Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joyce John Mukya (14 total)

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya michezo vimegeuzwa kuwa viwanja vya usheherekeaji wa sherehe mbalimbali na badala ya kuviendeleza kama viwanja vya michezo ambavyo vingeweza kuwasaidia vijana, wanawake na watoto katika kujenga, kufurahia kuimarisha afya zetu na kuchangamsha miili yetu na hata kutupa afya njema kila siku. Hatimaye viwanja hivyo vimegeuzwa kuwa sehemu ya kufanyia sherehe za Kitaifa na sherehe za Chama cha Mapinduzi (CCM). Mbaya zaidi viwanja hivi vimegeuzwa viwanja vya CCM, kwa sababu vyama vya upinzani hawaruhusiwi kufanya shughuli zao katika viwanja hivi isipokuwa Chama cha Mapinduzi tu. Nina ushahidi na hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie viwanja hivi vitumike kwa shughuli za michezo na kama ni shughuli nyingine basi kuwe na usawa na haki kwa sababu vyama au itikadi ni mapenzi ya mtu binafsi tu, lakini mwisho wa siku Utanzania wetu unabaki pale pale.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii kama nilivyoainisha hapo juu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea tatizo la wafanyakazi kutopata ajira za kudumu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nilishafanya kazi na Jumuiya kabla sijawa Mbunge kuanzia mwaka 2006 mpaka 2009 kama IT Assistant. Wakati najiunga pale nilikuta wafanyakazi wa temporary ambao wanafanya kazi kama vibarua, naweza kusema hadi leo hii ni muda wa miaka 10 na zaidi sasa, baadhi yao hawajaajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua toka kwa Mheshimiwa Waziri ni lini ajira za hawa wafanyakazi zitatangazwa ili waweze kuajiriwa? Kwa sababu wangekuwa hawatakiwi, wasingekuwepo kazini hadi leo hii. Naweza kukupa majina yao kama utahitaji pia na wengi ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine, ni Serikali yetu kutopeleka fedha za kuendesha Jumuiya kwa wakati. Mfano, tokea makubaliano ya bajeti iliyopita kati ya Partner States hadi leo hii nchi yetu ya Tanzania haijapeleka au kukamilisha mchango wake wa kuendesha Jumuiya hiyo. Hii ni aibu sana kwa nchi yetu na ukizingatia Jumuiya hii Makao Makuu yake yapo Tanzania. Ilitakiwa tuoneshe mfano kwa nchi wanachama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni wafanyakazi wa ngazi ya profession kutokupatiwa Diplomatic Passports. Kama yalivyokuwa makubaliano ya nchi wanachama, yaani Headquarters Agreement, wafanyakazi wa level hii wanaotoka nchi nyingine wana diplomatic passports isipokuwa nchi yetu. Hili nilishalisemea tena Bungeni mara mbili na Mheshimiwa Waziri akaahidi watapewa kwani ni haki yao, lakini hadi leo imekuwa ni hadithi tu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kujua ni lini watapewa haki yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wafanyakazi wa Jumuiya wamekuwa na shida ya kupata Work Permit. Ni aibu kubwa sana kwa hili jambo. Mtumishi ana mkataba wa miaka mitano, lakini bado Serikali haimpi Work Permit ya miaka mitano na kusababisha kero kubwa kwa nchi wanachama wanaokuja kufanya kazi nchini ambako ndiyo sehemu Headquarter ilipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Naomba Mheshimiwa Waziri anijibu maswali yafuatayo:-
(1) Ni lini Wizara hii itaanza kukaa na Wabunge wa EAC ili kujadili mambo mbalimbali, kama mtakavyojipangia ratiba, kama Wizara ya EAC ya Awamu ya Nne ilivyokuwa inafanya?
(2) Ni lini mtawapatia ofisi Wabunge wa Tanzania ambao wanaunda Bunge la Afrika Mashariki na waache kufanyia kazi hotelini au nyumbani mwao?
