Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joyce Bitta Sokombi (25 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utahudu viwanda na biashara na mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda; Mkoa wa Mara ni Mkoa ambao ulikuwa na Viwanda vikubwa, lakini sasa hivi vimekufa na viwanda hivyo ni MUTEX. Hiki Kiwanda cha MUTEX kimepoteza ajira nyingi sana za wananchi hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa hili. Ni vizuri Serikali ikajipanga tena upya kufufua kiwanda hiki. Vile vile ningependa kuishauri Serikali kutoa kipaumbele kwa kufungua mnada wa Tarime mpakani, hii itasaidia kutoa ajira kwa vijana na kuepukana na vitendo viovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mazingira; kutokana na tabianchi hii inayotokana na Mkoa wa Mara kuwa na wafugaji na upatikanaji wa chakula na maji ya mifugo hiyo na kuhamahama kwa mifugo (wanyama) na wingi wa mifugo hiyo wanakandamiza sana ardhi na kusababisha maji kutokupenya ardhini na kusababisha mafuriko na kutuama kwa maji ambayo yanapelekea mazalia ya mbu na kuleta kipindupindu na madhara mengine kwa binadamu na hata kwa mifugo yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu, hii ni sekta ambayo Serikali izingatie na kuipa kipaumbele.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu; pili, naishukuru familia yangu na tatu, namshukuru Kiongozi wangu wa Kambi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye upande wa uvuvi. Tanzania imekuwa ikiongoza Afrika Mashariki katika uvuvi wa ndani ya nchi na uvuvi wa maji baridi ambao ni kama mito pamoja na maziwa. Pia katika Maziwa Makuu, imekuwa ikiongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uvunaji mkubwa wa samaki hali ambayo inahatarisha uvunaji endelevu wa samaki. Kwa mfano, sasa hivi samaki kama sato, sangara, wamekuwa ni adimu sana katika Ziwa Victoria na bei yake pia imekuwa iko juu. Kwa mfano, ukichukulia kuanzia miaka mitatu iliyopita, samaki aina ya sangara ulikuwa ukimnunua sh. 5,000/= samaki wa kilo tano au kilo saba, lakini sasa hivi samaki huyo hakamatiki kutokana na uvuvi holela. Je, ni mkakati gani ambao Serikali imeuandaa kwa mwaka wa fedha ili kukabiliana na changamoto hii? Kuchoma nyavu kumekuwa na ugumu mkubwa wa kupata fursa za mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye kilimo. Tanzania tumebarikiwa sana kuwa na ardhi ya kutosha na yenye rutuba. Mimi ninatokea Mkoa wa Mara; Mkoa wa Mara tulikuwa tunalima sana zao la pamba na pia tulikuwa na Kiwanda cha Mutex ambacho kilikuwa kinafanya kazi kubwa sana, kilikuwa kinasaidia sana vijana pamoja na wanawake kupata ajira. Pia kiwanda hicho kimekuwa kikiinua sana pato la Taifa. Leo hii kutokana na kutokuwepo na ulimaji wa pamba, imekuwa ni shida kubwa sana na kiwanda hicho kimefungwa na kimekuwa kikisuasua. Je, Serikali iko tayari kuinua zao la pamba ili kiwanda hicho kifunguliwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, nitaongelea hapo hapo kwenye suala la kilimo. Mkoa wa Mara umepakana na nchi ya Kenya. Nchi ya Kenya imejikita sana kwenye zao la maua. Je, kwa nini Serikali yetu pia isijikite kwenye zao la Maua? Ukiangalia kwa mfano, Mkoa wa Mara umepakana sana na Wilaya ya Tarime ambapo iko karibu sana na nchi ya Kenya na hali ya hewa inafanana na nchi ya Kenya; kwa nini na sisi Tanzania tusijikite kwenye kilimo cha maua? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa mifugo. Mkoa wa Mara tuna ng‟ombe wengi wa kutosha, lakini wafugaji hawa wanatumia miundombinu ambayo si endelevu. Lazima Serikali ianze kuandaa mpango wa muda mrefu kwa ufugaji wa kisasa kwa sababu tutakapofuga kisasa itatusaidia sana. Pia Serikali iandae majosho na machinjio yawe ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa mwenzangu wa Mkoa wa Mwanza, amesema kwamba wao Wasukuma ni wanywaji wa maziwa na sisi wananchi wa Mkoa wa Mara ni wanywaji wakubwa sana wa maziwa na pia walaji wazuri sana wa nyama ya ng‟ombe. Kwa nini Serikali isiweke kipaumbele kuhakikisha kwamba hawa ngombe wanakuwa kwenye malisho mazuri kwa sababu maeneo mengi ya malisho hayapo. Maana mtu ukiwa na ng‟ombe zaidi ya 100 ni shida, utaenda kuwalishia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Serikali iweke kipaumbele kwenye suala la mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu fidia ndogo kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi na Serikali kushindwa kuwadhibiti tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyama akimuua mtu au binadamu fidia yake ni ndogo sana. Familia inalipwa shilingi 100,000 au wasipate kabisa kutokana na figisufigisu za viongozi wa eneo husika; lakini endapo mtu akikutwa kaua wanyama, fidia anayotozwa ni kubwa sana na ni kuanzia shilingi milioni sita na zaidi. Swali la kujiuliza je, kipi kina thamani kati ya binadamu na mnyama? Maana hii inaonyesha moja kwa moja kuwa Serikali yetu inathamini wanyama kuliko binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, iangalie sheria hii kwa umakini, kwani haiwezekani hata siku moja mnyama akawa na thamani kuliko mtu au binadamu. Ni vizuri wananchi wa eneo husika wapewe elimu ya kutosha juu ya fidia wanazostahili kulipwa maana kila mwananchi akijua juu ya umuhimu wa malipo wanayostahili kulipwa, naamini hakutakuwa na kelele kuhusiana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya mbuga au hifadhi wananyanyasika sana utafikiri watu hawaishi katika nchi yao (wakimbizi). Wananyanyaswa, wanafukuzwa kwenye maeneo yao wakati Serikali haijawaandalia maeneo ya kwenda kuweka makazi hayo. Ina maana wakati wananchi hao wanajenga, Serikali ilikuwa wapi? Ina maana ilikuwa inawaangalia tu wanapomaliza ndiyo iwaambie wananchi kuwa wamevamia hifadhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana na inasikitisha pia. Inabidi Serikali iwaangalie kwa upya wananchi hawa kwani wanaishi kwa hofu kubwa na maeneo hayo ni Maliwanda, Mihale, Mcharo, Serengeti, Hunyali, Kunzugu na Balili, hivyo vyote ni vijiji vya Wilaya ya Bunda. Kwa upande wa Serengeti ni Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Mbilikiri, Bonchungu na Robanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kuwadhibiti wanyama (tembo) wanaoharibu mazao ya wananchi bila kujali hasara wanayoipata wananchi hao. Kwanza kabisa bila kuwadhibiti tembo hao umaskini hautaisha, kila siku wananchi hawa wataendelea kuwa ombaomba kutokana na umaskini unaotawala kutokana na mazao yao kuliwa na tembo au kuharibiwa na tembo ama wanyama wengine waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ikajipanga upya juu ya jambo hili la kuwadhibiti tembo ili wananchi wanapolima mazao yao wavune na kupata chakula na wananchi wengine wanahamia ili wapate kuvuna mazao yao na kuyauza kwa ajili ya kusomesha watoto wao, lakini tembo wanamaliza mazao ya wananchi kabla hawajavuna na kuendelea kuwadidimiza wananchi hawa kuwa maskini. Ninaamini Mheshimiwa Waziri atalishughulikia suala hili kwa ukaribu ili kuwasaidia wananchi hawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite sana upande wa mawasiliano. Mkoa wa Mara mawasiliano ni shida hasa tukienda kwenye kata za Bunda upande wa Neruma, Nachonchwe, Vigicha, Ving‟wani na upande wa Tarime kuna Muriba na Yanungu. Hii ni asilimia kubwa sana ya watu ambao hawana mawasiliano na total yake inakuja ni 15,894 watu hawana mawasiliano. Mtu ukitaka kufanya mawasiliano inabidi uende kwenye mti yaani tunarudi kule kule enzi zile za Mwalimu Nyerere. Kwa kweli upande wa mawasiliano kwa Mkoa wa Mara inatia aibu. Naiomba Serikali ielekeze nguvu zake huko na kuhakikisha wale watu wanajione wako kwenye nchi yao na kwamba wanapata mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye upande wa uwanja wa ndege. Mkoa wa Mara tuna uwanja wa ndege mmoja tu na Mkoa wa Mara una historia kubwa sana ambayo haitafutika. Ni Mkoa ambao ametoka Baba wa Taifa, lakini uwanja wake wa ndege unatia aibu na unasikitisha sana. Tulitegemea uwanja wa ndege Musoma ndiyo uwe uwanja ambao ni wa mfano katika nchi yetu ya Tanzania. Hata kama tuna local airport basi iwe ni local airport yenye kiwango lakini uwanja wa Mara jamani unatia aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali ielekeze nguvu zote kwenye uwanja wa Musoma. Imefikia hatua tunasema sasa wana Mara na sisi tumechoka ina maana kwamba tunapohitaji kupanda ndege kwenye uwanja mzuri ni mpaka uende Mwanza au Dar es Salaam ina maana watu wa Mara hatufai kupanda ndege kwenye viwanja vizuri kwa hapa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nakuja upande wa barabara. Nitazungumzia barabara itokayo Manyamanyama kuelekea Musoma Vijijini. Barabara hiyo inapita katika vijiji vya Kangetutya, Kabulabula, Bugoji mpaka kufika Musoma Vijijini, kwa kweli hairidhishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea katika bajeti hii barabara hii angalau ingekuwa ya kiwango cha lami lakini gharama zake zimewekwa kwenye kiwango cha changarawe. Zile changarawe zinazowekwa ni za kiwango cha chini sana mvua inaponyesha barabara zile zinakatika. Kwa hiyo, hakuna mawasiliano ya barabara kutoka kule Musoma Vijijini kuja Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama mkulima anataka kuuza mazao yake ni lazima mtu atoke kule Musoma Vijijini aje Bunda, usafiri inakuwa ni shida sana kwa sababu watu wengi wenye magari wanaogopa kuweka magari yao yafanye biashara kwenye hizo barabara kwa sababu mtu anaona gari yake inaharibika.
Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwamba barabara hii inayotoka Manyamanyama kwenda Musoma Vijijini kwa kipindi kijacho inajengwa kwa lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa Kabulabula akitaka kuiona lami ni mpaka aje Bunda au mpaka aende Musoma Mjini, kwa kweli tunaomba na tunasema kwamba wananchi wa kule wamechoka na wanasikitika sana. Mkoa wa Mara mzima barabara ya lami ni ile inayotoka Mwanza - Tarime - Kenya, zile barabara zingine zote hazina lami na nilitegemea kwenye bajeti yetu hii angalau ningeona vipande vya lami lakini sivyo. Lami tumewekewa kilometa mbili tu, ni ndogo sana na ni shilingi bilioni mbili.
Kwa hiyo basi, naomba na naendelea kuishauri Serikali, kwa hizi kilometa mbili zilizowekwa kwa upande wa Mkoa wa Mara kusema ukweli haziridhishi, hazitoshi ziongezwe. Mkoa wa Mara una population kubwa sana kwa nini Serikali isihakikishe inaweka lami katika baadhi ya barabara za Wilaya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na kuishauri sana Serikali iwe makini inapokuwa inakaa kujadili na kupanga bajeti zake. Kwa sababu unapokaa na kupanga ili mradi tu umepitisha bajeti, kaa uangalie ni watu wangapi unaowaumiza. Ina maana wale watu wa vijijini hawatakuwa na maendeleo mpaka lini? Hiyo pia inazidisha kudidimia kwa uchumi wa mahali husika kwa sababu watu wameshazoea ile hali ya kila siku kwamba mimi ni mtu wa kijijini, barabara ni ya vumbi, hakuna lami, hizo lami tutaziona mjini mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ajikite sana katika Mkoa wetu wa Mara, tunaomba lami hasa kutoka Bunda kwenda Wilaya ya Musoma Vijijini na pia barabara ya Nata kwa Serengeti, kwa kweli tunaomba mtusaidie barabara za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwa upande wa Serengeti ni Wilaya ambayo ina uchumi mkubwa kwanza tuna mbuga ya wanyama na pia watu wengi wanatoka Arusha kuja Serengeti, lakini barabara zile hazipitiki. Hamuoni kwamba tunapoteza asilimia kubwa sana ya uchumi wa Tanzania kwa kupoteza watalii kuja Tanzania kutembelea mbuga ya Serengeti?
Kwa hiyo basi, naomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu fidia ndogo kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi na Serikali kushindwa kuwadhibiti tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyama akimuua mtu au binadamu fidia yake ni ndogo sana. Familia inalipwa shilingi 100,000 au wasipate kabisa kutokana na figisufigisu za viongozi wa eneo husika; lakini endapo mtu akikutwa kaua wanyama, fidia anayotozwa ni kubwa sana na ni kuanzia shilingi milioni sita na zaidi. Swali la kujiuliza je, kipi kina thamani kati ya binadamu na mnyama? Maana hii inaonyesha moja kwa moja kuwa Serikali yetu inathamini wanyama kuliko binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, iangalie sheria hii kwa umakini, kwani haiwezekani hata siku moja mnyama akawa na thamani kuliko mtu au binadamu. Ni vizuri wananchi wa eneo husika wapewe elimu ya kutosha juu ya fidia wanazostahili kulipwa maana kila mwananchi akijua juu ya umuhimu wa malipo wanayostahili kulipwa, naamini hakutakuwa na kelele kuhusiana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya mbuga au hifadhi wananyanyasika sana utafikiri watu hawaishi katika nchi yao (wakimbizi). Wananyanyaswa, wanafukuzwa kwenye maeneo yao wakati Serikali haijawaandalia maeneo ya kwenda kuweka makazi hayo. Ina maana wakati wananchi hao wanajenga, Serikali ilikuwa wapi? Ina maana ilikuwa inawaangalia tu wanapomaliza ndiyo iwaambie wananchi kuwa wamevamia hifadhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana na inasikitisha pia. Inabidi Serikali iwaangalie kwa upya wananchi hawa kwani wanaishi kwa hofu kubwa na maeneo hayo ni Maliwanda, Mihale, Mcharo, Serengeti, Hunyali, Kunzugu na Balili, hivyo vyote ni vijiji vya Wilaya ya Bunda. Kwa upande wa Serengeti ni Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Mbilikiri, Bonchungu na Robanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kuwadhibiti wanyama (tembo) wanaoharibu mazao ya wananchi bila kujali hasara wanayoipata wananchi hao. Kwanza kabisa bila kuwadhibiti tembo hao umaskini hautaisha, kila siku wananchi hawa wataendelea kuwa ombaomba kutokana na umaskini unaotawala kutokana na mazao yao kuliwa na tembo au kuharibiwa na tembo ama wanyama wengine waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ikajipanga upya juu ya jambo hili la kuwadhibiti tembo ili wananchi wanapolima mazao yao wavune na kupata chakula na wananchi wengine wanahamia ili wapate kuvuna mazao yao na kuyauza kwa ajili ya kusomesha watoto wao, lakini tembo wanamaliza mazao ya wananchi kabla hawajavuna na kuendelea kuwadidimiza wananchi hawa kuwa maskini. Ninaamini Mheshimiwa Waziri atalishughulikia suala hili kwa ukaribu ili kuwasaidia wananchi hawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii kuchangia Wizara ya Nishati na Madini. Nitajikita sana upande wa Nyamongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Nyamongo ulianzishwa na wananchi wenyewe pale Nyamongo na Serikali ikaleta wawekezaji kwa makubaliano kwamba watawajengea wananchi wa eneo husika watawawekea hospitali, watawawekea maji, watawajengea barabara yenye lami na pia watawajengea kituo cha afya. Matokeo yake hayo makubaliano mpaka leo hayajafanyika, watu wa eneo lile kwa kweli wanatia huruma na inatia aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haioneshi kwamba wale wananchi wako kwenye nchi yao, ukikaa ukiangalia eneo kwamba linachimbwa madini na kwamba yale makubaliano ya mwaka 2011 walivyoenda Mawaziri yakawa kwamba wao wanachimba ule udongo ili wale wachimbaji wadogo wadogo wawe wanaenda kuchambua ule udongo, matokeo yake wakienda kuuchambua wanapigwa risasi. Je, ni halali kwa mwekezaji kuja kumpiga raia wa Tanzania?
Mheshimiwa Waziri ninakuomba na nina kusihi, hakikisha unaweka mipango ambayo ni mizuri kuhakikisha wale wananchi wa Nyamongo hawapati shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia mkataba wa wale wawekezaji pale Nyamongo uwekwe wazi na mnatakiwa pia muwaulize kama mkataba ulikuwa ni kwamba kuwajengea wananchi kuwawekea lami katika barabara na kuwawekea vituo vya afya, kwa nini hayo makubaliano hayakufanyika?(Makofi)
Mheshimia Mwenyekiti, nitajikita pia upande wa Dangote, nimeenda Mtwara. Dangote amekuja kuwekeza hapa nchini eneo la Mtwara kwa lengo la kutumia gesi yetu ya Mtwara. Lakini matokeo yake Dangote hatumii gesi yetu ya Mtwara anatumia mafuta. Je, yale mafuta wanayoyaagiza, yanalipiwa kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia kuhusu REA. REA ni nzuri na imekuja kwa ajili ya kumkomboa mwananchi ambaye yuko kijijini, lakini mmewasahau wale wananchi ambao wako pembezoni kwenye vile vijiji. REA imepita mjini tu, wale wananchi walioko pembeni ni ile wanakaa tu wanaangalia umeme ule. Jamani tunaomba kama Serikali imeamua kumkwamua mwananchi aliyeko kijijini, tuhakikishe kwamba REA inaenda kwenye kila kijiji na vitongoji vyake kwenye kila eneo, siyo REA ipite upande wengine wapate umeme, wengine wasipate umeme. Ninamuomba Waziri wa Nishati na Madini, kwenye hili suala la REA aliwekee mkazo, kwa kweli inatia aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwa mfano kule Kangetutya, Kabulabula umeme umepita tu, wale walioko ndani ndani hawana umeme, watafikiwa na umeme lini? Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, jikite sana katika maeneo ya ndani msipitishe tu umeme eneo la barabarani, wale walioko vijijini kwa ndani nao wanahitaji umeme. Mwananchi amezaliwa miaka nenda rudi anatumia kibatari, basi angalau hata miaka hiyo iliyobaki jamani angalau na inabidi aende mjini, yeye awashe umeme ajue umeme huu unawakaje na una starehe gani. Siyo hata ku-charge simu inabidi aende mjini kwenye center zinaitwa, watafanya namna hiyo mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena Mgodi wa Nyamongo. Ninakusihi sana Mheshimiwa Waziri, ninakusihi mno, wale wananchi wa pale kwa kweli wanateseka, watateseka mpaka lini? Wewe ukiwa Waziri tena mwenyeji wa Mkoa wa Mara nina hakika kwamba utaenda kulifanyia kazi kuhakikisha Mkoa wetu wa Mara unainuka, wale wananchi wa eneo la Nyamongo hawatapata shida tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri ukiangalia hata kama wakichimba visima eneo hilo yale maji siyo salama kutokana na ile sumu inayomwagwa kwenye Mto Tigiti, maji inabidi wayafuate mbali sana. Ninamuomba Waziri wa Nishati na Madini atusaidie kwa hilo tujikwamue maana hayo mauaji yanayotokea Nyamongo kwa kweli ni aibu kwa Taifa letu. Wawekezaji wanakuja nchini wanakuwa wao ni bora kuliko Watanzania wenyewe tuliozaliwa katika nchi yetu. Tutaendelea kudharauliwa namna hii mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchukua nafasi hii kuunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kutoa ushauri wangu kuhusu mabaki ya mjusi wetu yaliyoko Humberg. Ni aibu kwa Serikali yetu na nchi yetu ya Tanzania kushindwa kuyarudisha mabaki ya mjusi wetu. Hayo mabaki tunaendelea kuwanufaisha Wajerumani na sio Watanzania. Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kuyarudisha mabaki hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuishauri Serikali ifanye jitihada na kila iwezalo kuweza kurudisha mabaki hayo ili yanufaishe Watanzania kwani Watalii watakuwa wanakuja kuangalia mabaki hayo kwa tozo ya kiingilio. Ili Serikali iweze kurudisha heshima yake kwa wananchi wake wa Tanzania ilete mabaki ya mjusi wetu yaweze kunufaisha Watanzania wenyewe na si vinginevyo, ni aibu kwa Serikali!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi za Balozi zetu zipo hoi, yaani zina hali mbaya sana. Nilitegemea safari hii Serikali ingeona umuhimu mkubwa sana na kuweza kutenga fedha za kutosha ili kukarabati hizo ofisi ili ziwe kwenye hali nzuri. Ni aibu unapokwenda nchi za nje, ukienda ofisi za Ubalozi wa Tanzania ni aibu kubwa, pia inatia uchungu kwa nchi yetu. Balozi zetu kuwa mfano wa ofisi mbaya kuliko kawaida, yaani kuliko nchi yoyote hapa duniani halafu Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anasema, watafungua Balozi zingine. Je, ni kwa gharama zipi? Kwa nini Serikali isione umuhimu wa kukarabati kwanza Balozi zilizopo halafu ndiyo ione umuhimu wa kufungua hizo ofisi za Balozi zingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuishauri Serikali ifanye jitihada ya kuwa na Ubalozi wa Uingereza hapa nchini kwetu. Kwani mtu ukitaka kuomba viza ya kwenda Uingereza ilikuwa lazima uende Nairobi, Kenya. Sasa hivi ukitaka viza ya Uingereza sio tena Kenya bali inabidi uende South Africa. Kwa nini Serikali isione umuhimu juu ya jambo hili kwani inaleta usumbufu mkubwa sana na kero kwa Watanzania. Natumaini Mheshimiwa Waziri, kati ya majukumu yake yote, aweke kipaumbele kwa Ubalozi wa Uingereza uwepo hapa Tanzania.