za Vijiji lakini watawala wa Idara ya Elimu wanazuia sasa watoto wasisome katika yale madarasa ya awali wapelekwe katika madarasa yaliyoko karibu na shule ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia umri wa yule mtoto ana miaka minne, atembee kilomita sita kwenda mahali ambako iko shule ya msingi, atembee kilomita sita kurudi. Huyu mtoto lazima atachukia shule lakini vilevile ni hatari kwake. Hayuko mtoto mdogo mwenye umri huu ambaye anaweza akatembea kwenda shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri ni kwamba; katika yale madarasa ambayo Serikali za Mitaa zimejenga au Serikali za Vijiji zimejenga na yako vizuri, Serikali iyasimamie yale madarasa ifuatilie kwa utaratibu mzuri ili kusudi watoto wale wasome kule kule wanakoishi na waweze kupata elimu kule kule wanakoishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala haya ya utawala huko vijijini, liko tatizo la posho na mkono wa ahsante kwa Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa. Bila kuwa na Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa hatuwezi kabisa kufanya chochote kama Serikali. Ni vizuri Serikali sasa ikaagiza rasmi kwamba kila Mwenyekiti wa Mtaa posho yake ni kiasi gani; maana ile posho sasa inakuwa ni ya kufikirika tu; inafikirika tu kwamba leo Halmashauri ina kiasi gani cha fedha basi apewe; haina basi anaambiwa leo Halmashauri haina kitu lakini ukifikiria kazi anayoifanya Mwenyekiti wa Kijiji ama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa Serikali ikatoa mwongozo rasmi kwamba, watendaji hawa, viongozi hawa waliochaguliwa na wananchi katika maeneo yale wanastahiki nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulimwengu wa sasa hayuko mtu ana uwezo wa kufanya kazi bila malipo. Hebu tuingiwe hata na huruma tu Serikali tuone kwamba watendaji hawa, Wenyeviti wa Mitaa na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji wana kazi kubwa wanayoifanya, wanaamshwa usiku, wanasuluhisha mambo mbalimbali kule vijijini, wanasimamia maendeleo, tunakwenda kule tunafurahia majengo yamejengwa vizuri lakini wao wenyewe hawana kipato chochote na wala hawapewi mkono wa ahsante wanapomaliza ile kazi yao ya kutumikia wananchi baada ya miaka mitano ikipita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la uwezeshaji wa vijana na akinamama. Tumeweka hii asilimia 10 lakini ukijaribu kuangalia asilimia 10 hii imekuwa bado haitoshelezi kuwawezesha hawa wananchi. Tuiombe Serikali sasa, ile fedha milioni 50 ambayo ilisema itaitoa, mchakato huu umekwenda muda mrefu mno na mchakato unapokwenda muda mrefu unakosa maana iliyokusudiwa matokeo yake unazalisha hadithi nyingine na kuona kwamba wananchi hawatatekelezewa ile ahadi. Hebu tuombe huu mchakato uende haraka iwezekanavyo ili kusudi fedha hiyo ipatikane na wananchi hawa wafanye maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Halmashauri zinafanya jitihada nyingi sana katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata ile asilimia 10, lakini asilimia hii 10 ni ndogo mno. Wenyewe tunajua kabisa hali ya Halmashauri zetu zilivyo hivyo tuone kabisa kwamba kama hii milioni 50 itapatikana itasaidia sasa kupunguza ile kiu ya wananchi kufanya maendeleo na kuwapa hamasa zaidi ili waweze kujikimu katika maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimalizie na suala la TASAF; Naipongeza sana TASAF kwa jitihada zote walizofanya, sana sana. Wanatusaidia sana, wamepunguza kiwango cha uhaba wa fedha kwa wananchi, lakini nafikiri waende mbele zaidi. Wafikirie sasa kwa fedha ile kidogo wanayowapa wawape malengo, kwamba ile ile fedha kidogo wananchi wale wajaribu kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine wawape time frame, kwamba fedha hii watapewa mpaka lini; kwa sababu kuna watu sasa wameshajisahau kabisa wanajua fedha ile sasa wao mpaka siku watakapokufa ndipo itakapokoma. Ni vizuri sasa wananchi wale wakaandaliwa, wakaambiwa fedha hii wanapewa mpaka lini na ikabuniwa miradi midogo midogo ya mazingira wanayotoka hawa wananchi ili waweze kuwasaidia, kwa sababu wote tunaamini kwamba hayuko mtu mwenye uwezo wa kumpa mtu fedha siku zote za maisha yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naipongeza sana TASAF na uongozi wake wote pamoja na Wizara inayosimamia kwa usimamizi mzuri. Tuombe sana wajitahidi sasa wabuni miradi midogo midogo, washirikiane na Mabaraza ya Madiwani kuona kwamba namna gani sasa fedha ile hata kama ni kidogo inaweza ikasaidia kuwawezesha wananchi wale ili kuwa na vitu endelevu kusudi kesho kama TASAF inakoma kutoa hiyo fedha wananchi wasijikute kama wameachwa jangwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami nachukua fursa hii kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake na Mawaziri wote waandamizi wenye Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli napenda nianze kabisa na suala la kilimo. Sisi kule Jimbo la Njombe Mjini ni wakulima na hatuna shughuli nyingine zaidi ya kilimo. Katika suala la kilimo nianze kabisa kwanza kwa kuipongeza Serikali na Waziri Mkuu mwenyewe binafsi, kwa kazi kubwa iliyofanyika kudhibiti lumbesa. Leo hii wananchi wa Njombe wanafurahia kilimo chao cha viazi kwa sababu lumbesa imedhibitiwa.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kiazi ni zao la msimu, naomba sana mikoa yote inayopokea viazi kutoka kwa wakulima wa viazi wa Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya iendelee kudhibiti lumbesa katika masoko yao hasa hasa Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Ruvuma, Mtwara na
kadhalika, ili tuweze kusaidia wakulima ambao wanalima zao hili la viazi. Leo hii wanafurahia bei ni nzuri na lumbesa imedhibitiwa naipongeza sana Serikali kwa jitihada hizo.
Mheshimiwa Spika, kilimo ndicho kinachoajiri Watanzania walio wengi. Naiomba Serikali, tunayo kazi kubwa sana ya kufikiria namna gani tunaweza tukasaidia vijana wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, ningependa kuishauri Serikali sasa ianzishe makambi maalum ya kilimo kama mashamba darasa makubwa ambayo yataweza kusaidia kuwaweka vijana mahali ambapo pana miundombinu sahihi ya kilimo; kuna maji, makambi ya kuishi, mashine za kilimo ili vijijini vijana waende pale wafundishwe kilimo bora, walime wapate mitaji, halafu baada ya muda watakuwa wamefikia umri wa kuweza kujiendeleza. Warudi sehemu nyingine wakaendelee na shughuli za kilimo. Kuliko leo kuwahamasisha vijana waende wakalime. Vijana hawa
kwenda kulima kwa jembe la mkono kwa maendeleo haya tuliyofikia, hawawezi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaanzisha Vyuo vya VETA na katika bajeti iliyopita nilisema, vyuo hivi tunavyoanzisha maana yake nini? Tunahamisha vijana kutoka vijijini kupeleka mijini. Tukianzisha makambi maalum ya kilimo kwa vijana na tukawawekea miundombinu sahihi, tutawawezesha
vijana hawa kubaki vijijini na kujishughulisha na kilimo katika mazingira yaliyoboreshwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali sasa iangalie tunapojenga Vyuo vya VETA na tujenge makambi maalum ya kilimo yenye mashamba makubwa ili kusudi vijana waweze kufanya hizo kazi katika mazingira yaliyoboreshwa. Huo ndiyo ushauri ninaoweza kuutoa kwa
Serikali juu ya suala la kilimo.
Mheshimiwa Spika, suala lingine kwenye kilimo linalosumbua ni mbolea. Mbolea ni muhimu sana katika kilimo, lakini iko mbolea ya ruzuku. Naiomba sana Serikali iongeze kiwango cha ruzuku kwenye mbolea hii. Mbolea hii ina matatizo makubwa mawili; kwanza kiwango ni kidogo
sana, lakini pili inafika kwa kuchelewa.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Njombe Mjini mbolea inafika mwezi wa kwanza. Sisi Njombe tunapanda mwezi wa Kumi na Mbili mwanzoni. Sasa unapotuletea mbolea kupandia mwezi wa kwanza, maana yake sasa unasababisha hii mbolea iende katika mikono isiyo salama.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie, wataalam nafikiri wapo; ni nini kinachowashinda kujua kwamba mkoa fulani msimu wa kilimo ni huu; mkoafulani msimu wa kilimo ni huu; matokeo yake wanakulazimisha ununue mbegu mwezi wa kwanza. Utapeleka wapi mbegu mwezi wa kwanza wakati wewe umeshapanda mwezi wa Kumi na Moja mwishoni? Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie itoe ruzuku ya kutosha na ihakikishe kwamba inaleta ruzuku hii katika muda ambao ndiyo muda wa kilimo kweli.
Mheshimiwa Spika, kingine ni suala la udhibiti wa mbegu. Mbegu za mazao zinahitajika kudhibitiwa. Pale Njombe kuna taasisi ya udhibiti wa mbegu, ina wataalam saba, ina gari moja inadhibiti mbegu kanda nzima; na hiyo kanda ni Mkoa wa Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa;
mikoa sita, gari moja; wataalam sita wanadhibiti mbegu. Ni jambo ambalo haliwezekani.
Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali iangalie utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba Kitengo hiki cha Udhibiti wa Mbegu na Ubora wa Mbegu kinapewa huduma inayotosha ili kusudi kiweza kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, vilevile hata sheria yake naomba iangaliwe, kwa sababu sheria ukikutwa na mbegu ambayo siyo mbegu halali, siyo mbegu safi, mbegu fake, faini yake ni ndogo sana. Kwa hiyo, mtu yuko tayari kuzalisha mbegu fake na kuuzia wakulima, kwa sababu anajua kwamba nikipigwa faini, itakuwa Shilingi bilioni 50 nami nimeshauza mbegu zaidi ya mabilioni ya pesa. Kwa hiyo, kwangu siyo tatizo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie Sheria ya Udhibiti wa Mbegu na ikiwezeshe kitengo hiki pale Njombe. Hawana hata maabara, wala store ya kutunzia mbegu. Wametunza tu mbegu hovyo hovyo. Mbegu ikileta tatizo kwa mkulima ukirudi taasisi ya mbegu,
ukichukua ile sampuli ya mbegu ambayo ililetwa na mzalishaji wa mbegu, ilishaliwa na panya. Kwa hiyo, hilo ni tatizo kubwa sana. Naiomba sana Serikali ikiangalie kwa jicho la pekee kile Kitengo cha Udhibiti wa Mbegu pale Njombe.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala lingine linalohusiana na mambo ya maliasili na hasa Kitengo hiki cha TFS. Sisi Njombe ni wazalishaji wakubwa sana wa mbao, miti, mijengo na makaa ya kupikia majumbani na kadhalika. Kitengo hiki hakijawa makini. Moja ya umakini ambao
nauona unaleta tatizo kwa kitengo hiki ni kwamba, kinaeleza Sheria ile ya Udhibiti wa Misitu na hasa suala la mkaa, kama vile nchi nzima tunafanana katika mazingira yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi Njombe tuna mazao ya misitu ya kupanda; tunalo zao la mti mmoja unaoitwa uoto au mlingo au muwati. Miti hii inapandwa kwa muda wa miaka mitatu mpaka minne inavunwa. Mazao yanayotoka hapo kwenye huo mti ni maganda ambayo yanachukuliwa
yanapelekwa viwandani kwa ajili ya ku-process mambo mengine huko viwandani. Vilevile matokeo mengine ni kuni, pia unaweza ukatengeneza mkaa. Sasa taasisi hii inasema kwamba mkaa sasa ni marufuku kuvuka Wilaya. Sisi Njombe milingo ni zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilidhani kwamba Tanzania Forest Service wanatakiwa waje Njombe walete nguvu za kutosha, wananchi wa Njombe wapande milingo mingi zaidi ili tufidie uzalishaji wa mkaa katika eneo lingine la nchi kusudi wananchi wengine waweze kupata mkaa. Huwezi kuzuia mkaa halafu hujaweka mbadala wa mkaa. Wananchi hawa watapikia nini; hasa wananchi kama wa miji mikubwa? Njombe kuna fursa ya kuzalisha hii miti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niombe TFS waje Njombe tushirikiane tuzalishe miti mingi, tuzalishe mkaa, wananchi katika nchi hii waendelee kutumia mkaa wakati tukiendelea kutafuta nguvu nyingine ya matumizi ya kupikia na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, vilevile wanaleta marufuku nyingine ambazo zinaleta kero kweli kwa wananchi. Wanasema ni marufuku kupakia mazao ya misitu kwenye pikipiki. Hivi hawa watu wa TFS wanaelewa maana ya mazao ya msitu? Maana yake kuna korosho humo ndani, ni marufuku
kupakia korosho kwenye pikipiki. Kuna kuni, ni marufuku kupakia kuni kwenye pikipiki; kuna mkaa. Sisi hatuharibu sana mazingira kwa maana ya kwamba tunatumia miti ya asili.
Kwa hiyo, wanapotoa hizi sheria au maelekezo naomba sana Serikali iangalie hii taasisi iweze kutoa maelekezo ambayo hayasababishi kero kwa wananchi. Unapotoa maelekezo kama haya kwamba ni marufuku kupakia mkaa au kuni kwenye pikipiki matokeo yake ni kwamba anapokuja Afisa mwingine wa Serikali, yeye anasema hii ni sheria, huruhusiwi kupakia mkaa kwenye pikipiki. Kwa hiyo, wananchi wananyanyasika kwa sababu tu hawa TFS wanatoa maelekezo ya jumla kwa nchi nzima. Mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini, siwezi kukubaliana kabisa na hili jambo, naiomba kabisa Serikali iweze kuwapa maelekezo ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, kingine, kuna kitu kinaitwa TP (Transit Pass). Naomba sana Serikali itusaidie sisi watu wa Njombe. Sisi ndio tunaozalisha mbao, miti, mijengo na kadhalika. Tukisafirisha mabanzi tu ndani ya Halmashauri ya Njombe, tunatozwa kitu kinaitwa Transit Pass. Sasa manufaa ya sisi kuwa na misitu ni nini? Tunapanda ile miti kwa jasho letu, tunazalisha miti kwa ajili ya wananchi wote, mbao na kadhalika; tukikutwa tu tumepakia kuni kwenye gari, pickup tani moja; Tanzania Forest Service wanataka tuwe na TP. Naomba Serikali iangalie tuweze kuondolewa TP wananchi wa Njombe ili kusudi tuendelee kuzalisha zaidi misitu, kwa sababu misitu tunayozalisha pale ndiyo inawasaidia
wananchi wote.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunikumbuka na kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kutokana na ufinyu wa muda nianze kwa kusema kwanza kabisa naunga mkono hoja. Pili, nitoe mapendekezo yangu juu ya masuala ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti yetu ya maji imepungua sana, licha ya kupungua na hata ile bajeti ambayo imekwenda ni asilimia 19 tu, na mimi naungana na wale wote wanaosema tuongeze kwenye tozo ya mafuta ili tuweze kupata fedha zaidi ili tupate maji zaidi kwa ajili ya vijiji vyetu huko Majimboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Serikali tutakapokubaliana kwamba tunaongeza tozo kwenye mafuta angalau kwa shilingi 50/= kwa lita basi mgawanyo wa fedha hizi uende sawa, isionekane tu kwamba upande fulani wa nchi ama upande fulani wa Majimbo ndio unapata fedha nyingi zaidi kuliko mwingine, kwa sababu tutakaolipia fedha kwenye mafuta ni Watanzania wote. Kwa hiyo, tupate kwa usawa, miradi yote ya maji igawiwe fedha kwa usawa.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais katika masuala ya maji anataka kumtua ndoo Mama wa Kitanzania na kasi ya Mheshimiwa Rais wako ambao hawaijui na wasioijua kasi Mheshimiwa Rais juu ya kumtua mama ndoo ni Wahandisi wa Maji walioko kwenye Halmashauri zetu, vilevile watu wa Idara ya Manunuzi wakiongozwa na Idara ya Manunuzi ya Halmashauri ya Mji wa Njombe pamoja na Mhandisi wa Idara ya Maji Njombe, hawana habari kabisa kwamba Mheshimiwa Rais anataka kumtua ndoo mama wa Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji ya Njombe haiendi, haiendi kwa sababu hawa watu wawili yaani Idara ya Manunuzi na Idara ya Maji hawana habari kabisa kama kuna kumtua mama wa Kitanzania ndoo ya maji kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana kwa kuwa, Idara hizi mbili Idara Manunuzi na Idara ya Uhandisi zipo chini ya TAMISEMI, TAMISEMI waziangalie Idara hizi ili kusudi waweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji kaka yangu Mheshimiwa Lwenge ni Injinia na kaka yangu Mheshimiwa Kamwelwe pia ni Injinia. Kadri tunavyofahamu teknolojia ya maji ilivyo rahisi haikupaswa sisi tukose maji, tunakosa maji kwa sababu ya uzembe wa wahandisi walioko kwenye Idara ya Maji huko kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji Njombe pamoja na Idara ya Manunuzi wanafanya manunuzi mwaka nzima, wanahangaika kufanya manunuzi, sielewi wananunua kitu gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi ya maji ya Igongwe imeshindikana kutekelezwa ndani ya Halmashauri ya Mji Njombe kwa sababu tu kwamba Idara ile ya Manunuzi imesimamia utaratibu wa manunuzi mwaka mzima, mpaka leo naongea hivi bado mkandarasi hajakabidhiwa mradi, bado anahangaika na taratibu za manunuzi. Mara sijui tusaini hiki, mara tusaini hiki.

Ninaomba sana kwa kuwa ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene wanaokufahamu sasa wanakujua wewe ni Mwanasheria, lakini mimi ninayekufahamu zaidi najua wewe ni fundi, tulisoma chuo kimoja. Walioko kule wanahitajika Technician ili wafanya ile kazi, Engineer ni mtu ambaye kwa kweli hana uwezo kabisa wa kushughulika na maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana tuweke vijana ambao wana moyo wa kushughulikia matatizo ya wananchi na wana uwezo mkubwa. Injinia kwanza anajisikia, kwenda kwenye mabonde yale ya maji na uinjinia wake anaweza kuona ni matatizo.

Kwa hiyo, ninaomba sana kwamba tuweke technician, vijana wadogo ambao wako tayari kuhakikisha kwamba maji yanapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi ya maji kule Njombe tuna shida sana ya miradi miwili ya maji, Mradi wa Lugenge na Mradi wa Ngalanga. Miradi hii imeathirika vibaya sana. Serikali imetoa fedha ndiyo, hata kama imetoa kwa kuchelewa lakini jinsi miradi inavyotekelezwa inatia huruma, mradi wa Lugenge ulikuwa ni mradi wa mwaka 2012 na ulikuwa ni mradi wa miezi tisa, leo hii ni miaka mitano mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiutembelea mradi unatia huruma, wananchi wale wanasikitika sana, mabomba yameachwa porini, mitaro imechimbwa na maji zaidi ya pale walipochimba. Intake zimejengwa hazijakamilika, Mhandisi yupo Mhandisi Mwelekezi yupo, Mhandisi wa Mkoa yupo, watu wote hao lakini mradi hauendi. (Makofi)

