Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kunti Yusuph Majala (17 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii nami katika Bunge hili niweze kuchangia Wizara inayoamua Watanzania leo tuendelee kuishi ama la. Wizara ya Afya ni Wizara nyeti sana, ndiyo inayosababisha sisi leo tuko humu ndani tukiwa na afya njema pamoja na Mwenyezi Mungu kutujalia. Wizara hii ni Wizara ambayo bado inachechemea. Wizara ambayo inakwenda kuamua hatima ya maisha ya Mtanzania, bado tunakwenda kuiletea mzaha na kufanya ushabiki kwenye maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni takribani miaka 55 ya uhuru, hatuna Vituo vya Afya ndani ya Kata zetu 3,990. Tuna vituo vya afya ambavyo havifiki 500, halafu tuko humu ndani leo tunajisifu, tunapongezana kwa makofi eti kana kwamba tunakwenda kufaulu. Hatufaulu, tunarudi nyuma na tunaendelea kutokuwatendea haki Watanzania. Hali ya hospitali zetu kwenye maeneo yetu tunakotoka; tuachane na hospitali hizi za mjini, hebu twende kule vijijini. Mheshimiwa Waziri hotuba yake nikiiangalia na kuisoma imelenga maeneo ambayo yako hapa mbele yetu. Haijatugusa kule vijijini!
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijijini hospitali zetu zinasikitisha, zinatia huruma, wananchi wetu wanapata tabu. Hospitali zisizokuwa na maji! Hospitali zisizokuwa na umeme. Mbali na maji na umeme, lakini hospitali hizi hazina Wauguzi, hazina Madaktari, hazina madawa! Tunawatakia nini hawa Watanzania? Shida yetu ni nini? Si mtwambie Chama cha Mapinduzi miaka 55 mmeshindwa kuleta hoja ya msingi ya kuweza kuokoa maisha ya Watanzania! Tunabaki tunapigiana makofi humu ndani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuachane tu na suala zima la hali mbovu za hospitali, uwepo wa hizo hospitali zenyewe! Mkoa wangu wa Dodoma wenye Wilaya saba, tuna Wilaya nne tu ndiyo zina hospitali; Wilaya tatu hizi hazina Hospitali za Wilaya. Mnaweza mkasema Wilaya ya Chemba ni mpya, Wilaya ya Bahi ni mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chamwino ambayo awali ilikuwa inaitwa Wilaya ya Dodoma Vijijini mpaka leo ambako Ikulu ipo ya Chama cha Mapinduzi, hawana hospitali wale wananchi! Wanatoka Vijiji vya Chamwino, Mtera huko imepakana na Iringa wanasafiri kuja Manispaa ya Dodoma kupata huduma. Hivi mnawatakia wema kweli hawa Watanzania wa Mkoa wa Dodoma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambieni tu ndugu zangu, katika mikoa ambayo inawakoa, bado inasuasua ni Mkoa wa Dodoma ndiyo ambao angalau mnaambulia, lakini Waswahili wanasema usimwamshe aliyelala, utalala mwenyewe. Ipo siku wananchi hawa watakuja kuchoka na mateso na ahadi kila kunapokucha, mnaenda kuwaahidi kwamba tutawaleteeni hospitali ambazo hamzipeleki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma zinazotolewa kwenye hospitali zetu, wenzangu wamesema, naomba niongezee. Niende huduma zinazotolewa kwenye huduma ya mama mjamzito. Huduma zinazotolewa kwenye hospitali zetu kwa mama mjamzito, zinawakatisha tamaa wanawake kwenda hospitalini ndiyo maana wengine wanaamua kuzalia majumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa kike ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 kwa Dini ya Kiislamu mtoto anaweza kuolewa hata miaka 14, 15, 16; mtoto huyu akiolewa akipata ujauzito akienda hospitalini kwa ajili ya kujifungua, hapewi huduma. Atapewa kashfa kibao, atapewa matusi ya kila aina na kumsababishia mtoto yule hata kukosa ujasiri wa kwenda kutimiza wajibu na jukumu lake katika Taifa lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha hizi zinatusababishia vifo vingi vinavyokwenda kuwapoteza akinamama, vinavyokwenda kuwapoteza watoto ambao tunahitaji kesho na wao waje watupokee mzigo huu tulionao katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wanawake ambao wana umri mkubwa kuanzia miaka 40, hawa nao imekuwa ni changamoto kwenye hospitali zetu. Wakifika Hospitalini, “limama jitu zima, limebebelea limimba mpaka leo linazaa! Hizo ni lugha ambazo zinatolewa na wafanyakazi wetu kwenye hospitali zetu. Mheshimiwa Waziri wewe ni mwanamke, unajua uchungu wa kuzaa…
MWENYEKITI: Siyo wote ni baadhi! Ni baadhi, siyo wote!
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni baadhi!
Mheshimiwa Waziri unajua jinsi wanawake tunavyopata tabu, lakini kuna mwanamke mwingine yawezekana kwenye usichana wake amehangaika kupata mtoto ameshindwa. Imefika umri wa miaka 40 huyu mtu kabahatika kupata hiyo mimba, asizae? Kwa nini baadhi ya hawa watumishi wasipewe onyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona wiki iliyopita Mbeya, Muuguzi alichomtendea yule mama aliyekuwa anajifungua pale, Mkuu wa Mkoa alikwenda pale hospitalini. Yule mama anaeleza kwa uchungu namna alivyofanyiwa na mhudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli tunataka kuwatendea haki hawa wanawake? Tunataka kweli wanawake hawa waendelee kuja kwenye hospitali zetu kwa ajili ya kupokea kejeli, matusi na kashfa! Ya kazi gani? Vifo vya wanawake vinasababishwa na hizi kashfa; wanawake wengi wanashindwa kwenda hospitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake pia tunashindwa kwenda Hospitali kujifungua mahali salama; siyo salama, pale napo tunakwenda kutafuta vifo vingine. Ukienda hospitalini, kaka yangu Mheshimiwa Kuchauka amesema, unaambiwa mwezi wako wa mwisho, mwezi wa Nane unaenda wa Tisa kwenda kujifungua, utaambiwa unapokuja njoo na ndoo; maeneo ambayo hayana maji, anaambiwa aende na maji mama mjamzito. Maeneo ambayo hayana umeme, mama anaambiwa aende na taa au mafuta ya taa ili aweze kupata huduma ya kuweza kutimiza wajibu wake na majukumu katika Taifa letu ya kuongeza Watanzania katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CHF, janga la Taifa hili. Tunawatwisha Watanzania mzigo juu ya mzigo. Mmeshindwa kupeleka dawa; ili mjifiche kwenye kichaka, mmeamua kuwaundia mradi unaoitwa CHF mwendelee tena kukusanya fedha zao, wakienda hospitalini hakuna dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, CHF hii watu wetu wamekwenda kujiunga; akienda hospitali na kadi ile akifika fursa pekee anayoipata kwenye ile kadi ama huduma pekee ni kwa ajili tu ya kumwona Daktari. Akitoka kwa Daktari, amepata dawa ni paracetamol. Awe anaumwa tumbo atapewa paracetamol, awe amevunjika mguu atapewa paracetamol, awe anaendesha atapewa paracetamol. Ugonjwa wowote huduma pekee atakayoipata ataambiwa paracetamol ndiyo dawa atakayoipata pale, akipata bahati sana ya kupata dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huyu mwananchi anauliza, hivi nimeambiwa na Serikali yangu nijiunge kwenye Mfuko huu ili niweze kuokoa maisha yangu. Hata pale ninapokuwa sina fedha nipate huduma, lakini leo hii wananchi wetu wametoa fedha zao na badala yake wanaenda kuambulia maneno ama kuoneshwa maduka ya kwenda kununua dawa. Mradi huu siyo rafiki kwa Watanzania. Mheshimiwa Waziri tunaomba aje na mbadala wa biashara hii ya CHF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata miradi mingine ya Bima ya Afya, NHIF; ukienda na kadi ile, ukifika pale, kwanza kabla hata hujaitoa, unauliza jamani dirisha la Bima ya Afya liko wapi? Bima ya Afya? Eeh! Mhudumu anaweza akakukata kushoto akaendelea na safari zake. Kama uko kwenye foleni hujauliza chochote, unaulizwa; unatibiwa cash au una Bima? Ukimwambia una Bima, anakwambia subiri, kaa pale! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe Wabunge imetutokea, mimi nikiwa ni mhanga. Nimeenda Dar es Salaam Agakhan pale. Nimefika nikawaambia naumwa, nina Kadi ya Bima ya Afya – NHIF. Nikaambiwa, dada tunaomba usubiri pale. Nilisubiri zaidi ya dakika 45, nikaona haina sababu ni heri ninyanyuke nijiondokee zangu nikatafute hospitali nyingine nitoe fedha niweze kutibiwa. Sasa sisi kama tuko humu ndani yanakuwa namna hiyo na hizo kadi zenu mlizotupa, walioko kule nje hawa ambao mnawakatia hivi vikadi vyenu inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, nami nianze na suala zima la maji. Suala hili limekuwa ni changamoto kubwa sana kwa Watanzania wa nchi hii. Nitazungumzia suala la maji kwa Manispaa ya Dodoma, lakini pia nitazungumzia suala la maji kwa Wilaya ya Chemba.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Chemba tuna Mradi wa Maji Ntomoko. Mradi huu umeanza mwaka 2014 na ulikuwa una gharama ya shilingi bilioni 2.8. Mradi huu ulitakiwa kuhudumia vijiji 18 lakini ni kwa bahati mbaya sana katika vijiji 18 vijiji nane vikaondolewa vikabaki vijiji 10. Kati
ya hivyo vijiji 10 hivi ninavyoongea hakuna kijiji hata kimoja ambacho kimepata maji kutokana na mradi huo na mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 2.4, maji hakuna.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Ntomoko ulidhamiria kupeleka maji kwenye kituo cha afya ambacho kinatumika kama Hospitali ya Wilaya ya Chemba. Hospitali ile haina maji, miundombinu ya maji imeshaharibika. Mwanamke mjamzito anapokwenda hospitalini kupata huduma ya kujifungua sharti ndugu zake waende na ndoo ya maji kichwani ili mwanamke yule aweze kupata huduma ya maji. Kama ndugu zake wakishindwa kwenda na maji mwanamke yule atapata huduma ya kujifungua, atafungashiwa uchafu wake atakwenda nao nyumbani kwake kwenda kupata huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la maji ni kero katika Taifa letu, ni shida katika nchi hii. Tatizo la maji katika Taifa hili siyo suala la upatikanaji wa vyanzo vya maji kwani tunavyo vya kutosha sana. Shida ya Taifa hili ni mfumo wa namna ya kuyasambaza maji hayo kuwafikishia Watanzania kwenye maeneo yao, vyanzo vya maji vipo vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maji ya Ntomoko ninayokwambia siyo maji unayokwenda kuyachimba bali ni maporomoko ya maji unakwenda kuyatega wananchi wanapata maji, imekuwa ni shida kweli kweli. Shilingi bilioni mbili watu wamelamba, wamekaa kimya, Watanzania wanapata shida na suala la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi niseme ule mradi kwa kuwa ulikuwa ukamilike mwezi wa Pili mwaka huu umeshindikana na hakuna sababu zozote za msingi ambazo Watanzania wa Wilaya ya Chemba wanapewa, tunaomba huo mradi uondolewe kwetu ili tutafutiwe mradi mwingine mbadala utakaoweza kuleta tija na utakaofanya wananchi wetu waweze kupata maji. Nimeamua kulisemea hili kwa Waziri Mkuu ili na yeye aweze kuona kwa jicho la pekee sana hususani kwenye ile hospitali ambayo watu wanakwenda kupata huduma pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye suala zima la maafa. Mfuko wa maafa uko kwenye ofisi ya Waziri Mkuu. Kama unavyojua nchi yetu imekumbwa na ukame na hali ya chakula katika Taifa letu siyo nzuri kwenye maeneo kadhaa na hususan katika Mkoa wangu wa Dodoma hali ya chakula ni mbaya sana. Nilisema hapa siku ya Jumatatu kwenye briefing kwamba Watanzania wa Mkoa wa Dodoma
kuna njaa ya kutosha na imekithiri.
Mheshimiwa Spika, hapa ninapoongea, debe la mahindi Dodoma Mjini hapa sokoni pale Mwembeni na Majengo ni Sh.23,000, kilo ya mahindi wanapima Sh.1,250. Kondoa debe ni Sh.25,000, Chemba ni Sh.27,000, Kongwa kwako pale Kibaigwa ni Sh.22,500. Sijaona kwenye kitabu cha Waziri Mkuu akituambia suala la ukame katika Taifa hili katika yale maeneo ambayo yana changamoto ya bei kubwa za mazao ni nini amekifanya au anatarajia kufanya kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii si sawa, hatuwatendei haki hawa Watanzania wetu. Watu wanakufa, watu wanajiua, wanaume Wilaya ya Kondoa wawili wameamua kujiua kwa sababu familia zao zimekosa chakula kwa muda wa siku tatu. Wanaume wanakimbia familia zao, wanawake ndiyo
wanaobaki kwenye majumba na watoto wao lakini mwanamke huyo naye mvua Dodoma safari hii haijanyesha ya kutosha. Hata vibarua mwanamke aende akalime apate fedha ya kununua kilo ya mahindi hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningetaka kujua ni lini Serikali itatuletea chakula watu wa Dodoma. Tunahitaji chakula watu wa Dododma na naamini hata wewe unahitaji chakula kwa ajili ya watu wa Kongwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu watu wa Dodoma tunaomba yale mahindi yanayooza Shinyanga tani 8,000 tunazihitaji watu wa Dodoma tuna shida na chakula, acheni kuozesha chakula wakati watu wanakufa kwa njaa. Kama ninyi upande wa pili hamuwezi kusema sisi tuacheni tuseme, tuko hapa kwa ajili ya kuwasemea Watanzania. Hatuko hapa kwa ajili ya kuona nafsi zetu ziko salama lakini kesho tutakuwa huko na sisi mitaani maana yake kazi hii siyo ya kudumu. Niombe nipate ufafanuzi kwenye suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye suala la Mahakama. Mahakama zetu zimekuwa ni changamoto kubwa sana hususani kwenye upande wa watumishi, lakini pia kwenye suala zima la miundombinu kwa maana ya majengo yako. Wilaya yangu ya Chemba haina hata hiyo
Mahakama ya Wilaya tu.
Mheshimiwa Spika, pili, Mahakama hizi za Mwanzo ambazo ziko kwenye Kata zetu kule chini ziko kwenye nyumba za watu ambao wamejitolea, lakini hata hao wahudumu unakuta kuna Karani mmoja na Hakimu mmoja anayeweza kuzunguka kwenye Kata zaidi ya nane, ameenda Kata chache sana ni Kata tano. Tuone ni namna gani tunaongeza Watumishi kwenye sekta hii ama kwenye Wizara hii ya Mahakama ili wananchi wetu waweze kupata huduma hii kwa urahisi lakini pili kwa uharaka ili waweze kuendelea na shughuli zingine. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, lingine ni migogoro ya ardhi. Kaka yangu Mheshimiwa Shabiby amezungumzia tu mgogoro wa kwako kule pamoja na kwake. Kuna mgogoro kama huo wa Kiteto, mgogoro uliko baina ya Wilaya ya Chemba pamoja na Wilaya ya Kiteto ukiwa unahusisha hifadhi ya WMA-Makame. Wananchi wanakufa kule, hakuna vyombo vya habari vinavyoweza kuwamulika watu kwa namna gani wanavyokufa.
Mheshimiwa Spika, hayo matrekta yamechomwa moto hivi ninavyoongea, watu wameshapigwa, kuna watu 18 wameshafungwa jela, Mahakama ya Kiteto lakini kuna watu 27 wapo lock up Kiteto mpaka leo. Kwa hiyo, suala hili la migogoro tungeomba sana lishughulikiwe. Wabunge tuliambiwa tuorodheshe migogoro iliyoko katika maeneo yetu, tumeorodhesha migogoro hii kwa nchi nzima lakini hatupewi ripoti migogoro hiyo imesuluhishwa kwa namna gani na imeishia wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kuona suala la migogoro ya ardhi ndiyo itakayokwenda kutuletea vita ya wenyewe kwa wenyewe. Bila kumaliza migogoro ya ardhi ndoto za kufikia Tanzania ya Viwanda ni hadithi za Abunuwasi. Haitakuwepo kwa sababu ardhi hiyo ndiyo tunayoitarajia Watanzania wetu waweze kutafuta malighafi mbalimbali ili tuweze kuendesha hivyo viwanda ambavyo tunavisema leo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana mgogoro wa Kiteto pamoja na Chemba ambao unahusisha pia Makame-WMA ambayo iko Kiteto ambayo hifadhi ile inawanufaisha watu wa Kiteto basi ufanyiwe kazi kwa haraka ili wananchi wale waweze kupata maeneo yao ya kuweza
kulima na waweze kujijengea uchumi wa familia zao lakini na Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa muda ulioweza kunipatia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa machache niliyonayo kwenye Wizara hii muhimu ambayo inakwenda kuwahudumia Watanzania walio wengi. Kwa kuanza, nami naomba niungane na wenzangu kwenye suala zima la TARURA. Kwenye suala zima la TARURA nitaomba niende kwenye muktadha tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunapitisha hapa hii taasisi ya TARURA, mwaka 2017, Serikali ilituhakikishia kwenda kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watumishi wetu ili waende wakatimize wajibu na majukumu yao kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania. Hata hivyo, ninapata kigugumizi na sijui ni kwa nini? Serikali baada ya kuletewa TARURA ikatoa watumishi, wahandisi (engineers) waliokuwa kwenye Halmashauri ikawapandisha na kuwapa nafasi mbalimbali; Meneja wa Wilaya, Meneja wa Mikoa na Wakurugenzi. Baada ya kuwakabidhi majukumu hayo, watu hawa tunavyoongea mpaka leo hii, muda huu nimesimama, dakika hizi ninazoongea, watu hawa kuanzia Meneja wa Wilaya, Meneja wa Mkoa na Wakurugenzi wote, miaka minne kasoro hakuna hata mtu mmoja mwenye barua ya kuthibitishwa kazini kwenye nafasi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu watu hawa wana barua za kukaimu. Wanakaimu miaka minne kasoro, lakini Serikali mpo, halafu ni Ofisi ya Rais, ambayo inakwenda kuhudumia Watanzania walio wengi kwenye Sekta muhimu inayokuza uchumi wa Taifa letu kutokana na kilimo! Mtu ambaye amethibitishwa kazini ni mtu mmoja tu, Mkurugenzi Mkuu wa TARURA, baba yangu Victor ndiye amethibitishwa kazini. Mtu ambaye alifanya kazi hii kwenye Taifa letu na ninatambua mchango wake mkubwa, amelitumikia Taifa lake, akastaafu, lakini akarudishwa tena kwa mkataba, yeye ndio mwenye barua ya kuthibitishwa kazini, wenzake wote wana barua za kukaimu mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Ummy, nakuamini katika uwajibikaji na uchapaji kazi. Kama tunataka kuwasaidia Watanzania na kukuza uchumi wa Taifa letu na watumishi wetu waweze kufanya kazi vizuri kwenye taasisi hii, naomba ukitoka hapa, kesho tunahitimisha bajeti yako, nenda kaanze na suala zima la kuhakikisha watumishi wetu wote wa ngazi ya Wilaya na Mkoa, Wakurugenzi wapate barua zao za kuthibitishwa kazini. Kama mnaona hawafai, waondoeni, tafuteni watu wanaofaa, wapeni mamlaka waweze kufanya kazi. Siyo kuwakaimisha watu miaka minne, ni kitu ambacho hakiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zinazokwenda kutokana na kukaimisha watu hawa na kutokuwa na mamlaka ya kwenda kutimiza wajibu na majukumu yao ripoti ya CAG inatuambia kutokana na udhaifu huo, TARURA kwa miaka mitatu mfululizo, nitaisema miwili tu mfululizo, imebaki na bakaa. Yaani fedha ambazo zimebaki bila kwenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2018/2019 TARURA walibaki na bakaa ya shilingi bilioni 72.3 ambazo leo Wabunge tunapiga kelele humu ndani zingeweza kwenda kufanya kazi. Hakuna mtu wa kufanyia maamuzi, yuko mtu mmoja pale, kazi zimelala, fedha zinarudi, halafu bado sijui tunataka kufanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019/2020 shilingi bilioni 1.5 ziko pale, zimerudi. Barabara tunalalamika, miundombinu ni mibovu, wananchi wanakufa barabarani kwa kukosa huduma za barabara, akina mama wajawazito wanashindwa kwenda kujifungua watoto wao, wanajifungulia barabarani kwa sababu tu ya jambo dogo ambalo tunatakiwa tulisimamie ili watu wetu waweze kupata hiyo huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu twende tukafanye hii kazi ya kwenda kuwathibitisha hawa watu kazini ili tuweze kufanya kazi ya kulijenga Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala zima la posho za Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Vijiji. Tuna chaguzi mbili; tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu. Madiwani tunafanya nao uchaguzi pamoja. Tukija kwenye suala la malipo tunawabagua Madiwani wakalipwe na Halmashauri kwenye mapato ya ndani, wakati watu hawa ndio tunaokwenda nao katika uchaguzi wetu. Ni kitu gani kinachosababisha Madiwani wetu wasiwekwe kwenye mfumo wa Serikali wa kulipwa mishahara yao na posho zao ili waweze kutimiza wajibu na majukumu yao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Madiwani leo ndio watendaji wetu wakuu kule chini. Sasa hivi tuko humu Bungeni, vikao vya Mabaraza ya Madiwani vinaendelea kule. Wao ndio wanaojua nini kinachoendelea kwenye kata zao, lakini watu hawa hawathaminiwi, tumewasahau. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali, tuone ni namna gani tunawatoa Madiwani wetu kuwaleta kwenye Serikali Kuu; mishahara walipwe na Serikali Kuu na vikao vyao pia vigharamiwe na Serikali Kuu ili tuachane na biashara ya kuendelea kuwakopa Madiwani kila mwaka na kila vikao na vikao vingine havifanyiki kwa sababu Wakurugenzi wanakuwa na kigezo cha kwamba hakuna fedha, kwa hiyo, siwezi kuitisha baraza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la Wenyeviti wetu wa Vijiji, Mitaa pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji na Wajumbe. Watu hawa nao pia ni watu ambao wanafanya kazi kubwa sana. Tukae tukijua Wenyeviti wa Vijiji pia ndio wanaoishi huko na ardhi zetu za vijiji ambavyo leo vimekuwa na migogoro mikubwa, chanzo kikubwa pia ni Wenyeviti wetu wa Vijiji kwa sababu hawana chochote mkononi.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanakwenda kule wanatafuta ardhi na Mwenyekiti akiambiwa bwana, Mwenyekiti mimi nina shilingi 50,000 hapa, wewe nikatie hapa kidogo tu. Mwenyekiti anaona sasa hii shilingi 50,000 wakati wewe umenisahau, nifanye nini? Anamkatia eneo pale, anachukua shilingi 50,000 yake, maisha mengine yanaendelea, tunakuja kurudi kwenye timbwili la kuanza kusuluhisha migogoro kwamba mimi nilipewa na Mwenyekiti wa Kijiji, huyu anasema hii ilikuwa ni hifadhi, huyu anasema vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Wajumbe wa Vijiji pamoja na Mitaa, watu hawa tukiwatoa Madiwani wakaenda Serikali Kuu, tuwarudishe Wenyeviti wetu wa Vijiji walipwe na Halmashauri kwa sababu tunakuwa tumeipunguzia Halmashauri mzigo wa kulipa Madiwani na hivyo waende wakaanze kuwalipa Wenyeviti wetu wa Vijiji kupitia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la ahadi ya shilingi milioni 50 kila Kijiji. Uchaguzi wa mwaka 2015 kwenye Ilani ya Chama cha Mpainduzi mliwaahidi Watanzania kuwapatia shilingi milioni 50 kila kijiji ili waweze kukuza uchumi kwenye maeneo yao.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ahadi iliyotolewa ilikuwa ya mwaka 2015 – 2020, nasi tulienda tukawaeleza wananchi juu ya jambo hilo kwamba tuliahirisha kufanya mambo mengine. Kwa hiyo, Ilani inayotekelezwa sasa ni 2020 - 2025. Kwa hiyo, hayo ya nyuma hayako kwenye tender hiyo sasa hivi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru naomba niendelee, nam-ignore tu Mheshimiwa Getere. Nimefunga, kwa hiyo, naomba aniache tu nisije nikatengua swaumu yangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaahidi wananchi wetu shilingi milioni 50 kwa ajili ya kwenda kuhuisha uchumi wao kwenye maeneo yao, lakini kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambaye yeye ndiye anaye-deal na vijiji vyetu, sijaiona hiyo milioni 50 humu. Nakumbuka mwaka 2017, nilichangia kwenye bajeti kuu ya Serikali na nikaambiwa…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mnzava.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe Taarifa mzungumzaji anayeendelea kwamba, ahadi ya milioni 50 ya kwenye ilani ya mwaka 2015 ilitekelezwa kwa namna mbalimbali ikiwemo kupeleka mikopo kupitia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri. Kwa sababu ya utekelezaji wa namna hiyo ndio maana wananchi walikiamini tena Chama Cha Mapinduzi kikashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa mwaka 2020. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hizi ahadi kila ahadi ilikuwa inajitegemea. Waliahidi vituo vya afya, waliahidi maji kumtua mwanamke ndoo kichwani, waliahidi barabara ambazo wameshindwa kuwathibitisha hata watendaji wa TARURA na waliahidi milioni 50. Kwa hiyo, tunachokitaka nataka kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI milioni 50 ya kila Kijiji ambayo ilani yao hiyo, kama watakuwa wanaandika ilani kila baada ya miaka mitano wanasema hii ilipita hatuwezi kutekeleza tunaanza na mpya, Waheshimiwa basi kwa kweli, tusiendelee kuwaibia Watanzania kwa style hii, lakini kama tunaendeleza yale yaliyokuwa yamebaki…