(3) Ni lini Serikali ya Tanzania itaanza kuwapa mikopo ya magari Wabunge wa EAC kama zinavyofanya nchi wanachama, mfano Kenya na Uganda, ili waache kutumia mishahara yao na posho kununua magari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee alipoishia mwenzangu Mheshimiwa Zubeda kuhusu walemavu. Walemavu wamekuwa wakidhalilishwa sana, walemavu wamekuwa hawasaidiwi kimatendo. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu katika ukurasa wa 47 amezungumzia
suala la walemavu lakini hakuna mkakati wowote unaoonesha kwamba walemavu watasaidiwa kimatendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kama ambavyo tunatoa asilimia 10 kwenye Halmashauri zetu kutoka kwenye own source, naomba kwenye asilimia hizo hizo 10 iwe ni lazima kwa wanawake asilimia tano wawepo walemavu at least watano au 10 kwenye watu 30 na walemavu wengine watano kwenye watu 30 ambao ni vijana. Naomba sana kwa sababu walemavu hawa wanaonekana kwa macho tofauti na wanawake na vijana ambao mara nyingi wamekuwa wakitumika kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasiasa mara nyingi wamekuwa wakiwatumia wanawake na vijana kwa ajili ya kuwatafutia kura kwa vipindi vya uchaguzi vijavyo lakini naomba sana suala la walemavu wamekuwa hawana msaada dhahiri unaoonekana. Naomba sana suala la walemavu, aliliongelea sana Marehemu Dkt. Elly Macha, naomba tumuenzi marehemu Mheshimiwa Macha kwa kuwasaidia walemavu wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hela za maendeleo; ni dhahiri kwamba Serikali yetu imeshindwa kabisa kuisaidia nchi hii kwa hela za maendeleo. Asilimia 34 tu mpaka bajeti inakwisha ya mwaka 2017, hakuna hela za maendeleo ambazo zimeenda kwenye Halmashauri zetu ambazo
zinaenda kuwasaidia moja kwa moja wananchi kule chini. Ingekuwa hakuna own source katika Halmashauri zetu, mfano, Arusha Mjini tunaendesha Halmashauri kutokana na own source zetu wenyewe. Mpaka Februari mwaka 2017 imeenda shilingi milioni 320 kati ya bilioni tatu ambayo ni asilimia 11 tu iliyopendekezwa mwaka 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tunavyoendelea hivi tunaenda kuua zile Halmashauri zetu, wananchi hawatapa maendeleo na kwa Halmashauri ambazo ziko vijijini hawana own source za maana, wanashindwa kuendesha vikao, wanashindwa kulipana hela za vikao, wanashindwa kufika kwenye vikao kutokana na umbali ama distance kulipana mafuta na gharama za usafiri kwa sababu tu Serikali haipeleki hela za maendeleo kule chini. Naomba sana hili mliangalie kwa jicho la pekee sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongele suala la utawala bora; kumekuwa na tabia mbaya sana Viongozi wa Serikali wanachukua madaraka mikononi na kuanza kutumia hela za Halmashauri au hela za Mikoa na Wilaya walizopangiwa kuanza kutumia bila kuwashirikisha Kamati za Fedha na Uchumi za Halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limetokea mwaka jana Septemba. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Mrisho Gambo aliita Walimu wa AICC pale Simba Hall akaongea nao, wakahojiana, Walimu 701 wakampa madai yao akamuamuru Mkurugenzi wa Jiji, Ndugu Athuman J.
Kihamia awalipe wale Walimu shilingi 169.8 milioni, hii siyo sawa. Hata kama Walimu wale walikuwa wanatakiwa walipwe zile pesa lazima ilitakiwa vikae vikao vya Kamati ya Fedha na Uchumi, lazima vikae vikao lakini siyo Mkuu wa Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anaumia sana na wale Walimu angeingia kwenye Mfuko wake wa Mkoa na kutoa hela kwa ajili ya kuwalipa wale walimu. Hilo alilofanya siyo sawa, alipoambiwa akasema nawakomesha na hapa nimeanza tu lakini mtakoma. Pesa zile zilikuwa kwa ajili ya kuwalipa Madiwani, ilikuwa ni stahiki za Madiwani kwa ajili ya vikao, kwa ajili ya vocha, kwa ajili ya usafiri lakini Madiwani ambao wanaongozwa na Chama cha CHADEMA walivumilia yote na leo wanaenda kwenye vikao wanalipwa sh. 40,000 mpaka
sh. 60,000 mbali walivyokuwa wanalipwa sh.120,000 kwa kikao kimoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la Faru Fausta; Serikali hii imejitanabaisha kuwa inapunguza matumizi na mpaka sasa hakuna mtu yeyote ambaye analipwa milioni 17 kwa mwezi, lakini Faru Fausta analipwa milioni 64 kwa mwezi hiyo ni mara tatu. Gharama za Faru Fausta huyo ambaye ni Mzee ana miaka 54 ni kwa ajili ya gari lake ambalo linabeba chakula chake, kwa ajili ya chakula kinachotoka nchini Kenya aina ya LASEMI, kwa ajili ya kulipa Walinzi 15 ambao wanamlinda kwa masaa 24 na nguvu za Kijeshi. Faru Fausta huyu ni Mzee lakini ukiongea na Wizara ya Maliasili wanakwambia eti kwamba anaingiza fedha nyingi za kigeni sawa na bilioni 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kama Wazungu au Watalii wanakuja Tanzania kumuangalia Faru Fausta peke yake. Naamini Watalii wanakuja Tanzania kuangalia utalii, kujifunza kutalii Tanzania lakini wakifika Tanzania wanakutana na Faru Fausta. Naomba sana Serikali kwa sababu inajidai kwamba inapunguza gharama na kutumbua majipu, ianze kumtumbua Faru Fausta