Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joyce John Mukya (7 total)

MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shida kubwa ya maji katika Mkoa wa Arusha especially Jiji la Arusha inatokana na tatizo la mgao wa umeme tatizo ambalo katika nchi yetu tunaona kabisa haliishi leo wala kesho. Kwa mfano, Arusha Mjini tulikuwa tunapata maji lita laki moja kwa siku lakini mwaka 2013 tunapata maji lita 45,000 na katika Kata ya Mushono ni magaloni matano kwa siku hadi kufikia sasa kwa wiki mbili unapata maji mara mbili. Tatizo hili limekuwa kubwa sana na hatuoni kama kuna mkakati madhubuti wa Serikali kusaidia tatizo hili kwa sababu shida kubwa ni ya umeme na umeme wa nchi hii hata siku moja haujawaka frequently. Ni nini mkakati wa Serikali kuhusu kusaidia kutatua changamoto hii kwa sababu umeme katika nchi hii bado ni wa mgao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri mradi huu ni wa muda mrefu, lakini shida ya maji katika Mkoa wa Arusha ni shida ya kudumu na ya muda mrefu sana kama ulivyosema katika jibu lako …
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi huu ni wa muda mrefu na shida ya maji katika Mkoa wa Arusha ni ya muda mrefu, nini mkakati wa Serikali kutatua kwa haraka tatizo hili ili wananchi wa Arusha wapate maji kwa haraka?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimfahamishe Mbunge vitu asivyovifahamu. Kwanza pale KIA tumeweka sub-station kwa ajili ya umeme wa KIA na maeneo ya pale tu. Ukienda Mererani, katika wachimbaji 10 wa Tanzanite wachimbaji tisa wanatumia umeme bila kulipa, wanaiba umeme. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba ukitaka umeme wa uhakika shughulika na wezi wa umeme wa Arusha, ahsante.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu sehemu ya pili ya swali lake kwamba mradi huu ni wa muda mrefu, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba ili tuweze kufanya kazi nzuri lazima kwanza tufanye usanifu ili tuwe na uhakika kabisa kwamba maji yatakuwepo ya kutosha maeneo yote. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avumilie na mpango unaoletwa na Serikali ni wa uhakika kwamba tupate maji ya kutosha mpaka mwaka 2025.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kumekuwa na tabia mbaya na chafu ya udhalilishaji wa hawa waajiri wa madini ya kuwapekua wafanyakazi sehemu za siri. Hii imefanyika katika Kampuni ya Tanzanite one kule wanapovuna madini ya Tanzanite, wanawapekua sehemu za siri hasa sehemu za kujisaidia haja kubwa. Je, hakuna njia mbadala ya kufanya zoezi hilo zaidi ya kuwadhalilisha hawa wafanyakazi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI,VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, anachokisema Mheshimiwa Mbunge, mimi mwenyewe nilikwenda pale Tanzanite one katika mgodi huo, nilikutana na changamoto hiyo kubwa ambayo wafanyakazi waliieleza mbele yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa ziara ile nilitoa maelekezo na taratibu zote za namna ya ukaguzi unavyopaswa kufanyika ili usidhalilishe utu wa wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika migodi hiyo. Maelekezo yalitolewa ya kwamba zipo taratibu za kufuata katika ukaguzi lakini siyo za kumdhalilisha mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maelekezo tayari yapo, kama vitendo hivi vinaendelea basi niwaombe wafanyakazi wale waripoti tuchukue hatua stahiki zaidi.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarehe 31Januari, 2018 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dokta Kigwangala alitoa ilani kwenye kiwanja Namba 4091 kilichopo eneo la Njiro Mkoa wa Arusha kwamba wale watu ni wavamizi, wamejenga eneo la Serikali la kiwanja kinachoitwa kwa jina la Tanzania Tourist Corporation.
Swali langu, kwa nini Mheshimiwa Kigwangalla Waziri wa Maliasili na Utalii asikutane na watu hawa kwa sababu watu hawa pia ni wamiliki halali eneo lile kwa sababu wana hati pia na licha ya hivyo haoni kama huu ni uzembe wa Serikali yenyewe na je, kwa nini wasimtafute aliyehusika kufanya ili kabla hajawahukumu wananchi waliojenga katika eneo lile?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ametoa hilo tamko ametoa siku 30 kwa wale watu waliovamia wajisalimishe waje zile documents halali ili kusudi Serikali iweze kutathmini na kuangalia kama kweli hayo maeneo wameyapata kihalali. Kwa hiyo, siku 30 baada ya hapo ndipo tutafanya uamuzi unaostahili.(Makofi)