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, utangulizi; awali ya yote napenda kunukuu katika kitabu Kitakatifu cha Biblia, Mithali, Sura ya 11, mstari wa 14; mstari huo unasema: “Pasipo mashauri Taifa hupotea, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya afya nchini; ni dhahiri hali ya uchumi wa nchi unayumba. Kuyumba huku kwa uchumi ni hatari sana katika sekta nzima ya afya. Kumekuwepo na malalamiko makubwa katika sekta ya afya kwa muda mrefu sasa na hayajatatuliwa. Takwimu zinaonesha huduma za afya na ustawi wa jamii zilikua kwa asilimia 8.1 mwaka 2014, lakini kwa mwaka 2015 ni asilimia 4.7 pekee. Hii ina maana kwamba, utoaji huduma za afya na ustawi wa jamii umepungua kwa asilimia 3.4. Hivi karibuni nilifanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Musoma, Mara ni kilio kwa kweli! Vitanda havitoshi, madawa hakuna, kiasi kwamba wanaokwenda hospitali wakiwa wanaugua malaria wanatoka na typhoid au kifua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kauli tata sana na za aibu kwenye sekta hii ya afya. Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekiri kuwepo kwa ukosefu wa dawa nchini, ndani ya Bunge hili, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake wanasema kuna dawa za kutosha katika Bohari ya Dawa Nchini (MSD). Wananchi nao wanalalamika kwa kukosa dawa mahospitalini. Huduma za tiba zinadorora kwa kuwa hakuna vifaatiba katika mahospitali mengi. Pamba na gloves zimeadimika, wagonjwa wanalazimika kwenda na pamba na gloves; akinamama na watoto wamekuwa wahanga wakubwa katika hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka kuna siku hapa Mheshimiwa Mbunge mmoja aliuliza swali kuhusu Mpango wa Serikali kupambana na ugonjwa wa fibroid kwa wanawake. Ni ajabu sana Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu kwa kubeza kuwa, fibroid siyo ugonjwa tishio kwa kiasi hicho. Lakini sisi akinamama tunajua ni kwa namna gani akinamama wenzetu wanasumbuliwa na ugonjwa huo. Fibroid kwa akinamama ni tishio na ni tishio kubwa sana maana sasa linawakumba mpaka mabinti wadogo. Hili suala siyo la kuchukulia kimzaha tu! Tunapoteza nguvukazi ya Taifa ha hatuoni mpango madhubuti wa Serikali katika kukabiliana na tatizo hili kama walivyofanya kwa ugonjwa wa malaria kwa akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko yangu kuona Serikali ikinunua ndege ambazo zinawanufaisha tabaka la watu wachache tu huku hakuna uwekezaji wa kutosha katika sekta ya afya ambayo inamgusa kila mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kusema, pasipo mashauri, Tanzania itapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la utawala bora; hakuna maendeleo kama hakuna utawala bora. Ndani ya Serikali hii, washauri mbalimbali na watalaam wamekuwa wazito katika kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Tatizo kubwa linaloitafuna Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kutokuzingatia misingi ya utawala bora, kufuata sheria, Kanuni pamoja na kuruhusu mawazo huru kwa kila Mtanzania. Utawala bora ni pamoja na kukaribisha mawazo kutoka katika maeneo mbalimbali bila kujali itikadi za vyama. Ni pamoja na kuwa na kifua cha kupokea changamoto ikiwa ni pamoja na kukosoa na kukosolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko yangu pale ninapoona Vyama vya Upinzani ambavyo ni jicho la pili la Serikali, ni jicho linaloweza kuona pale Serikali isipoweza kuona, ni mdomo wa kuwasemea wadau mbalimbali ikiwemo ninyi Wabunge wa Chama Tawala na Mawaziri pale ambapo mna mambo ambayo hamuwezi kuyasema waziwazi kwa Serikali kwa sababu ya hofu za nafasi au maslahi binafsi. Upinzani ni msaada kwa kuwa, ndiyo Serikali mbadala (Alternative Government). Tunapoona Mawaziri au Wabunge wakichukia Upinzani au kuwa na mawazo potofu kuwa, upinzani ni kupinga inashangaza sana!
Ni vema Waheshimiwa Wabunge wakapewa elimu ili kujua upinzani ni kitu gani ili linapokuja suala la kujadili mambo ya msingi ya kimaendeleo kwa faida ya nchi yetu waweze kuwa-change kwa kupokea, kuyachambua yale yanayofaa hasa katika kujadili Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maendeleo inakwama kutokana na sanaa katika mambo ya msingi. Mfano, Mkurugenzi anatumbuliwa tena kwa barua kutoka Ikulu halafu anapelekwa nje ya nchi kuwa Balozi; tunakwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi imekuwa na msururu wa kodi kwa wafanyabiashara wazawa tena wale wenye mitaji midogo. Maliasili kuna kilio kikubwa cha kodi hizo mfano, kodi ya kulipia magari, leseni, mageti na kadhalika. Hii ikiwa ni jumla ya kodi 32 katika biashara ya sekta ya utalii. Yaani inaweza kuchukuwa takribani miezi miwili mpaka mitatu katika kulipia kodi. Hii ni aibu kubwa kwa Serikali, ambayo inashindwa kuleta tija katika kuwasaidia watu wake ambao tayari wengi wao wanapambana na ukuta mkubwa wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, kuna baadhi ya viongozi wanabeza na kusema, eti Watanzania ni wavivu! Kwa wingi huu wa kodi ambao unawafanya wafanyabiashara kushindwa kuendelea kumudu biashara zao, Serikali haioni kuwa tunazalisha wimbi la majambazi na vibaka tena kwa bidii?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu kuwa, Serikali iangalie upya namna ya kukusanya kodi. Iangalie ni aina gani za biashara za kukusanya kodi na kwa kiasi gani ili kupunguza mzigo mkubwa uliowaelemea wafanyabiashara wadogo au wachuuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Watendaji wa Serikali na wanasiasa wakaheshimu kazi kubwa inayofanywa na upinzani. Mheshimiwa Rais aheshimu Sheria na Katiba ya nchi ambayo kimsingi inawaruhusu wanasiasa kufanya mikutano yao kwa uhuru na amani. Rais awe ni mfano wa kusimamia Sheria na Katiba ya nchi. Kila Kiongozi ataweza kutekeleza shughuli za maendeleo na kuleta tija katika Taifa endapo kuna uhuru na haki katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho; niombe Waziri wa Fedha aweze kupitia tena vipaumbele hivi vya mpango na kuangalia ni namna gani sekta ya utalii inaweza kuchangia zaidi. Kwa kuwa, awali sekta hii ndiyo ilikuwa inachangia pato kubwa la Taifa takirbani asilimia 27.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu, pili nipende kumshukuru pia Mwenyekiti wangu wa Chama cha CHADEMA na nipende kumpongeza kwa hotuba yake nzuri iliyoletwa hapa Bungeni yenye kuonesha dira na mdororo wa uchumi wa Tanzania juu ya bajeti yetu iliyoletwa hapa Bungeni. Bajeti iliyoletwa hapa Bungeni ni bajeti hewa, na nitaendelea kusema kwamba ni bajeti hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu moja. Ukiangalia Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ukurasa wa 35, kwenye Wizara ya Kilimo, zimetengwa asilimia 2.22, Wizara ya Viwanda na Biashara imetengwa asilimia nane, Wizara ya Afya asilimia 25. Mheshimiwa Waziri Mkuu, hii asilimia 25 unazipenda kweli afya za Watanzania, maana hii asilimia 25 ndiyo imebeba maisha ya afya zote za Watanzania juu ya
matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kwa kuchangia juu ya hii Wizara ya Afya; Serikali ya CCM iliahidi kujenga zahanati kwenye kila kijiji na kata na vituo vya afya. Swali la kujiuliza; kwa bajeti hii ya asilimia 25 fedha hizi zitakidhi kweli vigezo vya afya katika Tanzania yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika Mkoa wangu wa Mara, Hospitali ya Mkoa wa Mara ni jambo la kusikitisha na ni aibu, tena mahali ambapo anatoka Baba wa Taifa, hospitali haina hadhi kwamba ni hospitali ya mkoa. Mfano mdogo, CT scan, ile hospitali haina CT scan na mtu akitaka kufanyiwa hicho kipimo ni mpaka wampe rufaa kwenda Bugando, Mwanza na Bugando hiki kipimo hakipo, hakipo Bugando wala Sekou Toure, ni aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipimo cha CT scan kipo kwenye hospitali moja tu tena ni dispensary ya mtu binafsi, inakuwaje mtu binafsi anaweza kununua hii mashine lakini Serikali inashindwa, ni jambo la kujiuliza na ni jambo la kusikitisha. Pia wanapokwenda kufanya hicho kipimo kwenye hiyo dispensary gharama yake ni kuanzia 290,000 kuendelea, je, mwananchi mwenye kipato cha chini hiyo 290,000 ataitoa wapi? Moja kwa moja inaonesha kwamba Serikali haina nia nzuri juu ya afya ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda. Hospitali hii ni hospitali inayohudumia wilaya tatu, lakini ile hospitali imeandikwa Hospitali ya Wilaya ya Bunda lakini yale madawa yanayopelekwa pale ni ya kituo cha afya. Hakuna madaktari bingwa kisa tu hakuna mortuary. Ndugu zangu tambueni zile wilaya tatu ni wilaya zenye wananchi wengi na hakikisheni kwamba msipoiweka katika
hadhi nzuri ile Hospitali ya Bunda mnahatarisha maisha ya watu wa Mwibara, Musoma Vijijini na Bunda yenyewe na uzuri Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mheshimiwa Bulaya ameshalisemea sana suala la Hospitali ya Wilaya ya Bunda. Kwa hiyo basi, ninachoomba, Serikali iseme kwamba ni lini itaipa hadhi Hospitali hiyo ya Wilaya ya Bunda ili wananchi wa Wilaya ya Bunda na wao wawe na hali nzuri kwa kuona kwamba wilaya yao ina hospitali ya wilaya, inaleta sifa pia kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusiana na suala la maji Bunda; sasa hivi ni takribani miaka 10 Wilaya ya Bunda kila siku wanasema maji yataletwa matokeo yake mpaka sasa maji bado hayajaletwa. Kila siku mnasema chujio, hilo chujio litatengenezwa lini ili wananchi wa Bunda wapate maji salama. Tunaomba mradi wa maji Bunda ukamilike ili wananchi wale na hasa upande wa akinamama,
akinamama wanateseka sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwenda kuhangaika kutafuta maji na wakati maji yapo shida ni chujio. Kwa hiyo, tunachohitaji Wilaya ya Bunda inahitaji ipate maji salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda upande wa elimu bure. Naomba tu niseme ukweli, mshaurini tu Mheshimiwa Mtukufu kwamba hili suala tayari sasa hivi limeshashindikana ili liwe wazi kwa wananchi na ikiwezekana pia aombe tu msamaha kwa wananchi kwamba hili suala limeshashindikana ili wananchi wenyewe waweze kuchangia kusomesha watoto wao. (Makofi)
TAARIFA....
