Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Lathifah Hassan Chande (9 total)

MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. LATHIFAH H. CHANDE) aliuliza:-
Mji wa Liwale umebakia kuwa ni Wilaya pekee ya Mkoa wa Lindi ambayo haijanufaika na umeme wa uhakika wa gesi asilia. Umeme unaotumika ni wa jenereta mbili za diseli za kW 800:-
Je, ni kwa nini Serikali isitenge fedha ili kuiunganisha Wilaya nzima ya Liwale na umeme wa gesi asilia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Liwale unapata umeme kutoka Kituo cha Kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta kilichopo Liwale. Hata hivyo, gharama za uendeshaji wa mitambo hiyo inayotumia nishati ya mafuta ni kubwa sana. Kutokana na hali hiyo, Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa njia ya umeme itakayounganisha Wilaya ya Liwale na Wilaya ya Nachingwea ambayo kwa sasa inatumia umeme kutoka Kituo cha Kuzalisha umeme cha Gesi Asilia kilichopo Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua iliyofikiwa katika mpango huo ni ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 14.5 kutoka Nachingwea hadi Kijiji cha Luponda, ambapo ni kilometa 73 kutoka Liwale hadi Kijiji cha Nangano. Kazi hiyo, ilianza mwezi Agosti mwaka 2014 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba mwaka huu. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 3.5 na kwa kweli, inaendelea vizuri. Hata hivyo, sehemu iliyobaki ya kilometa 45 kati ya Luponda na Nangano inatarajiwa kukamilika kupitia utekelezaji wa Mpango wa REA awamu ya tatu.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Uzalishaji wa zao la ufuta limeongezeka kwa msimu wa mwaka 2015/2016 na kusababisha kushuka kwa bei ya ufuta sokoni:-
Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda cha kukamulia ufuta Wilayani Liwale?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa mavuno ya zao lolote yakiongezeka, bei yake sokoni inaweza kushuka. Sera ya Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi iweze kujenga viwanda na kuwekeza katika biashara. Kufuatia uhamasishaji huo, Mkoa wa Lindi una jumla ya viwanda 11 vya kukamua mafuta, viwili vikiwa mahususi kukamua mbegu za ufuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jukumu la msingi la Serikali limebaki katika kuhamasisha sekta binafsi, Wizara itaendelea kuhamasisha wawekezaji ili kuwekeza katika usindikaji wa mafuta ya ufuta Wilayani Liwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Wizara yangu katika kuhamasisha wajasiriamali wa Wilaya ya Liwale waweze kuwekeza katika usindikaji wa mbegu za ufuta. Kiwango cha ufuta kinachozalishwa Wilaya ya Liwale kwa sasa kinakidhi uwekezaji mdogo na wa kati ambao wananchi na wajasiriamali waliopo wakihamasishwa wanaweza kuwekeza katika usindikaji wa mbegu za ufuta.
Mhesjhimiwa Mwenyekiti, mashine ndogo sana ya kukamua mafuta ya ufuta, inakadiriwa kuwa na gharama kati ya shilingi milioni 10 mpaka 15 na mashine ndogo ni kati ya shilingi milioni 16 mpaka 200. Mashine ya kati inayoweza kukamua na kuchuja mara mbili (double refinery) inagharimu kati ya shilingi milioni 200 mpaka 500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika wananchi wakihamasishwa wanaweza kujiunga katika vikundi na kuweka mitaji yao pamoja na kuweza kununua mashine ambayo ina uwezo wa kuchuja mara mbili (double refinery) yenye kuzalisha mafuta yenye soko zuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai pia kwa Waheshimiwa Wabunge wawahamasishe wananchi walio katika Majimbo yenye kuzalisha mbegu za mafuta waweze kushiriki katika kuanzisha viwanda vya kukamua mafuta kwa viwango mbalimbali. Wizara itakuwa nyuma yao kutoa ushauri na mafunzo ya kiufundi pamoja na kuelekeza mahali mashine zinapopatikana kupitia Taasisi zake za SIDO, TEMDO na TIRDO.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Asilimia 85 ya wananchi wa Mkoa wa Lindi ni wakulima wa korosho, ufuta na mbaazi. Pamoja na juhudi kubwa za uzalishaji, wakulima hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za ukosefu wa masoko, ucheleweshwaji wa pembejeo na kuongezeka kwa ushuru:-
(a) Je, ni lini Serikali itawashirikisha wakulima hawa katika upangaji bei hasa zao la korosho badala ya Bodi pekee ambayo inapanga bila kuangalia gharama halisi za kulima?
