Primary Questions from Hon. Kunti Yusuph Majala (3 total)
MHE. KUNTI Y. MAJALA Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kike katika Shule za Msingi Birise na Donsee ambazo hazina walimu wa kike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, asante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya ukosefu wa walimu wa kike katika Shule ya Msingi Birise na Donsee zilizopo katika Halmashauri ya Chemba, Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imempeleka mwalimu mmoja wa kike katika Shule ya Msingi Donsee wakati ikiendelea na utaratibu wa kukamilisha kumpeleka mwalimu mwingine wa kike katika Shule ya Msingi Birise.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikijiandaa na mpango wa ajira na mgawanyo wa walimu wapya kwa Halmashauri zote nchini, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inazielekeza Halmashauri zote nchini kufanya msawazo wa walimu wa shule za msingi na sekondari kwa kuzingatia jinsia.
MHE. KUNTI Y. MAJALA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itasambaza umeme katika Kata za Handa, Lalta, Sanzawa na Mpendo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Yussuf Majala, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji ambavyo havijapata umeme katika Wilaya ya Chemba vikiwemo vijiji vya Kata za Handa, Lalta, Sanzawa na Mpendo vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ulioanza kutekelezwa mwezi Machi, 2021 na utekelezaji wa mradi huu utakamilika ifikapo Desemba, 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za mradi kwa Wilaya ya Chemba zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 umbali wa kilomita 681.4, msongo wa kilovoti 0.4 umbali wa kilomita 50, ufungaji wa transfoma 50 za 50kVA, pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali wapatao 1,100 kwa gharama ya takriban Shilingi Bilioni 27.3.
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto kubwa ya maji inayowakabili wananchi wa Mji wa Chemba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Yussuf Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya huduma ya maji inayowakabili wananchi wa Mji wa Chemba ambapo kwa sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni chini ya asilimia 50. Katika kutatua changamoto ya huduma ya maji katika mji huo, Serikali ina mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika katika mpango wa muda mfupi, kazi zilizopangwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika mji huo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ni pamoja na ujenzi wa matanki mawili ya kukusanya maji ya ukubwa wa lita 50,000, nyumba ya mitambo ya kusukuma maji, ununuzi na ufungaji wa pampu nne (4), ununuzi na ulazaji wa mabomba ya umbali wa kilometa 11.6. Kukamilika kwa kazi hizo kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita 50,000 kwa siku hadi lita 320,000 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali ilipata mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya Dola za Marekani millioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 nchini ukiwemo Mji wa Chemba. Maeneo yatakayonufaika katika utekelezaji wa Mradi huo ni pamoja na Paranga, Makamala, Kambi ya Nyasa, Gwandi, Chambalo na Chemba yenyewe. Ujenzi unatarajiwa kuanza wakati wowote katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 na umepangwa kutekelezwa kwa miezi 24.