Ukiuliza Wizarani Mheshimiwa Waziri anasema fedha ipo walete certificate. Mkandarasi anatengeneza certificate anampelekea Mhandisi, Mhandisi anatoa copy certificate analeta ile copy wizarani, nani atalipa kwa malipo ya copy? Kwa hiyo, huu ni uzembe wa dhahiri kabisa na uzembe wa makusudi, wanasababisha wananchi wakose huduma bila sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe Wizara ya Maji mtusaidie hasa huu mradi wa Lugenge, naomba mje muukague na mtusaidie kwa sababu huu mradi umeshapitisha miaka mitano. Leo hii mkisema bei ya mradi huu utekelezwe kwa gharama zilezile haiwezekani, hata kama utaratibu hauruhusu, lakini vifaa vilivyokuwa vinanunuliwa miaka mitano iliyopita vikinunuliwa leo bei zimebadilika. Niwaombe sana Wizara ya Maji mtusaidie, mje muangalie mradi wa Lugenge ili kusudi tuweze kuurekebisha, kwasababu wananchi wale wanashindwa kuielewa Serikali, na tumekuwa tukiwashawishi mara zote kwamba maji yenu mtapata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walishatengenezewa mabomba mitaani, mabomba hayana hata maji lakini intake hazijajengwa na mabomba hayajalazwa ya kukamilika. Kwa hiyo niombe sana Wizara sasa itusaidie, ituletee mtaalam aje afanye ukaguzi na atoe ushauri tufanye nini na mradi huu kwa sababu sasa hivi tunaona hata mkandarasi naye anasua sua.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mradi wa Ngalanga nao unaonekana kama umekosewa kufanyiwa designing kwa sababu wenyeji wanasema chanzo hakina maji kabisa na wanashangaa mabomba yanalazwa watapeleka nini? Kwa hiyo niombe sana miradi hii miwili ya Njombe ikaguliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, katika Kamati yetu tulitembelea baadhi ya miradi ya umwagiliaji, kwa kweli inasikitisha. Unakwenda pale Halmashauri ya Lindi kuna mradi unaitwa Ngongo mpaka CAG amesema mradi unakosa umeme. Tumetembelea mradi hakuna dalili ya mradi kuanza leo wala kesho, ni pori. Sasa unajiuliza mpaka CAG anasema bado umeme halafu kuna pori hakuna maji, hawajalima wala nini lakini unaambiwa bado tu umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mradi wa maji tulitembelea pale Tabora nao ni hivyo hivyo, bwawa limekauka, fedha nyingi imetumika. Kwa hiyo, niombe sana kama kuna uwezekano kwenye miradi ya umwagiliaji nchi hii, kama tunaamini itatuokoa basi hiyo idara ya umwagiliaji huko wizarani ifanyiwe maboresho kwa sababu designing zao zimeonyesha kwamba miradi ile haina tija kabisa wala haifanyi kazi na wala haielekei kwamba inaweza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, gharama za maji. Yuko mjumbe hapa jana ameongea kwamba hivi haya maji ni huduma au ni biashara? Ni kweli watumia maji wanapaswa kulipia gharama za maji lakini gharama zenyewe angalau ziwe zinaendana. Mji wa Njombe gharama ya maji ni juu sana, unit moja ya maji Njombe ni shilingi 855, na katika hiyo bei unalipa tena na service charge ya shilingi 2,000. Lakini maji tunayopata katika Mji wa Njombe ni maji ya mtiririko, mitaro ile tulichimba sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu Njombe maji yetu yale pamoja na kwamba ni ya mtiririko hayana mtambo wa kuyasafisha wala nini, yanavyotiririka huko toka Mungu alivyoyaumba basi mpaka ndani ya nyumba zetu. Sasa gharama hii inavyokuwa kubwa namna hii wananchi wa Njombe wanalalamika na kusema kwamba hii inakuwaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyofika aliambiwa jambo hili lakini akatoa maelekezo. Kwa hiyo, naomba tena idara ya maji, lifuatilie jambo hili. Ni kweli EWURA walikuja lakini je, unampambanisha EWURA na mwananchi wa kawaida? EWURA wale ni wataalam, mwananchi wa kawaida anaelewa nini? Haiwezekani kabisa kama anataka kulinda haki za wananchi wetu tuwapambanishe eti EWURA kwa sababu EWURA wanakaa wanaongea na mlaji. Mlaji anamsikiliza mtaalam wa idara ya maji anachosema, mtaalam wa Idara ya Maji ameshapiga hesabu zake pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo haiwezekani upandishe bei ya maji kutoka unit moja kutoka shilingi 395 mpaka shilingi 855 kwa mara moja? Una sababu gani na unakimbilia wapi? Umebanwa na nini cha pekee mpaka uamue kupandisha maji kwa gharama kubwa namna hii? Haiwezekani kwa sababu kama ninavyosema maji ya Mji wa Njombe ni maji ya mtiririko na gharama yake sehemu kubwa tulifanya wenyewe wananchi kwa kuchimba mitaro na wenyewe Idara ya Maji wamekuja wamekuta ule mradi upo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana na kama haiwezekani kupunguza maji basi Mamlaka ya Maji ya Mji wa Njombe iondolewe, Idara ya Maji irudishwe Halmashauri kusudi ishughulikiwe na Halmashauri kusudi ishughulikiwe na isimamiwe na Halmashauri. Tunaamini kwamba gharama za maji zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoiendea miradi hii ya maji niendelee kusisitiza kwamba tuombe sana mhandisi, idara ya maji ya Halmashauri ya Mji wa Njombe ije iangaliwe upya kwa maana ya watalaam wake na ikiwezekana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, asante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu TBC Taifa na TBC FM. Hali ya usikivu wa redio hii katika Jimbo la Njombe Mjini ni adimu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumbukumbu zangu sijawahi kusikia hata siku moja redio hii ya Taifa ikisikika ndani ya Njombe. Kwa mara ya mwisho niliwahi kusikia iliyokuwa Idhaa ya Biashara ya RTD miaka ya 1980, baada ya hapo sijawahi kusikia tena RTD wala TBC Taifa au TBC FM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Shirika la Utangazaji la Taifa liweze kufunga vifaa vinavyoweza kuifanya TBC isikike Njombe Mjini na viunga vyake ikiwemo kuweka angalau studio ndogo ili habari za Njombe ziweze kusikika, pia kuwafanya Wananjombe wanufaike na matunda ya maendeleo ya nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutokusikika kwa TBC FM Njombe tunaifanya Njombe isipate habari za uhakika na kuwafanya Wananjombe watengwe na Watanzania wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, redio hii inaendeshwa na kodi za Watanzania wote hivyo Njombe ni haki yetu kupata taarifa kutoka chombo hiki cha Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kukusihi tupate usikivu wa TBC FM Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwakunipa nafasi. Na mimi nianze kupongeza Wizara ya Ujenzi kwa hotuba nzuri ambayo tunayo mbele yetu na tunaendelea kuijadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na jambo la Njombe Mjini, nashukuru kwamba ahadi ya Rais naona inaelekea kwenye ukweli kwamba nimepata kilometa nne za barabara za mjini nashukuru sana naomba hiyo kazi ifanyike. Kwa sababu iko hapa kwenye kitabu bado sijajua utekelezaji utakuwaje lakini naona mtunda na mategemeo ni mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu ambalo linaleta shida katika mji wa Njombe, ziko alama za “X”. Alama zile zimewekwa na TANROADS, alama zile zinawatia umaskini wafanyabiashara na wananchi wa Njombe. Alama zile zimewekwa miaka mingi hazijulikani lengo lake ni nini, nyumba zile wananchi wanalipia kodi, Wizara ya Ardhi bado inawatambua kama ni wamiliki halali wa vile viwanja, lakini wale wananchi zile nyumba hawawezi kukarabati, kuziendeleza na wala wakienda nazo benki hawawezi kupata mkopo kwa kuweka dhamana zile nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku ni kuwatia umaskini wananchi, naomba Wizara ifanye maamuzi kama haina fedha za kuwalipa fidia ama kufanya marekebisho ya zile barabara basi ifute zile “X” mara moja na iwaruhusu wananchi waendelee na maendeleo yao na ifanye kwamba barabara ya Mjini Njombe iwe nyembamba kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tutaridhika kabisa na ile barabara ilivyo, na tuko tayari kufanya mji wetu uendelee kuwa bora, kuliko sasa mmetuweka katika maisha magumu, nyumba zimetiwa alama za “X” haziendelezwi, mji ni mchafu watu wanashindwa kuuendeleza. Naomba sana Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo suala la mji wa Njombe na alama za “X”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la barabara ya Ludewa - Njombe. Barabara hii inaanzia katika msitu wa Itoni pale Nundu, barabara hii naona imetengewa fedha shilingi bilioni 35; ni fedha kidogo mno kwa barabara hii. Lakini kingine ambacho ni cha kushangaza, barabara hii inaanzia kujengewa Lusitu kwenda Mawengi. Barabara inaanza kujengwa kilometa 50 ndani, naomba Mheshimiwa Waziri arudishe barabara hii ianzie Itoni kuelekea Ludewa na iongezwe fedha kwa sababu huku ndiko tunakozungumza kila siku habari ya Mchuchuma na habari ya Liganga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya Mchuchuma na Liganga imeanza kuzungumzwa kwenye mabunge tangu Bunge alijahamia Dodoma, tangia watu wengine humu ndani hawajazaliwa mpaka sasa wanakuwa Wabunge, Mchuchuma - Liganga na tunalalamika nchi haina fedha lakini tumeacha mali inalala Ludewa. Chuma kipo pale, tunataka kuanzisha viwanda, tutaanzisha viwanda gani bila chuma? Niwaombe sana tutengeneze barabara ya Ludewa ili kusudi tuweze kutoa kile chuma tufanye maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la TAZARA. Tunazungumza habari ya reli ya standard gauge, ni jambo jema na wengi wamesema sana juu ya reli na kwamba reli ni uchumi. Lakini hebu tujifunze kule TAZARA kuna shida gani? Tunahangaika na barabara ya Tanzania Zambia kuikarabati kila mwaka, mizigo yote ipo barabarani, reli tupu haina kazi. Tunazungumza habari ya bandari kavu, sisi wa Kusini na sisi tunasema kama bandari kavu inatakiwa na ni muhimu tuiweke Mbeya ili kusudi mizigo ya Kusini mwa majirani zetu ipite kwenye bandari kavu itakayojengwa Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikusema toka mara ya kwanza lakini dakika zangu tano namuachia jirani yangu ili na yeye apate nafasi ya kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la madaraja. Sisi tumeomba katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, tujengewe daraja katika kijiji cha Mamongolo kuvukia kijiji cha Lupira, Wilaya ya Makete ili kusaidia wananchi kule waweze kuvuka kwenda hospitali kupata matibabu. Kuna mto mkubwa pale hauna daraja, lakini nimejaribu kuangalia kwenye kitabu sijaona, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utakapo…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, mpaji wa yote, ambaye yeye ndiye ametuwezesha wote tuwepo humu ndani siku hii ya leo, tukifurahia maisha ndani ya nchi yetu yenye amani ya kutosha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya chini ya Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Wamekuwa ni Viongozi ambao wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa sana kwa sisi wawakilishi wa wananchi na hasa sisi tunaotoka maeneo ambayo yanajishughulisha na kilimo. Kwa kweli nawapongeza sana na nawashukuru na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu waendelee kutoa ushirikiano kwetu, tuendelee kushauriana na kusaidiana ili kuboresha maisha ya wakulima na wafugaji wetu kwa kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na chakula cha kutosha na tunaweza kuendesha nchi vizuri kwa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwakilishi wa wananchi kutoka Jimbo la Njombe Mjini, jina hili mjini ni jina tu lakini Jimbo langu mimi lina Halmashauri moja lakini lina Tarafa mbili. Tarafa moja ni ya mjini lakini Tarafa nyingine ni ya vijijini na ina kata kumi na tunajishughulisha na kilimo barabara. Moja ya mbinu za kilimo ambayo tunatumia ni vinyungu. Wiki iliyopita headlines nyingi sana za habari hapa nchini zilizungumzia vinyungu na leo naomba niongee habari ya vinyungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna Mbunge amesema yeye amekuzwa kwa pamba na samaki na mimi nasema nimekuzwa kwa vinyungu. Kila mwananchi anayetokea Mkoa wa Njombe na yeye amekuzwa kwa vinyungu. Vinyungu sisi kwetu ni kilimo muhimu sana. Hizi sheria zinavyotungwa ni vizuri sana zikafanyiwa utafiti wa kutosha, kwa sababu unapotuambia watu wa Njombe tusilime vinyungu, sisi tunasema na mpunga usilimwe, kwa sababu mpunga ndiyo unaolimwa mabondeni na mpunga ndiyo unatumia maeneo makubwa zaidi kuliko vinyungu. Kwa hiyo kwa kutuambia sisi tusilime vinyungu tu ni kutuonea na kutufanya sisi tuendelee kuwa maskini bila hata sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba wataalam, sawa najua kuna Sheria ya Vinyungu inayosema tusilime mita sitini kutoka kwenye mtiririko wa maji, lakini maji hayahifadhiwi bondeni, maji yanahifadhiwa mlimani, ndiyo maana wote tunaokumbuka miaka ya nyuma baada tu ya uhuru na miaka mingine kidogo, kilimo chochote lazima mkulima alime makinga maji ndani ya shamba lake. Makingamaji ndiyo yanayohifadhi maji kwa sababu maji yale yatakuwa hayatiririki yote na kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wetu wa kilimo leo hawaelekezi wakulima juu ya makingamaji, watu wa mazingira na wenyewe wameng’ang’ana tu kuhusu mita sitini. Ninachosema, mita sitini itakuwa ni kuwanyanyasa wananchi na kuwafanya wafe na njaa, lakini kama ni kweli maji yanahifadhiwa bondeni basi na mpunga usilimwe kwa sababu wenyewe ndiyo unaotumia maeneo makubwa zaidi ya mabondeni. Nafikiri ujumbe huo umefika, Mheshimiwa Waziri, naamini hata huko Mwanza nina imani kutakuwa na vinyungu tu, haiwezekani kusiwe na vinyungu, Tanzania nzima tunalima vinyungu wataalam waangalie upya utaratibu wa kuhifadhi maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya suala la vinyungu sasa niongelee suala la mifugo. Nilikuwa najaribu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kuna mambo yamenisikitisha sana. Tuna tatizo kubwa sana la ng’ombe wa maziwa, ng’ombe hawa ndio ambao wanaweza wakawa na manufaa makubwa sana kwa wakulima walio wengi, lakini idadi ya ng’ombe wa maziwa ni wachache mno na uzalishaji wetu uko chini mno, sasa unajiuliza, mashamba yote haya kwa nini hayazalishi ng’ombe. Mheshimiwa Waziri mwenyewe katika hotuba yake amekiri kwamba maziwa yamepungua kwa asilimia 2.3 na anasema kwamba moja ya matatizo ni kukosekana kwa malisho, kuna ukame na malisho yamepungua, ukweli ni kwamba hata uzalishaji wetu wa malisho ni kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Watanzania lazima tuangalie kwamba tunataka kufanya nini kwenye kilimo, tunataka kufanya nini kwenye mifugo. Mifugo ina uwezo wa kuwaajiri vijana wengi sana. Leo hii kuna watu wanalima nyasi wanasafirisha nje ya nchi, hivi hatuwezi kweli kuanzisha ma-block makubwa ya kulima nyasi na tukaweka vifaa vya kutosha na vijana wakafanya hizo kazi. Tatizo kubwa tulilonalo ni kwamba tunawaambia vijana waende shamba, kijana wa leo ameelimika hawezi kwenda kushika jembe kwa mkono, ni lazima tuhakikishe kwamba tunaweka vifaa na mazingira wezeshi ili vijana wale wasimamie hayo mashamba kwa urahisi, lakini tunavyosema tu waende shamba hawataweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wangeweza kulima nyasi za kutosha, wakazifungasha na wakazisafirisha, lakini vilevile wakapeleka maeneo mbalimbali ambayo yana uhaba wa nyasi na mifugo ikapata nyasi. Sisi tunazalisha nyasi viroba 684,000, viroba 600,000 ni nyasi za ng’ombe 900 kwa mwaka, sasa ng’ombe 900 watatupeleka wapi? Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ilione hilo, ianze kuweka mpango maalum wa kuhakikisha tunakuwa na mashamba makubwa ya nyasi ambayo yatakuwa na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watendaji wa Mheshimiwa Waziri kidogo nao wameteleza. Katika ukurasa wa 106 wanaeleza kwamba kuna kiambatanisho cha viwanda vya maziwa, naomba waangalie hapo kwenye kielelezo hicho kama kinaelezea maziwa, maana yake kielelezo kilichopo katika ukurasa huo kinaeleza habari ya mbegu mama. Sasa sisi wenye interest na viwanda vya maziwa tunapata taabu sana kujua. Kwa hiyo, kama taarifa hizo zipo tunaomba watuletee tuweze kuziona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, kwanza tuongeze uzalishaji wa mitamba hii lakini pia tuongeze ukubwa wa mashamba kwa ajili ya malisho. Kwa sababu tunazalisha mitamba michache sana kwa mwaka, mwaka ambao ilizalishwa mitamba mingi ni kati ya mwaka 2011 na 2017 ambapo ilizalishwa mitamba 800 kwa nchi nzima, nchi kubwa namna hii hatuwezi kuzalisha mitamba kiasi kidogo namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye usindikaji wa maziwa lipo tatizo. Tatizo ambalo mimi naliona sasa hivi tumeingiza VAT kwenye mtindi. Sasa viwanda hivi, kwa mfano pale Njombe tuna Kiwanda cha maziwa kinaitwa CEFA, kiwanda kile ni cha wafugaji, ni kiwanda cha ushirika, tumeingiza VAT kwenye mtindi, matokeo yake wananchi wale hawapandishiwi bei ya maziwa kwa sababu kiwanda kinaingia gharama. Kwa hiyo, naomba Serikali iliangalie sana hilo kama kweli tuna nia ya kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la kilimo, upimaji wa udongo; tunahangaika na mbolea sawa, mbolea ni muhimu sana kwa ajili ya kilimo na nini lakini lipo suala la msingi zaidi, ni lazima udongo wetu ujulikane, kwa sababu mbolea ni dawa, kwa hiyo tunatibu nini katika udongo wakati hatujui kwamba udongo unaumwa nini. Kwa hiyo, ni vizuri sana Serikali ikaona kwamba, ni kwa namna gani sasa kila halmashauri lazima iwe na kifaa cha kupimia udongo, hata kifaa kile kidogo tu ili kusaidia kupima udongo. Wataalam wamesema chokaa ya kilimo ndiyo chokaa inayoweza kusaidia kurekebisha udongo, hapa Dodoma kuna mgodi lakini sijaona kama Serikali iko serious na ule Mgodi wa Chokaa ya Kilimo. Chokaa hii tuichukue tuisambaze kwa wakulima ili waweze kuongeza mapato yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zana za kilimo; hatuwezi kwenda kwa jembe la mkono, hata siku moja, lakini hata haya matrekta yenyewe ambayo tunayapata, ubora wake ukoje. Leo hii ukienda hapo Kilimo Kwanza, ukiyaona yale matrekta labda yana miaka mitatu au minne jinsi yalivyomomonyoka yanatia huruma. Unaona kabisa kwamba hata kama kuna uzembe katika matumizi lakini hata ubora uko chini. Naomba sana, wanaoshughulika na matrekta wahakikishe kwamba matrekta yanakuwa bora na wananchi wanaweza wakayapata matrekta hayo wakayatumia kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, mikopo ya matrekta na yenyewe siyo rafiki kwa wakulima. Unamwambia mkulima alipe asilimia 50 halafu asilimia 50 iliyobakia ndani ya mwaka mmoja, ni mkulima gani atakayeweza namna hiyo, kwa hiyo hilo nalo ni jambo gumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu suala la mbolea. Naipongeza sana Serikali kwa mpango inayokuja nao. Angalizo ambalo naomba niiambie Serikali yangu ni kwamba, lipo tatizo, sasa hivi wenye mbolea (importers wa mbolea) tayari wana mbolea kwenye ma-godown. Serikali itakaposema mbolea kwa utaratibu huu ambao inaelekeza sasa watakwambia hiyo mbolea inayokuja Mheshimiwa Waziri tunaomba tuiuze mwakani kwa sababu sasa hivi stock imejaa. Kwa hiyo bei itabaki palepale na wananchi wataendelea kuumia. Kwa hiyo, niombe sana, kama kweli mchakato huu upo, umekaa vizuri, fanyeni haraka inavyowezekana ili wananchi waweze kupata mbolea kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tozo, Mheshimiwa Waziri ameondoa tozo nyingi sana, kweli zinaonekana zina manufaa, lakini nimwombe sana sisi tunaotoka maeneo yanayolima chai wameondoa tozo ya Vyama vya Msingi vya Wakulima ya Sh.500/= kwa kilo. Hii tozo aliyoondoa haimnufaishi mkulima na wala haitakaa irudi kwa mkulima, hii ni tozo ya majani makavu kiwandani. Ilikuwa ni tozo ambayo viwanda vilikuwa vinarudisha kwenye Vyama vya Msingi ili kusudi vyama vile viweze kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa unahitimisha hotuba yake atuambie hii Sh.5/= aliyotoa, je, Vyama hivi vya Msingi vitaendeleaje kufanya kazi kwa sababu hotuba ya Kamati imesisitiza kuimarisha ushirika, anapouondolea ushirika tozo hii anaufanya ushirika ukose uwezo wa kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja zetu mbili zilizopo hapa mezani, hoja ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niwapongeze sana Wenyeviti wetu, niwapongeze Wajumbe wa Kamati wote wa Kamati zote mbili, lakini nisiwe nimepungukiwa fadhira niishukuru sana Ofisi ya CAG kwa jinsi inavyotusaidia Wajumbe wa Kamati hizi mbili kutuwezesha kiutaalam lakini kutusaidia kutuongoza namna gani tunaweza kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuchangia hoja ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Halmashauri mbalimbali zimekaguliwa nasi tumejaribu kuwahoji Maafisa Masuuli kama taarifa zetu zinavyoonesha, tumetembelea baadhi ya Halmashauri, lakini jambo kubwa ambalo
ningependa nilizungumzie zaidi hapa ni tatizo kubwa la maji. Kwanza kabisa naomba mtambue ndugu zangu, Wabunge wenzangu pamoja na Serikali kwamba kimsingi maji hayana mbadala, panapotakiwa maji lazima yapatikane maji, tatizo kubwa la nchi yetu mpaka sasa hivi tuna shida kubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha ajabu kuliko yote maji ndiyo kitu ambacho kina teknolojia rahisi, sasa najiuliza tatizo liko wapi! Kama maji hata kwa asili tu watu walichimba visima, walitengeneza mifereji wakapata maji wakatumia, leo hii pamoja na maendeleo tunayosema tunayo tunashindwa kupata maji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika Halmashauri unakutana na shida mbili kubwa, shida ya kwanza unakutana na matatizo ya usanifu wa miradi ya maji, shida ya pili unakuta kwamba mwenye mfuko wa pesa yuko Wizarani Halmashauri imekaa tu pale, mradi unapotekelezwa yuko mtu hapa katikati anaitwa Mhandisi Mshauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mhandishi Mshauri anaajiriwa na Halmashauri, lakini mradi unapoharibika Halmashauri hana cha kusema, ukiwauliza wataalam wa Halmashauri wanasema Mhandisi Mshauri alishauri hivyo na alisimamia hivyo. Sasa unajiuliza kwa mfano, tumeenda mradi mmoja kule Tanga unaitwa Changarikwa, mabomba mita 300 yanapasuka siyo hiyo tu, hata katika Halmashauri yangu ya Mji Njombe mradi wa maji wa Utengule mabomba yanapasuka. Ukiwauliza wataalam wa Halmashauri wanasema Mhandisi Mshauri ndio aliyesimamia huu mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tujiulize sasa kama Mhandisi Mshauri kimekuwa ni kichaka tutafute njia nyingine ya kufanya. Kama Mkoani kuna Injinia wa maji, Halmashauri yenyewe ina Injinia ya maji kwa nini miradi wasisimamie wenyewe, teknolojia ya maji ni ndogo sana. Tunagawa fedha hizi kidogo kuwapa Wahandisi Washauri wakati tumeajiri Wahandisi ndani ya Halmashauri wapo na miradi inakwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye upande wa ubunifu wa hii miradi, unakwenda mahala unakutana na mradi umebuniwa ni borehole wamechimba kisima, lakini umefungwa mashine ya diesel ifue umeme halafu ule umeme uingie kwenye submersible pump uendeshe ile pump ya maji. Mwananchi wa kawaida hawezi kulipa maji hayo, hawezi kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kutembelea mradi wa Mkonze hapa Dodoma tumeona hali hiyo, kwamba imefikia mahali wananchi kisima wanacho, miundombinu ipo lakini wanashindwa kuuhudumia ule mfumo wakaamua kumpa mtu tu aendeshe. Mtu yule amevuta umeme zaidi ya kilometa mbili. Sasa unajiuliza Serikali imeshindwaje kuvuta umeme ukaingia kwenye ile pampu ya maji mpaka mtu binafsi amefanya?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya maji inaharibika kwa sababu wabunifu wa miradi au mafungu yanayoletwa yanakuja na maelekezo kwamba huyu ndio Mhandisi Mwelekezi, atasimamia mradi huo ama atawabunia huo mradi. Nitoe ushauri kwa Serikali, tufanye haraka tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini ili kusudi jambo la Maji lishughulikiwe na Wizara. Kama ni Wizara ishughulikie Wizara, kuanzia mwanzo ubunifu, usimamizi, utekelezaji, ulipaji na kila kitu. Kusiwe na kusigana kwamba Halmashauri mara Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii certificate nyingi za maji hazijalipwa. Wapi zimekwama? Haijulikani! Wakandarasi wamefanya kazi hawalipwi. Miradi ya maji inaharibika kwa sababu Mkandarasi anakuwa amefanya kazi lakini hajalipwa. Matokeo yake muda unakwenda mrefu halafu gharama zinaongezeka za mradi Mkandarasi anakuwa hayuko tayari kuendelea kutengeneza ule mradi. Kwa hiyo naiomba sana Serikali harakisheni huo mchakato wa kuunda Wakala wa Maji ambao mwaka jana tumelalamika sana hapa Bungeni, nina imani Serikali ni sikivu italifanya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Idara ya Uhandisi, unatembelea miradi ya ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali unashindwa kuelewa kwamba hivi huyu ni Mhandisi kweli ambaye anastahili kuitwa Mhandisi? Kwa mfano, tulienda Tanga kutembelea Shule moja ya Msingi unakwenda kuangalia limejengwa jengo la msalani kwa ajili ya wanafunzi, lakini wote tunajua msala wa wanafunzi unatakiwa uweje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamuuliza Mhandisi anasema aah! mchoro uliletwa hivyo. Sasa unajiuliza wewe Mhandisi ulishindwaje kushauri? Kwa hiyo, tuna shida kubwa sana hata kwa hawa Wahandisi wetu wa Halmashauri, fedha nyingi inakwenda lakini uwezo wao wa kusimamia hiyo fedha ya kusimamia miradi ni mdogo sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linaleta shida kwenye Halmashauri zetu ni uchache wa wataalam hasa Wakuu wa Idara. Halmashauri nyingi ambazo tumepitia mahesabu yake kuna upungufu mkubwa sana wa Wakuu wa Idara. Kwa hiyo, inapokuwa kwamba Halmashauri haina Mkuu wa Idara au Idara fulani Mkuu wake anakaimu, matokeo yake ni kwamba hata maamuzi yake yanakuwa na sura hiyo ya kukaimu kaimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza anakuwa hajiamini, anashindwa kutoa maamuzi, anashindwa kufikiria kwamba idara yangu hii iendeje na niipangeje. Naomba kama TAMISEMI tunataka tuende vizuri, hawa wataalam wetu basi tuwathibitishe mapema. Tutoe maelekezo kwa Wakurugenzi kwamba ikiwa kuna mazingira ya kukaimu yanatakiwa yawepo, basi wawepo Wataalam ambao wana sifa ndio wakaimu hizo nafasi halafu muda ukifika wathibitishwe ili kuondoa hiyo nafasi ambayo inakuja kuleta ombwe hapo baadaye kwamba maamuzi hayafanyiki, shughuli zinachelewa ni kwa sababu tu kwamba mtu hajathibitishwa, lakini tukumbuke kwamba wananchi wanakosa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ukiangalia ushirikishaji wa kiidara. Idara ya ujenzi inapokuwa inatekeleza mradi kwa mfano tunataka kutekeleza mradi wa afya, watu wa afya hawashirikishwi. Tumekwenda Tanga tumekuta Idara ya Maji inatekeleza mradi kwa ajili ya wananchi, lakini wakati huohuo kuna sehemu ya kunyweshea ng’ombe wanaita hozi, hozi za kunyweshea ng’ombe mtu wa mifugo hajui kabisa. Imejengwa hozi, ng’ombe hawezi kunywa yale maji. Sasa unajiuliza, hili hozi alikuwa anajengewa nani? Kwa hiyo hapo kuna tatizo la ushirikishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda mahali tumekuta kituo cha afya kimejengwa kizuri sana, lakini ukiangalia mahali lilipowekwa jengo la upasuaji inaonekana kwamba kwenye mpango wa ujenzi kulikuwa hakuna ushirikishwaji. Wamejenga lakini hakuna miundombinu sasa inayoweza kuunganisha kati ya jengo la upasuaji na majengo mengine ya kile kituo cha afya, matokeo yake jengo hilo la upasuaji halitumiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niseme kwenye mipango yetu ya wataalam wetu wa Halmashauri pamoja na wataalam elekezi wanaanzisha miradi lakini matokeo yake mradi unafika mwishoni, mradi ni wa maji unafika mwishoni wanapotaka kuwasha pampu za maji zianze kufanya kazi unaambiwa hapa pana low voltage. Sasa unajiuliza jamani hivi kuna maana gani ya kumweka mtu msomi hapa? Kama hakuweza kuliona hilo kabla akaona kwamba hapa pana low voltage, naleta pampu za maji zenye uwezo huu, niwasiliane na wanaohusika na maji ili wajue kabisa kwamba pampu za maji zinazoletwa hapa zina uwezo, zinaweza zikatumia umeme huu. Mradi umekamilika lakini wanashindwa kwenda kwa sababu tu pampu za maji hazifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni pale ambapo Wataalam wa Halmashauri pamoja na hawa Wahandisi Wasimamizi wanafikia mahala kuwalipa Wakandarasi kazi hazijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wa Halmashauri wanathibitisha kazi ya Mkandarasi wakati kazi haijakamilika. Nitatoa mifano hii ya Tanga kwa sababu ndiko ambako tumefanya ziara. Unakwenda pale unamuuliza Mhandisi wewe hapa kwenye tenki lenu umesema kuna level indicator iko wapi hapa kwenye tenki? Yule akiamini kwamba sisi ni Wanasiasa hatujui level indicator anatuambia level indicator ipo kwenye DP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimuuliza wewe level indicator inakaa kwenye DP? Ukimbana kidogo na kumtikisa ndiyo anakiri kwamba aah! Mkandarasi hakuweka, lakini ameshalipwa na alishakwenda na muda wa matazamio ulishapita. Kwa hiyo ni jambo la kusikitisha sana unapokuwa na wataalam ambao wanathibitisha na Serikali inatoa fedha halafu kazi inakuwa haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningelipenda nilisemee ni kama walivyosema wenzangu. Baadhi ya Halmashauri kweli Wakurugenzi wake hawatilii maanani sana wajibu wao kama Wakurugenzi, wakipewa hoja za Kamati hawajibu. Hii inaleta shida sana wamebuni utaratibu wanajua kabisa kwamba Kamati inakaa miaka miwili na nusu baada ya hapo Kamati itamaliza muda wake itaingia Kamati nyingine. Wanajua kabisa kwamba hoja kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali huwa inakwenda kwa muda maalum, muda huo ukipita hiyo hoja inakuwa hoja mfu hakuna atakayekuja kuibua tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naiomba Serikali iangalie ni kwa namna gani sasa iweke utaratibu pamoja na kwamba hizi hoja zingine zinakuwa hazijajibiwa, lakini uwepo utaratibu wa kusema kwamba hoja hizi zinafuatiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nisisitize tu kwamba maoni ya Kamati naomba yazingatiwe hasa lile ambalo tunasema kwamba tunaomba Bunge liazimie kwamba sasa iundwe Kamati Maalum, ifuatilie matatizo ya miradi ya maji katika nchi yetu, kwa sababu maji hayana mbadala. Bila maji nafikiri hamna ambaye leo angeweza kutokea humu ndani. Kama wote tungekosa maji tusingetokea ndani ya Bunge leo kwa sababu tumekosa maji. Kwa sababu maji hayana mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiunda Kamati hii ndiyo itasaidia kuieleza Serikali na kuionesha Serikali upungufu ulipo na kuona kwamba nini sasa kifanyike. Kwa sababu hakuna mahali ambapo tuna mradi wa maji mzuri wa mfano kusema kwamba mradi huu kwa kweli umetekelezwa bila matatizo. Mradi utaona umetekelezwa lakini mabomba yanapasuka, mradi umekamilika maji hayatoki, mradi umekamilika wananchi hawawezi kuundesha ule mradi kwa sababu ya gharama zake. Limejengwa bwawa la umwagiliaji hakuna wakulima wanaohusika na kilimo, limejengwa bwawa la umwagiliaji bwawa limepasuka. Kwa hiyo ni matatizo mwanzo mpaka mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mapendekezo ya Kamati Bunge hili liridhie na yawe ni maazimio ili kusudi yaweze kusaidia kutatua tatizo la maji. Tatizo la maji katika nchi yetu ndio tatizo kubwa na linamgusa kila mwanachi, tukitatua tatizo la maji tutakuwa tumetatua matatizo mengi sana, magonjwa yote ya matumbo yatakuwa yamekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie bajeti ya dawa za matumbo ni kiasi gani, matumbo wananchi wanaumwa kwa sababu tu ya kukosa maji, lakini wakipata maji safi maana yake tumeokoa hiyo fedha wananchi wote watakuwa na afya tutaendelea na miradi mingine. Kwa hiyo, niombe sana hilo lizingatiwe tutatue tatizo la maji kwa wananchi ili kusudi wananchi wetu wawe na maji na waweze kufanya maendeleo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hizi taarifa za hizi Kamati mbili. Kwanza kabisa, niwapongeze Wenyeviti wa Kamati jinsi walivyowasilisha kwa umahiri lakini niwapongeze vilevile wanakamati wote walioshiriki kuchakata taarifa hizo mpaka hapo zilipofikia, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la upungufu wa walimu kwenye shule hasa hasa za msingi. Tatizo hili ni kubwa sana na Serikali inachelewa sana kuajiri. Ukitaka kuona Taifa linajimudu ama linaenda vizuri kwa maana ya misingi yake inajitetea vizuri na linaangalia mbele kwamba litafika wapi ni kusimamia elimu. Tunapokuwa hatupeleki walimu shuleni maana yake hili Taifa linaenda kuwa mfu kesho. Watoto hawa wanakosa walimu, wenyewe kama watoto hawawezi kulalamika, lakini matokeo yake tutayakuta huko mbele ya safari kwamba tutakuja kuwa na Taifa ambalo linajiwajibisha kabisa lenyewe kwa sababu watoto hawa watakuwa wamekosa elimu na maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi umetokea mgao wa walimu na tulivyojaribu kufuatilia tuliambiwa ni fidia ya walimu wenye vyeti batili. Mimi katika Halmashauri yangu Mji wa Njombe sikupata mwalimu hata mmoja wakati wenye vyeti batili walikuwa 12, hapa nifanyeje, si nione kama kuna upendeleo? Kama jibu ni vyeti batili, sijapata walimu na mimi wenye vyeti batili walikuwa 12. Kwa hiyo, tukienda kwa utaratibu huo kama ni kweli ni vyeti batili tunagawa tugawe kwa usawa. (Makofi)

Naomba niiambie Serikali kwamba Halmashauri ya Mji Njombe ni jina tu, lakini yenyewe ina kata 13 na kata moja tu ndiyo mji lakini kata nyingine ni vijijini, kwa hiyo, tuichukulie kwa kigezo hicho. Leo hii Halmashauri ya Mji Njombe ina upungufu wa walimu 454, hivi hapa tutatoa elimu kwa hawa watoto, si tunawapeleka tu wakacheze shuleni mwisho wa siku wanatoka hawajapata elimu yoyote. Naomba sana hili liangaliwe kwa sababu elimu ni suala muhimu sana, tukicheza na elimu maana yake ndiyo tunaliua Taifa taratibu. Sisi tunaweza tukawa hatuoni kwa sababu sisi tumepata elimu, lakini kipo kizazi ambacho tunakilea sasa ambacho kinahitaji kupata elimu. (Makofi)

Mheshimwia Mwenyekiti, tumeambiwa watahamisha walimu kutoka sekondari, zoezi hilo linakwenda polepole mno utafikiri kwamba wanaofanya hilo zoezi sijui hawalijui au hawana uhakika au hawajiamini. Haioneshi kabisa kwamba hili zoezi ni la haraka kwa sababu kuna shida ya walimu mashuleni hasa ukizingatia sasa hivi limetolewa tamko la marufuku kuchangisha mashuleni. Madarasa ya awali na baadhi ya madarasa walikuwepo walimu wanajitolea lakini wazazi walikuwa wanachangia sasa hiyo kitu tumeambiwa ni marufuku, hivi hatma ya hawa watoto itakuwaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine matamko ya Serikali yanatia shaka kwa sababu unakuja kuona kwamba yalikuwepo madarasa ya awali katika maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa yanakwenda vizuri kabisa na wananchi walikuwa wanalipa ada kwa ajili ya watoto wao, Serikali ikasema darasa lolote lile la awali lazima liwe chini ya shule ya msingi, ni marufuku kuwa na darasa la awali nje ya shule ya msingi. Watoto wale wamepelekwa kule shule ya msingi hakuna walimu, wameondoka mahali ambapo kuna walimu, hivi nia hasa ya Serikali ni nini, kwamba watoto wapate elimu au ni mtizamo ambao mimi nauona kwa upande fulani una kama wivu au chuki kwamba hawa wenye shule za watoto wananufaika kwa hiyo tuwanyang’anye hawa watoto tuwapeleke shuleni. Mmewanyang’anya watoto mmewapeleka shuleni, shuleni kule wale watoto hawana walimu, matokeo yake mnawaathiri watoto hawa. Kwa sababu watoto hawawezi kulalamika hamuwezi kuona madhara yake, lakini tutambue sisi wote ni Watanzania leo sisi tunawawakilisha wananchi, lakini hawa Watanzania wa kesho wanakosa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ziko ramani zinatoka Wizara ya Elimu zinaitwa MESS Makao Makuu kitu kama hicho zinapelekwa mashuleni kwa ajili ya ujenzi wa shule. Tumepiga kelele sana humu ndani juu ya suala la watoto wa kike kujisitiri. Maelezo yanasema kila shule iwe na mahali maalum pa watoto wa kike kujisitiri Serikali hiyo hiyo inaleta ramani haina chumba cha kujisitiri. Sasa hayo maelezo anapewa nani na anatekeleza nani? Hebu tuangalie tunapotoa maelezo tuhakikishe kwamba maelekezo haya yanakwenda kujibu ile kiu ambayo wananchi na wawakilishi wao wanahitaji wapewe huduma. Kama Serikali haiwezi kwa sasa kuwapa watoto hawa taulo za kujisitiri basi hata iwajee chumba maalum. Maelekezo yanasema hivyo, lakini utekelezaji unakwenda kinyume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo jambo lingine, uko mkanganyiko kati ya taasisi mbili za Serikali, iko Idara ya Wakaguzi wa Elimu lakini iko Idara inashughulika na usalama mahali pa kazi. Wananchi wanajenga darasa ile idara inakuja kusema darasa hili halina mwanga wa kutosha wakati Wakaguzi wa Elimu wamekagua na wamepitisha hilo darasa, sasa hapo wananchi wafanye nini? Kwa hiyo, nafikiri Idara hizi za Serikali zijaribu kuona ni namna gani zinaweza kushirikiana ili kusudi wananchi wakifanya shughuli ikikamilika iwe imekamilika. Siyo Idara hii ya Serikali inaseme shughuli hii haina sifa, shughuli hii ina sifa. Kwa hiyo, naomba Idara za Serikali ziwasiliane katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni elimu ya ufundi. Sasa hivi tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, ndugu zangu Wabunge humu ndani nawaambieni hivi viwanda tunavyohamasisha vijengwe tunakwenda kulifanya hili Taifa kuwa la watwana kwa sababu vijana wetu hawana ujuzi, sasa ni nani atakayefanya kazi kwenye hizo taasisi? Tunasema VETA wakati inakwenda mwendo wa konokono hakuna mfano wake, hawana vifaa wala walimu, VETA wana mitaala ya miaka 70 iliyopita wanafundisha sijui calibrator, wanafundisha vitu vya ajabu ajabu ambayo havipo kwenye ulimwengu wa sasa wa utendaji hasa hawa ndiyo wanatakiwa kwenda kufanya kazi kwenye viwanda vinavyojengwa na tunafahamu viwanda vinavyokuja ni vya teknolojia ya kisasa. Kwa hiyo, tunakwenda kuwapeleka Watanzania mahali ambapo watakuwa wafagia uwanja, wapakia mizigo, ndiyo kazi wanazokwenda kufanya. Kama kweli tunahamasisha viwanda sisi kama Watanzania tuwapange vizuri vijana wetu wapate elimu nzuri ya kuweza kuajirika huko kwenye viwanda vyenye teknolojia ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la UKIMWI. Tafiti za UKIMWI zinanitatanisha sana, mimi ni Mbunge wa Njombe Mjini na ukiangalia kwenye taarifa za Serikali Njombe ndiyo tunaambiwa sisi tunaongoza kwa UKIMWI katika nchi hii, lakini hizi data ni za lini kwa sababu mimi hapa nahisi kuna kuonewa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za miaka kumi mpaka leo ndiyo zinatumika kwamba Mkoa unaoongoza kwa UKIMWI Tanzania ni Njombe, siyo kweli tutendeane haki. Kama mnataka kutoa utafiti wa kisasa na wa kitaalam fanyeni utafiti kila mwaka.

T A A R I F A . . .

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nina mashaka sana na takwimu hizi za Serikali juu ya suala la UKIMWI. Hata hivyo, kama kweli Serikali inatuona kweli sisi watu wa Njombe ndiyo tunaongoza kwa UKIMWI mbona haitusaidii kupunguza UKIMWI? Zana zile za kujikinga hatuletewi…

T A A R I F A . . .