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Tatizo hili linafanana kabisa na tatizo la pori tengefu la Loliondo ambalo limedumu kwa kipindi cha miaka 25 sasa au zaidi, tokea nchi hii imepata uhuru ni awamu nne zimepita za uongozi na zote zikiongozwa na Serikali ya CCM. Kila awamu ilikuwa inapeleka uongozi wake kule kwa ajili ya kuongea na wananchi kwa ajili ya mgogoro huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha aunde Kamati ya kwenda kushughulika na tatizo hili. Amepeleka ripoti na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla amepeleka ripoti lakini mpaka sasa hakuna ambacho kimefanyika;
Naomba kujua je, ripoti hizi, zinasema wananchi wale waendelee kuteseka au ni nini ambacho kiko chini ya carpet ambacho kinasababisha wananchi hawa wasipiwe suluhu, na haki yao kupitia mgogoro huo ambao umeikumba Serikali hii na nchi hii kwa muda mrefu kwa muda wa miaka 25 na zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa muda mrefu kumekuwa na tatizo na mgogoro huko Loliondo na mgogoro huu umedumu kwa miaka mingi. Hivi sasa Serikali kama ulivyosema mwenyewe imechukua hatua za kuunda kamati mbalimbali ikiwemo kamati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambayo ilileta mapendekezo na mapendekezo hayo yamepitiwa na Serikali, Serikali imefanya uamuzi ambao tumeufikia ni kutaka kuwa na chombo maalumu kitakachosimamia lile pori la Loliondo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Serikali inafanya mchakato wa kuanzisha hicho chombo au mamlaka ambayo itahusika na usimamizi wa pori hilo la Loliondo kwa usimamizi na ushirikiano wa wananchi wenyewe wa Loliondo. Hii ndiyo tunaamini kwamba itakuwa suluhu ya tatizo ambalo limedumu kwa muda mrefu katika lile eneo. Kwa hiyo, ni hivi karibuni tu tutaleta huo mwongozo na tutaleta hiyo mamlaka au tutaleta chombo hicho ambacho kitakwenda kusimamia tatizo hilo la Loliondo.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, mapema mwaka huu alifanya ziara katika Mkoa wa Arusha hususan katika Jimbo la Monduli na akatembelea Vituo vya Afya vya Makuyuni na Kigongoni. Vituo hivyo vilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi na kufikia kwenye lenta na aliahidi kuvimalizia mapema mwaka huu au mwaka kesho. Naomba maoni ya Mheshimiwa Waziri, je, ni lini atatoa fedha hizo za kumalizia Vituo hivyo vya Afya vya Jimbo la Monduli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli siku ile nilifika Arusha, nikafika Monduli na priority yetu ni kwamba tumeitenga pale na commitment tuliyoifanya ni kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mto wa Mbu ambapo tumezungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimewapongeza wananchi kwa juhudi kubwa wanayoifanya katika suala zima la ujenzi wa Vituo vya Afya. Kwa hiyo, ni commitment ya Serikali na tuko katika michakato ya aina mbalimbali, tutaweza kukamilisha mambo haya kwa kadri inavyowezekana.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tatizo hili linafafana kabisa na tatizo la Kijiji cha Ngarasero katika Jimbo la Ngorongoro, Mkoa wa Arusha. Je, ni lini Serikali itapeleka minara katika eneo hilo ili wananchi waweze kupata mawasiliano katika Kijiji cha Ngarasero?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ngorongoro ni moja kati ya maeneo ambayo nayo yana changamoto ya mawasiliano. Kwa baadhi ya sehemu ambazo zina changamoto, tayari tumekwishatuma watu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwenda kufanya tathmini ya mahali gani panatakiwa kwenda kuwekwa minara kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pindi watakapotuletea taarifa, tutatangaza tenda ili makampuni mbalimbali ya simu yajitokeze kwa ajili ya kujenga minara ili kutatua changamoto hiyo.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Shule ya Msingi ya Uhuru iliyoko Arusha ni shule pia yenye watoto walemavu, shule hii inashida pia ya miundombinu, vyoo vyake havifai ukizingatia kuwa walemavu wengi au baadhi ya walemavu ni wale ambao wanatambaa, ukiangalia vile vyoo ni vichafu, havifanyi kazi vizuri maji mpaka yanatitirika nje na tunavyoelewa ukiongelea swala zima la vyoo ni afya.

Je, Serikali itarekebisha lini miundombinu ile ya vyoo katika hile shule ya Uhuru ya Arusha Mjini ili kuwasaidia walemavua hawa watoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba nichukuwe fursa hii kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Arusha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi nikimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri


ya Liwale naomba nitumie fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Jiji Arusha kwa sababu nina uhakika wanavyanzo vya mapato vya kutosha, atizame namna gani wataweza kuboresha miundombinu ili wanafunzi wetu wenye uhitaji maalum wasome katika mazingira yaliyo bora.