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hii itakuwa Taarifa ya mwisho. Mheshimiwa Agness Mathew Marwa.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa Taarifa kwa muongeaji kwanza anatoa lugha ya maudhi, lakini kingine anatakiwa ajue kwamba, mpaka sasa hivi muda bado. Mama atayatekeleza yote, kwa hiyo, aache kashfa. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti malizia sekunde zako chache zilizobaki.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikushukuru. Hata ninyi wenyewe mmepoteana huko, yaani hamjui nini ambacho mnakifanya, kwa hiyo, mimi niwashauri tu na najua Mheshimiwa Mama Samia ni mwanamke ambaye anaweza kusimama na anasimama. Nina hakika atakuwa amenisikia na atakwenda kuwapoza Watanzania hiyo milioni 50 ili isiwe ahadi ya uwongo. Naye tunamwamini na mwanamke siku zote akimuahidi mtoto wake kwamba, nitakuletea pipi, basi akitoka akirudi anakuja na pipi, atakwenda kutekeleza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dakika chache ama sekunde chache zilizobaki, naomba niendelee na suala zima la mikopo ya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu kama wenzangu walivyosema. Mikopo hii kwenye halmashauri zetu nyingi imekuwa ni mikopo kichefuchefu naweza nikasema. Kwanza vikundi vinavyokopeshwa vina walakini na vikikopeshwa fedha hizo hazirudi, zikichukuliwa zimechukuliwa jumla. Ukihoji hakuna maelezo yoyote ya kina ya kutosha yanayokwenda kutoa majibu kuhusiana na mikopo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hii tulisema tuwapatie wanawake wetu na vijana na watu wenye ulemavu ili kuweza kupunguza familia tegemezi ambazo Serikali imekuwa ikiendelea kutoa mchango kwenye kupitia mfumo wa TASAF kwenda kuzisaidia familia tegemezi ama familia maskini. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara ya TAMISEMI iweze kuona na kufuatilia suala zima la mikopo hii ya asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa muda wako na Mungu akubariki sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali ambayo mwaka jana wakati tunachangia bajeti humu ndani ilijinasibu sana na tukawa tunaambiwa Waheshimiwa Wabunge tulieni bajeti ni ya kwanza.