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hizi za Serikali sawa tunakubaliana nazo kimsingi, lakini ukitokea ukame hapa, wale wanaokuwa wamefiwa na ng’ombe huko, Serikali inawapa ng’ombe; ikitokea njaa watu wanapelekewa misaada ya chakula. Sisi tuna UKIMWI, kwa nini hatusaidiwi? Kama sisi tuna UKIMWI, tupeni hiyo misaada basi tuione. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaichotaka Serikali ioneshe kweli kwamba Njombe wanateketea. Njombe ikiteketea, maana yake Watanzania watokosa chips, ndio wakulima wa viazi hao, watakosa maparachichi, mtakosa ma- housegirl mnaokuja kuwachukua Njombe na sisi tumepiga marufuku. Kwa sababu hawa watoto wetu mnawachukua kwa ajili ya kufanya kazi za ndani, nao ni sehemu ya kuchangia UKIMWI Njombe. Mnawaacha kwenye majumba yenu, hawana ulinzi wala uangalizi, wanaambukizwa UKIMWI wanarudhishwa vijijini kule, wanaenda kupaka vijana vijijini. Kwa hiyo, nawaomba sana, msije tena Njombe kuchukua ma-housegirl, tumekataa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu kwa leo ni hayo.
Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante wa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, mpaji wa yote kwa kutujalia afya njema mchana wa leo na tunaendelea kuijadili Bajeti yetu ya Mwaka wa Fedha wa 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niseme nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ujumla. Vile vile nawapongeza Mawaziri wote na Serikali yetu kwa ujumla kwa kazi nzuri wanazoendelea kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya nchi yetu na kwa manufaa ya Watanzania wote. Leo tumepata taarifa kwamba amekutana na Profesa John ambaye ndio Mkurugenzi wa Barrick, amefika na wamekubaliana kwamba tukae chini tuongee na Kampuni ya Barrick imekubali kutulipa Watanzania sehemu ya fedha ambayo tunaidai na tutarekebisha mikataba kuifanya nchi yetu ipate manufaa makubwa sana kwenye machimbo ya madini mbalimbali ambayo tunayo hapa nchini. Mheshimiwa Rais amesimamia kwa niaba yetu wote Watanzania. Tuna wajibu wa kumpongeza na kumwombea ili aendelee na kazi hiyo vizuri, tuweze kunufaika kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijikita kwenye bajeti iliyopo mbele yetu, nianze na suala la maji. Kuna miradi ya maji kwa kweli inasuasua sana. Kama ahadi ya Mheshimiwa Rais inavyosema, ni kumtua ndoo mwanamke wa Tanzania, lakini kwa mwendo huu tunaokwenda, sidhani kama tutafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi ya maji iliyopo katika Jimbo la Njombe Mjini, upo mradi wa maji ambao tumeambiwa kwamba tutapata fedha kutoka Serikali ya India, ni mkopo. Sasa hivi ni mwaka mzima, hakuna hata dalili ya hiyo fedha kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa kwamba documents na mikataba yote iko ofisini kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kwa taratibu za nchi na nchi. Hebu tuombe sasa basi hiyo fedha ipatikane ili Mradi huu wa Maji wa Njombe Mjini uweze kufanyika, vinginevyo wananchi wa Njombe wataendelea kuteseka sana na kuona kwamba Serikali haiwajali. Mji wa Njombe jinsi ulivyo, umezungukwa na mito pande zote mbili; ni jambo la kusikitisha sana kwamba tunapokuwa Njombe tunakosa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, miradi ya maji ya Njombe inasuasua sana na kinachofanya isuesue; na nimeshalalamika sana hapa Bungeni, inawezekana kabisa kwamba ndani ya Halmashauri ya Mji wa Njombe kuna shida ya wataalam. Tunaomba sana Wizara ya Maji na Umwagiliaji ikishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango waone namna gani wanaweza kutusaidia tupate wataalam wa kutosha waweze kusaidia hii miradi iweze kwenda ukiwemo Miradi Rugenge na Igogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiacha Miradi ya Maji ya Njombe nije suala la Liganga na Mchuchuma. Suala hili kwa kweli linasikitisha sana. Ni mradi ambao ni miaka mingi sana tumekuwa tukiuongelea. Wapo watu mpaka sasa wanazeeka wanaacha Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana ukizungumza habari ya Liganga na Mchuchuma, watu wanafikiri ni vitu ambavyo viko hapo hapo pamoja. Ni kwamba Liganga na Mchuchuma viko sehemu mbili tofauti na vina umbali zaidi ya kilometa 80. Kutoka Liganga kwenda Mchuchuma pana kilometa 80, lakini kinachotakiwa kuchimbwa ni chuma kilichopo Liganga na kuna makaa ya mawe yaliyopo Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kuvuna chuma hivi ni kweli makaa ya mawe ya Mchuchuma yatatumika yote kwenye chuma? Kama makaa haya yana matumizi mengine, basi makaa yaanze kutoka. Hivi makaa yanahitaji process gani? Kwa sababu tunachojua sisi, kwa
mfano ukienda kule Ruvuma wanakochimba makaa ya mawe, kiko kile kijiko kinachimba na crusher, vitu viwili tu; na magari yanasomba yanasafirisha makaa. Tuombe na sisi yale makaa yaanze kutoka tuanze kupata manufaa yake. Vinginevyo tuambiwe kwamba makaa ya Mchuchuma yanatosha kwa ajili ya kiwanda cha Liganga tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dalili ya mvua ni mawingu. Tunapotaka kuchimba chuma cha Liganga na tunapotaka kuchimba makaa haya ya Mchuchuma yatasafiri kwa barabara. Barabara ya Itoni – Manda ni ya vumbi na ipo kwenye ilani iliyopita na ipo kwenye ilani hii. Tumeambiwa itaanza kutengenezwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha iliyopatikana ni kuanzia kipande cha kilometa 60 kuanzia Mawengi mpaka Lusitu. Sasa kipande hiki ni kidogo sana, sehemu kubwa ya barabara itakuwa bado ya vumbi. Kama kweli hiki chuma kitatoka, maana yake kutakuwa na malori yanayosafirisha chuma kwa sababu tumeambiwa uzalishaji ni tani milioni moja kwa mwaka. Ukifanya hesabu ya kawaida tu kwamba lory libebe tani 30, ni malori 76 kwa siku yatabeba chuma. Kweli malori 76 yatapita barabara ya vumbi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi Wananjombe tunaona kabisa kwamba hatutendewi haki na hatuambiwi ukweli. Tunaambiwa tu kwa kuridhishwa kwamba huu ni mradi wa kielelezo, lakini hakuna cha kielelezo wala cha nini. Sasa tunasema tunataka kazi hii ianze, kama haianzi, basi habari ya kwamba Mchuchuma na Liganga ni mradi wa kielelezo, ifutwe na isiwepo, tuseme kabisa kwamba hii tumeiacha kwa sababu ni deposit ya miaka ijayo, karne ijayo na vizazi vijavyo. Ieleweke hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara sisi tunaihitaji, kwa sababu ukiacha Mchuchuma na Liganga, tunahitaji kusafirisha mazao. Chakula kingi kinatoka Ukanda wa Ludewa; viazi vinatoka Ukanda wa Ludewa, vije kwenye masoko yanayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Njombe – Ludewa inatakiwa iwe ya lami ili tusafirishe mazao. Kwa sababu tunaona katika nchi hii, sehemu nyingine zimetengenezwa barabara za lami, nasi tunahitaji barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, ndugu yangu Mheshimiwa Hongoli pale amelizungumzia. Sisi Njombe miti na mbao ni zao kama mazao mengine. Sasa figisufigisu na mizengwe inayowekwa kwenye mbao inatukatisha tamaa. Kwa sababu mkulima wa kawaida ana uwezo wa kuvuna miti yake na kuiuza sokoni. Vinginevyo, tuambiwe kuanzia sasa ni marufuku wakulima kuvuna miti yao; na maana yake ni marufuku wasipande miti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapanda miti, anapasua; akifika barabarani anaulizwa mashine ya EFD kwenye mbao. Jamani, hebu Serikali ifanye kazi, muwe mnajua na mazao ya wananchi wenu, kwa sababu mbao ni mazao ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hiyo, kuna kitu kinaitwa TP (Transit Pass). Sheria inasema, Transit Pass unadaiwa unapovuka Wilaya. Ndani ya Wilaya ya Njombe watu wanadaiwa Transit Pass; ukibeba kuni, Transit Pass; ukibeba mabanzi, Transit Pass; sasa inasikitisha sana kwamba wananchi hawa wanapanda miti; sehemu kubwa ya nchi hii haina miti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Njombe kupanda miti ni maisha ya kawaida humhimizi mtu. Sasa bado wanakuja kupata adhabu kwenye kuvuna. Kama tunataka twende pamoja tutunze mazingira na mkumbuke kwamba ukanda ule una vyanzo vingi sana vya maji, basi tusaidiane. Kitu kama Transit Pass naomba Serikali itoe ufafanuzi kwamba Transit Pass ikatwe nje ya Wilaya. Kwa mfano, kama unasafirisha mbao kwenda nje ya Wilaya uwe na Transit Pass, mabanzi yasiwe na Transit Pass, kuni zisiwe na Transit Pass ili wananchi wale waone kupanda miti kwao ni sehemu ya maisha ya kawaida na waweze kuona neema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la vijana. Vijana wa Kitanzania tumewasahau jumla! Ni jambo la kusikitisha sana! Kama tunataka kujenga Taifa bora lenye vijana wanaoweza kufanya kazi na kuitetea nchi hii, ni lazima tuweke mikakati muhimu sana na kabambe kwa ajili ya vijana. Vijana wa Tanzania wale tu wanaomaliza Kidato cha Nne kwa mwaka ni vijana 400,000 kwa matokeo ya waliofanya mtihani wa Form Four mwaka 2016. Waliochaguliwa kwenda Kidato cha Tano wapo 99,000. Vijana zaidi ya 300,000 wamebaki. Hakuna mpango wowote wa Kitaifa kuwasaidia. Kichaka tunachojificha ni asilimia 10 ya Halmashauri. Hivi are we serious? Vijana hawa watasaidiwa na asilimia 10 ya Halmashauri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali iseme upya kwamba vijana hawa tuwafanyie nini? Kama Wizara ya Fedha na Mipango mnataka fedha, tengenezeni walipakodi. Hawa ndio vijana walipakodi, wapewe maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikishauri hapa Bungeni, tuanzishe makambi kabambe kabisa ya shughuli za vijana, tuwawezeshe vijana kwa mkakati maalum ili vijana hawa waweze kuwa na kipato. Wakishakuwa na kipato watakuwa walipa kodi, lakini tunapowaacha hivi vijana 300,000 na mwakani 300,000 na mwaka mwingine 300,000, tunakuwa na vijana wazururaji, walalamishi, vijana ambao tutashindwa kuishi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, nianze kwa kusema naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali jinsi inavyofanya kazi. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Watendaji wote wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri Mkuu imeeleza kwamba bado tuna nafasi ya kuweza kukopa kama Watanzania kwa sababu deni letu ni himilifu. Naomba sasa tukope ili kusudi miradi ya maendeleo ambayo katika Jimbo la Njombe Mjini haitekelezeki, sasa itekelezeke. Mradi wa kwanza ni ujenzi wa barabara ya Itoni – Manda. Barabara hii miaka yote imekuwa ikiambiwa itajengwa ili kwenda Mchuchuma na Liganga, lakini haijengwi. Amewekwa mkandarasi kilometa 50. Kutoka Njombe ni kilometa 50 ndani ya Jimbo la Ludewa, lakini mkandarasi yule hana nguvu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha kuanzia Njombe mpaka linapoishia Jimbo la Njombe Mjini hakijaanza. Sasa tuombe kama fedha hiyo ya kukopa ipo. Kama Serikali ina fedha ya kutosha, iweke mkandarasi mwingine aanze kutengeneza barabara kutoka Itoni kwenda Manda ili kusudi tunaposema kwamba tuna mradi kielelezo wa Liganga, basi hata barabara iendane. Maana barabara ile ina uchumi mkubwa kwa wananchi lakini vile vile ina madini hayo yaliyopo huko ambayo tunahitaji yachangie uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni maji. Maji katika Jimbo la Njombe Mjini ni tatizo kubwa sana. Miradi ya maji haitekelezeki. Wakandarasi wako site lakini malipo yanachelewa sana. Yuko Mkandarasi anafanya kazi katika mradi wa Igongo, malipo yake yanachelewa sana; na tunajua kabisa kwamba hela ya maji ni hela ambayo wote tunachangia kupitia mafuta na kadhalika. Kwa hiyo, naomba sana, kama Wakandarasi wako site na wanafanya kazi, basi walipwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, ni msikivu na anajitahidi kufanya kazi vizuri, lakini tunajua kabisa kwamba matatizo yapo kwa Watendaji, lakini kwake kama Waziri na Naibu wake wanafanya kazi vizuri mpaka wanajitwisha na ndoo. Hii ni dalili kwamba kazi wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la maji ya Njombe Mjini. Mradi wa maji Njombe Mjini leo hii nasimama hapa Bungeni kwa mara ya tatu na kila bajeti inapokuja ya mwaka wanataja mradi wa Njombe Mjini tutapata maji kutoka Mto Hagafilo, lakini mradi ule haujatekelezwa mpaka leo. Tumeambiwa upo kwenye miradi ya miji 17, tunataka tuambiwe safari hii shida ni nini? Vinginevyo, tuambiwe kabisa kwamba mradi ule haupo ama upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kabisa kwamba iko miradi mikubwa katika mikoa mingine inatekelezwa na watu wanapata maji, lakini sisi pale Njombe maji yapo kilometa tisa yanatakiwa yafike katikati ya mji, tunashindwa kuyapata yale maji, kila siku tunaambiwa fedha ipo, tutafanyiwa lakini hatufanyiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la afya. Naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri inayofanya. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, sisi katika Jimbo la Njombe Mjini tumepewa shilingi milioni 500, tunajenga Kituo cha Afya pale Ihalula, lakini pamoja na ujenzi huo wa Kituo cha Afya, wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri wanajenga kituo kizuri sana cha afya katika Kata ya Makoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Makoo, Kata ya Ihalula na Kata ya Utalengoro ni Kata ambazo ziko mbali sana na mjini. Tunaomba, tutakapokuwa tumekamilisha kazi hizi, basi tupewe magari ya wagonjwa, lakini tupewe Waganga wa kutosha katika vituo hivi vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, iko Hospitali ya Mkoa ambayo inajengwa. Naishukuru sana Serikali kwa kutujengea Hospitali ya Mkoa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika, aliiona ile hospitali nzuri kabisa inayojengwa pale, lakini hospitali ile bado haijakamilika. Kwa sasa tunatumia Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, ndiyo imechukuliwa kama Hospitali ya Mkoa, lakini ina upungufu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chumba cha upasuaji, wagonjwa wa aina zote wanapasuliwa chumba hicho hicho. Hebu niambie, huku unapasua mtu labda amevunjika mguu halafu kuna dharura ya mama mjamzito, unafanyaje? Unamtoa huyu mgonjwa unayempasua mguu umwingize mama mjamzito? Kwa hiyo, tunaomba pale Hospitali ya Kibena, tujengewe angalau theatre ya ziada ili kusudi angalau tuweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndiye Mbunge wa watu wenye UKIMWI. Naiomba sana Serikali, kama sisi Njombe tuna UKIMWI na tumekuwa tukitangazwa kwamba hata data zetu ziko juu sana, basi tuhudumiwe. Huduma tunayoiomba, kwanza kabisa hatuna mashine ya kupima virusi vya UKIMWI (viral load). Sisi ndio tunaoonekana kwamba ndio waathirika wa kwanza, lakini inabidi tubebe sampuli za damu tupeleke Mbeya au tupeleke Iringa kwa ajili ya kupima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Njombe tupewe mashine hiyo ya kupima viral load ili tupime pale Njombe. Vile vile tupewe dawa kwa ajili ya magonjwa nyemelezi. Kama kweli Serikali inatutambua sisi kweli ni waathirika wa kwanza katika nchi hii kwa maradhi ya UKIMWI, basi tupewe dawa za kutosha za magonjwa nyemelezi na vitendanishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unaenda kufanya vipimo unaambiwa vitendanishi hakuna. MSD hawatoi vitendanishi, vitendanishi wanatakiwa kutoa Wizara ya Afya na Wizara ya Afya inachelewa kutoa. Linapokuja suala la kugawa Waganga, sisi tunaoumwa zaidi, tupewe zaidi Waganga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana tupo mjini, tunaambiwa ah, Hizi Halmashauri za Mjini tusiwape Waganga wa kutosha, lakini sisi tunaomba mtambue kwamba sisi ni wagonjwa zaidi na tunakiri hilo na tunaomba mtusaidie. Msiendelee kututangaza tu kwamba sisi ni wagonjwa zaidi, lakini hamtusaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Njombe Mjini hakuna hata kijiji kimoja ambacho umeme wa REA umewaka. Wakandarasi wanakuja, wanaulizia wanaondoka. Naomba sana, najua ndugu yangu Waziri wa Nishati yuko makini na tunawasiliana naye kwa karibu. Hebu awasimamie hawa watu wafanye ile kazi kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la elimu. Hapa nazungumzia habari ya mikopo ya elimu ya juu. Mikopo ya elimu ya juu inanyanyasa wanafunzi. Anakopeshwa mwanafunzi mwaka wa kwanza, mwaka wa pili hakopeshwi, atapata wapi fedha ya kuendelea kujisomesha? Matokeo yake wanaanza kuzurura mitaani, wanaomba misaada. Mara waje kwa Waheshimiwa Wabunge, mara waende wapi. Kwa hiyo, naomba Bodi ya Mikopo ikimkopesha mwanafunzi mkopo mwaka wa kwanza, ihakikishe kwamba huyo mwanafunzi anakwenda naye mpaka mwaka wa nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu bila malipo ni zuri sana na linawasaidia sana wananchi huko vijijini na wananchi wote kwa ujumla, lakini tatizo lake kubwa ni kwamba elimu bila malipo ingewekewa kiwango maalum kwamba kiwango cha chini kabisa ambacho Serikali itatoa kwa shule ni kiasi fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna shule ambazo zina wanafunzi wachache. Kuna shule zina wanafunzi 150. Kwa hiyo, ukichukua ile namba ya wanafunzi na kutoa ile fedha ya Serikali, unajikuta kwamba fedha ya matengenezo na michezo haipatikani pale shuleni. Kwa hiyo, naomba sana kuwe na angalau kiwango cha chini ambacho kinaanzia angalau kuweza kulipia zile gharama za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile liko suala la elimu msingi. Elimu msingi, watoto sasa hivi wako darasa la nne na watoto hawa kila nikisimama hapa wanasema kwamba itafika mahali tutakuwa na form one mbili; tutakuwa na form one waliosoma miaka saba, lakini tutakuwa na form one waliosoma miaka sita. Je, maandalizi yetu yakoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile suala la kuandaa Walimu kwa ajili ya elimu msingi limekwama. Ilikuwepo NACTE na NECTA, sasa zimeingia kwenye ushindani, kwamba Mabaraza haya mawili ya Mitihani yanavutana jinsi ya kutoa elimu kwa Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itoe maamuzi, kama tuliamua kwamba Taasisi ya Elimu ya Ufundi wajibu wake ni kusimamia mitihani yote ya ufundi ikiwemo ya Majeshi, Polisi na kadhalika, basi isimamie. Isirudi tena Wizara ya Elimu ikatoa mitihani mingine ikairudisha Baraza la Mitihani. Huku ni kuleta mkanganyiko na kuwavuruga Watendaji. Vilevile wapo wawekezaji katika masuala ya elimu, nao wanapata shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la Polisi. Nimetembelea Gereza la Njombe pale mjini. Pale kuna mahabusu wana miaka sita, saba mpaka kumi wanalalamikia suala la Polisi kwamba upelelezi unachelewa. Naomba sana, wanaotuhumiwa kwa mauaji upelelezi ukamilike ili kusudi kesi zao ziweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile liko suala la Mahakama. Mahabusu wa Gereza la Njombe wanailalamikia sana Mahakama. Moja, Njombe hatuna Mahakama Kuu, inakuja kwa vikao. Ikikaa kikao Njombe, haimalizi kesi, matokeo yake mahabusu wamelundikana sana katika Mahakama ya Njombe na wanasababisha ile mahabusu ionekane ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama inapokuwa haifanyi vikao na ikakamilisha zile kesi, ina maana inasababisha mlundikano wa mahabusu pale Magereza, matokeo yake kunakuwa na watuhumiwa wengi sana, halafu Gereza linaonekana ni dogo. Kwa hiyo, naomba sana, Idara ya Mahakama, namwona Mwanasheria Mkuu yuko hapa, tuone, tupeleke Mahakama Kuu Njombe ili kusudi Vikao vya Mahakama Kuu vifanyike Njombe. Kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshawadhihirishia Watanzania kwamba fedha katika nchi hii siyo tatizo. Kwa hiyo, naomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la mawakala wa pembejeo. Mawakala wa pembejeo waliosambaza mbolea mwaka 2015/2016 wamepekuliwa mara nane. Hesabu zao zimepitiwa mara nane, lakini hakuna Wakala hata mmoja aliyepewa jibu. Jamani, huu siyo uungwana. Kama watu hawa wamepekuliwa hivi, wapewe majibu.

(Hapa kengele ililiakuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafsi nami niweze kuchangia hoja hii ya Wizara ya Nishati iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya na baada ya hapo nijielekeze kwenye suala la umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Njombe Mjini tuna masikitiko makubwa sana, wengi wamesifia REA lakini Njombe Mjini tunasikitika kwa sababu hata kijiji kimoja hakijapata umeme wa REA. Utaratibu wanasema Njombe tunatakiwa kupata umeme kutokana na Mkandarasi anayetengeneza umeme kutoka gridi ya Taifa kwenda Songea. Mkandarasi yule anakumbwa na matatizo mengi tu, mara hana fedha, mara nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii hali inaleta sintofahamu sana kwa wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini na inasababisha hali ya siasa kuwa ngumu, lakini vilevile morali inapungua sana kwa wananchi wakisikiliza habari ya TANESCO na habari ya REA, wanaingiwa na kasumba kwamba kwa sababu lile Jimbo linaitwa Jimbo la Njombe Mjini na umeme wa REA ni wa vijijini, kwa hiyo Njombe haimo. Kwa hiyo, naomba sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja kufunga hotuba yake atuambie, Njombe tutapata lini umeme wa REA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana TANESCO na REA kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa ajili ya umeme wa kupeleka kwenye kwanda kipya tunachotaka kukijenga pale Lwangu, Kiwanda cha Chai. Naomba sasa Wizara na TANESCO wasaidie, msimamo ambao tumekubaliana kwamba kazi ile inaanza mwezi wa Sita kweli ianze, kwa sababu tumeshapata mwekezaji kwa ajili ya chai, chai ile wakulima wale wameshalima haina kiwanda. Kwa hiyo, naomba sana Kijiji cha Lwangu kipelekewe umeme kutoka Kilocha ili chai ile ianze kusindikwa pale kwenye Kijiji hicho cha Lwangu na wananchi waanze kupata fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwa Jimbo la Njombe na kwa maana ya Mkoa wa Njombe ni Mchuchuma na Liganga. Kwa kweli Wanamkoa wa Njombe tunasikitika sana kwa sababu Mchuchuma na Liganga ni hadithi ya miaka mingi sana, juzi nimesema na leo narudia, kwamba kwa kweli if we are serious na maendeleo ya nchi hii, Ujerumani imeendelea kwa chuma, chuma ndicho kilichoendeleza nchi, sasa chuma cha Liganga ni hadithi tu miaka yote, chuma Liganga, chuma Liganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamefanya kazi ya kuchepusha madaraja wakisema madaraja yaliyopo ni madogo, mitambo haitaweza kupitia, madaraja yale safari hii yamesababisha matatizo, maji yamejaa yameshindwa kupita, kisa ni kwamba wamechepusha madaraja ili wapitishe mitambo, hakuna cha mitambo, majani yameota. Wale Waheshimiwa waliokwenda kule kwenye migodi inasemekana kwamba wamegundua kuna madini mengine, wameanza kuchenjua hayo, habari ya chuma wameachana nayo. Sasa tuambiwe na Wizara, Mchuchuma ipo ama haipo! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine cha kusikitisha, Mchuchuma amepewa NDC. Watu wote humu ndani tunajua NDC ilivyo, hivi afya ya NDC ikoje jamani? NDC anaweza akachimba chuma! NDC haiwezi kuchimba chuma leo, uchumi wa NDC uko chini sana. Niwaombe sana Serikali muwe na maamuzi na kama mmesema kwamba Mashirika ya Hifadhi ya Jamii yaingie kwenye biashara inayoajiri watu wengi, migodi ile ya Mchuchuma na Liganga inatarajiwa kuajiri watu 30,000. Hayo Mashirika ya Hifadhi ya Jamii yapelekwe huko wafanye hizo kazi za kuchimba makaa kule Mchuchuma na chuma pale Liganga. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake aseme chochote juu ya Mchuchuma na Liganga ili tujue msimamo ukoje.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu TANESCO Njombe. TANESCO Njombe wana shida kubwa sana. Wapo vijana wachapakazi sana pale, wanajitahidi lakini ukatikaji wa umeme kutokana na hali ya hewa ya Njombe, mvua nyingi na miti mingi, mara nyingi sana miti inaangukia nyaya, hawana gari za kutosha, wana gari moja TANESCO Njombe. Wasafiri kilometa 70 upande mwingine wa Jimbo la Lupembe kwenda kuangalia tatizo la umeme, wakitoka huko warudi Jimbo la Njombe Mjini waende mpaka Luponde tena kuangalia umeme, unaweza ukakuta siku mbili Kiwanda kama cha Chai Luponde kinakosa umeme kisa TANESCO hawana gari ya kuwafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini na wakubwa wa TANESCO watakuwa wanasikia maneno haya. Naomba wawasaidie wale wachapakazi vijana pale Njombe ili wapate gari lingine la kufanya service kwenye lane za umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la viwanda. Sisi Njombe tuna viwanda, moja ya kiwanda tulichonacho ni Kiwanda cha Nguzo (TANWAT). TANWAT wameingia kwenye tenda ya kuomba ku-supply nguzo TANESCO, wamekosa. Ni jambo la kusikitisha sana! Masharti ambayo wameweka TANESCO na utaratibu waliouweka unasikitisha sana. Wametoa tenda hii South Africa tena ku-supply nguzo za umeme wakati Njombe kuna nguzo za umeme. Ni kweli inawezekana kiwango ambacho kinatakiwa ni kikubwa sana, ndiyo uwape South Africa shilingi bilioni 60 ku-supply nguzo TANESCO, halafu wazawa wananyimwa kwa kuwalambisha tu unawapa Sao Hill nguzo za shilingi bilioni 24!
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa hili nitakwenda ofisini kwake tukae tuongee tuliangalie. Haiwezekani kabisa, kwa sababu nguzo hizi hawa Makaburu wata-supply kwa miaka mitatu, ina maana viwanda vyetu vile sasa havitakuwa na kazi. Nasi kama Watanzania tunasema tunataka nchi iwe ya viwanda, ni lazima tuanze ku-favour viwanda vya ndani. Kama haiwezekani hiyo, basi hata viwanda haitakaa iwezekane. Maana yake watakuja watu wa viatu, watatengeneza viatu, tutasema viatu vya Tanzania vina udhaifu moja, mbili, tatu, havinunuliwi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, kama nguzo hizi kiwanda kile kimekaguliwa, ubora wa nguzo umekaguliwa, imeonekana kwamba ubora ni sahihi, kinachodaiwa ni kwamba hawana fedha, basi wangewapa hata kidogo tu ili wajijenge kiuchumi kesho waweze kuwa suppliers wazuri zaidi. Kwa suala la nguzo naomba niseme hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala haya yanayohusiana na suala la madini. Kule katika Jimbo la Njombe Mjini kuna mgodi wa madini katika Kijiji cha Uliwa. Mgodi ule ulisababisha ugomvi sana na wananchi kwa sababu tu leseni zilitolewa kwa watu wawili, wote wafanye utafiti katika eneo moja. Naomba sasa, kama utaratibu ndivyo unavyoruhusu, basi urekebishwe kwamba kama ni leseni inatolewa kwa mtu mmoja na idara hii inayohusika na leseni iwe inatoa kwa utaratibu mzuri ili kusaidia wananchi wale wasiingie kwenye mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, yuko mwekezaji mmoja yuko tayari pale kuchimba yale madini ya copper, basi mwekezaji yule apewe kibali aendelee na kazi kwa sababu anazunguka siku nzima, miaka inakwenda kazi haifanyiki; na wananchi wale hawajapata elimu ya kutosha kwamba je, ni utaratibu gani unatakiwa ufanyike ili waweze kupewa kitu kinachotakiwa, kama ni mrabaha wa kijiji au ni wa Halmashauri au wa nini. Matokeo yake ni kwamba wananchi wale wamesimama pale wanasema mwekezaji haingii na mwekezaji anasema nina leseni; na upande mwingine kuna sehemu kuna mwekezaji mwingine anasema naye ana leseni. Kwa hiyo, naomba sana Wizara isaidie uchimbaji wa yale madini katika Kijiji cha Uliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mhehsimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kupongeza Wizara hii ya Ardhi ambayo kwa kweli imeonyesha umahiri katika utendaji wake wa kazi, naipongeza sana. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nitazungumzia zaidi Jimbo la Njombe. Katika Mji wa Njombe kuna tatizo moja kubwa sana, wakati wa Wizara ya Ujenzi niliongea na leo Wizara ya Ardhi naomba niongee. Ninaloliongelea mimi ni zile alama za „X‟, zimewekwa alama za „X‟ kwenye nyumba ambazo Wizara ya Ardhi imetoa hati halali kwa wale wananchi. Matokeo yake ni kwamba zile hati walizonazo wale wananchi wanaendelea kuzilipia na kodi ya ardhi wanalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo ni kwamba mji ule sasa hivi ni mchafu kwa maana ya kwamba majengo yamechakaa na watu wanashindwa kuziendeleza zile nyumba zao. Kama tunavyofahamu kila mahali penye mji maana yake ndiyo mahali pa biashara, zile nyumba nyingi ni za wafanyabiashara, wanashindwa kutumia zile nyumba kama dhamana katika mabenki kwa sababu tu zina alama za „X‟.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara ya Ardhi kwa kuwa na yeye ni mnufaika na kodi ya ardhi ambayo wananchi wale wanalipa, waone ni namna gani watafanya kutatua tatizo hilo wakishirikiana na Wizara ya Ujenzi. Vinginevyo tukubaliane, barabara ile pale mjini ipunguzwe size, zile alama za „X‟ zifutwe ili wale wananchi waendelee kuzitumia zile nyumba zao kama dhamana katika mabenki kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi nyingi kwa Wizara ya Ardhi, liko tatizo la asilimia 30 za Halmashauri ambazo hazirudishwi. Halmashauri yangu ya Mji wa Njombe inadai zadi ya shilingi milioni 60 haijawahi kurudishiwa. Niombe sana Wizara hii iangalie na iweze kurudisha hiyo fedha ambayo Halmashauri imekusanya imeipelekea Wizara na Wizara haijarudisha ile asilimia 30 kwa Halmashauri. Tatizo tunalolipata pale ni kwamba hata kuwahamasisha wananchi waweze kuendelea kulipia kodi hiyo haiwezekani kwa sababu Mkurugenzi hayuko tayari kutoa fedha yake nyingine ili tuhamasishe wananchi walipe kodi ya ardhi ni kwa sababu tu Ardhi wenyewe kama Wizara hawarudishi ile asilimia 30. Kwa hiyo, nikuombe sana kaka yangu Mheshimiwa Lukuvi turudishie hiyo asilimia 30 ili ndugu zako tujenge zahanati kule na wadogo zako waendelee kutibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine tulilonalo Njombe ni bustani za mabondeni maarufu kwa jina la vinyungu. Nafikiri kaka yangu Mheshimiwa Lukuvi unafahamu vizuri sana sheria hii ya mita 60 Njombe inatuathiri sana kwa sababu kwanza mji wenyewe uko milimani halafu wananchi wale walio wengi ni wakulima wanatumia bustani kama sehemu ya kipato kwao. Kwa hiyo, tunapokuja kuwaambia wasilime tayari tunawaathiri kiuchumi na tunavuruga kabisa utaratibu wao wa maisha. Najua hii ni sheria lakini naomba tuangalie jinsi ya kuitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sababu zinazotolewa wakati mwingine zinakosa mantiki ya kisayansi. Watalaam wanatuambia tusilime mabondeni kwa sababu tunavuruga mfumo wa maji, tunasababisha maji sijui yafanye nini lakini tukumbuke kwamba tumekuwa tukilima kwa muda mrefu, sisi tumezaliwa tumekuta wazazi wanalima maji yale hayajawahi kukauka na yapo vilevile. Sasa hiyo hoja ya kuambiwa tunapungaza maji, tunapunguzaje maji? Kama kuna mahali yamepungua maji ni huko yalikopungua lakini siyo Njombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ni la kitalaam kwamba maji yanatunzwa mlimani, zamani Maafisa Ugani walihamasisha wananchi walime kwa matuta ili kutunza maji kusudi mvua ikinyesha maji yakifika kwenye tuta yatulie yaweze kuzama kwenda chini. Kwa hiyo, yakizama kwenda chini yale maji ndiyo baadaye yanakuja kutoka kule bondeni. Sasa leo tunaambiwa huku juu tulime kwenye sesa au tambarare lakini kule mtoni tusilime, kisayansi hiyo haikubaliki. Naona watalaam wa sayansi warudie tena kufanya utafiti wao ili sisi watu wa Njombe Mjini watuache tuendelee kulima vinyungu kwa ndiyo vinasababisha watu wa mjini mle chipsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Njombe Mjini tuna tatizo lingine linalohusiana na ardhi. Uwanja wa ndege wa Njombe Mjini uko mjini kabisa. Katika lile eneo la uwanja wa ndege wako wananchi wana nyumba zao pale na wanashindwa kuendeleza nyumba zao kwa sababu tu wanaambiwa wako eneo la uwanja wa ndege na hawalipi maduhuli yoyote ya ardhi.
Naomba Wizara hii ifanye utaratibu tuone kama wale wananchi ni kweli wako ndani ya eneo la uwanja wa ndege waambiwe rasmi wako ndani ya uwanja wa ndege na kama kuna fidia walipwe waondoke. Kama hawapo ndani ya eneo la uwanja wa ndege basi wapewe hati za ardhi ili kusudi waendeleze yale makazi yao na wazitumie zile nyumba zao kwa ajili ya uchumi. Kinyume cha hapo wale watu tunawafanya wanakuwa maskini, nyumba zinachakaa, wanaishi maisha ya wasiwasi wakiamini kwamba kuna uwanja wa ndege pale na wenyewe watu wa uwanja wa ndege hawasemi lolote juu ya maendeleo ya ardhi ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo na mimi niseme kidogo kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa. Shirika la Nyumba la Taifa walifika Njombe kutafuta eneo la kujenga nyumba na wakaonyeshwa eneo lakini kwa bahati mbaya sana ninasikitika kwamba Shirika la Nyumba hawajarudi tena Njombe. Taarifa niliyonayo ni kwamba walihitaji wapewe eneo la bure sasa Njombe eneo la kutoa bure halipo. Kwa hiyo, niwaombe sana Shirika la Nyumba, wakiona eneo lina thamani maana yake hata nyumba watakazojenga zitakuwa na thamani hivyo hivyo. Naomba waje tena Njombe wachukue lile eneo ambalo tumelitenga kwa ajili yao lakini watulipe fidia kwa sababu eneo la bure halipo na wao kwa upande mwingine zile nyumba si wanaziuza, kwa hiyo ni biashara. Kwa hiyo, wasione kwamba wanatakiwa wapewe eneo la bure kama fidia ya gharama za uendeshaji wa shirika lao, hapana, wasifanye namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Shirika la Nyumba hilo hilo wengi wamesema kwamba nyumba zao ni za ghali sana, ni kweli nyumba zao ni ghali sana. Hatufahamu sana ni gharama gani wanaingia lakini nafikiri shirika lijipange vizuri tu ifike mahali liwe na mifuko miwili, mfuko wa kuuza hizo nyumba za gharama lakini liwe na mfuko kwa ajili ya nyumba za wanyonge. Kwa hiyo, lijenge nyumba za wanyonge ili wanyonge wapate nyumba. Tusipofanya hivyo shirika litaendelea kulaumiwa lakini na lenyewe linashindwa kufanya vinginevyo. Niwaombe sana Shirika la Nyumba wasife moyo, wajitahidi lakini wasisahau kufika Njombe tuwape eneo lile lakini watulipe fidia ili waweze kujenga nyumba zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme na mimi naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na momi niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Awali ya yote, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, kwa kweli wanajitahidi, tunawaona wanakimbiakimbia, mara wako Njombe, Bukoba, Arusha kuangalia miundombinu mbalimbali ya shule na kuhakikisha kwamba watoto wa Kitanzania wanapata elimu nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni fundi na fundi niliyesoma kutoka shule ya sekondari ya ufundi na nikaenda chuo cha ufundi. Sasa hivi tunazungumza Tanzania ya viwanda lakini Tanzania hii ya viwanda tunayoizungumza kama vijana wetu wasipopata elimu ya ufundi ina maana kwamba vijana hawa wa Kitanzania watakuwa watumwa ndani ya nchi yao kwa sababu hawatakuwa na ujuzi wowote wa kufanya kazi katika viwanda hivyo ambapo wote tunasema tunaiendea Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ndiyo yenye jukumu la kutoa elimu na maarifa kwa Watanzania iache kufikiria kwamba ili kutoa elimu ya ufundi ni lazima tuwe na karakana kubwa sana, mashine kubwa sana, mitambo inayoendana na mitambo ya viwanda, hapana. Sisi wakati ule tunasoma ufundi tulisoma ufundi katika nyenzo ambazo zilituwezeshe kuwa mafundi mpaka leo tunafanya kazi hizo za ufundi na tunajivunia ufundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako nikuambie humu ndani kuna mafundi sita ambao tumesoma na tunaujua ufundi vizuri na tunafanya kazi ya ufunzi vizuri kabisa. Uwekezaji kwenye ufundi kwa level ya sekondari ni kiasi kidogo sana, unaweza ukawa na shilingi 500,000 ukaanzisha fani ya ufundi sekondari. Kwa mfano, ufundi wa kujenga unahitaji kuwa na pimamaji, ndiyo kifaa cha gharama kuliko vifaa vyote, pimamaji moja ni shilingi ngapi? Chukulia shule ya sekondari inahitaji pimamaji kumi, unahitaji kamba ya kunyooshea ukuta, ubao, mwiko na konobao, hapo tayari fani ya ufundi kwa maana ya practical imekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unahitaji kitabu cha ufundi kwa maana ya theory na kitabu cha ufundi kwa maana ya michoro. Kwenye theory unahitaji ubadilishe masomo mawili tu, ubadilishe somo la physics liwe engineering science, lakini uondoe somo la biology uingize somo la somo la urasimu ama ufundi wenyewe. Kwa hiyo, ni rahisi sana kuweka ufundi sekondari kuliko kujenga Vyuo vya VETA. Leo hii kila mtu hapa analia ajengewe Chuo cha VETA, tutajenga Vyuo vya VETA mpaka lini ili tuweze kuendana na kasi ya ufundi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu tuanzishe shule za sekondari za ufundi na si lazima kwenye shule ya sekondari ya ufundi tuanzishe fani sita au saba, tuanzishe shule moja, fani moja. Tunachukua shule moja tunaanzisha fani ya ujenzi, tunakwenda shule nyingine tunaanzisha fani ya umeme, shule nyingine tunaanzisha fani ya useremala, tunakwenda shule nyingine ya sekondari hivyo hivyo. Kwa hiyo, utakuja kuona jimbo zima ama nchi nzima sasa tunakuwa na shule nyingi za ufundi ambazo vijana wanapata maarifa na wakitoka pale wanakuwa tayari wanaanza kujitegemea. Tukisema tusubiri tuanze kujenga VETA, hela zenyewe sijui tunaomba wapi, wanaotupatia hela wana masharti, mpige magoti, mfumbe na macho, muombe na kuomba ndiyo hela zije, lini, tunachelewa, tufundishe ufundi vijana tujikomboe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wakisoma ufundi itawasaidia sana. Nataka niwaambieni wanaosoma ufundi sekondari wanakuwa ni mafundi wazuri kuliko mfano wake. Ufundi wa umeme unahitaji chini ya shilingi 500,000 kuanzisha umeme shuleni. Unahitaji bisibisi, koleo, kipande cha waya na kipande cha ubao, biashara imekwisha, huyo ni fundi. Hata akienda university atatumia vifaa hivyo hivyo kujifunza umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimwa Profesa Ndalichako hebu toa maamuzi angalau kila Halmashauri ianzishe shule moja ya ufundi kwa fani moja kama jaribio ili tuone tunakwendaje. Baada ya hapo tutafanya maamuzi kila Halmashauri iwe na shule ngapi za ufundi kadri watakavyoona mazingira, lakini kwenye maeneo yale ya wafugaji anzisheni mafunzo ya mifugo huko sekondari, watu wajifunze ufundi lakini kupitia fani za mifugo, sehemu za wavuvi wajifunze uvuvi sekondari kitaalum ili kusudi vijana hawa wakitoka hapo sekondari wawe tayari wana elimu ya kutosha kuliko kusubiri hizo VETA ambazo tunajua kwamba ni ngumu sana kuzijenga. Karakana zinazojengwa ni gharama sana, tunahangaika kujenga mabweni na kachalika, shule za kata zipo tuanzishe ufundi kwenye shule za kata angalau kila halmashauri au kila jimbo shule moja ya ufundi kadri watakavyoona mazingira yanaruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulishauri Serikali uko mkanganyiko ambao nauona katika ya NECTA na NACTE. NACTE wanasimamia mitihani ya ufundi katika vyuo vya kati, lakini NECTA wanasimamia mitihani ya shule ya msingi, sekondari na mitihani ya ualimu. NACTE imeanzishwa kwa sheria ambayo imeipa nguvu ya kusimamia vyuo vyote vya kati; vyuo vya majeshi, vya afya, vya mifugo, vya madini, lakini jambo la kushangaza kozi ya ualimu wa elimu ya msingi imekwenda NECTA, lakini imerudishwa NACTE kwa hoja kwamba ule mfumo ambao NECTA wanautumia kudahili na kutoa mitihani si mfumo ambao unaweza ukamjenga mwalimu kuja kuwa mwalimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeki, mimi nasema huu ni mkanganyiko, kama Wizara ya Elimu ndiyo iliyosimamia kuanzisha kwa NECTA na ikaagiza kwamba sheria ile iliyotungwa vyuo vyote vya kati viwe chini ya NECTA halafu yenyewe Wizara ya Elimu imeamua kujipendelea kuchomoa kozi moja tu ya ualimu wa primary na kubaki nayo kule kusema kwamba hii tunabaki nayo sisi. Wakati huo huo inaongezea masharti mengine kwamba chuo chochote kinachofundisha ualimu kisiwe na kozi nyingine hapo mahali yaani hawa watu wanaojifunza ualimu wakae wao tu kama walimu wasiwe na mtu mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani hii dunia ni pana, tunapowaweka wale walimu wakae hivyo tunamaanisha nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kozi ile ya walimu irudishwe NACTE na waisimamie na walishaweka mifumo mizuri ya kuhakikisha kwamba hata mwalimu wa primary ambaye yupo kazini arudi apate elimu zaidi na aweze kuendelea kielimu. Kwa sababu kozi ile ya grade A ilikuwa ni kozi ambayo mwalimu akisoma si sifa ya kuendelea na masomo yoyote anabaki pale miaka yote, lakini ukiangalia kwenye Sera mpya ya Elimu inataka walimu waliojiendeleza na waweze kuendelea zaidi.