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru lakini sitaipokea kwa sababu najua Waziri Mkuu atakuja kujibu hoja, tuseme tu ukweli elimu sio bure, Mheshimiwa Simbachawene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda upande wa hili suala lililopo Tanzania sasa hivi, ni hali ya kutisha hili suala la utekaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utekaji kwa kweli ni suala ambalo linatisha juu ya maisha yetu na juu ya maisha ya Watanzania. Kila mtu
anasimama hapa anaongelea juu ya utekaji, naomba wewe kama Mwenyekiti uliyekalia hiki kiti hapo mjiulize ni kwa nini kila mtu anasimama na kuongelea suala la utekaji? Halafu Waziri mwenye dhamana, Waziri Mkuu hajatamka kitu chochote mpaka dakika hii, kusema ukweli inasikitisha na ni jambo la aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoomba, Ben Saanane amepotea ni muda mrefu sasa umepita, Serikali imekaa kimya. Msanii Roma alitekwa lakini cha ajabu yule mtu kapatikana kwenda kujieleza matokeo yake Waziri wa Michezo eti anamsindikiza, unategemea yule msanii ataongea kitu gani cha ukweli? Ina maana Serikali inajua ni kitu gani kilicho nyuma yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimwa Mwenyekiti, kuhusu ndoa za utotoni, wazazi na Waheshimiwa Wabunge tunaomba tuwe kitu kimoja tuangalie namna gani tunaweza kumsaidia mtoto wa kike hasa wanaopata mimba wakiwa masomoni, Serikali ione namna ya kuwasaidia watoto hawa wanaokuwa na matumaini ya kuendelea na masomo lakini masomo yao hukatishwa kwa kupata mimba bila kutegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini wanapata mimba? Wanapata mimba kutokana na kudanganywa na wanaume kwa kupewa vitu vidogo vidogo ambavyo huwafanya kujisahau wajibu wao na kuingia kwenye mtego huo bila kutegemea, wengine hutokana na umbali mrefu wa mahali ilipo shule. Ili kupunguza idadi hii kubwa ya watoto kupata mimba ni lazima Serikali ihakikishe wanajenga hostel za kutosha kwenye mashule, hii itasaidia sana kupunguza uharibifu kwa watoto hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za mfumo wa elimu, kukosa falsafa ya elimu yetu, changamoto ya usawa wa elimu kuhusu mtoto wa kike na wasiojiweza, usimamizi mbovu wa elimu shuleni, utakuwa udhibiti ubora, uandaaji walimu, uwajibikaji mdogo kwenye elimu wadau wote, ubora hafifu ya ufundishaji, kukosa walimu bora wasio na hamasa hasa vifaa. Mazingira duni ya kujifunzia kama vile uduni katika miundombinu.

MheshimiwaMwenyekiti, kuhusu changamoto za miundombinu; madarasa 146,106 hii ni kwa shule za msingi. Madarasa 12,568 kwa shule za sekondari hii ni kutokana na taarifa ya Kamati. Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2017/2018 ni kujenga madarasa 2000 tu ya shule za msingi na sekondari ilihali mahitaji ni takribani 158,674 kwa asilimia moja hadi mbili tu kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu motisha kwa walimu; kutokana na malimbikizo ya mishahara shilingi bilioni 200 kutokana na madeni hayo kunashusha sana moyo wa walimu hawa kufanyakazi kwa moyo wa kufundisha, kwa sababu mwalimu huyu akipata haki yake bila usumbufu itamfanya afanye kazi kwa bidiii na moyo mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali Serikali iwaonee huruma watoto hawa wa maskini ambao wanarubuniwa na kuingia kwenye maisha ya ndoa ambazo hawajazikusudia. Naishauri Serikali ijitahidi sana kila shule iwe na hosteli za kutosha ili watoto wawe wanaenda kukaa shule hadi semister inaisha ndipo warudi nyumbani na wanapokuwa nyumbani mara nyingi watoto huwa chini ya uangalizi wa wazazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makosa ya vitabu; hadi sasa tayari vitabu 13,680,981 vya darasa la pili na tatu vimesambazwa mashuleni wakati vitabu vina makosa mengi sana. Kwa sababu vitabu takribani milioni sita vya darasa la kwanza vimechapishwa na vina makosa pia na vitabu hivi ni takribani ya milioni 18 ambavyo gharama yake takribani shilingi bilioni 108, hizi shilingi bilioni 108 ni fedha nyingi sana na Serikali haioni inalipa Taifa hasara maana fedha hizi zingeenda kujenga hostel kwenye shule zetu, zingesaidia sana kupunguza tatizo la watoto wetu kupata shida ya kwenda shule na kurudi au fedha hizo zingeweza hata kujenga madarasa ya kutosha kwenye shule za nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii nami nichangie Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Jambo la kwanza naunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni sekta kubwa ya ajira hapa nchini kwetu maana inaajiri takribani asilimia 70 ya Watanzania. Wizara hii hii ndiyo yenye kauli mbiu nyingi tulianza na kauli mbiu ya Baba wa Taifa ya Siasa ni Kilimo, ikaja Kilimo cha Kufa na Kupona cha Mheshimiwa Alhaji Ali Hassan Mwinyi, ikaja Kilimo Kwanza cha Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema siasa ni kilimo maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba kilimo kinagusa maisha ya kila mwananchi, kilimo kinagusa maisha ya kila Mtanzania lakini kilimo hiki hakijamkomboa Mtanzania huyu. Kwa mfano, katika Mkoa wa Mara, enzi za zamani nilipokuwa naenda kijijini kwetu Kabulabula wazee walikuwa wanalima sana pamba na ilikuwa inastawi kwa asilimia kubwa sana na ndiyo maana Mkoa wa Mara ulikuwa una viwanda vingi sana na mazao mengine kama mihogo na viazi vilikuwa vinashamiri sana, lakini sasa hivi wakulima hawa wanahangaika kutokana na uhaba wa mazao haya hayapati rutuba na hayakui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze hizi mbegu wanazozileta sasa hivi ni mbegu za aina gani, maana hazikui na zao la pamba limekufa katika Mkoa wa Mara halistawi tena. Mazao ya mihogo zao hili limekufa ni tofauti kabisa maana unapopanda mihogo inapokaa kidogo tu inapata ugonjwa wa ukungu, sasa sielewi hii mihogo inapopata ukungu tatizo ni kitu gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ni Mkoa ambao ulikuwa unategemea kwa kiasi kikubwa kilimo lakini kilimo hiki kinasuasua. Naomba Waziri atakapokuja atueleze ni mbadala wa mbegu zitakazoletwa katika Mkoa wa Mara ili watakapokuwa wanalima kama ni mazao ya pamba, mihogo na viazi vistawi kama vilivyokuwa vinaota zamani. Kwa sababu sasa hivi mkulima akipanda mbegu ya pamba kama ni heka tano, matokeo ya lile zao uvunaji wake ni kama heka moja tu. Tunaona ni namna gani zao la pamba linavyodidimia kutokana na uhaba au ubovu wa mbegu ambazo si stahili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi hii. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema. Kabla ya yote, napenda tu pia kumpa pole Mwenyekiti wangu wa Kanda, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mheshimiwa John Heche kwa kuumwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine pia napenda nisemee kitu kidogo, imesemewa hoja yake iliyotolewa hapa asubuhi; ni mbaya sana kumsema mtu ambaye anaumwa, yuko hoi kitandani. Ni vizuri mkamwacha akapona ndiyo aje aambiwe hayo maneno anayoambiwa ili ayajibu yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Mbunge hajakataa kiwanda kisijengwe Tarime, isipokuwa utaratibu ufuatwe unavyotakiwa na mwende mkawashirikishe wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuishauri Serikali kwamba Wizara ya Viwanda na Biashara ni vizuri ikaungana ikawa pamoja na Wizara ya Kilimo, kwa sababu bila kuwa na Wizara ya Kilimo, viwanda haviwezi kufanya kazi zozote kwa sababu wanaendesha viwanda kwa kutoa malighafi wapi? Maana malighafi inatoka kwa wakulima. Kwa maana hiyo basi, ni vizuri hizi Wizara zikaungana ili yale mazao yanayopatikana kutoka kwa wakulima yaende yakafanye kazi katika viwanda. Maana huwezi kusema mnafanya kazi katika viwanda kwa kutegemea mazao ya wakulima halafu Wizara yenyewe inajitegemea yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, viwanda vya mafuta; huwezi kuchenjua mafuta bila kutoka kwenye vitu kama karanga, mbegu za pamba, ufuta au alizeti. Kwa hiyo, basi ni vizuri hizi Wizara mbili zikaungana. Kwa mfano, katika Mkoa wa Mara tulikuwa na viwanda vingi sana, karibu viwanda kumi na kitu, lakini sasa hivi ni viwanda vitatu tu vinavyofanya kazi; na ni viwanda vya watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Waziri wa Viwanda na Biashara kwa nini asivifufue vile viwanda vya Mkoa wa Mara? Kwa mfano, kile Kiwanda cha MUTEX, kile kiwanda kilikuwa kinasaidia kutoa ajira nyingi sana kwa wakazi wa Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimshauri tu Mheshimiwa Waziri na Mkoa wa Mara una sifa kuu kubwa moja ambapo ametokea Baba wa Taifa. Ili kumuenzi Baba wa Taifa ni vizuri ikaonekana kwamba kuna kitu ambacho kinaleta manufaa kwa wananchi wake katika Mkoa wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini atavifufua vile viwanda vya Mkoa wa Mara? Maana tulikuwa na Kiwanda cha Mara Oil ambacho sasa hivi hakifanyi kazi; kuna Mugango Ginnery, tuna Jarif Ginnery, ORAM Ginnery; hivi vingine vilikuwa vya watu binafsi na Buramba Ginnery, vyote hivi havifanyi kazi.