Mimi jinsi ninavyoamini kati ya awamu zote zilizopita na zinazoendelea naweza nikasema kuwa, awamu itakayofanya vibaya na Watanzania watakuja kulia sana ni Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnawaahidi Watanzania mnaacha kutekeleza mliyoyaahidi mnakuja mnatekeleza mambo tofauti na vile mlivyoahidi, yaani mnaimba kama malaika mnakuja kucheza kama mashetani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mliwaahidi Watanzania kuwajengea barabara….

TAARIFA .....

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kuweza kuniruhusu niweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, wakati wagombea wakijinadi na vyama mbalimbali vikijinadi kwa Watanzania, vilikuwa vinanadi mambo mbalimbali ama shughuli mbalimbali za kijamii ambazo vyama hivyo


vitatekeleza kama vitapewa ridhaa.Mliwaahidi Watanzania kuwajengea barabara ili ziweze kupitika kwa mwaka mzima kipindi cha masika na kipindi cha kiangazi, hamjajenga barabara hata moja, mnawapelekea Watanzania waende wakawalipie motor vehicle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hujajenga barabara unaenda unampelekea mwananchi wa kijijini akakulipie motor vehicle na Wabunge mko humu ndani mnapiga makofi, wananchi wenu kule vijijini barabara zisizopitika kipindi cha masika waende wakalipe hii motor vehicle hii siyo sawa, kwenye Ilani ipi ya Chama cha Mapinduzi mstari upi, ukurasa gani uliandika kwamba mtaenda kuwalipisha Watanzania motor vehicle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii motor vehicle mmeamua kwenda kuwapelekea Watanzania kwa kupandisha mafuta ya taa, diesel na petrol yaani leo Watanzania wa nchi hii, umeme ni anasa, walibakia na mafuta ya taa, nayo mafuta ya taa yanaenda kuwa anasa kwa Watanzania. Mnaturudisha enzi za huko nyuma zama za kale za kwenda kuanza kutembea na vijinga kwenye vyumba kwa nini tunawafanyia Watanzania vitu vya namna hii ninyi? Hivi kwa nini hamna moyo wa huruma! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokwenda kupandisha mafuta ya taa wakati umeme umeshindwa kuwafikishia Watanzania unakwenda kuendeleza kumdhoofisha Mtanzania maskini aendelee kuwa maskini mpaka siku yake ya kufa, hii inajidhihirisha kuwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Ilani yenu inajidhihirisha kuwa hamjawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kwenda kuwaondoa Watanzania kwenye umaskini na ndio maana mnachokiadi hamtekelezi na mnajua mkitekeleza watu hawa wakiwa na uwezo wakawa na uchumi wao kwa story zenu hawatawachagua, kwa hiyo, mnabakia kila siku mnaahidi hiki mnaenda kutekeleza kitu kingine ili baada ya miaka mitano ikiisha mrudi tena kwenda kuahidi namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili suala la


kwenda kuhamisha motor vehicle kuwapelekea Watanzania waende wakalipe si sawa, si sawa kuwahamisha yaani motor vehicle ya Kunti nimpelekee mtu mwingine kule kijijini aende akanilipie motor vehicle, kila mmoja aende atimize wajibu na majukumu yake, Watanzania wale hawajatutuma sisi tununue magari, ni Watanzania wangapi wenye magari? Watu wengi waliopo vijijini hawana magari kwa hili suala nadhani halikai sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Wabunge mnasema kwamba eti ile shilingi 40 iende kwenye maji, unakumbuka tulipendekeza hapa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji tulisema tutoe shilingi 50 iende kwenye maji, leo mnasema 40 iende kwenye maji, aliyewaambie inaenda kwenye nani? Nani aliyewaambieni inaenda kwenye maji? Hii inapelekwa badala ya motor vehicle, motor vehicle itakatwa kule tukinunua mafuta ndio umelipa motor vehicle, kwa hiyo, hili suala si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la kodi ya majengo, Watanzania hawa wanajenga kwa shida kweli, lakini kitu cha kwanza Mtanzania huyu analipa kodi ya ardhi, Mtanzania huyu analipa kodi kwenye cement, kwenye nondo, kwenye bati, kwenye kila kitu mpaka mchanga anaochota ardhini ukisombwa pale anaulipia kodi, leo tena hivi vijumba vyao ambavyo wamejijengea kwa shida mnaenda tena kuwanyonya hawa Watanzania waende wakawalipieni tena kodi, tena mnaenda kuwapandishia kutoka shilingi 3,000 mpaka shilingi 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawataka nini hawa Watanzania wa watu yaillai toba maulana, wametukosea nini Watanzania? Hivi kuwapa ridhaa ya kuongoza nchi hii ndio imekuwa adhabu kwao? Waoneeni huruma hawa Watanzania, mlienda kuwapigia pushapu mpaka misamba ya suruali ikachanika, kwa hiyo, waoneni kwamba ile huruma waliowapeni basi hebu itumieni kuweni na moyo wa huruma kwa binadamu wenzenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kodi ya majengo si


sawa, mngekuja mimi nilikua najua hapa mngekuja mkasema kwamba kama mnataka kodi ya majengo basi vifaa vya ujenzi vipinguzwe kodi ama viondolewe kabisa, ili muweze kuchukua hiyo kodi ya majengo, hamtoi vifaa vya ujenzi vinapanda kwa kupandisha mafuta vifaa vya ujenzi vitapanda. Lakini pili mnawapandishia hivyo vifaa vya ujenzi mnakwenda tena mnawatoza na kodi za majengo huko waliko, jamani mnawakamua kiasi hiki wamewakosea kitu gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shilingi milioni 50, ni suala lile lile tunaimba kama malaika tunacheza kama mashetani, mliahidi hapa na mwaka jana tulisema, hili suala la milioni 50.

TAARIFA .....

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mdogo wangu Mariam nimsamehe bure tu, Jimbo lenyewe la Chemba halijui huyu, hiyo barabara imepita wala wananchi wa Chemba hawanufaiki na chochote kwenye lile Jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Chemba, tulieni ninyi nini mnachozomea kitu gani? Tulieni hiyo, vitulizeni taratibu cristapen iingie, vitulizeni visiwashe saa hizi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina dakika zangu tatu zimebaki naomba unilindie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la shilingi milioni 50, mliwaahidi Watanzania kila kijiji kuwapatia shilingi milioni 50, tunataka tujue shilingi milioni 50 ni lini au ni deni watakuja kuwadai waanzie wapi kudai shilingi milioni 50, hatujaziona kwenye kitabu cha Waziri humu shilingi milioni 50 ziko wapi? Mlijinasibu na shilingi milioni 50 leo mwaka wa pili, bajeti ya pili hii kitabu kinapita empty, hata dalili wala harufu wala sisikii Mbunge wa CCM akiongelea suala la shilingi milioni 50, ni lini hizo shilingi milioni 50 mtazitoa?

TAARIFA.....