(b) Je, ni lini Serikali italianzisha tena soko la uhakika la mazao ya wakulima baada ya kulifunga lile la awali Wilayani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikishwaji wa wakulima na wadau wa korosho katika upangaji wa bei ya korosho na mjengeko wa bei ni kwa mujibu wa Sheria ya Korosho ya Mwaka 2009. Kwa hali hiyo, kabla ya kuanza msimu mpya wa soko la korosho, wadau hukutana ambapo Wawakilishi wa wakulima huwa zaidi ya nusu ya wajumbe wote na kukubaliana kuhusu bei dira. Bei hii huzingatia wastani wa gharama za uzalishaji wa korosho ghafi shambani na hali ya soko la nje kwa kipindi kisichopungua miezi sita iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya kuweka bei dira ni pamoja na kumwezesha mkulima kuhimili ushindani wa soko kwa kuwa na uhakika wa kurudisha gharama zake za uzalishaji wa korosho ghafi katika msimu husika, pia juu yake huwekwa asilimia 20 ya faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu wa kupata bei dira ya korosho hufanyika baada ya utafiti wa kina wa gharama za uzalishaji wa korosho na kumsaidia mkulima kupata bei yenye maslahi sokoni kupitia mfumo wa soko wa stakabadhi ghalani. Kwa mantiki hiyo, upangaji wa bei dira ya korosho unashirikisha wakulima na huzingatia gharama halisi za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzisha masoko ya mazao mbalimbali kadri itakavyoonekana inafaa.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Halmashauri ya Mji wa Liwale imetumia takribani shilingi milioni 540 katika ujenzi wa mradi wa umwagiliaji katika Kata ya Mtawango, lakini mradi huo umejengwa chini ya kiwango na hakuna thamani ya matumizi ya fedha (value for money).
Je, Serikali ipo tayari kwenda kukagua mradi huo na kufanya uchunguzi ili kubaini kasoro za mradi huo na kuwawajibisha wote watakaobainika kuuhujumu mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Chande, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umwagiliaji wa Mtwango upo katika kijiji cha Mtawango, Kata ya Mbaya, Tarafa ya Liwale, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Mradi huu uliibuliwa nawananchi mwaka 2008 na una jumla ya eneo la hekta 230.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za uboreshaji zilianza mwaka 2009 kwa kufanya upimaji na usanifu wa awali. Katika mwaka 2011/2012 mradi huo ulitengewa fedha kiasi cha shilingi milioni 220 kupitia Mfuko wa Wilaya wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji kwa ajili ya ujenzi wa banio, uchimbaji wa mfereji mkuu mita 1,000, ujenzi wa vigawa maji vinne. Kazi hizo zilifanyika na kukamilika kulingana na matakwa ya mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 mradi ulitengewa fedha kiasi cha shilingi milioni 184 kwa ajili ya kusakafia mfereji uliochimbwa na mita 1,000 kujenga vigawa maji nane, kujenga ukuta wenye urefu wa mita 250 kwa ajili ya kukinga mafuriko, kujenga kivusha maji na kivuko kwa ajili ya watembea kwa miguu na mitambo. Kazi hizo zilifanyika na kukamilika kulingana na matakwa ya mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kasoro alizobainisha Mheshimiwa Mbunge, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, itaunda timu ya wataalam kwa ajili ya uchunguzi na endapo itabainika kweli kuna hujuma katika mradi huo, hatua stahiki zitachukuliwa kwa wahusika.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Serikali ilianzisha mradi wa kupeleka maji kwenye Mikoa ya Shinyanga, Tabora na Dodoma toka Ziwa Victoria Mkoani Mwanza; mradi huu ulisaidia upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na shughuli za kilimo.
Je, kwa nini Serikali isianzishe mradi kama huu kutoa maji kwenye Mito ya Ruvuma na Rufiji kwa ajili ya wakazi wa Lindi na mikoa jirani ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji na kusaidia shughuli za kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza miradi miwili mikubwa ya kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara/ Mikindani na Miji ya Mangaka. Kwa upande wa Manispaa ya Mtwara/Mikindani, Wizara imekamilisha taratibu zote za manunuzi hadi kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara/Mikindani pamoja na vijiji 26. Kwa sasa kinachosubiriwa ni kusaini mkataba wa kifedha baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kupitia Benki ya Exim.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mji wa Mangaka upembuzi yakinifu wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka katika mji huo pamoja na vijiji 26 umekamilika mwezi Oktoba, mwaka 2016. Kwa sasa kazi ya usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uanzishwaji wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji, Wizara itaendelea kutafuta fedha za kufanya utafiti ili kuwa na michoro na thathmini ya kiutaalam ili kutayarisha andiko litakalosaidia kutafutwa fedha za utekelezaji wa mradi huo kutoka vyanzo vya ndani na nje ya Serikali. Malengo ya miradi hii yote ni kutoa huduma ya maji safi na salama. Pia Serikali itaangalia uwezekano wa kuanzisha miradi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Lindi na mikoa jirani.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Mtama (Cashewnut Factory) kilichopo katika Jimbo la Mtama kilikuwa chini ya Bodi ya Korosho na kiliuzwa kinyemela kwa Kampuni ya Lindi Farmers ambayo ilikodishwa kwa kampuni ya Kichina ya Sunshine Industries Limited, kampuni ambayo inawalipa wafanyakazi ujira wa shilingi 70 hadi 80 kwa kubangua kilo moja ya korosho.