ambaye ni Mzee sana sasa hivi na wanasema kwamba nyumba yake ikishakamilika atatumia milioni 20.4 tu sawa sawa na milioni 244 kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado gharama hizi ni kubwa sana. Kule chini Ngorongoro wale Wamasai na wale wakazi wa Ngorongoro wanahangaika, hawana mahali pa kulisha mifugo yao, Serikali imeshindwa hata kuwajengea majosho kule juu kwa ajili ya kulisha mifugo yao, Faru Fausta ambaye ni Mzee anahudumiwa kwa milioni 64 kwa mwezi, hii siyo haki na siyo sawa kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie katika suala la elimu bure; elimu bure ni kwenye makaratasi tu, ukienda kule chini elimu bure hakuna cha elimu bure zaidi ya kulipa ile UPE. Walimu wamekuwa kwanza wanahangaika, hakuna walimu wa sayansi, hakuna walimu wa hisabati, imefikia wazazi wakae vikao na walimu na wanafunzi kutafuta walimu wa hisabati na walimu wa sayansi. Inabidi walimu wakae vikao na wanafunzi na wazazi kulipa walinzi, kulipa maji kwa ajili ya wanafunzi wao waweze kusoma, hii siyo sawa kabisa hapa hakuna elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Ma-DC na Ma-RC badala ya kupigana na Wapinzani kwenye Wilaya zenu na Mikoa yenu, tafuteni njia mbadala ya kusaidia a elimu bure ambayo ni sera ya Serikali yenu. Kama mnaweza kuchangisha hela za Mwenge, Mheshimiwa Gambo Arusha alinunua pikipiki 200 kwa kusaidiana na wadau wa Mkoa wa Arusha sasa Mheshimiwa Gambo fanya hili la elimu bure kwa watoto ambao wanakua sasa hivi. Naomba sana hili mliangalie kwa jicho la pekee kabisa, hakuna elimu bure hapa ni utapeli tu wa makaratasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende katika suala la utalii; suala la utalii tangu kodi na tozo za utalii zipande limekuwa halina faida kwa nchi yetu. Kama mnavyofahamu nchi ya Kenya ndiyo imekuwa mpinzani mkubwa sana kwetu kwa suala la utalii. Nchi ya Kenya imeondoa kodi ya VAT, nchi ya Tanzania imeweka kodi ya VAT, nchi ya Kenya imeondoa kodi kwenye magari ya utalii wakati wa matengenezo, nchi ya Kenya imeondoa Visa kwa watoto na kuwafanya watalii ambao wana familia waende Kenya na siyo Tanzania. Nchi ya Kenya imeondoa Park fees Tanzania vyote hivyo mmeviweka, Tanzania mnataka utalii wa aina gani ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Tanzania, naomba sana nchi yetu, naomba sana Waziri Mkuu anavyokuja kujibu utalii Tanzania umeshuka katika ukurasa wa 20 amesema kwamba utalii umepanda kwa asilimia 1.2 siyo kweli. Wageni hawa ambao wanaingia nchini ni wageni ambao wanakuja kwenye mambo ya kibiashara na mikutano lakini takwimu za utalii zinasema wageni wote wanaokuja Tanzania ni watalii siyo kweli, siyo watalii wa vivutio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wageni wengi wanatokea Rwanda, wanatokea Burundi, wanatokea South Africa na hii ni kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu anapopewa takwimu zipitie na watu wako, anapokuja hapa kwenye Bunge ziletwe
takwimu ambazo ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee mimea vamizi katika crater ya Ngorongoro. Kumekuwa na mimea vamizi sana katika crater ya Ngorongoro. crater ya Ngorongoro kuna uoto wa asili. Mimea vamizi imeharibu crater ya Ngorongoro, Waziri January Makamba alienda lakini
hali ni mbaya na mbaya zaidi mimea hii inakua kwa kasi sana. Sehemu ambako mimea hii inakua, wanyama hawawezi kwenda kula. Sasa inaharibu uoto wa asili kule. Naomba sana Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Waziri Mkuu ashirikiane… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. JOYCE Y. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo mbalimbali katika hotuba hii ya bajeti ya 2017/2018 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mazingira kwa mimi, ninavyofahamu au kutafsiri ni afya kwa maono ya kwamba mazingira yakiwa machafu yataathiri afya za binadamu, wanyama au viumbe hai chochote ikiwemo mimea. Kwa hiyo, naomba sana Wizara hii ipewe kipaumbele, kiuchumi kwani ndio Wizara inayolinda maisha na afya ya viumbe hai moja kwa moja na kama mazingira hayataangaliwa basi afya na viumbe hai zitakuwa hatarini wakati wowote. Matokeo yake ni kuhatarisha uhai wa viumbe hai kupitia magonjwa na upungufu wa virutubisho mbalimbali na hatimaye hata kuwasababishia vifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyoelewa wanyama, mimea tunashirikiana katika mambo mbalimbali ili kuweza kuishi mfano katika hewa ya oxygen na carbondixide. Hivyo basi, ni dhahiri mazingira ni kitu muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimea vamizi, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana katika maeneo mbalimbali ndani na hasa katika maeneo ambayo kuna mifugo na wanyama ambao wamekuwa wakitegemea majani, kama chakula. Mfano katika eneo la Ngorongoro kumekuwa na mimea vamizi sana na ambayo inakuwa kwa kasi sana siku hadi siku na kusababisha wanyama kuyatenga maeneo hayo yenye mimea vamizi (invasive).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimea hii pia imekuwa ikiharibu uoto wa asili katika eneo la Ngorongoro na kuvuruga kabisa ekolojia. Ningeomba sana Serikali ichukue hatua za haraka katika kutokomeza mimea hii na kuendelea kuitunza mbuga ya Ngorongoro ili iweze kuiletea nchi yetu watalii na kuingiza fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la mimea vamizi limelikumba eneo la hifadhi ya Mlima Rungwe ambayo ni aina ya miti inayoitwa Mipaina ambayo imekuwa ni tishio kubwa katika Mlima Rungwe. Miti hii imekuwa ikisababisha upotevu wa baianowai ya Mlima Rungwe uliopo Mkoani Mbeya na kupoteza uoto wake wa asili. Kama nilivyoshauri