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahisi Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi hawanielewi. Nimesema hivi jamani mlichokiahidi sicho mnachokitekeleza ni miaka miwili sasa, mliahidi shilingi milioni 50, mliahidi barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeahidi shilingi milioni 50 mmeenda kujenga uwanja wa Chato wa ndege! Hivyo ndiyo vitu shilingi milioni 50 mtaitoa lini? Siyo suala kwamba miaka Mitano, hivi vingine havikuwepo hata kwenye Ilani yenu, vimepatikanaje? Halafu unakuja unaniletea story hapa eti Ilani ya Chama cha Mapinduzi inanihusu nini mimi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Waziri akija hapa atuambie, shilingi milioni 50 ni lini zinaanza kutolewa kwa Watanzania wetu, ukidai ujue na kulipa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kupata fursa ya kuchangia Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi. Naomba nianze kuchangia Wizara hii, kwenye suala zima la migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hili la migogoro niseme tu Mheshimiwa Lukuvi amepata pongezi nyingi, lakini kwa Mkoa wa Dodoma kwa kweli kazi bado anayo. Nasema kazi bado anayo kwa sababu Mheshimiwa Lukuvi, atasema mambo kadhaa nitakayoyazungumza hapa hayahusiani na Wizara yake, lakini yeye ndiye tunajua Wizara yake inahusika na suala zima la makazi, bila ardhi makazi hayapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa yetu ya Dodoma, kuna kitu ambacho kinataka kuja kutengenezwa kinachofanana na kinachokuja kutengenezwa hapa KDA. Sisi Dodoma tuna msalaba unaitwa CDA, hii CDA ilianzishwa mnamo mwaka1973 kwa madhumuni na malengo ya kwenda kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kuja Manispaa ya Dodoma ama Mkoa wa Dodoma. Yapata leo miaka 43 makao makuu yapo ya chama tu, ya Serikali hayapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize Serikali mko hapa team nzima, huyo Waziri Mkuu yuko hapa mwakilishi wake, lakini Wizara mbalimbali ziko hapa. Wana Manispaa ya Dodoma wanataka kujua, kama suala zima la uanzishwaji wa kitu kinachoitwa CDA, ilikuwa dhumuni lake na malengo yake ni kwa ajili ya kuleta, Makao Makuu Dodoma imeshindikana, kwa nini hii CDA isirudi Dar es Salaam ambako ndiko kuna makao makuu ya nchi? Badala yake kuendelea kuwatesa na hao Watanzania wasio kuwa na hatia yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, CDA ilikuja ili ipange mji wetu vizuri, igawe viwanja vyetu lakini pili, iweze kuwapatia wananchi wa Manispaa ya Dodoma ardhi, waweze kuiendeleza, waweze kupata makazi yaliyo bora. Leo wananchi wa Manispaa ya Dodoma, hawana ardhi ambayo wamemilikishwa na CDA badala yake wamegeuzwa kuwa watumwa ndani ya wilaya yao, wanaitwa wavamizi kila kunapokucha wanabomolewa nyumba zao. Inasikitisha sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, wananchi hawa bila huruma CDA imekuja tangu mwaka 1973 kuna watu walikuwepo tangu mwaka 1959 kabla hata ya Uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Njedengwa pale walienda kuwavunjia watu wakampa eneo mtu mmoja tu, anaitwa Maimu, wakavunja nyumba 127, wakampatia maekari mtu mmoja anaitwa Maimu pale. Wananchi wetu wakawaacha hewani, wanateseka halafu leo wanataka kuendelea kuwashawishi Watanzania wa Manispaa ya Dodoma wabaki na CDA, hawaitaki CDA chukueni pelekeni kwenu, mnakoona kunafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii nimeona hapa kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, migogoro iliyoripotiwa ni migogoro miwili tu, (d) center na (c)center, si kweli. Nami nimshukuru Mheshimiwa Waziri hili begi lake alilonipa nimeweka haya ma-document ya CDA, ya wananchi haya, yako humu yamejaa haya humu, haya nimemletea. Mimi hili begi kazi yake nitakuwa nabeba makablasha ya wananchi, wanaoandika barua kwenye Ofisi zenu hamuwajibu, mnaitetea CDA, mnaenda mnakaa kwenye vikao vya Bodi ya CDA mnawaangamiza Watanzania wa Manispaa ya Dodoma, wamewakoseeni nini? Kwa nini mnawanyanyasa hawa watu kiasi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapimieni ardhi, wapeni ramani zenu, wapeni waende wakajenge, watu wanahangaika barabarani wanauza machungwa akinamama wajane, wana watoto wanasomesha, wanakwenda wanajijengea nyumba zao, mnaenda mnawavunjiwa, mnawaambia wavamizi. Mnachotaka ni nini, kuwaua? Waueni basi tujue moja kama hamuwataki, watu hao hao ndiyo wanaendelea kuwasitirini ninyi kupata kura, halafu bado mnaleta blabla hapa, za kuendelea kuwanyanyasa namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, safari hii mlipiga magoti na kupiga push up mwaka 2015 mwaka jana, 2020 nahisi mtaruka kichura chura. Kwa sababu hawa watu hawako tayari kuendelea na mateso haya na mwakilishi wa Waziri Mkuu aliyeko hapa, wananchi wa Kata zote 41 za Manispaa ya Dodoma, wanahitaji kukutana na ofisi ya Waziri Mkuu, ili waeleze manyanyaso na mateso wanayoyapata na hawa watumishi wa CDA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, CDA haisimamiwi na mtu yeyote ipo tu ina-hang hapo, inajifanyia mambo inavyotaka, inafunga ofisi tarehe 2 Februari, wamefunga ofisi eti kisa mfagizi kafiwa na mume wake, sisi mbona huwa hatuahirishi Bunge hapa mama yangu Stella amefiwa, mbona hatujaahirisha Bunge ili twende tukamzike mama yake Stella. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mume wa mfagizi wa CDA kafiwa wamefunga ofisi ambayo inahudumia zaidi ya watu 40,000 kweli ni mateso gani mnayowatesa hawa watu. Wana kikao tu cha kawaida cha kikazi wanafunga ofisi eti wamekwenda kwenye kikao, hawa watu kwa nini mnawaendekeza kiasi hiki? Hiki kiburi mnawapa ninyi Serikali. Laiti mngeamua kuwasimamia na mkawaambia lengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa CDA wangeshika adabu, wangefuata Kanuni na taratibu za nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wetu wanakwenda wanachukua ardhi zao, wakichukua ardhi badala ya kwenda kuwafanyia maboresho ya ardhi pale wawapimie watu mahali walipo, hawawapimii mahali wanawaambia tunapima upya. Wanawafukuza kwenye maeneo yao, wanaenda wanapima vile viwanja, wakipima viwanja wanawalipa fidia laki tano, kiwanja kinaenda kuuzwa milioni tano ama milioni nane, mwananchi gani anaenda kupata hiyo milioni nane ya kununua kiwanja. Ardhi umemkuta nayo mwenyewe, wana mashamba yao yaliyokuwa enzi na enzi, walikuwa wanayatumia kulima ardhi ya Dodoma hii haiongezeki inapungua, ila watu tunaongezeka. Kwa hiyo, ni lazima CDA muiambie na itambue, kwamba wanahitaji siku ngapi wakamilishe upimaji wa ardhi Manispaa ya Dodoma wafungashe vilago vyao waende wanakotaka kwenda, sisi Dodoma hapa tumechoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawawezi kufanya hiyo kazi, Mheshimiwa Lukuvi na Waziri Mkuu, wananchi wa Dodoma watakachokuja kukifanya wasije wakaleta lawama, wamechoka kunyanyaswa na mateso ya CDA. Hilo nimemaliza kwenye CDA, naomba lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wangu wanataka kukutana na Waziri Mwenye dhamana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa sababu Wabunge wa Majimbo hususani Jimbo la Dodoma Mjini, mmekuwa mkiwafunga midomo wasisemee suala la CDA. Alianza hapa Malole mwaka juzi mkamfunga zipu, eti ooh usiongee kwani ni ya nani, kama ni ya kwenu si mseme, kama na ninyi mnanufaika humo semeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Migogoro ya Swagaswaga ambayo najua iko kwa Mheshimiwa Maghembe, lakini suala lile la Swagaswaga, Mkungunero Dagram A mgogoro wa uliopo katika mpaka wa Chemba na Kiteto. Tunahitaji mpaka ule Waziri akautatue. Bunge la mwezi wa Pili, wazee wa watu walitoka Wilaya ya Chemba, wakaja kumwona Mheshimiwa Waziri wakamwelezea hali halisi iliyoko pale kati ya mgogoro wa Chemba na Kiteto, Mheshimiwa Waziri hata ile wakawapa maneno matamu, wakawarudisha wazee wa watu na wakawaahidi Waziri Mkuu anakwenda. Mpaka leo Waziri Mkuu hajawahi kukanyaga, wala harufu tu ya kusikia kwamba atakuja kwenda haipo, kwa nini wanawadharau hawa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawawezi kushughulikia, wawambie wajichukulie hatua wenyewe watajua nini cha kufanya huko, mpaka wasubiri watu wafe ndio wataona ving‟ora na magari 42 yanafukuzana yanakwenda kuangalia maiti za watu kule. Kwa nini mnafanya namna hii ninyi? Wananchi wa Dodoma wamewakoseeni nini? Tuambieni kama kuna makosa ambayo tumewakosea tuwaombeni radhi, ili na sisi tuweze kupata haki ya kuhudumiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kama maeneo mengine.
Maeneo mengine umefanya, Dodoma kwetu wewe ni sifuri na mbaya zaidi ulikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hii, usichokijua ni nini wewe Mheshimiwa Lukuvi, kipi usijchokijua kwa Dodoma hii ambayo umekaa kimya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ni mzuka tu! Suala la nyumba huko Swagaswaga na wapi huko niwaombe tu mwende wananchi wale, wazee wa watu wanalalamika huko, dharau hawazihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba, wakati Kamati zinaundwa nilikuwa mjumbe wa Kamati hiyo kabla sijabadilishwa, nilikwenda kuona nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba, nyumba zile sijui maana yake tulipoziona zilikuwa hazijaisha lakini tukaambiwa zikiisha zitakuwa nzuri, sasa sijui zinakuwaje nzuri kabla ya kwisha sijaelewa, chumba kinachokwenda kuwekwa mtu pale ukiweka kitanda cha futi tatu na nusu, utaweka na meza ndogo ya kuwekea mafuta ya kupaka, labda na kitana na dawa ya mswaki. Chumba huwezi kuweka kitanda cha tano kwa sita, nani siku hizi analeta biashara ya mbanano kwenye vyumba, vyumba vya kulala havina hadhi…
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu haujaonesha baadhi ya sekta katika kukuza pato la Taifa:-
(i) Sekta ya madini
(ii) Sekta ya Maliasili na Utalii
(iii) Bandari
(iv) Gesi
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kufahamu sekta ya madini itachangia kiasi gani? Hisa za Serikali katika miradi ya uchimbaji madini kwenye migodi ya Geita, Mwadui, Buzwagi, Tanzanite One na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu, uchimbaji wa gesi umeanza lakini katika mpango huu haujaonyesha ni kwa namna gani sekta hii itaongeza pato la Taifa. Pia ningependa kujua ununuzi wa vitalu mpaka sasa ni vitalu vingapi viko mikononi mwa wawekezaji na vinaingiza shilingi ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huu haujaonyesha sekta ya maliasili ina malengo kiasi gani. Napenda kujua mchango wa Serikali katika mpango huu wa 2017/2018. Kwenye upande wa Bandari pia uko kimya ni kwamba Bandari ndiyo inakufa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufike kwenye Tanzania ya viwanda ni lazima tuwekeze kwenye kilimo na siyo kilimo tu. Tunahitaji kilimo cha kisasa ili tuwe na malighafi kwa ajili ya viwanda. Pia kwenye mpango huu kilimo alichokitaja Mheshimiwa Waziri upande wa mazao ni mazao ya chakula tu. Ushauri wangu, tuongeze mazao ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Afya; ndani ya nchi sasa madawa yamekuwa tatizo, tusipoongeza fedha upande wa afya ni dhahiri kuwa katika viwanda tunavyotarajia kuvijenga tutaendelea kuajiri watu toka nje, hivyo tuna kila sababu ya kuboresha hospitali zetu ili tuwe na jamii yenye afya bora.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi na mimi ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Maji. Kwa kuwa dakika chache lakini Wizara hii nyeti naomba niende moja kwa moja kwenye kitabu cha Waziri na bahati nzuri mimi nina vitabu viwili vyote, cha mwaka jana na kitabu cha mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa Ntomoko ambao niliusemea pia katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Mradi huu wa Ntomoko unabadilishwa tu maneno kwenye vitabu vya Mheshimiwa Waziri. Kitabu cha mwaka wa jana alituletea mradi wa Ntomoko kwamba unahusisha Halmashauri mbili za Wilaya ya Chemba na Wilaya ya Kondoa. Kitabu cha mwaka huu hali ya huduma ya maji kutoka chanzo cha Ntomoko imeshindwa kukidhi mahitaji na kupunguza vijiji, yaani tunabadilishiwa maneno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mradi huu Mheshimiwa Waziri unalifahamu vizuri. Mradi wa Ntomoko ni disaster, haiwezekaniki. Leo mnakuja kutuandikia hapa ilhali mnajua kabisa nini kinachoendelea kuhusiana na suala zima la Ntomoko. Mheshimiwa Waziri, suala hili kama mnashindwa kuwawajibisha watu ambao wameweza kutenda dhambi kwa Watanzania wenzao kwa kupoteza fedha nyingi shilingi bilioni 2.4 wamezilamba, maji hakuna, wananchi wanapata shida ya maji, mna kazi ya kutubadilishia maneno kwenye vitabu, hatuwatendei haki wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hela zile si hela ambazo watu wale wanaomba, fedha ile wananchi wa Wilaya ya Chemba na wao ni miongoni mwa Watanzania wanaolipa kodi, wanatakiwa wapate hii huduma muhimu ya maji. Wilaya ile ina shida ya maji haijapatikana kuona. Kituo cha Afya cha Hamai hakina maji, nilisema, mwaka jana niliwaambia Wizara, mnaendelea kutubadilishia maneno kwenye hivi vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja, naomba aniambie suala la Ntomoko hatma yake ni nini? Wananchi wa Chemba tumesema huu mradi hatuutaki kaeni nao ninyi, tutafutieni mradi mwingine ambao tutapata maji. Hamuwezi kuwa mnaendelea kutubadilishia vijiji vyote, kata zote 26 hakuna maji. Mlitupa hivyo vijiji kumi navyo vimekuwa shida hakuna maji, mnataka nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya maeneo ambayo mnaendelea kufadhiliwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni miongoni mwa Mkoa wa Dodoma ndimo mnamopata kura humu, lakini bado hata hamuwakumbuki watu hawa, kwa nini mnafanya namna hiyo? Waswahili akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Sasa kama rafiki huyu mnamuona hana maana atakapokuja kupata rafiki mwingine msije mkamlaumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la maji DUWASA. Sijaona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kikiniambia kwamba kutokana na ujio wa Makao Makuu kuhamia Manispaa ya Dodoma ambayo ndiyo itakayobeba watu wengi, sijaona mpango mkakati wa upatikanaji wa maji katika Mji wa Dodoma. Tuna kata 41 katika Manispaa ya Dodoma, ni kata 18 tu ndizo zina maji; na katika hizo kata 18 haizidi mitaa 50 ambayo inapata maji katika hizo kata 18. Sasa tuna huu ujio, Mheshimiwa Waziri hujatuambia nini mkakati wa Serikali kuhakikisha maji yatapatikana pamoja na ongezeko kubwa la watu linalokuja kuingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, DUWASA hii ina majanga ya madeni kwenye taasisi za Serikali, na naomba nizitaje na utakapokuja hapa Mheshimiwa Waziri naomba uniambie madeni haya yatalipwa lini na taasisi za Serikali. Inakuwa ni aibu na ni masikitiko makubwa sana mwananchi wa kawaida anakatiwa maji, hapati maji mpaka alipe bili ya maji, taasisi za Serikali hamtaki kulipa maji mnadaiwa mabilioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, DUWASA inadai shilingi bilioni 1.9; kati ya hizo Jeshi la Polisi linadaiwa shilingi milioni 600, Magereza shilingi milioni 200; JWTZ inadaiwa shilingi milioni 100, JKT shilingi milioni 500, Makamu wa Rais… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzunguzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Ujenzi ambayo inahusisha barabara zetu pamoja na viwanja vyetu vya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala zima la ulipaji wa fidia kwa wananchi wetu wanaokwenda kupisha maeneo yanayokwenda kujengwa viwanja vya ndege, lakini pili na barabara zetu. Wizara ya Ujenzi kupitia Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Dodoma, Airport hii hapa iliwasimamisha wananchi wa eneo la Makole tangu mwaka 2016 mwezi Mei wakiwa wanahitaji maeneo yale kwa ajili ya kupanua uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja ule wananchi wale waliosimamishwa baadhi walilipwa lakini wengine waliobaki zaidi ya wananchi 57 mpaka leo hawajalipwa fidia na wamezuiliwa kuendeleza makazi yao na hakuna tamko lolote linaloendelea, wamebaki wako pale nyumba zinapata ufa, hawawezi kupaka rangi, hawawezi kufanya chochote, wameshabomoa na wameshaweka uzio tayari. Wizara ya Ujenzi kupitia kwa Mheshimiwa Waziri atuambie wananchi wale waliobaki kwenye Uwanja wa Ndege, Airport hii iliyoko hapa Makole, ni lini watalipwa fidia zao ili waweze kuondoka eneo lile na kama hawalipwi hawaoni sasa ni wakati wa kwenda kuwaruhusu waendelee na ukarabati wa makazi yao na kuwapa kibali cha kuendelea kuishi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hilo, kwa kuwa wamewachelewesha, waliwafanyia tathmini ya kuwalipa fidia tangu mwaka 2016 mwezi Mei, wamewakalisha muda wote zaidi ya miaka mitano, sita sasa; watakapokwenda kuwaruhusu kuishi kama hawawalipi fidia ya kuwaondoa hawaoni sasa kuna sababu pia ya kuwalipa kifuta jasho kwa kupoteza muda wao mrefu na kushindwa kuendeleza makazi yao hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna Uwanja wa Ndege wa Msalato hali kadhalika uwanja ule na wenyewe kuna wananchi waliotakiwa kupisha ujenzi wa uwanja ule, walilipwa zaidi ya wananchi 200 wakabaki wananchi 89; tangu mwaka 2011 mpaka leo wananchi hawa hawajalipwa. Pia nataka kujua wananchi hawa wanalipwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na ulipwaji wa fidia, nimeona hapa kwenye kitabu cha Waziri anasema uwanja huo wa ndege uko kwenye mchakato. Mchakato mpaka lini, zaidi ya miaka 10 kiwanja hiki ni mchakato tu. Waziri akija kuhitimisha hoja yake jioni ya leo, naomba kujua ni lini sasa kwa tarehe ili tuweze kujua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dodoma wa Msalato unakwenda kuanza ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala zima la barabara zetu. Nitazungumzia barabara moja muhimu sana kwa maslahi mapana ya wananchi wa mikoa minne. Tunafahamu fika barabara ndiyo uchumi wa Taifa letu. Bila barabara hauwezi kupata huduma ya afya au huduma yoyote ya msingi au kufanya shughuli zozote za kibinadamu. Tuna barabara ya kutoka Kilindi - Kiteto – Chemba (Dodoma) - Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii iliahidiwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa; miaka 10 imeisha barabara haijajengwa. Akaja Rais wa Awamu ya Nne akaahidi barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami; miaka 10 imepita barabara hii haijajengwa. Akaja Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ikawekwa kwenye Ilani ya CCM mwaka 2015 - 2020 imepita bilabial. Imewekwa kwenye Ilani ya mwaka huu 2020-2025, kwenye kitabu cha Waziri inasema barabara hii inakwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu; miaka 25 Ilani ya Chama cha Mapinduzi mnafanya upembuzi yakinifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo si sawa. Sisi wananchi wa Wilaya ya Chemba barabara pekee inayoweza kukuza uchumi wa wilaya yetu ni barabara ya kutoka Kilindi kuunganisha na Mkoa wa Singida. Kati ya kata 26 za Jimbo la Chemba; kata 12 ndizo zilizopitiwa na barabara hii. Tukijenga barabara hii kwa kiwango cha lami tutakwenda kukuza uchumi wa wilaya yetu kwa kuwa …