Kwa hiyo, naomba sana Wizara muangalie muwape nafasi hiyo NACTE waendelee na mafunzo ya ualimu. Najua mlisema kwamba mnamashaka na ile mitaala na kadhalika lakini naomba basi hayo mashaka muwe mnayaondoa haraka, kama mnaona mashaka hayaondoki haraka basi tuwatafute na waombezi wawaombee ili kusudi mashaka yenu haya yaondoke haraka ili kazi iende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naliona nalo ni muhimu sana nilichangie hapa ni kuanzishwa kwa chombo huru cha kusimamia elimu. Tunasema kwamba chombo hiki kitasaidia sana kupata elimu vizuri katika nchi yetu, kitasimamia kwa haki na kitahakikisha kwamba kila mmoja anayehusika na elimu anafuata utarabu. Unaona kabisa kwamba kwenye taasisi au Wizara nyingine kuna vyombo kama OSHA, EWURA, hizi ni regulatory bodies. Kwa hiyo, sisi elimu tuwe nayo basi kusudi elimu yetu sasa isiguswe na mtu, asitoke mtu alikotoka akasema hiki kiwe hivi, hiki kiwe hivi, ikae hivyo na isimamiwe hivyo naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala Sera ya Elimu ya mwaka 2014, suala hili leo hii ndiyo linaleta mkanganyiko. Sera mpya ya Elimu imeanza kutumika na watoto walioanza kutumia sera hii mpya leo wako darasa la nne. Niungane na Mheshimiwa Bulembo aliyesema kwamba hivi itakuwaje, tunaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa utuambie kwamba watoto hawa waliopo darasa la nne leo watafika darasa la sita ama wataishia darasa la saba ili kusudi hata wazazi huko mitaani tuwajenge kisaikolojia wawe wanajua nini kitafanyika. Sera hii ya Elimu pamoja na kuizindua wakati ilipozinduliwa maandalizi yalikuwa bado, ndiyo maana leo unaweza ukakuta sera ipo haina sheria, sera ipo haina kanuni, matokeo yake linaweza likatokea kundi lisilojulikana likaja likaipeleka Serikali Mahakamani kupinga sera hii na mkashindwa hata kujitetea kwa nini mnatoa elimu kwa kutumia sera hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana tufuate utaratibu wa sera, leteni sheria Bungeni, sheria ipitishwe wekeni na kanuni zake kusudi sera hii ikae vizuri. Vilevile andaeni vitabu na mviweke katika msingi kwamba zinafuata sera hiyo kuliko sasa tunaambia vitabu vya darasa la nne havipona wakati mwingine mnaambiwa mtaala upo lakini vitabu hakuna, mafunzo kwa walimu hakuna kwa sababu sera hii tumeiendea haraka mno. Kama tumeiendea haraka tujitahidi kwa sababu watoto sasa wako darasa la nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ufaulu. Ni kweli ufaulu unasikitisha, ni-declare interest kwamba mimi ni mmiliki wa shule, lakini ufaulu katika shule za umma unasikitisha. Kinachosikitisha si kingine si kwamba hakuna walimu, bali mazingira siyo mazuri Serikali ijitahidi kuweka mazingira mazuri. Hata kama unapata majibu rahisi, ukikutana na watendaji wa Serikali wanakwambia nyie private si mnachuja, huwezi kuchuja darasa zima lakini Serikali una uwezo wa kuchuja, una shule za vipaji Ilboro, Mzumbe, zipo zile shule na mmekuwa mkipeleka hao mnaowachuja vilevile. Kwa hiyo, mimi nafikiri Serikali iandae mazingira mazuri ili kusudi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja na nawatakia kila la kheri Wizara ya Elimu wafanye kazi vizuri.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyopo mbele yetu. Awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa uwasilisho wa bajeti nzuri ambayo tunaiona inatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la TRA. Katika Mji wa Njombe iko Ofisi ya TRA. Tunaposema kwamba ulipaji kodi unatakiwa uwe rafiki nadhani ni pamoja na mazingira ya kulipia kodi. Katika Ofisi ya TRA Njombe mazingira ni mabaya sana, jengo lile lina vyumba sita, limechakaa, linavuja lakini lina watumishi wachache sana. Matokeo yake ni kwamba kunakuwa na msongamano mkubwa sana, watu wanakwenda kulipa kodi siku mbili mfululizo anakaa TRA kulipa kodi.

Mheshimiwa Spika,Hii nayo inawavunja nguvu sana walipa kodi, niombe sana Serikali ilione hilo na itujengee jengo lingine lenye nafasi. Tuliambiwa kwamba kuna mpango wa kuhamisha TRA pale, lakini hatuoni kama kuna dalili ya kuhama leo wala kesho na makusanyo ya TRA Njombe ni zaidi ya bilioni 12 kwa mwaka. Kwa hiyo, haya ni makusanyo makubwa ukilinganisha na mikoa mingi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nikiacha suala la TRA niende kwenye suala la kilimo. Njombe ni wakulima na katika kilimo yako mambo ambayo ni msingi sana yakatekelezwa kwa wakati. Jambo la kwanza kabisa ni suala la miundombinu inayowahusu wakulima, wakulima wanahitaji miundombinu ya barabara ili waweze kusafirisha mazao kutoka katika mashamba kwenda katika masoko.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la pembejeo, pembejeo zimekuwa zikifika kwa kuchelewa sana kwa wakulima, hali ya barabara ni mbaya sana kwa wakulima. Niombe sana Serikali iangalie kwamba ni kwa namna gani sasa itaweza kuwawezesha wakulima wa mazao ya chakula na biashara waliopo katika Jimbo la Njombe Mjini ili kusudi waweze kufanya kazi yao vizuri, msimu wa mavuno waweze kusafirisha mazao vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna Kiwanda kipya cha Chai kimejengwa pale Rwangu, Njombe. Kiwanda kile kinahitaji chai nyingi sana na ile chai inalimwa maeneo mbalimbali sana ambayo hayana hata barabara. Kwa hiyo, ni jukumu sasa la Serikali kuona ni namna gani inawezesha kupeleka fedha za kutosha katika Jimbo la Njombe Mjini, kutengeneza barabara kwa ajili ya mashamba ya chai katika eneo lile.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia kilimo tunazungumzia na masoko, sasa hivi Njombe tumeanza kulima zao la parachichi na zao la parachichi linaiingizia fedha ya kigeni nchi. Sasa hivi tuna-export parachichi kwa wingi sana kutoka Njombe, lakini miundombinu yetu siyo rafiki. Kwa hiyo, inasababisha bei ya lile zao isiwe na ushindani, kwa sababu anatokeza mtu mmoja na kwa kuwa miundombinu inayotakiwa ni ile yenye ubaridi. Niiombe sana Serikali ilione hilo.

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu nikikumbuka huko nyumba wakati uwanja wa Ndege wa Songwe unajengwa tuliambiwa uwanja huu unajengwa Kusini kwa lengo kwamba uweze kusaidia kusafirisha mazao ya matunda na maua kwenda masoko ya Ulaya. Uwanja umekamilika, mazao yanalimwa lakini mpaka leo yanasafirishwa kwa malori. Wafanyabiashara wanasema mazao ya Njombe hayapati bei nzuri kwenye soko la dunia kwa sababu gharama ya usafiri iko juu sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wanasafirisha kwa malori kutoka Njombe mpaka Dar es Salaam, hebu tuone sasa hivi tumetengeneza wale wanaitwa white elephant au ni nini. Kwa sababu uwanja ule uko tayari, mazao yako tayari lakini hatuoni dalili ya kuona kwamba sasa tunaanza kuutumia ule uwanja. Tunakwenda na miradi mingi mikubwa, kama tunashindwa hii miradi ambayo ipo ilishakamilika ikiwemo TAZARA hakuna hata dalili ya kusafirisha mizigo kutoka Nyanda za Juu Kusini kupeleka kwenye masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaweza tukajikuta tunafanya miradi mikubwa mingine lakini bado ikawa haifanyi kazi. Sasa hivi tunakwenda kuhamasisha kuna soko kubwa sana ya njegere changa huko Ulaya na mahindi machanga yanahitajika yakiwa fresh, tunahitaji miundombinu ambayo itatusaidia kusafirisha haya mazao kwa ajili ya masoko ya huko Ulaya na haya mazao yanaleta fedha ya kigeni moja kwa moja. Naomba sana hilo jambo liweze kutiliwa maanani kwamba Uwanja wa Ndege Songwe na TAZARA - Makambako wawekewe miundombinu yenye ubaridi ili kusudi waweze kusafirisha haya mazao fresh kwa ajili ya masoko ya nje na wafanyabiashara hawa wapate unafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la maji. Katika Jimbo la Njombe suala la maji limekuwa gumu sana.

Nimeshangaa sana kuona kwamba inaonekana suluhisho la maji kwenye Mji wa Njombe na miji mingine ni kutungwa kwa sheria inayompa idhini Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa kodi. Jambo hili tumelizungumza miaka mitatu, miaka mitatu yote kwenye bajeti fedha inaoneshwa kwamba kuna miradi ya maji, kuna mkopo nafuu toka India. Kumbe tatizo ni sheria ilikuwa inagomba miaka mitatu!

Mheshimiwa Spika, nasikitika sana nikiangalia jinsi Baraza la Mawaziri na Serikali yetu ilivyosheheni wasomi jambo kama hili linachukua miaka mitatu kupata ufumbuzi, je, huo utekelezaji utakuwaje sasa? Sasa tunapitisha hii ili kusudi Waziri apate hiyo idhini, niombe sasa watekelezaji watakapoanza kutekeleza hii miradi, ikiwemo mradi wa maji wa Njombe Mjini waone kwamba mradi huu wananchi wamekosa huduma kwa miaka mitatu. Kwa hiyo, waende na kasi ya kufidia hiyo miaka mitatu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la fedha za maendeleo. Fedha za maendeleo kwenye Halmashauri zetu haziletwi na sisi ambao vyanzo vyetu kama vile vyanzo vya kodi ya majengo vimechukuliwa inatuumiza sana. Tumejenga zahanati, tunashindwa kuezeka, tumebaki na mapagale. Sasa nashindwa kuelewa kwamba ikiwa Serikali imechukua vyanzo vya mapato kama vya kodi ya majengo ikidai kwamba itafidia halafu haitufidii, tumejenga zahanati katika Kijiji cha Mamongolo, Kata ya Makoo; tumejenga zahanati Kifanyo, tumejenga zahanati Luponde, tumejenga zahanati Magoda tunashindwa kumalizia zahanati hizi kwa sababu tu hatuna fedha na Serikali fedha za maendeleo haituletei.

Mheshimiwa Spika, hebu niombe basi Serikali ione kwamba ili twende sawa kwa sisi ambao vyanzo vya mapato ambavyo ni haki yetu kabisa, vyanzo vya mapato vya kodi ya majengo vimechukuliwa, tupewe basi hizo pesa tuweze kumalizia hayo majengo. Kuna wakati wameita Wakurugenzi wa kila Halmashauri wamefika hapa wamepewa maelekezo, wameandika na kila kitu lakini mpaka leo fedha haitoki. Niombe sana jambo hili lifanyike ili kusaidia maendeleo ya maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la elimu. Ukiangalia kwenye kitabu cha Bajeti cha Mheshimiwa Waziri anasema nchi hii inawahitimu laki laki nane kila mwaka, lakini wanaopata bahati ya kuajiriwa ni wahitimu 40,000. Kwa hiyo, watu zaidi ya laki saba wanabaki bila ajira na watu hawa hawana ujuzi wowote zaidi ya kujua kusoma na kuandika. Kila wakati nasimama hapa naelezea kwamba hebu tusaidie nchi hii tuweke shule za ufundi katika shule za Kata ziwemo shule za ufundi.

Mheshimiwa Spika, watu wote hapa wang’ang’ana VETA, hatuna uwezo wa kujenga Vocational Schools leo zikatosheleza nchi hii, lakini njia rahisi ya kufanya tubadili baadhi ya shule za Kata ziwe shule za ufundi ili kusudi tuokoe kundi kubwa la vijana. Tutawasaidia vijana hawa watakuwa wamepata elimu ya ufundi ili waweze kujitegemea hivi hapa ugumu uko wapi au ni nani atamke? Naomba sana jambo hili lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtazamo wa walio wengi wanaona kabisa kwamba kitu cha ufundi ni kitu kikubwa sana lazima kuwe na ma-workshop kuwe na mashine za ajabu ajabu, lakini nimekuwa nikieleza hapa mara zote kwamba jambo hili wala siyo kubwa kiasi hicho. Hebu twende turudi chini tuangalie tulifanyie kazi, tuweke mpango ambao utasaidia angalau kila Halmashauri iwe na fani angalau moja mbili katika shule zake za Kata kuzifanya kuwa za ufundi ili ziweze kufundisha vijana wapate maarifa na baadaye waweze kujitegemea.

Mheshimiwa Spika, tusipofanya hivyo, tatizo la kujiajiri kwa vijana halitakaa lipate suluhisho, italeta shida sana kwa maana ya kwamba wanaomaliza elimu ya msingi na wanaomaliza elimu ya sekondari ni wengi sana. Kwa hiyo, elimu ya ufundi ndiyo ukombozi na elimu ya ufundi siyo inapatikana kwenye Vyuo vya Ufundi tu kwa maana ya VETA, tunaweza kabisa kuzifanya shule zetu za sekondari zikawa sehemu ya mafunzo ya ufundi na ikawa imesaidia vijana wengi kupata hayo maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja hii iliyopo hapa mbele yetu. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri na wataalam wote walioshiriki katika kuandaa mpango huu ili na sisi tupate fursa ya kuuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwanza kabisa kwenye viwanda, tunapozungumzia viwanda ni lazima tuwe na viwanda mama na wengi sana wamezungumzia habari ya Mchuchuma na Liganga. Hadithi ya Mchuchuma na Liganga sasa inafikia mahala itabidi hata watoto wetu tuwabatize majina hayo, kwa sababu hadithi hii ni ya miaka mingi sana. Mchuchuma na Liganga lakini ukweli wa mambo ni kwamba wengi tunaongelea Mchuchuma na Liganga tunafikiri Mchuchuma na Liganga viko mahala pamoja. Kutoka Liganga mpaka Mchuchuma kuna umbali wa takribani kilometa 80 au zaidi na Mchuchuma ni mahala ambapo makaa ya mawe yanapatikana. Na Liganga ni mahali ambapo chuma kipo sasa ukiangalia utaona kwamba tumeiweka hii miradi pamoja tukiamini kwamba ni mradi mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuona kwamba Serikali sasa ione itenganishe miradi hii, makaa ya mawe yaliyoko mchuchuma yaanze kutoka, kwa sababu utoaji wa makaa ya mawe hauitaji mitambo ya ajabu, hauhitaji vitu vikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachohitaji katika Mkoa wa Njombe tunahitaji barabara ile itengenezwe, tumeambiwa habari ya barabara miaka ilani ya uchaguzi iliyopita ilisema barabara ya Itoni - Manda, ilani hii kuna Itoni - Manda. Kumetengwa kilometa 50 barabara ina zaidi ya kilometa 150, lakini zimewekwa kilometa 50, hasa unaweza ukaona kwamba ni kiasi gani tuko serious. (Makofi)
Sasa tunahitaji nani muwekezaji aje awekeze kuchimba chuma kwa sababu pale tumekuwa tukisimulia mpaka hadithi za ajabu ajabu, kwamba chumba kile kikianza kuchimbwa malori 600 yatapita kila siku kwenye Mji wa Njombe kusafirisha chuma. Hasa barabara ya vumbi malori 600 hiyo itakuwa ni barabara kweli, hebu tuone are we serious kweli kuhakikisha kwamba kile chuma kinataka kutoka, are we serious kwamba tunataka yale makaa yatoke? Kwa hiyo, niombe sasa Serikali ione itenganishe miradi hii makaa yaanze kutoka kwa sababu makaa hayaitaji utaalamu sana. Lakini vilevile barabara hii ya Itoni - Manda itengenezwe ili kusudi sasa iweze kufanya kazi ya kupeleka maendeleo upande ule na mali zile ziweze kutoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ningependa kuliongelea leo ni suala la elimu, nimekuwa nikipitia katika kitabu cha mpango hiki ukurasa wa 53, unaeleza mpango kabambe wa elimu msingi. Ndugu zangu elimu msingi ni kitu kigumu sana kama nchi hii hatujawahi kupata maanguko makubwa tunakwenda kupata maanguko sasa kwenye elimu msingi, kwa sababu elimu msingi inaonyesha kwamba watoto walioko darasa la pili sasa wataishia darasa la sita. Ina maana kwamba mwaka 2011 watoto hawa watakuwa form one, lakini wakati huo huo wale walioko darasa la tatu na wao watakuwa form one.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ina maana shule za sekondari tulizonazo zitakuwa na mikondo miwili, na mkondo mkubwa ni huo wa watoto ambao wataishia darasa la sita kwa sababu hawa darasa zima litakuwa linaenda sekondari. Sasa tujiulize leo hii tuna suasua na shule zetu za kata hazijakamilika, kwanza watoto hawa watakuwa na umri mdogo sana kumtoa darasa la sita kumpeleka form one, je, atamudu masomo ya sekondari na atamudu umbali? Watoto wengine tumewapangishia mtaani, watoto wengine wanatembea umbali mrefu sana kwenda shule. Tuone sasa kama Serikali tunajipangaje kuhakikisha kwamba hii elimu msingi inatekelezwa, vinginevyo tutaenda kutesa watoto, tutaenda kuharibu elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo elimu kwa uma haipo, nani anajua leo hii kama mtoto aliepo darasa la pili ataishia darasa la sita na ataanza form one. Niwaombe sana Serikali hebu jaribuni kuona sasa pamoja na kueleza kwamba kuna mpango kabambe toeni elimu kwa umma ili kusudi umma ujue kwamba watoto walioko darasa la pili hawa wataishia darasa la sita na wataanza form one. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie suala la sekta binafsi, sekta binafsi ni tamu sana kuitamka katika midomo ya Serikali na wadau mbalimbali. Lakini ukija ukweli wake unakuja kuona kwamba kuna ugumu mkubwa sana wa sekta binafsi inakabiliwa nao. Kwanza kabisa sekta binafsi imekuwa kama yatima, haipati msaada wa aina yoyote zaidi ya maneneo lakini wamezungumzia kwamba bajeti ya kodi. Suala la kodi naomba liangaliwe sana sasa hivi karibu kila mtu anadaiwa…
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake na neema zake, mimi na wenzangu humu ndani hatujambo na tunaendelea na wajibu wa kuwakilisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Makamu wake kwa maana ya Naibu Waziri kwa kadri wanavyofanya kazi na wanavyosimamia masuala ya uchumi wa nchi yetu. Niseme awali kabisa napongeza mpango huu naunga mkono pia hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na suala la kilimo. Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa saba, kuna mahali anaonyesha kwamba mfumuko wa bei uko chini ya numeral asilimia tano. Sasa mfumuko huu wa bei wote tunajua kwamba kinachosababisha mfumuko wa bei uwe katika hali hiyo katika nchi yetu ni upatikanaji wa uhakika wa chakula kwa maana ya mahindi na mchele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama kweli tunataka wananchi wa nchi hii pamoja na mfumuko wa bei hii, kuwa chini namna hii waishi maisha yenye furaha basi tuwasaidie wakulima hawa. Wakulima hawa wanaishi maisha ya dhiki sana, mahindi yao hayana soko, pamoja na kwamba mahindi haya ndio yamewezesha nchi hii sasa mfumuko wa bei kuwa chini, lakini hali ya mbolea ni mbaya sana na hali ya pembejeo ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia mahali pengine nimeona kwenye mpango anaeleza kwamba kutakuwa na uunganishaji wa matrekata ya kutosha, lakini ukifanya utafiti mdogo tu makampuni yote ya matrekta yaliyopo Tanzania unayoyafahamu, hakuna kampuni inayouza trekta zaidi ya 200 kwa mwaka mzima. Na leo hii pale Kibaha, kuna yale matrekta mekundu yale wanalalamika kwamba hawajui watayauzaje kwa jinsi yalivyo mengi. Hebu tujaribu kuona tunalinganishaje mahitaji wa wakulima ya matrekta na uwezeshaji kutoka kwenye taasisi za kibenki. Lakini mikopo yetu mingi mikopo rafiki kwa wakulima, mabenki mengi yamekuwa na riba ya juu sana, lakini ukienda kwenye mabenki wanasema sisi kama benki hatuna riba ya juu, riba hii imewekwa na Serikali. Sasa Serikali mnataka nini, mnataka wakulima waneemeke, mnataka kupata hela nyingi kutoka kwenye riba. Hili ni jambo ambalo mnatakiwa mliangalie kama mkulima hawezi kukukopa benki na kulipa mkopo huo, maana yake hayo matrekta hayawezi kununulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana wakulima wa mahindi wapate uangalizi maalum ufanywe utaratibu maalum wa masoko, ni kweli tunahitaji mahindi kwa chakula katika nchi, lakini vile vile tunahitaji wakulima hawa waneemeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mnafahamu kabisa sisi kama nchi tunahitaji fedha ya kigeni. Katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini sasa hivi liko zao la parachichi. Zao hili limekosa watalaam, hebu niombe sana Serikali muangalie namna gani sasa mtazidisha wataalam kwenye hili zao kwa sababu hili zao ndio linaleta fedha za kigeni sasa. Matokeo yake sasa ni kwamba kila mteja anayekuja anakuja na standard zake, anakwenda kwa mkulima mwingine anasema ananunua parachichi kubwa, mwingine anasema ananuna parachichi ndogo, kwa hiyo kila mtu sasa amekuwa anaamua anachokitaka.

Lakini sio hiyo tu, hatuna nyumba maalum za kuhifadhia maparachichi kwa maana ya park house, lakini vilevile kuna tatizo la vifungashio vya mazao kama parachichi. Vifungashio vinakuwa imported lakini vina kodi kubwa na kadhalika. Kama kweli parachichi linaleta fedha ya kigeni basi naomba sana msaidie kama Serikali kuona kwamba zao hili sasa linapata mstakabali mzuri ili kusudi, wakulima wengi waneemeke, lakini vilevile hata nchi iweze kupata fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la miradi ya maji. Tunafahamu kwamba hatuwezi kufanya maendeleo kama hatuna maji. Lakini tunalo tatizo kubwa sana kwenye miradi ya maji, tuna fedha ambazo miaka yote tumesema ziko ring-fenced kwa ajili ya miradi ya maji. Lakini ukiangalia Waziri wa Maji au Wizara ya Maji hailipi wakandarasi on time, inachelewa sana kuwalipa wakandarasi. Hakuna mkandarasi tajiri Tanzania anafanya kazi ya maji, Makandarasi wanaofanya kazi ya maji ni makandarasi wenzetu tu malofa malofa tu, ananunua mabomba, analaza mabomba, akimaliza kulaza mabomba na yeye mwenyewe ameishiwa, aki-raise certificate Wizarani certificate ni miezi mtatu mpaka miezi minne, haiwezekani. Miradi hii haiwezi kukamilika hata kama tunasema tunataka kumtua mama ndoo haiwezekani, utamtuaje ndoo mkandarasi halipwi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba sana Serikali iangalie kwamba tunapopanga hii mipango tunaposema kwamba tunawapa wakandarasi kazi halafu wakandarasi wakishafanya kazi wa-raise certificate walipwe basi walipwe kwa wakati. Mkandarasi anatoa certificate miezi mitatu halipwi, tuliangalie sana hilo ili tuweze kusaidia.

Jambo lingine kwenye miradi, tunayo miradi ambayo ni miradi ya kuendeleza miji. Miradi hii ina mikopo kutoka World Bank, lakini miradi utekelezaji wake umekuwa ni wa mateso makubwa sana kwa Halmashauri zetu. Wanajenga stand, wanajenga masoko, wanajenga barabara, lakini wakandarasi kwenye mikataba wameandikiwa kwamba kutakuwa na msamaha wa kodi. Lakini unapopeleka msamaha wa kodi Wizarani, msamaha hautoki. TAMISEMI imefanya semina, imewaita watalaam wa Wizara ya Fedha, imeita wataalam sijui wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamewapa semina, wamewaelimisha wanaanza kutekeleza yale waliyowaelimisha ukifika Wizara ya Fedha hakuna msamaha wa kodi.

Naomba sana kama tunapanga mipango yetu, tunawapa watu semina tujue kabisa zile semina ni gharama ya Serikali, na ni fedha ile tunaipoteza. Kwa hiyo, tunapoanza utekelezaji miradi hii basi mara moja msamaha wa kodi uweze kutoka na miradi iweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije suala la biashara. Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, biashara nyingine ambayo wanafanya ni biashara ya mazao ya misitu. Lakini sisi kama Watanzania kama kweli tunataka maendeleo kwenye hizi biashara, hebu tuangalie style yetu ya kufanya biashara. Mazao ya misitu ya Nyanda za Juu Kusini ni mazao ambayo yanatokana na misitu ya kupandwa ambayo ni mbao, nguzo, magogo mbalimbali, fito na mijengo mbalimbali. Lakini iko sheria ya maliasili ambayo inakataza mazao ya misitu yasitembee usiku. Sasa unajiuliza sheria hiyo ni nzuri sawa, lakini mfanyabiashara anabeba mzigo kutoka Nyanda za Juu Kusini kwa maana ya Njombe, amebeba mbao, halafu akifika karibu anakaribia Dodoma kama mitaa ya huko Mpunguzi, saa 12 jioni ikifika lazima asimamishe gari alale pale. Lori la mzigo lililobeba mbao, lililobeba nguzo, lililobeba fito, linasimamishwa lilale hata kabla hata kuku hawajaingia kulala. Hivi kweli sisi tunataka kufanya maendeleo tunataka kufanya nini. Kama gari la mizigo limekaguliwa njia nzima toka alikotoka na mzigo amekaguliwa lakini anafika Mpunguzi ambako hazizalishwi mbao, haizalishwi nguzo, hakuna miti ya kupandwa lakini anapaswa kulala hapo mpaka asubuhi saa 12 jioni, aendelee na safari.

Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama unataka watu wawe na fedha na watu wafanye biashara, vikwazo vidogo vidogo kama hivi muwe mnavifuta mara moja ili kusudi watu wafanye biashara. Mimi sioni kama kuna sababu yoyote ya kuzuia watu wanaosafirisha mazao ya msitu hayakupandwa baada ya saa 12 jioni. Kwanza ameambiwa gari unayotumia kusafirishia liwe la wazi, amefanya gari limekuwa la wazi, usifunike na turubai, hajafunika na turubai, lakini bado anaambiwa saa 12 jioni mwisho. Ukikutwa na gari imebeba mbao saa 12:05 unapigwa faini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la elimu. Tunaiendea sana Tanzania ya viwanda, naomba sana Serikali iangalie uwezekano wa kuwa na vyuo vya uwalimu wa ufundi ili kusudi sasa waweze kutoka Walimu wengi waweze kufundisha katika shule zetu ili tuweze kupata mafundi wengi vinginevyo viwanda hivi tutawafanya vijana wetu wawe watwana, wawe watu wa kupakia maboksi, kufagia viwanja na kuchimba mashimo ya takataka. Lakini kama tunataka vijana hawa wafanye kazi za kitaalam viwandani ni kazi za ufundi. Kwa hiyo kazi ya kwanza ni tupate walimu wa kutosha wa Ufundi na waweze kutoa elimu kwa wanafunzi ili waweze kufanya hizo kazi za ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa walimu wa sayansi hali ni mbaya sana wewe shule ni ya sekondari miaka 10 lakini haina mwalimu hata mmoja wa physics naomba sana hilo liangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa name niweze kuchangia Kamati mbalimbali ambazo zimewasilisha taarifa zake leo ikiwemo Kamati ya UKIMWI, ambayo mimi pia ni Mjumbe katika Kamati hiyo. Awali ya yote nimpongeze sana Mwenyekiti wangu, kwa wasilisho lake lililo zuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi ya UKIMWI yana utata mwingi sana, lakini sisi kama nchi, nadhani sasa imefika wakati tuweze kuona kwamba ni nini tufanya ili tuweze kupambana na UKIMWI vilivyo. Kwanza kabisa nianze na jambo moja, uko ukinzani wa kisheria ambao unatuletea shida sana katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ndoa, inasema, mtoto anaweza akaolewa kwa ridhaa ya mzazi, akiwa na miaka 14, lakini Sheria ya UKIMWI inamtaka mtoto huyu apime kwa hiyari vizuri vya UKIMWI akiwa na miaka 18. Maana yake nini? Maana yake binti au kijana au hawa wanandoa, wakitaka kupima na hata kama wameshaoana, maana yake wafunge safari warudi kwa wazazi, wakawaambie wazazi wao kwamba sasa tunaomba mtusindikize Hospitali au kwenye kituo cha kupima, tukapime UKIMWI. Ni jambo ambalo linaleta utata sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali iangalie tufanye nini haraka iwezekanavyo ili hizi sheria zisikinzane. Haiwezekani mtoto huyu mwenye miaka 14 aende kwa mzazi akaombe kwenda kupima. Kwa hiyo, nayo inaleta shida katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linaleta shida katika mapambano dhidi ya UKIMWI, liko tatizo kubwa sana, ukisoma kwenye bajeti za Wizara UKIMWI ipo kwenye kipaumbele. Hata ukienda kwenye Halmashauri, mapambano ya UKIMWI yako kwenye kipaumbele, lakini ikija kwenye utekelezaji, liko tatizo kubwa. Ni kwamba haya mambo yanapitishwa na Bunge hapa, bajeti inatengwa, lakini ikifika kule Wizarani au ama kwenye Taasisi za Umma inawekwa tu, hakuna anayeifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia kwenye Kamati yetu ya UKIMWI, tukiita Taasisi za Umma, kuja kueleza afua za UKIMWI mahala pa kazi, unakuja kuta ndiyo Kamat imeundwa. Maana yake ni nini? Wito wa Bunge kuja kujibia afua za UKIMWI kwenye Taasisi zao za Umma ndiyo imewafungua macho kwamba kumbe liko jambo tunatakiwa kulijadili katika ngazi ya Wizara au kwenye ngazi ya Taasisi yetu ya Umma.

Mheshimiwa Spika, Taasisi nyingi kwa lugha ya kawaida hazikuweza kufika kwa wakati kwa sababu hazikuwa na cha kusema mbele ya Kamati. Kwa hiyo, wanakwambia tumeunda Kamati na ndiyo tumeanza. Unauliza Wizara nzima, kuna Watumishi wangapi kwa hiyari yao wamesema wao wana virusi vya UKIMWI, wanakwambia mmoja; wengine wanasema hakuna. Kwa hiyo, unaona kabisa kwamba kumbe jambo hili katika jamii linazoeleka na linaonekana ni jambo la kawaida. Kama linazoeleka na linakuwa jambo la kawaida madhara yake ni kwamba mapambano haya hatutafanikiwa. Kwa sababu hatuchukulii kama ni jambo hatari na linahatarisha maisha yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kutoa wito kama Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI kwamba Wizara na Taasisi za Umma zote mahala pa kazi, zihakikishe kwamba suala la UKIMWI, linajadiliwa na wale wote ambao wanaohusika wapime na waweze kupata majibu kujua kwamba hali zao za afya zikoje? Baada ya kujua hali zao za afya, basi waanze kufuata hizo afua za UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine ambalo linatusumbua sana kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI ni usiri. Usiri ndiyo unaoathiri sana katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Usiri huu sasa hivi inaelekea umetengenezwa na Taasisi zinazotoa huduma za Afya. Zamani hapo ilikuwa kuwawekea wagonjwa wa UKIMWI mahali maalum pa kutibiwa, pa kuchukua dawa na Mganga Maalum, ilikuwa ni jambo linaloonekana ni jambo la faragha na jambo linalowasaidia wagonjwa wa UKIMWI. Leo, hali hiyo imebadilika imekuwa sasa huo ndiyo unyanyapaa wenyewe, kwamba mtu hayuko tayari kwenda kule kwenye kituo cha kutolea huduma za dawa na vipimo, CTC.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri sana Serikali, hebu tuufute ule utaratibu wa CTC, wagonjwa wote sasa waende kwenye huduma ya kawaida; tukikaa kwenye mstari pale hospitalini, mimi mwenye virusi na mwingine asiye na virusi tukae pale tumwone Mganga huyo huyo, tutibiwe tuondoke. Tuache ile kwenda kuwaficha wagonjwa wa virusi mahali kwenye CTC na kuwapangia siku maalum, kwa sababu hiyo inasababisha sasa watu wengi zaidi; moja, waende hospitali za mbali sana kutafuta huduma, au vituo vya mbali sababu ya aibu, lakini pili, akikosa nauli ama uwezo wa kwenda huko mahali, matokeo yake anakuwa hawezi kwenda kupata zile dawa na anaacha kutumia dawa. kwa hiyo, nafikiri, tuondoe huo usiri na ugonjwa wa UKIMWI tuuone ni ugonjwa wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali za afua za UKIMWI zilipofikia sasa, zimefanya ugonjwa wa UKIMWI uonekane wa kawaida kabisa. Nampongeza sana Dkt. Maboko na Taasisi yake ya TACAIDS wanajitahidi sana kufanya vizuri na wanatoa elimu vizuri, lakini kikubwa hali ya bajeti ya Taasisi hii iko chini sana. Kwa hiyo, hiyo nayo itakuwa ni kikwazo kwa maana ya mapambano dhidi ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, suala la madawa ya kulevya; Taasisi ya Kupambana na Madawa ya Kulevya katika nchi yetu kwa kweli imefanya kazi kubwa sana, chini ya Dkt. Sianga. Tunatakiwa wote kama Watanzania tuwapongeze, lakini vile vile tuwaunge mkono. Hali tuliyokuwa tunaenda nayo kama nchi ilikuwa ni mbaya sana. Ilikuwa kila mahali unapokwenda, hukosi wanaoitwa mateja, lakini leo hii kumkuta teja ni kazi ngumu kidogo. Kwa hiyo, hii ni dalili kwamba Taasisi hii inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba Taasisi ya Kupambana na Madawa ya Kulevya peke yake, haiwezi. Sisi kama Watanzania, kama Wabunge ni lazima tuisaidie hii Taasisi. Serikali nayo iwekeze katika miundombinu ya kisasa ya kuhakikisha kwamba vifaa vya kisasa vya kupima na kutambua madawa ya kulevya vinakuwepo ndani ya nchi na vinaweza kusaidia Taasisi hii, kuweza kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwas Spika, jambo lingine ambalo ningeweza kuliongelea ni suala la elimu. Tunafahamu kabisa kwamba sasa tunatekeleza elimu bila malipo, lakini suala hili bado lina mkanganyiko mkubwa sana katika jamii yetu. Utakuta kwamba miundombinu mingi wananchi wamejenga; wamejenga madarasa, wamejenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi, lakini hayana samani mle ndani. Linapokuwa suala la samani inakuwa ni shida sana. Naomba sana Serikali itoe muongozo vizuri. Nafahamu kabisa kwenye mwongozo uliotolewa mara ya mwisho juu ya elimu bila malipo ilieleza kabisa kwamba jukumu la miundombinu ni jukumu la wananchi, lakini inapofika mahali fulani kuna mkanganyiko unatokea, baadhi ya sehemu hawatambui kwamba dawati ni sehemu ya miundombinu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anapoambiwa mzazi achangie dawati, lakini hapo kunatoa ukinzani; wako Maafisa wa Serikali wanasema hapana, hatakiwi kuchangia. Unajiuliza, mtoto anakwenda shuleni, atakalia nini? Fedha ya dawati iko wapi? Kwa hiyo, naomba sana, hili litolewe ufafanuzi mzuri ili kusudi tusiende kule tukakanyagana kati ya Watendaji na wananchi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la Ikama ya Walimu. Hali ya Walimu katika nchi yetu imekuwa mbaya sana. Shule nyingi hazina Walimu. Mimi nafikiri kupanga ni kuchagua. Kama tunaamini kabisa kwamba elimu ndiyo msingi wa kulifanya Taifa letu liwe bora. Naomba sana sasa Serikali ifanye maamuzi magumu kwamba ikamilishe Ikama ya Walimu. Inapokuwa inakamilisha Ikama ya Walimu kwenye shule zetu, vile vile iangalie, liko tatizo linajitokeza, Walimu wanastaafu, kwa sababu tunajua kabisa Mwalimu akistaafu maana yake atakuwa hayuko kwenye Utumishi, pale panakuwa na pengo.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri inafika mahali wanastaafu Walimu zaidi ya 30, hakuna hata Mwalimu mmoja anayeajiriwa katika Halmashauri ile. Mara ya mwisho tukaambiwa kwamba ikiwa waliopatikana na vyeti bandia, walikuwa 15, basi Halmashauri hiyo inarejeshewa Walimu 15. Kwa uhakika kabisa katika Halmashauri yangu ya Njombe Mjini, hilo halikufanyika. Walitolewa Walimu kati ya 15 na 18 lakini walioletwa ni Walimu wanne, kitu ambacho nimejaribu kuulizia na kufuatilia imeonekana ni tatizo kabisa.