(i) Je, Serikali ina taarifa ya kukodishwa kwa kiwanda hiki?
(ii) Je, Serikali inachukua hatua gani juu ya mazingira magumu ya wafanyakazi ambao hawana mikataba ya kazi katika kiwanda hiki ambacho kinamilikiwa na wageni?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Mtama kilibinafsishwa kwa kuuza hisa asilimia 100 kwa Kampuni ya Lindi Farmers Association ambayo inakimiliki. Kufuatia umiliki huo, kiwanda hicho kilikodishwa kwa makubaliano maalum kwa Kampuni ya Sunshine ili iweze kukiendesha.
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo taarifa kwamba Kampuni ya Sunshine Industrial Company Limited inaendesha kiwanda hicho kwa kubangua korosho kwa mkataba wa miaka mitano kuanzia mwaka 2013 hadi 2018 ambapo unahusisha kujenga, kuendesha na kuhamisha. Baada ya mkataba kumalizika mashine na mitambo vitakuwa mali ya Lindi Farmers Association. Uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni moja umefanyika tangu mkataba huo wenye gharama ya dola 100,000 kwa mwaka uliposainiwa.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuona viwanda vinafanya kazi na kuleta manufaa kwa Watanzania ikiwemo kutoa ajira, kulipa kodi na kuongeza thamani ya malighafi. Hata hivyo, msimu wa mwisho mwaka huu kiwanda hicho hakikupata korosho za kutosha kutokana na ushindani wa bei ya korosho ghafi na hivyo kupelekea wanunuzi kugombania korosho.
Mheshimiwa Spika, kuhusu usalama wa wafanyakazi viwandani, Serikali inaendelea kutoa wito kwa waajiri wote kuzingatia sheria za usalama kazini. Aidha, nitumie fursa hii kuzihimiza mamlaka zinazohusika na ukaguzi wa usalama kazini kusimamia kwa karibu sheria hizo. Pamoja na hatua hizo, waajiri wote wanapaswa kujiunga na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Fund – WCF) ulioanzishwa hivi karibuni na sheria yake kupitishwa na Bunge lako tukufu. Hii itawawezesha kunufaika pale wanapoumia kazini kutokana na majanga mbalimbali. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu tutaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria hiyo.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 6.4 kwa mwaka 2012 mpaka mwaka 2015 kwa ajili ya ukarabati wa kawaida wa barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye urefu wa kilometa 230 na barabara hii inawaunganisha watu wa Liwale na Wilaya za Lindi na Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam:-
Je, Serikali iko tayari kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Chande, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha kuwa kwanza makao makuu ya mikoa yote inaunganishwa kwa barabara za lami ambapo kwa sasa karibu mikoa yote nchini imeunganishwa kwa barabara za lami. Pili, kuunganisha nchi yetu na nchi za jirani kwa barabara za lami ambapo karibu 64% ya barabara kuu zimejengwa kwa kiwango cha lami. Tatu, ni kuhakikisha kuwa, barabara zote za mikoa ambazo nyingi zinaunganisha makao makuu ya Wilaya zinapitika majira yote ya mwaka. Kwa sasa barabara nyingi za wilaya zimejengwa kwa kiwango cha changarawe na zinapitika majira yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Chande, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nangurukuru – Liwale ni barabara ya mkoa inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi. Hivyo, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali yatakayoiwezesha barabara hii kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya shilingi bilioni 1.086 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya muda maalum na katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.76 kwa ajili ya kuendelea na ukarabati na matengenezo ya muda maalum kwa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015 imepanga kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Kwa sasa inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
MHE. LATHIFA H. CHANDE aliuliza:-