Pia tulikuwa na viwanda vya samaki; na hivi viwanda vya samaki, sasa hivi kinachofanya kazi ni kiwanda kimoja tu ambacho ni cha Musoma Fish. Sasa Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu kwamba wale wavuvi wanapovua samaki, kwa nini wasiwe wanapeleka kwenye kiwanda kuchenjua minofu ya samaki ambayo inasafirishwa kupelekwa nje ili wasilete usumbufu wowote, wawe wanachambulia pale pale Mkoani Mara?

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine kikubwa, ni lazima iwepo mikakati ya Wizara hizi mbili ili izingatie namna ya kumsaidia mkulima pamoja na kuweza kuwasaidia vijana wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na wimbi kubwa sana la migogoro ya ardhi hapa nchini; migogoro ya wakulima na wafugaji na migogoro hii inasababishwa na wawekezaji hasa maeneo ya hifadhi

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni Kata ya Kyanyari, wananchi wanateseka sana wamefukuzwa kwenye makazi yao kwa lengo la Serikali eti kupisha hifadhi. Wananchi hawa toka wamefukuzwa wanahangaika sana hadi sasa hawana makazi maalum ya kuishi na hawana matumaini ya maisha yao, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha inawapa makazi ya kuishi wananchi hawa pamoja na mashamba (maeneo) kwa sababu maeneo waliyofukuzwa ndiyo yaliyokuwa yanawasaidia kwa makazi pamoja na mashamba lakini kwa sasa hawana sehemu ya kulima na wananchi hawa walitegemea sana kilimo ili kuinua kipato cha maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwaondoa kwenye maeneo yao kumewaathiri sana wananchi wa Kata ya Kyanyari wanateseka na kutia huruma. Napende kuishauri Serikali iwe inawatengea maeneo mbadala kabla ya kuwahamisha wananchi kwa lengo la kupisha hifadhi tofauti na sasa kuwahamisha wananchi bila kuwatengea maeneo kwani wanapowaondoa bila kuwatengea maeneo wanategemea wananchi hao watakwenda wapi? Pia Halmashauri husika ihakikishe inasimamia na kutetea haki ya wananchi wake katika maeneo husika.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niane na sekta ya uvuvi.

Katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018 kuhusu rasilimali za uvuvi, Serikali ilitenga shilingi bilioni 2.2, na shilingi milioni 400 tu kama fedha za ndani kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya uvuvi pekee. Fedha hii ni ndogo sana ukilinganisha na matokeo tunayoyatarajia katika sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli usiopingika kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inataka kuwekeza kidogo huku ikitarajia matokeo makubwa sana. Sekta ya uvuvi ni sekta nyeti ambayo inachangia katika uchumi wa Taifa na pato la mtu mmoja mmoja katika maeneo mengi ya nchi yaliyozungukwa na maji. Jambo la kushangaza jamii za wavuvi zimekuwa ni jamii zinazoishi maisha duni sana pamoja na ugumu na changamoto nyingi wanazopitia wavuvi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa zana bora na za kisasa katika kufanya uvuvi wenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wamekuwa wakitozwa kodi nyingi huku miundombinu ikibaki vilevile. Wavuvi wa Tanzania hususani wa Mkoa wa Mara wamekuwa wakinyanyasika kwenye kulipa tozo nyingi, hawana uhakika wa mikopo na pia usalama wa kutosha wawapo katika shughuli zao usiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Norway imekua sana kiuchumi kwa kuwekeza katika sekta ya uvuvi pekee. Leo hii katika nchi za Ulaya, Norway ni nchi inayoongoza kwa kuwa na GDP kubwa ambapo sehemu kuwa ya Pato la Taifa hutokana na uvuvi tofauti na hapa nchini ambapo jamii ya wavuvi ndio jamii maskini wa kutupwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usafiri wa anga, uwanja wa ndege wa Musoma, katika mpango huu wa maendeleo 2017/2018 hakuna mahali panapoonesha mkakati maalum wa ukarabati wa uwanja wa ndege wa Musoma. Ni dhahiri uwanja huu ni muhimu sana katika kukuza sekta ya utalii kwa Kanda ya Serengeti. Uwanja wa Ndege wa Musoma ni wa muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sababu za kiuchumi uwanja wa ndege wa Musoma ni muhimu katika historia ya ukombozi wa nchi yetu. Uwanja huu umebeba historia ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hivyo ni muhimu kwa wageni wanaokuja nchini
kutembelea makazi ya Hayati Baba wa Taifa ambaye aliipigania ukombozi wa nchi hii kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni vema sasa Serikali ione umuhimu wa kuuweka uwanja huu katika vipaumbele vyake ikiwa ni pamoja na kuutengea fedha za kutosha na kukamilisha ukarabati kwa wakati kama vile ilivyofanya kwenye uwanja wa ndege wa Chato. Pamoja na hilo, uwanja huu utakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwani hata shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika Mkoani Mara zitaimarika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naamini Mkoa wa Mara una wasafiri au watumiaji wengi wa ndege wanaofanya biashra katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ikiwemo nchi jirani ya Kenya. Hivyo Serikali itueleze ni lini itakamilisha uboreshaji wa uwanja huu ili wananchi hawa waweze kunufaika. Naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii nami nichangie kwa maandishi kuondolewa kwa vitabu vibovu mashuleni.



Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita wachangiaji walisisitiza juu ya ubovu au kutokuwa na usahihi wa vitabu vya kufundishia mashuleni hivyo iliamuliwa viondolewe mashuleni, lakini cha kushangaza vitabu vile bado vipo mashuleni na kusababisha kufifia (kufifisha) kwa elimu yetu hapa nchini. Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe inaviondoa vitabu hivyo mashuleni haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Mloganzila; Chuo cha kujifunzia na kufundishia Madaktari Bingwa Mloganzila kimejengwa (kilijengwa) kwa madhumuni ya kufundishia Madaktari kwa mujibu wa kanuni za Madaktari ulimwenguni ya kwamba kila Hospitali Kuu ni lazima iwe na Chuo Kikuu cha kufundishia na kujifunzia Madaktari. Mimi naishauri Serikali kwamba chuo hiki kibaki kuwa chuo cha kufundishia na kujifunza na siyo kuwa Hospitali kama inavyotaka kufanywa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa elimu; kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ubora wa elimu hasa kwa shule za Serikali na hii inatokana na Serikali yenyewe kutotilia mkazo maslahi na motisha kwa Walimu na uhaba wa vifaa vya kufundishia mashuleni pamoja na umbali wa makazi na umbali wa shule.


Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo shule binafsi zimeboresha na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi, lakini nashangaa na inasikitisha sana kwa Serikali kutoa matamko ya kuzuia kukaririsha wanafunzi na kusababisha mrundikano wa wanafunzi wanaofeli mashuleni. Ushauri wangu Serikali iachane na kuzuia kukaririsha kwa shule binafsi ili waweze kuwajengea uwezo wale wanaoweza kufanya vizuri badala yake waboreshe shule za Serikali ili ziweze kutoa wanafunzi walio bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iache kutoa adhabu kwa Walimu ambao shule zao zimefelisha badala yake Serikali ifanye utafiti ili kujua kwa nini wanafunzi wanafeli ndio itoe adhabu na siyo kutoa adhabu bila kufanya utafiti.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi nami kuchangia kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua fika kwamba maji ni uhai, 2016/2017, fedha za maendeleo zilikuwa shilingi bilioni 915.1 lakini hadi kufikia Machi, 2017, zilitolewa asilimia 17.8 tu na 2017/2018 fedha za maendeleo zilikuwa shilingi bilioni 408.6 lakini hadi kufikia Machi, 2018 zilitolewa asilimia 22 tu, maana tumeona pia hata kwenye kitabu cha Kamati imeelezea hivyo kwa fedha za maendeleo na asilimia 1.8 tu kwa fedha za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Taifa ya Maji Fungu Namba 05 zimeainishwa shilingi bilioni 5.6 tu na hadi kufikia Desemba, 2017 hakuna fedha za ndani zilizotoka, zilitoka fedha za nje tu ambazo ni asilimia 1.8. Kufikia mwaka 2018 Serikali na wadau wa maji walijenga vituo 125,086 vya maji vijijini ambavyo ilikuwa vihudumie watu milioni 30.9, sawa na asilimia 85.2 ambao ni wananchi milioni 36.3 waishio vijijini. Jambo la kusikitisha vituo vinavyofanya kazi kati ya hivyo vituo vyote ni vituo 86,877 tu ambavyo vinahudumia watu milioni 21.7 sawa na asilimia 59.8 ya watu waishio vijijini. Kwa hiyo kuna hasara ya vituo 38,209 havifanyi kazi, sawa na asilimia 30.5 ya vituo vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu cha Waziri sijaona mahali popote ambapo wameelezea namna ya kuvikarabati vituo hivyo au kuhakikisha vituo hivyo vinafanya kazi. Sasa tunasema kwamba tunahitaji kumtua mwanamke ndoo kichwani, kwa hali hii ukiangalia kweli mwanamke wa kijijini tutamtua ndoo kichwani? Ndivyo wanavyoishi watu wengi vijijini, sisi tuko mijini maji yakikatika kidogo tu tunaanza kulalamika, je, wale akina mama wanaoamka saa kumi alfajiri kwenda kufuatilia maji? Haya, ameamka saa kumi alfajiri, kurudi saa sita mchaa! huyu mwanamke ataleta maendeleo kwenye familia kweli? Tunahitaji watu wa vijijini wawe na maendeleo, walete maendeleo, kwa hali hii anahangaikia maji muda wote maendeleo atayafanya saa ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishauri Serikali, hasa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango atueleze fedha zinazoidhinishwa za mwaka jana kwanza zilienda wapi? Zinavyoidhinishwa ihakikishwe fedha zote ziende kwa wakati ili miradi ifanye kazi kama inavyokusudiwa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, mimi ni mwanamke, nawaonea huruma sana wanawake wenzangu wa vijijini. Tunaomba tafadhali sana, tunajua pale Mheshimiwa Waziri wa Maji hakikisha unaongea na Waziri wa Fedha unapata pesa kwa wakati ile miradi ifanye kazi vijijini. Kwa mfano, Mkoa wangu wa Mara tumezungukwa na Ziwa Victoria mwaka jana niliongea hapa, tumezungukwa na Ziwa Victoria, lakini fikiria Serikali inaweza kutoa maji Ziwa Victoria inapeleka maji Shinyanga, lakini sisi wa Mkoa wa Mara hatuna maji, inasikitisha!(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tafadhali sana hakikisheni Mkoa wa Mara tunapata maji hasa Bunda hatuna maji ya kutosha, Musoma Vijijini hatuna maji ya kutosha. Pale Musoma tu tupo lakini hatuna maji ya kutosha, Tarime ni sehemu ya mjini tu, sehemu za vijijini watu hatuna maji ya kutosha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuchangia kwa maandishi. Nipende kusema ya kwamba sekta ya uvuvi ni rasilimali ya kujivunia sana hapa nchini kwetu na nchi yetu isingekuwa ya umaskini na kutegemea misaada kutoka nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, naongea haya kwa uchungu sana jinsi wavuvi wanavyonyanyasika kwenye nchi yao kwa kuchomewa nyavu zao eti hazina ubora wa kuvulia, huu ni uonevu wa hali ya juu sana, otherwise Serikali itoe nyavu mbadala zinazoruhusiwa na Serikali na si kuwakamatia wavuvi na nyavu zao na kusema hazina ubora.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali iache kutumia nguvu ya dola (vyombo vya dola) kuwanyanyasa wavuvi hasa wa Mkoa wa Mara. Ukatili unaofanywa na vyombo vya dola kwa wavuvi si sahihi kabisa.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ilete nyavu zinazotakiwa kwa wavuvi wa maeneo yote na si kuwanyang’anya nyavu zao na kuzichoma halafu mnawaacha hewani.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mifugo; ukatili wa wanyama kuwekwa chapa kwenye ngozi njia inayotumiwa na Serikali si sahihi kabisa kwani ng’ombe huugua na kupata maumivu makali sana, huu ni ukatili wa hali ya juu. Haki za wanyama ziko wapi? Ubora wa ngozi unapotea, utaiuza wapi ngozi yenye alama kubwa?

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali itafute njia mbadala badala ya kuwachoma na chuma cha moto ni vema wangewavalisha ring ambazo zinakua na alama au wawekwe alama kwenye masikio na si kwa kuwachoma alama kubwa hadi kusababishia maumivu kwa ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, hii tabia ya kutaka kupata leseni ya biashara ya ng’ombe eti lazima ujisajili Bodi ya TMB kwa shilingi 102,000 then unakata leseni ya export shilingi 2,500,000 na kila ukisafirisha mifugo ulipe shilingi 2,500 kwa kila ng’ombe mmoja (movement permit) then unalipa shilingi 5,000 kwa kila ng’ombe market fee bado shilingi 3,000 kwa kila ng’ombe kama kodi ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, nipende kuishauri Serikali ipunguze kodi kwa wafugaji wa maeneo yote. Nakumbuka mwaka jana baadhi ya maeneo kodi ilipunguzwa/kufutwa isipokuwa kwa mifugo tu. Ifikie mahali tumsaidie huyu mfugaji na siyo kumkandamiza.

Mheshimiwa Spika, Serikali itoe mwongozo nini mfanyabiashara wa ng’ombe anapaswa kuwa navyo ili kukidhi sifa za kusafirisha na kuuza ng’ombe ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na siungi mkono hoja ya hotuba ya uvuvi na mifugo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami namshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Wizara hii ya Kilimo kusema ukweli ni ndogo sana. Ukiangalia nchi yetu ni ya wakulima na wafanyakazi na haya makundi mawili asilimia 80 ni wakulima lakini bajeti inayotengwa hapa ni asilimia 4.8. Kusema ukweli hii asilimia haikidhi kabisa mahitaji ya wakulima hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea pia ni janga la kitaifa. Mbolea bei yake ni kubwa sana ukilinganisha na hali halisi ya wakulima wetu hapa nchini. Cha kushangaza mbolea hii hii haifiki kwa wakati. Kwa mfano, mkulima analima mazao yakishaota mbolea ya kupandia ndiyo inakuja, wakati tayari mkulima ameshalima mazao yake. Inapofika kipindi cha mkulima kuvuna mazao, mbolea ya kukuzia ndiyo inafika. Kwa hiyo, niishauri Serikali kwamba mawakala wawe wa maeneo yaleyale husika kwa sababu kama kijiji fulani kinajulikana kabisa, kama mkisema chagua wakala wao wenyewe wanajuana, kwa nini wasifanye utaratibu huu kuliko kuweka wale mawakala wanaochaguliwa na Serikali? Kusema ukweli hawa mawakala hawafanyi kazi bali ni wachakachuaji tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tuna upungufu wa mafuta hapa nchini. Kusema ukweli ni jambo la kushangaza na ni aibu kwa nchi yetu. Ukiangalia tuna wakulima wanaolima ufuta na alizeti, kwa nini tusiweke kipaumbele kwa wakulima hawa ili tuweze kuzalisha mafuta ya kutosha katika nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mazao kama mahindi mengi hufikia wakati huharibika, kwa nini tusitafute wataalam wakaweza kutengeneza mafuta ya mahindi? Hakuna mafuta mazuri sana kama mafuta ya mahindi na yanashindana na mafuta ya olive oil. Wewe mwenyewe unajua kabisa jinsi olive oil ilivyo ya bei ghali na mafuta ya mahindi ni hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaangalia viwanda vingi vinategemea sana kilimo. Kwa mfano, katika Mkoa wangu wa Mara Kiwanda cha MUTEX kilikuwa kinazalisha nguo zenye quality nzuri sana. Hata hivyo, sasa hivi wakulima wa Mkoa wa Mara hawalimi tena pamba kwani imekuwa ni janga la kitaifa kwa sababu mkulima atalima ataenda kuiuza wapi? Tuangalie namna ya kumfufua mkulima wa zao la pamba kwa sababu hivyo viwanda tunavyosema Tanzania ya viwanda tunategemea tutauza vitu gani katika hivyo viwanda au tutangeneza kitu gani katika viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tujitahidi sana kuwasaidia wakulima wetu katika nchi yetu kwa sababu tunategemea sana kilimo. Kama kweli tunategemea kilimo na kilimo kinatusaidia na tunavyoangalia kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo na asilimia kubwa kati yetu tumesomeshwa kutokana na kilimo walichofanya wazazi wetu sasa iweje leo hii tumdharau mkulima? Naomba tuweke kipaumbele kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni upatikanaji wa mikopo. Kusema ukweli tumemminya sana mkulima kwenye hili suala la mikopo. Tunatoa asilimia 2 tu unategemea mkulima itamsaidia kwa kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hizi benki naomba zifike vijijini. Benki hizi mara nyingi ziko mijini, wakulima vijijini mnategemea kwamba auze mazao yake apate nauli, aende kukopa kule mjini kwa kutumia mazao hayo hayo, kusema ukweli ni kuwatesa hawa wakulima. Kwa kweli naomba tuamshe akili zetu, Mheshimiwa Waziri naomba mnisikilize, tuamshe akili zetu tuwaone na tuweke kipaumbele kwa wakulima, tuwasaidie wakulima hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao hasa ya mahindi katika Mkoa wa Mara, kwa kweli limekuwa ni tatizo kubwa sana. Sasa hivi wakulima wengi wanalima mahindi kwa ajili ya chakula tu.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi hii na mimi niweze kuchangia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, nitaanza na ukamataji hovyo wa wauza mikaa. Naomba utambue kuwa mkaa ni kimbilio la wananchi kwa 95% mfano mwananchi wa Kaburabura, Bugoji, Salagana, Kangetutya umwambie atumie gesi ni kichekesho cha hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, kwanza vile usafirishaji wa gesi kutoka Mjini Musoma hadi ifike kusambazwa kwa wananchi huko vijijini ambako bado wanaamini kupika kwa kutumia kuni na mkaa, leo hii wananchi hao wananyanyasika kutokana na upatikanaji wa kupatikana (upatikanaji wa kuni) kwa kuni na mkaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatakiwa iwasaidie wananchi wake na siyo kuwanyanyasa kwa sababu leo hii mtu akikamatwa hata na gunia moja la mkaa ni shida na linaweza kumfunga. Serikali inazuia ukataji miti hovyo sasa kama mnawazuia wananchi hata kupata kuni mnategemea mwananchi wa kijijini atapika kwa kutumia nini? Kwani wale watendaji wenu wananyanyasa wananchi kule vijijini kwani hata mwananchi akikamatwa na mzigo wa kuni au gogo lililoanguka lenyewe anashtakiwa na viongozi wa eneo husika eti kwa nini hajachukua kibali.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali irekebishe kanuni zinazosimamia matumizi ya nishati ya mkaa kwani wananchi wengi wa vijijini hawajapata nishati mbadala ya kutumia kuni na mkaa.