katika bajeti ya Waziri Mkuu wakati nimechangia kwa kuongea, naiomba tena Serikali iangalie tatizo hili kwa karibu kabisa ili kuweza kuidhibiti mimea hii vamizi na kunusuru maeneo haya yaliyovamiwa na kibaya kabisa mimea hii imekuwa ikikausua hadi vyanzo vya maji na kusababisha ukame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa ukuta wa Pangani, ujenzi wa ukuta huu uliopo katika Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Pangani unaelekea kutokumalizika kwa wakati kama ilivyopangwa kumalizika Novemba, 2017, kama Serikali haitapeleka fedha za ndani kiasi cha 10% walichokubali kukitoa wakati ujenzi huu unaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zingine za nje zimeshatolewa na ujenzi unaendelea vizuri katika upande wa mashariki wa ukuta huo kwani fedha za ujenzi zimetoka nje kwa wafadhili na wametoa fedha zote. Changamoto kubwa ipo katika eneo la Pangadeco na ndio eneo ambalo lina wakazi wengi ukilinganisha na eneo la mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la Pangadeco ndiko wanategemea ile 10% ya fedha za ndani ambazo Machi, 2017 zilikuwa hazijatolewa hata shilingi moja. Naishauri sana Serikali ipeleke fedha hizo ambazo ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na kiasi kilichotolewa na wafadhili cha 90%, kama nilivyosema hapo mwanzo mazingira ni afya na kama hayatapewa kipaumbele yatahatarisha maisha na kusababisha vifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano katika Wilaya ya Ngorongoro imekuwa ya muda mrefu sasa na viongozi wamekuwa wanakuja kila mara na kuahidi kulishughulikia, lakini hawafanyi hivyo. Mfano, katika Kijiji cha Ngarasero, changamoto hii imekuwa ya muda mrefu sana. Tatizo la mtandao limekuwa sugu sasa na kufanya wananchi wanaoishi katika kijiji hiki kukosa mawasiliano ya redio tu. Naishauri sana Serikali ishirikiane katika kijiji hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ATCL; pamoja na mafanikio yaliyooneshwa na ATCL, inabidi Serikali iweke mikakati madhubuti ya soko ili kuifanya Kampuni ijiendeshe kibiashara na kuiletea nchi yetu mafaniko makubwa kiuchumi kupitia Sekta ya Usafiri wa Anga. Lazima Serikali iangalie ni mikakati ipi iliyotumika na nchi nyingine ambazo zimefanikiwa kujiendeleza kiuchumi kupitia huduma ya usafiri wa anga, mfano Ethiopia, Rwanda na UAE. Ni lazima kuwa na mikakati ambayo italeta ushindani baina ya makampuni mengine yaliyomo ndani ya nchi yetu ya Tanzania ikiwemo kubadili sheria ambazo zinabeba Kampuni nyingine ambazo zinafanya biashara sawa na siyo wazawa kama ilivyo ATCL. Mfano, Kampuni ya Fastjet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa kuwa hata fedha za mtaji wa kuanzia hazijatolewa zote na hata zinazotolewa, zinatolewa kwa kuchelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya ATCL, tumeona ahadi ya kuchukua madeni yaliyopatikana kwa ufisadi na uzembe ikitolewa bila kutimizwa kwa kipindi kirefu na kuifanya ATCL ianze kutumia mapato yake kulipia uzembe huu uliosababishwa na mipango mibaya ya usimamizi mbaya wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubinafsisha ATCL kwa Shirika la Ndege la SA (Afrika Kusini), mali nyingi za ATCL zilichukuliwa na Serikali na nyingine kuuzwa. Hii inalifanya shirika sasa kutokuwa na mali zake binafsi na kusababisha kuongezeka kwa gharama za juu za uendeshaji. Naiomba Serikali isaidie kurudisha mali hizi ili kulipunguzia shirika mzigo mkubwa sana wa kiuendeshaji ukizingatia ATCL ndiyo kwanza inaanza kufanya kazi. Tatizo hili linaweza kuifanya Kampuni hii kufilisika tena na hatimaye kuwa ATCL tena kama ilivyokuwa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itueleze, mali ziko wapi hasa? Kwa nani na lini zitarudishwa ili kuweza kulisaidia shirika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba Mheshimiwa Waziri akubaliane nami kuwa afya ya kiumbe hai yeyote inapotetereka na maisha yake pia yanakuwa hatarini wakati wowote. Kwa hiyo basi, afya ni kitu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu, kiumbe hai chochote ikiwemo mimea na wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Hospitali ya Kaloleni iliyopo Mkoa wa Arusha ambayo imekuwa ikitumika sana sehemu ya kusaidia magonjwa ya mlipuko mfano, kipindupindu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hii haina vifaa kama dawa na hata dawa za kawaida tu za kutuliza maumivu zinashindwa kupatikana katika hospitali