Mheshimiwa Spika, shida ya Walimu ni kubwa sana na ni shida ya nchi nzima. Kwa hiyo, naomba sana, tukamilishe idadi ya Walimu katika shule zetu, kwa sababu wananchi wanajenga miundombinu, wanajitahidi.

Mheshimiwa Spika, upande wa Sekondari hakuna shida kubwa sana, shida tu kwa Walimu wa Sayansi, hasa Shule za Msingi kuna shida kubwa sana. Inafika mahali ambapo wananchi wanaambiwa jamani, sawa mmeleta watoto shuleni, liko Darasa la Awali, hili darasa sasa hatuna Mwalimu, tunajadiliana sisi kama wazazi tunafanyaje? Sasa kunatokea upinzani, wengine wanasema ni elimu bure, wengine wanasema tuchangie jamani watoto wasome, mazingira kama hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Ikama ya Walimu iangaliwe sana na Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote niseme naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napende kusema kwamba, naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inayofanya. Katika Jimbo la Njombe tumepata maendeleo ambayo toka dunia kuumbwa haijawahi kutokea. Nitoe mfano mmoja tu, tumepelekewa maendeleo na Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika Kata ya Utalingolo katika Kijiji kijulikanacho kwa jina la Ihalula, mpaka leo nilipokuwa nafuatilia, maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni mbili, haijawahi kutokea. Naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumejengewa zahanati mahali pale ya shilingi milioni 500, tumepelekewa vifaa vya hospitali vya zaidi ya shilingi milioni 300, lakini tumepelekewa umeme kwa thamani ya shilingi bilioni moja. Naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inayofanya katika nchi yetu, lakini ni pamoja na maendeleo mengine makubwa yanayofanyika ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizi, yako mambo ambayo tungependa sana Serikali yetu ifanye. Ni- declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC. Tunakushukuru sana umetuwezesha tumefanya ziara nyingi sana katika Kamati yetu. Jambo kubwa nililoliona ni tatizo kubwa la maji katika nchi, lakini ni pamoja na Jimbo la Njombe Mjini, lina tatizo kubwa la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi mingi ya maji katika nchi yetu ukiiangalia imekosewa design. Kikubwa kinachofanyika ni kwamba, ndani ya Halmashauri husika hakuna wataalam wa maji. Halmashauri wanatafuta Mkandarasi au Msanifu wa mradi, anakuja msanifu wa mradi anasanifu mradi, baada ya kusanifu mradi anaikabidhi Halmashauri. Halmashauri inaupokea ule mradi haijui chochote. Ina Mhandisi pale naye hajui chochote. Vinaandikwa vitu ambavyo ikifika wakati wa kutekeleza mradi, mradi hautekelezeki. Hilo ndiyo tatizo kubwa katika Halmashauri zilizo nyingi ikiwemo Halmashauri yangu ya Mji wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Mji wa Njombe uko mradi unaitwa Igongwi, ni mradi wa vijiji sita kwa ajili ya maji, lakini mradi ule umesanifiwa na umeanza kutekelezwa na una lots kama tano au sita, lakini lot ya kwanza ni ya uzalishaji maji kwenye chanzo. Kwenye chanzo, kutokana na umbali na milima ilivyo, Msanifu ameweka mabomba ambayo hayawezi kufika kule. Sasa unajiuliza huyu Msanifu alifikaje kule aka-design mabomba mazito kiasi hicho ili yaweze kwenda kule?

Mheshimiwa Spika, nimeenda Halmashauri ya Ilemela, Mwanza, Msanifu amesanifu mradi wa maji wa kijiji uchimbwe mtaro kwenye mlima wa mawe. Matokeo yake imekuwa haiwezekani, Mkandarasi ameshindwa kufanya vile, imebidi ifanyike variation. Kwa hiyo, unajiuliza, hivi tuna Wahandisi wa Maji kweli katika Halmashauri zetu? Tuna wataalam wa maji kwenye nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeenda Halmashauri ya Ngara, Msanifu amesanifu tenki la maji lijengwe kwa matofali. Mkandarasi amejenga kwa mawe, tenki linavuja na kuna Mhandisi wa Halmashauri. Tumeenda Halmashauri ya Mheshimiwa Mwijage, mradi wa maji umekamilika hakuna mita inayoonesha kiasi gani cha maji kilichopo kwenye tenki. Unamwuliza Mhandisi wa Halmashauri anasema labda Mkandarasi ali-overlook. Sasa unajiuliza, yeye kama Mhandisi wa Halmashauri alikuwa wapi?

Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara ya Maji ifanye utaratibu mpya wa kupata Wahandisi sahihi wa Maji ili kusudi Wasanifu wanaposanifu miradi ya maji, ile miradi ikifika kwenye Halmashauri, wakiiwasilisha kwenye Halmashauri Mhandisi wa Maji mwenyewe auone ule mradi ni nini kimeandikwa na nini kinatakiwa kufanyika? Vinginevyo tutalalamika matatizo ya maji, fedha itapotea, Wakandarasi watashindwa kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwenye miradi ya maji, pamoja na upungufu ambao upo, Wizara na yenyewe inachelewa mno kufanya marekebisho. Wakandarasi wanaweza wakaleta taarifa kwamba hapa hili jambo halitekelezeki, lakini unaona kabisa Wizara inachukua muda mrefu sana kufanya marekebisho. Naomba sana Wizara ijitahidi kufanya marekebisho mapema ili miradi ya maji iweze kwenda.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni suala la biashara. Katika Halmashauri ya Mji, Njombe sisi sio wafanyabiashara per-se, lakini sisi ni wakulima, lakini mazao yetu ndiyo hayo tunayoyafanya kuwa biashara. Nizungumzie suala la mazao ya misitu hasa mbao, miti, nguzo na majengo.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumza kwamba mazingira ya kufanya biashara Tanzania ni magumu, sisi wakulima wa miti Njombe tunayaona hayo. Tunayaona kwa namna ipi?

Mheshimiwa Spika, sisi zao la miti ni zao la kawaida kama yalivyo mazao mengine kama korosho, wanaolima mpunga, mtama, mbaazi, na kadhalika. Inapokuja kwenye zao la miti kumewekwa sheria na taratibu nyingi sana. Taratibu ya kwanza ambayo inachelewesha maendeleo kwa wananchi hawa, ukitaka kuvuna miti yako, baada ya kuivuna, ili usafirishe mbao kuna kitu kinaitwa TP (Transit Pass). Sasa kama umeshavuna na unataka kusafirisha, ile Transit Pass inapatikana Makao Makuu ya Halmashauri. Kwa hiyo, mwananchi anapaswa kusafiri kilometa kadhaa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tuchukulie mwananchi anayetoka mwishoni kabisa mwa Jimbo la Njombe Mjini, kwa mfano Kata ya Makoo ambayo iko kilometa 70, lazima aje Njombe Mjini, akate TP ambayo thamani yake haizidi shilingi 3,000/= au shilingi 4,000/=, arudi kijijini akatafute usafiri asafirishe. Hiyo safari peke yake inamgharimu zaidi ya shilingi 20,000/=. Hiyo ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, ya pili, mazao haya ya misitu pamoja na kwamba jana Serikali ilizungumza hapa kwamba itaweka utaratibu rasmi, lakini mwananchi yule haruhusiwi kusafirisha ule mzigo kutoka kule kijijini kuleta sokoni baada ya saa 12.00 jioni. Sasa ukiangalia haya ni mazingira ambayo yanachelewesha maendeleo. Wananchi wanashindwa kusafirisha mazao yao ya kawaida kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Njombe, kama Mkoa, idadi yetu tuko 700,000 tu, lakini wenye nafasi ya kuchangia maendeleo, nguvu kazi, siyo zaidi ya 400,000. Sasa ukiangalia watu 400,000 tunachangia maendeleo, tunafanya nchi iweze kupata mbao, ipate nguzo, ipate miti, lakini vilevile tunachangia chakula, tunalima mahindi kwa wingi sana, tunalima viazi kwa wingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana, idara inayohusika na mambo ya misitu iangalie upya jambo hili. Inapokuwa inazuia wananchi wasiweze kufanya biashara eti kwa sababu saa 12.00 imefika, huku ni kuchelewesha maendeleo kwa makusudi. Niombe sana sisi wenye misitu ya kupandwa turuhusiwe kufanya biashara, zao letu la miti liwe kama zao la kawaida kama vile zilivyo mbaazi, pamba, mpunga, na kadhalika ili kusudi speed ya maendeleo iweze kupatikana kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, mnapotuwekea mazingira ya kuweka sijui vibali, utaratibu, kama hiyo TP hatukatai, iwepo, lakini ikatwe kijijini, kwa sababu kule kuna Mtendaji wa Kijiji ambaye ni Mtumishi wa Serikali. Idara ya Misitu ikasimu kwamba akitokea mwananchi ana miti yake anataka kusafirisha, mkatie TP kuliko asafiri kilometa 70 akakate TP arudi kijijini akaanze kusafirisha, inafika saa 12.00 hawezi kuondoka, asubiri siku ya pili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie hilo na ilione kwamba ni jambo linalochelewesha maendeleo wakati mahali kwingine tunakwenda haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumzia jioni ya leo katika kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni suala la elimu. Elimu yetu inapata shida, inapita wakati mgumu. Tunafanya elimu ipite wakati mgumu kwa sababu ya kutokutaka kubadilika. Kuna vitu tunavisimamia haviko sahihi.

Mheshimiwa Spika, tumeanzisha Shule za Kata. Shule za Kata leo zimekuwa bora sana na performance inaonekana kwenda kuwa juu sana. Nimekuwa nikishauri hapa na Wajumbe wengine walikuwa wakichangia hapa kwamba, katika Shule zetu hizo za Kata, tuanzishe michepuo ya ufundi. Jambo hili limekuwa gumu sana. Yaani limekuwa gumu. Kila mtu akisimama hapa anasema VETA, Serikali yenyewe ikisimama inasema VETA; lakini hizo VETA ukiangalia jinsi zilivyo, zitaweza kuchukua watoto wote hawa wanaohitimu Kidato cha Nne? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna ugumu wa kubadilisha shule angalau moja kila Halmashauri kuwa Shule ya Ufundi. Naomba sasa Serikali ilione hilo na iweze kusaidia hawa vijana. Vijana hawa wakipata Elimu ya Ufundi tutakuwa tumewasaidia, tutakuwa tumewapa ajira na tumewapa ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nina mashaka nalo sana, miaka ya nyuma wakati tuna Shule za Ufundi kama Ifunda Tech, Moshi Tech, Tanga Tech, Mtwara Tech, Ihungo na nyinginezo, kulikuwa na Chuo kinaitwa Dar es Salaam Technical College, lakini kilikuwa kinatoa Diploma ya Ualimu wa Ufundi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. (Kicheko)

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika hoja hii ya Wizara ya Maji ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitoe pongezi nyingi sana kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inayofanya. Nikisema juu ya Mheshimiwa wetu Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, alifanya ziara katika Mkoa wa Njombe na pale Njombe Mjini alituahidi kwamba kuanzia Septamba mkandarasi atakuwepo site kwa ajili ya maji ya Mji wa Njombe. Nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri na wewe mwenyewe ulithibitisha mbele ya Mheshimiwa Rais kwamba mkandarasi atakuwepo Njombe kwa ajili ya mradi wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana jambo hilo litekelezwe kwa sababu Mji wa Njombe unakua kwa kasi na una shida kubwa sana ya maji. Kwa kuwa shida ile ni kubwa na shida yenyewe inasikitisha kwa sababu Njombe kila bonde lina maji ya mwaka mzima sasa tunapokuwa na mji hauna maji na mabondeni kuna maji o hapo masikitiko yanaongezeka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wetu wa Wizara ya Maji kwa maana ya Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Maji tunawapongeza sana. Wanafanya kazi nzuri, ni wasikivu na wanachukua hatua pale tu ambapo tunakuwa tumeshawaeleza matatizo yaliyopo katika Majimbo yetu na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Njombe, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri umeingilia Mradi wa Igongwi ambao unaleta shida sana katika Jimbo la Njombe Mjini na nakushukuru sana kwa sababu kasi inakwenda vizuri. Niwaombe wenzangu kule Jimboni, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Mhandisi wa Maji na Mwenyekiti wangu wa Halmashauri wafanye haraka kadri ya maelekezo yako ili kusudi tuweze kumruhusu tena mkandarasi wa Lot One ya Igongwi ili vijiji vinavyoangukia katika mradi huo viweze kupata maji ambavyo Vijiji vya Uwemba, Njomlole, Luponde pamoja na Kitulila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Njombe kiko kijiji kinaitwa Lugenge katika Kata ya Lugenge, kina mradi ambao umekadiriwa kusaidia zaidi ya vijiji sita. Mradi huu ulikuwa ni wa miezi tisa lakini mpaka hivi tunavyoongea una miaka saba haujakamilika. Mheshimiwa Naibu Waziri unakumbuka tulifika katika kile kijiji na tuliona ule mradi, mkandarasi alituahidi kwamba ndani ya miezi mitatu atakuwa amefikisha maji kwenye tenki hadi dakika hii ninavyoongea mkandarasi yule hajamudu kazi ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mtusaidie wananchi wa Lugenge wapate maji. Miundombinu ya usambazaji na matenki ya Vijiji vya Lugenge, Kiyaula, Kisilo, Ihalula na Otalingolo yalishakamilika lakini miundombinu ya kuleta maji kutoka kwenye chanzo mpaka leo haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya tatizo kubwa tunalopata kwenye miradi ya maji, kadri nionavyo mimi hatuna mipango kwa maana ya Halmashauri kuwa na mpango wa maji wa Halmashauri kwamba tunatekeleza mradi upi, kwa ajili ya kijiji kipi, kwa gharama zipi na tukimaliza huu tunaenda upi. Niombe sana sasa Wizara itoe hayo maelekezo kwamba kila Halmashauri sasa iwe na mpango kwa maana kwamba kuwe na usanifu wa kila kijiji ili kuwezesha vijiji viweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Njombe Mjini kuna Vijiji kama Mtila, Lusitu, Idihani, Idunda, Ihanga, Uliwa, havina dalili kabisa ya kupata maji ya bomba. Niombe sasa Serikali isaidie kutoa maelekezo kwa Halmashauri kusudi vijiji hivi vifanyiwe usanifu, viwekewe mipango ya maji ili tujue kabisa kwamba katika utekelezaji wa mipango yetu ya maji vijijini ni lini itatekelezwa na kwa gharama zipi ili kusudi tunapowaeleza wananchi kwamba tuna jitihada ya kuleta maji hapa, wawe wanafahamu kwamba ni kweli jitihada ya kuleta maji inafanyika kuliko unasema kwamba una jitihada ya kuleta maji lakini hata usanifu haujafanywa, haijulikani ni lini maji yatapelekwa mahali hapo na ni nani atafanya kazi hiyo. Niombe sana jambo hilo liweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalalamika sana juu ya miradi ya maji lakini tatizo kubwa ambalo tunaliona sisi kama wawakilishi wa wananchi na hasa hasa katika Jimbo langu la Njombe Mjini ni tatizo la usanifu. Unaona kabisa kwamba usanifu umefanyika hasa hasa ile miradi ya vijiji 10, mimi katika Jimbo langu kuna mradi wa Vijiji vya Ngalanga na Utengule, usanifu umefanyika katika mazingira ambayo hayana maji na mkandarasi amepewa kazi ya kutekeleza ule mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naye katika utekelezaji wake anatekeleza kwa viwango vya chini sana. Anaweka mabomba ambayo hayawezi kuhimili pressure, unajiuliza ni nani hapa mwenye mapungufu, ni Mhandisi wa Maji wa Halmashauri, ni msanifu aliyesanifu mradi au mkandarasi? Hakuna teknolojia rahisi kama ya maji, inabidi wataalam wetu huko Wizara ya Maji watafakari na wajiulize kwamba ni kweli wanastahili kuendelea kutoa huduma katika Wizara hiyo? Kwa sababu haiwezekani teknolojia rahisi inashindwa kutoa huduma. Hivi kama leo tungefanya mabadiliko tukasema Wizara ya Maji ndiyo iwe Wizara ya Ujenzi, ina maana madaraja yangebomoka siku ya pili yake, barabara zingebomoka siku ya tatu yake, tungekuwa hatuna huduma kabisa. Teknolojia rahisi kama ya maji tunashindwa kweli kusafirisha maji yawafikie wananchi na tunaona Serikali inatoa fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, wataalam wa Wizara ya Maji wakishirikiana na Wahandisi wa Wizara ya Maji walale kwenye taaluma zao, wafanye kazi kitaalam. Sisi ni wanasiasa lakini tunafika mahali tunaona kabisa kwamba usanifu uliofanywa siyo sahihi kabisa lakini wao kwa vigezo vyao vya utalaam wanasema hivi ndiyo inavyotakiwa, kwa kweli inasikitisha sana. Mimi najua kabisa Waziri, Naibu Waziri na Katibu wetu Mkuu mko makini sana, hebu waangalieni hawa wataalam, kweli wana moyo wa dhati wa kuwasaidia Watanzania wapate maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunalo tatizo sana la watengenezaji wa vifaa vya mabomba. Watengenezaji wa vifaa vya mabomba wamekuwa wakiingia katika mitego ya gharama wakishirikiana na Maafisa Manunuzi katika maeneo mengine lakini wakati mwingine wanaingia kwenye mitego ya gharama wakishirikiana na wakandarasi. Mkandarasi BOQ inamuambia bomba labda la PN9 lakini kwa sababu bomba la PN9 ni la gharama kwa hiyo mkandarasi anaongea na mwenye kiwanda, mwenye kiwanda yuko tayari kugonga muhuri wa PN9 kwenye bomba la PN6 ama PN5 matokeo yake ule mradi unakuwa unavujisha maji mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama tunavyosema kwamba tujali viwanda vya ndani, naomba Serikali na sisi Wabunge tusimame pamoja tuwaambie wenzetu wanaotengeneza vifaa vya mabomba kama kweli wanataka tuendelee kuwaunga mkono ili kusudi uzalishaji wa vifaa vyao vya maji viweze kununuliwa na vitumike kwa wananchi basi wawe waaminifu, wakweli na wawe wanatengeneza vitu ambavyo ni imara kwa sababu haiwezekani Serikali itoe fedha nyingi wananchi hawapati huduma, yaani haiwezekani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, inafika mahali wakati mwingine mkandarasi anakwambia kabisa ni bora nikaagiza bomba kutoka nje ya nchi ni nafuu kuliko kununua ndani. Kwa hiyo, ina maana sasa hata kumuunga mkono huyo mzalishaji binafsi haisaidii kitu. Kwa hiyo, niombe sana kama itawezekana kwenye upande wa usanifu, Serikali iangalie sana kwenye usanifu pamoja na engineering cost kwa sababu hapa mahali pawili ndipo ambapo wakandarasi pamoja na watu wa manunuzi pamoja na consultants wanacheza na gharama za miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mbinu ya pekee ambayo inaweza ikasaidia. Kama inawezekana kabisa, tunao wahandisi katika idara mbalimbali za Serikali, tunao wahandisi wa Jeshi wako Mzinga, wako Suma JKT, tuwe tunawashirikisha kuona hizi engineers cost ziko sahihi kweli kwa sababu bila kufanya hivyo tunamuachia mhandisi na mtu wa manunuzi wanaweka ile engineers cost matokeo yake mradi unakuwa na gharama kubwa halafu unakuwa hautekelezi lakini ukishaona kwamba mahali panapoingia nafsi ya ulafi maana yake hata ufanisi wa kazi unashuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naunga mkono hoja na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia zawadi ya uzima. Nitumie fursa hii kwanza kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Wizara yake na watendaji wote wa Wizara ya Fedha. Pia niwashukuru na kuwapongeza sana Serikali yetu chini ya Rais wetu John Pombe Magufuli na watendaji wote, tumefanya kazi vizuri kwa pamoja katika Mpango uliopita na matokeo yameonekana na sasa tunaenda kujadili mpango kwa ajili ya mwaka wa fedha unaofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu na Waziri katika kitabu chake ameeleza kwamba mafanikio ya kilimo yamekwenda zaidi ya asilimia 100 lakini kusema kweli ni jambo la kusikitisha sana. Kilimo hiki ambacho kimetufikisha hapa tulipo kwamba nchi ina chakula cha kutosha na kimekwenda zaidi ya asilimia 100 si kilimo kile ambacho kimezalisha kwa nafasi ambayo tunasema ni sahihi, ni kwamba watu wamefyeka sana misitu, wamepanua sana mashamba lakini mashamba yenyewe tija kwa eka iko chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hali iko namna hii? Hali iko namna hii kwa sababu, moja, udongo wa nchi yetu haujapimwa. Wananchi wanatibu udongo kwa maana ya kutia mbolea ya kukuzia mazao yao lakini hawajui kama hitaji la udongo ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mbili wananchi hawa hawana Maafisa Ugani. Wizara ya Kilimo kama sikosei kuna kipindi haikuajiri Mabwana Shamba zaidi ya miaka 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni zana za kufanyia kazi. Tumeshuhudia makampuni mbalimbali ya matrekta mengine ya umma yameleta matreka katika nchi yetu matrekta yale mabovu, yamewatia hasara wananchi. Haiwezekani trekta unalimia msimu mmoja halafu inakufa. Tunashuhudia kabisa matrekta ya siku za nyuma yamekuwa imara na yamekuwa yakisaidia sana katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tunapokwenda kuandaa Mpango mwingine, tujipange vizuri tuhakikishe kwamba tunapata Maafisa Ugani wa kutosha katika maeneo yetu ya kilimo ili kusudi wananchi wapate wataalamu wa kutosha. Ni jambo muhimu sana wakulima wapate wataalamu wa kutosha tujipange tupime udongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye kitabu inaeleza kwamba kutakuwa na upimaji wa matabaka ya udongo basi hilo jambo lifanyike kwa sababu litaenda kuwasaidia wakulima. Mafanikio yake tuyaone kwamba wakulima sasa watumie eneo dogo halafu wazalishe zaidi lakini wanafyeka sana misitu na wanapanua sana mashamba ili kusudi wapate mazao mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwa taasisi zinazoleta vitendea kazi kama matrekta naomba Serikali iangalie. Kama kweli tunataka kuinua kilimo na kusaidia wakulima tuhakikishe kwamba zana za kilimo zinazoletwa kwenye nchi yetu ni imara na zinaweza zikawasaidia wananchi kwa muda mrefu kuliko sasa leo hii ni kilio, madeni waliyokopeshwa wananchi kwa ajili ya yale matrekta hayalipiki, taasisi zilizoleta matrekta zinalia hasara, mabenki yanalia hasara lakini matrekta ni mabovu. Huu ndiyo ukweli wenyewe, yale matrekta ni mabovu. Najua nayasema haya kuna watu watachukia lakini wacha wachukie tu, matrekta yale ni mabovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la masoko. Tutakapokuwa tumewawezesha wakulima tujitahidi kuongeza masoko. Leo hii tunazungumza habari ya soko la Congo lakini tunalenga upande mmoja zaidi upande wa kusafirisha mizigo tu lakini tukumbuke kabisa kwamba mazao ya kilimo vilevile yana soko Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini tunaomba sana ile bandari ikamilike. Mtakapokuwa mnapanga mipango hiyo sasa tunawashauri mkamilishe bandari ile na iweze kufanya kazi vizuri kusudi tuanze kupeleka mazao Congo. Siku mzigo wa Congo utakapokuwa haupo, mazao yetu ya kilimo yatakwenda Congo na kwa idadi ya watu ina maana wao ni wengi kuliko sisi kwa hiyo ina maana wanahitaji kula kuliko sisi ni soko mojawapo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Mchuchuma na Liganga. Mchuchuma na Liganga hata ukiangalia kwenye Hansard za Bunge sidhani kama kuna kipindi cha Bunge kiliwahi kupita bila kuongelea Mchuchuma na Liganga. Hebu sasa Serikali ifanye maamuzi ambayo yataifanya Mchuchuma na Liganga iweze kufanya kazi. Mmesema mmetenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi lakini vilevile mnasema mnataka kulipa fidia sehemu ya kupitisha njia ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke umeme utakuwa ni zao la Mchuchuma ili uende Liganga lakini kuna barabara zinazokwenda kule, iko barabara ya Itoni - Manda mpaka leo tunasema kilometa 30 tunapanga mpango wa maendeleo hapa naomba basi tukamilishe hii barabara kuanzia Itoni - Manda barabara ikamilike. Tunachoambiwa kila siku ni kwamba ile barabara ni ndefu sana ya zege nchi nzima hakuna barabara ndefu kama ile, haiwezi kutusaidia kama hii barabara haijaanzia Itoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa kama tunataka kufanya uwezeshaji migodi ile iweze kufanya kazi basi tujipange tuweze kutengeneza na barabara iweze kufika maeneo yale. Imekuwa ni bahati mbaya sana wataalamu wetu wanapopanga mipango unasikitika kuona kwamba wanaweza wakapanga kujenga, nichukulie mfano mmoja tu pale Njombe wamejenga Mahakama ya Mkoa lakini mradi ule ulikuwa ni wa kujenga Mahakama tu hakuna hata barabara kuifikia hiyo Mahakama yenyewe. Mkandarasi anapita porini mpaka kuifikia hiyo Mahakama yenyewe, hata itakapokuwa imekamilika hakuna fungu la kutengenezea barabara. Kwa hiyo, nafikiri tunapopanga mipango tuhakikishe kwamba kama tunajenga mradi kama Mahakama basi na mipango yake ya kujenga barabara kuifikia Mahakama hiyo iwepo kusudi itakapokuwa imekamilika iweze kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema hata Mchuchuma, tunaiendea Mchuchuma tutakapokuwa tunakamilisha kumpata huyo mbia ambaye atashiriki katika kuchimba madini haya basi aikute na barabara iko tayari lakini barabara hii ni barabara ya kiuchumi itasaidia sana kuhakikisha kwamba Mkoa wa Njombe unazidi kuleta uchumi wa kutosha ndani ya nchi. Huu ni mkoa unaozalisha chakula kwa wingi na itasaidia wananchi kufanya kazi zao vizuri lakini ndiyo maendeleo yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kwenye suala la barabara ambalo napenda kuishauri Serikali ni kwamba tunaposema tunataka barabara za kuunganisha mikoa kwanza tujiulize tunaunganisha huo mkoa na mkoa ili tupitishe kitu gani? Wakati mwingine tunaunganisha barabara mkoa na mkoa kwa wiki linapita gari moja tu lakini tumeacha barabara inayounga wilaya na wilaya na inapitisha mazao ya kutosha, inachangia uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mtizamo huo tuuangalie upya kwamba tunajenga barabara ambazo zitapitisha mazao, tuangalie zinapitisha nini. Tusijenge tu barabara sababu tu watu wapite, waseme tu kwamba tumeunganisha mkoa na mkoa, mmeunganisha so what, ili kifanyike nini? Itakuwa siyo msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuishauri Serikali ni suala la huduma za matibabu ya UKIMWI. Leo hii asilimia kubwa sana ya fedha au ya dawa wanazotumia waathirika wa UKIMWI ni za msaada. Tutambue moja huu msaada iko siku utakuwa na ukomo, ni lazima kwenye mipango yetu tuhakikishe kwamba tunajiwekea utaratibu wa namna gani tutajimudu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pekee kabisa kwenye suala la UKIMWI liko suala la watoto waliojikuta wamezaliwa na maambukizi ya UKIMWI, watoto hawa wana hali mbaya sana ya lishe. Kama Serikali kwenye mipango yetu ambayo tunaenda kuipanga sasa kwa ajili ya bajeti ijayo tulione hilo na tuhakikishe kwamba tunatenda kiwango kwa ajili ya kusaidia watoto ambao wameathirika na UKIMWI kwa sababu wamepata UKIMWI kutoka kwa wazazi wao. Watoto hawa wanapokuwa shuleni lishe ni duni sana na wanashindwa kusoma vizuri na magonjwa nyemelezi yanawasumbua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutokuwa na bajeti ya Serikali kwenye jambo la kuhudumia watoto waliothirika na UKIMWI watoto hao wengi sana tunawapoteza. Leo hii wagonjwa pekee waliobaki wanaumwa zaidi kutokana na tatizo la UKIMWI ni watoto ambao wamejikuta wana maambukizi kutokana na kuzaliwa na wazazi ambao walikuwa na maambukizi.

Kwa hiyo, ni ushauri wangu kwa Serikali itakapokuwa inapanga bajeti ihakikishe kwamba inaangalia kwa jicho la pekee kwamba tuwe na fedha ya kuweza kusaidia watoto hawa ili kusudi waweze kupata huduma bora ya chakula ili afya zao ziweze kuimarika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nashukuru sana kwa fursa. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu katika bajeti yetu ambayo tunaendelea kuijadili hapa Bungeni. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa mapaji yake kutuwezesha wote kuwa salama na tunaendelea na kazi yetu vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na watendaji wake wote, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu John Pombe Magufuli kwa jinsi alivyoweza kuangalia kipindi cha Hadubini cha TBC na kuwachukua wale wajasiriamali wawili, Ndugu Ngailo na Ndugu Mwafute kutoka katika Jimbo langu ambao wanafua umeme na wanasaidia wananchi wengine. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa lile alilolifanya na ninampongeza sana kwa hilo, lakini niseme tu kwamba bado wapo wengine, yupo Bwana Mhando yupo Kijiji cha Uliwa, lakini yuko Bwana Mwanyika yuko Uwemba pale anaunda mashine za maji basi kama Mheshimiwa Rais alivyosema, Mawaziri wanaohusika wajaribu kuangalia wataalam hawa ili waweze kusaidia maendeleo. Huyu anayeunda mashine za maji anaunda mashine za maji ambazo zinaendeshwa bila kutumia nguvu ya umeme, wala nguvu ya jua, wala nguvu ya mafuta. Zinatumia maji kwa maji, zinaitwa Hydraulic ram au kwa kifupi Hydram. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia sana kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha bajeti, lakini moja ya jambo ambalo ninaliona katika Wizara ya Fedha na bajeti nzima kwa ujumla ni kama vile suala la kodi imeachiwa Wizara ya Fedha na TRA, Wizara zingine zote ziko likizo kabisa hazina habari ya kodi wakati kumbe tungeweza kuhakikisha kwamba na Wizara zote zinasaidia kwa nguvu zote upatikanaji wa kodi. (Makofi)

Mimi ningelikwenda kwenye kodi moja tu ya Pay As You Earn, hii ni kodi ambayo wanatozwa wafanyakazi, lakini ziko Wizara ambazo zingeweza kusimamia ajira kwenye Wizara zao kupitia sekta binafsi, taasisi za sekta binafsi zikapata kuajiri watu wengi ili kusudi waweze kulipa Pay As You Earn. Kwa mfano, nikichukua Wizara ya Elimu, kwanza na-declare mimi ni mdau wa elimu, nikichukua Wizara ya Elimu kupitia NACTE. NACTE ndiyo inayosimamia vyuo vya kati. Viko vyuo vinakufa na chuo kinapokufa maana yake kinakosa wanafunzi na wafanyakazi wanakosa ajira, lakini watu wa elimu wao hawahangaiki, wacha tu kife wala siyo jukumu lao, lakini wajue kabisa kwamba pale kunakosekana ajira na Serikali inakosa kodi. Mwalimu mmoja mwenye mshahara wa shilingi 600,000 akikosa ajira katika chuo maana yake anashindwa kulipa Pay As You Earn ya shilingi 800,000 badala yake anakwenda kupewa kitambulisho cha machinga analipa shilingi 20,000.