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Msitu wa Kyanyari uko chini ya TFS, mpaka sasa katika Kijiji cha Nyamikoma, Mwibagi Kata ya Kyanyari, Butiama kuna wananchi walifukuzwa ili kupisha eneo la msitu lakini toka walivyofukuzwa hadi leo wananchi hao bado wananyanyasika kwani hawana makazi maalum na mashamba.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kyanyari wanateseka sana kwa kukosa maeneo ya kulima, niishauri Serikali kabla ya kufanya uhamisho kwa wananchi ili wapishe hifadhi ni vizuri iwaandalie maeneo kabla ya kuwahamisha ili wananchi wanapofurushwa wawe na eneo la kuweka makazi ya kudumu ya uhakika na sehemu ya mashamba ambapo wananchi watakuwa na uhakika wa kulima na kupata mazao ya chakula na biashara ili kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya elimu haiendani na uhalisia wa elimu yetu ya Tanzania kwa ilivyo sasa. Kwa hiyo naishauri Serikali ilichukue umuhimu wa mabadiliko ya sera ya elimu tuliyonayo hivi sasa ili tuboreshe elimu yetu ya Tanzania kama ilivyokusudiwa mfano, mitaala yetu inaelekeza wanafunzi kukaririshwa na siyo kuelewa na baada ya kuhitimu anafikiria kuajiriwa na si kuendelea na masomo ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya Walimu yaboreshwe; kama tunahitaji kuboresha elimu yetu ya Tanzania ni lazima maslahi ya Walimu yaboreshwe kwa kuwa ndio wadau wakuu na muhimu wa elimu kwani suala hili ni muhimu sana kwa kuwaletea morari Walimu wetu na pia Walimu hawa wataachana na mawazo ya tuition au kuuza karanga kwa ufupi kuwaza kufanya biashara ndogo ndogo ili kujiongezea kipato cha familia na kusabisha kutofundisha wanafunzi vizuri. Kwa hiyo, naishauri Serikali izingatie jambo hili la kuhusu maslahi ya Walimu kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo ibadilishe utaratibu wa michepuko bila kuangalia aina za masomo aliyofaulu bali waangalie alama ambazo mtu (mwanafunzi) amefaulu bila kubagua aina za masomo, kwa mfano, kwa sasa kipaumbele cha Bodi ni kwa wale wanaosoma masomo ya sayansi, ndio wanapewa kipaumbele kulingalisha na wanafunzi wanaosoma michepuo mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuboresha elimu ya Tanzania bila kuboresha kitengo hiki cha Ofisi ya Ukaguzi kukitengea fedha za kutosha kama vile usafiri ili waweze kuyafikia maeneo yote yanayotakiwa kukaguliwa kwa mujibu wa sheria kwa haraka na hii itarahisisha kufikia maeneo yasiyoweza kufikiwa kwa urahisi wakipata usafiri wa uhakika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nami nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, hasa kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti kwa miaka mitatu zimetengwa shilingi trilioni 13. Naitaka Serikali itueleze, tunapata ajira kiasi gani na return yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha nyingi za maendeleo kila siku tunaambiwa zinafanya upembuzi yakinifu. Maana toka nimekuwa Mbunge, sasa hivi ni mwaka wa nne, kila ukiuliza swali unaambiwa ni upembuzi yakinifu, sasa sijui huo upembuzi yakinifu utaisha lini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Sasa hivi Wilaya ya Rorya, TARURA haijapata fedha za maendeleo ya barabara takribani miaka miwili mfululizo na ukiangalia Wizara hii imetengewa pesa nyingi sana. Naomba tafadhali Mheshimiwa Waziri asikilize kilio cha wananchi wa Mkoa wa Mara apeleke fedha zikamalize ujenzi wa barabara ambazo zinatakiwa kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Musoma – Busekela ina kilometa 42, lakini fedha zilizopelekwa ni za kilometa tano tu, kilometa 37 bado hazijajengwa. Sasa sijui Mheshimiwa Waziri atatuambia ni lini zile kilometa 37 zitaenda kumalizwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Wanyele – Kitario imekatika na kila siku nimekuwa nikiizungumzia hapa kwenye maswali; na majibu yamekuwa ni yale yale ya marudio. Ile barabara ya Wanyele – Kitario ni barabara ambayo inahitaji kuwekwa daraja na ilishasababisha maafa. Kuna takribani watoto 20 walishafariki na nilishasema katika hili Bunge lako tukufu, lakini mpaka sasa hakuna hatua yoyote ambayo imeshachukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tafadhali, hizi mvua zinazonyesha, wasije tena watoto wengine wakaendelea kufa tukaendelea kupata maafa katika Mkoa wetu wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi viporo mingi tu. Kwa mfano, Bunda – Kisoria, Makutano – Sanzate, Mugumu – Tabora B, zinahitajika fedha kuweza kukamilisha miradi hii viporo. Mpaka leo hii hakuna pesa yoyote ambayo imeshapelekwa na barabara zile zimekaa tu, hatuelewi hatma ya hizi barabara. Tunaomba Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa kwenda kumalizia miradi hii viporo iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilivile kuna round about Tarime. Ile round about ya Tarime Mjini mara nyingi imekuwa ikisababisha madhara. Imesababisha ajali nyingi sana. Naishauri tu Serikali ihakikishe eneo lile inaweka angalau zile taa za kuongoza wale watu wa magari, hata wale waenda kwa miguu. Kwa mfano, kama ile barabara ya pale Mwenge kwenda Mjini, Mwenge kwenda Mikocheni, Mwenge kwenda Kawe, Mwenge Kwenda Ubungo, ni taa ambazo zinaongoza vizuri sana. Naishauri sana Serikali ione umuhimu kwa sababu ile keep left pale ni ndogo na eneo lile ni dogo sana. Naomba na kuishauri Serikali ituwekee taa eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda Uwanja wa Ndege wa Musoma, ule uwanja ni mdogo. Sasa hivi wanataka kuutanua ule uwanja uwe mkubwa, lakini kuna wale watu ambao wamezunguka lile eneo la Uwanja wa Musoma na wale watu walishawekewa X toka mwaka na miezi mitano mmoja sasa hivi. Wale watu walishafanyiwa tathmini, lakini watu waliofanya tathmini walifanya bila kuwashirikisha wananchi husika. Mpaka sasa wale wananchi hawajui hatma yao kwa sababu wanatembea tu hati, hawawezi kwenda benki kukopesheka wala kufanya kitu chochote cha maendeleo yoyote katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na kuishauri Serikali wakarudie kufanya tathmini kwa kushirikiana na wananchi wa eneo husika ili mtu anapofanyiwa tathmini ajue nyumba yake inafanywa tathmini kwa kiasi gani? Kwa sababu mnapofanya tathmini tu na kuondoka bila kumwambia mhusika kwamba tathmini tumefanya nyumba yako ina thamani ya kiasi fulani kwa kweli inasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda upande wa TBA. Kwa kweli TBA hawafanyiwi ushindani na makampuni binafsi, ndiyo maana kazi zao zimekuwa ni substandard. Matokeo mengi tunaona kazi nyingi za Serikali zinafanywa na TBA na kazi zao nyingi zimekuwa za kiwango cha chini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naongea hivyo kwa sababu gani? Kuna zile nyumba za mradi wa Bunju. Ule mradi, yaani kwa ushauri wangu mdogo tu, sana sana wangeanza kuweka social services kwa kuanza kuweka zahanati, wakaweka shule, wakaweka barabara nzuri ili mtu anapokwenda kule kwa sababu zile nyumba ziko pembezoni sana, angalau hata ziwe ni nyumba za kufikika kwa urahisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, zile nyumba malengo ilikuwa ni kwa ajili ya wafanyakazi na wafanyakazi wengi wamehamishiwa Dodoma, kwa maana hiyo zile nyumba zinakaa tu hazina wapangaji. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania wote kwa ujumla. Tunaona bajeti kwa miaka mitatu zimetengwa shilingi trilioni 13, nataka Serikali itueleze tunapata ajira kiasi gani na return yake ni nini? Fedha nyingi zinaenda kwenye upembuzi yakinifu, sijui huu upembuzi yakinifu utaisha lini ili ujenzi kamili uweze kuanza kwa sababu Wilaya ya Rorya, TARURA haijapata fedha za maendeleo ya barabara kwa miaka miwili mfululizo sasa.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Musoma – Busekela ni ya kilometa 42, lakini fedha zilizotolewa ni kilometa tano tu, bado kilometa 37. Zitaishaje bila fedha? Naishauri Serikali ipeleke fedha za kumalizia hizo kilometa 37 zilizobakia.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Wanyere – Kitaryo imekatika, hakuna mawasiliano sababu ya daraja. Kwa sababu Wizara hii imetengewa fedha nyingi, naishauri Serikali ifanye jitihada za haraka kuhakikisha inatengeneza barabara hii na daraja ambalo limeshaua watoto zaidi ya 20 ili kunusuru maafa mengine yasitokee.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara una miradi viporo vingi sana kama vile Bunda – Kisorya, Makutano – Sanzate, Mugumu – Tabora B zinazohitajika fedha ili kuweza kukamilisha miradi hii viporo.