hii na hata karatasi za kuandikia (description) hakuna. Ukienda Nurse anakwambia kanunue daftari kwa ajili ya kuandikia. Hata dawa ya kufungia kidonda tu, hakuna. Mashuka ya kulalia na kujifunika hatuna na idadi ya mashuka hayo ni 15 tu, lakini Serikali imeshindwa kupeleka hata hii idadi ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru inafanya kazi kama siyo Hospitali ya Rufaa kwa kukosa madawa na vifaa vingi vya matibabu na naona hata Serikali ilikosea kuipa hadhi ya Hospitali ya Rufaa, kama ilikuwa haijajiandaa kupeleka vifaa hata vile muhimu tu. Achia mbali MRI, lakini ultrasound, X-Ray, hazifanyi kazi. Kuna mashine mbili za X-Ray, moja ambayo ni nzuri inaweza kufanya au kupima vipimo vingi, haifanyi kazi kwa muda mrefu sasa na inayofanya kazi ni moja tu, ambayo haipimi vitu vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali iangalie hospitali hii na kuitendea haki kama Hospitali ya Rufaa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba ya Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uaminifu wa kibiashara; kutokana na kukiuka miiko ya kibiashara kwa kupandisha au kubadili kodi bila utaratibu wa kibiashara Tanzania sasa haiaminiki kwa mawakala wa kimataifa ambao ndio wauzaji wakubwa. Imefikia wakati sasa ma- agents wa kimataifa wanauza nchi zilizo nafuu kwa bei na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Tanzania imeongeza idadi ya kodi na tozo hadi kufikia 36 kutoka 14 – 16 zilizokuwepo awali. Bado kuna malipo ya TALA ya kila mwaka kutokana na mahali kampuni inapofanyia kazi zake za kitalii au kutoa huduma za kitalii kama ni kupandisha watalii milimani au kuwapeleka mbuga za wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahoteli, kuanzia Novemba, 2016 mahoteli mengi wageni wamepungua ukilinganisha na kipindi kabla ya VAT haijaingizwa. Kwa kweli idadi ya wageni imeshuka sana kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, hatuwezi kupata takwimu sahihi. Biashara ya utalii ni delicate sana na utachukua muda mrefu sana kurejesha imani ya mawakala na watalii wa dunia kwa ujumla kuiamini Tanzania katika sekta ya utalii. Athari ya maamuzi haya yataonekana kuwa makali zaidi katika kipindi cha mwaka 2018/2019/2020. Makampuni mengi hayana bookings za kuridhisha kwa miaka ya mbele kama ilivyo desturi ma-agents wengi wamebadili mwelekeo wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni/ushauri; Bunge liunde tume huru kupitia wadau pamoja na watalii wanaoingia na kutoka juu ya maoni yao kwa kivutio Tanzania. Ofisi za Kibalozi nje zitumike pia kupata taarifa za umaarufu wa kivutio Tanzania. Serikali kupitia Wizara husika zote zikae chini na kuangalia hali ya ushindani iliyopo duniani, Afrika, Afrika Mashariki na nafasi yetu katika ushindani huu kwa miaka kumi ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi zinazokusanywa sasa si za biashara mpya bali ni biashra ya nyuma. Tujiulize kuanzia mwaka 2018 na kuendelea tutakusanya nini? Makampuni mengi ya Kitanzania yatakosa uwezo wa kushindana na makampuni yenye mitaji mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isipuuze taarifa za makampuni mengi ya kigeni za kufunga biashara zao na kwenda nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi, Mawasiliano kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019. Nitakuwa na hoja tatu kama muda utatosha, kwa sababu muda ni mchache, naomba nianze moja kwa moja kwenye hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuongelea karakana ya kuhifadhi na kutengeneza ndege ambayo iko katika Uwanja wa Ndege Kilimanjaro. Karakana hii ilinyang’anywa kwa mwekezaji wa VIA Aviation ambaye alikuwa anaitwa Susan Mashibe Februari, 2016 ambaye aliambiwa alikuwa anatoa ushuru kidogo. Alikuwa analipa dola 3,000 kwa mwezi na Serikali inasema alikuwa anapata hela nyingi sana lakini alikuwa anatoa ushuru kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiulize Serikali, mpaka wanakubaliana awe analipa dola 3,000 alijipangia mwenyewe au waliandikishiana mikataba na yule mwekezaji ambaye ni VIA Aviation alipe dola hizo kwa mwezi. Kazi hii kaifanya kwa muda wa miaka 10 na yeye kwa sababu alikuwa anajua anatakiwa alipe dola 3,000 kwa mwezi ikabidi awe anatengeneza ndege nyingine ambazo siyo za ATCL lakini kwenye mkataba ilikuwa atengeneze ndege za ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunajua kwamba ndege za ATCL zimeanza kazi hivi karibuni. Ndege zilikuwa hazifanyi kazi lakini mwekezaji huyu alikuwa anatakiwa alipe dola 3,000 kwa mwezi, je, angefanyaje ili aweze kulipa dola hizo kwa mwezi kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji yule sasa hivi hana kazi lakini pia Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefungia vile vipuri na ndege za ATCL zinatengenezwa nje ya nchi kwa gharama kubwa sana. Vipuri vimefungiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na ndege hazitengenezwi tena katika uwanja huo bali zinapelekwa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, matengenezo madogo madogo ya ndege yafanyike pale katika karakana ya Kilimanjaro yaani Uwanja wa KIA kwa sababu kwa kupeleka ndege nje wanapoteza fedha nyingi sana za Tanzania na wakati pale KIA kuna karakana ya kutengeneza na kuhifadhi ndege za ATCL. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naelekea TBA, wazee wa expansion joint. TBA ambao wanahusika zaidi kutafuta viwanja kwa ajili ya Serikali, kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma mbalimbali, wamekuwa wanajenga nyumba hizi lakini hawajui kuzigharamia. Mfano mzuri ni hapa Dodoma katika eneo la Site One, Sengia (Area D), wamejenga nyumba pale kuanzia mwaka 1994 mpaka leo ni miaka 24, hawajawahi kurudia hata kupaka rangi ya ukuta wa nje achilia mbali kukarabati nyumba moja moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale unatafuta njia ya kuingilia kwenye compound, huoni njia kumejaa majani kila mahali. Mnakaa majumbani mwenu kwenye mikoa yenu lakini mkifika Dodoma kwa ajili ya Kamati na Bunge majani yamejaa kila mahali, eneo ni chafu, hakuna sehemu ya kupita, mkikaa baada ya siku mbili ndiyo hao TBA mnaona wanaanza kuja kufanya usafi na kufagia, walikuwa wapi wasifanye usafi wakati nyie hampo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hiyo, nyumba zile ambazo zina vyumba viwili wanalipa Sh.150,000 kwa mwezi, vyumba vitatu ni Sh.250,000 kwa mwezi, hela hizo zinakwenda wapi? Miaka 24 hata kama ni kurudisha gharama wamesharudisha gharama, kwa nini wanajenga majengo lakini hawayafanyii maintenance? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, hawa hawa TBA wanakwambia wanafanyia marekebisho nyumba za viongozi tu lakini pale Sengia, Site One wanakaa viongozi ambao ni Wabunge lakini nyumba zao hazifanyiwi matengenezo, zinafanyiwa matengenezo nyumba za Makatibu Wakuu ambao wanakuja kuhamia Dodoma kwa ajili ya Wizara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaambiwa wewe ambaye unataka kufanya matengenezo kwenye nyumba yako, baada ya kufanya matengenezo aidha uweke tiles au ubadilishe choo mkae na TBA tena chini mkubaliane gharama mpya ya kodi ya nyumba wakati mpangaji ametengeneza nyumba peke yake na kwa gharama zake. Kama TBA wanataka kweli hela kwa nini wasifanye matengenezo wao wenyewe na baada ya hapo wakaongeza hizo gharama za kodi za kila mwezi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo siyo sawa kabisa naomba sana hawa TBA wachukue jukumu lao la kujenga nyumba zao, wazifanyie ukarabati, zile nyumba zimechoka na kwao viongozi siyo Wabunge ni Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali. Naomba sana hawa TBA wazifanyie ukarabati zile nyumba kwani zimechoka.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba ya utekelezaji wa Kamati kama nilivyoainisha hapo juu. Tatizo la maji linazidi kuwa kubwa siku zinavyokwenda. Hii siyo kwa baadhi ya maeneo ya nchi bali kwa nchi nzima. Mfano katika Wilaya ya Arusha Mjini mahali ninapoishi tatizo hili limekuwa sugu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Njiro limekuwa na shida kubwa ya maji zinaweza zikapita hata wiki mbili au tatu bila kuona maji na wakati huo huo mvua zinakuwa zinanyesha. Nimeona kamati ilitembelea Mamlaka ya Maji AUWSA na kupewa taarifa kuhusiana na tatizo hili kama inavyoonekana katika ukurasa wa 45 -48.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona niseme kuwa wahusika wa Mamlaka ya Maji Arusha Mjini hawakusema ukweli kwa Kamati kuwa tatizo kubwa la maji Arusha Mjini linasababishwa na tatizo la umeme. Hili alithibitisha Felix Mrema mwaka 2015 wakati wananchi ilipobidi waandamane ili kuweza kujua nini hasa tatizo la maji katika Jiji la Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya maji katika Jiji la Arusha kwa siku ni lita milioni mia moja, (1000,000,000) lakini kutokana na mgao wa umeme uzalishaji umeshuka hadi kufikia lita milioni arobani na tano tu (45,000,000) kwa siku ambapo katika eneo la Moshono (Kata) uzalishaji umeshuka hadi kufikia galoni 100 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya sana katika nchi kwa ujumla kwa upatikanaji wa maji, ikizingatiwa Mkoa wa Arusha kuna Mlima Meru sijui maeneo ambayo ni makavu kabisa ikoje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwa maandishi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia katika bajeti hii ya Maji na Umwagiliaji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama na watoto ndiyo wanaoumia zaidi na tatizo la kukosekana maji nchini Tanzania. Kama inavyojulikana akinamama ndiyo wapishi katika familia zetu za Kiafrika pamoja na watoto kwa maana ya kuwafundisha kazi kwa ajili ya maisha ya baadae. Mfano, katika Jimbo la Ngorongoro Kijiji cha Naiyobi, Mkoani Arusha kuna kero kubwa sana ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu sasa, akinamama na watoto wanakesha hadi siku tatu kwenye bomba la kijiji kwa ajili ya kusubiria maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana tatizo la maji lishughulikiwe na kupewa kipaumbele