T A A R I F A

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti, kuna taarifa inatoka wapi sioni Mbunge akisimama. Waheshimiwa Wabunge ukisema neno taarifa inabidi usimame ili nikuone. Mheshimiwa Eng. Ulenge.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba tu kumpa taarifa mzungumzaji nafikiri ana lag behind the information. Barabara anayoitaja inakwenda kujengwa kilomita 20 na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alitamka hapa Bungeni; Phase I ilikuwa ni kilomita 50 lakini kutokana na scarcity ya bajeti kilomita 20 inakwenda kuanza kujengwa. Sisi watu wa Tanga tunaifuatilia kwa karibu kwa sababu ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Tanga. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niendelee kwa sababu yeye anazungumza biashara ya kilometa 20; kwako Tanga kuna lami mama sisi Chemba hatuna lami. Kwa hiyo, ukiniambia biashara ya kilometa 20 none of my business. Kwanza, hata hiyo kilometa 20 imeanza au iko tu kwenye maandishi? Bunge la Kumi na Moja tuliambiwa inakwenda kujengwa, haikujengwa. Kwa hiyo, tunachokitaka hapa na nachotaka kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kama barabara viongozi wetu wakuu wa nchi wanaahidi awamu zote mbili kipindi cha Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne, miaka 20 hamjajenga barabara leo mtu anakuja kuniambia kwamba wanajenga kilometa 20, so what? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii sisi Wanachemba na Mkoa wa Dodoma ndiyo itakayokwenda kutusaidia kujenga uchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. Serikali imekuwa ikisema humu ndani kwamba Halmashauri ambazo zitakuwa na uchumi mdogo au zitakazoshindwa kukusanya mapato zitakwenda kunyang’anywa; sisi Chemba hatuna chochote tunategemea kilimo, wakulima wetu wanaolima Wilaya ya Chemba, tunatarajia tuwe na miundombinu rafiki kuwezesha kuuza mazao ili tuweze kukuza uchumi wa Halmashauri lakini hatuna barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wafanyabiashara wa mazao wanakuja kununua mazao kwa wakulima wetu kwa bei ya chini kwa sababu ya miundombinu mibovu ya barabara. Wawekezaji wanashindwa kuja kuwekeza ndani ya Wilaya ya Chemba kwa sababu miundombinu ya barabara si rafiki atakuja kuwekeza ili afanye nini? Sisi tuna mapori mawili; (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Mkungunero na Pori la Swagaswaga, tunaweza kupata watalii kama tutakuwa na barabara hii ambayo itatusaidia kuendelea kujenga uchumi wa Halmashauri yetu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atakapokuja biashara hii ya kilometa 20, tutashughulika humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu jana walikuwa wanasema kuna upendeleo na ukiangalia ni kweli; kata 26 huna barabara ya lami hata kilometa moja halafu unasema uko sawa, kweli? Hata watoto nyumbani mzazi ukimnunulia huyu leo kaptura, kesho mnunulie mwingine, inakuwaje mtoto huyo huyo kila siku ndiye unayemnunulia kaptura halafu mwingine unamuangalia? Kwa akili ya kawaida kama binadamu atahisi yeye kabaguliwa au katengwa na mwisho wa siku mtoto yule ataanza kuishi maisha ya kujitenga. Hatuhitaji ndani ya Bunge hili na ndani ya Taifa letu tuanze kuonekana kwamba kuna mikoa ambayo yenyewe ndiyo mizuri zaidi na inastahili sana na mikoa mingine ambayo haistahili.


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Sera ya Wizara ya Ujenzi inakwenda kuunganisha barabara za mikoa kwa mikoa na wilaya kwa wilaya. Tuna barabara ya kutoka Mrijo Olboloti, inapita mpaka daraja la Simba Kelema tunaunganisha na Wilaya ya Kondoa. Kuna daraja pale lilikatika mkaenda kuwaambia eti TARURA ndiyo waende wakajenge daraja lile, TARURA ana uwezo wa kujenga daraja la namna gani? TARURA mnaowapa bajeti ya 30% TANROADS wanachukua 70%, TARURA wataweza kujenga daraja lile? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aniambie daraja lile la Kelema Simba Maziwani ni lini litakwenda kujengwa la uhakika ili tuondokane na adha ya Watanzania wetu wa Wilaya ya Chemba kusafiri kwa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna eneo lingine korofi sana; kuna eneo la Mto Bubu ambao unapita Kata ya Songolo, wakati wa kipindi cha mvua maji pale huwa yanajaa kweli kweli na abiria wanaposafiri wakikutana na ule mto ni lazima wasimame ili mto upite na wao waweze kuweza kupita. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha naomba atuambie maana wananchi wa Wilaya ya Chemba tunahitaji Daraja la Songolo ili kuokoa maisha ya wananchi wetu na watoto wetu wa shule kwa sababu tuna shule ya msingi na sekondari ambapo mwaka jana watoto wawili; mmoja wa sekondari na mwingine wa shule ya msingi walifariki kwa kusombwa na maji kutokana na lile daraja pale maana wanavuka kwenda shuleni.

Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja pia atuambie nini anachokwenda kufanya kuhusiana na daraja hili, hata kama ni la dharura tutengenezeeni wakati mnaendelea kujipanga ili muweze kutuwekea daraja linalostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa machache haya, nakushukuru kwa muda wako lakini fidia Uwanja wa Ndege wa Airport pamoja na Msalato naomba kujua hatma yake. Pia naomba kujua hatma ya kilometa 461 za barabara ya kutoka Kilindi mpaka Singida zikiwa zinapita Chemba. Nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kunipatia nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya Awamu ya Sita ambayo tunaianza mwaka 2021/ 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kuipongeza Serikali. Tangu lilivyoingia Bunge la Kumi na Moja kilio changu kilikuwa ni malipo ya Madiwani kupelekwa Serikali Kuu, hata wakati nachangia Wizara ya TAMISEMI nilisema kwamba tunaomba Madiwani wetu wakalipwe stahiki zao na Serikali Kuu ili kuwaondolea mzigo wa kukopwa…