Kwa hiyo, mimi nafikiri Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla sasa itoe jukumu rasmi kabisa kwa Wizara zote na kuwe na database kila Wizara ihakikishe kwamba inakuza ajira ya sekta binafsi kwenye Wizara yake na ipewe na malengo kwamba tunataka katika Wizara yako bwana uhakikishe kwamba unasukuma ajira inayoweza kuleta Pay As You Earn kiwango hiki. Wakiwa na malengo hayo watahakikisha kwamba wanasimamia taasisi zao zisiyumbe na nafasoi hiyo wanayo. Kwa mfano, NACTE tumeiondolea jukumu la kugawa wanafunzi kwenye vyuo, tumeomba wanafunzi waombe kwenye vyuo matokeo yake ni kwamba wanafunzi wanaoomba kwenye vyuo kwa mfano, Chuo kama cha Mpwapwa cha Mifugo wanaomba wanafunzi 800, wanaochukuliwa na chuo ni wanafunzi 400, ada inayolipwa na mwanafunzi yule kwneye Chuo cha Mpwapwa ni kubwa kuliko chuo cha private kwamba NACTE wangepewa hiyo nafasi maana yake wale wanafunzi wengine waliobaki wangewagawanya kwenye vyuo vya binafsi na wangeweza kulipa. Hilo lilikuwa ni suala la kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la ufungaji wa biashara, Mheshimiwa Waziri umezungumza vizuri sana, lakini ziko biashara huwezi kufunga. Kwa mfano, taasisi kama ya elimu hufungi, Maafisa wa TRA wamekuwa wakifunga account. Fikiria shule ya bweni, watoto wako shuleni wanahitaji kula, wanaweza wakaumwa, wanahitaji kupelekwa hospitali na nini, TRA wamefunga account za shule mpaka walipwe fedha yao, jambo hili linaumiza sana wamiliki wa mashule na linawafanya wamiliki wa shule wanashindwa kuhudumia watoto kwa sababu TRA wamefunga account. Mimi naomba utakapokuwa unajumuisha utuambie vitendo hivi vya kufunga account za taasisi kwa sababu taasisi kama shule huwezi kufunga, unafunga account za shule. Suala kama hili tunaliwekaje, naomba uliwekee ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia bajeti haijasema vizuri sana juu ya wakulima, lakini tunasema kwamba wakulima ndiyo wanaotusaidia katika nchi kuhakikisha kwamba mfumuko wa bei upo hapo ulipo ni kwa sababu wakulima wetu wamelima chakula cha kutosha, chakula ndani ya nchi kipo cha kutosha. Niombe sana wakulima hawa wasaidiwe. Pembejeo ziko ghali sana, wakulima hawa hawana mbegu bora, wakulima hawa hawana nyenzo za kilimo lakini wakulima hawa hawana wataalam wa kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe la kwanza kabisa ambalo serikali mnaweza mkafanya jitahidini sana kuhakikisha kwamba wakulima udongo unapimwa ili kusudi ajue kabisa anapotia mbolea kwenye shamba lake anatia mbolea anatibu nini kwenye ule udongo. Sasa hivi imekuwa ni mazoea tu wanatumia mbolea udongo haujapimwa, lakini tupate Maafisa Ugani na Maafisa Ugani hawa wapate vyombo vya usafiri ili kusudi waweze kuwafikia wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nadhani na sisi sasa tuombe wakulima tukutane na Mheshimiwa Rais tupeleke malalamiko yetu kwasabbau imeonekana kwamba sasa suluhisho la matatizo ni mpaka wadau wanaohusika na sekta hiyo wakutane na Mheshimiwa Rais. Sisi wananchi wa Jimbo la Njombe ni wakulima, tunalima sana viazi mviringo, tumelalamika sana juu ya lumbesa sana, lakini hakuna hata mmoja anayeshituka juu ya hiyo lumbesa. Lumbesa ina madhara. Madhara ya lumbesa kwanza kabisa inamnyonya mkulima, lumbesa inamuumiza yule mpakiaji wa ule mzigo. (Makofi)

Mimi ningedhani kwamba Wizara ya Afya ingetoa sasa vipimo kwamba binadamu anatakiwa kupakia au kubeba mzigo wenye uzito gani. Wale vijana wanaopakia ile mizigo wanabeba magunia yenye kilo 150 ni maumivu makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni kwamba mapambano haya ya lumbesa hivi leo neongea hapa kama watu wa vipimo wananisikia wataanza operation kesho Njombe na kuwaambia wananchi kwamba ninyi wananchi wa Njombe Mbunge wenu amelalamika juu ya lumbesa, sasa tunazuia lumbesa. Tunawaomba lumbesa ikazuiwe sokoni kwenye masoko makubwa kama ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na masoko mengine ndiko huko Lumbesa ianze kuzuiwa, lakini wasizuie wafanyabiashara njiani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiacha suala la kilimo, suala la miundombinu. Njombe tumelalamika sana, Jimbo la Njombe tumelalamika sana juu ya barabara ya Itoni - Manda. Barabara hii ndiyo barabara kuu ya kilimo. Kama kweli tunathamini wakulima, tunathamini shughuli za kusaidia nchi kupata chakula, hebu tuwezeshe hii barabara ya Itoni - Manda iweze kuwa bora, iweze kuwa ya lami. Fedha mnayotumia kama Serikali kukarabati ile barabara mara kwa mara ni nyingi ambayo mngeweza kutia lami kilometa moja moja leo hii ile barabara ingeshatiwa lami yote. Niombe sana barabara ya Itoni - Manda iweze kuangaliwa. (Makofi)

Jambo lingine ambalo sisi kama Njombe, kama Mkoa sasa ni suala la Mchuchuma na Liganga. Hili jambo limesemwa sana lakini nataka niwaambie hivi Serikali, hivi kuna ulazima gani wa kuhakikisha kwamba tunachimba chuma na tunachimba makaa ya mawe? Mimi ushauri wangu tuchimbe makaa ya mawe tuachane na chuma kwasababu makaa ya mawe yaliyopo pale tukichimba tani 300,000 kwa mwaka tutachimba miaka 150 wakati kile chuma tutachimba miaka 50 kitakuwa kimekwisha na makaa ya mawe ili uweze kuyachimba nyenzo ni chache, unahitaji bulldozer, unahitaji excavator, vitu viwili tu na malori ya kupakia makaa kupeleka sokoni. Hebu mtusaidie watu wa Njombe basi haya makaa yaweze kuchimbwa vinginevyo mkumbuke kama kuna kitu mkaitia Serikali kinaitwa rainfall alliance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rainfall alliance ni mkataba ambao Serikali iliingia leo hii chai inayolimwa na Magereza haiwezi kuuzwa kiwanda chochote kwa sababu wanasema ile ni forced labour, wafungwa hawaruhusiwi kuchuma chai. Sisi tukiwa shule za msingi tulichuma chai ya shule, leo hii haturuhusiwi kuchuma chai ya shule na kupeleka kiwandani. Kiwanda kinachonunua hiyo chai, chai yake haitanunuliwa kokote kule.

Sasa iko hoja inakuja huko duniani wanataka kupiga marufuku matumizi ya makaa ya mawe, sasa tutafika mahali haya makaa ya mawe ya Mchuchuma yatachacha na kwa sabbau tu tumeufungamanisha na mradi wa chuma. Hebu tuitenganishe hii miradi na tuhakikishe kwamba tunaanza kuchimba huu mkaa mara moja, kwa sababu hebu angalia kama ule mradi wa makaa ya mawe wa Ruvuma ule wa Ngaka, makaa yake tunapata shilingi ngapi na tukiongeza na huo wa Mchuchuma tungepata shilingi ngapi kama Serikali? Nafikiri tunajizuia wenyewe na tunaona kwamba maendeleo yetu yanakwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, sisi kama wananchi wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini tunaomba sana Serikali itusaidie na juzi nimeona Rais wa Congo alivyokuja na Rais wetu wanazungumzia juu ya biashara ya Congo na Tanzania na sisi tunaomba utusaidie ili kusudi tuweze kufanya hiyo biashara ya Congo na Tanzania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga, ahsante sana.

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwa Kamati ambazo zimewasilishwa mbele yetu leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la elimu. Kwanza kabisa niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wenzangu na tuipongeze Serikali yetu kwamba mfumo wetu wa elimu ni mzuri sana, mfumo wa elimu ni mzuri sana. Tatizo kubwa tulilonalo ni jinsi ya kuusimamia, hapo ndipo shida inapoanzia kwamba uwezo wetu wa kuusimamia mfumo mzuri huu uko chini mno, hatuwezi kabisa kuusimamia huu mfumo. Kwa hiyo, sasa kinachokuja kutokea baadaye ndio maana tunapata matokeo mabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano watu wanalalamika kusema watoto ujasiriamali, watu wanatoka wanamaliza mpaka vyuo vikuu hawawezi kujitegemea, sio kweli. Wasioweza kujitegemea baada ya kumaliza elimu hizi katika mfumo tulionao ni kwamba wao wenyewe tu hawako tayari kujituma, kwa sababu wanalazimisha kufanya vitu ambavyo wamesomea vilevile tu kama yeye amesoma degree ya sheria analazimisha akawe mwanasheria, lakini tunachosema kwenye elimu maana yake umepanua maarifa, licha ya kufanya hiyo taaluma maalum uliyosomea, lakini maarifa uliyapata, njia nzima uliyopita yanakuwezesha kuishi maisha mengine. Kwa hiyo, kila msomi anapaswa kuongeza akili ili aweze kutumia maarifa aliyopata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mfumo huu wa elimu ambao sasa tumeanza tunaita elimu msingi lipo jambo ambalo naiomba sana Serikali iangalie na ijaribu kutoa taarifa za mara kwa mara na kuna wakati nilishauri hapa kwamba kingekuwepo chombo fulani kinachoweza kuzungumza mara kwa mara juu ya hii elimu msingi; kwa sababu katika elimu msingi ifikapo mwaka 2021 itakuwa kwamba kidato cha kwanza kutakuwa na mikondo miwili, maana yake kutakuwa na wale walioishia darasa la saba na kutakuwa na wale walioishia darasa la sita na hawa wote wanaenda kusomea shule hiyo hiyo ya sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiwauliza wataalam wa elimu wanasema kwa sababu tumefikia asilimia 75 ya ku-recruit watoto wote shuleni. Definetly watakapokuja hao wengine na wenyewe wataingia kwenye mfumo huo, lakini miundombinu tuliyonayo kwenye shule zetu za sekondari bado ni kidogo mno, hatuna madarasa ya kutosha, maabara zile hazitakaa zitoshe kama ni ma-hall au mabwalo yatakuwa hayatoshi. Lakini vilevile shule nyingi mpaka leo bado zinajengwa mpaka leo bado zinajengwa; shule nyingi hazina madarasa, misalani ya kutosha na miundombinu chungu mzima ambayo inatakiwa watoto hawa iwatosheleze. Sasa tunaenda na huu mfumo wa elimu msingi ambao watoto wote sasa kufikia mwaka 2021 wote watakuwa wanaendelea na sekondari bila kuwabakiza au bila kuchagua pale katikati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana serikali ikaona ni namna gani itajipanga vizuri. Niipongeze imejaribu kuwaelimisha walimu, tumeona; pamoja na changamoto zilizokuwepo za walimu kufanya migomo hawapati posho za kutosha na nini kwenye yale mafunzo ya kuwapa hii elimu msingi, lakini angalau mmeliona hilo na katika sera mpya ya elimu mnajaribu kulifanyia kazi. Lakini kazi iliyobaki sasa ni kufanya maandalizi ya kutosha kuandaa, miundombinu ya kutosha na kuelimisha wananchi kwasababu watoto wale na wazazi hawaelewi mpaka sasa kama wataishia darasa la sita; ni vizuri sasa wakaelimishwa wakajiweka tayari kwamba tunaishia darasa la sita halafu tunaendelea na kidato cha kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kwamba Wizara ya elimu iache mikanganyiko; wapo maafisa kwenye Wizara ya Elimu wakiulizwa na wenyewe hawajui. Mahali kama Wizara ya Elimu na TAMISEMI ndipo tunapotegemea tupate majibu sahihi, wananchi wanapouliza maswali kama haya ya elimu msingi ni lazima watumishi na watendaji katika Wizara ya Elimu na TAMISEMI wawe na majibu sahihi. Kwa hiyo, nafikiri pamoja na hii sera ya elimu msingi ni vizuri sasa Wizara ya Elimu ikatengeneza hata vipeperushi tu kutoa hii elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuwa ipo Idara ya Ukaguzi ambayo ni idara ya udhibiti wa elimu; idara hii hatujaitendea haki; kwanza haina vitendea kazi na pili ina wakaguzi wachache sana. Sasa katika kuendesha elimu ndipo tunaposema mfumo wetu ndio wenye matatizo, kwenye elimu kuna mtaala, udhibiti ubora halafu kuna Baraza la Mitihani kwa ajili ya kutoa mitihani. Hawa wanaodhibiti ubora wao ndio wanaosimamia kuona mitaala inatekelezwa vilivyo? Halafu Baraza la Mitihani kazi yake ni kuleta mtihani na kufanyisha mitihani. Sasa unakuta kwamba hii Idara ya Ukaguzi haifanyi chochote na matokeo yake ni kwamba hawa wanaosimamia mitaala kwa maana ya walimu, shule na wanafunzi wenyewe wanaosoma halafu wanakuja baraza wanatoa mtihani.
Sasa naomba Serikali iangalie itafanyaje kuwezesha hii Idara ya Udhibiti Ubora kweli iwe Idara ya Udhibiti Ubora, kinyume chake idara hii kama isipopewa vitendea kazi, wasipokuwepo wakaguzi wa kutosha haina uwezo wa kusimamia elimu yetu. Kwa hiyo, mapungufu mengi tunayoyaona yapo kwenye hii Idara ya Udhibiti Ubora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiacha suala la elimu, nije kwenye suala la afya. Suala la afya yapo matatizo sio makubwa sana lakini ningependa niyasemee kidogo kwamba ipo shida ya tiba kwa watoto, huduma ya bure kwa watoto, wazee na akinamama wajawazito. Huduma hizi zinapotolewa zinaingiza gharama na wanaoingia gharama ni wale wanaosimamia ile hospitali kama ni Halmashauri ndio inaingia gharama. Sasa utaratibu wa Serikali kurejesha zile gharama ambazo Halmasahauri zimeingia upo chini sana. Kwa hiyo, niombe sana Serikali ione ilete zile fedha ambazo Halmashauri zimeingia gharama kutoa huduma kwa watoto, wazee na wajawazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo ningependa kuishauri Serikali itusaidie linaweza likawa ni la kwenye Halmashauri lakini tamko la Serikali lingeweza kutusaidia; matumizi ya magari ya wagonjwa. Mara nyingi sana tumeona magari ya wagonjwa ndio yanatumika kusafirishia wafu, sasa ni kinyume kabisa cha utaratibu yaani haiwezekani Halmashauri ina ambulance moja halafu ambulance hiyo hiyo bahati mbaya mtumishi amefariki inaondoka inaenda kilometa 800 kusafirisha mwili wa mtumishi aliyefariki, halafu Halamsahuri inabaki bila gari la mgonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba sana tamko la Serikali litolewe kwamba magari ya wagonjwayatumike kubebea wagonjwa, iwe ni bahati mbaya tu huyo ndugu yetu tunayemsafirisha kama mgonjwa amefariki ndio tunaweza kusema gari hiyo itumike kumrudisha alipotoka. Lakini kutumia gari la wagonjwa kwa lengo la kumpeleka marehemu kumsitiri hii sio sawa na wala sio sahihi kwa sababu inaacha pengo halafu Halmashauri inabaki haina gari la wagonjwa. Ningeomba sana Serikali ione hili na iweze kulikemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naunga mkono hoja za Kamati kama zilivyowasilishwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri ya kutuongoza Watanzania. Pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na watendaji wote wa Wizara yake kwa jinsi wanavyowajibika kuwahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika hoja tatu.
(i) Wakazi waliopo pembezoni mwa Uwanja wa Ndege Njombe.
(ii) Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Njombe.
(iii) Ujenzi wa barabara ya Itoni - Manda kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi waishio pembezoni mwa Uwanja wa Ndege Njombe Mjini hawatendewi haki na hawajui hatma yao. Naiomba Serikali itoe ufafanuzi juu ya wananchi hawa kwani hawafanyi maendelezo, hawapewi hati na wala hawakopesheki. Hii kwa kweli ni kuwanyima maendeleo, ni vizuri sana Serikali ikatoa ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Njombe katika Ilani ya CCM umetamkwa kwamba utawekwa lami. Niombe Serikali sasa itekeleze ahadi hii. Njombe sasa inakua kisiwani kwa kukosa huduma ya usafiri wa ndege kwa kukosa uwanja. Naiomba Serikali ituone na sisi Wananjombe tunahitaji uwanja ili tuendane na kasi na mafanikio ya nchi yetu kwa kupata usafiri wa ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Itoni - Manda nayo imo kwenye Ilani ya CCM. Ukiacha miradi ya kielelezo iliyopo Ludewa, maeneo ambayo barabara hii inapita ndiyo maeneo muhimu sana ya uzalishaji wa chakula, mbao, nguzo na chai. Wakulima na wafanyabiashara wametaabika kwa miaka mingi sana kwa kusafirisha mazao katika barabara hii. Serikali imeanza kazi ya kuweka zege barabara hii eneo la Mkiu hadi Mawengi kilometa 50 ndani ya Jimbo la Ludewa. Niishauri Serikali, kazi hii ianzie Itoni kuelekea Mkiu kwani itasaidia kuondoa ugumu wa usafirishaji wa mazao ya wananchi katika Kata za Uwembe, Luponde, Matola ndani ya Jimbo la Njombe Mjini na Kata ya Madope, Jimbo la Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi anavyotuongoza katika nchi yetu. Pia nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kuwezesha zahanati na vituo vya afya vya Jimbo la Njombe kupata dawa. Jimbo la Njombe lina changamoto nyingi za kiafya ikiwemo miundombinu, vifaa tiba, dawa na watumishi. Watumishi na wahudumu wa afya ni wachache sana. Katika Hospitali ya Kibeda Nesi moja anahudumia wagonjwa na kufanya usafi, ni kazi kubwa sana inayosababisha kushusha tija na kuleta manung’uniko kwa watumishi. Niiombe Serikali ilione suala hilo. Pia katika zahanati vijijini mhudumu akienda likizo huduma inasimama na wananchi wanakosa huduma.

Nitoe rai kwa Serikali iisaidie Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa kuiongezea watumishi wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Afya, lipo tatizo la tezi dume ambalo sasa linazidi kusababisha vifo vingi nchini. Niiombe Serikali iongeze nguvu katika kutoa elimu za utambuzi wa tatizo hili katika hatua za awali na tiba. Vilevile Serikali itoe elimu kwa waganga wengi ili waweze kufanya upasuaji mapema na kuepusha vifo visivyo vya lazima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Kwa dhati nampongeza sana Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako na msaidizi wake Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa Taifa letu. Naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoiendea Tanzania ya viwanda ambayo itaongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania, ajira hizi zitakuwa za vijana ikiwa tu wana ujuzi unaohitajika katika viwanda hivyo. Uwezo wa nchi yetu kwa maana ya Serikali kuanzisha vyuo vya ufundi hadi tukidhi mahitaji ya kila jimbo ama Wilaya kuwa na Chuo cha VETA kwa sasa ni kama miujiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma ya kuwa na vyuo vya kutosheleza kwa ajili ya vijana wetu wote naomba nitoe ushauri kwamba kila Halmashauri katika shule zake za sekondari ijenge karakana ya fani moja ya ufundi. Hii itatuwezesha kufanikiwa kwa haraka na kuwezesha vijana wote watakapokuwa wanahitimu kidato cha nne watakuwa wana ujuzi. Kwa mfano, Azania sekondari (umeme), Kisutu sekondari (upishi/hoteli), Malangali sekondari (ujenzi) na Mbeya Day (useremala). Kwa mfano, huu tutawezesha vijana wote kuwa na ujuzi wa kuwawezesha kuajiriwa na kujiajiri na kuwezesha kusukuma maendeleo kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutuletea Mpango huu wa maandalizi ya maendeleo wa mwaka 2018/2019.

Pia nitakuwa ni mchache wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ya kuiendesha na kuisimamia nchi yetu. Sisi Wana- Njombe kwa maana ya Jimbo la Njombe tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwamba tumepata mafanikio makubwa katika kipindi chake, tunajengewa kituo cha kisasa kabisa cha afya katika Kijiji cha Ihalula chenye thamani ya shilingi milioni 500, tunajengewa soko la kisasa katika Mji wa Njombe lenye zaidi ya shilingi bilioni nne lakini pia tunajengewa stendi ya kisasa kabisa katika Mji wetu wa Njombe. (Makofi)

Kwa hiyo, hayo ni mafanikio mazuri na nampongeza sana Mheshimiwa Rais na tunamshukuru sana kwa kutupatia hizo fedha za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na kuchangia Mpango wa Maendeleo ambao upo mbele yetu, sisi Njombe tunaitwa Njombe Mjini, lakini ni wakulima, kwanza kabisa nianze na suala la wakulima. Watu wengi wameongelea suala la mahindi, ni kweli kabisa suala la mahindi kiuchumi, mfumuko wa bei katika nchi yetu unashikiliwa na mahindi. Kama Serikali inaliona hilo na inataka kweli wananchi hawa wanaolima mahindi waweze kunufaika na kilimo, lakini vilevile waisaidie Serikali kuweza kushikilia mfumuko wa bei basi ihakikishe kwamba Serikali inawekeza vizuri kwa wakulima kwa maana ya kuwapa pembejeo, wataalam wa ugani na mbegu zilizo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Njombe kuna Kituo cha Usimamizi wa Mbegu Bora, kituo kile kina wataalam wachache, kina gari moja linatumika Kanda nzima kwa ajili ya udhibiti wa mbegu. Sasa hawa wakulima wanaolima mahindi na kile kituo ndio kinadhibiti mbegu za aina zote za mpunga, mahindi na kahawa, kwa kweli inaonekana kwamba tunafanya tu kwa sababu sheria imesema, lakini nia ya dhati ya kusaidia wakulima inaonekana haipo, wakulima wanauziwa mbegu fake, wanaletewa mbolea zisizofaa na kadhalika. Niombe sana tuimarishe huduma kwa wakulima wakati tunatambua kabisa kwamba mahindi ndiyo yanayoshikilia shilingi ya Tanzania iweze kuwa imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwa suala la wakulima, lipo zao la viazi Njombe ambapo vinadhurika sana. Viazi tunalima Mkoa wa Njombe lakini vilevile Mkoa wa Mbeya, Tanga na Kilimanjaro. Viazi vya Tanzania vinaathiriwa sana na viazi kutoka nje hasa katika ujazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu niombe sasa Serikali kupitia Idara ya Vipimo tutengeneze mifuko maalum kwa ajili ya zao la viazi. Mazao mengine kama kahawa na korosho yana magunia na viazi tuwekwe mifuko maalum ya viazi ambapo unajua kabisa piga ua mfuko huu hauzidi kilo 90 na huo ndio mfuko wa viazi, yeyote atayekutwa sokoni na mfuko tofauti na ile maana yake huyo awe ni mhalifu, itakuwa imeasaidia sana wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo zao la parachichi katika Jimbo langu la Njombe Mjini, parachichi za Njombe ni za export. Mwaka huu tume-export tani 700 lakini kwa bahati mbaya sana tuna-export kwenda nchi jirani na wale wa nchi jirani ndio wanapeleka Ulaya. Niiombe sasa Serikali itusaidie, wakulima hawa wa parachichi kwanza kabisa wapatiwe mbegu bora, lakini pia tupate wataalam kutoka Serikalini kwa sababu parachichi hizi ni za export maana yake tayari zitatusaidia kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba tatizo kubwa la parachichi ni kwamba hatuna pack house. Katika Halmashauri yetu tuna pack house moja tu na hawa wanaokuja kutoka nchi za nje kuchukua parachichi wanakuja na magari yao maalum yenye ubaridi. Kwa hiyo, Serikali ione kwamba kuna nafasi ya kuwekeza kwenye miundombinu ya ubaridi ili kusudi wananchi wanaolima parachichi waweze kupata mahali maalum pa kutunzia hizi parachichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kutokana na mfumuko wa kilimo hiki, wananchi wengi wameitikia sana na parachichi zinaendelea kuongezeka. Itusaidie kwamba sasa parachichi ziwe exported kutoka Njombe kwenda masoko ya nje Ulaya na kadhalika lakini tukipeleka Kenya maana yake wanatulipa Tanzanian shillings halafu wao ndiyo wanapata dola na sisi hapa tuna shida kubwa sana ya dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambao napenda kuliongelea ni umeme. Upo umeme wa REA Awamu ya Tatu lakini vilevile lipo suala la TANESCO. TANESCO ndiyo wanaweka umeme katika maeneo ya mijini pale Njombe tuna vijiji vilivyo karibu na mji kilometa tano kama Itulike havina umeme na havina umeme kwa sababu havimo kwenye REA, lakini vilevile vinatakiwa viwe TANESCO na uwezo wa TANESCO wa kupeleka umeme uko chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwenye bajeti itakayoandaliwa tuone TANESCO wanavyopewa miradi ya mjini angalau wapewe miradi unayokwenda mpaka kilometa tano, wanapewa mita 700, 600 au 300. Sasa utaona vijiji vilivyo karibu na mji havipati umeme, kwa hiyo, niombe sana hilo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufanikiwa kiuchumi tunahitaji barabara nzuri. Katika Jimbo langu la Njombe Mjini iko barabara inayoenda Ludewa inaitwa barabara ya Itoni – Manda. Awamu zote za uongozi zimekuwa zikiisemea barabara hii iwekwe lami, lakini mpaka leo katika Jimbo langu kazi hii ya kuweka lami haijaanza. Niombe sana katika Mpango ujao basi litekelezwe hili kwa sababu barabara hii inasaidia wananchi kusafirisha mazao ya kilimo lakini inasaidia vilevile huduma mbalimbali kwa Wilaya ya Ludewa na kuendelea mpaka Ziwa Nyasa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu, tunahamasisha viwanda lakini tusipowapa elimu watu wetu hapa tunarudisha umanamba. Vijana hawa wataingia kwenye viwanda hivi watafanya kazi ya kupanga vitu kwenye maboksi na hatutajivunia kwamba vijana wetu wamepata ajira, itakuwa wamepata ajira lakini watakuwa wamepata ajira ya kijungujiko na yenye manung’uniko. Watakuwa watu wa kuhangaika tu kukunja mashati kuweka kwenye mifuko, tuwape elimu vizuri ya ufundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu ya ufundi ambayo tunapaswa kuwapa vijana hawa iko elimu inaitwa industrial maintenance. Katika industrial maintenance vijana watajifunza mambo yanayohusiana na marekebisho ya mitambo mbalimbali ndani ya viwanda. Leo hii VETA mtaala wanaotumia kufundisha, wanafundisha watu kutengeneza vigae vya moto wa mkaa, ndiyo ataenda kufanya kazi kiwandani huyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, mpaji wa yote kwa kutujalia Wabunge wote kuwemo humu ndani na tunaendelea na kazi yetu vizuri. Pia nawapongeza sana watendaji wote wa Serikali, akiwemo Rais wetu na Mawaziri na wote wanaowasaidia kutimiza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la ujenzi kwanza kabisa niseme kwamba kwa kweli nasikitishwa sana na jinsi bajeti ilivyowekwa katika Mkoa wa Njombe na hasa katika barabara ya Itoni – Manda. Barabara hii ni miaka mingi sana imekuwa ikiahidiwa itawekewa lami na kipande cha kilometa 50 kimeshaanza kuwekewa lami ndani ya Wilaya ya Ludewa lakini hakisongi mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha inayotolewa ni ndogo sana kiasi ambacho kazi haiendi na maeneo yale ni ya uzalishaji mkubwa na ndiyo ghala la chakula kwa ajili ya wananchi wa nchi hii. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, hebu iwe serious, tunaposema tunataka kutengeneza barabara ya lami kwa ajili ya kuleta maendeleo katika maeneo yetu, basi iwekwe fedha ya kutosha na kazi iweze kwenda vizuri.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuliongelea ni barabara za mijini ambazo TANROADS huwa inajenga. Njombe Mjini ni Makao Makuu ya Mkoa, tumetengenezewa barabara ya lami mita 150. Sasa ukiangalia mobilisation ya vifaa vya lami kwenda wilayani au mkoani kama Njombe halafu vinakuja kufanya kazi ya mita 150 ni upotevu wa fedha. Siyo kwamba tunakataa tusitengenezewe, lakini hebu wabadilishe utaratibu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Makao Makuu ya Mkoa barabara haziridhishi kabisa lakini zinakuja kutengenezwa mita 150, mkandarasi anakuja pale kwa ajili ya barabara ya mita 150, anasafirisha grader, roller, escalator, malori na mashine za kumimina lami, anakuja kufanya kazi ya mita 150, hii inasababisha barabara iwe ya ghali sana. Kwa hiyo, niombe sana Njombe tutengenezewe barabara za mjini kwa sababu ni Makao Makuu ya Mkoa na hali ya barabara za mjini ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni uwanja wa ndege. Nimeona wanasema kwenye viwanja vya ndege ambavyo vimo na Njombe imo. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa nataka asema mipaka ya uwanja wa ndege iko wapi? Wananchi wale wanaozunguka uwanja wa ndege wa Njombe wanastahili nini? Wahame, waendelee kuwepo, watawalipwa fidia au wapime nyumba zao zile waendelee kuishi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu siku zote wananchi wale wa Njombe wamekuwa hawaelewi, wanaishi kwenye sintofahamu. Wanashindwa kuendeleza maeneo yao, hawapimiwi na uwanja wa ndege hawatoi taarifa yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ule uwanja wa ndege ni pori na unatusababishia vibaka pale mjini.

Niwaombe sana wakija hapa keshokutwa kuhitimisha bajeti yao waseme uwanja wa ndege wameshafyeka majani yote ndani ya uwanja hayapo. Kwanza uwanja wenyewe uko mjini, hawausafishi, wanatusababishia mji uwe mchafu. Vibaka wanatoka pale wanasumbua watu mtaani lakini vilevile wamefanya kama ndiyo dampo kwa ajili ya kutupa uchafu mbalimbali katika uwanja wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri anajitahidi sana kujenga barabara, lakini nimefanya utafiti mdogo, Jeshi la Polisi, Idara ya Trafiki wanabomoa barabara. Wanasimamisha malori mahali ambapo sio mahali maalum pa kusimamisha lori, matokeo yake barabara inamegeka mabega kidogo kidogo, wakiona pameshakuwa na mashimo pamemegeka sana wanahama wanaenda kuanzisha kituo mahali pengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ya Ujenzi wakae na Wizara ya Mambo ya Ndani wakubaliane Police Traffic watasimama wapi na watasimamisha magari wapi kwa sababu hii ni hasara kwa nchi. Kama sehemu za vivuko vya ng’ombe tumeandaa mazingira maalum kwamba ng’ombe wavuke mahali fulani, kwa nini malori yasiandaliwe mahali pa kusimamishwa? Wanaamua tu kwamba leo tusimame hapa, leo tusimame hapa, malori yanasimamishwa yanakwenda kandokando ya barabara yanaharibu barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu ni hayo, lakini naomba sana barabara za Mji wa Njombe ziangaliwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa barabara ya Itoni – Manda yenye urefu wa kilometa 211. Ujenzi wa kiwango cha zege kati ya Lusitu na Mawengi unasuasua sana. Naishauri Serikali kwamba barabara hii ipo ndani ya majimbo mawili au Wilaya mbili kwa maana ya Wilaya ya Njombe na Wilaya ya Ludewa na kazi imeanza ndani ya Wilaya ya Ludewa na kuruka kipande cha kilometa 52 kilichopo Wilaya ya Njombe ambacho ndicho kinaunga kwenye barabara kuu ya Makambako - Songea eneo la Itoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa pesa kidogo inayotenga kwa barabara hii, sasa iajiri mkandarasi mwingine aanzie Itoni ili kuweka imani kwa wananchi wa eneo la Jimbo la Njombe Mjini kwani ahadi ya lami kutoka Itoni ni ya muda mrefu sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kunipa nafasi nichangie katika hotuba iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ama kweli baniani mbaya kiatu chake dawa, Jeshi la Polisi wanalaumiwa lakini wanafanya kazi nzuri sana kwa sababu nasema kama polisi wasingekuwepo hali ingekuwaje? Usipomchokoza polisi hawezi kuhangaika na wewe, ukiona polisi wanashughulika na wewe ujue kwamba kuna kitu umekifanya kwamba umeenda kinyume na utaratibu na kinyume cha sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya, wote tupo salama siku zote za maisha yetu kwa sababu ya Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Njombe bado Serikali haijalitendewa haki vizuri, Jeshi la Polisi hawajatendewa haki vizuri kwa sababu Njombe ni mkoa toka mwaka 2013 lakini mpaka leo hawajajengewa jengo la polisi la mkoa, hakuna Ofisi ya RPC, hakuna nyumba za polisi, polisi wale wa Njombe wanafanya kazi vizuri lakini hawana makazi. Polisi 400 vijana hawana makazi, hakuna nyumba hata moja ya polisi Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo hiki nakiona kwamba hatuwatendei haki askari wetu na wakati mwingine tunaweza tukawalaumu polisi kwamba hawatimizi wajibu wao vizuri, lakini wakati mwingine pengine wanapata na msongo kutokana na mazingira ya kazi wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Kituo cha Polisi Njombe nafikiri Mheshimiwa Waziri alifika alikiona, kile kituo nadhani ni cha mkoloni nimezaliwa nimekikuta. Kile kituo kwanza kipo ndani ya mita 30 za barabara halafu ni kichakavu sana. RPC wa Njombe kila siku anabomoa kaukuta angalau aongeze apate chumba cha kumtosha kufanya kazi. Kwa kweli hadhi ya polisi kwa Njombe bado haijawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Jeshi la Polisi Njombe waangalie kwa namna gani wanaweza wakasaidia kama Wizara na kama Serikali kuona kwamba Jeshi la Polisi linakuwa na jengo lake, linakuwa na ofisi nzuri na wanaweza kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza; kwanza kabisa katika Mkoa wa Njombe Magereza Mkoa haijafika. Maafisa wa Magereza Njombe wakihitaji mahitaji yao ya kiofisa ni lazima waende Iringa. Sasa je tukubaliane hapa kimsingi kwamba Magereza wamegoma kuja Njombe ama wanakuja? Nami kama wananiambia wamegoma nipo tayari kumwambiwa mwenye nchi kwamba magereza wamegoma kuja Njombe. Tunahitaji watu wa magereza waje Njombe ili kusudi shughuli zinazohusiana na Jeshi la Magereza ziweze kufanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari Magereza Njombe wanafanya kazi nzuri sana, tarehe 2, nakumbuka ilikuwa Jumatatu ya Pasaka nilitembelea Magereza Njombe, niliongea na wafungwa, niliangalia makazi yao, lipo tatizo moja tu la msongamano lakini wafungwa wenyewe kwa maneno yao walitamka kwamba wanalelewa vizuri na wanatunzwa vizuri. Nilitembelea vyumba vyao vipo vizuri na wanasema kwamba maisha pale, ukiacha kwamba wao ni wafungwa na mahabusu lakini maisha ni mazuri na wanatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika nikamweleza Mheshimiwa Waziri, lakini nilipata fursa ya kuuliza swali hapa na nikawa na mahabusu mmoja pale alikuwa anaumwa, namshukuru sana alichukua hatua haraka na mahabusu yule ametibiwa. Tatizo kubwa la Magereza Njombe ni uchakavu na msongamano, lakini msongamano huu unatoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa msongamano unasababishwa na kesi zisizokwisha mahakamani na upelelezi ambao haukamiliki. Kwa hiyo, ni kati ya Jeshi la Magereza na polisi kwa maana kwamba polisi hawapelelezi kesi kwa wakati na magereza wanashindwa kuwatunza wale mahabusu vizuri kwa sababu ya nafasi ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalojitokeza ni kwamba Magereza Njombe wana maeneo ya mashamba, maeneo yale hayatumiki, yamekuwa mapori kwa miaka mingi sana. Niombe sana Jeshi la Magereza hebu waone ni kwa namna gani wanaweza wakayatumia yale maeneo, vinginevyo sisi kama wananchi wa Njombe tutayavamia yale maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi katika matumizi ya ardhi ni kwamba sisi tukivamia ardhi ile tukiilima wasije wakatulaumu, lakini ni wajibu wao kuhakikisha kwamba Magereza Njombe wanalima mashamba yale na wanayafanyia kazi ili kusudi tuondokane na mapori hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nililiona pale Magereza Njombe pamoja na uzuri niliouona ndani ya gereza, usafi na mazingira ya ndani ni kwamba yule afisa magereza anakaimu. Mheshimiwa Waziri hebu angalieni kwa nini yule anaonekana msomi na anamudu kazi vizuri, kwa nini aendelee kukaimu siku zote hizo kwa sababu inamsababisha anashidwa kutoa maamuzi kwa sababu ya kukaimu. Niombe sana waliangalie hilo kiutumishi waone namna gani wafanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uhamiaji haramu, nimeenda Gereza la Njombe nimekuta pale kuna watu wa Ethiopia 15 walikamatwa wakapelekwa mahakamani, wamehukumiwa wamemaliza kifungo lakini bado wapo gerezani, sababu wanasema hawajasafirishwa. Gereza lile ni dogo wanasababisha msongamano, halafu kesi imekwisha bado wanaendelea kuwepo gerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu niombe kama utaratibu wetu sisi ni kuwakamata hawa wanaoitwa wahamiaji haramu, basi tuangalie utaratibu mwingine wa kufanya, kwa sababu naamini kama tunaweza tukawakamata, kama tumewakuta kwenye lori tunamwambia dereva wa hilo lori, nyuma geuka, mbele tembea, rudi ulipotoka, kuliko anaenda kukamatwa Njombe anakaa Magereza ya Njombe anahukumiwa, matokeo yake anasabisha msongamano katika Gereza la Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo haya naona yapo sehemu nyingi sana katika nchi yetu kwamba Jeshi la Magereza linapata tabu kutunza hawa wahamiaji haramu. Kama ni watu wanaopita njia tu tuangalie sheria zimekaaje; kama inawezekana kuwasindikiza wakamaliza msafara wao tuwasindikize wavuke waende wanapokwenda kuliko tunaendelea kubabaika nao hapa. Kwanza wanakula sembe yetu ya bure, hawatakiwi kwenda kazini tumewapeleka mahakamani, tunatumia nguvu zetu nyingi kuwatunza bila hata sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliombe sana Jeshi la Uhamiaji waweze kuangalia hili jambo na Serikali iliangalie kwa umakini ili kusudi hawa watu waweze kurudi kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la usalama barabarani, tunashukuru sana Askari wa Usalama Barabarani wanafanya kazi vizuri lakini wapo miongoni mwao hawafanyi kazi vizuri. Askari wa usalama barabarani wamegeuza kile kitengo kwamba ni sehemu ya kipato, wananyanyasa sana vijana wa bodaboda na maaskari wa usalama barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeshatokea mahali pengine unakuta askari wa usalama barabarani amesimamisha gari katikati ya barabara halafu amefungua milango wa gari ili kusudi yule kijana asimame kwa ghafla au aingie porini ili amkamate, kuna sababu gani? Kwa sababu bodaboda zote zinajulikana ni za wapi, haiwezekani bodaboda ikawa inatoka Tabora kuja Dodoma haiwezekani. Kama ni bodaboda ya hapa Dodoma ni ya Dodoma na kama ni ya Njombe ni ya Njombe. Naomba vijana hawa waangaliwe, kama wana makosa basi wakamatwe kwa utaratibu wa ukamataji; wapo askari ambao kwa kweli ukamataji wao hauridhishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana tuwasaidie sana askari, tuwaelimishe vizuri ili kusudi ukamataji wao uweze kuwa ni ukamataji ambao unaweza ukamsaidia hata yule unayemkamata ajue ana kosa gani kuliko unapofungua milango ya gari halafu unataka mwenye bodaboda ajigonge kwenye milango ya gari au aingie porini ili umkamate, kwa hiyo ukamati huo sio ukamataji sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa muda. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vipimo, maduka yote yawe na mizani ya kupimia bidhaa zinazouzwa. Mizani hiyo iwe na uwezo wa kupima zaidi ya kilo 50 ili mteja akihitaji sukari ya kilo 50, cement ya kilo 50, unga wa ngano kilo 50, mbolea ya kilo 50 aweze kupimiwa, maduka mengi yanayouza bidhaa hizo hayapimi na kwa wafanyabiashara wasio waaminifu huwaibia wateja na kuwasababishia hasara wateja hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba za ubavuni kwenye malori ya mchanga Wizara iangalie viwango vya kuandika namba za ubavuni na hasa pale inapokuwa inaandikwa kwa mwaka wa pili, ada hii ni kero na haina uhalisia hivyo inasababisha maudhi na usumbufu kwa wamiliki wa magari hayo, nafahamu fika ni sheria na nia ni kumlinda mlaji, lakini