kwa ajili ya kuwasaidia akinamama hawa ambao wamekuwa wanateseka na tatizo la maji kwa muda wa miaka 20 sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Ngorongoro ni Jimbo la kitalii kupitia Crater ya Ngorongoro ambayo pia ni kati ya maajabu ya dunia. Kama inavyojulikana sekta ya utalii ni sekta inayoongoza kuliingizia Taifa letu fedha za kitalii na pia kuongoza kwa kuongeza pato la Taifa baada ya madini ya dhahabu kushuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Wilaya hii ipate ufumbuzi wa tatizo hili la maji ambalo limedumu kwa muda wa miaka 20 sasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia pia katika Wizara ya Kilimo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko bado ni changamoto kubwa kwa wakulima hapa Tanzania. Tanzania imezidi kuwa nyuma katika udhibiti wa masoko ya mazao ya kilimo kutokana na masharti magumu ya usafirishaji nje ya nchi. Hata katika taarifa ya Benki ya Dunia (WB) nchi yetu inaonekana ipo nafasi ya 56 kati ya nchi 62. Hii inasababishwa na ugumu wa kupata vibali vya kusafirishia mazao hayo nje ya nchi hii. Kwa Tanzania inachukua hadi siku zaidi ya 20 ili kukamilisha tararibu zilizopo ili kuweza kupata vibali wakati kiutaratibu kwa nchi zilizizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara zinahitajika siku si zaidi ya sita kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishauri Serikali ikazane kupunguza vikwazo kwenye upatikanaji wa vibali vya kusafirishia mazao nje ya nchi ili wakulima wa Tanzania pia waweze kufaidika na sekta hii ya kilimo. Uchumi wa Tanzania utatengemaa zaidi kama sekta ya kilimo itakuwa nzuri. Tukumbuke wakazi wengi wa Tanzania wanaishi vijijini na huko ndiko msingi wa kilimo ulipo. Wakulima wengi wanalima na kuishi vijijini, lakini cha kushangaza huko ndiko kuna matatizo kila siku. Kama uchumi kupitia kilimo ungekuwa mzuri hata maisha ya wananchi waishio vijijini yangekuwa na ahueni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa mazao ya mbegu za kilimo nchini bado ni changamoto kubwa. Nasema hivyo kwa sababu Serikali imetumia pesa nyingi sana kufanya uzalishaji huu lakini wakulima wengi hawana taarifa au hawajapata elimu ya kutosha kuhusiana na mbegu hizi ambazo nyingi sifa yake kubwa ni kuhimili ukame na kuzalisha mavuno mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara ya Kilimo kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima wa Tanzania ili mbegu hizi ziweze kutumika na hatimaye kuongeza kipato pamoja na mavuno mengi ya mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo makubwa ya ardhi yanamilikiwa na wakewezaji wachache, hii ni kwa ajili ya wakulima wadogo wengi kukosa kipato cha kutosha cha kumiliki ardhi na hivyo kukosa ardhi ya kutosha ya kufanya kilimo. Ugawaji wa ardhi umekuwa ukifanyika bila kumilikisha wenyeji wa maeneo husika na kusababisha tatizo kubwa la migogoro ya ardhi ambavyo hata Serikali imeshindwa kutatua katika sehemu nyingi hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuhusisha wenyeji wa maeneo husika wakati wa kumilikisha na kununua ardhi ili kutoa haki kwa kila mtu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo kubwa katika utoaji wa mikopo nchini, wakulima wadogo wadogo wamekuwa wakikosa fursa ya kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha ili waweze kuwekeza kwenye kilimo, na hii inatokana na wananchi wengi kutokuwa na hatimiliki ya ardhi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri na kuisisitiza Serikali kupeleka mikopo kwa wakulima wadogo hasa wa maeneo ya vijijini ambako ndiko wakulima wengi walipo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwa maandishi katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu haki ya kuishi; kama Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoeleza kwa kila binadamu, Mtanzania ana haki ya kuishi. Nasikitika kuona Jeshi la Polisi Tanzania limekuwa linakiuka Katiba ya nchi ambayo ni Katiba Mama au mwongozo ambao umewekwa na Bunge letu Tukufu ili tuweze kutekeleza majukumu yetu kwa haki na bila kuvunja sheria za nchi yetu ya Tanzania. Polisi wamekuwa wakivunja sheria za nchi mara nyingi sana kwa kukatiza maisha ya watu kwa kutumia silaha za moto, vitu vyenye ncha kali na mambo mengine kama vipigo kwa kutumia nguvu za ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa matukio haya ni Ndugu Aquilina Aquiline wa Chuo cha Usafirishaji yaliyotokea mwezi Februari, 2018 Jijini Dar es Salaam. Pia mauaji yaliyotokea kwa mdogo wa Mheshimiwa John Heche, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, lakini nashukuru kuwa Polisi aliyehusika Tarime ameshafikishwa Mahakamani na naamini haki itatendeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Polisi wafuate sheria zitokanazo na Katiba ya nchi ambayo ndiyo mwongozo wetu na Polisi wenyewe wamekuwa wakikamata raia yeyote anayekiuka sheria ya nchi, lakini wao wenyewe ndio wamekuwa mstari wa mbele kutotii sheria za nchi kupitia Katiba ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haki