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba tupunguze sauti tuwasikilize wachangiaji.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweze kuwalipa Madiwani wetu kupitia Serikali Kuu ili kuwapunguzia mtihani na msalaba mzito waliokuwa wanaubeba Madiwani kwa kukopwa na Wakurugenzi kwenye halmashauri zao. Kwa hiyo niwapongeze sana, na niipongeze sana Serikali kwa kuliona hilo na kuweza kuwapelekea Madiwani kwenda kuwalipa kwenye Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipendekeza hapa wakati nachangia Wizara ya TAMISEMI, kwamba Serikali ikipeleka Madiwani wetu kwenda kulipwa Serikali Kuu tuna watu hawa ambao pia wao ndiyo watendaji wetu wakuu huko chini baada ya Madiwani. Wenyeviti wa vijiji tunao ambao ndio wanafanya kazi kule nikapendekeza kwamba Madiwani tuwapeleke Serikali Kuu ili zile fedha zilizokuwa zinalipa Madiwani ziende na zenyewe zikasaidie kuwalipa posho angalau ya shilingi laki moja wenyeviti wetu wa vijiji, na wao waweze kutekeleza majukumu yao na wajibu wao kwa weledi kuliko sasa wanapata posho ya shilingi 10,000 na wakati mwingine hazilipwi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini hilo Mheshimiwa Waziri atakwenda kulichukua kama alivyoelekeza Mama, naamini watamshauri vyema, hali kadhalika na mama aweze kuona kwa jicho la kipekee kwa ajili ya kuwasaidia wenyeviti wetu wa vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa kwenye hotuba ya Waziri na ninaomba nianze na suala zima la kodi ya majengo. Wamesema Wabunge wengi, lakini na mimi naomba niseme hofu yangu kwenye suala zima la kodi ya majengo. Mheshimiwa Waziri anatuambia kwamba itakwenda kulipwa kwa mfumo wa LUKU na kila mwezi italipwa shilingi 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi ya majengo kwa kila nyumba ni shilingi 20,000. Ukilipa kila mwezi shilingi 1,000 kwa mwaka mzima utakuwa umelipa shilingi 12,000 hii shilingi 8,000 nani anaifidia? Niombe nisaidiwe ufafanuzi kwenye suala zima hili la kodi ya majengo. Lakini ukiangalia tu kwa uhalisia wa kawaida ni kitu ambacho hakiwezekani, kwamba mpangaji niende nikampe huo mzigo wa kulipa kodi ya jengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwenye kodi ya majengo pia ametuambia kwamba shilingi 1,000 na shilingi 5,000 kwenye nyumba yenye mita moja, na zile nyumba ambazo zina mita zaidi ya moja zinatengenezewa mfumo wao, ni lini zinakwenda kutengenezewa huo mfumo? Imekuaje watengeneze huo mfumo wa kodi ya jengo kwenye nyumba yenye mita moja wakashindwa kutengeneza huo mfumo wa nyumba yenye mita zaidi ya moja? Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri aende akakae na timu yake vizuri watengeneze namna bora ambayo tunaweza kwenda kukusanya kodi hii ya majengo ili tuweze kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 nikiwa nachangia bajeti hii nilisema kwamba Serikali imekuwa haipunguzi kodi kwenye vifaa vya ujenzi, lakini inakwenda kuongeza kodi kwenye vifaa vya ujenzi huku wanataka kodi kwenye majengo. Ukiangalia hapa kwenye ongezeko la ushuru wa forodha, Mheshimiwa Waziri amekuja na mapendekezo ya kuongeza ushuru kwenye bidhaa ya mabati asilimia kumi au Dola za Kimarekani 250. Sasa tunataka wananchi wetu waweze kujenga na kuishi kwenye nyumba bora leo unakwenda kuwaongezea kodi huko kwenye hizo bati ni mwananchi gani atakayeweza kwenda kujenga nyumba kwa kwenda kupandisha kodi ya mabati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaturudisha nyuma tena watu hawa watarudi nyuma, hawataweza kwenda kumudu gharama za kununua mabati na matokeo yake nyumba za mabati zitapungua tutakwenda kuanza kurudi kwenye nyumba za matope za full suit juu na chini kama enzi hizo tulizotoka huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalo nimuombe Mheshimiwa Waziri, kama umeamua kuchukua kodi ya majengo tunaomba basi punguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi; na kama mnaamua kuchukua kodi kwenye majengo basi huku kwingine tuache ili watu waweze kupumua na waweze kuona ni namna gani wanaweza kuichangia Serikali yao kwenye suala zima la kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye kuzungumzia suala la barabara zetu za kimkakati za kuunganisha mikoa pamoja na wilaya. Ili tuweze kukuza uchumi wetu; na Tanzania sisi tunategemea sana suala zima, la kilimo na kilimo bila barabara hatuwezi kupata tija kwenye kilimo. Sasa sisi mikoa minne, Mkoa wa Tanga, Manyara, Dodoma na Singida tuna barabara yetu ya kutokea Kilindi. Nilisema, kwamba, barabara hii ina ahadi ya marais watatu, Rais Awamu ya Tatu, Rais Awamu ya Nne na Awamu ya Tano waliahidi kuijenga barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na barabara hii sisi kwenye uchumi ndiyo barabara itakayoweza kusaidia wakulima wetu kuweza kupata tija kwenye mazao yao. Lakini pili, ni juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu amezindua zao la kimkakati kwenye mikoa mitatu, mkoa wa Dodoma, Singida pamoja na Simiyu. Kama barabara hizi hazitakwenda kupitika na hizi ndoto za mazao ya kibiashara ya kimkakati ambayo tunaenda kuyapeleka kwenye maeneo yetu, haya mazao pia itakuja kufikia hatua wananchi wamelima mazao haya lakini watakosa barabara za kuzipitisha mazao haya kwa ajili ya kwenda sokoni na kwenda kwenye viwanda vyetu. kwa hiyo mwisho wa siku hatutakuwa na tija kwenye suala zima la malengo ama na matarajio yetu ya kwenda kupandisha uchumi wa taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeiona barabara hii kwenye mpango, lakini kwenye bajeti mmeweka kujenga barabara kilometa 20. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, kwa umuhimu wa zao la alizeti ambalo tunalima Mkoa wa Dodoma na Singida niombe barabara hii Mheshimiwa Waziri ukaingalie kwa jicho la kipekee iende ikajengwe kwa haraka ili tuweze kupata tija kwenye suala la zao hili la mkakati ambalo Serikali mmeweza kuliona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana tena na suala hilo hilo la ujenzi wa barabara zetu hali kadhalika Serikali imekuwa ikipata kigugumizi sana kwenye suala zima la ulipaji wa fidia. Tunapokwenda kujenga barabara zote na maeneo mengine suala la ulipaji wa fidia Wizara ama Serikali mmekuwa mkipata kigugumizi na kuchelewesha ulipaji wa fidia ambao umetusababishia miradi mingi kushindwa kumalizika kwa wakati na hivyo hasara kwa wakandarasi wetu pamoja na kuchukua muda mrefu kumaliza miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mnapokwenda kutekeleza miradi ya kimikakati niwaombe sana, kwa suala la ulipaji wa fidia, fedha hizo zitoke kwa haraka na hatimaye tuweze kuwa tunakwenda kwa kadri ambavyo tunajipangia sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la utekelezaji wa bajeti na nitazisema wizara chache, pia suala zima la utekelezaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo kwenye wizara mbalimbali hali kadhalika Serikali imekuwa na kigugumizi sana. Waziri wa Fedha kwa kweli Wizara yako imekuwa na changamoto kubwa kwa kuwa mmekuwa mkichelewesha kupeleka fedha kwenye wizara zetu. Vilevile hata mkizipeleka pia hamzipeleki kama Bunge lilivyopitisha, mnapeleka kidogo kidogo ambazo mwisho wa siku haziendi kwenda kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo kwa kipindi cha miaka mitano Wizara hii imepelekewa fedha za maendeleo asilimia 19.3, lakini Wizara ya Mifugo kwa miaka mitano pia mfululizo wamepelekewa fedha za maendeleo kwa asilimia 21, yaani hata asilimia 30, 50 haijafika. Kwa hiyo tunaona ni kwa namna gani Wizara ya Fedha mnakwamisha maendeleo ya taifa letu kwa kuvuta miguu kwenda kupeleka fedha kwenye shughuli za maendeleo kwa ajili ya kuweza kuleta tija kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sheria ya Petrol kuongeza tozo ya mafuta ya taa, na Mheshimiwa Waziri pendekezo lake anasema anakwenda kuongeza tozo ya mafuta ya taa ili kudhibiti wafanyabiashara wakubwa wanaokwenda kutumia mafuta ya taa kuchakachua diesel na petrol. Mheshimiwa Waziri yaani umekaa na watalaam wako, mkachakachua, mkapanga, mkapangua mkazichanga karata ukaona mbinu rahisi ama njia rahisi ni kwenda kupandisha mafuta ya taa ambayo ndiyo nishati peke yake iliyobaki kwa wananchi wengi ambao bado hawajafikishiwa umeme vijijini?. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri niombe nenda kwenye suala zima la uongezaji mafuta ya taa hiyo shilingi mia moja uliyoiongeza, hebu nenda kajipangeni upya. Tunafahamu fika, hata wewe Iramba kwako unajua ni vijiji vingapi vyenye umeme? Nenda, watu leo bado wanatumia mafuta ya taa, tunapoendelea kuongeza huu mzigo wa shilingi mia kwa wananchi wetu haikusaidii, hata wewe utakuja kuulizwa ulikuwa na maana gani? tuwaache hawa watu, tafuta namna ya kuwadhibiti hawa wanaochakachua huku, punguza mzigo kwa mtanzania mnyonge asiyekuwa na hatia. Kwa hiyo nenda ukaondoe kodi hii ili wananchi wetu waweze kupata nafuu ya maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la shilingi mia moja pia kwenye lita ya kila mafuta ya petrol na diesel; nimalizie tu. Pia hili nalo nikuombe Mheshimiwa Waziri nenda kaliangalie, ukiongeza tozo tena kwenye petrol na diesel hali kadhalika maisha yatapanda, nauli zitapanda, vyakula vitapanda kwa sababu vinasafirishwa, kwa hiyo gharama ya maisha inakwenda kupanda huo mzigo anaenda kubeba mwananchi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie la mwisho. Ahadi nyingi za viongozi wetu waliopita zimekuwa zikisemwa humu ndani mara kwa mara na ni wajibu wetu kwa sababu ahadi ni deni; na siku zote ahadi zinazoahidiwa na viongozi wetu kwa mfano Mheshimiwa Rais au Makamu wa Rais ama Waziri Mkuu inakuwa ni taasisi siyo mtu binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwaka 2015/2020 Serikali Awamu ya Tano iliwaahidi Watanzania kuwapatia milioni 50 kila kijiji, lakini mpaka sasa bado sijawahi kuisikia wala kuiona hii milioni 50. Ahadi ni deni, Mheshimiwa Waziri wa Fedha niombe hii milioni 50, kwa kuwa ni ahadi kama ahadi zingine na wananchi wetu Watanzania waliopo huko bado wana matumaini wanasubiri milioni 50 kila Kijiji, niombe sasa hii milioni 50 kila kijiji itolewe ili wananchi wetu waende wakapate mitaji yenye tija na waweze kujenga uchumi wa taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi siku ya leo niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Afya na ninaomba nianze tu na suala zima la upungufu wa wahudumu wa Wizara ya Afya na naomba nilisemee kwa Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Dodoma ni Mkoa ambao umekwenda sasa kupata ongezeko kubwa sana la wageni kutoka nje na tuna Hospitali ya Rufaa kwa maana ya Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, lakini pia tuna Hospitali ya Benjamin na hospitali zingine za taasisi, lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana ya foleni ama msongamano kwenye hospitali hizi. Nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri ukija naomba utuambie wananchi wa Dodoma msongamano huu, mkakati wako ni nini wa kuepusha msongamano kwani watumishi kwa maana wageni wengi ambao wameingia ni watumishi wa Serikali na mara nyingi wanatumia kupata appointment na madaktari wanapofika pale hospitalini hawapangi foleni. Wenyeji wa Mkoa wa Dodoma wanapanga foleni Mheshimiwa Waziri mpaka siku tatu mtu hawezi kumuona daktari, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja uweze kuniambia suala hilo linatatuliwaje kwa udharura wa ongezeko la watu katika Mkoa wetu wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kusemea suala zima ni sera ya Serikali kwamba kila mkoa unatakiwa kuwa na Hospitali ya Mkoa, Wilaya kuwa na Hospitali ya Wilaya, lakini pili kata kuwa na vituo vya afya na vijiji kuwa na zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamekuwa wakisimama hapa wanalalamikia suala zima la hospitali za Wilaya na vituo vya afya. Mkoa wangu wa Dodoma una Wilaya saba, Wilaya tatu hatuna hospitali. Tumekuwa tukiomba fedha mara kadha wa kadha na fedha hizo hazitoki. Sasa Mheshimiwa Waziri suala la ongezeko la watu hapa Mkoa wa Dodoma linakwenda pia kuleta changamoto kubwa kwa sababu wananchi wa Wilaya za pembezoni zote wanapokosa huduma huko kwenye Wilaya zao wanakuja hapa Makao Makuu kwa maana ya Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Sasa leo Wilaya hizi hazina hospitali za Wilaya, lakini bado kuna msongamano mkubwa, naomba utuambie Mheshimiwa Waziri hizi Wilaya tatu nini hatma yake kwenye bajeti hii ya fedha ya mwaka huu 2018/2019. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Chemba ina kata 26. Kati ya kata 26 ni kata nne tu ndiyo ina vituo vya afya, lakini tuna kituo cha afya Kituo cha Hamai, kituo hiki nilikisemea Bunge lililopita ama kikao cha bajeti kilichopita. Hiki ndiyo kituo kinachotumika kama Hospitali ya Wilaya ya Chemba, lakini cha kustaajabisha na cha kusikitisha kituo hiki kina watumishi 16, kituo hiki hakina maji, kituo hiki hakina x-ray machine, kituo hiki hakina gari la wagonjwa. Kituo hiki acha tu kwamba kinahudumia kama kinakuwa kina-take charge ile ya wagonjwa wa Wilaya ya Chemba, lakini pia kinahudumia Wilaya ya Kiteto, kinahudumia Wilaya ya Chamwino, kinahudumia Wilaya ya Kondoa. Hivi vitu hebu tunaombeni muwe mnatuona na watu wengine huku, msiwe mnagawana gawana tu hizi fedha halafu watu wengine mnatusahau. Mngeacha hata kutujengea ule uwanja wa Chato kwa shilingi bilioni 42 mkatuletea hizi fedha zingeweza kutusaidia kujenga hizi hospitali zetu za Wilaya ikaweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hii shilingi trilioni 1.5 ambayo inapigwa pigwa chenga na Serikali mimi naamini ipo mahali, mlikuwa mnatikisa kiberiti, sasa tunaomba muitoe hadharini ije iende ikatekeleze shughuli za maendeleo kwa kutoa huduma ya afya, kwani tunaamini Mama Salma amesema kwamba bila afya hakuna uchumi. Mnatangaza Serikali ya viwanda, Serikali ya viwanda Watanzania wagonjwa hawana dawa, hakuna wahudumu, Tanzania ya viwanda iko wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba sana kwa jinsi mnavyojinasibu Serikali sikivu tunaomba usikivu huo uende kwenye shilingi trilioni 1.5 ikatuletee madawa na kulipa mishahara ya watumishi katika Taifa letu ili Watanzania waweze kwenda kuendelea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niseme kwamba hakuna Mbunge hata mmoja ambaye anaamini kwamba maji siyo muhimu. Nisikitike tu watu wanaopinga suala zima la kuundwa kwa tume ya kwenda kuchunguza hali halisi ya miradi ya maji kwenye maeneo yetu. Leo kama Wabunge tungekosa maji hakuna Mbunge hata mmoja angekuja humu ndani, hayupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uundwaji wa tume, Wabunge tunahitaji tume iundwe kwa sababu tumekuwa tukizungumza suala zima la ufisadi kwenye miradi ya maji, Serikali kwa maana ya Wizara mmekuwa hamtuelewi. Mwaka jana nilizungumza suala la Mradi wa Ntomoko, mwaka juzi hali kadhalika, mradi huu sikuwahi kupata majibu, uliendelea kupigwa danadana kwenye vitabu vya Waziri, safari hii hata kwenye kitabu cha Waziri Mradi wa Ntomoko haupo na matokeo ni mpaka Rais ndiyo amekwenda kutoa kauli ya kwamba waliotumia fedha za Mradi wa Maji Ntomoko wachukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tuna kosa gani Wabunge tukisema Mawaziri hawako tayari kwenda kufanya kazi na kusimamia miradi hii ya maji kwa ukamilifu wake? Kwa nini tukisema kwamba Mawaziri mmeshindwa, amebaki mtu mmoja peke yake ndiye anayetoa kauli za miradi na shughuli mbalimbali za Serikali kutendeka.

Suala la Ntomoko tumelisema hapa miaka nenda, miaka rudi, hamkuwahi kusema chochote na hamjawahi kuchukua hata hatua yoyote mpaka Rais amekwenda kuchukua hatua. Sasa ninyi Mawaziri kazi yenu ni nini, si bora mtoke wote abaki Rais Magufuli peke yake afanye kila kitu, ninyi mnafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upatikanaji wa maji nchini ni changamoto kubwa sana. Vijijini kuna shida ya maji wote humu ndani sisi ni mashahidi. Taabu hii wanaoipata ni wanawake wanaoishi vijijini. Mwanamke wa kijijini kulala kwake analala saa mbili, anaamka saa saba za usiku, saa tisa za usiku anatembea zaidi ya kilometa 20, 40 anakwenda kutafuta maji, anarudi mwanamke huyu amechoka bado anatakiwa kwenda kuihudumia familia yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini watoto wetu wa kike wanapata taabu kubwa sana. Leo watoto wa kike wanapata mimba za utotoni kwa sababu ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kutafuta maji na Serikali mnawakatalia watoto wetu wa kike kurudi shule wanapopata mimba za utotoni eti kwa sababu amepata mimba, akienda shuleni atakuwa ni mzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina dhamira ya dhati ya kwenda kumtua mwanamke na mtoto wa kike ndoo kichwani. Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kumdidimiza Mtanzania wa chini aendelee kudidimia kwenye shughuli za kiuchumi, elimu na hatimaye sisi Wabunge tulio wengi wa Chama cha Mapinduzi tunaopata maji safi na salama, elimu bora na familia zetu zinasoma vizuri ili watu hawa wanyonge wa huko chini watoto wao wasisome, wasipate maji safi na salama, wafe kwa maradhi, ili familia zenu viongozi wa Chama cha Mapinduzi waje waendelee kuliongoza Taifa hili. Dhambi hii Mwenyezi Mungu anawaona na hakuna malipo yanayokwenda kulipwa akhera, tutalipana hapahapa duniani na kila mmoja ataonja jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala zima la madeni ya taasisi za maji. Mwaka jana nilisema taasisi za Serikali zinadaiwa na Mamlaka za Maji zikiwemo Ofisi ya Rais, Ofisi ya Makamu wa Rais, JKT, Polisi na Magereza. Taasisi zote hizi za Serikali zinadaiwa na Mamlaka za Maji. Kibaya zaidi unakuta taasisi hizi zinadaiwa hazikatiwi maji, Mtanzania/ mwananchi wa kawaida anadaiwa mwezi mmoja tu hajalipa anakwenda kukatiwa maji, huu ni uonevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbaya zaidi Jeshi la Polisi kwa hapa Dodoma ilifanyika operesheni, walivyokwenda kukatiwa maji Jeshi la Polisi likaamua kukamata magari yote ya DUWASA pamoja na pikipiki, vifaa vyote vikakamatwa vikaenda kujazwa pale kwenye kituo cha polisi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi. Mimi naamini kuwa kila mtu anapofanya kazi anatakiwa anapopata ujira wake autumie bila ya mtu yeyote kumuingilia katika kipato chake. Wafanyakazi wa nchi hii wanafanya kazi na wanalipwa mshahara hakuna Serikali yoyote ya nchi hii inayokwenda kumpangia matumizi mfanyakazi yule ya mshahara wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini wakulima wanalima kwa shida, kwa taabu wanapovuna mazao yao mnataka kuwapangia namna ya kuyatumia mazao yao? Nimwombe Mheshimiwa Waziri akija hapa, pamoja na kwamba zigo hili tunamtwisha lakini yeye ndiye mwenye dhamana na Wizara hii, aje atuambie hivi ni kwa nini wakulima hawa ambao hamuwapi mbegu, wananunua mbegu kwa shida ambazo bei zake ni aghali, pembejeo mnachelewesha na wengine kwa mfano huku Dodoma sisi pembejeo za Serikali hatuzijui kabisa, hamuwasaidii kitu
chochote kile lakini mnataka kuwapangia namna ya kutumia mazao yao pale wanapokuwa wamevuna? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la mbegu za mahindi; kilo mbili ya mbegu ya mahindi inauzwa shilingi 14,000. Mwananchi huyu anapanda mbegu ile ya kilo mbili kwa shilingi 14,000, leo ndani ya Mkoa wa Dodoma, Wilayani kwangu Chemba wakulima wale wanauza debe la mahindi shilingi 2,500. Mbegu kanunua kilo mbili Sh.14,000 lakini debe la mahindi anauza shilingi 2,500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakulima tunachowataka ni nini? Yaani hii shilingi 2,500 anayouza hata nusu kilo ya dagaa hana uwezo wa kununua ili aweze kula. Mtu huyu anatakiwa kuuza madebe mawili apate shilingi 5,000 aende akanunue kilo moja ya sukari aweze kunywa chai ama uji na familia yake. Hiki kitu hakikubaliki na Mheshimiwa Waziri ukija mimi nitaomba unisaidie tu, umejipangaje na Wizara yako kuhusiana na upatikanaji wa mbegu ambazo zitapatikana kwa urahisi na kwa gharama ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la pili kuhusiana na migogoro ya ardhi. Tumeona migogoro mingi ya ardhi inayotatuliwa leo ni upande wa maliasili tu. Wakulima hawa pamoja na shida kubwa wanayoipata ya kulima chakula na sisi Wabunge tunakula chakula cha wakulima hao lakini mahali pa kulima nako pia imekuwa ni changamoto. Migogoro ya wakulima watu hao wanakufa kifo huku wakiwa wanajiona wao wenyewe wanakufa na kitanzi chao. Hawana watu wa kuwapigia kelele kwenye migogoro na wakisema wanaonekana ni wakorofi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri akija aniambie suala la migogoro ya ardhi ya wakulima nini mkakati wake kwenye bajeti hii ya fedha ya 2018/2019 ili wananchi wetu wakulima hawa ambao wanafanya kazi kubwa ya kutafuta chakula kwa ajili ya Taifa letu tuweze kuona namna gani migogoro hiyo inakwenda kutatulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akija naomba wakulima wangu wa Wilaya ya Chemba, eneo la Sekii pamoja na Champanda nataka aje aniambie mgogoro huu baina ya WMA ya Makame (Kiteto) na wananchi hawa kwenye vijiji hivi hatma yao ni nini? Wananchi hawa wameendelea kunyanyasika, mashamba yale ni ya kwao, Makame WMA wameenda kurudisha mpaka nyuma, matokeo yake watu wetu wanaenda kufyekewa mazao, si sawa sana. Mheshimiwa Waziri akija naomba anisaidie huu mgogoro unakwenda kuishaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala zima la madeni ya mbolea, wameongea Wabunge wengi. Siku za nyuma huko mwaka 2014 na kurudi nyuma, watu hawa pamoja na kuwa walikuwa wanafuja hizo nyaraka na kadhalika lakini walikuwa wanalipwa. Leo ni mwaka wa nne watu hawa hawajalipwa mnadai kwamba mnafanya uhakiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 mlituambia mnahakiki, mwaka 2017 mnahakiki, leo mnafanya nini? Mtaendelea kuhakiki mpaka lini? Hivi kwa Serikali na vyombo vyake vyote mlivyonavyo mmeshindwa kubaini nani anastahili kulipwa na nani hastahili kulipwa? Mheshimiwa Waziri akija tunaomba... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na mimi kwa kunipatia nafasi niweze kusema machache kwenye Wizara yetu hii ambayo imebeba Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika, mimi nitaomba nizungumzie suala zima la wagani (maafisa mifugo), lakini pili migogoro na tatu ni ushuru kwenye minada yetu na ntagusia kidogo suala zima la nyavu haramu.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wetu wengi walioko vijijini wana changamoto kubwa sana ya wagani ama maafisa mifugo. Kwanza maafisa mifugo hawajitoshelezi, lakini pili hao waliopo hawafanyi kazi ipasavyo kwa mujibu wa maadili yao ya kazi. Leo afisa ugani aliyeko kijijini yeye amekuwa ni mchuuzi. Analipwa mshahara na Serikali lakini bado anapohitajika kwenda kutimiza wajibu na majukumu yake mtu huyu ukimfuata atakwambia kwanzasina usafiri, hilo ni kweli hawana usafiri, lakini pili, akienda kufanya hiyo kazi atakwambia sasa unanipa shilingi ngapi; mtumishi huyu analipwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hawa watu, maafisa ugani waliopo tunaomba Wizara iweze kuwafuatilia mmoja baada ya mwingine kwa sababu wamekuwa ni kero na changamoto inayosababisha wakulima ama wafugaji wetu kuacha kuwatumia kutokana na biashara yao ya kutoa huduma, badala ya kutoa huduma kwa jamii, wanalipwa mishahara na kodi hizohizo za Watanzania, wanaacha kufanya hiyo kazi wanataka walipwe fedha nyingine ili waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maafisa ugani hawa bado wana shida ya vitendeakazi. Afisa ugani huyu uliyempeleka kwenye kata pale ana vijiji vitatu ama vinne; kutoka makao makuu ya kata mpaka kwenda Kijiji A unaweza ukakuta kuna kilometa 20 mpaka 30; vijiji vyetu hata vya Mkoa wa Dodoma unavijua jinsi vilivyo; mtu huyu hana usafiri, hana pikipiki wala baiskele. Hivi Serikali hii ya uchumi wa kati, Serikali ya viwanda tunaifikiaje hiyo ndoto bila kuwaboreshea maisha vitendeakazi vya hawa maafisa ugani wetu ili waweze kufikisha huduma kwa wakulima wetu?