Wananchi wa Mkoa wa Lindi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya hali duni ya huduma za afya kwa kuwa na uchache wa Wauguzi, Madaktari wa kawaida na wa akina mama na uhaba wa vifaa na dawa, lakini pia Vituo vya Afya na Zahanati hazitoshi:-

(a) Je, ni lini Serikali itaongeza Wauguzi, vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale?

(b) Hospitali ya Ruangwa kwa kipindi kirefu imekuwa haina huduma ya X-Ray hali inayowalazimu wananchi wa Wilaya ya Ruangwa kufuata huduma hiyo Lindi: Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hilo?

(c) Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa nyumba za Wauguzi na Mganga Mkuu katika Zahanati ya Mtawango katika Kata ya Mtawango, Liwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Lathifa Hasan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, Lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliajiri watumishi wa kada mbalimbali za Afya 6,180. Kati ya hao, 89 walipangwa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imepokea jumla ya shilingi milioni 345.5 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Aidha, upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vyote 242 vya kutolea huduma za afya Mkoani Lindi kuanzia Januari hadi Desemba, 2018 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Liwale ulikuwa ni kwa zaidi ya asilimia 91.9.

(b) Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa ilifungiwa mashine ya X-Ray mwaka 2015 ambapo mpaka Desemba, 2018 Wagonjwa 7,250 wamehudumiwa. Ni kweli kuna wakati mashine hii ilipata hitilafu na ikashindwa kufanya kazi, lakini hitilafu hiyo ilirekebishwa na mashine ya X-Ray inaendelea kutoa huduma. Mpango wa Serikali ni kuipatia hospitali hii X-Ray ya kisasa.

(c) Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ujenzi wa Zahanati pamoja na nyumba za Watumishi Mtawango ulikuwa ni mradi unaofadhiliwa na TASAF katika mwaka wa fedha 2015/2016 kujenga nyumba mbili kwa moja (two in one), ambapo fedha zilizopangwa na kutumika ni shilingi milioni 27. Hata hivyo, fedha hizo hazikutosheleza kumalizia ujenzi wa nyumba. Hivyo, Halmashauri imepanga kutenga shilingi milioni 10 katika bajeti ya mapato ya ndani ya mwaka 2019/ 2020 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Muuguzi na Mganga katika Zahanati ya Mtawango.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y MHE. LATHIFAH H. CHANDE) aliuliza:-

Serikali iliahidi Mji wa Liwale Kufanyiwa usanifu wa mradi wa maji:-

(a) Je, ni lini mradi huo uliofanyiwa usanifu utakamilika na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa Liwale?

(b) Je, ni kata zipi zilizopo katika Wilaya ya Liwale ambazo zitanufaika na mradi huo wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa ruksa yako kwanza naomba nitoe pole kwa wananchi wa Pangani na Chama cha Mapinduzi na wanaCCM wote kwa kuondokewa na Mzee wetu ndugu Hamis Mnegerwa ambaye ni Mwenyekiti wa chama chetu Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Pangani. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amin.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Chande, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Liwale ili kutatua changamoto hiyo, Serikali inatekeleza mipango ya muda mrefu na muda mfupi. Kwa upande wa muda mfupi katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imekamilisha mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika Mji wa Liwale.

Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni ukarabati wa kituo cha kusukuma maji, ununuzi na ufungaji wa pampu, ununuzi na ulazaji wa mabomba, usambazaji maji umbali wa kilometa 16 pamoja na ununuzi wa dira za maji 200 kwa gharama ya shilingi milioni 264. Kukamilika kwa mradi huo kumeongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kutoka masaa matano kwa siku hadi masaa 12 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa muda mrefu, Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni ambazo kazi hiyo imepangwa kufanyika mwaka wa fedha 2019/2020. Kukamilika kwa kazi hiyo kutatoa gharama halisi ya utekelezaji wa mradi mkubwa katika Mji wa Liwale pamoja na kuainisha kata zitakazonufaika na mradi huo.