ya usalama wa mtu na faragha; Jeshi la Polisi pia limekuwa na tabia mbaya sana ya kuingilia haki ya faragha na usalama wa mtu. Ni sawa Askari Polisi anaweza kukagua simu ya raia mara anapomtilia mashaka, lakini kwa siku za hivi karibuni imezidi, kwani Polisi baada ya kukagua simu au laptop ya mtu anabaki nayo kwa muda mrefu sana huku akiwa anafahamu password ya kifaa hicho. Hii ni hatari sana kwani simu au laptop inakuwa haina usalama tena kwa maana ya mambo yaliyopo ndani ya simu na kama inavyofahamika simu na mawasiliano yaliyopo kwenye simu ni siri ya mtumiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Jeshi la Polisi likague simu hizi na laptop na kuzikabidhi kwa mhusika mara tu wanapomaliza ukaguzi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uhusiano mkubwa kati ya sekta ya kilimo na ukuaji wa uchumi wa viwanda. Kama inavyoeleweka vision ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendeleza viwanda nchini na kukuza uchumi wa kati kupita viwanda hivyo, lakini ili viwanda viweze kuzalisha kwa kiwango ambacho kitazalisha vizuri na kukuza uchumi wa kati, tunahitaji material, human resource na haya kwangu ni mambo muhimu zaidi kwa viwanda vya ndani. Sasa kama tunavyofahamu kilimo sasa hivi hapa Tanzania hakipovizuri kutokana na hali ya uchumi wa wananchi kuwa chini kwa kushindwa kuhudumia mazao yao ipasavyo kutokana na huduma za pembejeo, mbegu, kuwa juu na vilevile hali ya hewa kwa sasa siyo nzuri sana kwa wastani wa mazao ya wakulima kilimo kinachangia takribani 65% ya malighafi zote za viwandani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali ihakikishe inaboresha kwanza kilimo na kuelekeza katika viwanda ambavyo vitaongeza thamani katika uzalishaji wa mazao mbalimbali. Mfano ya mifugo kama ngozi, maziwa, kwato, pembe, damu, ambavyo vyote hivi vinasaidia katika kutengeneza bidhaa mbalimbali kwenye viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, manyanyaso ya wafanyabiashara mbalimbali tokea Awamu ya Tano imeingia madarakani; kumekuwa na matatizo makubwa kwa wafanyabiashara nchini kama vile hawana uhalali wa kufanya biashara au kutafuta njia mbadala ya kujikimu katika maisha kama sekta nyingine zinavyofanya. Wafanyabiashara ndiyo walipakodi wakubwa katika nchi hii, lakini wamekuwa hawatendewi haki kabisa na biashara sasa hivi imekuwa ni kama kansa katika nchi yetu. Kodi zimekuwa nyingi zaidi ya 25 ili tu kuanzisha kampuni yoyote ya kibiashara nchini. Hili linafukuza hata investors ambao wanataka kuja nchini kuwekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali kuwasaidia wafanyabiashara katika kuhakikisha wanakua na mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuisaidia Serikali pia hata kufanikiwa katika kupata kodi kupitia biashara wanayofanya, lakini pia wafanyabiashara wanasaidia sana katika kuendeleza uchumi wa kati kupitia viwanda ambavyo ni vision ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. JOYCE J. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ndogo; kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilitenga fedha za maendeleo katika Fungu 38 - Ngome kiasi cha shilingi bilioni nane tofauti na shilingi bilioni mbili kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo kwa bajeti hii imetengewa shilingi bilioni sita kama nilivyoeleza hapo juu ni pungufu ya shilingi bilioni mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa, Fungu 39 fedha za maendeleo iliyokuwa imetengwa ni shilingi bilioni sita na iliyotolewa ilikuwa shilingi bilioni tano sawa na asilimia 83.33.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kutotekeleza bajeti ya maendeleo ya Wizara hii siyo tu kunafedhehesha Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania (JKT) lakini pia kunawaweka wananchi katika hali ya hatari kubwa. Hili nalisema hivi kwa kuwa yanapotokea matukio ya ghafla ya uharibifu hata wanaopelekwa kwa ajili ya kuweza kutoa msaada wa haraka ni Jeshi la Kujenga Taifa. Mfano, kufanya huduma za ujenzi mara tu yatokeapo majanga kama mafuriko yanapoharibu miundombinu kama vile madaraja, majengo ya Serikali kuharibika, ni hawa hawa wanajeshi ndiyo wanaitwa kwa haraka kufanya matengenezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kutopandisha vyeo Maofisa wa Jeshi kwa wakati kuna athari za moja kwa moja ikiwa ni pamoja na katika mishahara yao na pia katika pension zao, kwa hiyo askari aliyetakiwa kupandishwa cheo miaka miwili iliyopita halafu akaachwa akaja kupandishwa miaka miwili baadae atakuwa amepunjwa nyongeza yake ya mshahara ambapo ingetokana na cheo hicho na pia mapunjo hayo yanakwenda kuathiri pension za askari hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo napendekeza Serikali ilieleze Bunge hili kama tatizo gani linasababisha wanajeshi wasipandishwe vyeo kwa wakati na kama ni bajeti finyu? Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada wa askari hawa wanaotumikia nchi kwa moyo huku mahitaji yao yanapotekelezwa kwa wakati?