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la migogoro ya ardhi; limesemwa na Wabunge wengi lakini suala hili ni kama vile limetulia kidogo, limepoa, lakini linafanyika chini kwa chini, kuna mambo yanayoendelea huko huwezi kuamini. Naibu Waziri alifika Wilaya ya Chemba na Wilaya ya Kondoa, kwenye Pori la Swagaswaga pamoja na Mkungunero. Kuna watu walikamatiwa ng’ombe wao wakiwa wanachunga, si kwenye hifadhi, ni mpakani na hifadhi, wale watu wa hifadhi wakaenda wakawasukumia wale ng’ombe kwenye hifadhi wakawakamata.

Mheshimiwa Spika, walivyowakata wakaenda wakawaambia kila ng’ombe mmoja alipiwe shilingi laki moja. Watu wale wakasema hizo hela kwa sasa hatuna, wakawaambia nendeni mkatafute mrudi. Walivyorudi wakahojiwa kila mfugaji mmoja wewe ulikuwa na ng’ombe wangapi, mfugaji anasema nilikuwa na ng’ombe 200 anaambiwa ng’ombe hawa 200 mara 1000 tujumlishe. Lakini watu hawa walikuwa wakilipa hizo faini, wanapokabidhiwa ng’ombe hawafiki ng’ombe 200, mtu atapewa ng’ombe 150, atapewa ng’ombe 80. Wakiuliza ng’ombe wetu wengine wako wapi wanaambiwa ng’ombe wamepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya yanasononesha, mambo haya yanasikitisha, mambo haya yanahuzunisha na yanatia simanzi sana ndani ya taifa letu la Tanzania. Taifa hili, wakulima hawa, wafugaji hawa, huyu mfugaji anatakiwa alipe ada ya mwanafunzi, anatakiwa ale, anatakiwa afanye mahitaji yake yote kulingana na hawa ng’ombe wake. Umeenda umemchukulia ng’ombe wale, umemlipisha faini, unamtaka nini huyu mfugaji? Tanzania ya wanyonge ipi katika taifa letu leo la Serikali ya Awamu ya Tano? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa na Wizara bado hazina dhamira ya dhati ya kwenda kupambana na watu hawa ambao wameendelea kuwadhalilisha Watanzania walio wengi katika taifa hili ambao ndio walipa kodi na wao ndio wanalipwa mishahara na haohao walipakodi wanaowanyanyasa. Naomba watu wale ambao ng’ombe wao hawakurudishwa, Mheshimiwa Waziri ukija naomba uniambie watu wa Mkungunero na Swagaswaga waliokuwa wamekamatiwa ng’ombe wao, hawakurudi, naomba uniambie watu wale mnawachukulia hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Suala Zima la Ushuru wa Minada. Tunafahamu minada haipo kwenye vijiji vyote wala kwenye kata zote, tuna minada ambayo tumeiteua. Lakini ni kwamba katika minada hii, kumekuwa na ushuru wa usafirishaji na kwenda kuuza, mfano mwananchi anayetoka Kijiji cha Mlongia kwenda kuuza ng’ombe Mnada wa Soya, huyu mtu anatakiwa kukata ushuru…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kuniti, nakushukuru.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na mimi kwa kunipatia fursa ya kuweza ushauri wangu katika hotuba ya Mheshimiwa Rais. Nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyeweza kutujaalia uhai na afya njema imetusababisha tunaendelea kukutana katika ukumbi huu.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nisemee suala zima la huduma ya afya kwa Watanzania. Mheshimiwa Rais amesema kwenye hotuba yake kwamba tumeongeza vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali za wilaya na mikoa na ukarabati wa hospitali zetu za kanda. Kwenye hili, kujenga vituo vya afya kwa maana ya majengo, kujenga zahanati kwa maana ya majengo, kujenga hospitali za wilaya kwa maana ya majengo bila kuwa na dawa pamoja na vifaatiba na wahudumu kwenye hospitali zetu ni sawasawa na kutwanga maji kwenye kinu, mshahara wake ni kuloa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kama jinsi mlivyojenga haya majengo tunwaomba muende mkawaajiri watumishi wa Wizara ya Afya ili waende kwenye hospitali zetu hizo kuanzia zahanati mpaka hospitali zetu za rufaa waweze kupata huduma.

Pili, muende mkanunue vifaatiba. Asubuhi dada yangu Mheshimiwa Ritta aliuza swali kuhusiana na CT-Scan kwenye hospitali ya Mkoa wa Iringa. Lakini hata sisi Dodoma hapa, CT–Scan tunayo Ntyuka pale ni shilingi 200,000; ni Mtanzania gani anayeweza kumudu kipimo hicho? Kwa hiyo niombe Wizara na Serikali iweze kuona kwenda kununua vifaatiba hivi ili Watanzania wenzetu waendelee kupata huduma iliyo bora ya afya na waimarishe afya zao ili waweze kujenga uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala zima la maji; mwaka 2015 mlituahidi wakati wa kampeni mkatuambia mnakwenda kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani. Watanzania tukaenda tukapiga kura, ndoo ya mwanamke kichwani bado haijatulika kichwani. Bado mwanamke wa Kitanzania hususan anayeishi vijijini anateseka kutembea umbali mrefu akiwa na ndoo yake na mtoto mgongoni anatafuta maji.

Niiombe Serikali safari hii mkija kwenye suala zima la Wizara ya Maji, twendeni tukatenge bajeti ambayo haitakuwa bajeti ya maandishi na maneno na ya kusifiana humu ndani, twendeni tukatenge bajeti itakayokwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kama jinsi Mheshimiwa Spika tulivyokwenda kuwekeza kwenye miradi mikubwa Stiegler’s, tumenunua ndege. Basi vivyo hivyo hebu twende tukaone suala zima la upatikanaji wa maji ndani ya Taifa letu ili tuweze kuepuka maradhi, lakini pili tupate fursa ya kupoteza na kuokoa muda ambao tunautumia kwenda kutafuta maji. Muda ule utusaidie kujenga uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waswahili wanasema kitanda usichokilalia huwezi kuwajua kunguni wake. Tunapoomba suala zima la Katiba Mpya, sio kwamba tunaomba ili tuweze kujifurahisha. Tumekuwa hatuna imani na suala zima la Tume yetu ya Uchaguzi na unaweza ukasema Kunti unasema huna imani na Tume ya Uchaguzi mbona wewe uko humu ndani, mimi nilishiriki uchaguzi wa Jimbo yaliyotokea ni mengi. Kwa maoni yetu tunatamani hiyo Katiba Mpya ambayo yale maoni ya wananchi waliyoyatoa kwenye mapendekezo ya hiyo Katiba Mpya ambayo yatakwenda kutupatia Tume Huru ya Uchaguzi yanaweza kutujengea faraja sisi wa vyama vya upinzani pamoja na Watanzania kwenda kuamini tena kwamba tutakuwa kwenye Taifa letu uchaguzi wa huru na wa haki na wa kidemokrasia katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi kwa dakika hizo tano naomba niseme ya kwangu machache ambayo nitaweza kuyasema. Zaidi ya watanzania 75% wamejiajiri kwenye sekta ya kilimo. Lakini sekta hii ya kilimo ambayo ndiyo imeajiri watanzania walio wengi lakini ndiyo inayochangia uchumi wa pato la Taifa hili, lakini ndilo linalosababisha sisi watanzania tuendelee kuishi, Serikali imekuwa haitoi kipaumbele kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wenzangu waliotangulia kwenye suala zima la masoko naomba nizungumzie suala zima la upatikanaji wa pembejeo na suala zima la wagani kwenye sekta hii ya kilimo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha sasa alikuwa Waziri wa Kilimo kwenye Serikali ya Awamu ya Tano na alivyokuja akiwa Waziri wa Kilimo aliwatangazia watanzania kuhusiana na suala zima la upatikanaji wa pembejeo na hususan kwenye suala la mbolea akasema mbolea itakuwa kama Coca Cola. Sasa Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu umerudi huko huko jikoni nikuombe sana suala lile la pembejeo kwenye suala zima la mbolea ile Coca Cola ile tunaitaka safari hii kwenye bajeti hii tuone mbolea inapatikana kwa wakati na yenye tija kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye suala la pembejeo matrekta power tiller na vitu mbalimbali ambavyo vinakwenda kumsaidia mkulima huyu wa chini vimekuwa vikipatikana kwa shida sana. Hata hiyo mikopo ya matrekta imekuwa ni changamoto pia watu wanazungushwa kwelikweli lakini ili uweze kupata hata hilo trekta unatakiwa kuwa na hati. Wizara ya Ardhi nayo imekuwa ni changamoto hata kuwapatia tu zile ardhi za kimila wakulima wetu ili waweze kupata hati hizo waweze kwenda kukopa hayo matrekta.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kujiuliza Serikali ni moja hivi wanashindwaje kuwaamini hawa watanzania kwamba mtu huyu anajulikana anaishi Kijiji fulani ana ekari kadhaa mwenyekiti wa Kijiji yuko pale anamtambua ni kwanini Serikali imekuwa na kigugumizi kuhusiana na suala zima la utoaji wa mikopo ya pembejeo kwa wakulima wetu wadogo huko vijijini na badala yake tumeendelea kuwaacha wanateseka tuna Benki ya Kilimo ambayo inatakiwa kuwasaidia wakulima wa nchi hii haifanyi chochote hakuna mkulima mdogo hata mmoja anaekopeshwa na Benki ya Kilimo tunaambiwa ni Benki ya Kilimo kwenye makaratasi na majina. Ili tuweze kuleta tija kwenye benki hii niombe benki ya kilimo tuirudishe Wizara ya Kilimo ili iweze kuwahudumia wakulima wetu kule chini na hatimae waweze kunufaika na kodi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisemee suala na wagani, bado watanzania tunalima kilimo cha kujisukuma tu cha jana cha leo tunakwenda nacho hivyo hivyo. Wagani ndani ya nchi yetu pia kwenye sekta ya kilimo ni changamoto Wizara inayohusika na kuajiri Wizara ya Utumishi tunaombeni mtuambie shida ni nini inayosababisha kushindwa kuajiri wagani wakutosha kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wagani ni muhimu sana, tunaona hata watu wamoja moja ambao wanajitutumia wenyewe kwa jitihada zao kuweza kulima kilimo cha kuondokana na umasikini, kilimo cha kutoka kwenye mvua ya Mwenyezi Mungu kwenda kwenye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji bado wamekuwa wakikosa huduma hii ya ugani kwasababu tu ya Serikali kushindwa kuajiri wagani kwenye maeneo yetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe pia kama kweli tunahitaji tija kwenye sekta ya kilimo na tuweze kujenga na kuimarisha uchumi wa Taifa letu tuhakikishe kwenye bajeti hii inayokuja kwenye sekta ya kilimo twendeni tukaajiri wagani wa kilimo ili wakulima wetu waweze kupata hiyo huduma muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye suala la wagani suala la wagani wako TAMISEMI kwenye kilimo huku hawapo kwa hiyo, pale wanapokwenda kupata changamoto wagani hawa wanashindwa namna ya kuzifikisha mahali husika. Lakini mgani huyu unakuta mgani huyo ni mtendaji wa kata, mgani huyo ni Afisa Mifugo, mgani huyo huyo ndiyo hata yeye anashughulika na masuala ya kilimo kwa hiyo, unamkuta mtu mmoja ana majukumu kadhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba pia kwenye suala zima la wagani wanaohusiana na kilimo tuwarudishe Wizara ya Kilimo ili waende wakasimamiwe na Wizara yao na waweze kufuatiliwa na tuweze kupata tija kwenye suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie kidogo kwa dakika chache zilizobaki miundombinu tunafahamu vizuri nimalizie tu kidogo dakika moja tunafahamu tuna barabara za kimkakati…

