Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Kunti Yusuph Majala (1 total)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: heshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, mkiwa bado kwenye huo mchakato wa kwenda kupitia sheria na mambo kadha wa kadha, hata wewe pia unafahamu kuwa changamoto kubwa iliyopo baina ya wakazi wa Manispaa ya Dodoma na CDA, nini tamko lako kwa CDA kuhusiana na bomoabomoa zinazoendelea bila wananchi hao kulipwa stahiki zao?

Jambo la pili, endapo hamtakamilisha huo mchakato, mnawaambia nini Watanzania wa Manispaa ya Dodoma kwamba ahadi iliyotolewa ilikuwa ya uongo na kuwarubuni Watanzania ili mpate kura then muwapotezee? Kama msipofanya hivyo mnawaambia Watanzania wasiwachague tena kwa sababu mmekuwa na ahadi za uongo zisizotekelezeka? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimwambie usiwe na mashaka ya utekelezaji wa Ilani zetu na kwamba umeanza kutanguliza majibu ya wananchi msiwachague tena hilo siyo lako, wewe subiri tutekeleze ahadi zetu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Dodoma wakiwemo na wananchi wa Manispaa, jambo muhimu hapa ni kufanya maboresho ya Mji wa Dodoma ambako ni Makao Makuu ya Serikali. Kama ambavyo nimeeleza kwenye maelezo yangu ya msingi kwamba tayari Tume imeshaundwa wanaendelea kuharakisha zoezi hilo la kuhakikisha kwamba tunaondoka kwenye sheria iliyounda CDA ili kurudi kwenye sheria tuweze kuifanya CDA iweze kufanya kazi zile ambazo zitampa mwananchi haki ya kuweza kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo swali ambalo limesema wale ambao wanabomolewa na CDA, sasa hili ni lazima tufanye mapitio CDA utaratibu wanaoutumia, wanabomoa kwa ajili ya nini na je, maeneo hayo na wale wanaobomolewa wanatakiwa kupata stahili ya namna gani. Kwa sababu sheria tuliyonayo inamtaka popote ambako unataka kupatumia kwa kuondoa mali ambayo mwananchi amewekeza lazima uilipie fidia.

Kwa hiyo sheria ipo, lazima tuone tufanye mapitio tuone CDA sasa wanaendesha operation wapi na wanalipa au hawalipi ili tuweze kujua kama hawalipi kuna sababu gani za msingi za kutolipa, lakini haki ya kulipwa ipo pale na ninaamini CDA ipo ofisini kwangu, kwa hiyo nitafanyia mapitio halafu nitakupa taarifa.