gharama za kuandika namba hizo inamrudia huyo huyo anayelindwa. Hivyo nashauri Serikali iondoe ada ya kuandika namba ya ujazo kwa mara ya pili ili kuondoa gharama na kero kwa wamiliki. Kama ipo kwenye sheria ya msingi basi iletwe Bungeni na kama ipo ndani ya uwezo wa Wizara basi jambo hili liangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kabisa kudhibiti rumbesa ya viazi mviringo, hii ni aibu kwa wataalam wa Wizara kushindwa kudhibiti jambo la wazi kama hili. Serikali isaidie ujenzi wa parking house (cold room) ambazo zitawasaidia wateja wa matunda aina ya parachichi kuweza kununua matunda hayo na kuyaandaa vizuri kwa ajili ya masoko ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo utakuwa umewawezesha wakulima kuuza zao hili na kuisaidia nchi kupata fedha za kigeni kwani parachichi zinazolimwa Njombe zimepata soko nje ya nchi na hasa Ulaya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Njombe Mjini sasa wamepata zao la parachichi ambalo wananchi wamelipokea vizuri sana kila mwananchi sasa anashughulika na kilimo hiki. Wananchi hawa wa Jimbo la Njombe Mjini wanahitaji msaada kidogo sana wa Serikali, katika upatikanaji na usambazaji wa miche bora. Zao hili limepata soko kubwa sana nje ya nchi na hii itasaidia sana nchi yetu kuongeza pato la fedha za kigeni. Katika mauzo ya zao la parachichi nyenzo muhimu sana ni pack house (cold storage) ambazo mkulima hana uwezo wa kujenga na wanunuzi hawawezi kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie hili na inipe maelezo kwa niaba ya wakulima wa parachichi wa Jimbo la Njombe Mjini ni kwa namna gani inaweza kusaidia hili, Wizara iunde timu ya wataalam kusimamia kuendeleza zao la parachichi na kupima vihatarishi vyake ili tuweze kusaidia zaidi utaratibu wa masoko na mauzo kwa manufaa ya wakulima na nchi kupata fedha za kigeni.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, Ofisi ya TRA Njombe Mjini ni finyu sana kiasi kwamba inasababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi ambao wanafika TRA katika kuhitaji huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, suala la kodi ni suala muhimu sana na wananchi wa Njombe wamelipokea vizuri kwa kitendo cha mwananchi kushinda TRA ili alipe kodi hii imewavunja moyo sana walipa kodi. Ninachohitaji kufahamu ni lini Serikali itajenga jengo lenye nafasi ya kutosheleza mahitaji ya TRA- Njombe kwa kujenga jengo la kutosha Njombe, hiyo itasaidia sana kurahisisha kazi ya kukusanya mapato ya Serikali. Watumishi wa TRA ni wachache sana, ni lini Serikali itaongeza watumishi TRA Njombe?

Mheshimiwa Spika, mbao laini ni zao la kawaida kwa Njombe, wakivuna miti yao wanadaiwa risiti ya EFD. Nahitaji kufahamu kwa nini wakulima hawa wa miti wanapokuwa wanasafirisha mazao yao ambayo ni mbao wanadaiwa EFD receipt? Je, wakulima wa korosho nao wanatakiwa kuwa na EFD receipt au wakulima wa miti wanaonewa? Ni lini sasa Serikali itaweka ufafanuzi wa namna gani wakulima wa miti wanaweza kusafirisha mazao yao ya mbao?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali na Watendaji wote wa Serikali kwa kazi nzuri ya kuwahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Jafo na Naibu Mawaziri wake na Watendaji wote wa Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 10 ya vijana na wanawake; kauli ya Serikali kwamba kuanzia sasa fungu hili la vijana na wanawake halitatozwa riba ni jambo zuri. Ushauri wangu ni vizuri Serikali ijiridhishe suala la kodi ya mapato kwani TRA inatoza mapato Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS), hivyo ni vyema jambo hili likapewa ufafanuzi ni kwa namna gani pesa hizo zitapitia SACCOS bila kutozwa kodi ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ndiyo inayosimamia shule za msingi na sekondari. Hali ya uanzishaji wa vyuo vya ufundi VETA hapa nchini si ya kuridhisha na tunatoa elimu ya nadharia zaidi. Nashauri Serikali kufanya maamuzi ya kuagiza kila halmashauri iongeze mchepuo wa ufundi katika shule moja au mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo lazima kuanzisha fani zaidi ya moja katika kila shule ili jambo hili liwezekane kwa urahisi ni vizuri kuanzisha fani zenye gharama nafuu ili vijana wakimaliza kidato cha nne wawe na ujuzi wa kuwawezesha kuwapatia ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wa shule ya msingi wenye cheti cha daraja la IIIA, hawana fursa ya kujiendeleza na daraja la IIIA siyo sifa ya kujiendeza katika chuo chochote hapa nchini. Nashauri Serikali, TAMISEMI wakae na Wizara ya Elimu ili kozi iliyozuiwa na Wizara ya Elimu iliyokuwa ikisimamiwa na NACTE na kuendeshwa na vyuo vya kati kwa kuwapa maarifa zaidi Walimu hawa pia kuwawezesha kupata madaraja mapya kwenye kada ya Walimu wa daraja IIIA hii pia itatia morali kwa Walimu hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa inayojengewa Hospitali za Rufaa. Hospitali ya Mkoa wa Njombe imewekwa jiwe la msingi na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Waziri katika maelezo yake kabla kuwekewa jiwe la msingi mbele ya Mheshimiwa Rais na mbele ya umati wa wananchi wa Njombe Mjini, aliahidi hospitali yetu itaanza kazi mwezi Julai na maelezo hayo yalirudiwa tena wakati wa kumkaribisha Mheshimiwa Rais kuweka jiwe la msingi. Wananchi wa Njombe tungefurahi sana kuona Hospitali yetu mpya inaanza kutoa huduma kama alivyoahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jambo ambalo linanitia shaka wakati Mheshimiwa Waziri akiwasilisha bajeti yake hajaonesha bayana kama hospitali hii itafunguliwa kama alivyoahidi. Nimepitia Kitabu cha Hotuba sijaona kabisa fungu mahususi kwa vifaa vya hospitali vipya. Naomba wakati wa kuhitimisha hotuba, Mheshimiwa Waziri atoe kauli ya Serikali ndani ya Bunge kututhibitishia wananchi wa Mkoa wa Njombe kuwa hospitali yetu itaanza kutoa huduma kama alivyotuahidi. Vinginevyo namfahamisha mapema Mheshimiwa Waziri kwamba nitazuia shilingi ya mshahara wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Muswada huu wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa na maneno mengi sana lakini kubwa ni kutoa tu ushauri kwa Serikali ione ni kwa namna gani inaweza ikatusaidia na hasa katika mazingira yetu ya Halmashauri na mazingira yetu ya vijijini suala la utengenezaji wa taarifa. Kwa sababu wengi sana tunachangia juu ya taarifa kutoka Serikalini kwenda kwa wananchi na kadhalika, lakini ziko taarifa ambazo kutokana na mazingira yetu ya Halmashauri inabidi zitengenezwe ili wananchi wazipate. Kwa mfano taarifa zinazohusiana na masuala ya kilimo; wananchi wengi wamekuwa wakipata tabu sana kwenye masuala ya kilimo kwa sababu wanakosa taarifa.
Moja ya tatizo wanalopata ni kwamba mabadiliko ya hali ya hewa, ningeshauri sasa Serikali izielekeze Halmashauri zetu kila mazingira ilipo iweze kutengeneza taarifa ambazo zinaweza zikasaidia kuepukana na matatizo ambayo wakulima wanapata. Wakulima wajue kwamba sasa mazingira yalivyo ama hali ya hewa ilivyo mazao haya yanaathirika hivi. Kwa hiyo, imekuwa ikijitokeza mara nyingi wananchi wanakosa taarifa matokeo yake mazao yanaharibika mashambani kwa sababu magonjwa yanayoyakuta yale mazao yanajirudia mara kwa mara na wataalam wetu hawana hata benki ya taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri Serikali ione sasa kwamba katika sheria hii ielekeze Halmashauri ziweze kutengeneza taarifa ambazo zitawafaa wakulima na taarifa hizi zisiwe ni za kuombwa. Japokuwa wanasema unaweza ukaomba kwa siku kadhaa, lakini tuwe na utaratibu wa kwamba ziwekwe taarifa huria ambazo zinatolewa wananchi wanaziona, pia ziwepo taarifa za kuomba, tukisema mkulima aombe taarifa ya kujua hali ya hewa miaka mitatu iliyopita ilikuwaje ili aweze kutabiri miaka mitatu ijayo, itakuwa ni ngumu sana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuwepo na taarifa ambazo zinaweza zikasaidia shughuli za wananchi huko vijijini, tusihangaike tu na zile taarifa za magazetini, sijui za mikutano na kadhalika, zipo taarifa muhimu zinazoweza kusaidia wananchi wetu kupata maendeleo kutokana na mazingira wanayoishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kushauri ni kwamba Serikali ione ni kwa namna gani inaweza ikaongeza katika Muswada huu kwamba taarifa huria itolewe. Kwa mfano, kwenye suala la miradi, kama kuna mradi unafanyika mahali, wananchi wale wapelekewe taarifa ya wazi kwamba Halmashauri yetu imepokea fedha kwa ajili ya daraja na daraja hili litajengwa mahali hapa, fedha ni hii, mkandarasi ni huyu, BOQ ni hii. Siyo lazima mtu afunge safari akaombe, wananchi wangapi wana uelewa wa kuomba, wananchi wangapi wanafikiwa na Diwani kila siku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri taarifa nyingine tukaziweka zikawa ni taarifa huria kwamba Halmashauri hupokea fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, ikatoa zile taarifa wananchi wakajua nini kinaendelea kuliko unaona tu kazi inaendelea, kazi imesimama hujui nini kinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali ione ni jinsi gani itatumia nafasi hii ya Sheria hii ya Taarifa kuzielekeza Halmashauri kila mahali zilipo ziweze kutengeneza mfumo utakaosaidia wananchi kujua maendeleo yao, shughuli zao zinazoendeshwa pale kwenye zile Halmashauri ikiwemo kujua taarifa za hali ya hewa, taarifa za maradhi ili tujue tatizo hili linajitokeza baada ya miaka mingapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweka taarifa za namna hii itatusaidia sana kujua kama tatizo hili linajitokeza kila baada ya miaka mitatu, basi tunajua kwamba mwaka ujao kuna barafu kali itaunguza mazao, ni namna gani tuweze kujihami, namna gani tuweze kuendesha kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe na maneno mengi, ya kwangu ni hayo tu. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja hizi mbili zilizopo mezani kwa siku ya leo. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa ya kuendelea kuwa uhai, lakini pia niwapongeze sana wenyeviti wote wawili Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii lakini pia Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI Dkt. Tiisekwa; nawapongeza sana kwa kazi nzuri waliyofanya. Kwanza wanatusimamia vizuri kwenye Kamati zetu lakini leo wamewasilisha vizuri sana Taarifa za Kamati mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze na jambo moja, nianze na suala la elimu. Kwenye elimu tunahangaika sana juu ya suala la walimu, hali ya walimu ni mbaya sana, na sielewi kabisa kwamba sasa Serikali inajipangaje kwa sababu shule zetu hazina walimu, ni tatizo la Kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia ni mjumbe wa Kamati ya LAAC ukiangalia Taarifa za Mkaguzi wa Mahesabu ya Serikali unaona kabisa kwamba anaonesha mapungufu kwamba katika kila Halmashauri kuna upungufu mkubwa sana wa walimu na tatizo likishakuwa kubwa sana halafu ukawa huwezi kulitatua inafika mahali unaliona hili huliwezi unaamua kuliacha tu liendelee kama lilivyo na unalizoea unaona kama ni hali ya kawaida. Ni hali mbaya sana. Kwa mfano tu kwenye Halmashauri yangu ya Mji Njombe ina upungufu wa walimu mia nne. Niombe sana Serikali iangalie ni kwa namna gani itafanya iajiri walimu wa kutosha ili kusudi shule zetu pamoja na kwamba wananchi wanachangia ujenzi wa shule, Serikali inachangia nguvu za wananchi pia lakini kama hakuna walimu katika shule za msingi kama hakuna walimu wa sayansi itakuwa ni tatizo kubwa sana kwa maana watoto hawa hawatapa elimu iliyokusudiwa (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine tunahitaji vijana wetu wapate ujuzi; hawa vijana hawawezi kupata ujuzi kwa namna yoyote ile kwa sababu leo hii katika nchi yetu hakuna chuo kinachotoa walimu wa ufundi; hatuna chuo hata kimoja kinachotoa walimu wa ufundi. Watu wengi tunapenda vijana wapate elimu ya ufundi lakini ni ukweli usifichika kwamba hakuna chuo hata kimoja. Kuna chuo kidogo sana cha VETA pale Morogoro na hakina uwezo hata kidogo wa kutoa walimu wa ufundi; lakini vilevile mitaala ya ufundi inayofundishwa ni mitaala ya zamani sana. Mimi ni fundi, kwa hiyo ninajua nini kinafundishwa huko. Kwa kweli ufundi ulipofikia leo na ufundi wanaofundishwa vijana ni vitu viwili tofauti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niishauri Serikali ijitahidi sana kuhakikisha kwamba sasa inajenga vyuo na inafundisha walimu wa ufundi wa kutosha ili kusudi tutakapotaka kuwa na mafundi walimu wa kuwafundisha wawepo. Tutakaa tunasema tunahitaji ufundi VETA zianzishwe lakini walimu wako wapi? Walimu hakuna. Nchi hii hakuna vitabu vya ufundi vinavyoandikwa, havipo. Sisi tunataka mafundi lakini nchi hii vilevile hakuna mitaala ya ufundi ya kisasa, yaani hakuna; mitaala iliyopo ni ya kizamani sana. Kwa hiyo niombe sana Serikali iangalie kadri inavyowezekana na hasa hasa Wizara ya Elimu ijikite kuliona hilo; ni jambo gumu zito lakini ni la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake Mama Jenista, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa. Katika Wizara yao wameweka utaratibu wa kutoa ujuzi; ni utaratibu mzuri na vijana wengi wanapelekwa maeneo mbalimbali ili kupata ujuzi. Wengi hatuyajui hayo lakini kwa kweli ukiuona ule mpango umeinua vijana wengi na umewawezesha vijana wengi kupata ujuzi. Ni mpango mzuri unaosaidia sana katika kuhakikisha kwamba sasa Vijana wengi wanapata fursa kupata ujuzi. Niwaombe muendelee na kazi hiyo muimarishe zaidi lakini mpanue, msiende tu kwenye fani zile zile za useremala, ujenzi, ushonaji. Haiwezekani nchi nzima ikawa ya mafundi seremala na washonaji, tuweke na fani nyingine, twende kwenye fani za kilimo, uvuvi na mifugo ili sasa vijana hawa watawanyike sehemu pana zaidi ili wakatumie ujuzi huu na hivyo uweze kuwasaidia kuweza kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la elimu liko jambo moja baya sana. Serikali imetoa mitaala mipya, Serikali ina ruzuku ambazo zinatakiwa ziende shuleni; haipeleki zile ruzuku badala yake inapeleka ku-print vitabu Taasisi ya Elimu iki-print vile vitabu inaviandika kitabu hiki hakiuzwi na vile vitabu vinapelekwa moja kwa moja shuleni na kwa hiyo shule zisizo za Serikali zote hazipati vitabu. Sasa unajiuliza, hivi hawa wanaosoma shule zisizo za Serikali ni watoto wa nani? Hawa si Watanzania? Hakuna fursa hata chembe ya shule isiyo ya umma kupata kitabu kilichoko kwenye mtaala wa kisasa. Kwa hiyo niombe sana hilo Serikali ilione na ilitatue hilo tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tulipitisha hapa Sheria ya fedha, kwamba tozo kwenye shule zisizo za umma inayofanana ya fire isiwepo; lakini mpaka leo fire bado wanatoza; hivi mimi najiuliza sheria na waraka ni nini kikubwa? Maana wao wanadai hawajapelekewa waraka. Niwaombe wahusika, watu wa Wizara ya Elimu, wati wa Wizara ya Mambo ya Ndani waambieni hawa Askari wa Zimamoto sheria inasema usitoze fire kwenye Shule zisizo za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la UKIMWI. Tunalo tatizo kubwa la UKIMWI katika nchi yetu lakini tatizo tunavyoliendelea ni kama vile si letu. Hatuna mfuko imara kama nchi kwa ajili ya kukabiliana na UKIMWI tunategemea fedha za wafadhili; na fedha hizi za wafadhili zina masharti mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, MheshimiwaWaziri wa Fedha yupo, niombe sana sasa hivi ndiyo tunaandaa bajeti kwa ajili ya mwaka ujao tuhakikishe tunaweka kifungu cha Mfuko kwa ajili ya UKIMWI ili kusudi kama nchi tuweze kuwa na fedha yetu kwa ajili ya matatizo ya suala la UKIMWI; vinginevyo hawa wafadhili wakiondoka, na wanavyotuyumbisha itafika mahala tutashindwa kabisa kuhudumia wagonjwa wa UKIMWI. Hawa wafadhili muda wanaokatiza shughuli, kwa mfano kuna taasisi moja ilikuwa inafanya huduma ya UKIMWI katika Mkoa wa Njombe JHPIEGO mkataba umekwisha.

Sasa katika kipindi kile ambacho mkataba umeisha na wenyewe hawana fedha za kuendelea kuhudumia, wale wanufaika wa ile huduma sasa hawapati; na kwa sababu hakuna fedha ya Serikali ya kufidia pale kwa hiyo wale watu wanakuwa hawapati huduma inayostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Serikali, kwa kuwa sasa tunakwenda kwenye kikao kijacho ambacho kitakuwa ni cha bajeti; na sasa hivi ndiyo maandalizi yanafanyika tuanzishe Mfuko wa Nchi kwa ajili ya huduma ya UKIMWI kwa wananchi. Vilevile niombe sana wananchi wote wajitahidi kupima na Serikali ihamasishe upimaji. Watu wengi wanaogopa kupima ni uoga tu lakini tuhamasishane tupime ili kusudi tuweze kupata tiba ya UKIMWI kwa maana ya kupata tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza kwa siku ya leo. Niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Maliasili jinsi wanavyofanya kazi, ni kweli wameitia uhai Wizara ya Maliasili na kazi wanayofanya inaonekana kwa mapana na marefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini nikisimama hapa ninaongelea sana sana mazao ya misitu na mazao ya misitu ninayoongelea mimi ni mbao. Wizara hii kama ingejikita kwenye uzalishaji wa mbao laini ingeliweza kuisadia Serikali kupata mapato makubwa sana. Lakini kwa bahati mbaya sana imeacha uzalishaji wa mbao unafanywa kienyeji sana, ukiangalia jinsi miti ilivyopandwa katika Jimbo la Njombe Mjini, ukaangalia jinsi watu wanavyopasua kienyeji na kuacha west nyingi kwa maana ya kwamba upotevu wa mbao ni mkubwa sana na mbao zile kusafirishwa bila hata kufanyiwa treatment yoyote zinasafirishwa zikiwa ghafi pato kubwa la Serikali linapotea, wananchi wanakosa mapato, lakini na Serikali na yenyewe inakosa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali kupitia Wizara hii kwamba wahakikishe sasa wanafanya utaratibu wa kupata mashine zilizo bora ili kusaidia upasuaji wa mbao katika Jimbo la Njombe Mjini uwe wa kitaalam mbao zile tuwe kuzi-treat, tuweze kuzisafirisha na tuwe na mbao ambazo zina ubora wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiacha suala la uzalishaji wa mbao nije kwenye suala la usafirishaji. Suala la usafirishaji wa mbao limekuwa ni kero kubwa sana kwa wafanyabiashara wote wanaosafirisha mbao, lakini hata kwa matumizi binafsi ya mbao. Usafirishaji wa mbao unapakia mbao kwenye gari ukimaliza kupakia mbao hizo saa 11 jioni huwezi kusafirisha, ikifika saa 12 ukitembeza gari lenye mzigo wa mbao lazima upigwe faini.

Ndugu zangu tunakwenda na maendeleo sasa, maendeleo yetu yanakwenda kwa kasi sana, hii biashara kusimamisha magari ya mizigo saa 12 jioni yasisafiri na mzigo halafu yaanze kusafiri kesho yake saa 12 ya asubuhi tunawasimasisha kwa ajili ya nini? Na hasa hasa hizi mbao za miti ya kupandwa kwanza anayesafirisha ana leseni, ana vibali vyote, amelipa ushuru, kila kitu amefanya, lakini bado ikifika saa 12 jioni lazima asimame mzigo ulale hapo na kesho asubuhi uanze kusafiri. Yaani gari la mzigo linalala kabla kuku hawajaingia ndani na sisi tunatafuta maendeleo hatuwezi kufika kwa staili hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri unafanya kazi nzuri sana, Naibu Waziri unafanya kazi nzuri sana, Mkurugenzi wa TFS anafanya kazi nzuri sana na watu wake, lakini kwa hili kwa hili hebu angalieni mnafanyaje, vinginevyo leo shilingi hapa hamtoki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mwalikishi wa watu wa Njombe wenzangu tunaotoka Njombe na Iringa hatuwezi kukubali hili, tumekuwa tukiwaambieni mara kwa mara tunataka mbao zisafiri usiku na mchana watu wafanye biashara, biashara ifanyike, yaani haiwezekani mtu atoke na gari la mbao Njombe afike Mwanza baada ya siku nne wakati mwenzake aliyepakia viazi anafika Mwanza baada ya siku mbili hiyo haiwezekani kabisa. Lakini kwa kufanya hivyo kwa kuondoa utaratibu huo wa kutokusafiri usiku hakuna madhara ya aina yoyote kwa maana ya mapato ya Serikali, hakuna kodi itakayopungua, hakuna mapato ya aina yoyote yatakayopungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawaombeni sana hakikisheni mnarekebisha huu utaraibu haraka iwezekanavyo ili wafanyabiashara wa mbao na mazao mengine ya misitu zikiwemo mijengo, zikiwemo kuni, ukiwemo na mkaa. Tunalalamika misitu inaharibika, lakini tunawacheleweshea watu nishati Njombe sisi tuna miti maalum ya mkaa ya kupandwa, inaitwa uoto, au milingo. Ile miti ukitengeza mkaa ndiyo unaotumika katika familia mbalimbali watu mkaa wanataka kusafirisha wapelekee watu wasio na mkaa ili waokoe misitu sehemu nyingine ninyi mnasimamisha gari isitembee mkaa unalala watu wanashindwa kupata mkaa wa miti ya kupandwa matokeo yake wanatumia nishati nyingine, lakini wanakata miti ambayo ni miti ya asili niwaombe sana,.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika zoezi hili la miti ya mkaa ningeliomba sana Wizara hii kwa sababu yenyewe ndiyo inashughulika na upandaji wa miti na ndiyo inayoshughulika kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kutokata miti ya asili kwa kuwa Njombe sasa sisi tuna miti inayofaa kwa mkaa na tumekuwa tukipanda miaka yote. Lakini sasa hatuna uwezeshaji wa aina yoyote ile tunafanya wenyewe kama wananchi tumekuwa tukijitahidi na wananchi wa Njombe niwaambieni, wananchi wa Njombe hawatumi kazi, wananchi wa Njombe wanafanya hawana kikao na mtu kwenye suala la kazi, suala la bidii, suala la kilimo, suala la upandaji wa miti hawashauriani mtu yoyote wao wanajua ratiba yao ya maisha ya kila siku ni kupanda miti kwa ajili ya maendeleo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe sasa wataalam wa TFS na Wizara hebu jikiteni Njombe mpate miti mingi ipandwe kwa ajili ya mkaa ili kusudi wananchi wa nchi hii waweze kupata mkaa kutoka kwenye miti ya kupandwa badala ya kupata mkaa kutoka kwenye miti ya asili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kusisitiza suala la usafiri na usafirishaji wa mazao ya msitu ya mbao ya kupandwa. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri na watu wake wajitahidi kadri wanavyoweza leo atakapokuwa anahitimisha taarifa yake aseme lolote lile linalowezekana kuhakikisha kwamba mbao zinaweza kusafiri usiku na mchana; wakati huo wa zamani, kwanza sheria ukiangalia utaratibu huu wa kizamani sana wakati nchi haijaendelea, barabara hazijafunguka, hasa manufaaa ya kufungua barabara ni nini? Kama tumefungua barabara ya Dodoma, Iringa imekuwa ya lami lahafu unalaza mzigo Mtela maana yake nini, kuna maana ya, lazima tuone haya maendeleo mengine yaliyopatikana lazima kila Wizara sasa iyapokee iyatumie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TFS bado hamjatumia fursa hiyo ya kufunguka kwa barabara zetu, TFS hamjatumia fursa hiyo ya magari makubwa kuwepo ndani ya nchi yetu. Nakumbuka miaka ya zamani kama miaka kumi, 15 iliyopita gari kubwa kabisa lilikuwa ni Bedford au Isuzu, ilikuwa inabeba mbao 500, mabao 100, 250. Lakini leo gari inabeba bao 3,000 tumefanya maendeleo halafu unalilaza njiani tena unachelewesha maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana na kwa kufanya hivyo mtawapunguzia gharama wasafirishaji, moja kwa moja mtawapunguzia gharama wananchi, pia mtaifanya nchi ipate fedha nyingi kwa sababu gari linapotembea linakwenda lina rudi, linakwenda linarudi, linatumia mafuta na kwenye mafuta kuna ushuru wa Serikali. Kwa hiyo, mtakuwa mmeisaidia Serikali kupata mapato zaidi; kwa hiyo, niwaombe sana mlione hilo na mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa nafasi naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji wa hotuba ya ofisi yake. Pia naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, na Serikali yake kwa ujumla jinsi wanavyofanya kazi tumeona katika miaka yote minne iliyopita Serikali yetu imefanyakazi nzuri tumepata mafanikio makubwa sana maendeleo yameonekana nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kuipongeza Serikali niipongeze sana Serikali kwa janga hili ambalo sasa linatukabili la corona Serikali ina jitahidi kutoa elimu inajitahidi kukabili tatizo hili na imeandaa kila aina ya misaada kwa wananchi nikuombe sana niombe sana sasa Serikali ikiwezekana iwaandae wananchi zaidi juu ya hali halisi ya corona ilivyo duniani na watanzania waambiwe bayana kabisa kwamba hali hii ikiendelea kuwa mbaya itabidi tukae ndani. Hivyo kila mtu akae akijua kwasababu hii ndiyo hali ya dunia ilivyosasa kwamba kule ambako corona imechachamaa watu wote sasa wanakaa ndani si vibaya kwa Serikali yetu kutamka hivyo kwamba watanzania tujue kwamba kama hali itaendelea kuwa mbaya tutakaa ndani ili kuhakikisha kwamba tunaepukana na tatizo hili la corona.

Mheshimiwa Spika, lakini wako wadau wanajitahidi sana kutusaidia kutoa elimu kwa wananchi ni mpenzi sana kusikiliza Radio One kwa kweli wanajitahidi kweli kweli Radio One kutangaza kutoa muda wao wa asubuhi zaidi ya masaa matatu wanazunguka mitaani wakielimisha wananchi. Jana nimeshuhudia mtangazaji anaongea na mtu wa daladala, mtu wa daladala anasema nina maji nilikuwa na sabuni lakini sabuni yangu imeibiwa mtangazaji anatoa fedha yake mfukoni anampa mtu wa daladala kwamba nunua sabuni nyingine ili kusudi abiria wako waendelee kupata huduma. Kwa kweli ni jambo ambalo linaonekana vyombo vya habari vimehamasika na wananchi wengi wamehamasika. Kwa kweli naipongeza sana Radio One kwa hilo waendelee kutoa elimu kwa wananchi na vyombo vyote vya habari viendelee kutoa elimu.

Mheshimiwa Spika, nikiacha hiyo habari ya ugonjwa wa corona, nije kwenye hoja ya Waziri Mkuu tuna tatizo kubwa sana la maji kama nchi lakini sasa ni takriban tunakwenda huu ni mwaka wa tano tumekuwa hapa Bungeni tukiambiwa miji 26 itapewa fedha ya kutengenezewa miradi ya maji na huu ulikuwa ni mkopo toka India miaka mitano inakwisha toka tunaanza Bunge hili tumekuwa tukiambiwa miji 26 itapewa fedha miji 26 mara muambiwe sijui kuna sijui kuna no objection sijui mara nini yaani tunaweza kusema ni hadithi tu zimekwenda mpaka tumefika leo tunafika mwaka wa tano hakuna maji kwenye miji 25 na wananchi wanaendelea kutudai maji na sisi tumekuwa tukiahidi na Serikali imekuwa ikituahidi.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri Mkuu atakapokuwa anahitimisha hoja yake atuambie kwamba hii miji 26 ambayo tuliambiwa itapewa maji, ikiwemo mji wa Njombe ni lini sasa itapewa maji na kama hiyo ya India imeshindikana kwa sababu kama jirani ameshindwa kumpa mwanao chakula mwenye mtoto si umpe chakula mwanao? Au utaacha mtoto afe tu eti kwasababu jirani aliahidi atampa chakula. Kwa hiyo, nafikiri tubadilishe utaratibu tuendelee na utaratibu kama nchi tuipe maji hii miji kwasababu maji ni uhai, maji ni afya na maji ni maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nipongeze sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri kubwa anayoifanya ya kurithisha ujuzi. Kazi hii ya ujuzi ni kazi muhimu sana vijana wengi sasa wameanza kupata ujuzi ninachokiomba kwenye idara ile inayoshughulika na ujuzi ipanue nafasi iende mpaka kwenye nafasi za fani za kilimo, fani za ufugaji kwa sababu kilimo na mifugo ndiyo itaajiri watu wengi nimeona wanatoa kwenye ufundi wa magari, umeme, na nini hivi yaani katika vijana tulionao katika nchi hii hao mmewasaidia vijana wa mjini lakini vijana wa vijijini watasaidiwa kwa kupelekwa kwenye fani za kilimo na fani za mifugo tutakuwa tumewasaidia vijana wengi wa vijijini kupata ujuzi na tutumie vyuo vingi zaidi tusitumie vyuo hivi vitatu tu Don Bosco, DMI, DTI hapana tuende vyuo vingine.

Mheshimiwa Spika, iko private sector ina vyuo vingi tu ambayo inaweza ikasaidia kutoa ujuzi huu. Kwa hiyo, niombe sana hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu mliangalie na msaidie vijana wengi zaidi ili kusudi wapate ujuzi kwa sababu ujuzi pekee ndiyo utawafanya vijana wa nchi hii kuweza kujiajiri na kuweza kufanya kazi katika ulimwengu huu unaokwenda sasa watanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, nimeona katika hotuba ya Waziri Mkuu akizungumza habari ya benki ya kilimo. Benki ya kilimo imefanya kazi nzuri miaka mingi tumekuwa tukilalamika sana juu ya benki ya kilimo lakini kwa sasa benki ya kilimo inaonekana imefanya jitihada kubwa sana binafsi nimemuona Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kilimo akipita kwa wadau mbalimbali na wananchi mbalimbali kuhamasisha na kuangalia miradi ambayo wanaweza wakakopeshwa na benki

Mheshimiwa Spika, niombe Serikali iendelee kuisimamia hii benki na benki yenyewe iendelee kujituma zaidi kushuka chini kwa wakulima wa kawaida kama vile anavyofanya Mkurugenzi wao basi watumishi wote ndani ya benki ile wafanye hivyo kwamba wawatembelee wananchi waone mahitaji ya wananchi wakulima ni nini. Lakini mara nyingi nimekuwa nikisimama hapa mbele yako nikilalamika sana juu ya matrekta, matrekta mengi wanayokopeshwa watanzania ni mabovu, matrekta mengi wanayokopeshwa watanzania hayakidhi haja ya kilimo tunaletewa katika nchi matreka ambayo hayana sifa. Taasisi zote zinazoleta matrekta zinaleta matrekta zinaleta matreka ambayo kwa kweli uimara wake na ubora wake ni chini sana. Kwa hiyo, niombe sana Serikali ilione hilo.