NAIBU SPIKA: Nina orodha ndefu hapa Mheshimiwa.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja tu my dear kidogo tu dakika moja ningekuwa nimeshamaliza tuna barabara za kimkakati tangu Bunge la 10 tuliahidiwa barabara ya kutoka Kilindi kupita Chemba tunaenda kuungana na Singida barabara ile mpaka leo bado hatujaweza kuona nini mkakati wake. Niombe Wizara mtakapokuja kuja kuhitimisha tunaombeni tuione barabara ya kutoka Kilindi inayokwenda kupita Jimboni kwangu Chemba…

NAIBU SPIKA: Haya ahsante Mheshimiwa hiyo barabara umeshaitaja, kwa hiyo imeshasikika.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: …nakwenda kuunganisha na Mkoa wa Singida nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu ambayo inatusababisha tuendelee kuishi.

Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Pili wa Bunge hili, niliuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusiana na suala nzima la kilimo cha kutegemea mvua ya Mwenyezi Mungu. Waziri Mkuu majibu aliyoyatoa alisema kama Serikali inatoka sasa kwenye kilimo cha kutegemea mvua ya Mungu na kwenda kujikita kwenye kilimo cha tija, kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siku za nyuma sekta ya umwagiliaji ilikuwa Wizara ya Maji lakini kwa kuona ufanisi wake ni mdogo tukashauri sekta ya umwagiliaji itoke kwenye Maji iende Kilimo ili watu wa Kilimo waweze kuisimamia sekta hii na iweze kuleta tija ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini cha kushangaza na cha kustaajabisha baada ya sekta hii kutoka Wizara ya Maji kuletwa Wizara ya Kilimo mwaka 2020/2021bajeti iliyoisha mwaka jana, Wizara ya Kilimo, Sekta ya Umwagiliaji Fungu Na.5 ilipitishiwa au iliidhinishiwa shilingi bilioni 17, fedha za maendeleo za ndani zilikuwa shilingi bilioni 3 na fedha za nje zilikuwa ni shilingi bilioni 9. Sasa katika hizi fedha za ndani shilingi bilioni 3 Serikali haijatoa fedha hata shilingi moja kwa ajili ya kwenda kwenye umwagiliaji na badala yake fedha za nje wenzetu wakatoa shilingi bilioni 5. Tunasema Serikali tunakwenda kujikita kwenye kilimo chenye tija cha umwagiliaji mnatenga wenyewe bila ya kulazimishwa mnasema hii ndiyo tutakayoiweza hata kuitoa nako ni shughuli, imeshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najiuliza kama Bunge tuna sababu gani ya kukaa humu ndani na jadili na kupitisha fedha halafu haziendi kwenye kazi ambayo tumekwenda kuipitisha? Leo Fungu Na.5 linaomba fedha za maendeleo shilingi bilioni 5, shilingi bilioni 3 haikupewa shilingi bilioni 5 itapewa? Hivi vitu vinakwaza, vinakatisha tamaa, vinaturudisha nyuma na wakati mwingine tunaona hatuna sababu ya kuendelea kuchangia Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kwamba sekta hii ndiyo ambayo imeajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania. Hivi inasema imeajiri kwa wakulima mmoja mmoja kuhangaika huko kwa majembe ya mikono, kwa mikopo ya gharama kubwa, ilhali tuna Benki yetu ya Kilimo ambapo lengo na madhumuni ilikuwa ni kwenda kuwasaidia wakulima wetu kuweza kupata fedha na mitaji kwa ajili ya kuhakikisha wanakwenda kulima kilimo chenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe kwa Serikali kwa kuwa Benki ya Kilimo iko chini ya Benki Kuu ambayo masharti yake yanakwenda kubaki vilevile kama benki nyingine, tuone namna gani tunakwenda kuitoa Benki hii ya Kilimo ili tuweze kuipunguzia masharti wananchi wetu waweze kupata mikopo ya yenye tija na hatimaye waweze kilimo chenye tija.

T A A R I F A

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa naipokea.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba Wizara ya Kilimo wana Mfuko unaitwa Agriculture Trust Input Fund ambapo ni mfuko huu, pamoja kwamba ni mfuko chini ya Wizara uko one hundred percent commercial. Wanamkopesha mkulima anayetegemea mvua, wanamkopesha mkulima ambaye hapati masoko lakini katika kipindi cha miaka minne ambayo wamempangia kurejesha akisharejesha anakuta kuna interest ambayo inazidi asilimia 50 ya hela halizokopa. Kwa hiyo, matokeo yake watu wengi wanaona hakuna tofauti ya hela inayosimamiwa na Wizara ambayo ilipangwa kwa ajili ya kuwasadia wakulima na ile inayotoka kwenye benki za biashara.

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana.

SPIKA: Mheshimiwa Kunti unapokea taarifa hiyo?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nimshukuru kaka yangu Mheshimiwa Kanyasu, haya yote ndio tunayazungumza suala zima la kumsaidia mkulima, Serikali dhamira na nia yenu ni kuwasaidia wakulima kuweza kuhakikisha wanakwenda kupata fedha ama mikopo yenye riba nafuu na itakayokwenda kutolewa kwa muda mrefu hili waweze kuhakikisha kwamba wanalima mazao yao na wanapata fursa ya kuweza kuyauza kwa tija na hatimaye waweze kurejesha hiyo mikopo.

Mheshimiwa Spika, lakini stakabadhi ghalani Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa wamesema suala zima la stakabadhi ghalani na Mkoa wangu wa Dodoma tuliathirika sana na wakati wizara inatulekea stakabadhi ghalani Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Bashe alituita pale ukumbi wa Msekwa tulimkatalia tukamwambia stakabadhi ghalani kwa kuwa Serikali hamjajipanga kuleta stakabadhi ghalani kwa kuwa wananchi wetu hawana taarifa hawaelewe ni chochote. Lakini pili hamjaweza kuwasaidia wakulima wa Mkoa wa Dodoma na mpaka mfikie hatua ya kwenda kutuletea stakabadhi ghalani.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wao wana mabavu, wana vyombo vya dola wana kila kitu wakaamua kutuletea stakabadhi ghalani watu wetu walipigwa walinyanganywa mazao yao lakini pili mbaya zaidi Wilaya ya Chemba, Kata ya Mpendo tunapakana na Bahi shughuli zote na kata ile ndiyo inayolima ufuta kwa wingi Kata ya Mpendo wanapata huduma Wilaya ya Bahi, wakulima wa Mpendo walikuwa mazao yao wakivuna wanapeleka Bahi wanauza.

Mheshimiwa Spika, baada ya stakabadhi ghalani kwa kuwa zoezi hili lilikabidhiwa kwa Wakuu wa Wilaya wananchi na wakulima wa Kata ya Mpendo walikuwa wanalazimishwa awe ana kilo mbili awe ana debe moja awe na gunia atoke Mpendo kilometa 97 mpaka Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba pale kwenye ghala aende akaweke bodaboda ukikodi ni shilingi 35,000, kilo ya ufuta ni shilingi 2,000 ana debe moja ni Shilingi 40,000huyu mkulima mnamuinua kwa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana stakabadhi ghalani wabaki nayo wao Bashe aipeleke kule pamoja na Mheshimiwa Mkenda pelekeni kwenye majimbo lakini kwetu kwenye Mkoa wa Dodoma tunawashukuru kwa huduma hiyo lakini hatuhitaji hata kuisikia na nitakuwa wa kwanza kwa ajili ya stakabadhi ghalani sitaki kusikia stakabadhi ghalani sitaki kusikia stakabadhi ghalani ndani ya Mkoa wangu wa Dodoma. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, lakini nitumie fursa hii kukupongeza kwa nafasi uliyonayo. Hongera na naamini utakitendea haki kiti hicho. Naomba nianze kuchangia Wizara hii alipoishia Mheshimiwa Olelekaita kwenye migogoro ya hifadhi na watumiaji wengine wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Mkoa wa Dodoma tuna mapori mawili ambayo yako Wilaya ya Chemba na Wilaya ya Kondoa. Pori la Mkungunero ambalo lipo Kondoa na Pori la Swagaswaga ambalo lipo Wilaya ya Chemba. Pori hili la Mkungunero limekuwa ni kichaka cha Maafisa wa Wanyamapori kutesa Watanzania wasiokuwa na hatia eti kwa sababu tu wana ng’ombe, eti kwa sababu tu ni wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2019 nilizungumza ndani ya Bunge hili nikaeleza mateso na manyanyaso wanayopata wananchi wa wilaya ya Kondoa kwa Kata ya Keikei, Kata ya Kinyasi pamoja na Kata ya Itasu. Mheshimiwa Waziri nimekuja kwako mara kadhaa nikiwa nakulalamikia suala hili na ninyi Wizara mnasema kuna shida gani? Pale tumemaliza kabisa Mkungunero. Ukweli ni kwamba mnafukia kombe mwanaharamu apite wakati Watanzania wanaumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki mbili zilizopita kuna wananchi watatu ambao wamekamatiwa ng’ombe wao. Wawili wamelipa kwa makubaliano na Maafisa Pori wa Hifadhi ya Mkungunero. Mmoja akakataa akapelekwa Mahakamani, ng’ombe 50 kalipa shilingi milioni 10 faini. Hivi huyo mwananchi mkulima, mfugaji anayetegemea mifugo yake kwa ajili ya kuendesha maisha yake ya kila siku na kulichangia kodi Taifa hili, mnachomtafuta ni nini watu wa hifadhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, katika hifadhi ile kuna akina mama ambao wanafanya shughuli zao mbalimbali za kujitafutia uchumi, wamekuwa wakibakwa kwenye Hifadhi ya Mkungunero, wamekuwa wakipata mateso ya kurushwa kichurachura, kupigwa na kila aina ya mateso kadha wa kadha wanayoyapata kwa ajili ya hilo pori. Mheshimiwa Waziri, kuna shida gani? Serikali ni moja, chama kimoja, Mawaziri mnakaa kwenye Baraza la Mawaziri, mnashindwaje kukaa chini na kuweza kutatua mgogoro wa pori hili? Serikali Sikivu, Serikali ya wanyonge mnaotamani kuwapigania Watanzania, hawa Watanzania hawana hatia, ardhi haiongezeki Mheshimiwa Waziri, watu tunaongezeka.

Pori lile Mheshimiwa Waziri kwa akili tu ya kawaida, Warangi sisi hatuna mahali pa kwenda. Lile ndiyo eneo letu tumezaliwa kule, twende wapi? Tunaomba Pori ya Mkungunero, kagaweni eneo, tuachieni na sisi watoto na wajukuu tuendelee kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Swagaswaga Wilaya ya Chemba Kata ya Lahoda, pale kuna wafugaji; na ninashukuru Mheshimiwa Mpina amelisema. Kuna wafugaji mwaka 2018/2019, Mheshimiwa Mpina ukiwa Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Ulega akiwa Naibu Waziri wako; Mheshimiwa Ulega alienda Wilaya ya Chemba Pori la Swagaswaga akakutana na wafugaji waliokamatiwa ng’ombe wao wasiokuwa na hatia wamewekwa pale, hawana chakula, hawana maji, hawana dawa, hawana chochote. Ng’ombe wamekufa zaidi ya 500. Tulisema humu ndani, hamkutaka kusikia eti tu kwa sababu mnalinda uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji uhifadhi lakini siyo kwa maisha ya mateso ya namna hii mnayotufanyia Watanzania. Mkitushirikisha wananchi, tutaulinda huo uhifadhi kwa sababu na sisi tunautaka na tunauhitaji sana. Ila kama mtaendelea kutunyanyasa, kututesa na kutuonea, hata hao wahifadhi wenu mnaowaleta kule, ipo siku hapatatosha. Tutachoka kunyanyaswa, tutaamua kuchukua hatua mkononi, kitu ambacho sitamani kitokee. Mheshimiwa Aida amesema, kwake imeshatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mstaafu Mheshimiwa Mpina kasema. Zaidi ya ng’ombe 400 mpaka leo Wizara ya Maliasili hamtaki kurudisha ng’ombe wale, mnachotaka ni nini? Mmewapeleka wapi hao ng’ombe? Nani anao mpaka leo miaka miwili?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)