Mheshimiwa Spika, kuna round about ya Tarime inasababisha ajali za mara kwa mara. Naishauri Serikali iondoe hiyo round about badala yake ziwekwe taa za kuongozea kama vile Barabara ya Mwenge kwenda Mikocheni, Kawe, Mjini, Ubungo ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara una uwanja wa ndege ambao unapanuliwa (unaongezwa), kitu ambacho kinaathiri wananchi wanaozunguka (waliopakana) na uwanja huo kwani wananchi hawa walishafanyiwa tathmini takribani mwaka na miezi minne, lakini wananchi hawa hadi sasa hawajui hatma yao kwani tathmini imefanyika bila wao kujua nyumba zao zimefanyiwa tathmini ya shilingi ngapi.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ikarudie kufanya tathmini na suala hili liwe shirikishi kwa wananchi wenyewe na Serikali iwatengee (iwape) eneo lingine la kwenda kujenga nyumba nyingine pale ambapo watakuwa wameshalipwa fedha za kupisha uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Spika, TBA hawafanyiwi ushindani na makampuni binafsi ndiyo maana kazi za TBA ni substandard (kazi nyingi za Serikali zinafanywa na TBA matokeo yake majengo mengi hayakidhi viwango). Mfano mradi wa nyumba Bunju zinazojengwa na TBA haziko competitive hata kidogo kwani haziwezi kuingia kwenye ushindani kwa vile hazina viwango. Kwanza hazina (hakuna) social services kama vile zahanati, shule, barabara na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nyumba hizi hazinunuliwi? Ni kwa sababu bei iko juu sana kulinganisha na ubora wa nyumba zenyewe, kwani hadi sasa nyumba zilizonunuliwa ni chache sana, nyingi hazijanunuliwa, zimekaa tu na kuendelea kuharibika. Naishauri Serikali, hizi nyumba zipangishwe badala ya zinavyokaa zenyewe bila watu.

Mheshimiwa Spika, lingine katika Sekta ya Ujenzi; kati ya wakandarasi Watanzania asilimia 80, ni wakandarasi asilimia 20 tu ndiyo wanaopata kazi. Ni aibu kwa nchi yetu ya Tanzania. Ushauri wangu ni kwamba Serikali itoe ujuzi kwa Wakandarasi wetu ili tuweze kuwatumia kuokoa pesa zinazokwenda nje.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nami kwa kupata nafasi hii niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kuipongeza Kamati na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC ni Mujumbe wa PAC. Nitaongelea suala la TBA (Wakala wa Majengo Tanzania).

Mheshimiwa Naibu Spika, TBA ilipewa jukumu la ujenzi wa majengo kujenga Taasisi mbalimbali za Serikali nchini Tanzania na mkataba wenye gharama ya shilingi bilioni 24,068,482,278. Pesa hii ni ndogo sana ukilinganisha na mradi wenyewe jinsi ulivyo na kutokana na uhaba wa pesa iliyotolewa wkamba ni ndogo tunaona miradi mingi ya TBA inasuasua. Mapungufu yamekuwa mengi sana. Kutokana na hilo pia hata bill of quantity haikufuatwa. Kwa hiyo, kama haikufuatwa BOQ kumefanya gharama za mradi kutojulikana hadi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya serikali kutoa bilioni 24 tunaona kabisa ni jinsi gani miradi hii inayosimamiwa na TBA haifanyikazi kwa ukamilifu kwa sababu unakuta msimamizi mmoja wa mradi ana miradi miwili. Aende huku akasimamie mradi, atoke huku aende akasimamie mradi huu kwa hiyo unakuta mradi huu mwingine ambao anakuwa ameuacha unakua umesimama anaporudi kwenye huu mradi mwingine na huu nao unasimama. Na pia inabidi achukue vifaa hivi anavyotumia kujengea kwenye mradi huu mwingine, mradi (a) aende akachukue tena akajengee kwenye mradi (b) kwahiyo tunakuta kuna upungugfu mkubwa sana wa ufanisi wa kumaliza miradi kwa ufasaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; jengo la Makao Makuu ya Tume hapa Dodoma, TBA ilikuwa inafanyakazi pale kujenga lile jengo matokeo yake wameshindwa na baada ya kuona kwamba lile jengo halitaisha kwa wakati ikabidi sasa wachukuliwe SUMA JKT kwenda kumalizia ule mradi pale na hadi sasa SUMA JKT ndiyo bado inaendelea kujenga ule mradi ambao ulikuwa unasimamiwa na TBA.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaenda pia upande wa NHC; upande wa NHC miradi mingi nayo imetelekezwa yaani haieleweki kwamba hii miradi itakwisha au laa! Mfano; mradi ule wa Kawe 711; ule mradi una thamani ya shilingi bilioni 142. Bilioni 142 ni pesa nyingi sana lakini cha ajabu mradi unatelekezwa. Pesa ambayo imetolewa haijafanyakazi yoyote. Kwa kweli inakuwa ni kitu ambacho kinailetea hasara Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi wa CAG ulibaini pia ongezeko la gharama la shilingi bilioni 6.86 pesa ambayo haikutolewa maelezo yoyote hadi leo hii. Tunaomba tuelezwe kinagaubaga pia tuelewe kama Kamati hii bilioni 6.86 imetoka wapi na kwa sababu haikutolewa maelezo yoyote kwa hiyo hatujui mpaka sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba; iwe inatoa pesa kwa wakati. Itakapokuwa inatoa pesa kwa wakati, majengo yale yatakamilika kwa wakati na value for money itaonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru kwa kupata nafasi hii. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii nami niweze kuchangia Hotuba ya Bajeti. Kwa mtazamo wangu bajeti hii siyo Gender Responsive Budget bali ni bajeti ambayo inamkandamizi mwanamke. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu Serikali imerudisha ushuru kwa upande wa taulo za kike (Pedi). Hii ni kumfanya mwanamke huyu ambaye suala hili la hedhi ni la kimaumbile na lazimishi, kwa nini nitozwe kwa sababu hii ya kupata hedhi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuishauri Serikali iweke ruzuku na bei elekezi kwa wafanyabiashara wa pedi kwani bila kufanya hivi wafanyabiashara hawa kila mtu ajipangie bei yake itakuwa shida kwani pakiti moja ya pedi inauzwa Sh.1,500/=, ukiongeza hili ongezeko la thamani ambalo ni Sh.1,646.7 ambayo ni 1,647 x 18% ya VAT/100 = 296.406 or 297.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo 1,500 + 297 = 1,797 kwa kila pedi moja ya bei ya chini ambayo ni 1,500/=. Hii ni bei ya zamani tukiongeza ongezeko la thamani ya sasa pedi moja itauzwa kwa bei ya Sh.1,797.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za maendeleo, kilimo ni uti wa mgongo kwa nchi yetu. Zaidi ya 75% ya Watanzania ni wakulima na katika hiyo 75% wanawake ndio wanaojihusisha na kilimo lakini cha kushangaza fedha za maendeleo tunazotenga kila mwaka kwa mwaka 2018/2019 zimetengwa shilingi bilioni 98, hii ni aibu kwa nchi na Taifa kwa ujumla ukichukulia hii ni awamu ya Serikali ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hii ya kumkandamizi mkulima huyu kwani fedha zilizopelekwa ni 0.143% 41 bilioni, kwa kiwango hiki wanategemea watapata wapi malighafi wakati unaikandamiza sekta hii na badala yake wanawekeza kwenye vitu mfano, barabara, ndege, Stiegler’s George, tunaona ni kwa jinsi gani wanachukua hadi fedha za ziada za kwenye Kilimo, Afya, Elimu naomba itambulike kuwa watu ni kilimo, watu ni afya, watu ni elimu, watu ni maji. Mfano mzuri ni wa Abraham Lincoln alisema if you think education is expensive try ignorant kwa maana kama unafikiri elimu ni gharama jaribu ujinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii imekuwa haiwekezi kwenye elimu ndio maana tunapata changamoto nyingi kwani hakuna wabobezi wa kutatua changamoto hizi. Nipende kuishauri Serikali tuwekeze kwenye elimu ya kilimo bora chenye tija pia tuwekeze kuwatafutia wakulima masoko yenye uhakika na bei ya kutomkandamizi mkulima ili mkulima huyu afurahie kazi yake ya ukulima.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii. Nitachangia upande wa Sheria ya Ardhi, kipengele cha tisa kifungu cha 120A(3)(a)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona ni jinsi gani hii Sheria ya Ardhi ilivyowekwa, kwamba mtu anapokopa ni ndani ya miezi sita ripoti inatakiwa ipelekwe, kwa kweli muda ni mdogo sana. Tupo hapa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, kuwainua kiuchumi na kuwalinda, kuhakikisha wanapata haki zao sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba yawekwe mazingira mazuri kwa namna ya kuweza kumsaidia huyu mwananchi anayekopa kwa njia hii ya ardhi. Tukiangalia muda uliowekwa wa miezi sita ni muda mdogo sana, at least ungewekwa hata mwaka mmoja, tena hapo ni at least, hata huo mwaka mmoja bado tunaona kwamba pengine muda utakuwa bado hautoshi. Ukiangalia jinsi changamoto zilivyo nyingi, miezi sita haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia mtu hata kama ni mfanyabiashara amechukua mkopo, ndani ya mwaka mmoja ndiyo anaanza kuona faida. Kwa hiyo, hiyo miezi sita bado itakuwa ni midogo sana kwa kumwezesha mtu huyu kuweza kulipa ndani ya hii miezi sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria hii inamkandamiza mtu ambaye anakaa kijijini; watu wengi wanaokaa vijijini wana hatimiliki za kimila. Tayari hapa kwenye hiki kitabu cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kinaeleza kabisa kwamba mtu akiwa na hatimiliki ya kimila haruhusiwi kupata mkopo huu. Sasa hapa tunaona kabisa namna gani hii sheria inavyomkandamiza mwananchi au inabagua, yaani kuna watu wa vijijini ambao hawataruhusiwa kuchukua mkopo na watu wa mjini ambao wanaruhusiwa kuchukua huu mkopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuiangalie kwa umakini kwenye hiki kipengele cha 9 (3) Tutakaporekebisha vizuri kipengele hiki tutaweza kumsaidia mwananchi, maana lengo letu ni kumsadia mwananchi na sio kumkandamiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.