Mheshimiwa Spika, na mwisho kabisa ni suala la UKIMWI, tatizo la UKIMWI ni kubwa sana lakini ukubwa wa tatizo hili, sisi watanzania ni kama vile tumeufumbia macho. Kiwango chetu cha kutoa elimu kiende kwenye taasisi zilizochini kwa mfano halmashauri mimi ni mjumbe wa kamati ya Ukimwi lakini unakwenda pale halmashauri unakutana na watu ambao ni wajibu wao kutoa hiyo elimu lakini hawajui chochote hawatoi elimu na wala hawana data zozote niombe Serikali ilione hilo jambo liende lisimamiwe mpaka ngazi ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho kabisa ni mfuko wa UKIMWI ATF hatuna mfuko, tunao mfuko wa UKIMWI lakini Serikali haichangii hatuna tozo mahala ambalo linasaidia kuingia kwa ajili ya mfuko wa UKIMWI, tunategemea kupata huduma ya dawa hizi za Ukimwi ARV kutoka kwa wafadhili. Leo hii wafadhili wanapambana na corona na inawezekana corona ikawabana sana wakaendelea kuhudumia watu wao tu sisi ambao tunategemea msaada kutoka kwao tutakwama na tusipokuwa na ARV maana yake sasa watanzania tutaanza kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kuhakikisha kwamba inatafuta tozo yoyote ambayo watanzania tutachangia kwa ajili ya mfuko wa UKIMWI ili kusudi tuwe na mfuko wetu wa kujitegemea kuliko kutegemea wafadhili ambao leo hii mfadhili mkubwa ni Marekani, Marekani leo ana corona 200,000 na wanaendelea kupambana sasa atatukumbuka sisi kweli. Kwa hiyo, hii ni hatari sana kwetu na niombe sana Serikali iangalie hilo namna gani tutafanya tupate tozo ya aina yoyote ile iwe ni maalum kwa ajili ya masuala ya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana kwa fursa, ahsante sana. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali uliopo mbele yetu. Kwanza kabisa, nampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, jinsi alivyouwasilisha kwa umahiri na kutupa nafasi na sisi kama Wabunge tuweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Misitu. Suala hili la misitu kwa kweli kadiri tunavyokwenda linaonyesha kwamba sasa tunazidi kuelemewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaongeza adhabu juu ya adhabu; lakini lazima tujiulize, kwa nini adhabu za zamani ambazo tuliziweka zimetufikisha wapi? Kwa mfano, ipo adhabu iliyokuwa inapambana na teknolojia. Kuchana mbao kwa kutumia chain saw yale ni maendeleo ya kiteknolojia. Unapoweka adhabu kupambana na teknolojia, ina maana kwamba umekosa mbinu mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tukaangalia kwamba, ilikuwa ukiingia na chain saw msituni, ukikutwa faini ni shilingi milioni moja, lakini ile ni teknolojia. Teknolojia yenyewe haina matatizo, wenye matatizo ni watendaji ambao hawasimamii sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumo humu ndani ya Bunge leo tunatunga sheria, lakini hatuendi kusimamia hizi sheria. Ni vizuri sasa watendaji wajione kwamba wao ndio wenye wajibu wa kusimamia sheria na kuhakikisha sheria zinafuatwa. Leo tunaongeza adhabu kwa watu wanaofanya kazi za mali za misitu, lakini wasimamizi wameshindwa kabisa kusimamia hata zile sheria walizokuwa nazo. Hilo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni baya zaidi ni kwamba ukiingia na chain saw msituni ukikamatwa faini ni milioni moja. Kwa hiyo, mtu anaona ni furaha atakwenda msituni atakata miti haraka haraka, kwa sababu chain saw itamrahisishia kazi, atatozwa faini ya shilingi milioni moja, atakuwa amefanya kazi kwa haraka. Sasa tuone kwamba hili shirika la TFC ambalo ndilo linashughulikia kusimamia hii misitu, lisimamie vizuri sana sheria hizi ambazo zipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nashauri kwamba TFC ilisharidhia lakini sasa isimamie na itekeleze makubaliano ya mwaka 2013 ambayo yalishirikisha vijiji katika usimamizi wa misitu. Misitu ile ambayo ipo chini ya vijiji, leo hii ina hali nzuri zaidi kuliko misitu ambayo inasimamiwa na TFS. TFS hawafanyi kazi vizuri, misitu inakatwa na wenyewe wapo na magogo yanazidi kusafirishwa hasa katika misitu ile inayosimamiwa na TFS.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine, katika suala la adhabu, nashauri kwamba hawa watu wanaojishughulisha na mazao ya misitu watakaokamatwa na makosa, moja mali zao zitaifishwe. Sheria hii ipo, lakini haitaifishwi, kwa hiyo tunaendelea kulalamika. Sasa isimamiwe wataifishiwe hizo mali, lakini pili, watakapokuwa wanauza hizi mali kwa mnada ama kwa njia nyingine yoyote, yeyote aliyejishughulisha na kazi ya misitu kiharamu asiuziwe tena. Kwa maana nyingine ni kwamba wafisilisiwe ndiyo angalau itasaidia kupunguza hili tatizo la misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile lipo suala la misitu ya kupandwa. Nadhani kwamba sheria sasa ionyesha kwamba kuna mazingira ambayo misitu yake ni ya kupandwa kwenye miti kama Cariptus, Pines, Cyprus ni miti ambayo inapandwa. Sheria inawabana sana wale wananchi wenye ile misitu, hasa anapokuwa anasafirisha mazao yake hata kwa matumizi binafsi. Mtu anatozwa kodi ya misitu, anasafirisha kuni kutoka kwenye shamba lake.
Kwa hiyo, hii nayo tunaomba sheria iangaliwe ili kusudi tuondoe sheria zenye kero kwa wananchi, kwamba maeneo yale ambayo misitu inapandwa yenye uoto, caliptus au pine, basi kuwe kuna unafuu kwa wananchi ambao wanajishughulisha kwenye hii misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya sheria hii, naomba nichangie pia kuhusu Sheria ya Elimu ambayo inapaendekeza kifungo cha miaka 30 kwa yeyote atakayesababisha ujauzito kwa mwanafunzi. Naungana na sheria hii. Ni kweli yeyote atakayesababisha ujauzito kwa mwanafunzi, afungwe; lakini ushauri wangu ni kwamba kwa sababu ujauzito hakuna unaozidi miezi tisa.
Nashauri ili kuwa na uhakika kwamba kweli huyu mtu amehusika, basi vipimo vya DNA vifanyike ili kwamba mtu anayefungwa kweli awe amekosea.
Tutakuja kufunga watu halafu tutakuja kuona kwamba tumewaonea. Kwa sababu tendo lile linatendwa katika mazingira ya siri ya watu wawili; na huwezi kujua huyu mwanafunzi amefanya hivyo na watu wangapi, anaweza akamdandia mtu na akamng’ang’ania halafu akamsababishia matatizo ya miaka 30 jela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sheria hii ikatoa nafasi kwamba baada ya mtoto kuzaliwa, basi mtoto huyo apimwe tupate visibitisho vya DNA halafu ndiyo hukumu isomwe. Hii itakuwa imetoa nafasi ya uhakikia kabisa kwamba kweli huyu mtu ni mhalifu na hili kosa linamhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme jambo lingine, wapo watoto wa kiume ambao wanatunzwa na akina mama, sheria haisemi chochote. Wewe una mtoto wako anakwenda boarding school Tanga, umempa pocket money, akifika pale mjini anapokelewa na mama anatunzwa, matokeo yake anaacha shule. Kule anakotuzwa, anamrutubisha yule mwana mama mpaka anapata mjamzito: Je, hapa kosa linakuwa ni la nani? Mimi nadhani kwamba hapa kosa liwe la huyo mama anayemtunza mtoto wa kiume nyumbani kwake na ahukumiwe na yeye miaka mitano ama faini shilingi milioni tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiacha kwamba tusiweke adhabu kwa ajili ya akina mama ambao wanahusiana na watoto wa kiume wanafunzi, tutakuwa hatuwatendei haki wanaume na tutakuwa tunawafanya wanafunzi wa kiume waingie kwenye matatizo. Kwa sababu mtoto huyu akizaliwa; chukulia kwamba kijana yuko Kidato cha Nne, amesababisha ujauzito kwa mama mmoja huko mtaani, atakapoenda Kidato cha Tano, au cha Sita anaanza kusumbuliwa matunzo ya motto, mara nini, wakati mama yule ndiye aliyesababisha hiyo hali. Kijana alikuwa shule lakini yeye alifanya ushawishi wa kumfanya mama yule apate mtoto. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba sheria hapa iseme, maana yake hakuna sheria inayosema chochote juu ya mwanamama ambaye anamtunza mtoto wa kiume na kusababisha ujauzito kwake. Ilete usawa huo na ihakikishe kwamba huyu mama atakayefanya kitendo hiki na yeye jela miaka mitano ama faini milioni tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii iliyopo mbele yetu juu la Sheria ya Manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingi ni ushauri lakini katika ushauri huu nadhani ni vizuri sana tukajaribu kuangalia namna gani tunazisaidia halmashauri zetu kwa mfano katika suala la usafi. Suala la usafi ni gumu sana katika halmashauri zetu. Tunapoweka utaratibu huu wa manunuzi kwenye usafi ina maana kwamba tenda zetu zinafuata mwaka wa fedha na inakuwa ni muda wa mwaka mmoja. Sasa tujiulize kwamba ni nani ana uwezo wa kuwekeza vifaa vya usafi kwenye mji halafu akavitumia kwa mwaka mmoja halafu baada ya hapo mwaka unaofuata anakosa ile tenda! Jiulize hata kama ungekuwa wewe umenunua lori la kusomba takataka, umewekeza kwenye mradi wa kusomba takataka katika mji na umeshinda tenda lakini mwaka unaofuata bahati mbaya umekosa hiyo tenda, hilo gari utalipeleka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kama hili liliwahi kutokea pale Dar es Salaam miaka ya nyuma. Imetangazwa tenda ya kukusanya ushuru wa maegesho, mtu kawekeza, kafunga mashine za kisasa kabisa kukusanya ile ada ya parking mwaka uliofuata kakosa tenda mashine zile inabidi ang‟oe akaweke nyumbani, hazina kazi nyingine zaidi ya kuuza tiketi za parking. Kwa hiyo, nashauri kwamba ziko tenda ambazo lazima tuziwekee kipengele maalum kwa mfano kama ni suala la vifaa vya usafi ama usafi wa miji basi ni lazima Serikali ione kwamba hapa mwekezaji wake awe tofauti au anayeiomba hii tenda awe tofauti na tenda nyingine za kawaida. Kwa sababu mtu hawezi kununua magari kwa ajili ya kufanya usafi katika mji, ameshinda tenda, ame-operate kwa mwaka mmoja, mwaka unaofuata amekosa ile tenda. Sheria inawafanya halmashauri watangaze tenda kwa mtu mwingine na wewe unaikosa, sasa yale magari utafanya nayo nini, utakuwa huna kazi ya kufanyia yale magari. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie hilo na ione ni kwa namna gani inaweza ikasaidia halmashauri zetu kuwa safi. Miji yetu inashindwa kuwa misafi kwa sababu ya utaratibu wa kuwapata wakandarasi wa kufanya usafi katika miji. Hilo suala la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni la ujenzi katika halmashauri zetu. Ziko halmashauri zina vifaa vya ujenzi lakini havina sifa ya kufanya kazi ya ujenzi ndani ya halmashauri kwa kutumia fedha ambayo Serikali inaitoa ili kusudi barabara zitengenezwe na miradi mbalimbali ya ujenzi ifanyike. Naomba niishauri Serikali hapa, kwa zile halmashauri ambazo zimekamilisha seti ya vifaa kwenye kanuni ioneshwe kwamba wapate kibali kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI kuwaruhusu kutengeneza angalau barabara moja ili kusudi halmashauri na yenyewe iweze kupata ile fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, halmashauri ina wataalam, unakuta ina injinia na ndiye anayesimamia barabara zote kwa hiyo uzoefu anao. Matokeo yake tunakuja kutoa tenda ya mamilioni ya kujenga barabara zetu kwa mkandarasi aliyekuja na begi na jeans tu, anaanza kukodi vifaa vilevile vya halmashauri halafu anaanza tena kuwasumbua kulipa na anaanza kuhangaika kutafuta vifaa mahali pengine. Niombe sana Serikali iangalie hili kwa sababu halmashauri zimetumia fedha nyingi sana kununua vile vifaa vya ujenzi na vimekamilika. Kwa hiyo, angalau 25% kwenye miradi ya ujenzi ndani ya halmashauri, halmashauri iruhusiwe kuijenga na Serikali iwalipe kama inavyowalipa wakandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la Kamati ya Fedha kutokupitia wakandarasi waliopitishwa na Bodi ya Manunuzi. Naomba Serikali iangalie, jambo hili kwanza halicheleweshi mchakato wa aina yoyote kwa sababu vikao vile vya finance viko kila mwezi na vina ratiba yake. Suala la kupitisha au kuwapitia wakandarasi hawa linakuja pengine kwenye halmashauri mara moja au mbili tu katika mwaka, wala haihusiki kabisa kumchelewesha mkandarasi wala kuzuia shughuli ya aina yoyote ya mkandarasi lakini ile inasaidia kujiridhisha na kupanua maarifa. Kwa sababu ndani ya halmashauri wale Madiwani wanaoshiriki katika vikao vile vya finance wanauelewa mbalimbali, wanaweza wakasaidia kuishauri halmashauri namna gani mkandarasi huyu yupo na wanamfahamu namna gani. Sioni kama kuna haja ya kuiondoa hii Kamati ya Fedha ya Halmashauri kutokushiriki katika mchakato wa kuwa-award tenda. Niombe sana Serikali ilione hilo kwa sababu lenyewe lilikuwa halipunguzi chochote kwenye halmashauri badala yake lilikuwa linajaribu kuongeza ubora wa kazi ambayo Kamati ile ya tenda imefanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, nimefurahi sana sheria hii imekuja na utaratibu sasa wa kubishania bei kwamba mnajadiliana bei na supplier ili kusudi halmashauri iweze kupata huduma. Niiombe sasa Serikali, vinginevyo hapa tutasababisha matatizo kwa watendaji kwa sababu watatumia nafasi hii, watabishania bei, watapata bei nzuri lakini inapokuja kwenye malipo sasa, tutasababisha tatizo kubwa sana kama hatutalipa kwa wakati. Tukumbuke kwamba walikuwa wanaweka bei ya juu na ilikuwa inawasaidia kwa sababu fedha yao ilikuwa inakaa Serikalini. Leo hii tukijaribu kuangalia unaweza ukakuta kuna watu huko Magereza na kwenye Shule za Sekondari hawajalipwa. Kwa hiyo, niombe sana tunapofikia mahali pa kuanza kuitumia sheria hii malipo kwa suppliers yaweze kutolewa kwa wakati kwa sababu unapobishania bei ina maana kwamba utapata bei ya soko halafu unachelewesha malipo zaidi ya miezi sita maana yake hutaki huyo supplier aendelee kukuhudumia ndiyo unamuua kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mazingira ambayo supplier ana-supply chakula cha wanafunzi, akikataa kuleta chakula kwa sababu wewe hujamlipa maana yake watoto wale watalala njaa. Ukitaka kujua kichaa cha watoto wa shule wanyime chakula, watachoma shule, watapiga walimu, wao hawatajua kama ni supplier hajaleta chakula. Kwa hiyo, niombe sana suala hili liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kundi lingine ambalo ni dhaifu sana, kundi la wafungwa. Tusipoangalia utaratibu tunaouweka hawa wafungwa ndiyo tunaenda kuwapa adhabu ya mara ya pili ya kulala na njaa. Kwa sababu huyu supplier atasema naleta leo mnilipe pesa kesho, mtasema sawa, ataleta hakupewa fedha miezi inakwenda, siku nyingine haleti, wafungwa wanalala njaa na wafungwa kwa sababu hawana pa kulalamika maana yake sasa tutakuwa tunasababisha adhabu mara mbili ya adhabu waliyohukumiwa. Kwa hiyo, niombe sana, kama tunakubaliana sheria hii ni nzuri ipite basi niiombe Serikali ihakikishe kwamba kweli kila mmoja anatimiza wajibu wake, anahakikisha kwamba fedha inakuwepo, huyu supplier anatoa hiyo huduma na Serikali inamlipa kwa wakati. Hivi ndivyo tutaweza kusaidia hii sheria ifanye kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie tena kuomba, tafadhali sana halmashauri zenye vifaa vya ujenzi zipewe angalau zile kazi zilizoko kwenye mpango wa kazi kwa 25% ili kusudi na zenyewe ziweze kujijenga zaidi. Kwa sababu tunategemea miaka ijayo halmashauri ziweze kujitegemea zenyewe kwa kila jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja sheria hii iweze kutusaidia kupunguza gharama kwa Serikali. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimwa Mwenyekiti, awali ya yote, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia machache kwenye Muswada ulioko mbele yetu, Muswada wa kitaaluma wa Bodi ya Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema, naunga mkono hoja hii na naipongeza sana Serikali kwa kuleta hoja hii. Jambo la pekee ambalo napenda kulisema sana ni upande wa taaluma ya ualimu. Tumeshuhudia katika nchi yetu tukipita miongo kadhaa ya mafungu mbaliambali ya walimu, lakini kwa bahati mbaya sana mafungu haya yote yamekosa utafiti thabiti ambao unaweza ukasema kwamba mwalimu yule aliyekuwa anaitwa Mwalimu wa UPE alifundisha na alikuwa na upungufu gani? Tumekwenda baadaye tumekuwa na madaraja mbalimbali ya ualimu na sifa mbalimbali za kujiunga na vyuo vya ualimu, lakini mpaka leo hakuna anayeweza kusema kwamba kijana aliyehitimu kidato cha nne na kuwa na division four na akawa na point 28 akasoma taaluma ya ualimu, akapangiwa kazi ya kufundisha na akafundisha, alikuwa na upungufu upi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuundwa kwa Bodi hii, naamini kabisa kwamba sasa taaluma ya ualimu itasimamiwa vizuri. Nimeona hapa moja ya jukumu la Bodi hii ya Ualimu ni kusimamia taaluma ya ualimu. Tumeshuhudia siku za karibuni, kauli mbalimbali zikitolewa juu ya taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya ualimu, kumekuwa na kuyumba kwenye taasisi zisizo za Serikali na za Serikali. Vijana wanajiunga na vyuo lakini wanakatizwa masomo kwa kuambiwa kwamba hawana sifa. Kwa kuundwa kwa Bodi hii naamini kabisa sasa kwamba Bodi itaweka utaratibu mzuri ambao utasaidia kutoa mwelekeo na utaratibu ambao utawezesha sasa kila anayetaka kufanya kazi hii ya ualimu atakuwa anajua mapema kabisa kwamba sifa yangu ni ipi, nikasome wapi na nifanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeliona kwenye Muswada huu ni kwamba, Muswada huu kwenye majukumu ya Bodi imeeleza vifungu mbalimbali ambavyo Bodi itafanya kazi, lakini ukiingia ndani ya Muswada wenyewe unaeleza zaidi kama ni Muswada wa kusimamia maadili ya ualimu. Hii mimi inanitia mashaka sana kwa maana ya kwamba lengo zima la kuwa na Muswada linamezwa na kipande kidogo tu cha maadili ya ualimu. Sasa kama tutakuwa tunaunda Bodi ambayo itajikita tu kwenye maadili tu ya ualimu, basi niungane na wenzangu kusema kwamba tutafika mahali tutakuwa tunaunda vitu vingi halafu majukumu yake yatakuwa ni yale yale yanayojirudiarudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana katika suala hili tuwe makini sana kama Wabunge kuona kwamba hivi tunavyounda hii Bodi ni kweli inaenda kutatua tatizo lililopo? Au tunaunda Bodi kwa sababu tu chombo hiki kimedaiwa na watu wengi kiwepo basi kiwepo lakini majukumu yake yote hayatakuwepo. Kwa sababu maelezo mengi yaliyomo kwenye hii Bodi yanazungumzia tu nidhani ya walimu, adhabu na kukata rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye hiyo taaluma ya ualimu wenyewe, mbali ya kwamba hilo ni lengo limewekwa kwamba itasimamia utoaji wa elimu ya walimu sioni kwa ndani inaelezwaje kwamba itatoaje hiyo elimu, ni nani atawajibika na nini? Anyway kama alivyosema Mhshimiwa Balozi Dkt. Kamala kwamba hii ni hatua ya kwanza, lipite hili lakini tuombe sasa, next tuletewe kitu kingine ambacho kitajazilizia huu upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulisema, baada ya kupitisha huu Muswada, nina imani utapita, lakini baada ya kuupitisha, kuna kipengele ambacho Wizara inatakiwa iunde kanuni. Hapa ndipo kwenye tatizo. Tunaweza tukapitisha huu Muswada leo, sheria ikasainiwa na Mheshimiwa Rais, lakini kanuni zikachukua miaka. Kwa hiyo, ikawa kazi yote tunayoifanya hapa inakuja kuwa implemented labda baada ya miaka miwili au mitatu. Kwa hiyo, itakuwa maana nzima ya shughuli yote hii iliyofanyika huko nyuma inakua siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, kama kweli tumedhamiria kuweka mambo sawa kwenye suala hili la walimu wa Tanzania na kwa maana ya kwamba walimu hawa ndio wanaosimamia taaluma, basi tuhakikishe kwamba kanuni zinatungwa mapema, mara tu baada ya sheria kusainiwa ili kusudi sasa Bodi hii ianze kufanya kazi mara moja. Kwa sababu ukitunga sheria, ukaunda hiyo Bodi, lakini huna kanuni, hiyo Bodi inakuwa haiwezi kufanya kazi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena jambo lingine wakati wowote wa kutunga hizo kanuni na waangalie sana mgongano wa kimaslahi, kwa sababu tunafahamu kwamba tunaiangalia taaluma hii ya ualimu kwa maana ya kwamba wanaofundisha shuleni, lakini ukienda Baraza la Mithani utakuta kwamba asilimia 90 ya watumishi wa Baraza la Mitihani ni walimu; ukienda Taasisi ya Ukuzaji Mitaala, asilimia 90 ya watumishi wa pale ni walimu. Kwa hiyo, tuone kwamba vyombo hivi vingine ambavyo navyo vinashiriki katika zoezi zima la utoaji wa elimu vinashirikishwa vipi kwenye hizi kanuni ili kuondoa mgongano wa kimaslahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaweka kanuni ambazo zitaleta ukinzani kwamba Bodi ya Usajili ya Ualimu inamtaka mtumishi wa Baraza la Mitihani ambaye ni mwalimu ajisajili na amejisajili, lakini anapokuja kukutwa pengine amekiuka baadhi ya miiko ya Bodi ya Walimu analindwa na Sheria ya Baraza la Mitihani ama analindwa na Sheria ya Taasisi ya Elimu. Kwa hiyo, haya ni mambo muhimu sana kuyaangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake, niseme kwamba nimefurahishwa sana na Muswada huu na hasa kwenye kipengele cha kusimamia taaluma ya ualimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie katika hoja iliyoko mbele yetu inayohusiana na Muswada huu wa huduma ya utoaji maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama inavyojulikana, maji ni uhai na maji hayana mbadala. Mahali popote yanapohitajika maji, lazima yatafutwe maji na yapatikane. Huwezi kusema kwamba nitafanya jambo hili badala ya maji au kuna kitu utakitafuta ambacho kitafanya kazi badala ya maji. Kwa hiyo, ndiyo maana tunasema maji ni uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Wakala wa Maji Vijijini. Naomba Serikali ijipange vizuri. Tunaweza tukawa tunaanzisha vyombo lakini ufanisi ukabaki ule ule. Kadri nijuavyo mimi, tatizo la maji siyo Wakala na siyo wala siyo Halmashauri, tatizo la maji ni Serikali. Miradi mingi ya maji ambayo iko katika maeneo yetu nikichukulia mfano katika Jimbo la Njombe Mjini, tatizo kubwa la miradi ile ya maji ni Serikali yenyewe. Sasa sielewi hapa, tunaunda Wakala; itajibadilishaje Serikali yenyewe kwenda kufanya kazi kwa ufanisi katika miradi ambayo imekuwa ikiisimamia toka mwanzo? Serikali ndiyo imefanya designing, Serikali ndiyo imetafuta wasimamizi wa miradi, Halmashauri sawa imehusika katika mchakato wa kumtafuta Mkandarasi, lakini Serikali inatakiwa kutoa fedha kwa ajili ya kuwalipa Wakandarasi. Wakandarasi wa maji hawalipwi. Certificates zinakaa, zinachelewa kulipwa miezi mitatu, miezi sita, miezi nane.

Sasa je, huyu Wakala anayekwenda kuwa sasa ndio Msimamizi wa Maji Vijijini yeye atatoa wapi fedha? Sawa tunajua kuna Mfuko wa Maji utaanzishwa, lakini katika hili Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba tunaunda Wakala na hii Wakala wa Maji Vijijini itakuwa na fedha za kutosha kutekeleza miradi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo kubwa ninaloliona mimi ni suala la fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Miradi mingi ya maji imeharibika katika Majimbo mbalimbali kwa sababu Serikali imekuwa haitoi fedha kwa wakati, matokeo yake unakuja kuona kwamba mradi umeshindwa kufanikiwa, hautoi maji ama mradi unakuwa na phase tatu au nne. Phase za usambazaji maji zimekamilika, lakini phase zinazojenga vyanzo, hazijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo lingine ambalo pamoja na kuunda Wakala Serikali lazima iangalie, iko miradi ambayo ilikuwa na msamaha wa kodi, miradi ile, ule msamaha wa kodi hautoki. Sasa hata tukiunda Wakala, atafanikishaje hiyo miradi kama Serikali haitatoa huo msamaha wa kodi na kuweza kufanikisha miradi ya maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine tunaunda Sheria ya Huduma ya Maji na Mazingira lakini liko jambo ambalo lazima nalo tuliangalie kwamba je, tunataka huduma iwe nzuri, wananchi wapate huduma bora, lakini kuna mahali inafikia wakati, taasisi hizi za maji ambazo zinasimamia maji haziwi makini, matokeo yake wananchi wanapata maji ambayo siyo safi. Unakuta mabomba yanatoa maji siyo masafi, yanatoa maji machafu, yanatoa maji yana udongo. Je, hapa Serikali itajiwajibishaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ifike wakati kama ni EWURA au ni nani wanaosimamia walaji, tuwe na sheria ambayo inaweza ikasaidia wananchi kupata haki yao na kupata majisafi. Vinginevyo, tutakuwa tumeunda sheria nyingi, sheria ambazo zinawabana walaji tu wanaochafua vyanzo vya maji, wanaovunja mabomba, lakini yeye kama Wakala ama yeye kama mtoa huduma, anatoa maji yasiyo safi kwa wananchi. Anawajibikaje au sheria inamwajibisha namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la mkanganyiko wa kisheria katika masuala ya maji. Iko Sheria ya Mazingira ambayo inazuia matumizi ya maeneo ambayo huwa yamo ndani ya mita 60. Naomba sana Wizara ya Maji na watu wa Mazingira wajaribu kuiangalia hii sheria. Hii sheria iko vile, lakini ni sheria isiyotenda haki. Kwa sababu tumekuwa tukihoji mara nyingi sana kwamba hivi maji tunahifadhi wapi? Maji tunayahifadhi pale yanapotoka au maji tunayahifadhi kwenye milima? Sayansi ya kawaida inasema, maji yanahifadhi kwenye mlima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawapewi elimu ya kulima kilimo cha makinga maji; hawapewi elimu ya kuhakikisha kwamba katika maeneo yenye miinuko wanahakikisha wanalima matuta ili kuhakikisha kwamba mvua zikinyesha maji yale yasiporomoke kwenda mabondeni; maji yatuame kule kwenye milima, yanyonywe na ardhi ili yahifadhiwe kwenye ardhi, lakini matokeo yake sasa wataalam, mimi nahisi wamechukua taarifa sijui za kwa Wazungu, mimi nasema hawa Wazungu wametuzunguka tu, kwamba huwezi ukahifadhi maji pale yanapotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yanahifadhiwa mlimani.unahifadhi maji mlimani kwa kuweka makinga maji, kwa kupanda miti na kuhakikisha kwamba milima inakua na zulia ama carpet ili kusudi mvua zikinyesha ardhi iweze kunyonya maji na maji yale yatunzwe ndani ya ardhi ili yatoke kule kwenye chanzo kidogo kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapowaambia wananchi kwamba wasilime bondeni kwa sababu kule ni chanzo cha maji, kule siyo chanzo za maji. Kule ni sehemu ya kutokea maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana wataalam waliangalie hilo, waangalie hiyo Sheria ya Mazingira ili kusudi tuone wananchi wakipata huduma ya maji, lakini Serikali na yenyewe iangalie, inapoanzisha huu Wakala ihakikishe mtaji upo wa kutosha kuhakikisha kwamba, unatoka kwenye kuiacha Halmashauri kutoa huduma ya vyanzo vya maji na kugawa na kusambaza maji kwa wananchi, lakini Wakala huu uwe na ufanisi. Kinyume chake ni kwamba, tutakuwa tumeweka Wakala, lakini hatuna fedha ya kumsaidia kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Finance Bill ambayo tunaendelea kuijadili hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme mambo machache sana, nianze na suala la vitambulisho. Vitambulisho vya wajasiriamali ni muhimu sana na vimesaidia sana wajasiriamali wengi kuwa na utaratibu mzuri wa kufanya biashara zao. Hata hivyo, Serikali imetuahidi kwamba itatoa Waraka, naomba sana watakapokuwa wanatoa huo Waraka waangalie jambo moja la muhimu sana. Katika kodi zote ambazo tunalipa kupitia mishahara kuna kodi ya Pay As You Earn, wanaolipa ni wale tu ambao mishahara yao iko juu ya kima cha chini na hata wenye mishahara juu ya kima cha chini huwa inaondolewa kiwango cha kima cha chini cha mshahara halafu kiwango kinachobakia ndicho kinachotozwa kodi. Kwa hiyo, ningeomba sana hata kwa hawa wajasiriamali…

T A A R I F A

MHE. SULEIMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwalongo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Bungara.

MHE. SULEIMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana msemaji anayesema sasa hivi kwa kuunga mkono kwamba vitambulisho vya wajasiriamali virekebishwe. Nachomuunga mkono yeye Serikali kabla hatujatoka katika kikao hiki Wabunge wote tupewe orodha za wajasiriamali kwa kuwa waliahidi. Kabla hatujatoka Bungeni hapa tupate hiyo orodha.

Kwa hiyo, ninampongeza sana lakini ni vema wote tupate hizo orodha kama tulivyoahidiwa. Kwa hiyo, nakupongeza sana kijana wewe unaweza kuwa Waziri siyo Ubunge tu. Ahsante sana. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kuna muda huwa mnapenda masihara hivi lakini taarifa kwa mujibu wa kanuni zetu si kwa ajili ya kupongezana moja, lakini la pili taarifa siyo kwa ajili ya kuunga mkono anachozungumza mtu. Ndiyo maana huwa tunapigiana makofi kama unaunga mkono, siyo hoja ya kusimama ili umwambie unamuunga mkono la sivyo tutakuwa hatumalizi michango huu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwalongo, endelea.

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuliweka sawa hilo, naomba niendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu uko mkanganyiko mkubwa sana wa utoaji wa hivi vitambulisho kwenye maeneo yetu na umezua taharuki kubwa sana. Kwa hiyo, niombe sana Serikali iliangalie suala hili mapema na kama Serikali ilivyotuahidi kwamba italeta Waraka hapa utakaokuwa unaelekeza kwa sababu ziko kada ambazo zinapewa hivi vitambulisho au zinapaswa kupewa vitambulisho lakini ukiangalia kipato chao kiko chini ya kima cha chini cha mshahara ambao Serikali imeweka kama ndiyo kima cha chini cha Mtanzania kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ningeomba nirejee kwenye kodi ambazo kwenye Finance Bill iliyopita tuliweza kuzijadili hapa, kodi ya majengo. Tulisema nyumba zinazotozwa kodi ya majengo ni nyumba zote zilizoko kwenye miji lakini imetokea kwamba ziko Halmashauri za miji kwa mfano Halmashauri ya Mji wa Njombe, ni Halmashauri ya Mji lakini ina vijiji kata kumi. Sasa unapokwenda kutoza kodi ya nyumba kwenye vijiji vilivyoko ndani ya Halmashauri ya Mji kidogo inaleta shida. Mimi naomba sana Serikali iliangalie suala hili kwamba tuko tayari kulipa kodi hii ya nyumba kwenye Mji wetu wa Njombe na Mitaa ya Njombe na mitaa iliyoko vijijini yenye sifa ya mitaa lakini kwenye vijiji vilivyoko ndani ya mji, yaani vilivyoko ndani ya utawala wa Halmashauri ya Mji inaleta shida sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tabia ya wananchi wa vijijini watashindwa hata kujenga nyumba kwa uwoga tu kwamba nikijenga nyumba nzuri wataniletea kodi. Kwa hiyo, ningeomba sana Serikali iliangalie suala hili na nafikiri ni busara ya kawaida kabisa kama ni kijijini, sawa eneo la utawala linasema ni ndani ya Halmashauri ya Mji, lakini pale mahali ni kijijini kabisa. Kwenye Halmashauri yangu ya Mji Njombe Vijiji kama vile vya Mamongolo, Ng’elamo vipo zaidi ya kilometa 90 toka Njombe Mjini ambavyo kwa kweli ni vijiji kabisa. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iliangalie hili na iweze kutoa maelekezo kwa TRA kwamba maeneo ya vijijini hata kama yako ndani ya utawala wa Halmashauri ya Mji waweze kuona namna gani wanaweza wakasaidia kuwafanya hawa wananchi waweze kuishi bila kulipa hiyo kodi ya majengo kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la wigo wa kodi. Hapa tunalalamika sana juu ya mapato ya Serikali na mapato mbalimbali kwa ajili ya kuiwezesha Serikali yetu kufanya kazi vizuri. Wakati wa mchango wangu nilitoa ushauri kwamba Serikali iangalie namna gani itaweza sasa kuzipa majukumu taasisi zote za Serikali kwa maana ya Wizara zote za Serikali kuhakikisha kwamba zinakuwa na kitengo maalum kinachosimamia ajira kwenye sekta binafsi kwa sababu Wizara nyingi zimekuwa zenyewe sasa badala ya kukuza sekta binafsi ili ajira ikue ili tuweze kupata Pay As You Earn, zimekuwa hazijishughulishi kabisa na jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake zinavuruga kule kwenye sekta binafsi na kwa kuwa hazina jukumu la msingi la kuhakikisha kwamba mapato kupitia Pay As You Earn kutoka sekta binafsi yanakuwa ndiyo maana zinakuwa hazisimamii na zinaweza zikavuruga kabisa. Nilitoa mfano juu ya baadhi ya sekta za Serikali ambazo zinafanya shughuli kama hiyo.

Kwa hiyo, ningeomba sana Serikali ijitahidi sana itengeneze utaratibu rasmi ambao utasaidia sasa kuhakikisha kwamba kila Wizara, Idara ya Serikali kama kuna shughuli ya aina hiyo inafanywa na sekta binafsi basi iwekewe utaratibu rasmi ili iweze kuhakikisha kwamba na yenyewe inachangia na kukuza ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, Njombe tunapenda sana kulipa kodi na tuko tayari kulipa kodi lakini jengo letu la TRA kwa kweli linasikitisha sana. Ilikuwa ni kama vile nyumba ya kuishi au ilikuwa ni ofisi ndogo tu ya Mamlaka ya Pareto miaka hiyo na sasa ndiyo TRA Mkoa. Kwanza jengo ni dogo, limechakaa, linavuja lakini pia watumishi ni wachache sana. Wananchi wanakwenda pale kulipa kodi wanasubiri siku mbili yaani mwananchi yupo tayari kulipa kodi lakini anasubiria siku mbili msongamano ulioko ndani ya TRA ili alipe kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri nafikiri unanisikia, muangalie jengo la TRA Njombe mhakikishe kwamba Njombe wanapata jengo zuri na wanaweza kutoa huduma vizuri kwa wananchi. Maana haipendezi unaenda kulipa kodi halafu unapoteza na muda tena pale badala ya kwenda kufanya kazi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)